Search This Blog

Thursday, 23 March 2023

MATANGA YA ROHONI - 2

  

Simulizi : Matanga Ya Rohoni


Sehemu Ya : Pili (2)


Siku za mkutano zilikwisha Jijini Nairobi, Bosi Minja na Katibu Muhtasi wake Recho wakaongeza siku kadhaa za kujidai ndani ya Jiji la Mombasa. Walienda kujivinjari ndani ya fukwe za Mombasa kisha wakarejea Jijini Arusha mwishoni mwa juma tayari kujiandaa na kazi Jumatatu yake.
Safari ya nchini Kenya ilikuwa ni ya ushindi kwa Bosi Minja akiwa ameshafanikisha adhma yake ya kumbatiza Katibu Muhtasi wake Recho kuwa kimada wake rasmi. Walikuwa ni kama mke na mume, wakianza na penzi la siri lililopandwa Jijini Nairobi na kuja kuchipua Jijini Arusha. Sasa ikawa ni mwendo wa kazi na dawa, mpaka ikafikia hatua Recho baadhi ya siku za mwishoni mwa juma analala na kuamkia nyumbani kwa Bosi wake. Kila kiwanja cha starehe anachotia mguu Bosi Minja basi sako kwa bako na Recho wake.
Wakware wenzake wakawa hawachoki kumimina sifa lukuki na kumpa mkono wa tahania kuwa kaopoa kifaa chenye hadhi ya kimataifa. Sifa hizo zilimlewesha na kumvimbisha kichwa hali iliyomchochea kuzidi kumwaga pesa kwa Recho ili azidi kuvutia zaidi kwake. Ikafika hatua baadhi ya mwisho wa juma anakatiwa tiketi ya ndege kwenda saluni Jijini Nairobi.
Recho alimmeza Bosi Minja akiwa muungwana na kumtema akiwa mtumwa hana sauti hata kidogo, alitakalo Recho ndio huwa. Huku ndani ya kipindi kifupi akifanikiwa kufunguliwa miradi kadhaa binafsi ya kujiongezea kipato nje ya mshahara na kuanzishiwa ujenzi wa nyumba. Maendeleo binafsi ya Bosi Minja ilisimama, huku nguvu kubwa ya pesa akiiwekeza kwa kimada wake na kujisahau kabisa kutengeneza kesho yenye neema kwa familia yake. Kesho ambayo nguvu zitakuwa zimemuisha mwilini, shaibu wa umri ajira amestaafu hatokuwa na kitu cha kumsaidia zaidi ya vitega uchumi vyake alivyoviandaa.
Kama Recho angekuwa mwenyeji wa mikoa ya Pwani tungeweza kujichumia madhambi kuwa Bosi Minja amepigwa dunga, katiwa kwenye chupa kwa marogo ndio maana hafurukuti, haoni wala hasikii kwa Recho, lakini Recho ni Mchaga kabila ambalo mambo ya kupiga dunga kwao ni mbingu na ardhi.
Baadhi ya rafiki zake Bosi Minja walijua fika mwenzao kaingia choo cha kike lakini nani sasa wa kujitoa muhanga kumpa pwi na pwiriri kuwa huyo hawara yake sio atakupeleka kubaya!. Walijua fika ukimgusa kwa jambo hilo urafiki utavunjika kabisa zile neema za asali na maziwa wanazofyonza kwa Bosi Minja itakuwa historia.
Wakaamua kumlamba kisogo tu wakisubiria yamkute wamzodoe kuwa mwana kulitaka mwana kulipata. Mwezi mmoja tu tokea warudi safari yao ya kikazi, Jijini Nairobi, kikaibuka kisanga kipya na kizito kwa Bosi Minja. Kisanga ambacho kilimtikisa vilivyo na kuanza kumpotezea uelekeo wa kazi yake. Siku hiyo ya tukio alifika kazini asubuhi na mapema kama kawaida yake, akapokea bahasha kubwa yenye anuwani ya Jijini Nairobi.
Alipoifungua hiyo bahasha ndipo tafrani na patashika ya nguo kuchanika ilipoibuka. Barua ilimkata maini, na kumnyong'onyesha nguvu kabisa. Feni ilikuwa inapuliza ofisini kwake kawa kawaida lakini jasho jekejeke lilikuwa linamvuja mwilini. Alikuwa amevalia suti yake asubuhi hiyo lakini aliiona ni nzito sana ikabidi aivue.
Alitumiwa picha mbili za rangi, moja akiwa yupo juu ya kifua cha mwanamke, ambaye sura yake haionekani vizuri na ingine akiwa amelala fofofo amemkumbatia mwanamke. Alipoziona tu moyo wake ulianza kupiga haraka haraka. Kulikuwa na kikaratasi kidogo chenye kumpa maelekezo ya kitu cha kufanya pindi atakapopata picha hizo.
"Rechooo... Rechooo....njoo haraka ofisini kwangu " aliongea kwa hasira kwa kutumia simu ya mezani na kuikata. Bosi Minja hakutaka kulimbika mambo moyoni peke yake akataka ampashe na Recho ili wajadili pamoja kama wahanga. Akajiegemeza kwa kutumia kichwa chake kwenye kiti wakati anamsubiria Recho aje, huku anajaribu kuvuta kumbukumbu za siku ya tukio lililosababisha wapigwe picha hizo chafu.
Kumbukumbu zake zilimuelekeza kuwa mara ya mwisho baada ya kufanya manunuzi yao, walielekea kwenye starehe Baa moja inaitwa 'Black Diamond Bar & Grill' kilichopo maeneo ya Mpaka road, Westlands. Hapo wakalewa chakari mpaka wakafanya maamuzi ya kuchukua chumba katika nyumba ya wageni jirani na Baa hiyo. Baada ya hapo akawa hakumbuki chochote zaidi ya kujikuta asubuhi ameamka yupo kitanda kimoja na Recho. "Bosi nimekuja kukusikiliza mbona huniambii kitu..?" Recho alimshtua Bosi wake akiwa kwenye lindi zito la mawazo.
Alikuwa amefungua mlango wa ofisi, mpaka amevuta kiti amekaa, ameshatulia lakini Bosi Minja alikuwa hayupo kabisa kifikra. "My God..! Recho umeingiaje humu ndani sijakuona kabisa...!" aliropoka Bosi Minja akiwa hayaamini macho yake, alikuwa ametingwa kweli na mawazo, mpaka macho yake hayafanyi kazi yake ya maumbile ya kuona vitu.
Recho hakujibu kitu akawa amemtumbulia macho tu anasubiri kwa shauku kubwa kitu alichoitiwa. "Rechoo...tumeumbuka my LOVE yule mbwa wako uliyekutana nae pale Baa, Jijini Nairobi ukaja kumtambulisha kwangu kisha akajifanya msamaria mwema kutupeleka nyumba ya dharura ya kulala wageni kumbe alikuwa na lake jambo!" aliongea kwa huzuni Bosi Minja huku machozi kwa mbali yanamlengalenga akaweka kituo kifupi akatoa hanchifu yake na kuanza kufuta machozi, kisha akaendelea.
"Angalia hizi picha alizotupiga..na pesa anazodai tumpe vinginevyo anasambaza picha zetu, angalia angalia..huu sio utoto huu.. ! " akanyoosha mkono Bosi Minja anamkabidhi bahasha yenye picha Recho. "Yelewiiiiiiiiii.....Oooh.... Ooooh......Yesu na Maria...tumeumbuka Bosi wangu, lipa hizo pesa tuishi kwa amani vinginevyo nitakunywa sumu...mama yangu hawezi kunielewa kabisa, tutaweka wapi sura zetu hapa Jijini Arusha!" aling'aka Recho kwa sauti ya juu huku ameachama mdomo wake huku amesimama wima baada ya kuziona picha zile anatetemeka kwa hasira.
"Hiyo pesa aliyoitaja laki 2 ni nyingi sana.... lakini, naitoa wapi Rechoo...!" aliongea Bosi Minja kiunyonge akionyesha amekata tamaa, hajui cha kufanya. "Mchaga wa wapi wewe....zobaa fanya maarifa ulipe, vinginevyo sikuelewi aiseee wewe ndio umesababisha matatizo yote haya, mie sikupanga kwenda Nairobi wewe ndio ulinishawishi....!" alifoka Recho huku anapigapiga meza ngumi, ulikuwa huwezi kujua kama anaongea na Bosi wake. Ama kweli penzi ni kitovu cha uzembe, Recho alimpeleka harijojo Bosi wake.
Alishapandisha mzuka wake hashikiki tena, mpaka Bosi Minja akalegea na kukubaliana na mawazo ya Recho ya kuitafuta pesa kwa kila hali, kwa udi na uvumba, kwa jino na ukucha, kwa mapana na marefu mpaka ipatikane wafanye malipo. Bosi Minja hakung'amua kabisa kuwa analiwa bangu na Recho kwenye sakata hili la picha chafu. "Ookh....Uuukh......Uuukh.....Nakuf....aaah....." ghafla bin vuu bila kutarajia, wakiwa wameshafikia muafaka kuwa atalipa pesa haraka iwezekanavyo, kabla Recho hajatoka mle ofisini akaanza kutapika huku anayumba amepatwa na kizunguzungu kama vile anapulizwa na upepo wa kisulisuli. Akaanguka chini huku akiwa anahema juu juu kama vile pumzi zinataka kukata.
Bosi Minja alichanganyikiwa vilivyo akiwa haamini kinachomtokea siku ya leo. Aliona ni nuksi tupu inamuandama kuanzia asubuhi na mapema, kadhia dhidi yake zinafuatana mtawalia. Akaitisha gari himahima, akiwa amepatwa na kihoro na kumkimbiza haraka hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu. Njia nzima Bosi Minja alikuwa anasali anamuombea Recho afya yake itengamae akiwa amempakata mapajani mwake. Bosi Minja alikuwa maarufu kila kona ya Jiji la Arusha, hivyo hospitalini pale ilipojulikana kuwa Recho ni mtumishi wa 'Peace Corps-Tanzania' manesi na madaktari walikuwa wanakimbizana kwenye makorido kuhakikisha Recho afya yake inatengamaa.
Walijua tu kwa mchicha alionao Bosi Minja hatowaaacha mikono mitupu lazima atawapa bakshishi kama kifuta jasho. Bosi Minja nae alishinda hospitalini siku hiyo akishirikiana bega kwa bega na madaktari kuchunguza afya ya Recho. Akili yake ilivurugika kabisa, tokea asubuhi mpaka majira hayo ya jioni alikuwa hajatia chochote tumboni mwake mpaka ajue hatima ya kimada wake Recho. Ama kweli mapenzi ni zaidi ya upofu, huyo anayemuhangaikia moyoni mwake Bosi Minja hayupo kabisa. Thamani ya Bosi Minja kwenye moyo wa Recho ni kama mfano wa kululu la baharini, hata bure mtu mwenye akili timamu hapokei.
Mpaka kufika majira ya alasiri, tatizo linalomsumbua Recho likawa hadharani. Bosi Minja alipoitwa kwenye chumba cha daktari kiroho kilikuwa kinamdunda kusikilizia tatizo la Recho, asali wa moyo wake ni nini haswa kinachomsumbua. "Mtumishi wako amepimwa vipimo vyote, damu kubwa na ndogo amekutwa matatizo lukuki ikiwemo damu yake ina shida" akapumzika kuongea huku anaiweka miwani yake sawa daktari yule. Kusikia hivyo habari ya shida kwenye damu kijasho chembamba juu ya pua zake kikaanza kumvuja Bosi Minja.
Zama hizo UKIMWI ulikuwa unaogopeka hatari sana. Mawazo yalimpeleka kuwa tayari huenda na yeye ni muathirika hasa ukichukulia alikuwa anauza mechi kwa Recho bila kutumia kinga yoyote wala kupima afya zao. Akaanza kutetemeka kama mgonjwa malaria mwenye homa kali. "Vipi Bosi unaumwa nini? Pole sana itabidi ukacheki vipimo maabara haraka sana, nitakuandikia" aliongea daktari kwa msisitizo mkubwa baada ya kumuona Bosi Minja anatetemeka. "Hapana I'm OK... just nimeshtushwa na afya yake....ni binti mdogo sana! " alijifaragua na kuyeyusha ukweli halisi wa kitu kilichomsumbua, alitokwa na ulimi kabisa akabaki kujikanyagakanyaga. "Ni matatizo ya kawaida tu wala usijali ana presha ya kushuka, upungufu wa damu na infection katika damu... " Mganga mkuu wa hospitali ya mkoa ya Arusha alikuwa anamuelezea Bosi Minja kwa ufafanuzi zaidi.
"OK...OK...hivyo mmeshamuanzishia dozi?" aliuliza huku akishusha pumzi ndefu mithili ya mpira wa baiskeli uliopata pancha, huku wahaka wake sasa ukipungua. "Tumeshaanza matibabu yake kwa umakini mkubwa sana maana pia ni mjamzito mimba changa kabisa ya mwezi mmoja" aliongea Mganga yule huku anaandika baadhi ya maelekezo kwenye karatasi ya gharama zinazohitajika kulipiwa. Taarifa hiyo ya mimba ya Recho iliamsha chemuchemu ya furaha ndani ya moyo wa Bosi Minja bila kuidhihirisha hadharani mbele ya daktari asije kugundua kuwa kuna mahusiano ya kimapenzi baina yao. Alijiona hodari kwelikweli, kidume cha mbegu kwa kufanikisha kumpa mimba binti mchanga kama Recho. Baada ya maongezi hayo mafupi Bosi Minja akaondoka zake, huku akihakikishiwa kesho yake asubuhi Daktari wa zamu atakavyopita tu atampa ruhusa ya kurejea nyumbani. Kama kawaida yake Bosi Minja, Mlezi wa wana hakuwaacha madaktari na manesi wale kwa maneno matupu akawaachia chauchau kidogo ya shukrani.
Furaha ya Bosi Minja kutokana na taarifa ya ujauzito wa Recho ilikuwa haielezeki ikamsahaulisha kabisa kwa muda laki 2 anayotakiwa kuitoa kama kikomboleo picha zake ngono zisisambazwe na mjuba Martin. Akajiona kabisa anajiandaa kuitwa baba kwa mara ya pili, kwa maana ya kwamba Deborah atapata mdogo wake mpya. Alishaanza kupanga mipango kuwa atafunga ndoa ya kimila na Recho awe mke mwenza wa mama Deborah. Na aliapa kama mama Deborah atakataa kuongezewa mke mwenza, akajiona hawawezi kupikika chungu kimoja, basi yeye mama Debora ndio atakayefungasha virago amuachie ukumbi Recho na si vinginevyo, daima kipya kinyemi.
Uzuri wa Recho ulimsahaulisha Bosi Minja kuwa ya kale dhahabu na tabia bulibuli za mkewe zenye kuvutia ni msingi muhimu katika maisha ya ndoa kuliko mvuto wa umbile. Alitaka Recho akitoka hospitali akili yake itulizane isiwaze kabisa jambo lolote baya hivyo lazima alipe pesa haraka kwa Martin. Pesa za kumlipa Martin mmiliki wa picha zake za ngono alipanga auze moja ya nyumba zake ili apate pesa za kulipa kwa ajili ya kuizima aibu inayoelekea kumkabili mbele yao.
Aibu ambayo ingeweza hata kumpotezea kibarua chake hasa akichukulia Rais wa awamu ya pili, Mheshimiwa Ally Hassan Mwinyi kipindi hicho alikuwa hataki mchezo kazini. Alishatangaza kupitisha fagio la chuma kwa viongozi wazembe na wabadhirifu. Hivyo na yeye angeingizwa kwenye kundi la wazembe wanaoendekeza starehe na kuchafua sifa za watendaji wa serikali. Angeadhibiwa kwa kuigeuza ofisi ya 'Peace Corps-Tanzania' kuwa danguro kwa kuanzisha uhusiano na mtumishi wake mpaka wanajipiga picha za ngono kuashiria wamefikia kilele cha uasherati wao.
Taarifa ya ujauzito ilipomfikia pale kitandani Recho, ilileta mshtuko mkubwa, na kuyasukasuka mawazo yake. Taarifa hiyo aliona kama songombingo imeingia gotalo. Hakuipokea kwa mashamushamu kama ilivyozoeleka kwa akina mama wengi wanapopewa habari hiyo. Taarifa ya kubeba mimba kwa akina mama wengi hupokelewa kwa machozi ya furaha hasa kutokana na mateso ya msongo wa mawazo wanayoyapata wanawake wagumba. Yeye hakuwa tayari kuitwa mama kwa umri wake mdogo wa chini ya miaka 26. Mawazo mtambuka kichwani mwake yalikuwa yanamshauri aitoe mimba hiyo ili bado aendelee kula ujana kwanza kwa kusoza akiba ya Bosi Minja. Mawazo mengine yakimshawishi aitunze mimba hiyo ili aitumie kama mtaji wa kujitajirisha kiuchumi kwa Bosi Minja. Mbaya zaidi mimba yenyewe haikuwa ya Bosi Minja. Alikuwa anataka kubandikwa mzigo usio wake ili aendelee kufanywa chuma ulete wa kiuchumi. Dhana hii ya pili ya kuigeuza mimba kitega uchumi ikapata nguvu kichwani mwake. Akaanza kuingiwa na furaha taratibu.



Miezi ilikuwa inakatika haraka, ilikuwa imeshapita miezi 6 huku ujauzito wa Recho ukiwa mkubwa kabisa. Alishatambulishwa kwa wazazi wake Bosi Minja waliokuwa wanaishi Moshi Mjini katika maeneo ya 'Boma Ng'ombe' wakitokea Marangu. Recho alikuwa bado hajachoka, kazini anatimba kama kawaida kuchapa kazi. Siku ya siku likaibuka dili jipya la kupiga pesa za ofisi kwa Recho.
"Recho my LOVE, chapa hii barua ya majibu ya kuthibitisha tupo tayari kupokea pesa toka kwa wafadhili, kisha uilete nitie sahihi yangu, ibakie kwenye mafaili ya Uhasibu" yalikuwa ni maagizo ya Bosi Minja kwa Katibu Muhtasi wake. "Sawa...kwa hiyo zimeshaingia hizo pesa, na ni za nini..?!" aliuliza Recho kiunyenyekevu swali la kimtego, roho choko aliyoumbiwa nayo ilikuwa inamsumbua.
"Aaah...ni za ujenzi wa shule maalumu kwa ajili ya jamii ya wafugaji huko Longido, ni pesa nyingi sana karibia dola elfu 10. Muda sio mrefu tutaishi maisha ya peponi ha...ha...ha...ha..!" aliongea kwa madahiro huku anaangusha kicheko cha pesa. Bila kujua anauza siri za kambi kwa Recho, mtu mwenye silika za kijambazi lililokubuhu. Recho ndio aliyemfanya Bosi Minja auze nyumba yake ili kupata pesa ya kuzikomboa picha chafu. Picha ambazo Martin ndio alizipiga kwenye ile nyumba ya kulala wageni kwa maelekezo ya Recho ili wamkamue pesa wagawane. Pesa zilivyotoka hizo laki 2 wakagawana pasu kwa pasu. Na sasa Bosi Minja alikuwa analea mimba ya Martin bila kufahamu kuwa Martin ni mume mwenza wake.
Chambilecho mtalaka hatongozwi upya, ndicho kilichotokea kwa Martin na Recho, penzi lilianza kuchipuka upya tokea wakutane Nairobi siku ile. Mara kibao tu Martin alikuwa anajiiba anavuka boda na kuja kinyemela Jijini Arusha kuja kustarehe na Recho dhahiri shahiri, anajilia pweza gizani bila Bosi Ninja kung'amua kuwa mali zake zinaliwa.
Mpango wa Recho na Martin ilikuwa ni kumkamua Bosi Minja mpaka senti yake ya mwisho huku wakihakikisha mtoto wao anaandikishwa mali za kutosha kama mtoto wa Bosi Minja kisha wanatorokea zao Jijini Nairobi kuanza maisha mapya ya raha mustarehe. Leo bila kujua Bosi Minja anamwaga mchele mbele ya kuku, anaanika tena mpango wa pesa kibao mbele ya Recho bila kujua sifa zake zitamtokea puani.
Recho akatekeleza maagizo yale ya Bosi wake ya kuzichapa barua hizo huku sasa akiwa makini kuchunguza nyendo za Mhasibu na Bosi wake kufahamu lini pesa zitatolewa Benki ili aandae mipango yake mibaya dhidi ya pesa hizo za msaada. Recho nikukumbushe anatokea MOSHI, watoto wa Mjini wenye wanatania kuwa MOSHI maana yake ni "(M) MUNGU, (O) ONYESHA, (S) SEHEMU, (H) HELA, (I) ILIPO", hivyo Recho likija suala la mchongo wa pesa, alikuwa hana masikhara wala utani wa aina yoyote, alitumwa pesa toka kwao Machame. Ukiletwa mchongo wowote hata kama unaobidi kutoa roho ya mtu ili mradi pesa itapatikana yupo tayari kuutekeleza.
Taftishi zake Recho zikazaa matunda baada ya wiki mbili tokea barua ile iandikwe. Pesa zilitumwa na Bosi Minja akashinikiza kwa Mhasibu pesa zitolewe Benki kutoka kwenye akaunti ya shirika ili aingize kwenye akaunti yake binafsi maalumu kwa muda fulani ili atunishe riba. Siku hiyo Bosi Minja akiwa anafunga mlango wa Ofisi yake kwa ajili ya kurejea nyumbani kwake. Alikuwa anaonekana ana haraka sana siku hiyo ya Ijumaa alikuwa na safari ya kuelekea Moshi kwa ajili ya kwenda kuwaangalia wazazi wake.
"Bosi.... Samahani ule mzigo tayari, sijui nikukabidhi au ulale hapa hapa ofisini utauchukua Jumatatu..?" aliongea Mhasibu Mzee wa makamo aliyekuwa anajulikana kwa jina la Mr. Mbweku. Mhasibu ambaye alikuwa anafuata "STK" Sheria, Taratibu na Kanuni za kazi yake vilivyo. Hata hilo jambo la kuzitoa pesa za ofisi kinyemela hakulipenda kabisa Mr.Mbweku sema tu shinikizo la Bosi wake ndio lilimlazimisha kuvunja miiko ya kazi. "Hapana nitaondoka nazo, nitajua mwenyewe nitakapoenda kuziweka, nipatie huko mzigo...!" aliongea Bosi Minja huku ananyoosha mkono kulipokea lile Brifkesi jeusi lililojaa ngwenje za kutosha za pesa za kigeni kwa uso wa bashasha.
Recho masikio yake aliyategesha huku akishuhudia kila kitu kinachoendelea akijitia ametingwa na shughuli zake za uchapaji nyaraka mbalimbali. Akamuacha Bosi Minja atoke nje tu, akamfuata kabla hajaingia kwenye gari yake. "Mie naona twende wote Moshi tukawaone wazee wako, na bora nichukue mapumziko ya kazi wiki nzima sasa sijisikii vizuri kabisa, kitoto chako tumboni kimenichokesha mapema, kinanipiga miteke yake tumboni sina raha" aliongea Recho kwa sauti ya kudeka mbele ya mpenzi wake na Bosi wake.
"Hamna shida kwanza itakuwa vizuri sana hawajakuona karibia mwezi na nusu sasa, kachukue fomu ya ruhusa nikujazie haraka, ukajiandae...twende zetu" aliongea Bosi Minja huku akirudi tena ofisini akiwa ameambatana na Recho. Baada ya kukamilisha taratibu zote za kuondoka, Bosi Minja akaondoka zake na gari la Ofisi huku Recho akiondoka na taksi kwenda kujiandaa kwa ajili ya safari.
Bosi Minja alienda kuzihifadhi pesa zile nyumbani kwake, akiwa anajiamini usalama wa nyumba yake. Hakujua kabisa kama Recho katoa kopi funguo zote za nyumbani kwa Bosi Minja kinyemela. Malengo yake yalikuwa siku Jumatatu azipeleke pesa hizo Benki kwenye akaunti maalumu "Fixed Account" yenye riba nono kwa muda wa miezi 6 kabla ya kuanza kuzifanyia matumizi ya ujenzi wa shule hiyo ya kisasa. Malengo ya wafadhili yalikuwa ni kutoa elimu bora kwa watu masikini kwa gharama nafuu, ambapo kila mwanafunzi alitakiwa kwa siku alipe dola 1 au dola 20 kwa mwezi mzima. Kwa ada hiyo angepata vitabu, chakula na malazi. Ingejengwa shule ya msingi na sekondari kwenye eneo moja, huku siku za usoni Chuo Kikuu kingejengwa kwenye eneo hilo hilo. ulikuwa ni mradi wa kihistoria kuwahi kutokea nchini Tanzania.
Hapo kwenye mradi Bosi Minja akitegemea kufaidika maradufu kutokana na riba na pesa watakazochakachua wakati wa ujenzi wa shule hiyo. Usiku mbichi wa saa 1 usiku, ndipo walipoanza safari ya kuelekea Moshi, yeye na mpenzi wake Recho bila kujua Recho kashaandaa miundombinu ya kihalifu ya ukwapuaji wa pesa hizo.



Bosi Minja na mpenziwe Recho waliingia Moshi Mjini majira ya 3:45 usiku wakapokelewa kwa bashasha na wazazi wake Bosi Minja, kama kawaida ya Wachagga kwa kupenda nyama, wakakuta wamechinjiwa mbuzi mzima kisha akachomwa makhsusi kwa ajili yao.
Baada ya mapumziko mafupi, moto wa burudani ukawaka wakaanza kula nyama choma na kunywa mpaka manane ya usiku. Kesho yake Bosi Minja ilitakiwa arejee Arusha kwa ajili ya kumfuata Debora shuleni. Shule ilikuwa inafungwa kupisha mapumziko mafupi ya sikukuu ya 'Christmass' hivyo wazazi walikuwa wanahitajika kuwafuata watoto wao. Kulikucha salama familia nzima wakajumuika kupata staftahi ya mtori kwa chapati kisha baada ya kupita kitambo fulani, Bosi Minja aliaga kwa wazazi wake. " Baba na Mama nashukuru Mungu nimewakuta salama salimini, ila leo naondoka narejea Arusha kumchukua Debora shuleni. Mpenzi wangu Recho atabaki na nyie hapa kwa muda kabla ya kurejea Arusha. Afya yake kidogo ni mgogoro, dada Joyce anakuja nyumbani kukaa na Debora kipindi hiki cha likizo, pindi ikiisha tu likizo atakuja kukaa hapa na nyie nimemuomba afanye hivyo. Pia nimeagizia dada wa kazi anakuja kesho kukusaidieni kazi za nyumbani.
Hivyo nikutakieni kila la kheri muishi kwa amani na upendo, kwaherini". "Na sisi tunakutakia kazi njema, Mungu azidi kukushushia baraka zake ili uzidi kukutunza sisi wazazi wako. Tunajisikia fahari sana kupata mtoto mwenye mafanikio kama wewe, tena mwenye heshima na adabu kwa mkubwa na mdogo. Tunachowasisitizeni ni kuwa akijifungua msichelewe kufunga ndoa tu, hapo ndipo sisi wazazi wenu tunafurahi, safari njema" baba yake Bosi Minja nae alitia neno kisha wakapeana mikono ya kuagana na wazazi wake.
Baada ya hapo wakaenda chemba na mpenzi wake Recho wakateta mambo mawili matatu kisha wakapeperushiana mabusu motomoto wakaachana na kuagana. Recho akaambatana nae mpaka kibarazani alipoegesha gari yake Bosi Minja. Recho muda wote alikuwa anamsindikiza Bosi Minja kwa macho wakati anapanda gari lake huku machozi yanamtiririka, anajitahidi kuyazuia kwa kuyafuta hanchifu yake nyekundu. Bosi Minja akatoa kichwa chake nje ya kioo na kumuaga kwa mara ingine, "Goodbye my LOVE see you soon..Mwaaaaaah Mwaaaaaah" aliongea Bosi Minja huku anapunga mkono wake wa kulia akiwa ameshawasha gari lake. Recho nae akanyanyua mkono wake wa kulia akawa anaupunga hewani huku vilio vya kwikwi vinazidi.
Bosi Minja akang'oa nanga na kutokomea zake barabarani akitimua vumbi tu lililochanganyika na moshi wa gari. Machozi ya Recho yalikuwa ni machozi ya uchuro aliokuwa anamchuria Bosi Minja. Alikuwa anajua fika Bosi Minja atakaporudi tena nyumbani kwake hapa atarudishwa kwenye sanduku kama maiti. Kwanza hakuwa radhi kufunga ndoa na mtu aliyemzidi umri karibia mara mbili ya umri wake, atamtambulishaje mbele ya marafiki zake. Pili Bosi Minja alimdanganya hana mke, mkewe ameshafariki zamani na kumuachia mtoto mmoja wa kike, Debora lakini Recho pale ofisini ameshazifuma barua kadhaa alizozifungua kiujanjaujanja za Bosi Minja kutoka kwa mama Debora zikielezea masikitiko yake ya kutelekezwa na mumewe. Hivyo akilini mwa Recho alifuta kabisa wazo la kuolewa na mfadhili 'sponsor' wake Bosi Minja.
Wazazi wa Bosi Minja walikuwa wanaisubiria kwa hamu ndio hiyo. Wao kwao mama Debora walikuwa hawamuhesabu kama ni mke wa mtoto wao, joto baya la ukabila lilikuwa linachemka ndani ya vifua vyao. Kwao walitaka piga ua lazima mtoto wao pekee wa kiume, Joseph Minja awe na watoto damu ya kichaga kwa asilimia 100% kupitia kwa mke wa Kichaga.

Recho baada ya kulisindikiza gari la mpenziwe kwa macho akilishuhudia linapasua mitaa, linatimua moshi mweusi kuitafuta Arusha, akarejea ndani ukumbini anasogoa na mama mkwe wake. Ilipofika adhuhuri wakaelekea wote jikoni kutayarisha mlo wa mchana, huku baba yake Bosi Minja akiwa hayupo nyumbani ameelekea kusimamia miradi yake aliyofunguliwa na mtoto wake. Alikuwa anasimamia duka la vifaa vya ujenzi 'Hardware'.
Recho na mkwe wakiwa zao jikoni wanajipikilisha habari na mtu hawana, ghafla bin vuu... hali ya kiafya ya Recho ikaonekana kama inabadilika tena kwa mara ingine. "Aaaaah....Mamaaaaah.....Nakuuu..fw..... aaaaah.." ghafla tu Recho akaanza kulalamika maumivu makali ya tumbo, huku amelikamatia tumbo lake kuashiria ana maumivu makali, huku machozi kupukupu yanamtiririka. Taharuki kubwa iliibuka, ikabidi kindakindaki itafutwe taksi ya haraka ya kumkimbiza Recho hospitalini. "Nipele...keee...ni..."Huruma Dispensari" pliiiiiz...!" aliongea Recho kwa msisitizo mkubwa huku akionekana ana maumivu makali anaongea kwa kujigagamiza, lakini akiashiria hataki hospitali ya serikali.
Ikabidi dereva taksi atii maagizo aliyopewa na mgonjwa hala hala ili kumfikisha salama mgonjwa. Alipofikishwa hapo dispensari haraka haraka akapewa kitanda huku vipimo vya damu na mkojo vikichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Baada ya kupita muda mrefu kidogo vipimo vikatoka maabara, daktari akampa maelekezo mama mkwe wake Recho juu ya kinachomsibu. "Mama poleni sana, mgonjwa wenu anaendelea vyema hana ugonjwa wowote ila anahitaji mapumziko ya kutosha kutokana na ujauzito wake, hivyo hamtoruhusiwa kumuona mpaka kesho asubuhi, ili kuwapa madaktari na manesi muda wa kutosha wa kumhudumia kwa uangalizi wa karibu, msiwe na hofu mambo yote yanaenda kwa urari..!" aliongea mmoja wa madaktari ambaye ilionyesha ni mtu wanayefahamiana kinagaubaga na Recho, na ndio sababu Recho kuchagua dispensari hiyo.
" Sawa baba nimekuelewa, tunashukuru kwa msaada wenu maana mwenza wake yupo Arusha, hivyo sisi hapa ndio wazazi wake. Tunakutakieni kila la kheri Mungu awape maarifa ya uponyaji wake" aliongea mama mkwe wake Recho kwa uso wa bashasha akionekana amefurahishwa vilivyo na ripoti ya daktari. Wakaagana na daktari ili kupisha wagonjwa wengine waliokuwa foleni kupata nafasi ya kumuona daktari.
Mama yake Bosi Minja alipotoka hapo hospitali mguu kwa mguu, kwa mwendo wa matiti mpaka nyumbani kwa mama yake Recho kumpa taarifa za ugonjwa wa binti yake ya pekee na maendeleo yake hospitalini hapo. Alipomfikishia habari hizo wakapangiana kabisa zamu za kupeleka chakula hospitalini kuanzia hiyo kesho yake. Mama yake mzazi na Recho alikuwa roho juu juu akihofia binti yake mimba isije kuchomoka au akaenda na ulele ngoma kimoja mpaka akhera. Mama Recho alikuwa anamsubiria kwa hamu mjukuu wake mtarajiwa hasa ukichukulia upweke alionao wa mtoto mmoja tu, kama dawa. Alitarajia mjukuu wake huyo kumlea kama mboni ya jicho. Alishajiandaa kwa hilo kwa maana alimjua fika binti yake Recho bado hajajiandaa kuwa mama bora, ujana bado ulikuwa unamsumbua sana.
Ilipofika majira ya magharibi, mama Recho akamrudisha nyumbani kwake mkwe mwenzie kwa gari lake. Wakaagana huku wote wakipangiana asubuhi mama yake Bosi Minja kudamka mapema kabisa kwenda kuangalia maendeleo ya mgonjwa, huku mama Recho akipanga kwenda kupeleka chakula mchana.


"Daddy I want be a pilot what is your opinions..."(Baba mimi nataka niwe rubani wa ndege, nipe maoni yako). "Daddy where is my mummy?"(Baba, mama yangu yupo wapi?). "Daddy last month I left my chocolates in your room.."(Baba mwezi uliopita niliacha chocoleti zangu chumbani kwako.). Debora kwa umri wake wa miaka 4 alikuwa hachoshi yeye kutwa ni kuongea kama chiriku, anamtwanga maswali baba yake mpaka anakoma. Baba yake alikuwa hamkaripii wala kumfukuza kuwa anamsumbua, kwa sababu yeye kama Mwalimu kwa fani yake alikuwa anaelewa ubongo wa mtoto kipindi hicho upo safi na kiu kali ya kujifunza vitu vipya.
Alikuwa anajitahidi kumjibu maswali yote madogo madogo kila anapoulizwa. "Leo binti yangu unataka ule nini...likizo hii sitaki upate shida binti yangu" aliulizwa Debora na baba yake kwa kudekezwa. "Leo ataka akule "chips kuku na sodaaa" dadiii..." alijibu Debora kwa sauti ya kudeka huku tayari ameshamparamia mapajani baba yake.
"Shaka ondoa binti yangu....you are my queen...!" akijibu Bosi Minja huku akiwa ameshika tama shavuni anamuangalia Debora. Alikuwa anavusha mawazo anamuangalia jinsi Debora alivyofanana na mama yake, kwa umbo mpaka salihi wa tabia. "Debooo...mda wa kuoga umeshafika haya twende..." shangazi mtu alikuja kumchomoa Debora miguuni kwa baba yake.
"OK....aunty...nakuja.." aliongea Debora huku akimfuata shangazi yake, ambaye ukaribu wao ni kama nyoka na shimo, utasema ndio mama yake mzazi kwa jinsi walivyoshibana. Bosi Minja ikawa ni afueni kwake ya kumpotezea mawazo akaondoka na kwenda kuwasha gari kwenda kumnunulia binti yake chakula alichomuahidi kumnunulia usiku huo. Debora alizoeana sana na shangazi yake kutokana na ukaribu wao, yeye ndio alikuwa muda wote anapotoka shuleni anamlea mpaka siku anaporejea shule. Haikupita muda mrefu sana usiku mbichi ukiwa umeshaingia, Bosi Minja akarejea nyumbani akiwa na vifurushi vya manyamunyamu ya chakula cha familia nzima. Akatoka nje ya upenuni mwa nyumba na kwenda mubashara kumfungulia mbwa wake 'Jerry' kwenye kibanda chake huku kijana wa kazi za nje akiwa anaaga kurudi nyumbani kwake usiku huo.
"Sawa, usiku mwema ila kesho uwahi kudamka kuja si unajua Jumapili kuna kazi nyingi huenda tukapokea wageni hivyo usichelewe sana... ..chukua hizi pesa kidogo nawe uwaburudishe familia mwisho wa juma, kwaheri ya kuonana" aliagana Bosi Minja na kijana wake huku akifungua pochi yake iliyotuna minoti na kuchomoa noti moja ya shilingi 200 ya karatasi kisha akamkabidhi.
"Mungu Baba wa Mbinguni akubariki Bosi wangu..!" alishukuru huku uso wake wote ukiwa umevaa tabasamu kunjufu kutokana na pesa hiyo ya bonasi aliyopewa nje ya mshahara wake. Alipotoka tu, Bosi Minja akarudishia geti lake na kujifunga na kuingia ndani kujumuika na familia yake kwa pamoja. Wakakaa mesini wanakula mlo wao wa usiku 'Chips Kuku' raha mustarehe habari hawana.
Walipomaliza mlo wao, wakajongea sebuleni na kuwasha Video wakaanza kuangalia sinema ya kihindi inayoitwa 'HATYA-GOVINDA' filamu ambayo Debora alikuwa anaipenda mno. Kwa miaka hiyo Arusha nzima watu wanaomiliki video walikuwa hawazidi watu watano (5) na Bosi Minja alikuwemo katika watu hao. Walikuwa wakipita mitaani wananyooshewa vidole kuwa wale wanamiliki Video kutokana na uthamani wa kifaa hicho zama hizo. Ilikuwa ni filamu ndefu sana kama ujuavyo filamu za kihindi yenye kuhuzunisha na kufurahisha.
Ilipofika saa 6:30 usiku wakanyanyuka kwa ajili ya kwenda kulala wakiwa wamezidiwa na usingizi wa uchovu wa pilikapilika za mchana kutwa. Bosi Minja ndio alizidi kuzidiwa hasa kutokana na kukosa mapumziko ya uhakika kuanzia Ijumaa alivyotoka kazini. "Baba Debora nikitaka kusahau kesho tunataka twende kanisani misa ya kwanza, hivyo jiande kuamka mapema utupeleke na gari.....!" alitoa ombi lake shangazi yake Debora kwa kaka yake akiwa ameshashika kitasa cha mlango wa kuingilia chumbani kwake, chumba ambacho kipo mkabala na kile cha Bosi Minja.
"Haya...nikipitiwa tuamshane, Alamsiki..!" akajibu kisha wakatakiana usiku mwema. Mchaga na kanisani ni kama paka na maziwa, hata awe muovu vipi lakini mlango wa kanisa hawezi kuusahau, atakwenda kanisani wakitoka tu, biblia atapewa mtoto arudishe nyumbani wazazi wanakaa Baa sasa kugida Bia zao mpaka kuchwee.
Hawakuchukua muda mrefu tokea wapande vitandani kabla hawajapitiwa na usingizi mzito wa fefefe kutokana na uchovu. Manane ya usiku Shangazi yake Debora alikuwa ni wa kwanza kusikia vishindo vizito vya kuvunjwa kwa mlango wao wa mbele huku mbwa anabweka kwa fujo kuashiria kuna jambo baya. Kisha mbwa yule akatulia kubweka kama vile ametulizwa na kitu kwa kutoa sauti ya malalamiko kisha sauti ikakata mara moja.
Alikuwa tumbo moto akijua fika mambo yameshaharibika, akauvaa ujasiri wa ghafla kwa kufungua mlango, akatoka nje ya chumba chake, "Tulia hivyo hivyo kama bado unaupenda uhai wako vinginevyo tutakugeuza kuwa tambiko la risasi..." ilikuwa ni amri aliyopewa na mmoja wa wale majambazi waliovalia makoti marefu yenye kufunika vichwa vyao huku mmoja mwenye kitambi akijifunika mpaka sura yake kwa barakoa iliyoacha macho yake. Akagongwa kisogoni na kitako cha bunduki akapoteza fahamu hapo hapo kwenye korido. Bosi Minja ambaye alilala pamoja na binti yake Debora kitanda kimoja alivisikia vishindo vya kuvunjwa kwa mlango. Mwanzoni alidhania yupo ndotoni lakini baadae akatanabahi kuwa sio njozi ni ukweli wamevamiwa.
Umeme ulikuwa umezimika jengo zima kutokana na hitilafu bandia iliyosababishwa na majambazi wale kabla hawajavunja geti la kuingilia. "Deboo.. Debooo...amka ingia uvunguni mwa kitanda kuna watu wabaya wametuvamia, usipige kelele watakuua..." hima hima alimkurupusha usingizini binti yake na kumnong'oneza kisha akamnyakua juu juu akimsaidia kuingia uvunguni. Haraka haraka akiwa tumbo wazi na pajama yake akachukua funguo wake na kukimbilia kufungua kabati lake ile atoe bastola yake, akiwa na rajua ya kupambana na kujiokoa. "Tulia hivyo hivyo usitikisike" Bosi Minja alihisi ubaridi wa mdomo wa bastola akiwa katika kiza kile. Jambazi alipindukia chumbani nyatunyatu kwa kupitia juu ya dari kwenye uwazi wa silingibodi akitokea ukumbini. Jambazi yule akawasha kurunzi yake ndogo akarudi kinyumenyume huku amemnyooshea mdomo wa bastola Bosi Minja. Jambazi yule akafungua mlango kwa ufunguo wakaingia wenzake wawili ndani ya chumba, sasa wakawa watu watano, Bosi Minja, majambazi watatu pamoja na mtoto Debora chini ya uvungu.
"Geuka nyuma tuangalie..." alitoa amri mmoja wao huku wanammulika na mwangaza wa kurunzi machoni mwake. "Tumekuja kufuata dola elfu 10 zetu....umeziweka wapi?" Aliongea kwa sauti kali isiyo na chembe ya utani akionyesha ana uhakika anachokiongea. Kauli hiyo iliibua mshtuko mkubwa na wahaka katika moyo wa Bosi Minja. Akitafakari bila kupata majibu hawa wamejuaje hicho kiwango wakati ni siri baina ya watu watatu tu, yeye, mhasibu Mbweku na Recho, mpenzi wake. "Sina hizo pesa mnazozitaja, aliyekunyetisheni amewadanganya, mimi niko polo tu hohe hahe... " alijitutuma kujibu akijaribu kuangalia bahati yake ya kujiokoa kwenye kifo kama itatokea aitumie vizuri.
"Mpige risasi mpige risasi mwongo mkubwa....." alisikika mmoja wa wale majambazi mwenye kitambi akiongea kwa sauti ya kutafuna maneno kama mtu anayekula bazoka ili sauti yake isijulikane kwa urahisi. Amri hiyo ilitekelezwa kivitendo kwa mvua ya risasi kuanza kumiminwa kifuani mwake Bosi Minja. "Aaaaaaaah.......Mme.......ni.......u...... aaaaahh...." alillama akionekana ana maumivu makali, huku akiwa ametupwa chini kwa kishindo. Wakaanza kuvunja makabati, na kuanza kutupa vitu sakafuni, haikuchukua muda wakafanikiwa kuziona kwenye moja ya droo ya kabati zikiwa zimefungwa bandali bandali mipira ya rababendi. Yule jambazi mwenye kitambi baada ya kuona Bosi Minja tayari kashateketezwa kwa risasi za kutosha akavua maski yake ya usoni na kupiga ukelele wa furaha ya kuzitia mkononi pesa nyingi kiasi hicho kiurahisi.
Kilio cha maumivu cha Bosi Minja alipokuwa analalamika wakati shaba zimetua mwilini mwake, zilisababisha binti yake Debora ajikojolee kwa uwoga, huku anatweta kwa hofu akiwa uvunguni, akijua fika jambo baya limemsibu baba yake. Mkojo ule ulitiririka mpaka ukafika pale aliposimama yule jambazi mwenye kitambi bila mwenyewe kujua. Alikuwa ametingwa kumulika na kurunzi yake huku na kule wakati maburungutu ya pesa yanaposhindiliwa kwenye begi dogo la mgongoni. Nyaraka mbalimbali za umiliki wa mali nazo zinachukuliwa na kufinyangwa kwenye begi hilo.
Alipopiga hatua tu kwenda mbele akajikuta anateleza kwenye mkojo ule wa Debora na kupigwa mweleka mpaka chini. Debora akiwa chini ya uvungu sasa alifanikiwa kumshuhudia uso wake yule jambazi mpaka maeneo ya shingoni kiufasaha kabisa kwa msaada wa mwangaza wa kurunzi yake iliyodondoka sentimeta chache toka kichwani. Debora hofu ilizidi kumtawala akajua tayari ameshaonekana, lakini sudi ilikuwa upande wake yule jambazi hakuwa na muda wa kuangaza uvunguni haraka haraka akajizoa toka sakafuni.
"Pole...upo OK..Taita? " aliongea mmoja wa majambazi wale huku akimsaidia kunyanyuka. "Nipo fine hamna matata, ila tuondoke naskia maumivu makali ya kiuno na tumbo linakata... " alitoa maagizo huku akiwa amejishika kiunoni mikono yake kama mtu aliyefanya mazoezi magumu ya mwili akachoka. Koti lake lilikuwa limelowa damu ya kutosha tu iliyotiririka kutoka kwenye mwili wa marehemu Bosi Minja ambaye tayari alishakata roho na kurejea jongomeo. Wakaanza kuondoka huku akisaidiwa na yule mwingine kwa kumkokota mabegani. Mpaka walipofika mlango mkubwa wa kutokea wakaanza kushauriana. "Kinda wake wa kike amejificha wapi, lazima ateketezwe....!" alikumbushia mmoja wapo juu ya uwepo wa Debora. "Hana madhara achana nae maadamu pesa tumezinyaka tayari" aliongea yule mwenye begi la pesa. Wakafanikiwa kutoka nje ya geti mpaka wakalifikia gari lao lilipoegeshwa wakapanda. " Cobra sikia lakini ni muhimu huyo binti yake kupotezwa kama yupo asije kuwa shahidi dhidi yetu mahakamani" alitilia msisitizo jambazi kitambi baada ya kuanza kupata ahueni alipokaa kwenye kiti cha siti ya nyuma ya dereva. Ikabidi yule jambazi aliyejulikana kwa lakabu ya Cobra ashuke haraka ndani ya gari na kukimbilia ndani ya nyumba ile ya Bosi Minja yenye kiza totoro.
Alipoingia akaanza kumsaka Debora kila kona ya nyumba, kuanzia chooni, jikoni, chumbani, sebuleni mpaka chini ya uvungu mwa kitanda hamna kiashiria chochote uwepo wa Debora. Ikabidi wenzake wapige honi mbili za haraka haraka walipoona imefika robo saa hajatoka ndani ya nyumba. Cobra kusikia honi ile imepigwa akachomoka nduki spidi kama zote kuharakia garini yasiye mambo yakaharibika.
"Twendeni hayupo inaonyesha hajalala humo ndani" Cobra aliongea huku mwenzake akijibu kwa vitendo kwa kuwasha gari na kuliondoa eneo lile. Debora alitoweka kimiujiza bila wao kung'amua ama kweli waswahili wana msemo wao ya kuwa watoto ni malaika wa Mungu. Huenda msemo huu ulikuwa na mantiki, labda Debora alinyakuliwa kwenda mawinguni hasa ukichukulia hata kuzaliwa kwake ni kimiujiza.


Kulipopambazuka Jiji zima la Arusha lilizizima kwa taarifa ya kifo cha Bosi Minja 'Mlezi wa wana'. Vilio vilizagaa karibia kila kitongoji hasa kutokana na umaarufu wake. Alikuwa ni
kipenzi cha watu wa rika zote kuanzia vijana, akina mama na wazee. Alikuwa anajichanganya nao kwenye shida na raha zao bila ubaguzi wa hali zao. Jambo ambalo lilimjengea mapenzi makubwa na kufanikiwa kuiteka mioyo ya wana Arusha.
Wengi waliokuwa na nyadhifa kubwa na nyeti kama Bosi Minja walikuwa ni watu wa madahiro na kujisikia sana. Walikuwa wana viwanja vyao maalumu vya watu walalaheri kujimwayamwaya. Hata mialiko ya hafla ya sherehe na matukio ya msiba walikuwa wanabagua wapi waende na wapi wasiende.
Kadamnasi ya watu walijaa ndani na nje ya nyumba ya Bosi Minja kuja kutaazi wapate kujua chanzo hasa cha kifo chake. Ndipo wakafahamu kuwa ametwangwa risasi 5 za kifuani na majambazi kisha wakapora pesa ambazo hazijajulikana thamani yake na nyaraka kadhaa. Simulizi za majirani zikatoa shuhuda kuwa huenda majambazi hao walitumia bunduki zenye kiwambo cha kuzuia sauti kwa maana hakuna hata mmoja aliyesikia milio ya risasi hizo 5 zilizonyofoa roho ya Bosi Minja. Maiti ya Bosi Minja ilishaondolewa eneo la tukio baada ya polisi kumaliza taftishi yao ya awali.
Wananchi kadri masaa yalivyokuwa yanaondoka wakaanza kuondoka mmoja mmoja mpaka wakabaki watu wa karibu na marehemu Bosi Minja. ya kusafirisha mwili wa marehemu kuelekea Kilimanjaro ikaanza kupangwa na rafiki zake wa karibu. Rafiki zake hawakuwa watu mburumatari kiuchumi, hivyo walipanga kuandaa mazishi ya kifahari kuonyesha shukrani yao kwa wema waliotendewa na rafiki yao Bosi Joseph Minja katika uhai wake wa miaka 46 duniani. Jeneza lake walipanga kulinunua Jijini Nairobi, tayari alishatumwa mtu na vipimo vya jeneza wanalohitaji.
Magari ya kifahari yasiyopungua 20 yalipangwa kusindikiza mwili wa marehemu. Huku kwenye sekta ya chakula wakipanga kuangusha ng'ombe 50 na kupikisha mchele gunia 100. Wakati vikao vya mazishi nje vinaendelea nje, ndani Askari kanzu mmoja alikuwa na shughuli ya mahojiano na shangazi yake Debora ambaye alisharuhusiwa hospitali baada ya kupumzishwa kwa masaa kadhaa. Askari kanzu yule akamnyakua shangazi yake Debora kutoka kwenye msitu wa waombolezaji na kukaa nae chemba kwa ajili ya mahojiano ya kipolisi. Mahojiano ambayo walikuwa wanatarajiwa kutoa penyenye za wahusika wa ujambazi huo.
Askari kanzu: "Pole sana msiba, Mungu akupe subira. Mimi ni askari kanzu niliyopewa jukumu la upelelezi wa kifo cha Bosi Josephu Minja, hivyo nitaomba ushirikiano wako"
Shangazi: "Ahsante tumepoa ndio mipango ya Mungu haina makosa, hamna shida wewe tekeleza wajibu wako"
Askari kanzu: "Jina lako kamili unaitwa nani? "
Shangazi: "Naitwa Joyce Minja"
Askari Kanzu: "Umri wako ni miaka mingapi?"
Shangazi: "Umri wangu ni miaka 43"
Askari kanzu: "Umeolewa?"
Shangazi: "Hapana sijaolewa kwa sasa mimi ni Mjane..ila ninao Mji wangu maeneo ya Sanawari....!"
Askari kanzu: "Unafanya kazi gani?"
Shangazi: "Mkulima"
Askari kanzu: "Una uhusiano gani na marehemu Josephu Minja"
Shangazi: "Ni kaka yangu wa toka nitoke kwa baba na mama"
Askari kanzu: " Unaweza kuelezea vipi usiku wa tukio la kifo cha marehemu kaka yako! "
Shangazi: "Tulikula chakula cha usiku, kisha tukakaa sebuleni kuangalia filamu mpaka karibia na saa 6:30 usiku. Tukaagana kwenda kulala akiambatana na binti yake Debora. Tulipolala usiku wa manane ndipo nikasikia vishindo vya kuvunjwa mlango. Nilipotoka tu wakaniweka chini ya ulinzi na kunipiga na kitako cha bunduki kichogoni nikapoteza fahamu sikujua kinachoendelea. Nimekuja kuzinduka na kupata fahamu saa 12 asubuhi, huku nikiwa na maumivu makali ya kichwa. Nikakuta chumba cha kaka yangu marehemu Josephu Minja kipo wazi. Nikajikokota kwa msaada wa ukuta na kuingia ndipo nikakuta maiti ya kaka imelala sakafuni ikiwa na matundu kadhaa ya risasi mwilini mwake. Damu ilikuwa imegandiana kuonyesha aumeliwa masaa mengi yaliyopita. Nikataharuki na kujikuta naanza kumsaka Debora nijue kama na yeye yupo hai au ameuliwa. Ndipo nikamkuta kwenye tenga la kuwekea nguo chafu akiwa amejificha humo. Ile huzuni na majonzi tuliyokuwa nayo ndio tukapiga makelele ya vilio vya kuwaita majirani ndio wakaja kufahamu kuwa usiku wake tulivamiwa na majambazi".
Askari kanzu: "Je marehemu ameshawahi kukudokeza kama ana maadui wowote wanaomuwinda? "
Shangazi: "Hapana hajawahi na ninavyofahamu, marehemu kaka alikuwa ni kipenzi cha watu na hilo nadhani umeshuhudia mwenyewe namna halaiki ya watu walivyojazana hapo nje"
Askari Kanzu: "Marehemu ana mke na anaishi wapi huyo mkewe? "
Shangazi: "Marehemu anaye mke wa ndoa kwa sasa yupo masomoni wilayani Masasi, Mtwara"
Askari kanzu: "Nimeskia pia ana kimada wake hapa Jijini Arusha ni mfanyakazi wake wa ofisini kwake, Je wewe unalifahamu hilo? "
Shangazi: "Kashawahi kunitambulisha kwake kwa hiyo wifi yangu mpya na hata wazazi wangu wanamfahamu fika"
Askari kanzu: "Je yupo hapa msibani? "
Shangazi: "Hapana yupo Moshi kwa wakwe zake watarajiwa, walisafiri jana na marehemu kaka"
Askari kanzu: "Je dhana zako hazikupelekei kuwa yeye ni mtuhumiwa kwa sababu anajua siri nyingi za marehemu na hata kujua wapi pesa zinahifadhiwa?"
Shangazi: "Kwa kweli sifahamu na siwezi kujichumia dhambi za bure, maana kama kutengenezewa maisha huyo wifi yangu kafanyiwa mambo makubwa tu na kaka"
Askari kanzu: "Je unaweza kufahamu ni pesa kiasi gani zimeibwa, mbali ya hizo nyaraka zake binafsi?
Shangazi: " Siwezi kufahamu sikuwa msiri wake wa kunieleza mambo ya pesa zake"
Askari kanzu: "Umesema una mji wako, usiku wa kuamkia leo kuna dharura gani haswa iliyokusibu mpaka ukaja kulala kwa kaka yako na ndio usiku wa tukio la mauaji, huoni watu wanaweza kuwa na mashaka na wewe kuwa ni mhusika, kuwa umekuja kupanga mauaji ya kaka yako? "
Shangazi: "Yaani mimi kweli nimuue kaka Jose mimi kweli? " akaanza kuangusha kilio cha nguvu, kisha akanyama kulia akafuta machozi yake kwa kutumia upande wa kanga. "Kaka huwa anaiomba binti yake kila wanapofunga shule nije kukaa nae mpaka shule inapofunguliwa ndio narejea kwangu, sasa mtu akiwa na hisia mbaya dhidi yangu shauri yake, Mungu ndio mtetezi wangu dhidi ya watesi wangu" aliongea kwa hisia kali huku macho yake yakiwa mekundu kama nyanya iliyoiva na kususwa shambani na mkulima.
Askari kanzu: "Ahsante kwa ushirikiano wako, ila tutaelekea huko Moshi kwenda kuwahoji wazazi wako na huyo wifi yako huenda tukaambulia chochote kitu, na usinichoke kama nitarudi tena kijijini, lengo ni kuwatia mbaroni wahusika wote wa unyama huu waliomfanyia kaka yako"
Shangazi: "Ah...s... ante" alijibu kwa kilio cha kwikwi shangazi yake Debora huku akishindwa kuzuia mbubujiko wa machozi yake.
Askari kanzu yule akaaga na kuondoka zake huku akimuacha shangazi yake Debora akiungana na ndugu, jamaa na marafiki katika kuendeleza maombolezo ya msiba ule mzito wa kigogo wa Jiji la Arusha. Akina mama watu wazima walikuwa wanachukua muda mwingi kumfariji Debora ambaye alionekana kabisa kavurugwa kisaikolojia kwa sababu kashuhudia matukio mazito zaidi ya umri wake kuweza kustahimili. Fadhaa iliyowakuta hamna hata mmoja aliyekumbuka kumpa taarifa mkewe halali wa ndoa, mama Debora. Hasa kutokana na kwamba mama Debora hajawahi kukanyaga Arusha hata mara moja na Bosi Minja hakuwahi kujitambulisha kwa rafiki zake kuwa ana mke na ndio mama mzazi wa binti yake Debora. Walichokumbuka ni kupeleka taarifa kwenye Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kwa ajili ya kuwapasha ndugu zake na marafiki zake Tanzania nzima.


Mzee Minja usiku wa kuamkia Jumapili, usiku ambao mtoto wake marehemu Josephu Minja amechakazwa risasi na majambazi alilala kwa shida. Alikuwa mahamumu kichwa kinamgonga barabara na maumivu ya mgongo. Usingizi wote ulimpaa usiku kucha akiugulia. Mkewe nae chango la uzazi likawa linamkata utasema mwanamke mjamzito anataka kujifungua. Uchungu wa mwana aujuaye mzazi, hiyo ilikuwa ni taarifa wanapewa ya msiba mzito wa nguzo yao katika maisha ya uzeeni Bosi Minja. Mtoto ambaye ndio pekee amefanikiwa kufika elimu ya Chuo kikuu,wamehangaika nae kwa kukopa, kulima buni ili mradi aweze kutimiza ndoto zake za kielimu. Sasa ndio ulikuwa wakati wao wa kula pensheni ya malezi toka kwa kijana wao, hata hawajaanza kufaidi vizuri, Malaika mtoa roho anawakatisha starehe yao.
Mpaka kufika majira ya alfajiri ndio akapatwa na usingizi mzito. Mama yake Bosi Minja ikabidi ajikaze kisabuni hivyo hivyo kama ujuavyo nani kama mama!. Mama ukimuona ameugua akalala kitandani basi tambua huo ugonjwa ni wa hatari sana lakini kwa kawaida mama anaweza kuugua na wala watu wasifahamu kama ni mahamumu. Atapika chakula, atafua nguo za watoto, atafanya usafi wa nyumba, ataosha vyombo na majukumu yake mbalimbali ya kila siku bila kuchoka, bila kuwa na likizo miaka nenda miaka rudi. Mama yake marehemu Bosi Minja ilipofika asubuhi akajikaza kisabuni kama vile ni mzima wa afya hana chochote kinachomsumbua mwilini akaandaa mtori wake kwa ajili ya mgonjwa, mkwewe mtarajiwa Recho aliyelazwa 'Huruma Dispensari', moja ya kituo cha afya kilichokuwa kinatoa huduma bora Jijini Arusha kikiwa kinamilikiwa na mwekezaji Mzungu mwenye uraia wa Kenya.
Asilimia kubwa ya Madaktari wake walikuwa ni Raia wa Kenya. Mpaka kufikia saa 12:15 asubuhi alikuwa tayari ameshawasili kwenye viunga vya dispensari hiyo. Moja kwa moja akapitiliza mapokezi na kwenda kumuulizia mgonjwa wake kalazwa wodi gani. Nesi wa zamu alikuwa ni Bibi mtu mzima kiumri aliyeonekana yupo makini na kazi yake. Alikuwa anawasikiliza kwa makini wateja wanaokuja dawatini kwake na lugha nzuri ya kujali wateja. Akaelekezwa aelekee wodi ya wazazi, ikabidi apatwe na mshtuko usiomithilika. Ikabidi aulizie tena kwa mara ya pili, maana mgonjwa Recho kweli ni mjamzito ila siku za kujifungua zilikuwa bado kabisa sasa alikuwa anashangaa iweje apelekwe wodi ya wazazi. Alipopata ufafanuzi kiufasaha toka kwa yule Nesi ndipo akaelewa kuwa Recho amejifungua majira ya jogoo la pili.
Akaanza kutembea kuelekea kwenye wodi ya wazazi kwa haraka huku akitamani apaishwe kwa furaha sheshe aliyokuwa nayo ya kupata mjukuu. Alipofika akabisha hodi chumba alichoelekezwa kisha akafungua mlango na kuingia. "Waooooh.....hongera mwanangu na pole kwa maumivu" aliongea kwa furaha mama yake Bosi Minja huku akilitua chini kapu lenye chupa iliyojazwa mtori. "Ahsante nashukuru mama.." alijibu Recho kwa ufupi huku macho yake yakiangalia chini kwa aibu akikwepesha kabisa kuangaliana nae uso kwa uso.
Dhamira moyoni ilikuwa inamsuta Recho hasa kwa kuwa alikuwa anajua kabisa kwa zaidi ya asilimia 100 kuwa mtoto aliyemzaa masaa machache yaliyopita sio wa Bosi Minja. "Umetuletea mtoto gani, ni mume wangu au mke mwenza wangu.." aliuliza kwa shauku Bibi yule akitaka kufahamu jinsia ya mjukuu wake aliyezaliwa. "Ni mumeo, mtoto wa kiume...." alijibu Recho huku akijilazimisha kutia utani kwa shida sana. "Muda wa kuona wagonjwa umekwisha, tupisheni sasa tuwahudumie ahsanteni sana kwa kuja kuwafariji wagonjwa wenu" lilikuwa ni tangazo la nesi anayepita kila wodi na kengele yake akiipiga kuwaondoa ndugu wa wagonjwa. Mama yake Bosi Minja ikabidi akusanye kila kilicho chake akitoe zake.
Recho alikuwa amejifungua mtoto njiti wa miezi 7, hivyo alitakiwa akae hapo kwenye kituo cha afya kwa siku kadhaa huku mtoto akiwa anatunzwa kwenye vifaa maalumu vya kuhifadhia watoto njiti. Hima hima akitembea mashimashi na kapu lake akielekea kwenye kituo cha daladala kurejea nyumbani kwake kumpa taarifa mumewe juu ujio wa mjukuu wa mtoto wao Joseph Minja.

Mzee Minja aliamka toka usingizini majira ya mafungulia ng'ombe akiwa kidogo amepata ahueni. Baada ya kupiga mswaki na kuoga akaamua achome utumbo wake kwa kahawa chungu ya moto sana, iliyochanganywa na samli bila sukari "Bullet Coffee" bila mchapalo wowote wa kitafunwa. Hapo akajisikia nafuu sana.
Akatoa kiti chake nje ya kibaraza huku pembeni ana redio yake kubwa maarufu kwa jina la 'Mkulima' anasikiliza 'Redio Tanzania Dar es Salaam' (RTD) kipindi cha muziki zilipendwa asubuhi hiyo. "Hureeeh....Hureeeeeeh.....Ripu... Ripu...mkwe wetu Recho katuletea mnangu" alilipuka kwa furaha mama yake marehemu Bosi Minja baada ya kumuona mumewe kibarazani kabla hata ya salamu yoyote. "Ooooh....usiniambie mama Jose huyo kichanga kampata lini? Mbona maajabu..!" Mzee Minja alilaki mazungumzo ya mkewe kwa shauku kubwa. "Huo ndio uhalisia, kumbe changolililokuwa linaniuma usiku kucha lilikuwa ni la kumpokea mjukuu wangu jamani, amejifungua ila mtoto ni njiti, hivyo mama na mtoto wataendelea kubakia hospitalini" alitoa maelezo ya kina Bibi Deborah yaliyomshibisha mumewe.
"Daaah.....mnangu wetu atakosa mambo mengi ya taratibu za kimila nilitamani aje leo leo" aliongea Babu Debora kwa sauti ya manung'uniko, hasa kutokana na ushabiki wake wa mambo ya kimila.
"Usijali kikubwa ni kuwaombea uzima wao, mie ngoja niingie jikoni nipike mlo wa mchana, itabidi nimtume kijana akapeleke taarifa kwa mama yake mzazi Recho, maana hata taarifa hizi ana mipango ya kupeleka chakula mchana hivyo ni bora azijue mapema!" aliongea Bibi Debora huku akijiandaa kufungua kitasa cha mlango wa kuingilia ndani. Mila zao Wachaga, mtoto akishazaliwa mkunga aliyemzalisha mama huagiza majani yaitwayo kwa kichaga masunzuku ambayo huyachovya ndani ya maji ya uvuguvugu na kisha kumfuta nayo mtoto mwili mzima na kumpaka siagi mwili mzima. Baada ya hapo mtoto hupewa dawa fulani ili akitumia maziwa ya mama yasimdhuru kisha hupewa maji ya chemuchemu au ndizi iitwayo mrarao iliyovumbikwa ndani ya majivu ya moto kabla ya kumenywa ili ipate kuiva vizuri na kuwa laini.
Ndizi hii ikishaiva hutafunwa na kutemewa mtoto kinywani aimeze. Chakula hiki cha kwanza anacholishwa mtoto mchanga 'mnangu' huitwa kelya ketocha mana ulaka maana yake, chakula cha kutoboa koo la mtoto. Pia Ilikuwa mwiko kumuona mtoto kabla ya kutimiza miezi mitatu kutokana na imani kadhaa zilizokuwepo. Alama ya kuonyesha nyumba au mahali palipofanywa marufuku ni kusimika mti uitwao kwa kichagga sale ulio na majani yaliyopigwa fundo na kusimikwa karibu na mlango wa nyumba ya mzazi.
Mila hizo zote Babu Debora alitamani zitumike kwa huyo mjukuu wake mpya, lakini mambo yalikuwa nje ya uwezo wake. Akaendelea kubakia pale kibarazani anasubiria mkewe apike 'machalari' huko jikoni, moja ya chakula cha asili alichokuwa anakipenda sana Babu Debora. Muda ukazidi kuyoyoma mpaka ikafika saa 7:00 za mchana, ikasomwa taarifa ya habari ya adhuhuri mara baada ya taarifa hiyo ya habari iliyochukua takribani dakika 5 kwisha yakaanza matangazo ya vifo. Ikasikika sauti "Booooooooommm....!" kutoka kwenye redio ikiashiria kuanza kwa matangazo ya vifo.
Tangazo la kwanza tu kuanza kutangazwa na mtangazaji lilikuwa ni la msiba wa Bosi Minja. "Shirika la Peace Corps-Tanzania linasikitika kutangaza kifo cha Mratibu wake kanda ya Kaskazini, Bwana Joseph Minja kilichotokea usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake maeneo ya Philips kutokana na kupigwa risasi na majambazi. Habari ziwafikie Baba na Mama yake waliopo maeneno ya Boma Ng'ombe, Moshi, ndugu na jamaa zake waliopo Marangu, pia habari ziwafikie walimu wote wa Morogoro Sekondari mkoani Morogoro.Vikao vya maandalizi ya mazishi ya marehemu vinaendelea nyumbani kwake maeneo ya Philips. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi-Amiiin".
"Ooooh.....Oooh.....Yelewiiiiiiiii........Aaakh Aaakh.... Aaakh...!" alikuwa Babu Debora amepagawa anapiga kelele kama kama mtu aliyepandisha ruhani anahitaji kisomo cha ruqiya apate kutulia. Redio yake aliyokuwa muda wote ameikamatia mkononi aliiona kama kaa la moto, akaitupia kule na kupasuka vipandevipande. Mayowe yale yaliwavuta majirani, na mkewe nae ilibidi akurupuke toka jikoni ayaache machalari yake yanachemka na kwenda kuangalia mumewe kimemsibu nini.
Majirani wengi walikuwa tayari wamesharejea makanisani kwao, wanataka kupumzika na familia zao lakini ilibidi lazima waje kusikiliza kilio hicho hasa kama ujuavyo ukiona mtu mzima analia ujue kuna jambo sio bure. Ikabidi kwa shida sana awaeleze juu ya kifo cha Bosi Minja kilichotangazwa kwenye redio muda mfupi uliopita. Sasa eneo hilo likageuka kuwa msibani, vilio mtindo mmoja kila kona. Bosi Minja alikuwa ameshaondoka duniani amerejea jongomeo kwa Mola wake kwenda kuhesabiwa matendo yake ya duniani. Riziki zake za duniani tayari zilishakatika mali zake zote alizokusanya katika maisha yake ya dunia kwa njia ya halali au kwa dhuluma zilikuwa haziwezi kumfaa chochote huko jongomeo. Mpaka kufikia majira ya Alasiri maiti ya Bosi Minja ilifikishwa nyumbani ikiwa imesindikizwa na msururu wa magari ya kifahari ya waombolezaji kutokea Jijini Arusha.
Wazazi wa marehemu baada ya kujadiliana na kamati ya mazishi wakatoa tamko rasmi la familia kuwa mazishi yatafanyika siku ya Jumatano huko Marangu.


Mazishi ya Bosi Minja tayari yalishafanyika katika eneo la kata ya Marangu Magharibi ndani ya Wilaya ya Moshi Vijijini. Matanga ya msiba huo yaliwekwa huko huko Marangu, huku ndugu wa mbali na marafiki wakirejea majumbani kwao kuendelea na harakati zao za maisha ya kila siku wakiwaacha ndugu wa karibu wakiendelea na maombolezo yao kwa mpendwa wao Bosi Joseph Minja. Deborah kwa upande wake afya yake iliendelea kuwa tete, alikuwa kila anapokumbuka tukio lile la mauaji anaaanza kutetemeka kama vile mgonjwa degedege na ikifika usiku hasa usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili lazima ajikojolee kitandani. Walipompeleka hospitali kupimwa hakukutwa na shida yoyote, wakashauri tu tatizo litaondoka wenyewe baada ya kupita muda fulani. Kwa upande wa mama Deborah alikuja kukumbukwa siku ya Jumatatu wakati maiti inasafirishwa kuelekea Marangu ndipo wakatanabahi kuwa taarifa hajapewa na huenda hajui kifo cha mumewe. Ikabidi ipigwe simu kazini kwake hospitali ya Mkoa Morogoro. Napo walipopata taarifa hiyo ya huzuni wakapiga simu kwa Mkuu wa Chuo Cha Uuguzi-Mkomaindo Masasi. Wakajibiwa kuwa Chuo kimefungwa siku ya Jumamosi na mama Deborah ameondoka Chuoni siku ya Jumapili akiaga anaelekea Arusha kwa mumewe. Hivyo alipishana na taarifa nyeti sana ambayo ilikuwa ni muhimu kuipata. Kazini kwake mama Deborah wakatoa gari la kuwasafirisha watumishi wenzake wanaokwenda msibani wakiwa na ubani maalumu uliotolewa na ofisi pamoja na michango ya watumishi. Kama sio ubovu wa barabara ya Mikoa ya kusini kuja Dar es Salaam kuwa mbovu, huenda mama Deborah angewahi kumzika mumewe. Lakini safari ya kutoka Masasi mpaka Dar es Salaam ilimchukua wiki nzima, kutokana na Basi lao alilopanda la 'Mkaramo Bus Service' kunasa kwenye matope mara kwa mara kwenye maeneo korofi katika vijiji vya Mavuji, Matandu na Muhoro. Hivyo waliingia Jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi usiku. Usiku huo huo akakata tiketi ya Basi la kuelekea Arusha asubuhi yake siku ya Jumapili kwenda kuonana na mumewe Bosi Minja siku ya Jumatatu. Laiti angepitia Morogoro kwanza kabla ya kwenda Arusha huenda angepata taarifa za msiba toka kwa watu wa kazini kwake, pamoja na ndugu na jamaa, lakini kudra za Mwenyezi Mungu zilikuwa haziwezi kupunguza, ilishapangwa mama Deborah taarifa asizipate za msiba wa mumewe mpaka afike mwenyewe Arusha.
Wakati huo huo Askari kanzu yule yule aliyefanya mahojiano na Joyce Minja, shangazi yake Deborah baada ya wiki mmoja tokea kifo cha Bosi Minja akatua kazini kwa marehemu Bosi Minja siku ya Jumatatu, kuzidi kufanya taftishi zake huenda akanusa harufu ya muuaji wa Bosi Minja. Tayari Kaimu Mratibu mpya wa 'Peace Corps-Tanzania' alishateuliwa kuchukua nafasi ya Bosi Minja. Alishaanza kupiga mzigo kwa kuendeleza majukumu aliyoachiwa na mtangulizi wake Bosi Minja. Kama ujuavyoRecho alikuwa bado yupo likizo ya uzazi hajarudi kazini, huku mhasibu, Mr.Mbweku akiwa anaendelea kuchapa kazi kama kawaida yake bila kujua jumba bovu linataka kumbomokea yeye juu ya pesa zilizoibwa nyumbani kwa Bosi Minja. Yule askari akiwa amevalia nguo za kiraia alipitiliza moja kwa moja ofisini kwa Bosi mpya kwenda kujitambulisha na kueleza nia yake ya kuendesha uchunguzi wa kina ofisini hapo. Akafanya nae mahojiano ya kina na kisha kuchakuachakua nyaraka za siri za ofisi kwa zaidi ya masaa 3 mpaka akaanza kupata fununu ya anachokihitaji. "Mratibu mie nimemaliza kazi yangu ofisini kwako ila ningependa nifanye mahojiano na Mhasibu wako maana kuna nyaraka zinaonyesha marehemu Joseph Minja amekabidhiwa pesa sufufu na mhasibu wako siku ya Ijumaa, kidogo napata mashaka" aliongea yule Askari kanzu huku akijiandaa kunyanyuka kitini. "Hamna shida yoyote ngoja nikupeleke kwake huyo mhasibu" aliongea yule Bosi huku akisimama kitini kwake na yule askari akawa ameshasimama wakafuatana bega kwa bega kuelekea ofisini kwa Mr.Mbweku. "Hellow....Mr.Mbweku kutana na huyu Afisa usalama ana maswali yake machache anataka kukuuliza kuhusiana na msiba wa Bosi Minja" yule mratibu mpya alifanya utambulisho mfupi mara tu walipoingia ofisi ya Uhasibu. "Karibuni sana, nipo tayari kukueleza chochote unachokihitaji toka kwangu.." alijifaragua mhasibu kujibu lakini uhalisia moyo wake ulikuwa unadunda kwa uoga. Yule askari kanzu akanyoosha mkono wakasalimiana na Mr.Mbweku, mikono ilipogusana tu askari kanzu akajua tayari mhasibu presha juu jinsi kiganja kinavyotetemeka kama ameshikishwa donge la barafu. "Mie ngoja niwaacheni nikaendelee na majukumu mengine ya kikazi..." aliaga Bosi na kumuachia msala Mr.Mbweku yeye akiwa ameshajivua. Askari kanzu akaanza kumuweka kitimoto Mhasibu yule.
Askari kanzu: "Mimi ni Afisa mpelelezi natokea polisi Wilaya Arusha Mjini, ningependa kufahamu vitu vichache toka kwako..! "
Mhasibu: "Ahsante mie ndio mhasibu mkuu hapa kwa zaidi ya miaka 15, au wananiita Mzee wa 'STK' naitwa Mr.Mbweku Wa Mbweku"alijinasibu kwa uzoefu ili kumuondolea mashaka Askari yule. bila kujijua mbwembwe zake anaenda kujitundika kitanzi mwenyewe.
Askari Kanzu: "Nimefurahi kukutana na mzoefu wa kazi, hongera sana, hiyo STK ndio nini" alidodoswa huku akivutwa kwenye chambo kilichofungwa juu ya ndoano taratibu bila kujijua.
Mhasibu: "Ha.. ha.. ha.. ha...hiyo abbreviation 'STK' maana yake Sheria, Taratibu na Kanuni. Hivyo wamenipachika hilo jina kutokana na msimamo wangu hapa kazini katika kufuata sheria, taratibu na kanuni za utunzaji wa pesa za serikali" alijibu kwa kujiamini huku uoga ukiwa umeshaanza kumuondoka.
Askari kanzu: "Je sheria, taratibu na kanuni za serikali zimaruhusu kumpa mtu tu kinyemela pesa za serikali akaweke nyumbani kwake? " alitupiwa kombora zito Mr.Mbweku
Mhasibu: "Aah..Aah...haziruhusu kabisa, ni kinyume kabisa ukibainika kazi huna na hata kifungo kabisa....! " alijibu huku akianza kubabaika akiwa hajui lengo la swali hilo yule askari anakusudia nini.
Askari kanzu: "Vizuri kabisa, hivyo wewe kumbe hufuati 'STK' maana umpa pesa nying marehemu Bosi Minja akalale nazo kwake ili usiku umtumie majambazi sio! "
Mhasibu: "Uwongo..... nakaa kabisa aliyekuambia kama ni Bosi mpya ni majungu tu Uwongo mtupu.." alijibu kwa hasira akiwa amejua mambo yameshabumburuka tayari.
Askari kanzu: "Kama ni uongo nani kaweka hii saini yako ya makabidhiano ya pesa? Ili hali pia kwenye akaunti wewe ndio umezitoa pesa hizo zote zilizotumwa na wafadhili!" alizidi kugongelea msumari wa moto kwenye moyo wa Mr.Mbweku huku akimkabidhi nyaraka aliyoichukua ofisini kwa marehemu Bosi Minja.
Mhasibu: "Ni.. ni... .ni....saini yaangu......nisamehe marehemu alishinikiza nimpe pesa" alipatwa na kigugumizi cha ghafla baada ya kuona maji yamezidi unga kila kitu kipo dhahiri shahiri.
Askari kanzu: "Huo msamaha utakwenda kuuomba mbele ya hakimu mahakamani, na lazima nihakikishe nakufunga jela kwa kesi ya kula njama kuiibia serikali pia kwa kuhusika na mauaji ya Bosi Minja maana majambazi sio wanajimu watabiri tu kuwa kwa Bosi Minja nyumbani kwake kuna pesa ni lazima umehusika na mchongo mzima" alifoka kwa sauti ya kipolisi askari kanzu yule huku akivaa uso wa kazi na kutoa pingu zake ili amvike nazo mikononi Mr.Mbweku.
Mhasibu: "Mie sijahusika unanionea bure tu, duniani hamna haki mbele ya Mungu mtalipa nyie askari dhulma mnazinifanyia hizi" alilalamika huku akiwa tayari kashapigwa pingu zake anatolewa nje ya ofisi yake. Yule askari kanzu akatoa taarifa kwa Bosi wake kuwa anamchukua kwenda nae kituoni kwa ajili ya mahojiano zaidi. Njia nzima Mr.Mbweku alikuwa analia kama mtoto mdogo, akijutia uzembe alioufanya mpaka umemtia matatizoni.



zote kuanzia cheti cha mgonjwa mpaka kadi ya kliniki vilithibitisha bila kuacha mashaka kuwa kuanzia mchana wa Jumamosi mpaka kuamkia usiku wake wa kuamkia Jumapili, siku aliyouliwa Bosi Minja, Recho alikuwa mgonjwa amelazwa hospitalini hapo na hajaruhusiwa mpaka hii leo. Uzuri zaidi kwa Recho usiku wa mauaji alfajiri yake ndio wakati aliojifungua mtoto wake wa kiume. Mashaka ya Askari kanzu yalikuwa ni umbali wa dispensari aliyojifungulia ilipo na makazi ya wazazi wake Bosi Minja. Recho akajitetea kuwa alifuata huduma nzuri na madaktari bobezi kwenye hospitali hiyo.
Askari kanzu akawa ameishiwa hoja kutokana na suala la matibabu ni uhuru wa mtu binafsi ana hiari wa kuchagua hospitali ya kwenda, daktari wa kumtibu na hata aina ya matibu anayoyataka ni uhuru wa mteja. Anaweza kuamua kwenda kutibiwa kwenye mitishamba au hospitalini. Askari kanzu akabaki ametahayuri hana hata kipengele kimoja cha kumtia hatiani Recho.
Hata ushahidi wa kimazingira ulikuwa unamuokoa Recho, hasa kutokana na mtoto aliyejifungua kwao wao wakijua ni damu ya Bosi Minja, hivyo isingekuwa rahisi mtu amuue baba watoto wake kirahisi tu bila sababu ya msingi. Kwa msingi huo Recho akaruka kiunzi cha kutupiwa msala wa mauaji. Jeshi la polisi likafunga rasmi jalada la upelelezi wa kesi hiyo likiwa na mtuhumiwa mmoja tu ambaye ni Mhasibu Mkuu Mr.Mbweku. Hivyo aliendelea kusota rumande bila kupata dhamana akisubiria siku ya hukumu yake ya kesi ya mauaji na kula njama ya kuiba pesa nyumbani kwa Bosi wake Bwana Joseph Minja.
Recho akaruhusiwa atoke hospitalini na kichanga chake, lakini alitoka akiwa hana furaha ya mtoto aliyempata. Mtoto aliyezaliwa alikuwa ni mlemavu wa miguu yote miwili huku pia akiwa na shida ya uoni hafifu kwenye macho yake. Kuzaa mtoto mwenye afya mgogoro ambaye atakuwa tegemezi kwa wazazi wake maisha yake yote mpaka kifo ni moja ya mtihani mzito sana kwa wazazi. Martin alikuwa anajitahidi kumpa moyo kuwa ndio mipango ya Mungu inabidi avumilie ndio ukweli usioweza kubadilika.
Taratibu za mirathi ya marehemu Bosi Minja kwa muda kutokana na Recho kushughulikia afya ya mtoto wake. Baada ya kuonana na madaktari bingwa wa macho katika hospitali ya Taifa Muhimbili, tiba zao zikasaidia macho yake mtoto wa Recho yakarudia uoni wake wa kawaida. Suala la ulemavu wa miguu akashauriwa ampeleke mtoto wake India, China au Afrika ya Kusini. Maamuzi ya Recho yalikuwa ni kuhama Tanzania na kuhamia Jijini Nairobi akale maisha yake na Martin kwa uhuru bila kubanwabanwa. Kwanza akaandika barua ya saa 24 kuacha kazi 'Peace Corps Tanzania', akitoa sababu ya kutaka apate muda wasaa wa kumhudumia mtoto wale ambaye ni mlemavu.
Pili akaliamsha sakata la mirathi lililokuwa limelala. Kikao maalumu cha kujadili mirathi kikaandakiwa huku mtendaji kata wa serikali ya mtaa nae akihudhuria huku rafiki yake kipenzi Bosi Minja akiwa ndio ana barua ya wosia ulioachwa na marehemu. Siku ya kikao hicho ndio siku waliyokutana uso kwa uso kati ya mama Debora na Recho.
Kabla ya kikao ukafanyika utambulisho mfupi wa waliohudhuria pale, huku mama Debora akiwa amefura kwelikweli kwa hasira kwa kumfahamu mwizi wa mume wake. Recho kwa upande wake alikuwa wala hajali kitu, anasubiri bomu la barua ya wosia kulipuka hadharani familia isambaratike kwa fedheha. Recho alikuwa anakijua kila kitu kilichoandikwa ndani ya barua hiyo ya wosia na Bosi Minja, mstari kwa mstari, neno kwa neno. Anaikumbuka vyema mpaka siku ambayo Bosi Minja aliandika wosia huo kutokana na shinikizo lake.
"Recho..wewe ni binti mdogo sana kwangu lakini ninakiri kwa dhati ya moyo wangu ndani ya muda mchache tu umeuteka moyo wangu vilivyo na kunisahaulisha machungu ya kifo cha mke wangu mama Debora, naahidi kukupenda mpenzi wangu Recho mpaka mwisho wa uhai wangu...!" aliyatamka maneno hayo Bosi Minja akiwa amemkumbatia vilivyo Recho, usiku wa manane wakiwa ndani ya shuka moja kwenye 'Hoteli ya WhiteSands' Jijini Dar es Salaam walipokuja kula bata mara moja wakitokea Jijini Arusha.
"Mhhh mie siamini nyie wanaume hamuaminiki tena ndio hivyo unajua nimebeba mimba yako basi ndio utanibwaga muda sio mrefu na kutafuta kigori mpya" aliongea Recho kwa sauti ya kudeka akijifanyisha ana huzuni ya kusikiliza, akajipapatua kutoka kwenye mikono ya Bosi Minja na kukaa kwenye kingo ya kitanda huku akiwa ameshika tama.
" Niamini Recho...nikufanyie nini uniamini kuwa una thamani kuliko hata nafsi yangu mpaka wazazi wangu mbele ya wewe si lolote si chochote kwako mimi nimetia nanga sioni wala sisikii kitu, wewe kwangu ndio Kigoma mwisho wa reli" alizidi kujimaliza maneno ya uvunguni kabisa akijiacha mtupu bila kujibakisha. Hivyo ndio nafasi aliyokuwa anaitafuta Recho ijitokeze aitumie vizuri.
"Niandikie wosia wa umiliki wa mali mimi na mtoto wangu mtarajiwa kama unachokisema ni kweli na sio porojo za Abunuwasi, kufurahia penzi langu" aliongea Recho huku sasa akimsogelea na kuanza kuzichambua na kuzichezea ndevu za Bosi Minja kwa kutumia vidole vyake laini ambavyo havijawahi kufanya kazi za sulubu zaidi ya kutumika kuvunja mayai tu. "Nisogezee hiyo Brifkesi yangu nikate mzizi wa fitina kabisa, tena wewe ndio unipe maelekezo ya ugawaji wa mali zangu, mie nitakachofanya ni kukusaidia kukutajia orodha halafu wewe unanishauri hiyo nimgawie nani! " aliongea Bosi Minja huku akiwa analisubiria hilo Brifkesi aandike huo wosia kwenye nyaraka zake. Hiyo ndio siku Recho alivyoandikiwa urithi wa mali kochokocho.
Wana ukoo walikuwa wamejawa na kimuhemuhe cha kufahamu nani kapata nini na kakosa nini, walitegesha masikio yao kama antena kusubiria mgawanyo huo. "Mimi nikiwa kama rafiki wa marehemu Bosi Minja, nimekuja kuusoma waraka wa wosia wa marehemu juu ya mgawanyo wa mali zake" akaweka kituo cha mazungumzo yake huku anawatupia macho wana ukoo waliokuwa wamejazana pale ukumbini mpaka wengine wamekaa chini ya zulia. Recho alikuwa anachekea tumboni tu, akisubiria namna watakavyosambaratika baada ya wosia huo kuwa hadharani. "Miezi mitatu iliyopita rafiki yangu aliniita ofisini kwake pale Arusha, tukaongea mambo mengi sana kama ilivyo kawaida yetu kisha mwishoni kabisa ndio akanikabidhi huu wosia, kana kwamba marehemu alikuwa anatabiri kifo chake" alipofika hapo, mama mzazi wa Bosi Minja akawa analia kilio cha kwikwi amemkumbuka mtoto wake.
"Sasa barua imeanza kwa kusema, Mimi Joseph Minja nikiwa na akili zangu timamu, tena bila kushinikizwa na mtu yoyote nimeamua kugawa mali zangu, pindi tu nitakapofariki huu wosia ufanyiwe kazi. Nyumba yangu ya Moshi Mjini, maeneo ya Boma Ng'ombe, nyumba namba 32 Bloku B nimemkabidhi Recho na mtoto wake mtarajiwa. Kitalu changu cha uwindaji kilichopo Ngorongoro, kitalu F bloku XZ/21 nimemkabidhi mtoto wangu mtarajiwa kwa mpenzi wangu Recho. Viwanja vyangu viwili vilivyopo kijijini Marangu nimewakabidhi wazazi wangu baba na mama. Mwanangu Debora nimemkabidhi pagale langu lililopo Kihonda, Mkoani Morogoro. Duka langu la vifaa vya ujenzi litakuwa chini ya usimamizi wa mdogo wangu Joyce Minja mapato yatakayopatikana yawasomeshe watoto wangu na kuwatunza wazazi wangu" wosia ukawa umeishia kusomwa, kila mtu akabaki ametumbua macho yake kwa mshangao hawaamini wanachokisikia.
"Huko nyuma ya karatasi hamna maandishi yoyote maana sijasikia jina langu" aliuliza kwa shauku na jazba kubwa mama Debora akiwa haamini kama ametoswa kwenye wosia. "Wewe mie kwanza hata sikujui kama upo, mumeo alikuwa anatangaza umeshakufa ndio maana mie ikawa rahisi kumkubali, kumbe Bibi la Bibi upo hai, umefufuka kwa sababu ya mali za marehemu?" Recho alimpiga kijembe cha nguvu mama Debora, mpaka akakosa ustahamilivu, akasimama anataka akamvae maungoni Recho wazichape.
"Niacheniiii..... nasema Niacheniiiii nimfundishe adabu mwana hizaya mkubwa, malaya mharibu ndoa za watu huyu... " alifoka na kupayuka kwa sauti ya juu mpaka Debora ambaye alikuwa nje anacheza akaingia ndani kuangalia kulikoni. Ile Debora kuingia tu alipomuona Recho akaanza kulia huku anaogopa anarudi nyuma nyuma anakimbilia kwa shangazi yake Joyce na kujikunyata.
Zogo mtindo mmoja huku Baba yake Bosi Minja nae akiupinga wosia huo hadharani kuwa ni wa kughushi sio wosia sahihi. "Mwanangu Jose hawezi kuandika upumbavu huo unaotusomea hapo, toka hapa mara moja nisikuone la sivyo nitakushindilia mapanga ya kichwa" alifoka huku akinyanyuka kutaka kuelekea stoo kufuata upanga wake.



"Huo wosia hata ofisi yangu ya kata upo, nakala yake ipo hivyo ni juu yetu kukubaliana nao na kama tunaupinga basi tutumie vyombo vya kisheria tusitumie nguvu hasira hasara ndugu zanguni" aliongea mtendaji kata maneno ya busara kidogo yaliyosaidia kutuliza dhoruba na ghasia kwenye kikao kile.
Recho kumbe alijiandaa kuna vijana maalumu aliwategesha kama walinzi wake ili kama kikinuka tu waje kumuokoa, na ndivyo walivyofanya. Wale walinzi wake walivyo sikia mikikimikiki na mikingamo ya kwenye kikao kile wakambeba Recho juu juu na kutokomea nae kusiojulikana. Matusi ya nguvu yaliyokosa adabu za ukumbi yaliporomoshwa mbele ya Recho bila kujali kuwa mtoto mdogo kama Debora ambaye anasikia kila aina ya tusi lililotukanwa wakati huo.
Kikao kikasambaratika huku wana ukoo waligawanyika, wengine wakisema wanamuachia Mungu yeye ndio hakimu wa haki, kundi hili liliongozwa na mke wa Mzee Minja. Huku kundi la pili, ni la pili likitoa ahadi ya kwenda mahakamani kufungua kesi ya kupinga mirathi hiyo, wakionyesha mgawanyo wake ni batili haukuzingatia haki na usawa. Kikao cha mirathi kikamuibua Recho kama mshindi wa mali za urithi akiwa amerithishwa sehemu kubwa ya mali za marehemu kwa kuwa mpenzi wake chini ya mwaka mmoja, huku mkewe wa ndoa aliyeishi nae kwa zaidi ya miaka 9 mama Debora, akitoka patupu, bilabila.

Jambo la kunyimwa urithi na mume wake, lilimnyima raha sana mama Deborah na kumpa msongo mkubwa wa mawazo. Hakutegemea kama mumewe Bosi Minja atamletea dharau kiasi kile. Aliumizwa hasa na kitendo cha kumfadhilisha kumpa urithi mkubwa kimada tu kuliko hata yeye na wazazi wake. Kila shauri la mirathi walipokuwa wanataka kulipeleka mbele ya vyombo vya sheria walikuwa wanakutana na vigingi vizito. Recho alikuwa anatumia nguvu ya pesa zake kuwazima wasimsumbue. Mbaya zaidi akawafanyia kituko cha kufungia mwaka ambacho hawawezikukisahau maishani mwao mpaka wanakufa. Siku ambayo mama Deborah akiwa ndio anaaga kuwa kesho yake anarejea mkoani Morogoro, mchana wake. Wakiwa katika mazungumzo ya kutafakari mustakabali wao namna utakavyokuwa kutokana na giza nene linalowakabili mbele ya safari. "Haya haya ndugu wananchi tunapenda kuwatangazia kuwa kwa idhini tuliyopewa na mmiliki wa nyumba namba 32 Bloku B, leo ifikapo majira ya adhuhuri tutaendesha mnada wa hadhara wa mauzo ya nyumba hiyo, mnakaribishwa. Mnunuzi atawajibika kulipia asilimia 20% hapo hapo, na pesa iliyobakia ndani ya siku 7. Pia mnunuzi ataruhusiwa kuhamia leo leo kama atapenda kufanya hivyo. Ahsanteni sana" ilikuwa ni taarifa ya kushtua kwa familia ya Mzee Minja iliyokuwa inatangazwa kwa kutumia kipaza sauti. Nyumba ilikuwa inauzwa na wazazi wake Bosi Minja wapo ndani bado hawajahama. Wakawa hawana jinsi isipokuwa kuanza kuchakarika kuanza kutoa vitu nje ya nyumba kwa haraka kabla ya kuanza kwa mnada. Mpaka kufika majira ya alasiri mnada ulikuwa umeisha na mnunuzi ameshapatikana. Siku hiyo ilibidi wakalale stendi ya Mabasi na vifurushi vyao ili asubuhi kila mtu atawanyikie kwake. Wazazi wake Bosi Minja ilibidi wamtake radhi sana mama Deborah kwa ujinga walioufanya wa kumpokea hawara Recho kwa mikono miwili na kumpa heshima kama mke wa ndoa wa kijana wao. Majuto ni mjukuu walijua wanamkomesha mama Deborah kumbe na wao wameonja joto ya jiwe toka kwa Recho. Wazazi ilibidi warejee kijijini vichwa chini, waliondoka kwa mbwembwe na majitapo makubwa kuwa wanahamia mjini, mtoto wao Bosi huko kashawatengenezea maisha. Kumbe kijana wao amekuja kutengeneza maisha ya hawara na sio ya familia yake. Recho alihakikisha anauza kila kitu cha Bosi Minja katika mali zinazojulikana na familia huku akibakiza vitalu vya uwindaji kisha akahamia Jijini Nairobi kwa ushawishi wa mpenzi wake Martin. Walijipanga kwenda kufanya biashara nchini Kenya wakiwa na pesa za kutosha walizopora nyumbani kwa Bosi Minja. Recho na Martin ndio waliopanga ramani nzima ya mauaji huku wakimtumia kijana wa kukodi, anayeitwa kwa jina la kazi Cobra, maarufu Mjini Moshi kwa madili ya ujambazi iwapo tu ukimhakikishia mgao wa kutosha. Walijipanga kwenda kuanzisha vitega uchumi mbalimbali huku wakiishi raha mustarehe bila usumbufu wowote wa ndugu wa Bosi Minja. Waarabu wa pemba hujuana kwa vilemba, walijua fika Wachaga wenzao familia ya Bosi Minja wakiwaona wanaishi maisha ya kifahari wakiamua kubakia Tanzania kisha wakafanya uwekezaji lazima tu watawasumbua na kujipanga kulipa kisasi. Hivyo kuepuka usumbufu wao wakaamua afadhali wakajichimbie Jijini Nairobi wafaidi vizuri jasho la marehemu Bosi Minja. Kabla hawajatimka zao kuelekea Jijini Nairobi, Recho akapatwa na pigo la kwanza katika maisha yake. Mama yake mzazi alifariki katika ajali ya gari barabarani maeneo ya Chalinze akiwa anatokea Jijini Dar e Salaam na kufariki hapo hapo. Kifo hicho kilikuwa ni pigo kubwa sana kwa upande wake kwa sababu mama Recho alijitolea kukaa na mtoto wa Recho. Hakutaka kabisa mjukuu wake asafiri na Recho kwenda Jijini Nairobi. Hivyo baada ya mazishi kupita, Recho ikabidi aambatane na mwanawe Jijini Nairobi na mtoto wake huyo wa kiume aliyekuwa anajulikana kwa jina la Pesambili, jina alilopewa na Bibi yake mzaa mama. Pesambili alikuwa ni mzigo kwa mama yake, maana alikuwa hajiwezi kwa kila kitu kutokana na ulemavu wake hivyo kupelekea kuhitaji msaada wa kila kitu toka kwa mama yake. Mwezi tu baada ya kulizoea vizuri Jiji la Nairobi, akampeleka motto wake katika kituo cha kulea watoto Yatima kinachoitwa Cheryls Childrens Home and Learning Centre. Kituo hicho binafsi kilichopo Katika mtaa wa Dagorretti Corner hatua chache kutoka barabara ya Ngong kilikuwa kinakusanya watoto yatima kutoka mitaa duni mbalimbali wenye kuishi vibandani wametengenezewa mabweni na madarasa kama hatua muhimu ya maendeleo ya jamii kupitia elimu bora. Akawapiga usanii kuwa yule mtoto wake Pesambili ni yatima, alizaliwa na dada yake ambaye amefariki na baba yake hajulikani hivyo anataka awe anaishi hapo na atakuwa anakuja kumtembelea kila mwisho wa mwezi. Hapo ndio ikawa nafuu yake Recho sasa ya kufanya yake, kujirusha namna anavyotaka yeye. Walifungua Klabu ya Usiku inayoitwa Nairobee BY Night Club, ambapo ilikuwa inafunguliwa masaa 24 kwa siku. Ilikuwa ni Klabu iliyojipatia umaarufu mkubwa ndani ya muda mfupi kutokana na huduma zake za viwango vya hali ya juu. Pia kuhakikisha anawavuta wateja wakware kwa wasichana, Recho alikuwa anawasaka wasichana wabichi na warembo toka mitaa mbalimbali ya Jijini Nairobi ambao wanaishi maisha magumu na kuwapa ajira kwenye Klabu yake. Recho alikuwa ndio msimamizi mkuu wa biashara hiyo, huku Martin akijishughulisha na biashara haramu ya mihadarati. Hiyo ndio ilikuwa kazi yake tokea zamani inayomuweka Jijini Nairobi. Alikuwa anapewa mzigo wa madawa ya kulevya na Matajiri wakubwa halafu yeye anaufanyia udalali mzigo huo kwa kuusambaza mitaaani. Vijana wake wa kazi wa kusambaza mzigo mitaani, alikuwa anawapata mitaani Katika kitongoji cha Mlango Kubwa, katikati mwa jiji la Nairobi, sehemu lililopokuwa jalala hapo zamani. Eneo hilo ni kimbilio la watoto wa mitaani, ambapo wenyewe wanapaita kama makao makuu, hivyo alikuwa anaenda kuwachukua kwa ahadi za kujifanya kuwatafutia vibarua mbalimbali kisha anawashawishi kufanya biashara ya kuuza madawa ya kulevya. Hivyo walivyopata ngwenje za kutosha walizopora nyumbani kwa marehemu Bosi Minja, Martin akajikuta anashawishika kutaka kwenda mwenye ughaibuni kufuata mzigo wa mihadarati, Heroine na Cocaine ili aweze kupata faida sufufu. "Nakusudia kuanza kwenda Italia mimi mwenyewe kwenda kubeba mzigo wangu, kutumwa sasa basi" aliongea Martin akiwa anampa taarifa mpenzi wake juu ya maamuzi ya kusafiri kwenda nchini Italia. "Kila la kheri, maadamu umefanya taftishi ya kutosha kuwa tutapata pesa mie sina tatizo kikubwa umakini tu usije kupigwa changa la macho" aliongea Recho kijasiri bila uwoga wowote hasa dili lenyewe likiwa ni la pesa akili zilikuwa zinamruka kabisa. "Hamna shida, kuna rafiki yangu ameniunganisha na Zungu la mihadarati anaishi katika mji wa Catania, anatokea katika ukoo mmoja maarufu sana wa Cappello-Bonaccorsi.



Tumempigia simu kakubali kunipokea. Huko mimi safari zangu tatu tu, tutauchinja Afrika Mashariki yote tutajulikana kwa pesa zetu" aliongea Martin kwa majigambo na kiburi cha pesa. Baada ya siku kama tatu tu, Martin akakwea mwewe kuelekea Ughaibuni Jijini Catania nchini Italia. Baada ya kama miezi miwili akarejea Jijini Nairobi akiwa ameambatana na punda wake watatu (3) wa kubeba dawa za kulevya tumboni. Baada ya kama mwezi mmoja akarejea tena nchini Italia kwenda kufuata mzigo mwingine nchini Italia, baada ya mwezi mmoja tu akaondoka tena kwa mara ya tatu. Maisha yalizidi kuwanyooka, ndani ya miezi 6 tu Recho akaanza kujenga bonge la Hoteli lenye hadhi ya nyota 5 kisirisiri pembezoni mwa ufukwe wa bahari Jijini Dar es Salaam. Akaipa hiyo hoteli jina la 'Mercy Memorial Hotel' kama kumbukumbu ya marehemu mama yake mzazi. Mawazo ya Recho ni kuwa mradi huo mkubwa wa Hoteli, Martin hajui kinachoendelea alishamzunguka tayari. Pia alipanga kufanya njama majina ya mali zote wanazomiliki Jijini Nairobi kuzibadilisha zisomeke kwa jina lake, hasa ukichukulia kulikuwa hamna ndoa baina yao, hivyo saa yoyote Martin akimgeuka itakuwa imekula kwake Recho. Akafungua akaunti ya benki kisirisiri yenye jina lake pekee, sehemu kubwa ya mapato ya biashara akawa anayaficha kwenye akaunti yake ya siri. Kumbe Martin nae mtoto wa mjini, sio zoba wala bwege, mbumbumbu mzungu wa reli, asichokijua Recho ni kuwa kuna watu maalumu wa kuchunguza nyendo zake za miamala ya kipesa waliwekwa na Martin. Hao ndio waliomletea udaku kuwa Recho amefungua akaunti ya benki ya kwake peke yake pia anajenga bonge la Hoteli huko Kigamboni pembezoni mwa ufukwe wa bahari nchini Tanzania. Kila mtu aliyeuona uwekezaji ule wa Recho hakuacha kuusifia kwa uzuri wake, hali iliyorahisisha habari zake kusambaa kwa haraka. Martin alipopata taarifa hizo akiwa nchini Italia, alikasirishwa sana hasa akichukulia namna alivyoiweka roho yake rehani kwa kukubali kumpiga picha za utupu Bosi Minja Hotelini kule Nairobi kwa lengo la kuzitumia kujipatia pesa kwake kwa njia za haramu, pia namna alivyoshawishiwa na Recho kuivamia nyumba ya marehemu Bosi Minja usiku wa manane na kupora pesa za kigeni na kufanya mauaji. Dawa ya moto ni moto, hivyo akapanga kulipiza kisasi kwa Recho kwa kutumia washirika wake, vigogo wa serikali ya Kenya kumshikisha adabu Recho, bila kutumia silaha yoyote. Kisasi ambacho alipanga kimrudishe kijijini kabisa huko Moshi, akiwa na nguo zake mwilini tu akajipange moja. Tokea aondoke kwa mara ya tatu, miezi ikaanza kukatika, Martin hana dalili za kurejea Jijini Nairobi. Recho akaanza kupatwa na wasiwasi kuwa huenda kuna jambo baya limemkuta huko ughaibuni sio bure. Hofu kubwa ya Recho ilikuwa ni kwenye pesa waliyoitumbukiza kwenye biashara haramu za ughaibuni anazozifanya Martin. Baada ya miezi kama minne (4) ya kuwa roho juu, tokea kutoweka kwa Martin nchini Italia, siku moja usiku Recho alijiwa na kigogo wa jeshi la polisi Jijini Nairobi akiwa kwenye Klabu yake ya 'Nairobee BY Night Club' na kumpa taarifa ya taharuki na kushtua. Kigogo huyo alitua ndani ya gari la polisi na ving'ora juu vikimsindikiza. "Mshirika wako wa kibiashara Ndugu Martin Tenga ametiwa mbaroni nchini Italia akihusishwa kuwa na mashirikiano na kundi la hatari nchini Italia kwenye biashara ya dawa za kulevya. Hivyo kundi la wapelelezi wa Kimataifa toka nchi za Ulaya wametumwa Kenya wapo njiani kuja kuchunguza vitega uchumi vyake Martin na washirika wake wa kibiashara. Kwa kukusaidia tu nakupa masaa 24 utoweke nchini Kenya na kurejea kwenu Tanzania vinginevyo yatakayokupata tusije kulaumiana, maana lazima utakamatwa na kuozea jela maisha. Kuanzia kesho picha zako zitasambazwa kwenye njia zote za usafiri, majini, ardhini na angani kuwa ukamatwe hivyo hutoweza kuchoropoka mikono mirefu ya dola. Pia hapa tunapoongea hivi sasa nyumba yako imezungukwa na wana usalama wanakusubiri wakukamate ukalale rumande. Nitakachokusaidia ni kukupa eskoti ya polisi hivi sasa kwenye gari yangu watakusindikiza mpaka Namanga pale watakuvusha na kukupa nauli ya kufika kwenu Arusha" yalikuwa ni maelezo ya amri sio ombi, toka kwa Afisa huyo wa juu wa Jeshi la polisi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Martin, na Recho alikuwa analijua hilo. Kigogo yule wa polisi, alijifanya kama msamaria mwema hivyo alivyopata penyenye za ujio wa ugeni huo mzito wa kuja kumchunguza Martin akaona bora amuokoe mpenzi wa Martin, kumbe ni mipango haramu iliyosukwa kiufundi ikasukika vilivyo. Recho akawa amepewa nafasi ya kuchagua kusuka au kunyoa, akawa hana jinsi isipokuwa ni kutoroka usiku huo huo kupitia mpaka wa Namanga, Arusha. Mtoto wake Pesambili akawa amemtelekeza Jijini Nairobi, hakuwa na haja nae tena. Msemo wa mali ya bahili huliwa na wadudu ukatimia, na daima mali ya dhuluma haina baraka na hawezi kudumu na hata ikidumu haiwezi kuleta manufaa yaliyokusudiwa vile inavyopaswa. Karibia robo tatu (3/4) ya pesa waliyoipora nyumbani kwa marehemu Bosi Minja ikawa imetua mikononi mwa Martin. Recho alimchukia Martin kupita kiwango cha kawaida cha chuki, kwa kumlaghai kuingiza pesa kwenye biashara ya hatari asiyo na uzoefu nayo. Martin alimchezea picha ya kihindi Recho na kuamua kumfanyia dhulumati ya mali zote ajimilikishe yeye peke yake. Hakuwa amekamatwa alikuwa yupo huru nchini Italia anatumbua maisha kwenye biashara zake haramu mbalimbali. Akili yake haikuwa katika mapenzi ya dhati na Recho, aliona Recho ni macho juu mjanja sana, saa na wakati wowote anaweza kumgeuzia kibao hata yeye akamuua hivyo jambo lililo aula ni kummaliza mapema kabla hajawahiwa yeye. Sasa rasmi mali zote zikaangukia mikononi mwa Martin huku Recho akirejea Tanzania na nguo zake tu alizovaa mwilini tu. Hakupata hata nafasi ya kwenda benki kutoa pesa zake zilizomo kwenye akaunti yake. Njia nzima akiwa ndani ya Basi alikuwa analia mfululizo kama mtoto mdogo au mtu aliyefiwa na familia yake yote. Abiria wote ndani ya Basi walikuwa wanamshangaa yeye huku wakijitahidi kumnyamazisha lakini ilikuwa ni kama wanamwagia petroli kwenye moto, ndio kwanza anaongeza sauti ya kilio. Kichwani mwake Recho, alikuwa na mawazo lukuki hasa akiwaza kuwa anaenda kuwa mgeni wa nani Mjini Moshi au Jijini Arusha wakati aliuza kila kitu chake alichorithi kwa marehemu Bosi Minja pia aliuza kila kitu chake alichorithishwa kutoka kwa marehemu mama yake mzazi.



Tegemeo pekee lililobaki kwa Recho ni Hoteli yake ya 'Mercy Memorial Hotel' lakini bahati mbaya zaidi akiwa hana nyaraka yoyote ya umiliki wa Hoteli hiyo. Alikuwa anawaza wataangaliana vipi na Mashoga aliokuwa anawadharau na kuwafanyia nyoko, leo atakapotua Jijini Arusha itabidi akawapigie magoti wampe hifadhi.

SURA YA SITA
. Mama Deborah alishakata shauri ya kuhamia kijiji cha Mikongeni, kilichopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro. Kijiji ambacho taribani umbali wa kilomita 25 kutokea Morogoro Mjini. Alifanya maamuzi ya kuuza pagale la nyumba ya urithi aliyoachiwa binti yake Deborah. Alikuwa anajaribu kufuta kumbukumbu zote zilizoachwa na marehemu mume wake Bosi Minja ili aanze maisha upya. Pesa alizopata kwenye mauzo ya pagale hilo akaja kujengea kibanda cha miti kwenye kiwanja chake ili kama akibahatika kupanga nguvu ya kiuchumi siku za mbele aje kujenga nyumba ya tofali. Chambilecho lakuvunda halina ubani, tayari moyo wa mama Deborah ulisha chanikachanika kwa ajili ya vituko alivyofanyiwa na mumewe baba Deborah. Kila alipokuwa anamtafakari alikuwa anashindwa kummaliza. Kichwa kilishamvurugika, akajikuta tu Chuo anaacha, hataki tena kuendelea na masomo. Kazini napo akajikuta hawezi kurudi ataanzaje kwanza kuwaambia ameacha chuo kwa sababu hajisikii kusoma, lazima muajiri wake atamwambia ajieleze kwanini asifukuzwe kazi kwa uzembe. Afya yake ikawa inazidi kuzorota, anakonda kwa mawazo, unene wake wote kwisha kabisa akawa kimbaumbau kama mwiko wa pilau. Deborah nae afya yake ilikuwa ni tia maji tia maji, kuna wakati afya ilikuwa inaboreka lakini baada ya muda fulani anarudia tena afya mgogoro. Deborah pindi mwaka ulipopinduka tu alishaandikishwa Chekechea ya hapo hapo kijijini. Ilichukua muda kidogo kwa Deborah kuweza kuendana na mfumo mpya wa masomo. Alitoka shule ya 'Arusha International School' inayotumia lugha ya kimombo kufundishia mpaka shule ya kijijini inayotumia kiswahili, ambapo mwalimu inabidi atumie lugha ya kiluguru kuwafafanulia neno la kiswahili wanafunzi wake ambao karibia asilimia 90% walikuwa hawaijui kiufasaha lugha ya kiswahili. Deborah kudeka kote jule kulikishwa, 'sijui nataka chips kuku', sijui 'nataka kwenda swimming', sijui 'chai ya mkandaa chungu nataka ya maziwa' kulikuwa hamna tena. Sasa ilikuwa mwendo wa uji wa dona wa chumvi kwa mihogo au magimbi ya kuchemsha ndio aghalabu huwa kifungua kinywa chao yeyrme na mama yake. Mchana hapapikwi mpaka majira ya alasiri hapo ndipo patasongwa ugali kwa maharage au mboga za majani paliwe. Kula tena ndio mpaka kesho asubuhi. Maandalizi ya shuleni Deborah alikuwa anaamka mwenyewe anajiandaa kila kitu, kisha anamuasha mama yake ndipo anamchemshia uji na mihogo, anakula na kwenda moja kwa moja shuleni. Siku ya tarehe 08/04/1987 itabaki kuwa siku yenye kumbukumbu mbaya sana kwa Deborah katika maisha yake yote. Ikiwa ni takribani miezi minne (4) tokea ampoteze baba yake mzazi, mama yake alipatwa na ugonjwa wa kiharusi. Siku hiyo kama kawaida yake Deborah alidamka asubuhi na mapema, akajiandaa kisha akaenda kumuamsha mama yake. Akamuita mama yake kwa kumtikisa kitandani kwa zaidi ya nusu saa. Lakini kwa bahati mbaya mama Deborah alikuwa hawezi kuongea wala kunyanyuka pale kitandani, alikuwa ameshapooza mwili mzima na mdomo umeenda upande. Deborah akaanza kuangusha kilio cha nguvu, lakini hamna jirani yoyote aliyejitokeza kutoa msaada kutokana na kuwa wengi walishaondoka zako tokea alfajiri kuelekea mashambani mwao. Deborah ikabidi ajiongeze mwenyewe kwa kukimbilia kwa Mjomba wake Kobelo kwenda kutoa taarifa. Kwa bahati Mjomba Kobelo siku hiyo alichelewa kwenda shambani kwake kuna kazi za nyumbani kwake alikuwa anazimalizia kwanza. "Jee... Mwaaa...vipi tena Mjomba mbona asubuhi asubuhi... kulikoni? " aliuliza Mjomba Kobelo huku anautupa upanga wake pembeni baada ya kumuona Deborah anakuja mbio mbio huku analia. Deborah akajieleza kwa tabu kuwa mama yake hataki kuamka kitandani ampikie uji aende shule. Mjomba Kobelo kwa akili za kiutu uzima akagundua tu kuna shida sio bure, akakwea baiskeli yake na Deborah wake nyuma akanyonga pedeli mpaka nyumbani kwa dada yake. "Dada umerogwa dada...binadamu wabaya dada, nilikuambia mapema hukunisikiliza usijenge nyumba kwa mara moja hukunisikiliza" Mjomba Kobelo alikuwa analalamika kwa masikitiko baada ya kuiona hali ya dada yake. Himahima akamtia kwenye tenga dada yake na kumkimbiza kwa mganga wao wa familia babu Katimbwa huko Mkuyuni. Deborah ikabidi ahamie rasmi nyumbani kwa Mjomba wake, huku mama yake akiwa yupo kwa mganga anapata tiba mujarabu. Siku zikaanza kutotoa, mpaka ikafika miezi miwili kamilifu, hamna nafuu yoyote iliyopatikana toka kwa mganga. Ikabidi arudishwe nyumbani tu kusubiria kudra za Mwenyezi Mungu, hakupata nafuu yoyote. Hali yake ilikuwa inazidi kuwa mbaya kila uchwao. Nae mama mtu ikabidi ahamishiwe nyumbani kwa kaka yake Mjomba Kobelo kurahisisha huduma zake. Ingekuwa ngumu sana kwa kipato cha kijungu meko cha Mjomba Kobelo kugawanisha matumizi baina ya nyumba yake na nyumba ya dada yake. Kitendo cha Deborah na mama yake kuhamia pale nyumbani kwa Mjomba Kobelo, hakukumpendeza kabisa Shangazi yake Deborah, yaani mke wa Mjomba Kobelo. Kwake alichukulia ni kama mzigo wa ziada na wa kudumu umeingia kwenye familia yake. Familia yake tu, ya watoto 6 ilimtoa jasho, walikuwa wanailea kimkanda mkanda. Fauka ya hapo analetewa mgonjwa asiyejiweza kwa chochote mwenye kujisaidia haja zake zote hapo hapo alipo, anayehitaji kulishwa na kuogeshwa kila siku. Pia kaletewa mtoto ambaye ni yatima, hana baba ambaye ataleta matunzo yoyote, hivyo msemo wa mgeni njoo mwenyeji apone kwa Deborah ulikuwa hauna maana yoyote alikuwa ni mzigo wa misumari. Mzigo ambao watabeba jukumu lote la malezi na kumsomesha maisha yake yote mpaka aanze kujitegemea. Mke wa Mjomba Kobelo akaapa kiapo cha Yasini Mkubwa cha kuanzisha mapambano ya kufa au kupona kuhakikisha wageni hao wanaondoka hapo nyumbani kwake




Mke wa Mjomba Kobelo akaapa kiapo cha Yasini Mkubwa cha kuanzisha mapambano ya kufa au kupona kuhakikisha wageni hao wanaondoka hapo nyumbani kwake. Deborah kwa umri wake wa miaka 5, akaanza kufanyishwa kazi kama trekta shambani bila kuchoka. Alikuwa anaamshwa saa 9 za usiku, jogoo la kwanza na kuanza kufanyishwa kazi za nyumbani. Kwanza ataanza kufulishwa nguo za mikojo za mama yake, akitoka hapo, apewe biwi la vyombo vya chakula cha usiku wake aoshe, akimaliza hapo aanze kufagia uwanja. Atapumzika kidogo, binamu zake wakiamka wafuatane nae mtoni kwenda kuchota maji ya matumizi ya nyumbani.

Mpaka ukifika muda wa kuelekea shuleni, alikuwa yupo hoi bin taabani mwili wake hautamaniki. Shangazi yake, mwili wa Debora ndio ulikuwa ngoma yake, kila akijisikia kuchapa, basi hasira zake zitamalizikia kwenye mwili wa Debora. Alikuwa anampiga mithili ya ngoma, kila anapozembea kutekeleza majukumu anayopewa kutokana na utoto wake. Mama Debora alikuwa anashuhudia vibweka vyote anavyofanyiwa binti yake, lakini alikuwa hawezi kuongea anabaki kulia machozi tu, lakini ni kilio cha samaki, macho yanasombwa na maji tu. Mateso hayo mazito kwa Deborah kuliko kipimo cha umri wake ukichanganya na tukio alilokutana nalo utotoni la kushuhudia kifo cha kikatili cha baba yake mzazi Bosi Minja, kikasababisha awe na ugonjwa wa wasiwasi wakati wote anaishi kwa hofu tu.

Pia ilikuwa kila ikifika usiku wa siku ya Jumamosi kuamkia Jumapili, sasa ile ile aliyopigwa risasi baba yake, lazima ajikojolee kitandani. Akiwa amelala fefefe kitandani, ikifika manane ya usiku tukio lile lote la mauaji huwa linajirudia kama mkanda wa video akiwa ndotoni mpaka anajikojolea chapachapa hapo hapo. Akishtuka usingizini tayari kashachafua mazingira. Hilo jambo la kujikojolea kitandani likawa ni doa kubwa katika maisha yake Debora pale nyumbani kwa Mjomba wake. Ilikuwa ni fedheha na soni kubwa kwa upande wake, Shangazi yake alikuwa anasubiria watoto wa kijijini wote wameshaamka vizuri, ndio anatwisha kichwani tandiko lake na shuka za mikojo huku anatoa amri wamuimbie nyimbo mbalimbali za kebehi kumsindikiza mtoni kwenda kufua nguo zake za mikojo. "Kikojozi Kikojozi....nguo zake tuzitie moto...! " huo ndio ulikuwa wimbo pendwa kwa watoto hao huku wanagonganisha vifuu, vyuma na ngoma, wananyimwa kwa kumsindikiza kikojozi Debora.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog