Simulizi : Matanga Ya Rohoni
Sehemu Ya : Tatu (3)
Sasa ikawa hata binamu zake, watoto wa Mjomba Kobelo ambao analala nao chumba kimoja, nao wakijikojolea kitandani msala wanamuangushia Debora kuwa ndio kajikojolea, hivyo mvua ya viboko mwilini inamshukia Deborah. Kazini kwa mama Debora ikafika barua ya kufukuzwa Chuo kutokana na kutoonekana kwa kitambo kirefu Chuoni. Wafanyakazi wenzake wa hospitali ya mkoa wakapanga ziara ya kumtembelea nyumbani kwake kujua kulikoni, Chuoni hayupo na kazini hayupo. Walichokipata nyumbani kwa Mjomba Kobelo hawatokuja kukisahau maishani mwao. Mjomba Kobelo aliwatimua kwa upanga wake akiwatuhumu kwa uchawi uliosababisha dada yake awe kitandani kwa muda wote. "Mmemroga dada yangu mkijua akimaliza masomo yake angewanyang'anya vyeo vyenu, nisiwaone tena kung'aza pua zenu nyumbani kwangu hapa wanga wakubwa, la sivyo nitawacharanga kama nyama ya buchani" alifoka Mjomba Kobelo huku yupo kidari nje hana shati mwilini. Watumishi wale wenzake mama Debora kila mmoja alijua namna alivyochomoka kwenye dhahama ile ya Mjomba Kobelo. Wapo waliopitia madirishani, wengine waliwahi kupita mlangoni na wengine walipenya kwenye uzio wa mabua ili mradi kila mmoja wapo alikuwa Yarabi Mola anasalimisha roho yake. Hawakukanyaga tena nyumbani pale, ndio ukawa mwisho wa ajira mama Debora, hakuwa tena na mtetezi.
Tarehe 1/09/1990 itakuwa ni siku ya kukumbukwa vizazi na vizazi kwa jamii ya Watanzania hasa kutokana na ugeni mzito walioupokea siku hiyo. Ilikuwa ni Jumamosi majira ya mchana, kadamnasi ya watu wa dini zote, makabila mbalimbali ya Tanzania na wa rika zote watoto, vijana kwa wakubwa walikuwa wamejipanga pande zote za barabara inayotokea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakiwa na majani, maua na bendera katika mikono yao huku wakiimba nyimbo mbali mbali, wakipiga shangwe na vigeregere wanapunga hewani. Walikuwa wanasubiria kumpokea Bwana Karol Joxef Wojtyla maarufu kwa jina la Papa John Paul II aliyekuwa katika ziara ya kuzitembelea nchi za Kiafrika zikiwemo Tanzania, Rwanda, Burundi na Ivory Coast. Alikuwa ndio kiongozi mkuu kabisa wa madhehebu ya kanisa katoliki duniani kipindi hicho akiwa ametokea nchini Vatican. Umati huo wa watu wapo walioanza kujikusanya barabarani kuanzia majira ya Alfajiri kwa kimuhemuhe, hamu na shauku ya kumuona mgeni huyo mukhtari. Papa huyo aliwasili uwanja wa ndege, aliposhuka tu moja kwa moja akaibusu ardhi ya Tanzania kisha akanyanyuka na kulakiwa na mwenyeji wake aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Mheshimiwa Rais Ally Hassan Mwinyi. Ilipofika majira ya saa 9 alasiri mvua kali ya kidindia ikanyesha sana lakini maajabu watu hawakuondoka barabarani mpaka alipopita Papa na kuwapungia mikono. Wapo wanaoamini kuwa rekodi yake ya umati uliojazana katika viwanja vya jangwani kusikiliza hotuba yake, haijavunjwa mpaka leo licha ya ujio wa marais watatu mfululizo wa Marekani, yaani Bill Clinton, George W. Bush pamoja na rais kijana mwenye asili ya Afrika, Barack Obama.
Ziara hiyo ya Papa huyo aliyetokea kuwa kipenzi cha wengi ilikuwa ni ziara iliyolenga zaidi katika Juhudi za Kupambana na gonjwa sugu la UKIMWI, pia hayati Yohane Paulo wa II alilenga zaidi Katika namna bora zaidi ya kuwahudumia wakimbizi. Pia aliambatana na timu nzito ya watendaji toka Vatican waliokuwa wanashiriki kuendesha mazungumzo mbalimbali ya kidiplomasia katika nchi mbalimbali walizotembelea na serikali husika. Pia walikuwa wanapata nafasi ya kufanya mazungumzo na asasi za kiraia zinazojihusisha na makundi muhimu katika jamii kama haki za watoto, mayatima, wanawake na mengineyo. Kwa kuwa Papa hakuwa na ratiba ya kutembelea nchini Kenya, hivyo Mkurugenzi wa kituo cha kulea yatima cha Cheryls Childrens Home and Learning Centre, Bwana 'Peter Ochieng' kituo ambacho mtoto mlemavu 'Pesambili Martin Tenga' ambaye ametelekezwa na wazazi wake alikuwa analelewa, hakulaza damu akaja kuvizia nafasi ya kuzungumza na ugeni huo mzito nchini Tanzania akitokea Kenya. Kama ilivyo pana nia pana njia na mgaa gaa na upwa hali wali mkavu akapata nafasi ya kuongea na ugeni ule toka Vatican. Akaeleza kinagaubaga mipango, malengo, maono na madhumuni ya uanzishwaji wa kituo chake katika malezi ya watoto yatima ambao wengi katika wazazi wao wamefariki kwa ugonjwa hatari wa UKIMWI. Kwa jinsi Bwana Ochieng alivyokuwa ametabahari katika kujieleza kwa ufasaha, wakapendezwa sana na kituo hicho, wakampa ofa ya fastafasta kuwachukua watoto yatima 10 kwenda nao nchini Italia kwenda kuwasomesha mpaka elimu ya Chuo Kikuu. Pia wakamuahidi misaada lukuki itakayokuwa inatumwa kwenye kituo chake ikiwemo gharama za chakula, malazi na mavazi.
Mungu si Athumani, Pesambili mtoto wa Recho alitelekezwa huko Kenya akaula nae akawekwa katika orodha ya watoto wanaotakiwa kuelekea nchini Italia. Ujio wa Papa John Paulo II nchini Tanzania ukawa ni neema kwake ya mwanzo wa kutoboa katika maisha yake. Uchaguzi wa watoto hao ulisimamiwa na wao wenyewe wazungu wa Vatican, kuhofia figisufigisu za Waafrika kuchaguana kindugu na kirafiki. Walikuwa wanajua nje ndani usanii wa vituo vingi vya watoto yatima, ofa kama hizo za kusomeshwa wanaweza kuchaguliwa watoto ambao sio yatima na hata wakati mwingine watoto wa vigogo serikalini. Wale mawakala wa viongozi toka Vatican waliotumwa Jijini Nairobi kuchagua watoto wa kuelekea Italia, walipomuona tu Pesambili pale kituoni wakavutiwa nae kutokana na upole wake na werevu wake wakamuweka katika orodha hiyo ya watoto 10, ya wanaotakiwa kusafirishwa hasa wakimuonea huruma kutokana na ulemavu wake.
Pesambili akarudishwa katika nchi ya asili ya Babu yake mzaa mama, baba yake Recho, Bwana 'Francesco Gabrielebila' bila kufahamu kuwa anarudishwa katika mizizi yake. Alisafirishwa akiwa hamjui baba wala mama yake, na wala hajui asili ya wazazi wake ni wapi katika nchi za Kiafrika. Alipofikishwa tu nchini Italia, moja kwa moja Pesambili akapelekwa katika moja hospitali kubwa Jijini Roma, Italia inayoitwa 'Policlinico Universitario Agostino Gemelli'. Hospitali ambayo inamilikwa na Chuo Kikuu cha "The Università Cattolica del Sacro Cuore" wakiitumia hospitali hiyo pia kama hospitali ya mafunzo kwa wanafunzi wake wa kitivo cha Utabibu. Ilikuwa ni hospitali kongwe na ya pili kwa ukubwa katika hospitali zote za nchi nzima ya Italia. Walipomfanyia vipimo vya uchunguzi vya kina chini ya jopo la madaktari bingwa, majibu yakatoka kuwa anaweza kufanyia upasuaji wa kurekebisha mifupa yake na ataweza kutembea kutokana na kuwa bado mifupa yake haijakomaa. Mara moja shauri likapitishwa la kufanyika kwa upasuaji huo, ambao kwa baraka za Mwenyezi Mungu, upasuaji ukafanikiwa.
Baada ya miezi 6 tokea upasuaji ule ufanyike, Pesambili akaanza kutembea vizuri kabisa kama vile hajawahi kuwa mlemavu, kiasi kwamba hata mama yake Recho angefanikiwa kumuona, basi angekataa katakata kuwa huyo sio Pesambili wake
Baada ya kutoka hospitalini hakukaa sana kwenye kituo cha kulea watoto, bali ikaja familia ambayo ilikuwa inahitaji mtoto wa kulea, wakamuomba mtoto Pesambili wakaishi nae nyumbani kwao. Taratibu za kukabidhiwa zinafanyika, wakakabidhiwa jukumu la malezi ya Pesambili.
Maisha alishayapatia, alikuwa analelewa katika familia tabaka a'ali yenye pesa sufufu. Wakawa wanamlea na kumuengaenga mtoto Pesambili kama mboni ya jicho bila kumbagua rangi yake na asili yake.
Martin Tenga sasa alikuwa ni tajiri mkubwa tu, mwenye mtandao mpana wa biashara halali na haramu zinazomuingizia mamilioni ya pesa kwa mwezi katika nchi za Afrika Mashariki kuanzia Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Alijikita kwenye biashara za Mahoteli na Masupamaketi kwenye kila Jiji la Afrika Mashariki lazima ungekutana na athari zake za "Martino Royal Hotel" au "Martino Super market". Pia mapenzi yake ya mpira wa miguu hakuyaacha kamwe, akaanzisha shule ya timu ya mpira wa miguu inayoitwa 'Street Boys Academy' iliyokuwa inakuza vipaji vya soka kwa vijana wadogo wa mtaani kuanzia miaka 11-17.
Mawakala mbalimbali wa soka toka Barani Ulaya walikuwa wanafurika kwenye shule hiyo ya soka kuja kusaka vipaji vya kuwapeleka Ulaya kusakata kabumbu. Wadau wa soka walikuwa wanamuona Bwana Martin Tenga ndio kama mkombozi wa soka la Tanzania hasa katika zama ambazo soka la Tanzania lilikuwa limedorora vilivyo mpaka Rais Mwinyi wa awamu ya pili akazifananisha timu za Tanzania na kichwa cha mwendawazimu, kwa maana kila mmoja anajifundishia kunyoa. Huyo ndio Martin wa hadharani na shughuli zake rasmi zinazojulikana na wengi.
Nyuma ya pazia, Martin hakuwa mtu mzuri hata kidogo alikuwa anajishughulisha na biashara nyingi haramu haswa biashara ya mihadarati, utakatishaji wa fedha haramu na kamari. Pia ile shule yake ya mpira wa miguu ya 'Street Boys Academy' kilikuwa ndio kichaka cha kuwapata vijana wa mtaani wanaoenda kubeba madawa ya kulevya Ulaya. Vijana wengine alikuwa anawauza kwa makundi ya kihalifu sehemu mbalimbali duniani kwa kisingizo cha kuwa wamepata timu za kusakata kabumbu Ulaya.
Baadhi ya wadadisi wa mambo walikuwa wanatilia mashaka shule hiyo ya mpira kwa hoja ya kwamba hawajawahi kuvuna matunda ya wanafunzi waliotoka shule hiyo kuchezea timu ya taifa. Zaidi ya kuona Taifa Stars bado ilikuwa inaundwa na wachezaji toka Simba na Yanga tu. Hata hao mawakala waliokuwa wanakuja kutafuta vipaji hawakuwa mawakala kwelikweli bali ni washirika wake wa kibiashara haramu wanaokuja nchini kwa gia ya uwakala wa soka.
Vigogo wengi serikalini alijaribu kuwaweka kwa ukaribu ili mambo yake yasikwamishwe. Alikuwa na watu uhamiaji wa kushughulikia usafiri wa wageni wake toka ughaibuni na vijana wake wa kazi. Pia aliwaweka baadhi ya mapolisi, mahakimu na majaji mfukoni mwake huku wakiamua kesi zinazohusu maslahi yake anavyotaka yeye. Bila kusahau kwenye mamlaka za kutoza kodi za mapato alikuwa na vibaraka wake wanaomsaidia njia za panya za kukwepa kodi na tozo mbalimbali za serikali.
Kwa ufupi Martin katika nchi za Afrika Mashariki alijitengenezea ngome imara ya chuma isiyopenyeka kirahisi. Nchini Italia, mamlaka za usalama za nchi hiyo tayari zilishaanza kumshuku, wakaanza kuzichunguza nyendo zake bila yeye mwenyewe kufahamu. Ingia toka yake ya mara kwa mara nchini Italia huku biashara anayoifanya haswa nchini humo ikiwa haijulikani ndio kitu haswa kilichozifanya mamlaka za usalama zianze kumfanyia taftishi. Lakini harakati za kumtia mbaroni zilikuwa ngumu sana kuliko maelezo kutokana na ustadi wa hali ya juu wa kukwepa vyombo vya dola wa kundi alilokuwa anashirikiana nalo kwenye biashara zake haramu za mihadarati. Alikuwa anashirikiana na kundi hatari la Mafia linaloitwa 'Ndrangheta'.
Kundi ambalo hata vyombo vya dola lilikuwa linapata shida kuwakamata washirika wake kutokana na mizizi yake iliyojikita kiukoo hivyo kufanya zoezi la kupata siri zao za ndani kuwa ni gumu sana. Kundi hili asili yake ni eneo la kusini mwa Jiji la Calabria, nchini Italia, likiwa limeundwa kwa muundo wa ukoo. Kundi hilo kongwe la Kimafia ambalo asili inaanzia mwaka 1412 katika Mji wa Toledo huko Hispania. Huko Hispania kundi hilo lilianza kama ushirika wa kucheza kamari likitumia jina la 'Garduna', na baadae kusambaa mpaka katika mkoa wa kusini, mkoa uliogubikwa na umaskini mkubwa wa Calabria, Italia.
Mwanzoni miaka ya 1860's walipoanza kushika kasi na kujulikana, walianza na uhalifu wa kuteka watoto na kudai malipo ya kikomboleo, mpaka baadae walipopata nguvu ya kiuchumi ndipo wakajikita zaidi kwenye biashara za mihadarati, usafirishaji wa binadamu, utegaji wa mabomu, wizi, uporaji wa kutumia silaha, biashara ya magendo na kila aina ya uhalifu uliopo duniani. Pesa wanazopata kwenye uhalifu huo wakawa wanazitakatisha kwa kufungua Mahoteli, Maduka, Migahawa, Baa, na Mashamba. Ilikuwa inakadiriwa kuwa kundi hili linamiliki karibia asilimia 3% za uchumi wa nchi ya Italia, unao karibia dola bilioni 55, huku wakiwa na benki akaunti zao za siri katika Majiji ya Monte Carlo and Milan nchini Italia.
Muundo wake kundi hilo ulijigawa katika vikundi vidogo vidogo zaidi ya 160 vyenye wanachama zaidi ya 6000. Kila kikundi katika hivyo 160, muundo wake ulikuwa unaangalia udugu wa damu au kuoleana ili kupunguza usaliti miongoni mwao. Kilikuwa ni kikundi kilichojisambaza vilivyo katika sehemu kubwa ya dunia huku Marekani tu katika majimbo ya Florida na New York likikadiriwa kuwa na wanachama 100-200. Huku pia wakiwa na wanachama wao nchini Colombia, Spain, Germany, The Balkans, Canada, Australia mpaka Ulaya Magharibi.
Kulitokomeza kundi hilo ilikuwa ni ndoto za Alinacha, hata serikali ya Italia ilikuwa inalitambua hilo, walichokuwa wanachokifanya ni kupunguza tu madhara yake. Martin alikuwa anajifichia kwenye kivuli hicho kipana, na kumfanya awe salama wakati wote. Martin alikuwa chini ya ulinzi wa koo ya Cappello-Bonaccorsi, hivyo ilikuwa ni ngumu kufukua maovu yake. Kila uchao, mambo yakazidi kumnyookea kimaisha.
Huku nyumbani Tanzania, viongozi wa serikali wasiojua undani wake walikuwa wanamsifia na kumtaja Martin, kwenye majukwaa yao ya kisiasa kama mjasiriamali kijana, mwenye ufanisi, anayejituma kwa bidii katika kazi zake. Huku wakiwataka vijana kuacha kuilalamikia serikali bali wazitumie fursa ipasavyo kujiletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Miaka ilishaanza kuyoyoma, huku Martin akiwa amemsahau kabisa Recho, kama ujuavyo mla kunde anakuwa mwepesi kusahau kuliko mtupa maganda. Martin alikuwa anatembea na Mabodigadi wa kutosha kwa ajili ya ulinzi wake binafsi, na nyumba yake ilikuwa na mifumo ya ulinzi ya kisasa, kiasi kwamba kufanikiwa kuonana na Martin ilitakiwa ufanye kazi kwelikweli. Ulikuwa unaweza kusailiwa na walinzi wake zaidi ya 10, wakijiridhisha na sababu zako kuwa ni za msingi ndio utapata fursa ya kuonana nae.
Watu wengi mtaani walikuwa hawajawahi kumuona Martin kwa sura yake mubashara zaidi ya kumsikia jina lake kwenye redio likitajwa, au kumsoma magazeti na kupitia vitega uchumi vyake. Wajuzi wa mambo ya ndani ya Jiji la Dar es Salaam, wakawa wanavumisha kuwa ule wimbo wa 'Ogopa Tapeli' wa bendi ya Vijana Jazz Band ulioimbwa na marehemu Hemedy Maneti uliimbwa kwa lengo la kuwazindua watu wa Dar es Salaam na matapeli walioibuka ghafla katika Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Tapeli Mkuu, Kibopa Martin. Inasemekana Martin alimtapeli tajiri wa madini toka Arusha kwa kumpa ahadi ya kumuuzia nyumba mitaa ya Kariakoo. Kumbe nyumba yenyewe ni Msikiti wa Kwa Mtoro. Wakafanyiana makabidhiano ya pesa na hati feki ya umiliki wa nyumba hiyo vilifanyika. Ilipofika majira ya swala ya adhuhuri yule tajiri wa madini anashangaa kuona waislamu wanaingia kwenye nyumba yake wanaitana kwa adhana waje kuswali.
Tajiri akacharuka amepandisha mori anawafukuza waislamu kwenye nyumba yake aliyouziwa na Kibopa Martin. Ikabidi watu wamfungue macho na masikio kuwa ametapeliwa hiyo sio nyumba ya mtu ni msikiti. Hivyo mkasa ulivyofika kwa mwanamuziki Hemedy Maneti akaamua autungie kibao cha kuwatahadharisha Watanzania na matapeli aina ya akina Martin waliochukua ujanja na ujuba wa Ulaya na Nairobi na kuuleta Jijini Dar es Salaam.
SURA YA SABA
Recho akatua salama ndani ya Jiji la Arusha, huku Mashoga zake wote wakimkwepa. Wengi wao walikuwa tayari wameshaolewa wana waume zao na familia zao hawakuwa tayari kumpa hifadhi mtu asiye na mbele wala nyuma. Katika kuhangaika kwake huku na kule, kwa kufanya umalaya kwenye Mahoteli makubwa kwa kuwavizia watalii, akafanikiwa kupata senti kidogo alizopanga kuzitumia kwenda Ngorongoro kwa lengo la kuuza kitalu chake cha uwindaji alichorithishwa na marehemu Bosi Minja.
Hicho kitalu F bloku XZ/21 kilikuwa kipo Loliondo makao makuu ya wilaya na kati ya tarafa tatu zinazounda Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, kaskazini mwa Tanzania. Kihistoria, Loliondo ni jina lililotokana na kuwapo kwa miti mingi aina ya loliondo kwa jina la kitaalamu Olea capensis subsp, O.welwitschii katika moja ya msitu wa hifadhi wa Serikali, Kusini mwa mji wa Loliondo. Watanzania wengi wanaijua Loliondo kutokana na migogoro mingi ya ardhi na sifa ya Babu wa Kikombe, Mchungaji Ambikile Mwasapila. Wazungu wao wanaijua Loliondo kutokana na utajiri mkubwa wa rasilimali za wanyamapori, bioanuai '[biodiversity]' na 'ecosystem' yake ya asili hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa watalii, uwindaji na sehemu muhimu ya uwekezaji vitega uchumi vya utalii na upigaji picha.
Matarajio yake ni kukipiga bei kubwa kitalu hicho kisha pesa zake azitumie kujipanga upya kimaisha. Alishagundua kuwa Martin kampiga changa la macho na kumfanyia dhuluma ya mali zake zote zilizopo Jijini Nairobi. Na kwa sasa hana hata chembe ya nguvu ya kujaribu kupambana na Hivyo mategemeo yake ya mali yalibakia kwenye kitalu cha Loliondo na Hoteli yake ya Kigamboni ya 'Mercy Memorial Hotel'.
Alipofika Loliondo aliyoyakuta huko alitamani afe kabisa. Alikuta tayari kitalu kimeshauzwa kwa tajiri wa kiarabu toka Saudi Arabia 'Sheikh El-Khadoos Al-Aziiz'. Tena alitimuliwa kama mbwa na walinzi wa kitalu hicho huku wakimtishia kumfurumishia risasi mwilini kama akileta ubishi kuondoka eneo hilo. Alipoleta ubishi wake wa Kichaga wa sikubali, walinzi wale wa Kimeru mmoja wao akamfyatulia risasi zilizomkosakosa sentimeta chache kutoka kwenye kichwa chake. Ikawa ndio mwisho wake kukanyaga kwenye kitalu hicho bora kabisa kwa shughuli za uwindaji.
Martin tayari alishachezea nyaraka za umiliki wa kitalu na kutengeneza nyaraka bandia ambazo alizitumia kuuza eneo hilo kwa mwekezaji. Recho hakuwa na hamu tena ya kutaka sijui kufungua kesi, alijua fika ni kama kutwanga maji kwenye kinu tu, Martin ana mtandao mpana katika mihimili yote ya serikali, kamwe asingeweza kushindana nae.
Kwa kutumia visenti vyake vilivyobakia akaamua aje zake Jijini Dar es Salaam kufuatilia mali yake ya mwisho ambayo labda alikuwa anadhania bado ipo mikononi mwake. Alikuwa amebakiwa na nauli ya kutoka Arusha mpaka Dar es Salaam tu, hana akiba yoyote ya ziada. Akaamua liwalo na liwe atasafiri hivyo hivyo mpaka Dar es Salaam kujua hatima ya Hoteli yake ya 'Mercy Memorial Hotel'. Kwenye Basi alikaa siti moja na mwanachuo mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Walipobadilishana mazungumzo mawili matatu wakawa mashosti haswa. Akili yote ya Recho ilikuwa ni kwenye kipochi cha mkononi cha yule Mwanachuo. Mawazo yake alijua kuna pesa za matumizi kapewa kwao. Walipofika kituo cha Mombo, dereva akatoa mapumziko ya nusu saa kwa ajili ya kuchimba dawa na kupata chakula. Yule mwanachuo aliposhuka tu, Recho alibakia ndani ya Basi na kuanza kupekenyua kipochi cha yule dada.
Kwa bahati mbaya hakukuta pesa yoyote zaidi ya fomu ya kuitwa chuoni ya yule dada na baadhi ya vifaa vidogo vidogo vya kujiremba kama wanja, shedo na manukato . Fomu ambayo ilikuwa na orodha ya vifaa anavyotakiwa kununua siku ya kuripoti Chuoni. Alikasirishwa sana na kitendo cha kuzidiwa ujanja na yule dada wa Chuo kwa kutohifadhi pesa zake kwenye kipochi. Mwizi ni mwizi tu akaamua kuiba hiyo fomu kwa lengo la kumkomoa tu dada wa watu. Mipango yake ya kumuingiza mjini dada wa watu ilienda mperampera kinyume na matarajio yake.
Safari hiyo ndefu ya Arusha mpaka Dar es Salaam kwa kutumia Basi la 'Dar Express' ikahitimishwa saa 2 usiku kwa kuwasili Stendi ya Mabasi ya Mikoani ya Kisutu. Yule Mwanachuo kwa uso wa bashasha wakaagana na Recho huku akitafuta taksi itakayompeleka Mlimani, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Akiwa amejawa na kimuhemuhe cha kuyaanza maisha mapya ya Chuo Kikuu. Malengo ya Recho yalikuwa ni kufika usiku mwingi ili apate stara ya kulala ndani ya Basi mpaka asubuhi kisha ajue sehemu ya kuingilia.
Lakini kwa muda huo waliowasili ulikuwa bado ni usiku mbichi, hivyo abiria wote walishuka ndani ya Basi huku Recho nae akiwa hana jinsi zaidi ya kushuka. Madereva taksi walikuwa kwenye pilikapilika za kugombania wateja kwa ajili ya kuwapeleka majumbani kwao, huku Recho akisimama pembezoni mwa taksi zilizoegeshwa huku mkono mmoja upo shavuni. "Yaaah Habibty.....mbona umeshika tama kulikoni zungumza usaidiwe...!" aligutushwa Recho na sauti ya Babu mtu mzima, maarufu hapo stendi ya Kisutu kwa jina la 'Babu Tingisha'. Alikuwa ni mzee mwenye asili ya Kisomali mwenyeji wa mkoa wa Kigoma. Recho akaona kabisa mtu wa kumfaa wakati wa jua ameshajitokeza lazima achange vyema karata zake. Jina la Babu Tingisha, lilitokana na mapenzi yake kwa mchezaji wa Yanga SC enzi hizo katika miaka ya 90's mwanzoni aliyekuwa akiitwa Sanifu Lazaro 'Tingisha'. Mchezaji huyo walikuwa wanatoka wote Kigoma hivyo alikuwa ni kipenzi chake sana, mpaka watu wakampachika jina la Babu Tingisha.
"Babu Shikamoo....nimeibiwa ndani ya Basi na mmoja wa abiria wenzangu na mwenyeji wangu aliyetakiwa kuja kunipokea sijamuona mpaka sasa" aliongea Recho kwa sauti ya huzuni ambayo kila aliyemsikiliza alimwamini huku huku akijifanyisha kwenda pumzi njia mbilimbili. "Pole sana kwani umetokea wapi na unaelekea wapi...?" aliulizwa Recho swali kushtukiza na Babu Tingisha kwa shauku kubwa ya kutaka kujua. "Mimi ni Mwanachuo mpya wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, ndio nimekuja kuripoti..." aliongea Recho kwa kujiamini huku akinyoosha mkono wake wa kulia anamkabidhi ile fomu ya kujiunga na Chuo aliyoikwapua kwenye kipochi cha mwanafunzi.
SURA YA NANE
Deborah sasa alikuwa amefika darasa la saba kwa mbinde. Siku zilikuwa zinahesabika kwake za kuanza kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya shule ya msingi. Alikuwa amejitahidi kuruka viunzi vingi ambavyo kama sio majaliwa ya Rabana shule ingekuwa imemshinda zamani. Vikwazo fauka ya vikwazo vilikuwa vinamuandama kwenye harakati zake za masomo yake. Mchawi wake mkubwa na hasidi wa maendeleo yake alikuwa ni shangazi yake, ambaye alikuwa na roho ngumu mithili ya malaika wa mlango wa jehanamu. Licha ya ratiba yake ngumu aliyowekewa ya kuamshwa jogoo la kwanza, saa 9 za usiku na kuanza kazi za nyumbani kisha anaelekea shuleni hali ya kuwa amechoka, bado alipokuwa anarudi nyumbani hakuwa na mapumziko ya wasaa kama wanayopata binamu zake, watoto wa Mjomba Kobelo.
Majira ya magharibi alikuwa anapewa utumbo wa kuku na shingo zake kwenda Kilabuni kunapouzwa pombe za kienyeji kwenda kuuza asusa hiyo kwa walevi. "Usikanyage hapa nyumbani, mpaka ziishe hizo..!" hayo ni maagizo kama wimbo wa taifa ya kila siku toka kwa shangazi yake pindi anapomkabidhi sahani ya asusa hiyo kwenda kuuza Kilabuni. Kwa ufupi shangazi yake alimgeuza Deborah kuwa punda wa dobi, lakini Deborah alitapikia sandani mateso hayo ya shangazi yake. Mungu daima alikuwa yupo upande wa Deborah, asusa zake zilikuwa zinaisha kimiujiza hata kama siku hiyo biashara ni ngumu. Mitihani huko kilabuni ilikuwa ni mingi sana, walevi kama unavyowajua, mtindi ukishawapanda kichwani mara watake kumfanyia vitendo vya udhalilishaji kama kutaka kutomasa matiti yake machanga, mara watake kumchezea makalio yake, lakini alijitahidi kukabiliana navyo kadri ya upeo wa uwezo wake.
Mara nyingi akichelewa sana saa 6 usiku alikuwa ndio anarejea nyumbani. Ilifika hatua mpaka shangazi yake usiku huo akirudi kwenye biashara na ubao mkali tumboni anamnyima chakula ili kumvuruga tu kisaikolojia apoteze lengo. Lakini Deborah alizidi kuwa mvumilivu akijifanya punda na mkia wake, na kuamua kukomaa na masomo yake. Alijua ya kuwa hamna kitu ambacho kinaweza kumkomboa mtu masikini kama elimu, kama ujuavyo elimu ndio ufunguo wa maisha. Alikuwa akirudi toka kilabuni usiku huo kabla hajalala, lazima awashe koroboi yake na kujisomea madaftari yake walau hata kwa nusu saa ndio alale. Shuleni akili zake zilikuwa zinachaji sana, tokea aanze darasa la kwanza mpaka anafika darasa la saba alikuwa hajawahi kutoka nje ya 10 bora. Kila Mwalimu wake alikuwa anamsifia kwa uhodari wake wa masomo darasani na nidhamu. Deborah akawa ni kiigizo chema kwa wanafunzi wenzake pale shuleni.
"Wewe nyamafu unajisumbua bure kukesha kujisomea subiri ufeli mtihani mwezi ujao, uone posa zitakavyotiririka hapa, wa kusoma utakuwa wewe..ebo zima huko koroboi yako unawakera wenzake na mwangaza wako...!" yalikuwa ni baadhi ya maneno ya kejeli na dharau toka kwa shangazi yake pindi akiona koroboi imewashwa chumbani kwa Deborah. Shangazi yake alikuwa ni fundi wa kuuchonga mdomo, akianza kubwabwaja hachoki mpaka utatamani atie nanga ulimi wake. Maneno hayo hakuyachukulia kama ni kikwazo, bali aliyabeba kama changamoto ya kufanya vizuri darasani ili aje kuwa na maisha yake binafsi pia amsaidie mama yake mzazi ambaye sasa kwa zaidi ya miaka 10 alikuwa yupo kitandani tu mahamumu hajiwezi.
Wasichana wenzake wa rika lake pale Kijijini hawakuwa wanajali sana masomo, wao kutwa kucha akili yao ilikuwa kwenye michezo tu na kuwaza kuolewa. Walikuwa wanajua kusakata ngoma zote za asili za Kiluguru kuanzia mdundiko, mkwajungoma, mbeta, zembwela, mchiriku au mnanda, zembwe, Kihamba, gombesugu, na vanga. Maajabu ya Mungu, Deborah hakuwa anajua kucheza ngoma hata moja kati ya hizo, nadhani ni kutokana na damu ya Kichaga ya baba yake mzazi ilikuwa haipatani na ngoma hizo, pia alikuwa kila anapojaribu kujifunza anaona kiuno chake ni kigumu tofauti na wenzake viuno vyao vinazunguruka kama feni mbovu. Kila siku kwenye sala zake Deborah alikuwa anaomba afaulu shule ya bweni kwenye mtihani wake wa kumaliza elimu ya msingi ili aweze kuishi mbali na shangazi yake, fisadi kiwembe mjaa laana. Hakutaka yaliyowatokea binamu zake, watoto wa Mjomba Kobelo ya kukacha elimu nae yamkumbe. Binamu zake walipomaliza darasa la saba tu, hata kabla majibu hayajatoka tayari walishaozwa kwa wachumba zao. Wazazi pale kijijini Mikongeni walikuwa wanawashajiisha watoto wao wajifelishe makusudi mitihani yao ili kukwepa majukumu ya kuwasomesha sekondari. Hivyo asilimia kubwa ya waliokuwa wanafeli ilitokana na kuogopa wazazi wao watawachapa na kuwasusa iwapo watafaulu.
Deborah yeye kwa upande wake alikuwa anajitambua, hakusikiliza vishawishi vyovyote vya kujifelisha mitihani, alikuwa anasoma kwa bidii zote ili afaulu mitihani yake.
Siku ya kuhitimisha mitihani ya shule ya msingi ikawadia, Deborah akamaliza mitihani yake vyema huku akiwa na matumaini kibao ya kupasua mitihani hiyo kwa daraja la juu kutokana na wepesi wa mitihani hiyo kwa upande wake. Mara tu alipomaliza mtihani wake wa mwisho ikabidi kwa tahadhari tu akamsimulie Mwalimu Mkuu wake kuanzia utandu mpaka ukoko maisha yake yote pale nyumbani na hofu ya kuozeshwa kabla ya matokeo kutoka. Mwalimu yule alishangazwa na ukomavu wa Deborah na moyo thabiti kwa madhila aliyopitia. Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mzumbe, anayosoma Deborah, akiambatana na Mwenyekiti wa Kitongoji wakafuatana sako kwa bako na Deborah kwenda kuwachimba mkwara Mjomba Kobelo na mkewe. Waliwapasha kinagaubaga kuwa Deborah ni mwanafunzi anayetegemewa kufika mbali kielimu hivyo harakati zozote za kutaka kujaribu kumuozesha zitasababisha waozee jela. Mjomba Mkude na mkewe mjuba wakaufyata mkia na kugwaya, na kukubaliana na matakwa ya mkuu wa shule.
Siku hazigandi, matokeo ya mitihani ya kumaliza elimu ya shule ya msingi kwa mwaka 1996 yakatoka. Deborah akaongoza kwa upande wa wanafunzi wasichana kwa Mkoa mzima wa Morogoro. Kwa upande wa shule yao ya msingi Mzumbe, walifaulu watoto 20 kati ya wanafunzi 60, ila kati ya hao wote aliyebahatika kwenda shule ya bweni ni Deborah peke yake. Alichaguliwa kujiunga na shule ya watoto wenye vipaji maalumu vya kiakili, ya 'Msalato Girls', Dodoma. Furaha aliyokuwa nayo alitamani mama yake mzazi awe mzima wa afya ili aone mafanikio ya juhudi zake, lakini ndio hivyo tena mama yake alikuwa si mamati si hayati hajui kinachoendelea duniani wala akhera yupo yupo tu. Akaenda shuleni kwao Mzumbe na kupokewa kishujaa kuanzia na wanafunzi wenzake mpaka na walimu wake. Bahati nzuri mmoja wa walimu wa pale shuleni kwao, mtoto wake alikuwa anasoma 'Msalato Girls', shule hiyo anayotakiwa kusoma Deborah, hivyo akaanza kumuandikia kwenye karatasi mahitaji ya shuleni yanayohitajika ili aanze kujiandaa mapema kununua vifaa vya shule wakati wanasubiria fomu ya kujiunga na shule itumwe kwa Deborah. Deborah akashukuru sana walimu wake kwa malezi bora waliyompa kwa muda wote wa miaka 7 waliokaa na yeye pale shuleni, akaagana nao na kurejea nyumbani kwao akiwa na furaha sheshe.
Siku hiyo alishinda ndani na kimuhemuhe cha kumsubiria Mjomba wake Kobelo amuelezee kuhusu ufaulu wake. Aliporudi Mjomba wake tu, akamkimbilia shoti shoti kumpa habari ya ufaulu wake, lakini majibu aliyopewa yalimtibua nyongo. "Ukatafute mtu wa kukusomesha, huyo mama yako tu ni mzigo wangu tu kitandani zaidi ya miaka 7 sasa, na wewe uanze kuniongezea mzigo, hao hao waliokushawishi ujifaulishe mitihani ndio wakulipie ada..." aliongea Mjomba Mkude kwa hasira huku anaingiza baiskeli yake mkweche ndani ya nyumba. "Utakuwa umependelewa tu, wa kufaulu utakuwa wewe, wenzako wote utawakuta wameolewa wana Miji yao ukijichetua kujitia kwenda sekondari shauri yako. Kwanza na ukojozi huo ulionao shule nzima si itanuka mikojo tu he... heeee....hallow...hallow....shule ya mikojo... !" shangazi yake huyo nunda mla watu, mke wa Mjomba Kobelo akazidi kumshindilia na maneno ya kejeli na kebehi yaliyozidi kuuchanachana moyo wake Deborah na kumuongezea majonzi.
Alijikuta machozi yanamtiririka machoni mfululizo na kutengeneza mifereji ya machozi katika mashavu yake. Kifua cha Deborah kilimbana kwa hasira alizonazo, akapatwa na mkururu wa fikra hasi. Akajikuta hana mtu wa kumpa faraja zaidi ya kwenda kushtaki kwa mama yake mzazi ambaye ni mgonjwa yupo chumbani kwake. Akamkuta mama yake mzazi, amejikojolea mwili wote amelowana chapachapa hajabadilishwa nguo zake toka asubuhi. Kwanza akaanza kumpa huduma ya kwanza kwa kumsafisha mwili wake na kumvika nguo zingine. Alipomaliza kumbadilisha mama yake, akapiga magoti karibu na kichwa cha mama yake huku akichukua chake cha mkono wa kulia na kugusanisha na kiganja cha mkono wa kushoto wa mama yake. Akasogeza mdomo wake karibia na sikio la kulia la mama yake na kuanza kunong'ona na mama yake. "Mamaa... Mamaaa... Mamaaa..! najua unanisikia lakini unashindwa tu kunijibu, leo kwa mara ya kwanza nakuletea mashtaka yangu. Kwanza kwanini sisi tunaishi katika mateso makubwa namna hii, tumemkosea nini sisi Mungu?. Pili kwanini baba amekufa mapema na kutuacha peke yetu duniani tunateseka? kama kweli mwanaume ndio kichwa cha familia kwanini asingebakia hai atupambanie familia yake tuwe na maisha bora kama familia nyingine?. Kwa zaidi ya miaka 7 mfululizo tuliyoishi hapa nyumbani kwa Mjomba Kobelo, Shangazi hajawahi hata siku moja kunipa maneno ya faraja na matumaini. Ananiona mimi ni kama mtu baki, mtoto bunga na dufu la dufu sina msaada wowote hapa nyumbani. Daima amekuwa ni mtu wa kunikatisha tamaa, kunisimanga, kuniporomoshea matusi, na vipigo mfululizo kwenye mwili wangu kama ngoma vile. Nimejitahidi sana kuwa mvumilivu, kujipendekeza na kujibidiisha kwenye kila kazi anazoniagiza nizifanye lakini wapi, haoni wema wangu wowote. Sasa nimechoka manyanyaso ya shangazi, najiona kama nimeibeba dunia kichwani mwangu, sasa bora niitue chini nimeamua kutoroka nyumbani ninakwenda ninapokujua mimi, nisamehe kwa kukuacha peke yako, naamini Mungu atanilinda huko niendako na wewe atakupa afya njema tutakuja kuonana siku moja iliyopangwa na Mungu kwaheri" aliongea Deborah kwa uchungu mkubwa mbele ya mama yake, ambaye nae machozi yalikuwa yanamtiririka kwa kushuhudia mateso ya binti yake katika umri mdogo.
Alikuwa anashindwa tu kumuongelesha binti yake ila alielewa kila kitu alichoambiwa na binti yake. "Debooo....Debooo....wewe mbwa jike upo wapi? Usicheleweshe visusio kilabuni, unavyojichelewesha shingo za kuku zikibakia utafute kwa kulala usirudi hapa mpumbavu wewe..!" aliongea kwa hasira shangazi yake Deborah huku anafoka akiwa ameshamaliza kuandaa shingo za kuku na miguu ya kuku iliyofungwa na utumbo wa kuku tayari kwa kupelekwa kuuzwa kwenye klabu ya pombe za kienyeji. "Abeee...shangazi nakujaa samahani kwa kuchelewa..!" aliitika Deborah huku akijizoazoa toka chini pale alipopiga magoti chumbani kwa mama yake na kukimbilia kuitikia wito wa shangazi yake.
Magharibi hiyo alipoondoka nyumbani hapo kwa Mjomba wake, Deborah hakurudi tena akatokomea kimoja. Deborah alitoroka kimoja nyumbani kwao, na kuamua kuwa mtoto wa mtaani kukwepa manyanyaso na mateso ya shangazi yake. Kuondoka kwa Deborah nyumbani pale ilikuwa ni kwa lengo la mguu niponye, maana siku si nyingi subira ingemshinda wangeishia kuvaana maungoni na shangazi yake na watu wote wangemuona yeye ndio mtovu wa adabu.
'Pesambili' sasa makazi yake rasmi yalikuwa yapo Jijini Turin, nchini Italia. Baada ya kumaliza elimu ya chekechea, alipofikisha umri wa miaka 6 alianza masomo yake ya shule ya msingi kwa muda wa miaka 5. Aliandikishwa shule ya msingi ya serikali lakini yenye kutoa elimu yenye viwango inayoitwa 'Comprehensive School "Sandro Pertini" iliyopo Jijini Turin nchini Italia. Hakupata tabu sana kuizoea hali ya hewa ya Jijini Turin, kwa sababu ilikuwa haipishani sana na Jijini Nairobi alipolelewa utotoni mwake kwa muda.
Ndani ya miaka michache tu aliyokaa Jijini Turin, tayari akawa mjanja mjanja, alikuwa anaijua Turin mitaa na vichochoro vyake utadhani amezaliwa Italia. Alithibitisha kweli ana damu ya Kichaga kwa ujanja ujanja wake. Kila alipo Pesambili basi alikuwa na kundi wanafunzi wenzake wa Kitaliano wamemzunguka wanamsikiliza hadithi zake anazosogoa. Alikuwa fasaha wa lugha na bingwa wa kuyaumba maneno kinywani. Kamwe hakupata misukosuko yoyote ya ubaguzi wa rangi hasa kutokana na rangi yake ya uburushi aliyoipata kutoka kwa mama yake mzazi Recho na pia nywele zake laini za singa pia zilimbeba. Pia walezi wake walikuwa wanampa maisha ya hali ya juu kiasi kwamba shuleni kwao hamna mwanafunzi aliyethubutu kumnyanyasa Pesambili kwa sababu ya kiuchumi.
Waswahili wanasema usimfanyie ubaya mtu usiyemjua, ndio ilivyotokea kwa Mr.Lorenzo mlezi wa kijana Pesambili. Mr.Lorenzo baba yake ni Mzee 'Francesco Gabrielebila' baba yake mzazi na Recho. Hivyo kwa maana ingine ni kwamba Pesambili alikuwa analelewa na Mjomba wake kabisa wa damu bila kufahamiana. Mbaya zaidi Mzee Francesco alifanya siri, hakuwapa taarifa familia yake akiwemo mkewe kuwa amepata mtoto wa kike nchini Tanzania na jina lake ni Rachael. Ndio maana alimtelekeza Recho bila kuleta huduma za mara kwa mara kuogopa siri ya kuzaa nje ya ndoa isije kubumbuluka kwa mkewe nchini Italia. Kuna wakati Pesambili alikuwa anaenda nyumbani kwa Mzee Francesco, ambaye ndio babu yake wa damu bila kujua. Daima damu ni nzito kuliko maji, Mzee Francesco alikuwa akikaa muda mrefu bila kumuona Pesambili lazima ataagiza aletwe amuone.
Alikuwa ni Babu mpenda maisha ya kifamilia, hii ni kutokana na safari zake nyingi za Afrika enzi za ujana wake, hivyo alipendezwa na maisha ya umoja katika familia za Kiafrika. Pia huko mitaani anapovinjari Pesambili, kuna wakati alikuwa anakutana na baba yake mzazi kabisa, Mr. Martin Tenga pindi anapokuja Jijini Turin kwenye biashara zake akitokea Jijini Nairobi bila kufahamiana. Namna walivyokuwa wanaonana ilikuwa ni katika njia ya kustajabisha kabisa.
Pesambili na wanafunzi wenzake walikuwa wakitoka shule au wakati wa mapumziko wana tabia ya kuzunguka kwenye masoko maarufu ya Jijini Turin kufanya manunuzi. Basi la shule lilikuwa linawaleta na kuwarudisha katika masoko ya Mercato di Porta, Palazzo Balon, Torino Market of Porta, na Palazzo Mercato Centrale Torino. Mchezo ulikuwa hivi, Mr.Martin Tenga anapokuja Italia kupokea mzigo wake wa mihadarati kutoka kwa washirika wake wa kundi la Mafia la 'Ndrangheta', walikuwa kuna wakati wanampa mzigo wake kupitia Jiji la Catania na wakati mwingine Turin. Akiwa anapokelea Jijini Turin ili kuwakwepa wana usalama, alikuwa anajibadilisha na kujifanya kama fukara, ombaomba wa mitaani katika maeneo yenye watu wengi ya masokoni. Akitimiza anachokitaka toka kundi la Ndrangheta, anapotea mtaani kwa kitambo fulani kisha anarudi tena mtaani, hiyo ndio ilikuwa tabia yake.
Pesambili kutokana na kudhurura kwake mitaa ya sokoni mara kwa mara akajikuta anavutiwa kumsaidia sana ombaomba Martin, bila kujua kuwa anamsaidia baba yake mzazi kabisa ambaye sio mhitaji wa kweli ila yupo kwenye harakati zake haramu za biashara ya madawa ya kulevya. Pesambili alikuwa anapenda sana kutoa sadaka kutokana na maisha ya kidini aliyoyapata tokea utotoni.
Namna alivyokuwa anaupokea mzigo wake, Mr.Martin ilikuwa ni kwa namna ya njia za siri sana. Mpaka uwe Kachero bobezi ndio labda ungeweza kung'amua mchoro mzima wa uhalifu unavyochorwa mpaka mzigo unamfikia Martin. Mwenyekiti wa bodi wa kundi la Mafia la 'Ndrangheta' mwenyewe, Bwana 'Domenico Oppedisano', jitu lenye roho ngumu na mkatili, mwenye umri wa zaidi ya miaka 80 lakini ukimwona ukakamavu wake wa mwili utasema ndio kwanza ana miaka 40, alikuwa asubuhi na mapema akiwa na bajaji yake nyeusi ya matairi matatu anasambaza matunda masokoni. Alikuwa na shamba lake la matunda mbalimbali lenye ekari zaidi ya 500 hivyo akizugia kuwa matunda ndio biashara yake inayomuweka Jijini Turin. Lakini matunda yake hayakuwa matunda ya kawaida tu, ilikuwa ni kiini macho kwa ajili ya kuwakwepa Makachero, kwenye baadhi ya matunda yalikuwa yametobolewa kiutaalamu mkubwa kisha ndani yake kuna ujumbe maalumu unapenyezwa kwa mhusika wake aliyemkusudia kumpa hilo tunda. Ndani ya hayo matunda maalumu kulikuwa na ujumbe namna washirika wao wa biashara ya madawa ya kulevya watakavyopokea mzigo wao wa mihadarati. Kwa hiyo kama bajaji imepakia lumbesa ya matunda elfu 10, basi ndani yake kuna matunda maalumu zaidi ya 50 yenye kazi ya kusambaza ujumbe kwa wadau wake.
Watoto wa shule walikuwa wanampenda sana kununua matunda kwenye bajaji ya Babu 'Domenico Oppedisano' hasa kutokana na kuuza matunda yake kwa bei ya chee pia na ucheshi wake kwa watoto wa shule. Pesambili kwa sababu kalelewa katika maisha ya kumtukuza Mungu na upendo nyumbani kwa mlezi wake Mr.Lorenzo alijizoesha kila anaponunua matunda sokoni lazima anunue ya ziada kwa ajili ya kusaidia masikini, na kama Martin yupo basi ndio atamtanguliza kuwa wa kwanza kumsaidia. Akifika atamsalimia kwa adabu, kisha atampa msaada halafu watafanya maombi mafupi kwa Mungu kisha wanaagana kwa bashasha. Kutokana na ukaribu wao, ikafika wakati Martin na Pesambili wanasogoa maongezi kama marafiki vile wenye umri unaolingana bila kutambuana kuwa ni baba na mwana, na huyu ndio baba yake mzazi asiyemfahamu ambaye alimtelekeza kule Jijini Nairobi kwenye kituo cha watoto Mayatima.
Makachero wa Jiji la Turin, walishachoshwa na tabia za mazungu ya unga kuligeuza Jiji lao kuwa ni kitovu cha biashara ya mihadarati, hivyo wakaanzisha msako wa kimya kimya wa kuwanyakua Mazungu ya unga. Makachero hao wa Jijini Turin hawakuwa maboya walikuwa wanazisoma nyendo za Martin na Babu Domenico Oppedisano, kwa umakini mkubwa sana. Wakawa wanatafuta mbinu muafaka ya kuandaa mtego wa kumnasa Martin bila mwenyewe kushtukia. Wakaamua kumtumia Pesambili katika harakati zao za kumnasa Martin kijasusi, baada ya kugundua ukaribu wao baina yao na pia ingekuwa ni vigumu kwa Martin kushtukia kuwa Pesambili ni pandikizi la Makachero kwake. Pesambili bila kufahamu kuwa wana usalama wanamtumia yeye kama chambo cha kumnasa baba yake mzazi. Pesambili akakubali kuingia kwenye huo mpango mkakati wa kumtia mbaroni baba yake. Martin hakuwa na alifu bee tee za usalama wake kuwa hutakiwi kumuamini kupita kiasi mtu yoyote yule, na mara nyingi katika maisha umdhaniaye ndie kumbe sio. Ikala kwake siku zake za kuvuta hewa ya uraiani zikawa zinahesabika kwa vidole vya kiganja kimoja cha mkono.
?
Deborah baada ya kuhesabiwa idadi ya shingo na ndizi za kuchemsha anazotakiwa kwenda kuuza usiku ule Kilabuni kabla hajatoka akaingia chumbani kwake akajifungia. Akakusanya nguo zake chache na kuziweka ndani ya mfuko wa 'Rambo' akachukua na baadhi ya makaratasi yake muhimu akatumbukiza kisha akautupa ule mfuko nje ya nyumba kupitia dirishani. Akapiga magoti chini na kufumba macho akaanza kusali sala maalumu ya majitoleo kwa mama wa huzuni. Ni sala maarufu sana kwa waumini wakristo wa dhehebu la katoliki.
Akaanza kusali kwa hisia za hali ya juu huku akiwa amevifumbata viganja vyake vya mikono mpaka alipoanza kusema "Naweka roho fukara katika moyo wako uliotobolewa na panga nyingi za mateso. Unipokee mimi niwe mtumishi wako wa pekee na mshiriki wa mateso yako" akashindwa kujizuia mvua ya machozi ikaanza kumwagika toka machoni mwake. Akijiona kabisa ustahamilivu wake wa mateso ya shangazi yake kama ng'ombe wa gari umefikia kikomo.
"Wewe kenge..!.kujiandaa huko unachukua mwaka mzima? Au ushapata Mabwana huko Kilabuni ndio unajiremba wakuone mrembo sio..! Sasa wewe jicheleweshe afu ubakize hizi asusa ndio utanitambua mimi nani, sitoacha kukupiga mpaka unitajie jina langu la utoto kabla ya unyago nilikuwa naitwa nani ndio nitakuacha.." ilikuwa ni sauti ya maneno ya matusi ya shangazi yake, ambaye hachoki kuzoza maneno yasiyo na maana utasema anakunywa maji ya chooni. Sauti hiyo ndio iliyomzindua kwenye kilele cha sala yake. Shangazi yake alikuwa amevimba kama chura. Akajifuta machozi yake kwa kutumia viganja vya mikono yake kiunyonge kama aliyefiwa kisha haraka haraka akatoka chumbani mwake akabeba sinia lake la asusa kiguu na njia kuelekea Kilabuni.
Akazunguka nyuma ya nyumba yao mkabala na chumba chake, akabeba mfuko wake wa rambo na kuelekea Kilabuni. Giza lilishaanza kushika kasi kushitadi angani, akawa anaongeza mwendo ili mradi awahi kuuza na kumaliza biashara yake hiyo. Huku akiombea asikutane na mtu yoyote njiani anayemfahamu asije kupeleka umbea kwao kuwa amemuona na mfuko wa nguo. Mjomba wake nae alikuwa bado hajarudi nyumbani, ambaye kawaida yake akitoka kwenye shughuli zake kwanza anapitia kwenye pombe anapasha halafu anarudi nyumbani kuacha baiskeli yake na kwenda safari ya pili kuutwika mtindi kichwani.
Ghafla mno bila kutarajia akamuona mtu mbele yake kwa mbali anakokota baiskeli huku anayumbayumba njia nzima kama mnazi. Akapigwa nna tahayari kama aliyefumaniwa ugoni, miguu yake akaiona mizito kama nanga. Alijiona kuwa tayari ameshaumbuka na kukamatika, hima hima akaanza kutambaa kwenye nyasi kama nyoka akijisweka porini kwenye majani huku akilitua salama sinia la asusa lililofunikwa kwa juu. Akajiziba uso wake na mfuko wa rambo huku akisali kila aina ya dua asiwe Mjomba wake Kobelo. Alianza kutetemeka akijua tayari ameshakamatika hana ujanja. Kwanza atamhoji anaenda wapi na huo mfuko na iwapo atagugumiza maneno akiamua kuukagua akaukuta una nguo ndio mkong'oto utakapoanzia hapo. Pia atamhoji kwanini leo kapita njia ya vichochoroni na sio ile anayopita kila siku ana miadi gani au anajificha na nini. Hayo yote yalikuwa ni maswali magumu kwa Deborah ambayo lazima angekosa majibu yake.
Michakato ya yule mtu ikazidi kusogelea mpaka jirani na pale alipo Deborah huku sasa akisikia wazi wazi nyimbo inayoimbwa na yule mlevi. " Kamuacha MUME wake kafuata MDUNDIKO...MDUNDIKO...MDUNDIKO EEH...MDUNDIKOOOO... " huo ndio ulikuwa wimbo unaoimbwa kwa furaha sheshe na mlevi huyo. Deborah bila chembe ya mashaka akang'amua kuwa huyo ni Mjomba wake kabisa, sauti yake haiwezi kumpotea masikioni mwake. "Afu hapa kuna harufuuu...nzuriiii....ya nyama ya kuku...hapa...!" akaropoka Mjomba Kobelo kwa sauti ya kilevi huku anaegesha baiskeli yake pembeni na kuanza kusogelea kwenye fukutu la nyasi alilojibanza Deborah. Deborah harakati zote za Mjomba wake alikuwa anaziona vizuri tu, akaanza kuingiwa na wasiwasi kuwa Mjomba wake kamuona tayari hana ujanja. Moyo ukaanza kumpiga mbio mbio, huku jasho jekejeke mwilini linaanza kumvuja akijua kabisa kuwa amekamatika hana ujanja.
Akaanza kuhisi kama haja kubwa na ndogo zinagonga nguo ya ndani kwa kutaka kutoka bila ridhaa yake. Akajikaza kisabuni na kutulia kama mtu aliye usingizini. Ghafla Mjomba Mkude akasimama meta chache kutoka pale alipojificha Deborah. Akafungua zipu ya suruali yake na kuanza kuucharaza mkojo akilengesha pale pale alipojibanza Deborah. Bahati yake Deborah ule mkojo wote wenye harufu ya pombe ya kienyeji ukawa unatua juu ya mfuko wake wa rambo na kutiririkia kwenye nyasi. "Mizimu nyie mfaidi sana, sisi duniani huku tunakula majani nyie mnachinja kuku tu, shenzi zenu nyie....!" akaropoka kilevilevi baada ya kumaliza kujisaidia haja ndogo machakani, akageuka na kuielekea alipoegesha baiskeli yake na kuanza kuiburuza kuelekea nyumbani kwake, huku sasa akianza kuimba nyimbo za Kiluguru na kutokomea zake kwenye upeo wa macho ya Deborah.
Deborah akashusha pumzi ndefu kama aliyetua mzigo mzito, huku hofu yake yote iliyokuwa imemtawala ikiyeyuka kama siagi katika kikaango cha moto. Akajinyanyua pale kwenye kichaka akajitwika sinia lake la asusa kichwani huku mkono wake wa kushoto umekamatia furushi lake la nguo kiguu na njia Kilabuni. Mipango yake ilikuwa ni kutorokea Jijini Dar es Salaam.
Alikuwa anasoma kwenye vitabu, magazeti na kusikiliza kwenye redio uzuri wa Jiji la Dar es Salaam. Alijua huko anaweza kutafuta kibarua kitakachomuwezesha kupata pesa za kumtunza mama yake mzazi. Alishakata tamaa kabisa ya kuendelea na masomo ya sekondari. Ndoto zake za kufika elimu ya Chuo Kikuu zikayeyuka kama theluji kwenye jua. Mawazoni mwake aliweka dhana kuwa elimu ni fursa pekee wanayopata watoto wa tabaka a'ali katika jamii sio watu hohe hahe kama yeye Deborah. Ambaye ni yatima, hana baba na mama yu mgonjwa mahututi kitandani hajiwezi si kwa chumvi wala sukari. Kwake suala la usafiri wa kuelekea Dar es Salaam haikuwa shida kabisa.
Kulikuwa na taniboi wengi wa Malori yanayokuja kupakia nyanya katika Kijiji cha Kipera anajuana nao kutokana na kuja kunywa gongo katika Kilabu anachouzia asusa Deborah. Mwanzoni walikuwa wanamsumbua kumtaka kimapenzi huku wakimpa ahadi kemkem za kumtorosha na kuja kuishi nae Jijini Dar es Salaam. Walipomuona ni kichwa ngumu na ni msichana mwenye kujitambua utu na thamani yake wakaacha kumsumbua na kumzoea kama mdogo wao.
Hivyo Deborah alijiamini kuwa leo akiwalalamikia shida yake ya kutaka kuelekea Jijini Dar es Salaam hawatosita kumchukua. Hasa kwa jinsi alivyokuwa anashuhudia watu wengi tu wasio na uwezo wa kukata tiketi ya Basi walikuwa wanasafiri na Malori hayo ya kupakiza nyanya. Alipanga pesa atakayopata kwenye mauzo yake ya asusa iwe ndio pesa yake ya kununua masurufu ya safarini.
Ukifika Dar es Salaam hasa maeneo ya Kariakoo nyakati za usiku, utashangaa kuona watoto wengi wakiwa wamelala kwenye viambaza vya majengo mbalimbali. Watoto hawa mara nyingi hushinda mchana wakiomba fedha barabarani, wengine hufanya kazi ngumu kama vile kuosha magari, kubeba mizigo na wengine ni vibaka. Usishangae kuona watoto wadogo chini ya miaka 10 wakivuta sigara, bangi au gundi za viatu kama kilevi. Watoto hao wanajifunza kila aina ya maisha ambayo hawakustahili kabisa, lakini yote ni kutokana na kukosa mwongozo wa maisha.
Watoto hawa wanalala kwenye mazingira hatarishi kwa maana kwamba, hawana ulinzi wowote usiku, matokeo yake huishia kubakwa huku wavulana wakilawitiwa. Hamna anayejali ustawi na maslahi ya watoto hao wa mitaani maarufu kwa jina la Chokoraa.
Miongoni mwao watoto hao, Mbweku Jr nae alikuwa ni mmoja wao tena akiwa ni ghulamu wa miaka 14 tu. Baba yake Mhasibu Mkuu wa zamani wa Peace Corps Tanzania baada ya kufungwa jela miaka 30 hawakuwa na jinsi zaidi ya kurudi kijijini kwao, Kitomanga huko Lindi Vijijini. Huko kijijini maisha hayakuwa rahisi hata kidogo, mpaka ikafikia hatua kila siku wao wapo kwenye funga ya lazima bila kupenda wanashindia uji tu. Shuleni Mbweku Jr akawa haelewi chochote kinachofundishwa kutokana na njaa. Ndipo wakashauriana na mwanafunzi mwenzake watoroke kuja Dar es Salaam kutafuta maisha. Ndipo Mbweku Jr akatua Jijini Dar es Salaam na kuanza kuchuuza biashara ndogondogo mitaani. Ikifika usiku inabidi alale kwenye maboksi yaliyotandikwa mitaani.
Napo wakati wa kulala lazima upambane kupata nafasi. Kulikuwa na wababe wanaojifanya wanamiliki maeneo hayo. Hao wababe haulali kwenye maeneo yao mpaka wakuruhusu, na wakati mwingine unatakiwa uwape kitu kidogo kama pango ya malazi. Mbweku Jr akiwa ndio kwanza ana wiki mbili mtaani ameshaanza kuzoea hali ngumu ya maisha, jua, mvua na mbu vyote vyake ukamsibu mkasa uliomfanya atoroke Kariakoo na kukimbilia maeneo ya Feri Kigamboni kwenda kujificha.
Mkasa ulikuwa hivi, baada ya mikikimikiki ya kuonewa na wenzake kama ujuavyo kuku mgeni hakosi kamba mguuni, hali ikatulia kwa kupata hifadhi kwa njemba moja ambaye aijifanya msamaria mwema kwa Mbweku Jr. Lakini Mbweku Jr akaanza kupatwa na wasiwasi na huo wema wake huo anaomfanyia akijua fika atatakiwa kuja kuulipa maana siku zote bure aghali, hivyo akawa anaishi nae kwa tahadhari. Kilichokuwa kinampa mashaka MbwekuJr ni ukaribu wa huyo msitiri wake na mwarabu mmoja hapo Kariakoo mfanyabiashara maarufu kwa jina la 'Mwinyi Fuad', ambaye alikuwa hatajwi kwa wema katika midomo ya watu. Ilikuwa kila siku saa 4 usiku lazima apite na gari yake maeneo yao ya kujibanza, ataongea na wale wababe kisha anaondoka zake.
"Dogo langu Mbweku kuna Galacha mmoja anataka kukupa maisha, nimeona bora nikuunganishe wewe hilo dili usiniangushe" alipewa taarifa MbwekuJr na huyo mmoja wa Watemi wao aliyekuwa anajulikana kwa jina la 'Bruce Master'. "Dili gani hilo..?" aliuliza MbwekuJr kwa udadisi mkubwa huku akikiweka vizuri kilago chake cha kulalia lakini huku anamtazama usoni bila kupepesa macho. "Punguza presha dogo, utauchinja muda sio mrefu utatuhama sisi wenzako..!" aliongea kwa kebehi na ahadi za kifaurongo. "Pii..Piii...Pipiiiii...." kabla hata Bruce Master hajamalizia maongezi yake honi ya kwenye gari aina ya NOAH lenye vioo vya giza ilikuwa inapigwa mfululizo.
"Yap.. Yap...Taita mwenyewe huyo ngoja nikamsikilize, nitakuja kukupa jibu" akakurupuka mbio mbio 'Bruce Master' tena akipekua ili kumuwahi bazazi Mwinyi Fuad kwenye gari yake. "Psiiiii.....Psiiiii......Psiiii....! Dogo njoo mambo yameiva" alipayuka yule mbabe kumuita MbwekuJr aje pale kwenye gari ya mwarabu Mwinyi Fuad. Kiunyonge sana, kijana Mbweku baada ya kujishauri mara kadhaa akajinyanyua na kuwafuata pale garini. "Mpe chake kabisa, ajue sio kazi ya kisanii...!" aliongea Bruce Master akijifanya kutetea maslahi ya kijana Mbweku. Mwinyi Fuad akajibu kwa vitendo bila kutamka neno lolote ulimini, akavuta droo ya siti ya upande wa abiria kiti cha mbele na kuchomoa fuba la noti nyekundu za shilingi mia mbili zimefungwa kwa pamoja. Kisha akachomoa noti zenye thamani ya shilingi elfu mbili (Tshs 2,000/=) na kunyoosha mkono akitaka kumkabidhi kijana Mbweku. Mwinyi Fuad alikuwa anamzuzua MbwekuJr kumuonyesha kuwa yeye ni mtu aliye ghariki ukwasi hana shida ya pesa.
Mbweku akataka kupokea lakini akasita kidogo kupokea. Akarudisha mkono wake kisha akauliza huku amemkazia macho Mwinyi Fuad bila hofu yoyote, "Samahani Mzee unanipa hizi pesa ni za kazi gani? maana ninavyofahamu mimi hamna cha bwerere hapa duniani..!" . "Kwani weye hujamuambia huyu?" akafoka Mwinyi Fuad kwa hasira, uso wake ukiwa ule umepigwa na taharuki anamsumbua anamuangalia Bruce Master kuwadi wake wa kumtafutia wasenge. Akajitia kutaka kuzirudisha pesa zake kwenye droo ya gari. "Mwana unaniangusha...si nimekuambia ana kazi, wewe pokea kwanza acha ushamba Mjini hapa dogo shauri yako, unadhani wote wanaomiliki magari mazuri na majumba wangekuwa malofa kama wewe wangepata? Wangekuwa mpaka leo wanauponda wa fisi mitaani. Uchumi unaukalia dogo halafu unalalamika shida shida.... ..rudi basi kijijini kumsaidia mama yako kulima umekuja kufanya nini Mjini kama huwezi kujitoa mhanga kwa vitu vidogo tu.....!" Bruce Master alijifanya kumfunda kihuni huku sauti yake ikionyesha kabisa ameghadhibika kwa ukaidi ulioonyeshwa na MbwekuJr mbele ya mfadhili wake.
"Tena kama unakataa kazi, hapa kwenye himaya yangu uhame kabisa ukatafute kwa kulala kwa washamba washamba wenzako..!" alizidi kuporomosha maneno ya karaha kwa MbwekuJr. Baada ya maongezi ya vitisho vya hapa na pale MbwekuJr akapokea zile pesa kwa shingo upande, akazitia mfukoni na kukubali kupanda kwenye gari la Mwinyi Fuad. Akiahidiwa kuwa wanaelekea Bandarini kuna kazi ya kupakua mizigo kupakia kwenye Lori la Mwinyi Fuad. Wakati wanaondoka, MbwekuJr bado roho yake ilikuwa haimtumi kabisa, kupakua mizigo tu ulipwe pesa nyingi kama elfu mbili, mizigo hiyo ya aina gani, lakini akapiga moyo konde na kusubiria kitakachotokea, huko huko mbele ya safari. Alishajipanga kama atafanyiwa vitendo vya kikhabithi atapambana nae mpaka kifo, piga ua hatokubali. Wakatoka na gari vizuri huku akifunga vioo vyote vyenye kiza na kwenda kuligeuza gari katika mzunguko wa Uhuru na kushika uelekeo wa barabara ya kuelekea maeneo ya Posta. "Mpenzi unaitwa nani, nimeshasahu jina lako? " alivunja ukimya Mwinyi Fuad huku akijilazimisha kutabasamu. Moyo wa Mbweni ulipasuka vipande vipande baada ya masikio yake kusikia anaitwa kwa jina la mpenzi.
Akajikuta anapatwa na kigugumizi cha ulimi katika kutaja jina lake, huku akifanya kazi ya ziada kusema na moyo wake utulize hasira. Kengele ya tahadhari ilishagonga kichwani mwake, kuwa Mwinyi Fuad sio mtu mzuri hata kidogo, pesa zake hazina sada na sudi zinataka kumuingiza motoni kesho yaumu kiama mbele ya Mola wake. "Usiogope mchumba, tena una sura ya matlai shamsi wa kiume, mie nataka uwe mpenzi wangu, nipo tayari kukulipia mahari na nitakufanyia mambo mengi mazuri na kuboresha maisha yako ukikubali kuwa mpenzi wangu..!" aliongea kwa sauti ya kubembeleza huku akiwa anampapasa mwilini MbwekuJr kimahaba kwa mkono wa kushoto huku mkono wa kulia umeshikilia steringi ya gari.
MbwekuJr alikuwa anatetemeka mwili mzima kwa hasira, alikuwa anatamani amrushie mangumi pale pale amalizane nae baradhuli mjaa laana huyu, mwenye kutumia nguvu ya pesa zake kuwalawiti watoto wa watu kutokana na shida zao za kimaisha. "Kweli Mjini kuzito nilikuwa naambiwa tu sasa nayashuhudia mwenyewe, yaani huyu anataka kunioa mtoto wa kiume?" alikuwa anawaza mkururu wa mawazo kichwani mwake MbwekuJr. Busara zikaongoza kichwani mwa Mbweku kwa kuhofia asije kusababisha ajali ya barabarani pindi akiamua kumshughulikia njiani Alikuwa anajiamini kwa umbile lake kubwa la miraba minne licha ya kuwa na umri mdogo, asingeshindwa kumuadabisha Kibopa Mwinyi Fuad. Utulivu wa MbwekuJr bila kumpatua mikono yake, Mwinyi Fuad akajua kijana wa watu kashakubali ndio akazidisha vituko vya kumchezea Mbweku. Mara ampapase kifua chake, ajaribu kubinyabinya chuchu zake, mara mkono uhamie kupapasa tumbo lake ili mradi alikuwa ni mshenzi wa tabia.
Mwinyi Fuad na yeye akapatwa na mihemko na kutoa miguno ya kimahaba akionekana ni galacha mkubwa kwenye sekta ya mapenzi haramu ya jinsia moja. Mara tu, wakawa wameshafika ufukwe wa 'Coco Beach' kutokana na kutokuwa na msongamano wa magari barabarani. Fukwe ya Coco ambayo ipo Msasani Peninsula, sehemu hii ni maarufu pia kwa kuuza vitu kama mishkaki na muhogo wa kuchoma, hivyo nyakati za mchana familia nyingi za Jijini Dar es Salaam hupenda kwenda kupumzikia hapo. Mwinyi Fuad alikuwa ameshapandisha pepo la ulawiti kama la watu wa Sodoma na Gomora enzi za Nabii Lutu, akaegesha gari pembeni ya ufukwe, akazima taa za gari na kushuka haraka haraka nje ya gari huku akivua nguo zake zote, akibaki uchi wa mnyama kama alivyozaliwa.
MbwekuJr alizidi kugwaya nafsini mwake akiwa haamini kama huyu ndio yule Mwinyi Fuad, mtu mahashumu mpaka kwa viongozi wa chama na serikali nchini. Pia ni mtu wa ibada, khamsa swalati, kipindi hakitoki msikitini, kumbe ni mtu bunga kiasi hichi. MbwekuJr akawa anameza machungu kifuani mwake. Akiwa hajakaa vizuri, akastukia mlango wa gari unafunguliwa kwenye siti aliyokaa kwa nguvu huku akivutwa na kutupwa chini ya mchanga wa pwani kijana MbwekuJr. Kabla hata MbwekuJr hajatanabahi nini kinachotaka kumkuta, tayari alishavamiwa pale chini na kuanza kuvuliwa pensi lake nyeusi la dangirizi mpaka likafika magotini na Mwinyi Fuad huku akiwa anahemea juu juu tayari anajiandaa kumfanyia vitendo vichafu kijana wa watu.
MbwekuJr alishafanya maamuzi ya kujilinda kufa au kupona, mfukoni alikuwa na kisu chake cha kukunja. Akajilegeza kama kweli anataka aingiliwe bila shida huku anaupeleka taratibu mkono wake wa kushoto nyuma ya mfuko wenye kisu, mpaka akakifikia kisu chake. Mwinyi Fuad akapunguza kumkandamiza kwa nguvu akijua shughuli imeisha kwa kijana kashakubali kulawitiwa, ndio maana haleti makeke ya ubishi. Likawa ni kosa kubwa sana kwa Mwinyi Fuad, kama umeme kijana MbwekuJr alijigeuza na kuchomoa kisu kisha akamshindilia kisu chake tumboni mwake na kukipeleka kushoto na kulia kikatili sana." Shabaaash ...kufa mwanaharamu wewe" alipiga ukelele wa ujasiri ghulamu MbwekuJr huku akikoroga kisu chake pande zote za tumbo kukatakata utumbo wa Mwinyi Fuad.
"Aaaaaaah....Nakuff...waaahaah.....!" alitoa sauti ya kugugumia maumivu mara moja tu huku akijigaragaza kwenye mchanga. MbwekuJr alibaki amepigwa na butwaa huku mkononi amekishikilia kisu chake mkono wa kushoto anatwetwa kwa hasira mithili ya farasi wa mashindano. Baada ya kupita dakika kadhaa MbwekuJr akatanabahi kuwa amefanya mauaji ya Mfanyabiashara Mwinyi Fuad. Akakimbilia mpaka karibia na maji ya bahari kisha akataka kukitupa kisu chake kwenye maji ya bahari, ili kupoteza ushahidi lakini akasita kufanya hivyo. Akabadili maamuzi ya kukitupa akaamua kukisafisha na maji ya bahari. Alipomaliza tu, akakikunja na kukirudisha mfukoni mwake. Alishaamua hiyo silaha yake asiitupe inaweza kumsaidia siku za usoni kuwaadabisha wajuba kama Mwinyi Fuad. Akanawa damu mikononi mwake na kuipangusa damu iliyodondokea kwenye fulana yake na kuanza harakati za kutaka kutoroka eneo la tukio. Akausogelea kwa karibu mwili wa Mwinyi Fuad na kumuona kwa msaada wa mbalamwezi angani anageuzageuza macho huku anakoroma kwa nguvu yupo katika ghari ghari ya mauti, huku damu zinabubujika kama maji toka tumboni mwake huku utumbo wote ukiwa nje umetapakaa kwenye mchanga wa bahari. Bamvua la maji kujaa lilianza kushika kasi, huku maji yakiwa yamebakiza mita chache kuifikia ilipo maiti ya Mwinyi Fuad.
Akairuka ile maiti na kulisogelea gari la marehemu Mwinyi Fuad. Akaifungua droo kwa urahisi kwa kuwa mlango wake ulikuwa wazi. Akaikuta droo hiyo imehifadhi burungutu la pesa alilokuwa analitumia muda wote wakiwa garini kumshawishi nalo akubali kulawitiwa nae. "Kiendacho kwa mganga hakirudi, hizi pesa ni mali yangu" alijisemea kimoyomoyo huku tabasamu pana likichanua usoni mwake, usifanye mchezo na pesa sabuni ya roho. Akazibeba zile pesa kwenye bahasha yake na kuanza kukimbia kuelekea asipokujua, akiamua kufuata njia ya barabara alipofika barabarani tu akaanza kutembea, akijua ameshasalimika. Ghafla bin vuu akaliona gari la polisi linakuja kasi kwa mbele yake. Jasho jekejeke lile la uoga likaanza kumtiririka chini ya kwapa zake, huku akijilaumu kwa maamuzi ya hasira ya kumuua Mwinyi Fuad. Mbaya zaidi kisu alichokitumia kwenye mauaji hayo alikuwa nacho mfukoni, hivyo ushahidi umeshakamilika akikamatwa na kufikishwa kizimbani mbele ya Jaji. Akawa anavuta taswira kama ya siku ile baba yake mzazi anahukumiwa mbele ya Jaji kule Arusha, jinsi familia yao ilivyohuzunika kwa hukumu ile. MbwekuJr akawa anavaa viatu kama vya baba mzazi jinsi atakavyohukumiwa na Jaji. "Mbweku wa Mbweku nakuhukumu kunyongwa mpaka kifo kutokana na mauaji ya Mwinyi Fuad Katika Ufukwe wa Coco" akikuwa anaisikia sauti nzito ya Jaji inarindima masikioni mwake.
Akazidi kuongea kasi ya mwendo wake huku sasa akianza kulikanyaga daraja la Salenda "Selander Bridge" lakini anatetemeka kama mlevi wa gongo, kihoro kimemkamata huku akipatwa na maumivu mfano wa tumbo la zingizi lile linalomkamataga mama mjamzito baada ya kujifungua. Daraja hilo lililopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam, Tanzania linaunganisha kaskazini magharibi mwa jiji la Dar es Salaam na mjini kati na maeneo jirani ya Kinondoni na Oyster Bay. "Hey....wewe kijana simama kwanza, upo chini ya ulinzi kwa amri halali ya jeshi la polisi...!" ilikuwa ni sauti kali toka kwa mmoja wa mapolisi ikimuamuru MbwekuJr asimame. Sauti ile mithili ya radi ya polisi yule ilipopenya katika ngoma za masikio ya MbwekuJr, ilimzindua kutoka kwenye mawazo yake ya kizimba cha mahakama, hakusubiria aitwe tena kwa mara ya pili. Akajikuta miguu yake inapata nguvu za ghafla na inaanza kuchanganya kwa kasi ya ajabu mfano wa mwanariadha mahiri anayeshindania medali ya dhahabu. Alijua fika akizubaa amekwisha maana amesha tomasa ugenge kwa kumchoma kisu na kumuua tajiri mwenye Jiji lake, Mwinyi Fuad.
Lile daraja lilikuwa lina urefu usiopungua meta 85, akajikuta mita hizo anazikata ndani ya sekunde zisizozidi 30 mpaka kwenye kingo ya daraja. Akatupa macho yake nyuma kuwaangalia wale polisi kwa upeo wa macho yake akaona gari lao linarudi nyuma. Haraka haraka bila kupepesa macho akaning'inia kwenye bomba lililolazwa juu ya daraja, kwa kitambo kifupi kwa mtindo wa kukongoya kama mtu anayehesabu moja, mbili mpaka tatu akijiandaa kuruka. Kisha bila kuchelewa akajitupa chini ya daraja mithili ya komandoo wa Jeshi aliyekubuhu katika mafunzo anayejirusha kutoka kwenye parachuti angani. Laahaulah..! Ama kweli mbuzi wa masikini hazai, wakati MbwekuJr akiwa angani anajirusha chini ya daraja kwa bahati mbaya sana, bahasha yenye minoti aliyopora kwenye gari la marehemu Mwinyi Fuad ikamponyoka mkononi na kutumbukia kwenye mkondo wa maji unaotiririka kwa kasi kuelekea baharini. Akajikuta anahuzunika na kuweweseka kwa muda kama mtu aliyetupiwa ndumba vile kutokanao na uzembe alioufanya mpaka mfuko wenye pesa ukamporonyoka mkononi.
Machozi kapakapa yalikuwa yanamtiririka mpaka macho yake yakasharabu wekundu kwa uchungu wa kupoteza ngwenje sufufu ambazo zingekuwa ndio mkombozi wake wa maisha magumu yanayomkabili. Ama kweli MbwekuJr alikuwa mahuluku tabu, ndio takdiri toka kwa Mola wake muumba wa mbingu na ardhi. Akapiga moyo konde na kujishajiisha nafsini mwake kuwa kikubwa kwa sasa jambo la usoni mwake ni kujiokoa kwanza, hima hima akaanza kutafuta mbinu muafaka ya kujisalimisha kwanza na janga la usoni mwake, asije kutia maji maziwani bure. Muhimu kwake kwa kipindi kile ilikuwa ni kuwachenga wana usalama chenga ya mwili wasimkamate, vinginevyo jela itamuita. Maana kanuni inajulikana ukikamatwa na polisi wa Kiafrika kama una pesa lazima wakutoe upepo kutegemeana na ukubwa wa kesi ili kuwatia kidaka mdomoni, na yeye alikuwa yupo majalala hana kitu mfukoni. Wana usalama wale walimtilia mashaka MbwekuJr kutokana na kutembea kwake kwa haraka haraka huku akionekana ana wasiwasi halafu yupo peku bila viatu, ndio maana wakaona wajiridhishe huenda ni mhalifu wa usiku.
Walipoona MbwekuJr anapewa wito wa kusimama yeye badala ya kutii amri halali ya polisi anaamua kutundika miguu mabegani kwa kasi ya ajabu, wakaweka dhana kuwa MbwekuJr ni mhalifu, wakamtia katika taksiri. Dereva wa Difenda lile la polisi akaanza kulirudisha gari kisengerenyuma kwa haraka huku wamewasha taa zote. Wakashuka toka garini polisi wasiopungua watano wakiwa na bastola zao, tayari kumsaka mjuba wao MbwekuJr. Walijipanga wamtege kwa chachu kisha wamnase kwa ulimbo, ili mradi asiweze kuwatoroka kirahisi. Mshikemshike wa msako wa MbwekuJr ukaanza kwa fujo zote kama ujuavyo harakati za mapolisi wetu wakilitaka jambo lao huwa hawashindwi kitu.
SURA YA KUMI
Recho nyota yake ilizidi kung'aa kiuchumi. Ngwenje alizokuwa analipwa na Washefa wake kwenye kazi yake mpya kuuza mwili zilikosa kifani. Zilimtosha kupanga nyumba nzima peke yake katika eneo la Sinza na kujipatia usafiri binafsi wa kukata mitaa akiwa Jijini Dar es Salaam. Katika wanawake wa kwanza kwanza Jijini Dar es Salaam kumiliki gari la kifahari zama hizo la aina ya 'Korando' toleo jipya. Mpaka ikafika hatua anawaponda kwa kejeli wale wanaouponda wa fisi au kupanda usafiri wa umma kwenye mizunguko yao ya kila siku ndani ya Jiji. Alishajiapiza kamwe hawezi kupanda daladala hata kama gari yake italeta matatizo, alikuwa yupo tayari akodishe taksi hata kama ni siku nzima. Alishafanikiwa kukata miaka kadhaa Jijini Dar es Salaam huku jina lake likiwa maarufu kwenye kumbi na klabu zote kubwa za starehe Jijini.
Bendi zote kubwa za muziki wa dansi hapa nchini kwenye nyimbo zao wakawa wanatia vionjo vya kulitaja jina lake. Mara kwenye nyimbo anaimbwa "utasikia dadaa Rechooo, una sura nzuri kama malaika" na sifa kedekede za kumpamba mafuta kwa mgongo wa chupa. Nae Recho alivyokuwa mpenda misifa, akitajwa tu alikuwa anacheka na kuterema kisha lazima asimame toka kitini kwenda kuwatuza wanamuziki wote wa bendi.
Katika harakati zake za umalaya, Recho akaibua fursa nyingine nchini Jijini Nairobi. Akafanya maamuzi ya kurudi tena huko kwa mara ya pili baada ya kukatika miaka kadhaa tokea afukuzwe ndani ya masaa 24 na kudhulumiwa Klabu yake ya "Nairobee By Night". Kilichomsukuma arudishe majeshi tena Jijini Nairobi ni fursa ya kuwadaka watalii wa kutokea ughaibuni wanaotua Jijini Nairobi. Kenya ilikuwa na wasaa mkubwa wa kupokea watalii kutokana na kuwa na shirika la ndege lenye nguvu la 'Kenya Airways' kulinganisha na Tanzania ambayo shirika lake la ndege la 'ATC' lilikuwa lipo mahututi linapumulia gesi likiwa na kidege kimoja tu tena chakavu. Maelfu ya watalii kutokana na kutoka nchi za Ulaya walikuwa wanamiminikia Kenya wakiaminishwa na propaganda kuwa Mlima Kilimanjaro upo Kenya. Kisha wakija kutanabahi kuwa Mlima huo, upo Tanzania wanakuwa tayari fedha nyingi za kigeni wamezitumia nchini Kenya na Tanzania kuambulia mabaki tu. Hivyo Recho akaona Nairobi ataweza kuibua madanga ya kizungu yenye pesa sufufu hivyo kuzidi kujiimarisha kiuchumi.
Na kwakuwa Jiji la Nairobi analijua nje ndani, haikumpa ugumu kulizoea tena Jiji hilo kwa haraka. Sasa akawa mtu wa kambi popote, anakaa Nairobi wiki mbili kisha anarejea Jiji Dar es Salaam, anazunguka kama popo baina ya Majiji hayo mawili. Baada ya miezi kadhaa tu akafanikiwa kutengeneza mirija ya kuingiza pesa za kutosha. Katika hangaika yake ya kusaka pesa haramu, akafanikiwa kumnasa kiruka mito wa kizungu, kutoka nchini Italia wa rika lake kabisa ambaye kwa jina alikuwa anajulikana kama Mr.Lorenzo. Huyu mzungu, buzi lake jipya alikuwa ni baba mlezi kabisa wa mtoto wa Recho, Pesambili. Mr.Lorenzo alikuja Afrika Mashariki kwa gia ya utalii lakini kiuhalisia alikuja kuangalia fursa kwa ajili ya kazi haramu maalumu. Kazi ambazo zilikuwa zinamuingizia Mr.Lorenzo mabilioni ya pesa katika nchi mbalimbali za Kiafrika alizowekeza.
Nchini kwao Italia alikuwa anajipambanua kama Mfanyabiashara maarufu mwenye kumiliki kampuni ya kuzalisha na kusambaza filamu za wanyama pori 'Wildlife'. Kampuni hiyo ya Mr. Lorenzo ilikuwa inajulikana kama 'Talking Trees and Animals Creative(TTAC)-Films Company LTD. Baadhi ya serikali za nchi za Kiafrika zilikuwa zimeingia nae mkataba wa kuwatangazia vivutio vyao vya kitalii. TTAC-Films Company Ltd, ilijipambanua kama moja ya kampuni bora kabisa ya filamu Jijini Turin nchini Italia. Lakini sirini kampuni hiyo ilikuwa inazalisha pia filamu za ngono zinazorekodiwa maeneo tofautitofauti katika nchi mbalimbali za Afrika. Nchi nyingi za Afrika zilikuwa zimepiga marufuku kwa raia kushiriki kuandaa filamu za ngono, na zilikuwa zimeweka adhabu kali kwa watakaobainika. Hivyo kampuni ya TTAC-Films Company LTD inayomilikiwa na Mr.Lorenzo ikawa inafanya shughuli hizo kinyemela kinyume na utaratibu. Kwa kuwahadaa washiriki hao kwa kuwapa fedha sufufu ili mradi wasikatae kurekodiwa filamu hizo.
Shughuli hizo walikuwa wanazifanya kwa usiri mkubwa sana. Mr Lorenzo na wahuni wenzake walikuwa wanakwenda kuzuru nchi mbalimbali za Kiafrika kwa kutumia hati feki za kusafiria wakijifanya kama watalii wenye kuvutiwa na mali asili za Afrika kumbe wanafanya pia utalii wa ngono. Mr.Lorenzo kwa Recho alijitambulisha kwa jina bandia la 'Luis Van Odergaard', Mdachi wa Uholanzi, akijifanya ni Mfanyabiashara wa vito vya madini. Hakutaka kabisa Tengo amjue undani wa shughuli yake anayoifanya. Na Recho nae mara tu baada ya kufariki mama yake akajibadilisha jina na kuanza kujiita 'Recho Kavishe', akitumia ubini wa ukoo wa babu yake mzaa mama. Hakutaka kabisa kulisikia jina la baba yake mzazi Mzee 'Francesco' ambaye kwanza alikuwa hajawahi kumtia machoni na wala kupata huduma zake za matumizi. Alikuwa anamchukia baba yake mzazi kupita maelezo hasa kutokana na maamuzi ya kumtelekeza hali ya kuwa mama yake alikuwa anamuambia kuwa baba yake ni mkwasi wa mali huko nchini Italia alipo.
Maisha yao ya usanii na ulaghai yakasababisha ndugu wa baba mmoja wasitambuane na waangukie katika mapenzi motomoto bila kufahamu kuwa wao ni ndugu wa damu kabisa. Mwanzoni Mr.Lorenzo alimchukulia Recho kama walivyo malaya wengine tu aliowahi kupita nao, lakini kadri siku zinavyokwenda akajikuta anazidi kumpenda Recho, amesalitika vilivyo. Tokea aanze kuyajua mapenzi alikuwa hajawahi kustareheshwa kwa ufundi mkubwa kama anavyofanyiwa na Recho. Akakata shauri kuwa lazima Recho awe wake peke ajifaidie anavyotaka yeye. Akampa masharti kuwa akitaka awe mpenzi wake aachane na shughuli ya uchangudoa atamfanyia mambo makubwa maishani mwake.
Recho baada ya kumgundua kuwa Mr.Lorenzo ni pochi nene, sio pangu pakavu tia mchuzi nile hakuwa na shida kutimiza masharti aliyotakiwa kuyatekeleza ya kuachana na biashara ya kujiuza mwili wake. Mr.Lorenzo kuonyesha amekufa na kuoza kwa Recho akamuuliza amfungulie mradi gani wa kujikimu kimaisha. Recho alifurahi sana na kuona wakati wa kulipa kisasi kwa mpenzi wake wa zamani Martin Tenga umetimu. Recho bila kupepesa macho, akataka kufunguliwa biashara ya Hoteli, na kumtaka Mr Lorenzo amnunulie 'Martino Royal Hotel' iliyopo Jijini Dar es Salaam, Hoteli ambayo ilikuwa sokoni inapigwa bei. Baada ya Bwana Martin Tenga kushikiliwa huko nchini Italia, ndugu zake wakashindwa namna ya uendeshaji wa Hoteli hiyo ya kifahari hivyo wakaiweka sokoni kwa mteja yoyote atakayejitokeza.
Hoteli hiyo ya kifahari yenye roshani 10 ilikuwa inauzwa milioni 200 taslimu. Mr.Lorenzo alichofanya ni kutekeleza ombi la kimada wake huyo kwa moyo mmoja kwa kufanya taratibu zote za manunuzi ya Hoteli hiyo. Hati ya manunuzi ya Hoteli hiyo iliandikishwa kuwa Hoteli hiyo inamilikiwa kwa ubia kati ya mzawa Recho na mwekezaji Mr.Lorenzo. Hivyo Recho alikuwa na furaha sheshe kwa kufanikisha kuirudisha Hoteli yake aliyoiasisi kwenye mikono yake mwenyewe kisha akaporwa kilaghai na mpenziwe wa zamani Martin Tenga ambaye alikuwa hataki hata kumsikia wala kumuona. Alitamani sana Recho, Mr.Martin Tenga arudi nchini Tanzania na aone jinsi Hoteli aliyodhulumu ilivyotua tena mikononi mwa Recho.
Kwa upande wake Mr. Lorenzo alikuwa anaendelea na shughuli yake haramu kwa kificho sana, bila Recho kushtukia kazi yake inayomleta mara kwa mara katika nchi za Afrika Mashariki.
Wasichana wa kucheza filamu hizo za ngono alikuwa hapati shida kuwapata, kutokana na tabia ya wasichana wengi wa Majiji hayo makubwa ya Afrika Mashariki kuanzia Nairobi, Kigali, Kampala, Bujumbura na Dar es Salaam kuendekeza utajiri wa mezani. Ule utajiri wa bila kutoka jasho kwa kutumia uzuri wa maumbile yao. Maisha yakawa yanasonga baina ya wapenzi hao wapya ambao ni kaka na dada wasiotambuana.
Lakini kama kawaida yake Recho kwenye pesa huwa ana simile, akili yake inaruka na kuwaza kufanya dhuluma, akaandaa mpango wa kumuondoa kwenye umilki wa Hoteli hiyo Mr.Lorenzo, kabla kibao hakijamgeukia na kufanyima unyama wa kutisha na Mr.Lorenzo. Unyama ambao ulimuacha mgonjwa kitandani maisha yake yote.
Deborah alishaanza kuwa mzoefu wa mitaa ya Kisutu stendi ya Mabasi ya mikoani. Alishakata miezi miwili tokea atue Jijini Mwezi Novemba. Alipata kibarua cha kuuza kioski cha kuuza vitafunwa na vya vinywaji baridi kwa abiria na Wafanyabiashara ndogo ndogo kuzunguka eneo hilo la Kisutu. Haikumchukua muda kuzoea biashara maeneo hayo, hasa ikichukuliwa kuwa ana uzoefu wa biashara hizo kwa zaidi ya miaka 4 kutokea kule Kijiji Mikongeni, Morogoro. Kioski alichokuwa anauza kilikuwa kilikuwa kinamilikiwa na Koplo Marieta, Askari wa kituo cha polisi, Msimbazi, Kariakoo. Deborah alikuwa anamchukulia Koplo Marieta kama malaika mkombozi kwake. Hivyo ni kwa namna alivyomchomoa katika mikono ya polisi wenzake waliotaka kumfungulia kesi ya uzembe na uzururaji kisha wamrudishe kijiji kwao tena. Siku ile aliyotoroka nyumbani kwao alifanikiwa kupata msaada wa usafiri wa kumfikisha Jijini Dar es Salaam kama alivyotarajiwa.
"Sasa mwanangu Deborah tumeingia tayari Jijini Dar es Salaam, tutakushusha hapa Buguruni, tutakupakiza kwenye daladala litakalokushusha stendi ya Mabasi ya Kisutu kama ulivyoelekeza kuwa mwenyeji wako yupo huko" aliongea dereva Babu Juma kwa sauti ya uchovu wa safari, akimuelekeza Deborah kuwa wameshawasili ndani ya Jiji. Babu Juma alikuwa ameendesha gari lake usiku kucha bila kupumzika tena akiwa ameutwika mtindi wa pombe za kienyeji kichwani mwake. "Ahsante sana Babu Juma tutaonana tena Mungu akipenda, nakutakia kazi njema" Deborah alishukuru huku akiunda tabasamu moja matata usoni mwake. Shukrani hiyo ilikuwa ni kutokana na msaada wa bure aliopewa na dereva yule. Baada ya hapo akaanza kukusanya kifurushi chake cha nguo akijiandaa kushuka chini ya gari lile.
Deborah aliwadanganya akina Babu Juma na Taniboi wake kuwa mwenyeji wake anamsubiria kumpokea stendi ya Mabasi ya Mikoani ya Jijini Dar es Salaam. Wakati ukweli wa mambo ni kuwa hakuwa na ndugu wala rafiki katika Jiji hilo la Dar es Salaam. Alichokuwa anajipa moyo ni kuwa Mungu atampa stara asiadhirike ugenini. Aliamini bila kwa yakini isiyo na mashaka kuwa kwa baraka za Mola atapata msamaria mwema atakayemuangalia kwa chakula, mavazi na malazi. Walikuwa wameingia Jijini Dar es Salaam asubuhi asubuhi wakiwa wametoka Morogoro tokea manane ya usiku.
Akawashukuru na kuagana nao, akiwaongopea amekuja Jijini Dar es Salaam kusoma masomo ya ziada 'Tuition' kwa ajili ya kujiandaa na masomo ya kidato cha kwanza kwa mwaka ujao wa 1997. Aliposhuka tu kwenye Lori lile, Taniboi nae akawa nae bega kwa bega kumtafutia Daladala kama alivyoomba. Basi hizo ndogo zilikuwa zinaitwa 'Daladala' kutokana na kutoza nauli ya shilingi 5 kwa safari. Deborah kwa bahati nzuri alipata siti ya dirishani, hivyo macho yake yalikuwa yamekodoka barabarani utasema anakata roho kutokana na kushangazwa na uzuri wa maghorofa na magari yanayopishana barabarani kwa kasi kubwa. Tokea anapata akili timamu mpaka anavunja ungo, alikuwa hajawahi kupata mtoko wowote wa safari hata walau wa kufika Morogoro Mjini. Hivyo hiyo ndio ilikuwa ziara yake ya kwanza kubwa katika maisha yake.
Daladala lile alilopanda bila kuchelewa likamshusha Kisutu kama alivyohitaji huku likiendelea na safari zake kuwafikisha abiria wengine. Aliposhuka tu pale stendi na kuuona umati wa watu stendi pale, moyo wake ukamlipuka kwa uoga. Kilichokuwa kinamshangaza watu wale walikuwa wanaongea Kiswahili cha haraka haraka kama ndege tena chenye kukatisha maneno. Lugha ambayo ilikuwa inampa wakati mgumu sana kuelewa wanaongea kitu gani haswa. Hofu ilimjaa zaidi baada ya kuona kila mtu alikuwa ameshika hamsini zake ametingwa na mambo yake hamna hata mmoja wa kumuuliza hali yake mgeni na anahitaji msaada gani. Alitegemea ukarimu wanaofanyiana kijiji kwao huku Mjini uwe maradufu.
Akaanza kuuchukia Mji huo kuanzia muda huo huo kutokana na watu wake kukosa utu na ubinadamu. Kiu ya maji na njaa ilikuwa imemkamata vilivyo asubuhi hiyo utasema yupo kwenye mfungo. Deborah akaanza kutupa macho yake huku na kule kutafuta walau kisima cha kujichotea maji ya kunywa kama kule kijijini kwao. Pia alitarajia huenda atauona mti wa mchungwa au muembe walau abahatike kuchuma tunda ashibishe minyoo tumboni. Kwa bahati mbaya hakuambulia kiti chochote katika alivyovitamani. Zaidi ya kuziona embe chache na machungwa yamepangwa kwenye meza za wachuuzi wadogo wadogo zinauzwa.
Alishangazwa sana kuona matunda wanayogaiana bure kijijini kwao mpaka wanyama kama nyani na tumbili wanajipocholea bwerere huku Mjini yanauzwa kwa bei ya kuchupa. "Hawa watu wa Mji huu, nimewanyooshea mikono na wana dhambi sana, embe za shamba la Bi. Pembe kule kijijini tunajiokotea bure tu" alinong'ona moyoni mwake. Akawa amejikunyata kwenye banda la wasafiri akiwa amejichanganya na wasafiri wengine wanaosubiri Mabasi ya kuelekea mikoani, huku akizichanga karata zake kichwani mwake kuitafakari hatima yake. Kwenye akiba yake kibindoni alikuwa na shilingi 55 taslimu, alizozipata katika mauzo ya shingo za kuku, ndizi na sinia za kuuzia asusa hizo zote alizipiga bei.
Alijitahidi kuvumilia njaa na kiu ili mradi asikiguse kibubu chake cha akiba lakini ilipofika majira ya adhuhuri, uzalendo ukamshinda. Usicheze na tumbo wewe, ndio maana watu wazima na heshima zao wanapokea rushwa, wanajiingiza kwenye ufisadi, wanawake wanajiuza miili yao, ukiwauliza kisa tumbo. Ikabidi aishiwe ujanja, asije kuanguka njaa bure na pesa anayo. Kiunyonge kabisa ikabidi afungue kibubu chake na kujongea banda la jirani la mama lishe na kuagiza chakula, akala, akashiba na kuendelea kutafakari kitu gani cha kufanya kadri saa zinavyozidi kwenda. Mpaka kufika majira ya magharibi, asilimia kubwa ya abiria walikuwa tayari wameshatawanyika zao mmoja mmoja kuelekea majumbani kwao kupumzika. Mabasi ya kutokea mikoani asilimia kubwa yalikuwa yameshawasili zao.
Kiza kikaanza kutanda angani huku mawingu mekundu yakizidi kupotea kuashiria usiku mbichi unakaribishwa. Hofu ikazidi kushamiri katika moyo wa Deborah huku akianza kujutia kwanini hata alichukua maamuzi magumu na ya hasira ya kuja Jijini Dar es Salaam bila kujipanga. Akazidi kujipa nasaha za majuto ni mjukuu kuwa siku zote hasira ni hasara. Na daima mwanadamu hutakiwa kufanya maamuzi wakati una hasira sana au una furaha sana, lazima utapotoka katika maamuzi yako. Sasa alijiona kabisa anapatwa na fedheha ugenini, sehemu ambayo hamna mtu yoyote anayemfahamu kwa kina. Wasela wa stendi nao hawakutaka kujivunga, tayari wakaanza kuiona fursa ya kujiegesha kwa Deborah usiku huo. Walishazoea kujipatia wasichana wa mahonyo wanaozagaazagaa stendi hapo. Kwao suala la magonjwa ya zinaa kama UKIMWI, sijui Kaswende, Kisonono na mengineyo ilikuwa ni hadithi za alinacha zisizo na mashiko. Walichokuwa wanajali wao ni kuitimizia nafsi hawaa zake inazohitaji.
Hofu ikazidi kushamiri katika moyo wa Deborah huku akianza kujutia kwanini hata alichukua maamuzi magumu na ya hasira ya kuja Jijini Dar es Salaam bila kujipanga. Akazidi kujipa nasaha za majuto ni mjukuu kuwa siku zote hasira ni hasara. Na daima mwanadamu hutakiwa kufanya maamuzi wakati una hasira sana au una furaha sana, lazima utapotoka katika maamuzi yako. Sasa alijiona kabisa anapatwa na fedheha ugenini, sehemu ambayo hamna mtu yoyote anayemfahamu kwa kina.
Wasela wa stendi nao hawakutaka kujivunga, tayari wakaanza kuiona fursa ya kujiegesha kwa Deborah usiku huo. Walishazoea kujipatia wasichana wa mahonyo wanaozagaazagaa stendi hapo. Kwao suala la magonjwa ya zinaa kama UKIMWI, sijui Kaswende, Kisonono na mengineyo ilikuwa ni hadithi za alinacha zisizo na mashiko. Walichokuwa wanajali wao ni kuitimizia nafsi hawaa zake inazohitaji. Wakaanza kumsarandia waondoke nae wakafanye yao, kila mmoja anamwaga sera zake na kutupa ndoano yake yenye chambo kwa shauku na mshawasha mkubwa wa kumuingiza mtegoni Deborah.
"Sistery....mambo vipi kama hauna mwenyeji, utaondoka na mimi uskonde, tuliza wahaka na jakamoyo...!" alichombweza mmoja wa vijana hao huku akijichekesha chekesha. "Jimmy..achana nae huyu dada ni wa kwetu kabisa toka Mji kasoro bahari lafudhi zake tu unaziskia kabisa. Naondoka nae mimi huyu, huu mkwaju wa maana haswa, toka Milima Uluguru..." aliongea mhuni mwingine kwa swaga za lafudhi za vijana wa Mjini akibishana na hasimu mwenzie.
Deborah hakujishughulisha nao, anawapiga kijicho pembe akawa amebaki amejikunyata, Amejivika ujasiri wa Simba wakati moyoni alikuwa na uoga wa kunguru huku akisali na kuomba kila aina ya dua wasije kumfanyia vitendo vya kifedhuli. Tayari usiku mbichi ulikuwa umeshaingia, kiza kilisha shamiri mawinguni huku nyota angani zikijitutumua kutoa nuru yake walau kufifisha makali ya giza kadri zinavyoweza. Wale wajuba wa stendi baada ya kumuona Deborah sio anuwai ya wasichana wanaojiokotea, wakaamua kutokomea zao vichwa chini kama kuku mwenye mdondo. Walikwenda kujaribu mawindo mengine, hiyo ndio ikawa salama na pona ya Deborah.
Usiku huo akala tena 'chips dume' za muhogo, na kusukumizia na maji ya kidebe, akarudi tena kwenye majlisi yake. Alikuwa ameshachanganyikiwa hajui hata cha kufanya. Taswira ya Jiji la Dar es Salaam kwa namna alivyokuwa anaisikia kwenye redio na kuisoma kwenye vitabu shuleni, na uhalisia wake ilikuwa ni mbingu na ardhi. Fikra zake zikimtuma kuwa amekuja kwenye Jiji la asali na maziwa kumbe yupo kwenye Jiji la shubiri mwitu. Jiji ambalo ni sehemu ya hatari kwa ustawi wa mwanadamu kuishi. Kadri muda ulivyokuwa unasonga ndio wavulana wadogo wadogo, machokoraa wanaolala kwenye stendi za Mabasi wakavamia banda la abiria. Wengine wakawa wanazidi kumjongelea Deborah, ili mradi tafrani mtindo mmoja.
Wakiwa baadhi yai wanatokwa na udenda wa fisi wa kufuata mkono wa binadamu udondoke ale. Walianza kumjongelea na kumuuliza maswali yasiyo na kichwa wala miguu, mpaka Deborah akaona kabisa dalili zote za kubakwa zipo waziwazi akijilegeza. Akapanga achomoke pale alipo, akajibanze kwenye kibanda chenye ulinzi wa mgambo. Alishakata shauri kuwa kesho jua likichomoza tu anakata tiketi ya kurejea nyumbani kwao Morogoro. Alishapanga atamuomba msamaha Mjomba pindi watakapoonana ana kwa ana. Mawazo yaliwaza kuwa siku akirejea, shangazi yake atamdunda kama paka mwizi. Kwanza alifahamu kuwa kijiji kizima kitakuwa kimeshapata taarifa zake za wizi wa shingo za kuku na sahani yake. Machozi yalianza kumlengalenga Deborah, akijiona kabisa yeye ni fungu la kukosa, na daima wambili havai moja.
Ghafla bin vuu....Deborah akiwa hana hili wala lile akashtukia Difenda la polisi limetua pale Stendi ya Kisutu likiwa na askari wapo kwenye kamatakamata ya wazembe na wazururaji. Wale vijana wahuni walipoiona tu ile gari kila mmoja wao mguu begani, kuhofia kutiwa mbaroni. Wale waliozubaa wote wakakamatwa akiwemo na Deborah. Msemo wa kuku mgeni hakosi kamba mguuni ukatimu kwa Deborah. "Wewe unafanya nini hapa sasa hivi usiku huu msichana mdogo kama wewe..!" alibandikwa swali Deborah na mmoja wa maafande wale, yakifuatiwa na mkururu wa maswali ya kipolisi kutoka kwa maaskari wengine.
Deborah akabakia kujing'ata ulimi tu, hawezi kabisa kujitetea, akiwa pia haamini kama amedakwa na wana usalama. Baada ya kushindwa kujieleza kwa ufasaha nae akasombwa na polisi wale kwenye msako huo wa usiku kwa kutupiwa kwenye Difenda. Kisha moja kwa moja akaenda kutupwa selo ya kituo cha polisi Msimbazi, kusubiria kuwekwa kitimoto cha maswali ya ziada. Deborah alikuwa anamwaga mchozi mithili ya ngamia anayetaka kuchinjwa akiwa katika majuto makubwa juu ya maamuzi yake ya hasira ya kutoroka nyumbani namna yalivyomponza. Kwa akili zake za utoto alijua kukamatwa na polisi ndio tiketi ya kufungwa jela.
Walipofikishwa kituoni, wakatenganishwa, wanawake kwao na wanaume kivyao. Baada ya hapo wakaanza kuhojiwa kila mmoja kivyake vyake sababu ya kukamatiwa huko mitaani. Ilipofika zamu ya Deborah, akaingizwa kwenye chumba cha askari mwanamke. Huko ikabidi autapike ukweli wake wote anaoujua kuhusu yeye mbele ya Koplo Marieta. Alimueleza kinagaubaga bila kuficha kitu mpaka sababu iliyomfanya akimbie nyumbani kwa Mjomba Kobelo kukwepa mateso ya shangazi yake. Koplo Marieta, kama binadamu mwenye moyo wenye nyama, imani ikamuingia akashikwa na uchungu mkubwa kutokana na mateso aliyoyapitia Deborah katika umri mdogo.
Hivyo akafunga nae ahadi ya kumchukua, ataishi nae nyumbani kwake kisha utakapofika muda wa kuripoti shule atampa pesa ya ada aende akasome. Deborah akawa amechomokea kwenye tundu la sindano chupuchupu yamkute mambo. Toka hapo Deborah akahamia rasmi nyumbani kwa Koplo Marieta kwenye kota za polisi hapo hapo Msimbazi maghorofani. Shida, tabu na mateso yote aliyopitia akayazika kwenye kaburi la sahau, kutokana na jinsi Koplo Marieta alivyokuwa anamjali. Akapumzishwa kazi za kipagazi na sulubu alizokuwa anafanyishwa na shangazi yake kule kijijini. Kazi yake mpya katika siku za fadhili wakati anasubiria muda wa shule kufunguliwa ikawa asubuhi na mapema kabisa anadamka kwenda Kisutu kwenye Kioski cha biashara kinachomilikiwa na mfadhili wake Koplo Marieta kusaidia kuuza biashara hiyo.
Deborah alikuwa anakaa hapo kibandani mpaka saa 1 mpaka 2 usiku ndio anarejea nyumbani kwa miguu tu. Kutoka Kisutu mpaka Msimbazi alikuwa anatumia takribani nusu saa, na kwa namna Deborah alivyokulia Kijijini umbali huo ulikuwa ni mfupi sana kwake. Siku za kupelekwa shule zilikuwa inakaribia, huku ada yake akiwa ameshakabidhiwa bado kununuliwa mahitaji madogo madogo ya kujikimu. Kwa jinsi Deborah alivyokuwa makini na pesa yake ya ada alikuwa anatembea nayo kila anapokwenda, akilala na kuamka nayo akiwa ameihifadhi katika nguo yake ya ndani. Akiwa Deborah amejistarehe nafsini mwake akijua muda sio mrefu ndoto yake ya mafanikio kielimu itaanza kutimia, akakumbwa na tukio baya sana maishani mwake.
Matanga ya rohoni ambayo alishaanza kuyasahau yakaibuka upya tena katika wakati usio muafaka, ikiwa ni siku tatu kabla ya shule kufunguliwa.
Deborah akatekwa na mtu asiyejulikana. Mtu huyo, aliyemteka alikuwa ni mrefu wa umbo, ana kifua kipana, akiwa anapenda kuvaa miwani nyeusi machoni mwake na kofia ya pama kichwani mwake. Hiyo yote ilikuwa ni mbinu kabambe ya kuficha wajihi wake usijulikane kisawasawa. Alijizoesha karibia wiki nzima kwenda kwenye kioski kunywa soda baridi kwa sambusa kila inapofika muda wa saa 1 usiku. Alikuwa ni mcheshi haswa atamtania Deborah na muuzaji mwenzake, akiwa ni mtu hadhiri haswa. Siku ingine atajitia kuwapa ofa ya soda na wao wanawe, wakamzoea akawazoea, kumbe ana lake jambo.
"Naona ndio muda wako wa kuondoka huu, nisubirie nimalize soda yangu tuondoke wote na mimi naelekea huko huko unakokwenda wewe..!" alizungumza yule jamaa baada ya kumuona Deborah anaagana na mwenzake ambaye yeye alikuwa anaishi Mbagala. "Mhhhh....kwani mie unajua ninakwenda wapi?" Deborah akauliza swali la kidadisi akiwa amepigwa na bumbuwazi baada kushtushwa na maelezo ya yule mtu kuwa anapajua anapoishi hivyo kupatwa na mshawaha nafsini mwake wa kutaka kumdadisi. "Rafiki yangu mwema na mzuri kama wewe nishindwe kujua unapoishi? Yatakuwa maskhara hayo, wewe unaishi Msimbazi kwenye kota za manjagu, nyumbani kwa Koplo Marieta...!" aliongea kwa kujiamini mtu yule huku akikita chupa yake ya Pepsi juu ya meza kuashiria amemaliza soda yake aliyokuwa ameinywa kwa mtindo wa tarumbeta.
Deborah akawa kama mtu aliyeshikwa na kihoro, akijiuliza maswali lukuki nafsini mwake akishangazwa na mgeni huyu kumjua mpaka anapoishi. Wakawa wanatoka wote kwa pamoja nje ya Kioski, mguu kwa mguu Deborah akiwa mbele. "Lakini mimi sina haja ya lifti nikikatisha hapo katikati natokea soko la Kariakoo tayari nipo nyumbani nimefika hivyo ahsante kwa wema wako, labda siku ingine" ghafla aligeuka nyuma Deborah na kuanza kujieleza kwa kujiamini huku akiwa amemtumbulia macho bila uoga. Deborah aliyakumbuka maneno ya wosia ya mfadhili wake Koplo Marieta ya kuwa, Jiji la Dar es Salaam watu wenye utu ni wachache sana wengi ni mbwa kasoro mkia waliovaa sura za kibinadamu, kutokana na tabia.
Hivyo hakuwa tayari kuambatana na mtu asiyemfahamu kwa kinagaubaga. Walikuwa tayari wawili hao wameshalifikia gari la yule jamaa aina ya 'Toyota Hilux Double Cabin' yenye vioo vya giza aliyokuwa ameiegesha meta chache pembeni ya kioski. "Haya nimekuelewa, hamna noma siku ingine nitakupa lifti utakapopenda wewe, chukua basi hii zawadi yako, uchangamshe kinywa......!" alijibu yule jamaa huku akitoa pipi mbili mfukoni, moja akinyoosha mkono kumpa Deborah na ingine akaifungua haraka haraka na kuitumbukiza kinywaji akianza kuimung'unya mbele ya Deborah. "Ahsante sana,ubarikiwe..!" alijibu Deborah huku akiipokea na kuanza kuimung'unya pipi ile mbele ya yule mgeni. Aliona bora amridhishe mgeni huyo asije kumuona ana madahiro kwa wateja.
Uso wa yule jamaa mwanzoni alipokataliwa lifti uliliwa debe, lakini Deborah alipoanza tu kuimung'unya pipi ile, akaunda tabasamu la ushindi lenye kufu ya furaha. Deborah ghafla akakimbilia tena kwenye Kioski kama mtu aliyegutushwa na kitu cha kuogofya. Mwenzake wa kioski alikuwa nae anajiandaa kufunga anaingiza viti ndani ya kibanda, tayari kwa kurejea sehemu anayoishi. Deborah alipomfikia yule mwenzake akawa anamuongelesha mambo mawili matatu, kama maagizo na maelekezo fulani aliyokuwa amesahau kumpa mwenzake wakati wakaagana. Yule mtu alikuwa ameegemea mlango wa mbele ya siti ya abiria kama vile bado anamsubiria Deborah.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment