Search This Blog

Thursday 23 March 2023

CABO' DELGADO - 1

 

IMEANDIKWA NA :  BADI M. BAO
*********************************************

Simulizi : Cabo' Delgado


Sehemu Ya : Kwanza (1)


Makaburi ya mashujaa wa vita vya dunia, Kijijini Mahiwa, Lindi.
Kadamnasi ya watu walikuwa wamekusanyika wakiwa wamejikunyata vikundi vikundi. Nyuso zao zimegubikwa na majonzi na huzuni katika makaburi ya mashujaa wa vita vya dunia vya kwanza, yaliyopo kijijini Mahiwa.

Kijiji ambacho kipo katika Wilaya ya Lindi Vijijini katika Mkoa wa Lindi. Waombolezaji hao walikuwa wamekusanyika katika harakati za kuhitimisha shughuli ya arobaini kutokana na msiba wa Bi.Josephina Charles Nyagali aliyezikwa kwenye makaburi hayo ya mashujaa. Ni makaburi ambayo hayatambuliki Kitaifa lakini wenyewe wenyeji wanalitambua na kulienzi kuwa ni eneo walilolazwa mashujaa wa vita vya dunia.

Anga nayo ilitandaza wingu zito, lililofunika jua utadhania nalo lilikuwa linajumuika na waombolezaji kwenye kumaliza msiba huo. Kijiji kilifurika wageni mahashumu wa ndani na nje ya nchi waliokuja kuhitimisha msiba huo. Miongoni mwa wageni hao, alikuwepo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Nchi ya Msumbiji, Mheshimiwa Allan Fernando, aliyetumwa kumwakilisha Rais wa Msumbiji katika msiba huo.

Pia alikuwepo Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini Msumbiji Bwana Jacob Steven au maarufu kwa lakabu ya Komandoo 'JS' akiwa ni mteule mpya kwenye idara hiyo. Pia alikuwemo katika msafara huo toka nchini Msumbiji, Daktari Anabella Munambo akiwa ni Daktari Mkuu katika hospitali mpya ya "Quelimane Central Hospital" iliyopo katika jimbo la Zambezi. Hao walikuwa ni baadhi tu ya vigogo wazito toka msafara viongozi wa Msumbiji.
Kwa upande wa Tanzania, mkururu wa vigogo nao walifurika kijijini Mahiwa, kuanzia wa Mkoa na wa Kitaifa. Mawaziri, Makatibu Wakuu na Mkuu wa Idara ya Usalama ya Taifa Bwana Mathew Kilanga alikuwepo kundini. Wasioelewa kinachoendelea na kushangazwa na ugeni ule mzito pale kijijini walikuwa wanajiuliza bila kupata majibu.

Swali kubwa vichwani mwao lilikuwa "huyu Bi.Josephine Nyagali alikuwa ni nani haswa katika historia ya nchi ya Tanzania mpaka apate bahati ya kulazwa malaloni pamoja na wanajeshi mashujaa waliokufa katika vita vya kwanza vya dunia?". Heshima ya Bi.Josephina kuzikwa hapo, ilitokana na babu yake mzaa baba, hayati "Nyagali Wa Nyagali" aliyekuwa mpiganaji wa Jeshi la Mjerumani enzi za vita vya dunia na kuzikwa katika makaburi hayo. Vita vya Mahiwa katika ya Mjerumani na Muingereza vilipiganwa mwaka 1917.

Ambapo Jeshi la Mjerumani likiongozwa na Jenerali Paul Emil von Lettow-Vorbeck walichuana vikali na Jeshi la Muingereza likiwa chini ya uongozi wa Luteni Jenerali Jacob van Deventer. Vita hivyo vya Mahiwa vilisababisha vifo vya askari si chini ya 2,000 wengi wao wakiwa ni Wanajeshi wa upande wa Uingereza. Katika baadhi ya Wanajeshi waliofariki, babu yake Bi Josephina, Koplo Nyagali Wa Nyagali nae alikuwemo, akabahatika kuzikwa eneo hilo na baadhi ya wanajeshi wachache waliozikwa hapo.

Pia mtoto wake Bi.Josephina, Kachero Manu ndio ambaye alipendekeza mama yake mzazi azikwe hapo kando ya kaburi la babu yake mzaa mama, kwenye eneo ambalo hata yeye Kachero Manu atakavyofariki atapendelea azikwe hapo. Muda wote wa shughuli hiyo Dr.Anabella, Kachero Manu na Komandoo 'JS' walikuwa hawaachani wamegandana kama kupe. Wasiowafahamu wakadhania ni watoto mapacha walioachwa na marehemu Bi.Josephina Nyagali wanafarijiana wenyewe kwa wenyewe.

La hasha..! hawakuwa na udugu wowote wa damu, ila walikuwa ni marafiki waliosafishiana moyo ambao kufahamiana kwao katika urafiki huo ulitokana na kazi pevu waliyoshirikiana kuifanya siku chache zilizopita huko nchini Msumbiji. Dr.Anabella alishindwa kuyazuia machozi yake wakati anaweka shada la maua juu ya kaburi la Bi.Josephina. Alivuta taswira jinsi mama yake na baba yake mzazi na nduguze walivyochinjwa kikatili shingo zao na wahusika hao hao waliopoteza uhai wa mama mzazi wa rafiki yake.

Wote watatu walikuwa wanafarijiana na kumpoza mpambanaji mwenzao Kachero Manu aliyefikwa na maswahibu mazito. Kachero ambaye alifiwa na mama yake mzazi kwa kuchinjwa kikatili na mahasimu zake toka nchini Msumbiji katika usiku wa kuamkia siku ya Wapendanao "Valentine Day" ya mwaka 2016. Yeye hakuwahi kuhudhuria mazishi ya mama yake kwa sababu alikuwa na safari ya muhimu sana ya kikazi nchini Msumbiji isiyowezekana kughairishwa kwa sababu yoyote ile. Hivyo alivyorejea toka safarini, ikabidi aunganishe moja kwa moja Kijijini kwao Mahiwa kwenye maandalizi ya arobaini ya kuhitimisha msiba wa mama yake.

Kwa uzalendo wake huo wa kukubali kukacha kushiriki msiba wa mama yake mzazi kwa ajili ya kujitoa mhanga kwa maslahi ya Taifa la Tanzania na Msumbiji, ndio maana nchi ya Msumbiji na Tanzania kwa ujumla wakaipa uzito shughuli hiyo kwa kutuma wawakilishi wao wazito. Baada ya shughuli zote zilizopangwa kufanyika hapo makaburini kuhitimishwa, na kuashiria msiba huo kumalizika kwa kupanda msalaba juu ya kaburi la marehemu, msafara huo ukarejea nyumbani kwao Kachero Manu kwa ajili ya kutoa rambirambi zao.

Mpaka kufikia majira ya saa 12:30 magharibi shughuli zote zikawa zimehitimishwa na wageni mbalimbali wakaanza kurudi kwenye makazi yao waliyofikia kabla ya kurejea makwao.
"Mbona huufanyii kazi msemo wa waswahili ule wa Mgeni njoo Mwenyeji apone, unaniacha mrembo naenda kulala peke yangu Mjane mimi, wewe wa wapi wewe....!" alisema Dr.Anabella kiutani, akimpa shutuma rafiki yake Kachero Manu wakati tayari anajiandaa kupanda gari aliloandaliwa na serikali tayari kwa kuondoka. "Ng'ombe wa kuazima anakamuliwa wima, nisingekuacha bahati yako mmiliki yupo hapa msibani anakaba mpaka penati, hapa alipo amefura kwa hasira, wivu juu yako..!" alijibiwa Dr.Anabella huku akipewa tahadhari ya kuwa makini na mchumba wake Kachero Manu, Faith Magayane.

"Kwaheri...niagie kwa niaba yangu, maana asubuhi nimemsalimia kaninunia utasema mie mke mwenza wake, na Wamakonde tunavyoogopeka kwenye sekta ya chumbani, alipo hana amani kabisa na mimi...!" alisema Dr.Anabella, huku wakikumbatiana kwa sekunde kadhaa na Kachero Manu nyuso zao zikiwa na bashasha mpwito mpwito kisha akapanda kwenye gari na kuondoka msibani.

Komandoo JS alikuwa amejitenga kando wanapeana michapo na mkongwe mwenzake Bosi Mathew Kilanga. Hawa walikuwa ni maswahiba wakongwe waliofanya pamoja mafunzo ya Ukomandoo na sasa wote ni Wakuu wa Idara za Usalama wa Taifa, katika nchi za Msumbiji na Tanzania.

Kachero Manu akawaacha waendelee kusogoa na kukumbushiana enzi zao, na kuamua kujumuika na familia yake wakiendelea kubadilishana mawazo mbalimbali. Giza likazidi kutanda eneo ile na watu wa karibu kuanza kurejea majumbani kwao na wa mbali kuondoka zao ili maisha ya kawaida yapate kuendelea.


Februari ya huzuni na majonzi
"Piga risasi wale kule wanakimbia, fanya haraka sana hamna kuwaonea huruma manyang'au hawa. Hamna kuwachekea wezi wa rasilimali za nchi yetu ya Msumbiji" ova ova. "Sawa mkuu tutawapa kipigo cha mbwa koko" ova ova ". Msiache majeruhi hakikisheni vizuri wafe mara moja hatuna bajeti ya kutibu majeruhi, na hakikisheni mizoga mnawafukia katika mahandaki kuficha ushahidi ova ova".

Yalikuwa ni maelekezo ya kwenye redio za upepo baina ya Afisa Mkuu, Operesheni maalumu ya kutokomeza wahamiaji haramu kwenye jimbo la Cabo-Delgado, Inspekta Jenerali Mark Noble kwenda kwa askari wake waliokuwa wametawanywa mitaani kuwashughulikia wahamiaji hao. Milio ya risasi na mabomu ya machozi yalisikika kwenye kila kichochoro cha kijiji cha Namanhumbire, kilichopo kilometa 30, mashariki mwa Jimbo la Cabo-Delgado.

Hakuna mhusika waliyemkusudia kwenye operesheni hiyo aliyesalimika, wote walikumbwa na dhahama na sekeseke hilo. Balaa na belua kubwa ilizuka ndani ya Jimbo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini ya rubi. Magari ya polisi yakiwa yamejaza polisi idadi ya kutosha yalikuwa yanaranda mitaani pamoja na magari maalumu ya kumwaga maji ya kuwasha kwa waandamanaji nayo yalikuwepo, yamekaa mkao wa tayari tayari kwa lolote.

Msako wa mtaa hadi mtaa, nyumba hadi nyumba, chumba hadi chumba, duka hadi duka ulikuwa unaendelea kuwabaini hao wanaoitwa wahamiaji haramu. Ving'ora vya magari ya polisi vyenye sauti ya kuogofya vilikuwa vinasikika kila kona. Cha kushangaza zaidi kwenye msako huo walengwa wakuu hawakuwa raia wa mataifa mengine bali walikuwa ni Watanzania.

Tena wengi wao ni wale wanaoishi kwa kufuata sheria za nchi kwa kupata viza ya kuingia Msumbiji na pia wakapata hati za ukazi. Mpaka kufikia majira ya saa tano usiku ya siku hiyo tayari mamia ya watu walikuwa wamefariki na wengine kujeruhiwa vibaya. Akina mama nao walikuwa wahanga wa uhalifu huo, wakajikuta wamebakwa hobelahobela na askari hao. Watoto wadogo wakajikuta wengine wao wamekuwa mayatima bila kutarajia. Mali za thamani kubwa zinazomilikiwa na Watanzania hao zikaporwa na askari hao madhalimu. Wale majeruhi waliosalimika wakapokonywa nyaraka zao muhimu kama vitambulisho na hati za kusafiria ili waonekane waliingia Msumbiji kwa kuzamia bila kufuata sheria.

Ili kuficha takwimu halisi za waliofariki, maiti hizo zilikusanywa na kuzikwa kwenye kaburi la pamoja la halaiki ili kupoteza ushahidi wa unyama uliofanyika. Walikuwa wanaogopa tukio lisije kuvuta macho na masikio ya wapenda haki na amani duniani, wakaanza kupaza sauti zao wakakitia kitumbua chao mchanga, wakaja kujikuta wapo kwenye mahakama ya uhalifu duniani iliyopo kule "The Hague", Uholanzi, wamepandishwa kizimbani.

Vyombo vya habari vya nchini Msumbiji vikalishwa habari potofu na Maafisa hao madhalimu walioendesha zoezi hilo haramu lenye malengo mahususi nyuma ya pazia. Wakazidi kuupotosha umma kwa kuwalisha matango pori kuwa waliouliwa ni wahalifu na wahujumu uchumi waliokuwa wanapora na kuchimba madini ya nchi ya Msumbiji kinyume na taratibu za nchi.

Wakasisitiza kuwa wahalifu hao walikuwa wamejihami kwa silaha kali za kivita, hivyo wameuliwa wakati wa mapambano ya ana kwa ana ya kurushiana risasi na wanausalama. Pongezi mbalimbali zikawa zinapeperushwa na viongozi wa juu serikalini kwa Bwana mkubwa, Inspekta Jenerali Mark Noble kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuzihami rasilimali za nchi ya Msumbiji.

Silaha za kivita zinazosemekana kukamatwa eneo la tukio zikawa zinaonyesha kwenye runinga ili kuthibitisha umma wa Watu wa Msumbiji kuwa waliouliwa ni wahalifu wasiostahili kuonewa hata chembe ya huruma. Watanzania mamluki waliohongwa ngwenje za kutosha wakajifanyisha wamekamatwa kwenye tukio hilo, baadhi yao wakiwa wameshikishwa silaha, na kujitia wanatoa ushuhuda mbele ya vyombo vya habari kuwa walikuwa ni genge la uhalifu lililokuwa limejipanga kwa mbinu za medani za kivita, hivyo wanaomba msamaha toka vyombo vya dola.

Magazeti yakapambwa na picha za Afisa Mkuu kwenye operesheni hiyo, Inspekta Jenerali Mark Noble akisifiwa kama shujaa wa nchi, mzalendo na mfia nchi wa kiwango cha kutukuka. Mmoja wa Mawaziri waandamizi, hakubaki nyuma kubariki operesheni hiyo akatoa ahadi ya donge nono kwa askari wote walioshiriki kuwashikisha adabu wahalifu hao wa Cabo-Delgado, iwe motisha kwao kuzidi kujitolea kiuzalendo katika siku za usoni.

Watanzania wachache waliofanikiwa kutoroka kwenye sokomoko hilo, wakaja kutoa ripoti ya kina ya tukio hilo nchini Tanzania. Wakapaza sauti zao kwa kutumia vyombo vya habari, wakitaka ufanyike uchunguzi huru.

Ikabidi sasa Inspekta Jenerali wa Polisi wa Tanzania afunge safari mpaka nchini Msumbiji kwenda kuonana na Mkuu mwenzake wa Jimbo la Cabo-Delgado Bwana Mark Noble ili wayaweke sawa. Baada ya majadiliano ya karibia wiki nzima baina yao, Inspekta Jenerali wa Tanzania akarejea. Alipokanya tu ardhi,pale Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, waandishi wa habari walijikusanya wakiwa na kimuhemuhe na kiherehere cha kujua kilichojiri katika kikao hicho cha ujirani mwema baina ya vigogo hao wawili wa polisi.

"Tumekubaliana kimsingi pande zote mbili kwamba wahalifu siku zote hawana mipaka. Hii mipaka iliyowekwa na Wakoloni isitufanye tukashindwa kupambana na uhalifu na hasa haya makosa yanayovuka mipaka ni lazima tushirikiane. Na kikubwa zaidi ni kubadilishana taarifa na kufanya operesheni za pamoja, mara kwa mara” maelezo hayo mepesi ya uzani wa nyoya la kuku ya Inspekta Jenerali wa Tanzania yakaonyesha kabisa amezidiwa kete na mwenzake Inspekta Jenerali Mark Noble kwa kupewa taarifa za uwongo juu ya tukio hilo.

Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza, vijana wa Mjini wanasema "Alilishwa matango pori na kutiwa ndimu juu ya matukio hayo hatarishi". Ndugu, jamaa na marafiki wa wahanga wa tukio hilo, wakakata tamaa ya kuona haki inatendeka kwa ndugu zao walioathirika kwenye uhalifu huo. Taarifa hiyo ilibaraganya kabisa ukweli halisi wa tukio hilo, kwani ilionyesha kama vile matukio hayo hayajafanywa kabisa na polisi wa Jimbo la Cabo-Delgado, bali ni mtifuano baina ya wahalifu wa Tanzania na Msumbiji.

Wakati shuhuda za wahanga wenyewe zinasema kuwa polisi wa Cabo-Delgado ndio watuhumiwa haswa wa vitendo hivyo wakishiriki kuvilinda vikundi vya kihalifu mitaani. Mategemeo na matarajio yao waathirika wa matukio hayo yalikuwa ni kuletewa taarifa yenye fusuli ya kutosha isiyoacha hata chembe yoyote ya mashaka. Ushindi ukawa umeelemea mikononi mwa genge hilo la wahalifu lililopo ndani ya mfumo rasmi wa nchi.

Walilolikusudia genge la wahalifu ndani ya mfumo rasmi likawa limeshatimu, wakiwa wamefanikiwa kumuongopea mpaka Inspekta Jenerali wa nchi ya Tanzania. Bila kujua ya kwamba wamekumbatia waya wa umeme mkubwa vifuani mwao utawateketeza bila kuacha masalio yao.

Chambilecho "Daima hamna marefu yasiyo na ncha, na haki siku zote ni kama mfano wa boya majini, haiwezi kufichwa kwa kuzamishwa, tabia ya haki siku zote ni kuelea juu".
Idara ya Usalama wa Taifa, Tanzania ilikuwa macho kodo, haijalala usingizi wa pono. Iikuwa ipo kwenye pembe za chaki inafuatilia matukio hayo kwa umakinifu na ukaribu zaidi. Wahalifu hao walichokoza nyuki, wakati wa kukiona kilichomtoa kanga manyoya ulikuwa unakaribia kwa upande wao.


Matukio hayo ya uhalifu yanayowawinda Watanzania pekee hayakukoma. Yakazidi kushamiri na kutamalaki katika Jimbo hilo la Cabo-Delgado lenye kusifika kwa utajiri mkubwa wa madini ya rubi nchini Msumbiji.

Watanzania hao wanyonge na madhulumu hawakuwa na mtetezi wa kuwasemea na kuwaokoa. Wakawa wanapopolewa mitaani kama mbogo msituni anavyowindwa na majangili.

Likaja kutokea tukio lingine la kutisha, tukio ambalo likavifanya Vyombo vya Usalama vya Tanzania vikose simile, na kuamua sasa kwa kauli moja kuwashughulikia Mafioso wote wa Jimbo la Cabo-Delgado wanaopenda kuwachokoa Watanzania.

Ilikuwa ni tarehe 08/02/2016 ya huzuni, simanzi na majonzi makubwa kwa nchi ya Tanzania. Watanzania wapatao 16 walipigwa risasi na kufariki hapo hapo huku makumi kadhaa wakijeruhiwa wakati wakiwa kwenye maduka yao ya kubadilisha fedha za kigeni na kununulia madini, kisha wakaporwa pesa zote na madini yao.

Watanzania hawa walikuwa wakiishi na kufanya kazi katika eneo lenye madini ya rubi liitwalo Montepuez, kwenye Jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa nchi ya Msumbiji.

Yalikuwa ni mauaji ya kinyama na yasiyokubalika kwa jamii ya watu waliostaarabika. Mauaji ambayo yalisababisha kilio katika kila kona ya nchi ya Tanzania, Bara na Visiwani, huku wananchi wakigubikwa na simanzi isiyomithilika na joto la hasira likichemka vifuani mwao.
Lakini kabla ya mauaji hayo, wiki mbili zilizopita serikali ya eneo hilo ilitoa muda wa siku 5 kwa raia wote wa Tanzania wapatao 5,000 waishio hapo Cabo Delgado kuondoka mara moja na kurudi nchini kwao Tanzania.

Hii haikuwa taarifa yenye kupendeza hata kidogo masikioni mwa wananchi wa Tanzania, hasa wakikumbuka udugu wa asili kati ya wananchi wa Tanzania na Msumbiji. Ni kama vile kuna watu walikuwa wanachezea sega la nyuki ili kuwagombanisha ndugu wa damu walioshibana.

Ni tukio ambalo lilileta simanzi na fadhaa kubwa kwa ndugu wa wahanga na Watanzania kwa ujumla. Mikasa hio endelevu ilikusudia kuchimbia kaburini mahusiano mema baina ya hizi nchi mbili.

Ilitaka kufuta mema yote ya siku za kisogoni yaliyotendwa na Watanzania kwa watu wa Msumbiji. Watanzania wengi haikuwahi kuingia akili mwao wala katika fikra zao hata siku moja kuwa itafika siku Watanzania watatendewa unyama kama huu na ndugu zao wa Msumbiji.

Ndugu zao kabisa wa damu wanaotenganishwa tu na mipaka ya wakoloni. Katu hawakutegemea msaada wao wa asali na maziwa katika kipindi cha kupigania Uhuru wa Msumbiji kutoka kwenye makucha ya mabeberu wa Kireno malipo yake yangekuwa shubiri.
Watu wa Msumbiji baada ya kufanikiwa kumng'oa Mkoloni, wakaanza kupigana vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuzalisha maelfu wakimbizi. Bado Watanzania hawakuwafungia vioo ndugu zao, waliwakaribisha kwa mikono miwili waje nchini mwao, wakaishi nao kwa amani na utulivu. Wakashirikiana nao kutwa kucha katika shida na raha, katika mvua na jua bila utengano wowote.

Bila ya shaka tukio hili la mauaji ya watu 16 likasababisha uhusiano baina ya nchi ya Tanzania na Msumbiji kwenda zigizaga, Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake nchini Msumbiji ukawa upo makini kufuatilia na kutoa msaada unaohitajika kwa wahanga wote wa machafuko hayo.

Pia ubalozi ukajitwika jukumu zito la kuwarejesha nyumbani wahanga wote wa kadhia hii mbaya, huku wakitega sikio kusubiri tamko toka kwa viongozi wa juu wa nchi ya Msumbiji.
Lakini ukimya ukazidi kutawala toka kwenye Vyombo vya Dola vya Msumbiji utasema waliokufa ni nguruwe pori wasio na thamani yoyote.

Kwa upande wa maadui wa Umoja wa nchi za Kiafrika, chokochoko hiyo baina ya nchi ya Msumbiji na Tanzania kwao ilikuwa ni furaha sheshe.

Mabeberu hao walikuwa wanajimwashamwasha pindi wakiona nchi huru za Kiafrika zinavyogombana wenyewe kwa wenyewe.

Lengo lao kubwa ni kuona Afrika nzima inaingia kwenye machafuko ya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyo nchi za Congo, Sudani Kusini, Afrika ya Kati, Somalia, Mali na kwingineko ili wajichotee rasilimali bwerere bila jasho.

Lengo la mabeberu hao lilikuwa ni kuziona nchi za Afrika, kamwe hazijikomboi kutoka kwenye lindi la umasikini, ujinga na maradhi.

Walitamani wawe ni nchi ombaomba na tegemezi kwao miaka nenda miaka rudi. Moto wa kuni za fitina ulishawashwa na kuchochewa na maadui, ni busara tu za viongozi wa Tanzania na Msumbiji ndizo zinalizokuwa zinahitajika kuzuia uhasama na kukatana baina ya nchi zao.


Tarehe 11/02/2016 siku 3 baada ya mauaji hayo ya Msumbiji, muda wa saa 4:30 usiku kwa majira ya saa za Afrika Mashariki, Kachero nambari wani nchini Tanzania Bwana "Manu Yoshepu" maarufu kwa lakabu ya “Mwiba wa Tasi” ndio alikuwa anaingia nyumbani kwake maeneo ya Mbezi-Juu akiwa hana hili wala lile.

Alikuwa anaishi eneo linaloitwa “Kwa Pembe” akiwa amechoka vibaya kutokana na mazoezi magumu aliyotoka kuyafanya muda mfupi uliopita. Alikuwa ameloa jasho chepechepe mwili mzima huku anatwetwa kwa uchovu.

Alikuwa amejiwekea ratiba yake binafsi kuwa akitoka ofisini kwake saa 9:30 Alasiri juu ya alama maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam, huwa anapitia ukumbi wa kufanyia mazoezi "GYM" maeneo ya Mwenge jengo jirani na kiwanda cha madawa ya binadamu cha SHELLYS.

Huwa anafika hapo kwenye ukumbi kisha anafanya mazoezi mazito kwa muda wa masaa yasiyopungua mawili mpaka saa 12 ya jioni. Hapo atafanya mazoezi ya kuongeza pumzi kwa kuendesha baiskeli na kukimbia, pia atafanya mazoezi ya kuongeza stamina katika mwili kwa kubeba vitu vizito, mwisho anamalizia kwa mazoezi ya viungo.

kisha akitoka hapo mazoezini atapitia kwenye jengo la maduka ya kuuzia bidhaa maarufu kama "Mlimani City Mall" iliyopo barabara ya Sam Nujoma kununua mahitaji mbalimbali ya nyumbani anayohitaji. Kwa kawaida maduka ya hapo unaweza kupata kuanzia bidhaa za chakula, nguo, vifaa vya elektroniki na kila kitu unachohitaji kinapatikana hapo.

Kama hana ratiba ya kujipikia nyumbani siku hiyo basi akitoka "Mlimani City Mall" atapitia kwenye mgahawa mdogo ulio nje ya "Mlimani City Mall" uliopo mkabala na kituo maarufu cha kujazia mafuta vyombo vya moto cha "TOTAL", hapo atakula chakula chake cha chajio atakachopenda.

Ila mara nyingi usiku huo halafu chakula kizito sana kinakuwa chepesi kukwepa kutoka kitambi. Kisha baada ya hapo ataondoka na gari yake pendwa aina ya "Nissan Navara" rangi nyeusi akipitia njia ya 'Makongo Juu' anakuja kutokezea Goba Kati, kisha anashika njia ya uelekeo wa kulia kwake mpaka muda wa saa 1:30 ya usiku mbichi anakuwa tayari amesharejea maskani kwake zamani.

Ambapo akifika nyumbani atapumzika nusu saa kisha ataanza mazoezi ya karate na taikondo kwa muda wa nusu saa tena, siku yake kwa upande wa mazoezi inakuwa inaishia. Baada ya hapo ataenda kuoga bafuni kwake kwa ajili ya kujiandaa kupumzika.

Alikuwa akipenda ataangalia televisheni yake mpaka saa 4 au 5 usiku halafu anaenda kujitupa kitandani kwake. Kama hajisikii kuangalia runinga basi atajichimbia ndani ya maktaba yake kujisomea vitabu mbalimbali vya kujiongezea ufahamu na maarifa.

Hiyo ndio ilikuwa ratiba yake ya mizunguko ya baada ya kazi aliyojipangia na kuiheshimu vilivyo ratiba yake. Ikifika mwishoni mwa juma ndio anapumzika nyumbani muda wote hatoki ila kwa dharura au kuwatembelea ndugu, jamaa na marafiki. Ila siku hiyo alichelewa mno kurudi nyumbani, na sababu ilikuwa wazi kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari yaliyoshonana barabarani.

Foleni ya magari ilianzia maeneo ya Mwenge mpaka kufika Ubungo kwa hiyo magari yalikuwa yanakwenda kwa mwendo wa kinyonga au kama msafara wa Bwana na Bibi harusi wanaoelekea kwenye ukumbi wa kufanyia tafrija. Kwa kuwa yeye ni mzoefu wa Jiji la Dar es Salaam hilo halikumpa shinikizo wala wahaka wa moyo, zaidi ya kubaki kuchukia tu moyoni.
Maana Jiji la Dar es Salaam ni Jiji ambalo huwezi kukadiria utafika kwa muda muafaka sehemu unayoikusudia. Jiji hili wewe unaijua saa ya kutoka tu lakini saa ya kufika ni majaliwa yake Mola. Ukiwa mgonjwa huwezi kufika kwa wakati hospitalini, ukiwa muajiriwa huwezi kuripoti kibaruani kwako kwa muda muafaka na ukiwa mwanafunzi ukifanya masihara daima utakuwa unachezea viboko vya walimu wako.

May 8, 2020
Thread starter
Add bookmark
#2
Umbali ambao unapaswa kutumia nusu saa tu kufika unaweza ukatembea kwa masaa mawili kutegemeana na mabadiliko ya siku na siku ya msongamano wa magari. Na bado kila siku bandarini yalikuwa yanaingizwa magari mapya utasema yaliyopo hayatoshi. Foleni hizo barabarani zilikuwa zinachangiwa na mengi, ikiwemo ulimbukeni wa matumizi ya magari. Hapo ndio unakuta familia moja inaleta barabarani kwa siku gari zaidi ya 4.

Baba, Mama, Watoto na Mtumishi wa nyumbani kila mmoja anatoka na gari lake. Pia ubovu wa miundombinu ya barabara nacho ni chanzo kikubwa cha kusababisha msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam. Ndio maana serikali katika kutatua changamoto ya msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, ikabuni njia mbalimbali kama mabasi ya mwendokasi maarufu kama UDART, ili watu washawishike kuacha magari yao nyumbani watumie usafiri wa umma. Pia ikajenga barabara ya kupita juu kwa juu kwenye makutano ya barabara eneo la TAZARA maarufu kwa jina la "Mfugale Flyover".

Pia serikali katika kuzidi kutatua changamoto ya foleni ikaanzisha ujenzi barabara ya njia nane kutokea eneo la Kimara Mwisho kuelekea Chalinze. Foleni hiyo siku hiyo iliharibu kabisa mipango yake ya kufika nyumbani kwa wakati.

"Nadhani serikali ikihamia rasmi Dodoma na ikahamisha ofisi zake na watumishi wake, magari yatapungua sana hapa Jijini. Pia kama itaboresha huduma muhimu kama afya na elimu huko Mikoani pia itapunguza wimbi la watu wanaokuja Dar es salaam kusaka matibabu na kukata kiu ya elimu katika Vyuo mbalimbali vilivyopo Jijini Dar es Salam.

Pia kama itawasaidia wakulima kupata masoko ya uhakika ya mazao yao itawasaidia watu wa vijijini hasa vijana kujikita kwenye kilimo kubakia huko huko walipo wasihamie Dar es salaam kusaka vibarua viwandani na kufanya uchuuzi wa bidhaa mitaani",

alikuwa amezama kwenye fikra tunduizi kichwani mwake huku akiwa ameshikilia usukani wake wa gari lake ambalo lilikuwa linajivuta taratibu kwenye mnyororo huo wa magari. Mpaka alipoingia barabara ya Chuo Kikuu cha ardhi "UCLAS" ndipo foleni ikakatika akawa anaendesha gari yake kwa madahiro yote, kwa kujinafasi bila kikwazo chochote.

Alipofika nyumbani kwake getini, akapiga honi mara mbili, mlinzi kirungu wake akaja mbio mbio kumfungulia geti. "Shwari hapa, kuna la zaidi? " alisalimia Kachero Manu huku anashusha kioo chake cha gari wapate kusikilizana vizuri na mlinzi wake. "Tumesalimika Mkuu amani tupu, shaka ondoa." alijibu kiunyenyekevu huku akiunda tabasamu pana usoni mwake.

"Haya usiku mwema, kazi njema..!" akaaga kwa sauti ya kichovu kisha akapita zake getini na kwenda moja kwa moja kulisweka gari lake kwenye sehemu maalumu aliyoitenga kwa ajili ya maegesho ya magari. Baada ya kulizima gari lake, akatoa begi lake lenye kompyuta kutoka kwenye gari akalipachika begani kisha akawa anakagua usalama wa mazingira ya nje ya nyumba yake.

Macho yake yalikaribishwa na mandhari nzuri ya bustani ya maua na nyasi za ukoka iliyonawiri, inayotunzwa kiumaridadi mkubwa. Baada ya kushangaa hapo nje kwa muda mchache tu, akaingia zake ndani ya nyumba yake hiyo ya kisasa ya roshani moja.
Nyumba ambayo kuanzia mchoraji wa ramani mpaka fundi muashi aliyeijenga walisugua bongo zao vilivyo na kuzitendea haki fani zao. Kila mtu aliyeiona nyumba hiyo kwa mara ya kwanza alistaajabishwa na uzuri wake.

Wapo ambao hawakuamini kama hiyo nyumba ipo Tanzania, wapo waliofikicha macho yao kujidhania labda wapo ndotoni wanaota mchana mchana, na wapo wale wenye vijiba vya roho waliozusha kuwa sio nyumba yake ni ya serikali. Na pia kuna waliokataa kama nyumba hii imejengwa na mafundi wazalendo wa hapa hapa nyumbani Tanzania.

Ilimradi uzuri wa nyumba hii ulikuwa wa kupigiwa simulizi kwenye kila kona kwa kila aliyebahatika kuitia machoni. Bosi wake kazini walikuwa wanagombana na Kachero Manu juu ya nyumba hiyo. Alikuwa anamtaka aipangishe kisha apewe nyumba ya kawaida ya kuishi na serikali. Kiusalama mtu nyeti kama Kachero Manu hakutakiwa kuishi nyumba ya kifahari itakayoibua mjadala wa kuleta taftishi kwa watu juu ya aina ya kazi anayoifanya.

Mubashara tu alivyoingia ndani alielekea jikoni kwenye jokofu lake la kisasa aina ya “Samsung” yenye mlango unaoitwa “French door”. Jokofu ambalo ilikuwa limejazwa mashrabu mbalimbali kochokocho kuanzia maji ya chupa, soda, juisi na vinywaji mbalimbali vikali. Moja kwa moja akaichomoa chupa ya maji yenye ujazo wa lita 1 kutoka kweye trei yake, akaifungua na kuanza kufakamia chupa hiyo ya maji baridi kama anafukuzwa kutokana na kiu kali aliyo nayo kutokana na mazoezi.

Baada ya sekunde 25 akawa tayari ameshaimaliza chupa yake. Alikuwa anayapenda sana maji hayo safi aina ya “USAMBARA SOFT DRINKING WATER” maji matamu sana kutoka safu ya milima ya Usambara, Tanga kutoka kwenye kiwanda cha Predeshee mmoja anaitwa "Zombe" ambaye anajulikana Mji mzima wa Tanga.

Akaitupa chupa ile ndani ya pipa la kutupia takataka. Baada ya kutoka jikoni akashika uelekeo wa kuelekea kwenye chumba cha kulala. Nyumba ya Kachero Manu ilikuwa na chumba tatu huku kila chumba kikiwa kinajitegemea choo na bafu na sehemu ya kubadilishia nguo.

Chumba hizo zilikuwa zipo kwenye roshani ya kwanza. Pia ilikuwa na jiko la kisasa lililosakafiwa kwa umaridadi na marumaru kutoka nchini Hispania. Nyumba hiyo ilikuwa na sehemu pana ya kulia chakula iliyotenganishwa na vioo na sebule kubwa iliyowekwa kutani mwake paneli za plastiki za “polypropylene” (PEPP) zenye kazi ya kuzuia sauti (sound proof), ambavyo hivi vyote vilikuwa vimejengwa chini ya nyumba.

Kiasi kwamba ukiwa sehemu ya kulia chakula unaweza kuwaona watu waliokaa sebuleni ila huwezi kusikiliza mazungumzo yao, utakachoambulia ni kuona midomo yao inacheza cheza wakati wa maongezi yao. Ndani ya uzio kulikuwa na uwanja wa kuchezea mpira wa mikono wa basketi bila kusahau bwawa kubwa la kuogelea huku ikiwa imezungukwa na ukuta mkubwa wenye urefu usiopungua meta 10.

Alielekea moja kwa moja chumbani kwake ili ajimwagie maji na kulala moja kwa moja maana kwa kawaida huwa analala saa tano juu ya alama ila siku hiyo alikuwa amechoka kupitiliza.
Alipoufikia mlango wa chumbani kwake akachomoa ufunguo kutoka kwenye suruali yake akafungua mlango na kuingia ndani ya chumba. Akawasha taa akalivua begi lake la mgongoni lenye kompyuta mpakato "laptop" ndogo ya kisasa na kuliweka juu ya meza ndogo, na simu zake mbili za mkononi nazo akaweka juu ya meza hiyo, meza ambayo kwa kawaida anaitumia kufanyia shughuli zake za kuandikia akiwa chumbani humo kama hajisikii kwenda maktaba.

Kisha akaamua apitilize bafuni kwake. Akiwa tayari ameshika kitasa cha mlango wa chumba cha kubadilishia nguo zake anajiandaa kukinyonga kimpe ruhusa ya kuingia akasikia muito wa simu yake unalia mlio ambao ulimshtua sana. Mapigo ya moyo wake yakaanza kwenda mbio mithili ya saa mbovu akijua tu kuna jambo kubwa lipo mbele yake litamkabili tu.

Mshtuko ulimpata kwa sababu huo ni mlio maalumu aliouweka kwa ajili ya kuitambua simu anayopigiwa na Bosi wake Mkuu, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Akazidi kushikwa na tumbo joto, moyoni mwake akiyakinisha kuwa kuna tukio kubwa limetakadamu ndio maana Bosi wake huyo anamtafuta kwenye simu.

Akaachana na kitasa hicho akageuka na kukimbilia moja kwa moja kwenye meza yenye simu hiyo. Bado swali lilikuwa linajifanyia takiriri kichwani mwake anajiuliza mara mbili mbili "Saa tano na dakika mbili usiku huu, Bosi anapiga simu kuna dharura gani? mbona sio kawaida yake?".

Kisha haraka haraka akaipokea kabla haijakatika kwa kubonyeza kitufe cha kupokelea simu na kuisogeza simu kwenye sikio lake la kushoto kisha akatangulia kumsalimia "Shikamoo Kiongozi". Alijizoesha kumuita Bosi wake kwa jina la "kiongozi", kisha akaitikiwa na kubandikwa swali la ghafla,"Marhaba kijana wangu Manu, umeangalia taarifa ya habari ya televisheni ya "AZAM TWO" ya saa 2:00 usiku leo?".

Kachero Manu akajibu kwa unyenyekevu mkubwa "Hapana Kiongozi", nimechelewa kurudi nyumbani kutokana na foleni ya barabarani, je kuna tukio gani nilifuatilie Kiongozi?. Bosi akamjibu haraka haraka "nenda kawahi sasa hivi kuangalia marudio ya taarifa ya habari muda huu saa tano usiku, ufuatilie kwa umakini kusikiliza tukio la kuuawa na kujeruhiwa na kufukuzwa kwa Watanzania waishio katika jimbo la Cabo-Delgado, huko Msumbiji kisha kesho asubuhi saa tatu kamili asubuhi bila kuchelewa tukutane ofisini kwangu.

Pia simu yangu nikiikata tu ufanyie kazi ujumbe nitakaokutumia haraka iwezekanavyo", kisha kabla Kachero Manu hajatoa maelezo yoyote, Bosi wake akawa tayari ameshakata simu yake zamani sana. Hapo hapo akafahamu Bosi wake kakasirika kutokana na kutokuwa na habari na tukio hilo nyeti kwa usalama wa nchi.

Moja ya sifa ya Kachero bora ni kuwa na habari anazohitaji Kiongozi wake kwa wakati muafaka, hatakiwi kuwa mtu boya boya au mtu zumbukuku mzungu wa reli asiyefahamu kinachoendelea ulimwenguni na nchini mwake kwa ujumla. Akiwa bado kapigwa na butwaa hajui hata pa kuanzia akasikia mlio wa meseji kuashiria kuwa kuna ujumbe umetumwa kwake, akaupuuzia kwanza, hakutaka kuufungua.

Himahima akakimbilia sebuleni kuwasha king'amuzi chake cha AZAM-TV akaanza kuitafuta chaneli ya "AZAM-TWO" kwa kutumia kisengeretua chake, kwa bahati akakutana na taarifa ya mwandishi wa televisheni ya "AZAM-TWO" Mkoani Mtwara, Ndugu "Mohammed Mwaya" anadadavua kwa ufasaha maelezo ya mauaji hayo ya tarehe 8/02/2016 na manyanyaso yanayoendelea huko katika Jimbo la "Cabo-Delgado" kwa ufasaha na umahiri mkubwa.

Alipomaliza kuangalia taarifa hiyo akazima televisheni yake na kuamua kuisoma meseji ya kwenye simu yake iliyoingia punde tu. Ujumbe huo aliotumiwa ulikuwa unasomeka kama ifuatavyo; "Black Bag Job kwa Birdwatcher toka Msumbiji, anakusubiria haraka sana kwenye uwanja wa mpira Chambezi, Bagamoyo usiku huu, fanya hima uende kuonana nae".

Alipomaliza tu kuusoma ujumbe huo akajikuta anafumba macho yake huku anazidi kuishiwa nguvu kabisa, ikabidi kwanza avute kiti chake na kukaa chini. "Kazi imeanza upya, kufa au kupona, mgeni wa usiku mwenye ujumbe wangu..!" alijisemea mwenyewe kimoyomoyo huku anazidi kuogelea kwenye bahari ya fikra.

Akajikaza kisabuni akanyanyuka kitini na kwenda kuoga haraka haraka ili aondoke usiku huo huo kuelekea Bagamoyo. Wakati anaoga mawazo yalimjaa kichwani kuwa lazima atapewa kazi ya kwenda Msumbiji. Alichukia sana moyoni moyoni mwake hasa kipindi hiki ambacho alipanga awe karibu zaidi na mchumba wake kuzidi kupalilia penzi lake.

"Kazi yetu hii ya Ukachero ni kama starehe ya mbwa kukalia mkia wake, kwa maana tunapata muda mfupi wa kustarehe lakini muda mwingi tunakuwa kwenye tabu na mahangaiko" aliwaza Kachero Manu huku anajipakaza povu sabuni mwilini mwake na kuiruhusu mvua ya maji ya bomba la juu ianze kulowanisha mwili wake. Alivyomaliza kuoga, akaingia chumbani kwake kwa ajili ya maandalizi ya safari. Akavalia fulana yake nyeupe na suruali ngumu ya dangirizi ya rangi buluu bila kusahau kubeba bastola yake ndogo yenye kiwambo cha kuzuia sauti.

Alivyojiona yupo tayari kwa kuondoka akaangalia simu yake akaanza kuperuzi mitandao ya kijaamii kama "FACEBOOK" na "WHATSUPP", akatuma meseji mbili tatu za mahaba kwa mchumba wake kisha akazima mtandao wa simu yake. Akazima taa ya chumbani mwake na kufunga mlango wa chumba chake tayari kwa kuanza safari ya kuelekea Bagamoyo usiku huo.

Wakati anaelekea kwenye maegesho ya magari alikuwa akizidi kuwaza na kuwezua mkutano wake wa kesho saa 3:00 asubuhi na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa nchi. Alipazwa kwa fikra za jambo analoitiwa na Bosi wake kesho kazini. Alitambua tu wito wake unakuwa ni wito wa kupewa shughuli maalumu ya kufanya ambayo inakuwa na sura ya kufa au kupona.
Vinginevyo angemsubiria tu afike kazini kesho asubuhi ndio ampashe hiyo taarifa. Akajuta kidogo kwa Mungu kwa kumpa kazi inayompatia mkate wake wa siku kupitia kuiweka roho yake rehani chini ya vivuli vya risasi. Sawa waswahili wanasema fuata nyuki ule asali lakini wanasahau pia fuata nyuki upate manundu usoni, kazi yake ilikuwa ni sawa na kuchezea shilingi karibu na tundu la choo.

Akaweka nadhiri kama atatumwa aende "Cabo-Delgado-Msumbiji" akifanikiwa kurudi salama atahakikisha anafunga ndoa haraka na mpenzi wake wa siku nyingi tokea wapo mwaka wa kwanza Chuo Kikuu-Dodoma (UDOM). Mrembo mwenye uzuri wa shani kama angekuwa ni jamii ya ndege angekuwa ni tausi, alikuwa anaitwa "Faith Magayane" anayeishi Dodoma akifanya kazi katika benki ya KCB tawi la Dodoma kama Afisa mikopo.

Alikuwa ni mlimbwende wa viwango vya kimataifa mwenye sifa ya kupewa ithibati ya uzuri na shirika la viwango la kimataifa la "ISO". Njia nzima Kachero Manu wakati anaendesha gari lake kuelekea Bagamoyo alikuwa anavuta fikra kwa mtriririko wa matukio moja baada ya jingine namna walivyokutana na mpenzi wake enzi wapo Chuo Kikuu. Chuo kizima kuanzia Wahadhiri mpaka Wanachuo wenzake walikuwa wanalimezea mate ya fisi penzi la mrembo huyu mkamilifu wa kila idara katika mwili wake kuanzia sura, sauti, umbile, makalio, miguu, kiuno na kila kitu chake utakipenda tu utake usitake.

Vijana wa mjini wangesema "Faith Magayane" alikuwa ni kama maji, upende usipende, utayatamua tu usipoyanywa, utakutana nayo kwenye chakula, au utakutana nayo bafuni wakati wa kuoga. Mrembo huyu kama jina lake linavyosema basi na tabia zake zilisadifiana hivyo hivyo alikuwa ni mwenye imani na muaminifu.

Alikuwa hapapatikii wala kushobokea pesa za Mapredeshee na Vibopa wa Jiji la Dodoma. Ilishawahi kutokea siku moja, mmoja ya mawaziri wastaafu alienda benki anapofanyia kazi mrembo huyu. Wakati anahudumiwa na mrembo Faith akampa bahashishi ya milioni 5 na akamuachia na kadi ya mawasiliano yenye namba zake za simu amtafute akitoka kazini. Lakini wahuni wanasema "aliisoma namba", hata kutumiwa meseji ya asante hakuambulia.
"Kiendacho cha mganga hakirudi", pesa zote hizo milioni 5 alizohongwa, aliamua kuzipeleka kwenye kituo cha watoto yatima kilichopo maeneo ya kitongoji cha Msalato. Hakuwa kama wale warembo ambao kutokana na uzuri wao basi sehemu zao za siri zinapata tabu kutokana na tamaa ya pesa.

Tuachane na mrembo Faith hadithi na simulizi zake namna alivyokuwa anawapa tabu vigogo wenye pesa na ahadi kemkem kwake au wahadhiri wa chuo wenye uchu wa fisi na ahadi za kumpa daraja la juu kwenye mitihani yake, hao wote simulizi zao haziwezi kuisha leo wala kesho, wewe tosheka tu kuwa uzuri wa Faith Magayane sio wa dunia hii, ni moto wa kuotea mbali.

Ukaribu wa Kachero Manu na mchumba wake ulianzia siku ya kwanza tu kuja kuripoti chuoni. Wote walipanda basi moja la "SHABIBY LINE", na kwa bahati walikaa siti sambamba. Sasa safari ya kutoka Dar es salaam mpaka Dodoma ni zaidi ya masaa 8 kwa mwendo wa wastani ingekuwa ni vigumu kukaa pamoja masaa yote bila kupiga stori mbili tatu baina yao. Hapo ndipo ukaribu ulipoanzia, walibadilisha namba zao za simu. Wakawa wanasalimiana mara kwa mara kwa kupigiana na kutumiana meseji. Kwa kuwa walikuwa wanasoma kozi tofauti kuna wakati mpaka wiki mbili mtawalia hawatiani machoni.

Kachero Manu alikuwa anasoma kozi ya Digrii ya mambo ya kudhibiti uhalifu "Criminology" na Faith alikuwa anasoma Digrii ya Uhasibu. Faith alimpenda sana Kachero Manu kutokana tu na upole wake na ustaarabu wake. Maana wengi wa wanaume waliokuwa wanaomba namba ya simu ya Faith walishindwa kudhibiti nafsi zao, waliishia kumtongoza siku hiyo hiyo kutokana na pupa na haraka zao.

Walisahau msemo wa wahenga wa kuwa "haraka haraka haina baraka" na "subira yavuta kheri". Wao walikuwa wanafanyia kazi msemo mwingine wa wahenga wa "ngoja ngoja yaumiza matumbo" lakini kwa Faith waliula wa chuya. Hakuwa wale wasichana wanaoitwa mitaani "maharage ya Mbeya", maji mara moja tu umekula tayari.

Mpaka walipofika mwaka wa kwanza muhula wa mwisho ndipo penzi zao likaanza kuchipua kwa kasi. Ilitokea siku moja isiyo na jina walienda kupata chakula cha pamoja katika kantini ya Chuo. Ghafla mvua kubwa ya kidindia ikaanza kunya. Bahati nzuri Kachero Manu alikuwa amebeba mwavuli wake kutokana na wingu lililokuwa limetanda siku hiyo. Hivyo wakawa wanautumia kujikinga na mvua wakati wanaondoka kurejea hosteli.

Njiani mvua ikazidi kutamalaki, zikaanza sasa kupiga radi za sauti ya kuogofya, Faith akajikuta tu bila kupanga amemkumbatia Kachero Manu kwa hofu ya radi. Matiti yake madogo na laini yaliyochongoka kama konzi na kusimama dede yakamchoma choma kifuani Kachero Manu. Nae bila kufanya ajizi akajishtukia ameutupa mwavuli wake kando na amemkumbatia kindakindaki hataki kumuachia. Mapigo ya moyo wake yakawa yanadunda kama moyo unataka kuchomokea kifuani, kutokana na kupandwa na hawaa ya nafsi.

Akajikuta anatamka kwa sauti ya mahaba "Faith nakupenda sana kuliko kitu chochote hapa duniani, wewe ni msichana wa maisha yangu yote". Faith nae hakulaza damu hii nafasi ya kupendwa na mwanume aliyekuwa anamtamani kwa udi na uvumba. Akisubiria kwa hamu na tashiwishi kubwa, siku ya kuambiwa kuwa anapendwa naye. "Nami nakupenda pia Manueli, usije utesa moyo wangu, ninakukabidhi funguo zake uufanye utakavyo" wewe alijibu Faith kwa sauti nyororo ya puani. Kuja kushtukia, wote wawili wameloana mvua chapachapa na mwavuli wameshautupa kando muda mrefu.

Hapo ndipo safari yao ndefu ya mapenzi ilipoanzia na kama ingekuwa mapenzi ni kitabu huo ndio ungekuwa ukurasa wao wa kwanza. Baada ya hapo Kachero Manu akasafiri kwenda nchi za ng'ambo kwa zaidi ya miaka mitatu lakini Faith alifanikiwa kuvishinda vishawishi akatunza ubikira wake na uaminifu kwa mchumba wake. Alitamani siku ya ndoa yake avikwe kisarawanda.

Mila za kabila lao, mwali ambae ni bikira alikuwa anavikwa nguo nyeupe kiunoni inayoitwa kisarawanda na bibi yake mzaa kuthibitisha ubikira wake. Lilikuwa ni penzi la siri hamna mtu alifahamu mahusiano yao mpaka Faith anamaliza chuo. Wengi walijua anaringa sana maana hawajawahi kumuona hata kusimamishwa chemba na mvulana yoyote pale chuoni, kumbe mchumba wake yupo Marekani.

Hakuwa kama wale wasichana malimbukeni wanaojitangaza kwenye mitandao kila akipata mchumba mpya. Sasa Kachero Manu mipango yake ili afunge nae ndoa haraka mpenzi wake Faith.

Ulishapita muda mrefu wa kuweza kumsoma tabia zake na alijiridhisha pasina mashaka yoyote kuwa Faith anafaa na ana vigezo vyote vya kuwa mama mtarajiwa wa watoto wake. Alishamtambulisha tayari kwa baadhi ya ndugu na jamaa zake ilibakia yeye tu kwenda kujitambulisha rasmi kwa wazazi wa mpenzi wake, ili taratibu zinazofuata za ndoa zifuatie.

Alitambua wasichana warembo ambao ni waaminifu kama mpenzi wake Faith katika zama zetu hizi ni wa kutafuta na tochi au darubini ya kuangalizia vijidudu. Wasichana wengi warembo mitaani ni wahonyoaji au vijana wa mjini wamewapa lakabu ya wachunaji mabuzi hawana mapenzi ya dhati. Wanachoangalia ni kama wewe ni pochi nene ili aweze kukutumia umlipie pango la nyumba, uweze kumpeleka kwenye maduka makubwa kwa ya kufanya nanunuzi ya nguo na viatu vya gharama, uwezo wa kumpeleka kwenda kustarehe ziara za kitalii nchi za Ughaibuni.

Pia huyo mwanaume awe anafanya kazi yenye mshahara sufufu, awe anamiliki gari la kifahari na kuwa na nyumba yake. Lakini wanawake hao wakijiwa na mwanaume asiye na ukwasi ili wajenge maisha yao kwa pamoja kuanzia chini hawana muda nao. Kachero Manu alianza kutamani afanikiwe walau kuacha mtoto duniani kama atapoteza uhai kwenye kazi zake za Kikachero ambazo uhai na umauti ni asilimia hamsini kwa hamsini vinatenganishwa na uzi mwembamba sana. Maana walilishana yamini yeye na mchumba wake kutoshiriki tendo la ndoa kabla ya ndoa ili waepuke kuzaa nje ya ndoa.

Hawakutaka watoto wao wapachikwe majina yasiyofaa na jamii kama mtoto wa haramu au mtoto wa kikopo. Pia wazazi wa mchumba wake walikuwa ni wafia dini wazuri wa Madhehebu ya Kisabato. Wakwe zake hao hawakuwa tayari binti yao ajifungue mtoto nje ya ndoa. Kwao ilikuwa wanahesabu ni laana kama binti yao akizaa nje ya ndoa. Hivyo Kachero Manu aliandaa "jazua" maalumu ya kumtuza mchumba wake siku ya ndoa kwa ajili ya kutunza ubikira wake.

Alipanga kumzawadia gari ndogo ya kisasa, atakalotumia kuendea kazini. Vikao vya familia ya akina Kachero Manu vya kujiandaa kupeleka posa vilishaanza kukaliwa. Tayari alishateuliwa mmoja wa wajomba zake kwa kupewa jukumu la kupeleka posa na kiasi cha pesa kama kifungua mlango nyumbani kwa wazazi wa Faith Magayane.

Mjomba mtu alikuwa anasubiri Kachero Manu apungukiwe na majukumu ya kikazi aweze kupewa ruksa ya kupeleka posa ya mpwa wake. Sasa mambo yanakaribia kukamilika, ghafla linaibuka jipya hili la "Cabo-Delgado" ambalo "piga ua" alijua atatumwa yeye tu. Akawa anawaza kama akipewa jukumu la kwenda Msumbiji kitumbua cha posa kitakuwa kimeingia mchanga tayari, na hana uchaguzi, kazi kwanza mapenzi baadae.

Ingawa alijua mpenzi wake Faith ataumia sana kwa kuvurugika kwa mipango yao kabla hawajatimiza ndoto zao.

Akiwa kwenye lindi zito hilo la mawazo hayo ya mpenzi wake akashtuliwa na honi nzito sana ya Lori lililokuwa lipo mbele yake kwenye hiyo barabara ya kuelekea Bagamoyo. Ilikuwa nusra limpige dafrao lakini bahati ikaangukia kwake, kwa umahiri mkubwa akalikwepa. Akajutia sana uzembe wake wa kuruhusu mawazo yamtawale akiwa barabarani, tena katika nyakati mbaya za giza la usiku.

Akaanza kuwa makini barabarani sasa mawazo yake akiyaelekeza kwenye kazi. Alikuwa anakaribia Chambezi, kwenye Shamba la Utafiti linalomilikiwa na Wizara ya Kilimo, kwenda kuonana na Jasusi Mtanzania mwenye nyaraka za siri alizitorosha toka nchini Msumbiji.


SURA YA PILI
Ofisini kwa "Kiongozi" tarehe 12/02/2016, saa 3:00 asubuhi
Jina lake rasmi anaitwa Bwana Mathew Kilanga au ukipenda muite kwa lakabu ya "Kiongozi" au "Mti mkavu hauchimbwi dawa". Alikuwa ni Kachero Bobezi na mkongwe aliyeanza kuhudumu katika Idara ya Usalama wa Taifa tokea enzi za Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alijiunga na idara hiyo tokea mwaka 1970 mara tu alipomaliza mafunzo yake ya JKT kambi ya Makutupora, Dodoma. Kambi ambayo ipo takribani kilometa 25 kutokea Dodoma Mjini.

Kujiunga kwake kwenye idara nyeti kama hiyo haikuwa kwa ganda la ndizi, bali Hii ilitokana na bidii na nidhamu kubwa aliyokuwa anaionyesha kipindi chote cha mafunzo yake ya JKT. Akiwa JKT alitunukiwa nishani ya Uongozi bora, Nidhamu na Ukakamavu siku ya kuhitimu mafunzo yake mbele ya Mgeni Rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa kipindi hicho Mheshimiwa Saidi Maswanya.

Kisha baada ya kusajiliwa kwenye idara hiyo, akapelekwa Ughaibuni nchini Urusi kwa muda wa miaka 6 mtawalia kwenda kufanya kozi mbalimbali za Ujasusi. Baada ya hapo alirudi nchini mwaka 1976 akahudumu katika idara ya usalama kwa miaka mitatu mpaka 1979 ilipozuka vita vya Kagera, baina ya mahasimu wawili wa enzi hizo, Tanzania na Uganda.

Rais wa nchi ya Uganda wakati huo wa vita alikuwa ni "Nduli Iddi Amini Dada". Katika medani ya vita Bwana Mathew Kilanga alikuwa ni mmoja wa vijana machachari sana waliofanikisha ushindi maridhawa wa jeshi la Tanzania. Alifanikiwa kuingia mpaka viunga vya Jiji la Kampala, Uganda akiwakwepa maafisa usalama wa Nchi ya Uganda kwa mbinu ya kipekee kabisa.

Alijifanya yeye ni mwanamke mfanyabiashara wa vitenge toka Mombasa, Kenya aliyejitanda vazi la baibui lenye mahadhi ya pwani. Alipofanikiwa kupeleleza alichotumwa akaleta mrejesho wa penyenye za udhaifu na nguvu ya jeshi la Uganda ilipo. Baada ya kumalizika vita hivyo, alikuwa ni miongoni mwa mashujaa waliotunukiwa nishani ya heshima ngazi ya juu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hiyo kama haitoshi, mwaka 1981 akapelekwa nchini Israel kwa ajili ya mafunzo mazito na magumu ya Ukomandoo Daraja la-I kwa muda wa miaka miwili. Mafunzo ambayo kwa nchi zote za Afrika, waliteuliwa vijana 25 tu ambao ni shupavu na wenye nidhamu. Lakini waliofanikiwa kuhitimu mafunzo hayo ni watano pekee, akiwemo Mathew Kilanga toka Tanzania, Okola Ochoga wa Uganda, Kwesi Appiah wa Ghana, Ahmed Taleeb wa Misri na Jacob Steven wa Msumbiji.

Wengine wote waliobakia walikufa kabla ya kumaliza mafunzo yao na wengine walipata ulemavu wa kudumu kama kuvunjika miguu na upofu wa macho hali ambayo iliwafanya washindwe kuhitimu mafunzo yao. Alivyorejea nchini mwaka 1983 ndipo alipokabidhiwa rasmi rungu la madaraka makubwa ya kuiongoza Idara ya Usalama huku akifanikiwa kuiletea heshima kubwa idara hiyo ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Ndio zile zama za hofu ya kuwa vichaa wengi barabarani ni "Makachero vidole" au kwenye kila maskani mtaani kuna "Kachero kidole", mbinu hizo zote zilikuwa ni mipango thabiti ya Bwana Mathew Kilanga kuhakikisha nchi inakuwa katika hali ya usalama na amani wakati wote. Nje ya Tanzania moja ya kazi zake za kukumbukwa ni namna alivyokabidhiwa jukumu la kuratibu vikosi vya Afrika vilivyomuondosha madarakani tarehe 25/03/2008, Rais wa zamani wa visiwa vya Anjouan Kanali Mohammed Bacar.

Ambaye alikuwa ana'ang'ania kubaki madarakani kinyume na katiba ya nchi. Hivyo Kiongozi Mathew Kilanga ndio aliandaa mpango mkakati uliosababisha Kanali Mohammed Bacar abwage manyanga mwenyewe bila kupenda. Pia Bwana Mathew Kilanga anakumbukwa kwa namna alivyozima mapinduzi ya kijeshi ya Rais wa Burundi yale ya tarehe 3/05/2015, yaliyotaka kumtoa madarakani Mheshimiwa "Pierre Nkurunzinza" akiwa mkutanoni nchini Tanzania. Kiasi ya kwamba nchi ya Burundi mpaka leo inammezea mate ya uchu Bwana Kilanga, akahudumu nchini kwao kama mshauri wa Rais wa mambo ya usalama.

Hizi shughuli zote zilizompatia ujiko Bwana Kilanga, aliziratibu chini ya mwongozo wa kijana wake makini kwa kazi, kijana "Manu Yosepu" au kwa jina la kazi la utani akijulikana kama "Mwiba wa tasi". Kijana ambaye Bwana Mathew Kilanga ukimuamsha hata usiku wa manane ukamwambia kuna jukumu zito na gumu la kumtoa mtu mharifu mfu ambaye yupo kuzimu na anahitajika kurudishwa duniani akiwa hai aje kuhukumiwa, basi bila kusita atakwambia hilo jukumu hilo mkabidhi "Manu Yosepu" ataliweza.

Kwake yeye kijana wake huyo alimuona ni moja ya lulu za Bara la Afrika ambazo ni adimu sana kupatikana, na huenda wanazaliwa mara moja tu katika kila karne moja.

Bwana Kilanga umri ulikuwa umemtupa arijojo sasa, akiwa ameshakula chumvi ya kutosha akiwa na umri takribani wa miaka 70 na ushee. Alishafanya majaribio kadhaa ya kuandika barua zaidi ya mara 10 akiomba kustaafu kazi ili apumzike na jukumu la utumishi wa umma lakini kila wakati jibu toka kwa wakubwa wake wa kazi lilikuwa ni moja tu, "Taifa bado linakutegemea, hatuna mbadala wako".

Ila alishapanga liwalo na liwe kuwa ikifika mwaka 2020 liwake jua, inyeshe mvua lazima aondoke kazini. Akisimamia vyema jukumu lake la Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge akijaaliwa uzima ndio utakuwa mwisho wa utumishi wake kwa usalama wa nchi. Hasa akijivunia ameshawapika vijana mahiri kama akina Kachero Manu Yosepu wakapikika, hivyo hana sababu ya kuwa mkiritimba wa kung'ang'ania utumishi wa umma, mwisho aje kufia ofisini bure. Kutokana na ajira hii alikuwa anakosa muda timilifu wa kucheza na wajukuu zake, pia muda wa kusimamia mashamba yake ya mifugo na kilimo huko kwao Madaba, Ruvuma.

Lakini jana yake tu alikabidhiwa na wakubwa zake jukumu la kuchunguza mauaji ya huko Cabo-Delgado, Msumbiji ndio maana akampigia simu Kachero Manu ili amkabidhi jukumu hilo. Yeye mwenyewe alishafika kazini tokea saa 12:30 asubuhi na alikuwa hajakaa chini anazunguka zunguka ndani ya ofisi yake kama kishada kinachosukumwa na upepo, hatulii sehemu moja.

Bwana Kilanga mikono yake alikuwa kaitumbukiza kwenye mifuko yake ya suruali akiwa amevalia Kaunda suti ya rangi ya kijivu, soli ya viatu vyake vya mokasini rangi nyeupe vinatoa mlio wa malalamiko kila vinapogusa sakafu ya ofisi yake. Alizama kwenye tafakuri pevu ya kupangilia mbinu mbalimbali za kutumia ili kufanikisha kuwatia mbaroni wahalifu.
Yeye alikuwa anajifananisha na kocha na Kachero Manu ndio mchezaji wake.

Timu ikifanikiwa kupata ushindi sifa zinaenda kwa wachezaji, lakini ikifungwa lawama zinaenda kwa kocha. Hivyo yeye ndio jumba bovu daima linamuangukia yeye mambo yakienda mlama. Kila wakati alikuwa macho yake hayabanduki kwenye saa yake ya mkononi kuangalia kama muda umefika wa mkutano wake na kijana wake. Ilivyobaki nusu saa akaeleka mpaka dirishani na kuanza kuchungulia magari yanayopita chini ya ghorofa na kuelekea kwenye maegesho ya magari.

Kwenye kikao hicho kulikuwa na vigogo wengine waalikwa toka idara nyeti mbalimbali za serikalini, hivyo kijinga cha moto cha kuwamulika wahalifu wa Cabo-Delgado popote walipo kilikuwa kinategemewa kuwashwa rasmi ofisini hapo saa 3:00 asubuhi. Mpaka kufikia saa 2:30 asubuhi juu ya alama, vigogo wote walikuwa wameshawasili kwenye ofisi za Bwana Mathew Kilanga, wakapokelewa na kukirimiwa vinywaji.

Sasa wakajitega mkao wa kula wakiwa macho juu wanamsubiria Kachero Manu aje wampe maagizo ya kutekeleza.




Ofisi hizo za Bwana Mathew Kilanga, ambapo mkutano huo mzito ulipangwa kufanyikia humo, zilikuwa zipo katika jengo maarufu Jijini Dar es Salaam la "Benjamin William Mkapa Pension Tower" roshani ya 5 katika mtaa wa Azikiwe.

Zamani jengo hili lilikuwa linajulikana kama "Mafuta House". Ilikuwa ni ofisi ya wastani isiyo na mbwembwe nyingi kama zinavyokuwa Ofisi za vijana wa Mjini, huku akisaidiwa na Katibu Muhtasi wake mwanamke kisura, makini na mwerevu "Kokunawa Rweikiza" mhaya mzaliwa wa Bukoba vijijini.

Alikuwa mwanamke kidosho lakini anayejitambua vilivyo, Waingereza wanasema "Beauty with brain" hivyo hakupata tabu sana kufanya kazi na Bosi Mathew Kilanga. Wengi walishindwa kuendana na kasi ya Bwana Mathew Kilanga katika utendaji wake wa kazi wa kasi na viwango. Lakini Koku yeye akawa anamjulia Bwana Mathew Kilanga, akawa anajifanya yeye ni mithili ya jini mchapa kazi, hachoki.

Hali hiyo ikamfanya adumu nae kwa muda wa miaka isiyopungua 8 mfululizo bila kuharibu kazi yoyote anayoagizwa kutekeleza, wala kupewa barua ya karipio kazini ya kuharibu kazi.
Alikuwa anaishi maeneo ya Kigamboni ili asiwe anachelewa kufika kazini kwa wakati na hata ikitokea dharura ya kuhitajika kazini usiku wa manane iwe rahisi kwake kuripoti kazini. Maana sumu namba moja ya kushindwa kupatana damu zenu na Bwana Mathew Kilanga ilikuwa ni kuchelewa kuripoti kazini katika muda ambao anaokuhitaji. Sumu namba mbili ni kushindwa kutekeleza majukumu ya kikazi aliyokupa uyatekeleze.

Kwa kulitambua hilo ndio maana akafanya maamuzi ya kuhamia Kigamboni kwenye nyumba ya kupanga ili kazi yake iwe na ufanisi. Tarehe 12/02/2016, Kokunawa aliingia ofisini tokea saa 6:05 za usiku, akiwa na kazi moja tu ya kupokea barua pepe za taaarifa za kiintelijinsia kutoka Ofisi ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mtwara. Pia alikuwa anapokea taarifa kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji. Kisha taarifa hizo za kiintelijinsia alikuwa anazidurufu na kuzipeleka kwa Bosi wake Bwana Mathew Kilanga azipitie kwa ajili ya kuzifanyia kazi na kama kuna zinazohitajika kujibiwa zijibiwe.

Kwa ufupi ni kwamba alikesha mfano wa nesi wa zamu anavyokesha na wagonjwa wake wenye hali mbaya. Mida ya saa saa 3:05 asubuhi majira ya dhuha, jua likiwa limeshachomoza vizuri kabisa linamwaga katika uso wa dua miale yake ya rangi ya shaba, mifugo imeshafunguliwa kwenye malishoni zamani, Kachero Manu Yosepu alikuwa ndio kwanza anapanda ngazi kwa madaha kuelekea roshani ya 5 ofisini kwa Bosi wake kama vile hana haraka..

Kachero Manu Yosepu alikuwa hapendi kutumia "Lift" anapopanda ngazi za jengo la ghorofa lolote lile. Huo ulikuwa ni utamaduni wake aliojiwekea na huwezi kumbadilisha asilani. Kwake yeye mtambo huo unaotumika kubebea watu kutoka roshani za chini na kuwapeleka roshani za juu kwenye majengo makubwa alikuwa anauona ni maalumu kwa wagonjwa, wazee, watoto na akina mama wajawazito.

Ilikuwa ni moja ya mazoezi yake ya kuimarisha misuli ya miguu katika upandaji wa ngazi. Bwana Mathew Kilanga alishaanza kuulizia kwa Sekretari wake kama Kachero Manu kashatia nanga ofisini. Ilipofika saa 3:08 asubuhi Kachero Manu akagonga mlango wa ofisi kisha akanyonga kitasa bila kusubiri sauti ya kukaribishwa kuingia ndani. Akapokewa kwa tabasamu mwanana la Sekretari wa Bosi wake, Kokunawa.

Moto wa utani baina yao hao watani wa jadi ukatawala kama kawaida yao wanapokutana. "Habari za asubuhi dada "Koku" uliyehajiri kuja Jijini kwa hisani za mbio za mwenge wa uhuru, Bukoba wanasemaje? alitania Kachero Manu kumtania Kokunawa.

"Habari za asubuhi ni nzuri, Bukoba nimeongea nao mambo yao ni mpwitompwito, hongera zako unaetoka usingizini, mimi na Bosi wako tuko kazini tokea saa 6 usiku wa jana, kupenda kwako kitanda kutakuotesha kitambi shauri yako ushindwe kazi zote mbili za nyumbani na za ofisini zinazokupa mkate wako wa siku" wakacheka wote kwa pamoja kicheko cha nguvu huku wakigonganisha viganja vyao vya mikono.

"Kazi za nyumbani lazima zitushinde na bodaboda lazima watusaidie hamna jinsi, kwa maana maisha yanavyotukimbiza mchakamchaka, Mungu pekee ndio anajua" aliongea Kachero Manu huku akiwa ameinamia dirisha la Sekretari huyo huku amepinda mgongo wake ili waonane vizuri sura zao.

"Sasa Afisa mzima kama wewe, mshahara mnono na marupurupu kochokocho unalalamika maisha magumu je sisi wenye mishahara ya mkia wa mbuzi tutasema nini..!" alisema Kokunawa kwa sauti ya kinyonge akionekana anachokiongea sio utani kinatoka moyoni mwake, akiwakilisha kilio cha watumishi wengi wa umma cha kulipwa mishahara kiduchu isiyoendana na gharama halisi za maisha ya kila siku.

Ghafla bin vuu wakiwa kwenye soga zao simu ya mezani ya Sekretari Kokunawa ikaita tena, ilikuwa inapigwa toka kwa Bosi akiulizia kama Kachero Manu kasharipoti ofisini, akajibiwa ndio ameingia hivi sasa.

Alivyokata simu tu, Kokunawa akamwambia Kachero Manu "Kaka yangu kimenuka huko, ukisikia hasira za ndovu kumla mwanawe ndio leo, fanya haraka uende Babu yako anasema hana muda wa kupoteza kukusubiria wewe, na sauti yake inaonyesha kashaanza kukasirika, si unamjua Bosi wako kama kazaliwa na kazi vile". "Sawa ngoja nimuone haraka, tutaonana nikitoka nataka nikupeleke kula mlo wa usiku kwenye hoteli kubwa kubwa binti mrembo upumzike kula senene kila siku" akajibu Kachero Manu huku akitokomea kwenye veranda ya kuelekea kwenye mlango wa ofisi ya Bosi wake, akimuacha Sekretari Kokunawa yupo hoi kwa kicheko hana mbavu.

Alivyofika akagonga hodi na kufungua mlango moja kwa moja. Alipoingia ofisini ndani, Kachero Manu alijikuta anapigwa na bumbuwazi baada ya kuona Bwana Mathew Kilanga yupo na wageni wengine wawili ambao sio wageni katika macho ya Kachero Manu.

Ukweli wa kutoka sakafu ya moyo wake hakupendezwa na uwepo wa wageni wale kwenye mazungumzo nyeti kama yale. Kachero Manu akapotezea ule mfadhaiko alioshikwa na akajizuia kuonyesha hasira zake, akasalimia "Shikamoo Kiongozi, habari za asubuhi"...! kisha akawasalimia wale wageni waalikwa wengine wawili kwa tabasamu lenye bashasha feki.

Bosi wake alimkuta bado amesimama hajakaa kwenye kiti chake, akajibu salamu hiyo. "Habari za asubuhi ni mbaya sana, karibu kiti ukae" huku akimuashiria kwa mkono kiti cha kukaa. "Ahsante sana...!" akajibu Kachero Manu, kisha akavuta kiti kilichopo tupu akakaa na akatoa kompyuta mpakato yake kutoka kwenye begi lake akaiwasha, kisha akaitafuta pragramu ya uandishi ya "microsoft word" tayari kwa kuandika vitu vya msingi kwenye majukumu ya kazi atakayopewa na wakubwa zake hao.
ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog