Search This Blog

Thursday 23 March 2023

HUBA LA MISS TANZANIA - 1

 

IMEANDIKWA NA :  BADI M. BAO
*********************************************

Simulizi : Huba La Miss Tanzania

Sehemu Ya : Kwanza (1)


Mchakamchaka chinja la mgambo limelia, asiye na mwana aeleke jiwe, hoi hoi, shamrashamra, vifijo na nderemo vilitawala nyumbani kwa bwana na bibi Shamsi Sakuzindwa aliyekuwa anaozesha binti yake mpendwa mwenye kupendeza kama lilivyo tamu jina lake, Zabibu.

Ilikuwa ni siku ya hitimisho la uchumba wao wa zaidi ya miaka mitatu mfululizo wa kijana Shebby na Zabibu. Vijana ambao penzi lao lilikuwa mithili ya mapacha au kumbikumbi wanaoambatana pamoja kila wakati kwenye kila kiunga cha jiji la Dar es Salaam. Kijiji kizima cha Mzundu kilichopo wilayani Handeni, mkoani Tanga, siku kilikuwa kimepiga kambi nyumbani hapo karibia juma zima kuhakikisha ndoa hiyo inapita kwa amani na usalama. Walikuja kuwapongeza wawili hao kwa kuonyesha mfano halisi wa ujasiri wenye busara wa kufunga ndoa na kuishi kama mke na mume na si mahawara kwenye uchumba sugu kama ilivyo kwa vijana wengi ambao wanaiogopa ndoa kama ukoma.


Kama ujuavyo, ndoa si kitu cha mchezo mchezo kwa kuwa ni kutimiza amri ya Mwenyezi Mungu na kudhihirisha kukua kiakili na kimwili pia. Usiku wake kulikuwa na mkesha wa ngoma za jadi za kabila lao la Wazigua, ngoma za Mkweso na Machindi zilizovurumishwa mpaka liamba zikiburudisha wageni waalikwa. Asubuhi yake sherehe ya kitamaduni ikatamatishwa, ikawa sasa ni sherehe rasmi ya ndoa ya kiislamu ikihitimisha sherehe nzima za juma lote. Dufu, ngoma maarufu katika hafla za kiislamu zikawa zinapigwa na kuchezwa kwa mitikisiko yenye kuvutia katika masikio na macho ya mtazamaji toka kwa vijana wa madrasa ya hapo hapo kijijini Mzundu. Sauti za kuvutia za nyimbo za kaswida zinazoimbwa kwa lafudhi ya lugha ya kiarabu na kiswahili zilisikika. Sauti ambazo zilikuwa zikiambatana na milio ya nai na zumari huku midundo ya dufu za aina mbalimbali kama ogani, namba wani, besi, kibakubaku na nyinginezo nyingi zikawa zinadundwa kwa ustadi wa hali ya juu.

Siku hiyo mashamushamu yake yalikuwa sio ya kawaida, hata ndege angani na wanyama porini nadhani nao walipashika habari ya sherehe hiyo kuwa Zabibu kapata mchumba sasa anaolewa, kutokana na hekaheka na pilikapilika zilizoambatana na furaha sheshe ya wanakijiji hao. Waoaji walikuwa wanatokea jijini Dar es Salaam, na tayari walikuwa wameshawasili katika viunga vya kijiji hicho wanavinjari na motakaa zao za gharama tayari kumnyakua mwali, fujo zao tu kila mtu alijua, majogoo ya mjini hayooo yamekuja kuwika kijijini.

Walikuwa wamekuja na sanduku zima la vihendo maalumu kwa ajili ya bibi harusi, na familia yake, kama nguo, seti za mapambo ya dhahabu, viatu na vikorokoro vingi tu vya kuchombeza shughuli hiyo ili mradi ifane vile inavyopaswa kutokana na hadhi ya mrembo Zabibu. Bila kusahau moja ya bidhaa za mahari ya kimila walizoagizwa kuja nazo siku ya harusi kama tundu la mwigazi, ambaye ni kuku mtetea na vifaranga vyake saba, blanketi na mkongojo wa babu.

Mama mzaa chema hakuwa nyuma katika tafrija hiyo, furaha yake ilikuwa fokofoko akijifunga kibwebwe kiunoni kusakata burudani mbalimbali zilizokuwa zimeipamba siku hiyo adhimu kwa familia yao. Ndugu, jamaa na majirani kila wakati walikuwa wanamzingira na kumsukasuka kwa ajili ya kumpa mkono wa pongezi, wengine wanampa tuzo ya pesa, vitenge na kuitakia sherehe hiyo iwe ya heri na fanaka. Kwenye upande wa maakuli na mashrabu nako kulikuwa ni moto wa gesi, hii bila kusahau ni sekta muhimu kabisa kwenye sherehe yoyote ile ipate kufana. Si unajua Tanga kwa misosi ndio kwenyewe!. Sasa unafikiria nini kwenye mambo kama hayo? Usipime unaambiwa, wanawake wao mikono yao ina uchawi maalumu wa upishi wa ngano, basi kupitia ngano wanaweza kukutengenezea sambusa, visheti, maandazi, chapati, kalimati na vinginevyo vingi katika mahanjumati.

Kwa waliokuwepo hapo kijijini siku hiyo, walifaidi hadi kusaza mahanjumati. Kama ilivyozoeleka katika sherehe nyingi, huwa kuna muda maalumu wa chakula na mara nyingi huwa ni katikati au mwishoni mwa sherehe. Sasa unaambiwa kwenye sherehe hiyo ya ndoa ya Zabibu, hayo mambo hayakuwepo, chakula kilikuwa kinaliwa mwanzo mwisho, yaani watu walikuwa wanakula huku ratiba nyingine zikiendelea. Kwenye sekta hiyo familia ilijipanga haswa ng'ombe liliofutwa kodi na mbuzi wa kutosha waliangushwa, kupikia madikodiko na masontojo ya anuwai mbalimbali kuanzia samaki wa kupaka, rosti za nyama, rosti maini, chai ya maziwa, chai ya rangi, chapati, maandazi, vitumbua, na mbwembwe kochokocho za mapishi ya ngano.

Ilikuwa ni sherehe ambayo ilipangwa iache gumzo kijijini hapo karibia miongo kadhaa. Minyoo ya matumbo ya wanakijiji siku hiyo ilishtuka kwa kuvamiwa na chakula jadidi wasichokizoea. Maana vyakula vya asili vinavyopendelewa kuliwa na kabila la Wazigua ni ugali. Ambao unapikwa kutokana na unga wa mahindi yaliyokobolewa na kuvundikwa kwa muda mrefu kabla ya kusagwa au kutwangwa. Baada ya kusagwa hutoa unga mweupe na laini sana. Ugali huo huliwa na mboga za asili kama vile, Kungujulu, Sunga, Kididi, Mnavu, nyama za pori na uyoga, lakini siku hiyo walikuwa wanalishwa chakula cha tabaka aali katika jamii.

Gharama za fujo zote hizo zilibebwa na ofisi anakofanyia kazi binti yao Zabibu. Alikuwa ameajiriwa kwenye moja ya benki za kigeni inayovuma kwa sasa nchini Tanzania ijulikanayo kama 'Turkish Commercial Bank' (T.C.B) akiwa kama afisa uhusiano. Mbali ya ufadhili huo walimuandalia pia sherehe kabambe ya kukata na shoka jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mlimani City Hall punde tu atakaporejea jijini Dar es Salaam. Sherehe ambayo vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi vilishanunua haki miliki ya kurusha tukio hilo kwa mamilioni sufufu.


Wataachaje kurusha tukio hilo la ndoa ya Miss Tanzania kipenzi cha wananchi, jina lake lilikuwa tamu kama peremende midomoni mwao, asiye na skendo yoyote ya ufuska, wala tabia mbovu za kuchefua jamii!. Hayawi hayawi sasa yakawa, muda uliokuwa unasubiriwa kwa hamu wa kupitishwa kwa nikaha hiyo baina ya Zabibu na mumewe mtarajiwa Shabani Zomboko dereva taksi za UBBER, mzawa wa Kariakoo au maarufu kwa rafiki zake kwa jina la 'Shebby-Zoo' ukawadia. Vyombo vya habari kochokocho kuanzia magazeti, televisheni, redio, blogu mbalimbali za mitandao za kijamii nazo hazikuwa nyuma kuja kurusha taarifa ya hafla hiyo kutoka kijijini.

Vyombo hivyo vilitaka kupaisha habari hiyo ya ndoa ya mlimbwende Zabibu Shamsi, mshindi wa taji la mrembo wa nchi, Miss Tanzania. Motakaa za kila aina zilitapakaa kijijini pale, kupamba mandhari ya sherehe hiyo, zikitokea pande mbalimbali za Tanzania kujua kushuhudia tukio hilo adhimu. Yalikuwa ni magari ya mashoga zake Zabibu na rafikize Shebby walikuja kuwaunga mkono kwenye tukio ambalo hata malaika wa mbinguni hupiga vigeregere kwa furaha pindi wapendanao wanapofunga ndoa.

Pia Mwenyezi Mungu, khalaka wa ardhi, mbingu na vilivyomo baina ya mbingu na ardhi nae anafurahi sana, pindi wanaadamu wanapochukua maamuzi ya kufunga pingu za maisha. Lakini aksi yake Ibilisi, shetani mkuu anakuwa na huzuni na hasira za kupitiliza pindi ambapo watu wanapofanya maamuzi ya kuungana kuwa mwili mmoja. Kwasababu anakosa wateja wake katika dhambi yake pendwa ya uzinifu, anaona wamemuacha solemba kwenye mataa. Nikaha hiyo ilipangwa kufungwa majira ya dhuhaa katika wakati wa mafungulia ng'ombe, baina ya saa 2-3 asubuhi katika msikiti wa ijumaa wa hapo kijijini, kisha sherehe zote kwenda kuhitimishwa nyumbani kwa bibi harusi. Huko kwa bibi harusi ndipo watu watakula, watakunywa na kucheza kutwa nzima mpaka majira ya usiku mbichi ndio itakuwa tamati yake.

Bwana harusi Shebby-Zoo akiwa amesindikizwa na wapambe zake ithnani wa chanda na pete, wa toka utotoni. Wamecheza mpira wa chandimu wote mpaka sasa wamekuwa wakubwa bado ni maswaiba. Walikuwa tayari wamewasili msikitini wanasubiri kukabidhiwa jiko lao la Kizigua warudi nalo jijini Dar es Salaam wakaendekeze libeneke la sherehe upya. Walikuwa wamevalia kanzu zao nyeupe nadhifu na majoho ya rangi ya kijani yenye ufito wa rangi ya samawati kwenye kola zake, huku vichwa vyao vikifunikwa na kofia za kuziua kwa mkono za rangi ya kahawia. Bwana harusi alikuwa anatembea na mkongojo wa urembo ili mradi kuleta nakshinakshi na mvuto wa muonekano wake. Kwa ujumla Bwana harusi na wapambe wake walipendeza sana machoni pa watazamaji.

Sheikh Ayoub Makoja, shaibu kiumri, unaweza kumkadiria miaka 50-55 kama ukipewa mtihani wa kumpachika umri wake, imamu mkuu wa msikiti huo nae alikuwa nadhifu katika vazi la kanzu yake nyeupe na kilemba kichwani, huku akiwa ana kitabu cha rejista ya ndoa na kitabu kingine maaalumu cha hotuba ya ndoa huku anahesabu tasbihi mkononi. "Salaam Aleikum nyie Wazaramo, karibu sana Handeni, ha.. ha... ha.." Sheikh Ayoub aliwasalimia waoaji, akawataniana kwa bashasha huku pia anapeana nao mikono. "Waleykum salaam Sheikh, ndio tumekuja kumbeba jumla jumla tumpeleke Uzaramoni, binti yenu wa Kizigua" walijibu salamu kwa pamoja kisha mmoja wa mpambe wa Bwana harusi akaujibu utani huo wa Sheikh. "Mmemaliza mahari lakini? Maana zamani enzi sisi tupo vijana kama hujamaliza mahari huondoki na mke!. Unabakia hapo hapo ukweni" alizungumza Sheikh Ayoub na waoaji wale huku wakisubiria watu wazidi kujazana msikitini kushuhudia akidi hiyo.

"Aaaah...Sheikh unatuonaje sisi, Wazaramo hatujazoea kuishi kwa mikopo, sisi ni maskini jeuri tumemaliza mahari yote na vihendo juu tumezidisha" alijibu mpambe yule ambaye alikuwa ni fundi wa matani. "Vizuri sana mnaonyesha mmepania, ila zamani hali ilikuwa tete sana. Wazee wa mila walikuwa wanaandaa tukio linaitwa Kulagasama. Hilo ni tukio la kuagwa kwa waliooana mara baada ya kukamilisha mahari na taratibu zote za kimila. Katika mila za Kizigua, ilikuwa mtu anapofunga nikaha, yeye na mkewe hutakiwa kukaa katika familia ya mke wake huyo kwa muda fulani ili aweze kukamilisha mahari kama alikuwa hajamaliza. Hivyo akimaliza kulipa mahari na mambo mengine yanayohitajika, huomba ruhusa toka kwa wakwe zake ili akaanzishe maisha yake na mkewe. Alikuwa kama akishindwa kulipa ataendelea kuishi upande wa mkewe kwa maisha yake yote na hata kama akifariki atazikwa upande wa ukweni kama ukoo wa upande wa mume hautamlipia, ila kama wakimlipia watapewa mwili kuzika upande wa mume. Lakini sasa mna raha sana mila na desturi sehemu nyingi hazifuatwi ipasavyo" alisimulia kwa uso wa bashasha Sheikh Ayoub mambo jinsi yalivyokuwa enzi zao wako barobaro mambo yalivyokuwa.

"Sheikh unachosema ni ukweli kabisa wala hatukubishii, kila zama na kitabu chake, siku hizi kuanzia sherehe za unyago, jando, harusi hamna tena ngoma za asili, sasa ni mwendo wa muziki wa singeli tu kwenda mbele" alizungumza kuchangia mazungumzo mpambe mwingine wa Bwana harusi, huku Bwana harusi mwenyewe akiwa amejiinamia chini, amefumbata viganja vyake vya mkononi. Inaonyesha alikuwa kwenye tafakuri nzito juu ya jambo analotaka kulielekea katika historia ya maisha yake. Tukio ambalo litambadilisha sasa na kuitwa mume wa Zabibu, pia tukio ambalo Mwenyezi Mungu akiwabariki watapata matunda ya ndoa, ambayo ni watoto, hivyo atakuja kuitwa baba fulani.

"Assalamu alaykum warahmatullah wabarakaatuhu jamiaaa.." Sheikh alikatisha mazungumzo baada ya kuona idadi ya watu wameshajazana pomoni msikitini wanasubiria shughuli ya kufungisha ndoa ianze, kisha akawasalimia kwa salamu maarufu kwa waislamu. "Waalekum salaam warahmatullah wabarakatuhu" wakajibu wote kwa nidhamu na taadhima salamu toka kwa Sheikh wao. "Sasa tunataka tuanze ibada ya kufungisha ndoa.

Mtume wetu Muhammad (S.A.W) ametufundisha kuwa Kukamilika ndoa lazima kwanza yatimie masharti yafuatayo:
kwanza ipatikane Idhini ya Walii. Alhamdulillahi baba mzazi wa muolewa yupo hapa Mzee Shamsi kashafika msikitini. Pili, Kuridhika kwa bibi harusi mtarajiwa. Hivyo hili sharti tutatuma watu nyumbani kwa bibi harusi kumuuliza kama hii ndoa anaifahamu na ameridhia. Sharti la tatu ni kutimia kwa tamko la ndoa yaani Ijaab na Qabuul, yaani iijab na qubuul iliyounganishwa kwa tamko la ndoa au yenye kufidisha maana hiyo. Sharti la nne ni kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu. Na mwisho Kubalighi na kuwa na utambuzi baina ya wanandoa, hivyo haifai kuwepo kwa ndoa ikiwa mmoja wapo ni mwendawazimu au mdogo kwa umri na bado hajabaleghe. Sasa kabla sijaanza khotuba ya ndoa, ningependa shahidi mmoja wa upande wa muoaji na mwingine kutoka kwa muolewa waelekee mubashara mara moja nyumbani kwa Bibi harusi wakamuulize kama anazo habari ya hili tukio linalotaka kuendelea hapa msikitini.

Tunawapa muda wa nusu saa muwe mmesharejea, Inshallah maa-salaaam" alitoa maelezo yenye ufasaha Sheikh Ayoub, mara moja akanyanyuka mmoja wa wapambe wa Bwana harusi na mwakilishi wa kikeni wakaelekea nyumbani kwa Mzee Shamsi, baba wa Zabibu. Baba mzazi wa Zabibu na waumini wengineo wakabakia ndani ya msikiti wanabadilishana mambo mawili matatu. Zikapita sekunde, dakika, sasa yakawa masaa walioenda nyumbani kwa mwali hawajarejea. Taharuki ikaanza kutawala mule msikitini, zogo la minong'ono likaanza kusambaa mle msikitini.
JE NDOA ITAFUNGWA KWELI AU BIBI HARUSI KALALA MITINI??



"Takbiiir....Takbiiiiir" ,alitamka kwa sauti ya juu Sheikh Ayoub maneno ya kiarabu yenye maana ya Mtukuzeni Mwenyezi Mungu. Waumini wote wakaitikia msikitini wakaitikia "Allahu Akbar...Allahu Akbar....", wakimaanisha Mwenyezi Mungu ni mkubwa. "Ndugu zanguni tuweni na ustahamilivu na subira, Qur' an Iinasema, inna-llah maa swaabirina, hakika ya Allah yupo pamoja na wenye subira, tuache zogo msikitini hii ni nyumba ya Allah na sio marikiti hapa, sehemu ambayo unaweza kubwabwaja upendavyo.

Nimeshatuma watu wengine waende kujua kulikoni huko mbona wanachelewa tunawapotezea watu muda bure, Pia tunawapiga simu sasa hivi tutawajuzeni kilichojiri, ahsantum" alitoa nasaha Sheikh Ayoub baada ya kukerwa na makelele ya waumini msikitini. Simu zilizokuwa zikipigwa nyumbani nazo hazikuwa na majibu ya kueleweka, yenye nakisi na mashaka mengi kuliko matumaini. Mpaka kufika muda wa jua la mtikati mbivu na mbichi zikawa dhahiri shahiri, kweupe. Kama ni jipu ni pwaaaah...! likawa limepasuka.


Penyenye zisizo na chembe ya mashaka zilizofika msikitini zilisema Bibi harusi Zabibu Shamsi Sakuzindwa alikuwa amejiua, kwa kujichoma kisu tumboni. Taarifa hizo za kifo zilivyosambaa mule msikitini, zikasababisha simanzi, huzuni, taharuki na sononeko katika mioyo ya ndugu, jamaa na marafiki wa wana ndoa hao tarajaji, ambao ndoa yao ilishaingia mdudu, haiwezekani tena kufungishwa. Kila mtu alitawanyikia njia yake, kutoka mle msikitini. Wapo waliosahau makubazi yao kutokana na kuchanganyikiwa na taarifa hizo ngeni kijijini kwao.


Mkosi na balaa wa sampuli hiyo ulikuwa ni wa kwanza kutokea kijijini hapo. Vidinga popo na wale akina habari kauzwa wakawa wamepata cha kusimulia vijiweni. Simulizi zao juu ya kifo cha Zabibu zikawa ukweli kidugu lakini ndimu na chumvi kibao ili mradi kunogesha porojo zao. Kijiji kukawa ni taharuki mtindo mmoja, hali ilikuwa mchafukoge, harusi ikageuka kuwa matanga.


Chakula kilichoandaliwa kwa ajili ya sherehe kikageuka kuwa cha matanga. Hadithi ya penzi tamu la kusisimua kati ya Zabibu, Miss Tanzania na Shebby Zoo ikafikia tamati. Hamkani mambo yakawa sio shwari tena, habari hiyo ikasambaa Tanzania nzima na viunga vya nchi za jirani. Tukio la mrembo ambaye amewahi kutwaa taji la Miss Tanzania kujiua kikatili tena siku ya harusi yake ilikuwa ni habari ya kushtua na kuogopesha sana. Swali la kila mtu alilokuwa anajiuliza ni kuwa amepatwa na maswaibu gani mlimbwende huyo mpaka afikie hatua ya kuyaondosha maisha yake kikatili namna hiyo tena bila kuacha ujumbe wowote unaoweza kuibua fununu za kifo chake.

Ilipofika majira ya jua la utosini tayari askari kanzu si chini ya wanne wakiongozwa na mpelelezi mkuu wa kituo kikuu cha polisi cha Handeni, Inspekta Hamduni walikuwa walikuwa wameshatia timu msibani. Walikuwa wanasubiria kwa hamu na wanakijiji ili waweze kupata fununu ya chanzo cha kifo hicho. "Poleni na msiba" alisalimia Inspekta Hamduni kwa baba wa marehemu. "Ahsante tumepoa ingawa siamini kilichotokea, Mwana kaita mjima ...... hahumile ooooh ooooh Mungu wangu" alijibu Bwana Shamsi huku akiwa anajifuta machozi kwa ncha ya vidole vyake huku anazungumza Kilugha kuwa mtoto kafariki kijana wala hajaumwa.

Mama Zabibu, mke wa Bwana Shamsi alikuwa nae hajiwezi, alilia mpaka akapoteza fahamu, alipozinduka akawa hata sauti haitoki tena, amebaki kuwa kama zuzu. "Mara ya mwisho kabla ya kifo chake, marehemu Zabibu alikuwa na nani?" alitupiwa swali baba wa marehemu. "Mimi nilikuwa msikitini nasubiria kumuozesha binti yangu, sikuwepo nyumbani ila kupitia simulizi za mashuhuda niliambiwa mpaka dakika za mwisho alikuwa na kungwi wake Bi Maua na ndio alimsindikiza mpaka msalani" alijibu baba wa marehemu Kiutulivu bila papara yoyote.

"Alishawahi kukudokezea dukuduku lake lolote linalomsumbua kabla ya ndoa yake binti yako?" aliendelea Inspekta Hamduni kuuliza maswali huku anarekodi mahojiano hayo kwenye kinasa sauti chake cha kisasa. "Hapana, hata mimi nimeshangazwa na uamuzi wake binti yangu, namuachia Allah tu nisije kukufuru bure" alijieleza baba Zabibu. "Ahsante kwa ushirikiano wako, usisite kutupa taarifa iwapo utapata fununu zozote zitakazosaidia upelelezi wetu! Pia nitaomba kuonana na kungwi wa marehemu Bi maua, huenda ana chochote kitu cha kutuhabarisha" alihitimisha mahojiano yake na baba wa marehemu.

Bi Maua akapewa taarifa za wito akawa anakuja himahima huku moyo unamdunda kwa uoga.
JE BI MAUA NI MHUSIKA MBONA ANAOGOPA KUKUTANA NA POLISI KAMA HANA HATIA?


Hofu yake Bi Maua ilikuwa ni kuangushiwa nyumba bovu la mauaji kama uwajuavyo baadhi polisi wetu, kwenye matatizo wao kwao ndio neema ya kuvuna kipato, ganda la muwa la jana chungu kaona kipato. Fauka ya hapo ni wavivu wa kufanya upelelezi wa kina, hivyo anaweza kukushikilia usaidie upelelezi ukaishia unaozea jela, hilo ndilo lilikuwa linampa uoga wa kukutana na afande, Bi Maua.


Inspekta Hamduni: "Naitwa Inspekta Hamduni, nimekuja kwenye uchunguzi wa wa kifo tata cha Zabibu. Nitajie majina yako matatu kamili"(Alianza mahojiano Inspekta na Bi Maua mara baada ya kufika)


Bi Maua: "Naitwa Maua Hassani Kipande"

Inspekta Hamduni: "Umri wako! "

Bi Maua: "Miaka 50 natimiza mwisho wa mwezi huu! "

Inspekta: "Kazi yako! "

Bi Maua: "Mimi nimejiajiri,ni kungwi wa kufunda wali, pia nauza dawa za mvuto katika mahaba kama ndere na zinginezo"

Inspekta Hamduni: "Umeolewa? "

Bi Maua: "Hapana Bwana afande sijabahatika"(alijibu Bi Maua kwa aibu huku ameinamisha kichwa chini)

Inspekta Hamduni: "Sasa unawafunda kitu gani hao wali wakati hata ndoa hujawahi kuolewa! "(Aliuliza huku anatabasamu Inspekta)

Inspekta Hamduni:" Anyway tuyaache hayo ni mambo yako binafsi sipaswi kuwaingilia, eheee....ulijuana vipi na marehemu Zabibu"

Bi Maua: "Namfahamu tokea akiwa msichana mbichi anasoma shule ya msingi hapa kijijini miaka hiyo"

Inspekta Hamduni: "Ilikuaje mpaka akakuchagua wewe kuwa ni kungwi wake wa kumfunda kwenye ndoa yake! "

Bi Maua: "Mama yake mzazi ni shoga yangu, hivyo ilivyokuja posa, wakalipa 'gubula lomo', ndio mama yake akanipa kazi ya kumfunda binti yake juu ya maisha ya ndoa.

Inspekta Hamduni: "Hiyo gubula lomo ndio nini sijaelewa fafanua tafadhali!"

Bi Maua: "Hiyo ni kifungua kinywa, kwa mila zetu Wazigua, mshenga akija kuleta posa lazima alipe kifungua kinywa"

Inspekta Hamduni: "Ulikaa na marehemu siku tokea maandalizi ya ndoa mpaka siku ya ndoa"

Bi Maua: "Nimekaa nae siku tatu pamoja na hii ya ndoa"

Inspekta Hamduni: "Je kuna dalili zozote za hatari uliziona kwake kama viashiria atakuja kujiua? "

Bi Maua: "Hamna dalili kubwa sana, ila nilichokiona alikuwa na msongo mkubwa wa mawazo hali iliyompelekea kutokuwa mzingativu wa ninachomuelekeza. Mie nikajua ni dharau zao hawa kizazi kipya na hasa ukichukulia ni mmoja wa wasichana waliowahi kushinda taji la ulimbwende la Miss Tanzania"

Inspekta Hamduni: Unaweza kutuelezea dakika za mwisho kuwa nae zilikuwaje? "

Bi Maua: Aliamka akiwa na afya nzuri tu, ila kama ninavyosema alikuwa mnyonge sana, tukawa tunajua ni uoga tu wa ndoa ambao unawapata wanawake wengi tu. Tukampamba akapambika vilivyo, kisha tukawa tumekaa nae ndani tunasubiria ndoa ipite msikitini. Muda wote alikuwa ametingwa na simu yake ya mkononi, mara aingie Instagram, mara aingie Whatsapp. Yote nilikuwa nashuhudia kwa sababu nilikuwa jirani nae.

Ghafla akaomba udhuru amebanwa na haja anataka kwenda msalani. Hivyo nikamsindikiza kwa kumshikilia kwa nyuma nguo yake ndefu isije ikapita kukomba vumbi njiani. Tulipofika msalani akaniachia simu yake nimshikie yeye akaingia ndani.

Dakika zikaanza kupita mpaka ilipotimu nusu saa nikaanza kupatwa na wasiwasi huenda amezidiwa na ugonjwa labda kapatwa na tumbo la kuhara au kaanguka chooni kapitiwa na jini. Nikaanza kumuita bila majibu yoyote. Ndio nikaja kutoa taarifa wakaja wababa kuvunja mlango wa choo, hamadi! Tukamkuta amelala kuegemea sinki la choo cha kukaa huku akiwa amejichoma bisu kubwa tumboni na utumbo wote umetawanyika sakafuni. Alikuwa anapumua kwa mbali sana, ndipo hekaheka za kumkimbiza zahanati ya kijiji inafanyika, lakini akapoteza uhai njiani kabla hajafika huko"( akamaliza maelezo yake marefu huku machozi ya uchungu yanamtiririka mashavuni )


Inspekta Hamduni: "Alikwenda kujisaidia huku akiwa na kisu mkononi au kisu ulimbebea wewe? "

Bi Maua: "Itakuwa aliktayarisha mapema akakificha huko huko mie sikumbebea kisu" alijibu Bi Maua swali ambalo uso wake ulionyesha lilimkera mno.

Inspekta Hamduni: "Hiyo simu yake ipo wapi? "

Bi Maua: "Kwa bahati bado ninayo sijaikabidhi kwa ndugu wa marehemu" alijibu Bi Maua huku anafungua pochi lake la rangi ya pinki.

Inspekta Hamduni: "Ahsante napokea kama kidhibiti, nitairejesha mara baada ya uchunguzi wangu kukamilika. Ahsante kwa ushirikiano wako mzuri nikikuhitaji tena sitosita kukutafuta"

Bi Maua: "Ahsante Bwana afande, karibu tena" alijibu Bi Maua huku ananyanyuka kwenye kiti chake alichokalia kipindi chote alichowekwa kiti moto na Inspekta Hamduni. Inspekta Hamduni alitamani aongee pia na mama wa marehemu lakini alikuwa sakimu wa hali yupo taabani hajiwezi.

Mume mtarajiwa wa marehemu Shebby Zoo nae alikuwa hoi bin taabani, alipatwa na mshtuko mkubwa sana wa kuharibika siku muhimu sana ya ndoa yake na mpenzi wake waliopendana kwa dhati. Baada ya dodoso ya hapa na pale, Inspekta Hamduni akaruhusu taratibu za kutoa maiti hospitalini ziendelee kwa ajili ya mazishi baada ya kujiridhisha kuwa marehemu amejiua mwenyewe.

Pia Inspekta Hamduni alikabidhi simu ya marehemu kwa familia baada ya kugundua laini zake zimenyofolewa, ni ganda tupu. Ilionyesha kuwa marehemu aliamua kupoteza ushahidi wowote wa mawasiliano yake ya mwisho.

"La Ilaha Illa Allah La Ilaha Illa Allah La Ilaha Illa Allah Muhammad Rasuul-llah..." ilisikika sauti ya Sheikh Ayoub Makoja ikipaa hewani kuwaimbisha umati wa waombolezaji waliofurika kuja kumsindikiza marehemu Zabibu katika makaburi ya kijini hapo Mzundu. Mazishi yalifanyika majira ya adhuhuri siku ya pili yake tokea kuaga dunia kwa Zabibu.

Waombolezaji nao wakawa wanaitikia matamshi ya Sheikh Ayoub huku wanatembea polepole na jeneza lililobeba mwili wa Zabibu likiwa mabegani mwao wanamsindikiza malaloni kwake. Umati wa waombolezaji waliokuja kuhani msiba wa Zabibu ulikuwa ni historia kwa pale kijijini.Vyombo vya habari kwao ilikuwa sherehe kubwa, maana walikuwa wanakusanya taarifa mbalimbali za tukio hilo kwa umakini mkubwa wapate kuwapasha walaji wao wa habari.
ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog