Search This Blog

Monday 27 March 2023

HEKAHEKA! - 2

  


Simulizi : Hekaheka!

Sehemu Ya Pili (2)



Kuona vile sikuwa mbishi, nikanyoosha mikono yangu juu nikiamini kuwa kitendo chochote cha kuendelea kuleta ubishi kwa wale maofisa wa usalama kingeweza kuyagharimu maisha yangu.


Niliponyoosha mikono yangu juu nikaamuriwa niiweke mikono kisogoni kisha nigeuke na kuuelekea ukuta. Nikafanya kama nilivyoamuriwa bila kuhoji.


Mmoja wa wale maofisa usalama akanisogelea haraka na kwa tahadhari kubwa kisha akaanza kunipekua kama nilikuwa na silaha yoyote, huku wale maofisa wengine wakiwa makini kuhakikisha sileti matata yoyote na endapo ingetokea nimeleta purukushani yoyote waweze kunituliza kwa wepesi zaidi.


Wakati nikipekuliwa nikajaribu kuhoji sababu za wao kutaka kunikamata namna ile kama jambazi sugu lakini nikaambiwa kuwa nitalijua kosa langu baadaye kwani nilikuwa nahitajika kwa mahojiano kidogo na kama ningeonekana kutokuwa na kosa basi ningeachiwa mara moja.


Sikuleta matata yoyote, hivyo nilifungwa pingu mikononi kisha nikachukuliwa hadi kwenye chumba kimoja maalumu katika jengo lile pale kiwanja cha ndege ambacho kilikuwa na utulivu wa kupita kiasi.


Na hapo tukawakuta maofisa wengine watatu ambao niliamini kuwa walikuwa ni maofisa wa usalama wa taifa walionikaribisha kwa tabasamu bashasha.


Nilisimama nikabaki kuwatazama, wakati huo wale maofisa walionileta mle ndani walikuwa bado wamenizingira huku wakiwa makini kuhakikisha kuwa sipati fursa yoyote ya kuleta rabsha.


Mpaka hapo bado sikuwa na hofu kabisa kwani nilifikiria kuwa yawezekana walikuwa wamenifananisha na mtu mwingine na baada ya mahojiano mafupi na kugundua kuwa mimi si yule mtu waliyekuwa wakimdhania basi wangeniomba radhi na kuniachia huru niende zangu.


“Kuanzia sasa upo chini ya ulinzi,” aliniambia mmoja wa wale maofisa wa usalama wa taifa tuliowakuta mle ndani, ambaye alionekana kuwa mkuu wa usalama au kiongozi wa wale maofisa wengine.


“Kwanini nawekwa chini ya ulinzi wakati hata siambiwi kosa langu ni nini?” nikauliza huku nikishangaa.


“Usijali, utaelezwa sasa hivi, keti tafadhali,” alisema yule ofisa mkuu wa usalama aliyeonekana kuwa kiongozi wa wale maofisa wengine akinikaribisha kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza ndefu iliyokuwa na umbo mstatili, ambayo nyuma yake lile jopo la wale maofisa usalama wa taifa walikuwa wameketi. Macho yao yote yalikuwa kwangu.


Nikaketi taratibu huku nikiyatembeza macho yangu taratibu kuwatazama wale maofisa usalama mmoja baada ya mwingine kabla ya kuweka kituo kwa yule ofisa mkuu wa usalama, ambaye wakati huo alikuwa ameketi mbele yangu tukitazamana.


Sikuwa na shaka yoyote kuwa nilikuwa nimefikishwa pale kwa sababu moja muhimu ya mahojiano wakihitaji kupata taarifa fulani walizodhani pengine nilikuwa nazifahamu.


Katika mahojiano kama yale nilifahamu kuwa ushirikiano wangu ndicho kilikuwa kitu pekee ambacho kingeweza kuniweka salama na kuniepushia matatizo zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa katika kipindi kile harakati dhidi ya ugaidi duniani zilikuwa zimepamba moto kutokana na ugaidi kushika chati.


“Sijui nikuite Brown Senga, Godwin Sengerema au kwa jina la sasa la Maximilian Banda?” hatimaye yule ofisa mkuu wa usalama alivunja ukimya huku akinikazia macho.


Nikashangaa sana kusikia nikihusishwa tena kwa mara nyingine na jina la Brown Senga, hata hivyo, kilichonishangaza zaidi ni kuongezeka kwa jina la Godwin Sengerema. Nikajiuliza kulikuwa na nini kinaendelea kwa huyo mtu aliyeitwa Brown Senga!


Hata hivyo, pamoja na kujiuliza maswali yale nilijitahidi kuuficha mshangao wangu.


“Niite Maximilian Banda, hayo mengine si majina yangu,” nilimjibu yule ofisa wa usalama kwa sauti tulivu huku nami nikimkazia macho.


“Okay, nitakuita Maximilian kama unavyotaka…” alisema huku akiachia tabasamu.


“Kwa kifupi tulipata taarifa zako tangu tu ulipotua jijini Nairobi kwamba ulikuwa unakuja Dar es Salaam na mimi nikazipokea taarifa hizo kwa shauku huku nikiamini kuwa utatusaidia katika uchunguzi wetu wa mambo kadhaa ya kihalifu yaliyotendeka nchini wiki mbili zilizopita,” alisema yule ofisa mkuu wa usalama huku akiweka kituo kidogo na kunitazama kwa uyakinifu.


“Sina kitu chochote ninachoweza kuwasaidia kuhusu uhalifu, kwa kifupi sijui chochote,” niliongea kwa sauti tulivu huku nikiendelea kumkazia macho yule ofisa usalama.


Hata hivyo yule ofisa wa usalama alionekana kunipuuza, nilipomtazama wala sikuona tashwishwi yoyote katika uso wake.


“Pengine bado hujaelewa vizuri uzito wa jambo hili au taarifa tunazozihitaji kutoka kwako na hujui kwanini wewe upo hapa… hii ni kuhusiana na hali ya usalama wa nchi hii,” yule ofisa mkuu wa usalama akasema kwa msisitizo huku akiendelea kunitazama na macho yake yaliyokuwa yamehifadhi ghadhabu.


“Bado sijaelewa, ni nini kinachohusiana na usalama wa nchi hii ambacho mimi nina taarifa zake?” niliuliza kutaka kupata uhakika wa kile alichokuwa anakisema yule ofisa wa usalama kuhusiana na kutaka taarifa kutoka kwangu.




“Pengine bado hujaelewa vizuri uzito wa jambo hili au taarifa tunazozihitaji kutoka kwako na hujui kwanini wewe upo hapa… hii ni kuhusiana na hali ya usalama wa nchi hii,” yule ofisa mkuu wa usalama akasema kwa msisitizo huku akiendelea kunitazama na macho yake yaliyokuwa yamehifadhi ghadhabu.


“Bado sijaelewa, ni nini kinachohusiana na usalama wa nchi hii ambacho mimi nina taarifa zake?” niliuliza kutaka kupata uhakika wa kile alichokuwa anakisema yule ofisa wa usalama kuhusiana na kutaka taarifa kutoka kwangu.


“Unaweza kutuambia, ulikuwa wapi kipindi chote tangu ulipoondoka nchini?”


“Nadhani hati zangu za kusafiria zinajieleza vizuri, unaweza kuangalia tu,” nikasema.


“Jibu swali uliloulizwa,” ofisa mwingine wa usalama akaniambia kwa ukali.


“Nilikuwa jijini Amsterdam nchini Uholanzi,” nilijibu kwa utulivu.


“Ulikuwa huko kwa muda gani?”


“Ndiko ninakoishi, zaidi ya miaka kumi sasa,” nilijibu huku nikijaribu kujiuliza kama kulikuwa na uhusiano wowote kati ya ugaidi na muda nilioishi nchini Uholanzi.


“Una uhakika?”


“Kwa asilimia mia moja! Hata ukiulizia kwenye ubalozi wa Tanzania nchini Netherland watakuthibitishia kwani wanazo taarifa zangu,” nikasema kwa kujiamini sana.


Yule ofisa wa usalama akaniangalia kwa makini kwa kitambo kirefu huku akionekana kutafakari kwa kina jambo ambalo sikulifahamu.


Nilipowatazama wale maofisa wengine wa usalama nikawaona wakinikodolea macho kwa namna ambayo sikuelewa mara moja.


“Mizigo yako iko wapi?” akaniuliza tena.


“Hapa nina hili begi dogo, begi langu kubwa bado sijalichukua,” nilisema huku nikijiuliza walikuwa wakitaka nini kwenye mizigo yangu.


“Okay, tunahitaji kuifanyia upekuzi mizigo yako maana tunazo taarifa kuwa unafanya biashara ya mihadarati,” alisema yule ofisa usalama kwa msisitizo huku akijiamini.


“Sasa nina uhakika kabisa kuwa mmemkamata mtu asiye sahihi. Mimi sifahamu chochote kuhusu mihadarati, na mfanyabiashara wa mihadarati mnayemtafuta siye mimi niliye mbele yenu,” niling’aka huku nikishindwa kuuficha mshtuko wangu.


“Uongo huwa ni suluhisho la muda mfupi katika kutatua tatizo la kudumu. Labda nikwambie tu kuwa huwa siwavumilii watu waongo. Taarifa zetu ni madhubuti na tumejiridhisha kuwa wewe ndiwe bosi wa mtandao wa wafanyabiashara wa mihadarati nchini,” akaniambia yule ofisa mkuu wa usalama kwa kujiamini kabisa.


“Naomba uniamini, mmemkamata mtu asiye sahihi. Sifahamu chochote kuhusu mnachosema na sijui kwanini mnaendelea kunishikilia hapa kwa mahojiano. Mimi si mhalifu na sina rekodi ya uhalifu achilia mbali kuhojiwa na polisi,” nilijitahidi kuongea kwa utulivu nikijaribu kujitetea.


Yule ofisa usalama akanitazama kwa uyakinifu zaidi na kwa utulivu mkubwa huku akitabasamu, kisha akachukua mkoba wake mdogo mweusi uliokuwa chini ya ile meza na kutoa bahasha kubwa ya khaki.


Hapo ndipo alipotoa pasi mbili za kusafiria, moja ikiwa ni pasi ya Tanzania na nyingine ilikuwa ya Rwanda, kijitabu kidogo pamoja na nyaraka zingine, akavimwaga juu ya ile meza huku akiniomba nivitambue vile vitu kama ni vyangu au la.


Ile pasi ya kusafiria ya Tanzania niliitambua mara moja kuwa ilikuwa ni ile pasi yangu ya kusafiria niliyokuwa nimeikabidhi kwa yule mrembo ofisa uhamiaji pale dirishani, lakini ile pasi ya pili ambayo ilionesha kuwa ni ya Rwanda sikuitambua japo ilinishtua kidogo.


Ilikuwa na picha yangu lakini ikiwa na jina la Brown Senga na ilinitambulisha kama raia wa Rwanda. Pasipoti ile ilikuwa imegongwa mihuri ya Viza zilizoonesha kuwa nimewahi kuingia katika nchi za Uingereza, Ufaransa, Israel, Libya, Urusi, Ethiopia, Zimbabwe, Zambia na nchi nyingine nyingi.


“Bila shaka kabisa hiyo pasipoti ya Tanzania yenye jina la Maximilian Banda ni yangu, lakini hiyo pasipoti ya Rwanda siitambui kabisa na wala sijawahi kuiona,” nilisema huku nikionesha kushtushwa sana.


“Una uhakika kuwa hii pasipoti siyo yako?” aliniuliza yule ofisa usalama huku akiwa kanikazia macho.


“Sijawahi kumiliki pasipoti ya Rwanda, achilia mbali kufika katika nchi hiyo, kwani nyie mmeipata wapi?” nilisema kwa kujiamini lakini nikiwa na mshangao mkubwa.


“Na hii nakala ya pasipoti ni ya nani?” aliniuliza yule ofisa usalama huku akiinua karatasi moja miongoni mwa zile karatasi zilizokuwa pale juu ya meza na kunionesha akiwa bado kanikazia macho akinitazama kwa uyakinifu.


Nikaitazama kwa makini ile karatasi na kugundua kuwa ilikuwa ni fotokopi ya pasi ya kusafiria mali ya Tanzania, ambayo pia ilikuwa na picha yangu lakini ikiwa na jina la Godwin Sengerema.


Hapo nikahisi joto kali sana likiibuka ndani ya mwili wangu na muda ule ule akili yangu ikaanza kushindwa kufanya kazi yake sawasawa, nikahisi kuwa akili yangu ilikuwa imepigwa shoti kali ya umeme hatari wenye nguvu nyingi, hivyo kuzifanya shughuli za mwili wangu kusimama kwa ghafla kama niliyekuwa nimepigwa kumbo na ugonjwa hatari wa kiharusi.


Nikahisi labda wale maofisa usalama walikuwa sahihi kuhusu utambulisho wangu kuwa mimi ni Brown Senga, pengine nilikuwa nimepotelewa na kumbukumbu zangu na kudhani mimi ni mtu mwingine kabisa.


Nimewahi kusoma machapisho fulani kuwahusu watu waliowahi kupotelewa na kumbukumbu, jambo ambalo kwa kitaalamu huitwa amnesia. Watu hao walipoteza kumbukumbu zao wakawa hawana uwezo wa kukumbuka taarifa zao za nyuma na hata utambulisho wao halisi.


Kwa mfano mtu anayeitwa Juma akashindwa kukumbuka kuwa yeye ni Juma wa sehemu fulani na kudhani yeye ni Jacob wa sehemu nyingine kabisa. Wakati mtu mwingine hukosa kabisa uwezo wa kuhamisha taarifa mpya kutoka kwenye hifadhi ya kumbukumbu za muda mfupi kwenda hifadhi ya kumbukumbu za muda mrefu, na kushindwa kukumbuka mambo kwa muda mrefu.


Nilianza kuhisi kuchanganyikiwa, huku ubaridi mwepesi ukinitambaa mwilini mwangu na kuzifanya nywele zangu kusisimka. Hivi mimi ni nani? Maximilian Banda? Brown Senga? Au Godwin Sengerema?


Nilishindwa kusema chochote, nikabaki nashangaa. Jambo moja likanijia akilini mwangu kuwa, inawezekana nilikuwa naota ndoto ya kutisha na mara ningeamka kutoka usingizini ningekuta kila kitu kikiwa cha kawaida.


Hata hivyo kutokana na mazingira yale niliamini kuwa ile haikuwa ndoto, bali ni kweli nilikuwa nahojiwa na watu wa usalama kuhusu utambulisho wangu.


Niliendelea kuitumbulia macho ile fotokopi kwa kitambo kirefu huku wale maofisa wa usalama wakinitazama kwa makini, kisha nikashusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani. Nilifumbua mdomo wangu ili kusema lakini sauti ikawa haitoki, hivyo nikatingisha kichwa changu kukana kuifahamu ile pasi ya kusafiria.


“Kama wewe siye mwenye pasi hizi, tuambie hivi vitu ni vya nani na mbona vina picha yako?” yule ofisa usalama aliniuliza huku macho yake yakianza kumwiva kwa hasira.


“Kwani nyinyi mmevitoa wapi hivyo vitu?” nikamuuliza yule ofisa usalama.


Hakunijibu bali alichukua kile kijitabu kidogo akakifungua kurasa mbili tatu huku akinionesha. Niliyapeleka macho yangu kwenye zile kurasa zilizofunuliwa nikayaona maandishi yaliyokuwa yamemeandikwa mambo mengi sana lakini kwa lugha tofauti tofauti.


Nilijaribu kuyasoma yale maandishi lakini ilikuwa vigumu kuelewa ni nini hasa kilikuwa kimeandikwa ndani yake, kwani lugha iliyokuwa imetumika katika yale maandishi ilikuwa ni lugha iliyotumia alama zaidi.




Nilijaribu kuyasoma yale maandishi lakini ilikuwa vigumu kuelewa ni nini hasa kilikuwa kimeandikwa ndani yake, kwani lugha iliyokuwa imetumika katika yale maandishi ilikuwa ni lugha iliyotumia alama zaidi.


Sikuelewa kabisa, hivyo nilitingisha kichwa changu kukana kufahamu chochote juu ya kile kitabu.


Yule ofisa wa usalama alitaka kusema neno lakini akasita na kunitazama kwa kitambo kisha akaniamuru sasa tutoke twende nikachukue mizigo yangu ili wafanye upekuzi kuona kama sikuwa nimebeba mihadarati katika mizigo niliyotoka nayo Amsterdam.


Hapo ndipo nilipojua kuwa nilikuwa katika lindi kubwa la matatizo huku ubongo wangu ukishindwa kufanya kazi kwa haraka, suluhisho pekee nililokuwa nalo moyoni ilikuwa ni kuomba Mungu anisimamie, kwani nilijua kabisa kuwa sikuwa na kosa, na kama ni njama za wabaya wangu basi zilikuwa zimekamilika na leo ilikuwa imefika siku yangu.


Nikajiuliza itakuwaje endapo wangepekua na kukuta kulikuwa na dawa za kulevya kwenye mizigo yangu!


Nikaanza kufikiria kuhusu vichwa vya habari vya magazeti jinsi ambavyo vingepambwa na habari zangu kesho yake kuwa, ‘Kinara wa biashara ya unga akamatwa uwanja wa ndege’.


Nikamfikiria mchumba wangu, Susan Stephens raia wa Uholanzi na binti yetu Pamela niliowaacha jijini Amsterdam jinsi watakavyopatwa na mshtuko mkubwa baada ya kusikia kuwa nimekamatwa katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam nikiwa na dawa za kulevya.


Nilianza kujilaumu kwani wiki mbili kabla wakati nikijiandaa kwa safari ya kuja Tanzania, Susan aliniomba sana niahirishe safari hadi wakati mwingine lakini nikamkatalia.


Pia nikawafikiria ndugu zangu walioko ziwani kijijini Manda na maeneo mengine jinsi ambavyo wangepatwa na mshtuko mkubwa baada ya kusikia kuwa mimi ni kinara wa biashara ya dawa za kulevya na kwamba nimekamatwa na dawa za kulevya katika uwanja wa ndege.


Muda ule ule ikanijia yakini kuwa huenda watu wa usalama walikuwa wameniwekea dawa za kulevya katika mizigo yangu ili waniangamize.


Hata hivyo, nililifuta wazo hilo haraka huku nikipiga moyo konde baada ya kujiuliza kwanini watu wa usalama waniwekee dawa za kulevya, kwani walikuwa na ubaya gani na mimi hadi waniwekee dawa za kulevya kwenye mizigo yangu? Waniangamize kwa lipi nililokuwa nimewakosea?


Lakini kwa ajili ya tahadhari nilimgeukia yule ofisa mkuu wa usalama aliyekuwa akinihoji nikamwambia kuwa sitokubali kugusa mizigo yangu bila kuwapo mashahidi, isijekuwa mizigo yangu ilikuwa imewekewa hizo dawa za kulevya, kwani nilipotoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Schiphol jijini Amsterdam mizigo yangu ilikuwa imekaguliwa na ilikuwa salama.


Hoja yangu kubwa kwao ilikuwa kupata uhakika kutoka kwao kuwa walikuwa wananijua vizuri kiasi cha kuthibitisha kuwa kweli mimi nilikuwa kinara wa biashara na msafirishaji wa dawa za kulevya.


“Sisi tunazo taarifa zako kamili kuwa wewe si tu mfanyabiashara wa dawa za kulevya, bali yapo mengine mengi ya kutisha,” aliniambia yule ofisa mkuu wa usalama na kuongeza kuwa wao walikuwa wanafanya kazi kutokana na taarifa za kiintelijensia zilizokuwa zikiwafikia.


“Kwa hiyo, baada ya kupata taarifa zangu kuwa mimi ni mfanyabiashara wa dawa za kulevya, nyie mmechunguza kutafuta ukweli?” nilimuuliza yule ofisa mkuu wa usalama kwa sauti tulivu.


“Ndiyo maana leo tumekukamata baada ya ujanja mwingi wa kuruka mitego ya vyombo vya dola. Lakini pia unatafutwa na polisi wa Zimbabwe, Rwanda na Ethiopia kwa kupanga matukio ya uhalifu,” alisema yule ofisa mkuu wa usalama kwa kujiamini kabisa.


“Si kweli, sijawahi kufika katika nchi hizo na sijakanyaga ardhi ya Tanzania kwa takriban miaka kumi na mbili tangu nilipoondoka, ni wapi niliporuka mtego? Isitoshe sina historia yoyote ya uhalifu achilia mbali kuhojiwa na polisi kwa kosa lolote lile,” nilisema huku nikishangaa sana.


“Ni kweli, kama Maximilian Banda hujakanyaga Tanzania kwa takriban miaka kumi na mbili, hilo halina ubishi kwani hata pasipoti yako inajieleza, na kama Brown Senga au Godwin Sengerema hujawahi kufikishwa polisi kwa kosa lolote… lakini bado haiwezi kukufanya kuwa mwadilifu kwani umekuwa ukiratibu shughuli zote za uhalifu.”


Kwa maneno hayo ndipo nilipopata uhakika kuwa walikuwa wamenifananisha na mtu mwingine kabisa, maana sijawahi kutumia majina hayo.


“Mmekosea sana, mimi sina uwezo wowote wa kuratibu shughuli za uhalifu, kwanza mimi ni mwoga sana na katika maisha yangu sijawahi hata kushuhudia kuku akichinjwa sembuse kupanga mipango ya uhalifu kwa binadamu wenzangu!” nilisema huku nikishangaa.


“Uongo wa kipuuzi kama huo hauwezi kuaminika hata na mtoto mdogo,” alisema tena yule ofisa mkuu wa usalama kwa sauti tulivu lakini akionekana kuidhibiti ghadhabu iliyoanza kuibuka ndani yake.


Baada ya mabishano makubwa na kukurukakara za hapa na pale kuhusu suala la mimi kukubali kufanyiwa upekuzi wa mizigo yangu, mara akatokea mwanamama aliyejitambulisha kwangu kuwa ni Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.


Alinihakikishia kuwa wale wanausalama ni serikali na siyo wahuni. Wasingethubutu kuniwekea dawa za kulevya katika mizigo yangu, hivyo akanisihi sana kwa upole nikubali kupekuliwa ili wajiridhishe kabla ya kuendelea na mambo mengine.


Niliomba apatikane shahidi nje ya wale maofisa wa usalama wa kushuhudia mizigo yangu kabla ya kufanyiwa upekuzi lakini hakuna mtu aliyekubali kuchukua dhima ile katika maofisa waliokuwa kazini pale uwanja wa ndege jioni ile.


Hata hivyo, baada ya kitambo kirefu yule Meneja wa Kiwanja cha Ndege alichukua dhima ya kuwa shahidi na hapo ndipo upekuzi ukafanyika kuanzia kwenye mizigo yangu hadi mwilini. Hakuna dawa yoyote ya kulevya iliyopatikana.


Hawakuridhika wakanipeleka katika choo maalumu cha kutolea dawa za kulevya kwa njia ya haja kubwa. Kwa hofu nikashindwa kabisa kujisaidia pale.


Hata hivyo, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuona choo kama kile. Kilikuwa ni choo cha aluminium na kilikuwa tofauti kabisa na vyoo vingine vya pale uwanjani, hiki kilikuwa cha aina yake, kisafi sana kiasi kwamba mtu ungeweza hata kutengewa chakula na ukala bila ya kuhisi kinyaa.


Nilitegemea kuwa baada ya kukosa dawa za kulevya katika mizigo yangu wangenirejeshea uhuru wangu na kuniachia niende zangu nyumbani. Lakini haikuwa hivyo.


Walinirudisha tena kwenye kile chumba cha mahojiano. Sasa wakaacha habari za dawa za kulevya, wakahamia katika masuala ya uhalifu na vikundi vya kigaidi. Hapo nikashangaa sana!




Hata hivyo, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuona choo kama kile. Kilikuwa ni choo cha aluminium na kilikuwa tofauti kabisa na vyoo vingine vya pale uwanjani, hiki kilikuwa cha aina yake, kisafi sana kiasi kwamba mtu ungeweza hata kutengewa chakula na ukala bila ya kuhisi kinyaa.


Nilitegemea kuwa baada ya kukosa dawa za kulevya katika mizigo yangu wangenirejeshea uhuru wangu na kuniachia niende zangu nyumbani. Lakini haikuwa hivyo.


Walinirudisha tena kwenye kile chumba cha mahojiano. Sasa wakaacha habari za dawa za kulevya, wakahamia katika masuala ya uhalifu na vikundi vya kigaidi. Hapo nikashangaa sana!


Je, nini kitaendelea?...


“Tueleze, washirikia wenzako wako wapi na silaha mlizopora ili kutekeleza mipango yenu haramu mmezificha wapi?” yule ofisa mkuu wa usalama aliniuliza mara tu nilipoketi kwenye kiti mbele yake.


“Sifahamu chochote kuhusu silaha wala mipango haramu kama unavyosema,” nikamjibu yule ofisa mkuu wa usalama nikionesha kuchoshwa na maswali yao.


Yule ofisa usalama alinitazama kwa makini zaidi kisha akaongea kwa msisitizo huku akiendelea kunitazama.


“Nimekwishakuonya kuwa huwa siwavumilii kabisa waongo, elewa mimi ni mtu mwema sana lakini siyo mpumbavu kama unavyodhani, tumeelewana?”


“Nimekuelewa lakini mimi sifahamu chochote kuhusu uhalifu wala silaha unazosema na sina washirika wowote katika uhalifu,” nikaongea kwa msisitizo.


“Tuambie wenzako wako wapi na silaha mlizopora mmezificha wapi?” akazidi kuniuliza kwa kusisitiza.


“Wenzangu akina nani?”


“Wenzako ulioshirikiana nao kuvamia bohari kuu ya silaha na kupora silaha ili kufanya matukio ya ugaidi hapa nchini, tunajua mna mtandao mpana na wewe ndiye kiongozi wa ugaidi huu!”


“Kwa kweli sifahamu chochote kuhusu huo mtandao wa uhalifu unaosema wala hizo silaha.”


“Mmezificha wapi?” sasa yule ofisa mkuu wa usalama aliongea kwa sauti kali huku akianza kushindwa kudhibiti hasira zake.


“Kwa jinsi ninavyopenda amani kama ningekuwa na taarifa zozote kuhusu uhalifu mnaonituhumu nadhani nisingeshindwa kuwapa taarifa hizo,” nikajitetea huku nikiwa nimechanganyikiwa.


Yule ofisa usalama alinipuuza, badala yake akaruhusu tabasamu la kifedhuli kuchanua usoni kwake, kisha nikamuona akimpa ishara fulani kwa kichwa ofisa mmoja wa usalama aliyekuwa amesimama kando, ishara ambayo sikufahamu maana yake.


Na hapo yule ofisa usalama aliyepewa ishara ile akaondoka haraka na kufungua mlango kisha akatoka ndani ya chumba kile akielekea nisikokujua.


Wakati huo huo nikamuona yule ofisa mkuu wa usalama akiinuka na kuanza kupiga hatua taratibu kunisogelea huku akiwa amekunja uso wake na kutengeneza matuta usoni.


Nilimtazama kwa wasiwasi wakati akizidi kunisogelea huku nikiwa sijui anataka kufanya nini. Nilitamani kuinuka na kutimua mbio lakini sikuweza, hivyo nilisubiri kuona mwisho wake.


“Ni vyema ukasema ukweli vinginevyo utapata mateso makali sana, maana tunachohitaji ni taarifa zote muhimu kabla ya hii nchi haijaangukia kwenye machafuko,” yule ofisa usalama akaninong’oneza sikioni maneno yaliyonishtua sana.


Kisha akasimama na kunitazama kwa kitambo huku akiuma mdomo wake wa chini. Nilibaki kimya nikiwa nimemtumbulia macho maana sikujua nimjibu nini.


“Hivi unadhani tumekuleta hapa ili kupiga stori au kupoteza muda wetu!” yule ofisa mkuu wa usalama akanionya na kisha muda uleule alianza kupiga hatua taratibu kurudi kule alikotoka na kuketi kwenye kiti chake huku akinitazama kwa hasira.


“Pengine bado hujaelewa vizuri uzito wa jambo hili lililosababisha vifo vya askari wetu na wananchi wasio na hatia, na kwanini wewe upo hapa…” alisema yule ofisa na kuongeza.


“Kwa akili yako ulidhani kusafiri nje ya nchi kila unapokuwa umeandaa matukio ya uhalifu ili yatokee wakati wewe uko nje ya nchi tusingeweza kubaini kama wewe ndiye uliye nyuma ya mipango hii?” yule ofisa mkuu wa usalama akaniuliza huku akiendelea kutabasamu.


Sikujibu kitu bali nilibaki nikimtazama kwa mshangao huku hasira ikiwa imenikaba kooni. Sikujua kwanini nilikuwa nikiulizwa maswali ambayo kwa kweli sikuwa na majibu yake!


Muda huo huo ule mlango ukafunguliwa kisha yule ofisa usalama akaingia akiwa ameongozana na mwanamke mmoja mrefu kiasi aliyevaa gauni fupi jepesi la rangi ya pinki na mtandio mwepesi huku ndani ya lile gauni akiwa amevaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu.


Yule mwanamke alifika na kusimama mbele yangu, na hapo nikainua uso wangu kumtazama usoni, haikunichukua muda mrefu kumtambua.


Alikuwa ni yule mwanamke chotara mwenye mtoto niliyesafiri naye kutoka Nairobi hadi Dar es Salaam. Lakini safari hii hakuwa na mtoto wake wala mizigo.


Yule mwanamke alinitazama kwa makini huku chuki ya waziwazi dhidi yangu ikijionesha kwenye macho yake wakati akinitazama.


“Unamfahamu huyo mwanamke aliyeko mbele yako?” yule ofisa mkuu wa usalama akaniuliza kwa udadisi.


“Hapana, simfahamu kabisa,” nikajibu huku nikitingisha kichwa changu kukataa.


“Una uhakika kuwa humfahamu?” aliniuliza tena huku akiwa amenikazia macho.


“Kweli simfahamu na sina sababu ya kuongopa,” nikamjibu yule ofisa usalama kwa kujiamini.


“Mbona yeye anakufahamu?”


“Hilo mimi sijui, labda muulizeni ananifahamu kivipi, ila kitu pekee ninachojua ni kwamba tumesafiri wote kwenye ndege moja ya KLM ingawa yeye alipandia Nairobi, basi!” nikajibu kwa hakika, hata hivyo jibu langu lilionesha halikunisaidia.


“Babra…” yule ofisa usalama akamwita yule mwanamke chotara.


“Abee!” yule mwanamke chotara ambaye sasa nilimtambua kwa jina la Babra aliitika kwa unyenyekevu huku akiyaondoa macho yake kutoka kwangu na kuyahamishia kwa yule ofisa usalama aliyemwita.


“Unamfahamu huyu mtu aliyeketi mbele yako?”


“Ndiyo namfahamu,” alijibu Babra kwa kujiamini huku akiyarudisha macho yake kwangu.


“Unaweza kutuleza unamfahamu kivipi?” yule ofisa usalama akamwuliza Babra kwa sauti tulivu.


“Namfahamu kama shemeji yangu, anaitwa Brown Senga ingawa yeye anataka watu wamwite Godwin Sengerema, na alikuwa anaishi na mdogo wangu Jasmine ambaye walikutana miaka sita iliyopita,” alianza kuelezea Babra huku akinitazama kwa chuki.


“Enhe, endelea kutuelezea jinsi unavyomfahamu,” yule ofisa usalama akasema huku akibetua kichwa chake.


“Niseme tu kuwa mwanzoni nilimuona ni mtu mchesi, mstaarabu na mwema sana kwani alionesha kumpenda sana mdogo wangu Jasmine ingawa nilimuona kuwa alikuwa na wivu sana kwa Jasmine, hivyo kila wakati alimpapatikia na alikuwa tayari kumtimizia chochote alichokitaka…” alinyamaza na muda huo nilimuona akimeza funda la mate kutowesha koo lake.


“Lakini kilichonishangaza ni kuwa alikuwa akikwepa sana kuongelea mambo yaliyohusu familia yake na wala hakupenda kupiga picha huku akisisitiza kuwa uhusiano wake na Jasmine usiwe wa wazi na ujulikane na watu wachache sana akidai kuwa hakutaka kumwingiza Jasmine katika hatari. Nilishangaa na nilikuwa nikimuuliza sana kuhusu kazi aliyokuwa akiifanya, maana nilimfahamu kama mfanyabiashara wa madini, hivyo niliuliza biashara hiyo ilihusianaje na kumuingiza Jasmine katika hatari, lakini Brown hakupenda sana kuongelea mambo ya kazi yake, na ilionekana kuwa hata Jasmine alikuwa akikubaliana naye kwa kila kitu!


“Alikuwa mtu wa safari nyingi sana na za ghafla na siku zote alikuwa na marafiki tofauti ambao sikuwa nikiwaelewa. Nikamshawishi Jasmine kuwa makini na amchunguze taratibu kabla hajaamua kuishi naye ili kufahamu zaidi undani wake na awafahamu wazazi wake na jamaa zake, lakini Brown aligundua na kumtaka Jasmine asipende kunisikiliza mimi kwani nilikuwa nataka kumpotosha, ili mradi wao walikuwa wanampenda sana na alimtimizia kila kitu bila ya matatizo yoyote hakukuwa na haja ya kuchunguzana.


“Siku moja nilikwenda kuwatembelea walipokuwa wanakaa, Brown alikuwa ametoka, nikamkuta Jasmine akifanya usafi chumbani kwake huku akipekua kila sehemu na kuiona bunduki aina ya SMG iliyokuwa imefichwa mahala fulani ndani ya kabati la ukutani. Jasmine alinionesha na sote tulishikwa na wasiwasi sana kwani tulianza kuhisi kuwa Brown alikuwa akijishughulisha na vitendo vya uhalifu. Jioni aliporudi kutoka kazini Jasmine alimuuliza kuhusu ile bunduki na Brown alimuelezea kuwa yeye kama mfanyabiashara mkubwa wa madini alipaswa kuwa na silaha kama ile kujilinda, kwani huko migodini wanakumbana na watu wa kila aina na kumuonya Jasmine kuwa asiitoe siri ile kwa mtu yeyote.”


“Lakini pia alipoona mimi ninazidi kuwa na mashaka naye waliamua kuhama walipokuwa wakiishi na kuhamia sehemu nyingine ambayo sikuijua na wakaamua kubadilisha namba zao za simu, na ninahisi pia alimkataza Jasmine asiwasiliane na mimi, na kwa kuwa alimpenda sana Brown akamsikiliza. Sikutaka kujishughulisha nao na kwa muda huo mimi na mume wangu tukawa kwenye pilika pilika za kuhamia jijini Nairobi nchini Kenya.





“Lakini pia alipoona mimi ninazidi kuwa na mashaka naye waliamua kuhama walipokuwa wakiishi na kuhamia sehemu nyingine ambayo sikuijua na wakaamua kubadilisha namba zao za simu, na ninahisi pia alimkataza Jasmine asiwasiliane na mimi, na kwa kuwa alimpenda sana Brown akamsikiliza. Sikutaka kujishughulisha nao na kwa muda huo mimi na mume wangu tukawa kwenye pilika pilika za kuhamia jijini Nairobi nchini Kenya.


“Lakini kwa muda mfupi niliomfahamu Brown niligundua kwamba alikuwa ni mtu wa mambo mengi na marafiki wengi sana, walioonekana wana nyazifa tofauti wakiwemo wanajeshi, waliokuwa wakifika pale nyumbani kwake mara kwa mara lakini kwa uficho na kila walipofika walitumia muda mrefu na Brown wakiwa peke yao maktaba wakijadili mambo fulani waliyoyajua wenyewe. Na kwa kuwatazama tu usingeshindwa kugundua kuwa wote waliokuwa wakifika pale walikuwa na tabia zinazofanana, wacheshi, wakarimu na marafiki wazuri kama alivyo Brown,” Babra alinyamaza kidogo, akayahamisha macho yake kutoka kwangu na kutazama kando huku akionekana kuwaza mbali sana.


“Unaweza kuwakumbuka baadhi ya hao watu waliokuwa wakifika hapo kwa Brown kuonana naye?” yule ofisa mkuu wa usalama alimuuliza Babra huku akionekana kuwa makini zaidi.


“Kwa kweli walikuwa wakija watu wengi wa aina tofauti kama nilivyoeleza, ila kwa kuwa mimi sikuishi pale ilikuwa vigumu kuwambuka labda kama itokee nionane nao tena. Ila yupo mmoja ninayemkumbuka kwa jina moja la Trésor, kwani mara nyingi nilikuwa nikimsikia Brown akimtaja wakati akimwita hivyo na alikuwa akiongea naye mara kwa mara kwenye simu,” alisema Brown huku akinitazama kwa jicho la wizi.


“Ni nani huyo Trésor?” aliuliza tena yule ofisa wa usalama.


“Alikuwa rafiki mkubwa wa Brown na kwa haraka niliweza kubaini kuwa alikuwa mtu wa Rwanda kwa mwonekano wake na hata lafudhi ya Kiswahili chake, na bila shaka walikuwa wakifanya biashara pamoja kwani mara nyingi alikuwa akimpitia pale kwake,” alisema Babra huku akishusha pumzi.


“Kwa hiyo baada ya wao kuhama pale walipokuwa wakiishi na wewe kuhamia Nairobi ikawaje?”


“Kilipita kitambo kirefu bila kuonana nao wala kusikia habari zao lakini siku moja nilishangaa nilipomuona Jasmine akifika nyumbani kwangu jijini Nairobi kunisalimia na nilipomuuliza amepajuaje akaniambia kuwa Brown ndiye aliyemuelekeza na kwamba yeye hakutaka tujue kama yupo pale jijini Nairobi kutokana na shughuli alizokuwa akizifanya,” alisema Babra kwa huzuni na mara nikamuona kama aliyekuwa anafikiria kitu fulani, muda huo huo nikaiona michirizi ya machozi kwenye mashavu yake.


“Sikujua Brown alipajuaje pale kwangu, na katika maongezi yetu niligundua kuwa Jasmine alikuwa amebadilika sana kitabia, alikuwa ametumbukia kwenye ulevi na utumiaji wa dawa za kulevya, na hakuwa tena mtu wa kuaminika kwani alijiingiza kwenye masuala ya uhalifu wa mitandaoni, uhalifu wa kutumia silaha na hata utapeli,” alisema huku akiwa analia.


Muda wote ule wale maofisa wa usalama walikuwa kimya wakimsikiliza Babra huku wakinitazama kwa makini. Nilijikuta nikivutiwa kukisikiliza kile kisa kumhusu mtu aliyeitwa Brown Senga na kusahau kuwa yale maelezo yalikuwa yakitolewa ili kunikandamiza nionekane nina hatia ya uhalifu.


“Siku mbili tangu nionane na Jasmine likatokea tukio la kutoweka kwa kaimu mkurugenzi wa masuala ya teknolojia wa tume ya uchaguzi nchini Kenya (IEBC), Christopher Chege Msando na kisha akapatikana akiwa ameuawa katika eneo la Kikuyu lililo viungani mwa mji wa Nairobi baada ya kuteswa sana. Katika upelelezi wa watu wa usalama ilisemekana kuwa siku ile alikuwa na msichana mmoja chotara ambaye walikuwa wanamsaka na walipoonesha picha za CCTV nilishtuka sana baada ya kumtambua yule msichana kuwa alikuwa Jasmine, kwa kweli nilishtuka sana, nikajaribu kuwasiliana na Jasmine bila mafanikio,” alinyamaza na kufuta machozi.


“Ndipo baada ya miezi kadhaa nikasikia kuhusu tukio la wizi wa pesa kwenye Benki ya Wananchi lililomhusisha pia Jasmine. Kwa kweli huyu bwana kamsababishia mdogo wangu matatizo makubwa kwa kumwingiza kwenye uhalifu kisha yeye akatokomea tusikokujua…” alibwata Babra huku akinielekezea kidole kwa hasira.


“Siyo kweli, mwongo mkubwa huyu mwanamke, naomba msimuamini maneno yake,” nikamkata kauli huku nikiongea kwa kujiamini.


“Kama unadhani kuwa yeye ni muongo kwanini hujiulizi kuwa tumezipata wapi taarifa zako na nyaraka zako zikiwemo pasipoti zako kama siyo yeye aliyesaidia kutupa taarifa zako?” yule ofisa usalama akaniuliza huku akinitazama kwa ukali.


“Mimi siye mmiliki wa pasipoti hizo na wala sijui habari hizi mmezitoa wapi! Kama taarifa zenu mmezipata kutoka kwa mwanamke huyu amewadanganya, simjui na wala sijawahi kumuona kabla ya leo,” nilisema kwa kubwata huku donge la hasira likiwa limenikaba kooni.


“Sioni sababu kwanini nikusingizie, Brown, kwanza sina ugomvi na wewe hata kama umesababisha kifo cha mdogo wangu. Inamaana hukumbuki kuwa uliwahi kumtorosha Jasmine ukampeleka kuishi kwenye jumba lako la kifahari huko Avenue Gikondo jijini Kigali? Hukumbuki ulivyokuja kumuumiza baadaye na kuyafanya maisha yake yawe ya majonzi?” Babra akasema kwa kusisitiza na kuniacha na mshangao usioelezeka.


“Hukumbuki kuhusu lile tukio la uporaji pale Benki ya Wananchi? Uliamua kumtumia Jasmine kwenye ule wizi kwa kuwa uliona umezitawala akili zake na ulipofanikiwa azma yako ukamwacha afe. Au kwa kuwa Jasmine amekufa na hawezi kujitetea tena basi huoni taabu kumkana?” aliniuliza Babra kwa hasira huku akitokwa machozi. Sasa alikuwa analia kwa uchungu mkubwa.


Loh! Maelezo ya Babra ambaye wakati wote alikuwa amesimama mbele yangu yakasababisha tumbo langu lianze kunisokota kama niliyevamiwa na maradhi mabaya ya kipindupindu.


Maelezo yake ni kama aliyepigilia msumari wa mwisho katika jeneza langu tayari kwa safari ya maziko. Nilikuwa nimesingiziwa vibaya kiasi kwamba sikufahamu haraka nijitetee vipi na badala yake nikabaki mdomo wazi huku koo langu likikauka.


Sikuwa na shaka yoyote kuwa njia ya kuelekea gerezani ilikuwa nyeupe kwangu na mwisho wangu ulikuwa umewadia, na hapo nikaanza kuilaani vibaya nafsi yangu huku nikijuta kupata wazo la kurudi Tanzania.


Kwa maneno yale ya Babra, kwa kweli hali ya mambo ilivyokuwa kwa wakati huo ikawa imenichanganya sana na kuanza kunikatisha tamaa. Niliona ni kama lilikuwa tukio la kufikirika lakini haikuwa vile, kwani lilikuwa ni tukio la kweli na lililonishangaza sana.


Hata hivyo, niliona kuwa kukaa kimya na kuuruhusu uongo ule uaminike isingefaa.


“Muongo mkubwa huyu mwanamke, msimuamini maneno yake hata kidogo,” nikaongea kwa kujiamini.

ITAENDELEA


0 comments:

Post a Comment

Blog