Simulizi : Laiti Ningejua
Sehemu Ya Pili (2)
Kwa kweli nilikata tamaa sana hasa kwa kuchukulia kuwa nilikuwa tayari nimepoteza muda wangu mwingi eneo lile, na hasa nilipoanza kuwaza kuwa kutokana na hali ile nisingeweza tena kupata nafasi ya kuwahi dili la pesa jijini Dar es Salaam.
Baada ya taarifa zile nilianza kuhisi njaa ikiniuma na tumbo langu likisokota, hivyo nilichowaza muda ule ilikuwa ni kutafuta kwanza mgahawa wowote uliokuwa jirani na eneo lile ili nipate kwanza mlo wa nguvu baada ya hapo ningepanga nini cha kufanya.
Nilitoa simu yangu na kutafuta namba ya Yeriko Kyando, jamaa yangu ambaye tulikuwa tumebaliana kukutana jioni ya siku ile kwenye ofisi yangu iliyokuwa eneo la Buguruni Rozana.
Nilipoipa ile namba nikapiga lakini namba ilikuwa haipatikani, nikataka kupiga tena lakini nikakumbuka kuwa siku mbili zilizokuwa zimetangulia Yeriko aliniambia kuwa simu yake ilikuwa na tatizo la betri, kwani ilikuwa haikai na chaji muda mrefu. Nikaishiwa kabisa nguvu.
Hali ile ikanifanya nipate wazo la kuwasiliana na jirani yangu Jonas Odilo, ambaye tulikuwa tukiishi nyumba moja eneo lile lile la Buguruni Rozana. Lengo langu lilikuwa ni kutaka kumweleza kuhusu hali halisi ya usafiri na kwamba alipaswa kumtafuta Yeriko ili amweleze kuwa nilikuwa nimekwama Kibiti, na kwamba uwezekano wa kuondoka hapo sikuuona.
Hivyo nikaitafuta namba ya Jonas kwenye orodha ya namba nilizokuwa nimehifadhi katika simu yangu ya mkononi, nikaipata na kupiga na mara simu ikaanza kuita, sekunde chache baadaye Jonas alikuwa amepokea simu nami nikamweleza lakini akaniambia kuwa hata yeye hakuwa Dar es Salaam muda ule, alikuwa amekwenda Kibaha kwenye shughuli zake.
Nilipokata simu nilimsogelea mtu mmoja aliyeonekana kuwa mwenyeji wa eneo lile na kumuuliza kama ningeweza kupata chakula kizuri, bila kusita akanionesha mgahawa mmoja uliokuwa unaitwa la ‘Victoria’, ambao ulikuwa jirani na kituo kimoja cha kujazia mafuta cha Gapco, pale Kibiti.
Nilianza safari ya kuelekea katika ule mgahawa wa Victoria ambao haukuwa mbali sana na eneo lile nililokuwa nimesimama, nilipofika nilitafuta sehemu nzuri nikaketi, na mara mhudumu mmoja mcheshi akanifuata huku akiachia tabasamu bashasha la makaribisho.
Nilimwagiza aniletee ugali wa dona, kuku wa kienyeji na maziwa mtindi, kisha nikaanza kufikiri namna ya kujinasua kutoka katika janga lile la kukosa usafiri.
Nilifikiria sana ni jinsi gani ningeweza kuondoka pale Kibiti pasipo kupata jibu, mara nikakumbuka kuwa sikuwa nimechukua namba ya Adnan, ningemweleza pengine angekubali kuniazima gari moja, maana niliamini kuwa walikuwa na magari mengi, ili niende Dar es Salaam halafu ningeangalia namna ya kumletea siku nyingine.
Hata hivyo, kwa muda ule nisingeweza tena kumpata, maana wala sikujua aliishi sehemu gani pale Kibiti. Mara likanijia wazo jingine kuwa ni bora nichukue bodaboda lakini nimweleze dereva wa bodaboda kuwa ajitahidi kuendesha kwa makini bila papara.
Hata hivyo nikawaza kuhusu gharama za bodaboda kuitoa Kibiti hadi Dar es Salaam ingekuwa ghali sana. “Kwa kweli sina ujanja, sijui nifanyeje…”
“Karibu chakula, kaka,” sauti ya yule mhudumu aliyeniletea chakula ilinizindua kutoka kwenye mawazo yangu. Nilimtazama kisha nikaachia tabasamu la shukurani huku nikinawa mikono yangu.
Kisha nikawa napata mlo wangu taratibu huku kichwani nikiendelea kufikiria juu ya safari yangu ya kurudi jijini Dar es Salaam, ki ukweli nilidhamiria kuondoka pale Kibiti kwa namna yoyote ile, ije mvua au lile jua.
Nilipomaliza kula kile chakula, ambacho kiukweli kilikuwa kitamu sana, nilipumzika kidogo kisha nikaagiza chupa kubwa ya lita moja na nusu ya maji baridi na kuanza kunywa taratibu huku nikiendelea kuwaza jinsi ambavyo ilikuwa muhimu kwangu kufika jijini Dar es Salaam siku hiyo.
Hata hivyo, katika mawazo yangu nilijikuta napata wakati mgumu sana kiasi cha kuingia katika hali ambayo wataalamu huiita ‘interpersonal conflict’, yaani nilikuwa napanga na kupangua katika mawazo yangu pasipo kufikia muafaka.
Nilikuja kushtuka baada ya kuangalia saa yangu na kugundua kuwa ilikuwa imeshatimia saa kumi na moja ya jioni nikiwa bado nimeketi pale pale kwenye mgahawa, hivyo nikaanza kuhisi kuwa nilikuwa nimetumia muda mwingi kukaa ndani ya mgahawa ule nikibishana mwenyewe ndani ya nafsi yangu pasipo kufikia mwafaka.
Nilianza kujishtukia kwani nilidhani kuwa wahudumu wa ule mgahawa walikuwa wakinishangaa kuona kuwa watu walikuja wakahudumiwa na kuondoka zao lakini mimi niliendelea kukaa pale pale nikionekana kuwaza mbali.
Sikuwa na uhakika kama walinishuhudia wakati mwingine nikionekana kuongea peke yangu, maana hali hiyo humpata mtu anapokuwa katika ‘interpersonal conflict’.
Nilimuita yule mhudumu wa ule mgahawa aliyenihudumia nikamlipa pesa ya ule mlo niliokula. Niliporudishiwa chenji yangu nikachukua begi langu na kutoka nje ya ule mgahawa kisha nikaanza kujivuta taratibu kurudi katika eneo la stendi ya mabasi huku wale wahudumu wakinitazama kwa makini.
Nilipofika pale stendi nilipowaacha wengine nikaangaza macho yangu huku na kule na haraka nikagundua kuwa wale abiria wengi waliokuwa eneo lile wakisubiri usafiri hawakuwepo tena ila wapiga debe wachache waliokuwa eneo lile wakizunguka zunguka.
Hali ile ikanifanya niingiwe na wasiwasi zaidi kuwa huenda usafiri wa dharura ulikuwa umepatikana wakati mimi nilipokuwa nimekaa ndani ya ule mgahawa nikiwa natafakari.
Nilimfuata kijana mmoja ambaye mwanzoni nilimkuta akipiga debe katika ile stendi nikamuuliza kama kulikuwa na usafiri wowote ulioondoka kuelekea jijini Dar es Salaam katika kipindi kile ambacho mimi sikuwepo pale stendi.
Yule mpiga debe aliniambia kuwa hapakuwa na basi lolote, achilia mbali gari binafsi lililosafirisha abiria kutoka pale kuelekea sehemu yoyote, na akanifafanulia kwa kina kuhusu agizo lililotolewa na viongozi wa madereva wa magari ya abiria nchini Tanzania kuwa usafiri ulikuwa umesitishwa kabisa kwa safari zote nchini.
Wakati yule mpiga debe akinieleza hivyo nikawa nayatembeza macho yangu taratibu kulikagua eneo lile huku nikiziangalia nyuso za watu waliokuwa bado wamesimama pale.
Katika uchunguzi wangu dhidi ya watu wachache waliokuwa eneo lile mara nikajikuta macho yangu yakivutiwa kumwangalia msichana mmoja aliyekuwa amesimama peke yake mbali kidogo na eneo lile akiwa ameshika kiuno.
Nilipomtazama kwa makini yule msichana nilimuona ni kama na yeye alikuwa amekatishwa tamaa sana na tamko lile la kusitishwa kwa usafiri wa kuelekea jijini Dar es Salaam. Nikajaribu kuyasoma mawazo yake lakini sikuweza kufahamu mara moja alikuwa akiwaza nini muda ule.
Alikuwa msichana mrefu na mweupe wa asili, si ule weupe wa mkorogo bali ule wa asili wenye ung’avu wa kuteleza. Umri wake ulikuwa hauzidi miaka 25, alikuwa mwembamba lakini akiwa na umbile lililovutia mno na mwenye haiba nzuri ya kuvutia.
Kwa yeyote awaye mwanaume rijali hapana shaka kama angemuona msichana yule asingeacha kukiri kuwa alikuwa ni moto wa kuotea mbali, kwani kwa mlingano wa macho tu, msichana yule alitoa tafsiri ya kuwa na ule uzuri usiomithilika ambao ungeweza kumliwaza, kumpumbaza na hata kumlaza kitandani mtu yeyote aliye buheri wa afya.
Kutokana na jinsi alivyokuwa mtu yeyote asingesita kusema kuwa huenda alikuwa mmoja kati ya wasichana wachache sana ambao huenda walikusudiwa kuumba malaika, ila wakashushwa duniani kimakosa. Hawa ndio wale ambao huitwa nusu malaika!
Alikuwa amevaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu bahari iliyokuwa inambana na ilikuwa na matobo matobo mbele katika maeneo ya mapaja yake na kuifanya miguu mizuri iliyotazamika kuonekana vizuri.
Juu alikuwa amevaa fulana nzito ya rangi la samawati iliyoyafanya matiti yake yenye ukubwa wa wastani yaliyochongoka mbele na yaliyoonekana kuwa na hasira ya kutoboa fulani hiyo yaonekanae vizuri, na juu ya fulani hiyo alikuwa amevaa shati zito la rangi ya bluu la kitambaa cha kadeti.
Miguuni alikuwa amevaa buti ngumu za kike zilizokuwa zimemtoa bomba zaidi na kumfanya apendeze sana kwa mapigo ya msichana wa kileo. Mgongoni alikuwa amebeba begi dogo na mkononi alikuwa ameshika pochi nzuri nyeusi ya kike.
Kwa mwonekano wa haraka tu niliweza kutambua kuwa wazazi wake walikuwa ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha, maana mavazi yake yalikuwa ya gharama kubwa ingawa kwa mtazamo wa haraka ungeweza kudhani ni ya kawaida.
Pia niliweza kung’amua kuwa alikuwa amevaa vito vya thamani kama vile dhahabu na kadhalika ingawa alikuwa amevificha ndani ya fulani na shati lake. Vitu vyote hivyo kwa pamoja na asili ya urembo wake vilimtoa katika sura ya mrembo matata aliyekuwa amekolea sana!
“Oh my God, she’s so pretty! She’s such an angel” niliwaza huku nikimtazama kwa makini yule msichana.
Kwa nukta chache nilihisi kama moyo wangu ulisahahu mapigo yake, na mara yalipoanza nilijikuta nikivuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani, kisha nikazishusha taratibu.
Sikujua kwa nini nilipatwa na mshtuko kiasi kile baada ya kumuona yule msichana, lakini nilichokifahamu kwa wakati ule ni kitu kimoja tu, kwamba nilivutiwa sana kumtazama msichana yule, huku nikiwa na uhakika kabisa kuwa alikuwa hafahamu chochote kuwa nilikuwa nikimtazama kwa kificho. Hali ile ikanifanya niendelee na udadisi wangu.
Mara nikamuona yule msichana akiinua mkono wake kutazama saa yake ya mkononi kisha akakunja sura yake akionekana kushtuka sana.
Nilipoichunguza vizuri, japo alikuwa amesimama mbali kidogo nami, niligundua kuwa ilikuwa ni saa ghali sana ya kike aina ya Swatch Skinmesh, ambayo bei yake ilikuwa si haba, kwani haikuwa chini ya Pauni elfu tisini za Uingereza.
Kisha nikamuona akifungua pochi yake na kutoa simu yake ya mkononi kutoka kwenye ile pochi kisha akaanza kutafuta namba fulani ili apige, mara nikajikuta nikianza kupiga hatua kumfuata pale alipokuwa amesimama.
Wakati naanza kumfuata nikamuona akisogea kando zaidi na kwendaa kuketi ameketi kwenye kibanda kimoja kilichokuwa eneo lile, kisha akawa anangea na simu huku akionekana kukata tamaa. Nilihisi kuwa maelezo ya wale wapiga debe pale stendi yalimfanya aondoe kabisa matumaini ya kupata usafiri.
Hatimaye miguu yangu ikawa myepesi ghafla na hivyo kujikuta nikipiga hatua zangu za haraka kumsogelea huku uso wangu ukianza kutengeneza tabasamu la kirafiki. Msichana yule akawahi kugeuka na kunitazama wakati nilipokuwa nikimkaribia na hapo nikamsalimia kwa kumpungia mkono huku uso wangu ukitengeneza tabasamu la kirafiki.
Msichana yule alinitazama kwa mshangao kidogo kuanzia chini hadi juu kana kwamba alikuwa akijaribu kukumbuka kama aliwahi kuniona mahala. Hata hivyo hakunijibu, bali alisogea mbali zaidi na mimi huku akiendelea kuongea na simu kwa muda mrefu sana akionekana kulalamika, na mara kadhaa aligeuza shingo yake kunitupia jicho la wizi.
Wakati akiendelea na maongezi yake kwenye simu nikagundua kuwa idadi ya watu waliotarajia kusafiri ilikuwa ikiendelea kupungua taratibu pale kwenye ile stendi ya mabasi ya Kibiti huku dalili za kusafiri zikizidi kufifia.
Hivyo, akili yangu ikaanza kuchangamka nikianza kufikiria njia mbadala ya kunifikisha jijini Dar es Salaam. Nikiwa katika hali ile mara nikamuona yule msichana akiinuka pale alipokuwa ameketi na kumfuata kijana mmoja aliyekuwa amesimama kando ya eneo lile akiangaza macho yake huku na kule kama aliyekuwa akisikilizia jambo.
Nilimuona yule msichana akizungumza na yule kijana na baada muda mfupi wa maongezi yao nikamuona yule kijana akigeuka kututazama mimi na watu wengine wawili watatu tuliokuwepo katika eneo lile kisha akatuonesha ishara ya kuuliza kama tulikuwa tayari kusafiri kwenda jijini Dar es Salaam.
Nilijisogeza haraka pale walipokuwa wamesimama na kupitia maongezi yao nikaelewa kuwa kulikuwa kumepatikana usafiri wa mtu binafsi wa kuelekea jijini Dar es Saalaam.
Hivyo yule kijana alikuwa ni mhusika mmojawapo wa gari lile ambalo kwa mujibu wa maelezo yake ni kuwa gari hilo lilikuwa limeegeshwa nyuma ya kituo cha kujazia mafuta kilichokuwa jirani na eneo lile cha Gapco.
Alituambia kuwa walikuwa wameliegesha gari lao kule nyuma ya kituo cha kujazia mafuta cha Gapco kwa kuhofia kufanyiwa fujo na madereva wa magari ya abiria endapo wangeliegesha gari lile pale stendi na kutafuta abiria.
Sikuwa na wasiwasi wowote na yule kijana kwani katika hali na mazingira kama yale usafiri wa magendo wa namna ile ulikuwa ni jambo la kawaida kufanyika katika stendi yoyote ile, hususan pale inapotokea shida ya usafiri.
Nikamuuliza yule kijana kuwa nauli ingekuwa shilingi ngapi kutoka Ikwiriri hadi Dar es Salaam na hapo akanieleza kuwa alikuwa akitoza shilingi elfu kumi na mbili kwa kila abiria mmoja.
Sikuona kwa nini nijivunge, hata kama ingekuwa shilingi elfu therathini ningesafiri tu, niligeuka kuwatazama wale wengine, hususan yule msichana nikitaka kufahamu wao walikuwa wakilichukuliaje suala lile.
Wote walionekana wako tayari kusafiri kwa gharama yoyote, ingawa mmoja alianza kulalamika kuwa nauli ilikuwa juu kidogo.
Tuliongozana na yule kijana hadi kule nyuma ya kile kituo cha kujazia mafuta cha Gapco ambako walikuwa wameliegesha gari lao.
Wakati tukitembea kuelekea kule nyuma ya kile kituo cha kujazia mafuta mara kwa mara yule msichana alikuwa akinitazama katika namna ambayo sikuweza kuielewa. Baada ya mwendo mfupi wa safari yetu hatimaye tukawa tumekifikia kituo kile cha kujazia mafuta cha Gapco cha Kibiti.
Tulipolikaribia vizuri eneo lile mara nikaliona gari moja aina ya Toyota Land Cruiser Prado lenye muundo wa kizamani la rangi ya samawati likiwa limeegeshwa kando ya kituo kile cha kujazia mafuta. Lile gari ingawa lilikuwa la muundo wa kizamani lakini lilionekana kuwa bado imara na lenye uwezo mzuri wa kumudu safari.
Mle ndani tulikuta kuna watu watano. Mbele kulikuwa na dereva wa lile gari, mwanaume wa makamo aliyekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka arobaini hadi arobaini na tano, alikuwa mrefu na mweupe.
Macho ya yule dereva yalikuwa makali na alikuwa amevaa baragashia nyeupe ya kufumwa. Alikuwa ameketi nyuma ya usukani kwenye ile siti ya dereva akionekana kuendelea kusubiri abiria na siti ya abiria upande wa kushoto wa dereva ilikuwa tupu.
Ile sehemu ya siti za abiria ya katikati nyuma ya dereva kulikuwa tayari kuna watu wanne, wote vijana ambao kwa mtazamo wa haraka tu hawakuzidi miaka therathini. Kati yao mmoja alikuwa ni mwanadada mfupi mnene.
Niliwasalimia wale watu waliokuwa mle ndani ya lile gari kiungwana na wote wakaitikia kwa pamoja. Yule kijana aliyetuleta aalitufungulia mlango wa nyuma ambako ndiko kulikokuwa na siti tupu.
Mimi sikujali, badala yake nilijitoma ndani ya lile gari na kuketi kwenye siti za nyuma za kutazamana. Wale abiria wengine pia wakapanda na hivyo kukawa na nafasi moja tu iliyokuwa imebakia.
Yule msichana alifungua ule mlango wa mbele kwenye siti ya abiria upande wa kushoto wa dereva lakini yule kijana aliyetuleta alimtaka akae nyuma kwa kuwa siti ile ilikuwa tayari ina mwenyewe.
Yule msichana alisimama pale akionekana kukata tamaa huku akiwa hataki kukaa kule nyuma, aliminya midomo yake huku akishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani. Yule kijana akasikika akimweleza kuwa hakuna usafiri mwingine, hivyo kama angebaki ingekuwa ni shauri lake mwenyewe.
Nilimuona yule msichana akinyanyua mabega yake juu na kubetua midomo yake huku akionekana kubadili msimamo wake pale alipoona hakuna namna nyingine ya kusafiri.
Alikuja kule nyuma ya lile gari na kuingia kisha akaketi mbele yangu upande wa pili kwenye siti iliyokuwa mkabala na mimi, na kutokana na muundo wa siti za lile gari mtindo ule wa ukaaji ukatufanya tujikute tukitazamana.
Muda ule ule nikamuona mwanamume mmoja wa makamo aliyekuwa amevaa suti maridadi akija haraka eneo lile akitokea kwenye ule mgahawa wa Victoria huku akiwa amebeba brifukesi yake nzuri ya gharama katika mkono wake wa kulia na mkono wake wa kushoto alikuwa ameshika chupa kubwa ya lita moja na nusu ya maji safi.
Alipofika kwenye lile gari alishika kitasa cha mlango ule wa mbele wa ile gari, akavuta na kufungua kisha aliingia na kuketi kwenye ile siti ya abiria upande wa kushoto wa dereva. Muda ule ule nikaliona gari moja aina ya Toyota Land Cruiser Pick-up likipita pale na kusimama kwenye kile kituo cha kujazia mafuta.
Ndani ya lile gari kulikuwa na wanaume watatu, dereva na mtu mmoja walikuwa wameketi mbele na mtu mwingine alikuwa amesimama kule nyuma ya lile gari. Wote walikuwa warefu na wenye miili imara iliyojengeka. Nilijikuta nikivutiwa sana kuwaangalia wale watu ingawa sikujua kwa nini nilijikuta nikivutiwa sana kuwaangalia.
Muda ule ule nikamuona mwanamume mmoja wa makamo aliyekuwa amevaa suti maridadi akija haraka eneo lile akitokea kwenye ule mgahawa wa Victoria huku akiwa amebeba brifukesi yake nzuri ya gharama katika mkono wake wa kulia na mkono wake wa kushoto alikuwa ameshika chupa kubwa ya lita moja na nusu ya maji safi.
Alipofika kwenye lile gari alishika kitasa cha mlango ule wa mbele wa ile gari, akavuta na kufungua kisha aliingia na kuketi kwenye ile siti ya abiria upande wa kushoto wa dereva. Muda ule ule nikaliona gari moja aina ya Toyota Land Cruiser Pick-up likipita pale na kusimama kwenye kile kituo cha kujazia mafuta.
Ndani ya lile gari kulikuwa na wanaume watatu, dereva na mtu mmoja walikuwa wameketi mbele na mtu mwingine alikuwa amesimama kule nyuma ya lile gari. Wote walikuwa warefu na wenye miili imara iliyojengeka. Nilijikuta nikivutiwa sana kuwaangalia wale watu ingawa sikujua kwa nini nilijikuta nikivutiwa sana kuwaangalia.
Endelea...
Mara nikamuona yule mtu aliyekuwa amesimama kule nyuma ya lile gari akishuka kisha akatazama huku na kule na kuharakisha kuvuka barabara na kuja moja kwa moja upande tuliokuwepo.
Wakati akivuka kuja upande tuliokuwepo nikawaona wanaume wawili wakitoka ndani ya ule mgahawa wa Victoria na kupanda kwenye lile Toyota Land Cruiser Pick-up lililomshusha yule mtu, na hapo lile gari likaanza kuondoka na kuingia barabara iliyoelekea Dar es Salaam.
Muda ule ule yule kijana aliyekuwa ametuleta pale kwenye lile gari akazunguka kwenda kwenye mlango wa dereva, nikamuona yule dereva akijipapasa mifukoni, na kama aliyegutuka akatugeukia, lakini kabla hajasema chochote yule jamaa aliyeshuka kwenye lile gari Toyota Land Cruiser Pick-up akasogea mlangoni kwa dereva.
Alipokuwa pale nikashtushwa sana na macho yake makubwa yaliyoonesha uchovu lakini yalikuwa ni aina fulani ya yale macho yaliyoashiria shari. Alikuwa na uso mrefu uliokuwa umetulia na ijapokuwa alikuwa amevaa kofia aina ya kapelo na miwani midogo myeusi ya jua aliyokuwa ameipandisha juu ya uso wake.
Aliposimama pale mlangoni kwa dereva akawa anachungulia mle ndani kiaina akionekana kama aliyekuwa anamtafuta mtu fulani ndani ya lile gari tulilopanda, kwani alipochungulia alikuwa akitutazama usoni kiaina. Dereva akamtazama kwa makini.
“Vipi kuna mtu unamtafuta?” dereva wa lile gari alimuuliza yule jamaa.
“Hapana, nilitaka kujua kama mnaelekea Dar,” yule mtu alimwambia yule dereva huku akiendelea kututupia jicho la wizi.
“Ndiyo, tunaelekea Dar lakini tayari gari limeshapendeza, si unaona mwenyewe,” yule dereva alimwambia yule mtu huku akiendelea kumtazama kwa macho ya udadisi.
Yule jamaa alishusha pumzi na kulizunguka akiendelea kutuangalia kwa makini, kisha akaondoka zake. Muda wote nilikuwa namtazama kwa makini na sura yake ikanitia mashaka.
Sikujua kwa nini nilikumbwa na hisia mbaya juu yake, hata hivyo, niliamua kuzipuuza hisia zangu na kuanza kuifikiria safari yangu ya kurudi Dar es Salaam.
Mara yule dereva wa lile gari tulilopanda akageuka tena nyuma na kuanza kudai nauli, alitutazama kwa utulivu huku akitengeneza tabasamu jepesi usoni mwake.
Bila kupoteza muda kila mmoja alitoa fedha na kumpa, nami bila kuchelewa nikachukua pochi yangu kutoka mfukoni na nilipoifungua nikahesabu noti zenye thamani ya nauli iliyohitajika na kumpa yule dereva kama malipo ya nauli yangu.
Yule dereva alizipokea zile fedha na kuanza kuzihesabu taratibu huku ukimya ndani ya lile gari ukitawala. Kisha alichukua noti kadhaa kutoka kwenye zile fedha na kumpa yule kijana aliyetuleta. Kisha akawasha gari tayari kwa safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam, niliitazama saa yangu nikagundua kuwa ilikuwa imeshatimu saa kumi na mbili jioni.
Yule dereva aliliondoa lile gari kwa mbwembwe huku akiwa makini kutazama barabarani na kuingia kwenye barabara ya Dar es Salaam na mbele kidogo tukalipita lile gari aina ya Toyota Land Cruiser Pick-up likiwa limeegeshwa kando ya barabara huku nyuma yake kukiwa na alama ya pembe tatu (triangle) kama ishara ya kutambulisha kuwa gari lile lilikuwa limepata hitilafu.
Nje ya lile gari kulikuwa na wale wanaume wawili, dereva wa lile gari na mtu mmoja aliyekuwa amekaa mbele walioonekana wameinamia kwenye boneti la gari lililokuwa limefunguliwa wakiwa wanalitengeneza. Nikaangalia huku na kule lakini sikuweza kuwaona wale wanaume wengine wawili waliopandia pale kwenye kituo cha kujazia mafuta cha Gapco.
Tulipowapita nikawaona wakiinua sura zao na kugeuka kulitazama gari letu kwa makini sana kana kwamba kuna kitu kilikuwa kinawashangaza.
Tuliendelea na safari yetu huku dereva akiwa makini zaidi kutazama barabarani. Miale hafifu ya jua la machweo ilikuwa mbioni kutoweka angani na kiza kilikuwa mbioni kuchukua nafasi yake. Dereva aliendesha kwa kasi akiifuata barabara ile iliyoelekea Dar es Salaam huku taratibu tukianza kuuacha mji wa Kibiti nyuma yetu.
Nilikuwa nimezama katikati ya tafakuri nzito nikifikiria jinsi nilivyoweza kukosa dili la pesa kizembe, lakini sikukata tamaa, niliamua kutoa simu yangu na kumpigia tena simu Yeriko, nilitafuta namba ya Yeriko kisha nikapiga. Mara ikaanza kuita na haukuchukua muda ile simu ikapokelewa.
“Hello!” niliisikia sauti ya Yeriko upande wa pili wa simu iliyonipa nguvu.
Haraka sana niliumjulisha kilichokuwa kimenisibu mara baada ya kusalimiana. Yeriko alinifahamisha kuwa nisiwe na wasiwasi kwani hata yeye alikuwa amepata udhuru, hivyo dili letu lilikuwa bado lipo pale pale na tungeweza kukutana kesho yake, ila alinitaka niwasiliane naye mara tu nikifika jijini Dar es Salaam.
Muda mfupi baadaye tukawa tumeuacha kabisa mji wa Kibiti nyuma yetu na muda ule sauti pekee iliyokuwa ikisikika mle ndani ya gari ilikuwa ni sauti ya muungurumo wa injini ya lile gari.
Lile gari lilikuwa likienda mwendo wa kasi ingawa yule dereva alionekana kuwa makini sana huku akionekana pia kuizoea vizuri ile barabara, na wakati safari ikiwa inaendelea nikaanza kumchunguza yule msichana mrembo nikitafuta namna ya kumzoea.
Nilimuona akiwa ameelemewa sana na usingizi, nadhani kwa sababu ya uchovu, na muda huo giza lilikuwa limeanza kutanda angani, hata hivyo, dereva wa lile gari aliwasha taa kubwa za mbele na mwanga mkali wa taa zile ulijitahidi kulifukuza giza lile lililokuwa limetanda mbele yetu huku tukizidi kutokomea mbele zaidi.
Hakuna aliyekuwa akiongea muda huo na hivyo mle ndani ya gari kulitawaliwa na kiasi kikubwa cha ukimya wa namna yake. Nilimtazama yule msichana mrembo, sikuona tashwishwi yoyote katika sura yake kama ilivyokuwa kwa abiria wengine ndani ya lile gari, na kila mmoja alionekana kuchoka sana.
Uso wa yule mrembo ulikuwa umepoteza kabisa nuru na utulivu, kwa namna nyingine nilimuona akiitupia jicho saa yake ya mkononi mara kwa mara na kusonya na mara akaonekana kuzama kwenye fikra fulani.
Mwendo wetu ulikuwa siyo wa kubabaisha tukikatiza katikati ya pori na baada ya mwendo mfupi wa safari yetu mbele kidogo tukawaona watu kadhaa waliokuwa wakilisimamisha gari letu, hata hivyo dereva hakusimama na muda mfupi baadaye tukayavuka majengo ya Shule ya Sekondari ya Kibiti yaliyokuwa upande wetu wa kushoto.
Tuliendelea kukatisha katikati ya msitu mnene wenye giza zito huku manyunyu ya mvua yakianza kudondoka hali iliyofanya barabara ile izidi kutisha wakati ule wa usiku.
Tulipishana na magari mawili matatu wakati tukiipita barabara ya kuelekea Nyamisati, muda wote dereva alikuwa yuko makini sana huku akiendesha kwa mwendo kasi lakini wenye tahadhari za aina zote.
Kisha tukaanza kukatisha katikati ya makazi ya watu tukiuvuka mji mdogo wa Bungu ambao kwa wakati ule wa usiku nyumba za makazi ya watu zilionekana kama vichaka kwani wakazi wake wengi walikuwa wamekwisha ingia majumbani.
Safari iliendelea na ilionekana kuwa ndefu lakini yule dereva wetu alikuwa makini mno akiendelea kuendesha kwa mwendo kasi na hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake muda wote wa safari yetu.
Tuliendelea kukatisha katikati ya msitu mnene wenye giza zito huku manyunyu ya mvua yakianza kudondoka hali iliyofanya barabara ile izidi kutisha wakati ule wa usiku.
Tulipishana na magari mawili matatu wakati tukiipita barabara ya kuelekea Nyamisati, muda wote dereva alikuwa yuko makini sana huku akiendesha kwa mwendo kasi lakini wenye tahadhari za aina zote.
Kisha tukaanza kukatisha katikati ya makazi ya watu tukiuvuka mji mdogo wa Bungu ambao kwa wakati ule wa usiku nyumba za makazi ya watu zilionekana kama vichaka kwani wakazi wake wengi walikuwa wamekwisha ingia majumbani.
Safari iliendelea na ilionekana kuwa ndefu lakini yule dereva wetu alikuwa makini mno akiendelea kuendesha kwa mwendo kasi na hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake muda wote wa safari yetu.
Endelea...
Huku tukizidi kuvuka msitu mnene, vichaka na kona mbalimbali za ile barabara ya Dar es Salaam, niliwatazama tena wale abiria wenzangu ndani ya gari na kuwaona wote wakiwa hoi kwa usingizi kutokana na uchovu wa kutwa nzima.
Ni mimi na dereva tu wa lile gari ambao hatukuwa tumesinzia, na katika ukimya ule, nilijikuta nikianza kuwaza namna ambavyo ningeweza kupanua ofisi yangu ya Buguruni au hata kufungua kampuni nyingine kubwa ya ushauri wa masuala ya kibiashara na masoko na kuwaajiri vijana mbalimbali wenye utaalamu wa biashara na masoko kama wangu.
Kwa takriban mwaka sasa nilikuwa nakwenda kutoa mada katika ofisi mbalimbali jijini Dar es Salaam na maeneo ya jirani, nikiwa kama mtaalamu wa masuala ya kibiashara na masoko kwa watu waliopenda kuwezeshwa mawazo kazini kwao, zikiwemo kampuni mbalimbali zilizohitaji kuwapa wafanyakazi wao semina ya biashara lakini walikuwa na tatizo la muda.
Ni Yeriko ndiye aliyenishauri kufikiria namna nyingine ambayo ingeweza kuniingizia fedha nyingi kutokana na taaluma yangu ya biashara na masoko, kwani nimewahi kushuhudia baadhi ya wajasiriamali wakubwa walioendelea na kuingiza fedha nyingi kwa kuzungumza tu, tena kwa hesabu za dakika.
Mwanzoni nilipoanza kutoa mada nilikuwa nikitoza fedha kidogo, lakini namna nilivyotoa huduma yangu, ilinitangaza kwa kiwango kikubwa na kuniwezesha kupata watu wengi zaidi. Taratibu nilianza kufanikiwa na niliamini kuwa hatimaye ningekuwa mmoja wa watoa mada maarufu nchini na Afrika Mashariki.
Wakati nikiendelea kuwaza, nilianza kuzidiwa kwa mawazo na uchovu wa kutwa nzima, niliinamisha kichwa changu, na hapo nikaanza kusinzia lakini nilishtuka baada ya hisia mbaya kunijia akilini na hapo haraka nikainua kichwa changu na kuyapeleka macho yangu kuangalia nyuma tulikokuwa tunatoka.
Mara nikaiona miale mirefu ya mwanga mkali wa taa za gari moja lililokuwa linakuja nyuma yetu kwa mwendo wa kasi zaidi. Macho yangu yalivutiwa kulitazama lile gari namna lilivyokuwa likija kwa kasi na kutukaribia nyuma yetu, huku akili yangu ikianza kutafakari juu ya gari lile kwa jinsi lilivyokuwa likizidi kutusogelea.
Baada ya muda mfupi hatimaye lile gari likawa limetufikia na sasa lilikuwa nyuma yetu, takriban mita ishirini hivi kutoka lilipokuwa gari letu. Mara likaanza kutupita kwa kasi ya ajabu.
Tukio lile likamfanya dereva wetu apunguze mwendo wa gari na kuliruhusu lile gari lipite kwa uhuru na kuendelea na safari yake. Wakati likitupita nikapata wasaa mzuri wa kulichunguza na hapo nikagundua kuwa lilikuwa ni lile gari Toyota Land Cruiser Pick-up tulilolipita kando ya barabara pale Kibiti likiwa limeharibika.
Hisia mbaya zaidi zikanijia na kunifanya nianze kuswali kimoyomoyo nikimuomba mola atuepushe na balaa lolote, japo sikuwa mtu wa kwenda msikitini. Mara tu baada ya lile gari Toyota Land Cruiser Pick-up kutupita, nikaliona likipunguza mwendo ghafla na kwenda kutuzuia kwa mbele.
Kitendo kile cha lile gari Toyota Land Cruiser Pick-up lililotupita kupunguza mwendo ghafla mbele yetu huku likituzuia kikamfanya dereva wa gari letu kukanyaga breki za ghafla huku akijitahidi kwa kila namna kulikwepa lile gari huku ufundi wake katika udereva ukionekana kugonga mwamba.
Kutokana na mwendo wake alionekana kushindwa kuhimili na hivyo gari letu liliyumba na kuserereka huku magurudumu yakilalamika kwenye ile barabara ya lami.
Hata hivyo, alikuwa amekwisha chelewa, akaligonga lile gari kwa nyuma na kusababisha taa za mbele za gari letu kuvunjwa vibaya na ngao ngumu ya nyuma ya lile Toyota Land Cruiser Pick-up lililokuwa limesimama mbele yetu.
Muda ule ule nikawaona watu watatu waliokuwa nyuma ya lile gari Toyota Land Cruiser Pick-up wakiruka kutoka kwenye gari huku wakiwa wameshika vyema bunduki zao aina ya Sub Machine Gun na kuzielekeza upande ule tuliokuwepo.
Sasa nilikuwa na uhakika kabisa kuwa zile hisia mbaya zilizokuwa zikinijia kabla zilikuwa sahihi, na tukio lile likanidhihirishia kuwa hatukuwa salama, kwani tulikuwa tukielekea kukabiliana na utekaji kutoka kwa wale watu, na wakati nikitafakari kuhusu jambo hilo nilijikuta nikishikwa na hofu kubwa na taharuki isiyoelezeka.
Sikuwa na shaka na wala sikuhitaji mtu yeyote kunieleza kuwa mambo hayakuwa shwari tena, hivyo nilipaswa kufanya maamuzi ya haraka kabla sijashuhudia jambo baya likitokea mbele ya macho yangu, ambalo lingeacha taswira isiyoelezeka ndani ya akili yangu.
Kabla sijajua nifanye nini nikamuona dereva wa gari letu aliyekuwa amepagawa baada ya kuhisi jambo baya lilikuwa mbioni kutokea, akifanya jambo lisilotarajiwa, kwani aliingiza gia ya kurudi nyuma na hapo hapo kukanyaga pedeli ya mafuta na kulifanya gari letu lianze kurudi nyuma kwa mwendo wa kasi ya ajabu.
Sasa gari letu lilikuwa linarudi nyuma kwa kasi ya ajabu, hata hivyo, hatukuweza kwenda umbali mrefu zaidi kwani muda ule ule sote tulishtushwa na mlio mkali wa risasi zilizopasua kioo cha mbele cha gari letu na kulifanya lile gari liende likiyumbayumba barabara nzima.
Katika taharuki ile gari lile likaanza kuserereka likielekea kando ya barabara na kuanza kuingia vichakani kwa mwendo ule ule wa kasi huku likiyumba na kisha kwenda kugota kwenye mti mkubwa uliokuwa takriban mita hamsini nje kabisa ya ile barabara. Kitendo cha lile gari letu kugota pale kwenye ule mti mkubwa kikanifanya nigonge kichwa changu na kusikia maumivu makali yaliyosambaa hadi mgongoni.
Kabla sijajua nifanye nini mara nikasikia milio mingine kadhaa ya risasi ikirindima kama radi kuelekea kule tulikokuwa na hapo nikashuhudia kile kioo cha mbele cha gari letu kikitawanywa na kusambaa huku vipande vidogo vidogo mfano wa chenga chenga vikitumwagikia mwilini na kuendelea kuzua hali ya taharuki.
Kwa nukta chache nilihisi kama vile moyo wangu ulisahau mapigo yake, nilichoweza kusikia kusikia muda ule ilikuwa ni yowe dogo la hofu kutoka kwa yule dereva wa gari letu kisha nikamuona akiangukia kwa mbele kwenye usukani wa lile gari na kutulia kimya huku kifo kikiwa tayari kimemchukua. Waswahili wangeweza kusema kuwa; ‘hakuomba maji’.
Muda ule ule abiria wenzangu ndani ya lile gari walianza kupiga mayowe ya hofu, hata hivyo ule haukuwa muda wa kushauriana kwani nilijua fika ni nini ambacho kingefuatia baada ya pale. Niliweza kushuhudia zile risasi zilizorindima zikiwa zimekifumua vibaya kichwa cha yule dereva a gari letu na kutoboa bodi la lile gari.
Risasi nyingine zilikuwa zimeacha matundu mawili yakivuja damu katika sehemu ya kifua cha abiria mtu wa makamo aliyekuwa ameketi siti ya mbele upande wa kushoto kwa dereva na nyingine kupita hadi kwa abiria mwingine aliyekuwa ameketi nyuma ya yule abiria wa mbele katika ile siti ya katikati.
Kwa kweli sikuwahi kuingia na hofu kubwa maishani mwangu kama hofu iliyonipata siku ile, hata hivyo, katikati ya hofu ile sikuona namna nyingine yoyote ya kujiokoa haraka katika mkasa ule, hivyo nilichokifanya ilikuwa ni kuvuta haraka kabali ya ule mlango wa nyuma ambako tulikuwa tumeketi.
Niliivuta ile kabali ya mlango na kuinyonga huku nikijaribu kuusukuma ule mlango kwa nguvu, lakini ule mlango haukufunguka kwa kuwa ulikuwa umepinda kidogo na kubonyea kwa ndani kutokana na gari lile kugonga ule mti mkubwa, hivyo nikaamua kuufungua kwa teke moja la nguvu.
Ule mlango ulisalimu amri na kufunguka, lakini kabla sijashuka kutoka ndani ya lile gari nikajiwa na wazo la kumuokoa yule mrembo ambaye muda ule alionekana kama aliyekuwa amepigwa bumbuwazi na presha ilikuwa imepanda na hivyo kumfanya asijue la kufanya.
Nilikuwa nimejiwa na wazo la kumuokoa kwani sikuona sababu ya kujiokoa mwenyewe huku nikimwacha yule mrembo auawe kinyama katika mazingira ambayo nilidhani ninawajibika kufanya hivyo. Bila kuchelewa nikamshika mkono na kumsukumia nje ili ashuke, lakini alionekana kuendelea kushangaa.
Nilipotupa macho yangu kule barabarani muda ule nikawaona majambazi wawili kati ya wale watatu waliokuwa wameruka kutoka ndani ya lile gari aina ya Toyota Land Cruiser Pick-up wakikimbilia kuja kule lilikokuwa lile gari letu, huku wakiwa wameshika vyema bunduki zao mikononi.
Sikutaka kuendelea kushangaa tena, nikamnyanyua yule msichana mrembo kutoka kwenye siti yake kisha nikaruka naye nje ya lile gari na kutua chini kwa miguu yangu.
Kutokana na kiza kilichokuwa kimetanda katika eneo lile nilishindwa kuona vizzuri sehemu niliyorukia na kujikuta nikitua kwenye bonde dogo na hivyo mguu wangu wa kushoto ukashtuka na hapo nikasikia maumivu makali sana kwenye kifundo cha mguu wangu wa kushoto yaliyopanda hadi juu ya goti.
Kutokana na kiza kilichokuwa kimetanda katika eneo lile nilishindwa kuona vizzuri sehemu niliyorukia na kujikuta nikitua kwenye bonde dogo na hivyo mguu wangu wa kushoto ukashtuka na hapo nikasikia maumivu makali sana kwenye kifundo cha mguu wangu wa kushoto yaliyopanda hadi juu ya goti.
Hata hivyo, sikujali yale maumivu makali ya mguu wangu niliyoyahisi, nilimbeba juu juu yule msichana mrembo na kujitahidi kuondoka haraka kutoka eneo lile huku nikikimbilia kichakani.
Sikuweza kufika mbali kwani nilihisi mguu wangu ukipinda, kisha nikaanguka huku nikiwa bado nimembeba yule msichana mrembo, hata hivyo, kwa namna ya ajabu nilijikuta nikimuinua juu yule mrembo huku nikijipinda na kulalia mgongo huku yule mrembo akiangukia juu ya kifua changu.
Kitendo kile cha kuanguka chini na yule mrembo kunilalia juu kikamzindua kutoka kwenye lile bumbuwazi, na hapo nikamuona akitazama huku na kule kwa hofu kubwa na kutaka kupiga kelele. Niliwahi kumziba mdomo wake huku nikimsukuma haraka kumuondoa eneo lile.
“Tafadhali kimbilia kichakani kabla hawajafika,” nilimnong’oneza sikioni yule mrembo huku nikimsukuma aondoke haraka eneo lile na kwenda kwenye kichaka kikubwa ambacho hakikuwa mbali kutoka pale chini tulipokuwa tumeangukia.
Yule msichana mrembo alionekana kuganda juu yangu kama sanamu akiwa ameanza kuchanganyikiwa na hivyo kumfanya asijue lipi la kufanya na kwa wakati gani.
Muda ule walee abiria wengine walikuwa wametaharuki na kuanza kutimua mbio ovyo wakikimbilia barabarani huku wakipiga kelele ovyo kwa hofu. na hapo milio mingine kadhaa ya risasi ikavuma tena hewani, kufumba na kufumbua nikawaona watu watatu miongoni mwa wale abiria wakitupwa hewani na kupiga mayowe ya uchungu.
Wale watu walipoanguka chini walitulia kimya huku uhai ukiwa mbali na nafsi zao, kwani zile risasi zilizofyatuliwa zilikuwa zimepenya kwenye maeneo nyeti ya kichwa na kifua na kuacha matundu makubwa yaliyokuwa yanavuja damu.
Milio ile ya risasi ikamzindua tena yule msichana mrembo, nami nikazidi kumsisitiza kwa sauti yenye kusihi na kushawishi sana kuwa akimbilie kichakani kabla wale majambazi hawajafika pale na kutuona tukiwa katika hali ile. Maneno yangu yakamfanya anitazame kwa makini kama vile alikuwa amesikia habari mpya kabisa masikioni mwake.
Nikamsukuma kwa nguvu nikimtaka aondoke haraka eneo lile, safari hii aliinuka haraka pasipo upinzani wowote, nikamuona akitimua mbio huku akiwa ameinamisha mgongo wake kuelekea kwenye kichaka cha lile pori lililokuwa kando ya ile barabara.
Nikiwa bado nimelala pale kwenye majani, nilimtazama yule msichana mrembo namna alivyokuwa akipotelea kwenye kile kichaka hadi alipotoweka kabisa machoni kwangu, nami nikaubana mguu wangu wa kushoto uliokuwa na maumivu makali na kuanza kutambaa kama nyoka, haraka nikapotelea gizani huku nikielekea kwenye kile kichaka.
Muda ule abiria wengine wanne waliobaki walisambaratika kwa hofu kila mmoja na njia yake wakikimbilia porini na hivyo kusalimisha roho zao. Nilifanikiwa kufika pale kwenye kichaka japo kwa taabu nikamkuta yule mrembo akiwa kajikunyata kwa hofu kubwa huku akilia kwa uchungu kilio cha kwikwi.
Sikuwa na shaka kabisa kuwa yule mrembo pale kwenye kichaka alikuwa amechanganyikiwa kutokana na hali ile ya taharuki aliyokuwa ameishuhudia na kuna wakati alitaka kupiga yowe la hofu lakini niliwahi kumziba mdomo wake baada ya kuhisi hatari ambayo ingetukabili pindi wale wauaji wangelisikia yowe lake.
Wale wauaji wawili waliisogelea ile gari yetu kwa tahadhari wakati yule jambazi wa tatu alikuwa amesimama kwa mbali kule barabarani akionekana kulinda eneo lile pamoja na kuwalinda wale wawili endapo hatari yoyote ingetokea.
Mara nikamuona mmoja kati ya wale wauaji wawili waliokuwa wamesima kwenye lile gari akianza kusogea taratibu kuelekea pale kwenye kile kichaka tulichokuwa tumejificha mimi na yule msichana mrembo huku akielekeza mtutu wa bunduki yake pale kichakani.
Yule mrembo akaingiwa na kiwewe na kutaka kutoka ili akimbie lakini niliwahi kumdaka na kumzuia kwa mikono yangu yenye nguvu ili asikimbie, kisha nikamziba mdomo wake kwa nguvu ili asipige kelele. Ni wazi kabisa kuwa kwa muda ule alikuwa amechanganyikiwa na hakujua hatari ambayo ingempata endapo angejaribu kukimbia.
Wakati nikiwa nimemziba mdomo yule mrembo nikaamuona yule muuaji akizidi kusogea pale kwenye kichaka kwa kupitia uwazi wa matawi na majani katika kile kichaka, niliweza kumuona vizuri yule mtu wakati akitembea kwa tahadhari kusogea pale.
Kiza kilichokuwepo katika eneo lile hakikunizuia kumtambua yule muuaji kutokana na umbile lake na hata utembeaji wake, alikuwa ni yule jamaa aliyeshuka kwenye lile gari Toyota Land Cruiser Pick-up pale jirani na kituo cha kujazia mafuta cha Gapco cha Kibiti na kuja kuuliza usafiri wa kwenda Dar es Salaam kwenye gari letu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment