Simulizi : Huba La Miss Tanzania
Sehemu Ya : Nne (4)
Mchakamchaka chinja la mgambo limelia, asiye na mwana aeleke jiwe, hoi hoi, shamrashamra, vifijo na nderemo vilitawala nyumbani kwa bwana na bibi Shamsi Sakuzindwa aliyekuwa anaozesha binti yake mpendwa mwenye kupendeza kama lilivyo tamu jina lake, Zabibu.
Ilikuwa ni siku ya hitimisho la uchumba wao wa zaidi ya miaka mitatu mfululizo wa kijana Shebby na Zabibu. Vijana ambao penzi lao lilikuwa mithili ya mapacha au kumbikumbi wanaoambatana pamoja kila wakati kwenye kila kiunga cha jiji la Dar es Salaam. Kijiji kizima cha Mzundu kilichopo wilayani Handeni, mkoani Tanga, siku kilikuwa kimepiga kambi nyumbani hapo karibia juma zima kuhakikisha ndoa hiyo inapita kwa amani na usalama. Walikuja kuwapongeza wawili hao kwa kuonyesha mfano halisi wa ujasiri wenye busara wa kufunga ndoa na kuishi kama mke na mume na si mahawara kwenye uchumba sugu kama ilivyo kwa vijana wengi ambao wanaiogopa ndoa kama ukoma.
Kama ujuavyo, ndoa si kitu cha mchezo mchezo kwa kuwa ni kutimiza amri ya Mwenyezi Mungu na kudhihirisha kukua kiakili na kimwili pia. Usiku wake kulikuwa na mkesha wa ngoma za jadi za kabila lao la Wazigua, ngoma za Mkweso na Machindi zilizovurumishwa mpaka liamba zikiburudisha wageni waalikwa. Asubuhi yake sherehe ya kitamaduni ikatamatishwa, ikawa sasa ni sherehe rasmi ya ndoa ya kiislamu ikihitimisha sherehe nzima za juma lote. Dufu, ngoma maarufu katika hafla za kiislamu zikawa zinapigwa na kuchezwa kwa mitikisiko yenye kuvutia katika masikio na macho ya mtazamaji toka kwa vijana wa madrasa ya hapo hapo kijijini Mzundu. Sauti za kuvutia za nyimbo za kaswida zinazoimbwa kwa lafudhi ya lugha ya kiarabu na kiswahili zilisikika. Sauti ambazo zilikuwa zikiambatana na milio ya nai na zumari huku midundo ya dufu za aina mbalimbali kama ogani, namba wani, besi, kibakubaku na nyinginezo nyingi zikawa zinadundwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Siku hiyo mashamushamu yake yalikuwa sio ya kawaida, hata ndege angani na wanyama porini nadhani nao walipashika habari ya sherehe hiyo kuwa Zabibu kapata mchumba sasa anaolewa, kutokana na hekaheka na pilikapilika zilizoambatana na furaha sheshe ya wanakijiji hao. Waoaji walikuwa wanatokea jijini Dar es Salaam, na tayari walikuwa wameshawasili katika viunga vya kijiji hicho wanavinjari na motakaa zao za gharama tayari kumnyakua mwali, fujo zao tu kila mtu alijua, majogoo ya mjini hayooo yamekuja kuwika kijijini.
Walikuwa wamekuja na sanduku zima la vihendo maalumu kwa ajili ya bibi harusi, na familia yake, kama nguo, seti za mapambo ya dhahabu, viatu na vikorokoro vingi tu vya kuchombeza shughuli hiyo ili mradi ifane vile inavyopaswa kutokana na hadhi ya mrembo Zabibu. Bila kusahau moja ya bidhaa za mahari ya kimila walizoagizwa kuja nazo siku ya harusi kama tundu la mwigazi, ambaye ni kuku mtetea na vifaranga vyake saba, blanketi na mkongojo wa babu.
Mama mzaa chema hakuwa nyuma katika tafrija hiyo, furaha yake ilikuwa fokofoko akijifunga kibwebwe kiunoni kusakata burudani mbalimbali zilizokuwa zimeipamba siku hiyo adhimu kwa familia yao. Ndugu, jamaa na majirani kila wakati walikuwa wanamzingira na kumsukasuka kwa ajili ya kumpa mkono wa pongezi, wengine wanampa tuzo ya pesa, vitenge na kuitakia sherehe hiyo iwe ya heri na fanaka. Kwenye upande wa maakuli na mashrabu nako kulikuwa ni moto wa gesi, hii bila kusahau ni sekta muhimu kabisa kwenye sherehe yoyote ile ipate kufana. Si unajua Tanga kwa misosi ndio kwenyewe!. Sasa unafikiria nini kwenye mambo kama hayo? Usipime unaambiwa, wanawake wao mikono yao ina uchawi maalumu wa upishi wa ngano, basi kupitia ngano wanaweza kukutengenezea sambusa, visheti, maandazi, chapati, kalimati na vinginevyo vingi katika mahanjumati.
Kwa waliokuwepo hapo kijijini siku hiyo, walifaidi hadi kusaza mahanjumati. Kama ilivyozoeleka katika sherehe nyingi, huwa kuna muda maalumu wa chakula na mara nyingi huwa ni katikati au mwishoni mwa sherehe. Sasa unaambiwa kwenye sherehe hiyo ya ndoa ya Zabibu, hayo mambo hayakuwepo, chakula kilikuwa kinaliwa mwanzo mwisho, yaani watu walikuwa wanakula huku ratiba nyingine zikiendelea. Kwenye sekta hiyo familia ilijipanga haswa ng'ombe liliofutwa kodi na mbuzi wa kutosha waliangushwa, kupikia madikodiko na masontojo ya anuwai mbalimbali kuanzia samaki wa kupaka, rosti za nyama, rosti maini, chai ya maziwa, chai ya rangi, chapati, maandazi, vitumbua, na mbwembwe kochokocho za mapishi ya ngano.
Ilikuwa ni sherehe ambayo ilipangwa iache gumzo kijijini hapo karibia miongo kadhaa. Minyoo ya matumbo ya wanakijiji siku hiyo ilishtuka kwa kuvamiwa na chakula jadidi wasichokizoea. Maana vyakula vya asili vinavyopendelewa kuliwa na kabila la Wazigua ni ugali. Ambao unapikwa kutokana na unga wa mahindi yaliyokobolewa na kuvundikwa kwa muda mrefu kabla ya kusagwa au kutwangwa. Baada ya kusagwa hutoa unga mweupe na laini sana. Ugali huo huliwa na mboga za asili kama vile, Kungujulu, Sunga, Kididi, Mnavu, nyama za pori na uyoga, lakini siku hiyo walikuwa wanalishwa chakula cha tabaka aali katika jamii.
Gharama za fujo zote hizo zilibebwa na ofisi anakofanyia kazi binti yao Zabibu. Alikuwa ameajiriwa kwenye moja ya benki za kigeni inayovuma kwa sasa nchini Tanzania ijulikanayo kama 'Turkish Commercial Bank' (T.C.B) akiwa kama afisa uhusiano. Mbali ya ufadhili huo walimuandalia pia sherehe kabambe ya kukata na shoka jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mlimani City Hall punde tu atakaporejea jijini Dar es Salaam. Sherehe ambayo vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vilishanunua haki miliki ya kurusha tukio hilo kwa mamilioni sufufu.
Wataachaje kurusha tukio hilo la ndoa ya Miss Tanzania kipenzi cha wananchi, jina lake lilikuwa tamu kama peremende midomoni mwao, asiye na skendo yoyote ya ufuska, wala tabia mbovu za kuchefua jamii!. Hayawi hayawi sasa yakawa, muda uliokuwa unasubiriwa kwa hamu wa kupitishwa kwa nikaha hiyo baina ya Zabibu na mumewe mtarajiwa Shabani Zomboko dereva taksi za UBBER, mzawa wa Kariakoo au maarufu kwa rafiki zake kwa jina la 'Shebby-Zoo' ukawadia. Vyombo vya habari kochokocho kuanzia magazeti, televisheni, redio, blogu mbalimbali za mitandao za kijamii nazo hazikuwa nyuma kuja kurusha taarifa ya hafla hiyo kutoka kijijini.
Vyombo hivyo vilitaka kupaisha habari hiyo ya ndoa ya mlimbwende Zabibu Shamsi, mshindi wa taji la mrembo wa nchi, Miss Tanzania. Motakaa za kila aina zilitapakaa kijijini pale, kupamba mandhari ya sherehe hiyo, zikitokea pande mbalimbali za Tanzania kujua kushuhudia tukio hilo adhimu. Yalikuwa ni magari ya mashoga zake Zabibu na rafikize Shebby walikuja kuwaunga mkono kwenye tukio ambalo hata malaika wa mbinguni hupiga vigeregere kwa furaha pindi wapendanao wanapofunga ndoa.
Pia Mwenyezi Mungu, khalaka wa ardhi, mbingu na vilivyomo baina ya mbingu na ardhi nae anafurahi sana, pindi wanaadamu wanapochukua maamuzi ya kufunga pingu za maisha. Lakini aksi yake Ibilisi, shetani mkuu anakuwa na huzuni na hasira za kupitiliza pindi ambapo watu wanapofanya maamuzi ya kuungana kuwa mwili mmoja. Kwasababu anakosa wateja wake katika dhambi yake pendwa ya uzinifu, anaona wamemuacha solemba kwenye mataa. Nikaha hiyo ilipangwa kufungwa majira ya dhuhaa katika wakati wa mafungulia ng'ombe, baina ya saa 2-3 asubuhi katika msikiti wa ijumaa wa hapo kijijini, kisha sherehe zote kwenda kuhitimishwa nyumbani kwa bibi harusi. Huko kwa bibi harusi ndipo watu watakula, watakunywa na kucheza kutwa nzima mpaka majira ya usiku mbichi ndio itakuwa tamati yake.
Bwana harusi Shebby-Zoo akiwa amesindikizwa na wapambe zake ithnani wa chanda na pete, wa toka utotoni. Wamecheza mpira wa chandimu wote mpaka sasa wamekuwa wakubwa bado ni maswaiba. Walikuwa tayari wamewasili msikitini wanasubiri kukabidhiwa jiko lao la Kizigua warudi nalo jijini Dar es Salaam wakaendekeze libeneke la sherehe upya. Walikuwa wamevalia kanzu zao nyeupe nadhifu na majoho ya rangi ya kijani yenye ufito wa rangi ya samawati kwenye kola zake, huku vichwa vyao vikifunikwa na kofia za kuziua kwa mkono za rangi ya kahawia. Bwana harusi alikuwa anatembea na mkongojo wa urembo ili mradi kuleta nakshinakshi na mvuto wa muonekano wake. Kwa ujumla Bwana harusi na wapambe wake walipendeza sana machoni pa watazamaji.
Sheikh Ayoub Makoja, shaibu kiumri, unaweza kumkadiria miaka 50-55 kama ukipewa mtihani wa kumpachika umri wake, imamu mkuu wa msikiti huo nae alikuwa nadhifu katika vazi la kanzu yake nyeupe na kilemba kichwani, huku akiwa ana kitabu cha rejista ya ndoa na kitabu kingine maaalumu cha hotuba ya ndoa huku anahesabu tasbihi mkononi. "Salaam Aleikum nyie Wazaramo, karibu sana Handeni, ha.. ha... ha.." Sheikh Ayoub aliwasalimia waoaji, akawataniana kwa bashasha huku pia anapeana nao mikono. "Waleykum salaam Sheikh, ndio tumekuja kumbeba jumla jumla tumpeleke Uzaramoni, binti yenu wa Kizigua" walijibu salamu kwa pamoja kisha mmoja wa mpambe wa Bwana harusi akaujibu utani huo wa Sheikh. "Mmemaliza mahari lakini? Maana zamani enzi sisi tupo vijana kama hujamaliza mahari huondoki na mke!. Unabakia hapo hapo ukweni" alizungumza Sheikh Ayoub na waoaji wale huku wakisubiria watu wazidi kujazana msikitini kushuhudia akidi hiyo.
"Aaaah...Sheikh unatuonaje sisi, Wazaramo hatujazoea kuishi kwa mikopo, sisi ni maskini jeuri tumemaliza mahari yote na vihendo juu tumezidisha" alijibu mpambe yule ambaye alikuwa ni fundi wa matani. "Vizuri sana mnaonyesha mmepania, ila zamani hali ilikuwa tete sana. Wazee wa mila walikuwa wanaandaa tukio linaitwa Kulagasama. Hilo ni tukio la kuagwa kwa waliooana mara baada ya kukamilisha mahari na taratibu zote za kimila. Katika mila za Kizigua, ilikuwa mtu anapofunga nikaha, yeye na mkewe hutakiwa kukaa katika familia ya mke wake huyo kwa muda fulani ili aweze kukamilisha mahari kama alikuwa hajamaliza. Hivyo akimaliza kulipa mahari na mambo mengine yanayohitajika, huomba ruhusa toka kwa wakwe zake ili akaanzishe maisha yake na mkewe. Alikuwa kama akishindwa kulipa ataendelea kuishi upande wa mkewe kwa maisha yake yote na hata kama akifariki atazikwa upande wa ukweni kama ukoo wa upande wa mume hautamlipia, ila kama wakimlipia watapewa mwili kuzika upande wa mume. Lakini sasa mna raha sana mila na desturi sehemu nyingi hazifuatwi ipasavyo" alisimulia kwa uso wa bashasha Sheikh Ayoub mambo jinsi yalivyokuwa enzi zao wako barobaro mambo yalivyokuwa.
"Sheikh unachosema ni ukweli kabisa wala hatukubishii, kila zama na kitabu chake, siku hizi kuanzia sherehe za unyago, jando, harusi hamna tena ngoma za asili, sasa ni mwendo wa muziki wa singeli tu kwenda mbele" alizungumza kuchangia mazungumzo mpambe mwingine wa Bwana harusi, huku Bwana harusi mwenyewe akiwa amejiinamia chini, amefumbata viganja vyake vya mkononi. Inaonyesha alikuwa kwenye tafakuri nzito juu ya jambo analotaka kulielekea katika historia ya maisha yake. Tukio ambalo litambadilisha sasa na kuitwa mume wa Zabibu, pia tukio ambalo Mwenyezi Mungu akiwabariki watapata matunda ya ndoa, ambayo ni watoto, hivyo atakuja kuitwa baba fulani.
"Assalamu alaykum warahmatullah wabarakaatuhu jamiaaa.." Sheikh alikatisha mazungumzo baada ya kuona idadi ya watu wameshajazana pomoni msikitini wanasubiria shughuli ya kufungisha ndoa ianze, kisha akawasalimia kwa salamu maarufu kwa waislamu. "Waalekum salaam warahmatullah wabarakatuhu" wakajibu wote kwa nidhamu na taadhima salamu toka kwa Sheikh wao. "Sasa tunataka tuanze ibada ya kufungisha ndoa.
Mtume wetu Muhammad (S.A.W) ametufundisha kuwa Kukamilika ndoa lazima kwanza yatimie masharti yafuatayo:
kwanza ipatikane Idhini ya Walii. Alhamdulillahi baba mzazi wa muolewa yupo hapa Mzee Shamsi kashafika msikitini. Pili, Kuridhika kwa bibi harusi mtarajiwa. Hivyo hili sharti tutatuma watu nyumbani kwa bibi harusi kumuuliza kama hii ndoa anaifahamu na ameridhia. Sharti la tatu ni kutimia kwa tamko la ndoa yaani Ijaab na Qabuul, yaani iijab na qubuul iliyounganishwa kwa tamko la ndoa au yenye kufidisha maana hiyo. Sharti la nne ni kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu. Na mwisho Kubalighi na kuwa na utambuzi baina ya wanandoa, hivyo haifai kuwepo kwa ndoa ikiwa mmoja wapo ni mwendawazimu au mdogo kwa umri na bado hajabaleghe. Sasa kabla sijaanza khotuba ya ndoa, ningependa shahidi mmoja wa upande wa muoaji na mwingine kutoka kwa muolewa waelekee mubashara mara moja nyumbani kwa Bibi harusi wakamuulize kama anazo habari ya hili tukio linalotaka kuendelea hapa msikitini.
Tunawapa muda wa nusu saa muwe mmesharejea, Inshallah maa-salaaam" alitoa maelezo yenye ufasaha Sheikh Ayoub, mara moja akanyanyuka mmoja wa wapambe wa Bwana harusi na mwakilishi wa kikeni wakaelekea nyumbani kwa Mzee Shamsi, baba wa Zabibu. Baba mzazi wa Zabibu na waumini wengineo wakabakia ndani ya msikiti wanabadilishana mambo mawili matatu. Zikapita sekunde, dakika, sasa yakawa masaa walioenda nyumbani kwa mwali hawajarejea. Taharuki ikaanza kutawala mule msikitini, zogo la minong'ono likaanza kusambaa mle msikitini.
JE NDOA ITAFUNGWA KWELI AU BIBI HARUSI KALALA MITINI??
"Takbiiir....Takbiiiiir" ,alitamka kwa sauti ya juu Sheikh Ayoub maneno ya kiarabu yenye maana ya Mtukuzeni Mwenyezi Mungu. Waumini wote wakaitikia msikitini wakaitikia "Allahu Akbar...Allahu Akbar....", wakimaanisha Mwenyezi Mungu ni mkubwa. "Ndugu zanguni tuweni na ustahamilivu na subira, Qur' an Iinasema, inna-llah maa swaabirina, hakika ya Allah yupo pamoja na wenye subira, tuache zogo msikitini hii ni nyumba ya Allah na sio marikiti hapa, sehemu ambayo unaweza kubwabwaja upendavyo.
Nimeshatuma watu wengine waende kujua kulikoni huko mbona wanachelewa tunawapotezea watu muda bure, Pia tunawapiga simu sasa hivi tutawajuzeni kilichojiri, ahsantum" alitoa nasaha Sheikh Ayoub baada ya kukerwa na makelele ya waumini msikitini. Simu zilizokuwa zikipigwa nyumbani nazo hazikuwa na majibu ya kueleweka, yenye nakisi na mashaka mengi kuliko matumaini. Mpaka kufika muda wa jua la mtikati mbivu na mbichi zikawa dhahiri shahiri, kweupe. Kama ni jipu ni pwaaaah...! likawa limepasuka.
Penyenye zisizo na chembe ya mashaka zilizofika msikitini zilisema Bibi harusi Zabibu Shamsi Sakuzindwa alikuwa amejiua, kwa kujichoma kisu tumboni. Taarifa hizo za kifo zilivyosambaa mule msikitini, zikasababisha simanzi, huzuni, taharuki na sononeko katika mioyo ya ndugu, jamaa na marafiki wa wana ndoa hao tarajaji, ambao ndoa yao ilishaingia mdudu, haiwezekani tena kufungishwa. Kila mtu alitawanyikia njia yake, kutoka mle msikitini. Wapo waliosahau makubazi yao kutokana na kuchanganyikiwa na taarifa hizo ngeni kijijini kwao.
Mkosi na balaa wa sampuli hiyo ulikuwa ni wa kwanza kutokea kijijini hapo. Vidinga popo na wale akina habari kauzwa wakawa wamepata cha kusimulia vijiweni. Simulizi zao juu ya kifo cha Zabibu zikawa ukweli kidugu lakini ndimu na chumvi kibao ili mradi kunogesha porojo zao. Kijiji kukawa ni taharuki mtindo mmoja, hali ilikuwa mchafukoge, harusi ikageuka kuwa matanga.
Chakula kilichoandaliwa kwa ajili ya sherehe kikageuka kuwa cha matanga. Hadithi ya penzi tamu la kusisimua kati ya Zabibu, Miss Tanzania na Shebby Zoo ikafikia tamati. Hamkani mambo yakawa sio shwari tena, habari hiyo ikasambaa Tanzania nzima na viunga vya nchi za jirani. Tukio la mrembo ambaye amewahi kutwaa taji la Miss Tanzania kujiua kikatili tena siku ya harusi yake ilikuwa ni habari ya kushtua na kuogopesha sana. Swali la kila mtu alilokuwa anajiuliza ni kuwa amepatwa na maswaibu gani mlimbwende huyo mpaka afikie hatua ya kuyaondosha maisha yake kikatili namna hiyo tena bila kuacha ujumbe wowote unaoweza kuibua fununu za kifo chake.
Ilipofika majira ya jua la utosini tayari askari kanzu si chini ya wanne wakiongozwa na mpelelezi mkuu wa kituo kikuu cha polisi cha Handeni, Inspekta Hamduni walikuwa walikuwa wameshatia timu msibani. Walikuwa wanasubiria kwa hamu na wanakijiji ili waweze kupata fununu ya chanzo cha kifo hicho. "Poleni na msiba" alisalimia Inspekta Hamduni kwa baba wa marehemu. "Ahsante tumepoa ingawa siamini kilichotokea, Mwana kaita mjima ...... hahumile ooooh ooooh Mungu wangu" alijibu Bwana Shamsi huku akiwa anajifuta machozi kwa ncha ya vidole vyake huku anazungumza Kilugha kuwa mtoto kafariki kijana wala hajaumwa.
Mama Zabibu, mke wa Bwana Shamsi alikuwa nae hajiwezi, alilia mpaka akapoteza fahamu, alipozinduka akawa hata sauti haitoki tena, amebaki kuwa kama zuzu. "Mara ya mwisho kabla ya kifo chake, marehemu Zabibu alikuwa na nani?" alitupiwa swali baba wa marehemu. "Mimi nilikuwa msikitini nasubiria kumuozesha binti yangu, sikuwepo nyumbani ila kupitia simulizi za mashuhuda niliambiwa mpaka dakika za mwisho alikuwa na kungwi wake Bi Maua na ndio alimsindikiza mpaka msalani" alijibu baba wa marehemu Kiutulivu bila papara yoyote.
"Alishawahi kukudokezea dukuduku lake lolote linalomsumbua kabla ya ndoa yake binti yako?" aliendelea Inspekta Hamduni kuuliza maswali huku anarekodi mahojiano hayo kwenye kinasa sauti chake cha kisasa. "Hapana, hata mimi nimeshangazwa na uamuzi wake binti yangu, namuachia Allah tu nisije kukufuru bure" alijieleza baba Zabibu. "Ahsante kwa ushirikiano wako, usisite kutupa taarifa iwapo utapata fununu zozote zitakazosaidia upelelezi wetu! Pia nitaomba kuonana na kungwi wa marehemu Bi maua, huenda ana chochote kitu cha kutuhabarisha" alihitimisha mahojiano yake na baba wa marehemu.
Bi Maua akapewa taarifa za wito akawa anakuja himahima huku moyo unamdunda kwa uoga.
JE BI MAUA NI MHUSIKA MBONA ANAOGOPA KUKUTANA NA POLISI KAMA HANA HATIA?
Hofu yake Bi Maua ilikuwa ni kuangushiwa nyumba bovu la mauaji kama uwajuavyo baadhi polisi wetu, kwenye matatizo wao kwao ndio neema ya kuvuna kipato, ganda la muwa la jana chungu kaona kipato. Fauka ya hapo ni wavivu wa kufanya upelelezi wa kina, hivyo anaweza kukushikilia usaidie upelelezi ukaishia unaozea jela, hilo ndilo lilikuwa linampa uoga wa kukutana na afande, Bi Maua.
Inspekta Hamduni: "Naitwa Inspekta Hamduni, nimekuja kwenye uchunguzi wa wa kifo tata cha Zabibu. Nitajie majina yako matatu kamili"(Alianza mahojiano Inspekta na Bi Maua mara baada ya kufika)
Bi Maua: "Naitwa Maua Hassani Kipande"
Inspekta Hamduni: "Umri wako! "
Bi Maua: "Miaka 50 natimiza mwisho wa mwezi huu! "
Inspekta: "Kazi yako! "
Bi Maua: "Mimi nimejiajiri,ni kungwi wa kufunda wali, pia nauza dawa za mvuto katika mahaba kama ndere na zinginezo"
Inspekta Hamduni: "Umeolewa? "
Bi Maua: "Hapana Bwana afande sijabahatika"(alijibu Bi Maua kwa aibu huku ameinamisha kichwa chini)
Inspekta Hamduni: "Sasa unawafunda kitu gani hao wali wakati hata ndoa hujawahi kuolewa! "(Aliuliza huku anatabasamu Inspekta)
Inspekta Hamduni:" Anyway tuyaache hayo ni mambo yako binafsi sipaswi kuwaingilia, eheee....ulijuana vipi na marehemu Zabibu"
Bi Maua: "Namfahamu tokea akiwa msichana mbichi anasoma shule ya msingi hapa kijijini miaka hiyo"
Inspekta Hamduni: "Ilikuaje mpaka akakuchagua wewe kuwa ni kungwi wake wa kumfunda kwenye ndoa yake! "
Bi Maua: "Mama yake mzazi ni shoga yangu, hivyo ilivyokuja posa, wakalipa 'gubula lomo', ndio mama yake akanipa kazi ya kumfunda binti yake juu ya maisha ya ndoa.
Inspekta Hamduni: "Hiyo gubula lomo ndio nini sijaelewa fafanua tafadhali!"
Bi Maua: "Hiyo ni kifungua kinywa, kwa mila zetu Wazigua, mshenga akija kuleta posa lazima alipe kifungua kinywa"
Inspekta Hamduni: "Ulikaa na marehemu siku tokea maandalizi ya ndoa mpaka siku ya ndoa"
Bi Maua: "Nimekaa nae siku tatu pamoja na hii ya ndoa"
Inspekta Hamduni: "Je kuna dalili zozote za hatari uliziona kwake kama viashiria atakuja kujiua? "
Bi Maua: "Hamna dalili kubwa sana, ila nilichokiona alikuwa na msongo mkubwa wa mawazo hali iliyompelekea kutokuwa mzingativu wa ninachomuelekeza. Mie nikajua ni dharau zao hawa kizazi kipya na hasa ukichukulia ni mmoja wa wasichana waliowahi kushinda taji la ulimbwende la Miss Tanzania"
Inspekta Hamduni: Unaweza kutuelezea dakika za mwisho kuwa nae zilikuwaje? "
Bi Maua: Aliamka akiwa na afya nzuri tu, ila kama ninavyosema alikuwa mnyonge sana, tukawa tunajua ni uoga tu wa ndoa ambao unawapata wanawake wengi tu. Tukampamba akapambika vilivyo, kisha tukawa tumekaa nae ndani tunasubiria ndoa ipite msikitini. Muda wote alikuwa ametingwa na simu yake ya mkononi, mara aingie Instagram, mara aingie Whatsapp. Yote nilikuwa nashuhudia kwa sababu nilikuwa jirani nae.
Ghafla akaomba udhuru amebanwa na haja anataka kwenda msalani. Hivyo nikamsindikiza kwa kumshikilia kwa nyuma nguo yake ndefu isije ikapita kukomba vumbi njiani. Tulipofika msalani akaniachia simu yake nimshikie yeye akaingia ndani.
Dakika zikaanza kupita mpaka ilipotimu nusu saa nikaanza kupatwa na wasiwasi huenda amezidiwa na ugonjwa labda kapatwa na tumbo la kuhara au kaanguka chooni kapitiwa na jini. Nikaanza kumuita bila majibu yoyote. Ndio nikaja kutoa taarifa wakaja wababa kuvunja mlango wa choo, hamadi! Tukamkuta amelala kuegemea sinki la choo cha kukaa huku akiwa amejichoma bisu kubwa tumboni na utumbo wote umetawanyika sakafuni. Alikuwa anapumua kwa mbali sana, ndipo hekaheka za kumkimbiza zahanati ya kijiji inafanyika, lakini akapoteza uhai njiani kabla hajafika huko"( akamaliza maelezo yake marefu huku machozi ya uchungu yanamtiririka mashavuni )
Inspekta Hamduni: "Alikwenda kujisaidia huku akiwa na kisu mkononi au kisu ulimbebea wewe? "
Bi Maua: "Itakuwa aliktayarisha mapema akakificha huko huko mie sikumbebea kisu" alijibu Bi Maua swali ambalo uso wake ulionyesha lilimkera mno.
Inspekta Hamduni: "Hiyo simu yake ipo wapi? "
Bi Maua: "Kwa bahati bado ninayo sijaikabidhi kwa ndugu wa marehemu" alijibu Bi Maua huku anafungua pochi lake la rangi ya pinki.
Inspekta Hamduni: "Ahsante napokea kama kidhibiti, nitairejesha mara baada ya uchunguzi wangu kukamilika. Ahsante kwa ushirikiano wako mzuri nikikuhitaji tena sitosita kukutafuta"
Bi Maua: "Ahsante Bwana afande, karibu tena" alijibu Bi Maua huku ananyanyuka kwenye kiti chake alichokalia kipindi chote alichowekwa kiti moto na Inspekta Hamduni. Inspekta Hamduni alitamani aongee pia na mama wa marehemu lakini alikuwa sakimu wa hali yupo taabani hajiwezi.
Mume mtarajiwa wa marehemu Shebby Zoo nae alikuwa hoi bin taabani, alipatwa na mshtuko mkubwa sana wa kuharibika siku muhimu sana ya ndoa yake na mpenzi wake waliopendana kwa dhati. Baada ya dodoso ya hapa na pale, Inspekta Hamduni akaruhusu taratibu za kutoa maiti hospitalini ziendelee kwa ajili ya mazishi baada ya kujiridhisha kuwa marehemu amejiua mwenyewe.
Pia Inspekta Hamduni alikabidhi simu ya marehemu kwa familia baada ya kugundua laini zake zimenyofolewa, ni ganda tupu. Ilionyesha kuwa marehemu aliamua kupoteza ushahidi wowote wa mawasiliano yake ya mwisho.
"La Ilaha Illa Allah La Ilaha Illa Allah La Ilaha Illa Allah Muhammad Rasuul-llah..." ilisikika sauti ya Sheikh Ayoub Makoja ikipaa hewani kuwaimbisha umati wa waombolezaji waliofurika kuja kumsindikiza marehemu Zabibu katika makaburi ya kijini hapo Mzundu. Mazishi yalifanyika majira ya adhuhuri siku ya pili yake tokea kuaga dunia kwa Zabibu.
Waombolezaji nao wakawa wanaitikia matamshi ya Sheikh Ayoub huku wanatembea polepole na jeneza lililobeba mwili wa Zabibu likiwa mabegani mwao wanamsindikiza malaloni kwake. Umati wa waombolezaji waliokuja kuhani msiba wa Zabibu ulikuwa ni historia kwa pale kijijini.Vyombo vya habari kwao ilikuwa sherehe kubwa, maana walikuwa wanakusanya taarifa mbalimbali za tukio hilo kwa umakini mkubwa wapate kuwapasha walaji wao wa habari.
Waombolezaji toka pande mbalimbali za Tanzania na dunia kwa ujumla walijumuika. Watu maarufu katika jamii kuanzia Wanasiasa, Viongozi wa dini, Wafanyabiashara, Wanamichezo, na Wanamuziki nao walihudhuria msiba huo. Nyuso zao zilikuwa ni kioo cha kuonyesha kiwango cha huzuni kilichobebwa na nyoyo zao. "Mtume Muhammad...Mtume Muhammad...!!" alipayuka Sheikh Ayoub kwa sauti ya juu, waombolezaji wakawa wanamuitika "Swall-a-llahu Alaihi Wasalaam". Alikuwa anawatuliza waombolezaji wakae kimya, ili shughuli ya kuusitiri mwili wa marehemu ipate kuanza.
"Salaam Aleikum ndugu waombolezaji mliokuja kumsindikiza binti yetu Zabibu Bint Shamsi ambaye amerejea kwa Mola wake tokea jana asubuhi. Nafahamu nyote mna hamu kubwa ya kuingia kaburini, lakini hatuwezi kuingia wote kaburi ni finyu" akapumzika kuongea kumeza mate kidogo kisha akaendelea.na mazungumzo yake. "Sasa wafuatao ndio watakaoingia kaburini kuiwakilisha. Kila nitakayemtaja jina aporomokee kaburini, nao ni kaka wa marehemu Hilali Shamsi, mjomba wa marehemu Jumanne Kizinguto, Ustaadh Kalonji na Sheikh wetu Ayoub, ahsante sana" akashukuru mshereheshaji baada ya kuhakikisha wote waliohitajika kwenda kuingia kaburini wameshashuka tayari. Hekaheka za kuushusha mwili kaburini zikaanza huku kaburi likiwa limefunikwa shuka nzito kuzuia watu kuchungulia namna maiti inavyoswekwa ndani ya mwanandani, ambacho kina kichumba chembamba sana kilichopo ndani ya kaburi.
"Leteni ubao, miti na nyasi" ilisikika sauti ya Sheikh Ayoub ndani ya kaburi akiagiza vitu hivyo ili kuzibaziba upenyo ndani ya kaburini. Baada ya dakika kama 7 wakawa tayari wameuhifadhi mwili sasa ikabaki shughuli ya kushusha mchanga kaburini. Watu wakawa wanashindana kupokezana chepe ili kurushia mchanga kaburini. Baada ya kama robo saa kaburi likawa tayari limeshasawazishwa, huku mti maarufu kwa jina la mashahidi ukawa umechomekwa eneo la kichwani.
Jumamosi moja ambayo alikuja mapumzikoni nyumbani kwake toka shambani kwake alipanga atoke mtoko wa kwenda ufukweni mwa bahari. Kilipita kitambo kirefu bila kutia mguu kiwanja chochote kile cha starehe. Shebby alishang'amua na kupitishwa kwa vitendo jinsi mapenzi yanavyotesa, jinsi yanavyoweza kusababisha kifo, maziwa si msaada tena kwa sumu ya penzi. Pia alishajifunza moyo uliyojeruhiwa kwa mapenzi hauwezi kukingwa kwa vazi la chuma lililozunguka mwili mzima. Fauka ya hayo, kila aliyetambua hali yake anayopitia alikuwa anamfanyia maombi tu.
Ila watu wenye roho za kigaidi walikuwa wanamuona ni mwanaume tepetepe, mwenye mapenzi ya kihindi yenye maigizo ya nyimbo nyimbo na vilio vingi. Laiti hawa watu wakatili wangeonjeshwa walau suduthi ya maumivu yake Shebby, tungekuwa tumeshawazika tayari.
Siku hiyo akapatwa na mshawasha wa kwenda kujiburudisha ufukweni mwa bahari. Alijiandaa zake mapema mapema kwa usafi wa mwili wake, juu alivalia jezi ya buluu inayovaliwa na timu ya Chelsea ya nchini Uingereza, kuthibitisha yeye ni shabiki kindakindaki wa timu ya darajani pale Jijini London, Uingereza. Huku chini akivalia trakisuti rangi nyeusi ina mabaka ya buluu kuzunguka magotini, na raba zake za rangi ya maziwa chapa 'Adiddas'. Kwa kweli alipendeza vilivyo kimuonekano, nguo zilimkaa vilivyo mwilini hasa kutokana na umbo lake la kimazoezi.
Adhuhuri ilivyotimu akajisogeza kwenye kituo cha daladala, kuvizia usafiri wa umma, mkombozi wa wanyonge, daladala zinazoelekea stendi ya Makumbusho zikitokea Mbezi. Hakutaka kuganda kituoni kusubiria usafiri huo wa kibongo ambao hauna uhakika nao utafika saa ngapi. Akaamua atembee mdogomdogo usafiri umkute njiani ili nae anyooshe miguu. Hazikupita hata dakika tano akiwa ameshafika maeneo ya shule ya sekondari ya binafsi maarufu kwa jina la 'Libermann' akapata usafiri huo.
Kwa bahati ilikuwa ni mwishoni mwa juma daladala zinakuwa hazijazi nyomi ya kutisha, akabahatika kupata siti ya kuketi ya upande wa dirishani. Suka alikuwa fundi kwelikweli wa kulikamua gari lake alikuwa haliendeshi gari lake kwa mwendo wa mzofafa kama yupo harusini, alikuwa anajua abiria wanawahi kwenye pilikapilika zao za siku. Ghafla wakajikuta wameshafika kituo cha 'Massana Hospital' meta chache kutokea barabara ya 'Mwai Kibaki Road' au kwa jina la zamani 'Bagamoyo Road', Shebby Zoo akapatwa na mfadhaiko wa moyo na simanzi, akawa amejiinamia. Alitoneshwa donda la moyo baada ya kuitia machoni hospitali hiyo ilimpa kumbukizi mbaya sana maishani mwake aliyowahi kuipitia katika kipindi cha mapenzi yake na Zabibu.
"Sorry sana Bwana Shabani,mpenzi wako amepata miscarriage...mimba imeharibika, tutakaa nae kwa siku moja zaidi kumchunguza. Maana katuambia amekunywa soda ndipo dalili zikamuanza za maumivu.." alikuwa anafanya kumbukizi ya miaka minne iliyopita, majibu aliyopewa na daktari, siku alipomkimbiza kwa dharura mchumba wake Zabibu hospitalini hapo baada kuanza kutokwa na damu sehemu za siri. Maelezo ambayo yaliupasua moyo wake vipande vipande na kuzima ndoto yake ya kuitwa baba.
"Mwanangu angejaaliwa uhai sasa angekuwa na 4 years sasa angekuwa vidudu anahesabu tu kwa kimombo one..two..three!. Mwanangu angekuwa ni zawadi tosha niliyoachiwa na mpenzi wangu Zabibu, na angenipunguzia uchungu wa kifo cha mama yake" alizidi kuzama kwenye dimbwi la mawazo.
"Afrikana kituo...., Afrikana wa kushuka oyaaa...changamkeni, wa kupanda pandeni na wa kushuka fastaa msiuweke usiku, ni mwendo wa panda mti kata mti" maneno ya kondakta wa daladala ile ndio yalimuibua juu Shebby kutoka kwenye kina kirefu cha bahari ya mawazo alichokuwa anaogelea. Akajizoazoa kitini na kuharakia mlangoni kushuka.
"Oyaaaah...nauli mzee baba hamna stafu humu...hapa ni pesa tu" kondakta alimkumbusha Shebby Zoo ambaye kutokana na kutingwa na mawazo alishasahau kulipa nauli ya daladala. "Oooh...Samahani, nilipitiwa" akajibu Shebby huku anamfinyangia noti ya shilingi elfu tano. Akarudishiwa chenji yake ya shilingi elfu nne mia tano, kondakta akaruhusu gari kwa kupiga kofi bodi ya daladala, ikakitoa zake huku inafurumusha moshi angani.
Shebby Zoo akarudi nyuma kidogo ya barabara kulikuwa na bajaji zimepaki zinasubiri abiria huku pembeni ya bajaji hizo zilizojipanga kulikuwa na meza ya muuza magazeti, akaisogelea kushangaa magazeti ya siku hiyo. Baada ya kusoma vichwa vya habari akapendezewa na gazeti la michezo linaloitwa 'Kabumbu Uwanjani' akalilipia na kujinyakua pale mezani. "Broo...karibu hii hapa nikuhudumie tunapakia kwa zamu" alikaribishwa na mmoja wa waendesha bajaji. Shebby hakujibu kitu akaingia moja kwa moja, na kumpa maelekezo, "Nipeleke Jangwani Sea Breeze Resort tafadhali..". Muendesha bajaji akatii kwa vitendo ombi hilo.
Iliwachukua takribani dakika kumi na mbili na nusu mpaka kufika ufukweni hapo. Akamalizana nae malipo ya gharama za usafiri. Akawa anajongea kwa mwendo wa pole ndani ya hoteli ile. Akaingia ndani na kulipia kiingilio kisha moja kwa moja akaenda kwenye midule yenye kivuli cha makuti na kuketi. Mara moja mhudumu wa hoteli akamchangamkia kwa kumfuata pale alipokaa na kumuongelesha. "Kaka yangu karibu sana, nakusikiliza mahitaji yako". "Ahsante naomba hiyo karatasi ya orodha ya vyakula na vinywaji".
Akakabidhiwa na yule dada mhudumu ile karatasi ya Menu, akaanza kuisoma. huku ameiinamia kisha akanyanyuka na kumuongelesha yule dada mhudumu. "kinywaji Fanta Orange kisha niletee....Fried Chicken with Salads..". "Nimekuelewa, chakula itabidi usubirie kati ya dakika tano mpaka kumi" akasema yule dada huku Shebby akikubaliana nae kwa kuinamisha kichwa chake. Mhudumu yule alipoondoka zake,akalifungua gazeti lake la michezo na kuanza kuperuzi kurasa zake kujua kilichojiri katika ulimwengu wa soka Tanzania na duniani kwa ujumla.
Taratibu alishaanza kuizoea hali ya kutokuwa pamoja na mpenzi wake Zabibu. Zamani enzi za uhai wa mamsapu wake Zabibu walikuwa wanagandana kama luba, popote alipo Shebby na Zabibu yupo. Mpaka baadhi ya wanaowafahamu ambao wanawatakia heri wakawapachika lakabu ya 'Love Birds'. Mahasidi, wale wenye vijiba vya roho nao hawakuacha kuropoka maneno ya asidi dhidi yao, wapo waliowasimanga kuwa wanaishi maisha ya tamthilia ya kufikirika.
Wapo walioenda mbali zaidi na kusema kuwa Shebby Zoo amemloga Miss Tanzania, amemwendea kwa wataalamu wa mitishamba Zabibu ili tu amkubali kuwa mpenzi wake. Kigezo chao kikubwa kilikuwa haijawahi kutokea dereva taksi kama Shebby eti afaidi huba la Miss Tanzania mwenye viwango vyake kama Zabibu, ambaye Mapredeshee na Maofisa wenye milundi ya mali wanalizengea huba lake.
Akiwa amezama kwenye gazeti lake pendwa la michezo, akashtukia anagongwa begani. "Komredi upoo..!siamini kama nimekutia machoni, kitambo kirefu sana hujaonekana viwanja kama hivi. Pole sana na matatizo yaliyokupata ndio dunia ilivyo kikubwa subira tu" alizungumza huyo jamaa yake Shebby aliyevalia fulana nyeusi zenye na maandishi ya kijani kifuani yaliyoandikwa 'RAJA SAFARI TOURS'. "Ohooo...Kenny daah kitambo sana mzee wa pori hatujaonana ila ndio mbiringe mbiringe za maisha, mie nimeshapoa, yamepita" alijibu huku akiwa amesimama kumlaki mgeni yule wanayefahamiana kitambo.
Mhudumu akawa tayari ameshaleta chakula pale mezani. "Aisee...dada yangu msikilize na huyu anachotumia, bili zote juu yangu naomba Kenny usikatae ukarimu wangu kwako maana wewe moja haikai wala mbili pia haikai" alitoa angalizo Shebby huku wote wanakaa kwenye viti. "Sawa bwana umeshinda mie niletee Coca-cola bariiiidiii basi niisuuze roho yangu na joto hili la Bongo" aliagiza Kenny, huku anamsindikiza kwa macho yule mhudumu anavyotembea mzofafa.
"Bado tu Kenny...hujaacha tabia zako za kupenda totoooz..." alimchomekea baada ya kuona Kenny amekodolea macho kwenye miondoko ya yule dada. "Ng'ombe hazeeki maini afu si unajua kazi na dawa, sie watu wa pori hawa viumbe adimu sana kule ha...ha...ha... " alijisifia Kenny sifa yake ya ukware kwa akina dada. "Kulikoni mbona hapa tena na sare za kazi? " aliuliza Shebby baada ya kumuona hajavaa libasi za kuja kupumzika ufukweni. Maana juu alivaa hilo fulana yake, huku chini akivaa dangirizi ya buluu na safari buti nyeusi.
"Aaah...acha tu, nimekuja na wageni wangu Wataliano niliwapeleka mbuga ya Serengeti sasa nimerudi nao leo, wametaka wapate mlo mchana hapa kisha nawarudisha hotelini walipofika. Kesho wanaamsha kurejea kwao Itali" alieleza nia na madhumuni ya uwepo wake pale. "Daah...Waitali kavu sana, ni wababe na ni wabahili kuwa makini maana hata bakshishi zao ni kiini macho, anaweza kukupa tip ya dola 100 kumbe ni feki ha.. ha . ha... ha.." wakafa kwa kicheko wakichambua janja janja ya Waitali.
Kama ulikuwa hufahamu, Shebby na Kenny wamewahi kufanya kazi pamoja kwenye kampuni ya kuongoza watalii ya RAJA SAFARI TOURS kwa zaidi ya miaka 6, baadaye Shebby kibarua kikaota nyasi, akajiingiza kwenye taksi za UBBER huku Kenny akiendelea kulisongesha mpaka leo hii wanayokutana. " Unayosema ni kweli tupu hawa bwana kama Waswahili tu wana roho ya korosho. Watalii toka Swiss na nchi za Skandinavia kwa ujumla wapo poa sana, wale unaweza kuvuna mpaka bakshishi ya dola 1000 kwa safari moja" aliendeleza mada dereva Kenny huku wanashushia mazungumzo yao na vinywaji vyao waliyoagiza.
"Kuna safari moja bwana, nilienda watalii toka Norway, mbuga ya Mikumi basi kabla hatujatoka huku walianza kunitangazia dau langu la bakshishi. Wakaniambia nikiwaonyesha Simba watanipa dola 150, nikiwaonyesha Tembo dola 100, chui nae dola 150, na hawana longolongo hapo hapo wakiwaona wanakupa chako" alichagiza mazungumzo Shebby huku akiwa amemaliza chakula anachokonoa nyama zilizonasa kwenye meno yake kwa vijiti maalumu. Sasa ukiwabahatisha pale 'KIA Airport' halafu wakikuambia uwapeleke BOMA MASAI hapo ndio umekula bingo, maana huwa nawatia ndimu kuwa kuingia BOMA MASAI kushuhudia mila na tamaduni za kabila la Wamasai kila mtalii lazima alipe dola 20. Sasa ukiwa na vichwa 10 tayari unazo dola 200, kule kwa Wamasai wao tozo yao wanataka shilingi elfu ishirini na saba tu" alitoa siri namna waongoza watalii wanavyopata kipato cha ujanja ujanja kupitia watalii.
Wakiwa kwenye mazungumzo yao, wakikumbushiana michapo mbalimbali ya enzi wapo pamoja kazini, ghafla bin vuu simu ya Kenny ikaanza kuita. "Daaah..!tayari itakuwa wanataka kuondoka. Hellow..!OK...OK..i'm coming right now..!!" Ebana mie nawapeleka wazungu wangu wakapumzike. Ahsante kwa kuchati tutafutane bana usijitenge" wakaagana huku wakibadilishana namba za simu.
Akapiga hatua kama tatu tu, ghafla akageuka Kenny, "Mungu wangu weeeh...! Nikitaka kusahau jambo muhimu kwelikweli. Kuna barua yako, bahasha kubwa ilitumwa pale ofisini kwetu yapata miezi sita sasa. Kila nilipokutafuta kwenye simu sikukupata hewani, na nilishawahi kuja kwako Goba mara moja lakini hukuwepo sasa sijui tunafanyaje....?"
MAMBO YANANOGA SASA,BARUA INA MIEZI 6 INA NINI HIYO BARUA TENA????
ENDELEA KUFUATILIA HADITHI HII
Kila nilipokutafuta kwenye simu sikukupata hewani, na nilishawahi kuja kwako Goba mara moja lakini hukuwepo sasa sijui tunafanyaje....?" aliulizwa Shebby na rafikiye Kenny. "OK...vizuri ahsante wa taarifa nitaangalia namna ya kuipitia jumatatu ofisini kwenu kabla sijaenda shambani" alishukuru Shebby huku wakipeana mikono tena kwa mara ya pili. Shebby akawa anaendelea kula upepo mwanana wa bahari, sehemu ambayo feni haiwashwi labda uwe majinuni ndio utawasha feni ufukweni mwa bahari. Alivyochoka kukaa akaaanza kutembea pembezoni mwa bahari ili mradi lengo lake la kujipumzisha likatimia vilivyo. Ilipotimia muda wa magharibi akaanza harakati za kurejea nyumbani kwake. Mpaka kufika majira ya saa tatu kasoro usiku, akawa tayari kashawasili nyumbani kwake.
Ghorofa za ofisi ya RAJA SAFARI TOURS zilikuwa zipo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, katika makutano ya mtaa wa Ohio na Sokoine Drive. Lilikuwa ni jengo lenye mvuto wa kipeke yake kwa jinsi lilivyosanifiwa kimaridadi likiwa na roshani tano. Ilimchukua takribani dakika 45 Shebby kufika ofisini hapo kutokea nyumbani kwake Goba. Alidamka asubuhi na mapema kwa malengo akishachukua hiyo barua aliyoambiwa jana afanye mipango ya kupitia sokoni Kariakoo kwa ajili ya kupata mahitaji ya shambani kwake kama madawa ya kudhibiti wadudu wa mazao shambani kisha ndio aelekee porini kwake Kiwangwa akajichimbie. Sasa Jiji alikuwa analiona halina thamani tena kwake bora ajichimbie porini tu kusakanya pesa za shambani ndio kazi iliyobakia kwake. Hakutilia uzito wowote barua hiyo anayoitiwa, alikuwa anajua ni barua tu kama zingine, ila alikuwa anadhania huenda barua hiyo inatoka wizara ya ardhi kukumbushia malipo ya kodi ya viwanja na nyumba ya familia yao iliyopo Kariakoo. Pia alipanga kama itakuwa ni barua ya ardhi, basi pia atapitia benki kabisa kulipia ili amalizane nao kabla hawajacharuka kutaka kuuza mjengo na viwanja vyao. Miaka nenda miaka rudi, alikuwa anatumia anuani ya posta ya kazini kwake kwa zamani kwa ajili ya mawasiliano yake ya barua. "Hellow...Sada za masiku upo bado... ? " alisalimia kwa uso wa bashasha Shebby huku anampa mkono dada huyo wa mapokezi ya wageni wenye kuhitaji kukodisha magari kwa ajili ya safari zao za kitalii na safari zingine zozote binafsi au za kiofisi katika kampuni hiyo ya RAJA SAFARI TOURS. "Aaah...Aaah...Aah..ni wewe kweli kaka yangu au mzimu wako... ! Siamini kaka yangu Shebby, umeamua kutupa jongoo na mti wake sawa bwana, Mungu anakuona ujue" alijibu salamu dada yule huku akiwa analalamikia kitendo cha Shebby kukata mguu ofisini kwao. "Afu nilisahau pole na matatizo ya msiba, sikuwa na taarifa kabisa za ndoa yako, ila habari nilizipata kwenye mitandao na magazeti, Mungu akupe faraja na subira kubwa" alizungumza Sada huku uso wake ukivaa huzuni kwa msiba wa mpenzi wake Zeddy. "Nimepoa kabisa sina hata kinyongo ndio mitihani ya duniani ingawa ni ngumu sana kukubaliana na kilichotokea. Halafu pia nisamehe nakiri sikutoa taarifa kwa watu wengi sana, sikutaka kukupeni takilifu ya kunichangia, kama ujuavyo kipato sasa hivi kimekuwa kigumu sana, unakuta mtu kwa mwezi ana mzigo wa kadi za harusi karibia tano na wote wanambananisha kwenye kona kuwa lazima awachangie" alishukuru na kujitetea kwanini hakuwapa taarifa za harusi yake. "Anyway... nina haraka kidogo sijui Kenny nimemkuta?" aliuliza Shebby akimjulisha kilichomleta pale ofisini. "Kenny katoka kidogo kaelekea uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kawapeleka wageni wake, ila kuna mzigo kaniachia kasema ukifika nikukabidhi" alijibu dada yule wa mapokezi huku akigeukia nyuma ya kabati lake kuchomoa hiyo bahasha aliyokabidhiwa, huku Shebby akiwa anaisubiria bahasha hiyo huku ametia mikono yake kwenye mifuko ya suruali yake anapiga mluzi. "Haya ahsante sana, tutaonana dada yangu usijali mambo ni tumbitumbi hayajatulia bado, wewe ni kama hirizi hapa kamwe huwezi kuacha kazi, mhindi kakurogezea" aliaga Shebby kwa utani wote wakafa kicheko na kupeana mikono ya kwaheri. Shebby akawa anatoka sasa ya ofisi hiyo iliyopo roshani ya pili, akaamua ashuke chini ya jengo kwa kutumia ngazi na sio lifti. Akatembea mpaka alipofika chini ya jengo akakutana na kibao kikubwa chenye nembo ya kampuni hiyo ya RAJA SAFARI TOURS, akawa anakumbukia siku yake aliyofutwa kazi pale ofisini. "Iko veve naendekeza sana mapenzi kuliko kazi, habari zako zote ninazo sitaki kukuona unakanyaga tena hapa ofisini kwangu, sitaki watu wavivu hapa, kabidhi kila kitu changu cha kiofisi" mwangi wa sauti ya mhindi yule Patel ulikuwa inajirudiarudia tukio la miaka sita iliyopita kila nilipoiangalia nembo ile. Akashukuru Mungu tukio lilipita na maisha yanasonga mbele kwa mbele sasa yupo Kiwangwa anakomaa na mananasi. IIlikuwa ni kampuni yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 40 kwenye shughuli za usafirishaji hasa watalii katika mbuga mbalimbali za Tanzania. Ilikuwa ni kampuni ya familia ya Bwana Rajeev Patel iliyohamia Tanzania kutokea nchini India na kuamua kujikita kwenye shughuli hiyo. Ilikuwa na magari ya aina mbalimbali ya usafirishaji zaidi ya 200 kwa idadi. Wafanyakazi hapa walipapenda sana kufanya kazi kwa sababu alikuwa anawajali na kuwalea kama familia yake tofauti na tabia za wawekezaji wengi wa kihindi ambao wanawafanya wafanyakazi wao kama watumwa. Yeye Bwana Rajeev dereva yoyote alikuwa akiendesha gari miaka mitatu mfululizo bila kosa lolote la kinidhamu anakukopesha gari linakuwa lako kisha anakukata kidogo kidogo kwenye mshahara. Ilikuwa ni bahati mbaya sana kukuta dereva wa RAJA SAFARI TOURS kumkuta yupo choka mbaya kimaisha, apeche alolo, wengi wao walikuwa wanamiliki nyumba zao na magari yao wenyewe na Shebby alikuwa tayari ameshanunua kiwanja . Ndio maana siku Shebby anafukuzwa kazi kama mbwa kila mfanyakazi pale RAJA alishangaa sana, hawakujua kuna nini baina yao, siri ya mtungi aijuaye kata. Maana haikuwa kawaida ya Bwana Patel kumkoromea mtumishi wake namna hiyo, wakayaacha kama yalivyo. Alipofungua mlango wa gari lake tu kabla hajafunga mlango akapata kimuhemuhe cha kufungua bahasha hiyo kubwa ya rangi nyekundu ili kufahamu kuna ujumbe gani ndani yake. Mapigo ya moyo wake yalikuwa yanaenda kasi, alishaanza kuhisi sio barua ya kiserikali kama alivyodhania mwanzoni. Maana bahasha nyingi za serikalini ni za rangi ya kaki na wakati mwingine huwa zinakuwa na nembo ya taifa ya Adamu na Hawa, lakini hiyo ilikuwa ni bahasha ya rangi ya nyekundu mpauko, kutokana na kuwa ilishaanza kuchoka kwa kubadilika rangi kutokana na kupigwa vumbi muda mrefu. Vidole vilikuwa vinamtetemeka kama mlevi wa gongo wakati anachana gundi ya bahasha hiyo. Ule mwandiko wa juu ya bahasha ndio ulimuogopesha, ulikuwa ni mwandiko ambao karibia asilimia 99% anaujua mwandishi wake. Alichokuwa anatafuta ni uthibitisho tu kuwa ni kweli huyo huyo anayemjua ndio mwandishi wa barua hiyo au hati zao tu zimeshabihiana?. Kufungua tu ile bahasha na kutoa vilivyomo , Loooh Salalee weee.! ni yule yule mtu aliyekuwa anamhisi ndio mwandishi wa barua hiyo ndefu. Barua ambayo imekuja kutonesha kidonda chake cha huba katika moyo upya. Damu za kidonda hicho kilichokuwa kinakaribia kupona sasa kwa takribani muda wa miezi sita ya kukiuguza. Barua imekuja kuchubua upya majeraha ambayo kupona kwake hakuwezi kutibiwa na daktari bingwa wa upasuaji wa moyo, si kule hospitali ya Apollo, India wala sio Daktari bingwa Mohamed Janabi wa Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), pale hospitali ya taifa Muhimbili. Bahasha ikamdondoka chini ya miguu yake ndani ya gari pale kwenye siti ya dereva. Akafanikiwa kuiokota bahasha huku jasho jekejeke likawa linamtiririka utasema yupo katikati ya jangwa huko Darfur, Sudani muda wa jua la mtikati ambapo joto la nje ni kali sana hufikia wakati mwingine mpaka sentigredi 40. La hasha...! hayupo Darfur, yupo Jijini, Dar es Salaam lakini kilichompandisha joto si kingine, bali ni joto la huba, huba la Miss Tanzania, mlimbwende wake, marehemu Zabibu. Alikuwa ameleta salamu za huba lao toka kuzimu. Alichofanikiwa Shebby ni kuifungia barua ile kwenye droo ya kuhifadhia nyaraka zake ndani ya gari na pia kupata nguvu za kumpigia simu dereva wake wa taksi yake ya UBBER anayoiendesha. Taksi ambayo kwa siku hiyo Shebby aliichukua kwa makubaliano kuwa afanyie misele yake ya mjini akimaliza mizunguko yake amkabidhi yeye arejee shambani kwenye kupiga jembe kama kawaida. "Hellow..Sheni, samahani nipo RAJA SAFARI TOURS njoo nifuate sijisikii vizuri kabisa kifua, mapigo ya moyo siyaelewi kabisa tafadhali njoo haraka! " akakata simu yake. Mapigo ya moyo yaakanza kupungua taratibu akaanza kujihisi kichwa kinauma na kizunguzungu kikali, akapoteza fahamu hapo hapo, hajui tena linaloendelea duniani. Barua toka kuzimu, yenye ujumbe tatanishi toka kwa mpenzi wake Zeddy ikawa imezua kasheshe upya.
Baada ya siku mbili za kulazwa katika hospitali ya Agakhan iliyopo jijini Dar es Salaam karibu na barabara ya Ufukoni, Shebby alikuwa tayari kupewa ruhusa. Afya yake iliimarika vilivyo hivyo alikuwa hana budi kuruhusiwa arejee nyumbani kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa. Uzuri wa mambo Daktari Shaqeel wa Agakhan ni mmoja wa Madaktari waliomhudumia kisaikolojia miezi sita Iliyopita alipoletwa toka Tanga akiwa hajitambui. Na ni daktari ambaye kwa kawaida ana maneno mengi kama kitabu mgonjwa akimsikiliza tu maneno yake anajiona amepona kabla ya kuanza matibabu. "Bwana Shabani, afya yako ipo mikononi mwako mwenyewe, ukiamua kujiua ni wewe mwenye na ukiamua kuishi kwa furaha ni wewe mwenyewe, kupanga ni kuchagua"aliongea Dr.Shaqeel kwa sauti ya huruma akionyesha hapendezwi na suala la kudorora tena kwa afya ya mgonjwa wake mara kwa mara. "Narudia tena, tatizo lako sio lenye kuhitaji kumeza vidonge vya kuondosha msongo wa mawazo, bali ni tatizo la kisaikolojia tu. Nakuomba ufuate kanuni zile nilizokuwa nakufundisha na ukaamua kuzifuata ipasavyo mpaka kwa muda wa miezi sita afya yako ikatengamaa na kuimarika vilivyo. Nitakupa na kitabu kipya kimetoka hivi karibuni tu kinaitwa 'A Widow’s Guide to Healing' kitakusaidia sana. Lakini nilipokufanyia vipimo leo kuna tatizo jipya nimeligundua kwako uniazime masikio yako" alisema Dr.Shaqeel huku anaweka miwani yake vizuri kisha akaanza kuuma kizibo cha peni yake ya kuandikia kana kwamba anasitasita kuendelea na kulieleza hilo tatizo. "Nipasulie ukweli tu Dr.Shaqeel, sasa nimeshakata shauri la kubadilika. Nimeshajifuma ujinga wa bure ninaoufanya, na tatizo la ujinga hauna kikomo hivyo nikiendelea na hii hali nitateseka mpaka siku naingia kaburini. Hivyo wewe Daktari wewe mwaga tu mchele kwenye kuku wengi moyo wangu upo tuli umetulizana raha mustarehe kama Sultani bin Jelebi" alizungumza Shebby kwa kujiamini, kwa sauti iliyokuwa inaonyesha kweli ameamua kubadilika. Alishatambua kukasirika au kuhuzunika ukiwa na tatizo wala haikusaidii kuondosha tatizo ulilo nalo bali mambo hayo yanaweza kuchochea matatizo mapya zaidi ambayo haukuyatarajia. Kama yeye Shebby tayari alikuwa kamkosa mpenzi wake walioshibana lakini akiendekeza msongo wa mawazo atakuja kuzalisha matatizo mapya kama shinikizo la damu, mshtuko wa moyo na hata kansa. "Mhh...Mhhiii..." alikohoa Dr.Shaqeel kuliweka sawa koo lake huku akishangazwa na ujasiri wa simba nyikani uliomvaa ghafla bin vuu mgonjwa wake Shebby. Kabla ya kuendelea na kitu kipya anachotaka kumuambia Shebby kuhusiana na tatizo jipya la kiafya lililoibuka kwake akafungua faili lililopo mezani kwake kisha akaanza kuongea "Tulipopima damu yako safari hii, tumekuta ni chafu....nikawaambia.....!" "Chafu kivipi sikuelewi ujue Bwana daktari.." alikatiza Shebby maongezi ya Dr.Shaqeel huku anapigapiga meza ngumi kwa kishindo. Maneno ya daktari yalipenya kama mshale wa sumu katikati ya moyo wake hasa baada ya kuona mambo yanazidi kuharibika kwa upande wake badala ya kupata tahfifu anazidishiwa uzito fauka uzito. "Punguza presha na munkari, Laa tahzani lazima nikuambie ukweli siwezi kukuficha na daima ukweli ndio utakuweka huru. Umegundulika kuwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa UKIMWI baada ya vipimo vya damu kubwa. Ila kuishi na virusi ni jambo lingine na kuumwa ugonjwa wa UKIMWI ni jambo lingine. Ukizingatia kanuni bora za afya na lishe bora kama zinavyoshauriwa na washauri nasaha utaweza kuishi kwa matumaini raha mustarehe. Utaweza kutimiza ndoto zako mbalimbali ulizojipangia kimaisha kama kujiendeleza kwa kipato, elimu, kupata watoto, na mengineyo mengi tu kama wanayofanya wasio na virusi vya UKIMWI. Je una swali lolote kuhusiana na virusi vya UKIMWI?" aliulizwa Shebby na Dr.Shaqeel baada ya kuelezwa kinagaubaga namna ya kuishi kwa matumaini. Alishusha pumzi ndefu zilizotoa sauti, huku akikodoa macho yake kama bundi na kuyapepesa macho hayo kama mtu aliyebumburushwa usingizini, kuonyesha kapashwa habari mpya, ambayo ni nzito na mbaya sana aliyokuwa haitarajii. Kichwani mwake akiwaza namna wagonjwa UKIMWI wanavyokonda kama samaki ng'onda ndio na yeye atakuja kuwa hivyo. Pia akawa anafikiria namna watu wanavyo wanyanyapaa wagonjwa UKIMWI kama mtu mwenye ukoma. Kikapita kitambo kirefu kidogo huku akiwa Shebby amejiinamia kama kobe anayetunga sheria bila kuzungumza kitu chochote huku Dr.Shaqeel akiwa kajiweka tayari tayari kwa lolote. Maana taarifa za damu ya mtu kuwa chafu kila mmoja huipokea kivyake katika binaadamu. Wapo ambao wanataka kutembeza kipondo kwa daktari aliyempa taarifa hiyo na wapo ambao wanapoteza fahamu na hata kufa hapo hapo hivyo alijiandaa kukabiliana na lolote lile. Alishapigilia msumari mwingine kwenye moyo wa Shebby, ila ukweli wa mambo msumari uliomchoma mja hutokea pale pale ulipoingilia. Alishusha pumzi ndefu hufyu kijana Shebby huku akichegama mgongo wake kwenye kiti alichokalia akionyesha amechoka kutokana na ujumbe mzito aliopewa. Taarifa ya daktari ilimtingisha kichi kichi, alikuwa amepoa kama tangopepeta, kisha akafungua mdomo wake kuzungumza. "Nimepokea kwa masikitiko taarifa hii ya hali mpya ya afya yangu, moyo wangu umevunjika keche keche, lakini maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga na hata hili jipya ulilonipa leo nitakabiliana nalo bila vikwazo vyovyote, sitotetereka tetere kama wafanyavyo wengine wakipata habari ya msiba ugongao moyo kama huu wa UKIMWI. Siwezi kusema taarifa hii haitonisumbua nitakuwa ni muongo, itanisumbua kimawazo lakini naamini baada ya muda nitakaa sawa sitoendelea kutepwereka tepwere la hasha!. Ila kinachonistaajabisha ni kuwa wiki moja kabla hatujataka kufunga ndoa na mke wangu tulipima vipimo vya UKIMWI katika moja ya hospitali kubwa tu ya binafsi hapa jijini Dar es Salaam na majibu tuliyopewa sote tuliyafurahia mimi na mchumba wangu mara tu tulipofahamu kuwa afya zetu ni njema. Sasa hapo ndipo ninapotatizika, ina maana vipimo vyao ni feki au nyie mmekosea? " aliulizwa Shebby swali gumu linalohitaji jibu gumu ili kumkinaisha vilivyo. "Vipimo vyako hata mimi vilinishtua sana, ikabidi nichukue damu upya mimi mwenyewe, kisha niingie maabara mimi mwenyewe kufanya vipimo. Majibu yangu na yale ya awali ya mtaalamu wa maabara yakalingana. Hivyo hospitali mliopima mara ya kwanza unaweza kuta wapo sahihi pia, kwa maana ukipima ukakuta hauna virusi vya UKIMWI unatakiwa urudie tena kupima baada ya kupita miezi mitatu" alimfafanulia vyema ili kumuondoa wasiwasi. Baada ya mazungumzo hayo yaliyogeuka kuwa ya kirafiki zaidi kuliko uadui, Dr.Shaqeel akaagana kwa kupeana mikono na mgonjwa wake kwa kumkabidhi kile kitabu cha kujisomea alichomuahidi. Uzuri wa Shebby kimombo kilikuwa hakimpigi chenga ingawa kaishia darasa la saba pale shule ya msingi Ilala, Boma lakini kukaa kwake muda mwingi na wazungu huko mbugani wakati wa kazi kulimnufaisha vilivyo kuijua lugha kiundani. Shebby akawa anatoka ofisini kwa Dr.Shaqeel huku yupo mnyonge haamini kama matatizo yote yanamuandama yeye, "ama kweli huu ni mwaka wa tabu kwangu" aliwaza Shebby huku akiwa tayari kashatoka nje ya jengo la hospitali, anajiandaa kuliita gari lake limrudishe nyumbani. Mawazo yalimjaa fori fori hajui ashike lipi na aache lipi.
Shebby alikuwa juu ya kitanda chake cha samadari, nje angani giza totoro nyumba nzima akiwa yupo peke yake anagaragara usingizini macho meupe pee hayana hata lepe la usingizi. Alikuwa anabingirika bingiri bingiri na kutangatanga kwenye kitanda kile kama kuku anayetaka kutaga. Barua yake iliyomsababishia kasheshe la kulazwa Agakhan alishaichukua kwenye gari na kuiweka nyumbani. Alipanga kesho yake akishapata staftahi ya asubuhi aisome ajue kuna ujumbe gani mahususi toka kwa Zabibu. "Lo masalala! Itakuwa ndani yake hiyo barua kaeleza chanzo chake cha kujiua. Itakuwa alijiandaa kumbe, akanicheza shere bure mtoto wa mwenziwe. Kesho Inshallah nitajua mbivu na mbichi za tukio zima lililosababisha ndoa yetu ikwame, ikanyorora nyororo" mawazo yalikuwa yanaendelea kumtafuna ila sasa kwa unafuu sio katika hali ya kumtetelesha afya yake. Afanalek! Huu UKIMWI nao mie nimeupataje? tokea nianze mahusiano na kipenzi changu Zabibu katu Yasin mkubwa! naapa sijawahi kuchepuka, Mwenyezi Mungu azizi na baswiru wa kila kitu ni shuhuda wa hilo" mkondo wa mawazo mbalimbali yalikuwa yanatiririka kichwani mwake. "Katika mahusiano yangu na Zabibu tulikuwa na utaratibu wa kupima mara kwa mara afya zetu sasa huyu mdumu kapitia wapi, au ndio uchawi tena wazee wataalamu wa fani ya mduni wamefanya yao dhidi yangu? Hawakupenda nimdhibiti mrembo mkali kama Zabibu wakaamua wanitumie makombora? Au labda umepitia kwenye mashine za kunyolea nywele kwa kinyozi mitaani? Mashine ambazo usafi wake ni tia maji tia maji! " maswali lukuki yasiyo na majibu ndio yalimfanya awe macho mpaka manane ya usiku. Fikra zake hazikutaka kabisa kupeleka tuhuma za kuambukizwa UKIMWI na mpenzi wake Zabibu, kwa sababu alikuwa anamjua fika uaminifu wake kwake ni wa kiwango cha kutukuka. Akaanza kuleta fikra na kumbukizi siku ya kwanza namna walivyokutana na mpenziwe Zabibu. Maana kila wapendanao wana sampuli ya peke yao iliyowakutanisha, kuna wanawake wengine waume zao ni makondakta wa daladala walikutaniana ndani ya daladala wakati wanakoromeana kurudiashiana chenji. Wengine wamefahamiana kwenye mitandao ya kijamii kupitia Facebook, Whatsapp, Instagram na mingineyo. Mbali ya hao, wengine wamekutana kwenye nyumba za ibada ili mradi kila binadamu wapendanao wamekutana kivyao vyao.
"Shebby iko kuja kazi hapa, takiwa wewe peleka warembo kule Saluu, nenda kwa keshia upate njuruku zako" alipewa maelezo Shebby akiwa ndani ya ofisi ya Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya RAJA SAFARI TOURS alikuwa anapewa maagizo na Bosi wake mhindi mwenye kiswahili kibovukibovu utasema amekuja Tanzania wiki iliyopita, kumbe ni mzaliwa wa hapa hapa babu na babu zake. Tatizo la jamii ya kihindi linalowafanya washindwe kuongea kiswahili fasaha ni kujitenga na watu wa ngozi nyeusi, wao daima wanaambatana wao kwa wao. "Sawa nimekuelewa Bosi wangu ondoa shaka nitawafikisha salama Inshallah..." alijibu Shebby huku ananyanyuka kotini kuelekea ofisini kwa mhasibu kupewa masurufu ya safari. "Shebiiiii...iko tahadharisha wewe jiepushe, kaa mbali na hao wanawake..tafadhali tapata tatizo bure" alisikika Bosi mkuu akimuasa vilivyo? kujitenga na kuwatamani hao wateja wake, Shebby akiwa wakati ameshafungua mlango wa kutokea nje. "Ondoa shaka Bosi wangu, rekodi zangu unazijua vizuri, sina uhusiano usiohusu kazi na mteja wangu" alimtoa mashaka Shebby, Bosi wake. "Sawa...mimi aminia wewe ndio maana chagua wewe, safari njema" Bosi akaridhishwa na majibu ya Shebby wakaagana. Ofisi ya uhasibu na ya Mkurugenzi mkuu zilikuwa pua na mdomo, milango yao inatazamana. Alipotoka tu akapiga hatua kama tano tu akafungua mlango wa ofisi ya uhasibu
Nimeambiwa masurufu yangu ya safari yapo tayari! " ilikuwa ni kifungua mazungumzo cha Shebby baada ya kusalimiana na mhasibu mkuu wa kampuni. "Hewala! Upo sahihi, tia saini yako hapa, ni masurufu ya siku tano sawa na shilingi laki tano na milioni moja ya kujaza mafuta ya kwenda na kurudi na tahadhari kwa tatizo lolote litakalotokea huko" akielekeza mhasibu huku anampa kitabu cha kuweka saini ya kuchukua pesa hizo. Shebby akasaini kitabu hicho huku akiwa na furaha sheshe ya kusafiri kuelekea pori. "Unawapeleka warembo waliofanikiwa kuingia fainali za Miss Tanzania kwenye hifadhi ya wanyama ya Selous. Maelekezo yao ni kuwa uwafuate kesho kambini kwao Hyatt Regency, The Kilimanjaro hotel saa 12:00 asubuhi" alimfafanulia hizo pesa ni za shughuli gani. Shebby akawa ametega sikio ndi hataki apitwe na neno huku akiwa amenyamaza zii. "Ok..nimeelewa, kwa maana nikichomoka nao kesho Jumapili, Alhamisi usiku natakiwa niwarudishe jijini sio ndio Kiongozi? " aliuliza swali kutaka uhakika. "Ewaa! Ndio maana yake, maana watapumzika Ijumaa na Jumamosi, Jumapili ndio fainali yenyewe ya walimbwende, ngoma uwanjani! " alitilia tashididi maelekezo yake. Wakaelewana na kuagana. Siku ya siku ikafika msafara wa kuelekea Hifadhi ya Selous na walimbwende wa nchi nzima ukaanza. Msafara ulianzia kambini kwao niliwadamkia asubuhi na mapema, nikawa nawasaidia kuwaingizia mabegi yao kwenye gari. Mbwembwe zao za miondoko yao katika kutembea ilikuwa ni burudani tosha, wapo waliokuwa wanatembea kwa kutetemeka kama upanga uliotiwa tahabibu. Kwa kawaida safari ya mbugani huwa ni safari ndefu na yenye kuchosha lakini uwepo wa visura wale wacheshi na wachangamfu ambao wakikupa tabasamu hata kama ulikuwa na njaa tumbo unalihisi limejaa kwa shibe. Selous ni pori la akiba kubwa kuliko yote nchini Tanzania, pia ni ya pili kwa ukubwa duniani baada ya hifadhi ya Yellowstone iliyopo nchini Marekani. Hifadhi hii ipo katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Eneo hilo la hifadhi ni kubwa kwa makadiro kushinda nchi 70 duniani ikikadiriwa kuwa na eneo sawa na nchi ya Kostarika (Amerika ya Kati) na takribani mara mbili kuliko nchi ya Ubelgiji. Nikiwa fani yangu ni kama dereva na muongoza watalii (tour guide) na mpishi wangu nikiambatana na walimbwende kumi na Matroni wao wawili jumla tukiwa msafara wa watu kumi na nne nikaamua niwafikishe Selous kupitia barabara ya Kibiti-Lindi kwenye lango la Mtemere. Kulikuwa na njia ya mkato ya kupitia Kisarawe yenye umbali wa kama kilomita 150 lakini barabara ilikuwa ni mbovu na ulikuwa ni msimu wa masika, hivyo nikahofia hatari ya kunasa kwenye matope. Tulivyoanza safari walikuwa na mbwembwe na shamrashamra nyingi lakini safari ilivyokolea wengi wao walikuwa wamelala usingizi wa pono. Maajabu ni kuwa mrembo mmoja jina lake Zabibu muda mwingi alikuwa anajisomea kijitabu chake kidogo cha sifa za wanyama mwitu, kuonyesha yupo makini na ziara ile. "Sasa kaka Shebby naskia hifadhi hii inaitwa kiutani shamba la bibi kwanini mpaka imepewa jina hilo? " ilikuwa ni sauti nyororo ya kama ndege zuwaridi toka kwenye kinywa cha Zabibu ilipenya kwenye ngoma za masikio yangu akifanya udadisi. Sauti yake Zabibu na umbile lake vilikuwa vinashabihiana kwa uzuri. Uzuri wa Zabibu hausimuliki wala kuandikika kwenye vitabu ukaumaliza, tosheka tu kujua alikuwa na ngozi laini kama sufi, nyeupe kama mchanga wa peponi yenye kumeremeta hata akiwa kwenye giza totoro la usiku wa maneno, pua yake ya upanga na shingo yake ndefu kama twiga ilimfanya kila mwanaume rijali mwenye kumtupia jicho kwa mara ya kwanza atarudia tena na tena bila kuchoka kumtazama kama ilivyo chovya chovya inavyomaliza buyu la asali"Swali zuri, ni kweli hii hifadhi ya Wanyapori Selous ilijulikana kama shamba la Bibi enzi za wakoloni. Hii ni kutokana na mtawala wa Kijerumani aitwaye Kaiser Wilheim II ambaye alimzawadia mkewe hifadhi hii kama kumbukumbu yake ya kuzaliwa" alijibu Shebby kwa maelezo safi kama msahafu huku sasa wakiwa wameshatembea karibia masaa 6 barabarani umbali wa zaidi ya kilomita 250. "Daah...natamani niuone uzuri wa Selous mpaka wapendanao wanazawadiana, maana kaacha kumpa mbuga ya Serengeti, Manyara, Mikumi, Tarangire na nyinginezo kaamua kumpa Selous kwa vyovyote vile ina kitu Special" alijibu Zabibu, huku wakicheka kwa pamoja. "Lo lo lo! miaka yote kumbe ulikuwa hujui kama Selous ndio baba lao, ila tu bado haijatupiwa jicho la pekee" alikubaliana na mawazo ya Zabibu juu ya uzuri wa hifadhi hiyo. Wakawa ni mwendo wa stori mtindo mmoja kama vile wamejuana kitambo kirefu sana. Sasa warembo wale walianza kuchangamka baada ya kuuona mji wanakaribia kufika. Baada ya muda wa nusu saa tukawasili Behobeho /Cordura Camp ambapo hapo ndipo tulipanga tupate mlo wa mchana, na muda huo ulikuwa ni adhuhuri tayari. Hapo tulikuta wazungu wengi wameshaanza eneo hilo. "Muongozaji hapa pana kitu gani mbona watu wamejaa fori fori?" aliuliza mmoja wa matroni wa warembo wale. "Hapa ndio kuna kaburi la muasisi wa hii hifadhi. Jina limetokana na Mwingereza Frederick Selous aliyekuwa mwindaji wakati wa kuanzishwa kwa ukoloni katika Afrika ya Kusini na Mashariki na ambaye aliuawa katika Tanzania ya leo akiwa mwanajeshi wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia" nilimjibu yule matroni. Tukatelemka wote kasoro Zabibu peke yake alibakia ndani ya gari. "Zabibuu...mbona unatutenga hivyo hutaki kula pamoja na sisi eeh..." nilimtania huku nikimaanisha kweli ashuke tukale wote tayari alishanikamata mawazoni ndi ndi ndi, kila wakati namuwaza yeye na kujiona ni kiumbe mwenye bahati sana kuwahi kuwa karibu na Zabibu. Nikakumbuka methali kule shule ya msingi isemayo Bi Mariamu hana siri, wakimaanisha mapenzi ni kikohozi hayafichiki. "Aah...najisikia nimeshiba, ukila wewe Shebby ndio na mimi nimeshiba tayari" alizungumza kiutani huku akiachia tabasamu pana lililouacha mwanya wake katika meno yake mazuri ukioneka dhahiri shahiri. "Huyu binti ni mrembo wa Shani, akilikosa hilo taji la Miss Tanzania nitajua kweli uchawi upo! " niliwaza kichwani mwangu huku nikimtabiria ushindi mchana kweupe. Tukamuacha Zabibu tukaelekea hotelini kabla ya kuanza rasmi kuzunguka mbugani. Baada ya kumaliza mlo wangu, nikaamua kufungasha chips kavu na kuku wa kukaanga nikamletea Zabibu. "Pori ni pori dada yangu, nimekuletea hivyo ukitaka vitupe lakini nimetimiza wajibu wangu" nilisema kumuambia Zabibu wakati namrushia kifuko cha chakula pale kwenye siti yake alipokaa huku akabaki ananiachia tabasamu moja matata sana huku macho yake makubwa kayalegeza kama mwali amekula kungumanga anasubiria kutambulishwa kwa mchumba wake. Moyo wangu mapigo yake yakawa yanapiga duku duku kama saa mbovu, nguvu ya huba ikawa imeanza kupenya. Nikaanza kumlaani shetani kwa pepesi zake za tashwishi anazozivuvia kwenye moyo wangu. "Shebby unaota ndoto za alinacha mchana kweupe wa jua kali, huyo Zabibu hauna kufu nae, hadhi yake ni kama mwezi angani humfikanii kamwe, huyo atakuwa anamegwa penzi lake na kigogo mkubwa, musharafu katika jamii, achana nae" nilikuwa ninawaza, mawazo yaliyonisaidia kunirudisha kwenye hali yangu ya kawaida nikafutika futi moyoni mwangu tamaa yangu ya mwili kwake. "Ahsante kaka yangu Shebby kwa ukarimu wako ubarikiwe kwa kujali" alishukuru Zabibu kwa zawadi ile ya kipaseli cha kuku na chips kavu. "Usijali, take easy.." alijibu Shebby huku tayari akiwa analiondosha gari sasa wanaitafuta Matobwe umbali wa zaidi ya kilomita 86 mbele yao. Mpishi wangu mzee Shukuru akawa ametingwa na kukata mananasi kwa ajili ya kuwapa Mamiss wale washushie mlo wao kwa matunda. "Naomba ndugu muongoza watalii uwaelezee warembo wangu wanategemea kuona nini pindi wakiwa ndani ya hifadhi katika siku zote tutakazokaa humu ndani?" aliuliza mmoja wa matroni wao huku warembo wale wakiwa wamekaa mkao wa kuniazima masikio yao niwape shule. "Ahsante kwa swali, hifadhi hii ya Wanyamapori ya Selous inasifika kwa kuwa na Mandhari tulivu naya kuvutia (total wilderness). Uoto wa asili wenye mbuga za wazi na uwanda wa miombo umeenea karibu robo tatu ya hifadhi, ukiwa na miti aina ya mitunduru, mininga na milama. Magharibi mwa hifadhi hii kuna mbuga za nyasi pamoja na miti ya mitagalala.Aidha kuna mikoche ambayo inaweza kufikia urefu wa mita 25. Mikoche hiyo huonekana kwa wingi kando kando ya mto Rufiji. Selous ina idadi kubwa ya wanyamapori wa aina mbalimbali hususani, tembo, simba, chui, nyati, nyumbu, pundamilia, ngiri, twiga, fisi, kongoni, pofu, pongo, kuro utepe mweupe, tandala, ndege wa aina mbalimbali zaidi ya spishi zipatazo 450, nyoka wa aina mbalimbali ambao huonekana kwenye misitu na kwenye mito.Viboko na mamba huonekana kwa wingi wakivinjari ndani ya mto Rufiji na kwenye maziwa ndani ya hifadhi. Sifa hizo zimeifanya hifadhi hii tangu mwaka 1982 imeingizwa katika orodha ya UNESCO ya Urithi wa Dunia", nikawapa jibu maridhawa ambalo walikubaliana na maelezo yangu kutokana na uzuri wa mandhari wanayoiona. Maswali yakawa ni bandika bandua sasa ili mradi wakati kiu yao ya utalii. Nilikuwa natembea mwendo mdogo mdogo ili wapate kuishuhudia mandhari kwa uzuri zaidi. Walikuwa visura wale wameshughulishwa na kupiga picha wanyama kwa kamera zao na wengine kwa kutumia simu zao. Hali ikawa si hali ilipofika majira ya alasiri, ghafla bin vuu tembo mkubwa akiwa ameongozana na mtoto wake alikuwa anakuja wangu wangu mbele yetu. "Tafadhalini kaeni kimya, kila mtu aombe kwa imani ya dini yake tupo kwenye hatari, na hamna tena kula mananasi, harufu ya mananasi inawavutia sana tembo" nilitoa amri kama tupo jeshini inayohitaji utekelezaji tu bila kuanza kuhojihoji kwanini.
PICHA CHINI DEREVA SHEBBY AKIWA JUU YA KABURI LA MGUNDUZI WA MBUGA YA SELOUS
Hali ikawa si hali ilipofika majira ya alasiri, ghafla bin vuu tembo mkubwa amekuwa ameongozana na mtoto wake alikuwa anakuja wangu wangu mbele yetu. "Tafadhalini kaeni kimya, kila mtu aombe kwa imani ya dini yake tupo kwenye hatari, na hamna tena kula mananasi, harufu ya mananasi inawavutia sana tembo" nilitoa amri kama tupo jeshini inayohitaji utekelezaji tu bila kuanza kuhojihoji kwanini. Nikaanza kulirudisha gari langu kwa revasi, kinyumenyume huku tembo yule anatufuata bila kuchoka. Wawindaji haramu, waliifanya hifadhi ya Selous kuwa shamba la bibi kweli, kwa kujiwindia tembo, nyati na wanyama wengineo vyovyote wanavyopenda. Udhibiti juu ya majangili hao ulikuwa mgumu kutokana na ukubwa wa hifadhi hiyo iliyokusanya zaidi ya vijiji 89 katika hiyo mikoa minne. Mpaka nilipopata upenyo wa kugeuza gari nikaligeuza haraka haraka na kurejea kule tulipotoka. Wale warembo wote walikuwa wapo kimya, wamepigwa na taharuki ya uoga. Jioni kabisa tukaianza tena safari ya kuelekea kule tunakokukusudia, tukafanikiwa kufika salama kijiji cha Tagalala ambapo hapo ndio ilikuwa kambi yetu tuliyoichagua. Ziara yetu ilikuwa ni yenye kufana sana. Niliwatembeza maeneo tofauti kuanzia maporomoko ya maji ya Stieglers katiika mto Rufiji, ziwa Tagalala, Mnze, Nzelekela, Siwandu, Utunge na Mzizimia na Maji moto ambavyo vyote ni vivutio muhimu kwa utalii na kuvua samaki Sport fishing katika hifadhi ya Wanyamapori Selous. Nikawatembeza
maeneo mengine yanayotumika kwa ajili ya uwindaji wa kitalii. Baadhi ya sehemu za shughuli za utalii wa kuona wanyama (Game viewing), utalii wa kutembea, utalii wa boti. Mpaka ukatimu muda wa kurejea jijini Dar es Salaam. Ila penzi ni kikohozi halijifichi, wenzake na Zabibu walikuwa wameshanizoea wananitania shemeji shemeji. Waliona tuna ukaribu usio wa kawaida kati yangu na Zabibu. Alikuwa kila wakati wa kula chakula lazima awe pembeni yangu, na kwenye kila jambo alikuwa hakubali kuwa mbali na mimi. Siku ya Alhamisi mchana tukaanza msafara wa kurejea Jijini Dar es Salaam, mpaka kufikia majira ya usiku mbichi nikawarejesha kambini kwao. Wakati najiandaa kulitoa gari kwenye maegesho ya Hyatt Regency ili kukirejesha gari langu ofisini nikakabidhi gari. Nikashtukia Zabibu kachomoka kutokea eneo la mapokezi ya hoteli ananifuata, "Shebby......Shebby.....nisubiri pleaaase....! " nilimsikia vizuri nilikuwa bado sijapandisha kioo cha gari upande wa dereva. Nikazima gari kisha nikashuka chini, sikutaka mazungumzo yetu mpishi mzee Shukuru ayasikie maana nae alikuwa mpambe wa Bosi, akifika kazini anaweza kutapika kila kitu bila kusaza kitu. "Shebby.....ahsante kwa ukarimu wako nimefurahia sana safari, ila nakualika kwenye hafla ya fainali ya Miss Tanzania siku ya Jumapili tafadhali usikukose kuja kwako ndio furaha yangu. Nimekuletea hii kuponi ya tiketi utakayoitumia kukaa V. I. P. pale hivyo usipokuja nitakuona tu na utakuwa umeniangusha" alizungumza Zabibu kwa sauti ya kubembeleza huku ameinamisha shingo yake pembeni kwa huruma. " Duuuh....lakini......" alianza kujibu Shebby, "Lakini nini....sitaki kusikia cha lakini,faraja yangu ni kukuona basi, kwaheri" alimkatiza mazungumzo yake Shebby huku akimzuia kuzungumza kwa kidole chake cha shahada. Kisha akaaga haraka haraka kuanza kukimbilia ndani ya hoteli kwani kwa sheria za kambi hakutakiwa kuwa nje ya kambi. Shebby alibaki ameganda kama sanamu la chumvi lililogandishwa, akawa kama kapigwa shoti ya umeme, haamini anachokishuhudia machoni mwake. Zali la mentali la kupendwa na kisura mwenye viwango vyake vya ubora unaokubalika kimataifa. Kisura ambaye hana kasoro kuanzia kwenye unyayo mpaka kichwani kwenye nywele zake. Tofauti na wasichana wa uswazi aliozoea kukimbizana nao kila siku uzuri wao ni wa kutafuta na tochi. "Uswazi kwetu ukimkuta binti ana sura nzuri, basi matiti yake makubwa kama ananyonyesha kambi ya yatima, sio wakamilifu kwenye kila idara kama Zabibu toto la Kitanga" niliwaza nikiwa nimesimama pale pale nje ya gari pembeni kidogo namsindikiza kwa macho Zabibu. Mpaka alipofungua mlango wa hoteli na kunipungia mkono, na mie nikampungia na kurejea kwenye gari kiunyonge kulirejesha ofisini.
Usiku wake siku hiyo ya Alhamisi tulikesha tunatumiana meseji za chombezo zenye ujumbe wa mahaba na Zabibu mpaka manane ya usiku. Sasa ikawa rasmi Zabibu ni mpenzi wangu mpya, ameshaingia kwenye himaya yangu nikaona kama nimeokota embe dodo chini ya mti wa mwarobaini au kama vile nimeokota madini ya lulu pembezoni mwa ufukwe wa bahari. Katika dunia hii kila jambo hutanguliwa na ishara, hata mvua huwa hainyeshi ghafla, utaziona ishara za mawingu. Na huba mwanzowe ni jicho, kisha hufuata maneno matamu matamu ya kunawirisha nyoyo mpaka mnafanya maagano ya kuwa pamoja. Wahenga walituambia, kuwa ukiona zinduna na ambali iko nyuma. Hivyo nilishajiona Zabibu na mimi tutafika mbali sana katika penzi letu. Kama kanikubali nikiwa kapuku, kipato cha wastani huku akiwatolea mbavuni vigogo wenye pesa sufufu na madaraka yao, akaamua kunichagua mimi ninayeganga maisha, kweli amenipenda kwa dhati furaha ya kweli inakuja katika maisha yangu.
Usiku wa fainali za Shindano la Miss Tanzania ukawadia lilofanyika usiku wa Jumapili yake na kushuhudia Queen Zabibu Shamsi Sakuzindwa kuibuka na ushindi katika mashindano hayo na kutawazwa rasmi kuwa ni Miss Tanzania.
Tukio hilo nalikumbuka vizuri sana kama vile ninashuhudia jua la utosini la saa 6 mchana.
Ilikuwa ni Jumapili ya usiku mbichi kuanzia saa 1:30 usiku, washabiki walianza kumiminika katika ukumbi maarufu kwa burudani wa Mlimani City Hall. Watanzania wengi walitamani kuhudhuria siku hiyo ila viingilio vilikuwa ni vya bei ya kupaa. Wale wenye vipato vya pangu pakavu tia mchuzi hapa, ikabidi wakabaki majumbani mwao wanafuatilia kwenye runinga zao huku wanalaumu kuwa Kamati ya Miss Tanzania imeweka mbele tamaa ya pesa kwa kuweka kiingilio cha fainali hizo kuwa ni kati ya shilingi 100,000 na 200,000, kiasi ambacho ni kikubwa mno kwa Mtanzania wa kawaida. Mpaka kufika saa 2:00 usiku, ukumbi ukawa umejaa pomoni hamna hata pa kutema mate. Mimi niliwasili ukumbini mapema kidogo ingawa nilipata rabsharabsha za hapa na pale. Walinzi wa ukumbi na wakaguzi wa tiketi hawakuamini kama ni tiketi yangu kweli ile inayoniruhusu kwenda kukaa viti vya V. I. P. maana viti hivyo vilitawaliwa na mawaziri, wafanyabiashara wakubwa na watu mukhtari wenye wadhifa wao katika nchi za Watanzania. Na kila wakati kamera za waandishi wa habari zilikuwa zinawamurika watu wao wenye sharafu zao. Mwanzoni wakahisi labda nimemuibia mtu au nimeokota hiyo tiketi. "Kijana sema ukweli wako ni yako kweli au umeiokota? Usije pata matatizo bure mwenyewe akifika! " aliniuliza mmoja wa wakaguzi huku ananikazia macho. "Ni tiketi yangu kabisa, wewe kazi yako ni ukaguzi wa uhalali wa tiketi, usiingilie undani wa mtu! ' nilimjibu kwa ufedhuli,maana dawa ya moto ni moto. "Achana nae Bwana mruhusu, pesa za siku hizi hazina adabu, tofauti na pesa ya zamani ilikuwa ina watu na ukoo maalumu" alizungumza mkaguzi mwenzake aliyeonyesha busara kubwa. Ndipo nikaruhusiwa kupita mlango maalumu wa V. I. P. Tayari mashindano hayo yalishanitumbukia nyongo kwa dharau niliyoonyeshwa mlangoni, nusura nifanye maamuzi magumu ya kurudi zangu maskani. Ila nikawa namfikiria mpenzi wangu Zabibu nitamuumiza vibaya sana, hasa ukichukulia wenzake wote tiketi zao waliwapa familia zao ili waje kuwatia hamasa ya ushindi pindi wakiwaona, ila yeye Zabibu kaamua tiketi yake anitunuku mimi nije kumtia nguvu akiwa jukwaani. Nilipokaa kwenye eneo hilo la viti vya V. I. P nilikuwa mdogo kama kidonge cha piritoni, maana nilizungukwa na vigogo kila pande yangu ya shimaali, yamiini, mbele na nyuma yangu. Maongezi yao yalikuwa ni ya biashara kubwa kubwa za bilioni za pesa, nikabaki nimebung'aa tu nakodoa macho,nabaki nachezea simu yangu Tekno ya Mchina, ikabidi na sauti niipunguze kabisa, isije kuita mbele yao nikawasumbua wanene wa nchi. "Kijana changamkieni fursa za biashara, leo ofisini kwangu zimekuja kampuni za kutoka Uarabuni, Saudi-arabia na Qatar wanahitaji mbuzi wenye thamani ya bilioni 50 kwa mwezi, kama unaweza kuchangamkia hiyo fursa tuonane kesho ofisini" alinizungumzusha waziri wa biashara huku akinikabidhi kadi yenye mawasiliano yake. Nikaipokea na kubaki najilazimisha kutabasamu. Maana nilikuwa naona kama ananichezea shere, ananieleza fursa za mabilioni ya pesa wakati ndio kwanza nimenunua kagari cha biashara ya taksi- UBBER cha mkopo kazini kwa dhamana ya nyumba ya familia. Mambo yalimuendea sheshe mpenzi wangu Zabibu, akafanikiwa kuingia kwenye tano bora ya wale wanaowania taji hilo. Minong'ono ya Mapredeshee niliokaa nao jirani nao, ilinivunja nguvu kabisa ya kufanya mahusiano ya kwelikweli na Zabibu. Nilipanga nikitoka pale ukumbini namtumia meseji kuwa mimi na yeye mahusiano yetu yafe. Ilihitaji roho ya paka kuweza kuvumilia njama zilizokuwa zinapangwa na wale vigogo bila kujua kuwa Zabibu ni mpenzi wangu." Huyu mrefu kuliko wote mwenye jina tamu kama zabibu zenyewe huyu wangu. Nakula nae sahani moja, nampa mkataba wa kutangaza bidhaa za kampuni yangu, safari za China nyingiii naenda kumla huko huko ha...ha..ha..." alizungumza tajiri mmoja mwarabu mwenye kampuni ya kuuza vifaa vya umeme vya majumbani. "Ha.. ha.. ha..mwenye kisu kikali ndio atakula nyama, mie nataka nitafune wote hawa tano bora kabla hawajachakaa maana mashindano ya mwakani vinakuja vipuri vipya vyenye kilomita sifuri" akachagiza mwenzake huku wanapongezana kwa ujinga wao kwa kugongesheana glasi ya vinywaji vyao. Aheri nivunje nae uhusiano kabla sijafika nae mbali huyu Zabibu ni bahari kubwa anagombewa na watu wazito. Ikafika kipindi cha maswali kila mrembo anachagua swali la kujibu, kati ya linalohusu sekta ya afya, utalii, haki za watoto na akina mama, ajira kwa vijana na uchumi wa nchi. Zabibu akachagua swali la masuala ya utalii, ambapo aliulizwa kama angekuwa waziri wa utalii angefanya mbinu gani ili kupandisha idadi ya watalii wanaoitembelea nchi yetu?. Akalijibu kiufasaha mkubwa swali hilo ukumbi mzima ulisimama huku unapiga makofi kuashiria kawabwaga wenzake vibaya sana. Muda ukafika wa kumtangaza mshindi wa taji hilo baada ya kujumlisha idadi ya kura toka kwa majaji watano. Mshereheshaji wa sherehe akamtangaza Zabibu Shamsi kuwa ndio mshindi wa taji hilo la Miss Tanzania kwa mwaka huo. Ukumbi mzima ukaripuka kwa mayowe, shangwe na vigeregere kuonyesha wamekubaliana na na maamuzi ya majaji hamna upendeleo wowote uliofanyika. Zabibu alikuwa na furaha isiyomithilika mpaka akawa anamwaga machozi ya furaha, huku wale Mapredeshee wanahangaika kuwatafuta waandaaji wa mashindano hayo kwa malengo ya kunasa namba za simu za warembo hao. Zabibu akafanya tukio ambalo lilinipaisha ukumbi mzima na kila mtu kujiuliza mimi ni nani katika jamii mpaka nimeopoa mlimbwende wa nchi kama yule. Kabla hajavikwa taji lake la kichwani na mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Naibu Waziri Mkuu wa nchi. Alichomoka kule stejini na kuja mpaka pale nilipokaa mimi akaninyanyua kitini na kunikumbatia kwa furaha. "Ahsante Honey...kwa kuja, sikutegemea kama utakuja kunitia nguvu, pia nashukuru sana maelezo yako mazuri kule kwenye hifadhi ya Selous ndio yameniwezesha kujibu swali la masuala ya utalii kiufasaha mkubwa, bila wewe hili taji nisingelipata. Usiniache usiku huu naondoka na wewe Mwaaaaah....Mwaaaah...!" alininong'oneza sikio kisha akanipa mabusu mawili motomoto ya shavuni kisha akaniachia na kurudi stejini. Macho ya ukumbi mzima yakawa yamenigeukia mimi, huku vyombo vya habari nao wakiwa ndio wamepata habari ya kuandika, wakinimulika na kamera zao. Mgeni rasmi akamkabidhi zawadi yake ya gari aina ya 'Toyota Highlander New Model'. Baada ya hapo akaanza kuhojiwa na vyombo vya habari mubashara anaonekana Tanzania nzima.
Mbele ya wafanyakazi wenzangu nilijipiga kibobwe nikajifanya sijali kufukuzwa, lakini nilipotoka nje ya jengo la RAJA SAFARI TOURS na kukanyaga tu lami ya barabarani machozi yakaanza kunimwagika kwa uonevu niliofanyiwa. Nikafanikiwa kupata daladala ya kuelekea nyumbani Mwembechai, lakini kimwili nilikuwa ndani ya daladala ila kimawazo nilikuwa nipo kwenye nyumba ya familia Kariakoo, ninawaza hali itakavyokuwa siku ya mnada hapo kesho, jinsi dalali atakavyokuwa anatamba kwa mbwembwe, huku akijitawanya kwa mapana na marefu na kipaza sauti chake. "Milioni 7 mara ya kwanza, milioni 7 mara ya pili, milioni 7 mara ya tatu....tooop top..! , ameshinda mpeni nyumba yake, hongera sana kalipie kwa keshia asilimia 25% zako" . Nikawa navuta taswira jinsi mama yangu, ambaye ni kikongwe atakavyokuwa anatoa machozi kwa kujutia kwanini alikubali kunipa hati ya nyumba kwenda kukopea, huku ndugu zangu wakinilalamikia kwa kuwasababishia nyumba yao ipigwe shoka. Ilifika hatua nikawa natamani baragumu la siku ya kiama lipulizwe muda huo huo ili dunia iwe ndio mwisho niepuke fedheha iliyopo usoni mwangu. Mbona mimi sina tabia nzito kama zamani sasa ni mtu mwema ninayeweza kusuhubiana na mtu yoyote, lakini yule ponjoro nimemkosea nini lakini, ya rabi stara!. Sina roho choko, naridhika na kile ninacholipwa sijawahi hata kupiga nyoka mafuta ya gari kama wafanyavyo madereva wasio waaminifu" mawazo yaliendelea kujikita mizizi akilini mwangu. "Mwembechai washukajii piga chiniii....Mwembechai waendaji choma ndani..." nilishtuliwa kutoka kwenye dimbwi hilo la mawazo na sauti ya mvumo wa radi ya kukwaruza ya kondakta wa daladala ile. Ndipo nikatanabahi kuwa nimeshafika maeneo ya nyumbani kwangu. Nikajizoazoa hima hima toka kitini na kuharakia mlangoni kabla daladala halijaondoka. Nikavuka barabara bila hata kuangalia vizuri magari yanayopita kwa kasi, nusra nigongwe na lori la kusambaza bidhaa madukani. "Wewe mshambaaa....utakufaaa, ndio nyie mliokuja mjini kwa mbio za mwenge" niliporomoshewa maneno ya kejeli ya kila sampuli na walimwengu wasio na hata chembe ya huruma. "W-houf...!" nilishusha pumzi ndefu sikuwajibu kitu zaidi ya kumshukuru Rabana kwa kuniepusha na ajali ya asubuhi asubuhi, nilikuwa nimepatwa na pumbao la nafsi sijielewi. Laiti wangeingia kichwani mwangu na kukuta mambo yalivyo tumbi tumbi wasingenihukumu kwa kosa za uzembe barabarani. Yalikuwa ni makosa yangu kushuka bila kuchukua tahadhari kwa umakini lakini hiyo yote ilitokana na mazonge kichwani ya kufukuzwa kazi. Nikawa ninawaza Jiji hili lilivyo gumu kuishi bila kazi sijui maisha yatakuwaje!."Hivi tu mtu utakuta ana ajira lakini maisha yake vuru vuru sasa sembuse upo benchi apeche alolo huingizi hata senti tano nyeusi!" bado lundo la mawazo lilikuwa limetawala kichwani mwake. Nilipokuwa nakaribia kufika nyumbani nikaona mtiti wa akina mama nyumbani kwangu nilipopanga, mpaka nikadhania labda ni msiba. Walikuwa wamejikalia kibarazani pote sambejambe bila nidhamu wala taadhima. Ikabidi nichepuke kidogo kwenye kiduka cha Mangi nyumba ya jirani nijitie nakunywa soda ili niyasome mazingira kunani pale nyumbani. Ndipo nikawasikia mazungumzo yao waziwazi kumbe yalikuwa ni vijembe tu dhidi yangu na Zeddy wangu. "Mama Sele nakuambia huyu mzaramo mwenzako ametushinda tabia, mchawi kabisaa kamuendea kwa kalumanzila binti wa watu mpaka amezuzuka zuzu, haiwezekani Miss Tanzania wetu jana tumekesha tunamshangilia kwenye runinga leo aje kuamkia usingizini kwenye mabanda yetu haya ya uswahili tena analishwa misumari akitoboko utumbo akatutie aibu huko Miss World ha ha haaaaa...hoi.. hoi.. hoi.. hallo.. hallo.. ya dagaa kauzu kwa teeembeleee" alizungumza mama mmoja wapo mpangaji mwenzangu ambaye nilikuwa namheshimu sana, nilijua ni jirani wa huba na hawa, kumbe jirani mnafiki sikutegemea abadaan kataan kama ipo siku atanisengenya na kunikebehi nyuma ya mgongo wangu." Mie kuhemwa naona mrembo anakuja kibarazani kwangu chaka chaka kupima mkaa wa kikopo, kumbe ndio mchumba wa Shebby..sasa atatulizana maana walikuwa wanakuja wanawake wa kila sampuli yeye ni zoa zoa tu. Ila yatamkuta mambo hao Mamiss wanahitaji matunzo hana pesa za kumuengaenga binti mrembo kama yule" alizungumza maneno ya uwongo, uzandiki na uzushi mtupu mama Sele kuwa mimi ni mpenda vidosho wakati hasha lillahi! sipo hivyo. Walizama kwenye porojo zao za hamrere hamrere, bandika bandua ili mradi baraza lao la umbea lilichachamaa kwa vijembe. Nikachomoka pale dukani kwa Mangi kwa kasi huku nikiwa na soda yangu mkononi na kuwapita kwa kupasua kati kati yao bila salamu yoyote kwao. Kwa ghaidi nilizokuwa nazo, ningewakwapua mikwaju laiti angethubutu mmoja wao kujishaua kunisalimia. Wakabaki wameduwaa,wameshukwa na nyuso zao, wamenitumbulia macho kwa uoga utasema wanaaga maiti. Hawakutegemea kuniona wakati ule kurudi nyumbani. Walijua fika kuwa nimewasikia kila kitu walichosema, maana walimuona mtu amesimama pale dukani kawapa mgongo ila hawakujua kama ndio mimi. Wakatawanyika kla mmoja akashika njia yake anayoijua mwenyewe. Siku zote mwisho wa ubaya ni aibu na fedheha isiyobebeka machoni mwa waja. Namshukuru Mwenyezi Mungu alinipa stahamala ya uvumilivu ningewashushia kipigo ningekuwa nimepanda kimbunga kwa lengo kuvuna tufani"Hodii ngo ngo ngo Hodii ngo ngo ngo," nilibisha hodi mlango wa kuingia kwenye chumba changu. Zabibu alikuwa ametulizana chumbani Anachambua dagaa kauzu wa Mwanza raha mustarehe kama sultan bin Jerehe habari hana huku anaangalia vipindi vya televisheni. "Oooh..! Waaaoh baby huyoo, karibu tena " alikurupuka na kufungua mlango Zabibu na kunikaribisha ndani. Alikuwa amevalia jezi zangu za timu ya Chelsea na trakisuti yake maana hakuwa na nguo za kubadilisha. "Ahsante my love, umeshindaje lakini" nilijikaza kisabuni kwa kujibu salamu yake kiuchangamfu." Mbona hunisifii nimetinga jezi za vijana wa darajani au sijapendezaa?" alijilalamisha kwa kudeka huku anajigeuzageuza mwili wake kimadoido. "Oooh! Sorry baby nimesahau mawazo mengi , bundi analia....upande wangu. " nikajibu kwa ufupi na kwenda mubashara kukaa pwetepwete kwenye kochi mojawapo kisha nikaendelea kumpa ufafanuzi . "Mambo hamkani si shwari tena!, nimefukuzwa kazi bila utetezi wowote". Nikawa nimejiinamia kwa kushika tama mashavuni mwangu nimeishiwa mipango sina alifu wala bee, kilichokuwa kinanitesa zaidi suala la nyumba ya familia basi hamna kingine. Hasa nikikumbuka nilianza maisha ya ununda ya kutoroka nyumbani na kurejea tokea nikiwa darasa la saba, hivyo suala la ajira haikuwa shida kubwa sana, tatizo sasa lilikuwa kwenye mnada. "Beeebi...umefukuzwa kwa kosa gani, mbona kama ujio wangu kwenye maisha yako kumefungua balaa, nuksi na fali mbaya kwako nisamehe bebiiii.....sio kosa langu ni kosa la moyo wangu kukupenda" akawa Zabibu ameingiwa na kimuyemuye huku akaanza kuangusha kilio cha kwi kwi, huku ananipigia magoti. "Acha dhana za kufikirika hizo my love!, mie tatizo langu linaloniny'ong'onyesha ni mkopo wa lile gari langu ninalolifanya UBBER, nimeambiwa mpaka kesho saa 4:00 niwe nimerejesha la sivyo nyumba ya familia kule Kariakoo inapigwa mnada, hicho ndicho kinaninyima raha mpenzi wangu!" nilijikaza kuzungumza baada ya kuona mpenzi wake kumbe nae ni moyo wa wake ni nyumba ya udongo hauwezi kuhimili vishindo. "Kuna kitu nimekumbuka mpenzi wangu ngoja nimeagizia begi la nguo zangu toka kwa shoga yangu, mchana nina kipindi chuo usiku nitakuja tena kukupa jibu kama ninaweza kukusaidia au laah!" alipata ujasiri wa ghafla Zeddy akafuta machozi yake na kunipa matumaini ya msaada. "Kweli mpenzi wangu Zabibu alinisaidia kwa hali na mali nyumba ya familia haikuuzwa" nilikuwa ninanong'ona kwa sauti ya chini huku usingizi ukinivamia kwa nguvu bila huruma, haukutaka usingizi huo kuniacha niendelee kumaliza kumbukizi zangu zote za maisha ya misukosuko, yenye milima na mabonde niliyoyapitia na mchumba wangu Zabibu tokea nakutana nae mpaka anachukua maamuzi ya kujitoa uhai wake.
Shebby alikuwa yupo katika ofisi za Mkurugenzi wa Kampuni ya Firdaus Trading and Shipping LTD zilizopo barabara ya Kawawa nyuma ya majengo ya Chuo Kikuu Huria. Ofisi hizo zilikuwa zinajishughulisha na biashara ya mbalimbali ikiwemo ya kuuza na kununua madini ndani na nje ya nchi. Ilikuwa inamilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania Bwana Nadeem Massawe. Lengo, madhumuni na nia ya kukanyaga ofisi hizo lilikuwa ni kutaka kuonana uso kwa uso na mkurugenzi mkuu huyo wa kampuni bwana Nadeem. Ugumu sasa ulikuwepo kwenye kuonana nae bwana mkubwa huyo. Mara nyingi shida za wenye kutaka kuonana nae zilimalizwa na wasaidizi wake. Hakuwa mtu wa kujichanganya na watu wala vyombo vya habari. Watanzania wengi walikuwa wanamjua kwa matendo yake mema kwa jamii lakini hawamjui kwa sura. "Kuna nini mbona watu wamejazana hapa chini" lilikuwa ni swali la kwanza kuuliza Shebby baada ya kuwasili ndani ya uwanja uliozungukwa na geti, uwanja ambao ndani yake kulikuwa na majengo pacha ya roshani 10. "Wewe itakuwa mgeni hapa eeh..! Hapa hali ipo hivi karibia mwaka wa tatu, kila ikifika siku ya Ijumaa, siku ya ibada kwa waumini wa kiislamu, bwana mkubwa huyu Mwenyezi Mungu amuingize peponi huwa na tabia ya kutoa sadaka kwa mafukara, masikini, yatima na wajane" alijibu mmoja wa watu wazoefu wa mazingira yale. "Kupata tajiri mwenye uchamungu kama huyu ni nadra sana, Allah amlinde na amkuzie mali zake, amuepushe na husuda za mahasidi-Amiiin..." mzee mmoja wa makamo alishadidia mazungumzo hayo huku mkononi akiwa amefumbata burungutu la pesa kuonyesha tayari kashapata kamgao chake. Shebby alikuwa anachekea tumboni kimoyomoyo alivyosikia Nadeem anasifiwa uchajimungu. Kwa umati ule wa watu, Shebby akaona itakuwa ngumu kuonana nae bwana Nadeem. Inasemekana watu huanza kufurika hapo kuanzia manane ya usiku kupanga foleni, nae Mkurugenzi mwenyewe anawasili baada ya kusali swala ya Alfajiri. "Kwa hiyo siwezi kumuona Kabisa kwa leo? " aliuliza Shebby akiwa ameshaanza kukata tamaa, hasa ukichukulia kuzipata zilipo ofisi hizo imemchukua karibia siku tatu kudodosadodosa. "Siku zingine rahisi kumpata ni siku za Jumatatu na Alhamisi, siku hizo anarudi nyumbani kwake mapema sana kwa sababu anafunga swaumu za sunnah hivyo anawahi kufuturu" alisema mmoja wa wasimamia usalama wa eneo lile. Shebby akaondoka eneo lile kiunyonge huku akiwaza na kuwazua jinsi atakavyojipenyeza mpaka afanikiwe kumuona. Wakati anataka kuondoka akapata mawazo mapya, "leo ni siku ya Ijumaa kwa vyovyote ataende msikitini kuswali pindi atakaporudi nitamvizia kwenye lifti nipande nae hapo ndio nitatapika dukuduku langu kwake. Barua iliyoachwa na marehemu Zabibu ndio iliyompelekea Shebby kuwa na uhitaji wa kuonana na Kibosile Nadeem. Akajibanza kwenye moja ya mahema yaliyojengwa kwa ajili ya kupumzikia wageni wanaotembelea eneo hilo. Akiwa pale anasomasoma magazeti aliyokuwa ameyanunua siku hiyo akamuona kwa mbali Kibosile Nadeem akiwa na mlinzi wake binafsi anapanda gari kuondoka eneo lile la maegesho, akatabasamu, alipoangalia saa yake ya mkononi ilikuwa ni saa 6:00 kamili mchana, akajua sasa lazima tu atakuwa anaelekea msikitini kuswali swala ya Ijumaa. Shebby alikuwa ni tariku swala, msikitini kwake ni kama kituo cha polisi, mara ya mwisho ni siku aliyotaka kumuona Zabibu. Alikuwa hajali cha siku ya Ijumaa, wala mwezi wa ramadhani wala sikukuu ya Eid alikuwa na mzio mkubwa na msikiti. Maisha yake ya kushinda mbugani na wanyama, nae kulimfanya awe kama hayawani hajali mambo ya ibada. Mpaka kufika majira ya alasiri, Bwana Nadeem alikuwa bado hajatia mguu ofisini kwake. Shebby akaanza kuwa na wasiwasi huenda ndio kakitoa kimoja hatorudi ofisini. Pesa ziliendelea kutolewa kwa wenye mahitaji maalumu na wasaidizi wake. Ilipofika majira ya saa 11:00 jioni akakata tamaa kabisa ya kuonana nae kabisa. Akanyanyuka kwenye kiti na bahasha yake ya kaki mkononi na magazeti yake akijongea getini tayari kwa kuondoka eneo lile akajipange upya. Hakupiga hata hatua tano akasikia mvumo wa gari la Bwana Nadeem linataka kuingia kwenye jengo lile. Chapuchapu Shebby akabadili uelekeo na kwenda kwenye moja kwa moja kwenye jengo la ofisi kwa ajili ya kumvizia kwenye lifti." Kijana mbona umesimama hapo kwenye lifti muda mrefu kulikoni? " walikuja wana usalama wawili wakimzongazonga Shebby baada ya kumuona kwenye kamera za ulinzi za jengo.
Mbele ya wafanyakazi wenzangu nilijipiga kibobwe nikajifanya sijali kufukuzwa, lakini nilipotoka nje ya jengo la RAJA SAFARI TOURS na kukanyaga tuwlami ya barabarani machozi yakaanza kunimwagika kwa uonevu niliofanyiwa. Nikafanikiwa kupata daladala ya kuelekea nyumbani Mwembechai, lakini kimwili nilikuwa ndani ya daladala ila kimawazo nilikuwa nipo kwenye nyumba ya familia Kariakoo, ninawaza hali itakavyokuwa siku ya mnada hapo kesho, jinsi dalali atakavyokuwa anatamba kwa mbwembwe, huku akijitawanya kwa mapana na marefu na kipaza sauti chake. "Milioni 7 mara ya kwanza, milioni 7 mara ya pili, milioni 7 mara ya tatu....tooop top..! , ameshinda mpeni nyumba yake, hongera sana kalipie kwa keshia asilimia 25% zako" . Nikawa navuta taswira jinsi mama yangu, ambaye ni kikongwe atakavyokuwa anatoa machozi kwa kujutia kwanini alikubali kunipa hati ya nyumba kwenda kukopea, huku ndugu zangu wakinilalamikia kwa kuwasababishia nyumba yao ipigwe shoka. Ilifika hatua nikawa natamani baragumu la siku ya kiama lipulizwe muda huo huo ili dunia iwe ndio mwisho niepuke fedheha iliyopo usoni mwangu. Mbona mimi sina tabia nzito kama zamani sasa ni mtu mwema ninayeweza kusuhubiana na mtu yoyote, lakini yule ponjoro nimemkosea nini lakini, ya rabi stara!. Sina roho choko, naridhika na kile ninacholipwa sijawahi hata kupiga nyoka mafuta ya gari kama wafanyavyo madereva wasio waaminifu" mawazo yaliendelea kujikita mizizi akilini mwangu. "Mwembechai washukajii piga chiniii....Mwembechai waendaji choma ndani..." nilishtuliwa kutoka kwenye dimbwi hilo la mawazo na sauti ya mvumo wa radi ya kukwaruza ya kondakta wa daladala ile. Ndipo nikatanabahi kuwa nimeshafika maeneo ya nyumbani kwangu. Nikajizoazoa hima hima toka kitini na kuharakia mlangoni kabla daladala halijaondoka. Nikavuka barabara bila hata kuangalia vizuri magari yanayopita kwa kasi, nusra nigongwe na lori la kusambaza bidhaa madukani. "Wewe mshambaaa....utakufaaa, ndio nyie mliokuja mjini kwa mbio za mwenge" niliporomoshewa maneno ya kejeli ya kila sampuli na walimwengu wasio na hata chembe ya huruma. "W-houf...!" nilishusha pumzi ndefu sikuwajibu kitu zaidi ya kumshukuru Rabana kwa kuniepusha na ajali ya asubuhi asubuhi, nilikuwa nimepatwa na pumbao la nafsi sijielewi. Laiti wangeingia kichwani mwangu na kukuta mambo yalivyo tumbi tumbi wasingenihukumu kwa kosa za uzembe barabarani. Yalikuwa ni makosa yangu kushuka bila kuchukua tahadhari kwa umakini lakini hiyo yote ilitokana na mazonge kichwani ya kufukuzwa kazi. Nikawa ninawaza Jiji hili lilivyo gumu kuishi bila kazi sijui maisha yatakuwaje!."Hivi tu mtu utakuta ana ajira lakini maisha yake vuru vuru sasa sembuse upo benchi apeche alolo huingizi hata senti tano nyeusi!" bado lundo la mawazo lilikuwa limetawala kichwani mwake. Nilipokuwa nakaribia kufika nyumbani nikaona mtiti wa akina mama nyumbani kwangu nilipopanga, mpaka nikadhania labda ni msiba. Walikuwa wamejikalia kibarazani pote sambejambe bila nidhamu wala taadhima. Ikabidi nichepuke kidogo kwenye kiduka cha Mangi nyumba ya jirani nijitie nakunywa soda ili niyasome mazingira kunani pale nyumbani. Ndipo nikawasikia mazungumzo yao waziwazi kumbe yalikuwa ni vijembe tu dhidi yangu na Zeddy wangu. "Mama Sele nakuambia huyu mzaramo mwenzako ametushinda tabia, mchawi kabisaa kamuendea kwa kalumanzila binti wa watu mpaka amezuzuka zuzu, haiwezekani Miss Tanzania wetu jana tumekesha tunamshangilia kwenye runinga leo aje kuamkia usingizini kwenye mabanda yetu haya ya uswahili tena analishwa misumari akitoboko utumbo akatutie aibu huko Miss World ha ha haaaaa...hoi.. hoi.. hoi.. hallo.. hallo.. ya dagaa kauzu kwa teeembeleee" alizungumza mama mmoja wapo mpangaji mwenzangu ambaye nilikuwa namheshimu sana, nilijua ni jirani wa huba na hawa, kumbe jirani mnafiki sikutegemea abadaan kataan kama ipo siku atanisengenya na kunikebehi nyuma ya mgongo wangu." Mie kuhemwa naona mrembo anakuja kibarazani kwangu chaka chaka kupima mkaa wa kikopo, kumbe ndio mchumba wa Shebby..sasa atatulizana maana walikuwa wanakuja wanawake wa kila sampuli yeye ni zoa zoa tu. Ila yatamkuta mambo hao Mamiss wanahitaji matunzo hana pesa za kumuengaenga binti mrembo kama yule" alizungumza maneno ya uwongo, uzandiki na uzushi mtupu mama Sele kuwa mimi ni mpenda vidosho wakati hasha lillahi! sipo hivyo. Walizama kwenye porojo zao za hamrere hamrere, bandika bandua ili mradi baraza lao la umbea lilichachamaa kwa vijembe. Nikachomoka pale dukani kwa Mangi kwa kasi huku nikiwa na soda yangu mkononi na kuwapita kwa kupasua kati kati yao bila salamu yoyote kwao. Kwa ghaidi nilizokuwa nazo, ningewakwapua mikwaju laiti angethubutu mmoja wao kujishaua kunisalimia. Wakabaki wameduwaa,wameshukwa na nyuso zao, wamenitumbulia macho kwa uoga utasema wanaaga maiti. Hawakutegemea kuniona wakati ule kurudi nyumbani. Walijua fika kuwa nimewasikia kila kitu walichosema, maana walimuona mtu amesimama pale dukani kawapa mgongo ila hawakujua kama ndio mimi. Wakatawanyika kla mmoja akashika njia yake anayoijua mwenyewe. Siku zote mwisho wa ubaya ni aibu na fedheha isiyobebeka machoni mwa waja. Namshukuru Mwenyezi Mungu alinipa stahamala ya uvumilivu ningewashushia kipigo ningekuwa nimepanda kimbunga kwa lengo kuvuna tufani"Hodii ngo ngo ngo Hodii ngo ngo ngo," nilibisha hodi mlango wa kuingia kwenye chumba changu. Zabibu alikuwa ametulizana chumbani Anachambua dagaa kauzu wa Mwanza raha mustarehe kama sultan bin Jerehe habari hana huku anaangalia vipindi vya televisheni. "Oooh..! Waaaoh baby huyoo, karibu tena " alikurupuka na kufungua mlango Zabibu na kunikaribisha ndani. Alikuwa amevalia jezi zangu za timu ya Chelsea na trakisuti yake maana hakuwa na nguo za kubadilisha. "Ahsante my love, umeshindaje lakini" nilijikaza kisabuni kwa kujibu salamu yake kiuchangamfu." Mbona hunisifii nimetinga jezi za vijana wa darajani au sijapendezaa?" alijilalamisha kwa kudeka huku anajigeuzageuza mwili wake kimadoido. "Oooh! Sorry baby nimesahau mawazo mengi , bundi analia....upande wangu. " nikajibu kwa ufupi na kwenda mubashara kukaa pwetepwete kwenye kochi mojawapo kisha nikaendelea kumpa ufafanuzi . "Mambo hamkani si shwari tena!, nimefukuzwa kazi bila utetezi wowote". Nikawa nimejiinamia kwa kushika tama mashavuni mwangu nimeishiwa mipango sina alifu wala bee, kilichokuwa kinanitesa zaidi suala la nyumba ya familia basi hamna kingine. Hasa nikikumbuka nilianza maisha ya ununda ya kutoroka nyumbani na kurejea tokea nikiwa darasa la saba, hivyo suala la ajira haikuwa shida kubwa sana, tatizo sasa lilikuwa kwenye mnada. "Beeebi...umefukuzwa kwa kosa gani, mbona kama ujio wangu kwenye maisha yako kumefungua balaa, nuksi na fali mbaya kwako nisamehe bebiiii.....sio kosa langu ni kosa la moyo wangu kukupenda" akawa Zabibu ameingiwa na kimuyemuye huku akaanza kuangusha kilio cha kwi kwi, huku ananipigia magoti. "Acha dhana za kufikirika hizo my love!, mie tatizo langu linaloniny'ong'onyesha ni mkopo wa lile gari langu ninalolifanya UBBER, nimeambiwa mpaka kesho saa 4:00 niwe nimerejesha la sivyo nyumba ya familia kule Kariakoo inapigwa mnada, hicho ndicho kinaninyima raha mpenzi wangu!" nilijikaza kuzungumza baada ya kuona mpenzi wake kumbe nae ni moyo wa wake ni nyumba ya udongo hauwezi kuhimili vishindo. "Kuna kitu nimekumbuka mpenzi wangu ngoja nimeagizia begi la nguo zangu toka kwa shoga yangu, mchana nina kipindi chuo usiku nitakuja tena kukupa jibu kama ninaweza kukusaidia au laah!" alipata ujasiri wa ghafla Zeddy akafuta machozi yake na kunipa matumaini ya msaada. "Kweli mpenzi wangu Zabibu alinisaidia kwa hali na mali nyumba ya familia haikuuzwa" nilikuwa ninanong'ona kwa sauti ya chini huku usingizi ukinivamia kwa nguvu bila huruma, haukutaka usingizi huo kuniacha niendelee kumaliza kumbukizi zangu zote za maisha ya misukosuko, yenye milima na mabonde niliyoyapitia na mchumba wangu Zabibu tokea nakutana nae mpaka anachukua maamuzi ya kujitoa uhai wake.
Shebby alikuwa yupo katika ofisi za Mkurugenzi wa Kampuni ya Firdaus Trading and Shipping LTD zilizopo barabara ya Kawawa nyuma ya majengo ya Chuo Kikuu Huria. Ofisi hizo zilikuwa zinajishughulisha na biashara ya mbalimbali ikiwemo ya kuuza na kununua madini ndani na nje ya nchi. Ilikuwa inamilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania Bwana Nadeem Massawe. Lengo, madhumuni na nia ya kukanyaga ofisi hizo lilikuwa ni kutaka kuonana uso kwa uso na mkurugenzi mkuu huyo wa kampuni bwana Nadeem. Ugumu sasa ulikuwepo kwenye kuonana nae bwana mkubwa huyo. Mara nyingi shida za wenye kutaka kuonana nae zilimalizwa na wasaidizi wake. Hakuwa mtu wa kujichanganya na watu wala vyombo vya habari. Watanzania wengi walikuwa wanamjua kwa matendo yake mema kwa jamii lakini hawamjui kwa sura. "Kuna nini mbona watu wamejazana hapa chini" lilikuwa ni swali la kwanza kuuliza Shebby baada ya kuwasili ndani ya uwanja uliozungukwa na geti, uwanja ambao ndani yake kulikuwa na majengo pacha ya roshani 10. "Wewe itakuwa mgeni hapa eeh..! Hapa hali ipo hivi karibia mwaka wa tatu, kila ikifika siku ya Ijumaa, siku ya ibada kwa waumini wa kiislamu, bwana mkubwa huyu Mwenyezi Mungu amuingize peponi huwa na tabia ya kutoa sadaka kwa mafukara, masikini, yatima na wajane" alijibu mmoja wa watu wazoefu wa mazingira yale. "Kupata tajiri mwenye uchamungu kama huyu ni nadra sana, Allah amlinde na amkuzie mali zake, amuepushe na husuda za mahasidi-Amiiin..." mzee mmoja wa makamo alishadidia mazungumzo hayo huku mkononi akiwa amefumbata burungutu la pesa kuonyesha tayari kashapata kamgao chake. Shebby alikuwa anachekea tumboni kimoyomoyo alivyosikia Nadeem anasifiwa uchajimungu. Kwa umati ule wa watu, Shebby akaona itakuwa ngumu kuonana nae bwana Nadeem. Inasemekana watu huanza kufurika hapo kuanzia manane ya usiku kupanga foleni, nae Mkurugenzi mwenyewe anawasili baada ya kusali swala ya Alfajiri. "Kwa hiyo siwezi kumuona Kabisa kwa leo? " aliuliza Shebby akiwa ameshaanza kukata tamaa, hasa ukichukulia kuzipata zilipo ofisi hizo imemchukua karibia siku tatu kudodosadodosa. "Siku zingine rahisi kumpata ni siku za Jumatatu na Alhamisi, siku hizo anarudi nyumbani kwake mapema sana kwa sababu anafunga swaumu za sunnah hivyo anawahi kufuturu" alisema mmoja wa wasimamia usalama wa eneo lile. Shebby akaondoka eneo lile kiunyonge huku akiwaza na kuwazua jinsi atakavyojipenyeza mpaka afanikiwe kumuona. Wakati anataka kuondoka akapata mawazo mapya, "leo ni siku ya Ijumaa kwa vyovyote ataende msikitini kuswali pindi atakaporudi nitamvizia kwenye lifti nipande nae hapo ndio nitatapika dukuduku langu kwake. Barua iliyoachwa na marehemu Zabibu ndio iliyompelekea Shebby kuwa na uhitaji wa kuonana na Kibosile Nadeem. Akajibanza kwenye moja ya mahema yaliyojengwa kwa ajili ya kupumzikia wageni wanaotembelea eneo hilo. Akiwa pale anasomasoma magazeti aliyokuwa ameyanunua siku hiyo akamuona kwa mbali Kibosile Nadeem akiwa na mlinzi wake binafsi anapanda gari kuondoka eneo lile la maegesho, akatabasamu, alipoangalia saa yake ya mkononi ilikuwa ni saa 6:00 kamili mchana, akajua sasa lazima tu atakuwa anaelekea msikitini kuswali swala ya Ijumaa. Shebby alikuwa ni tariku swala, msikitini kwake ni kama kituo cha polisi, mara ya mwisho ni siku aliyotaka kumuona Zabibu. Alikuwa hajali cha siku ya Ijumaa, wala mwezi wa ramadhani wala sikukuu ya Eid alikuwa na mzio mkubwa na msikiti. Maisha yake ya kushinda mbugani na wanyama, nae kulimfanya awe kama hayawani hajali mambo ya ibada. Mpaka kufika majira ya alasiri, Bwana Nadeem alikuwa bado hajatia mguu ofisini kwake. Shebby akaanza kuwa na wasiwasi huenda ndio kakitoa kimoja hatorudi ofisini. Pesa ziliendelea kutolewa kwa wenye mahitaji maalumu na wasaidizi wake. Ilipofika majira ya saa 11:00 jioni akakata tamaa kabisa ya kuonana nae kabisa. Akanyanyuka kwenye kiti na bahasha yake ya kaki mkononi na magazeti yake akijongea getini tayari kwa kuondoka eneo lile akajipange upya. Hakupiga hata hatua tano akasikia mvumo wa gari la Bwana Nadeem linataka kuingia kwenye jengo lile. Chapuchapu Shebby akabadili uelekeo na kwenda kwenye moja kwa moja kwenye jengo la ofisi kwa ajili ya kumvizia kwenye lifti." Kijana mbona umesimama hapo kwenye lifti muda mrefu kulikoni? " walikuja wana usalama wawili wakimzongazonga Shebby baada ya kumuona kwenye kamera za ulinzi za jengo.
Kijana mbona umesimama hapo kwenye lifti muda mrefu kulikoni? " walikuja wana usalama wawili wakimzongazonga Shebby baada ya kumuona kwenye kamera za ulinzi za jengo. "Nilikuwa nina shida ya kuonana na Bwana Nadeem sasa kila ninavyojitahidi sipati nafasi ndio nikaamua bora nije nimtegee hapa, samahani sana nimekosa" alijieleza kwa ufasaha alishajua kimenuka tayari. "Angalia bwana mdogo utapata matatizo bure Bosi anatumia lifti ya peke yake inayoenda moja kwa moja mpaka ndani ya ofisi yake. Kama una shida nae rasmi nenda kwa sekretari wake uombe nafasi utakuja kupata matatizo bure" aliongea mmoja wa wale wana usalama. "Haya potea haraka sana eneo hili mara moja" alitoa amri mlinzi mwingine, amri ambayo ilimfanya Shebby aondoke haraka eneo lile la jengo akiwa ameshakata tamaa. Kigiza cha magharibi kilikuwa kinaanza kuinyemelea anga.
"Zabibu, binti mrembo uliyeumbwa ukakumbuka, niliyekutegemea na kukuamini hata kukusifia mbele ya marafiki zangu, kumbe ndio ulikuja kunivurugia maisha yangu yote?. Sasa sina mbele wala nyuma ama kweli kikulacho kinguoni mwako, umdhaniaye ndiye kumbe siyo. Tambua Zabibu kama unaweza kunisikia huko jongomeo ulipo, mtu anaposaliti katika mapenzi, maana yake ametekwa na tamaa binafsi. Anashindwa kutambua kwamba yeye ni mpenzi wa mtu, kwa hiyo anatakiwa kulinda penzi la mwenzake kwa udi na uvumba, kwa hali na mali. Inamaana hukujua kama unachokifanya ni dhuluma ya hali ya juu dhidi yangu?. Ukweli ni kwamba unapoanzisha uhusiano na mtu, maana yake umeamua kumpa hatimiliki ya penzi lako. Kwa hiyo ukienda kulitoa kwa mwingine, huo ni ubinafsi uliopitiliza. Unakuwa umeingiliwa pepo mchafu kama sio jini mahaba kwa kuona kwamba unaweza kuwa tu unatoa rasilimali za ndani ya mwili wako mwenyewe kirahisirahisi. Zabibu umenionyesha tabia mbaya na dharau kubwa sana. Kabla ya kuamua kuwa na mimi na kuweka maagano tuwe wapenzi kwanini usingeniambia kabla kwamba huwezi kuishi pamoja na mimi kama mwili mmoja, wewe ni kiruka njia tu, msichana wa mahonyo, upo kama siti ya daladala panda shuka na kila abiria?. Yote uliyonikosea sina kinyongo na wewe nimekusamehe, ila tambua daima wema hauozi na dhambi haisahauliki ndio maana siwezi kuzika kaburi la sahau kwa yote uliyonisababishia maishani mwangu. Ni kweli mengi uliyafanya kwa lengo la kunisaidia kwenye misukosuko yangu, lakini ulisahau kuwa furaha ya kweli haitafutwi kwenye batili bali furaha ya kweli hujengwa juu ya misingi ya ukweli, haki na uaminifu. Kabla ya kuchukua maamuzi yoyote unayosema uliyokuwa unayafanya kwa malengo ya kuninusuru na maadui zangu basi tungeshauriana. Ila hao michepuko yako yote iliyonitia kwenye misukosuko na matatizoni bila kujua kuwa chanzo cha matatizo yangu yasiyokwisha maishani mwangu. Matatizo ambayo yaliyokuwa yananiandama usiku na mchana, kumbe chanzo ni mahusiano yangu na wewe!. Lazima niwabatize kwa mara ya pili kwa moto wa risasi kutoka kwenye mtutu wa bunduki. Yasin mkubwa! naapa Lazima niwashikishe adabu, ili wasiendelee kufanya pesa zao ni fimbo ya kuchapia wanyonge na kuteketeza mamia ya wasichana wasio na hatia kwa kisingizio cha mashindano ya warembo, kumbe kwao ni mashindano yao wameyageuza kuwa ni danguro la warembo. Natangaza rasmi kuvaa gwanda za uhalifu kwa mara ya pili baada ya kustaafu kitambo sana. Mnanifanya wewe Zabibu na michepuko yako mnirudishe nifukue kaburi la sahau kwenye mambo ya uhalifu. Mwenyezi Mungu natanguliza kwanza kuomba msamaha kwako kwa ninachokusudia kuwalipizia, nafsi yangu i dhaifu sana kusamehe, sitoweza kuvumilia waponde maisha yao kwa furaha na familia zao, hali ya kuwa mimi ni kama mpapai dume sina uwezo tena wa kurutubisha mwanamke yoyote dunia hii. Kisasi changu kwao kitakuwa ni tiba na kinga kwa wasichana wengine wasiokuwa na hatia wanaotegemewa kudhulumiwa kingono na watu wenye umri sawa na wazazi wao mabinti hao" mawazo yalikuwa yanatembea kwenye kichwa cha Shebby kama mkondo wa umeme wa gridi ya taifa unavyotembea huku machozi ya hasira yanamtiririka mashavuni mwake akiwa juu ya kitanda chake baada ya mizunguko tasa ya kutwa nzima isiyo na faida. Mizunguko iliyoshindwa kabisa kumkutanisha na mtu muhimu kwake, Bwana Nadeem. Shebby alikuwa ni mtoto wa uswahilini haswa, kazaliwa Kariakoo mtaa wa Narung'ombe, shule ya msingi Ilala Boma. Utotoni madrasa ya kusoma dini ya kiislamu alipelekwa, mtaa wa jirani wa Nyamwezi kwa Maalim Kidevu, alisoma mwezi mmoja na ushee Maalim Kidevu ambaye anasifika kwa kunyoosha watoto watukutu kwa mikwaju lakini kwa Shebby alisalimu amri mwenyewe. "Mzee Zomboko mwanao nakukabidhi sitaki kumuona tena madrasani kwangu anatia mguu, nitafungwa bure huyu ni nunda amefurutu ada kwa tabia yake mbovu" alifoka Maalim Kidevu, mapovu yanamtoka baada ya Shebby na rafiki yake kutokomea na sahani la pilau kwenye tafrija ya walima. Sahani hiyo maalumu kwa ajili ya Maalim Kidevu, ilikuwa imeshindiliwa nyama za kutosha na viazi ulaya. Shebby na wenzake kinara kilipokwisha tu wakanyanyuka kwenda jikoni kutoa taarifa Maalim Kidevu kawatuma sahani Yake maalumu ya pilau iliyotayarishwa kwa ajili yake anataka kuwahi kula ana hafla nyingine amealikwa. Walipokabidhiwa sahani lile ikawa ni historia halikuonekana tena. Hizi paukwa pakawa za kuaga kuwa anaenda shule lakini anaishia kubadilisha sare za shule kisha anajichanganya sokoni Kariakoo kubebea wateja mizigo yao kwa ujira ya shilingi ishirini ya chuma kafanya sana. Yupo darasa la sita tayari kashalazwa poliso Msimbazi zaidi ya mara tatu kwa utapeli wa wizi wa simu kwa kuwapa wateja miche ya sabuni. Mzee Zomboko ndio papatu papatu ala kuli hali akafanya maamuzi magumu ya kumuhamishia mtoto wake Jijini Arusha kwa shangazi yake akasomee huko huenda huko akatulia kwa kubadilisha mazingira. Ikawa ni kama wameruka mkojo wakakanyaga kinyesi, huko ndiko akaenda kuwa mtukutu maradufu. Akakutana na wa Arachuga wakamfundisha matumizi ya kila anuwai za mihadarati, akageuka kuwa mkabaji mzuri wa vipochi vya akina mama na mikoba yao usiku. Hiyo elimu ya darasa la saba ikamshinda akatokomea mtaani kimoja. Huko mtaani alishiriki kila aina ya uhalifu ikiwemo ujambazi wa kutumia silaha na uporaji wa magari. Harakati za kudhibiti uhalifu Jijini Arusha zilipopamba moto, wakawa vibaka na majambazi wanauliwa hobelahobela na wananchi wenye hasira kali kila uchao, ikabidi Shebby na baadhi ya wenzake wabadilishe gia angani waibukie kwenye sekta ya utalii kwa kujifanya waongoza njia kupandisha watalii Mlima Kilimanjaro kwa kubeba mizigo yao. Uongozaji wa watalii taratibu kukambadilisha, akaona uhalifu haulipi kamwe bora asake ajira itakayompa mkate wake wa siku kwa njia za halali. Ndipo katika pilikapilika zake za maisha ndio akaja kuangukia tena Jijini Dar es Salaam akijikita kwenye kampuni ya RAJA SAFARI TOURS akiwa kama muongoza watalii mbugani. Sasa hawa Mapredesheee waliokuwa wanamuadhibu Shebby kwa kumalizia hasira zao eti kwa sababu tu amefanikiwa kuuteka moyo wa Miss Tanzania mpaka anawapuuza wao licha ya kumiliki mali kochokocho. Sasa walikuwa wamemrudisha rasmi Shebby yule wa Arachuga, mkatili kupita maelezo, jasiri asiyeshindika, asiyekata tamaa anapokusudia kulitekeleza jambo lake. Uzuri maadui zake wote walitajwa ndani ya barua hiyo toka kuzimu iliyokuwa na karatasi zisizopungua 12. Walitajwa kwa majina na uovu walioufanya dhidi ya Shebby kwa kigezo cha kulipiza kisasi kwa kuwapokonya tonge mdomoni la huba la Miss Tanzania. Kutokana na ukubwa wa baadhi yao waliotajwa na Zabibu na nguvu walizonazo ndio maana Shebby alihitaji msaada wa mtu mkubwa kama wao, Bwana Nadeem ambaye nae ni mtu mzito kwenye jamii ya watu wazito. Lakini wehu wa Shebby ni kuwa hajawahi kuonana na Bwana Nadeem uso kwa uso hata siku moja zaidi ya kumuona kwenye vyombo vya habari tena mara moja moja sana kwa nadra. Leo mchana uliopita ndio kafanikiwa kumtia machoni mubashara tena akiwa kwa mbali. Sasa iweje mtu hakujui asilani umtegemee eti ndio awe nguzo yako ya mapambano. Shebby alikuwa ana funguo za siri za utajiri wa Bwana Nadeem, ambazo hamna anayefahamu siri hiyo zaidi ya Mwenyezi Mungu na Shebby basi. Hicho ndicho alichokuwa anajivunia Shebby na kuapia Yasini mkubwa lazima aonane nae ana kwa ana kisha akishafikisha ujumbe wake kwa Bwana Nadeem atakuwa mtumwa wake, yeye ndio atakuwa anamuendesha atakavyo.
"Motoo..... Motooo...... Motooo... msaada tafadhali....motoooo tunakufaaa...mje mtusaidieeee...!" zilikuwa ni kelele zinazopigwa kwenye redio ya upepo na Bwana Nadeem akiwa eneo la Oldivai ndani ya hifadhi ya Ngorongoro. Waongoza watalii walikuwa wanatumia redio za upepo kuwasiliana katika kuelekezana masuala mbalimbali ya mbugani, kama kujulishana maeneo muhimu walipo wanyama kwa wingi ili iwe wepesi kwa watalii kuwaona wanyama wote wanaowatamani. Shebby akiwa na watalii wake kupitia kampuni anayofanyia kazi kipindi hicho kabla hajaajiriwa RAJA SAFARI TOURS alikuwa ni mmoja ya waokoaji wa mwanzo mwanzo kabisa kufika eneo la tukio. "Ooh..jamani hitilafu ya umeme wa gari imesababisha gari langu kulipuka wakati nipo nje ya gari nalikagua tatizo lake, ndani nina mtalii mmoja wa kiume na mtoto wake wa miaka mitano, kila kitu chetu kimeungua kwenye ajali hii, kuanzia vitambulisho vyangu vya kazi mpaka simu zangu na mabegi yangu, Ooh...my God mkosi gani huu umeniumba!" alijieleza Bwana Nadeem Massawe kwa uchungu mkubwa huku mikono yake ipo kichwani akisikitika vibaya sana kwa pigo hilo la ajali ya moto. Mshikemshike eneo la tukio ukashika kasi, kila mtu akatingwa na jaribio lile la kuzima moto, lakini juhudi zilikuwa kama kilio cha samaki machozi yanabebwa na maji tu, moto ulikuwa umekolea kisawasawa hauna utani wa msalie Mtume. Bwana Nadeem akaondolewa eneo lile, huku taratibu za kumpeleka hospitali kwa matibabu ya mshtuko ule kisha polisi kwa maelezo zaidi zikaendelea. Shebby kumbukumbu zote za tukio hilo lilikuwa linajirudia vizuri kabisa.
Shebby alikuwa nje ya jengo lililomkabala na benki ya Posta tawi la Mkwepu jijini Dar es Salaam huku pembeni yake yupo Bwana Nadeem wakiwa wamesimama nje ya duka la nguo. "Nimekuja kuitika wito wako, lakini karibia robo saa huniambii ulichoniitia bado" alivunja ukimya uliotawala baada ya kuwa wamesalimiana kisha Shebby akazama kwenye bahari ya luja, dimbwi zito la mawazo akifanya kumbukizi ya ajali ya moto iliyomkuta Bwana Nadeem karibia miaka saba na ushee iliyopita. "Oooh....sorry! sina jambo kubwa sanaa, nataka uninunulie bastola mbili za kisasa uzisajili kwa jina lako, pia nahitaji gari la kisasa lenye kasi la kuzungukia mitaani, bila kusahau niingizie fasta milioni 200 tu kwanza kwenye akaunti ya benki, nikihitaji pesa zaidi sitosita kukuambia. Haya yote ufanye ndani ya siku mbili tu sina muda wa kupoteza na sio ombi ni amri" alizungumza Shebby kwa sauti kavu yenye mamlaka inayomaanisha hayupo kwenye maigizo wala maonyesho ya vichekesho vya jukwaani.
Nadeem uso wake hapo hapo ukabadilika ukawa na rangi ya nyekundu huku midomo inamchezacheza inataka kuongea lakini anashindwa kutokana na hasira alizonazo. Jasho jeke jeke lilikuwa linamtiririka usoni na makwapani utasema amewekwa kwenye tanuri la kuokea mikate. Usicheze na mchaga kwenye pesa zake, fanya nae utani kwenye mambo yote ila sio pesa zake mtaonana wabaya. "Wewe kumbe boya eeeh, jeta mkubwa wewe...unadhania nimetoka kwetu Moshi kuja mjini Dar es Salaam kuuza sura bure bure, nimekuja kutafuta pesa. Hupati hata senti tano yangu nyeusi, ng'oo..fanya utakalo usinitishe, pumbavu wewe.... !" alizungumza kwa hasira huku akitilia msisitizo kuwa pesa hatoi na kujitapa yeye ni kiparamoto haswa kwenye ubabe hana utani na pesa yake. "Ha.. ha.. ha.. ha...unajifanya kuonea ubahili urithi wa familia ya marehemu Dr.Steven Hasselbank? Toka lini mali zako umezipata kwa jasho lako, muuaji mkubwa wewe usiye na huruma, uliyekosa junaya usoni mwako. Uliyewateketeza kwa moto baba na mwana kwa lengo tu la kuwaibia pesa zao mzomzo za kigeni, sasa kama umemwaga ugali mimi nataka kumwaga mboga ili biashara zako ziende mbagombago jambazi mkubwa wewe, uliyestahili kitanzi cha shingo" alifoka kwa sauti ya juu Shebby kumzodoa Bwana Nadeem. Alimpa vidonge vyake kwa kutumia maneno ya kukata maini. Bwana Nadeem kwenye barua aliyopewa alikuta maneno ya kikombo, yasiyonyooka aliandikiwa tu na Shebby "NAJUA SIRI NZITO YA UTAJIRI WAKO-TAFADHALI TUONANE HARAKA VINGINEVYO TUTAONANA WABAYA NINAO USHAHIDI WOTE".
Sasa hapa leo alipotajiwa Dr.Steven Hasselabank, daktari wa Kiholanzi aliyekuja kutalii Tanzania akaishiwa kutiwa moto ndani ya gari kihujuma na Bwana Nadeem kisha kuibiwa mkoba wake wenye pesa za kigeni zaidi ya dola $30,000/=. Bwana Nadeem baada ya kugundua mtalii wake anayemzungusha mbugani anatembea kishamba na mamilioni ya kutosha ya dola za Kimarekani akafanya vitimbi vya kumfungia ndani ya gari baada ya kupora mkoba huo, kisha akasababisha hitilafu feki ya umeme wa gari na kusababisha gari zima kulipuka. Baada ya hapo alichimbia mkoba wenye pesa porini na kuanza kupiga simu ya upepo na kutangaza madai ya kuwa imetokea hitilafu gari limelipuka bahati mbaya. Wakati wa harakati za uzimaji moto, Shebby alibanwa na haja akachepuka porini kidogo ndipo alipookota funguo ya gari la Nadeem na kitambulisho chake vimedondoka porini. Hapo hapo Shebby akanusa harufu ya mchezo mchafu, akaweka ahadi ya kufuatilia maisha ya Bwana Nadeem kuona kama yatabadilika kwa haraka ina maana moja moja atanathibisha mabadiliko hayo ya kimaisha na wizi kwa watalii wake aliokuwa anawazungusha. Katika hali ya kawaida isingewezekana moto ushike ghafla halafu funguo wa gari uwe njia, pia porini alienda kufanya nini mpaka kitambulisho kikampotelea huko maporini. Shebby kwa mikwara yake akajifanya amesusa mazungumzo yale anaondoka eneo lile.
"Sasa...mbona hivyo rudi tuyamalize kwanza" alijiongelesha Nadeem kwa sauti ya kupooza huku anamvuta mkono wake. "Oyaaa...nakuambia niache, husikii? nitakupasua sasa hivi tuzalishe tafrija ya damu hapa, sina muda mchafu wa kupoteza na watu wenye kiburi cha pesa zao" alizungumza kibabe akijifanya hataki tena kumbe moyoni mwake alikuwa anamtikisia kiberiti. "Samahani mkubwa tuyamalize bwana, hutaniwi? " alijilazimisha kutabasamu hali ya kuwa moyoni anaungua kwa fukuto la joto la hasira. Aliona mtu anakuja tu kilaini kudai pesa wakati yeye katoa roho za watu wawili ndio akazipata pesa. "Sawa tuyamalize kamata hii namba ya akaunti yangu uweke mzigo, na hapa hatujamalizana naomba ulinzi wako nikipata msukosuko wowote, wala usisikitike, roho ya marehemu huwa haiondoki dunia hadi ilipe kisasi hivyo haupo salama kabisa Bwana Nadeem kikubwa ni kufanya kila ninachotaka ufanye, kwaheri...!" alizungumza kwa kujiamini, kiburi na majivuno kisha akamkabidhi kikaratasi na kuondoka zake eneo lile. Nadeem akabaki ametumbua macho tu kama samaki wa kuvuliwa na mabomu, huku amekishikilia kipande cha karatasi chenye akaunti ya benki ya Shebby anayeteseka mikono. Usicheze wewe na Mchaga kwenye masuala ya pesa.
Mkurugenzi mkuu wa RAJA SAFIRI TOURS Bwana Patel Rajeev, alikuwa sio mtu wa starehe kama walivyo matajiri wenzake. Watu walikuwa wanajiuliza wapi anapotumia pesa zake ni wapi. Maana kama kumiliki nyumba, alikuwa ni mpangaji tu, nyumba anayoishi bado ilikuwa ni ya shirika la nyumba (NHC). Hata magari anayotembelea yalikuwa ni ya kawaida sana ukilinganisha na hadhi yake. Umri wake nao ulikuwa unaenda harijojo, alikuwa ni shaibu wa miaka 66 huku watoto wake watatu wote wakiwa wanaishi nchini Canada wakiwa wanasoma vyuo vikuu. Tanzania Alibakia yeye na mkewe tu wanasukuma siku za kuishi.
Waswahili wanasema kila binadamu duniani lazima awe na ulevi wake, asiye na hili ana lile. Wapo ambao ulevi wao ni kushabikia mpira, wengine ni unywaji wa vileo, wengine kupenda vidosho na ulevi mwingine. Bwana Pateli alikuwa hana ulevi wa pombe, wala sigara inavyoshikwa mkononi hajui inavyoshikwa, wala bangi hata majani yake hayajui namna yalivyo. Lakini ulevi wake mkubwa ambao watu wengi hawaujui ni kupenda kwake vimwana. Kwa ajili ya warembo, Bwana Pateli alikuwa yupo tayari kugharamia kiasi chochote kile. Hakuwa sawa kisaikolojia, alikuwa anugua ugonjwa wa kupenda ngono kupitiliza kitalamu unaitwa 'Sexual disorder' au 'Mania'. Alikuwa na makuwadi wake maalumu wanaolipwa mishahara wa kumsakia vimwana vya kustarehe navyo kila kona ya Jiji kuibua vipaji vipya.
Huko kwenye mashindano ya urembo ya Miss Tanzania, baadhi ya wakufunzi wa warembo walikuwa ni makuwadi wake wa kumuunganisha na mabinti wakali. Lakini maajabu ya fimbo ya Musa kumeza nyoka wa Farao, licha ukware wake wote kwa wanawake, pia alikuwa ni basha anawaharibu vijana wadogo wadogo wa kiume Jijini Dar es Salaam kuwa watoto si riziki, au michicha mwiba. Wanaomjua vizuri Bwana Pateli wanasema kati ya vijana kumi wanaopenda maisha ya bwerere Jijini Dar es Salaam, wasiotaka kujishughulisha na kazi, wakaa vijiweni basi vijana wawili mpaka watatu wameshawahi kupitiwa na Bwana Pateli. Naam..! alikuwa ni basha haswa anayewalawiti vijana mabarobaro kwa ahadi za kuwapa maisha bora. Wapo aliwapata kwa ahadi za kuwanunulia bodaboda, wapo anaowapata kwa kuwapa pesa na nguo za gharama za kutambishia vijana wenzao mitaani, ili mradi kila mmoja alinasa kwa chambo chake maalumu.
Namna Bwana Pateli alivyomnasa Zabibu, ilikuwa kupitia watu wake. Makuwadi wake wa kamati ya Miss Tanzania walishamuonyesha vifaa vipya vya kutoka navyo, huku akiwaahidi madonge nono ya pesa wakifanikisha. Furaha yake sheshe ya kuonyeshwa vifaa hivyo vipya, akaamua kutoa ofa maalumu ya wiki moja kwa warembo wote walioingia fainali kwenda kutembelea hifadhi ya Selous. Hivyo kitendo cha Shebby kumpindua Bosi wake kwa Zabibu, ilikuwa ni kama amekanyaga nyaya za umeme mkubwa, lazima anase tu. Hasa ukichukulia alishamtahadharisha asubuhi na mapema kabla hajawapeleka warembo Selous, kuwa ajiepushe na warembo hao. Hivyo Shebby alipochezea sharubu za simba wa kihindi akamshukia vilivyo bila huruma kwa kumfukuza kazi mara moja kisha kufukua makaburi yake ya madeni.
Bwana Pateli alijua ameshafunga kazi kwa Shebby ameshamshikisha adabu, amemkomoa tayari. Alidhania Shebby ni mjinga wa jinga, dufu la dufu, mtu hariri, asiyeweza kujitetea chochote. La hasha! Kumbe alikuwa anajidanganya mchana kweupe, Shebby alikuwa mtu kocho wa mapambano na adui zake, anajipanga kuja kivingine kulipiza kisasi. Tena kisasi alichotaka kukilipa ni kisasi kisicho na usawa kutokana na madhara makubwa waliyomsababishia.
Shebby alikuwa ndani ya gari yake 'Subaru Forester New Model', mpya aliyonunuliwa na Nadeem ikiwa ni katika utekelezaji wa makubaliano yao. Gari ambayo ilikuwa na uwezo wa kutimua vumbi mithili ya gari za mashindano. Ilikuwa ni majira ya saa 6 za usiku alikuwa anafuatilia nyendo za Bosi wake wa zamani Bwana Pateli, ambaye katika upelelezi wake aligundua siku ya jumapili usiku lazima atatoka na gari kuu kuu aina ya 'Suzuki Grand-Vitara' anaelekea nayo mitaa ya fukwe za Mbweni, akifika hapo atakaa kama nusu saa kuna bodaboda itakuja alipoegesha gari yake kisha huyo dereva bodaboda anaingia kwenye gari ya Bwana Pateli. Kinachoendelea humo ni siri yao lakini Shebby alihisi kuna vitendo vya kishoga vinaendelea humo.
Baada ya kuzisoma vizuri nyendo za Bwana Pateli kwa muda wa wiki tatu mfululizo sasa akaamua siku ya arobaini yake imefika. Ilipopaki gari ya Bwana Pateli na alipojibanza Shebby kwenye mikoko ya baharini ilikuwa karibia umbali wa meta 50. Alikuwa haoni kinachoendelea kwa sababu Bwana Pateli alishazima taa za gari yake anamsubiria basha wake aje wafanye laana zao. Punde si punde bodaboda iliyokuwa inakuja kwa kasi ikaegeshwa ubavuni mwa gari la Bwana Pateli. Bodaboda hiyo iliwasili baada ya Shebby kusubiria kwa zaidi ya dakika 20 mle kwenye mikoko huku maji kujaa ya bahari yakiwa yamemfika usawa na goko zake lakini alikuwa anavumilia apate kutekeleza alilolikusudia. Kwanza kulipa kisasi cha dhuluma ya kimapenzi aliyofanyiwa mpenzi wake Zabibu mpaka kumpelekea kujiua kutokana na msongo wa mawazo uliopitiliza, pili kumfukuza kazi kwa uonevu na kukaribia kutaka kuiuza nyumba ya familia yao kwa lengo tu la kumkomoa.
Yule bodaboda alipofungua mlango wa gari na kuingia tu, Shebby akawapa muda wa robo saa kisha awavamie wakiwa katikati ya kilele cha hanjamu zao. Shebby katika kutaka kuamsha upya hasira zake ili asimuonee huruma Bosi wake huyo wa zamani akaanza kukumbuka mstari kwa mstari maelezo ya Zabibu yanayomhusu Bwana Pateli kwenye barua yake toka kuzimu. "......Mpenzi wangu Shebby sijapata kupenda mwanaume kama nilivyokupenda wewe na ndio maana niliamua kukuzawadia kizinda changu katika usiku wa kwanza wa kukutana na wewe na wala sitojutia kwa hilo kwa sababu nilikupenda kupita maelezo. Licha ya kuwa nilikuwa ninasumbuliwa sana na wanaume hasa wenye mali mzomzo za kuweza kukutengenezea jambo lako lolote lile kimaisha unalohitaji toka kwao lakini niliwakataa kwa sababu walikuwa wananitamani tu kutokana na uzuri wa umbo langu, ila hawanipendi kwa dhati ya mioyo yao. Siku ile unakuja kunipa taarifa za kufukuzwa kazi na nyumba ya familia yenu kutaka kuuzwa moja kwa moja nilifahamu fika mhusika ni Bosi wako, Bwana Pateli. Kwa sababu tokea ile safari yetu ya kutembelea hifadhi ya Selous, matroni wetu Madam Jenipher alikuwa ananisumbua sana, ananiambia mmiliki wa kampuni yako ya RAJA SAFARI TOURS ananipenda sana na yupo tayari kunifanyia jambo lolote ili mradi nimkubalie. Nikawa simpi jibu lolote zaidi ya kumwambia ngoja nifikirie kwa sababu kama ningemjibu moja kwa moja Madam Jenipher kuwa huyo mhindi wake simtaki angeweza kunitibulia mipango yangu ya ushindi wa taji la Miss Tanzania labda kwa kunipakazia kwa majaji kuwa sina nidhamu kambini na mengineyo mengi ya kuzusha. Ndio maana siku niliyotwaa taji la Miss Tanzania wakati tupo pamoja kwenye gari yako Shebby walikuja wadada wawili kunirai nitoe jibu kwa Madam Jenipher, nilichowajibu ulikisikia pale kuwa awapeleke watoto wake kwa huyo mshefa anayetaka kwenda kuniuza kwake biashara ya ukahaba. Bosi wako Pateli kumbe alipopewa jibu la mimi kukataa Na Madam Jenipher tena wakatia chumvi na pilipili kuongeza ladha ya jibu lao kuwa dereva wako yaani wewe Shebby ndio umepindua meza kibabe. Kilichofuata nadhani mwenyewe shahidi ukafukuzwa kazi na deni la mkopo ukatakiwa ulilipe ndani ya masaa 24. Hukuwa na sehemu ya kutoa pesa wala mimi sikuwa nazo hizo pesa. Sasa nyumba ya familia yako kama ingeuzwa chanzo ingekuwa ni mimi Zabibu. Mimi ndio nilikupenda wewe kabla wewe hujanipenda, kama nisingekuingiza majaribuni kukupa kadi ya kuja kwenye fainali za Miss Tanzania na kulazimisha kuondoka na wewe usiku ule kamwe usingepata matatizo yaliyokupata. Hivyo sikuwa na budi bali nijitoe sadaka ili kurekebisha mambo yako na familia yako. Sadaka ambayo hata kama ni ya kuhatarisha uhai, heshima na utu wangu ili mradi tu nikuokoe katika janga zito ulilokuwa nalo. Samahani sana nisamehe mpenzi nikakudanganya ninaenda chuoni nina vipindi mchana. Lakini ukweli ni kuwa sikuwa na vipindi vyovyote siku hiyo bali nilikata shauri niende moja kwa moja ofisini kwako nikaonane na Bosi wako Bwana Pateli nimuambie kuwa nimemkubali kuwa na yeye ili baadae niokoe jahazi kwa upande wako. Nilipofika ofisini kwako mchana ule moja kwa moja nikaenda kuonana nae kwa bahati nilimkuta. Aliponiona tu alinitambua kwa sababu alishapewa na Madam Jenipher hadi picha zangu za nusu utupu tunazopiga tukiwa wenyewe wakati tunaogelea na nyinginezo. Akaanza kunilaumu kwanini namkataa yeye ana pesa nyingi sana hapa nchini na huko Canada wanapoishi watoto wake. Akanipa ahadi kemkem kuwa yupo tayari kulitekelezea kama nitamkubali na niachane na wewe kapuku, usiye na mbele wala nyuma. Nikampa sharti moja tu, asiuze nyumba ya familia yako ndio nitakubali kufanya nae mapenzi. Mara moja akatekeleza sharti hilo kwa kuwapigia simu kampuni ya udalali waache mipango yao yote ya kuuza nyumba yenu ya familia.Baada ya hapo, Bosi wako Pateli akawa ni mtu wa pili duniani tokea nizaliwe kufanya nae tendo la ndoa. Akanifanyia ufedhuli wake usiku kucha bila kuchoka tena akiwa amemeza vidonge vya kuongeza nguvu za kiume kwa lengo la kunikomoa tu. Nyumba yako ikasalimika, nakumbuka ulinipigia simu asubuhi na mapema kuwa umetaarifiwa kuwa nyumba ya familia yako haitouzwa tena, kazini kwako wamekusamehe deni lako kutokana na utendaji wako kazi wa kutukuka wameona wakikudai ni kama wanakukomoa, kwa furaha yako tu ukaomba jioni nikitoka chuo tuonane ili kujipongeza. Ukweli ile simu yako uliyopiga niliipokea nipo kifuani mwa Bosi wako Bwana Pateli iliniuma sana na machozi yalinitiririka hasa kwa kuwa ulikuwa haujui yanayoendelea nyuma ya pazia. Nilifanya yote kwa ajili ya upendo wangu kwako Shebby na sio kwamba mimi ni malaya natafuta pesa...." Shebby alipomaliza kipande cha kumbukumbu hiyo chafu inayomhusu Bosi wake Bwana Pateli akakurupuka kwa hasira toka kwenye mikoko aliyojibanza na kuelekea kwenye gari la Bosi wake kwenda kumaliza uhai wa mjuba huyo wa kihindi.
Kulipokucha asubuhi habari iliyobeba gumzo la jiji siku hiyo ilikuwa ni ya kuuliwa kinyama kwa mfanyabiashara wa Kiasia, mmiliki wa kampuni ya RAJA SAFARI TOURS, Bwana Pateli. Maiti yake iliokotwa pembezoni mwa ufukwe wa Coco Beach ikiwa pembeni na maiti ya kijana mwingine wa Kiafrika muendesha bodaboda. Ilikuwa ni bina kwa jamii mtu ambaye ni mahashumu kama Bwana Pateli kufa kifo dhalili kabisa na cha aibu.
"Afadhali sana, nampongeza aliyefanya hili tukio, huyu babu ametuharibia sana vijana wetu Jijini kwa jeuri ya pesa zake, amepata malipo stahiki na uovu wake, lakini watu walimwogopa kutokana na pesa zake" alinoa ulimi wake mmoja wa wananchi mwenye hasira kali huku akimnyambua marehemu Pateli juu ya tabia zake chafu za ukware. Maneno aliyoropoka mwananchi yule ni ya lolololo yasiyo na mantiki yoyote katika jamii iliyostaarabika.
"Aaaah....kosa ni kosa tu, muuaji mie simpongezi kama alichukizwa na vitendo vya Bwana Pateli angeripoti polisi na sio kujichukulia sheria mkononi, kama kila raia akikosewa akaamua kuchukua sheria mkononi nchi itakuwa vuruvuru na mchafukoge kama Somalia, hamna haja basi ya kuwa na vyombo vya dola na mahakama, kama mnaona hukumu zenu mitaani ni bora kuliko hukumu ya mahakama" alitoa indhari mmoja wa raia baridi, mwenye busara zake akionyesha kuchukizwa haswa na mihemko ya mwananchi yule anayeshangilia kifo cha Bwana Pateli.
Mitandao yote ya kijamii ilitikisika na kuzizima kwa tukio hilo la kutisha kwa mtu ambaye ni mausufu katika jamii mwenye kampuni kubwa iliyotoa ajira za moja kwa moja ya zaidi ya Watanzania 200. Vyombo vya dola hususani polisi nao hawakuwa nyuma, walikuwa nao wanahaha huku na kule kuhakikisha wanamtia mbaroni muuaji kwa haraka sana ili kuondoa hofu ya usalama kwa wawekezaji wa ndani na wa nje. "Mie mpaka sasa sijafahamu lengo la muuaji ni nini, maana hajachukua kitu chochote zaidi ya kuwaua Bwana Pateli na kijana yule! " alizungumza mmoja wa maofisa wa polisi kwenye kikao cha dharura cha maafisa upelelezi wa mkoa wa Dar es Salaam.
"Inaweza ikawa ni mauaji ya kisasi, na kisasi kinaweza kuwa ni kutoka kwa mfanyabiashara mwenzake labda wamedhulumiana" alichangia mazungumzo mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Kinondoni. "Sio lazima iwe kisasi cha biashara inaweza kuwa pia mmoja wa wazazi ambae mtoto wake amewahi kulawitiwa na Bwana Pateli kuamua kulipiza kisasi" mmoja wa maofisa hao alizidi kupanua wigo mpana wa majadiliano ya upelelezi wa mauaji hayo.
"Mie kidogo nitofautiane na wachangiaji wenzangu waliopita, nimezichunguza zile maiti mbili lakini kwenye maiti ya Bwana Pateli kuna vitu vya ziada viwili vinavyotatanisha " aliingilia mazungumzo hayo kachero Millan aliyekuja kumuwakilisha kamanda wa polisi wa wilaya ya Temeke ambaye muda mwingi alikuwa kimya akisikiliza hoja za wenzake. "Eheee...vipi hivyo maana waziri wa mambo ya ndani hapa ameshatuma meseji anataka ripoti ya tukio hili saa 8:00 mchana wa leo.. " aliingilia mazungumzo kamanda wa polisi wa mkoa wa Dar es Salaam akiwa na kimuhemuhe cha kupata taarifa sahihi la tukio hilo ili asije kuonekana ni mzembe na wakubwa zake akatumbuliwa.
"Kwanza kwenye maiti ya Bwana Pateli amekatwa sehemu yake ya siri na imechukuliwa, hii inaweza kuwa ni kisasi cha mapenzi au mambo ya kishirikina. Lakini pili kwenye paji lake la uso chini kidogo ya kidoti cha rangi nyekundu wanachojichora Wahindu, kuna maandishi madogo kama ya mhuri wa moto umeandika "Next stop IFM" sasa hapa tujadili haya mambo mawili dhana moja wapo inaweza kuwa ipo sahihi" alimalizia mawazo yake ambayo yaliamsha mjadala mpya wakiwa ndani ya chumba mahususi kilichopo kwenye wizara ya mambo ya ndani.
Picha za marehemu zinazoonyesha maandishi hayo madogo yakakuzwa kwa kamera maalumu zikasambazwa mezani, na wote wakathibitisha ni kweli maandishi hayo yameandikwa. Mjadala ukaendelea kulindima kwa zaidi ya masaa manne wakibishana kwa hoja mbalimbali za kichunguzi, mpaka wakafikia hitimisho huenda muuaji anataka kuua wanafunzi wa chuo cha usimamizi wa fedha "IFM" hivyo ikaamuliwa ulinzi mkali sana wa jeshi la polisi uwekwe chuoni IFM kumdhibiti muuaji huyo anayeonyesha ana kiu ya damu.
Ukaguzi mkali ukawa sasa unafanyika wakati wa kuingia na kutoka chuoni hapo, ili mradi kuzuia mpenyo wowote wa mhalifu kutekeleza uovu wake. Pia maamuzi mengine ni kutafuta watu maarufu wakiwemo viongozi na wafanyabiashara wenye ufupisho wa majina yenye herufi tatu 'IFM' ili wapewe ulinzi maalumu wa masaa 24 wa jeshi la polisi. Kamanda wa polisi akatangaza kwenye vyombo habari kuwa wananchi wachukue tahadhari kabla ya hatari na iwapo wakiona dalili zozote za viashiria vya mtuhumiwa wa mauaji wasisite kutoa taarifa haraka sana kwa vyombo vya dola.
Jeshi hilo pia likaomba msaada toka vyombo vingine vya usalama ndani ya nchi ili kumbaini mhalifu wa tukio hilo mara moja. Huku familia ya Bwana Pateli ikitangaza kiangaza macho cha milioni 10 kwa yoyote atakayefanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa. Baada ya kutangazwa dau hilo sasa ikawa fujo mtindo mmoja, vidinga popo na habari kauzwa wakaingia kazini kupekenyua taarifa za maisha binafsi ya Bwana Pateli huenda wakaambulia fununu zozote zitakazowawezesha kujiingizia milioni 10 ya machombozi bila jasho, hasa kipindi hiki ambacho pesa za magumashi bila kufanya kazi halali ilikuwa haipatikani abadaan kataan.
Mihangaiko yote hiyo ya vyombo vya dola, Shebby alikuwa anachekea tumboni tu anakula kuku kwa mrija, akijiandaa kwa kushusha kombora lingine kwa maadui zake wote waliotajwa na Zabibu kwenye barua yake yenye kurasa 12. Huku akiwa amewaachia vyombo vya usalama mashaka tipitipi yenye kina kirefu wanachoshindwa kuogelea kumkata mhalifu wao. Shebby alipania haswa kuwashukia maadui zake kwa mkururo wa misiba mpaka awamalize wote.
Bahari ya mapenzi tuliyozama mimi na wewe mpenzi wangu Shebby ilikuwa ni kubwa kwa wale waliowahi kuogelea. Bahari ambayo masikini na matajiri, wote lazima waogelee katika vina vyao tofauti tofauti kwa kadri ya ufundi wao wa kuogelea. Ni bahari yenye mkondo wa kina kirefu uliozungukwa na viumbe wa hatari wenye kuogofya, dhoruba, vitimbi na mawimbi makubwa yenye nguvu kama ukiamua kuivinjari vilivyo bahari hiyo. Bahari halisi kwa kawaida huwa inaweza kuwa na viumbe wakubwa sana kama nyangumi au papa .
Lakini bahari hiyo hiyo pia wanaishi viumbe wadogo sana kama dagaa, viumbe ambao hawana uwezo wa nguvu za kuwashinda majemedari wakubwa wa bahari kama Nyangumi na Papa. Kwenye bahari ya mapenzi, wenye pesa zao sufufu na madaraka makubwa katika jamii ndio wao hujifanya ni Nyangumi na Papa wa bahari hiyo, huku wakitumia pesa zao na madaraka yao vibaya kuwaonea wanyonge katika starehe zao za mapenzi. Mimi na wewe tulikuwa ni kama dagaa au samaki wadogo baharini, tulikuwa madhaifu tunawindwa kufanywa mboga na samaki wakubwa, tusingeweza kuhimili dhoruba na vitimbi vya wakubwa wa bahari ya mapenzi asilani.
Fisadi papa mwingine wa mapenzi yetu baada ya Bosi wako Bwana Pateli alikuwa ni mhadhiri wangu wa chuoni Profesa Nolan Kaganda, ambaye alikuwa ananimendea kutoka na mimi kimapenzi kwa uchu wa kumchuruzika udenda kama fisi tokea nikiwa mwaka wa kwanza tu pale chuoni IFM. Ila vitimbi vyake na nyavu zake alizokuwa anatumia kunitega vilifeli vibaya kwa muda wote wa miaka miwili pale chuoni. Nilikuwa ninamrusha kwa sababu hakuwa ananifundisha somo lolote kwa mwaka wa kwanza mpaka wa pili hivyo alikuwa hana ujanja wowote wa kufanya mapenzi na mimi bila ridhaa yangu maridhawa.
Kasheshe lilikuja kuibuka pale nilipofika mwaka wa tatu muhula wa mwisho nikawa nimeingia kwenye anga zake. Alikuwa anatufundisha somo la takwimu 'Statistics', somo ambalo lilikuwa ni homa ya jiji kwa wanafunzi wengi wenye mzio na somo la hesabu. Somo ambalo kama hujuavyo ni homa ya jiji kwa wanafunzi wengi mashuleni kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari. Yeye akawa ndio anatumia hiyo fursa ya ugumu wa somo lake kama tiketi ya kung'oa wasichana warembo anaohitaji kustarehe nao kimwili. Kipindi hicho pia umaarufu wangu na urembo wangu shuleni ukawa dhahiri shahiri haswa kutokana na ushindi wangu wa taji la Miss Tanzania, hivyo akanizidishia chuki dhidi yangu.
Kwa kuwa nilikuwa nimemkataa kwa kipindi kirefu, testi zake zote darasani nilikuwa ni mtu wa kufeli tu mpaka ilipofika mtihani wa mwisho wa marudio maalumu kwa watu waliofeli kwenye mtihani wa kwanza. Mtihani ambao kama ningeshindwa kufaulu mtihani huo ningefukuzwa chuo moja kwa moja bila msalie Mtume hivyo kupoteza matumaini yangu yote ya kuhitimu shahada yangu ya Chuo kikuu. ikabidi niweke silaha chini na kwenda kumsujudia ili nifaulu mtihani wake kwa kumbembeleza anisamehe kama nimemkosea jambo lolote.
Yeye alikuwa ndio ameshikilia shahada yangu mkononi mwake, alikuwa ameshika mpini mimi nimekamatia makali hivyo ujanja wowote dhidi yake ningeishia kukatwa na kisu hicho. Nikaomba miadi ya kukutana nae ili tuyajadili kiustaarabu tuweze kuyamaliza vizuri. Akaniita ofisini kwake na kujifanya ni mtu baridi sana kwangu hana shida kabisa na mimi na kuanza kunishushia lawama lundo, kwa kushindwa kumpa ushirikiano mapema mpaka imefika hatua ya mwisho ya kukaribia kufukuzwa chuo kwa kufeli.
Kitu cha mwisho nachokumbuka nilipokuwa ofisini kwake alichonifanyia alinikaribisha keki na soda huku mazungumzo yetu yanaendelea. Kinywaji ambacho baada ya kunywa tu sikufanikiwa kulimaliza, baada ya muda mfupi, nikajikuta napoteza fahamu, sitambui kinachoendelea. Nilipozinduka nilijikuta tayari amenibaka, akaniomba sana msamaha, na kuonyesha sura ya kujutia na kukiri kanifanyia hivyo kutokana na kuniona sieleweki misimamo yangu hali ya kuwa amelisaka penzi langu msitu na nyika bila mafanikio kwa muda wa miaka miwili.
Nilitoka ofisini kwake kwa uchungu mkubwa hasa kwa kunifanyisha mapenzi bila ridhaa yangu. Lakini wapi ningeenda kushitaki nikaeleweka kama kweli nimebakwa?. Jamii yetu iliyotawaliwa na mfumo dume, daima sisi wanawake ni watu wa kuonekana tuna makosa hata kama hatuna dhunubu yoyote. Wengi wangeishia kunilaumu kuwa nimeyataka mwenyewe kama kweli sikuwa na nia ya kumtega mhadhiri wangu kwanini nilikubali kujifungia nae ofisini tukiwa watu wawili tu?.
Bado hata wewe mpenzi wangu ningekuja kukuhadithia mkasa wangu kwa Profesa Kaganda lazima ungenibeza tu kuwa nimeyataka, katu usingeniamini. Machozi yangu yakawa kama machozi ya samaki baharini hayaonekani yanatokomea kwenye maji. Lakini bado shahada yangu ilikuwa ni muhimu kwangu, chukulia kama ningemshitaki kisha akanishinda lazima angenishukia kwa pigo takatifu la kunifelisha mtihani wangu wa mwisho hivyo ningetoka kapa chuoni miaka mitatu bila shahada. Vyombo vya habari vya udaku na mitandao ya kijamii yote ingenihukumu kuwa Miss Tanzania kakosa digrii kwa kuendekeza anasa chuoni, jambo ambalo lingeniumiza maradufu maisha yangu yote.
Baada ya hapo nilipofika nyumbani kwako usiku nikakulalamikia maumivu ya tumbo yaliyotokana na unywaji wa soda, maumivu ambayo yalisababisha nilazwe hospitali binafsi ya Massana na kupelekea kupoteza ujauzito wako nilioushika toka kwako. Hivyo ndio namna nilivyogeuzwa kuwa asusa ya Profesa Kaganda bila ridhaa yangu, akawa ni mtu wa tatu kufaidi penzi langu tokea nimekuja duniani, lakini pia akinisababishia niondoke duniani bila kukuachia mtoto hata wa dawa anayetoka kwenye mifupa yetu"
Shebby alikuwa anaoga bafuni usiku huo mbichi wa saa 1:30 kujiandaa kwenda kumshughulikia Profesa Kaganda hivyo alikuwa anakumbukia akiwa bafuni kipande cha barua kilichomtaja kinagaubaga ubaladhuli wake Profesa Nolan Kaganda. Uzuri barua hiyo ya kurasa 12 Shebby alikuwa ameikariri kichwani kama hivyo haitoshi bado kila siku alikuwa kabla ya kulala anairudia kuisoma akali ya mara tano. Kumbukizi hiyo ikampa amsha amsha ya kufanya haraka kwenda kumuwahi Profesa kwenye mkahawa wake maarufu anaopenda kupata mlo wake wa usiku akamshikishe adabu kisha kumtanguliza jongomeo, akhera.
Shebby akiwa yupo kamili gado kwa kupiga matukio mengine ya kutikisa jiji alikuwa anaegesha gari yake kwenye uwanja wa Biafra-Kinondoni mbele ya Chuo Kikuu Huria 'Open University of Tanzania (OUT)'. Akashuka nje ya gari lake, akaangalia saa yake ya mkononi akatabasamu ilikuwa ni saa tatu kasorobo ya usiku. Alichofanya Shebby kwanza ni kutafuta lilipo duka la kuuzia dawa za binadamu 'Pharmacy' iliyopo jirani na hapo eneo la Biafra usiku huo.
"Habari za usiku dada yangu, pole sana na kazi!" alisalimia Shebby baada ya kufungua mlango wa duka hilo la madawa na kuingia ndani. "Ahsante sana, usinipe pole nipe hongera, Tanzania ya sasa kauli mbiu ni 'Hapa kazi tu' mpaka kieleweke " akajibu mhudumu yule kwa bashasha wakaangua kicheko wote kwa pamoja. "Sijui nikusaidie nini kaka yangu, nipo tayari kukuhudumia" alivunja furaha ile ya kicheko mhudumu yule ambaye dalili zote zilionyesha anakaribia kufunga duka lake. "Dada yangu mie nina aleji ya macho, yanakuwa mekunduu sasa naomba unisaidie dawa ya macho 'Altazine' nikaminyie jichoni nipate kulala vizuri maana yanawasha kwelikweli" alijieleza Shebby kwa ufasaha. "Hiyo dawa ipo pole sana thamani yake ni shilingi elfu nne tu za Kitanzania" alijibu yule dada huku akiitafuta dawa hiyo kutoka kwenye shelfu za kutunzia dawa na kumkabidhi dawa hiyo Shebby.
"Mhhhh...mbona sio hii, naona wameandika 'Visine Eye drops' wakati mie nahitaji Altazine, nyie wauza madawa bwana wakati mwingine wababaishajiii...." alizungumza Shebby kwa hasira kidogo baada ya kuona jina ni tofauti na dawa aliyoiagiza. "Baba yangu usikasirike dawa ni hiyo hiyo tofauti ni majina ya kibiashara tu 'brand name' hiyo dawa uliyoitaka ya Altazine ina majina kochokocho. Altazine inajulikana pia kama Geneye Extra, Geneyes, Opti-Clear, Optigene 3, Redness Relief, Redness Relief Original, Visine, Visine Maximum Redness Relief, Vision Clear hayo yote ni majina yake" alifafanua kiufasaha kuonyesha hajakaa pale dukani bure bure bali amekaa kwa sababu amesomea elimu ya famasia. "Samahani sana kwa kutoheshimu taaluma yako lakini nyie wenyewe ndio mnatuchanganya majina yote hayo ya kazi gani sasa" aliomba msamaha Shebby huku akijitetea kwa mkoroganyiko huo uliotokea.
"Unachotakiwa wewe kuzingatia ni viambata vyake vya kwenye 'Generic Name' ambayo ni tetrahydrozoline ophthalmic ambayo kazi yake ni kupunguza kipenyo cha mishipa ya damu inayoelekea kwenye jicho ili kupunguza jicho kuwa na rangi nyekundu" Alifafanua kwa weledi mkubwa, ufafanuzi ambao ulimshibisha vilivyo Shebby. Hakuwa na muda wa kupoteza, akailipia dawa yake ya macho na kutimka zake haraka haraka kuelekea Break Point.
Profesa Kaganda alikuwa tayari kashawasili kwenye mkahawa wa 'Break Point Restaurant' uliopo maeneo ya Kinondoni. Shebby baada ya kuzisoma nyendo za Profesa Kaganda kwa zaidi ya wiki moja, akagundua ratiba yake akitoka chuoni IFM kufundisha, aghalabu anapitia Break Point ya Kinondoni anapata mlo wake wa usiku, kisha anaendeleza moja moto, moja baridi kabla ya kurejea nyumbani kwake Salasala. Shebby na yeye alishajifanya kijiwe chake ni Break Point cha kupatia mlo wake ili mradi azisome vizuri nyendo za mlengwa wake. Shebby akapita vichochoro vya ndani kwa ndani mpaka akaja kuibukia Break Point ndani ya mwendo wa takribani dakika 10 tu. Alipoangalia kwenye maegesho ya magari Shebby akatabasamu, baada ya kuliona gari la Profesa limeegeshwa nje ya mkahawa.
Shebby akiwa amevaa kofia yake ya pama ya rangi ya kahawia na miwani yake nyeusi, huku juu akiwa amevalia jaketi la baridi la kisasa rangi nyeusi lenye michirizi ya rangi ya uzurungi lililotengenezwa kwa ngozi ndani yake akiwa na fulana ya Polo ya rangi ya kijani bila kusahau sarawili yake ya dangirizi nyeusi yenye mifuko mifuko mingi na safari buti zake. Kwa ufupi alikuwa anaonekana ni mtanashati na maridadi kwa mavazi, lakini moyo wake ndani ulikuwa mweusi ti ti ti kwa kiu ya kulipiza kisasi kwa wote waliomaharibia huba lake kwa Miss Tanzania. Mkahawa siku hiyo ya Ijumaa ulikuwa umeshona watu vilivyo utasema kuna chakula na vinywaji vya bure kumbe wanalipia pesa zao. Watu wa mataifa mbalimbali kuanzia wazungu, wahindi, waarabu na Waafrika ambao wana maisha bora, sio mahohe hae, pangu pakavu tia mchuzi. Walikuwa wanakula na kunywa huku wanazungumza kwa furaha kubwa.
Kama kawaida yake Profesa Kaganda alikuwa ni mtu mpekepeke asiyependa kujichanganya na watu akiwa kwenye starehe zake, alikuwa amejitenga kwenye meza ya kukaa watu wanne, wakiwa wapo wawili tu. Shebby moja kwa moja akaenda kuungana nao sasa wakawa watu watatu. "Good evening waungwana...!" alisalimia Shebby na kukaa kiti mkabala na mbaya wake. Wakaitikia salamu ile huku wanamkaribisha kwa bashasha kama ujuavyo ukarimu wa Watanzania wakikutana utasema ni ndugu wa familia moja kwa namna wanavyochangamkiana. Mhudumu akamfuata Shebby kwa ajili ya kumsikiliza mahitaji yake. "Niletee Wali kwa nyama ya nyati iliyopikwa chukuchuku tu kwa nyanya, kwa upande wa kinywaji niletee juisi yoyote ya matunda unayoipenda wewe ninywe! " aliagiza Shebby kwa mhudumu yule. Ambaye alitii maagizo ya mteja wake na kwenda kupeleka oda yake jikoni.
Break Point ni mkahawa ambao ulikuwa unasifika jijini Dar es Salaam kwa mapishi ya nyama za porini, kuanzia nyati, swala na nyinginezo. Hilo ndio jambo ambalo lilikuwa pia linamvutia Profesa Kaganda kula milo yake hapo. Alikuwa ni msomi ambaye hana mke nyumbani kwake anaishi kinembanemba tu. Alishawahi kuwa na mke wa Kijerumani aliyewahi kuzaa nae watoto wawili wa kiume akiwa masomoni nchini Ujerumani. Kilichotokea baina yao mpaka ndoa hiyo kuvunjika ni siri yao na Manani, lakini kwa muda mrefu watu wanaomjua hawajahi kumuona mkewe wala watoto wake. Alikuwa ni mtu wa kula bata kwa kwenda mbele hana majukumu yoyote ya kifamilia zaidi ya kujihudumia yeye mwenyewe tu.
Alipoletewa chakula chake akawa Shebby anakishambulia kwa pupa chakula kile kitamu hasa ukichukulia alikuwa na njaa kali. Kipindi chote wapo watatu kwenye meza walikuwa wanabadilishana mazungumzo mbalimbali ya mambo yanayoendelea nchini Tanzania kuanzia siasa mpaka kwenye burudani. Huku Shebby akitafuta nafasi ya kumfanyia tukio alilolikusudia Profesa Kaganda. Fursa adhimu aliyokuwa anaisubiria kwa hamu ikawadia, yule mwenzao kwenye ile meza akawaaga, akanyanyuka zake kuondoka. Mezani wakabaki wawili tu, Profesa Kaganda na Shebby, mahasimu wawili wasiopikika chungu kimoja, utamu zaidi ukichagizwa kwa mmoja kumtambua mwenzake wakati mwingine hamjui mwenzake.
Laiti Profesa Kaganda angefahamu kuwa mbele yupo wakala wa Ziraeli malaika mtoa roho za waja, Wallahi angetimua mbio zile za Kibanga ampiga mkoloni. Lakini ajuaye ya ghaibu ni Rabana, mlango wa funguo za siri anazo yeye tu hajamuwakilisha yoyote.
"Waitress...Weeeeh...Waitressssss.....kuja hapa ongeza bia moja ya mwisho hapa kisha ulete bili yangu, nikalale zangu mieee...." alimuita mhudumu Profesa Kaganda huku akiwa ndio amemaliza msitu wa bia zilizotapakaa mezani pale. Alipoagiza tu kabla hajaletewa akanyanyuka kuelekea msalani kujisaidia. Hapo hapo Shebby kachomoa kutoka kwenye mfuko wake wa dangirizi dawa yake ya macho na kuiminyia matone kama manne tu kwenye glasi ile aliyokuwa anaitumia kunywea pombe zake Profesa Kaganda.
"Usifungue kwanza hiyo bia yake msubiri kwanza arudi, maana kaka yangu huyu akilewa ana matata sana yaani" alizungumza Shebby baada ya mhudumu Kuja kwa ghafla na bia aliyoagizwa na kutaka kuifungua. Hali iliyopelekea Shebby aidondoshe ile dawa yake chini kwa uoga kwa malengo ya kuwa ataiokota mhudumu akiondoka zake. Akamdanganya pia mhudumu kama yule Profesa ni kaka yake wa damu ili kuwafanya wahudumu wa pale waamini kuwa ni wamoja. "Yaani....kumbe hata nyie wanandugu mnamjua vizuri eeeh huyu Profesa akiwa hajautwika mtindi ni mtu mzuri sana, hariri hanaga shida na mtu lakini shida yake akilewa tu mhhhhhh...fujo tupu mtindo mmoja mara anapapasa papasa wahudumu miili yao kimahaba utasema kaingia balehe juzi juzi" aliongea mhudumu yule akionyesha kuchoshwa na tabia chafu za Profesa Kaganda.
Huo ndio unyanyasaji wa kijinsia mashuhuri sana kwa wahudumu wa baa na mikahawani wanaofanyiwa na wateja wao pindi wakilewa lakini hamna wa kuwapazia sauti kutokana na unyanyasaji huo wa mashambulio ya aibu. Kwanza wakipaza sauti zao watafukuzwa kazi mara moja na wamiliki wa maeneo wanayofanyia kazi kwa kisingizio cha kuwa mteja ni mfalme hivyo umridhishe chochote akitakacho. Tegemeo lao pekee la kutetea haki zao lilibakia kwa ' CHODAWU' Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Mahotelini, Majumbani na Huduma za Jamii, lakini wapi chama hicho kilikuwa kwenye usingizi mzito wa pono, si hayati si mamati wapo wapo siku zinasonga.
"Safi sana kwa kunisubiria, mteja ni mfalme maana usalama siku hizi ni mdogo wewe binti lazima nishuhudie unavyofungua" alizungumza Profesa Kaganda baada ya kutua pale mezani na kumuona mhudumu amesimama na bia yake anamsubiria yeye. "Kweli Bwana broo...siku hizi dunia inakaribia machweo kabisa kila aina za uhalifu unaovuma zama hizi" alijifaragua Shebby huku moyoni akijua tayari kashamuingia mkenge Profesa Kaganda. Akafunguliwa bia ile Profesa kisha kwa heshima na taadhima dada yule akaimimina bia ile kwenye glasi iliyofanyiwa mambo mambo na Shebby. Bila kuchelewa ilipojazwa tu kinywaji kile, Profesa akainyanyua juu kwa juu huku anaanza kuigiza kwa mtindo wa tarumbeta bila kupumzika, kisha alipoitua chini ilikuwa ipo tupu.
Alipoishika bia yake ili ajimiminie tena kwa mara ingine akawa kama mtu mwenye kizunguzungu anasitasita. "Profesa nini tena..?" Shebby alijishebedua kumuuuliza wakati anajua tayari Altazine imeshafanya vitu vyake mwilini. "Naa...ji... si..ki... a dizz....ne...ssss, ni...pe.....leke...... kwe...nye ga...riiii..." alizungumza kwa shida sana akiwa analalamika kuhisi kizunguzungu.
Shebby ndio fursa aliyokuwa anaitaka hiyo akaanza kumnyanyua kwa kutumia mabega yake anamburuta anamtoa nje ya mkahawa ule. Hamna aliyejali sana tukio hilo walijua tu ni mlevi aliyezidiwa na kileo anasaidiwa kupelekwa nyumbani kwake na ndugu yake au msamaria mwema. Ikawa ndio mwisho wa Profesa Kaganda kuonekana kwenye uso wa dunia hii.
?
Ofisi za Bwana Mathew Kilanga, Mkuu wa kitengo cha siri cha usalama wa nchi, zilikuwa zipo katika jengo la "Benjamin William Mkapa Pension Tower" roshani ya tano katika mtaa wa Azikwe. Zamani jengo hili lilikuwa linajulikana kama "Mafuta house". Ilikuwa ni ofisi ya wastani isiyo na mbwembwe nyingi, huku akisaidiwa na katibu muhtasi wake mwanamke makini na mwerevu "Kokunawa Rweikiza" mhaya mzaliwa wa Bukoba vijijini.
Alikuwa mwanamke kidosho haswa lakini anayejitambua vilivyo, hivyo hakupata tabu kufanya kazi na Bosi Mathew Kilanga. Tofauti na makatibu muhtasi hawa wa kizazi kipya utakuta anamhudumia mteja huku anapaka rangi ya mdomo, mara anachati na simu yake kwenye mitandao ya kijamii huku wateja wanamsubiria, ili mradi tafrani tupu. Waliowahi kufanya nae kazi kigogo huyu wa ushushu wengi walishindwa kuendana na kasi yake katika utendaji wake wa kazi. Lakini Koku yeye akawa anamjulia haswa bwana Mathew, mpaka sasa akawa amedumu nae kwa muda wa miaka isiyopungua kumi mfululizo bila kuharibu kazi yoyote anayoagizwa kutekeleza, wala kupewa barua ya onyo kazini la kuharibu kazi.
Kokunawa wiki yote iliyopita tokea alipouliwa mfanyabiashara Pateli kinyama alikuwa akiingia ofisini asubuhi saa 1:30 muda wa kurudi nyumbani haujulikani, siku akiwa sana saa 4:00 usiku, lakini kutoka saa 6:00 usiku ilikuwa ndio kawaida. Alikuwa na kazi ya kupokea barua pepe za taaarifa za kiintelijinsia kutoka ofisi ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam kisha kuzipeleka kwa mkuu wake wa kazi kwa utekelezaji. Taarifa hizo za kiintelijinsia alikuwa anazidurufu na kuzipeleka kwa Bosi wake Bwana Mathew Kilanga azipitie na kama kuna zinazohitajika kujibiwa zijibiwe kwa haraka ili mradi suala la Bwana Pateli kuuliwa na watu wasiojulikana ilikuwa ni dosari kubwa kwa vyombo vya usalama. Kwa ufupi ni kwamba Koku alikuwa anakesha mfano wa nesi wa zamu anavyokesha na wagonjwa wake.
Mida ya saa saa 4:30 usiku Kachero Manu Yosepu alikuwa ndio kwanza anapanda ngazi kuelekea sakafu ya tano ofisini kwa bosi wake. Kachero Manu Yosepu alikuwa hapendi kutumia "Lift" anapopanda ngazi za jengo la ghorofa. Huo ulikuwa ni utamaduni wake na huwezi kumbadilisha. Ilikuwa ni moja ya mazoezi yake ya kuimarisha misuli ya miguu katika upandaji wa ngazi. Bwana Mathew Kilanga alishaanza kuulizia kwa sekretari wake kama Kachero Manu kasharipoti kazini usiku huo au bado. Uzuri wake kutoka anapoishi Kachero Manu na ofisini kwao ni mwendo wa robo saa tu kwa kutembea. Ilipofika saa 4:36 usiku Kachero Manu akagonga mlango wa ofisi kwao kuelekea kwa mkuu wake wa kazi kisha akanyonga kitasa bila kusubiri kukaribishwa akapokewa na tabasamu mwanana la sekretari wa bosi, Kokunawa. Habari za usiku dada "Koku", Mkesha wa watu wasiojulikana unaendeleaje? alitania kachero Manu kumtania Kokunawa kawa kawaida yao. "Habari za usiku ni mbaya , hongera zako unaetoka usingizini, mimi na bosi wako tuko kazini toka asubuhi saa 1:30, ila kupenda kwako usingizi kutakuotesha kitambi shauri yako ushindwe kazi zote mbili za nyumbani kwa wifi na za ofisini zinazokupa mkate wako wa siku, ooh wewe haya tu" wakacheka wote kwa pamoja kicheko cha nguvu kwa mapigo ya utani wa Koku.
Ghafla simu ya mezani ya sekretari Kokunawa ikaita tena, ilikuwa inapigwa toka kwa bosi akiulizia kama kachero Manu kasharipoti ofisini, akajibiwa ndio ameingia hivi sasa. Alivyokata simu tu, Kokunawa akamwambia Kachero Manu "fanya haraka bosi anasema hana muda wa kupoteza, amekuwa mkali kama pilipili na sauti yake inaonyesha kashaanza kukasirika, si unamjua bosi wako kama kazaliwa na kazi vile utasema Tanzania ya baba yake mzazi". "Sawa ngoja nimuone haraka, tutaonana nikitoka nataka nikupeleke kula mlo wa usiku kwenye hoteli kubwa kubwa binti mrembo upumzike kula senene kila siku" akajibu Kachero Manu huku akitokomea kwenye veranda ya kuelekea kwenye mlango wa ofisi ya bosi wake, akimuacha sekretari Kokunawa yupo hoi kwa kicheko hana mbavu.
Alivyofika akagonga hodi na kufungua mlango moja kwa moja kisha akasalimia "Shikamoo Kiongozi, habari za usiku huu". Bosi wake alimkuta bado amesimama hajakaa kwenye kiti chake, akajibu salamu hiyo. "Habari za usiku ni mbaya sana, karibu kiti ukae" huku akimuashiria kwa mkono kiti cha kukaa. Ahsante sana akajibu kachero Manu, kisha akavuta kiti akakaa na akatoa kompyuta mpakato yake kutoka kwenye begi lake akaiwasha, kisha akaitafuta pragramu ya uandishi ya "mikrosofti wordi" tayari kwa kuandika vitu vya msingi kwenye majukumu ya kazi atakayopewa. Kikapita kimya cha kama dakika moja, bosi akakohoa kikohozi kikavu, kisha nae akaja kuvuta kiti chake akakaa. Akachukua chupa yake ya kahawa akamimina kikombe kimoja kikubwa akaifunga, kisha akapiga mafunda matatu mfululuzo huku amefumba macho yake mithili ya mnywaji pombe haramu ya "Gongo", kuonyesha uchungu wa kahawa hiyo.
Halafu akaisogeza chupa pale alipoketi kachero Manu kumpa ishara kuwa anaruhusiwa kunywa kahawa akipenda, kisha akaanza kuongea huku anamkazia macho Kachero Manu. "Mtu asiyejulikana amefanya tukio baya tena, muda mfupi uliopita kamuua Profesa Kaganda mhadhiri nguli wa Chuo cha usimamizi wa fedha 'IFM'". akaweka kituo cha mazungumzo yake kisha akamimina tena kahawa kwenye kikombe akaendelea na mazungumzo yake. "Sasa agizo toka kwa wakubwa juu wamependekeza wewe ndio uhakikishe unakomesha mauaji haya ya hovyo hovyo yanayochafua taswira ya Tanzania kimataifa, nchi ambayo tunajulikana kama kisiwa cha amani.
Tunafahamu kuwa wewe ni Kachero maalumu wa matukio makubwa ya kimataifa, huwa hatukusumbui kwenye matukio ya kihalifu madogo madogo, lakini kwa hili tunaomba sana utusaidie. Maana wananchi wa zama hizi ni waelewa sio wajinga huwezi kuwadanganya kuwa tunafuatilia tu, lazima tuonyeshe juhudi za kweli kukabiliana na mauaji haya hobelahobela yasiyojulikana chanzo. Maana Tatizo la Watanzania kila tukio la hovyo kama hili watalinasibisha na siasa hata kama chanzo kikiwa ni kingine. Tunatambua kazi yako ya kutukuka kule Cabo-delgado, Msumbiji (Soma Riwaya CABO-DELGADO) ulivyowatia adabu vibaraka wa makaburu, pia kule Kigali ulipomshikisha adabu kahaba aliyetishia maisha ya viongozi wa serikali na wafanyabiashara (Soma Riwaya DILI LA COVID 19), na kazi zako lukuki za kuwaadabisha wahujumu wa amani na usalama wa nchi.
Sasa hauna muda wa kupoteza, ndani ya wiki moja tu mtuhumiwa awe amekufa nataka nione maiti yake au awe yupo hai namtaka nimuone anapandishwa kwenye karandinga la magereza Kuelekea Mahakamani ili haki itendeke. Ripoti kamili walipofikia polisi kwenye upelelezi wao wa tukio hili ipitie kwa katibu muhtasi dada yako Koku ameshakuandalia. Kwa kuanzia sasa hivi kwanza uelekee eneo la tukio kwenye mkahawa wa Break Point, Kinondoni upate penyenye zinazoweza kukusaidia katika upelelezi wako. Jeshi la polisi limenyoosha mikono juu, zigo umetwishwa wewe, kachape kazi" alimalizia maongezi yake mafupi Bwana Mathew Kilanga.
Wakaagana nae haraka haraka Kachero Manu akafanya hima kwenda kwa katibu muhtasi wao kuchukua nyaraka ili awahi eneo la tukio kabla ushahidi haujaharibika. Mbona mnuno kama wote, kama vile umenyweshwa uji wa shubiri kulikoni mwenzetu" katibu muhtasi Koku kama kawaida yake alimpiga kijembe Kachero Manu wakati alikuwa anajua fika kila kitu kilichosababisha aitwe ofsini Kachero Manu usiku huo.
" Acha utani Bibi kimeshanuka tayari huko, Babu yako kashanitibulia mapumziko yangu usijifanye hujui kitu, kasema nikabidhi kila kitu tena kwa haraka asije kunikuta hapa bado nipo ninasogoa kikazuka kisanga kipya" aliongea kiunyonge Kachero Manu kiunyonge mkubwa kuonyesha hajapendezwa na majukumu aliyopewa ila ndio kazi aliyoajiriwa nayo hana budi kutimiza wajibu wake.
Ilibaki kidogo tu apinge yeye kukabidhiwa jukumu hilo wakati wapo vijana wengi idarani wachanga ambao wangeweza kupewa jukumu hilo. Kwake yeye alijifananisha na nyundo inayotaka kuondosha uhai wa inzi, wakati kofi moja tu kungetosha. Ila aliposikia yeye kusimamia upelelezi huo ni agizo toka mamlaka za juu, akanywea akawa hana ujanja tena bali ni utekelezaji tu.
Mbio za sakafuni huishia ukingoni, hivyo janja janja yote ya Profesa Kaganda ya kuwanyanyasa kingono watoto wa walalahoi waliopata bahati ya mtende ya kusoma elimu ya chuo kikuu ikageuka kuwa ni historia. Alisahau kabisa msemo wa wahenga, yakuwa tamaa mbele mauti nyuma. Mabinti ambao walikuwa wanategemewa na familia zao zenye kipato cha kijungu meko, waje kuwakomboa kutoka kwenye lindi la umaskini, yeye Profesa badala ya kuwa daraja la kuwavusha kwenye mto wa ufukara, na kuwapeleka katika nchi ya maziwa na asali yeye akajigeuza kuwa mamba wa kuwatafuna vidosho hao mtoni bila huruma.
Majuto ni mjukuu, akawa sasa yupo ndani ya friza mochwari huko Muhimbili tayari kuandaliwa kupelekwa kuzikwa huko kwao Bukoba kwenye mashamba ya ndizi. Kachero Manu alitinga ndani ya muda muafaka huku akikuta bado maiti haijaondoshwa eneo la tukio. Maiti ya Profesa Kaganda ilikutwa imekatwa sehemu zake za siri, huku ikiwa imepigwa risasi eneo la moyo ipo ndani ya gari imelazwa. Aliyegundua maiti hiyo alikuwa ni mlinzi wa eneo hilo baada ya kuona wameingia watu wawili kwenye gari kisha akatoka mmoja tu tena kwa haraka na kutokomea zake kisha gari haiondoki. Alipokwenda kufanya taftishi kulikoni kwa kuchungulia kwenye kioo cha gari, ndio akakutana na kimbwanga hicho cha kushtusha.
Kwa kutumia vifaa vyake vya kazi Kachero Manu akiwa amevaa vikinga mikono yake, akachunguza anachokitaka kisha akapiga picha kadhaa anazotaka na kutoa maagizo kadhaa kwa wana usalama waliokuwa wanafuata muongozo wake kuhusiana na kwenda kuhifadhi mwili wa Profesa gwiji wa mambo ya takwimu. Mhudumu aliyewahudumia Profesa na Shebby kwenye meza yao akaitwa na kuhojiwa ili atoe maelezo nyoofu yanayoweza kusaidia upelelezi huo.
Kachero Manu: "Habari yako na pole na matatizo, ehee... unaitwa nani, na una umri gani? "
Mhudumu: " Nimeshapoa tayari, naitwa Angela Chama, mwezi Desemba mwaka huu natimiza miaka 26"(Alijibu huku anajifuta machozi kwa hanchifu yake nyeupe)
Kachero Manu: "Ehee..unafahamu nini kuhusu marehemu Profesa Kaganda maana wewe ndio mshukiwa namba moja, maana umemuhudumia mwanzo mwisho mpaka akazidiwa na kileo"
Mhudumu: " Mama weeeeh...kaka polisi muogope Mungu wako, mie ninahusikaje hapo jamani ?"(Alilala mhudumu Angela huku anaanza kububujikwa na machozi ya nguvu)
Kachero Manu: "Tuliza mzuka, nieleze sasa unachokijua kama kweli wewe sio mhusika! "(Kachero Manu alikuwa anatabasamu lengo lake limeshatimia la kumpanikisha Angela ili atapike kila kitu anachokijua)
Mhudumu: "Sawa!.Profesa alikuja hapa mkahawani kwetu kama kawaida yake majira ya kama moja usiku. Bahati nikawa mimi sina mteja wa kumhudumia nikamkaribisha kwenye meza iliyo tupu akakaa hapo nikaanza kumhudumia.
Baadae waliongezeka wateja wengine wawili wakakaa nae pamoja. Baadaye mmoja wao alijitambulisha kwangu kama ni ndugu yake na Profesa baada ya kutaka kufungua bia ya Profesa alipoenda msalani akanizuia. Baadae waliondoka pamoja akiwa anamkokota, Profesa akionekana amezidiwa na kileo. Hivyo ndivyo kwa ufupi ninavyofahamu tukio hilo"
Kachero Manu: " Je huyo aliyejitambulisha kama ndugu, umeshawahi kumuona hapa mkahawani katika siku za nyuma? "
Mhudumu: "Hapana kwakweli na alikuwa haonekani vizuri kwa sababu alivaa kofia kubwa ya pama na miwani usoni"
Kachero Manu: "Uliwahi kumtilia mashaka kama ni mtu muovu? "
Mhudumu: "Hata chembe sikumshuku,maana kipindi nataka kufungua kinywaji cha mwisho cha Profesa wakati hayupo mezani Profesa alinikataza kata kata kuwa nimsubirie kwanza Profesa arudi msalani ndio nifungue kwa kuhofia masuala ya kiusalama. Pia kwa jinsi walivyokuwa wanaongea wawili hao kwa bashasha ni kama vile wanafahamiana sana"
Kachero Manu: "Je imeshawahi kutokea siku za nyuma Profesa kuzidiwa na kinywaji mpaka kubebwa?"
Mhudumu :" Sijawahi kushuhudia nikiwepo zamu kumuona amezidiwa labda kwa siku ambazo sipo kazini! "
Kachero Manu: "Sasa kwanini hukutilia mashaka kuwa kama kuna jambo baya limemkumba?".
Mhudumu: "Aaaah..mmhhhh..(Kijasho chembamba kikawa kinamvuja mhudumu yule hana cha kujibu)
Kachero Manu: "Au hujaelewa swali, nirudie tena kuuliza? "(Alitilia msisitizo huku akimkazia machoni kuonyesha yupo kazini hatanii)
Mhudumu: "Nimeelewa swali, siwezi kumjibia marehemu kwa sababu siku hazifanani, huenda alianza kupata moja moto moja baridi viwanja vingine hapa akaja kusuuzia tu. Hiyo inatokeaga tu mara nyingi kwa walevi hata wale nguli"( Alijibu kiumakini yule dada mhudumu).
Kachero Manu: "Ahsante kwa ushirikiano wako, sitosita kukutafuta tena kwa mahojiano zaidi ikibidi kufanya hivyo. Ila kanionyeshe meza waliyokuwa wamekaa na nadhani mlipewa maagizo msiondoshe kitu chochote mezani hapo! "
Mhudumu: "Tulipokea maagizo hayo na tumeyafanyia kazi, hakuna kilichoondolewa eneo la tukio" alijibu mhudumu yule kwa kujiamini akiwa sasa uoga wote umemuisha, huku akinyanyuka kuelekea kwenye meza waliyokuwa wameketi Profesa Kaganda na Shebby.
Walipofika hapo kwenye meza, Kachero Manu akakagua vilivyo meza hiyo na mabaki yaliyobaki ya pombe ya Profesa Kaganda yale ya kwenye chupa na kwenye glasi. Akaamrisha iende kupimwa kwenye ofisi ya mkemia mkuu. Kabla hajaondoka pale mezani akaona dawa ya kutibu ugonjwa wa macho chini ya meza, ambayo iliyofunguliwa kuonyesha kuwa imetumika tayari ikiwa imetelekezwa eneo la tukio. Kwa Kachero makini kila kitu chochote eneo la tukio ni msaada mkubwa kukufikisha kwenye uchunguzi sahihi. Kachero Manu akatabasamu kisha akavaa vikinga mikono yake na kuiokota dawa hiyo na kuifadhi kwenye vyombo vyake maalumu. Baada ya hapo akawa ameshamaliza taftishi yake aliyoikusudia, huku muda ukiwa umeyoyoma, saa ikisoma saa 7:15 usiku.
Nilipozinduka nilisimuliwa na manesi wanaonihudumia kuwa niliokolewa na polisi wa doria mtaani waliopigiwa simu na wasamaria wema. Polisi hao walifanya juhudi kubwa ya kunichomoa kutoka kwenye mikono ya wananchi wenye hasira kali kwa kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya raia hao. Polisi wale wakanibeba mzobemzobe kwenye gari lao mpaka hospitali ya taifa ya Muhimbili. Nilizindukia hospitalini Muhimbili nikiwa nimetundukiwa dripu za damu. Niliambiwa nilizimia kwa zaidi ya masaa 7, na nilipoteza damu nyingi sana. Shukrani za pekee kwa madaktari wa hospitali ya taifa Muhimbili, kwa juhudi zao za kuokoa uhai wangu vinginevyo ningekuwa marehemu tayari. Mkono mmoja wa kushoto nilikuwa nimefungwa pingu iliyounganishwa na kitanda cha chuma, kuashiria nje ya wodi kuna askari maalumu anayechunga usalama wangu. Kila nilipokuwa nafikiria tukio zima, nikilikumbuka machozi yalikuwa yananibubujika kama maji bila kikomo. Nikakubali matokeo kuwa mkubwa ni jaa, hivyo sina budi kupokea misukosuko toka kwa Maulana kwa moyo mkunjufu, huku nikiamini Mungu pekee ndio atakayenitakatisha kutoka kwenye tuhuma hizo chafu walizonibambikizia, zisizo na kichwa wala miguu. Mwili wangu ulikuwa umepambwa na mishono ya nyuzi za madaktari katika harakati zao za kudhibiti upotevu wa damu mwilini mwangu. Sindano ya ganzi ilipoisha nguvu yake, maumivu ya mwilini mwangu yalikuwa makali hayaeleweki utasema kuna mtu amechukua kisu kikali cha buchani ananicharanga nacho mwilini. Njaa ilikuwa kali lakini hamna wa kuniandalia chakula zaidi ya uji wa hospitalini niliyoletewa na nesi wangu muuguzi. Hakuna ndugu wala jamaa aliyejitokeza pale hospitalini labda kutokana na ukosefu wa taarifa za tukio baya lililonikumba. Baadhi ya manesi na madaktari walianza kuninyanyapaa na kuniangalia kwa sura ya mabezo baada ya kupata taarifa kuwa nimechezea kipigo kutokana na jaribio la ubakaji kwa mwanafunzi. Nikamshukuru Mungu wamechelewa kujua mpaka wamenipa huduma zote stahiki vinginevyo wangenitelekeza mapokezi mpaka ningefariki. Wananchi walikuwa tayari wameshanihukumu kwenye mahakama zao za mtaani kuwa mimi ni mbakaji nimestahiki malipo ya uovu wangu. Maneno ya ahlan wa sahalan ya binti yule mwanafunzi kuwa nimembaka tayari yalishaniletea ngondo na wanajamii. Wanajamii ambao walionekana wamechoshwa haswa na kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto wadogo vinavyofanywa na watu wazima, bila kuchukuliwa adhabu stahiki na vyombo vya dola. Kila raia mwema aliyepata taarifa ya kutaka kubaka, waliniona mimi ni mlanisi wa chusu, kifo kilikuwa halali yangu. Tayari wana habari wa mtaani walishasambaza habari zangu kwenye mitandao ya kijamii yote kuwa Mchumba wa Miss Tanzania, Zabibu ameshushiwa kipigo kwa kutaka Kubaka mwanafunzi maeneo ya Makongo. Lengo la Naibu Waziri Mkuu Dr.Sanko la kunichafua heshima na hadhi yangu katika jamii kulitumia, ili tu kumfanya mpenzi wangu Zabibu akasirike kisha animwage na yeye apate upenyo wa kumtwaa jumla jumla Zabibu. Kwenye mitandao ya kijamii huko watu walikuwa wananiona mkia wa mbuzi tu, sina thamani hata chembe. Kisanga changu kilipomfikia Zabibu huko ughaibuni kwenye mashindano, moyo wake ulimpasuka haswa. Dunia ya sasa ni kama kijiji kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hivyo ndani ya muda mfupi taarifa zikamfikia kupitia mtandao wa kijamii wa 'Instagram' na makundi ya 'Whatsapp'. Taarifa ambazo zlimfedhehesha na kumhuzunisha vilivyo huku akiwa haamini kama kweli Shebby anayemjua yeye anaweza kufanya tukio kama hilo la aibu. Taarifa ambayo ilisababisha maandalizi ya Zeddy kwa ajili ya mashindano hayo yadorole vilivyo, na siku ya fainali hizo za Miss World alifanya vibaya sana kwa kushika mkia kwa warembo wa dunia nzima. Aliporejea tu nchini Tanzania akanikuta tayari nipo rumande gerezani nimeshapandishwa kizimbani zaidi ya mara mbili. Akafanya hima hima pa mtima pamoyo kuja kunitembelea gerezani, huku nikimuapia haki tena kuwa sina hatia, waja wananipakazia.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment