Search This Blog

Thursday, 23 March 2023

MATANGA YA ROHONI - 4

  

Simulizi : Matanga Ya Rohoni


Sehemu Ya : Nne (4)


Alikuwa anapiga miluzi huku kidole cha shahada cha mkono wa kulia kinauzungusha ufunguo kwa mbwembwe zote. Deborah akaanza kuja mpaka usawa wa ile gari, akawa ananyanyua mikono kama vile anaomba msaada fulani, huku kipochi chake cha mkononi anataka akitupe. Akaanza kuyumba kama mtu mwenye kisunzu au mlevi aliyezidiwa na pombe. "Naomba msaada wako najiskia vibaya sana, macho yanaishiwa nguvu, nifikishshshsh......!" Deborah alizungumza kwa shida kabla hata hajamaliza maelezo yake akataka aanguke chini.

Jamaa akamdaka hewani kabla hajakita sakafuni na hima hima akamfungulia siti ya mbele na kumbeba akamuweka vizuri na kufunga mlango. Akakimbilia kufungua mlango wake wa dereva na kuwasha gari. Akang'oa nanga kwa mwendo wa kasi, kila mtu aliyeshuhudia tukio lile akabaki amepigwa na butwaa asijue kilichotokea. Kilikuwa ni kitendo cha utekaji kilichotekelezwa ndani ya muda wa kufumba na kufumbua, ikionyesha tukio limefanywa na mtu mzoefu wa kazi hizo.

Deborah akawa ameshatekwa na mtu asiyejulikana na kupelekwa sehemu isiyojulikana kwa madhumuni yasiyojulikana. Sasa mambo yakawa mchafukoge kwa upande wa Deborah, hakuna mtu yoyote aliyeshuhudia tukio akawa na uthubutu wa kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi au kumpasha habari mtumishi mwenza wa Deborah pale kwenye kioski.

Kila mtu aliyeshuhudia tukio alikuwa anaogopa kukamatwa ili kuisaidia polisi kwa kosa lisilo lake. Kama ilivyo tabia za wakati wa Jiji la Dar es Salaam, kila mtu akashika hamsini zake kama vile hamna tukio lililotokea. Giza jeusi likatanda tena katika maisha ya Deborah, matanga ya moyoni mwake yanapiga hodi kila uchao kwa upande wao.

SURA YA KUMI NA MOJA
"Mwana Side-Boy..... sio mwenzetu tena, kaula mbaya huko South anasukuma E- class Mercedes Benz, aah....hiki kijiwe noma sana" aliongea mmoja wa wanachama wa majlisi ya wahuni wanabadilishana mawazo. "Kweli hata mie nimeletewa hizo habari na Timammy yupo Mtoto wa Mzee Fakii wa Vijibweni, ananiambia mara ya mwisho walivyoonana nae alifikia hatua hadi kumiliki kadi nyeusi ya benki 'FNB Bank'. Hiyo kadi nasikia inamaanisha mtu ana zaidi ya Rand milioni 1 kwenye akaunti yake benki" aliongea kwa uchungu kijana mwingine huku anapuliza hewani moshi wa sigara bwege maarufu kwa jina la bangi.

"Bangi, nipe mabawa unipeperushe hewani mpaka South kwa Mjomba Madiba kama ndege, nikale bata mie..." alizidi kuyasasambua maneno kijana yule kwa hisia kali huku anajinuwizia kwa kutumia moshi wa bangi anaojifukiza nao kichwani. "Kwa hiyo hapa mpango mzima ni kuona namna gani na sisi tumainika, tusibakie kuwa washangiliaji tu wa mafanikio ya wenzetu" Mbweku alichangia mawazo huku nae akigongea kwa ishara ya kidole kuwa apitishiwe sigara bwege asuuze akili yake.

"Hamna kulala dogo Mbweku hapa ni amsha amsha na kesha mpaka che tupo Bondeni kwa Mjomba Madiba, ndio maana nimekuunganisha kwenye ule mchongo wa kazi ya Ubaunsa pale 'Martino Royal Hotel' sasa ukambwelembwele wewe mwenyewe. Pale ukifika "How are you" nyingiii na "Yes Yes Mzungu Kala Mafenesi" za kutosha kwa Watasha na kuwachangamkia, Zali la Mentali likikudondokea haina shanapa wala kwepesha unasanda tu, tutajuana mbele kwa mbele" alijibiwa Mbweku na mmoja wa mtu ambaye aliyeonekana kama ndio kiongozi wa kijiwe chao.

Walikuwa wanajikusanya kijiwe wanapeana michapo ya nchi za ughaibuni yenye sura ya hadaa kwa rangi na hali. Hayo ndio maisha yalikuwa maisha mapya ya kijana Mbweku akiwa Kigamboni. Maisha ya kulala kwenye Meli mbovu, maboti na mitumbwi. Maisha ya kula kwa donesheni ya kupiga ugali wa shirika kwa samaki wa kupora kwa wavuvi. Maisha ya kuvizia usiku abiria wanaoshuka kwenye Pantoni na kuwapora ndio ikawa kazi yao. Vijana hao walikuwa hawajali wala hawabali juu ya mustakabali wao wa maisha ya baadae. Mambo yote haramu mutlaki kama ulevi, unyang'anyi, uzinzi, kupigana na mengineyo yalikuwa ndio matendo yao ya kawaida.

Simulizi zile za kuzamia nchi za ughaibuni "Stowaway" zilikuwa zinamsisimua vilivyo Mbweku, hivyo akaazimia lazima azamie Bondeni na kama fursa ikiruhusu Ulaya kabisa. Miaka hiyo kiu ya vijana kutaka kuikimbia nchi yao ya Tanzania ilikuwa kubwa sana. Wapo waliokuwa wanataka kwenda Ughaibuni kwa malengo ya kutabahari katika fani mbalimbali za elimu katika Vyuo Vikuu bora duniani, wengine kufanya kazi au kutembea. Wengi wao katika vijana hao kilichokuwa kinawasukuma kwenda nje ni mseto wa uchumi mbaya, umaskini na kutaka tu kufahamu mambo. Hali hiyo yote ilichagizwa na ukosefu wa ajira kutokana na serikali kuacha kuajiri kutokana na uchumi mbovu wa nchi.


Sasa rasmi kijana Mbweku, baada ya kuhangaika huku na kule akajikuta amepata bahati ya kibarua rasmi cha ulinzi na kufanya usafi kwenye mazingira ya Hoteli ya 'Martino Royal Hotel'. Akawa amejitapua kwenye kundi la vijana hawana kazi hawana bazi, kazi yao kukaa vibarazani kupiga ubwete tu. Hoteli ambayo waasisi wake Mr.Martin Tenga na Recho ndio waliosababisha baba yake mzazi kijana Mbweku afungwe jela kutokana na pesa walizokwapua nyumbani kwa marehemu Bosi Minja. Hawa Mabosi wake ndio waliosababisha Mbweku na familia yake kwa ujumla waishi maisha yasiyo na mbele wala nyuma.

Kwa tabia za MbwekuJr za kutopenda kudhulumiwa haki zake, kama angetambua kuwa Bosi wake Recho, mmiliki wa hiyo Hoteli ndio chanzo cha yeye kuishi maisha magumu yaliyochangia aachane na shule na kuwa chokoraa mtaani, pangechimbika vilivyo. Sala na matumaini ya MbwekuJr ilikuwa ni siku moja afanikiwe kimaisha ili akawachukue kutoka kijijini mama yake na wadogo zake ili waishi pamoja kama zamani.


Mkasa wake wa mauaji ya Kibopa Mwinyi Fuad uliishia hewani, hata Mbweku mwenyewe hakuamini namna lilivyopotezewa. Alikuwa kila siku asubuhi anadamkia kwenye meza za wauza magazeti kufanya taftishi ya taarifa ya mauaji ya Mwinyi Fuad. Lakini akashangazwa taarifa hiyo haikupewa kipaumbele na vyombo hivyo vya habari. Ndugu wa Mwinyi Fuad walitaka kusitiri aibu ya ndugu yao, ya kukutwa amefariki uchi wa mnyama ufukweni mwa bahari tena usiku. Maana Jiji zima walikuwa wanatambua tabia zake chafu katika jamii.

Wakatembeza chai kwa baadhi ya waandishi wa habari wasio waaminifu ili kuhakikisha hakuna redio wala gazeti lolote litakalotoa taarifa ya msiba huo hadharani. Maiti yake siku ya pili yake tu, ikaenda kuzikwa kwao Pangani, Tanga. Huo ndio ukawa mwisho mbaya wa baradhuli Mwinyi Fuad, katika safari yake ya kurejea jongomeo kwa Mola wake. Kufichwa kwa siri hiyo ya kifo hicho na familia ikawa ni nafuu kwa jeshi la polisi kutokana na ugumu wa kumpata muuaji uliopo.



Msichana mrembo mweusi mng'avu wa rangi, mrefu mwenye umbo la penseli. Uzuri wake wa sura ni wa shani, alikuwa yupo katika kilele cha milki ya usingizi akiwa ndani ya kasri ya kifahari ya aushi iliyopigwa umaridadi na mafundi waashi bobezi katika fani ya ujenzi. Pandikizi hilo la jumba ambalo kwa mtazamo wake, kila mtu atakayeiona lazima atatamani aishi ndani yake walau kwa saa chache. Alilazwa juu ya samadari ya thamani a'ali. Kiyoyozi kilikuwa kinafanya kazi yake ya kuleta ubaridi ndani ya chumba kile chenye wasaa wa kutosha alicholala kisura huyo mbichi. Juu ya dari kulifungwa bodi zilizopakwa rangi nyeupe huku taa mbili zilizozungushiwa marembo marembo ya kung'ara yaliyotengenezwa na madini ya 'Zabarjad' zikiwa zinawaka. Chini ya sakafu kulitandikwa zulia nene lenye rangi nyekundu mithili ya uwaridi. Ukutani kulikuwa na makabati mawili yaliyofungwa kwa funguo zenye kuning'inizwa. Bila kusahau ala za muziki laini zilizopangiliwa mipigo yake ilikuwa inasikia kwa mbali ndani ya chumba kile.

Kwa jinsi alivyokuwa kwenye usingizi mzito, kwa mtazamo tu hakuwa ni mtu wa kuamka muda mfupi ujao. Ghafla bin vuu mlango wa chumba chake yule msichana ukafunguliwa, akaingia daktari mmoja mrefu wa umbo, amevalia miwani yake, kidevuni amenyoa nywele zake mtindo wa duara huku akiziachia nywele za kionjamchuzi zikiungana na zile za kidevuni. Kwapani alikuwa amefumbata mkoba wake wa rangi nyeusi. Alikuwa amefuatana na mzungu mmoja unyounyo bila kuachiana nafasi kubwa baina yao. Yule daktari akaenda mubashara mpaka pale kitandani akampima mapigo ya moyo na joto la mwili la yule msichana kisha akaandika maelezo mafupi kwenye kidaftari chake kidogo chenye gamba gumu la rangi ya kahawia. Baada ya hapo akamtoa damu kubwa ya mkononi kwa kutumia bomba la sindano akahifadhi damu ile kwenye kichupa maalumu. Kisha akamlegeza nguo yake ya ndani aliyovaa msichana yule, akamtanua miguu yake kidogo kisha akamfanyia vipimo kwenye sehemu zake za siri. Muda wote yule mzungu alikuwa anamuangalia yule msichana kwa jicho la uchu wa huba.

"My God..Black beauty Black beauty....!" aliropoka yule mzungu akishindwa kujizuia hisia zake kwa msichana yule aliyezama katika usingizi wa pono akionekana ana furaha ya kupindukia akiwa ameshikwa na raghba ya kumzimikia kimapenzi. Yule daktari akabaki anatabasamu na kufunga kidaftari chake baada ya kumalizia maelezo yake ya mwisho na kumfuata yule mzungu. Daktari yule akamnong'oneza kitu Mzungu yule kwenye sikio la kushoto kisha wakatoka nje ya chumba kile. Yule mzungu alipotoka nje ya vyumba vile akaingia kwenye gari yake kisha warembo waliojiweka pembeni yake wakilizingira gari lile hawataki kumpa nafasi ya kutoka. Akashusha kioo chini na kuchomoa burungutu la pesa za kigeni kisha akamwaga hewani, akawapiga ukope na kutabasamu. Warembo wale wakawa sasa wanagombaniana ngwenje zile. Ndipo yule mzungu akapiga honi ili afunguliwe geti la kutoka nje ya Kasino hilo la vigogo.

Mlinzi wa Kasino hilo la roshani hima hima akafungua geti kuruhusu gari hilo litoke. Yule daktari nae baada ya muda akaagana na mlinzi yule akaondoka zake kwa kutumia usafiri wake binafsi aliokuja nao usiku huo. Warembo wale walikuwa kama wapo kambini ndani ya kasri lile linalotumika kama danguro. Mapaja yao warembo yalianikwa waziwazi huku chuchu zao zikicheza kifuani pale walipokuwa wakipiga hatua wakitembea kwa madahiro pindi wanapomlaki mteja.

Makalio yao ndio usiseme kwani hizo gauni laini walizovaa ziliwachora vyema hasa kutokana na kuwabana vilivyo. Wengine walikuwa chini wamevalia vichupi vya kuogelea na juu wana viblauzi vyepesi. Visura hao walikuwa wanatamanisha kweli hasa kwa mtu mkware, angeweza hata kufanya maamuzi ya kufuja urathi kwa kuhonga nyumba aliyoachiwa wa wazazi.

Danguro hili la siri la kifahari lililopo eneo la Sinza Kijiweni lilikuwa linamilikiwa na Recho. Vigogo pekee ndio walikuwa wanaweza kumudu gharama zake, mtu fukara fuke hata ajichange kipato chake cha mwaka mzima asingeweza kumudu gharama zake. Mpenzi mpya wa Recho, mzungu Mr.Lorenzo alikuwa hajui kitu juu ya uwepo wa danguro hilo la siri. Alichofanya Recho ni kwenda kuweka poni benki hati ya Hoteli ya Martino Royal Hotel waliyokuwa wanaimiliki kwa pamoja kati yake na mwandani wake Mr.Lorenzo. Kisha akachukua mkopo mkubwa wa mamilioni ya shilingi na kuja kununua nyumba ya roshani maeneo ya Sinza kisha akaifanyia ukarabati wa ngumu kuiongezea hadhi na thamani. Kupitia biashara hiyo ya danguro Recho akajikuta anajiingizia pesa kochokocho ambazo hazitozwi kodi hata chembe tofauti na biashara ya Hoteli ambayo macho ya serikali yote yalikuwa hapo ili kupata pesa za kuendesha nchi.

Sera ya serikali ya awamu ya tatu, chini ya Rais 'Benjamin William Mkapa' ilikuwa na mikakati madhubuti ya kukusanya vizuri maduhuli ya ndani yanayotokana na kodi ili nchi ipunguze utegemezi wa wafadhili toka nchi za ng'ambo. Wafadhili ambao daima misaada yao ilikuwa inaambatana na masharti magumu yenye kuvunja maadili ya utu na uhuru. Recho akausoma mchezo mapema akaamua awekeze nguvu kwenye biashara haramu ya danguro. Nia na malengo yake yalikuwa sio kurejesha mkopo benki. Alitaka benki waipige bei Martino Royal Hotel ili awe amejivua ushirika na Mr.Lorenzo. Kilichomsukuma Recho afanye yote hayo, ni kutokana na kugundua kuwa Mr.Lorenzo anamficha vitu vingi sana, hasa kutokana na tukio la kuzifuma hati za kusafiria za Mr Lorenzo zenye majina tofautitofauti ya bandia. Pia alikuwa anaweza kupotea Tanzania kwa zaidi ya miezi 3 asijulikane alipokwenda akiwa kwenye mishemishe zake za kurekodi filamu. HIvyo usiri wa Mr.Lorenzo ukamfanya Recho achukue tahadhari kabla ya hatari kwa kuamua kumzunguka mwekezaji mwenza wake. Alimuona Mr.Lorenzo ni kama nyoka mwenye mwendo wa mzizimo, anayejificha uhalisia wake.

Akajigeuza panya kuuma huku akipuliza kwa mpenzi wake Mr.Lorenzo. Kumbe mwenzake Mr.Lorenzo hakuwa bunga, ni mtoto wa mjini, kazaliwa Jijini Turin kakulia Turin maujanja yote anayajua. Tabia za Mr.Lorenzo zilikuwa kama samaki kitatange, mjanja kupitiliza ingawa kimuonekano anaonekana ni fala, bwege mtozeni. Alikuwa ana watu wake mawakala sehemu nyeti kama benki, uhamiaji na kwingineko ambao wanamuunga taarifa mbalimbali za harakati zake. Wakamnyetisha mkanda mzima namna Recho alivyoweka bondi benki hati ya Hoteli. Hivyo akajipanga akitua tu Bongo, atampiga tukio la hatari Recho litakalomfanya ajute kuzaliwa. Tukio ambalo alifahamu kwa vyovyote vyombo vya dola vitamuwinda vimtie mbaroni jambo ambalo Mr.Lorenzo hakutaka litokee hivyo alijiandaa kugura kikafiri kurejea kwao nchini Italia.


Recho kwa upande wake, wasichana wa danguro lake wengi wao alikuwa anawapata kwa njia za utekaji. Alikuwa ana vijana wake wa kazi, genge la wahuni wanaozunguka mitaani kusaka vipaji. Hivyo likaanza kuibuka wimbi la matukio ya wasichana kupotea mitaani bila kufahamu kuwa wanaenda kugeuzwa kuwa watumwa wa ngono kwenye danguro la Recho. Walikuwa wanapofikishwa hapo kwenye danguro, wanapimwa afya zao na daktari kisha wanaanza kuzoeshwa matumizi ya pombe na madawa ya kulevya. Pia wanalipwa pesa sufufu zinazowashawishi waendee kubakia kwenye ulingo huo wa uchangudoa ili waweze kumudu kuishi maisha ya anasa.

Yule msichana mrembo aliyekuwa amelazwa kitandani alikuwa ni Deborah. Akiwa ndio kwanza ametekwa mtaani na kuletwa ndani ya danguro hilo. Danguro ambalo kutoroka kwake ingekuwa ni ndoto ya mchana, au ni lenye kustaajabisha mfano wa mbwa kuvaa nguo. Alikuwa amefungiwa katika chumba kilichopo roshani ya tano. Mpaka kuifikia roshani ya tano ulikuwa unakutana kwenye kila korido na mlinzi mmoja mwenye silaha. Walinzi hao namba wani walikuwa na maumbo ya miraba minne na sio vimbaumbau kama mwiko wa pilau. Walishapewa maagizo ya wazi kuwa wasiruhusu mwanamke yoyote au mgeni yoyote kuingia bila kibali kutoka kwa mmiliki Recho.

Uzuri wa mambo vibali hivyo alikuwa anatembea navyo Recho kwenye gari yake, hivyo kuzidi kutengeneza ugumu wa mtu yoyote kutoroka au kuingia humo. Hivyo Deborah alikuwa ana wiki moja tu ya kuachwa arudie kwenye hali ya kawaida baada ya hapo, ndio angeanzwa kuharibiwa kisaikolojia kwa mihadarati na kuwa teja rasmi na mtumishi wa danguro hilo. Bila muujiza wa Mungu wake, asingeweza kamwe kufua dafu kama akiamua kutoroka kwenye jumba lile. Deborah kama angejaribu kutaka kutoroka angefilia mbali kutokana na kipigo angechopokea toka kwa walinzi hao.


"Mwana harashi mkubwa huyu binti ameshafilisi Kioski changu, wema wangu umeniponza kumbe mkora wa kutupwa, msakeni popote alipo, mkimkamata ama zake ama zangu pumbavu zake sana....!" alikuwa anafoka Koplo Marieta mbele ya askari wenzake huku mishipa ya shingo imemsimama, mapovu meupe ya hasira yanamtoka pembezoni mwa kinywa chake, wakati anaripoti kituoni kwa polisi wenzake juu ya tukio la kutoroka kwa Deborah.

Koplo Marieta alikuwa anatetemeka kwa hasira utasema amevumbikwa na homa. "Lakini haonekani kama ni mwana hizaya, anaonekana ni Binti anayejitambua labda kapatwa na jambo baya tusimhukumu kwanza, muda ni mwalimu mzuri....!" alitetewa Deborah na polisi mmoja wa kike jirani yake Koplo Marieta ambaye alikuwa anamfuatialia kwa makini nyendo za Deborah akiwa nyumbani. "Watu wahalifu makini daima ni wapole, wanaficha madhambi yao kwenye upole wao...!" alitia shadda msimamo wake Koplo Marieta akionekana hataki kusikia la muadhini wala la mchota maji msikitini, yeye alisha hesabu kuwa Deborah kamuingiza mjini."Afande nilikutahadharisha mapema siku ile juu ya uamuzi wako wa kumkaribisha nyumbani huyo Binti hukunisikiliza, nilikuambia kinagaubaga kuwa hawa watoto machokoraa ni kama kunguru hawafugiki, wameshazoea maisha ya kubakwa, kulawitiwa, na uporaji huko mitaani, daima mbwa ni mbwa tu hawezi kugeuka mbuzi" Afande mwingine wa kiume nae akiwa amevimba kama mvua ya masika aliongezea chumvi kwenye kidonda cha maumivu ya moyoni cha Koplo Marieta.

Koplo Marieta ilibidi aelezee tukio zima lililotokea, ya kuwa Deborah hajarudi nyumbani jana usiku mpaka ilipofika che hajafika maskamoni. Akaelezea pia kuwa amedamka asubuhi na mapema kwenda Kisutu kwenye Kioski, muuzaji mwenzake Deborah hafahamu kitu chochote kama hajafika nyumbani kwa maana waliagana salama salimini jana yake, huku wakiahidiana kukutana mapema iwezekanavyo asubuhi yake. Baada ya majadiliano ya kina, askari wale wakaafikiana kwa kauli moja, wavunje kikao kile kisha waingie mitaani wamsake Deborah popote alipo kisha akamatwe aje kujibu tuhuma zake za wizi wa kuaminika. Deborah alihesabiwa ametoroka na ngwenje za kutosha, za kulipia ada shuleni na zingine za mauzo ya siku ya kwenye Kioski. Msako ulikuwa unafanyika kwa haraka na umakini mkubwa ili kujaribu kuokoa baadhi ya pesa alizotoroka nazo kabla hajazifuja. Askari wale kwanza walimbinya vilivyo kibarua wa pale kwenye Kioski cha Koplo Marieta, viboko vikimwandama mwilini masikini Binti wa watu, wakiweka dhana huenda ni mchezo walioshirikiana na Deborah. Lakini hawakuambulia kitu baada ya kuonyesha hafahamu chochote katika njama hizo za Deborah. Walipowahoji baadhi ya vijana wa pale Stendi wapo waliotoa shuhuda kuwa walimuona anapanda gari usiku huo lililoegeshwa jirani na Kioski. Maelezo hayo yakazidi kuongeza chachu kuwa tayari Deborah alishaanza kushiriki mambo ya mapenzi mpaka anafuatwa na wenye magari usiku.

Siku zikaanza kuyoyoma, bila kuleta matokeo chanya ya kukamatwa kwa Deborah. Koplo Marieta alijaribu kupekua kwenye begi lake la nguo alilolitelekeza kwa matumaini huenda akambulia picha za Deborah na nyaraka zingine zinazoweza kusaidia taftishi ya kukamatwa kwake, lakini hakuambulia kitu. Deborah maisha yake alikuwa anayaendesha kama mwanajeshi, kila kitu chake muhimu kilikuwa kwenye pochi yake ya mkononi. Ilipofika siku ya 5 tokea atoweke, Koplo Marieta akabwaga manyanga, akakubali matokeo na kuamua kumshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea. Lakini kama ujuavyo kanuni asilia inasema dhambi daima haisahauliki na wema hauozi. Uwe mwema kadri utakavyokuwa mwema kwa watu, lakini bado watu watakumbushia dhambi zako za nyuma ulizowahi kuwatendea. Hivyo mazuri yote aliyowahi kuyatenda Deborah kwa muda mfupi alioishi na Koplo Marieta akawa ameyachafua, mema yote Koplo Marieta akayaweka kwenye kaburi la sahau.

Ama kweli usilolijua ni kama usiku wa giza nene, na daima ukipatwa na jambo au kuletewa habari usiyo na uhakika nayo, iweke deke kwanza usikimbilie kuhukumu utakuja kujutia maamuzi yako pindi ukweli ukidhihiri. Polisi wale walichokuwa hawakifahamu ni kuwa Deborah alikuwa yupo mateka ndani ya pandikizi la jumba akiwa haifahamu hatima ya usalama wake. Alikuwa yupo katika msongo mkubwa wa mawazo akiwa halifahamu lengo la watekaji wale kwake.

Mbweku Jr alikuwa ndio anatoka kazini asubuhi yake, akiwa ameshushwa na daladala katika kituo cha Manzese Argentina na mkururu wa mawazo kichwani. Mbweku Je alikuwa amehamishiwa kikazi eneo la Sinza Kijiweni kuwa ni mlinzi wa getini kwenye danguro linalomilikiwa na Bosi wake Recho. Alihamishwa kutoka 'Martino Royal Hotel', Kigamboni na kuletwa huku mjini, hivyo ikambidi apangishe chumba maeneo ya Manzese ili kumuwepesishia kufika kazini kwa haraka, tofauti na kama angeendelea kuishi Kigamboni. Mipaka yake ya kazi ilikuwa ni kuishia getini tu, huko ndani ya nyumba kulikuwa na walinzi wengine mahususi kwa kazi za ndani ya jengo.


Usiku wa kuamkia asubuhi aliyokuwa anatoka kazini, kulitokea jambo zito kwa upande wake jambo ambalo ndilo lilikuwa linampa mawazo lukuki kichwani mwake. Jambo ambalo alijiwekea adhima ya kuelekea gereza la Ukonga kwenda kuonana na baba yake mzazi ampasulie ukweli wa mambo asubuhi ile ile. Kutokana na siri aliyoiona, mawazo ya Mbweku Jr yalikuwa yanamtuma huenda baba yake alikuwa na watoto wengine wa nje ya ndoa ambao hawafahamiki na familia yao. Bahati mbaya sana, baba yake mzazi Mbweku Jr alianza kuugua maradhi tofauti tofauti kule gerezani Arusha, hivyo akahamishiwa gereza la Ukonga lililopo Jijini Dar es Salaam ili kumuweka karibu na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya urahisi wa matibabu.

Mbweku Jr alishapewa taarifa hizo za baba yake kuhamishiwa gereza la Dar es Salaam na mmoja wa wajomba zake aliyekutana nae bila kutarajia katika viunga vya maeneo ya Manzese Darajani. Enzi hizo Manzese Darajani kilikuwa ni moja ya kivutio kikubwa kwa wageni wanaokuja Jijini Dar es Salaam wakitokea mikoani. Wananchi hao wa mikoani wengi wao ilikuwa lazima waje Manzese walipande daraja hilo la kisha kupiga nalo picha za kwenda kuonyesha wenzao huko mikoani kuwa wamekanyaga daraja refu la Jjijini Dar es Salaam. Hivyo siku moja Mbweku Jr akiwa kwenye harakati za kuelekea Sinza kibaruani hana hili wala lile ndipo akagongana uso kwa uso na Mjomba wake huyo. Katika kubadilishana mazungumzo baina yao, ndipo akapata taarifa za baba yake mzazi kuletwa gereza la Ukonga. Hivyo akawa anajipanga siku atakayokuwa yupo mapumziko kazini aende kumtembelea amjulie hali na kumueleza maendeleo yake toka alivyowaacha uraiani.

Lakini kwa tukio alilolishuhudia kazini kwake usiku wake aliamua siku hiyo hiyo lazima aende gereza la Ukonga hasa ukichukulia siku hiyo ilikuwa ndio mwisho wa juma, siku ambayo wafungwa wanaruhusiwa kutembelewa na ndugu, jamaa na marafiki zao. Alipofika chumbani kwake, akawasha jiko lake la stovu kisha akabandika sufuria la maji ya chai, haraka haraka akabadilisha sare zake za kazi, akavaa malapa yake na kubeba bakuli lake chakavu la plastiki kwa ajili ya kwenda kununulia mihogo ya kukaanga kwa mama muuza mtaa wa pili kutokea nyumba anayoishi.

Nakuona tu unachomoka wima kama mlingoti, kwani hujui usafi wa choo ni zamu yako, mwanaume mzima lakini ovyoooo kabisa, masharubu kama paka wa baa vile, nakodi yako ikiisha Billahi wa Rasuli utahama nyumba hii siku hiyo hiyo..…!” alikoroma mama mwenye nyumba akimchamba kijana Mbweku Jr kutokana na kuzembea usafi wa msalani. Narudi mama yangu siondoki, nakumbuka vizuri zamu yangu, nisamehe kama ninakukwaza.! Alijibu Mbweku Jr kiunyenyekevu mkubwa huku anachapa lapa zake kutoka kwenye kizingiti cha mlango.

He..Heeeee.Hallow eeeeeh.mama yako nani hapa, mie naweza kuzaa lidume kama wewe, usinizeeshe babu wewe, ukome kuniita mama yako iwe mwanzo na mwisho mwana halulu mkubwa wewe! alizidi kufoka Bibi Mwazani, ajuza ambaye ni mjane alikuwa hapunguzi miaka 65 kwa haraka haraka lakini alikuwa anaupenda ujana balaa. Kila wiki atanunua dera jipya, mara aweke kigodoro usiku kucha nyumbani kwake na vimbwanga vingine kochokocho ambavyo kiuhalisia vilitakiwa vifanywe na wanawake vijana.

Watoto wake walimsema kwa tabia zake mbovu mpaka wakachoka, wakaamua kumsusia nyumba peke yake, aendeleze ufisadi wake nje ya mboni za macho yao. Kawaida yake alikuwa hapendi wapangaji wanawake, au wana ndoa kwenye nyumba yake ya urithi wa mumewe. Alikuwa anapenda barobaro ili ashiriki nao kwa kuwarubuni kimapenzi. Na kwa jinsi vijana wa kileo wanavyopenda mserereko wa kimaisha walikuwa wepesi tu kuzini na Bi. Mwazani ili mradi mambo yao yawaendee vyema. Sasa ugomvi wao mkubwa na mpangaji wake Mbweku mpaka kufikia kutoleana maneno makali ulianzia kwenye mambo ya kunyimana unyumba. Mbweku Jr alikataa kuwa mpenzi wa Bi.Mwazani, licha ya kufanyiwa vibweka na mitego ya kila ya aina ya kimahaba.

Siku za mwanzoni Mbweku Jr kuhamia hapo, Bi. Mwazani alikuwa anadamka alfajiri, siku akijua Mbweku Jr amelala kazini usiku wake. Basi hapo atajipikilisha chapati za mayai na rosti ya maini kisha anamuandalia Mbweku Jr utasema ni mumewe. Mchana wake atamuita Sheikh wa msikiti wa jirani amchinjie jogoo lililofutwa kodi kwa ajili ya pilau ya Mbweku Jr. Kijana wa watu alikuwa anajilia vinono vyake na penzi hatoi kwa Bibi wa watu. Siku waliyogombana kimoja na kuwa mahasimu wasiopikika chungu kimoja, Bi.Mwazani alileta maigizo kuwa kazidiwa na ugonjwa akiwa kibarazani huku akijua wapangaji wake wote wapo vibaruani kasoro Mbweku Jr ndio kabakia nyumbani. Majirani wakapiga kelele baada ya kumuona anazidiwa na kutoa sauti ya kuweweseka kutokana na tashdidi ya ugonjwa. Mbweku Jr ikabidi atimue mbio kutokea ndani akija wangu wangu kumuwahi mama mwenye nyumba wake. "Msinipeleke hospitali, huyu ni jini Khanziri kanipumzisheni kitandani nitapata nafuu baada ya muda msijali" aliongea kwa tabu Bi.Mwazani huku akiwafanyia kiini macho cha kiwango cha lami bila wao kutambua. Ikabidi wakubaliane na matakwa yake, wakambeba mzobemzobe mpaka chumbani kwake wakambwaga kitandani mwake.

Wale watu baki walipotoka chumbani, Bi.Mwazani akajitia kumuagiza maji ya kunywa ya chupa Mbweku Jr. Alipoyaleta maji yale, wakiwa wawili tu chumbani ndipo alipokutana na kituko cha kufungia mwaka. Bi.Mwazani alibakia mtupu uchi wa mnyama, amesaula nguo zake zote amebakiza lundo la shanga kiunoni. Akawa bibi wa watu anamlalamikia Mbweku Jr kwa sauti ya kimahaba ile inayotokea puani kuwa anamtesa sana kwa kumnyima penzi lake, hasa akiona kifua chake Mbweku Jr kilichotanuka kama mataruma ya reli, hivyo amuonjeshe huba atulize ashki na hawaa ya nafsi yake.

Ikabidi Mbweku Jr atumie akili za kuzaliwa, akazichanga vyema karata zake kuepuka mtego huo ulioenda shule. Maana vinginevyo Bi Mwazani angeweza kumzushia kesi ya ubakaji, kesi ambayo asingechomoka abadani kutokana na kukutwa chumbani kwa Bibi. Jamii yote inayopenda kutenda bila kutafakari, inayopenda kuongea bila kupima, moja kwa moja wangetoa hukumu kuwa Mbweku Jr ni mbakaji. "Ngoja basi nikanywe chai nishibe, ndio tuanze upasuaji unaoutaka, uskonde hata mie nakupenda sana sema nilikuwa nakuogopa kukuambia usije kuniona sina adabu" alijitutumua Mbweku Jr kumuongelesha kimahaba Bibi wa watu huku akimpa matumaini feki, mpaka bibi akaingia kwenye mstari.

Akapewa ruhusa ya kutoka chumbani mule kwenda kunywa chai huku Bi, Mwazani akiwa amejawa na furaha fokofoko anapulizia marashi, utuli na manukato chumba kizima maandalizi ya ujio wa Mbweku Jr chumbani kwake aje kumpagawisha. Yakawa yanakatika masaa, Mbweku Jr kajifungia chumbani kwake habari na mtu hana. Mpaka kufika majira ya alasiri Bi.Mwazani akakata tamaa huku uso wake ukibeba soni na fedheha ya hali ya juu ya kuzidiwa akili na mjukuu wake kabisa kiumri, na kuamua kuzindua vita rasmi vya uhasama na Mbweku Jr. Hiyo ndio ilikuwa sababu ya Mbweku Jr kuandamwa asubuhi asubuhi hata hajapumzika tayari ameanza kumjazia nzi mbele ya majirani.

Mbweku Jr alivumilia kwa sababu siku zake za kuishi Tanzania zilikuwa zinahesabika alishajipangia hana siku tatu mbele lazima atazamia Afrika ya Kusini. Alishajiandaa kwa masurufu ya safarini, kutokana na kudunduliza sehemu ya pesa zake za mshahara. Baada ya kujishibia mihogo yake kwa chai ya mkandaa, akaingia zake bafuni akaanza usafi wa choo na bafu kama mama mwenye nyumba wake Bi.Mwazani alivyoagiza. Alipomaliza akajimwagia maji na kujiandaa kuelekea Ukonga, Gerezani. Akalifunga vizuri geto lake, mkononi akiwa na bahasha nzito ya kaki, ndani yake bahasha hiyo ina jambo zito analotaka kwenda kumuonyesha baba yake gerezani. Kisha akampita Bi.Mwazani kibarazani akiwa amefura kwa hasira dhidi yake, anatamani hata awe na uwezo wa kummeza kama chatu.

Mbweku Jr hakumjali, akampita bila kumuaga, na kuelekea dukani kwa Mangi kununua mazagazaga kama sabuni, nyembe, dawa ya mswaki, mswaki na vikorokoro vingine vya kumbebea baba yake gerezani. Alipofika kituo cha daladala, hakuchelewa sana kabla hajapata gari la kuelekea Ukonga. Njia nzima alikuwa anawaza namna baba yake atakavyomshangaa kwa kumuona mabadiliko yake ya kimwili na kiakili. Pia alikuwa na kimuhemuhe cha kufahamu ukweli na undani wa kilichomo ndani ya bahasha ile.



"Mbweku Wa Mbwekuuuuu.........!" "Naaam Afande.....", aliitwa mfungwa Mbweku na askari magereza wa zamu akaitika haraka haraka, aje kumuona mgeni wake aliyemtembelea magereza siku hiyo ya kutembelea wageni. "Babaa....Babaaa....Babaaaa....nini hasa kinakusibu Babaaa.....!" alijikuta Mbweku Jr anaongea kwa hisia kali mpaka machozi yakaanza kumtiririka na kuyalowesha mashavu yake. Mzee Mbweku alipigwa na pumbao na mzubao wa muda fulani akionekana hayaamini macho yake kumtia machoni tena barobaro wake mkubwa baada ya kutenganishwa nae kwa miaka kadhaa. Bila kujibu kitu akamfuata kijana wake na kumkumbatia kwa nguvu mpaka nae akamwaga mchozi wa nguvu. Eneo lile la makutano ya wafungwa na ndugu zao likageuka kama msibani kwa muda kutokana na vilio vilivyokuwa vimetawala.

Askari magereza alikuwa anawaangalia baba na mwana kwa jicho la huruma na imani, moyoni mwake utasema akitamani awe na mamlaka ya kuwaruhusu waondoke wote kwenda nyumbani, lakini La hasha, mwenye mamlaka hayo ya kuwasamehe wafungwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mheshimiwa Rais pekee. "Mimi ni mahamumu mwangu, kisukari, shinikizo la damu na matatizo ya moyo yote ni magonjwa yangu. Lakini sasa mimi sijambo, nawashukuru sana madaktari wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa huduma wanazonipa...! " alijieleza kitu kinachomsibu mwilini mwake mpaka akakondeana akabakia mifupa tupu, kitu ambacho kilimuogopesha sana mtoto wake Mbweku Jr. Mtoto mtu akabaki kutikisa kichwa tu, kuashiria hakubaliani na maelezo ya baba yake, huku moyoni mwake akitambua fika hiyo nafuu ya baba yake ni ile sijambo ya Kiswahili, ya kuanua ngoma juani.

Wakaongea mambo mengi baina yao, wakikumbushiana hadithi za siku za nyuma huku baba akionyesha kusikitishwa sana na kitendo cha Mbweku Jr kukacha shule na kuingia mtaani. Mbweku Jr alijitetea sana mpaka baba yake akamuelewa kuwa ni kweli hakuwa na jinsi lazima tu angeacha shule. Ila akampa wosia huku Jijini aishi vizuri na watu, aviogope vya watu kama ukoma ndipo watu watampenda vinginevyo ataliacha Jiji kwa fedheha. Pia akamuasa asiache kuwaangalia kijiji mama yake mzazi na wadogo zake kwa jicho la huruma, awainamishie bawa la unyenyekevu walau kwa kuwatumia senti ya sukari na unga.

"Baba nisije nikasahau, hii picha yako ulipiga na watu gani, imechakaa na ni ya siku nyingi sana..! " aliuliza Mbweku Jr wakati akiwa tayari ameikabidhi ile picha kwenye mkono wa baba yake huku moyo wake unadunda kwa nguvu akisubiria jibu la baba yake, alikuwa makini kutazama mabadiliko ya uso wa baba yake. "Mmhhhh.....umeipata wapi hii picha?, daah....hawa ni marehemu Bosi Minja huyu aliyekaa katikati na huyu kulia kwetu alikuwa dereva wetu anaitwa Nicco. Hii picha ilipigwa siku ambayo Bosi wetu huyu Mr.Joseph Minja anaripoti kazini pale katika ofisi za Peace Corps-Tanzania. Umeipata wapi hii picha sikumbuki kama ilikuwa kwangu hii picha...! " aliuliza kwa mara ya pili kwa msisitizo na kiudadisi huku amemkodolea macho mtoto wake.

"Hii nimeikuta kwa msichana mmoja, huko kazini kwangu nikamuibia bila yeye kufahamu, mara tu nilivyoiona sura yako, basi nikajua huenda huyo dada ni mtoto wako wanje ya ndoa" alijibu Mbweku Jr huku anairudisha tena ile picha kwenye milki yake ndani ya bahasha akiwa anatabasamu. "Mhhh.....hapana, sina mtoto nje ya ndoa zaidi ya nyinyi wanangu kipenzi,asije akawa ni binti wa Bosi wangu Minja, maana marehemu aliacha mtoto mmoja wa kike anaitwa Deborah kama sijasahau, maana miaka imepita.

Nimemkumbuka kwa sababu alikuwa anakuja nae kazini mara nyingi tu huyo binti yake. Pia kuna mwanamke mmoja chotara wa kizungu, alikuwa katibu muhtasi wetu pale ofisini akiitwa Recho inasemekana alizaa nae mtoto mmoja wa kiume ingawa tetesi zinasema alibambikiwa tu Bosi hakuwa mtoto wake wa damu..!" aliongea kiunyonge Mzee Mbweku huku akionekana anavusha mawazo yake kuyapelekea mbali sana, akikumbukia matukio ya siku za nyuma kabla hajafungwa. "Unasemaje baba?.., Huyo katibu muhtasi wenu akiitwa Recho..? kama vile namfahamu asije kuwa ndio Bosi wangu ninapofanyia kazi baba....!" aliongea Mbweku Jr kwa tashwishi kubwa huku akisubiria jibu la baba yake, litoe ithibati. Moyoni alikuwa anachekelea, kuwa kama Bosi Recho akiwa ndio mtumishi mwenza wa baba yake enzi wakiwa kazini alipanga kwenda kujitambulisha rasmi kwake. Hisia zikimtuma kuwa huenda Recho akamkabidhi kitengo kizito chenye ulaji, na safari ya kwenda Afrika ya Kusini lazima aioteshe mbawa.

"Huenda akawa ndio huyo, maana huyo Recho, dereva wetu Nicco wakati nipo gerezani Arusha alishawahi kunitembelea siku moja akanieleza kuwa sasa ameuchinja, ni mwanamke tajiri sana, anamiliki Hoteli kubwa Jijini Dar es salaam kwa ushirikiano na mpenzi wake, hiyo Hoteli inaitwa 'Martino Royal Hotel'. Nicco akanieleza vitu vingi sana mpaka tukafikia hitimisho huenda Recho ndio alimuua Bosi wetu Minja kwa ushirikiano na huyo mjuba mwenzako Martin ili wapore pesa ambazo zimesababisha mimi niozee jela...!" aliongea kwa hisia kali huku machozi yanazidi kumtiririka Mzee Mbweku, mpaka Mbweku Jr akawa anajitahidi kumfuta machozi baba yake. Maongezi yao, yaliendelea wakimuongelea Recho, wakifafanuliana wajihi wake mpaka Mbweku Jr akajiridhisha bila mashaka kuwa huyo Bosi wake wa sasa nwanamama ndio Recho huyu aliyekuwa Katibu Muhtasi kazini kwa baba yake.

"Muda umekwisha mmebakiza dakika 2 tu, muagane sasa.." aliongea yule askari magereza huku akiwapitia wafungwa wengine waliotembelewa na ndugu zao akiwakumbushia suala la muda kwisha. "Baba mie nasafiri kwenda nchini Afrika ya Kusini saa na wakati wowote kuanzia sasa, hii ni taarifa tu nakupa sihitaji ushauri wako.. !" aliongea Mbweku Jr akiwa ameshasimama lakini anachemka kwa hasira dhidi ya Recho, amekunja ndita mpaka akajikuta machozi yanamlengalenga. "Safari njema, wewe sasa ni mkubwa upo katika utawala wako binafsi, nakujua wewe ukilazimisha jambo lako lazima liwe unavyotaka ndio tabia yako toka utotoni. Ila kikubwa ni kama nilivyokupa nasaha, usijaribu kufanya chochote cha kulipiza kisasi kwa Recho. Kwanza hatuna ushahidi wa asilimia 100% kuwa yeye ndio mporaji wa pesa zilizoibwa ofisini, pili ana nguvu ya kipesa atakupoteza wewe na kizazi chako chote akikugundua umeijua siri yake kuwa yeye ndio muuaji wa Bosi Minja. Pia nakuomba kabla hujasafiri kwenda huko unakotaka kwenda upite Bagamoyo kwa Sheikh Maarifa akufanyie dua ya safari, wakati tupo kazini enzi zetu watumishi wengi tulikuwa tungongana kwake kunyoosha mambo yetu" aliongea Mzee Mbweku huku akisimama na kuvichukua vitu vya zawadi alivyoletewa na mtoto wake baada ya kuwa vimeshakaguliwa na askari magereza kuhusu usalama wake.

"Sasa huyo Sheikh Maaarifa anaishi Bagamoyo gani maana Bagamoyo ni kubwa baba...! " alizidi kuuliza Mbweku Jr huku akionekana amekubaliana na ushauri wa baba yake, wa kwenda kwa mtaalamu. "Haya ondoka zako, karibu tena siku nyingine…" askari yule akamfukuza Mbweku Jr. Mzee Mbweku akawa anaondoka zake kurejea gerezani huku anampungia mkono wa kwaheri mtoto wake. Mbweku Jr alibakia amesimama kama sanamu, alitamani aondoke na baba yake warudi nyumbani pamoja, wakafanye maisha kama zamani. Mbweku Jr nae hakupoteza muda akatoka nje ya gereza na kuingia zake mtaani.

Alipoangalia saa yake akaona ni saa 6 mchana, hivyo bado anao muda wa kutosha kabla ya kuingia kazini saa 12 jioni. Akaingia mtaani kutafuta penyenye wapi anapopatikana Sheikh Maarifa huko Bagamoyo. Hiyo ndio tabia halisi ya Muafrika kuabudu mizimu na kushinda kwa Waganga, hata asome mpaka Chuo Kikuu, awe Tajiri wa dunia lakini bado mambo yake atayaendesha kwa nguvu za ndumba. Pia akitoka kwa Sheikh Maarifa, kuna vitu vya kazi alitaka kuvinunua kwa ajili ya kumtorosha Deborah usiku wa leo ili na yeye atoroke kimoja. Sasa alihisi kuna hisia kabisa za kumuunganisha yeye na Deborah. Picha ile aliyompelekea gerezani baba yake aliifuma katika makorokoro yaliyomo kwenye mkoba aliokutwa nao Deborah pindi alipoletwa na mtekaji wake pale kwenye danguro. Aliona kabisa wao ni wahanga wa vitendo vya kishetani vya Recho, hivyo akapatwa na pashawa la moyo ya kumsaidia Deborah. Ingekuwa ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu kumtelekeza kwenye jumba lile lenye kila aina ya Ufirauni.



SURA YA KUMI NA MBILI


“Youu…fala mkubwa, hanisi wewe unachelewa kufungua geti, unataka kazi au hutaki? “ alifoka na kutoa matusi ya nguoni Bosi Recho kwa mlinzi Mbweku Jr ambaye alikuwa yupo kama hayupo usiku huo kutokana na mawazo kichwani mwake. Recho alikuwa akiutwika mtindi kichwani basi kinywa chake hakikosi kutoa maneno tepetepe yenye matusi ndani yake. Sasa adhabu yako gari tunaliacha nje, ulilinde ole wako kiibiwe kitu utakiona kilichomtoa kanga manyoa, kenge mkubwa wewe..Bebiiii.... Bebiii... shuka kwenye gari tukale raha zetu.. alionge Recho kwa hasira akitoa maagizo mapya kwa Mbweku Jr kisha akimuita dereva wake, ambaye alikuwa ndio mpenzi wake wa siri ambaye Mr.Lorenzo hamfahamu. Walianza kwa kificho lakini kama ujuavyo penzi ni kikohozi halifichiki sasa walikuwa wanajiachia waziwazi dhahiri shahiri.

Nisamehe Bosi sirudii tena, usingizi ulikuwa unataka kunimiliki aliomba msamaha Mbweku Jr kwa sauti ya unyenyekevu huku amefumbata mikono yake kifuani kuonyesha majuto yake kwa uzembe alioufanya kazini. Halafu dogo jiangalie sana, punguza dharau ukiwa kazini, umeskia wewe, utarudi kuwa chokoraa shauri yako.. aliongea maneno ya kukereketa, yenye kukata maini yule dereva mdogo tu kiumri, mchepuko wa Bosi Recho, aliyekuwa anajulikana kwa jina la Beka, halafu akamsogelea kwa karibu kisha akamtemea mate usoni mlinzi Mbweku Jr. "Bebiii...muda unayoyoma achana nae mbwa koko huyo...! " aliongea Recho kwa sauti ya kilevi na dereva wake, wakakumbatiana viuno vyao kimahaba huku wanapigana mabusu motomoto, wanapeana nyama ya ulimi kwa sauti za kunong'ona, wanaelekea zao kwa mwendo wa kinyonga kwenye moja ya chumba kilichopo kwenye roshani hiyo kwenda kujivinjari, wakazamishane kwenye kina cha bahari ya mapenzi.

Mbweku Jr akiwa ameumuka uso kwa hasira na ghaidhi ya kutemewa mate na hawara wa Bosi wake. Alikuwa amepandwa na mori wa kutaka kulipiza kisasi, lakini akawa anajitahidi kutuliza hasira zake asije kuharibu mambo ya msingi. Walivyotoweka mabaradhuli wale kwenye upeo wa macho yake, kabidi amshtue mlinzi mwenzake aliyekuwa anarandaranda nje ya ukuta aje kukaa ndani, wabadilishane ili yeye atoke nje kulinda gari kama alivyoagizwa na Bosi Recho. Amri hiyo ya Mbweku Jr kulinda gari ena nje ya geti, ikawa ni kama kumpa paka kazi ya kulinda maziwa, tena kwenye siku ambayo Mbweku kaipanga ndio siku yake ya kutoroka. Himahima kwa ustadi mkubwa akavunja kioo cha gari upande wa abiria na kuzama ndani ya gari hilo la Recho. Akawasha kurunzi yake ndogo na kuanza kufanya speksheni. Akaona mkoba wa Bosi Recho umetuna ameusahau ndani ya Korando lake, akiwa ameuacha chini ya sehemu ya makanyagio ya miguu yake. Bila ajizi akaufungua mkoba huo na kukutana na pochi nene ya ngozi iliyotuna, akashawishika kuifungua pia kujua kilichomo. Alipoifungua tu, akakodoa macho yake kwa mshangao, yakatamani yasifunge tena. Aliziona noti nyingi sana zimepangwa kiufundi mkubwa ili ziweze kuenea kwenye pochi hiyo. Moyo wa Mbweku Jr ulilipuka kwa furaha sheshe huku akijiona ana bahati ya mtende ya kuua ndege wawili kwa wakati mmoja. Mbele ya pesa kila binadamu ana mate ya fisi, hadiriki tamu na daima hutaka zaidi na zaidi, ndio maana mabilionea duniani kila siku wanaanzisha vitega uchumi vipya hawatosheki.

Malengo sasa yakawa ni kumtorosha Deborah na pia kujilipa nusu hasara kwa pesa alizokwapua Recho nyumbani kwa Bosi Minja. Kwenye hilo fuba la pesa alilolifukutua kwenye pochi zilikuwa ni noti mchanganyiko pesa za kigeni na za madafu. Bila kulazia damu, Mbweku Jr akazichukua zote na kuzisunda vizuri ndani ya chupi yake ya kubana aina ya V. I. P. Akaendelea na upekenyuzi wake kwenye droo za gari mpaka akaliona zigo la vibali vya kuingia ndani ya jengo.

Akachukua vibali viwili vilivyokuwa vimeshasainiwa tayari na Recho himahima akashuka garini, huku akiombea Mungu wasitoke mapema Recho na hawara yake Beka. Kilichokuwa kinampa ujasiri ni kuwa kwa kawaida wakiingia kujivinjari wapendanao hao huwa wanatoka Alfajiri, hivyo atakuwa tayari kishatoroka zake Baada ya kufanikisha zoezi lile. akiwa bado Mbweku Jr anachukua doria kule nje anazunguka huku na kule. Kila wakati akiangalia saa yake ya mkononi kama kuna kitu anakisubiria kwa hamu. Ilimchukua kama dakika 45 kitu alichokuwa anakisubiria kwa hamu kikatokea.

Gari nyeupe aina ya Corolla, ikafika pale kwenye danguro la siri na kusimama nyuma ya gari la Recho. Kabla hajapiga honi, Mbweku Jr akamuwahi pale pale mbio mbio dereva wa lile gari, na kwenda kugonga kioo cha mlango wa dereva. Dereva wa Corolla lile baada ya kumuona Mbweku Jr akiwa ndani ya sare za kazi akatambua ni mlinzi, bila hofu yoyote akashusha kioo cha gari lake na kuongea. "Hellow...habari yako, mimi daktari nimekuja kwa mgonjwa wangu yule dada wa jana, kibali changu hiki hapa...!" aliongea yule daktari kwa kujiamini, akiwa ameuvalisha uso wake tabasamu pana huku akitoa mkono wake wa kulia nje ya dirisha akionyesha kibali chake. Hilo ndio likawa kosa yule daktari, Mbweku Jr alizuga kama anakipokea kibali kile, akafanya shambulizi la ghafla na la kuumiza mno. Daktari akashtukia tu amekabwa kabali nzito ya mbao shingoni mwake. Akajaribu kufurukuta huku na kule kujitoa kwenye mikono ya Mbweku Jr, lakini ikawa ni kazi bure, mpaka akalegea na kutulia.

MBweku Jr alikuwa na mshipa wa nguvu wa kuzaliwa nao, mikono yake imekomaa utasema anakula saruji. Mbweku Jr alipojiridhisha kuwa daktari yule ameshazimia, mbele hayuko na nyuma hayuko, akafungua mlango wa dereva na kutoa koti refu jeupe la kidaktari lililokuwa limetundikwa kwenye siti ya abiria kiti cha mbele. Kisha Mbweku Jr akajongea mafichoni kwa haraka alipoficha begi lake la safari umbali wa kama meta 10 kutoka lilipoegeshwa gari la daktari. Akabadilisha nguo zake za sare za kazi na buti za kazi na kuvaa za nguo zake za kawaida na viatu vyake kisha akatinga juu yake koti la kidaktari aliloiba. Akachukua pia kamba ndefu na ngumu yenye kifundo cha chuma kutoka kwenye begi lake na kuitia kwenye mmoja wa mifuko ya koti lile la kidaktari. Akajirekebisha koti alilovaa na kujiaminisha kuwa yupo vizuri sasa, anaweza kuingia ndani ya geti kuelekea kwenye jengo kumuokoa Deborah.



Mbweku Jr alifanikiwa kuwavuka walinzi wote huku akiwa tayari ameshaelekezwa wapi alipo Deborah. Alikuwa anaisikia sauti ya mbwa kwa mbali akibweka woo woo bila kufahamu kuwa huyo ni mbwa wa Mr.Lorenzo, akapuuzia. Alileta ujanja kwa mmoja wa walinzi kuwa amesahau chumba Ambacho Deborah amehifadhiwa. Mbweku Jr alikuwa amewatangulia kuingia ndani ya mjengo akina Jimmy, Mr.Lorenzo na genge lao kwa mpishano wa kama takribani nusu saa. Alikuwa anazipanda ngazi huku akiwa anakimbia pukutu pukutu mithili ya farasi wa mashindano akiwa na hamu ya kumuokoa dada yake Deborah. Kasheshe jipya likaibuka kwa Mbweku Jr alipokifikia chumba cha Deborah. "Vipi Daktari mbona unahangaika, funguo wako upo wapi? "aliuliza mmoja wa walinzi huku anamfuata Mbweku Jr kwa kasi ya ajabu huku akiiweka silaha yake vizuri. Mbweku Jr kijasho chembamba cha uoga kikaanza kumvuja, alijiona kabisa amekamatika kizembe sana. Mawazo yake yalikuwa huenda mlango utakuwa wazi au funguo upo hapo hapo mlangoni, kumbe daktari alikuwa na ufunguo wake maalumu wa kuingilia. "Kama umeupoteza wako sio shida, twende kwa Bosi Recho tukamgongee chumbani kwake ukamuelezee akuazime wa kwake, maana kiongozi wao hawa wanawake Miriam amerudi nyumbani kwake leo halali hapa, yeye pia ana ufunguo wake" aliongea yule mlinzi baada ya kumfikia Mbweku Jr kwa ukaribu zaidi. Kusikia kuwa anataka kupelekwa kwa Bosi Recho, moyo wa Mbweku Jr ulianza kudunda kwa uoga kama saa kweche ya mezani, akijihesabu kabisa ameshakamatwa. "OK...wazo zuri sana, twende kwa Bosi Recho....!" Mbweku Jr akajitutumua kuongea kiujasiri huku akiuweka mkoba wake vizuri na kumfuata nyuma nyuma yule mlinzi mwenye silaha akijitia kupiga miluzi. Mbweku Jr hakuwa na uthubutu katu wa kumvamia yule mlinzi kwa sababu hakuwa na ujuzi wowote wa kutumia silaha ya moto. Alichopanga ni kuwa kuwa akipata upenyo tu atundike miguu mabegani kuepusha masaibu yatakayomsibu toka kwa Recho pindi akimgundua kuwa sio yule daktari wake aliyemuagiza kumchunguza afya Deborah. Kadri alivyokuwa yule mlinzi anapunguza mwendo kuashiria kama vile wamekaribia chumba alichokuwepo Recho na hawara yake katika roshani ileile aliyohifadhiwa Deborah, matumbo ya Mbweku Jr yalianza kumchezacheza huku akizidi kuzama katika bahari ya luja akiwazia mustakabali wake. Mungu si Athumani, Mbweku akajitia kuweka mkono wake wa kushoto kwenye mfuko wa koti lake la udaktari. Akashtuka mshtuko wa furaha kwa mbali, aligusa kitu kigumu kama chuma mfano wa ufunguo. "Aaaaah....tumehangaika bure kumbe funguo niliusweka ndani ya koti langu bwana...!" aliongea kwa sauti ya juu Mbweku Jr na kujilazimisha kujichekesha. " Basi hamna tatizo kaendelee na kazi maana hapa mwenye nilikuwa naogopa kumsumbua Bosi Recho maana kumuamsha usingizini angekuwa moto balaa" alijibu yule mlinzi huku akianza kushika ngazi za kushuka roshani ya chini kama vile kuna kitu anafuatilia. Mbweku Jr akaanza tena kurudi chumbani kwa Deborah kwa mwendo wa kasi. Kwa upande wake Deborah alikuwa ameshashtuka toka kwenye usingizi wa mang'amung'amu unaotokana na kuzidiwa na kileo pia na ndoto za kutisha za kifo cha baba yake mzazi. Aliposhuka alijikuta amepiga makelele huku akiwa tayari ameshajikojolea kitandani. Ndoto ya kifo cha kikatili cha baba yake alikuwa anaiota mara nyingi akiwa na msongo wa mawazo katika usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili. Haraka haraka akaamka akaenda kubadilisha nguo zake za mikojo msalani na kutoa mashuka kitandani na kutandika mapya. Akavaa nguo zingine alizozichukua kwenye kabati kisha akarudi kitandani pake Kichwa kilikuwa kinambangua vilivyo kwa maumivu makali, huku akiwa anajutia kwa kitendo chake cha kunywa pombe. Hakuwa na uwezo wa kubadili kitu, daima asiyeangalia jambo mwanzoni kwa kulifanyia upembuzi yakinifu kabla ya kulifanya huishia ningalijua. Akaanza kuogopa kutumia kinywaji cha aina yoyote ndani ya chumba kile. Alikuwa ameshafungiwa ndani kama mwari kwa zaidi ya saa 24 bila kuangaziwa na jua la nje ya nyumba. Akiwa nae kichwani kazama kwenye bahari ya luja pale kitandani akiyawazia maisha mapya ya ukahaba anayotarajia kuyaanza muda sio mrefu, ghafla bin vuu akashtukia kelele za ufunguo unaogombana na kitasa cha mlango wa chumba ili kuruhusu mlango kuwa wazi mtu apate kuingia ndani. Akakurupuka haraka haraka na kukaa pembeni ya kitanda, macho yakitazamia kukutana na Miriam, mwanamke aliyejitambulisha kwake kama ni kiongozi ndani ya ule mjengo. Alipanga kutaka kupambana na Miriam kwa hali na mali mpaka aweze kutoka ndani ya jengo lile. Hakuwa tayari kufanywa mboga kirahisi labda awe maiti. Kwa mshangao mkubwa akamuona daktari anaingia ndani ya chumba kisha akaufungua mlango kwa ufunguo. Deborah akazidi kuchanganyikiwa, huku akijiuliza maswali lukuki yasiyo na majibu kuhusu huyu daktari. "Nani kakuambia mie mgonjwa, mie sikubali nataka kutoka humu sitaki kuendelea kukaa humu....!" alijikuta Deborah amepata nguvu za kuongea kwa sauti ya juu huku akianza kulia kilio cha kwikwi. "Shiiiiiii.....! Nyamaza Deborah nimekuja kukuokoa usiwe na hofu hata chembe na mimi, upo sehemu mbaya sana, utapoteza muelekeo wako wote kimaisha ukiendelea kukaa humu...!" aliongea Mbweku Jr akiwa ameuegemea mlango wa chumba kile. Mbweku Jr akaanza kuvua koti lake alilovaa na kulitupa pembeni huku akitoa kamba yake aliyoikusudia kumuokolea Deborah. "Samahani...wewe ni nani kwani, Askari umetumwa na mama Koplo Marieta kuja kuniokoa?" aliuliza Deborah kwa furaha akiwa hayaamini macho na masikio yake. Mbweku Jr hakumjibu kitu, akaanza kupambana na kuvunja dirisha, mpaka akafanikiwa kwa utundu wake. "Njoo haraka, jitahidi kugangamala utakapokuwa unashuka na hii kamba mpaka chini ya jengo, ukicheza tu umevunja miguu au kifo hili jengo ni refu sana" alitoa amri ya kijeshi Mbweku Jr akiwa hana muda wa kupoteza kabisa na kumpa tahadhari Deborah ya usalama wake. Akambeba Deborah na kumpitisha dirishani kisha akamshikisha kamba ya kushukia chini ya jengo. Wakati Deborah anajiandaa kuanza kushuka, zikaanza kusikika sauti za kuogofya. "Paaah.....Paaaah.....Paaaaah....", "Maamaaaaah.....nakufaaaaaaah..." Deborah alipiga kelele yenye sauti kubwa kisha akanyamaza akiwa bado anaserereka na kamba ile, baada ya kusikika kwa vishindo vya sauti za risasi mfululizo ndani ya lile jengo. Mbweku Jr nae hakujivunga kwa kutumia kipande kile kile cha kamba aliyokuwa anaitumia Deborah na yeye akaanza kushuka nayo kabla ya kugundua kuwa kamba hiyo imekatika haijafika mpaka chini, hivyo lakini akashuka hivyo hivyo kabla ya kukutana na janga jipya kabla hajatua chini. Kilisikika kishindo kizito sana cha baadhi ya sehemu za jengo lile la kifahari kubomoka vibaya kutokana na mabomu yaliyolipulika kwenye lile jengo. Vishindo hivyo vya sauti za risasi na mabomu likazusha tafrani na taharuki kubwa isiyotegemewa na wakazi wa Sinza usiku huo wa maneno. Mayowe na makelele ya kuomba msaada yakawa yanasikika kila kona ya kitongoji cha Sinza kilichofikiwa na sauti ile ya kutisha katika pindapinda la usiku wa manane tulivu.


Asubuhi na mapema jua lilipochomoza, watu walikuwa wamejazana pomoni ndani ya nyumba mpaka nje ya ukuta wa fensi, wa danguro la siri lililokuwa likimilikiwa na Recho. Walikuwa wamejikunyata wakiwa na hali ya huzuni na majonzi kutokana na tukio la kutisha lililotokea usiku wake. Maelfu ya watu hao walitoka pande mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam, na wengine walikuwa bado wanaendelea kumiminika kama siafu, tokea walipopashwa habari kupitia kwenye redio, televisheni na wale Vidinga popo juu ya kutokea kwa milipuko ya mabomu na milio ya risasi kwenye danguro hilo la siri huko Sinza Kijiweni. Wanajeshi wa jeshi la wananchi "JWTZ" na polisi wote kwa pamoja walikuwa wanashirikiana kuhakikisha hali ya usalama inarejea eneo hilo kwa haraka. Helikopta za jeshi nazo zilikuwa zinaruka angani kujaribu kuchunga na kuimarisha hali ya usalama wa eneo hilo. Kwenye milipuko hiyo iliyotokea usiku wa manane, watu kadhaa walisadikiwa kufariki hapo hapo na wengine kujeruhiwa vibaya. Hakuna mkazi wa Jiji aliyependa kusimuliwa tukio hilo la kihistoria katika nchi ya Tanzania, alitaka akashuhudie mwenyewe kwa macho yake kisanga hicho, ikiwa ndio mara ya kwanza kusikika uhalifu wa kulipua jengo unafanyika. Siku hiyo Sinza kutokana na hekaheka zake iligeuka kama sehemu zenye machafuko huko Darfur nchini Sudani na Kandahar nchini Afghanistani. Wale wakazi wenye roho nyepesi kama karatasi kwa uoga, tayari zamani walishakimbilia Stendi ya Kisutu kwenda kutafuta usafiri wa kurejea kwenye Mikoa yao, huku wakienda kusikilizia hali ya usalama irudi kuwa nzuri. Watu walikuwa wamejikusanya vikundi vikundi vidogo vidogo vya midahalo wakibadilishana mawazo na kuhadithiana namna uhalifu huo ulivyotekelezwa. "Penyenye nilizozipata ni kuwa walinzi 6 wa ndani ya jengo wamefariki, pia mlinzi wa getini mmoja tu ndio kapona mwingine mwili wake haujaonekana inasadikiwa amefariki kwa kufunikwa na kifusi" aliongea Habari kauzwa aliyekuwa anajifanya ana siri nyeti za tukio hilo. Umahiri wake wa kupangilia maneno ukawafanya watu wameguke vipande vipande kutoka kwenye vikundi vyao kwenda kumfuata yeye waweze kupata nyepesi nyepesi. "Inasemekana hili ni danguro la siri linalotumiwa na Vigogo wa nchi, mama mmiliki wa hili danguro nae ni miongoni mwa majeruhi hao wenye hali mbaya. Wasichana wasiopungua 20 nao wameaga dunia, waliosalimika ndio wametoa siri zote za kilichokuwa kinafanyika kuhusu utumwa wa ngono. Polisi mpaka sasa inamshikilia mzungu mmoja anaitwa Mr Lorenzo ikimhusisha na tukio hili ambaye ni hawara wa siku nyingi wa huyo mama mjengo. Haki ikitendeka wataumbuka wengi, kuna wanawake watumishi wa serikali na taasisi zake, watumishi wa Mabenki nao walikuwa wanakuja humu kwenye danguro kujipatia kipato haramu cha ziada. Wote majina yao yametajwa na mkubwa wao anaitwa Miriam ambaye nae mpaka sasa yupo mikononi mwa polisi anasaidia uchunguzi" alizidi kubwabwaja huko jamaa maneno kedekede yenye uzandiki na chumvi ndani yake ili kunogesha simulizi zake kwa dhumuni tu ya kuvutia hadhira yake inayomsikiliza. Ghafla fujo na varangati zikaanza kuibuka tena upya ndani ya eneo lile, watu wakaanza kukanyagana na kuumizana baada polisi ya kuanza kuwatawanya watu waliokuwa ndani ya jengo na kuwataka watoke nje kabisa ya fensi. Kikosi cha uokaji kilikuwa ndio kimefika muda sio mrefu ili kutafuta miili ya waliofunikwa na vifusi, hivyo walihitaji utulivu katika utendaji kazi wao. Waandishi wa habari wa televisheni za 'DTV', ITV zote za Jijini Dar es Salaam na 'TVZ' ya Zanzibar hawakubaki nyuma nao, walitingwa na kazi ya kurekodi video na kupita kufanya mahojiano na watu mbalimbali waliojitokeza kwenye umati ule ili wapate kuwahabarisha watazamaji wao. Wandishi wa habari wa redio na magazeti nao walichakarika huku na kule ili mradi nao wapate habari ya kuihabarisha jamii. Daktari aliyeshambuliwa na Mbweku Jr mpaka kuzimia nae alikuwa anategemewa kuwa msaada mkubwa kwa polisi pindi atakapopata nafuu huko hospitalini alipokimbizwa baada kukutwa yupo mahututi. Makachero wa polisi walikuwa nae bega kwa bega ili akizinduka tu awape habari ya kilichomkuta eneo lile. Mr.Lorenzo alikuwa na moyo wa kitoto sana, ndio aliyewapa mabomu ya kutega vijana wa Jimmy walipoingia ndani ya jengo kuruka ukuta. Lengo lilikuwa iwapo atashindwa lengo lake la kumuadabisha Recho lazima alitie hasara jengo hilo lisiweze kumfaidisha Recho maisha yake yote. Hivyo kilichokea yule mlinzi wa jengo aliyekuwa amefuatana na Mbweku Jr wakaachana karibia na mlango wa chumba alichomo Bosi Recho alipokuwa anashuka chini ya jengo ndio akakutana uso kwa uso na akina Mr.Lorenzo, Jimmy na wenzake. Ndipo mapigano kwa njia ya kurushiana risasi yakaanza kusikika. Beka mpenzi wa siri wa Bosi Recho kusikia milio ile ya risasi akajua majambazi wamevamia jengo nae akatoka nje ya chumba na silaha kwenda kuongeza nguvu. Vurugu mtindo mmoja ya vilio vya wanawake ndani ya jengo lile wakitaka kujiokoa kwa hali na mali vikamfanya Mr.Lorenzo ashikwe na taharuki, akafanya maamuzi ya kulipua mabomu yaliyotegwa kuzunguka jengo kwa kutumia saa yake ya mkononi, akihofia Recho asije kuchurupuka kwenye mtego wake. Polisi wa doria nae kusikia vishindo hivyo nao wakatia timu na kulizingira jengo zima na kufanikiwa kumtia mbaroni Mr.Lorenzo na mshirika mmoja wa Jimmy, huku Jimmy na mwenzake wakipoteza uhai kwenye mashambulizi ya risasi. Kizungumkuti na kitendawili kikabakia kwa Mbweku Jr na Deborah, je walifanikiwa kutoroka nje ya jengo au ni miongoni mwa wahanga waliofunikwa na vifusi. Mbweku Jr alitajwa na mlinzi mwenzake aliyesalimika kuwa walikuwa wanalinda wote, na daktari baada ya kuzinduka hospitalini alimtaja mlinzi wa nje ya jengo ndio aliomkaba shingo nusura kufa. Hivyo Mbweku Jr nae akawekwa katika orodha ya watuhumiwa wanaotafutwa kwa udi na uvumba kama yupo hai ili aunganishwe kwenye kesi hiyo ya mauaji ya halaiki. Mawazo ya polisi ni kuwa Mbweku Jr huenda nae ni mshirika wa Mr.Lorenzo katika uhalifu huo. Recho alikuwa mahututi amepoteza fahamu katika chumba maalumu cha wagonjwa mahututi 'ICU' anapumulia mashine akipigania uhai wake, haja kubwa na ndogo zote anajisaidia hapo hapo.

SURA YA KUMI NA TATU
Mr.Martin Tenga na vijana wake wabebaji mihadarati walisota kwenye rumande maalumu inayoitwa 'Casa Circondariale' wakiwa wanasubiria hukumu yao. Watuhumiwa wanaoshikilia kwenye 'Casa Circondariale' nchini Italia kwa kawaida huwa wanasongamana, hivyo kila siku Mr.Martin Tenga na vijana wake walikuwa kila siku wanaomba kwa Mungu hukumu yao ipitishwe ili wahamishwe kutoka kwenye jela hizo. Ndani ya 'Casa Circondariale' kila chumba walikuwa wanalazwa kwenye chumba kidogo watu 6. Walikuwa wanachanganywa pamoja na wahamiaji haramu wanaozamia nchi za Ulaya kupitia nchi ya Italia. Baada ya kesi yao kuunguruma kwa muda wa miaka 3 hukumu yao ikatoka. Mr.Martin Tenga akahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, huku vijana wake wakifungwa kila mmoja miaka 20. Baada ya kifungo hicho wakahamishiwa kwenye jela maalumu za wafungwa zinazoitwa 'Carcere Giudiziaro'. Huko kidogo kukawa na unafuu, hamna msongamano wa wafungwa. Gereza alilofungwa Martin na vijana wake lilikuwa linaitwa 'Museo del Carcere "Le Nuove' likiwa lipo Jijini Turin. Ndani ya gereza hilo ilikuwa ruksa kutembelewa na ndugu, jamaa na marafiki kila siku saa 9:00 alasiri. Kwa upande wa chakula walikuwa wanalishwa vyakula vya Kitaliano kama Resotto, Pasta na baadhi ya siku wanapikiwa Lasagna. Mwanzoni ilikuwa ni ngumu sana kuzoea vyakula vya Kitaliano hasa ukichukulia Mchaga alishazoea kula ndizi, mchemsho na nyama za kuchoma. Pia ndani ya gereza hilo kulikuwa na jiko la kupikia la gesi kwenye kila chumba hivyo mfungwa alikuwa anaruhusiwa kujipikia chakula chake anacholetewa na ndugu zake. Hivyo maisha ya jela hayakuwa na ugumu wa maisha kama zilivyo jela za nyumbani Tanzania. Kikubwa walichokuwa wananyimwa ni uhuru wa kufanya mambo yao binafsi. Mr.Martin Tenga kila wakati alikuwa anazama katika lindi la mawazo hasa akifikiria kuwa atakapomaliza kifungo chake atakuwa mzee wa zaidi ya miaka 60, je ataenda kuanzaje maisha ya mtaani huko Tanzania. Alijua fika huko Kenya na Tanzania kila kitu chake katika vitega uchumi vyake vitakuwa vimeshafujwa. Hivyo mawazo makubwa yalikuwa yanamsonga kuwa anaenda kuwa mmoja wa wazee wa mitaani. Mzee ambaye atakuwa hana makazi ya kuishi, hana uhakika wa mlo wake wa siku, pia hana uhakika na matibabu yake pindi atakapougua. Moyoni akawa anaomba siku za kumaliza kifungo chake ziende taratibu kwa mwendo wa kobe, maana huko mbeleni ilikuwa ni giza tu. Kingine kilichokuwa kinampa mawazo ni kitendo cha kukosa mtoto katika maisha yake ambaye angeweza pengine kuwa msaada mkubwa sana katika maisha yake ya uzeeni. Akawa anajutia kitendo chao cha Kifirauni walichokifanya na hawara yake Recho cha kumtelekeza mtoto wao mlemavu, Pesambili kwenye nyumba watoto yatima kule Kenya. Kwa muda waliomtelekeza Pesambili kule Jijini Nairobi, Kenya kwa sasa alikuwa anaweka dhana kuwa sasa atakuwa ghulamu mkubwa aliyebaleghe tayari wa zaidi ya miaka 15. Baada ya kupita miaka 6 tokea afungwe jela, Mr.Martin Tenga akapokea mgeni, mfungwa mwenzake kwenye chumba chake cha gereza. Mfungwa huyo mpya hakuwa mwingine bali ni Mr.Lorenzo. Mr.Lorenzo hukumu yake huko nchini Tanzania kutokana na kosa lake la kulipua jengo la roshani ya Recho na kusababisha mauaji ya watu lukuki, alihukumiwa kifungo cha maisha jela. Pia kosa la pili la kukutwa na filamu za ngono za wasichana mbalimbali wa Afrika alihukumiwa kifungo cha miaka 15. Hivyo adhabu hizo mbili zikawa anazitumikia sambamba. Balozi wa Italia nchini Tanzania akaongea na wizara ya mambo ya ndani kuhusiana na suala ya kumhamisha Mr.Lorenzo akatumikie kifungo chake nchini kwake Italia. Wizara ya Mambo ya Ndani, haikuwa na kipingamizi, ikaruhusu Mr.Lorenzo asafirishwe mpaka nchini Italia. Ndipo Mr.Lorenzo akapelekwa gereza alilofungwa Mr.Martin Tenga, na wakapangiwa chumba kimoja. Hawakuchelewa kujenga uswahiba baina yao hasa baada ya kuwa wote wanaongea kiswahili na pia wameshawahi kuishi Tanzania. Ujio wa Mr.Lorenzo ukawa ni neema kwa Mr.Martin Tenga, kutokana na Mr.Lorenzo kuletewa chakula kila wiki cha kupika toka nyumbani kwao. Hivyo wakawa wanashirikiana katika kupika kwa pamoja na kila kitu wakifanya kwa pamoja. Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza, hawa maswahiba wapya wawili, Mr.Martin Tenga na Mr.Lorenzo walikuwa ni mtu na shemeji yake, kwa maana ya kwamba Mr.Martin amezaa mtoto na Recho ambaye ni dada wa damu wa Mr.Lorenzo. Mtoto mwenyewe wa Mr.Martin na Recho ndio huyu Pesambili ambaye anaishi nyumbani kwa Mr.Lorenzo.




Ujio wa Mr.Lorenzo ukawa ni neema kwa Mr.Martin Tenga, kutokana na Mr.Lorenzo kuletewa chakula kila wiki cha kupika toka nyumbani kwao. Hivyo wakawa wanashirikiana katika kupika kwa pamoja na kila kitu wakifanya kwa pamoja. Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza, hawa maswahiba wapya wawili, Mr.Martin Tenga na Mr.Lorenzo walikuwa ni mtu na shemeji yake, kwa maana ya kwamba Mr.Martin amezaa mtoto na Recho ambaye ni dada wa damu wa Mr.Lorenzo. Mtoto mwenyewe wa Mr.Martin na Recho ndio huyu Pesambili ambaye anaishi nyumbani kwa Mr.Lorenzo.

Wakati Pesambili anasubiria kujiunga na masomo ya Chuo Kikuu baada ya kumaliza elimu ya kidato cha sita, akakabidhiwa na babu yake jukumu rasmi la kupeleka mahitaji ya baba mlezi wake, Mr.Lorenzo. Hapo ndio kwa mara ya kwanza tokea kuzaliwa kwake, Pesambili akaanza kuonana na baba yake mzazi uso kwa uso bila kutambuana.

Pesambili, tayari majibu yake ya mitihani ya kidato cha sita yalishatoka. Alifaulu kujiunga na masomo Utabibu katika Chuo Kikuu cha Turin, 'University of Turin', alikuwa anasubiria tu muhula mpya wa masomo uanze2 akaanze maisha mapya ya Chuo Kikuu. Alichaguliwa kujiunga na kitivo cha 'Medicine and Surgery' akiwa mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika mitihani ya kumaliza kidato cha 6. Pesambili alikuwa na furaha sana kufanikiwa lengo lake la kusomea Udaktari likiwa linakaribia kutimia.

Pesambili alikuwa na ndoto kubwa ya kuwa Daktari Bingwa wa Upasuaji, kutokana na huduma aliyopewa yeye utotoni ya upasuaji mpaka akaweza kutembea. Akaweka adhima na nia ya kuwa akiwa mkubwa nae atasomea Udaktari wa Binadamu ili nae aje kutoa huduma kwa wahitaji mbalimbali kama alivyosaidiwa yeye. Alipanga akimaliza Chuo Kikuu akafanye kazi katika nchi yoyote ya Afrika, hiyo ndio iwe sadaka yake kwa Mungu, aliyemtoa kwenye kituo cha watoto yatima na kumleta Ulaya. Nchi aliyoipanga kwenda kujitolea kufanya kazi, ni ile ambayo itakuwa ni ya ni ya asili ya wazazi wako. Kitu ambacho kilikuwa kinamuumiza kichwa ni kuwafahamu ndugu zake kwa upande wa baba na mama.

Taarifa aliyowahi kupewa na Babu yake wa kuasili, baba mzazi wa Mr. Lorenzo ni kuwa alichukuliwa kwenye kituo cha yatima katika moja ya nchi za Afrika, hivyo moja kwa moja mawazo yake yakampa kuwa wazazi wake wameaga dunia ndio maana alipelekwa kwenye kituo cha yatima. Bahati mbaya zaidi, Pesambili alikuwa hajijui jina lake hilo la Pesambili alilopewa na Bibi yake mzaa mama. Mr.Lorenzo alipomuasili tu, akambatiza tena upya na kumpa jina jipya la 'Trezguet Lorenzo', na hilo ndio jina alilolitumia kusomea shule. Hakuwa analipenda kabisa jina hilo la kizungu kwa asilimia 100%, ila hakuwa na jinsi. Alizidi kuchukia kuishi nchini Italia hasa kutokana na kuibuka wimbi jipya la ubaguzi wa rangi lililoanza kuibuka kwa kasi. Kuna wakati alikuwa akiingia kwenye Daladala, abiria wazungu wanampisha siti aketi peke yake.

Akikatisha mitaa ya wahuni wanambwekea sauti za nyani. Hali ambayo haikumkatisha tamaa bali ilimjenga kisaikolojia na kumshajiisha afanye bidii katika masomo ili akaungane na Waafrika wenzake kujiletea maendeleo yao binafsi hasa katika uboreshaji wa sekta ya Afya.
Kitendo cha kwenda mara kwa mara kule gerezani kumtembelea baba mlezi wake Mr.Lorenzo, Pesambili akajikuta anajenga mazoea na Mr.Martin Tenga pia. Kama waswahili wasemavyo damu ni nzito kuliko maji, alijikuta tu katokea kumpenda kwa kumsafishia nia bila kufahamu kuwa huyo ndio baba yake mzazi, huku yeye akijua ni rafiki wa Mr.Lorenzo.

Lakini kabla hawajazoeana vya kutosha na baba yake kidudu mtu kikaingilia kati. Wafungwa wote wa gereza lile la 'Museo del Carcere "Le Nuove' wakasambaratishwa kwa kutawanywa magereza mbalimbali ya nchini Italia. Hiyo ilitokana na taarifa za kiintelijinsia toka kwa mashushushu wa serikali kunusa harufu ya mpango wa kundi la Kimafia 'Ndrangheta' kutaka kutorosha gerezani baadhi ya washirika wao. Na kwa kuwa Mr.Martin Tenga alikuwa ni mshirika wao, akahisiwa nae alikuwa kwenye orodha ya wafungwa waliokuwa wanahitaji kutoroshwa gerezani, hivyo akahamishiwa gereza la siri lenye ulinzi mkali saa 24.

Pesambili nae kwa upande wake muda wa kujiiunga na Chuo Kikuu tayari kwa kuanza masomo yake ya Udaktari ukatimu. Ndio ikawa kimoja haonekani tena mitaani Jijini Turin, ametingwa na shule huku mwenyewe akitaka asijiingize kwenye jambo lolote litakalomtoa nje ya masomo. Darasa lao wanaosomea fani ya Utabibu lilikuwa lina wanafunzi 100, huku ngozi nyeusi ni Pesambili peke yake. Mwanzoni wanafunzi wenzake na baadhi ya Wahadhiri walikuwa wanamdharau wakichukulia kuwa mtu mweusi hana anachokiweza zaidi ya kupenda ngoma na starehe. Hakuwajali yeye akawa anajipanga kuwaonyesha kazi darasani.

Masomo yalivyoanza kuchanganya vizuri na kuanza Mitihani kila Mwanachuo alimheshimu na kumhusudu Pesambili. Kila Mtihani alikuwa anapata maksi kuanzia asilimia 90% kwenda juu kwenye masomo yote muhimu kwa daktari kama Anatomia 'Anatomy', Fiziolojia 'Physiology' na mengineyo. Umahiri wake kwenye masomo ukamfanya awe maarufu Chuo kizima kuanzia Wanachuo mpaka Wahadhiri wote.

Chuo tayari kilishaanza kumtongoza Pesambili kwa kumpa ahadi za mshahara mnono na marupurupu ya kutosha kama atakubali kubakia Chuoni hapo awe Mhadhiri pindi akimaliza masomo yake. Pia hospitali mbalimbali kubwa barani Ulaya walishaanza kusikia sifa zake nao wakaingia kwenye mkumbo wa kumgombea Pesambili. Wote hao Pesambili aliwaruka kimanga na kuwakatalia kuwa hayupo tayari kuingia makubaliano na mtu yoyote mpaka atakapomaliza masomo yake.

Maajabu ya kipekee kwa Pesambili ni kuwa usiku alikuwa kwa baadhi ya siku lazima amuote usingizi baba yake mzazi Mr. Martin Tenga, huku akilini akijiaminisha kabisa kuwa sio sura ngeni kabisa machoni mwake. Alikuwa kila akijaribu kuvuta hisia za kumbukumbu zake kuwa wapi alishawahi kuonana na mfungwa mwenzake wa baba yake mlezi, akili ilikuwa inagoma kabisa kukumbuka. Lakini pia bado suala la kutokujua asili yake na ya wazazi bado lilikuwa linamtafuna Pesambili. Siku alikuwa anaona zinachelewa za yeye kumaliza Chuo ili alishughulikie rasmi suala la kuitafuta asili yake na pia kuulizia ni gereza gani Mr.Martin Tenga amefungwa akamtembelee na kumdadisi vyema, huenda akafahamu walionana wapi kwa mara ya mwisho kabla ya kukutana tena gerezani.

Chambilecho siku hazigandi, miaka 5 ya kumaliza masomo kwa Pesambili ikawa imetimu, akachaguwa kwenda kufanya mazoezi vitendo katika Jiji la 'Barletta', moja ya Jiji lenye wakazi masikini nchini Italia. Hayo ndio yalikuwa mapenzi ya Dr. Pesambili au ukipenda Dr.Trezguet Lorenzo kwenda kutoa huduma kwa watu masikini, ambao shukrani yao kwake itakuwa ni kumuombea dua kwa Mungu.


Gandhi Square, eneo maarufu hapa mitaa ya Carlton Centre ndani ya Jiji la Johanesburg ndio ulikuwa moja ya mtaa maarufu sana kwa Mbweku Jr akiwa ameshakata miaka ndani ya Jiji hilo tokea atue nchini Afrika ya Kusini. Ulikuwa ni mtaa ambao Watanzania wengi utawaona wanazurura mitaani. Si ajabu ukakuta kwenye mtaa mzima watu wote wanaongea kiswahili. Haya yalikua maeneo duni sana, machafu, yananuka kila aina ya harufu. Wabongo wengi walikua ni vibaka, wanategeshea barabarani kwenye alama za pundamilia 'zebra cross' ambapo msongamano wa watu ni mkubwa sana. Kisha wanawazonga watu, na kuwakwapulia mali zao. Wadada na wamama walikua wanalizwa sana vitu vyao vya thamani kama simu za mkononi, fedha na vipochi vyao. Wengi wa hawa wabongo walikua kama mateja, wamechoka sana wanapolala ndio hapo hapo wanapokojoa.


Mbweku Jr alikuwa ameshatua nchini Afrika ya Kusini kiwepesi kabisa kuliko matarajio yake. Aliponea kifo kwenye tundu la sindano yeye na Deborah kwenye mlipuko wa mabomu katika jumba la Recho kule Sinza Kijiweni. Pia wakafanikiwa kuruka viunzi vya walinda usalama ambao walikuwa wanamsaka Deborah kwa kosa la kumuibia mfadhili wake Koplo Marieta. Usiku ule walikuwa wanawapita bila kusimamishwa barabarani tena wakiwa wanatembea mashimashi bila usafiri wowote tena kifua mbele bila kuogopa kitu. Deborah alikuwa anashangazwa sana kwanini watu wengine wanasimamishwa na kuhojiwa ila wao wanapita bila kuulizwa kitu chochote. Mbweku Jr alikuwa anatabasamu tu hana hata chembe cha hofu wala uoga wowote. Moyoni mwake mwake alikuwa anajua kila kitu kwanini inatokea vile hawakamatwi na wana usalama, mpaka akafanikisha mpango wake kabambe wa kutorokea nchini Afrika ya Kusini salama salimini huku akimuacha Deborah mikononi mwa rafiki yake kipenzi Timammy kwa ajili ya uangalizi wake wa kila kitu.

Mbweku Jr nae alikuwa ni miongoni mwa vijana hao vibaka wa mitaani, akiishi maisha ya kuungaunga na kubangaiza yasiyo na mbele wala nyuma. Nyumba ya kuishi alikuwa anakaa gheto na vijana wenzake kwenye chumba walichopangisha katika mtaa wa 'Polly Street', kulikuwa na jengo moja limechakaa kiasi, ndipo hapo maskamoni pake. Maamuzi yake ya kuja nchini Afrika ya Kusini licha ya ugumu wa maisha anayoishi hakuyajutia sana hasa kutokana na taarifa zake za msako kusambaa mpaka Afrika ya Kusini. Habari zilimfikia kuwa anasakwa kama nyara ya taifa na wana usalama kutokana na mlipuko wa jengo kule Sinza, na picha zake zimesambaa kila kona ya nchi kuanzia kwenye magazeti na mitaani, akituhumiwa kuwa ni mmoja wa walipuaji wa hilo jengo.

Aliishia kusononeka moyoni kutokana na kusingiziwa kitu asichohusika nacho kabisa hali ya kuwa ukweli wote alikuwa anaujua kinagaubaga kuwa sio mhusika wa tukio hilo. Moyoni alikuwa anahuzunika kuhusu yule daktari aliyemshushia kipigo, hakuwa na taarifa zake kama alisalimika au alipoteza uhai. Pia alikuwa hajui kama Bosi wake Recho aliokoka kwenye milipuko ile au nae alikuwa ni mhanga wa tukio hilo. Alichokuwa anajutia sana ni kitendo chake cha kukubali kuziacha pesa zote sufufu alizopora kwenye gari la Bosi wake Recho kwa rafiki yake aliyekuwa nae kijiwe kule Kigamboni, Timmamy.

Huyu ndio alimlaghai na kumtia ndimu vilivyo Mbweku Jr kuwa aache pesa zote atoroke yeye kama yeye bila kitu chochote huku akimtisha kuwa mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, askari wa uhamiaji wa Msumbiji ni wakatili na wababe, watampora kila kitu chake na kumuacha patupu. Wakaweka makubaliano ya mdomo na Timmamy kuwa hizo pesa awekeze kwenye biashara ya pamoja, na mwaka wowote atakaorudi salama watagawa mali nusu kwa nusu. Pia katika makubaliano alimuomba Timmamy kila akipata muda asikose kumtembea baba yake mzazi gerezani na kumpelekea mahitaji mbalimbali hasa ukichukulia ni mgonjwa hivyo anahitaji uangalizi wa karibu.

Timmamy ndio aliyemuelekeza Mbweku Jr afikie 'Polly Street' Jijini Johanesburg. Kwa jinsi Timmamy alivyokuwa anajinadi kijiweni na kujimwambafai kuwa anaishi maisha mazuri huko nchini Afrika ya Kusini, alichokikuta Mbweku Jr ni tofauti kabisa, ni kama mbingu na ardhi. Gheto moja walikuwa wanaishi watu 15 chumba kimoja, wakiwa wamepanga magodoro chini utasema wanalala matanga msibani. Alichokuwa hafahamu Mbweku Jr ni kuwa kuna ujanja na udanganyifu hali ya juu sana, katika uwanda huu wa kidigitari unaofanywa na Watanzania wanaoishi Ughaibuni. Kwa mfano kijana anayeishi nchi za Ulaya au Afrika ya Kusini anaweka picha zake nyingi kwenye mitandao kama Facebook, Instagram au Twitter akijionyesha mwenye tabasamu, afya murua, mavazi ya kisasa na vilevile mazingira safi na mandhari za kuvutia, akiwa ameegemea gari la kisasa ili tu kuwakoga vijana wenzake ambao kwa bahati nzuri kwake wapo nchini Tanzania, ambako mazingira ya Ughaibuni wanayaona kama mazingaombwe kwao. Mpaka wengine wanafikia hatua ya kujutia kuzaliwa nchini Tanzania na kutamani hata kama wangekuwa mbwa huko Ughaibuni lakini sio kuishi Tanzania. Lakini, ndani ya picha hizo kuna matatizo makubwa ambayo hakuna anayeweza kuyajua bila kusafiri na kwenda kuishi huko japo kwa muda mfupi.

Hayo ndio yaliyomkuta Mbweku Jr kwa jinsi alivyokuwa anatamani maisha ya Ughaibuni kutokana na hadithi za paukwa pakawa za kijiweni kule Kigamboni sasa zilikuwa hadithi hizo zinamtokea puani, anaula wa chuya. Akakuta maisha ya Ughaibuni yamejaa msongo wa mawazo ambao siyo wa kawaida na kuna wakati hasa wageni wanaingia katika majaribu mbalimbali hata ya kutaka kujinyonga kwa msongo wa mawazo. Ndipo alipojikuta Mbweku Jr na vijana wenzake toka Mataifa mbalimbali ya Afrika ambao wamezamia nchini Afrika ya Kusini na maisha kukuta yanakwenda mchafukoge na kujikuta wakijiingiza katika biashara hatari ya kuuza dawa za kulevya katika mitaa mbalimbalimbali ya nchi hiyo ili wapate kipato cha kujikimu.

Kwa wanaopenda maisha ya bwerere ili kukabiliana na ugumu wa maisha ya huko Ughaibuni haishangazi kumkuta kijana wa kiume wa Kitanzania akijivinjari na mke wake mwenye umri ambao ni sawa na bibi wa kumzaa mama au baba yake, hivyohivyo kwa msichana kumkuta akiwa na babu yake ukiuliza utaambiwa maisha na makaratasi. Makaratasi ni nyaraka za kukuwezesha kuishi kama raia wa ukiwa katika nchi za Ughaibuni na kupata mahitaji yote ambayo ni ya lazima kwa raia wa nchi hiyo, hasa unapokosa kazi kwa hiyo wengi huona kama wamepata aina fulani ya ushindi.




katika majaribu mbalimbali hata ya kutaka kujinyonga kwa msongo wa mawazo. Ndipo alipojikuta Mbweku Jr na vijana wenzake toka Mataifa mbalimbali ya Afrika ambao wamezamia nchini Afrika ya Kusini na maisha kukuta yanakwenda mchafukoge na kujikuta wakijiingiza katika biashara hatari ya kuuza dawa za kulevya katika mitaa mbalimbalimbali ya nchi hiyo ili wapate kipato cha kujikimu. Kwa wanaopenda maisha ya bwerere ili kukabiliana na ugumu wa maisha ya huko Ughaibuni haishangazi kumkuta kijana wa kiume wa Kitanzania akijivinjari na mke wake mwenye umri ambao ni sawa na bibi wa kumzaa mama au baba yake, hivyohivyo kwa msichana kumkuta akiwa na babu yake ukiuliza utaambiwa maisha na makaratasi.

Makaratasi ni nyaraka za kukuwezesha kuishi kama raia wa ukiwa katika nchi za Ughaibuni na kupata mahitaji yote ambayo ni ya lazima kwa raia wa nchi hiyo, hasa unapokosa kazi kwa hiyo wengi huona kama wamepata aina fulani ya ushindi.


Siku, wiki, miezi na miaka ikawa imekatika, sasa ilitimu miaka 10 taslimu, sawa na muongo mmoja tokea Mbweku Jr atoroke nyumbani, Tanzania. Sasa hamu ya kurudi nyumbani ikawa inamsonga kila wakati hasa ukichukulia maisha kila siku zinavyosonga yalikuwa yanakuwa magumu sana. Kulianza kuibuka vitendo vya chuki na ubaguzi 'Xenophobia' dhidi ya wageni nchini Afrika ya Kusini na kutikisa dunia. Vitendo ambavyo havikuweza kuvumiliwa na wapenda haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi duniani. Wageni walikuwa wanawindwa kwa ajili ya kuuliwa na kuharibiwa mali zao na raia wa nchi ya Afrika ya Kusini, wakiwatuhumu wamekuja nchini kwao kuziba ajira zao, hivyo kuwataka warejee nchini mwao.

"Masela wangu safari ya kurudi nyumbani Tanzania kwa upande wangu imeiva, siwezi kuvumilia kuishi maisha ya kujificha kama popo" aliongea kiunyonge Mbweku Jr akionekana kukata tamaa kabisa ya kuendelea kuishi maisha ya tabu na mashaka ugenini. Walikuwa wapo chumbani usiku wanabadilishana mawazo namna ya kukabiliana kikamilifu na vita dhidi yao inayofanywa na wenyeji. "Mwana acha kutuzingua, kila mtu ataondoka kwa namna alivyokuja, mimi binafsi yangu nitazikwa kwenye ardhi ya Mzee Madiba, maisha ya nyumbani Tanzania siyawezi tena, nimeondoka kwa zaidi ya miaka 20 halafu nirudi mikono mitupu hamna atakayenielewa. Hivyo hapa hamna mtoto mdogo wa kumpa ushauri, wewe si ulikuja kichawi huku Bondeni basi rudi kichawi vilevile" aliongea kwa jazba na hasira jamaa aliyekuwa anajulikana kwa jina la 'RAS' na wenzake akionekana kukerwa na maneno Mbweku Jr ya kukata tamaa ya kutaka kurudi nyumbani Tanzania.

Maneno ya kebehi toka kwa RAS kuwa Mbweku Jr amekuja kichawi nchini Afrika ya Kusini yaliamsha vicheko ndani ya chumba kile huku Mbweku Jr akiwa amejiinamia tu kichwani amejawa na mkururu wa mawazo, huku nae ameshikwa na hasira kama mbogo anatamani wachapane ndondi ili heshima irudi mahali pake. Wengi wao walikuwa hawaamini hadithi ya ujio wa Mbweku Jr nchini Afrika ya Kusini wa kimiujiza. Alivyowasimulia waliona kama ni ndoto za Alianacha, anawaongopea tu. Hasa wakijiangalia wao namna walivyoisotea kuitafuta Afrika ya Kusini. Mbweku Jr hakutilia maanani kebehi zao hasa akichukulia ukweli halisi alikuwa anao yeye. Kebehi hizo zikamkumbusha Mbweku Jr namna alivyosafiri ndani ya siku 3 mfululizo bila kikwazo chochote mpaka nchini Afrika ya Kusini, akajenga tabasamu la furaha usoni mwake. Akakumbukia tukio zima kwa mtiririko sahihi kabisa akiwa kijana mdogo wa miaka 17 mwenye umbo lililojengeka, wakati anafanya kibarua cha ulinzi katika danguro la Bosi Recho alipomtembelea baba yake gerezani. "Baba mie nasafiri kwenda nchini Afrika ya Kusini saa na wakati wowote kuanzia sasa, hii ni taarifa tu nakupa sihitaji ushauri wako !" aliongea Mbweku Jr akiwa ameshasimama lakini anachemka kwa hasira dhidi ya Recho, amekunja ndita mpaka akajikuta machozi yanamlengalenga. "Safari njema, wewe sasa ni mkubwa upo katika utawala wako binafsi, nakujua wewe ukilazimisha jambo lako lazima liwe unavyotaka ndio tabia yako toka utotoni. Ila kikubwa ni kama nilivyokupa nasaha, usijaribu kufanya chochote cha kulipiza kisasi kwa Recho. Kwanza hatuna ushahidi wa asilimia 100% kuwa yeye ndio mporaji wa pesa zilizoibwa ofisini, pili ana nguvu ya kipesa atakupoteza wewe na kizazi chako chote akikugundua umeijua siri yake kuwa yeye ndio muuaji wa Bosi Minja. Pia nakuomba kabla hujasafiri kwenda huko unakotaka kwenda upite Bagamoyo kwa Sheikh Maarifa akufanyie dua ya safari, wakati tupo kazini enzi zetu watumishi wengi tulikuwa tungongana kwake kunyoosha mambo yetu" aliongea Mzee Mbweku huku akisimama na kuvichukua vitu vya zawadi alivyoletewa na mtoto wake.


Siku hiyo Mbweku Jr alivyotoka hapo gerezani mchana huo, baada ya kuuliza uliza kwa watu, akaelekezwa kuwa kufika kwa Sheikh Maarifa apande gari za kuelekea Bagamoyo kisha ashuke maeneo ya mbele ya Kiromo. Akifika hapo dereva bodaboda yoyote atakayemuuliza kuwa anataka kufika kwa Sheikh Maarifa atamfikisha. Mbweni hakujivunga, na asiyesikia la mkuu huvunjika guu, huo ndio ushauri wa baba yake alikuwa hana budi lazima aende kwa Sheikh Maarifa akapate dua na baraka za safari ya Afrika ya Kusini. Mpaka kufika majira ya saa 9:30 alasiri alikuwa tayari yupo katika viunga vya Sheikh Maarifa, akikutana na wateja wengine wanaosubiria huduma.

"Sheikh kaenda kuswali msikitini, baada ya swala ndio ataendelea na huduma tena" aliongea mmoja wa wahitaji wa huduma ya Sheikh akimpasha Mbweku Jr alipoulizia. Mbweku Jr akawa hana budi kufanya subira, huku akitafuta nafasi kwenye jamvi maalumu la wateja na kuketi chini baada ya kuvua viatu vyake. Pale zikaanza soga mbili tatu juu ya umahiri wa Sheikh Maarifa namna alivyotabahari katika fani ya falaki na uaguzi wake. "Huyu Babu ni kiboko sana, akitaka kuchuma nazi, wala haitaji mkwezi yeye anachofanya ni kuomba dua zake tu basi ule mnazi unajipinda mpaka kwenye usawa wa mikono yake, anachuma kisha anauombea unarudi kama zamani" aliongea mteja wa Sheikh wa lugha ya tashiwishi na hamasa kuonyesha Sheikh ni gwiji kwelikweli katika fani yake.

"Huyu Sheikh anatisha sana katika fani, akitaka kusafiri hana haja ya kupanda gari, huwa anakaa kwenye jamvi lake anafanya kisomo tu anapaa, kwa kweli amepewa makarama sana na Mwenyezi Mungu" mwingine nae alichangia maongezi pale jamvini. Maongezi ambayo yalimtia nguvu na kumshajiisha Mbweku Jr kuwa kweli hajafunga safari bure, amekuja kwa kigogo haswa kama alivyoelekezwa na baba yake. Wakati maongezi yanaendelea baina yao, akajidhihirisha mbele yao, mtu shaibu kiumri, mrefu wa wastani, rangi ya maji ya kunde, amevaa libasi aina ya kanzu nyeupe pee isiyo na chembe ya doa kwa umaridadi wake, mkononi kabeba tasbihi na miguuni kavalia makubazi ya rangi ya hudhurungi. Alikuwa anakuja mbele yao akitokea msikitini huku midomo yake na ulimi wake unaonekana kutikisika na vidole vyake vikihesabu tasbihi kuonyesha alikuwa anamdhukuru Mwenyezi Mungu. Kila mmoja pale kwenye jamvi akazidisha kukaa mkao wa heshima na taadhima.

"Asalamu Aleikum Warahmatullah Wabarakatuhu jamia" alitoa salamu kwa sauti nzito yenye kuonyesha ni mtu mwenye kujiamini, huku akielekea moja kwa moja kuketi kwenye kiti tupu kilichokuwa kimetengwa mbele yao. "Waleikum Salaam" waliitikia watu wote kwa pamoja waliokuwa wamekaa pale jamvini. Huku kila mmoja akiwa amesinyaa kama magome ya miti, akitega masikio yake kama antena kusubiria maelekezo maridhawa toka kwa yule mtu mahashumu kwao. "Sheikh ametingwa na ugeni mzito toka Uarabuni hivyo kwa leo mimi ndio nitatoa huduma kwenu, nianze na wewe kijana Mbweku unaonekana una safari nzito ya haraka, elekea kwenye kilinge kile pale" alifungua maongezi kwa kutoa maelezo mafupi lakini safi kama msahafu yenye kuonyesha yeye sio Sheikh Maarifa mlengwa wao. Mbweku aliposikia utambulisho ule alipatwa na unyonge kidogo wa moyo juu ya uwezo wa huyu msaidizi wa Sheikh. Lakini mashaka na wahaka wake moyoni ulikuja kuondoshwa mara moja baada ya kutajwa kwa jina lake na kuelezwa sababu iliyomleta Bagamoyo hata kabla hajafungua mdomo wake kujieleza. Alichokuwa hafahamu Mbweku Jr ni kuwa mbabe huyo wa fani ya falaki alikuwa anatumia kitabu kinachoitwa 'Majmu Saatul Khabar', kitabu ambacho kwa imani zao waganga hao kilikuwa kina kanuni za kufuatwa za kujua matukio ya kila saa kwa kila mtu.

Mbweku Jr alipopewa maelekezo yale akasimama na kuelekea kwenye kilinge hicho cha kibanda cha miti kilichoezekwa kwa makuti ya mnazi na kuzungushiwa bendera nyekundu na nyeupe zilizochorwa herufi mbalimbali za lugha za maruhani. Mbweku Jr akaelekezwa akae juu ya kinu cha kutwangia huku akiwa amefumba macho yake asione kinachoendelea ndani ya Kilinge kile. Akaanza kuzisikia sauti mbalimbali za kuogofya zilizomfanya ashtuke kama mtu aliyekanyaga kaa la moto. Yule msaidizi wa Sheikh alipoingia hapo Kilingeni tu sauti zile zikakoma. Akaamrishwa afumbue macho, alipofumbua tu, ghafla bin vuu likapita bonge la paka jeusi lina shingo nene kama mbuyu amevikwa lundo la hirizi zilizoshonana kama ushanga. Paka lile likaenda kutulizana katikati ya miguu ya mtaalamu akazunguruka mara 7 mfululizo kisha akatoka nduki kukimbilia kusipojulikana. Kipindi chote hicho Mbweku Jr alikuwa roho juu juu, jasho jekejeke la uoga linamtiririka chini ya makwapa.

Mtaalamu yule hakumjali Mbweku Jr akaanza kumsomea kisomo kirefu cha zaidi ya saa moja. Baada ya hapo akaelekezwa akakae chini ya mti wa Mkungu kusubiria jani litakalo dondoka wenyewe kisha alipeleke kwa mtaalamu. Alisubiria chini ya mti kwa takribani dakika 29 ndipo jani hilo alilokuwa analisubiria kwa hamu likaanguka. Haraka haraka akaliokota hilo jani huku akiwa na furaha sheshe mpaka akalifikisha kwa msaidizi wa Sheikh. Mbweku Jr alivyokabidhi akaachwa kwenye kilinge, huku mtaalamu yule akiingia chemba kushughulikia lile jani. Zikawa zinasikika sauti za mnyama kama kondoo kulalamika kwa maumivu ya kuchinjwa chwa, huku damu zake kondoo huyo zikichiririka chiriri chiriri. Baada ya kama nusu saa hivi Sheikh yule akatoka kule chemba huku akiwa ana uso uliojaa bashasha. "Kazi yako tayari, utasafiri salama salimini, bila shida yoyote. Utatakiwa kuanza msafara wa kuelekea nchini Afrika ya kusini saa 10:29 usiku, pale ambapo, mapambazuko ya asubuhi yanakaribishwa. Ndio maana lile jani limedondoka baada ya dakika 29. Na hii ni hirizi iliyoshonwa kwa ngozi ya kondoo na ndani yake kuna jani la mkunguu na vifaa vingine vya kazi, utaivaa kiunoni kuanzia sasa na hamna Askari yoyote atakayeweza kukukamata. Na utakapofika mpakani mwa Msumbiji na Tanzania, omba kuonana na mkubwa wao wa kazi, atakapokuja muambie shida yako atakusaidia. Tayari nimeshamvuta na kumkata ulimi hatoweza kujitetea chochote mbele yako. Nakutakia safari njema, utaweka kwenye kapu lile pesa ya vifaa na sadaka yako ya ufundi" aliongea yule mtaalamu huku akiruhusu Mbweku atoke ili aingie mtu mwingine mhitaji wa huduma ya uganga.

"Ahsante sana Sheikh, Mwenyezi Mungu akubariki, kazi njema" aliongea Mbweku Jr akitoka nje ya kilinge na ile hirizi yake. Kwa usongo tu akaamua aivalie pale pale hata kabla hajafika nyumbani. Mbweku Jr kwa furaha aliyonayo akawa anarukaruka kwa furaha kama mwanambuzi. Hiyo hirizi ndio Mbweku Jr anaamini ilimsaidia usiku wa tukio la kumuokoa Deborah kuweza kupita barabara mbele ya mapolisi bila kusemeshwa chochote. Pia imani yake ikamtuma kuwa alipofika mpakani, yule Mkuu wa Uhamiaji wa upande Wa Msumbiji alimruhusu kupita bila kumuuliza hati ya kusafiria tena akimsaidia kumuombea usafiri wa gari la kumfikisha nchini Afrika ya Kusini. Simulizi hii alivyowapa wenzake hakuna aliyemwamini walijua ni Ablakadabra za kusukuma muda tu, lakini huo ndio ukweli halisi kwake.

Baada ya mazungumzo yao mule chumbani, Mbweku Jr alipanga asubuhi na mapema ataenda kujiandikisha ubalozini kwa ajili ya kurudishwa Tanzania kuepuka machafuko. Mbweku Jr hakuwa na wasiwasi wa kuishi maisha magumu atakaporejea nchini Tanzania, kwani alijua mgao wake wa pesa atakaoupata kwa rafiki yake kipenzi waliyeshibana kama chanda na pete, Timammy utamuwezesha kuishi maisha mazuri anayoyataka yeye. Penyenye alizokuwa anazipata toka kwa Vidinga popo wa nyumbani Tanzania ni kuwa Timammy ni tajiri mkubwa anayemiliki vituo vya kuuza mafuta 'Petrol Station' kila kona ya Jiji la Dar es Salaam. Alikuwa pia anamiliki nyumba za ghorofa za kupangisha lukuki katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Wazo lake la kwanza alilopanga pindi akipokea mgao wake ni kujenga mjengo wa kuishi. Kisha akaenda kijijini kuifuata familia yake waishi pamoja kama zamani. Pia alipanga kufunga ndoa haraka sana, na mwanamke wa ndoto zake kila alipokuwa anawaza alikuwa ni Deborah. Alikuwa anamuona Deborah kuwa ni mwanamke aliyetimia katika idara zote. Kuanzia uzuri wa umbo, tabia ya uvumilivu katika maisha na usomi. Deborah alimsimulia Mbweku Jr madhila na manyanyaso yote aliyowahi kupitia maishani mwake. Wasiwasi pekee aliokuwa nao Mbweku Jr ni juu ya kumkuta Deborah akiwa bado hajaolewa au kupata mchumba. Akilini alishajiandaa kisaikolojia kukubali matokeo kama akimkuta kashawekwa kwenye himaya ya mtu. Kosa alilokuwa anajijutia ni uoga wake kama fisi ni kutomueleza ukweli Deborah mapema kabisa kuwa anampenda sana na anatamani aje kuwa muhibu wake wa kufanya nae maisha ya ndoa. Hofu kubwa iliyomzuia kumtapikia Deborah hisia zake ni kwanza kuogopa ataonekana ametoa msaada wa kumuokoa kule kwenye danguro kwa lengo la kujifaidisha kimwili. Pili aliogopa asije kumchanganya kimasomo, badala ya kutili mkazo kwenye shule atageukia kuwazia mapenzi tu hivyo kusababisha afeli vibaya masomo yake, kama ujuavyo penzi ni kitovu cha uzembe. Na kwa kuwa penzi lake kwa Deborah lilikuwa ni la dhati kabisa hakutaka yeye kuwa ndio kikwazo cha kumfanya Deborah ashindwe kutimiza ndoto zake. Matumaini pekee yalibakia kwa rafiki yake Timammy ambaye alimdokezea juu ya mapenzi yake ya dhati kwa Deborah na kumuomba amsaidie kwa hali na mali kutimiza ndoto zake.

Mwalimu wa zamu: "Jina lako unaitwa nani? "
Mwanafunzi: "Naitwa Deborah Minja"
Mwalimu wa zamu: "Fomu yako ya kujiunga na shule ipo wapi? "
Deborah: "Imeibiwa na vitu vyangu vingine..!"
Mwalimu wa zamu: "Pole sana, umetokea Mkoa gani na umemaliza shule gani? "
Deborah: "Nimetokea Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Mvomero, shule ya msingi Mikongeni, "
Mwalimu wa zamu: "Haya nisubiri nikaangalie jina lako kwenye ofisi ya Mwalimu wa Taaluma" aliongea Mwalimu yule huku akinyanyuka na daftari lake mkononi akimuacha ofisini mwake Deborah peke yake. Baada ya kitambo kifupi kupita akarejea akiwa ameambatana na mwanafunzi mwengine aliyevalia sare zake nadhifu za shule.
Mwalimu wa zamu: " Sasa Deborah utafuatana na huyu mwenzako, atakupeleka bwenini kwao, atakupeleka kwa Mhasibu ukalipie ada kabisa. Pia tambua umechelewa na una bahati ya mtende, kesho kutwa kuna Mitihani ya mchujo, watakaofeli wanarudishwa shule za sekondari za kawaida tambua kuwa Msalato ni shule ya watoto wenye vipaji vya akili, hivyo ujiandae vyema na mitihani katika muda huo mfupi" aliongea Mwalimu yule kwa ukarimu na umakini mkubwa.
Deborah: "Ahsante sana Mwalimu nitafuata ushauri wako" aliongea Deborah huku akisimama na kuanza kubeba sanduku lake huku yule mwenzake akimsaidia kubeba godoro lake.
Mwalimu wa zamu: Haya usome kwa bidii si umeona kaka yako kafunga safari toka Dar es Salaam mpaka Dodoma kukuleta shule ili usome kwa bidii" alizidi kuchagiza maneno ya hamasa Mwalimu yule kwa Deborah akimkumbushia Timammy, rafiki yake Mbweku Jr ambaye alijitolea kumnunulia vifaa vya shule, kumpa pesa ya ada pamoja na matumizi na kumleta shuleni, Jijini Dodoma. Pesa yote hiyo, Deborah alidhania imetoka mfukoni mwa Timammy, kumbe ni pesa ya mfadhili wake Mbweku Jr ambaye alimuokoa kule kwenye danguro la Recho, Sinza Kijiweni.

Baada ya kumaliza mikikimikiki yote ya siku nzima ya usajili pale shuleni akawa ametulia bwenini kwake, katika bweni linalojulikana kama 'Mwongozo' akawa yupo kwenye tafakari nzito ya furaha iliyochanganyika na huzuni, hali iliyomsababisha machozi ya furaha yamtiririke kama ngamia. Kwanza alikuwa haamini macho yake kama kweli kafanikiwa kutua shuleni kutimiza ndoto zake za kielimu hasa akikumbukia vimbwanga vizito alivyopitia kuanzia kule nyumbani kwa Mjomba Kobelo, kutoroka kwake, kukamatwa na polisi, kuokolewa na mfadhili wake Koplo Matuta, kutekwa kwake na kuhifadhiwa kwenye danguro la Bosi Recho hadi kuokolewa na Mbweku Jr.
Hakuchukua muda mrefu kuzoea mazingira ya shuleni pale, ndani ya muda mfupi akawa anajulikana kama mmoja wa wanafunzi vinara wa Masomo ya Sayansi. Mazingira ya shule yakampenda akanawiri kama mti uliopata mbolea. Tatizo kubwa lililokuwa linamsumbua ni la kujikojolea kila unapofika usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili. Ile ndoto ya ukweli juu ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya baba yake ilikuwa inajirudia mara kwa mara. Hali ambayo ilikuwa inamfanya ajikojolee kwa uoga, na akishtuka usingizini anajikuta ameshachafua kitanda kwa mikojo. Wanafunzi kama uwajuavyo hawana dogo, habari zile za umbea wa kuwa Deborah ni kikojozi licha ya urembo wake na akili zake darasani zikasambaa kwa kila mwanafunzi.

Wapo waliokuwa wanamkebehi dhahiri shahiri kwa kumuita 'Mrembo Kikojozi' na wengine 'Kipanga Kikojozi' na majina kochokocho ya dharau na kashfa. Taarifa ilipofika kwa Matroni wao ikabidi amuite Deborah na kumhoji kulikoni. Ikabidi amuelezee mkasa mzima wa namna alivyoishuhudia sura ya mmoja wa wauaji wa marehemu baba yake. Mkasa ambao ulimkumba tokea akiwa kinda wa Chekechea na namna unavyomtesa mpaka leo. Mwalimu yule akamuonea huruma sana na kumpa pole nyingi kwa mkasa huo mbaya uliomkuta. Tokea siku ile Mwalimu yule akashusha mkwara mzito sana kuwa yoyote atakayegundulika anamkebehi Deborah hatua kali dhidi yake zitachukuliwa ikiwemo hata kufukuzwa shule. Tangazo hilo likawa kidogo limesaidia kutuliza hali ya hewa na kumfanya Deborah aanze kufurahia tena maisha ya shule. Hali hiyo ya kudharauliwa ndio ikawa ni kichocheo chake cha kusoma kwa bidii. Usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili akauchagua uwe ni usiku wa kukesha kusoma ili kuepuka aibu ya kujikojolea kitandani. Timammy kumbe nae alikuwa amekufa na kuoza kwa Deborah. Kila inapofika Jumamosi ya mwisho wa mwezi ya kutembea wanafunzi 'Visiting Day' Timmamy akawa anahudhuria na zawadi kedekede kuanzia sabuni za kuogea, manukato, mpaka vyakula vya makopo. Ukarimu aliokuwa anafanyiwa Deborah akaanza kuingiwa na mashaka, kuwa ipo siku tu isiyo na jina atalazimika kuvilipa hivyo vitu. Alianza kumuona Timammy ni adui mpenzi kama moto ulivyo, siku yoyote utakuja kumuunguza.

Hakuna marefu yasiyo na ncha, Timammy akashindwa kuficha hisia zake, kipindi ambacho Deborah yupo kidato cha 3, siku moja Timammy alivyomtembelea akavunja ukimya. Akaamua apasue ukweli uliopo moyoni mwake kwa Deborah. "Deborah wewe sasa ni mkubwa, mwakani unatimiza miaka 18, hivyo natamani ukimaliza tu shule kidato cha nne nataka nifunge ndoa na wewe". Timammy aliamua kufunguka liwalo na liwe, tayari alishavunja ahadi ya rafiki yake Mbweku Jr ambaye alidokeza kuwa ana mipango ya muda mrefu na Recho. Deborah pale pale alipokaa alisimama bila kuagana na Timammy na kutokomea zake kuelekea kusipojulikana. Timammy akaachwa mdomo wazi haamini kama kweli Deborah kamuacha solemba kwa kumfanyia jeuri. Deborah alikuwa amechefukwa na kuvurugwa na maneno ya mkahawani ya Timammy. Alimuona kabisa kuwa ni mharibifu asiye na mapenzi ya kweli kwake. Kwa sababu alimuona hajali kabisa masomo yake bali anajali kutimiza hawaa ya nafsi yake. Timammy fedheha na soni ilimkumba, akashikwa na ubaridi wa moyo, hakuamini kama Deborah atamuonyesha dharau kiasi kile, hasa ukichukulia tayari ameshaanza kutengeneza Jijini Dar es Salaam. Wanawake walikuwa wanamgombea ili awaoe wao kutokana na utajiri wake. Deborah alipotoka pale breki ya kwanza ni kwenda kushtaki kwa Mwalimu wa nidhamu. Akamuelezea kinagaubaga bila kuficha kitu, huku akiomba Timammy afutwe kabisa kwenye orodha ya majina ya ndugu zake wanaoruhusiwa kumtembelea shuleni. Ikabidi Timammy atolewe nje ya fensi ya shule chini ya ulinzi mkali wa walinzi wa shule. Timammy aliona kuwa amekashifika vya kutosha na chokoraa aliyeokolewa kwenye mdomo wa simba na rafiki yake Mbweku Jr sasa ameota mapembe. Akawasha gari lake na kuliondosha kwa kasi akirejea Jijini Dar es Salaam, huku akijiapiza lazima amshikishe adabu vya kutosha, mpaka afanikishe kumfanya mke wake iwe kufa au kupona.



SURA YA KUMI NA NNE
Bosi Recho baada ya kuponea kifo kwenye tundu la sindano, kwenye mlipuko wa jingo lake la ghorofa uliofanywa na Mr.Lorenzo, akajikuta amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika kitengo cha mifupa cha Muhimbili Orthopaedic Institute MOI. Alipopokelewa tu akapelekwa moja kwa moja katika chumba cha wagonjwa mahututi ICU. Takribani mwezi mzima alikuwa hana fahamu tokea apokelewe hospitalini hapo. Madakatari bingwa walikuwa wanakesha kufanya mdahalo wa namna ya kuokoa maisha ya Bosi Recho. Baada ya majadiliano ya kina kati ya madaktari na ndugu wa Bosi Recho, wakafikia muafaka kuwa kama wana uwezo wampeleke mgonjwa wao kwenye hospitali kubwa huko ughaibuni kama nchini Afrika ya Kusini au India, lakini hapa nchini Tanzania matibabu yake yameshindikana kufanyika kutokana na kuwa na majeruhi mabaya. Ndugu zake Recho, walikuwa ni watu hohehahe wenye kipato cha kijungu meko, hivyo hawakuwa na uwezo wa kumpeleka kokote kule kwa ajili ya matibabu. Ikabidi wafikie maamuzi ya kupiga bei mali zote za Recho zilizopo Jijini Dar es Salaam ili pesa zitakazopatikana zitumike kulipia matibabu nje ya nchi na matunzo yake muda wote wa matibabu. Hatimaye Recho akasafirishwa mpaka nchini Afrika ya Kusini kwa ajili ya kuanza matibabu.

Alipelekwa kutibiwa katika hospitali inayoitwa “Busamed Hillcrest Private Hospital iliyopo Jijini Durban. Hiyo ni moja ya hospitali bora nchini Afrika ya Kusini katika orodha ya Hospitali bora 20. Ilikuwa ni hospitali yenye vyumba vya upasuaji vya kisasa, wodi za hadhi ya juu za kulaza wagonjwa, pia ilikuwa na Madaktari na Manesi bobezi katika kazi yao ya utabibu. Gharama ya siku ya matibabu kwa matibabu ya Recho hospitalini hapo ilikuwa ni shilingi elfu 50 za Kitanzania. Recho alifanyiwa upasuaji zaidi ya mara 37 katika sehemu mbalimbali za mwili wake, mpaka akaanza kupata nafuu. Ila angalizo walilotoa ni kuwa atakuwa mlemavu wa kutembelea kiti katika maisha yake yote yaliyobakia hapa duniani. Kwa huduma murua alizokuwa anazipata hapo hospitalini, baada ya kupiita muda wa miezi 9 akaanza kuongea bila shida ila hawezi kusimama, ni mtu wa kulala kitandani tu. Pesa zote alizokwenda nazo huko nchini Afrika ya Kusini zikaisha, ikabidi zikauzwe mali zake zingine za Jijini Arusha na Kilimanjaro ili ziweze kupatikana pesa za kuendelea kumtibu. Kwa hiyo rasmi Bosi Recho akawa ni muflisi, hana senti yoyote aliyoibakiza benki wala mali yoyote. Hakuwa tena na mikogo yake, ujanja wote ulishamuisha. Baada ya kukaa hospitalini kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, ndugu zake wakaomba rasmi warudi nae nyumbani Tanzania, kutokana na kuhofia kushindwa kufanya malipo kama ataendelea na matibabu huko. Wakarudi nae Tanzania, na kupelekwa moja kwa moja kwa mama yake mdogo, aliyekuwa anaishi katika Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro. Sasa akawa ni mtu wa kutembea na kiti cha kukokotwa na magurudumu maalumu kwa walemavu. Akaanza sasa kuhangaika kwenda kwenye Makanisa ya Kilokole kwa ajili ya maombezi, akiweka matumaini huenda akafanyiwa miujiza na Wachungaji akapona na kuanza kutembea kama zamani. Akaamua rasmi kuokoka, kwa kuachana na starehe za dunia na kujiunga na makanisa ya Kilokole akiachana na dhehebu lake la Katoliki.

Upele ukawa umempata mkunaji, akawa hataki kusikia kuitwa jina la kifupisho la Recho, akawa anataka aitwe kiukamikifu jina lake la 'Rachel Francesco Gabriele'. Wapo wanaomfahamu tokea enzi zake wakambeza kuwa ng'ombe akivunjika mguu hana jinsi tena hurejea zizini, lakini Recho akayapuuza maneno yao na kumshika Mungu kikamilifu. Akaanza kuuvaa tena mkufu wa shingoni aliopewa zawadi na bibi yake mzaa baba. Mkufu ambao ulikuwa na kidani chenye herufi ya kwanza ya jina lake 'R'. Mkufu ambao aliutelekeza kitambo kirefu tokea ahamie nchini Kenya na mpenzi wake wa zamani Martin Tenga. Nyumbani kwa mama yake mdogo pakageuka kama kanisa vile, Wachungaji wa kiroho wanapishana kumfanyia maombi. Recho akatubia dhambi zake zote, huku dhambi ya kumtelekeza mtoto wake Pesambili kwenye kituo cha watoto yatima ikiendelea kumtafuna moyoni. Akaweka nia kuwa pindi akipata nafuu atafanya ziara nchini Kenya kuulizia wapi alipo mtoto wake.

Alijua kuwa mtoto wake kama atakuwa hai, sasa atakuwa ni kijana mkubwa kabisa, ambaye amekosa mapenzi ya mama kwa asilimia 100%. Akawa anajijutia kwa kumpa uyatima usio na sababu mtoto wake hali ya kuwa ana wazazi wake waliohai. Siku zikasonga hali ya kuwa bado Recho hajaanza kutembea mwenyewe zaidi ya kuendelea kutumia kiti cha magurudumu ya kukokotwa.

Deborah alikuwa amebakisha mwizi miwili tu kuanza mitihani ya kumaliza elimu ya kidato cha 6. Kwa muda wa miaka 6 yote ya elimu ya Sekondari alisoma shule hiyo hiyo moja tu, ya 'Msalato Girls'. Alikuwa ni miongoni mwa wakongwe wa shule, tena mkongwe ambaye hajawahi kukanyaga likizo nyumbani hata siku moja tokea ripoti shuleni. Kama waswahili wasemavyo kuwa ukimuona nyani mzee ujue amekwepa mishale mingi, huyo ndio alikuwa Deborah, alipitia misukosuko mingi akiwa shuleni mpaka kuweza kufikia kidato cha 6. Kwanza miaka 6 yote, alikuwa hajakanyaga nyumbani akiogopa kurudi kwa Mjomba wake Kobelo. Pili Timammy baada ya kuonyeshwa utovu wa nidhamu na Deborah kwa kukataliwa ombi lake la kukubali kuolewa nae akimaliza elimu ya kidato cha 4, akakacha kulipa ada. Ikabidi Deborah aombe eneo pale shuleni la kulima bustani. Akawa analima mchicha halafu anauza mchicha kwa shule kwa ajili ya kulisha wanafunzi mboga za majani. Pesa alizokuwa analipwa akawa anapotumia kwa ajili ya ada na kujinunulia mahitaji yake mengine ya kujikimu. Sasa hamu yake ilikuwa ni kumaliza shule ili apate nafasi ya kurejea nyumbani kwao kwa Mjomba wake baada ya kupotezana nao kwa zaidi ya miaka 6.

Shauku yake kubwa ilikuwa ni kwenda kumuona mama yake mzazi amjulie hali yake. Kila alipokuwa anamuwaza mama yake machozi yalikuwa yanamtoka. Alikuwa hajui kama yupo hai au amefariki.
Siku ya sherehe ya mahafari ya wanafunzi wa kidato cha 6 ikawadia. Wanafunzi hao walikuwa wameshikwa na furaha chekwachekwa ya kumaliza elimu ya sekondari. Walijiona wameshakuwa wakubwa wakiwa wamebakiza miezi michache tu waanze ya Chuo Kikuu. Walikuwa wanajiona kama vile wameshakula ng'ombe mzima wamebakiza mkia tu. Deborah nae hakubaki nyuma, alikuwa na furaha sheshe kupita hata wanafunzi wenzake wote. Hii ni kutokana na kukaribia kufanikisha ndoto zake za kielimu. Deborah alijipara, akajikwatua na kupendeza vilivyo. Sherehe zilipoanza, Deborah ndio alikuwa kinara wa kuongoza kwaya ya shule inayotumbuiza mbele ya hadhira wakiwemo wageni waalikwa. Sauti yake nyororo na namna alivyokuwa ananengua mwili wake ilikuwa ni burudani tosha kwa kila mtu aliyehudhuria hafla ile. Mgeni rasmi alikuwa ni Mfanyabiashara mkubwa tu Jijini Dodoma, maarufu kwa jina la Mrs.Tonny. Alikuwa ni mama wa makamo ambaye alikuwa anamiliki maduka mbalimbali ya kuuza vito vya thamani. Pia alikuwa anamiliki machimbo ya madini ya Tanzanite huko Mererani, Arusha. Watu wengi walikuwa hawamfahamu mumewe mama huyo zaidi ya kumjua kwa jina la Mrs.Tonny. Ukafika wakati wa kugawa vyeti na kutoa tuzo kwa wanafunzi vinara wa masomo mbalimbali.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog