Search This Blog

Monday, 27 March 2023

HEKAHEKA! - 5

  


Simulizi : Hekaheka!

Sehemu Ya Tano (5)



“Utanisamehe sana kwani sikupenda tufikishane huku ila ni wewe ndiye uliyenilazimisha kufanya hivi, hata hivyo muda wa kujiokoa bado unao. Unaweza kujiokoa kwa kutuambia ukweli kwani bado hujachelewa sana,” alisema Madame Pamela huku akinikazia macho yake.


Mimi sikumjibu kitu kwani muda wote nilikuwa nalia kwa uchungu huku nikiilaani nafsi yangu iliyonituma kuja Tanzania, nilijilaumu kwanini sikumsikiliza Susan aliponiomba niahirishe safari yangu pengine hayo yasingetokea.


Muda ule ule nikamuona Madame Pamela akiibonyeza ile swichi ya umeme pale ukutani, mara nikaanza kupigwa shoti kali ya umeme iliyonitetemesha mwili mzima, nikahisi miale mikali sana ya moto wa umeme ikinishtua kisha ikaanza kutambaa na kusambaa haraka sana mwilini mwangu.


Nikajikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka ambayo sijawahi kuyahisi maishani mwangu yakitambaa mwili mzima, mwili wangu wote ulikuwa unatetemeka huku nikitokwa na jasho jingi.


Nikaanza kupiga kelele kama niliyekuwa nimepigiliwa msumali utosini, hali yangu ilianza kuwa mbaya sana na kumfanya Madame Pamela aibonyeze ile swichi pale ukutani kuizima na hapo nikahisi ahueni kidogo, hata hivyo nilijihisi kizunguzungu kikali sana huku nikihisi kutaka kutapika.


“Bila ya shaka sasa upo tayari kutuambia washirika wenzako wako wapi na silaha mlizopora mmezificha wapi?” aliuliza Madame Pamela akiwa amenikazia macho, sura yake haikuonesha chembe yoyote ya utani.


Nilibaki kimya nikimtumbulia macho maana sikujua niseme nini ili niaminike mbele ya yule mwanamke.


“Brown, nadhani unaelewa fika jibu la swali langu, nasubiri unijibu vinginevyo utakufa kifo cha mateso makali,” alisema Madame Pamela akionekana kupandwa na hasira.


“Nimekwisha waambia mimi sifahamu chochote, niueni mnasubiri nini sasa!” nilisema kwa hasira huku nikitamani nisimame nimchape kibao yule mwanamke.


“Ooh, kumbe wewe ni jeuri!” alisema Madame Pamela huku akiachia tabasamu la dhihaka kisha aliiwasha tena ile swichi ya umeme pale ukutani.


Nikahisi tena miale mikali sana ya moto wa umeme ikinishtua na kuanza kusambaa haraka sana mwilini mwangu, nikapiga yowe kali nikiwasihi waniache na wakati huo nikawa nikiisikia sauti yangu namna ilivyokuwa ikisafiri na kutengeneza mwangwi kwenye kuta za kile chumba.


Niliendelea kupiga yowe huku kile kizunguzungu kichwani kikizidi kuongezeka na hatimaye nikaacha kupiga yowe kwani nilihisi kuishiwa nguvu lakini Madame Pamela hakuonesha kujali kwani alisimama akinitazama tu huku akitabasamu.


Yale mateso yaliendelea zaidi hadi pale nilipoonekana kuanza kuishiwa na nguvu ndipo alipoizima ile swichi. Kisha alisogea akasimama mbele yangu, kisha alinitazama kwa kitambo na kuongea kwa sauti ya chini kama aliyekuwa akininong’oneza.


“Ni afadhali utuambie ukweli, Brown, nadhani umekwisha sikia habari zangu na unajua kwanini nimekabidhiwa jukumu la kuongoza taasisi hii nyeti ya usalama wa taifa, huwa sivumilii ujinga, mimi ni mtu mwema sana lakini siyo mpumbavu na nipo tayari kukubadilishia staili endapo hii itaonekana haikufai.”


“Sasa unataka niseme nini? Kweli mimi sifahamu chochote,” nilimwambia kwa kumsihi.


“Kumbuka mimi ni mpelelezi wa kimataifa na ninao uwezo mkubwa wa kijasusi kuliko wewe…” Madame Pamela aliniambia akiwa katika uso usio na masikhara


“Unafahamu kila kitu, Brown, usinidanganye,” aliongeza huku akinikazia macho.


“Sijui chochote, wewe fanya ulilokusudia,” nilisema kwa hasira maana niliona hata ningesema nini bado nisingeweza kumridhisha yule mwanamke.


“Okay! Wewe ni jasusi uliyekubuhu, nadhani umedhamiria kufa kiume… usijali, ninayo njia nyingine itakayokulazimisha kuongea,” aliniambia Madame Pamela huku akiachia tabasamu la kifidhuli kuchanua usoni mwake.





“Unafahamu kila kitu, Brown, usinidanganye,” aliongeza huku akinikazia macho.


“Sijui chochote, wewe fanya ulilokusudia,” nilisema kwa hasira maana niliona hata ningesema nini bado nisingeweza kumridhisha yule mwanamke.


“Okay! Wewe ni jasusi uliyekubuhu, nadhani umedhamiria kufa kiume… usijali, ninayo njia nyingine itakayokulazimisha kuongea,” aliniambia Madame Pamela huku akiachia tabasamu la kifidhuli kuchanua usoni mwake.


Endelea...


“Achana na porojo kwamba ukikamatwa katika uwanja wa kivita hata ukisema ukweli adhabu yako bado itabaki palepale. Mimi nakuahidi kama utaonesha ushirikiano na kutubu nipo tayari kushauri usamehewe na ninaamini watanisikiliza,” alisema Madame Pamela huku akiendelea kutabasamu.


Sikusema kitu bali nilibaki kimya huku nikimtazama bila kuonesha tashwishwi yoyote usoni kwangu kwani nilishachoshwa na maswali yake.


Madame Pamela alinitazama kwa uyakinifu na kushusha pumzi kisha nikamuona akimweleza jambo komandoo mmoja na hapo yule komandoo akaondoka eneo lile haraka kuelekea kwenye mlango wa chuma wa kile chumba, alifungua na kutoka.


Baada ya kitambo kifupi ule mlango wa chuma ukafunguliwa kisha akaingia akiwa amemuongoza mtu mmoja mrefu mwenye umbo kakamavu hadi mbele yangu, ilinichukua muda mrefu nikimtazama yule mwanamume huku nikijiuliza niliwahi kumuona wapi maana sura yake haikuwa ngeni machoni mwangu.


Baada ya kutuliza vizuri mawazo yangu nikamkumbuka vizuri yule mtu, alikuwa ni yule mtu niliyemuona kwenye picha moja kati ya zile picha nne nilizooneshwa kule kwenye chumba cha mahojiano cha uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, katika picha iliyotuonesha tukiwa watatu: mimi, yeye na Jasmine.


Niliweza kumtambua japo alikuwa amechakaa vibaya, alikuwa akivuja damu nyingi kifuani na maeneo ya usoni na alikuwa amelegea nadhani kwa sababu ya mateso makali huku nyuso mbili za makomandoo ambazo hazina utani zikiwa zimesimama pembeni yake tayari kwa lolote.


Hata hivyo, uso wa yule mwanamume haukuwa na hata chembe ya mashaka wala uoga. Nadhani alikwishazoea yale mateso na alikuwa mkomavu katika nyanja kama zile.


Yule mwanamume alisimama akanitazama kwa makini kisha akaonekana kushtuka sana baada ya kuonesha kunitambua. Ile sura ya ujasiri aliyokuwa nayo ghafla ikayeyuka na badala yake woga ukatawala usoni kwake.


“Brown, ils vous ont? Nous avons fini mon frère,” alisema yule mwanamume kwa lugha ya Kifaransa ambacho nilikuwa nakielewa kiasi na hapo nilielewa kuwa alimaanisha: Wamekukamata? Tumekwisha ndugu yangu.


“Qui es-tu? Je ne te connais pas!” Wewe ni nani? Sikufahamu! Nilimuuliza yule mwanamume kwa Kifaransa changu kibovu huku donge la hasira likinikaba kooni.


“C'est moi Trésor… Trésor Ibingira. Je suis désolé, quelqu'un leur a tout dit, ils savent tout,” alisema kwa huzuni akimaanisha: Ni mimi Trésor… Trésor Ibingira. Nasikitika sana, kuna mtu kawaeleza kila kitu kuhusu wewe, wanajua kila kitu.


“Mimi sikujui na wala sielewi unaongea nini!” nilimwambia yule mtu huku nikimeza mate kutowesha hasira kifuani kwangu.


“D'accord! Mais je pense…” Sawa! Lakini nadhani…


“Trésor, nous ne vous avons pas amené ici à discuter avec votre copain” Trésor hatujakuleta hapa kupiga stori na rafiki yako. Madame Pamela alimkatisha Trésor kwa ukali kwa Kifaransa na kumfanya Trésor ashtuke sana na kugeuka kumtazama Madame Pamela kwa mshangao.


“Êtes-vous choqué, pensez-vous que je ne connais pas le français?” Unashtuka, ulidhani sijui Kifaransa? aliuliza Madame Pamela baada ya kumwona Trésor akishangaa.


Kuanzia hapo nikatambua kuwa huyu ndiye Trésor aliyekuwa akisemwa na Babra kuwa alikuwa rafiki mkubwa wa Brown, ambaye mwanzoni wakati anaingia alikuwa akijiamini lakini sasa alionekana kunywea sana. Alishusha pumzi huku akinyanyua mabega yake juu na kuyashusha.


“Eleza jinsi ulivyofahamiana na huyu mtu aliyeko mbele yako hadi kujihusisha na ugaidi, vinginevyo utakufa hapa hapa mbele yake,” alisema Madame Pamela kwa ukali kidogo, sura yake ilikuwa imebadilika kabisa na sasa alivaa sura ya kazi.


“Nitasema yote na sina sababu ya kuendelea kuficha maana kama huyu naye amekamatwa sina tena matumaini, niliamini yeye angeweza kuniokoa…” alisema Trésor kwa masikitiko.


“Huyu ni rafiki yangu mkubwa, anaitwa Brown Senga. Yeye ndiye kiongozi na mpangaji mkuu wa mambo yote, nimefahamiana naye mwaka 1994 nilipokuwa na miaka kumi na mbili wakati yalipozuka mauaji ya halaiki nchini Rwanda, mimi niliponea chupuchupu nyumba yetu ilipovamiwa usiku wa manane na watu niliowatambua vema na familia yangu kuchinjwa wote huku nyumba yetu ikiteketezwa kwa moto, peke yangu tu nilipona,” alianza kusimulia Trésor.


“Uliponaje?” Madame Pamela alimuuliza.


“Nilitoka mara moja kwenda uani kujisaidia, ndipo walipovamia nyumba na kuua watu wote, hata hivyo mimi wasingeweza kuniua kwa kuwa babu yangu alikuwa amenipa kinga…”


“Kinga? Kinga ipi inayoweza kukuokoa na mauaji!” aliuliza Madame Pamela huku akicheka kwa dharau.


“Miezi sita kabla ya machafuko babu yangu alifariki dunia, lakini kabla hajafa alikuwa amenipa siri kuwa kungetokea machafuko makubwa hivyo akaniachia bangili lenye umbo la nyoka anayekula mkia wake lililokuwa limechongwa kwa mti wa mpingo, akaniambia nilitunze na niwe nalivaa muda wote kwani litanilinda na nitapita popote, nitafanya chochote lakini sitakamatwa. Kwa macho ya kawaida ilikuwa ni kitu kidogo lakini lilikuwa na kazi kikubwa…


“Basi usiku ule wa siku ya machafuko baada ya kuuliwa familia yangu nilikimbia na nikaumalizia usiku porini, juu ya mti. Sikupata usingizi kabisa. Picha kamili ya kuvamiwa nyumbani mwetu ilikuwa inanijia waziwazi. Nilizisikia kelele za sauti ya mama yangu na wadogo zangu zikipasua anga kwa uchungu wa mateso waliyoyapata huku roho zao zisizo na hatia zikitoka,” alisema Trésor kwa uchungu huku akitokwa na machozi.


“Mwili ulinisisimka kila nilipowakumbuka waliohusika na ukatili huo. Moyoni nilijilaumu sana kwanini nilikimbia. Ningerudi ndani na kupambana nao uso kwa uso, potelea mbali hata kama na mimi ningeuawa, na kuanzia siku ile nikajikuta nikianza kutamani kufanya mauaji kwa kila niliyedhani alihusika katika kuiteketeza familia yangu, hata kwa kutoa amri tu.


“Baadaye nilijiondosha mtini mara tu kulipopambazuka, nikatembea mwendo mrefu mpaka nilipotokea barabarani, ambapo niliwaona watu kama ishirini hivi wakijitokeza kutoka msituni upande wa pili wa barabara... walikuwa wanaume kadhaa, wanawake wa makamo na watoto. Mwanzoni niliwaogopa lakini nilipokumbuka kuwa nina kinga niliyopewaa na babu nikajipa moyo na kuwasogelea.


“Baada ya kuwauliza walikokuwa wanaelekea walinijibu kuwa hawajui waendako na hawakujua hata wamefikaje pale. Mara mlio wa gari dogo aina ya Nissan pickup lililokuwa likija kwa mbali ulitushtua wote, wenzangu wakajitosa msituni na kuniaacha mimi nimesimama pale peke yangu nikilitazama gari hilo likija, likiyumba huku na huku kama kwamba dereva wake hakumudu kuliongoza vizuri,” Trésor alinyamaza kidogo na kufuta machozi kisha akameza mate na kuendelea.


“Nikiwa nimesimama palepale ghafla misuli ya tumbo langu ikaanza kutetemeka na kukakamaa. Bila kufikiria nikainua mkono wangu na kulikazia macho lile bangili lenye umbo la nyoka anayekula mkia wake kana kwamba nilikuwa natazama saa maana ndivyo nilivyokuwa nimeelekezwa na babu. Mtetemeko wa misuli ya tumbo langu ukatulia, nikaushusha mkono wangu. Zilibaki hatua chache gari kunifikia, nikalipungia mkono.


“Lilisimama kwa kuseleleka na kuyumba. Kulikuwa na watu wazima sita na mtoto ndani ya lile gari, mbele kulikuwa na dereva mwanamume, mwanamke na mtoto mmoja niliyekuwa nimemzidi kama miaka miwili, na nyuma ya gari kulikuwa na wanaume watatu na mwanamke mmoja. Muda huo huo wanaume watatu wakiwa na mapanga waliruka kutoka nyuma ya gari hilo hata kabla halijatulia kuyumba na kunizunguka huku mapanga yakiwa juu, huku mmoja wao akiwa ameshika bunduki aina ya rifle.



“Nikiwa nimesimama palepale ghafla misuli ya tumbo langu ikaanza kutetemeka na kukakamaa. Bila kufikiria nikainua mkono wangu na kulikazia macho lile bangili lenye umbo la nyoka anayekula mkia wake kana kwamba nilikuwa natazama saa maana ndivyo nilivyokuwa nimeelekezwa na babu. Mtetemeko wa misuli ya tumbo langu ukatulia, nikaushusha mkono wangu. Zilibaki hatua chache gari kunifikia, nikalipungia mkono.


“Lilisimama kwa kuseleleka na kuyumba. Kulikuwa na watu wazima sita na mtoto ndani ya lile gari, mbele kulikuwa na dereva mwanamume, mwanamke na mtoto mmoja niliyekuwa nimemzidi kama miaka miwili, na nyuma ya gari kulikuwa na wanaume watatu na mwanamke mmoja. Muda huo huo wanaume watatu wakiwa na mapanga waliruka kutoka nyuma ya gari hilo hata kabla halijatulia kuyumba na kunizunguka huku mapanga yakiwa juu, huku mmoja wao akiwa ameshika bunduki aina ya rifle.


Endelea...


“Waliniuliza nilikuwa nafanya nini pale nikawaambia kuwa nilikuwa nakimbia machafuko, wakanishangaa nilikuwa nakimbiaje huku nimesimama katikati ya barabara, wakati wenzangu niliokuwa nao walikimbia na kuniacha peke yangu! Nikawaambia kuwa wao wameogopa, wakakimbia. Yule mwanamume aliyekuwa ameshika bunduki aina ya rifle akaniambia ‘Panda haraka tuondoke’ huku akinivuta garini. Ndivyo nilivyonusurika na kufahamiana na Brown ambaye ndiye yule mtoto aliyekuwa ndani ya gari na mwanamume aliyekuwa ameshika bunduki aina ya rifle ndiye baba yake na mama yake ni yule mwanamke aliyekuwa ameketi mbele,” alisema Trésor na kuweka kituo na kufuta tena machozi yaliyokuwa yakimdondoka kisha alinitazama kwa kituo akionekana kufikiria jambo.


Sasa chumba kizima kilizizima kwa ukimya, sikuweza kusema chochote isipokuwa nilibaki nikimtazama Trésor kwa mshangao mkubwa.


“Brown, Je suis désolé mon frère (Brown, samahani kaka yangu), sina namna nyingine isipokuwa kueleza ukweli,” alisema Trésor huku akinyanyua mabega yake juu na kuyashusha.


“Tulipofika Tanzania, nilikwenda kuishi kambini Benaco kwa kipindi kirefu na nilipoyazoea maisha ya Tanzania nikaanza kujishughulisha na biashara ndogondogo mbalimbali zilizonikutanisha na watu wengi, Brown yeye hakukaa sana kambini kwa kuwa baba yake alikuwa na pesa, aliondolewa pale kambini na sikujua alikwenda wapi akaniacha mimi kambini, ila nilisikia kuwa alibadilisha jina na kupelekwa kusoma katika shule nzuri, akaelimika na baadaye kwenda nje ya nchi na hatukuonana tena hadi tulipokuja kukutana tukiwa watu wazima.


“Katika pilikapilika zangu za kimaisha nilikutana na Asteria Buregeya, mwanamke wa Kinyambo aliyekuwa akiishi Nyakahanga wilayani Karagwe na alijishughulisha sana na biashara ya siri ya uuzaji wa silaha za moto. Washirika wake wa karibu sana walikuwa wanajeshi wa Rwanda waliokuwa na mbinu za kuzipata silaha hizo, kuzitoa na kisha kumkabidhi yeye awauzie waliozihitaji. Wakati huo vurugu zilikwishaisha nchini Rwanda na waliohusika na uanzilishi wa machafuko yale walitiwa mbaroni na baadhi yao kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa Arusha, Tanzania.


“Nikiwa na Asteria, nilijihesabu kuwa miongoni mwa watu waliokuwa na bahati ya pekee. Nilikuwa na uhuru wa kuchagua silaha niitakayo kuanzia SMG, AK 47, Winchester 73 hadi 38 police Special. Asteria pia alinitambulisha kwa vijana wa kazi wawili watatu ambao wasingeogopa kuingia hata Ikulu kupambana na walinzi na kuchukua chochote mradi wapewe maelekezo sehemu kilipo hicho kitu.


“Tukaanza kufanya uhalifu na uporaji wa ng’ombe na mali zingine na kuzivusha hadi nchini Rwanda, wakati huo mimi nikiwa na silaha imara… 853 Magnum yenye kiwambo cha kuzuia sauti na ambayo niliweza kuibomoa vipande vipande na kuibeba bila kutiliwa mashaka. Nikiwa na lile bangili lenye umbo la nyoka anayekula mkia wake nililopewa na babu yangu niliweza kufanya uhalifu bila kukamatwa na siku moja ndipo nikakutana na Brown nikiwa katika harakati zangu za uhalifu. Ilikuwa siku ambayo mimi na wenzangu tuliiteka gari yake kwenye pori la Hifadhi ya Moyowosi mkoani Kigoma, na kuanzia hapo tukashikamana na nikajiunga upande wake aliponieleza kuhusu mikakati yake,” alihitimisha Trésor.


Kwa maneno yale ya Trésor nilijikuta naishiwa nguvu, nikaona mwisho wangu ulikuwa umewadia na hapo nikaanza kulaani vibaya nafsi yangu huku nikijuta kuja Tanzania.


“Hilo bangili bado unalo, na mbona safari hii halikukusaidia usikamatwe?” Madame Pamela aliuliza kwa dharau.


“Ningekuwa nalo unadhani mngenikamata kibwege bwege!” alisema Trésor huku akinyoosha mkono wake wa kushoto uliokuwa mtupu kumuonesha Madame Pamela na kuangua kicheko cha dharau.


“Lilipotea wiki mbili zilizopita katika duka la kubadilisha fedha za kigeni la Universal linalomilikiwa na Mgiriki mmoja pale Mnazi Mmoja, kwenye lile tukio la uporaji wa aina yake wa dola za Marekani zaidi ya elfu kumi na pesa za mataifa mengine ambazo hata sikumbuki idadi yake. Ni tukio hilo ndilo lililowafanya ninyi na polisi kunisaka kwa udi na uvumba na kunikamata…


“Nakumbuka niliingia mle dukani nikaanza kutembea dizaini kama nimechuchumaa mfano wa mdudu kaa, na kuwafanya watu wahisi labda nilikuwa na matatizo ya akili lakini hawakujua nilifanya kwa makusudi kabisa. Wakati wakishangaa nikainua mkono wangu na kulikazia macho lile bangili lenye umbo la nyoka kana kwamba nilikuwa natazama saa na hapo misuli ya tumbo langu ikanitetemeka na damu kusambaa mwilini hadi kinywani mwangu. Haikuwa kazi rahisi kwani nilikutana na upinzani mkali lakini niliwamudu wote waliokuwemo na baada ya mapambano nikaondoka na pesa lakini sikukumbuka kama nililidondosha lile bangili au ilikuwaje, lakini hadi nakamatwa juzi nilikuwa bado sijaliona!” alisema Trésor kwa huzuni.


“Kwa hiyo unaamini ulikamatwa kwa sababu ulikuwa umepoteza lile bangili la nyoka wa mpingo anayekula mkia wake lililokuwa linakulinda?”


“Bila hivyo mnadhani mngenipataje?” aliuliza Trésor.


“Pumbavu! Unajidanganya sana, sisi huwa hatuzuiwi na mazingaombwe katika kazi ya upelelezi. Miaka mitatu Israel kujifunza ujasusi wa kisayansi unadhani bado unaweza kuniaminisha na hadithi zako za uchawi wa kufikirika za bangili la nyoka wa mpingo anayekula mkia wake! Uliza habari zangu uambiwe, nimekwisha fanya kazi kubwa na za hatari itakuwa hizi hadithi za bangili la nyoka wa mpingo!” alifoka Madame Pamela huku akijigamba mbele ya Trésor.


“Kilichofanya tukupate ni kwamba tunavyo vyanzo vingi vya kutuletea taarifa, hasa baada ya kukuona kwenye kamera za usalama ndani ya lile duka la kubadilisha pesa za kigeni, tukaunganisha na lile tukio la uporaji fedha kwenye Benki ya Wananchi na kugundua kuwa kwa vyovyote mshiriki ni mmoja, kwani hata siku ya uporaji sehemu zote ilikuwa ni Ijumaa ya mwisho wa mwezi. Ndiyo maana tulipokukamata cha kwanza ilikuwa ni kutafuta taarifa za Brown Senga,” aliongeza Madame Pamela na kunitupia jicho.


Nilibaki kimya pasipo kusema neno lolote kwani sikuona sababu ya kuendelea kukana kuwa mimi si Brown Senga kama walivyoamini. Madame Pamela alinitazama kwa kitambo kisha akamgeukia tena Trésor.


“Sawa, tunajua kuwa na wewe ulishiriki kwenye tukio la kigaidi la uporaji wa silaha katika bohari kuu ya silaha, hebu tueleze mlikozifichwa silaha hizo,” Madame Pamela alimwambia Trésor huku akiwa amekunja uso wake.


Trésor aligeuka haraka na kunitazama huku uso wake ukionekana kuwa na hofu kubwa.


“Chochote atakachowaleleza ni uongo, simjui huyu mtu na wala sijawahi kukutana naye,” nikasema kwa hasira kabla Trésor hajajibu lakini nikashtukia nikizabwa kofi la nguvu usoni lililonifanya kuona vimulimuli mbele ya macho yangu.


“Shut up! Hujaulizwa wewe, unakimbilia kujibu!” Komandoo aliyenichapa kibao akafoka.


Nikasonya kwa hasira huku nikigeuza shingo yangu kumtazama yule komandoo, nikamtemea mate, kutahamaki nikazabwa kofi la pili lililonifanya kuyahisi maumivu makali sana yaliyosambaa haraka hadi shingoni hadi mgongoni.


“Trésor, tueleze ni wapi mmeficha silaha!” Madame Pamela akamwambia Trésor kwa ukali kidogo.




“Chochote atakachowaleleza ni uongo, simjui huyu mtu na wala sijawahi kukutana naye,” nikasema kwa hasira kabla Trésor hajajibu lakini nikashtukia nikizabwa kofi la nguvu usoni lililonifanya kuona vimulimuli mbele ya macho yangu.


“Shut up! Hujaulizwa wewe, unakimbilia kujibu!” Komandoo aliyenichapa kibao akafoka.


Nikasonya kwa hasira huku nikigeuza shingo yangu kumtazama yule komandoo, nikamtemea mate, kutahamaki nikazabwa kofi la pili lililonifanya kuyahisi maumivu makali sana yaliyosambaa haraka hadi shingoni hadi mgongoni.


“Trésor, tueleze ni wapi mmeficha silaha!” Madame Pamela akamwambia Trésor kwa ukali kidogo.


Endelea...


“Ukweli japo mimi ni mshirika wa karibu wa Brown lakini naapa sijui mahali zilikofichwa kwani mkakati wote anaujua yeye na watu wengine wasiozidi watatu ambao mimi siwafahamu, mimi nilikuwa mtu wa kusubiri kupewa amri tu,” alisisitiza Trésor na kuniacha na mshangao usioelezeka.


“Na kuhusu washirika unaowafahamu?” aliuliza Madame Pamela.


“Wote ninaowafahamu ndio wale niliowataja, siwajui wengine labda muulizeni mwenyewe,” alisema Trésor huku akiyakwepa macho yangu na kuinamisha uso wake chini kwa hofu.


“Wapi mmezificha silaha, au unataka tukurudishe tena chumba cha mahojiano ndipo useme ukweli, siyo?” Madame Pamela alimuuliza Trésor kwa ukali.


“Nimewaambia Brown ndiye anayejua kila kitu, mimi ningekuwa najua zilipo ningewaambia, mbona haya mengine nimesema! Najua hata nikificha bado adhabu inayonikabili ni kifo tu,” alisema Trésor.


“Mimi naona mmeamua kupandikiza watu wenu ili mnikomoe, huu ni uongo mkubwa na ninaapa kuwa lazima niwashtaki kwenye mahakama ya haki za binadamu,” niling’aka kwa hasira.


“Kama unadhani kuwa Trésor ni muongo kwanini usijiulize tuliipata wapi ile picha mliyopiga wote mkiwa na Jasmine, au hujiulizi zile nyaraka zako zikiwemo zile pasipoti na kijitabu chenye mipango yako haramu tulivipataje kama siyo yeye aliyetusaidia kuvipata?” Madame Pamela akaniuliza huku akinitazama kwa udadisi.


“Nimekwishawaambia mimi siitwi Brown. Sijui mmewatoa wapi hawa watu wanaotoa ushahidi wa uongo dhidi yangu, na mkakubali kudanganywa kiasi hiki! Muulizeni kila kitu yeye ndiye atakuwa anafahamu kuhusu hiyo mipango na ugaidi mnaonituhumu nao,” nilijitetea lakini haikuonekana kusaidia.


Madame Pamela alimpa ishara yule komandoo ya kumwondoa Trésor na kumrudisha alikomtoa. Wakati Trésor akiondolewa Madame Pamela alinigeukia akanitazama kwa uyakinifu huku akiachia tabasamu la ushindi.


“Sasa niambie, washirika wenzako wako wapi na silaha mmezificha wapi?” aliniuliza kwa sauti tulivu.


Sikumjibu bali niliendelea kubaki kimya huku nikimkodolea macho kwani nilionesha kuchoshwa na maswali yake.


Alishusha pumzi ndefu huku akiendelea kutabasamu na baadaye tabasamu lake liligeuka kuwa kicheko, kisha nikamuona yule komandoo aliyetoka na Trésor akirudi na muda huo huo Madame Pamela akawapa ishara fulani wale makomandoo ambayo sikufahamu maana yake.


Mara nikawaona wale makomandoo wakinisogelea kwa ukakamavu mkubwa, na kwa haraka sana wakanifungua zile pingu zilizokuwa zimefungwa kwenye mikono na miguu yangu pale kwenye kile kiti cha umeme kilichokuwa kikitumika kunisulubu.


Nikiwa bado nashangaa ghafla wale makomandoo wakanishika miguu yangu na kunivuta wakinishusha kwa nguvu kutoka pale kwenye kile kiti hali iliyonifanya nitue pale chini sakafuni kwa matako na kunifanya nisikie maumivu makali sana yaliyosambaa mwili mzima.


Nilijaribu kujitetea lakini ilikuwa kazi bure kwani walianza kunishushia kipigo cha mateke mwilini mwangu na kujikuta nikiishiwa na nguvu na kulala sakafuni kama mfu.


Wale makomandoo waliporidhika kuwa kile kipigo kilikuwa kimenilegeza kiasi cha kutosha, wakaanza kuniburuza kibabe kuelekea kule kwenye lile tangi kubwa lililokuwa limejengwa kwa vioo ambalo ndani yake lilikuwa limejazwa maji.


Walinibwaga pale chini jirani na lile tangi la maji. Nikiwa pale chini nikihema kwa nguvu kutokana na kile kipigo nilimuona Madame Pamela akinisogelea taratibu huku wale makomandoo wakinizunguka na hapo nikafungwa kamba mikononi.


“Tuambie wenzako wako wapi na silaha mmezificha wapi?” aliniuliza Madame Pamela kwa hasira.


“Wenzangu akina nani?” nilimuuliza kwa hasira.


“Unaoshirikiana nao kufanya ugaidi”


“Sifahamu chochote kuhusu ugaidi unaouzungumzia…”


Nilikatishwa na kipigo cha mateke ya mgongoni, kabla sijajua niseme nini mara nikabebwa mzobe mzobe na wale makomandoo kisha nikarushwa na kuangukia ndani ya lile tangi la maji. Matukio yote yale yalifanyika kwa haraka sana.


Nikajua sasa walikuwa wamedhamiria kunitesa kwa kunizamisha ndani ya lile tangi la maji kwa kufungulia umeme ulioungwa ndani ya lile tangi la maji ili kunipiga shoti mbaya na ikiwezekana kuniua kabisa.


Nikakumbuka kuwa niliwahi kusoma habari kuhusu matumizi ya mbinu za ukatili na utesaji kwa kuwaweka watuhumiwa kwenye maji, kuwakosesha usingizi, kuwapiga shoti ya umeme na kila aina ya utesaji ili kupata siri kutoka kwa magaidi.


Nilisimama na yale maji ndani ya lile tangi yaliishia usawa wa kifua changu. Nikiwa sijui kilichokuwa kinaendelea ghafla nikapigwa shoti kali ya umeme iliyonitetemesha mwili mzima huku nikihisi ngozi yangu ikiunguzwa na moto wa umeme uliokuwa ukisambaa haraka sana mwilini mwangu.


Nikajikuta nikiwa katikati ya maumivu makali sana yasiyoelezeka, nikaanza kutetemeka kama niliyekumbwa na ugonjwa mbaya wa degedege.


Nilifumbua mdomo wangu kupiga kelele za kumuomba Madame Pamela asitishe yale mateso lakini sauti yangu haikuweza kutoka, kila nilipopiga kelele niliisikia sauti yangu ikiishia ndani ya akili yangu.


Kwa mbali nikasikia mlango wa kile chumba ukigongwa kwa nguvu kisha ukafunguliwa na hapo nikasikia sauti ya vishindo vya watu waliokuwa wakija mbio kule kwenye lile tangi huku wakipiga kelele kumtaka Madame Pamela asitishe yale mateso.


Muda ule ule nikaanza kujiona nikipaa angani kwa kasi ya ajabu sana, na nilipofika juu zaidi nikajikuta nikianza kushuka chini kwa kasi ile ile na kisha nikatumbukia kwenye shimo refu sana lililokuwa na kiza kilichotisha.


Na mara giza zito likatanda kwenye mboni zangu za macho huku taratibu nguvu zikianza kuniishia na mwili wangu ukilegea, mapigo yangu ya moyo nayo yakaanza kudorora, mwishowe nikahisi roho yangu ikifika njia panda…




* * * * *




Nilizinduka nikajikuta nipo kwenye chumba kikubwa nikiwa nimelala kwenye kitanda kikubwa cha chuma cha futi nne na nusu kwa sita, nikiwa nimelalia foronya laini na mto wa kuegemeza kichwa.


Ndani ya chumba kile kulikuwa na hewa safi iliyokuwa ikisambazwa taratibu na kiyoyozi kilichokuwa juu ya dari ya kile chumba iliyokuwa imetengenezwa kwa gypsum nzuri ya rangi nyeupe na katika sehemu za dari ile kulining’inizwa taa nzuri.


Nilikuwa nimerudiwa na fahamu zangu na sikujua nilipoteza fahamu kwa muda gani, hisia zangu zilinitanabaisha kuwa nilikuwa nimerudiwa na fahamu huku nikikumbuka vizuri masaibu yote yaliyonitokea kule kwenye chumba cha mateso makali.


Sikuwa na uhakika kama nililetwa pale kwa gari, mkokoteni, machela au niliburuzwa kama ilivyotokea kule kwenye chumba cha mateso, kwa kuwa sikuwa na fahamu yoyote nilipokuwa nikiletwa pale.


Hata hivyo, jambo hilo halikuwa la muhimu sana kwangu. Jambo lililokuwa la muhimu ni kwamba nilikuwa bado nipo hai, na hivyo nikataka kujua nilikuwa wapi.


Mambo sasa yananoga, ni nini kitaendelea? Fuatilia kuujua mwisho wa Hekaheka...





Sikuwa na uhakika kama nililetwa pale kwa gari, mkokoteni, machela au niliburuzwa kama ilivyotokea kule kwenye chumba cha mateso, kwa kuwa sikuwa na fahamu yoyote nilipokuwa nikiletwa pale.


Hata hivyo, jambo hilo halikuwa la muhimu sana kwangu. Jambo lililokuwa la muhimu ni kwamba nilikuwa bado nipo hai, na hivyo nikataka kujua nilikuwa wapi.


Endelea...


Niliyatega masikio yangu kwa makini huku nikijaribu kutafakari kuwa pale nilikuwa wapi. Sikusikia sauti ya kitu chochote na utulivu ndani ya chumba kile ulikuwa ni wa hali ya juu kiasi kwamba nilianza tena kuingiwa na hofu.


Nilijaribu kujiinua kutoka pale kitandani nikahisi maumivu makali yakisambaa mwilini sambamba na kichwa kuuma huku nikihisi kizunguzungu na mwili wangu ulikuwa umedhoofika sana mithili ya mlevi aliyeamka na uchovu wa pombe.


Nilipojichunguza vizuri nikagundua kuwa nilikuwa nimefungwa bandeji na plasta maeneo mbalimbali ya mwili wangu. Kilichonishangaza zaidi ni kwamba nilikuwa nimevaa nguo zangu safi zilizokuwa kwenye begi langu tofauti na zile nilizokuwa nimevaa wakati nikiteswa, pia sikuwa nimefungwa pingu.


Kingine nilichogundua ni kuwa nilikuwa nimefunikwa kwa shuka safi la rangi ya samawati, nikashtuka. Niligeuza shingo yangu kuyatazama vizuri mandhari ya kile chumba na kugundua kuwa hakikuwa chumba nilichokizoea, na wala hakikuwa kile chumba cha mateso.


Hiki kilikuwa chumba maalumu kilichoonekana kama ni wadi maalumu ya VIP kikiwa na mitambo ya kisasa ya tiba ya hali ya juu yenye kumsaidia mgonjwa kupumua na mingine ya kusoma mapigo ya moyo jinsi yanavyoendelea.


Nikajikuta nikishikwa na mshangao huku nikiwaza pale nilikuwa wapi na nilifikaje!


Nilishangaa kuona kulikuwa na meza ndogo upande wangu wa kulia na juu ya ile meza kulikuwa na trei ndogo ya aluminium iliyokuwa na vifaa vyote muhimu vya tiba kama mikasi, bandeji, plasta, dawa ya kukaushia vidonda, mabomba ya sindano, glovu, chupa ya maji, bilauri na dawa za vidonge ambazo sikuzifahamu.


Baadhi ya vile vifaa vilikuwa vimefunguliwa na kuachwa wazi kitendo kilichoashiria kuwa tayari vilikuwa vimekwisha tumika.


Kando kidogo ya kile kitanda kulikuwa na stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyokuwa imetundikiwa chupa mbili, moja ilikuwa chupa ya maji aina ya Dextrose 5% yaliyokuwa yamechanganywa na fulani dawa maalumu, na nyingine ilikuwa ni chupa ya damu.


Macho yangu yakapata uhai kidogo na nilipochunguza kwa makini nikagundua kuwa mirija ya zile chupa ilishuka hadi kwenye mkono wangu wa kulia na mwishoni kulikuwa na sindano mbili zilizokuwa zimechomekwa kwenye ule mkono na kupeleka maji na damu kwenye mishipa yangu ya damu.


Niliziangalia zile chupa zilizokuwa zimetundikwa kwenye chuma kwa makini na kushusha pumzi, kisha nikafumba macho yangu nikijaribu kutafakari.


Japo nilikuwa bado sijaelewa pale ni nilikuwa wapi lakini nilishangaa sana kujiona nikiwa ndani ya chumba kilichoonekana kuwa na mifumo ya kisasa kabisa ya uchunguzi kwa mgonjwa.


Nikaanza tena kujiuliza pale ni hospitali gani na nilifikaje lakini sikupata jibu, nikaanza kuyatembeza macho yangu taratibu huku na kule katika kutathmini vizuri mandhari yale. Nia yangu ilikuwa kuona kama kulikuwa na kielelezo chochote ambacho walau kingenifanya kuhisi pale nilikuwa katika hospitali gani.


Hata hivyo, nilipiga moyo konde na kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuniweka hai hadi wakati ule nikiamini kuwa Mungu alikuwa ametenda muujiza wake. Sikutaka kujiuliza maswali mengi kwa kuamini kuwa mambo mengine ningekuja kuyafahamu baadaye.


Nilitamani ile isiwe ndoto, niligeuza shingo yangu kuutazama mlango wa kile chumba kwa makini nikauona ukiwa umefungwa ingawa sikuweza kufahamu kama ulikuwa umefungwa kwa funguo au ulikuwa umerudishiwa tu.


Hata hivyo nilishindwa kuthibitisha kwani afya yangu ilikuwa dhaifu sana kiasi cha kushindwa hata kunyanyuka na kuketi pale kitandani.


Kutoka pale kitandani nilipolala nilibaki nikiwa mtulivu huku nikiutazama ule mlango wa kuingilia mle ndani, nikawa najiambia kuwa chochote ambacho kingetokea ingenipasa nisubiri tu kwani afya yangu ilikuwa dhaifu sana kuweza kuleta upinzani. Hivyo sikuwa na namna ila kuendelea kujipa subira.


Nikiwa bado nautazama ule mlango mawazo mengi yalikuwa yakipita kichwani mwangu na kunifanya nijihisi kama kiumbe kigeni katika sayari mpya.


Muda ule ule nikashtuka kuona kitasa cha ule mlango kikizungushwa taratibu kisha ule mlango ukasukumwa na kufunguka, nikajikuta nikiingiwa na hofu huku moyo wangu ukipoteza utulivu katika kiwango cha hali ya juu.


Niliyafumba haraka macho yangu nikatulia nikijifanya bado sijarudiwa na fahamu ili niweze kujua kwanini nilikuwa pale na nini kilikuwa kinaendelea pale.


Nilisikia kishindo cha mtu aliyekuwa akiingia na kisha akatembea kuja pale kitandani, kisha nikashtuka baada ya kuhisi mkono ukinigusa kwenye paji langu la uso.


Nilifumbua macho yangu taratibu kisha nikageuza shingo yangu kutazama upande ulikotokea ule mkono na kumuona mwanamume mnene na mrefu akiwa amesimama huku akinitazama kwa huruma.


Kwa haraka niliweza kugundua kuwa alikuwa na umri uliokaribia miaka hamsini, maji ya kunde na misuli imara ya mikononi iliyotuna kikamilifu vilimfanya aonekane kama bondia mkongwe. Alikuwa na uso mpana huku miwani yake mikubwa ikiwa imeyahifadhi macho yake makubwa.


Alikuwa amevaa suruali ya rangi nyeusi, shati la samawati na juu yake alivaa koti refu jeupe la kidaktari huku shingoni kwake akiwa amening’iniza kifaa cha kupimia mapigo ya moyo ambacho kitaalamu kiliitwa stethoscope.


“Vipi Maximilian, unajisikiaje?” yule daktari aliniuliza baada ya kugundua kuwa nimeamka, hata hivyo sauti yake ilikuwa ya chini kana kwamba hakutaka watu wengine wasikie alichokuwa akiongea.


Kwanza nilisita baada ya kusikia nikiitwa kwa jina langu halisi, nikajiuliza niko wapi na nini kilikuwa kinaendelea. Nikashusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikimeza mate kuitowesha hofu ndani yangu.


“Nasikia maumivu ya mwili na kichwa, halafu ninahisi kizunguzungu na mwili umedhoofu sana,” hatimaye nikasema kwa sauti tulivu huku nikimtazama yule daktari kwa makini.


“Usijali, utapona… ulipoteza damu nyingi mwilini ila naamini utakapomaliza hii chupa ya tatu ya damu utapata afueni, kama hali yako haitabadilika,” alisema yule daktari aliyeonekana mchangamfu, mkarimu na rafiki kwa wagonjwa huku akinitazama kwa makini.


“Chukua hivi vidonge vya kutuliza maumivu, ukimeza utapata nafuu kabisa,” aliniambia huku akinipa vidonge viwili vya kutuliza maumivu na bilauri ya maji.


Wakati nikivichukua vile vidonge na kuvitupia mdomoni niliitupia jicho saa yake aliyokuwa ameivaa mkononi na kugundua kuwa ilikuwa inasomeka saa tatu na robo.


Muda ule miale ya jua la saa tatu asubuhi ilikuwa imepenya dirishani na kutuama chumbani na kuenea hadi pale kwenye kitanda nilipolala. Ni dhahiri kuwa joto la miale ile ya jua la saa tatu asubuhi lilikuwa limeamsha homa hafifu mwilini mwangu.



“Chukua hivi vidonge vya kutuliza maumivu, ukimeza utapata nafuu kabisa,” aliniambia huku akinipa vidonge viwili vya kutuliza maumivu na bilauri ya maji.


Wakati nikivichukua vile vidonge na kuvitupia mdomoni niliitupia jicho saa yake aliyokuwa ameivaa mkononi na kugundua kuwa ilikuwa inasomeka saa tatu na robo.


Muda ule miale ya jua la saa tatu asubuhi ilikuwa imepenya dirishani na kutuama chumbani na kuenea hadi pale kwenye kitanda nilipolala. Ni dhahiri kuwa joto la miale ile ya jua la saa tatu asubuhi lilikuwa limeamsha homa hafifu mwilini mwangu.


Endelea...


Niligida mafunda kadhaa ya maji yaliyokuwa kwenye ile bilauri nikivisukumia ndani vidonge vile kisha nilimrudishia yule daktari ile bilauri huku nikimtazama kwa utulivu.


“Pole sana…” yule daktari aliniambia huku akiachia tabasamu la kirafiki. Kisha alitoa mashine ndogo ya kupimia shinikizo la damu na mapigo ya moyo.


“Samahani, nataka niangalie mwenendo wa presha na mapigo ya moyo wako…” alisema yule daktari.


Aliifunga ile mashine kwenye mkono wangu wa kushoto kisha akaanza kuipampu kwa muda na mara presha [pressure gauge] ikaanza kupanda juu.


Niliyafumba macho yangu huku nikibana pumzi kutokana na ile mashine kuanza kubana kwenye mkono wangu na kusababisha maumivu kidogo.


Baada ya kitambo fulani yule daktari alianza kulegeza taratibu kifungo fulani kidogo kilichokuwa pembeni, mara nikasikika sauti ya ‘hisssiii’ huku pressure gauge ikishuka taratibu, na wakati huo namba zilikuwa zikijiandika kwenye kioo kidogo juu ya ile mashine.


Nilikuwa makini kutazama pale kwenye namba lakini niliishia kuona maandishi SYS 110 na chini yake kukiwa na maandishi DIA 60, huku chini zaidi kukiwa na maandishi PULSE 72. Hata hivyo, sikujua maana yake ila nilihisi kuwa zile namba zilimaanisha presha ya damu yangu na mapigo ya moyo.


Nikamuona akiweka rekodi kwenye faili alilokuja nalo na kunitazama.


“Naona presha yako inaanza kuimarika, una 110 juu ya 60 ambayo siyo mbaya na moyo wako unapiga mara 72 kwa dakika,” alisema na kuchukua vifaa vyake kisha akaanza kupiga hatua zake haraka kuondoka, sikutaka aondoke bila kunitegulia kitendawili changu, hivyo nikamtupia swali.


“Samahani dokta, hapa nipo wapi?” nikamuuliza huku hofu ikinitambaa taratibu.


Yule daktari aligeuza shingo yake na kunitazama kwa kitambo kisha nikamuona akishusha pumzi za ndani kwa ndani. Hata hivyo sikuweza kuona tashwishwi yoyote usoni kwake.


“Usijali, utafahamu baadaye kidogo, ila upo kwenye mikono salama,” alijibu na kuanza kuondoka haraka lakini nikamwita tena kitendo kilichomfanya ageuke tena kunitazama huku akionesha uso wa mashaka kidogo.


“Nini kilitokea na hapa ni wapi?” nilimuuliza tena yule daktari huku nikiyapuuza maneno yake na kumkazia macho, na hapo nikamuona akiyakwepa macho yangu na kutazama kando huku akishusha pumzi ndefu.


“Kwani tatizo lako nini? Nimekwambia uko kwenye mikono salama,” aliongea kwa ukali kidogo yule daktari huku akionekana kuanza kukerwa na maswali yangu, kisha aliyapeleka macho yake kutazama dirishani kama mtu aliyekuwa anawaza jambo fulani.


“Nisamehe, sikupaswa kukujibu kwa ukali,” alisema yule daktari huku akijipiga kofi dogo kwenye paji lake la uso kisha akapandisha mabega yake juu na kushusha pumzi ndefu.


“Kwani nimelazwa hapa tangu lini?” nilimuuliza tena huku nikiendelea kuyapuuza maneno yake na kumkazia macho.


“Leo ni siku ya nne tangu uletwe hapa,” yule daktari alinijibu huku akishika kitasa cha mlango na kukinyonga. Kabla hajatoka kabisa nikaongea neno lililomfanya ageuke tena kunitazama.


“Dokta nasikia njaa.”


“Usijali utaletewa chakula sasa hivi,” alisema yule daktari na kutoka nje haraka, ilionekana kama vile hakupenda kuulizwa maswali.


Mara tu yule daktari alipoondoka mle chumbani ile hali ya upweke ikanirudia tena pale kitandani huku nikiupisha utulivu kichwani mwangu.


Nilibaki nikiwa nautazama ule mlango huku nikizidi kuhisi kuchanganyikiwa kidogo kutokana na tabia ya yule daktari ya kuonesha kuyakwepa maswali yangu na kutotaka kuongea na mimi.


Na hapo fikra zangu zikahamia kutafakari juu ya Madame Pamela na wale makomandoo waliokuwa wakinitesa kwa kuwa nilionekana gaidi mwenye taarifa nyeti ambazo serikali ilizihitaji kwa gharama yoyote. Je, Madame Pamela aliwezaje kuniacha hai?


Kisha likanijia swali, je, ni nani wale walioingia ndani ya kile chumba na kumtaka Madame Pamela asitishe mateso wakati nilipokuwa nateswa kwa kupigwa shoti ya umeme ndani ya lile tangi la maji? Kwanini walimtaka Madame Pamela asitishe kunitesa?


Nilizidi kushangaa, sikusita kujiuliza ni nani aliyelipia gharama zote za matibabu yangu kwa kipindi chote cha siku nne tangu niletwe pale!


Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani huku moyo wangu ukiendelea kupoteza utulivu, hasa nilipokumbuka kauli ya Madame Pamela aliponiambia kuwa ‘hatajali kuhusu kifo changu, ikiwa sitaki kusema ukweli ni lazima ningekufa tu’!


Hata hivyo akili yangu ilianza kugoma kuamini kama nilikuwa hai nikihudumiwa kwenye chumba kilichokuwa na mifumo ya kisasa kabisa ya uchunguzi kwa mgonjwa. Nikajikuta nikibaki kwenye mkanganyiko usioelezeka, huku akili yangu ikianza kuniambia kuwa huenda pale nilikuwa ndotoni.


Ili kuhakikisha kama kweli sikuwa naota nikajifinya kidogo kwenye shavu langu la kushoto ili nione kama sikuwa naota. Finya yangu ya mashaka ilinifanya nitumie nguvu kubwa na hivyo nilipata maumivu makali sana.


“Ooh shit!” nikang’aka kwa sababu ya maumivu makali niliyoyahisi.


Ni kweli sikuwa naota na nilikuwa hai lakini swali lililoendelea kunisumbua lilikuwa, niliokokaje kutoka kwenye kifo kilichotokana na mateso makali na hata kuteswa kwenye kiti cha umeme kabla sijatumbukizwa kwenye tangi lililojazwa maji lililounganishwa na mfumo wa umeme? Jambo hilo likabaki kuwa kitendawili!


Hali ile ikasababisha jasho jepesi lianze kunitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu japo mle ndani hakukuwa na joto, aina fulani ya joto la woga wa aina yake lilinitambaa mwilini na mapigo ya moyo wangu yakaanza kwenda mbio isivyo kawaida!


Kila nilipomfikiria Madame Pamela nilijikuta nikikosa amani, nikahisi kuwa japo nilikuwa hai lakini hicho kisingekuwa kigezo tosha cha kunifanya niamini kuwa nilikuwa katika mikono salama. Kwa hiyo nikajionya kuwa makini zaidi.


Hata hivyo, sikuwa na namna yoyote ya kufanya kwani chochote ambacho kingeweza kutokea nilipaswa kukabiliana nacho maana kama Madame Pamela na wale makomandoo wangetaka kunidhuru au kuniua wasingeshindwa, kwani uhai wangu ulikuwa mikononi mwao.


Hatimaye nikameza funda kubwa la mate nikijitahidi kuyachuja mawazo yale kichwani mwangu na wakati huo zile dawa za kutuliza maumivu nilizomeza zikifanya kazi yake mwilini mwangu.


Na muda ule ule nikashuhudia tena kitasa cha mlango wa kile chumba kikizungushwa taratibu kisha ule mlango ukasukumwa ndani na kufunguka.


Nilimuona mwanamke mmoja mnene ambaye niliweza kumtambua kwa mavazi yake kuwa ni muuguzi akiingia mle ndani huku akiwa amebeba kikapu kilichokuwa na hotpot dogo la chakula, mabakuli mawili yaliyokuwa na mfuniko, sahani, kijiko kikubwa cha kupakulia na kingine cha kulia chakula.


Nyuma ya yule muuguzi alifuatia yule daktari aliyetoka mle chumbani dakika kadhaa zilizokuwa zimepita akiwa amebeba bilauri pamoja na chupa kubwa ya maji ya kunywa.


Waliingia na kuviweka vile vyombo juu ya meza ndogo kando ya kile kitanda. Moyo wangu ulilipuka kwa furaha baada ya kuona kile chakula nikajua sasa nipo salama, lakini furaha yangu ikayeyuka ghafla baada ya kumuona Madame Pamela akiingia huku ameongozana na walinzi wawili.




Nyuma ya yule muuguzi alifuatia yule daktari aliyetoka mle chumbani dakika kadhaa zilizokuwa zimepita akiwa amebeba bilauri pamoja na chupa kubwa ya maji ya kunywa.


Waliingia na kuviweka vile vyombo juu ya meza ndogo kando ya kile kitanda. Moyo wangu ulilipuka kwa furaha baada ya kuona kile chakula nikajua sasa nipo salama, lakini furaha yangu ikayeyuka ghafla baada ya kumuona Madame Pamela akiingia huku ameongozana na walinzi wawili.


Endelea...


Madame Pamela alikuwa amevaa suti nadhifu ya kike ya rangi ya kijivu ya ‘single button’ iliyokuwa imemkaa vyema na kumpendeza sana, wale walinzi wake pia walikuwa wamevaa suti nyeusi na miwani myeusi.


Moyo wangu ukapiga kite kwa sekunde kadhaa huku nikihisi mwili wangu ukifa ganzi na mara ubaridi fulani wa aina yake ukaanza kunitambaa mwilini huku mapigo ya moyo wangu yakibadili mwendo wake na kuanza kwenda mbio isivyo kawaida!


Nikabaki nimemtumbulia macho Madame Pamela kana kwamba nilikuwa nimemuona zaraili mtoa roho. Mwanzoni sikuona tashwishwi yoyote kwenye uso wake, bali alisimama akawa akinitazama kwa makini.


Wasiwasi mwingi ukanijaa, nikaanza kuhisi kuwa nilikuwa nimefuatwa kwa ajili ya mahojiano kwa mara nyingine na ikiwezekana nipate mateso makali kuliko niliyopata mwanzo hadi nicheue taarifa walizokuwa wakizihitaji.


Nilifungua mdomo wangu kutaka kusema lakini nikajikuta nikibaki mdomo wazi huku donge la fadhaa likinikaba kooni.


Hata hivyo, tabasamu jepesi la upendo nililoliona usoni kwa Madame Pamela na macho yake makubwa yaliyonitazama kwa upole tofauti na siku ile ya kwanza alipokuwa akinihoji kwenye kwenye chumba cha mateso makali, vikaufanya moyo wangu utulie kidogo.


“Unaendeleaje, Bwana Maximilian?” Madame Pamela akaniuliza kwa sauti ya upole huku akitabasamu.


Swali lake likanishtuka sana, mwanzoni nilidhani kuwa labda nilikuwa sijasikia vizuri aliponiita kwa jina la Maximilian badala ya jina la Brown Senga walilokuwa wakiniita mwanzo!


Nikafungua mdomo wangu kutaka kujibu lakini nilijikuta nikishindwa kusema chochote kwa kuwa nilikuwa njia panda. Kwa kweli sikumwelewa kabisa huyu mwanamke!


Wazo la kwamba labda nilikuwa ndotoni likanijia tena lakini akili yangu ikakataa, hivyo mara hii milango yangu ya fahamu ikawa makini zaidi huku nikiishirikisha akili yangu kikamilifu katika kuniletea taarifa sahihi za kuaminika kama nilichokisikia kutoka katika kinywa cha Madame Pamela kilikuwa sahihi au lah!


“Usihofu, najua una maswali mengi sana akilini mwako na pengine unadhani labda uko ndotoni,” alisema Madame Pamela akiniangalia kwa uyanikifu huku akionekana kuyasoma mawazo yangu.


“Pole sana,” alisema tena kwa sauti ya upole baada ya kuniona nikiwa bado nipo kimya huku nikimkodolea macho. Na hapo akaufanya moyo wangu ulipuke kwa furaha isiyopimika.


“Ahsante,” nikamjibu huku nikijaribu kuyasoma mawazo yake kuona kama uso wake ulimaanisha kile alichokuwa akikisema au lah!


Kuna wakati nilidhani labda alikuwa akinitega ili kujua kama nimepata nafuu ili nirudishwe tena katika chumba cha mateso makali kuhojiwa.


“Pole kwa yote yaliyotokea, nilipopata taarifa kuwa unaendelea vizuri nikashukuru sana, na nilipoambiwa kuwa umeamka nikaona vema nije mwenyewe kukuona na kuongea na wewe mambo fulani…” alisita kidogo na kugeuza shingo yake kuwatazama wale watu wengine waliokuwemo mle ndani ya kile chumba.


“Nahitaji nafasi kidogo ya kuongea na Maximilian, kama hamtojali,” alisema Madame Pamela akiwaambia wale watu huku akisogea na kuketi kwenye kiti kilichokuwa kando ya kile kitanda.


Niliwaona yule daktari, muuguzi na wale walinzi wake wawili wakitoka ndani ya kile chumba na kutuacha peke yetu, hapo nikajikuta nikianza kufarijika zaidi na tukio lile la kuondoka kwa wale walinzi wa bosi wa usalama wa taifa na kutuacha peke yetu.


Kisha Madame Pamela aligeuka kunitazama kwa makini akionekana kama aliyekuwa akiwaza mbali sana au akijishauri jambo kama aniambie au la.


Hata hivyo, sikuthubutu kufungua mdomo wangu kuongea chochote bali nilibaki kimya nikimtumbulia macho bila kusema chochote. Kikapita kitambo kifupi cha ukimya kisha kama aliyegutuka alitaka kusema neno lakini akasita na kuvitazama vile vyombo vya chakula vilivyokuwa juu ya meza.


“Samahani, unapaswa kula kwanza ili upate nguvu kisha tutaongea, maana niliambiwa una njaa sana,” alisema Madame Pamela huku akiinuka na kulifunua lile hotpot.


Nilipotupa jicho langu kuangalia ndani ya lile hotpot nikagundua kuwa kulikuwa na mchemsho wa ndizi na samaki aina ya sato. Pia aliyafunua yale mabakuli mawili yaliyokuwa na mifuniko, bakuli moja lilikuwa na mboga za majani na saladi na jingine lilikuwa na matunda mchanganyiko.


Kwa msaada wa Madame Pamela nilifanikiwa kunyanyuka kidogo na kukiegemeza kichwa changu kwenye mto niliokuwa nimeugemezea ukutani pembeni ya kitanda. Wakati huu nilisikia kichwa changu kikipwita kwa maumivu kana kwamba nilikuwa nimebebeshwa mzigo mzito sana.


Madame Pamela akachukua sahani na kijiko kikubwa na kuanza kunipakulia chakula kisha akaonja kidogo na kunipa huku akionekana kukifurahia sana kile chakula.


Nami sikujivunga, nikakipokea kile chakula na kwa kuwa nilikuwa nina njaa sana, nilikifakamia bila kujali maumivu ya mwili niliyokuwa nayo wakati huo.


Wakati nakula kile chakula Madame Pamela alikuwa akiniangalia kwa uyakinifu sana katika namna ambayo sikuweza kuielewa na sikujua alitaka kuongea nami kuhusu nini. Hata hivyo, sikutaka kuisumbua tena akili yangu kuwaza, yote niliamua kumwachia Mungu.


Nilimaliza kula kile chakula ambacho kiukweli kilikuwa kitamu sana, kisha Madame Pamela akavitoa vile vyombo na kuvisogeza kando.


Kikapita tena kitambo kirefu cha ukimya, hakuna aliyesema neno kati yetu. Na baada ya muda mrefu nikamuona akivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akikohoa kusafisha koo lake. Hapo nikajua sasa mahojiano yameanza.


“Maximilian… ni kwamba tangu tulipokukamata pale uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere hatukuridhika bali tuliendelea kuchunguza, hivyo ilibidi nitume watu wangu kufuatilia kwa umakini mkubwa taarifa zako kwenye ubalozi wetu huko Amsterdam na kwingineko, kwa mujibu wa taarifa za kiintelijensia zilizokuwa zimetufikia…” hatimaye alivunja ukimya Madame Pamela.


“Hadi wakati ule nakuja pale CMI kwenye chumba cha mateso bado taarifa tulizokuwa tukizipata kuhusu wewe zilikuwa zikitukanganya kidogo, kiasi kwamba ilinishangaza sana kuona uliwezaje kuwepo katika maeneo zaidi ya moja kwa wakati mmoja! Nikahisi huenda wewe si binadamu wa kawaida!


“Muda ule nilipokuwa nakuadhibu mle kwenye lile tangi la maji waliingia maofisa wetu wawili wa usalama waliokuja na taarifa fulani za kiitelijensia zilizonifanya kusitisha yale mateso, ingawa tayari ulikuwa umepoteza fahamu baada ya kupigwa na shoti ya umeme na hali yako ilikuwa mbaya sana,” alisema Madame Pamela kwa huzuni.


“Kwa kifupi tu, taarifa hizo zilihusu kugunduliwa kwa eneo ambalo zilikuwa zimefichwa silaha ambazo ndizo zilizokuwa zimeibwa kule kwenye bohari ya silaha na zilikuwa zitumike kufanyia ugaidi, hivyo nikawaamuru wale makomandoo wakuwahishe hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi ya Lugalo kwa ajili ya matibabu lakini wakihakikisha unawekewa ulinzi ili usiweze kutoroka hadi pale tutakapojiridhisha na zile taarifa kisha tukufungulie mashtaka ya ugaidi,” alipofika hapo aliweka kituo na kuangalia kando huku akivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu akionekana kuwaza mbali kidogo.


Kauli hiyo ikaufanya moyo wangu upige kite kwa nguvu huku kijasho chembamba kikianza kunitoka, hofu ikiwa imeanza kuniingia moyoni nikamtazama Madame Pamela kwa wasiwasi huku nikianza kuhisi hali ya hatari iliyokuwa ikinikabili.





“Kwa kifupi tu, taarifa hizo zilihusu kugunduliwa kwa eneo ambalo zilikuwa zimefichwa silaha ambazo ndizo zilizokuwa zimeibwa kule kwenye bohari ya silaha na zilikuwa zitumike kufanyia ugaidi, hivyo nikawaamuru wale makomandoo wakuwahishe hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi ya Lugalo kwa ajili ya matibabu lakini wakihakikisha unawekewa ulinzi ili usiweze kutoroka hadi pale tutakapojiridhisha na zile taarifa kisha tukufungulie mashtaka ya ugaidi,” alipofika hapo aliweka kituo na kuangalia kando huku akivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu akionekana kuwaza mbali kidogo.


Kauli hiyo ikaufanya moyo wangu upige kite kwa nguvu huku kijasho chembamba kikianza kunitoka, hofu ikiwa imeanza kuniingia moyoni nikamtazama Madame Pamela kwa wasiwasi huku nikianza kuhisi hali ya hatari iliyokuwa ikinikabili.


Endelea...


Nilimkodolea macho kwa wasiwasi kama vile nimeona guruneti lililokuwa limetelekezwa mle chumbani na magaidi wa kundi la al-Shabab na wakati wowote lilitaka kulipuka. Madame Pamela alinitazama kwa makini na kuachia tabasamu la kirafiki ili kunitoa hofu.


“Mchana wa siku ile kuna vijana wadogo walikuwa wanachunga mifugo yao katika msitu wa Kazimzumbwi mkoani Pwani, eneo ambalo ni karibu na kijijini kwao! Wakati wakiwa ndani ya huo msitu wa Kazimzumbwi wakaokota bomba la PVC lililokuwa limefichwa, na baada ya kulifungua ndani walikuta lilikuwa na bastola na vitu vingine kadhaa vilivyowatia shaka.


“Wale vijana wakawataarifu wazazi wao ambao nao wakautaarifu uongozi wa serikali ya kijiji, ndipo ikashauriwa vitu vile vipelekwe polisi! Baada ya vitu hivyo kupelekwa polisi, vikachunguzwa na kukakutwa ramani ambayo polisi waliitilia shaka.


“Haraka sana polisi waliifuatilia ile ramani ndipo ikawapeleka moja kwa moja kwenye handaki dogo ndani ya ule msitu wa Kazimzumbwi. Kutokana na vitu vilivyokutwa ndani ya lile handaki polisi wakapata wasiwasi kuwa inawezekana walikuwa wanashughulika na jambo kubwa na nyeti zaidi kuliko uwezo wao, kwani kiliwachostaajabisha ni kuwa handaki lile lilichimbwa kiustadi na kujengewa kwa ndani kwa vitofali vidogo vidogo na lilikuwa lina mpangilio wa hali ya juu wa kiwango cha kijeshi. Na hapo ndipo idara yetu ilipotaarifiwa kuhusu jambo hili,” alinyamaza Madame Pamela na kuinuka kisha akaanza kupiga hatua akizunguka zunguka mle ndani.


Nilibaki kimya nikimtazama Madame Pamela kwa wasiwasi, sikujua kwanini alikuwa akinieleza yale yote, na sikujua kama bado walikuwa wakidhani kuwa nilikuwa nahusika na uhalifu ule, hivyo alikuja ili nimpe taarifa nyingine zaidi! Muda huo huo nikahisi tena ubaridi wa woga wa aina yake ukinitambaa taratibu mwilini.


Niliendelea kumtazama Madame Pamela wakati akizunguka zunguka kwa muda mle chumbani kisha akageuka kunitazama huku akilamba midomo yake iliyoanza kukauka.


“Tulipopewa taarifa zile haraka sana niliwatuma watu wangu huko na walipowasili iliwachukua saa kadhaa tu kung’amua kuwa vitu walivyovikuta ndani ya lile handaki dogo vilikuwa vinahusiana moja kwa moja na mtu anayeitwa Brown Senga au Godwin Sengerema, vitu ambavyo imetuchukua muda mrefu tukihangaika kutafuta taarifa zake. Kisha watu wangu wakachunguza alama za vidole walizozikuta kwenye lile handaki na zilionekana kutofautiana sana na alama zako za vidole jambo lililozidi kutuchanganya, lakini alama zile zilifanana sana na alama za vidole kwenye nyaraka za Brown Senga.


“Ndipo tulipoanza kuhisi kuwa ninyi ni watu wawili tofauti ingawa mnafanana sana kwa karibu kila kitu. Mle ndani ya lile handaki pia tulikuta kijarida kidogo kinachohusu kituo cha siri cha mafunzo ya karate na ujasusi nchini, pia taarifa za uwepo wa mahandaki mengine mawili ya aina ile, moja likiwa katika pori la Hifadhi ya Moyowosi mkoani Kigoma na jingine likiwa wilayani Kongwa katika mkoa wa Dodoma, yote yalifanana kwa jinsi yalivyochimbwa kiustadi na kujengewa kwa ndani kwa vitofali vidogo vidogo kama lile lililokutwa katika msitu wa Kazimzumbwi mkoani Pwani…” alinyamaza na kumeza mate.


Nilibaki hoi kwa taarifa zile za kiintelijensia ambazo zilisababisha nywele zangu zisisimke kichwani.


Madame Pamela alinitazama kwa makini na kuachia tabasamu pana la kunifariji kisha akasogea pale kwenye kiti na kuketi tena.


“Nimekueleza yote haya ili ufahamu ni kwa namna gani hatulali kuhakikisha nchi hii inakuwa salama lakini wakati mwingine tunakuwa katika mazingira tata yenye mkanganyiko wa taarifa, hasa kwa mambo makubwa kama haya yanayohusu usalama wa nchi na wananchi wake,” alisema Madame Pamela na kuweka tena kituo.


“Kwa kutumia taarifa zilizokuwa ndani ya kile kijarida kidogo kinachohusu kituo cha siri cha mafunzo ya karate na ujasusi nchini tukaanza kumfuatilia Brown Senga mpaka tukafanikiwa kumpata na kumkamata akiwa kajichimbia mafichoni Dodoma kwenye maktaba yake ya siri iliyosheheni nyaraka mbalimbali za kijasusi, na ndani ya maktaba hiyo kulikuwa na kila kitu ambacho angekihitaji, silaha, nyaraka za kijasusi, kifurushi cha kujikimu, dawa za dharura za huduma ya kwanza, fedha nyingi za kigeni na za Tanzania nadhani ni zile zilizoporwa katika Benki ya Wananchi…


“Pia kulikuwa na majarida ya mazoezi ya kawaida na ya kijeshi na vitu vingine vingi ikiwemo mtambo maalumu wa udukuzi wa mawasiliano wa Satellite GPS and Traces wenye mvuto wa hatari uliotengezwa kwa madini ya Uranium ambao ulikuwa umefungwa kwenye kompyuta maalumu ukifanya kazi ya kufuatilia taarifa na mawasiliano yote ya simu, kompyuta na vifaa vyote vya kielektroniki viwezavyo kutumia Intaneti…


“Tulimkamata wakati akiandaa mkakati wa mwisho wa namna ya kutekeleza tukio kubwa la mauaji ambayo angeyafanya kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wiki ijayo katika siku ya Mei Mosi, kwani walitega mabomu mawili yenye nguvu kubwa karibu na jukwaa kuu na alikuwa na saa ambayo akiibonyeza tu yanaanza kujihesabu na ikifika kumi yangelipuka na kuifanya nchi hii iingie kwenye taharuki isiyoelezeka… kama hufahamu siku ya Mei Mosi ni siku kubwa sana ya wafanyakazi ambayo inakusanya wafanyakazi na viongozi mbalimbali wa serikali kwa ajili ya kusherehekea, na mwaka huu imepangwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye atakayekuwa mgeni rasmi siku hiyo.


“Mpango huo wa mauaji ulikuwa umepewa jina la ‘Operation Underground Elimination’ na ndani ya huo mpango kulikuwa na orodha ya washirika wote katika mtandao wa kigaidi aliouongoza, baadhi yao ni wanasiasa, maofisa wa jeshi, vigogo waliowahi kutumbuliwa serikalini kwa tuhuma mbalimbali, wafanyabiashara wakubwa na watu kutoka nje ya nchi waliopewa jina la ‘wafadhili’. Wengi wao hasa waliopo hapa nchini tayari tumekwisha wakamata na wengine bado tunawasaka kwa udi na uvumba popote walipo duniani, tutawakamata na kuwafikisha katika mahakama ya ugaidi.”


Kauli ile ya Madame Pamela ikawa imeamsha nguvu mpya kwenye mwili wangu na hapo hapo nikajihisi kupona.


“Kwa kuwa wewe umeingia kwenye matatizo haya makubwa yaliyokaribia kuyagharimu maisha yako kutokana na kufanana sana na Brown Senga, Rais amenituma nije kukuomba radhi na kukueleza kuwa serikali inaomba radhi na itakupa dola laki moja za Marekani kama fidia,” alisema Madame Pamela na kusimama.


Nilijikuta nikiyasahau machungu yote kutokana na furaha kubwa niliyokuwa nayo, kisha kitambo kifupi cha ukimya kikapita tena mle ndani huku wote tukizama kwenye tafakuri. Madame Pamela alinitazama jinsi nilivyokuwa nikionesha furaha isiyoelezeka.


Nilifungua mdomo nikataka kusema lakini sauti ikagoma, nilikosa kabisa neno la kusema na hivyo nikajikuta nikiwa nimeganda kama sanamu nikimkodolea macho yule bosi wa usalama wa taifa utadhani nilikuwa nimegeuka sanamu!


Mara kikohozi kidogo kikanitoka, na nyuma yake wimbi la machozi ya furaha lilikuja mbio, machozi ya furaha yakamwagika na kuanza kulowesha mto niliokuwa nimeegemeza kichwa changu utadhani milizamu iliyopasuka.


Nilijaribu kuyazuia machozi lakini nikashindwa, sikuwa na namna nyingine yoyote ya kuyazuia yasitoke, hivyo niliyaacha yamwagike huku nikiendelea kumtumbulia macho yule bosi wa usalama wa taifa bila kusema chochote.


Muda wote Madame Pamela alikuwa akinitazama kwa tabasamu kisha akatoa simu ya mkononi kutoka kwenye mkoba wake na kunipa. Nilipoitazama vizuri ile simu nikagundua kuwa ilikuwa ni simu yangu iliyochukuliwa pale uwanja wa ndege na watu wa usalama nilipokuwa nahojiwa.


“Kwa sasa unaweza kuwasiliana na yeyote utakaye, tumekwisha wasiliana na familia yako na kuwaeleza kuwa ulipofika Dar es Salaam ulipata matatizo ya kuvamiwa yaliyosababisha ulazwe hospitali, hatukutaka kuwaeleza jinsi tukio lilivyotokea kwani haya mengine yatabaki kuwa siri kati ya serikali na wewe,” alisema.


Nikashusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikiachia tabasamu.


“Halafu huwezi kuamini, kumbe wewe ni kaka binamu, babu yako mzaa mama na babu yangu mzaa baba walizaliwa kwa baba mmoja na mama mmoja! Mungu akuponye haraka, mdogo wangu, na nimeambiwa kuwa huenda ukaruhusiwa kutoka hospitali baada ya siku tatu au nne kama hali haitabadilika. Nitarudi tena baada ya siku mbili kukuona,” alisema Madame Pamela na kunipapasa kwenye paji langu la uso katika namna ya upendo.


Kisha alipiga hatua zake taratibu kuufuata mlango na alipoufikia alishika kitasa cha ule mlango na kukinyonga taratibu, mlango ukafunguka, akachungulia nje na kugeuka kunitazama kwa tabasamu.


“Nilisahau kukwambia, Susan na Pamela wapo hapa kukuona,” alisema na kutoka nje akiuacha mlango wazi, na muda huohuo nikamuona mchumba wangu Susan na binti yetu Pamela wakiingia. Nilipata mshangao mkubwa uliochanganyika na furaha isiyoelezeka.


“Asante Mungu,” nilijikuta nikisema kwa furaha huku nikiwatazama kwa makini na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani. Machozi ya furaha yakaanza tena kunitoka na kuulowesha mto niliolalia.


MWISHO.



0 comments:

Post a Comment

Blog