Search This Blog

Thursday, 23 March 2023

HUJUMA NZITO - 2

  

Simulizi : Hujuma Nzito

Sehemu Ya : Pili (2)


"Tupa silaha yako chini mara moja na nyoosha mikono juu..!" sauti kali mithili ya radi ya ilimgutusha yule mwanajeshi huku taa ya veranda ya juu ikiwa tayari imeshawashwa na Kachero Manu, sasa wanaonana ana kwa ana.

Yule mwanajeshi hakuwa zoba mwenye kukubali kusalimu amri kilaini tu, akazuga kama anataka kutupa bastola yake chini lakini akageuka ghafla na kuanza kuvurumisha risasi kama mvua kuelekea upande alipo Kachero Manu.

Kachero Manu alikuwa yupo makini vinginevyo maafa yangemkuta. Akakwepa risasi zile kwa kujibiringisha chini huku na kule na yeye akijibu mapigo. Shambulio ambalo lilimsaidia sana kwa upande wake kwani moja ya risasi ilitua sawia kwenye kiganja cha mkono cha yule mwanajeshi kilichoshika ile bastola yake. Bastola ikamponyoka huku akigugumia maumivu makali kwa mayowe ya sauti ya juu.

Hakutaka kumpa adui yake fursa ya kujipanga hata kidogo, akamshindilia risasi nyingine ya tumboni. Risasi ambayo ilimsababisha yule mwanajeshi ainame chini akiwa ameshikilia tumbo lake. Akamfuata adui yake kwa kujifutua akijua tayari ameshamaliza kazi. Alipomkaribia tu ndipo akatanabahi kosa alilofanya, chamoto alikiona.

Hasimu yake alinyanyuka ghafla na kurusha teke lililotua sawia kwenye kifua cha Kachero Manu na kumsababisha aende chini kulamba sakafu kwa mara ya kwanza. Hakumpa nafasi anyanyuke, akamuwahi na kumkwida fulana yake ya juu maeneo ya shingoni huku amemkandamiza goti lake shingoni.

Kachero Manu akakusanya mate yake na kumtemea usoni yule hasimu wake. Yale mate yalitua sawia kwenye jicho a kushoto la yule mwanajeshi, hapo hapo hakumchelewesha, akajitutumua na kumsukumia pembeni.
Kachero Manu akapata nafasi ya kusimama na yule mwanajeshi akajizoazoa nae akasimama, wakawa wanatazamana wote wanatweta kama mafahari mawili.

Kachero Manu kwa namna alivyomuona yule mwanajeshi namna alivyojitega katika ukunjaji wa ngumi zake na namna aivyoiweka miguu yake akajua kabisa staili ya mapigano anayoitaka kucheza nae.
Hivyo hakutaka kumlealea tena alitaka majilipo mapema kabisa. Alijua fika ukicheka na nyani shambani utayavuna mabua. Na mtu yoyote anayetumwa kwake kuja kumuangamiza kwa vyovyote atakuwa ni mtaalamu bobezi wa sanaa za mapigano.

Kachero Manu alimtishia kama anataka kumpiga ngumi ya usoni yule jamaa akakwepesha uso wake. Akashtukia tayari kashapigwa mtama, akala mweleka sakafuni kwa mara nyingine tena.
Alipokuwa anajikongoja kutaka kusimama kwa mara nyingine tahamaki akashtukia teke zito na lenye kasi likitua kichwani mwake na kumsababisha aanze kuyumba yamini wa yasari kama mlevi aliyezidisha kileo. Kisha akaanguka chini chali damu zinamvuja mdomoni na puani dalili ya kuonyesha hawezi tena kujitetea, kwisha habari yake.

"Sema nani amekutumaaa.....nani amekutuma kuja kuniuaaaaah..?" Kachero Manu alikuwa anamfanyia mahojiano kwa sauti ya kufoka huku anamtikisa kichwa chake ili ashtuke. Masikini ya Mungu yule mwanajeshi alikuwa yupo katika sakarati mauti anaiaga dunia kuelekea jongomeo, kupona kwake ni takdiri. Kila akijaribu kuongea mapovu ya damu yaliyochanganyika na mate yalikuwa yanamvuja huku anautafuna ulimi wake.

Baada ya sekunde kadhaa akazimika kabisa, akiwa tayari ameshakata roho yake. Bila kuchelewa akaanza kumfanyia speksheni kwenye nguo zake huenda akaambulia chochote kitu. Akamkuta na kitambulisho cha kazi kuthibitisha kuwa ni mwanajeshi halisi wa Tanzania akiwa na cheo cha Kapteni. Alipozidi kupekenyua kwenye kibegi chake huko ndio akakutana na vimbwanga vilivyoanza kumpa mwangaza wa upelelezi wake.

Alimkuta ana vitambulisho viwili, vyenye muelekeo wa kisiasa. Kimoja ni cha chama cha upinzani cha "National Movement Party" (NMP) na kingine cha "Nyasa Empire Supporter (NES)", kuonyesha kuwa anaunga mkono kusimamishwa kwa Dola ya Nyasa. Kilichokuwa kinastaajabisha kadi zote mbili zilikuwa na sahihi moja ya Mwenyekiti wa chama cha NMP, Dr. Patrick Ndomba.

Pia hiyo kadi ya NES ilikuwa na nembo ya picha ya mmoja wa waasisi wa wapigania uhuru wa nchi hii, Mheshimiwa Oscar Kambona akiwa ameshikilia mwenge wa uhuru huku akiwa yupo juu ya ziwa Nyasa.
"Sasa naanza kunusa harufu ya mchezo mchafu kwenye sakata hili kuna kitu kinataka kutengenezwa hapa" aliwaza Kachero Manu.

Akaanza kuumba ushahidi wa kimazingira kichwani mwake juu kifo cha Dr.Pius Chilembwa ambaye ni Mnyasa na Dr.Patrick Ndomba nae ni Mnyasa.
Akawa anajiuliza pia "kwanini picha ya Mheshimiwa hayati Kambona pekee ambaye nae pia ni Mnyasa itumike na sio wapigania uhuru wengine waliovuja jasho na damu kwa ajili ya nchi hii kwanini hawa wamchague Mheshimiwa Oscar Kambona pekee. Na kwanini wajiite "Nyasa Empire Supporter" (NES) ina maana wanataka kuigeuza Tanzania kuwa Dola mpya inayoitwa Nyasa?".

Hayo ni maswali yaliyokuwa yanampasua kichwa Kachero Manu huku sasa yakimpa mwangaza halisi katika upelelezi wake. "Nitaelekea msibani Ziwani nimeshapata mashaka kama kweli huyu mtu kweli kafariki au changa la macho anataka kukwepa mkono wa sheria huyu mshenzi. Kama akiwa hajafariki ama zake ama zangu popote alipo nitamfurumusha mpaka nimfikishe kwenye vyombo vya dola" alikula kiapo huku akijiandaa kupiga simu kitengo maalumu waje kuichukua maiti ya yule mwanajeshi.




Kachero Manu ndani ya kaburi la Hayati Dr.Pius Chilembwa

"Sasa ni wakati kusomwa kwa historia ya marehemu, itahudhurishwa historia hiyo na pacha wa marehemu anaitwa Bwana Alex Chilembwa, karibu sana" alizungumza mshehereshaji wa mazishi hayo ya hayati Dr Pius Chilembwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa fedha za ndani na nje wa Benki Kuu, aliyeaga dunia nchini Afrika ya Kusini kwa ajali ya gari juma moja lililopita.

Umati forifori wa waombolezaji toka pande mbalimbali za dunia walihudhuriwa kuja kufanya taazia ya msiba huo. Waombolezaji hao walikuwa ni katika ndugu, jamaa, marafiki na watu waliowahi kufanya kazi na hayati Dr. Pius Chilembwa. Kadamnasi hiyo ya watu ilizizima kwa vilio vya kwikwi na majonzi makubwa wakisubiria kusomwa historia hiyo.

Waombolezaji hao walivalia fulana nyeupe zilizochapwa juu yake maeneo ya kifuani picha ya Dr.Pius Chilembwa huku ikisindikizwa picha hiyo na maneno madogo chini yake "Pumzika kwa Amani Dr. Pius Chilembwa Tutakukumbuka daima milele". Misa ya kuombea msiba huo ilikuwa tayari imeshakamilika, yamebaki mambo machache ya kumalizia mazishi hayo.

Akanyanyuka kitini kiunyonge mdogo wake marehemu anayejulikana kama Bwana Alex Chilembwa huku mkononi akiwa amekamatia karatasi nyeupe iliyochapishwa historia nzima ya marehemu huku anaelekea sehemu maalumu ya jukwaa dogo lililotengwa kuzungumzia.
Alikuwa ameulamba suti nadhifu za rangi nyeusi, ndani ya suti hiyo alivalia shati jeupe na tai ya rangi nyekundu.

Miguuni alivalia viatu vya ngozi rangi ya kahawia. Baada ya kupiga hatua kadhaa, tayari akawasili kwenye jukwaa. Akaisogelea maiki ya kuzungumzia, kisha akajikohoza kidogo kwa ajili ya kulisafisha koo lake akijiandaa kuzungumza.
Akavua miwani yake ya macho kisha akachomoa hanchifu yake kutoka kwenye mfuko wa suruali ya suti yake, akajifuta machozi, na kupenga mafua mepesi kwenye pua zake, kisha akarejesha machoni miwani yake na hanchifu mfukoni mwake.

Umati wote ulitulizana tuli kama maji mtungini wakiwa tayari wameshamuazima masikio yao. Akainamia karatasi yake na kuanza kuzungumza kwa sauti ya mikwaruzo iliyochanganyika na kilio chepesi.

"Bwana Yesu Asifiwe sana...Wapendwa waombolezaji wenzangu, Mabibi na Mabwana mliohudhuria, ifuatayo ni historia fupi ya marehemu Dr.Pius Chilembwa ambaye ni kaka yangu wa damu tulizaliwa siku moja tarehe 2/02/1961 kwa kupishana masaa kadhaa katika zahanati ya hapa hapa kijijini Kwambe karibu na Mbamba Bay katika wilaya ya Nyasa.
Kwa bahati mbaya sana baba yetu mzazi alifariki tukiwa na umri wa miaka miwili hivyo akajitokeza msamaria mwema, mjomba wetu kiukoo hayati Kapteni Meshack Wandawanda aliyekuwa anafanya kazi jeshini enzi hizo jeshi likiitwa Kings African Rifles (K. A. R) baadae JWTZ katika kambi ya Lugalo.

Hivyo tukahamia Jijini Dar es Salaam kwenda kuishi nae kama sehemu ya familia yake. Akatulea kwa huruma na upendo bila kutubagua wala kutunyanyapaa. Marehemu Dr.Pius alianza darasa la kwanza mwaka 1971 na kuhitimu darasa la saba mwaka 1977. Baada ya kuhitimu elimu ya msingi alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya wavulana ya 'Songea Boys' ambapo alisoma hapo kwa muda wa miaka 6 mfululizo na kufanikiwa kuhitimu elimu ya sekondari tahasusi ya masomo ya biashara mwaka 1983 kwa daraja la kwanza.

Hayati Kapteni Wandawanda, mfadhili wetu alifurahishwa sana ufaulu wa kiwango cha juu wa marehemu Dr.Pius. Akampatia marehemu udhamini wa masomo nchini Uingereza kwa ajili ya elimu ya juu ya Chuo Kikuu. Akasoma katika Chuo Kikuu cha Stanford na kuhitimu shahada ya kwanza na ya udhamili kwa mfululizo mwaka 1988.
Akarejea nchini na kuajiriwa moja kwa moja katika Benki kuu ya Tanzania kama mchumi daraja la kwanza. Mwaka 1996 akaanza masomo yake ya shahada ya uzamivu katika Uchumi, kwenye Chuo Kikuu cha Stanford tena na kuhitimu mwaka 2000.

Pia marehemu amehudhuria semina na kozi lukuki ndani na nje ya nchi.
Tokea hapo Dr.Pius akawa ni mwenye kupanda vyeo mfululizo mpaka mwaka 2010 alipoteuliwa kwenye cheo chake alichofia nacho cha Ukurugenzi wa fedha. Marehemu ameacha mke na mtoto mmoja ambao wote wanaishi nchini Uingereza kwa miaka kadhaa sasa.

Mpaka mauti yanamfika alikuwa tayari ametimiza umri wa miaka 58 na miezi kadhaa.
Marehemu ameacha pengo lisilozibika katika familia yake na kazini kwake kwa ujumla. Daima tutakukumbuka Dr. Pius Chilembwa. Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe-Amiiiin" akawa amemaliza tayari kusoma hotuba yake huku akiwa sasa hajiwezi tepwetepwe kwa kilio cha kwikwi mpaka akawa anasaidiwa na watu kurejea kwenda kuketi kwenye kiti chake.

"Huyo marehemu Dr.Pius na huyu Alex aliyesoma hotuba wamerandana kama korosho, kuna watu wana damu kali aisee..kama mtu mgeni huwezi kuwatofautisha kamwe lazima uwachanganye tu. Kuanzia kutembea, kuongea na kila kitu tofauti yao kubwa ipo kwenye tabia huyu Alex ana hasira sana, wakati Dr.Pius alikuwa ni mpole kupitiliza, amepooza kama mkojo wa ngedere, enzi za uhai wake hata kuua mbu alikuwa hataki anamuonea huruma. Ama kweli wema hawadumu duniani" alikuwa ananong'ona mmoja wa waombolezaji waliokusanyika maziarani akimnong'oneza mwenzake ambaye ilionekana haijui vizuri familia hiyo.

Kachero Manu nae alikuwa yupo jirani yao anawasikiliza kinagaubaga kila wanachoongea watu hao. "Alaaah...kumbe ni mapacha wa yai moja eeh..hii picha ni tamu sana, hapa kuna jambo tu hata uso wa Bwana Alex mdogo wa marehemu uso wake umeshindwa kabisa kuvaa uhusika wa msiba ingawa amejitahidi kuigiza. Sisi tuliosoma masomo ya saikolojia tumejifunza namna ya kusoma lugha ya muonekano wa nje wa mtu.

Hapa tunachezewa mchezo ingawa hatuujui huo mchezo tunaochezeshwa na hawa wajuba" alikuwa amezama Kachero Manu kwenye lindi zito la mawazo. Kinachoendelea pale msibani akaona ni usanii mtupu.
Baada ya kusomwa salamu za rambirambi toka kwa makundi mbalimbali aliyowahi kusuhubiana nayo marehemu kuanzia shuleni, mtaani mpaka kazini kwake sasa ikafikia hatua ya mwisho ya kushusha mwili wa marehemu kaburini.
Mpaka kufikia majira ya alasiri mwili unaosadikiwa kuwa ni wa Dr. Pius Chilembwa ukawa umeshapumzishwa katika nyumba yake ya milele kwenye mavani maalumu ya ukoo wa Chilembwa.

Mazishi yake yalikuwa ni ya kihistoria kijijini hapo kutokana na umati wa watu uliofurika kijijini hapo kumsindikiza safari yake ya mwisho.
Wapo waliofananisha umati huo uliohudhuria mazishi hayo na umati uliohudhuria mazishi ya hayati Oscar Kambona mwaka 1997 kijijini hapo. Hekaheka sasa zikahamia kwa wenye motokaa za waombolezaji kukimbizana kuwahi kwenda kulala Songea Mjini jioni ile ili kesho yake wadamkie msafara wa kurejea jijini makwao.

Kachero Manu alikuwa amevalia pama lake alilolishindilia sawia kichwani mwake huku akiwa machoni amevalia miwani nyeusi, na kategesha mzuzu feki kidevuni mwake ili asiweze kugundulika kirahisi na watu wanaomuwinda.
Yeye hakuwa na mpango wa kuondoka siku hiyo. Alishakata shauri usiku wake kulivamia kaburi la marehemu Kininja apate sampuli za kupeleka maabara kufanya vipimo vya DNA ili kujithibitisha kama ni kweli uliozikwa mavani ni mwili wa Dr Pius Chilembwa au ni kanyaboya.

Uzuri wa mambo Benki Kuu walikuwa na utaratibu wake binafsi wa vigogo wake wote wakubwa kutunza hali zao za kiafya zilikuwa zimehifadhiwa kwenye data kanzi kuu ya serikali. Kuanzia magonjwa yao yote wanayoumwa pamoja na DNA zao zilikuwepo zilikuwa zimehifadhiwa, kwa ajili ya kudhibiti usalama. Hivyo kupatikana kwa sampuli ya Dr.Pius ilikuwa ni suluhisho la mzizi wa fitina.

Kachero Manu alikuwa anawachora tu bila wao kujua watu anaowadhania walikuwa pale msibani kwa lengo la kumsaka yeye. Hakutaka kupambana nao kwa sababu sio lengo lililomleta kijijini pale.
Kitendo cha marehemu kuzikwa nje kidogo ya nyumba za familia yao, hali iliyompa urahisi Kachero Manu kufanya vitu vyake alivyopanga. Kuna mlinzi mmoja shaibu kiumri, alipewa kibarua cha muda cha ulinzi kaburini kwa kuhofia vibaka wanaoweza kuja kufukua mwanandani na kuiba vito vya thamani na nguo alizovikwa maiti.

Maadui wa Kachero Manu hawakudhania kabisa kama hasimu wao anaweza kuwa na mawazo ya kuvamia kaburi hilo usiku wa manane kwa ajili ya kufanya taftishi. Vinginevyo lazima wangeimarisha ulinzi madhubuti kwenye kaburi la anayesadikiwa kuwa ni Dr.Pius Chilembwa.
Jua lilipozama tu, Kachero Manu baada ya kujilia bada yake kwa dagaa iliyoandaliwa maalumu kwa waombolezaji pale msibani, akazugazuga pale kwenye matanga mpaka saa saba kasorobo za usiku.

Akaanza kujiandaa kuelekea makaburini.
Watu pale msibani walikuwa tayari wengi wao wameshalala. Wanakoroma kwa kuzidiwa na usingizi unaotokana na uchovu wa shughuli nzima za kufanikisha mazishi. Akiwa na zana zote muhimu kwa kazi yake alizozichukua kutoka garini mwake, akachepuka pale matangani na kutokomea zake maziarani alipozikwa Dr.Pius Chilembwa. Ilimchukua kama nusu saa tu ya kutembea kufika eneo stahiki.

Uzuri pale makaburini kulikuwa na miti iliyopandwa vizuri hivyo haikumuwia vigumu Kachero Manu kujificha kwenye vivuli vya miti iliyotapakaa hapo. Akawa anasogelea kwa mwendo wa kunyatia mpaka akawa yupo kama meta saba au sita kutoka alipo yule mlinzi upanga. Aliyekuwa amevalia koti kubwa la baridi linaloburuta mpaka chini, huku chini ametinga buti kubwa ambazo kwa muonekano zilikuwa hazimtoshelezi.

Kichwani alivalia kofia ya mzula aliyoishindilia mpaka kwenye paji lake la uso. Mkononi mlinzi yule aliukamatia upanga wake ambao ulikuwa umeshamtoka mkononi kutokana na usingizi wa pono huku anajijambia mashuzi tu ya ugali wa muhogo kwa dagaa aliokula msibani.

Kachero Manu akaanza kumkaribia bila kutengeneza mchakato mkubwa wa sauti za nyayo zake. Mpaka akamfikia na kusimama mbele yake. Wakati yupo kwenye harakati za kuchovya dawa za kulevya kwenye pamba ili amnusishe puani apoteze fahamu, yule mlinzi akaanza kuchezesha miguu kama mtu anayetaka kuamka usingizini. Ikabidi asitishe kwa muda mchakato wake wa kutaka kumkaba pua kwa muda huku akijiandaa kupambana nae.



Kachero Manu akaanza kumkaribia bila kutengeneza mchakato mkubwa wa sauti za nyayo zake. Mpaka akamfikia na kusimama mbele yake. Wakati yupo kwenye harakati za kuchovya dawa za kulevya kwenye pamba ili amnusishe puani apoteze fahamu, yule mlinzi akaanza kuchezesha miguu kama mtu anayetaka kuamka usingizini. Ikabidi asitishe kwa muda mchakato wake wa kutaka kumkaba pua kwa muda huku akijiandaa kupambana nae.

Mara kikasikika kishindo kizito cha mashuzi kilichoambatana na harufu kali ya kuchukiza katika pua, toka kwa yule mlinzi akiwa usingizini. Ilibaki kidogo tu aangushe kicheko, hali ambayo ingeharibu kazi yake yote kwa kumzindusha usingizini mlinzi yule. Lakini akafanikiwa kujizuia na kuweza kuchekea tumboni mwake.


"Inaonyesha ameshiba ndi ndi ndi ugali wa muhogo kwa dagaa Nyasa za pale msibani" aliwaza huku huku akimnusisha dawa hizo za kulevya kwa kutumia pamba puani mwake. Baada ya sekunde kadhaa tu, mlinzi yule akaanguka chini kabisa kutoka kwenye kiti kile cha plastiki kama mzigo.

Himahima mara tu baada ya kumuona mlinzi yule ameshazimia, na kujiridhisha na usalama wake, akaanza sasa harakati za kupekechua kaburi kupitia pembezoni mwa kaburi kwa kunyofoa matofali ya pembeni.

Haikuwa kazi ngumu sana kwa sababu matofali yalikuwa bado hayajakomaa. Akaanza kuchapa mzigo wa nguvu kuhakikisha anamaliza haraka jukumu lake. Baada ya nusu saa tu akafanikiwa kutumbukia ndani ya kaburi.

Alipotua ndani ya kaburi, akakutana na giza zito la ndani ya kaburi lile lililosakafiwa marumaru ya gharama ndani yake. Kwa giza lile zito la kaburini na fukuto lake kama angekuwa mtu mwenye roho nyepesi angetoka mbiombio kwa jinsi kunavyoogofya.

Lakini kwa kuwa yeye ni galacha wa mapambano, akapiga moyo konde na kuamua liwalo na liwe lazima amalize taftishi yake iliyomleta ndani ya kaburi. Akawasha kurunzi yake yenye mwangaza mkali kwa ajili ya kumuwezesha kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Kwa kutumia bisibisi zake maalumu na vifaa vingine vya kazi akafanikiwa kulifumua jeneza. Alipopochungulia kuangalia mwili uliolazwa ndani ya jeneza lile akashikwa na taharuki isiyomithilika. Jasho jekejeke likaanza kumtiritika mwilini, huku hasira nzito ikitamalaki moyoni mwake. Mara moja hisia zake zikamtuma kuwa huyu sio marehemu Dr. Pius Chilembwa kabisa, ni kanyaboya tu.

Maiti iliungua vibaya kuanzia usoni mpaka kifuani ili kuwaaminisha watu kuwa amefia kwenye ajali ya moto. Kimtazamo ilikuwa ni maiti ya pande la mtu lenye miraba minne. Kwa kutumia kamera yake maalumu yenye uwezo wa kuchukua picha gizani kwa ufanisi akaipiga picha za kutosha ile maiti na kuchukua sehemu ya mwili kama sampuli ya kwenda kupima DNA ya ile maiti.

"Kama marehemu Dr.Pius wanasema amefanana na pacha wake Bwana Alex yule niliyemuona msibani, basi huyu sio Pius kabisa nakataa. Maana Alex mwili mwake ni kimbaumbau mwiko wa pilau, sasa imekuwaje pacha wake kuzikwa tu awe mwili nyumba" alikuwa anawaza Kachero Manu huku akiwa sasa yupo kwenye harakati za kuchomoka nje ya kaburi, akiwa ameshabeba kila kitu chake. Alipofanikiwa kufika juu ya kaburi akachomokea nje ya kaburi.

Yule mlinzi bado alikuwa amepoteza fahamu, hajitambui. Akajaribu kurudishia baadhi ya matofali kadri anavyoweza kisha akatokomea zake kwa haraka.
Usiku ule ule akaanza msafara wa kuondoka kijijini pale Kwambe kurejea Jijini Dar es Salaam kwa kupitia njia ya Tunduru, Masasi, Lindi mpaka Dar es Salaam. Njia nzima Kachero Manu alikuwa na furaha sheshe akianza sasa kuwa na matumaini ya kuwatia mbaroni wahusika wote ni suala la muda tu.


"Jaribu kufikiria maiti ile inavuta pumzi
ndefu, kisha inaanza kujikohoza kwa dhumuni la kuweka sawa koo halafu kwa sauti yake anatamka, "Mimi sio Dr.Pius Chilembwa. Niliuliwa na hawa wahaini waroho wa roho za watu kwa tamaa zao za madaraka".

Yaani nilitamani ile maiti inipe hiyo taarifa Kachero Yasmine nilipokuwa tayari nimeshashuka ndani ya kaburi na kuiangalia ile maiti. Nimeamini asilimia kwa zaidi ya asilimia 100% yule sio Dr.Pius Chilembwa kabisa" alikuwa Kachero Manu anamsimulia Kachero Yasmine tukio zima la kaburi linalosadikiwa kuzikwa Dr.Pius Chilembwa.

Pacha wake huyo wa kazi Kachero Yasmine, kila alichokuwa anasimuliwa alijaribu kuweka nukuu zake. Tayari alishatia timu kitambo Jijini Dar es Salaam na akiwa tayari ameshaanza kazi mpya katika kituo chake cha kazi Benki kuu katika harakati za kuwabaini waliokwapua pesa za nchi.

"Sasa una mpango gani maana tayari njia nyeupe hii ya kuwakamata bila kuacha chembe ya shaka katika ushahidi, hasa tukifanikiwa kutegua mtego namna ya mbinu walizotumia kuzikwapua pesa hizo" aliuliza Kachero Yasmine kwa mshawasha huku akijimiminia chai ya nyongeza kwenye kikombe chake. Alikuwa anasukumizia mchapalo wake wa makalimati na chapati walizokuwa wanakula usiku huo ili wakalale. Muda ulishasonga sana hawakuwa na muda wa kuandaa chakula chao cha usiku.

Walikuwa wapo kwenye nyumba waliyopangishiwa na idara ya usalama maeneo tulivu ya Mbweni, Jijini Dar es Salaam. Kuonana kwao ilikuwa ni kuanzia saa 4:00 usiku na kuendelea pindi wanaporudi toka kwenye mishe mishe zao za siku. Muda huo ndio walikuwa wanautumia kupeana dondoo mbili tatu za shughuli zao za kipelelezi zinavyokwenda.
Wanapokutana wanabadilishana mawazo namna ya kuboresha utendaji kazi wao. Wakiwa hawajachoka walikuwa wanapika wenyewe kwa ushirikiano, kama huyu akipepeta mchele kwa ajili ya kuupika wali wa nazi huyu anatayarisha mchuzi na mbogamboga ili mradi walikuwa wanashirikiana kila kitu kama umoja wa siafu.

"Mipango yangu ni kwenda nchini Afrika ya Kusini kupeleka sampuli kwenda kupima DNA za huu mwili unaodaiwa wa Dr.Pius Chilembwa lakini kesho usiku naenda kuonana na mmoja wa wanajeshi wakongwe waliowahi kufanya kazi jeshini enzi hizo "Kings African Rifles (K. A. R) nimeshatuma mualiko kwake nimekubaliwa mara moja nimeambiwa niende kesho usiku nikaonane nae" alifafanua Kachero Manu kumfafanulia Kachero Yasmine kinachofuata katika upelelezi wake.

"Sasa hiyo DNA si ungepimia hapa hapa Tanzania, yanini kubeba mpaka nchini Afrika ya Kusini, unajipa mikazi isiyo na kichwa wala miguu" alichangia mazungumzo Kachero Yasmine huku sasa akianza kupiga miayo ya usingizi kuashiria muda sio mrefu ataanza kusinzia.

"Hapana siwezi kufanya upuuzi huo, hawa watu siwaamini hata kidogo. Sijui mtandao wao una mkono mrefu kiasi gani sitaki kufanya makosa. Kwanza pesa ni za serikali wewe Mpemba unataka kuzionea ubahili ha... ha.... ha.. ha" alielezea Kachero Manu sababu zake za uchunguzi kuamua ukafanyikie nchini Afrika ya Kusini ni kutaka ukamilifu wa mambo bila uchunguzi kuingiliwa na mtu.

"Sasa mie nishachemsha, macho naona ni mazito kufunguka na kesho nina kiporo kizito kazini. Nikutakie usiku mwema Bosi wangu Tchaooo..!" aliaga Kachero Yasmine huku ananyuka kitini pake na kukusanya vyombo walivyolia maakuli pale mezani walipokaa kusogoa na kuvipeleka jikoni ili akauchape usingizi.

"Pole sana kalale zako, ila mlango wangu sifungi ukikabwa na vibwengo ndotoni njoo chumbani kwangu si unajua tupo Mbweni huku karibu na bahari, vibwengo ndio nyumbani kwako huku oooh" alitania Kachero Manu wakafa kicheko kwa pamoja, huku Yasmine hataki kujibu kitu chochote usingizi umemlevya tayari anakitamani kitanda tu.

Mara baada ya Kachero Yasmine kuingia zake chumbani. Kachero Manu akazima taa ya sebuleni na ya kwenye varanda, kisha akajisogeza kwenye pazia dirishani. Akalisogeza pembeni kidogo akaanza kuchungulia dirishani kukagua usalama, akamuona mlinzi wao wa getini yupo macho na silaha yake anazunguka huku na kule akitekeleza majukumu yao. Akatabasamu akifurahishwa na umakini wa mlinzi huyo katika kazi. Akarudishia pazia sehemu yake kisha akaelekea moja kwa moja chumbani kwake kulala.

SURA YA NNE
Kapteni Wandawanda ndio muasisi wa hujuma nzito..

"USIKU wa kuamkia Januari 21, 1964, mjukuu wangu sitousahau kamwe mpaka naingizwa kaburini. Kuna siku ambazo historia rasmi ya Tanzania haipendi kuzikumbuka, lakini haitaweza kuzisahau kamwe. Hasa kutokana na hekaheka zake na matukio yake yaliyotokea usiku huo niliokutajua. Usiku kwa kawaida huonekana ni mrefu sana na tulivu, lakini usiku huo wa maasi, saa zilikuwa zinayoyoma kwa haraka sana.

Risasi zilikuwa zinamiminwa na wanajeshi waasi kama njugu kila upande wa Jiji la Dar es Salaam, yamini, yasari, angani na ardhini ili mradi hali ya hewa ilitifuka ikawa mchafukoge. Wanajeshi tulionekana kama tumechanganyikiwa au kama wavuta bangi, lakini la hasha! tulikuwa na akili timamu tena tulikuwa na madai yetu ya msingi yanayotusukuma tufanye vimbwanga hivyo tulivyofanya usiku huo. Haya unayoyashuhudia huko Somalia ya leo au Syria au Iraqi ndio yalishuhudiwa ndani ya Tanganyika mpya kwa siku chache.

Wananchi huko mitaani walipatwa na taharuki hasa baada ya kuona mambo yanaenda borongoborongo kuliko walivyotegemea. Matumaini yao ya kuipata Tanganyika huru yenye amani na usalama waliona kabisa yanaanza kuyeyuka kama mshumaa, hasa wakiwa hawajui ukomo wa vurugu hizo utachukua muda gani. Tukio letu hilo Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alilielezea kuwa ni siku ya aibu sana kwa Taifa".
Wakati jeshi hilo la Tanganyika enzi hizo likiasi; siku hiyo hiyo, na saa hiyo hiyo, majeshi ya Kenya na Uganda nayo yaliasi kwa staili hiyo hiyo kwa mkupuo." Meja mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ, Bwana Marwa Chacha alifungua mazungumzo yake ya simulizi hiyo ya kusisimua kwa Kachero Manu aliyemtembelea maskani kwake usiku huo kwa mualiko maalumu.

Aliomba miadi ya kukutana na Meja huyo mstaafu ili huenda akaambulia dondoo za mlezi wa marehemu Dr.Pius Chilembwa, Kapteni Wandawanda ambaye walikuwa wote kituo kimoja cha kazi jeshini enzi hizo. Meja Marwa alikuwa shaibu wa umri kimuonekano tu hata kama asipokuambia.
Kwa hesabu ya haraka takribani miaka 80 hivi na ushee alikuwa hapungui lakini ukimuangalia bado ni mkakamavu haswa kutokana na shughuli zake za kila siku zinazotumia nguvu. Alikuwa bado anaweza kusoma gazeti kwa macho yake mwenyewe bila msaada wa miwani na shambani bado anaingia mwenyewe kila siku kupiga jembe la mkono.

Meja huyo mstaafu alikuwa anaishi maeneo ya kitongoji cha Picha ya Ndege, kilichopo Kibaha katika Mkoa wa Pwani. Alikuwa anaishi yeye na mkewe tu huku watoto wao wote khamsa wakiwa wamesambaa mikoa mbalimbali ya Tanzania katika harakati zao za kujitafutia maisha bora.

Akaweka kituo kwenye simulizi yake aliyoifungua kwa mbwembwe kwa muda. Akajikohoza kidogo kuliweka koo lake vizuri na kujaza ugoro kwenye kiko chake kwa kutumia vidole vya mkono wake wa kushoto na kukiwasha ili aanze kuvuta tumbaku lake. Baada ya kuvuta mikupuo kama miwili akapulizia moshi angani. Macho yake mekundu yakasindikiza wingu la moshi huo kisha akatabasamu kidogo kuonyesha ametibu alosto yake ya kiu ya tumbaku iliyokuwa imemkamata, akaendelea na maongezi yake.

"Kwa Tanzania, maasi haya yalitokea wiki moja tu baada ya mapinduzi ya umwagaji damu ya kule visiwani, Zanzibar, Januari 12, 1964; na usiku huo wa maasi hayo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar Field Marshal John Gidion Okello, alikuwa na mazungumzo na Mwalimu Nyerere Ikulu, Dar es Salaam, katika hali ya kubadilishana mawazo juu ya hali ya Zanzibar.
Ambapo Mwalimu Nyerere alikuwa anampa nasaha Bwana Okello afanye kazi kwa imani na Rais Abeid Amani Karume. Huyu Bwana Okello ndio mhandisi mkubwa wa vuguvugu la mabadiliko ya kudai uhuru katika nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla.

Sasa turejee kwenye maasi yetu, mpaka leo mjukuu wangu haijafahamika vizuri aliyepanga na kutekeleza maasi hayo; lakini swali kuu linaloulizwa bila kupata jibu ni je, ilikuwaje mpaka majeshi ya nchi tatu za Afrika Mashariki kipindi hicho Kenya, Uganda na Tanganyika kuasi siku na wakati ule ule, juma moja tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar?.

Akili yoyote iliyosalimika na kasumba ya ushabiki lazima italeta hisia kuwa injinia wa haya maasi kwa vyovyote ni mmoja. Dhana moja inajitokeza kwamba, kwa kuwa John Okello, mzaliwa wa Lang'o, Uganda, ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar, na pia kwamba aliwahi kuishi nchini Kenya kabla ya kwenda Zanzibar miezi michache kabla ya Mapinduzi; huenda alikuwa na mkono wake katika maasi hayo. Bwana Okello alijitapa pia kushiriki vita vya Mau Mau nchini Kenya, miaka ya 1950 vilivyopiganwa katika harakati za kupigania uhuru wa Kenya.

Ipo dhana nyingine kwamba, inasemekana huenda Oscar Kambona alikuwa na mkono wake kwenye hayo maasi". Alipomgusa Mheshimiwa Oscar Kambona kwenye simulizi yake, Kachero Manu alikuwa ameegemea kiti lakini sasa akajiweka mgongo wima, Meja Marwa alimkuna kunako hasa anapopataka haswa. Akaishikilia kalamu yake vizuri kwa mkono wake wa kushoto kwa ajili ya kujiandaa kuchukua dondoo muhimu.

"Watu wanajiuliza kwa nini wanajeshi tulimsikiliza yeye Oscar Kambona wakati huo huo baadhi yetu sisi wanajeshi wakimtafuta Mwalimu Nyerere hadi viwanja vya Ikulu, kwa shari au vinginevyo?. Nadhani unatamani haswa nikupasulie dhahiri shahiri kuwa nani kati ya Okello na Kambona alituongoza kwenye maasi hayo haramu ha.. ha... ha... ha..!.

Lakini katika miiko ya kijeshi siri ya kambi haiuzwi unakufa nayo moyoni. Wewe mwenyewe mjukuu wangu utajua kwa jinsi nitakavyokusimulia tu tuliza munkari na wahaka" aliongea Meja Marwa huku akinyanyuka kitini kwa haraka na kuomba udhuru anaelekea msalani kujisaidia nje ya nyumba pembezoni mwa upenuni mwa nyumba.



Kachero Manu akapata wasaa sasa wa kufanya utalii wa bure kwa kutumia macho yake kuichunguza nyumba ya Meja Marwa pale sebuleni walipoketi. Kwa msaada wa mwangaza hafifu pale sebuleni akaanzia juu kushuka chini, kwenye mbao za dari zinazoshikilia bati kuukuu aliona kikundi cha panya bila aibu wanakimbizana usiku ule kama vile wanacheza mchezo wa kitoto wa foliti, huku buibui wakiwa wametandaza nyumba yao sehemu kubwa ya dari.

Akaanza kuyashusha macho yake taratibu mpaka yakatua kwenye madirisha ya mbao yaliyoanzwa kutafunwa na mchwa. Akaona vipande vya kanga kuukuu na vipande vya maboksi vimetumika kuziba uwazi uliopo kwa ajili ya kupunguza makali ya upepo wa baridi la usiku.

Hakuchoka kufanya taftishi zake, alipotupa macho yake sakafuni akakutana na udongo ulioshindiliwa vyema ukamwagiwa maji kwa ajili ya kutuliza vumbi lisitimke mle ndani. Huku sebule ikiwa imepambwa na samani chakavu na za kizamani zenye umri wa zaidi ya miaka 15 kwa mtazamo. Zikionekana kabisa hazijawahi kung'arishwa tokea zilipoingizwa kwenye nyumba hii.

Akiwa amezama kwenye lindi la tathimini yake, ghafla akashtushwa na kelele za kulalamika za mlango wa bati wa kuelekea uani. Mwenyeji wake Meja Marwa akarejea toka msalani na kuisogeza karibu yao karabai inayoangazia pale sebuleni huku mkononi akiwa sasa ameshikilia kidaftari chake kidogo chakavu.

"Nimechelewa kidogo kuna nyaraka hii nilikuwa naitafuta stoo huko uani, bahati nzuri nimeliona daftari langu la kumbukumbu. Hii taa imeshaanza kupunguza mwangaza, sina uwezo wa kuvuta umeme, pensheni yangu ya mwezi ni ya kijungu meko haitoshi hata kuilisha familia lishe bora" alizungumza Meja Marwa kwa sauti ya manung'uniko akionyesha kabisa hajaridhishwa na namna wazalendo, walinda usalama waliochangia nchi hii kuitwa kisiwa cha amani namna wanavyopunjwa maslahi yao.

Baada ya mazungumzo kadhaa nje ya mada, Meja Marwa akaendelea na simulizi yake. "Kupata majibu ya maswali nani chachu ya maasi hayo, hatuna budi kuangalia kwa ufupi matukio kadhaa yaliyotangulia maasi ya nchi hizo tatu, kuona kama yana uhusiano wowote. Tanganyika ilirithi Jeshi kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza baada ya uhuru, Desemba 9, 1961, likijulikana kama Kings African Rifles (K. A. R) na baadaye kuitwa Tanganyika Rifles (TR) na kutokana na maasi hayo ya Januari, 1964 likaitwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Katika kipindi kufuatia uhuru, ili kukidhi matarajio ya Watanganyika, zilitakiwa hatua za haraka kuhakikisha nafasi zote za juu serikalini na taasisi zake, zinashikwa na Wazalendo. Huu ni utamaduni uliokuwa umejengeka kwa nchi zote za Kiafrika zilizokuwa zikipata uhuru.

Hiyo hali ilikuwa ndio inaonekana kuwa uhuru wa kweli umepatikana kinyume chake watu walikuwa wanaona ni kama kiini macho tu, wamepewa uhuru wa bendera. Baadhi ya vigogo ndani ya chama cha TANU wakawa mbogo, wakaona Nyerere anawalea wakoloni hataki kuwafurumusha, anapeleka mambo aste aste, hapo ndipo yakaanza malumbano ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Tawala, Tanganyika African National Union (TANU).

Wapo waliomuambia Nyerere wazi wazi kuwa alikuwa anairudisha Tanganyika katika enzi za Ukoloni.
Hivyo kwamba uhuru haukuwa na maana kwa Watanganyika kwa kushindwa kwake kuwapa vyeo Waafrika. Na kwamba wapo waliopoteza mali zao, kazi zao na hata kuhatarisha uhai wao ili tu kumfurusha mkoloni sasa iweje uhuru umepatikana yeye anawadekeza tena!.

Ili kuepusha shari, na ili Chama kisifarakane, wakawapa nafasi wafitini, Mwalimu akaachia ngazi nafasi yake ya Uwaziri Mkuu Januari 16, 1962 na kurejea kijijini kwake Butiama kuimarisha Chama kama Mwenyekiti wa Taifa wa TANU; na Rashid Mfaume Kawawa akachukua Uwaziri Mkuu wa nchi.

Naye Oscar Kambona, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Elimu, akawa Waziri wa Mambo ya Ndani badala ya George Kahama. Wote wawili hao wakaachiwa jukumu zito la kazi ya kuwaondoa Wazungu katika vyeo walivyokuwa bado wanashikilia haraka bila visingizio. Kazi ya kwanza ya Oscar Kambona sasa akiwa kama Waziri wa Mambo ya ndani ilikuwa ni kumtimua Kamishna wa Polisi Mwingereza, 'Mr. M.S Wilson' na kumteua mzalendo 'Elangwa Shaidi' kuchukua nafasi hiyo.

Zoezi hili la kuwapokonya madaraka wazungu lilifanywa kwa kasi ya kutisha kiasi cha kuishitua jamii ya Kimataifa. Desemba 1962, ulifanyika Uchaguzi Mkuu ambapo Mwalimu Nyerere alichaguliwa kuwa Rais Mtendaji wa kwanza. Kwa hiyo, Januari 1963, Mwalimu alirejea madarakani kama Rais wa kwanza wa Tanganyika na kusitisha mara moja zoezi hilo.

Hali ambayo ilichochea hasira kali toka kwa viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, ambao waliapa kutolala usingizi, wala kuupa nafasi uamuzi wa Mwalimu wa kusitisha zoezi la kuwapa madaraka Watanganyika. Wakaanza kumuona Mwalimu kuwa kama nae ni mkoloni tofauti ni rangi tu, Waingereza nyeupe na Nyerere nyeusi.

Kwa ujumla Nyerere alikuwa yupo sahihi, unapotaka kufanya mabadiliko hufanyi kwa ghafla tu lazima kuwe na maandalizi. Hata mtoto mchanga hapelekwi moja kwa moja toka kuacha kunyonya ziwa la mama mpaka ugali, lazima aanze uji mwepesi, uji mzito kisha ndio ugali mlaini mpaka anafikia hatua ya kula ugali mgumu.
Matata yalianza usiku wa Januari 20, kuamkia 21 usiku huo, siku ambayo Okello alikuwa na mazungumzo na Mwalimu, Ikulu usiku. Lakini ilipofika saa 7:50 alfajiri, Januari 21, Mkuu wa Kikosi cha kwanza cha Tanganyika Rifles (TR), Brigedia Patrick Sholto Douglas, aliamshwa nyumbani kwake na sauti ya baruji na vingora, karibu na kambi ya Jeshi ya Colito (sasa Lugalo Barracks).

Alipotoka nje, aliona askari wake 12 wakikamatwa na wenzao wenye silaha na kutiwa mahabusu. Ndipo alipofahamu kwamba, nusu ya askari 800 wa Kikosi hicho walikuwa wameasi. Aliweza kutoroka yeye na familia yake hadi katikati ya Jiji, akaiacha familia kwa Balozi wa Australia, kisha akakakimbilia kwa Afisa mwenzake, eneo la Oyster Bay. Akiwa huko, akampigia simu Oscar Kambona, akamwomba msaada naye akakubali, kupeleka ndege tatu Kikosi cha Pili huko Tabora, kuleta askari waliokuwa bado waaminifu kwa Serikali.

Douglas na Kambona hawakujua kwamba, tayari waasi walikuwa wamefunga barabara iendayo uwanja wa ndege; kwa hiyo, marubani walirudi mbio; naye Douglas akakimbilia kwenye Ubalozi wa Uingereza, akajificha kwa siku tano hadi Januari 25. Douglas alikuwa amempigia simu Mkuu wa Polisi, ambaye alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Makamu wa Rais, Rashidi Kawawa, eneo la Ikulu na kumwamsha, kisha hao wawili kwa pamoja, wakaenda kumpa habari Mwalimu. Mwalimu alipoelezwa juu ya maasi hayo, alilipuka kwa hasira na ghadhabu kubwa papo hapo; akataka kwenda yeye mwenyewe kukutana na Waasi hao ili wamweleze sababu za kitendo hicho cha aibu.

Ndipo watu wa Usalama walipojenga hoja nzito kumzuia, na hoja hiyo ikamwingia. Akakubali kuteremka matawi ya chini, kisha yeye, Kawawa na Mama Maria Nyerere, wakatorokea mahali kusikojulikana wakitoroshwa na mlinzi wao Bwana Peter Bwimbwo.
Wakati huo, tayari waasi walikuwa kwenye lango kuu la Ikulu wakimtafuta. Mwenyezi Mungu ni mwema kwetu Watanzania huenda waasi wangempata wangefanya tukio la kuistaajabisha dunia.

Kufikia saa 9:00 alfajiri, waasi walikuwa tayari wamekamata kambi ya Colito, hii kambi ya jeshi inayoitwa Lugalo hivi sasa, kisha waasi wakajigawa vikundi vitatu na kuingia mjini. Kikundi kimoja kilibakia kulinda kambi ya Colito, mimi nilibaki kwenye kile kinacholinda kambi ya hiyo ya Colito. Kikundi cha pili, kikiongozwa na Sajini Francis Higo Ilogi, ndicho kilichokwenda Ikulu kumtafuta Rais; wakati kikundi cha tatu kililinda barabara kuu zote mjini.

Kikundi cha Sajini Ilogi kilipofika Ikulu, kilishauriwa na mmoja wa Maafisa Usalama wa Taifa, wamwone kwanza Waziri Oscar Kambona; nao wakakubali kufanya hivyo. Wakaenda hadi kwa Kambona na kumleta Ikulu, na kumweleza kwamba walikuwa wamewakamata na kuwaweka mahabusu maafisa wake (Wanajeshi) 16; na kwamba, kama alikuwa tayari kusikiliza malalamiko yao, afuatane nao hadi Colito. Kambona hakuwa na budi bali ni kukubaliana nao.

Hapa sasa nisikilize kwa makini mjukuu wangu, Ni ujasiri gani huo; ni kujiamini vipi kwa Kambona, kwamba bila ulinzi wala woga, tena akiwa amepanda gari la Mkuu wa Polisi tu, aliweza kukubali kuandamana na askari wenye silaha, na hasira kali, kwenda Colito Barracks (Lugalo)?. Hilo ni swali gumu sana linalohitaji majibu ya kina sio ya kurashiarashia tu.

Ukimwondoa Nyerere na Kawawa, ambao walikuwa na kila sababu ya kujificha, kulikuwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Job Malecela Lusinde; kwa nini Kambona hakumshirikisha, kama aliona mambo yalikuwa salama kiasi hicho?. Hapo ndipo baadhi ya watu wanakwenda mbali zaidi kusema kwamba, huenda Kambona alihusika na maasi hayo" Kachero Manu akaanza kutikisa kichwa kuonyesha somo sasa linaanza kumuingia huku akabaki anatabasamu kwa jinsi Babu Meja Marwa anavyojua kujenga hoja na kuzitetea kiustadi mkubwa wakati anaunganisha na kunyumbulisha matukio.

"Huko Colito Barracks, walipompeleka walimweka Kambona mtu kati, wakimtaka aamue papo hapo, pamoja na mambo mengine, kuondolewa mara moja kwa Maafisa wa Kiingereza Jeshini, na nafasi zao zishikwe na Wazalendo. Walitaka pia mishahara iongezwe maradufu, kwa zaidi ya asilimia mia, kutoka shilingi 105/= hadi shilingi 260/= kwa mwezi. Bila kuonyesha kwamba ameyakubali au kuyakataa madai yao, Kambona aliomba wateue wawakilishi wachache ili wafuatane naye hadi Ikulu kwa mashauriano na Mwalimu Nyerere.

Ndipo Kiongozi wa waasi, Francis Higo Ilogi mzaliwa wa Bukene, Tabora, mtu mmoja mwenye roho ngumu, na mkomavu kama mti mkavu asiyetaka masikhara wala utani kwenye jambo lake akiamua, alikataa mara moja na kusema, Tunataka kila kitu leo hii, Yowe zikasikika, Apigwe risasi, apigwe (Kambona) huyo!. Tayari baadhi ya wanajeshi wakakoki silaha zao wakimnyooshea midomo ya mitutu yao Bwana Oscar Kambona kusubiria amri ya kumpiga risasi itoke kwa kiongozi wao Bwana Hilogi.

Kambona alipoona hali ni tete akauliza haraka haraka: Mnataka nani awaongoze? Lilitajwa jina la Alex Nyirenda; lakini likakataliwa kwamba alikuwa na majivuno, madahiro na kujisikia sana hafai kuwa kiongozi. Akatajwa Luteni Elisha Kavana, akapitishwa kwa kauli moja na kuvishwa kofia ya Brigedia Douglas.

Kambona alikataa kutia sahihi makubaliano, kwa madai kwamba mpaka ashauriane kwanza na Rais. Ndipo kikundi chote cha Ilogi kikafuatana naye sako kwa bako kwenda Ikulu kwa Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kubatiza uteuzi huo wa Luteni Elisha Kavana.

Walipofika huko, askari hao walijipanga barabara yote iingiayo Ikulu, lakini Sajenti Ilogi aliwakataza wasiingie ndani, alitumia nguvu kweli kwelikweli kuwatuliza mpaka wakamuelewa. Ndipo wakamruhusu Kambona pekee ndio aingie ndani Ikulu kwenda kuonana na Nyerere. Wakati huo kumbe Nyerere alikuwa ametoroka zaidi ya saa mbili zilizopita. Baada ya mashauriano kwa muda na wasaidizi wa Rais pamoja na mama mzazi wa Mwalimu, Kambona alitoka nje na kuwatangazia waasi hao kuwa Rais ameyakubali madai yao.

Lakini askari hao wakapiga kelele mwongo huyo! Rais hayumo ndani; mpige risasi, mwongo huyo!. Kambona akawa ametindinganya mambo tena kwa mara ya pili. Hata hivyo sudi bado ilikuwa upande wake Kambona, waliondoka wameridhika, wakarejea kambini siku hiyo. Hima, Kambona aliwaondoa maafisa wa Kiingereza na kuwasafirisha kwao kupitia Nairobi.

Akiwatangazia wananchi kupitia Redio Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC), Kambona alisema: Huyu ni Waziri wenu wa Mambo ya Nje na Ulinzi; Serikali ingalipo Kumekuwa na kutoelewana baina ya askari Waafrika na maafisa wa Kiingereza katika Jeshi. Baada ya kuingilia kati shauri hili, sasa askari wamerudi kambini.

Hata hivyo, hakusema lolote juu ya Nyerere, wala mahali alikokuwa. Je, ni kweli mambo yalikuwa yamekwisha? Kwa nini Nyerere hakutokea hadi siku mbili baada ya askari kurejea kambini? Kwa nini askari hao waliasi tena siku nne baadaye na Nyerere kulazimika kuita majeshi ya Uingereza kuja kuzima maasi?.
Haya maswali yote mjukuu wangu ni magumu hatuwezi kupata majibu kwa haraka haraka kwa uchambuzi wa usiku huu pekee!.

Ninachoweza kukuambia ni kuwa kwa kawaida Kambona alijua au alikuwa amearifiwa mapema kuhusu maasi ya Dar es Salaam katika vitengo vya usalama vya Tanganyika na maofisa wa Kiingereza ambao bado walikuwa wakiitumikia Serikali ya Tanganyika, lakini hakuchukua hatua yoyote kuikabili hali hiyo hadi pale ilipotokea. Mmoja wa maofisa hao ni Luteni Kanali Rowland Mans. Ilidaiwa kuwa mara kwa mara, Kambona, akiwa Waziri wa Ulinzi, alikuwa akiwatembelea maofisa wa ngazi za chini katika kambi ya Colito, na mara nyingine bila kuonana na viongozi wakubwa wa kambi hiyo.

"Leo asubuhi nilikuwa nasoma kitabu kimoja cha utafiti wa Ndugu Nestor Luanda katika kitabu hicho "Tanganyika Mutiny", ameeleza humo kuwa Kambona alianza kufika mara kwa mara katika Makao Makuu ya Jeshi mwishoni mwa 1963 na aliwaambia maofisa wa kijeshi wa Kiingereza kwamba alitaka wawe wameondoka nchini ifikapo mwishoni mwa 1964, je hayo maelezo yana ukweli kwa kiasi gani?" Kachero Manu aliingilia kati mazungumzo ya Meja Marwa kwa swali, huku akijiandaa kunukuu majibu ya swali lake.

"Unajua mjukuu wangu Kambona alitaka maofisa wengi wa Kitanganyika wapewe vyeo haraka, jambo ambalo Waingereza walidai haliwezi kutendeka kwa ghafla kama alivyotaka. Kuanzia hapo maofisa hao wakaanza kuwa na wasiwasi kuwa chochote kinaweza kutokea. Ingawa uhusiano wa maofisa wa kijeshi wa Uingereza na Waziri Kambona ulianza kupungua, huo si ushahidi wa kutosha kueleza kuwa Kambona alihusika kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja", alijibu kimtego wa kijanja akiwa hataki kumhukumu Kambona moja kwa moja jambo ambalo Kachero Manu alishamshtukia kuwa Meja Marwa ni mjanja kama sungura, anaingia na kutoka kwenye mtego.

"Sasa kuna mwanajeshi mmoja anaitwa Kapteni Wandawanda alikuwa anatokea Mbamba Bay ni Mnyasa nasikia nae mlikuwa nae jeshini kipindi hicho lakini akapata utajiri wa maajabu maajabu akawa anamiliki mali lukuki kipindi hicho zilizotokana na uasi, je unamkumbuka vizuri?" Kachero Manu sasa aliona muda umeshakwenda sana akamuulizia swali la kumchomekea mlezi wa mapacha Dr.Pius na Alex Chilembwa, na hili swali ndio lilikuwa swali haswa lililomleta.

"Huyo mtu unayemtaja hafai kabisa ni hayawani mkubwa. Kwenye yale machafuko kama ujuavyo kwenye msafara wa mamba na kenge wapo, sisi lengo lilikuwa ni kudai wazungu waondoke na maslahi bora lakini baadhi ya wenzetu akiwemo Kapteni Wandawanda walikosa maadili walikuwa wanapita mitaani kupora mali za wananchi. Kwa namna hiyo wapo baadhi yetu akiwemo yeye walitajirika sana kwa uhalifu huo walioufanya mitaani. Baadae aliachana na jeshi na kwenda kuishi nchini Uingereza akitumbua utajiri haramu aliojikusanyia.

Mfano nakumbuka tukio moja kipindi maasi hayo yalivyosababisha ghasia nyingi mitaani, hususani Mtaa wa Msimbazi maeneo ya Kariakoo. Maeneo mengi ya katikati ya mji risasi zilirindima. Mwarabu mmoja eneo la Magomeni, kwa kuona duka lake linavamiwa, kwa hasira zake alimpiga risasi mwanajeshi mmoja aliyejulikana kwa jina la Kassim na kumuondosha duniani hapo hapo bila kuomba maji. Koplo Nashon Mwita, ninatoka nae mkoa wa Mara, ambaye alishuhudia mauaji hayo, alirudi kambini kujizatiti. Akiongozana na askari mwingine, Luteni Mwakipesile, pamoja na wanajeshi wengine, walifika Magomeni na kummiminia risasi Mwarabu huyo, kulipiza kisasi kama mbwai iwe mbwai tu. Kana kwamba haikutosha, waliiteketeza nyumba yake kwa moto. Katika nyumba hiyo, inasemekana, Mwarabu huyo aliteketea na familia yake ya watu 15" alijibu kiufasaha Meja Mwita huku akionekana hana hata lepe la usingizi na kumbukumbu yake kichwani inachaji mithili ya ghulamu wa miaka 15 vile.

"Sasa je Wanyasa mlikuwa nao jeshini hawakuwa wanajivuna kuona mtu wa kabila lao kama Kambona ndio katuliza machafuko hivyo wao ni watu muhimu sana katika nchi hii?" alichomekea swali la kimtego ili apate penyenye zinatakazompa mwangaza zaidi wa upelelezi wake.

"Aaaaah...hiyo kujivuna mtu wenu akiwa anafanya vizuri ni kawaida mbona, sio wao tu Wanyasa peke yao mbona hata sisi watu wa mkoa wa Mara tulikuwa tunajivuna Nyerere katokea kwetu, hivyo hiyo sio mbaya. Ubaya ni kama kuna upendeleo yule kiongozi anaufanya kwa watu wa kabila lake huku anawabagua wa makabila mengine hilo ndio jambo baya sana kwa ustawi wa jamii yenye usawa, machafuko yanaweza kutokea wakati wowote ule kama vita vya Watusi na Wahutu kule Rwanda.

Ila nakumbuka Siku za usoni baada ya Nyerere na Kambona kutofautiana mitazamo mbalimbali ya kiitikadi katika namna ya kuiendesha Tanzania mpaka kupelekea Kambona kutoroka nchini Tanzania na kuhajiri nchini Uingereza, baadhi ya Wanyasa jeshini na hata huko mitaani walijisikia vibaya sana.

Huyo Firauni Kapteni Wandawanda alikuwa anaropoka maneno hatari kwa ustawi wa Umoja wa nchi kuonyesha kuwa Kambona kaonewa na nadhani pia jambo hilo lilichangia yeye kuacha kazi. Maana Kambona alikuwa anaonekana ni kama mtu namba mbili kwa ubora wa uongozi akitoka Nyerere. Hasa sononeko kwao lilizidi sana baada ya nyimbo mbalimbali za kashfa na kejeli dhidi ya Kambona zilipokuwa zinaimbwa mashuleni na jeshini.

"Sasa baada ya kupatikana Uongozi mpya wa Jeshi, je wale waliofanya fujo walichukuliwa hatua zozote au walisamehewa?" alichomekea swali la mwisho huku muda ukiwa umeenda sana karibia saa saba kasorobo za usiku alipotupa jicho kwenye saa yake ya mkononi.
"Mjukuu wangu ilipofika Jumamosi ya Januari 25, 1964, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mwalimu Nyerere aliomba msaada kutoka Serikali ya Uingereza kunyamazisha maasi ya kijeshi yaliyokuwa yanazidi kusambaa katika Tanganyika, yalifika mpaka kambi ya Tabora na Nachingwea huko Lindi. Hatimaye makomandoo wa Uingereza waliwasili kwa helikopta na kuwanyanganya silaha waasi. Jioni ya siku hiyo hiyo maasi ya Tabora nayo yakazimwa. Maasi hayo, hasa katika kambi ya Colito( Lugalo), yalizimwa baada ya makomandoo hao wa Uingereza kutua na kuanza kulipua lango la mbele la kambi hiyo.

Mara moja askari walioasi walijisalimisha. Kikosi cha Uingereza kiliongozwa na Brigedia Patrick Sholto Douglas. Waasi watatu waliuawa katika operesheni hiyo. 20 walijeruhiwa na wengine 400 walikamatwa, na wengine walitoroka, sisi wengine tulishatubia tulikuwa tunaiunga mkono serikali ya Nyerere, tuliona maji yameshazidi unga.

Kwa njia hiyo Rais Nyerere alirejea madarakani, lakini historia ya Tanganyika ikabadilika moja kwa moja.
Wiki tatu baada ya maasi (Feb. 16, 1964), Nyerere aliitisha mkutano wa hadhara Viwanja vya Jangwani na kuwaambia Watanganyika hivi: "Wanajeshi walioasi walidanganywa na wahuni wachache. Wendawazimu walikuwa wawili, watatu. Wale wengine waliswagwa tu kama ng'ombe wanaoenda malishoni. Wakivutishwa bangi, wakaja mjini kutenda maovu. Tukaenda kwa Mwingereza. Bwana Mwingereza tusaidie utuondolee balaa hili". Baada ya maasi hayo, Mwalimu Nyerere alianza kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa hakuna kosa linalorudiwa.

Hatua ya kwanza alianza kukamata wote waliohusika, kisha akapiga marufuku gazeti la Nation la Kenya linalomilikiwa na Aga Khan kutouzwa katika Tanganyika. Kwanini marufuku hayo? Gazeti hilo (Nation) lilitoa taarifa sahihi lakini yenye raghba na chumvi nyingi kuhusu kuangushwa kwa serikali yake. Kupunguza uwezekano wa mfarakano wa mawazo, akawabadilisha makamanda wa Kiingereza akaweka wa Kiafrika. Wakati huo huo, akateua kamati ya kutafakari mabadiliko ya kikatiba ambayo yataifanya Tanganyika kuwa nchi ya kidemokrasia ya chama kimoja kisheria na kiuhakika. Uso wake Nyerere ulikuwa na simanzi sana.

Hakuna hata Mtanganyika mmoja aliyeuawa kwa miaka yote 17 ya kupigania Uhuru wa Tanganyika. Lakini sasa baada ya uhuru Watangayika wameuawa. Jumanne ya Aprili 21, Mwalimu Nyerere alimwapisha Sir Ralph Wildham ndani ya Ikulu ya Dar es Salaam kuwa Jaji Mkuu wa Tanganyika, na kumwambia awashughulikie kikamilifu wanajeshi waliofanya jaribio la kuipindua serikali yake hapo Januari 19, 1964.

Ndipo Sir Wildham akatangaza rasmi kuwa wanajeshi wa Kambi ya Colito waliotaka kuiangusha serikali watafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu, Aprili 27, 1964. Wakati huo huo Rais alimteua Kapteni Abdallah Twalipo (35) na Kapteni Lukias Shaftaeli (39), wote wakiwa ni wanajeshi wa jeshi la Wananchi, kuwa wajumbe wa mahakama ya kijeshi. Sir Wildham akawa Rais wa mahakama hiyo.
Baada ya uteuzi huo, Mkurugenzi wa Mashitaka, Herbert Wiltshire Chitepo, alisema angewaita mashahidi 25. Kesi hiyo iliendeshwa kwa siku chache na hatimaye hukumu ikatolewa. Ijumaa ya Mei 15, 1964, siku 19 baada ya kufanyika kwa Muungano wa Tanzania, wanajeshi walioasi katika Kambi ya Colito walihukumiwa, lakini adhabu zao zilikuwa tofauti.

Sajini Francis Hingo Ilogi alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, Koplo Aliche miaka 10, Koplo Baltazar miaka 10, Private Jonas Chacha miaka 10, Private Pius Francis miaka 10. Wengine ni Private Patric Said John aliyehukumiwa miaka 10, Sajini Lucas miaka 10, Kapteni Kamaka Mashiambi miaka 10, Kapteni Benito Manlenga miaka 10, Private Dominicus Said miaka 10, Kapteni Andrea Dickson miaka 5, Private Hamidus miaka 5 na Roger Mwanaloya miaka 5.

Wanajeshi walioshitakiwa lakini hawakupatikana na hatia na hivyo kuachiwa huru ni Koplo Peter Mbasha, Private Ernao Msafiri, Private Gerado Raphael, Kapteni Mahara Magom na Kapteni Moses Kawanga" alimalizia mazungumzo yake huku anawasoma majina wanajeshi hao kupitia kwenye daftari lake kuukuu la kuhifadhia kumbukumbu zake alilolifuata pindi alipoelekea msalani.

Hapo ndipo Kachero Manu akang'amua kwanini aliporudi msalani alisogeza taa karibu yake, kumbe alikuwa anajiandaa kumsomea majina ya waasi.
Baada ya mazungumzo hayo wakaagana na kuahidi kumfanyia mpango wa kumsaidia kumvutia umeme nyumbani hapo kwa kutumia tashiwishi yake kwenye idara ya usalama.

"Nilichojifunza hapa inaonyesha akina Kapteni Wandawanda na baadhi Wanyasa wenzake wachache waliona kama wameonewa hivyo waliamua kujipanga, wajukuu zao waje kuchukua uongozi wa nchi kulipiza kisasi cha Babu yao Kambona. Ndio maana hata hawa akina Dr.Pius Chilembwa walipelekwa wakawasomeshwe elimu bora ughaibuni ili watumie elimu yao kuandaa mapinduzi ya kiakili sio kwa kutumia nguvu" yalikuwa ni baadhi ya mawazo yanayopita kichwani mwa Kachero Manu wakati anasukuma gari lake kwa mwendo wa wastani anaelekea nyumbani Mbweni. Muda ulikuwa umeshasonga mno usiku ule na yeye alishaanza kushikwa na uchovu wa usingizi.


SURA YA TANO

Jina la Kachero Manu chungu midomoni mwa wahujumu kama shubiri..

"Jamaa ni hatari sana, anatisha kama njaa, anashambulia kwa kugonga kama nyoka mwenye sumu kali, kamuua kikatili sana Kapteni Koba, ambaye ni komandoo wa kutegemewa kwenye operesheni nyingi za kijeshi nchini Tanzania.
Tulimrudisha makusudi toka Darfur kiujanja anapohudumu kwenye jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa (UN) ili aje kumshughulikia huyu Kachero Manueli Yoshepu, lakini tahamaki kachemsha, na kwa ujumla tumegonga mwamba. Mwili wa Kapteni Koba nimeushuhudia kwa macho yangu ukiwa mochwari kule hospitali ya Muhimbili.

Kusema ukweli umechakazwa vibaya hautamaniki huwezi kuuangalia mara mbili. Utasema amegongwa na gari barabarani kumbe ni vipigo vitakatifu toka huyu mshenzi, mjuba Manueli Yoshepu. Ripoti ya polisi ilivyoandikwa ni kuwa ameuawa kwenye tukio la ujambazi, hivyo hatozikwa kwa heshima za kijeshi kwa hadhi ya cheo chake ni kama ameliaibisha jeshi.

Kiongozi wetu ukiongea na Mkubwa kwa busara zake naomba umwambie awape kifuta jasho familia ya Kapteni Koba ili kuwafuta machozi maana alikuwa ni mshirika wetu muhimu katika harakati za kuisimika Dola ya Nyasa nchini Tanzania. Pia itatupa moyo sisi wa kupambana kuhakikisha ndoto yetu ya kuisimika Dola ya Nyasa inatimia tena kwa haraka".

Chew Master kama anavyojulikana na washirika wenzake wa mpango dhalimu, lakini ni kigogo mkubwa wa jeshi la polisi alikuwa anatoa taarifa ya kuhuzunisha kwenye kikao cha dharura kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili tukio lililoshindikana la mauaji ya Kachero Manu.

Jukumu la mauaji alibebeshwa Chew Master na akaahidi kulitekeleza kwa ufanisi ndani usiku huo huo lakini, Kachero Manu amegeuka fupa la chupa lililomshinda fisi kutafuna.

"Halafu mmepata taarifa ya kustusha kijijini Kwembe, kule kaburini kwa Dr.Pius Chilembwa feki?" aliuliza mmoja wapo wa wana kikundi kile mle kwenye chumba cha mkutano wao. "Wewe ndio wa kutujuza maana shughuli za mazishi yote yalikuwa ni jukumu lako, kuanzia usafiri, mazishi, chakula mpaka ulinzi..!" alichangia mmoja wapo, huku kila mmoja akipatwa na wahaka wa moyo wa kutaka kufahamu kumetokea nini huko maziarani.





"Halafu mmepata taarifa ya kustusha kijijini Kwembe, kule kaburini kwa Dr.Pius Chilembwa feki?" aliuliza mmoja wapo wa wana kikundi kile mle kwenye chumba cha mkutano wao. "Wewe ndio wa kutujuza maana shughuli za mazishi yote yalikuwa ni jukumu lako, kuanzia usafiri, mazishi, chakula mpaka ulinzi..!" alichangia mmoja wapo, huku kila mmoja akipatwa na wahaka wa moyo wa kutaka kufahamu kumetokea nini huko maziarani.


"Taaarifa niliyoipata ni kuwa mlinzi wa kaburi la marehemu Dr.Pius niliyemuweka amekutwa asubuhi akiwa ameleweshwa madawa ya kulevya amelala fo fo fo hajitambui. Lakini kaburini kuna dalili kama lilitobolewa ingawa limeonekana limezibwa tena, na mwili upo kama tulivyouzika," alitoa ripoti hiyo iliyowapa jambamoto na wahaka mkubwa wana mkutano wote kwenye ukumbi ule.

Maana walijua fika kama siri yao ya kuidanganya mamlaka ya nchi kuwa Dr.Pius Chilembwa ni marehemu hali ya kuwa ni mzima wa afya, ikigundulika patachimbika.

Dr.Pius marehemu kanyaboya ndio huyo wanayemuita kwenye kikao chao kwa jina la Mkubwa, alikuwa anakula zake maisha nchini Afrika ya Kusini na kuja Tanzania kwa mficho akitumia hati feki ya kusafiria. Pindi akiwa nchini inabidi mdogo wake, pacha wake Alex awe mafichoni kwa muda ili watu wasitambue kama huyu ni Dr.Pius ambaye ni marehemu.


"Mie ushauri wangu ni kuwa wala tusipigwe na taharuki mpaka tukashindwa kupanga mipango ya kumdhibiti huyu mpumbavu Kachero Manuel. Siwezi kuamini sisi na akili zetu mtu mmoja tu atusumbue, mpaka atunyime usingizi..!" alizungumza mmoja wa wajumbe wa mkutano ule wa siri.

"Kama atakuwa ni yeye huyo basi atakuwa ni mzuka maana mie nilihudhuria mazishini ulinzi ulikuwa mkali sana na yeye alikuwa ni muwindwa namba moja. Mawakala wetu wote tuliwapa picha ya Kachero Manu. Na maagizo yetu kwao yalikuwa wazi wakimuona mtu hata anayefanana na yeye ni kumtandika risasi kwanza kisha ndio uhakika wa kuwa ni yeye au sio ufanyike. Hivyo kuniambia kuwa huyu mjuba alikuwepo msibani na ameshafanya yake mimi nakula yamini kuwa hakuwepo labda ni mzuka wake" mjumbe mwingine aliongea kwa kujiamini, kuelezea namna hali ya ulinzi alivyoiona msibani.

"Mie nakubaliana na wewe kuwa ulinzi ulikuwa madhubuti na kama mlikuwa hamjui nilichukua mamluki wa Kizulu toka nchini Afrika ya kusini ambao hata lugha ya kiswahili kwao ni shida ili kama wakimkamata iwe ni utekelezaji wa vitendo na sio wa maneno mengi ya mahojiano" alizungumza kwa kujigamba Chew Master huku akiwa amevua miwani yako na kuiweka juu ya meza, anaongea kwa kutumia mikono yake kuonyesha msisitizo wa kile anachokiongea.

"Sasa kwa tahadhari tu, tutawapa taarifa watu wetu wote waliopo kwenye taasisi za upimaji wa DNA za hapa Afrika Mashariki ili kama kuna chochote amenyofoa kaburini anataka kufanya vipimo vyake aangukie pua.

Pia sasa tutazidi kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu yetu ya nchi kavu, baharini na njia ya anga kuona kama anataka kutoka nje ya nchi kumsaka Dr.Pius maana hatujui kwenye mpambano wake na mwanajeshi wetu Luteni Koba huenda ameropoka mambo yoyote sisi hatujui.

Hivyo lazima tuwe na tahadhari maili 100 mbele yake kimtazamo" alifunga kikao muwakilishi wa Dr.Pius katika kikao kile kabambe cha siri kilichofanyika usiku wa manane kwa lengo la kuandaa mikakati ya kumziba mdomo Kachero Manu, ambaye shughuli yake pevu ilikuwa inawanyima usingizi wadau wa harakati za kuisimamisha Dola ya Nyasa.

Paka anampenda panya kwa mapenzi ya maki

Nathanieli Banda au wana mtandao wenzake wa "Nyasa Empire Supporter" (NES) wakimfahamu sana kwa jina mpachiko la kimombo "Masterminder". Alikuwa ametinga suti yake nadhifu ya kahawia na viatu vyake vya rangi nyeusi ngozi halisi, ametulia ndani ya mgahawa uliopo kwenye Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo barabara ya Kivukoni.

Ilikuwa ni Hoteli ya kifahari yenye mandhari tulivu sana inayokuwezesha kuburudisha mboni za macho yako kwa kuiangalia mubashara Bahari ya Hindi mpaka mwisho wa upeo wa macho yako.
Ama kwa hakika siku hiyo Nathanieli alikuwa amependeza sana kimuonekano, vijana wa mjini wanasema "aliamua kuvunja kabati".

Alikuwa ana muonekano mithili ya Bwana harusi anayesubiria saa na wakati tu akakabidhiwe jiko mbele ya Baba mchungaji. Alikuwa ni kijana wa makamo mwenye kila aina ya mafanikio ambayo kila barobaro wa kileo anayaota awe nayo maishani mwake.

Kwa upande wa elimu alikuwa ametabahari vya kutosha, kwa shahada zake mbili za Uzamili. Moja ikiwa ni ya uchambuzi wa mifumo ya kompyuta aliyoipata nchini Afrika ya Kusini "Cape Town University" na ingine ni ya usimamizi wa fedha aliyoipata hapa hapa nchini, Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro.

Ukija kwenye kibarua cha kumuingizia mkate wa siku, alikuwa ni Afisa Mwandamizi katika Benki Kuu ya Tanzania (BKT) Makao Makuu, Jijini Dar es Salaam. Ajira ambayo ilikuwa inampa mshahara mnono na marupurupu kochokocho kwa mwezi. Pesa ambayo ilimfanya ayaendeshe maisha yake anavyotaka yeye yasonge na sio kuendeshwa na maisha yatakavyo.

Vidosho wenye kupenda kuwapapatikia wanaume tabaka a'ali, walikuwa wamejaribu kumtega Nathanieli kwa kila aina ya mitego na tashwishi lakini wapi, walishindwa kufua dafu. Mahusiano yake ya kimapenzi alikuwa anayaweka sirini sana, kiasi kwamba ilikuwa ni ngumu kumng'amua mpenzi wake. Habari kauzwa na Vidinga popo walipata uwanja wa kumchafua kwa kusambaza habari za uwongo za kimahusiano ya Nathanieli.

Wapo waliosema "anaye mchumba mrembo wa shani lakini anaishi Bondeni kwa Mzee Madiba, nchini Afrika ya Kusini". Walipata kani ya kuropoka hivyo kutokana na safari zake za huko zisizokauka. Chambilecho "akutukanae hakuchagulii tusi", wapo walioamua kupitiliza kumchafua kabisa wakavumisha kuwa "jogoo lake halipandi mtungi ndio maana anajitia hana mpango na warembo walioumbwa wakaumbika".

Maneno yote hayo ya lolololo Nathanieli aliyapuuza, hakuwa na muda mchafu wa kujiosha mbele yao wazandiki wa mambo. Ulevi wake mkubwa Nathanieli uliokuwa unajulikana na watu wengi ni upenzi wake kupitiliza wa motokaa za kileo. Alikuwa anabadilisha magari ya kisasa ya kutembelea kama vile mtu anavyobadilisha libasi zake.

Lakini kama ujuavyo hamna mkate mgumu mbele ya chai ya mkandaa, na ugumu wa siagi kiboko yake kisu, Nathanieli majivuno na nyodo zake zote za kuwadharau wanawake wa Kitanzania ziliyeyuka mbele ya mrembo Yasmine. Tokea siku ya kwanza tu kuripoti kwake kazini kwa Kachero Yasmine pale Benki Kuu na kutambulishwa mbele ya watumishi wenzake, Nathanieli tayari alishashikwa na gagaziko la moyo juu ya huba la Yasmine.

Bila kuchelewa kwa kuhofia ngoja ngoja huumiza matumbo akaanza kumfukuzia kwa kutega nyavu na kurusha ndoano zake zenye chambo cha udaga kwa Yasmine. Lakini kinyume na matarajio yake, hakuwa kisura wa mahonyo mwenye kubabaikia wenye nazo. Baada ya kupigwa kalenda kwa zaidi ya miezi miwili leo ndio alikubaliwa na Yasmine mualiko wake wa mlo wa usiku katika hoteli hiyo ya kifahari.

Yasmine kukubali kwake kukutana faragha na Nathanieli hakukuwa kibubusa tu. Bali kutokana na speksheni zake za muda mfupi tu pale ofisini kwake BKT alinusa harufu na kuona kuna dalili za uhusika wa Nathanieli kwa kiasi kikubwa kwenye ushiriki wake wa ukwapuaji wa mabilioni ya pesa zilizopotea.

Nathanieli furaha aliyokuwa nayo siku hiyo ilikuwa haisemeki baada ya kukubaliwa ombi lake na Kachero Yasmine. Ndio maana siku hiyo aliamua kuvunja kabati kabisa kwa kuvalia libasi za kutungua toka Ughaibuni na kujipulizia marashi ya ukwasi pia toka nchi za ng'ambo ili mradi tu awe nadhifu mbele ya mahabuba wa moyo wake. Ilipofika majira ya magharibi Nathanieli alikuwa tayari ameshawasili eneo la miadi kwa kutumia moja ya gari zake za kifahari aina ya "Range Rover Spot" rangi ya kijivu.

Lakini tokea awasili eneo la miadi, muda ulikuwa unazidi kuyoyoma Yasmine alikuwa bado hajang'aza uso wake. Kila wakati macho yake Nathanieli yalikuwa hayabanduki mlangoni ili amuone anapowasili.
Na pia macho yake yalikuwa hayabanduki kwenye saa yake ya mkononi kuangalia namna mishale yake ya saa hiyo inavyoshinda kusukuma muda mbele. Kadri saa zilivyoenda matiti, moyo wake ukaanza kupigapiga kwa haraka akianza kupatwa na wasiwasi wa kuachiwa manyoya na Yasmine kwenye majilisi hiyo aghali hapa Jijini.

"Huyu Binti mjanja mjanja kama sungura asije akawa ameamua kuniacha solemba. Muache aruke aruke mimi ndio "Masterminder" kama hanifahamu, lazima nimuingize kwenye mtego wangu" mkondo wa mawazo hasi ulikuwa unatiririka katika ubongo wake. Kila anapojaribu kumtafuta hewani kwenye simu yake, anajibiwa namba anayopiga haipatikani.

Ilipofika majira ya saa 2:00 usiku, Nathanieli tayari ameshaanza kukata tamaa juu ya hudhuri ya Yasmine, ghafla bin vuu...bila kutarajia, mlango mkubwa wa kuingilia alionekana msichana mmoja mrembo sana akiwa anatembea kwa madahiro. Alionekana anaingia huku anaangaza macho yake yasari na yamini kama vile kuna mtu anamsaka ila bado hajamtia machoni mwake.

Kimuonekano alikuwa ni hirimu, ana sura ya mvuto, macho yake legevu ya ukubwa wa wastani yaliyorembuliwa kama vile amekula kungumanga. Kifua chake cha wastani kilibarikiwa chuchu za kusimama zinazotaka kutoboa sidiria yake mithili ya ncha ya mkuki. Umbo lake lilikuwa limejengeka vyema na kuunda namba nane hasa kutokana na kiuno chake kubonyea katikati kama mdudu nyigu.

Alivutia mno kumtazama msichana huyo si kwa nywele zake laini na ndefu za Kisomali alizokuwa amezifunga kwa nyuma kwa mtindo wa mchicha, bali hata kwa ngozi yake ang'avu yenye kumesamesa kama taa ya aladini nyikani kwenye kiza kinene cha usiku. Kwa mwendo wake wa maringo tu aliwaacha midomo wazi watu wote waliomuangalia akitembea mle mgahawani.

Hatua zake alikuwa anaziachia sakafuni mithili ya mshindani wa mashindano ya ulimbwende. Wapenzi watazamaji wa mrembo yule wengine waliokuwa wanajipatia maakuli yao ya usiku, wengine walijikuta wanakosea badala ya kupeleka chakula kwenye mdomo ili kishuke tumboni, wakajikuta wanapeleka puani na wengine shavuni hali iliyopelekea kujimwagia ovyo chakula kama watoto wadogo. Ili mradi macho yao yalishikwa na mshawasha wa umbea.

Nathanieli alijikuta nae anapigwa na bumbuwazi, maruweruwe na mapigo ya moyo wake kusimama kwa sekunde mbili na nusu akiwa haamini kama yule ndio kweli Yasmine aliyemuweka doria karibia saa mbili ametokea.
Kisha akajikuta anapatwa na nguvu za ajabu akajikaza kisabuni na kujizoazoa kitini, akasimama na kujikuta anachanganya miguu yake kwa kujilazimisha mithili ya mtoto mdogo anayejifunza kutembea kwenda kumlaki.

"Ooooh...Waaaooh..! Yasmine Mpenzi wangu..karibu sana majilisi, siamini kama umetimiza miadi yako....!" alijikuta tu anaropoka Nathanieli kama mwehu mwenye kupandisha wazimu wakati wa mwezi mchanga. Wakati huo huo anamsaidia kutoa pochi yake ya rangi ya pinki kwapani ili aibebe yeye.

Bila hiana wala kinyongo Yasmine akamuachia pochi ile huku akiwa ameachia tabasamu pana lililoacha wazi sehemu ya meno yake ang'avu yaliyopangika kiufundi mkubwa na kuachia mwanya mdogo na kusababisha mbonyeo kwenye mashavu yake. Kisha kwa sauti yake laini ya kubembeleza usiku ule tulivu akaongea, "Samahani sana Mpenzi kwa kuchelewa....unajua hili Jijini lenu foleni sana, tofauti na kwetu Visiwani".

"Usijali naelewa cha muhimu ni kuwa umefika basi" alijibaraguza Nathanieli kujibu kwa lugha ya kinyenyekevu kuwa hamna tatizo lolote huku anachekacheka ovyo kama majinuni. Wakawa wameshafika kwenye meza maalumu aliyoichagua Nathanieli wakaketi vitini.
Yasmine alikuwa amevalia kisketi kifupi cha kubana cha dangirizi chenye rangi ya bahari buluu kilichoyaacha sehemu kubwa ya mapaja yake meupe wazi.

Kwa juu alivalia brauzi nyeupe nyepesi iliyombana vyema. "Umenisubiri sana? aliuliza Yasmine kwa sauti ya kudeka huku akiwa anachezea ufunguo wake wa gari kwa mkono wake wa kushoto.
"Nakuuliza wewe ujue, kwamba je umenisubiria sana..?" Nathanieli macho yake na mawazo yake yalikuwa yanashangaa mapaja mororo ya Yasmine, akiwa haamini kama huyu kweli ameumbwa na Jalali au amejiumba mwenyewe kutokana na kutokuwa na kasoro yoyote ya kimwili labda ya kitabia.

"Aaaah..! Samahani nilikuwa mbali sana mawazo yangu, ndiyo nimekusubiri sana muda mrefu yani mpaka nilibaki kidogo tu kukata tamaa, tahamaki ukatokea alizungumza Nathanieli kwa sauti ya kitetemeshi kama mtu aliyekurupushwa usingizini.
"Basi mie ngoja niondoke kumbe upo na mimi hapa kimwili tu lakini kifikra haupo nami unawaza michepuko yako mingine hukoooo....!" akatikisa kiberiti Yasmine huku akijitia kunyanyuka na kuchukua kibegi chake na kutaka kuanza kunyanyua hatua zake.

Weeeeh...! Nathanieli alikuwa mdogo kama piritoni anaona kabisa tonge linamponyoka mbele yake wakati tayari limeshafika kinywani. Alishapagawa anatetemeka huku anaweweseka kama mgonjwa degedege.

"Tafadhali....! Nisamehe sana, nimekosa sana nipe nafasi ya pili...! Tulia basi nikuambie ukweli nini nilichokuwa nakiwaza, nadhani utastaaajabishwa na maelezo tafadhali nipe nafasi ya kunisikiliza..!" alibembeleza Nathanieli huku amepiga magoti na Yasmine alishasimama tayari. Akajitia amemsamehe na kurudi kuketi tena kwenye nafasi yake. "Siku nyingine usijaribu kunifanyia hivyo, mie sipendi dharau hata kidogo" aljifanya amekuwa mkali kama pilipili kichaa.

"Hivi kwanini Yasmine unautesa moyo wangu kiasi hicho? hivi nizungumzie lugha gani nyepesi na rahisi upate kunielewa kuwa sina hali juu yako nipo mahamumu, ukipenda unifunge tu kwenye gereza la chumba cha chini kabisa katika sakafu ya moyo wako. Nimekufa juu ya penzi lako unanichelewesha tu mwenyewe kunizika moyoni mwako. Mimi ni mateka wako wa vita ya huba, nimesalimu amri nipo tayari kukukabidhi kila kitu changu, unifanye nitakavyo" akasita kuzungumza kwa muda akameza mate.

"Tafadhali sana Yasmine usiendelee kunipa mateso ya moyo, maisha yangu bila wewe ni sawa na kula chakula kisicho na chumvi, sipo tayari kuona nakukosa maishani mwangu. Mungu alipomuumba baba yetu Adamu alipomuona ni mpweke hana furaha kule bustanini Edeni, akamletea mwenza wake wa kumliwaza ambaye ni Hawa. Na mimi kipindi chote cha maisha yangu sikuona mwanamke anayeweza kuniondolea upweke na kunipa furaha maishani, mpaka nikajiona sina bahati duniani ya kubahatika kupata mwenza.

Lakini pindi ulivyojitokeza wewe pale kazini sasa naona kama nimeshapata mahabuba muafaka kwangu. Tangu ujio wako pale ofisini kwetu naona ni kama nyota jaha inayonifanyia upendeleo wa makusudi kwangu kuangaza mchana wa jua kali kwa kusaidiana na jua....!!" Nathanieli Banda alikuwa anajimaliza tu kwa kushusha mashairi matamu matamu ya kubembeleza, kudekeza akilimendea penzi la Kachero Yasmine Abeid lakini wapi kilikuwa hakieleweki kitu.

Binti wa Kipemba aliyelowea Zanzibari alikuwa mgumu kama chuma cha pua, na sio maharage ya Mbeya maji mara moja umekula. Alimkazia haswa kuwa hayupo tayari kuwa mpenzi wake, yupo pale kikazi tu na sio mambo mengine.
Hayo mashairi ya leo yalikuwa ni muendelezo tu, simu ya Yasmine ilikuwa imejaza meseji za mahaba toka kwa Nathanieli, mfanyakazi mwenzake katika kitengo kimoja cha kudhibiti fedha za nje na ndani. Kitengo ambacho Bosi wake alikuwa marehemu Dr.Pius Chilembwa, akisaidiwa kwa karibu na Nathanieli Banda na mwanamke mwingine akiitwa Flora Tarimo, na Makatibu Muhtasi wao wawili.

Kwa ujumla kitengo hicho nyeti kilikuwa na watu watano tu. Hivyo kifo cha Dr.Pius kikafanya idara hiyo iwe na watu wanne huku Kachero Yasmine Abeid akihamishiwa kitengo hicho akitokea Zanzibari. Nafasi ya Dr.Pius Chilembwa ilikuwa ikikaimiwa na Nathanieli Banda, hivyo alikuwa ni Bosi wa Yasmine kwa muda.

Baada ya mazungumzo ya hapa na pale wakanyanyuka kwa pamoja kwenda kuchota chakula wakaanza kupata chakula cha chajio kwa pamoja kwa kuwa usiku ulikuwa umeshafika. Sasa wakawa wanaendelea na mazungumzo yao huku sasa Nathanieli akiitumia fursa hiyo vilivyo kwa kuendelea kubembeleza penzi la mfanyakazi mwenzake.

"Hivi mimi na wewe tukiwa wapenzi, wafanyakazi wenzetu watatuchukuliaje kwa mfano! Si italeta taswira mbaya kwa taasisi yetu yenye heshima ya kutukuka itaonekana ni kama danguro. Mie naomba niendelee kukuheshimu kama kaka yangu tu na si vinginevyo, tusivuke zaidi ya hapo, samahani sana kama jibu langu kwako litakuwa limekukera na kuleta gharika ya moyo" Kachero Yasmine alijibu ombi la kuwa wapenzi toka kwa Nathanieli akiwa tayari ameshamaliza kula huku akijifanya anakwepesha macho anamuonea aibu. Anatafuna moja ya kucha zake katika kidole kidogo cha mkono wa kulia.

Jibu ambalo liliupasua na kuuchanachana vipande vipande moyo wa Nathanieli. Hakutegemea kupewa jibu kama hilo na kisura Yasmine. Nathanieli alijua tayari ameshamaliza kazi, ni kama anamsukuma mlevi kwenye mlima, sasa anaona binti anambadilikia kama kinyonga.

"Kwanza kinachonishangaza sana kaka Nathanieli ni kuwa kama uzuri basi Flora ni mzuri maradufu yangu mimi na katu sijaona kasoro yake katika tabia anachukuliana na kila mtu, kwanini unitongoze mimi na sio Flora ambaye mpo pamoja kitambo kirefu idarani?" Kachero Yasmine alizidi kumdodosa ili ajianike kila kitu kwa kutumia nguvu ya mapenzi tu.

"Swali zuri, Flora alikuwa chakula ya Bosi sasa siwezi kula sahani moja na Bosi sio adabu asilani" alijtetea Nathanieli kwa mafumbo, kiasi kwamba Kachero Yasmine alikuwa anataka mambo yawekwe hadharani na sio kufungwa fungwa kwenye bahasha.

"Unajua sijakuelewa bado unavyosema kuhusu Flora, kuwa ni chakula ya Bosi niweke sawa..!". Aliuliza Kachero Yasmine akiwa na tashiwishi ya kufahamu ukweli kinagaubaga.
"Ninamaanisha ya kuwa nisingeweza kutoka kimapenzi na Flora kwa sababu alikuwa ni mpenzi wa siri wa Bosi wetu wa idarani marehemu Dr.Pius Chilembwa, kuanzia Ijumaa kila wiki alikuwa hawaonekani kazini na Bosi wanakula bata ndefu tu, kifo cha Bosi ni pigo sana kwa Flora, hivyo namheshimu kama mjane wa Bosi wangu" aliweka wazi dhahiri shahiri ufafanuzi wa maelezo yake Bwana Nathanieli.

"Oooh.... masikini ya Mungu pole yake, nilikuwa siyajui hayo sasa naanza kuelewa, ndio maana mara nyingi siku ya Ijumaa hafiki kazini mpaka nikawa najiuliza kulikoni ana matatizo gani? Nadhani kwa sababu alishajizoesha toka zamani kuifanya kuwa sio siku ya kazi kwa upande wake. Pia kuna wakati anaonekana kama ni mtu mnyonge ana mawazo mengi sana" alinogesha mazungumzo hayo Kachero Yasmine kwa kukoleza umbea.

"Kunikataa mimi unachezea bahati kubwa sana Yasmine, mimi ni Gavana mtarajiwa wa Benki Kuu, ni suala la muda tu, sasa unadhani mie nikiwa mumeo halafu Gavana unatarajia nini...!" Nathanieli alichepusha mazungumzo na kumrudisha Yasmine kwenye lengo la kumpa mualiko ule, hata akajikuta kwa nguvu ya penzi anaropoka siri za ndani za NES hata zisizotakiwa kuzungumza mbele za watu ili mradi tu amuingize kwenye reli. Sasa aliamua kubadilisha gia angani kwa kumtega kwa kutumia nyadhifa ya cheo chake tarajaji.

Yasmine akajifanya ameshikwa na taharuki kupata taarifa hiyo mpya ya Ugavana akajifanya kama amejigonga kweli kweli na kukipapatikia hiko cheo cha kindotondoto anachokiota Nathanieli cha Ugavana.

"Oooh! Kweli jamani mpenzi wangu..au kamba tu za paukwa pakawa!!, unataka kupewa cheo cha Ugavana? nitajidaije mie nitakapoutangazia umma call me Mrs. Gavana, ha.. ha... ha.... ha...Hongera sana..!" alijitia kustaajabishwa kwelikweli na cheo hicho huku sasa akiwa amemuinamia Nathanieli kifuani kwake huku mkono wake wa kushoto unazichezea ndevu za Nathanieli.

"Eeeeh...ndio hivyo mubashara hamna chenga, mimi sio mtu mdogo kwenye hiyo serikali ijayo, ila siri yako usimwambie mtu mpenzi wangu. Kuna mgombea Urais ambaye ana nguvu kubwa ya zaidi ya asilimia 100% kushinda uchaguzi mkuu ujao wa mwakani. Kaniahidi kwa maandishi kabisa hiyo ni uhakika kabisa haina longolongo mbele ya mwanasheria wangu Ila narudia tena ni siri yako usimwambie mtu yoyote yaani wewe ndio wa kwanza kukupa siri hii hata mama yangu mzazi, kipenzi changu Bi Marieta wa kule Mbamba Bay sijawahi kumwambia habari hii abadaan katan" alijikuta Nathanieli anajikaanga kwa mafuta yake mbele ya adui yake bila kufahamu.

Yasmine moyoni mwake alikuwa na furaha maradufu isiyopimika katika mizania za kupimia furaha ya mwanadamu. Hasa kutokana na jambo lililomleta BKT kuchunguza linaanza kufungua wenyewe bila papara wala kokoro. "Simwambii mtu mpenzi.....kuwa na amani kabisa" aliongea alijiapiza kuifanya siri ahadi ya Ugavana aliyopewa kuwa ataificha.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog