IMEANDIKWA NA : BISHOP HILUKA
*******************************************
Simulizi : Hekaheka!
Sehemu Ya Kwanza (1)
DAR ES SALAAM, SAA 12:30 JIONI.
SAUTI laini ya mwanadada mrembo mhudumu wa ndege aina ya Airbus A340-600 ya shirika la ndege la Uholanzi la KLM tuliyoiabiri, ilinizindua kutoka usingizini.
Sauti ile ilikuwa ikiwatangazia abiria wote kufunga mikanda ya siti zao tayari kwa kujiandaa na tukio la kutua kwa ndege hiyo katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere kipo umbali wa kilomita 12 kusini magharibi mwa jiji hilo la Dar es Salaam ambalo ni jiji kubwa zaidi nchini Tanzania.
Usingizi ukiwa haujaniisha sawasawa niliyafumbua macho yangu taratibu, kisha nikayatembeza taratibu mle ndani ya ndege nikitazama huku na kule, na kwa kufanya vile, nikagundua kuwa abiria wenzangu wote mle ndani ya ndege walikuwa macho na tayari walikwisha funga mikanda ya siti zao tayari kwa tukio lile la kutua kwa ndege.
Niliwatazama haraka haraka na hapo nikajua kuwa ni mimi tu ndiye ambaye nilikuwa nimepitiwa na usingizi wakati yule mwanadada mrembo mhudumu wa ndege ile alipokuwa akitutangazia abiria wote kufunga mikanda kabla ya tukio la kutua kwa ndege.
Tulikuwa tumesafiri tukiwa angani kwa takribani saa nzima tangu ndege yetu iliporuka katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta jijini Nairobi nchini Kenya hadi Dar es Salaam.
Kupitia ukuta msafi ya vioo vya dirisha la ile ndege niliweza kuona sehemu kubwa ya bahari ya Hindi, barabara zote kuu zilizokuwa zinaingia na kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam, makazi ya watu na hata eneo la Mto Msimbazi uliokuwa ukitapisha maji yake katika pwani ya Bahari ya Hindi.
Kiujumla sehemu kubwa ya mandhari ya jiji la Dar es Salaam ilinivutia sana kwa uoto wake wa asili wa kijani kibichi kama ilivyokuwa katika nchi nzima ya Tanzania iliyo na mito mingi yenye maji ya kutosha.
Nilipiga mwayo mrefu wa uchovu huku nikiendelea kustaajabu maendeleo makubwa niliyokuwa nikiyashuhudia katika jiji la Dar es Salaam yaliyofikiwa katika kipindi kifupi tu cha miaka kumi.
“Aisee! Ni bahati iliyoje kurudi tena katika nchi yangu nzuri na tajiri kama hii, I real love my country,” (Naipenda nchi yangu) nikanong’ona nikiiambia nafsi yangu mwenyewe.
Usingizi wa takribani saa nzima safarini, tangu tuliporuka kutoka kiwanja cha ndege cha Jomo Kenyatta jijini Nairobi hadi Dar es Salaam, ulikuwa umenipunguzia kwa kiasi kikubwa uchovu wa safari ndefu ya kutoka katika jiji la Amsterdam nchini Netherland (au huitwa Uholanzi) nilikokuwa nikiishi.
Wakati ndege yetu ikizunguka angani kutafuta uelekeo mzuri wa kutua, nikatumia nafasi ile kutazama nje, kupitia ukuta msafi wa vioo vya dirisha nikayaona machweajua yakiwa yamepaka rangi ya damu huku jua lenye kutua likijificha nyuma ya wingu, ati kutughilibu tusilione wakati linaingia upande wa pili wa dunia.
Kisha niliyahamisha macho yangu kutoka kule na kuyaangalia mandhari ya kupendeza ya eneo lililozunguka kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere kupitia ukuta msafi wa vioo vya dirisha pale nilipokuwa nimeketi.
Nilitazama nje nikiyastaajabia mandhari ya kupendeza ya eneo lile la uwanja wa ndege, nikajiuliza kama ni kweli kile kilikuwa ni kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere cha jijini Dar es Salaam au labda rubani alikosea, kwani nilichokuwa nakishuhudia ilikuwa ni kiwanja kikubwa, kizuri na chenye majengo ya kisasa.
Kudhihirisha mshangao wangu, niliivua miwani yangu myeusi mikubwa niliyokuwa nimeivaa muda wote wa safari yangu ikifunika macho yangu, na hapo nikaangalia vizuri kule nje.
Hapo ndipo nilipoyaona vizuri zaidi mandhari ya kupendeza ya uwanja ule yaliyonivutia kwa mpangilio wake mzuri wa majengo, hasa lile jengo kubwa lililokuwa bado jipya la kituo nambari tatu cha uwanja wa ndege, maarufu kama ‘terminal 3’.
Jengo lile la kituo nambari tatu lilikuwa kubwa na refu zaidi kuliko yale majengo mengine ya vituo nambari moja na nambari mbili, na lilikuwa lina migahawa na maduka ya kisasa, na ofisi mbalimbali za utawala zikiwemo ofisi za uhamiaji za nchi ya Tanzania kwa ajili ya wageni waliokuwa wakifika nchini kupitia ule uwanja wa ndege.
Nikakumbuka kuwa nilisoma kwenye mtandao wa intaneti mara kadhaa kuwa lile jengo lilikuwa na uwezo wa kuruhusu ndege kubwa 24 kwa wakati mmoja na abiria milioni 6 kwa mwaka, pale nilipokuwa natafuta habari kuhusu maendeleo ya nchi yangu, na nilipokuwa najiandaa kuja Dar es Salaam.
Niliachia yowe dogo la mshangao nikizidi kuajabia maendeleo yale ya haraka yaliyofikiwa, kwani nilipokuwa naondoka nchini miaka kumi na mbili iliyopita kwenda Ulaya hali ya ule uwanja haikuwa kama nilivyokuwa nikiishuhudia sasa.
Niliporidhika kuyatazama mandhari ya eneo lile nikageuza shingo yangu kuwatazama abiria wenzangu wawili waliokuwa wameketi kwa utulivu jirani yangu na macho yangu yakaangukia kwenye uso wa abiria mwanamke aliyekuwa ameketi pembeni yangu kwenye siti ya katikati.
Mara tu macho yetu yalipogongana, tukajikuta wote wawili tukiachia tabasamu bashasha.
Abiria yule alikuwa ni mwanadada chotara aliyekuwa mchanganyiko wa Mswahili na mzungu, nadhani kutoka Ulaya mashariki, kama si Mgiriki basi Mturuki. Kwa mwonekano wa haraka tu niliweza kugundua kuwa alikuwa na umri wa miaka kati ya therathini na therathini na mbili.
Mwanadada yule alikuwa ameketi na mtoto mmoja wa kike aliyeonekana kuwa na miaka mitatu. Wakati huo yule mtoto alikuwa amepitiwa na usingizi huku akiwa amezuiliwa vyema na mkanda wa siti ya ndege ile.
Kwa uzoefu wangu kwa wadada warembo, haraka niliweza kugundua kuwa abiria yule alikuwa na umbo la kuvutia la kimiss, mwenye weupe wa asili na hakuwa mwanamke wa kumtizama mara moja tu ukamwacha.
Mwonekano wake ulinitanabaisha kuwa alikuwa mrefu kiasi na mwenye haiba ya kuvutia sana, alikuwa na mashavu mfano wa chungwa na nywele zake zilikuwa ndefu zilizokuwa nyeusi tii za kichotara ambazo alikuwa amezisuka mtindo wa mkia wa pweza.
Niliweza kuziona vyema nywele zake zilizokuwa zimeangukia mgongoni kwani alikuwa amezifunika kwa mtandio mwepesi wa rangi ya njano uliozifanya zionekane vyema.
Nyusi zake alikuwa amezitinda vizuri na kuzipaka wanja, na kope zake zilikuwa zimerembwa vyema na hivyo kuyafanya macho yake makubwa kidogo na legevu yenye kung’ara kama nuru yaonekane vizuri na kupendeza.
Alivaa gauni fupi jepesi la rangi ya pinki lililohifadhi vyema umbile lake na ndani ya lile gauni alikuwa amevaa suruali ya jeans ya bluu.
Miguuni alikuwa amevaa sendozi ngumu za kike zilizotengenezwa kwa ngozi imara ya mamba.
Nilipomtazama kwa makini nikagundua kuwa sikuwa nimemchanganyia macho vizuri kabla ya hapo, japo tulikuwa tumeketi katika siti zilizokuwa jirani, na tulisafiri pamoja muda wote tangu ndege yetu iliporuka kutoka katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Jomo Kenyatta, jijini Nairobi ambako ndiko alikokuwa amepandia.
Mara nikashtuka kuwa hadi muda huo sikuwa nimefunga mkanda wa siti yangu, hivyo haraka sana nikafunga ule mkanda wa siti na kujiweka sawa kwa tukio la kutua kwa ndege.
Na wakati huo huo mtikisiko kidogo ukatokea mle ndani ya ndege mara baada ya magurudumu ya ndege ile kuanza kutua kwenye ardhi ya kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere, hata hivyo, baada ya kitambo kifupi hali ya utulivu ikarejea tena.
Wakati ndege yetu ikikimbia kwa kasi kwenye barabara ndefu ya lami maarufu kama ‘runway’ iliyokuwa imewekwa alama elekezi ili kuwaongoza marubani wa ndege, yule mwanamke chotara akaonekana kunitazama kwa uyakinifu zaidi na hapo hapo akaonekana kushtuka sana.
Nilipomkazia macho nikamuona akijaribu kuuficha mshtuko wake na kujifanya kutabasamu kiurafiki, lakini niliweza kuyasoma vizuri mawazo yake kupitia macho yake makubwa kiasi na kugundua kuwa hakuwa tu ameshtuka sana baada ya kuniona, bali pia macho yake yalionesha chuki fulani dhidi yangu.
“Brown!” hatimaye yule mwanamke chotara aliita huku akionekana kulazimisha tabasamu.
“Long time no see!” (Siku nyingi sijakutia machoni!) aliongeza kabla sijasema chochote huku akiendelea kunitazama kwa makini.
Hata hivyo, japo alijitahidi kutabasamu lakini uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote wakati akinisemesha na macho yake yalionesha chuki fulani dhidi yangu.
“Who is Brown?” (Brown ndiyo nani?) nilimuuliza yule mwanadada chotara huku nikionesha mshangao.
“Kwani wewe siyo Brown Senga? I have been searching you,” (Nimekuwa nikikutafuta) aliniambia huku akiendelea kunitazama kwa mtazamo ule ule ulioonesha chuki na mashaka kwangu.
“I’m not Brown, you have mistaken me to someone else,” (Mimi siyo Brown, umenifananisha na mtu mwingine) nilisema huku nikiachia tabasamu.
“I don’t think so (Sidhani), au ndo hata jina umeamua kubadilisha kabisa!” alisema huku akiendelea kunitazama kwa mashaka.
“Believe me, I am not Brown (Niamini, mimi si Brown) …na sijawahi kutumia jina hilo, nina hakika utakuwa umenifananisha na mtu mwingine kabisa,” nilisema kwa msisitizo huku nikijaribu kumtazama kwa makini, nilikuwa najaribu kukumbuka kama tuliwahi kuonana sehemu.
“I am sorry!” (Samahani) alisema na kugeuzia shingo yake kutazama upande mwingine huku akionekana kama mtu aliyekuwa amekasirishwa sana na majibu yangu.
Hata hivyo, sura yake ilikuwa ngeni kabisa machoni kwangu, lakini nikajikuta nikitamani kutaka kumfahamu zaidi yule mwanadada chotara.
“Maybe you can remind me, where did we meet?” (Labda unaweza kunikumbusha, tulionana wapi?) nilimuuliza huku nikimtazama kwa uyakinifu.
Aligeuza shingo yake akanitazama kwa kitambo kifupi huku akionekana kama aliyekuwa akitafakari jibu zuri la kunipa, kisha aliuma mdomo wake usio mdogo wala mkubwa uliokuwa umekolea ‘lip shine’ ya rangi ya pinki na kutingisha kichwa.
“I am so sorry once again… (Samahani kwa mara nyingine…) inawezekana kweli nimekufananisha,” alisema yule mwanadada akionekana kuniomba radhi kisha aliikunja sura yake na kutazama kando huku akionekana kuwaza mbali.
“It’s okay… it happens, take it easy,” (Ni sawa… huwa inatokea, usijali) nilisema kwa sauti tulivu nikijaribu kumtoa shaka ili asije akajihisi vibaya. Hata hivyo nilijikuta nikitamani sana kufahamu kilichokuwa kinaendelea akilini kwake, maana kwa jinsi alivyokuwa akinitazama ilinishangaza sana.
Kichwani kwangu nilibaki na maswali, nilijiuliza: je, kwanini alikuwa amenitazama namna ile? Kwanini alionekana kushtuka sana baada ya kuniona? Na kwanini baada ya kumwambia kuwa mimi sikuwa Brown Senga akaonesha hasira zaidi?
Hata hivyo, japo maswali yale yalinitesa lakini nilijifanya kama sijagundua lolote kuhusu mtazamo wake kwangu, nikashusha pumzi za ndani kwa ndani.
Wakati nikijaribu kujiuliza maswali kuhusu yule mwanadada chotara mara nikaiona ile ndege yetu ikipunguza mwendo na kugeuza, kisha ikaingia katika barabara nyingine ya lami ambayo pia ilikuwa imechorwa alama elekezi ili kuwaongoza marubani wa ndege, kisha ikaelekea jirani na majengo ya kiwanja kile cha ndege.
Muda huo huo nikayapeleka tena macho yangu kutazama nje na mara moja nikaona kiza kikianza kuchukua nafasi ya mchana na mwanga wa taa za pale uwanjani ukapenya hadi ndani ya ndege kupitia ukuta msafi wa vioo vya madirisha, na hapo nikakumbuka kuitupia macho saa yangu ya mkononi.
Nilipoitazama saa yangu nikagundua kuwa tayari ilikuwa imetimia saa kumi na mbili na dakika therathini na tano za jioni, nikajua kuwa tulikuwa tumesafiri angani kwa muda wa dakika sitini tu, tangu tuliporuka kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta, jijini Nairobi hadi kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Muda ule nikajifanya kujinyoosha huku nikipiga mwayo mrefu lakini nikiwa makini zaidi kumchunguza kwa jicho la wiziwizi yule mwanadada chotara.
Uchunguzi wangu ukanifanya kubaini kuwa hata yule mwanadada naye alikuwa bado yupo makini zaidi akinitazama kwa jicho la wizi huku akiendelea kuonesha wasiwasi fulani usoni kwake.
Hata hivyo, sikutaka kumnyima nafasi ile ya kunitazama, hivyo nikawa nazuga kutazama nje kupitia vioo vya dirisha la ile ndege nikijifanya kulishangaa lile jengo jipya la kituo nambari tatu la uwanja wa ndege wa Julius Nyerere.
Pamoja na yote lakini macho ya yule mwanadada hayakuhama kwangu badala yake yalikuwa makini zaidi kufuatilia kwa karibu kila tukio nililokuwa nikilifanya.
Nikaanza kujiuliza, je, ni kweli alikuwa akinifanisha na mtu fulani aliyemfahamu au kulikuwa na jambo jingine nyuma ya pazia? Na kama ni kweli alinifananisha na mtu mwingine, ni kipi kilichomfanya ashtuke kiasi kile baada ya kuniona? Je, huyo mtu aliyeitwa Brown Senga alikuwa na nini hasa kilichomfanya jambo yule mwanadada kushtuka?
Hata hivyo, sikuweza kupata majibu ya haraka ingawa nilipania kumuuliza tukakapokuwa tumeshuka kwani nilihisi kuwepo jambo fulani kati ya mwanadada yule na huyo mwanamume aliyeitwa Brown Senga. Nikahisi huenda nilikuwa nafanana na mtu huyo ndiyo maana aliniuliza kama nimeamua kubadili jina!
Mara likanijia wazo kuwa huenda huyo Brown Senga aliwahi kumuumiza huyu mwanamke, maana si kwa kushtuka kiasi kile!
Muda mfupi baada ya ndege yetu kusimama kwenye kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere na milango ya ile ndege kufunguliwa huku ngazi zikiwekwa sawa, tulifungua mikanda ya siti zetu na muda huo abiria wakaanza kushuka taratibu.
Nilimtupia jicho yule mwanadada chotara mwenye mtoto nikamwona akihangaika kuchukua mzigo wake mdogo kutoka sehemu maalumu ya kuwekea mizigo kwenye sehemu ya juu ya ile ndege huku akiendelea kunitazama kwa jicho la wizi.
Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani huku nami nikijisogeza jirani na nilipokuwa nimeweka mzigo wangu, kisha nikachukua begi langu dogo la mgongoni kutoka sehemu ile maalumu ya kuwekea mizigo na kujiunga kwenye foleni ya abiria waliokuwa wakishuka.
Wakati huo yule mwanamke chotara mwenye mtoto alikuwa mbele kabisa jirani na mlango wa kutokea akionekana mwenye haraka ya kutaka kushuka.
Mara tuliposhuka kutoka kwenye ile ndege tukalikuta basi moja maalumu la pale uwanja wa ndege likitusubiri, tuliingia kwenye lile basi kisha likatupeleka hadi kwenye jengo la kituo nambari mbili cha kiwanja kile cha ndege cha Julius Nyerere.
Pale nje hali ya hewa ya joto ikanikumbusha kuwa tayari nilikuwa nimeikanyaga ardhi ya jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania, nchi niliyokuwa nimeiacha takribani miaka kumi na mbili iliyopita na kwenda kuishi ughaibuni katika jiji la Amsterdam nchini Netherland.
Tulishuka kutoka kwenye lile basi maalumu na kuingia ndani ya lile jengo la kituo nambari mbili tukipita katika lango moja kubwa lililokuwa na maandishi makubwa meusi juu yake yaliyoandikwa ‘International Arrivals’.
Lile jengo pia lilikuwa na migahawa na ofisi mbalimbali za utawala zikiwemo ofisi za uhamiaji za nchi ya Tanzania kwa ajili ya wageni waliokuwa wakifika nchini kupitia ule uwanja wa ndege.
Japo kiza kilikuwa kimekwishaingia hakikunizuia kuivaa tena miwani yangu myeusi ya jua na kufunika macho yangu kisha nikatinga kofia yangu nyeusi ya pama na kuanza kutembea taratibu huku begani nikiwa na lile begi langu dogo la mgongoni.
Mara nikamuona yule mwanadada chotara akinitupia jicho la wizi na kuharakisha kuelekea kwenye dirisha moja la ofisi za uhamiaji pale uwanjani.
Nikajikuta nikishikwa na shauku ya kutaka kujua nini hasa kilichokuwa kimejificha nyuma ya fikra za yule mwanamke, hivyo nami nikaharakisha nikijipenyeza haraka ili kulifikia lile dirisha la ofisi za uhamiaji zilizokuwa pale uwanjani na kisha nikapanga foleni nyuma yake.
Hata hivyo, nilijikuta nikiwa mtu wa sita katika mstari wa foleni yangu, mbele yangu wakinitangulia watu watano. Mtu wa kwanza katika foleni hiyo alikuwa mwanamume mmoja wa makamo, alikuwa mzungu mrefu na mwembamba akiwa amevaa shati jeupe na sweta la kijivu juu yake, huku chini akivaa kaptura nyeusi ya kadeti yenye mifuko mikubwa pembeni na miguuni alivaa raba.
Nyuma ya yule mwanamume mzungu alikuwa kasimama yule mwanadada chotara mwenye mtoto. Kisha walifuata wazee wawili, mwanamke na mwanamume, walioonekana wana asili ya Afrika Magharibi kutokana na mavazi yao. Niliweza kuwabaini kuwa walikuwa ni mke na mume walioishi maisha marefu ya ndoa yenye furaha.
Yule mwanamke alikuwa nadhifu na mrefu kiasi, alikuwa amevaa vazi la kitambaa cha bazee lililoshonwa na kudariziwa vizuri na kichwani alikuwa amevaa kilemba kikubwa.
Yule mwanaume alikuwa mrefu, alivaa joho la kitambaa cha bazee lililodariziwa vizuri shingoni kwa nyuzi za dhahabu na kofia ya kitambaa kile, na alikuwa na ndevu nyingi zilizokizunguka kidevu chake akiwa amevaa miwani ya macho.
Baada ya wale wazee alifuata mwanamume mmoja ambaye kiumri alionekana asingezidi miaka arobaini, akiwa amevaa shati la rangi ya samawati lililokuwa na mistari ya rangi ya bluu iliyokolea na suruali ya jeans, alikuwa mrefu kiasi na maji ya kunde, uso wake ulikuwa wa umbo duara na muda wote alikuwa anatabasamu.
Pamoja na kwamba Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilikuwa kimebadilika sana tofauti na wakati nilipoondoka miaka kumi na mbili nyuma lakini bado hakikuwa na tofauti kubwa na viwanja vya ndege vingi vya barani Afrika.
Ila kwa wakati huo kulikuwa na pilikapilika nyingi zaidi za wasafiri waliokuwa wakiingia na kutoka jijini Dar es Salaam na hata barabara zilizowekwa alama elekezi ili kuwaongoza marubani wa ndege zilikuwa zimeongezeka na zilikuwa ndefu zaidi tofauti na wakati ule, hivyo kuruhusu ndege nyingi za ukubwa mbalimbali kutua pale kiwanjani.
Nikiwa bado nimesimama pale kwenye foleni nikisubiri zamu yangu ifike macho yangu yalikuwa yamevutiwa sana na namna ndege zilivyokuwa zikitua na kuruka pale kiwanjani lakini akili yangu ilikuwa imejikita katika kumfikiria yule mwanadada chotara mwenye mtoto. Nafsi yangu sasa ilikuwa ikitamani kujua kilichokuwa akilini mwake.
Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikiendelea kusubiri zamu yangu ifike niweze kulifikia lile dirisha dogo lenye kuta za vioo mbele yangu lililokuwa limemuhifadhi mkaguzi wa pasi za kusafiria.
Hata hivyo, nikaamua kuutumia muda ule kumchunguza vizuri yule mwanadada chotara mwenye mtoto huku nikijaribu kuyasoma mawazo yake.
Nilimuona akinitupia jicho la wizi wakati akihudumiwa na mara akarudishiwa pasi yake ya kusafiria kisha akanikata tena jicho na kuondoka haraka eneo lile wakati nikiwa bado nimesimama nikisubiri wale watu watatu waliokuwa mbele yangu wahudumiwe kwanza.
Kazi ya ukaguzi wa hati za kusafiri ilienda haraka haraka na hatimaye wale watu wote waliokuwa mbele yangu wakahudumiwa na kuondoka na sasa zamu yangu ilikuwa imefika.
Nilisogea pale kwenye lile dirisha huku nikitupa macho yangu kutazama mazingira ya eneo lile, nikawaona watu kadhaa niliowatambua mara moja kuwa ni maofisa wa usalama wakitokea na kuangaza huku na kule wakiwa makini huku wengine wakijongea taratibu eneo lile nililokuwepo.
Sikuwatilia maanani kwa kuwa niliamini kuwa walikuwa katika majukumu yao ya kawaida kuhakikisha eneo lile linakuwa salama, nikashusha pumzi za ndani kwa ndani na kupenyeza pasi yangu ya kusafiria kwenye dirisha dogo la kioo la kile chumba kidogo huku nikichungulia kuangalia mle ndani.
Na hapo macho yangu yakatua kwenye uso wa msichana mmoja mlimbwende aliyeonekana kuyazingatia vema maadili ya kazi yake kwa uchangamfu wa sura yake.
Msichana yule ofisa uhamiaji akaipokea pasi yangu ya kusafiria huku akinipa pole kwa uchovu wa safari na kuliachia tabasamu lake maridhawa lililozichanganya ghafla fikra zangu na kuzigalagaza vibaya hisia zangu.
Niliiegemeza mikono yangu juu ya sakafu ya kipande kidogo cha ubao mfupi kilichokuwa mbele ya lile dirisha huku nikiinama kidogo ili niweze kuliona vizuri tabasamu la msichana yule, kisha nikaivua miwani yangu myeusi iliyokuwa imefunika macho yangu.
Macho yetu yalipogongana tena kila mmoja alijikuta akitabasamu na hapo nikajikuta nikivutiwa zaidi na uzuri wake. Sura yake ilikuwa ndefu kiasi na pua yake ndefu mithili ya pua ya Kihabeshi.
Alikuwa amevaa gauni la rangi ya pinki la kukata mikono lililolichora vyema umbo lake na kuishia sentimita chache juu ya magoti yake huku mpasuo mfupi wa gauni hilo ukiliacha nusu wazi paja lake. Juu ya lile gauni alikuwa amevaa kitopu cheusi na miguuni alivaa skuna, viatu vyeusi vilivyokuwa na visigino virefu.
Hakuwa mweusi wala mweupe kwa rangi na alikuwa na shingo ndefu kiasi iliyobeba mabega ya kike na shingoni alikuwa amevaa kidani cha dhahabu chenye herufi ‘W’ kilichokuwa kimening’inia kifuani kwake na kuzama katikati ya matiti yake madogo mfano wa embe dodo changa.
Mdomo wake ulikuwa mdogo uliokuwa umekolea ‘lip shine’ ya rangi ya chokoleti pamoja na vishimo vidogo mashavuni mwake vilivyoweza kumfanya mwanaume yeyote rijali ababaike kidogo kwa uzuri wake wakati alipomtazama.
Niliachia tabasamu kabambe la uchokozi na kumfanya yule ofisa uhamiaji abaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa akinikodolea kwa macho yake makubwa ya kike lakini malegevu yaliyokuwa yamerembeshwa kwa wanja maridadi uliochorwa mfano wa mwezi mwandamo.
Yule msichana aliendelea kuduwaa akinitazama kwa makini kana kwamba alikuwa amemuona malaika wa muujiza akiwa amesimama mbele yake akisubiri kumtunuku zawadi bora iliyotukuka.
Sikumlaumu yule msichana pindi nilipomuona ameduwaa akinitumbulia macho na kujikuta akisahau wajibu wake kwa muda.
Naam, sikumlaumu na wala sikushtuka kwani nilifahamu fika kuwa nilikuwa nimependeza sana, isitoshe nilikuwa miongoni mwa wanaume wenye mvuto kwenye macho ya wasichana warembo kama huyo aliyekuwa mbele yangu.
Kwa mtazamo wa nje mtu yeyote asingesita kunifananisha na mtu yeyote mashuhuri, awe ni mfanyabiashara mkubwa, msanii maarufu wa muziki, muigizaji wa filamu au mwanamitindo wa mavazi ya kiume.
Kama kawaida yangu, nilikuwa katika mwonekano wangu nikiwa nimetinga suti yangu nyeusi ya bei ghali aina ya Dunhill, shati maridadi la rangi ya samawati aina ya Levi’s, tai ya bendera ya taifa shingoni na kiatu ghali cha ngozi miguuni.
Pia nilivaa saa ya mkononi ya madini ya dhahabu aina ya Quatz na kofia nyeusi kichwani aina ya pama na nilijipulizia manukato ya gharama kubwa aina ya Clive ambayo bei yake ilikuwa si haba, kwani ingetosha kabisa kuwa bajeti ya mwezi mzima ya familia ya kipato cha kawaida.
Nikiwa na umri wa miaka therathini na mbili, nilionekana kuwa na sura ya kitoto yenye muonekano uliomfanya mtu yeyote aliyeniona adhani kuwa nisingeweza kuzidi miaka ishirini na mbili ingawa nilishapita miaka hiyo.
Nilikuwa mrefu na mwenye umbo kakamavu la kimichezo lililofanana na wachezaji wa NBA, ligi ya mpira wa kikapu nchini Marekani na nilikuwa na ndevu nyingi nilizokuwa nimezinyoa katika mtindo wa ‘O’.
“Hujambo Miss Tanzania?” nilimsalimia kwa utani yule msichana baada ya kumwona akiwa ameduwaa, hata hivyo hakuitikia salamu yangu badala yake alizidi kutabasamu tu na kuitupia jicho pasi yangu ya kusafiria katika namna ya kuikagua.
“Maximilian Banda…” nilimsikia akilitamka jina langu taratibu pasipo kunitazama.
“Yap! Hilo ndilo jina langu, vipi umewahi kulisikia popote?” nilimuuliza yule msichana huku nikiendelea kutabasamu.
“Sijawahi ingawa akina Maximilian wapo wengi sana hapa Tanzania, ila hili jina la Banda hmm… si la asili ya nchi hii,” alisema yule msichana mrembo huku akiinua uso wake na kunitazama kwa makini.
“Kwani hili nalo ni jina lako?” yule mrembo aliniuliza huku akinikazia macho kwa makini.
“Kwani jina langu hasa ni nani?” nilimuuliza yule mrembo huku nikionesha kushangaa kidogo.
“Kwanini unaitwa Maximilian Banda na siyo Brown Senga?” aliniuliza tena akionekana kulipuuza swali langu.
“Kwa sababu naitwa Maximilian Banda na siyo Brown Senga,” nilijibu kwa utani.
Hata hivyo kuna kitu kilinishtua kidogo baada ya kumsikia yule mrembo akilitaja jina la Brown Senga, na hii ikiwa ni mara ya pili kulisikia lile jina likitajwa tangu nifike pale uwanja wa Julius Nyerere.
“Okay, kwa hiyo wewe ni Maximilian Banda!” aliuliza katika namna ya kushangaa huku akishusha pumzi ndefu.
Niliachia tabasamu, akilini mwangu nikadhani labda alipenda tu kunisikia nikiongea kwani vibali vyangu vya kusafiria ambayo wakati huo alikuwa navyo yeye vilikuwa vikieleza wazi kabisa utambulisho wangu.
“Ndiyo maana yake,” nilijibu kwa sauti tulivu huku nikiendelea kumtazma kwa tabasamu.
“Ulikuwa wapi kipindi chote tangu uondoke nchini?” yule mrembo alinitupia swali jingine kabla sijasema chochote.
“Amsterdam, Uholanzi,” nilijibu huku nikimtazama yule mrembo kwa kujiamini.
“Ulikuwa huko kwa madhumuni gani?”
“Huko ndiko ninakoishi, ila hapa nchini nimekuja kusalimia jamaa zangu, una lingine mrembo?” nikamtania huku nikizidi kumtazama kwa tabasamu.
“Kabila lako?” aliniuliza akionekana kutoujali utani wangu.
“Mtanzania,” nikamjibu.
“Kila Mtanzania ana kabila, sasa wewe kabila lako ni lipi?” aliniuliza akiwa amenikazia macho huku uso wake ukionesha kuwa mbali na utani.
Swali hilo likanifanya nimkazie macho yangu kwa mshangao kwani sikuelewa maana ya swali lake, hasa ikizingatiwa kuwa kabila langu na taarifa zangu zote zilikuwa kwenye zile nyaraka zangu za kusafiria, nikabaki nimeshikwa na mduwao.
“Je, huku ndiko tulikofika Watanzania siku hizi kuulizana makabila? Mbona huu si utamaduni wetu Watanzania kuulizana makabila, hasa kwa kuwa tuna makabila zaidi ya mia moja na ishirini,” nilisema huku nikimkazia macho kisha nikaongeza.
“Hata hivyo, mbona nyaraka zangu zinajieleza waziwazi kuhusu taarifa zangu likiwemo kabila langu!”
Msichana yule mrembo hakujibu kitu badala yake aliendelea kunikodolea macho kwa makini, safari hii tabasamu lilikuwa limeyeyuka kabisa usoni kwake na sura ya kazi ilikuwa imejitokeza.
Alionekana kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani na kuyaondosha macho yake kutoka kwangu, kisha akayatuliza kwenye mashine ya ukaguzi wa pasi za kusafiria iliyokuwa mbele yake.
Wakati huo mimi sikuwa na hili wala lile, niliendelea kusubiri nihudumiwe kisha niondoke zangu nikitaraji kumkuta yule mwanadada chotara mwenye mtoto kule kwenye eneo la kuchukulia mizigo. Nilikuwa nimedhamiria kufanya jambo, jambo mwafaka, ili kujua kilichokuwa akilini mwake!
Niliivaa tena miwani yangu myeusi na kutupa macho yangu kando na mara nikaweza kubaini kuwa nilikuwa nikitazamwa na wasichana wengine wawili warembo, wakaguzi wa pasi za kusafiria waliokuwa kwenye vibanda vya jirani.
Kisha niliyahamisha macho yangu kutazama mazingira ya eneo lile, nikawaona wale maofisa wa usalama wakiwa wanarandaranda eneo lile karibu kabisa na nilipokuwa nimesimama huku wakinitazama kwa uyakinifu zaidi.
Maofisa wale walionekana kama ni watu waliokuwa wananifananisha au waliokuwa na shauku ya kutaka kuniona kama siyo kuzungumza na mimi.
“Nadhani wanafikiri mimi ni mtu fulani mashuhuri au pengine msanii maarufu,” nikawaza.
Hata hivyo sikuwatilia maanani sana, niliyarudisha macho yangu kwa yule msichana aliyekuwa kwenye kile kizimba mbele yangu nikawa namuona akikukuruka na pasi yangu ya kusafiria akiitia katika mashine na kuitoa mara kadhaa.
Fikra iliyonijia kwa haraka wakati huo ilikuwa kwamba pengine ile mashine ilikuwa mbovu na harakati zile pengine zilikuwa ni namna ya kurekebisha mitambo.
Kisha nilimuona akiyahamisha macho yake toka kwenye kioo cha ile mashine yake na kugeuka kunitazama kwa makini bila kusema neno halafu akayarudisha macho yake tena kwenye kioo cha ile mashine lakini uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote na hapo moyo wangu ukapiga kite.
“Maximilian, mbona kama taarifa zako zinanikanganya!” kauli yake ikanifanya nipumbazike kidogo huku nikimtazama kwa makini kabla ya kumjibu.
“Zinakungakanya ki vipi!? Kwani kuna nini umekiona kwenye taarifa zangu kisicho cha kawaida?” niliuliza kwa kujiamini huku nikimkazia macho kwa makini yule mrembo ofisa uhamiaji.
“Utaelewa tu baadaye… hebu kwanza weka vidole vyako vya mkono wa kulia hapo,” alisema yule mrembo ofisa uhamiaji huku akinionesha sehemu maalumu ya kuweka vidole.
Kisha nilimuona akiyahamisha macho yake toka kwenye kioo cha ile mashine yake na kugeuka kunitazama kwa makini bila kusema neno halafu akayarudisha macho yake tena kwenye kioo cha ile mashine lakini uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote na hapo moyo wangu ukapiga kite.
“Maximilian, mbona kama taarifa zako zinanikanganya!” kauli yake ikanifanya nipumbazike kidogo huku nikimtazama kwa makini kabla ya kumjibu.
“Zinakungakanya ki vipi!? Kwani kuna nini umekiona kwenye taarifa zangu kisicho cha kawaida?” niliuliza kwa kujiamini huku nikimkazia macho kwa makini yule mrembo ofisa uhamiaji.
“Utaelewa tu baadaye… hebu kwanza weka vidole vyako vya mkono wa kulia hapo,” alisema yule mrembo ofisa uhamiaji huku akinionesha sehemu maalumu ya kuweka vidole.
Nilipoweka vidole akayapeleka macho yake tena kutazama kwenye kioo cha ile mashine, kisha nikamuona akiachia mguno, mara akawa kama aliyejishtukia na kuinua macho yake kunitazama huku akiachia tabasamu ambalo mwanzoni sikuelewa liliashiria nini. Taratibu lile tabasamu lilianza kugeuka kicheko.
Nilibaki nikishangaa huku nikimtazama yule mrembo ofisa wa uhamiaji kwa makini zaidi.
“Samahani kaka, itabidi usubiri kidogo kwa mahojiano mafupi na watu wa usalama,” hatimaye yule mrembo ofisa wa uhamiaji akanambia na kubonyeza kitufe fulani kilichokuwa juu ya meza yake.
“Mimi!?” nilishtuka sana na kumuuliza huku nikimkazia macho kwa udadisi yule mrembo ofisa wa uhamiaji na hapo hapo nikagundua kuwa uso wake ulikwishabadilika na kuwa mbali kaabisa na mzaha.
“Ndiyo, wewe!” alinijibu na kuanza kumhudumia mtu mwingine.
Mara nikapata wazo la kutazama kando yangu, na hapo nikawaona wale maofisa wa usalama wakiwa tayari wamejigawa na kunizingira kila upande. Safari hii walikuwa sita na walikuwa wakinitazama kwa uyakinifu zaidi.
Nilipowatazama kwa makini nikawaona wawili wakiwa upande wangu wa kushoto, wawili upande wangu wa kulia na wawili walikuwa wamesimama nyuma yangu huku wakijitahidi kuweka ulinzi madhubuti kwa kulizingira lile eneo nililokuwa nimesimama.
Walikuwa ni watu wenye miili mikubwa iliyoshiba chakula na mazoezi magumu, hivyo kujengeka vyema, na nilipozitazama sura zao nikagundua kuwa zilitawaliwa na mazingira yenye utata.
Kwa mtazamo wa haraka tu usingeshindwa kubaini kuwa walikuwa ni watu wasiokuwa tayari kuvumilia upuuzi wa namna yoyote. Nilizungusha macho yangu kuwatazama mmoja mmoja kisha nikageuka kumtazama tena yule mrembo ofisa uhamiaji kwa namna ya kuuliza ‘kulikoni?’.
Sikuona tashwishwi yoyote katika uso wa yule mrembo, alikuwa akinitazama kwa makini huku akiwa ameuma mdomo wake wa chini. Nikashusha pumzi za ndani kwa ndani na kumeza funda kubwa la mate kutowesha koo langu lililoanza kukauka.
“Sisi ni maofisa wa usalama, tunakuhitaji kwa mahojiano mafupi,” alisema mmoja wa wale maofisa usalama.
Sikuzungumza kitu chochote badala yake taratibu nikayetembeza tena macho yangu kuwatazama wale maofisa wa usalama mmoja baada ya mwingine na sikuwa na hakika kama hawakuwa makomandoo kutokana na mwonekano wao.
Wanne kati yao walikuwa wamevaa suti maridadi za rangi nyeusi na wengine kijivu, na walionekana kuvaa vifaa maalumu vya mawasiliano masikioni mwao. Nilipowachunguza vizuri nikawaona kama waliokuwa wakiwasiliana na watu wengine kupitia vile vifaa maalumu vya mawasiliano.
Wale wengine wawili walikuwa wamevalia sare rasmi za jeshi la polisi huku wakiwa wameshika fimbo maalumu ambazo hupewa maofisa wa polisi na mmojawapo alikuwa na simu za upepo mkononi mwake. Maofisa wote walikuwa makini zaidi wakinitazama kama vile fisi wenye uchu waliokuwa wanautazama mzoga.
Mmoja kati ya wale wawili wenye sare za jeshi la polisi alikuwa na cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP). Niliweza kukifahamu vizuri cheo chake kufuatia alama ya ngao, nembo ya Adam na Hawa na nyota moja mabegani mwake.
Mwingine niliweza kumtambua kuwa alikuwa na cheo cha Mkaguzi wa Polisi kutokana na alama ya nyota mbili mabegani mwake.
Maofisa usalama wote walionekana ni watu makini sana na macho yao yalikuwa yakinitazama kwa umakini mkubwa katika namna ya kunikagua. Walitazamana na kuonesha kukubaliana na jambo fulani.
Taratibu wasiwasi ukaanza kuniingia, hisia zangu zikaniambia kuwa kulikuwa na jambo baya lilikuwa likielekea kunitokea pale uwanjani.
Nilijikuta nikishikwa na hofu na taharuki isiyoelezeka na hapo hapo moyo wangu ukashikwa na mfadhaiko na kuanza kwenda mbio isivyo kawaida.
Japo sikuelewa kosa langu lililonifanya kutakiwa na watu wa usalama kwa ajili ya mahojiano lakini nilihisi ujasiri ukinipotea kabisa na moyo wangu ukizidi kupoteza utulivu, huku kijasho chepesi kikinitoka mwili mzima.
Sikuwa na namna yoyote ya kufanya bali kusubiri chochote ambacho wangeniambia, maana sikuwa na namna ya kuepuka mahojiano yale au kutoka eneo lile kwani hata pasi yangu ya kusafiria ilikuwa bado imeshikiliwa.
Hivyo, nilifumba macho yangu taratibu na kuanza kumuomba Mungu aniokoe katika hatari yoyote iliyokuwa mbele yangu na kusiwepo jambo lolote baya, bali kama ni mahojiano basi yawe ya kawaida tu kisha niachwe huru niende zangu.
Kisia mwenyewe jinsi nilivyohamanika kujikuta katikati ya maofisa wa usalama walionihitaji kwa mahojiano. Kichwa changu kilizunguka, na ndani yake mseto wa hamu ya kutaka kumuwahi yule mwanadada chotara mwenye mtoto, hasira, hofu na tamaa vilichanganyika.
Ilielekea kuwa wale maofisa usalama na hata maofisa wakaguzi wa pasi za kusafiria pale uwanja wa ndege walikuwa na taarifa zangu mapema na walikuwa wakinisubiri kwa hamu kubwa, kwani nilipotoa pasi yangu kwa yule mrembo ofisa wa ukaguzi wa pasi ndipo shughuli za kupanga kunishughulikia zilipoanza.
Hata wakati yule mrembo alipokuwa akiitia katika mashine pasi yangu ya kusafiria na kuitoa mara kadhaa nadhani ilikuwa ni namna ya kuhakikisha kuwa mimi ndiye huyo mtu waliyekuwa wakimwinda na kumsubiri pale uwanja wa ndege, na sasa nilikuwa nimepatikana na nimeingia mwenyewe kwenye mtego na kunasa.
Nikiwa bado nimesimama pale nikajaribu kujiuliza, nini ilikuwa sababu ya wale maofisa wa usalama kutaka kunihoji ilhali niliamini kuwa sikuwa na kosa lolote na wala sikuwahi kuwa na historia yoyote ya uhalifu, achilia mbali kufikishwa polisi kwa tuhuma zozote.
Hata hivyo, nilipiga moyo konde huku nikijitahidi kuifukuza hofu iliyoanza kuniingia kwa kuwa nilikuwa natambua kuwa harakati dhidi ya ugaidi zilikuwa zimepamba moto na labda nilitakiwa kwa mahojiano mafupi kutaka kujua nyendo zangu.
Nikiwa bado nimesimama pale nikajaribu kujiuliza, nini ilikuwa sababu ya wale maofisa wa usalama kutaka kunihoji ilhali niliamini kuwa sikuwa na kosa lolote na wala sikuwahi kuwa na historia yoyote ya uhalifu, achilia mbali kufikishwa polisi kwa tuhuma zozote.
Hata hivyo, nilipiga moyo konde huku nikijitahidi kuifukuza hofu iliyoanza kuniingia kwa kuwa nilikuwa natambua kuwa harakati dhidi ya ugaidi zilikuwa zimepamba moto na labda nilitakiwa kwa mahojiano mafupi kutaka kujua nyendo zangu.
Hapo nikakumbuka kuwa wiki mbili zilizotangulia nilikuwa nimesoma kwenye mtandao wa intaneti na baadaye kuona kwenye televisheni habari za matukio mawili yaliyodhaniwa kuwa na chembechembe za ugaidi yaliyotokea nchini Tanzania kwa kufuatana.
Tukio moja lilihusu mlipuko wa guruneti uliokuwa umetokea katika mkutano wa kampeni ya ‘Uzalendo’ ambao Waziri Mkuu ndiye aliyetarajiwa kuwa mgeni na badala yake akawakilishwa na Mkuu wa Mkoa, Daniel Luhopelo.
Katika tukio lile lililotokea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam watu 6 walipoteza maisha, 83 walijeruhiwa akiwemo Daniel Luhopelo, huku 10 wakiwa katika hali mahututi.
Tukio la pili lilihusu uvamizi na uporaji wa silaha za kivita kwenye bohari kuu ya silaha iliyokuwa katika eneo la Kwembe nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na katika uvamizi huo askari kadhaa waliuawa.
Kwa matukio yale na mengine ambayo sikuyafahamu nikaamini kuwa walipaswa kujiridhisha kuwa hali ya amani inatamalaki nchini na mimi sikuwa tishio kwa usalama wa nchi hii, hasa kwa kuwa nilionekana mgeni.
Hata hivyo, sikujua kabisa wala sikutarajia kuwa mshtuko mkubwa ulikuwa unanisubiri mbele yangu!
Mara nikawaona maofisa usalama wawili waliokuwa wamevaa suti wakifunua makoti yao na kunionesha bastola zao zilizokuwa zimechomekwa vyema kwenye mishipi kiunoni, kisha yule kamishna msaidizi wa polisi akanitaka kunyanyua mikono yangu juu.
Niligwaya sana na mwili wangu ulianza kutetemeka lakini sikutaka kabisa kuionesha ile hali ya kugwaya, hivyo nilibaki nikiwatazama kwa makini na kuhoji kwanini ninyooshe mikono yangu juu kama mtuhumiwa wakati sikuambiwa kosa langu.
Mara nikamuona mmoja wa wale maofisa wa usalama akiitoa bastola yake na kuishika vizuri akiielekeza kwenye kichwa changu huku akiniamuru ninyooshe mikono yangu juu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment