Search This Blog

Thursday 23 March 2023

HUJUMA NZITO - 1

 

IMEANDIKWA NA :  BADI M. BAO
*********************************************

Simulizi : Hujuma Nzito

Sehemu Ya : Kwanza (1)



Sakarati mauti ya Kapteni Wandawanda Jijini London, Uingereza

Marafiki, ndugu na jamaa wa karibu wa Kapteni mstaafu Wandawanda wakiwa wamegubikwa na nyuso za huzuni, walionekana wamejikusanya sehemu moja, ndani ya hospitali ya "St Thomas' Hospital" iliyopo nchini Uingereza, ndani ya Jiji la London katika barabara ya Westminster Bridge SE1 7EH.

Kwa Watanzania walio wengi, wenye umri wa kuanzia miaka 30 na fauka ya hapo, jina la hospitali hiyo sio geni kwenye masikio yao. Ndani ya jengo la hospitali hiyo, Baba wa Taifa la Tanzania, Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliaga dunia tarehe 14/10/1999.

Ndugu na jamaa hao ambao wengi ni Watanzania waishio nchini Uingereza, walijikusanya hospitalini hapo sio kuadhimisha kifo cha mpendwa wao Hayati Nyerere, bali walikuja kufuatilia kwa ukaribu hali ya afya ya kipenzi chao, Kapteni Wandawanda, aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ndani ya hospitali hiyo.

Kila mmoja wao alishikwa na daka la roho, wanajitahidi kadri wawezavyo kufarijiana wao kwa wao. Walishindwa kabisa kuyazuia machozi kutoka kwenye mboni za macho yao yasichuruzike kutokana na uchungu wa nafsi zao. Walishajiandaa kisaikolojia kupokea taarifa yoyote mbaya juu ya mgonjwa wao.

Kapteni huyo mstaafu wa Jeshi la Wananchi, JWTZ, Bwana Wandawanda alikuwa anapitishwa na Mola wake kwenye sakarati mauti. Katika hali hiyo, mtu anakuwa baina ya uhai na kifo, hivyo huanza kutapatapa katika kupigania roho yake. Kuna wakati alikuwa anapata nafuu na kuleta matumaini ya kupona, kisha hali yake inabadilika ghafla na kumfanya apumue kwa misaada wa mipira ya gesi.

Ghafla bin vuu katika viunga vya hospitali hiyo, likaonekana gari la kifahari la Kijapani, aina ya "Honda Accord" lenye rangi ya kahawia linaingia ndani ya uzio wa hospitali. Likaegeshwa gari hilo kwenye eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya maegesho ya magari.

Wakashuka watu wawili, na kumuacha dereva pekee kubakia ndani ya gari hilo. Watu hao mmoja wapo alikuwa ni mwanamama mweusi wa rangi yake, mrefu kiasi, shaibu wa umri hapungui miaka 70. Mwenzake aliyeambatana nae alikuwa ni kijana wa makamo chotara wa kizungu mkononi amefumbata mkoba mdogo wenye rangi nyeusi.

Huyo mwanamke ni mke wa Kapteni Wandawanda aliambatana na mwanasheria wao, anayesimamia masuala ya urathi katika familia hiyo. Walikuja hospitalini hapo mintarafu kuitikia wito maalumu wa kushtukiza toka kwa Kapteni Wandawanda.

Walipoingia tu ndani ya jengo la hospitali na kukatiza eneo lililotengwa watu kupumzikia, watu wawili miongoni mwa wale ndugu na marafiki waliokuja mapema hospitalini hapo wakanyanyuka vitini na kwenda kuwalaki kwa nyuso za bashasha.
Baada ya habari sijambo na kusogoa kwa dakika mbili tatu, msafara wa watu wanne ukaongozana sako kwa bako kuelekea kwenye lifti kwa ajili ya kuisubiria iwapeleke roshani za juu alipolazwa Kapteni Wandawanda.

"Najiona sina uhai mrefu, saa na wakati wowote kuanzia sasa Malaika mtoa roho nahisi atanitembelea kwenye kitanda changu hicho cha mauti kwa jinsi ninavyougua" alifungua maongezi yake Kapteni Wandawanda kwa watu wake waliomzunguka kitandani.

Walikuwa wamejifungia ndani ya chumba cha mgonjwa hiyo wakisikiliza wosia wake. Baada ya kumeza mate kwa sekunde kadhaa, akaendelea na hotuba yake iliyowatia kiwewe na kuibua taharuki kubwa nafsini mwao.

"Hivyo nimewaita mke wangu na mwanasheria wangu ili muwakabidhi nyaraka zangu za siri nilizozitunza kwa ajili ya vijana wangu hawa wawili" alisema kwa tabu Kapteni Wandawanda huku sasa macho yao wote ndani ya chumba kile yakiwaelekea vijana wale wawili walioambatana nao toka chini ya jengo la hospitali.

Walikuwa ni vijana rika la makamo wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Oxford kilichopo nchini Uingereza, moja ya chuo chenye hadhi ya juu sana nchini humo. Wote walikuwa wanasomea shahada zao za Uzamivu, wakiwa ni waajiriwa katika taasisi tofauti ndani ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vijana hao walikuwa hawakauki nyumbani kwa Kapteni Wandawanda anayeishi katika mtaa wa Cannon Street, Jijini London. Mmoja wao kati yao, alilelewa na kusomeshwa tokea akiwa kinda na Kapteni Wandawanda, huku mwingine waliunganishwa nae na kabila. Wote watatu walikuwa wana asili ya kabila la Nyasa, linalozunguka Ziwa Nyasa.
Enzi za afya yake, walikuwa wawili hao walikuwa ni wabaraza kwenye majilisi, nyumbani kwa Kapteni Wandawanda mpaka manane ya usiku wanasogoa. Walikuwa wanapanga na kupangua mipango yao ya siri, ambayo hata mwandani wa Kapteni haifahamu vizuri kwa undani wake.

"Naomba mwanasheria wangu Mr.Harrison Ferguson uwakabidhi rasmi kimaandishi mkoba wangu mweusi uliokuja nao wenye nyaraka zangu mbalimbali nilizozitunza tokea harakati za ukombozi wa nchi ya Tanganyika toka kwenye makucha ya Mkoloni. Mkazisome kwa umakini na kuzifanyia kazi, mkifanikisha kuyatekeleza yaliyomo humo, mifupa yangu itarukaruka kwa furaha nikiwa jongomeo, mwili wangu umeoza. Mtatimiza ndoto yetu, wazee wenu wa Nyasa tuliyoshindwa kuitimiza kwa miongo kadhaa. Aluta kontinua kila la heri, Dola ya Nyasa itasimama kwa jasho na damu".

Alimalizia maongezi yake mafupi Kapteni Wandawanda huku sasa machozi ya uchungu yanambubujika akiwa yupo juu ya kitanda chake cha mauti.

Baada ya kitambo cha muda wa nusu saa tu, shughuli zote za makabidhiano hayo ya nyaraka hizo zikamalizika. Wote kwa pamoja kama walivyokuja, wakaondoka vichwa chini kama kuku wenye mdondo.
Wakawaacha madaktari na manesi wakifanya kazi yao waliyosomea ya utabibu, kujaribu kuokoa uhai wa mpendwa wao Kapteni Wandawanda.


Wingu zito latanda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dodoma

Yalikuwa ni majira ya usiku mbichi wa saa 1:30 za usiku, kikao kizito kilikuwa kinarindima ndani ya jengo la Makao Makuu mapya ya Jeshi la Polisi yaliyopo Jijini Dodoma. Ulinzi madhubuti uliimarishwa nje na ndani ya jengo hilo la mkutano, lenye roshani nne lililokuwa zamani likitumiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Dodoma.

Ulinzi wa eneo hilo ulikuwa ni wa kutumia kikosi cha farasi, mbwa, kikosi cha mabomu ya machozi na askari wengineo wakiwa wanarandaranda maeneo hayo ili mradi kuhakikisha kuna usalama wa kutosha kwa wakuu hao.

Kikao hicho muhimu kwa mustakabali wa ulinzi na usalama wa nchi kilikuwa kinaongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini-(MJP) mwenyewe huku vigogo wote unaowajua wewe wa jeshi hilo kutokea ngazi ya Mikoa yote Tanzania mpaka Taifani walikuwa wamekusanyika kwenye kikao hicho adhimu na cha siri.

Vigogo hao walichafuka vyeo mabegani mwao kama uchafu, kila mmoja kwa muktadha huo alikuwa ametingwa na kuandika nukuu na dondoo mbalimbali zinazoelekezwa na Bosi wao huyo. Wote walijawa na wahaka katika mioyo yao hawajui kitaisha saa ngapi kikao hicho kilichoanza tokea majira ya alasiri na pia hawafahamu maamuzi yatakayopitishwa na kikao hicho.

"Tokea historia ya kuanzishwa kwa Jeshi letu la Polisi hapa nchini hatujawahi kupata mtikisiko na msukosuko mkubwa kama huu, wa kiasi kikubwa cha pesa nyingi, zaidi ya bilioni 560 kukwapuliwa kwa mkupuo katika Benki tatu kubwa kwa pamoja kwa njia za kieletroniki. Mbaya zaidi mtu ambaye tulimtegemea kuwa angeweza kutupa muongozo na dira ya namna ya kufuatilia sakata hili kubwa kwa ukaribu na umakini, Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya fedha za nje na za ndani wa Benki Kuu, nae taarifa nilizonazo zilizonifikia dawatini kwangu hivi punde tu ni kuwa amepata ajali mbaya ya moto kwenye gari akiwa nchini Afrika ya Kusini.

Taftishi za awali zinasema ameteketea mwili wake vibaya kabisa na amefariki dunia" aliweka kituo cha mazungumzo yake MJP huyo huku akianza kulipuna jasho lake jekejeke lililokuwa linatiririka kwenye paji la uso kwa mkono wake licha ya baridi kali la usiku la Jijini Dodoma.
Hii ilikuwa ni dalili ya kuonyesha kuwa maji sasa yamezidi unga kwa upande wake.

"Sasa kwa kumalizia nawaacheni mkae nyinyi wenyewe mjichinje kibudu na kisu chenu, mjipange vilivyo kwa kujadili ikifika saa 6:00 usiku wa leo, mezani kwangu niwe nimepata jina la mpelelezi makini mwenye viwango vyake ambaye atapewa hili jukumu zito la kupeleleza na kufahamu hizi pesa zimekwapuliwa na watu gani wasioitakia nchi yetu mema katika juhudi zake za kujikwamua na lindi la umaskini. Kila mmoja ameshakabidhiwa kablasha la nyaraka za kuthibitisha wizi huo, lipo hapo mezani kwake na alisome vizuri. Ahsante sana kwa kunisikiliza, Aluta Kontinua" MJP akaagana nao na kutokomea zake kwa haraka pale ukumbini akisindikizwa na mpambe wake.


Maneno ya MJP kuwa uhalifu huu ni wa kihistoria yalikuwa yamewasuta vichwani mwao vilivyo vigogo hao. Ulikuwa ni ukweli usiopingika abadani. Jeshi la polisi tokea kuanzishwa kwake rasmi Agosti 25, 1919 na serikali ya kikoloni ya Uingereza kwa tangazo katika gazeti la serikali namba Vol.1No.21-2583 kuwa Jeshi la Polisi Tanganyika limeanzishwa rasmi, mpaka leo hii ikiwa si chini ya miaka 100 kulikuwa hakujawahi kutokea wizi wa kiasi kikubwa cha pesa kiasi hicho katika matawi tofauti ya benki hapa nchini.


Ilipofika majira ya saa 5:15 usiku, vigogo hao kwa kauli moja ya bila upendeleo wakamteua Inspekta Mengi Matunda, kutoka Polisi Makao Makuu kuongoza timu ya uchunguzi huo.
Wakampatia muda wa mwezi mmoja tu kuhakikisha anakamilisha taftishi yake ili wahusika waweze kutiwa mbaroni. Vigogo hao walijawa na matumaini makubwa na Inspekta Mengi hasa kutokana na umri wake mdogo wa miaka 28. Pia umahiri wake katika kuchapa kazi, bila usongombwingo.

Utendaji wake kazi wa kutukuka ulichangia apandishwe vyeo kwa mserereko. Na ndio alikuwa kwanza na mwezi mmoja tu na ushee tokea amerudi masomoni nchini Israeli. Hivyo hilo likawa ndio jukumu lake la kwanza kukabidhiwa akiwa bado wa motomoto.

Inspekta Mengi akala kiapo cha utii na uaminifu mbele ya vigogo wale huku akiwapa ahadi ya kutekeleza jukumu hilo gumu kwa juhudi, maarifa na vipawa vyake vyote. Saa 6:00 za usiku juu ya alama jina la Inspekta Mengi Matunda likawa lipo mezani mwa MJP kuwa ndio kabebeshwa msalaba huo mzito kwa Jeshi zima la Polisi.

Ilipotimu majira ya alfajiri ya siku hiyo hiyo tokea kutangazwa kwa Inspekta Mengi Matunda kuongoza timu hiyo ya uchunguzi, wingu zito tena jeusi zaidi likazidi kutanda kwenye jeshi hilo la polisi nchini.

Habari mbaya zikaanza kusambaa alfajiri hiyo kama upepo, kuwa Inspekta Mengi Matunda amekutwa ameuliwa kikatili nyumbani kwake maeneo ya Veyula, Makutupora, nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Hilo tukio lilitokea si zaidi ya masaa 7 tokea kuteuliwa kwake. Taharuki ikazidi kumea ndani ya watendaji wakuu wa Jeshi hilo la polisi. Kuthibitisha kuwa uchunguzi wa jambo hilo ni mgumu sana mithili ya kumeza kaa la moto bila kuishia kupata vidonda mdomoni.


Hamkani mambo si shwari tena kila kona ya nchi
Kulipokucha asubuhi na makucha yake, gumzo la Jiji zima la Dodoma, makao makuu ya nchi na Tanzania yake kwa ujumla wake kuanzia mijini mpaka vijijini, lilikuwa ni kifo cha kikatili cha Inspekta Mengi Matunda. Ambaye alikutwa barazani kwake nyumbani akiwa ametumbuliwa matumbo nje na kutobolewa macho yake.
Lilikuwa ni tukio geni kwao la kihalifu lenye munasaba wa ukatili mkubwa kiasi hicho, kwani kwao matukio kama hayo walikuwa wanayasikia kwenye redio na kuyaona kwenye runinga kwenye nchi za jirani lakini sio Tanzania kisiwa cha amani.
Wananchi wa kawaida walipatwa zaidi na taharuki huku wakifanya hisabati za mlinganyo vichwani mwao kuwa kama kigogo a'ali kabisa wa Jeshi la Polisi kama Inspekta Mengi Matunda anauliwa kikatili bila huruma vipi usalama wa raia wa kawaida, wale akina yakhe utakuwaje!.
Mitandao ya kijamii nayo yote ililipuka kwa simulizi hiyo ya kutisha ya kifo hicho cha Inspekta. Wapo waliokuwa wanamsifia ujasiri wake wa kupambana wakisema hakufa kikondoo kuelekea jongomeo kama anaenda harusi, alijitoa jihadi ya nafsi yake kupigania uhai wake.
Wakielezea kuwa alipambana vilivyo na maadui zake na kusababisha damu kutapakaa nyumba nzima kuanzia chumbani kwake mpaka kibarazani kuthibitisha hakufa kirahisi. Pia walikuwepo wale watu wa kupondaponda kila kitu, wakilishutumu Jeshi la polisi kutoa ajira kiushikaji kwa kutumia vimemo vya huyu barobaro wa Shangazi au ni banati wa Mjomba, hali ambayo inayopelekea kutokupata askari makini wenye ujuzi a'ali katika fani zao.
Wakati mitandao hiyo ya kijamii ikiwa bado inazizima na kurindima kwa tukio hilo likaibuka jambo lingine jipya kabisa lililotikisa umayamaya nchi nzima. Ikaandikwa mitandaoni kuwa benki hizo tatu kubwa katika nchi zimetishia kufunga matawi yao ya benki nchi nzima kama hawatohakikishiwa usalama wa pesa za wateja wao.
Ikasemwa wameipa serikali muda wa mwezi mmoja kutafuta ufumbuzi wa suala hilo vinginevyo watahamishia mitaji yao katika nchi za jirani zenye kuhitaji huduma zao kwa udi na uvumba. Siri ikawa si siri tena mambo yakawa hadharani kuwa kuna upigwaji mkubwa wa pesa, zaidi ya bilioni 560 umetokea nchini.
Taklifu isiyotegemewa ikaibuka katika jamii, mambo yakawa hamkani si shwari tena kwa mara nyingine, mchuma janga hula na wa kwao. Misururu mirefu ya Watu kama mabehewa ya treni ya kuelekea Kigoma, ikawa inaonekana kwenye benki mbalimbali wakiwa wananyofoa fedha zao kwenye mashine za kutolea pesa wakahifadhi kwenye vibubu na mchagoni majumbani mwao.
Wapo waliokuwa wanaingia ndani ya benki kabisa kwa wale wanaotaka kutoa pesa sufufu zaidi ya milioni moja na wengine wakiwa wapo kwenye mashine za benki wakiwa katika harakati za kuchomoa pesa zao wakitimiza misemo ya wahenga 'tahadhari kabla ya hatari', 'mchelea mwana mwisho hulia na yeye'.
Soko la hisa na mitaji nako mambo hayakutungamana. Mauzo ya hisa yakashuka kwa kasi mithili ya mbio za duma porini, kuashiria wawekezaji wameingiwa na baridi ya mioyo kwa uwoga wa usalama wa mitaji yao.
Hali ilishakuwa tete tayari, baraza la mawaziri likaitwa Ikulu kujadili hali ya mambo kwenda mrama na namna wanavyoweza kudhibiti. Ndani ya wiki mbili tu tokea kutokea kwa matukio hayo, uchumi wa nchi ulianza kutoa viashiria vya kutetereka.
Chama kikuu cha upinzani cha "National Movement Party" (NMP) kinachoongozwa na Dr.Patrick Ndomba nacho kilicharuka vilivyo kuinanga serikali kwa uzembe uliosababisha mdororo huo wa kiuchumi. Wakawa sasa wanazunguka kuushambulia serikali nchi nzima.
Wakapita kuichachafya na kuishitaki serikali mbele ya wananchi. Chambilecho 'ganda la muwa la jana chungu kaona kivuno', kauli mbiu yao ilikuwa viongozi wa chama tawala ni genge la wapigaji wasio na uchungu wa hali za walalahoi.
Kauli hizo za uchochezi ziliamsha chuki na hasira kwa wananchi dhidi ya serikali yao iliyopo madarakani. Pia uchaguzi mkuu nao ulikuwa ndio unanukia, ilibakia miezi kama saba tu kufanyika. Watabiri na wachambuzi wa upepo wa mambo ya kisiasa walishaanza kubashiri juu ya kuanguka kwa chama tawala kama hali ya uchumi itaendelea kuzorota na kudorora.
Baadhi ya wachambuzi hao wa masuala ya kisiasa wakajaribu mpaka kufananisha kuanguka kwa chama tawala cha KANU cha nchini Kenya kutokana na wananchi kuchoshwa na vitendo vyao vya ufisadi wakati wapo madarakani tokea nchi ipate uhuru wake.
Kikao cha baraza la mawaziri likakabidhi rasmi jukumu la kuhakikisha pesa hizo zilizoibwa zinarejeshwa haraka na wahusika wanafikishwa kizimbani likakabidhiwa kwa Usalama wa Taifa. Jeshi la polisi waliombwa kukaa kando kidogo ila wawe tayari kusaidia pindi wakihitajika.
Mkuu wa Usalama wa Taifa Bwana Omega Mtanika akawa amekabidhiwa rasmi mzigo huo kwa taarifa rasmi ya barua toka Ikulu. Mambo yakawa inogile, asiye na mwana aeleke jiwe, kumekucha mapambano rasmi yakazinduliwa.

Kachero Manu atoweka kimaajabu
"Ngriii...... Ngriii.... ..Ngriii....Ngriiiii.!" simu ya mezani anayoitumia Katibu muhtasi wa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Bwana Mtanika, Kokunawa ilikuwa inaita mfululizo bila kukoma. Himahima Kokunawa akiwa yupo mezani kwake, amejawa na lepelepe la usingizi unaotokana na uchovu akanyanyua mkono wa simu kivivu na kuuweka sikioni kusikiliza maelekezo anayotaka kupewa muda huo.
"Hellow..!! Koku vipi umeshampata huyu mtu? ananipa presha sasa, ataniua siku si zangu kwa mawenge anayonisababishia..!" aliuliza Bwana Mtanika huku sauti yake kavu ikiwa inaonyesha kabisa amechukizwa na utovu wa nidhamu wa Kachero Manu.
Alikuwa anasakwa na Bosi wake kwenye simu yake ya kiganjani tokea majira ya asubuhi alivyopata maagizo ya Ikulu, lakini mpaka wakati huo majira ya saa 5:00 usiku alikuwa bado hajapatikana hewani.
"Nimemtafuta hewani tokea uliponiagiza, lakini sijampata. Nikafanya maamuzi ya kumtumia meseji kwenye simu yake kuwa anitafute pindi akipata ujumbe wangu. Majira ya alasiri simu yangu imeonyesha kabisa kuwa amepata meseji yangu lakini hajanitafuta. Nilipojaribu kupiga namba yake sasa majibu ninayopata kuwa hiyo namba haipo kabisa niangalie vizuri ili nipige tena" alifafanua Kokunawa usumbufu anaoupata kutoka kwa Kachero Manu kumpata kwenye simu yake. Alinawa mikono ya lawama nae akionyesha amechoshwa na vimbwanga vyake.
"Huyu asitusumbue hajui kuwa hili suala sasa ni maslahi ya nchi na agizo limetoka Ikulu, hivyo wasiliana na mtu wetu wa mamlaka ya mawasiliano 'TCRA' ili kufahamu simu yake Kachero Manu inatumika sana akiwa mkoa gani ili nimfuate mimi mwenyewe. Alivyo mpuuzi hapa ofisini ameaga yupo msibani kwao Lindi lakini nina uhakika hayupo huko ni janja yake ya kutaka mapumziko tu. Mie nilimpitishia barua yake ya ruhusa sikujua kama yatajitokeza haya, sasa ananivua nguo mbele ya wakubwa wangu. Haya utanipa jibu haraka wapi alipo...!" akakata simu kwa hasira Bwana Mtanika bila kumpa wasaa Kokunawa wa kuongea chochote kitu.
Baada ya kama robo tatu saa hivi jibu likaja kuwa Kachero Manu huenda yupo Arusha amejichimbia. Hii ni kutokana na simu yake ya kiganjani kusoma katika minara ya Arusha kwa karibia wiki nzima sasa.
Bwana Mtanika akaamrisha usiku huo huo afanyiwe oda ya tiketi ya kuondoka kesho yake asubuhi na mapema. Alitaka aondoke kwa ndege inayoelekea Arusha aweze kuonana nae Kachero Manu huko huko Arusha ana kwa ana kesho yake.
Ni kweli walipatia kwa asilimia zote, Kachero Manu alijichimbia zake Arusha anakula zake bata raha mustarehe. Ilikuwa ni kawaida yake pindi akitaka mapumziko ya kazi anatafuta sehemu tulivu ya kupumzisha akili yake.
Anapokuwa mapumzikoni huwa hataki kabisa usumbufu wa kidudu mtu yoyote, hiyo ndio ilikuwa shida yake. Kuna wakati hata mkewe, Bi Faith Magayane muajiriwa wa benki ya KCB tawi la Dodoma alikuwa anakuwa hajui wapi alipo mumewe ila yeye alishamzoea tayari hivyo alikuwa hampi shida.
Bwana Mtanika, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa nae hakuwa na muda wa kupoteza wa kumsubiria Kachero Manu arejee mwenyewe. Alikuwa anakubali kuvumilia vituko na viroja vyote vya Kachero Manu kutokana na umuhimu wake pindi anapokabidhiwa majukumu mazito na magumu. Majukumu ambayo kwa akili ya kibinadamu usingeweza kuamini kuwa linatekelezeka.
Tabia yake Kachero Manu ni kupenda kuomba dua za shari zimfike kuliko heri ili akabiliane nazo hizo shari kwa nguvu ya Mungu. Mwenyewe imani yake ilikuwa kuwa unapopambana na misukosuko ndipo unapokomaa kifikra na kimwili katika kuweza kukabiliana na shida nzito zinazokuja siku za usoni mwako.
Ilipofika majira ya dhuha kama saa 3:00 za asubuhi ya siku ya pili yake, Bwana Omega Mtanika alikuwa tayari ameshatua Jijini Arusha tayari kuanza kumsaka kijana wake mtukutu. Uzuri alikuwa anamjua vizuri kijana wake kwa kupenda starehe hivyo alijua hatopata shida kumsaka kijana wake.
Alikuwa analijua Jiji la Arusha nje ndani na kila kichochoro chake. Enzi za ujana wake Bwana Mtanika amewahi kupitia mafunzo katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli kilichopo nje kidogo ya Arusha. Hivyo kila mwisho wa juma alikuwa anakuja kuzurura kama mbwa koko kwenye kila kina ya Jiji.
Breki yake ya kwanza baada ya kuwasili Bosi Mtanika ilikuwa ni ndani ya Hoteli ya kisasa Jijini Arusha, inayoitwa "New Palace Hotel-Arusha". Alipofika hapo moja kwa moja akaenda mapokezi kuonana na mhudumu. "Habari yako mwanangu, nahitaji huduma ya chumba hapa...!" alisalimia Bwana Mtanika mhudumu wa Hoteli aliyoko zamu muda huo.
"Sijambo Babu shikamoo...! Chumba kipo utapata bila shida, ngoja nikuchagulie chumba kizuri sana kwako kitakachokusuuza roho yako" alijibu kiuchangamfu yule mdada wa mapokezi kwa lafudhi ya kichaga.
"Samahani nina kijana wangu nataka nifahamu kama nae kafikia hapa yapata wiki sasa, nimepoteza mawasiliano nae..!" alimkatiza yule dada aliyekuwa yupo kwenye kompyuta yake ametingwa anaipekenyua kutafuta nafasi ya chumba.
"Eeeh...anaitwa nani huyo niangalie kama bado yupo maana vijana hapa wapo kibao tu..!" aliuliza yule dada huku anamuangalia usoni kwa umakini. "Somebody Manuel...!" alijibu kwa kimombo huku nae anamkazia macho mhudumu yule.
"Ooooh.....mrefu hivi mwili wake umejengeka kimazoezi, ana kifua cha taruma la reli hivi. Kama ni huyo namfahamu ni mteja wetu kalipia hapa wiki mbili lakini leo siku ya tatu haonekani, hajarudi ila vitu vyake vipo bado chumbani kwake..!" alieleza wajihi kwa ufasaha yule dada kuonyesha kuwa Kachero Manu ni mtu maarufu hapo Hotelini.
"Huyo huyo wala hujakosea mwanangu" alisema Bwana Mtanika kwa sura ya bashasha akiona ameshampata kwa wepesi kijana wake mtukutu anayemtaka kwa udi na uvumba.
"Basi kama ni hivyo, nitakuweka chumba kinachotazamana na chumba chake ili muwe karibu. Yeye anaishi chumba namba 802 hivyo nitakuweka chumba namba 806, sasa je utalipia kwa kadi ya benki au pesa taslimu na utakaa siku ngapi?" alipigwa swali na mhudumu yule ili aweze kujaza kiufasaha taarifa zake.
"Nitalipia kwa kadi ya Benki tafadhali sina pesa taslimu, ni siku moja tu nitalala, kesho mapema naondoka zangu" akajibu huku anafanya kwa vitendo kuiweka kadi ya benki kwenye mashine ya kukata fedha kwa njia ya kieletroniki.
"Sasa kama hajarudi siku tatu mtawalia je hamna wasiwasi wowote juu ya usalama wake? mbona hamtoi ripoti polisi huenda yamesibu mabaya je?" aliuliza swali la kichokonozi huku anaondoka zake taratibu pale kaunta kuelekea upande wake wa kulia kwenye lifti ya kumpeleka roshani ya 8 katika jengo hilo lenye roshani 10.
"Ha.. ha.. ha..hatuna wasiwasi nae yule chapombe sana kijana wako, tena leo Ijumaa hapa kuanzia saa 12 jioni mpaka saa 2:30 usiku tuna saa za furaha, vinywaji vinakuwa ni bei chee lazima atarudi muda huo nimehisi. Maana anastahabu pombe kama amezaliwa kwenye wodi iliyopo ndani ya kiwanda cha pombe, wakati mwingine anazidiwa mpaka anajilaza kwenye ngazi" alizidi kubwabwaja huyo mhudumu kumchambua Kachero Manu kama karanga na kumuacha uchi mbele ya Bosi wake bila kujua kuwa anamchomea utambi.
Bosi Mtanika akabaki anatabasamu tu huku anatikisa kichwa chake huku anaondoka zake kuelekea chumbani. Tayari alishafika kwenye lifti akaingia na kuiamuru iondoke.
"Kachero Manu amepatwa na maswahibu gani mpaka amegeuka kuwa mlevi buda hivi mpaka kuwa na raghba kubwa!" alikuwa anawaza kwa masikitiko muda wote Bwana Omega Mtanika akiwa ndani ya lifti.
Maana anachofahamu Kachero Manu ni mnywaji tena sio wa kila siku lakini mara ghafla tu anapata sifa zake mbaya za ulevi wa kupitiliza. Hivyo fikra zake zikamtuma kuwa atakuwa na tatizo tu linalomsumbua sio bure.
Alipofika tu kwenye roshani yake akashuka kwenye Lifti na kuharakisha kuingia chumbani mwake. Baada ya kitambo kifupi akatoka chumbani kwake na kuukabili mlango wa chumba namba 802 anachoishi Kachero Manu. Akaangaza macho yake kwenye veranda hiyo ya vyumba, upande wa kushoto na kulia hakumuona mtu yoyote.
Kisha kwa kutumia kifaa maalumu akafanikiwa kufungua mlango wa chumba hicho kijasusi na kuingia ndani kisha akajifungia. Alitumia kadi ya sensa ambayo ukisogeza karibu na kitasa, kinawaka taa nyekundu kisha kitasa kinawaka tena rangi ya bahari buluu ya kukupa ruhusa ya kuingia chumbani.
JE ATAKUTA NINI CHA KUSTAAJABISHA CHUMBANI KWA KACHERO?




Bila kuchelewa akaanza upekuzi wa haraka haraka, mpaka kweli akasuduku kuwa hiki chumba ni cha kijana wake. Alijiridhisha baada ya kuona baadhi ya nguo zake na vitambulisho vyake vya uwongo na ukweli. Akakuta simu zake za mkononi zipo kwenye mtoto wa meza zimezimwa.

"Huu mshenzi sana sisi tunamsaka ndio kwanza simu zote kazima kabisa na kuzitelekeza chumbani mwake, haya ngoja nione, lazima atakuwa amepandwa na kinyamkela kichwani sio bure" aliwaza Bwana Mtanika huku akiwa anatoka na kurudishia mlango kisha kuingia chumbani kwake kujipumzisha tayari ilishakuwa adhuhuri.

Alikuwa amevimba kama samaki bunju kwa hasira hasa kwa usumbufu anaopewa na Kachero Manu. Akakata shauri kama leo hatofanikiwa kumtia machoni kesho atarejea Jijini Dar es Salam na kuingia mwenyewe mzigoni kuwasaka wahalifu. Lakini alijiapiza Kachero Manu ajiandae kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwepo kushushwa cheo.

"Dawa yake kwenda kumtupa kwenye jeshi jipya la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu lililoanzishwa akawe kama mkufunzi. Siku zote ashinde na wanyama huko porini siku akili zake zikimkaa sawa akaja kuomba radhi nitamfikiria, lakini sio upumbavu huu anaoufanya" alikuwa anawaza fikra nzito nzito Bosi Mtanika huku ana akiwa amejawa na hamaki, stahamala yake ikiwa ni sifuri.

Akiwa kwenye hali hiyo ya mawazo akajishtukia bila kupenda anasombwa na mawimbi ya usingizi mzito wa pono kutokana na utu uzima wake wa miaka 65 uliomlaza mpaka majira ya alasiri.

"Kulipwa mishahara mizuri inayokidhi mahitaji yako pia nao ni uzalendo, Uchaguzi ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani na mimi najitosa kwenye dimba la siasa nikastakimu maisha bora huko Bungeni. Wazee wangu huko jimbo jipya la Uchaguzi la Mahiwa, Lindi Vijijini wameniomba nikagombee Ubunge.

Ila bado sijachagua chama nitakachopeperusha bendera yao.
Naachana na kazi za kitumwa, nakoswakoswa risasi kuitetea nchi yangu, lakini bado nalipwa mshahara mkia wa mbuzi, huku wapiga maneno ya lololo kule Bungeni, tena wakati mwingine wanasinzia tu wakiamka wanapiga madawati kuunga mkono hoja mfu, wanalamba mshiko wa nguvu.

Mhudumuu...!! Mhudumuuuu...!! Ongeza pombe hapa kama kawaida yangu nakesha mpaka lyamba maisha ni bambam wasinichanganye imetosha... maji ya shingo yamenifika hapaaa mimi sio bwege tena" alikuwa Kachero Manu anaroroma amecharuka kama mbogo huku pombe imeshamtawala kichwani, amekuwa chordo chupa na kizibo chake hajali chochote, kama amechanganyikiwa vile.

Kipindi chote anacholeta ushume na kuzua suitafahamu hapo "Arusha By Night Bar" au wenyewe vijana wa Jijini Arusha wameipa jina la utani la "Makalio Bar", Bosi wake alikuwa amekaa pembeni anamuangalia tu kijana wake anavyojimwambafai.

Bwana Mtanika kijasho chembamba kilimvuja kidogo mpaka kupanasa mahali Kachero Manu alipokita kambi. Kwanza jioni alimsubiria pale "New Palace Hotel Arusha", roshani ya pili kulikuwa na Baa ndogo inaitwa "Turaco Bar" akivizia huenda akaja kunywa bia za punguzo za bei lakini hakutokea.

Giza lilipozama, akazurura kwenye Baa mbili tatu za mitaani mpaka akaja kumfumania Kachero Manu amebarizi "Arusha By Night" iliyopo maeneo ya Mianzini njia ya lami ya kuelekea Sanawari.
Bwana Mtanika hakuwa na muda wa kupoteza, akamfuata pale pale alipokaa huku amezungukwa na warembo anatumbua maisha.

"kijana simama njoo haraka pale kwenye meza yangu" aliongea akiwa nyuma ya mgongo huku anampiga begani Kachero Manu na kisha kurejea kukaa kwenye meza yake.

Sauti ya Bwana Mtanika ilikuwa kama bomu la nyuklia kwenye ngoma za masikio ya Kachero Manu. Sauti hiyo ilimfanya kutokuwa na roho wala uhai. Moyo wake ulikuwa unadunda mtindo mmoja kama vile unataka kuchomoka. Kwanini asiwe na wasiwasi Kachero Manu?, Wahenga wanasema chezea mshahara usichezee kazi, na kazi mbaya ukiwa nayo, ngoja uikose kwanza ukione cha moto, hicho ndicho kilichompa wahaka wa moyo.

Alimjua fika Mudiru wake ni mkono wa chuma hakawii kumtilia kitumbua chake mchanga. Akavua kofia yake ya pama nyeusi, akasimama na kugeuka nyuma ili amuangalie yule aliyemuita kuthibitisha kama ni yeye anayemdhania au sauti tu zinafanana maana duniani wawili wawili.

"Mzee Shikamoo....sana tena nisaaa.... m..e... he.. sana, niko chini ya miguu yako..!" aliomba msamaha huku pombe ikiwa imeshakata kichwani, ububu kiziwi wake wote kwisha kazi. Alishavuta kiti tupu na kukaa pembezoni mwa Bosi wake. Alikuwa kama kifaranga cha kuku kilicholowana mvua, anayesubiri huruma ya mama yake amfunike na mbawa zake.

Alikuwa haamini kama kweli kang'oa nanga kumfuata yeye toka Jijini Dar es Salaam mpaka Baa za Uswahilini huku Arusha. "Haya kalipe pesa za watu tuondoke mguu kwa mguu na wewe mpaka Hotelini kwako tutayazungumzia huko sio hapa" alitoa amri kwa sauti inayohitaji utekelezaji tu sio kubembelezana tena.

Hakuwa na jinsi zaidi ya kusimama kitini na kuwaacha viruka njia wake wanang'aza macho. Kachero Manu akatembea mpaka kaunta, kisha akalipia gharama zote za pombe alizokunywa. Baada ya hapo akaondoka eneo lile la Baa na Bosi wake huku mikono yake ipo nyuma, kichwa chini amejawa na hamaniko.

Kaumu nzima pale Baa walikufa kwa kicheko, mtu ambaye ni mbabe wao na anayewaburudisha kila siku kwa kuwachezea rumba na kuwapa hotuba za bure kapata mbabe wake.
Wapo waliosema baba yake mzazi kamfuata kamtishia kumtolea radhi hapendezwi na mtoto wake kuwa chapombe.

Wapo waliosema ni Bosi wake katoweka kazini kwa siku kadhaa hivyo kamfuata. Ilimradi kila mmoja pale Baa aliyeshuhudia tukio lile alibuni maoni yake binafsi.


Walipofika "New Palace Hotel-Arusha" kikao kifupi cha halahala kikafanyika chumbani kwa Bosi wake, chumba namba 806.

"Kama una malalamiko yoyote ya maslahi yako ni bora uniambie lakini sio utovu wa adabu huu unaoonyesha. Wewe mwenyewe unajua namna gani ninavyopigania maslahi yenu vijana wangu wote wa idarani. Tazama jinsi mishahara yenu ilivyopanda maradufu kulinganisha na kada zingine hata kama umeidharau unaita mshahara wa mkia wa mbuzi hausitiri makalio.

Sasa nimebakiza masuala ya posho ya mazingira magumu tu ndio napambana kuhusu hilo liingizwe kwenye bajeti ijayo itakayosomwa Bungeni hivi karibuni" alifungua mazungumzo yao Bosi Mtanika kwa sauti ya huzuni akionyesha kukerwa haswa na utovu huo wa nidhamu kabla hajaanza kumueleza lengo la ujio wake Jijini Arusha.

Bosi Mtanika alikuwa ni kiongozi mwenye idili na itifaki na watumishi wa idara yake anayoiongoza ya usalama wa taifa. Alikuwa anawalea kama wajukuu zake anaenda nao aste aste, lakini pindi wakimkorofisha anawashukia kwa ukali kama simba mwenye njaa nyikani.

"Nimekosa nisamehe Bosi nilipitiwa tu na Ibilisi, ila posho ya mazingira magumu ya kazi ni jambo la kulizingatia sana. Uliangalie kwa macho mawili, leo mkata viuno huko anaimba Bongo fleva kwa kubana pua jukwaani anaishi maisha ya matumaini kuliko sisi walinda amani wa nchi.

Ambao tunalala maporini huku vitanda vyetu ni kwenye miti, sauti za mbu na risasi ndio muziki wetu kule porini. Wanyama wakali ndio familia zetu na ndio marafiki zetu, inakatisha tamaa sana Bosi. Tunadanganyana kama wanywa mtori kuwa nyama tutazikuta chini siku tukistaafu lakini tunaishia kukosa hata rehe ya fulusi.

Mfano familia zetu huko kijijini waliotusomesha kwa kuuza mashamba yao ili kutulipia ada wakitegemea tutawakomboa kwenye lindi la umasikini sasa wanaishi kwa tabu, kuna wakati wanakosa hata pesa za kusagia mkungu" alikuwa anazungumza kwa uchungu Kachero Manu akitetea maslahi yao wana usalama kwa ujumla, anampasulia maneno hadidi bila kumung'unya maneno Bosi wake.

"Sawa nimepokea maoni yako, ondoa fundo moyoni, nitayafanyia kazi kwa haraka. Haya haki inaambatana na wajibu sasa kuna jukumu zito unatakiwa ulitekeleze kwa haraka ndio maana nimekufuata mwenyewe, nadhani umesikia kilichotokea kwenye mabenki yetu matatu makubwa hapa nchini?" aliuliza Bosi Mtanika sasa akihamisha mada ya madai ya maslahi bora kumrudisha kwenye kazi.

"Abwa!...Hiyo ni habari mpya kwangu sijui chochote kinachoendelea hapa nchini, aisee... kumetokea nini?" aliuliza Kachero Manu kwa tashiwishi kubwa huku akiwa ametumbua macho na kuyataarisha masikio yake kwa udadisi wa kupewa taarifa mpya.

"Habedari! Kweli ulikuwa unaishi kibwege sana unapenda ureda tu kama sio Kachero bobezi vile unanitia aibu sana toka lini umeanza kuwa boya hivyo..!, Sawa...tuyaache ni hivi pesa zaidi ya bilioni 560 zimeibwa kwa mkupuo katika benki tatu tegemo hapa nchini. Nazo ni Benki za "Turkish Commercial Bank" (TCB), Benki ya makabwela ya "Umoja Ni Nguvu Benki" (UNB) pamoja na "Youth and Women Bank" (YWB) kwa njia ya kieletroniki". Akajikohoza kidogo na kujiweka sawa kitini alipoketi kisha akaendeleza maongezi yake.

"Hatujafahamu wahujumu hao walitumia muda gani kukamilisha zoezi lao hilo ovu ila tokea kugundulika wizi huo ni ndani ya wiki moja tu imepita. Mbaya zaidi Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya fedha za nje na ndani wa Benki Kuu nae amefariki kifo cha kutatanisha nchini Afrika ya Kusini kwa ajali ya moto kwenye gari " akaweka kituo cha mazungumzo yake na kumuomba ampe kinywaji chake pendwa aina ya Klabu Soda kwenye friji dogo la mule chumbani.

Kachero Manu akanyanyuka, akijibu kwa vitendo kwenda kuchungulia kwenye jokofu dogo la mule chumbani kama kweli kipo hicho kinywaji alichoagiza. "Mhhhh....Bosi humu hamna hicho kinywaji unachohitaji kuna vile vinywaji vya wanafunzi wa shule ya vidudu.!." alizungumza Kachero Manu wakajikuta wanakufa wote kwa vicheko.

"Ngoja nishuke chini roshani ya kwanza, pale "Turaco Bar" watakuwa nazo tu..!" akafungua mlango na kuanza kuelekea roshani ya kwanza kwa kuita lifti ije roshani namba 08 kisha impeleke kwa haraka roshani ya 01. Punde si punde ikaja lifti ikitokea roshani ya 09, ilipofunguka tu mlango akapupia kupanda.

Aliwakuta watu wawili ndani ya ile lifti tayari wakiwa wamepanda. Ikaanza kushuka chini sasa wakiwa watu watatu, yeye Kachero Manu, na Mzee mmoja wa makamo ambaye Kachero Manu alimuona pale chini mapokezi wakati wanakuja na Bosi Mtanika pamoja na mtumishi mmoja wa Hoteli.

"Yule Babu mpana wa mwili, mwenye upara amevalia kaunda suti ya rangi ya kahawia kafikia chumba gani na anaondoka lini?" aliuliza yule Mzee wa makamo akionekana kama ana wasiwasi mkubwa kumuuliza mtumishi wa Hoteli huku Kachero Manu akiwa kimya anawasikiliza kwa makini lakini anajifanya ametingwa na kusoma meseji zilizoingia kwenye simu yake za muda mrefu huku anatabasamu.



"Yule Babu mpana wa mwili, mwenye upara amevalia kaunda suti ya rangi ya kahawia kafikia chumba gani na anaondoka lini?" aliuliza yule Mzee wa makamo akionekana kama ana wasiwasi mkubwa kumuuliza mtumishi wa Hoteli huku Kachero Manu akiwa kimya anawasikiliza kwa makini lakini anajifanya ametingwa na kusoma meseji zilizoingia kwenye simu yake za muda mrefu huku anatabasamu.

"Yule amefika asubuhi ila sijui anaondoka lini na wala sifahamu amefikia chumba gani labda ukaulizie pale mapokezi kama una shida nae" alijibu yule mtumishi kwa ufupi na kwa ufasaha.

Mara lifti ikawa imetua roshani ya 01. Kachero Manu himahima akashuka na kuelekea mlango wa Baa kuchukua kinywaji pendwa cha Bosi wake huku akiwaacha wale wenzake wanaelekea chini kabisa ya jengo.

Kwa bahati nzuri akakipata kile kinywaji na kuanza kupandisha kwenda roshani ya 08 kwa kutumia ngazi huku anazipanda kwa haraka kama moja ya mazoezi ya kuimarisha misuli ya miguu yake. Alijiona mzito sana wa mwili kutokana na kupuuzia mazoezi kwa siku kadhaa.

"Yule jamaa nahisi kabisa anamuulizia Bosi wangu, na wamesalimiana vizuri kama watu wanaojuana pale chini kwanini hakumuuliza yeye mwenyewe mpaka amfanyie taftishi nyuma ya mgongo wake kupitia mtu wa pembeni kuna jambo sio bure...!" Kachero Manu alikuwa anatafakari mazungumzo ya wale wenzake mle ndani ya lifti.

"Ooh...pole kwa usumbufu na ahsante sana..!" alishukuru alipokitia mkononi kinywaji chake huku tayari ameshaanza kuimimina kwenye glasi na kuanza kuigida kwa mkupuo. "Usijali Mkuu kuwa na amani" alijibu Kachero Manu huku akichukua nafasi yake kwenye kiti alichokalia mwanzo. Mazungumzo yao yalikuwa marefu yaliyowaacha macho kodo mpaka manane ya usiku bila kupitiwa na lepe lolote la usingizi.

"Sasa muda umekwenda matiti, katu hatuwezi kudadavua kila kitu usiku huu tukapata hitimisho sawia. Kikubwa kesho kutwa tukutane ofisini Jijini Dar es Salaam tukajipange vizuri. Maana sasa wapinzani wa chama tawala ndio wamepata sauti ya kuropoka wanavyojisikia wao, na ni kweli huwezi kuwadhibiti kwa kuwafunga midomo maana wanachosema ni ukweli mtupu pesa zimekwapuliwa.

"Kuwafunga mdomo ni kuwakamata wahusika na kuwapandisha kizimbani wapate hukumu yao stahiki na si vinginevyo. Hata yule Mzee wa makamo tuliyesalimiana nae pale chini mapokezi wakati tunakuja hapa ni Kiongozi mkuu mpya wa upinzani wa Chama kinachoitwa "National Movement Party" (NMP), Dr.Patrick Ndomba.

Nadhani yupo ziara ya kanda ya kaskazini kwa lengo hilo hilo la kuinanga serikali". Alipotajwa yule Mzee kuwa ni Kiongozi wa chama cha upinzani, moja kwa moja Kachero Manu akaanza kuunganisha nukta kutokana na maongezi aliyoyasikia ndani ya lifti muda mchache uliopita.
"Hivyo Kachero Manu tunakutegemea usituangushe.

Uwe makini sana maana tunahisi kikulacho ki nguoni mwako lazima kuna watu ndani ya mfumo wetu wa usalama wa nchi wapo kwenye hiki kikundi cha uhalifu" akatamatisha mazungumzo yao Bosi Mtanika huku wakipanga namna watakavyoondoka kesho.

Wakaafikiana kila mtu asafiri kivyake kama walivyokuja kuepusha kushukiwa jambo lolote lililopo baina yao. Maana walishahisi mtandao wa wahalifu hao ni mrefu sana hasa wakifananishia namna Inspekta Mengi Matunda alivyouliwa ndani na saa chache tu tokea kujulikana kuwa amepewa jukumu hilo zito. Wakaagana kwa ahadi za kukutana tena kesho kutwa siku ya Jumapili ofisini Jijini Dar es Salaam.

SURA YA PILI
Kindumbwendumbwe kwa Kachero Manu

Mudiru Omega Mtanika aling'oa nanga Alfajiri ya siku ya Jumamosi kwa njia ya ndege akitumia usafiri wa taksi iliyomfikisha mpaka uwanja mdogo wa ndege wa Jijini Arusha uliopo njia ya kuelekea Babati, mkoani Manyara. Akafanikiwa kutua salama salimini Jijini Dar es Salaam, akimsubiria kijana wake Kachero Manu awasili wamalizie mpango mkakati wao.

Kachero Manu yeye alipanga aondoke Jumapili na ndege ya saa 2:30 asubuhi kwa ndege ya shirika la ndege la ATCL. Shirika ambalo lilikuwa limeshajifia zake, lakini sasa lilikuwa limerudi tena sokoni kwa ari mpya na nguvu mpya huku likiwa na ndege zinazofanya safari ya Arusha za asubuhi, mchana na usiku.

Alikata tiketi yake kwa kutumia mmoja wa wakala maarufu sana wa usafirishaji watalii nchini Tanzania, kampuni ya "Lake Nyasa Safari Tours", kampuni ambayo ilikuwa pia inatoa usafiri kwa wateja wake kuwatoa kwenye Mahoteli yao walipofikia na kuwafikisha kwenye uwanja wa ndege mdogo wa Arusha.

Ilipofika majira ya saa 1:00 asubuhi siku ya Jumapili, alikuwa yupo tayari kwa safari. Alishapata staftahi nyepesi iliyoandaliwa pale pale hotelini kwake. Sasa alikuwa amejipumzisha kwenye sofa pale mapokezi anasoma magazeti mbalimbali ya siku hiyo ya Jumapili. Pembeni yake ana kibegi chake kidogo cha safari, anasubiri kuja kuchukuliwa na usafiri kwa ajili ya kuelekea Uwanja wa ndege.

Ilipotimu saa 1:15 asubuhi shapu likaja basi dogo la rangi nyeupe likiwa na chata ya "Lake Nyasa Safari Tours" ubavuni mwake, kuonyesha ni gari linalomilikiwa na kampuni hiyo. Huku pia likiwa limepambwa na michoro mbalimbali ya wanyama pori kutia nakshi nakshi muonekano wa Basi hilo.

Upesiupesi Kachero Manu alipoliona tu akatokeza nje ya jengo la Hoteli akiwa amefumbata mkononi begi lake kisha akatoma ndani ya gari. Humo akajumuika na abiria wenzake wapatao 14 waliokuwa tayari wameshapanda. Wengi wa abiria hao wakiwa ni wa kutoka nchi za Ughaibuni kutokana na muonekano wa rangi za miili yao.

Kabla Basi halijaondoka pale Hotelini, dereva akapiga simu kwa Mkuu wake wa kazi, kuthibitisha kuwa ameshawapakia wateja wao wote aliopangiwa kuwachukua. Hamna aliyejali maongezi hayo ya dereva na Bosi wake kila mmoja alishika hamsini zake.

Msafara wa kuelekea Uwanja wa ndege bila ajizi ukaanza kwa mwendo wa wastani huku dereva akiwaburudisha abiria wake kwa kuwafungulia muziki laini usiochosha masikioni kusikiliza. Pia mhudumu wa kiume ndani ya Basi hilo, alikuwa anapita kwa kila abiria kugawa peremende za kuchangamsha mdomo.

Baridi kali ilikuwa inapuliza asubuhi hiyo, lakini abiria wote walivalia libasi za kuwawezesha kuhimili vishindo vya baridi kali ya Arusha. Kila mmoja alikuwa ameshughulishwa na jambo lake huku wengine wanajisomea vitabu mbalimbali vya kuongeza maarifa na vya burudani. Kachero Manu aliendelea kuperuzi magazeti yake aliyobeba Hotelini.

Msafara ulivyofika kwenye mzunguko wa mnara maarufu wa Azimio la Arusha tu mara baada ya ya kuyapita makaburi ya Kaloleni, simu ya kiganjani ya Kachero Manu ikaanza kuita mfululizo bila kukoma. Kisha simu ikakata akiwa kwenye harakati ya kuitoa kiunoni kwenye kasha lake maalumu la ngozi la kuifadhia simu.

Ghafla akiwa kwenye harakati za kuichunguza namba inayomtafuta, simu yake ikaanza tena kuita. Sasa hakujivunga tena kuipokea, himahima akabonyeza kitufe cha kuruhusu kupokelea simu.

"Hellow.....Morning, I'm fine..eeeeh...eeheeee yeah...daaaah...it is true...thank you very much....may God Bless You so much...., I'm coming right now..No problem...see you soon..!" akakata simu huku uso wake ukiwa umepigwa na taharuki isiyoelezeka.
"Aisee..dereva samahani sana simamisha gari haraka nishuke, kuna kitu muhimu sana nimesahau hotelini pale "New Palace Hotel-Arusha". Nitakuja mwenyewe kwa usafiri wangu binafsi usijali wewe endelea na safari usije kuwachelewesha ndege bure abiria wenzangu kwa uzembe wangu....!".

Aliomba Kachero Manu gari lisimame na dereva bila makeke yoyote akatii kwa vitendo kwa kuanza kupangua gia zake mpaka akalisimamisha gari.
Chapuchapu kama mtu aliyekurupushwa na hatari akashuka na kibegi chake kidogo cha mkononi na kutoa ruksa ya basi lile kuondoka eneo lile.

Tahamaki Basi likaondoka zake linamtimulia moshi tu angani. Alipotupa macho yake kuangaza huku na kule kutafuta usafiri mara akaliona bodaboda moja linakuja pale pale usawa aliposimama kwa kasi.


Bila kufanya ajizi akaanza kulipungukia mkono lipunguze mwendo wake. Dereva wa bodaboda akatii ishara ile ya mkono kivitendo kupunguza mwendo wake. Akaisimamisha pikipiki yake meta chache kutoka pale aliposimama.

"Mshefa habari yako unaenda wapi nikukimbize fasta?" aliuliza yule muendesha bodaboda akiwa na kimuhemuhe cha kumpata abiria wa mapema asubuhi hiyo. Kwake aliona kama ni sudi kuanza kupata abiria asubuhi hiyo na mapema.

"Habari yangu ni nzuri tu, naomba nipeleke haraka Hotelini pale "New Palace Hotel-Arusha" mkabala na Ofisi za Mkuu wa Mkoa", aliitikia salamu na kujieleza anapotaka kwenda. "Hamna noma napafahamu fika, rukia twende fasta" alijibu yule dereva bodaboda huku akijitayarisha kuliondosha pindi tu akikwea kiti cha abiria.

Akaparamia bila kutia neno na msafara wa kurejea Hotelini ukaanza. Alikuwa ameisahau chumbani kwake chaja yake ya kisasa ya simu. Haikuwa chaja ya simu ya kawaida, kitaalamu ikiitwa "Cellphone Charger Spy Camera". Mbali ya kutumika kuchajia simu, ilikuwa na uwezo wa kufanya kazi kama kamera ya siri.
Alikuwa anaitumia kwenye kazi zake mbalimbali za kipelelezi, ndio maana akakubali kuvunja safari yake kuifuata.

Sasa asubuhi ile wakati anaondoka pale Hotelini aliisahau kwenye soketi ya umeme chumbani kwake. Hivyo mhudumu wa usafi alipoiona akatoa taarifa mapokezi, ndipo akakumbushwa kwa kupigiwa simu.
Ilimchukua dakika kama 5 tu hivi kufika Hotelini na kukabidhiwa amana yake.

"Sasa kijana moyo wangu umetulizana naomba nikimbize mpaka uwanja wa ndege maana nimeshachelewa muda wa kuripoti fanya uwezavyo nisiikose ndege", alitoa maagizo akiwa na moyo mkunjufu baada ya kukipata kifaa chake cha kazi.


"Hamna shida Mangi, andaa elfu 16 tu Bosi wangu, buku ya kutoka pale nilipokuchukua mpaka hapa na elfu 15 ya kutoka hapa mpaka Uwanja wa kupandia mwewe" alijibu yule dereva bodaboda kwa sauti ya bashasha akionekana ana furaha ya kismati cha kazi kumtembelea asubuhi na mapema, huku akianza kuliondosha pikipiki lake kwa mbwembwe.

Muda halisi wa kuripoti kwa abiria ulikuwa ni saa 2:00 asubuhi. Kwa maana walikuwa wamebakiwa na dakika takribani 25 tu za kuchapa mwendo. Bodaboda ilipeperushwa vilivyo kwa kuvutwa mafuta vile inavyotakiwa huku upepo wa kasi unavuma kuipiga miili yao iliyositiriwa na majaketi.

Walipokaribia maeneo ya "Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania" (TARI), Kituo cha Siriani-Arusha, wakaanza kuona wingu zito la moshi angani limetanda kuashiria kuna tukio la moto. Dereva bodaboda akapunguza mwendo huku wanakaribia taratibu eneo hilo la tukio. Umati wa watu, wakubwa kwa wadogo ulikuwa unakimbilia eneo hilo kuashiria kuna jambo baya limetokea katikati ya barabara.

"Hii tabia yetu ya Watanzania kukimbilia sehemu ya hatari kama ajali bila tahadhari itakuja kutugharimu siku moja" aliongea yule bodaboda kwa sauti ya masikitiko huku akiwa tayari ameegesha pikipiki mbali kidogo na eneo la tukio.

"Itugharimu mara ngapi si umesikia maafa ya ajali ya lori la mafuta kulipuka Mkoani Morogoro mpaka sasa zaidi ya watu 100 wamefariki na majeruhi kadhaa wapo hospitalini wanapigania roho zao, sisi aliyeturoga kafa tayari. Hapo watu wanatafuta picha na video za kurusha kwenye mitandao ya kijamii ili waonekane watu wa kupata habari nyeti kwa haraka, ushamba mtupu" alitilia mkazo Kachero Manu maneno ya dereva yule wa bodaboda akiwapondea wananchi wale wasioogopa hatari ya moto.

"Jamani Eeeh....! mama weeeh...! Pale hatoki mtu, gari imelipuka tunahisi ni bomu. Basi dogo lililokuwa limebeba watalii na dereva wao wote wanateketea na moto hivi sasa. Tanzania yetu haipo salama tena na hawa magaidi wa Al-shabaab toka Somalia". Alikuwa anasimulia kwa sauti kubwa yenye kubeba hisia juu ya tukio hilo mmoja wa shuhuda aliyotoka eneo hilo. Mikono yake ikiwa ipo kichwani akionekana amesikitishwa mno na tukio hilo.

"Twende zetu uwanjani hayatuhusu, zimamoto wenye kazi yao watakuwa wameshapewa taarifa tutachelewa bure..!" Kachero Manu alimkurupusha kwa maagizo dereva bodaboda huku kichwani akiwaza. "Kumekucha kindumbwendumbwe upande wangu kimeanza asubuhi na mapema hivi..!, ningekuwa marehemu hivi sasa na mimi kwenye lile Basi, namshukuru sana Mola wangu siku zangu za kuishi bado sana".

Basi la "Lake Nyasa Safari Tours" lililokuwa limebeba wateja wao kuwapeleka uwanja wa ndege lilikuwa limelipuliwa na bomu lililotegwa barabarani. Kama sio kupigiwa simu ya kuja kuifuata chaja yake ya simu aliyoisahau pale hotelini, Kachero Manu huenda angekuwa ni mmoja wa marehemu walioaga dunia.
ITAENDELEA,....




Basi la "Lake Nyasa Safari Tours" lililokuwa limebeba wateja wao kuwapeleka uwanja wa ndege lilikuwa limelipuliwa na bomu lililotegwa barabarani. Kama sio kupigiwa simu ya kuja kuifuata chaja yake ya simu aliyoisahau pale hotelini, Kachero Manu huenda angekuwa ni mmoja wa marehemu walioaga dunia.

Mpaka saa 2:05 asubuhi ile walikuwa tayari wameshawasili uwanja wa ndege, lakini habari za mlipuko ule zilishaenea zamani eneo lile la uwanjani huku watu wakiwa vikundi vikundi kujadilia tukio hilo. Kachero Manu akamalizana malipo na dereva bodaboda yule huku akimshukuru wakaagana kwa salama, kisha Kachero akaingia zake ndani ya jengo.

"Hizi nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama zisiposhirikiana kwa nia thabiti kuwadhibiti magaidi wa Al-shabaab wa Somalia kila siku tutaishia kulialia tu na kuomboleza" aliongea mmoja wa watumishi wa pale uwanja mdogo wa Arusha kwa hasira na majonzi makubwa.

"Sasa angalia wale idadi ya watalii waliouliwa toka mataifa mbalimbali kwa vyovyote nchi zao zitawatangazia wananchi wao wasije kutalii Tanzania kwa kuwa hakuna usalama. Haya madege ya ATCL serikali inayonunua kwa kodi za wananchi bila amani na usalama tutafugia kuku nakuambia..!" alichangia mazungumzo hayo mmoja wa hao watumishi wanaosogoa muda huo.

Kachero Manu alitulia kimya kama maji mtungini anawasikiliza tu huku akifahamu fika tukio kuwa hamna cha Al-shabaab wala nini. Isipokuwa ni hujuma ya waziwazi ambayo anaihusianisha moja kwa moja na matukio aliyosimuliwa na Bosi wake Omega Mtanika.

Ilipofika majira ya saa 3:00 ndege ya ATCL aina ya "Bombadia" ikapaa zake angani kuelekea Dar es Salaam kupitia uwanja wa kimataifa wa KIA-Kilimanjaro. Ilishathibitika tayari kuwa abiria wote kwenye lile Basi dogo la "Lake Nyasa Safari Tours" wameteketea wote pale pale eneo la tukio. Mpaka saa 6:00 mchana Kachero Manu akawa tayari ameshawasili ofisini kwake kwenye jengo la "Benjamin Mkapa Tower" lililopo maeneo ya Posta Mpya.

"Mnoko upo wewe ndio umenichongea kwa Bosi mpaka kaja kunifuata Arusha, haya umeshinda wewe...!" Kachero Manu alikuwa anamsalimia kwa utani Katibu Muhtasi wa Bosi wake, Kokunawa.
"Mhhh....usiniangushie jumba bovu kwa uzembe wako mwenyewe kazini, ni tabia ya mbaazi zikikosa mvua kusingizia jua usinitishe mtoto wa watu bure...!" alijibu Kokunawa kwa kujiamini huku wakiendelea kutaniana hapa na pale.

"Vipi Mzee mwenye usalama wa nchi yake kashafika ofisini?" alibadilisha mada akivaa sura ya kazi. "Amefika lakini katoka kidogo kuna ajali ya Arusha ilimshtua kidogo tulidhania na wewe umo, lakini nilipokutafuta ukaniambia umesalimika nikamfahamisha, akaniaga anatoka akasema hachele....." kabla hajamaliza maelezo yake Bosi Omega Mtanika akawa ameshatia timu ofisini.

"Aaah..Manu siamini kijana wangu kama umesalimika Mungu yu mwema wakati wote" alizungumza kwa uso wa bashasha huku wanapeana mikono ya salamu na kukumbatiana kwa furaha sheshe.

"Nashukuru sana Mungu nimepenya mauti kwenye tundu la sindano ni siku yangu ya kifo ilikuwa haijafika tu, maana siku na saa ikifika hamna mjanja wa kutengua" alijibu kwa unyenyekevu Kachero Manu. "Mungu bado ana makusudi na wewe kwa ajili ya ukombozi wa Watanzania kwa vibaraka, walafi wenye uchu na mali za Watanzania" Bosi Mtanika akatilia tashididi mazungumzo hayo.

Baada ya kumaliza kusalimiana, wakaongozana sako kwa bako kuelekea ofisini kwake. Wakamuacha Kokunawa ameinamia kompyuta yake ametingwa na majukumu yake.
Kachero Manu akageuka wakati anajiandaa kufunga mlango wa ofisi ya Bosi wake huku anamuangalia Kokunawa kwa huruma na kuwaza, "Kazi hii haina dini aisee leo Jumapili hata kanisani tumeshindwa kwenda, Mungu atusamehe hatuna jinsi". Akafunga mlango na kujongea kwenye meza kuu iliyopo ofisini humo.

"Coffee or Green Tea?" aliuliza Bosi Mtanika kumuuliza Kachero Manu huku akiwa amesimama pembeni ya birika la umeme la kuchemshia maji ya moto. "Nipe Green Tea usiweke maziwa hata tone tafadhali..!" alijibu huku anazungusha kiti chake cha kuzunguka kushoto na kulia. Baada ya kitambo cha dakika takribani 2 wakaanza kuburudika na vinywaji vyao vikavu bila mchapalo wowote.

Mazungumzo wakayafungua tena rasmi sasa kuendeleza majadiliano yao yaliyoanzia siku ya Ijumaa kule Arusha. "Nilichopanga kwanza, Kachero Yasmine Abeid afanyiwe mpango wa kupatiwa kazi Benki kuu, afanywe kama amepata uhamisho tokea Zanzibari kuja Tanzania bara, sasa akiwa pale ataanza kufukunyua yaliyojificha, maana ni rahisi kumshinda adui kutokea ndani kuliko ukiwa nje.

Maana kwa vyovyote kuna watu wa Benki Kuu wamehusika na sakata hili. Pili ningependa hiyo wiki ijayo ambayo wanasema mazishi rasmi ya Mkurugenzi mkuu wa fedha yatafanyika nihudhurie mazishi yake. Maana nimeulizia maiti itasafirishwa toka Afrika ya kusini kesho kutwa siku ya Jumanne, kisha Jumatano wataaga hapa Dar es Salaam baada ya hapo itapelekwa kwao Nyasa kwa mazishi. Sasa ningependa kuhudhuria huko huenda tukanusanusa na kuambulia kitu chochote" alieleza mipango yake Kachero Manu mbele ya Bosi wake ambaye wakati wote anamsikiliza alikuwa anatabasamu akijua sasa kazi imeanza.

"Sawa yote hayo uliyoyaomba yatatekelezwa tutakupa taarifa rasmi ya mazishi ni kijijini gani ili ujipange. Pia sasa hivi ninatoa maagizo iandikwe barua ya uhamisho wa Kachero Jasmine, pacha wako wa pete na kidole ili pale akafanye kazi yetu pale Benki Kuu, maana tunao pale watu wetu wa idara lakini bure kabisa wameshindwa kung'amua uhalifu".

Kawaida moto wowote mkubwa lazima uanze na cheche. Sasa iweje vijana wao waliopenyezwa Benki Kuu kwa siri wasiambulie kitu, hilo ndilo lilimkasirisha mno Bosi Omega Mtanika. "Haya kuwa makini katika majukumu yako, nakutakia kila la kheri. Maana kama kweli ile ajali walikulenga wewe na kama wamegundua haujafa lazima watakujia tena kukuangamiza.

Uhalifu ni kama uchawi, maana mchawi akianza kula nyama za watu haachi kutokana na utamu wake.
Hivyo hivyo kwa wahalifu kuacha ni ngumu kutokana na kunogewa na maslahi machafu ya bila jasho wanayoyapata" alimpa tahadhari kijana wake, huku Kachero Manu akimtoa wasiwasi na kuomba asimsahau kwenye sala zake kisha wakaagana, na kuondoka zake tayari kwa kazi.


Anyamazishwe kwa mtutu wa bunduki

"Yule Kachero wao namba moja amenusurika kwenye mlipuko wa bomu tulilotega barabarani. Kijana wetu amemuona anapanda ndege Arusha ya kuja Dar es asalaam. Pia idadi ya waliokufa ni pungufu kwa mtu mmoja kuliko idadi tuliyoitarajia hivyo kuthibitisha amepona mtegoni wetu.

"Bwana Mkubwa" wetu amekasirishwa mno na uzembe uliofanyika wa kushindwa kumuua yule tegemeo lao la Idara ya Usalama Kachero Manu. Anataka maelezo ya kina, tatizo lilikuwa ni nini mpaka tumeua wasio husika huku mhusika akiachwa anadunda, unaweza kueleza chochote wewe "Chew-Master" maana wewe ndio mkuu wa mipango yetu yote ya siri ya kuwateketeza maadui zetu" aliongea muwakilishi wa huyo anayeitwa "Bwana Mkubwa" ambaye wengi wao walikuwa hawamjui kwa sura wala kwa jina lake halisi zaidi ya kumsikia tu kwa cheo chake hicho.

Huyu "Chew Master" ni jina lake la utani, alikuwa ni kigogo mzito ndani ya Jeshi la Polisi ambaye alikuwa yupo upande wa waliokwapua mabilioni ya pesa katika mabenki. Ndio aliyevujisha siri ya jukumu alilopewa Inspekta Mengi Matunda na ndio maana ikawa rahisi sana kuuliwa ndani ya muda mfupi tu tokea akabidhiwe jukumu hilo. Tamaa ya maisha mazuri kwa haraka haraka zilimfanya aingizwe kwenye genge ovu la wahaini wenye lengo la kuigeuza nchi ya Tanzania kuwa Dola ya Nyasa "Nyasa Empire".

"Hata mimi sifahamu kilichotokea mpaka sasa, labda ana jeshi la mizimu lililompaisha kutoka eneo la ajali. Lakini robo saa kabla ya bomu kulipuka tulimuuliza dereva akathibitisha abiria wote amewapakia na anawaleta uwanja wa ndege. Labda dereva kama angekuwa hai angetusimulia huyu mjuba alishukaje kwenye gari mpaka amenusurika.

Hata mkitaka uthibitisho wa mawasiliano ya mwisho ya dereva na mkuu wake wa kazi mnaweza kuyapata kupitia kampuni ya simu. Kikubwa hamna haja ya kulaumiana hapa ni kumtafuta mtu makini wa kwenda kumshughulikia usiku huu wa leo. Anyamazishwe kwa mtutu wa bunduki" alizungumza kwa kujiamini "Chew-Master" huku anatikisa mguu wake wa kushoto kwenye kiti alichokalia kwa kiburi.

"Nimekuelewa sana, sasa nani utakayemtuma kumshughulikia usiku huu mie nataka asubuhi kutakapopambazuka serikali wawe wanatoa vilio tu. Wanyooshe mikono juu kwa kusalimu amri, watuachie nchi yetu tuifanye tunavyotaka sisi kuitawala" aliongea kwa wahaka mkubwa wa kutaka Kachero Manu afe tu kwa haraka, mwakilishi wa huyo kiongozi wao, "Bwana Mkubwa".

"Kuna kijana wetu yupo Jeshini ni makini sana tena ni komandoo, hivyo tumemchomoa toka Darfur nchini Sudani mara moja anapohudumu kwenye Jeshi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri tayari ameshawasili wakaonyeshane undava wenyewe kwa wenyewe. Nimeshampa taarifa yupo njiani anakuja nusu saa kutoka sasa nitakutana nae nimpe maelezo yote.

Amenihakikishia atamsambaratisha bila kipingamizi chochote" "Chew Master" aliongea kwa majigambo, akimpamba na kumpaka manukato kijana wake huyo wa kazi.
"Ehee! !...Mpango wa ugawaji wa kadi za siri wanachama wetu watiifu unaendeleaje, Dr. Patrick Ndomba nakusikiliza wewe sasa" mjadala sasa ulihamia kwa Mwenyekiti wa "National Movement Party" (NMP) ambaye alikuwa na jukumu la kugawa kadi ambazo zitawawezesha kuwajua wafuasi wao kindakindaki watakaotumika kutimiza mpango wao wa siri muda muafaka utakapowadia.

"Nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa maelezo mafupi tu, lengo letu tulisema tugawe kadi laki 7. Lakini mpaka sasa tumeshagawa kadi laki 2.5 kwa hiyo mambo yanaenda vizuri sana na kila tunayempa fikra zetu za kimapinduzi anashawishika na kua tayari kutusaidia kwa hali na mali. Tumekubalika kwenye makundi yote muhimu katika jamii kuanzia walimu mpaka jeshini huko kote tumeshawalisha sumu za kimapinduzi kwenye fikra zao.

Mfano walimu tuliowaingiza kwenye mpango wetu, wao tayari wameshaanza mgomo baridi wanaingia darasani lakini wanawafundisha pumba tu wanafunzi wao. Lengo ni kuwa matokeo ya mitihani ya Taifa katika mwaka huu wa uchaguzi yawe mabaya maradufu ili kuzidi kuchochea hasira za wananchi wazimalizie kwenye sanduku la kupigia kura" alitoa maelezo yake kiufasaha Dr.Patrick Ndomba Mwenyekiti wa chama cha upinzani.

Kikao hicho kizito kikaendelea kujadili ajenda mbalimbali za kuingamiza nchi huku "Chew Master" akiwaacha wenzake kwa ajili ya kwenda kupika mipango ya kumuangamiza Kachero Manu. Ajenda zingine zilizokuwa zinatamalaki ni kuhusiana na mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa fedha wa Benki kuu (BOT) Dr.Pius Chilembwa aliyeaga dunia nchini Afrika ya Kusini.
"Mazishi ya Dr.Pius yanatakiwa yabebe hadhi yake na mchango wake mkubwa kwetu. Naomba vijana wetu wanaofanya kazi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere wafanye kazi yao kwa weledi. Wasikubali kabisa jeneza kufunguliwa itakuwa ni kama kuikashifu maiti" alitilia msisitizo juu ya kuheshimiwa kwa jeneza la mchoraji ramani mkuu wa mpango mzima wa wizi huo wa mabilioni ya pesa katika mabenki.

Kikao hicho cha siri kikafungwa usiku wa manane huku kila mtu akiingilia upande wake kwa ajili ya kujiandaa kurejea makazini Jumatatu kutokana na kwisha kwa mapumziko ya mwisho wa juma. Pia masikio yao waliyategesha juu juu kama antena kutegeshea kupata taarifa ya kifo cha Kachero Manu ili walipuke ripuripu.

3. SURA YA TATU

Kachero Manu majaribuni tena mbele ya adui sumsum

Usiku tulivu wa Jumapili ya kuamkia Jumatatu, Kachero Manu alikesha akiandaa miundombinu mbalimbali ya kufanikisha kazi yake. Alijipangia Jumatatu kutakapokucha tu kuanza kutafuta nyumba ya kupangisha watakayoishi na pacha wake wa kazi Kachero Yasmine binti wa Kizanzibari. Mshirika wake ambaye walifanya nae kazi nzito katika kukidhibiti kishindo cha gaidi "Maso Maso" katika "Msako wa Mwehu" kule katika mapango ya Amboni, Tanga.

Ilipofika majira ya saa nane usiku, baada ya kumaliza kazi zake akaamua aingie zake chumbani kwake kulala. Huku akiyakinisha kuwa yupo salama salimini. Kutokana na uchovu uliokuwa unamkabili, hakuchukua raundi ndefu kitandani kabla usingizi wa pono haujampitia. Usingizini akaanza kupitiwa na njozi za sampuli mbalimbali za kuogofya.

Bila kutarajia, ghafla bin vuu alikurupuka usingizini baada ya kuota njozi mbaya kuwa kuna jambazi anataka kuja kumvamia na kumfanyia unyama. Akaheshimu machale yake, akajinyanyua kitandani taratibu kisha akadaka bastola yake ya mkononi aliyokuwa ameisunda chini ya mto wa kulalia. Mbiombio akapitia dirishani na kuporomoka mpaka chini ya ghorofa kwa ajili ya kufanya doria.

Chumba chake kilikuwa na dirisha la dharura ambalo lina uwezo wa kufunguka lote kisha limeunganishwa na kamba madhubuti unayoweza kuitumia kuning'inia mpaka ukafika chini ya nyumba.
Ndoto yake kumbe ilikuwa ni ya kweli, ilikuwa inampa bishara mbaya mbele yake. Alipotua chini akaona taa ya veranda imewashwa huku kuna pandikizi la mtu sumsum ananyata. Alikuwa amevalia gwanda za jeshi na mgongoni ana kibegi kidogo anaanza kupanda ngazi za kuja vyumbani roshani ya kwanza mkononi amekamatia bastola.

Alishangaa sana kuona mbwa wake mkali sana habweki hata kidogo. Akahisi kwa vyovyote kuna jambo baya dhidi yake. Alipoangaza vizuri macho yake kumsaka mbwa huyo akamuona amekufa kwa kupigwa risasi ya kichwani. Alikuwa hana mlinzi wa nyumbani zaidi ya mtumishi anayekuja kufanya usafi na shughuli zote za nyumbani kuanzia asubuhi na kuondoka jioni.

Akazunguka fasta kutokea upande alioutumia kushukia akaja mpaka kibarazani kwa tahadhari kubwa. Akausukuma kidogo mlango wa barazani, tahamaki ukafunguka. Ulikuwa umeshavunjwa, ila umerejeshwa geresha tu. Akaingia na kuanza kumfuata sako kwa bako bila yule adui kugutuka kuwa anaviziwa kwa nyuma na Kachero Manu.
Uzuri taa zilikuwa zimezimwa hivyo ingekuwa ngumu kuonana kirahisi.

Mwanajeshi yule hakuwa na tahadhari kubwa ya kuangalia nyuma yake wakati anapandisha ngazi za kumfikisha roshani ya kwanza. Alishajua Kachero Manu kalala usingizi wa pono ule wa fe fe fe hasa ukichukulia ni usiku mnene.
Alipofika mlangoni kwa utundu wake wa kikomandoo, akafanikiwa kuufungua mlango wa kumpeleka vyumbani. Kwenye roshani hiyo ya kwanza kulikuwa na vyumba vitatu vya kulala vinavyojitegemea kwa huduma zote pamoja na vyoo viwili vya nje na mabafu mawili ya nje.

Akasita kuingia kidogo yule adui, kisha alipojiridhisha usalama wake akaanza kuingia bila kuwasha taa huku akitumia kurunzi yake ndogo aliyoishika mkono wake wa kushoto. Alijiweka tayari akijiandaa kuanza kufanya speksheni ya mahali alipolala Kachero Manu chumba kwa chumba.

"Tupa silaha yako chini mara moja na nyoosha mikono juu..!" sauti kali mithili ya radi ya ilimgutusha yule mwanajeshi huku taa ya veranda ya juu ikiwa tayari imeshawashwa na Kachero Manu, sasa wanaonana ana kwa ana.



Alipofika mlangoni kwa utundu wake wa kikomandoo, akafanikiwa kuufungua mlango wa kumpeleka vyumbani. Kwenye roshani hiyo ya kwanza kulikuwa na vyumba vitatu vya kulala vinavyojitegemea kwa huduma zote pamoja na vyoo viwili vya nje na mabafu mawili ya nje.

Akasita kuingia kidogo yule adui, kisha alipojiridhisha usalama wake akaanza kuingia bila kuwasha taa huku akitumia kurunzi yake ndogo aliyoishika mkono wake wa kushoto. Alijiweka tayari akijiandaa kuanza kufanya speksheni ya mahali alipolala Kachero Manu chumba kwa chumba.
ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog