Search This Blog

Thursday, 23 March 2023

CABO' DELGADO - 2

  

Simulizi : Cabo' Delgado


Sehemu Ya : Pili (2)


Kikapita kimya cha kama dakika moja utasema shetani kapita vile. Bosi Kilanga akajikohoza kikohozi kikavu, kisha nae akaja karibu yao na kuvuta kiti chake akakaa.

Akachukua chupa yake ya kahawa akamimina kikombe kimoja kikubwa akaifunga, kisha akapiga mafunda matatu mfululuzo huku amefumba macho yake mithili ya mnywaji pombe haramu ya "Gongo", kuonyesha uchungu wa kahawa hiyo. Halafu akaisogeza chupa pale alipoketi Kachero Manu kumpa ishara kuwa anaruhusiwa kunywa kahawa, kisha akaanza kuongea huku anamkazia macho. Wale wageni wengine nao wakaongeza umakini kwa ajili ya kushiriki mazungumzo hayo.

"Kama ulivyoona jana kwenye taarifa ya habari ya jana AZAM-TWO usiku kuhusiana na madhila ya Watanzania wenzetu waishio nchini Msumbiji. Sina haja ya kurudia kukuelezea kile ulichokiona kwenye televisheni kama nilivyokuelekeza uangalie. Sasa haya matukio yametikisa mahusiano ya kidiplomasia ya nchi zote mbili Tanzania na Msumbiji.

Jana Rais wa wa Msumbiji amenukuliwa katika televisheni ya taifa ya Msumbiji "Televisão dê Moçambique" akihutubia taifa kuwa amesikitishwa na matukio hayo yaliyojitokeza. Rais huyo pia tayari ameagiza vyombo vya dola vya Msumbiji vichunguze chanzo cha madhila hayo na wahusika wote wachukuliwe hatua, pia ametumia fursa huyo kuwaomba radhi wananchi wa Tanzania kwa matukio hayo aliyoyaita ya kishenzi na kinyama yasiyoendana na utu wa kibinadamu.

Pia ameahidi kuandika barua rasmi yenye maelezo ya kina kwa serikali ya Tanzania ikielezea sakata lote kwa ujumla na njia za kufuata ili lisijirudie tena siku za usoni. Lakini habari za kiintelijinsia za kushtua toka Mtwara tulizozipata jana jioni ni kuwa mara baada ya matukio hayo kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa iliyo chini ya Mkuu wa Mkoa ilipitisha maamuzi ya kuwatuma askari kanzu 6 kwenda kupata ithibati ya habari, lakini tokea waondoke tarehe 9/02/2016 hawajulikani walipo mpaka hivi sasa ninavyozungumza na nyinyi.

Ubalozi wetu nchini Msumbiji umejaribu kufanya kila linalowezekana kuwatafuta, lakini leo ni siku ya 4 haijulikani kama wapo hai au wameshafariki. Na mbaya zaidi habari zilizonifikia asubuhi hii ni kuwa machafuko yanayowalenga Watanzania yameanza kusambaa katika Wilaya zingine za Jimbo hili la Cabo-Delgado.

Ripoti toka ubalozini kwetu zinasema Watanzania waishio katika wilaya za "Mueda" na "Palma" nao wameporwa mali zao na kuchaniwa hati zao za kusafiria kwa makusudi ili kuhalalisha kuwa wamekuja nchi Msumbiji kinyume cha sheria. Kwenye msafara wa mamba na kenge wapo hatukatai kuwa lazima wapo Watanzania waliokuwa wanaishi kinyume na sheria za Msumbiji, kwa maana ni wahamiaji haramu lakini hilo halihalalishi vitendo walivyofanyiwa vinakiuka sheria na haki za binadamu za umoja wa mataifa.

Kwa hali ilivyo inaonyesha dhahiri serikali ya Msumbiji imeshindwa kuwalinda raia wetu wa Tanzania. Iwe wameshindwa kwa bahati mbaya au kwa kukusudia, sisi hatufahamu maana moyo wa mtu ni kichaka. Inavyoonekana pia kuna kikundi cha watu ndani ya serikali ya Msumbiji wanatumika na mabeberu kutoka ughaibuni kutaka kuvuruga mahusiano mema yaliyopo kati ya Tanzania na Msumbiji yaliyoasisiwa na Baba wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na muasisi wa chama cha kupigania uhuru wa Msumbiji "FRELIMO" Bwana Erduado Chivamba Mondlane tokea mwaka 1962, kisha mahusiano yakatiliwa nguvu na Rais wa kwanza wa Msumbiji Bwana Samora Machel.

Sasa maagizo niliyopokea jana usiku toka kwa wakubwa huko serikalini, maagizo ambayo yakanilazimu nikupigie simu usiku huo huo ni kuwa wanataka tuchunguze nini chanzo cha fujo hizo na nani yupo nyuma ya hawa wanaotumika kuvuruga mahusiano mema baina ya hizi nchi mbili, ili watiwe mbaroni na sheria iweze kuchukua mkondo wake dhidi yao.

Sasa nakuagiza unatakiwa ujiandae kusafiri kwenda Msumbiji kwa kazi hii maalumu. Kazi ambayo serikali ya Msumbiji hatutaki wajue kuwa tumetuma Kachero wetu kuchunguza ndani ya nchi yao, itaharibu mahusiano yetu mema na itakiuka pia mikataba ya Umoja wa Mataifa ya kutokuingilia uhuru wa ndani wa nchi ingine.

Lakini hatuna jinsi Watanzania wenzetu wananyanyasika, wanaporwa mali zao na hata kuuliwa na askari kanzu wetu tuliowatuma wametoweka. Hivyo ni jukumu letu kulinda maslahi ya raia wetu hata kama ni nje ya mipaka yetu. Sina maongezi zaidi kama kauli mbiu ya Tanzania hivi sasa ya "HAPA KAZI TU", naomba ukachape kazi uwashikishe adabu vibaraka wa mabeberu mpaka wajutie uovu wao ili iwe funzo na fundisho kwa watu wengine wanaotamani kuichokonoa Tanzania yetu iliyojengwa katika misingi imara ya umoja, mshikamano na amani na Baba yetu wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hii kazi naomba imalizike mtondogoo ukihesabu kuanzia kesho, ukizidisha sana iwe juma moja kamilifu. kuanzia sasa naomba ukitoka hapa utamuona Katibu Muhtasi wangu "Kokunawa" atakukabidhi makabrasha yote yenye taarifa zote za yanayoendelea Msumbiji mpaka jana usiku pia atakupa makabrasha ya historia ya mahusiano ya kidugu yaliyopo baina ya Msumbiji na Tanzania, ili upate kufahamu nini unachoenda kukitetea, yakujenge uzalendo wako uone upuuzi wanaoufanya hawa vibaraka wa mabeberu.

Pia atakupa hati zako za kusafiria na tiketi za ndege, akaunti za benki mbalimbali na mawasiliano yote ya mtu wetu muhimu nchini Msumbiji Bwana Jacob Steven atakayekupa msaada wowote unaouhitaji ukiwa Msumbiji". Muda wote Bosi alikuwa anaongea huku Kachero Manu anamsikiliza kwa umakini mkubwa sana ili asije akapitwa na mambo muhimu, huku kukiwa kuna jambo anaogopa kusahau analiandika kwenye kompyuta yake.

"Mie nimemaliza je una lolote unataka kuongea?" aliulizwa Kachero Manu, huku macho sita ya watu watatu yakimkodolea yeye kama washabiki wa mpira wanavyomuangalia mchezaji mpira mahiri anayesakata kabumbu uwanjani.

"Sina lolote, ila leo alasiri nitaonana na yule kijana niliyeonana nae jana usiku Bagamoyo, ameniahidi kunipatia kifaa kingine cha kieletroniki kilichohifadhi nyaraka zingine nyeti, amesema nitamkuta "New Star Hotel", Mwenge saa 10:00 alasiri, huenda nikikamilisha kuzisoma nitakuwa na lolote la kuongea lakini kwa sasa sina chochote..!" aliongea Kachero Manu huku akijiandaa kuzima kompyuta yake.

"Nakutakia maandalizi mema ya safari, kuwa makini sana taifa linakutegemea, Watanzania zaidi ya milioni 55 na ushee wameweka matarajio kwetu sisi watu wa Usalama ya kuwalinda hatutakiwi kuwaangusha hata kidogo na ndio kiapo cha kazi yetu tulichokiapa cha kulinda maslahi ya nchi yetu kwanza hata ikibidi kupoteza uhai wetu.

Hawa wenzangu uliowaona hapa nafahamu unawajua kiundani, wanatoka idara mbalimbali ndani ya serikali nao ni wanakamati walioteuliwa kushirikiana na sisi, wamekula viapo vya utumishi wa umma hivyo hatuna wasiwasi nao" alimaliza maelezo yake marefu yenye kusisimua Bwana Mathew Kilanga Mudiru wa Idara ya Usalama wa Taifa, nchi nzima.

"Sawa Kiongozi nimekuelewa kama nilivyokueleza nitasoma hizo nyaraka za siri kwa kina nikimaliza nitakujuza lini nitaondoka kuelekea Msumbiji kutekeleza wajibu niliotumwa na taifa langu nilipendalo kwa dhati la Tanzania. Nadhani safari itakuwa baada ya siku mbili maana nahitaji muda mpana wa kupitia makabrasha vizuri sana ili nijue wapi pa kuanzia" alijibu Kachero Manu kwa unyenyekevu na kujiamini.

Baada ya maelezo ya Kachero Manu Bosi wake akaonyesha kuafikiana nae. Bosi wake akawa wa kwanza kusimama na wale wageni waalikwa ambao muda mwingi walikuwa ni wasikilizaji tu huku wakichukua nukuu mbalimbali za maandishi kwenye vipengele wanavyoona vinawafaa, nao wakasimama.

Wakaagana kwa kupeana mikono, Kachero Manu akahisi ugumu wa kiganja cha Bosi wake Bwana Mathew Kilanga, shaibu wa miaka 70 lakini bado mkakamavu. Kilikuwa kiganja hicho cha mkono ni kigumu mithili ya jiwe la kusugulia gaga za miguuni katika nje ya mabafu ya nyumba za uswahilini kule maeneo ya Tandale na Mbagala.

"Kuwa makini kijana wangu, usiache kumtafuta Bwana Jacob Steven ni komandoo mwenzangu mstaafu, atakusaidia sana utakapokwama" alisema kwa kumnong'oneza sikioni. Hakujibu kitu bali alitikisa tu kichwa chake kuonyesha ishara ya kukubali kupokea ushauri huo na kufungua mlango wa ofisi na kutoka nje.

Alichokuwa hakifahamu Kachero Manu kuhusu ukakamavu wa Mudiru wake wa kazi Mzee Kilanga ni kuwa alikuwa ni mwanaume wa shoka, kwanza anaamka jogoo la kwanza saa saa kumi za alfajiri kufanya mazoezi magumu, yakiwemo mazoezi ya kukimbia na tairi la trekta milimani. Hivyo umri kwake ulikuwa ni namba tu lakini mwili ulikuwa fiti mithili ya kijana wa miaka 30.

Kachero Manu Akawa anatembea kwenye korido kuelekea mahali alipo Katibu Muhtasi Koku huku ameinamisha kichwa chini kama kobe anayetunga sheria, mkononi amebeba mkoba wa kompyuta yake mawazo kibao yamemzonga.

Alishtushwa na sauti ya Katibu Muhtsasi wa Bosi wake dada Kokunawa, "kulikoni mbona kama umepewa taarifa ya kulazimishwa kuchumbia maiti pole sana...!" alirushiwa kijembe na Kokunawa.

Kachero akashtuka toka kwenye dimbwi la mkururu wa mawazo na kisha akatabasamu, akasema "Ahsante...Kwanza wewe mbaya sana hukunipa taarifa kama kuna wageni wengine zaidi ya Bosi, pili kazi imeanza upya tena natakiwa nisafiri na kila kitu nitakipata toka kwako, naomba tumalizane kabisa nipe kila kinachonihusu niondoke zangu mie, pia Bosi kasema usisahau kunifungia senene wa kutafuta njiani maana huko Msumbiji chakula chao kikuu ni panya kwa ugali wa muhogo, na mie si unajua nataka kuchumbia kwa Wasabato sasa wakwe zangu nitakosa mwana na maji ya moto, wakisikia nimekula panya tu watanipa kadi nyekundu mke nitanyimwa tena mchana kweupe kabisa" alisema Kachero Manu kumuambia Kokunawa huku anamkonyeza ukope wa jicho kiutani.

Wote wakaangusha kicheko cha furaha sheshe isiyo kifani, maswahiba hawa wa kazini. Kachero Manu akavuta kiti cha wageni akaketi, akawa anamsubiria Kokunawa amkabidhi makabrasha yote kama alivyoagizwa ili aondoke zake.

Kokunawa akabakia ameinamia mtoto wa meza yake kuyatoa makabrasha anayotakiwa amkabidhi. Akiwa pale kwenye kiti, wale wageni wawili nao wakatoka ofisini mwa Bosi Mathew Kilanga wakamkuta Kachero Manu ametulia tuli anasubiria mzigo wake aondoke zake. Mmoja wapo katika wale, mfupi, mnene ana kitambi kikubwa kampa mpiga ngoma ya besi katika bendi ya shule fulani, akajitia kumpa mkono wa kumuaga.

"Safari njema kijana wetu, Mungu akufunike kwa rehema zake" aliongea kwa sauti kubwa huku Kachero Manu akijilazimisha kwa mara ingine kutabasamu. Hisia zake zilikuwa zinamtuma mapema kabisa kuwa huyu sio mtu mzuri. Alikuwa hana ushahidi wowote ila dhana ikimtuma hivyo na hakutaka kupuuzia dhana na hiyo ndio moja ya tabia ya Kachero makini.

Kokunawa alipozipata nyaraka zote alizotakiwa amkabidhi, akaziweka kwenye bahasha ngumu akaifunga vizuri bahasha hiyo kwa gundi na kumkabidhi mkononi. "Nikutakie kazi njema, Mungu akutangulie akushushie malaika wake wa ulinzi, urudi salama My Bestfriend forever..!" aliombewa dua na Kokunawa huku machozi yakiwa yanamlenga lenga kwa mbali kwenye mboni zake za macho.

Kokunawa alitambua rafiki na Mkuu wake wa kazi, Kachero Manu anaenda kuupanda mlima mrefu ulioko mbele yake huko Cabo-Delgado, wenye vigingi, vichuguu, vichaka na makorongo juu yake. "Ahsante dada Koku usijali, nitawashinda na kurudi salama nikiwa na zawadi ya ushindi" alijibu Kachero Manu kwa ufupi.

"Eheee... nimekumbuka kitu nikitaka kusahau sasa vipi lini sasa nikutoe ile ofa ya mlo wa usiku niliyokuahidi usijisahaulishe mrembo" Kachero Manu alitaka kupotezea mawazo ya kuonewa huruma na kikubwa alikuwa hapendi kuanza kutiwa uoga kuwa anaenda kufanya jambo gumu.

"Aaah...mchumba wako yule mtu wa kanda ya ziwa kama mimi, sisi wenyewe tunajijua kwa wivu, usitake nitiwe kilema bure kama mtaalamu wa ofa sana kawape watoto mayatima, mie nalipwa mshahara mnono Babu wewe sibabaishwi na ofa zako uchwara...!" alijibu kwa mbwembwe zote akiipangulia hewani ofa ya kununuliwa mlo.

"Shauri yako kwenye miti hamna wajenzi ngoja nikawape ofa watoto warembo wa kimakonde huko Msumbiji, ambao nasikia wamefundwa na makungwi hodari na hawana madahiro na mbwembwe kama nyie akina nshomile wajivuni wakubwa nyie...!" akajibu Kachero Manu kimasihara wakafa tena kwa kicheko wote kwa pamoja.

"Ebibi kwaheri asije akanikuta hapa Mzee wako nikageuziwa kibao cha uzembe kazini nikafukuzwa kazi, huko mtaani wananchi wanasema vyuma vimebana sijui nitakuwa mgeni wa nani bila ajira, chezea mshahara usichezee kazi, tchaoooo....!" akaaga Kachero Manu na kufungua mlango wa kutokea ofisini kwa Katibu Muhtasi wao bila kusubiria madongo atakayorushiwa.

Muda ulikuwa unasoma ni saa 4:30 asubuhi, hivyo moja kwa moja Kachero Manu akafanya maamuzi ya kuelekea nyumbani kwake kujipumzisha kwa ajili ya kujiandaa na miadi yake ya saa 10:00 alasiri, ya kuonana na kijana Alex Turabu toka nchini Msumbiji.


Kachero Manu alitoka nyumbani kwake majira ya saa 8:45 mchana akijiwekea kadirio la mpaka kufikia saa 10:00 alasiri atakuwa ameshakanyaga katika eneo la Hoteli mpya ya 'New Star Hotel'.

Alipeana miadi ya kukutana na mtumishi mwenzake mchanga wa Idara ya Usalama kijana Alex Turabu. Kijana huyu alikuwa anasomea Udaktari wa Falsafa 'PhD' katika Chuo Kikuu cha 'Joaquim Chissano University' kilichopo Jijini Maputo.

Alikuwa katika mpango wa mabadilishano ya wanafunzi katika ushirikiano wa kielimu kati ya Tanzania na Msumbiji. Katika mpango huo baadhi ya wanafunzi toka Msumbiji walikuwa wanapewa udhamini wa masomo katika Vyuo Vikuu vya Tanzania, hali kadhalika hivyo hivyo, kwa wanafunzi wa Tanzania kwenda Msumbiji.

Katika mpango huo, Alex Turabu akachomekwa, akijifanya ni mwanafunzi anayesomea magonjwa ya mimea 'Plant Diseases', kumbe yupo kazini analinda maslahi ya nchi yake ya Tanzania huko ughaibuni. Kijana Alex alikuwa mahiri wa kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kireno na Kimakonde utasema ni mzawa wa Msumbiji kumbe ni Mdigo wa Tanga.
Sekeseke la mauaji ya yanayowalenga Watanzania yalipoanza tu akaanza kuyafanyia taftishi matukio hayo. Akafanikiwa kukusanya taarifa za kutosha zenye usahihi, tatizo likabakia namna atakavyosafirisha nyaraka hizo bila kutiwa mbaroni.

Inspekta Jenerali 'Mark Noble' na washirika wake walihakikisha wanaweka ulinzi mkali mpakani unaodhibiti Watanzania wanaotoka na kuingia nchini Msumbiji. Bahati aliyoipata kijana Alex Turabu ya kupenya ni wakati wa kuja kufanya utafiti wake nchini Tanzania kwenye magonjwa ya mihogo kama batobato na michirizi ya kahawia alifuata na Profesa wake anayemsimamia.

Mizigo yake ya nyaraka za shule akaichanganya na mizigo ya Profesa wake, hivyo ikapita kiulaini kabisa bila purukushani zozote za kupekuliwa. Walipofika Tanzania wakafikia kiota kipya kabisa cha 'New Star Hotel' kilichopo maeneo ya Mwenge, na kila sehemu wanayokwenda lazima waambatane, Bwana Alex akiwa kama mkalimani wake.

Siku aliyomchomoka na kumkabidhi nyaraka za siri Kachero Manu, alimuongopea kuwa kapigiwa simu ya ghafla na mlinzi anayelinda majaribio yake ya utafiti wa mihogo huko Chambezi kuwa kuna moto umewashwa kwenye shamba la mmoja wa wanakijiji unaweza kuunguza majaribio yake.

Hivyo kwa mbinu hiyo akafanikiwa kumtoroka kiaina kwenda kukabidhi nyaraka za siri lakini kikwazo kikabakia kwenye nyaraka laini 'soft copy' alizokuwa amezihifadhi kwenye kifaa maalumu chenye mafaili yenye nywira ya siri. Kifaa hicho alikuwa nacho Profesa wake usiku huo anafanyia kazi baadhi ya nyaraka za mwanafunzi wake.

Hivyo Alex akakusudia leo saa 10:00 alasiri saa chache kabla hawajaelekea Uwanja wa ndege kupaa hewani na Profesa wake kurejea nchini Msumbiji, lazima waonane kwa mara ya pili, 'New Star Hotel' alipofikia maeneo ya Mwenge ili aweze kumkabidhi.

Mpaka kufikia saa 9:30 Alasiri alikuwa amefanikiwa kufika kambi ya jeshi ya Lugalo kituo cha daladala kinachoitwa 'Super'. Alipoangalia saa yake ya mkononi tena, Kachero Manu akatabasamu akijiamini kuwa ndani ya dakika 10 zilizobaki kama pale Mwenge Mataa kutakuwa hamna foleni atakuwa ameshawasili 'New Star Hotel'.

Alipofika Mwenge Mataa akakutana na nyororo ya foleni isiyosimulika. "This is too much indeed...Afrika tunapoteza pesa nyingi kutokana na foleni za barabarani, Vyama vya siasa vina jukumu la kuwasimamisha kwenye Chaguzi wagombea Uongozi wenye maono na nia thabiti ya kutatua kero za wananchi kama hizi za miundombinu ya usafiri, afya, elimu na kadhalika. Wasipeane vyeo kwa misingi ya udugu, udini na ukabila bali uwajibikaji uwe ndio kigezo mama... !" alifoka Kachero huku anajimwagia sera za siasa peke yake ndani ya gari, anapigapiga ngumi kwenye usukani wa gari yake kwa hasira.

Alipotupia jicho tena kwenye saa yake ya mkononi akaona inasoma saa 9:50 alasiri, hii ni kuonyesha amebakiza dakika 10 tu kufikia muda wa miadi. Akatoa simu ya mkononi na kuitafuta namba ya kijana Alex aliyompa jana.

Alikuwa anataka kumfahamisha juu ya foleni hiyo hivyo awe na subira. Alichoshangazwa simu aliyokuwa anapiga ikawa inaita bila kuleta majibu mpaka ikakatika. Akarudia tena mara ya pili kuipiga simu ya Alex ikaita kidogo halafu ikakatwa.

Alipopiga tena mara ya tatu, akakutana na jibu lililompa mashaka, ni lile linalosema "Mtumiaji wa simu unayempigia hapatikani kwa sasa, jaribu tena baadae". Hapo hapo machale yakamcheza akahisi kuna jambo litakuwa limetokea kwa yule kijana wao, iweje mpaka simu yake ikatwe.

Akapiga simu kwa kijana wake wa gereji hapo hapo maeneo ya Mwenge aje kulichukua gari. Baada ya dakika 10 yule kijana wake wa gereji akawasili wakakabidhiana gari.

Kachero Manu akashuka kwenye gari na kudaka bodaboda akashika uelekeo wa kuelekea 'Mlimani City Mall'. Foleni ilikuwa imezidi kutia fora uelekeo wa kwenda mpaka Ubungo.

"Lazima kuna ajali imetokea sio bure foleni hii" alijisemesha Kachero Manu kwa sauti ya wastani ili kuweza kudukua taarifa zozote kutoka kwa huyu bodaboda. "Sio ajali kaka yangu, nasikia kuna mauaji yametokea muda mfupi uliopita kwenye hiyo Hoteli mpya ya 'New Star Hotel', watu wawili wameuliwa kikatili, hivyo askari ndio wamefunga kwa muda pale kwenye mzunguko wa barabarani mbele" alijibu Bodaboda huyo huku wakiwa wamefika kituo cha Daladala cha Lufungila.

Maelezo yale ya muendesha bodaboda yalikuwa kama mkuki wa moyo kwa Kachero Manu, na kuamua kufanya maamuzi ya haraka mara moja bila kupepesa macho. "Nishushe hapa hapa tafadhali" aliongea huku akirukia chini wakati hata kabla bodaboda haijasimama vizuri. Akatoa noti ya shilingi 5,000/= halafu bila kusubiria chenji akaanza kukimbia kuelekea uelekeo wa 'New Star Hotel'.

Dereva bodaboda alijaribu kumpayukia Kachero Manu arudi kuchukua chenji yake lakini wapi, akatia pamba masikioni na kuzidi kutimua mbio. Bodaboda yule akabakia amepigwa na bumbuwazi huku kwenye fikra zake akitilia mashaka utimamu wa akili wa abiria wake yule. Fikra za Kachero Manu zilimtuma kuwa aliyeuliwa lazima mmoja wapo atakuwa ni kijana wake Alex tu na sio mwingine.

"Pisha pisha, sogea pembeni...!" alitoa amri Kachero Manu huku mkono wake wa kushoto unapepea angani na bastola mkononi. Alikuwa ameshauvaa uso wa kazi, macho yake yanaonyesha kuwa fanya fyoko akudonyoe risasi, hataki masihara na kiumbe chochote kwenye kazi. Akafanikiwa kupenyapenya mpaka ndani ya Hoteli hiyo.

Ndani humo, askari kanzu lukuki wa jeshi la polisi walikuwa wametanda wanaendelea na uchunguzi wao kwa kufanya mahojiano na watumishi mbalimbali wa Hoteli hiyo. Akaonyesha kitambulisho chake cha kazi, wakamruhusu nae aungane nao katika harakati za kuwabaini wahalifu hao.

"My God....They will pay the price of this crime..!" aliropoka Kachero Manu baada ya kuuona mwili wa kijana Alex Turabu ukiwa umelazwa chali sakafuni, damu zinamchuruzika kutokea kifuani huku ametobolewa macho. Akawa anakumbuka taswira ya jana yake usiku walipoongea na kuonana na Alex kwa mara ya kwanza na ya mwisho, kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa Chambezi, Bagamoyo.

Alipoangaza ndani ya chumba kile kuangalia kama ataambulia chochote kitu kwenye upelelezi wake, akaona vitu mbalimbali zimetawanyika sakafuni kuonyesha kuna vitu walikuwa wanavitafuta chumbani mule wale wahalifu. Pia akashuhudia matone ya damu yamesambaa sehemu mbalimbali za chumba mpaka kwenye mashuka, kuonyesha kuwa Alex hakufa kikondoo, alipambana nao maadui zake hakukubali kusalimu amri kwao kirahisi.
Kachero Manu akafanikiwa kuingia kwenye chumba kingine alichoelekezwa napo kuna mauaji yametokea. Kilikuwa ni chumba mkabala na kile alichouliwa Alex. Huko akakutana na mwili wa mtu mzima wa makamo umri wake takribani kama miaka 55, nae akiwa amelazwa kifudifudi tumbo wazi na chini amevalia pajama rangi nyeupe, akiwa amepigwa risasi ya kisogoni damu zinamchuruzika toka kichwani.
Akatanabahi kuwa huyo ni Profesa wake kijana Alex, raia wa Msumbiji aliyekuja kumsimamia utafiti wake kwenye zao la muhogo kama alivyosimuliwa na Alex jana yake usiku. Hapo baada ya kufanya speksheni ya muda mfupi ile ya haraka haraka hakuambulia kitu chochote kinachoweza kumsaidia kubaini wahalifu wa tukio hilo.
Mwishoni kabisa kabla hajafanya maamuzi ya kuondoka Hotelini pale akapatwa na wazo. Akaomba kufanya mahojiano na Meneja wa Hoteli hiyo ya 'New Star Hotel', akakaribishwa kwa moyo mkunjufu kwenye Ofisi ya Meneja.
Kachero Manu: "Habari yako Bwana Meneja, mimi ni Afisa upelelezi toka Polisi Makao, Makuu Tanzania, kwanza pole na matukio haya yaliyotokea Hoteli mwako" alijitambulisha huku akidanganya kituo chake cha kazi kwa makusudi.
Meneja: "Habari yangu ni nzuri, namshukuru Mungu, tumeshapoa ingawa ni tukio lililotusikitisha kwa sababu litatupotezea wateja kwenye Hoteli yetu mpya", kwa kutupaka matope kuwa hatuna ulinzi madhubuti "
Kachero Manu: "Je tukio mmeligundua utokeaji wake saa ngapi? "
Meneja: " Tukio tumeligundua saa 8:45 mchana baada ya mhudumu wetu kushuhudia damu inavuja chini ya mlango wa kijana Alex, ndipo tulipofungua mlango tukakuta ameshafariki. Tulipotaka kwenda kumpa taarifa huyu Mzee wake aliyekuja nae pamoja nae tukakutana ameuliwa kinyama" aliongea kwa uchungu mkubwa huku machozi yakianza kumlengalenga.
Akachomoa hanchifu yake toka kwenye mfuko wa suruali yake na kuanza kuyadhibiti machozi yasibubujike kwa kuyafuta kisha akairudisha.
Kachero Manu: "Pole sana, jikaze tumalizie mahojiano yetu, je kuna watu wowote unamuhisi kuhusika na matukio haya?
Meneja: "Mmmhhh..... Kuna wateja wanne waliingia kwa kupishana siku moja na hawa marehemu, wanazungumza Kireno na Kimakonde, hao tunawahisi kwa sababu wametoweka wote kwa pamoja. Pia usiku wa kuamkia leo nimepewa taarifa kuwa manane ya usiku alikuja Mzee mmoja amechanja chale za kimakonde usoni kuonana nao wageni waliotoweka ingawa hatujui walichokuwa wanaongelea, kaondoka majira ya alfajiri jogoo la kwanza"
Kachero Manu: "Nitahitaji kwenda kwenye chumba chenye CCTV Kamera, nikawaangalie sura zao hao washukiwa"
Meneja: "Bila ya shaka Mkuu" akajibu huku akinyanyuka kitini na kuongoza njia mguu kwa mguu kuelekea kwenye chumba cha kuhifadhi mtambo wa Kamera.

Hisia za Kachero Manu dhidi ya Bwana "Andenga Kazimoto", Meneja Mkuu Shirika la Gesi na Mafuta, Tanzania (SGMT) kuwa ni kibaraka wa wahalifu wanaoua raia wa Tanzania nchini Msumbiji zilianza kujipa taratibu.
Utakumbuka Kachero Manu siku alivyoitwa Ofisini kwa Bosi wake wa Idara ya Usalama Bwana Mathew Kilanga kukabidhiwa jukumu la kuelekea nchini Msumbiji katika Jimbo la Cabo-Delgado kufanya taftishi yakinifu ya kuwabaini wahalifu wanaowafanyia unyama Watanzania, alikosa imani kabisa na mmoja wa wajumbe waalikwa wa kikao kile.
Hakuwa na ushahidi wala sababu kuwa na dhana mbaya dhidi yake isipokuwa ni hisia zake tu ndio zilimuongoza kuwa sio mtu mzuri na hakustahiki kuhudhuria kikao kile. Sasa hisia zake dhidi ya Bwana Andenga Kazimoto kumbe zilikuwa sahihi. Gari yenye namba ya usajili ya Shirika la Gesi na Mafuta, Tanzania (SGMT) ndio lililokuwa limetumika kuwaleta washukiwa hao wa mauaji katika Hoteli ya 'New Star Hotel' siku ya kwanza walipowasili Hotelini hapo.
Hii ni kutokana na picha mnato za CCTV-Kamera alizozichunguza Kachero Manu. Busara zikamuongoza kutokufanya pupa ya kumtia mbaroni Bwana Andenga Kazimoto ili washirika wake wasigutuke mapema wakaharibu ushahidi. Kwa kawaida nyoka anagongwa kichwani ili afe kirahisi, hivyo kichwa cha wahalifu hawa ni Jimboni Cabo-Delgado, hana jinsi lazima aende huko.
Pia hata kama angefanya maamuzi ya kumtia mbaroni, bado ulibakia kuwa ni ushahidi wa kimazingira tu usingetosha kumuhusisha kwa asilimia 100% Bwana Andenga Kazimoto. Pia kwenye kamera hizo, alifanikiwa kuzinyaka picha za wahalifu idadi yao 5 na kuamuru siku ya pili yake tu zichapishwe kwenye magazeti mbalimbali kusaidia upatikanaji wao vidagaa hao mamluki wa uhalifu.
Huku kiangaza macho cha shilingi milioni 5 kikiwekwa kwa mtu atakayefanikisha kutoa taarifa za kukamatwa kwa mhalifu yoyote katika hao. Wa kwanza kugundulika katika vidagaa hao wa uhalifu alikuwa ni Mzee mmoja wa kimakonde anayejulikana kama Mzee Mnangwa. Mzee huyu alikuwa ni mmoja wa walinzi vibarua wa muda mrefu tokea miaka ya 70's kwenye Shamba la Utafiti la Chambezi, Mjini Bagamoyo.
Wakazi wa pale walikuwa wanamfahamu kama kibarua tu, mlinzi wa shamba lakini kumbe alikuwa ni zaidi ya wanavyomjua. Huyu Mzee ni veterani wa Jeshi la ukombozi wa nchi ya Msumbiji kupitia kambi ya vijana ya FRELIMO enzi hizo. Alikuja Tanzania na wenzake kupata mafunzo ya kijeshi katika kambi ya Ruvu, Mkoani Pwani.
Baada ya kurejea nchini kwao kuendesha mapambano ya Kivita na Wakoloni wa Kireno na nchi ya Msumbiji kufanikiwa kupata Uhuru mwaka 1975, Mzee Mnangwa na baadhi ya wenzake walirudishwa Tanzania kwa mara ya pili kinyemela, wakiwa kama majasusi mwenye kulinda maslahi ya nchi ya Msumbiji nchini Tanzania.
Mzee Mnangwa akapangiwa eneo la Bagamoyo, maisha kwake yakawa yanasonga, akipata kibarua cha kuzugia cha ulinzi katika mashamba ya Chambezi kumbe ni jasusi. Akawa anaishi kwenye kitongoji chenye idadi lukuki ya Wamakonde, kinaitwa 'Makondeko', jirani kabisa na shamba la Chambezi.
Ndipo vibaraka wa Dola walipozitilia mashaka nyendo za kijana Alex na Profesa wake wakamkabidhi rungu la kuwadodosa na kuwapekenyua kama kweli wapo kwenye utafiti wa kilimo au wana ajenda zao nyuma ya pazia. Mzee Mnangwa alifanikiwa kuzipata namba za gari la Kachero Manu aliloenda nalo shambani Bagamoyo usiku usiku wakati anaenda kukutana na kijana Alex.
Kama ujuavyo zege halilali, Usiku huo huo akazileta zile namba kwa waliomtuma ambao walifikia pia 'New Star Hotel'. Mpaka kufikia majira ya alfajiri wakafanikiwa kulitambua kuwa hilo ni gari la Kachero nambari wani wa nchi ya Tanzania. Hivyo hukumu ya kifo ikasomwa toka Jimboni Cabo Delgado, nchini Msumbiji kuwa Alex na Profesa wake wauliwe kwa njia yoyote.
Kachero Manu baada ya kupata penyenye za kutambuliwa kwa Mzee Mnangwa, akatuma vijana wake mahiri kuelekea Bagamoyo kuhakikisha wanamtia mbaroni mzee huyo. Kachero Manu alikuwa anamsubiria kwa hamu kubwa ili awe ndio chanzo cha kuwataja wahusika waliomtuma. Vijana wa kazi walivyorudisha mrejesho walikuja na majibu ya kukatisha tamaa.
Baada ya kuelezea kuwa Mzee Mnangwa ameyeyuka kama samli juu ya kikaango cha moto, hajulikani alipotokomea. Kila aina ya juhudi ilifanyika ili kumtia mbaroni lakini wakaambulia manyoya tu, ameshawachurupuka tayari.
Kachero Manu akaanza kuumiza kichwa mpaka akaamua ajilipue kwa kumfuatilia dereva wa gari la "Shirika la Gesi na Mafuta Tanzania" (SGMT) ili huenda akatoa penyenye za wapi alipowachukua wale wahalifu na wapi walipo hivi sasa. Alichokutana nacho kwenye taftishi yake hiyo kilitisha mno.
Afisa Rasilimali watu wa Ofisini kwake alitoa taarifa kuwa ameanza likizo yake ya mwaka tokea jana yake. Alipoenda nyumbani kwake ndipo akakutana na tukio la kutisha na kuogofya. Alikuta nyumba yake imefungwa kama vile wakazi wake wamesafiri safari ya mbali. Alipofanikiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo kwa utundu wake anaoujua, akakuta maiti ya dereva huyo, mkewe na mtoto wake mmoja mchanga, wote wameuliwa kinyama wakiwa wamefungwa kamba.
Hii hali aliyokutana nayo ikampa hofu kubwa Kachero Manu na kumuongezea umakini kwa kutambua ya kuwa anapambana na genge la wahalifu ambao wapo makini sana, hawataki kuacha hata chembe ya ushahidi utakaosababisha watiwe hatiani.
Sasa rasmi Kachero Manu akatakiwa asafiri kichwa mchunga kuelekea Msumbiji akiwa hana bee wala chee ya sehemu atakayoenda kuwafuma Mafioso hao wa Cabo-Delgado.


SURA YA TATU
Kachero Manu “Mwiba wa Tasi”
Kachero anajulikana kwa jina la ubatizo kama 'Emmanuel Joseph' akiwa ni mtoto wa pekee katika familia ya Mzee Joseph Mbali na Bi.Josephina Nyagali. Alizaliwa mwaka 1985 kipindi cha hekaheka za Uchaguzi wa Rais wa Awamu ya Pili, Ndugu Ali Hassan Mwinyi, katika kijiji cha Mahiwa kilichopo wilaya ya Lindi Vijijini.
Baba yake mzazi Mzee Joseph taaluma yake alikuwa ni dereva aliyeajiriwa katika hospitali ya Misheni ya Nyangao, na mama yake Bi Josephina alikuwa ni mama wa nyumbani tu, anayejishughulisha na kazi za kilimo na ujasiriamali mdogo mdogo.
Sasa huyu kijana wao alipachikwaje hili jina la "Manu Yoshepu"?. Hili jina ni mbwembwe tu za utamkaji katika kabila lake la asili la Wamwera. Jina kama Emmanuel wao wanaita "Manu", na Joseph wanalitamka "Yoshepu".
Katika nchi hii, Wamwera ni moja ya kabila ambalo wana lugha ya kiswahili yenye vionjo vya aina ya kipekee kabisa. Mfano sentensi ya kiswahili ukisema "Nataka kuvua nguo" wanasema "Nataka kuchojoa nguo", pia ukisema "huyu ana sura mbaya" utawasikia wakisema huyu "ntu ana sura ya kunyata" na vionjo vinginevyo vingi vitakavyokufanya uwapende tu utake usitake.
Kabila hili tabia zao za ujivuni hutaniwa kuwa mapacha zao ni Wahaya. Mtu wa kabila hili akienda shule hutomtaka kwa hizo mbwembwe zake. Wamwera ni kabila linalopatikana kwa wingi katika mkoa wa Lindi katika maeneo ya wilaya ya Nachingwea, Ruangwa, na Lindi vijijini.
Inasemekana asili yao ni Kaskazini Magharibi mwa nchi ya Msumbiji. Waliingia Tanzania katika kipindi cha kati ya karne ya 12 mpaka 16 wakimkimbia kiongozi wao mkatili akiitwa Sultani Sadala.
Kwa asili Wamwera ni mashujaa sana, hasa ikikumbukwa katika vita ya Majimaji, Wamwera wa Nachingwea wakiwa juu ya milima Ilulu, walishiriki bega kwa bega kwenye vita hivyo, wakiwaporomeshea mawe na mishale askari wa Kijerumani.
Manu alilelewa katika maadili mufti kabisa ya dini ya Kikristo, madhehebu ya Kikatoliki. Manu tokea utoto wake hakuwaki kuwa goigoi abadani. Daima alikuwa ni mtoto shujaa, mkakamvu, mchapakazi, mwerevu na mwenye umbile lililogangamala la kikubwa. Kiasi kwamba wengi walikuwa wanajua anadanganya umri wake kama wanavyodanganya watu wa nchi za Afrika ya magharibi kama Naijeria, Ghana, Togo na Cameroon ili wapate kucheza timu za soka la kulipwa huko Ulaya.
Ukakamavu wake unaokumbukwa na kijiji kizima, ni kwenye tukio lililotokea akiwa darasa la 6. Tukio lake hilo lilikuwa la kumkimbiza mwizi aliyepora mkoba wa mwalimu wake wakati wa mashindano ya shule za msingi UMITASHUMTA yaliyokuwa yanafanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Mahiwa.
Alikimbizana na huyo kibaka kwa umbali wa kilometa 4, akafanikiwa kumtia mbaroni kibaka huyo peke yake maeneo ya Nyangao Sokoni. Mpaka walivyofika raia wema kumuokoa kibaka huyo walikuta tayari kashavimbishwa manundu ya kutosha usoni mwake na Manu.
Kutokana na uwezo huo mkubwa wa mbio aliouonyesha wa kumkimbiza umbali mrefu mwizi huyo bila kuchoka, kamati ya UMITASHUMTA Mkoa kwa kauli moja ikampitisha moja kwa moja kuwa mshiriki wa mbio ndefu za meta 5000 Kitaifa bila kushindanishwa na mwanafunzi yoyote.
Alipomaliza elimu ya shule ya msingi mwaka 1998 alichaguliwa kujiunga na sekondari ya wavulana “SONGEA BOYS” akiwa ni miongoni mwa wanafunzi bora 10 kwa mkoa mzima wa Lindi. Lakini mama yake Manu, Bi. Josephina alikuwa ni muumini mzuri sana wa madhehebu ya kikatoliki, tena Mfia dini haswa akafanya maamuzi ya kumpeleka mtoto wake katika shule ya Sekondari ya Seminari ya Namupa, ambayo ni kijiji cha jirani tu kutoka Mahiwa.
Lengo alitaka mtoto wake aje kuwa Padri amtumikie Mungu, katika maisha yake yote ya duniani. Mtoto wao akadurusu Namupa Seminari mpaka kidato cha 6 mwaka 2005 akafaulu kwa kiwango cha daraja la I na pointi 5 katika mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi "HGE". Baada ya hapo akachaguliwa kujiunga na Seminari Kuu ya Peramiho, huko Ruvuma kuendelea na masomo ya Upadri.
Lakini siku zilivyokuwa zinasonga akawa kashapoteza wito wa kuitumikia dini katika maisha yake yote. Hasa ukichukulia kwa wazazi wake yeye alikuwa ndio mtoto wao wa pekee, hivyo kama angejiunga na upadri maana yake ni kuwa wazazi wake wasingepata wajukuu hata wa dawa. Hivyo kupelekea kupunguza idadi ya wana ukoo wao.
Akaamua kufanya maamuzi magumu na mazito ya kukacha masomo ya Upadri na kuamua kujiunga na Chuo Kikuu cha Dodoma, akisomea shahada ya sanaa ya mambo ya kudhibiti uhalifu "BA Criminology". Akiwa mwaka wa kwanza tu Chuo Kikuu mwaka 2006 ndipo Bosi wake Mathew Kilanga alipoenda kuwafanyia usaili wa kujiunga na idara ya usalama wa nchi.
Hasa ukichukulia digrii ya “Criminology” ilikuwa ndio imeanza kufundishwa hapa nchini na Chuo Kikuu cha Dodoma kikiwa ndio chuo pekee kinachofundisha elimu ya kupambana na uhalifu.
Katika darasa lao la wanafunzi 20 ni “Manu” pekee ndiye aliyefikia viwango vya Bosi Mathew Kilanga. Ikabidi aombewe ruhusa ya kusimamisha masomo ya Chuo Kikuu kwa muda kwa ajili ya kupelekwa nchini Marekani kwenye mafunzo ya juu zaidi ya usalama na ukomandoo kwa muda wa miaka mitatu (3), kwa masharti ya kupewa ajira pindi tu akifanikiwa kumaliza vizuri mafunzo yake.
Hapo ndipo alipotenganishwa na mpenzi wake, asali wa moyo wake Faith Magayane. Lakini kutokana na umahiri wake katika medani za mapambano ilibidi amalize mafunzo yake kwa muda wa miaka miwili pungufu kwa mwaka mmoja.
Tukio lililomjengea historia ya kukumbukwa na idara zote kubwa duniani za usalama ni kitendo chake cha kumtoboa utumbo kwa bahati mbaya mwalimu wake wa sanaa za mapigano kutoka China wakati anajifunza mtindo wa mapigano ya kutumia ncha za vidole unaitwa “Dim Mak”.
Kutokana na tukio hilo mwalimu wake huyo alipendekeza apewe cheti cha kuhitimu kabla ya muda na hapo hapo akapachikwa jina la utani na wanachuo wenzake la “Mwiba wa Tasi”.
Tasi ni aina ya samaki asiye na magamba anapatikana baharini ila ana miba mbaya sana, ikikuchoma maumivu yake yanaweza kudumu hata wiki nzima. Sasa wenzake walifananisha tukio lake la kudonyoa utumbo wa mwalimu wake wa Kichina kwa kutumia vidole na maumivu ya mwiba wa tasi.
Aliporejea nchini Tanzania mwaka 2008, akapewa ajira rasmi ya kuitumikia Idara ya Usalama akianzia na cheo cha Kachero Msaidizi, na mtihani wake wa kwanza mwezi mmoja tu baada ya kurejea nchini ikawa ni kushirikiana na kikosi cha Umoja wa Afrika kumuondoa madarakani muasi Janali Mohammed Bacar wa visiwa vya Anjouan.
Vikosi vya Comoro na vya Umoja wa Afrika vikijumuisha majeshi ya Tanzania na Sudan, vilianza uvamizi wao katika mji mkuu wa Nzouni-Mutsamadu na katika uwanja wa ndege. Kachero Manu ndio alikuwa mtu wa kwanza kuingia katika Kasri la Kanali Mohamed Bacar linaloitwa "Dar el Najah" huko Anjouan, si mbali na mji mkuu wa Mutsamadu.
Aliingia kwenye jumba hilo kupitia mfumo wa maji taka wa hapo mtaani, na ilibaki kidogo tu amtie mbaroni kwa mikono yake mwenyewe ila Kanali Muhammed akawahi kutoroka kwa kutumia ndege ndogo ya kukodi iliyoruka kutoka kwenye uwanja mdogo wa nyumbani kwake na kukimbilia nchini Madagascar.
Baada ya kuitekeleza kazi hii kwa uaminifu na umahiri mkubwa, akapandishwa cheo mpaka kuwa Kachero namba moja wa nchi nzima. Kisha mwaka 2009 akarejea Chuo Kikuu cha Dodoma kuendelea na masomo yake ya shahada ya kwanza, ambayo aliimaliza mwaka 2012.
Kitendo chake cha kurejea tena Dodoma ndio kilimfanya mpenzi wake Faith Magayane atafute kazi Jijini Dodoma ili awe karibu na Kachero Manu aweze kupalilia vizuri penzi lake lichanue bila shida. Alivyomaliza masomo yake akajenga nyumba yake maeneo ya Mbezi juu, wilaya ya Kinondoni, Dar es salaam akawa anaishi huko tokea mwaka 2014 mpaka sasa.
Chambilecho "Mzigo mzito mtwishe Mnyamwezi", sasa Kachero Manu alikuwa amepewa mtihani mzito wa kwenda Msumbiji kuchunguza chanzo cha machafuko dhidi ya Watanzania wanaoishi huko. Muda wa mapumziko kwake ulikuwa umeisha, alitakiwa aende kuwa kinara kwenye uwanja wa vita, akavuje jasho na damu, kufa au kupona, punda afe, mzigo ufike.
Kwake yeye "Mwiba wa tasi" ilikuwa ni ufahari mkubwa kuaminiwa na Taifa lenye vichwa zaidi ya milioni 55. Minghairi ya hiyo, lakini pia kurudi nchini Msumbiji sehemu ambayo ndio asili za mababu zake wa kimwera kwake ilikuwa ni moja ya fursa adhimu.
Kama ujuavyo kwa asili Msumbiji na Tanzania ni ndugu wa damu, hivyo alikuwa na hamu ya kuwatambua vinara wa chokochoko hizo zinazoendelea. Kisha awashikishe adabu iwe onyo kali kwa wengine wenye kutamani kuchafua mahusiano maridhawa baina ya Tanzania na Msumbiji. Mahusiano yaliyorithishwa na mababu tangu na tangu.

Historia ya Uhuru wa Msumbiji
Kachero Manu kwa muda wa siku mbili mtawalia, kuanzia tarehe 12/02/2016 alikuwa amejifungia ndani nyumbani bila kutoka nje kama mwali anayetawa. Alikuwa anapata mahitaji yote muhimu maskamoni, akimuagiza mtumishi wake wa kiume wa nyumbani amletee kila anachohitajia.
Kwanza kabisa alianza kubukua kabrasha la faili la rangi nyeusi lenye karatasi nyeupe ila zimepoteza nuru yake kutokana na kukaa muda mrefu kwa zaidi ya miaka 56. Alipoanza kulisoma akarejesha kumbukumbu zake miaka ile yupo Sekondari, Seminari ya Namupa anasoma somo la Historia, moja ya masomo ambayo alikuwa analimudu kwa kiwango cha juu sana.
Humo akakuta historia ya chama cha ukombozi cha Msumbiji chenye jina la lugha ya kireno "Frente de Libertação de Moçambique" (FRELIMO). FRELIMO ilianzishwa mwaka 1962 na muasisi wa ukombozi wa Msumbiji Bwana "Edwardo Mondlane" kwa msaada mkubwa wa Rais wa Tanganyika wakati huo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Lengo la FRELIMO ilikuwa ni kuiweka huru nchi ya Msumbiji na dahari ya dhulma za mkoloni wa Kireno. Makao makuu ya FRELIMO yakawa ni Dar és Salaam kwa muda wa miaka 13 kuanzia 1962-1975. Ili kuhakikisha nchi za Kusini mwa Afrika zinapata ukombozi, Mwalimu Nyerere aliunda kamati maalumu, wakiwemo Jenerali Sarakikya, Brigedia Hasheem Mbita, Kanali Ally Mahfoudh, na Kanali Ameen Kashmeer.
Hivyo vichwa vilivyoteuliwa na Nyerere vilikuwa ndio injini ya kuamsha vuguvugu la kupigania Uhuru wa Msumbiji. Wakaanza kupokea vijana wa Msumbiji mwishoni mwa 1964 waliokuwa wanasoma Vyuo Vikuu nchini Ureno, lakini wakakacha masomo yao kwa sababu ya kutaka kupigania uhuru wa Msumbiji kutokana na kusukumwa na wimbi la uzalendo wa nchi yao.
Baadhi ya vijana hao walikuwa ni Samora Machel, Philipe Magaie, Joachim Chisano, Raimundo Pachinuapa na Marcelino Dos Santos. Vijana hawa walipewa mafunzo kamili ya kijeshi na ya kisiasa kisha wakapelekwa Algeria kwa mafunzo zaidi, hasa ukichukulia kipindi hiko Algeria walikuwa wametoka kwenye vita ya kumuondoa Mfaransa.
Hivyo Algeria ilichukuliwa kama ni sehemu sahihi ya kujifunza mbinu za medani ya vita. Serikali ya Cuba nayo haikubaki nyuma kwenye kuunga mkono harakati za kupigania Uhuru wa nchi za Kiafrika, ikamleta nchini Tanzania Balozi Pablo Ribalta.
Huyu balozi ndiye, ambaye alikuja kama mshauri wa mbinu za ukombozi na ndio alifanikisha ujio wa bingwa wa vita vya msituni Ernesto Che Guevara 1965. Che Guevara, Muajentina huyu mwenye misimamo mikali ya siasa za kimapinduzi, kwanza alifanya mkutano na viongozi wote wa ukombozi wa kusini mwa bara la Afrika. Kwa bahati nzuri kwenye mkutano huo, kiongozi wa FRELIMO, Bwana Mondlane nae alihudhuria.
Kikubwa Che Guevara aliwasisitiza kushikamana kwa umoja baina yao ndio silaha yao kubwa itayowawezesha kuyaangusha majeshi makubwa, tena yenye silaha na zana nzito za kivita. Sumu hizi walizolishwa akina Mondlane na mwanaharakati wa kutukuka Bwana Che Guevara zikawasha moto wa mapambano katika mioyo yao na kuunguza kabisa chembechembe zote za uoga katika miili yao.
Vijana wa Msumbiji wale waliopelekwa nchini Aljeria, walivyorudi nchini Tanzania walipelekwa moja kwa moja kambini eneo linaloitwa "Farm seventieen "Nachingwea, Lindi. Huko kambini sasa wakaanza kuandaliwa kwenda kuanzisha vita vya ukombozi kwa njia ya mtutu wa bunduki.
Wapiganaji hao wa FRELIMO hawakuwa wengi, walikuwa hawazidi hata elfu moja (1,000), lakini idadi kubwa ilikuwa ni wanajeshi wa Tanzania (JWTZ). Alipofika kwenye maelezo hayo, Kachero Manu akapigia mstari, na kuanza kufanya tafakuri jadidi na kuanza kujiuliza.
"Inawezekana vipi watu ambao wamesaidiwa kujikomboa kwa kutumia mali na damu za raia wa nchi nyingine leo wawageuke kuwafukuza nchini mwao tena kwa ukatili, ubakaji na mauaji?. "Lazima tu kuna nguvu ya mabeberu toka za Ughaibuni lakini wanaficha ajenda zao za siri kwenye migongo ya watu wa Msumbiji wale wasiofahamu historia ya Uhuru wa nchi yao na wenye tamaa za kujinufaisha kiuchumi bila kujua thamani ya Watanzania kwao".
Kisha akaendelea kuperuzi kabrasha hilo humo akakutana na maelezo kina yakielezea jinsi Kanali Mahfoudh Mtanzania chotara wa kiarabu aliyehitimu mafunzo ya kikomandoo namna alivyofanikiwa kujipenyeza kwenye kambi za Wareno huko katika miji ya Cabo-Delgado na Xai-Xai kufanya upelelezi wa kujua nguvu za jeshi la Wareno na udhaifu wao.
Hapo tena Kachero Manu akavuta tafakuri jadidi, "ina maana Wareno toka mwanzoni walijikita Cabo-Delgado, na sasa machafuko dhidi ya Watanzania yameanzia Cabo-Delgado, hapa kuna kitu maalumu chenye mahusiano kati ya wakoloni na huu mji wa Cabo-Delgado sio bure" alitafakari kwa kina Kachero Manu.
Akatambua hapa kuna siri nzito imejificha ambayo inabeba fumbo kubwa la machafuko hivyo anahitajika kuitegua siri hiyo na kuiweka bayana. Na kama akifanikiwa kuitegua hiyo siri ndio kitajulikana kiini halisi cha machafuko dhidi ya Watanzania wasio na hatia yoyote. Kisha humo akaendelea kusoma akakuta namna mapambano yalivyoendeshwa kwa muda wa miaka 13 mpaka Uhuru kamili wa Msumbiji ulivyopatikana tarehe 25/06/1975.
Kingine cha kilichomstaajabisha kwenye nyaraka hizo ni kuwa Marais wote wa Msumbiji kwa awamu zote waliishi Tanzania, kuanzia Samora Machel, Dr.Joachim Chissano, Armando Gwebuza na mpaka Rais wa sasa Filipe nyusi wote kwa ujumla waliishi katika kambi mbalimbali za hapa Tanzania kuanzia Nachingwea, Tunduru, Liwale na Kongwa. Kwa ufupi unaweza ukaleta hitimisho kuwa Tanzania ndio Chuo Kikuu cha kuwapika Marais wa nchi ya Msumbiji.
"Huu nao ni uthibitisho wa wazi kuwa huwezi kutenganisha mafanikio ya Msumbiji na nchi ya Tanzania" aliwaza Kachero Manu. Baada ya kumalizana na kabrasha hilo akafungua lingine linaloelezea kwa kina vita baina ya wapigania uhuru wa Msumbiji dhidi ya Wareno iliyoanza tarehe 25/09/1964. Ambapo wapigania uhuru wa jeshi la ardhini walivamia ofisi za serikali ya Wareno zilizopo Cabo Delgado, huku jeshi hilo kllikitokea nchini Tanzania.
Hii ikampa udadisi wa kutaka kulifahamu kinagaubaga Jimbo hilo la Cabo-Delgado. Ikabidi avute mtoto wa meza yake ya kusomea, akaitoa ramani ndefu kama mkeka. Akafungua ramani hiyo kubwa ya nchi ya Msumbiji na viunga vyake vyote iliyokuwa imehifadhiwa humo kisha akaitundika ukutani. Akawa analitafuta jimbo la Cabo-Delgado kwa kutumia fimbo yake nyembamba, mpaka akaliona kwenye ramani.
Akakuta ni jimbo lililopo kaskazini kabisa mwa nchi ya Msumbiji. Likiwa na kilomita za mraba zisizopungua 82,625 na idadi ya wakazi isiyopungua watu milioni 2,333,278, likiwa ni jimbo lenye wilaya 16. Huku makabila matatu yakitamalaki ndani ya jimbo hilo, nayo ni Makonde, Makua na Mwani. Makao makuu ya jimbo yakiwa yanaitwa Pemba na miji mingine muhimu ni Montepuez na Mocimboa da Praia.
Baada ya kumaliza kuisoma kwa kina ramani hiyo kwa ujuzi mkubwa hasa ukichukulia shuleni alikuwa mahiri sana kwenye somo la Jiografia usomaji wa ramani 'Map Reading'.
Akaanza kupitia ripoti mbalimbali za kiuchunguzi zinazoelezea hatua mbalimbali zilizochukuliwa mpaka sasa na jeshi la polisi nchini Msumbiji lakini hakuona chochote cha maana zaidi ya maelezo ya mkahawani yasiyoweza kumsaidia chochote kwenye kazi yake mpya anayoitarajia kuianza.
Akaona kazi ni mbichi kabisa anatakiwa aanze uchunguzi wa alifu kwa ujiti. Akafunga makabrasha akaweka nia ya kuelekea Cabo-Delgado kuanza kazi mara moja bila kuchelewa.


SURA YA NNE
"Safari ya Cabo-Delgado yaingia nyongo"
Tarehe 14/02/2016 saa 11:00 kamili alfajiri mwanana yenye kibaridi chepesi, ikiwa ni siku ya Jumamosi, Kachero Manu maarufu kwa jina la "Mwiba wa Tasi" alikuwa amedamka mapema sana kuliko kawaida yake.
Kama sio safari ya kikazi iliyopo mbele yake kwenye hiyo siku angekuwa yupo karibu na mchumba wake kipenzi Faith Magayane wanaendelea kuufaidi usingizi wao. Walipanga siku hiyo ya Wapendanao "Valentine Day" kukicha tu wajiandae kwenda Mbuga ya wanyama ya Mikumi, mkoani Morogoro kufurahia miaka 8 ya safari ya mapenzi yao yalioanza kumea na kuchipua wakiwa tokea Chuo Kikuu cha Dodoma "UDOM".
Sikukuu hiyo ambayo iliyozoeleka sana kwenye tamaduni za Wazungu, lakini kutokana na utandawazi kushamiri na dunia kuwa kama kijiji, ilikuwa pia inaazimishwa mpaka katika nchi za Kiafrika kama Tanzania.
Ila kazi kwanza mapenzi baadae, ilikuwa hamna jinsi lazima Kachero Manu aondoke kwa haraka sana Tanzania kwenda nchini Msumbiji kutekeleza majukumu yake ya kitaifa aliyokabidhiwa kazini kwake. Alipoamka kitandani akafanya mazoezi ya viungo kwa muda wa kama robo saa kisha akaenda kujimwagia maji maliwatoni.
Baada ya kutoka bafuni akaanza maandalizi ya safari. Wakati anavaa ndipo akakumbuka kuwa alipolala saa 6:00 usiku baada ya kumaliza kudurusu nyaraka zake muhimu alitaka mapumziko timilifu hivyo akaamua azime simu zake zote asipate usumbufu wowote.
Akaelekea sehemu alipozihifadhi simu zake na kuziwasha. Simu anayoitumia sana kwa shughuli za kiofisi alipoiwasha haikuwa na ujumbe wowote, akashukuru Mungu maana kama angekuwa ametafutwa na Bosi wake halafu hakupatikana ungekuwa msala mwingine kwa upande wake.
Alipoiangalia simu yake ya matumizi binfasi akakutana na namba ya simu ya Mjomba wake imempigia saa 7:15 usiku kwa zaidi ya mara 8 wakati namba yake haipo hewani.
"Mjomba kama kawaida yake ikifika mwishoni mwa juma ni kupiga vizinga tu vya kuomba hela ya pombe...!" alipuuzia kwanza kumtafuta Mjomba wake hewani akiona simu hiyo haina kipaumbele chochote. Akaanza kuitafuta namba ya mpenziwe Faith ili waagane vizuri kabla hajapaa.
Alishamgusia kwa juu juu kuhusu safari ya ghafla inayomkabili tokea juzi, lakini Faith aliona kama vile anataniwa tu na muhibu wake. Akaipiga simu ikaanza kuita kisha ikapokelewa. "Baby ina maana huko kazini kwenu hamna mwingine wa kutumwa hiyo kazi ila wewe tu?" ilikuwa ni sauti ya mang'oro na kulalamika ya mpenzi wake baada tu ya kupokea simu hiyo.
Hakukuwa na salamu wala nini, alikuwa ametibuka nyongo kwelikweli. "Baby usijali ni ndani ya wiki moja tu nitakuwa nimesharejea kikubwa niombee dua tu nirudi salama, natamani sana nibaki na wewe asali wa moyo wangu ila majukumu ya kikazi ndio yananilazimisha niwe mbali nawe" alijibu Kachero Manu kwa sauti ya kubembeleza hakupenda kabisa kumpa maudhi mpenzi wake.
"Mhhh....haya isije ikawa unaniongopea unaenda safari ya kikazi kumbe unaenda na mchepuko wako huko Cabo-Delgado, na kwanini kwanza mpaka usafiri siku ya wapendanao usingesubiri ipite kwanza, wenzangu wote ofisini watakuwa na wapenzi wao mimi peke yangu nitabaki peke yangu kama kinda wa njiwa aliyefiwa na wazazi" mpenzi wake Faith aliendelea kujilalamisha huku analia kwenye simu kilio cha kwikwi akionyesha haipendi kabisa hiyo safari.
Ongea yake ilionyesha ana joto joto la wivu limeshampanda. Ilibidi Kachero Manu atumie zaidi ya nusu saa kumlainisha mpenzi wake, kwa maneno ya mahaba ya kumtoa nyoka pangoni mpaka akaeleweka. Mwishoni Faith akakubali matokeo kuwa hawezi kuitengua safari hiyo, akamtakia safari njema ingawa alihuzunika sana kushindwa kuwa pamoja na mchumba wake siku kubwa kama hiyo.
Hakuna mtu aliyefahamu kama Kachero Manu anaelekea Mtwara isipokuwa Bosi wake Mzee Mathew Kilanga tu, hata mpenzi wake Faith alimuaga kwa ujumla tu kuwa anaenda Cabo-Delgado lakini atakavyosafiri hakuwa anafahamu atasafiri kwa njia gani.
Kawaida ya Kachero Manu huwa hana imani na mtu yoyote inapokuja suala la usalama wake kwenye kazi. Baada ya hapo akaelekea mesini kupata staftahi ya mkate uliopakwa siagi, mayai mawili ya kuchemsha na kahawa kavu isiyo na sukari. Baada ya hapo akabeba kibegi chake tayari kwa safari.
Ghafla akiwa ameshafunga mlango wa chumbani kwake anaelekea kwenye ngazi aanze kushuka chini, akasikia mlio wa kengele ya nyumba yake kuashiria mtu anataka kuingia ndani ya nyumba. Akaweka chini kibegi na kuanza kushuka ngazi kwa haraka kutaka kujua nani anayegonga mlango.
"Samahani Bosi...mzigo wako umeletwa toka manane ya usiku na mwanadada mmoja, alikuja na gari la kifahari kasema ni zawadi yako ya Valentine Day..!" aliongea Mlinzi wa getini kiunyenyekevu mkubwa huku akiwa anakabidhi boksi hilo kubwa wastani lililonakshiwa kwa mapambo ya rangi nyekundu kwa nje kuashiria ni zawadi maalumu ya siku ya wapendanao.
"Ahsante..!" alijibu kwa ufupi huku akilipokea boksi lile lililokuwa na uzito wa wastani. "Mwanadada..! Gari la kifahari...Tena zawadi ya Valentine..!" yalikuwa maswali anayojiuliza kwa udadisi Kachero Manu wakati anapandisha ngazi kurudi chumbani kwake akiwa amejawa na tashiwishi ya kulifungua boksi hilo ili kujua nani aliyetuma zawadi hiyo kwake.
Zaidi ya mpenzi wake Faith hakuwa na mazoea ya kutumiana zawadi na wanawake. Akaingia chumbani na kujibweteka juu ya tandiko kisha vidole vyake ndio vikawa vinaongea vikianza kulifungua boksi hilo. Alipolifungua tu kwanza akakutana na kadi kubwa imefungwa kwenye karatasi maalumu ya zawadi yeye mng'aro 'gift paper', akaiweka pembeni hiyo kadi akili yake ikiwa ipo kwenye zawadi ya ndani ya boksi.
Ghafla bin vuuu....akapigwa na mshtuko wa mwaka huku akilitupa kwa nguvu boksi hilo alilokuwa amelishikilia juu ya kitanda kwa uoga. Kijasho chembamba kikaanza kumvuja juu ya paji lake la uso licha ya kuwa kiyoyozi kilikuwa kinafanya kazi huku akitwetwa kwa nguvu. Mapigo ya moyo yalianza kukimbia kwa kasi utasema moyo unataka kumchomoka kifuani.
Akawa ametumbua macho yake kuelekea alipolitupia boksi hilo kama fundi saa aliyepoteza nati ndogo sana ya saa anayoitengeneza. Alikuwa haamini kitu ambacho macho yake yanamshuhudisha asubuhi hiyo kilazima. Machozi yakaanza kumvuja bila kizuizi chochote, alishindwa kabisa kujizuia. Alichokiona kwa macho yake kilikuwa ni chenye kuogofya kwenye mboni za macho yake, hakuna cha ukomandoo wakati wa shida, maumivu yanakuwa ni yale yale kama binadamu wengine.
JE KACHERO MANU KAPOKEA ZAWADI GANI YA VALENTINE DAY????
ENDELEA KUFUATILIA


RIWAYA: "CABO-DELGADO-PART 05
Kichwa cha kipenzi chake, mama yake mzazi, Bi. Josephina Nyagali kilichokatwaa kwa mtindo wa kuchinjwa na panga kilikuwa ndio kipo ndani ya boksi la zawadi aliloletewa usiku wa manane nyumbani kwake. Kilichokuwa kinamliza ni kifo cha kikatili cha mama yake mzazi, tena akiwa hana hatia yoyote masikini wa Mungu. Yeye akiwa ndio chanzo cha mama yake kupoteza hai kutokana na maelezo ya kwenye barua aliyoikuta ndani ya boksi hilo ikiwa na maandishi makubwa tu. Barua hiyo ilikuwa ikisomeka kama ifuatavyo;
"TUNAJUA UNAJIANDAA KUJA CABO-DELGADO KARIBU SANA MACHINJIONI, LAKINI TAMBUA YA KWAMBA BAADA YA SHINGO YA MAMA YAKO MZAZI, ITAFUATIA YA BABA YAKO MZAZI, YA MCHUMBA WAKO NA JAMAA ZAKO WA KARIBU. KWA USALAMA WAKO NA WA FAMILIA YAKO KAMA KWELI UNAWAPENDA USITHUBUTU KUKANYANG'A CABO-DELGADO"
BY-"BOB-CHINANGA"
Majuto ni mjukuu Kachero Manu akaanza kujilaumu kwa maamuzi yake ya kuzima simu usiku kucha uliopita. Huenda simu zilizopigwa na Mjomba wake zilikuwa zinamfahamisha juu ya tukio hilo. Pia huenda tarishi aliyetumwa kuleta mzigo huo wa kichwa nyumbani kwake angefanikiwa kumtia mbaroni. Akili zikamrudia akatanabahi kuwa yeye ni mtoto wa kiume lazima ajikaze kisabuni ili mambo yaweze kwenda.
Hapo hapo akapiga simu hospitali yao ya kitengo maalumu waje kukichukua kichwa hicho ili wafanye harakati za kukituma Kijijini Mahiwa kikaunganishwe na mwili wa mama yake. Hakuwa na jinsi zaidi ya kusafiri tu kuelekea Cabo-Delgado, kazi yake ya ulinzi wa amani ya nchi ilikuwa ni kazi ya kutanguliza maslahi ya nchi kwanza kabla ya maslahi binafsi.
Alishajipanga kisaikolojia kuwa ataenda kuhani msiba wa mama yake mzazi kama akifanikiwa kurejea salama toka nchini Msumbiji. Hamu kuja kuliona kaburi la mama yake ikawa ni kichocheo kwake cha kujitahidi kuwa na tahadhari ya hali ya juu ili asiuliwe akiwa kwenye uwanja wa vita.
Akampigia simu Bosi wake akimuelezea kwa kinagaubaga mkasa mzima uliomkumba muda mfupi Kabla hajasafiri. Bosi Mathew Kilanga, akampa pole na kumhakikishia kuwa serikali itashirikiana na familia kwa niaba yake kuhakikisha inampa mama yake maziko yenye hadhi ya juu. Wakaagana kwenye simu na Kachero Manu kujiandaa kuelekea Uwanja wa ndege tayari kwa safari.

Kachero Manu alifunga mkanda ndani ya ndege aina ya "Bombardier Dash-8 Q400" kikwangua anga kipya kabisa, mali ya shirika la ndege la Tanzania-ATCL akielekea zake Manispaa ya Mtwara. Alikuwa ameshakabidhiwa na Sekretari wa Bosi wake "Kokunawa" tiketi ya ndege ya kuelekea nchini Afrika ya kusini-Johannesburg, kisha ndege ya kuunga kwenda Pemba makao makuu ya jimbo la Cabo-Delgado.
Taarifa alizopata ni kuwa kuna ndege zaidi ya tano zinazoenda Pemba kwa wiki kutokea Johannesburg, nyingi zikiwa zimejaza watalii. Pia alishapewa hati ya kusafiria mpya yenye jina jipya la Hassan Ibn Hussein, mzaliwa wa Kisiwani, Unguja. Alikuwa amepanga aingie Cabo-Delgado kama mtaalamu wa mambo ya elimu ya kale, anayetafiti majengo ya asili yaliyojengwa na Mreno nchini Msumbiji.
Ili kuendana na muonekano wa utamaduni wa Waunguja kabla hajaondoka alishaenda Kariakoo msikiti wa Kwamtoro ambao upo karibu na soko kuu la Kariakoo, Dar es Salam kununua kanzu na barakashia za kutosha bila kusahau tasbihi ya kiislamu atakayotumia kuzugia kumsabihi Mwenyezi Mungu akiwa barabarani. Aliondoka kwa usafiri wa teksi ya UBBER iliyomfuata nyumbani kwake Mbezi juu na kumpeleka mpaka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
Kachero Manu akiwa ndani ya vazi la kanzu rangi ya samawati huku akiwa amevaa makubazi ya rangi nyeusi yenye mkanda katikati unaotenganisha kidole gumba na vidole vingine, huku kichwani akiwa amevalia kofia ya kushonwa na mkono ya rangi nyeusi bila kusahau mkono tasbihi ya rangi ya kijani anaichezesha chezesha laiti ungefanikiwa kumuona ungedhania ni Shekhe wa Mkoa fulani mwenye unyenyekevu na utiifu mkubwa kwa mola wake.
Lakini kabla hajatoka nyumbani kwake kuelekea uwanja wa ndege tayari machale yalishamcheza kusafiri na ndege ya moja kwa moja mpaka nchini Afrika ya kusini. Hasa kutokana na tukio la kuuliwa kwa mama yake mzazi na kukatwa kichwa kisha akatumiwa kichwa hicho, zilikuwa ni salamu kwake kuwa anapambana na genge kubwa la waharifu ambao wana ujuzi na maarifa makubwa.
Hivyo akabadili mawazo ya kwenda Afrika ya kusini na ndege ya shirika la Afrika ya kusini badala yake akakata shauri ya kwenda Msumbiji kwa njia ya barabara kupitia Mtwara kwa ndege ya ATCL. Akaingia kwenye mtandao wa ATCL kupitia kwenye simu yake ya kiganjani, akatoa oda ya tiketi ya Mtwara ya asubuhi akapata na akailipia tiketi ya saa 5:00 asubuhi kwa njia ya pesa mtandao.
Hivyo akawapiga chenga ya mwili maadui zake waliokuwa wanamsuburia kwa hamu wampokee kwa kumteka kwenye Uwanja wa ndege wa Oliver Tambo, Jijini Johanesburg. Akiwa angani akawa anapanga na kupangua namna atakavyoingia katika jimbo la Cabo-Delgado bila kujulikana na maadui zake, huku tukio la kuchinjwa kwa mama yake mzazi akiwa ameshalizika kwenye kaburi la sahau.
Ilikuwa ni safari ya dakika 45 tu kutoka Dar es Salaam mpaka uwanja wa ndege wa Mtwara. Aliposhuka akafanya haraka kutoka nje ya uwanja hakuwa na muda wa kupoteza, nje ya uwanja akakutana na kundi kubwa la madereva taksi wanaogombania wateja. Akaichomoa miwani yake yenye vioo vya giza toka kwenye koti lake, akaifuta miwani hiyo kwa kitambaa laini akaivaa kuzidi kuficha wajihi wake.
Huku akiwa anaburuza begi lake la matairi akaenda kwa mmoja wapo wa wale madereva aliyekuwa amejitenga na wenzake hana papara na wateja. "Salamu Aleikum Ustaadhi, sema nikupeleke wapi bei zangu poa tu hatuwezi kushindwana" aliongea kistaarabu yule dereva huku tayari ameshafungua buti la gari lake kujiandaa kupakiza begi. Akamuambia ampeleke kwenye nyumba ya wageni ambayo ina utulivu mkubwa, haina fujo fujo na haipo mbali sana na kituo cha mabasi.
"Nitakupeleka "Lole Grand Lodge" iliyopo mtaa wa Chikongola utafurahi na roho yako" alisema huku tayari ameshapakiza begi lile kwenye buti na kulifunga. Msafara ukaanza kuelekea kwenye nyumba hiyo ya wageni huku akiwa amekaa siti ya nyuma. Macho yake alikuwa anayatupa, kuangaza huku na kule kupitia kioo cha madirishani ili mradi kuchunga usalama wake wake.
Hakutaka kuanza kupoteza mpambano mbele ya adui zake hata kabla bado mechi haijaanza Mjini Cabo-Delgado. Ndani ya robo saa tu wakawa wameshawasili katika Nyumba hiyo ya wageni. Akamalizana nae malipo yake kisha akatoa begi lake na kutokomea ndani ya jengo hilo.
Bahati nzuri akapata chumba bila shida yoyote. Alivyolipia chumba chake tu, akaanza kunusanusa kama mbwa wa polisi, kuikagua nyumba nzima kujiridhisha usalama. Akagundua kuwa kumefungwa mfumo wa CCTV-Kamera unaorekodi matukio yote hapo "Lodge".
Akatabasamu kisha akaingia chumbani kwake kuweka begi lake na kuweka vitu sawa chumbani kwake. Nako akajipa kama dakika 10 za kukikagua usalama wa chumba, akihofia asije akawa amejiingiza kwenye mdomo wa mamba bila mwenyewe kutanabahi akaja kulia kilio cha kusaga na meno.
Baada ya kujiridhisha, akakifunga chumba kisha akatoka kuelekea kwenye mgahawa mdogo wa hapo hapo alipofikia. Maana njaa ilikuwa inamkwangua vilivyo tumboni utasema ana ugomvi na minyoo ya kwenye utumbo. Alijiwahi mapema kula kabla kasheshe halijanza maana Kachero Manu akiwa na jambo linalomshughulisha hakumbuki kula mpaka atulizane.
Akamuita mhudumu mgahawa akasalimiana nae, kisha akaomba karatasi ya MENU yenye orodha ya vyakula mbalimbali vinavyopikwa hapo mgahawani. Akaipitia haraharaka kisha akataka kuagiza, Ugali kwa samaki samsuli rosti.
"Inachukua muda gani kuandaliwa chakula ninachokitaka"? aliuliza huku akiwa amemkazia macho mhudumu kwa umakini.
Akajibiwa na mhudumu wa upande wa vyakula, "oda yoyote unayotoa ni ndani ya dakika ishirini hadi nusu saa kutegemeana na aina ya chakula unachohitaji". "Basi naomba Ugali kwa samsuli rosti, usiweke chumvi nyingi tafadhali " alisema Kachero Manu kumwambia mhudumu yule.
"Hamna shida, mteja ni mfalme kwetu, je utapenda kinywaji gani nikuletee pia" aliuliza mhudumu yule." "Nitahitaji juisi ya matunda halisi lakini baada ya kumaliza mlo wangu nitakuambia nahitaji juisi ya kitu gani" alijibu kimkato bila kustawisha maneno.
Ndugu msomaji samaki samsuli kama humjui ndio yule alikuwepo kwenye picha ya senti tano ya enzi za Nyerere, ni samaki mwenye mnofu wakati mwingine anaitwa ng'ombe wa baharini unaweza hata kumpikia pilau. Baada ya dakika ishirini na tano kupita, kilihudhurishwa chakula chake mezani.
Akaanza kukishambulia kwa pupa mithili ya mtu aliye kwenye mashindano ya kula au mkimbizi wa Somalia aliyekosa chakula kwa muda wa wiki nzima. Aliupiga mlo huo bila kusaza mabaki yoyote, sahani nyeupe kabisa utasema imetoka kuoshwa.
Alipomaliza akaagiza juisi ya ndimu yenye sukari chache sana kwa ajili ya kushushia mlo. Akanywa, na mara baada ya kumaliza akaletewa bili yake akailipia na kisha moja kwa moja akaenda kulala tayari kwa kujiandaa na safari ya kuondoka usiku kwa usiku kuelekea Msumbiji.

Usiku wa heka heka
Kachero Manu aliamka saa kumi na moja jioni baada ya mapumziko mafupi aliyoyafanya. Alijikuta amelala kwa muda wa masaa manne mfululizo bila hata kushtuka usingizini, dalili ya kuonyesha amechoka sana.
Akafanya mazoezi ya kunyoosha viungo ya muda wa robo saa kisha akaelekea maliwato moja kwa moja akajimwagia maji ya baridi. Alipomaliza akaanza kujiandaa na safari, wakati wa kuvaa nguo ndani akavaa fulana aina ya "ballistic vest" yenye uwezo wa kuzuia risasi kupenya.
Kisha akachagua kuvaa nusu kanzu yake nyeusi mtindo wa Pajama toka Pakistani ili imuwezeshe kupambana kirahisi hasa katika mitindo ya urushaji wa mateke itakapobidi kupambana, pia rangi nyeusi inakufanya usionekane kirahisi hasa kwenye giza hivyo kumpa wakati mgumu adui yako kukutambua.
Chini akavalia viatu vya 'kung-fu' ili kuepusha sauti wakati wa kutembea. Akakagua vifaa vyake vyote muhimu kama vipo salama ikiwemo kalamu maalumu ya kipelelezi 'spy pen' yenye uwezo wa kuchukua video kwa muda wa nusu saa, kupiga picha na kurekodi sauti mpaka umbali wa meta 50.
Bila kuwasahau rafiki zake muhimu sana anaowatumia inapobidi kuondosha roho ya mtu duniani, bastola zake mbili za kisasa aina ya Glock G42 zilizotengenezwa na kampuni toka Australia.
Alipomaliza ukaguzi wake na kujiridhisha kuwa kila kitu kipo katika mustawa sahihi akalifunga vizuri begi lake. Akachomoa pochi lake la kuhifadhia pesa na vitambulisho nalo akalifanyia uhakiki wa haraka haraka. Akakuta kadi zake mbili za benki za Msumbiji kadi moja ya benki ya United Bank of Africa (UBA) na ingine ni ya benki ya Barclays zote zikiwa zimejazwa mkwanja wa kutosha wa kumuwezesha kuishi nchini Msumbiji hata mwaka mzima kama itabidi.
Akasifu kimoyomoyo kazi nzuri ya Sekretari wa ofisini kwao mrembo Kokunawa, kwa kuratibu safari yake kwa viwango kabisa. Ilipofika majira ya usiku mbichi wa saa moja, aliufungua mlango wa kwenye chumba chake kwa tahadhari kubwa, huku macho yake akiyageuza kama kinyonga. Bahati nzuri hakuonwa na mtu yoyote wakati anaufungua mlango. Kabla hajaanza kutembea kwenye veranda ya kuelekea mapokezi, akiwa amesimama pale pale mlangoni pake akiutoa mkono wake nje ya mlango na sehemu ya kichwa chake, akachomoa kifaa chake chenye ukubwa wa kalamu ya kuandikia kinaitwa kitaalamu "Laiser pointer" cha rangi nyeusi akakielekeza kifaa hicho usawa wa Kamera ya CCTV iliyopo juu ya mlango wa kuingilia mapokezi.
Alivyoelekeza kile kifaa hapo hapo CCTV-Kamera ikaacha kurekodi matukio yote kutokana na kuunguzwa na miale ya kifaa chake kile. Uso wake ukavaa tabasamu la ushindi, akakirudisha mfukoni kile kifaa, kisha akatoka nje ya mlango. Akaurudishia mlango aste aste bila kuufunga na funguo kuepusha kelele za funguo kusikika. kisha akachomoa kitambaa chake cha kujifutia jasho akafuta alama za vidole kwenye kitasa cha mlango.
Hakutaka kudharau nguvu ya adui yake hata kidogo, hivyo alichukua umakini mkubwa kwenye kila hatua tokea mwanzo. Akatembea na veranda kinyume na ofisi ya mapokezi akajikuta ametokeza kwenye mlango wa nyuma unaotenganisha vyumba na bustani ya upande wa nje. Kwa bahati mlango ulikuwa umerudishiwa tu, akaufungua na kutembea kama umbali wa meta 10, juu ya kibaraza cha vitofali vilivyolazwa juu ya ardhi 'pavement blocks', akarusha begi lake nje ya ukuta kwanza. Kisha bila kufanya ajizi akajikunja na kuruka ukuta wa kutokea nje kama samaki mkizi. Ukuta ambao ulikuwa na urefu wa zaidi ya meta 7 na juu yake kuna nyaya za umeme maalumu kwa ajili ya kudhibiti wezi.
Akatokemea zake kichochoroni kwenye giza, nia na madhumuni yakiwa ni kuelekea Stendi Kuu ya Mabasi ya Mkoa. Akafanikiwa kupenyapenya kwa kuhangaika bila kumuuliza mtu mpaka akatokeza Stendi Kuu, akashukuru Mwenyezi Mungu.
Stendi Kuu ya Mtwara Mjini, ni Stendi ambayo ina mzunguko wa watu wengi kipindi cha kuanzia majira ya jogoo la kwanza mpaka kufikia magharibi, baada ya hapo kunakuwa na watu wachache tu wenye kujipatia bidhaa za majumbani katika maduka yaliyozunguka stendi hiyo lakini hamna wasafiri. Kachero Manu alivyofika Stendi hapo, kwa usiku ule hakukuwa na Basi dogo la kuelekea Wilaya ya Masasi ambapo anahitaji kwenda.
Lengo lilikuwa afike kwanza Masasi kisha hapo atapanda tena usafiri wa kwenda Wilaya mpya ya Nanyumbu akavizie usafiri wa kuelekea nchini Msumbiji. Akaanza kubuzibuzi maeneo ya hapo hapo Stendi huku akiweka matumaini huenda ukajitokeza usafiri wa ghafla bin vuu, na kama ikishindikana hana budi atasubiria mpaka alfajiri apande Basi dogo.
Mungu si Athumani bwana, kwa bahati nzuri katika kuhangaika kwake kupata usafiri, likaja gari dogo aina ya "Toyota Pick-up" limezungushiwa turubai kwa nyuma, lilikuwa ni gari la idara ya Halmashauri, Wilaya mpya ya Nanyumbu. Gari hilo lilimpeleka Afisa Elimu Wilaya Mjini Mtwara, alikuwa anasafiri kesho yake na ndege ya saa kumi na mbili asubuhi kutokea Mtwara kwenda Dar es Salaam. Dereva huyo alijiongeza, akaamua apate vichwa viwili vitatu wakati anarejea Nanyumbu ili kupunguza ukali wa maisha.
Wenyewe watumishi wa umma wana msemo wao wa kuonyesha kuwa maisha ni magumu kuwa vyuma vimebana hivyo inabidi vilainishwe. Sheria ilikuwa inamkataza kabisa dereva wa gari la serikali kumpakiza mtu asiye mtumishi ndani ya gari la serikali, ila tamaa ya kipato cha ziada ndio ilikuwa inamilikiwa avunje sheria. Walikuwa ni abiria wawili tu usiku huo wenye nia ya kufika Nanyumbu, nao ni yeye Kachero Manu na msichana mmoja mbichi.
Katika maongezi yao na Kachero Manu wakati wanaanza safari alijitambulisha kuwa ni Mwalimu mpya, bobezi wa somo la "Sayansi-kimu" wa shule ya msingi anaenda kuripoti kituo kipya cha kazi akitokea Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Dodoma.
Umbali kutoka Mtwara Mjini mpaka kufika Nanyumbu ni kama kilometa 282 kwa mwendo wa wastani. Kachero Manu aliamua kuingia Cabo-Delgado Kininja kwa kutumia njia ya barabara kupitia daraja jipya linalounganisha Msumbiji na Tanzania.
Pia ipo njia ya rahisi zaidi ya kuingia Msumbiji kupitia kivuko cha kijiji cha Kilambo kilichopo kilometa 40 kutoka Mtwara mjini, ila kipindi cha masika hasa cha mwezi Februari sio nzuri sana kutumia njia hiyo kwa sababu mto unajaa maji sana, na ni rahisi kupata ajali ya kivuko. Hivyo kwa kuufanyia kazi msemo wa kimombo unaosema "Short cut wrong cut", au waswahili tuna msemo wetu "rahisi aghali", Kachero Manu akaamua atumie njia ya daraja la Mtambaswala ili afike safari yake salama.
Akafanya maamuzi ya bora azunguke njia ndefu lakini awe na uhakika wa usalama wa safari yake. Lile gari likaondoka Mtwara Mjini usiku ule wa saa mbili na dakika kumi, huku Kachero Manu akipiga mahesabu yake kwa mwendo wa kawaida wa mwendokasi wa 80-120 km/hr akakadiria wataingia Mangaka, Makao Makuu ya Wilaya ya Nanyumbu muda wa saa sita usiku.
Gari lilikuwa linaendeshwa kwa kasi na barabarani hakukuwa na askari wa barabarani wale wenye vitochi vya kudhibiti mwendokasi wa gari kama mwenge wa uhuru. Ilipofika muda wa saa 5:15 usiku ikiwa imebaki kama kilometa 15 kufika mwisho wa safari, Kachero Manu hakutaka kupoteza muda alimshukuru Mungu kwake yeye alijiona ameshafika tayari.
Bila kupoteza muda akamuangalia yule mwalimu mwanamke abiria mwenzake gwiji wa "Sayansi-kimu" alikuwa yupo hoi, amezidiwa usingizi wa samaki pono anayumba kushoto na kulia kama mwali anayenema. Akatumia mwanya huo vizuri kwa kutelemka pole pole kutoka kwenye gari bila kishindo. Akashika mlango wa nyuma ya "pick-up" akateremka taratibu mithili ya mjusi anayeogopa kubanwa na mlango akatokomea kwenye kichaka pembezoni mwa barabara.
Akaanza kuambaa ambaa pembezoni mwa barabara huku akijiandaa kujificha kwenye kichaka iwapo itatokea gari au pikipiki barabarani itakayomulika mwanga. Baada ya mwendo kama wa saa moja wa kutembea na miguu akawa ameshafika Mangaka Mjini muda kama saa 7:20 usiku.
Kwa bahati mbaya muda ulikuwa umeyoyoma sana, watu wengi wapo majumbani kwao wamelala. Katika zunguka zunguka yake mitaani, akakutana na kijiwe kimoja cha madereva bodaboda na kabakia bodaboda mmoja tu kavalia barakashia ya kiislamu huku ameliinamia pikipiki lake.
Bodaboda wana tabia ya kuogopa abiria hasa nyakati za usiku hii ni kutokana na uporwaji wa pikipiki zao na hata kuuliwa, lakini Kachero Manu mavazi yake ya kiislamu yalimbeba aonekane ni mwema akatanguliwa kusalimiwa na dereva bodaboda yule "Assalamu Alekum" ustaadh..". Kachero Manu akajibu "Waleikum salaam kijana", haraka haraka dereva bodaboda akadakia kumuuliza "vipi unaelekea kwenye sherehe ya Maulidi ya wilaya? hii ilitokana na mavazi ya Kiislamu aliyotinga usiku ule.
Kachero Manu akatabasamu kuwa mbinu yake ya kuvaa uhusika usio wake umeanza kufanikiwa mpaka sasa anaitwa Ustaadhi. "Hapana, mie nataka nielekee "Cabo-Delgado" sijajua usafiri unakuaje hapa wa kufika huko?" alisema huku analikumbatia vizuri begi lake. Akajibiwa na bodaboda, kwamba usafiri unaanza saa nne asubuhi, ila sasa inapata wiki magari hayaendi Cabo-Delgado kutokana na machafuko yanayoendelea huko.
"Kabla ya machafuko kulikuwa kuna daladala nne zinatoka huku kwenda Cabo-Delgado na mbili zinarudi, ni daladala za Kibopa mmoja wa Mtwara mjini anaitwa "Panchoo Jalaby" ila leo una bahati sana ustaadhi wangu inaelekea wewe kweli ni mtu wa Allah sana, kuna madrasa imetoka Wilaya ya Montepuez, Cabo-Delgado imealikwa na kwa kawaida huwa wanaondoka saa 9 za usiku safari zao, nakushauri uwahi kwenda ukaongee na dereva mapema hivi sasa akufanyie mpango" alisema kwa kirefu muendesha pikipiki yule huku akiwa tayari ameshalitia moto pikipiki lake analiungurumisha.
Dereva huyo aliyekuwa anayedadavuliwa na muendesha bodaboda, asili yake ni Tanzania, lakini alikuwa ana zaidi ya miaka 30 yupo Msumbiji na amepata uraia huko huko Msumbiji. Alikuwa ni maarufu sana huyu Mzee, anajulikana Mangaka nzima na vitongoji vyake. Bila kuchelewesha muda Kachero Manu akamlipa bodaboda Sh.1,500/= ili amfikishe nje ya msikiti mkuu wa Mangaka ambapo hayo maulidi yalikuwa yanafanyikia hapo.
Alipofikishwa wakaagana na bodaboda akawa anaangaza angaza kutafuta gari kubwa aliloelekezwa linalotoka Montepuez, hakuliona gari lolote zaidi ya kuona magari madogo madogo, pikipiki na baisikeli za waumini waliokuja maulidini. Akashikwa na taharuki kuwa huenda kadanganywa na yule bodaboda ili labda apate tu pesa za kumsafirisha hadi hapo Maulidini. Akasimama na begi lake pembeni anaushangaa umati mkubwa wa waislamu wale wanaimba kaswida na kuyumbayumba kwa furaha mipigo ya ngoma za dufu wakiwa wapo umbali wa meta kama 20 kutoka pale aliposhushwa na dereva bodaboda. Akaamua kuegemea kwenye mti wa Msonobari wa jirani akiwa ametulizana kama kobe anayetunga sheria, akitafakari kitu cha kufanya.
Ghafla bin vuu akiwa hana hili wala lile, akasikia muungurumo wa lori aina la Isuzu linakaribia eneo la shughuli linajongea pembeni ya Msonobari ule ule alioegemea. Dereva alipofika sehemu aliyoikusudia kuegesha gari lake, akazima gari kisha haraka haraka akashuka chini ya gari. Akasogea pembeni kidogo ya gari lake yule dereva, akaingiza mkono mfukoni akachomoa paketi ya sigara rangi ya dhahabu. Kachero Manu kwa mbali akafanikiwa kusoma maandishi ya paketi hiyo kwa kutumia mwangaza hafifu wa taa ya Mungu, mbalamwezi chapa ya juu ya maandishi meusi yaliyokolezwa jina la "Kingdom".
Hizi ni sigara kutoka nchini Afrika ya kusini zinazopatikana kwa wingi nchini Msumbiji. Kachero akawa anajipanga namna ya kumvaa dereva akaanza kutafakari. "Inaonyesha hili gari baada ya kuwashusha wanafunzi wa Madrasa kuna sehemu ilikwenda sasa ndio inarudi tayari kuwachukua kwa safari".
Dereva alipovuta mikupuo mitatu ya sigara na kutoa moshi angani, Kachero Manu bila kupoteza muda akamkabili dereva uso kwa uso kujaribu bahati yake kuomba nafasi ya kusafiri kwenye gari. "Salamu aleikum, natumaini wewe ndio dereva wa hili gari eeh?" alisalimia na kutupa swali kabisa. "Bila ya shaka Ustaadh wangu, hujakosea sijui nikusaidie nini?" akajibu dereva huku aliweka sigara yake pembeni kumsikiliza Kachero Manu. Bila kujivunga Kachero Manu akakohoa kidogo ili kulisafisha koo lake ili sauti itoke vizuri kisha akaanza kujieleza.
"Nina shida ya kwenda Cabo-Delgado kikazi, sasa usafiri ni shida sana wiki nzima nipo hapa ninatangatanga hamna usafiri wowote, sasa nimeelekezwa wewe unaelekea Cabo-Delgado hivyo naomba unisaidie kama kuna uwezekano huo tafadhali...!", alidanganya uwongo mtakatifu uliopangika ukajipanga vizuri.
Uwongo ambao hata mbele ya Jalali unakubalika kwa ajili ya manufaa ya safari hiyo kwa nchi ya Tanzania. Akajibu yule dereva kwa ufupi, "huogopi mauaji yanayoendelea huko? Watanzania wenzako wanatoroka wewe ndio unajipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa mamba?". "Kutokana na kazi zangu za utafiti wa mambo ya kale inanibidi tu maana naskia mbali ya machafuko haya ya kibaguzi kwa Watanzania pia kuna kikundi cha kigaidi hapo Cabo-Delgado hofu yetu ni kuwa magaidi wasije wakalipua majengo ya kale kama walivyofanya wale magaidi wa kule Timbuktu, nchini Mali, tukakosa kuandika historia sahihi kwa vizazi vijavyo", aliongea Kachero Manu kwa msisitizo mkubwa akijifanya ana uzalendo na kazi yake, kumbe ni jasusi wa Kimataifa.
"Sawa mimi nitakusaidia kukupa msaada wa usafiri kwenye hili lori lililobeba wanafunzi wa madrasa, ila uwe makini sana maana Watanzania Cabo-Delgado hawapo salama, mimi mwenyewe napata staha kwa sababu nimeishi Msumbiji zaidi ya miaka 30 na nimeolea Msumbiji lakini bado naonekana kama kidudu mtu. Heshima tuliyokuwa tunaipata Watanzania wakati wa utawala wa awamu ya kwanza wa Samora Machel ni mbingu na ardhi ukilinganisha na sasa. Wanawabagua Watanzania lakini tayari wameanza kubaguana wenyewe kwa misingi ya makabila, ukanda na dini ndio unakuta vikundi vya kigaidi vimeanza kuibuka" aliongea dereva wa Lori lile la Madrasa.
Bila kupoteza muda Kachero Manu akatumia fursa ya muda mchache uliobaki kabla ya safari kuanza kumdadisi dereva yule mambo mawili matatu yanayoendelea Jimboni Cabo-Delgado. Dereva yule aliyeonyesha fika kutopendezwa kabisa na mambo yanayoendelea nchini Msumbiji hivyo akawa anafunguka vilivyo mambo mbalimbali.
"Sasa kwanini watoto wadogo mnawapandisha kwenye lori gari ambalo sio rasmi kwa abiria, ina maana Cabo-Delgado yote hamna Mabasi na Daladala kubwa"? alitupa swali la taftishi. Dereva yule kabla hajajibu, alimuangalia Kachero Manu kwa umakini kisha akapiga pafu la mwisho la sigara yake akaupumulia moshi wake angani, kisha akakitupa chini kipisi na kuisaga kwa kisigino cha soli ya kiatu chake.
Kisha akamsogelea kwa ukaribu akaanza kumuelezea kwa kunong'ona, "ndugu yangu hii ni mipango tu ya kimaisha hapa hamna sherehe ya dini kikweli, bali kuna uharamia mkubwa unaendeshwa. Hapa haipiti miezi 3 utaskia kuna sherehe ya kidini inafanyikia Nanyumbu, lakini kinachofanyika hizi sherehe zinafadhiliwa na tajiri mmoja tena Mkristo anaishi Cabo-Delgado, inasemekana huyo anajishughulisha na biashara haramu nyingi tu hasa za mipakani, hata haya machafuko dhidi ya Watanzania inasemekana ndio anafadhili.
Ukikodiwa kuwaleta wanafunzi, basi mtapakia mzigo wa magendo kwenda Tanzania na mnaporudi Cabo-Delgado mtapakia mzigo wa haramu kama meno ya tembo au madini. Madini yanayoibiwa huko Mererani, Jijini Arusha yanatoroshwa kwenda kuuzwa nchini Afrika ya kusini. Hivyo kwenye lori inapangwa mizigo chini kisha baada ya hapo inatandikwa mikeka ya wanafunzi kukakaa chini, ndio maana hawapendi kukodi Mabasi..!". "
Anaitwa nani huyo tajiri? alidodosa kachero Manu swali fupi ambalo alihisi litamfungulia wepesi wa kuanzia upelelezi wake akiwa Jimboni Cabo-Delgado. Dereva kabla ya kujibu akaangalia kulia na kushoto kama mtu anayesikiliza maongezi yao, akionyesha ana hofu moyoni mwake kumtaja huyo kigogo.
Kisha akavuta pumzi kwa nguvu akijianda kulitamka jina la huyo tajiri. "Anaitwa "ALF.....! " kabla dereva hajamalizia kutamka jina hilo kikamilifu akaskia anaitwa jina lake.
NANI HUYO ANAMUITA JINA DEREVA ANAPOJIANDAA KUMTAJA KIONGOZI WA MAFIOSO WA CABO-DELGADO?
ENDELEA KUFUATILIA



Anaitwa nani huyo tajiri? alidodosa kachero Manu swali fupi ambalo alihisi litamfungulia wepesi wa kuanzia upelelezi wake akiwa Jimboni Cabo-Delgado. Dereva kabla ya kujibu akaangalia kulia na kushoto kama mtu anayesikiliza maongezi yao, akionyesha ana hofu moyoni mwake kumtaja huyo kigogo.
Kisha akavuta pumzi kwa nguvu akijianda kulitamka jina la huyo tajiri. "Anaitwa "ALF.....! " kabla dereva hajamalizia kutamka jina hilo kikamilifu akaskia anaitwa jina lake.
"Mzee Masebbo eeeh.... muda unayoyoma huu, tutafika asubuhi sana iwe msala kwetu kwa waliokodisha gari oooh...!" ilikuwa ni sauti ya taniboi wake akimpa msisitizo waondoke haraka kuelekea Jimboni Cabo-Delgado. Dereva yule akakurupuka kama vile amemuona simba kichakani, akamwambia kachero Manu.
"Twenzetu safari imeiva tutaongea zaidi Cabo-Delgado. Nitafute rafiki yangu naishi mtaa wa Ruvuma nyumba namba 23B, haya twende maana wenyewe wanataka saa 12:00 asubuhi uwe umeshafika". Kachero Manu akaitikia kwa vitendo kwa kubeba begi lake mkononi na kumfuata dereva nyuma nyuma wakielekea kupanda Lori lile tayari kwa safari.


SURA YA TANO
Safari ya kuelekea Cabo-Delgado ilianza kama saa 9:15 usiku kutoka pale uwanja wa sherehe ya maulidi.
Kachero Manu alikuwa amepanda nyuma ya lori akijichanganya pamoja na wanafunzi wa madrasa pamoja na Maustaadhi na Taniboi wa gari.
Safari ilipoanza tu ndani ya muda mfupi tu, Kachero Manu akagundua kitu toka kwa yule Taniboi wa dereva Masebbo, alikuwa anamuangalia sana kwa jicho pembe la kuibia. Ingawa kulikuwa na mwangaza hafifu wa mbalamwezi angani, Kachero Manu alitambua kuwa sio mtu mzuri kwake.
Akajifanya kama hamuoni, anasinzia huku anajaribu kupasua kitobo kwenye mikeka waliyokalia watoto wa madrasa kwa kutumia mkasi wake mdogo aliouchomoa mfukoni mwake. Lengo alitaka ajihakikishie kama kweli kuna mzigo wa meno ya tembo umebebwa na hilo lori kama alivyodokezewa na mzee Masebbo.
Lakini hakufanikiwa kuona kitu baada ya kutoboa mkeka. Meno yale yalipangwa kwa ustadi mkubwa kisha yakazuiwa na mbao ngumu zilizopangwa na juu ya mbao ndio ikawekwa mikeka ya kukalia wanafunzi wa madrasa, hivyo kila alipokuwa akipitisha mkasi ukawa unagota kwenye mbao.
"Inaonyesha hili gari halikuwepo hapo kwenye sherehe ndio lilienda kupakia mzigo", aliwaza Kachero Manu akiwa tayari ameshaurudisha mkasi mfukoni. Akapotezea huo mpango wake na kuamua kujiegemeza kwenye begi lake akiutafuta usingizi.
Alimuona Mzee Masebbo ni kama malaika msaidizi ambaye ametumwa kumrahisishia kazi yake katika namna asiyoitarajia. Akashukuru kwa hatua aliyofikia, hasa ya kumtambua tajiri wa kuvusha biashara haramu, jina lake linaanza na herufi tatu “ALF”.
Akajijengea mawazo chanya huenda huyu ndio kiini cha machafuko yote. "Kwanini machafuko yameanza kwa Watanzania, Wafanyabiashara wa madini!" ndio swali lililokuwa linamsumbua kichwani mwake. Wafanyabiashara ambao biashara zao zinaendana na huyu tajiri “ALF”. "Je anawaogopa Watanzania wanahatarisha biashara zake?" aliendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu ya papo kwa hapo.
Alikuja kushtuka yupo kwenye dimbwi hili la mawazo wapo juu ya daraja jipya linalounganisha Tanzania na Msumbiji. Ni daraja lenye urefu wa meta 720, limejengwa kusini mwa Tanzania eneo la Mtambaswala wilaya ya Nanyumbu kuelekea upande wa Kaskazini wa Msumbiji wa jimbo la Gabo-Delgado.
Akawa anahesabu nguzo za daraja ambalo lina nguzo 18, akapata nguzo 9 zipo upande wa Tanzania na 9 zingine zilizobaki ni nguzo za upande wa Msumbiji. Akatabasamu kwa sababu alisoma kwenye moja ya kabrasha kuwa ujenzi wa daraja hilo la la Umoja la kuvukia mto Ruvuma ni matokeo ya wazo lililotolewa na Marais waasisi wa nchi mbili ambao ni Hayati Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Samora Machel wa Msumbiji mwaka 1975.
Marais hao walikuwa na lengo la kuunganisha nchi za Tanzania na Msumbiji kupitia mikoa ya Mtwara upande wa Tanzania na Gabo Delgado upande wa Msumbiji. Kachero Manu akatamani mawazoni mwake kuwa Nyerere na Samora wangekuwepo hai leo waone ndoto yao ya kuunganisha nchi zao ilivyotekelezwa na warithi wao.
Lakini wangekuwa hai pia wangepatwa na kihoro kutokana na mpasuko uliopo baina ya wananchi wa nchi zao mbili kinyume na matarajio yao. Marais hao walitaka wananchi hao wawe wamoja kama ndugu mpaka kupelekea kupatikana kwa Umoja wa Afrika.
Usingizi ukaanza kumnyemelea mpaka akaanza kuwa nusu amelala nusu yupo macho, ghafla bin vuu akashtuka usingizini kwa kuona dereva mzee Masebbo anapangua gia kudhihirisha kuwa anapunguza mchepuo wa wa gari. Akakaa vizuri kisha akajituliza na kuchungulia kwenye ncha ya turubai inayounganisha kwenye vyuma vya lori ili ajue sababu ya kupunguza mwendo.
Akashuhudia kwa mbali kuna askari takribani 6 mpaka 7 ambao wamening'iniza bunduki mabegani mwao. Gari likasota pole pole mpaka likasimama. Kachero Manu akajua tayari kimenuka mambo hamkani sio shwari tena, akajipa subira kuona mwisho wake.
Liliposimama tu askari mmoja akasogelea mpaka usawa wa mlango wa dereva huku wengine wakibaki kwa nyuma yake usawa kama wa mita 5, kisha kwa sauti kubwa yule askari akamsalimia dereva kwa kireno.
"Como você esta"( habari yako), dereva Mzee Masebbo akajibu "eu estou bem"(nipo vizuri) , "De onde você esta vindo?" (mnatokea wapi?), "A partir de Nanyumbu, Tanzania" (Tunatokea Tanzânia), "Todos os cidadãos? "(wote ni raia wa Msumbiji?) , akajibu Mzee Masebbo "sim"(ndio) lengo la yule askari alikuwa anataka kufahamu huyu dereva anajua kireno.
Kama angeshindwa kujibu tu kimbembe kingeanza hapo, baada ya kujiridhisha na majibu akaanza kuzunguka gari kuanzia mbele mpaka nyuma. Kipindi hicho dereva Masebbo anahojiwa, tayari yule Taniboi ameshashuka zamani chini ya gari anaongea na baadhi ya askari wale kirafiki.
Kisha askari mmoja wapo mwenye umbo la miraba minne mithili ya mchezaji wa mpira wa kikapu wa ligi ya NBA-Marekani, katika wale aliokuwa anaongea nao Taniboi ghafla akachomoka na kurukia kwa nyuma kwenye lile lori.
Kachero Manu akajikausha bila kutikisika huku akijiweka tayari kwa lolote litakalotokea. Hakusema chochote yule askari ndani ya umati ule wa watu huku akiwa amewasha tochi yake kali anamulika kama vile kuna kitu anakitafuta. Akazidi kusogea kwa ukaribu mpaka akafika pale alipokaa Kachero Manu, kisha akasimama mbele yake kabisa.
Kachero Manu alijiinamia chini uso wake huku akisali kila aina ya dua apate kukiepuka kikombe cha kukamatwa na maadui zake kabla hata hajawasili uwanja wa vita, Jimboni Cabo-Delgado. Ghafla askari yule akamkwida Kachero Manu kwenye nusu kanzu yake aliyovaa juu na kumnyanyua juu kwa nguvu.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog