Search This Blog

Wednesday 22 March 2023

UKURASA WA GAIDI - 4

  

Simulizi : Ukurasa Wa Gaidi 

Sehemu Ya : Nne (4)


"Hivi blaza mbona unapenda kusumbua watu kwa maswali ya kiboya.Mi nilikuona kama mstaarabu kumbe hovyo tu.Au tuseme hujui kusoma.Pita uone utakavyo chezea vitasa hadi ujinyee".Alijibu kwa jazba dreva yule huku akinyoosha kidole mahali fulani kama vile anataka Kumuonesha Mick kitu fulani upande wa kushoto kwake.

Mick alipogeuka kutazama upande ule ndiyo kwanza aliona kibao kilichoandikwa " ILANI. NI MARUFUKU KUPITA BARABARA HII NYUMA YA KAMBI.UKIPATIKANA UTAONA CHA MOTO."Kibao kile kilijieleza.

"Bas poa blaza.Shika hii ya maji."Aliongea tena Mick huku akimkabidhi dreva yule noti tatu za shilingi elfu kumi kumi.Ustaarabu wa dreva yule alioonekana nao mara ya kwanza ukarudi tena wakati huu alipokuwa akipokea fedha hii na kushukuru huku akiwa kama haaminikama kuulizwa swali moja tu la kipuuzi ambalo amejibu kwa jazba kumempa pesa yote hii kabla hata ya mchana.Tabasamu lilichomoza usoni mwa dreva huyu ambaye sekunde chache zilizopita alimjibu Mick kwa ghadhabu.Ama kweli pesa ni sabuni ya roho.

"Hawa madreva wa magari makubwa sijui wana matatizo gani.Yaani akili zao wanazijua wenyewe".Aliwaza Mick wakati akiwa amerudi ndani ya gari lake.

"Lakini mbona mimi nimepita barabara ile na nimeshuka na kukaa zaidi ya dakika ishirini bila kubugudhiwa na mtu.Au kamera zimekufa."Alijiuliza Mick.Alihisi taa nyekundu kuwaka kichwani mwake.Yeye kama mwana usalama yeyote,alihisi kuwepo kwa mchezo mchafu.Ndiyo.Kwa nini kamera ziharibiwe.Kwa nini magaidi walipita njia ile.Alipojaribu kuunganisha mambo haya,Mick alihisi kuwa kuna jambo limejificha nyuma yake,hii haikuwa 'Coincidence'.

Mick aliendesha gari lake kurudi ' safe house' huku akiwaza jambo hili na lile.Mwisho aliamua kuwa muda utatoa majibu muafaka wa maswali aliyojiuliza kichwani mwake,japo muda hausubiri mtu



Vipi umepata jipya lolote".Mick alimuuliza swali Clara mara tu alipoingia katika ofisi yao ndani ya 'safe house'.

"Dah ....nimepata baadhi ya mambo ambayo yamezaa ugumu katika kung'amua kipi ni kipi."Clara alijibu jibu lililosababisha Mick avute kiti kilichokuwa sambamba na meza nyingine ili aweze kusikiliza vizuri alichomaanisha Clara.Clara wakati huu wote alikua akiongea huku akibonyeza bonyeza hapa na pale katika keyboard ya kompyuta yake.

"Enhee....Hebu nieleze ni nini hicho kigumu".AlihojiMick.Wakati huu maajenti wote walikuwa wamekaa katika viti vyao vilivyokuwa na meza zilizobeba kompyuta juu .Clara alibonyeza hapa na pale katika kompyuta.Mara mbele yao kulikokuwa na 'screen' kubwa, pakaonekana taswira ya kile ambacho Clara alikuwa akikifanya katika kompyuta yake,kile ambacho Clara alitaka wote wakione.Kisha akaanza kuzungumza kwa sauti iliyowafikia wote vizuri.

"Kwanza kabisa ,nilifanikiwa kuvunja kuingilia mfumo wa kamera za CCTV za pale kambi ya JKT Mafinga, kwa lengo la kutazama video kama ambavyo Mick alinielekeza.Lakini hakuna kilichoonekana kurekodiwa,yaani kitaalamu ningeweza kusema kuwa yawezekana zimeungua au 'connection' zimefeli.Ili kuhakikisha kama nilichokiwaza ndicho nikawasiliana na mtu mmoja yuko pale jeshini, ni rafiki yangu wa miak mingi na yupo katika kitengo cha utaalam wa kompyuta. Nilimuuliza ' kijanja janja' kuhusu kamera zao.Nilijifanya kuwa nataka kuwea kamera kama zile nyumbani kwangu.Na hapo hapo nikamdadisi kiundani kuhusu kamera zao,nayeye akanijibu kiufasaha bila kujua kuwa namdadisi."Clara alinikohoza kidogo kuweka koo sawa kisha akaendelea kuongea .

"Katika mazungumzo yetu,niligundua kuwa kamera ile upande wa nyuma wa kambi iliungua tangu wiki iliyopita.Kuna kifaa waliagiza kutoka nje ya nchi ndicho kilichochelewesha kwa matengenezo kufanyika kwa kuwa bado hakijafika labda hadi wiki ijayo.Hapo nikaamua kutumia njia nyingine ambayo mara ya kwanza sikuiwaza kwa karibu.Lakini kabla sijawaeleza kuhusu hilo ngoja niwaeleze kitu kimoja ambacho nadhani wengi hatukifahamu sana.Hasa nyie ma 'field agents' kwa kuwa wakati kinafanyika nyinyi mlikuwa mafunzoni nje ya nchi.Labda mnakifahamu juuu juu tu lakini nadhani hamkifahamu kiundani.".Aliongea Clara,akaweka kituo kisha akaendelea kuongea tena.

"Miaka mitano iliyopita wakati ambao wengi wenu mlikwenda nje ya nchi kupata mafunzo yanayohusiana na idara hii,taarifa za kiintelijensia zililetwa mezani kuhusiana na kugundulika kikundi cha magaidi ambacho kilikuwa kimeweka makazi yake huko Tanga katika mapango ya Amboni.Wengi wetu tulipata habari hii kwa kuwa ilisambaa sana duniani.Ila tu kitu ambacho wengi hawakukijua ni kuwa dhumuni la magaidi hawa walikuwa wakijiandaa kuvuruga uchaguzi mkuu wa kwanza wa awamu ya nne.Walipanga kuwaua wagombea wa vyama pinzani vyenye nguvu vitakavyoingia katika kinyang'anyiro hicho.Lengo lao kuu lilikuwa ni kuwachanganya wananchi wenye hasira kwa kukishutumu chama tawala kuhusika na mauaji hayo ili vurugu kubwa zitokee.Wakati ambao vurugu zingetokea kubwa sana basi wenyewe wangeingia nchini na kuifanya nchi kuwa kama Somalia ilivyo leo hii. Kitu ambacho bado kilikuwa katika upelelezi hadi leo hii ni kuwa, wanufaika wa mambo hayo ni akina nani,na palikuwa na hisia ambazo hadi sasa ni ngumu kuthibitisha,kwamba kuna wahusika kutoka ndani ya nchi yetu ambao wangenufaika zaidi."Aliongea kwa tuo Clara kisha akaendelea kuongea.

"Lakini kwa bahati nzuri mashushushu wetu wakaling'amua swala hilo na kulileta mezani.Mara baada ya kupata taarifa za kutosha kadri ya ilivyowezekana kuwahusu,jeshi la wananchi likavamia eneo hilo ili kuwaangamiza.Japo walifanikiwa lakini mazingira yalionesha sehemu ya wahusika wa kundi hilo walitoroka muda mchache kabla ya vikosi vya majeshi yetu kufika.Wasiwasi wa kuwepo wahusika wa mpango huo ndani ya nchi ukaongezeka kwa sababu kutoroka kwa baadhi ya wahusika kulihisiwa kutokea kwa sababu ya kuvuja kwa taarifa.Swala hili nalo limeendelea kuchunguzwa hadi hivi leo na wapelelezi wa majeshi yetu,lakini muafaka bado haujapatikana."

"Kwa sababu hiyo ,serikali ikaamua kujitahadharisha kwa kuingia gharama kuimarisha ulinzi hasa maeneo ambayo pengine ilihisiwa yangeweza kuvamiwa.Kati ya njia zote za kuimarisha ulinzi maeneo mbalimbali ya nchi,mojawapo ilikuwa ni kununua kamera za CCTV za kutosha na kuzifunga maeneo yote hatarishi, na barabara zinazoelekea huko kwa umbali fulani.Sehemu ya maeneo hayo ilikuwa ni pamoja na kambi za JKT na JWTZ pamoja na vituo vya polisi hasa vile vikubwa nchi nzima. Wasiwasi ulikuwapo zaidi maeneo haya kutokana na matukio ambayo nchi yetu imeyaona ya vituo vyetu vya polisi kuvamiwa na watu wasiojulikana na kupora silaha kisha kutokomea nazo."

"Kamera zilizofungwa katika maeneo ya kambi za majeshi yetu,zilipita katika mikono ya wataalamu wachache wa teknolojia kutoka kitengo cha intelijensia cha jeshi la wananchi cha MI(Military intelligency) kwa siri kubwa sana.Wataalamu hawa walipandikiza 'Memory chip' ndogo sana ndani ya kamera hizo ambazo zina uwezo wa kutunza kumbu kumbu za muda mrefu sana bila kuhitaji kufuta kumbu kumbu zingine.Chip hizi ziliwekwa ndani ya kamera kitaalamu,hivyo kamera zile zina uwezo wa kuhifadhi kumbu kumbu katika mifumo miwili.Katika kamera yenyewe na katika mfumo wa kurekodi wa kawaida.Hivyo hata mawasiliani kati ya kamera na vifaa vinavyotunza kumbu kumbu ndani ya jeshi,bado kamera ziliendelea kurekodi na kutunza kumbukumbu hapohapo katika kamera.Hii ni siri inayofahamika na watu wachache sana."Alimaliza kuonge Clara kisha akaanza tena kuzungumza.

"Sasa katika haya yaliyojiri leo hii, nilipoingilia mfumo wa kamera za pale kambi la jeshi la Mafinga , na kugundua kugundua kuharbiwa kwa mfumo wa ndani wa kutunza kumbukumbu,ilibidi niingilie mfumo wa siri wa nje wa kutunza kumbukumbu.Hapo nikakuta kumbu kumbu bado zimetunzwa vizuri tu.Ila tu nadhani nihitilafu fulani ilitokea wakati mfumo ulipoharibika, kumbukumbu zilizopo zimeishia wiki mbili zilizopita.Lakini kwa kushauriana na wataalamu wengine wa kompyuta ndani ya idara,tumeonelea tuchunguze matukio yaliyotokea kuanzia miezi mitatu iliyopita hadi mwisho wa rekodi, nadhani kuna kitu tutakipata."Alimaliza kuongea Clara.

"Duh ...kazi ngumu bado.Unafikiri unaweza kukufuatilia video hiyo kwa muda gani".Alihoji Mick.

"Nikisaidiana na wenzangu, nadhani ndani ya masaa 72 nitakuwa nimemaliza".Alijibu Clara.

"Ok......basi wacha tuendelee kufuatilia habari hizi ,nakutegemea sana kwa utakayoyapata humo"Aliongea Mick kisha akanyanyuka na kutoka katika ofisi hiyo.

********************************************************************


SAA TISA ALASIRI KESHO YAKE.

Timu nzima ya maajenti idara ya CTI walikuwa katika ofisi yao wakiwa kimya na umakini wa hali ya juu.Mbele yao alikuwepo ajenti Morris,mtaalamumwingine wa 'data analysis' katika idara ya CTI, alikuwa akielekeza kitu kilichofuatiliwa kwa ukaribu sana na wanaidara wote ndani ya chumba hiki.

"Jamani kwa bahati nzuri kazi ya kufuatilia matukio katika kumbukumbu zilizorekodiwa kati iamera za jeshi katika kambi ya jkt Mafinga,imekwisha kabla ya muda tulioomba na tumefanikiwa kupata kitu ambacho labda kinaweza kuleta ufumbuzi kiasi chake. Kitu tulichokiona kipo katika kipande hiki cha video kilichorekodiwa na kamera wiki tatu siku kadhaa zilizopita."Alimaliza kuongea Morris kisha akabonyeza katika kompyuta yake hapa na pale, video iliyokuwa katika kompyuta hiyo,ikaanza kuonekana katika screen kubwa iliyokuwa mbele ukutani.

Kilikuwa ni kipande kifupi cha video.Lilionekana gari aina ya Rangerover vogue nyeusi likifunga breki pembezoni mwa barabara, ile iliyopita nyuma ya kambi la jeshi jkt Mafinga.Barabara ile ambayo ajenti Mick alipita jana yake. Mara baada ya gari hilo kusimama, video hiyo inamuonesha mtu aliyevalia sare za jeshi akilisogelea gari hilo.Mtu huyu alione kana kwa upande wa nyuma kisogoni.Hii ilimaanisha alitokea upande ambapo kamera zile zipo kisha akazipa kisogo. Mtu huyo akaenda hadi mahali gari lilipopaki ,mlango wa nyuma upande wa kulia wa gari huku akiwa bado ameipa kamera kisogo.Akagongakatika kioo cha gari,hapo kioo kikashushwa kisha mlango ukafunguliwa.Mtu huyu aliyevalia sare za jeshi akapanda gari lile, mlango wa gari ukafungwa na gari likaanza kuondoka taratibu .

"Vipi kuna kitu sijui mmegundua, kabla mtu huyu hajapanda gari kuna kosa alilofanya ambalo ndilo limeikamatisha sura yake kwetu"..Aliuliza Morris huku akirudisha video nyuma na kuisimamisha katika kipande kilichoonesha mtu huyu asiyefahamika akigonga katika dirisha la gari lile.

"Hapana kwa kweli mimi naona huyu jamaa alikuwa makini sana kiasi cha kutogeuka nyuma hata kidogo hivyo itahitaji nguvu kubwa kumtambua".Alijibu ajenti Paul ambaye alikuwa kimya tangu mwanzoni mwa kikao hiki huku wana idara wengine baadhi wakitingisha vichwa kuonesha nao walikuwa wanawaza kama Paul.

"Lakini hakuwa makini kwa kiasi cha kutosha kuificha sura yake kikamilifu".Aliongea tena ajenti Paul huku akitabasamu.Sura za wanaidara wengine zikamuangalia kwa mshangao wa kumaanisha kuuliza alikuwa anamaanisha nini.

Hapo ajenti Morris aka'zoom'kile kipande cha video alichokisimamisha. Katika kipande kile cha video, yule mtu alipokuwa akigonga kioo cha dirisha la gari huku akizipa kisogo kamera, taswira yake ilionekana kupitia kioo cha gari lile.

"Hahaaaa....bingo.Safi sana .Kazi nzuri sana."Alicheka kwa sauti ajenti Mick huku wengine wakipongeza hilo kwa kutikisa vichwa.

"Japo taswira haionekani vizuri,tunaweza kutumia programu ya 'face matching' ambayo kama mtu huyu kama ni askari basi ataonekana kupitia mtandao wa wanausalama wa idara ya MI.Hilo ndiyo bado hatujalifanya hadi sasa."Alimaliza kuongea Morris.Wakati huo Clara aliyekuwa karibu na Morris,akabonyeza hapa na pale na programu ile aliyokuwa akiisema Morris ikaonekana katika screen kubwa ukutani.

Clara aliiunganisha taswira ile iliyoonekana katika kioo cha gari lile na mamia elfu ya picha za askari waliowahi kutumikia majeshi ya Tanzania tangu nchi ilipoanza kuwa na majeshi yake yenyewe hadi sasa.Kwa kupitia programu ile ya kufananisha, picha zilianza kubadilika badilika kwa kasi sana. Zoezi lilichukua dakika tatu hadi pale picha iliyofanana ilipoonekana katika screen ile kubwa.

"Match found 92%". Programu ile iliandika hivyo kwa kumaanisha kuwa taswira ile imepata picha inayofanana nayo kwa asilimia 92.Kwanza kabisa maajenti wote wakafurahi kwa kuwa kazi ilionekana imekuwa rahisi sana kwa kuwa wamempata mtu ambaye walau wakimbana ataleta mwanga wa wapi pa kuanzia kuifanya kazi ya kuwakamata walengwa wao.Lakini waliposoma mwisho wa maelezo yaliyokuwa pembeni mwa picha ile,waliona maandishi yaliyokuwa na rangi nyekundu yaliyoandikwa kwa herufi zenye umbo kubwa zaidi ya zingine,pengine ili zionekane vizuri kwa wengine.Maandishi haya ya mwishoni ndiyo yalisababisha kitendawili kingine kitokee ambacho ni kigumu zaidi kukitegua.

*************************************************************************;*************************

'Anaitwa John Karobota,alizaliwa mwaka 1970,alisoma chuo kikuu cha Dar es salaam kozi ya civil engineering,aliajiliwa najeshi la wananchi Tanzania JWTZ mwaka 1995".Hayo yalikuwa ni baadhi ya maelezo yaliyoonekana katika 'profile' ya mtu huyu ambaye sasa alijulikana kuwa anaitwa John Karobota.

Baada ya maelezo mengi katika 'profile' hiyo,mwishoni kabisa kulikuwa na neno lililoonekana kama muhuri mwekundu 'DECEASED'.Hii ilimaanisha kwamba mtu huyu alikwishafariki.Na chini ya neno hilo kulikuwa na maelezo yaliyo gongelea msumari wa mwisho kwa maajenti hawa wa CTI waliodhani kwamba sasa wangepata mwanga wa kesi hii wanayoifuatilia."Alifariki mwaka 1998 tarehe7,Agosti katika shambulio la kigaidi ubalozi wa Marekani Dar es salaam Tanzania.Alikiwa ubalozini hapo katika kushughulikia 'Visa' yake ya kwenda Marekani ambako alitakiwa kwenda kuongeza mafunzo ya kijeshi,katika kudumisha ushirikiano wa Marekani na Tanzania.Mara baada ya shambulio la kigaidi kutokea,maiti yake ni miongoni mwa maiti ambazo hazikuonekana,hivyo ikakadiriwa kuwa miongoni mwa watu walioteketea kabisa kwa moto na kufariki,kwa kuwa chumba alichokuwamo wakati wa tukio ni kati ya pande zilizodhurika kabisa."

Haya maelezo yalichanganya vichwa vya maajenti hawa wa idara ya C.T.I.Labda ni kwa kutambua kuwa ile programu waliyoitumia kufananisha taswira ya huyu mtu waliyekuwa wanahangaika kumtambua na picha za askari wote wa nchi hii,ilikuwa ni teknolojia ya hali ya juu sana ambayo hutumiwa hata na idara za intelijensia za mataifa yaliyo katika ulimwengu.wa kwanza.Yaani ni ya teknolojia ya hali ya juu sana kiasi kwamba haiwezi na haijawahi kutoa majibu ya uongo.Sasa leo hii inaonesha taswira ambayo imepatikana kutoka katika kumbu kumbu zilizorekodiwa wiki mbili zilizopita,ni ya sura ya mtu aliyefariki mwaka 1998, yaani miaka kadhaa iliyopita.

Swali lililozunguka katika vichwa vya vijana hawa wakakamavu wenye weledi wa juu katika kazi yao ni ,"mtu aliyefariki mwaka 1998, ni kwa namna gani aonekane tena katika video hii ya wiki mbili zilizopita?".

"Lakini hapo mwishoni, maelezo yanaonesha kuwa mwili wake haukupatikana na ikahisiwa tu kuwa pengine ni miongoni mwa watu walioangamia kabisa.Kama ni hivyo mimi nadhani tusiumize vichwa sana bila sababu.Ni wazi kuwa John Karobota aliokoka na tukio hili.Nadhani sasa tusijiulize 'yawezekana vipi' bali tujiulize namna tunavyoweza kumpata."Aliongea ajenti Mick na wengine wakamuunga mkono kwa kutikisa vichwa.

"Alichokisema ajenti Mick ni ukweli.Kuanzia sasa John Karobota anaingia katika 'list' ya watu wanaosakwa zaidi na idara hii.Ni mtuhumiwa namba tatu kuanzia sasa.Sasa natoa majukumu.Ajenti Paul utakwenda Mikocheni B Dar es salaam.Pale kuna ndugu yake John Karobota. Ni ndugu yake wa karibu sana.Nenda kampeleleze kuhusu habari hizi.Kama ikibidi,unaruhusiwa kutumia nguvu.Utatumia helkopta kwenda huko. Ajenti Mick wewe utakwenda pale kambini Mafinga utaonana na mkuu wa kambi lile bwana Aloyce Mwasambili,uanzie pale kazi ya kumbaini huyu John Karobota.Taarifa ya ujio wako ataipata kabla wewe haujafika pale."Alitoa maagizo mkurugenzi wa idara,ambaye tangia mwanzo wa kikao hiki alikuwa kimya akisikiliza na kutafakari.

Maajenti wakatawanyika kuendelea na majukumu yao.Mkurugenzi naye akarudi katika ofisi yake binafsi



J.K.T MAFINGA

Saa kumi na mbili na nusu jioni.

Ndani ya moja kati ya ofisi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),mlango uligongwa gongwa na mtu aliye nje.Sauti nzito ya mtu aliyekuwa ndani ilisikika ikisema "karibu".Mlango ulifunguliwa kisha ajenti Mick-reuben akiwa amevaa suti nyeusi iliyomkaa vyema ikisindikizwa na shati jeupe na tai nyeusi huku sikioni akiwa amevaa kifaa maalum cha mawasiliano kinachoitwa 'Tube Coiled Earpiece'.Kijana huyu alifunga mlango nyuma yake baada ya kuingia kisha akakaa katika kiti kilichokuwa mbele ya meza huku akitazamana na yule aliyekaa nyuma ya meza, mtu mzima mmoja ambaye alionekana kama mwenye umri kati ya miaka 50 hadi 55 hivi.

"Naitwa Mick-reuben kutoka C.T.I, nadhani ulipata ujumbe kuhusu ujio wangu".Aliongea kwa nidhamu kijana huyu huku akiwa katika hali ya utulivu wa hali ya juu.

"Ok, nimepata habari kutoka makao makuu na ndiyo maana niko ofisini hadi sasa.Mimi naitwa Aloyce Mwasambili.Ni mkuu wa kambi hili la Hapa mafinga.Nimepewa maagizo nikupe ushirikiano kwa kila utakachokitaka.Sijui nikusaidie nini kijana wangu."Aliongea kwa nidhamu pia mzee huyu ambaye mabegani alichafuka kwa nyota kadhaa.Alionekana kuwa mtu kwenye cheo cha juu.

"Kubwa hapa ni kuhusu tukio lililotokea na ambalo bado ni la moto kwa taifa letu na mataifa mengine.Tukio la kutoroka kwa gaidi wa kimataifa Omar al-Mahmood. Namna pekee ya kujua aliko kirahisi ni kwa kuwatambua baadhi ya watu wanaotuhumiwa kusaidia kutoroka kwake. Moja ya watu wanaotuhumiwa kuhusiana na tukio hili ni mtu ambaye hapo mwanzo alidhaniwa kuwa ji marehemu tangu mwaka 1998.Lakini katika upelelezi imegundulika kuwa yupo hai na anahusishwa moja kwa koja kwa kuhusika na tukio hili kwa namna moja au nyingine.Tumemtambua mtu huyu,kwa jina anaitwa John Karobota.Kwa kuwa hakufariki, ninaweza kusema kuwa alipotea akiwa na cheo cha luteni katika jeshi la wananchi,yaani JWTZ."Alianza kujieleza Mick kisha akaacha kwa muda kidogo kumuacha mwenyeji wake ayatafakari haya kabla hajaendelea kumueleza kwa kina.

"Sasa picha iliyopatikana inayotushuhudia kuwa mtu huyu yupo hai , imerekodiwa na kamera za kambi hii kwa hiyo tunaamini mtu huyu alikuwapo ndani ya kambi hii aidha kwa muda mrefu au kwa muda mfupi.Picha yenyewe ya mtu huyo ni hii hapa,sijui kama unaweza kuitambua".Alimaliza kueleza Mick huku akitoa 'Tablet' kutoka katika mfuko wa suruali aliyoivaa, kisha akapapasa kioo hapa na pale kisha picha waliyoipata ya John Karobota ikaonekana vizuri kabisa.Ni picha ya muda mrefu,lakini mkuu wa kambi hii bwana Aloyce alionekana kuitambua mara baada ya kuiangalia kwa sekunde chache tu.

"Picha hii siyo ngeni kwangu......Ahaa....Nadhani nimekumbuka kitu.Miezi kama mitatu hivi iliyopita,nilipigiwa simu kutoka makao makuu ofisi ya C.D.F(Mkuu wa Majeshi Tanzania). Simu hii ilipigwa na katibu muhtasi wa C.D.F, ambaye alinipa maagizo kuhusiana na ujio wa mtu huyu, kwamba atakuja katika kambi hii kwa muda mfupi kwa sababu ya kazi maalum anayoifanya katika mipaka ya nchi upande huu wa nyanda za juu kusini,yaani katika mkoa wa Mbeya kisha ataondoka.Kwamba hapa ndiyo itakua kituo chake kikuu wakati wote atakaokuwa akifanya kazi hiyo. "Alijieleza kwa maelezo ya mwanzo mkuu huyu wa kambi kisha akanyamaza kidogo akionekana kufikilia jambo fulani kwa kina kabla hajaendelea.

"Nilitambulishwa jina lake.Anaitwaaaaaaaa (huku akitafuta kitu katika makabrasha mengi yaliyokuwa katika droo za meza yake na kisha kutoa bahasha moja ya ukubwa wa 'A4'.akaifungua haraka na kutoa karatasi mbili zilizounganishwa kisha akaiangalia kwa haraka), yes....Anaitwa Jeremiah Mwakibinga.Cheochake ni Luteni. Lakini hiyo picha uliyonionesha haina utofauti sana na sura yake.Labda tu hiyo picha naweza kusema inamuonesha akiwa kijana zaidi ya alivyokuja hapa, au labda kama ni ndugu yake aliyefanana kwa asilimia mia."

"Na hii ni barua yake aliyokuja nayo na pia nilitumiwa ' email' kwa anwani ya makao makuu ya jeshi( huku akibonyeza hapa na pale katika keyboard ya kompyuta iliyo mezani pake) ambayo ni hii hapa".Alimaliza kuongea mkuu huyu wa kambi huku akimgeuzia Mick kompyuta yake ili aweze kuona barua pepe ile.

"Wewe umewahi kuzungumza na katibu muhtasi wa C.D.F kabla"Alihoji Mick Reuben.

"Ndiyo nimewahi kuzungumza naye zaidi ya mara ya tatu na hii ilikuwa ni ya nne.Tena kwa namba hiihii tangu nilipoteuliwa kuwa mkuu wa kambi hii miaka mitano iliyopita."Alijibu mkuu huyu wa kambi hii ya JKT.

Kisha mara tu alipojibu akaonekana kukumbuka kitu kwa ghafla ambacho ni kama kilimshitua kidogo.

"Lakini, kuna kitu nimekumbuka ambacho sijawahi kukifikiria hapo mwanzo.Nilipoongea naye mara ya mwisho,sauti yake ilikuwa kama inakwaruza hivi, siyo ile niliyowahi kuisikia kabla.Na siku ile alikuwa akiongea kama mtu aliyechangamka sana tena kirafiki kuliko kawaida ya siku zingine ambapo huwa anazungumza akiwa yupo siriasi , tena kwa sauti kama ya ki-amri amri hivi."Alimalizia kuongea mkuu huyu wa kambi,Aloyce Mwasambili.

Kengere ya hatari ikalia katika kichwa cha Mick.Tayari alikwishaunganisha maelezo haya na mambo ambayo yeye alikuwa akiyahisi, na kung'amua jambo katika kichwa chake.

"Ahsante.Ila kwa kukumbushana tu nadhani unafahamubkuwa tuliyoongea hapa ni siri kubwa na hakuna mtu anatakiwa kufahamu.Nikikuhitaji tena nitakutafuta.Naomba niondoke na barua hii kwa upelelezi zaidi pia naomba unitumie barua pepe hiyo uliyotumiwa katika anwani hii( huku akimuandikia anuani ile)." Akamaliza kuongea Mick.

"Haina shida.Nafurahi tu kama maelezo yameweza kukusaidia kwa lolote.Wakati wowote utakaponihitajiunakaribishwa sana".Aliongea mkuu wa kambi kisha wakapeana mikono na Mick.Mick akaondoka huku akionekana kufikiria mambo kadhaa kichwani.

******;********************************************************************************************

"Nimefanyia utafiti ile barua uliyokuja nayo pamoja na barua pepe.Nikianza na barua.Imefanana na barua za makao makuu ya jeshi kwa asilimia kubwa sana.Asilimia chache zilizobaki kufika asilimia mia iko katika muhuri uliopigwa katika barua hii.Kama unavyoona, muhuri wa jeshi uko katika umbo la duara.Lakini nikifananisha na barua nyingine kutoka makao makuu ya jeshi, zinatofautiana kidogo katika kipenyo kwa milimita moja na nusu.Pia umbali kati ya herufi na herufi umetofautiana kwa umbali ambao haiwezekani kutambua kwa macho ya kawaida.Mimi mwenyewe nimeng'amua hayo baada ya kui'scan' katika kompyuta na kutumia programu maalum ya kompyuta inayoweza kupima vitu hivyo."

"Nimeitafiti barua pepe ambayo ilitumwa kwa mkuu wa kambi ya jeshi Mafinga.Nimetafiti pia na namba ya simu ambayo mkuu wa kambi ya JKT Mafinga anadai kuwa ilipigwa kutoka makao makuu ofisi ya C.D.F na katibu wake.Vyote hivyo,yaani barua pepe na simu vilitumika kuwasiliana kutokea eneo la ofisi za mamlaka ya mapato (TRA) Mbeya. Ninadhani mpigaji simu na mtumaji wa barua pepe hiyo alikuwa mtaalamu au aliwezeshwa na mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano na inawezekana alitumia programu maalum kufanya mawasiliano hayo.Programu hiyo inamsaidia mtumiaji kuingilia mawasiliano ya mtu mwingine,na hivyo nadhani mawasiliano ya ofisi ya C.D.F yaliingiliwa. Nathubutu kusema mtaalam wa teknolojia aliyehusika kufanya haya yawezekana ni mtaalamu wa hali ya juu sana kuweza ku-'hack' hata mawasiliano ya taasisi kubwa kama ofisi ya mkuu wa majeshi".

"Kwa sababu hiyo ninaweza kuhitimisha kuwa mawasiliano hayo pamoja na barua ile ni feki na wala hazihusiani na ofisi ya C.D.F."Alimaliza kuongea Clara.Wasikilizaji wake walikuwa ni ajenti Mick,mkurugenzi wa C.T.I, Maajenti wengine watatu wa C.T.I pamoja na mtu mmoja aliyekuja pamoja na mkurugenzi wa C.T.I ambaye wengine walikuwa bado hawajamfahamu.

"Kwanza naomba niwatambulishe mgeni wetu huyu. Kutokana na majukumu kuwa mengi, raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa George Katumba amemteua Josephat Moses kutoka idara ya usalama kitengo cha ulinzi wa rais,kuwa makamu mkurugenzi wa idara ya C.T.I. Sahani kwa kuwa mpaka wakati huu amekwisha kuhudhuria kikao chake cha kwanza ndani ya idara bila nyinyi kumgundua.Hii ni kwa sababu rais ameagiza aanze kazi mara moja."Aliongea mkurugenzi wa C.T.I na wanaidara waliokuwemo katika kikao hiki wakapiga makofi kama ishara ya kumkaribisha mgeni huyu.

"Lakini pia ,kutokana na alichokigundua Mick pamoja na maelezo haya ya ajenti Clara, basi ninadhani kuna umuhimu wa ajenti Mick na ajenti Clara kwenda kwenda huko Mbeya ofisi za mamlaka ya mapato TRA mkaanzie hapo.Wengine tutaendelea kutoa usaidizi kutokea hapahapa ofisini. Mtapata usaidizi wote mtakaouhitaji."Alimaliza kuongea mkurugenzi wa C.T.I.

Dakika ishirini baadaye,Ajenti Mick pamoja na Ajenti Clara walikuwa ndani ya helkopta iliyo na chapa ya polisi wakielekea Mbeya .

***************************************




Ofisi ya Mamlaka ya mapato mkoani Mbeya (TRA).

Asubuhi ya siku iliyofuata,iliwakuta Mick na Clara ndani ya tawi la benki ya NMB Loleza,ambalo lipo ndani ya wigo wa ofisi za mamlaka ya mapato TRA,yaani zimepakana.Siku hii ilikuwa inatimia wiki moja na siku moja tangu walipoanza kulifuatililia jambo hili.Kwa upande wao,walikuwa ndani ya muda.Tena walikuwa katika kasi nzuri sana katika kufanya kazi yao.

Ndiyo.Ukifananisha na miezi mitatu ambayo wamepewa, ambayo ni sawa na wiki kumi na mbili, wao walikuwa wameanza kuuona mwanga katika wiki ya kwanza tu.Kwa maana nyingine bado kulikuwa na wiki kumi na siku kadhas mbele yao kabla kikomo cha muda wao hakijafika.Japo walichokipata hadi sasa kilikuwa kidogo tu, na kilisababisha kugundua mtuhumiwa mwingine tena badala ya kusaidia kujua maficho ya watuhumiwa wao wa kwanza kabisa (Abdallah na Omar),lakini ilikuwa na afadhali kuliko wasingegundua lolote hadi sasa. Wahenga walisema "Heri kenda shika kuliko kumi nenda rudi".

Asubuhi hii,Mick na Clara walikuwa mbele ya meza ya meneja wa tawi hilo la benki.

"Jina langu naitwa Inspekta Joseph Agoth na mwenzangu huyu ni Inspekta Julieth Goodluck.Tumetoka makao makuu ya jeshi la polisi .Nadhani ulipata taarifa za ujio wetu"Alitoa utambulisho Mick kwa kutumia majina yao bandia.

"Ndiyo.Nilipewa taarifa na nimeagizwa niwape ushirikiano wowote kadri ya mtakavyotaka.Sijui niwasaidie nini."Alijibu meneja huyu.Kiumbo alikuwa mfupi na mnene japo hakuwa na kitambi.Kwa lugha nyingine tungeweza kumuita 'miraba minne'.

Mick alimueleza walichokihitaji kwa kifupi.Dakika kadhaa baadaye ,meneja huyu alikuwa akiminya hapa na pale katika moja ya kompyuta zilizokuwa ndani ya ofisi ile.

Ni kompyuta hii ambayo ndiyo ilitumika kuonesha,na kutunza kumbukumbu za mambo yote yaliyokuwa yanarekodiwa na kamera za 'CCTV' zilizofungwa ndani na nje ya tawi hili la benki.Kwa kuwa tawi hili la benki liliungana na jengo la ofisi za TRA,basi kamera za tawi hili la benki ziliweza kurekodi hata kinachoendelea nje ya ofisi hizo. Na hicho ndicho Mick na Clara walichokuwa wanakitaka.

Wakati huo meneja huyu wa tawi la benki ,alikuwa akibonyeza hapa na pale kutafuta moja ya video iliyorekodiwa miezi kadhaa nyuma.Ni ile siku ambayo simu na barua pepe vilitumika kuwasiliana na mkuu wa kambi la jeshi la JKT Mafinga kutokea eneo la ofisi za TRA na kudhaniwa kuwa mawasiliano hayo yalifanyika kutokea ofisi ya mkuu wa majeshi nchini C.D.F. Mawasiliano haya ambayo baadaye yalihusishwa moja kwa moja na tukio la kutoroshwa kwa gaidi, ndiyo yaliyowaleta Mick na Clara hapa leo.

Kwa utaalamu wa Ajenti Clara,alikwishatambua siku na muda ambao simu ile ilipigwa na muda ambao barua pepe ilitumwa. Lakini kwa ushauri wa kitaalamu wa ajenti Clara, alionelea ni bora wafuatilie zaidi simu hii iliyopigwa kuliko barua pepe.Labda kwa utaalamu wake aliona ni rahisi zaidi.

Katika kuchunguza kitaalamu kuhusiana na simu hiyo, Clara aliweza kutambua 'IMEI number'ya simu iliyotumika kumpigia mkuu wa kambi ya Mafinga.Kwa kutambua namba ya IMEI, aliweza kutambua aina ya simu iliyotumika kupiga.Ilikuwa ni simu aina ya MOTOROLA C113.

Kwa sababu hiyo walichokuwa wanakifuatilia maajenti hawa wa C.T.I katika video hii,ni kujaribu kuangalia kama watamuona mtu yeyote katika video hii anayewasiliana kwa kutumia simu ya aina hii ili waweze kumfuatilia kitaalamu.

Kipande cha video walichokuwa wanatazama kilikuwa kidogo sana ,ambacho walikipakua kufuatana na muda ambao Clara alidai ndiyo hiyo simu ilipigwa.

Siyo kwamba video hiyo haikuonesha mtu aliyekuwa akizungumza kwa simu, La hasha.Video ilionesha watu wengi tu ambapo wengine walikuwa wanaongea na simu na wengine walikuwa wanaminyaminya simu zao hapa na pale.

Tatizo ni kwamba,siku hii ambayo walikuwa wakiitafiti,siku ambayo video hii ilirekodiwa,ilikuwa ni moja ya siku ambazo wafanyabiashara na wamiliki wote wa vyombo vya moto Mkoa wa Mbeya walikuwa wanahakiki leseni zao katika ofisi hizi za TRA.Kwa hiyo kipande hiki cha video,japo kiwa kilikuwa kifupi sana kisichozidi dakika mbili, lakini kilionesha kundi kubwa sana la watu waliokiwa nje ya ofisi za TRA wakisubiri foleni ya uhakiki huu.Kwa hiyo katika kundi hili kubwa la watu waliokuwa katika kila kona na waliorekodiwa na kamera nne tofauti za usalama kutokana na pembe walizokaa, ilikuwa ni bigumu kuweza kumng'amua muhusika wao ambaye vielelezo vyao viliwaaminisha kiwa lazima alikuwa miongoni mwa watu waliokiwa katika kundi hili.

"Hebu mkuze huyo jamaa anayeonekana pembeni katika kamera namba tatu".Aliongea Mick baada ya kimya kutawala kwa dakika kadhaa tangu waanze kufuatilia video hii.Clara akabonyeza hapa na pale katika keyboard ya kompyuta picha ile ikakua kisha 'akaigandisha'.Picha hii ilimuonesha kijana mmoja aliyekuwa pembeni kabisa na wengine.Sikionialishikilia simu aina ya Motorola C113,alionekanaakiongea.Clara alituma kipande kile katika kompyuta yake kwa mtindo wa picha, kisha akaiingiza picha ile katika programu maalum ya kijasusi kisha akbonyeza hapa na pale katika keyboard ya kompyuta .

Mara ikatokea picha inayoonekana vizuri ikiambatana na maelezo pembezoni mwa picha hiyo.

Hata kabla ya kusoma maelezo ya utsmbulisho wa mtu huyo,hii ilikwishamaanisha kwamba pengine wamempata mtu waliyekuwa wakimtafuta.

Kuonekana katika kumbukumbu za mtandao wa kijasusi,tayari ilimaanisha mtu huyu ni muhalifu ambaye amewahi kutafutwa na idara za ujasusi.Kutafutwa na majasusi ilimaanisha kuwa anayetafutwa ana kesi kubwa za kuhusishwa na uhalifu mkubwa unao hatarisha maisha au maslahi ya kundi kubwa la watu. Pengine muhusika amewahi kuhusishwa na ugaidi.

Hili lilihitimishwa baada ya kusoma maelezo yake pembeni.

"James Omolo Ekeni, raia wa Nigeria, Umri miaka 48.Anatafutwa na vyombo vya usalama kwa kutoa ufadhili kwa magaidi wa kundi la Boko Haram. Pia amehusika katika kutekeleza matukio ya kigaidi ndani ya Afrika na nje ya Afrika".Yalikuwa ni maelezo yaliyoandikwa kwa lugha ya kiingereza.Pia kulikuwa na maelezo mengine mengi chini ya picha hii ambayo yote yalimuhusu mtu huyu.

"Nadhani tumepata tulichokuwa tunakitafuta.Sisi ngoja tukuache ndugu Meneja.Ahsante sana kwa ushirikiano uliouonesha.".Akaongea kwa sauti Mick,kusudi asikike kwa meneja ambaye kwa muda sasa alikuwa amekaa mbali kidogo na ile kompyuta aliyokuwa anaitumia Mick na Clara,ili kuwapisha wafanye mambo yao ya kiusalama kwa uhuru.

"Haina shaka.Mnakaribishwa sana wakati wowote nami nitawapa ushirikiano kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wangu."Alijibu meneja wa tawi la benki la NMB kisha wakapeana mikono kabla ya Mick na Clara kuondoka.

****;*;********************************************************************************************

SAFE HOUSE

Usiku wa saa nne na robo, siku hii ambayo ajenti Mick na ajenti Clara walikuwa wametambua uhusika wa James Omolo Ekeni kutokana na ushahidi walioupata katika ofisi ya TRA Mbeya, ajenti Paul alikuwa akiongea na mkurugenzi wa C.T.I. Ilikuwa ni kuhusu kazi ambayo ajenti Paul alitumwa kuifanya Kinondoni, Dar es salaam kukutana na ndugu wa Luteni John Karobota.

"Leo asubuhi ,nimekutana na ndugu yake John Karobota,bwanw Edward Karobota. Kazi haikuwa ngumu sana kwa sababu niligundua huyu Edward ni mropokaji sana na ni mtu anayependa sana majivuno.Kwa hivyo ilikuwa rahisi sana kumuingia.Tumeongea mambo mengi sana.Lakini muhimu zaidi aliweza kunionesha hata picha ambazo waliwahi kupiga pamoja na John Karobota enzi hizo kabla ya kusemekana kufa.

Moja kati ya picha hizo na ambayo ilinivutia sana ni ile iliyopigwa mwaka 1996,miaka miwili kabla ya John Karobota kupotea.Picha hiyo inaonesha watu watatu ambao ni John Karobota, Edward Karobota pamoja na huyu mtu wa tatu ambaye ndiye ananipa mashaka (Huku akimuonesha mkurugenzi picha ile).

"Hii sura mbona kama ni ya yule gaidi wa Nigeria nimesahau kidogo jina lake".Aliongea Mkurugenzi wa C.T.I kwa kuhoji huku sura ikionekana kujiuliza kitu.

"Upo sawa kabisa.Anaitwa James Omolo Ekeni.Hapo alikuwa bado hajapata umaarufu katika nyanja hii ya ugaidi".Aliongea Paul.

"Kweli uzee umeanza kunijia kwa kasi.Leo asubuhi tumetoka kumuongelea na Mick halafu mara hii nimemsahau.Ni yeye mwenyewe.Na kuanzia sasa James Omolo Ekeni anapewa namba nne kati ya watu wanaotafutwa zaidi katika idara hii."Aliongea Makassy,mkurugenzi wa C.T.I.

"Unajua mara ya kwanza nilipoambiwa kuwa suala hili lipo mikononi mwetu,nilipata shauku sana ya kufuatilia.Sasa hivi ndiyo napata shauku zaidi ya kufuatilia jambo hili kwa kuwa naona sasa linazidi kutuhusu kwa mambo yetu ya ndani ya nchi.Watuhumiwa tulio wagundua hadi sasa wananifanya nifikiri kuwa kuna uwezekano lile suala la wabaya wetu kutaka kuivuruga nchi uetu kuifanya kuwa kama Somalia, bado linaendelea chini chini.Kama tusingeomba kulifuatilia hili suala la gaidi kutoroshwa, basi kuna mambo mengi ambayo tusingegundua na hapo mbeleni nchi yetu ingelia kilio kikubwa sana. Lakini pia.............." Mkurugenzi Makassy alisita kidogo kuendelea kuongea.Alihisiuwepo wa mtu mlangoni aliyekiwa akisikiliza maongezi haya kati yake na ajenti Paul.

"Vipi mzee mbona umeacha kuongea ghaf......"Paulalianza kumhoji mkuu wake lakini Mkurugenzi Makassy aliweka kidole mdomoni kwa ishara ya kusema 'sshhhh'. Paul akaelewa na kukaa kimya huku akigeuka nyuma kwa utulivu na kutazama kule mlangoni ambako mkurugenzi wa idara alikuwa anaangalia. Kupitia upenyo wa chini ya mlango waliweza kuona kivuli cha mtu.Muda huo huo wakasikia mnyato wa mtu akiondoka pale mlangoni.

"Kazi inazidi kuwa ngumu. Inaonekana tuna wasaliti hadi ndani ya ofisi. Nadhani ndiyo tafsiri pekee ya kile tulichokiona hapa sekunde chache zilizopita.Kwa kuwa hatujajua ni nani alikuwa anatusikiliza kwa siri haya tunayoongea nadhani hili suala tulifanye sisi wanne.Yaani sisi tulio ndani ya ofisi yangu na waliopo Mbeya."Aliongea mkurugenzi Makassy.

"Kweli kabisa mkuu.Wote tunajua kuwa katika mambo ya usalama, wasaliti ni watu hatari zaidi kuliko hata maadui wenyewe.Ni vyema tusiwabusishe tena watu wengine hadi pale tutakapowatambua wasaliti kama wapo ndani ya ofisi.Japo kazi itakuwa ngumu lakini heri ugumu wenye uhakika kuliko urahisi ulio na unafiki ndani yake."Aliongea Paul.

Kisha baada ya hapo, wakaongea mengi zaidi huku wakiwa makini sana.Kisha Makassy akawasiliana na Mick-Reuben ambaye yupo na Clara Mbeya na kumjulisha kuhusu hisia za kuwepo kwa msaliti ndani ya ofisi yao.

Wakakubaliana kuwa sasa mawasiliano yanayohusiana na upelelezi unaoendelea yatakuwa yanawahusisha Mick, Clara, Paul, mkurugenzi Eliakim Makassy, na Rais George Katumba.

******************



Ajenti Mick na Ajenti Clara walikuwa ndani ya gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin.Walikuwa wamefika Iyunga wakielekea Mbalizi walikokuwa wameweka makazi katika 'guest house'moja ya hadhi ya chini kabisa.Tangu wafike Mkoa wa Mbeya hadi leo hii ni siku nne zilikuwa zimepita.Walikuwa wamekwisha kukaa 'guest house' tatu tofauti kwa sababu za kiusalama.Na walipendelea kukaa katika nyumba za kulala wageni za hali ya chini sana kwa kuwa walitambua kwamba hata kama adui wanawafuatilia , basi wasingeweza kuwapata kirahisi kama ambavyo wangewapata kirahisi iwapo wangekaa katika hoteli kubwa na maarufu.

Mpaka sasa Mick na Clara walikuwa bado wanapeleleza ni namna gani ambavyo wangeweza kumpata John Karobota.Walijua kumpata John kungewarahisishia kukusanya taarifa juu ya James Omolo, Abdallah Yusoof na hatimaye Omar Al-Mahmood na hatimaye kuweza kuwakamata.Labda waweza kujiuliza kwa nini walichagua kumtafuta John Karobota kwanza ndipo wawapate wengine.

Kutokana na kuwa John Karobota alikuwa ni mMtazania aliyezaliwa na kukulia ndani ya nchi,idara iling'amua kuwa ukusanyaji wa taarifa kumhusu yeye (John) ingeweza kuwa rahisi kuliko kuwafuatilia watuhumiwa hawa wengine ambao ni watu wa nje ya Tanzania.Kwa mfano; ilikuwa rahisi na ingekuwa rahisi zaidi kukusanya taarifa za John Karobota kutoka kwa ndugu zake,shule alizosoma,chuo alichosoma, na hata kwa waliowahi kuwa rafiki zake miaka ile kabla hajasemekana kufa kwa kuwa upatikanaji wa haya yote ni ndani ya nchi yetu kuliko kufuatilia taarifa hizi kwa upande wa watuhumiwa wengine yaani James, Abdallahna Omar ambao ni kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.

Wakati huu gari lilikuwa limefika usawa wa ofisi za shirika la reli la TAZARA mkoa wa Mbeya ambazo zipo mita chache kutoka stendi ya daladala ya Iyunga.Mick alikuwa akiendesha gari kwa kasi ya kawaida sana.Sikioni alikuwa amevaa kifaa cha mawasiliano na alikuwa anawasiliana na Mkurugenzi wa C.T.I bwana Makassy.Pamoja na kuendesha gari akiwa anawasiliano lakini hakupoteza umakini barabarani kabisa.Na zaidi ya hilo pia kuendesha huku akiwasiliana, hakukumpotezea uwezo wa kung'amua na hisia kwamba kuna magari mawili au pengine zaidi ya mawili.yaliyokuwa yanamfuatilia kwa kuachana kwa umbali wamita kama hamsini hivi.

Katika mkoa wa Mbeya,ukitokea katikati ya mji kuelekea Mbalizi,eneo la nje pembezoni mwa wilaya ya Mbeya mjini, kuna foleni kali sana ya magari, mengi yakiwa ni ya abiria ambayo inaishia eneo hili la TAZARA. Baada ya hapo,kutoka TAZARA kuelekea huko Mbalizi, ni magari machache ya abiria, watu binafsi pamoja na magari makubwa.Hivyo doleni hupungua sana kutokea TAZARA kuendelea mbele kuelekea Mbalizi.

Mick alikwisha kuhisi kufuatiliwa na magari haya kilomita mbili nyuma kabla ya kufika TAZARA.Lakini kwa kuwa huko nyuma foleni ilikuwa kubwa,hili lilimnyima Mick kupata uhakika kwamba ni kweli alikuwa anafuatiliwa au ni hisia zake tu.Sasa wakati huu akiwa amefika TAZARA, kwa kuwa foleni haikuwepo kabisa,ndipo alianza kupata uhakika kwa asilimia nyingi sana kuwa ni kweli magari yale yalikuwa yanamfuatilia.

Wakati huu Mick alikuwa amekwishamalizakuwasiliana,hivyo umakini ukaongezeka mara dufu. Wakati huo huo Clara alikuwa akianzaa bunduki aina ya UZI pamoja na bastola aina ya Beretta tayari kwa mapambano.Mick akapewa bastola huku Clara akikamata vyema bunduki ile aina ya UZI.

Wakati huo ndipo Mick akaanza kuendesha gari kwa kasi kubwa sana.Yale magari ambayo Mick aliyahisi yanawafuatilia nayo yakaongeza kasi na 'kumuungia Mick tela.Magari haya yalikuwa na Land Rover na VAN.Risasi zikaanza kurushwa kuelekea gari walilopanda Mick na Clara.

Mick aliendesha gari kwa mkono mmoja wakati mkono mwingine ukiwa umekamata bastola aina ya beretta na kufyatua risasi kujibu mashambulizi.Clara naye akahamia siti ya nyuma ya gari hilo na kisha kujibu mashambulizi kwa kutumia bunduki yake dhidi ya magari haya yaliyo kuwa nyuma yao.

Kurushiana risasi huku kuliendelea kwa muda kama wa dakika tano hivi huku magari yote yakiwa katika.kasi kubwa sana.Magari yalikiwa yameiacha barabara ya lami na sasa yalikuwa katika barabara ya vumbi,maeneo ya mashamba nje pembeni mwa mji.

Mick alinyonga usukani kulia kwake na kuingia ndani ya shamba moja la mahindi. Kisha akakanyaga pedeli ya mafuta hadi mwisho.Gari likapita ndani ya shamba hilo kwa kasi ku wa sana huku likilaza na kukanyaga mahindi mengi.Hapo angalau Mick akawaacha maadui wale kwa umbali kiasi.

Baada ya kuona amewaacha adui mbali kidogo Mick akafunga breki kisha yeye na Clara wakashuka na kutokomea huku wakifichwa na mahindi ya shamba hilo yaliyostawi vyema.Kisha Mick akavaa tena kifaa cha mawasiliano na kuwasiliana tena na mkurugenzi wake mzee Makassy.

"Sasa nawaona kwa picha mnato za satellite.Hao watu wanaowafuatilia wako mita mia mbili kutoka hapo mlipo wanakuja kwa miguu.Wako kumi jumla."Mick alimsikia Makassy akiongea kwa kupitia kifaa cha mawasiliano alichovaa sikioni.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog