IMEANDIKWA NA : JAPHET NYAN'GORO SUDI
*********************************************
Simulizi : Msako
Sehemu Ya : Kwanza (1)
“KWA NINI UMEMCHAGUA POKA KINGU, wakati siku za karibuni kumejitokeza mafundi wengi wa kufanya mauaji, kwa ustadi wa hali ya juu?’’
“Huyu anafaa! Aliongea Ngongoseke
“Ndiyo niambie sasa, kwa nini anafaa?
“Poka Kingu ni mvivu.” Akajibu Ngongoseke kwa utulivu huku akifikiri.
“Uvivu ni sifa nzuri ya kumchagua mtu?” Mzungumzaji wa upande wa pili wa simu, ambaye ni mzungu. Akauliza kwa mshangao.
“Hasa!” Ngongoseke akasisitiza.
“Yaani unataka mtu mvivu, kwenye kazi ngumu na hatari kama hii?” Mzungu huyo akauliza, kutoka upande wa pili wa simu. Katika mshangao usiyoelezeka.
“Ndiyo! Nimepitia mafaili takribani saba, niliyoletewa mezani, yenye sifa za watu ninaowahitaji, kwa ajili ya kazi hii. Nimejiridhisha kuwa, Poka Kingu ana vigezo vya kuwazidi wengine. Kutokana na kazi ninayotaka ifanyike.” Akaongea Ngongoseke kwa hakika. Mkono wake mmoja ameshika kiwambo cha simu sikioni, mkono wake mwingine, ukipapasa waya wa simu hiyo ya mezani.
“Sifa yenyewe ndiyo iwe uvivu?”
“A killer on the payroll isn't good for business. Sitaki mazoea, nataka msisimko wa kazi.” Ngongoseke akasisitiza.
“Unadhani mtu aliyeko kwenye orodha ya malipo, hafai kwa kazi hiyo?” Mzungumzaji wa upande wa pili, akauliza kwa udadisi. Akionekana kutoridhishwa na uamuzi wa Ngongoseke.
“Vidole vyao ni vizito kwa shabaha, mishipa yao imejaa mafuta kwa sababu wanalipwa mishahara minono na kula ovyo. Hawana njaa wala mdadi wa kazi.” Akafafanua Ngongoseke.
“Hii kali! Yaani uvivu umekuwa sifa kwa muuaji tishio!” Akashangaa Mzungu simuni.
“Sitaki mtu anayeua kwenye muda wa nyongeza, yaani, extra time killer. Mtu ambaye ananiweka kwenye wasiwasi kwa muda mwingi. Nataka muuaji anayekamilisha kazi yake bila kutoa jasho, ndani ya sekunde za awali za tukio.” Ngongoseke akafafanua.
“Okay! Sifa nyingine ni ipi?”
“Poka Kingu anaweza kuishi kama mzimu. Kwa vile ana hulka ya uvivu, hapendi kupambana na mtu kwa muda mrefu. Hivyo hujua namna ya kujificha na kuua haraka, pale anapopata nafasi finyu ya kufanya hivyo. Kwenye kazi hii, sitaki mtu wa kuremba. Kumbuka watu tunaokwenda kupambana nao, hawastahili kupata nafasi ya kuishi mara mbili. Lazima wafe hata kwenye mpenyo mdogo wa kupitisha wembe.
“Uvivu wake umemfanya awe mtu anayeshika rekodi ya juu barani Afrika. Rekodi ya kuua watu wengi ndani ya muda mfupi zaidi kwa mapambano ya ana kwa ana. Uvivu umemfanya awe stadi wa mapigo ya kifo, kwa vile asivyopenda kupoteza muda. Hapendi kushughulika na mtu au jambo fulani kwa muda mrefu, kwa vile anavyopenda kupumzika na kustarehe. Hivyo amejifunza kupiga mapigo machache ya kifo. Hataki kumpiga mtu muda mrefu. Namfananisha na wembe upitavyo kwa wepesi kwenye mnofu wa nyama. Huyu atatufaa sana. Inadhaniwa kuwa ndiye mtu makini anayeweza kuua haraka bila silaha.” Ngongoseke akaweka kituo huku akitazama picha ya Poka Kingu kwenye jalada juu ya meza iliyokuwa mbele yake.
“Okay! sikuwahi kuwaza kuwa uvivu unaweza kuwa sifa ya muuaji hatari wa kukabidhiwa kazi hatari kama hii.” Mzungu akaongea kwa shauku huku wasifu wa Poka Kingu ukionekana kumuelea vyema.
“Wauaji wasio makini hawaoni shida kukwambia, watu uliowatuma kuwaua wamewaponyoka kwa bahati mbaya. Japo watakuambia kuwa wamefanikiwa kuwajeruhiwa vibaya. Mbaya zaidi, watakueleza kuwa hawafahamu aliyenusurika kuuawa amekimbilia wapi. Poka Kingu hafanyi makosa ya namna hiyo. To me, when a serial killer have to kill the same target twice in one week, then there's either something wrong with his skills or something wrong with instructions. Nataka akipiga amepiga, tumesahau na tunaongelea habari nyingine.” Alisema Ngongoseke huku akiweka msisitizo kwa lugha ya Kiingereza.
“Okay! Sasa naanza kuafikiana na wewe. Hata hivyo bado nina shaka.”
“Shaka gani?” Ngongoseke akauliza kwa udadisi.
“Poka Kingu yuko kifungoni, tena kwenye gereza la wafungwa hatari, linalolindwa kwa ulinzi mkali, masaa ishirini na nne, siku saba kwa wiki. Bila shaka kumbukumbu zangu ziko sahihi, sivyo?” alihoji Mzungu huyo
“Upo sahihi kabisa. Usijali suala hilo niachie mimi. Unajua huwezi kujua kila kitu kabla ya kuanza kutekeleza jambo lenyewe. Ujuvi wa jambo huja wakati jambo hilo likiwa linaendelea kutendeka. Kukaa na kusubiri ujue kila kitu kabla ya kuanza kutekeleza jambo, ni sawa na kupoteza muda. Tunachotakiwa ni kuwa tayari kwa mambo yasiyojulikana.” Ngongoseke akajitapa na kuongeza.
“Tunachopaswa kufanya sasa ni kutafuta watu wa kufanya nao kazi. Wiki chache zijazo, nitakuwa nimetengeneza timu ya kazi na kuanza fujo ndani ya jiji hili la Dar es Salaam.”
“Hebu niambie juu ya hiyo timu unayotarajia kuitumia.” Mzungumzaji wa upande wa pili, akazidi kuhoji.
“Poka, Naomi, Misanya, Nyoso na Mheshimiwa, wataongoza timu hiyo katika mazingira na nyakati tofauti.” Ngongoseke akabainisha mpango wake.
“Mh! Mbona sioni mchanganyiko mzuri kati ya Poka Kingu na yule mrembo Naomi?” Mzungu akatia shaka kwa mara nyingine.
“Hawa viumbe wawili, ni kama pande mbili za sarafu. Hazifanani lakini zinafanya thamani ya pesa. Ni kama jua linavyotawala mchana, na mbalamwezi unavyoangaza usiku, vyote huangaza dunia. Naomi na Poka wanaunganishwa na hewa iliyopo pande zote, yaani, mchana na usiku. Uwanja wa Poka Kingu ni sehemu ya jua kali na misukosuko. Sehemu yenye upole na mwanga hafifu wa mbalamwezi, yenye hamasa za mahaba, ni ya Naomi Nanalungu. Wote wapo kwenye sayari moja ya matukio ya kutisha, wakiishi kwa kuvuta hewa moja, mchana na usiku.” Ngongoseke akafafanua nadharia yake kwa ujivuni.
“Kwa hivyo Poka unamfananisha na Jua, anafanya kazi mchana kwenye mazingira magumu. Naomi kama mwezi, anafanya kazi usiku kwenye mazingira laini yenye mahaba. Umesema wanaunganishwa na hewa ambayo iko mchana na usiku. Sasa hewa ndiyo nani kwenye nadharia yako?” Mzungu akahoji.
“Hiyo sehemu ya hewa ndiyo mimi. Sionekani lakini nitawaunganisha vyema.” Ngongoseke akaongea kwa utulivu na kuweka kituo. Baada ya ukimya mfupi wa tafakuri, mtu wa upande wa pili akasema.
“Lo! Nimevutiwa sana na mkakati wako. Nadhani mpango wetu utafanikiwa bila shaka.” Kauli hiyo ikafuatiwa na kimya kifupi.
“Nataka Tanzania ichafuliwe, nataka kusiwe na ripoti yoyote kuhusiana na gesi ya Mtwara. Sijui nikueleze vipi ili uelewe namna wakubwa watakavyofurahi, baada ya kufanikiwa kwa tukio hili. Makampuni takribani kumi na tano ya nchi za ulaya na Marekani, yatasaini mkataba wa kuendelea kununua gesi kutoka PAW & Company. Mpango huu ukishindwa, makampuni yote yatakimbilia kwenye gesi ya Mtwara. Ambayo itakuwa rahisi kwao kununua, na upatikanaji wake ni endelevu wa muda mrefu, kutokana na siasa tulivu za Tanzania”
“Hivi sasa kampuni zote zimeshaweka angalizo kuwa hazina hakika kama zitaongeza mkataba wa kununua gesi kwetu. Baada ya kutathimini angalizo lao hilo, tumejiridhisha kuwa zinasubiri hiyo ripoti ambayo inaandaliwa sasa kuhusu gesi ya Mtwara. Ni wazi kuwa tukiharibu utaratibu mzima wa ripoti hiyo katika kiwango ambacho kitaifanya Tanzania itake siyo chini ya mwaka mmoja kuandaa ripoti nyingine. Tutakuwa tumefanikiwa kuyalazimisha makampuni hayo kuendeleza mkataba wa kibiashara baina yetu. Nasi tutawabana walau mkataba mpya uwe wa miaka kumi, ili hata kama Tanzania ikijipanga upya, ikute tumeshatawala soko. Hivyo kazi hii ni muhimu sana kwako na kwetu, bwana Ngongoseke.”
“Ondoa shaka! Japokuwa inaonekana ni kazi ngumu, lakini itafanyika tu. Nikimaliza hii kazi, nitakuja Washington kununua zile nyumba, ulizoniambia habari yake. Nifanyie mpango.” Ngongoseke akaongea kwa hakika, huku akisimama.
“Bila shaka. Kesho nitakutumia picha za nyumba unazoweza kununua, zilizopo maeneo mazuri.” Mzungu akaongea kwa matumaini, upande wa pili wa simu.
“Nitashukuru sana. Basi tutawasiliana wiki ijayo baada ya mambo kuanza.” Ngongoseke akasisitiza.
“Sawa! Natarajia kusikia kasheshe huko. Nimetuma malipo ya awali, malipo ya pili yatafanyika nitakapopata kiboksi cheusi cha kurekodi safari ya ndege. Malipo ya mwisho yatafanyika pale itakapothibitika, kuwa timu yako imefanikiwa kuondoa na kuharibu nakala zote za ripoti ya gesi ya Mtwara.” Mzungu akafafanua.
“Mtathibitishaje kuwa nakala zote zimefutwa?” Ngongoseke akahoji.
“Ni rahisi sana.”
“Kwa vipi?”
“Tanzania itakapoanza upya mchakato wa kupima na kuandika ripoti mpya kuhusu; mchanganuo, aina, ubora na thamani halisi ya gesi ya Mtwara. Jambo ambalo litawachukua takribani mwaka mzima kulifanya. Hapo tutajua kuwa mpango wetu ulifanikiwa na kampuni yetu itakuwa imefanikisha azma yake. . Na ndiyo hapo tutajua kuwa ulifanya vema kazi yako.”
“Nashangaa unatia hofu wakati unajua rekodi yangu ya kazi.”
Njoo tena saa 12:00 jioni.
BAADA YA KUMALIZA MAONGEZI YALE, Ngongoseke akatembea kwa utulivu akizunguka ndani ya chumba alichokuwa akifanyia yale maongezi. Bado alikuwa akitafakari maongezi yaliyopita. Vilevile akitathmini kazi iliyokuwa mbele yake.
Jina lake kamili anaitwa Ngongoseke Amos Nkwija. Akiwa na umri wa miaka arobaini na sita lakini tayari anaogelea katika mafanikio ya hali ya juu ya hapa duniani. Mafanikio ya kifedha na kiuchumi. Kwa wanaomfahamu, mafanikio hayo haikuwa ni jambo la ajabu wala bahati mbaya. Maana angekosaje kuwa na mafanikio wakati Mungu alimtunuku akili njema ambayo alionekana kuitumia vyema. Wakati shetani alimvika ukatili na ujasiri wa kufanya mambo gizani na kuweza kuingia sehemu ambazo haziingiliki kwa urahisi?
Safari yake ya mafanikio ilianza kama utani tu. Alianza kwa kuuza mawazo na mipango, kwa kuwasaidia matajiri kupanga mipango mizuri ya uwekezaji. Akitumia vyema talanta ya akili aliyopewa na Mungu. Haikumchukua muda mrefu kubaini kuwa, siyo kila mtu mwenye pesa ana akili. Isipokuwa wenye pesa ni wale watu wanaojua kutumia akili za wenzao, kuweza kupata pesa na kuongeza pesa. Hivyo Ngongoseke, kwa miaka kadhaa akajikuta kama walivyo vijana wengi ambao hutumia akili zao na taaluma, kuwapa au kuwaongezea pesa watu wengine kwa makubaliano ya kulipwa visenti vichache, mwisho wa mwezi.
Lakini ikatokea siku ile ambayo Ngongoseke akapata ukatili na ujasiri ovu, ndipo mambo yalipobadilika. Alivitumia vipawa vyake vyote, kupora mali za matajiri wachache waliokuwa wakitumia akili yake kujinufaisha. Sasa yeye ndiyo akawa zaidi yao, akiitumia akili yake vyema, ukatili na ujasiri wa kishetani kutengeneza pesa. Kwa muda mfupi Ngongoseke akajikuta ameingia kwenye ramani ya watu wenye utajiri mkubwa wa kuogopwa.
Pamoja na kuwa na watoto watatu, ambao wote wanaishi na kusoma ulaya, lakini hukuwa na mke. Mama wa watoto hao hawakuwepo. Si kwa bahati mbaya wala mapenzi ya Mungu, bali hilo liliamuliwa na Ngongoseke mwenyewe. Mtu mwenye akili ambazo siyo za kufanyia majaribio, akipanga jambo amepanga, yeyote hawezi kosoa. Akipangua amepangua, hakuna wa kupanga. Mtu mwenye akili kubwa yenye shabaha kali, ya kuweza kuunganisha mambo mengi kwa muda mfupi na kuweza kuona matokea tarajiwa kwa uwazi. Akili hizo ndiyo zilizomtuma kumuua kwa siri kila mwanamke aliyezaa naye. Alitaka wanawe wasiwe na mama, wawe wanawe peke yake.
Jumba hili alilokuwa akiishi, lilikuwa kielelezo tosha kuwa alikuwa akiogelea katika utajiri wa kutisha. Ni katika jumba hili la kifahari ndiyo alikuwa akifanya mzungumzo ya simu na mzungu huyo wa upande wa pili. Utajiri wake ulikuwa miongoni mwa watu wanaotafuta namna tofauti za kutumia pesa, wenyewe wanaita kuchoma pesa, hivyo hawabishani bei na hawanunui vitu vya bei nafuu. Jumba lake lilikuwa kwenye kitongoji chenye makazi ya watu wakwasi. Muonekano wa jumba hilo la kifahari ulivuta macho ya wapita njia kwa namna lilivyopendeza. Ukiliangalia unapata tafsiri halisi ya utajiri uliowekezwa kwenye jumba hilo. Bustani kubwa yenye ndege wa rangi tofauti za kupendeza, bwawa kubwa kuogelea, bar ya ndani ya nyumba na sehemu mbalimbali za starehe. Nafsi ya mtu yeyote ingeweza kujihisi burudiko la kifahari kuwepo eneo hilo. Jumba hilo kubwa lililindwa kwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi au mtu yoyote kuingia na kutoka bila ridhaa ya mwenyeji. Ngongoseke hakuajiri mlinzi isipokuwa kijana mmoja, ambaye kazi yake ilikuwa kuhudumia, bustani ya kupendeza ya jumba hilo.
* * *
USIKU WA SIKU HIYO ambayo Ngongoseke alitoka kuongea kwa simu na yule mzungu wa nje ya nchi, Halfan Mwaruko, askari wa Kituo cha Polisi cha Msimbazi, jijini Dar es Salaam alikuwa akiandika majina ya washukiwa wa uhalifu waliokuwa wamefikishwa kituoni hapo usiku huo.
Ilikuwa saa tatu na robo usiku, washukiwa watatu kati ya sita waliochukuliwa maelezo yao na kuswekwa rumande walikuwa wanawake.
“Nyinyi wanawake sogeeni hapa!” Akafoka kwa sauti ya ukali.
“Taja jina lako.’’ Akaanza na mwanamke wa kwanza kufika.
“Joanita Mwaikambo.” Mwanamke huyo akachukuliwa maelezo kisha akaswekwa mahabusu. Mwingine akafuatia.
“Joan Mwainunu.” Afande Halfan akamtazama mwanamke huyo kwa udadisi, kisha akaanza kumchukua maelezo kama yule wa awali huku akipiga mwayo hafifu. Alipomaliza akachukua maelezo ya mwanamke wa mwisho. Lakini kabla hajaandika, akamtazama msichana huyo kwa mshangao.
“Jina lako?’’ Akauliza huku akimtazama msichana huyo mrembo mwenye mavazi yaliyochafuka, kuashiria kukamatwa kwake kulikuwa mshikemshike.
“Jo…Mwa.”
“Acha mzaha! Ndiyo jina gani hilo?” Afande Halfan akatilia shaka. Akamtazama msichana huyo kwa udadisi. Macho yake hatimaye yakaweka kituo kiunoni kwake kwa sekunde kadhaa, kabla ya kumeza mate na kumwangali usoni.
“Hilo swali labda ungewauliza wazazi wangu.” Msichana huyo akajibu kwa dharau.
“Jo Mwa!’’ Afande Halfan akarudia kutamka jina hilo lililoonesha walakini kichwani mwake.
“Hujakosea.” Akasisitiza msichana huyo kwa sauti ya kilevi.
Afande Halfan akaandika maelezo ya msichana huyo huku akitingisha kichwa, nusu kukubali nusu kukataa. Wakati akiendelea kuandika, mara akaingia mkuu wa kituo hicho cha polisi, katika mavazi yake ya kiafande.
“Sajini! mahabusu yetu imejaa na leo ni ijumaa. Hivyo nimefanya utaratibu baadhi ya hawa mahabusu wapelekwe gereza maalumu hadi jumatatu.” Mkuu wa kituo hicho cha polisi akaweka bayana.
“Ndiyo afande.” Sajini Halfan akaitikia kwa saluti.
* * *
Saa nne asubuhi ya siku iliyofuata, ndani ya gereza maalumu jijini Dar es Salaam, timu ya watu wanne ilikuwa ikifanya kazi yake kwenye gereza hilo.
“Zimebaki dakika kumi tu!’’ Mmoja akafoka.
“Chumba kiko upande gani?’’ Mwingine akauliza.
“Usiniambie kuwa umesahau ramani...?” Mmoja akauliza kwa mashaka. Baada ya ukimya mfupi mwenzake akapendekeza.
“Bila shaka nadhani ni ule mlango wenye rangi nyekundu pale mbele.” Mwingine akasisitiza kwa sauti ya kunong’ona. Walipoufikia mlango huo na kugundua kuwa ulikuwa umefungwa. Kitasa cha mlango huo kilifumuliwa kwa risasi mbili kisha mlango ukasukumwa kwa teke kali. Mlango huo ulipofunguka, watu hao hatari wakajikuta wakitazamana na chumba kidogo sana, mfano wa chumba cha lifti kwenye jengo refu la ghorofa.
Ndani ya chumba hicho alikuwepo mtu mmoja dhaifu sana. Mtu huyo alikuwa amesimama katikati ya chumba hicho. Miguu na mikono yake, imefungwa madhubuti kwa minyororo. Mtu huyo alitia shaka na huruma kama kuku aliyesimama chini ya mti baada ya kunyeshewa sana na mvua.
Ilikuwa wazi kuwa alisimama ghafla, baada ya kusikia hatua za watu hao kuukaribia mlango wa chumba hicho. Vumbi jepesi lililotibuka baada ya watu hao kufanya uvamizi, lilikuwa limesambaa kila mahali humo ndani. Mtu huyo alikuwa akitetemeka kwa vile alivyokuwa dhoofu, dhahiri akionekana mwenye afya dhaifu.
Kilikuwa chumba kidogo ndani ya jengo kubwa, lililozungukwa na ukuta mrefu wenye ulinzi mkali. Ndani ya jengo hilo kulikuwa na wafungwa wachache, ambao kila mmoja alifungwa kwenye chumba chake kama huyu. Lilikuwa gereza moja maalumu la jijini Dar es Salaam.
“Mfungueni haraka tuondoke. Hamsikii kelele za ving’ora?” Kiongozi wa wavamizi hao wa gereza, akawatahadharisha wenzake. Kisha akamtazama mfungwa huyo mbele yake kabla ya kusema.
“Nakuonya! Usilete hila yoyote, vinginevyo risasi yangu moja ya kichwa, itahitimisha uhai wako humu ndani.”
Mtu huyo alikuwa amevaa magwanda meusi, kofia nyeusi ya mfuko yenye matundu mdomoni na machoni, na miwani myeusi yenye vishikio vyekundu. Mtu mwenye umbo kubwa na kovu la kutisha juu ya jicho lake la kushoto. Mara baada ya amri yake. Mvamizi mwenzake, mfupi kwa kimo, mwenye shingo nene na nywele nyingi. Alimsogelea yule mfungwa kwa tahadhari ndani ya hicho chumba.
“Jonas! wewe nenda kawashe gari na kuiweka tayari. Hatuna muda wa kupoteza, tukiingia tu ni kuondoka. Mwambie yule mheshimiwa atangulie, tutamkuta La Grado Casino. Nahofia asijeshindwa kasi ya matukio tukampoteza hapa.” Kiongozi wao akapendekeza. Mtu huyo aliyeitwa Jonas akaondoka bila kutaka ufafanuzi wa ziada, dhahiri akionekana kumwogopa kiongozi wao.
“Weka mikono yako kichwani.” Akasema yule mtu mfupi mwenye shingo nene. Amri yake ilipotekelezwa, akamsogelea yule mfungwa.
“Haya tembea mbele!” Akaamuru tena.
“First…., I need my lunch! Napenda chakula cha hapa. Haraka ya nini jamani? Mwili uliokufa haufi tena.” Yule mfungwa akaongea kwa sauti dhaifu yenye kujiamini.
“Wewe fala! hivi umemsikia vizuri Misanya? Yaani unaokolewa halafu unaleta masharti?” Yule mvamizi mfupi mwenye shingo nene, akafoka kwa hasira na kumchakaza yule mfungwa kwa mapigo manne yaliyokusudiwa tumboni. Hata hivyo akastaajabu kuona hakuna pigo hata moja lililompata. Pamoja na mfungwa huyo kufungwa kwa minyororo, mikononi na miguuni, lakini aliweza kukwepa mapigo yote ya mvamizi huyo mfupi na kujihami kwa kutupa mapigo mawili safi, yenye athari. Mvamizi akajibu mapigo kwa ngumi mbili makini za shingoni, zilizompunguza ukaidi yule mfungwa.
“Pumbavu..!” Mtu mfupi akafoka kwa hasira.
“Usiwe na hasira kijana..” Alisema mfungwa kwa sauti dhaifu. Akayatafuta mate kinywani kabla ya kuendelea
“Wakati wa ujana watu wengi huwa tuna ndoto moja; kwa mfano kutumikia taifa kama walimu, madaktari, wanajeshi na mengineyo. Wengi wetu ndoto hizo hufutika haraka, baada ya kuvutwa na mambo ambayo huja kugundua ni muhimu zaidi kuliko hizo ndoto. Mambo kama vile kuwa na familia, kupata pesa au kuasi tu. Wengine hugundua kuwa siyo rahisi kubadilisha jamii wanazotoka, watu hao hubadilika na huwa kama mimi. Watu ambao huamua kutumia vipawa vyao kwa njia mbaya. Wewe na mimi tuko kwenye kundi moja, maana sioni tofauti ya mimi na wewe kwa kweli. Hivyo twende taratibu tu, usijifanye mtakatifu kwa vile mimi nimesimama hapa wewe umesiamama hapo!’’ Yule mfungwa akaongea kwa sauti thabiti.
“Tofauti yetu ni kuwa, wewe ni mfungwa, mimi niko huru!’’ Akadakia yule mtu mfupi huku akimsogelea tena yule mfungwa.
“Hakuna mtu amewahi kukamatwa kwa mauaji au makosa aliyofanya. Wote waliokamatwa ni kwa sababu walishindwa kupangilia vizuri mauaji ama makosa hayo. Kilichofanywa wafungwe ni kwa sababu ushahidi dhidi yao ulipatikana, yaani walishindwa kupangilia vema makosa yao na kuyaficha baada ya kufanya. Lakini wapo wengi huko nje ambao wanaitwa watakatifu ila kwa sababu tu wanajua kuficha makosa na dhambi zao, amabazo ni kubwa kuliko iliyofanya mimi niwe hapa.” Alisema yule mfungwa kwa sauti ya chini.
“Hebu acha mahubiri wewe, hatuna muda wa mahubiri hapa. Lazima tuondoke hapa haraka. Tunataka kukutoa hapa gerezani uwe huru” Alisema Misanya, ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa wavamizi wa gereza.
“Sawa, najua hamjaja kunisaidia, bali mna shida na mimi. Siku zote ujue kuwa, ukiwa na manufaa makubwa mikononi mwa watu wasiosahihi, wewe si huru tena. Wewe kuwa hapa na mimi hatuna tofauti, nguruwe mchanga wewe! shenzi!.” Yule mfungwa akafoka na kuongeza tena, “Nguruwe wakubwa wakikosa chakula, nguruwe wachanga kama wewe wanaliwa. Huna tofauti na maji ya kutawadhia. Inashangaza maji kama hayo kujinadi kuwa masafi kuliko mkono wa mtawadhaji.” Mfungwa akaongea kwa tabasamu
“Sawa, najua hamjaja kunisaidia, bali mna shida na mimi. Siku zote ujue kuwa, ukiwa na manufaa makubwa mikononi mwa watu wasiosahihi, wewe si huru tena. Wewe kuwa hapa na mimi hatuna tofauti, nguruwe mchanga wewe! shenzi!.” Yule mfungwa akafoka na kuongeza tena, “Nguruwe wakubwa wakikosa chakula, nguruwe wachanga kama wewe wanaliwa. Huna tofauti na maji ya kutawadhia. Inashangaza maji kama hayo kujinadi kuwa masafi kuliko mkono wa mtawadhaji.” Mfungwa akaongea kwa tabasamu la dhihaka.
“Wewe! hebu mwache huyo, siyo kiwango chako. Mpe hiki chakula kwanza. Ndiyo maana nilikusisitiza tuje na mlo huo. Namjua huyu fala! tabia zake ni za ajabu sana.” Akasisitiza kiongozi wa wavamizi mwenye magwanda meusi, akimwamuru mvamizi mwingine mrefu na mweupe, mwenye nywele nyekundu na sura ya tabasamu.
Sauti ya ving’ora vya magari ya polisi, ikazidi kuhanikiza jirani na eneno lile. Wote wakaingiwa na hofu. Kiongozi wa kundi hilo akaanza kuona shida. Shida ya namna ya kuweka sawa uwiano kati ya mipango na ufinyu wa muda. Aliona muda ulikuwa ukikimbia wakati mipango ilikuwa ikienda taratibu. Alipoitupia macho saa yake ya mkononi, akajikuta akilaani mwenendo wa majira ya saa hiyo.
“Sijui kama waliopanga mipango walizingatia hilo!’’ Akawaza kabla ya kusema.
“Nadhani ni bora tumchukue kwa nguvu kabla polisi hawajafika. Hili gereza ni dogo lakini lina wafungwa muhimu sana. Hivyo najua vitakuja vikosi vya imara.” Mtu mfupi mwenye shingo nene akapendekeza huku akijishikashika usoni baada ya kipigo. Alikuwa amefura kwa hasira. Alitaka kumshushia mfungwa kipigo lakini bosi wake aliwahi kumzuia.
“Bora upambane na jeshi la watu mia kuliko kumlazimisha huyu mpuuzi kuondoka hapa. Haya Poka kula haraka, tunatakiwa kuondoka hapa haraka sana.” Kiongozi wa wavamizi akaongea kwa utulivu huku akitazama upande ambao kulikuwa na lango kuu la kuingilia. Mahali kulipokuwa na miili ya walinzi wa eneo hilo.
“Wewe nawe nenda katusubiri kwenye gari, jiandaeni na kuandaa vifaa endapo kutatokea makabiliano na polisi. Mwambie Naomi atupokee.” Kiongozi akasisitiza.
“Naomi ndiyo nani?’’ Akahoji mtu huyo aliyepewa maelekezo.
“Oooh! Okay! Jo…Mwa.” Akatoa maagizo huku akichomoa bastola yake kisha. akamwangalia yule mfungwa aliyemwita kwa jina la Poka wakati akimalizia kula. Kasi aliyotumia kula ilikuwa wazi kuwa hakuwa mtu wa kawaida. Baada ya kula alifanya kama anajinyoosha, hapo sauti ya mifupa kujiweka sawa ikasikika mwilini, kama vijiti vikavu vilivyokanywagwa na buti za jeshi msituni.
“Twende zetu, Poka kuwa makini. Nadhani sina haja ya kujitambulisha kwako kuwa mimi ni mtu wa namna gani.” Alisema yule jamaa mwenye magwanda.
“Usihofu Luteni Misanya, siwezi kuwa mkorofi kwa mkombozi wangu. Hasa baada ya kunipa chakula kitamu kama hiki.” Kauli ya Poka ikakatishwa na mlio wa risasi. ‘Hakuna namna, Life is too short to spend another moment imprisoned by the will of another’ Poka akawaza wakati akijiweka tayari kwa vitendo.
“Kazi imeiva.” Luteni Misanya akaongea kwa kihoro huku akifikiri hatari iliyokuwa mbele yao.
* * *
“SAJINI HALFAN, HEBU TUELEZE VIZURI. Ina maana siyo wewe uliyeandika hili jina?’’ Inspekta Lucas Mwenda akauliza kwa mshangao.
“Nakumbuka majina ya wasichana wawili yalikuwa yanafanana afande. Mmoja alijitambulisha kwa jina la Joanita Mwaikambo. Mwingine alijitambulisha kuwa anaitwa Joan Mwainunu. Halafu yule wa tatu, akajitambulisha kuwa anaitwa Jo Mwa. Nilimuuliza mara mbilimbili huyu msichana wa tatu, maana siyo kawaida kupata majina ya namna hiyo kwenye makabila ya hapa nchini.” Sajini Halfan akafafanua.
“Ulipomuuliza alisemaje?’’ Inspekta Lucas akadadisi.
“Alisema swali hilo nilitakiwa kuwauliza wazazi wake!’’ Sajini Halfan akafafanua huku akionesha kukereka na maswali hayo. Mahojiano haya yalichukua saa nne.
“Kwa hiyo Sajini unataka kutuhakikishia kuwa, hukuandikisha majina mawili yanayofanana? Maana kwa mujibu wa kitabu cha taarifa za awali pale kituoni, jina la Joan Mwainunu limeandikwa mara mbili na hakuna jina la Jo Mwa, kama unavyotuaminisha!’’ Inspekta Lucas akaonesha dukuduku lake.
“Hapana! Inawezekana kuna kitu hapo. Joan Mwainunu iliandikwa mara moja. Ni ajabu kuwa hakuna jina la Jo Mwa!’’ Sajini Halfan akaonesha mshangao wa dhahiri usoni.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment