Search This Blog

Monday 27 March 2023

HADI LINI - 5

  


Simulizi : Hadi Lini

Sehemu Ya Tano (5)


“Na kwa nini atoke humu chumbani akiwa analia?” Ibrahim aliuliza huku akiendelea kumkazia macho Pamela.

“Nikuulize wewe, pengine analia kwa vile nimemweleza msimamo wangu,” Pamela alijibu kwa kujiamini huku akimtulizia macho Ibrahim moja kwa moja machoni pasipo kukwepesha macho yake.

“Msimamo gani uliomweleza?” Ibrahim aliuliza kwa pupa huku naye akimtulizia macho Pamela.

“Swali hilo ingependeza zaidi kama ungemuuliza mama mwenyewe,” Pamela alijibu na kugeuka kutazama nje akionekana kumpuuza mumewe.

Ibrahim alimtazama Pamela kwa makini na kushusha pumzi, akauma midomo yake akionekana kuzuia hasira zake, kisha alianza kuranda randa mle chumbani huku akiwa kainamisha kichwa chake, mikono yake akiwa kaiweka nyuma na akionekana kuwaza mbali sana.

Pamela aliendelea kusimama pale pale akiendelea kutazama nje, naye alikuwa akiwaza mbali sana. Ibrahim alikuwa anageuka mara kwa mara kumwangalia Pamela kwa jicho la hasira, na baada ya kuranda randa kwa kitambo kifupi alimfuata huku akimkazia macho. Akasimama hatua moja mbele yake na kumtulizia macho kwa hasira huku akimnyooshea kidole chake.

“Hakika mwalimu wako wa somo la kiburi na jeuri anafanya kazi yake vizuri sana.”

“Ni kweli, hasa baada ya mwalimu wa somo la upendo, nidhamu na uvumilivu kushindwa kazi yake!”

“Sasa, kama ameshindwa kazi ni bora angekushauri uondoke nyumbani kwangu na siyo kunifanyia ufedhuli kiasi hiki!”

“Nilichukuliwa kwa wazazi wangu kwa taratibu zote, japokuwa naweza kuondoka kisheria lakini ninawajibika kuwapa wazazi wangu na wa kwako heshima inayostahili!” Pamela alisema kwa utulivu huku akiendelea kumtulizia macho Ibrahim pasipo kupepesa.




“Heshima inayostahili ni kumwacha mwanamke aliyenizaa atoke humu ndani akiwa analia?” Ibrahim alimwuliza Pamela akiwa amekerwa sana.

“Nadhani analizwa na yale unayopaswa kuyatenda ambayo hata mimi nayasubiri kwa hamu.”

“Kwani unataka nini hasa kutoka kwangu?”

“Hujui au unapenda kusika wakati natamka? Haipendezi kuuliza jambo ambalo unalifahamu vizuri!”

Ibrahim alimtazama kwa hasira, akataka kusema neno lakini akasita na kushusha pumzi kwa uchungu, donge la hasira lilionekana kumkaba kooni kwake. Alitamani amshike Pamela na kumtupa kutoka kule ghorofani hadi chini ili afe. Alimeza mate kutowesha koo lake lililoonekana kukauka kisha akashusha pumzi ndefu huku akionekana kuizuia hasira zake.

“Okay, ni jambo gani unalotaka toka kwangu, talaka?”

“Nadhani hilo ni la kwanza,” Pamela alimjibu ibrahim kwa kujiamini huku akiendelea kumtulizia macho yake.

Ibrahim aliachia tabasamu la dharau na kubetua kichwa chake kukubali, alijionesha kuwa alikuwa hajali chochote na alikuwa tayari kwa lolote, isitoshe suala la talaka kilikuwa kitu ambacho alikitamani muda mrefu, na sasa ilikuwa jambo rahisi kuliko alivyokuwa ametarajia.

“Naona umeitafuta na utaipata sasa hivi, nipe dakika moja tu,” Ibrahim alisema kwa kujiamini huku akiendelea kutabasamu kwa dharau.

“Naisubiri kwa hamu kubwa, wala usijaribu kabisa kunitisha,” Pamela aliongea kwa sauti iliyobeba dharau huku akionekana kushindwa kuficha hasira zake, donge la hasira lilizidi kumkaba kooni.

Ibrahim aliivua pete ya ndoa kutoka kwenye kidole chake na kumpa Pamela huku akimtazama kwa chuki, “Nilijua tu toka siku ile kwa mkuu wa wilaya kuwa ungeidai siku moja.”

Pamela aliipokea ile pete bila kusita wala kujiuliza huku uso wake ukipambwa na tabasamu, kisha naye akaivua pete yake ya ndoa kutoka kwenye kidole chake na kunyoosha mkono kumpa Ibrahim, “Kama ndivyo ulivyotarajia sawa, na wewe chukua pete yako uliyonivalisha kinafiki.”

Ibrahim aliachia tabasamu pana la dharau usoni kwake huku akiipokea ile pete, akaiweka kwenye mfuko wa suruali yake huku akionesha kutokujali kabisa. Muda ule alikuwa anajihisi mwepesi mno baada ya kuutua mzigo mzito uliokuwa umemwelemea kwa muda mrefu.

“Okay, sasa nasubiri kuondoka kwako haraka humu ndani ili nipate kupumua,” Ibrahim alimwambia Pamela na kumfanya aangue kicheko cha dharau huku akimtazama Ibrahim kwa dharau kuanzia unyayoni hadi kichwani.

“Naona wewe ungetangulia kuondoka humu ndani ndiyo ingekuwa vizuri zaidi wakati mimi nikisubiri iwapo wakili wangu atamaliza shauri letu mapema.”

Ibrahim alishtushwa sana na kauli ile, akamkazia macho Pamela huku hasira ikijionesha waziwazi kwenye macho yake, “Umesema nani atamaliza shauri letu?”

“Utamuona panapostahili akisaidiana na wanaostahili kufanya yote yanayostahili kwetu,” Pamela alijibu kwa kujiamini huku akishika kiuno chake na kumtazama Ibrahim kwa dharau.

Ibrahim aliondoka kutoka eneo lile kwa hasira huku akionekana kuchanganyikiwa na kwenda kusimama kule nje kwenye balcony, Pamela aliendelea kusimama pale pale. Ibrahim alisimama pale nje akiangalia chini ya lile jengo kwa muda, akamuona yule mlinzi akiwa ameketi juu ya kiti chake pale kwenye kibanda cha ulinzi huku akitazama kule juu kwenye balcony kwa wasiwasi.

* * * * *

Baada ya Ibrahim na mama yake kupishan kwenye ngazi na Mama Bigirimana kupita akiwa analia, Mzee Tugiramahoro na Mama Ninziza Bernice walikuwa bado wameketi pale pale wakijadiliana kuhusu hatma ya binti yao. Mara wakashtushwa sana kumuona Mama Bigirimana akiingia tena pale sebuleni kutokea kule nje alikouwa na mumewe akiwa analia kwa uchungu huku akifuatwa nyuma na mumewe aliyejaribu kumfariji.

Mama Bigirimana aliketi kwenye sofa huku akiendelea kulia kwa huzuni kilio cha kwikwi, alijiinamia kwa huzuni huku akijitahidi kuzuia machozi yaliyokuwa yakimtoka lakini hakuweza kufanikiwa. Mzee Tugiramahoro alimtazama yule mama jinsi alivyokuwa akilia na kuinuka huku akishika kiuno chake, akageuza shingo yake kumtazama mkewe na kumpa ishara ya kumtaka watoke nje wakazungumze faragha mambo yanayowahusu.

Mama Ninziza Bernice alimtazama mumewe kwa wasiwasi, akataka kukataa lakini hakuwa na namna nyingine yoyote ya kufanya, hasa alipokumbuka kuwa walikuwa wameitwa pale kuja kujaribu kutafuta muafaka na kunusuru ndoa ya binti yao, hivyo akajikuta akiwa hana njia nyingine isipokuwa kuinuka na kutoka nje kumfuata mumewe huku akimtupia jicho Mama Bigirimana aliyekuwa analia.

Mama Ninziza Bernice alimkuta mumewe akiwa kasimama kwenye ile baraza ya nyumba akiwa anamsubiri huku mikono yake akiwa kaiweka nyuma. Mama Ninziza Bernice alisimama huku akimwangalia mumewe kwa wasiwasi mkubwa.

“Unajua hadi sasa sielewi… hivi hapa tumeitwa tuje kufanya nini! Maana muda wote naona uchuro tu wa watu kulia ovyo kama vile kuna msiba!” Mzee Tugiramahoro alimwambia mkewe huku akimtazama kwa makini.

“Ni kweli hata mimi sielewi, lakini ni wajibu wako wewe kumuuliza mzee mwanzako!” Mama Ninziza Bernice alimjibu mumewe kwa utulivu lakini akiwa na uso uliotawaliwa na wasiwasi.

“Kama unyumba wa binti yangu hakuna ni heri watuambie tujue moja, lakini nasema kabisa umtafutie pa kumpeleka maana mimi sikai na watoto walioachika.”

“Lakini hukumuoza mtoto akiwa hana kwao, na siyo wote wanaoachika hawafai… sasa katika mazingira kama haya ndiyo umwache tu aendelee kuteseka eti kwa vile ulimuoza?” Mama Ninziza Bernice alisema kwa mshangao huku akionekana kukerwa sana na yale maneno ya mumewe, donge la hasira lilimkaba kooni.

“Nasema hivi, kama unamuunga mkono basi wewe na yeye mtakwenda kutafuta kiota chenu cha watalikiwa… tena safari yenu muianzie hapa hapa na siyo kwangu.”

Mama Ninziza Bernice alitaka kusema neno lakini akashindwa, donge la hasira lilizidi kumkaba kooni na kumfanya aanze kulia kwa uchungu. Mumewe alimtazama kwa hasira.

“Nasisitiza, akiachika mtu hapa asirudi nyumbani kwangu!” Mzee Tugiramahoro alisema kwa msisitizo na kuondoka akimwacha mke wake pale nje, akaingia sebuleni na kumkuta Mzee Bigirimana akiendelea kumtuliza mke wake ambaye alikuwa bado analia kwa uchungu kilio cha kwikwi. Mzee Tugiramahoro alifika na kusimama huku akiwatazama kwa makini.

“Niwie radhi mzee mwenzangu, naomba tutoke nje tukatete kidogo kama wanaume,” Mzee Tugiramahoro alisema huku akimkazia macho Mzee Bigirimana.

Mzee Bigirimana aliinua shingo yake kumtazama Mzee Tugiramahoro kwa wasiwasi kidogo, akashusha pumzi na kuinuka huku akimwacha mke wake bado analia kilio cha kwikwi. Walitoka nje ambako walimkuta Mama Ninziza Bernice akiendelea kulia kwa uchungu.

“Ingia ndani bibie, tuna mazungumzo ya kiume hapa,” Mzee Tugiramahoro alimwambia mkewe huku akishusha pumzi.




Mama Ninziza Bernice aliwatazam wale wanaume kwa mashaka kidogo huku akiinuka na kuingia ndani huku akisindikizwa na macho ya wale wazee wawili, alipoingia ndani wakaketi pale kwenye sofa. Mzee Tugiramahoro alitoa paketi ya sigara kali, akatoa humo sigara mbili huku moja akiiwasha na kuanza kuvuta na sigara nyingine akanyoosha mkono wake kumpa Mzee Bigirimana. Mzee Bigirimana alikataa kwa kutingisha kichwa.

Mzee Tugiramahoro alipiga mkupuo mkubwa wa sigara na kuutoa moshi taratibu huku akiutazama kwa makini jinsi ulivyokuwa ukipanda juu na kupotelea hewani. Akapiga mkupuo mwingine na kutoa moshi mwingi, kisha akageuza shingo yake kumtazama Mzee Bigirimana.

Mzee Bigirimana alikuwa ameketi kimya kabisa akimwangalia mzee mwenziye kwa makini. Akashusha pumzi na kusimama kisha akaanza kuzunguka zunguka pale barazani huku akitazama juu, mikono yake akiwa ameiweka nyuma akionekana kuwaza mbali sana.

“Siku hizi tunazaa kenge na siyo watoto kabisa!” Mzee Bigirimana alisema kwa huzuni.

“Inategemea, maana si watoto wote ambao ni kenge, wapo wanaofaa kabisa,” Mzee Tugiramahoro alisema katika hali ya utulivu huku akiendeleaa kuvuta sigara yake taratibu.

“Wapo kweli wala sikatai, lakini si mimi na bwana mwenye mji huu,” Mzee Bigirimana alisema huku akimtupia jicho mzee mwenzake.

“Kwa nini unasema hivyo?” Mzee Tugiramahoro alimtazama kwa makini na kuuliza huku akipiga mkupuo mwingine na kutoa moshi mwingi.

“Kinachomliza mama yake ndicho ambacho yeye kadhamiria kukifanya!”

“Ni kipi hicho cha ajabu?” Mzee Tugiramahoro aliuliza kwa shauku huku akimkazia macho Mzee Bigirimana.

“Eti anataka kumtaliki mkewe na pengine aoe mwanamke mwingine!” Mzee Bigirimana alisema kwa huzuni.

“Kama akili yake ndivyo inavyomtuma basi amtaliki, lakini mimi sirejeshi mahari na wala binti yangu hatarudi nyumbani kwangu,” Mzee Tugiramahoro alisema kwa hamaki huku donge la hasira likimkaba kooni. Muda ule alianza kuiona ile sigara chungu.

“Hapana, tusikose hekima, mzee mwenzangu, wacha tuwaite wote wawili na kisha tuwahoji maana ndilo tuliloitiwa na mkwe wangu!”

Mzee Tugiramahoro alimtazama Mzee Bigirimana kwa kitambo kirefu pasipo kusema neno kisha alipiga mkupuo mwingine mkubwa wa moshi na kuutoa na kukitupa chini kipande cha sigara kilichobakia na kukisigina kwa mguu wake.

“Bahati ya binti yangu ni mbaya sana, walikuja vijana wengi tu wa maana waliotaka kumuoa nikakataa, kumbe sikujua kama namtumbukiza kwenye pango la mbwa mwitu,” Mzee Tugiramahoro alisema kwa huzuni maneno yaliyoonekana kumchoma na kumkera sana mzee mwenziye.

Mzee Bigirimana alimkazia macho mzee mwenziye huku hasira zikianza kumpanda, “Nadhani sasa tusianze kutukanana kirejareja, mimi si mjinga na wewe unafahamu hilo… cha msingi ni kuzungumza na watoto wetu ili tuwaweke sawa.”

“Tuwawekeje sawa wakati tayari mwanao anamuona binti yangu kama chawa!” Mzee Tugiramahoro alimuuliza mzee mwenziye huku hasira zikianza kumtambaa mwilini mwake na kuyafanya maungo yake kuzizima.

Mzee Bigirimana alitaka kusema neno lakini akasita na kushusha pumzi. Kisha wale wazee walibaki wakitazamana pasipo kusema neno kwa kitambo kirefu. Mzee Tugiramahoro alitoa sigara nyingine na kuiwasha kisha akapiga mkupuo mkubwa na kutoa moshi mwingi huku akihema kwa nguvu.

* * * * *

Akiwa pale kwenye balcony Ibrahim aliendelea kutazama kule chini kisha kama aliyekumbuka kitu akaondoka na kurudi chumbani, akaanza kuranda randa mle ndani huku akiwa kainamisha uso wake, alionekana kuwa katika dimbwi la mawazo.

Muda ule Pamela alikuwa amepiga magoti akipanga vizuri nguo zake ndani ya kabati kubwa la nguo la ukutani. Ibrahim alikuwa anageuka mara kwa mara kumtazama Pamela huku akiwa na donge la hasira.

“Kabla sijasahau, naomba ukitaka kuondoka hakikisha kwanza umenitayarishia kabisa orodha ya mali yangu humu ndani.”

“Kila kinachostahili kufanywa tayari kipo kwa wakili wangu, wewe tengeneza listi yako ukampe wakili wako,” Pamela alimjibu Ibrahim huku akiendelea kupanga nguo zake ndani ya lile kabati.

“To hell with your lover boy,” Ibrahim alifoka kwa hasira na kumkwida Pamela kwa ghadhabu. Pamela hakuogopa bali alionekana kumshangaa sana Ibrahim.

“Mimi tena? Siyo wewe na mlolongo wa malaya wako wa ushirika?” Pamela alimuuliza Ibrahim huku akimtazama kwa mshangao.

Ibrahim alionekana kuhamaki sana, akamnyanyua Pamela na kumsukuma kwa ghadhabu, Pamela akaanguka pale sakafuni na kuinuka haraka huku akimtazama Ibrahim kwa tabasamu, kisha akatingisha kichwa chake kwa dharau.

Akiwa bado anatingisha kichwa kwa dharau alishtuliwa na kibao kikali cha ghafla ambacho hakukitegemea kilichotua kwenye shavu lake la kushoto, akaanguka sakafuni huku lile tabasamu likiyeyuka na badala yake hofu ikachukua nafasi yake.

Pamela alijishika shavu lake huku akimtazama Ibrahim kwa hofu kubwa akiwa haamini kilichotokea, mdomo wake wa chini ulikuwa umechanika kidogo na damu zilianza kumtoka kwenye mdomo wake. Alifuta damu huku donge la hasira likizid kumkaba kooni.

“Unanipiga!” Pamela alimwuliza Ibrahim kwa mshangao huku akiinuka kutoka pale sakafuni, akasimama huku akimkazia macho, ni wazi hasira zilikuwa zinachemka ndani kwa ndani. Ibrahim hakumkawiza, akampiga teke lililotua kwenye tumbo lake na kumdondosha chini huku akilishika, akaanza kulia kwa uchungu sauti kubwa.

Sauti ya kilio chake ilipenya na kusambaa kila mahali, kuanzia pale sebuleni walipokuwa wameketi wale kina mama, barazani walipokuwa wamekaa wale wazee wakiongea hadi kule chumbani walikokuwa wamelala watoto wao Nduwimana na Samantha.

Mama Ninziza Bernice na Mama Bigirimana walinyanyuka kutoka kwenye sofa walipokuwa wamekaa huku wakitazamana kwa wasiwasi, walionekana kujaribu kusikiliza kwa makini ili kubaini sauti hiyo ilikuwa ya nani na ilitokea wapi. Mama Ninziza Bernice akamshika mkono Mama Bigirimana na kuanza kulia kwa uchungu.

“Mwanao anataka kuniulia binti yangu,” Mama Ninziza Bernice alisema kwa huzuni huku akitokwa na machozi.

Mama Bigirimana alimtazama Mama Ninziza Bernice kwa wasiwasi na bila kusubiri alianza kukimbilia kule nje huku akiita kwa sauti kubwa yenye hofu, “Baba Ibrahim, mwanao anamuua mtoto wa watu!”

Wakati Mama Bigirimana akiwa anakimbilia kule nje, Mzee Bigirimana naye alikuwa anaingia ndani mbio huku akiwa na wasiwasi mkubwa, wakakumbana mlangoni na kupiga mweleka sakafuni kwa mshindo mkubwa uliowaacha wakigaragara.

Mama Bigirimana alitoa ukelele wa maumivu huku akishika tumbo lake, Mzee Bigirimana alijizoazoa na kuinuka kutoka pale sakafuni huku akikunja uso wake akionekana kusikilizia maumivu, akahema kwa nguvu huku akimtazama mke wake pale sakafuni kwa makini.





Mama Bigirimana alimtazama Mama Ninziza Bernice kwa wasiwasi na bila kusubiri alianza kukimbilia kule nje huku akiita kwa sauti kubwa yenye hofu, “Baba Ibrahim, mwanao anamuua mtoto wa watu!”

Wakati Mama Bigirimana akiwa anakimbilia kule nje, Mzee Bigirimana naye alikuwa anaingia ndani mbio huku akiwa na wasiwasi mkubwa, wakakumbana mlangoni na kupiga mweleka sakafuni kwa mshindo mkubwa uliowaacha wakigaragara.

Mama Bigirimana alitoa ukelele wa maumivu huku akishika tumbo lake, Mzee Bigirimana alijizoazoa na kuinuka kutoka pale sakafuni huku akikunja uso wake akionekana kusikilizia maumivu, akahema kwa nguvu huku akimtazama mke wake pale sakafuni kwa makini.


ENDELEA...


Kule chumbani Pamela aliendelea kulia kwa uchungu mkubwa akiwa bado yupo pale sakafuni kashika tumbo lake. Ibrahim alisimama huku akimtazama kwa hasira, akamnyooshea kidole chake kwa hasira na kumfuata pale sakafuni akitaka kumpa kichapo kingine. Hata hivyo, hakuwahi kwani mlango wa chumbani kwao ulipigwa kumbo na kumfanya Ibrahim ashtuke sana na kugeuka kuangalia kule mlangoni.

Akamuona Nduwimana akiingia mbio ndani ya chumba chao pasipo hata kubisha hodi na kusimama huku akimtazama baba yake kwa chuki. Pamela akiwa bado yupo sakafuni alimuona Nduwimana na kujinyanyua huku akiendelea kulia kwa uchungu.

“Tafadhali niache niwalee wanangu,” Pamela alisema huku akijizoa zoa kutoka pale sakafuni.

“Huyu mama yako ni jeuri na mjinga sana, sasa atakula jeuri yake,” Ibrahim alimwambia Nduwimana huku akisonya. Kisha akataka kumfuata tena Pamela akitaka kumwadhibu lakini Nduwimana aliyekuwa akimtazama baba yake kwa chuki alimshika miguu yake na kumng’ang’ania huku akipiga kelele na kulia kwa sauti kubwa.

“Mwache mama yangu! Mwache mama!” Nduwimana alikuwa anasema huku akilia.

Ibrahim alijaribu kujinasua kutoka kwenye mikono ya Nduwimana lakini Nduwimana aliendelea kumng’ang’ania pasipo kumwachia huku akizidi kupiga kelele na kufanya sauti yake na ile ya mama yake zizidi kupaa na kusambaa hewani hata katika eneo la jirani katika ule usiku tulivu.

Mzee Bigirimana na Mama Bigirimana walipanda ngazi mbio kuelekea kule juu huku wakiwa na wasiwasi mkubwa. Nyuma yao walifuatwa na Mzee Tugiramahoro na mkewe ambao walikuwa wakipanda ngazi huku wakiwa na wasiwasi mkubwa.

Mzee Bigirimana na Mama Bigirimana walipofika kwenye korido wakitaka kuelekea kwenye chumba cha Ibrahim na Pamela wakashtulia na Samantha aliyewapita mbio akielekea kule kwenye chumba cha wazazi wake huku akilia kwa uchungu. Alipoufikia mlango wa chumba cha wazazi wake aliupiga kumbo, akaingia na kuuacha mlango ukiwa wazi.

Mama Bigirimana na Mzee Bigirimana walisimama ghafla na kurudi nyuma wakionesha nidhamu katika kuendeleza mila na desturi za Kiafrika za kutotaka kuona kile kilichokuwa kinaendelea ndani ya chumba cha watoto wao. Muda huo huo Mama Ninziza Bernice na mumewe nao wakafika na kusimama nyuma yao, wote wakiwa na wasiwasi mkubwa. Kisha wakawa wanasikilizia kwa makini sauti za vilio kutoka mle chumbani.

Nduwimana aliendelea kumng’ang’ania baba yake huku akilia, Samantha alipoingia alimkumbatia mama yake ambaye alikuwa bado yupo sakafuni, wote wakawa wanalia kwa uchungu na kufanya kile chumba kigeuke ukumbi wa simanzi na vilio kutoka kwa mama na watoto wake.

Ibrahim alibaki amesimama pasipo kufanya chochote, Pamela akainuka kutoka pale sakafuni na kujikung’uta mavumbi kisha akamkumbatia Samantha kwa uchungu huku akifuta machozi na kwenda kuchungulia kwenye ule mlango uliokuwa wazi. Akawaona wazee wote wanne wakiwa wamesimama pale nje ya mlango huku wakiangalia kwenye ule mlango kwa wasiwasi.

Mama Bigirimana alipomuona tu Pamela akashusha pumzi za ndani kwa ndani huku akionesha mashaka yake. “Mwanangu, uko salama kweli?” alimwuliza Pamela huku akishindwa kufika hofu aliyokuwa nayo.

“Hapana mama, nimo mashakani.”

“Mama, naomba niitie mumeo haraka, mwambie namhitaji huku chini,” Mzee Bigirimana alimwambia Pamela huku akiwa amepandwa hasira.

“Sawa, baba,” Pamela alisema na kuufunga ule mlango nyuma yake akiwaacha wale wazee bado wamesimama pale pale wakiendelea kuutazama ule mlango wa chumbani kwa wasiwasi.

Mzee Tugiramahoro na mke wake wakaangaliana kisha yule mzee akampa ishara mke wake amfuate kule chini huku akigeuka kuondoka na kuzifuata ngazi za kurudi sebuleni, mkewe naye akaondoka, wakaanza kushuka ngazi huku kila mmoja akiwa na hisia nzito.

Wakati wakiwa wanateremka zile ngazi taratibu Mzee Tugiramahoro alikuwa anasonya kwa hasira huku akionekana kukasirishwa sana na kitendo cha Ibrahim kumpiga Pamela.

“Yaani jitihada zangu zote za kumkuza mtoto wa kike leo hii navuna ufedhuli huu!” Mzee Tugiramahoro alisema kwa huzuni huku akigeuza shingo yake kumtazama mkewe.

“Binti yangu si fedhuli na sikumlea kifedhuli, hivyo hastahili kutendewa anayofanyiwa hapa, na laiti angelikuwa na baba mwenye kumpenda basi leo angesimama kidete kumtetea,” Mama Ninziza Bernice alisema kwa masikitiko.

“Kwa hiyo, unamaanisha kuwa mimi simuonei uchungu binti yangu, siyo?”

“Kama una uchungu basi fanya kile kinachostahili ili kumnusuru mwanao katika uonevu huu anaofanyiwa… tupo kwenye nchi yetu kwa nini tunyanyasike utadhani ni wakimbizi?”

Mzee Tugiramahoro alionekana kuguswa sana na yale maneno ya mkewe, akamwangalia kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akilamba midomo yake iliyoanza kukauka, kisha hakuongea tena, akawa anashuka ngazi kimya kimya huku akionekana kuzama kabisa kwenye lindi la mawazo.

Walipofika pale sebuleni, Mama Ninziza Bernice aliketi kwenye sofa huku akiwa bado ana wasiwasi, mumewe alikataa kuketi na kubaki akiwa amesimama huku amejishika kiuno. Sasa donge la hasira lilizidi kumkaba kooni na kumfanya apumue kwa shinda. Alisonya kwa hasira na kuanza kukunja mikono ya shati lake kisha akakwida suruali yake tayari kwa lolote.

“Nawasubiri waje! Leo watanitambua!” Mzee Tugiramahoro alisema kwa hasira huku akitazama kule kwenye ngazi. Muda huo huo Mzee Bigirimana na mkewe walionekana wakiziendea zile ngazi kisha wakaanza kushuka taratibu huku wakiongea kwa sauti ya chini. Mzee Bigirimana alikuwa akimuangalia mke wake kwa masikitiko.

“Hivi fedheha gani hii anafanya mwanao! Kama ni kuacha mke amwache basi na aoe mwingine, kwani ana shida gani, mali anayo ni mwanamke gani atamkataa?” Mzee Bigirimana alimwambia mkewe na kumfanya yule mama agune.

“Kuoa ovyo kuna athari zake, hivi unafikiri ni nani mlezi mzuri wa watoto zaidi ya mama?”Mama Bigirimana alisema huku akionekana kutoafikiana kabisa na maneno ya mume wake, alitingisha kichwa chake taratibu kukataa kata kata.

Mzee Bigirimana aligeuza shingo yake kumwangalia mke wake kwa makini, akaonekana kuguswa na yale maneno, alishusha pumzi huku akibaki kimya. Muda ule walikuwa wamefika pale sebuleni na kuwakuta wazee wenzao wakiwa wanawasubiri. Mzee Tugiramahoro alipowaona akawapokea kwa maneno makali huku akianza kutamba pale sebuleni.

“Nasema hivi, nangojea maiti ya binti yangu lakini na mimi leo nitaacha maiti ya mtu mwingine ndani ya nyumba hii,” Mzee Tugiramahoro alisema kwa hasira huku akiranda randa kwa ghadhabu.

“Mzee mwenzangu, najua uchungu ulio nao lakini jaribu kutuliza jazba kidogo… kumbuka kuwa hata jina lako la Tugiramahoro lina maana ya ‘tuwe na amani’,” Mzee Bigirimana alijaribu kumsihi mzee mwenziye.

“Jina ndiyo kitu gani! Yaani nivumilie mwanangu anaumizwa eti kwa kuwa jina langu linamaanisha amani! Na kama kijana wako ameweza kumpiga binti yangu mbele yangu, vipi pale wanapokuwa wenyewe tu?” Mzee Tugiramahoro alisema kwa hasira na kurusha mikono yake juu kudhihirisha hasira aliyokuwa nayo juu ya Ibrahim.




Mzee Bigirimana anamtazama Mzee Tugiramahoro kwa wasiwasi. Anataka kusema lakini anasita na kushusha pumzi.

* * * * *

Alipoufunga ule mlango na kuwaacha wale wazee nje, Pamela alisimama akamtazama Ibrahim kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Muda ule Ibrahim alikuwa amesimama huku amewashika watoto wake, mmoja mkono wake wa kulia na mwingine mkono wake wa kushoto. Pamela aliwasogelea wale watoto na kuwashika mikono kwa upole.

“Nendeni mkalale wanangu, hivi sasa ni saa nane usiku,” Pamela alisema kwa sauti tulivu akijaribu nkuwashawishi wale watoto.

Nduwimana na Samantha walimtazama mama yao kwa wasiwasi kisha wakageuza shingo zao kumtazama baba yao kwa hofu na kuondoka bila ubishi, lakini wakiwa na wasiwasi. Pamela aliwatazama wale watoto kwa upole huku akiachia tabasamu. Walitoka na kuufunga ule mlango nyuma yao.

Pamela akaufungua ule mlango na kuwachungulia ili kuhakikisha wameondoka na kuelekea kwenye vyumba vyao kisha akaufunga tena mlango nyuma yake na kumkabili Ibrahim.

“Unaitwa na baba yako huko chini,” Pamela alimwambia Ibrahim huku akimtazama kwa makini.

Ibrahim alimtazama Pamela kwa kitambo kifupi na kushusha pumzi kisha akageuka kuutazama mlango. “Nakwenda kuwaeleza wazee kwamba hunifai na ninakutwanga talaka.”

“Kwangu itakuwa ni bonge la barafu jangwani,” Pamela alisema huku akiachia tabasamu lililokuwa limebeba chuki.

Ibrahim aliinua mkono wake kutaka kumpiga kibao Pamela lakini akasita, kisha akageuka na kuanza kuondoka lakini kabla hajatoka kabisa aligeuka kumtazama Pamela kwa chuki.

“Utajuta nikikuacha,” Ibrahim alisema huku chuki ikijionesha wazi wazi usoni kwake.

“Kama wewe ndiye mfalme wa upendo na faraja n’tajuta,” Pamela alisema huku naye chuki ikijionesha wazi wazi usoni kwake. Wakatazama kwa sekunde kadhaa bila kusema. Kisha Ibrahim akasonya na kuondoka huku akiubamiza ule mlango kwa hasira. Pamela alishusha pumzi huku akitingisha kichwa chake kwa huzuni.

Ibrahim alianza kushuka ngazi taratibu akiwa na wasiwasi kidogo, alipokaribia kufika sebuleni akasimama na kuchungulia pale sebuleni na kumuona baba yake akiwa kasimama huku amejishika kiuno akitazama kule kwenye ngazi kwa hasira, Ibrahim akaonekana kusita sana. Alisimama pale kwa sekunde chache akionekana kujishauri kama ashuke au akaidi agizo la wazee na kurudi chumbani kwake.

Mzee Tugiramahoro pia alikuwa amesimama akiwa kajiandaa kwa lolote, alikuwa anaranda randa pale sebuleni huku akigeuka mara kwa mara kumwangalia Mzee Bigirimana. Mama Ninziza Bernice na Mama Bigirimana wao walikuwa wameketi kwenye sofa kwa utulivu lakini wakiwa na huzuni iliyochanganyika na wasiwasi.

Ibrahim alijipa ujasiri na kuanza kuzishuka zile ngazi taratibu, aliamini kuwa ndiye mwenye uamuzi wa kumuacha mwanamke yule na kuoa mwanamke mwingine na hakuna yeyote wa kumpangia aishi vipi kwenye nyumba yake. alishuka na kufika pale sebuleni, akasimama huku akiwatazama wale wazee akijitahidi kuzuia hofu iliyokuwa inataka kuutawala moyo wake.

Mzee Bigirimana alimkazia macho Ibrahim yaliyoashiria hasira alizokuwa nazo, na wakati huo huo Mzee Tugiramahoro alikuwa anamwangalia Ibrahim kwa hasira huku akiwa ameuma midomo yake.

Mama Bigirimana na Mama Ninziza Bernice walikuwa wanamwangalia Ibrahim kwa wasiwasi. Ibrahim akasimama karibu na baba yake huku akijaribu kuachia tabasamu pana usoni kwake. Bahati mbaya hakujua nini kilichokuwa akilini kwa baba yake wakati huo.

“Bwana mkubwa, hatukuitwa hapa na mkeo kuja kuoneshwa jinsi ulivyo hodari wa kupiga mke, kama ni huo umwamba sisi hatukuona faida yake enzi zetu,” Mzee Bigirimana alimwambia Ibrahim huku akimtazama kwa makini, hata hivyo Ibrahim aliendelea kutabasamu huku akionesha kujiamini.

“Lakini, baba…” Ibrahim alianza kusema lakini akakatizwa na kibao kikali cha ghafla kilichotua kwenye shavu lake kutoka kwa baba yake na kumwangusha pale sakafuni. Ibrahim alitahayari sana na kujishika shavu lake akiwa haamini kilimchotokea, alimkodolea macho baba yake kwa wasiwasi.

Mzee Bigirimana alimtazama kwa hasira huku akikaa sawa, alikuwa amekunja ngumi tayari kwa mpambano endapo Ibrahim angetaka kuleta matata, akafoka kwa ghadhabu, “Simama sasa unipige mimi kama unavyompiga mtoto wa watu.”

Ibrahim alitaka kusema neno lakini maneno yakawa hayatoki mdomoni, akajizoa zoa kutoka pale sakafuni na kusimama akiwa katahayari sana huku akiendelea kujikuna kwenye lile shavu. Mzee Tugiramahoro aliwatazama Mzee Bigirimana na mwanawe kwa zamu na kutingisha kichwa chake kwa masikitiko.

“Wala haitasaidia kumpiga huyu bwana mdogo, naomba tu umweleze kuwa nashukuru sana kwa yote aliyomfanyia binti yangu, hivi sasa nasubiri ampe talaka usiku huu ili alfajiri niondoke naye.”

Mzee Bigirimana alimwangalia Ibrahim kwa hasira. “Haya baba nadhani umemsikia mkweo, kamtwange talaka mkeo na mimi nikuachie radhi yangu niondoke usiku huu huu, wala sina haja ya kusubiri kukuche.”

Ibrahim aliwatazama wale wazee kwa unyonge sana, akashusha pumzi za ndani kwa ndani. “Mimi niseme nini sasa wakati binti yenu tayari kishaamua kuupeleka unyumba wetu kwa wakili ili akaachwe na mahakama.”

Mzee Tugiramahoro akashituka sana na kumkodolea macho Ibrahim, alionekana kushangaa sana na kumkodolea macho kana kwamba alikuwa ameona kitu cha ajabu sana. Kisha akatingisha kichwa chake kwa nguvu zote.

“Sijazaa mtoto wa kwenda kudai talaka mahakamani!” Mzee Tugiramahoro alisema huku akishusha pumzi.

“Lakini hiyo ndiyo hali halisi, sasa mnatarajia nini kutoka kwangu? Kwa kweli mnanionea bure!” Ibrahim alisema kwa unyonge mkubwa.

Mzee Bigirimana akamkodolea macho Ibrahim akiwa haamini kile alichokisikia na kutingisha kichwa chake taratibu kukataa. “Haiwezekani! Yaani mwanamke adai talaka hivi hivi tu!”

Ibrahim aliwatazama kwa makini na kuinamisha kichwa chake chini, akakunja sura yake iliyotengeneza matuta madogo usoni huku donge la hasira ya kupigwa kibao na baba yake likiwa limemkaba kooni. Mzee Tugiramahoro akiwa bado anashangaa, alimsogelea Ibrahim huku akimkazia macho.

“Wewe si ndiye mumewe, tueleze sababu inayomfanya mkeo adai talaka mahakamani, kama ni kweli hayo usemayo!”

“Hakuna kingine ni wivu tu, anadai haki sawa eti kwa vile yeye kasoma na siyo kama mama yangu,” Ibrahim alisema kwa huzuni huku akitingisha kichwa chake kwa huzuni.

Mzee Bigirimana aligeuka kumtazama mkewe kwa makini kisha akayarudisha macho yake kumwangalia Ibrahim. “Usawa wa namna gani anaoudai mkeo?”

“Usawa wa kimaisha ili aweze kwenda baa na kunywa pombe kama mimi, aweze kujiamulia chochote kile mwenyewe bila kupangiwa, na pengine anataka kufuga ndevu kama wanaume walivyo!” Ibrahim alisema kwa kujiamini huku akiinamisha kichwa chake.

Kikazuka kitambo kirefu cha ukimya huku sebule yote ikizizima kwa ukimya ule, kila mmoja alionekana kuzama kwenye tafakari nzito kuhusu kauli ile aliyoitoa Ibrahim.

Mzee Bigirimana alivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu huku akionesha kuyaamini yale maneno ya Ibrahim kwa asilimia zote.

“Kama mazingira ndiyo haya, nakushauri mpe talaka haraka na nitahakikisha unapata mke atakayetambua wazi kwamba mwanamke siku zote ni kajakazi tu kwa mwanaume, azae na kulea watoto basi,” Mzee Bigirimana alisema huku akipumkua kwa nguvu.




Mama Bigirimana akamtazama mumewe kwa jicho kali huku akiguna, akatingisha kichwa chake kwa huzuni huku akionekana kutofautiana kabisa na yale maneno ya mumewe. Wakati huo huo Mzee Tugiramahoro alimsogelea mkewe na kuongea naye kwa sauti ya chini.

“Umesikia mambo ya binti yako? Kumbe kibiritingoma ni yeye… tangu lini mwanamke akawa huru akiwa kaolewa, na haki hiyo aipate wapi?”

Mama Ninziza Bernice alionekana kukerwa zaidi na maneno ya mume wake, akamwangalia kwa makini na kushusha pumzi huku akitingisha kichwa chake taratibu.

“Sidhani kama maneno haya yana ukweli wowote, binti yangu namjua vizuri, hajawahi na hana tabia kama hiyo!” Mama Ninziza Bernice alisema kwa kujiamini na kuwafanya watu wote wageuke kumtazama kwa mshangao. Donge la hasira lilikuwa limemkaba kooni na kumfanya aanze kulengwa na machozi, alimtazama Mzee Bigirimana kwa makini.

“Naomba niitieni binti yangu nimsikie mwenyewe mbele yenu, na kama ni kweli haya asemavyo mwanenu basi usiku huu huu nitaondoka naye, maana kibaya chako ni chako, vizuri waachie wenye navyo.”

Mzee Tugiramahoro alimtazama mke wake kwa makini na kuonekana kuafiki maneno yake huku akionesha kutokuwa na msimamo, hakujua asimamie upande upi. Sasa donge la hasira lilikuwa limesimama kwenye koo lake na kumfanya ashindwe kupumua vizuri, akaona kuwa hakuwa na namna nyingine ya kuliondoa isipokuwa kusema kile alichodhani kuwa ni sahihi.

“Bwana mdogo, unaweza kuwadanganya watu wote kwa muda fulani tu lakini siyo muda wote. Sisi si wajinga kama unavyodhani japo hatukusoma kama wewe, ikiwa umepanga kumwacha binti yangu basi mwache kwa usalama ila usitake kutafute sababu zisizoeleweka, lakini nataka nikwambie kabisa sitakubali bali nitapigania haki yake hadi mwisho…” Mzee Tugiramahoro alisema na kuwafanya watu wote wamtazame kwa mshangao uliochanganyika na wasiwasi.

“Na mimi nataka ukamwite binti yangu ili nimsikie mwenyewe mbele yako, kisha nitajua cha kufanya,” Mzee Tugiramahoro aliongeza huku akimkazia macho Ibrahim.

Ibrahim alimtazama Mzee Tugiramahoro kwa wasiwasi, akataka kusema neno lakini akasita sana na kuonekana kutahayari sana. Aliendelea kumkodolea macho yule mzee kwa wasiwasi kwa kitambo fulani kisha akainamisha kichwa chake kutazama chini huku akishusha pumzi ndefu.

“Nadhani umewasikia wakwe zako, nenda kamwite mkeo, mbona bado upo hapa?” Mzee Bigirimana alimwambia Ibrahim kwa sauti iliyojaa hasira huku akimkazia macho.

Ibrahim alishusha pumzi ndefu akionekana kusita sana, akamtupia jicho la wasiwasi Mzee Tugiramahoro.

“Sisi siyo wajinga, hatuwezi kuacha shughuli zetu huko tukaja hapa kuchezeshwa kama vikaragosi! Itashangaza sana mke atuite kuja kusaidia kutafuta ufumbuzi wa ndoa yake halafu eti kumbe huyo huyo ndiye amekwenda kutafuta talaka mahakamani! Huu si upuuzi wa karne!” Mzee Tugiramahoro alisema huku akimkazia macho Ibrahim.

“Ni kweli… mimi sitaki kumtetea mwanangu, ukweli ni bora usemwe kuliko kuficha ficha, maana hatukuja hapa kuwatenganisha wanetu ila kuwaweka sawa ili waishi vizuri na kulea watoto wao…” Mama Bigirimana ambaye muda mwingi alikuwa kimya alisema kwa huzuni.

Mama Ninziza Bernice alitaka kusema neno lakini akashindwa, machozi yakaanza kumtoka na kutiririka kwenye mashavu yake. Mzee Bigirimana alitaka kusema lakini hatia ikamkaba kooni na kubaki kimya akiwatumbulia macho wazee wenzake.

“Kama hali ndiyo imefikia hapa sitakuwa na furaha tena iwapo binti yangu ataendelea kuishi kwenye nyumba hii, ni bora niondoke naye!” Mama Ninziza Bernice alisema kwa huzuni huku akifuta machozi.

Kauli ile ikaonesha kumuogopesha sana Mama Bigirimana ambaye alimtazama Mama Ninziza Bernice kwa wasiwasi kisha akageuka kumtazama Ibrahim.

“Kama akili yako imefikia hatua hiyo ya kutaka kumwacha mkeo ili uoe mwanamke mwingine, nasema huyo mwanamke sitakuwa na radhi naye na wala hataingia humu ndani, na utakapooa tu nakuachia laana, bora nijue kuwa sina mtoto kuliko kunitia aibu kiasi hiki!” Mama Bigirimana alisema kwa hasira na kufunika uso wake kwa viganja vya mikono yake, machozi yalianza kumtoka.

Ibrahim alikuwa amechangayikiwa kabisa, aliwatazama wale wazewe bila kujua afanye nini, kikazuka tena kitambo kirefu cha ukimya pale sebuleni, kila mmoja alionekana kutafakari kwa kina. Ibrahim alikuwa ametahayari sana, akainamisha kichwa chake chini kwa wasiwasi.

Mzee Bigirimana alikuwa akimtazama kwa makini huku naye akionekana kuwaza mbali sana, kisha akakohoa kidogo kurekebisha sauti yake.

“Haya baba, nadhani umewasikia mama zako… wewe ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ikiwa kusuka ama kunyoa. Mimi sitii tena neno hapo…” Mzee Bigirimana alisema huku akishusha pumzi.

“Hapa suluhu ni moja tu, akamwite mkewe ili tusikie na upande wa pili, mimi sioni sababu ya kumlazimisha huyu bwana aendelee kuishi na mke ambaye tayari ameshaamua kumwacha,” Mzee Tugiramahoro alisema kwa sauti iliyoashiria kuwa alikuwa na hasira.

“Jamani, kutokana na maelezo tuliyoyapata kutoka kwa mkwe wangu yanadhihirisha kabisa huyu bwana ni muongo, sioni kwa nini tusiamue tu,” Mama Bigirimana alijaribu kushauri.

“Tunaamuaje katika mazingira ya aina hii, kumlazimisha mtu aishi na mtu aliyemchoka ni hatari sana, ni bora tukubaliane na uamuzi wake hata kama hatuupendi ili asije akamuua bure!” Mzee Tugiramahoro alisisitiza huku akionekana wazi kutotaka suluhu.

“Kwa maana hiyo, tusichukue hatua yoyote eti kwa sababu tutaonekana tumemlazimisha! Kwani tulichoitiwa hapa na mkwe wangu ni nini kama si kutafuta suluhu?” Mama Bigirimana alihoji huku naye akianza kukosa uvumilivu.

“Ndiyo maana nataka huyo aliyetuita hapa aitwe ili tutakapoamua tuwe tumepata nafasi ya kuwasikia wote wawili na wao tuwape nafasi, ili tukiamua basi tuamue mbele yao wote wawili,” Mzee Tugiramahoro alisisitiza.

Watu wote wakaonekana kuafikiana na maneno yale bila kipingamizi, kisha macho yote yakamtazama Ibrahim kwa makini huku kikizuka kitambo kingine cha ukimya mzito.

Ibrahim alionekana kugwaya sana, akawatazama wale wazee huku akitamani kulia. Aliinuka na kwenda kuanguka miguuni kwa Mama Bigirimana na Mama Ninziza Bernice, akaishika miguu yao huku akitokwa machozi.

“Mama zangu, naomba mnisamehe. Nimewakosea sana wazazi wangu, na siyo nyinyi tu, nimemkosea pia Pamela mke wangu, watoto wangu na nimeikosea nafsi yangu vile vile…” Ibrahim alisema kwa huzuni.

“Nenda kamuombe msamaha mkeo kwanza, kisha mje wote hapa tuyazungumze,” Mama Bigirimana alisema huku akimkazia macho Ibrahim.

Ibrahim alinyanyua uso wake kumtazama mama yake kwa huzuni, kisha akasimama akiwa mnyonge mno na kuondoka kutoka eneo lile huku akitazamwa na macho ya wale wazee wote kwa makini. Alizipanda ngazi taratibu na kupotelea ghorofani.




Alifika kwenye mlango wa chumba chake na kusimama, akajifuta machozi na kufungua mlango na kuingia chumbani huku akiufunga mlango nyuma yake, kisha akasimama pale mlangoni akiuegemea ule mlango, akamwangalia Pamela huku akiwa amekunja sura yake na kushusha pumzi.

Pamela alikuwa ameketi kitandani akiwa kajiinamiaakiwa anawaza mbali sana. Alipohisi ujio wa Ibrahim mle ndani aliinua uso wake kumwangalia, macho yake yalikuwa yanadhihirisha chuki aliyokuwa nayo kwa Ibrahim. Alimtazama kwa sekunde chache kisha akageuza shingo yake kuangalia upande mwingine huku akiendelea kuonesha chuki yake kwa mumewe.

“Hivi ni mambo gani haya yasiyoisha?” Ibrahim alimuuliza Pamela huku akimtazama kwa makini. Pamela akamkata jicho Ibrahim bila kusema neno.

“Hata kama ni kudai haki, ni haki ipi inapatikana kwa kumletea nyodo unayetaka akupe hiyo haki?” Ibrahim alisema kwa sauti tulivu lakini kavu.

“Tafadhali naomba uniache. Sitaki kabisa kuendelea kubishana na wewe saa hizi!” Pamela alisema huku donge la hasira likizidi kumkaba kooni.

”Unan'letea jeuri ya kwenu, siyo? Mi naongea na wewe kistaarabu lakini wewe unaleta jeuri! Kwa taarifa yako hata ukinuna mimi ndiye mwanaume humu ndani, wewe utabaki kuwa mwanamke tu wa kulea watoto basi!” Ibrahim alisema huku hasira mpya ikifumuka ndani yake.

Pamela alimtazama Ibrahim kwa makini kuanzia juu na kumshusha hadi chini, akakunja sura yake na kuinuka kisha akaelekea nje kwenye balcony akionekana kutomjali mumewe, kitendo kile kikaonekana kumkera sana Ibrahim.

“Hmm! Najuta sana kukuoa…” Ibrahim alisema kwa huzuni.

“Hata mimi najuta kuolewa na wewe, tena najuta majuto ya Firauni!”

Ibrahim alimtazama Pamela kwa makini kisha akapiga hatua kumfuata kule kwenye balcony na kusimama mbele yake, alimtazama kwa kitambo kirefu na kushusha pumzi ndefu kwa masikitiko.

“Kilichobaki ni kukutwanga talaka tu nikaoe mwanamke wa kwetu Tanzania.”

“Kaoe hata kesho, kwani unadhani nababaika! Ila ujue tu kuwa haki yangu haitapotea na watoto wangu hawawezi kulelewa na mwanamke mwingine kama bado niko hai.”

Ibrahim akaduwaa asijue la kufanya, alimkodolea macho Pamela huku akihisi donge la hasira likianza kumkaba kooni, akaminya midomo yake akionekana kuzuia hasira. Hata hivyo, alionekana kuchanganyikiwa zaidi na kukosa neno la kusema. Akashika kiuno chake kwa mikono yake miwili na kusimama akimtazama Pamela kwa makini.

Mawazo kibao yakaanza kupita kichwani kwake; alijiuliza inamaana Pamela alikuwa amekusudia kweli kuachwa au alikuwa anatingisha kiberiti ili aone kama kimejaa njiti? Na kama ni kweli alikuwa amekusudia kuachwa, ilimaanisha kuwa alikuwa amekwisha pata mwanaume mwingine? Na kama sivyo kulikuwa na nini alichojivunia?

Ibrahim alifikiria sana akakosa majibu, hata hivyo akajipa moyo kuwa hata kama Pamela angeondoka, hakuwa mwanamke peke yake duniani, mbona wapo wengi tu wazuri na wachapakazi, kama Jeanine…

Alipomkumbuka Jeanine akasita sana, ikamjia picha ya fumanizi pale nyumbani kwa Jeanine. Hakuipenda sana ile picha ya kumfumania mwanamke aliyekuwa akimpenda na kumuamini sana akiwa na mwanamume mwingine! Hasira zikamchemka zaidi ndani kwa ndani na hapo akajikuta akisonya kwa hasira.

Pamela aligeuka kumtazama Ibrahim kwa makini akadhani kuwa ni yeye aliyekuwa akimsonya. Ibrahim aligundua akajibaraguza huku akilazimisha tabasamu lililoonekana usoni lakini moyoni akiwa ana roho iliyojaa uchungu. Alionesha wasiwasi mwingi, akamwangalia Pamela kwa makini huku akiendelea kuonesha tabasamu.

Pamela aliketi pale kwenye kiti cha kupumzikia kilichokuwa kwenye balcony huku akimtazama Ibrahim kwa makini, macho yake yalikuwa yanaonesha uchungu. Akatingisha kichwa kwa huzuni.

Ibrahim alimtupia jicho la wizi na kuonekana akijishauri kama aendelee kumsemesha au aondoke zake. Akashusha pumzi na kuuma midomo yake huku akiwaza kidogo, kisha anamsogelea na kupeleka mkono wake wa kulia kwenye uso wa Pamela kwa uangalifu huku akiachia tabasamu, si kwa kulazimisha.

“Usiniguse!” Pamela aliusukuma mkono wa Ibrahim kwa hasira na kumfanya Ibrahim aminye midomo yake huku akimtazama kwa makini, alimtazama kwa kitambo kirefu bila kusema neno. Wakabaki wanaangaliana kama majogoo waliotaka kupigana.

Kisha Ibrahim alikwenda kujiegemeza kwenye ukuta wa ile balcony huku akionekana kufikiria kidogo, kiukweli muda ule alikuwa amechanganyikiwa zaidi na hakujua afanye nini. Alijishika kichwa chake kwa mikono yake miwili na kuinamisha kichwa chini. Pamela akamwangalia kwa makini bila kusema neno.

Baada ya muda wa sekunde kadhaa, Ibrahim alimtazama Pamela, akamsogelea tena na kukaa sakafuni mbele yake huku akiishika miguu ya Pamela na kuanza kutembeza mikono yake kwenye miguu ya Pamela, kuanzia magotini mpaka unyayoni. Pamela hakumzuia bali alibaki kimya akimtazama kwa makini.

“Pamela, naomba unisamehe… ni kweli nilitaka kukuacha lakini nimegundua kuwa wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu na chaguo kutoka kwa Mungu… tafadhali usinihini nafasi ya kuwa mimi pekee ninayestahili kuchezea miguu hii,” Ibrahim alimsihi Pamela na kuegemeza kichwa chake juu ya magoti ya Pamela.

Donge la hasira lililizidi kumkaba Pamela kooni, alimwangalia Ibrahim kwa makini huku akiona kama aliyekuwa akimchezea akili yake, machozi yakaanza kumtoka na kumdondokea Ibrahim, ambaye aliinua uso wake kumwangalia Pamela kwa mshangao.

“Usilie, nadhani anayestahili kulia ni mimi, na wala siyo wewe Pamela… kitu gani kinachokuliza?” Ibrahim alimuuliza Pamela huku akimtazama kwa makini.

“Naomba niache tafahdhali… silii kwa sababu nakupenda ila kinachoniliza ni hayo maigizo yako,” Pamela alisema huku akimsukuma kando Ibrahim na kuinuka, akasimama na kujiegemea kwenye ukuta wa balcony, macho yake akayaelekeza kutazama kule chini ya ghorofa huku akionekana kuwaza mbali.

Ibrahim alibaki akiwa amepiga magoti pale pale sakafuni huku akimkodolea macho Pamela huku akionekana kuchanganyikiwa zaidi, alitamani kulia.

“Nimegundua kuwa kumbe muda wote wa ndoa yetu ulikuwa hunipendi, ulikuwa unatafuta sababu ili tugombane uondoke!” Ibrahim alisema kwa huzuni.

Pamela akageuka kumtazama Ibrahim kwa mshangao, alimkazia macho akiwa na maswali mengi kichwani kwake yaliyokosa majibu.

“Imekuwaje huyu mwanaume akabadilisha ghafla msimamo wake wa kutaka kuniacha na kuwa mpole kiasi hiki! Ni nini kimetokea kule sebuleni alikokuwa ameitwa na wazee? Je, amelazimishwa kuja kuniomba radhi au ni kweli amegundua kuwa mimi ndiye mwanamke wa maisha yake kama anavyodai?” Pamela aliwaza na kukosa majibu.

Alimtazama Ibrahim kwa makini huku yale maswali na mengine mengi yakizidi kuzunguka kwenye akili yake na kuonekana kumchanganya zaidi, hata hivyo aliapa kuendelea kukaza kamba ili aone mwisho wa maigizo ya Ibrahim.

“Kama umegundua kuwa nilikuwa sikupendi sijui unasubiri nini sasa, fanya kile ambacho umegundua kuwa nakisubiri kwa hamu,” Pamela alisema huku akimtazama Ibrahim kwa makini.





“Hivi jema kwako ni lipi, tuendelee kugombana na hatimaye tuachane ili watoto wetu wateseke au tusameheane na tuanze ukurasa mpya?” Ibrahim alimuuliza Pamela huku akionesha mshangao mkubwa.

“Ukurasa mpya kauanze na mwanamke mpya, na mimi niache nianze ukurasa mpya kivyangu.” Pamela alisema na kumfanya Ibrahim ashtuke sana.

“Kama umekusudia kuachwa hapa sahau, mimi najua kuoa tu sijui kuacha,” Ibrahim aling’aka kwa hasira.

“Na ulipotaka kuniacha hukujua kama hujui kuacha? Naona unajitekenya na kucheka mwenyewe! Nasema hivi, leo bila talaka yangu humu ndani hakukaliki wala hakulaliki,” Pamela alisema kwa ukali huku akimkazia macho Ibrahim.

“Hivi uko yakini Pamela?” Ibrahim alimuuliza Pamela kwa mshangao.

“Niko yakini kabisa, nafahamu ninachokisema!” Pamela alijibu huku akiendelea kumtulizia macho Ibrahim.

Ibrahim akazidi kuchanganyikiwa, alimtazama Pamela kwa kitambo kirefu na kushusha pumzi, kisha akatingisha kichwa chake kwa masikitiko na kuondoka, akaelekea kwenye mlango, akaufungua na kutoka nje kimya kimya huku akiufunga ule mlango nyuma yake.

Pamela alimtazama kwa mshangao wakati akiondoka na kushusha pumzi, kisha akaketi pale kwenye kiti cha kupumzikia pale kwenye balcony. Baada ya muda mfupi alisikia hodi inabishwa mlangoni, akainuka na kwenda kufungua mlango na kuchungulia nje, akamuona Mama Bigirimana akiwa amesimama pale mlangoni akiwa na sura iliyosawajika kidogo.

“Mama yangu, kulikoni! Mbona tumepata taarifa za kutatanisha?” Mama Bigirimana alimuuliza Pamela huku akiwa bado katika sura iliyosawajika.

“Habari zipi za kutatanisha, mama?”

“Tumeambiwa eti hutaki kumsamehe mumeo ila unachodai ni talaka tu?”

Pamela akaachia mguno ulioambatana na tabasamu, alipotaka kusema neno Mama Bigirimana akamkatiza.

“Kama hutajali wazazi wako wanakuhitaji mara moja huko sebuleni. Najua hivi sasa ni usiku wa manane na ungependa kupumzika lakini nia yetu ni njema tu, mama yangu,” Mama Bigirimana alisema huku akishusha pumzi.

“wala usijali mama, nakuja sasa hivi,” Pamela alisema na kurudi chumbani huku akiufunga mlango nyuma yake.

Mama Bigirimana aliutazama ule mlango kwa wasiwasi kisha akazifuata ngazi na kuanza kushuka akielekea sebuleni. Pale sebuleni kimya kizito kilikuwa kimetawala, watu walikuwa wameketi wakiwa wametahayari huku kila mmoja akiwaza lake na wakionekana kusubiri kwa hamu kusikia kilichokuwa kinaendelea. Ibrahim alikuwa ameketi akiwa kajiinamia kwa huzuni.

Mama Bigirimana alifika pale sebuleni peke yake bila Pamela huku akiwa anatembea taratibu na kuwafanya wote wageuze shingo zao kumtazama kwa wasiwasi.

“Anakuja!” Mama Bigirimana alisema huku akiketi juu ya kochi baada ya kuona macho yote yalikuwa yanamtazama kwa wasiwasi.

Haikuchukua muda Pamela akafika pale sebuleni na kusimama akiwatazama wale wazee kwa mashaka kidogo. Mama Bigirimana alisogea na kuacha nafasi kidogo huku akimuashiria Pamela aketi jirani yake. Pamela alikwenda kuketi pale na kubaki kimya akiwatazama wale wazee kwa wasiwasi.

Kisha macho yake yakatua kwa Ibrahim ambaye alikuwa ameinamisha uso wake kutazama chini, hofu ikaanza kumtambaa Pamela mwilini mwake. Kitambo kifupi cha ukimya kikazuka pale sebuleni huku wale wazee wakitazamana kwa makini, kisha Mzee Tugiramahoro akakohoa kidogo kurekebisha sauti yake.

“Haya mama, hebu tuambie, kulikoni! Mbona tumepata taarifa za kutatanisha?”

Pamela alimtazama baba yake kwa makini kisha macho yake yakahama na kuwatazama wale wazee wengine, na mwisho akamalizia kwa Ibrahim na kushusha pumzi.

“Ndiyo baba, nadai talaka, ni Ibrahim ndiye anayeleta utatanishi kwa kutotoa talaka!” Pamela alisema na kuwafanya wale wazee wamwangalie kwa mshangao mkubwa.

Mzee Tugiramahoro alionekana kukerwa mno na ile kauli, hasira iliyochanganyika na mshangao mkubwa ikaibuka ndani yake.

“Hivi u mzima kweli wewe, au una wazimu?” Mzee Tugiramahoro alimuuliza Pamela kwa sauti kali.

“Mungu apishe mbali, sina wazimu, sikupagawa, sikurogwa na wala sina kichaa. Najua ninachokifanya baba! Nisaidieni kumwambia Ibrahim kuwa nataka talaka yangu sasa hivi!” Pamela alisisitiza huku akionekana kujiamini.

Mzee Tugiramahoro alitaka kusema lakini akasita na kugeuza shingo yake kumtazama mkewe kisha akainua mabega yake juu na kuyashusha akionekana kuchanganyikiwa huku akiwa hana la kufanya.

Wazee wote walionekana kuchanganyikiwa, walimtazama Pamela wakiwa hawaelewi ni kipi kilichomfanya awaite, maana mwanzoni walidhani alikuwa amewaita pale kuja kutatua mgogoro wa ndoa yao lakini sasa alionesha kuwa alitaka wamsaidie kudai talaka! Mama Bigirimana alimwangalia Pamela kwa huzuni.

“Mama, ni sababi zipi hasa zimekufanya utake mumeo akutaliki?” Mama Bigirimana alimuuliza Pamela kwa sauti tulivu.

Pamela alimtazama yule mama huku aking’atang’ata midomo yake na kufikicha ncha ya nguo aliyokuwa amejitanda kichwani.

“Ni kwa sababu nampenda sana na ninathamini maendeleo yake… mama!” Pamela alijibu huku akiiangalia ile ncha ya nguo na kuwafanya watu wote wamwangalie kwa mshangao.

Wale wazee waliendelea kumwangalia Pamela kwa muda kisha wakaangaliana wenyewe kwa wenyewe. Ibrahim aliduwaa na kubaki akimwangalia Pamela kwa mshangao zaidi.

“Sasa, kama unampenda sana na unathamini maendeleo yake mbona unataka akuache?” Mama Bigirimana alimuuliza Pamela huku mshangao ukiwa haujamtoka usoni kwake.

Pamela alinyanyua uso wake na kuwaangalia kwa makini wale wazee, hasa Mzee Tugiramahoro na Mzee Bigirimana. Akaonekana kusita na kumeza mate huku akimtupia jicho Ibrahim. Muda ule Ibrahim alionekana kuchanganyikiwa zaidi, jasho lilikuwa linamtoka.

“Kwa sababu sioni sababu kwa nini tumlazimishe kuishi na mtu aliyepanga kumtaliki badala ya kuheshimu maamuzi yake, mbona yeye haulizwi kwa nini alitaka kuniacha na kuoa mwanamke mwingine na kwa nini sasa hivi ananiona nafaa?”

Kauli ile ikafanya pazuke tena ukimya, wale wazee wote wakabaki kimya wakimtazama Pamela kwa makini. Mama Bigirimana akashusha pumzi ndefu huku akibetua kichwa chake akionekana kumwelewa Pamela na kuafikia naye.

“Hilo nalo neno! Mimi nipo upande wako mama, wanaume wanapaswa watambue kuwa mwanamke si mtumwa, tena wewe umekuwa muungwana sana, mwanzo alipokuja hapa alisema yake lakini sasa hayasemi… kwa nini tumuonee haya mtu asiyetuonea haya?”

Ibrahim aliwaangalia wale wazee huku akionekana kugwaya sana. Aliinamisha uso wake akiwa hana la kusema, machozi yalianza kumlengalenga. Pamela alimtazama Ibrahim kwa makini huku akijitahidi kuyazuia machozi ambayo yalianza kumtoka.

“Baba Samantha, nakupenda sana, kwa nini nisikuache huru ukaishi na mwanamke unayempenda. Ulipanga kuniacha ili uoe mwanamke anayekufaa na sasa unaniomba msamaha kwa kuwa wazee wamekulazimisha kufanya hivyo, sijui hapa pendo liko wapi? Hivi utalazimishwaje kuishi na mwanamke uliyemchoka eti kwa kuwa wazee wamekulazimisha? Ndiyo maana nataka unitaliki ili uwe huru kutafuta pendo la kweli…” Pamela alimwambia Ibrahim kwa sauti tulivu.

“Mwambie mama, mwambie mpumbavu huyu,” Mama Bigirimana alidakia na kuwafanya watu wengine wageuke kumwangalia kwa mshangao.

Sasa machozi mengi yalikuwa yanamtoka Ibrahim, alitaka kusema neno lakini akashindwa kuwa kuwa maneno yalikuwa hayatoki, akaanza kulia kilio cha kwikwi. Muda ule ule aliinuka, akamfuata Pamela na kuanguka miguuni kwake kisha akaishika miguu yake huku akiendelea kulia kwa uchungu.

Pamela alimtazama Ibrahim kwa huzuni, akajitahidi kuyazuia machozi yake. Mzee Tugiramahoro aliinuka na kumfuata Ibrahim, akamshika mabega na kumnyanyua kutoka pale alipokuwa amelala, kisha akampa ishara Mama Bigirimana akimtaka ainuke na kumpisha Ibrahim.

Mama Bigirimana alitii na kupisha, Mzee Tugiramahoro akamkalisha Ibrahim kando ya Pamela na kunyanyua kiganja cha mkono wa Pamela kisha akakikutanisha na kiganja cha mkono wa Ibrahim.

“Pamela, mumeo amejua makosa yake na sasa anataka muanze upya, sioni kwa nini usimsamehe…” Mzee Tugiramahoro alisema na kuwatazama wazee wengine.

“Na ikiwa mimi ni mzazi wenu, basi kwa niaba ya wazazi wenzangu wote naiombea kwa Mungu ndoa yenu idumu zaidi na zaidi, isiwe na migogoro tena wala visasi,” Mzee Tugiramahoro alisema na watu wote pale sebuleni wakaitikia, “Amina!”


MWISHO.


0 comments:

Post a Comment

Blog