Search This Blog

Thursday, 23 March 2023

CABO' DELGADO - 4

  

Simulizi : Cabo' Delgado


Sehemu Ya : Nne (4)

"Waheshimiwa wajumbe wenzangu kwa heshima na taadhima napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kupewa nafasi hii ya kuwasilisha taarifa ya kitengo changu nyeti. Kwa ufupi zoezi limefanikiwa kwa zaidi ya asilimia tisini (90%), tumefanikiwa kuwafurusha Watanzania walio wengi waliohajiri nchini kwetu kutoka Tanzania na tumedhibiti uingiaji wao nchi Msumbiji hasa maeneo yetu ya kujidai ya Montepuez kupitia mipakani. Na propaganda tunazozisambaza katika vyombo vya habari, ni kuwa tunawaondosha wahamiaji haramu wa mataifa yote sio Tanzania pekee, ambao wanaishi bila kibali cha ukaazi nchini Msumbiji". Akapumzika kuongea Bwana Mark kwa muda akameza mate kisha akaendelea.
"Lakini leo asubuhi saa moja tulipokea taarifa za kiintelijinsia za uingiaji wa mtu anayedhaniwa ni Kachero kutoka Tanzania kupitia njia ya daraja la umoja la Mtambaswala linalounganisha Tanzania na Msumbiji. Hasa tulivyowakamata na kuwaua wale wapelelezi sita toka mkoa wa Mtwara tulitegemea lazima atatumwa mtu toka Tanzania kuja kutuchunguza. Tulipotaka ripoti kwa askari wetu wa ukaguzi mipakani ambao ni sehemu ya mfumo wetu, tukakuta amewaua askari wetu 6 wa mpakani.
Pia tukapata penyenye zake muhimu toka kwa kidinga popo mmoja. Ndipo kumfuatilia mpaka kwenye vituo vya taksi vya Mji wote wa Montepuez. Kwa bahati nzuri mpaka kufikia muda wa saa 6:30 mchana tukafanikiwa kuelekezwa alipo huyo mtu kuwa anaweza kuwa amefikia Nzuwa Lodge. Tulipofika hapo tulipojitambulisha ni Maafisa Usalama tukakagua Kompyuta ya kujifadhia kanzi ya wageni lakini hakuweka taarifa zake na alikuwa ametoka.
Wanasema aliwaambia amechoka ataandika baadae, lakini yote ni janja janja yake tu. Tulipoingia chumbani kwake hakuwepo tukafanya ukaguzi wetu hatukupata lolote la kutusaidia zaidi ya kukuta mavazi yake ya kanzu na tasbihi, na begi lake lenye vitu vingine kabisa. Hivyo tukaenda nyumbani kwa dereva aliyesaidia kumuingiza Msumbiji kwa mficho huku tukiwa nia ya kurudi kumsaka tena Nzuwa Lodge.
Huko nyumbani kwa dereva ndipo tulipojua kuwa huyu mtu ni hatari sana, alifanikiwa kumdhibiti mwanausalama mwenzangu Jimmy, inaonyesha alikuwa anafuatilia nyendo zetu na mpaka ripoti za sasa hivi kwa watu wetu tuliowaacha Nzuwa lodge wanasema hajarudi mpaka sasa hivi na kahamisha vitu vyake vyote ingawa chumba alikilipia. Hivyo namalizia kwa kusema tayari Tanzania wamejibu mapigo kwa kuleta mtu wao kuja kutuchunguza na mpaka sasa vijana wangu wa kazi 7 ameshawapeleka jongomeo. Tusipokuwa makini nae tutaumbuka, Tanzania wakitaka jambo lao huwa hawashindwi, ahsante sana ndugu wajumbe". Alimalizia Inspekta Jenerali Mark hotuba yake iliyowasilishwa kiufasaha na weledi mkubwa.
Ukumbi mzima ulizizima kwa hofu na uwoga kama vile wamemwagiwa maji ya baridi. Kipindi chote cha uwasilishaji wa ripoti hizi, Kachero Manu alikuwa ndani ya gari lake "Volvo s60" gari la kipelelezi lililofungwa vifaa vya kisasa vya kudaka sauti kutoka kwenye ukumbi wa mkutano. Hivyo kila kitu kinachozungumzwa anakisikia, na anakirekodi.
Walichokuwa hawafahamu ni kuwa yule fundi umeme wa Nantilius hoteli, aliyeingia kwenye chumba cha mkutano kurekebisha hitilafu pindi ulipokatika umeme alikuwa ni Kachero Manu na alifanikiwa kufunga vifaa vya kunasa sauti kutoka kwenye ukumbi namba 03 wa mkutano.
Pia simu za baadhi ya vigogo zilizokuwa zinachajiwa ukumbini mule zote zilikuwa zinadukuliwa na Kachero Manu bila wao wenyewe kujua. Kila mmoja mule ndani akawafahamu kwa majina yao na magari waliyokuja nayo usiku ule kwenye mkutano ule.
Akawa yupo ndani ya gari anasikiliza mazungumzo yao kwa kutumia kifaa kinaitwa "personal sound amplifier" ni vifaa vinavyotumiwa sana na Makachero wanapopeana taarifa wakiwa umbali mrefu, hasa wakiwa kwenye misafara ya viongozi wa kitaifa. Ilipofika zamu ya kuwasilishwa ripoti ya udhibiti wa kitengo cha madini, gesi na mafuta, ndio moja ya ripoti iliyompa mshtuko mkubwa Kachero Manu.
Hapo iliwasilishwa ripoti kuonyesha nchini Msumbiji imegundulika gesi mapipa bilioni 20 katika pwani yake inayopakana na Tanzania. Mapipa ambayo yataingiza pesa dola za kimarekani bilioni 39, na zitaweza kuikwamua Msumbiji kutoka kuwa miongoni mwa nchi ya 7 kwa umaskini duniani.
Kilichomshangaza Kachero Manu ni mikakati ya kampuni ya "Monte Branco Ltd" kuhujumu uchimbaji wa gesi Tanzania, ili kuwafukuza wawekezaji kwenye sekta ya gesi Tanzania. Mikakati ilikuwa ni kutumia sintofahamu ya kizungumkuti cha watu wa mkoa wa Mtwara Tanzania kuzuia gesi isisafirishwe mpaka Dar es salaam mpaka watakapopewa ithibati ya namna watakavyonufaika na gesi inayochimbwa mkoani kwao.
Kumbe "Monte Branco Ltd" walipandikiza mamluki wao watakaohamasisha raia wa kawaida wafanye fujo ili kuwatia khofu wawekezaji waone Tanzania sio sehemu salama kwa uwekezaji. Pia kwenye vigogo wa serikali ya Tanzania wanaohusika na gesi kuhujumu kwa kuweka kodi zisizo na kichwa wala miguu, sera mbovu za uwekezaji na masharti magumu kwa wawekezaji ili wakimbie Tanzania. Kisha wao "Monte Branco Ltd" watakapodhibiti biashara ya gesi na mafuta nchini Msumbiji wauze kwa bei ya kupaa bila ushindani kutoka Tanzania.
Hivyo maazimio ya kikao ilikuwa ni kumuita nchini Msumbiji Meneja Mkuu wa masuala ya gesi na mafuta wa Tanzania, Bwana Andenga Kazimoto, ambaye ni mamluki wa Bwana Alfredo kwa upande wa Tanzania ndani ya siku mbili zijazo. Ili akutanishwe na Bwana Alfredo ana kwa ana kutoa ripoti za siri na nyaraka nyeti za alipofikia katika mikakati yake ya hujuma.
Kachero Manu alivyosikia jina la Mkurugenzi Andenga Kazimoto linatajwa tu fikra zake zikarudi siku ya kwanza kuitwa Ofisini kwa Bosi wake Mathew Kilanga alivyomtilia mashaka Bwana Andenga Kazimoto kuwa sio mtu mzuri hata kidogo. Sasa leo alikuwa anakithibitisha kile kitu ambacho alikuwa anakidhania kuwa ni kweli. Kachero Manu alichukizwa sana na ulafi wa kiongozi huyu ambaye alikuwa ni mtu msharafu na mwenye heshima kubwa nchini Tanzania na kujitambulisha mbele ya jamii kuwa ni mchapakazi na mzalendo mwenye kuitakia mema nchi yake.
Hapo ndipo akafahamu kwanini alikuwa huyu Bwana Andenga alikuwa anapenda sana vyombo vya habari. Ilifika hatua hata sherehe ya kipaimara tu ya mjukuu wake basi ataita vyombo vya habari si chini ya vitatu ili mradi tu asikauke midomoni mwa Watanzania. Pia Bwana Andenga alikuwa na urafiki na uswahiba uliopitiliza na matajiri wapenda sifa jiji Dar es Salaam, jambo ambalo kimaadili ya uongozi ilikuwa haileti muruwa mzuri.
Akaamini msemo wa wahenga "Kikulacho kinguoni mwako", na "chema chajiuza kibaya chajitembeza". Akajisemea Kachero Manu nafsini mwake "kumbe Tanzania wapo viongozi na watendaji ambao ni wachapakazi wazuri tu lakini kwa kuwa hawapendi kuuza sura kwenye vyombo vya habari basi wanaonekana ni wavivu na mapoyoyo".
Kachero Manu akaendelea kuwaza baadhi ya viongozi wa serikali ambao ni mfano wa kuigwa. "Mfano katika Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Mkoa wake Bwana "Anthony Mtaka" ni mmoja wa watendaji bora kuwahi kutokea nchini Tanzania. Anapendwa kuanzia na watoto, wazee, vijana, akina mama na watumishi wa serikali katika mkoa wake lakini sio kiongozi mpenda kiki katika vyombo vya habari".
Ikafika zamu ya kuwasilisha ripoti ya tenda mbalimbali za serikali zilizopelekwa Monte Branco Ltd, ndipo jina la Dr.Muganyizi lilipotawala kikao. Ilielezwa kuwa mradi wa PEMOVACHA kwa upande wa serikalini umeshapita na hamna kikwazo chochote, ila tatizo lipo kwa mwakilishi wa Benki ya ADB Dr. Muganyizi huyu alionekana ni kikwazo maana inahitajika aweke saini yake tu pesa zitoke.
"Nakuamrisha wewe Inspekta Jenerali Mark Noble huyu mtu afuatwe nyumbani kwake usiku huu wa leo, ukitoka hapa tu uende nyumbani kwake utafute nyaraka ya siri ya "PEMOVACHA PROJECT" ambayo lazima umlazimishe aweke saini yake kwa mtutu wa bunduki ili benki iweze kutoa pesa na baada ya hapo auwawe ikifika asubuhi tuwe tunajiandaa kutuma rambirambi tu, hawezi kujifanya ana uchungu na pesa za msaada kwa wana Msumbiji kuliko sisi wazawa wenyewe huu ni muendeleo wa kiherehere cha Watanzania kujitia wana uchungu sana na nchi za wenzao, sasa wajiandae kupokea maiti ya msomi wao tegemeo pale uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere.
Taarifa tulizonazo toka kwa watu wetu wa ofisini kwake Dr. Muganyizi wanasema huwa nyaraka muhimu zote anapenda kutembea nazo huwa hana imani na mtu yoyote. Na huyo Kachero wao anayejiita Hassan ibn Hussein kama tulivyopata taarifa zake toka Nzuwa Lodge, asakwe na aletwe akiwa hai kwanza aonane na Bosi Alfredo ana kwa ana tujue ana kitu gani anakijua kuhusu sisi kisha nae auliwe. Tutaonana kesho kutwa tarehe 17/02/2016 kwa wale watu maalumu wanajua muda wa mkutano kwenye kiwanda cha kusindika korosho karibu na soko la Baraca," alimalizia mwakilishi wa Bwana Alfredo kwa kufunga kikao hicho saa sita kasoro dakika tano usiku, waalikwa wote wakatawanyika.
Mwenyewe Bwana Mkubwa Alfredo hakuhudhuria mkutano huo, kutokana na kutingwa na majukumu ya kikazi nje ya nchi. Pia ilikuwa ni tabia yake haonekani ovyo mbele za watu kuleta tabia ya kuogopwa katika mioyo yao.



SURA YA TISA
Hali bado ni tete Jijini Dar es Salaam
Bosi Mathew Kilanga, Mkuu wa Idara ya Usalama nchini Tanzania, alikuwa hajapata usingizi wa starehe kwa siku ya tatu mfululizo tokea tarehe 14/02/2016 siku ambayo Kachero wake mtiifu Manu alipoaga kuwa anaelekea Cabo-Delgado, Msumbiji.
Alikuwa analala usingizi wa mang'amung'amu utasema kitanda chake kina kunguni kutokana na kuzongwa na mawazo juu ya kazi aliyomkabidhi kijana wake kachero Manu kama itakamilika kwa wakati aliompangia.
Kwa mtu ambaye ana umri zaidi ya miaka 70 kama yeye, ni mbaya sana kwa afya kukosa usingizi wa utulivu. Ingeweza kumpelekea kupata magonjwa kama ya mshtuko wa moyo na shinikizo la damu. Ukosefu huu wa usingizi haukuwa wa bure bali ulisababishwa na kutopata taarifa zozote za Kachero Manu tokea aondoke, sio arafa yake, wala barua ya pepe, wala simu.
Akajawa na hofu na wasiwasi wa jakamoyo, "je ni mzima Kachero Manu? au katekwa na maadui kauawa na yeye kama walivyopotea Maafisa upelelezi 6 kutoka mkoa wa Mtwara". Pia ukosefu wa usingizi ulikuja kutokana na maswali anayoulizwa na wakubwa wake wa kazi, kuwa amefikia wapi kwenye uchunguzi wa matukio ya Msumbiji dhidi ya raia wa Tanzania.
Uongozi katika zama hizi za uwazi na utandawazi ni shida sana. Uwajibikaji wa serikali ukilegalega katika kutatua changamoto za wananchi, hukumu yao dhidi watawala hufanyika kwenye sanduku la kupigia kura. Wanaadhibiwa na wananchi kwa kunyimwa kura zitakazowapa mamlaka ya kukamata dola. Hivyo viongozi wa serikali walikuwa wanahitaji majibu ya haraka kutoka kwa Mkuu wa Usalama wa Taifa ili waweze kuwajuza raia kinachoendelea.
Hali ilikuwa tete pia kwa Katibu Muhtasi wake, dada Kokunawa. Maana sasa alikuwa anakaa mkesha ofisini kama nesi wa zamu ya usiku kwa ajili ya wagonjwa mahututi. Kila wakati alikuwa yupo kwenye mtandao anasubiria barua pepe ya ripoti kutoka kwa Kachero Manu. Akaamua awe anarudi nyumbani saa 7 usiku lakini ikifika saa 12:30 asubuhi tayari yupo ofisini.
Ikafikia wakati baadhi ya wafanyakazi wa usafi kwenye jengo la ofisi yao wakawa wanadhani analala ofisini. Maana jioni wanapoondoka ofisini wanamuacha na asubuhi wanapowahi mapema kuja kusafisha jengo wanamkuta kashafika zamani.
Kazini kwao watu wa ofisi za jirani kila mmoja akawa na tafsiri yake kwa Kokunawa, wapo waliokuwa wanadhani hajaolewa na wala hana mchumba. Kumbe ni mchumba wa mtu na mtarajiwa wake alikuwa yupo nje ya nchi kimasomo.
Huko mtaani kwake majirani zake walikuwa wakimuona anajifanya mzungu na anajidai hana muda wa vikao vya umbea mtaani, hana muda wa kuhudhuria msiba wala sherehe ya mtu yoyote pale mtaani. Kumbe hawajui hata Kokunawa alikuwa hapendezwi na mazingira ya kazi yake namna yanavyomuweka mbali na jamii inayomzunguka na hata ndugu zake.
Maana ilikuwa ni kawaida kwake wakati mwingine yupo likizo lakini anakatishwa likizo yake kwa sababu ya kikazi. Kokunawa akiwa katika lindi la mawazo ya kazi yake, ghafla akaona meseji ya barua pepe yenye kichwa cha habari "Mwiba wa Tasi:Cabo-delgado", akajua kazi imeanza huko akatabasamu na kushusha pumzi ndefu mithili ya mtu aliyenusurika kupigwa dafrao na gari barabarani.
Akaifungua, kisha akaisoma na kuidurufu kisha akaweka kwenye faili na akapeleka ripoti hiyo ya Kachero Manu mezani kwa Bosi Mathew Kilanga. Akafunga ofisi na kuanza msafara wa kurejea nyumbani kwake Kigamboni ilikuwa imeshafika saa saba kamili usiku tarehe 16/02/2018. Alijua Bosi wake sasa ataanza kulala kwa raha maadamu amepata taarifa ya kijana wake Kachero Manu toka Jimboni Cabo-Delgado.

Mahasimu uso kwa uso nyumbani kwa Dr.Muganyizi
Mara baada ya kikao cha siri cha 'Monte Branco Ltd' kufungwa haraka haraka saa 6:45 usiku, Kachero Manu akatuma ujumbe wa barua pepe mfupi ofisini Dar es salaam ukitaka Meneja Mkuu wa Mafuta na Gesi Bwana Andenga Kazimoto afuatiliwe kwa karibu na wana usalama na mali zake zote anazomiliki na akaunti zake za benki zifuatiliwe miamala yake na kuhakikiwa.
Pia washirika wake wa karibu nao wachunguzwe kwa ukaribu na apewe taarifa yoyote kama atakuwa na safari ndani siku mbili hizi, na asizuiwe kusafiri. Lengo la Kachero Manu lilikuwa ni kutaka kumkamata Bwana Andenga Kazimoto katika ardhi ya Msumbiji akiwa na ushahidi kamili wa nyaraka za siri anazokuja kuziuza kwa Bwana Alfredo.
Baada ya kutuma barua pepe alishuka kwenye gari kwa haraka akaanza kuzunguka kwenye maegesho kuitafuta gari anayohisi wataitumia wabaya wake kwenda kufanya mauaji ya Dr.Muganyizi. Gari aina ya "Toyota Land cruiser" rangi nyeupe yenye namba inayoanzia na MBA-08...ambayo aliliona lilipomfuatilia kule Nzuwa Lodge. Alizunguka karibu eneo zima la maegesho ya magari, hakuona gari lenye namba hizo. Kijacho chembamba kikaanza kumvuja usoni, akashtushwa roho yake huenda kapigwa chenga ya mwili na wabaya wake.
Ingawa ilikuwa ni msimu wa baridi, kijacho kilitokana na hisia za kutorokwa na maadui zake bila kuwaona na hasa ukichukulia yeye ndio pekee anafahamu kuwa Inspekta Jenerali Mark ndio kapewa jukumu la kumuua Dr.Muganyizi.
Alipokuwa karibu na kukata tamaa, akapata wazo jipya la kwenda kwa mlinzi wa getini anayeandika namba za magari yanayoingia na kutoka hotelini, akajua hapo getini ndipo atapata majibu kuwa hilo gari lipo au limeshaondoka.
Akatembea kama meta 10 kwa mwendo wa kupega mpaka kwenye kibanda cha mlinzi wa getini. Alipofika akasalimiana nae "Hellow... habari za usiku kijana wangu, aisee nimepigiwa simu na mteja wenu mmoja, kaniambia kaharibikiwa na gari lake yupo hapa hotelini kwenu, gari lake limekataa kuwaka sasa simu yangu imezima chaji na nimelitafuta hapa maegesho silioni, sasa sijui unanisaidiaje?", alimaliza uwongo wake mtakatifu Kachero Manu huku akimkazia macho mlinzi yule.
"Wewe unatokea wapi? Alipigwa swali papo kwa hapo na mlinzi yule. "Mimi ni fundi magari wa kampuni ya magari ya kukodishwa ya "PAPADIOT"" alidanganya tena Kachero Manu huku akimkazia macho bila kupepesa.
Mlinzi yule alionyesha amechoka choka hataki usumbufu akaashiria kwa kidole, "kama hapa maegesho ya mbele hujaliona hilo gari unalolisaka basi fuata njia hii kwa mbele kushoto kuna maegesho ya chini kwa chini kwa baadhi ya magari maalumu huenda gari unalolitafuta lipo huko" alielekeza mlinzi yule huku akisogelea kiti chake ili aendelee kusinzia zake.
Akaaga Kachero Manu bila mlinzi yule kuitikia, kwa mwendo wa haraka tena akafanikiwa kuingia kwenye maegesho ya chini kwa chini. Kwa bahati nzuri gari hilo analolisaka liliegeshwa usawa na lango la kuingia.
Akalisogelea gari hilo, akachomoa mfukoni mwake mkungu wa funguo malaya na bahati ilikuwa kwake hakukuwa na mtu yoyote kule chini. Akajaribisha funguo kama sita zote zikawa zinagoma, akaijaribisha funguo ya saba mara mlango wa gari ukafunguka.
Bila simile akafungua mlango wa gari, akaingia akafunga. Akafungua droo ya upande wa siti ya mbele ya abiria kwa msaada wa kurunzi yake ndogo aliyoiwasha na kuanza kupekua. "Shabaaashi.......! kumbe nimepatia kwelikweli hii ni gari ya Inspekta Jenerali Mark Noble..! " aliropoka hivyo baada ya kuona kadi ya umiliki wa gari hilo.
Akairudisha hiyo kadi kisha akaenda kujibanza chini ya siti ya nyuma kabisa akimsubiria mbaya wake. Akaangalia saa yake ilikuwa inasoma saa 7:15 usiku. Akawaza kuwa leo mkesha mwingine bila usingizi, lakini alishazoea maana katika mafunzo ya Ukomandoo huwa wanakaa miezi miwili mfululizo bila kulala.
Mchana kutwa wanafanya mazoezi, ikifika usiku ni kuimba nyimbo za hamasa mpaka kunakucha tena. Hivyo hili la kukosa usingizi halikumpa tabu sana. “Kwanza Mwanausalama utapataje usingizi mororo haliyakuwa raia ambao wanakulipa mshahara kwa kodi zao hawana amani”, alijisemeza peke yake moyoni mwake huku akijipa hamasa ya mapambano.
Akawa yupo makini kumsubiria Inspekta Jenerali Mark aje waende pamoja nyumbani kwa Dr.Muganyizi kama ataamua yeye mwenyewe kutekeleza jukumu hilo kama alivyoagizwa na wakubwa wake. Nyumbani kwa Dr.Mganyizi ndio alipanga kuwe machinjio ya Inspekta Jenerali Mark Noble.
Akawa anavuta taswira namna serikali ya Msumbiji inatakavyoduazwa na itakavyofanya maombolezo ya Kitaifa kwa kifo cha Inspekta Jenerali Mark Noble. Wakati kwa upande wa Tanzania itakuwa ni furaha fokofoko kwa kuliangamiza joka jangwa la hatari kwa uhai wa Watanzania.

Upepo mwanana wa ziwa Nkwita ulikuwa unavuma usiku huo na kuleta hali ya hewa safi na yenye kuvutia kwa wakazi wa maeneo ya jirani na ziwa. Pembezoni mwa ziwa kulikuwa na msitu wa savana wenye miti inayovutia ndege wa kila aina kufanya makazi yao. Watalii toka sehemu mbalimbali walikuwa wanavutika kulitembelea ziwa Nkwita kwa ajili ya shughuli za kitalii.
Dr.Muganyizi alikuwa anaishi karibia na ziwa Nkwita katika Mji wa Pemba, makao makuu ya Jimbo la Cabo-Delgado umbali wa takribani saa moja kwa kutumia usafiri wa gari ukitokea Nautilus Hoteli, sehemu kilipofanyika kikao cha Mafioso wa Cabo-Delgado na kutoa hukumu ya kifo kwa Dr.Muganyizi.
Lilikuwa ni eneo tulivu sana lililojitenga na mji. Maofisa wengi wa taasisi za kimataifa wanaofanya kazi katika Mji wa Pemba na vibopa wa Mji walikuwa wanaishi huko kujiepusha na fujo fujo na makelele ya mjini. Kwa Tanzania tungefananisha na maeneo ya Masaki au Oysterbay.
Inspekta Jenerali Mark Noble alichelewa kutoka Nantilius Hoteli usiku ule, alikuwa anapokea taarifa juu ya usafirishwaji wa maiti ya kijana wake Jimmy kuelekea kwa wazazi wake Jijini Maputo. Huyu Jimmy alipigwa risasi na Inspekta Jenerali Mark nyumbani kwa dereva Masebbo kutokana na kutaka kutoboa siri za Mafioso wa 'Monte Branco Ltd' kwa Kachero Manu.
Baada ya hapo aliulizia hali ya mpakani kama hakuna lolote jipya, akapewa taarifa kila kitu kipo shwari. Kisha baada ya hapo ndio akapanga aelekee nyumbani kwa Dr.Muganyizi kutekeleza maagizo ya kikao cha usiku huu aliyopewa.
Alivyoingia ndani ya gari hakuchukua tahadhari yoyote na hilo ndio lilikuwa kosa lake, ndani ya gari alimpakiza adui yake namba moja Kachero Manu bila yeye mwenyewe kujua. Alipowasha gari lake tu akafungulia wimbo wa mwanamuziki wa Kimarekani “Louie V Gutta” unaoitwa “Kill The Streets” upate kumburudisha akiwa safarini.
Wimbo ambao huwa daima anapotaka kwenye kufanya tukio la mauaji huwa anaupenda kuuskiliza ili umpe morali kutokana na mashairi ya wimbo huo. Humo humo ndani ya gari lake akabusha bangi lake na kuanza kulipuliza bila aibu.
Kwa Cheo chake kama Inspekta Jenerali hakutakiwa kuwa mvunjivu namba moja wa sheria. Tabia yake ilifanana na Daktari anayekukataza usivute sigara utapata kansa wakati yeye ndio mvutaji aliyekubuhu. Au sawasawa na Sheikh anayehubiria waumini wake msikitini kuwa fuateni maneno yangu msifuate matendo yangu.
Baada ya dakika kama 45, Inspekta Jenerali Mark na Kachero Manu walikuwa tayari wameshafika maeneo ya karibu na nyumbani kwa Dr.Muganyizi. Aliegesha gari mtaa wa pili yake kutoka nyumba anayoishi Dr.Muganyizi. Ilikuwa ni mitaa ya kishua kweli kama wanavyopenda kuiita vijana wa mjini.




Baada ya dakika kama 45, Inspekta Jenerali Mark na Kachero Manu walikuwa tayari wameshafika maeneo ya karibu na nyumbani kwa Dr.Muganyizi. Aliegesha gari mtaa wa pili yake kutoka nyumba anayoishi Dr.Muganyizi. Ilikuwa ni mitaa ya kishua kweli kama wanavyopenda kuiita vijana wa mjini.
Yaani ni mitaa ambayo nyumba zake zimejengwa kwa mpangilio maalumu, kwa ramani za kwenye video na huku barabara zake zimepandwa bustani za miti mirefu yenye kutunzwa kiustadi mkubwa. Huku pembezoni mwa barabara kukiwa na taa za barabarani zinazotumia jua zenye kutoa mwangaza wa wastani usiokera kwa mpita njia.
Barabara zake zilikuwa zimewekwa lami yenye viwango vya hali ya juu. Akashuka haraka haraka Inspekta Jenerali Mark Noble, akachomoa bastola yake akaishika mkono wa kulia inapepea akasahau hata kufunga milango kwa funguo kutokana na pupa zake za kutaka kumnyofoa roho Dr.Muganyizi. Hilo likawa ni kosa namba mbili la kumpa nafasi ya kushuka Kachero Manu kutoka siti za nyuma bila shida na kwa haraka.
Alivyoshuka tu akatoa upepo tairi zote nne za gari la Inspekta Jenerali Mark, ili kama wakizidiana ujanja huko ndani nyumbani kwa Dr.Muganyizi asiweze kumtoroka kirahisi. Kachero Manu akawa anamfuata nyuma nyuma Mark bila Mark kutambua kuwa anafuatwa. Kuna wakati Inspekta Mark akigeuka nyuma kwa machale yake, inabidi ajifiche kwenye kivuli cha miti ya barabarani.
Walipoingia mtaa wa pili, nyumba ya tatu upande alioingia kushoto kwake ndipo alipokuwa anaishi Dr.Muganyizi. Kachero Manu akajibanza kwenye kivuli cha miti iliyopandwa kwa mstari nyumba ya pili kabla kufika kwa Dr Muganyizi. Ilikuwa ni nyumba kubwa imezungushiwa ukuta mrefu wenye meta zisizopungua sita huku ukiwa ukuta huo umenakshiwa kwa rangi nyeupe, huku juu yake kukiwa na nyaya za umeme maalumu kwa ajili ya kuzuia wezi. Na taa za duara zilikuwa zimezunguka ukuta wote kwa ajili ya kuleta mwangaza wa usalama.
Ni nyumba ambayo gharama ya ukuta wake tu unajenga "Nyumba Mjinga" zetu hizi za uswahilini kama 20 na chenji inabaki ya kununulia gari ndogo ya kutembelea mfano wa aina ya "Mark-X". Akaamua ampe dakika 20 kabla hajamshtukiza, huku robo saa zikiwa ni za kupambana na kikwazo chochote.
Zilipopita dakika 10 tu akasikia risasi ya kwanza imepigwa. Akajua kazi imeanza akakurupuka haraka haraka toka mafichoni kuelekea nyumbani kwa Dr.Muganyizi huku akiwa kaichomoa bastola yake mkononi. Akasogea kwa tahadhari kubwa sana mpaka akafika getini, akatulia kidogo akachungulia kwenye uwazi mdogo wa kwenye geti.
Akamuona mlinzi wa getini akiwa na sare zake za rangi ya kaki na kofia nyeusi, na buti nyeusi miguuni, anaogelea katika dimbwi la damu huku bunduki yake imelala pembeni yake anapigania roho yake katika siku yake ya mwisho ya uhai wake wa kufaidi ugali wa duniani.
Alikuwa amelala chali meta kama 5 kutoka usawa wa geti akafahamu ile risasi aliyosikia akiwa nje ya nyumba itakuwa amepigwa huyu mlinzi na Inspekta Jenerali Mark Noble.
“Huenda huyu mlinzi alimuona Mark wakati anaingia kwenye nyumba hivyo labda alimfuata ili kupambana na Mark kwa bahati mbaya hakufahamu kama Mark ni mzoefu wa mapambano, labda alijua ni kama majambazi tu wa kawaida” aliwaza Kachero Manu. Akajiuliza "je aingie kupitia getini kwa tahadhari kubwa au ni mtego anachezewa sinema la kihindi aweze kunaswa kiwepesi?".
Kwa Kachero makini kila unachokitilia mashaka lazima ukifanyie kazi usikipuuzie hata kidogo. Akaghairisha kupitia getini, akarudi kuzunguka ukuta akaparamia kwenye mti miongoni mwa miti iliyopandwa kuzunguka nje ya ukuta kwa pembezoni mwa ukuta.
Alivyofika usawa wa juu kidogo ya ukuta ule wa meta 6 akaruka kutoka kwenye mti na kupaa juu ya nyaya za umeme za ukuta mithili ya mpiga mbizi kwenye bwawa la kuogelea anavyojirusha. Akatua salama kwa mtindo wa sarakasi kwenye nyasi za ukoka za ndani ya ukuta.
Aliponyanyuka akaanza kuisogelea ile maiti mpaka akaifikia huku akiwa na tahadhari kubwa. Akaipiga mateke kidogo, ikabakia imetulia akajihakikishia kweli amekufa sio mtego kwake. Akairuka ile hakuwa na muda wa kupoteza kuichunguza sana asije baradhuli Mark akapata nafasi ya kupoteza uhai wa Dr.Muganyizi.
Akaanza kutembea kwa minyato usawa wa pembezoni mwa bustani ile ya nyasi za ukoka inayoizunguka nyumba mpaka akalifikia karibu dirisha la jiko la ndani. Akaona taa ya jikoni inawaka. Akasogelea dirishani kabisa akakuta dirisha lililotengenezwa kwa madini ya aluminium limefungwa. Akatoa kibati kidogo toka mfukoni mwake akaingiza kibati hicho kufyatua kifungio cha dirisha akakandamiza kibati kikafyatuka. Bila ajizi akasukuma kwa upole dirisha ili lisipige kelele akafanikiwa kulifungua.
Akarukia jikoni, alipoingia, akawa anaskia sauti anayohisi ni ya Mark ya kufoka, "yuko wapi Bosi wako Dr.Muganyizi? kama unamficha hutaki kusema alipo nikigundua nasambaratisha ubongo wako kwa risasi". "Bosi kaniaga anasafiri ila hajaniambia anasafiri kwenda wapi" alijibu huyo mtu kwa sauti ya kutetemeka ilyojaa uwoga wa kupigwa risasi. Katika uhai wake kijana yule leo ndio siku ya kwanza kasikia mlio wa risasi ile iliyompiga mlinzi wa getini.
“Sasa tulia hivyo hivyo”, alisema Inspekta Jenerali Mark, akatoa kamba ya manila ndefu toka kwenye mfuko wa suruali yake akaanza kumfunga kamba kijana yule za mikono na miguuni kwa kuikaza mpaka damu ikawa inapita kwa tabu. Kisha alipomaliza akamsokomezea matambara machafu ya nguo mdomoni ili asiweze kupiga kelele, kisha akarudi tena Mark chumbani kwa Dr.Muganyizi ambapo alikuwa amemkosa mara ya kwanza.
Kachero Manu akasubiri kidogo akaona ukimya umetawala kwa muda. Akanyonga kitasa cha mlango wa jikoni unaotenganisha na ukumbi wa kulia chakula, ukafunguka akaufungua kwa umakini mkubwa ili usitoe kelele akapita akaingia ukumbi wa chakula, akapitiliza mpaka kwenye veranda ya kuelekea vyumba vya kulala.
Huko ndipo alipomuona kijana kafungwa kamba, huku damu zinamvuja mdomoni na puani kila akipumua kutokana na kipigo kizito kisicho na chembe ya huruma alichopokea toka kwa Mark. Alipomkaribia yule kijana akawa anamuona yule kijana ameelekeza macho yake usawa wa mlango wa chumba kimojawapo.
Kachero Manu, akatambua anapewa ishara ya macho kuwa kuna mtu kwenye hicho chumba, na mtu mwenyewe si mwingine bali ni Inspekta Jenerali Mark Noble. Hivyo akamsogelea yule kijana kwa tahadhari huku macho yake yapo uelekeo wa kile chumba. Alipokaribia akakuta mlango upo wazi na Mark ametingwa na kupekua chumbani humo ametupatupa vuruvuru nguo na mafaili mbalimbali chini.
Ilionyesha kama kuna nyaraka za siri anazitafuta chumbani mule kwa Dr.Muganyizi huku mkononi mwake kuna bastola ambayo ameishika kizembezembe kwa kujiamini yupo peke yake ndani ya chumba.
Alichofanya Kachero Manu ni kumshitukiza,"tupa bastola chini na nyanyua mikono juu" alifoka kwa sauti ya juu yenye mamlaka isiyo na chembe ya mzaha. Inspekta Mark moyo wake ulilia paaah..!, alipatwa na mshtuko mithili ya mtu aliyefumaniwa na mke wa mtu saa 6 ya mchana ya jua la utosi.
Hakutegemea usiku ule wa manane kuwe na mtu atakayemsumbua kwa kufuatilia nyendo zake. Akatii amri mara moja na kutupa bastola chini. "Yupo wapi Dr.Muganyizi"? aliulizwa Mark na Kachero Manu. "Sifahamu alipokwenda" alijibu Mark kwa sauti ya kujiamini. Alianza kuondosha uoga alijua akizubaa atakufa kifo cha kijinga bila kupambana. Akaanza ujanja wa kuchelewesha muda.
Akaongea Mark, "wewe maluhuni unajiita Hassan ibn Hussein mpelelezi toka Tanzania" kisha akaangua kicheko cha kebehi. "Utanijua hivi punde..", alijibu Kachero Manu. "Haya rudi kinyumenyume mpaka usawa wa kitanda" alitoa amri huku anaingia vizuri kwenye chumba cha Dr.Muganyizi, hilo lilikuwa ni kosa kubwa.
Inspekta Mark




Inspekta Mark alirudi nyuma nyuma, kama hatua tatu halafu akajifanya kama kajikwaa kitu anataka kuanguka kwa kuugongesha mguu wake wa kushoto juu ya mguu wake wa kulia kisha kama umeme akajibidua sarakasi hewani akatua miguu yake juu ya kifua cha Kachero Manu ambaye hakujiandaa na shambulio la ghafla na alikuwa anatembea kuingia chumbani.
Shambulio ambalo lilimwangusha kizembe mpaka chini na bastola yake mkononi ikadondoka chini. Haraka haraka Inspekta Mark akajizoa chini kuikimbilia bastola yake, Kachero Manu naye bila ajizi akainuka na kumpiga teke aina ya "SAVATE".
Huo ni upigaji wa teke ambao asili yake ni nchini Ufaransa. Huwa ukipigwa na fundi wa upigaji lazima utenguke kiungo labda uwe na bahati ya mtende kuota jangwani, na ndio hiyo bahati ilimkuta Mark. Hilo teke halikutua vizuri kwenye maungio ya goti liliteleza kidogo kutokana na kuwa katika mwendo wa kuiendea bastola yake ndio ikawa salama yake likamuangusha chini lakini akiwa na maumivu makali.
Akajikaza kisabuni akanyanyuka ghafla na kutupa makonde ya haraka haraka kama matatu, makonde mawili yakampata Kachero Manu kisawa sawa yakampasua kwenye kona ya mdomo. Damu zikaanza kuvuja taratibu, akarusha konde la tatu usawa wa jicho la kushoto la Kachero Manu, Kachero akalikwepa kiustadi mkubwa.
Mark akapatwa na wazo jipya baada ya kutambua Kachero Manu ni farisi katika fani ya mapambano, na asingeweza kumshinda kirahisi. Akaanza kurudi kinyumenyume mpaka akakaribia usawa wa dirisha la chumbani alilotumia kuingilia chumbani kwa Dr.Muganyizi.
Kachero Manu akadhani ni mbinu ya kujipanga kwa shambulio akasimama kwa umakini anamsubiria maana alitia akili Inspekta Jenerali Mark sio wa kawaida kwenye sanaa za mapigano.
Kumbe ile ilikuwa ni "janja ya jani kula hindi bichi", kama nyani vile aligeuka kwa haraka kwa kudandia kitanda kisha akaparamia dirisha la chumbani kwa Dr.Muganyizi alilotumia kuingilia akatokomea nje ya nyumba kisha akatimkia mtaani kwenye giza totoro.
Kachero Manu alisimama kama kapigwa ganzi alishangazwa na umahiri wa Inspekta Mark, hakutegemea kama Mark atamkimbia usiku ule. Akatanabahi kuwa Inspekta Mark atakuwa amepitia mafunzo makubwa sana ya sanaa za mapigano.
Alifahamu Mark hatoweza kuitumia gari yake kwa kuwa kaitoa upepo, lakini kwa kasi aliyotoka nayo hapa ingetosha kutafuta mbinu mbadala za kuondoa eneo lile. Akaamua aachane kwanza afahamu alipo Dr.Muganyizi maana ndio kipaumbele cha kwanza kumuokoa yeye na sio kumsaka Mark.
Kachero Manu akaiendea bastola yake akaiokota akamrudia yule kijana aliyefungwa kamba kwenye veranda. Akamfungua kamba zote na kisha akaanza kumuuliza, "wewe ni nani humu, pole sana.." alisema Kachero Manu.
”Mimi ni msaidizi wa kazi za nyumbani, kibarua wa Dr.Muganyizi” alijibu kijana Yule. ”Sasa Dr. kalala wapi usiku huu”? aliuliza Kachero Manu kiudadisi ili apate ukweli mahali alipo.
"Dr kasafiri kwenda Tanzania na ndege ya saa moja usiku wa kuamkia leo, kaenda kuangalia familia yake kipindi hiki cha mwezi wa mwezi wa pili katika mapumziko ya siku ya wapendano "Valentine Day". Kasema atarudi wiki ijayo” alimalizia maelezo yake kijana Yule.
Kachero Manu akatabasamu akajua Dr.Muganyizi bado siku zake za kuishi zipo sana hapa duniani, kakikwepa kifo chake mbele ya mtutu wa Inspekta Jenerali Mark. Pia akatambua Dr.Muganyizi safari zake zilikuwa za siri maana hata mamluki watoa taarifa kwa watu wa Alfredo wa kazini kwake hawakufahamu hiyo safari.
”OK.. kuwa na amani kijana endelea na maisha yako, ikiwezekana katoe taarifa kituo cha polisi, kwaheri...” akaondoka Kachero Manu bila kumpa nafasi yule kijana ya kujibu chochote, akatokomea zake nje ya nyumba, usiku ule kama wa saa tisa kasoro dakika kumi.
Huku ving'ora vya gari za polisi vikisikika kwa mbali akafahamu huenda majirani wametoa taarifa baada ya kusikia mlio wa risasi iliyomuua mlinzi wa nyumba ya Dr.Muganyizi au Mark kawashtua polisi waje kumtia mbaroni.
Akafanya haraka kupotea eneo lile ili asije kufanywa asusa kwenye jambo asilohusika nalo, wakamtoa kafara.


SURA YA KUMI
Kachero Manu aonyeshwa cha mtema kuni
Nyumba ya Dr.Muganyizi usiku huo ikazingirwa na mapolisi lukuki waliokuja kuchunguza mauaji yaliyotokea ndani ya nyumba hiyo.
Kachero alipotoka nyumbani kwa Dr.Muganyizi, akawa hajui anaelekea wapi maana hata eneo alilokuwepo alikuwa halijui linaitwaje kutokana ugeni wake. Kama ujuavyo "kuku mgeni hakosi kamba mguuni". Lakini akafanya haraka kuondoka eneo lile asije kukutwa na polisi akapewa kesi ya mauaji ikawa habari ingine tena.
Akatembea kwa muda wa kama robo saa kwa miguu. Akiwa anakata mitaa usiku huo, akakutana na "taksi bubu" moja inapiga tripu za mitaani. Akafanya maamuzi ya kuisimamisha kwa kuipungia mkono. Dereva yule akatii amri na kuisimamisha gari yake.
Alichomwambia dereva taksi yule ni kitu kimoja tu, apelekwe Nautilus Hoteli. Akafikishwa salama salimini hapo hotelini na ile taksi. Kabla hajashuka kwenye taksi bubu, akamuuliza dereva taksi, "wapi naweza kupata sehemu nzuri ya kulala lakini ya gharama ya kawaida hapa Naitilus hoteli ni matawi ya juu sana sipawezi" akadanganya wakati alikuwa na pesa sufufu za kumuwezesha kulala hata Hoteli ya nyota 5 hata kwa muda wa mwaka mzima.
Lengo lilikuwa ni kutopoteza muda na kutafuta sehemu ya haraka ya kulala ili asubuhi ikifika ajue anajipanga vipi kuwakabili mabaradhuli wa Alfredo. Haraka haraka dereva yule akajibu, "nenda "Pemba Magic Lodge" ipo kama kilometa 3 kutokea ufukwe wa Wimbi hapo ni sehemu tulivu huwezi kukosa nafasi usiku huu" alimalizia maelezo yake dereva taksi akitumia ulimi wake wa ulimbo kumnasa Kachero mtegoni.
Akalipa pesa aliyotajiwa akaingia ndani ya Nautilus Hoteli kuchukua gari yake ya kazi 'Volvo s60' aliyoacha maegesho ya magari tokea saa 3:05 usiku alipowasili eneo hilo. Gari ilikuwa imechafuka matope ya barabarani halitamaniki hata kuliangalia.
Alipolisogelea gari yake akatabasamu kwa jinsi ilivyofanikisha salama safari yake ya kumtoa Montepuez mpaka Pemba kwa muda mfupi sana, akamsifu kimoyomoyo Komandoo "JS" kwa kumchagulia gari lenye ufanisi mkubwa.
Akaingia ndani ya gari akawasha gari huku anaitafuta ilipo 'Pemba Magic Lodge' kwa kutumia mtandao wa simu yake ya mkononi, akarekebisha GPS yake kwenye simu ikawa inamuelekeza barabara za kupita mpaka kumuwezesha kufika karibu na ilipo 'Pemba Magic Lodge' ndani ya nusu saa tu kutokea Nautilus Hoteli.
Akiwa ndani ya gari bado hajang'oa nanga, akawasha Kompyuta yake mpakato kwa ajili ya kutuma taarifa ofisini za kuhusu Dr.Muganyizi. Taarifa aliyotuma ilieleza kuwa Daktari anatafutwa kwa udi na uvumba ili auliwe na Mafioso wa Cabo-Delgado, hivyo azuiwe asirudi kwanza nchini Msumbiji, asalie Tanzania mpaka hali ya usalama wake itakavyotengamaa.
Pia ahojiwe haraka ili kufahamu ni watu gani walikuwa wanahitaji kupewa tenda ya ujenzi wa barabara katika mradi wa "PEMOVACHA", na apewe ulinzi madhubuti yeye na familia yake.
Ikiwezekana alipendekeza wapelekwe mafichoni kwenye nyumba maalumu za usalama wa taifa 'safehouse' kuhofia mtandao mpana wa Alfredo kuwanyakua. Baada ya kutuma taarifa hiyo nyeti akazima kompyuta yake akahifadhi vizuri vifaa vyake muhimu kwenye sanduku dogo lililopo chini ya miguu ya kukanyagia breki.
Safari yake fupi ya kuelekea 'Pemba Magic Lodge' kwa ajili ya kulaza mbavu zake ikaanzaa, ili kesho yake aendeleze libeneke lake la kuwatafuta mahasimu zake. Baada ya muda wa nusu saa akawasili kwenye jengo moja jirani na Pemba Magic Lodge. Hisia zake hazikumtuma kabisa kuegesha gari lake hapo kwenye nyumba ya wageni. Akaamua kutii hisia zake bila kupingana nazo. Akafunga vizuri gari lake akashuka na kamzigo chake cha nguo chache.
Alichokuwa hajui Kachero Manu ni kuwa ile "taksi bubu" iliyombeba maeneo ya nyumbani kwa Dr.Muganyizi, ilikuwa ni ya mmoja wa wakala wa Inspekta Jenerali Mark. Baada ya Mark kufanikiwa kumtoroka Kachero nyumbani kwa Dr.Muganyizi alitoa taarifa kwa wakubwa wake juu ya ujio wa Kachero Manu katika Mji wa Pemba, na namna alivyopambana nae kindakindaki nyumbani kwa Dr.Muganyizi.
Ikapangwa mikakati kabambe ya kumkamata kupitia 'taksi bubu' na nyumba za kulala wageni zote usiku huo. Pia ulinzi wa barabarani uliimarishwa vilivyo ili asiweze kuwatoroka tena. Zikasambazwa 'taksi bubu' zaidi ya 20 usiku ule zikijifanya zinatoa huduma kwa watembea kwa miguu usiku ule.
Yule dereva alivyomuacha Kachero Manu pale nje ya Naitilus Hoteli alipeleka taarifa moja kwa moja juu ya Kachero Manu kuwa atafikia 'Pemba Magic Lodge'. Hivyo hiyo ikachaguliwa kuwa ni sehemu muafaka kufanyia Umafia wao usiku ule.
Kingine kilichompa uhakika dereva taksi juu ya

Alichokuwa hajui Kachero Manu ni kuwa ile "taksi bubu" iliyombeba maeneo ya nyumbani kwa Dr.Muganyizi, ilikuwa ni ya mmoja wa wakala wa Inspekta Jenerali Mark. Baada ya Mark kufanikiwa kumtoroka Kachero nyumbani kwa Dr.Muganyizi alitoa taarifa kwa wakubwa wake juu ya ujio wa Kachero Manu katika Mji wa Pemba, na namna alivyopambana nae kindakindaki nyumbani kwa Dr.Muganyizi.
Ikapangwa mikakati kabambe ya kumkamata kupitia 'taksi bubu' na nyumba za kulala wageni zote usiku huo. Pia ulinzi wa barabarani uliimarishwa vilivyo ili asiweze kuwatoroka tena. Zikasambazwa 'taksi bubu' zaidi ya 20 usiku ule zikijifanya zinatoa huduma kwa watembea kwa miguu usiku ule.
Yule dereva alivyomuacha Kachero Manu pale nje ya Naitilus Hoteli alipeleka taarifa moja kwa moja juu ya Kachero Manu kuwa atafikia 'Pemba Magic Lodge'. Hivyo hiyo ikachaguliwa kuwa ni sehemu muafaka kufanyia Umafia wao usiku ule.
Kingine kilichompa uhakika dereva taksi juu ya mtu aliyembeba ndio anayetafutwa ni matone ya damu kwenye fulana ya Kachero Manu upande wa bega lake la kushoto. Matone yalitokana na makonde mawili ya kona ya mdomo aliyopigwa na Inspekta Jenerali Mark Noble wakati wa mapigano nyumbani kwa Dr.Muganyizi. Sasa wakati dereva kawasha taa ya gari kupokea malipo yake akaona damu damu. Akajua huyu ndio mlengwa anayesakwa na akina Mark.
Hivyo ujio wa Kachero Manu pale 'Pemba Magic Lodge' ulikuwa unafahamika tayari. Alipofika tu kuulizia chumba cha kulala, aliambiwa vyumba vimejaa ila kimebaki chumba kimoja tu. "Una bahati sana kaka yangu kimebaki kimoja chumba namba "4A" tena kilishawekwa oda ila hakutokea huyo mtu mpaka saa 6:00 usiku, ndio maana tunakiuza tu sasa..!" alisema msichana ambaye ni mhudumu wa mapokezi ya wageni kwa sauti nyororo yenye kuonyesha imebeba ukweli ndani yake huku uso wake umevaa bashasha mwanana.
"Nipe hicho hicho, nachohitaji ni kupumzika usiku huu, kama sitokipenda kesho Inshallah utanibadilishia chumba...!" alisema huku akiwa amelifumbata kwa mkono wa kushoto begi lake dogo lenye nguo zake huku vifaa vyake muhimu vyote vya kazi akiwa ameviacha kwenye gari aliyoamua kuiacha kwenye maegesho ya jengo la maonyesho ya sinema lililopo takribani meta 200 kutokea 'Pemba Magic Lodge'. Ambapo hapo alipoliacha kulikuwa na magari kadhaa yaliyoegeshwa kwenye eneo hilo ya watu wanaoangalia burudani ya filamu usiku huo.
Aliamua kufanya hivyo ili ayasome vizuri mazingira ya eneo analotaka kufikia ili kama atapata matatizo ajue njia za kutorokea kirahisi. Alipokabidhiwa funguo na kuelekezwa chumba kilipo huku akimpa mgongo mhudumu, yule msichana mshirika wa mabaradhuli wa Alfredo akaunda tabasamu la ushindi katika sura yake akajua wameshamkamata mtuhumiwa wao kiulaini sana, bila rabsha zozote.
Alipofungua tu chumba chake, kabla hata hajafanikiwa kuwasha taa, alihisi hewa ya chumba sio rafiki kabisa, ni nzito sana. Alijiona anaanza kuishiwa nguvu akataka kurudi nyuma asiingie hobelahobela chumbani mume mpaka afanye taftishi kwanza. Lakini alikuwa ameshachelewa, alishtukiwa anapigwa na kitu kizito kwenye kisogo chake na kujikuta macho yake yanaingia giza zito na kujiona anazama kwenye shimo refu lisilofika mwisho. Akaanza kupiga kelele ili apate msaada wa haraka lakini sauti yake haitaki kutoka. Macho yake yakafumba na kupoteza fahamu pale pale.
Taarifa zilipofika za ujio wa Kachero Manu kwenye nyumba ya wageni ya "Pemba Magic Lodge" haraka haraka wakatumwa vijana wa kazi wakachague chumba watakachomshughulikia Kachero Manu.
Wakaingia na kupulizia gesi inaitwa "Methoxyflurane" kwa jina la utani inaitwa "knockout gas" (KO-Gas) ni gesi ambayo ukivuta tu hapo hapo unajiskia kulala usingizi mzito.
Kwa kuijua zaidi hii ndio gesi waliyoitumia Makachero wa Shirika la Kijasusi la Urusi (FSB) waliyoitumia kuwakamata magaidi waliowateka watu zaidi ya 1,000 katika Ukumbi wa maonyesho wa Dubrovka Theatre Jijini Moscow mwaka 2002. Mpaka ilipopulizwa hii kemikali ndio mateka wakafanikiwa kuokolewa.
Watekaji wa Kachero Manu walivyopulizia gesi hiyo wakakifunga vizuri chumba namba "4A" kisha wakaingia chumba namba "4B" ambacho kilikuwa kinatazamana na chumba cha mtego wa Kachero. Alipofungua tu mlango wake nao wakatoka na kiroba cha kokoto cha ujazo wa kilo zisizopungua 60 wakampiga nacho kisogoni akapoteza fahamu, wakaondoka nae.
Afya ya Kachero Manu haikuwa afya mgogoro ndio maana alipoteza fahamu tu, hakuaga dunia vinginevyo mimi na wewe kama tungepigwa na kiroba chenye ujazo huo tungekuwa hivi sasa tupo kaburini zamani sana tunasubiri siku ya kupulizwa parapanda la hukumu na Malaika Israfili huko jongomeo.


SURA YA KUMI NA MOJA
Kachero Manu ndani ya handaki la mateso
Kachero Manu alizinduka saa 10:30 Alasiri ya siku iliyofuata akiwa hafahamu mahali alipo. Alikuwa katika mghafala mkubwa wa kutokumbuka namna alivyofika hapo kitandani alipolazwa. Alikuwa ametimbika vilivyo, uso wote umevimba kutokana na tashdidi ya vipigo toka kwa wajuba waliomteka.
Licha ya kuzimia mule chumbani, walikuwa na hasira nae wakawa wanampiga kama vile yupo mzima na fahamu zake. Walichukizwa sana na kitendo chake cha kumuwinda Inspekta Jenerali Mark Noble na kuhatarisha uhai wake, mtu mahashumu sana Jimboni Cabo-Delgado.
Alijikuta yupo juu ya kitanda kidogo cha chuma na springi huku akiwa amefungwa miguu na mkono wake wa kulia kwa kamba huku akiwa yupo uchi wa mnyama kama siku alivyokuja duniani kutoka kwenye mfuko wa uzazi wa mama yake. Mkono wake wa kulia ukiwa umetundukiwa dripu la kuongeza damu mwilini na mkono wake wa kushoto umefungwa pingu. Kilikuwa ni chumba kidogo chenye uwezo wa kukaa kitandaa cha futi nne kwa sita na kuingia watu watatu mpaka wanne.
Kilikuwa ni chumba chenye mwangaza hafifu sana huku madirisha yake madogo matatu kama matundu ya vyoo vya uswahilini yakiwa juu kabisa hivyo kukisababishia chumba kukosa nuru ya kutosha. Alipofumbua macho tu akaanza kujiuliza "amefikaje hapo?".
Alipoanza kuvuta kumbukumbu namna alivyofika hapo, maumivu ya kichwa makali yakaanza kutawala katika mwili wake, akaamua afumbe macho tena. Ghafla akawa anasikia michakato ya nyayo za viatu vya kike vinakaribia kwenye mlango wa chumba chake. Akafumbua macho na kuangalia geti dogo la chuma, lililo kuu kuu lenye kutu.
Akasikia mgombano wa funguo na kufuli la geti wa kama sekunde takribani 40 kisha geti likafunguka akafumba macho kidogo huku anachungulia kwa jicho pembe. Akaingia ndani mwanamke mrefu wa rika la takribani si chini ya miaka 37, mrembo wa shani, ambaye mwanaume mwenye jicho la nje lazima achepuke nae akipata fursa.
Ni mwanamke ambaye hutegemei afanye kazi za ofisini labda awe Daktari au Mhasibu, bali unategemea awe anafanya shughuli za mitindo na ulimbwende. Aliingia akiwa amevaa shingoni mwake kifaa cha kupimia mapigo ya moyo ya mgonjwa na koti jeupe huku amebeba trei mkononi. Alivyokaribia kitandani akamtikisa Kachero Manu kwa kutumia mikono laini ya kike.
Kachero Manu akasisimkwa mwili na kupandwa na mihemko ya hamu ya kukumbatiana na mwanamke huyo. Akayapuuza mawazo hayo kisha akazuga kama ndio anaamka katika usingizi mzito. "Kunywa dawa za kupunguza maumivu" alisema yule Daktari kwa sauti ya upole na ukarimu huku akiwa anatabasamu.
Akaonyesha nje meno yake ya mbele, mazuri yaliyoacha mwanya, mpaka Kachero Manu akajiona kabisa anapata nafuu ya ghafla. Akatoa dawa kutoka kwenye trei ndogo nyeupe iliyokuwa na kikombe kichakavu cha bati kilichokuwa kinatoa harufu kali ya mkojo kuonyesha ni kikombe kilichochukuliwa chooni kikiwa na maji yake.
Akaitikia kwa kichwa kuonyesha kukubaliana na maelekezo ya Daktari yule mwanamke kisha akawekewa vidonge kwenye ulimi na kumeza vidonge vile vya maumivu kwa maji ya kikombe kichafu cha chooni kwa msaada wa Daktari. kwa mtindo wa kugugumia Kisha hapo hapo baada ya kumeza dawa, akafumba macho yake kuonyesha anahitaji mapumziko zaidi.
Dripu ya damu ilikuwa imebaki robo ujazo kuisha yote ili chupa ibaki tupu. Akasikia sauti ya viatu vya yule Daktari kuondoka huku anamchungulia kwa kupepesa macho, mpaka alipofika mlango akageuka kisha akamwambia "sasa umepata nafuu ulikuwa umezimia kwa zaidi ya saa zisizopungua 12, na ulipoteza damu nyingi sana hiyo ni chupa ya nne kuongezewa. Utakuja kuchukuliwa muda sio mrefu na "NACATANAS" ukahojiwe", alisema yule Daktari kwa sauti ya huzuni, Kisha akafungua geti akalifunga na kufuli akaondoka zake.
Sauti ya mlio wa viatu vya Daktari ikaanza kupotea masikio mwa Kachero Manu mpaka ikapotea kabisa. Akaanza kuvuta taswira kumbukizi ya namna alivyokamatwa. Akakumbuka mara ya mwisho alifika hadi kwenye nyumba ya kulala wageni na haikumbuki vizuri jina lake kisha akajishtukia yupo mikononi mwa maadui.: CABO DELGADO-PART 19




Sauti ya mlio wa viatu vya Daktari ikaanza kupotea masikio mwa Kachero Manu mpaka ikapotea kabisa. Akaanza kuvuta taswira kumbukizi ya namna alivyokamatwa. Akakumbuka mara ya mwisho alifika hadi kwenye nyumba ya kulala wageni na haikumbuki vizuri jina lake kisha akajishtukia yupo mikononi mwa maadui.
Akajilaumu namna alivyoshindwa kuchukua tahadhari ya kutosha na kuingia kichwa mchunga. Pia akaanza kujiuliza hao "NACATANAS" watakaokuja kumhoji ni akina nani hasa..!. Akajaribu kutikisa miguu yake kupima uimara wa kamba za miguuni ikawa ndio kama anaziongezea nguvu ya kuikamata vizuri miguu yake.
Akatulia kidogo kisha akapata wazo jipya la kuondosha dripu ya damu kisha atumie huo mkono kujifungua kamba aweze kujiokoa. Kabla hajaanza harakati zake hizo akasikia vishindo vya miguu ya watu wanakuja kwenye chumba chake, na giza lilianza kushitadi kwenye chumba chake ikabidi asitishe harakati zake hizo.
Alipoangaza macho juu ya dari akaanza kuona panya wakubwa wakubwa wanakimbizana kama vile wanacheza mchezo wa kitoto wa 'foriti' juu ya dari chakavu iliyojaa vumbi la toka mkoloni aondoshwe Msumbiji. Akatulizana kusubiri majaliwa yake toka kwa watekaji wake.
Ghafla baada ya kukurukakara za kufungua kufuli, ukafunguliwa mlango wakaingia watu wawili vipande vya watu. Sura zao ni za kunyata ambazo zinachukiza machoni kama ukibahatika kuwaangalia. Sura ambazo zimejaa makovu na majeraha mbalimbali ilyoshonwa kama nguo yenye viraka. Sura zao watu hao kama utamuonyesha picha zao mama mjamzito wa mimba changa ya wiki mbili tu itatoka mimba hiyo hapo hapo bila hata kutumia vidonge vya kuporomosha mimba na atalazwa hospitalini kwa kihoro.
Miili yao ilikuwa mikubwa vijana wa kileo wanaita "mwili nyumba", mmoja wapo ni mfupi, andunje kibushuti haswa jicho lake la kushoto chongo huku mguu wake mmoja wa kushoto anauvuta kwa mbali, kwa maana ni mfupi kuliko mwingine.
Na huyu mwingine ni mrefu sana kampita yule mcheza basketi wetu wa Tanzania anayetuwakilisha vyema Kimataifa "Hasheem Thabeet" kwa sentimeta chache sana.
Huku macho yao wote wawili yamepambwa kwa rangi nyekundu mithili ya nyanya iliyoivia shambani ikasuswa kuchumwa na mkulima akaachiwa ndege ajipocholee atakavyo. Hizo ni dalili ya kuonyesha ni wavutaji bangi wazuri tu.
Wote walivalia singlendi nyeusi kifuani zina maandishi meusi yameandikwa "NACATANAS" kuziba milima miwili mikubwa vifuani mwao. Fulana ambazo zilikuwa zinazoonyesha ukubwa wa matiti yao kutokana na ubebaji wa vyuma vizito na ukubwa wa lishe wanazokula.
Miguuni walikuwa wamevalia safari buti rangi ya kahawia. "Wewe mwanaharamu amka wakati wako umefika wa kufa kifo cha kijinga bila kujitetea, haupo Hotelini hapa..!" aliongea kwa kufoka yule baradhuli chongo ambaye anaitwa "Bob Chinanga", kumwambia Kachero Manu.
Huyu Bob-Chinanga na timu yake ndio waliotumwa na Inspekta Jenerali Mark Noble kwenda Kijijini Mahiwa kwenda kukata kichwa cha mama mzazi wa Kachero Manu baada ya kupewa taarifa za ujio wake na Bwana Andenga Kazimoto.
Huku yule mwingine mrefu ambaye anaitwa "Nanga Boy" ambaye hakuonekana kuwa ni mtu wa maneno mengi ya mkahawani ila ni mtu wa vitendo akawa anamfungua kamba za miguuni Kachero Manu. Mikono yake ilipogusa miguu ya Kachero Manu, Kachero alihisi kama ameguswa na chuma, kutokana na ukakamavu wa viganja vya mikono yake yule baradhuli.
Ilikuwa viganja vya mikono vimekomaa kama ubao utasema damu imefanya mgomo kutembelea vidole vyake vya mikono. Alipomaliza kumfungua kamba za miguuni, akahamia kufungua kamba ya mkono wa kushoto kisha akachomoa na kutupa pembeni dripu ya damu pembeni. Kisha akamfunga kitambaa cheusi usoni.
Hapo hapo Kachero Manu akaanza kupiga chafya mfululizo kutokana na vumbi pia kilikuwa kina harufu kali ya bangi. Halafu akamkwida Kachero Manu kwa kutumia ngozi ya tumboni akambeba begani mwake mzobemzobe kichwa chini mikono ya baradhuli "Nanga Boy" imekamatia chini ya mapaja akatoka nae nje ya chumba.
Kachero Manu hajui anapelekwa wapi na wajuba wale. Alichohisi ni kuwa walitembea hatua chache wakawa wanashuka chini ya ardhi kwenye ushoroba mwembamba na mteremko mkali. Kadri walivyokuwa wanashuka chini ndipo hali ya hewa ikaanza kubadilika kuwa nzito zaidi na kiza kikazidi kushitadi.
Kuna wakati anajigonga kwenye kiwambaza cha njia hiyo ya chini kwa chini huku wanaburudishwa na sauti za panya wanaokimbizana njiani kwenye giza lile na harufu ya kuchukiza kwenye pua zao. Waliposhuka kama mwendo wa dakika 20 kwenda chini akahisi wanapita njia yenye tope zito lililovunda.
Kichwa chake kinachoning'inia chini kuna wakati kinagusa kwenye tope lile lenye uvundo mzito wa harufu ya vitu vilivyooza kama mabaki ya chakula na maji machafu ya chooni. Kisha wakasimama mahali fulani.
Likafunguliwa lango kisha akatupwa kwenye chumba kilichoonyesha sakafu yake ni ya kokoto ngumu kutokana na kuumizwa na vijiwe hivyo. Alipotua sakafuni akaanza kunusa harufu ya mikojo yenye harufu ya pombe za kienyeji huku anaugulia maumivu ya mgongo.
Akiwa hajui nini cha kufanya akabebwa tena na kuweka kwenye kiti cha chuma kisha mikono yake ikafungwa juu ya bomba kama za kuning'iniza nyama buchani na miguu yake ikafungwa chini ya kiti, kisha akafunguliwa kitambaa alichofungwa usoni. Akatambua sasa yupo kwenye handaki lenye mwanga hafifu sana limejaa dhana mbalimbali za mateso.
Kulikuwa na mashoka na mapanga yaliyogandana damu na mabaki ya ubongo wa mwanadamu. Kulikuwa na mabomba ya sindano za kuchomea ng'ombe na chupa mbalimbali za dawa zikiwa zimetawanyika chini, pia kulikuwa na viti vya mateso vya umeme na minyororo ya kufunga na kufungua kwa kufuli. Kilikuwa ni chumba kinaweza kuingiza watu 10 kwa pamoja bila kubanana sana.
Ukutani kuliandikwa maneno mengi mengi ya lugha ya kireno yenye lengo la kuleta vitisho vya kisaikolojia. Mfano kulikuwa na maneno kama "Matar" likiwa na maana ya "fanya mauaji", pia neno kama "desgraçado" likimaanisha "mtoto wa haramu" na maneno mengi ambayo hakuwa anafahamu maana yake.
Ila aliona neno moja limeandikwa ukutani "Gorongosa Camp". Akawa anajiuliza "hili neno "Gorongosa" nimeliona wapi?". Alipovuta kumbukumbu zake vizuri akakumbuka alilisoma hilo jina kwenye nyaraka za siri la faili rangi nyeusi alilopewa Ofisini Jijini Dar es Salaam.
Akakumbuka ilikuwa ni jina la moja ya kambi ya mateso ya FRELIMO waliyokuwa wanaitumia wakati wanapambana katika vita ya wenyewe kwa wenyewe na kundi la RENAMO. Ndani ya hiyo kambi hiyo ya Gorongosa enzi hizo za vita kulikuwa na kila aina ya ukatili na mateso, akatambua yupo kwenye eneo la hatari sana.
"Kama eneo hili linafananishwa na kambi ya Gorongosa nitapona kweli? " alijiuliza nafsini mwake Kachero Manu huku hofu ikianza kutawala nafsini mwake. "Jina lako kamili ni nani na umekuja kufanya nini"? alishtukizwa na swali kutoka kwa Bob Chinanga huku Kachero akiwa kwenye lindi la mawazo.
"Mimi naitwa "Hassan Ibn Hussein" nafanya kazi kama mtafiti wa mambo ya kale kutoka Zanzibar, Tanzania Visiwani" alijibu kwa kujiamini huku amemtumbulia macho. "Hatujawahi kusumbuliwa ndani ya hii kambi na kidudu mtu wa aina yoyote sasa tutakufunza namna ya kusema ukweli, bila kushinikizwa" alisema yule baradhuli mrefu "Nanga Boy" huku akijiweka sawa kuanza kushusha kipigo kitakatifu.
Aliendelea kusema "Unajifanya mkaidi, kichwa mchungu ngoja tukutie adabu...!" kisha akamchapa kibao kimoja cha kelbu kwenye shavu la kushoto. Kachero Manu aliona nyota nyota nyingi sana usoni mwake na mwezi mchanga mwandamo mmoja, akapiga kelele za maumivu kama abiria aliyesahau mzigo kwenye daladala lenye haraka na lililojaza abiria la kuelekea Mbagala.
Kisha akashtukia nyundo nzito ya kupasulia mawe imetua utosini, hakuweza kuikwepa kwa sababu macho alikuwa amefumba kutokana na kibao kile cha shavuni. Nyundo ile ilisababisha damu ianze kububujika kwa nguvu, kisha yule baradhuli mfupi akawasha kiberiti akamwagia ndevu za Kachero Manu mafuta ya taa kisha akawasha moto zilipoanza kuungua ndevu, akawa anapiga kelele kwa maumivu makali sana huku kinywa kipo wazi hapo hapo yule mfupi akaingiza koleo kinywani mwa Kachero Manu akakamata jino moja la juu akaanza kuling'ang'ania ndani ya dakika moja akawa ameng'oa jino moja bila ganzi huku damu zinamwagika ovyo usoni mwake.
Huku yule mwingine anamchapa mgongoni na mkia wa samaki taa. Mkia ambao ukichapwa nao mwilini miba zake zinanasa kwenye ngozi ukivuta unachana ngozi na damu zinamwagika. Mateso na maumivu ya Kachero Manu yalikuwa makubwa, hayasemeki na wala hayaelezeki. Kabla hajapewa nafasi ya kupumua, kuugulia maumivu akashtukia anapigwa ngumi mfululizo za tumboni kama 6 hivi akajikuta anatoa mashuzi mfululizo bila kizuizi.
Ngumi ambazo kama ukipigwa mimi na wewe tusio na mazoezi, ambao mazoezi yetu ni kupiga matonge tu kwenye sahani ya chakula unaweza kutapika vipande vya utumbo wako na kuaga dunia bila kuchelewa. Akaanza kutapika nyongo hasa ukikumbuka alikula tokea jana yake jioni. Alikuwa sasa ametimiza saa 13 bila kutia chochote kitu tumboni.
Kisha akaanza kuhisi macho yake kuwa mazito, kwa mbali akaskia kengele imebonyezwa, kisha ndani ya dakika 3 wakaingia vijana wawili wakamfungua kwenye kiti na kumfunga tena kamba vizuri kisha wakambeba kama maiti kumtoa mule kwenye chumba cha mateso. Alichofanikiwa kusikia kwa mbali ni maneno ya kuwa "kamtupeni kwenye selo kubwa" kisha akapoteza fahamu kabisa.



SURA YA KUMI NA MBILI
"Mjue Daktari wa handaki la mateso"
Moja ya kazi ambayo ina miiko yake madhubuti hapa duniani ukiachilia kazi ya Ualimu basi ni kazi ya Udaktari. Ni kazi ambayo siku ya mwisho ya kuhitimu elimu hiyo, madaktari hula kiapo cha utii wa maadili ya kazi yao.
Kiapo ambacho huwa kinawafunga kutenda kazi zao kwa kufuata weledi wa kazi yao hiyo kwa kuwataka kuwahudumia wagonjwa wao bila ubaguzi, wawe na moyo wa huruma na uvumilivu na kutanguliza kuokoa uhai wa wagonjwa wao kwa gharama yoyote.
Ni kazi ya wito ambayo hautakiwi kutanguliza maslahi yako binafsi, kazi ya udaktari ni kama vile umechagua kifo ni bora kwako kuliko uhai, ndio maana ukitokea mlipuko wa ugonjwa wowote wa hatari wa kuambukiza kama "Ebola", "Covid-19" na mengineyo huwezi kusikia madaktari wametoka nduki na kuwatelekeza wagonjwa wao hospitalini.
Sasa ukiona mtu ni daktari kama alivyo Dr.Anabella anashirikiana na wahalifu kwa kutoa huduma kwa wagonjwa na amepewa Cheo kama "Daktari wa Mateso", kengele ya tahadhari lazima ilie kichwani mwako.
Lazima utajiuliza zaidi ya mara mbili, "huyu daktari anaijua kweli miiko ya kazi yake au anatanguliza mbele maslahi yake binafsi au nini kimemsibu mpaka anashirikiana na wahalifu?". Lakini kumbe mazonge na maswahibu tunayokumbana hapa duniani huwa kuna wakati yanawabadilisha watu wema kuwa waovu na waovu kuwa wema.
Mfano wapo watu hapo zamani walikuwa majambazi, walawiti, wanyang'anyi lakini wakarejea kumtumikia Mungu wao baada ya kupatwa na ajali, au magonjwa yasiyotibika. Na wapo watu ambao zamani walikuwa swalihina sana, kwenye nyumba za ibada hawakosekani, wanashinda mahospitalini kuangalia wagonjwa, wanatoa zaka na sadaka kila wakati lakini misukosuko ya walimwengu iliyowasibu ikawabadilisha na kuwafanya wawe watu waovu maishani, Ibilisi mwenyewe ambaye ni Shetani Mkuu anasubiri nyuma.
Nakama na misukosuko aliyokumbana nao maishani mwake, Dr.Anabella pamoja na familia yake ndio iliyomsababisha ajiunge na kundi hili ovu na katili la NACATANAS linaloongozwa na Inspekta Jenerali Mark Noble.
Dr."Anabella Julio" ni mzaliwa wa kijiji cha Nthoro katika wilaya ya Montepuez, nchini Msumbiji. Alizaliwa mwaka 1979 miaka minne tokea kupatikana uhuru wa Msumbiji. Alimaliza masomo yake ya udaktari wa binadamu katika chuo kikuu cha "The Eduardo Mondlane University" kilichopo ndani ya viunga vya Jiji la Maputo, nchini Msumbiji. Hicho ndio Chuo Kikuu kikubwa zaidi nchini Msumbiji kikiwa na uwezo wa kudahili wanafunzi takribani elfu 40 katika kila mwaka wa masomo.
Baba yake mzazi, Mzee "Julio Munambo" alikuwa ni mkulima mdogo wa mihogo na korosho. Ni Mzee ambaye amewahi kuishi Tanzania kwa miaka 13 mtawalia katika kambi ya wakimbizi ya Rutamba mkoani Lindi. Hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 1971-1984.
Alitoroka Msumbiji kama mkimbizi na kuja kuishi Tanzania, kipindi cha vita baina ya Wareno na Wapigania Uhuru wa FRELIMO. Baada ya uhuru wa Msumbiji uliopatikana mwaka 1975, Mzee Mnambo alikuwa ana mipango ya kurudi nyumbani akalijenge Taifa lake changa. Ila vilipoibuka vita ya wenyewe kwa wenyewe baada ya Uhuru kati ya vyama hasimu nchini Msumbiji, chama cha RENAMO na FRELIMO akakata shauri la kuendelea kubakia Tanzania mpaka amani ya kweli ipatikane nchini Msumbiji.
Dr.Anabella, kifungua mimba wa Mzee Mnambo, akawa ni mhanga wa sarakasi zisizokoma baina ya FRELIMO na RENAMO. Akajikuta anazaliwa na kukulia ukimbizini nchini Tanzania bila hata kuwahi kunusa harufu ya udongo wa nchi yake ya asili. Sarakasi ambazo zilizaa Mkataba wa NKOMAT na kusababisha Dr.Anabella anapelekwa nchini Msumbiji na baba yake kwa mara ya kwanza katika maisha yake.
Chama cha RENAMO kiliundwa mwaka 1975 kilikuwa kikipinga sera za ukomonisti za chama tawala cha FRELIMO. Chama hiki kilianzishwa kwa msaada wa serikali ya wazungu wa Rhodesia (Zimbabwe) na serikali ya makaburu wa Afrika ya Kusini.
Lengo la wazungu kuanzisha na kuipa misaada RENAMO ilikuwa ni kuivunja nguvu serikali ya Msumbiji inayoongozwa na FRELIMO kuwasaidia wapigania uhuru wa Afrika ya kusini na Zimbabwe. Baada ya uhuru yakaibuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji kati ya chama cha FRELIMO na RENAMO, mapigano ambayo yalikuwa ni janga la kimataifa kwa wapenda amani na uhuru wote duniani.
Miundo mbinu kama shule, vyuo, hospitali na barabara ziliharibiwa, wananchi waliuliwa na kuchinjwa ovyo kama kuku, huku wengine wakiambulia ulemavu wa maisha na maelfu kwa maelfu ya wakazi wa Msumbiji hasa waishio kaskazini walitorokea nchini Tanzania kama wakimbizi.
Duniani tumepata kuona na kusikia vikundi mbalimbali vya waasi ambao ni wakatili kama Talebani wa kule nchini Afghanistani, au Al-Shabaab wa kule Somalia na makundi mengineyo lakini hawafikii hata robo ya ukatili wa askari wa RENAMO, waasi hao walikuwa kiboko yao.
Katika baadhi ya simulizi za kuelezea ukatili wao zinasema ulikuwa ukikamatwa na waasi wa RENAMO kama ukiwa adui yao unaulizwa swali kwa lugha ya Kimakonde "ulambela kununa au kusunala"? (Unachagua kununa au kucheka). Ukichagua kununa unatobolewa mdomo wa juu na wa chini kisha unafungwa na kufuli, ukichagua kucheka unakatwa midomo ya juu na chini.
FRELIMO ilifanya makosa kadhaa ya kiufundi yaliyowafanya wakazi wa upande wa Kaskazini mwa nchi kuiunga mkono RENAMO licha ya kwamba walitambua kuwa sio kundi sahihi kwao. Moja ya makosa yaliyofanywa na FRELIMO baada ya nchi kupata uhuru ni kunyakua nafasi nyingi za juu za uongozi na kuwapatia watu wa kusini mwa Msumbiji, hivyo watu wa kaskazini kujiona kama ni watoto wa kambo. Wametengwa ndani ya nchi yao waliyoipigania uhuru wake kwa kuvuja jasho na damu, kwa kupoteza uhai na mali zao.
Pia sera za Ukomonisti zilitekelezwa vibaya na baadhi ya viongozi wa FRELIMO. Mpaka ikafikia hatua baadhi yao kuamuru makanisa na misikiti ifungwe kwa kigezo cha kwamba Msumbiji ni nchi ya kisekula isiyo na dini yoyote. Maelfu ya viongozi wa dini walinyanyaswa na kuteswa mpaka wengineo kuikimbia nchi yao ya Msumbiji.
Zipo taarifa ambazo zinaenezwa sana na wafuasi wa RENAMO kuwa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa FRELIMO alipata kuingia kanisani siku moja na nyundo yake mkononi inapepea hewani kama kishada. Kwa kutumia nyundo ile akavunjavunja 'Altare' siku ya Ibada ya Jumapili huku waumini wamejaa pomoni kanisani na kutangaza Msumbiji hairuhusu ibada zozote.
Mapigano kati ya makundi haya hasimu, FRELIMO na RENAMO yalizidi kushika moto zaidi mara baada ya Maafisa wa usalama wa serikali ya Msumbiji kumuua Bwana "André Matsangaissa" kiongozi mkuu wa RENAMO. Bwana Matsangaissa mwanzoni alijiunga na FRELIMO mwaka 1972 kisha baada ya uhuru mwaka 1975 aliajiriwa kama mwanajeshi akapewa cheo cha "Mfawidhi Mkuu wa Kikosi" (quartermaster).
Kituo chake cha kazi kilikuwa maeneo ya Dondo karibu na Beira, akihusika na manunuzi, uhifadhi na ugawaji wa vifaa vya jeshi. Baada ya muda mfupi tu akafukuzwa kazi akituhumiwa kwa wizi kisha akapelekwa jela ya Gorongosa.
Sasa mwaka 1977 kambi ya Gorongosa ikavamiwa na wazungu wa Rhodesia wakamtorosha Bwana "André Matsangaissa" wakaenda nae Rhodesia baadae akatangazwa kama mkuu wa kikundi cha RENAMO.
Kwa hiyo FRELIMO wakawa wanapambana na mtu ambaye anawajua nje ndani katika medani zao za kivita, ni kama kinyago walichokichonga wenyewe kinawatisha sasa.
Amani ya kwanza kati ya FRELIMO na RENAMO ilianza kupatikana tarehe 16 mwezi Machi mwaka 1984 kuliposainiwa mkataba maarufu unaitwa "NKOMAT ACCORD". Mkataba huu ulikuwa ni kati ya serikali ya Msumbiji ikiwakilishwa na Rais Samora Machel na Waziri Mkuu wa serikali ya kikaburu ya Afrika ya Kusini kipindi hicho Bwana P. W. Botha.
Huyu Kaburu Botha ndiye ambaye wazalendo weusi wa Afrika ya kusini wanamuita kwa jina la utani la "The great crocodile". Ile miaka ambayo watoto wa shule wanapigwa risasi hadharani 1976 huko Afrika ya kusini, na mpaka filamu maarufu ya Sarafina ikaigiza tukio hilo la kinyama, huyu Bwana mkubwa Botha alikuwa ndio Waziri wa ulinzi na baadae kuanzia mwaka 1984-1989 alikuja kuwa Rais wa Afrika ya kusini.
Huyu ndio ndio mhandisi aliyeufuma na kuusuka vilivyo mkataba wa NKOMAT. Mkataba huo uliweka matakwa ya serikali ya Msumbiji kuacha kusaidia wapigania uhuru wa Afrika ya kusini wa chama cha "African National Congress"(ANC), pia uliwataka serikali ya makaburu kuacha kuwapa msaada wa vifaa na pesa chama cha upinzani cha RENAMO.
Mkataba huu ulikuwa ni pigo takatifu kwa wapigania uhuru wa ANC na nchi zote zilizokuwa zinazosaidia kupatikana kwa uhuru wa Afrika ya kusini.
Siku ya kusainiwa kwa mkataba huo, Marais wote wa SADC kuanzia Mwalimu Nyerere, Keneth Kaunda na wenzao walisusia mkataba huu hawakutokea kwenye sherehe licha ya kwamba Rais wa Msumbiji Bwana Samora aliwapa mualiko.
Waliona ni kama vile Rais Samora amewasaliti, amekuwa mbinafsi kwa kujali maslahi yake kwa kuamua kukaa meza moja na adui yake wanafaidi mapochopocho na mahanjumati wakati wapigania uhuru wenzao wa nchini Afrika ya Kusini wanateseka.
Baada ya mkataba wa NKOMAT kusainiwa, Mzee "Julio Martine Munambo", baba wa Dr.Anabella aliamua kurejea nchini Msumbij. Akiambatana na mkewe, Binti yake mkubwa, Anabella, na wadogo zake Anabella wakiume wawili, Munambo Jr na Athanas. Hawa watoto wote walikuwa wanarejea Msumbiji kwa mara ya kwanza, kwa maana walizaliwa katika kambi ya wakimbizi hawaijui hata Msumbiji inafananaje kimuonekano.
Mzee Julio Munambo akaanza maisha mapya katika kijiji chao cha asili ya mababu zake cha "Nthoro".
Kipindi hicho kulikuwa na watu wachache vijijini, wengi wao wakiwa wamekimbia kutokana na mfumo ulioachwa na RENAMO vijijini unaoitwa "Gandira". Mfumo huo ulitaka vijiji viwe vinazalisha chakula kwa ajili ya wapiganaji wa RENAMO, pia wanakijiji wahusike kusafirisha bidhaa na silaha za RENAMO na pia wanawake wa kijiji baadhi yao wawe ni watumwa wa kingono wa wanajeshi wa RENAMO.
Kipindi hicho cha miaka ya 1980's chama cha RENAMO kilikuwa kina nguvu zaidi katika Majimbo ya Kaskazini na Mashariki kuliko hata FRELIMO. Sasa huu mfumo wa Gandira ulikuwa unasababisha baadhi ya wanakijiji wakimbilie tena Tanzania hasa msimu wa kilimo kwenda kufanya vibarua katika mashamba ya wanakijiji wa mpakani ili wafaidike na jasho lao.
Watanzania walikuwa wakiwapata hawa vibarua wanashangilia maana "Wamakonde" wa Msumbiji kwa uhodari wao wa kulima waliwapa lakabu ya "trekta", hawachoki kwa haraka wakiingia shambani.
Katika mazingira magumu hayo hayo aliyoyakuta Mzee Julio alihamasisha na kuamsha ari mpya na nguvu mpya kwa wanakijiji wenzake akiwaelekeza namna nzuri ya kuboresha maisha yao na kuwa bora kupitia kilimo. Hasa ukichukulia ametoka kuishi maisha ya kambini ambayo ni maisha ya nidhamu na utiifu kama shuleni.
Pia alijifunza mfumo wa uendeshaji wa vijiji vya Ujamaa na Kujitegemea kutoka Tanzania alipoishi kwa muda mrefu hivyo mpaka kufika mwaka 1992 wakati wa mkataba wa kusitisha mapigano ya yenyewe kwa wenyewe kati ya FRELIMO na RENAMO unasainiwa. Ndani ya muda mfupi kwa hamasa na ushawishi wa Mzee Julio Munambo, kijiji cha "Nthoro" kikawa ni kijiji cha kupigiwa mfano kwa katika namna ya kujiletea maendeleo yao, kati ya vijiji vyote vya Jimbo la Cabo-Delgado.
Kwa umoja wao walijenga shule ya msingi hapo hapo kijiji kwao, shule ambayo ndio Dr.Anabella alianzia hapo darasa la kwanza mwaka 1989 na kumaliza 1995. Mwanzoni masomo yalikuwa magumu kwa Dr.Anabella kwa sababu yalikuwa yanafundishwa kwa lugha ya Kireno na sio kwa lugha yake ya asili ya kimakonde, lakini baada ya muda mfupi alikuwa anaongea kireno kizuri kana kwamba kazaliwa katika viunga vya "Lisbon" huko nchini Ureno.
Alipomaliza elimu yake ya msingi akafaulu kwenda kusoma sekondari katika shule ya sekondari Montepuez. Alisoma hapo kwa muda wa miaka mitano mfululizo. Kwa mfumo wa elimu ya nchi ya Msumbiji, elimu ya sekondari imegawanywa mafungu mawili, kidato cha kwanza mpaka cha tatu mwisho halafu ukifaulu unaendelea kidato cha tano na cha sita kwa muda wa miaka miwili.
Alivyomaliza sekondari alifaulu vizuri sana, alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi kumi bora kwa jimbo zima la Cabo-Delgado na akiwa ni wa kwanza katika wilaya yake ya Montepuez. Siku ya kutoka kwa matokeo na kujulikana kuwa binti yao mpendwa Anabella kachaguliwa Chuo kikuu bora kuliko vyote nchini Msumbiji cha 'Eduardo Mondlane' kusomea Shahada ya Udaktari wa Binadamu "Doctor of Medicine" ilikuwa ni hoihoi, shangwe, nderemo, vigeregere na vifijo kijijini kizima.
Walimuona kama ndio mkombozi wao kielimu atakayekuja kuwatoa kwenye utumwa wa umasikini uliotopea na kuwaletea maisha bora kwa kutumia kipawa chake cha elimu.
Furaha ya kusomea udaktari Dr. Anabella ilitumbukia nyongo kuanzia mwaka 2008 akiwa ndio yupo mwaka wa mwisho wa masomo yake. Hiyo ni baada ya kuwa wazazi yake hawapatikani mara kwa mara kwenye simu ya mkononi kama alivyozoea kuwasiliana nao. Na siku akibahatika kuongea na baba yake basi alikuwa anaonekana ni kama mtu mwenye wasiwasi mwingi. Kama vile kulikuwa kuna kitu wanamficha binti yao wakihofia wasije wakamchanganya kwenye masomo yake.
Subira yavuta heri, Aliweka nia thabiti moyoni mwake, Dr. Anabella kuwa akimaliza masomo yake ataenda kijijini kwao kiguu na njia kutafiti nini kinachowasibu wazazi wake haswa. Na kama akikuta kuna matatizo yasiyotatulika kwa haraka itabidi awachukue wazazi wake na kwenda kuishi nao katika Jiji la Maputo. Huko ndio alipanga aendeshe maisha yake baada ya kumaliza Chuo Kikuu. Ingawa alijua ni ngumu sana kwa baba yake mzazi kukubali kuondoka kijiji cha Nthoro, kijiji ambacho ameshiriki kwa asilimia nyingi kukipa hadhi inayoonekana leo akiwa kama muasisi.
Alikuwa anatamani arudi kijijini mara kwa mara ila umbali ulikuwa ni kikwazo kikubwa. Kutoka Maputo mpaka Montepuez kwa usafiri wa gari ni zaidi ya saa 35, na kulipa nauli ya ndege ambayo angetumia saa 2 tu hakuwa nazo hizo pesa, hivyo ikawa kila mwaka anarudi mara moja nyumbani kusalimia familia yake.


"Kiu ya kisasi ya Dr.Anabella"
Zikiwa zimebaki wiki mbili tu Dr. Anabella arejee nyumbani kwao kijiji cha Nthoro akiwa tayari ni mhitimu wa fani ya Udaktari, furaha yake ilikuwa haielezeki. Alikuwa anawaza furaha ya wazazi wake jinsi itakavyokuwa. Akawa anavuta picha sherehe kubwa atakayoandaliwa na kijiji ya kuhitimu masomo yake.
Akakumbuka sherehe yake ya unyago maarufu kama "Chiputu" aliyofanyiwa kipindi ana miaka 12 namna ilivyopambwa na ngoma za utamaduni za "Mapiko" zilizorindima wiki nzima. Na akakumbuka namna vyakula vya kila aina na nyama za kila aina kama panya, nyoka, nguruwe na vinginevyo vililiwa siku hiyo na kusazwa.
Nikumegee siri moja ndugu msomaji, Wamakonde wa Msumbiji wana tofauti kidogo na Wamakonde wa Tanzania. Wamakonde wa Msumbiji wengi wao hawachagui nyama ya kula wana msemo wao wa kimakonde kuwa "chiumbile Nnungu chakumemena" wakimaanisha "kila alichokiumba Mungu kinatakiwa kiliwe".
Dr.Anabella ilikuwa akipita mitaa mbalimbali ya jiji la Maputo kama mitaa ya "Bustani ya Tunduru", mitaa ya stesheni huko kote alikuwa hakosi kununua zawadi ndogo ndogo kama za nguo kwa ajili ya wazazi na ndugu zake wa karibu ambao bado walikuwa wanaishi kijijini ambao hawakuendelea na masomo ya juu kama yeye Dr.Anabella.
Ilikuwa tarehe 13/04/2009 itabaki kuwa ni siku ya kumbukumbu mbaya sana kwa Dr.Anabella mpaka siku anakufa. Ni siku ambayo iliamsha kiu yake ya kulipa kisasi kwa wabaya wake wote. Siku hiyo aliamka na taarifa mbaya sana kutoka kijijini kwao Nthoro.
Usiku wa kuamkia siku hiyo alikuwa zamu ya usiku kucha katika hospitali ya "Maputo Central Hospital" alipokuwa anafanya mazoezi ya vitendo ya Udaktari, hivyo hakupata muda wa kuangalia taarifa ya habari kwenye runinga. Aliporudi nyumbani alfajiri moja kwa moja akapitiliza chumbani kuuchapa usingizi.
Alipoamka asubuhi baada ya kuoga wakati anafanya maandalizi ya chai ya asubuhi akaweka televisheni ya Afrika ya kusini ya "SABC NEWS" ndipo alipoona habari ya kusikitisha ya mauaji ya baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha Nthoro, waliouwawa kwa kukatwa katwa mapanga na viungo vyao kukusanywa kama nyama za buchani.
Akataharuki na kuamua kupiga simu kijiji kwao ili kufahamu usalama wa familia yake, ikawa namba za wazazi wake na wadogo zake wote hawapo hewani ndio akazidi kuchanganyikiwa. Hamu ya chai ikatoweka kabisa, ikabidi aende kwa muuza magazeti mtaani kwao kutafuta gazeti lolote lenye habari hizo za kusikitisha. Kwa bahati nzuri akapata gazeti la "Expresso da tarde" linalotoka kila siku.
Humo ndipo akapata habari kuwa zaidi ya wanakijiji 50 wameuliwa. Wameuawa kikatili kwa mapanga na mashoka kwa kukatwa vichwa vyao na watu wasiojulikana. Aliposoma orodha ya wahanga aliishiwa nguvu na kuzimia palepale pembeni mwa kibanda cha kuuza magazeti. Alikuta miongoni mwa majina ya waliofariki ni familia yake yote.
Alizinduka akijikuta yupo hospitali huku amezungukwa na madaktari wenzake wakimfariji kwa maneno ya kumtia moyo kuwa maisha lazima yaendelee anatakiwa kukubaliana na matokeo. Kwa bahati nzuri uongozi wa hospitali na wafanyakazi wenzake wakamchangia pesa ya kutosha kuendeshea mazishi. Akarejea kijijini kwao kushughulikia mazishi ya wazazi na ndugu zake.
Baada ya shughuli za matanga kupita, siku moja akiwa anapangapanga vitu vizuri nyumbani kwao ili aweze kurejea Jijini Maputo, akaendelee na maisha yake mapya, ndipo alipofungua sanduku la marehemu baba yake. Humo kwenye sanduku alikutana na taarifa iliyompa mshtuko mkubwa wa moyo na taharuki jadidi.
Aliifuma barua ya siri aliyoiandika marehemu baba yake mzazi na kuihifadhi kwenye sanduku hilo. Barua iliandikwa juu ya bahasha maandishi makubwa yanasomeka "NACATANAS". Alipoifungua na kuisoma hiyo barua alilia sana siku hiyo, kutokana na maelezo yaliyoandikwa na baba yake kuhusu kundi la "NACATANAS".
Majonzi ya msiba yakaibuka upya moyoni mwake. Ndio akafahamu kwanini baba yake siku za mwisho za uhai wake alikuwa hana maisha ya furaha kama zamani ambapo ilikuwa haipiti wiki atampigia simu mtoto wake chuoni kuulizia afya yake na maendeleo yake.
Mipango yake ya kurejea Maputo akaizika rasmi. Akaapa kuwa kuanzia sasa hatolia tena kwa sababu kilio kinapunguza hasira na kuondoka joto la hasira moyoni, badala yake atalipa kisasi kwa wote waliohusika kuiteketeza familia yake kikatili.
Akaweka nadhiri kuwa fursa itakavyopatikana lazima atawatekeza NACATANAS kwa mkono wake mwenyewe na wote waliohusika kufanya mauaji ya kikatili kwa familia yake. Kila uchao nyakati za Alfajiri akawa anazuru makaburi ya wazazi wake na kula yamini ya kulipiza kisasi. Kiu ya kisasi ikatawala katika fikra za "Dr.Anabella".



SURA YA KUMI NA TATU
Kachero Manu kifungoni ndani ya Selo kuu
Kachero Manu alitupwa selo kuu usiku wa giza totoro na akiwa hana fahamu kabisa. Alikuja kuzinduka katikati ya usiku akiwa anatetemeka na baridi, alipoangaza kwenye chumba hicho akaona mambo ya kutisha na kuogofya zaidi ya kule selo ndogo alipotolewa. Kwake aliona ni mfano wa mtu aliyeruka mkojo na kukanyaga kinyesi.
Kulikuwa na mwangaza hafifu wa kurunzi ya taa ya karabai iliyowekwa juu ya meza chakavu ya mbao. Akayaona majeneza kama 7 yamepangwa safusafu na kufungwa na kufuli za chuma cha pua. Alikuwa anasikia kwa mbali sana sauti hafifu za watu wanapiga kelele ndani ya yale majeneza wakilalamika kutokana na kukosa pumzi lakini sauti zao hazitoki vizuri.
Yale majeneza ndani yake kulikuwa na wadudu wakali kama nge na tandu pamoja na mende kwa lengo la kuwanyima usingizi mateka waliletwa humu kwenye selo kuu. Alipoangaza pembezoni ya meza yenye kurunzi akaona lundo la mabaki ya mifupa ya binadamu na mafuvu ya vichwa yamekusanywa pamoja kwenye magunia, ambayo yamezidiwa na mizigo mpaka mifupa mingine imejitokeza nje.
Akatulia na kuwaza, akajisemea moyoni mwake asipotumia akili za kuzaliwa imsaidie kutoroka humu, hatoweza kutoka salama. Atafia Cabo-Delgado na maiti yake haitoonekana tena, itatupwa katika mto Ruvuma, iwe chakula cha samaki.
Akawa anawaza jinsi kifo chake kitakavyomsikitisha mpenzi wake Faith Magayane ambaye walipanga huu mwaka usiishe wawe ni mke na mume mpaka kifo kiwatenganishe. Akawaza jinsi baba yake kule Mahiwa watakavyopokea taarifa ya kifo chake kwa mshtuko mkubwa, baada ya kumpoteza mkewe kwa kuchinjwa na kumpoteza mtoto wake ndani ya wiki moja. Pia Bosi wake Mzee Mathew Kilanga na Taifa kwa ujumla litapigwa na mshtuko mkubwa, litakuwa limempoteza Kachero wake mzoefu aliyepikwa akapikika kwa miaka kadhaa.
Ghafla Kachero Manu akiwa kwenye mkururu wa mawazo, akashtushwa na sauti ya kikohozi, ni kama kikohozi cha mtu aliyepigwa na baridi kali ya mule ndani. Akatulia kidogo, hakutaka kuyaamini kwa haraka masikio yake. Akasikia tena kwa ufasaha sauti ya mtu anaye jikohoa. Akaangaza macho yake chumba kizima kumtafuta huyo mtu. Kwenye kona ya chumba upande wa kushoto akafanikiwa kuona kwa tabu sana kama vile kuna mtu amelala juu ya kitanda. Akafanya maamuzi ya kumfuata kwa kujiviringisha ili akamfahamu huyo aliyelazwa. Huenda akapata msaada kwake wa kumsaidia kutoka ndani ya selo.
Akaanza kusota kwa njia ya kubiringika taratibu anajigeuza mwili mzima mzima kwa sababu alifungwa kamba za mikononi na miguuni. Akawa anasota huku anaugulia maumivu kwa sababu kulikuwa na misumari na vyupa vilivyovunjwa ovyo ndani ya kile chumba. Alikuwa anachomwa na ile misumari iliyopigiliwa chini ya sakafu kwa lengo la mateso kwa mateka. Akajikaza kisabuni hivyo hivyo, alijua kama atajidekeza kesho ndio mwisho wake wa kuishi duniani.
Hasa akikumbukia mazungumzo aliyoyanyaka kule Nantilus Hotel kuwa kesho kutwa usiku, tarehe 18/02/2016 kutakuwa na kikao kikubwa. Kikao ambacho Mkuu wa Mafioso wa Cabo-Delgado, Alfredo atakuwepo na mgeni wao toka Tanzania Bwana Andenga Kazimoto atakuja akiwa na nyaraka zote za siri alizozikwapua nchini Tanzania. Pia aliagizwa Inspekta Jenerali Mark Noble ahakikishe anamkamata Kachero Manu na kumleta kwenye kikao hicho ili ahojiwe kisha kuuliwa jambo ambalo tayari walishafanikiwa kumkamata.
Hivyo kwanza alijiamini mateso yote anayopewa ni vitisho tu lakini ahadi ni lazima apelekwe mbele ya kikao hicho akiwa yupo hai. Fursa ambayo alikuwa anaitamani sana ya kupelekwa kwenye kikao kikubwa cha washirika wa siri wa kampuni ya Monte Branco Ltd. Hivyo akajifariji hata kama huyo anayemfuata ambaye anakohoa kitandani atakuwa ni adui yake hana ubavu wa kumuua yeye kabla hajaonana na Bwana Alfredo.
Akaendelea kuburuzika kwa tabu, ilimchukua kama takribani dakika 38 mpaka kufika pembezoni mwa kitanda kile. Alipomkaribia yule mtu akamuona kwa tabu anajilazimisha kuunda tabasamu usoni mwake. Kachero Manu akajipa matumaini ni mtu mwema, asilani hawezi kuwa adui. Nuru ya matumaini ya kuokoka ikawa imechanua katika moyo wake, mithili ya mmea unavyochangamka pindi ukinyunyiziwa maji.
Alipomkaribia karibu zaidi akamsikia yule mtu anajikohoza tena kisha akaongea “Kiongozi tupo pamoja, usiogope, njoo karibu yangu zaidi”.
Kusikia hivyo Kachero Manu akaongeza bidii ya kujiburuza, baada dakika 3 akawa amelifikia tofali lililoweka kwa pembeni jirani na tendegu la kitanda. Akaegesha kichwa chake kwa tabu kisha, akamuuliza yule jamaa "wewe ni nani na umeletwa humu kwa kosa"? .
Yule jamaa bila ajizi akajitambulisha, “Mimi Naitwa Koplo Hamduni, wa Kituo kikuu cha Polisi Mtwara mjini, nimeambiwa ujio wako na Dr.Anabella Yule mwanadada anayetutibu mateka wa humu selo” akaongea Koplo Hamduni huku amekenua meno yake ya rangi ya manjano, machafu kutokana na kutopigwa mswaki kwa muda wa wiki nzima.
Kachero Manu akaanza kupata matumaini ya kutoka mule kwa kumtumia yule daktari ambaye hata jina lake alikuwa halijui, lakini alionyesha ana utu nafsini mwake. Kisha bila kusita akamkumbushia tena swali alilouliza, ”hujajibu swali langu ni kosa gani limekuleta humu selo ya kifo?” ingawa hisia zake zilimtuma kuwa huenda huyu ni miongoni mwa askari wapelelezi 6 waliotumwa Cabo-Delgado ambao inasemekana wamekamatwa na kuuliwa hivyo ikasababisha atumwe yeye.
Koplo Hamduni kwa sauti hafifu ya kukwaruza yenye kusikika kwa mbali akaanza kumsimulia mkasa wao wote tokea walivyoondoka Mtwara mpaka kufika Cabo-Delgado na namna kila mmoja wao alivyokamatwa. Mkasa ambao ulimsaidia sana kachero Manu kupata picha halisi ya chanzo cha machafuko dhidi ya Watanzania, Jimboni Cabo-Delgado.



Safari ya Koplo Hamduni na wenzake Jimboni Cabo-Delgado
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mtwara chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ilitoa maagizo kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa-(RPC) kutuma vijana wake kwenda Jimbo la Cabo-Delgado, Msumbiji kuchokonoa chanzo cha machafuko dhidi ya Watanzania wanaoishi huko.
Hivyo kikosi cha askari kanzu 6 wakiongozwa na Koplo Hamduni waliteuliwa kwenda huko wakiwa wamejikamilisha ipasavyo. Safari ya Koplo Hamduni na askari kanzu wenzake 5 ilikuwa ni kwa mafungu, wenzao 2 walitangulia kwa njia ya anga na 4 waliobaki walisafiri kwa njia ya nchi kavu.
Wale wa njia ya anga walitoka Mtwara na ndege ya shirika la ndege la ATCL mpaka Dar es Salaam. Kisha wakaunganisha moja kwa moja na ndege ya shirika la ndege la Msumbiji Linhas Aéreas de Moçambique, Ltd (LAM), ambayo huwa inatoka Dare s Salaam mpaka Pemba nchini Msumbiji, mara mbili kwa wiki.
Pemba ndio Makao Makuu ya Jimbo la Cabo-Delgado. Kisha wakaondoka Pemba kwa usafiri wa daladala kuelekea Montepuez tayari kuwasubiria wenzao wanaokuja kwa usafiri wa basi waungane pamoja. Walitumia hekima za wahenga zinazosema “usiweke mayai yote kwenye kapu moja, kapu likidondoka hutoi kitu”, walikuwa wanachukua tahadhari ili baadhi wakikwama wengine watimize lengo walilotumwa, afe beki afe kipa lengo litimie.
Koplo Hamduni na wenzake watatu waliosafiri kwa njia ya barabara safari yao iliyoanzia nyumba ya wageni ya “Chilindima” iliyopo Mtwara Mjini, mtaa wa pili tu toka stendi kuu. Hapo huwa ndio Gesti wanayopenda sana kufikia Wafanyabiashara wanaoelekea Cabo-Delgado na kuna daladala inaanzia safari zake hapo hapo nje ya gesti asubuhi na mapema.
Hivyo Koplo Hamduni na wenzake nao walijifanya ni Wafanyabiashara wanaelekea huko Cabo-Delgado wakaanza kupata alife bee tee za huko wanakoelekea kutoka kwa Wafanyabiashara wengine. Ingawa malengo yao ilikuwa wakifika wajitambulishe kama waandishi wa habari wa kimataifa ili waingie kirahisi eneo la tukio.
Walianza safari yao asubuhi kwa daladala iliyowafikisha mpakani mwa mto Ruvuma. Hapo walivushwa kwa mtumbwi mpaka ng'ambo ya Msumbiji kisha wakapanda daladala za kuelekea Msimbwa, nauli yake ni kama Mitikashi 400 kwa pesa za Msumbiji. Walipofika Msimbwa wakalala tena kwenye gesti ya “Marehemu Mzee Yahya”, ni gesti maarufu sana kwa Watanzania wanaoelekea Msumbiji.
Ila Gesti za Msumbiji ni kichefuchefu tupu kama hujazoea hasa zile za kawaida ustaarabu hamna kabisa. Mfano huwa hawaweki kandambili za kuingilia chooni inabidi ubebe za kwako mwenyewe la sivyo utapekua chooni. Pia chumba kinawezakuwa kina choo cha ndani "self-contained" lakini kumbe mnatumia watu wawili tofauti wa chumba tofauti kila mtu ana mlango wake wa kuingilia chooni.
Kutokana na mazungumzo na wazoefu wa kusafiri kwenda Montepuez,Jimboni Cabo-Delgado akina Koplo Hamduni wakafanya maamuzi tena wajigawanye asubuhi yake. Kwa kuwa hawakuwa na askari mwenye uwezo wa kufanya tarjama ya lugha Kireno kwa Kiswahili, wakaamua koplo Hamduni akapande gari linaitwa “Micula”. Hizo ni gari za kigogo mmoja wa zamani wa serikali ya Msumbiji huwa hazisimamishwi na askari usalama yoyote barabarani. Wale wenzake wakaondoka na basi la "ManingNice" zinazotoka Msimbwa kwenda Montepuez. Wenzake walikuwa afadhali wanaambulia maneno mawili matatu ya lugha ya Kireno hivyo hawakuwa na uwoga wowote wa askari wa Msumbiji iwapo itatokea wamesimamishwa njiani na kuhojiwa.
Askari wa Msumbiji ni wasumbufu sana na hata kama wanajua Kiswahili na Kiingereza wanajifanya kuongea Kireno ili wakukamate mgeni unayeenda nchini kwao kwa mara ya kwanza, ili wakusumbue wakuombe kitu kidogo.
Mfano askari anaweza kuingia kwenye gari la abiria akasalimia kwa kireno wakati wa asubuhi akasema “Boa-ndia”(habari za asubuhi), wewe unatakiwa umjibu “Boa-ndia shefuu”(Habari ni nzuri mkuu). Sasa askari anakuwa makini kuangalia abiria ambaye mdomo wake haujatikisika, akikugundua anakujua wewe ni mgeni, lazima akung'ang'anie kama ruba.
Anakufuata kwa mbwembwe zote kibonde wake, akikufikia atakuliza tena “Vai para aonde?”(Unakwenda wapi). Huo sasa hapo ni mtego wa panya, usijaribu kabisa kujibu “Montepuez”. Ukijibu hivyo tu wanajua huyu ndio Mtanzania kama kawaida yao anaenda kwenye machimbo ya rubi chamoto utakiona. Wewe ukiulizwa jibu tu sehemu ingine labda "Nampula" au "Mweda" lakini usitaje kuwa unaenda "Montepuez" kuwa ndio unapoelekea. Ukivuka kikwazo hicho, litakuja swali lingine “Vai para fazero ke?”(Unakwenda kufanya nini). Ukipigwa swali hilo wewe mjibu kwa upole kabisa, “Vizitari meo limao”(kumtembelea ndugu). Pia jiandae na usumbufu kibao, kama onyesha kitambulisho, ukiruka viunzi vyote mwishowe lazima atakuambia tu, “Dala refureshiko”. Yaani anakuomba ela ya soda, tayari hapo anataka uzunguke mbuyu ili akuache uende kwa salama, hapo sasa unaweza tu kumpa Mitikashi 50 unamalizana nae kwa usalama.
Hivi vikwazo vyote wale askari kanzu waliviruka wote 6 wakakutana Montepuez wakiwa salama salimini. Baada ya masimulizi marefu, Kachero Manu alimkatiza Koplo Hamduni, kwa swali la udadisi, "sasa ilikuwaje mpaka mkashikwa wote kama mlifika salama Montepuez?". Koplo Hamduni akaendelea na simulizi yake. "Tulifika salama na tukaelekea mpaka eneo la tukio katika kijiji cha Nthoro, tuliingia kijijini tukijifanya ni wandishi wa habari wa kimataifa wa haki za binadamu kutoka Afrika ya kusini na ndani ya siku mbili tulipata habari nyingi sana za kipelelezi toka kwa wananchi wakazi wa pale kijijini, lakini tunahisi kuna shinikizo la kigogo serikalini anayeshirikiana na hawa mabaradhuli, ambaye alikuwa anaogopa ukweli halisi ukianikwa ukajulikana kimataifa, taswira ya Msumbiji itachafuka na huenda baadhi ya viongozi wasio waadilifu wakapelekwa katika mahakama ya uhalifu ya Kimataifa. Tulikuta taarifa za mauaji makubwa ya mwaka 2009 ya wanakijiji kukatwa mapanga na watu wanaojiita "NACATANAS", mpaka leo hawajakamatwa sasa ukijumlisha na tukio hili jipya la Watanzania. Hivyo tukakamatwa na kuletwa kwenye hii selo na hamna yoyote aliyefanikiwa kutoroka toka humu, wenzangu wameshakufa hata mimi sina uhai mrefu ni mipango tu ya Dr.Anabella mie na wewe tukutane nikiwa hai na walitupokonya kila kitu chetu tulichokipeleleza". Baada ya kusikia maelezo hayo akashusha pumzi ndefu Kachero Manu.
"Mligundua nini chanzo cha machafuko haya yanayoendelea ya Montepuez"? aliuliza tena kiudadisi. Koplo Hamduni akajikohoza kuliweka koo lake sawa, ili aweze kuendelea na simulizi ya rubi iliyolowa damu ya Montepuez, Jimboni Cabo-Delgado.
Simulizi yake ilikuwa ni msaada mkubwa sana kwa Kachero Manu. Lakini sasa alianza kuongea kwa shida na alikuwa akikohoa anatema makohozi ya damu. Kachero Manu akaongeza umakini kumsikiliza alifahamu huyu hana muda mrefu atakuwa maiti mtarajiwa, anaelekea jongomeo.
“Eneo la Montepuez upande wa kaskazini-mashariki mwa jimbo la Cabo-Delgado iligundulika rubi yenye thamani ya juu kabisa duniani mwishoni mwa mwaka 2008. Eneo lenye madini ya rubi ni zaidi ya hekta za mraba 33600. Rubi hiyo iliyogunduliwa Msumbiji ni sawa na asilimia arobaini (40%) ya rubi yote iliyopo duniani. Ugunduzi uliopongezwa na shirika la Marekani “Gemological Institute of America” na kuitwa ni ugunduzi wa karne ya 21.
Aina za hizo rubi zilizogunduliwa Montepuez ni aina ya kifaru Rhino Ruby (40.23 carats) na macho ya dragoni Eyes of the Dragon (45 carats). Iligunduliwa na mkulima mdogo anayeishi eneo la kijiji cha Nthoro. Ilikuwa ni kawaida yao kuchimba chimba na kuuza kwa wageni vimawe vidogo.
Sasa yale mawe yalipelekwa nchini Thailand kuuzwa, yalipopimwa na wataalamu wakataka kufahamu wapi yalipotokea madini hayo ya rubi ndio ikajulikana ni Montepuez, Jimbo la Cabo-Delgado, Msumbiji. Kigogo wa serikalini kutoka chama cha FRELIMO ambaye aliwahi kuwa gavana wa Cabo-Delgado siku za nyuma. Alipopata taarifa za ugunduzi huo akanunua ardhi ya wakulima wadogo wa eneo hilo. Huyu kigogo alikuwa na kampuni yake aliyoisajili iliyokuwa inajihusisha na uuzaji wa jumla na rejareja wa vifaa vya ofisini. Ila baada ya ununuzi wa ardhi hiyo akaisajili kampuni yake kama mchimbaji wa madini ya rubi na kisha akaingia ubia na kampuni moja ya Kiingereza inayojihusisha na madini ya rubi ya ambayo ni kampuni kubwa sana duniani inayojishughulisha na uchimbaji na uuzaji wa madini ya rubi. Walipoingia ubia wakatengeneza kampuni moja mpya inayoitwa “Cabo-Delgado Ruby Mining”(CRM) ambapo kampuni ya Uingereza ikachukua asilimia sabini na tano (75%) ya hisa za kampuni na asilimia ishirini na tano(25%) ya hisa zikachukuliwa na kampuni ya kigogo mstaafu wa Msumbiji.
Kampuni ya "CRM ikapewa kibali halali cha serikali ya Msumbiji cha uchimbaji cha miaka 25 cha kuchimba eneo ya ekari 81,000. Sasa tatizo likaibuliwa na wachimbaji wadogo wadogo wakajikuta wanaondolewa kwenye maeneo yao ya uchimbaji. Na inasemekana hawa wachimbaji wadogo wadogo walikuwepo wengi wao ni wenyeji wa Msumbiji lakini pia Watanzania, Wasenegali na Wasomali pia walikuwepo.
Sasa inavyoonyesha kuna kampuni moja inaitwa "Monte Branco Ltd" ilitaka kujiingiza nayo kwenye biashara ya uchimbaji wa rubi bila kufuata sheria za Msumbiji na wala kulipa fidia halali kwa wazawa ambao ndio wamiliki halali wa ardhi ya vijiji vya Nthoro na Namanhumbir, ambavyo ndio vijiji vyenye rubi nyingi. Sasa ghafla kukaibuka kikundi kinajiita “NACATANAS” ambacho hakijulikani nani hasa mmiliki wa hiki kikundi. Wakawa wanapita kupiga mapanga wachimbaji ambao wanajifanya viherehere kutetea haki za wenzao.
Kampuni ya "CRM" ikakanusha kuwa haihusiki na kikundi hicho kwa sababu wao wana vibali vya serikali vya kumiliki eneo hilo, sasa vidole vya lawama vinaelekezwa kwa hawa "Monte Branco Ltd" kuwa huenda ndio wanaofadhili hawa NACATANAS ili kupandikiza hofu kwa jamii halafu na wao waweze kujitwalia eneo la kuchimba rubi. Ingawa hizi zote ni hisia hamna ushahidi kamili wa kuthibitisha kuwa wao ni wahusika, na daima vikundi vikubwa vya kimafia huwa haviachi alama za ushahidi kirahisi, hivyo ni juu yako “Kiongozi” kwenda ndani zaidi kufanya upelelezi kuwagundua kama hawa "Monte Branco Ltd" wanahusika au hapana na hicho kikundi cha NACATANAS nani mmiliki wake, maana kila mwananchi anawataja hao ndio wanaofanya fujo machimboni".
Ghafla akaanza kukohoa mfululizo Koplo Hamduni baada ya kukaribia kumaliza simulizi yake. Akaanza kuhema kwa nguvu kama mtu aliyetwishwa mzigo mzito kichwani. Kisha akamalizia simulizi yake “Kii..o…oo.ngozi nak..uta…kia kazi njeeee..ma.....Aluta Kontinua!” kisha akatumbua macho kodo angani akakata roho kuelekea kwa Mola wake.
Machungu ya Kachero Manu ya kumshuhudia Koplo Hamduni anafariki mbele ya macho yake yalikuwa hayaelezeki nae akajikuta machozi yanamtiririka kwa uchungu. Akashukuru Mungu kwa kumkutanisha na Koplo Hamduni aliyempatia maelezo mazuri. Maelezo ambayo yalimpa mwangaza mkubwa kwenye taftishi yake na yamemrahisishia kazi yake aliyotakiwa kuifanya kwa kiasi kikubwa.
Akakumbuka kuna wakati kwenye maisha binadamu unaweza ukapatwa na balaa na ukalaumu Mungu kumbe ndani ya hilo balaa Mungu kaweka neema ndani yake. Inamaanisha yeye alivyotekwa kuletwa huku selo aliona ni balaa lakini kumbe amekuja kukutanishwa na Koplo Hamduni ambaye amempa taarifa nyeti sana.
Akasifu uhodari wa Koplo Hamduni, kwani ya muda mfupi wa siku chache tayari alishajikusanyia taarifa muhimu sana za upelelezi. Akajisemea huyu kama asingefariki ningependekeza kwa Bosi Mathew Kilanga aletwe Makao Makuu akapewe mafunzo zaidi na angekuwa msaada kwa idara yetu ya usalama. Lakini haikuwa bahati yake kashapoteza uhai wake.
Akaanza kujiburuta Kachero Manu kurudi eneo alilotupwa na wale vijana wawili waliopewa maagizo ya kumpeleka kwenye selo kubwa.


SURA YA KUMI NA NNE
Dr.Anabella anasa ripoti nyeti nyumbani kwa Inspekta Jenerali Mark Noble
Dr.Anabella baada ya kusoma barua iliyoachwa na marehemu baba yake iliyoelezea dhuluma kubwa waliyofanyiwa ya kuporwa ardhi yao na vitisho walivyokuwa wanapokea kutoka kwa kikundi cha "NACATANAS", ikabidi azime ndoto zake zote za kufanya kazi ndani ya Maputo Jiji kuu la Msumbiji.
Wanakijiji aliwakuta wameshakata tamaa sasa wakawa wanamtazama yeye kama ndio msomi wa kijiji mwenye jukumu la kuwaonyesha dira na njia ya kupata haki zao kutokana na dhuluma wanazofanyiwa. Dr.Anabella akavaa koti la uanaharakati na kuliweka kando koti la Utabibu wa binadamu kwa muda. Akaitisha mkutano wa wahanga wote, kisha wakachagua kamati ya kijiji ya kufuatilia haki zao. Hatua ya kwanza ya ufuatiliaji ilikuwa ni kutoa ripoti polisi na kujua walipofikia Kwenye upelelezi wao. Hatua ya pili ilikuwa ni kufanya mazungumzo na mgodi wa 'Cabo-Delgado Ruby Mining'-("CRM") uweze kulipa fidia na kuisaidia jamii kujijenga upya baada ya kuhamishwa maeneo yao ya asili.
Juhudi za Dr.Anabella zilizaa matunda chanya kwani mgodi wa 'Cabo-Delgado Ruby Mining'-("CRM") ulikubali kujenga nyumba mpya kwa ajili ya familia 500 za wana kijiji cha Nthoro katika eneo jipya. Nyumba hizo zilijengwa kwa thamani ya dola za kimarekani milioni 10. Pia walikubali kujenga soko, hospitali, shule, kanisa, msikiti, chuo cha ufundi na eneo la makaburi.
Upande wa hawa wahalifu wa 'NACATANAS' taarifa ya hatua walizochukuliwa na vyombo vya dola ikawa ni danadana za nenda rudi nenda rudi toka jeshi la polisi. Mwishoni mwa mwaka 2012, baada ya kuona usumbufu wa Dr.Anabella umezidi kikomo katika ufuatiliaji wa sakata hilo, Inspekta Jenerali mwenyewe wa Jimbo la Cabo-Delgado Bwana Mark Noble akajibebesha mwenyewe zigo. Akajiteua kuwa ndio awe anashughulika na upelelezi wa sakata la machafuko ya machimboni.
Mark safari za kijiji cha Nthoro zikawa sasa hazikauki, kila wakati anafanya mikutano ya siri na ya wazi na kamati ya Dr.Anabella anajifanya anashughulikia tatizo lao kumbe "kikulacho ki nguoni wako" kumbe wangejua kuwa Mark ndio kiongozi mkuu wa "NACATANAS" yeye ndio anawapangia matukio yote, na alikuwa anatumia nafasi yake ya Ukuu katika jeshi la polisi kuwakwepesha na mkono wa sheria. Ndio maana NACATANAS wakawa hawafanyi uhalifu wao kwa mficho, wakiringia ukaribu wao na Inspekta Jenerali Mark Noble.
Ule ukaribu wa Dr.Anabella na Mark na kufahamiana kwao kwenye suala la wanakijiji kukazalisha kujuana zaidi. Wakajikuta wameingia katika mahusiano ya kimapenzi bila wenyewe kutarajia.
Katika vitu vilikuwa vinamkosesha majibu ya moja kwa moja Dr.Anabella na kumpa mawazo juu ya mpenzi wake Inspekta Jenerali Mark toka siku za mwanzo mwanzo za mahusiano yao ni utajiri wa kupindukia aliokuwa nao Mark.
Nchi ya Msumbiji ipo miongoni mwa nchi 10 masikini duniani, haina mishahara mikubwa kwa watumishi wa umma. Mfano kima cha chini cha Mshahara ni Mitikashi 2,900 sawa na kama Sh. 100,000/= ya Tanzania. Lakini Inspekta Jenerali Mark Noble alikuwa anamiliki majumba ya kifahari karibia katika kila wilaya ya Cabo-Delgado. Alikuwa anabadilisha magari ya kifahari kila wakati na vitega uchumi mbalimbali. Baadhi ya likizo zao walikuwa wanaenda Jijini Paris, Ufaransa na Dubai kutumbua raha za dunia.
Dr.Anabella kila anapomuuliza kwa kumchokonoa wapi alipopata utajiri wa kupindukia, alikuwa anakuja juu kama moto wa kifuu hataki kufuatiliwa mambo yake binafsi.
Kitu kingine kilichokuwa kinamkera Dr.Anabella kwa mpenzi wake Inspekta Jenerali Mark, ni tabia ya ulevi wa kupindukia hasa anapokuwa na msongo wa mawazo. Tabia ambayo Dr.Anabella alikuwa tayari wavunje hata mahusiano yao ya kimapenzi. Ila Mark kila mara alikuwa anaomba msamaha na kutoa ahadi kemkem za kutorudia tena lakini "lakuvunda halina ubani" baada ya muda anarudia tena yale yale ya zamani kama sio yeye aliyahidi kwa viapo kabisa kuwa hatorudia pombe.
Siku moja baradhuli Mark alirudi nyumbani usiku wa manane akiwa amelewa chakari. Akaingia kwenye chumba cha kujisomea nyumbani kwake akawa anapitia nyaraka zake za kwenye mkoba wake aliorudi nao akapitiwa na usingizi wa fefefe hapo hapo mezani. Dr.Anabella alifanikiwa kumvua viatu mpenzi wake na kumburuza mpaka kitandani kwake na kumlaza.
Ila wakati anamtoa mezani Dr.Anabella aliona bahasha kubwa ya kaki imechapwa maandishi rangi nyeusi kwa herufi kubwa "CONFIDENTIAL". Jakamoyo likamuwaka kifuani kwake na dukuduku la moyo la kutaka kufahamu hiyo barua inahusu nini na siri iliyopo.
Akaamua aende kuisoma huenda atapata majibu ya maswali anayojiuliza kila leo kuhusiana na shughuli za Inspekta Jenerali Mark nje ya shughuli rasmi za jeshi la polisi hasa akitilia wasiwasi ukaribu wa kupitiliza wa Inspekta Jenerali Mark na vigogo wa kampuni ya Monte Branco Ltd. Ilifikia hatua hadi kupewa ofisi ya kufanyia shughuli zake ndani ya ofisi za kampuni hiyo.
Akaanza kuifungua hiyo bahasha huku vidole vinatetemeka akiombea Mark asije kushtuka usingizini ukazuka msala mpya kwake. Alipoifungua tu hiyo bahasha akakuta kuna barua ya onyo imetoka kwa Alfredo Bosi mkuu wa "Monte Branco Ltd" ikimlaumu sana Mark kwa uzembe wa upotevu wa madini yao ya rubi huko nchini Thailand uliofanywa na vijana wa Kitanzania waliotumwa Thailand na Inspekta Mark Noble, wakaleta ujanja wao wa Kariakoo na kutokomea na mzigo wa madini wote bila kuleta hata senti moja.
Hapo akatambua kumbe Mark utajiri wake unatokana na madini ya rubi, na kule kujifanya amezoeana nao vigogo wa kampuni hiyo sio bure ni kwa kazi maalumu ya kuwalinda na mkono mrefu wa dola. Hiyo barua ikampa udadisi sasa wa kupekua nyaraka zingine zilizopo kwenye mkoba huo, humo ndio akakuta taarifa ya mchezo mzima wa biashara ya rubi ya Montepuez.
Humo akakuta kwamba michezo mbalimbali wanayofanya katika kusafirisha ni kuwatumia Wafanyabiashara wenye vibali vya Msumbiji vya kusafirisha madini nje ya nchi. Ambao wanaandikiwa barua ya kutoka Wizara ya Madini kuonyesha aina ya madini, uzito na yanapoelekea na wanasindikizwa mpaka Uwanja wa ndege na vijana wa Inspekta Jenerali Mark Noble halafu kuna kamisheni unawalipa.
Njia nyingine ni kutorosha madini ya Msumbiji kupitia nchini Kenya. Wanawatuma vijana wao wanabeba madini kwa njia za panya mpaka nchini Kenya. Wakifika Kenya wanayaacha madini kastamu. Wanaacha na vibali vyao, Maafisa wa kastamu wanayapokea na kutoa risiti, kisha wanaenda kuomba viza ya kwenda Thailand baada ya siku mbili wanakuwa tayari wamekamilisha taratibu zote. Wanachukua madini yao bila gharama zozote wanayapekeka nchini Thailand kwa ndege ya Kenya Airways au ndege ingine yoyote yenye safari ya huko.
Hii mbinu ni kama wanawatumia wasafirishaji ambao sio wazawa hivyo wanaogopa watanyimwa viza na mamlaka za Msumbiji. Wakifika Thailand wanalipia vibali husika uwanja wa ndege kisha wanaruhusiwa kuingia nayo madini Jijini Bangkok, Thailand. Wakitoka Bangkok wanasafiri kwa Basi kwenda jimbo la Chanthaburi lililopo kusini mashariki mwa nchi ya Thailand. Jimbo lililo umbali wa takribani saa tatu au wanaweza kupanda ndege za ndani. Huko Chanthaburi ndio kuna gulio kuu la rubi kila siku ya Ijumaa na Jumamosi.
Huko ndiko Matajiri kutoka Australia, nchi za mbalimbali za Ulaya na nchi za Scandavia wanachuana kununua madini hayo kwenye mnada. Alishangazwa Dr.Anabella aliposoma imeshawahi kuuzwa rubi ya gramu 30 kutoka Montepuez kwa dola za kimarekani milioni 1($1,000,000).
Nyaraka zilizomchefua zaidi Dr.Anabella ni alipoona orodha ya wapokea mshahara wa kikundi cha "NACATANAS", hapo ndio akajua kumbe joka lililohusika na mauaji ya familia yake yupo nae nyumba moja anakula nae na kulala nae.
Alikaribia kupoteza fahamu kwa kugundua muuaji yupo nae miaka yote nyumba moja, kumbe ametajirika kwa mgongo wa damu ya familia yake. Alitamani aende jikoni akabebe kisu kikubwa kile kisu kinachotumika kuchinjia mbuzi wa sikukuu ya Pasaka amchome nacho kifuani amalize shughuli mara moja.
Lakini akajipa subira ili amteketeze wakati muafaka ukifika na aweze kusambaratisha Mafioso wote wa biashara haramu ya madini ya rubi. Dola haitomuelewa hata kidogo kama akifanya mauaji chumbani. Alijua muda sahihi kwake utawadia wa kutekeleza kisasi chake. Daima subira yavuta kheri ingawa chelewa chelewa utakuta mwana sio wako, hivyo akajiona anatakiwa afanye jambo muafaka, katika nyakati muafaka na mahali muafaka.
Nyaraka zote za siri alizosoma usiku ule, Dr.Anabellah hakuziacha bure. Alizitoa nakala kwa kutumia mashine iliyomo kwenye chumba cha kujisomea, akahifadhi sehemu salama akisubiri muda muafaka wa kutoa ushahidi wake kwenye vyombo husika itakapobidi.




Nyaraka zote za siri alizosoma usiku ule, Dr.Anabellah hakuziacha bure. Alizitoa nakala kwa kutumia mashine iliyomo kwenye chumba cha kujisomea, akahifadhi sehemu salama akisubiri muda muafaka wa kutoa ushahidi wake kwenye vyombo husika itakapobidi.
Dr.Anabella hakutaka kumuonyesha dalili yoyote Inspekta Jenerali Mark Noble kuwa sasa anafahamu kinagaubaga kumhusu mafungamano yake na wamiliki wa kampuni. Alificha siri yake moyoni huku anatamani fursa ya kuwa karibu na vigogo wa Monte Branco Ltd, ambao ndio wahusika namba moja wa kifo cha wazazi wake na nduguze ijitokeze.
Ikatokea wakati mmoja kiwanda kikubwa cha kusindika korosho cha Monte Branco Ltd kinataka daktari wa kusimamia hospitali ya kiwanda. Mark ikabidi akamfanyie mpango mchumba wake Dr.Anabella ale shavu hiyo ajira. Bila kufanya ajizi akakubali hiyo nafasi mara moja bila pingamizi lolote. Rasmi Dr.Anabella akawa yupo kiwandani anafanya kazi. Majukumu yake ikawa ni kuwapa matibabu madogo madogo wafanyakazi wa kiwanda na pia kuandaa rufaa za wagonjwa wanaohitaji matibabu zaidi katika hospitali kubwa.
Mategemeo ya Dr.Anabella alidhani labda na vigogo wa Monte Branco Ltd watakuwa wanatibiwa pale wao na familia zao ili awamalize taratibu kwa madawa ya sumu. Kumbe ikawa tofauti, vigogo wote walikuwa wanatibiwa hospitali kubwa za Jijini Maputo na Cape-Town, Afrika ya kusini.
Alibaki kidogo tu aache kazi kwa sababu lengo lake aliona haliwezi kutimia kwa haraka. Ndipo ilipokuja nafasi aliyokuwa anaisubiria kwa hamu ya kukata kiu yake ya kisasi. Daktari Mkuu wa selo ya mateso ya mabaradhuli ya 'Gorongosa Camp' alipata ajali mbaya ya barabarani katika wiki ambayo Koplo Hamduni na wenzake wamekamatwa. Ikabidi atafutwe Daktari wa dharura msiri wa kuendesha matibabu ya kambi hiyo ya siri kwa mateka. Na ni kazi iliyokuwa na marupurupu makubwa, na baradhuli Mark alikuwa ndio mkuu wa Gorongosa Camp hivyo haraka haraka akamteua mchumba wake 

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog