Sehemu Ya Tatu (3)
Kule chooni Jaka alifunga zipu ya suruali yake na kugeuka huku akichomekea vizuri suruali akiwa katika hatua ya kutoka pale chooni baada ya kujisaidia.
Hakupiga hatua nyingine zaidi.
Muddy na Alphonce Ng’ase walikuwa wamesimama huku wakimtazama, na mara moja alijua kuwa balaa lilikuwa limemfika, kwani alimkuwa wazi kuwa wale jamaa walikuwa wamemsimamia namna ile kwa nia moja tu, nayo si kumsalimia.
Huku moyo ukimwenda kasi na akili yake ikifanya kazi ya ziada kujaribu kutafuta namna ya kujikwamua, alitupa jicho kulia kwake na hakuona chochote cha kumsaidia. Akatupa jicho kushoto nako akakuta hali ni hiyo hiyo. Aliona ajabu kwa nini walikuwa peke yao mle chooni ambapo kwa kawaida vyoo vya kumbi za starehe huwa haipiti dakika tano bila kuwa na mtu au watu wakijisaidia.
Aliinua macho yake na kuchungulia juu ya mabega ya wale jamaa na kugundua kuwa wale jamaa walikuwa wameufunga mlango ule kwa ndani ili kuhakikisha kuwa Jaka hafanikiwi kutoka mle chooni kabla hawajatimiza azma yao mbaya.
“Oi! Vipi tena tough guy, umeshituka kutuona rafiki zako wapenzi?” Muddy alimuuliza kwa kejeli huku akimsogelea. Jaka alipiga hatua mbele kuuwahi mlango huku akiwapisha wale jamaa.
“Samahani, naomba kupita...”
Alphonce Ng’ase alimdaka koo huku akimkemea kwa ukali.
“Sisi tunaongea na wewe halafu unajidai huelewi sio? Pumbavu!”
Hapo hapo Muddy akamtandika teke kali sana la mbavu, naye akahisi maumivu makali, mguno wa uchungu ukimtoka pasi kupenda. Aliinua mikono yake akijaribu kuuondoa mkono wa Alphonce uliomkaba koo, lakini Alphonce alimwachia koo haraka kabla Jaka hajamgusa na hapo hapo akamshindilia ngumi tatu za haraka haraka, mbili kwenye chembe, na moja ikimpata kwenye taya.
Jaka alilia kwa kipigo kile huku akipepesuka. Muddy aliruka na kumbabatiza teke la kifua lililomsukuma hadi ukutani, ambapo alipigiza mgongo na kisogo chake vibaya sana. Alihisi mlipuko wa kiza ukipita machoni mwake na miguu ikamuwia mizito. Alijitahidi kujizatiti kimakabiliano, lakini maumivu makali kutokea kisogoni kwake yalim[oteza kabisa muelekeo. Na kama hilo halikutosha, wale jamaa waliokuwa wamedhamiria kutompa kabisa nafasi ya kujitetea kimakabiliano walimvurumishia mvua ya mapigo bila ya huruma akiwa amebabatizwa pale ukutani, huku wakimiminiwa matusi kem kem. Nguvu zilimwishia Jaka, na huku akihisi kizunguzungu alidondokea magoti pale msalani, na alikuwa anaelekea kuangukia uso pale sakafuni wakati Alphonce Ng’ase alipomdaka koo. Alibaki akitweta huku uzito wake wote ukiwa umeegemezwa kwenye mkono wa Alphonce Ng’ase aliyemdaka koo. Alijaribu kuuinua uso wake ili amtazame yule jamaa aliyemdaka koo lakini hakuweza kwani macho yake yalimuwia mazito sana.
“Hizo zilikuwa ni salamu kutoka kwa Joakim...na nyingine zitafuata, Pusi wee!” Alphonce alimkoromea, kisha akamwachia na Jaka akaanguka sakafuni kama mzigo. Hapo hapo Muddy alimtandika teke la mbavu lililotoa mguno hafifu kutoka kwa Jaka.
Wale jamaa walibaki wakimwangalia kwa dharau akiwa amelala pale sakafuni kabla ya kugeuka na kutoka nje kimya kimya, wakimwacha Jaka akigaagaa kwenye mikojo na damu pale sakafuni.
Jaka alijaribu kuinuka bila ya mafanikio. Maumivu makali yalimtambaa mwilini na alihisi fahamu zikimpotea upesi mno. Alijaribu kutambaa kuelekea mlangoni huku akitoa sauti za kuomba msaada lakini sauti ilikuwa imemkauka na nguvu zilizidi kumwishia. Hatimaye alidondosha kichwa chake juu ya mkono wake uliolala pale sakafuni kwa kukata tamaa na kubaki akiwa amelala kifudifudi pale chooni bila ya kujali harufu kali ya mikojo na damu nyingi iliyokuwa ikimtoka puani na mdomoni. Akili yake ilitawaliwa na jambo moja tu muda ule...Moze.
Alijua kuwa baada ya kumfanyia yale waliyomfanyia wale jamaa wangeenda kwa Moze...
Sijui watamfanya nini tu maskini Moze wangu huko…
Wazo hilo lilimpa nguvu. Alijikurupusha na kupiga goti moja pale sakafuni huku akihisi maumivu makali mwilini na kichwani. Alipojaribu kuinua mguu wa pili alishindwa na kuanguka tena sakafuni kwa kishindo huku akihisi kiza kikitanda mbele ya macho yake.
Fahamu zikampotea.
_____________________
Kule ukumbini Raymond Mloo aliangalia saa yake kwa mara nyingine tena na kuwageukia Moze na Rose waliokuwa pamoja naye pale mezani.
“Jamani, mbona Jaka amechelewa sana kutoka...” Kabla hajamaliza kauli yake aliwaona Alphonce Ng’ase na mshirika wake wakitokea sehemu za kule msalani kwa mwendo wa haraka hali wakiangaza huku na huko. Mara moja alihisi hatari kwani aliuelewa fika uhasama uliojitokeza baina ya Jaka na Joakim, na alijua kuwa Alphonce na Muddy walikuwa ni marafiki wakubwa wa Joakim.
“Ooooh, Shiiit!” Aliropoka na kutoka mbio kuelekea kule chooni.
Kwa sekunde kadhaa Moze na Rose walibaki wakiwa wamepigwa butwaa pale mezani pasina kuelewa kilichokuwa kinaendelea. Kisha Moze naye akakurupuka na kutoka mbio kumfuata Raymond huku akiita jina la Jaka kwa kelele. Na hata wakati anaendelea kufanya hivyo, alimuona Raymond akitokea sehemu za eneo la kujisaidia wanaume huku akiwa anamburura Jaka kwa taabu. Moyo ulimlipuka na alihisi miguu ikimwisha nguvu. Akasimama palepale alipokuwa, macho yakiwa yamemtumbuka.
Jaka alikuwa ametapakaa damu sehemu ya mbele ya shati lake na jicho lake moja lilikuwa limevimba vibaya.
“Brown...! Brown! Oh, Mungu wangu! Ni nini tena kimetokea sasa?” Alibwabwaja huku akipepesuka kuelekea kule alipokuwa wanatokea Raymond akiwa nusu amembeba, nusu anamkokota Jaka. Baadhi ya wanachuo, wahudhuriaji wengine na wahudumu waliokuwepo pale ukumbini nao walianza kuelekea kule alipokuwa akitokea Raymond kujaribu kutoa msaada na kutaka kujua kilichotokea.
“Gari! Tafuta gari upesi!” Raymond alifoka huku akiendelea kumburura Jaka.
Kufikia hapo Moze na Rose walikuwa wakilia kama wajinga. Muda mfupi baadaye walikuwa ndani ya teksi wakielekea kituo cha afya cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Waliamua kwenda huko kwa kuwa ndipo mahala pekee ambapo walijua kuwa Jaka angeweza kupata huduma bila maswali mengi wala kuhitajika kutoa pesa za matibabu, wakizingatia kuwa wote walikuwa ni wanafunzi wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu ya hospitali za nje ya chuo kikuu. Teksi ilikuwa inaendeshwa kwa mwendo wa kasi sana kuwarejesha chuoni, Raymond akiwa kiti cha mbele kando ya dereva hali Jaka akiwa amelazwa kwenye kiti cha nyuma akiwa amelaza kichwa chake kwenye mapaja ya Moze na miguu yake ikiwa kwenye mapaja ya Rose. Kutokea kwenye kile kiti cha nyuma, sauti za wale akina dada zilisikika zikilia taratibu.
Jaka alilazwa pale hospitali ya Chuo Kikuu kwa wiki mbili. Ndani ya wiki ya kwanza akiwa pale hospitali alikuwa akipoteza na kurudisha fahamu mara kwa mara kutokana na maumivu makali yaliyotokea kichwani na kwenye mbavu.
Mama yake alikwenda kumuona pale hospitali na alikuwa pamoja na Moze kando ya kitanda alicholazwa mwanaye kwa muda wote huo, ukiachilia mbali nyakati kadhaa ambazo Moze alilazimika kwenda darasani. Katika muda waliokuwa pamoja, Moze alipata fursa ya kumueleza mama Jaka mkasa wote mpaka ikafikia hatua ile.
Mama Jaka alizipokea habari zile kwa masikitiko makubwa.
“Lazima hao vijana wafunguliwe mashtaka Moze, lazima!” Mama Jaka alisema kwa hasira.
“Ni kweli…lakini patahitaji ushahidi mama, na kwa mujibu wa taarifa zilizopo, hakukuwa na mtu yeyote aliyeshuhudia wale vijana wakimpiga Jaka…Ray alimkuta akiwa amelala sakafuni kule msalani akiwa peka yake!”
“Si unasema aliwaona hao vijana rafiki zake Joakim sijui…wakitokea kule kule msalani? Ushahidi gani tena unahitajika hapo?”
“Aliwaona wakitokea usawa wa eneo la msalani, sio msalani kwenyewe!”
Mama Jaka aliuma meno kwa hasira.
“Kwani mwanangu alikutwa akiwa ameibiwa chochote huko msalani alikoachwa baada ya kipigo?” Aliuliza.
“Hapana mama…”
“Sa’ si unaona? Huwezi kusema kuwa hao waliompiga ni vibaka Moze…lazima hao watakuwa ni watu wenye kisasi au ugomvi naye tu! Sasa watu hao ni akina nani kama si hao akina Joakim? Hapa Jaka akipona tu ni kuwafungulia mashtaka…yote yakaelewekee huko huko!” Mama alikuja juu.
Moze alimtazama yule mama kwa muda.
“Sawa mama…lakini, mi’ nasomea sheria ujue. Na ingawa natal asana hawa jamaa wachukuliwe hatua…bado najua ni jinsi gani itakuwa vigumu kuwatia hatiani kwa kosa hili, japo mioyoni mwetu tunajua kuwa ni wao ndio waliohusika…!” Moze alimwambia mkwewe mtarajiwa.
“Tutapambana kisheria tu mwanangu! Hawa jamaa hawawezi kumfanya hivi mwanangu halafu tuwaangalie tu!” Mama Jaka aliazimia.
“Sawa mama. Basi tutakuwa pamoja katika hilo mwanzo mwisho. Nilitaka tu ujue hali halisi ili kupunguza kiwango cha kukatishwa tamaa pindi hitimisho la kesi hii litakapokuwa tofauti na matarajio yetu…” Moze alimalizia.
___________________
Taarifa za kipigo alichopokea Jaka zilimfurahisha sana Joakim. Alikuwa na uhakika kabisa kuwa baada ya kipigo kile, Jaka asingethubutu tena kumletea jeuri na kwamba mtoto Moze angemkubalia matakwa yake kwa kuhofia usalama wa mpenzi wake. Na ndio sababu alishindwa kuyaamini macho yake pale Moze alipofika chumbani kwake na kumwambia kuwa alikuwa ana maongezi na yeye.
Ilikuwa ni kiasi cha saa kumi na moja za jioni hivi, wiki moja tangu Jaka apate kile kipigo na Joakim alikuwa peke yake chumbani akijaribu kujisomea.
“Oh, Ka…karibu Moze...karibu...ingia tu mpaka ndani...” Joakim alimkaribisha Moze huku akianza kuisifu bahati yake. Moze alisimama kando ya mlango ndani ya chumba kile kidogo huku akimtazama kwa ghadhabu. Lile jicho la chuki alilokuwa akitupiwa na Moze lilimfanya agwaye kidogo na abaki akimkodolea macho ya viulizo yule binti.
Walitazamana kwa sekunde kadhaa bila ya yeyote kusema neno.
“Moze...vipi, naona leo umeamua kunitembelea, lakini nakuona kama...” Alianza kuongea, lakini hapo Moze akamkatisha.
“Joakim, kilichonileta hapa ni kitu kimoja tu, nacho ni kukujulisha kuwa iwapo unyama walioufanya rafiki zako kwa Jaka wangu unatokana na mimi kukataa kuwa kimada wako, basi mtu wa kupata adhabu ile alikuwa ni mimi na sio Jaka!”
Joakim alibaki mdomo wazi. Hakutarajia kuambiwa maneno kama yale.
“Ah, Moze…”
“Kitu ninachotaka wewe Joakim ukielewe ni kuwa mimi sikupendi na sitakupenda maisha yangu yote! Kwa hiyo huna utakalofanya ambalo litabadilisha msimamo wangu katika hilo na wala usijidanganye kuwa kuwatuma hao marafiki zako kufanya kitendo cha kijinga na cha kipumbavu kama kile kunaweza kubadilisha msimamo wangu na kunifanya nikubaliane nawe...na kama una mawazo hayo basi nakusikitikia sana Joakim kwani kwa hakika utakuwa ni mwenye kufilisika kibusara!” Maneno yale yalimchoma sana Joakim, lakini sio kama alivyochomwa na chuki ya wazi dhidi yake iliyo jidhihirisha usoni kwa yule mwanadada. Alibaki akimtazama Moze kwa mshangao na woga kwani Moze alikuwa kama mtu aliyepandwa na mashetani.
“Moze… Mimi sio...”
“Funga domo lako Joakim! Mimi sio mpumbavu hata kidogo na wala usijaribu kujidanganya kuwa wewe hukuhusika katika tukio lile...wewe ndio chanzo cha mambo yote haya na ndio maana na mimi nimekuja kwako ili nikupe yangu machache. Liwalo na liwe, mi’ niko tayari!”
“Nakubali Moze, lakini naomba uelewe kuwa mimi...”
“Nyamaza kimya Joakim nikueleze! Mi’ najua kuwa hata tukiwafungulia mashitaka hatutashinda hata kidogo, maana nyie ni watoto wa vigogo. Lakini huwezi kuushinda uthabiti wa moyo wangu na penzi lililomo ndani yake kwa Jaka! Kwa hiyo nimekuja kukueleza ukweli wa moyo wangu Joakim, nao ni kwamba mimi sikupendi! Sikupendi, sikupendi, sikupendi! Na wala sitaki kupendwa na wewe hata kidogo! Sasa kama wewe unadhani unanitaka sana kiasi cha kutaka kuniulia mpenzi wangu, basi leo ndio nimekuja ili unifanye hicho cha maana mno kwako hata utake kumuua mwenzako kwa ajili ya hicho ukitakacho kwangu! Lakini ujue kuwa mimi sikupendi na sitokupenda daima...tumeelewana?”
Heeeh!
Joakim aligwaya maradufu. Aliingiwa na woga wa ajabu kutokana na maneno ya yule binti na jinsi alivyoonesha chuki ya hali ya juu kwake.
“Haya mimi hapa sasa nimekuja! Fanya unalolitaka uniachie mpenzi wangu aishi!” Moze alimfokea kwa hasira huku akimkazia macho yaliyojaa hasira.
“Moze sikiliza...” Joakim aligwaya lakini Moze hakuwa na muda wa kusikiliza.
“Fanya basi, mbona maelezo mengi? We’ si kidume? Onesha basi huo udume wako!”
Tahayari ilimwingia Joakim na alijikuta akikaa kwenye kiti taratibu huku macho yake akiwa ameyainamisha chini.
“We’ si unanitaka sana? We’ si umezoea kila mwanamke unayemtaka ni lazima umpate? Sasa nimekuja ufanye hicho cha muhuimu sana kwako na ambacho huwezi kukipata sehemu nyingine isipokuwa kwangu, eeennh?” Moze aliendelea kumkemea kwa hasira.
Joakim alibaki kimya tu, wazi kuwa hakuwa ameitarajia hali ile.
“Fanya sasa!” Moze alizidi kumkemea, na Joakim alijikuta akimnyooshea Moze mkono wake kumwashiria kuwa anyamaze kama jinsi askari wa barabarani anavyofanya wakati akiashiria magari yasimame.
“Basi Moze! Inatosha, usipige kelele tafadhali...” Alisema huku bado akiwa ameinamisha uso na amemuinulia mkono namna ile.
“Nisipige kelele how? Mpenzi wangu yuko taabani huko anapoteza fahamu hovyo hospitalini kwa sababu ya upumbavu wako halafu unaniambia nisipige kelele?” Moze alimjia juu.
“Moze, nimesikia yote uliyoyasema dadaangu. Sasa naomba utoke tu humu ndani na baada ya hapo sitakusumbua wala kukufuata tena! Naomba haya mambo yaishie hapa hapa! Mimi sikuhusika na hilo la kupigwa Jaka ingawa kiukweli halikunihuzunisha hata kidogo. Hata hivyo, samahani kwa yote yaliyotokea...kweli kabisa!” Joakim alimjibu kwa tahayari kubwa huku akiwa bado ameinamisha uso wake.
Ikawa zamu ya Moze kutoamini masikio yake. Alimtazama yule jamaa aliyejiinamia kama kuku aliyenyeshewa mvua.
“Kweli...?” Alijikuta akiropoka lile swali bila ya kujitambua.
Joakim aliinua uso wake taratibu na kumtazama usoni kwa muda.
“Nakubali kuwa nimekuwa na tabia chafu kwa akina dada wengi hapa chuoni, lakini kwa hakika Moze nilipokutaka wewe nilikutaka kwa penzi la dhati na la kweli kabisa. Lakini kwa kuwa leo umenihakikishia kuwa penzi lako siwezi kulipata, basi nakuahidi kuwa sitakubughudhi tena wewe wala mpenzi wako na naomba msamaha kwa yote yaliyotokea.” Joakim alimwambi kwa uchungu na tahayari kubwa.
Moze alimtazama kwa kutoamini, na kwa mbali alihisi akiingiwa na huruma kwa yule kijana.
Hakuwa na la kusema. Hakujua aseme nini. Bila ya kuongeza neno zaidi, aligeuka na kutoka nje ya chumba kile huku machozi yakimtiririka na moyo ukimwenda mbio.
Eeh, Mungu wangu! Bila shaka sasa penzi langu litaendelea kwa amani!
Alijiwazia huku akijifuta machozi, akirudi bwenini kwake. Ambalo hakulijua ni kwamba amani bado ilikuwa mbali sana na penzi lake.
10
Jaka alifumbua macho ghafla na kukutana uso kwa uso na Joakim Mwaga, ambaye haraka aliinua mikono yake yote miwili kwa ishara ya amani huku akiketi taratibu kando ya kile kitanda alichokuwa amelalia Jaka pale Hospitali. Walibaki wakitazamana kwa muda huku kila mmoja akiwa na mawazo tofauti juu ya mwenzake, hasira ikijidhihirisha wazi usoni kwa Jaka.
Ilikuwa ni saa mbili na nusu za usiku na Jaka alikuwa amepitiwa na usingizi peke yake kwenye wodi ile ndogo, kabla ya kushtuka ghafla na kukutana macho kwa macho na hasimu wake.
Jaka alijaribu kujiinua kutoka pale kitandani ili akabiliane na adui yake lakini hakuweza kufanya hivyo haraka kama jinsi alivyotaka, na Joakim alimuwekea mikono mabegani na kujaribu kumlaza tena pale kitandani.
“Tulia Jaka....usiwe na wasiwasi kwani sikuja kwa shari kama unavyodhani...” Alimwambia.
Jaka alimtazama kwa mashaka na kutazama pembeni.
“Unataka nini tena kwangu Joakim...umekuja kutazama kazi waliyokufanyia jamaa zako?” Alimuuliza bila ya kumtazama.
“La Hasha, Jaka. Nimekuja kukuomba msamaha kwa yote yaliyotokea...kwa kweli sikutegemea kama yangefikia hatua hii...”
“We’ unataka kunieleza nini? Baada ya yote haya bado unapata moyo wa kuja kuniambia samahani? Halafu unategemea mimi nikusamehe?” Jaka alimjibu kwa hasira.
“Jaka, mi’ najua kuwa huwezi kuniamini. Lakini ukweli ni kwamba mimi sikuwatuma kabisa akina Alphonce waje wakupige na wala sikujadili nao kitu chochote kuhusiana na hili jambo lililotokea...”
“Sasa unataka msamaha wa nini? Joakim usitake kunifanya mimi mpumbavu...”
“Naomba msamaha kwa sababu najua kuwa akina Alphonce walichukua hatua waliyochukua kwa sababu wanaamini kuwa mimi ni rafiki yao na wewe umenipiga...kwa hiyo wao waliona ni wajibu wao kulipiza kisasi kwa niaba yangu ingawa mimi sikuwatuma...”
“Na unataka kuniambia kuwa ulisikitika sana baada ya kusikia kuwa nimebondwa na hao rafiki zako?” Jaka aliuliza kwa kebehi huku akizidi kumtazama kwa hasira.
“Bila kukuficha Jaka kwanza nilifurahi sana...yaani kabla ya...” Joakim hakumalizia alibaki akiangalia chini kwa aibu. Kisha akainua kichwa chake na kumtazama Jaka.
“Lakini baada ya hapo nilijua kuwa jambo lililofanyika lilikuwa ni la kipuuzi na lisilo na manufaa...hivyo naomba haya mambo yaishe tu Jaka…na...we should be friends, eeenh?” Alimwambia, akimalizia kuwa walipaswa wawe marafiki. Jaka alimtazama kwa muda na kutoa mguno wa kukereka kabla ya kugeuza uso wake pembeni. Muda mrefu ulipita hata Joakim alianza kupata mashaka kuwa huenda Jaka alikuwa amepitiwa na usingizi. Hatimaye Jaka aliuliza huku akiwa bado ameuelekeza uso wake pembeni.
“Umemaliza Joakim?”
“Jaka, najua kuwa nakuweka katika wakati mgumu. Lakini nataka nikuhakikishie kuwa kuanzia leo hutasikia tena bughudha yoyote kutoka kwangu...na kuwa kuanzia leo sitakuwa tena pamoja na chochote kitakachofanywa na Alphonce, Tony au Muddy....kwa sababu sioni sababu ya kupigana, kutishana na kuumizana namna hii...hasa kwa watu wasomi kama sisi ambao tunatakiwa tuwe tunatatua matatizo yetu kwa nguvu za hoja tu na sio vinginevyo...”
Jaka alimgeukia na kumtazama kwa makini.
“Ni nini zaidi unachotaka kutoka kwangu, Joakim?” Alimuuliza.
“Sina chochote zaidi nitakacho kutoka kwako Jaka…zaidi ya hayo niliyokueleza. Najua kuwa huniamini na unanichukia sana...lakini huo ndio ukweli...nimebadili mtazamo.”
“Basi kama ni hivyo, mi’ naona ukweli utajionesha wenyewe Joakim, wala hakuna haja ya kusema maneno mengi...au vipi?”
“Sawa kabisa...”
Walikaa kimya kwa muda kabla ya Joakim kuinuka na kuaga huku akimpa mkono wa urafiki. Jaka alibaki akimtazama akiwa amelala pale kitandani huku mawazo mengi yakipita kichwani mwake.
“Ni mapema sana kupeana mikono Joakima…we nenda tu kwa sasa!” Jaka alimwambia. Joakim hakuonekana kuumizwa na jibu lile. Aliutazama mkono wake aliokuwa amemnyooshea Jaka, kisha akaurudisha na kuutumbukiza mfukoni mwa suruali yake.
“Fair enough…” Alimwambia, akimaanisha kuwa alidhani uamuzi wa Jaka ulikuwa sawa tu kwa wakati ule, kisha akaendelea, “Ugua pole, Jaka…”
Akageuka na kupiga hatua kadhaa kuelekea mlangoni, kisha akasimama na kumgeukia.
“Jaka...” Alimwita huku akimtazama machoni. Jaka alimtazama kwa macho ya kuuliza.
“...Moze anakupenda sana rafiki yangu...wala usiwe na shaka juu ya hilo hata kidogo!” Alimwambia na kubaki akimtazama Jaka huku akitabasamu, kisha aligeuka na kutoka nje ya wodi ile haraka. Jaka aliona mchanganyiko wa hisia katika lile tabasamu la Joakim kabla hajatoka nje ya wodi ile. Alibaki akiwa amelala pale kitandani akiutafakari ujio wa Joakim, hususan yale maneno yake ya mwisho, na lile tabasamu lake kabla hajatoka nje ya wodi ile.
Lilikuwa ni tabasamu lenye mchanganyiko wa simanzi kubwa…na....kitu kingine...
Kitu kama wivu hivi...
Asubuhi ya siku iliyofuata mama yake alifika pale hospitali na kumsisitizia juu ya haja ya kuwafungulia mashitaka wale mahasimu wake. Baada ya kupiga kimya kirefu cha tafakuri, Jaka alikataa kabisa kufungua mashitaka.
“Lakini kwa nini mwanangu? Unataka kuwaachia waendelee kuwa huru baada ya yote haya?” Mama yake alisaili kwa kutoamini.
Jaka aliendelea kuwa na uso wa tafakuri.
“Tunaweza kujaribu kuwashitaki na kupoteza muda, mama…lakini hatutashinda. Na mitihani ya kumaliza chuo ndio inakaribia…kwa nini nipoteze muda wa kujisomea na kujiandaa kwa mitihani kupambana vita ninayojua wazi kuwa nitashindwa? Tuachane nao tu mama…angalau nipate muda wa kujisomea. Si ndilo lililonileta hapa from the very beginning?” Alimwambia mamaye kwa upole.
Mama mtu aliguna.
“Sasa una hakika gani kuwa wao wataachana nawe baada ya hapa?” Alimuuliza mwanaye.
“Si wameshinda? Wamenipa kipigo…nimelazwa masiku tele…wameridhika. Hawatanisumbua, kama hatutawasumbua. Tukubali kushindwa tu kwa sasa, mama …”
Majibu yale yalionekana kumridhisha mama yake kidogo. Muda mfupi baadaye aliaga na kumuacha Jaka akiwa na mawazo tele. Kwa namna fulani ule ujio wa Joakim ulimfanya atake kuona hatma ya yale waliyoongea, na hakika hilo asingeweza kulifikia iwapo angeanza kushitakiana na akina Alphonce mahakamani, ambako alikuwa na hakika kabisa kuwa wasingeshinda.
Je, Joakim alikuwa ametumwa ili kumpoteza malengo asichukue hatua za kuwashitaki akina Muddy?
Alijiuliza.
Hapana, kwani alijua kuwa na wao walijua wazi kwamba hatakuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani.
Alijijibu.
Au ni kweli Joakim alikuwa amedhamiria yale aliyoyasema, kwa anataka waache tofauti zao na wawe na amani?
Alijiuliza tena.
Kama ni hivyo, alitaka sana kuona akina Tony watakuwa na mtazamo gani juu ya hilo.
Aliazimia.
Na ile dalili ya wivu niliyoiona usoni kwa Joakim usiku uliopita? Mbona kana kwamba iliashiria kuwa bado alikuwa ana njama dhidi ya Moze? Je, haiyumkini kuwa Joakim na wenzake walikuwa wamepanga kumfanyia Moze jambo baya ili kuendelea kumkomoa? Kwani ni adhabu gani kali kwa adui yako zaidi ya kumuumizia wale awapendao?
Alijitia shaka zaidi.
Kama ni hivyo, alidhamiria kuwa makini sana na kila hatua ya Joakim. Na ndipo alipojipitishia uamuzi wa kutomwambia yeyote juu ya ule ugeni wa Joakim pale hospitali usiku uliopita…mpaka pale atakapopata uhakika juu ya dhamira halisi ya ujio ule.
Ni uamuzi uliogeuza mtiririko wa matukio yote yaliyofuatia baada ya kuruhusiwa kutoka pale hospitali.
_____________________
Siku tatu baadaye aliruhusiwa kutoka pale hospitali.
Ilikuwa ni furaha isiyo kifani kwa Moze kukutana tena na mpenzi wake nje ya yale mazingira ya hospitali. Walikumbatiana na kubusiana kwa uroho wa huba iliyomea. Ilibidi siku ile Raymond akalale chumba cha rafiki yao mwingine, na Jaka akalala na mpenziwe mle chumbani, akidekezwa ukomo wa kudekezwa.
Lakini katikati ya mudekezana huko, walipata muda wa kutosha kujadili mustakbali wao baada ya tukio lile. Moze akamueleza juu ya mjadala wake na mama Jaka na namna asivyounga mono hija ya kuwashutaki akina Muddy huku wakiwa na ushahidi mwembamba sana kuwapa ushindi. Jaka akakubaliana na hoja ile na akamfahamisha jinis alivyoongea na kumshawishi mama yake kuachana na swala la kufungua kesi.
“Oh, bora ilivyokuwa hivyo Brown…maana ingekuwa ni kupateza muda na kuzidi kujikosesha amani!” Moze alisema, na Jaka akaafikiana naye, moyoni akiificha sababu kuu iliyomfanya alipinge lile wazo la kuwashitaki wale jamaa.
Alimtazama mpenziwe, na akaiona hofu iliyokuwa usoni kwake dhidi ya wale mahasimu wao, na kwa mara nyingine akajipongeza kwa ule uamuzi wake wa kutosema lolote juu ya yale yaliyopitikana baina yake na Joakim kule hospitali, kwani alijua kwa vyovyote Moze angelitafsiri jambo lile kuwa ni njama tu ya Joakim na hivyo kuwa na wahka zaidi.
Moze naye kwa upande wake hakutaka kabisa kumweleza Jaka kuwa alikwenda chumbani kwa Joakim, tena akiwa peke yake, na kumkemea kama alivyofanya wakati Jaka alipokuwa amelazwa hospitalini. Kwani naye alijua fika kuwa Jaka angechukizwa sana na kitendo kile ambacho baadaye hata yeye mwenyewe alikiri kuwa kilikuwa sio tu cha kijinga, bali pia cha hatari sana.
“We’ una wazimu Moze...una wazimu tena si kidogo!” Rose alimfokea sana siku ile alipomweleza kuwa alikwenda chumbani kwa Joakim kumkemea.
“…unajua angeweza kukubaka kule wewe? Halafu ungesema umebakwa wakati umejipeleka mwenyewe chumbani kwake fala wewe?”
“Mi hasiri ilinielemea Rose…jinsi walivyomfanya Brown…”
“Hasira za mkizi hizo wewe! Je ungemkuta na wale wenzake? Si ndio umgekuwa asusa tu kule wewe? Halafu siye tungemueleza nini Jaka, eenh?”
“Ah, Rose…”
“Hakuna cha Aaah Rose hapa bwana! Hivi we’ mbona sometimes unakuwa dunderhead sana wewe lakini?” Rose alizidi kumfokea siku ile, akimuuliza kwa nini mara nyingine anakuwa hamnazo namna ile.
Moze alibaki akimkodolea macho tu, asiwe na la kusema. Na hata alipojaribu kujieleza kuwa alikuwa akiendeshwa na hasira na alikwenda kwa Joakim bila ya kufikiri bado haikutosha kumnyamazisha Rose.
“Ninachojua Moze ni kuwa umefanya jambo la kipumbavu sana ambalo lingeweza hata kukupotezea maisha yako!” Rose aliendelea kumkemea huku akifungua kabati lake la nguo na kuanza kupanga nguo zake zilizokuwa zimewekwa kitandani baada ya kufuliwa.
Moze alimtazama Rose kwa mshangao.
“Ningepoteza maisha yangu...?”
“Moze, wasichana kadhaa wamekuwa wakipoteza maisha hapa chuoni kwa vifo vya kutatanisha-tatanisha tu...au wewe hulijui hilo? Au unajidhani wewe ni nani hata usiwe miongoni mwa hao wanaokufa vifo visivyoeleweka hapa chuoni?” Rose alimjibu huku akiwa bado amemgeuzia mgongo akipanga nguo zake kabatini.
“Ha! Kwani Joakim ndio....”
“Kwani Joakim ndio nani! Ile mobu yake unaiona ni mobu ya mchezo ile? Tazama jinsi walivyomfanya Jaka. Joakim naye si ndio kundi moja na hao waliompiga Jaka wakiongozwa na Tony?” Rose alimjibu huku akimgeukia na kumnyooshea kidole kwa jazba.
Moze alibaki akimtazama tu huku akiwa amepigwa na butwaa. Taratibu Rose alirudia kazi yake ya kupanga nguo huku akimalizia, “Na najua kuwa Jaka akisikia kuwa umefanya jambo la kilofa kama hilo hatapendezewa hata kidogo!”
Moze alikaa kwenye kiti taratibu na kujiinamia akiwa amejishika kichwa kwa mikono yake miwili. Hakuwa na la kusema.
Aseme nini wakati yote aliyoambiwa na Rose siku ile yalikuwa ni kweli isiyopingika?
Kwa hofu ya kumkera mpenziwe na kumzidishia mashaka zaidi, aliamua kutomweleza kabisa kuhusu safari yake kule chumbani kwa Joakim, na yale yaliyopitikana baina yao.
Aliisukuma pembeni kumbukumbu ile kutoka akilini mwake na kujilaza kifuani kwa mpenziwe.
“Oh, nina furaha sana kuwa umepona na tuko pamoja Jaka…!” Alimnong’oneza.
“Yeah…mimi pia kisura…na nakuhakikishia kuwa haya yote hayatapoteza pendo lililopo baina yetu!” Jaka naye alimnong’oneza.
Kwikwi ya kilio ilimchomoka Moze, na akamkumbatia kwa nguvu zaidi mpenziwe.
___________________
Siku mbili baadaye, akiwa anajisomea chumbani kwake Jaka alishtushwa na hodi iliyobishwa mlangoni kwake. Hakuwa akitarajia mgeni lakini alihisi anaweza kuwa ni mgeni wa Raymond ambaye alikuwa kwenye kipindi darasani. Kwa kuwa mlango ule haukuwa umefungwa kwa ufunguo, alipaza sauti kumkaribisha mbishaji wa hodi ile.
Mlango ulisukumwa na Tony, Muddy na Alphonce Ng’ase waliingia mle ndani kwa vishindo, Alphonce aliyekuwa wa mwisho kuingia akiukomea kwa ndani mlango ule.
Kengele za hatari zikavuma kwa nguvu akilini mwake wakati akiwatazama wale jamaa huku akiinuka taratibu kutoka kitini alipokuwaamekaa na kusimama katikati ya chumba kile.
“Oyaa mambo gani haya sasa! Mbona mnaingia na kufunga mlango wangu kwa ndani...mnataka nini tena?” Aliuliza kwa hasira huku akiwatembeza macho kwa zamu wale jamaa. Tony alimtazama kwa dharau kabla ya kumjibu kwa swali.
“Tumekuja kukujulia hali tu.” Alphonce alimwambia. Jaka akawatazama kwa kutoamini, na akakutana na macho yenye chuki ya wazi dhidi yake.
“Jamani mi’ s’taki balaa saa hizi...” Jaka alianza kujitetea.
“Oh, Yeah…? Basi labda balaa inakutaka wewe...?” Alphonce alimkatisha.
“Akh, mbona siwaelewi…?”
“Kwani vipi Jaka...? Hutaki marafiki zako tuje tukujulie hali?”
“Mimi sio rafiki yako Tony, na wala si rafiki wa yeyote kati yenu...naomba muwe wastaarabu kidogo tu na mtoke humu ndani. Sasa hivi!”
Tony aliendelea kumtazama huku akitikisa kichwa taratibu kwa masikitiko ya kebehi.
“Aaah...hasira za nini mshikaji...? Sisi tumepata habari kuwa Joakim hataki tena ugomvi na wewe na anataka muwe marafiki...” Tony alimjibu huku akiendelea kumtazama kwa kebehi.
Kumbe Joakim alidhamiria yale aliyoyasema!
“Sasa hilo kwako ni tatizo?” Jaka alimuuliza kwa jeuri, na hapo hapo Muddy alikurupuka na kumtupia kofi kali ambalo halikumpata Jaka kwani Tony aliwahi kumzuia.
“Tulia, Muddy!” Tony alimfokea, kisha akamgeukia Jaka kwa hasira.
“Wakati mimi naongea ni vyema unisikilize kwanza kabla ya kudakia kwa maneno yako ya jeuri, you know what I’m sayin’? ” Alimkoromea, akimalizia kauli yake kwa ule msemo wa kiingereza cha kimarekani aliozoea sana kuutumia.
“Sasa masharti namna hiyo unipangie siku nikija chumbani kwako, hapa uko chumbani kwangu hivyo amri yangu ndiyo inayotawala…tokeni nje ya hiki chumba sasa hivi!” Jaka naye alimkoromea, Muddy na Alphonce walitoa miguno ya kuonesha kuchukizwa na namna kiongozi wao alivyokuwa akijibiwa.
“Kaa mbali nasi Jaka, usitake kabisa kutufuatilia katika nyendo zetu, you know what I’m sayin’?” Tony alizidi kumkoromea, na Jaka akamshangaa.
“Khah! Nyendo zenu? Ni nyendo zipi hizo nilizozifuatilia? Na kwa taarifa yako, hilo la kukaa mbali nanyi mbona ni jepesi sana tu kwangu?” Jaka aliuliza kwa hasira huku akimkazia macho Tony. Tony alimrudishia jicho kali.
“Sisi sio wapumbavu Jaka. Hiyo mbinu ya kujitia katika urafiki na Joakim ili upate kujua tunafanya nini sisi tumeshaish’tukia zamani sana...na ndio maana tumekuja kukushauri kuwa kaa mbali nasi kwa kukaa mbali na Joakim...kwa usalama wako. Si umeona promo tuliyokutolea kule Billicanas?” Hatimaye alimjibu kwa sauti ya upole huku bado akiwa amemkazia macho, akimaanisha kuwa kile kipigo alichopokea kule Billicanas kilikuwa ni mfano tu wa mambo mabaya wanayoweza kumfanyia.
“Basi kama hilo ndilo tatizo, kaa ukijua kuwa tayari limeshatatuka. Kwa sababu sio mimi niliyetaka urafiki na Joakim bali ni yeye ndiye aliyenifuata na kutaka tuwe marafiki...kwa hiyo njia nzuri kwako ni kumfuata Joakim na kumshauri kuwa akae mbali nami...hapo hata mimi utakuwa umenirahisishia sana kazi kwa sababu sina haja na urafiki au mahusiano yoyote na watu wa jamii yenu...”
“We’e bwana mbona unajitia unajua sana kutoa majawabu wewe?” Ng’ase alifoka kwa hasira huku akimsogelea Jaka, na Jaka akajiweka sawa kimakabiliano.
“Nimekwambia kaa kimya Ng’ase!” Tony alimfokea, na kumgeukia tena Jaka.
“Sisi tunaondoka. Lakini ukae ukijua kuwa tumeshakuonya. Ukipuuza basi ujue safari hii tutamwendea malaya wako na sio wewe tena.” Tony alimwambia kwa hasira, kisha akageuka na kuanza kutoka ndani ya chumba kile.
“Lets go!” Aliwaambia na kuwaashiria wafuasi wake, ambao walimfuata baada ya kumtupia Jaka mitazamo ya ghadhabu, naye alibaki akiwa amesimama katikati ya chumba kile akiwa amefura kwa ghadhabu.
_____________________
Gari jeusi aina ya Toyota Chaser lilisimama mbele ya geti kubwa nje ya moja kati ya majengo mengi yaliyozagaa katika eneo la bandari ya Dar es Salaam. Dereva wa lile gari alisoma maandishi makubwa yaliyokuwa yameandikwa juu ya geti lile, yaliyosomeka ST. STANZA CANNED FISH (E.A.) COMPANY. Alipiga honi mara mbili na kubaki akisubiri garini mwake.
Lile jengo lile llilikuwa ni ofisi pamoja na kiwanda cha kusindika samaki wa Tanzania na kuwahifadhi kitaalamu katika makopo tayari kwa kuuzwa ndani na nje ya nchi, na hivyo kuipatia Tanzania fedha za kigeni na kuiongezea kipato kampuni ile kubwa.
Hii ilikuwa ni moja kati ya makampuni mengi ya kigeni nchini, ikiwa ni matunda ya sera ya Serikali ya Tanzania ya kuhamasisha uwekezaji kutoka nje ya nchi na biashara huria. Kampuni hii inayomilikiwa na raia mmoja wa Kolombia, nchi iliyopo Amerika ya Kusini, pia huingiza samaki wa makopo kutoka Kolombia na kuwauza hapa nchini. Hivyo, St. Stranza Canned Fish Company ilikuwa ni kampuni ya kuagiza samaki waliosindikwa kutoka bahari ya Carribean nchini Kolombia kuja nchini Tanzania, na pia ilisafirisha samaki waliosindikwa kutoka bahari ya Hindi hapa Tanzania na kuwauza nchi mbalimbali za Amerika ya Kusini hasa Kolombia ambako Kampuni hiyo pia ilikuwa na ofisi zake.
Katika kufanikisha biashara zake hizi, kampuni hii kubwa ilimiliki meli zake yenyewe kwa ajili ya kusafirisha shehena zake za samaki na malighafi mbalimbali baina ya Tanzania na nchi mbalimbali za ulimwengu ambapo Kampuni hiyo ilipeleka bidhaa zake.
Kwa hiyo, St. Stanza Canned Fish Co. ilileta mahusiano mazuri ya kibiashara sio tu baina ya bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania na bandari maarufu za Santa Marta na Barranquilla za kule Kolombia, bali pia na bandari nyingine nyingi ulimwenguni.
Geti lilifunguliwa na dereva wa ile Chaser akaliongoza gari lake kuingia ndani ya uzio mkubwa wa eneo la kampuni ile ya kimataifa kabla ya kusimama tena umbali wa kama mita kumi na tano mle ndani ambapo kulikuwa kuna kizuizi kingine. Askari mwenye silaha alilisogelea lile gari kwa ukaguzi mwingine tena. Kampuni ya St. Stanza ililipa kipaumbele sana swala la ulinzi na usalama ndani ya maeneo yake.
Dakika chache baadaye Toyota Chaser iliegeshwa kwenye maegesho maalum kando ya lango kuu la kuingilia ndani ya ofisi zile za St. Stanza, na Tony akateremka kwa madaha huku akiwa amevaa miwani myeusi iliyoficha macho yake. Alikuwa amevaa shati jeupe la mikono mirefu lililomkaa vyema na suruali pana ya rangi ya kahawia ambayo pia ilimpendeza sana. Tai yake pana iliyokuwa na mchanganyiko wa rangi ya kahawia na weusi ilienda sambamba na rangi ya viatu vyake vya ngozi ambavyo vilikuwa vyeusi; sawa na rangi ya mkanda wake wa ngozi aliouvaa kiunoni juu ya suruali ile. Mkono wake wa kushoto ulikuwa umebeba mkoba mdogo wa kiofisi, maarufu kama Briefcase.
Kinyume na watu wengine aliowakuta wakisubiri kwenye eneo la mapokezi ndani ya ofisi ile, yeye alipitisliza moja kwa moja na kupanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza na pekee ya jengo lile, ambapo alitokea kwenye korido fupi iliyomfikisha kwenye mlango mpana wa kioo, uliomuwezesha kumuona mrembo aliyekuwa nyuma ya dawati kubwa na ghali nyuma ya mlango ule. Alipoufikia tu ule mlango ulijifungua wenyewe naye akapita ndani. Alisalimiana na yule mwanadada, na kama kwamba alikuwa amezoea ujio wa Tony ofisini pale, yule dada alimuashiria kuwa mkono wake kuwa apite moja kwa moja kuuelekea mlango mwingine mle ndani, uliokuwa kulia kwa lile dawati alilokuwa amekalia yule katibu muhtasi.
Tony alifuata maelekezo yale na kuuendea ule mlango alioelekezwa, uliokuwa na kibao kidogo cha shaba nyekundu kilichoandikwa neno moja tu, “DIRECTOR.” Aligonga mara mbili kwenye mlango ule, kisha taratibu akafungua na kuingia ndani ya ofisi ya thamani mno, iliyopambwa kwa zulia zito sakafuni na seti ya sofa ya kifahari sana. Kuta za ofisi ile zillikuwa zimepambwa kwa picha mbalimbali za meli zinazomilikiwa na kampuni ya St. Stanza na ramani mbali mbali zilizoonesha njia kadhaa za meli hizo baharini. Meza kubwa ilikuwa mbele ya dirisha pana la kioo lililotoa mandhari nzuri ya bandari ya Dar es Salaam kutokea pale ofisini.
Mtu mrefu alikuwa amesimama mbele ya dirisha lile akiangalia mandhari ile ya kuvutia kule nje, akiwa amemgeuzia Tony mgongo. Alikuwa amevaa suti kubwa ya kuvutia ya rangi ya kijivu. Tony alimtazama yule mtu na kuteremsha macho yake juu ya ile meza kubwa iliyokuwa imepangwa makaratasi na mafaili kadhaa kwa unadhifu mkubwa mno. Macho yake yakatua kwenye kibao kidogo kilichonakshiwa kwa ustadi mkubwa na kusoma kwa mara nyingine tena maneno yaliyochingwa kwa nakshi nzuri kwenye kibao kile:
MR. RAUL PINTO GARCIA
DIRECTOR
“Karibu Tony.” Raul Pinto Garcia alimkaribisha huku bado akiwa amemgeuzia mgongo, akiangalia nje ya dirisha lile pana. Sauti yake ilikuwa ni kama ya mtu aliyekuwa akijaribu kuongea wakati akiwa amepaliwa na moshi wa sigara hivi, na ingawa aliongea kiswahili kizuri, bado kulikuwa kuna lafudhi ya kigeni kwenye kiswahili chake.
Tony aliketi kwenye moja ya viti viwili vilivyokuwa mbele ya ile meza na kusubiri. Raul aligeuka taratibu na kumtazama kwa muda, kisha akarudi pale mezani na kuketi kwenye kiti cha kifahari sana kilichokuwa nyuma ya meza ile.
Mkurugenzi na mmiliki wa St. Stanza Canned Fish Company alikuwa na nywele ndefu nyeusi mithili ya zile za kihindi ambazo alizilaza nyuma na kuzifunga kwa kisogoni, akiacha mkia mdogo wa nywele ukining’inia. Uso wake mrefu ulikuwa na macho madogo yenye mboni kali za buluu ambazo zilifanya tofauti kubwa sana na rangi ya nywele zake. Rangi ya ngozi yake haikuwa “nyeupe”kama jinsi wazungu wengine walivyo bali ilikuwa ni mchanganyiko wa rangi hiyo na weusi fulani ambao ulimfanya aonekane kuwa na rangi ya kahawia kidogo.
Raul Pinto Garcia alikuwa ni raia wa Kolombia.
“You okay, Tony?” Raul alimjulia hali Tony kwa kimombo huku akitabasamu.
Alikuwa na mdomo mpana na mwembamba na tabasamu lake liliishia hapo hapo: mdomoni. Macho yake makali hayakuonesha dalili yoyote ya tabasamu kiasi kwamba hata wewe ungeweza kuamini iwapo ungeambiwa kuwa ule mdomo uliotabasamu na yale macho vilikuwa ni viungo vya watu wawili tofauti kabisa.
Raul hakuwa na ndevu za aina yoyote na pua yake ilikuwa ni nyembamba na ndefu.
“I’m cool, man...what’s up? Umeniita...” Tony alijibu salamu ile huku akimtazama Garcia kwa wasiwasi kwani macho ya mkolombia yule ambayo daima yalikuwa yakimtazama mtu kama kwamba yaliweza kuona mpaka ndani kabisa ya moyo wa mtu, yalimtisha Tony siku zote. Garcia aliafiki kwa kichwa kuwa ni kwlei alikuwa amemuita, na Tony alibaki kimya akisubiri kuambiwa aliloitiwa, ingawa alikuwa anajua kuwa litakuwa linahusiana na biashara kama kawaida.
Bila ya kuongeza neno, Garcia alivuta droo na kutoa kijichupa kidogo ambacho ndani yake kulikuwa kuna vidonge vyeupe vilivyoshabihiana kwa muonekano na vile vya dawa ya maumivu ya Panadol, na kukiweka mezani taratibu kisha kwa kidole chake cha shahada akamsukumia Tony kile kichupa na kujiegemeza kitini kwake huku akimtazama Tony kwa utulivu wakati akikiinua kile kichupa na kukitazama kwa makini. Baada ya kukigueza-geuza kile kijichupa, Tony alitoa kidonge kimoja na kukitazama kwa karibu zaidi.
Kwa haraka haraka kilionekana kuwa ni kidonge cha kawaida tu cha maumivu, kama Panadol.
Lakini kilikuwa tofauti kabisa na kidonge cha “kawaida”.
Badala ya kuandikwa “Panadol”, sura ya kidonge kile ilionesha picha ndogo ya mbwa mwenye mabawa aliyekuwa katika hatua ya kupaa. Tony alikibonyeza kidogo kile kidonge na mara moja kilimong’onyoka na kutoa unga laini sana, na mara moja akajua ni kwa nini kile kidonge hakikuwa “Panadol” ya kawaida.
Kwa kutaka kuhakikisha hisia zake hizo, aliunusa kidogo ule unga uliotokana na kidonge kile na hapo alipata ladha ya ile hisia ya ajabu ambayo huipata kila mara anapovuta ule unga ambao wengi huuita wa haramu, ingawa tangu alipovutishwa kwa nguvu na mtu mmoja aliyemjua kwa jina moja tu la Puzo kiasi cha miaka miwili iliyopita, Tony alishindwa kabisa kuelewa ni nini uharamu wa unga ule ambao yeye ulimfanya ajisikie furaha na kumfikisha kwenye daraja ya juu kabisa ya ubora wa kibinadamu. Tangu siku hiyo Tony hakuweza kabisa kuacha kutumia madawa ya kulevya.
Ili kuendelea kumfichia siri ile, Puzo alimtaka Tony awe tayari wakati wowote atakapohitajika kupeleka mzigo wa madawa yale haramu kwa wateja mbalimbali wa Raul Pinto Garcia na wakati huo huo kuhakikisha kuwa anapata wateja wengine wengi wa kuwauzia unga ule. Ilikuwa ni muhimu sana kwa Tony kuwa utumiaji wake wa madawa ya kulevya uwe siri, kwani kama habari ile ingeanikwa kwenye vyombo vya habari ingemchafulia sana jina baba yake, mzee Anthony Wanzaggi, ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha vita dhidi ya madawa ya kulevya nchini kutokana na umaarufu wake.
Tony hakuwa na ujanja, kwani masharti ya Puzo yalikuwa wazi. Akubali kuwa wakala wa madawa ya kulevya kwa wateja mbalimbali atakaoelekezwa, au siri itoke nje na yeye asipate tena unga ule ambao tayari alikuwa ameshafikia hatua ya kutoweza kufanya lolote bila ya kuupata - kwa lugha ya kigeni, Tony alishakuwa drug addict.
Tony hakuwa na uamuzi zaidi ya kukubali matakwa ya Puzo.
Na ndio sababu leo hii alijikuta akiitikia wito mwingine tena kutoka kwa Raul Pinto Garcia ambaye aliendesha biashara hii haramu nyuma ya kivuli cha biashara halali chini ya kampuni yake ya St. Stanza Canned Fish Company.
Tony aliinua uso wake na kumtazama Raul.
“Hii ni mali safi sana, Raul...imeingia lini?” Alimwambia na kumuuliza kwa bashasha kubwa.
“Ni mali safi na ghali sana...ni wateja wachache sana wanaoweza kumudu kununua mali hiyo...na hao ni mimi tu ninayeweza kudiriki kuwaona.” Raul alijibu.
Tony alimtazama bila ya kusema neno, akitafakari uzito wa maneno yale. Alielewa kuwa Raul alikuwa na wateja wake muhimu ambao ni yeye tu aliyewajua. Wateja hao walikuwa ni maafisa wa balozi mbalimbali hapa nchini pamoja na baadhi ya maafisa wa ngazi za juu serikalini, wafanyabiashara maarufu, waigizaji na wengine kama hao... hizo zilikuwa ni tetesi tu ambazo Tony alizisikia kutoka kwa Puzo lakini hakuwa na uhakika nazo. Lakini sasa alianza kupata uhakika na tetesi zile na moyo ukamsisimka alipojaribu kufikiri uzito wa kashfa itakayotokana na siri kama hiyo kugundulika.
Alijiuliza iwapo na watu hao muhimu walianza kutumia madawa yale ya kulevya kwa kupenda kwao wenyewe na kisha kujikuta kuwa hawawezi tena kuacha, au na wao waliingizwa katika mtego ule kama jinsi yeye alivyoingizwa...na kwa mara nyingine tena alikubali moyoni mwake kuwa Raul Pinto Garcia alikuwa ni mtu mwenye nguvu na kauli kubwa sana kwa baadhi ya watu muhimu nchini kiasi cha kumfanya aendelee na biashara ile ya “haramu” nyuma ya kivuli cha biashara nzuri ya halali bila ya wasiwasi wowote.
“Kwa hiyo?” Hatimaye alimmuliza huku akimuinulia nyusi kusisitiza swali lake.
Badala ya kumjibu, Raul alivuta mkoba wa kiofisi uliofana na ule aliyokuja nao Tony na kuuweka juu ya meza. Aliufungua ule mkoba na Tony alishuhudia vijichupa kama kile alichokuwa nacho mkononi mwake vipatavyo kumi hivi vikiwa vimefungwa pamoja kwa mpira katika mafungu mawilli ya vitano-vitano. Raul aliufunga tena ule mkoba na kumkabidhi Tony na Tony akamkabidhi Raul ule mkoba aliokuja nao ambao ulikuwa mtupu.
“Utaenda Kilimanjaro Hyatt Hotel, na hapo utaomba kuwasiliana kwa simu na mtu aitwaye Johann Schultz. Akipokea simu hyo mtu wewe utakaa kimya mpaka aongee. Neno lake la kwanza litakuwa ni swali…atakuuliza, “Is the nest is full?”.
Tony alinyanyua zaidi nyusi zake, na Raul akaendelea, “Ndio. Atakuuliza hivyo, nawe utamjibu kiufiupi tu, kwa kusema “Yes”, kisha utampa ile simu yule mtu wa mapokezi na huyo mteja atampa maelekezo yule mtu wa mapokezi kuwa akuruhusu kwenda chumbani kwake…ambako utatajiwa namba ya chumba na huyo mtu wa mapokezi…”
“Duh!” Tony aliguna.
“Oh yes. Hii ni mali adimu sana na lazima kuwe na umakini wa hali ya juu. basi utakwenda mpaka chumba utakachoelekezwa ambapo utaingia na utasikia maji yakimwagika bafuni kama kwamba huyo mteja anaoga. Wewe utauweka mkoba huo juu ya kitanda na kuondoka haraka sana...kutakuwa hakuna kuonana na mteja, tumeelewana?” Raul alimpa Tony maelezo kwa utulivu huku akimtazama kwa makini kwa macho yake makali.
Tony aliyasikiliza maelezo yale kwa makini na kuafiki kwa kichwa kuwa alikuwa amemuelewa.
“Hiyo inamaanisha kuwa iwapo mtu atakayepokea simu ataanza kwa kuongea neno tofauti na hilo nililokuwambia, au akionesha kubabaika au kusita kidogo tu, basi haraka sana utafute njia ya kutoweka kutoka eneo hilo. Puzo atakuwa nawe muda wote ingawa wewe hutamwona, hivyo atakusalimisha bila matatizo...sawasawa?” Raul alimwambia kwa msisitizo mkubwa. Tony alimkodolea macho na kumeza funda kubwa la mate huku akipepesa macho.
“Sa…sawasawa...nimekuelewa…”
“Ni vyema uwe umenielewa, bwa’mdogo!” Raul alimsisitizia kwa kitisho, na kimya kikatanda kwa muda mle ndani.
Baada ya madawa yale haramu kuingia nchini kutoka Kolombia kwa kutumia meli za St. Stanza, yalihitaji kusambazwa kwa wateja mbalimbali sio tu hapa nchini bali pia hata nchi za jirani za Uganda, Burundi, Kenya na nyinginezo, ambako bidhaa “halali” za St. Stanza Canned Fish Company ziliuzwa. Katika nchi zote hizi, Raul alikuwa na wasambazaji wake ambao mwenyewe aliwaita Couriers, na ambao hawakuwa wakijuana kabisa wao kwa wao. Hivyo Tony alikuwa ni mmoja tu kati ya couriers wengi waliotawanywa katika kila kona ya nchi na kila kona ya miji mikubwa hapa nchini. Yeye aliwekwa maalum kwa ajili ya wateja waliokuwa ndani ya eneo la Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, ingawa mara kwa mara alitumika kwa kazi za nje ya eneo hilo kutokana na ukweli kuwa eneo la Chuo Kikuu bado halikuwa likifanya vizuri kibiashara.
Baada ya kimya kile kifupi, Raul alivuta tena droo na kutoa kitita cha fedha na kumtupia Tony pale juu ya meza. Tony alikichukua kitita kile na kukitazama kwa karibu. Zilikuwa ni shilingi laki mbili kamili za kitanzania.
Tony alitabasamu na kuinuka huku akipeana mkono na Raul.
“Iwapo hili zoezi la leo litaenda vizuri, kutakuwa kuna mzigo mwingine kama huo baada ya siku chache...Puzo atawasiliana nawe.” Raul alimwambia wakati wakiagana.
“No problem.” Tony alijibu huku akiondoka akiwa na ule mkoba wenye madawa ya kulevya.
___________________
Akiwa amejilaza chali kitandani, Jaka aliendelea kujiuliza ni kitu gani hasa ambacho Tony na wenzake walikihofia kutokana na “urafiki” kati yake na Joakim Mwaga. Wao walihisi kuwa Jaka alijifanya rafiki wa Joakim ili apate kuchunguza “nyendo” zao, kitu ambacho si kweli kabisa...lakini ni nyendo gani hizo ambazo wao walihisi Jaka alikuwa anataka kuzifuatilia?
Ni mambo gani hasa walikuwa wakiyafanya ambayo hawakutaka Jaka, au mtu mwingine yeyote, ayajue kiasi cha kudiriki kwenda kumtisha na kumkanya dhidi ya urafiki wake na
Joakim? Urafiki wenyewe ni urafiki gani? Ingawa tangu mwanzo hakuwa na nia ya kuwa “rafiki” na Joakim, ule ujio wa akina Tony ulimletea picha kuwa huenda Joakim alimuendea kwa nia ya kweli ya kutaka kumaliza tofauti zao, jambo ambalo ni wazi kuwa wenzake wale hawakulitarajia, na hivyo baada ya Joakim kuwaambia nia yake ile, wakakurupuka.
Aliguna na kumung’unya midomo kwa kuvuta tafakuri zaidi. Kadiri alivyozidi kufikiri ndivyo alivyozidi kukubaliana na wazo lililokuwa likimjia kila mara kichwani mwake; Tony na wenzake walikuwa wanaogopa.
Sasa kwa nini waogope? Kila mara alipojiuliza swali hilo alipata jibu jingine moja tu; Tony na wenzake walikuwa wanaogopa kwa sababu walikuwa wana mambo mabaya sana wanayoyafanya.
Kwa sababu walikuwa wanaogopa sana kujulikana kwa mambo yao hayo, wakachukua hatua ya kukurupuka tu na vitisho badala ya kutumia akili. Hiyo ni kawaida ya watu wenye madhambi-huwa ni waoga na wenye wasiwasi muda wote kuwa huenda madhambi yao yamegundulika.
The guilty are afraid.
Kwa kutokutumia kwao akili, kitendo kile cha kwenda kumuwekea vitisho dhidi ya uhusiano wake na Joakim kilikuwa kimeamsha udadisi mkubwa kichwani mwake, badala ya kuzuia udadisi huo ambao kabla ya hapo haukuwepo kabisa.
Kwa hakika ilikuwa haileti maana hata kidogo. Maana pekee ambayo Jaka aliweza kuikokotoa kutokana na tukio lile ni kuwa huenda hata hao akina Tony wenyewe hawakuwa na uhakika iwapo Joakim alikuwa anajua lolote kuhusu hayo “mambo ” yao... jambo ambalo Jaka hakutaka kuliamini kwani Joakim ,Tony, Ng’ase na Muddy wote walikuwa ni kundi moja.
Na kama Jaka akikubali swala kwamba Joakim alikuwa hajui lolote kuhusu “mambo” ya Tony na wale wenzake wawili, basi hiyo ilimuweka Joakim kwenye nafasi moja mbaya sana, nafasi ya kutoaminika na wale wenzake, na wakati huo huo kutoaminika na Jaka vilevile.
Ukweli huo pia ulimrudisha kwenye jambo jingine ambalo lilishapita kichwani mwake mara kadhaa tangu atembelewe na akina Tony mle chumbani mwake…kuwa Joakim alikuwa anasema kweli siku ile alipomtembelea pale hospitali. Jamaa alikuwa anataka wasameheane kiukweli na wawe marafiki.
“Unawaza nini?”
Alishtuka kutoka kwenye mawazo yake na kupeleka mkono wake kwenye kichwa kilichokuwa kimelazwa juu ya kifua chake pale kitandani na kukipapasa taratibu. Moze alijiinua na kuegemea kiwiko cha mkono wake wa kushoto, akamtazama mpenzi wake huku akimpapasa kifuani kwa mkono wake wa kuume.
“Unawaza nini Brown...?” Moze alimuuliza tena huku akimtazama usoni.
“Mmnnhh...nilikuwa nasinzia...” Jaka alidanganya kivivu huku akiendelea kumpapasa mpenziwe sehemu ya nyuma ya kichwa na shingo yake. Moze alimtazama kwa muda.
“No, Brown...ulikuwa husinzii. Ni nini kinachosumbua kichwa chako mpenzi?” Alimkatalia na kumuuliza tena huku akimbusu kivivu katikati ya kifua chake. Jaka alitoa mguno hafifu huku akihisi mwili ukisisimshwa kwa busu lile la kimzaha tu. Aligeuza uso wake pembeni wakati Moze akichora viduara vidogo vidogo kukizunguka kitovu chake kwa kidole chake cha shahada na kumfanya Jaka ajigeuze geuze kitandani kivivu huku akiendelea kubaki kimya.
Ukweli ni kwamba hakujua aanze vipi kumweleza Moze kuhusu mawazo aliyokuwa nayo kwa sababu yeye mwenyewe yalikuwa hayamwingii akilini.
“Au unawaza kuhusu mambo ya akina Joakim?” Aliendelea kuuliza Moze.
Yaani umepiga mle mle! Nawaza ni kwa nini Tony na wenzake wanaogopa sana kuwepo kwa urafiki baina yangu na Joakim Mwaga.
“Hapana Moze...sina ninachowaza mpenzi...nilikuwa nasinzia.”
“Kweli?”
“ Kweli.”
Moze alimtazama kwa muda kisha taratibu alikilaza kichwa chake kifuani kwa mpenzi wake huku akiendelea kumpapasa tumboni taratibu. Jaka naye alianza kumpapasa mgongoni kivivu huku akiendelea na mawazo yake.
Lazima kuna sababu ya kuwatia hofu Tony na wenzake...na iwapo nitaijua, huenda sababu hiyo ikawa ndiyo njia pekee ya kujihakikishia usalama wangu na wa mpenzi wangu…
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
______________________
“Mimi naona yule jamaa hajui lolote, Tony.” Muddy alikuwa akimwambia Tony, na Alphonce “Al Pacino” Ng’ase aliafikiana naye kwa kichwa huku akiwa amekunja uso kwa mawazo. Walikuwa chumbani kwa Tony.
Tony aliwatazama kwa hasira huku akitafuna kucha za vidole vyake. Alikuwa amekasirika sana, kwani alijua kwamba baada ya tukio lile, Jaka ndio angeanza rasmi kukitafuta kitu ambacho wao walikuwa wanataka asikijue...
Lile lilikuwa ni kosa, tena kosa kubwa sana. Alijua kuwa iwapo Jaka akipata japo wazo tu juu ya kile walichokuwa wanakifanya, basi angewaamshia matatizo mengi sana ambayo mwisho wake ungekuwa ni kuozea jela. Kujulikana kwa habari za kuhusika kwake katika madawa ya kulevya kungemletea athari kubwa baba yake na hilo ndilo jambo ambalo Tony alilihofia sana.
Alizidi kughadhibika alipomkumbuka Puzo ambaye ndiye aliyemtia katika mtego huu ambao kadiri alivyozidi kuendelea kutumia madawa yale ya kulevya, ndivyo ulivyozidi kuwa mgumu kujinasua.
Kwa vyovyote vile ni lazima habari hizi zisijulikane...hata kidogo!
“Una uhakika gani kama hajui lolote, Muddy?” Hatimaye aliuliza.
“Kama angekuwa anajua, basi pale tulipomwendea ni lazima angejaribu kututishia usalama wetu juu ya hilo...kwamba tumwache aendelee na mpenzi wake naye anyamaze kimya kuhusu dili zetu...lakini hakusema hivyo...” Muddy alijibu.
Lakini tuna uhakika gani iwapo Jaka hataanza kulifuatilia swala hili kwa undani zaidi? Je akigundua na kuviarifu vyombo vya dola? Nini itakuwa hatima yangu...? Bila shaka Raul ataniua....yaani huo ndio utakuwa mwisho wangu hapa duniani!
“Tulishafanya kosa tangu mwanzo...la kumdharau yule jamaa. Sasa nagundua kuwa yule jamaa ni hatari sana...” Tony aliendelea kuwaza kwa sauti, bila kutilia maanani iwapo wale wenzake walikuwa wanamsikia au la.
“Sasa tufanya nini kuhusu hilo?” Muddy aliuliza Muddy.
“Aah...mi’ naona tuachane naye tu...” Ng’ase aliingiza hoja.
Tony alimtupia jicho kali sana, na Ng’ase akambetulia mabega.
“Mmeshaanza kumwogopa sio?” Tony alifoka kwa hasira, na bila ya kusubiri maoni ya wenzake akaendelea, “Siwezi kuruhusu mtu yeyote kutishia usalama wa maisha yangu, mimi. Jaka anaelekea kuwa tishio kwa usalama wangu, kwa sababu nina hakika kabisa kuwa iwapo sasa hivi hajui kitu, basi atafanya kila hila mpaka ajue ni nini tunafanya ili atumie kujua kwake huko kuwa kama ngao yake na fimbo ya kutuongozea sisi tufanye atakavyo...na hilo siwezi kulikubali kabisa, you know what I’m bloody sayin’ ?”
“Ahh, hakuna anyemuogopa Jaka hapa bwana! Si umeona jinsi tulivyomdidimiza masumbwi kule Bills? We’ sema nini kifanyike wanaume tuingie kazini!” Muddy alimjia juu.
“Akh, si huyu Ng’ase anataka kuleta habari za kuogopa-ogopa hapa!” Tony naye alimjia juu huku akimtupia Ng’ase jicho la pembeni.
“Ah, mi siogopi! Nimetoa wazo hilo kwa kuwa jamaa ameonekana hajui lolote so sikuona sababu ya kuamsha mashetani yaliyolala, au vipi bwana? Halafu…kama tayari Joakim ameshaanza kuonesha dalili za kutaka amani, kwa nini na siye tusiachane naye ili tuendelee na harakati zetu bila kuwa na mashaka na nini Jaka anafanya?” Alphonce alitetea hoja yake.
“Hilo la Joakim tutalishughulikia baadae, ila kwa sasa maamuzi juu ya Jaka lazima yafanyike!” Tony alidakia.
“Sasa sisi mawazo yetu ndo yalikuwa hayo…kama wewe una wazo tofauti ndo uliweke wazi hapa!” Ng’ase alimjibu. Kwa mara nyingine Tony alimkata jicho, kisha akatazama pembeni.
“Hapa lazima tutafute njia ya kuhakikisha kuwa hata kama Jaka akijua kuhusu mambo haya, hatothubutu kumwambia hata mama yake mzazi.” Tony alisema huku bado uso wake ukionesha mawazo mengi.
Wenzake waliendelea kumtazama bila ya kusema neno.
“Toeni mawazo sasa! Hivyo mnavyokaa kimya maana yake nini? Mjue mi’ nikizama na nyie mnazama pia...mkiruhusu Jaka atuzamishe basi mjue kuwa hatuna chini ya miaka ishirini jela…” Tony aliiacha kauli yake ikielea hewani na kuwatazama wenzake kwa zamu.
Muddy alimeza funda la mate na kuuliza huku macho yakimtembea.
“Sasa wazo si umeshalitoa Tony? Suala hapa ni tunalitekelezaje hilo wazo…”
“Yeah Tony…Muddy is right. Swala sio wazo…swala ni namna gani ya kulitimiza!” Ng’ase alimwambia.
Tony hakujibu haraka. Alifikiri kwa muda kisha akawapa maelekezo kuwa kuanzia muda ule walitakiwa wafuatilie nyendo zote za Jaka na Joakim, na kuwa waripoti kwake tukio lolote litakaloonekana kuwa si la kawaida kutoka kwao.
“Muddy utakuwa na jukumu la Joakim na wewe Ng’ase utakuwa na jukumu la Jaka...” Alimalizia maelekezo yake.
“Halafu wewe utakuwa unafanya nini wakati sisi tunawafuatilia hao jamaa?” Ng’ase aliuliza.
“Mimi nitacheza na yule malaya wa Jaka...Moze.” Tony alijibu kwa sauti ya kunong’ona huku akiwa amemkazia macho Ng’ase. Kwa mara nyingine wale wenzake walitazamana kwa kutokuelewa.
“Ngoja kwanza Tony...kwani yule binti anahusika vipi tena...?” Hatimaye Muddy aliuliza kwa mashaka.
“Yea! Joakim si ameshaamua kuachana na yule demu? Na si’ tulikuwa katika mbinde hizi kwa sababu ya Joakim kumtaka yule binti...sasa Joakim hamtaki tena yule binti. Mi’ naona yule demu tumuache kama alivyo!” Ngase aliongezea.
“Sasa hivi swala lililobaki ni baina yetu na Jaka...yule demu hana umuhimu tena kwetu!” Muddy naye aliunga mkono hoja.
“On the contrary, yule demu ndio turufu yetu pekee ya kumyamazisha Jaka for good! ” Tony aliwajibu wenzake huku akichanganya lugha, akimaanisha kinyume na mawazo yao, Moze ndio alikuwa pekee ya kumfunga Jaka mdomo milele.
Wenzake waliendelea kumtazama kwa nyuso zilizoonesha wazi kuwa walikuwa wanataka ufafanuzi zaidi. Tony alianza kuranda-randa mle chumbani huku akiongea kwa sauti ya kunong’ona na kuwatazama wenzake kwa zamu.
“Swala hapa ni kuhakikisha kuwa Jaka anakosa kauli wala uwezo wa kufanya lolote iwapo ataamua kufuatilia nyendo zetu na kubaini kuhusu maswala yetu...kitu ambacho najua atakifanya kwa sababu sisi wenyewe tumeshafanya kosa la kuamsha udadisi wake juu ya hilo kwa kwenda kumtisha chumbani kwake kabla hatujawa na hakika kuwa anajua au la, au iwapo ni kweli alikuwa anafuatilia nyendo zetu au la...you know what I’m sayin’? Nd’o maana nataka nyendo zake yeye na za Joakim zifuatiliwe ili kuhakikisha hilo.”
Aliketi kitandani huku akiendelea kuongea.
“Iwapo Jaka atafanikiwa kugundua siri yetu, njia nzuri na rahisi kwake kutulipizia kisasi kwa yote tuliyomfanyia na pia kujihakikishia amani ya mapenzi yake na yule malaya wake ni kutoa ripoti tu kwenye vyombo vya dola...tena hata kwa simu tu, na sote tutauona mwisho wetu...”
“Lakini mpaka hapo bado sijaona ni jinsi gani yule msichana atahusika katika kujiokoa kwetu, Tony...swala ni kuachana kabisa na yule binti bwana...” Ng’ase alidakia huku bado akionesha kuwa hajaafiki swala la kumuingiza Moze katika mzozo ule.
“Yea, Tony...it will just complicate matters, bwana. Achana na huyo mwanamke kabisa!” Muddy alidakia akimaanisha kuwa kumwingiza Moze katika swala lile kutazidi kukoroga mambo bila ya sababu. Kama kwamba hakusikia maneno ya wenzake, Tony aliendelea kutoa mpango wake wa kumdhibiti Jaka, “...lakini vilevile, Jaka atashindwa kwenda kutoa ripoti popote hata kama atabaini ukweli iwapo na mpenziwe pia ni mtumiaji wa hayo madawa ya kulevya, you know what i’m sayin’? ”
Mohammed “Muddy” Shomari na Alphonce Ng’ase waliyasikia maneno yale ya mwisho ya Tony na wakabaki wakimkodolea macho rafiki yao kwa muda huku wakijaribu kuichuja maana halisi ya maneno yale. Taratibu walianza kuulewa mkakati wa yule mwenzao aliyekuwa akiwatazama kwa makini.
“Oh! Mungu wangu yaani unamaanisha...”
“Yaani ninamaanisha kuwa nitahakikisha kwamba na Moze pia anakuwa mtumiaji wa bwimbwi kama jinsi nilivyowafanya wengine, na hivyo atakuwa mteja wetu kama jinsi wengine walivyo hapa chuoni.” Tony alidakia kwa sauti ya kunong’ona huku mdomo wake ukifanya tabasamu baya sana.
“Duh!” Ng’ase aliishia kuguna tu.
“Ndio. Nikishatimiza hilo, Jaka hatakuwa na ujanja hata kidogo...nadhani sasa mmeipata picha kamili.” Tony alisema, na taratibu wale wenzake waliafikiana naye kwa vichwa.
Siku ile ile, bila ya kujua ni nini mahasimu wake walikuwa wanapanga dhidi yake na mpenzi wake, na kwa kuhofia vitimbi vingine kutoka kwa akina Tony na pia kwa kuwa alishadhamiria kuanza rasmi kufuatilia nyendo za wale maadui zake, Jaka alimshauri na kufanikiwa kumshawishi Moze kuhama pale chuoni kwa muda na awe anaishi nyumbani kwao. Walikubaliana kuwa kuanzia siku iliyofuatia Moze angehamia nyumbani kwao na angekuwa akihudhuria masomo kila siku pale chuoni na kurejea kwao.
Bila ya yeyote kati yao kujua, uamuzi ule uliepusha balaa kutoka upande mmoja na kulihamishia upande mwingine.
____________________
Siku nne baadaye, Moze aliongozana na kundi la wasichana wenzake wapatao watano hivi wakitoka darasani kuelekea bweni namba tatu, maarufu kama Doug Hammaskjold, ambamo yeye na Rose walikuwa wakiishi. Akiwa amezama kwenye mazungumzo na wenzake huku wakicheka kwa sauti, hakumuona Tony aliyekuwa amesimama miongoni mwa abiria waliokuwa wakisubiri mabasi kwenye kituo cha daladala kilichokuwa kikitazama na duka la vitabu la pale chuoni.
Kutoka pale kituo cha basi, Tony aliangalia saa yake na kugundua kuwa ilikuwa ni saa kumi na moja na dakika ishirini za jioni. Alijiondoa pale kituoni na kuelekea sehemu ya baa iliyokuwa kando ya bwalo la kulia chakula lililokuwa jirani na duka la vitabu la pale chuoni. Alishaona alichokuwa anakitaka. Kilichobaki kilikuwa ni kusubiri wakati muafaka tu. Na baada ya siku ile alijua kuwa Jaka hatakuwa tishio tena kwake.
Kule kwenye lango la kuingilia ndani ya bweni namba tatu, Moze aliagana na wale wenzake na kuendelea moja kwa moja kuelekea usawa wa baa ya Udasa ili akapandie daladala kwenye kituo cha Udasa kuelekea Mwenge, akiwaacha Rose na wale wasichana wengine wakiingia ndani ya eneo la bweni lile. Wakati wale wenzake wote wakielewa kuwa alikuwa anakaa kwao kwa muda kutokana na wazazi wake kusafiri naye kuwajibika kuwaangalia wadogo zake mpaka wazazi wake watakaporejea, ni Rose tu ndiye aliyeijua ukweli juu ya sababu halisi iliyomfanya Moze ahamie nyumbani kwao kwa kipindi kile.
_____________________
Saa tatu baadaye Rose alitoka bafuni akiwa amejifunga taulo lililofunika kiwiliwili chake kuanzia juu ya matiti yake ya duara na kuishia juu kidogo ya magoti yake. Kwa mwendo wa mbwembwe alielekea chumbani alimokuwa akiishi na Moze huku akipiga mbinja laini kuigiza wimbo wa muibaji maarufu wa bongofleva alioupenda sana, mkononi akiwa ameshika kibeseni kidogo cha sabuni, mswaki na funguo za chumba chao ambacho alikuwa amekifunga kabla ya kwenda bafuni.
Alifungua mlango na kuingia ndani huku akiusukuma kwa kisigino chake ili kuufunga na kuelekea moja kwa moja kwenye kabati la nguo huku akiendelea kupiga mbinja zake. Alikuwa katika hatua ya kutoa taulo alilojitanda huku akifungua mlango wa kabati lile kwa mkono wake mmoja wakati kwa kona ya jicho lake alipoona kitu kama kivuli kikipita haraka kutoka upande mmoja kwenda mwingine na haraka aligeuka kutazama upande wa mlangoni ambapo ndipo alipohisi kitu kile kilikuwa.
Alipata mshituko mkubwa sana alipoona kuwa hakuwa peke yake mle ndani na hapo hapo ukelele wa woga ulimtoka. Haraka sana mkono wa Tony ulichomoka na kuongeza sauti ya redio iliyokuwa kando ya kiti alichokalia pale pembeni ya mlango na ukelele wa Rose ukamezwa na sauti ya redio ile.
Huku macho yakiwa yamemtoka pima na midomo ikimcheza kwa wasiwasi, Rose alibaki akiwa amesimama huku amelishikilia kwa nguvu taulo pale kifuani pake akimkodolea macho yule jamaa. Akilini alikuwa akijiuliza ni jinsi gani yule mtu aliweza kuingia ndani ya chumba kile bila ya yeye kujua wala kuhisi mpaka dakika ya mwisho kabisa. Alihisi matumbo yakimkata kwa woga, na magoti yake yakaanza kumuishia nguvu yakifuatiwa na vile vidole vilivyoshikilia lile taulo pale kifuani. Alianza kutetemeka mwili mzima.
“Um…Umeingiaje humu wewe...toka, toka sasa hivi!” Rose alijaribu kumkemea Tony, lakini hata yeye mwenyewe alijua kuwa kwa sauti ile asingeweza kumtisha hata mtoto mdogo, kwani ilitoka kwa kitetemeshi kikubwa mno. Tony aliendelea kumtazama tu huku uso wake bado ukiwa na tabasamu baya lililodhihirisha nia mbaya zaidi. Taratibu aliinua mkono wake wa kushoto kutoka nyuma ya kiti alichokuwa amekalia na kuuweka juu ya paja lake. Macho yalizidi kumtoka Rose alipoona kisu kirefu na chembamba kikichomoka ghafla kutoka kwenye mpini wa “Spring Knife” uliokuwa kwenye mkono ule uliovikwa glovu nyembamba ya mpira.
“Hooooohhh…!” Rose alitoa mguno wa woga huku akirudi nyuma, na kwa wepesi usiotarajiwa Tony alimrukia na kumdaka koo kwa mkono wake wa kulia ambao nao pia ulikuwa umevikwa glovu. Rose aliihisi ncha kile kisu ikimtomasa-tomasa tumboni.
“Un…unataka nini kwah…kwah…kwangu wewe…?” Rose alibwabwaja kwa woga mkubwa kabisa.
“Kaa kimya na utaendelea kuishi!” Tony alimkoromea kwa sauti ya kuogofya. Rose alimeza funda la mate na kufinya macho kuzuia machozi yaliyoanza kumtiririka. Moyo ulikuwa ukimdunda kwa kasi ya ajabu na alijihisi kubanwa na haja ndogo.
“Sina haja na wewe Rose...” Tony aliendelea kumkoromea, na Rose alishangaa kumsikia Tony akimtaja kwa jina. “ ...shida yangu ni Moze...where is she?”
Alilegeza kidogo ile kabali na Rose alikohoa kwa nguvu huku akimjibu kwa woga mwingi kuwa Moze hakuwepo pale chuoni. Tony alimchapa kofi kali sana la uso kwa mkono wake wa kulia na kumbana tena koo.
“Usin’tanie wala usin’danganye mimi Rose...n’takuumiza! Moze yuko wapi. Si nimewaona mkirudi naye kutoka darasani jioni hii nyie?”
“Kweli hayupo, Tony…hayupo! Kaenda nyumbani kwao...kweli kabisa...naomba uniachie!” Rose alimjibu kwa kuomboleza, akilia wazi wazi.
“Kama unataka kupoteza maisha yako basi kwangu ndio njia ya mkato, you know what I’m sayin’? Sema upesi sana! Moze yuko wapi na kwa nini hayumo humu ndani saa hizi!” Tony alimnong’oneza kwa hasira huku akimsogezea uso wake kiasi mashavu yao yakagusana. Rose alifinya macho huku akijitahidi kuuweka uso wake mbali na ule wa yule muhuni huku akilia na kubwabwaja kuwa Moze hakuwepo pale chuoni kutokana na kusafiri kwa wazazi wake naye kulazimika kwenda kukaa na wadogo zake nyumbani kwao.
“Usin’danganye mimi wewe!” Tony alifoka na kumchoma Rose kwa ncha ya kisu chake kikali juu kidogo ya kitovu na damu ikaanza kumchuruzika.
“Kweli kabisa nikwambiavyo kaka’angu...Moze hayupo kabisa hapa chuoni sasa hivi...mi’ niko peke yangu...Oh, Mungu wangu...kwani kosa langu ni nini jamani?” Rose alizidi kujitetea na kulalama. Tony alimtomasa tena kwa ncha kali ya kisu chake shavuni na kuanzisha mchirizi mwingine wa damu.
“Kosa lako ni kuwa unasema uongo Rose...unasema uongo ili kumtetea Moze. Je, uko tayari kufa kwa ajili yake?” Alimuuliza kwa sauti ya kuogopesha.
“Hapana...hapana jamani, naomba unisamehe...” Sasa Rose alikuwa akilia kama mtoto. Tony alimtazama kwa makini, na akaona kuwa alikuwa anasema ukweli.
Alisonya kwa hasira na kulaani kwa tusi zito kitendo cha kumkosa Moze. Alijaribu kufikiria kwa haraka haraka ni hatua gani ifuate kwani sasa tayari alikuwa amekwisha potea stepu na kumpata tena Moze itakuwa vigumu sana. Rose aliendelea kulia huku akijaribu kujichomoa kutoka mikononi mwa Tony.
“Tulia!” Tony alimfokea, na kumshindilia ngumi ya tumbo. Rose alijipinda kwa maumivu huku akigumia kwa uchungu, na hapo hapo Tony alimnyanyua na kumtupia kitandani, taulo likimtoka na kumwacha akiwa uchi wa kuzaliwa. Rose alijaribu kupiga kelele kwa woga, akijua anaelekea anabakwa, lakini Tony alimrukia pale kitandani na kumlalia mgongoni huku akimbana mdomo wake kwa mkono wake wa kulia na akiwa amemuwekea ncha ya kisu chake shingoni.
“Tulia! Tulia kimya, la sivyo n’tachanachana kishingo chako hicho, pumbavu!” Tony alimnong’oneza kwa sauti ya kutisha sana, na mara moja Rose alitulia huku akimeza vilio vyake kwa taabu, macho yakiwa yamemtoka pima na moyo ukimwenda mbio vibaya sana.
“Umekuwa mtoto mbaya sana Rose...na mimi nimekasirika sana, you know what I’m sayin’...?” Tony aliendelea kumnong’oneza na Rose alizihisi pumzi zake nyuma ya shingo yake, mwili ukamfa ganzi kwa woga.
“...nimekasirika kwa sababu itanibidi nikufanyie wewe mambo niliyotaka kumfanyia Moze. Na yote hayo ni kwa sababu ni wewe mwenyewe ndiye uliyesababisha kwa kukataa kunieleza mambo ninayotaka unieleze, you know what I’m sayin’.mrembo?”
Rose alitikisa kichwa kwa nguvu huku akitoa miguno lakini Tony alikuwa amembana vizuri sana mdomo wake na hivyo hakuweza kusema lolote.
“Sasa nitaanza kwa kukubaka kwa sababu ndivyo nilivyopanga kumfanyia rafiki yako ...”
Na hata wakati akisikia maneno yale mabaya Rose aliuhisi uume wa Tony ukivimba nyuma ya mapaja yake na woga wake ukazidi maradufu, naye akazidi kujitutumua bila mafanikio huku akitoa miguno ya fadhaa.
“...jambo litakalokuokoa na kubakwa leo hii ni kuniambia ukweli tu, baby...you know what I’m sayin’...”
Rose alitikisa kichwa kwa nguvu sana kuashiria kuafikiana na wazo lile.
Tony alikaa kimya kwa muda huku akiwa bado amemlalia mgongoni kabla ya kumuuliza huku akimwachia mdomo wake taratibu.
“Najua ni kweli kuwa Moze hayupo hapa chumbani, jambo ambalo sijui ni kwamba amekwenda wapi...”
“Kwao!” Rose alijibu huku akitetemeka. Tony alimpa muda amalize kwikwi zake kabla ya kumuuliza tena.
“Nakuami. Sasa ni kwa nini amekwenda kulala kwao leo hii, na usiniambie habari ya kwenda kukaa na wadogo zake!”
“Kwa…kwa sababu...Jaka alimwambia kuwa...kuwa mtaweza kuja kumfanyia ubaya...” Rose aliangua kilio upya baada ya kutoa jibu hilo.
Hapo Tony alijua kuwa Jaka alikuwa amemzidi kete.
Kwa mara nyingine tena.
“Shit!” Alilaani huku akiinuka kutoka pale mgongoni kwa yule binti na kubaki akiwa amesimama katikati ya chumba kile huku uso wake ukisajili ghadhabu nyingi. Rose alikurupuka na kulinyakua taulo lake, akajisitiri mwili wake huku akilia kwa uchungu.
“Kaa hapo hapo!” Tony alimfokea huku akimnyooshea kisu na Rose aliruka kwa mshituko kisha akatulia pale kitandani huku akiwa anabubujikwa na machozi.
“Tafadhali naomba uondoke we’ kaka... mimi mbona sina kisa na wewe...?”
“Shut-the fuck-Up, mbwa koko wee! Huoni kuwa najaribu kufikiri hapa?” Tony alimkemea, na Rose aliruka kama kwamba amepigwa kwa karipio lile. Tony alikuwa akijaribu bila mafanikio kuelewa ni jinsi gani Jaka alijua kuhusu njama yake ile. Hakuweza kuamini kuwa Muddy na Ng’ase nao walikuwa wameamua kumgeuka na kumtahadharisha Jaka kuhusu dhamira yake ya kumdhuru Moze ili kumdhibiti Jaka. Lakini wakati huo huo alikumbuka ni jinsi gani wazo lake hilo lilivyopingwa vikali na wale wenzake...kabla ya kuwaelewesha na wakaelewa...au hawakuelewa? Au walijifanya wameelewa lakini tayari walikuwa wameshaamua kutokumuelewa?
“Shit!” Alilaani kwa sauti.
Kwa vyovyote Rose atawaeleza tu akina Jaka juu ya tukio hili la leo, kwa hiyo hata kama akina Muddy hawajamgeuka, Jaka atajua tu kuhusu mkasa huu...na akijua sijui atazusha balaa gani tena! Lazima Rose afungwe mdomo...lazima!
Nje ya mlango wa chumba kile zilisikika sauti za wasichana wengine wakipita kuelekea vyumbani mwao huku wakifanyiana utani kwa kelele. Rose aliruka kukimbilia mlangoni huku akipiga kelele za kuomba msaada, lakini kelele zake zilimezwa na sauti kubwa ya muziki uliokuwa ukitoka kwenye redio yake na Tony aliwahi kumdaka kabla hajaufikia ule mlango na kumtupia tena kitandani. Akamtandika makofi manne makali sana ya haraka haraka, na Rose aliangua kilio cha kwikwi na kukata tama. Tony alikuwa amemkazia macho ya ghadhabu huku akiwa amemuwekea ncha ya kisu chake shingoni na akimwashiria kuwa akae kimya kwa kuweka kidole chake cha shahada juu ya mdomo wake.
Sauti za wale wasichana zilipopotea Tony alisimama taratibu na kumtazama kwa muda mrefu bila ya kusema lolote huku Rose akimkodolea macho ya woga na midomo ikimcheza. Kisha alimuona Tony akichomoa kichupa kidogo kutoka mfukoni mwake na kutoa kidonge kimoja kati ya kadhaa vilivyokuwa ndani ya kichupa kile. Alikibonyeza baina ya kidole chake cha gumba na shahada na kubaki na unga laini mweupe baina ya vidole vile.
Kwa mshangao mkubwa Rose alimshuhudia Tony akiupeleka puani kwake unga ule na kuuvuta wote kwa mkupuo mmoja.
Heh!
Tony alifumba macho yake huku akitoa mguno wa burudani kutokana na hisia alizozipata kutoka kwenye unga ule huku akitikisa kichwa chake. Taratibu alifumbua macho yake na kumtazama Rose aliyekuwa akimkodolea macho kwa mshangao uliochanganyika na hofu kubwa, kwani jambo alilolishuhudia pale lilimaanisha kitu kimoja tu ambacho hakutegemea kukiona maishani mwake ukiachilia mbali kutoka kwenye sinema na kusoma kwenye vitabu vya waandishi wa nchi za magharibi.
Tony alikuwa anatumia madawa ya kulevya!
Pamoja na kwamba iwapo angetokea mtu akamwambia kuwa Tony alikuwa anatumia madawa yale asingeshangaa hata kidogo, bado kitendo cha kumuona kwa macho yake akiutumia unga ule hali wakiwa wawili tu mle ndani kilimletea hofu isiyosemekana. Mwili wote ulimwingia baridi na alihisi kichechefu kikali sana.
“...you know what I’m sayin’ ...?” Tony alikuwa akimsemesha huku akimsogelea.
Rose alishtuka na kukurupuka kutoka pale kitandani, akijaribu tena kukimbilia mlangoni huku akiwa amelikumbatia kwa nguvu taulo lake kuusitiri mwili wake. Kwa hatua moja Tony aliruka na kusimama mbele yake huku akimnyooshea kisu kwa vitisho. Rose alisimama akikikodolea macho kile kisu kwa woga huku akilia na akibwabwaja maneno yasiyoeleweka. Tony alianza kumsogelea huku akiwa anamlengeshea kile kisu, naye alikuwa akirudi nyuma kwa woga.
“Unataka kuishi, Rose?” Tony alimuuliza huku akimsogelea.
Rose aliitikia haraka haraka kwa kichwa huku machozi yakimbubujika. Tony alitoa kicheko cha kebehi huku uso wake ukionesha kufurahishwa sana na hali ile.
“Mi’ n’takuacha uishi iwapo utakuwa tayari kushirikiana nami katika kazi yangu, you know what I’m sayin’?”
Rose aliendelea kurudi nyuma huku akiitikia maneno yale kwa kichwa.
“Wewe hutamwambia Moze wala Jaka kuwa mimi nilikuja kumsaka Moze hapa...actually, hutamweleza mtu yeyote kuhusu mambo yaliyotokea humu ndani leo hii, you know what I’m sayin’...?”
Kwa mkono wake wa kulia alitoa kidonge kingine na kukibonyeza na kunusa tena ule unga mweupe huku akitoa miguno ya kuburudishwa na unga ule . Rose aliendelea kurudi nyuma na kuitikia kwa kichwa huku woga ukizidi kumtawala.
“...na siku Moze akija...you know wharrasssayeeein’...siku akija tu…utahakikisha kuwa unamkawiza hapa na unakuja kuniita popote pale ili nije nimfanyie vitu vyangu, okay?” Tony aliendelea kumsemesha taratibu huku maneno yake yakitoka kwa tabu kama kwamba ulimi ulimuwia mzito ghafla. Rose alifika mwisho wa chumba kile na kubaki ameegemea ukuta huku akitikisa kichwa, safari hii kwa kuyapinga yale maneno ya Tony.
“No! Ooh, no way! Hapana! Hapana jamani...sitaki, sitaki!” Alibwata huku macho yakiwa yamemtoka pima.
Kwa hatua moja Tony alimrukia pale ukutani na kumbana koo kwa mkono wake wa kulia huku akimuwekea ncha ya kisu chake kikali ndani ya tundu yake ya pua na kumkemea kwa ukali hali nyuso zao zikiwa zimetengana kwa milimita chache sana.
“Don’t you ever say sitaki to me again, you know what I’m sayin’...? Ever!” Alimkemea vikali, akimkanya asirudie tena maishani mwake kumtamkia neno ‘sitaki’, na Rose alitumbua macho kwa woga huku akijaribu kupiga ukelele ambao haukutoka, kwani sauti ilimkauka ghafla. Haraka sana Tony alibadilisha mkono na kumbana koo kwa mkono wake wa kushoto ambao sasa ulikuwa umeshika kile kisu na kumuelekezea ncha kali ya kisu kile kwenye sikio lake la kushoto. Rose alitulia kimya na kubaki akitembeza mboni za macho kuufuata mkono wa kulia wa Tony, ambao sasa ulikuwa umeshika kidonge kingine cheupe. Tony alimsukumia usoni kile kidonge.
“Sasa wewe na mimi tutapata “dope” pamoja kwanza, you know what I’m sayin’?” Alimwambia huku akikibinya kile kidonge na kutoa unga ambao alimsogezea taratibu puani kwake.
Khah!
Rose alitikisa kichwa huku akitupa miguu yake kwa nguvu kujaribu kujiepusha na balaa lile la kuvutishwa unga wa kulevya. Lakini kila alivyotikisa kichwa chake ndivyo ncha kali ya kisu cha Tony ilivyozidi kumchoma na kumtoa damu. Kelele zake hazikutoka kabisa kwani Toni alizidi kumkandamiza koo kwa mkono wake wa kushoto.
“Tulia, Pusi mkubwa! Tulia!” Tony alimkoromea huku akizidi kumbana pale ukutani. Rose alifanikiwa kuchomoa mkono wake mmoja na huku akiwa amelishikilia taulo kifuani kwa mkono mwingine, alimtupia Tony mkono wake usoni huku akiwa amechanua vidole vyake vyenye kucha ndefu, lakini Tony alikwepa shambulio lile na hapo hapo akamchanja shingoni kwa kisu chake kikali. Rose alitoa kilio cha maumivu huku akihisi mchirizi wa damu ukiteremka kutoka pale alipochanjwa na kumlowesha kifuani. Hapo hapo Tony alilaza ubapa wa kisu kile juu ya koo lake na kumshurutisha atulie. Rose alibaki akitweta na kutembeza macho huku midomo ikimtetema na moyo ukimwenda mbio wakati akiushuhudia mkono wa Tony ukimsogezea ule unga puani kwake.
“Hapana... si..ttakii…!” Rose alibwabwaja bila mafanikio wakati Tony akimuwekea ule unga chini ya tundu za pua yake.
“Usiogope mrembo wangu...utanishukuru sana baadaye kwa kukupatia raha hii...you know? ” Tony alikuwa akimwambia kwa sauti ya kubembeleza. Rose alibana pumzi ili asiuvute ule unga haramu ndani ya mapafu yake, lakini hakuweza kubana pumzi kwa muda mrefu na alipozidiwa alivuta pumzi nyingi kwa ghafla, na hapo unga wote uliokuwa chini ya pua yake ulivutwa ndani ya mapafu yake. Macho yake yalisajili woga mkubwa sana, kwani alijua kuwa tayari alikuwa ameshauvuta unga ule. Ameshavuta unga wa kulevya…dawa ya kulevya…unga haramu! Alianza kutetemeka mwili mzima huku akihisi kuishiwa nguvu za mikono na miguu.
“Ooh! Ttch, ttcha, ttcha...unaogopa mrembo wangu? Mbona kuna wenzako wengi tu wanaotumia hii kitu na wanaishi kama kawaida tu? Usiwe mwoga tu…ukiwa mwoga basi ndipo utakapodhurika...kama Margareth...unamkumbuka Margareth?” Tony alikuwa akimwambia kwa kuchombeza, na Rose akamakinika kwa maneno yake yale. Alimkazia macho ya kuuliza huku akimtazama kama kwamba ndio kwanza anamuona. Kichwani mwake alikuwa akihisi vitu vya ajabu-ajabu tu ambavyo hajawahi kuvihisi hata siku moja...na kweli ilikuwa ni hisia ya ajabu...hisia ya raha isiyo kifani...raha ya ajabu.
Lakini Tony alikuwa anamsemesha...anamsemesha nini? Margareth? Margareth...?
“Humkumbuki marehemu Margareth, Rose? Marehemu Margareth Mfinanga...?”
Hapo Rose alikumbuka. Margareth Mfinanga, mwanafunzi mwenzao aliyejiua kwa kunywa sumu nyumbani kwao miezi michache iliyopita...
“Hah!” Rose alitoa sauti ya mshangao pale picha iliyokuwa ikichorwa na Tony ilipojidhihirisha akilini mwake.
Ina maana Margareth alijiua baada ya kuvutishwa unga wa kulevya na Tony? Kama anavyonifanyia mimi hivi sasa?
Lakini mawazo yake hayakuwa yakienda sawa sawa kichwani mwake, kwani alizidi kupata mchanganyiko wa zile hisia za ajabu zilizomfanya ashindwe kutafakari zaidi juu ya Margareth...
“Anhaa....umemkumbuka sasa, eenh?” Tony alimwmabia baada ya kuona mabadiliko usoni kwake, na kuendelea, “…basi Margareth alikufa kutokana na woga wake wa kuyoyoma nah ii kitu....you know what I’m sayin’? Sasa sitaki na wewe uwe kama Margareth...” Hapo hapo akamsogezea tena unga ule puani kwake. Rose alitikisa kichwa na kubwabwaja kwa taabu, kwani sasa mdomo wake uliuhisi mzito sana.
“Hapana...sit...takih! Hai...wez...zekannn...kanih...”
“Ooh! Inawezekana sana tu mrembo wangu, tena sana tu...! Au unataka kuwa kama...kama...kama nani tena huyu...? Yaa....unataka kuwa kama Mwantumu Mlawa?” Tony aliendelea kumnong’oneza huku akimuwekea tena unga ule puani.
Eh, kumbe na Mwantumu naye ilikuwa hivi…?
Rose alichanganyikiwa, na akajikuta anauvuta bila kipingamizi ule unga.
Oh, Mungu wangu…n’shanasa tena miye sasa!
Hapo wazo lilimpitia kichwani mwake kuwa akiendelea kumuendekeza shetani yule basi atakuwa ni mtumwa wa yale madawa yake ya kulevya milele. Na hapo alielewa ni kwa nini Mwantumu Mlawa na Margareth Mfinanga waliamua kujiua...
Kwa nguvu zake hafifu zilizobakia alimshindilia goti la korodani yule bazani, na Tony alitoa yowe la maumivu huku akipepesuka akiwa amejishika uume wake. Aliinua uso wake kwa hasira na kumtazama yule binti. Rose aliishiwa nguvu na aliangukia magoti pale sakafuni huku akitweta. Alijihisi kama kwamba alikuwa akielea hewani huku zile hisia za ajabu zikizitawala fahamu zake. Alikaa chini na kuinua uso wake kuelekea darini, nako aliona vitu vingi vya ajabu vikimshukia usoni mwake. Alifumba macho na kujisika kichwa mithili ya mtu aliyekolewa na midadi.
Ule unga ulikuwa ukimlevya kwa kasi sana.
Tony alimtazama yule binti na mara uso wake uliokuwa umekunjamana kwa ghadhabu ukalainishwa na tabasamu pana, kwani alijua kuwa alikuwa amefanikiwa. Kuanzia wakati ule Rose alikuwa "mteja wake", na hivyo angeweza kujipatia fedha zaidi kwani kila mara Rose atakapohitaji dozi ya unga ule wenye raha itabidi amtafute yeye; na yeye hatompa bure…vile vile, sasa Rose atafanya lolote atakalomtaka afanye…
Tabasamu lake likabadilika na kuwa kicheko.
Alimsogelea Rose ambaye sasa alikuwa akigaragara pale sakafuni bila ya kujitambua. Rose alifumbua macho na kumuona Tony akiwa amemuinamia huku akitabasamu, naye akatabasamu kipumbavu bila ya kuelewa ni kwa nini alikuwa anafanya vile. Tony alipiga goti kando yake pale sakafuni na kuanza kumpapasa mapaja yake.
Rose alijua kuwa lile halikuwa jambo zuri, lakini hakuelewa kwa nini lilimfanya ajihisi burudani namna ya hali ya juu. Na hata pale wazo lile lilipokuwa linapita kichwani mwake, wazo jingine likadakia na kumkumbusha kuwa huwa anahisi burudani zaidi anapofumba macho.
Akafumba macho.
"Unaona jinsi inavyopendeza unapopata madope mrembo wangu?" Rose alimsikia Tony akiuliza kwa sauti ya kunong'ona huku akiendelea kumpapasa sehemu nyeti za mwili wake, naye akabaki akibwabwaja kurudia tena na tena yale maneno mawili ya mwisho yaliyotamkwa na Tony huku akizidi kujihisi raha isiyo na kifani.
"…tena hauko peke yako…" Tony aliendelea kumtomasa tomasa huku akimnong'oneza, "… hata Grace Wanjau pia anatumia madope…anatumia hii kitu…"
"Grace Wanjau…madope…" Rose aliyarudia maneno yale bila ya kujitambua.
"Na Imelda Athanas pia…" Tony aliendelea kumtajia wasichana wengine wanaotumia madawa ya kulevya pale chuoni huku akizidi kumpapasa. Sasa Rose alikuwa amelegea kabisa, hakuwa na habari na mambo aliyokuwa anafanyiwa naTony wakati ule.
Taratibu Tony alilivutia pembeni lile taulo alilokuwa amejifunga Rose na kumuacha Rose akiwa amelala pale chini akiwa uchi wa kuzaliwa.
Alimtazama yule binti kwa macho ya uchu huku akifungua mkanda wa suruali yake…
__________________
Cocaine ni madawa ya kulevya yenye nguvu sana yatokanayo na mmea aina ya coca upatikanao zaidi huko Amerika ya Kusini, kwenye nchi kama vile Venezuela,Peru, Kolombia na Panama. Mmea huu hukua kwa urefu wa kiasi cha futi zipatazo tatu hadi saba na huwa na aina tofauti, kama vile "Huanaco Coca", ambao huwa una mchanganyiko wa rangi za kijani na kahawia na wenye majani yenye urefu upatao inchi moja hadi tatu.
Aidha, kuna "Truxillo Coca", ambao huwa na rangi ya kijani iliyofifia na majani madogo zaidi ya yale ya Huanaco Coca, na hunukia kama majani ya chai.
Majani ya aina zote hizi mbili za Coca ni machungu pindi yatafunwapo na humsababishia mtafunaji hisia ya ganzi kwenye ulimi na mdomoni.
Watu wengi wa nchi hizi za Amerika ya Kusini hasa kule mashambani, hutafuna majani haya pamoja na ndimu ili kuwafanya wasijisikie uchovu au njaa. Majani ya m-coca, pindi yakaushwapo huweza kutumika kwa dawa ambapo hutoa madawa kadhaa yenye manufaa kwa binadamu kama vile Tropacocaine, Hygrine na Cocaine yenyewe.
Ingawa hapo mwanzo Cocaine ilikuwa ikitumika kwa shughuli za ki-matibabu, matumizi ya madawa haya yamekuja kugundulika kuwa na madhara zaidi kwa mwili wa binadamu kuliko manufaa. Hii ni kutokana na ugunduzi kwamba ingawa Cocaine inaweza kutumika kwa kuzuia maumivu wakati wa Operesheni kadhaa mahospitalini kwa kusababisha mishipa midogo ya damu kukaza na hivyo kupunguza kutoka kwa damu wakati wa operesheni, madhara yake ni makubwa zaidi kwa binadamu kiasi kwamba nchi zote duniani zimepiga marufuku utumiaji wa madawa haya kwa shughuli zozote zile, ziwe za kimatibabu au za kujiburudisha kwa kutumia madawa hayo kama kilevi cha kujiletea faraja. Cocaine ni kichangamsho kinachomfanya mtumiaji awe na bashasha fulani. Huongeza utendaji wa fahamu za kibinadamu au huzichangamsha kwa hali ya juu kabisa. Vile vile utumiaji wa madawa haya husababisha kuongezeka ghafla kwa mapigo ya moyo na huzidisha mkandamizo wa damu.
Utumiaji wowote wa cocaine, pamoja na kuleta madhara katika mwili pia humjengea mtumiaji wa madawa hayo matamanio ya ajabu kwa madawa hayo kiasi cha kumfanya ashindwe kufanya kitu chochote bila ya kutumia madawa hayo. Kwa maana hiyo, mara mtu akishaanza kutumia madawa hayo, huwa ni vigumu sana kuacha; kwa lugha ya kitaalamu, watu wa aina hii huitwa "Drug Addicts", yaani watu wanaoishi kwa kutegemea madawa ya kulevya.
Watumiaji wa madawa haya huwa wanafanya hivyo kwa kutaka kufaidi ile hisia ya raha ya hali ya juu ipatikanayo katika hisia za mtumiaji muda mfupi baada ya kuvuta au kutumia cocaine. Wengi kati ya watumiaji wa madawa haya walianza kutumia kwa vile tu marafiki zao walikuwa wanatumia, lakini baadaye wakajikuta kuwa ni watumwa wa madawa haya.
Cocaine hii ya haramu mara nyingi huwa katika hali ya unga mweupe laini wenye madawa aina ya Cocaine Hydrochloride, ambayo ndiyo yenye madhara yote ikichanganywa na madawa mengine. Mara nyingi hutumiwa kwa kunuswa puani, au kwa kutumia sindano ambapo cocaine ikiwa katika hali ya maji maji hudungwa kwenye mishipa ya damu ya mtumiaji ili kupata hisia ya hali ya juu zaidi kwa haraka zaidi.
Watumiaji wa madawa haya hufanya hivyo kwa kuitafuta ile "hisia ya kujiweza" au euphoria itokanayo na madawa haya. Hisia hii humfanya mtumiaji ajihisi mwepesi zaidi, makini na mwenye uwezo wa kufanya lolote lile hapa duniani. Wengine hujiona kuwa na uwezo wa kufikiri zaidi wakishatumia madawa haya kuliko kawaida.
Lakini mara nyingine, utumiaji wa cocaine humletea mtumiaji hisia kali za mchecheto, papara na hofu zisizo na msingi.
Kwa kawaida madhara ya unga huu huondoka kichwani kwa mtumiaji baada ya dakika ishirini au arobaini hivi, kutegemea na uwezo wa fahamu za mtumiaji kuhimili madawa hayo; baada ya muda huo, mtumiaji hujihisi kufadhaika na huwa mnyonge sana, na matokeo yake hutaka sana kupata dozi nyingine ya unga ule ili kurudisha tena zile hisia za kujiweza. Hivyo mtumiaji hujikuta akiendelea tu kutumia madawa haya na kuwanufaisha wafanya biashara ya unga huu haramu.
Ni hali hii ya uraibu wa madawa haya ndio iliyoifanya, na inayoendelea kuifanya, biashara ya madawa haya, sio cocaine tu, bali pia mandrax, heroin na mengineyo, kuwa ya faida sana. Biashara ilivyozidi kukua, waendeshaji wakaitawanya sehemu nyingi za dunia ili kuzidi kuvuna faida kutokana na soko pana la biashara hii.
Utumiaji wa unga au madawa haya ukizidi huweza kusababisha matatizo makubwa ya akili ambayo huwafanya wale watumiao kuwa na mashaka na woga kila wakati. Hisia hii huweza kuendelea kwa mawiki au hata miezi tangu kutumiwa kwa madawa hayo.
Kazi kubwa kwa wauzaji wa madawa haya ni kuwapata wateja, lakini mara wakishawapata wavutaji wa unga au madawa hayo, huwa ni kazi ya wateja hao kuwatafuta wafanyabiashara hao kwa kila hali mpaka wapate madawa hayo, kwani mtu akishavuta unga ule, ni vigumu sana kuacha kuwa mteja. Na pindi akisha kuwa mteja, atatoa kiasi chochote ili apate japo dozi kidogo tu ya unga ule haramu.
_____________________
Rose alifumbua macho taratibu na kuyatembeza ndani ya chumba chake. Alihisi maumivu karibu mwili mzima na alishangaa kujikuta amelala sakafuni akiwa uchi. Alijiinua taratibu na kuegemea ukutani. Alipopeleka mkono wake katika sehemu ya uuke wake aligundua mara moja kuwa alikuwa ameingiliwa kimwili bila yeye mwenyewe kujitambua, ingawa kwa mbali alikuwa ana kumbukumbu ya kufanya tendo hilo. Alikunja uso na kuangaza tena mle chumbani huku akihisi kichefuchefu na woga mwingi. Tony alikuwa akimwangalia huku akitabasamu kwa dharau akiwa amekalia kiti kile kile alichokuwa amekalia wakati Rose alipomuona kwa mara ya kwanza ndani ya chumba kile. Uso ulimbadilika na macho yakamtumbuka. Alilinyakua taulo lake lililokuwa kando yake pale sakafuni na kujifunika mwili wake na kubaki akimkodolea macho yule muhuni huku midomo ikimtetemeka.
“W-We! Umenifanya nini…! Eeenh? Sema upesi…!” Hatimaye aliropoka kwa woga uliochanganyika na hasira huku akiendelea kumkodolea macho Tony, kwani alishapata jibu la kilichotokea baina yake yule jamaa mle ndani.
Tony aliendelea kumchekea kwa dharau. Rose alitikisa kichwa chake kwa nguvu kuukataa ukweli uliozidi kujijenga akilini mwake. huku na huku kwa kuchanganyikiwa na kumtazama tena Tony aliyekuwa akiendelea kumchekea kwa dharau na kebehi.
“Um, Umenibaka! Umeniba…” Hakuweza kumalizia kwani uzito wa jambo lile ulikuwa ukizidi kumwelemea kadiri alivyokuwa akilitamka neno lile na akaishia kuangua kilio huku akificha uso wake kwa viganja vya mikono yake. Tony alizidi kupandisha sauti ya redio iliyokuwa mle chumbani huku akiendelea kumtazama kwa dharau.
Kwa uchungu Rose alijitahidi kujizuia kulia na kumtazama Tony kwa hasira.
“Ondoka humu ndani…Ondoka upesi, mbwa we!” Alimkemea kwa hasira huku machozi yakiendelea kumbubujika, na hasira zilimzidi alipoona kuwa Tony khakumtilia maanani hata kidogo. Na hata pale alipokuwa akizidi kumtazama kwa hasira yule jamaa, alimuona Tony akimtikisia kichwa kwa masikitiko ya kejeli.
“Kweli unataka niondoke mrembo wangu? Umeisahau raha ya ajabu niliyokupa muda mfupi tu uliopita? Nikiondoka utapata wapi tena raha kama ile, eeenh? Hapana mrembo wangu… mimi nadhani wewe hutaki niondoke, ila hutaki kusema…sasa na mimi kwa kukusaidia, siondoki!” Alimwambia kwa mbwembwe, na Rose hakuamini masikio yake. Alibaki mdomo wazi huku akimtazama yule jamaa.
Huyu jamaa kichaa nini?
“Ooo yeah! Ukweli unaitaka sana ile raha uliyoipata kwenye ule unga Rose…na pia unaitaka tena ile raha niliyokupa hapo chini…sa’ kwa ni’i usiwe mkweli tu kwa nafsi yako mrembo, you know what I’m sayin’? ” Tony alizidi kumchombeza kwa ungeaji wake mithili ya wa kibogoyo, na akazidi kumchefua Rose.
Kwa fadhaa kubwa Rose alijikubalia moyoni kuwa alikuwa ametendewa unyama na udhalilishaji mkubwa kabisa mle ndani usiku ule, na hakuwa na namna ya kufuta kile kilichomtokea.
Ee Mungu wangu wa mbinguni…kwa nini lakini umeacha nikutwe na mambo haya?
Mara alihisi nguvu zikimwisha mwilini kama jinsi puto linavyoishiwa na upepo. Alibaki mdomo wazi akimtazama yule jamaa ambaye bado alikuwa akitabasamu kwa dharau. Alijaribu kujiinua akashindwa. Alijaribu kuinua mkono wake ili ajizibe mdomo kuzuia matapishi aliyokuwa akiyahisi kumjia kwa kasi lakini mkono wake ulikuwa mzito sana na hakuweza kuusogeza hata kwa milimita moja. Kwa uchungu alianza kulia huku akijitapikia kama mtoto mdogo na Tony akiendelea kumtazama kwa dharau.
Rose alibaki akiwa ameegemea ukuta huku akiwa ametawanya miguu yake pale sakafuni akitweta, matapishi yalikuwa yamemtapakaa kuanzia chini ya mdomo wake, kifuani, tumboni, mapajani na hata pale sakafuni. Akiwa ameishiwa nguvu kabisa pale sakafuni, alianza kujihisi unyonge wa hali ya juu uliochanganyika na uchovu wa ajabu.
Ah, sasa unyonge gani tena huu jamani…!
Alijikuta akiikumbuka ile raha na faraja ya ajabu aliyoipata muda mfupi uliopita baada ya kuvutishwa ule unga wa ajabu.
Hivi kweli inawezekana mtu kupata faraja kama ile hapa duniani…?
Simanzi ilimtawala alipogundua kuwa alikuwa anatamani kupata tena faraja ile iliyotokana na kuvuta unga ule wa haramu. Hali ile ilimtia woga mkubwa na akaanza kutetemeka mwili mzima.
Ina maana na mimi ndio nimeshakuwa mlevi wa madawa ya kulevya? Coccaine! Lakini…si nimevuta kidogo tu! No...hapana, sijavuta…nimevutishwa…sasa kwa nini tena na mimi nautamani?
Muda wote huo Tony alikuwa akimuongelesha lakini yeye hakuwa akitilia maanani maongezi yake.
Mungu wangu! Kwa nini ? Kwa nini nimekubali huyu shetani anivutishe maunga yake haramu? Oh! Mungu wangu! Mungu nisaidie nisitamani tena…Mungu wangu….
Taratibu alianza kulia tena huku akijaribu kukabiliana na kizunguzungu kilichokuwa kikimjia kwa nguvu sana.
Lakini ilielekea kama kwamba Mungu hakuwa upande wake, kwani ile hamu ya kuuvuta tena ule unga ilizidi kumkolea kadiri kile kizunguzungu kilivyokuwa kikizidi kumwelemea, na kadiri alivyokuwa anajitahidi kujizuia, ndivyo unyonge ulivyozidi kumtawala. Alibaki akibubujikwa machozi huku akimtazama Tony kwa shingo upande huku akihisi kichwa kikimuwia chepesi sana. Alikuwa kama mbwa aliyekutana na Chatu, na akajua kuwa hana la kufanya isipokuwa kukubali kuwa chakula cha Chatu tu.
Huku akiendelea kumtazama kwa dharau Tony alidondosha kifuko kidogo cha nailoni kilichokuwa na ule unga haramu ndani yake pale sakafuni, sio kidonge kama kile alichomvutisha hapo mwanzo.
Huku akielewa fika ni kitu gani kilikuwa ndani ya kifuko kile, Rose alikitazama kifuko kile na kumeza funda kubwa la mate huku akihisi kasi ya mapigo ya moyo wake ikiongezeka. Alifumba macho na kugeuza uso wake pembeni katika jitihada ya kushindana na matamanio ya kukiokota kile kifuko, kukirarua na kuunusa kwa pupa unga ule. Machozi yalizidi kumbubujika.
“Tafadhali sana nakuomba uondoke Tony…Please…!” Alibwabwaja huku akiwa amefumba macho yake, lakini mara ile ile aliyafumbua na kugeukia kule alipokuwa amekaa Tony, kwani hata yeye mwenyewe hakuitambua sauti yake kwa jinsi ilivyotoka kwa mkwaruzo na kitetemeshi cha hali ya juu. Tony alikuwa akimuangalia kwa makini, akiangalia jitihada yake ya kushindana na tamaa ya kupata “dozi” nyingine ya unga ule haramu.
Taratibu Rose alishusha macho yake na kukitazama kile kifuko chenye ule unga mweupe kilicholala pale sakafuni. Moyo ulimwenda mbio na alianza kuhema kwa nguvu.
Matatizo gani haya…? Kitu gani kitaniokoa kutoka kwenye madhila haya? Au nikiuvuta tena ule unga hali hii itaondoka…? Lakini ule ni unga wa haramu…sitakiwi kuuvuta wala kuutazama…!
Kwa taabu sana Rose alianza kujivuta kuusogelea ule unga. Mwili wote aliuhisi mzito wakati akitambalia tumbo na kuacha mgongo na matako yake vikiwa wazi kukisotea kile kifuko chenye ule unga mweupe ambacho Tony aliangusha karibu sana na miguu yake. Alinyoosha mkono wake ili akichukue huku akitweta kwa uchovu, nia yake wakati ule ilikuwa ni kukirarua kile kifuko na kuusukumia puani kwa pupa ule unga uliokuwa ndani yake.
Mara ile ile Tony alishusha mguu wake na kukikanyaga kiganja chake ambacho tayari kilikuwa kimeshakikamata kile kifuko. Kwa uchungu na mshtuko Rose aliinua uso wake na kumtazama kwa macho ya kuuliza. Taratibu Tony aliinama na kumsogezea sura yake mbaya usoni huku bado mguu wake ukiwa umekanyaga mgongo wa kiganja cha msichana yule aliyelalia tumbo bila nguo pale sakafuni.
“Unaijua thamani ya unga uliomo ndani ya kifuko hicho mrembo wangu?” Tony alimuuliza kwa sauti ya kunong’ona huku akitabasamu kikatili. Rose alibaki akimtazama kwa mshangao huku akiwa amefinya uso kwa maumivu ya kukanyagwa kiganja chake na akitweta kwa hamu ya kuumiminia unga ule ndani ya tundu za pua yake.
“Thamani yake ni buku kumi na tano…unazo ?” Tony aliendelea kumueleza kwa sauti ile ile ya kunong’ona, akimaanisha kuwa thamani ya unga ule ilikuwa ni shilingi elfu kumi na tano.
“Ndio! Ndio…ninazo. Nipe…! Usinikanyage tafadhali…!” Rose alijibu kwa pupa huku akitikisa kichwa kama vile Tony alikuwa akimchelewesha kwa maswali yake.
“Sawa...lakini kwa sasa sitaki pesa. Nataka ufanye vile nitakavyokueleza, you know what ‘am sayin’? ”
Rose aliafiki kwa kichwa haraka haraka huku akibubujikwa na machozi.
“That’s my girl! Mi’ namtaka Moze, you know what am sayin’? Wewe imekuwa bahati mbaya sana kwako kuwepo humu ndani badala yake, you know what am sayin’…sasa siku Moze akija tu, nataka uje unijulishe haraka sana, you know what am sayin’?”
“Sawa! Sawa…lakini mi’ sijui unakaa chumba gani…” Rose alijikuta akikubali kila alilokuwa akielezwa ili tu apate kuondokana na mateso yale na kujipatia tena ile faraja ya upeo wa juu kabisa aliyowahi kuipata katika maisha yake.
“Sitaki uje chumbani kwangu, Pusi wee! Uje pale Baa kando ya Kafeteria, unaelewa?”
Rose alikubali kwa kichwa huku akiwa ametumbua macho.
“Kila siku mi’ nipo pale kuanzia saa tatu ya usiku…sawa?” Tony aliendelea na Rose aliafiki tena kwa kichwa, kabla ya kuongezea: “Sawa…nitakuja kukwita Moze akija…nipe basi tafadhali!”
“Bado sijamaliza mrembo wangu…sitaki umueleze mtu yoyote kuhusu habari hii, umenielewa wewe? Ukisema tu, sikupi tena dozi nyingine ya unga maishani mwako, halafu tuone kama utaendelea kuishi hapa duniani, nyau wee!” Tony alimkoromea, kisha aliinua mguu wake kutoka kwenye kiganja cha Rose, ambaye kwa mikono ya kutetemeka alianza kukirarua kwa papara kile kifuko, akatoa kiasi kikubwa cha unga ule na kuupeleka puani kwake huku akihema kwa nguvu. Tony alimdaka mkono kabla haujaufikisha unga ule puani, na Rose aliinua uso wake na kumtazama kwa mshangao uliochanganyika na ghadhabu.
“Usiwe mjinga wewee! Ukibwia unga wote huo kwa mkupuo utakufa sasa hivi! Huo utautumia leo na kesho. Kesho kutwa nitamtuma kijana wangu akuletee dozi nyingine, you know what am sayin’?”
“Oke…Oke…h!” Rose alijibu kwa papara huku akiona maelezo ya Tony yalikuwa yakimchelewesha tu. Lakini bado Tony aliendelea kuushikilia mkono wake, naye alianza kuuvuta ili Tony auachie.
“Na hiyo kesho kutwa utayarishe kabisa kiasi cha pesa nilichokutajia, sawa mrembo wangu ?"
“Sawa!”
Tony alimpimia kiasi kidogo cha unge ule, kisha akamuachia mkono wake. Alijiegemeza kitini na kumuangalia yule binti akiupeleka ule unga aliompimia puani mwake na kuuvuta kwa nguvu huku akifumba macho na kutikisa kichwa.
Tabasamu jingine la ushindi likashamiri usoni kwake, kwani alijua kuwa pale alikuwa amefanikiwa. Jaka alikuwa amechelewesha tu mafanikio ya mpango wake wa kumpata Moze, lakini hakuwa ameuzima moja kwa moja. Taratibu alitoka nje ya chumba kile akimuacha Rose akigaragara sakafuni huku akiwa amefumba macho akiburudika na maruweruwe ya unga ule haramu.
Nje ya chumba kile aliangaza taratibu pande zote za korido na kufarijika baada ya kuona kuwa hakukuwa na mtu yeyote aliyemuona akitoka mle ndani. Aliangalia saa yake na kuona kuwa ilikuwa saa moja na nusu za usiku. Ulikuwa ni muda wa chakula cha jioni na hivyo wakaazi wengi wa vyumba vya jirani walikuwa wameelekea Kafetaria kupata mlo. Aliingiza mkono kwenye mfuko wa suruali yake na kutoa ufunguo alioutumia kufungulia mlango wa chumba kile na vyumba vingi vingine pale chuoni. Ulikuwa ni ufunguo ambao wengi huuita " Ufunguo Malaya" au Master Key. Aliufunga kwa nje mlango ule, akijua kuwa Rose alikuwa ana ufunguo wake kule ndani. Hakutaka mashoga zake waje na kumkuta akiwa katika hali ile kule ndani. Alirudisha ufunguo wake mfukoni na kuondoka taratibu huku akipiga mbinja.
______________________
Rose alifumbua macho taratibu kutoka kwenye usingizi mzito huku akihisi kichwa kikimgonga sana. Alipiga mwayo na kuitupia macho juu ya meza yake ya kusomea, na kugundua kuwa ilikuwa ni kengele ya simu yake iliyokuwa pale mezani ndiyo iliyomuamsha kutoka kwenye usingizi ule mtamu. Alijiinua taratibu kutoka pale kitandani huku akiachia mwayo mwingine na kusimama akiwa uchi katikati ya chumba kile. Huku akihisi kizunguzungu na njaa kali, alijikongoja na kuinyakua ile simu, akabofya sehemu iliyoizima ile kengele kutoka kwenye simu ile, naye akaketi kwenye kiti kilichokuwa kando ya mlango na kutazama saa iliyokuwa ikionekana kwenye ile simu yake ya kisasa.
Ilikuwa ni saa kumi na mbili na nusu za asubuhi.
Alijiinamia akiwa ameegemeza paji lake la uso kwenye viganja vya mikono yake. Matukio ya siku iliyopita yalianza kumrudia kichwani mwake na moyo ukaanza kumwenda mbio.
Alikumbuka jinsi alivyomkuta Tony mle ndani alipoingia kutokea bafuni na jinsi Tony alivyomtesa na kumtisha kwa kisu. Aliinama kujitazama chini ya titi lake ambapo Tony alimtoboa kwa ncha ya kisu. Damu ilikuwa imekauka na kuganda kulizunguka jeraha lile.
Alikumbuka jinsi Tony alivyofanikiwa kumvutisha unga wa madawa ya kulevya…alikumbuka hisia alizozipata baada ya kuvuta unga ule, na hapo mwili wote ulimfa ganzi kwani kumbukumbu hiyo ilienda sambasamba na kumbukumbu kwamba Tony alimwingilia kimwili wakati akiwa katika hali ya kulevywa na unga ule. Haraka sana alipeleka mkono wake katika sehemu ya uuke wake. Manii yaliyokauka yalikuwa yamemgandia katika sehemu ile na sehemu ya ndani ya mapaja yake.
Alijihisi kichefuchefu na machozi yalianza kumlenga lenga.
Tony ameniingilia kimwili bila ya ridhaa yangu! Amenibaka…! Hivi ni kweli haya mambo yamenikuta mimi au ninaota?
Wazo la kwamba sio tu amevuta unga ule haramu bali pia amebakwa na mtu yule mchafu na mshenzi, tena bila ya kondomu lilimletea hofu nyingine mbaya zaidi…
Itakuwaje iwapo atakuwa ameniambukiza ukimwi? Mungu wangu, balaa gani hili!
Alikumbuka jinsi alivyobaki akiwa amejilaza pale sakafuni baada ya Tony kuondoka. Hakuwa na kumbukumbu ni vipi au saa ngapi alipanda kitandani…
Machozi yalianza kumbubujika.
Huku akijifuta machozi alijiinua taratibu na kuanza kujichemshia maji ya chai kwa birika la umeme lililokuwa mle ndani. Kipindi cha kwanza kilikuwa kinaanza saa mbili asubuhi hivyo ilibidi aanze kujiandaa, lakini alitaka apate chai kabla ya kuoga wala kupiga mswaki. Alianza kunywa chai taratibu huku akiwa amesimama akitazama nje kwa kupitia dirishani. Alijua kuwa ikifika saa moja na nusu Moze atampitia pale chumbani ili waelekee darasani.
Moze!
Alibaki ameduwaa na kikombe mkononi akimfikiria Moze…
Tony alikuwa anamtakia nini Moze?
Mwili ulimsisimka. Roho ilimuuma sana na kuanza kumfikiria rafiki yake huku maswali kem kem yakimjaa kichwani.
Ina maana alitaka kumfanyia Moze mambo yale aliyonifanyia mimi jana?
Kwa hiyo Tony alitaka kumfanyia mambo yale Moze ili kumlipizia kisasi Jaka kwa kumpiga Joakim Mwaga na kuwatia aibu Tony na wenzake?
Mbona mambo haya ni ya upuuzi mtupu? Inawezekana kweli yote hii ikawa ni kwa sababu hiyo tu? Hapana, lazima kuna sababu nyingine…sasa ni sababu gani hiyo?
Alibaki katika hali ile kwa muda mrefu, akiwaza na kuwazua.
Kama ni kisasi tayari wameshalipiza…si wameshamlaza Jaka hospitali kwa wiki mbili? Sasa hiyo haitoshi? Isipokuwa…isipokuwa kama Tony anafanya vile kama sehemu ya kazi yake…kwamba Tony huwalazimisha wanafunzi, hasa wasichana pale chuoni kuvuta ule unga ili apate kuendelea kuwauzia na kujipatia pesa…lakini mbona Tony ana uwezo mzuri tu wa fedha? Baba yake anajiweza sana…Ah!http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Rose alisonya na kurudi kuketi kwenye kiti. Alishindwa kuelewa mambo yale yalikuwa na maana gani.
Mambo pekee aliyoyaelewa ni kuwa hakuwa tayari kuruhusu mambo aliyofanyiwa yeye yaje yamkute Moze. Na pia hakuwa tayari kuendelea kuvuta madawa ya kulevya maishani mwake .
Lazima nimtahadharishe Moze kuhusu jambo hili…nitamweleza Jaka…lazima…!
Lakini alimkumbuka Tony.
Tony alisema kuwa nikisema tu hatonipatia tena dozi ya unga…
“Poa tu, kwani mi’ n’na haja na huo unga? Kabla ya jana si nilikuwa naishi tu bila ya huo unga?” Alijisemea kwa sauti.
Sasa baada ya jana je…?
Sauti nyingine ndogo ikamuuliza kutoka ndani kabisa ya nafsi yake.
“Oh, God!”
Taratibu alienda kitandani na kupeleka mkono wake chini ya mto na kutoa kile kijifuko kidogo cha unga alichoachiwa na Tony. Aliuangalia unga ule kwa muda mrefu huku moyo ukizidi kumwenda mbio. Unga ambao alipewa na Tony kwa sharti la kumsaliti rafiki yake mpenzi…
Aliendelea kuutazama unga ule huku mkono ukimtetemeka na machozi yakianza kumtoka tena. Kwani alipokuwa akiutazama unga ule, alijua wazi kuwa alikuwa anautamani…tena kwa kiasi kikubwa kabisa. Alikuwa anautamani unga ule tangu alipoamka pale asubuhi, ila alijaribu kujisahaulisha kwa kunywa chai na kujipa moyo kuwa hakuwa akiuhitaji, lakini sasa ukweli ulikuwa umedhihiri na machozi yalimtoka kwa kujisikitikia maisha yake…
Maisha yangu sasa yatakuwa mikononi mwa unga huu haramu…na ili niweze kuupata itanibidi nikubaliane na sharti la Tony, nimsaliti rafiki yangu mpenzi…
“Oh! Masikini Moze…masikini miye…! Hivi ndivyo nilivyodhalilika hadi kufikia hatua hii? Jana Tony ameninajisi kwa ajili ya unga huu! Na sasa anataka nimtoe kafara rafiki yangu mpenzi kwa ajili ya unga huu huu! Sijui baada ya hapo atataka nifanye nini tena kwa ajili ya hu huu unga…na itanibidi niendelee kufanya tu vyote atakavyotaka ili niendelee kupata unga huu… mpaka lini, Eeenh? Mpaka lini Mungu wangu?” Aliongea peke yake kwa sauti ya kuomboleza, machozi yakimbubujika.
Alilia!
Alilia kwa uchungu kusikitikia jinsi maisha yake yalivyoharibika katika muda mfupi sana, bila ya kutarajia.
“Yaani leo unga huu ndio unanifanya nishirikiane na yule shetani mkubwa baradhuli asiye na maadili katika kumsaliti Moze? Ili na Moze naye awe kama mimi? Hapana! Hapana! Hapana!” Alizidi kujiongelesha peke yake, na kubaki akiwa amejikunyaka kinyonge kitandani.
Najua Tony ataniua nikiwaeleza Moze na Jaka juu ya jambo hili, lakini potelea mbali! Kama Tony amenishinda kwa kunivutisha huu unga, basi nitahakikisha kuwa anashindwa kumnasa Moze katika mtego wake huu haramu…nitahakikisha hivyo!
Alikumbuka jinsi Tony alivyokuwa akimtesa kwa kisu mle chumbani na mwili ulimsisimka. Na hapo alikumbuka maneno ya Tony wakati akimlazimisha kuvuta unga ule.
Unataka kuwa kama Margareth Mfinanga…?
Aliketi wima kitandani alipolikumbuka swali lile la Tony.
Tony ni muuaji.
Sasa alielewa ni kwa nini Margareth alijiua. Jasho lilianza kumtoka kwani alielewa ni jinsi gani kisa chake kilivyokuwa kinaelekea kufanana na kisa cha Margareth Mfinanga, kama jinsi alivyokielewa baada ya kutafakari yale maneno ya Tony.
“This guy is a real bastard!” Rose alipayuka kwa sauti huku jasho likizidi kumtoka, akimaanisha kuwa kwa hakika Tony alikuwa ni mwanaharamu kweli kweli. Aliutazama ule unga na hamu ya kuuvuta tena ilimjia. Alifumba macho na kugeuza uso wake pembeni.
“Lazima nimueleze Jaka…lazima nimueleze Moze…najua Tony ataniua tu…!” Sasa alikuwa anaongea peke yake kama mwendawazimu mle ndani.
“Sasa kama yeye atataka kuniua kwa hilo, basi pia hatafanikiwa!”
Huku machozi yakiendelea kumbubujika, alianza kupanga vizuri vitu vyake mle chumbani na kukiondoa kile kijifuko kilichokuwa na ule unga ambao bado alikuwa anashindana na nafsi yake dhidi ya kuuvuta tena ndani ya mapafu yake. Hamu ya kuuvuta ule unga ilikuwa kubwa sana na kadiri alivyokuwa akijizuia, ndivyo alivyozidi kuchanganyikiwa.
Baada ya hapo alichukua karatasi na kalamu na kuviweka juu meza. Kisha alivuta droo ya meza ile na kutoa kichupa kidogo cha plastiki chenye rangi nyeupe na kukitikisa kidogo ili kuhakikisha kama hakikuwa kitupu. Mlio wa vidonge vilivyokuwa ndani ya kichupa kile ulimthibitishia kuwa hakikuwa kitupu.
Alichukua glasi na kujimiminia maji kutoka kwenye jagi lililokuwa juu ya meza ile, na bila ya kujali idadi, alibugia vidonge vyote vilivyokuwa ndani ya kile kijichupa na kuvimeza kwa kunywa maji yaliyokuwa kwenye ile bilauri. Alikiacha kile kichupa kikianguka sakafuni kikiwa kitupu naye akaanza kuandika kwenye ile karatasi aliyoiandaa pale mezani.
Plasta iliyokuwa imebandikwa kwenye ubavu wa kile kijichupa ilikuwa imeandikwa neno moja tu.
Chloroquine.
____________________
Moze alifungua mlango wa chumba chao pale chuoni na kusimama ghafla pale kizingitini. Ilimchukua sekunde kadhaa kwa akili yake kutafsiri kile ambacho macho yake yalikiona ndani ya chumba kile, ambacho hakutarajia kabisa kukiona maishani mwake. Alitupa chini madaftari na vitabu vyake huku akipiga kelele na kubakia amejishika kichwa ilhali amekodoa macho kumtazama rafiki yake.
Rose alikuwa akigaagaa sakafuni akiwa uchi huku mwili wake ukijitupa tupa huku na kule na koo lake likitoa sauti za ajabu mithili ya mtu aliyepandwa na mashetani. Pale chini palikuwa pametapakaa matapishi yaliyochanganyika na damu, na Rose alikuwa akigaragara juu ya matapishi yake.
Huku akipiga kelele Moze alimkimbilia rafiki yake pale chini na kupiga magoti kando yake, akamshika kujaribu kumzuia asijizidi kujitupa tupa pale sakafuni namna ile.
“Rose! Rose! Ni nini kimetokea! Ni nini kimetokea…??” Alibwabwaja huku machozi yakimtiririka, akisikia vishindo vya wanafunzi wenzao wakikimbia kuelekea pale chumbani. Na hata pale alipokuwa anamuuliza Rose maswali hayo, Rose alitoa mguno mkubwa wa uchungu huku macho yamemtumbuka, mchirizi mzito wa damu ukimtoka kinywani na kutiririkia shavuni kwake.
“Mungu wangu, Rose! What happened? Umekuwaje jamaniii...?” Moze aliuliza huku akilia kwa hamaniko. Alivuta upande wa kanga na kumfunika rafiki yake huku akimnyanyua kwa taabu na kumlaza mapajani kwake. Rose alikunja uso kwa maumivu makali aliyoyapata na kumtazama rafiki yake. Uso wake ulionyesha hofu kubwa na alijitahidi kumweleza rafiki yake yaliyomsibu.
“Moze!” Aliita kwa sauti ya kukwaruza iliyochanganyika na kikohozi.
“Nini Rose…umekuwaje rafiki yangu…?” Moze alimwitikia huku akiwa amechanganyikiwa vibaya sana, na hapo macho yake yakaangukia kwenye mkono wa kulia wa Rose ambao ulikuwa umekamata karatasi na kalamu kwa nguvu sana kiasi kwamba ile karatasi ikawa imefinyangwa vibaya sana. Alitaka kuichukua ile karatasi, lakini Rose aliukwepesha mkono wake na badala yake, alimshika Moze sehemu ya mbele ya blauzi yake kwa mkono wake wa kushoto na kumvuta ili nyuso zao ziwe karibu zaidi.
“...You…know..wha…whaa…what…” Hakuweza kumaliza, kwani ghafla mwili wake wote ulijipinda kutokea kiunoni kuja juu, na hivyo kuipinda nyuma shingo yake huku akitoa ukelele mrefu wa maumivu ulioishia na kutoa povu jingi kinywani.
Moze alipiga kelele kwa woga na hapo hapo alihisi watu wengi wakiwa wanaingia ndani ya chumba kile wakiuliza maswali mengi. Moze aligeuza shingo yake kuwageukia wanafunzi wenzake waliokusanyika mle ndani.
“Hospitali! Tumpelekeni hospitali haraka…!” Moze alibwata huku akibubujikwa na machozi.
“Hapana...! No time! Nisikilize Moze…!” Rose aliropoka kwa taabu na haraka. Moze alimgeukia rafiki yake pale chini na kabla hajasema lolote, Rose aliendelea kwa taabu, “..You..know….what Iam saying!…you know wha…at…Iam….sayi…ing!”
Kwisha kusema hivyo alihema kwa nguvu na kugeuza uso wake pembeni, akabaki akiweta kama mtu aliyetoka kukimbia mbio ndefu. Moze alibaki amepigwa na butwaa.
“ Nini!?” Moze hakuelewa kabisa ni nini Rose alikuwa anasema. Mara ile msichana mwingine alikuja na bilauri ya maziwa.
“Moze, mpe glasi ya maziwa labda ameji-over dose…!” Alisema yule msichana naye akiwa na wasiwasi na hofu kubwa hali wengine wakilia kwa woga. Haraka sana Moze aliichukua ile bilauri na kuipeleka mdomoni kwa Rose.
Rose alijua kuwa hawezi kuishi. Hakutaka tena kuishi. Alitaka amtajie Moze jina la mtu aliyemsababishia madhila yale kabla hajafa. Lakini cha ajabu ni kwamba jina la yule mtu lilimtoka kabisa kichwani mwake. Alichokumbuka ni yale maneno yanayokera tu ya yule mtu mbaya. Lakini Moze alikuwa haelewi. Alijiona akizama kwenye shimo refu lenye kiza kizito. Hasira zilimpanda…
Kwa nini Moze haelewi…?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Moze!” Sasa Rose alifoka kwa nguvu na kumshitua Moze.
“Hapana, usiongee kitu Rose…kunywa maziwa kwanza...halafu twende hospitali.” Moze alijitahidi kumwambia huku woga ukizidi kumwelemea.
Rose aliinua mkono wake wa kushoto na kumshika Moze kwa nguvu nyuma ya shingo na kumvutia kwake, na wakati huo huo akijiinua kutoka mapajani kwa Moze. Mlio wa king’ora cha gari la kubebea wagonjwa ulisikika ukielekea katika eneo la bweni namba tatu na Moze alipata moyo wakati akijitahidi kumtuliza rafiki yake huku akiyakinga yale maziwa yasimwagike. Rose aliipiga kofi ile bilauri ya maziwa kwa mkono wake wa kulia, nayo ikatupwa pembeni na kuvunjika huku maziwa yakiwamwagikia wote wawili pale chini.
“Ayyaaaaaaaah!” Wale wenzao walipayuka kw apamoja/
“ Rose !” Moze naye alimkemea mwenzake kwa mshangao.
Bila kujali Rose alitoa macho kwa hasira na kumtazama Moze moja kwa moja machoni.
“You..know what Iam saying…!” Kwa nguvu zake za mwisho zilizobakia alimwambia Moze kwa ukali. Baada ya kusema maneno yale, Rose alijibwaga tena mapajani kwa Moze huku akimtazama rafiki yake kwa huzuni kubwa.
Safari hii Moze aliyasikia vizuri yale maneno na alijua kuwa halikuwa swali bali ilikuwa ni taarifa. Lakini bado hakuweza kuelewa ni kwa nini Rose alikuwa anang’ang’ania kumwambia maneno yale.
“Whaaa…?” Moze alianza kumuuliza rafikiye lakini hapo alimuona rafiki yake akikodoa macho darini, kisha Moze akaihisi shingo ya Rose ikilegea na kichwa chake kikalalia upande mmoja. Alianza kutoa sauti za kukoroma huku pumzi zikimtoka kwa shida.
“No, Rose NOOO! No, rafiki yangu, No please, jamaniiiii!” Moze alipayuka kwa wahka huku akimkumbatia rafiki yake. Rose akamuwia mzito sana mikononi kwake, akamuweka tena mapajani mwake na kumtazama kwa woga mkubwa.
Rose alimtazama kwa jichola kukata tama, kisha akatoa kikohozi hakifu.
Akakata roho.
11
“Detective Sergeant ”, yaani Sajenti-Mpelelezi, John Vata aliinuka kutoka kwenye kochi la kifahari alilokuwa amekalia na kumtazama yule binti aliyeingia ndani ya sebule ile na kujitambulisha huku akimpa mkono. Moze aliupokea mkono ule huku naye akijitambulisha. Wote waliketi kwenye makochi huku Sajenti Vata akimshukuru Mungu kwa kumjaalia yule binti urembo wa kuvutia na umbo la kupendeza. Macho ya yule binti yalikuwa mekundu na yaliyovimba kutokana na kulia kwa muda mrefu. Vata alihisi ni kutokana na kifo cha rafiki yake.
“Sielewi kwa nini unataka kuonana na mimi kwa sababu tayari askari wengine walishanihoji maswali mengi sana kule chuoni…sasa leo siku ya nne tangu nifiwe na rafiki yangu bado mnanifuatafuata tu hadi nyumbani kwetu, hata sipati nafasi ya kuhuzunika kwa faragha! Ni nini ambacho bado hamjaelewa?” Moze alimuuliza yule sajenti bila ya kuficha jinsi alivyokereka. John Vata aliendelea kumtazama kwa utulivu bila ya kusema neno lolote, akaachia kiasi cha kama dakika mbili hivi zipite, kisha akaenda moja kwa moja kwenye kuuliza maswali yake badala ya kujibu shutuma alizotupiwa na yule mrembo.
“Ulikuwa rafiki na marehemu kwa muda gani?”
Moze alizungusha juu mboni za macho yake kwa ishara ya kuchoshwa na swali lile kwani alikuwa ameshalijibu hapo awali na sasa ilikuwa ni marudio.
“Miaka ipatayo mitatu sasa…”
“Ulijua katika muda huo kuwa Rose alikuwa anatumia madawa ya kulevya?”
Swali lile lilikuwa jipya kwa Moze na lilimshitua sana. Alibaki mdomo wazi huku akimtazama yule askari kama kwamba alikuwa ana wazimu.
“Rose atumie madawa ya kulevya? Never! Rose hakuwa akitumia madawa ya kulevya wala kilevi cha aina yoyote ile hapa duniani afande!” Alimjibu kwa jazba. John Vata alimtazama kwa muda, kisha akamtupia swali.
“Una hakika?”
Moze alimtazama yule Sajenti kwa hasira huku macho yake yakilengwa na machozi na midomo ikimcheza. John Vata alijua kuwa lile swali lilimkera sana yule binti, lakini hakujali.
“Una uhakika gani kuwa Rose hakuwa akitumia madawa ya kulevya?” Vata aliuliza tena.
“Sikiliza sajenti, tena sikiliza vizuri…Rose alikuwa rafiki yangu mpenzi. Hakuna jambo lolote ambalo angelifanya nami nisilijue, au mimi nifanye jambo Rose asilijue, hivyo ndivyo urafiki wetu ulivyokuwa, na ndio maana nina uhakika na jibu ninalokupa...tulikuwa hatufichani kitu.” Moze alimjibu kwa hasira. John Vata alibaki akimtazama tu yule binti kwa uso ulioficha hisia yoyote ambayo angekuwa nayo wakati ule. Hali hiyo ilimfanya Moze aendelee.
“...kwa hiyo ninapokuambia kuwa Rose hakuwa hivyo ambavyo wewe unataka niseme alikuwa, ujue ninasema hivyo nikiwa na uhakika na ninachokisema, sawa afande?”
John Vata aliendelea kumtazama kwa utulivu bila ya kusema neno. Tabia hii ilionekana kumchanganya akili Moze na kumfanya ashindwe kudhibiti ghadhabu zake. John Vata aliamini kuwa mtu akijibu swali kwa ghadhabu na kuchanganyikiwa, mara nyingi hutoa jibu lililo moyoni mwake, ambalo mara nyingi huwa ndio lililo karibu zaidi na ukweli. Ni mbinu ambayo imemletea mafanikio makubwa sana huko nyuma.
“Una sababu nyingine yoyote zaidi ya hiyo inayokufanya uamini kuwa Rose hakuwa akitumia madawa ya kulevya?” Alimchapa swali jingine.
Moze aliguna na kutikisa kichwa kwa masikitiko kabla ya kumjibu yule askari.
“Afande, ile bia tu Rose alikuwa haigusi, sasa leo uje uniambie kuwa Rose alikuwa akitumia madawa ya kulevya? Hapana afande. Rose hakuwa akitumia madawa ya kulevya...!” Moze alimalizia jibu kwa kuangua kilio kutokana na kuzidiwa na machungu ya tuhuma zile chafu dhidi ya rafiki yake marehemu. John Vata aliendelea kumtazama bila ya kusema neno. Alimuacha alie na atoe machungu yake bila ya kumuingilia. Baada ya muda Moze alinyamaza na kuanza kujifuta machozi kwa upande wa khanga aliyokuwa amejitanda.
“Pole sana.” Hatimaye Vata alimpa pole na Moze aliipokea kwa kichwa. Vata alimpa dakika kadhaa kabla ya kuendelea kumsaili.
“Eeenh...Moze, kama ujuavyo, rafiki yako amejiua...sijui unaweza kuwa na wazo lolote ni kwa nini aliamua kufanya hivyo?”
“Kwa kweli sijui ni kwa nini aliamua kuchukua uamuzi huo, kwa sababu jioni kabla ya siku ya tukio, alikuwa katika hali yake ya kawaida tu.”
“Kwa hiyo nikikwambia kuwa kuna uwezekano kuwa rafiki yako aliuawa utakubaliana na mimi?”
Moze alishtushwa na swali lile. Hakufikiria kabisa kitu kama kile.
“Sijui...sijui, kwa kweli. Lakini Rose hakuwa na uhasama na mtu yeyote kiasi cha kufikia hatua ya mtu kutaka kumuua...” Moze alijibu huku akionesha wazi kuwa Vata alikuwa akizidi kumchanganya kwa maswali yake. Vata alitazama saa yake na kumtazama Moze kwa muda, kama kwamba alikuwa anajaribu kumpima ataweza kuhimili kiasi gani uzito wa swali alilotaka kumuuliza; kisha alimuuliza: “Umeshawahi kutumia madawa yoyote ya kulevya maishani mwako?”
Moze alikuwa kama mtu aliyepigwa kofi usoni. Alimtazama kwa hasira, na kwa utaratibu mno, kama mtu anayetaka maneno yake yaeleweke vema, alimjibu huku akimtazama moja kwa moja machoni.
“Sajenti John Vata…kama umekuja hapa kunitukana na kunivunjia heshima, basi nakuomba sasa hivi uinuke na utoke humu ndani. Na mimi naijua sheria vile vile! Sasa naona lengo lenu ni kunichanganya tu! Mara Rose kauawa...mara alikuwa anatumia madawa ya kulevya...sasa tena imekuwa mimi ndiye mtumiaji madawa, mbona hamueleweki?” Alibaki akitweta huku akiendelea kumkazia macho Vata, ambaye aliendelea kumtazama kwa utulivu. Hii hali ilizidi kumkera, akaendelea, “Sasa sikiliza Sajenti…mimi sina muda wa kupoteza zaidi kwa kusikiliza maswali yako ya kipuuzi. Ondoka! Ondoka na usirudi tena. Mimi na wewe tutaongea mahakamani. Kanifungulie kesi ya kutumia hayo madawa ya kulevya nami nitafurahi kuja kujibu tuhuma hizo mahakamani, sio hapa nyumbani kwetu. Sawa? Toka!”
Baada ya kusema hivyo Moze alibaki akitweta huku akimtazama Vata kwa ghadhabu. Vata alibaki akimtazama tu yule binti huku akiwa ameinua nyusi zake na akipapasa ndevu zake za juu ya mdomo kwa utulivu wa hali ya juu. Hakuwa na papara wala wasiwasi. Hali hii ilizidi kumkera Moze. Alikuwa akihema kwa nguvu, kifua chake kikipanda na kushuka haraka haraka kufuatisha pumzi zake za ghadhabu. John Vata alijiweka sawa pale kwenye kochi na kushusha pumzi ndefu.
“Mimi natoka katika idara maalum ndani ya jeshi la polisi inayoshughulika na makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya. Katika wilaya ya Kinondoni, makao ya idara hii yako katika kituo cha polisi cha OysterBay...” Vata alianza kumueleza kwa utulivu kama kwamba hakusikia maneno yote yaliyosemwa na Moze.
“...sio mara ya kwanza kwa kifo kama hiki kutokea pale Chuo Kikuu, lakini kwa vile hii ndio mara ya kwanza kwa vifo hivi kuhusishwa moja kwa moja na madawa ya kulevya, ndio maana idara yangu imechukua jukumu la kuendesha uchunguzi wa kifo hiki, kinyume na hapo awali ambapo kituo cha polisi cha Mlimani ndicho kilichokuwa kikiendesha uchunguzi wa vifo hivyo...” Alinyamaza kidogo, kwani wakati huo mama Moze aliingia pale sebuleni akiwa na sinia lenye vikombe viwili vya chai na visahani vidogo viwili vyenye biskuti.
Aliwakaribisha chai na wote walishukuru. Alitoka na kuwaacha waendeleee na maongezi yao, na Vata aliendelea kuhabarisha.
“Katika chumba ambamo Roze alifariki, ambamo na wewe ndimo unamoishi pale chuoni, kumepatikana kiasi kidogo cha unga wa madawa ya kulevya aina ya Cocaine ukiwa kwenye kifuko kidogo cha nailoni, na mwingine ukiwa umemwagika juu ya zulia la mle chumbani, wakati kiasi kingine cha unga huo kilionekana kutapakaa ukutani...sijui unafahamu nini juu ya hilo?”
Moze alionekana kushtushwa sana habari ile kiasi kwamba hasira zake zote ziliyeyuka mara moja na nafasi ya hasira zile ikachukuliwa na mashaka na mshituko.
“Niliona unga kidogo pale juu ya zulia, lakini sikijua ni unga gani na wala sikuutilia maanani kabisa...” Alisema kwa mashaka makubwa kabisa.
“Baada ya wale askari waliokuhoji mara ya kwanza kutoa ripoti ya kupatikana kwa unga huo, na baada ya unga huo kuthibitishwa kuwa ni Cocaine, uchunguzi wote wa kesi hii umehamishiwa moja kwa moja mikononi mwa idara inayohusika na udhibiti na ufuatiliaji wa madawa ya kulevya hapa nchini…na ndio maana mimi leo nimekuja tena kwako ili kuanza uchunguzi wa idara yangu katika kesi hii.” Alimalizia John Vata.
“Kwa hiyo wewe ndiyo umetoka kwenye hiyo idara ya...”
“Narcotics Department, ndiyo...na nipo hapa kuomba msaada wowote unaoweza kuutoa katika kutatua kesi hii. Kwani tuna imani kuwa tukiijua sababu ya kifo cha Rose, tutakuwa tumepata chanzo kizuri sana cha kutufikisha kwenye chimbuko la biashara hii ya madawa ya kulevya.”
“Dah! Sawa...sasa…unadhani mimi nitaweza kusaidia vipi Sajenti?”
“Mimi nadhani wewe unajua ni kwa nini Rose aliamua kujiua...kwa sababu hadi anakata roho alikuwa mikononi mwako...” Hapo Moze alifumba macho na mwili ulimsisimka kwa kumbukumbu zilizomjia. “...na bila shaka kuna maneno fulani ambayo Rose atakuwa amekuambia au ameyatamka katika dakika zake za mwisho, ambayo tunadhani yanaweza kutupatia mwanga juu ya swala hili.”
“Mimi sijui ni kwa nini Rose aliamua kujiua afande! Nami pia nakubali kuwa Rose alikuwa anataka kuniambia neno au kitu...ila tu kile alichokuwa akikisema kilikuwa hakileti maana yoyote...she was very delirius, man...!”Moze alimjibu, akimalizia kwa maneno ya kimombo yaliyomaanisha kuwa Rose alikuwa akibwabwaja vitu visivyoeleweka tu katika zile dakika zake za mwisho.
“Ni nini hasa alichokuwa akikueleza, au akijaribu kukueleza…? Hebu niambie namna ilivyokuwa, neno kwa neno…kadiri unavyoweza kukumbuka”
“Ah, afande! Yaani ni utata tu, kwani neno pekee alilokuwa akijaribu kunieleza ni...you know what I am saying...you know what I am saying...zaidi ya hapo hakusema neno lingine...mpaka leo hii sielewi ni kwa nini neno hilo lilikuwa na umuhimu sana kwake kwa wakati ule, au alitaka nielewe nini kwa maneno yale...it was very scary, Sajenti.” Moze alimjibu, akimalizia tena kwa kuchomekea maneno ya kimombo, akimaanisha kuwa hali aliyokuwa nayo Rose kabla ya kukata roho ilimtisha sana.
Vata alionekana kumakinika sana na maelezo yale. Alikunja nne, kisha hapo hapo akaikunjua na kuikunja tena kwa mguu mwingine.
“Aha! Yaani…kutokana na maneno hayo ni kwamba alikuwa akimaanisha kuwa wewe unajua ni nini Rose alikuwa anasema, sio?”
“Ndio. Hiyo ndio maana yake. Lakini kwangu hayakuleta, na wala hayaleti, maana yoyote...”
John Vata alimtazama Moze kwa muda bila ya kusema neno. Kisha aligeuka pembeni na kuendelea kukaa kimya, akifikiri juu ya yale maelezo ya Moze, akichezesha-chezesha ule mguu wake mmoja uliolazwa juu ya mwingine pale kochini. Hatimaye alimgeukia tena Moze.
“Rose aliandika barua kabla ya kifo chake...”
“Ambayo hakuwahi kuimalizia...” Moze alidakia.
John Vata aliafiki kwa kichwa huku akimkabidhi Moze kipande cha karatasi alichokitoa kwenye mfuko wake wa shati.
“Barua hiyo ndiyo hii?”
Moze aliipokea ile karatasi kwa mikono ya kutetemeka na kuitazama. Ilikuwa bado ina mikunjo- mikunjo, na ilikuwa imechanika kidogo.
Ilikuwa karatasi nyeupe, yenye urefu wa inchi zipatazo kumi hivi na upana wa inchi saba. Mwandiko ulioandika maneno machache yaliyokuwa juu ya karatasi ile ulikuwa dhaifu na wa kitetemeshi, ila Moze hakuwa na shaka kabisa kuwa ulikuwa ni mwandiko wa rafiki yake Rose.
“Ndiyo hii.” Alijibu huku akimrudishia Vata ile karatasi.
“Una uhakika huu ni mwandiko wa Rose?” Kama aliyekuwa akisoma mawazo yake, Vata alimuuliza. Moze aliafiki kwa kichwa na wote walibaki kimya kwa muda. Moze akijifuta machozi yaliyokuwa yakimchuruzika, ilhali Vata akisoma kwa mara nyingine kile kilichoandikwa kwenye ile karatasi.
Rafiki mpendwa Moze,
Samahani sana kwa uamuzi nilioamua kuuchukua, kwani najua utakuhuzunisha sana.
Naomba tu uelewe ya kuwa huu ni uamuzi wa busara zaidi kwangu hivi sasa na kwa maisha yako.
Moze, nimeamua kufanya hivi kwa sababu nimeshindwa kabisa kukusaliti kwa huyu mtu mbaya ambaye tayari ameyaharibu kabisa maisha yangu, nawe itabidi uwe makini san
Kilichofuatia baada ya hapo ni michoro isiyoeleweka, kama vile baada ya kufikia hapo tu kitu, au mtu alimshitua kiasi cha kufanya michoro ile isiyoeleweka kwenye ile karatasi, halafu hakuendelea tena kuandika.
“Inaelekea Rose alikuwa anataka kukuachia tahadhari fulani dhidi ya mtu fulani.” Vata alisema huku akimtazama Moze usoni. Moze aliuma mdomo na kuafiki kwa kichwa.
“Na wewe unadai kuwa ujumbe huu hauleti maana kwako.”
Halikuwa swali. Ilikuwa ni sentesi kamili iliyotolewa kama shutuma. Moze alimtazama yule askari kwa mshangao.
“Unadhani mimi nasema uongo nikisema hivyo?”
“Kwangu mimi huu ujumbe uko wazi kabisa...yaani wewe ungetakiwa uelewe ni nani Rose anayemzungumzia kwenye barua hii.”
“Sasa hilo ndilo ambalo halileti maana kwangu afande, kwa sababu sijui ni nini Moze anachozungumzia kwenye hiyo barua…na wala sijui ni nani huyo anayemtaja kwenye hiyo barua, na huo ndio ukweli.”
Vata alimtazama kwa muda bila ya kusema neno. Kama yule binti angekuwa anasema uongo kwa namna fulani angeweza kugundua, lakini aliona kuwa yule binti alikuwa akisema ukweli, na hii iliifanya kazi yake iwe ngumu kuliko alivyotarajia.
Ni nani huyu anayeongelewa kuwa ni mtu mbaya kwenye barua ya Rose?
Kwa nini uamuzi wa Rose kujiua uwe ndio salama ya Moze?
Rose alishindwa kumsaliti Moze katika lipi, hata akaona ajiue?
“Inaelekea Rose aliamua kujiua ili akuokoe wewe kutokana na hatari fulani Moze, halafu wewe unasema kuwa hujui lolote juu ya jambo lote hili?” Vata aliendelea kusaili.
“Sajenti, mimi ningekuwa naelewa kitu juu ya mambo haya nisingekuwa na sababu ya kuficha. Ukweli ni kwamba sielewi kitu chochote!” Moze alijibu kwa sauti iliyochanganyikiwa.
“Rose hakuwa na rafiki yeyote wa kiume, ambaye labda angeweza kumdhuru kwa namna yoyote ile ?”
“Hakuwa na rafiki yeyote wa kiume afande.”
“Je wewe?”
“Je mimi vipi?”
“Huna rafiki yeyote wa kiume?”
“Niliye naye hawezi kumdhuru Moze wala mimi. Ni mtu mzuri sana na wala hana tatizo lolote juu ya urafiki wangu na Rose.”
“Niandikie jina lake na mahala anapoweza kupatikana, ikiwezekana na namba yake ya simu.” Vata alimwambia huku akimsogezea kijitabu kidogo cha anuani na kalamu. Moze alitekeleza. John Vata aliutazama mwandiko wa yule binti wakati akiandika na kuufananisha kwa kichwa na ule aliouona kwenye barua iliyosemekana kuwa imeandikwa na Rose.
Ulikuwa ni mwandiko tofauti.
Kimya kilitawala kwa muda mrefu, kisha John Vata aliinuka ghafla.
“Bado kuna maswali mengi juu ya kifo cha rafiki yako Moze, hivyo nitarudi tena wakati wowote.” Alimwambia huku akimtazama moja kwa moja usoni. Moze aliafikiana naye kwa kichwa huku naye akiinuka kutoka pale kwenye kochi alilokuwa amekalia.
John Vata alitoka kuelekea mahala alipoegesha gari lake la polisi nje ya nyumba ile bila ya kuongeza neno zaidi.
Kikombe cha chai na biskuti alivyokaribishwa na mama Moze vilikuwa havijaguswa.
___________________
John Vata alikuwa amesimama kwenye chumba kidogo kilichokuwa ndani ya ofisi ya Dokta Felix Mgunda, mtafiti wa kitabibu wa polisi anayeshughulika na uchunguzi wa maiti zitokanazo na vifo vya jinai. Alipofika katika ofisi ile iliyopo ndani ya Hospitali maarufu ya serikali ya Muhimbili, alikaribishwa kwenye chumba kile na Dokta Mgunda mwenyewe, ambaye alimtaka asubiri kidogo pale ndani kwani alikuwa akimalizia kuichambua maiti nyingine kwenye chumba kingine, kikubwa zaidi, kilichokuwa upande wa pili wa ofisi ile.
Badala ya kuketi kitini, Vata alikuwa akiranda randa huku na huko mle ndani, akimsubiri tabibu yule makini. Dokta Mgunda hakuwa na muda wa kupoteza na alikuwa ana kumbukumbu ya hali ya juu, hivyo alipoingia tena mle ndani dakika kumi baadaye alianza kuongea moja kwa moja.
“Umekuja juu ya swala la Rose wa Chuo Kikuu, Sajenti Vata...ni nini hasa ulichokuwa unataka kujua juu ya kifo chake?”
John Vata alitabasamu kidogo kutokana na jinsi Dokta Mgunda alivyokuwa akiendesha ofisi yake. Alikuwa ni mtu mfupi, mnene na mwenye upara uliong’aa sehemu ya juu ya kichwa chake, ingawa alikuwa na nywele nyeusi mno kisogoni na pembeni ya kichwa kile kikubwa.
“Tuanze na sababu ya kifo chake.”
“Sababu halisi ya kifo chake...” Dokta Felix Mgunda alivuta droo ya meza iliyokuwa mbele yake na kutoa faili jembamba. Alifunua ukurasa mmoja wa faili lile na kulilaza mezani mbele ya macho yake, na kuendelea bila kusoma kutoka kwenye lile faili, “...ni kupasuka kwa mishipa midogo inayopeleka damu moyoni na kusababisha kusimama kwa mzunguko mzima wa damu na hivyo kuufanya moyo ulipuke ghafla na kusimama...”
“Kwa nini unasema sababu halisi...kuna sababu nyingine, au...”
“Hali hiyo ya kupasuka mishipa hiyo midogo ya damu imesababishwa na marehemu kumeza vidonge vingi vya Chloroquine kwa mkupuo...sasa Chloroquine in itself, if properly administered , haisababishi kifo, ndio maana nikasema kuwa sababu halisi ni kule kupasuka ile mishipa kulikotokana na marehemu kubwia vidonge vingi vya dawa hiyo.” Mgunda alifafanua kwa utaratibu kama anayemuelezea kitu mtoto mdogo huku akichanganya na lugha ya kiingereza, jambo ambalo Vata alilizoea.
“Kuna dalili yoyote katika mwili wa marehemu za kuonesha kuwa kulikuwa kumetumika nguvu dhidi yake kabla ya kumeza vidonge hivyo?”
Mgunda alimtazama Vata kwa muda, kisha alimjibu:
“Sajenti, mimi nitajibu kutokana na matokeo ya uchunguzi wangu, hayo mambo mengine ni juu yako mwenyewe. Swala la kwamba nguvu ilitumika lipo, lakini iwapo ilitumika kabla au baada ya kumeza vidonge hivyo haliko ndani ya taaluma yangu kujua. Sawa?”
“Sawa.”
“Kuna alama za mbali sana kwenye shavu la kulia la marehemu ambazo zinaashiria kuwa alipigwa kofi kali.”
Vata alimsikiliza Mgunda kwa makini.
“Pia kuna michubuko katika sehemu ya mbele ya shingo ya marehemu, ambayo inaweza kuwa imetokana na aidha kukabwa au kukandamizwa na kitu au mkono uliovikwa glovu au kitu kama hicho.”
“Hakukuwa na alama za vidole mwilini mwa marehemu?”
“Vijana wa alama za vidole waliupitia mwili wa marehemu hatua kwa hatua, Sajenti. Alama za vidole zipo lakini sio kwenye maeneo yaliyojeruhiwa au yaliyoshikwa kwa kupigwa....ripoti hiyo si unayo Vata?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ninayo. Ni alama za wale wasichana wanafunzi wenzake waliokuwa wakijaribu kumsaidia baada ya kumkuta akiwa katika hatua za mwisho za kuaga dunia pale chumbani kwake. Kingine chochote?”
Sasa Dokta Mgunda alikuwa anasoma kutoka kwenye lile faili.
“Kulikuwa kuna majeraha mawili katika mwili wa marehemu ambayo yanaweza kuwa yamesababishwa na kitu chenye ncha kali...kama kisu chembamba au bisibisi..au kitu chochote chenye ncha kali...” Hapo Vata alionesha kumakinika zaidi na taarifa ile. “...jeraha moja lilikuwa upande wa kushoto wa uso wa marehemu, chini kidogo ya sikio la upande huo. Jeraha jingine kama hilo ilikuwa chini ya titi la kulia la marehemu.”
John Vata alikunja uso akitafakari habari zile. Dokta Mgunda alibaki kimya akimtazama, kama vile anayempa muda wa kuyaelewa vizuri mambo aliyomueleza.
“Nadhani alilazimishwa kumeza vile vidonge ili ionekane amejiua...” Vata alijisemea peke yake kwa sauti huku akimsahau kabisa Dokta Mgunda.
“Ningekuwa mimi nisingedhani hivyo.” Dokta Mgunda alimjibu taratibu. Vata aliinua uso wake na kumtazama kwa macho ya kuuliza. Mgunda aliendelea kumtazama bila ya kusema neno jingine. Vata akauliza.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment