Search This Blog

Monday, 27 March 2023

GARI LA KUKODI - 3

  



Simulizi : Gari La Kukodi

Sehemu Ya Tatu (3)

amekwishavaa bukta na fulana, akaelekea mlangoni na kusimama nyuma ya Joyce.


“Pendo amezidiwa hawezi kupumua vizuri, anatapatapa huku akilalamika maumivu…” Winifrida alisema kwa hofu huku akilia kilio cha kwikwi baada ya mlango kufunguliwa na kuwaona Sammy na Joyce wakimtazama kwa wasiwasi.


Bila kusubiri, Joyce na Sammy walikimbilia kwenye chumba alikokuwa amelala Pendo na kumkuta akiwa anatapatapa huku akihema kwa shida. Pendo alipowaona alianza kulalamika maumivu ya mikono na miguu.


Kwa kuwa Sammy alielewa zile dalili ziliashiria tatizo gani kwa Pendo, hakusubiri, alichukua haraka simu yake na kumpigia dereva mmoja wa teksi jirani yao ili wamkimbize Pendo hospitali.


* * * * *


Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu ya asubuhi, sauti ya aina yake iliyoburudisha ya maji ya baharini yaliyokuwa yanachapa kingo za baharini ilipenya kwenye madirisha makubwa ya chumbani hadi pale kitandani walipolala Zainab na Mr. Oduya.


Mr. Oduya alijigeuza na wakati huo huo Zainab naye alijinyoosha kisha akamkumbatia. “Good morning, my darling!” Zainab alimsalimia Mr. Oduya huku akikishika kidevu chake kwa utani kama vile mjukuu akimtania babu yake.


“Morning, my darling!” Mr. Oduya aliitika huku akipiga miayo na kuachia tabasamu, kisha akaongeza, “Mungu ni mwema, tumeamshwa salama.”


“Mungu ni mwema kweli kweli,” Zainab naye aliirudia ile kauli huku akiachia tabasamu.


Mr. Oduya alijinyoosha kisha akainuka na kuketi pale kitandani, miguu yake ikakanyaga sakafuni, alishusha pumzi na kuinuka huku akiendelea kujinyoosha na kusogea upande wa pili ilipokuwa simu yake ya mkononi, akaichukua na kuiwasha, kwani ilikuwa imezimwa.


Alikuwa amelazimika kuizima simu yake kwani shughuli iliyofanyika usiku wa kuamkia siku ile ilikuwa supa. Zainab alikuwa amemtaka aizime ili kusiwe na kitu chochote cha kuingilia faragha yao, naye akatii.


“Sihitaji simu yoyote saa hizi, nimekuja kwa ajili yako, ni mimi na wewe tu hadi lyamba…” Mr. Oduya alikumbuka kuambiwa na Zainab usiku kabla hawajalala.


Usiku wa kuamkia siku ile Mr. Oduya alipofika Paradise Club ilikuwa imeshatimu saa nne za usiku. Alimkuta Zainab akiwa amejifunga khanga moja tu nyepesi na alipogonga mlango haraka Zainab alimfungulia na kumrukia, akakumbatia kwa mahaba.


“Waoo… pole mpenzi wangu, naona umechoka sana,” Zainab alimwambia huku akiupokea mkoba wa kiofisi aliokuwa kaubeba na kuupeleka moja kwa moja chumbani.


“Asante sana, mke wangu mpenzi,” Mr. Oduya alisema huku akimfuata Zainab kule chumbani, kisha akajipweteka juu ya kitanda.




Zainab alimsogelea akaimvua koti lake kisha alimvua viatu na soksi, halafu akamfungua tai yake shingoni na kufungua vifungo vya shati lake huku akimtazama usoni kwa tabasamu.


“Samahani mpenzi, naomba nikufungue mkanda wa suruali,” Zainab alisema kwa sauti tamu ya mahaba akiomba ruhusa kwa Mr. Oduya.


Mr. Oduya alimtazama kwa makini na kuachia tabasamu huku akishusha pumzi.


“Darling!” Mr. Oduya aliita kiwa sauti ya kunong’ona.


“Abee!”


“Unaweza kufanya chochote, mwili huu ni mali yako.”


“Asante sana mpenzi, unapaswa kuhudumiwa maana unachoka na kazi nyingi, una mambo mengi ya kufanya, pole sana ninajua akili yako haijatulia.”


“Asante sana, mpenzi wangu, ndiyo maana nakupenda kuliko kitu chochote,” Mr. Oduya alisema na kupitisha mkono wake kichwani, kuanzia kwenye paji la uso kuelekea usogoni na alipofika mwisho wa kichwa alipitisha mkono wake shingoni mwake na akawa kama anayejinyoosha.


Kisha aligeuka upande wa kushoto na kulia huku akitoa miguno ya uchovu hasa.


“Pole sana. Umeshakula?” Zainab alimuuliza Mr. Oduya huku akiivua suruali yake na kumwacha akiwa na boksa tu.


“Hapana sijala,” Mr. Oduya alijibu huku akijilegeza.


“Sijui utakula kwanza ndiyo ule au unakula kwanza halafu ndiyo utakula?” Zainab alimuuliza Mr. Oduya kwa sauti laini ya mahaba na kumfanya Mr. Oduya amwangalie kwa makini kabla ya kuachia tabasamu lililozaa kicheko hafifu.


“Kabla hujajibu ngoja kwanza nikupunguze uchovu,” Zainabu alisema kabla hata Mr. Oduya hajajua ajibu nini.


Haraka bila kuchelewa, Zainab alimsukuma Mr. Oduya, akaanguka chali pale kitandani kisha alimgeuza vyema akalalia tumbo lake kisha alipanda juu yake akakaa vyema, alichukua mafuta laini (lotion) aliyokuwa ameyaandaa na kuanza kumpaka Mr. Oduya eneo la mgongoni na shingoni kisha akaanza kumsinga kwa ufundi wa hali ya juu. Wenyewe huita kumfanyia masaji.


Mr. Oduya alitulia kimya wakati Zainab akifanya kazi yake kwa ufundi, alikuwa akifurahia sana kila kitu alichokuwa anafanyiwa na Zainab.


“Darling, yaani namna unavyonikanda najisikia burudani hasa, kwa kweli nimemisi sana kufanyiwa haya mambo,” Mr. Oduya alisema huku akihisi faraja ya aina yake.


“Usijali mpenzi, nimekuja Tanzania kwa ajili yako… hii ndiyo kazi yangu,” Zainab alisema huku akiendelea kuukanda kanda mgongo wa Mr. Oduya, kisha akashuka mapajani na baadaye akapanda hadi shingoni, mpaka kichwani.


Hadi muda huo Mr. Oduya alikuwa kazidiwa, kwani macho yake yalishabadilika na kuwa mekundu kabisa. Hii ndiyo faraja aliyokuwa akiikosa ndani ya ndoa yake na kuamua kuitafuta nje ya ndoa yake. Hakika kwenye ndoa nyingi mambo kama haya hukosekana.


Wanawake wengi ni wavivu sana kwenye ndoa zao, na ndiyo maana shetani ameweza kutumia mbinu hii kusambaratisha ndoa nyingi… cha ajabu wanawake hawa wanajituma sana kwenye uzinzi lakini kwenye ndoa zao wala hawajitumi!


Baada ya kazi ile ya kusingwa, kilichofuata kiliiongeza njaa ya Mr. Oduya mara dufu, alihisi kizunguzungu kutokana na garidwe la aina yake alilochezeshwa na Zainab, gwaride lililomuacha akihema ovyo kama bata.


Walipomaliza waliingia maliwatoni, kilikuwa chumba kikubwa cha maliwato yenye hadhi yake yaliyoweza kumsahaulisha majonzi hata aliyefiwa na ampendaye.


Waliingia kwenye jakuzi na kutulia humo miili yao ikiwa inakandwa na maji ya uvuguvugu…


“Unawaza nini, mpenzi?” sauti ya Zainab ilimzindua Mr. Oduya aliyekuwa amesimama wima akimkodolea macho Zainab pasipo kumuona.


“Ah, wala usijali… nilikuwa nayakumbuka mautundu yako,” Mr. Oduya alisema huku akipiga miayo mfululizo na kuchukua taulo lake, akajifunga kiunoni kisha akaelekea jikoni. Alitengeneza vikombe viwili vya kahawa na baada ya dakika chache alirudi chumbani, kikombe kimoja akampatia Zainab.


“Welcome, my darling,” Mr. Oduya alisema kwa mahaba huku akiachia tabasamu pana usoni kwake.


“Thank you,” Zainab alisema huku akiinuka, akajifunga kipande cha khanga nyepesi kifuani na kukaa pembeni ya Mr. Oduya.


“No, darling…” Mr. Oduya alisema huku akitingisha kichwa chake taratibu. “Ukiona nimekaa, unatakiwa kukaa hapa,” alisema huku akijipigapiga juu ya paja lake.


“Kaa hapa mpenzi wangu…” Mr. Oduya alisisitiza na kumfanya Zainab aangue kicheko hafifu cha mahaba huku akiinuka na kumkalia juu ya paja lake, kisha wakawa wanakunywa kahawa taratibu.


Walipomaliza kunywa kahawa wakaelekea maliwato, walijimwagia maji na kurudi chumbani wakiwa wamepata nguvu mpya. Mr. Oduya alivaa bukta na kukaa kitandani kisha akaanza kuvuta mkoba wake wa kiofisi, Zainab alimtazama kwa makini na kuufuata ule mkoba.


“Darling, nikusaidie?” Zainab alimuuliza kwa sauti ya mahaba.


“No… unajua sipaswi kukusumbua na kukuchosha, wewe ni malkia… isitoshe mwanamke siyo roboti, relax…” Mr. Oduya alisema huku akimpapasa Zainab mgongoni kwa mahaba.


“Wala hunisumbui mpenzi, it’s just loves, najisikia tu kukusaidia…” Zainab alisema lakini akakatishwa na mlio wa sauti ya kengere ya mlangoni iliyoita kwa fujo huko sebuleni na sauti yake kupenya hadi chumbani, wakatazamana. Ni kama walikuwa wanaulizana ‘ni nani?’


Zainab alitoka chumbani akaelekea sebuleni na kuchungulia kwenye tundu maalumu la mlangoni lenye kioo cha lenzi, akamuona Lilian akiwa amesimama nje ya mlango. Akashusha pumzi na kuufungua mlango.


“Ooh, Lilian… karibu mdogo wangu, naona umeniwahi,” Zainab alisema huku akisogea kando kumpisha Lilian aingie.


“Asante sana madame, habari za asubuhi?” Lilian alisema huku akiingia na kusimama pale sebuleni.


“Nzuri Lilian… unaweza kuendelea na kazi, kama kutakuwa na chochote utaniita nipo chumbani,” Zainab alimwambia Lilian na kurejea chumbani alikomwacha Mr. Oduya.





“Nzuri Lilian… unaweza kuendelea na kazi, kama kutakuwa na chochote utaniita nipo chumbani,” Zainab alimwambia Lilian na kurejea chumbani alikomwacha Mr. Oduya.


* * * * *


Saa nne asubuhi siku ya Jumapili, katika chumba kikubwa cha wadi maalumu ya VIP ya Hospitali ya Dar Group iliyopo barabara ya Nyerere jirani na Tazara, jijini Dar es Salaam, Sammy alikuwa amesimama kando ya kitanda alicholala Pendo, akionekana mwenye huzuni.


Chumba kile kilikuwa kikubwa chenye vitanda viwili na dirisha kubwa lililokuwa linaingiza hewa safi, na juu kulikuwa na dari nzuri iliyotengenezwa kwa gypsum ya rangi nyeupe na katika sehemu za dari ile kulining’inizwa taa nzuri na pangaboi.


Kitanda alicholala Pendo kilikuwa cheupe cha chuma chenye godoro nene la foronya laini na mto laini wa kuegemeza kichwa. Pendo alikuwa bado anapumua kwa shida kutokana na kusumbuliwa na tatizo la seli mundu lililosababisha kupungukiwa damu na matatizo ya kupumua.


Kando ya kile kitanda kulikuwa na stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyokuwa imetundikiwa chupa ndogo ya damu na mrija wake ukipeleka damu kwenye mshipa wa damu mkononi kwa Pendo.


Kando ya ile stendi ya chuma kulikuwa na meza ndogo na juu yake kulikuwa na trei ndogo ya chuma iliyokuwa na vifaa-tiba kama mkasi, plasta, bomba la sindano, glovu, chupa kubwa ya maji, bilauri na dawa za vidonge kwa ajili ya tatizo la seli mundu.


Baadhi ya vile vifaa vilikuwa vimefunguliwa na kuachwa wazi kitendo kilichoashiria kuwa tayari vilikuwa vimekwisha tumika.


Winifrida alikuwa ameketi kwa utulivu juu ya kitanda cha pili mle chumbani akimtazama Pendo kwa huzuni, alionekana mbali kimawazo na machozi yalikuwa yanamlenga machoni. Chumba kilikuwa na ukimya wa aina yake.


Muda ule ule mlango wa kile chumba ulifunguliwa, Daktari wa magonjwa ya watoto, Daktari Beda Msimbe aliingia akiwa ameongozana na muuguzi wa wodi ile ya watoto


Daktari Msimbe alikuwa mwanamume mfupi mnene na rangi ya ngozi yake ilikuwa ya maji ya kunde, akiwa na umri wa miaka hamsini na saba alikuwa na nywele fupi zenye mvi kiasi na uso wake ulikuwa mpana huku miwani yake mikubwa ikiwa imeyahifadhi macho yake makubwa.


Alikuwa amevaa suruali ya kitambaa cha kadeti cha rangi ya khaki, shati kubwa jeusi lililokuwa na mistari myeupe ya pundamilia na juu yake alikuwa amevaa koti refu jeupe la kidaktari na kuning’iniza shingoni kwake kifaa maalumu cha kupimia, kwa kitaalamu kiliitwa ‘stethoscope’.


Daktari Msimbe alikwenda moja kwa moja kitandani kwa Pendo akapishana na Winifrida aliyeinuka na kutoka nje. Daktari Msimbe alisimama akimchunguza Pendo kwa macho na kumgusa kwenye paji la uso wake, kisha aliiangalia kwa makini damu iliyokuwamo ndani ya chupa aliyotundikiwa Pendo.


Aliangalia kwa makini jinsi matone ya damu yalivyokuwa yakidondoka na kuingia kwenye mrija maalumu uliopeleka damu kwenye mshipa wa damu mkononi kwa Pendo na kuonekana kuridhika kisha alipeleka macho yake kusoma maelezo kwenye faili la ugonjwa wa Pendo alilokuwa amelishika mkononi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.


Baada ya kusoma maelezo kwa kitambo kifupi aliinua uso wake kumtazama muuguzi mmoja aliyefuatana naye, wakaonekana kuongea jambo fulani kwa lugha ya kitabibu, kuhusiana na tatizo la Pendo. Yule muuguzi alibetua kichwa chake kukubali.


Muuguzi alikuwa mwanamke wa umri wa kati ya miaka ishirini na nane na therathini, mrefu wa wastani, si mweusi wala si mweupe kwa rangi. Alikuwa na mashavu mfano wa chungwa na alikuwa na nywele nyingi kichwani, nyeusi fii.


Alikuwa amevaa gauni jeupe refu na pana kiasi lakini lililokuwa limeushika vyema mwili wake na kulichora vyema umbo lake kubwa. Kiunoni alikuwa amevaa mkanda mpana mweusi na kofia ndogo nyeupe ya kiuguzi yenye lesi iliyofunika sehemu ya utosi wa mbele kichwani kwake.


Baada ya mazungumzo mafupi ya kitabibu kati ya Daktari Msimbe na muuguzi, Daktari Msimbe aliandika taarifa fulani kwenye lile faili la ugonjwa wa Pendo kisha alimgeukia Sammy aliyekuwa amesimama kando ya kile kitanda akionekana mwenye huzuni.


“Poleni sana na kuuguza, Mungu atamsaidia mtoto na atakuwa sawa,” Daktari Msimbe alisema na kuachia tabasamu.


“Asante sana daktari,” Sammy alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani na kumeza mate kutowesha koo lake lililokauka.


Kisha Daktari Msimbe aliachia tabasamu pana la kufariji na kuanza kupiga hatua kuondoka, alifungua mlango na kutoka huku akifuatwa na yule muuguzi.


Kule nje Winifrida alikuwa amesimama na kujiegemeza kwenye ukuta wa korido pana na ndefu iliyozitenganisha zile wodi, alionekana kutafakari sana. Aligeuka kumwangalia Joyce aliyekuwa ameketi kwenye benchi huku akiongea na simu.


Muda huo huo alimuona muuguzi mmoja wa kiume aliyekuwa akipita eneo lile akisukuma kiti cha magurudumu kilichokuwa kimekaliwa na mgonjwa mmoja aliyeonekana kama nusu mfu huku akiwa ametundikiwa chupa ya maji na mrija wake ulipeleka maji kwenye mshipa wa damu wa mkono wake wa kulia.


Joyce akiwa na uso wenye huzuni aligeuza shingo yake kumwangalia yule mgonjwa na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiendela kusikiliza simu. Alionekana kukubali jambo kwa kubetua kichwa chake na kuvuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu. Muda mwingi alionekana kama aliyekuwa katikati ya mtihani mgumu sana.


“Ni kweli mama, lakini hapa nipo njia panda… hali ya mjukuu wako hadi sasa siyo nzuri kabisa…” Joyce alisema huku akivuta kamasi nyepesi kutokana na machozi mepesi yaliyokuwa yakimtoka machoni.


Aliyazungusha macho yake na kumwona Winifrida akiwa amejiegemeza kwenye ukuta huku akifuta machozi yaliyomtoka, Joyce alimtazama kwa makini na kuonekana kusita kidogo, kisha alishusha pumzi za ndani kwa ndani.



“Haya mama, ngoja nione itakavyokuwa halafu nitakupigia simu kukujulisha… lakini nisingependa kabisa kuikosa fursa hii muhimu kwangu!” Joyce alisema na kukata simu yake akionekana kuchanganyikiwa.


Aliinuka na kuondoka haraka eneo lile, akaingia wodini na kusimama karibu na Sammy huku akimwangalia Pendo kwa makini, huzuni ilikuwa inajionesha waziwazi kwenye macho yake. Sammy aligeuza shingo yake kumtazama Joyce, wakatazamana bila kusema neno. Joyce alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kubetua juu mabega yake.


* * * * *


Saa saba mchana Paradise Club, Zainab alikuwa ameketi kwenye sofa sebuleni akisoma magazeti ya siku ile, uso wake ulikuwa umeliinamia gazeti moja la kila siku lililokuwa limeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, hali iliyoonesha kuwa alikuwa amenogewa na habari iliyoandikwa gazetini.


Ilikuwa ni habari-muendelezo iliyohusu kutoweka kwa mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi wa gazeti la MamboLeo, Abbas Dalali, ambaye hakuna yeyote aliyejua yupo wapi, na kama ni mzima au mfu.


Kabla ya hapo, Zainab alikuwa amesoma habari nyingine mbili, moja ilihusu mke kumuua mumewe kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali, na nyingine ilihusu mume kumuua mkewe kwa kumbanika kwenye mkaa wa moto kama ndafu. Hizi ni habari alizokutana nazo kwenye magazeti karibu yote ya siku ile.


Hii ndiyo Tanzania ambayo utafiti ulionesha kuwa ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoongoza kwa watu wake kutokuwa na furaha! Ndiyo maana kila kukicha habari za matukio ya wenzi kuuana zilitawala!


Lakini… mbona hata nchi zilizoendelea zenye watu wanaoishi kwa furaha bado matukio kama hayo yalikuwepo, tena ni kwa kiwango kikubwa? Zainab alikumbuka kushuhudia matukio mengi ya mke kumuua mume au mume kuua familia yake yote, au mtoto kuua wazazi wake nchini Canada na hata Marekani!


“Sasa nini kifanyike?” alijiuliza bila kupata jibu huku akiyatupa yale magazeti kando. Alikumbuka kuwa hata yeye aliwahi kutuhumiwa kumuua mumewe Hemed miaka kumi na miwili iliyopita, na vyombo vya habari viliandika sana kuhusu hilo.


Zainab alimeza funda kubwa la mate kutowesha koo lake lililokuwa limekauka, alitamani sana habari ile ya mauaaji ya Hemed ibaki kuwa hadithi ya kutunga, hakupenda kukumbuka, lakini haikuwa hivyo. Mawazo sasa yalianza kupita kichwani kwake utadhani alikuwa akitazama sinema, aliyakumbuka maisha ya kijijini Mkuzi katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, alikozaliwa akiwa mtoto wa tatu na wa mwisho kwa mama, Bi Rehema, ambaye hakuwahi kuolewa.


Zainab ndiye mtoto pekee aliyesoma hadi kumaliza kidato cha nne ingawa hakuwa na ujuzi wowote wa maana, kwani hata hiyo elimu ya kidato cha nne aliimaliza kwa mbinde baada ya baba yake mzazi, Adam Semaya kufa na mama yao kuugua ugonjwa wa ajabu.


Zainab alipozaliwa aliwakuta dada zake wawili waliomtangulia, Nuru Mhina na Zuena Shauri ambao kila mmoja alikuwa na baba yake na hakuna kati yao aliyewahi kumfahamu baba yake, ni Zainab pekee aliyebahatika kumfahamu baba’ake, ingawa hata yeye alikuwa mtoto wa nje ya ndoa, kwani Bi Rehema hakuwa mmoja wa wake wanne wa Adam Semaya.


Japo maisha ya Bi Rehema hayakuwa mazuri lakini alijitahidi sana kuhakikisha binti zake wanasoma. Alikubali kufanya kazi dhalili katika mazingira magumu mno, kiasi cha kumuondolea utu na heshima kwa jamii ili tu binti zake wapate elimu aliyoamini ingewakomboa toka katika lindi la ufakiri.


Aliwahimiza sana binti zake kusoma kwani hakutaka na wao waishie alikoishia yeye, akiwa na wasiwasi kuwa kama angekufa wasingepata msaada kwa ndugu, kwa kuwa yeye alikuwa na ndugu wachache sana aliowafahamu upande wa mama yake, ambao hawakuwa ndugu wa damu, na hakumjua ndugu yeyote upande wa baba.


Bi Rehema hakujua alikotokea mama yake wala ndugu wa baba’ake, na siku zote alikuwa akisononeka zaidi, kwa kujua kuwa binti zake pia wangefuruka na kuishi maisha ya kubangaiza kijijini kama yeye endapo wasingetia bidii kusoma, ndiyo maana aliwahimiza sana kusoma.


Lakini maisha yalibadilika sana baada ya binti zake wakubwa, Nuru na Zuena kupachikwa ujauzito, kwa nyakati tofauti, wakiwa sekondari na kufukuzwa shule. Nuru hakurudi nyumbani, alitorokea kusikojulikana! Lakini Zuena alirudi kulea ujauzito wake nyumbani, na alipojifungua mtoto hakukaa hata mwezi akafa. Zuena akawa amekosa mwana na masomo, hivyo aliondoka nyumbani na kuelekea Arusha na kuanzia hapo hakuna tena aliyejua taarifa zake.


Kuanzia hapo Bi Rehema alianza kuumwa hiki na kile na miaka kadhaa baadaye Mzee Semaya alikufa ghafla baada ya kuanguka chooni, wakati huo Zainab alikuwa kidato cha kwanza. Hali ya Bi Rehema ilibadilika zaidi, alianza kuwa mtu wa kuuguzwa. Hakuna aliyejua alikuwa anaumwa ugonjwa gani, walipima na kupima lakini hawakuona ugonjwa wowote.


Aliendelea kuugua tu. Mara alalamike kuhusu miguu, mara alalamikie maumivu ya mgongo, mara kichwa! Ili mradi, hakukuwa na machweo yaliyopita asiwe katika hali ya kulalamikia maumivu. Katika kuhangaika huku na kule ikasemekana kuwa alikuwa amelogwa. Waliambiwa kuwa mchawi wake alikuwa ni mke mkubwa wa Adam Semaya


Lakini Daktari wa afya ya akili wa Hospitali Teule ya Muheza aligundua kilichokuwa kinamsumbua na kuwaeleza kuwa alisumbuliwa zaidi ni msongo mkali wa mawazo. Hili la msongo mkali wa mawazo hakuna aliyelielewa, hivyo walichagua kuamini katika ushirikina kuwa alilogwa, kwani ilikuwa rahisi kwao kuelewa hilo kuliko kuambiwa mawazo yakizidi huleta ugonjwa.


Zainab alikuwa na miaka kumi na nane alipomaliza kidato cha nne huko Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe. Rafiki wa baba yake aliyeitwa Julius Mhilu, ambaye alikuwa mhariri wa gazeti moja maarufu jijini Dar es Salaam, alimfanyia mpango wa kumpatia kazi katika hoteli ya kitalii ya Kilimanjaro, kwani alikuwa akifahamiana na wakubwa wengi serikalini.


Zainab hakwenda popote kwa ajili ya mafunzo ya kazi hiyo kama wafanyavyo wasichana wengine, kwa kuwa alipenda sana kufanya kazi, hivyo ilimchukua muda mfupi tu kuimudu kazi hiyo.


Alifanya kazi kwa bidii huku akijitahidi sana kumsaidia mama yake mgonjwa, kwa kutuma fedha kidogo nyumbani kila mwezi, kwani wakati huo ni yeye pekee aliyebakia kumsaidia mama yake kwa kuwa dada zake wote hawakuwepo nyumbani na hakuna aliyejua walikokuwa, isitoshe hakukuwa na mtu mwingine wa kumsaidia mama yao.


Ni katika hoteli ile ya Kilimanjaro ndipo siku moja alikutana na Hemed Kimaro, mfanyabiashara wa madini. Kama ilivyokuwa kwa dada zake, Zainab alikuwa msichana mrembo kweli kweli na kila mwanamume alikuwa yuko tayari kutoa roho yake ili amuoe.




Hemed alishindwa kuvumilia baada ya kumwona Zainab na kuamua kuingia mzima mzima kwenye mbio za kumfukuzia. Aliporusha ndoano hakuamini baada ya kuona akiibuka na ushindi. Hawakuwa na muda mrefu wa mazungumzo, na huo mfupi ulitosha kabisa kuwajulisha kuwa kila mmoja alitokea kumpenda mwenziwe. Miezi michache baadaye wakafunga ndoa.


Miezi ikaanza kusonga na hatimaye mwaka mmoja ukakatika lakini Hemed hakuwa mjuzi wa masuala ya ndoa, aliyachukulia kama jambo la kawaida sana na hakujali hisia za mwenzi wake wala kumfikisha alikotaka kufika kimapenzi. Muda mwingi alikuwa ‘bize’ na biashara zake na akirudi nyumbani amechoka, analala, wakati Zainab alitaka kufurahia ndoa yake…


Miaka mingine miwili ikapita tangu na hali ilikuwa ile ile, hatimaye mwaka wa nne ukafika lakini mambo haya kubadilika, yalibaki kuwa yale yale! Tena yalianza kuwa mabaya zaidi. Hemed alikuwa bize zaidi kiasi cha kuchelewa hata kurudi nyumbani na wakati mwingine hadi usiku wa manane. Siku moja Zainab alilala sebuleni kumsubiri mumewe kwa saa nyingi lakini hakurejea kabisa.


Hata aliporejea siku iliyofuata Zainab alimkabili kumuuliza alilala wapi, lakini alijibiwa kirahisi rahisi tu, Zainab kwa kumpenda mumewe alijitahidi kuvumilia akiamini kuwa huo ulikuwa ni upepo mbaya tu uliokuwa ukipita na muda si mrefu maisha yangesonga vyema.


Kutahamaki mwaka wa tano! Zainab alishangaa, mwaka wa tano katika ndoa lakini mambo ni yale yale na hawakuwa na mtoto, wala Hemed hakuonesha kushtuka. Ni wazi Hemed aliendelea kuchukulia mambo ya ndoa kirahisi rahisi.


Usiku Zainab alikuwa hapati usingizi, muda mwingi alikuwa anawaza kuhusu hatma ya ndoa yake, akibaki peke yake alikuwa analia tu, donge la hasira lilimkaba kooni na hakuweza kulihimili mpaka atoe kilio. Siku moja alijiuliza sana na kuamua kupeleka shauri lao kwa wifi yake mkubwa, Dk. Salma Oduya.


Hapo ndipo mume wa wifi yake, Mr. Oduya alipopata mwanya wa kuwa na ukaribu na Zainab na baadaye kupenyeza ushawishi wake, haikuchukua muda wote wawili wakagundua kuwa kila mmoja alihitaji faraja lakini wote walionekana kuikosa katika ndoa zao. Hawakuwa na njia nyingine isipokuwa kuitafuta nje ya ndoa na hatimaye Zainab akapata ujauzito…


_____


“Madame, kuna tatizo lolote?” sauti laini ya Lilian ilipenya hadi kwenye ngoma ya masikio ya Zainab na kumzindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Aliinua uso wake kumtazama Lilian aliyesimama mbele yake na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akilazimisha tabasamu.


Lilian alikuwa amesimama pale kwa kitambo kirefu akimsemesha Zainab lakini ilionesha kuwa Zainab alikuwa mbali kimawazo. Alimtazama Zainab kwa macho yenye udadisi na mkononi alikuwa ameshika bilauri na chupa ndefu ya mvinyo mwekundu wa bei ghali aina ya Romanee-Conti uliotengenezwa nchini Ufaransa.


“Kinywaji chako hiki hapa, madame,” Lilian aliongea kwa sauti tulivu huku macho yake yakiendelea kuweka kituo kwenye uso wa Zainab.


Na hapo Zainab akakumbuka kuwa alipokuwa anasoma magazeti alimuagiza Lilian kumtafutia mvinyo mwekundu wa Kifaransa aina ya Navette de Marseille au Romanee-Conti.


“Ah, usijali mdogo wangu… weka hapo,” Zainab alisema huku akimuonesha Lilian ilipo meza, alijitahidi kuupamba uso wake na tabasamu na kuyakwepa macho ya Lilian. Alikuwa analengwa na machozi kutokana na kukumbuka mengi katika maisha yake ya zamani.


Kumbukumbu zile zilikuwa zimemuumiza sana, hasa kwa kuwa mama yake Bi Rehema alikufa kwa msongo mkali wa mawazo miezi miwili tu baada ya yeye Zainab kutuhumiwa kushiriki katika mauaji ya mumewe, Hemed.


“Asante sana mdogo wangu, unaweza kuendelea na kazi zako kama nikihitaji kitu nitakujulisha,” Zainab alimwambia Lilian baada ya kuona alikuwa bado amesimama mbele yake akisubiri maagizo. Lilian aligeuka na kuondoka haraka kutoka eneo lile, akaelekea jikoni huku akiwa na wasiwasi.


* * * * *


Saa saba mchana katika ofisi za Mr. Oduya zilizo ghorofa ya sita ya jengo la ghorofa kumi na mbili lililomilikiwa na Mr. Oduya, jengo lililokuwa katika barabara ya Bagamoyo eneo la Kijitonyama jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara huyo na mgeni wake, Balozi Aldolf Mageuzi, walikuwa wanabadilishana mawili matatu.


Ni Balozi Mageuzi aliyeomba kuonana na Mr. Oduya mchana ule, na yeye hakuweza kukataa ombi lake kwa kuwa alikuwa mmoja kati ya watu muhimu na walioheshimika sana. Balozi Mageuzi alikuwa kati ya washauri muhimu sana wa Rais wa Tanzania, Dk. Yohana Funguo, hasa katika masuala ya diplomasia, ulinzi na usalama wa taifa.


Ni kwa sababu ya kutambua umuhimu wake ndiyo maana mchana wa Jumapili ile Mr. Oduya aliondoka Paradise Club akimwacha kipenzi chake Zainab, badala yake alitenga muda ili aweze kuonana na Balozi Mageuzi.


Balozi Mageuzi alifika pale kuongea na Mr. Oduya ili kujua upepo wa kisiasa kwa upande wake ulikuwaje, hasa baada ya kushuhudia vuguvugu la urais ndani ya Chama Cha Ukombozi (CCU) likizidi kupamba moto, kwani Rais Yohana Funguo alikuwa mbioni kumaliza muhula wake wa pili.


“Niseme ukweli, upepo wa kisiasa si mbaya, unavuma vizuri sana licha ya changamoto za hapa na pale kutok kwa washindani wangu lakini nimekwisha jiweka vizuri sana kwani nina sapoti kubwa ya mabilionea wa Paradise Club na wamekubali kufadhili kampeni zangu nchi nzima,” Mr. Oduya alimwambia Balozi Mageuzi.


“Ni jambo zuri lakini kumbuka awamu hii siyo ile ya Rais Sakaya Mkiete, hii ni ya Dk. Funguo, na mfumo wote ndani ya CCU umebadilika, sidhani kama hao mabilionea wana ushawishi mkubwa ndani ya chama, labda nje ya chama. Hata hivyo, bado sina wasiwasi na nguvu yako ingawa hupaswi kujipa uhakika sana,” Balozi Mageuzi alisema huku akimwangalia Mr. Oduya kwa makini.


“Kwa nini unasema hivyo, Balozi?” Mr. Oduya aliuliza huku akimkazia macho Balozi Mageuzi.


“Kwa hali ilivyo, hamasa ya kuwania uteuzi imeongezeka sana ndani ya chama. Ila bado imeendelea kuwa siri ni nani na nani watajitosa kuwania uteuzi. Lakini najua mheshimiwa Tumbo na Dk. Hussein Abbas watawania…” Balozi Mageuzi alisema na kuongeza.





“Ni jambo zuri lakini kumbuka awamu hii siyo ile ya Rais Sakaya Mkiete, hii ni ya Dk. Funguo, na mfumo wote ndani ya CCU umebadilika, sidhani kama hao mabilionea wana ushawishi mkubwa ndani ya chama, labda nje ya chama. Hata hivyo, bado sina wasiwasi na nguvu yako ingawa hupaswi kujipa uhakika sana,” Balozi Mageuzi alisema huku akimwangalia Mr. Oduya kwa makini.


“Kwa nini unasema hivyo, Balozi?” Mr. Oduya aliuliza huku akimkazia macho Balozi Mageuzi.


“Kwa hali ilivyo, hamasa ya kuwania uteuzi imeongezeka sana ndani ya chama. Ila bado imeendelea kuwa siri ni nani na nani watajitosa kuwania uteuzi. Lakini najua mheshimiwa Tumbo na Dk. Hussein Abbas watawania…” Balozi Mageuzi alisema na kuongeza.


Sasa endelea...


“Dk. Hussein Abbas japo anaonekana kama asiye na nia lakini kwa taarifa nilizonazo atawania nafasi ya kuteuliwa na chama, ni mmoja kati ya wanachama wenye nguvu kubwa kwenye chama na kwa siku za hivi karibuni nguvu yake imeongezeka na kutishia vigogo wenzake serikalini ambao nao wana dhamira kama yake…”


“I see! Kumbe mambo ni moto moto kiasi hicho!” Mr. Oduya alionesha kushangaa sana.


“Hivi nikuambiavyo tayari mheshimiwa Tumbo ameanza kampeni za chini kwa chini ili kutafuta uungwaji mkono katika zoezi la kura za maoni na katika vikao vya juu vya uteuzi ndani ya chama…”


“Niseme ukweli, sikutegemea kama Dk. Hussein Abbas angeonesha nia ya kutaka kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taarifa nilizo nazo ni kwamba anaandaliwa kuwa Rais wa Zanzibar, ndiyo maana nilifikiria kumshirikisha kwenye mikakati yangu ya urais!” Mr. Oduya alisema kwa mshangao.


“Hakuwa akitaka ila wazee wamemuomba. Na jambo hili limesababisha makundi ndani ya chama, lipo kundi linalomsapoti Dk. Hussein Abbas na lingine linamshabikia Mheshimiwa Tumbo, kwa hiyo kuna mchuano mkali wa chini kwa chini kati ya vigogo hawa wakubwa serikalini. Kumbuka hawa waliwahi kuwa maswahiba wakubwa lakini kwa sasa wamekuwa mahasimu wakubwa. Kwa ufupi hiyo ndiyo hali halisi ilivyo ndani ya Chama,” Balozi Mageuzi alisema na kutingisha kichwa chake kwa huzuni.


“Nimekuelewa Balozi, kama Dk. Hussein Abbas naye anatafuta nafasi ya kuungwa mkono kugombea urais basi tutegemee mnyukano mkubwa kati yake na mheshimiwa Tumbo. Wawili hawa watakigawa chama katika sehemu mbili, sipati picha mtikisiko utakaokuwepo ndani ya chama katika uteuzi, ndiyo maana naamini kuwa mwisho wa siku ni mimi nitakayeibuka mshindi, japo shaka yangu kubwa ni mheshimiwa Tumbo kutumia siasa za majitaka…” Mr. Oduya alisema huku akijiweka sawa kwenye kiti chake.


“Kweli kabisa, kuna kila dalili za mpasuko ndani ya chama, hawa vigogo wameanza kukigawa chama katikati na hilo ndilo hasa limenifanya nitake kukuona. Cha kwanza nijue msimamo na pili nikupe taarifa ambazo naamini bado hujazipata,” Balozi Mageuzi alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.


“Zipi hizo?” Mr. Oduya aliuliza kwa shauku huku akimkazia macho Balozi Mageuzi.


“Sipendi kukuficha rafiki yangu lakini ni ukweli usiopingika kuwa utapata wakati mgumu sana kuteuliwa ndani ya chama kwa sababu ya vigogo hawa wawili kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama na wewe nguvu yako kubwa iko nje ya chama. Hivi sasa kuna mkakati maalumu wa kumshawishi Rais ili jina lako likatwe kabla ya kufika Halmashauri Kuu. Juzi usiku kulikuwa na kikao cha siri Chattle Hotel na mwenyekiti wake alikuwa Katibu Mkuu wa Chama, Dk. Bazil Uledi…” Balozi Mageuzi alisema na kunyamaza kidogo, akailamba midomo yake iliyoanza kukauka.


“Ninazo taarifa za uhakika kuwa mheshimiwa Tumbo tayari ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama na wajumbe wengi wa kanda yote ya kusini, pwani na kwa sehemu kubwa ya kanda ya magharibi. Kuna mtandao makini na wa siri umeundwa ili kuhakikisha wanashinda, kusema kweli hawalali, wanafanya kazi usiku na mchana…” Balozi Mageuzi aliongezea.


Maneno yale yalimshtua sana Mr. Oduya, alibaki ameduwaa huku akihisi joto kali mwilini na jasho jepesi likianza kumtambaa sehemu mbalimbali za mwili wake, koo lake lilikauka ghafla na nywele zikamsimama kichwani kwa hofu.


“Wanahangaika usiku na mchana kwa kuwa hofu yao kubwa ni wewe, wanaogopa wakikuachia upenyo kidogo utawashinda kwani jina lako linatajwa sana katika orodha ya watu wenye sifa na uwezo wa kuiongoza nchi hii, kutokana na misaada mbalimbali ambayo umekuwa ukiitoa kwa vikundi vya walemavu, akina mama na vijana,” Balozi Mageuzi alisema baada ya kuona Mr. Oduya yupo kimya akimtumbulia macho.


“Kwani mheshimiwa Rais anasemaje kwenye hili? Umebahatika kusikia chochote kuhusu mtu anayemuunga mkono?” hatimaye Mr. Oduya alimudu kuuliza, hata hivyo bado alikuwa na wasiwasi.


“Sijamsikia kusema chochote, lakini natambua urafiki wenu ulivyo mkubwa, yeye ni mmoja wa watu wanaokukubali, na wapinzani wako wanajua hilo, ndiyo maana hawapati usingizi… hivi sasa wanawatumia watu wa Usalama wa Taifa kukusanya kila taarifa ya kashfa inayokuhusu ili wampelekee Rais,” Balozi Mageuzi alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.


Kilipita kitambo kirefu cha ukimya, kila mmoja alikuwa kimya akitafakari. Sasa Mr. Oduya hakuhisi tena joto kali mwilini bali alianza kukihisi ubaridi mkali ukimtambaa mwilini mwake.


“Lakini usihofu, najua yupo mtu mmoja muhimu sana, kama utaweza kumshawishi ajiunge na upande wako utakuwa umemaliza vita kabla hata hujafika kwenye uwanja wa mapambano…”


“N-nani?” Mr. Oduya aliuliza kwa pupa huku uso wake ukianza kuonesha matumaini.


“Makamu Mwenyekiti wa Chama, mzee Fabian Magulu… kama umegundua huyu mzee anakubalika sana, ndiye mwenye ushawishi mkubwa siyo tu ndani ya chama bali hadi serikalini na ndiye alikuwa nguzo muhimu ya ushindi na mafanikio yote ya Rais Funguo, wakati akiwania kipindi cha pili cha urais. Unakumbuka alipigwa sana vita ili aishie kipindi kimoja,” Balozi Mageuzi alisema na kumfanya Mr. Oduya avue koti lake na kulitundika kwenye kiti chake, sasa hakuwa akihisi tena baridi.



“Unajua sina ukaribu sana na mzee Magulu japo tunafahamiana, sijajua nitamuingiaje!” Mr. Oduya aliuliza kwa sauti tulivu.


“Usipate taabu, ndiyo maana nipo hapa kukusaidia, nipe wiki moja tu nitakuelekeza nini cha kufanya ila kama utakuwa tayari kufuata ushauri wangu…”


“Kwa nini nisifuate ushauri wako wakati ni wewe ndiyo umenifumbua macho?” Mr. Oduya alisema huku akionesha uso wenye matumaini mapya, sura yake sasa ilikuwa imejenga tabasamu pana.


* * * * *


Saa kumi na moja na dakika arobaini jioni ilimkuta Madame Norah akiwa ameketi kwenye kochi kubwa la sofa ndani ya ukumbi mkubwa wa kisasa wenye jukwaa zuri la kisasa lililokuwa linatazamana na viti vingi vya kisasa kwa ajili ya burudani au kufanyia mikutano. Kulikuwa na seti moja ya masofa yaliyokuwa yamepangwa kwa namna ya kulizunguka lile jukwaa.


Ukumbi ule ulikuwa katika jumba zuri la kifahari la ghorofa tatu lililokuwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi katika eneo la Mikocheni, likiwa limezungukwa na miti mirefu ya kivuli. Eneo lile lilikuwa la majumba ya kifahari ya makazi ya kisasa ya watu wenye ukwasi, yaliyozungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika.


Jumba lile lilikuwa limezungukwa na ukuta uliofungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi juu yake na lilikuwa na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri.


Madame Norah alikuwa mrefu na mweupe mwenye umbo la kupendeza japo alikuwa na umri mkubwa, alikuwa amevaa blauzi ya bluu ya mikono mirefu, suruali ya Jamsuit ya rangi nyekundu iliyolichora vyema umbo lake refu maridadi lenye kiuno chembamba lakini imara kikiwa kimebeba minofu ya mapaja iliyokaza kutokana na mazoezi.


Miguuni alikuwa amevaa viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio vya rangi ya bluu na harufu nzuri ya manukato ghali aliyokuwa amejipulizia mwilini ilitamalaki mle ukumbini


Japo alijitahidi kuonekana mchangamfu sana lakini macho yake yalionesha huzuni fulani, hakuwa na furaha kabisa. Alikuwa mbali kimawazo japo alionekana kama alikuwa anamwangalia msaidizi wake na mtayarishaji wa kipindi chake maarufu cha Madame Norah Show, Jessica Walari.


Wakati huo Jessica alikuwa anatoa maelekezo kwa wapigapicha za mnato na video wakati wakichukua picha za matukio mbalimbali za wabunifu wa mavazi waliokuwa wakiandaa mavazi na kuivalisha ‘midoli’ mikubwa iliyokuwepo eneo lile.


Pale kwenye masofa alipoketi Madame Norah pia kulikuwa na wageni wachache mashuhuri waliofika kumuunga mkono Madame Norah katika shughuli zake za kusaidia jamii. Kushoto kwa Madame Norah aliketi kijana mmoja mtanashati asiyezidi miaka therathini na tano, aliitwa Florian na alikuwa mpenzi wa Madame Norah.


Florian alikuwa mweupe, mwenye ngozi nyororo na umbo kakamavu la kimichezo, alikuwa amevaa fulani nyekundu na suruali ya jeans ya rangi ya bluu. Kichwani alivaa kofia nyekundu aina ya kapelo na miguuni alivaa raba ndefu na ngumu za rangi nyekundu.


Kama walivyo vijana wengi wenye tabia ya kupenda wanawake waliowazidi umri kwa sababu ya kutaka fedha zao, Florian hakuona aibu kuambatana na Madame Norah kila alipokwenda, na muda ule alikuwa amejiegemeza kwenye sofa katika hali ya mahaba.


Kuna muda alimnong’oneza jambo Madame Norah wakati akiongea na wageni wake, Madame Norah aligeza shingo yake kumtazama Florian na kuachia tabasamu pana la kimahaba, kisha alinyoosha mkono wake na kumgusa shingo yake.


Florian alikuwa ameweka mkono wake wa kulia juu ya paja la Madame Norah kisha aliuchukua mkono wa kushoto wa Madame Norah, moja kwa moja akaupeleka kwenye uso wake, aliupitisha kwenye paji la uso wake na kumfanya Madame Norah kuligusagusa paji lake.


Muda ukafika wapiga picha wakaweka tayari kamera zao kuzielekeza jukwaani kwa Madame Norah, kisha Jessica alitabasamu na kumpa ishara ya dole gumba kuwa wapo tayari kuanza kuchukua picha ya kilichowaleta pale.


Madame Norah alinong’ona jambo kwenye siko la Florian na kumfanya aachie kicheko hafifu cha mahaba. Madame Norah alitabasamu na kumpiga piga Florian mgongoni kwa mahaba, kisha Florian aliinuka taratibu na kuondoka akimwacha Madame Norah na wageni wake pale jukwaani.


Madame Norah alishusha pumzi za ndani kwa ndani, akaketi vizuri kwenye sofa, na baada ya kupewa ishara na Jessica, alianza kwa kujitambulisha na kuwatambulisha wageni wake kisha akaeleza lengo lake.


“Kwanza niweke wazi, maonesho ya mwaka huu yatakuwa tofauti kidogo na miaka mingine, tumeandaa kitu kinachoitwa Live from the Red Carpet kitakachowafanya watu wote wawe sehemu ya onesho. Litakuwa onesho kubwa kuwahi kufanyika Afrika kwani tumewaalika wabunifu na wanamitindo wakubwa duniani na lengo likiwa kutunisha mfuko ili kuwajengea makazi bora wazee wasiojiweza sambamba na kituo na shule ya watoto wenye ulemavu na waishio katika mazingira magumu chenye miundombinu rafiki kwa elimu yao na makazi. Itakuwa shule ya aina yake na ya kimataifa kwani baadaye tutaweza kupokea hata watoto kutoka maeneo mengine ndani na nje ya nchi…” Madame Norah alisema huku akiachia tabasamu.


“Kupitia Madame Norah Foundation tutazidi kutatua matatizo mbalimbali ya watoto na wazee wasiojiweza ambao ni kundi linaloonekana kusahaulika sana. Tumekuwa tukitoa misaada mbalimbali kwenye vituo vya yatima na hospitalini kusaidia watoto wadogo na hata wazee, tumekuwa tukisaidia huduma za afya, chakula na mambo mengine. Katika utafiti tulioufanya mwaka jana tumegundua kuwa kundi moja limesahaulika sana, ni la watoto wenye ulemavu. Kundi hili linazidi kuongezeka na wanakumbana na changamoto nyingi sana…” Madame Norah alinyamaza kidogo na kumeza mate ili kutowesha koo lake lililoanza kukauka.




“Kwa miaka kumi sasa tangu niingie katika tasnia ya ubunifu na mitindo, mwaka huu tutayatumia maonesho haya kuandaa pia chakula cha hisani na kuwakaribisha watu mbalimbali mashuhuri, taasisi za serikali, mashirika na watu binafsi ambao watachangia fedha. Na hata tusipofikia lengo la kiasi kilichokusudiwa kukusanywa hatutaacha kujenga… kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Simamia ndoto yako usijali wengine wanasema nini’.” Madame Norah alimaliza hotuba yake na kuachia tabasamu.


Baada ya kutambulisha lengo lake waandishi wa habari walimuuliza maswali ambayo aliyajibu kwa ufasaha kisha alianza kuwatembeza waandishi na wageni kuwaonesha sehemu mbalimbali na kazi walizokuwa wanazifanya pamoja na hatua mbalimbali za ubunifu wa mavazi ndani ya lile jumba.


Baada ya kuwatembeza eneo lote Madame Norah aliagana na wageni wake kisha akaelekea kwenye ofisi yake binafsi iliyokuwa juu kabisa, kwenye ghorofa ya tatu ya lile jumba la kifahari.


Aliingia ofisini kwake na kuketi kwenye kiti kirefu cha kuzunguka cha kiofisi cha ngozi halisi kilichokuwa na magurudumu madogo yaliyokiwezesha kusogea.


Ilikuwa ofisi nzuri yenye samani za bei ghali, ikiwa na kiyoyozi aina ya Boss kilichokuwa kikisambaza hewa safi mle ndani, zulia nene la manyoya la rangi nyekundu sakafuni, meza kubwa ya kiofisi ambayo juu yake kulikuwa na kompyuta moja aina ya IMac Retina 5K ya inchi 27, kidau cha wino, mhuri na kichupa kidogo chenye wino mweupe wa kufutia maandishi.


Pembeni kulikuwa na meza nyingine ndogo ya kioo ya pembe nne na juu yake kulikuwa na chupa kubwa ya mvinyo mwekundu aina ya Navette de Marseille na bilauri, chini ya ile meza kulikuwa na magazeti na majarida mbalimbali ya mitindo.


Meza hiyo ilikuwa mbele ya kochi moja kubwa jeusi la sofa na ukutani juu ya ile meza ya kioo kulikuwa na shubaka la vitabu lililokuwa na vitabu na mafaili yenye nyaraka mbalimbali yaliyopangwa kwa ustadi mkubwa.


Upande wa kulia kulikuwa na madirisha mapana ya kioo yaliyokuwa na mapazia mepesi marefu ya rangi ya samawati, na pembeni kabisa kulikuwa na mlango ulioelekea kwenye maliwato maalumu ndani ya ofisi ile.


Pia kulikuwa na kabati kubwa la ukutani lenye mbao zilizosanifiwa kwa ustadi wa hali ya juu na kulikuwa na kioo kirefu cha kujitazama, pembeni yake kulikuwa na jokofu ukubwa aina ya BOSS lililojazwa vinywaji mbalimbali vya kumchangamsha yeyote aliyeingia humo, hata kama angekuwa amechoka sana baada ya kazi ngumu.


Akiwa na huzuni, Madame Norah alivuta droo moja ya meza yake na kutoa picha tatu, aliziangalia kwa kitambo na kushusha pumzi za ndani kwa ndani huku akionekana kukata tamaa.


Zilikuwa picha zake za zamani, akiwa bado binti tineja. Picha moja ilimuonesha akiwa na wadogo zake wawili, wote wa kike, wakiwa wamesimama nje ya nyumba yao ndogo ya nyasi kijijini kwao Mkuzi Wilaya ya Muheza. Picha hiyo ilipigwa kama kumbukumbu baada ya kupata matokeo mazuri ya darasa la saba.


Madame Norah alikuwa amevaa gauni refu la zambarau lenye maua ya rangi mchanganyiko na alikuwa na miaka kumi na tano, wadogo zake mmoja alikuwa na miaka kumi na moja na mwingine alikuwa na miaka mitatu.


Picha ya pili aliipigia shuleni wakati huo akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Usagara jijini Tanga, alikuwa na wanafunzi wenzake na picha ya tatu alikuwa na kijana mmoja mtanashati wakiwa katika mkao wa kimahaba.


Aliitazama kwa kitambo kirefu ile picha ya tatu, mara matukio fulani ya zamani yakaanza kumjia akili kwake, alikuwa kama aliyekuwa anaangalia kipande cha filamu ya kuhuzunisha. Ilikuwa ni mchanganyiko wa picha mbalimbali za msichana mrembo wa miaka kumi na nane akiwa analia kwa uchungu katika chumba kidogo chenye mwanga hafifu wa taa.


Msichana huyo alikuwa mwenye huzuni nyingi na alitazama mbele yake kwa huzuni, wakati huo sauti ya mwanamume ilisikika ikimtaka aondoke haraka na haakutakiwa kuonekana tena pale. Kisha sauti ya mtoto mchanga akilia nayo ikasikika…


Madame Norah alizinduka kutoka kwenye yale mawazo, akaangaza macho yake huku na huko na kugeuka kujitazama kwenye kioo kirefu cha kujitazama, alijitazama kwa kitambo akionekana mwenye huzuni kubwa.


Michirizi ya machozi ilionekana kwenye mashavu yake na muda huo alianza kulia kwa uchungu kilio cha kwikwi. Alijiegemeza kwenye kiti chake huku akikumbatia zile picha kifuani kwake, akatoa leso na kupenga kamasi.


Sasa mawazo yalimjaa kichwani, alikumbuka juu ya taabu zote alizokumbana nazo maishani mwake mpaka kufikia pale. Jina lake halisi aliitwa Nuru Mhina.


Alikuwa na shahada zote za mwanamke mrembo, ingawa aliachishwa shule akiwa kidato cha nne, wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na nane, baada ya kugundulika alikuwa na ujauzito wa miezi sita. Alikabidhiwa barua aliyotakiwa kuipeleka kwa mzazi wake nyumbani, lakini asifike baada ya kukumbuka maneno ya mama yake:


“Unakwenda sekondari na umeshakuwa mwali sasa, kasome na uchunge sana kukaribiana na wanaume. Elimu ndiyo urithi wako pekee na siku ikitokea umefanya ujinga ukapata ujauzito basi utafute kabisa pa kwenda, usirudi hapa nyumbani…”


Mama yake alikuwa amemtolea uvivu wakati akijiandaa kwenda kuanza kidato cha kwanza jijini Tanga. Wakati huo alikwishatimu miaka kumi na tano na chuchu za usichana zilikuwa zimechomoza kifuani kwake kama embe dodo changa na kutishia kutoboa kila blauzi aliyovaa. Alikuwa na uzuri wa asili na ulimbwende wake uliwaka kama karabai gizani.


Lakini huko shule maisha yalikuwa magumu sana, alianza kuwa na kesi za shule kila iitwapo leo; hakuwa mtoro wala mjinga bali alikuwa na kesi za kukosa fedha ya michango ya hiki na kile. Hata fedha ya ada ilikuwa inalipwa kwa mbinde sana, kuna wakati alirudishwa nyumbani, wanakijiji wakachangishana ili kusaidia ndipo fedha ikapatikana. Kiujumla maisha yalimpigisha kwata na shule aliiona chungu.


Maisha ya shida yalimfanya ajiulize kwa nini hakuzaliwa kwenye familia zenye ahueni kama wanafunzi wenzake? Mama na wadogo zake walilazimika kula mlo mmoja tu, tena kwa shida ili yeye aweze kusoma.




Alijitahidi kuivumilia ile dhiki lakini mambo yalianza kufikia ukomo wa uvumilivu. Alipoingia kidato cha nne alikuwa anaelekea kutimiza mwaka wa kumi na nane tangu kuzaliwa, lakini kwa sababu maisha yalimpigisha kwata ungeweza kudhani alikuwa anaikimbilia miaka therathini tangu alione jua. Usichana wake ulishambuliwa na utu uzima uliomjia ukiwa umevikwa koti la umasikini.


Lakini hadi wakati huo hakuwa amemfahamu mwanamume, alikuwa bado bikira! Ni katika kipindi hicho vishawishi vilizidi na yeye alitamani sana apendeze kama wasichana wenzake, hasa rafiki zake Mainda Shelukindo na Johari Mcharo. Nguo zake zilikuwa zimechakaa na hakuwa na viatu vya maana.


Ilifikia kipindi alitamani atafute fedha. Angezipataje sasa? Hakukuwa na njia nyingine ya kuzipata isipokuwa kufanya kama rafiki zake, hasa Mainda aliyekuwa akimsaidia mara kwa mara kalamu na madaftari, na wakati mwingine alimpa hata nguo zake na viatu alivyovichoka. Lakini hakumpa hivi hivi bali alimsema kwanza kwa kutochangamka. Walikuwa wakimshangaa, walidhani labda alitaka kuwa Mtawa!


Taabu ilikuwa kwamba hakuwa ameyazoea mambo ya umalaya. Haikuwa haiba yake kuukabidhi mwili wake kwa mwanamume kabla ya ndoa ili apewe fedha za kutatua matatizo yake. Hata hivyo, vishawishi kutoka kwa Mainda na Johari vilimpa kisebusebu. Roho ilimchonyota na fedha aliitaka.


Tena aliitaka sana tu na ushawishi wa rafiki zake ulivyomvika nguvu, Nuru akayavua mashaka na kuamua kujitosa. Ni wakati huo ndipo alipokutana na kijana wa aina na kariba yake. Kijana huyo aliitwa Rafael Jengo na alikuwa mtanashati kweli kweli.


Rafael ndiye aliyemwondolea ‘utoto’ wake na kumwingiza katika dunia ya watu wazima. Ndiye yeye aliyejitokeza kuwa faraja na furaha yake katika maisha yale ya shule, tangu alipoufahamu ulimwengu huu.


Walianza taratibu, siku za mwanzo zilikuwa za maumivu makubwa, hata hivyo, hakuwa na namna. Kwani ukitaka kula sharti uliwe! Alijikaza kwa kuwa alifahamu anapaswa kuvumilia ili afanikiwe kama rafiki zake, hasa Mainda. Akakomaa kweli kweli na baadaye akazowea.


Sasa alipopewa barua ya kumkabidhi mzazi wake hakuona sababu ya kurudi nyumbani, aliamua kwenda moja kwa moja eneo la Ngamiani alikokuwa akiishi Rafael, mwanamume aliyemkatizia ndoto yake ya kusoma ili aje kuwa mwanasheria.


Alimkuta Rafael akiwa na msichana mwingine nyumbani, walikuwa kitandani watupu kama walivyozaliwa. Nuru alishindwa kuvumilia. Msirimbi wa kipaji cha uso wake uliumuka, milizamu ikatutusika chini ya masikio yake kama iliyopulizwa, na mara kikamtoka kikohozi kikubwa na michirizi ya machozi ikapasuka machoni mwake.


Alilia kwa uchungu mkubwa mbele ya Rafael lakini mwenzake akakana kumfahamu yeye wala ujauzito wake. Kuona hivyo, Nuru hakutaka makuu, aligeuka akaondoka zake huku akilia kwa uchungu. Jambo moja lilimjia kichwani, atafute vidonge anywe ili afe yeye na mtoto wake tumboni.


Sauti nyingine ilimwambia mtoto tumboni hakuwa na kosa na yeye hakutakiwa kukata tama, kwani hakuwa wa kwanza kupata ujauzito akiwa shuleni. Sasa hakuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kwenda kuomba hifadhi kwa rafiki yake Mary Mgaya aliyekuwa anaishi eneo la Kiriwani, barabara ya Pangani, nje kidogo ya jiji la Tanga.


Nuru alikuwa amefahamiana na Mary aliyewahi kuishi kijijini Mkuzi kwa mama’ake mdogo, wakati huo Nuru akisoma shule ya msingi. Hivyo Nuru alimwomba Mary asimwambie yeyote kama yeye aliishi kwake. Alijifungua mtoto mzuri wa kike, kisha alirudi tena Ngamiani nyumbani kwa Rafael na kumbwagia yule mtoto, yeye huyo akatorokea jijini Dar es Salaam.


Huko jijini Dar es Salaam alitafuta kazi kila sehemu, mwishowe aliajiriwa kazi ya kutunza nyumba na mama mmoja, mke wa meneja rasilimali-watu wa kiwanda cha Bora. Alilipwa mshahara kidogo wa kujikumu kwa mwezi, chakula bure, malazi bure, nguo alizozichoka mama mwajiri bure. Akatae? Ili iweje?


Maisha mapya yakaanza. Kutokana na uzuri wake wa asili haikuchukua hata mwezi akamfadhaisha baba mwenye nyumba na kumtisha mama mwajiri. Matokeo yake alitupiwa virango, akalipwa mshahara wake na nauli juu, kisha akatakiwa kuondoka mara moja na kurudi kwao Tanga.


Hakurudi. Afuate nini? Kwanza maisha ya nyumbani kwao yalikuwa magumu sana, maisha ya kuishi na mzazi mmoja tu wa kike, tena ya jembe na mpini wake! Halafu angemwambia nini mama yake? Aliamua kubaki Dar es Salaam. Kwa nini? Aliyekuwa baba mwenye nyumba alikuwa amenogewa na sasa alipanga kumlipia kodi kwa siri ili waendelee kubanjuka.


Alipewa fedha nyingi kisha akatafuta chumba eneo la Magomeni Makuti. Chumba chake hakikuwa kikubwa, kilikuwa cha kawaida ila hakikutofautiana na stoo, kilibeba kitanda kidogo cha futi tatu na nusu kwa sita pamoja na majukumu yote ya sebule, jiko, stoo na mengineyo.


Nyumba aliyopanga ilikuwa ya vyumba kumi, sita kwenye nyumba kubwa na vingine vinne vya mabanda ya uani. Alikuta wapangaji wengine, wengi wakiwa wasichana kama yeye, hivyo akawa amepata marafiki. Wakati huo ahueni ndogo ya maisha ilishamtembelea, alikuwa amepata wa kumpa vya kumuwezesha hata kupanga chumba kama kile.


Miezi miwili tu tangu ahamie hapo akapata kazi katika kampuni moja ya samani za ofisini na majumbani kama mkaribisha wateja, baada ya kumfurahisha mfadhili wake.


Nuru alianza kubadilika, alinawiri na kuwa mrembo kweli kweli, hata shoga zake walianza kumuonea donge. Chuki ikaanza kumea baina yao. Hakujali, kwani alikuwa na marafiki wengi wa kiume kuliko wa kike. Na ni hao ambao aliwahitaji zaidi. Mtaa ule akauhama na kwenda kuishi Kijitonyama, na hata jina alibadilisha, hakuitwa tena Nuru bali Madame Norah.


Katika kipindi hicho alifanya makosa mara tatu, mara ya kwanza aliruhusu ujauzito bila taarifa wala hiyari, hakumjua aliyempa ujauzito huo wala hakuhitaji mtoto. Suluhu ikawa kuutoa. Haikuchukua muda mrefu mimba nyingine ikanasa. Nayo akaitoa.


Mwaka mmoja baadaye akanasa ya tatu iliyomhenyesha kweli kweli! Hata hivyo, fedha kidogo alikuwa nayo, akampata daktari mmoja asiye na huruma aliyefanya kazi yake barabara, lakini yeye aliponea chupuchupu.





Baada ya mwaka mmoja na nusu wa kufanya kazi katika kampuni ya samani za ofisini na majumbani aliachishwa kazi na kuanzia hapo hakutaka tena kuajiriwa, badala yake, alizidi kujitafutia riziki kutoka kwa wanaume mbalimbali, hakujali yupi ajaye, yeyote alikuwa sawa tu kwake ili mradi tu amkatie fedha za kutosha.


Siku moja jioni akiwa katika mawindo eneo la Hoteli ya Mawenzi, alikutana na kijana mmoja wa kizungu kutoka Sweden, Karl Johan. Madame Norah akamfurahisha kweli kweli Karl, kiasi cha kukiri kuwa ingawa alishatoka na wasichana wengi lakini kwa Madame Norah alipiga saluti, sasa aliamua kuchonga mzinga.


Karl akampeleka Madame Norah nchini Sweden, lakini mambo hayakwenda kama alivyopanga. Waliachana huku akimpa fedha nyingi za kujikimu pindi akirudi Tanzania. Lakini Madame Norah hakurudi Tanzania. Afuate nini?


Aliamua kubaki huko huko Sweden akihangaika na haikuchukua muda akaangukia katika penzi la mzungu mwingine aliyeitwa Andreas Gunnar. Andreas aliwahi kuwa balozi wa Norway nchini Tanzania na walikutana katika klabu ya usiku ya Tradgarden iliyopo barabara ya Harmmaby Slussvarg, jijini Stockholm.


Hapo ndipo bahati ya Madame Norah ilikuwa ikimsubiri, Andreas alikolea kweli kweli, kwanza akaamua kumpeleka shuleni akiwa na miaka 24 kumalizia masomo yake. Alimaliza na kupata ‘Daraja B+’, kisha alisoma katika Chuo cha Ubunifu cha Beckmans jijini Stockholm.


Kisha Andreas alimnunulia lile jumba la kifahari la ghorofa tatu eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam na jumba jingine la vyumba vinne katika mji wa Göteborg, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sweden. Hakuishia hapo, alimsaidia kuanzisha duka kubwa la vipodozi na nguo za kike jijini Dar es Salaam.


Baada ya uhusiano wao uliodumu miaka kadhaa waliachana, Madame Norah akajiongeza na kuanzisha kampuni aliyoiita Nuru Group iliyokuwa mkusanyiko wa kampuni za vipodozi ya Madame Norah Cosmetics & Fashion; pamoja na kampuni ya Nuru Media iliyomiliki vituo vya Nuru FM na Nuru TV.


Miaka michache baadaye alifungua kampuni ya samani za nyumbani na ofisini aliyoiita Madame Norah Furniture Centre na mgahawa wa kisasa wa Nuru Foods Café (NFC) katikati ya jiji la Dar es Salaam…


Pamoja na mafanikio hayo bado hakuishi maisha ya furaha, alikuwa mtu mwenye maisha ya huzuni muda mwingi japo alijitahidi kuonekana mwenye furaha mbele ya watu. Tatizo nini? Kwanza suala la mtoto wake aliyembwaga kwa Rafael kule Ngamiani Tanga lilimsumbua sana.


Kwa umri wake asingeweza kupata mtoto mwingine kwani alikwisha toa mimba takriban nne na daktari wa mwisho alimtoa kizazi chake. Hakuwa akijua kama mtoto aliyembwaga nyumbani kwa Rafael kule Ngamiani alikuwa mzima au hata yeye alikufa kwa moto.


Alikuwa amekwenda Tanga kumtafuta Rafael baada ya kutoka Ulaya lakini taarifa alizozipata kule zilimchanganya sana, ile nyumba aliyoishi Rafael katika makutano ya barabara ya 10 na Mnyanjiani haikuwepo tena na badala yake ilijengwa nyumba nyingine mpya.


Alipouliza aliambiwa iliteketea kwa moto baada ya kutokea hitilafu ya umeme na kuua watu wanne waliokuwa wamelala ndani akiwemo mtoto mdogo. Hakuna aliyekuwa na kumbukumbu ya majina ya waliokufa! Bahati mbaya Madame Norah hakuwahi kumuuliza Rafael alitokea wapi, huenda angelikwenda kwao kupata uhakika…


Mara mlango wa ofisi yake ukagongwa na kumzundua Madame Norah kutoka kwenye lindi la mawazo. Alifungua mikono yake iliyokumbatia picha zake za usichana kifuani na kufuta haraka machozi yaliyomchuruzika kwenye mashavu yake, kisha alitoa leso na kupenga kamasi huku akizificha zile picha kwenye droo na kujiweka sawa.


Muda ule aliisikia vyema sauti ya mtoto ikilia kwa uchungu masikioni mwake na kuacha mwangwi moyoni na kwenye ubongo wake. Mlango ukagongwa kwa mara ya pili.


“Pita!” Madame Norah alisema kwa sauti tulivu huku akijiweka sawa kwenye kiti chake.


Mlango ulifunguliwa na msaidizi wake Jessica alichungulia na kumwona kisha akaingia ndani. Kwanza alisita, akasimama akimwangalia Madame Norah kwa udadisi na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Lakini hakuuliza.


“Unasemaje Jessica?” Madame Norah aliuliza huku akijaribu kuifanya sauti yake isikike ya kawaida.


“Madame, yule dada wa ile demo ya kipindi cha fashion amekuja,” Jessica alisema huku akiwa bado anamtazama Madame Norah kwa udadisi.


“Okay, mpeleke ukumbini anisubiri nakuja.”


Jessica alitoka, akaufunga mlango nyuma yake na kumwacha Madame Norah peke yake akiendelea kutafakari.


Jessica alikwenda moja kwa moja kwenye ukumbi kulikokuwa na wabunifu wa mavazi, alimkuta Joyce akiwa amesimama akiwatazama kwa makini wabunifu wa mavazi wakati wakikamilisha kazi zao za siku ile.


Alimchukua hadi kwenye makochi ya sofa na kumwonesha sehemu ya kuketi ili amsubiri Madame Norah. Wakati akiketi mara akamuona Madame Norah akija kwa mwendo wa madaha, akasimama na kumlaki, wakasalimiana na kuketi kwa mazungumzo.


Muda wote Joyce alikuwa anazungusha macho yake kustaajabu mandhari ya kupendeza ya eneo la ukumbi wa kisasa wa lile jumba la kifahari la Madame Norah.


Madame Norah alimtazama kwa tabasamu, hata hivyo, bado alihisi huzuni ndani ya moyo wake ikishindwa kwenda likizo japo kwa muda. Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na wakati huo huo Joyce aligeuza shingo yake kumtazama. Wakatazamana na kujikuta wakitabasamu.


Kwa mara ya kwanza, Madame Norah alihisi faraja kwa mbali moyoni mwake na huzuni ikipotea taratibu baada ya kuliona tabasamu la Joyce. Muda huo huo Florian alitokea na kumsalimia Joyce kisha aliketi ubavuni kwa Madame Norah, akaupitisha mkono wake nyuma juu ya bega la Madame Norah na kujiegemeza kwenye kochi.


Madame Norah alimtazama Florian kwa tabasamu na kunong’ona jambo kwenye sikio lake, Florian alimtupia jicho Joyce na kuinuka, akaondoka akiwaacha. Madame Norah alimtazama Joyce na kuachia tabasamu. Kisha kilifuata kitambo fulani cha ukimya.


“Unajua kwa nini nimekuita? Nilipoiona demo ya kipindi chako ilinishtua sana… Ilinikumbusha kitu fulani cha miaka mingi iliyopita!” Madame Norah alianza kusema na kuvunja ukimya.


“Baada ya hapo nikaanza kutafuta taarifa zako ili nikufahamu vizuri, niseme tu nimeipenda sana creativity yako na juhudi unazozionesha katika kutimiza ndoto zako. Keep it up, my dear.”


Endelea kufuatilia stori hii ya kusisimua ili kuujua mwisho wake. Ujue kwa nini tunaifuatilia taxi, ni ya nani na ina nini hiyo taxi?...




Madame Norah alimtazama Florian kwa tabasamu na kunong’ona jambo kwenye sikio lake, Florian alimtupia jicho Joyce na kuinuka, akaondoka akiwaacha. Madame Norah alimtazama Joyce na kuachia tabasamu. Kisha kilifuata kitambo fulani cha ukimya.


“Unajua kwa nini nimekuita? Nilipoiona demo ya kipindi chako ilinishtua sana… Ilinikumbusha kitu fulani cha miaka mingi iliyopita!” Madame Norah alianza kusema na kuvunja ukimya.


“Baada ya hapo nikaanza kutafuta taarifa zako ili nikufahamu vizuri, niseme tu nimeipenda sana creativity yako na juhudi unazozionesha katika kutimiza ndoto zako. Keep it up, my dear.”


Sasa endelea...


“Thank you, Madame,” Joyce alisema huku akiachia tabasamu, alihisi fahari kubwa kupewa sifa na mtu kama Madame Norah.


“Creative thinking kama yako ni muhimu sana katika kutimiza ndoto ya mtu, na tofauti kubwa kati ya mtu aliyefanikiwa na wengine ni moja tu, kuthubutu…” Madame Norah alisema na kunyamaza kidogo, alimtazama Joyce kwa kitambo kirefu kisha akaangalia kando. Huzuni ilianza kujionesha tena usoni kwake.


Joyce hakuelewa kilichokuwa kikiendelea akilini kwa Madame Norah, alibaki kimya akisubiri kusikia zaidi kutoka kwa mtu aliyemhusudu na kutamani kufuata nyayo zake.


“Kuthubutu…” Madame Norah alirudia tena neno lile la mwisho, kisha akaongeza, “Lakini huwezi kupata uthubutu kama bado unategemea kupangiwa kila kitu na mwanamume. Mimi nimefika hapa baada ya kutambua kuwa ili niendelee ninapaswa kuwa bosi wa maisha yangu mwenyewe.”


Joyce alishtuka sana, akainamisha kichwa chake. Aliona kuwa Madame Norah alikuwa anampa mtihani mkubwa sana. Hata hivyo, Madame Norah alikuwa ameyasoma mawazo yake, akaachia tabasamu.


“Samahani kwa kukwambia haya, wewe ni sawa na binti yangu… ni kwamba huko nyuma nimewahi kutendwa na mwanamume niliyempenda kuliko chochote, aliniharibia maisha yangu na baadaye akanifukuza kama mbwa nyumbani kwake, wakati huo nilikuwa binti mdogo tu, na kilichofuata baada ya hapo sipendi hata kukikumbuka…” Madame Norah alisita kidogo na kufuta machozi yaliyoanza kumtoka.


Joyce alihisi kuingiwa huzuni lakini hakuweza kusema lolote, alibaki kimya akimtumbulia macho.


“Kisha nikawa na uhusiano na wanaume kadhaa lakini wao pia walitaka kunitumia tu. Ninashukuru mmoja wao ndiye alinisaidia kufika hapa nilipo, lakini kwa sasa sitaki mume, sitaki kuwa chini ya mwanaume. Huyu kijana niliyenaye sasa ni kwa ajili ya kujifurahisha tu na siyo kwa ajili ya mapenzi. Ninao uwezo kama wanaume, ninatoa amri na wao wanatekeleza, hivyo sina haja ya mwanamume atakayeniweka chini ya amri zake. Ninaamini katika falsafa ya kuwa: utafanikiwa tu endapo wewe ndiye bosi wa maisha yako!” Madame Norah alisistiza na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.


“Ila kwa wewe uliyeolewa sikushauri umwache mumeo kama hakuzuii kutimiza ndoto yako na usianze kujiona uko juu yake… I know you have an amazing husband and a very strong marriage,” (Najua una mume makini na ndoa imara) Madame Norah alisema na kuachia kicheko hafifu.


Joyce aliachia tabasamu na kuangalia kando akiyakwepa macho ya Madame Norah.


“Unachotakiwa ni kumfanya akuamini na kukusaidia kufikia ndoto yako, kama kweli anakupenda,” Madame Norah alisema na mara akaonekana kukumbuka jambo. Alimwita Jessica.


“Nisamehe sana, binti yangu, nimesahau hata kukuuliza utatumia kinywaji gani?” Madame Norah alimuuliza Joyce kwa upole baada ya Jessica kufika.


Joyce alimtazama Jessica kwa makini huku akizungusha macho yake kujaribu kufikiria, alivuta pumzi za ndani kwa ndani na kuminya midomo yake. “Mm… nitakunywa chochote,” hatimaye aliongea baada ya kufikiria kidogo.


“Tuna chai, kahawa, soda, juisi za boksi, bia za kopo, mvinyo mweupe na mwekundu… sijui ungependa nini?” Madame Norah aliuliza tena kwa sauti tulivu huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Joyce.


“Naomba juisi ya boksi… kama ipo tropical nitafurahi zaidi,” Joyce hakutaka kujivunga, alisema bila wasiwasi wowote.


“Okay, chukua funguo uende ofisi kwangu, chukua tropical juice kwenye jokofu langu, na mimi niletee chupa yangu ya mvinyo wa Navette de Marseille, ipo juu ya meza yangu,” Madame Norah alimwambia Jessica huku akimkabidhi funguo za ofisi yake.


Jessica alipokea kisha aligeuka na kuondoka haraka kutoka eneo lile, akaelekea kwenye ngazi za kuelekea juu. Madame Norah alishusha pumzi huku akimtupia jicho Joyce na kuachia tabasamu.


“Kwa kweli sijui kwa nini ninasukumwa sana kutaka kukusaidia ili uweze kutimiza ndoto yako, nimefikiria hata kukutafutia personal assistant ambaye nitamlipa…”


“Asante sana, mama… sijui nikushukuru vipi!” Joyce alisema huku akiinamisha kichwa chake mbele kwa heshima zote na kuikunjia mikono yake kifuani kuonesha shukrani za kipekee.


“Usijali… usijali, hata hivyo nina ushauri mdogo kwako, kama kweli unataka kufanikiwa basi simamia ndoto yako bila kujali nani atasema nini juu yako, na usikubali kukatishwa tamaa! Hii imekuwa siri kubwa ya mafanikio yangu,” Madame Norah alisema kwa sauti tulivu ya upole.


Muda ule ule Jessica alifika akiwa amebeba chano chenye vinywaji na bilauri, akakiweka juu ya meza ndogo iliyokuwa mbele yao kisha aliwakaribisha. Joyce aliitazama saa yake ya mkononi na kushtuka sana, ilikuwa imeshatimu saa mbili za usiku.


Mara simu yake ikaanza kuita, aliitazama kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani. Uso wake ulikuwa umesawajika kidogo kwani ilikuwa ni simu kutoka kwa mumewe Sammy na hakujua angemjibu nini.


Madame Norah alimtazama kwa makini, alijua kwa vyovyote vile, kuna jambo lilimsumbua.


“Ni mumeo huyo, bila shaka!” Madame Norah aliongea kwa sauti tulivu huku macho yake yakiweka kituo kwenye uso wa Joyce. Joyce alibetua kichwa chake kukubali na hapo Madame Norah alimuashiria apokee simu.


“Ooh… mjibu kuwa upo njiani ili usije ukamkwaza, ngoja nikuwahishe mara moja na gari yangu,” Madame Norah alimwambia Joyce huku akiinuka.


Joyce alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kubofya kitufe cha kupokelea, akaiweka simu kwenye sikio.




“Nipo njiani nakuja!” Joyce alisema na kusikiliza kidogo huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani, “Haya!” alisema na kukata simu kisha aliinuka na kuchukua boksi lake la juisi. Wakatoka kuelekea kwenye gari la kifahari la Madame Norah.


* * * * *


Zilikuwa zimekwisha pita wiki mbili tangu Sammy aliposimamishwa kazi katika hoteli ya kitalii ya Udzungwa Beach Resort, kipindi chote hicho hakuwa amemweleza mkewe, kila siku alidamka alfajiri na kufanya mazoezi kama ilivyokuwa kawaida yake, kisha akajitayarisha na kuondoka kwenda Ilala Sharif Shamba kwa rafiki yake Elli.


Hata hivyo, katika kipindi kile cha wiki mbili alikwisha fika Udzungwa Beach Resort mara tatu kwa ajili ya kufuatilia stahiki zake.


Siku ya kwanza alimkuta Dk. Masanja aliyemtaka arudi kazini mara moja lakini alikataa akibainisha kuwa hakutaka tena kuajiriwa bali alitaka alipwe stahiki zake ili afanye shughuli zake. Dk. Masanja hakuwa na namna nyingine ila kutoa maagizo kwa mhasibu kuandaa hesabu na kumtaka Sammy arejee siku iliyofuata saa nne asubuhi.


Siku iliyofuata Sammy alifika ofisini kwa Dk. Masanja saa nne asubuhi kama walivyokubaliana lakini alisita baada ya kumkuta Mr. Oduya ndani ya ile ofisi akimsubiri. Dk. Masanja alimtoa wasiwasi Sammy kuwa Mr. Oduya hakuja kwa ubaya na kumtaka aketi kwenye moja ya viti vilivyokuwa ofisini.


Sammy aliketi lakini akiwa bado ana mashaka. Muda wote tangu alipoingia mle ofisini Mr. Oduya alikuwa yupo makini akimtumbulia macho kupitia juu ya miwani yake aliyoivaa kwa kuilegeza.


Pamoja na kuwa na wasiwasi lakini bado Sammy aliwasalimia kwa adabu kisha Dk. Masanja alimweleza kuwa ameshawasiliana na mhasibu na kila kitu kilikuwa kinakwenda vizuri, pia alimweleza kuwa Mr. Oduya alifika pale akitaka wazungumze.


“Kabla hatujaendelea mbele, vipi maisha yanakwendaje?” Mr. Oduya alimuuliza Sammy huku akitabasamu, macho yake yalikuwa yameweka kituo usoni kwa Sammy.


“Maisha yanakwenda vizuri sana,” Sammy alijibu kwa kujiamini huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.


“Vizuri… nimesikia kuwa hutaki tena kurudi kazini, kwa nini hutaki kazi?” Mr. Oduya aliuliza tena huku akiendelea kumkazia macho Sammy.


“Kwa sababu sitaki kuendelea kuwatumikia watu wasio na shukurani, ninaowaingizia fedha nyingi ili wanilipe mshahara, sasa ninataka kuwa bosi wa maisha yangu mwenyewe…” Sammy alisema kwa sauti tulivu huku akijitahidi kuizuia hasira iliyoanza kuchipua ndani yake.


“Mr. Kambona, naomba nisikilize kijana wangu, najua wewe bado kijana na una ndoto nyingi, ungependa kuwa na maisha mazuri zaidi, umiliki kampuni yako mwenyewe, watoto wako wasome kwenye shule bora zaidi na pengine nje ya nchi, utembelee magari ya kifahari na mambo mengine kadha wa kadha… nimekuja hapa lengo langu ni kutaka kukusaidia kutimiza ndoto zako…” Mr. Oduya alisema na kunyamaza kidogo, akameza mate kutowesha koo lake.


“Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikipata sifa zako kuwa wewe ni mwanamkakati mzuri sana wa kiufundi na matukio ndiyo maana umeipaisha sana hoteli hii na kupata tuzo nyingi… lazima niwe mkweli, unastahili makubwa zaidi, ndiyo maana niliposikia hutaki tena kazi nikataka uwe mshirika wangu kwenye masuala yangu ya…”


“Hilo haliwezekani, Mr. Oduya. Siwezi kuwa na ushirika na wewe,” Sammy alimkatiza Mr. Oduya huku akitingisha kichwa chake taratibu.


“Kama hilo haliwezekani then you’ll never make it,” Mr. Oduya alimwambia Sammy huku akitabasamu kwa dharau.


“Now you’re threatening me, Mr. Oduya,” (Kwa hiyo sasa unanitishia, Mr. Oduya) Sammy alimwuliza Mr. Oduya huku akihisi damu mwilini mwake ikichemka na kwenda kasi kwenye mishipa yake ya damu.


“This is not a threat, young man, this is a warning…” (Hiki siyo kitisho, kijana, hili ni onyo) Mr. Oduya alisema kwa sauti tulivu huku akiendelea kutabasamu kwa dharau.


“Kama hutataka kushirikiana nami basi hutaweza kufanikiwa kwenye mambo yako, ninaweza kuyafanya maisha yako kuwa magumu zaidi,” Mr. Oduya aliongeza.


“Tafadhali, mzee, usijaribu tena kunitisha…” Sammy alisema kwa hasira na kusimama, sura yake ilikwisha badilika na sasa alikuwa ameikunja na kutengeneza matuta madogo madogo usoni.


“Calm down, Mr. Kambona. Lengo la Mr. Oduya ni zuri sana ni kwa vile hujamwelewa tu,” Dk. Masanja aliingilia kati kumtuliza Sammy.


Sammy hakutaka kuketi, huku akionesha kujiamini aligeuka na kuanza kupiga hatua kutoka nje. Mr. Oduya alibaki akimtumbulia macho, wakati Sammy akijongea mlangoni na kutoka.


Sammy alipotoka alipita kwa katibu muhtasi wa Dk. Masanja, mwanadada Salha Hamisi. Alimuaga kwa upendo pasipo kuonesha kama alikuwa amekerwa kule ndani, kisha akatoka na kuanza kuelekea nje ya jengo lile. Alipokuwa akipita eneo la mapokezi kuelekea kwenye lango kubwa ili atoke nje akamuona Salha akimjia mbio mbio huku akimwita.


“Unasemaje Salha?” Sammy alimuuliza Salha huku akigeuka kumsubiri.


“Bosi Masanja anakuita,” Salha alisema huku akihema kwa nguvu kutokana na kukimbia.


“Bosi wako anataka nini tena kwangu?” Sammy aliuliza huku akikunja sura yake.


“Sijui, wewe nenda kamsikilize, amesisitiza sana uende,” Salha alisema huku akimtazama Sammy kwa makini.


Sammy alifikiri kidogo, akawa kama anajishauri kisha akakata shauri kutorudi tena kwenye ofisi ya Dk. Masanja siku ile.


“Mwambie nitarudi siku nyingine, kwa sasa kuna sehemu natakiwa nifike kabla ya saa sita mchana,” Sammy alimwambia Salha na kuanza kupiga hatua za haraka kuondoka eneo lile huku akimwacha Salha anashangaa.





Sammy alipotoka pale alielekea moja kwa moja kwenye mgahawa wa Elli’s, Ilala Sharif Shamba. Lakini hakumsimulia Elli wala yeyote kuhusu kilichokuwa kinaendelea kati yake na Mr. Oduya.


Baada ya siku mbili alirudi tena Udzungwa Beach Resort na kwenda ofisini kwa mhasibu wa kampuni kufuatilia suala la kulipwa stahiki zake. Haikuchukua siku nyingi akawa amepewa hundi, sasa akawa anatarajiwa kupata fedha ambazo zingemwezesha kukamilisha ndoto yake…


Siku ya Jumamosi na Sammy alikuwa nyumbani, hakujisikia kwenda popote, alihitaji kutulia na kupanga mambo yake vizuri kuhusu hatua ambayo ingefuata baada ya kukabidhiwa hundi yake siku mbili zilizokuwa zimeitangulia siku ile.


Pia siku ile alihitaji nafasi ya kumweleza mkewe kwa utulivu kuhusu matatizo yaliyojitokeza kazini kwake na mipango yake ya baadaye kisha angempa nafasi aongee ili asikie mawazo yake, huu ulikuwa ushauri alioutoa kwa Elli aliyemweleza kuwa, ‘kuambiana ukweli ni muhimu katika kuijenga familia’.


Siku ile alikuwa ameamka alfajiri kama ilivyokuwa kawaida yake akafanya mazoezi, kisha aliingia maliwatoni na kujiweka sawa, akarudi kitandani kulala. Alihisi uchovu hivyo uamuzi wake ulikuwa ni kulala tu hadi pale ambapo angehisi kuchangamka.


Ilipotimu saa tatu na nusu, akiwa bado yupo kitandani alishtuliwa na mlio wa ujumbe mfupi kwenye simu yake ya mkononi. Alinyoosha mkono wake kuichukua na kufungua sehemu ya ujumbe mfupi. Ulikuwa unatoka kwa Elli: “Njoo hapa Ilala twende Kinondoni, kuna gari zuri sana limepatikana…”


Sammy aliachia tabasamu pana huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani. Aliinuka na kuingia maliwato, akashevu ndevu zake vizuri kwa mashine maalumu ya kunyolea ndevu huku akikinga mkono wake kwenye bomba la maji na kunawa uso wake huku akijifuta kidevu chake vizuri kwa maji, alipomaliza alijitazama kwenye kioo.


Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kupapasa kindevu chake akionekana kuridhika, akabetua kichwa chake na kutoka chumbani, alielekea sebuleni alipomkuta mkewe ameketi, akamuaga kuwa alikuwa amepata ujumbe mfupi uliomtaka afike kazini mara moja, kwani kulikuwa na kazi ya dharura. Akatoka na kuelekea kituo cha daladala.


* * * * *


Saa nne ya asubuhi ilimkuta Zainab akiwa amejiegemeza ukutani chumbani kwake, alikuwa kitandani karibu kabisa na dirisha akiangalia nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha, alikuwa akitazama mandhari nzuri ya kupendeza ya Paradise Club.


Alikuwa akiangalia kwenye lile eneo la maegesho ya magari akitaraji kumuona Mr. Oduya wakati akiingia. Hakuwa na raha kiasi fulani ingawa alionekana kujilazimisha. Kitu alichokuwa amekishuhudia asubuhi ile kilikuwa kimekataa kabisa kumtoka akilini mwake.


Hii ilikuwa ni baada ya kustafustahi na kuwasha runinga kisha aliweka chaneli ya taifa na kutazama taarifa ya habari, nia yake ilikuwa kujua kilichojiri duniani, hasa kwa kuwa tangu afike nchini alikuwa akishinda ndani na hakuruhusiwa kabisa kutoka nje.


Hakuwa na shida ya kutoka nje kwani kila alichokitaka basi Lilian alikuwepo kumhudumia. Alikuwa kama malkia aliyekuwa akipewa huduma zote za kimalkia ndani ya jumba la kifalme. Akikohoa tu Lilian huyu hapa kumsikiliza!


Taarifa ya habari ya asubuhi ile ilipofikia ukomo wake alitazama kipindi cha mapitio ya magazeti, kisha aliamua kubadilisha chaneli na kuweka ya burudani iliyorushwa na Nuru TV. Hapo ndipo alipokutana na kitu kilichoufanya moyo wake kumpasuka paa!


Akili yake ilianza kupoteza utulivu huku mitupo ya mapigo ya moyo wake ikiongezeka kasi! Alitaka kupuuza kile alichokuwa akikiona akidhani labda alikuwa ndotoni, hata hivyo, milango yake ya fahamu ilikuwa makini zaidi, na aliishirikisha akili yake kikamilifu katika kumletea taarifa za kuaminika.


Akajiambia kuwa wala haikuwa ndoto bali ni kitu halisi. Hali ile ikasababisha jasho jepesi lianze kumtoka mwilini huku mwili wake ukipigwa ganzi.


“Oh my God!” Zainab alimaka kwa mshtuko huku akiikodolea ile runinga, hakuamini kabisa alichokiona. Alivuta pumzi ndefu ndani kisha alizishusha taratibu huku akiulegeza mwili wake na kujiegemeza pale kwenye sofa. Hata hivyo, alihisi kulikuwa na mtu aliyekuwa akimwangalia, akageuza shingo yake na kumuona Lilian aliyekuwa anapita kuelekea jikoni na kugundua kuwa alikuwa akimtazama kwa jicho la wizi.


“Vipi dada, kuna shida yoyote?” Lilian alimuuliza Zainab baada ya macho yao kugongana.


“Hapana, nimevutiwa sana na huyo mama anayeongea kwenye hiyo chaneli ya burudani,” Zainab alijibu huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.


“Aah, huyo ni mwanamama anayejituma kweli kweli! Wengi wanamsifia kwani amekuwa mfano bora kwa wanawake wengi… ana mafanikio makubwa sana. Hiyo Nuru TV ni ya kwake, pia anamiliki kituo cha redio cha Nuru FM, mgahawa wa kisasa wa Nuru Foods Café na kampuni kubwa la vipodozi na nguo za Kike la Madame Norah Cosmetics & Fashion na mali zingine kibao,” Lilian alisema na kumfanya Zainab asisimkwe zaidi.


“Kwani ni Mtanzania na anaishi hapa hapa Tanzania?” Zainab aliuliza huku akishindwa kuficha mshtuko wake, alionekana kushangaa sana na muda wote macho yake yalikuwa yameweka kituo kwenye ile runinga.


“Ndiyo, ni Mtanzania ‘piwa’ na anaishi hapa hapa jijini Dar es Salaam, asili yake ni kutoka Mkoa wa Tanga…”


“Anaitwa nani?” Zainab alimtupia Lilian swali jingine huku akionekana kuwa na shauku.


“Anajulikana zaidi kwa jina la Madame Norah…”


“Madame Norah!” Zainab alidakia akiwa haamini alichokisikia.


“Ndiyo, Madame Norah. Ni mwanamke aliyejitosheleza hasa, anamiliki pia majumba ya kifahari eneo la Mikocheni alikoweka makao makuu ya ofisi za Nuru Group na eneo la Makumbusho kwenye vituo vyake vya redio na televisheni. Wanasema kuwa pia ana majumba Ulaya…” Lilian alisema maneno yaliyozidi kumchanganya Zainab na kujikuta akiishiwa nguvu.




“Anaitwa Madame Norah!” Zainab aliwaza na kumeza funda kubwa la mate kutowesha koo lake lililokauka ghafla, aliyakaza macho yake kutazama kwenye runinga. Alijiuliza: Je, ndiye yeye yule aliyekuwa akimtafuta miaka yote hii au alikuwa amemfananisha? Na kwa nini atumie jina la Nuru kila mahali? Hapana huyo ndiye yeye!


Aliwaza, asingeweza kukosea na wala macho yake yasingeweza kumdanganya. Ila lile jina la Madame Norah ndilo lililomchanganya kidogo, ni tafauti na lile alilokuwa akilifahamu. Hata hivyo, watu hubadili majina yako, huenda hata yeye alilazimika kubadilisha jina!


“Mbona hata mimi nimebadili jina langu, badala ya Zainab Semaya sasa naitwa Suzanne Ross!” Zainab aliwaza na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.


“Nimewahi kusikia habari za Madame Norah mara kadhaa kila nilipofuatilia habari za Tanzania wakati nikiwa Canada, ila sikujua kama mwenye jina hilo ndiye huyu ninayemshuhudia muda huu kwenye runinga!” Zainab alizidi kuwaza, uso wake ulizidi kupambwa na mshangao mkubwa.


Kwa kweli ile habari aliyokuwa ameisikia kutoka kwa Lilian ilikuwa imemsisimua sana, hata hivyo, akili yake ilikuwa bado ikisumbuka katika namna ya kutaka kufahamu mengi yaliyomhusu Madame Norah.


Alimtazama kwa makini Madame Norah pale kwenye runinga, alikuwa mrefu na mweupe mwenye umbo la kupendeza, alikuwa amevaa blauzi ya bluu ya mikono mirefu, suruali ya Jamsuit ya rangi nyekundu iliyolichora vyema umbo lake refu maridadi lenye kiuno chembamba lakini imara kikiwa kimebeba minofu ya mapaja iliyokaza.


Madame Norah alikuwa akiongea na waandishi wa habari kutambulisha shughuli zake. Zainab alichukua rimoti ya runinga iliyokuwa juu ya mkono wa lile sofa alilokalia na kuongeza sauti.


“…mwaka huu tutayatumia maonesho haya kuandaa pia chakula cha hisani na kuwakaribisha watu mbalimbali mashuhuri, taasisi za serikali, mashirika na watu binafsi ambao watachangia fedha. Na hata tusipofikia lengo la kiasi kilichokusudiwa hatutaacha kujenga… kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Simamia ndoto yako usijali wengine wanasema nini’.”


Zainab alishusha pumzi huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Madame Norah wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari huku tabasamu bashasha likiwa halimtoki usoni kwake. Zainab alikuwa na uhakika kuwa huyo ndiye na wala hakuwa amemfananisha.


Sasa alifikiria kuahirisha safari yake ya kurudi nchini Canada ili kuweka kwanza mambo sawa, aliamua kumsubiri Mr. Oduya ambaye alikuwa amemtuma mtu kwenda ofisi za shirika la ndege la Uholanzi la KLM kufanya mpango wa safari.


Ndipo Zainab alipoinuka na kuelekea chumbani kwake, akaketi kitandani. Akili yake ilizidi kusumbuka: huyu Madame Norah alikuwa wapi miaka yote hiyo na aliwezaje kufikia mafanikio makubwa kiasi kile, kama alivyosikia kutoka kwa Lilian?


Sasa kichwa chake kilianza kulemewa na mawazo, alikuwa akijiuliza maswali yaliyokosa majibu, kwani mwenye majibu alikuwa ni Madame Norah mwenyewe. Muda huo Zainab alikuwa ameketi jirani na dirisha akiyatazama magari yote yaliyoingia na kutoka katika eneo lile la Paradise Club akitaraji kumwona Mr. Oduya ili amsaidie kumpata Madame Norah.


“Enhee! Afadhali amefika,” Zainab alijiambia huku akiliangalia gari la Mr. Oduya aina ya Range Rover Velar la rangi nyeupe lilipokuwa likiegeshwa eneo maalumu la maegesho la Paradise Club, kisha akamwona Mr. Oduya akishuka na kushika mkoba wake wa kiofisi, akaanza kutembea kwa haraka kuelekea kule ndani huku akimwacha dereva wake ndani ya gari akisubiri.


Zainab alijiandaa kumkabili, baada ya dakika chache mlango wa chumbani kwake uligongwa, akakimbilia kuufungua.


“Waoo! Pole sana mpenzi wangu, pole na kazi,” Zainab alimwambia Mr. Oduya huku akimpokea ule mkoba na kuupeleka moja kwa moja mezani.


“Asante sana, mpenzi, mbona unashinda chumbani muda wote?” Mr. Oduya aliuliza huku akishusha pumzi. Alikaa kitandani.


“Nimeingia muda si mrefu,” Zainab alisema, na kama kawaida yake, alimvua koti Mr. Oduya na kufungua tai yake na kumfungua shati lake vifungo kisha akamvua viatu na soksi.


“Nimefanikiwa kila kitu nilichokuwa nakifuatilia…” Mr. Oduya alisema baada ya Zainab kumaliza kazi yake na kuketi kando yake huku akimtazama kwa makini.


Zainab alishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akaitupia jicho saa yake ya mkononi. Saa nne na dakika arobaini. Alimtazama Mr. Oduya kwa kitambo kirefu, uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote.


“Vipi mpenzi, kuna tatizo lolote, naona kama hufurahii hiki kinachokueleza!” Mr. Oduya alimuuliza Zainab baada ya kuuona uso wake ukiwa hauna tashwishwi na yeye yupo kimya bila kuchangamka kama ilivyokuwa kawaida yake pindi walipokuwa pamoja.


“Nimeamua kuahirisha safari yangu…” Zainab alisema kwa sauti ya chini iliyobeba huzuni.


“What?” Mr. Oduya alimaka kwa mshangao mkubwa huku akimtazama Zainab kwa makini.


“Siwezi kuondoka tena hadi nionane na mtu mmoja muhimu sana,” Zainab alisema huku akiyatuliza macho yake kwenye uso wa Mr. Oduya. Alionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema.


“Ni mtu gani muhimu kuliko mimi? Mbona sielewi umepatwa na nini, mpenzi wangu?” Mr. Oduya aliuliza, uso wake ulikuwa bado una mshangao.


“Nimemuona dada yangu mkubwa, unakumbuka niliwahi kukueleza kuhusu familia yangu na jinsi dada yetu mkubwa alivyotoroka baada ya kupata ujauzito wakati nikiwa nina miaka sita…”


“Ndiyo nakumbuka.”


“Leo nimemuona… I need to see her,” Zainab alisisitiza.


“Umemuona wapi? Naona sasa unatafuta matatizo na ikigundulika kuwa upo nchini huoni kama itatuletea sote matatizo!” Mr. Oduya aliongea huku uso wake ukionesha mashaka.


“Wala hakutakuwa na tatizo lolote. Nimemuona kwenye televisheni, ninachokuomba mume wangu, fanya vyovyote uwezavyo unikutanishe naye, hata kwa kumleta hapa, nahitaji sana kuongea naye.”


“Sasa nitampata wapi, na anaitwa nani?”


“Madame Norah…”


“What?” Mr. Oduya alishtuka sana, akamkazia macho Zainab kwa mshangao. “Is Madame Norah your elder sister?” (Madame Norah ni dada yako mkubwa?)


“Yes, she’s my sister, blood sister,” (Ndiyo, ni dada’angu wa damu) Zainab alisema huku akilengwa na machozi.


Endelea kufuatilia stori hii ya kusisimua ili kuujua mwisho wake. Ujue kwa nini tunaifuatilia taxi, ni ya nani na ina nini hiyo taxi?... 



“Nimemuona dada yangu mkubwa, unakumbuka niliwahi kukueleza kuhusu familia yangu na jinsi dada yetu mkubwa alivyotoroka baada ya kupata ujauzito wakati nikiwa nina miaka sita…”


“Ndiyo nakumbuka.”


“Leo nimemuona… I need to see her,” Zainab alisisitiza.


“Umemuona wapi? Naona sasa unatafuta matatizo na ikigundulika kuwa upo nchini huoni kama itatuletea sote matatizo!” Mr. Oduya aliongea huku uso wake ukionesha mashaka.


“Wala hakutakuwa na tatizo lolote. Nimemuona kwenye televisheni, ninachokuomba mume wangu, fanya vyovyote uwezavyo unikutanishe naye, hata kwa kumleta hapa, nahitaji sana kuongea naye.”


“Sasa nitampata wapi, na anaitwa nani?”


“Madame Norah…”


“What?” Mr. Oduya alishtuka sana, akamkazia macho Zainab kwa mshangao. “Is Madame Norah your elder sister?” (Madame Norah ni dada yako mkubwa?)


“Yes, she’s my sister, blood sister,” (Ndiyo, ni dada’angu wa damu) Zainab alisema huku akilengwa na machozi.


Sasa endelea...


“Oh my God!” (Mungu wangu!) Mr. Oduya alisema huku akiwa haamini alichokisikia. Alimtumbulia macho Zainab kwa muda, akajikuta akiachia mdomo wake wazi kwa mshangao zaidi. “Ni kweli mnafanana, tena mnafanana sana!” alisema huku akiachia mluzi mdogo wa mshangao.


Kisha kilipita kitambo kirefu cha ukimya, walibaki wakitazamana kila mmoja akimezwa na ulimwengu wa tafakuri kabla Mr. Oduya hajachukua simu yake ya mkononi na kutafuta namba za Adam Mafuru. Alipozipata alipiga na kusikiliza.


“Mr. Mafuru,” Mr. Oduya aliita mara tu alipogundua kuwa Mafuru alikuwa amepokea simu. Uso wake ulikuwa na mikunjo.


“Yes, Boss,” sauti ya Mafuru ilijibu kwa adabu.


“Naomba ufike hapa Paradise Club mara moja, kuna jambo muhimu sana unatakiwa kulifuatilia, it’s urgent please,” Mr. Oduya alisema huku uso wake uliondoa mikunjo, kisha ukaunda tabasamu pana.


“Okay, Boss,” Mafuru alijibu. Mr. Oduya akakata simu na kushusha pumzi za ndani kwa ndani, aligeuka kumtazama Zainab huku akiendelea kutabasamu.


“Don’t worry, my darling, kila kitu kitakwenda sawa,” Mr. Oduya alisema na kumfanya Zainab aruke kwa furaha na kumkumbatia.


“Thank you, darling, thank you very much,” (Ahsante mpenzi, ahsante sana) Zainab alisema huku akimporomoshea Mr. Oduya mabusu mfululizo.


* * * * *


Saa nne na dakika arobaini asubuhi, Elli na Sammy walikuwa wanatoka ndani ya mgahawa wa kisasa wa Elli’s uliopo Ilala Sharif Shamba na kuingia ndani ya gari la kifahari aina ya BMW X6 xDrive 50i la rangi nyeupe mali ya Elli, lililokuwa kwenye maegesho ya magari ya mgahawa ule.


Elli aliwasha gari na kuliondoa taratibu kutoka kwenye yale maegesho ya magari ya mgahawa wa Elli’s akazunguka na kuelekea kwenye geti kubwa la kutokea la jengo lile, akaliingiza barabarani huku akiendesha kwa umakini mkubwa. Ilikuwa safari ya kuelekea Kinondoni B.


Kutoka pale mgahawa wa Elli’s gari lilikata kona na kuingia upande wa kushoto likaifuata barabara ya Uhuru iliyokuwa na msongamano wa magari muda ule, hivyo Elli alilazimika kuendesha kwa mwendo mdogo.


Safari yao iliendelea huku wakiwa kimya, kila mmoja alikuwa akitafakari, walivuka eneo la Bungoni kisha wakayavuka majengo ya Kituo cha Amana Vijana, na mbele yake wakavuka vibanda vya wasusi wa Kimasai vilivyokuwa upande wao wa kushoto na kuingia upande huo huo wa kushoto wakiifuata barabara ya mtaa wa Mafao.


Kwa kuwa barabara ile haikuwa na msongamano Elli aliongeza mwendo akiyapita majengo ya ghorofa ya Shirika la Nyumba la Taifa eneo la Ilala na baada ya safari fupi hatimaye wakaja kukutana na barabara ya Kawawa.


Barabara ya Kawawa ilikuwa moja ya barabara kubwa na maarufu sana jijini Dar es Salaam iliyoanzia eneo la Veta Chang’ombe katika makutano ya barabara za Nyerere, Chang’ombe na Kawawa na kuishia katika eneo la Kinondoni Morocco kwenye makutano ya barabara za Ali Hassan Mwinyi, Mwai Kibaki, Bagamoyo na Kawawa.


Elli aliingia kushoto akaifuata barabara ile ya Kawawa kuelekea Magomeni. Muda wote Sammy alikuwa yupo kimya akiwaza mbali sana, muda wote macho yake yaliangalia nje wakati gari likipita eneo la Msimbazi Centre kisha likavuka eneo la Kigogo Sambusa na baadaye Kigogo Mbuyuni, kwenye mzunguko wa barabara za Kawawa na ile ya Kigogo.


Pilika pilika za wakazi wa jiji la Dar es Salaam zilikuwa zimeshamiri muda ule kwani eneo lile lilionekana kuwa na watu wengi, pikipiki na magari yaliyopishana kwenda sehemu mbalimbali zaa mji.


Walipovuka eneo la Kigogo Mbuyuni walianza kuteremsha bonde la Msimbazi kisha mbele kidogo Elli aliongeza mwendo ili kulipita lori la wazoa taka lililokuwa mbele yao. Kisha waliivuka barabara ya Mikumi upande wao wa kushoto huku wakipishana na magari mengi yaliyoingia katika barabara ile.


Baada ya safari fupi wakaanza kukivuka kituo cha daladala cha Magomeni Mikumi, Sammy akayatupa macho yake kutazama upande wake wa kulia, ng’ambo ya ile barabara ya Kawawa na kuiona yadi moja ya magari yaliyotumika, iliyokuwa na magari yasiyozidi ishirini yakiwa yameegeshwa kwenye uzio yakisubiri wanunuzi.


Sammy aliyatazama kwa makini yale magari na kuliona gari moja lenye muundo wa kizamani aina ya Cadillac DeVille jeupe. Moyo wake ukapiga paa! Aliendelea kulikodolea macho lile gari wakati Elli akivuka eneo lile kuelekea kwenye taa za kuongozea barabarani za Magomeni, kwenye makutano ya barabara za Kawawa na ile ya Morogoro.


“Stop the car,” Sammy alisema ghafla huku akilikodolea macho lile gari na kumshtua Elli aliyegeuza shingo yake kumtazama kwa mshangao.


“Nimesema simamisha gari!” Sammy alisema tena, safari hii kwa sauti ya juu kidogo.


“Nini!” Elli aliuliza huku akikanyaga breki kwa nguvu pasipo kufikiri, gari likajivuta na kusota kwenye ile barabara pana huku likiyumba, bahati nzuri gari halikutoka nje ya barabara.


Muda huo huo walisikia sauti ya breki kali kutoka nyuma yao, dereva wa daladala linalofanya safari zake kati ya Gongolamboto na Masaki lililokuwa nyuma yao alikuwa akihangaika kukanyaga breki ya ghafla na kufanya gari lile liserereke na kusimama kando ya barabara.


Kwa sekunde chache ilitokea taharuki ndani ya lile daladala, abiria walitaharuki sana. Daladala liliposimama walianza kutoa lugha kali ya matusi kwa Elli, wengine waliishia kusonya tu na mmoja wao aliinua juu kidole chake cha kati kuonesha hasira zake.




Elli hakuwajali, alilipeleka gari lake kando kabisa ya barabara kwenye barabara ndogo ya waenda kwa miguu na kuliegesha huku akimuomba msamaha dereva wa daladala aliyeonekana kuchukizwa na tukio lile. Eneo lile lilikuwa jirani kabisa na kituo cha mafuta cha Gapco.


Sammy aliteremka haraka na kuelekeza macho yake kuangalia kule kwenye yadi ya magari kulikokuwa na lile gari aina ya Cadillac DeVille, kisha alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kushika kiuno chake.


“Nimeiona gari ninayoitaka,” Sammy alimwambia Elli, bila kusubiri alianza kupiga hatua zake haraka kuelekea kule kwenye yadi ya magari, akavuka barabara ya Kawawa na kutokea upande wa pili wa barabara. Hapo hakuwaza kitu kingine chochote bali alichowaza ni jinsi ambavyo angemiliki lile gari. Elli alibaki kimya akimtazama Sammy kwa mashangao.


Elli aliwasha gari lake akaingia upande wa kile kituo cha mafuta na kulizungusha kisha akarudi tena barabara ya Kawawa na kukunja kuelekea upande wa kulia akimfuata Sammy. Alimkuta Sammy akiwa anaongea na kijana mmoja, mfanyakazi wa yadi ile ya magari.


Kabla hajajua wanaongea nini akamwona yule kijana akichukua funguo kisha akaanza kuondoka kumfuata Sammy ambaye tayari alikuwa amesimama akilitazama gari moja jeupe lenye muundo wa kizamani aina ya Cadillac DeVille. Elli alimfuata Sammy lakini kabla hajauliza chochote Sammy alimweleza kuwa alitaka kununua lile gari, Elli akashangaa sana!


Elli hakuwa na uhakika kama Sammy alikuwa ameushirikisha ubongo wake kabla hajafikia uamuzi wa kutaka kununua lile gari lenye muundo wa kizamani. Lakini Sammy alisisitiza kuwa alikuwa akilihitaji lile gari kwa sababu ya upekee wake.


“Kwanza ni gari lenye upekee, pili lina muundo wa kizamani na tatu ni zuri sana,” Sammy alisema na kuingia ndani ya lile gari.


“Na vipi kuhusu ubora wake? Usije ukanunua gari ukaliendesha mwezi mmoja tu kisha lianze kukuendesha wewe!” Elli aliuliza akiwa bado ana mashaka.


“Hili ni gari zima kabisa, ni kama jipya licha ya uzamani wake, kwa kuonesha hivyo tunampa garantii ya miezi sita, kama ataona lina matatizo ruksa kulirudisha,” alisema yule Mwarabu kwa kujiamini.


Sammy alitia ufunguo na kuwasha injini ya lile gari, gari likaunguruma bila shida yoyote. Sammy akapiga lesi huku akinesa nesa kwa mbwembwe na kuonekana kuridhika. Akaachia tabasamu.


* * * * *


Saa sita mchana Joyce alikuwa anawasili katika jumba la kifahari la Madame Norah lililozungukwa na ukuta mrefu wenye mfumo wa uhakika wa ulinzi na geti kubwa jeusi mbele yake. Jumba lile lilikuwa limejengwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi eneo la Mikocheni.


Toka kwa mbali uzuri wa jumba lile la ghorofa tatu ulionekana wazi, mandhari yake ilizungukwa na miti mirefu na mikubwa ya kivuli aina ya ‘Quercus virginiana’, kulikuwa na barabara ya lami yenye usafi wa hali ya juu iliyokuwa ikieleka katika jumba hilo na kupandwa miti ya kivuli iliyovutia na maua aina ya ‘lotus’.


Kulikuwa na ukimya mkubwa eneo hilo. Joyce alisimama nje ya lile geti kubwa jeusi kisha akabonyeza kitufe cha kengele na mara geti dogo kando ya lile geti kubwa jeusi likafunguliwa, mlinzi mmoja aliyekuwa wamevaa sare maalumu za kampuni binafsi ya ulinzi akachungulia na kumuona Joyce kisha akaachia tabasamu.


Alimsalimia kwa bashasha zote huku akimpisha aingie ndani. Hakumuuliza maswali yoyote kwa kuwa alimfahamu, kwani alikwishafika hapo mara mbili kabla ya siku ile na tayari walikuwa na taarifa kuwa angefika siku hiyo.


Joyce alipoingia ndani ya ule uzio walinzi wawili waliokuwa katika kibanda cha walinzi upande wa kulia wa lile geti walimsimamisha, mmoja wao alichukua kifaa maalumu cha kukagulia akamkagua kuona kama alikuwa na silaha yoyote na alipohakikisha kwamba hakuwa na silaha yoyote wakamruhusu aendelee na safari yake.


Joyce alipiga hatua zake taratibu kuelekea kwenye baraza kubwa ya mbele iliyokuwa na mlango mkubwa wa kuingilia ndani ya lile jumba, alikuwa akikatiza katikati ya bustani nzuri ya maua ya kupendeza aina ya ‘lotus’ na katikati ya bustani ile kulitengenezwa njia nzuri ya kutembea kwa miguu kwa vitofali vidogo vinavyovutia.


Kabla hajafika kwenye ile baraza kubwa ya mbele iliyokuwa imepangwa seti moja ya makochi meusi ya sofa alimuona Madame Norah akitoka ndani ya lile jumba akiwa ameongozana na msichana mmoja aliyekadiriwa kuwa na miaka kati ya ishirini na sita na ishirini na nane.


Alikuwa msichana mrefu na mrembo hasa, alikuwa na nywele nyingi nyeusi za kibantu zisizotiwa dawa, begani alitundika mkoba mzuri wa kike wa rangi ya pundamilia uliogharimu fedha nyingi.


Alikuwa amevaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu, blauzi nyekundu ya mikono mirefu na viatu vyekundu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio. Mkononi alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe.


Madame Norah alikuwa amemuona Joyce wakati akiingia, hivyo aliachia tabasamu na kumpokea kwa bashasha zote.


“Hello Joy, karibu sana, binti’angu. Habari za huko utokako?” Madame Norah alimsalimia Joyce kwa bashasha huku akimkumbatia na kumbusu kwenye shavu.


“Nzuri tu, mama. Shikamoo!” Joyce alisema huku akiachia tabasamu.


“Marhaba, pole na majukumu,” Madame Norah aliitikia huku akimwachia Joyce na kusimama akimtazama kwa makini. Macho yake yaliweka kituo usoni kwake.


“Ahsante sana mama, vipi na wewe unaendeleaje?”


“Sijambo kabisa, mumeo na wajukuu hawajambo?” Madame Norah aliendelea kumuuliza Joyce huku akijihisi faraja kubwa sana kila alipokutana naye. Alimchukulia kama binti yake wa kumzaa.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog