Search This Blog

Thursday 23 March 2023

ZAWADI TOKA IKULU (2) - 5

   

Simulizi : Zawadi Toka Ikulu (2)

Sehemu Ya : Tano (5)



“ sema Shida yako”

“nahitaji kuonana na Mzee Gao”

“mzee Gao hayupo”

“Na Von Gao nimemkuta”

“Von yupo safarini nchini China wiki ya tatu sasa”

“Ooooh! Sawa mzee akirudi mwambie kijana wake Alfred Mwaka nilikuja ninashida mhimu sana nimerejea juzi kutoka ujerumani afanye juu chini nionane naye maana nitaondoka ndani ya siku mbili zijazo”

“Sawa kaka salamu zitafika”

Kimbo alitoka na kuvuka barabara upande wa pili kisha aliita bodaboda na kutokomea.


Mwaka ni waziri wa zamani wa taifa hili pia ambaye alikuwa na kijana wake ambaye ni maarufu sana na alikuwa rafiki mkubwa mno wa Von Gao mbali na wazazi wao kuwa marafiki pia wao walishibana vilivyo.

Kimbo kaamua kutumia jina hilo ili kumuondoa hofu mzee Gao maana akisikia jina Kimbo kuna uwezekano wakutoroka nchini jina la Mwaka kwa ukaribu uliopo na kutoonana kwa muda mrefu na Alfred bila shaka ingekuwa rahisi sana kuingia.


Kimbo baada ya kwenda umbali mfupi anapishana na msafara wa magari ya Mzee Gao ukirejea nyumbani hapo kwa papo akamuamru dereva wa pikipiki kurudi. Walirudi na baada ya kufika alikamkabidhi yule dereva ujira wake kisha yeye akalisogelea tena lile geti. Baada ya kugonga kengele Yule kijana alimuangalia Kimbo kwenye kamera za getini na bila kujua aliamini kuwa Alfred amerudi akapiga simu kwa Mzee Gao kumkumbusha habari za Alfred Mwaka na mzee Gao akaruhusu afunguliwe mlango mlinzi alifungua geti bila kujua amevaa suruali iliyo na nge ndani yake na tayari kafunga mkanda sijui ataivuaje?.


Ni kosa ambalo kijana huyu mdogo aliyeajiriwa na kampuni ya ulinzi ya K.K. Security hatokuja kulisahau maishani mwake mpaka anazikwa. Kimbo aliingia akiwa kavalia suti yake ya rangi ya bahari moja kwa moja kwa muonekano wake nadhifu hakuna aliyemtilia shaka na kwa bahati nzuri kwake ila ni bahati mbaya mno kwa bwana Gao kwani alimkuta mzee Gao ameketi sebureni na yuko peke yake. Mzee Gao alibaki kaduwaa ni uso kwa uso kwa mara nyingine tena na hasimu wake wa miaka mingi namzungumzia Kimbo. Mzee Gao alianza kutetemeka huku jasho likimtweta. Machozi yalianza kumshuka hakutegemea na alimini wazi kuwa anakutana na Alfred Mwaka ila ujio wa Kimbo ulimduwaza. Mbaya zaidi yeye na na Kimbo ni mahisimu wakutupwa na imekuwa kawaida sasa kuwa ujio wa Kimbo kwa Mzee Gao daima huwa hauko salama. Na leo ni mara ya pili anakutana na Kimbo baada ya kuaminishwa kuwa Kimbo ameeshafariki lakini anamuibukia kama mzimu.


Mzee alikuwa akitetemeka asijue nini chakufanya Kimbo alifika na kuketi karibu yake kisha akamuangalia kwa dharau huku akitabasamu. Mzee Gao alikuwa kimya akiwaza na kuwazua nikweli siku yake ilikuwa imeharibika kuliko kawaida ni kitu ambacho hakukitarajia. Mbali na uoga aliokuwa nao lakini aliamini wazi kuwa Kimbo amekuja kuchukuwa nafsi yake na kamwe hata muacha salama. Mzee Gao hakujua Kimbo amekuja kwa sababu gani, ila alihisi huenda kaja kulipa kisasi kwa matendo aliyomtendea nyuma. Kimbo anaingiza mkono kwenye mfuko wa ndani wa koti lake na kutoka na bastora aliiweka sawa na mazungumzo yakaanza.

Je, Kimbo anahitaji nini kwa mzee Gao…





Kimbo alimuangalia mzee Gao kuanzia juu mpaka chini kisha akatabasamu, bila shaka alifurahishwa na jinsi mzee huyu alivyokuwa na hofu. Maana muda wote amekuwa akitetemeka kwa hofu huku jasho likimtweta bila kujua lakufanya.

“Mzee Gao wewe na mwanao ni mabingwa wa drama siyo?”

“Hapana mwanangu hayo mambo mbona yalishapita, mimi sina tatizo na wewe Gao”

“Nikweli hukuwa na tatizo baada ya kugundua kuwa nimeesha kufa”

“Si hivyo Gao nilishajutia makosa yangu na sidhani kama kuna haja yakuchukiana mwanangu, tusameheane tu maana yalishakwisha hayo”

“Oooh! Vizuri kumbe yalikwisha?”

“Hakika na nakuhakikishia baba yangu, hayo yaliisha na ukizingatia umri wangu mimi kwa sasa haustahili kuendelea kutengeneza maaduni ila marafiki vita ya Gao na Kimbo iliisha. Tumuombe Mungu atusamehe kwa makosa yote tuliyofanya mimi na wewe kipindi nakutumia katika shughuli zangu haramu kumbuka tumeangamiza roho za watu wengi na wengine kuwasababishia ulemavu, tukiachilia mbali maumivu tuliyoyaacha kwa ndugu na jamaa zao wa karibu hiyo ni laana tosha niliyojizolea.”

“Umenena vyema Mwanaharamu wewe, nashukuru kwa kunikumbusha ila wambie miungu wako hilo halijanileta”

“Aaah! Kimbo! Baba kwani kimekuleta nini……. Kuchukua roho yangu?

“Bila shaka nitaondoka nayo iwapo maswali haya hayatajibiwa kwa ufasaha, na kwa hili sitanii ushirikiano wako ndiyoponapona yako ukinichanganya tu basi ujue mauti yanakuhusu.”

Kimbo alisisitiza huku akiielekeza vyema bastora yake kifuani kwa Mzee Gao. Gao alihisi haja ndogo inampita huku akiongea haraka bila kujua alichokiongea. Hii yote ni sababu ya hofu maana alimjua vyema Kimbo, anaijua historia yake na matendo yake ya nyuma akishika siraha huwa hatanii ni binadamu aliyetengenezwa na kupandikizwa roho ya shetani mtoa roho.


Kimbo alijiweka sawa kwenye sofa la kifahari alilolikalia lililofunikwa na kitambaa cha manyoya chenye nakshi ya rangi ya chuichui na weupe wa seruji. Ili kuhakikisha usalama wake Kimbo alinyanyuka na kuufunga ule mlango wa sebureni na sasa wanabaki wawili ndani.

“Ninahitaji majibu yakweli na mafupi yatakayonisaidia mimi na kuokoa maisha yako wewe sawa?”

“Hakuna shida Kimbo niko hapa na nitakusaidia chochote utakachotaka”

“Sawa swali la kwanza nataka kujua mwanao Von Gao yuko wapi?”

“Alisafiri wiki mbili zilizopita yuko Beijing China”

“Kwa shughuli Gani?”

“Sifahamu kiundani zaidi ila ninahisi ni biashara zake binafsi”

“mnawasiliana?”

“Hapana toka ameondoka hatujawasiliana, maana hajanitafuta na mimi sina namba zake mpya anazotumia huko nje”

“Eeeh! …. unaweza kuniambia ni nani anahusika na utekaji wa Familia ya Jamae Justine?”

“Kimbo hilo sifahamu ila kwa taarifa nilizozipata ni kwamba wametekwa na magaidi na hawa magaidi wanahitaji fedha nyingi sana ili waweze kuwaachia, ninaona kwenye vyombo vya habari kila siku umekuwa ni majadala mzito, magaidi wanahitaji fedha nyingi trioni nane siyo pesa ya mchezo.”

Kimbo alitabasamu kidogo huku akimwangalia mzee Gao maana mchezo uliokuwa ukichezwa hapo katikati ulimshangaza kwani anagundua kuwa mzee Gao hajui kama mwanae ndiye aliewateka hawa watu, Kimbo anatarifa zakutosha ingawa hajathibitisha ila anaamini wazi kuwa mzee Gao ni baadhi ya watu wanaohusika moja kwa moja katika utekaji wa familia ya rafiki yake kipenzi Jamae Justine.


Mazungumzo yao yalikuwa hayana hata chembe ya urakini hivyo utani uliwekwa pembeni na Kimbo alijikita katika kuupeleleza ukweli juu ya maisha ya rafiki yake kipenzi Jamae aliyetekwa pamoja na familia yake.

“Mzee unanijua vizuri hivyo naomba tu utambue kuwa Kimbo hajaja kupiga stori nyumbani kwako nitakifumua hiki kifua sasa hivi kisha nitamalizana na walinzi wako maana unanijua siogopi kufa maana unajua nilishakufa zaidi ya mara mbili sasa hata mimi ninashangaa kwanini bado niko hai.”

“Nalielewa hilo Kimbo si kama sielewi na ndiyo maana natoa ushirikiano sijabisha”

“ninauliza kwa mara nyingine ni nani aliyehusika na utekaji wa Jamae Justine na familia yake?”

“Sijui na siwezi kukudanganya Kimbo kwa hili ninaapa mbele ya mwenyezi sina tarifa kamili juu ya utekaji huu”

“Mimi ninajua aliyemteka ni Von Gao na anashirikiana na Bilionea Dominic Martine”

“Kimbo unauhakika na hilo, Bilionea huyu mkanada?”

“Tena bila hofu Von hayuko Beijing kama unavyodhani yupo hapahapa nchini na nimekuja kukujulisha tu kuwa ninaujua mchezo wote unaochezwa, hakuna gaidi anaehitaji trioni nane isipokuwa familia ya Gao na Martine ndizo zinauhitaji huo utajiri”

“Nihakikishie hicho unachokisema”

“Uhakika ni kwamba siku Jamae amepotea na familia yake ndiyo siku ambayo Von alikuaga amesafiri, uongo?”

“Nikweli ila huo ni ushahidi wakitoto, kwani kusafiri kwake siku ya kutekwa Jamae kuna uhusiano gani na tukio la kutekwa?, wewe ni mpelelezi bwana umefanya kazi usalama wa taifa hili miaka nenda rudi utanipaje mimi ushahidi wakitoto namna hii”

“Oooh! Unauona ni ushahidi wa kitoto siyo?” Basi Kimbo alitoa simu yake mfukoni akazifungua zile video za magaidi walizokuwa wakizituma kwenye vyombo vya habari pamoja na picha alimuonesha mzee Gao na kumwambia.

“Anaejiita mwanao huyu hapa anasema yuko Beijing lakini ndiye amesimama kama mkuu wa hawa vibwengo wanaojiita magaidi na ndiye anaeongea na kutoa amri ngumu kwa rais akiomba kulipwa pesa, pamoja na kufunika sura yake lakini bado ukiliangalia umbo lake unamtambua wazi kuwa huyu ni Von. Angalia haya mabega, angalia hiyo mikono, haya mbali na umbo hebu sikia sauti yake pamoja na kuwekewa mawimbi na kuongezwa uzito lakini mimi nimeifahamu na hata wewe ukiisikiliza kwa makini utagundua hii ni sauti ya mwanao sikia anavyotamka maneno, sikia anavyovuta maneno. Pia angalia hili kovu kwenye mkono wake wa kusho kovu aliloumia wakati akicheza na mbwa miaka kumi na mitano iliyopita, nalo utalikataa kuwa hulitambui kuwa liko kwenye mwili wa Von Gao mwanao kipenzi? Hayo ni tisa lakini kumi hiyo saa aliyovaa ni zawadi uiyompa wewe siku akihitimu shahada yake ya sheria huko Marekani na ni moja ya saa azipendazo kuliko kawaida, mzee Gao unataka ushahidi gani kuamini kuwa huyu ni Von Gao?”

mzee aliinama chini kimya bila kujua atajibu nini maana zinakuwa ni tarifa ngeni kwakwe, ushahindi aliooneshwa kupitia simu ya Kimbo ni ushahidi wa kweli na sasa ndo anaanza kuujua ukweli kuwa Von yupo nyuma ya mchezo unaochezwa dhidi ya serikali na wala si magaidi kama alivyojua awali.


***

Bado jamii haijapata muafaka juu ya hiki kinachoendelea masaa yanazidi kuyoyoma kuielekea siku ya pili ambayo ndiyo ilihesabika kama mwisho wa makubaliano yaliyowekwa na magaidi kwa rais Manguli. Wakati Ikulu ya rais Manguli ikiitafuta suruhisho ya tatizo hili hali haikuwa nzuri kimashauriano, kwani kulikuwepo mvutano mkubwa baina ya wanasiasa wakongwe ambao ni washauri wa rais Manguli na kushindwa kuufikia mwafaka kwa haraka zaidi. Mjadala ulijikita katika jambo moja tu nalo ni kuitafuta suluhu juu ya utekwaji wa familia ya Jesca Manguli mtoto wa rais aliyetekwa na kikundi cha magaidi. Kikundi hiki kinadai donge nono la shilingi trioni nane ili waweze kuiachia familia hiyo ya watu watatu ambao ni baba, mama na mtoto.


Katika mjadala huu wapo waliokubali watu hawa walipwe ili kunusuru maisha ya familia hiyo, lakini wapo waliolipinga kabisa swala hilo na kusema magaidi wasilipwe. Mvutano haukuleta suluhu, wengine walishauri nguvu ya jeshi itumike ili kuwaokoa mateka hao na pia kuziokoa fedha zilizoweka kama dhamana, lakini hoja yao ilipingwa na swali moja ambalo liliuliza wangewapata wapi hao watekaji ilhali mawasiliano yao yamefungwa na si rahisi kuwafatilia kwa njia ya mtandao?. Busara ilitumika ingawa kuna wakati wazee hawa ilibidi hata kukoseana adabu kutokana na hoja zao za kulitetea taifa.


Masirahi yaliwekwa mbele na maisha ya wananchi yaliwekwa mkono wa kushoto, mvutano huu ulikatishwa na sauti iliyosema “sasa tumebakiwa na dakika tano tu na tunahitaji kauri ya mwisho kutoka kwenu” baada ya kauri hiyo kutolewa na rais sasa ukimya ulitanda na hakuna aliyethubutu kufungua kinywa chake kunena. Dakika zikakata sekunde zikayoyoma na hatimaye saa mbili kamili usiku ilitimia bila kuupata muafaka wa moja kwa moja na sasa maamzi yamebaki kwa rais mwenye, kilichosubiriwa ni kile atakachokitamka rais basi itakuwa sheria. Ingawa kila mmoja alisali kivyake wapo walioomba aitoe kafara familia ya binti yake. Lakini wapo walioomba akubali kuwalipa magaidi maana pesa makaratasi hara ni kupoteza roho za watu. Kila kona ya taifa hili watu walikusanyika makundi makundi kwenye radio na televisheni pia wapo waliojaza vifurushi kwenye simu zao wakiingoja saa mbili kamili ya usiku ili wapate kujua nini kitajiri iwapo masaa aliyopewa mtawala wao yataisha.


Wakati taarifa ya habari ikianza kuruka urushaji wa picha ulibadirika ghafla na tarifa ya magaidi ilijitokeza mbele ya runinga za watazamaji, mafundi mitambo hawakuhaisha hata vichwa vyao maana wanajua haiwezekani kuzuia kitu hicho kilikuwa kiko juu ya uwezo wao. Bilashaka hakuna aliyeshitushwa na hali hiyo na ikawahivyo kwa televisheni zote za ndani ya nchi pamoja na radio.

“Manguli kiongozi usiye na haya, usiye na huruma, usiye na upendo hata kwa kizazi chako mwenyewe, tulikuagiza uwe umejihudhuru toka saa mbili ya jana usiku lakini ulitupuuza. Tukaagiza tena uwe umetulipa fedha zetu mpaka kufikia saa mbili ya leo usiku pia umepuuza nadhani kunakitu tunahitaji kufanya maana familia hii haina umhimu katika maisha yako na mimi ninakuhakikisia leo utakishuhudia hicho unachokingoja.”

Jesca alisogezwa kwenye uso wa kamera huku wakiwa wamemuwekea kisu shingoni.

“Mweleze baba yako atulipe hizo fedha haraka iwezekanavyo tunampa dakika kumi tu la sivyo tutakuchinja mbele ya macho yake na jamii nzima inayokutazama saa hivi”

“Tafadhali baba ….ninakuomba walipe hizo pesa watatuua si watu wazuri, hawana huruma. Baba unakosa huruma kweli hata kwa mimi mwanao wa kumzaa tena mwanao pekee wa kike, tazama nimekamatwa kwa wiki tatu sasa mimi pamoja na mume wangu, leo nadhalilishwa mbele ya vyombo vya habari mataifa kwa mataifa wananiangalia. Baba lakini bora tungekuwa peke yetu mimi na mume wangu mtazame mwanangu Eric mjukuu wako kichanga anateseka pasipo kuwa na kosa lolote,. Ndugu zangu viongozi na washauri wa baba yangu pamoja na wanachi kwa ujumla pazeni sauti kumhimiza baba yangu afanye hima kuyaokoa maisha yetu tutauwawa, watatuua hawa watu na tutakufa kinyama baba usitutoe kafara kwa tamaa ya madaraka tafadhari ukishindwa kuwalipa jihudhuru.”

Baada ya Jesca kueleza hayo mbele ya kamera kila alieitizama habari ile alitokwa machozi kwa uchungu, mama mzazi wa Jesca alikuwa akilia kwa uchungu.


Sasa Kiongozi huyo wa magaidi anamchukua Eric mikononi mwa mama yake Jesca kisha anamlaza kwenye Gogo kubwa la mti lililokuwa mbele yao, gogo hilo lilijaa damu iliyokauka kama litumikalo buchani. Kamera zilizorusha matangazo moja kwa moja zilielekezwa pale na kiongozi huyo alichukua jambia lake na kulielekeza juu kwa nguvu zote ni ishara ya kukitenganisha kiwiliwili cha kichanga hicho maana kisinge uhimili mshindo wa jambia lile iwapo lingetua. Wakati huo Eric alikuwa akilia kwa uchungu, mama Eric alipiga yowe kuomba msaada ambao haukupatikana. Jamae akiwa amejaa hasira misiri ya mbogo lakini asijue lakufanya maana alikuwa kafungwa minyororo aliishia kujiinamia huku akilia kwa uchungu. Jambia lile lilishushwa kutoka juu kwa kasi ya ajabu likisukumwa na misuri ya mikono ya mwanaume aliyoshiba vyema bila shaka likatua lilipokusudiwa, ni Sauti za vilio vilisikika kwa huzuni na uchungu usioelezeka.Huku kiza kikiwa kimetanda kila mahali na hakuna chombo cha habari kilichokuwa hewani….. ni huzuni ya taifa zima kila mtu alilia kwa kabila lake.





Kifo cha Eric mbele ya macho ya ya watu haikuwa habari nzuri kwa rais, mama Jesca alikuwa amezilai kutokana na taarifa hiyo yakaushitusha aliyoina kupitia runinga, huku walinzi na wasaidizi wakijaribu kumpatia huduma ya kwanza. Mzee Manguli sasa anagundua kuwa wale magaidi walikuwa hawatanii bali walichokifanya walimaanisha, alianza kujuta kwanini hajafikia muafaka mapema tazama sasa yanayoanza kutokea ndani ya familia yake. Anakumbuka walichomwambia kuwa watafanya walichokusudia, na sasa aliamini wazi kuwa hawa watu hakuna wanachoshindwa na huenda ile familia nzima wameiteketeza maana walionekana kutokuwa na masihara. Na hili lilijidhihilisha maana taarifa ilitoweka baada ya umeme kukatika je, nani anajua kilichoendelea baada ya hapo, jibu ni hakuna hakuna aliyejua ukweli kuhusu uwepo au kutokuwepo kwa familia ya Jamae Justine tena katika dunia hii.


Kukatika kwa umeme ghafla wakati tukio hilo likiendelea niwazi kuwa wale magaidi walikamilisha mauaji ya Eric pasipo na shaka, mtoto huyu mdogo ambaye ni kijukuu pendwa wa rais Manguli hatuko nae tena katika ulimwengu huu, ameondoka kama malaika kichanga huyu. Wasaidizi wa rais wanajaribu kutafuta simu za watu katika maeneo mbalimbali ili kujua hatima ya hiyo tarifa lakini kila mmoja alijibu alivyojua yeye maana umeme ulikatika pote, na wale wanaotumia umeme wa nchi jirani mfano Uganda huko mkoa wa Kagera wao walidai tarifa ilitoweka ghafla na hakuna kilichoendelea mpaka sasa hakuna televisheni ya nchini inayofanya kazi zote hazipo hewani. Maswali yalizidi kujaa vichwani na kushindwa kuujua ukweli je amekufa au yu hai?. Ni swali ambalo kila mtu alijiuliza, waweza kuhoji kwanini mtoto huyu aligeuka kuwa gumzo lakini bilashaka jibu utalipata kuwa wazazi wake ni watu waliopendwa na kufatiliwa sana na jamii lakini hofu haikuwa kwa Eric tu bali walihofia pia maisha ya Jamae na mkewe huenda mauaji yao yalifuata .


Nyumbani kwa rais sasa hakukaliki mama Jesca amezinduka na alikuwa akimlaumu mumewake kwa kushindwa kuilinda familia, alilia kwa uchungu akijuta kuipoteza familia ya Mwanawe wa kike pekee aliye mpenda kwa dhati na kumlea katika mazingira hatari mpaka leo kakua ameolewa na kuwa na familia harafu anampoteza kizembe kwa kuhusishwa na harakati za masuala ya kisiasa mama alilia sana kiukweli alitia huruma hakuna aliyetegemea. Mama Jesca alilalamika kwa uchungu hakika ungemsikia mama wa watu alitia huruma mno. Maneno makali na yakutia huzuni yalimfanya kila aliyekuwa karibu yake aangue kilio si kutokwa machozi tu bali kuangua kilio. Maneno yaliyomtoka mama Jesca hakika yaliuchoma kila moyo hai wa binadamu uliokuwa hapo karibu kwani hata mlinzi wa rais kwa mara ya kwanza alishuhudiwa akidondosha chozi, mama alisikika akisema.

“Ulimwengu nimeukosea nini mimi?........ huenda haikupangwa nikuzae mwanangu au haikupangwa uishi katika dunia hii, maana tangu nikiwa na ujauzito wako ulinitesa na nusu nipoteze maisha… juhudi za madaktari zilikuokoa ukiwa na miezi saba tu ukatoka tumboni kwangu ukiwa hai….. huku ukiniacha kwenye chumba mahututi kwa takribani wiki nzima nikiyapigania maisha yangu pasipo hata chembe ya fahamu kichwani mwangu … lakini kwa kudra za mwenyezi mungu niliweza kunyanyuka tena baada ya takribani mwezi mzima nikiwa hospitali na hapo ndipo nilianza juhudi za kuyaokoa maisha yako kutoka miezi saba na kilo zisizofika hata mbili mpaka ulipotimu miezi tisa nikiwa hospitali kwa uangalizi maalumu niliruhusiwa kutoka.” Mama Jesca aliangua kilio kwa uchungu kisha akaendelea.

“staki kusema mateso niliyopitia kwa baba yako baada ya ujio wako nikihusishwa na kutoka nje ya ndoa, ni kesi iliyonitesa miaka na miaka nikiwa sina amani ndani kwangu na hatimaye vipimo vya vinasaba vilituliza ghasia za vipigo na matusi ndani kwetu hapo ukiwa na umri wa miaka kumi na miwili, …. Mwanangu kipenzi sijayazungumzia magonjwa yaliyokuandama wakati ukiwa mtoto yakasababisha nikasuswa na hata kukukatia tamaa, maradhi ya moyo na pumu ni magonjwa ambayo sitayasahau kamwe yalinifanya nikae nchini India kwa miaka takribani mitatu nikikupigania, maana hakuna aliyeamini kuwa utapona Mungu alisimama upande wako na akakuepushia ukawa salama.” Ni maneno yaliyotia uchungu sana na wakati akiyasema hayo mzee Manguli alikuwa kimya kajiinamia huku watu wakiziba midomo kwa aibu. Na wengine wakijaribu kumsihi mama Jesca asiendelee kuyazungumza hayo maneno kwani yalishapita na hayakufaa kusikilizwa na wasaidizi kwani ni siri za ndani.

“Hapana msinizuie kusema, niacheni niseme huenda leo huyu mwananume ataelewa nijinsi gani ninajisikia vibaya pale mwanangu anapopatwa na matatizo yaliyosababishwa na shughuli zake au matakwa yake” mama Jesca alikuwa akilia kwa uchungu wakati akiyazungumza hayo.

“ tunaelewa mama lakini hapa si mahara pake kuyazungumza haya… hizi ni siri za ndani” mzee Kato alilivalia njuga swala hili ili lisiendelee kuufaidisha umma, mzee huyu ambaye ni mmoja wa washauri wa rais pale Ikulu kwa miaka mingi na alisifika kwa busara zake.

“Mzee Kato pamoja na hayo yote ni lipi kosa la mwanangu? Au kumpenda mtoto wa masikini? … masikini mwanangu alianza kuwindwa kama nguruwe pori kwa mwaka sasa. Manguli hunafadhira …. Hufadhiriki mume wangu. Ninaikumbuka mipango yote yakumuangamiza Jamae wakati akiwa na mahusiano ya awali kabisa na mwanao najua ilishindikana kwa uwezo wa Mungu lakini hukufurahi kabisa binti yako kuolewa na Jamae na nadhani hiki kinachoendelea mpaka leo huenda unahusika kwa asiliamia miamoja”

“Aaah sasa unafika mbali mke wangu, najua nilikosea na niliomba radhi lakini kwa hili sasa unanionea, nawezaje kumteka mwanangu na hasa kumuua mjukuu wangu tena damu yangu halali ili nipate nini mimi Manguli mimi hapana mke wangu rekebisha kauli.”

“haushindwi mume wangu maana ninakujua kuliko unavyojijua, sina mtoto wa kike tena katika maisha yangu … siasa umemtoa kafara mwanangu na sasa ninabaki mpweke mimi … Baba Jesca umeamua bila aibu kumtoa mwangu kafara …. Jamani mwanangu mimi uchungu unauma, Jesca mwangu nenda salama… Nenda mama tutaonana kwa Mungu mbinguni ,msalimie mjukuu wangu Eric mama aliangua kilio upya” ni huzuni ndiyo iliyotawala hakukuwa na mashauriano tena, kila mtu alikuwa kachoka na hakukuwa na nguvu yakufanya lolote bali vitambaa vilizidi kulowa machozi na kuzikwangua kamasi zilizoambatana na machozi ya uchungu ndani ya pua za wahusika.


******************


“Nimefanikiwa kuukata umeme kote nchini na hata walipokuwa wakirushia matangazo yao hao magaidi umeme umekatika hivyo hawataweza kurusha tena matangazo yao hivyo nakuhakikishia hakuna tukio linaweza kuendelea kwa giza lile lakini pia mshituko walioupata lazima watafute namna yakujipanga kwa muda maana hawakutarajia hivyo sasa tumia huo muda bila kukosea” alisema Elisha Ngami.

“Oooh sawa pia unaweza kuzuia namna wanayoitumia katika urushaji wao wa matangazo ili hata baadae wakipata njia mbadala washindwe?, maana ninahofu wakipata jenereta wanaweza kukamilisha walichokikusudia” Kimbo alihoji

“Ni rahisi iwapo hawana teknolojia mpya wanayoitumia tofauti na hii ambayo nimeigundua na kuidukua tayari ila itachukua muda kidogo”

“ Ni kama muda gani?”

“ masaa matatu yanatosha”

“Ila usiwe na shaka nimeesha uvuruga mfumo wao wa kompyuta na ndiyo mfumo pekee wanaoutegemea, pia nimevuruga mfumo wa shirika la umeme nchini na haitakuwa rahisi kwao kutoa huduma kwa usiku huu hata wakiweza itawachukua muda mrefu kugundua maana nimewachezea kiteknolojia zaidi, mamlaka ya mawasiliano haipo hewani hivyo nimezuia urushwaji wote wa matangazo ya radio na televisheni pia kwa kifupi niseme tu kwamba nchi haina aina yoyote ya mawasiliano”

“Kwanini umefanya hivyo Elisha”

“ Nafanya hivi ili hata wakipata njia mbadala ishindikane kurusha matangazo yao maana vyombo vyote vya habari haviko hewani na wao wanategemea radio na televisheni kurusha matangazo yao”

“ sawa mkuu nashukuru kwa hilo, fanya hivyo endelea kuwadhibiti mpaka tukamilishe na nitashukuru sana kaka” Kimbo alikata simu yake huku akivaa vizuri koti lake lililokuwa na kila aina ya siraha, bastora, visu na mabomu yakurusha kwa mikono, alikuwa amevalia kikamilifu mithiri ya komando aendae vitani ungemuona hakika usingemtofautisha na waigizaji mashuhuri wa sinema za kivita tuwaonao kwenye kaseti za video. Alifika na akagonga mlango taratibu na baada ya muda mlango ulifunguliwa.



MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog