Search This Blog

Thursday, 23 March 2023

MSAKO WA MWEHU - 4

 


Simulizi : Msako Wa Mwehu

Sehemu Ya : Nne (4)





Jamaa yule baada ya kuona Kachero Manu ameshachomoa bastola yake akaona isiwe tabu akaruka ukuta na kukimbia zake, akimtelekeza yule mwenzake aliyekuja nae. Mjuba mwingine mle chooni alibaki ameduwaa baada ya kusikia shaba zinarindima nje ya choo akajua kimenuka tayari. Akatoka mkukumkuku nje ya choo huku mkononi ameshika bastola yake.
Ile kutokeza tu nje akakutana na mdomo wa bastola, "tupa chini bastola yako, la sivyo nitasambaratisha ubongo wako sasa hivi" alisema kwa ukali Kachero Manu akiwa amemnyooshea mdomo wa bastola. Yule jamaa akaitupa chini bila ubishi na akanyoosha mikono juu. Kosa alilofanya Kachero Manu ni kutaka kuchungulia chooni kuangalia usalama wa kijana wa 'Chops CarWash'. Jamaa alionekana mzoefu wa kazi, akamshambulia kwa kurusha teke na kufanikiwa kudondosha bastola ile wakapanga mikono sasa watifuane vilivyo.
Kachero Manu alitaka pambano liishe raundi ya kwanza, akarusha teke moja la ubavuni ambalo uzito wake kama Mwalimu Kashasha yule mchambuzi wa Michezo "TBC-FM" angeliona kasi yake angethibitisha kuwa lina uwezo wa kuchana mifupa ya mbavu vipande vidogo vidogo. Tahamaki jamaa alichofanya ni kukaza mifupa ya mbavuni teke likadunda kama kitenesi.
Haraka haraka akabadili mbinu, akaamua sasa atakuwa anampiga kwa kumdokoa kwa lengo la kumchosha kama mbinu ya bondia bingwa nguli duniani kupata kutokea katika historia ya masumbwi, Mohamedi Alli. Mbinu hiyo ilifanya kazi na kuleta tija haraka baada ya muda mfupi jicho la kushoto na la kulia la yule mjuba yakaanza kuvuja damu, huku midomo yake yote miwili imepasuka haina hali. Jamaa akawa amepandwa na hasira akaja kumvamia Kachero Manu na kumbeba jumla jumla na kumtupa chini, mtupo ambao Kachero Manu alianguka kichwangomba kwa kugongeshwa kwenye ukuta.
Haraka haraka akajizoa pale sakafuni na kusimama. Yule adui akawa anacheka kicheko cha dharau cha kikwakwa huku meno yake ya susa yenye uchafu wa moshi wa sigara ukijionyesha dhahiri shahiri. Kachero Manu akameza mate machungu ingawa alikuwa kwenye maumivu makali. Akaamua ambadilishie mbinu za mapigano, jamaa ikawa akirusha ngumi anazikwepa halafu anamtandika chembe kidevu mbili za dabodabo.
Jamaa akaishiwa mbinu akabaki kutegemea maguvu yake, akaja kwa kasi na kumzoa tena Kachero Manu kwa kuikamata miguu yake kwa pamoja na kumnyanyua tena akiwa na lengo la kwenda kumbamiza kwenye ukuta. Alichofanya Kachero Manu nikukusanya nguvu na kumpiga kichwa cha katikati ya kichwa kwenye kidazi. Mbinu ambayo ilisaidia sana damu zikaanza kumchuruzika kwenye upara wake yule adui akaanza kuyumba kama mlevi, huku anaona kisunzi.
Usifanye mchezo na kichwa cha Komandoo wewe, kina nguvu zaidi ya jiwe fatuma. Kachero Manu kila akiona damu ndio mori wake unapanda, marshimarshi akaanza kumshambulia kwa kasi kwa mateke na mangumi baada ya sekunde kama 40 adui akawa ameshapiga dafrao yupo chini anatapatapa, huku kwenye suruali yake ameshajiachia ngama na mkojo. Akaifuata bastola yake na kumuwekea mtutu wake sikioni huku amemkandamiza goti lake kifuani mwake.
"Chiiifu Chiiifu nisamehee Chiifu..." aliomba msamaha yule adui. "Nani kakutuma uje umteke huyu kijana"?, tamaa Chiiifu, imeniponza nisamehe... Chiifu" alikuwa anaongea kwa takilifu mjuba yule. Gari za polisi zikawa zinasikika kwa mbali zinakuja eneo la tukio, maana ile milio ya risasi kule chooni ilisababisha mkukumkuku miongoni mwa wahudumu na wateja wao. Paka wa baa kwao ikawa ganda la muwa la jana chungu kaona kivuno, wanajisosomola kuku choma na mishikaki iliyotelekezwa na wateja mezani wanaokikwepa kifo.
Kachero Manu akakimbilia chooni na kumkuta yule kijana anatapatapa kwenye dimbwi la damu, huku kisu kimechomekwa ubavuni mwake, kisu ambacho kiliroromoa donda kubwa ubavuni mwake. Yule kijana alipomuona tu Kachero Manu akaanza kuongea kwa tabu huku analalamika,"Menejaaa.....ana...niuaaa....ana.... sem....aaa nime.....ku.... paa siriiiii". Haraka haraka Kachero Manu akapiga simu ya dharura waje wamchukue wamkimbize hospitalini kuokoa maisha yake.
Alipotoka nje ya choo tu akamkuta yule jamaa aliyepambana nae amezimia. Akapishana nao wana usalama wanaingia yeye ndio anaondoka na gari yake, huku akimpigia simu Kachero Yasmine kuhakikisha usiku huu wanamtia mbaroni mmiliki wa "Chops CarWash & Garage" na Meneja wake, ambao ni Baba na Mwana, ili wasaidie upelelezi wa kubaini wahusika wa mauaji ya Wabunge na dereva wao.

Mipango ya mauaji ya Wabunge namna ilivyotekelezwa ndani ya "Chops Carwash & Garage"
Mzee Hafeedh Abdullah mmiliki wa "Chops Carwash & Garage" akiwa ni mkandarasi mwenye vitega uchumi mbalimbali Afrika Mashariki na Kati, alikuwa pia ndio mfadhili mkuu wa ugaidi kwenye ukanda huo. Baada ya kutungwa kwa sheria ya ugaidi mwaka 2002 Bungeni, alichukizwa na sheria hiyo akiita kuwa ni ya ukandamizaji. Akaweka nia ya dhati ya kulipiza kisasi kwa Wabunge, waliopitisha sheria hiyo. Hivyo akanunua baadhi ya maeneo jirani na hapo Bungeni kwa kutumia majina tofauti tofauti.
Ilivyokuja mipango hii mipya kutoka "Al-shabaab" ya kuipa shinikizo serikali ya Tanzania wafunge balozi yao nchini Kenya ndio akaanzisha gereji na sehemu ya kuoshea magari inayoendana na hadhi ya Waheshimiwa. Mbaya zaidi viongozi wetu wengi hawapo makini kwenye kuchunga usalama wao. Dereva anapewa jukumu la kupeleka gereji anayoijua yeye na sehemu ya kuoshea magari anapopataka dereva, wanakula katika migahawa ya mitaani bila kuchunga usalama wao.
Mpango wa kwanza wa kutekeleza mauaji ya Wabunge kupitia kemikali ya kwenye vibomba vya kutawadhia hotelini ulivyobumburushwa na Kachero Manu, haraka haraka ukapangwa mkakati namba mbili wa kuwaua kupitia magari yao. Mauaji yalipangwa yafanyike siku ya ijumaa, siku hiyo hiyo ya hitimisho la maombolezo ya kitaifa hasa baada ya Tanzania kupuuza vitisho vya Al-shabaab" vya kupewa wiki moja watekeleze vinginevyo wataleta maafa tena.
"Maso Maso" baada ya kufanikiwa kuwapiga chenga ya mwili wana usalama kule hotelini, Dodoma akapata hifadhi nyumbani kwa Bwana Hafeedh Abdallah, ambaye ndio mfadhili wake wa masomoni kule Uingereza. Miaka ya karibuni Bwana Hafeedh Abdallah alikuwa anapatikana sana Jijini Dodoma hasa baada ya serikali kuhamia huko. Yeye shughuli zake za ukandarasi asilimia 85% zilikuwa zinategemea tenda za magumashi toka kwa watumishi wala rushwa wa serikalini.
"Sasa utatekelezaje hayo mauaji kijana wangu "Maso Maso" maana si unajua sasa Wabunge wanalindwa ile mbaya baada ya siri zetu kuvuja kwenye vyombo vya usalama? " alikuwa Mzee Hafeedh Abdallah anamsaili 'Maso Square The Duduman' ili asije kufanya kosa litakalowagharimu. "Unajua nimepanga kuwawekea sumu kwenye magari yao, sumu ambayo baada ya kuanzia nusu saa mpaka lisaa limoja baada ya kuvuta hiyo sumu inaleta madhara unakufa mara moja", alieleza "Maso Maso". "Utawekaje sasa hizo sumu si unajua magari ya vigogo hao yanachungwa sana" alizidi kudadisi Mzee Hafeedh, alitaka atolewe wasiwasi usioacha mashaka.
"Teh teh teh teh..labda nchi zingine sio Tanzania, nchi hii unakuta Hakimu kawahukumu majambazi kifungo cha miaka 30 jela halafu bado anaishi uswahilini, na jioni atakuja baa kupata kilaji. Ndio maana zamani enzi za mkoloni viongozi walikuwa wana maeneo yao maalumu ya kuishi yanayolindwa, wana sehemu zao maalumu za kustarehe ndio maana kulikuwa na ile 'Leaders Club' pale Dar es Salaam, lakini sasa mambo yanaenda shaghalabagala ukitaka kuleta madhara kwa kiongozi ni dakika sifuri tu" alizungumza "Maso Maso" kwa majigambo na kujitapa kuonyesha anaijua kazi yake ya ugaidi nje ndani.
"Sasa nimepanga kuweka sumu kupitia mfumo wa kipoza hewa wa gari. Nitakachofanya magari ya waheshimiwa yakifika kuoshwa nitafungua A/C Filter kisha naweka kemikali yangu ambayo wakiwasha kiyoyozi tu baada ya lisaa limoja dereva na kigogo wake wanapokelewa akhera leo hii, wataivuta hiyo kemikali sumu wakati hewa baridi inapuliza kiyoyozi ndani ya gari lao" alimaliza maelezo yake marefu yaliyomkinaisha na kukata kiu yake kibopa Hafeedh Abdallah, hivyo akapitisha mkakati huu.
Ndio ikapangwa siku ya Ijumaa wafanyakazi wa gereji na wote wanaohusika na 'Carwash' waambiwe wasije kazini, ili kumpa fursa "Maso Maso" apige kazi yake ya mwisho kuiadabisha Tanzania kisha wote watoroke kwenda kujificha huko mafichoni. Mzee Hafeedh Abdallah tayari alishaacha vitega uchumi vya siri vingi kwa majina ya watu tofauti tofauti ili kuificha serikali isikamate mali zake. Hivyo alikuwa na uhakika wa kuishi mafichoni mpaka kifo chake bila shida yoyote ya pesa.
Baada ya Kachero Manu na Kachero Yasmine kupewa taarifa ya msiba wa Wabunge hao, na Mkuu wao wa kazi, Bwana Omega Mtanika, ikawabidi wakimbilie hospitali ya mkoa ya Dodoma "General" kuangalia miili ya wahanga. Walikuta umati wa wakazi wa Jiji la Dodoma wamefurika mochwari ya Dodoma. Uvumi mitaani ulienea magari zaidi ya magari 10 yamegongana na kusababisha vifo vya mamia ya watu. Hawakujua kama kuna ugaidi ndani ya tukio hilo.
Bahati na ngekewa ilikuwa upande wake Kachero Manu, kuna dereva mmoja wa mmoja wa Wabunge wale alikuwa bado yupo hai ila yupo kwenye hali mbaya, anapitia sakaratu mauti. Hizo taarifa alizipata toka kwa Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali walipoenda kuhojiana nae.
Kachero Manu alikesha chumba cha wagonjwa mahututi, "Intensive Care Unit"- (I. C. U) akimsubiria dereva huyo apate nafuu huenda akaambulia chochote kitu. Mishale ya saa tisa usiku uvumilivu wake ulilipa, kama wanavyosema mvumilivu hula mbivu, yule dereva alipata nafuu kidogo na alifanikiwa kueleza sehemu ya mwisho waliyopitia kabla ya tukio ni 'Chops Carwash'. Lakini baadae hali ilibadilika akaaga dunia. Ila alichoshukuru Kachero Manu ni kupata sehemu ya kuanzia upelelezi wake.

SURA YA KUMI NA MOJA
Mke wa Kachero Manu mikononi mwa magaidi
Siku ya Jumatatu, Kachero Manu aliamka majira ya saa tatu asubuhi akiwa buheri wa afya. Kwa wiki nzima iliyopita alikuwa hajapata utulivu wa maana wa kupumzisha mwili na nafsi, mpaka Jumapili usiku akaamua akalale nyumbani kwa mkewe Bi.Faith Magayane. Mamsapu wake alikuwa anaishi maeneo ya karibu na Viwanja vya Maonyesho ya Nane Nane-Nzuguni katika nyumba ya kupangisha yenye chumba tatu, jiko na sebule. Ilikuwa ni nyumba inayoendana na hadhi yake kama mtumishi wa umma katika sekta binafsi.
Alipoamka usingizini Kachero Manu alikuta tayari mkewe kashang'oa nanga kuelekea kibaruani kwake. Usiku walikesha na mkewe wanapeana michapo ya hapa na pale ya matukio mbalimbali, mpaka mechi za Wanandoa wakacheza, mwishowe wakajikuta wamelala mishale mibaya. Alipoamka kitandani alikwenda kwanza kunawa uso na kusafisha meno yake, kisha akafanya mazoezi binafsi ya viungo kama muda wa robo saa, kisha akaenda kuoga, akavaa vizuri na kuelekea mesini.
Hapo alikuta tayari kashatayarishiwa kifungua kinywa na mkewe. Alikuta kuna sahani ya matunda mchanganyiko iliyofunikwa na kawa yenye maandishi ya kimahaba. Pia akakuta hotipoti limejaa kande za mahindi mabichi na chai nzito ya maziwa kwenye chupa kubwa. Bila kufanya ajizi akaanza kujichana vilivyo, alimaliza akaenda kuosha vyombo jikoni kisha akawa anajiandaa kuondoka zake.
Akiwa anajiandaa kufunga mlango wa nyumba simu yake ya mkononi ikaanza kuita. Akaichomoa simu kuangalia akaona ni namba ngeni kwake akaipokea. "Hellow....unazungumza na Afisa Rasilimali Watu kutoka Benki ya KCB-Dodoma naitwa 'Martin Hoseah', nadhani nazungumza na mume wa mfanyakazi mwenzetu 'Faith Magayane'?". Mapigo ya moyo ya Kachero Manu yakalipuka na kupatwa na ususuavu wa moyo. Akaanza kujiuliza, "mke wangu kafariki, katekwa au kapata ajali,? mbona sijawahi kupigiwa simu toka kazini kwake hata siku moja,?" aliwaza Kachero Manu mpaka akajisahau hajatoa majibu ya swali aliloulizwa.
"Hellow.. Hellow.." yule Afisa alipoona hamna majibu akakata simu yake. Baada ya sekunde kadhaa kupita akaanza kupiga upya, Kachero Manu akakurupuka kama katoka ndotoni na kuipokea. Yule Afisa akaeleza anachokikusudia. "Samahani mkeo hajafika kazini mpaka sasa na hapatikani kwenye simu yake ya mkononi na hatuna taarifa zake zozote mpaka sasa hivi tunavyoongea". "My God, amepatwa na maswahibu gani tena, maana nyumbani kadamka asubuhi na mapema kuja huko kazini! labda tusubirie Kwanza tutaendelea kujuzana" alijibu Kachero Manu, wakaagana kwa maafikiano ya kupeana taarifa ya juu kinachoendelea katika sakata hilo la kupotea kwa mkewe.
Baada ya simu kukatwa ikabidi arudi kukaa sebuleni kwenye sofa na kuanza kutafakari kitu cha kufanya. "Nini kimempata mahabubu wangu Faith!, mbona tumelala raha mustarehe na asali tumelambishana mpaka usiku wa manane, tena mechi ya patashika nguo kuchanika!. Hajaniambia lolote kama kuna mbaya wake labda anamuwinda kwa kisasi. Itakuwa labda amepata ajali au kifo inabidi sasa hivi nielekee hospitali ya Mkoa kabla sijaendelea na chochote mkururu wa fikra ulikuwa unasafiri katika kichwa cha Kachero Manu.
Akaamua na yeye kujaribu kuipiga simu ya mkewe kupitia namba zake mbalimbali alizo nazo kwenye simu yake zote zikawa hazileti majibu yoyote zaidi ya lile jibu pendwa la simu iliyozimwa la kuwa “mtumiaji wa simu uliyempigia hapatikani jaribu tena baadae. Akajaribu kupiga kwa baadhi ya marafiki zake, nao hawakuwa na majibu ya kueleweka zaidi ya paukwa pakawa. Hakutaka kabisa kuwapigia ndugu na wazazi wa mkewe kuogopa wasijepatwa na taharuki juu ya uhai wa mtoto wao, na kuharibu uchunguzi wote.
"Lazima nipite Hospitali ya Mkoa kwanza kuulizia, vinginevyo nitaharibu kazi za watu bure kama sitofahamu usalama wa mke wangu kwanza" alijisemea mwenyewe wakati anajiandaa kutoka nyumbani. Akafunga mlango wa nyumba yao na kisha kupanda ndani ya gari lake ili aondoke zake kwenda hospitali ya Mkoa, akaanze kuhemea taarifa za mkewe kama zipo. Akiwa ameshaweka funguo kwenye swichi ya gari ili awashe aondoke zake, akaisikia simu yake inaita tena. Sasa hivi akafanya pupa kuichomoa kiunoni alijua labda ni mkewe Faith anapiga kumtoa wasiwasi juu ya usalama wake au labda ni yule Afisa Uajiri wa Benki ya KCB amepata taarifa mpya. Kuangalia akaona ni namba ya kachero Yasmine, akaipokea.
"Hellow...Bosi habari yako natumaini umeamka salama salimini wa afya, huyu Kareem Abdallah Meneja wa "Chops Carwash & Garage" tayari nilishamtia mbaroni toka saa sita usiku kama ulivyoagiza nifanye hivyo ila baba yake mzazi ametuachia manyoya hajulikani alipo, na vijana wangu wa kazi wanasema kuna dalili ameshatoroka maana hajaonekana popote pale kwenye viwanja vyake vya kujivinjari. Huyu mtoto wake tutazaa nae tupo nae huku chimbo letu kijiji cha Zuzu hapa hapa Dodoma mpaka sasa hajatoa ushirikiano wowote" alimaliza maelezo yake Kachero Yasmine kwa mkuu wake wa kazi.
"Good job..sasa mie nitakuja huko baada ya saa mbili kuona tunafanyaje, maana huyo ndio kabeba ramani nzima ya magaidi wa "Al-shabaab" yaliyosababishwa na gereji yake" akamalizia maongezi Kachero Manu wakaagana zao.
Hakutaka kumpa hiyo taarifa ya kupotea mkewe Kachero Yasmine aliogopa atamchanganya na kumpotezea umakini. Saa tano kamili asubuhi akawa ndio anawasili kwenye maegesho ya Hospitali ya Mkoa ya Dodoma kuangalia uwezekano wa kumpata mkewe akiwa mgonjwa au marehemu.

Kareem Abdullah, Meneja wa kampuni ya "Chops Carwash & Garage" mpaka sasa alikuwa ametumikia saa 12 akiwa ametimbika na kupigika vilivyo katika kituo cha siri cha kuwahoji watuhumiwa wa ugaidi. Baba yake mzazi alishatorokea mafichoni kwenda kujichimbia kusikojulikana.
Kituo hiko kilikuwa kipo katika barabara ya kuelekea kijiji cha Zuzu, katika jengo la zamani la NMC "National Milling Company" Kufika kilipo hiko kituo ilitakiwa uifuate barabara ya kuelekea Arusha (Arusha Road) kama unatokea katikati ya Jiji la Dodoma kisha unakata kushoto kuifuata barabara ya Kizota. Utatakiwa uende barabara ya vumbi na changarawe kwa zaidi ya kilometa 35 ndipo utakapokikuta kituo hicho kikiwa kipo pembezoni kabisa mwa reli.
Kachero Yasmine na vijana wake wa kazi walimuwekea mtego nje ya nyumba yake Bwana Kareem Abdallah. Kwenye muda ya saa 6:15 usiku wakati anarejea nyumbani kwake. Wakamteka juu kwa juu na wala hakuleta ubishi wowote, hivyo wakamsafirisha usiku kwa usiku mpaka kwenye kituo chao walichokiteua kwa kazi hiyo maalumu.
Kituo kilikuwa na watu maalumu wa utesaji wanne wanaopokezana zamu masaa 12, wakiingia wawili wawili. Ukiwaona walikuwa ni kama mapacha jinsi wanavyofanana majumbile yao. Walikuwa warefu, weusi tii, wamejazia mwili wa kimazoezi huku vifua vyao vikiwa ni vipana vimetengeneza mikato mikato kutokana na ubebaji wa vitu vizito na milo bora inayonawirisha miji yao hiyo. Sura zao zilikuwa zinatisha hazina chembe ya upendo wala huruma hata kidogo, huku macho yao daima yakiwa ni mekundu. Meno yao makubwa huku yakiwa yamejivika ukungu kutokana na uwingi wa idadi ya sigara wanazovuta kwa siku.
Kareem Abdallah Meneja na mtoto wa mmiliki wa 'Chops Carwash & Garage' alivyobwagwa kituoni hapo na Kachero Yasmine alipokelewa na hao wazee wa kazi. Ambao kwanza walimgombania kama mpira wa kona unavyogombaniwa na wachezaji wote wa timu mbili pinzani. Tahamaki baada ya dakika kama 10 tu alikuwa hatamaniki usoni kwa idadi ya manundu na mipasuko. Ghafla akapata umbile la macho ya chawa kama ya Wachina. Kisha baada ya hapo akawekwa kwenye kiti cha umeme halafu unawashwa umeme anapigwa shoti za umeme mpaka akazimia.
Akapewa huduma ya kwanza alipozinduka akawekwa kwenye chumba kilichofunguliwa muziki kama wa disko la mitaani, muziki ambao umefunguliwa mpaka sauti ya juu, wakamfungia humo. Hapo tena akakesha mkesha wa lazima bila kupenda mpaka kulipokucha.
Ilipofika saa mbili asubuhi akaletwa mbele ya Kachero Yasmine kwa ajili ya mahojiano. "Swali langu ni moja tu, yuko wapi mfanyakazi wako wa gereji aliyefanya kazi siku ya Ijumaa na kutokomea kusipojulikana"? aliuliza Kachero Yasmine mara baada ya Meneja huyo mhalifu kuletwa mbele yake. "Simfahamu mie ni Meneja tu, kila kitu mhusika ni mmiliki, nadhani mkimpata yeye mtapata majibu kamili" alijibu kiujeuri akionekana kuwa ni mnyonge kuonyesha amechoshwa na mateso ya usiku.



Ilipofika saa mbili asubuhi akaletwa mbele ya Kachero Yasmine kwa ajili ya mahojiano. "Swali langu ni moja tu, yuko wapi mfanyakazi wako wa gereji aliyefanya kazi siku ya Ijumaa na kutokomea kusipojulikana"? aliuliza Kachero Yasmine mara baada ya Meneja huyo mhalifu kuletwa mbele yake. "Simfahamu mie ni Meneja tu, kila kitu mhusika ni mmiliki, nadhani mkimpata yeye mtapata majibu kamili" alijibu kiujeuri akionekana kuwa ni mnyonge kuonyesha amechoshwa na mateso ya usiku.
Akawa hana jinsi ya kumlazimisha kwa sababu wanachunga haki za binadamu hakupenda wazidi kumpa mateso zaidi bila sababu. Jukumu lao ni kupepeleza ushahidi utakaomtia hatiani wakimpelekea mbele ya vyombo vya sheria. Akaamrisha arudishwe selo huku wakihakikisha wamempatia chakula cha kushiba.
Kachero Yasmine baada ya mahojiano na yule Meneja mtuhumiwa, akawasha kompyuta yake mpakato na kujiunga na kifurushi cha mtandao. Akatuma moja ya barua pepe. Akawa amebaki kusubiria majibu, baada ya dakika 5 akajibiwa. Muda wote alikuwa anatabasamu pana la ushindi kisha akafungua akaunti feki ya mtandao wa kijamii wa "Facebook". Kisha akatuma picha zake alizopiga katika mapozi mbalimbali. Akiwa bado yupo kwenye mtandao hajatoka, akaona akaunti moja yenye picha ya msichana yenye jina la "NUSRA COMMITTEE" inamuomba urafiki.
Haraka haraka akakubali urafiki huo aliomuomba. Akaanza kutumiwa kwenye akaunti yake feki mada mbalimbali za umuhimu wa ndoa kwa mwanamke wa kiislamu. Akafunga kompyuta yake huku akishukuru kwa hatua aliyoifikia sio haba. Kachero Yasmine alikuwa anakifanyia kazi kikadi alichodondoshewa na "Maso Square The Duduman" pale hotelini.
Kikadi kilikuwa na anuani ya barua pepe. Ambayo Kachero Yasmine aliitumia kutuma taarifa zake. Ndipo mpaka alipokutanishwa na "NUSRA COMMITTEE" sasa alikuwa anasubiria nini kitakachojiri. Alishakisia kuwa "NUSRA COMMITTEE" inahusika na kutafutia wachumba wanawake kwa wanaume. Alipoichunguza alikuta ni akaunti maarufu sana kwa wadada wa kiislamu kwa wakaka wenye kusaka wenza wao wenye maadili ya Kiislamu. Umaarufu wa "NUSRA COMMITTEE" ulivuma zaidi baada ya kuwa wenza wakikubaliana inagharamia gharama zote za sherehe ya ndoa kwa kiwango walichoweka cha bajeti. kisha kama mume hana kazi wanamjaribu kama anafaa wanamtafutia shughuli maalumu ambayo ni siri yao na mhusika.
Kachero Yasmine jina lake tayari lilishawekwa kwenye orodha ya wanaotafuta wachumba, lengo akitaka kuleta ufukunyuku wa kufahamu hao wasichana mamia kwa mamia wanapelekwa wapi baada ya ndoa, wao na waume zao.

Kachero Manu alikuwa ameshafika kwenye kituo kidogo cha kuwashikilia magaidi katika jengo la "NMC" ya zamani kama saa mbili yaliyopita akitokea Hospitali ya Mkoa. Ambapo hakupata taarifa yoyote kuhusiana na mkewe pamoja na kupewa maneno matamu ya ahadi ya kupewa taarifa pindi atakapofikishwa hapo.
Hakutaka kwanza kuwahusisha polisi wasije kuvuruga mambo, mkewe akapata matatizo. Ikabidi sasa hana jinsi zaidi ya kumsimulia Kachero Yasmine juu ya kutoweka kwa mkewe. "Sasa tunafanyaje Bosi,?" aliuliza Kachero Yasmine akionekana ameshachanganyikiwa baada ya kupewa penyenye hizo.
"Hatuna njia yoyote zaidi ya kwanza tusubirie kama ametekwa tuone masharti yao wanataka nini!" alijibu kiunyonge Kachero Manu. Kweli kisu kilikita kwenye mfupa alikuwa ameshikwa pabaya. Wakiwa bado wapo kwenye taharuki hiyo iliyowakumba simu ya Kachero Manu ikaanza kuita. Akaitoa kiunoni mwake, kucheki ni namba mpya, akaanza kutetemeka anagitagita kuipokea kama anavyotetema mlevi wa pombe kali iliyomkolea mwilini.
Akawa hana jinsi zaidi ya kuipokea, "Hello....Hello..nani mwenzangu?" aliuliza Kachero Manu baada ya kubonyeza kitufe cha kupokelea simu. "Hamna cha mwenzangu hapa, fungua "Whatsapp" yako uone utamu utamuni, tunavyojipocholea teh.. teh.. teh.." kisha akakata simu huyo mpigaji. Kachero Manu akawa bado amepigwa bumbuwazi. Alikuwa kwenye dimbwi la mawazo Kachero Manu, kijasho chembamba kikaanza kumvuja licha ya kuwa kiyoyozi mle ofisini kilikuwa kinatema baridi ya kutosha.
Ikabidi haraka haraka awashe data kwenye simu yake, na Kuingia kwenye mtandao wa "Whatsapp" akaona kuna video imetumwa kwa namba ngeni asiyoifahamu ambayo haipo kwenye orodha ya namba za watu wenye mawasiliano na yeye. Akaanza kutetemeka vidole vyake kubonyeza ile video ili aone inahusiana nae nini mpaka atumiwe yeye na asisitiziwe kabisa kuwa aangalie!. Akavaa vazi la ujasiri, wa liwalo na liwe yeye ni mtoto wa kiume, na matatizo ni sehemu ya maumbile ya maisha ya mwanadamu akaifungua.
Hamadi...! Simu ikamponyoka mpaka chini ikaenda kuangukia karibu kabisa na miguu ya Kachero Yasmine kwa mshtuko wa yale aliyoyaona kwenye simu yake. Kachero Yasmine muda wote alikuwa anamuangalia tu namna Bosi wake anavyopitia kipindi kigumu ambacho hajawahi kumuona anakipitia tokea waanze kufanya kazi pamoja. Alikuwa anaonekana kama mtu bozibozi tofauti na jinsi anavyomfahamu kuwa ni mtu jasiri na shupavu. Akamsaidia kuiokota simu na kumrejesha mwenyewe. Kachero Manu akaichukua simu na kuingia tena "Whatsapp" akaipunguza sauti ya spika ya simu yake, na kuruhusu video ianze kucheza tena.
Maskini weeeh..Masalale! ilikuwa ni video ya ngono, mkewe Kachero Manu amerekodiwa anaingiliwa kwa nguvu, mtungo na mijitu miwili mishababi iliyoshibiana, sumsum haswa miili yao ukiitazama na imejaaliwa dhakari kubwa mithili ya punda kilongwe. Mijitu ambayo kwa juu imefunika nyuso zao kwa maski nyeusi, ili isijulikane uhalisia wao. Ilikuwa inaonyesha mkewe Kachero Manu amefungwa kwenye kingo za kitanda na kamba madhubuti akiwa hana nguo yoyote kaachwa uchi kitandani. Wakawa wanamsukasuka kwa zamu huku analalamika kwa sauti ya juu maumivu ya vitendo vya kifedhuli vya kuingiliwa kinguvu anavyofanyiwa.
Alivyoimaliza kuiangalia video hiyo fupi ya dakika 3, Kachero Manu machozi yakaanza kumtiririka kama maji mashavuni mwake, huku akichomoa hanchifu chake na kuanza kujifuta machozi. "Vipi Bosi sikuelewi ni msiba, maana unagogoteza maneno yasiyoeleweka kama umepandwa na ruhani kichwani?, Faith amepona kweli jamani..!" aliuliza Kachero Yasmine. Akawa Kachero Manu hana nguvu ya kumjibu mwenzake zaidi ya kumpa simu ajionee unyama anaofanyiwa mkewe na watekaji.
Kachero Yasmine nae hakuwa na hali kwa jinsi alivyoiona hiyo video, ilikuwa ni unyama usiomithilika kutazama kwa mwenye akili iliyosalimika labda mwenye akili hamuma ndio atafurahia unyama huo. Wakawa wameshang'amua kuwa mkewe Kachero Manu ametekwa na watekaji hawajatoa kitu wanachokitaka kutokana na utekaji huo. "Kama watekaji watahitaji mshumbi wa pesa nipo tayari kukwangua akaunti zangu zote kwa ajili ya mke wangu hata ikibidi kukopa pesa benki nipo tayari ili mahabubu wangu awe huru" alisema Kachero Manu kumwambia mwenzake Yasmine wakati wanatafakari nini cha kufanya na kubadilishana mawazo.
Ghafla wakiwa kwenye majadiliano hayo, simu ya Kachero Manu ikaanza kuita, sasa halahala bila kuchelewa akabonyeza kitufe cha kuruhusu mpigaji wa simu asikike anachotaka kusema.
"Haya Baba nadhani umeona mwenyewe, kwanza nikupongeze memsapu wako ni fundi sana kitandani vijana wangu mahabithi wa tabia wameniambia wamefurahi sana, tena furaha isiyo kifani yaani ile fokofoko kustarehe na memsapu wako, haya tuyaache uamuzi ni wako, kama unamtaka mkeo akiwa salama tunaomba saa sita usiku leo hii umlete mateka mnayemshikilia Bwana 'Kareem Abdallah', Meneja wa "Chops Carwash & Garage" katika uwanda wa bonde la Mzakwe karibia na mashamba ya zazibu ya Mjerumani-DODEP, maelezo zaidi utayapata huko huko, kinyume chake hautompata tena.
Wale vijana wa kazi, waliompa shughuli mkeo hainehaine! nimewazuia mimi tu wasiendelee kujilia uroda, walishambeba juu juu sasa hivi wakamfanyie radidi tena.
Vinginevyo watakesha nae kitandani. Tunakupa hadhari usijaribu katu kuleta ujanja wowote, ukihalafa tu utampoteza mkeo, kwanza ongea nae mkeo akusalimie.." baada ya kupita kitambo kifupi akaanza kusikia sauti ya mkewe iliyojaa majonzi na simanzi, "Pliiiz Beeebiii...help me pliiiz i'm in great trouble" akanyang'anywa simu alipoanza kukatwa hapo hapo simu hiyo kabla hajaendelea kuzungumza zaidi na mumewe.
Kachero Manu akabaki amenyong'onyea hajui cha kufanya bado ameishikilia simu yake sikioni. Akapata nguvu za kujaribu kuipiga tena ile namba ya wale watekaji ikawa haipatikani kuonyesha imezimwa tayari. Akajaribu kupiga maradufu lakini jibu likawa ni lile lile linalokera masikio yake asilotaka kulisikia.
Ikabidi Kachero Manu ampe mchapo mzima Kachero Yasmine na namna watakavyoweza kufanya maneva ya kivita ya kumuokoa mke wake na bado adui agonge mwamba asiweze kuwatoroka.



Kachero Manu, alivyotoka ofisini kwa Meneja Bwana Kareem Abdallah tayari alikuwa kwenye rada za magaidi. Kuna vijana kama wanne walikuwa wanashinda pale gereji kama mafundi lakini wapo pale kwa kazi maalumu. Wakapewa jukumu la kumfuatilia nyendo zake. Hasa baada ya kuuliza maswali yanayohusisha kampuni ya 'Chops Carwash & Garage' na vifo vya Wabunge watano na madereva wao.
"Nimewaiteni kikao kifupi, naomba mfuatilie yule jamaa mtu aliyeingia ofisini kwangu sasa hivi. Namba zake za gari nakukabidhi wewe Jimmy mhakikishe hapotei kwenye rada zetu, mpaka tutakapopata maelekezo toka kambi kuu Jijini Tanga nini tumfanye" alifungua mazungumzo kwenye kikao kifupi Bwana Kareem Abdallah kilichofanyika ofisini kwake punde tu baada ya kutoka kwa Kachero Manu.
"Vipi tunaruhusiwa kuondosha uhai wake kama atatushtukia na kuamua kupambana na sisi?". Aliuliza Jimmy ambaye ndio alikuwa kiongozi wao huku akionekana umri wake ni takribani kijana wa makamo ya miaka 45, anayeikimbilia miaka ya rushudi. "Ikibidi hamna jinsi ila sitegemei iwe hivyo, wewe Jimmy achana na fikira tasa, wewe ni mzoefu wa mambo ya uhalifu tokea utoto wako, kumbuka wewe ukiwa na miaka 10 tu mwaka 1991 ulikuwa unawafanya watu wa Jiji la Dar es Salaam wanalala saa 12 jioni, kwa kuogopa kundi lako la watoto wenzako enzi hizo la 'Komando Yosso', hivyo sitegemei ushindwe kumfuatilia kwa umakini Mlugaluga kama yule" aliongea Bwana Kareem Abdallah, huku Jimmy akitikisa kichwa chake kuonyesha anakubali kile kinachoongewa na Bosi wake kuwa yeye alikuwa ni jambazi sugu kwa zaidi ya miaka 34.
Bila kuchelewa Jimmy akagawa majukumu kwa wenzake na kuanza kazi mara moja, kila mmoja akatawanyikia upande wake kutimiza majukumu yake. Wawili kati yao ndio wale aliopambana nao Kachero Manu kule chooni pale "Chako ni Chako bar" baada ya kuzuka suitafahamu baina yao.
Jimmy na mwenzake ndio waliomsindikiza Kachero Manu mpaka wakapajua nyumbani kwake bila ya yeye mwenyewe kutanabahi chochote. Hakuwahi kuwazia kama anaweza kufuatiliwa nyendo zake. Maana magaidi ni waoga sana ndio maana wanafanya matukio yao kwa kuvizia. Jimmy ambaye mwenyewe akipenda sana kujiita "Komando Yosso Veterani" alipopewa taarifa za kutekwa kwa Bosi wao Bwana Kareem, moja kwa moja akamtuhumu Kachero Manu kuhusika na figisufigisu zilizompata Bosi wao.
Nae akapanga mipango ya kulipiza kisasi kwa kumteka mkewe, ili wamtumie kama chambo cha kumrejesha Bosi wao kutoka mafichoni. Ili kuleta tashiwishi ya kufanya maamuzi ya haraka ya kumrejesha Bwana Kareem bila kusita wakawatumia wataalamu wao katika uhalifu wa kucheza na kompyuta wanaojua kuchezesha video. Wakampiga picha ya sehemu ya juu ya memsapu wake Kachero Manu, kuanzia chini ya kifua kuja juu, kisha wakaichanganya kiutaalamu mkubwa na mojawapo ya video za mcheza filamu za ngono nguli.
Ikawa ukiiangalia hiyo video utaamini moja kwa moja kuwa mke wa Kachero ndio anafanyiwa vitendo hivyo vya kifedhuli. Kwa sababu chini ya titi la kushoto la mke wa Kachero Manu kulikuwa na kovu dogo ambalo lilikuwa linaonekana dhahiri shahiri kwenye ile video feki.
Mbinu ambayo ilishafanikiwa tayari Kachero Manu alisharudisha mpira kwa golikipa, alishakubali yaishie. Hata siku moja usicheze na nguvu ya mapenzi, hamna boflo ngumu mbele ya chai ya mkandaa. Ilikuwa inasubiriwa muda tu Bwana 'Kareem Abdallah' akombolewe na washirika wake. Alijutia sana kwa uzembe wake laiti angekuwa ameongeza umakini angeshagundua kuwa kuna watu wanamwinda. Hamna mtu wa kawaida alikuwa anafahamu kama yeye ataenda kulala kwa mkewe hata Kachero Yasmine hakufamu wapi Bosi wake amelala usiku ule.
Ila alijiapiza "kwa vitendo hivi hobelahobela walivyomfanyia mke wangu nitahakikisha ninawatia adabu kwa mikono yangu mwenyewe mpaka wajutie uhuni walionifanyia" machozi yakawa yanamtiritika kama mtu mdogo, usicheze na maumivu ya kuchapiwa mke tena fauka ya kuchapiwa tena kwa mtindo wa mtungo na wahuni. Ambao afya zao hazijulikani kama wamesalimika na UKIMWI au magonjwa mengine ya zinaa.
Maumivu yake ni zaidi ya msiba. Aliona wamemfanyia unyama wa hali ya juu. Alikuwa anajijutia mkewe amemuingiza kwenye matatizo yasiyomhusu. Maana yeye mkewe alikuwa ni mtu rahimu na matendo yake ni hasanati hajawahi kumfanyia mtu yoyote matendo hasaisi yasiyoendana na utu.
"Wamenivua nguo hadhari, siwezi kuficha aibu hii, kujaribu kuficha ni sawa na kujikinga jua kwa kutumia ungo, nitauweka wapi uso wangu pindi wakiamua kuzirusha hizi video chafu kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook, Jamiiforums na hata Utube" alizidi kuwaza huku machozi yanazidi kutiririka kutoka kwenye mboni za macho bila kizuizi. Maji yalimfika shingoni Kachero Manu, magaidi walijua kulenga kunako.

Serikali ilipitisha maamuzi ya kuwa msako wa "Maso Square The Duduman" na genge lake la magaidi uwe ni wa kimya kimya. Ila picha za "Maso Square The Duduman" zikawa zimetawanywa kila kona ya nchi kuwa anatafutwa kwa udi na uvumba. Yeyote atayefanikisha kupatikana kwake aliahidiwa donge nono la milioni 100, na kuhakikishiwa ulinzi wa vyombo vya dola maisha yake yote.
Hata kwa misiba iliyotokea ya waheshimiwa wabunge na madereva wao, serikali iliamua maombolezo yawe kimya kimya, kusiwe na hashuo na kila mtu azikwe bila kutangaza kwa upana habari hizo kwenye vyombo vya habari. Lengo likiwa ni kumfanya adui asijue nini kinachopangwa na pia kuondosha hofu ya usalama kwa wananchi hivyo kuzorotesha uchumi wa nchi.
Ilipofika saa 12:00 jioni Kachero Yasmine alipowasha data tu ya simu yake ili apate kurambaza habari kwa njia ya mtandao, akaona meseji zimetiririka kwenye akaunti yake feki ya "Facebook". Kufungua tu alipoisoma tu akaanza kutabasamu, "Vipi Yasmine mbona furaha kama zote kulikoni unanipa jaka moyo" alichombeza Kachero Manu, kidogo kidogo alishaanza kuizoea hali ya kutekwa kwa mkewe. "Nimependwa na gaidi "Maso Maso" mwenzio anataka kunioa na picha yake kanitumia teh teh teh" alijibu kwa kujigamba Kachero Yasmine kuonyesha tayari ameshamuingiza kwenye mtego wa mapenzi. "Nilijua tu ile siku namna alivyokuwa anakuangalia alionyesha kabisa amekuzimikia vibaya sana, hongera sana Mrs. Maso Square keki ya harusi itakatwa kwa mtutu wa mtutu wa bunduki" aliongea Kachero Manu, utani ambao ulimuacha Kachero Yasmine akiwa hana hali kwa kicheko huku akimueleza Bosi wake alichowasiliana na "Maso Maso".
Nimeshampa masharti yangu kama anataka kunioa ndio nasubiria majibu yake". "Ila ukiangalia hii picha iliyotumwa ni ya kwake pasina shaka yoyote ila ni kama imechezewa kiutaalamu mkubwa ili usimgundue kuwa ni yeye anayetafutwa kwa hali na mali na vyombo vya dola, angalia sana sana haya masharubu hasa kwenye ncha hii inayogusa mashavu ni ya kuweka kabisa sio yake" alichangia mawazo yake Kachero Manu wakati anaiangalia kwa makini picha aliyotumiwa Kachero Yasmine na "Maso Maso" huku akionyesha masharubu hayo kwa ncha ya kidole chake cha shahada.
Wakaachana na habari za "Maso Maso", wakajisahaulisha kwa muda habari zake na kuchukua sasa ramani ya bonde la maji la Mzakwe ili waangalie wapi wataweza kutega mtego wao wa kuwafanya magaidi wasiwatoroke. Hilo ndio jukumu kubwa lililokuwa linawakabili mbele yao.
"Ehee...unaona hili bonde la Mzakwe lipo ndani ya bonde la Makutupora, na hiki ndio chanzo cha maji cha Jiji la Dodoma, sasa yumkini kuna ulinzi wa kutosha wa kulinda eneo hili la chanzo cha maji cha jiji. Pia kambi ya jeshi la kujenga taifa ya Makutupora ipo jirani na shamba la zabibu la DODEP, hawa wakijileta hawawezi kutoka kamwe" aligutuka kwa sauti kubwa Kachero Yasmine huku anasoza kidole kwenye ramani iliyokuwa imetandikwa mbele yao, baada ya kuitafakari ramani hiyo.
"Upo sahihi mia kwa mia hapa ramani inaonyesha kabisa njia za kuingilia kwenye shamba la zabibu ni mbili tu, unaweza kupitia njia ya Makutupora jeshini au ukapitia kijijini Veyula ukiliacha shamba la zabibu la kanisa unakata kulia, sasa hawa nadhani wamechagua hili eneo kututisha kuwa wana nguvu kubwa mpaka mateka wanampokelea karibu na kambi ya jeshi lakini ni mikwara tu, ni kama kelele za chura tu haziwezi kumzuia tembo kunywa maji" alizidi kuichambua Kachero Manu ramani ya bonde la Mzakwa.
"Kizuri zaidi ukiangalia kuanzia hapa tembea uwanda huu wote mpaka unakatiza hapa kijiji cha Mchemu wote hawa wamehamishwa wasije kuharibu chanzo cha mazingira, hivyo hapa ni pori hata tukilianzisha sokomoko hamna madhara yoyote kwa wananchi, bibi harusi wa gaidi mikono inawasha kabla sijaenda kuolewa na "Maso Maso", huko itakuwa ni mwendo wa majuba tu na kuswali tu saa zote sitopata muda tena wa kuipigania nchi yangu" aliendelea kuwekea tashdidi tafsiri ya ramani huku akichomekea utani Kachero Yasmine, utani ambao ulimchekesha Kachero Manu na kuzidi kumuondolea uchungu wa kutekwa kwa mkewe.
Wakaendelea kuisasambua ramani vilivyo, nje ndani mpaka wakakubaliana kuwa Kachero Yasmine atakuwa upande wa barabara inayotokea kijijini Veyula na Kachero Manu ataingilia barabara kuu ya kupitia jeshini, ili kama wakikimbia kwa kupitia njia ya kijijini Kachero Yasmine awazushie tifu. Somo la usomaji ramani ya dunia nzima ilikuwa ni moja ya somo la mtaala wao wa kikachero. Walikuwa wanafundishwa kitabu kimoja kinaitwa "The Red Atlas" kilichoandikwa na Bwana John Davies na Alexandaer Kent kikielezea namna Muungano wa Kisovieti ulivyofanikiwa kutengeneza ramani ya dunia nzima kwa mbinu mbalimbali.
Hivyo kuisoma ramani ya kijpande cha Mkoa ilikuwa kama kumsukuma mlevi kwenye utelezi. Hiyo ramani ya bonde la Mzakwe kwao ilikuwa maarifa tu ya somo la Jiografia kidato cha nne. Walichukua kama nusu saa tu kupata muwafaka wa pamoja baada ya kuhitalifiana hapa na pale katika namna ya kuwakabili maadui. Lakini mwishowe wakapata suluhisho la pamoja watakalolifuata. Wakawa tayari wameshapandwa na raghba ya kupambana na adui.
Wakaanza kutayarisha silaha zao na vifaa vingine wanavyohitaji kwa ajili ya usiku wa rabsha rabsha unaokuja. Walikuwa wamekaramka kwa furaha utasema wanaenda kuhudhuria harusi kumbe wanaenda kuziweka rehani roho zao kwenye usiku wa kufa au kupona.



Usiku wa sokomoko katika Bonde la Mzakwe
Majira ya saa tano na nusu usiku, giza likiwa limetanda huku anga ikiwa imepambwa na idadi sufufu ya nyota na kipande kiduchu cha mwezi kilichojikata kuashiria tumeshaingia katika mwanzo wa mwezi mwandamo kwa mahesabu ya mzunguko wa mwezi.
Kachero Manu akiwa peke yake na mateka wake ndani ya gari yake aina ya "Subaru Forester" alikuwa ndio anaiacha taratibu barabara ya lami ya Arusha na kukata kona ya barabara ya kulia kuelekea barabara ya vumbi, yenye mashimo kochokocho yaliyojaza maji tobi kuonyesha mvua kubwa ilinyesha siku za karibuni. Pia njia hiyo inayoelekea kwenye shamba la mizabibu la DODEP ilikuwa na makorongo ya kutosha. Alikuwa anaendesha kwa kufuata maelezo toka kwa watekaji wa mkewe. Ambapo walimtaka asifuatane na mtu yoyote zaidi ya mateka wao Bwana 'Kareem Abdallah' peke yake.
"Simamisha gari hapo hapo ulipo kisha ushuke chini na Bwana Kareem" ilikuwa ni maelezo anayopewa Kachero Manu kupitia kwenye simu yake. Kila amri aliyopewa jibu likawa ni hewala! tu kwa Kachero Manu.
Maadui walikuwa wameshika mpini na yeye kakamata makali, hivyo wangeweza kumgeuza wanavyotaka. Alikuwa hawaoni walipojificha maadui zake. "Itakuwa wamejificha humu porini mapema sana, hivyo wamenichora mpaka namna nilivyoingia humu ndani ya eneo" aliwaza Kachero Manu huku akiwa amezima gari na kushuka na mateka wake ambaye bado alikuwa kwenye hali nzuri ya kiafya.
"Tembea mpaka kwenye ule mti wa mwarobaini uliopo mbele yako ukiwa na Bwana Kareem, hakikisha hauna simu wala silaha yoyote ile mfukoni". Kachero Manu akawa anatii kwa kufuata maelekezo aliyopewa. Alipotembea kwa mwendo wa kama dakika 3 akiwa hana hili wala lile, ghafla bin vuu likajitokeza gari linakuja kutokea pembezoni mwake upande wa kushoto kwa kasi huku limewasha taa zote kwa mwanga mkali.
Akiwa hajajua nini cha kufanya gari likawa tayari limeshafika likiwa limefungua mlango tayari, huku likiwa bado halijazimwa wakamdaka Bwana Kareem na kumtupia nyuma ya gari huku mkewe Kachero Manu nae akitupwa chini kama mzigo. Kisha gari likaondoka kwa mchepuko wa kasi kama gari za mashindano ya mbio kuelekea njia ile ile aliyoweka mtego Kachero Yasmine.
Mara moja bila kuzubaa Kachero Manu akambeba mgongoni mkewe akawa anakimbia nae kurudi kwenye gari yake aliyoiacha meta kadhaa aweze kwenda kumsaidia kachero Yasmine. "Pole sana baby, ndio matatizo ya dunia uliyoyapata hayana mwenyewe, haya uliyoyaonja ni thumuni tu yale ninayoonja mumeo kila siku katika kazi zangu" alisema huku anamuweka sawa kwenye kiti mkewe. Ambaye alijibu kwa ishara ya kutikisa kichwa tu kuashiria wapo pamoja katika shida na raha.
Alikuwa amevishwa vazi la kiislamu la baibui nyeusi lilisitiri mwili wake wote. Akawa analalamika baridi kali, ikabidi akilaze kiti na kuchukua koti lake na kumvika yeye kisha akamlaza kwa upole.
Wakati anajiandaa kuwasha swichi ya gari lake, ghafla akaanza kusikia mirindimo ya risasi mfululizo kutokea upande ule ule walioelekea wale magaidi. "Kazi imeanza Ustaadhati Yasmine anawabatiza magaidi kwa mtutu wa bunduki" alijisemea pole pole Kachero Manu.
Akaanza kulitoa gari taratibu kuelekea upande ule ule walioelekea magaidi. Akaendesha mpaka sehemu fulani yenye kichaka akaiegesha. Kisha akabeba mtutu wake kukimbilia eneo la tukio bila kuaga kwa mkewe, akimuacha anakoroma akiwa ameshonwa na usingizi mzito unaotokana na uchovu wa sulubu za watekaji zilizomkosesha mapumziko ya raha.

Kachero Yasmine akiwa amejificha kwenye fukutu la nyasi, akiwa amejitandazia nyasi mwili mzima ulikuwa huwezi kudhani kama amejificha mtu kwenye kichaka hicho. Mwili wake ukiwa umevikwa kombati maalumu zilizokuwa zimechafuka matope kutokana na kutuama kwa maji kwenye eneo alilokuwepo.
Alikuwa ameshajichimbia hapo kwenye kichaka kwa karibia saa tatu timilifu, huku akiomba Mungu magaidi wapite njia hiyo. Walijua fika hawawezi kupita njia kuu ya jirani na kambi ya jeshi watapewa kichapo cha mbwa koko. Kuna wakati bonge la joka lenye urefu zaidi ya futi 8 lilimtambaa mwilini kuanzia kwenye buti miguuni, na kutambaa mpaka kuja kutokezea kichwani kwa kupanda kwenye kofia yake na kutokomea zake kwenye kichaka, likiwa kwenye harakati zake za kuwinda mawindo yake. Kwa ujasiri mkubwa bila kujitikisa aliliacha limfanye linavyotaka.
Mbu nao hawakubaki nyuma kumletea kero ya udungaji wa maumivu, lakini hawakuwa kikwazo kwake kutimiza lengo lake. Kuna wakati upepo ulivyokuwa unapuliza na miti kutingishika, huku sauti ya vyura ikirindima kwenye vifereji vidogo vidogo. Popo nao walikuwa katika harakati zao za kujitafutia maisha usiku huo wanahama mti mmoja na kuhamia mwingine. Ulikuwa ni msitu wenye kuogofya hasa nyakati za usiku kwa mtu mwenye roho nyepesi. Ukichanganya sauti ya mvumo wa upepo, kelele za vyura, na mtikiso wa matawi ya miti kulikuwa kunapatikana burudani fulani ya sauti yenye kuvutia inayobembeleza kwa msikilizaji na mwili kupata raha. Hiyo hali ikawa inataka kupelekea kope za macho yake ziwe nzito, usingizi ulikuwa unataka kuanza kumnyemeleza na kumpiga dafrau kipindi cha hatari.
Lakini akikumbuka ukubwa wa nguvu za adui ambaye ana nguvu ya kiuchumi, askari watiifu wanaopiga kwa malengo ya kusimamisha utawala wa kiislamu na waliofuzu mafunzo, usingizi wote ukayeyuka kama samli ndani ya moto. Akashtukizwa na kelele za gari linalokuja kasi huku limewasha taa zote kuashiria kuna hatari. Likiwa kwenye umbali wa kama mita kumi akaikoki vizuri silaha yake aina ya "Submachine Gun" aliyoifanyia utundu kuongeza manjonjo yake.
Bila kujiuliza mara mbili mbili akaanza kuzifyatua risasi kama njugu mfululizo, huku akilenga usawa wa kiti cha dereva na abiria. Kachero Yasmine alikuwa ni mtaalamu wa matumizi ya mkono wa kushoto, hakukosi shabaha kijinga akikuwinda risasi. Lengo la kupiga mfululizo ilikuwa ni kuwachanganya maadui wajue kama wamezingirwa na wapiganaji wengi. Mbinu ilijibu vyema, magaidi walipigwa na taharuki, lilikuwa ni shambulizi la kushtukiza kwao hawakutegemea kuzingirwa kirahisi.
Walianza kupiga risasi mfululizo bila mpangilio wowote. Kachero Yasmine kuzima mzizi wa fitina, akabahatisha kubutua matairi ya mbele yote ya gari lao, kwa kuwa lilikuwa kwenye kasi kubwa likayumba na kwenda kujibamiza kwenye mti mkubwa na kuzalisha kishindo kikubwa, na kupelekea gari kupinduka vibaya zaidi ya mara nne, kisha likatulia tuli.
Akasubirishia kama robo saa kuona labda kuna mtego wametegewa akaona kimya. Akawa anachomoka porini huku anakuja wanguwangu kwa kujiamini, akashtukia risasi mbili zinapigwa uelekeo ule ule anakokwenda, akajitupa chini haraka haraka na kuanza kutambaa. Kachero Manu akaanza kuita kwa sauti ya kupaliza iliyokuwa inasikia vizuri "Yasmiiiinee... njoo game is over...!".
Kachero Yasmine alivyosikia hivyo akasita kujitokeza mpaka alivyoisikia tena na kuhakikisha ni sauti ya Kachero Manu akajitokeza mbele ya gari la maadui na kulakiwa na Kachero Manu ambaye nae ndio alikuwa anafika, wakakutana ndindaninda.
“Kazi zuri Kachero Yasmine, nilivyokuwa nazisikia njugu zinatemwa nikajisemea kazi ipo leo Mpemba kashapandisha maruhani yake, maana anuwai yako ya ufyatuaji wa risasi imejipambanua kwangu, wakasalimu magaidi wenzao huko kuzimu" alitoa pongezi Kachero Manu huku akamkumbatia akisifu umahiri uliomfanya awe kama mtazamaji mpira uwanjani, ambaye anashangilia magoli yaliyofungwa na wachezaji.
"Na wewe ahsante kwa kuokoa uhai wangu nilijua nimewamaliza wote kumbe kuna mmoja alikuwa ananivizia nije anidokoe vizuri" Kachero Yasmine alitoa shukrani kwa mwenzake. Ni ukweli tungerudisha jina tu Pemba maana alikuwa pale pembeni ya mti anakuvizia tu ujilete" alijibu Kachero Manu kiufahari. Mara moja bega kwa bega wakaanza upekuzi mle ndani ya gari aina "Jeep kibanda wazi" la maadui.
Wakakuta kulikuwa na magaidi wapambanaji wa kiume 4 pamoja na dereva wao, na mateka wao waliyemkomboa Bwana Kareem Abdallah wakiwa wote wamepoteza maisha. Huku tafrija ya damu ikiwa imetapakaa kwenye gari. Damu ambayo ilitokana na mipigo ya risasi kutoka kwenye silaha ya Kachero Yasmine na kutokana na majeraha ya ajali mbaya ya gari lao. Wakamkuta pia mwanamke mmoja akiwa bado anapigania roho yake amezimia anapumua kwa mbali lakini ana majeraha makubwa kichwani.
"Huyu tumkimbize hospitalini hapo jeshini, tuombe gari la wagonjwa wampeleke Hospitali ya Mkoa" alitoa ushauri wenye mbolea Kachero Yasmine. "Upo sahihi feli bilahi kupona au kutokupona ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu" aliongea Kachero Manu kuonyesha kukubaliana na ushauri wa mwenzake. Wakati wanamuweka nguo zake vizuri ikaonekana bahasha nzito ngumu ya kaki imechimbiwa kwenye nguo ya ndani inachungulia. Ikabidi Kachero Yasmine aitoe, na kuanza kuifungua kwa kuchana gundi yake ngumu iliyogandishwa. Alipofanikiwa kuifungua zikajitokeza pesa za kigeni dola za kimarekani kitita kisichopungua dola $10,000 baada ya kuhesabiwa kwa haraka haraka. Kisha wakakuta na barua imevirigiwa kwenye bahasha ndogo. Akapatwa na udadisi wa kuifungua, alipoifungua tu, Kachero Manu kwa msaada wa tochi akaanza kummulikia Kachero Yasmine asome




Ilikuwa ni barua iliyoandikwa kwa maandishi ya lugha ya kiarabu. Akaisoma mpaka akafika mwisho, kisha akavuta pumzi kubwa Kachero Yasmine. "Ina nini hiyo barua?" alishindwa kuvumilia Kachero Manu maana alikuwa haelewi chochote kutoka kwenye ile barua, kwake ilikuwa ni makorokocho tu kama ya watoto wa chekechea.
"Usijali Bosi wangu, huyu tumuombee azinduke ana mengi ya kutuelezea tena atatufikisha mpaka kwa mama yake "Maso Maso", maana hii ni barua ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Huenda huyu ni posta wao. Wakafanya haraka kumuingiza kwenye gari kisha Kachero Yasmine akalikimbiza mpaka hospitali ya jeshi. Baada ya hapo Kachero Manu akapiga simu kwa askari wa kikosi maalumu waje kuondosha mizoga kimya kimya kabla hakujakucha na kuvuta hisia za waandishi wa habari.
Hii ilikuwa ni operesheni chinjachinja adui kimya kimya, mpaka gaidi wa mwisho atiwe mbaroni. Baada ya hapo akarejea kwenye gari lake na kumpeleka hospitali mkewe wamcheki afya yake kisha baada ya hapo ndio warejee nyumbani. Alikuwa anaonekana amesakarika kutokana na uchovu na njaa.

SURA YA KUMI NA MBILI
Ngome ya Al-shabaab ndani ya Wilaya ya Kilindi - Tanga
Watu 4 kwa idadi ambao ni wafuasi wa "Al-Shabaab" walifika Wilayani Kilindi tokea mwaka 2008. Walikuwa wametokea Somalia wakiwa wameiva vilivyo mafunzo ya ugaidi. Malengo ya Al-shaaab yalikuwa ni kusimamisha ngome zao imara katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki. Kuanzia Mombasa-Kenya, Tanga, Zanzibari, Rufiji-Tanzania na Pemba ya Msumbiji. Wageni hao walifikia katika Kijiji cha Lwande, kwa muda waliishi na wanakijiji wa Lwande, na wanakijiji wakawa wamewapokea kama waislamu wenzao.
Walikuwa ni watu rahimu na wenye tabia zenye kunukia mauwaridi kijiji kizima. Kila mtu alitamani awafanye kuwa ni marafiki wa familia yake au kama wakitaka kuoa au kuongeza wake basi waje kuolea kwenye mji wao. Walikuwa ni mahodari wa kazi mbalimbali kama kilimo na ujenzi majumba.
Kizuri zaidi walikuwa wanaonekana ni watu wanaomshiriki Mwenyezi Mungu kupita maelezo. Msikitini nako wakaaminiwa kuendesha baadhi ya vipindi vya swala. Walionekana wanasoma Kurani kwa kuipendezesha masikioni mwa msikilizaji.
Wakaanza kusambaza fitina za chini kwa chini kuwagombanisha waislamu wa kijijini wenyewe kwa wenyewe na viongozi wao bila wenyewe kujua kuwa wanapigwa majungu na wageni hao. Wanapita huku na kuzusha uwongo huu na wataenda kule na kuzusha zogo jipya.
Waislamu wa kijijini pale wakaanza kupoteza umoja wao, vurumai na kitimutimu mtindo mmoja kikaibuka, ikawa mwendawazimu kaingia nyumba ya shetani. Waumini wakawafurusha viongozi wao wa msikiti wakiwatuhumu kuwa hawana elimu ya dini, wanawasomea Qur'ani majaka na kuisoma kimakosa kwa kuimong'onyoa. Rungu la uongozi sasa wakakabidhiwa vijana hao wageni wa "Al-shabaab".
Ikawa ni kama kumpa paka kazi ya kulinda maziwa. Wakaanza sasa vibweka vyao baada ya kudhibiti uongozi. Baada ya muda walianza kutoa mafundisho ambayo hayaendani na utamaduni wa Kitanzania. Mfano wakaanza kufundisha elimu ya mazingira ni haramu mutlaki. Hivyo watoto wa Kiislamu wasome Madrasa pekee wasipelekwe shule za elimu dunia.
Wakaanza kupandikiza chuki dhidi ya waislamu wanaofanya kazi serikalini kuwa wamesharitadi. Wakifa wasizikwe kiislamu kwa sababu wanaitumikia serikali ya Kisekula isiyoamini dini. Kutokana na mafundisho hayo butu, yaliyojaa shonde. Baadhi ya wananchi wakang'amua wanapoelekea sipo. Wakaanza kuwahoji wapi wanatoa mafundisho hayo ya ajabu. Wakafarakana na wanakijiji wakajitenga na kununua eneo lao kisha wakajenga msikiti unaitwa "Madina".
Lengo kuupa msikiti wao jina hilo ilikuwa ni kufananiza kitendo cha Kiongozi wa dini ya Kiislamu Ulimwenguni, Mtume Muhammad (S.A.W) kufanya hijra kutoka Mji wa Makkah kuelekea Mji Madina alipofanikiwa kuisimamisha Dola ya Kiislamu.
Wafuasi wao sasa waliendelea kuongezeka na wengi wakitokea Jijini Dar es Salaam, Kigoma na Singida. Wengine walitokea nchi za jirani kama Kenya na Somalia. Kiongozi Mkuu wa msikiti huo akijulikana kwa jina la "Master" ambalo lilikuwa maarufu Kilindi nzima. Huyu alipachikwa jina la "Master" baada ya kuanza kuutumia msikiti wa Madina kama sehemu ya kufanyia mazoezi na mbinu za kigaidi.
Walifahamika kuwa ni magaidi walipoanza kunyanyasa wenyeji kwa kupora mashamba ya wenyeji bila fidia. Maelezo yao kwa wenyeji ilikuwa ni kwamba ardhi ni mali ya Allah, na wao wametumwa na Allah kusimamisha utawala wake duniani hivyo ni haki kwao kuichukua bila fidia. Idadi ya wageni katika kambi hii ikaanza kuongezeka zaidi kadri miezi inavyozidi kusonga. Baadae wakajitanua hadi katika msitu wa Dibungo, katikati ya Kilindi na Bagamoyo.
Katika msitu huo walihodhi ardhi yenye ukubwa wa ekari 500 iliyonunuliwa na Bwana Kareem Abdallah, Meneja wa "Chops Carwash & Garage". Katikati ya eneo hili wakajenga uwanja wa mazoezi. Kwa nje walijenga vibanda kuzunguka eneo hili, na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia katikati ya msitu huu. Pia walijenga msikiti katika msitu huu, na walikuwa wanafanya mazoezi mara mbili kwa siku. Walikuwa wanafanya mazoezi saa 11 alfajiri baada ya kumaliza swala ya asubuhi na saa 11 jioni baada ya kumaliza shughuli zao za kilimo na ufugaji.
Uhusiano kati ya wafuasi hawa wa "Al-Shabaab" na wanakijiji wa maeneo yaliyozunguka kambi yao hii ulizidi kuzorota siku hadi siku. Wenyeji wengi ni wafugaji, lakini wafuasi hawa wa "Al-Shabaab" walianzisha utaratibu wa kutoza kodi ya mifugo au faini ya mifugo kwa ngombe wanaoingia kwenye msitu huu. Hatari iliyo kubwa zaidi, kambi hii ikawa inatumika kutoa mafunzo kwa vijana ambao wakionekana wameiva tayari wanasafirishwa kutoka Kilindi, kupitia Mombasa na kwenda Somalia kujiunga na kundi la al-Shabaab, wao na wake zao waliotafutiwa kupitia mtandao 'Facebook' kupitia akaunti ya 'NUSRA COMMITEE'.
Usiku walikuwa wanajiliwaza kwa kuangalia video, mikanda ya vita vya Jihadi sehemu mbalimbali duniani. Kulikuwa na mikanda yenye mafundisho ya "Al-Shabaab", yenye kusisitiza kuwa Afrika Mashariki imekamatwa na makafiri, hivyo wanafundishwa namna ya kuikomboa kijeshi. Mpaka kufikia mwaka 2013 ikawa ni kambi ya siri iliyojiimarisha vilivyo yenye zana za kivita toshelevu.
Hivyo "Maso Square The Duduman" baada ya kukamilisha kazi aliyotumwa Tanzania ya kulipua jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani na kuua vigogo kadhaa na kuifanikisha vizuri aliteuliwa kwenda kuiongoza kambi hiyo kubwa ya Kilindi akitoa amri zote kutoka mafichoni. "Maso Maso" alikuwa anaishi katika mapango ya Amboni, yeye na wateule wake wachache na wanamgambo wao wachache.
Huku ndiko alikuwa akiletewa ripoti zote za kinachoendelea kwa njia ya maandishi tu. Alikuwa hatumii simu wala kompyuta wala chombo chochote cha elektroniki. Ilikuwa ni kama kujaribu kumpitisha ngamia kwenye tundu la sindano kama utataka kumkamata "Maso Square The Duduman". Mpaka kumfikia yeye ilitakiwa upambane na "Makomandoo" zaidi ya 25 ndio uwafikie kundi la "Wasagaliwa" 10 mgambo waaminifu. Wasagaliwa hao toka nchini Somalia walikuwa ni wanaume mahanithi ambao hawatamani mwanamke kimaumbile kwa namna walivyozaliwa, hivyo huwezi kuwashawishi wamsaliti "Maso Square The Duduman" kwa pesa kwa sababu wanalipwa vizuri wala kwa wanawake kwa sababu hawana matamanio.



Bi Mwantumu sasa anakula pweza gizani, matunda ya mwanawe
Bi. Mwantumu ilipita kama miezi 8 tu tokea mwanawe apatwe na umajinuni ndipo alikuja kung'amua mtoto wake kumbe ni mwehu feki. Kwanza alianza kuona viroba vya mchele, sukari, ngano na maharage havikauki nyumbani kwake kutoka kwa wanaojiita wasamaria wema, waliovalia mavazi ya kiustaadhi. Waliokuwa wanajifanya wanamuonea huruma kutokana na sakata la mwanawe pekee wa kiume kuugua uchizi. Akawa anajiuliza hapati majibu "hivi wenye watoto vichaa wote wanapata huduma kama hizo au yeye tu!".
Baada ya siri kubumburuka baada ya picha za mtoto wake kuhusishwa na ugaidi kuanza kusambazwa na serikali, wale wasamaria wema wakakata mguu. Walikuwa wanahofia vyombo vya dola watalala nao yombo. Aliyempasha kuhusu ugaidi wa mwanawe alikuwa ni shosti wake yule yule wa kufa na kuzikana Bi.Mwazani.
Siku hiyo isiyo na jina Bi.Mwazani alipata nakala ya gazeti pendwa kwa habari za kiuchunguzi Jijini Dar es Salaam la "Motomoto" likiwa limechambua makala inayomhusu "Maso Maso" namna anavyohusika na ugaidi wa matukio kedekede nchini Tanzania. Halahala bila ajizi kiguu na njia, Bibi asiyetulia maskamoni kwake kama amekula miguu ya kuku, Bi.Mwazani mpaka kwa shoga yake akiwa na nakala yake mkononi.
"Hodi hodii baada ya salamu mwanetu katuvua nguo tupo uchiii huko mitaani, hatuna pa kufichia nyuso zetu" alikuwa ni Bi.Mwazani huku tayari kurupukurupu huyo ameshaingia mpaka sebuleni na kujipweteka kwenye sofa pweteee. Huyo ndio Bi Mwazani alikuwa hawezi kulala na umbea, muda wote akipata umbea moyo wake unakuwa unapaparika, koo lake linamuwasha, anatafuta wa kumsimulia ndio roho yake itulie. Kuiweka habari anayoisikia kiporo alikuwa hawezi. Shoga yake alipopewa mchapo wote na Bi Mwazani ikabidi aitafute miwani yake na kujisomea mwenyewe uzuri alipitia madarasa ya ngumbaru hivyo kusoma haikuwa shida. Bi Mwantumu alibaki hoi bin taabani amechoka na vituko vya mtoto wake.
"Mie nimezunguka kwa waganga na waganguzi na mpaka nilisurika kubakwa na mganga, Shekhe Mbonde kule Rufiji. Nikaponea chupuchupu ili yeye apone uchizi kumbe alikuwa anatuzuga tu eeeh...ameuza jina lake kwa kina cha povu mwanangu..!" aliropoka Bi Mwantumu huku ameshika tama shavuni. Sasa mambo yakawa kweupe hadhiri kuwa mwanawe ni gaidi namba moja nchini anayesakwa kwa udi na uvumba na vyombo vya dola. Bi Mwazani alivyoaga kurudi kwake baada ya kuutua umbea kama kawaida yake na kibomu juu.
"Shoga kama mchele wetu ule wa msaada wa wale Maustaadhi umebaki nijulie hali na mimi, jiko nyumbani limenuna, na mwanetu Maso kashalitifua huko tifuu sijui kama hatukurudi kwenye kula chakula cha jela ugali au wali wa mtama kama njiwa vile". Ikabidi rafiki yake Bi Mwantumu abaki anatabasamu tu, huku anakwenda kumchotea kilo za mchele zilizokuwa zinamalizikia tena, mbwa ukimjua jina hakusumbui, Bi Mwantumu anamjua shoga tokea utotoni alishamzoea vibweka vyake.
Sasa Bibi wa watu ikawa kila akipita mitaani watu wanamsoza vidole. Wengine kutaka kumrusha roho kabisa wale wenye roho za ikidi na inda, watovu wa adabu wakawa wanaenda kudurufu picha nyingi zenye tangazo la kutafutwa kwa mwehu "Maso Maso" halafu wanakuja kumbandikia picha mpaka mlangoni pake bibi wa watu, asubuhi akiamka anakutana nalo mlangoni kumkera tu bibi wa watu. Binadamu wabaya wewe acha tu unaocheka nao mchana hao hao usiku ndio wanaokung'ong'a.
Bado mapolisi, wale akina afande kunyoa mabwenzi kama ndege shore wanaokuja kupiga kambi kutaka kumtoa upepo bibi wa watu kwa kumtisha kumrundika ndani. Bado vijana wa mtaani waliposikia dau la milioni 100 kwa atakayeripoti alipo "Maso Maso" zikawa zinawatia wazimu. Wapo waliokuwa wanakesha mtaani kusubiria nazi mdondo huenda atajitokeza nyumbani kwao walau siku moja wakatoe ripoti kwenye vyombo vya dola.
Mashababi wengine wakawekeana zamu kula chabo kwa doria mpaka usiku wa maneno wakiwa na ndoto huenda siku moja akateleza kuja kumsalimia mama yake. Bado mabanati wazuri, wenye uzuri wa zuhura, vidosho vya nguvu wenye maumbile ya kusababisha kadi za Benki na pochi za Mapredeshee zipate ugonjwa wa degedege la kutaka kuwahonga. Eti nao walijileta kwa Bi Mwantumu kujifanya kuomba kazi ya uhadimu wa kazi za ndani.
Ama kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni, kweli walimbwende wanataka kuja kujipaka masizi kwenye kusugua sufuria za Bi Mwanatumu!. La hasha si kweli hata kidogo, nia na madhumuni kumpekunyua tu Bi Mwantumu huenda anaweza kuropoka siku moja akaelezea mahali alipojificha mwehu "Maso Maso" au kumuona akija nyumbani kwa mama kwa kificho, wakajichukulie kiangaza macho kwenye vyombo vya dola. Ili mradi Bi Mwantumu alikuwa kwenye shida tamaamu haswa.
"Maso Maso" nae akili yake ilikuwa inachemka barabara hakuwa zumbukuku ulimwengu uko huku, ikabidi abuni mbinu mpya ya kupeleka msaada na kufanya mawasiliano na mama yake mzazi. Mbinu ikawa kila usiku wa Alhamisi ya mwisho wa mwezi kuna dua maalumu ilikuwa inafanyika nyumbani kwa mama yake. Alikuja siku moja "Maso Maso" nyumbani kwao Sinza kuhudhuria dua majira ya magharibi akiwa amejibadilisha kama mwanamke wa kiislamu aliyevalia juba zuri kuja kuweka mambo sawa na kuomba msamaha kwa mama yake.
Hakuna hata mmoja aliyemtambua baki wakware tu wale wasioogopa hata wanawake waliovaa mavazi ya heshima wakabaki wanataka kumchombeza watoke nae kimapenzi. Akabaki anawachora tu kwenye kizoro chake kilichoziba uso wake na kuacha macho tu anawasanifu mngenijua mimi ni nani ningewadonyoa risasi za tumbo. Huku mkononi ameshika tasbihi kujifanya hataki mchezo kwenye utajo wa Allah hata kidogo.
Sheikh Jamsheed, Shekhe maarufu Sinza yote na vitongoji vyake ndio alikuwa anaongoza hiyo dua alikuwa ndio amepewa jukumu la kumpa pesa na barua Bi Mwantumu Kila itakapobidi na akatambulishwa kwa mama "Maso Maso". Alikuwa ni Shekhe mwenye heshima na sharafu kubwa Sinza nzima. Shekhe ambaye hakuna mtu angemuhisi kuwa ni jasusi la "Al-shabaab".
Watu wakaanza kushangazwa mambo yake Bi Mwantumu yanamuendea vyema hayateteleki lakini hawamuoni jembe lake "Maso Maso" kuleta mafao yoyote. Mpaka majirani wakaanza kupata wivu mama ambaye mwanawe chizi anaishi maisha mazuri, wao wenye watoto timamu wa akili wanaishi maisha ya kubangaiza, akhera hawapo na duniani hawapo kwa tashididi ya maisha magumu wanayoishi.

Kachero Manu atinga ndani ya msikiti katika msitu wa Dibungo
Msikiti wa Dibungo maarufu wenyewe wakiuita kwa jina la "Masjidi Dibungo El-Jihaad" ulikuwa umejengwa katikati ya msitu kwa matofali ya kuchoma. Na kuezekwa na bati kuukuu. Ulikuwa una ukubwa wa wastani ukiwa na uwezo wa kuingiza waumini si chini ya 250 kwa pamoja. Ukiwa unatumia taa za mwangaza wa jua "Solar Power", zilizozunguka msikiti mzima.
Ndani ya msikiti kulitandikwa majamvi ya kufumwa na mkono yaliyoenea msikiti wote. Mbele ya msikiti kulikuwa kuna kikopesa ambacho ndio mihirabu anayoitumia Imamu kukaa kipindi anapotaka kuendesha ibada ya swala. Siku hiyo majira ya saa mbili na nusu usiku baada ya swala ya Isha, waumini zaidi ya 200 walikuwa wametulizana tuli wanamsikiliza mmoja wa viongozi wao aliyekuja kuzungumza nao. Haikuwa kawaida yao mida hiyo kuongea, ilikuwa swala ya Isha inapoisha tu, kila mmoja anaupasua msitu kurejea kwenye majumba yao yaliyopo umbali wa kilometa 2 mpaka 3 yaliyojengwa kuzunguka msitu huo. Ilikuwa ni ngumu kwa mtu mgeni kugundua kama kuna msikiti huo katikati ya msitu.
Kachero Manu alikuwa ndio kwanza amewasili msituni majira ya Magharibi na moja kwa moja akiwa na begi kubwa na mgongoni alifikia msikitini hapo akiwa na mwenyeji wake. Kilichomtisha Kachero Manu ambaye alikuwa amevalia mufti, vazi la kanzu nyeupe na kofia ya kufuma kwa mkono ni kitendo cha kuona waumini wote msikitini wamebeba silaha zao zipo pembeni yao, kasoro yeye. Huku wakiwa wanasikiliza viongozi wao kwa utiifu mkubwa bila kutikisika wala kuchezacheza. Kama ndege angeweza kujaribu kutua kwenye kichwa cha mmoja wapo wa hao wanamgambo waliomo msikitini muda huo angeweza kutulizana bila shida yoyote. Kwa muonekano wa juu juu namna alivyowachunguza wote hawakuwa Watanzania pekee, na hili lilijulikana baada ya mzungumzaji kufafanua baadhi ya mambo tata kwa kutumia lugha ya Kiingereza, na kuna wakati kuchomekea maneno ya Kisomali. Pia walionekana ni wanamgambo wenye afya zao wenye miili iliyoshiba na kukubali mazoezi magumu. Pia walionekana wana 'umoja wa huba na hawa' miongoni mwao. Na sio ule umoja wa mashaka wa paka na panya.
Ikaanza kusomwa ripoti ya wiki kupitia kwa mmoja ya wakufunzi wa mgambo hao kwa kutumia kipaza sauti. Ripoti ambayo pia ilimtisha Kachero Manu kiasi fulani kutokana na matukio yaliyokuwa yanatajwa. Ripoti ilieleza wiki iliyopita wamekufa wanamgambo wawili, mmoja kutokana na kudonyolewa na panga tumboni wakati wa mazoezi na mwingine kutokana na kulipukiwa na bomu wakati anajifunza kulitega.
"Kama kwenye mazoezi tu wanauana kikweli je kwenye mechi si kuna hatari hawa watu..!" alikuwa anawaza Kachero Manu huku akiwa amekunja miguu yake kwenye jamvi alilokalia huku ameinika kichwa chake chini kama kobe anayetunga sheria. Mara baada ya kumalizika kusomwa kwa ripoti fupi kuliambatana na tukio la kuja hadharani kwa mmoja wa viongozi wao wakubwa wa kikundi hicho cha "Al-shabaab" kutoka mapango ya Amboni, Tanga. Ambaye muda wote wa kusomwa kwa ripoti alikuwa ametungamana kwenye mihirabu mbele ya msikiti anapokaa Imamu akiwa amejifunika na kilemba. Akakaribishwa na kujitokeza mbele ya wale wanamgambo ambao walianza kuzidi kubanana pamoja na kupandwa na tashiwishi ya kumsikiliza kwa makini.
Hali hii ilithibitisha kuwa kiongozi huyo ni mtu adimu sana haonekani ovyo hadharani. Viongozi wao wakuu kuonekana kwao ni kwa nadra na wakijitokeza hadharani basi kuna tangazo muhimu ameleta, au kuna kiongozi amekuja kuvuliwa mbeleko au kuna adhabu amekuja kuleta kwa watu wakosefu. Kachero Manu alikuwa yupo kwenye safu za katikati akawa anasikia minong'ono toka kwa wale wana mgambo alioketi nao jirani. "Mullah Chambuso leo katutembelea, Allah ni mkarimu sana kutupa bahati ya kutukutanisha na kipenzi chake na mfia dini madhubuti asiyeteteleka inshallahu taala atakuwa amekuja na habari njema" alisema mmoja wapo katika wale wanaonong'ona kwa hisia kubwa za kuonyesha utiifu kwa kiongozi wake.
"Huyu ni wa peponi kabisa anachosubiria ni kifo akastarehe zake na wasichana wa peponi amekwishapigana vita vya jihadi ngumu sana zaidi ya 10 duniani, nchini Somalia, Yemeni, na Afghanistani na kote ameacha alama zake" alinogesha mazungumzo mwenzake kuonyesha nae anamkubali sana 'Mullah Chambuso'. Kisha yakapigwa makofi kuonyesha sasa wakae kimya bwana mkubwa "Mullah" anataka kuanza mazungumzo.
Akawa amesimama akiwa amezungukwa na Makomandoo watatu kwa nyuma yake waliobeba mitutu ya bunduki. Alikuwa amevalia suruali rangi nyeusi ya mtindo wa pajama, huku juu amevalia nusu kanzu na kizibao kizito cha rangi ya kijani, huku chini amevaa buti za jeshi rangi ya maziwa. Uvaaji wa viatu ndani ya msikiti huo nalo ni jambo lililomtatiza Kachero Manu. Tokea utoto wake kule Mahiwa, Lindi alikuwa anaona waislamu wakiingia msikitini wamevua viatu lakini hawa jamaa tena wafia dini wanaingia na viatu mpaka msikitini.
Kwa umbile lake alikuwa ni kibushuti mfupi haswa, pandikizi la mtu akiwa ni mweusi tii kama pipa la lami huku uso wake ukiwa una makovu ya kutosha kuonyesha amepitia mikiriti na mikutuo mbalimbali ya mapigano. Huku macho yake yakiwa na makengeza, macho kumberu. Alikuwa amefuga ndevu lakini zilikuwa zimemkataa hazijanawiri vilivyo, hazina rutuba zikawa kuna sehemu kidevuni zimejikusanya kama mkutano wa inzi. Kichwani alikuwa amejifunga kilemba cha rangi nyeupe kilichokuwa kinang'ara vilivyo. Alikuwa anatisha ukimuangalia mwonekano wake hakuwa na uso wa jamala wala wenye haiba ya mvuto. Uso wake haukuvaa hata chembe la tabasamu, ulimvimba kama mvua ya masika. Alikuwa akiongea anaunguruma kama radi, sauti ya punda. Akaanza hotuba yake fupi iliyojaa amri na vitisho.



Kwa umbile lake alikuwa ni kibushuti mfupi haswa, pandikizi la mtu akiwa ni mweusi tii kama pipa la lami huku uso wake ukiwa una makovu ya kutosha kuonyesha amepitia mikiriti na mikutuo mbalimbali ya mapigano. Huku macho yake yakiwa na makengeza, macho kumberu. Alikuwa amefuga ndevu lakini zilikuwa zimemkataa hazijanawiri vilivyo, hazina rutuba zikawa kuna sehemu kidevuni zimejikusanya kama mkutano wa inzi. Kichwani alikuwa amejifunga kilemba cha rangi nyeupe kilichokuwa kinang'ara vilivyo. Alikuwa anatisha ukimuangalia mwonekano wake hakuwa na uso wa jamala wala wenye haiba ya mvuto. Uso wake haukuvaa hata chembe la tabasamu, ulimvimba kama mvua ya masika. Alikuwa akiongea anaunguruma kama radi, sauti ya punda. Akaanza hotuba yake fupi iliyojaa amri na vitisho. "Salaam Aleikum Jamiiia, ama baada ya salamu sina mengi, kwanza nimeletewa taarifa tumepata 'Mujaahidu' mmoja amesilimu na moja kwa moja amekuja kwenye viwanja vya jihadi" akavuta pumzi kidogo kabla akaendelea. Zikaanza kulipuka kelele za vishindo vya sauti za maneno ya kiarabu "Takbiiiiiir......Allahu Akbaru, Takbiiiiiir.......Allahu Akbar" wakionyesha wamefurahia kwa huyo mgeni aliyeamua kuachana na maisha ya anasa za kidunia na kuamua kujiunga nao maporini kuja kupigania vita vya jihadi. Hapo alikusudia kuwapa taarifa za ujio wa Kachero Manu pale msikitini kwao.
Kisha baada ya vishindo hivyo akaendelea, "kizuri zaidi nimepata taarifa aliwahi kupitia jeshini lakini akashindwana nao hao madhalimu akaacha kazi miaka kama mitano iliyopita, kwa hiyo msisite kumtumia kwenye baadhi ya mambo" akakoma kuzungumza huku macho ameyakazia alipo Kachero Manu.
"Asalaaam Aleikuuum ndugu zangu katika imani ya haki, mimi ndugu yenu nilikuwa naitwa 'Raphael Kitokambali' lakini baada ya kuiona taa ya Uislamu sasa naitwa Abubakari" akasimama kuendelea kujitambulisha Kachero Manu baada ya vishindo vizito tena vya takbira vilivyokuwa vinakaribia kutaka kuezua paa la msikiti huo wa matofali ya kuchoma. "Nimechagua jina la Aboubakr kwa sababu nimesikia alikuwa rafiki wa karibu sana wa Mtume Muhammad (S.A.W). Na mimi nitafanya bidii mpaka niwe karibu na kiongozi wa harakati hizi za jihadi. Hivyo mimi ni ndugu yenu katika imani, wazazi wangu wamenitenga baada ya kusikia nimeingia kwenye imani hii mpya, ahsanteni sana" akamaliza na kukaa chini, akiongea maneno aliyokaririshwa vilivyo na Kachero Yasmine.
Wakawa wanamfuata na kumkumbatia kwa kumpa pongezi juu ya tukio lake hilo adhimu. Kisha yule mgeni mhashamu akaendelea na hotuba yake."Lakini pia kuna jambo tusha, baya la usaliti limetokea hapa kambini" akapumzika kidogo. Kila mmoja akawa ameshikwa na wasiwasi wanatazamana wenyewe kwa wenyewe. Walijua tayari pepo mchafu anataka kupita wajiandae. Kila mmoja kiroho kikawa kinamdunda kama saa mbovu, maana walijua adhabu ya msaliti ni kifo.
"Mke wa ikhwa mwenzetu mmoja katoroka na amana yetu ya Dola za Kimarekani $10,000 alizopewa afikishe sehemu yapata miezi miwili iliyopita. Kawauza wenzake, wakauliwa kinyama huko bonde la Mzakwe, Dodoma yeye katokomea na pesa zetu. Sasa tumechunguza tumegundua mumewe nae ni mhusika wa njama hiyo. Mleteni hapa haraka sana laanatu-llah ziwe juu yake maluuni mkubwa huyu" alizungumza kwa jazba na raghba kubwa ya kumuadabisha msaliti. Baada ya kutoka hiyo amri ikawa ni mikikimikiki ya kumuingiza ndani ya msikiti kupitia mlango wa katikati ya msikiti aliyehisiwa kuwa ni msaliti huku akiwa amefungwa kamba za miguuni na mikononi, kamba zilizokazwa ndindindi zilizomfanya asiweze kufurukuta.
Kachero Manu alikuwa anashuhudia mubashara tukio hilo, ambalo chanzo chake anakijua nje ndani, mwanzo mwisho. Yeye na Kachero Yasmine ndio waliokoa maisha ya 'Ukhti Rayhaan' ambaye anatuhumiwa kutoroka na Dola $10,000 za magaidi. Walimkuta amezimia na kujeruhiwa vibaya kwenye ajali siku magaidi walipojileta kwenye bonde la Mzakwe, na kuchakazwa vibaya na Kachero Yasmine. Baada ya ambushi hiyo, wenzake waliuawa kinyama na yeye kuponea chupuchupu huku akikutwa na kitita cha Dola za Kimarekani $10,000 kwenye nguo zake za ndani na barua zikiwa njiani kuelekea kwa mama yake "Maso Maso", Bi Mwantumu.
Alipozinduka hospitalini baada ya kukataa katakata kutoa ushirikiano mwishowe alikubali kuuza siri za magaidi waliomtuma, hii ilikuwa ni baada ya kuhakikishiwa usalama wake. Alijieleza yeye akiwa binti anayesomea fani ya Udaktari ngazi ya Chuo Kikuu alishawishiwa kuacha chuo na kwenda kujiunga kwenye kikundi cha ugaidi cha "Al-shabaab" nchini Somalia. Waliporejea Tanzania moja kwa moja wakatua Wilayani Kilindi yeye na mumewe aliyekutana nao huko huko Somalia. Kutokana na kujitolea kwao katika jihadi yeye akachaguliwa kuwa ni mmoja wa wana baraza la shura, wasiri wa ndani wa "Maso Square The Duduman" .
Mpaka akaaminika kufanywa tarishi wake wa kupeleka barua huku na kule. Hivyo mara ya mwisho alitumwa kupeleka pesa na barua kwa mama mzazi wa "Maso Maso", Bi Mwantumu lakini pia alitakiwa kupitia Dodoma kwa Bwana Kareem Abdallah achukue barua ya siri ya kuileta kwa "Maso Maso" yenye kuelezea namna serikali walivyochukua hatua baada ya shambulizi dhidi ya wabunge wake. Ndipo akakutana na sokomoko la kukuta mwenyeji wake Bwana Kareem Abdallah meneja wa Chops Carwash & Garage ametekwa.
Hivyo kwanza akasaidia kumtorosha baba yake mzazi Bwana Kareem Abdallah kumpeleka mafichoni Tanga, kisha akatia nia ya kushiriki ukombozi wa Bwana Kareem ili apewe hiyo barua kisha ndio aelekee Dar es Salaam kwa Bi. Mwantumu. Ndipo yakamkuta yaliyomkuta mpaka akanaswa mikononi mwa Makachero mahiri wanaopambana na magaidi.
'Ukhti Rayhaan' ndio aliyetoa maelekezo kuwa mzigo wa pesa na barua alikuwa anaupeleka kwa 'Shekhe Jamsheed' wa Sinza ambaye yeye ndio angeufikisha siku ya dua Alhamisi ya mwishoni mwa mwezi. Ndio ukachezwa mchezo wa pata potea wa Kachero Manu akajifanye amesilimu katika msikiti unaoongozwa na Shekhe Jamsheed.
Kisha baada ya hapo ajenge nae Shekhe Jamsheed mazoea mpaka amuingize kwenye harakati za "Al-shabaab" huko Kilindi, Tanga. Pata potea ikajibu vizuri, Shekhe Jamsheed ndani ya mwezi mmoja tu akamshiba Kachero Manu na kumfanya mwandani wake mpaka kuanza kumtapikia sumu za "Al-shabaab" kuwa ni kundi lililo katika haki, ila vyombo vya habari vya nchi za kimagharibi ndio vinawachafua kwa kusambaza propaganda chafu dhidi yao. Kachero Manu akaanza kuigiza anapendezwa sana na zile shemere za hadithi za Al-shabaab. Ndipo Shekhe Jamsheed akampa mchongo wa Kilindi Kachero Manu bila kujua anampeleka adui mwenye nia ya kuisambaratisha "Al-shabaab" itoweke Afrika Mashariki, watu waanze kuishi kwa amani na usalama kama zamani.
Mikono yake Kachero Manu ilikuwa inamsisimuka akawa anatamani anyanyuke aende akalianzishe tifu, awadunde kumuokoa mumewe 'Ukhty Rayhaan' lakini nafsi yake ikamuambia vuta subira, daima mwisho mwema ulio mzuri huwafikia wenye subira.
Kwa mkululu huu wa watu zaidi ya 200 ndani ya msikiti tena wakiwa na silaha za kivita hata uwe Komandoo wa dunia ukianzisha ugomvi utegemee tu kunyakuliwa kama mwewe anavyomnyakua kifaranga cha kuku.
Yule anayetuhumiwa kuwa msaliti akatupwa miguuni mwa 'Mullah', akawa anamuangalia 'Mullah' kwa macho ya huruma huku machozi ya huzuni yanamtiririka akitaraji shufaa yake huku jasho jekejeke limetotesha kanzu yake.
Ilikuwa ni siku yake ya mashaka fundo katika siku yake ya mwisho maishani. 'Mullah' akawa anamsinzilia kwa macho yake makali yule msaliti. 'Mullah' alikuwa akipitisha maamuzi ndio yamepita hivyo, alikuwa na tabia ya kisonoko mtamba na ukoko, haambiliki kamwe. Akaletewa jambia kubwa lile la kuchinjia ngamia aliyefutwa kodi huko Arabuni.
Akaanza kulizungushazungusha hewani kwa madaha na mbwembwe, halafu anatishia kama ndio anaanza kuchinjia, umati wote macho yanawatoka juu juu kwa hofu. Alivyolizungusha mara ya tatu na kulitua chini jambia halikurudi bure likatua kwa kasi shingoni na kutenganisha kichwa na kiwiliwili vipande viwili kwa kuikata mishipa ya damu na neva ya shingoni. Damu zilikuwa zinachuruzika kwa kasi mithili ya bomba chakavu la "DAWASA" lililopasuka mtaani.
Wakajitokeza watu wamevaa makoti meupe kama madaktari wakiwa na machela yao wakaibeba maiti na kuondoka nayo kwenda kuizika kusikojulikana. Biashara siku hiyo ikawa imeishia hapo mmoja, kila akatawanyikia upande wake kichwa chini, huku wengine wanashtakia njia kama kuku mwenye mdondo huku Kachero Manu akipewa rafiki atakayekuwa anaishi nae chumba kimoja hapo kambini.


Ilimchukua takribani miezi miwili tu, kila mmoja kambini kumfahamu Kachero Manu kwa jina la 'Komandoo Aboubakr' ni mtu wa shoka. Hii ilitokana na bidii na kujituma kwake kwenye mazoezi. Alikuwa pia anawapa mbinu na maneva mpya mpya za kivita ambazo ni ngeni kwa ufahamu wao.
Aliwafundisha kuanzia mbinu mpya za upigaji wa risasi, namna ya utegaji wa mabomu, na mbinu za utekaji. Sifa zake zilipaa mpaka zikafika mapango ya Amboni anakoishi "Maso Square The Duduman" na wateule wake. Sifa pia zikamrudia Shekhe Jamsheed kwa kuwaletea namba moja ya hatari sana kama 'Komandoo Aboubakr'. Na hayo yote ndio aliyokuwa anayatarajia Kachero Manu.
Wakati mwingine alipopata nafasi ya kuchokonoa mwenendo wa mambo pale kambini alifanya hivyo kwa utaalamu mkubwa. Ili yule mwenye ufahamu mkubwa azinduke mwenyewe kuwa kundi hili alilojiunga haliko katika njia ya sawa. "Swaahibu wangu 'Abuu-Fadhli' hivi haya matukio tunafanyaga tunaenda kutega mabomu sokoni au kwenye umati wa watu tunawaua watu wasio na hatia na sisi wenyewe tunajiua ni sahihi kweli?, mie naona ilibidi tukamlipue adui na sio hawa madhaifu akina mama, vikongwe na watoto ambao hawana hatia na hata kutushambulia kwa jiwe hawawezi, vipi mtazamo wako maana mie ni mgeni katika dini ya uislamu nisije kuonekana nakufuru imani yetu tukufu ya uislamu" alijitia kuuliza Kachero Manu kwa heshima na taadhima kubwa kumuuliza sanjari wake baada kutoka kupewa mpango kazi wa miezi sita ijayo usiku katika kikao cha wanamgambo wote.
Ambapo ilipangwa yakalipuliwe mabomu kwenye mechi za mpira wa miguu na mengine masokoni ili kuwashtua watawala kuwa "Al-shabaab" bado ina nguvu Afrika Mashariki. Wakiwa katika kitanda chao cha dabodeka Kachero Manu akiwa amening'iniza miguu yake chini huku mwenzake amejilaza kitanda cha chini, yule sanjari wake hakujibu swali aliloulizwa bali alinyanyuka na kuelekea mpaka mlangoni. Kachero Manu akaingiwa na wasiwasi huenda swali limemkera mwenzake na kumfanya amuone yeye sio mfia dini kama wao. Akawa amesisimkwa na malaika mwilini, akakaa vizuri mkao wa kazi hisia zilimtuma huenda mwenzake ameenda kubeba silaha amshindilie risasi za kutosha hivyo asibweteke kibwegebwege. Alipofika mlangoni akafunga mlango kwa funguo, kisha akazima taa ya chumbani na kurudi kitandani pake, kisha akatulia kama kuna kitu anatafakari.
Kisha akaanza kumjibu, "Komandoo Aboubakr leo umeleta hoja yenye mashiko ambayo sikutegemea mtu mgeni kwenye dini kama wewe uweze kuileta. Wengi wetu tunafuata mambo kama nyumbu tu, Shekhe au Kiongozi wa dini akisema sisi tunafuata tu kibubusa bila kuhoji hicho alichozungumza Shekhe ni maneno ya Mwenyezi Mungu toka kwenye Q'urani au maneno yake yanayotokana na hawaa ya nafsi yake! " alizungumza Abuu-fadhli kwa hisia za ndani, kisha akaendelea. "Hilo jambo ulilolichokonoa hata mimi nilikuwa ninalitafakari sipati majibu sahihi na ya kina. Kwa mfano kuua mtu asiye na makosa ya kuua mtu tumekatazwa kwenye Q'urani".
Wakaendelea na mazungumzo yao yaliyowaweka macho kodo mpaka manane ya usiku, yakipaza usingizi wao. Kutokea hapo wakazidi kuwa marafiki wa chanda na pete, kila alipokuwa 'Komandoo Aboubakr' (Kachero Manu) habanduki Abuu-fadhli, amejibandika nae. Huku Kachero Manu akimfunda rafiki yake mbinu madhubuti za kivita, ambazo ni adimu akiwa na malengo ya kumtumia kama msaada kwake wa kuisambaratisha hii kambi siku za usoni.
Baada ya kupita miezi kadhaa tena yakatoka maagizo toka kambi kuu, mapango ya Amboni, ambapo ndipo anapoishi gaidi mkuu "Maso Square The Duduman", ya kumteua 'Komandoo Aboubakr' kuwa ni Kiongozi Msaidizi wa kambi ya Dibungo. Kila mwanamgambo wa "Al-Shabaab" kambini hapo alipopata taarifa hizo alikubaliana moja kwa moja uteuzi huo bila kuleta ukaidi. Ikaandaliwa hafla ya kumpa mkono wa baia wa kukubaliana na uteuzi wake.
Hapo sasa akawa na uwezo wa kuingia bohari kuu ya silaha na vifaa vya kijeshi bila kikwazo chochote. Fursa ambayo kwake ilikuwa ni kama nafasi ya dhahabu, aliitumia ipasavyo kukamilisha nia yake ya undumilakuwili (Double Agent). Mchana alikuwa anafanya majukumu ya Al-qaeeda kama 'Komandoo Aboubakr' na nyakati za usiku anajigeuza kuwa Kachero Manu anaenda kutega mabomu ya ardhini kuzunguka kambi nzima, mpaka alipokamilisha zoezi lake. Na hakutiliwa mashaka hata chembe na walinzi wa usiku wa kambi kutokana na cheo chake.
Nyota yake ikazidi kung'ara zaidi sasa akapewa barua ya kupandishwa cheo, akatakiwa ahamie kambi kuu ya mapango ya Amboni. Barua ilimtaka akaripoti kambini haraka iwezekanavyo. Gaidi mkuu "Maso Square The Duduman" alikuwa anaondoka kwa muda na baadhi ya Makomandoo wazoefu hivyo kambi kuu ilitakiwa iongezewe nguvu na watu makini kama Kachero Manu ambaye wenyewe wakimfahamu kama 'Komandoo Aboubakr'.
Siku ya siku, majira ya saa tatu usiku wakiwa wamejifungia chumbani kwao, Kachero Manu akampa taarifa rafiki yake. "Swaahibu wangu mie ndio naelekea Amboni, safari yangu imeiva hivyo huku tena nakata mguu, kesho asubuhi na mapema jua litakapoanza kupasua matlai natakiwa niwe Amboni. nasikitika kutengana na wewe lakini nitafanya juu chini tuungane tena hata kwa kuwashawishi viongozi wetu" yalikuwa ni maneno ya Kachero Manu kwa rafiki yake kipenzi Abuu-fadhli. " Nikutakie kazi njema, ila ninachokuonya ni kuwa makini sana yale mapango ni balaa unaweza kujikuta unatoweka usipofuata masharti yake" alipewa nasaha za tahadhari na rafiki yake, maana alimjua Kachero Manu mtundu mtundu muda mfupi tu aliokaa nae ameona shughuli yake.
"Unaonyesha kama unayafahamu vizuri sana hayo mapango swaahibu wangu eeh?" aliuliza Kachero Manu swali la kudodosa. "Nayajua vizuri sana na kila kichochoro na kijia chake, marehemu Baba yangu alikuwa ni mmoja wa wahifadhi wa yale mapango akiwa muajiriwa wa serikali hivyo tumecheza sana mapangoni" alijibu kwa kujiamini. Ndipo zikaanza stori za mapango hayo, yenye hadithi za kusisimua zilizomuacha Kachero Manu mdomo wazi lakini zikimpa mwangaza wa makazi mapya anayoenda kuishi.

SURA YA KUMI NA TATU
Mipango ya ndoa ya Maso Maso na Kachero Yasmine inapangwa
Ni saa 2:30 usiku kwa majira ya saa za Afrika Mashariki na Kati, Kachero Yasmine alikuwa ameegesha gari yake ya kisasa yenye rangi nyeusi aina ya "2017 Nissan Murrano" pembezoni mwa barabara ya 'Survey' inayoelekea Chuo Kikuu cha Ardhi "Ardhi University". Ndani ya gari kiti cha nyuma alikuwepo mwanaume aliyevalia kanzu nyeupe na kofia, akiwa amepindua kiti na kujilaza.
Walikuwa wameshakaa kuwasubiria wageni wao wanaotarajia kuonana nao kwa zaidi ya nusu saa. Tayari alishaanza kuvuta hisia za watu wanaopita njia hiyo kutaka kufahamu kilichomuweka hapo. "Dada habari yako samahani umepatwa na shida yoyote unahitaji msaada? nimekuona umesimama hapa muda mrefu..!" ilikuwa ni kauli ya mlinzi wa kampuni binafsi anayelinda eneo la Chuo Kikuu. "Hapana kuna mtu namsubirishia amenipa ahadi tukutane hapa" akajibu Kachero Yasmine huku tayari gari alilokuwa analisubiria lilikuwa limeshapiga taa za ishara na kwenda kwa mbele yake kisha linasimama.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog