Search This Blog

Thursday 23 March 2023

MATANGA YA ROHONI - 5

  

Simulizi : Matanga Ya Rohoni


Sehemu Ya : Tano (5)

Deborah akageuka tena kuwa gumzo kutokana na kukomba zawadi zote za masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu. Walimu wake wanaofahamu undani wa maisha yake walijawa na furaha ya ajabu. Deborah wakati wote alikuwa analia machozi ya furaha kwa ushindi wa masomo hayo, akiwa amewaburuza wanafunzi wenzake wenye kupata mahitaji yote muhimu kwa wakati bila vikwazo vyovyote. "Nimefurahishwa sana na matokeo ya Bi.Deborah Kunambi, ninatoa ahadi ya kumpatia kibarua katika moja ya ofisi yangu mpya itakayofunguliwa Mjini Morogoro, pia ninatoa ahadi ya kumsomesha elimu ya Chuo Kikuu kwa kozi yoyote atakayochaguliwa" hayo yalikuwa ni sehemu ya maneno ya mgeni rasmi Mr.Tonny katika hotuba yake yaliyoibua shangwe na vigeregere katika ukumbi mzima.

Deborah ikabidi anyooshe mikono angani kumshukuru Mungu kwa baraka ya kupata kibarua Mjini Morogoro kitakachomfanya aweze kumtunza mama yake mzazi bila shida. Baada ya sherehe ile kwisha, msaidizi wa tajiri Mrs.Tonny, akampatia Deborah anuani za mawasiliano atakazozitumia kuwasiliana nao ili aweze kupangiwa kituo cha kazi mara tu akimaliza shule.




Nimefurahishwa sana na matokeo ya Bi.Deborah Kunambi, ninatoa ahadi ya kumpatia kibarua katika moja ya ofisi yangu mpya itakayofunguliwa Mjini Morogoro, pia ninatoa ahadi ya kumsomesha elimu ya Chuo Kikuu kwa kozi yoyote atakayochaguliwa" hayo yalikuwa ni sehemu ya maneno ya mgeni rasmi Mr.Tonny katika hotuba yake yaliyoibua shangwe na vigeregere katika ukumbi mzima. Deborah ikabidi anyooshe mikono angani kumshukuru Mungu kwa baraka ya kupata kibarua Mjini Morogoro kitakachomfanya aweze kumtunza mama yake mzazi bila shida. Baada ya sherehe ile kwisha, msaidizi wa tajiri Mrs.Tonny, akampatia Deborah anuani za mawasiliano atakazozitumia kuwasiliana nao ili aweze kupangiwa kituo cha kazi mara tu akimaliza shule.

Baada ya siku kadhaa kupita wakaanza mitihani ya kumalizia elimu ya kidato cha 6. Walipomaliza tu mitihani Deborah himahima akaelekea zake Morogoro kwenda kuripoti kazini kisha akamuone mama yake mzazi kwa mara ya kwanza baada ya kupotezana na mama yake kwa baada ya miaka 6 kupita. Laiti angelijua madhila ya mbeleni yatakayomsibu, asilani asingethubutu kukanyaga Morogoro.

Yalimsibu matanga ya rohoni yaliyomsababishia aishie gerezani kwa muda usiojulikana. Yale yale yakajirudia, ya mbuzi masikini hazai, na kama akizaa basi atazaa tasa tu. Juhudi zote za Deborah katika masomo yake ili aje kuishi kivulini, akajikuta zinakwamishwa na mahasidi wasiomtakia heri katika maisha yake. Maisha yake kila siku yalikuwa yanazalisha idadi kubwa ya maadui kuliko marafiki.

Mwaka 2002, Deborah alivyoikanyaga tena Morogoro kwa mara ya pili tokea atoroke nyumbani kwa Mjomba, sasa ulikuwa ni Mji wa wajanja. Mabadiliko ya Mji yalikuwa ni makubwa mno ya kimaendeleo ndani ya kipindi kifupi tu cha takribani miaka 6. Watu wake nao walionekana kuwa wamenawiri na ni wenye kufurahia maisha. Kulikuwa na wanaume kwa wanawake wanaojua kuvaa, wapenda burudani na wanaojua kuzisaka pesa kwa hali na mali. Ni mji uliofikia viwango vya kuitwa kwa jina la 'Jiji kasoro bahari' kutokana na upatikanaji wa kila kitu kinachotakiwa kasoro uwepo wa Bahari Hindi tu.

Tajiri mwanamama Mrs.Tonny mfadhili mpya wa Deborah alikuwa ni mtu maarufu na mahashumu kwenye kila kona ya Mji wa Morogoro huku akiwa na nyumba za kifahari kwenye maeneo wanaoishi watu wazito ya Forest na Rock garden. Mitaa yote kuanzia Mafisa, Msufini, Kilakala, Ngoto, Kingo, Mlapakoro, Boma road, SUA, Vibandani, Relwe magorofani, Kigurunyembe, Madizini na kwingineko kote huko alikuwa anajulikana, usicheze na pesa sabuni ya roho, ukiwa nayo kila mtu atakunyenyekea na kukuheshimu kuanzia wakubwa kwa watoto wote watakuabudu. Deborah aliwekwa aishi kwenye moja ya nyumba yake Mrs.Tonny iliyoko maeneo ya Liti huku nyumba hiyo ikiwa na ulinzi madhubuti wa saa 24. Ndani ya nyumba hiyo aliwakuta wasichana wenzake wengine wawili ambao nao ni wafanyakazi katika shughuli za Mrs.Tonny. Walikuwa wanachukuliwa nyumbani na gari na kurudishwa toka kazini na gari. Inapofika mwishoni mwa juma, Bosi wake Mrs.Tonny anakuja kuwachukua na kwenda nao muziki kwenye viwanja mbalimbali vya starehe. Walikuwa wanabadilisha viwanja watakavyo, mara waende Shimoni Morogoro Hotel, wakati mwingine Rock Garden na maonyesho ya 'Forest Hill' ili mradi Deborah alikuwa anaishi maisha ya hali ya juu ambayo hajawahi kuyaishi tokea azaliwe.

Akamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjaalia kuishi maisha ya ndoto zake mapema kabisa hata kabla hajamaliza Chuo Kikuu. Baada ya kupita muda wa wiki mbili tokea aanze kazi, akaomba ruhusa ya Siku 2 kwenda kuwasalimia ndugu na jamaa zake Kijijini Mikongeni. Mrs.Tonny akamruhusu kiroho safi kabisa huku akimtaka kuhakikisha Jumatatu asubuhi na mapema kuhakikisha anaripoti kazini. Akampatia na bakhshishi ya nakidi ya pesa za kushika mkononi kwa ajili ya matumizi ya hapa na pale. Deborah alifurahi mno, ikiwa ndio pesa yake ya kwanza kutia mkononi tokea aanze kufanya kazi kwa jasho lake mwenyewe. Deborah akapitia soko kuu la Mjini Morogoro na kununua masurufu ya kubeba nyumbani. Akanunua zake sukari, mchele, sabuni na bidhaa mbalimbali za nyumbani. Bila kusahau alinunua pia vitenge kwa ajili ya shangazi yake na binamu zake. Hakuwa tayari kulipiza ubaya kwa ubaya, bali alitaka kulipa ubaya kwa wema, ili Shangazi yake ajifunze kitu.

Deborah mawazoni mwake alitaka pindi akirudi kazini, aanze harakati za kutafuta chumba cha kupangisha ili amchukue mama yake aishi nae pamoja. Aliona kabisa kuwa wakati wa kumtunza mama yake umefika. Ingawa pia akawa anatafakari, kama akimchukua akaanza kuishi nae halafu ukifika muda wa kujiunga na Chuo Kikuu itakuwaje, nani atakaa kumtunza mama yake. Mawazo hayo yakamuingiza katika bahari ya fikra, akipanga na kupangua kichwani mwake. Baada ya kukamilisha mahitaji yake akaeleka stendi ya Daladala zinazoelekea Mzumbe kwa ajili ya kwenda nyumbani kwa Mjomba wake. Baada ya kupata nafasi kwenye Daladala hiyo, kitambo kifupi tu msafara wa kuelekea Mzumbe ukaanza. Njia nzima, Deborah alikuwa anawaza namna watakavyotazama uso kwa uso na Shangazi yake. Alipanga kuwangukia miguuni Mjomba na Shangazi yake kwa kuwaomba radhi kwa utovu wa nidhamu alioufanya wa kutoroka nyumbani. Matumaini yake ni kuwa watamsamehe na tena wakijua sasa anajitegemea mwenyewe na anashika pesa zake, heshima na adabu kwake itaongezeka maradufu. "Mikongeni Mikongeni...achia bodi, abiria piga chini mnauweka usiku...!" ilikuwa ni sauti ya kondakta wa Daladala iliyomshtua Deborah na kumfanya akurupuke hima hima kwenye kiti alichokuwa amekalia. Kondakta akamsaidia kushusha mizigo yake, kisha gari ile ikatimka zake.

Deborah akabakia amepigwa na bumbuwazi kwa muda akiwa haamini jinsi mazingira yalivyobadilika na kumbabaisha vilivyo. Akajongea pembeni ya duka moja jirani na barabara na kupumzika kwenye mti wenye kivuli kwa muda akiyasoma mazingira. Barabara yote ilikuwa imepigwa lami, huku nyumba nyingi zikiwa hazipo. Kijasho chembamba kikaanza kumvuja akiwa hayaamini macho yake kama kweli amepotea nyumbani kwao kabisa. Sehemu ambayo ameishi kwa zaidi ya miaka 10, akivijua vichochoro vyote lakini leo anarudi nyumbani haioni nyumba ya Mjomba wake wala za majirani zake.

"Habari za leo kaka, samahani, hapa zamani kulikuwa na nyumba nyingi tu sizioni imekuwaje?" aliuliza Deborah kwa yule huku akijitega kwa umakini kusubiria jibu. "Ahaaa...inaelekea dada ulipotea siku nyingi sana, kuna mradi wa barabara na bomba la maji ulipita hapa, wenye nyumba wakalipwa pesa za fidia na kuvunjiwa nyumba zao, yapata miaka 5 sasa...!" aliongea yule muuza duka huku akianza kuhudumia wateja wengine waliofika dukani pale. Jibu lile lilikuwa kama kaa la moto kwa Deborah, jasho jekejeke likaanza kumvuja mwilini, akiwa hayaamini masikio yake kwa kile alichokiita. "Kaka Unasemaje?...kwa hiyo wamekwenda wapi?" alijikuta Deborah anaropoka kwa sauti ya juu, huku akiwa anakaribia kutaka kulia machozi, alimuona kama ameongea Kichina. "Ndio hivyo hivyo ulivyosikia, sio jukumu kujua wapo wapi..!" alijibu yule muuza duka kwa hasira akionekana hapendwi kusumbuliwa tena. Deborah ikabidi asogee pembeni kiunyonge akiwa haamini anachokishuhudia na kukisikia, aliona kabisa lengo lake la kumuona mama yake mzazi limeota mbawa. Mawazo yake yakahamia kwa mama yake mzazi akianza kushikwa na hofu kama bado ni mzima wamehama nae au amefariki. Alikuwa hana be wala che kuhusu familia yake mahali ilipo hivi sasa.

Njaa ikaanza kumkamata vilivyo, ikabidi asogelee mkahawa wa eneo la jirani hapo hapo na barabara ili apate kifungua kinywa. Alipoingia akaukuta mkahawa umeshona watu kochokocho, kila mtu anapata staftahi awahi kwenye mizunguko yake ya kutwa. Deborah akaenda moja kwa moja kwenye meza iliyobakia tupu ikiwa na mtu mmoja tu mwanaume wa makamo. Alipofika Deborah akasalimiana na yule mwanaume kisha akavuta kiti na kumuita mhudumu. Mhudumu alipokuja, Deborah akaagizia vitafunwa na chai ya mkandaa. Kilichomshangaza Deborah ni kumuona yule kaka aliyekaa nae meza moja akiwa anamuangalia sana kwa kuibia, kwa kijicho upembe. Deborah hakujali sana, akajua ndio wanaume walivyo, tamaa zao zipo nje nje, alipoletewa chakula akaanza kukishambulia kama anafukuzwa kutokana na njaa aliyokuwa nayo.

Ilimchukua takribani dakika 10 kumaliza kifungua kinywa kile, akiwa ameshiba kifu kifaya. Alipokuja mhudumu kutaka kutoa vyombo na kuchukua pesa, yule kaka akavunja ukimya kwa kuongea na mhudumu. "Bili yake changanya na yangu ukate pamoja" aliongea huku akifungua pochi yake na kuchomoa noti ya shilingi elfu 5 na kumkabidhi mhudumu yule. Deborah akabakia amepigwa na butwaa, akiwa anatafakari iweje analipiwa chakula kirahisi tu na mtu asiyefahamu, hakupenda kabisa kuwa jeta, kama walivyozoea madada wa Mjini wanaopenda vya bwerere. Kengele ya tahadhari ikagonga kichwani mwake, hasa akikumbukia maneno aliyowahi kuambiwa na mama mlezi wake Koplo Marieta, ya kuwa Mjini hakuna kitu cha bure.

"Dada yangu usishtuke sana, mie nakufananisha ndio maana kila wakati nilikuwa nakukodolea macho, na ndio maana nimekulipia bili yako kuwa na amani" aliongea yule kaka kwa sauti ya kujiamini huku akisitisha maongezi kidogo na kuchomoa kijiti cha kuchokonolea meno kwenye kikopo chake cha plastiki kisha akaendelea na maelezo yake. "Wewe ulikuwa unaishi kwa Mzee Kobelo pale jirani na barabara ya sasa hivi au nakufananisha, maana jina lako nimelisahau" aliongea huku amemkazia macho Deborah, muonekano wake ulionyesha ni mtu matawi ya juu sio mwenye kipato cha kijungu jiko. "Ndio mimi wala hujakosea, wewe ni nani kwani?" alijibu Deborah kwa sura ya bashasha huku sasa akijiandaa kumfahamu yule mtu mgeni machoni mwake ambaye ameonyesha kumfahamu vilivyo, alishakubali shingo upande kulipiwa bili yake. "Mimi ni Alex mtoto wa Mwalimu Mwenda" alijitambulisha kwa ufupi huku akimpa nafasi Deborah ya kukumbuka. "Ahaaaaah...Alex kaka yake rafiki yangu Devota jamani, za masiku kaka yangu nilisha kusahau" aliongea Deborah kwa furaha sheshe akiwa sasa na shauku ya kufahamu mambo mengi yaliyopita hapo Kijijini kwao Mikongeni. "Usijali ni ngumu sana wewe kunikumbuka, mlikuwa wadogo sana kama sio wewe kuwa rafiki wa mdogo wangu Devota nisingekukumbuka kirahisi, sura yako ni ile ile kitoto wazungu wanasema una 'baby face'" aliongea huku akichomekea utani uliowafanya waangushe kicheko cha nguvu.

"Kwanza pole na msiba wa mama yako, nilisikia umefiwa na sasa mmehamia wapi baada ya nyumba yenu kuvunjwa?" alitoa taarifa ambayo iliuchanachana kabisa moyo wa Deborah, ilimjaza kimuyemuye cha nafsi na kumvuruga kabisa matumbo yake. Akaanza kuhema kimjusi kama mbwa koko aliyefukuzwa mitaani. Deborah akashindwa kujizuia, akajikuta anaangusha mchozi wa nguvu, wa kimyakimya kutokana na taarifa hiyo iliyomletea takilifu. "Pole sana, kuwa na subira ndio dunia ilivyo sisi sote ni wapita njia" aliongea kwa huzuni yule kaka akionyesha kujutia kwa maneno yake yaliyoamsha hisia hasi kwa Deborah. Deborah alitaka kukikisa maneno akawa anashindwa kuongea kitu kumuuliza nani aliyekata kamba, ikabidi ajikaze kisabuni mbele za watu mule mkahawani asije akachafua hali ya hewa, akapata nguvu sasa ya kumhoji vizuri huyo mama yake alifariki lini.

.Ikabidi ajieleze kinagaubaga kuwa alitoroka karibia miaka 6 iliyopita ndio anakanyaga tena hivi sasa, hivyo hajui hata walipohamia familia yake. Alex nae hakuwa na majibu ya kina ya nani haswa aliyefariki kati ya Shangazi mtu na mama yake mzazi, maana wengi walikuwa hawajawahi kumuona mama yake mzazi, na walikuwa wanajua Shangazi yake ndio mama yake mzazi. Kukata mzizi wa fitina, ikabidi yule kijana Alex ajitolee wafunge msafara mpaka makaburini wakaangalie kaburi. Kwa maelezo ya Alex ni kuwa huo msiba ulitokea mwaka juzi wakati yupo mwaka wa mwisho Chuo Kikuu cha SUA-Morogoro. Uzuri wake makaburini kutokea pale Mkahawani hapakuwa na umbali mrefu sana, wakaamua watembee kwa miguu tu. Mizigo yake Deborah aliamua kuomba ihifadhiwe hapo hapo mkahawani ataifuata baadae. Njia nzima Deborah alikuwa amejawa na wasiwasi usiomithilika, akiwa na hofu huenda kweli mama yake mzazi ameshatangulia jongomeo. Kijana Alex akawa anajitahidi kumnyamazisha na kumtia moyo kuwa hata kama kweli mama yake atakuwa amefariki basi huo hautakuwa ndio mwisho wa dunia, lazima agangamale.

Makaburi ya kuzikiana ukoo wa Kunambi yalikuwa upande wa kushoto karibia na Mbuyu, ukiingia tu ndani ya uzio wa kuzunguka makaburini hapo. "Hili ndio kaburi linaloonekana ni jipya, ila nashangaa hata halijajengewa" aliongea Alex wakati wanafanya speksheni ya kulitafuta kaburi alilozikwa mama yake. "Naanza kuamini aliyefariki ni mama yangu tu, ndio maana hata kujengea hawajakumbuka, hata msalaba walioupanda jina limefutika tayari" aliongea Deborah akiwa amepiga magoti mbele ya kaburi amejiinamia akiwa na huzuni furufuru nafsini mwake, mvua ya machozi inabubujika mashavuni mwake. "Deborah usilie sana, jikaze huzuni yako ndio yangu, twende turudi nyumbani tujipange namna ya kuwatafuta ndugu zako, hapo ndipo tutaupata ukweli wote" aliongea Alex kwa sauti ya kubembeleza, anampigapiga kwa upole mgongoni huku anamfuta machozi Deborah kwa kutumia hanchifu yake. Deborah akawa anajihisi faraja na raha ya ajabu, inayoupoza moyo wake kama umewekwa kwenye jokofu kutokana na maneno ya kubembelezwa toka kwa Alex. Kwa miaka 21 ya Deborah tayari alishaanza kushikwa na hisia za kupenda kwa mara ya kwanza katika maisha yake. Kwa upande wake nae Alex joto la huba nalo lilikuwa limeshamkamata vilivyo kwa Deborah akisubiria muda muafaka amfungukie.

Baada ya kitambo kifupi, wakaanza kuondoka na Alex, huku Deborah akiwa kama kondoo anafuata tu hajui anapopelekwa na Alex. Kwa hali aliyokuwa nayo Deborah kipindi hicho, alikuwa anamuona Alex ndio kama mkono wake wa kulia. Alex akaanza kumpunguzia machungu kwa kumsimulia habari za rafiki yake wa kufa na kutokana, Devota ambaye walipoteza mawasiliano na Deborah. Taratibu Deborah akaanza kurudi kwenye hali yake ya kawaida.

"Jisikie upo nyumbani Deborah, karibu sana..! " Alex alimkaribisha Deborah ndani ya nyumba yake anayoishi katika eneo la Chuo Kikuu Cha Mzumbe. Ilikuwa ni nyumba ndogo ya kisasa, yenye vyumba vitatu, choo na bafu, ukumbi na jiko ndani yake. Sebule hiyo ilikuwa imepambwa kwa mapambo yenye widadi yenye kumvutia mtu yoyote mwenye kubahatika kuikodolea macho. Zilikuwa ni nyumba daraja nambari wani maalumu kwa kuishi Wahadhiri wa Chuo hicho. Alex alikuwa ni mhadhiri msaidizi anayefundisha masomo ya Uchumi. Aliajiriwa Chuo hicho mara baada ya kumaliza Chuo Kikuu cha SUA akisomea mchepuo wa Uchumi Kilimo.

"Ahsante sana kaka Alex, shemeji yupo wapi aniletee maji ya kunywa" alijibu Deborah akiwa na kimuyemuye huku akichomekea swali lenye utani wa kweli akitaka kufahamu kama Alex anaishi peke yake au tayari ameshaoa. "Shemeji yako ndio amekuja leo rasmi, sasa ndio ameingia kwenye nyumba hii kwa mara ya kwanza" Alex hakulaza damu, akatumia fursa hiyo hiyo kujieleza kwa mafumbo. Deborah akaelewa Alex anachomaanisha akabakia kujing'ata vidole tu, anatafuna kucha zake anaangalia pembeni kwa aibu. Kweli Deborah alikuwa msichana mwenye maadili ya kale bado akitongozwa anakula kucha, wakati wasichana wenzake wa Mjini siku hizi hawali kucha wanakula pesa zako.

Alex hakutaka kuonyesha tamaa ya fisi, alikuwa anamuingiza taratibu kwenye mtego wake. Kabla hajamtamkia wazi nia yake ya kumfanya awe mchumba wake alitaka kwanza Kumchunguza Deborah kama kweli anafaa kuwa mke, ili akijiridhisha ndio amtamkie rasmi ombi la uchumba. Alex akanyanyuka sofani alipokuwa amekaa akaenda kuwasha runinga yake, na kuweka mkanda wa video wa sinema ya Kihindi. Kisha akarudi kwenye sofa wakaanza kuangalia kwa pamoja huku wakiwa wamekaa kwenye sofa moja, lenye uwezo wa kuwakalisha watu 3 kwa pamoja. Baada ya dakika kama 5 tu, Alex akaaga kwa Deborah. "Sasa niliacha kidogo, mie ngoja nikafue nguo zangu ili ziwahi kukauka si unajua kesho kutwa ni kazini" akazungumza Alex huku akiwa anasimama akianza kupiga hatua kuelekea bafuni. "Aaaaah...zima tu runinga yako, tutaenda kufua wote, nikakusaidie..!" aliongea Deborah nae huku akinyanyuka kumfuata Alex sako kwa bako. Alex akaanza kuchekea tumboni akiona Deborah tayari ameshafaulu mtihani namba moja, akionekana ni mke kweli anayefaa 'wife material' haonyeshi mikogo. Wakaanza kufua wote huku wakikumbushiana hadithi mbalimbali za kitambo cha nyuma, enzi wapo Kijijini.

Mpaka kufika muda wa saa 8:00 mchana, wakawa wameshamaliza kufua nguo. "Sasa twende tukajiandae tukale kule Mkahawani muda umeshakwenda tayari" Alex aliongea huku akielekea chumbani kwake. "Hapana, hatuwezi kwenda kula mkahawani kama wageni, bora tupike hapa hapa wenyewe" Deborah alipinga kwa nguvu zote, bila kufahamu kuwa anapewa majaribu na Alex. Baada ya mabishano mafupi, rai ya Deborah ikapita. Ikabidi ajiandae kuingia jikoni kukarangiza mapishi kwenye jiko la gesi. Alex kwa utundu wake tu makusudi akakorofisha mrija wa mtungi wa gesi unaoingia kwenye jiko, ili tu azidi kumpima Deborah, kama kweli anaweza kuvumilia shida. "Kama gesi imegoma ngoja niingie mtaani kuulizia mkaa tupike kwa jiko la mkaa" kuongea hivyo Deborah tayari alishadaka mfuko wa Rambo akachukua pesa juu ya kabati na kuingia mtaani. Alex akabaki na furaha sheshe akiwa amejiridhisha kuwa Deborah anafaa kuwa mke, shule haijambadilisha tabia yake.

Ndani ya dakika chache alizochomoka Deborah, Alex akaitwaa simu ya Deborah aina ya 'Twanga Pepeta' na kuanza kupekenyua meseji, akitarajia huenda akakuta meseji ya mapenzi. Lakini akajikuta anatoka hola bila kuambulia meseji yoyote ya mahaba, zaidi ya meseji za Bosi wake Mrs.Tonny na za wateja wake wa dukani. Alex kwa taftishi yake ya haraka haraka akajiridhisha kuwa Deborah ndio msichana anayefaa kuwa mchumba wake. Baada ya kama robo saa Deborah akarudi na mkaa wake, akakimbilia jikoni kwenda kupika huku akimuacha Alex anaangalia zake sinema sebuleni. Mpaka kufika saa 10 alasiri chakula kilikuwa tayari kipo mjini kinasitiriwa matumboni mwao. Walipomaliza kula, Alex akampisha Deborah chumbani kwake apumzike, yeye akabakia kujipumzisha sebuleni, huku wakipanga saa 12 jioni waingie mtaani kusaka taarifa za wapi alipohamia Mjomba Kobelo.

Deborah mawazoni mwake wakati yupo kitandani, yalijaa Alex tupu. Alimuona ni mwanaume ambaye ana elimu kubwa, ana kazi nzuri lakini hana maringo na hapendi umangimeza kama walivyo wanaume wengi wenye kipato walivyo. Akajiapiza kuwa Alex akimtamkia tu kuwa anampenda hatomzungusha kamwe, atamkubalia mara moja. Ghafla bin vuu Deborah akapitiwa na usingizi wa pono akiwa juu ya kitanda cha Alex.

Mr.Martin Tenga, alipotolewa gerezani kule Jijini Turin, alikuja kutupwa kwenye gereza lililopo ndani ya Mji wa Barletta. Mji ambao ni mdogo wenye wakazi wasiozidi laki moja, uliopo Kusini Mashariki mwa nchi ya Italia. Ndani ya gereza jipya, hali ya hewa ilimkataa kabisa Mr.Martin Tenga, kila siku zinavyosonga mbele afya yake ilikuwa inadorora. Vipimo vya kina vilipofanyika ikagundulika ana kansa ya ini 'Liver Cancer', hivyo sasa akawa kama Lori la kubeba mkaa, linavyokuwa tripu Shamba, tripu Gereji, na yeye akawa leo yupo gerezani kesho yupo hospitalini. Hali yake ilivyozidi kuwa mbaya akahamishiwa katika hospitali ya 'Ospedale Barletta'. Hapo ndipo alipokutana kwa mara ya pili na mtoto wake wa damu, 'Pesambili' au ukipenda 'Dr Trezguet'.

Pesambili alipangiwa kufanya mafunzo ya Udaktari kwa vitendo katika Mji wa Barletta. Lakini kutokana na umahiri wake, Wahadhiri wake wakamnyooshea mkono. Akawa anaachiwa kufanya mpaka upasuaji wa wagonjwa. Siku isiyo na jina akiwa kwenye mizunguko ya usiku wodini kuangalia maendeleo ya wagonjwa wake ndipo wakatiana machoni kwa mara ya pili. Pesambili alikuwa anapita kitanda kwa kitanda, kuangalia hali za wagonjwa wake. Alipofika kwenye kitanda cha Mr.Martin Tenga, akasita kuendelea na ziara yake kwa muda. "Amicoooo.....Amicoo....!" aliita Pesambili kumuita Mr.Martin Tenga, kwa furaha baada ya kuona chata ya mchoro wa mamba kwenye shingo ya Mr.Martin Tenga aliyojichora, alama ambayo Pesambili alikuwa anaiona mara kwa mara wakati anamsaidia kule sokoni, Turin. "Amicoooo...! " alijitahidi kujibu kwa tabu sana huku akipepesa macho kumuangalia huyo Daktari anayemuita rafiki kama anamfahamu vile. Pesambili akatabasamu na kuanza kumuongelesha huku akimkumbushia kuwa walionana gerezani kule Jijini Turin akiwa chumba kimoja na baba mlezi wake Mr.Lorenzo, pia akampasha kuwa walikuwa wanaonana sokoni, mara kwa mara Jijini Turin, akiwa kama ombaomba wa vyakula, na alikuwa yeye Pesambili anampa sana msaada. Mr.Martin Tenga akabakia anatabasamu kwa furaha baada ya kukumbuka wema wa Pesambili enzi anajifanyisha ni masikini mitaani kabla hajafungwa gerezani, akiwa haamini kama kweli yule mtoto wa shule ya msingi, mwana wa panopano, rafiki yake kipenzi leo ndio Daktari mbele yake.

Pesambili akasoma faili la mgonjwa yule ambaye ni baba yake wa damu ila tu hawajuani. Aliposoma faili lile inaonyesha ana kansa ya ini iliyotokana na unywaji wa pombe kali, hivyo anahitajika kufanyiwa upandikizaji wa ini "Liver Transplant". Haraka haraka akaagiza vipimo vya damu, mkojo na DNA vfanyike usiku huo huo. Pesambili akajiweka kwenye orodha ya watu watakaomtolea damu Mr.Martin Tenga, hivyo na yeye damu ikafanyiwa vipimo. Majibu ya vipimo vya damu na DNA ya Mr.Martin Tenga na Pesambili yalimshangaza sana, mtumishi wa maabara kwa jinsi yalivyorandana. Majibu ambayo yalithibitisha kuna nasaba ya damu baina ya Mr.Martin Tenga na Daktari Pesambili au ukipenda Dr.Trezguet. Ikabidi usiku huo huo aitwe Dr.Pesambili kule maabara afahamishwe kitu kilichogundulika kwa bahati nasibu. Pesambili akapatwa na gagaziko la moyo, akaamrisha waanze kurudia tena upya vipimo, majibu yakawa ni kama yale yale ya mwanzoni. Dr. Pesambili akawa sasa ana furaha sheshe iliyochanganyika na huzuni akiwa haamini anachokishuhudia pale hospitalini. Alikuwa anaona kinachotendeka mbele yake ni zaidi ya muujiza wa Mtume Musa kuipasua bahari ya Shamu kwa fimbo yake na kuwapitisha wana wa Israeli baharini. Vipimo vilishuhudia kabisa bila chenga kuwa Dr.Pesambili, baba yake ni huyu mgonjwa mahututi Mr.Martin Tenga.

Akaona ulikuwa ni mpango wa Mungu yeye kuamua kuchagua kufanya kazi kwenye Mji wa watu masikini wa Barletta, kumbe na baba yake yupo huku anateseka gerezani kwa ugonjwa. Mawazo mengi yalimsonga kichwani mpaka akifikiria kuwa siri ile ya kuwa Mr.Martin Tenga ni baba yake mzazi huenda baba yake mlezi Mr.Lorenzo alikuwa anaifahamu fika ila hakutaka kumwambia. Akazidi kujiuliza kuwa alikuwa anamficha kwa faida ya nani?. Na kama hawajuani kwanini walikuwa wanaishi chumba kimoja?. Je Mr.Lorenzo hakupata kusimuliwa chochote na Mr.Martin Tenga kuhusu mtoto wake aliyemtelekeza kwenye kituo cha yatima.
Kulipokucha tu, mgeni wa kwanza kumtembelea Mr.Martin Tenga alikuwa ni Pesambili. Kwa jinsi alivyomshuhudia baba yake akiwa kwenye mateso makali, alishindwa kujizuia kumwaga machozi, bila Mr.Martin kung'amua kuwa mtoto wake anamlilia. Dr.Pesambili akapata matumaini kuwa huenda mama yake mzazi nae yupo hai, ila swali jipya kichwani likaja kwanini walimtelekeza kwenye kituo cha yatima wakati yeye sio yatima?. Au walimnyanyapaa kwa sababu ya ulemavu wake wakaona atakuwa mzigo kwao?. Kadri alivyokuwa anawaza ndivyo alivyokuwa anashindwa kujizuia machozi yake yasimbubujike. Ikabidi Dr.Pesambili arudi ofisini kwake kwanza ili apate utulivu wa kujipanga namna atakavyokuja kuongea na baba yake, huku akijitambulisha rasmi kwake.

Akiwa katika hali ya huzuni na simanzi, ghafla Dr.Pesambili akaisikia kengele ya hali ya tahadhari imelia kwa zaidi ya mara tatu kuashiria kuna mgonjwa wa dharura anayehitaji huduma ya haraka kuokoa uhai wake. Ikabidi Dokta Pesambili akurupuke mbio mbio utasema swala anayemkimbia Simba nyikani, kwenda kuungana na Madaktari wenzake kwenda kutoa huduma na msaada kwa wahitaji bila kujali hali aliyo nayo. Tahamaki alichokiona baada ya kufika chumba cha dharura, kilimsababishia mapigo yake ya moyo yazidi kwenda mbio maradufu. Baba yake mzazi, Mr.Martin Tenga alikuwa yupo kwenye sakaratu mauti kitandani anapigania roho yake. Saa na wakati wowote alikuwa anaaga dunia, hakukuwa na njia yoyote ya kuokoa uhai wake. Dr.Pesambili hakuwa mtu wa kukata tamaa kirahisi akaanza kupambana, alikuwa anahangaika huku na kule kuhakikisha anajaribu kuokoa uhai wa baba yake. Lakini kama unavyo, jitihada haiwezi kushindana na kudra ya Mola, Mr.Martin Tenga akaaga dunia, akihitimisha safari yake ya uhai wa duniani. Dr.Pesambili alitoa kilio mithili ya mtoto mdogo aliyetelekezwa jangwani bila msaada wowote, ukichukulia amemjua baba yake halisi saa chache tu zilizopita halafu kabla hajajitambulisha kwa baba yake, wasameheane kiroho safi na kuelezwa asili yake baba yake ni wapi, ghafla tu bin vuu anakata kamba na kurejea jongomeo bila hata kusema kwaheri ya kuonana.

Alikuwa na uchungu mkubwa sana Madaktari na Manesi ambao tayari tetesi zilishawafikia juu ya uhusiano wa Dr.Pesambili na marehemu Mr.Martin Tenga iliwabidi wafanye kazi ya ziada kumpoza machungu ya kumpoteza baba yake mzazi. Watu wa gereza alilokuwa amefungwa Mr.Martin Tenga wakapewa taarifa juu ya msiba wa mfungwa wao, nao bila ajizi wakaja kuuchukua mwili ili wakausitiri kwa taratibu zao za kisheria. Dr.Pesambili ikabidi ajieleze kwa uongozi wa gereza kinagaubaga uhusiano wake na marehemu mpaka akaruhusiwa kushiriki mazishi ya baba yake. Baada ya mazishi kupita Dr.Pesambili akajaribu kufuatilia gerezani labda kuna mawasiliano ya ndugu wa karibu wa Mr.Martin Tenga yalihifadhiwa na marehemu ili aweze kuwasiliana nao, akaambulia patupu. Kwa kuwa muda wake wa mafunzo kwa vitendo ulikuwa umebaki miezi michache, akaona bora avumilie mpaka amalize ili awe huru kabisa kuanza uzinduzi rasmi wa kusaka ndugu zake wa damu. Msako usio na kikomo mpaka ahakikishe anawatia machoni ndugu zake wa damu. Na tumaini la pekee lililobakia ni baba yake mlezi Mr.Lorenzo. Kupitia Mr Lorenzo aliamini ataupata ukweli wa wapi alimtoa huko Afrika mpaka kumleta nchini Italia.



"Nikutakie kazi njema mpenzi wangu, mimi ngoja niwahi Kibaruani, leo nina kipindi saa 3:00 asubuhi, nakutegemea Jumamosi jioni utakuja tena nyumbani Mzumbe" aliongea Alex huku akimkumbatia kwa nguvu Deborah wakiwa tayari wameshashuka nje ya gari la Alex. "Nashukuru sana mpenzi, nikutakie kazi njema, ila nisamehe sana kwa yaliyotokea juzi usiku sio kusudi langu kabisa" aliongea Deborah huku machozi yakianza kumlengalenga akionekana kujutia tukio hilo alilolifanya nyumbani kwa Alex. "Usijali na ondoa mashaka tupo pamoja katika shida na raha, mwishoni mwa juma tutaanza kutafuta ufumbuzi wa tatizo lako, nimekusamehe kiroho safi" alijibu Alex huku akirudia kumkumbatia tena kwa mara ya pili na kuanza kumpeperushia mabusu motomoto mashavuni mwake Deborah. "Wewe malaya baridi unataka kazi kweli au umeshanogewa na mapenzi unataka ukawe kahaba tena? " ilikuwa ni sauti kali iliyojaa hasira furifuri toka kwa Bosi wa Deborah, Mrs.Tonny aliyekuwa amesimama meta chache kutoka waliposimama Deborah na Alex akiwachora mubashara namna wanavyo onyeshana mahaba hadharani. Sauti ile kutoka kwa mtu wa karibu na Deborah, anayoifahamu fika hata kama akiamshwa usiku wa manane, ilizua wahaka na mshituko mkubwa katika moyo wa Deborah, himahima akajipapatua kwa nguvu kutoka kwenye ya Alex na moja kwa moja akageuk kisha akapiga magoti na kuvikutanisha vidole vya viganja vyake vya mkono pamoja na kuviweka chini ya kidevu chake. "Samahani sana Madame...nipo chini ya miguu yako sirudii tena kuzembea kazini, nisamehe....! " aliongea Deborah kwa sauti iliyojaa uoga na majuto huku akitambaa kwa magoti kumfuata Bosi wake Mrs.Tonny pale alipokuwa amesimama. "Wewe kijana potea haraka kwenye upeo wa macho yangu kabla sijakutwanga risasi, mpumbavu wewe na kigari chako cha mkopo unataka kuniharibia binti yangu...!" aliendelea kufoka Mrs.Tonny huku kibao sasa kikimgeukia kijana Alex, akiwashiwa moto wa shari. Kwa mkwara tu, Mrs.Tonny akachomoa bastola yake kwenye pochi yake, na kutishia kama anataka kupiga risasi kwenye tairi ya upande wa kushoto wa gari akachimba chini jirani na tairi. Alex haraka haraka akaingia kwenye gari yake akaiwasha na kutokomea zake kwa kasi kubwa kusipojulikana akiwa na kiwewe akiepuka shari kamili inayomnyemelea. "Wewe mjinga unanidanganya unaenda kuangalia familia yako, kumbe unaenda kukutana na mahawara zako, hapa Mjini kuwa makini, ukimuona kijana anamiliki gari tu tayari umeshampapatikia, unataambukizwa UKIMWI shauri yako mpumbavu wewe, haya fungua duka mie naondoka zangu...! " alifoka Mrs.Tonny huku akimrushia funguo za duka hilo la vito Deborah na kuanza kupiga hatua kadhaa kuelekea kwenye gari lake kisha akasita kwenda na kugeuka nyuma. "Ebu lete hiyo simu yangu, maana hiyo simu ndio inakufanyia ukuadi na kuhangaika na viruka mito wako" aliongea huku tayari akiwa ameshafika alipo Deborah. Bila ubishi wowote akasalimisha simu kwa Mrs Tonny huku akiwa amejawa na aibu na soni hana hata ujasiri wa kumuangalia usoni mfadhili wake. Kiunyonge akajivuta na kumkabidhi funguo mlinzi amsaidie kufungua geti la dukani. Machozi yalikuwa yanambubujika usoni Deborah akiona kabisa Mrs.Tonny anamuonea na kumletea mtima nyongo kwenye penzi lake jipya ambalo ndio kwanza ameanza kupanda mbegu za upendo hata kuchipua bado. "Sasa nina miaka 21, sio mwanafunzi na nina haki ya kuwa na rafiki ninayemtaka mimi sasa iweje aniporomoshee matusi ya nguoni mimi na mpenzi wangu Alex, au ana ajenda gani ya siri dhidi yangu? Sasa Alex si anaweza kughairisha kunichumbia, na ukichanganya na kituko cha aibu nilichomfanyia Alex Jumamosi usiku ndio kabisa atatafuta mchumba mwingine" hayo yalikuwa ni baadhi tu mawazo ambayo yanapita kichwani mwa Deborah kipindi chote alichokuwa anasubiri milango ya duka ifunguliwe. Kwa ufupi siku nzima ya Deborah ilikuwa imeharibika, kwa kujawa na soni na simanzi kubwa moyoni mwake. Aliona kabisa mfadhili kaamua kumpanda kichwani kwa makusudi na kutia mchanga kwenye kitumbua cha penzi lake. Mpaka akawa anajiuliza huenda Bosi wake kaamka vibaya leo kuna kitu kinamvuruga, kwa maana tokea wameanza kufanya kazi pamoja hajawahi hata kumkemea lakini leo bila kosa lolote mpaka anafikia hatua ya kuchomoa bastola hadharani na kurusha risasi. Siku hiyo hata chakula hakuwa na hamu nacho kabisa, hisia za njaa tumboni mwako ziliyeyuka kabisa, akageuka kama mfungaji wa swaumu. Akaanza kufikiria hali ya mpenzi wake Alex huko alipo. Akaanza kumuonea huruma kwa kuingizwa kwenye matatizo yasiyo mhusu. Akakumbuka jinsi siku za Jumamosi na Jumapili Alex alivyojitoa mhanga kwake kumsaidia kuwasaka ndugu zake kwa udi na uvumba bila kuchoka. Juhudi ambazo zilikuwa tasa hazikuzaa matunda kwa maana hawakufanikiwa kufahamu wapi alipoelekea Mjomba Kobelo na familia yake. Saa za kufunga duka siku hiyo alikuwa anaziona zinaenda taratibu sana kwa mwendo wa kinyonga. Kwa amri yake alitamani afunge sasa hivi akajipumzishe zake hasa ukichukulia yupo kwenye kizungumkuti cha kutofahamu kama mama yake mzazi yu hai au amefariki, pia hajui alipo Mjomba wake na familia yake halafu Bosi wake Mrs.Tonny anamletea maswaibu mengine mapya ya kutaka kumpeperushia ndege mnana wake, Alex. Ilipofika saa 1:30 usiku gari linalotumika kuwarudisha nyumbani likawasili dukani kwa Deborah kuja kumchukua. Alikuwa tayari ameshafunga mahesabu ya siku hiyo, hivyo harakati za kufunga mlango wa duka zikaanza. Baada ya dakika 10 akawa ameshafunga duka na kumkabidhi funguo za duka dereva wa Bosi wake tayari kwa kurejea nyumbani. Kwenye gari walikuwa watu 4 kama kawaida, dereva na waliobaki ni wasichana wauzaji wa maduka ya Bosi wao Mrs.Tonny. Siku hiyo kadri walivyokuwa wanataniana Deborah alikuwa mtulivu tuli kama maji mtungini, kichwani ameshavurugwa. Walipofika nyumbani Deborah akapitiiza moja kwa moja mesini kula mlo wa chajio, usiku mbichi ulikuwa tayari umetimu. Mtumishi wa nyumba alikuwa tayari ameshapika chakula na kurejea kwao. Alipokula tu moja kwa moja akaenda kuoga na kujifungia zake chumbani kwake. Usingizi siku hiyo ulimpaa kabisa hautaki kuja, mawazo yote yapo kwa Alex. Alifahamu fika huenda hivi sasa Alex anamtafuta kupitia simu yake ya mkononi, lakini anaona kimya tu bila kufahamu kuwa simu amepokonywa na Bosi wake.

SURA YA KUMI NA TANO
"Habari za kazi, nimekuja kumuulizia ndugu yetu anaitwa Deborah Kunambi..! " aliongea kwa kujiamini dereva wa mfanyabiashara Timammy aliyetumwa kumuulizia Deborah huku Timammy mwenyewe akiwa amebakia kwenye gari. "Hee...kumbe yule Deborah ana ndugu wenye uwezo eeh, sie tukimjua ni fukara mwenzetu tu, maana ana muda mrefu hajawahi kurudi kwao likizo....! " alijibu yule mlinzi wa getini huku macho yake akiyaelekeza kwenye kukagua daftari lake kuangalia wanafunzi ambao wameshaondoka tayari shuleni, kwa wale waliomaliza shule na wanaosafiri likizo. "Yule kiburi chake tu, ndugu anao sema mjeuri tu..! " akaongopa yule dereva kuanua ngoma juani. " Ndio kawaida ya watoto wenye akili nyingi wanakuwa na misimamo sana. Hapa inaonyesha ameshachukuliwa saa mbili zilizopita, angalia hii anuani" aliongea yule mlinzi huku akimkabidhi yule dereva kikaratasi alichokiandika jina na anuani ya mtu aliyemchukua Deborah shuleni. "Oooh....sawa huku Morogoro ni kwa ndugu zake upande wa baba akina Kunambi, lakini hatukuwasiliana nao...!" aliongopa yule dereva huku akichukua kile kikaratasi na kuagana haraka haraka na yule mlinzi. "Kaka hata ya chai huachi kidogo, maana mie nimekusaidia tu ulitakiwa uende kule kwa Mwalimu wa zamu, si unaona mnyororo wa wazazi waliowafuata watoto kule.....! " alijichekesha yule mlinzi akiomba pesa kwa dereva wa Predeshee Timammy huku akimuonyesha kwa kidole mstari wa wazazi katika ofisi ya Mwalimu wa zamu. Yule dereva bila hiana wala kutia neno akachomoa mfukoni noti ya shilingi 500/= akamkabidhi mkononi. Yule mlinzi alishukuru kweli kutokana na ukata uliokuwa unamkabili, utasema amepewa kipande cha almasi kumbe mia 5 tu. "Ngoma ishakuwa ngumu Bosi, kinda Deborah kashachurupuka...!" aliongea dereva kiunyonge huku ameegemeza kichwa chake kwenye kiti chake cha dereva, wakati anamkabidhi kikaratasi chenye anuani ya mtu aliyeondoka na Deborah pale shuleni. "Uuuuuuhhh......Shabaashi..! usimwambie, kashanizidi ujanja..! Huyu Binti piga ua ni wangu, mie siwezi oa mwanamke mwingine zaidi yake, natambua kuwa nimempita zaidi ya miaka 10 taslimu lakini yule ana mvuto fulani utakaonituliza mimi, kwa njia yoyote Deborah atakuwa mke wangu tu, siwezi kukubali mtu yoyote anizidi kete kwa Deborah" alijikuta anaropoka kwa hasira Predeshee Timammy akijiapiza kumpata Deborah. Dereva wake akabakia amepigwa na butwaa mdomo wazi, akijiuliza haswa huyu Bosi wake kapatwa na mswaibu gani haswa mpaka haoni wala hasikii kwa binti wa shule. Deborah kwa upande wake alishamsahau Timammy tokea amfurushe siku aliyomtongoza kule shuleni alipomtembelea. Alijua Timammy ameshakoma kumfuatilia na ilishapita takribani miaka 3 bila kusikia chochote toka kwake na ada alishakata mguu kumlipia akajua ameshakasirikiana nae kimoja. Kumbe mwenzake bado alikuwa yupo kichwani mwake anampigia mahesabu makali. Hesabu ya kwanza alipiga kuwa Deborah atakuwa ameishi maisha magumu sana shuleni, na matokeo ya kidato cha 4 yalivyotoka alivyoona kachaguliwa pale pale akajua sababu kubwa ni ya kiuchumi. Hivyo akajua atakapomaliza kidato cha 6 atakuwa hana pa kufikia hivyo atamnyakua kiulaini kama mwewe kwa kifaranga cha kuku. Lakini kumbe karata namba moja imeshafeli sasa alitakiwa achange upya karata zake, ndani ya Mji wa Morogoro, ajue wapi alipo Deborah amchomoe. "Sasa Bosi tunafanyaje, maana humo hata namba ya simu haipo, labda tuulizie hilo sanduku la posta lililoandikwa hapo mmiliki wake ni nani" aliongeleshwa Timammy na dereva wake baada ya kuonekana ametulia kimya muda mrefu anavusha mawazo. "Yap.. Yap..hapo umeongea jambo la msingi ndio maana nimekufanya uwe dereva wangu kwa sababu wewe ni mwerevu mno, sasa hiyo kazi nitamkabidhi wakala wangu mmoja anafanya kazi Shirika la Posta, makao makuu, akishaleta jibu sasa huyo aliyemchukua mpenzi wangu Deborah nitapambana nae kwa jasho na damu" alikuwa anaongea Timammy kwa msisitizo huku anapigapiga ngumi pembeni ya mlango wa siti ya abiria. Yule dereva bichwa lilivimba kwa misifa aliyomwagiwa, maana hiyo kazi ya ukuwadi kwa Mabosi wao ndio ilikuwa moja ya njia ya kuongeza kipato cha ziada kwa baadhi ya madereva wasiojitambua kama yeye. Baada ya muda mfupi, safari ya Timammy kurejea Jijini Dar es Salaam ikaanza, lakini akiwa ni mnyonge kupitiliza hasa kutokana na kuzidiwa kete. Walikuwa wamechoma mafuta kwenye gari toka Jijini Dar es Salaam mpaka Dodoma umbali wa zaidi kilometa 450 bila mafaniko yoyote. Ndio akakumbuka ule msemo wa vijana wa mitaani kuwa wakati unasubiri embe liive ndio uchume, wenzako wanalila hivyo hivyo likiwa bichi kwa kutumia chumvi. Ndio yaliyomtokea kwa Deborah, kamsubiria apevuke, wajanja wameshamdaka juu kwa juu. Usilolijua ni kama usiku wa giza, Alex alikuwa anaenda kutumbukia kwenye janga zito la kupambana na watu wenye pesa zao, kisa ni penzi la Deborah. Kibaya zaidi Timammy amekulia kwenye mfumo wa maisha ya kijiweni yaliyojaa kina aina ya uharamia, ghiriba na ukhabithi, yeye kwake suala la kumwaga damu ya mtu anapolitaka jambo lake ni dakika sifuri tu.

"Mtumiaji wa simu unayempigia hapatikani kwa sasa, jaribu tena baadae, ahsante" ilikuwa ni sauti ya mwanadada inayotoka kwenye mtandao wa simu ikimuelezea Alex kuwa simu ya Deborah imezimwa haipo hewani. Alex alizidi kuchanganyikiwa majira hayo ya akakiri akiwa ametulizana tuli sebuleni kwake kwa utulivu murua utasema anaaga maiti. Muonekano wa nje alikuwa anaonekana ametulia lakini ndani ya serikali ya kichwa chake kulikuwa na mkururu wa mawazo kinzani yanapita kama mkondo wa maji yanayotumika toka sehemu moja kwenda ingine. Chambilecho mwenye kupenda ni jura wala hana maarifa na mwenye kupenda hana usono asijapopata akitamanicho, hiyo ndio hali aliyokuwa amekumbwa nayo kijana Alex. Kilichokuwa kinampa mawazo zaidi si kingine bali ni mustakabali wake na Dendesha katika safari ya penzi lao jipya ambalo limeanza na mkosi. Hasa akikumbukia tukio la tishio la kutaka kupigwa risasi na mama mfadhili wa Deborah asubuhi asubuhi na mapema. Katika maisha yake Alex hajawahi hata kutishiwa maisha na kitu chochote hata mithili ya kuchanjwa na wembe achilia mbali risasi. Kisanga cha kuchomolewa mguu wa kuku hadharani na Mrs.Tonny kilimsababishia cheche za mkojo zilowanishe nguo yake ya ndani, na kumfanya akimbize gari lake kuelekea kusikojulikana kutokana na kiwewe. Fahamu zilikuja kumkaa sawa ma kujishtukia yupo Dakawa anaelekea Jijini Dodoma, wakati alitakiwa ashike uelekeo wa barabara ya Iringa ili aweze kufika kijijini Mzumbe anapoishi na kufanya kazi. Mpaka kufanya maamuzi ya kushika njia sahihi itakayompeleka nyumbani kwake tayari majira ya mafungulia ng'ombe yalishatimu na kipindi chake darasani kilishamkosa bila kutoa taarifa yoyote ofisini na kwa wanafunzi wake hali ambayo ilizusha taharuki kutaka kufahamu amepatwa na maswahibu gani. Alipopigiwa simu ikabidi adanganye kuwa hajisikii vizuri vizuri kuacha, ni mahamumu hivyo alijihimu Morogoro Mjini kupata vipimo kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Moja kwa moja akapitiliza maskamoni kwake na kuanza kutuma meseji kwenye simu ya Deborah kutaka kufahamu mkasa wao umeishiaje. Lakini kitu cha kustaajabisha kwa upande wake meseji zote zaidi ya 8 alizotuma zilifikia, kuonyesha bado hazijapokelewa upande wa pili. Ndipo apofanya maamuzi ya kuanza kumpigia simu kujua kulikoni, jibu alilokuwa analipata kutoka kwenye simu yake ni sauti nyororo ya msichana inayosema "Mtumiaji wa simu unayempigia hapatikani kwa sasa, jaribu tena baadae, ahsante". Jibu ambalo lilikuwa linazidi kuvuruga na kuzalisha cheche za wahaka katika moyo wake. Kijasho chembamba cha uoga wa kuwa huenda penzi lao tamu la siku mbili tu ndio limefikia tamati. Penzi ambalo ndio kwanza limepandwa mbegu yake hata kuchipua bado, tayari limeshapigwa zongo na Mrs.Tonny, mfadhili wa muhibu wake Deborah. "Huenda Deborah kasikiliza ushauri wa mfadhili wake kuwa mimi ni bangai tu, mbabaishaji, tapeli wa Mjini wa mapenzi, hivyo kaungana nae, hivyo Deborah ameamua kuifukua mbegu ya penzi letu ili lisiote kabisa" alikuwa anawaza kijana Alex akiwa ameshika tama juu ya sofa lake pale sebuleni. Hali ya hewa ilikuwa ni baridi msimu huo wa kipupwe lakini jasho jekejeke lililokuwa linalomtiririka Alex utasema ni mtumishi wa tanuri la kuchoma mikate yupo jikoni anafanya mambo yake. "Huenda mfadhili wake kaamua kumpokonya simu yake na kuizima ili asiweze kamwe kuwasiliana na mimi kwa njia ya simu ya mkononi" alizidi kuwaza Alex dhana tofautitofauti dhana ambazo badala ya kumletea faraja ya moyoni zilizidi kumletea masumbuko yasiyo na mwisho. "Pia huenda ameamua kumpokonya simu na kumtimua kazi" aliwaza tena lakini dhana hii serikali ya kichwa cha Alex ikaipinga kwa nguvu zote, kwa hoja ya kwamba, kama Deborah angekuwa ametimuliwa kwa Mrs.Tonny basi kimbilio lake la pekee kwa Mjini Morogoro angekuwa ni yeye Alex kutokana na kutokufahamu wapi walipo ndugu zake mpaka sasa. "Ila anaweza kufukuzwa na mfadhili wake na kwangu asitie mguu kabisa, kutokana na kituko cha kujikojolea usiku wa kuamkia Jumapili niilipompisha alale kitandani kwangu na mimi kwenda kulala chumba cha wageni. Huenda tukio hilo limemsononesha sana na kuona ya kuwa limemvunjia hadhi na heshima yake, hivyo ameona bora ajihukumu mwenyewe kwa kuvunja penzi letu" aliendelea na mawazo yake kinzani. "Ila atakuwa wa ajabu basi kama ukikojozi wake ndio umemfanya avunje penzi letu, maana mimi nimemsamehe siku ile ile baada ya kunisimulia ni tatizo linalojirudia rudia kwake kutokana na kushuhudia sura ya mmoja wa Majambazi wauaji wa marehemu baba yake". Mawazo hayo yalikatishwa na kishindo kilichosikia kupitia mlango wa uani, kishindo mfano wa mtu aliyegonga mlango na kumfanya Alex akurupuke mbiombio toka sebuleni kwenda kujua kulikoni. "Huenda Deborah amefukuzwa, ameamua kuhamia rasmi nyumbani kwangu na mabegi yake, kaamua apite mlango wa uani kwa kuona aibu kwa watu kupitia mlango wa barazani" hizo ndio fikra za Alex wakati anachomeka funguo kufungua mlango wa uani. Alipofungua akabaki amepigwa na butwaa hana la kufanya, kumbe kIlikuwa ni kishindo cha paka wawili wa nyumba za jirani wanaogombania mabaki ya chakula cha usiku kwenye pipa la taka nje ya nyumba yake. Kinyonge akawa hana namna zaidi ya kuufunga tena mlango wake na kurejea sebuleni akiwa amekosa raha na buraha. Kabla hajakaa chini ndipo akakumbuka tumboni hajatia chochote tokea alivyoamka asubuhi na kuwahi kumkimbiza kazini kwake Deborah. Kabla hajakaa akageuka na kupitiliza uelekeo wa jikoni kwenda kuangalia chochote kitu kwenye jokofu lake la kuhifadhia vyakula anuwai mbalimbali. Alipofungua akakutana na maziwa freshi mabichi na robo tatu ya slesi za mkate ukiwa umefungwa vizuri. Akawasha jiko la gesi na kubandika sufuria la kuchemshia maziwa. Baada ya dakika takribani 3 maziwa yakawa tayari yamechemka. Akayamimina kwenye chupa ya kuhifadhia joto la vimiminika, akaweka mezani. Akachukua silesi 6 za mkate na kuanza kuzipaka siagi tayari kwa kula. Baada ya dakika kama 10 akawa tayari ameshashiba, alipotupia macho kwenye saa yake ya mkononi aliyoivaa akaona majira ya adhuhuri yameshatimu. Akakata shauri kuwa hicho kifungua kinywa alichokula ndio pia mlo wake wa mchana, hana haja tena ya kupika itakuwa ni ulafi kama akipika tena. Aliposhiba kidogo akili ikamtulia akaamua aende kujipumzish sha chumbani kwake na kukata shauri ya kuwa kama mpaka majira ya Alasiri atakuwa Deborah hapatikani kwenye simu ataenda kumsaka huko Mjini kwenye nyumba anayoishi aweze kupata jibu moja tu, kuwa bado mapenzi yao yapo au ndio yameshakufa ili ajue cha kufanya. Na kama akijua kuwa amezima simu makusudi kwa taadi yake tu basi ndipo atakubaliana na msemo wa wahenga wa unaosema usimjaribu mlevi na kutegemea shukrani abadani. Alikuwa hapajui wapi anapoishi Deborah kwa ufasaha ingawa alishamuelekeza lakini penye nia pana njia, liwalo na liwe hawezi kushindwa kufika.



Dr.Pesambili alitua barani Afrika nchini Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa mtu mzima tokea achukuliwe akiwa ni mtoto mdogo kutoka kule nchini Kenya. Aliwasili Tanzania katika nchi ya asili ya wazazi wake, bila yeye mwenyewe kufahamu. Alikuwa amepata kibarua katika taasisi ya Afya yenye makao makuu nchini Marekani inayoitwa "The Centers for Disease Control and Prevention (CDC)", iliyo na matawi yake katika nchi mbalimbali duniani. Taasisi hiyo ilikuwa na miradi ya Afya nchini Tanzania, Mkoani Morogoro hivyo Dr.Trezguet au ukipenda Dr.Pesambili alikuwa ni mmoja wa Wafanyakazi kwenye taasisi hiyo. Alivyopangiwa kituo hicho kipya cha kazi, Dr.Pesambili alijawa na furaha sheshe. Furaha hiyo ilitokana na tamaa yake ya kwenda kuzuru nchi Kenya, sehemu ambayo alipewa taarifa na baba yake mlezi, Mr.Lorenzo kuwa ndipo alipochukuliwa kutoka kwenye kituo cha watoto yatima.

Dr.Pesambili baada ya kumaliza mafunzo yake ya vitendo alimzuru baba yake mlezi gerezani na kumdadisi vya kutosha kutaka kujua wapi ilipo asili yake. Ndipo Mr.Lorenzo bila kupepesa macho akamchana waziwazi kuwa alichukuliwa na msafara wa Papa John Paulo (II) kutoka kwenye kituo cha watoto yatima, Jijini Nairobi. Tokea hapo Dr.Pesambili akaanza kusaka nafasi za kazi kwenye Taasisi za Kimataifa kwa kutumia mtandao akilenga hasa maeneo ya nchi za Afrika Mashariki. Chambilecho mgaagaa na upwa hali wali mkavu, juhudi zake zikajibu akapata kazi nchini Tanzania. Furaha yake ya kupata kazi Tanzania ilitokana na kuwa kupitia somo la Jiografia alijua fika Tanzania na Kenya ni nchi majirani, wanaounda Jumuiya moja ya Afrika Mashariki, hivyo itamuwia wepesi kwake kukanyaga ardhi ya Kenya akitokea Tanzania, ili kuisaka asili yake. Taasisi ya "The Centers for Disease Control and Prevention (CDC)" mkoani Morogoro walikuwa wanajishughulisha na kutoa huduma za Afya majumbani, kwa kutumia magari maalumu, hospitali inayotembea kwa kuwapatia vipimo vya magonjwa bure na kuwapa matibabu. Nguvu kubwa ya hospitali inayotembea 'mobile hospital' ilielekezwa vijijini, sehemu ambazo kulikuwa na shida ya uwepo wa hospitali za kisasa.

Shirika la Afya Duniani 'WHO' kwa kawaida linapendekeza, daktari 1 atibu wagonjwa 300, lakini kwa Tanzania hali ilikuwa ni mbaya, daktari 1 huwa anatibu wagonjwa zaidi ya 20,000, hivyo Taasisi ya "The Centers for Disease Control and Prevention (CDC)" ikaonelea bora iwekeze nguvu vijijini kwenye upande wa kuboresha Afya. Kijiji alichokuwa anafanyia kazi Dr.Pesambili ndio kijiji ambacho alikuwa anaishi Mjomba Kobelo.


Mjomba Kobelo, alishahama zake kutoka kijiji cha Mikongeni na kuhamia kijiji cha Nyandira Mgeta wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Mkewe yule mkorofi sana aliyekuwa haishi kumshushia vipigo shadidi na mateso Deborah alifariki kifo cha ghafla siku chache tu baada ya Mjomba Kobelo kupokea malipo yake ya fidia ya kuhamishwa eneo walilokuwa wanaishi. Alikufa kutokana na mshtuko wa moyo baada ya Mjomba Kobelo siku moja kurudi nyumbani amelewa akija na stori za kuibwa pesa zote za fidia. Baada ya maziko tu, haukupita siku nyingi Mjomba Kobelo akahama kijiji na binti zake pamoja na dada yake mgonjwa, mama Deborah kuhamia kijiji kipya. Ndipo Dr.Pesambili katika mapito yake ya shughuli za kikazi akajikuta anafika katika nyumba ya Mjomba Kobelo. Akafanikiwa kumuona mama Deborah akiwa kwenye hali mbaya ya kupooza mwili. Dr.Pesambili kwa jinsi alivyokuwa na uchungu wa kukosa mama, alihuzunika sana kumuona mama Deborah wamemtelekeza, hapati huduma stahiki. Hima hima akamuanzishia matibabu, na kumuanzisha pia mazoezi ya viungo. Baada ya miezi kama mitatu (3), mama Deborah taratibu akaanza kuimarika afya yake. Kutokana na huduma mbovu nyumbani kwa Mjomba Kobelo, ikabidi Dr.Pesambili ajitolee kukaa nae mgonjwa wake nyumba moja na yeye.

Kwa Mjomba Kobelo kiroho safi akakubali, kwake ikawa ni nafuu kubwa kitendo cha Dr.Pesambili kumchukua mama Deborah na kuishi nae chini ya paa moja. Mgonjwa zamani hali yake ilikuwa mbaya sana kutokana na kukosa faraja toka kwa wauguzi wake. Lakini sasa chini ya mikono ya Dr.Pesambili alikuwa anapata lishe bora, huduma bora za afya na ushauri nasaha wenye kumpa matumaini mapya katika maisha yake. Baada ya kupita miezi sita (6) mama Deborah akaanza kutembea kwa kuchechemea kwa msaada wa fimbo. Ila kitu kibaya zaidi, homa ile ya kupooza ilimfanya mama Deborah asahau kumbukumbu nyingi sana maishani mwake.

Ilikuwa inakadiriwa kuwa itamchukua kama muda wa mwaka mmoja na nusu kuweza kufanikiwa kurudisha kumbukumbu zake za miaka ya nyuma. Mbaya zaidi Mjomba Kobelo akahama tena toka kijiji kile na kutokomea kusipojulikana huku Binti zake wote wakiwa wameshaolewa wanaishi na waume zao, kila mtu na lake bila hata kumpa taarifa Dr.Pesambili. Maendeleo ya Kiafya ya mama Deborah kila uchao yalikuwa yanampa faraja kubwa sana Dr.Pesambili, sasa mama Deborah kwake akageuka ndio kama mama yake mzazi. Akaajiri mtumishi maalumu wa kumpa huduma zote mama Deborah. Lakini Dr.Pesambili alikuwa anamlea mama yake wa kambo bila kufahamu. Mama Deborah nae alikuwa hajui kitu chochote kama Dr.Pesambili huyu mfadhili wake na daktari wake, mama yake mzazi ni Recho, ambaye ndio hasimu wake mkubwa, aliyemdhulumu mali za marehemu mumewe Bosi Minja na kumsababishia msongo wa mawazo uliosababisha mpaka apooze mwili. Mungu aliamua kumtumia Dr.Pesambili kumfanyia wema mama Deborah ili kufuta ubaya wa mama yake mzazi alioufanya kwa mama Deborah.

Mkataba wa kazi ulipoisha, Dr.Pesambili hakutaka kuongeza tena kandarasi yake. Aliamua rasmi makazi yake kuyafanya yawe Jijini Dar es Salaam. Alipolipwa mafao yake tu akanunua nyumba maeneo ya Mikocheni na kuhamia rasmi akiambatana na mama Deborah, ambaye kadri siku zilivyokuwa zinasonga alikuwa anazidi kuimarika kiafya. Sasa rasmi akazindua harakati za kumtafuta mama yake mzazi, kwa udi na uvumba. Ikabidi apange safari ya kuelekea Jijini Nairobi, Nchini Kenya kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Cheryls Childrens Home and Learning Centre. Kituo hicho kinachomilikiwa na mtu binafsi, Mr.Ochieng kilikuwa kipo Katika mtaa wa Dagorretti Corner hatua chache kutoka barabara ya Ngong, Jijini Nairobi. Wakaagana vizuri na mama Deborah huku mama Deborah akimtakia kila la heri kwenye safari yake hiyo. Miadi walipeana kuonana baada ya wiki 2, ndipo Dr. Pesambili atarejea Jijini Dar es Salaam, hivyo akamuacha nyumbani na mtumishi wa kumpa huduma.

Alex na Deborah baada ya kumaliza mambo ya kesi, sasa walikuwa wanapika na kupakua pamoja, wanalala kitanda kimoja, wakijifunika shuka moja. Walikuwa ni wapenzi rasmi wapendanao 'Love Birds' wasiojificha tena, kila kitu hadharani. Muda wa kazi ulikuwa unapoisha tu, basi popote utakapomuona Alex basi Deborah yupo nae sako kwa bako. Wale wenye vijiba vya Roho, mahasidi wasiopenda kuona watu wakipendana mapenzi ya kweli, roho zao zilikuwa zinakaribia kuwachomoka kwa wingi wa chuki katika mioyo yao.

Chuki zilianzia Ofisini kwake Alex, wapo wasichana waliokuwa wanajiona wana sifa na vigezo vya kuwa wapenzi wa Alex kutokana na uvaaji wao nadhifu wa nguo za gharama na namna wanavyojua kwenda na wakati, lakini tahamaki Alex kadondokea kwa Deborah. Mwanamke ambaye kwa mtazamo wao ni mshamba, nywele zake anasuka mtindo wa twende kilioni. Magauni yake ya mshono wa mfuko wa mashineni kama muimba kwaya kanisani, na ngozi yake ya asili haipakwi cha ziada zaidi ya mafuta ya mgando. Walichokuwa hawakifahamu ni kuwa Alex alikuwa anatafuta mke mwema na sio gubegube linalojishebedua kwa uzuri wake.

Baada ya miezi mitatu (3), majibu ya Deborah ya kidato cha 6 yakatoka, huku akiwa amepata ufaulu wa daraja la kwanza. Alikuwa amechaguliwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 'UDSM' kusomea Uhandisi wa Chakula 'Food Engineering'. Alijawa na furaha chekwachekwa kwa kuchaguliwa kozi hiyo ambayo ingempa wigo mpana wa kujiajiri mwenyewe kwa kufungua kiwanda cha kusindika vyakula hasa katika zama ambazo ajira rasmi zilikuwa ni finyu sana. Lakini furaha yake hiyo ilitumbukia nyongo baada kutokupata mkopo toka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi Tanzania 'Higher Education Student's Loan Board'(HESLB). Vigezo vyote vya kuweza kupatiwa mkopo alikuwa anakidhi lakini Mrs.Tonny ndio aliyechafua hali ya hewa. Kumbuka alimpa ahadi ya kumfadhili kwenye elimu ya juu hivyo Deborah katu hakujishughulisha na kujaza fomu za maombi ya mkopo huo. Lakini mpenzi wake Alex akatekeleza msemo wa ukipenda boga penda na ua lake, hivyo akajivika rasmi mzigo wa kumsomesha. Alex hakutaka kufuata maneno ya mtaani ya kuwa mchumba hasomeshwi utakuja kulia kilio cha kusaga na meno. Alimuamini Deborah zaidi ya hata anavyoiamini nafsi yake, ya kuwa hawezi kamwe kuja kumgeuka pindi atakapohitimu masomo yake ya Chuo Kikuu.

Kwa kutumia mshahara wake, Alex akakopa pesa za kumlipia ada Deborah na matumizi ya kujikimu chuoni. Muda wa kuripoti Chuoni ulipowadia, Alex akamsindikiza Deborah mpaka Chuoni. Wakakamilisha taratibu zote za Chuo zinazohitajika na Deborah akapangiwa kuishi Hosteli za Mabibo zilizopo barabara ya Mandela jirani na eneo la Ubungo. "Mpenzi Deborah, nakutakia masomo mema, kikubwa kumbuka kulinda ahadi yetu, ya kuwa tutakuja kuoana pindi utakapomaliza Chuo. Jitahidi kujilinda na vishawishi vya kila aina. Upo ndani ya Jiji la Dar es Salaam lenye watu wa kila sampuli, wenye uwezo hata wa kukuhonga nyumba na magari ili mradi wavuruge penzi letu. Lakini kumbuka pia maisha ya Chuo ni matamu sana lakini ni mafupi mno, ukivuruga muelekeo wako ndani ya miaka 4, utakuja kujutia maisha yako yote, hivyo akili kumkichwa chako" alizungumza Alex kwa hisia kali, nasaha ambazo zilimtoa machozi Deborah pindi walipokuwa wanaagana hapo Mabibo Hosteli.


Deborah hakuwa na maneno mengi zaidi ya kushukuru kwa hisani ya kusomeshwa na mpenzi wake, kipindi ambacho aliona kabisa ndoto yake ya kielimu inataka kutoweka. "Nakuahidi sitokuangusha, nitalilinda penzi letu kwa hali na mali, na nitasoma kwa bidii ili kuhakikisha ninapata maarifa stahiki. Nakuahidi pindi nikimaliza Chuo nitafungua kiwanda cha kusindika nyanya kule kule Mzumbe, na hutojuta kwa pesa ulizonilipia ada, tutakuwa matajiri wakubwa tu. Nataka siku moja tukae meza moja na hasimu wetu Mrs.Tonny tukiwa tunaongea lugha moja ya uwezo wa kipesa" aliongea Deborah kwa furaha huku akimpa matumaini makubwa mpenzi wake Alex.

Wakaachana, siku zikaanza kusonga, miezi kadhaa ikakauka, huku Deborah akijihesabia kuwa yupo sasa yupo salama salimini, ndani ya mikono ya mtu makini kama Alex. Likizo ndogo zote alikuwa lazima arejee Mzumbe kwa Alex. Nae Alex kwa upande wake, majukumu ya kazi yaliongezeka hivyo kumfanya muda mwingi awe anautumia ofisini. Akitoka saa 1 asubuhi kurudi kwake ni saa 1 usiku. Sana sana mapumziko yake rasmi yalikuwa ni siku ya Jumapili, hali ambayo ilimlazimu kuajiri mtumishi wa kike wa kuja na kuondoka kwa ajili ya usafi wa nyumba, kufua nguo na kupika chakula. Kabla ya kuajiri mtumishi huyo, alipata baraka zote za Deborah hasa baada ya kuthibitisha uzito wa majukumu aliyo nayo mpenzi wake hivi sasa.

Lakini kama ujuavyo ya kuwa Deborah ni mtu wa mikosi, daima hawezi kupata starehe ya kukesha mpaka che, lazima tu kitokee kitu cha kuchafua hali ya hewa, akajikuta anaingia kwenye mgogoro wa mapenzi na Alex. Mgogoro ambao ulisababisha penzi lao lisambaratike vipande vipande, na kumuacha Deborah yupo njia panda hajui cha kufanya.

Mgogoro wao ulianza wakati wa likizo ndogo ya karibu na mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka, Deborah akiwa ndio kwanza amerejea toka Chuoni, ghafla yule dada wa kazi za ndani akatoweka bila taarifa. Simu yake ikawa kila ikipigwa ili kufahamu ana tatizo gani lililomfanya asije kazini ikawa haipatikani. Wakakubali matokeo kuwa huenda kazi imemshinda au kapata sehemu nyingine yenye maslahi zaidi ya hapo.
Asubuhi yake iliyofuatia, wakati Alex yupo kazini hana hili wala lile, Deborah akiwa kwenye harakati za usafi wa nyumbani akaifuma barua iliyokuwa imesokomezwa chini ya sofa ukumbini. Kichwa cha habari juu ya bahasha ya barua hiyo, alipokisoma tu kilimpa mshtuko mkubwa Deborah. Jasho jekejeke likaanza kumtiririka mwilini mwake huku mapigo ya moyo wake yakienda mbio. Akajikuta anaishiwa nguvu na kuamua kukaa kitako chini ya sakafu ili aisome vizuri barua hiyo mbaya. Akajikuta ghafla anatetemeka mwili mzima kama mgonjwa aliyepigwa na homa kali. Vidole vya mikono vilikuwa vinamtetemeka mithili ya mnywaji gongo aliyekubuhu. Kwa ufupi Deborah alijihisi kufa kufa.

Hakuamini mtu aliyemwamini na kumthamini kama Alex angeweza kumtenda kiasi hicho. Kilichokuwa kinampa mawazo ni kuwa ataiweka wapi sura yake kwa mashosti zake wa Chuoni ambao kutwa kucha alikuwa anawatambia kuwa amepata mpenzi mwenye kujiheshimu na anayempenda kwa dhati. Licha ya wenzake kumtahadharisha kuwa asiweke matumaini asilimia 100% kwa mwanaume, lakini Deborah alikuwa anamkingia kifua Alex. Sasa leo kupitia barua hiyo alikuwa anaonjeshwa asali kwa ncha ya kisu. Deborah akajikaza Kisauni na kujitutumua kuifungua barua hiyo.


Barua ambayo juu ya bahasha kulikuwa na maandishi ya herufi kubwa, "KWAKO MPENZI ALEX". Ndani ya barua sasa kulikuwa kunasomeka kama ifuatavyo; "Mpenzi Alex, nimeamua kukuachia ujumbe huu kama nilivyokuelekeza kwenye meseji ya simu yako kuwa utaukuta chini ya sofa lako unalopenda kukalia. Nimeamua kupotelea kusipojulikana kutokana na shinikizo lako la kutaka nitoe mimba uliyonipa ili mchumba wako asijue kama nina mimba yako. Nakutakia kila la heri katika maisha yako na huyo mchumba wako unayempenda sana kuliko mtoto wetu aliye tumboni mwangu. Nitamlea peke yangu bila kuhitaji msaada wako wowote lakini hesabia huna mtoto na mimi". Deborah alipomaliza kusoma barua hiyo alijikuta anajiona anaishiwa nguvu na kujilaza kwenye zulia la pale sebuleni. Kifua chake kilikuwa kinafukuta fukuto la joto la hasira dhidi ya Alex. Mawazo lukuki yalimvamia kichwani mwake, huku Ibilisi akimpandia kichwani na kumshadidia ajiondoshe uhai wake. Alijilaumu sana kukubali kuwa mpenzi wa Alex bila hata kupata nafasi ya kumchunguza tabia zake kiundani.

"Ina maana kipindi chote nipo Chuoni, huyu dada wa kazi alikuwa ndio alikuwa anajinafasi, ama kweli paka akitoka panya hutawala" alijisemea kimoyomoyo Deborah na kuamua kuinuka pale alipojilaza. Akili yake ilimuambia aifiche ile barua, ili aone mwisho wa sinema hiyo mpya kwake ya mapenzi baina ya Alex na dada wa kazi. Deborah akiwa hana hili wala lile, akashtukia mlango wa barazani unafunguliwa kwa kishindo, kisha Alex akaingia ndani ya sebule. Bila kuzungumza na mtu yoyote akaenda kukaa kwenye sofa lile lile aliloelekezwa kuna barua yake.

"Kulikoni mbona salamu unatuvamia, umepatwa na maswaibu gani mwenzangu mbona unanitisha..!" alisema Deborah huku akijikaza kutokumuuliza chochote kuhusiana na barua ile ili amuone kama atakuwa mkweli na kueleza kinagaubaga bila mficho. "Aaaah....take easy hamna kitu nimekuja kunywa chai tu, tayari umepika..?" aliongea Alex huku akilazimisha tabasamu. "Tayari ipo mezani, ingawa hukunipa taarifa kama utakuja kunywa chai nyumbani maana huna kawaida hiyo ukiwa kazini" Deborah alizidi kumfunga Alex ili kumtengenezea mazingira ya kuelezea kitu kinachomsumbua. "Hapa si nyumbani kwangu? usiwe na mashaka nimeamua tu kukufanyia surprise..twende basi tukapate wote staftahi" alijibaraguza Alex huku ameuviringisha mkono wake kwenye kiuno cha Deborah. "Ahsante mpenzi, lakini mie nimeshakunywa, sasa naenda kujipumzisha chumbani sijisikii vizuri, nimekunywa dawa za kutuliza maumivu " alisema Deborah huku akiutoa mkono wa Alex kiunoni mwake na kuelekea moja kwa moja chumbani kwao. "Pole sana, kapumzike unono..." alisema Alex huku akimuangalia Deborah namna anavyomalizikia kuelekea chumbani kwao.

Alex alivyomuona Deborah ameshamalizikia kuingia chumbani akarudi kwa kasi pale sebuleni mpaka kwenye sofa lake analopenda kukalia. Akalinyanyua kuitafuta barua aliyoelekezwa na mtumishi wake aliyetoweka. Alex tokea alipopata ujumbe wa kwenye simu ya mkononi, alikosa amani kabisa ya kuendelea kufanya kazi ofisini. Alijutia kitendo cha kumkubalia kuwa mtumishi wake wa nyumbani, mpaka akamuingiza kwenye mtego uliosababisha atembee nae kimapenzi. Siku ya kwanza Alex kumuona dada huyo alivyokuwa kuomba kazi hakuamini kama kweli dada huyo anatafuta kazi za ndani hasa kutokana na urembo wake wa shani. Urembo ambao ulimbabaisha Alex vilivyo na kumkubalia ombi lake, huku akijifanya kuomba ushauri kwa mpenzi Deborah ili kuondosha fikra potofu. Mpaka anavyopokea ujumbe huo wa simu alishakuwa ametembea nae si chini ya mara mbili. Lkini anachokumbuka ni kuwa mara zote alizofanya nae mapenzi alitumia kondomu, hakufanya ngono uzembe sasa mimba hiyo amepataje, ni kitu kilichokuwa kinamfanya achanganyikiwe vilivyo.

"Kama Deborah aking'amua nitambeba na mbeleko gani apate kunielewa kuwa ni shetani tu amenipitia..! " alijisemea peke yake Alex kimoyomoyo huku akiwa anaendesha lile sofa alilonyanyua. Deborah mchezo wote anaoufanya Alex wa kuitafuta barua chini ya sofa alikuwa anaushuhudia kupitia upenyo wa mlango wa chumbani. Alipojifanya anaenda kulala, ilikuwa ni janja ya nyani tu, ili kumpa nafasi Alex ya kujitawala sebuleni. Deborah akajithibitishia mubashara bila chenga kuwa Alex ni kweli kambandika mimba dada wa kazi kutokana na juhudi zake za kutaka kuinyakua barua hiyo. Deborah akajikokota kinyonge mpaka kitandani na kujitupa kama furushi la mwizi. Macho yake yalikuwa yanabubujikwa machozi bila ukomo, huku akiwaza na kuwazua maamuzi ya kufanya juu ya penzi lao. Mawazo mengine yakimshawishi aachane na Alex aanze maisha yake upya katika ulimwengu wa huba, lakini kikwazo kikaja kwenye suala la kusomeshwa, nani atakuwa tayari kumlipia ada ya Chuo Kikuu na gharama zingine kama anavyofanya Alex. Akajiona kabisa analazimika kuwa mtumwa wa Alex kwa sababu tu za kiuchumi lakini tayari alishamfuta thamani kwenye moyo wake.

"Koh...Koh....Koh....Koh....fungua mlango...!" ilikuwa sauti nzito iliyoshiba ikishinikiza yeyote aliyekuwa ndani ya nyumba ya Alex afungue mlango. Deborah akiwa jikoni anakarangiza maakuli ya jioni, wito huo ukamshtua kidogo. Akawa anasikilizia wito huo akijaribu kutaka kutanabahi sauti hiyo ni ya nani. Alipozidi kusikia wito huo ukitaka mlango ufunguliwe, ikabidi akurupuke na kanga moja kwenda kufungua mlango huo kujua kulikoni. Alipoufikia mlango huo na kuufungua mshtuko wa ghafla ulimshika. Alihisi mapigo ya moyo wake kama yanataka kusimama kwa ghafla. Akajikuta miguu yake haina ushirikiano na sehemu ya juu ya mwili wake, ikaanza kushindwa kuhimili uzito wake, akajikuta anachegama mlango huo ili kupata msaada wa kuegemeza mwili.

Alimuona Alex akiwa amefungwa pingu za mikononi huku machozi yanamtiririka machoni mwake. Deborah alikuwa anatamani afungue mdomo wake aulize kulikoni lakini akajikuta anapatwa na gagaziko la ulimi hawezi kuongea chochote. "Ingia ndani, unatuchelewesha fisadi mkubwa wewe" aliongea yule mtu mwenye sauti nzito aliyekuwa anagonga mlango. Walikuwa ni askari kanzu wawili wameambatana na Mtendaji kata wakimleta Alex nyumbani kwake. Majirani nao waliokuwa wamebakia nyumbani muda huo nao wakaanza kujongea kutaka kujua kulikoni.

"Dada habari yako, sisi tumekuja kufanya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa huyu Bwana Alex kutokana na tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake. Hivyo tumekuja kukagua mitihani ya wanafunzi wake aliyosema amehifadhi nyumbani kwake ili wana usalama iwasaidie kwenye taftishi yao dhidi ya mhadhiri Alex. Hivyo kuwa na amani kwa sababu tumekuja kisheria" alisema Mtendaji Kata nia na madhumuni ya ujio wao pale nyumbani. "Sawa hamna shida, kwani amefanyaje mpaka mnamtia pingu kama jambazi? " alijitutumua Deborah kuuliza kwa tabu akitaka adadavuliwe kwa undani tuhuma hizo. "Dada usichoelewa kitu gani, huyu jamaa yako tumemkata ofisini kwake leo saa 9 alasiri akijiandaa kufanya mapenzi na mwanafunzi wake ofisini kwake..! " aliongea yule askari kwa kufoka huku akimhimiza Alex asonge ndani ya nyumba hiyo akaonyeshe mahali anapohifadhi nyaraka za wanafunzi wake. Deborah akabaki amesimama mlangoni amebung'aa kwa mshangao anawasindikiza kwa macho. Alex wakati wote alikuwa anatikisa kichwa kuonyesha hakubaliani na tuhuma hizo, ukweli halisi wa tukio hilo alikuwa anaujua Alex na huyo mwanachuo aliyetoa taarifa kwa vyombo vya dola juu ya kusumbuliwa rushwa ya ngono ili apewe maksi za kumfaulisha kwenye somo analofundisha Alex.

Baada ya nusu saa ukaguzi wao ukakamilika huku wakiondoka na mitihani ya wanafunzi waliyoikuta nyumbani kwa Alex. "Naomba umfahamishe mama yangu mzazi tukio lote..!" aliongea Alex kumpa maagizo Deborah huku akikwepesha macho hataki kuangaliana uso kwa uso na Deborah. Alichofanya Deborah ni kuitikia kwa kichwa, kuonyesha kuwa atatekeleza maagizo hayo. "Mshahara wa dhambi ni mauti, umeumbuka Alex, umempa mimba dada wa kazi na leo leo kabla jua halijakuchwa unapigwa kofi lingine la rushwa ya ngono, Ahsante sana kwaheri..!" alisema Deborah baada kulisogelea gari la wazi lililotumika kumbeba Alex kwa upande wa nyuma. Alex hakuwa na kitu cha kujibu, soni ilimjaa usoni kwake, macho yake yamemwiva wekundu.

"Kumbe barua chini ya sofa kaichukua Deborah..!, ama kweli siku ya kufa nyani miti yote" hizo zilikuwa ndio fikra za Alex wakati huo. Gari hilo likaondoka eneo hilo kwa manjonjo likiwaacha majirani midomo wazi kila mtu anasema lake. Deborah haraka haraka akaingia ndani ya nyumba na kujifungia kwa komeo. Alijua majirani wale habari kuuzwa ndio wakati wao muafaka wa kuja kuchokonoa mambo ya watu. Watamuingia kwa gia za kumpa pole kisha waanze kumdadisi undani wa tukio la Alex. Alipoingia ndani Deborah akatuma meseji kwa mama yake mzazi Alex akimuelezea tukio zima kisha akazima simu yake kukwepa maswali, baada ya hapo akaanza kupanga nguo zake na vifaa vyake mbalimbali kwenye begi lake la safari. Alishajua penzi lake na Alex ndio limekufa rasmi, kwani lazima atafungwa jela kwa kosa la kuomba rushwa ya ngono.

Moyoni mwake aliyakinisha asilimia 100% kuwa Alex amehusika hasingiziwi hasa akirejea tukio la kumtundika mimba dada wa kazi. Pia hata kama angeendelea kukaa hapo lazima angetimuliwa katika nyumba na Uongozi wa Chuo cha Mzumbe ili kupisha watumishi wengine wasio na makazi. Kilichokuwa kinambangua kichwa ni kuwa anaelekea wapi akitoka hapa nyumbani kwa Alex, na nani atamlipia ada Chuoni na kumpa pesa za matumizi hali ya kuwa ni kesho kutwa tu Chuo kinafunguliwa. Chakula chake alichokuwa anakipika jikoni hakuwa na hamu nacho tena, akakitekeleza huko huko. Akiwa na begi lake pembeni akaa juu ya sofa sebuleni anatafakari. Muda ulikuwa inayotoka, magharibi ilikuwa inakaribia, muda muafaka aliopanga kuondoka huku kukiwa na kigizagiza kukwepa fedheha mbele ya majirani. Ghafla bin vuu akakurupuka kwenye sofa na kuanza kufungua begi na kuchambua vitu vyake pembeni ya begi kana kwamba kuna kitu anatafuta. Akaunda tabasamu jepesi baada ya kukiona kitu alichokuwa ananitafuta. Alikuwa anatafuta kadi yenye anuani na namba za simu za mfadhili wake mpya Timammy alizompa siku alipomchomoa mikononi mwa Mrs.Tonny kule mahakamani kwa kumuwekea dhamana. Tokea siku ile alipomtafuta mara moja na hakumpatana hewani hakujisumbua tena kumtafuta. Lakini leo alikuwa ametumbukia kwenye dhiki yenye kuhitaji utatuzi wa haraka hakuwa na jinsi zaidi ya kumtafuta tena, kama ujuavyo mficha ugonjwa mauti humuumbua. Sakata lake lilimfikisha mahali pa kuchagua kusuka ama kunyoa, hivyo ampige pande Timammy afukuzwe Chuo kwa kukosa ada au amtafute Timammy amuombe tena msaada wa kusomeshwa ili aweze kuhitimu Chuo.

Deborah alijawa na matumaini kuwa atamuelezea kila kitu Timammy kuwa Mrs.Tonny ndio alimuingiza chaka asiombe mkopo kwa kujimwambafai kuwa atamsomesha akaishia kumtelekeza machakani. Akatoa simu yake kwenye pochi la mkononi, na kuanza kuingia namba kwa ajili ya kuipiga simu ya Timmamy. Bila mafanikio yoyote namba zote za Timammy zilizokuwa zimeorodheshwa kwenye kadi ile zilikuwa hazipatikani. Jasho jekejeke likaanza kumvuja Deborah huku machozi yakianza kumlengalenga upya machoni mwake. Matumaini yake aliyaona kabisa mithili ya mshumaa uliowashwa kwenye uelekeo wa upepo mkali. Akaanza kuvuta tafakuri jadidi ya maisha yake upya tokea azaliwe mpaka leo yupo Chuo Kikuu akajiona kabisa hajawahi kabisa kuishi maisha ya kula bata kama walivyo wenzake, yeye kila siku kidagaa kinamuozea yeye tu. Machozi sasa yakaanza kumtiririka kwa wingi bila kizuizi na kilio cha kwikwi. Ghafla akanyamaza kulia, akatoa hanchifu yake kwenye pochi yake na kujifuta machozi yote. Akachomoa noti ya sh.5,000/= na kufungua mlango wa sebuleni atoke nje. Alipanga kwenda duka la dawa kununua vidonge ili avibugie afilie mbali. Alishakata tamaa ya kuishi, hakuona tena thamani ya maisha ya dunia, kwake aliona bora awafuate wazazi wake waliotangulia jongomeo. Kabla hajanyonga kitasa cha mlango, simu yake ikaanza kuita kwa fujo. Akairudia alipoangalia ilikuwa ni namba binafsi 'private number' akaikata na kuizima simu kabisa kisha akairudisha kwenye kipochi tena.

Akachomoka mbio mbio kuelekea duka la dawa, bila kutanabahi kuwa ile simu aliyoikata ni ya mfadhili wake Timammy aliyekuwa anamtafuta kwa udi na uvumba muda mchache uliopita. Ama kweli hasira hasara, Deborah alikuwa kama vile anapiga teke furushi la pesa, anapishana na ngekewa. Baada ya dakika takribani 10 Deborah akawa anarejea akiwa na tembe zake mkononi. Akiwa meta chache kabla ya kufika nyumbani akashtuka kuona gari la kifahari aina ya 'Vanguard' limeegeshwa upenuni kabisa mwa nyumba ya Alex. Akasita kwenda mbele akasimama, akiwa ameshtushwa roho yake kuwa huenda amekuja kukamatwa yeye sasa. Akiwa bado amepigwa na mzumbao akaliona lile gari limeamshwa linageuzwa na kuanza kuja uelekeo wake pale aliposimama. Deborah hakuwa na simile tena, akageuka, akavitupa vile vidonge na kutaka kuanza kutimua mbio, tayari alikuwa ameshachanganyikiwa, anaona kabisa penzi lake na Alex linampiga pute furaha yake katika maisha. Kichwa chake kilikuwa ni kama dampo ya mawazo machafu ya kila aina. Tahamaki lile gari likawa limefunga breki karibia kabisa na miguu yake, Deborah akaanguka mpaka chini kutokana na kiwewe cha hofu iliyomsonga moyoni mwake. Akaharakisha kunyoosha mikono yake juu anahema kwa kutweta kuonyesha kuwa anahitaji amani amesalimu amri. Lile gari lilifungwa vioo vyeusi lisivyoruhusu kumuona aliyekuwa ndani ya gari. Kioo cha gari upande wa siti ya mbele ya abiria kikaanza kushushwa taratibu mpaka aliyekaa siti ile akaonekana dhahiri.

"Deboraaaah.....usikimbie ni mimi Timammy nimekufuata...!" aliongea mtu aliyekuwa amekaa siti hiyo akiwa amevaa miwani yenye vioo vyeusi. Akaivua miwani yake na kufungua mlango wake akashuka chini na kumsogelea Deborah pale alipokaa kwenye mchanga. Akanyoosha mkono wake mrefu kutaka kumpa msaada Deborah wa kuinuka toka ardhini. Deborah alinyoosha mkono wake lakini kwa wasiwasi bado akiwa amepigwa na butwaa kaachwa mdomo wazi. Hofu yake ilikuwa haamini kama kweli huyu ni Timammy alidhania labda ni mzuka wake Timammy. "Haiwezekani mtu niliyempigia simu robo saa iliyopita tena sikumpata hewani ghafla awe amefika mpaka kwenye nyumba ninayoishi" aliwaza Deborah. "Najua unajiuliza maswali kibao na hupati majibu kuhusu ujio wangu, kwa ufupi sakata la mchumba wako kuomba rushwa ya ngono limetangazwa mapema sana kwenye redio na televisheni, na mie nilikuja kijiji cha Mlali hapo jirani na Mzumbe nikiwa kwenye harakati za kutafuta eneo la kufungua kiwanda cha kusindika nyanya ndio nikaonelea nichepuke mara moja kuja kuangalia usalama wako..! " aliongea Timammy kwa kujiamini bila kupepesa macho wala kutafuna maneno, kauli ambayo kidogo iliondosha hofu katika moyo wa Deborah. Kama ujuavyo ukiwa kwenye dhiki na shida hata akili inapunguza uwezo wake wa kuchanganua mambo kwa upana. Mtu mwenye njaa anafikiria kwa msaada wa tumbo lake, kichwa chake kinaenda likizo.

Deborah akajinyanyua ardhini na kujikung'uta mavumbi kwenye sketi yake. Baada ya maongezi mafupi ya kusafiana nyoyo baina yao, Deborah akaingia ndani kufuata begi lake aweze kuondoka na Timammy. Moyo wa Timammy ulijawa na furaha fokofoko kutokana na kukaribia kutimiza ndoto yake ya kumfanya Deborah awe mke wake wa kufanya nae maisha. Msichana ambaye amemsubiria kwa zaidi ya miaka 6 na ushee ili aweze kumtia kwenye himaya yake. Timammy ndio aliyeandaa mipango yote ya maangamizi kwa Alex bila Alex na Deborah kutanabahi kuwa ni adui yao. Baada ya Timammy na dereva wake kumkosa Deborah kule shuleni na kuelekezwa kuwa yupo Morogoro. Katika juhudi zao za kumsaka wakafanikiwa kuelekezwa kuwa anafanya kazi dukani kwa Mrs.Tonny. Walipofika hapo dukani ndio wakapata hadithi ya Deborah kuwekwa ndani rumande kwa kosa la wizi wa vito vya thamani. Kwa jinsi Timammy anavyomfahamu Deborah kwa tabia zake njema, moja kwa moja akajua ni zengwe tu lililosukwa na Mrs.Tonny, mwanamke ambaye anamjua kinagaubaga kuwa ni tajiri lakini ana tabia za kikhabithi sana.

Uzuri wake Mrs.Tonny alikuwa anamuogopa vibaya sana Timammy kutokana na mtifuano mkali waliowahi kuzozana katika kugombea tenda mbalimbali zenye ulaji serikalini. Ndio maana ikawa rahisi kwa Timammy kumaliza kesi ya Deborah kiulaini kama kumsukuma mlevi. Kikwazo pekee kilichokuwa kimebakia mbele Timammy alikuwa ni Alex. Akaitafuta mbinu iliyoenda shule ili kumchomoa Deborah kwa Alex, hakutaka kutumia mbinu ambazo Deborah zitamfanya amgundue yeye kama ndio mpishi faraka katika penzi lake na Alex kwa kutumia kuni za fitina. Timammy Kwa ujuba wake uliotopea angeweza kumuua Alex au kumtia kilema chochote ili ajitwalie kirahisi Deborah ila akaamua kutumia njia za kisayansi ambazo itakuwa ngumu Deborah kugundua kuwa yeye ndio mhusika wa matatizo ya Alex.

Akatumia fursa ya upweke wa Alex pindi mpenziwe alipokuwa Chuoni kumpenyeza dada wa kazi ambaye ni mrembo wa haja kumtia mtegoni Alex, akafanikiwa kunasa. Ndipo ukasukwa mpango yule dada ajisingizie amepata ujauzito na apotee kimoja ila ahakikishe taarifa zinavuja kwa Deborah. Ramani ya tukio zima ikachorwa kiustadi mkubwa kuwa siku hiyo hiyo inayovuja habari ya ujauzito wa dada wa kazi kabla jeraha la moyo wa Deborah halijakauka, atoneshwe tena ili amchukie kimoja Alex. Ndipo akapangwa msichana mrembo, mmoja wa wanafunzi wa Alex aingie ofisini kwa Alex kisha askari kanzu wavamie wamkamate Alex kwa kigezo cha kuomba rushwa ya ngono. Waandishi wa habari na wapiga picha wakapewa chao kuhakikisha wanaripoti tukio la Alex kiufasaha na kwa kuongeza chumvi zaidi ili kuzidi kuchafua hali ya hewa. Sasa mipango ya Timammy ilikuwa inakaribia kutimu, Deborah anaingia kwenye himaya yake kiulaini mithili ya mbwa mbele ya chatu.

Punde si punde Deborah akatoka na begi lake, kisha akaacha funguo za nyumba ya Alex kwenye nyumba ya jirani huku akimpa maelekezo kuwa mama yake Alex atakuja kuufuata ufunguo hapo, kisha akaingia kwenye gari la Timammy na kutokomea zao, usiku mbichi huo wa saa moja na robo usiku. Deborah mchezo aliokuwa anaucheza wa kutaka auni toka kwa Timammy ilikuwa ni kama kurudisha tende Manga, kamwe asingepata faraja anayoitarajia. Auni iliyokuwa inatolewa na Timammy kwa Deborah ilikuwa ni kwa malengo maaalumu.


SURA YA KUMI NA NANE
"Umesema ni mwaka 1990 eeh....ngoja niangalie faili la mwisho, tukikosa taarifa zako humo ndio basi tena, sina jinsi ya kukusaidia rafiki yangu" aliongea Bwana Joram Peter Ochieng Mkurugenzi wa kituo kikongwe cha yatima Jijini Nairobi kinachojulikana na kwa jina la Cheryls Childrens Home and Learning Centre. Walikuwa wamejifungia kwenye ofisi ya kisasa yenye ukubwa wa wastani iliyopambwa kwa samani nzuri za kuvutia, huku kiyoyozi kikifanya kazi barabara na kuzalisha hali ya hewa ya kuvutia.

"Sawa nitashukuru ukinisaidia" aliongea kinyonge Dr.Pesambili akionyesha dalili za kukata tamaa ya kupata taarifa zake zilizosajiliwa kwenye kituo hicho pindi alipokuwa analelewa kwenye kituo hicho cha yatima kwenye miaka hiyo ya 90's. Alikuwa ameshakaa ofisini hapo kwa zaidi ya dakika 45 wakizisaka nyaraka zenye taarifa zake. Kibaya zaidi mmiliki wa kituo mstaafu Mzee Peter Ochieng ambaye ndio alimpokea Dr.Pesambili akiwa kinda wa miaka 2 alikuawa ameshastaafu, anajilia zake pensheni yake huko maeneno Kisumu.

"Mmmhhhhh..........kuna hii karatasi ya usajili inaonyesha jina la mtoto wa kiume ni Pesambili, mlemavu wa miguu aliokotwa na mlinzi wa klabu ya starehe ijulikanayo kama 'Nairobee BY Night Club'" aliongea kwa mshawasha yule Mkurugenzi huku akiwa ananyofoa hiyo karatasi kutoka kwenye faili hilo alilokuwa ameliinamia kitambo kirefu na kumkabidhi Dr.Pesambili. Dr.Pesambili alipoipitia kwa umakini machozi ya huzuni yakaanza kumtiririka akivuta hisia za kulijua kwa mara ya kwanza jina lake halisi la utotoni la Pesambili. Siku zote tokea apate akili anajijua anaitwa 'Trezguet Lorenzo' na ndio jina la kwenye hati yake ya kusafiria na alilolitumia kwenye vyeti vya shuleni. "Huyu ndio mimi kabisa....! " alisema kwa msisitizo mkubwa Dr.Pesambili tena kwa lugha ya kiswahili fasaha kutokana na kuishi kwake Tanzania kitambo kirefu pia baba yake na babu yake mlezi nchini Italia nao walikuwa fasaha wa lugha ya kiswahili.

"Lakini hapo inaonyesha mtoto alikuwa ni mlemavu wa miguu na wewe ni mzima, hapo inashangaza kidogo" aliuliza Mkurugenzi yule swali la kidadisi huku akiyaweka sawa masikio yake kutaka kulisikia jibu maridhawa toka kwa Dr.Pesambili. "Ni hadithi ndefu, lakini kwa ufupi nimefanyiwa operesheni ya kurekebisha mifupa ya miguu nikiwa mtoto kabisa" aliongea kinyonge Dr.Pesambili. Baada ya mazungumzo mafupi, Dr.Pesambili akachomoa kitabu chake cha hundi akaandika cheki ya Ksh.10,000/= kama msaada wake kwa kituo huku akiahidi kukitafutia wafadhili mbalimbali kituo hicho.

Akatoka nje ya Ofisi na kufanya ziara fupi katika mabweni wanayotumia watoto hao kuishi, akaongea nao na kuwapa nasaha fupi zenye kuleta matumaini katika maisha yao ya siku za usoni. Watoto wale wakafurahi sana kuona mwenzao kama wao aliyepitisha maisha yake hapo kituoni ametoboa maisha. Akapiga nao picha ya pamoja, kisha akaagana nao na kuingia mtaani rasmi kumsaka mlinzi wa klabu ya "Nairobee BY Night" ambaye taarifa rasmi zinasema yeye ndio alimuokota.


"Naomba unipeleke klabu moja inaitwa Nairobee BY Night...!" alisema Dr.Pesambili kumuambia dereva taksi mmoja aliyekuwa ameegesha gari yake mtaani jirani kabisa na kituo cha watoto yatima alichotoka. "Wewe ni mgeni Jijini Nairobi eeeh...?" aliuliza kwa mshangao mkubwa yule dereva huku akimuangalia usoni Dr.Pesambili. "Eeeh...sio mwenyeji hapa Nairobi..!" alijibu Dr.Pesambili huku akisubiri jibu muafaka. "Hamna Klabu yenye jina hilo inayosema, nina miaka 5 Jijini Nairobi, naijua mitaa na vichochoroni vyote yakiwemo majumba ya starehe lakini sijawahi kuisikia hiyo Klabu unayoitaja" alisema yule dereva huku akimchangamkia mteja mwingine aliyekuwa anahitaji taksi.

Dereva yule akaondoka zake na mteja mpya, akimuacha Dr.Pesambili kwenye mataa asijue la kufanya. Akaanza kutembea kwa miguu barabarani akipasua mitaa kuelekea katikati ya Jiji huku akitafakari kitu cha kufanya akifika huko Mjini. Kwa upande wake maji yalishazidi unga, hajui hata cha kufanya huku uoga ukimtawala kuwa kama hiyo Klabu ni kweli haipo basi kumpata Mlinzi wa Klabu aliyemuokota itakuwa ni kama kamari ya kumtafuta mwanamke bikira ndani ya wodi ya wazazi. Alishaanza kukata tamaa kama kweli atafanikiwa kuipata asili ya wazazi wake. Dr.Pesambili alikuwa anauchapa wa fisi katika mitaa ya Jiji la Nairobi hataki taksi wala nini, kuanzia mitaa ya Moi Avenue, Tom Mboya, Kimathi, Biashara na kwingineko kote aliivuruga akiulizia kila anayekutana nae kuhusu Nairobee BY Night Club, lakini hakuwa anapata ushirikiano wowote. Katika Jiji la Nairobi kila mtu alikuwa anajali hamsini zake, watu wake sio marafiki kama walivyo Watanzania.

Harakati zake hizo zikamfanya atiliwe mashaka na na kuanza kumulikwa na vyombo vya Dola bila yeye mwenyewe kufahamu. Kenya ilikuwa imetoka kwenye Uchaguzi Mkuu wa tarehe 27/12/2002, uchaguzi ambao ulimuingiza madarakani Rais mpya Mheshimiwa Mwai Kibaki kupitia chama cha "National Rainbow Coalition (NARC)". Uchaguzi ambao ulishuhudia anguko la chama kikongwe barani Afrika cha "Kenya African National Union" (KANU) kilichokuwa madarakani tokea nchi ya Kenya kupata Uhuru mwaka 1963. Kwa kuwa siasa za Kenya zilikuwa zimetawaliwa na ukabila, wapo waliokuwa hawapendi nchi itawaliwe na Mheshimiwa Mwai Kibaki toka kabila kubwa la Kikuyu, kabila ambalo lilikuwa linapendelewa tokea enzi za utawala wa Mkoloni hivyo kulikuwa na tetesi za watu wa makabila madogo madogo kama Luhya, Luo, Kalenjin, Kamba, Kisii na mengineyo kuwa na mikakati ya kujipanga upya kuhakikisha wanachukua madaraka kwa njia ya kufa au kupona katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2007. Hivyo katika kutaka kulidhibiti jambo hilo lisitokee mashushushu walikuwa wamemwaga mitaani kama utitiri kunusanusa njama zozote za wahalifu wenye nia ya kuleta machafuko nchini Kenya.

Dr.Pesambili akiwa amejipumzisha kwenye Mkahawa mmoja wapo uliopo Jijini Nairobi anapoza koo kwa kupata soda baridi ili aendelee na harakati zake, akastukia anawekwa chini ya ulinzi mkali na maaskari kanzu lukuki. Alipofanyiwa taftishi ya kutosha na kutakiwa aonyeshe hati yake ya kusafiria na nyaraka zingine Nyeri akajikuta hanayo hata moja. Kijasho chembamba kilimvuja juu ya paji lake la uso kwa hofu kubwa. Kumbe alidondosha baadhi ya nyaraka zake kule kwenye kituo cha watoto Yatima alipotoka cha Cheryls Childrens Home and Learning Centre". Alipoteza nyaraka hizo akiwa katika harakati za kujumuika nao watoto yatima katika shughuli mbalimbali za kupiga nao picha, kupata nao maakuli ya pamoja na nyinginezo. Mashushushu wale kusikia hana nyaraka zozote halali, yupo yupo tu wakageuka mbogo dhidi yake na kumgombania mithili ya mpira wa kona, tayari wameshamhisi ni mtu hatari kwa usalama wa nchi ya Kenya.

Dhana zao ziliwatuma kuwa ni mmoja wa mamluki toka Mataifa kibeberu ya Ughaibuni aliyetumwa kupandikiza chokochoko nchini Kenya. Akiwa anashangaa hajui kinachoendelea dhidi yake akastukia anavikwa pingu mikononi na kufunikwa na mfuko mweusi usoni kisha akatupwa kwenye gari na kupelekwa kusipojulikana. Njia nzima alikuwa anapokea kichapo kitakatifu cha mbwa mwizi huku anahojiwa kwa kuulizwa alichokuja hasa kukifanya nchini Kenya akitokea huko kwao Italia. Walipoona hana chochote cha maana anachokiongea wakaacha kumtesa, Dr.Pesambili akasikia tu wanaongelea kuhusu "Shimo la Tewa".

Dr.Pesambili alijawa na hofu furifuri moyoni mwake hajui wapi anapopelekwa, hasa akichukulia amekuja nchini Kenya kwa amani kabisa, yeye wala sio mhalifu kwenye maisha yake hajawahi hata kumwaga damu ya mdudu mdogo kama mbu sembuse mwanadamu.

Mbweku Jr alipozinduka alijikuta yupo wodini ndani ya gereza la Segerea. Gereza hilo la mahabusu lilikuwa ni gereza ambalo watuhumiwa wengi hawapendi wapelekwe huko. Walikuwa wanakufananisha na Jahanamu kutokana na shida na madhira yanayopatikana huko. Wale watuhumiwa wenye nguvu ya kipato walikuwa wanahangaika huku na kule kwa njia za panya na kupenyeza mlungula kwa Maafisa wasio waadilifu ili mradi ndugu zao wapelekwe gereza la Keko lakini sio Segerea. Segerea kipindi hicho Mbweku Jr ametupwa huko, kulikuwa na shida ya maji balaa. Hali ambayo ilisababisha mahabusu waugue magonjwa ya ngozi maarufu kwa jina la 'burudani'.

Pia Segerea kulikuwa na msongamano wa mahabusu wa kutisha, gereza lilikuwa na uwezo wa kuhifadhi watu takribani 750 lakini kuwa wakati walikuwa wanafurika mahabusu zaidi ya 2,000 hali iliyokuwa inapelekea mahabusu kulala watatu watatu kwenye godoro moja kwa mtindo wa "mchongoma". Mtindo ambao ulimtaka mtuhumiwa kila baada ya masaa matatu kupita ndio anaruhusiwa kujigeuza kitandani kulalia ubavu mwingine.

Jambo la yeye kutupwa Segerea lilimpa mashaka makubwa Mbweku Jr kama kweli rafiki yake Timammy wapo pamoja na yeye kwenye shida na raha. Alitegemea Timammy kwa umaarufu wake alionao ahangaike juu chini ili apelekwe gereza lenye nafuu kidogo, lakini aliona kama ametelekezwa. Kingine kilichomsikitisha ni kitendo cha kutoletewa huduma zozote za kibinadamu na Timammy kipindi chote cha msoto akiwa gerezani. Mahabusu alikuwa anaruhusiwa kuletewa chakula na bidhaa mbalimbali kama sabuni, dawa ya meno, na miswaki lakini tokea atupwe Segerea hakuona hata mche mdogo tu wa sabuni ya kufulia unaouzwa Sh.1,000/= uliotoka kwa rafiki yake Timammy wakati yeye Mbweku Jr alikuwa anaamini ana hisa kibao tu katika utajiri anaomiliki Timammy.

Mbweku Jr akatumia busara na hekima, hakutaka kumhukumu moja kwa moja rafiki yake kuwa amemfungia vioo ametupa jongoo na mti wake, akampa udhuru kuwa huenda ametingwa na majambo mbalimbali ya harakati za kimaisha anaziweka sawa kwanza kisha atamrudia yeye. Baada ya wiki kadhaa kuyoyoma akaanza kuyazoea maisha ya jela. Maisha ya kuamka na kula kwa filimbi, unakula unachopewa na sio unachokitaka. Unafungiwa selo kulala kwa amri ya Afisa magereza hata kama hauna usingizi. Ikabaki kazi ya kupelekwa mahakamani na kurudishwa mahabusu wakati kesi yake ikitajwa na kupangiwa tarehe.
.

Kilichomshtua Mbweku Jr na kujua kuwa hawapo pamoja na Timammy ni kitendo cha kushindwa hata kumuwekea Wakili wa kumtetea mahakamani, mpaka serikali ikampatia Wakili wa kumtetea. "Hisia zangu kutoka kwenye sakafu ya mtima wangu wa moyo sasa zinanituma Timammy, rafiki yangu kipenzi hanitaki tena nirudi uraiani, na huenda yeye ndio amenichomea utambi pale Mahakamani kwa Hakimu kuhusu kesi hii ninayohangaishwa nayo siku tumeonana na nikamuomba anilipie faini. Ama kweli duniani wewe tenda wema nenda zako usingoje shukrani, na fadhila ya punda ni mateke daima dawamu...!" aliwaza kwa hasira Mbweku Jr huku amekunja ndita kwenye paji lake la uso anapigapiga ngumi zake nzito kwenye kiwambaza cha selo. Akaanza kukumbukia siku aliyomkabidhi burungutu sufufu la fedha za kigeni Timammy, alizopora kwenye gari ya Bosi Recho . Ngwenje ambazo zimempa heshima Timammy kutoka mtu asiyejulikana mpaka kuwa mtu mahashumu katika Nchi, akiongea kila mtu anamtetemekea.

Kwa kuwa alikuwa hana jinsi ya kufanya, akafunika kombe mwanaharamu apite kwa kunyanyua mikono juu na kumshukuru Jalia kwa yote yaliyomfika huku akisubiri hatima yake ya hukumu atakayopewa. Baada msoto wa takribani mwaka mmoja na nusu gerezani wa kupigwa danadana kesi yake, sasa ikaanza kusikilizwa. Hapo ndipo likaibuka zengwe jipya kabisa lililozidi kumkata maini na kumtibua nyongo, Mbweku Jr. Mawakili tofauti wanaomtetea yeye wakaanza wimbi la kujitoa kumtetea bila kutoa sababu zenye mashiko mbele ya Mheshimiwa Jaji. Jambo ambalo lilimfikirisha vilivyo Mbweku Jr akitaka haswa kujua kindakindaki sababu za hao Mawakili kumkacha bila mafanikio.

Mungu si Athumani, ndipo mmoja wa Wakili wake wa mwisho kujitoa alipojivika mabomu na kumpasulia ukweli bayana, kinagaubaga bora bila kupepesa macho kuwa wanashinikizwa na tajiri Timammy wajitoe kwenye kesi kwa tishio la hata kupotezwa uhai wao kama wakijifanya vichwa ngumu. Hapo sasa Mbweku Jr ndipo alipoyakinisha kweli isiyo na chembe ya mashaka kuwa kikulacho ki nguoni mwako, na Timammy kweli ni zaidi ya Ibilisi adui nnasi kwa ususi wa vitimbi na vibweka vyake dhidi yake mtawalia visivyo na ukomo.

" Natangaza vita yenye kishindo kikuu na Timammy, nitatoroka gerezani kwa mbinu yoyote ile, nikimpata ama zake ama zangu, lazima nimuonyeshe cha mtema kuni, nimtie adabu mpaka akijue kilichomtoa kanga manyoya...! " alikula yamini ya moyo Mbweku Jr huku mishipa ya shingo imemsimama dede kwa hasira dhidi ya Timammy. Kiapo hicho kiliashiria kuvunjika rasmi kwa usuhuba baina yao uliodumu kwa miaka kadhaa tokea wakiwa maskani kule Kigamboni, na sasa Mbweku Jr alimtangaza Timammy ndani ya serikali yake ya moyo kuwa ni hasimu wake namba moja. "Nitamuangamiza Timammy na uzao wake wote, sitobakisha mbwa yoyote mwenye mafungamano nae, dawa ya moto ni moto na daima wapambanapo mafahali wawili ziumiazo ni nyasi, mie sitolijali hilo" alizidi Mbweku Jr kula yamini ya moyoni akiwa peke yake juu ya godoro amejipumzisha mchana mmoja wapo ndani ya gereza hilo la Segerea.

Lakini Timammy nae hakuwa zumbukuku ulimwengu upo huku, alikuwa anamjua fika rafiki yake Mbweku Jr ni mtata haswa hawezi kukubali kuishia gerezani, lazima atalala mbele akiona giza limezidi mbele yake hamna mapambazuko. Na kama akifanikiwa kuchoropoka kuja uraiani patakuwa hapakaliki, lazima pachimbike hivyo nae alijipanga kwa mbinu madhubuti za Kimafia kumuangamiza Mbweku Jr huko huko akiwa gerezani. Hivyo ngoma ikawa droo, mchuzi moto ugali moto, Mbweku Jr anawindwa bila mwenyewe kung'amua kuwa roho yake imewekwa rehani, Timammy ameipandia dau.


Siku moja ilipofika majira ya magharibi, mahabusu wote wakiwa tayari wameshakula mlo wa chajio na wameshafungiwa ndani ya selo kikasikika kishindo kikubwa cha mlipuko kama wa bomu kisha umeme ukazimika gereza zima, likageuka giza totoro. Kilikuwa ni kishindo cha mlipuko wa transfoma linalohusika na kusambaza umeme maeneo ya Segerea karibia na gereza na maeneo ya jirani. Mpaka giza likawa limeanza kutamalaki mawinguni, umeme ukawa bado haujarudishwa na TANESCO, hali iliyojulisha kuwa hitilafu ya umeme iliyotokea ni kabambe isiyo ya kitoto.

Ghafla tu Mbweku Jr akajikuta amebanwa na haja ndogo anahitaji kutabawali kwa haraka sana ili kibofu chake cha mkojo kipate unafuu kwa kutoa uchafu mwilini. Akajizoa toka kwenye godoro lake la ulimi wa ng'ombe alilokuwa amebahatika kulala peke yake na kushika uelekeo wa msalani. Akaambaa na korido mpaka akajitokeza kwenye eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya vyoo na mabafu lililopo ndani ya Selo hiyo hiyo. Wakati anazidi kwenda mbele akiwa gizani, machale yakaanza kumcheza Mbweku Jr, nywele zake zikaanza kumsisimuka, vinyweleo vya nywele ya ngozi yake vikamsimama dede, akageuka nyuma yake kuangalia kama kuna mtu anamfuatilia ili apate kuchukua tahadhari mapema. Akahisi kama kuna mtu amejificha nyuma ya moja ya tanki kubwa la kuhifadhia maji alilolipita nyuma yake baada tu ya yeye kugeuka nyuma.

Mbweku Jr akazidi kupatwa na ushawishi wa kutaka kumjua ni nani anayemfuatilia kizani kwa kutumia mwangaza wa mbalamwezi. Tayari damu ilianza kumchemka mwilini, mikono yake ikimchezacheza akipandwa shauku ya kutaka kumvunja mtu. Akamgeuzia mgongo adui na kuanza kuchanganya mwendo huku mkono wake wa kushoto umekamatia juu ya suruali kwenye maeneo ya sehemu za siri kujionyesha amezidiwa na mkojo, akakunja kulia kuelekea kwenye vyoo akiyaacha mabafu yakiwa yamejipanga upande wa kushoto kwake. Akapishana na mtu mmoja tu aliyekuwa anatokeza upande wa vyooni, Mbweku Jr akainamisha sura yake asijulikane, alishapanga kumshikisha adabu huyo mjuba anayemfuatilia.

Alipokata tu upande wa kulia mbele yake kulikuwa na pipa la plastiki la kuhifadhia maji ya kujitawadhia pindi ukiwa chooni. Mbweku Jr kama umeme akajitumbukiza ndani ya pipa hilo lililokuwa na maji robo kwa mtindo wa kupiga mbizi, huku akiacha kichwa tu kikiwa kinaelea juu juu. Baada ya muda wa nusu dakika akasikia vishindo vya miguu ya yule jamaa anakuja wangu wangu bila kuchukua tahadhari yoyote akasimama jirani kabisa na pipa lile la maji anaangaza usalama wake kabla hajavamia vyooni kumsaka Mbweku Jr. Mbweku Jr kama mzimu vile akaibuka kutoka kwenye pipa la maji akiwa nyuma ya mgongo wa yule jambazi kisha akajikohoza kidogo, yule jamaa mkononi akiwa ameshika bastola akageuka nyuma, macho yakamtoka kama mjusi aliyebanwa na mlango. Alishikwa na kihoro akiwa haamini kama ameingizwa mkenge kwenye mtego wa Mbweku Jr kaingia mzima mzima.

Mbweku Jr bila kuchelewesha habari, akajirusha mzima mzima kama samaki mkizi akitokea kwenye pipa na kumkumba yule mjuba wote wakaanguka sakafuni kwa mlio wa pwataaaaah. Kikiri kakara ikaanza baina yao wakiviringishana mieleka wakipimana nguvu ya ugali. Bastola ikawa imemponyoka mkononi na kuangukia meta kadhaa kutoka walipokuwa wanapimana ubavu. Wote wakanyanyuka kwa pamoja toka sakafuni na kuanza mtifuano mkali wa kukata na shoka baina yao. Mbweku Jr akawa anavurumisha mvua ya makonde kadhaa lakini yakawa yanayeyukia hewani, yanashindwa kumlenga sawa sawa adui yake, dalili za kukosa umakini kutokana na kuacha mazoezi kwa muda mrefu.

Mbweku Jr akajikuta kibao kinamgeukia yeye anaanza kuchakazwa ngumi mfululizo za usoni. Ndani ya muda mchache tu tayari alishapasuliwa chini ya jicho la kushoto. Akazuga kama amezidiwa na kipigo kile kumbe hamna mtu sugu duniani kama yeye. Vile amejiinamia chini yule adui akaanza kuelekea ilipo bastola yake akiifuata ili aje ammalize Mbweku Jr akiwa amempa kisogo Mbweku Jr. Hilo likawa ni kosa kubwa kwake la kufungia uhai wake, Mbweku Jr alijirusha hewani kama chui anayevizia mawindo yake na kumkaba shingo yake kwa nguvu kisha bila ajizi akaizungusha na kunyonga hapo hapo. Yule jamaa akapoteza uhai wa wake pale pale bila hata kuomba maji ya kunywa ya kupunguzia uchungu wa sakarati mauti wakati Malaika wa kifo anapochomoa roho ya mtu.

Himahima akaanza kumfanyia speksheni mwilini, kwenye suruali yake yule mjuba akakutana na vipisi visivyo idadi vya sigara bwege maarufu kwa jina la bangi pamoja na kikaratasi kidogo cheupe. Akamchomolea simu yake mfukoni yule adui kwa msaada wa mwangaza wa tochi ya simu akaanza kukisoma kile kikaratasi. Akabakia amepigwa na mzumbao wa sekunde kadhaa baada ya kusoma ujumbe ulioandikwa kwenye kikaratasi kile. Kilikuwa kinasomeka kama ifuatavyo;
"MBWEKU JR SELO NO. 06". Akakifinyanga kikaratasi hicho na kukitupia kwenye shimo la choo. Mbweku Jr haraka haraka bila kulaza damu akamburuza adui yule mpaka kwenye moja ya vyoo na kumfungia humo akiwa amemkamatisha kabisa bastola yake kukamilisha ushahidi. Baada ya hapo akajisaidia zake na kujiweka sawa kwa kuosha eneo lenye mpasuko usoni mwake kabla hajarejea selo kwa kutumia msaada wa nuru ya mwezi.

Akashukuru Mungu kwa kuwa hamna mtu hata mmoja aliyeshuhudia tukio lile la mauaji alilolifanya. Akarudi zake Selo kulala huku akisubiria mapambazuko yafike ili mbivu na mbichi za mhusika zijulikane. Usiku mzima Mbweku Jr alilala usingizi wa mang'amung'amu, anaweweseka kutokana na mpambano wake na mjuba yule aliyekosa chembe ya junaya mpaka anamfuata na bastola jela. Mbweku Jr alikuwa anawaza huyu adui yake aliyemuua muda mfupi uliopita katumwa na nani na kwa maslahi gani. Kilichokuwa kinambangua kichwa zaidi ni kitendo cha huyo adui kufanikiwa kuingia jela tena akiwa na silaha ya moto. Akajikuta anajisumbua bure kujifikirisha bila kupata majibu ya haraka kwenye maswali anayojiuliza.


"Tabia ya ukweli huwa haujifichi, hata kama ukiufunika ipo siku utajiweka uchi hadharani, adui yangu anashirikiana na baadhi ya Maafisa magereza wasio waaminifu kutaka kuniangamiza...!" aliwaza Mbweku Jr akijipa moyo wa kumfahamu mtu aliyemtuma mapema iwezekanavyo. Huyu jambazi alikua ni mtu wa pili kuuliwa na Mbweku Jr katika maisha yake, wa kwanza akiwa ni Kibopa Mfanyabiashara wa kiarabu wa Kariakoo, Bwana Mwinyi Fuad aliyetaka kumlawiti kinguvu wakati yupo chokoraa mtaani.
Kulipokucha tu tayari habari za kifo cha yule mtu zilisambaa kama upepo. Kilichowashangaza watu ni namna alivyoingia gerezani chini ya ulinzi mkali hali ya kuwa sio mahabusu. Ikagundulika kuwa askari magereza wawili waliokuwa lindoni usiku wametoweka, hawajulikani walipo. Hivyo dhana za Mbweku Jr dhidi ya Maofisa wa Magereza hazikuangukia patupu. Askari Magereza walitoroka baada ya kula njama na Timammy za kumuingiza mhalifu ndani ya gereza, hivyo njama zao zilivyofeli ikabidi walale mbele kukwepa mkono mrefu wa sheria.

Timu ya wapelelezi toka polisi makao makuu wakiwa na wapelelezi bobezi wakatua gerezani kuchunguza lengo la mhalifu huyo kuingia gerezani. Baada ya uchunguzi wao ikaonekana mhalifu huyo ameuliwa na mmoja wa mahabusu baada ya kuzidiwa nguvu katika kujitetea zake. Msako kabambe wa mule mule ndani ya gereza ukaanza wa kumtafuta mahabusu aliyehusika na mauaji hayo. Mpaka giza linazama walishindwa kumbaini mhusika zaidi ya mahabusu kadhaa kutiliwa mashaka akiwemo Mbweku Jr kutokana na majeraha aliyokutwa nayo. Ikatolewa amri mahabusu hao wahamishwe, kupelekwa kwenye magereza mengine. Ndipo Mbweku Jr akahamishiwa usiku usiku katika gereza la Ukonga. Moyoni Mbweku Jr kusikia anapelekwa Ukonga alijawa na furaha fokofoko isiyoelezeka. Furaha yake ilitokana na mchanyato wa mambo mengi, ikiwemo mazingira mazuri ya kuishi na uwezekano wa yeye kutoroka gerezani na kurejea mtaani. Sala na dua zake alikuwa anaombea kila kitu kiende anavyotegemea iwe. Pia pale Segerea alikuwa amejitahidi kutafuta penyenye za baba yake mzazi aliyemuacha gereza la Ukonga kabla hajazamia nchini Afrika ya Kusini lakini hakuambulia kitu. Hivyo huko Ukonga akategemea huenda atapata habari hizo anazozisaka.

Timammy safari hii hakutaka kufanya makosa ya kiufundi kabisa, alipanga kufa au kupona lazima amuoe Deborah. Aliamua kumtengeneza kwa kutumia kamati ya ufundi. Lengo lake namba moja lilikuwa ni kumuachisha Chuo moja kwa moja abakie nyumbani ili iwe rahisi kumuoa. Alijua akimpa sera za kumuachisha Chuo, itakuwa ni kumtafuta muhali Deborah hivyo lazima ajiongeze kwa kutumiwa uchawi ili aache chuo apende au asipende. Akaamua kumuendea kwa Mganga, gwiji wa ulozi ajulikanaye kama Bi.Havijawa. Huyu Bibi alikuwa anaishi katika kisiwa cha Kwale. Kwale ni kisiwa kidogo katika Bahari Hindi mbele ya pwani ya Tanzania upande wa kaskazini wa delta ya mto Rufiji. Kisiwa hicho ni sehemu ya kata ya Kisiju kwenye wilaya ya Mkuranga katika Mkoa wa Pwani.


Kwale imetambuliwa na wataalamu wa akiolojia kuwa kati ya vituo vya awali vya biashara ya pwani iliyokuwa chanzo cha utamaduni wa Uswahilini. Kwa hiyo mambo yote ya kiswahili swahili unayoyajua wewe na usiyoyajua huko ndio chimbuko lake. Yale sijui masuala ya mtu kugeuzwa paka, kujaza tumbo la mwizi wako kwa kutumia pampu ya baiskeli mpaka tumbo lake linamaanisha huko yalikuwa mambo madogo sana. Bi. Havijawa utaalamu alirithishwa na Baba yake mzazi.

Baba yake alivuma sana siku alivyoaga dunia, ndio watu wengi nchini Tanzania walimfahamu. Inasemekana kuna Shambaboi mmoja wa shamba la mzungu huko Rufiji alituhumiwa kesi ya ubakaji enzi za Mkoloni. Baba mzazi wa Bi.Havijawa akamfanyia dawa ya kumgeuza jinsia yule mtuhumiwa. Mahakamani Hakimu akamuachia huru mtuhumiwa baada ya kuthibitika pasina mashaka kuwa ni mwanamke hivyo hana uwezo wa kubaka kutokana na jinsia yake. Furaha ya mtuhumiwa huyo wa kiume aliyegeuzwa jike ilimtumbukia jongo baada ya kutoka Mahakamani na kuelekea moja kwa moja kwenye Kisiwa cha Kwale na kupishana na jeneza la mganga wake, baba yake Bi.Havijawa akipelekwa makaburini. Ikabidi amwage kilio cha karne na kutoboa siri baina yake na marehemu Mganga kuwa amempa jinsia ya kike nae anataka arudishie jinsia yake ya kiume. Hivyo sasa mikoba yote ya Uganga alikuwa ameachiwa Bi.Havijawa, Mapredeshee na Viongozi mbalimbali walikuwa wanamiminika Kisiju kwa Bi.Havijawa.

Timammy akapeleka jina la Deborah na la mama yake mzazi Deborah kwa Bi. Havijawa, akamfunga vilivyo kwa makafara ya kishetani na kumpa ahadi ya kuwa Chuo ndio kwaheri Deborah hatosoma tena.
Timammy akajitutumua kifaurongo kujitia kumlipia ada ya Chuo na pesa ya matumizi Deborah hali ya kuwa anamnanga kisogoni, akijua kabisa ya kuwa Chuo ndio kwaheri kwa Deborah. Aliporudi chuoni Deborah akaanza kukumbana na mauzauza ya kuogofya na kutisha Anatoka zake hosteli vizuri salama salimini lakini kosa lake akiingia tu darasani. Macho yake yanakosa nuru kabisa anakuwa mpofu na kiziwi kabisa. Akitolewa nje ya darasa mzima kabisa hana shida yoyote. Timammy alipoletewa mashtaka hayo na Deborah akajitia kuzunguka nae mahospitalini mpaka Nairobi wakafika, lakini kila aliporudi Chuo mambo yakawa yanabaki vile vile salama ya balawa. Ndipo Deborah rasmi akasalimu amri na kuacha Chuo.

Sasa ndio ikawa nafasi rasmi ya Timammy kutupa ndoano yake, ambayo bila ajizi ikamnasa mzima mzima Deborah. Ilikuwa ni ngumu kwa Deborah kumkataa tena Timammy hasa ukichukulia wema aliomtendea usio na kifani. Deborah alianza kupima tokea kulipiwa ada ya kwanza ya kuanza elimu ya sekondari, kuokolewa na kifungo cha jela kilichotaka kumkumba kutoka kwa Mrs.Tonny, na kulipiwa ada na kupewa hifadhi pindi ambapo mpenzi wake Alex alipotiwa ndani kwa tuhuma za kuomba rushwa ya ngono. Pia Timammy akamlipia gharama za Chuo Kikuu na bila kuchoka kazunguka nae kwenye tiba ya macho bara na visiwani mpaka Jijini Nairobi. Hakuona fadhila ya kumlipa Timammy zaidi ya kumkubalia matakwa yake.

Timammy akawa na furaha sheshe iliyopitiliza mipaka kutokana na kufanikiwa kumtia katika milki yake Deborah. Timammy roho yake ilikuwa imesuuzika vilivyo, akatokea kumtunuku chochote anachokihitaji Deborah. Sasa Deborah akageuka kuwa mwanamke tajiri 'BossLaddy' akishirikishwa kwa ukaribu katika biashara zote za Timammy kiufasaha. Katika kukata kiu yake ya kielimu aliyoshindwa kuipata Chuo Kikuu cha Dar es Saalam akajiunga na Chuo Kikuu Huria 'Open University of Tanzania' akawa anajisomea akiwa nyumbani. Katika harakati zao za kujivinjari penzi lao jipya, Deborah akajishtukia amenasa ujauzito. Ikabidi harakati za kufunga ndoa baina yao zianze kusukwa.

Timammy akamshinikiza Deborah kuwa lazima abadili dini yake ili wafunge ndoa ya Kiislamu. Baada ya mvutano wa hapa na pale na hasa ukichukulia Timammy ndio alishika mpini huku Deborah akiwa ameshika makali, ikabidi abadili dini kwa shingo upande ili mradi tu ndoa ipite. Moyo wa mwanadamu umeumbwa kumpenda yule mwenye kuutendea wema, kutokana na wema alioufanya Timammy kwa Deborah alishafanikiwa kuuteka moyo wa Deborah vilivyo. Kila alichokuwa anakiamrisha Timammy kinatekelezwa kama kumsukuma mlevi vile. Timammy aljiona amekuwa jabali wa maisha kayapatia vilivyo kwa kumzidi kete adui yake namba moja kwa sasa ambaye ni Mbweku Jr.


Siku moja asubuhi Timammy akiwa yupo nyumbani amejipumzisha, anasubiria kupata habari tamu kupitiliza kwa njia ya simu ili ajihakikishie kuishi maisha ya raha mustarehe na Deborah wake bila bughudha ya mtu yoyote, akajikuta anapigwa simu yenye maudhui ya kukera. "Hellow...Hellow...Bosi Bosi mambo sio mazuri, kijana tuliyemtuma gerezani akammalize Mbweku Jr amezidiwa nguvu kauliwa na Mbweku Jr. Hapa sasa kuna hekaheka za kuwahamisha baadhi ya wafungwa ili watawanywe magereza tofauti, na Mbweku Jr yupo katika orodha ya wafungwa hao, nitakujuza anapelekwa wapi kwaheri...!" taarifa ilitoka kwa mmoja wa askari magereza mshirika wa Bosi Timammy akimpa taarifa ya tukio zima.

Taarifa hiyo ikamsababishia shinikizo la damu Bosi Timammy na kupelekea kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya huduma ya kwanza. Alishaanza kukihofia kivuli cha Mbweku Jr, alishamuona ameshindikana kuuliwa kwa njia za kawaida.

SURA YA KUMI NA TISA
Dr.Pesambili alikuja kutupwa katika gereza linaloitwa Shimo la Tewa lililopo Mjini Mombasa, Kenya. Hili lilikuwa ni moja ya gereza linalotumika kuhifadhia magaidi tokea milipuko ya Balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania. Alipowasili hapo na kuvuliwa mfuko mweusi usoni alijaribu kuyazungusha macho yake kama dira kuangalia mandhari isiyovutia ya gereza lile. Baada ya kupokelewa tu, wakamtupia ndani ya selo kwa mtindo wa varange kama mnyang'anyi vile.

Selo hiyo iliyokuwa haipitishi mwangaza wa kutosha, alifungiwa kwa muda wa siku mbili mtawalia bila kutolewa nje. Selo ambayo sakafu yake ilikuwa ya mchanga yabisi kama ardhi ya jangwani. Riha mbaya ya mikojo na vinyesi ilisikika ndani ya selo ile dalili za kuonyesha unajisaidia mume mule ndani. Harufu ile ilimchefua chefu chefu na kumkoroga tumbo lake na kusababisha aanze kutapika bila breki. Paa lake lilikuwa ni refu sana, lililopambwa na utando wa nyumba za buibui, pamoja na ukoko wa kutosha wa vumbi.

Panya walikuwa wanakimbizana kwenye mbao za paa utasema wapo kwenye mashindano fulani. Selo ile ilikuwa na vidirisha vidogo sana, vilivyo juu na kupitisha mwangaza wa jua hafifu. kuonyesha Chakula chake pia kilikuwa cha kudonoa, akipewa kombe la uji asubuhi, uji ambao haina chumvi wala sukari anapewa mlo wa mwingine wa aina ya kipara cha babu chafuka moshi kwa kutowezea maharage mabovu saa 9 alasiri hiyo ndio nitolee mpaka kesho yake. Maharage hayo hayana dawa ya mboga wala hayajaungwa na kitunguu.

Alishikwa na msongo mkubwa wa mawazo hatima yake itakuwaje, Akianza kujiona yu kama mfu. Alitamani abebwe na kwenda kutupwa kwenye mtungi usioisha maji, huko akaliwe na samaki wakubwa kama papa na nyangumi iwe mwisho ya maisha yake ya ulimwenguni. Alitamani mfukoni awe na zile njiti ambazo ukikuna kichwa chake tu kinakupa moto aweze kuunguza selo yote iwe hadithi tena.

Kwa hali mbaya ya gereza lile alianza kuomba Mungu asiwekwe muda mrefu, vinginevyo ataanza kucheza gitaa bila kuujua wimbo wenyewe, kutokana na kupatwa na ukurutu wa ngozi. Alishangazwa sana na ufanyaji kazi wa Wanausalama wa nchi za Kiafrika kwa kutanguliza mateso kwanza kabla ya kujihakikishia kuwa huyo mtu ni mhalifu. Wanausalama hao walikuwa na nafasi ya kujiridhisha usahihi wa taarifa kupitia Ubalozi wa Italia nchini Kenya kwa sababu Dr.Pesambili alikuwa ni raia wa Italia. Matumaini yake pekee yalibakia kwa Bwana Joram Peter Ochieng Mkurugenzi wa kituo cha kulelea yatima cha Cheryls Childrens Home and Learning Centre alipopoteza nyaraka zake muhimu. Alitumaini huenda atazichukua nyaraka hizo na kuzipeleka polisi ili mwenye nazo atafutwe.

Siku zote mbili alikuwa hajafanyiwa mahojiano yoyote zaidi ya kula na kulala tu. Ilipofika siku ya tatu alfajiri na mapema akaja kutolewa kule selo, wakamfungua pingu alizofungwa miguuni na mikononi, kisha akapewa kifungua kinywa cha kutosha tu, chai ya mkandaa iliyojazwa fori fori kwenye kikombe cha plastiki na nusu mkate uliopakwa siagi. Dr.Pesambili akaanza kukibwakia bwaku kile chakula utasema anaishi kwenye kambi za wakimbizi kwenye shida ya chakula.

Aliona miujiza imemtembelea, watu ambao wenye roho za kishetani kwa zaidi ya siku tatu wanampa mateso shadidi bila sababu yoyote kisha ghafla bin vuu tu wanabadilisha gia angani na kujigeuza kuwa malaika, wanaanza kumtendea wema. Baada ya kumaliza kula akaletewa maji ya kuoga yaliyochemshwa chem chem na bwerasuti za michezo mpya za kubadilisha. Huko bafuni wakati anaoga ilibidi awe anajishikiza ukutani, vinginevyo Parr! mpaka Makka! na meno unavunja kutokana kubingirika bingiri bingiri bingiri na sakafuni. Weusi ulitanda ukutani na chini kutokana na uchafu uliorundikana kwa miongo kadhaa. Maji machafu bafuni kule yalikuwa yanachiririka chiriri chiriri, yakisambaa kila kona ya jengo.

Hofu ikaanza kumtawala moyoni mwake Dr.Pesambili kutokana na wema anaotendewa kwa ghafla tena bila kupewa maelezo yoyote. Alishawahi kusomaga taarifa za nchi za Afrika namna zinavyowajali wafungwa wanaotaka kunyongwa kwa kuwapikia chakula kizuri ili kuwaondosha mawazo. Sasa aliona hiyo hali ndio kama inataka kumtokea yeye ya kufanywa kama jogoo, mchana analishwa mchele, jioni anachinjwa cha kisha analiwa kwenye wali mezani.

"Ondoa hofu kijana tunakupeleka kwa Mkuu wa Polisi, Kaunti ya Mombasa, yeye ndio ataamua hatima yako kama kukuachia huru au kutupa amri tuendelee kukushikiria" aliongea mmoja wa askari wale waliofanana kwa sare zao na maumbile mfano wa njiti za kiberiti. Alipofikishwa mbele ya Mkuu yule mambo yakajipa, akaachiwa huru bila masharti yoyote huku akisindikizwa kwa msafara wa polisi mpaka alipofikia. Yule Mkuu wa Polisi, alikuwa Mzee mtu mzima, rangi ya nywele zake kichwani utasema amejitwika machicha ya nazi, anayesubiria miezi michache tu kustaafu utumishi wake wa umma. Shamba lake la meno kinywani mwake lilianza kukauka halitoi matunda, kutokana na mapengo dalili ya kuelekea kuwa kibogoyo miaka michache ijayo.

Mkuu huyo kabla ya kuhamishiwa Mombasa alikuwa anafanya kazi Jijini Nairobi kwa miaka mingi. Hivyo aliposoma maelezo ya Dr.Pesambili akavutiwa kuonana nae kutokana na maelezo yake kuonyesha kuwa baba yake mzazi Dr.Pesambili, Mr.Martin Tenga alikuwa ni rafiki yake miaka hiyo. Huyu ndio polisi ambaye alimfukuza Recho, mama yake Dr.Pesambili kwa mbinu chafu akishirikiana na Mr.Martin Tenga ili wapore mali zake zilizopo Jijini Nairobi. "Mama yako ni Mchaga, raia wa Tanzania, aliondoka Kenya miaka mingi sana. Alikuwa anatokea Mkoa wa Arusha au Kilimanjaro sikumbuki vizuri sana, na kabla ya kuja Jijini Nairobi aliwahi kuajiriwa kwenye Shirika moja linaitwa Peace-Corps Tanzania ", maelezo hayo ya Mkuu yule wa polisi, yalikuwa ni kama dawa inayotibu maradhi yake yote ya msongo wa mawazo wa kumkosa mama yake.

Akaamini maneno ya wahenga ya kuwa tumbo la shari huzaa heri, akawashukuru sana kimoyomoyo Askari Kanzu waliomkamata mtaani kule Jijini Nairobi. Kutokana na shari yao ya kumkamata imemlaimishia njia ya kufahamu sehemu alipo mama yake kiurahisi kabisa. Bila kupoteza muda baada ya kufikishwa Jijini Nairobi akarejea kule kwenye kituo cha watoto yatima kufuata nyaraka zake. Kwa bahati nzuri alikuta wamezihifadhi sehemu salama huwa wakiwa na matarajio kuwa lazima atarudi tena kuzifuata nyaraka zake hizo.

Siku ya pili yake tu akakwea pipa kurejea zake Jijini Dar es Salaam tayari kwa kujipanga upya kuanza msako rasmi dhidi ya mama yake mzazi. Aliyaona gerezani kule Shimo la Tewa alipewa onyo ayafutike futi moyoni mwake asimsimulie mtu, vinginevyo atajikuta matatizoni. Maana hamna aliyeingizwa humo akatoka salama salimini, ni yeye tu alipata bahati ya mtende kuota jangwani.

Aliporejea Jijini Dar es Salaam, Dr.Pesambili akajikuta anafuraha mbili bila kutarajia. Alimkuta mama Deborah ambaye anaishi nae chini ya paa moja, afya yake imeimarika vilivyo kuliko kawaida. Pia alishaanza kurudisha kumbukumbu zake kichwani taratibu. Akaanza kumkumbuka binti yake wa pekee kwenye hii dunia Deborah pamoja na ndugu na jamaa zake akina Mjomba Mkude. Akapatwa sana na tashiwishi na wahaka wa kutaka kufahamu wapi walipotokomea mpaka akaokotwa na Dr.Pesambili.

Ikabidi Daktari amkalishe kitako na kumuelezea mkasa wake mzima wa kuugua kwake mpaka alivyofanya maamuzi ya kumbeba jumla jumla. Swali la wapi alipo Deborah likakosa majibu toka kwa Dr.Pesambili, hivyo wakaweka adhima afya yake itakapotengamaa wataanzisha operesheni ya kumsaka Deborah popote alipo aweze kuungana na mama yake. Siku zilivyokuwa zinazidi kusonga ndipo alipozidi kunawiri na kutakata, mpaka akaacha kabisa kutembelea gongo akawa anatembea kwa kuvuta mguu kwa mbali. Katika mazungumzo yao kama mama na mwana, ndipo Dr.Pesambili akagundua kuwa mama Deborah ni nesi kwa fani yake. Jambo hilo lilimfurahisha sana Dr.Pesambili kwani aliona ndoto zake za kutaka kufungua hospitali kubwa ya kisasa itatimia kwa urahisi kutokana na kuwa karibu na mtu mzoefu wa shughuli za hospitali.

Dr.Pesambili kwa vijisenti vyake alivyodunduriza wakati anafanya kazi Morogoro akafanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Tuangoma, Kigamboni ekari 20 mahususi kwa ujenzi wa hospitali. Mipango ya Dr.Pesambili sasa ikawa akitoka tu kumtafuta mama yake mzazi Jijini Arusha na Kilimanjaro basi ahamishie nguvu zake kwenye ujenzi ili aanze hata walau na jengo moja. Wawili hao sasa ikawa kiba kibandika kiba kibandua kila wakati wanatembea pamoja, wasiojua kitu baina yao walidhania ni mama na mwana kwa jinsi walivyoshibana.

"Mama nitaomba kesho unisindikize Jijini Arusha, ninaelekea kwenye ofisi za 'Peace-Corps Tanzania'......hivyo ingekuwa bora tuambatane wote kwa pamoja na wewe upate kuchangamsha mwili" alisema Dr.Pesambili wakiwa wapo wawili tu mesini ndio kwanza wamemaliza mlo wao wa usiku. Mama Deborah kusikia Peace Corps Tanzania moyo wake ulimlipuka kama taa ya chemli iliyoishiwa mafuta inavyolipuka.

Mawazo yake yakarudi kisengerenyuma sana mpaka yakafikia mwaka 1986, akikumbukia mumewe alivyopata madaraka makubwa ya kuongoza shirika hilo, na mpaka madaraka hayo kuwa ndio sababu ya kifo chake kuuliwa na majambazi. "Mama mbona hunijbu kitu umebaki umeshangaa tu kulikoni, upo mzima?" aliuliza Dr.Pesambili akiwa ameshashikwa na hofu huenda afya ya mama Deborah inataka kuanza kubadilika.

"Nipo fiti mwanangu kuwa na amani, nimekumbuka tu miaka ya nyuma nimewahi kufika Jijini Arusha, mume wangu anafanyakazi shirika hilo hilo ulilolitaja" aliongea kiunyonge mama Deborah huku akijiweka sawa kutaka kufahamu anachokwenda haswa kukitafuta Dr.Pesambili huko kwenye ofisi za 'Peace-Corps Tanzania'. "Nilipokuwa Jijini Nairobi katika harakati za kumsaka mama yangu mzazi, nimepata penyenye za kuaminika zisizo na hata chembechembe ya mashaka kuwa mama yangu mzazi ni Mtanzania na yupo Jijini Arusha au Moshi, nikaambiwa amewahi kufanya kazi kwenye ofisi hizo, ndio maana nimeamua kuanzia taftishi yangu hapo..!" alisema Dr.Pesambili sasa akiwa ana amani ya moyoni baada ya kuondokwa na hofu yake dhidi ya afya ya mama Deborah ambaye sasa alikuwa anamuona ni kama mama yake rasmi.

Mama Deborah mapigo ya moyo wake yakaanza kwenda mbio, baada ya kusikia kuwa mama yake Dr.Pesambili amewahi kufanya kazi Peace-Corps Tanzania tena katika miaka ambayo mumewe alikuwa ndio Bosi hapo. "Ina maana huyu Dr.Pesambili ndio mtoto wangu wa kambo kwa Bi mdogo wa mume wangu?" alijiuliza hilo swali nafsini mwake mama Deborah, lakini akalipuuzia kwa muktadha kwamba Dr.Pesambili kampa taarifa kuwa baba yake mzazi amefariki gerezani nchini Italia hivyo kwa vyovyote vile hawezi kuwa ni mtoto wa mumewe Bosi Minja.

Wakaendelea na maongezi yao usiku huo huku mama Deborah akiweka nia ya kuelekea Marangu kwa wakwe zake kuwasalimis kutokana na kupotezana na kwa miaka mingi. Mpaka ilipofika saa 4:00 usiku wakaagana kwenda kulala, kuipumzisha miili yao wakijiandaa kwa safari ya kesho yake asubuhi kuelekea Jijini Arusha. Usiku kucha mama Deborah hakupata usingizi mtamu, alishikwa na kimuhemuhe cha kwenda kuwatembelea ukweni kwake Marangu, ili akamjue haswa mtoto wa kiume wa Bosi Minja ni nani na yupo wapi kwa sasa.




Licha ya wafungwa wengi na vijiwe mitaani kulisifia gereza la Ukonga kwa sifa kemkem kuwa ni zuri lakini kwa mtazamo wake Mbweku Jr jela ilikuwa ni jela tu hata siku moja haiwezi kufanana na Hoteli ya nyota tano. Tamaa yake ilikuwa ni kufanya vyovyote awezavyo aweze kuwa huru uraiani. Sumu haionjwi kwa ulimi, ukitaka kujua mateso na bughudha za jela ombea siku moja uende huko ndio utajua tamu na chungu yake. Kulikuwa na watuhumiwa huko gerezani tokea walipokamatwa hadi kufikia miaka 3 kesi zao hazijawahi kusikilizwa Mahakamani, na wengine walikuwa wamebambikiziwa kesi na polisi wanahangaika nazo nenda rudi.

Mbweku Jr alipoletwa Ukonga, siku za mwanzoni alikuwa anachungwa kama mboni ya jicho ili mradi asilete rabsha na ghasia zozote. Ripoti zilizofikishwa pale Ukonga juu ya Mbweku Jr zilijaa chumvi, zikivumisha kuwa Mbweku Jr ni mahabusu hatari sana, hivyo jina lake lilivuma mithili ya papa baharini. Hii yote ilikuwa ni mbinu chafu za rafiki yake Timammy ili kumdhibiti Mbweku Jr asije kufanya mbinu za kutoroka. Masazo ya ndovu majani makavu, pesa za watu wakubwa kama Timammy zilikuwa zinaleta uharibifu katika jamii kwa kuwaonea watu wanyonge kama akina Mbweku Jr. Alikuwa anatengwa haruhusiwi katu kuchanganyika na mahabusu wenzake.

Akaanza kupelekwa kwenye chakula na pingu, chooni na pingu huku askari magereza mwenye mtutu mgongoni mwake. Pia kulala kwake nako shida tupu, analala na pingu mikononi, anafunguliwa pingu za miguuni peke yake. Mbweku Jr alishaanza kukata tamaa ya kutoroka nje ya gereza hilo lenye ulinzi madhubuti. Baada ya kupita miezi kadhaa ya uangalizi wakaanza kumpa uhuru wake kama watuhumiwa wengine. Alishangazwa sana na mabadiliko hayo ya ghafla asiyoyatarajia.

Baada ya kupita siku kadhaa akapata ugeni uliomtembelea gerezani. "Mimi ni Mwanasheria wa Bosi Timammy amenituma nije kumuombea msamaha kwa kukutelekeza gerezani. Ametoa ahadi kuanzia sasa ya kukuhudumia kwa hali na mali, pia ameniagiza niandae mkataba wa makabidhiano ya mali zako, na ameahidi kufanya juu chini utoke gerezani kwa haraka" yalikuwa ni maelezo ya mgeni yule kwa Mbweku Jr. "Mjumbe hauliwi, mwambie vitendo vyake ndio vitanijulisha kuwa kweli anataka suluhu na mimi" alijibu Mbweku Jr kwa ufupi huku akionyesha hana haja ya mazungumzo zaidi huku akinyanyuka na kumuacha mgeni amebaki amepigwa na butwaa kaachwa mdomo wazi, akimshangaa jinsi Mbweku Jr alivyokuwa masikini jeuri. Maana ilivyo ada ni kuwa mtu aliye kwenye shida, mazonge yamemsonga hana miiko wala makuu haja yake ni nafuu tu.

Maneno ya mwendawazimu hayana maana lakini ni maneno, majibu ya Mbweku Jr yalipomfikia Bwana Timammy kweli akayafanyia kazi kwa vitendo. Tokea siku ile mchana wake tu mabadiliko yakaanza mara moja. Mbweku Jr akaanza kuletewa chakula kilichopikwa nyumbani kikiwa kimewekwa kwenye vyombo maalumu vya thamani utasema yupo Hoteli ya nyota 5. Mchana akiletewa wali uliokolezwa nazi na mchuzi wa samaki uliotiwa nazi shatashata basi jioni ataletewa chai ya maziwa na chapati za maziwa ili mradi, Bosi Timammy alianza kuonyesha msamaha kwa vitendo.

Huko Mahakamani nako hali ya hewa ikabadilika kabisa, upepo ukaanza kuvuma upande wake, Jaji alikuwa amecharuka akitaka ushahidi wa kesi hiyo kukamilika ndani ya mwezi mmoja vinginevyo atamuachia huru mtuhumiwa Mbweku Jr. Sasa Mbweku Jr akaanza kuwa na imani na Timammy kuwa kweli ameamua kujirudi kwa vitendo. Akaamini moyoni mwake kuwa kweli shetani alizeeka hugeuka kuwa malaika. Akaanza kuhesabu siku tu za yeye kurejea uraiani akadake mali zake aanze maisha mapya ya raha mustarehe yasiyo na rabsharabsha.

Alipanga akipata mgao wake ni kwenda kujichimbia nje ya mji na kuanza maisha yake upya. Asichokijua Mbweku Jr ni kuwa Na iwapo akifanikiwa kumuangamiza basi dunia kwake itakuwa ndio kama pepo yake iliyoletwa ardhini kabla hajafika.

Timammy alibadilisha mbinu za mashambulizi dhidi yake, aliamua kumuweka karibu adui yake ili iwe rahisi kwake kumuangamiza. Na kweli Mbweku Jr akanusurika na kifo chupuchupu apelekwe jongomeo kwa usafiri wa jeneza usiotumia mafuta kama gari. Lilikuwa ni shambulio la mwisho toka kwa Timammy dhidi ya Mbweku Jr. Jaribio lake la mauaji lilikuwa kupitia chakula anacholetewa na Timammy. Mauti mamoja maziko mbalimbali, sio lazima umshambulie adui yako kwa njia chafu, unaweza kumshambulia kistaarabu na ukapata natija ile ile uliyoikusudia, huo ndio mpango wa Timammy aliousuka dhidi ya Mbweku Jr.

Timammy aliona kabisa, Mungu kampa neema zote za dunia lakini kuna kidudu mtu mmoja ndio anamnyima raha kutumbua kwa furaha neema hizo nae ni Mbweku Jr. Lakini kumbe Mbweku Jr hakuwa juhali, zumbukuku ulimwengu uko huku, katika vitu ambavyo Mbweku Jr alikuwa makini nacho basi ni chakula. Alikuwa anajaribu kuwa makini kila anapoletewa lazima ahakikishe mletaji yule amekionja ndio anakipokea.

Chambilecho maziwa ya ng'ombe wa kuazima hunywewa mnywaji amesimama, katu hakumpa imani ya asilimia 100% Timammy juu ya wema anaomfanyia hivyo kila kitu alikuwa anakiendea kwa tahadhari kubwa. Lakini siku ambayo chakula chake kiliwekwa sumu kilipokelewa na Askari magereza peke yake, tena ambaye alijiweka karibu nae sana kwa kila kitu, akaniambia, wakaaminiana kuwa kuna kaurafiki baina yao. "Leo chakula kimeletwa mapema sana, nikaona nisikusumbue nimeamua nikupokelee akakionja yule mletaji kipo fiti usiwe na wasiwasi" alisema yule Askari wakati anamkabidhi vyombo vyenye chakula Mbweku Jr huku anakwepesha kugonganisha macho baina yao. Mbweku Jr hakutia neno, lakini kajoto ka wasiwasi kikamvaa mwilini mwake, ila akapuuzia kutokana na yule askari aliyemkabidhi ni mtu wake sana hakuwa na chembe ya mashaka nae.

Mbweku Jr alishaumia tayari, alisahau kuwa mazoea papai kwa kijiko, yanakupunguzia uwezo wa kufikiri. Aliyemfaa Mbweku Jr na kumuepusha na kifo cha sumu ni askari mwenzake na yule askari rafiki yake ambaye alikuwa nae lindo moja. Alimkonyeza kwa kumpa ishara juu ya chakula kile. Hakushuhudia mwenzake anavyokionja hivyo akahisi kuna janja janja inataka kufanyika kutokana na uwongo anaosema mwenzake. Pia alimsoma mwenzake namna alivyojawa na hofu na wasiwasi mwingi kipindi chote anapokabidhi chakula kile kwa Mbweku Jr. Chakula kile Mbweku Jr akaenda moja kwa kukitupa chote kwenye pipa la taka kikawe kalamu ya wadudu na ndio ukawa mwisho wa chakula kuletewa toka uraiani kwa Timammy.

Walishanyoosha mikono kuwa Mbweku Jr ameshindikana, kama ni mchawi basi yeye ndio gwiji wao. Mbweku Jr baada ya kujifanya zuzu kwa muda mrefu na kuwaaminisha kuwa hana madhara tena, kiasi kwamba wakazidi kupunguza umakini dhidi yake ukafika wakati wa kuwaachia manyoya tu. Mbegu za leo haziwi miti keshoye, tayari alishatumia muda mrefu kuwasoma walinzi wa gereza na sehemu gani kwake rahisi kuitumia kutoroka Kilaini. Alijua mpango wake wa kutoroka ni wa hatari sana, kufa au kupona na daima mchele haukosi ndume hivyo alijitayarisha kwa chochote kile kitakachompata.
Mipango yake ilikuwa ni kutoroka kupitia Lori la kubebea takataka gerezani.

Utakumbuka siku Mbweku Jr anapewa taarifa za kuletwa Ukonga alikuwa na furaha sheshe kutokana na kufahamiana na mtu anayehusika na Lori la takataka. Lori hilo Mjomba wake alikuwa ndio utingo wake. Huyu ndio Mjomba aliyempa taarifa Mbweku Jr za baba yake kuhamishiwa gereza la Dar es Salaam kutokea Jijini Arusha walipogongana mtaani maeneo ya Manzese baada ya kupotea kitambo kirefu.

"Uncle...Uncle...mimi kijana wako Mbweku, tuongee kidogo nina shida...!" alinong'ona Mbweku Jr huku akimkaribia Mjomba wake aliyekuwa ametingwa na kazi ya kupakiza takataka ndani ya Lori hilo. Mbweku Jr alimfuata Mjomba wake baada ya kujihakikishia kuwa ndio yeye kwa kumchunguza kiumakini kwa muda mrefu tokea ahamishiwe gereza lile. Kuna baadhi ya siku alikuwa hata anamsaidia kupakiza taka kwenye gari, ila Mjomba mtu hamtambui Mbweku Jr kutokana na kupoteana kwa muda mrefu sana.

"Mjomba.... Mjomba.... siamini Mjomba kama ndio wewe Mjomba..!, umefikaje humu"? alijikuta anaropoka yule Mjomba wake Mbweku Jr huku akikiachia kifurushi cha takataka kikidondoka chini alichokuwa amekishikilia mkononi. Damu ni nzito kuliko maji, Mjomba mtu alipomuangalia kwa umakini sana, akagundua huyu kweli ni mtoto wa dada yake, ambaye taarifa walizonazo ni kuwa yupo nchini Afrika ya Kusini,hivyo alishangazwa na kumuona yupo mule gerezani. Ikabidi Mbweku Jr aanze kumfungulia kitabu cha maelezo Mjomba wake, akianzia tokea alipotorokea nchini Afrika ya Kusini mpaka kujikuta tena yupo gerezani.

Mjomba nae akampa taarifa kuwa baba yake mzazi Mbweku Sr ameachiwa huru kwa msamaha wa Rais, na sasa yupo Kijiji cha Kitomanga, Mkoani Lindi anajishughulisha na kilimo. Kisha mwishoni akamdokezea nia na madhumuni yake ya kutaka kutoroka ili kukwepa kifungo cha maisha au kunyongwa, na tumaini pekee lililobakia kwake la yeye kukwepa mkono wa dola ni yeye Mjomba wake kumsaidia kutoroka gerezani. Mjomba mtu mwanzoni alikuwa anasitasita kukubaliana na mipango hatari ya mpwa wake. Alikuwa anatafakari kwa kupima kwenye mizania ya usawa madhara na madhila yatakayomkabili iwapo atagundulika uhusika wake wa kumtorosha Mbweku Jr. Ikabidi Mbweku Jr afanye kazi ya ziada kumrai, kumlainisha na kumtongoza Mjomba wake mpaka wakaenda sawa. Wakakubaliana wiki ijayo ndio iwe wiki ya kutoroka.


Siku ya miadi ilipofika Lori hilo la kubeba takataka badala ya kuingia gerezani saa 9 alasiri kama ilivyo kawaida yake, likaingia saa 11 jioni. Kwa bahati nzuri siku hiyo Wafungwa karibia wote wazima kwa wagonjwa walikuwa wamejikongoja, wamekusanyika kwenye jengo moja wanaangalia mpira wa mechi ya miguu. Ilikuwa ni mpambano baina ya Yanga na Simba, mpambano ambao kwa kawaida huwa unateka hisia za washabiki na wapenzi wa soka, wake kwa waume katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, habari hawana.

Mbweku Jr alikuwa amebakia Selo peke yake anapanga na kupangua mbinu mbalimbali za kuteleza toka gerezani. Lakini pia masikio yake yalikuwa yamemsimama dede kama dishi la televisheni linalosubiria kudaka mawimbi ya televisheni akiisikilizia Lori la takataka ujio wake. Muda wote Mbweku Jr alikuwa roho juu juu akilisubiria gari hilo lifike. Alipoona muda unayoyoma halitokei akaanza kukata tamaa, alishadhania Mjomba wake amebadilisha maamuzi yao waliyokubaliana. Sasa kabla hajaanza kuwaza kitu cha kufanya ili ajiokoe gerezani akasikia mlio wa Lori hilo la taka.

"Afandeee... Afandeee...!" aliitwa Askari Magereza pekee mwenye silaha na Mbweku Jr ili kumsikiliza shida yake, huku Askari wengine wote nao wakiwa wametekwa na laghwi ya mpira wa miguu, wamesahau kabisa jukumu lao la ulinzi walilokabidhiwa. Kilichopo fuatia hapo ni yule Askari kuja kuzindukia Muhimbili akiwa mahututi, hoi bin taabani. Alimfuata kizembe Mbweku Jr bila kuchukua tahadhari yoyote, hapo hapo akajikuta anapigwa ngwala moja matata sana na kulamba sakafu bila kupenda, kabla hajajua kinachoendelea akashtukiwa anapigwa kisogoni na kitako cha bunduk yakei na kujikuta analala fefefe usingizi wa kuzimia.

Mbweku Jr akamburuta askari yule mpaka ndani ya Selo hiyo iliyokuwa tupu bado.. Hima hima akachomoka zake kuelekea kwenye gari la taka. Baada ya hapo ilibakia historia tu kuwa mule gerezani kulikuwa na mtu anaitwa Mbweni Jr. Sakata la Mbweku Jr kutoroka lilizua kasheshe nzito gerezani.Mkuu wa gereza na baadhi ya Maaskari wake walijikuta wanapewa uhamisho wa kikazi bila kupenda kwa uzembe. Wafungwa na Mahabusu waliobakia gerezani walimlaani Mbweku Jr upeo wa juu wa kumlaani, kutokana na hali ngumu aliyowaachia.

Ile hali ya kudekezana na kuachiana ikatoweka kabisa. Mianya yote ya uzembe katika ulinzi ikatiwa Korokoroni, sasa ikawa kazi kazi tu hamna kuchekeana tena, Mbweku Jr alishawapa funzo kuwa ukimchekea nyani utayavuna mabua. Msako wa Mbweku Jr huko uraiani ukawa ni wa kimya kimya, ili kuhofia asije kugutuka kama anasakwa na pia kuhofia kuzua taharuki ndani ya nchi juu ya uzembe wa vyombo vya dola kwenye masuala ya ulinzi na usalama. Mbweku Jr tayari alishaenda kujichimbia kijiji kwao Kitomanga, huko Lindi kupata baraka za wazazi kabla hajarejea kudai haki zake zote kwa rafiki yake Timammy.

Msako wake ukawa kama moto wa kifuu, ilipopita miezi 3 tu wakaachana nae, maadamu alivyotoroka hakuua mtu, taratibu wakakubali matokeo kuwa Mbweku Jr amewazidi kete, maisha lazima yaendelee kama kawaida. Bosi Timammy nae kupitia vidinga popo vyake vya gerezani akapata taarifa juu ya utoro wa Mbweku Jr. Sasa nae akaanza kuishi kwa hofu na mashaka hana tena furaha ya maisha.

Siku za mwanzoni alikuwa anatumia muda mwingi wa mchana kujifungia ndani na kutoka usiku kama popo. Baadae alipoona mambo yake yatakwama ikabidi hana jinsi lazima atoke kama zamani kwa uangalizi maalumu. Kila alipokuwa anakwenda alikuwa anazungukwa na kikundi cha walinzi shupavu na makini wanaopenda kufa kuliko kuishi. Deborah bado alikuwa hajui chochote kinachoendelea kwa mumewe Timammy licha ya kuona mabadiliko yasiyo ya kawaida. Hakutaka kuhoji zaidi kutokana na hekaheka na misukosuko ya ujauzito wake.


SURA YA ISHIRINI
Dr.Pesambili na mama Deborah walifikia katika Hoteli yenye hadhi ya nyota 4 inayoitwa 'Palace Hotel-Arusha' iliyopo katika barabara ya Makongoro. Ilikuwa ni Hoteli tulivu isiyo na fujo kama inavyokuwa nyumba ya wavuvi. Kutokana na uchovu wa safari walijikuta wanalala fefefe mpaka majira ya mafungulia ng'ombe, jua limeshachomoza vilivyo. Baada ya kujimwagia maji maliwatoni kila mmoja kivyake wakajikuta wanakutana kwenye Mkahawa kwa ajili ya staftahi ya asubuhi, hali ya kuwa miili yao imepata tahafifu dhidi ya uchovu.


Kilichofuatia baada ya kuonana asubuhi hiyo ni kupeana jambo sijambo kama ilivyo ada ya binadamu wote wenye akili timamu. " Shikamoo mama, umeamkaje mie nipo vizuri nashukuru...!" alisalimia Dr.Pesambili huku akiwa yupo mbele ya mama Deborah amekamatia sahani yake anachagua vyakula kwenye bufee iliyokuwa imesheheni anuwai mbalimbali za michapalo kuanzia mayai ya kuchemsha, ndizi mchemsho na za kukaanga, soseji, mikate, maharage, vipande vya kuku wa kukaanga. Ilikuwa ni bufee ambayo kama wewe ni mtu mlafi bora usisogelee kabisa yasije kukuta yale yaliyohadithiwa kwenye kitabu kuhusu Manenge na Mandawa.


"Marhaba mwanangu na mimi naendelea vyema namshukuru Bwana...tule haraka tuwahi huko Ofisini tusije kuwakosa wenyeji wetu...!" aliongea mama Deborah akiwa anajimiminia kwenye bakuli lake uji wa ulezi. Wakajongea kwenye meza yao wakaanza kukishambulia chakula chao. Kila mmoja alikuwa mkimya ametulizana kama maji mtungini, anakula huku anatafakari mustakabali wa matokeo ya ziara yao ya leo katika ofisi za 'Peace Corps-Tanzania'. Dr.Pesambili alikuwa anawaza jinsi atakavyomfahamu mama yake mzazi na kuonana nae kwa mara ya kwanza.


Tayari alishamsamehe kwa kitendo chake cha kumtelekeza kwenye kituo cha watoto yatima. Pia mawazoni mwake alijua itamchukua muda kusahau tukio hilo, hasa kutokana na kwamba katika maumbile ya mwanadamu, dhambi uliyowahi kuifanya huwa haisahauliki. Ukiwa mtu muovu kisha ukageuka na kuwa mtu swalihina, bado walimwengu watakumbukia maovu yako tu. Utawasikia wanasema "siku hizi amemrudia Mungu wake lakini zamani enzi zake alikuwa mwizi, mnyang'anyi, mlawiti na mengineyo mengi tu katika dhunubi zake mtu huyo alizowahi kufanya siku za nyuma". Mama Deborah nae nae alizama katka bahari ya luja kimawazo, akifikiria kama huyo mama yake Dr.Pesambili ndio mwanamke aliyempora mume wake halali wa ndoa takatifu ya kanisani na kisha kushiriki njama za kuondosha uhai wa mumewe kwa lengo la kujitajirisha kwa pesa za wizi na urithi na kwenda kula mbwende na hawara yake. Huyo mwanamke ndio aliyemsababishia awe mgonjwa mahututi kitandani kwa zaidi ya miaka 15 na kumpotezea kazi yake na familia yake kwa ujumla kwa kukomba mali zote za familia.

Kwa upande wa pili wa shilingi, Dr.Pesambili, mtoto wa huyo hasimu wake ndio kamrudishia tena matumaini ya uhai. Kamtoa kitandani ambako tayari alishakufa kimawazo na kimwili, akisubiria ahadi ya kifo cha kiroho ije kutekelezwa na Malaku mauti. Na bado kama haitoshi anamhudumia kama vile ni mama yake mzazi kwa kila kitu anachokihitaji. Alipofika hapo akajikuta machozi yanamtiririka na kulowanisha mashavu yake bila mwenyewe kupenda. "Mama nini tena kimekusibu mbona unalia tena kulikoni?" aliuliza Dr.Pesambili huku tayari akiwa ameshachomoa hanchifu yake kuanza kumfuta machozi yale kiupendo kabisa.

"Hamna shida, nimetafuna pilipili vibaya wakati nakunywa supu hii" alitunga uongo wa haraka kuzima maswali zaidi, huku nae akitoa kitambaa chake kupenga mafua. Dr.Pesambili kwa utaalamu wake wa saikolojia alielewa kinagaubaga kuwa anafichwa kitu na mama Deborah. Hakutaka kumghasi, alijua tu muda sio mrefu atang'amua kinachomsonga mama Deborah. Walipotoka hapo Mkahawani, roshani ya kwanza wakashuka mpaka nje ya Hoteli na kukodisha taksi ya kuwapelekea Ofisi za 'Peace Corps-Tanzania'.

Mama Deborah, Dr.Pesambili na dereva wao walikuwa ndani ya taksi ukimya umetawala, dereva anahangaika kuinyonga sukani ya gari lake na kukanyaga mafuta ipasavyo ili gari lielekee ueleleo wa sawa. Watu wema hawadumu Bwana, gari yangu ya kwanza niliinunua kupitia kazi za Bosi wa zamani wa Ofisi za 'Peace Corps-Tanzania', mimi ndio nilikuwa dereva wake kipenzi anapokuwa na safari binafsi nje ya saa za kazi" alisema yule dereva wao mtu mzima aliyeonekana ni mwingi wa habari, akivunja ukimya uliokuwa umetawala huku wakiwa wanakaribia Ofisi hizo wanakiona kibao chake kwa mbali. "Alikuwa anaitwa nani huyo Bosi....?" alidakia mazungumzo mama Deborah huku akiwa na wahaka wa kutaka kumfahamu, kwa jinsi umri wa dereva huyo ulivyo moja kwa moja mawazo yake yakamuelekeza huenda anayeongelewa hapo ni mumewe.

"Huyo Bosi alikuwa anaitwa Joseph Minja, Mungu amlaze mahali pema peponi, alikuwa na roho nzuri sana, ana nakidi ya pesa, watu wamejenga majumba hapa Arusha kwa ajili yake. Alikuwa akiingia Baa basi kila mtu anafurahia, ila Bwana akaenda kumvaa msichana mdogo, gubegube la Kimachame, chotara wa kizungu anaitwa 'Recho Miondoko', Katibu Muhtasi wake akamkamua pesa vilivyo na nasikia ndio alipanga njama za kifo Bosi Minja kupitia majambazi aliowatuma. Baada ya hapo nasikia yule msichana alikimbilia nchini Kenya huko kula maisha" alizidi kuropoka yule dereva bila kujua anaumiza hisia za abiria wake. Maelezo hayo ya dereva yalitosha kuuchanachana vipande moyo wa Dr.Pesambili na kupata picha halisi ya tabia za mama yake. Jina la mama yake alitajiwa anaitwa Recho ila ubini wa babu yake mzaa mama ndio alikuwa haujui, sasa haya maelezo yalikuwa yanazidi kumfikirisha, yakimpa mawazo tata.

Maelezo hayo ya dereva pia hayakumuacha salama mama Deborah, kwani dereva alikuwa anaanika hadharani maisha ya ulimbukeni ya mumewe Bosi Minja. Akaamini msemo wa masikini akipata, matako hulia mbwata hasa akikumbukia shida walizopitia wakati mumewe ni Mwalimu wa Morogoro Sekondari, anapokea mshahara mkia wa mbuzi kumbe maisha yalivyomnyookea akawa mtu wa kutapanya fedha zake kwa israfu kwenye Mabaa kwa kuzipiga shoka pesa zake. Kila mmoja katika wao, machozi yalikuwa yanamlengalenga ila anajitahidi kuyazuia kuepusha maswali toka kwa mwenzake.

Dr.Pesambili akamalizana nae dereva yule, akatimka zake na gari lake akiwaacha wateja wake wanaingia ofisini kupata huduma waliyoikusudia. Wakajitambulisha pale mapokezi kisha Dr.Pesambili akaelezea nia na madhumuni yake ya kuonana na Bosi Mkuu wa Ofisi. Wakaelekezwa sehemu ya kupumzikia wageni huku wakikaribishwa soda, chai na kahawa kavu kwa mwenye kuhitaji. Waliwekwa kwenye orodha ya mzunguko wa watu wanaosubiria kuonana na Mkurugenzi wa 'Peace Corps-Tanzania'. Ilipofika zamu yake Dr.Pesambili kuingia, wakaamua waingie wote wawili. Walipoingia, wakajitambulisha kisha Dr.Pesambili akaanza kueleza shida yake. Muda wote wakati Dr.Pesambili anajieleza, mama Deborah uso ulikuwa haubanduki kwenye moja ya ukuta uliokuwa na picha mbalimbali za Wakurugenzi waliopita katika Ofisi hiyo ya 'Peace Corps-Tanzania'.

Jicho lake likatuama kwenye picha ya marehemu mume wake Bosi Minja. Akiwa amevalia suti nyeusi na tai, akatabasamu. Akajikuta machozi yanamporomoka bila kupenda akikumbukia zama bora enzi za uhai wa mumewe. "Hapa kwenye huo mwaka unaotaja, mtumishi tunayemfahamu alikuwa anaitwa 'Rachel Francesco Gabriele'....na picha yake hii hapa...!" ilikuwa ni sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa Peace Corps-Tanzania akimkabidhi picha ya Recho mkononi mwa Dr.Pesambili. "Whaaaaaat.......anaitwa nani?" aliuliza kwa sauti ya kugutuka Dr.Pesambili na kumfanya mama Deborah nae akae mkao wa kula kufuatilia mazungumzo baina ya Mkurugenzi na Dr.Pesambili. "Nimesema anaitwa 'Rachel Francesco Gabrielle', ila mara ya mwisho inaonyesha alipata urithi wa nyumba ya Bosi wake aliyezaa nae. Maeneo ya Moshi Mjini, maeneo ya Boma Ng'ombe, nyumba namba 32 Bloku B. Alipewa urithi yeye na mtoto wake mchanga anaitwa Pesambili Joseph Minja....!" maelezo hayo ya Mkurugenzi ilikuwa kama vile anapigilia msumari wa moto kwenye utosi wa mama Deborah baada ya kusikia kusikia huyu Dr.Pesambili ndio mtoto anayesadikiwa kuwa wa mumewe.

"Nttiiiiiiiiiiiiiiih......!" kilikuwa ni kishindo kizito cha kuanguka kwa mama Deborah kutoka juu ya kiti mpaka chini ya sakafu. Kisha akatulizana tuli bila kutikisika. Hamkani mambo yakawa si shwari tena Ofisini mule, hekaheka za kumkimbiza mama Deborah hospitalini. Mazungumzo kati ya Dr.Pesambili na Mkurugenzi yule ndio yalivurugikia hapo. Dr.Pesambili kila alipojitahidi kusikiliza mapigo ya moyo wa mama Deborah yalikuwa yameshuka sana yapo chini kuliko kawaida. Akawa muda wote amejishika kiunoni anatikisa kichwa kuonyesha ameshaanza kukata tamaa kama kweli mama Deborah atapona au atakufa fi.

"Mzee samaki wako wazuri sana, ukiwapata wazuri kama hawa wa leo usisite kuniletea nyumbani....! " alisema Bosi Timammy kumuambia mvuvi mmoja wapo aliyekuwa amejengeka kisawasawa misuli yake, kichwani ana msitu wa nywele zilizounguzwa na chumvi ya maji bahari. Pia alikuwa amefuga ndevu, masharafa na masharubu yake ameyasokota kama Karl Peters yule mkoloni wa Kijerumani. Viganja vyake vya mkono vilikuwa vigumu sana kama mbao ya Mninga na mikono yake imeshupaa kutokana na mazoezi ya kupiga makasia wakati anaendesha mtumbwi baharini.

Ngozi ya mwili ilikuwa imekaushwa vilivyo na maji chumvi ya bahari, ikiwa ngozi hiyo haijui bei ya rosheni dukani inauzwaje. "Ahsante Bosi wangu, mie Bosi mzigo wangu ni wa motomoto siuzagi samaki wa mochwari aliyevundikwa kwenye mabarafu nyumbani ni pale pale nilipopelekwa na dereva wako wiki iliyopita eeeeh...? " aliuliza mvuvi yule kiunyenyekevu. "Ndio pale pale, ukifika wewe jitambulishe tu kuwa umeleta samaki, nitaacha taarifa zako kwa mlinzi na mke wangu pia...!" huo ndio ukawa mwanzo wa mahusiano mapya baina ya Bosi Timammy na Mbweku Jr. Mahusiano yao yalianzia katika ufukwe wa Kunduchi kwenye mnada wa samaki.

Wateja wengi walikuwa wanampenda Mbweku Jr kutokana na ujuzi wake wa samaki wa baharini. Hamna samaki ambaye alikuwa hamjui jina kuanzia Changu doa, Perege, Fumi, Pono, Tasi, Kibua, Samsuli, Kolekole, Taa na wengineo lukuki tu katika anuwai za samaki. Na raha ya biashara ya samaki Bwana uwajue majina yao na namna ya kuwapika vizuri ili ufurahie mlo wako. Mfano umwambie mteja, ukitaka kumfaidi samaki Taa, umchanganye na futari ya muhogo wa nazi au umwambie kuwa huyu Samsuli ndio nyama ya ng'ombe ya baharini unaweza hata kupikia pilau.

Mbweku Jr alisharudi Jijini Dar es Salaam tayari akijiandaa kulipa kisasi kwa Timammy. Kipindi chote alichojichimbia kijijini alikuwa anajaribu kila Jumapili kuhudhuria kanisani na kuungama dhambi zake, huku akifunga nadhiri ya kumsamehe hasimu yake Timammy lakini juhudi zake hizo zikawa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Kwa ufupi alishindwa kabisa kumsamehe Timammy hasa akivikumbuka vimbwanga alivyomfanyia. Ikabidi lazima aje Jijini na kuanza kupeleleza nyendo za Bosi Timammy, ili kisasi kitibu majeraha yake ya moyo yanayovuja damu. Ndipo alipong'amua kuwa Bosi Timammy ni mpenzi mkubwa wa samaki na soko lake kubwa ni Kunduchi mnadani. Katika mahusiano hayo mapya, Mbweku Jr alikuwa anamtambua nje ndani Timammy lakini Timammy maskini ya Mungu hamtambui kabisa Mbweku Jr kutokana na kuchujuka kulikotokana na msoto wa maisha magumu.

Hawa mahasimu wapya walikuwa hawajatiana machoni kwa zaidi ya miaka 8, zaidi ya kuonana juu juu mara moja pale Mahakamani. Laiti Timammy angekuwa anamuangalia kwa umakini Mbweku Jr lazima angemtambua tu, kama ujuavyo mtu wako ni wako tu hawezi kukupotea machoni. Ila tatizo katika ulimwengu huu wa rakadha tunaoishi, ukiwa hohe hahe, kipato cha kijungu meko hakuna mtu anakuangalia kwa umakini. Wakikuangalia wanajua saa na wakati wowote utawabomu kwa kuwalalamikia shida zako.

Fursa ya kufanikiwa kufika nyumbani kwa Bosi Timammy bila kipingamizi ndio aliyokuwa anaivizia Mbweku Jr kwa udi na uvumba. Alijipanga aiteketeze familia yote ya Timammy kwa kutumia sumu atakayoiweka kwenye samaki. Tokea atoroke jela ilikuwa imeshapita nusu mwaka, Timammy alishaanza kupunguza umakini kwenye ulinzi wake, akijidanganya kuwa tayari Mbweku Jr ameshakubali matokeo kwa kushusha silaha chini kuwa yeye Timammy ni Taifa Kubwa haiwezekaniki. Hakujua kumbe simba mpole ndio mla watu, na daima mla kunde husahau lakini mtupa maganda kamwe hasahau. Mbweku Jr uhasama wake na Timamny aliona hauwezi kamwe kupata suluhu hapa duniani labda suluhu hiyo ikafanyike mbele ya Mola Mwenyezi kwenye mahakama iliyojaa uadilifu.

Hapa duniani kwenye mahakama zetu zilizojaa Mahakimu ,Majaji na Wazee wa baraza wapenda mlungula aliona kabisa hatoweza kumkabili Timammy mtu aliyejitengenezea naizesheni ya kutosha kwenye mihimili yote mitatu ya dola. Mfano huko bungeni kulikuwa na wabunge ambao pesa zao za kampeni kila kipenga kikipulizwa lilikuwa ni jukumu kake Bosi Timammy. Kulikuwa na Majaji nao baadhi yao amewatia mfukoni anagharamikia mpaka mapumziko yao na familia zao nje ya nchi kila inapofika mwishoni mwa mwaka.

Ni ununda tu na ujasiri wenye chembechembe za wehu wa Milembe usio mfanowe wa Mbweku Jr uliokuwa unamsukuma kuendeleza mapambano na Timammy, kubwa la maadui. Safari za kwenda na kurudi nyumbani kwa Timammy kukamfanya mpango wake wa kuiteketeza familia ya Timammy autie kapuni kimoja, na kuachana nao kabisa. Alifanikiwa kumuona mke wa Timammy ni Deborah, mwanamke wa ndoto yake, tena akiwa ameshajazwa mimba kubwa tu, tumbo limemuelemea kama mpiga ngoma kubwa wa bendi ya jeshi. Usicheze na nguvu ya mapenzi wewe, Samsoni wa kwenye biblia licha ya ubabe na maguvu yake dhidi ya Wafilisti lakini mbele ya penzi la Delila akajikuta nguvu zake zote zinayeyuka mithili ya siagi iliyowekwa kwenye kikaango kilichokolea moto.


Akamuona Deborah kwenye mavazi ya stara ya kiislamu tena akiitwa kwa jina la kiislamu la Faizah na masuria wake kochokocho wa kumhudumia. Mbweku Jr akazidi kumchukia Timammy hasa baada ya kugundua amemfunga bao la maudhi kwa kutumia kisigino cha mguu wake. Aliona ni dharau kubwa sana kumchukulia mwanamke wake ambaye alishampa tahadhari tokea siku ya kwanza anamtambulisha Deborah kwa Timammy, tena akasomeshwa kwa pesa za Mbweku Jr halafu hatimaye anakuja kumpokonya tonge mdomoni na mimba kamtilia kabisa.

Wakati bado akili yake inatafakari kitu cha kumfanyia akaona tukio linalojirudia pale nyumbani kwa Bosi Timammy ambalo akaona ni fursa kwake ya kwanza kujiweka vizuri kiuchumi apumzike maisha ya tabu kwa muda.

Kwa zaidi ya mara tatu mtawalia, Mbweku Jr alipokuwa anapeleka samaki hasa muda wa magharibi, lazima atakuta gari la kifahari la Mkurugenzi au Meneja wa mojawapo ya benki kubwa nchini limeegeshwa kwenye yadi nje ya nyumba ya Bosi Timammy. Mbweku Jr akahisi kuna kitu kibaya kitakuwa kinafanyika ndani ya nyumba ya Timammy na hawa Vigogo wa benki.

Kilichozidi kumpa wasiwasi ni kitendo cha Vigogo hao kuja nyumbani hapo bila madereva wao, kuonyesha kuna siri fulani wanataka kuificha. Kuna siku moja Mbweku Jr baada ya kuuza samaki wake alipotoka nje ya nyumba ya Timammy akatafuta sehemu na kujibanza ili kuchunguza kinachoendelea. Ilipofika majira ya saa 4:00 usiku akaona kitu kama mabegi mawili makubwa yanapandishwa ndani ya gari kisha likaondoka. Hisia zake zikamtuma kuwa hizo ni pesa zinasafirishwa kinyemela bila ulinzi wowote. Hisia za Mbweku Jr zilikuwa sahihi, kuna mchezo mchafu ulikuwa unafanyika kati ya Bosi Timammy na baadhi ya Maofisa wa benki wasio waaminifu. Baadhi ya Matajiri walikuwa wanacheza michezo na Maofisa wa benki, kwamba wanapewa pesa zIlizowekwa na wateja kama mkopo lakini sio mkopo rasmi. Wanapewa nje ya taratibu za kibenki wafanyie biashara halafu wanazirudisha kinyemela. Pesa hizo kwenye vitabu vya benki zinaonekana zimo ndani ya benki lakini kiuhalisia pesa hizo zinazungushwa mitaani na akina Timammy.

Mbweku Jr akaandaa shambulio takatifu namba moja kwa Timammy la kumshtua kuwa siku zote dhuluma hailipi, na mali ya dhuluma haina baraka kama ilivyo mali ya mtu bahili inavyoishia kuliwa na wadudu. Siku aliyoipanga ya tukio lao alitia bastola yake ya bandia, toi alilolinunua sokoni Kariakoo. Kila aliyemuona nalo toi hilo akiwa amelitia kwenye kikapu kule pwani kwenye samaki katika watu wake wa karibu akajitetea anampelekea mtoto wake ya kuchezea.

Ilipofika jioni kama kawaida yake akapeleka samaki kule nyumbani kwa Timammy na kupokewa na mke wake Timammy Bi.Faizah, ambaye ndio Deborah mwenyewe.
"Babu muuza samaki, kuanzia kesho usilete utapumzika kwanza, nategemea kusafiri na mume wangu tunaelekea nchini Afrika ya kusini siku zangu za kujifungua zimekaribia. Chukua hii namba yangu ya simu utanipigia baada ya wiki mbili kuniuliza kama tumerudi....!" aliongea Deborah akiwa amejitanda ushungi wa Manga wenyewe hamna hata unywele uliojitokeza nje sio ule wa kizushi wa kiswahili, utasema Mwarabu vile kama ungemuona. " Ahsante mama, hamna shida Mungu ni mwema panapo majaaliwa..!" alijibu Mbweku Jr huku anabonyeza batani za simu yake chakavu iliyofutikafutika baadhi ya namba zake akijitahidi kuingiza namba za simu alizopewa na Deborah.

Maumivu yalikuwa makali haswa ya kuitwa babu na mwanamke wa ndoto zake. Wakati kiumri Timammy alimzidi Mbweku Jr kwa zaidi ya miaka 5, ila ndio mambo ya pesa tena. Ukiwa na pesa kamwe huzeeki na ukizeeka bado utaitwa Mzee kijana. Akalipwa pesa zake za samaki, wakaagana. Kumbe Mbweku Jr siku hiyo alipanga kuwaadabisha kwa pigo namba moja. Moja kwa moja akapitiliza saluni akanyoa nywele vizuri, ghafla akageuka kijana. Baada ya hapo akakodisha chumba gesti bubu moja uswahili akaoga, alibadilisha nguo na kujiandaa kwa tukio.


Mama Deborah alikuja kuzindukia hospitalini baada ya kupoteza fahamu kwa saa kadhaa. Alipopata nafuu akabakia kulia hana cha kuficha tena mbele ya Dr.Pesambili. Ikabidi aufunue ukweli aliokuwa ameuficha moyoni mwake kwa muda mrefu, kwa kumueleza Dr.Pesambili kuwa mama yake ndio aliyeivuruga ndoa yake mpaka kusababisha kifo cha mumewe, Bosi Joseph Minja. Kama haitoshi akamuelezea namna alivyomtumia yeye Dr.Pesambili akiwa mtoto mchanga kubeba urithi wa mumewe kwa kudanganya familia kuwa Dr.Pesambili ni mtoto wa Bosi Minja.

Alipotoka hospitalini mama Deborah, ikabidi wafuatane mguu kwa mguu na Dr.Pesambili mpaka Marangu kwa wazazi wake Bosi Minja kwenda kuanika ukweli kuwa yeye sio mtoto wa Bosi Minja. Ikabidi yafanyike matambiko ya asili kusaidia kuondosha mikosi kwa Recho, mama yake Dr.Pesambili kwa kuchafua ukoo wa Minja kwa kuleta mtoto asiye na nasaba nao ya damu. Baada ya wiki moja wakarejea Jijini Dar es Salaam kuendelea na maisha yao ya kawaida. Lakini Dr.Pesambili akiwa amelipia matangazo ya kumsaka mama yake mzazi kwenye magazeti, redio na televisheni. Siku zikawa zinayoyoma lakini mama yake hakujitokeza kama alivyotarajia, mpaka akaanza kuhisi huenda mama yake mzazi amefariki dunia.


Hata hivyo akamshukuru Mungu kwa hatua aliyoifikia ya kumtambua mama yake ingawa hajawahi kumtia machoni.
Dr.Pesambili ilibidi taarifa za kufanikiwa kumtambua mama yake azifikishe yeye mwenyewe Jijini Turin kwa babu yake mlezi. Ilibidi azifikishe hasa baada ya kuona mfanano wa ubini wa baba mzazi wa jina la mama, "Francesco Gabriele". Ikabidi Babu wa watu aungame ukweli kuwa Rachel, mama mzazi wa Dr.Pesambili ni mtoto wake ambaye alimtelekeza tokea akiwa mtoto mdogo bila kutoa huduma zozote. Hivyo ikabidi Dr.Pesambili aitwe Jijini Turin Italia, atambuliwe rasmi kama Mjukuu mkubwa wa Mzee Francesco Gabriele. Mzee wa watu kwa furaha yake ikabidi akate nusu ya utajiri wake ampatie Dr.Pesambili. Sasa rasmi Dr.Pesambili akageuka kuwa bilionea kijana. Utajiri ambao ulimtembelea katika wakati muafaka, wakati ambao alikuwa na ujenzi wa hospitali yake ya kisasa anayoijenga Jijini Dar es Salaam.


Lakini kwa upande wa pili taarifa ya kama Recho ndio mama mzazi wa Dr.Pesambili, iliibua simanzi na majonzi makubwa kwa baba mlezi wa Dr.Pesambili, Mr.Lorenzo. Mr.Lorenzo alishapata msamaha wa kifungo chake kutokana na mwenendo mwema aliouonyesha gerezani. Hivyo ujio wa taarifa hiyo ulimkuta Mr.Lorenzo yupo uraiani, alipoonyeshwa picha ya Recho na Dr.Pesambili akamtambua mara moja kuwa ndio mwanamke aliyemsababishia matatizo yote ya kufungwa jela. Akajilaumu kumbe alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na dada yake wa damu kabisa kwa baba mmoja bila kujua. Ingawa lawama alizitupa pande zote, kwa baba yake mzazi kwa kuficha kama ana mtoto Tanzania. Pia lawama ziliangukia kwa Recho kwa kuamua kuficha ubini wake halisi, hali iliyosababisha wasifahamiane. Wote kwa pamoja wakazika tofauti zao kwenye kaburi la sahau, na kuamua kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo.


Aliporejea Tanzania, Dr.Pesambili bila kuchelewa ndani ya wiki tatu tu hospitali yake ya kisasa, yenye roshani zaidi ya 20 ikawa imesimama. Hospitali hiyo akaipa jina la 'Huruma General Hospital'-(HGH). Akaajiri madaktari bora na vifaa vya kisasa, kiasi kwamba watu wakaipa hospitali hiyo lakabu ya "Muhimbili Ndogo". Mama Deborah nae akaula kwenye hospitali hiyo. Akawa ni mmoja wa Wakurugenzi wa hospitali hiyo anayesimamia rasilimali watu. Kutokana na uzoefu wake katika mambo ya hospitali, ndani ya muda mfupi kila Mfanyakazi wa afya Tanzania akawa anatamani akafanye kazi 'Huruma General Hospital'-( HGH). Madaktari wakongwe na wapya wote wakawa wanachuana kutafuta kazi kwenye hospitali ya Dr.Pesambili.

Wagonjwa nao, kimbilio lao likawa Huruma General Hospital-(HGH). Huko walikuwa wanapata tiba ya viwango vya juu, tena ya kiustaarabu bila kufokewa wala kutusiwa na watumishi wake. Mpango wake Dr.Pesambili sasa ukawa ni kufungua matawi kila kanda ya nchi ili kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaofurika hospitalini hapo wakitokea Mikoani.

Kulipokucha gumzo la Jiji likagubikwa na kifo cha Meneja wa Benki maarufu nchini, aliyekutwa anaelea juu ya maji baharini. Yule Meneja aliamua kujihukumu mwenyewe kwa kujiua baharini ili kukwepa mkono wa sheria. Maana alijua tu lazima ataozea jela kwa kifungo atakachufungwa. Gari lake lilikutwa limetelekezwa katika makutano ya barabara za Dr.Barack Obama na Magogoni. Maafisa Usalama, walipofanya uchunguzi wao wakagundua mara ya mwisho alifanya sana mawasiliano ya simu ya kuonana na Bosi Timammy. Upelelezi ukaanzia kwa Bosi Timammy, akakamatwa na kuwekwa ndani kusaidia upelelezi. Katika nyaraka zilizofumwa nyumbani kwa Bosi Timammy ndio ikagundulika kuwa walikopeshana pesa za Benki milioni 500 kinyemela "offline" bila kufuata taratibu za kawaida za mikopo ya kibenki.

.Katika sekeseke hilo la mumewe kukamatwa, Deborah akashikwa na uchungu wa mimba wa ghafla kutokana na mshtuko wa kukamatwa kwa mumewe Bosi Timammy. Ikabidi akimbizwe katika hospitali ya 'Huruma General Hospital'-(HGH) ili kuokoa uhai wake na wa mtoto. Kama bahati tu, mama Deborah asubuhi moja akiwa kwenye harakati zake za ukaguzi wa shughuli za wodi ya wazazi ndipo akakutana na mtoto wake kwa mara ya kwanza baada ya kupoteana kwa zaidi ya miaka 12 lakini hawakutambuana. Mama Deborah alichoshangazwa ni kuona mgonjwa anayemdhania ni mtoto wake ana jina la kiarabu, anaitwa Bi. Faizah Timammy.


Mama Deborah akaamini kweli duniani wawili wawili na alishindwa hata kuongea nae kutokana hali mbaya aliyokuwa nayo Deborah na tayari mtoto wake mchanga alishafariki. Mchana wake Mama Deborah akakwea mwewe kuelekea Jijini Arusha kusimamisha ujenzi wa Huruma General Hospital-(HGH) tawi la kaskazini. Usiku wake alivyolala mama Deborah ndipo alipoanza kuona mauzauza ndotoni. Alikuwa amemuota mgonjwa aliyelazwa hospitalini kwao Bi.Faizah Timammy ndio Deborah wake wanacheka na kufurahi pamoja baada ya kupoteana kwa muda mrefu. Alipoamka akaipuuzia kuwa huenda ni ndoto tu haina maana yoyote. Usiku wake ndoto ile ile kama ya jana yake ikajirudia vile vile, ikabidi asiipuuzie tena arejee Jijini Dar es Salaam akampeleleze vizuri yule mgonjwa. Tahamaki mgonjwa kesharuhusiwa nyumbani. Namba za simu alizoziandikisha hospitalini ni za mumewe ambaye yupo korokoroni anapambana na hali yake ili akwepe kifungo kimagumashi.


Bahati nzuri Maabara kulikuwepo na sampuli ya vipimo vyake vya damu. Walivyoitumia kufanya vipimo vya DNA, majibu yakathibitisha pasina kuacha mashaka kuwa Bi. Faizah Timammy ndio Deborah Kunambi mtoto wa mama Deborah wa kumzaa. Kwanza akamshukuru Mungu kwa kumpa uhai mtoto wake na maisha mazuri mpaka wamefanikiwa kuonana bila kutambuana. Sasa ikawa mshikemshike kwa wote wawili, mchuzi moto ugali moto kwa kila mmoja, Dr.Pesambili anamsaka mama yake mzazi Recho na mama Deborah anamsaka binti yake Deborah.

Mbweku Jr pesa zake alizompora Meneja wa Benki akaamua kuwekeza kwenye kampuni ya usafirishaji majini. Aliamua kuwekeza kwenye kitu ambacho anakipenda. Utoto wake wote amecheza kwenye ufukwe wa bahari mpaka kuzamia kwake kwenda nchini Afrika ya Kusini alitokea ufukwe wa Kigamboni. Kampuni yake ilikuwa inaitwa "Express Boat Transport" (EBT)-Ltd, lakini hakuna mtu alikuwa anafahamu kama mmiliki ni Mbweku Jr.

Aliajiri vijana wasomi wa Chuo Kikuu wakawa wanamuendeshea kampuni, huku akiwa na timu ya wanasheria wanaoendesha mambo yake, yeye mwenyewe yupo pembeni anafanya shughuli zake binafsi. Bado alikuwa anajipanga kumpa pigo la mwisho Takatifu hasimu wake Timammy. Hakutaka kabisa kumuua tena alitaka ampe adhabu ambayo mwenyewe atajiona hastahili tena kuishi duniani. Alijua tu licha ya Timammy kuwekwa ndani hawezi kufungwa jela kutokana na mtandao wake wa uhalifu unaomlinda.


Alichokitabiri ni kweli kikaja kikatokea. Timammy hakufunguliwa kesi yoyote kutokana na shahidi mkuu, Meneja wa Benki kukosekana. Bosi Timammy akarudi uraiani huku amemkuta mkewe kapoteza ujauzito wake. Maisha ya Mbweku Jr yakawa yamejaa bashasha mpwitompwito wakati maisha ya Bosi Timammy yakawa mvangemvange hayana starehe tena. Wakati huo huo alishawaweka vijana wake wa upelelezi wanafuatilia nyendo za Bosi Timammy bila mwenyewe kujua kama anafuatiliwa. Baada ya miezi mitatu tu, Bosi Timammy akanasa kwenye mtego mwingine wa Mbweku Jr. Timammy alikuja kukodisha boti kwenye kampuni ya Express Boat Transport-(EBT) -Ltd.


Alikuwa anataka kupelekwa kwenye kisiwa cha Mbudya yeye na mke wake kwa kutumia boti ya kisasa, nambari wani kwa ubora. Walikuwa wanataka utulivu wa nafsi zao baada ya kila mmoja kutoka kwenye misukosuko. Bosi Timammy akiwa ametoka rumande, na Deborah ametoka kwenye kupoteza ujauzito wake. Waliweka oda wiki moja kabla ya tukio lenyewe, hali ambayo ilimpa uwanja mpana wa Mbweku Jr kujipanga kutekeleza tukio analolikusudia.


Siku ya siku ikawadia ya Bosi Timammy na mkewe Deborah kupelekwa kisiwa cha Mbudya. Msafara wa kuelekea kisiwani ulianzia katika Hoteli ya Whitesands kwa kutumia boti daraja la kwanza linalomilikiwa na kampuni ya Express Boat Transport-(EBT) -Ltd. Ilikuwa ni boti yenye kila kitu ambayo kuikodi kwa saa gharama yake ni milioni 5. Bosi Timammy aliikodi kwa kulipia saa 10. Boti ikang'oa nanga, ikiwa na abiria watano, nahodha wa boti na sarahange wake, Bosi Timammy, Deborah na khadimu wao mmoja wa kike. Nahodha, alikuwa mwili nyumba, amejengeka misuli utasema anakula sementi, huku kichwani alivalia kofia ya pama iliyoficha sehemu ya uso wake, huku akionekana yupo makini na kazi yake ya kulisongesha boti lifike linapotakiwa. Sarahange alikuwa kijana mdogo tu aliyemaliza Chuo Kikuu, aliyevalia mavazi nadhifu ya kibaharia. Alikuwa na jukumu la kuwapatia takrima ya kahawa na vinywaji mbalimbali wanavyohitaji abiria wao.

Nahodha alikuwa anaiendesha boti hiyo kwa mwendo wa kinyonga, ili kuwapa fursa maridhawa wateja wao ya kifurahia mandhari ya baharini. Kuna wakati alikuwa analeta mbwembwe za kulizima boti na kuliacha boti hilo lisukwesukwe na mawimbi ya bahari kwa kupelekwa pande za yamini na shimari. Huku nahodha huyo anazunguka kwenye boti anaongea na sarahange wake kisha safari inaendelea tena. Hayo yote yalikuwa ni madahiro na manjonjo ya kuwathibitishia kuwa kampuni ya Express Boat Transport-(EBT) -Ltd hawabahatishi katika fani, wana manahodha waliofurutu ada katika uendeshaji wa vyombo vya majini. Muda wote wa safari Bosi Timammy alikuwa amemkumbatia mkewe, kichwa cha Deborah kipo kifuani pake. Wanacheka, wananong'onezana, wanatabasamu pamoja ilimradi, waliweka pembeni shida zao zote na kuamua nuzuha hiyo ya kisiwani iwe ni ponyo na faraja kwa mazonge yote waliyoyapitia katika maisha yao.

Walipowasili Kisiwani walijikuta wametumia zaidi ya dakika 50, kwa safari ya takribani robo saa mpaka dakika 20. Yule khadimu wao aliposhuka tu, akaanza harakati za kuwasha majiko maalumu waliyokuwa wamekuja nayo kwenye boti. Majiko hayo yalikuwa ni kwa ajili ya kuchomea nyama ya mbuzi, kuku na samaki wabichi. Bosi Timammy na Nahodha wake wakapanda boti kwa mara ya pili kwa ajili ya kuvua samaki watakaowaleta kwa ajili ya kuchomwa kwenye jiko. Bosi Timammy ni katika vitu alikuwa anapenda katika maisha yake ni uvuvi wa samaki wa kitalii. Walipanga kwenda bahari kuu, hiyo ikiwa ni zaidi ya maili 12 kutoka pwani na sio chini ya himaya ya taifa lolote. Wakavaa nguo za kazi wakibeba na dhana za kazi za uvuvi wakajitoma baharini tayari kwa msafara wa mara ya pili. Hiyo ilikuwa ni majira ya mafungulia ng'ombe, jua bado halijachanganya vya kutosha. Wakatembea kwa zaidi ya maili 6 bila kuzungumzishana, kama kawaida yake Bosi Timammy akiweka mbele kiburi chake cha pesa. Ghafla bin vuu....Nahodha yule akazima injini ya boti.

"Huu ni ufala, nalipia pesa kochokocho halafu mnaweka mafuta kidebe, wewe una akili kweli au taahira..!" Bosi Timamny tayari alishajaa upepo kwa hasira baada ya kuona boti limezima tena wakiwa kina kirefu cha bahari. "Samahani Bosi tulijisahau, ngoja nifanye mawasiliano na wenzangu walete msaada wa haraka....!" alijibu Nahodha yule kinyonge sana huku akiendelea kuishindilia kofia yake kichwani kuzidi kuficha wajihi wake. "Nipe namba ya Meneja wako, wewe lazima ufukuzwe kazi leo mjinga mkubwa wewe...!" alifoka Bosi Timammy na bila kutarajia akamuezeka kibao cha nguvu shavuni yule Nahodha. Shambulio ambalo liliamsha chemchem ya hasira kwa Nahodha yule na kujibu mapigo kwa kumrushia teke la shingo Bosi Timammy, akaanguka mpaka chini kama gunia la mahindi.

"Mshenzi mkubwa wewe utanitambua leo, nitakuchakaza mpaka unitajie jando langu nilifanyiwa pori gani na ngariba wangu anaitwa nani..!" alisema kwa hasira yule Nahodha wa boti ambaye sasa alishatupa pembeni kofia yake na kuidhihirisha sura yake hali. "Khaaaaah....kumbe wewe ni best Mbweku Jr Shikamooo sana...!" Bosi Timammy kiherehere chote kilimuisha na kutumbukiwa na nyongo baada ya kugundua kuwa Nahodha wake aliyemchapa kibao ni Mbweku Jr.

."Ha.. ha.. ha....Mwanaharashi mkubwa wewe, pesa zangu zipo wapi? Deborah niliyekukabidhi akiwa na kizinda chake umsomeshe mpaka mwisho wa elimu yupo wapi? Baba yangu niliyekukabidhi umpelekee huduma Jela yupo wapi? Mbweku Jr rafiki yako aliyekuomba tu umlipie faini Mahakamani baada ya kukamatwa kwa uhamiaji haramu nchini Afrika ya Kusini yupo wapi? Au umeshamuua baada ya kumtumia jambazi jela na kumletea chakula cha sumu?" alikuwa Timammy anasomewa risala ya kifo wakati ameshakabwa koo yupo chini amelazwa kwenye ya boti.


"Ni...sa....me....he...... nipo....ta... yari.....kukupa....haki zako zote...!" aliongea kiunyonge kwa sauti ya kilio cha kwikwi chenye majuto ndani yake, huku boti iliyoitwa kutoa msaada na Mr.Mbweku Jr Nahodha feki ikiwasili eneo la tukio. Hofu ya Bosi Timammy ikazidi kuongezeka akijua fika hawa huenda ni maharamia wa Kisomali wenye michezo ya kuteka Meli kwenye bahari kuu. Wameitwa na hasimu wake wamchukue wakamtupe huko kwenye kina kirefu zaidi akaliwe na papa na nyangumi. Ghafla akaona timu ya watu wanashuka wakiambatana na baadhi ya Mameneja wake mwenyewe wa kampuni, pamoja na baadhi ya Watumishi wa Benki wakiwa na Brifkesi zao.

Bosi Timammy alizidi kunyong'onyea vilivyo wala hajui nini kinachotaka kufanyika mbele yake. Akajutia nafsini mwake kwa kuendekeza tamaa na uroho wa mali, ama kweli mbio za sakafuni huishia ukingoni. "Eheee....elezea hapa mbele ya mashahidi namna utakavyonilipa pesa zangu zote.....!" aliongea Mbweku Jr mbele ya watu wale waliokuwa wanafika idadi yao kama 6 hivi. Bosi Timammy alikuwa mnyonge kupitiliza, uso umemshuka kwa aibu utasema ni mzee wa miaka 80. "Usitake kunitibua nyongo, elezea mbele ya hadhira hii namna ulivyonidhulumu pesa zangu na kutaka kuniua ili nisije kudai mgao wangu, maana watu wasidhani ninakudhulumu, kwa kawaida mtenda akitendewa huona kaonewa.....!" alizidi kufoka Mbweku Jr ameshapandisha ruhani wake wa ugomvi huwezi kumuambia kitu akakuelewa.


Ikabidi Bosi Timammy ajikaze kisabuni, na kuanza kuelezea mkasa mzima wa chanzo cha utajiri wake na madhila mbalimbali aliyoyafanya juu ya swahibu wake Mbweku Jr. Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili ikaamriwa, yafanyike makabidhiano ya mali zote za Bosi Timammy kwa Mbweku Jr kisheria. Timu ile ya Wanasheria sasa ukageuka uwanja wao wa kumsainisha nyaraka mbalimbali Bosi Timamu za makabidhiano ya mali. Uzuri tayari walishafanya speksheni ya mali zote anazomiliki Bosi Timammy na nyaraka zote za umiliki zililetwa na Watumishi wake waandamizi. Bosi Timammy bila pingamizi lolote akasaini nyaraka zote, na pesa zake zikahamishwa na Watumishi wa Benki pale pale kwa kutumia dhana zao za kazi na kuingizwa rasmi kwenye kampuni ya Express Boat Transport-(EBT)-Ltd. Baada ya kama muda wa kama saa 2 shughuli ile ikafikia tamati.

. Sasa rasmi baada ya kikao kile Bosi Timammy akageuka kuwa Mlalahoi na sio Mlalaheri tena. Mbweku Jr ili kuwachagiza wale Watumishi Waandamizi wa Bosi Timammy wasije kufanya hujuma kwenye Biashara, akawaahidi wote kutowafukuza kazi, waendelee na nyadhifa zao kama kawaida. Kilichobadilika kwao ni Mmiliki tu wa Kampuni. Ile timu ikaondoka zao, huku wakiisindikiza boti ya Mbweku Jr na Bosi Timammy mpaka ifike Kisiwa cha Mbudya.


"Tuondoke mke wangu sijisikii vizuri kiafya....." ilikuwa ni kauli ya Bosi Timammy baada ya boti kutia nanga ufukweni. Nyama za mbuzi na kuku walionona wenye kuchuruzika mafuta zikawa haziliki tena. Njia nzima wakati wanarudi hamna mtu aliyekuwa anamzungumzisha mwenzake mpaka Deborah alipovunja ukimya. "Mume wangu isije kuwa hii mikosi inatuandama kwa sababu hatuishi vizuri na ndugu, jamaa na rafiki zetu. Hivi yule rafiki yako Mbweku Jr aliyenihadithia kuwa alifia nchini Afrika ya Kusini kwa matumizi ya mihadarati, ndugu zake unawasaidia kweli? Tufanye walau tukawaone mie kwa upande wangu yule alikuwa kwako ni zaidi ndugu na kwangu yule ni zaidi ya kaka, Mungu amlaze mahali pema peponi......Ameeen! " Aliongea Deborah kwa hisia kali mpaka machozi yanamtiririka huku bila kujua anapiga bomu Ikulu, amelenga pale pale anapopata Mbweku Jr kuwa ukweli ujulikane kuwa mumewe ni mmoja wa Mafioso.

"Kumbe, mimi Mbweku Jr nimeshakufa tayari na kuzikwa...! Wewe mbwa koko hata aibu huna..! " alijikuta Mbweku Jr anaingilia mazungumzo hayo, huku akiwa tayari ameivua tena kofia yake hali ambayo ilimfanya Deborah sasa amtambue dhahiri shahiri. Kipindi hicho Boti ilikuwa inaendeshwa na Sarahange anapata uzoefu wa kuwa Nahodha kivitendo, hivyo Mbweku Jr alikuwa yupo jirani na Bosi Timammy, mkewe Deborah na khadimu wao.


"Khaaah....Kaka Mbweku Jr kumbe upo hai kaka? Kwanini lakini rafiki yako, mume wangu Timammy kanidanganya wewe ni marehemu, mmegombana nini haswa mpaka kufikia hatua hiyo ya kuleteana uchuro wa kifo jamani.....!" alilalama Deborah kwa uchungu mkubwa na kuangusha kilio kizito mpaka anajigaragaza chini. Fujaa akaonekana Bosi Timammy amekurupuka kwenye boti na kujitosa ndani ya bahari. Bosi Timammy alishindwa kuhimili vishindo vya aibu atakayoipata mbele ya mkewe pindi ukweli halisi ukianikwa hivyo, alifanya maamuzi ya kujiua majini.

MWISHO






0 comments:

Post a Comment

Blog