Simulizi : Hadi Lini
Sehemu Ya Nne (4)
“Ndiyo, usiku huu maana raha ya mchuzi uunywe ukiwa bado wa moto.”
Ibrahim alitaka kusema neno lakini akasita, alimtazama baba yake huku akionesha uso wa mashaka, akaitazama tena saa yake ya mkononi na kushusha pumzi.
“Sawa, baba!” hatimaye alisema huku akabetua kichwa chake kukubali, kwani hakuwa na namna nyingine yoyote ya kufanya isipokuwa kukubali.
Alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiuma mdomo wake wa chini na kuanza kupiga hatua kuelekea ghorofani. Akaanza kuzipanda zile ngazi haraka haraka hadi ghorofani na kutokea kwenye korido pana iliyokuwa inatazamana na milango miwili.
Pia kulikuwa na milango mingine miwili katika korido nyingine fupi iliyokuwa kushoto na upande wa kulia uliokuwa mwisho kabisa wa ile korido.
Ibrahim hakusimama bali alikwenda moja kwa moja hadi kwenye mlango wa mwisho kabisa wa ile korido fupi, akafika na kushika kitasa cha mlango, akakinyonga na kuusukuma ule mlango. Mlango ukafunguka na kumruhusu kuingia mle chumbani.
Ibrahim akajitoma chumbani na kusimama katikati ya kile chumba huku akimtazama mke wake, Pamela Tugiramahoro, ambaye alikuwa kasimama kwenye mlango wa kuelekea kwenye kibaraza kidogo cha ghorofani (balcony) huku akiangalia juu kwa unyonge, sura yake alikuwa kaikunja na kutengeneza matuta madogo usoni. Ibrahim alimtazama kwa kitambo kifupi na kuachia tabasamu la kebehi.
Pamela alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka therathini na nane. Alikuwa msomi aliyehitimu Shahada ya Sanaa katika Sosholojia (B.A. in Sociology) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alikuwa amepata nafasi ya kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ufadhili maalumu wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), wakati huo yeye na familia yake walikuwa wakiishi nchini Tanzania na kufuatia machafuko yaliyokuwa yakiendelea nchini Burundi.
Pamela alikuwa Mrundi halisi, kwa baba na mama yake, akiwa mtoto wa kwanza kati ya watoto saba, watatu walikuwa wa kike na wanne walikuwa wa kiume. Paamela alikuwa na umbo kubwa lililokuwa linavutia sana, likiwa limesheheni vema na kunesanesa, likifanya kila jicho lililokuwa linamuona kumtazama mara mbili mbili pasipo kukinai.
Alikuwa mrefu wa wastani na mweupe kwa rangi ya ngozi yake, lakini haaukuwa ule weupe wa kujichubua bali weupe wa asili. Rangi yake ilikuwa na mng’aro wa aina yake na ilipendeza sana, ikiwa na mvuto wa pekee kiasi cha kumfanya kuonekana alikuwa bado msichana mdogo tofauti na umri wake. Pia hakuwa akihitaji kabisa vikorombwezo vya aina yoyote kuinakshi ngozi yake.
Ukiangalia macho yake, hmm… yalikuwa ni yale macho yanayoita kwa mng’aro sadifu, yakiambatana na kope nyingi nyeusi ambazo ziliachia nafasi kwa nyusi ili zipate kujidai.
Midomo yake ilikuwa minene yenye kingo nyepesi na mikunjo midogo midogo. Sauti yake ilikuwa ya upole kila alipoongea, na kikubwa zaidi kilichokuwa kinakamilisha uzuri na mvuto wake ilikuwa upole wake. Kwa kweli Pamela hakuwa mwanamke wa kumtizama mara moja tu ukamwacha.
Urafiki wa Pamela na Ibrahim ulianzia ufukweni mwa Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam, katika ufukwe wa Cine Club, maarufu kama Mikocheni kwa Warioba, ambako Pamela akiwa na rafiki zake aliokuwa anasoma nao Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walikuwa wakichezea mchanga uliokuwa kandokando ya bahari, walikuwa mara warushiane mchanga mara waangushane kwenye maji.
Mchezo ulipowanogea Pamela akachota mchanga ili kumwagia mwanachuo mwenzake, bahati mbaya kusudio lake likashindikana baada ya mchanga ule kukwepwa na mlengwa, kisha akammwagia mwanamume mmoja aliyekuwa amekaa jirani kabisa na eneo lile.
Kuona vile Pamela akaduwaa na kujiziba mdomo wake kwa hofu kubwa. Bila kufikiria mara mbili mbili yule mwanamume aliinuka na kumkabili Pamela ambaye bado alikuwa ameduwaa, akamfikia na kuanza kumporomoshea matusi ya nguoni pasipo hata kumpa nafasi ya kujitetea. Kama hiyo haitoshi alimkwida akitaka kumpiga.
Pamela aliingiwa woga mkubwa na kutetemeka asijue la kufanya huku wale rafiki zake wakijikunyata kwa woga wasijue la kufanya. Kijana mmoja mtanashati aliyekuwa akipita eneo lile akajongea mahali hapo haraka na kumshika yule mwanamume kwa nguvu, akamvuta kumuachanisha na Pamela na kumsukuma kando huku akimkazia macho.
“Kaka, siyo vizuri kugombana na watoto wa kike…”
“We umeona jinsi alivyonifanyia lakini, au unasema tu?” yule mwanamume alisema huku akiwa amekasirika.
“Wewe ni mwanamume na hawa ni watoto wa kike, utajitia matatani bure, mpotezee!” yule kijana mtananshati alimweleza na kumgeukia Pamela.
“Dada’angu, waambie wenzako kama ni michezo mkafanyie mbali, si unaona hapa kuna watu wamekaa!” yule kijana alisema kwa upole akimwambia Pamela.
Wakati huo yule mwanamume ambaye alishapandwa na hasira alipiga kite cha hasira na kushika kiuno huku akimtazama Pamela kwa makini. “Bahati yako!” alisema kwa hasira na kuondoka kabisa eneo lile huku akijifuta mchanga.
Pamela na rafiki zake walimshukuru yule kijana mtanashati na kuondoka eneo lile kisha wakasogea mbele kidogo, lakini si kwa ajili ya kuendelea kucheza bali walianza kuvaa nguo zao. Walishaona kuwa tayari ufukwe ule ulikuwa umeingia nuksi!
Walivaa nguo zao na kuanza kuondoka kutoka eneo lile, na wakati wakielekea barabarani Pamela akamwona tena yule kijana mtanashati aliyekuwa amemuokoa asipate kichapo akitembea taratibu mbele yao akielekea upande ule ule waliokuwa wanaelekea.
“Asante sana kaka, maana bila wewe sijui ingekuwaje leo kwa yule jamaa!” Pamela alimwambia yule kijana baada ya kumfikia.
“Usijali, dada’angu, hapa mjini kila mtu ana stress zake,” yule kijana mtanashati alijibu huku akiachia tabasamu.
Pamela alijikuta akivutiwa sana na ustaarabu wa yule kijana, hivyo alipunguza mwendo. Yakafuata mazungumzo kidogo ya kufahamiana, ndipo yule kijana mtanashati alipojitambulisha kwa Pamela kuwa aliitwa Ibrahim Bigirimana na alikuwa anafanya kazi Benki Kuu ya Tanzania.
Waliongea kwa kitambo kifupi na wakati walipokuwa wanaagana kwa kushikana mikono, Ibrahim alimpa Pamela kitu fulani mkononi. Pamela alikipokea kile kitu na kuufunga mkono wake vyema, kisha akawakimbilia rafiki zake waliokuwa wametangulia mbele bila kukitazama.
Walipofika kwenye kituo cha daladala cha Kwa Warioba Pamela aliufungua mkono wake kuangalia na kuiona ‘business card’ iliyokuwa na jina, cheo, anwani, mawasiliano na eneo la ofisi alizokuwa anapatikana Ibrahim.
Siku chache baadaye Ibrahim alipokea ujumbe mfupi kutoka kwa Pamela wa kumjulia hali, na yeye akaamua kupiga simu, na hapo ndipo urafiki ukazaliwa, baadaye ukawa mwanzo wa ukaribu wao uliofuatiwa na uchumba.
Baada ya Pamela kumaliza chuo, taratibu zingine zilifuatwa na hatimaye yeye na Ibrahim walioana kwa ndoa iliyofungwa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, kisha sherehe kubwa ya harusi ikafanyika nyumbani kwao Ibrahim, kwenye ukumbi wa hoteli ya kitalii iliyopo kwenye mandhali ya kuvutia ya ufukwe wa Ziwa Tanganyika mjini Kigoma, Kigoma Hilltop Hotel.
Ndoa hiyo ilikuwa imeridhiwa na kupata baraka kutoka pande zote mbili bila kinyongo chochote. Baada ya pale Ibrahim na Pamela wakaanza maisha mapya ya ndoa. Baada ya mwaka mmoja wa ndoa yao wakapata mtoto wa kiume, ambaye Pamela aliamua kumpa jina la Nduwimana, lilikouwa na maana ya “Nipo kwenye mikono salama ya Mungu” kwa lugha ya Kirundi.
Kupatikana kwa mtoto Nduwimana kulizidisha furaha ya ndoa. Lakini ni katika kipindi hicho hicho Pamela akakumbwa na msukosuko baada ya yeye na jamaa zake kutakiwa kurudi kwao, Burundi, katika kile kilichoitwa operesheni ya kuwarudisha wahamiaji haramu. Pamela aliporudi Burundi aliamua kutafuta kazi na hakuchukua muda akapata kazi katika taasisi ya kimataifa ya World Vision International Burundi.
Kwa kuwa Ibrahim alimpenda sana Pamela, aliamua kufanya utaratibu wa kuacha kazi Benki Kuu ya Tanzania na kumfuata Pamela nchini kwao Burundi, kwani muda mrefu alikuwa akivutiwa kuishi jijini Bujumbura.
Kwa kuwa alikuwa na elimu nzuri na uzoefu wa miaka kadhaa alioupata kutoka Benki Kikuu ya Tanzania, ikawa rahisi sana kwake kupata kazi, hakuchelewa, akapata kazi katika Benki ya Biashara ya Burundi (Commercial Bank of Burundi).
Miaka miwili baadaye wakapata mtoto wa pili wa kike, wakampa jina la Samantha ambalo ni jina maarufu sana la mtoto wa kike miongoni mwa wazazi nchini Burundi, na mara nyingi waliwachukulia watoto wa kike wenye jina hilo kama wasichana wa daraja la juu, waliozaliwa katika neema.
Ni wakati huo Ibrahim alimtaka Pamela kuacha kazi ili apate nafasi ya kulea watoto wake, kwa kuwa hakupenda watoto wake walelewe na msichana wa kazi. Ibrahim aliahidi kumpenda zaidi Pamela na kumtunza yeye na wazazi wake, kama ambavyo alivyokuwa akiwatunza wazazi wake.
Aliahidi pia kumvumilia mkewe mpaka mwisho wa maisha yao, maneno ambayo yalimpa faraja kubwa Pamela na hakuwahi kufikiria kabisa kuwa mambo yangekuja kugeuka!
Furaha katika familia ile ilizidi baada ya mwaka mmoja, maana Ibrahim aliacha kazi Commercial Bank of Burundi na kuchukuliwa na CRDB Bank Burundi, baada ya benki hiyo kuanzishwa nchini Burundi, na yeye akawa Meneja Mkuu wa benki hiyo, nafasi iliyomfanya kuwa mmoja wa watu wenye mafanikio makubwa jijini humo na kuzidi kumuongezea marafiki kutoka kila kona.
Miaka ikaanza kusonga, na taratibu Ibrahim akaanza kubadilika, upendo wake kwa Pamela ukaanza kupooza kwa sababu sasa alianza kupata mialiko mbalimbali iliyomkutanisha na warembo wengi waliokuwa wanamlilia. Pia kutokana na kipato chake kuwa kikubwa alijikuta akianza kuingia kwenye maisha ya anasa na starehe za kila aina.
Akaanza kuchelewa kurudi nyumbani, wakati mwingine hadi usiku wa manane, na siku moja ilionekana kama alichelewa sana kurudi basi Pamela alilala pale sebuleni kumsubiri kwa saa nyingi lakini hakurejea kabisa. Hata Ibrahim aliporejea siku iliyofuata Pamela alipomkabili kumuuliza alilala wapi, alionekana kubezwa na hakuweza kujibiwa.
Pamela akajitahidi sana kuvumilia akiamini kuwa huo ulikuwa ni upepo mbaya tu uliokuwa ukipita na muda si mrefu maisha yangeendelea. Kutahamaki miaka miwili ikawa imepita na mienendo mibovu ya Ibrahim ikaendelea kuchukua hatamu, ikafikia kipindi Pamela akaanza kujiuliza: ina maana Ibrahim alikuwa hatambui tena umuhimu wake!
Ni kweli Ibrahim alikuwa ameanza tabia za kuchelewa kurudi nyumbani lakini siku zilivyozidi kwenda hali ilizidi kuwa mbaya zaidi. Usiku Pamela hakupata usingizi, muda wote alikuwa anawaza kuhusu hatma ya ndoa yake na Ibrahim. Akawa analia usiku kucha, donge la hasira lilimkaba kooni na hakuweza kulihimili mpaka atoe kilio. Akajiuliza, hali ile ingeendelea hadi lini?
Alitamani kuikimbia nyumba yake lakini hakuweza kuondoka na kurudi kwao bila kupewa talaka, kwa sababu baba yake mzazi alikuwa mkali mno na kama angeenda kwao basi angeishia kufukuzwa nyumbani kama mbwa koko. Pamela akatamani kuiomba talaka yake lakini kibaya zaidi Ibrahim hakuwa amewahi kumtamkia kuhusu talaka hata siku moja. Jambo hilo kwake likawa tatizo kubwa, hivyo akawa anavumilia tu huku akiishi utumwani katika nyumba yake.
Hata mzigo wa majukumu juu ya wazazi wake na wadogo zake ungemuelemea sana Pamela kama angeamua kuondoka kwa Ibrahim, ni afadhali basi angekuwa anafanya kazi mahali walau angeweza kupata faranga mbili tatu ambazo zingeweza kukidhi mahitaji yake na ya wazazi wake, lakini wakati ule hakuwa na kazi, mume wake alikuwa hajamruhusu kufanya kazi kwa kauli ya kwamba yeye alikuwa anao uwezo wa kumhudumia kwa kila kitu. Na kama mume amesema hivyo, je, mke angebisha nini?
Hali ilipozidi kuwa mbaya zaidi Pamela aliamua kupigania haki yake, kwanza kwa kumkabili Ibrahim na kumtaka wakae, wayazungumze na kutatua matatizo ya ndoa yao, lakini Ibrahim alimpuuza. Kuona hivyo Pamela akaamua kwenda kuitafuta haki yake kwenye taasisi mbalimbali za watetezi wa jinsia na hata katika taasisi za kisheria lakini kote huko ilishindikana kwa sababu Ibrahim alidharau mwito kutoka katika taasisi hizo, alipata jeuri kwa sababu ya nafasi yake iliyomfanya kukutana na wakubwa wa nchi.
Pamela alipoona kote huko imeshindikana, ndipo akafikia uamuzi kuwa “liwalo na liwe!” maana alijiuliza, je, angeendelea kuvumilia mateso yale hadi lini? Ndiyo maana aliamua kukata mzizi wa fitina kwa kuwaita wazazi wa pande zote ili sasa aweke wazi kuhusu msimamo wake juu ya ndoa yake na Ibrahim. Kama noma na iwe noma!
Na sasa Ibrahim alikuwa amesimama akimtazama mkewe katika ule usiku usiosahaulika kamwe kwenye kumbukumbu zake, ulikuwa usiku wa kizaazaa! Ibrahim aliendelsa kumkodolea macho Pamela ambaye alikuwa chumbani kwake akiwa kasimama kwenye kibaraza cha ghorofa (balcony) akiangalia mbingu kwa unyonge.
Kilikuwa chumba kikubwa na chenye nafasi ya kutosha ambacho upande wa kulia na wa mbele wa kile chumba kulikuwa na madirisha mapana yenye vioo yaliyokuwa yamefunikwa kwa mapazia marefu na mepesi. Dirisha moja lilikuwa limeungana na mlango uliokuwa unatokea kwenye balcony, sehemu alipokuwa amesimama Pamela.
Upande wa kushoto ukutani kulikuwa na kabati kubwa la nguo la ukutani na kando ya kabati lile kulikuwa na meza nzuri nyeusi ya kioo. Juu ya meza hiyo kulikuwa na seti moja ya runinga kubwa Flat screen katikati ya spika mbili za sistimu ya muziki wa Home threatre.
Katikati ya chumba kulikuwa na kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita chenye nakshi nzuri za kupendeza, upande wa kulia wa chumba. Upande huo wa kulia kulikuwa na mlango mwingine wa chumba kidogo cha maliwato.
Upande wa kushoto wa chumba kulikuwa na seti moja ya makochi ya sofa nadhifu na ya kisasa juu ya zulia zuri lenye rangi za ngozi ya Pundamilia. Katikati ya makochi hayo kulikuwa na meza ndogo ya mbao iliyokuwa na umbo la nusu duara. Juu ya ile meza kulikuwa na kibakuli kidogo cha majivu ya sigara, kibiriti kimoja cha gesi, kasha tupu la miwani ya macho na simu ya mezani.
Dirishani kwenye balcony kulikuwa na ua kubwa zuri kwenye chungu cha udongo na kando ya ua hilo kulikuwa na kiti kimoja cha kupumzikia kilichokuwa kinatazama nje. Pembeni ya kile kiti kulikuwa na meza fupi ya mbao yenye droo mbili.
Ibrahim alimtazama Pamela kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akaachia tabasamu la kebehi.
“Naona unatazama juu kama vile unatarajia Mungu akushushie mume mwingine zaidi yangu!”
Pamoja na kutambua uwepo wa Ibrahim mle chumbani lakini Pamela hakugeuka kumtazama bali aliendelea kutazama kule juu bila kuonesha dalili yoyote ya kumsikia mumewe.
Ibrahim alionesha kukerwa mno, akaiweka briefcase yake sakafuni na simu zake akaziweka juu ya meza ndogo ya mbao yenye umbo la nusu duara, kisha akaanza kupiga hatua kumfuata Pamela. Alimfikia na kusimama nyuma yake huku akimwangalia kwa hasira iliyokuwa imechanganyika na jeuri.
“Mapokezi gani haya, halafu eti mwanamke anataka apendwe!” Ibrahim alisema huku akimtazama Pamela kwa dharau.
Pamela aligeuza shingo yake kumtazama Ibrahim kupitia juu ya bega lake bila kuonesha hisia zozote za kumjali, kisha akageuzia shingo yake upande mwingine akionekana kumpuuza. Ibrahim akapandwa zaidi na hasira na kushika mabega ya Pamela, akamgeuza kwa nguvu.
“Naona wewe na hao wazee sasa mnanitafuta kwa jambo, nasema hamtaniweza!” Ibrahim alibwata kwa hasira huku akimkazia machp Pamela.
Pamela alimkazia Ibrahim kwa chuki kubwa na kukunja sura yake, akaitoa mikono ya Ibrahim kwenye mabega yake na kurudi nyuma hatua moja akiwa bado kakunja sura yake.
“Nitashukuru iwapo utauacha moyo wangu utulie, tafadhali sana niache!” Pamela alisema huku akimtazama Ibrahim kwa makini.
Ibrahim alimsogelea tena na kumshika mabegani kisha akaanza kumtingisha kwa nguvu akionekana kupandwa zaidi na hasira. “Unanifanyia kiburi siyo? Nitakupiga sasa hivi au unadhani nawaogopa hao wazee?” Ibrahim alizidi kubwata huku akimtazama Pamela kwa hasira.
“Ni heri uniue kabisa maana nimechoshwa na maisha haya. Nitaishi hivi hadi lini?” Pamela alisema huku akiitoa tena mikono ya Ibrahim mabegani kwake. Ibrahim alimkazia macho akimtazama kwa makini na kucheka kwa dharau huku akitingisha kichwa.
“Huna lolote, najua ni wivu tu unakusumbua, tena wivu wa kijinga,” Ibrahim alisema huku akishusha pumzi.
“Sikuolewa nikuonee wivu bali nikupende na kukutumikia, na wala si kugeuzwa kijakazi wa mahaba!” Pamela alisema huku akimwangalia Ibrahim kwa makini na kutingisha kichwa chake kwa huzuni. Kisha alipiga hatua taratibu kujitenga na Ibrahim, akasimama hatua chache na kumwangalia kwa makini kuanzia chini hadi juu, kisha anaangua kicheko hafifu kilichokuwa kimebeba uchungu.
“Eti wivu! Utoke wapi katika unyumba duni kama huu!” Pamela alisema huku akiendelea kucheka kwa uchungu.
Kauli ile ikaonesha kumchukiza zaidi Ibrahim, alimsogelea Pamela kwa hasira na kunyanyua mkono wake akitaka kumzaba kibao, lakini Pamela alikinga mkono wake kwa ujasiri aakionesha kutomuogopa mumewe. Ibrahim akamwangalia Pamela kwa hasira na kusonya.
“Kama unyumba wangu ni duni, unangoja nini basi nyumbani mwangu? Si uondoke ukatafute anayeona anakutosheleza!” Ibrahim alisema huku akimtazama kwa hasira.
“Nangoja talaka! na itapendeza zaidi ikiwa ni kifo!” Pamela alijibu kwa dharau. Ibrahim alimkazia macho Pamela na kuachia kicheko cha dharau, kisha anasonya.
“Yaani ufedhuli wako ndiyo unanifanya nikuone kinyaa siku hizi,” Ibrahim alisema huku akishushas pumzi za ndani kwa ndani.
“Ulitaraji nini wakati una msururu mrefu wa mahawara, unadhani mke nyumbani atakuwa na thamani gani?” Pamela alisema na kumfanya Ibrahim akunje sura yake akimkazia macho Pamela.
“Thibitisha kama una ushahidi juu ya madai yako,” Ibrahim alisema huku akimsogelea Pamela, lakini Pamela alirudi nyuma akimkwepa mumewe.
“Ushahidi uliopo machoni kwa Mungu unanitosha, na ninaamini atanilipia.”
Ibrahim alitaka kusema neno lakini hatia ikamkaba koo, akabaki kushangaa akimtumbulia macho Pamela. Muda ule mlango wa chumba chao ukagongwa taratibu mara mbili. Ibrahim aligeuka kuutazama ule mlango akionekana kujishauri, kisha alipiga hatua na kwenda kuufungua kisha akachungulia nje, akamuona Nduwimana akiwa amesimama nje ya mlango wa kile chumba akiwa na wasiwasi.
“Unasemaje? Kwanini hujalala hadi wakati huu?” Ibrahim alimuuliza Nduwimana huku akiwangalia kwa makini.
“Ni mtoto gani mwenye mapenzi na baba yake atalala kabla ya kumuona? Lakini kwa wanangu imekuwa bure kabisa kuwa na baba asiyependeka!” Pamela alidakia kwa uchungu.
Ibrahim aligeuka kumtazama Pamela huku akionekana kukerwa mno na maneno yake.
“Siongei na wewe tafadhali, niache niongee na mwanangu, na naomba usiingilie!” alimwambia Pamela kwa hasira, kisha akageuka kumtazama Nduwimana na kuachia tabasamu. “Enhe, unasemaje mwanangu?”
“Babu anakuita!” Nduwimana alimjibu baba yake huku akiwa anamtazama kwa wasiwasi.
“Haya nakwenda sasa hivi, na wewe nenda ukalale ili kesho usichelewe shule.”
“Kesho ni Jumapili, hakuna shule.”
“Ooh! Hata kama hakuna shule ulitakiwa uwe umelala saa hizi. Sikuwaambia muwe mnalala mapema?”
Nduwimana alibaki kimya akiwa hana la kusema, alimtazama baba yake kwa wasiwasi, akataka kusema neno lakini akasita na kuondoka taratibu. Ibrahim aliamtazama kwa makini huku akimsindikiza kwa macho hadi alipofika kwenye mlango wa chumba chake.
Kisha Nduwimana alishika kitasa cha mlango na kugeuka kumwangalia baba yake kwa wasiwasi, akalazimisha tabasamu na kumpungia mkono kisha akaingia chumbani kwake.
Ibrahim aliachia tabasamu na kupunga mkono wake kisha akaufunga ule mlango wa chumba chake na kumgeukia Pamela, alimtazama kwa muda kisha akatingisha kichwa.
“Umekwisha wajaza maneno ya uzushi wazee na sasa wanataka kunijia juu. Sijui kwa kufanya hivyo ndiyo utapata faida gani?”
“Hata kama wangelikuwa vipofu wasingeshindwa kubaini maisha na mateso ya nyumba hii!”
“Mateso gani, kwani huli ama kulala humu ndani?”
“Nitaupataje usingizi, unyumba si kula na kulala tu!”
“Kumbe kuna nini cha zaidi?”
“Nenda kaonane na wazazi wako pengine watakueleza.”
Ibrahim alimtazama Pamela kwa muda bila kusema chochote, kisha aligeuka na kufungua mlango taratibu. Akataka kutoka lakini akasita na kugeuka kumtazama Pamela kwa hasira.
* * * * *
Kwenye ile sebule, Mzee Bigirimana alikuwa kasimama akiwa anatingisha kichwa chake kwa huzuni, alisonya huku akimkazia macho mke wake, kisha akageuza shingo yake kuwatazama Mzee Tugiramahoro na mke wake walioonekana kuzama katika mazungumzo wakiongea kwa sauti ya chini.
Mzee Bigirimana alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kugeuza tena shingo yake kumtazama mke wake. “Hivi ni mtoto gani huyu umenizalia?” alimuuliza mkewe kwa hasira.
“Si ulitaka mtoto wa kiume, sasa?” Mama Bigirimana alijibu huku akionekana kushangaa kidogo.
“Lakini si mtoto fedhuli kama huyu!”
“Alaa, leo amekuwa fedhuli, siyo?”
“Inamaana wewe huoni kama anatuaibisha sana?”
“Hivi toka lini mwembe ukazaa parachichi au umesahau ulivyokuwa zama zako! Anayoyafanya mwanao ndiyo hayo hayo uliyokuwa unayafanya wewe enzi hizo!”
“Lakini hiyo ilikuwa kijijini na wewe ulikuwa mshamba tu si kama mkweo ambaye amesoma na ana madigirii yake!”
“Mwanamke ni mwanamke tu popote pale alipo na katika mazingira yoyote yale anastahili kuthaminiwa na kuheshimiwa,” Mama Bigirimana alijibu akionekana kukerwa sana na ile kauli ya Mzee Bigirimana.
“Lakini si kama anavyofanya mwanao kwa mtoto wa watu,” Mzee Bigirimana alisisitiza kwa sauti ya chini.
“Ni kweli, lakini pilipili za kale hazitofautiani na za leo!”
Mzee Bigirimana alitaka kusema neno lakini akasita na kumtazama mke wake kwa makini, ni dhahiri alionesha kuchukizwa, akamnyooshea kidole katika hali ya kumuonya. Hata hivyo alishindwa kuvumilia kutokana na hasira iliyoanza kuchemka ndani kwa ndani na kujikuta akipandisha sauti yake kwa ukali.
“Kwa hiyo unataka kusema nini sasa, usiache nikakutia vibao saa hizi!”
“Mwenzangu umenipiga vibao vingapi ndiyo nishangae leo! We piga tu ili roho yako iridhike!” Mama Bigirimana alisema huku akimtazama mumewe kwa makini.
Mzee Bigirimana alitaka kusema neno lakini akasita na kugeuka kuwaangalia Mzee Tugiramahoro na Mama Ninziza Bernice kwa wasiwasi.
Wakati huo wale wazee walionesha kushtuka na kugeuka kuwatazama wazee wenzao kwa mshangao. Mzee Bigirimana akajibaraguza huku akilazimisha tabasamu.
Mzee Tugiramahoro alishusha pumzi na kugeuka kumtazama mke wake kwa mshangao, kisha akatingisha kichwa chake kwa masikitiko makubwa akiendelea kumkazia macho mke wake.
“Naujutia sana unyumba wa binti yangu kwa kweli,” Mzee Tugiramahoro alimwambia mke wake kwa sauti ya chini iliyojaa masikitiko.
Mama Ninziza Bernice alimtazama kwa makini na kuonekana kukerwa, alimwangalia mumewe kwa makini na kutingisha kichwa. “Hata sijui unajuta nini wakati mahari uliyapokea kwa mbwembwe na fahari kubwa!”
Mzee Tugiramahoro alikunja sura yake kwa hasira na kumkazia macho mkewe. “Lakini sikumuoza binti yangu ili afanywe hivi!”
“Basi mwelezeni kijana wenu, hii si karne ile ya unyonge wa mwanamke, sijui mnadhani mwanamke ataendelea kufanywa hivi hadi lini?”
Mzee Tugiramahoro alifikiria kidogo na kuinamisha kichwa chake chini, wakati huo mkewe alimtupia jicho Mzee Bigirimana ambaye muda wote alikuwa anarandaranda pale sebuleni huku akiwa anatazama upande zilipokuwa ngazi za kuelekea juu.
Mzee Tugiramahoro anainua na kumuona Mzee Bigirimana akiwa anarandaranda sebuleni, yeye na Mama Ninziza Bernice wanabaki kumtazama Mzee Bigirimana kwa mshangao.
“Hatukuja hapa kuoneshwa ufedhuli wa namna hii!” Mzee Bigirimana alikuwa anaongea kwa hasira kisha aligeuka kuelekeza kidole chake kwa Mzee Tugiramahoro, “Siku nilipopeleka mahari kwa rafiki yangu nilitambua kuwa atakuwa kapata mkwe bora na siyo mkwe duni kama mwanangu.”
“Sasa wewe zungumza na mwanao vizuri na mimi wacha nimfuate mkwe wangu huko juu nikamtulize ili mambo haya yaishe,” Mama Bigirimana alisema na kuinuka bila kusubiri, akaanza kutembea taratibu na kuzikwea ngazi kuelekea juu. Pale kwenye ngazi akapishana na Ibrahim aliyekuwa anashuka ngazi na kumtazama kwa wasiwasi.
Ibrahim alisimama akitaka kuongea na mama yake lakini yule mama alimpita pasipo kusimama wala kumtazama. Ibrahim akabetua mabega yake na kushusha pumzi kisha akaanza kushuka ngazi taratibu.
Mama Bigirimana aligeuka kumtazama Ibrahim kwa makini na kutingisha kichwa chake kwa masikitiko huku akiendelea kuzikwea ngazi haraka.
Ibrahim alipofika pale sebuleni alisimama na kumwangalia baba yake kwa wasiwasi, kisha akageuza shingo yake kuwatazama wakwe zake huku akionesha uso wa mashaka kidogo.
“Nasikia unaniita!” Ibrahim alimkabili baba yake akiwa bado ana uso wenye mashaka.
“Kwani nilisemaje? Sikukwambia kuwa nina mazungumzo na wewe usiku huu huu?” Mzee Bigirimana alisema huku akionesha kukerwa kidogo na lile swali la Ibrahim, kisha akageuza shingo yake kuwatazama Mzee Tugiramahoro na mkewe, akashusha pumzi ndefu na kumtazama tena Ibrahim.
“Naomba twende faragha hapo nje tukaongee kidogo.”
Ibrahim alisita kidogo, hofu ilikuwa inamtambaa mwilini na muda ulr alihisi kijasho chembamba kikimtoka. Alimtazama baba yake kwa makini na kuminya midomo yake, kisha akatoka nje.
“Mzazi mwenzangu, ukimaliza mazungumzo na mwanao na mimi nitahitaji kuzungumza na wewe,” Mzee Tugiramahoro alimwambia Mzee Bigirimana alipomuona akijiandaa kutoka nje kumfuata Ibrahim.
Mzee Bigirimana aligeuka kumtazama mzee mwenzie kwa uso wenye mashaka kidogo, akaminya midomo yake kutafakari kidogo, kisha akabetua kichwa chake kukubali.
“Sawa, mzazi mwenzangu,” alisema na kutoka nje haraka. Mzee
* * * * *
Mama Bigirimana alipofika kule juu alisimama kwenye mlango wa chumba cha Pamela, akaonesha kusita sana huku akitazama huku na huko, kisha akabisha hodi mlangoni akiwa na uso wenye wasiwasi kidogo. Alisubiri kwa kitambo kifupi na kugonga tena, lakini alipokuwa akianza kugonga mara ya pili mlango ukafunguliwa na kumfanya kushtuka sana.
Pamela alitoa kichwa chake nje kuchungulia, akamuona Mama Bigirimana na kuachia tabasamu la makaribisho. “Karibu mama,” Pamela alisema huku akimtazama yule mama kwa makini.
“Mwanangu, naomba tuzungumze kidogo, nafahamu kuwa usiku umekwenda mno na ungependa kupumzika,” Mama Bigirimana alimwambia Pamela kwa sauti tulivu huku akimtazama kwa wasiwasi.
“Usijali mama, haya niliyo nayo kwa kweli yanafanya usingizi kwangu kuwa sawa na kijiji cha mbali sana ambacho siwezi kukifikia kwa urahisi.”
“Basi naomba tukazungumzie huko chumbani kwetu kwani huku kwenu si haki niingie.”
“Mama, naheshimu sana mila na desturi za Kiafrika lakini katika mazingira kama haya si vibaya tukazungumzia huku huku chumbani kwetu,” Pamela alisema na kumsisitiza yule mama huku akimpisha aingie ndani.
Mama Bigirimana alionekana kusita sana, akainamisha uso wake kufikiria sana lakini mwisho alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akimtupia jicho Pamela. Muda wote Pamela alikuwa anamwangalia kwa makini kwa macho ya kumsisitiza aingie ndani ndani.
Baada ya kuonekana akijishauri kwa kitambo kifupi hatimaye Mama Bigirimana alikubali kuingia chumbani japo kwa shingo upande, akaingia akiwa na wasiwasi na kupita haraka akaelekea moja kwa moja kwenye balcony.
Pamela alimtazama kwa makini kisha akamfuata na kumkaribisha kwenye kiti cha kupumzikia kilichokuwepo pale kwenye balcony. Mama Bigirimana aliketi kwenye kile kiti kando ya ua kubwa zuri lililokuwa kwenye chungu cha udongo. Pamela naye akaketi jirani huku akimtazama kwa makini.
Mama Bigirimana alimtazama Pamela kwa muda akiwa na shaka kidogo, alionekana kutafuta maneno ya kuongea kisha akatingisha kichwa chake kwa huzuni.
“Binti yangu, najua mateso unayoyapata lakini kama mke hebu jaribu kuvumilia, haya yana mwisho. Hivi unadhani mimi nisingekuwa mvumilivu ningekuwa na baba yenu hadi leo?”
Pamela alimtazama yule mama kwa makini na kutingisha kichwa chake taratibu kwa huzuni huku akibetua mabega yake juu na kuyashusha.
“Mama, kumbuka kuwa hakuna kitabu chochote duniani kinachoamuru mimi kama mwanamke niishi maisha kama haya, eti kwa kuwa nimeolewa!”
“Nafahamu, hata mimi inaniumiza sana tangu uliponielezea hali halisi iliyopo hapa nyumbani, lakini elewa kuwa sisi mama zako pia tumetokea huko huko na tuliweza kuyavumilia yote.”
“Natambua lakini wakati ule ulimwengu wa mwanamke ulikuwa umegubikwa na giza la unyonge. Hivi mama, unadhani mambo haya yatavumiliwa hadi lini?”
Mama Bigirimana alikunja sura yake na kuwaza kidogo kisha akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akionekana kukata tamaa. Alimtazama Pamela kwa wasiwasi kidogo.
“Sasa unataka tufanyeje mama, maana hivi sasa baba yako amemweka chini mumeo ili amrekebishe.”
“Mama, mwanao amekuwa sugu na sidhani kama anaweza kubadilika, ninachotaka mimi ni kimoja tu ili nami nipumue kwa kweli.”
Mama Bigirimana alimkazia macho Pamela kwa wasiwasi, alitaka kusema neno lakini akasita, maana alikuwa hapendi kabisa kusikia kuhusu suala la Ibrahim na Pamela kuachana kwa namna yoyote ile. Alimpenda sana mkwe wake kwa kuwa alikuwa mwanamke mvumilivu, msomi, aliyejituma na mlezi mzuri kwa watoto.
“Ni nini tufanye basi, labda roho yako itaridhika?” hatimaye yule mama alimuuliza Pamela huku akimkazia macho kwa wasiwasi.
“Hakuna kingine mama, naomba mmwambie anipe talaka yangu tu,” Pamela alisema huku akiyakwepa macho ya Mama Bigirimana na kutazama kando, alikuwa akiyazuia machozi yaliyokuwa yanamlenga.
Mama Bigirimana alishtuka sana kusikia maneno yale kutoka kwa mkwewe, alimkazia macho akiwa haamini alichokisikia. Kwa nukta kadhaa akili ya Mama Bigirimana iligoma kabisa kukubali kuwa alichokisikia ni kile kilichokuwa kimetamkwa na Pamela, au labda alisikia vibaya, badala ya neno “muafaka” yeye kasikia neno talaka! Kwa kifupi, Mama Bigirimana alidhani kuwa huenda alisikia vibaya.
“Unasemaje, mama?” Mama Bigirimana alimuuliza Pamela kwa wasiwasi ili kuhakikisha kama alichokuwa amekisikia kutoka kwenye kinywa cha Pamela kilikuwa sahihi na siyo hisia zake.
“Nasubiri talaka yangu tu, mama yangu… lakini si kama mimi napenda talaka ila ndicho kitu alichokusudia mwanao!” Pamela alisema kwa sauti tulivu huku akimtazama mkwewe kwa makini.
Mama Bigirimana alinyanyua mikono yake na kushika kichwa chake kwa huzuni, akataka kusema neno lakini akashindwaa na kubaki akimtumbulia macho Pamela huku akiwa ameduwaa kwa mshangao mkubwa kana kwamba alikuwa ameona kitu cha kushangaza sana. Kwa nukta kadhaa akili ya yule mama iligoma kabisa kukubali. Hata hivyo, lile neno ‘nasubiri talaka yang utu…’ liliendelea kujirudia akilini mwake na kutengeneza mwangwi uliomkera sana.
Mama Bigirimana anaitoa mikono yake kichwani na kuziba masikio yake huku akikunja uso wake kana kwamba eneo hilo kuna kelele zinazomkera, machozi yanaanza kumtoka.
* * * * *
Kwenye ile baraza kubwa ya mbele ya ile nyumba, Mzee Bigirimana alikuwa akiongea na Ibrahim huku wakiwa wameketi kwenye makochi ya sofa. Mzee Bigirimana alimtazama Ibrahim kwa makini na kukunja sura yake kwa hasira, akasonya kwa huzuni huku akitingisha kichwa chake.
“Sikiliza bwana mdogo, mkeo hakutuita hapa sisi na wazazi wake kuja kuwatembelea… nadhani hilo unalifahamu vyema.”
Ibrahim alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akilazimisha tabasamu ingawa uso wake ulionesha kinyume chake, akanyanyua mabega yake juu huku akibetua midomo yake.
“Nafahamu baba, lakini sijui kama unafahamu kuwa mkweo siku hizi amekuwa kituo cha uzushi!”
“Kituo cha uzushi ki vipi wakati mengi ya wazi yanaonekana?”
“Najua kuwa tayari mmekwisha jazwa mengi ya kuzushwa…” Ibrahim alisema kwa namna ya kujitetea huku akimkazia macho baba yake.
Mzee Bigirimana alitingisha kichwa chake kwa hasira huku akipumua kwa nguvu kama mtu aliyekuwa amemaliza mbio ndefu za marathoni, akamnyooshea kidole Ibrahim kwa hasira.
“Bwana mdogo, elewa kuwa mimi siyo mtoto mdogo, na uendako wewe ndiko mimi nilikotokea.”
Ibrahim alitaka kusema neno lakini baba yake hakutaka kumpa nafasi ya kuongea, alikunja uso wake uliotengeneza matuta madogo usoni.
“Sikiliza… wewe ni mwanamume na una uhuru wa kufanya utakalo, wala hakuna anayeweza kukupangia. Kama unaweza basi oa mwanamke mwingine wawe wawili, maana hata dini yako inakuruhusu, ila kama huwezi basi mwache mtoto wa watu aende kwao na siyo kumnyanyasa kama hivi!”
“Nadhani hilo la pili ndiyo linaleta maana zaidi, kwani nimeshachoka kwa kweli!” Ibrahim alisema kwa kujiamini zaidi huku akibetua kichwa chake. Tabasamu lilionekana kuupamba uso wake.
“Umesemaje!” Mzee Bigirimana alimuuliza Ibrahim akiwa haamini alichokisikia, mshituko ulijitokeza waziwazi kwenye uso wake.
“Nataka kumuacha ili nioe mke mwingine,” Ibrahim alimwambia baba yake kwa sauti tulivu na kwa msisitizo huku akiyaelekeza macho yake kutazama mbele kwenye kibanda cha mlinzi. Mlinzi alikuwa ameketi kwenye kiti chake kwa utulivu akiwatazama Ibrahim na Mzee Bigirimana kwa mashaka.
Mzee Bigirimana alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akiwa hajui aseme nini, aliinamisha kichwa chake na kufikiria kidogo kisha akainua uso wake na kumtazama Ibrahim, akataka kuongea neno lakini maneno hayakutoka kinywani mwake. Akatingisha kichwa chake kwa huzuni huku akiendelea kumtazama Ibrahim.
Ibrahim aliinuka na kufungua mlango mkubwa wa barazani, akaingia ndani akimwacha baba yake pale akiwa bado ameduwaa. Alipoingia ndani alipita pale sebuleni na kuelekea moja kwa moja kwenye ngazi huku akiwapita wakwe zake wakiwa bado wameketi kwenye sofa wakiendelea kujadili mambo kwa sauti ya chini.
Walipomuona akipita waligeuza shingo zao kumtazama kwa mshangao, kisha wakaangaliana wasijue kilichokuwa kikiendelea ndani ya ile nyumba.
Ibrahim alizifikia ngazi za kuelekea juu na kupishana na mama yake aliyekuwa anashuka mngazi akitokea ghorofani huku akiwa analia kwa uchungu mkubwa, mikono yake yote miwili alikuwa kaiweka kichwani. Ibrahim alisimama huku akimtazama mama yake kwa mshangao, akajaribu kumsimamisha.
“Mama, kuna nini tena huko juu?” alimuuliza mama yake huku akimkazia macho kwa wasiwasi.
Mama Bigirimana alionesha ishara ya kutaka aachwe, akampita Ibrahim bila hata kumwangalia usoni wala kumjali na kupita pale sebuleni akiwapita Mzee Tugiramahoro na Mama Ninziza Bernice ambao walikuwa wameketi wakiwa bado wanashangaa, akaelekea moja kwa moja kule nje ya nyumba alikokuwa ameketi Mzee Bigirimana.
Ibrahim akiwa bado amesimama pale kwenye ngazi akimsindikiza mama yake kwa macho yenye mshangao, alijaribu kuwaza akijaribu kubashiri ni jambo gani huenda lilikuwa limetokea kule juu? “Au pengine mama na Pamela wamepishana kauli? Na kama wamepishana, kwa nini?” Ibrahim aliwaza na kukosa jibu.
Alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akibetua mabega yake na kuanza kupanda ngazi haraka akielekea kule juu kisha akaongoza moja kwa moja chumbani kwake. Alifika mlangoni na kuupiga kumbo ule mlango, mlango ukafunguka. Ibrahim akajitoma mle ndani huku akiwa amefura kwa hasira.
Alimkuta Pamela akiwa amesimama katikati ya kile chumba akiwa anatazama nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha ambalo pazia lake lilikuwa limefunuliwa kidogo na kumruhusu mtu aliyekuwa mle ndani kuweza kuona nje. Inrahim alisimama akamtazama Pamela kwa hasira.
Hasira zilikuwa zinamchemka ndani kwa ndani, akamsogelea huku akizidi kuhisi donge la hasira likizidi kumkaba kooni kiasi cha kushindwa hata kupumua.
“We mwanamke, umemfanyia ufedhuli gani mama yangu?” Ibrahim alimwuliza Pamela huku akipumua kwa nguvu, alipoona kimya akamshika mabegani kisha akamgeuza kwa hasira. Wakabaki wanatazamana, Pamela alimwangalia Ibrahim kwa makini huku akijitahidi kuwa mtulivu zaidi, japokuwa alikuwa amebanwa na donge la hasira kooni.
“Nakuuliza umemfanyia ufedhuli gani mama yangu?”
“Nimfanyie kitu gani mama wa watu?” Pamela alijibu kwa sauti yenye utulivu pasipo kuonesha hasira wala dharau yoyote kwa Ibrahim.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment