Simulizi : Gari La Kukodi
Sehemu Ya Tano (5)
“Kwani mimi nina tofauti gani na watu wengine?” Joyce aliuliza huku akimkazia macho Dynamo Plus.
“Wewe ni mtu mkubwa, watu kama ninyi muda mwingi mko bize, sina hakika hata kama mnapata muda wa kusikiliza nyimbo zetu,” Dynamo Plus alisema huku akipitisha ulimi kuilamba midomo yake mikubwa.
“Nina ukubwa gani mimi!” Joyce alisema na kuangua kicheko hafifu, akaendelea, “Tuyaache hayo, Aisha yuko wapi siku hizi? Nimemmisi sana,” Joyce aliuliza huku macho yake yakiwa yameweka kituo usoni kwa Dynamo Plus.
“Aisha dada’angu! Kwani mnafahamiana?” Dynamo Plus aliuliza kwa mshangao baada ya kufikiria kidogo.
“Ni best wangu sana, nilisoma naye kidato kimoja Sekondari ya Wasichana ya Tabora.”
“Anaishi Sweden siku hizi. Nimefurahi sana kukufahamu dada…” Dynamo Plus alisema na kuonekana kusita kidogo na kuachia kicheko hafifu huku akishika kichwa chake kuonesha kuwa amelisahau jina la Joyce.
“Joyce… Mrs. Joyce Kambona,” Joyce alisema huku akiachia tabasamu.
“Oh yes, dada Joyce… you are a fashion designer, right?” Dynamo Plus alisema huku akimtazama Joyce kwa makini. Joyce aliachia tabasamu pana zaidi la bashasha.
“Yeah! How do you know?” Joyce aliuliza huku akihisi furaha moyoni kwa kuwa Dynamo Plus alionesha kumfahamu.
“Nadhani tumewahi kukutana, pia nimekuwa nikisikia habari zako. Hasa Madame Norah amekuwa anakuongelea sana. She real admires you!” Dynamo Plus alisema na kumfanya Joyce azidi kujisikia fahari baada ya kugundua kuwa kumbe watu walikuwa wanaongelea habari zake.
* * * * *
Saa kumi alasiri, kwenye viunga vya maegesho ya magari vya mgahawa wa kisasa wa Elli’s, mtangazaji na mtayarishaji wa kipindi maarufu cha ‘Mbunifu Wetu’ katika kituo cha runinga cha Mzizima, Maximilian Njamba alikuwa amesimama kwa mbali akionesha kidole chake lilipokuwa limeegeshwa gari aina ya Cadillac DeVille lenye muundo wa kizamani likiwa na kibao cha “Taxi” juu yake.
Maximilian Njamba alikuwa mwanamume wa makamo mwenye umri wa kati ya miaka arobaini na tano na hamsini, si mrefu wala mfupi kwa kimo, pia hakuwa mwembamba wala mnene na alikuwa na sura ya ucheshi muda wote.
Alasiri ile Maximilian alikuwa amevaa kofia nyeusi ya pama, shati la mikono mirefu la pundamilia, suruali pana ya kijivu na viatu vyeusi ya ngozi miguuni.
Alikuwa amefika katika mgahawa wa kisasa wa Elli’s baada ya kuambiwa na rafiki yake kuhusu uwepo wa gari aina ya Cadillac DeVille lililosajiliwa kuwa teksi, alipoliona alijikuta akiupenda sana ubunifu uliotumika kulifanya lile gari kuwa la kibiashara.
Muda ule alikuwa ameshika kipaza sauti chenye nembo ya Mzizima TV akiwa mbele ya mpiga picha wake. Alikuwa akielezea jinsi alivyovutiwa sana na ubunifu uliotumika kwenye lile gari aina ya Cadillac DeVille.
Hii ilikuwa baada ya kumtafuta mmiliki wa gari lile, Sammy Kambona na kutaka kufanya naye mahojiano lakini Sammy alikataa katakata na kumuonya Maximilian asijaribu kulipiga picha gari lake bila idhini yake.
Kwa kuwa Maximilian aliiona ile teksi kama njia nzuri ya kuhamasisha ubunifu aliamua kuitumia ile fursa adimu ili kuwavutia watazamaji wa kipindi chake waweze kuhamasika kufikiria ‘nje ya boksi’ kwa kufanya vitu ambavyo watu wengine wangedhani haviwezekani.
Lakini tatizo lilikuwa ni Sammy, alikuwa amekataa kuhojiwa wala kupigwa picha, hivyo Maximilian aliamua kuvizia, pindi Sammy alipoingia ndani ya ule mgahawa wa Elli’s, akasimama kwa mbali lakini akihakikisha lile gari linaonekana kwenye kamera na kumtaka mpiga picha wake kulivuta gari karibu ili liweze kuonekana vyema.
Baada ya mpiga picha kuweka sawa mitambo yake na kumpa ishara kuwa alikuwa tayari, Maximilian alianza kazi iliyompeleka pale huku akiwa makini.
“Huu ni ubunifu wa hali ya juu sana, ila tunasikitika mmiliki wake amekataa kufanya mahojiano nasi, tungefahamu alifikiria nini kulifanya gari hili aina ya Cadillac DeVille lililotengenezwa zaidi ya miaka hamsini iliyopita kuwa teksi! Kwa kweli hii ni teksi inayovutia hasa, na kila mtu angependa kuwa abiria wake…” alisema yule mtangazaji wa kipindi maarufu cha ‘Mbunifu Wetu’ kilichorushwa na Mzizima TV.
“Na cha ajabu zaidi, licha ya kuwa ni gari la kizamani lakini ni kama mpya, haina matatizo yoyote na inaweza kukufikisha kokote uendako pasipo hofu ya kuharibika njiani… sasa ngoja nisikie maoni ya wakazi wa jijini Dar es Salaam kuhusu gari hili,” alisema Maximilian na kuelekea mtaani akijaribu kupata maoni ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Aliwauliza hasa wakazi walioishi jirani na eleo la mgahawa wa Elli’s kama wameshawahi kuliona gari aina ya Cadillac DeVille la muundo wa kizamani lililokuwa likitumika kama teksi na nini maoni yao kuhusu gari lile.
Wapo wakazi waliosema kuwa hawajawahi kuliona na wale walioliona walionekana kusifia sana akili ya kibunifu iliotumika kulifanya lile gari aina ya Cadillac DeVille la muundo wa kipekee kuwa teksi, wakidai kuwa lilikuwa ile hali ya upekee ingeweza kuwavutia watu wengi kutaka kuwa abiria wake na hivyo kulifanya gari liwe bidhaa adimu.
Wapo waliodai kuwa japo walikuwa wameliona ndani ya siku chache tu lakini tayari lilikwisha fahamika sana utadhani lilikuwa lina zaidi ya mwaka mmoja, wote walikiri kuwa wangependa kuwa abiria siku moja kutokana na upekee wake.
* * * * *
Saa moja jioni Sammy alikuwa anatoka ndani ya mgahawa wa kisasa wa Elli’s uliopo Ilala Sharif Shamba na kutembea haraka akikatiza kwenye viunga vya maegesho ya magari vya mgahawa ule, akalifikia gari lake aina ya Cadillac DeVille na kufungua buti la gari.
Alitoa supana, akaanza kukifungua kibao chenye maandishi ya “Taxi” kilichokuwa kimepachikwa juu ya gari na kukitoa, kisha akakificha ndani ya buti la gari. Alipomaliza akafunga buti na kuingia kwenye gari.
Jioni ile aliokuwa na mawazo na alichoka sana, nadhani ilitokana na pilika pilika za kutwa nzima za kupeleka abiria huku na kule ambazo hakuwa amezizoea. Alifunga mkanda wa siti yake na kuliondoa gari taratibu kutoka kwenye maegesho ya magari ya ule mgahawa wa Elli’s na kuingia barabarani.
Muda huo gari lilionekana likiwa halina kibao cha kulitambulisha kuwa ni teksi, aliamua kufanya vile kila siku alipotaka kurudi nyumbani hadi siku ambayo angemweleza ukweli mkewe.
Saa moja jioni jiji la Dar es Salaam lilikuwa limemezwa na pilika pilika za aina yake za watu zilizoshamiri katikati na kwenye viunga vya jiji hilo kubwa zaidi Tanzania na hali ya hewa ilikuwa ya joto sana kama kawaida ya jiji hilo.
Uso wa Sammy ulikuwa umesawajika, alikuwa na mawazo mengi kwani hakutegemea kama Winifrida angeweza kugundua siri yake mapema vile kuwa lile gari lilitumika kama teksi. Aliendesha gari lake kwa utulivu hadi alipofika nyumbani kwake eneo la Tabata Chang’ombe.
Akionekana kuchoka sana, alifika mbele ya nyumba yake kwenye geti kubwa la mbele akapiga honi mara moja tu na kuinamisha kichwa chake kwenye usukani akisubiri kufunguliwa geti, mara usingizi mwepesi ukamchukua.
Alikuja kushtuliwa na Winifrida aliyekuwa anagonga kwenye kioo cha dirisha lake, Sammy aliinua kichwa chake kumtazama Winifrida, akaachia tabasamu na kuliingiza gari lake ndani kisha akalizima na kushuka akibeba mkoba wake wa kiofisi.
Alitembea taratibu kuelekea ndani na mlangoni akapishana na Joyce aliyekuwa akielekea dukani. Walisalimiana na Sammy akaingia ndani na kuelekea moja kwa moja chumbani kwake alikokwenda kuuweka mkoba wake wa kiofisi na kuanza kuvua nguo zake.
Alianza kwa kuvua koti lake na kulitupa kitandani, akalegeza tai yake na kuivua ikifuatiwa na shati, vyote akavitupia kitandani kisha akavua viatu na kuviweka kwenye stendi maalumu ya viatu, halafu akavua soksi na kuzitupia kitandani na mwisho akavua suruali na kutoa mkanda kisha akaitupia kitandani. Alipomaliza alivaa bukta na fulana nyepesi.
Akachukua shati lake alilovua na kuanza kusachi kwenye mifuko ya shati, akatoa vijiti vitatu na nusu vya kuchokonolea meno na kuvitupa ndani ya kapu dogo la taka lililokuwa limewekwa kwenye kona moja mle chumbani.
Kisha alichukua koti lake na kupekua kwenye mifuko akianza na mifuko ya nje kabla hajahamia mifuko ya ndani, akatoa kadi fulani mbili tatu, mojawapo ikiwa ile kadi aliyopewa na abiria wake mzungu na karatasi fulani, akaviweka kando na kuchukua suruali yake.
Alianza kukagua mifuko ya mbele kwanza kwa kutoa nje vitambaa vyake, akatoa simu yake ya mkononi na kuiweka kitandani, kisha alitomasa mfuko wa nyuma lakini hakuhisi kitu. Aliamua kuingiza mkono uliotoka patupu! Hakukuwa na kitu.
Akaiachia suruali ile ikaanguka chini kisha akashika kiuno akionekana kufikiria kidogo. Alionekana kung'aa macho akionekana kujiuliza maswali kisha akatazama kitandani. Alionekana kushtuka na kutoka chumbani haraka, akamkuta Winifrida akiwa ameketi sebuleni.
“Hebu niangalizie pochi yangu, nadhani nimeiacha ndani ya gari,” Sammy alimwambia Winifrida na kujibwaga juu ya sofa, mara akagutuka na kuinuka haraka, akaingia chumbani kwake kwa kujikongoja.
Aliuchukua mkoba wake wa kiofisi na kuufungua, akaangalia ndani na kuiona pochi yake. Akaifungua na kuziona fedha, alizihesabu kwa macho. Zilizokuwa kama noti kumi na mbili za shilingi elfu kumi kumi na noti nyingine kadhaa za elfu tano tano na elfu mbili mbili. Sammy aliachia tabasamu na kuiweka vizuri pochi yake ndani ya droo iliyokuwa kando ya kitanda.
Kisha alizichukua nguo zake pamoja na soksi na kuzitumbukiza kwenye tenga la nguo chafu lililokuwa limewekwa sehemu fulani ndani ya kile chumba. Kama aliyekumbuka kitu, aligeuza shingo yake na kujiangalia kwenye kioo kirefu cha meza ya vipodozi. Kisha alitoka kuelekea sebuleni na hapo akawaona Winifrida na Joyce wakiingia huku wameongozana.
“Sijaiona,” Winifrida alimwambia Sammy.
“Usijali nimekwisha iona, ilikuwa kwenye mkoba wangu!” Sammy alisema na kujibwaga tyena kwenye sofa, akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akifumba macho yake. Alionekana kuzama kwenye mawazo.
Winifrida aliketi kwenye sofa huku akimtazama Sammy kwa kuvizia vizia. Joyce alielekea moja kwa moja jikoni na baada ya muda mfupi aliandaa meza kwa ajili ya chakula cha jioni na kusogea mbele ya Sammy, akasimama kwa heshima.
“Karibu chakula, Baba Pendo,” Joyce alisema huku akimwangalia Sammy kwa makini usoni.
Sammy alishtuka na kufumbua macho yake, akamtazama Joyce kwa kitambo kidogo bila kusema neno, kisha aliachia tabasamu kwa mbali na kujizoazoa taratibu kutoka pale kwenye sofa na kuelekea kwenye meza ya chakula.
“Naona leo hauko sawa, kuna tatizo?” Joyce alimuuliza Sammy huku akiwa bado anamwangalia kwa udadisi.
“Nimechoka tu,” Sammy alisema huku akiketi kwenye kiti chake.
Meza ya chakula ilikuwa imejaa mapochopocho: kulikuwa na wali mweupe, mchuzi mzito wa kuku, bakuli lenye nyama za kuku, bakuli la maharage yaliyoungwa kwa nazi, bakuli la mboga za majani, bakuli la saladi, matunda mchanganyiko kwenye sinia pamoja na jagi la maji ya kunywa na bilauri nne.
Ilikuwa imekwishatimu saa mbili na nusu usiku wakati Sammy na familia yake wakikaa mezani kwa ajili ya chakula cha jioni. Joyce alimnawisha Sammy mikono, kisha akamnawisha Pendo na kuwakaribisha.
Winifrida alinawa mikono huku akiendelea kumtazama Sammy kwa kuvizia vizia, kila mmoja alijipakulia chakula kwa kadiri ya tumbo lake, Winifrida alikuwa akimtazama Sammy kwa jicho la wizi wakati akijipakulia chakula.
Sammy alijipakulia wali wa kumtosha kwenye sahani, akawekea mchuzi wa kuku na kumwagia maharage kwa wingi, kisha aliweka mboga za majani nyingi na kujisogezea huku akiketi kitako. Alionekana kupoa sana jambo lililomshangaza kila mtu isipokuwa Winifrida, kwani yeye alifahamu ukweli kwa nini Sammy alikuwa amepoa sana siku ile.
Joyce alikuwa akimtupia Sammy jicho la wizi wakati akisogeza poti la chakula, akampakulia Pendo kidogo na kumwekea mchuzi mzito wa kuku na maharage kisha akampa na kuanza kujipakulia chakula chake mwenyewe, alipomaliza alianza kula taratibu.
Winifrida naye alijipakulia chakula huku Sammy akimtazama kwa makini, hakusema kitu lakini alionekana kuwa na donge moyoni. Alitamani kumwambia Joyce ni wapi alimkuta Winifrida akiwa na mwanamume lakini alihofu siri yake ingefichuka.
Pendo alimtazama baba yake kwa udadisi, Sammy naye alishusha macho yake kumtazama Pendo akiwa mtulivu sana. Akachota chakula na kuanza kula.
Siku hiyo meza ya chakula ilitanda ukimya mzito wakati wote wa chakula, hakuna aliyeongea na kilichokuwa kikisikika muda ule kilikuwa ni mgongano wa vijiko na vyombo vingine vya mezani, wakati wakila.
* * * * *
Saa sita na nusu usiku Winifrida, mtoto wa kike mchache wa miaka lakini mwingi wa maneno, alikuwa ameketi kitandani chumbani kwake, akiwa amejiegemeza kwenye ukuta akiwaza. Usiku huo ulikuwa mrefu kwake kuliko kawaida na usingizi ulikuwa adimu.
Rohoni mwake mlikuwa na shauku kubwa. Alipomaliza kula usiku ule aliingia chumbani kwake akapanda juu ya kitanda chake, si kulala bali kuendelea na fikra zake zisizokuwa na mwisho kuhusu Jackson. Kijana mtanashati na mcheshi sana.
Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kugeuza shingo yake kumtazama Pendo aliyekuwa katika sayari ya mbali muda ule akikoroma, alikuwa akivuta pumzi taratibu na kuzishusha.
“Hmm, utoto raha sana! Unakuwa huru na huna stress, hufikirii maisha wala mapenzi kama ilivyo kwa wakubwa,” Winifrida aliwaza.
Alizungusha macho yake kukitazama kile chumba chao kwa makini kana kwamba alikuwa akikiona kwa mara ya kwanza, akafumba macho yake, mawazo yalizidi kumsonga usiku huo, aliwaza vitu vingi: alifikiria masomo, maisha, mapenzi. Alimwaza Jackson, kijana aliyetokea kumpenda sana. Alitamani usiku ule angekuwa na Jackson mle chumbani, wakiwa wao wawili tu. Lakini hakukuwako!
Kilichokuwa pamoja naye usiku ule, ukimwacha Pendo aliyelala fofofo kitandani, ni mito miwili mikubwa, alifumbua macho yake na kuutazama mto mmoja, akauvuta kisha aliubana kifuani kwake na kuubusu.
“Jackson,” Winifrida aliuita ule mto huku akiyafumba macho yake, “Nakupenda sana mpenzi wangu. Tafadhali niambie kama nawe wanipenda kwa dhati.”
Kisha alitegesha sikio lake kwenye ule mto akifanya kama anayesikiliza, kwa mbali katika sikio lake la mawazo alimsikia Jackson wa ndotoni akimjibu, “Winnie, mpenzi wangu, ni wewe peke yako ninayekupenda hapa duniani. Nakupenda na nitaendelea kukupenda hadi mwisho wa maisha yangu…”
Winifrida alihisi mapigo ya moyo wake yakiongezeka maradufu na joto lake likizidi kupanda. Akaubusu tena ule mto kama aliyepatwa na wazimu. Hakuamini kama yote yale alikuwa anafanya na ule mto, wala Jackson hakuwako.
Aliendelea kuubusu ule mto mpaka aliporudiwa na fahamu. Akaona haya, japo Pendo alikuwa amelala na hapakuwa na mtu mwingine aliyeuona upumbavu wake. Aliusukuma ule mto pembeni, akaridhika kuwa alikuwa na Jackson muda ule.
“Lo, Jackson! Laiti ningekuwa na uwezo ningehama naye hapa duniani, nikajifiche naye pahala pa peke yetu, sina hofu ya pute wala vijicho, ni mimi na yeye tu, kutwa kucha,” Winifrida aliwaza na kushusha pumzi.
Akakumbuka alivyokutana na Jackson mara ya kwanza, ilikuwa mwaka uliokuwa umetangulia, miezi sita tu iliyokuwa imepita, wakati huo Winifrida akiwa kidato cha tatu na Jackson akiwa kidato cha nne. Ilikuwa ni katika mashindano ya ujirani mwema yaliyofanyikia Shule ya Sekondari ya Azania na kuzikutanisha shule kongwe za jijini Dar es Salaam.
Siku ile wanafunzi wa Zanaki walipanda jukwaani kuonesha mchezo wa kuigiza ulioitwa ‘Hadi Lini!’ na yeye Winifrida alicheza nafasi ya mhusika mkuu. Ulikuwa mchezo uliomwelezea mwanamke jasiri aliyepambana kunusuru ndoa yake pale mumewe aliyempenda alipoamua kumsahau na kumpenda mwanamke mwingine, baada ya kufanikiwa.
Winifrida alicheza nafasi ya mke mtii kwa ndoa yake ambaye mume wake alipata penzi jipya. Alicheza nafasi hiyo kwa uthabiti na kuuvaa uhalisia wa kweli, hasa pale aliposimamia kile alichokiamini na kuwafanya nusu ya watazamaji wasisimkwe na kupiga kelele za shangwe.
Walipomaliza tu onesho lao Jackson alimfuata alipokuwa amesimama na wenzake na kumpongeza. Winifrida alibinya mikono yake kwa shauku, raha iliyoje kupongezwa na kijana kama Jackson. Ni yeye Winifrida aliyetamani kumpongeza kwanza Jackson kwa onesho lake lililomsisimua kila mtu ukumbini. Ni Jackson aliyepanda jukwaani kabla yao.
Jackson alikuwa amejaaliwa sauti tamu na kipaji cha kuimba na alipokuwa jukwaani kila mtu alipagawa! Winifrida alihisi damu ikimchemka, roho ikamlipuka, miguu ikamcheza na moyo kumpapatika.
Kwa kweli Jackson alijaaliwa sauti nzuri na alijua hasa kuburudisha mashabiki awapo jukwaani, ndiyo maana haikuwashangaza wengi kuona wimbo wake wa ‘Nadhiri Yangu’ aliokuwa ameuachia kipindi hicho ukifanya vizuri sana kwenye vituo mbalimbali vya redio na runinga kuliko hata nyimbo za wakongwe.
Inaendelea... (62)
Sasa Jackson na Winifrida walikuwa wamesimama wakitazamana kwa makini, kila mmoja alikiona kitu fulani kwenye macho ya mwenzake. Penzi changa! Kwa muda mfupi tu waliosimama na kupongezana ulitosha kuwajulisha kuwa kila mmoja alikuwa amevutiwa na mwingine. Na kuanzia siku hiyo ukawa mwanzo wa kuchipua kwa penzi lao, ingawa hadi wakati huo hawakuwa wamekutana kimwili.
Kabla ya hapo, Winifrida hakuwa akijihusisha kabisa na uhusiano wowote wa kimapenzi japo hakuacha kubughudhiwa kila alipopita mtaani, kama alivyojiwekea nadhiri kutojiingiza katika uhusiano wa kimapenzi hadi amalize shule, ni hivyo hivyo alivyoishi. Hakuringia uzuri wake lakini hakutaka pia usumbufu unaopitiliza kutoka kwa wavulana.
Kuanzia kidato cha kwanza hadi hapo alipofikia alikuwa na msimamo thabiti sana, hata hivyo, maringo yake yalifichwa na werevu wake darasani. Ilikuwa ni warembo wachache sana wa aina yake waliofanya vizuri kimasomo, jambo hilo liliwavutia walimu na wanafunzi waliopenda maendeleo kimasomo.
Lakini sasa Jackson alikaribia kumfanya aivunje nadhiri yake aliyojiwekea. Japo alikuwa amemwambia Jackson asubiri kwanza amalize kidato cha nne lakini Jackson alikuwa na maneno matamu sana yaliyokaribia kumtia wazimu.
Winifrida alianza kuwa mzembe darasani, badala ya kumsikiliza mwalimu, mawazo yake yote yalikuwa kwa Jackson.
Ndiyo maana haikushangaza siku ile mchana aliamua kutoroka shule na kuandamana na Jackson kwenda nyumbani kwao Kiwalani, alikuwa tayari kwenda kumpa penzi, lakini kaka yake Sammy… ah, sijui alitoka wapi na kutibua mipango yao!
Winifrida alijiona kuwa hakuwa huru kama wasichana wenzake. Alidhani kuwa hapa duniani hakuna kitu kizuri kuliko uhuru; uhuru wa kufanya apendacho duniani.
Kwa mara ile ile aliutamani ukubwa ikiwa udogo maana yake ni kudhibitiwa, lakini pia aliuchukia ukubwa ikiwa maana yake kudhibiti wadogo. Sasa alikwisha ingia katika mtihani mgumu wa mapenzi. Alimfikiri Jackson kila wakati, akimwona kila pahala, tangu katika sahani ya chakula hadi kitandani.
Alichukua begi lake la madaftari na kupekenyua sehemu fulani kwenye mifuko ya lile begi na kutoa simu yake ya mkononi aliyokuwa akiificha ili isionwe na kaka yake au wifi yake. Ilikuwa ni simu aina ya Huawei aliyonunuliwa na Jackson ili kuwarahisishia mawasiliano.
Alifungua sehemu ya kuhifadhi majina na kulitafuta jina la Jackson, alipoliona alilitazama kwa makini akitamani kumpigia simu, lakini akasita.
Mara akakumbuka jambo na kuinuka haraka, akalifuata kabati la nguo na kulifungua, akapekua pekua kwenye nguo zake na kutoa kadi ndogo ya kuhifadhi kumbukumbu kwenye simu (Micro SD). Ni kadi aliyoipata kwenye gari la Sammy siku ya kwanza tu Sammy alipokuja na gari nyumbani.
Winifrida aliketi juu ya kitanda, akatabasamu huku akiiangalia kwa makini ile kadi ndogo ya kuhifadhi kumbukumbu kwenye simu kisha akageuka kumwangalia Pendo aliyekuwa anakoroma. Aliifungua ile simu na kuiweka ile kadi ndani yake.
Ile kadi ilionekana kujaa picha, sauti na video. Winifrida alipotaka kuingiza picha zake yakatokea maandishi kwenye kioo cha simu yake: “Micro SD is Full do you want to format it?” Winifrida alishusha pumzi huku akiangalia juu, aliwaza kidogo na kuuma midomo yake.
Alitaka kufuta vitu vilivyokuwemo lakini akasita na kuamua kuifungua ile kadi kuona kilichokuwemo. Alikuta picha kadhaa za jengo la kisasa lenye chumba chenye vifaa ambavyo hakuvielewa, video moja na sauti ya kurekodiwa. Aliamua kuisikiliza ile sauti na alichokisia kilimtisha sana.
Ilikuwa ni rekodi ya maongezi ya simu kati ya mtu mmoja aliyeonekana kuwa ni mwanasiasa au mtu mwenye mamlaka makubwa serikalini na muuaji wa kukodiwa. Katika maongezi yao walikuwa wanapanga mikakati ya mauaji ya mtu waliyekuwa wakimtaja kwa jina la JM.
Winifrida aliyasikiliza kwa makini maongezi yao huku akihisi kuogopa mno. Ubaridi wa woga wa aina yake ulimtambaa mwilini na mapigo ya moyo wake yalibadili mwendo wake na kwenda mbio isivyo kawaida! Nywele kichwani kwake zilisimama na mwili kusisimka. Hakumaliza kusikiliza maongezi, akayaondoa na kuamua kutazama ile video.
Lahaula! Alijilaumu kwa nini aliitazama ile video. Ilikuwa video ya mauaji ya kutisha, hakuamini alichokiona, alidhani labda ni sinema ya kutengenezwa. Lakini alipoitazama vizuri alihisi ilikuwa na uhusiano na yale maongezi aliyoyasikia awali. Hata hivyo, kuna jambo lilimshtua zaidi, gari la Sammy lilionekana kwa mbali!
“Lilifuata nini gari la Sammy kwenye ile video ya mauaji?” Winifrida alijiuliza swali lile na maswali mengine kibao: Je, mauaji yale yalikuwa yanahusiana vipi na Sammy? Ile kadi ya kumbukumbu kwenye simu aliyoikuta kwenye gari la Sammy ilifikaje? Je, Sammy alikuwa anaelewa chochote kuhusiana na yale mauaji?
Winifrida alijawa na hofu kubwa. Kichwa chake kilikuwa kimejawa na mawazo na kuchanganyikiwa kwa wakati mmoja. Alijihisi moyo wake ukilemewa na msukumo mkubwa wa damu na asijue la kusema. Hakuwa na majibu ya yale maswali.
Aliogopa sana na kuitoa ile kadi haraka, akaificha kabatini huku akihisi kama Sammy alikuwa akimchungulia dirishani, kwa mara ya kwanza alianza kumwogopa kaka yake. Alipanda kitandani, akajilaza na kujifunika shuka gubigubi huku akijikunyata kwa woga.
Taxi imeanza kuzua mambo! Usikose kuifuatilia simulizi hii ya kusisimua ili kuujua mwisho wake. Ciao...
- (63)
“.
SASA ENDELEA...
* * * * *
Saa tatu na nusu asubuhi, katika Shule ya Sekondari ya Zanaki, Winifrida alikuwa ameketi darasani akiwa mkimya mno jambo lililowashangaza wanafunzi wenzake, kwani haikuwa kawaida yake kutulia vile. Kwa tabia yake ya uchokozi kwa wengine na sauti yake kali ilikuwa rahisi kuhisi uwepo wake, na siku ambayo hakufika shule kila mtu angejua kuwa hayupo.
Hata hivyo, kimya cha siku ile kilikuwa cha sauti tu, kwani kichwani mwake mlikuwa mmejaa mawazo yaliyokuwa yakisokotana na kumfanyia kelele ambazo mtu yeyote hakuweza kuzisikia ila yeye mwenyewe.
Hakuwa na furaha kabisa moyoni mwake kutokana na kumbukumbu mbaya ya picha alizozishuhudia usiku uliokuwa umetangulia kwenye kadi ya simu aliyoiokota kwenye gari la kaka yake.
Ndani ya darasa lile la kidato cha nne kulikuwa na utulivu mkubwa, wanafunzi walikuwa wakimsikiliza mwalimu wao wa sayansi, Mwalimu Josephat Igembe. Hata hivyo, Winifrida aliyeonekana kama alikuwa akimsikiliza Mwalimu Igembe kwa makini, aliishia kumwangalia tu pasipo kusikia chochote alichoongea, mawazo yake yote yalikuwa mbali kabisa, nje ya zile kuta nne za darasa.
Kila mara alijitahidi kuyarudisha mawazo yake yawemo darasani, na hata alipopata nafasi ya kumsikiliza mwalimu, Kiingereza chake kilikuwa rahisi sana, lakini ule ujumbe uliokuwemo katika maana ndiyo uliokuwa mgumu. Winifrida aliviajiri viungo vyote vya mwili wake vimfikishie ujumbe, lakini wapi!
Maneno yaliteleza kinywani mwa Mwalimu Igembe utadhani maji yakiteremka mlima, kwa hali hiyo aliacha wazi masikio yake na kuyasabiria maneno ya mwalimu yule ili kuelewa maana ya neno moja moja.
Mara alishangaa kuona wanafunzi wenzake wote wakigeuka kumtazama kwa mshangao, na yeye akawatazama kwa mshangao. Kabla hajujua kulikoni, akashtuliwa na sauti ya Mwalimu Igembe, “Winifrida, mbona ni swali rahisi kabisa, sijui kwa nini unafikiria kiasi hicho!”
Winifrida alimkodolea macho Mwalimu Igembe, hakujua ajibu nini kwani hata swali lenyewe hakuwa amelisikia. Alishusha pumzi ndefu huku akiiminya midomo yake.
“Okay, mwingine anayejua jibu lake atusaidie, naona Winifrida leo hayuko sawa, pengine akili kazisahau nyumbani!” Mwalimu Igembe alisema na kuwafanya wanafunzi wote, isipokuwa Winifrida, wacheke. Hata hivyo, hali hiyo ilimfanya Winifrida ashushe pumzi za ahueni japo alikuwa anatweta kama aliyekuwa amekoswa na risasi.
“Sijui nifanye nini sasa? Naona hali hii inaanza kuathiri hata masomo yangu! Naogopa nikimuuliza kaka naweza kusababisha matatizo makubwa na nikimwambia wifi sijui kama atanielewa! Na hata akinielewa itakuwaje endapo ni kaka Sammy ndiye mhusika wa tukio lile? Halafu watakapojua kuwa nina simu watataka kujua nimeipata wapi? Ah… Mungu niepushe na balaa hili…” Winifrida aliwaza, mara mawazo yake yote yalivutwa na picha za tukio la mauaji, sasa alikuwa kama anaona tukio lile likifanyika mbashara mbele ya macho yake
Aliwaona wanaume wawili ambao walizishika bastola zao sawasawa kwenye mikono yao, wakazielekeza kwa mwanamume mmoja na kummiminia risasi kama mvua, kisha wakamweka kwenye kiroba na kukiburuta kuelekea nje…
Winifrida alijikuta akipiga kelele kwa nguvu bila kujitambua, darasa zima wakageuka kumtazama kwa mshangao. Mwalimu pia aliacha kufundisha na kugeuka kumtazama kwa mshangao, hakuelewa nini kilikuwa kimemsibu Winifrida siku hiyo.
"Is she dreaming?” (Anaota?) Mwalimu Igembe aliwauliza wanafunzi wengine huku akishangaa sana.
Darasa lote wakacheka kwa nguvu, lakini kicheko chao kilikatika ghafla baada ya kumwona Winifrida akilia kwa hofu huku akitetemeka sana, na kabla hawajajua kilichokuwa kinaendelea walimwona akisimama na kutoka nje mbio huku akilia.
“Zaituni, mfuate ujue ana tataizo gani?” Mwalimu Igembe alimtaka mwanafunzi mmoja wa kike aliyekuwa rafiki mkubwa wa Winifrida kumfuata.
Zaituni aliinuka na kutoka nje haraka kumfuata Winifrida huku wanafunzi wengine wakibaki wamepigwa na butwaa. Darasa lote lilikuwa na utulivu mkubwa sana.
* * * * *
Saa nne kasorobo asubuhi, Sammy na Elli walikuwa wanaingia katika ofisi za West Car Rentals zilizopo kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo la ghorofa mbili lililoko katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi eneo la Upanga Mashariki, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kujadiliana kuhusu mwenendo wa biashara ya Sammy hatimaye walikubaliana kwenda kumwona rafiki wa Elli aliyemiliki kampuni ya ukodishaji magari kwa ushauri zaidi, wakiamini kuwa Sammy angejifunza mengi na pengine kubadili mtazamo wake kuhusu biashara ya teksi.
Walipoingia ndani waliurudishia mlango taratibu na kusimama wakiwatazama watu sita waliowakuta mle ndani wakiwa wamekaa kwenye makochi, katika eneo la mapokezi ya ofisi ile, kati yao Waafrika walikuwa wawili vijana na wazungu wanne, wanawake wawili na wanaume wawili.
Wale watu waliokuwa mle ndani waligeuza shingo zao kuwatazama Sammy na Elli, kasoro mwanadada mmoja aliyeonekana kutingwa mno na shughuli kwenye kompyuta yake.
Mwanadada yule aliitwa Cynthia West, alikuwa na umri wa miaka 25, sura yake ilikuwa ndefu kiasi na pua ndogo ndefu. Alivaa sketi fupi iliyoishia sentimita chache juu ya magoti yake, ilikuwa nyeusi yenye miraba myeupe, blauzi nyeupe ya mikono mirefu na viatu vyeusi vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio
Alikuwa chotara wa kizungu mwenye shingo ndefu kiasi iliyobeba mabega ya kike na shingoni alivaa kidani cha dhahabu kilichoning’inia kifuani kwake na kuzama katikati ya uchochoro wa matiti yake ya ukubwa wa wastani.
Elli na Sammy waliwasalimia kwa Kiswahili wale watu waliowakuta mle ndani. Ni wale Waafrika pekee walioitikia ile salamu kwa pamoja, kasoro wale wazungu na yule mwanadada aliyeko kwenye kompyuta.
Kisha Sammy na Elli waliwasalimia wale wazungu kwa Kiingereza huku wakipunga mikono yao ya kulia na kuwafanya wale wazungu waitikie kwa bashasha zote.
Muda huo yule mwanadada aliyeko kwenye kompyuta aliinua uso wake mara moja na kuwaangalia Sammy na Elli. Macho yake yakagongana na yale ya Elli na Sammy. Yule mwanadada akaachia tabasamu pana na kurudisha macho yake kwenye kompyuta.
“Cynthia, hujambo dada’angu?” Elli alimsalimia yule binti kwa bashasha.
“Sijambo, kaka Elli, shikamoo,” Cynthia alisema huku akiacha kuchapa huku akiendelea kutabasamu.
“Marahaba. Pole na kazi,” Elli aliitikia huku akimsogelea.
“Asante, karibuni sana,” Cynthia aliitikia kisha akageuza shingo yake kumtazama Sammy huku akiendelea kutabasamu.
“Shikamoo,” alimsalimia Sammy kwa hesima zate.
“Marhaba, za kazi?” Sammy aliitikia huku naye akitabasamu.
“Nzuri,” Cynthia alisema huku akiyarudisha macho yake kwenye kompyuta mara moja na kuyarudisha tena macho yake kuwaangalia wageni wake huku akionekana ni mtu mwenye furaha muda wote.
Kabla Elli hajamuuliza Cynthia chochote mlango wa ofisi ile ulifunguliwa na mwanamume mmoja mnene na mrefu aliyefuga rasta aliingia. Alikuwa pia chotara wa kizungu na aliitwa McDonald West. Alipowaona Elli na Sammy aliwasogelea haraka huku akimtazama Elli kwa mshangao kama vile hakuwa ametegemea kumwona pale muda ule.
“Umepaa?” McDonald alimdaka Elli juu kwa juu bila hata ya salamu.
“Wala sijapaa, barabara tuliyojia haikuwa na foleni kabisa, askari wa usalama barabarani walikuwa wakiziita gari, nadhani kuna mkubwa fulani alikuwa anaandaliwa kupita,” Elli alisema huku akinyoosha mkono wake kumsalimia McDonald. Wakasalimiana kwa furaha kisha McDonald aliwakaribisha ofisini kwake.
Kilikuwa ni chumba cha ofisi cha ukubwa wa kawaida chenye samani chache muhimu za kiofisi. Kulikuwa na zulia lenye rangi za bendera ya taifa la Tanzania sakafuni, meza kubwa ya kiofisi ambayo juu yake kulikuwa na kompyuta aina ya Acer i5 na kioo cha flat, kiti kirefu cha ngozi halisi cha kiofisi chenye magurudumu madogo yaliyokiwezesha kusogea, na kilikuwa kinazunguka.
Mbele ya ile meza kulikuwa na viti viwili pamoja na kochi moja la sofa kwa ajili ya wageni, meza ya kioo ya pembe nne na chini ya meza ile kulikuwa na magazeti na majarida kadhaa yaliyoandikwa “Dar Guides”. Juu ya meza ile kulikuwa na vitabu, nakala chache za magazeti ya siku ile na nakala kadhaa za ramani kubwa ya Tanzania ikionesha maeneo ya vivutio vya utalii.
Kwa pembeni kulikuwa na rafu iliyopangwa vitabu na majarida chungu nzima ya utalii na ukutani kulikuwa na ramani kubwa ya Tanzania, yenye kuonesha maeneo mbalimbali yenye vivutio. Elli na Sammy waliketi kwenye viti vilivyokuwa mbele ya meza ya McDonald.
“Uliponipigia simu nilikuwa maeneo ya Muhimbili nikadhani huenda ningekuwahi, enhe nipe habari?” McDonald alisema baada ya Elli na Sammy kuketi kitako.
“Ni kama nilivyokueleza, huyu ni ndugu yangu, anaitwa Sammy…” Elli alianza kuelezea huku akimwoneshea Sammy kwa McDonald.
“Sasa, ngoja kwanza niwatoe hawa jamaa hapo mapokezi, wametokea Uswisi jana na walipaswa kuwa safarini kuelekea Iringa leo hii…” McDonald alisema na kuinuka, akatoka nje ya ofisi yake akiwaacha Sammy na Elli.
Muda huo huo simu ya Sammy ilianza kuita, alipoiangalia kwa makini akagundua kuwa ilikuwa simu kutoka kwa Dk. Masanja. Sammy alisita kidogo kisha akaamua kuipokea.
“Hello!” alisema mara tu alipoiweka kwenye sikio. Akasikia mwangwi wa sauti yake ukimrudia, akashtuka. Hii ilimaanisha kuwa simu ilikuwa imewekwa sauti ya juu ‘Loud speaker’ ili kumwezesha mtu au watu wa upande wa pili kusikia yanayoongelewa upande wa pili wa simu pasipo kuiweka sikioni.
“Hujambo, kijana wangu?” ilikuwa sauti ya Dk. Masanja aliyeongea kwa sauti tulivu.
“Sijambo, shikamoo.”
“Marhaba, vipi unaweza kuwa na nafasi ufike hapa ofisini kwangu leo?” Dk. Masanja alisema kwa sauti tulivu.
“Leo! Sidhani kama nitaweza kufika, nipo mbali kidogo, labda kesho kama itawezekana,” Sammy alisema huku akionesha kusita. Akasikia sauti ya Mr. Oduya ikiongea upande wa pili wa simu kumtaka Dk. Masanja amuulize alipo ili wamfuate. Sammy alishtuka kidogo, hata hivyo hakutaka kumwonesha Elli kuwa alishtuka.
“Kwani upo wapi, naweza hata kukufuata huko huko uliko!” Dk. Masanja alimuuliza Sammy.
Sammy alibaki kimya kwa muda akifikiria nini aongee, kwani alianza kuhisi kuwa kulikuwa na jambo lisilo la kawaida likiendelea. Alikumbuka jinsi alivyogombana na Mr. Oduya walipokutana ofisini kwa Dk. Masanja pale alipomtaka awe mshirika wake. Akajiuliza, huyo mzee alikuwa anamtakia nini!
“Sammy, are you there?” Dk. Masanja aliuliza kwa wasiwasi baada ya kuona kimya.
“Mmh… kwani ulikuwa unasemaje mzee, wangu? Labda naweza kukujibu hata humu kwenye simu.”
“Ah, kuna mambo haipendezi kuyaongea kwenye simu, ndiyo maana nilitaka kujua upo wapi!”
“Kuna tatizo lolote?” Sammy aliuliza huku akikunja sura yake na kuminya midomo.
“Hakuna, kuna mambo fulani nataka nikushirikishe,” Dk. Masanja alisema na kushusha pumzi.
“Unishirikishe?” Sammy aliuliza huku akiwa bado amekuja sura yake.
“Ndiyo, kwani kuna ubaya kukushirikisha? Au mimi na wewe tumeshakuwa na uadui siku hizi?”
“Hakuna ubaya, lakini kwa leo haitawezekana. Nipo nje ya mji na ninatarajia kurudi kesho.”
“Kesho saa ngapi nikutegemee?”
“Ngoja nione halafu nitakujulisha,” Sammy alisema na kukata simu, akashusha pumzi za ndani kwa ndani. Elli alimtazama kwa makini.
(65)
“Nani?”
“Dk. Masanja, meneja mkuu wa Udzungwa Beach Resort, eti anataka kuniona!”
“Sasa, kwani…” Elli alitaka kusema neno lakini akakatizwa na mtu aliyefungua mlango wa ile ofisi. Wote wakageuka na kumwona McDonald akiingia.
* * * * *
Winifrida alipotoka darasani alikimbilia nyuma ya jengo la darasa huku akilia kilio cha kwikwi na kusimama ukutani, aliyazungusha macho yake kutazama huku na kule akihisi kijasho chembamba kikimtoka licha ya kuwa eneo lile lilikuwa na upepo na ule ulikuwa ni msimu wa baridi. Moyo wake ulikuwa umepoteza kabisa utulivu.
“C’mon, Winnie, just relax,” alijiambia mwenyewe akijipa moyo kuwaasiwe na wasiwasi. Alivuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani kisha akazishusha taratibu huku akiminya midomo yake yenye maki.
“Relax baby, things gonna be alright…” Winifrida alijiambia kwa sauti kana kwamba alikuwa akimwambia mtu mwingine. Kisha alianza kujifuta jasho kwa kitambaa laini kilichokunjwa kwa umaridadi.
Muda huo huo akamwona Zaituni akimjia huku akiwa na wasiwasi. Zaituni alimsogelea na kabla hajasema chochote Winifrida alimwashiria kuwa amwache kwanza.
Zaituni alitii, Winifrida akaendelea kufuta machozi huku Zaituni akimtazama kwa mshangao. Walibaki kimya kwa kitambo kirefu kila mmoja akiwa anatafakari, kisha Winifrida alishusha pumzi za ndani kwa ndani.
Zaituni hakuweza kuvumilia alimuuliza Winifrida kama alikuwa na tatizo lolote huku akiwa amemtulizia macho usoni. Winifrida hakutaka kuongea hivyo alimweleza Zaituni kuwa hakujisikia vizuri na alihitaji kwenda nyumbani kupumzika.
* * * * *
Saa sita mchana, Joyce alishuka kutoka kwenye teksi na kumlipa dereva wa teksi fedha yake kisha akaanza kupiga hatua zake taratibu na kwa mwendo wa madaha akilisogelea jengo la Nuru TV. Muda huo alikuwa amevaa gauni zuri la kitenge lililodariziwa vizuri kwa nyuzi za dhahabu na kuushika mwili wake wenye umbo maridhawa la namba nane.
Mkononi alikuwa amevaa bangili kadhaa za pembe, kilemba kikubwa kichwani na begani kwake alikuwa ametundika mkoba mzuri wa kike wa pundamilia uliomgharimu fedha nyingi.
Wakati akitembea aliliona gari dogo aina ya Range Rover Sport L494 la rangi ya bluu la mwanamuziki Dynamo Plus likiingia katika viunga vya maegesho vya jengo la Nuru TV na kuegeshwa kwenye eneo lile
Joyce alisimama huku akijishika kiuno chake, alionekana kuwa na shauku ya kuonana na mwanamuziki Dynamo Plus ambaye muda huo alikuwa anashuka kutoka kwenye gari lake akiwa na watu wengine wawili. Mlinzi wake na meneja wake, Bob Tole.
Dynamo Plus alikuwa amevaa suruali ya jeans rangi ya bluu ya kubana iliyochanwa chanwa maeneo ya mapajani hadi kwenye magoti na kuacha matobo, fulana ya kata mikono na jaketi la bluu juu yake. Usoni alivaa miwani mikubwa ya jua iliyoficha macho yake, kofia aina ya kapelo kichwani na mkononi alikuwa ameshika simu mbili kubwa za kisasa.
Aliposhuka kwenye gari alianza kupiga hatua kubwa akielekea ndani ya jengo huku akiwa amewekwa katikati na mlinzi wake aliyekuwa kushoto kwake na meneja wake, Bob Tole kulia kwake. Joyce alimsogelea haraka huku akiachia tabasamu pana, akamdaka juu kwa juu bila hata salamu.
“Afadhali nimekuona, ninataka kukushirikisha kwenye project yangu…” Joyce alisema huku akinyoosha mkono wake kumsalimia Dynamo Plus. Dynamo Plus naye alinyoosha mkono wake huku akiachia tabasamu.
“Project gani tena, dada Joy?” Dynamo Plus aliuliza huku akilamba lips zake kubwa.
“Ngoja tuingine ndani nikupe proposal yangu… kwa kifupi nataka tuingie mkataba ili uwe unatumia mavazi yangu kwenye maonesho yako, najua kila mmoja wetu atabenefit. Wewe utapata mavazi bure kutoka kwangu lakini utasaidia kunitangazia biashara. Sijui unasemaje?” Joyce alisema huku akimtulizia macho yake Dynamo Plus.
“Mmh!” Dynamo Plus aliguna kidogo huku akiminya midomo yake mikubwa, kisha aligeuza shingo yake kumtazama Bob Tole huku akikunja sura yake, alionekana kufikiria kidogo, ingawa hakuonesha kukubaliana na wazo hilo.
Kilizuka kitambo kifupi cha ukimya. Joyce aliendelea kumtulizia macho yake akiwa na shauku ya kusikia majibu yake.
“Si wazo baya lakini sidhani kama itawezekana,” Dynamo Plus alisema huku akimtazama Bob Tole na kutingisha kichwa chake taratibu kuonesha kutokukubaliana na wazo la Joyce, kisha alianza kupiga hatua taratibu kueleka ndani.
Joyce alishusha pumzi ndefu akionesha kukata tamaa, hata hivyo alimfuata Dynamo Plus taratibu.
“Nadhani ingekuwa busara kama ungeiona kwanza proposal yenyewe kabla hujaikataa offer yangu,” Joyce alisema huku akimshika Dynamo Plus begani.
Dynamo Plus aliachia tabasamu na kuilamba tena midomo yake huku akimtupia jicho Bob Tole kama aliyekuwa anatafuta ushauri.
“Nadhani si wazo baya, tuione kwanza proposal yake kabla ya kuamua,” Bob Tole alishauri.
“Okay, utampatia meneja wangu aione kwanza, halafu tutajua la kufanya,” Dynamo Plus alimwambia Joyce kisha akaelekea kwenye chumba kimoja cha studio za Nuru TV.
* * * * *
Katika barabara ya Morogoro kwenye majengo ya Umoja wa Vijana mwanadada Nyaso Gilbert alikuwa anatokea ndani ya jengo dogo lililo upande wa barabara ya Morogoro, kisha akaanza kutembea haraka huku akiyatupa macho yake huku na kule kutafuta teksi.
Nyaso alikuwa amevaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu mpauko iliyombana kiasi na kulichora vyema umbo lake refu maridhawa lenye tumbo dogo na kiuno chembamba na juu alivaa blauzi ya rangi ya pinki. Shingoni alivaa kidani cha dhahabu chenye herufi “N”.
Miguuni alikuwa amevaa raba ngumu za rangi ya bluu na begani alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi ya bluu wa thamani kubwa. Uso wake ulikuwa umefichwa na miwani myeusi.
Muda huo huo aliliona gari aina ya Cadillac DeVille la muundo wa kizamani lililokuwa na kibao chenye maandishi ya “Taxi” juu yake likisimama mbele ya jengo la Shree Tanzania Swaminarayan Mandal, jirani na jengo alilokuwa akitokea, kisha watu wawili vijana wenye asili ya Kiasia wakashuka na kumlipa dereva.
Baada ya wale watu kushuka gari lile lilianza kuondoka taratibu kutoka eneo lile na kuifuata barabara ya Morogoro, Nyaso aliyekuwa akitembea kwa mwendo wa haraka kuelekea kule lilipokuwa gari alianza kupunga mkono wake juu kumwashiria dereva asimame.
“Taxi! Taxi!” Nyaso aliita kwa nguvu wakati lile gari likianza kumpita na kumfanya Sammy akanyage breki na kuliegesha gari lake kando ya barabara, akamsubiri huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
Nyaso alilikimbilia gari na alipolifikia akafungua mlango wa nyuma na kuutupia mkoba wake kwenye siti kisha akaingia na kuketi huku akihema kwa nguvu.
“Nipeleke Makumbusho,” Nyaso alisema huku akishusha pumzi ndefu. Sammy aliliondoa gari lake taratibu bila kusema neno akaifuata barabara ya Morogoro hadi alipofika usawa wa viwanja vya Tanganyika Legion, kwenye taa za kuongozea magari barabarani katika eneo la Bakhresa, akakata kuingia barabara ya Mazengo.
Aliifuata barabara ya Mazengo na mbele kidogo akaikuta barabara ya Faya iliyokatiza kutoka kushoto kuelekea upande wake wa kulia, akaivuka na kuendelea mbele hadi alipoukuta mtaa wa Kibasira, akakata kushoto kuifuata ile barabara na mbele kidogo akaukuta mtaa wa Isevya ulioingia kulia kwake.
Aliifuata barabara ile ya Isevya akipita nyuma ya viwanja vya Don Bosco na kwenda kutokea barabara ya Malik. Hapo akakunja na kuingia kushoto akiifuata ile barabara ya Malik na mbele kidogo akaikuta barabara ya Umoja wa Mataifa iliyowapeleka hadi kwenye taa za kuongozea magari barabarani za Sarenda.
Hapo Sarenda akakunja na kuingia kushoto akiifuata barabara ya Ali Hassan Mwinyi, na safari ya kuelekea Makumbusho ikaendelea. Muda wote walikuwa kimya na hakuna yeyote kati yao aliyeonekana kumfahamu mwingine, japo Sammy alikuwa mume wa Joyce na Nyaso alikuwa msaidizi wa Joyce.
Nyaso alitoa simu yake ya mkononi na kutafuta namba za Joyce kisha akapiga simu na kuiweka kwenye sikio lake la kushoto huku akiuma midomo yake, baada ya simu kuita kwa sekunde kadhaa alisikia simu ikipokelewa na Joyce.
“Da’ Joy, nimefanikiwa na sasa narudi, jiandae nakuja kukuchukua twende zetu Ubungo Plaza,” Nyaso alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
Sammy alimtupia jicho Nyaso kupitia kioo cha katikati cha gari lake cha kuangalia nyuma. Alimtazama kwa makini sana na kukunja sura yake akionekana kujiuliza kama alikwisha muona sehemu yoyote. Hata hivyo hakuweza kumfahamu, hivyo safari iliendelea huku wote wakiwa kimya.
Gari lilipofika eneo la Makumbusho Nyaso alimwonesha Sammy eneo ambalo alipaswa kusimamisha gari lake, ilikuwa ni kando ya barabara ya Bagamoyo jirani na jengo la Nuru TV. Sammy hakuzima injini ya gari, alijiegemeza kwenye siti yake kisha alimtupia jicho Nyaso aliyeonekana akiangaza macho yake kutazama kwenye jengo la Nuru TV, kisha akatoa tena simu yake na kupiga namba ya Joyce.
“Da’ Joy, njoo basi nimeshafika. Nipo hapa kando ya barabara nakusubiri… haya fanya fasta basi,” Nyaso alisema huku akiminya midomo yake.
Sammy aliyatupa macho yake kutazama kule alikokuwa akiangalia Nyaso na kumwona mkewe Joyce akitokea ndani ya jengo la Nuru TV akiwa ameshika simu yake na kuanza kutembea haraka huku akitupa macho yake kuangalia huku na huko.
Sammy alishtuka sana na kujikuta akipagawa, moyo wake ulishikwa na mfadhaiko na kuyasahau mapigo yake kwa nukta chache. Mapigo yalipoanza tena alivuta pumzi ndefu, akazishusha taratibu huku mwili wake ukiingiwa na ganzi iliyoyafanya maungo yake yazizime!
Sammy alimtazama Joyce kwa macho yaliyojaa hofu kisha aligeuka kumtazama Nyaso, akataka kumuuliza jambo lakini akasita na kugeuka tena kumtazama Joyce kwa hofu. Muda huo hakujua afanye nini. Alijiwa na mawazo kuwa aondoe gari haraka, lakini sauti nyingine ikamwambia hakuwa na haja ya kuondoka bali asubiri, kwani kuna kitu kilikuwa mbioni kutokea.
Akiwa katika kutafakari mara akamwona mwanamuziki Dynamo Plus akitoka haraka ndani ya lile jengo na kuanza kumwita Joyce. Joyce alisimama kugeuka kumsubiri Dynamo Plus huku sura yake ikiwa na shauku ya kusikia uamuzi wake juu ya ile proposal aliyompa.
“Meneja wangu amenihakikishia kuwa proposal yako imekaa vizuri sana, naomba tupate lunch huku tukizungumza vizuri namna tunavyoweza kufanya kazi pamoja,” Dynamo Plus alimwambia Joyce huku akitabasamu.
Joyce alionekana kufurahi sana, alijikuta akimkumbatia Dynamo Plus huku akiachia tabasamu pana, kisha alimwachia na kumshika mkono, wakaongozana kuelekea kwenye kantini iliyopo nyuma ya jengo lile huku wakiwa wameshikana mikono na kutembea kama wapendanao.
Sammy alishusha pumzi za ahueni huku akiyakaza macho yake kuwatazama kwa makini. Alifurahia kwa kitendo cha Joyce kurudi alikotoka lakini hakufurahishwa kwa kitendo cha kumwona akiwa na mwanamuziki Dynamo Plus. Alitamani ashuke na kwenda kuwazaba makofi lakini akajizuia sana. Kwa kweli hakujua afanye nini!
Mara simu ya Nyaso ikaanza kuita, Nyaso aliitazama kwa makini na kuipokea kisha akaipeleka moja kwa moja kwenye sikio lake.
“Nyaso, kuna jambo la muhimu sana limejitokeza, ni kuhusu ile proposal yetu hivyo natakiwa kuongea na Dynamo Plus tuone cha kufanya, wewe nenda tu ukaniwakilishe,” Joyce alisema.
“Okay, basi haina tatizo da’ Joy…” Nyaso aliitikia na kukata simu kisha akamtazama Sammy ambaye alikuwa bado anaangalia kule kwenye jengo la Nuru TV huku donge la wivu likiwa limemkaba shingoni.
“Twende Ubungo Plaza, Boss wangu amepata dharura,” Nyaso alimwambia Sammy na kujiegemeza kwenye siti.
Sammy aligeuka kumtazama Nyaso kwa makini, alitaka kumuuliza kitu lakini akasita na kushusha pumzi, kisha akaliondoa gari lake taratibu pasipo kusema kitu huku akiendelea kuangalia kule walikoelekea Joyce na Dynamo Plus.
Usikose kuifuatilia taxi ili kujua inaelekea wapi...
(67)
Aliendesha gari lake huku donge kavu la wivu uliochanganyika na hasira likiwa limemkaba kooni, alijisikia vibaya sana, alidhani kwamba alikuwa amemruhusu mkewe kutimiza ndoto yake kumbe alikuwa akimsogeza mbuzi karibu na chui!
Ilibaki kidogo tu apate ajali barabarani, mawazo yake yalikuwa kwa mkewe Joyce na Dynamo Plus yaliyomfanya akose umakini barabarani, kichwa chake kilikuwa kimevurugwa.
Sasa alikuwa na mgogoro wa ndani kwa ndani (interpersonal conflict), sauti moja ilimwambia arudi akamfumanie mkewe, kisha awape kipigo wote wawili, lakini sauti nyingine ilimwambia asifanye hivyo kwa kuwa hakuwa na uhakika kama walikuwa na uhusiano wa kimapenzi. Isitoshe angeweza kujiharibia kwa kuwa Joyce angegundua kuhusu siri yake ya kuendesha teksi.
“Vipi kaka, kuna tatizo lolote?” Nyaso alimuuliza Sammy akiwa ameitambua hali ya kukosa umakini iliyojitokeza baada ya kutaka kusababisha ajali kwa mara ya pili wakati wakivuka taa za kuongozea magari barabarani katika eneo la Tume ya Sayansi na Teknolojia.
Sammy alijishtukia na kumtazama Nyaso, akaachia tabasamu huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani, “Wala hakuna tatizo,” alijibu na kuongeza mwendo akiitafuta Bamaga.
* * * * *
Saa tatu kasoro robo ya usiku iliwakuta Sammy, Joyce na Winifrida wakiwa kwenye meza ya chakula wakila kimyakimya, kila mmoja alikuwa akitafakari lake. Muda huo Pendo alikwisha kula tayari alikuwa chumbani amelala.
Muda wote wakati wa mlo Sammy alikuwa anawaza mambo mbalimbali yaliyomjia kichwani kwake. Alifikiria kuhusu mwelekeo wa biashara yake baada ya mazungumzo yake na McDonald West na kudhani kuwa muda mwafaka wa kuongeza magari mengine mawili ulikwisha fika.
Changamoto kubwa ilikuwa ni jinsi ya kupata magari mazuri na ya kipekee ambayo yangemwezesha kuukabili ushindani. Alitamani sana kupata magari kama lile alilokuwa nalo sasa. Pia aliwaza kuhusu kile alichokishuhudia kule Nuru TV, alipomwona mkewe akiwa ameongazana na mwanamuziki wa kizazi kipya, Dynamo Plus huku wameshikana mikono.
Donge la hasira lililochanganyikana na wivu lilikuwa bado limemkaba kooni kwake. Lakini pamoja na mawazo kumwandama, chakula kilishuka vilivyo kutokana na ustadi wa mapishi ya mkewe. Hata hivyo, muda wote Joyce hakujua kilichokuwa kikiendelea kwenye akili ya mumewe, yeye alifurahia chakula alichopika mwenyewe.
Winifrida alikuwa mtulivu sana muda wote wa chakula tofauti kabisa na kawaida yake, alimtazama Sammy kwa jicho la kuibia huku akionekana kuwa mbali kimawazo. Alikuwa akijaribu kulinganisha maisha ya kaka yake Sammy na kile alichokishuhudia kwenye video ya mauaji na kuzidi kuchanganyikiwa.
Walimaliza kula na Winifrida akatoa vyombo, kisha walishushia matunda na baadaye maji, halafu Winifrida aliwaacha akaingia chumbani kwake kujipumzisha.
Sammy na Joyce walikwenda kuketi sebuleni kwenye masofa kila mmoja akiwa na kijiti mdomoni akijaribu kuondoa masalio ya nyama pamoja na masalio mengine kwenye meno. Waliketi pale kwani Joyce alitaka kufuatilia mfululizo wa mchezo wa kuigiza wa “Gereza la Kifo” uliorushwa kwenye runinga.
Hata hivyo, mawazo ya Sammy hayakuwa kwenye runinga, alikuwa anapanga jinsi ya kumuuliza mkewe kuhusu uhusiano wake na mwanamuziki Dynamo Plus.
Hakutaka kukurupuka kwani angeweza hata kujichongea endapo mkewe angegundua kuwa ile teksi iliyokusudiwa kumchukua na kumpeleka Ubungo Plaza ni gari la mumewe Sammy, na hata aliyekuwa akiendesha teksi ile hakuwa mwingine zaidi ya mumewe mwenyewe.
Ni dhahiri uso wa Sammy haukuonesha furaha ingawa alijitahidi kuwa na furaha mbele ya Joyce.
Joyce aliligundua jambo hilo baada ya kumtupia jicho mara kwa mara, alijaribu kuivumilia hali ile lakini alishindwa na kuamua kuvunja ukimya.
“Naona leo ni kama huna furaha, nini kimekukera, mume wangu?” Joyce aliuliza kwa sauti tulivu huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Sammy, alimwangalia kwa makini.
Sammy alimtazama mkewe na kujaribu kutabasamu lakini bado alishindwa kuficha wivu na hasira. Alipumua kwa nguvu, na kujiegemeza kichovu kwenye sofa huku akimtazama mkewe kwa umakini. Wivu na udadisi vilimsonga kwa pamoja. Alihisi labda mkewe alishampa ‘tunda’ Dynamo Plus au mwanaume mwingine. Donge la hasira na wivu lilizidi kumkaba kooni.
Joyce alipinda midomo yake upande wa kushoto na kushusha pumzi ndefu kama aliyemaliza mbio ndefu.
“Unajua, kwa siku za karibuni, hasa siku hizi mbili nimeona umebadilika kwa kiasi fulani tofauti na kawaida yako, sijajua tatizo ni nini hasa!” Joyce alisema huku akiminya midomo yake kisha akashusha pumzi.
“Inawezekana nikawa na mabadiliko lakini ni kwa sababu nakupenda sana. Mwenyewe unajua jinsi tulivyoanza uhusiano wetu hadi kufunga ndoa…” Sammy alisema na kusita kidogo, akavuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu akionekana kutafakari kwa sekunde kadhaa kabla hajayahamishia macho yake kumtazama tena Joyce ambaye muda huo alikuwa kimya akimtazama kwa makini.
“Nimekuruhusu kwa moyo mmoja kwenda kwa Madame Norah ili uweze kutimiza ndoto yako ya siku nyingi, ila nadhani uhuru niliokupa unaweza kuniumiza siku moja…” Sammy alianza kufunguka lakini Joyce alimkatisha kwa upole huku akionekana kushtuka kidogo.
“Kwa nini unasema hivyo, kwani umeona nini kutoka kwangu?” Joyce aliuliza huku uso wake ukionesha mshtuko wake.
“Hapa si suala la nimeona nini kwako bali unapaswa kutambua kuwa wewe ni mke wangu wa ndoa, ni mimi mwenye haki ya kuushika na kuutomasa huo mwili wako. Nakuomba jichunge sana usije kurubuniwa na wasanii na baadaye ukanisaliti kisa unatimiza ndoto…” Sammy alisema huku akijizuia kukasirika.
(68)
“Sammy, naona sasa umefika mbali jamani! Kwa nini unifikirie hivyo? Unajua tulikula kiapo cha uaminifu siku ile kanisani. Ingawa siwezi kusema kuwa sikumbani na vishawishi… nakumbana navyo na wakati mwingine najuta ni kwa nini nilizaliwa mrembo, lakini sijawahi kukusaliti. Kwanza ni dhambi kubwa!” Joyce alisema kwa huzuni huku akimtazama Sammy kwa makini.
Walitazamana kwa kitambo kifupi. Joyce alikuwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Sammy huku akionekana kuhuzunishwa sana na maneno ya mumewe. Alishusha pumzi.
“Sipendi kukuona katika hali hii. Najihisi kuumia sana unapoanza kuniwazia mambo ambayo sifikirii kuyafanya. Labda kama hupendezwi mimi kwenda kwa Madame Norah au kuna mambo fulani umeyaona kwangu ni vyema ukayaweka wazi badala ya kuniongelea kwa mafumbo…” Joyce alisema kwa sauti iliyoonesha kutetemeka baada ya donge la simanzi kuanza kumkaba kooni.
“Ngoja nikuulize… hivi tokea tuoane hujawahi kunisaliti? Hujawahi kutongozwa huko nje kweli? Achana na hawa wasanii wanaofinyafinya macho kila wakiona mwanadada mrembo, yaani mtu akomae kabisa?” Sammy alimuuliza Joyce akimtulizia macho usoni ili aweze kumsoma.
Joyce alionesha kushtuka sana na uso wake ulionesha maumivu makubwa. Alifungua mdomo na kutaka kusema lakini maneno yakawa hayatoki.
“Labda nifupishe mambo, kuna mtu amekuona ukiwa na mwanamuziki Dynamo Plus mnatembea mkiwa mmeshikana mikono kwa mahaba, unaweza kunieleza kuna nini kinaendelea kati yako na huyo kijana?” Sammy aliuliza kwa sauti tulivu akijitahidi kuzuia hasira.
Uso wa Joyce ulikuwa bado unaonesha maumivu makubwa, alimtazama Sammy kwa kitambo na kutingisha kichwa chake taratibu huku akivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu.
“Wala hakuna chochote kibaya kinachoendelea kati yetu,” Joyce alisema kwa sauti iliyoashiria huzuni.
“Kumbe kuna nini! Kama hakuna kibaya kinachoendelea basi kuna kizuri kinaendelea, unaweza kunieleza hicho kizuri ni kipi?” Sammy aliuliza huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Joyce.
“Unajua… sikuwa nimekueleza kabla kwa kuwa sikujua ni msanii gani angekubali proposal yangu, isitoshe ni msaidizi wangu ndiye niliyekuwa nimemkabidhi jukumu hilo. Kwa kifupi kuna dili huenda nikaingia na Dynamo Plus la kutangaza mavazi yangu. Leo nilipoonana naye tulipanga na kukubaliana tukutane tena kesho ili kuona namna kila mmoja wetu anaweza kufaidika na mkataba huo kabla hatujausaini,” Joyce aliongeza kwa upole kabisa huku akimtazama Sammy kwa makini.
Japo alijitahidi kujielezea vizuri mbele ya Sammy lakini uso wake ulikuwa umesawajika. Sammy alibaki kimya akimtazama kwa utulivu huku akianza kujilaumu moyoni baada ya kuona kuwa alikuwa amemfikiria vibaya mkewe.
Joyce alishusha pumzi, hamu ya kuangalia mchezo wa kuigiza wa “Gereza la Kifo” kwenye runinga ilikuwa imetoweka, hakuweza tena kuuangalia hadi kipindi kilipoisha na kingine kilikuwa mbioni kuanza. Sebule ilikuwa imegubikwa na ukimya, kila mmoja alikuwa akitafakari ya kwake.
Joyce alimsogelea Sammy, akaweka kiganja chake shavuni pa mumewe huku akimtazama kwa ukaribu. Wakatazamana. Joyce akajaribu kutabasamu lakini sura yake ilishindwa kuficha huzuni aliyokuwa nayo. Sammy aliliona hilo na kujikuta akiwa hana jinsi zaidi ya kumwomba msamaha mkewe kwa kumkwaza.
“Unajua… moyo wa mtu ni kichaka, mtu anakuwa na vitu vingi kichwani na moyoni. Sisi wanawake tunaishi katika mazingira magumu sana. Sikatai kuwa tunakumbana na vishawishi vingi na wakati mwingine mtu unashindwa ufanye nini, ila inakuwa siri yako,” Joyce aliongea kwa sauti ya kitetemeshi.
“Kwa maana hiyo, kuna wanaume wameshawahi kufanya mapenzi na wewe? Kwa hiari au kwa nguvu?” Sammy aliuliza kwa udadisi. Wivu ulianza kumsonga moyoni.
“Sijamaanisha hivyo.”
“Sawa, vyovyote iwavyo, naomba usije ukanisaliti, nitakapogundua nitaumia sana,” Sammy alisema kwa sauti tulivu iliyojaa hisia.
Joyce alitingisha kichwa taratibu na kuinamisha sura yake, hakutaka kumpa Sammy fursa ya kuona matone ya machozi yaliyoanza kumchuruzika machoni.
“Naomba uniruhusu niende kulala,” alisema na kunyanyuka bila kusubiri ruhusa, akambusu Sammy kwenye paji la uso na kuanza kupiga hatua akielekea chumbani.
“Mama Pendo, naomba ukae kidogo,” Sammy alimwambia Joyce mara alipoanza kuvuta hatua kuelekea chumbani, na bila hiyana Joyce alirudi akaketi na kuinamisha uso wake chini akijaribu kuyaficha machozi yaliyokuwa yakimtoka.
Sammy alimtazama kwa kitambo na kushusha pumzi akijaribu kujiaminisha kwamba ni yeye peke yake aliyekuwa akiyafaidi mapenzi matamu ya mkewe, ingawa hakuwa na uhakika kutokana na uzuri aliojaaliwa mkewe.
Joyce alikuwa bado amejiinamia. Sammy alitaka kusema neno lakini akasita baada ya kumwona mtangazaji Maximilian Njamba wa kipindi cha runinga cha ‘Mbunifu Wetu’ akitangaza huku akilionesha gari aina ya Cadillac DeVille lenye kibao cha “Taxi” juu yake.
Sammy alishtuka sana, aligeuza shingo yake kumtazama Joyce na kumwona akiinua uso wake, akainuka haraka na kusimama mbele yake kwa namna ya kumziba asiweze kuona kilichokuwa kinaoneshwa kwenye runinga, kisha alichukua rimoti haraka na kuzima runinga kabla Joyce hajaona.
Akamshika Joyce kwa upole na kumnyanyua taratibu kwa mahaba, lengo likiwa kumwongoza waelekee chumbani lakini akashituka sana baada ya kugundua kuwa mkewe alikuwa analia! Mwili wake ulikuwa ukitikisika kutokana na kilio cha kwikwi, alionekana alishindwa kujizuia kulia.
Joyce alipogundua kuwa Sammy ameyaona machozi yake akalipuka, alianza kulia huku akitamka maneno ambayo Sammy hakuweza kuyatafsiri, yalikuwa yamechanganyikana na kilio. Hali hiyo ilimtisha Sammy kwani haikuwahi kutokea hapo kabla. Maswali mengi yalipita ndani ya kichwa chake, akihofu huenda Joyce aligundua jambo kutoka kwake, au aliambiwa na Winifrida kuhusu kile alichokuwa amemficha.
“Dah! Hii sasa kali!” Sammy aliwaza huku akihisi ubaridi ukimtambaa mwilini.
Machozi yaliendelea kumtiririka Joyce. Aliinamisha uso wake chini huku akitia huruma. Alijitupa kifuani pa mumewe na kumkumbatia. Sammy naye alimkumbatia kisha alianza kumfuta machozi kwa kiganja chake cha mkono, akambusu katika paji la uso na kukilaza kichwa chake kifuani pake.
“Nini kimekusibu, mbona hata sielewi?” Sammy aliuliza kwa wasiwasi.
Kilio cha mkewe kilipungua na sasa alionekana kuweweseka. Sammy akaanza kumbembeleza huku akimwomba radhi kama kuna jambo lolote baya alilomkwaza huku akimsihi amueleze yaliyomsibu hadi kulia kiasi kile. Joyce alikusanya nguvu ili aweze kumweleza mumewe yaliyomsibu.
“Unajua, mume wangu, ghafla nimejikuta nikiwa kwenye wakati mgumu sana…” Joyce alianza kusema kwa sauti ya chini iliyobeba huzuni na mitetemo.
“Nimejaribu sana kujizuia nisilie mbele yako lakini nimeshindwa. Naona aibu hata kukueleza…” Joyce alisema na kuanza tena kulia lakini Sammy akambembeleza.
Joyce hakuona tena sababu ya kumficha kitu mumewe japo aliona aibu sana kumweleza. Alikusanya nguvu zote na kumtazama Sammy kwa huzuni, sura yake ilikuwa imesawajika.
“Ah… wacha tu nikuambie ukweli… ni kweli nilipanga kwenda kuonana na Dynamo Plus kesho, lakini…” Joyce alisita kidogo, akashusha pumzi huku akimtazama Sammy kwa wasiwasi. Alianza kuchezea vidole vyake huku akimtazama mumewe kwa machale.
“Sema, lakini nini?” Sammy alimsaili huku hisia mbaya zikianza kumwingia.
“Naomba usinichukie kwa kusema ukweli… nilikuwa nakwenda kuisaliti ndoa yetu kama njia ya kumshawishi kupata mkataba,” Joyce alisema na kuanza kulia tena.
Sammy alishtuka sana, alihisi mwili wake ukipigwa shot ya umeme kutokana na kile alichokisikia, japo angeweza kutarajia kitu kama hicho lakini hakutegemea kusikia kutoka kwa mhusika mwenyewe. Pamoja na mshituko, alijikaza na kuuma midomo, mapigo ya moyo wake yalikuwa yakienda mbio isivyo kawaida.
Muda wote Joyce alikuwa analia kilio cha kwikwi, Sammy alikuwa anamwangalia tu bila kufanya chochote. Sura yake kaikunja kwa hasira. Joyce aliendelea kulia kwa muda, kisha akajifuta machozi kwa kutumia upande wa kanga na kupiga magoti mbele ya Sammy ili kuomba msamaha.
Sammy alimsukuma kwa nguvu na kumfanya aanguke sakafuni chali, akashangaa sana kwa tukio lile. Alimtazama Sammy kwa hofu na kujikaza, akaacha kulia na kujikusanya kutoka pale sakafuni, akasimama.
“Baba Pendo, tafadhali usikasirikie, naapa haki ya Mungu sijawahi kukusaliti, sijui shetani gani alitaka kuniingia!” Joyce alisema kwa sauti ya chini ya kusihi kisha alianza kulia tena huku akifutika kichwa chake kwenye kifua cha mumewe.
“Hivi nyie wanawake mkoje, huyo mjinga mwenye mdomo mkubwa anawapa nini hadi mnazuzuka naye kiasi hiki? Au kutaka mkataba ni lazima mjiuze?” Sammy alihoji kwa ukali huku akimmuondoa Joyce kutoka kifuani pake. Alikuwa akihema kwa nguvu kutokana na hasira.
“Sasa nini kilichokufanya uniambie ukweli wakati ulifanya siri!” Sammy aliuliza huku akimkodolea macho Joyce.
“Nisamehe, mume wangu, najua unanipenda sana na kunijali ndiyo maana nimeshindwa kujizuia kulia mbele yako. Maneno yako yamenichoma sana hadi nimejiona mpumbavu, utadhani ulikuwa umeufunua moyo wangu ukaanza kuyasoma mawazo yangu, ningekuwa na moyo wa jiwe usingegundua chochote lakini moyo wangu ni wa nyama!” Joyce alisema huku akijikunyata mbele ya Sammy akiwa na hofu, hakuwahi kumwona Sammy ameghadhabika kiasi kile.
Muda wote Sammy alibaki kimya akiwa ameyatuliza macho yake usoni kwa Joyce. Macho ya Joyce hayakuficha chochote kiovu. Alikuwa ameuweka moyo wake bayana mbele ya mumewe.
“Nisamehe sana, mume wangu, naapa siwezi kukusaliti kabisa,” Joyce alisema kwa sauti ya huzuni.
Sammy alitaka kusema neno lakini akasita, moyo wa imani ukamwingia. Alimshika mkono Joyce na kumvutia kifuani kwake, akamkumbatia kwa kitambo, kisha akamwongoza kuelekea chumbani.
* * * * *
Saa nne usiku Mr. Oduya alikuwa ameketi kwenye ofisi yake binafsi ndani ya jengo lake la kifahari la ghorofa mbili lililokuwa katika eneo la Mikocheni jirani na Rose Garden. Lilikuwa jumba kubwa lenye uwa mpana na bustani ya kupendeza.
Ndani ya jengo hilo ndimo kulikuwa na ofisi pana yenye mazingira nadhifu na yaliyovutia kwa mpangilio wa samani za kisasa, ikiwa na zulia nene jekundu la manyoya sakafuni na meza ndefu ya ofisini yenye viti kumi na vinne. Viti saba upande wa kushoto na viti vingine saba upande wa kulia.
Mr. Oduya alikuwa ameketi kwenye kiti chake kikubwa cha kuzunguka kilichokuwa na magurudumu yaliyokiwezesha kusogea akiwa nyuma ya meza yake kubwa ya kiofisi mwisho wa ofisi ile upande wa kushoto. Alikuwa ameegemea kiti chake cha kiofisi akiwasikiliza wageni wake kumi na wanne.
Wageni hao walikuwa wajumbe wa kamati maalumu ya fitna na ushindi, muda huo walikuwa katika kikao maalumu chini ya uenyekiti wa Meneja Mkuu wa Udzungwa Beach Resort, Dk. Masanja na katibu alikuwa Balozi Mageuzi. Ajenda kuu ya kikao ilikuwa kupanga mikakati jinsi ya kumsaidia Mr. Oduya kushinda kinyang’anyiro cha kusaka nafasi ya kuteuliwa na Chama Cha Ukombozi kugombea urais wa nchi.
Katika muda ule, upepo mwanana ulikuwa unavuma kutokana na mvua ya rasharasha iliyokuwa inanyesha na kuyasonga songa mapazia marefu yaliyokuwa yamefunika madirisha matatu makubwa mle ofisini. Mara simu ya mkononi ya Mr. Oduya ikaanza kuita na kumshtua. Alipoitazama kwa makini akagundua kuwa mpigaji alikuwa mwanasheria wake, Adam Mafuru.
Mr. Oduya aliminya midomo yake huku akikunja sura, aliitazama saa yake ya mkononi huku akionekana kutafakari kidogo na kushusha pumzi, alijiondoa kutoka pale kwenye kiti alipokuwa ameketi na kuwataka radhi wageni wake, akatoka na kuelekea nje ya ofisi.
Alisimama ukumbini karibu na dirisha, akayatupa macho yake kuangalia nje na kuipokea ile simu kisha akaipeleka moja kwa moja kwenye sikio lake.
Mambo yanazidi kunoga, nini kitafuta baada ya hapo? Usikose kufuatilia kisa hiki cha kusisimua...
(70)
“Unasemaje?” alimdaka Mafuru juu kwa juu pasipo hata salamu.
“Boss, nimeliona gari!” Mafuru alisema kwa sauti iliyoonesha wasiwasi na yenye kitetemeshi.
“Gari gani?” Mr. Oduya aliuliza kwa pupa huku akiwatupia jicho wageni wake.
“Cadillac DeVille uliloagiza liteketezwe…” Mafuru alisema na kumfanya Mr. Oduya ahisi kama mwili wake ukiraruka vipande viwili. Moyo wake ulipiga mshindo mkubwa! Alihisi pumzi zikimpaa na moyo wake ukianza kwenda mbio isivyo kawaida.
“Una uhakika?” Mr. Oduya aliuliza akihisi labda hakuwa amemsikia vizuri. Muda huo pumzi zilizotoka hazikulingana na zile zilizoingia kwenye mapafu yake.
“Ndiyo, wa asilimia zote,” Mafuru alisema kwa msisitizo.
Mr. Oduya alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akiwa haamini alichokuwa akielezwa na Mafuru.
“Umeliona wapi?” aliuliza kutaka uhakika.
“Kwenye televisheni, kuna mtangazaji wa televisheni alikuwa analionesha kwenye kipindi chake cha Mbunifu Wetu…” Mafuru alisema na kumfanya Mr. Oduya ahisi kizunguzungu.
Alijiegemeza kwenye ukuta huku akipitisha mkono wake wa kulia kichwani akianzia kwenye paji la uso wake hadi kisogoni. Kwa mara ya kwanza alihisi kuogopa sana. Hakuwa na neno, kikazuka kitambo kirefu cha ukimya mzito, Mr. Oduya alianza kupiga hatua za taratibu kuzunguka pale ukumbini.
Habari ile aliyopewa na Mafuru ilikuwa imemshtusha sana. Taratibu ghadhabu ilianza kuchipua ndani yake.
“Una uhakika ni gari letu?” hatimaye Mr. Oduya aliuliza tena baada ya ukimya wa muda mrefu. Sauti yake ilikuwa ya kutetemeka kutokana na hofu na hasira kwa pamoja.
“Sana, hata rangi yake bado ni ileile haijabadilishwa, ndiyo maana nimekupigia simu, mzee,” Mafuru alijibu kwa sauti iliyoashiria wasiwasi mkubwa.
Kikapita tena kitambo kifupi cha ukimya, kisha Mr. Oduya akakata simu. Sasa alijiona yu hatarini kuliko hata hatari yenyewe. Akatafuta namba za Spoiler na kumpigia simu.
“Nakuhitaji hapa kwenye ofisi ya Mikocheni jirani na Rose Garden haraka iwezekanavyo!” Mr. Oduya alisema kwa sauti yenye kuashiria ghadhabu.
“Nipo mbali, bosi,” Spoiler alisema kwa sauti yenye wasiwasi kidogo.
“Silas!” Mr. Oduya aliita kwa kufoka kisha akapiga ngumi ukutani. “Uwe mbali ama karibu, nakuhitaji hapa Mikocheni haraka!” aliposema hivyo akakata simu yake na kurudi ofisini alikokuwa amewaacha wageni wake.
Alikuwa yu moto haswa na kichwa chake kilikuwa kinamgonga huku mikono ikimtetemeka. Alihisi baridi ya hofu ikipenya hadi kwenye mifupa na mapigo ya moyo wake yalidunda dabali. Muda ule alihisi hakuwa huru nafsini mwake hata kidogo. Alitamani kupiga yowe la hasira na sauti yake ikamsaliti. Kwa nini apige yowe, haoni kama angewapa watu faida?
Wageni wake walimtazama kwa mshangao mkubwa jinsi alivyobadilika. Ukimya mkubwa ulitamalaki ndani ya ile ofisi pana iliyojaa watu kumi na watano. Ulikuwa ukimya uliomfanya kila mtu mle ndani akiogope hata kivuli chake! Mr. Oduya aliketi kwenye kiti chake akiwa na fadhaa.
“Kuna tatizo lolote?” Balozi Mageuzi aliuliza baada ya kumwona Mr. Oduya akiwa amenywea kama aliyekuwa amepigwa na shoti ya umeme.
“Kuna tatizo dogo la kiufundi limejitokeza,” Mr. Oduya alijitutumua na kumjibu Balozi Mageuzi, moyo ulikuwa ukimwenda msobemsobe.
“Tatizo hilo linahusiana na masuala yetu ya siasa?” Dk. Masanja naye alimuuliza haraka huku akimkodolea macho kwa wasiwasi.
“Hapana, ni tatizo la kifamilia, natakiwa kulishughulikia haraka na kila kitu kitakuwa sawa,” Mr. Oduya alisema huku akijipa ujasiri uliokuwa umetoweka muda mfupi uliopita.
Kisha aliwaomba wajumbe waahirishe kikao ili apate muda wa kushughulikia jambo la dharura lililojitokeza usiku ule na kulikamilisha kabla hakujapambazuka. Baadhi ya wajumbe walijaribu kumdadisi lakini hakuwa tayari kuwaleleza jambo lenyewe. Hawakuwa na nanmna nyingine zaidi ya kukubali. Wakaondoka kwa makubaliano ya kukutana siku nyingine, katika sehemu nyingine itakayopangwa.
Alipobaki peke yake Mr. Oduya aliitazama saa yake ya mkononi kwa minajili ya kujua muda. Ilikuwa saa sita na robo usiku. Mishale ya saa na dakika kwenye simu ilimfanya azidi kupungukiwa subira. Zilikaribia kutimia saa mbili tangu alipomtaka Spoiler afike nyumbani kwake. Alisema yupo mbali, mbali ya wapi? Mr. Oduya alijiuliza.
Alitoka nje na kusimama chini ya mti wa kivuli kwenye uzio wa jumba lile, jirani na kilipo kibanda cha walinzi kando ya geti kubwa la kutokea. Muda ule eneo lile lilikuwa na ukimya mno.
Kulikuwa na watu wanne, Mr. Oduya mwenyewe, dereva wake Madjid na walinzi wake binafsi wawili waliokuwa makini kuhakikisha usalama upo. Hata hivyo, walinzi wale hawakushangaa kumwona Mr. Oduya akiwa pale muda huo akizunguka zunguka, mikono kaiweka nyuma na kichwa kakiinamisha chini.
Ilikuwa kawaida yake alipokuwa na mambo nyeti kuitumia nyumba ile kwa ajili ya kukutana na washirika wake, kwa mambo nyeti. Wakati mwingine alikuja pale alipokuwa amekorofishana na mkewe Dk. Oduya, kwani ilikuwa inatokea kiasi cha kumfanya mzee ashindwe kulala nyumbani.
Mara wakasikia muungurumo wa gari likija eneo lile na kusimama kwenye eneo maalumu la maegesho nje ya jumba lile. Kutokana na haraka aliyokuwa nayo, Mr. Oduya hakusubiri, alimtuma dereva wake achungulie nje kuona ni nani aliyekuwa amefika pale. Madjid alichungulia haraka kwa tahadhari na kumweleza Mr. Oduya kuhusu ujio wa Spoiler.
Spoiler alikuwa peke yake ndani ya gari na hakuteremka, alibaki kwenye usukani akiwa ametahayari. Mr. Oduya alitoka na kwenda kumkabili Spoiler. Alimtazama kwa macho yaliyokuwa yakiwaka kwa ghadhabu.
“Kwa nini uliniongopea?” Mr. Oduya alimuuliza Spoiler kwa sauti yenye ghadhabu.
Spoiler alishtuka sana, alimtazama Mr. Oduya kwa hofu akiwa haelewi kilichokuwa kinaendelea. Alifungua mdomo wake kutaka kuuliza lakini sauti yake ikamsaliti, hakuna kilichotoka mdomoni. Akapandisha mabega yake juu na kuyashusha.
(71)
“Gari ulilipeleka wapi?” Mr. Oduya aliuliza tena huku akionekana kuchemkwa kwa hasira. Alizidi kumkodolea macho Spoiler.
“Gari gani?” Spoiler aliuliza kwa mshangao uliochanganyika na wasiwasi.
“Cadillac DeVille nililoagiza liteketezwe miaka mitatu iliyopita.”
“Mbona lilikatwakatwa kisha likauzwa kama chuma chakavu!” Spoiler alisema huku mshangao ukiwa haujamtoka usoni.
“Una uhakika?” Mr. Oduya alimuuliza Spoiler akiwa bado amemtulizia macho yake usoni.
“Nilimpa kazi hiyo Jonas Odilo, yule jamaa wa duka la vipuri vya magari pale Shaurimoyo na alinihakikishia kuwa ameifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa kama nilivyomwambia.”
“Kama lilikatwakatwa mbona leo limeoneshwa kwenye televisheni. Kwanza kwa nini umwachie mtu kulikatakata wakati wakati nilikutaka uliteketeze mwenyewe na kisibaki kitu?” Mr. Oduya aliuliza tena na kulamba midomo yake iliyokuwa imekauka.
Spoiler hakuna na jibu, alimkodolea macho Mr. Oduya huku akiihisi ghadhabu ambayo ingemshukia muda wowote.
“I’m disappointed, very disappointed,” (Nimefadhaika, tena sana) Mr. Oduya alisema huku akimtazama Spoiler kwa hasira.
Spoiler alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiuinamia usukani wa gari lake kama mtu aliyeelemewa na mzigo mzito wa mawazo. Alitulia hivyo kwa sekunde kadhaa mpaka alipokusanya nguvu. Kisha alikiinua kichwa chake na kumtazama Mr. Oduya huku akitikisa kichwa chake kulia na kushoto. “Basi atakuwa ametuzunguka.”
Mr. Oduya alionekana kuduwaa. Alitulia akimtazama Spoiler kwa hasira.
“Kwa hiyo nifanye nini, mkuu?” hatimaye Spoiler aliuliza kwa fadhaa kama punguani aliyeingoja kwanza akili yake irudi toka ilikokimbilia.
“Unaniuliza ufanye nini?” Mr. Oduya alifoka kwa hasira. “Ina maana hujui cha kufanya?”
“Hapana mkuu!” Spoiler alisema haraka huku mapigo ya moyo wake yakienda mbio isivyo kawaida, “nilidhani labda una jambo la kuniambia. Hata hivyo usijali, kutakapopambazuka nitajua cha kufanya,” Spoiler alisema na kuwasha gari lake kisha akamuaga Mr. Oduya na kuanza kuondoka.
“Silas!” Mr. Oduya aliita, Spoiler alikanyaga breki na kugeuza shingo yake kumtazama Mr. Oduya kwa wasiwasi.
“Naomba kazi hiyo iwe nadhifu ambayo haitaacha alama yoyote nyuma ya kukutilia mashaka,” Mr. Oduya aliongeza. Spoiler aliitikia kwa kichwa na kuliondoa gari lake kwa mwendo wa kasi uliosababisha magurudumu yachimbe ardhi.
* * * * *
Saa tatu asubuhi, ndege ya shirika la ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Airbus 220-300 ilikuwa ikizunguka angani kutafuta uelekeo mzuri wa kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kilicho kilomita 12 kusini magharibi mwa jiji la Dar es Salaam.
Ndege hiyo ilikuwa inatokea jijini Mwanza ikiwa na abiria takriban mia moja. Kati ya abiria walioabiri ndege hiyo alikuwemo mwanadada Tunu Michael, aliyekuwa anatokea jijini Mwanza.
Tunu ambaye hakuwa amezidi miaka therathini, alikuwa msichana mrefu na maji ya kunde na mwenye umbo matata lenye kuweza kuitaabisha vibaya nafsi ya mwanaume yeyote. Alikuwa na nywele fupi na laini alizozitia rangi ya dhahabu. Alikuwa na sura ya duara yenye macho legevu na pua ndefu, midomo yake ilikuwa na kingo pana kiasi zilizopakwa rangi nzuri ya pink.
Alikuwa na vishimo vidogo mashavuni mwake vilivyofanya wanaume wababaike kidogo kwa uzuri wake kila walipomtazama. Asubuhi ile alikuwa amevaa blauzi ya pinki ya mikono mirefu iliyoyaficha vyema matiti yake imara madogo na suruali nyeupe ya jeans iliyombana na kuzuiwa na kiuno chake chembamba kiasi chenye misuli imara.
Miguuni alikuwa amevaa viatu vya ngozi vya rangi ya pink vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio na kumfanya azidi kuonekana mrembo kwelikweli. Mbali ya urembo aliokuwa nao, alikuwa msomi akiwa amebobea kwenye masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), kiasi cha kucheza na kompyuta kwa kadri alivyotaka.
Wakati ndege aina ya Airbus 220-300 ilipokuwa ikielekea kutua, Tunu alikuwa akitazama mandhari tulivu ya kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere kupitia dirishani, aliajabia uzuri wa kiwanja hicho, hasa jengo namba tatu la abiria, ambalo lilikuwa limekwisha anza kutumika.
Akiwa ameanza kuzama kwenye mawazo akifikiria kile alichokuja kukifanya jijini Dar es Salaam, mara akashtuliwa na mtikisiko mdogo uliotokea mle ndani ya ndege baada ya magurudumu ya ndege ile kugusa kwenye ardhi ya kiwanja cha ndege.
Ndege ilianza kwenda kasi ikipita katika barabara ndefu iliyotiwa lami na kuwekwa michoro elekezi kwa rubani wa ndege, kisha ikapunguza mwendo na kwenda kusimama mbele ya jengo namba mbili la kiwanja cha ndege.
Muda mfupi baada ya ndege kusimama na milango ya ile ndege kufunguliwa huku ngazi zikiwekwa sawa, abiria walianza kufungua mikanda ya siti zao na kuanza kushuka taratibu.
Tunu aliinuka kutoka kwenye kiti chake, akahangaika kuchukua begi lake dogo la rangi ya kijivu kutoka sehemu maalumu ya kuwekea mizigo kwenye sehemu ya juu ya ile ndege na kujiunga kwenye foleni ya abiria waliokuwa wakishuka.
Waliposhuka kwenye ndege waliingia kwenye jengo namba mbili la kiwanja cha ndege huku akili yake ikijikita katika kutafakari ni kwa namna gani atafanikiwa kutimiza kile kilichompeleka Dar es Salaam.
Baada ya muda alikuwa ametoka ndani ya lile jengo na kutokezea eneo la mbele la ule uwanja wa ndege katika sehemu kulipokuwa na maegesho ya magari.
Aliangaza macho yake huku na huko akionekana kutafuta kitu kisha akatoa simu yake na kuanza kutafuta namba fulani kutoka kwenye orodha ya majina ndani ya simu, kabla hajapiga akahisi mkono wa mwanamume ukimshika begani na kumshtua.
Aligeuka kumtazama aliyemgusa na kumwona mwanamume mmoja mrefu, mwenye umbo kakamavu la kimichezo akimtazama kwa uso wa tabasamu la furaha. Alikuwa na sura ya ucheshi na umri wake haukuzidi miaka therathini na mbili, alikuwa amevaa shati la kitenge la mikono mirefu, kofia nyeusi ya pama, suruali ya bluu ya dengrizi na viatu vya ngozi miguuni.
“Karibu sana Dar es Salaam,” yule mwanamume alisema huku akikumbatiana na Tunu.
“Ahsante sana, Victor,” Tunu aliitikia kwa furaha huku akimwachia yule mwanamume.
“Nisamehe kwa kuchelewa kidogo kuja kukupokea, gari langu liliniletea shida wakati najiandaa kuja, ilibidi niliache kwa jamaa yangu na nichukue gari lake ili nikuwahi,” Victor alisema huku tabasamu usoni kwake likizidi kuchanua.
“Oh! pole sana, hata hivyo hujachelewa,” Tunu alimtia moyo Victor, kisha aliongeza, “Vipi hapa Dar, kazi zinaendeleaje?”
“Hapa mambo ni faya kama ulivyotuacha. Naona siku hizi hata hupumziki, mwezi uliopita ulikuwa nchini Israel, juzi umetoka Afrika Kusini na leo tena kiguu na njia umekuja Dar es Salaam!” Victor alisema na kumfanya Tunu acheke kidogo.
“Unajua huwa siwezi kulala wakati naona kuna kazi inanisubiri,” Tunu alisema huku akianza kupiga hatua taratibu, “Hata hivyo, nilitakiwa niende jijini Arusha kuna kazi moja natakiwa nikaifanye wiki hii, lakini nimelazimika kuiweka pembeni kwanza ili kuja kumalizia kwanza kiporo changu nilichokiacha miaka mitatu iliyopita.”
“Hujaniambia hasa ni kazi ipi unayokuja kuifanya Dar?” Victor alimsaili Tunu huku akiwa na shauku.
“Usijali, muda ukifika utaijua. Kwa sasa wacha nipambane kwanza na hali yangu,” Tunu alisema huku akiangua kicheko hafifu.
Walilifikia gari alilokuja nalo Victor, aina ya Toyota Rav4 jeusi na kuingia kisha safari ya kuondoka kiwanjani pale ikaanza. Kwa dakika zisizopungua tano walisafiri katika barabara nzuri ya lami ya kutokea pale kiwanjani iliyokatisha katikati ya bustani nzuri ya maua, na muda mfupi baadaye walilivuka geti la kutokea.
Ndani ya gari walikuwa wawili tu na muda wote hakuna aliyemsemesha mwenziwe, Tunu alikuwa amezama kwenye kutazama mandhari yale baada ya kutengana nayo kwa muda mrefu. Walipofika mwisho wa barabara ile Victor alikunja kona kuingia kulia akiifuata barabara ya Nyerere iliyoelekea katikati ya mji akiwa katika mwendo wa wastani.
* * * * *
Saa tatu asubuhi kwenye duka la kuuza vipuri vya magari, katika mtaa wa Lindi eneo la Shaurimoyo jijini Dar es Salaam, Spoiler aliyekuwa ameghadhabika sana alimbamiza Jonas Odilo kwenye meza katika ofisi ndogo iliyokuwa ndani kwenye duka la kuuza vipuri vya magari. Spoiler alikuwa ameipandisha juu miwani yake myeusi ya kuficha macho.
Jonas alikuwa mwanamume mwenye umri wa kati ya miaka 35 na 40, alikuwa mfupi mnene mwenye misuli imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu na kumfanya aonekane kama bondia. Alikuwa na nywele fupi na uso mpana uliotulia kama maji ya mtungini. Asubuhi hiyo alivaa suruali nyeusi ya jeans na shati la rangi ya samawati lenye mistari ya bluu.
Alikuwa na uso uliotahayari na alimtazama Spoiler kwa hofu kubwa. Spoiler alikuwa amefika pale akiwa ameongozana na Dulla Mcomoro mwenye umbo kakamavu kama wachezaji wa mpira wa kikapu wa Marekani aliyekuwa amesimama karibu ya mlango akiwa makini kuhakikisha watu walioko nje hawajui kilichokuwa kinaendelea ndani ya ofisi ya duka hilo.
Dulla Mcomoro alikuwa amevaa miwani myeusi ya jua iliyokuwa imeyaficha macho yake makubwa na mekundu yenye uchovu lakini yaliyokuwa na kila dalili ya kuonya na muda wote.
Spoiler aliyazungusha macho yake kuangalia ndani ya ofisi ya Jonas ndani ya lile duka la kuuza vipuri vya magari akiwa kakunja sura yake, alikuwa bado kamkandamiza Jonas juu ya meza. Jonas alimtupia jicho Spoiler kwa hofu. Alipumua kwa shida akiwa bado amekandamizwa kichwa chake juu ya meza.
Spoiler alitoa kisu chake kutoka kwenye ala yake iliyokuwa kiunoni na kukisogeza karibu ya macho ya Jonas aliyekiona na kuanza kutetemeka kama aliyepagawa na mapepo.
“Kwa nini ulitusaliti?” Spoiler alimuuliza Jonas huku akimkazia macho yenye ghadhabu.
“Ni tamaa tu ndugu yangu. Jamaa alinishawishi nimuuzie, kwa kuwa alikuwa anasafiri nalo kwenda Botswana nikamuuzia!” Jonas alijaribu kujitetea kwa sauti ya kitetemeshi. Spoiler alimwinua na kumbana ukutani. Akamkodolea macho yake yenye kutisha huku akimuelekezea kisu shingoni.
Jonas alifumba macho yake huku akiendelea kutetemeka. Alimeza funda kubwa la mate kutowesha koo lake lililokauka ghafla.
“Gari uliliuza kwa nani?” sauti ya Spoiler ilimshtua Jonas na kumfanya afumbue macho yake na kukutana na macho yaliyokuwa yakiwaka kwa ghadhabu.
“Nimelisahau jina lake lakini ninazo nyaraka zote tulizoandikishana wakati wa kuuziana,” Jonas alisema kwa woga na hapo Spoiler akamwachia na kumsukumia kwenye meza.
“Zilete haraka, vinginevyo nitakuua.”
Jonas alifungua droo ya meza yake na kutoa faili kubwa, akaanza kulipekua kwa takriban dakika mbili na kutoa karatasi fulani, akampa Spoiler kwa mkono uliotetemeka. Spoiler alizipokea na kuzitupia jicho haraka haraka, kisha akaziweka mfukoni na kumkabili tena Jonas.
Dulla Mcomoro aliitupia jicho la wasiwasi saa yake ya mkononi na kuchungulia ndani ya kile chumba cha ofisi walichokuwemo Spoiler na Jonas.
“Tumebakiwa na sekunde hamsini tu,” Dulla Mcomoro alimwambia Spoiler huku akimwonesha saa yake.
“Ngoja nimalizie kazi,” Spoiler alisema huku akimkandamiza Jonas kwenye ukuta na kumwelekezea kisu chake. Muda huo huo wakasikia sauti za watu wawili wakiingia ndani ya lile duka na mmoja alikuwa anamwita Jonas.
Spoiler alishtuka na kumwachia Jonas. Alimtazama kwa ghadhabu na kurudisha kisu chake kwenye ala yake, kisha aliivaa miwani yake myeusi ili kuficha macho yake yenye ghadhabu.
“Hatujamalizana bado, nitarudi!” Spoiler alisema na kugeuka kisha akaanza kupiga hatua kutoka eneo lile haraka. Aliwapita wale wateja wawili wanaume waliokuwa wamesimama mle dukani wakisubiri kuhudumiwa.
(73)
Alifika kwenye gari lao aina ya Toyota Hilux double cabin la rangi ya bluu lililokuwa na namba bandia na kumkuta Dulla Mcomoro akiwa ameketi kwenye usukani na gari likiwa linaunguruma taratibu. Akapanda na gari likaondoka kwa kasi kutoka eneo hilo huku watu waliokuwepo eneo lile wakiwa hawajui kilichokuwa kimefanyika mle ndani ya duka la kuuza vipuri.
Jonas akiwa bado ana hofu, alitoka kwenye chumba kidogo cha ofisi yake na kuwatazama wateja waliokuwa wanamsubiri. Alikuwa na uso uliosawajika sana na mapigo ya moyo wake yalikuwa yakienda mbio isivyo kawaida.
“Samahani jamani, leo sifanyi biashara kuna sehemu natakiwa kwenda,” Jonas alisema na kuanza kufunga milango ya duka lake huku akiwa na wasiwasi. Wale wateja walishangaa sana, walijaribu kumuuliza kama kulikuwa na tatizo lakini hakuwa tayari kueleza chochote.
Alipomaliza kufunga milango akaingia kwenye gari lake aina ya Toyota Carina na kuondoka haraka akipanga kutofungua duka hadi pale ambapo angehakikisha hali ni shwari, kwani hakutaka kina Spoiler wakirudi tena wamkute pale dukani. Aliondoka akiwaacha wateja wake wanashangaa.
* * * * *
Gari aina ya Toyota Rav4 jeusi lililokuwa likiendeshwa na Victor lilikuwa katika mwendo wa wastani kaatika barabara ya Nyerere eneo la Kamata likielekea Mnazi Mmoja. Victor alikuwa makini barabarani na wakati huo Tunu alikuwa ameketi kwenye siti akiwa anaangalia nje kupitia ukuta msafi wa kioo wa dirisha la gari hilo.
Alikuwa amezama akilitazama anga la Maanani. Kwa dakika zote alizoketi ndani ya lile gari tangu Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere alikuwa akiwashuhudia walimwengu wakiwa katika pilika pilika za kuisaka fedha ndani ya jiji la Dar es Saalaam katika siku ile mpya.
Alijikuta tu akitamani afike haraka alikokuwa amepanga kwenda asubuhi ile kabla hajaelekea nyumbani kupumzika, na alikuwa akiomba kimoyomoyo amkute mtu aliyekuwa akimfuata pale Mnazi Mmoja. Kimtazamo tu ungeweza kutambua kuwa Tunu alikuwa katika wakati mgumu sana.
Kichwani kwake alikuwa na maswali mengi sana yaliyokosa majibu. Alijiuliza kama kwa miaka mitatu tangu alipolazimika kuondoka Dar es Salaam, ni nini kilichokuwa kikiendelea? Alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu kisha akaegemeza kichwa chake kwenye siti na kufumba macho yake.
Fadhaa ilijitokeza kwenye uso wake, aliapa kutorudi nyuma, hasa alipokumbuka masahibu yaliyompata miaka mitatu iliyopita yakikaribia kuyagharimu maisha yake. Muda wote Victor aliendesha kimya na alikuwa akimtupia jicho Tunu bila kusema neno.
* * * * *
Saa nne kasoro dakika kumi, katika mapokezi ya kituo cha televisheni cha Mzizima eneo la Mnazi Mmoja, Sammy alikuwa amesimama mbele ya kaunta ya mapokezi ya kituo kile cha televisheni akifoka. Alikuwa anapumua kwa nguvu huku akiwakazia macho wahudumu wa mapokezi.
Sehemu ya mapokezi ya kituo cha televisheni cha Mzizima ilikuwa katika sehemu ya chini ya jengo la ghorofa kumi na mbili lililopo barabara ya Lumumba jirani na bustani ya Mnazi Mmoja.
Sehemu ile ilikuwa na umbo la nusu duara iliyozungukwa na meza nzuri ya kaunta ya mbao ya mti wa mpodo na ilikuwa ikitazamana na viti vyeusi vya ngozi laini kwa ajili ya wateja waliofika hapo na kusubiri kuhudumiwa.
Kulikuwa na wahudumu watatu pale mapokezi, wawili wanawake na mmoja mwanamume waliokuwa katika sare zao nadhifu za kazi, mashati meupe ya mikono mirefu yenye kola za rangi ya kijivu yakiwa na nembo ya Mzizima TV kifuani na suruali za rangi ya kijivu. Shingoni walivaa wamevaa tai ndogo nyeusi zilizowapendeza.
Kwenye viti vyeusi vya ngozi laini vya kusubiria kulikuwa na wateja wawili watatu waliokuwa wameketi wakimtazama Sammy kwa mshangao wakati akifoka mbele ya wale wahudumu wa mapokezi.
“Naona ananitafuta ubaya, nilikataa kabisa gari langu lisipigwe picha, kwa nini apige picha bila ruhusa yangu na kurusha kwenye kipindi chake? Naondoka lakini mwambieni huyo mtayarishaji kuwa tutakutana mahakamani!” Sammy alisema kwa hasira na kuanza kuondoka.
Alitoka nje akiwa bado ana hasira, aliusukuma mlango mkubwa wa kioo na kutoka nje kisha akaanza kuzishuka ngazi takriban kumi za varanda pana yenye sakafu nzuri ya tarazo na kupishana na Tunu aliyekuwa anaingia ndani ya lile jengo. Wakati wakipishana walitazamana kwa makini. Hakuna aliyemsalimia mwingine lakini macho yao yaliongea zaidi ya ambavyo wangeongea kwa midomo yao.
Tunu alizikwea zile ngazi za varanda haraka haraka kisha akausukuma mlango mkubwa wa kioo na kutokomea ndani. Alitokea kwenye sehemu ya mapokezi ya kituo cha televisheni ya Mzizima na kwenda moja kwa moja hadi kwenye mapokezi ya kile kituo cha televisheni.
Alifika na kusimama mbele ya mhudumu mmoja wa kiume. Kabla hajamuuliza chochote akamuona Maximillian, mtangazaji wa kipindi cha “Mbunifu Wetu” aliyekuwa akija pale mapokezi huku akiwa na wasiwasi. Maximmilian alikuwa akiyazungusha macho yake kutazama huku na huko kwa wasiwasi.
“Kaondoka?” Maximillian alimuuliza yule mhudumu wa kiume.
“Eeh! Ila kakasirika huyo! Amesema mtakutana mahakamani,” yule mhudumu alisema, kisha akamgeukia Tunu, “Anti, nikusaidie?”
Tunu aliyekuwa akimtazama Maximillian alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kugeuza shingo yake kumtazama yule mhudumu mara moja.
“Nilitaka kumuulizia huyu kaka, bahati nzuri nimemuona,” Tunu alimwambia yule mhudumu kwa sauti tulivu na kumkabili Maximillian, “Samahani, kaka’angu!”
Maximillian aligeuza shingo yake kumtazama Tunu kwa makini. Tunu aliachia tabasamu pana la kirafiki huku akimsogelea. Maximillian naye alijikuta akiachia tabasamu, huku akionekana kuvutiwa na Tunu. Walitazama kwa sekunde chache kila mmoja akiwa kimya. Macho yao yaliongea mengi kuliko ambavyo wangeweza kuongea kwa mdomo.
Taxi imezua mambo. Kujua kitakachoendelea usikose kufuatana nami katika safari hii ya kusisimua...
(74)
“Enhe, nikusaidie!” hatmaye Maximilian alimudu kumuuliza Tunu.
Tunu alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kuonekana kama aliyekuwa akitafuta neno la kuongea.
“Jana usiku katika kipindi chako nimeliona gari aina ya Cadillac DeVille nikawa very interested…” Tunu alianza kujieleza, akasita na kuzungusha macho yake kuwaangalia watu waliokuwa wameketi kwenye eneo la kusubiria pale mapokezi. Wale wahudumu wa mapokezi na Maximillian wakatazamana, kisha wakamtazama Tunu kwa makini.
“Nahitaji kuonana na mmiliki wa gari hilo, sijui utanisaidiaje kaka’angu!” Tunu alisema huku akishusha pumzi. Maximilian alishusha pumzi na kulamba midomo yake.
“Mmh… hata sijui nisemeje, sina namba zake na hadi sasa tuna ugomvi. Alikuwepo hapa na ameondoka dakika chache tu zilizopita, nadhani mmepishana hapo nje,” Maximilian alisema huku akiegemeza kiwiko cha mkono wake juu ya meza ya mapokezi.
Tunu alishika kiuno chake na kukunja sura yake akionekana kuwaza kidogo. Kisha alimtazama Maximilian, “Hakuna sehemu yoyote unayoijua labda naweza kumpata?”
Maximilian alifikiria kidogo akionekana kujishauri, kisha alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu.
“Nenda pale kwenye mgahawa wa kisasa wa Elli’s, Ilala Sharif Shamba, mara nyingi huwa anakuwepo pale kwa rafiki yake. ila usimwambie kama mimi ndiye nimekuonesha,” Maximilian alimwambia Tunu.
“Usijali, kaka’angu. Nashukuru sana, nikiwa na chochote nitarudi tena kwako,” Tunu alisema na kuanza kupiga hatua taratibu kuondoka eneo lile huku macho ya Maximillian na wale wahudumu wa mapokezi yakimsindikiza hadi alipotoka nje ya jengo.
Alifika kwenye maegesho ya magari ya lile jengo la kituo cha televisheni ya Mzizima na kuingia ndani ya gari, alimkuta Victor akiwa amejiegemeza kwenye siti yake akiwa anasinzia.
“Twen’zetu. Naomba nipeleke Sinza nikapumzike,” Tunu alisema huku akifunga mkanda wa siti yake.
“Umempata uliyekuja kumtafuta?” Victor aliuliza kwa shauku huku akimkazia macho Tunu.
“Sijampata, nitamfuatilia tena baadaye!” Tunu alijibu kwa kifupi kisha akajiegemeza kwenye siti yake na kufumba macho.
Victor hakuongeza neno jingine, aliwasha gari na kuliondoa taratibu, akaingia barabara ya Lumumba na kwenda mbele alikokutana na barabara ya Morogoro, akakunja kuingia kushoto akiifuata barabara ile ya Morogoro. Ilikuwa ni safari ya kuelekea Sinza.
* * * * *
Saa tano ya asubuhi Joyce alikuwa ameketi kwenye sofa sebuleni kwake akitazama runinga, hata hivyo macho yake yalitazama runinga lakini akili yake haikuwa kwenye runinga, alikuwa mbali sana kimawazo, japo alionekana mtulivu sana.
Siku ile hakujisikia kutoka kwenda sehemu yoyote, alitaka kubaki ndani akipumzika baada ya kile kilichotokea kati yake na mumewe usiku wa siku iliyotangulia. Alishusha pumzi na kujilaza juu ya sofa.
Siku ile ilionekana kuwa ndefu sana kwa Joyce kuliko kawaida, hadi wakati huo alikuwa hajatia kitu chochote tumboni na hakuwa akihisi njaa, alikuwa peke yake nyumbani baada ya Sammy kutoka kwenda kazini kwake na watoto kwenda shule. Alijihisi mpweke sana.
Katika upweke ule alijikuta akizama kwenye tafakari, alikumbuka jinsi alivyokutana na Sammy kwa mara ya kwanza, walivyoanza uhusiano wao hadi walipofunga ndoa.
Alikumbuka kuwa alikutana na Sammy kwa mara ya kwanza miaka minane iliyokuwa imepita akiwa safarini kutoka Tanga akielekea jijini Dar es Salaam kuanza kazi ya ukatibu muhtasi baada ya kumaliza masomo yake ya uhazili katika Chuo Cha Uhazili tabora.
Ni siku hiyo hiyo Sammy alikuwa anatoka kutembelea vivutio vya mapango ya Amboni yaliyopo umbali wa kilomita 8 kutoka jijini Tanga katika barabara kuu inayoelekea Mombasa.
Ilikuwa saa kumi na mbili na dakika tano alfajiri ya siku ya safari yake ilimkuta akiwa bafuni anaoga na alitakiwa kuondoka saa kumi na mbili na nusu. Huaminika kuwa wanawake huchukua muda mrefu sana katika kujiandaa, kuanzia kuoga, kujipodoa na hata kuvaa nguo. Joyce alimaliza kuoga katika muda usiozidi dakika kumi, kisha alitoka haraka, akaingia chumbani mwake.
Kwa mara ya tatu, aliitupia jicho la wasiwasi saa yake ya mkononi iliyokuwa juu ya meza ya vipodozi, akajifuta maji haraka haraka. Zilikuwa zimebaki kama dakika tano tu tu kabla ya muda wa basi kupita uliokuwa umeandikwa kwenye tiketi yake, basi hilo lilikuwa likitokea jijini Tanga.
Kwa kawaida kutoka nyumbani kwao hadi kituo cha basi ingemchukua zaidi ya dakika arobaini na tano kama angetembea kwa miguu, lakini ilimchukua dakika tatu tu kufika kituo cha basi. Dereva wa pikipiki iliyomchukua kumpeleka hapo kituoni alikuwa ni kama nusu kichaa kutokana na mwendo wake wa kasi.
Joyce hakuamini kwamba angeweza kuwahi na kujiunga na wasafiri wenzake katika kituo cha basi kabla ya basi la Tahmeed halijapita.
Alipofika kituoni alitafuta sehemu nzuri akasimama. Siku ile alikuwa amevaa gauni zuri la kitenge cha wax lililokuwa limeshonwa na kudariziwa kwa nyuzi za dhahabu na kuushika mwili wake huku likilichora vyema umbo lake maridhawa na kichwani alikuwa amevaa kilemba kikubwa.
Kama ilivyokuwa imeandikwa, ndani ya dakika mbili tu basi la Tahmeed likawafikia na kusimama kituoni, Joyce akajiunga na wasafiri wengine kupanda ndani ya lile basi. Wakati akiingia kondakta wa lile basi alijikuta amebabaishwa sana na uzuri wa Joyce kiasi cha kusahau hata majukumu yake.
Kondakta alijikuta akipiga mluzi mdogo wa mshangao uliowafanya baadhi ya abiria walioketi jirani na mlango kumtazama kwa mshangao kabla ya macho yao kuhamia kwa Joyce. Si wanawake wala wanaume, wote walijikuta wakimkodolea macho Joyce huku wakiyasanifu mengi ya huba mbele ya hua aliyejitanashati kikweli kweli mbele ya macho yao!
Joyce alikuwa amebeba begi lake la safari lenye magurudumu lililokuwa na ukubwa wa wastani mkono wake wa kulia. Akiwa na uhakika kuwa macho yote yalikuwa yakimtazama, alijifanya hajui kilichokuwa kinaendelea, akapiga hatua taratibu huku akiangaza macho yake kuangalia namba za siti.
Alikuwa akiitafuta siti namba ishirini na nne. Aliiona na kuanza kukukuruka kuweka vizuri begi lake kwenye sehemu maalumu ya kuwekea mizigo iliyokuwa sehemu ya juu ndani ya lile basi.
Kumbe muda wote macho ya kijana mmoja mtanashati aliyekuwa ameketi dirishani katika siti namba ishirini na tano yalikuwa kazini yakimkagua Joyce tangu miguu iliyosimamia vidole hadi kwenye mikono iliyokuwa inasokomeza begi kwenye eneo maalumu la juu la kuwekea mizigo. Kijana huyo aliitwa Samuel Kombona au Sammy kwa kifupi.
Joyce alipomaliza kuuweka vizuri mzigo wake aliketi, muda huo dereva wa basi alikuwa ameshaliondoa gari huku wakiwaacha wasindikizaji wao wakipunga mikono yao.
“Habari yako, kaka!” Joyce alimsalimia Sammy huku akiyakwepesha macho yake baada ya kugundua kuwa abiria huyo alikuwa anamtazama usoni kwa makini.
“Nzuri tu, za utokako?” Sammy aliitikia na kumpiga swali papo hapo huku akimkazia macho usoni kwa tabasamu.
“Nzuri,” Joyce alijibu kwa ufupi na kutoa simu kubwa ya kisasa aina ya ‘Samsung’, akawasha data na kufungua mtandao wa facebook kisha akaanza kuperuzi, hali iliyoonesha kuwa hakutaka kumpa nafasi Sammy kuendelea kumsaili.
“Umpendaye hajambo?” Sammy alimtupia swali la uchokozi licha ya kumwona akiwa bize na simu yake lakini Joyce akajifanya hajamsikia na kubaki kimya akiendelea kuperuzi kwenye simu yake.
Wakati akiperuzi kuna wakati alijikuta akicheka na wakati mwingine alisonya. Baadhi ya abiria walikuwa wakigeuza shingo zao kumtazama ingawa hakuna aliyejua anacheka au kusonya nini!
“Na mimi natamani nicheke kidogo,” Sammy alishindwa kuvumilia, hivyo akajikuta akimsemesha kwa sauti tulivu ya chini.
Joyce aligeza shingo yake na kumtazama mara moja bila kusema neno, kisha akayaondosha macho yake kwa Sammy na kuyarudisha kwenye simu yake. Kitendo kile kikamfanya Sammy aanze kujilaumu kwa kuwa alianza kuonekana kuwa anajipendekeza na pengine ndiyo maana Joyce aliamua kumdharau.
“Samahani kama nimekuwa msumbufu kwako,” Sammy alimwambia Joyce na kujiegemeza kwenye siti yake.
Joyce hakunijibu bali alimtupia jicho la wizi huku akiachia tabasamu la aibu. Sammy hakutaka makuu, akachukua kitabu cha hadithi chenye jina la The Devil in Love kilichoandikwa na Barbara Cartland na kukifungua, akaanza kusoma ingawa akili yake ilikuwa kwa Joyce.
Kitendo kile kilimfanya Joyce apate nafasi nzuri ya kumsaili Sammy, alimtazama kwa makini kuanzia usoni hadi unyayoni na kushtuka kidogo japo alijaribu kuuficha mshtuko wake. Aligundua kuwa hakuwa amemchanganyia vizuri macho kwa kuwa alimchukulia Sammy kama mmoja wa vijana wahuni wasiopenda kupitwa na kila kilichofichwa ndani ya sketi.
Wakati Joyce akiendelea kumtazama Sammy katika namna ya kumsaili, Sammy aligeuza shingo yake kumtazama Joyce na mara macho yao yakagongana, wakajikuta wote wawili wakiachia tabasamu. Kwa hakika tabasamu la Sammy lilifanikiwa kuziteka hisia za Joyce kwani Joyce alijikuta akipumbazika na utanashati wa Sammy.
“Naitwa Sammy… Samuel Kambona,” Sammy alijitambulisha huku akimtazama Joyce kwa utulivu. Uso wake uliendelea kupambwa na tabasamu la kirafiki.
Joyce alisita kidogo na kumtazama Sammy huku tabasamu maridhawa la aibu likiendelea kuchomoza usoni mwake na kuusuuza mtima wa Sammy.
“Nafurahi kukufahamu,” Joyce alisema kisha akampiga swali la papo kwa papo, “Ulisema unataka kucheka?”
Swali lile lilimshtua Sammy kwani hakuwa amekumbuka kuwa alikuwa amemwambia kuwa na yeye alitamani acheke wakati Joyce alipokuwa akiperuzi simu huku wakati fulani akionekana kucheka.
“Hapana nilikuwa nakutania,” alisema huku akiachia kicheko hafifu.
“Ooh, kumbe!” Joyce alisema huku naye akiangua kicheko hafifu. “Naitwa Joyce…” aliongeza huku akionekana kuanza kuchangamka zaidi.
Kuanzia hapo stori kati yao zikakolea, na huo ndiyo ukawa mwanzo wa kufahamiana kwao, walipofika Dar es Salaam mapenzi yakachipua na miezi michache baadaye posa ikapelekwa…
_____
Mlio wa simu ya mkononi iliyoanza kuita ulimshtua sana Joyce na kumzindua kutoka kwenye lindi la mawazo, alinyoosha mkono wake kuichukua huku akiinua kichwa na kutazama kwa makini, moyo wake ukapasuka pah! Jasho jepesi likaanza kumtoka mwilini. Ilikuwa ni simu kutoka kwa Dynamo Plus.
Huku mwili wake ukimtetemeka kwa hasira aliikodolea ile simu kama aliyekuwa akilitazama bomu ambalo lilibakiza sekunde chache tu kabla halijalipuka, akakunja sura yake na kushusha pumzi huku akiendelea kuitazama ile simu bila kuipokea hadi ikakatika.
Simu ilianza kuita tena, Joyce aliiangalia tu pasipo kuipokea, aliiacha ikaita hadi ikakatika. Dakika moja baadaye ujumbe mfupi wa maneno ukaingia. Ulikuwa unasomeka: “Mbona hupokei simu, unapoteza bahati mtoto.”
Joyce alisonya na kuufuta ujumbe ule, wakati akitaka kuizima simu akasikia sauti ya muungurumo wa gari lililosimama nje mbele ya geti kubwa la nyumba yao, kisha akasikia honi za gari kumwashiria afungue geti. Aliitupia simu juu ya sofa na kukimbilia nje. Akachungulia getini na kuliona gari la Sammy.
Alionekana kushtuka kidogo baada ya kuliona gari la Sammy nyumbani kwani haikuwa tabia ya Sammy kurudi nyumbani muda ule. Hata hivyo hakutaka kuonesha mshtuko wake, akafungua geti huku akiachia tabasamu lililochanganyika na hofu.
Alimkodolea Sammy macho aliyeshuka kutoka kwenye gari na kutazama saa yake ya mkononi. Taratibu akaanza kupiga hatu kuelekea ndani. Joyce alifuata nyuma taratibu. Wakaketi sebuleni.
“Nilidhani ungekwenda kusaini mkataba!” Sammy alimwambia Joyce huku akimtulizia macho Joyce.
Joyce alimtazama mumewe kwa mshangao akiwa kakunja uso wake. Muda huo Sammy alikuwa hamtazami bali anatazama kwenye dari.
“Sikuelewi!” Joyce alisema huku akimkazia macho Sammy, ni wazi alikuwa amekerwa na kauli ya Sammy.
“Asiyemwelewa mwenzake ni wewe au mimi?”
- (76)
Joyce alimtazama mumewe kwa huzuni na uso wenye kutia huruma, alitingisha kichwa chake kwa masikitiko, kiganja chake cha kushoto kikiwa kimeshikilia paji lake la uso.
“Nilidhani yameisha, mume wangu!” Joyce alisema kwa huzuni.
“Hayawezi kwisha kirahisi rahisi hivyo,” Sammy alisema huku akigeuza shingo yake kumtazama Joyce.
Muda huo huo simu ya Joyce ikaanza kuita. Joyce alishituka sana ila alijikaza na kuuma meno. Aliitazama ile simu kisha akamtazama Sammy kwa wasiwasi. Wakatazamana.
Sammy alinyoosha mkono wake na kuichukua ile simu, akaitazama kwa makini na kuona namba ngeni isiyo na jina. Alimtazama Joyce kwa macho makali. Joyce alionekana kuwa na hofu na kujikunyata pale alipokaa.
“Pokea simu yako,” Sammy alisema kwa sauti iliyoashiria hasira huku akimpa Joyce ile simu.
Joyce alikataa kuipokea ile simu kutoka kwa mumewe. Alikuwa anatetemeka kwa hofu.
“Kwa nini unakataa kupokea, kwani unajua ni ya nani anapiga?” Sammy aliuliza kwa ukali huku akiendelea kunyoosha mkono wake kumpa simu Joyce.
“Wala sihitaji kumjua mpigaji,” Joyce alisema huku akinyanyua mabega yake juu kama ishara ya kutotaka kuipokea. Ile simu ikakatika.
Kabla Sammy hajasema chochote wakasikia sauti ya mtu akigonga geti huku akiita “Mama Pendo!” ilikuwa ni sauti ya jirani yao, Bibi Stumai. Joyce alibaki kajikunyata kwa hofu huku akimtumbulia macho mumewe.
“Nenda kamsikilize shoga yako huko nje,” Sammy alisema huku akijiegemeza kwenye sofa.
Joyce alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu, akajizoazoa kutoka pale kwenye sofa na kuelelekea nje.
* * * * *
Gari aina ya Toyota Hilux double cabin la rangi ya bluu lililokuwa na namba bandia lilikuwa limeegeshwa kwenye mtaa mmoja mtulivu katika eneo la Tabata Mawenzi. Ndani ya gari hilo kulikuwa na wanaume wawili, Spoiler na Dulla Mcomoro waliokuwa makini sana kuitazama nyumba moja ya kifahari iliyozungushiwa ukuta mrefu wenye uzio wa umeme. Mbele ya ukuta wa ile nyumba kulikuwa na geti kubwa jeusi.
Ukuta wa nyumba ile haukumruhusu mtu aliyeko nje kuona chochote kilichomo ndani ya nyumba hiyo kutokana na urefu wake. Kilichoonekana ukiwa nje ya ile nyumba ilikuwa miti miwili mikubwa ya kivuli na paa la kijani la nyumba ile. Ilikuwa ni sehemu tulivu sana lakini pia ya kifahari.
Spoiler na Dulla Mcomoro walikuwa wanafuatilia kujua kila aliyeingia au kutoka ndani ya nyumba ile. Spoiler alikuwa ametulia tuli akiwa makini sana kana kwamba alikuwa ameambiwa kungetokea kitu cha ajabu muda wowote.
Zilikuwa zimeshapita takriban dakika ishirini tangu wafike eneo lile baada ya kubaini kuwa aliyenunua gari aina ya Cadillac DeVille aliishi katika nyumba ile, kwa mujibu wa nyaraka walizozichukua katika duka la kuuza vipuri vya magari la Jonas Odilo, lililopo mtaa wa Lindi eneo la Shaurimoyo.
Hawakuwa na papara, waliamua kubaki ndani ya gari ili kufanya uchunguzi kabla hawajashuka na kwenda katika nyumba ile. Hadi muda ule hawakuwa wamemuona mtu yeyote kuingia au kutoka ndani ya nyumba ile, hali ilikuwa ya ukimya mno. Wakaanza kupatwa na wasiwasi iwapo nyumba ile iliishi watu.
Wakiwa bado wanafuatilia kila kinachotokea katika eneo lile mara wakaliona garo dogo aina ya Toyota Lexus RX jeusi likifika katika nyumba ile, likapiga honi na baada ya sekunde kadhaa lile geti kubwa likafunguliwa, gari likaingia ndani.
Ilichukua takriban dakika tano tu geti likafunguliwa na lile gari likatoka na kuingia barabarani, likaondoka. Spoiler akamtaka Dulla Mcomoro asogeze gari.
Dulla Mcomoro alilisogeza gari na kusimama mbele ya lile geti kubwa. Wakashuka haraka na kubonyeza kengele iliyokuwa kando ya geti, sekunde chache baadaye mlango wa lile geti ukafunguliwa, mlinzi mmoja wa Kimasai akatoa kichwa kuchungulia na kuwaona.
“Habari zenu?” yule mlinzi aliwasalimia huku akiwaangalia kwa macho ya kuwasaili.
“Nzuri. Habari za hapa?” Spoiler alimjibu yule mlinzi huku akimtazama kwa makini. Wakati huo Dulla Mcomoro alikuwa anachungulia kwenye uwazi wa ule mlango wa geti kutazama ndani.
“Sijui niwasaidie nini?” yule mlinzi aliwauliza huku akiwakazia macho, alionekana kuwa makini zaidi na kazi yake.
“Sisi ni wageni wa Dk. Mloka,” Spoiler alisema kwa kujiamini zaidi na kumfanya yule mlinzi amkazie macho kwa mshangao.
“Dk. Mloka!” yule mlinzi aliuliza kwa mshangao mkubwa, “Kwani Mloka yupi mnamtaka?” akaongeza huku akiwaangalia kwa udadisi, bado mshangao uliendelea kujionesha usoni kwake.
Spoiler na Dulla Mcomoro wakaangaliana na macho yao kuzungumza, kengele ya tahadhari ikalia kichwani kwa Spoiler, akashusha pumzi na kumtazama tena yule mlinzi.
“Kwani hapa siyo nyumbani kwa Dk. Mloka?” Spoiler aliuliza huku naye akijifanya kuonesha mshangao.
“Hii ni nyumba ya Dk. Mloka lakini mbona yeye amefariki dunia miaka miwili iliyopita!” yule mlinzi alisema huku akiwa bado anawatazama kwa makini.
“Kwa hiyo hapa anaishi nani kwa sasa?” Spoiler akamwahi kabla hajafanya chochote.
“Anaishi mkewe, Dk. Marina na watoto wake.”
“Hivi sasa kuna nani ndani?” Spoiler aliuliza huku akijaribu kuchungulia ndani kupitia upenyo mdogo ulio wazi wa mlango wa lile geti.
“Kwani ninyi mnamtaka nani hasa?” yule mlinzi akawauliza baada ya kufikiria kwa kitambo huku akionesha wasiwasi.
“Basi tunaomba tuonane na mama, mke wa Dk. Mloka, maana sisi ni jamaa zake marehemu Dk. Mloka,” Spoiler alisema huku akisogea karibu na yule mlinzi.
“Jamaa zake Dk. Mloka halafu hamjui kama alishakufa! Itabidi msubiri hapa ili nikaulize ndani kwanza, maana siwafahamu na wala sikutaarifiwa kama kuna wageni wa aina yenu watakuja hapa leo!” yule mlinzi alisema huku akijiandaa kuufunga ule mlango wa geti.
Mambo yanazidi kunoga, mlinzi ameonesha kuwashtukia kina Spoiler. Je, watafanikiwa kuingia ndani na kupata taarifa kuhusu mmiliki wa sasa wa gari wanalolitafuta? Vipi kuhusu Sammy na mkewe Joyce, moto utapoa? Na Tunu je, ana mission gani iliyomleta Dar es Salaam? Winifrida atakuja na jipya lipi? Endelea kufuatilia stori hii ya kusisimua ili kuujua mwisho wake...
(77)
Spoiler na Dulla Mcomoro wakaihisi hatari iliyotaka kutokea, bila kusubiri na kwa kasi ya umeme Spoiler akampiga pigo moja la haraka yule mlinzi kabla hajafunga ule mlango wa geti, pigo hilo lilimpeleka chini, kisha akaruka bila kishindo kama paka na kumkaba kabali matata pale chini iliyomfanya apoteze fahamu.
Wakati hayo yakitendeka Dulla Mcomoro alikuwa makini kuchunguza eneo lile kama kulikuwa na mtu yeyote aliyeona tukio lile, aliwaona watu wachache wakiwa na hamsini zao na hakuna aliyejishughulisha kuwatazama. Haraka akachungulia ndani lakini hakuona mtu mwingine yeyote.
“Shwari!” Dulla Mcomoro alimwambia Spoiler ambaye muda huo alikuwa amemvuta haraka yule mlinzi na kumficha kwenye maua, wakasaidiana kumwingiza kwenye kibanda maalumu cha mlinzi kilichojengwa kando ya lile geti kubwa la nyumba hiyo kisha wakaufunga ule mlango wa geti kwa ndani kumzuia mtu aliyeko nje asiweze kuingia ndani.
Dula Mcomoro alikuwa makini kuhakikisha hakuna aliyeona tukio lile wakati Spoiler akimpekua haraka haraka yule mlinzi na kuchukua simu yake ya mkononi kisha wakamfungia kwenye kile kibanda na kuelekea katika mlango mkubwa wa barazani wa kuingilia sebuleni.
Ilikuwa ni nyumba kubwa ya kisasa iliyokuwa na madirisha makubwa ya vioo na baraza kubwa mbele yake. Nje ya nyumba ile upande wa kulia kulikuwa na banda la wazi la kuegeshea magari na kulikuwa na gari moja la kifahari aina ya Toyota Landcruiser GX V8 jeusi lililokuwa na milango sita.
Sehemu nyingine ya mandhari ya nyumba ile ilizungukwa na miti miwili mirefu na mikubwa ya kivuli ambayo matawi yake yalikuwa makubwa na yalitengeneza vichaka vilivyosababisha kivuli kizito na kiza wakati wa usiku.
Sehemu ya mbele ya ile nyumba ilikuwa imezungukwa na bustani nzuri ya maua ya kupendeza yaliyotoa harufu nzuri na katikati ya bustani ile kulitengenezwa njia nzuri ya kutembea kwa miguu kwa vitofali vidogo vilivyokuwa vinavutia.
Wakiwa hapo barazani Spoiler akagonga mlango lakini hakuna mtu aliyejibu wala kufungua mlango. Akagonga tena, safari hii aligonga kwa nguvu, wakasikia nyayo za mtu zikija na mara mlango ukafunguliwa, msichana mmoja aliyeonekana wazi kuwa ni mfanyakazi za ndani akachungulia nje.
Yule msichana alikuwa mfupi na maji ya kunde, alikuwa na mwili mkubwa kiasi na kifua kipana kilichobeba maziwa makubwa ya mviringo, sura yake ilikuwa ya kitoto tofauti na mwili wake na alionekana hakuzidi miaka ishirini na tano.
Alikuwa na nywele ndefu alizozisuka mtindo wa twende kilioni, alivaa dela refu na apron nyeupe juu yake, ikionesha kuwa kabla mlango haujagongwa alikuwa jikoni akiandaa maakuli. Alisimama akiwatazama akina Spoiler mara moja na kutupa macho yake kutazama getini, hakumwona mlinzi na kuonekana kushtuka kidogo, akawasalimu akina Spoiler kwa woga.
“Mama yupo?” Spoiler alimtupia swali baada ya kujibu salamu yake.
“Yuko chumbani kwake amelala, anaumwa,” yule msichana alijibu baada ya kufikiria kwa sekunde kadhaa huku akiendelea kuwatazama akina Spoiler kwa wasiwasi.
“Nani mwingine yupo ndani?” Spoiler aliuliza kwa sauti tulivu huku akimtazama bila kupepesa macho.
“Yupo peke yake,” yule msichana alijibu huku uso wake ukishindwa kuficha wasiwasi aliokuwa nao. Aliendelea kuwatazama Spoiler na Dulla Mcomoro kwa zamu.
“Kwani humu ndani mnaishi watu wangapi?” Spoiler alimtandika swali jingine na kumfanya aachie mguno wa mshangao uliosikika kwa wote.
“Kwani nyiye ni kina nani?” yule msichana aliuliza kwa mshangao huku uso wake ukishindwa kuficha mshangao wake.
“Jibu swali unaloulizwa, we msichana,” Dulla Mcomoro alisema kwa ukali kidogo huku akifunua shati lake kumwonesha bastola yake iliyofichwa kiunoni.
Yule msichana aliiona ile bastola na kuingiwa na hofu, alimeza funda kubwa la mate kutowesha koo lake lililokauka ghafla na kushusha pumzi.
“Tunaishi wanne…” yule msichana alijibu kwa hofu.
“Watu wengine wamekwenda wapi?”
“Kaka Frank na mkewe wametoka muda si mrefu, wameenda kazini.”
“Okay, tupeleke chumbani kwa mama, tunahitaji kuongea naye,” Spoiler alimwambia yule msichana kwa sauti tulivu lakini iliyoamuru huku akimkazia macho yaliyowaka kwa ghadhabu.
Yule msichana alishusha pumzi, akaonekana kama aliyekuwa akijishauri, lakini alipokumbuka kuhusu ile bastola kiunino kwa Dulla Mcomoro akaogopa sana na kuwaongoza ndani. Waliingia na kuivuka sebule kubwa yenye samani zote muhimu za kisasa, ilikuwa imepambwa kwa seti mbili za makochi ya sofa ya kifahari yaliyokuwa yamepangwa katika mtindo wa kuizunguka.
Pia ilikuwa na zulia zuri la rangi nyekundu sakafuni na katikati kulikuwa na meza nzuri ya kioo iliyokuwa na umbo la yai ikizungukwa na stuli ndogo nne za sofa. Spoiler aliitupia jicho la haraka ile subule akijaribu kuyasoma mazingira ya nyumba ile.
Walielekea upande wa kushoto wakaifuata korido moja fupi na pana iliyokuwa na milango mitatu, milango miwili ilikuwa upande wa kushoto na mmoja ulikuwa upande kulia, mwisho kabisa wa ile korido. Yule msichana akawaongoza hadi kwenye ule mlango wa mwisho na kusimama mbele ya ule mlango huku akiwaangalia kwa hofu.
“Mlango wa chumba chake ni huu hapa,” yule msichana alisema kwa sauti ya kutetemeka huku akiwaonesha mlango.
“We Shamila, unaongea na kina nani?” sauti kali ya mwanamke ilisikika ikitokea ndani.
Yule msichana alishtuka, akawafanyia ishara akina Spoiler kwamba sauti ile waliyoisikia ndiyo sauti ya mama.
“Mama, ni wageni wako wanataka kukuona,” yule msichana alisema kwa wasiwasi huku akijikunyata.
“Nani aliyekuruhusu uwalete huku, kama ni wageni wangu kwa nini wasinisubiri sebuleni? Sauti ya Dk. Marina iliuliza kwa ukali toka chumbani.
- (78)
Kabla Shamila hajajua ajibu nini Spoiler alikishika kitasa cha mlango na kukinyonga huku akiusukuma mlango kwa nguvu, kumbe haukuwa umefungwa na ufunguo. Ulifunguka na Spoiler akajitoma ndani haraka huku akimwashiria Dulla Mcomoro amfuate.
Dulla Mcomoro alimshika Shamila na kumtanguliza, wakaingia ndani. Kilikuwa chumba kikubwa na chenye nafasi ya kutosha kikiwa na madirisha mawili mapana ya vioo yaliyokuwa yamefunikwa kwa mapazia mepesi marefu.
Katikati ya chumba kulikuwa na kitanda kikubwa cha samadari cha futi sita kwa sita chenye nakshi nzuri za kupendeza, upande wa kulia wa chumba kulikuwa na meza kubwa ya vipodozi yenye vioo viwili virefu vya kujitizama. Upande wa kushoto kulikuwa na mlango wa kuingia katika chumba kidogo cha maliwato.
Dk. Marina alishtushwa sana kwa kitendo cha kuwaona wanaume wawili asiowafahamu wakiingia chumbani kwake bila ruhusa, aliinuka haraka kutoka pale kitandani alipolala huku akitaka kupiga kelele kwa hofu lakini Spoiler alimwahi, akakitoa kisu chake na kumwonesha akiwa amemkazia macho ya ghadhabu.
Dk. Marina, daktari bingwa wa watoto wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, iliyopo eneo la Upanga Magharibi jijini Dar es Salaam, alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka arobaini na nane, alikuwa mrefu wa wastani mwenye mwili mkubwa na rangi ya maji ya kunde. Alipokiona kisu kikubwa cha springi kikimetameta mbele yake akanywea.
“Mnafanya nini ndani kwangu? Kwanza ninyi ni akina?” Dk. Marina aliuliza kwa hofu huku akijikunyata pale kitandani na kuwatazama akina Spoiler na Dulla Mcomoro kwa zamu.
“Mama, hatuko hapa kwa ajili ya kukudhuru, tunahitaji taarifa fulani toka kwako kisha tutaondoka zetu na kuwaacha salama,” Spoiler alisema kwa sauti tulivu huku akimkazia macho.
“Who are you guys?” Dk. Marina aliuliza na kushusha pumzi.
“Huna haja ya kutufahamu, sisi ni watu wazuri sana na tumekuja hapa kuzungumza nawe mambo kadhaa, ila kama utataka kuleta ujanja ujanja sisi ni wabaya sana hata shetani anatuogopa, we can destroy you in a second,” Spoiler alisema kwa sauti ya kufoka kidogo.
“Taarifa gani mnaitaka toka kwangu?” Dk. Marina aliuliza tena huku hofu ikiwa imemtawala.
Spoiler alimgeukia Dulla Mcomoro aliyekuwa bado kamshika Shamila na kumpa ishara ya kumfungia bafuni. Dulla Mcomoro alimkokota Shamila akampeleka katika bafu lililokuwa ndani ya chumba cha Dk. Marina, akamfungia huko baada ya kumpekua ili kuhakikisha hakuwa na simu wala kifaa chochote cha mawasiliano.
“Tunazo taarifa kuwa miaka mitatu iliyopita, mwezi Oktoba mumeo aliuziwa gari aina ya Cadillac DeVille la muundo wa kizamani, tupo hapa kwa kuwa tunalitaka gari hilo,” Spoiler alisema huku akiwa makini kumtazama Dk. Marina.
“Cadillac DeVille?” Dk. Marina alishtuka kidogo na kumtazama Spoiler kwa mshangao, kisha akaendelea, “Ni kweli tuliwahi kununua gari la aina hiyo miaka mitatu iliyopita lakini kwa sasa hatunalo, tumeliuza.”
“Mmeliuza lini na nani aliyelinunua?”
“Limeuzwa mwezi uliopita ila mimi simjui aliyelinunua kwani ni Frank ndiye aliyeliuza…” Dk. Marina alijaribu kujitetea.
“Frank ndiyo nani?”
“Mwanangu mkubwa, yeye anafanya biashara ya kuuza magari.”
“Tutampataje?”
“Nani?”
“Frank. Tunahitaji kujua ni nani aliyelinunua hilo gari.”
“Alikuja hapa muda mfupi uliopita, ameondoka na mkewe kwenda ofisini kwao, show room ya Magomeni Mikumi,” Dk. Marina alijibu huku akijiuliza wale watu ni kina nani waliomvamia kwa sababu ya kuulizia gari la kizamani!
“Magomeni Mikumi ipi?”
"Barabara ya Kawawa, karibu na kituo cha daladala cha Magomeni Mikumi kama unaelekea Ilala,” Dk. Marina alisema na kuwatajia jina la yadi hiyo ya kuuza magari.
“Mmeliuza mwezi uliopita, eeh! Kipindi chote lilikuwa wapi?” Spoiler aliuliza baada ya kufikiria kwa kitambo.
Dk. Marina alitaka kusema akasita na kumeza funda kubwa la mate kutowesha koo lake lililokauka, kisha akashusha pumzi. “Kwani shida yenu ni nini hasa, mbona sielewi?”
“Okay, nipe simu yako,” Spoiler alimwambia Dk. Marina huku akinyoosha mkono wake.
“Mmetaka taarifa nimewapa lakini bado mnataka na simu yangu, ya nini?” Dk. Marina alisema kwa huzuni.
“We mama, umeambiwa toa simu yako, hatuhitaji maswali,” Dulla Mcomoro alisema kwa ukali huku kinyanyua shati lake kumwonesha bastola iliyotuama kiunoni kwake na kumfanya Dk. Marina kuingiwa woga kwa namna Dulla Mcomoro alivyokuwa anamwangalia, akanyoosha mkono wake kumpatia simu Spoiler.
Spoiler aliipokea ile simu na kuizima kisha akatoa betri. Alimpa ishara Dulla Mcomoro kumleta Shamila kutoka bafuni kisha wakawafunga wote wawili kwa kamba na kuwaziba mdomo yao ili wasiweze kupiga kelele.
“Utatusamehe, mama, hatuna namna nyingine ya kufanya, mtabaki hivi kwa muda, tukishamalizana na Frank atakuja kuwafungulia,” Spoiler alimwambia Dk. Marina, wakatoka na kuufunga mlango wa chumba kwa funguo.
Walipofika nje waliingia ndani ya gari lao, wakaondoka kuelekea Magomeni Mikumi.
* * * * *
Saa kumi na mbili jioni jua lilikuwa limekwisha anza kuzama jijini Dar es Salaam na kwa mbali kiza kikianza kuchukua nafasi yake, anga la rangi nyekundu lilikuwa likinywea katika ukungu upande wa magharibi.
Tunu alishuka kutoka kwenye teksi, akatazama kushoto na kulia kwake halafu akavuka barabara akielekea upande ule wa magharibi, alipiga hatua taratibu kwa madaha kuelekea kwenye jengo moja lenye kuta safi za vioo na juu yake kukiwa na bango kubwa jeupe lenye maandishi makubwa mekundu yakisomeka MILAN CLUB & SPA. Chini ya bango lile kulikuwa na maandishi madogo yanayosomeka ‘Just enjoy every moment.’
Tunu alikuwa amevalia gauni zuri la kitenge cha wax lililoshonwa kwa mtindo wa ‘Ankara midi tube dress’ likiishia juu kidogo ya magoti yake, likaushika vyema mwili wake na kulichora umbo lake maridhawa. Nywele zake fupi na laini alizozitia rangi ya dhahabu alikuwa amezichana vizuri na macho yake aliyafunika kwa miwani mikubwa ya jua. Miguuni alivaa viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio na begani alining’iniza mkoba mzuri wa kike.
Katika eneo lile la MILAN CLUB & SPA kulikuwa na magari machache yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho ya magari na watu wachache waliokuwa wamesimama nje ya Club ile wakiendelea na mazungumzo yao. Watu wale waligeuza shingo zao kumtazama Tunu kwa matamanio na wengine walimsemesha wakati alipokuwa akikatiza eneo lile kuelekea kwenye mlango mkubwa wa mbele wa kuingilia ndani ya ile Club, hata hivyo hakuwatilia maanani badala yake aliendelea na hamsini zake.
Wakati akiukaribia ule mlango mkubwa wa mbele wa Club ile alizamisha mkono wake ndani ya mkoba wake na kutoa simu yake ya kisasa aina ya Iphone X iliyokuwa inaita. Akapokea na kuiweka kwenye sikio lake, “Hello, yeah ndiyo kwanza nafika… kwani wewe uko wapi?” Akasikiliza kidogo na kubetua kichwa chake, “Okay!”
Alikata simu kisha akairudisha ndani ya mkoba wake na kuzama ndani ya Club bila kujishughulisha na wanaume walioendelea kumtazama kwa matamanio na wengine wakimwita, kwani hali kama ile alikwishaizoea. Alipoingia ndani alikwenda moja kwa moja kukaa mwishoni kabisa mwa ukumbi wa baa.
Punde kidogo akatokea mwanamume mmoja mfupi kiumbo lakini mkakamavu akiwa na mwili uliojengeka kwa mazoezi na sura yake ilionesha unyenyekevu mkubwa tofauti na tabia yake halisi ya ubabe, unyama na wendawazimu. Alikuwa amevalia sweta jepesi lililoungana na kofia iliyofunika kichwa chake, suruali ya kadeti na buti ngumu nyeusi miguuni na usoni alivaa miwani myeusi ya jua.
Mwanamume huyo alitazama huku na kule kabla hajaelekea sehemu aliyoketi Tunu. Kabla hawajasalimiana, kila mtu akatazama kushoto na kulia kwake kabla ya kuendelea na mengine.
“Umenishtua sana uliponipigia simu kuniambia unanihitaji haraka,” yule mwanamume alisema na kushusha pumzi. Uso wake ulionesha wasiwasi kidogo.
“Kinachokushtua nini! Una soo gani hadi ushtuke baada ya kuona simu yangu?” Tunu alimuuliza yule mwanamume huku akiachia kicheko hafifu. Kabla yule mwanamume hajajibu, alitazama tena huku na kule kana kwamba alikuwa hapaamini mahala pale.
“Usihofu, Bob,” Tunu alimwambia kwa sauti ya chini. “Hapa hamna kamera, pia unadili na mtu makini kuliko maelezo.”
Yule mwanamume alishusha pumzi za ahueni lakini kabla hajasema lolote mhudumu wa Club ile akafika na kuwasalimia kwa tabasamu bashasha la kibiashara kisha akawataka radhi kwa kuchelewa kuwahudumia.
Yule mhudumu alikuwa msichana mwenye umbo kubwa lililofichwa ndani ya sare na miguu minene. Nywele zake ndefu zilikuwa zimefunikwa na kofia maalumu ya Club ili kuzuia kuharibu vinavyotiwa mdomoni.
“Naomba tuletee chupa kubwa ya Dompo na glasi mbili,” Tunu aliagiza na kutoa fedha, akampa yule mhudumu ambaye alipokea na kuondoka haraka.
Alipotoka wakaendelea kuteta wakipanga hiki na kile, baada ya dakika chache yule mhudumu alirudi na kuweka ile chupa ya dompo na bilauri mbili kwenye meza, alipotaka kurudisha chenji Tunu akamwambia abaki nayo. Alishukuru kisha akaenda zake huku akitabasamu.
Tunu na yule mwanamume wakaendelea kuteta huku sasa wakiwa wanalainisha makoo yao kwa kinywaji kile, mzao wa mzabibu kutoka Dodoma. Baada ya dakika ishirini tangu walipokutana pale yule mwanamume aliinuka, akajiondokea taratibu akimwacha Tunu bado kaketi ananywa kinywaji chake taratibu.
Tunu alikuwa ametulia tuli akiendela kunywa taratibu huku akitafakari kuhusu kazi iliyo mbele yake kwa kitambo kirefu kidogo, muda wote alizungusha macho yake kutazama huku na kule kulichunguza eneo lile. Alipomaliza kinywaji chake aliitupia jicho saa yake ya mkononi na kushtuka, ilionesha kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa mbili ya usiku.
Alichukua simu yake kutoka kwenye mkoba wake na kuandika ujumbe mfupi kisha akautuma na kuinuka, akatoka nje ya jengo la MILAN CLUB & SPA, alisimama pale akishangaa kuona eneo lile kulikuwa na wasichana wengi waliokuwa wakirandaranda nje. Walikuwa wa kila sampuli: wembamba kwa vibonge, warefu kwa wafupi, wenye sura mbovu na warembo, wote walikuwa wamevalia mavazi yaliyowaacha nusu utupu.
Tunu alishusha pumzi, akaanza kupiga hatua taratibu kuelekea kando ya eneo lile sehemu kulipokuwa na maegesho ya teksi, mara akasita baada ya kumwona mwanamume mmoja mrefu aliyekuwa amemwegemeza msichana mmoja kibonge ukutani wakiongea. Yule msichana alikuwa na kiuno chembamba na makalio makubwa na alivaa sketi fupi sana iliyoacha sehemu kubwa ya mapaja yake wazi na juu alivaa kitopu chepesi kilichoacha wazi sehemu kubwa ya kifua, matiti na tumbo lake.
Yule mwanamume alizungusha macho yake kuangalia huku na huko kisha akamwinamia yule msichana kibonge na kunong’ona jambo kwenye sikio lake. Yule msichana alishtuka sana, akamwangalia yule mwanamume kwa mshangao mkubwa na kuachia tabasamu huku akijiziba mdomo wake kwa viganja kuzuia kicheko.
Yule mwanamume alimtazama yule msichana kwa tabasamu na kumkumbatia kwenye kiuno lakini akashtuka na kugeuka nyuma, alimwona Tunu akiwa amesimama akiwaangalia kwa makini. Alimwachia yule msichana akitaka kujificha lakini alikuwa amechelewa.
Tunu aliendelea kumtazama, tazama yake ilikuwa ya dharau akimshusha na kumpandisha kuanzia juu hadi chini na chini hadi juu, kisha akabinua midomo yake na kusonya. Yule mwanamume alimtazama Tunu huku uso wake ukipambwa na aibu, hata hivyo alilazimisha tabasamu.
- (80)
“Mambo, Tunu!” yule mwanamume alimsalimia Tunu huku akijichekesha. Tunu hakumjibu bali alimwangalia kwa makini kwa kitambo. “Kuna mtu namuulizia hapa, nimeambiwa siku hizi anafanya kazi hapa!” alisema bila kuulizwa.
“Malaya wa kiume!” Tunu alisema kwa dharau na kuachia msonyo, kisha alibana pua yake na kuyarudia maneno ya yule mwanamume, “Kuna mtu namuulizia hapa, nimeambiwa siku hizi anafanya kazi hapa!…” kisha aliachia pua yake, akatema mate chini na kutingisha kichwa chake kwa huzuni, “Bora hata nilivyokupiga chini.”
“Mimi Malaya! Haya wewe usiye malaya unatafuta nini hapa?” yule mwanamume aliuliza huku akimkodolea macho Tunu.
“Mimi sipo hapa kujiuza. Natafuta mwanamume bora kuliko wewe usiyejielewa.”
“Sasa ndiyo natambua kuwa nilifanya uamuzi sahihi kuachana na wewe. Kahaba mkubwa!” yule mwanamume alisema huku akisonya kwa dharau.
“Nyoo! Hayo ni maneno ya mkosaji!” Tunu alisema na kubinua midomo yake kwa dharau, “Eti ulifanya uamuzi sahihi kuachana na mimi! Uamuzi upi sahihi wakati ulikuwa unanibembeleza usiku na mchana nisikuache!”
Yule mwanamume alitaka kusema neno lakini hatia ikamkaba kooni, akabaki akimtumbulia macho Tunu bila kusema neno. Tunu aliachia kicheko cha dharau na kuanza kupiga hatua za madaha kuelekea kwenye maegesho ya teksi akimwacha yule mwanamume anashangaa.
Dereva mmoja wa teksi, kijana mwenye sura yenye bashasha zote za kirafiki akawahi kumfungulia mlango wa mbele wa teksi yake wakati alipokuwa mbioni kuyafikia yale maegesho ya teksi nje ya MILAN CLUB & SPA.
Hata hivyo, Tunu hakutaka kukaa mbele badala yake alizunguka na kufungua mlango wa nyuma wa teksi ile, akaingia ndani na kuketi. Yule dereva wa teksi kuona vile haraka akaufunga ule mlango aliomfungulia Tunu kisha haraka akazunguka na kufungua mlango wa dereva na kuingia.
“Nikupeleke wapi, bibie?” yule dereva alimuuliza Tunu huku akimtazama kwa macho ya matamanio.
“Leo nitaenda kwako,” Tunu alimwambia yule dereva huku akimtazama kwa tabasamu.
“Kwangu?” yule dereva alishtuka sana na kumkodolea macho Tunu kwa mshangao mkubwa kana kwamba alikuwa ameona kiumbe cha ajabu kutoka sayari ya mbali.
“Kwani haiwezekani kwenda kwako? Naona umeshtuka sana!” Tunu alisema huku akiachia kicheko hafifu.
“Nimeshangazwa maana mimi nina mke, tena ndoa yangu bado changa. Sitaki kuletewa songombingo na waifu!”
“Hahaa, nilikuwa nakutania mwaya! Naomba nipeleke ELLI’S,” Tunu alimwambia yule dereva wa teksi huku akijiegemeza kwenye siti.
Yule dereva wa teksi akamtazama kidogo Tunu na kutikisa kichwa chake katika namna ya kuashiria kuwa alikuwa amemwelewa. Aliwasha gari na muda uleule ile teksi ikaanza kuyaacha yale maegesho.
* * * * *
Saa moja na ushee usiku katika ofisi za Mr. Oduya zilizo ghorofa ya sita ya jengo lake la ghorofa kumi na mbili lililopo katika barabara ya Bagamoyo eneo la Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Mr. Oduya alikuwa yupo ofisini kwake.
Alikuwa ameketi nyuma ya meza yake kubwa ya ofisini mwisho wa ofisi ile upande wa kuume akiwa katika uso wa kusawajika huku akiwa ameegemea kiti chake cha ofisi na kuweka miguu yake juu ya meza. Kama kawaida alikuwa amevalia suti nadhifu na viatu vya ngozi halisi ya mamba. Aliketi huku mche wa sigara ukiteketea taratibu kwenye pembe ya mdomo wake. Sura yake ilionesha wazi kuwa mambo hayakuwa salama kabisa.
Wakati huo Spoiler na Dulla Mcomoro walikuwa wanaingia baada ya mizunguko mingi ya hapa na pale ili kuhakikisha wanakamilisha kazi waliyotumwa kuifanya. Ukimya ulikuwa umetawala ndani ya ofisi ile ukawafanya Spoiler na Dulla Mcomoro watembee taratibu kama waliokuwa wananyata huku wakisikia sauti hafifu ya hatua zao wakati walipokuwa wakikatisha kuelekea kwenye viti ili kuketi.
Spoiler alikwenda moja kwa moja kwenye meza ya Mr. Oduya huku akimtazama kwa utulivu na kumkabidhi bahasha kubwa ya khaki aliyokuwa ameishika mkononi ikiwa na karatasi ndani yake. Mr. Oduya alinyoosha mkono wake kuipokea ile bahasha kisha akajiegemeza vizuri kwenye kiti chake cha ofisini.
Aliifungua na kutoa nyaraka za manunuzi ya gari aina ya Cadillac DeVille lililokuwa limenunuliwa na Sammy katika yadi ya kuuza magari ya Magomeni Mikumi. Mr. Oduya alizitazama kwa makini huku mche wa sigara ukiendelea kuteketea taratibu kwenye pembe ya mdomo wake na macho yake yakizipitia mstari kwa mstari zile nyaraka.
Kabla hata hajamaliza kusoma nyaraka zile moyo wake ukapoteza utulivu na kijasho chepesi kikaanza kumtoka sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Samuel John Kambona!” alilitamka jina hilo kwa sauti ya chini kama aliyekuwa ananong’ona. Jina lilijiumba na kujirudia akilini kwake likiacha mwangwi. Alihisi kulisikia jina hilo mara kadhaa, si hivyo tu bali alimfahamu hata mmiliki wa jina lenyewe ambaye kwa mujibu wa nyaraka zile, ndiye mnunuzi wa gari lile.
Mr. Oduya alichukua simu yake na kutafuta namba za Dk. Masanja, meneja mkuu wa hoteli ya Udzungwa Beach Resort na kupiga ili kupata uhakika. Majibu aliyopewa yalimfanya ajihisi kukanganyikiwa, akili yake ilijaribu kukataa kabisa kukubaliana na taarifa ile na kile alichokishuhudia kwenye katika nyaraka zile za ununuzi wa gari.
Alijitahidi kuwa makini zaidi na akiishirikisha akili yake kikamilifu katika kumletea taarifa za kuaminika, kwani mambo yale hayakuwa yanamwingia kichwani kabisa! Ni vipi Sammy ameendelea kujitokeza katika harakati zake za kuusaka urais wa Tanzania na kugeuka kuwa kitisho?
Aliinua uso wake na kutazama juu akionekana kuwaza mbali. Wakati huo Spoiler na Dulla Mcomoro walikuwa kimya kabisa wakimtazama kwa wasiwasi. Akiwa katika hali ile mara hisia mbaya zikamjia na hapo mapigo ya moyo wake yakaanza kwenda kasi isivyo kawaida, hasa alipowaza kuwa huwenda wapinzani wake kisiasa walikuwa na fununu fulani kuhusiana na lile gari na wangeweza kulitumia kummaliza.
Dah! Mambo yanazidi kunoga. Nini kitaendelea? Usikose kuwa nami kwenye safari hii ya kusisimua
MWISHO WA SEASON 1
ENDELEA KUFUATILIA SEASON 2
MWISHO
0 comments:
Post a Comment