Search This Blog

Monday 27 March 2023

LAITI NINGEJUA - 1

 

IMEANDIKWA NA : BISHOP HILUKA

*******************************************

Simulizi : Laiti Ningejua

Sehemu Ya Kwanza (1)



HII haikuwa mara yangu ya kwanza kufika wilaya ya Rufiji hususan katika mji wa Ikwiriri, mji mdogo uliopo kusini kwa Dar es Salaam katika Mkoa wa Pwani. Nilikuwa nimefika hapo Ikwiriri mara moja na hii ilikuwa ni mara yangu ya pili.


Kwa kiasi fulani sikuwa mgeni kabisa wa mazingira ya Ikwiriri ingawa mara ya kwanza nilipokwenda katika mji ule sikukaa kwa zaidi ya siku tatu. Kama ilivyokuwa mara ya kwanza, safari hii tena nilipokwenda katika mji wa Ikwiriri nilikuwa pale kibiashara na nilifikia nyumbani kwa rafiki yangu, Amir Ngwali, aliyekuwa anaishi Barabara ya Mtunda nje kidogo ya mji wa Ikwiriri.


Kama kawaida yangu, siku ile pia nilikuwa katika mwonekano wa kileo zaidi nikiwa nimevaa suruali ya jeans ya rangi nyeusi, buti ngumu za ngozi miguuni, shati maridadi la rangi ya samawati aina ya Levi’s nililokuwa nimelichomekea vizuri kiunoni, saa ya mkononi aina ya Seiko na kofia nyeusi ya kapelo.


Kwa ujumla nilikuwa mtanashati niliyejipenda mno kuanzia ndani ya chumba changu hadi mwili wangu, ilikuwa ni nadra sana kunifumania nikiwa nimerudia kuvaa nguo niliyoivaa jana yake.


Nikiwa katika umri wa miaka therathini nilikuwa mrefu na maji ya kunde mwenye umbo la kimichezo, nilikuwa mcheshi sana na mtu wa kujichanganya na watu wengine.


Sikuwa mbumbumbu, nilikuwa nina elimu nzuri tu ya biashara, kwani nilihitimu shahada ya kwanza ya Biashara katika Masoko (B.Com. in Marketing) kutoka katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), miaka mitano iliyokuwa imepita.


Baada tu ya kumaliza masomo yangu ya biashara pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilizunguka kutafuta ajira lakini baadaye nikaamua kujiajiri mwenyewe baada ya kuona mshahara niliokuwa nikitajiwa ulikuwa hauendani na matarajio yangu.


Kimsingi niliamua kuwa mtu wa dili au ukipenda unaweza kuniita ‘mishen tauni’, na ili kufanikiwa zaidi katika dili zangu niliamua kuwa mtu wa kujichanganya sana.


Tabia yangu ya kujichanganya na watu wa aina mbalimbali kwenye dili ambazo zingine wala hazikuhitaji kisomo na bila kujali elimu yangu, kwa kiasi fulani zilinifanya nianze kupata mafanikio makubwa kimaisha na kufanya watu walionifahamu kunipachika jina la utani la ‘the Jackal of all trades’, yaani dalali wa biashara zote.


Nilifanikiwa kufungua ofisi yangu ya udalali na ushauri wa biashara iliyokuwa katika eneo la Buguruni Rozana, na nilikuwa nimeajiri watu sita, mimi nikiwa ndiye mkurugenzi mtendaji wa kampuni.


Pia nilikuwa nimejenga nyumba kubwa ya kisasa iliyokuwa nje ya jiji la Dar es Salaam, katika eneo la Zingiziwa, Chanika na pia nilimiliki viwanja viwili vitatu katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.


Katika maisha yangu ua utafutaji, sikupenda kabisa kujihusisha na wasichana ndiyo maana ilikuwa vigumu sana kunikuta na msichana. Lakini kwa vile binadamu hawana dogo wakaanza kusema eti huenda nilikuwa na matatizo mwilini mwangu, ndiyo maana nilikuwa naishi peke yangu licha ya kuwa na uwezo na pia kushobokewa na warembo.


Wakati najiandaa kuondoka pale nyumbani kwa Amir nikiwa mbioni kurudi jijini Dar es Salaam yalipo makazi yangu, ilikuwa yapata saa nne asubuhi, Amir na mke wake, Mwanamvua Mbonde walinisindikiza huku wakilalamika kuwa nimekuwa nikifika Ikwiriri na kukaa siku moja au mbili tu kisha naondoka, walitamani siku nyingine nikae pale kwa zaidi ya wiki.


Pia Mwanamvua alikuwa haachi kulalamika akitaka amuone mke mwenzake, kwa maana nyingine ni kwamba alikuwa akinisisitiza nioe ili washerehekee harusi yangu kabla ujana haujaisha maana sasa nilianza kuelekea kwenye utu uzima.


Tulipotoka nje ya nyumba ya Amir nikawaona watu wawili-watatu wa bodaboda waliokuwa wameegesha pikipiki zao chini ya mti mkubwa kando ya ile barabara iliyokuwa ikielekea Mtunda, na walikuwa umbali wa kama mita hamsini hivi kutoka katika ile nyumba ya Amir.


Katika umbali ule dereva mmoja wa bodaboda mjanja akaniwahi haraka kabla ya wenzake hawajashtuka baada ya kuhisi hitaji langu. Aliponiona tu alipiga honi huku akiniashiria nipande ile bodaboda, na kama vile haitoshi aliiwasha bodaboda yake haraka na kunifuata pale pale nje ya nyumba ya Amir tulipokuwa tumesimama.


Kwa mwonekano tu yule dereva wa bodaboda alikuwa ni mtu mzima aliyekadiriwa kuwa na umri usiopungua miaka arobaini na tano. Alikuwa mrefu na mwembamba mwenye sura ya ucheshi na alikuwa amevaa shati la bluu na jaketi jeusi, suruali ya kijivu na raba miguuni.


Alitusalimia kwa bashasha huku akionekana kutaniana na Amir, kisha nikapanda kwenye ile bodaboda pasipo hata kusubiri. Mara tu nilipopanda kwenye ile bodaboda yule dereva wa bodaboda akanisemesha kwa lugha ya Kindengereko na alipoona kuwa sielekei kumuelewa aliamua kubadili lugha na kunisemesha kwa Kiswahili.


“Kwani wewe si mtu wa hapa Ikwiriri?” yule dereva wa bodaboda akaniuliza kwa mshangao.


“Mimi siyo Mndengereko, mimi ni mtu wa Kigoma,” niliongea kwa utulivu huku nikimtazama kwa makini.


“Oh! Kumbe wewe ni Muha wa Kigoma? Karibu sana Ikwiriri. Mimi ni Mndengereko al-watan hapa Ikwiriri. Hakuna asiyenifahamu hata ukimuuliza mtoto mdogo tu atakwambia anamjua Kindeka mzee wa mabodaboda ni nani, au siyo Amir?” alisema yule dereva wa bodaboda kwa tambo nyingi huku akigeuza shingo yake kumtazama Amir na kuachia kicheko hafifu.


Amir na mke wake pia walicheka kicheko hafifu bila kusema neno. Mimi nilibaki kumtazama tu yule yule dereva wa bodaboda kwa makini huku nikiachia tabasamu laini ambalo baadaye likageuka kicheko hafifu.


“Lakini si kila mtu anayetoka Kigoma ni Muha, yapo pia makabila mengine kama Wabembe, Watongwe, Wamanyema…” nilimwambia yule dereva wa bodaboda, ambaye sasa nililifahamu jina lake kuwa aliitwa Kindeka.


“Kumbe!” akadakia yule dereva wa bodaboda kabla hata sijamaliza maelezo yangu huku akionekana kushangaa sana.


“Ndiyo, si hao tu, pia utawakuta Wanyamwezi, Wasukuma, Wafipa na watu wenye asili ya Congo, Rwanda na Burundi,” nikazidi kumweleza yule dereva wa bodaboda na kuzidi kumshangaza.


“Ooh, kwa hiyo wewe ni kabila gani?” aliniuliza yule dereva bodaboda huku akigeuza shingo yake kunitazama usoni kwa shauku kubwa ya kutaka kujua.


“Mimi ni Mmanyema ingawa siwezi kuzungumza lugha ya Kimanyema kwa sababu nimekulia jijini Dar es Salaam.”


Maelezo yangu yakamfanya yule dereva wa bodaboda ageuke kabisa na kunitazama usoni kwa makini kisha akaangua kicheko hafifu kabla kuniambia.


“Sishangai kwa nini vijana wengi wa zama hizi hawajui kuzungumza lugha zao za asili, wengi wanadhani labda ni ushamba au labda ni kutokwenda shule,” alisema yule dereva wa bodaboda huku akiangua tena kicheko.


Maelezo yale yakatufanya watu wote kwa pamoja tuangue kicheko cha katikati ya maongezi na kabla kicheko kile hakijafika ukomo wake, yule dereva wa bodaboda akageuka tena na kuniuliza, “Lakini bado hujaniambia tunaelekea wapi, Bosi?”


“Nipeleke stendi ya mabasi ya kuelekea jijini Dar es Salaam,” nilimjibu yule dereva wa bodaboda kwa utulivu huku nikiwa nimekwisha kaa vizuri na begi langu nikiwa nimelivaa mgongoni.


“Ooh, kumbe unaelekea Bongo? Nilisahau kama umeniambia unakaa Dar es Salaam!” akasema yule dereva wa bodaboda na kuangua tena kicheko hafifu na kuongeza, “Au kwa sasa unaishi hapa kwetu Ikwiriri?”


“Hapana, bado naishi Dar es Salaam, Ikwiriri nakuja kutembea tu mara moja moja,” nilimjibu yule dereva wa bodaboda kisha nikawaaga wenyeji wangu, Amir na mkewe kwa bashasha zote.


Kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia wakati yule dereva wa bodaboda akiiondoa ile bodaboda kutoka pale kwenye nyumba ya Amir. Hakuwa na mbwembwe kama ilivyokuwa kwa vijana wengi waliokuwa wakiendesha bodaboda kupenda kupiga lesi.




Aliendesha mwendo mfupi na mbele akakata kona na kuingia upande wa kulia akiifuata barabara iliyokuwa inatoka Lindi kuelekea Dar es Salaam, na wakati tukiingia kwenye ile barabara ya Lindi – Dar es Salaam nikakumbuka kumuuliza bei yule dereva wa bodaboda.


“Nimesahau hata kuuliza, hivi ni shilingi ngapi kutoka hapa hadi stendi ya mabasi ya kuelekea Dar es Salaam?”


“Unadhani nina bei basi! Shilingi elfu moja tu, Bosi wangu,” yule dereva wa bodaboda akaniambia huku akiingiza gia.


“Basi haina noma, ila twende taratibu maana mimi ni mwoga sana wa ajali, hasa za bodaboda,” nilisema huku nikijiweka sawa kwenye siti ya nyuma ya ile pikipiki.


“Wala usihofu, Bosi wangu, maana hata mimi huwa sipendi kukimbizana kama hao vijana wenzako, ndiyo maana watu wengi hupenda usafiri wangu,” alisema yule dereva wa bodaboda huku akipishana na gari dogo lililokuwa linatoka katikati ya ule mji kuelekea barabara ya Lindi.


Safari yetu ikaendelea taratibu tukiwa katika barabara ile ya Lindi - Dar es Salaam huku yule dereva wa bodaboda akinielezea jinsi alivyolazimika kukatisha masomo yake akiwa kidato cha tatu ili kutunza wadogo zake baada ya wazazi wake wote kufariki kwa ajali ya basi.


Kiujumla alioneka kuwa mcheshi sana na alijua kutengeneza mazingira yaliyomfanya abiria wake kuwa rafiki yake wa karibu. Sikushangaa kwa nini mwanzoni aliniambia kuwa watu wengi walipenda usafiri wake. Wakati tukiendelea na safari mara nikakumbuka kumuuliza kitu yule dereva wa bodaboda.


“Hivi saa hizi nitaweza kweli kupata basi zuri la kuelekea Dar es Salaam? Unajua huwa sipendi kusafiri na ile mikangafu, ambayo ukisafiri nayo hakikisha una panadol, maana ukifika unakokwenda lazima utakuwa hoi!”


“Ondoa shaka, Bosi!” yule dereva wa bodaboda akaniambia kabla ya kuendelea, “Muda huu ndiyo muda mzuri wa kupata magari mazuri yanayotokea Lindi na maeneo mengine, ikiwa bahati yako utayakuta pale stendi. Hapo ni wewe tu kuchagua unalotaka na linakufikisha hadi Mbagala, Dar es Salaam.”


Kisha kikafuata kitambo cha ukimya huku yule dereva wa bodaboda akipangua gia, na baada ya kitambo kifupi cha safari yetu hatimaye tukawa tumetokea sehemu ilipokuwa stendi ya mabasi ya kuelekea jijini Dar es Salaam katika ule mji wa Ikwiriri.


Yule dereva wa bodaboda akataka kwenda kunishushia kando ya kituo cha maegesho ya bodaboda cha pale stendi ya Ikwiriri, hata hivyo, kwa kuwa sikutaka kusumbuliwa na wapiga debe waliokuwa katika eneo lile nikamwambia anishushie mbele kidogo ya stendi ile.


Bila kupoteza muda nikachukua waleti yangu kutoka mfukoni na kutoa noti moja ya shilingi elfu moja, nikampa yule dereva wa bodaboda na wakati akiipokea na kuihifadhi vizuri kwenye pochi yake nikamwambia, “Nashukuru sana kwa usafiri.”


Yule dereva wa bodaboda akanitazama huku uso wake ukitengeneza tabasamu la kirafiki na wakati huo huo akiitia ile pochi yake mfukoni.


“Ondoa shaka, Bosi wangu, wakati wowote ukifika hapa Ikwiriri na kama ukihitaji usafiri wa bodaboda we niulizie tu, naitwa Kindeka. Ningekupa namba yangu lakini bahati mbaya kwa sasa sina simu, niliidondosha nilipokwenda Mtunda kwenye shughuli ya mtoto wa dada’angu.”


Ili kumuonesha kuwa nilikuwa pamoja naye niliamua kubetua kichwa changu kukubali huku nikitabasamu katika namna ya kumuonesha kuwa asijali kwani mimi nilikuwa nimeafikiana vizuri na hoja yake.


“Ndiyo hivyo, Bosi wangu,” alisema yule dereva wa bodaboda kwa huzuni kidogo huku akiuma mdomo wake wa chini.


“Hakuna shaka, ndugu yangu, wala usijali siku nyingine nikiwa nakuja Ikwiriri nitakutafuta, hata kwa kumpigia simu Amir ili akupe taarifa kuhusu ujio wangu,” nilimweleza yule dereva wa bodaboda huku nikiliweka vizuri begi langu mgongoni kisha nikaanza kuondoka taratibu.


“Safari njema Bosi, wasalimie sana huko Dar es Salaam,” yule dereva wa bodaboda aliniambia na kuniaga kwa kunipungia mkono huku tabasamu lake la kibiashara likizidi kuchanua usoni kwake, kisha akageuza pikipiki yake na kushika uelekeo wa kule tulipotoka.


Niligeuka kuitazama ile bodaboda namna ilivyokuwa ikitokomea katika barabara ile ya Lindi kisha nikashika uelekeo wa kwenye lile eneo la stendi ya mabasi katika mji wa Ikwiriri. Saa yangu ya mkononi ilionesha kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa nne na robo asubuhi.


Jua lilikuwa limeanza kuingia kwenye mawingu na hali ya hewa kwa wakati ule ilikuwa ya baridi ya kiasi na siyo kama lile joto lililozoeleka katika ukanda wa pwani. Pilika pilika za watu zilikuwa zimeshamiri nyakati hizo za asubuhi na hivyo kuufanya mji ule wa Ikwiriri kuchangamka.


Nilifika na kusimama pale katika stendi ya mji wa Ikwiriri na kama yalivyokuwa maeneo mengi ya stendi za mabasi hususan katika miji midogo, stendi ile pia ilikuwa imetawaliwa na pilikapilika za hapa na pale za kibinadamu.


Kulikuwa na wachuuzi kadhaa wa biashara ndogondogo maarufu kwa jina la Machinga, wauzaji wa mahindi na matunda kwenye masinia, wauzaji wa korosho na pia kulikuwa na migahawa kadhaa midogo kwa ajili ya kuuza vyakula kwa wasafiri. Na bila kusahau maduka madogo ya bidhaa mbalimbali yaliyokuwa yakizunguka eneo la ile stendi ya mabasi ya mji wa Ikwiriri.


Niliwaona wapiga debe wawili watatu wa eneo lile la stendi ya mabasi walionipokea kwa bashasha zote, hata hivyo, hali niliyoikuta katika stendi ile ilinitia wasiwasi kidogo.


Nilishuhudia abiria wengi waliokuwa wamezagaa katika stendi ile huku mizigo ikiwa imejazana katika jengo la ofisi ya usafirishaji kwa namna ya kuashiria kuwa huduma za usafiri zilikuwa zimesitishwa kwa muda, ingawaje wapiga debe wa eneo lile la stendi walikuwa wakiendelea kupiga debe kuwaambia abiria kama mimi tuliokuwa tukiendelea kufika eneo lile kuwa tusiwe na hofu kwani tutapata tu usafiri.


Hatimaye nikaamua kuwauliza abiria wenzangu niliowakuta katika eneo lile la stendi kuhusu kilichokuwa kikiendelea pale, na baada ya kudadisi nikagundua kuwa safari za mabasi, si Ikwiriri peke yake bali nchi nzima, zilikuwa zimesitishwa kwa muda usiojulikana kutokana na mgomo wa madereva wa mabasi kwa nchi nzima.


Abiria mmoja mtu mzima alinieleza kwamba madereva wote wa mabasi nchi nzima walikuwa wanasubiri tamko kutoka kwa viongozi wa chama cha madereva ambao walikuwa kwenye mazungumzo na serikali yaliyokuwa yanaendelea muda ule jijini Dar es Salaam, na baada ya kuafikiana lingetolewa tamko ndipo safari zingeanza tena kama kawaida.


Kwa kweli hali ile ilinikatisha tamaa kwani nilianza kuona kulikuwa na dalili za kutofika jijini Dar es Salaam kwa siku ile, na kama nisingefika Dar es Salaam siku hiyo inamaanisha kuwa ningekuwa nimekosa dili nono la fedha.


Niliendelea kusimama pale huku nikijishauri nini cha kufanya na hatimaye nikaamua kutafuta namna yoyote ile ya kunifikisha Mbagala jijini Dar es Salaam kabla ya jua kutua ili niwahi dili la fedha, ambazo ingekuwa ni dhambi kubwa kama nisingezitia kibondoni.


Nikiwa bado nipo katika eneo lile la stendi ya mabasi ya Ikwiriri nikaanza kuyatembeza macho yangu eneo lile katika namna ya kuzichunguza sura za abiria waliokuwa eneo lile waliokuwa wakisubiri usafiri wa kuelekea sehemu mbalimbali za nchi.


Kwa kufanya vile nikagundua kuwa vijana walikuwa wachache sana katika eneo lile ukilinganisha na akina mama na wazee. Niligeuza shingo yangu kutazama huku na huko nikionekana kukata tamaa.





Niliendelea kushangaa shangaa pale stendi ya mabasi kwa zaidi ya saa tatu lakini hali ilikuwa ni ile ile na hakukuwa na dalili yoyote ya kupata usafiri wa kunifikisha jijini Dar es Salaam.


Hata hivyo, wapiga debe katika eneo lile waliendelea kutusisitiza tuwe na subira kwani kikao kilikuwa kinaendelea jijini Dar es Salaam na wakati wowote wangefikia mwafaka. Kwa kuwa nilikwishaanza kuchoka, nilishika kichwa changu na kufumba macho yangu nikaanza kuwaza mbali sana.


Maswali mengi yalikuwa yakipita kichwani kwangu pasipo kupata majibu, lakini kubwa lilikuwa ni iwapo nilitakiwa niendelee kuvuta subira au ningerudi nyumbani kwa Amir nikasubiri hadi siku ambayo ule mgomo wa madereva wa mabasi ungesitishwa.


Lakini nilijikuta nikipingana kabisa na wazo la kurejea nyumbani kwa Amir ili nisubiri hadi mgomo uishe, sikupenda kulala tena pale Ikwiriri.


Nilivuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani kisha nikazishusha taratibu, nikaona busara ilikuwa ni kutembea tembea kidogo eneo lile ili kujaribu kutafuta namna yoyote ya kuondoka pale, hivyo taratibu nikaanza kupiga hatua zangu nikiifuata barabara ile iliyoelekea Dar es Salaam kana kwamba nilikuwa nimeamua kwenda Dar es Salaam kwa miguu.


Hata hivyo swali moja likanijia akili kwangu, nilikuwa nakwenda wapi na kama ningekosa kabisa usafiri wa kunipeleka jijini Dar es Salaam ningefanya nini, lakini sikupata jibu.


“Today is going to be a very long day,” (Leo itakuwa siku ndefu sana) niliwaza huku nikiendelea kutembea taratibu, kichwa change nilikuwa nimekiinamisha na macho yangu yakiangalia chini kana kwamba nilikuwa natafuta jibu la maswali yangu kwenye ardhi.


Wakati natembea taratibu nikiwa katikati ya barabara nilikuwa nikigeuza shingo yangu mara kwa mara kutazama nyuma yangu, na nikiwa nimeanza kukata tamaa mara nikaliona gari dogo aina ya Toyota RAV4 lililokuwa likija nyuma yangu kwa mwendo wa kasi.


Nilishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani huku nikisimama katikati ya barabara na kuanza kupunga juu mikono yangu yote miwili kumtaka dereva asimame. Ghafla nilijikuta nikiwa nimepata nguvu mpya na sauti fulani ndani yangu ilikuwa ikinisisitiza kuendelea kupunga mikono yangu juu.


Sikujua ni kwa nini nilipata matumaini mapya baada ya kuliona gari lile na sikujua iwapo nilitakiwa kuendelea kuitii ile sauti ndani yangu iliyoniambia niendelee kupunga mikono yangu na nisitoke pale katikati ya barabara.


Dereva wa lile gari hakuonesha dalili zozote za kutaka kusimama, aliwasha taa za mbele za gari lake kuniashiria kuwa niondoke katikati ya barabara, lakini nilikaidi na kuendela kusimama pale pale katikati ya barabara huku nikizidi kupunga mikono yangu yote miwili juu kwa nguvu kumtaka dereva wa gari asimame.


Hatimaye yule dereva aliyeonekana kuwa na umri kama wangu alikanyaga breki kwa nguvu na gari lake likasota na kuyumba kwenye ile barabara ya lami huku akijaribu kunikwepa.


Hatimaye lile gari lilisimama huku yule dereva akisonya kwa hasira na kukunja ngumi huku akipiga ngumi katikati ya usukani wa gari lake kwa hasira, muda ule lile gari lilikuwa limesimama hatua chache tu mbele yangu.


Dereva wa lile gari alikuwa kijana wa umri wangu mwenye asili ya Kiarabu, japokuwa alikuwa ameketi lakini niliweza kubaini kuwa alikuwa mrefu na mwenye umbo kubwa, alikuwa amevaa kofia aina ya kapelo kama yangu na alivaa miwani myeusi ya jua.


Alishusha kioo cha dirisha na kunitazama kwa makini huku akionekana kukerwa sana na kitendo changu cha kumlazimisha kusimama wakati hakuwa na mpango wa kusimama.


Bila kujali namna alivyokuwa akinitazama au kuniwazia, nilimsogelea na kusimama kando ya kioo cha dirisha lake huku nikijaribu kutengeneza tabasamu la kirafiki katika kujaribu kumfanya anisikilize na kulipa uzito ombi langu.


Wakati namsogelea yule dereva alibaki kimya akiendelea kunitazama kwa makini huku akiwa amekunja sura yake kiasi cha kutengeneza matuta madogo madogo usoni kwake.


Nilisimama pale dirishani kwake nikamshuhudia akinitazama kwa utulivu mkubwa japokuwa macho yake yalikuwa yameficha hasira na kiburi. Wakati nataka kumsalimia nikamuona akitaka kusema kitu kisha akasita na kukunjua uso wake, kisha nikamuona akiachia tabasamu bashasha la urafiki lililonipa ahueni kidogo.


“Hey nigga! What are you doing here?”(Unafanya nini hapa?) alimaka yule dereva kwa furaha huku akinitupia swali mara tu niliposimama usawa na dirisha lake.


“It’s you Bilali, right? Long time no see!” (Ni wewe Bilali, au siyo? Siku nyingi sana sijakutia machoni!) yule dereva aliendelea kuongea kwa furaha huku akishusha pumza ndefu bila hata kunipa muda wa kujibu maswali yake.


Nilimtazama kwa makini nikijaribu kukumbuka kama niliwahi kumuona sehemu yoyote, lakini sikuweza kukumbuka, ingawa sura yake haikuwa ngeni kabisa machoni kwangu. Nikajiambia kuwa huenda alikuwa mmoja wa watu niliowahi kufanya nao biashara.


Yule dereva aligundua hilo, akaipandisha juu miwani yake aliyokuwa amevaa na kunikazia macho huku akinitazama kwa makini bila kupepesa macho.


“Don’t you remember me, Bilali? It’s me, Adnan Fahad, tulisoma wote pale Benjamin Mkapa High School…” mara tu alipovua miwani yake na kuanza kujitambulisha kwangu nikamkumbuka vyema.


Nilijikuta nikiruka kwa furaha baada ya kutambua kuwa kumbe dereva yule alikuwa ni ‘school mate’ wangu, maana sasa matumaini ya kupata usafiri wa kunifikisha jijini Dar es Salaam yalikuwa yamefufuka upya.


Nikakumbuka kuwa ni kweli nilisoma na Adnan Fahad darasa moja pale Benjamin Mkapa High School na baada ya kumaliza pale tuliendelea kukutana hadi pale alipoondoka nchini na kuelekea Afrika Kusini takriban miaka saba iliyokuwa imepita.


Nikakumbuka kuwa wakati tukisoma pale Benjamin Mkapa, Adnan na familia yake walikuwa wakiishi eneo la Ilala katika Mtaa wa Tanga, wakati huo mimi nilikuwa nikiishi na kaka yangu katika eneo la Buguruni nyuma ya kituo cha daladala cha Rozana. Tulipomaliza shule Adnan alianza kujishughulisha na biashara ya kuuza magari na spea za magari ya Kijapani.


Mara ya mwisho kuonana na Adnan ilikuwa ni pale alipokuwa akisafiri kwenda Afrika Kusini wakati mimi wakati huo nilikuwa nimejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea biashara.


Nilimtazama Adnan kwa tabasamu, na yeye aliendelea kunitazama huku akitabasamu, kisha nikanyoosha mkono wangu kumsalimia. “How are you doing?” (Hujambo?)


“I’m okay… I’m doing fine, my friend,” (Niko poa… sijambo, rafiki yangu) alinijibu Adnan huku akitoa mkono wake na kunipa, alionekana mwenye siha njema.


“You are too fat, that’s why I almost forget you. When did you come back from South Africa?” (Umenenepa sana, ndiyo maana kidogo nikusahau. Umerudi lini kutoka Afrika Kusini?) nilimuuliza huku nikimtazama kwa makini.


“It’s been a year now since I came back,” (Ni mwaka sasa tangu nirudi) alisema Adnan na kuendelea, “Si unajua Mzee Fahad alifariki dunia? Kwa hiyo familia ikanitaka nirudi ili kusimamia miradi aliyoiacha.”


“C’mon, man, don’t tell me!” (Wacha wee, usiniambie!) nilimaka kwa mshtuko mkubwa sana huku nikimkazia macho Adnan. “Mzee Fahad amefariki dunia! Lini?” niliuliza nikiwa bado nina mshtuko mkubwa.




“It’s been a year now since I came back,” (Ni mwaka sasa tangu nirudi) alisema Adnan na kuendelea, “Si unajua Mzee Fahad alifariki dunia? Kwa hiyo familia ikanitaka nirudi ili kusimamia miradi aliyoiacha.”


“C’mon, man, don’t tell me!” (Wacha wee, usiniambie!) nilimaka kwa mshtuko mkubwa sana huku nikimkazia macho Adnan. “Mzee Fahad amefariki dunia! Lini?” niliuliza nikiwa bado nina mshtuko mkubwa.


Endelea...


“Mbona umeshapita mwaka na ushee sasa tangu alipofariki dunia! Tulizika na tayari tumekwisha sahau…” alinijibu Adnan kisha kama aliyekumbuka jambo akanitupia swali. “Why are you here, what are you doing here, Bilali?” (Mbona uko hapa, unafanya nini hapa, Bilali?)


“Naelekea Dar es Salaam, lakini nimekwama hapa kwa takriban saa nne sasa sababu ya mgomo wa madereva wa mabasi nchi nzima,” nilimwambia Adnan kwa huzuni


“Daah… Pole sana ndugu yangu, bahati mbaya na mimi naishia Kibiti. Lakini kama hutajali, naweza kukusogeza hadi hapo Kibiti najua ukifika hapo huwezi kukosa namna ya kufika jijini,” aliniambia Adnan huku akiniashiria nizunguke upande wa pili niingie kwenye gari.


Nami sikujivunga nilizunguka upande wa pili wa lile gari nikafungua mlango wa nyuma wa abiria na kupanda ndani ya gari.


Ndani ya gari lile kulikuwa na watu wengine watatu, mwanadada mmoja mrembo wa Kiarabu ambaye sikuweza kumtambua alikuwa ameketi kwenye siti ya mbele kushoto kwa dereva, na kwa mwonekano wa haraka tu ungeweza kubaini kuwa ki umri hakuwa amezidi miaka ishirini na nane.


Kwenye siti mbili za nyuma kulikuwa na kijana mdogo wa kiume ambaye nilipomtazama mara moja tu niliweza kuhisi kuwa alikuwa ni mtoto wa Adnan kwa kuwa walifanana sana.


Alikuwa na umri wa kukadiria wa miaka mitano hivi na alikuwa ameketi kwenye siti ya katikati na kando yake aliketi mwanadada mwingine mrembo wa Kiarabu ambaye nilipomuona tu nikamtambua mara moja kuwa alikuwa ni dada wa Adnan aliyeitwa Jameela.


Jamila alikuwa mdogo kwa Adnan, japokuwa wakati ule mimi na Adnan tulipokuwa tunasoma pale Benjamin Mkapa High School Jameela alikuwa bado yupo shule ya msingi, lakini sura yake haikuwa imebadilika, hivyo niliweza kumtambua mara moja.


Wakati naingia na kuketi kule nyuma, Jameela alikuwa akinitazama kwa tabasamu la bashasha, akanisalimu kwa bashasha zote huku akionekana kubabaika kidogo na utanashati wangu. Niseme tu kuwa nilikuwa miongoni mwa vijana wachache sana waliokuwa na mvuto wa hali ya juu kwa wasichana warembo wa sampuli ile ya Jameela.


Nami niliitikia ile salamu yake kwa bashasha na kumuuliza habari za siku nyingi lakini Jameela alinijibu kwa kifupi huku akionesha kuwa na uoga fulani hivi, mara kwa mara alikuwa akimtupia jicho la wizi Adnan, jicho lililokuwa limebeba hofu fulani.


Baada ya kusalimiana na Jameela niligeuza shingo yangu kumtazama yule mwanadada mwingine aliyekuwa ameketi kule mbele kushoto kwa dereva, nikamsalimia pia kwa bashasha ili isionekane kuwa nilikuwa nabagua. Wakati wote huo nikiwasalimia wale wasichana Adnan alikuwa kimya akinitazama kwa makini.


Nilipomaliza salamu Adnan akanitambulisha kwa yule mwanadada aliyekuwa ameketi kwenye ile siti ya abiria ya mbele kushoto kwake kuwa alikuwa ni mke wake, Ada Abdulaziz, na yule mtoto aliyekuwa ameketi kule kwenye siti ya nyuma alikuwa mtoto wao na alikuwa amempa jina la baba yake, Fahad.


Alipomaliza utambulisho ule akaniuliza kama na mimi nilikuwa nina mke na watoto. Swali lile likanifanya nitabasamu kidogo huku nikimtupia jicho la wizi Jameela ambaye wakati wote huo alikuwa anatabasamu tu huku akiviminyaminya vidole vya mikono yake kama mtoto aliyekuwa anadeka.


Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha nikamjibu Adnan kuwa nilikuwa bado sijaoa na wala sikuwa na mchumba. Jameela akaonesha mshangao mkubwa uliochanganyika na furaha na kuniuliza swali kuwa iliwezekanaje kwa mwanaume mzuri kama mimi kusema kuwa nilikuwa sijaoa na sikuwa na mchumba?


Nilimjibu kuwa nilikuwa bado natafuta mwenza wangu kwa kuwa niliamini kuwa mke mwema hupatikana kwa subira na muda ukifika hakuna kitu ambacho kingenizuia kuoa. Nilisema na kuangua kicheko hafifu.


Wakati nilipokuwa nikiongea maneno yale niligundua jambo moja, ilionekana wazi kuwa swali la Jameela halikuwa limemfurahisha kabisa Adnan, kwani aligeuka na kumkata jicho lililoashiria kuchukizwa. Kwa swali lile ilionekana kana kwamba Jameela alikuwa amefanya dhambi fulani kubwa ambayo ilimshangaza hata shetani.


Nilibaki kimya na muda ule ule Adnan aliliondoa gari na safari ya kuelekea Kibiti ikaanza. Kuanzia hapo hakukuwa na stori tena, tulisafiri tukiwa kimya kabisa kwa kitambo kirefu hadi pale nilipoamua kuanzisha maongezi kwa kumuuliza Adnan ni wapi walikokuwa wakitoka.


“Tunatoka Lindi kwenye shughuli ya harusi ya mdogo wake waifu, tulienda juzi na ndoa ilikuwa jana,” Adnan aliniambia.


“Okay… na Kibiti kuna nini tena?” nilimsaili Adnan katika namna ya kutaka kuwachangamsha baada ya kuhisi hali fulani ya ukimya ndani ya lile gari.


“Ooh, hivi sijakwambia? Kabla mzee Fahad hajafariki dunia alikuwa kahamishia makazi yake Kibiti ambako alifungua miradi mbalimbali, ile nyumba ya Ilala aliamua kuipangisha,” alisema Adnan na kunifanya nishangae kidogo.


“Ooh, kumbe! Bahati mbaya tangu ulipoondoka kwenda South Africa nilifika mara moja au mbili tu pale nyumbani Ilala halafu nikakata mguu, hivyo nikawa sijui kinachoendelea,” nilimwambia Adnan.


“Kuna siku moja tu, nadhani ilikuwa mwaka juzi, nilikutana na kaka yako Feisal nikiwa katika mishemishe zangu, akaniambia kuwa bado uko South Africa,” nikaongeza.


“Kama ni mwaka juzi kweli nilikuwa South Africa. Hata hivvyo, mbona sikuondoka moja kwa moja, nilikuwa narudi nyumbani nakaa siku mbili tatu kisha kuondoka! Si unajua tena unapokuwa na mke hutakiwi kuwa mbali kipindi kirefu, utashangaa siku unarudi home unakuta mkeo ameolewa,” alisema Adnan huku akigeuza shingo yake kumtazama mkewe na kuachia kicheko hafifu.


Wote tukajikuta tukiangua kicheko. Lakini muda wote wa mazungumzo yetu Jameela alikuwa mkimya sana na sasa alikuwa ameegemeza vizuri kichwa chake kwenye siti huku akinitupia jicho la wizi mara kwa mara. Nilivyomchunguza niligundua kuwa alikuwa akitamani sana kuchangia maongezi lakini ni wazi alikuwa akimuogopa sana kaka yake.


Kutokana na hali ile hisia fulani hivi ndani yangu zikaanza kunipata na kunifanya nihisi hali isiyokuwa ya kawaida kukaa karibu na Jameela, ingawa hiyo haikuwa mara yangu ya kwanza kukaa karibu na Jameela, kwani alipokuwa akisoma Sekondari ya Kisutu, Adnan aliniomba niwe namfundisha hesabu kwa kuwa nilikuwa bingwa wa hesabu darasani.


Na kipindi chote hicho nilikuwa nikimchukulia kama dada yangu wa tumbo moja na yeye aliniona kama kaka yake, sawa na alivyokuwa akimchukulia Adnan, na sikuwahi hata siku moja kufikiria kama ningeweza kuanzisha uhusiano wowote wa kimapenzi na binti yule.


Hivyo nilianza kujiuliza kwa nini Jameela alikuwa akinitazama kwa jicho la aina ile tena kwa wizi kana kwamba alikuwa ameniona kwa mara ya kwanza! Hata hivyo, sikutaka kumnyima nafasi ile ya kunitazama, hivyo mara kwa mara nikawa nikizuga kutazama nje ya gari lile kupitia kioo kisafi cha dirisha.


Niligundua kuwa jicho la Jameela lilipokuwa likiniangalia kwa namna moja au nyingine lilikuwa linazidi kuamsha hisia zangu na kuyaruhusu mawazo mengi kuanza kupitia kichwani kwangu, nilianza kujiuliza maswali mengi pasipo kupata majibu: kwanza kwa nini alishangaa sana na kuonesha furaha pale aliposikia kuwa nilikuwa sijaoa na wala sikuwa na mchumba?


Je, swali lake kuwa iliwezekanaje kwa mwanaume mzuri kama mimi kusema kuwa sijaoa na sina mchumba liliashiria nini kwa mtazamo wake, kwamba sikupaswa kusema vile au ilikuwa ni dhambi kwangu kutokuwa na mke wala mchumba?


Maswali hayo na mengine mengi yalizidi kupita kichwani kwangu, hata hivyo, sikutaka kuyapa sana nafasi maana sikujua Jameela alikuwa anawaza nini juu yangu. Huenda aliniona kama kijana mhuni fulani asiyeweza kuishi na mwanamke au pengine nilikuwa mtu fulani asiye na mbele wala nyuma!


“Hivi mnakabilianaje na hali hii mbaya ya kiusalama hapo Kibiti?” nilimuuliza Adnan baada ya kitambo kirefu cha ukimya ndani ya lile gari..


“Kwa kweli hali ni mbaya, hata hivyo serikali inajitahidi sana kudumisha usalama ingawa kuna kitu wengi hawakijui kuhusu haya mauaji yanayoendelea,” alisema Adnan na kunifanya nikae vizuri kusikia mambo niliyokuwa siyajui juu ya yale mauaji yale yaliyojumuisha maeneo yote ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji .




Mtunzi Bishop Hiluka


Maswali hayo na mengine mengi yalizidi kupita kichwani kwangu, hata hivyo, sikutaka kuyapa sana nafasi maana sikujua Jameela alikuwa anawaza nini juu yangu. Huenda aliniona kama kijana mhuni fulani asiyeweza kuishi na mwanamke au pengine nilikuwa mtu fulani asiye na mbele wala nyuma!


“Hivi mnakabilianaje na hali hii mbaya ya kiusalama hapo Kibiti?” nilimuuliza Adnan baada ya kitambo kirefu cha ukimya ndani ya lile gari..


“Kwa kweli hali ni mbaya, hata hivyo serikali inajitahidi sana kudumisha usalama ingawa kuna kitu wengi hawakijui kuhusu haya mauaji yanayoendelea,” alisema Adnan na kunifanya nikae vizuri kusikia mambo niliyokuwa siyajui juu ya yale mauaji yale yaliyojumuisha maeneo yote ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji .


Endelea...


“Kuna mambo makubwa mawili nyuma ya mauaji haya ambayo ni chuki za kisiasa, na chuki za wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi…” alisema na kugeuza shingo yake kunitazama.


“Ki vipi, hebu nielezee vizuri maana sisi huko Dar es Salaam tumekuwa tukisikia tu mara ni wapinzani ndiyo wanaofanya hivyo, mara eti ni kikundi cha wafuasi wa alshabab, na maneno mengine kibao. Hivi wewe unayachukuliaje hasa mauaji haya?” nilimuuliza Adnan nikiwa na shuku kubwa ya kusikia.


“Kwa wasiojua kinachoendelea huku kwetu watasema hivyo, maana nchi hii kila mmoja anasema lake, na mtayasikia mengi tu…” alisema Adnan, na kuendelea.


“Ujue kuna kitu kimoja, ukweli…” alisema na kusita, mara nikamsikia akiguna. Nilipomtazama kwa makini nikamuona akionekana kushtuka sana huku akikodoa macho yake kutazama kwenye dashibodi ya gari.


Nami nikayapeleka macho yangu kutazama pale kwenye dashibodi ya lile gari na kuona taa ndogo ya njano ikiwaka na mshale wa mafuta ukienda kombo, na hapo nikajua kuwa mafuta kwenye lile gari yalikuwa yakielekea kuisha.


“Dah, nilisahau kabisa kuongeza mafuta tulipofika pale Ikwiriri, naona yanaelekea kuisha. Sijui kama yatafanikiwa kutufikisha pale Kibiti Lake Oil ili tujaze mafuta mengine,” Adnan alisema kwa wasiwasi huku akigeuza shingo yake kumtazama mke wake ingawa sauti yake ilikuwa tulivu.


Hata hivyo, aliendelea kuwa makini sana kuudhibiti vizuri usukani wa lile gari kwenye kipande kile korofi cha barabara.


“Hmm, mafuta yameisha kabisa!” Ada aligutuka na kumtazama Adnan kwa wasiwasi.


“Hayajaisha kabisa, ila kwa sasa tunatembelea rizevu,” alisema Adnan huku akiongeza kasi ya gari.


“Naamini Mungu atatusaidia yataweza kutufikisha Kibiti Lake Oil Petrol,” safari hii Ada aliongea kwa hisia fulani iliyoonesha kukata tamaa. Hata hivyo, Adnan hakutia neno lolote bali alikuwa makini zaidi akiyakaza macho yake barabarani.


Baada ya kitambo kirefu cha safari tukakivuka kile kipande kile kifupi korofi cha barabara na hapo Adnan alikanyaga pedeli ya mafuta na gari ikaongeza mwendo ikipita katikati ya msitu, na tulipokwenda mbele zaidi kama kilomita tano hivi tukaanza kukiona kituo cha kujazia mafuta cha Kibiti Lake Oil Petrol kikiwa mbele yetu upande wa kulia kwetu.


Sasa sikuwa na mashaka kuwa kituo kile cha kujazia mafuta ndiyo kile alichokuwa amekizungumzia Adnan hapo awali. Muda mfupi uliofuata akachepuka na kuingia upande wa kulia na kwenda kuegesha gari kwenye upande wenye pampu ya kujazia mafuta ya petroli chini ya paa kubwa la kituo kile cha Kibiti Lake Oil.


Pale Kibiti Lake Oil kulikuwa na magari mawili, gari moja lilikuwa aina ya Noah na jingine lilikuwa ni roli la mafuta lililokuwa limeegeshwa kando ya kile kituo cha kujazia mafuta. Mbali na magari yale mawili hapakuwa na dalili ya gari jingine lolote eneo lile. Kulikuwa na wafanyakazi kama watatu niliowaona katika eneo lile, kati yao wawili walikuwa wa kike na mmoja wa kiume wakiwa wamevaa sare maalumu za kituo kile cha Kibiti Lake Oil.


Adnan aliliegesha gari lake mbele ya msichana mmoja aliyekuwa amesimama kwenye pampu moja na bila kupoteza aliinama na kubonyeza kitufe fulani cha kufungua mfuniko wa tenki la mafuta.


Kisha bila kuchelewa alitoa pochi yake mfukoni na kuifungua kisha akahesabu na kutoa noti tano za shilingi elfu kumi kumi na kufungua mlango wa gari yake, akashuka. Aliposhuka nilimuona akisimama jirani na yule mfanyakazi wa kike wa kile kituo cha kujazia mafuta na kumpa zile noti.


Zoezi la kujaza mafuta likafanyika kwa muda mfupi tu, kisha muda huo huo Ada alishuka kutoka kwenye gari na kuonekana akinong’ona jambo kwa Adnan. Baada ya kujaziwa mafuta Adnan aliufunga ule mfuniko wa tenki la mafuta kisha yeye na Ada wakachepuka kidogo kwenda kwenye vyoo vya kile kituo cha Kibiti Lake Oil, nadhani walikwenda kushusha haja ndogo.


Niligeuza shingo yangu kumtazama Jameela ambaye muda wote alikuwa kimya kabisa kainamisha uso wake chini huku aking’ong’ona kucha zake za vidole vya mkono wa kulia, akionekana kuwa mbali sana kimawazo.


Sikutaka kujivunga, nikaona kuwa ule ndiyo ulikuwa wakati mzuri wa kuongea naye ili kujua kilichokuwa kikiendelea kati yake na kaka yake, maana ilionekana kama hakuwa huru mbele ya Adnan. Hivyo nikaamua kuutumia mwanya ule ambao Adnan na Ada walikuwa wamekwenda kujisaidia kumuuliza maswali Jameela.


“Jameela, what’s wrong with you?” (Jameela, una tatizo gani?) nilimuuliza huku nikimtazama kwa makini.


“Nothing!” (Hakuna!) alinijibu huku akiwa haniangalii machoni.


“You didn’t tell me, are you also married?” (Hukuniambia, na wewe umeolewa?) nilimtwanga Jameela swali jingine ambalo lilimfanya anitupie jicho na kuachia tabasamu dogo huku akiviminyaminya vidole vya mikono yake.


Nilimuona Jameela akishusha pumzi za ndani kwa ndani na kubaki kimya kwa kitambo kidogo kama aliyekuwa akifikiria au akitunga jibu la kunipa, kisha akanitazama moja kwa moja machoni huku akiendelea kunionesha tabasamu lake maridhawa.


“I’m not married, ila familia tayari imeshanitafutia mchumba,” Jameela alisema kwa sauti tulivu huku akitupa macho yake kutazama kule kwenye vyoo vya kile kituo cha kujazia mafuta cha Kibiti Lake Oil.


“Umetafutiwa mchumba na familia! Hadi karne hii bado yapo mambo ya kutafutiana wachumba!” nilisema huku nikionesha kushangazwa sana na maelezo yake.


“So, where is your fiancé?” (Kwa hiyo, mchumba wako yuko wapi?) nilimuuliza Jameela kwa shauku huku nikiendelea kumkazia macho kwa mshangao. Jameela aliminya midomo yake huku akishusha pumzi ndefu.


“He’s in Oman, I’ve never seen him, but Adnan and my mother know him,” (Yuko Oman, mimi sijawahi kumuona, ila Adnan na mama wanamfahamu) alinijibu Jameela huku akionekana kutofurahia maongezi yale na ilionesha wazi kuwa ama alikuwa hampendi au hakupenda kuulizwa kuhusu mchumba huyo.


“It’s very strange!” (Ni ajabu sana!) nilishindwa kujizuia kushangaa. Japokuwa Jameela hakuonesha kuyafurahia maongezi yale lakini nilikuwa na shauku ya kutaka kujua mengi zaidi kutoka kwake, ingawa nilishindwa kuyauliza kwa sababu nilihisi donge fulani la wivu lilikuwa likinikaba kooni.


“When are you going to be married?” (Lini mtaoana?) nilimuuliza tena.


“He’s waiting for me to finish my studies, nikimaliza tu ndipo process zingine zianze,” alisema huku akiinamisha uso wake kutazama chini.


“Okay! I’m sure you will definitely get married sooner when you finish your studies,” (Nina uhakika mtafunga ndoa mara moja mara tu utakapokuwa umemaliza shule) nikamwambia Jameela huku moyoni nikihisi wivu jambo lililoanza kunishangaza. Tangu lini nikaona wivu juu ya Jameela niliyemchukulia kama dada’angu, mdogo wangu!


“If God wishes…” (Kama Mungu akipenda) Jameela aliongea kwa unyonge na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani kisha akageuka tena kutazama kule kwenye vyoo vya kile kituo cha kujazia mafuta.


Kitendo cha Jameela kutazama kule kwenye vyoo vya kile kituo cha kujazia mafuta kikanifanya nami kugeuza shingo yangu kutazama upande ule kisha nikamtazama Jameela kwa udadisi zaidi.


“Kwani unasomea nini?” nilizidi kumuuliza maswali huku nikishangaa.


“Nasomea sheria University of Dar es Salaam, nipo mwaka wa mwisho,” alisema huku akiminya midomo yake na kuachia tabasamu laini lililozidi kunichanganya.





“Ooh! I’m sure he’s very luck wherever he is, to have a beautiful wife who is a lawyer to be, (Nina uhakika ana bahati sana kokote aliko, kupata mke mwanasheria mtarajiwa) nilisema kwa utani huku nikiachia kicheko hafifu. Jameela alibaki kimya pasipo kuonesha tashwishwi yoyote.


“I wish I would also look for a lawyer,” (Natamani na mimi pia nitafute mwanasheria) niliongea kwa utani huku nikiendelea kucheka kicheko hafifu.


Kauli hiyo ilimfanya Jameela anikate jicho ambalo sikuweza kuelewa lilikuwa na maana gani, alitaka kusema neno lakini akasita na kushusha pumzi ndefu kisha akainamisha uso wake chini akionekana kuwaza mbali.


Nilimtazama kwa makini nikajikuta napata uhakika kwamba hakuwa akiyafurahia kabisa maongezi yale, sikujua ni kwa nini alionesha hali ile ya kutoyafurahi mazungumzo yale ilhali mwanzoni tulipokuwa tukija nilimuona akitamani sana kuchangia mazungumzo!


Maswali mengi yalianza kuzunguka kichwani kwangu lakini nilifikia uamuzi wa kukaa kimya ili nisije nikamkwaza zaidi. Nilipotupa macho yangu kule kwenye vyoo vya kile kituo cha kujazia mafuta nikawaona Adnan na Ada wakirudi taratibu kwenye gari.


Jameela alinitazama kwa makini na kushusha tena pumzi zake ndani kwa ndani, akatoa haraka simu yake kutoka kwenye mkoba wake mdogo na kunipa akiniomba niandikie namba yangu ya simu.


Niliipokea ile simu na kuandika haraka namba yangu kisha nikamrudishia ile simu, nikamuona akiipiga ile namba pale pale na simu yangu ilipoita aliachia tabasamu na kukata simu.


Kisha aliirudisha simu yake kwenye mkoba na kuegemeza kichwa chake kwenye siti kama mwanzo na kufumba macho yake akijifanya kuwa amepitiwa na usingizi.


Niliitazama kwa makini ile namba ya simu ya Jameela iliyoonekana kwenye kioo cha simu yangu na kuihifadhi kwenye sehemu maalumu ya kuhifadhia majina ndani ya simu huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani, kisha nikairudisha simu yangu kwenye mfuko wa suruali.


Adnan na mkewe Ada wakafika na kuingia kwenye gari, wakanitaka radhi kwa kuchelewa kidogo na hapo safari yetu ikaanza tena tukiondoka eneo lile na kuingia barabarani.


Tulikwenda kitambo fulani cha safari nikaanza kuuona mji wa Kibiti kwa mbali wenye nyumba nyingi. Nyumba hizo baadhi zikiwa ni za kisasa na nyingine kuukuu kama za vijijini na baada ya muda tukaanza kukatisha katikati ya makazi ya watu katika barabara ile.


Tuliendelea kukatisha katikati ya yale makazi ya watu katika mji ule mdogo kisha tukaingia eneo ambalo wenyeji walipaiya mjini, muda huo ilikuwa tayari imetimia saa nane mchana.


Adnan aliniacha katika stendi ya mabasi ya Kibiti na kunitakia safari njema endapo nitabahatika kupata usafiri. Nilimshukuru sana Adnan na kuwatakia wote safari njema ya kule walikokuwa wakielekea, pia nilimtaka anifikishie salamu zangu kwa mama na wanafamilia wengine.


Mara tu nilipokanyaga miguu yangu katika stendi ya mabasi ya Kibiti nilishtuka kukuta hata pale Kibiti abiria waliokuwa wanasubiri usafiri wa kuelekea maeneo mbalimbali walikuwa wengi sana na walionekana kukata tamaa.


Nilisimama pale nikiwa sijui nifanye nini, nilianza kuchunguza eneo lile kuona kama kungekuwepo uwezekano wa kutafuta njia mbadala ya kuweza kunifikisha Dar es Salaam lakini sikuona chochote zaidi ya bodaboda zilizokuwa zikizunguka eneo lile.


Nilitaka nikodi bodaboda ili inipeleke Dar es Salaam lakini haraka sana nikalipinga wazo hilo, kwani niliwahi kushuhudia jamaa zangu watatu kwa nyakato tofauti wakifa kwa ajali ya bodaboda, sababu ikiwa ni kutaka kuwahi waendako. Nikapiga moyo konde nikiamini kuwa ingetokea gari binafsi iliyoelekeas Dar es Salaam na kutuchukua.


Nilisimama pale kituoni kwa takriban dakika arobaini nikijaribu kubahatisha kama ningeweza kupata usafiri lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo hali ilivyozidi kutananisha.


Nikaamua kuzunguka zunguka eneo lile huku matumaini ya kupata usafiri wa kuelekea jijini Dar es Salaam yakiwa yameanza kutoweka kabisa, hii ilikuwa ni baada ya wapiga debe kunieleza kuwa viongozi wa madereva walishindwa kuafikiana na serikali kuhusu madai yao katika kikao chao kilichokuwa kikifanyika jijini Dar es Salaam.


Kwa hali hiyo, ilimaanisha kuwa safari zote za nchi nzima kwa kutumia mabasi zingeendelea kusitishwa hadi wafikie muafaka na serikali kuhusu madai yao. Taarifa zile zilipowafikia abiria pale kituo cha mabasi Kibiti zikaibua zogo la aina yake, hasa kwa abiria ambao walikuwa wamekata tiketi ambao walianza kudai warudishiwe nauli zao.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog