Simulizi : Msako Wa Mwehu
Sehemu Ya : Tatu (3)
??? ????? ?????
Baada ya kumaliza kusoma Kachero Yasmine, akatabasamu, uso wake ukala mbwende kisha akamuangalia Kachero Manu ambaye nae alikuwa amemkodolea macho kwa hamu kumsubiria Yasmine aseme chochote kitu nafsi yake ipate faraja.
"Malizana na huyo mjuba wako kigogo wa Polisi anayekula kivuli cha Jeshi la Polisi, tuanze kumsaka huyu mwehu Maso Maso ana mengi sana ya kutueleza, ushahidi wa kimazingira umeanza kumfunga kuwa anahusika na mlipuko uliotokea Wizarani". Kachero Manu akajenga tabasamu la furaha usoni mwake akashuka haraka na kuagana nae, kisha akafanya haraka kuingia ndani ya hoteli na moja kwa moja akaelekea mapokezi.
"Karibu sana mgeni wetu, malazi yapo tumebakiwa na "single room" na "mini deluxe room" tu" alikaribishwa Kachero Manu kwa unyenyekevu mkubwa na mhudumu kisura wa mapokezi katika hoteli ile. "Ahsante sana, naomba nivione baadhi ya hivyo "Mini Deluxe Room" nione ubora wake" akajieleza Kachero Manu. "Usiwe na mashaka kabisa ubora wake ni wa kutukuka, vigogo wengi wa serikali hapa ndio nyumbani kwao, na hivi tunavyoongea na wewe kimebaki kimoja tu, chumba kingine kimechukuliwa na mteja ameingia sasa hivi punde tu" alijifaragua kwa maringo yule dada wa mapokezi.
"Any way no problem, nipe hiko chumba kilichobakia nisije kukosa mwana na maji ya moto" alisema Kachero Manu huku akiombea wawe jirani na huyo mgeni, hasimu yake. Akapewa daftari la wageni la kujaza taarifa zake. Akalifungua na kuanza kujaza taarifa zake lakini akawa anajaza huku anatabasamu pana sana. "Ushindi unanukia kiulaini kabisa" alijiwazia moyoni. Alichokuwa anafurahi ni kuona huyu kigogo huyo, Inspekta Haroub Farouq kaweka moja ya namba ya simu iliyopatikana kwenye daftari la kichaa "Maso Maso". "Inaonekana hii ni namba walikuwa wanapigiana wakiwa na mawasiliano ya faragha" aliwaza Kachero Manu.
Kwenye lile daftari la "Maso Maso" kulikuwa na namba zaidi ya 20 ambazo Kachero Manu zote alizihifadhi kichwani na kuweza kuziimba kwa kichwa. Na zote namba hizo walipofuatilia TCRA zilionekana zimefungwa hazitumiki. "Inaonyesha wana mtandao mpana mpaka kwenye kampuni za simu, wakitaka kuongea siri zao wanazifungulia kwa muda kisha zinafungwa na kufutwa mazungumzo ya siri yaliyorekodiwa" aliendelea kuwaza Kachero Manu.
Alipomaliza kujaza taarifa akasindikizwa na mhudumu yule mpaka chumbani kwake akiwa amesaidiwa kubebewa brifkesi yake ndogo nyeusi. Walipofika tu chumba namba 10B, wakamuona Inspekta Haroub Farouq anatoka kwenye chumba kinachotazama namba 10A huku akiwa amevalia sare zake za jeshi la polisi zikiwa zimechafuka vyeo mabegani mwake kama uchafu vile.
"Dada hiki chumba sitaki watu wa usafi au mtu yoyote aingie mpaka siku nitakapoondoka pia funguo nitakuwa nazo mwenyewe" alisema yule kigogo wa polisi ikiwa ni amri na sio ombi huku anatokomea zake kwenye korido za hoteli ile kutoka zake nje, huku akitembea kwa mwendo mzofafa kwa kiburi cha cheo chake kikubwa. "Huyu mteja wenu anaonekana mtata sana eeeh" alichokonoa Kachero Manu, akibahatisha huenda akaambulia chochote anachokijua huyu dada juu ya Inspekta Haroub Farouq.
"Simfahamu kwa kweli maana mie ni mgeni hapa kazini, kesho kutwa ndio natimiza mwezi kamili anajitia hanjamu mwenyewe wala hanipi presha mie " alijibu yule dada kwa nyodo huku analiweka brifkesi la Kachero juu ya meza, akaaga na kuondoka zake. Kachero Manu akazuga kama anajifungia chumbani kwake yule binti mhudumu ilivyopotea tu michakato ya nyayo zake masikioni mwa Kachero Manu, akafungua mlango wake na kutoka nje ya chumba chake.
Akatoa mfukoni mwake kibati kidogo mithili ya ATM-kadi ya benki akasogelea chumba alichotoka kigogo yule, akabonyeza namba za mlango wa chumba kile akakiingiza kibati kile mlango ukajimanua wenyewe bila kokoro zozote. Akaingia haraka na kuufunga tena kama iliyofungwa. Alivyoingia chumbani kwa Inspekta Haroub bila kupoteza muda akaenda moja kwa moja kwenye kabati la ukutani la chumbani kwa bahati lilikuwa limeegeshwa tu. Akavuta mlango wake ukafunguka, lilikuwa ni kabati lenye nafasi ya kutosha kukiwa na chemba nne, juu kulia na kushoto mbili na chini hivyo hivyo. Chemba za juu zinajitegemea mlango wake mmoja na chemba za chini nazo zinajitegemea mlango wake. Chemba ya chini kushoto alikuta ndipo alipohifadhi begi lake kubwa la nguo. Hakukuta zaidi ya begi hilo. Akarudi mezani alipoangalia chini ya meza akakuta kuna mkoba wa rangi nyeusi umetunatuna umefungwa kwa zipu tu. Akautoa chini na kuufungua, akakuta kuna makaratasi mengi mengi, ila akavutiwa na mafaili madogo mawili yaliyohifadhi nyaraka kimpangilio. Akaanza kuzipiga picha kwa kutumia simu yake ya kisasa zile nyaraka ambazo kwa haraka haraka aliziona zitamsaidia kwenye kazi yake.
Lilikuwa ni zoezi lisilozidi dakika 5 tu, akawa ameshamaliza kupiga picha. Wakati anafunga na kujiandaa kuelekea kwenye kabati afungue begi akasikia sauti ya mitembeo ya viatu vya kipolisi inakaribia kuishia mule chumbani alipo. Haraka haraka akafunga mkoba vizuri na kuurudisha mahali pake kisha akakimbilia kwenye kabati akafungua chemba ya upande wa kulia na kujificha kisha akairudishia.
Hisia zake zilimtuma sahihi kwa zaidi ya asilimia 100%. kuwa Inspekta Haroub Farouq alikuwa amerejea tena chumbani mwake ghafla huku anaongea kwa simu kwa sauti ya jahara, inayosikika wazi kabisa.
Mara moja Kachero Manu akatoa maagizo kwa Afisa Usalama wa Taifa wa Mkoa wa Dodoma awatafutie sehemu salama Wabunge wote wanaokuja kwenye hitimisho la maombolezo, kwenye nyumba maalumu za Usalama wa Taifa 'Safe House' na wapewe ulinzi mkali. Kisha wakaanza kupanga mipango sasa wa kuwatia mbaroni kwa pamoja usiku wa leo Inspekta Haroub Farouq na mwehu "Maso Maso" watakapokuwa pamoja chumbani.
Walipomaliza mipango yao tayari, wakaelekea mgahawani hapo hapo hotelini kupata mlo wa mchana wa nguvu kisha wapumzike. Wakati wapo mgahawani kwenye simu yake Kachero Manu ikaonyesha alama ya kutumiwa barua pepe. Alipoifungua na kuisoma akakuta Katibu Muhtasi wao Kokunawa kamtumia picha na video za CCTV-Kamera za majengo jirani na sehemu kulipotokea mlipuko walizohitaji. Wakarudi tena chumbani kwa mara ya pili kuanza kuzichambua picha kwa umakini. Wakawa wanaona namna "Maso Maso" anavyoingia na kutoka kama chumbani kwake katika jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani utasema ni chooni kwake. Wakayakinisha asilimia 100% kuwa "Maso Maso" alikuwa hakauki ndani ya jengo la Wizara kipindi chote cha kabla ya milipuko ya kigaidi.
Wakaamua wajipumzishe, kwa ajili ya kuirudishia miili yao nishati yake asilia. Kachero Yasmine akatandika mito chini ya zulia la chumbani mule mwa Kachero Manu, akiwa anajiandaa kujipumzisha. Kachero Manu akiwa amebaki kitandani peke yake akamchombezea utani kachero Yasmine, "Ndio tatizo la kufanya kazi na watoto wa Mashekhe kutwa wao mawazo yao kuogopa kuoga janaba tu, unajitesa bure kulala chini wakati kitanda kikubwa hiki ni futi 6*8, uje hapa kitandani tulale mzungu wa nne".
"Ha ha ha ha...sumu haipimwi makali yake kwa ncha ya ulimi, safari moja huanzisha nyingine, usije kunitia vishawishini, na majaribuni nikashindwa kuhimili ukanitia dhambini ukanivunja kizinda changu bure nikakosa kuvikwa kisarawanda siku ya ndoa yangu kwa kupoteza usichana wangu kwa jitu la ajabu na katili kama wewe, ambaye anapata pesa za kutambia Mjini kwa kutoa roho za watu" alijibu Kachero Yasmine kwa utani. "Nawe kweli mtu wa Zenji Kijukuu cha Sultani bin Jerebi, sasa hiyo kisarawanda ndio nini maana yake, umenitoa kapa"?, aliuliza Kachero Manu.
"Ha... ha... ha...ndio shida ya kufanya kazi na Mmwera, watu wa tunumba tunumba sana na kujishebedua kama wanajua kumbe wanaungua jua tu, kisarawanda ni nguo nyeupe anayovikwa mwanamke bikira kiunoni siku ya ndoa yake anaposindikizwa kupelekwa kwa mumewe" alijibu Kachero Yasmine kwa uso wa bashasha huku akisubiria dongo maridhawa toka kwa mkuu wake wa kazi.
"Kwa hiyo unataka kuniambia umri huo huo ulionao wa miaka yako 28 bado unayo yenyewe au Mchina tu ha ha ha? unataka kumshughulisha mpenzi wako akupe tunu na tamasha usiyostahili! aliuliza Kachero Manu huku akiwa anatabasamu pana, swali ambalo halikupata jibu la moja kwa moja toka kwa Kachero Yasmine zaidi ya kicheko na kurushiwa mito kitandani alipokaa, kuonyesha hataki utani wake ule wa kuulizwa swali la uhalisia wa ubikira wake.
Kisha wote wakaendeleza utani wa hapa na pale mpaka wakapitiwa na usingizi mwepesi huku wanapulizwa na kiyoyozi chenye sentigredi 15. Miili yao ikipata nguvu mpya tayari kwa mshikemshike wa usiku wa kumtia mbaroni Inspekta Haroub na kichaa wake feki "Maso Maso The Duduman".
Kisengerenyuma hadi 23/09/2014
Masoud Masoud alikuwa ndio anaripoti chuo kikuu cha "Stanford University" akiwa kama mwanafunzi wa kitivo cha Uhandisi wa Mitambo "Mechanical Engineering". Kukanyaga kwake Ulaya kwa Masoud Masoud akitokea mitaa ya uswahilini Sinza ilikuwa ni kama ndoto ya alinacha tena ya mchana wa saa sita, jua limesimama dede, alikuwa haamini kabisa.
Majumba ya kifahari, magari ya kisasa, mabasi ya mwendokasi na treni za umeme aliyokuwa anayashuhudia tu kwenye filamu na televisheni sasa alikuwa anayaona mubashara kwa mboni za macho yake. Wiki ya kwanza ya mwelekeo "Orientational Course", haikuwa na durusu za darasani. Ilikuwa ni wiki ya kufanya usajili wa chuo, kuonyeshwa benki ilipo ili kufungua akaunti, kuelekezwa maduka ya kununua bidhaa, na sehemu zote muhimu kwa mahitaji ya mwanadamu.
Ilipoanza wiki ya pili, ndio masomo yakaanza rasmi. Shule ilikuwa ngumu kama ilivyo kawaida ya shule ya uhandisi, haitopata kuwa rahisi hata siku moja mpaka dunia itakavyotoweka. Ndio maana wahandisi wanapenda sana watambulike kama Injinia fulani ili kujimwambafai kidogo kufidia machungu ya ugumu wa shule.
Masoud Masoud licha ya ugumu wa masomo alikuwa anaweza kwenda nayo sambamba, huku akiwagaragaza vibaya watoto wa kizungu. Baadhi ya wanafunzi wenzake wakampachika jina "Maso Square The Duduman" kuonyesha kukubali utabe wake katika masomo. Lakini baada ya masomo kwisha darasani alijikuta yupo mpweke kupitiliza hana sehemu ya kwenda, hana mtu wa kumtembelea wala kumjulia hali. Vyakula vya nyumbani kama ugali, wali wa nazi, mihogo ya kuchemsha, magimbi na mengineyo mengi akawa anayakosa. Akaanza kutamani kurejea nyumbani, Tanzania, Waingereza wanasema alipatwa na "Home Sickness".
Mwanachuo mwenzake aliyekuwa mkubwa kwake kiumri, kijana wa kutoka Sudani, kwa jina anaitwa Mudrah Mudriki, aliyekuwa anasomea Shahada ya Sheria. Ambaye ni chotara wa baba Msudani na mama Mzanzibari akatumia hiyo fursa ya upweke wa "Maso Square The Duduman" kumzoea kwa haraka sana, na akafanikiwa.
"Kwanza rafiki yangu Masoud tuanze kwa kuwekana wazi usione matreni ya umeme, ukaona majumba mazuri ukaona Mahoteli na Mikahawa mikubwa mikubwa au ukaona mabenki makubwa huku Ulaya ukadhani Waafrika kwa Wazungu wote wanaishi kwa raha. La hasha ni wachache sana, maisha ya Ulaya yamejaa msongo wa mawazo ambao siyo wa kawaida na kuna wakati hasa wageni wanaingia katika majaribu mbalimbali hata ya kutaka kujinyonga. Ndio maana kama umefuatilia vyombo vya habari jana Waziri Mkuu wa Uingereza kamchagua Waziri wa Upweke. Miongoni mwa malengo ya kuwekwa Wizara ya Upweke ni kukabiliana na upweke unaowakabili watu wazima, wale waliopoteza wapendwa wao, wale wasio na watu wa kuzungumza nao ama hata kugawana fikra na uzoefu" yalikuwa ni maneno ya nasaha ya Mudrah kwa rafiki yake Masoud ya kumfanya asijisikie mpweke. "Sawa nakuelewa rafiki yangu, lakini lakini kwanini sasa kule nyumbani Tanzania hata kwenu Sudani watu wanatamani kuzamia Ulaya kuja kutafuta maisha bora, wakati huku hamna starehe yoyote ya maisha?" aliuliza "Maso Square The Duduman" kwa rafiki yake aliyemsafishia nia na kumuamini.
"Tatizo nadhani ni lile lile tu la kuzuzuka na maroshani wanayoyaona yameota kama uyoga, na vitu vya anasa wanavyoviona. Laiti wangefahamu haya yanayotukuta, Balozi zao za nchi za Ulaya kule nyumbani Afrika wangefugia kuku kwa kukosa watu wanaokimbilia kuomba visa", alijibu kwa umakini Mudrah swali aliloulizwa na rafiki yake Masoud.
Kutokea hapo wakawa wapo kama mapacha, utasema ni "Sunche" na "Kapeto" unapomuona Mudrah ndio umemuona Maso, ukimuona Maso basi ndio umemdiriki Mudrah.
Kidogo kidogo "Maso Square The Duduman" akaanza kuizoea hali ya Uingereza. Wakawa sasa wapo bega kwa bega kila mahali, mambo yao wanayafanya kwa mkono mmoja, sio kwenye kuangalia mechi za kandanda ligi ya Uingereza, sio kwenda muziki, na kwenye kila aina ya starehe.
"Maso Square The Duduman" alimuona rafiki wa kweli ni Mudrah kwa sababu alijitoa wakati yupo kwenye taklifu ya kuyazoea maisha ya Ulaya. Wakawa kama kijibwa na mwanawe, lakini kwa kiasi kikubwa "Maso Maso" alikuwa ameshajenga utegemezi mkubwa kwa Mudrah, na hilo ndio jambo Mudrah alikuwa analitaka, na kulitamani litokee nalo likajipa.
Ikajitokeza ghafla tu Mudrah kakata mguu kwa rafikiye Maso bila taarifa yoyote. Akawa sio wa kumpigia wala kupokea simu ya swahiba wake Maso, wala si wa kujibu barua pepe anayotumiwa na rafiki yake. Hiyo hali ilidumu kwa muda wa si chini ya wiki mbili.
Mbaya hata akienda chumbani kwa Mudrah hapatikani, mlango umefungwa. Na akiwaulizia sanjali wenzake wa kozi ya sheria nao wanasema hawamuoni daima dawamu darasani. Maso akaanza kupata upweke wa mwanzoni, ukamrudia kwa kasi. Akapatwa na daka la roho kwa kumkosa bila taarifa rafiki yake kipenzi walioshibana. Akaanza kupatwa na msongo wa mawazo, na kuanza kupoteza hamu ya kula mpaka akaanza kuwa gofu la mtu mithili ya mgonjwa UKIMWI.
Mwaka wa masomo kuhitimisha muhula wa pili ulikuwa ndio unakaribia kwisha, akawa anajifikiria ndio kwanza anamaliza mwaka mmoja na bado miaka mitatu mbele yake. Masharti ya mfadhili wake ni kubakia Ulaya mpaka amalize Chuo ndio atarudi nyumbani Tanzania. Mbaya zaidi huku nyumbani kwao mama yake alipigwa mkwara na mfadhili kuwa asimsumbue kabisa mtoto wake masomo ni magumu, mtoto wake akifeli hata somo moja tu hatomlipia tena gharama za masomo na maisha.
Ikabidi Bi. Mwantumu awe anawasiliana kwa nadra sana na mtoto wake, jambo ambalo lilizidi kumuongezea upweke kipindi ambacho alikuwa anahitaji mfariji. Ghafla bin vuu, siku moja usiku akiwa amekaa nje ya bustani za hosteli maalumu kwa Wanachuo, akiwa ameshakata tamaa ya kuishi Ulaya, anatafakari kitu cha kufanya. Akajitokeza rafiki yake Mudrah Mudriki katika uoni wa macho yake kama mzuka vile.
Maso akiwa amepigwa na butwaa na kushikwa na gagaziko la ulimi, hayaamini macho yake "Assalaamu Aleikum rafiki yangu kipenzi wa moyoni" aliwahiwa kusalimiwa na Mudrah huku wakikumbatiana. Badala ya kujibu salamu, Maso haraka haraka akamtupia swali, "ulipotelea wapi ulinipa wahaka wa moyo usiomithilika kubeba nisiyoyaweza kifuani mwangu, kitu gani nilikukera uniambie kabla wakati haujazidi kwenda matiti nikuombe radhi tusameheane turudi kuwa washirika wa chanda na pete kama zamani". "Maso Square The Duduman" alikuwa anaongea kwa hisia za ndani ya moyo mpaka machozi yalikuwa yanamlengalenga.
Alikuwa ndio kwanza anatimiza miaka 21 bado anahitaji muongozo na faraja ya watu wa karibu. Mudrah Mudriki rafiki mkia wa fisi ukimshiriki atakufilisi alikuwa anafurahi kimoyomoyo kuwa lengo lake linakaribia kutimia muda sio mrefu la kumtumbukiza Maso kwenye shimo refu ambalo kuchomoka kwake itahitajika kudra za Rabana tu.
Kiuhalisia Mudrah Mudriki alikuwa Mwanachuo feki, alitumwa kazi maalumu ya kumuingiza "Maso square The Duduman" kwenye kundi la kigaidi la "Al-shabaab". Mchongo wote ulichongwa na mwarabu mmoja Mfanyabiashara na Mkandarasi maarufu nchini Tanzania 'Hafeedh Abdullah', ambaye ndio aliyemrubuni Bi.Mwantumu kuwa anataka kumsaidia kumsomesha mtotowe Uhandisi huko Ughaibuni ili aje kumuajiri kwenye kampuni zake zilizosambaa Arabuni na Afrika. Akamzuga ameamua kumsomeshea mwanawe kwa sababu yeye ni mwanamke mjane na pia kutokana na mtoto wake kufanya vizuri kwenye mitihani yake ya Kitaifa. Akamuingiza kingi kuwa Mwenyezi Mungu katika vitabu vya dini amesisitiza sana kuwajali wajane na mayatima kama Maso. Mfanyabiashara huyo Hafeedh Ibn Abdullah alikuwa ana ushirika na kampuni za Ukandarasi wa majengo nchini Sudani tokea mwaka 1989.
Hivyo Osama Bin Laden alivyokuja kuishi nchini Sudani kuanzia mwaka 1991-1996 alivyotafuta washirika wake wa kufanikisha ajenda zake za kigaidi siku za usoni akamsajili kibopa Hafeedh Ibn Abdullah kuwa ndio msimamizi mkuu wa shughuli za "Al-qaeda", Ukanda wa Afrika Mashariki. Chambo chao cha udaga kilikuwa kinakaribia kumnasa samaki muhimu kwao katika karata ya ugaidi.
Walitambua kabisa ugaidi katika karne ya 21 unahitaji watu wenye ubongo unaochemka sana kama "Maso Maso" ambaye alikuwa amemaliza shule katika sekondari ya watoto wenye vipaji maalumu vya kiakili, Mzumbe Sekondari. Mapambo yoyote dhidi ya adui yako katika zama za sayansi na teknolojia zilikuwa zinahitaji akili nyingi kuliko nguvu nyingi.
"Rafiki yangu samahani sana nimeipata njia ya kunikurubisha kwa Mola wangu. Mie nimeamua kujitenga na wewe kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema kwenye Qur'an Surat Mujaadalah, surah ya 58 aya namba 22; "Hutokuta watu wanaomuamini Allaah na Siku ya Mwisho kuwa wanafanya urafiki na kuwapenda wanaompinga Allaah na Rasuli Wake, japo wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao (Allaah) Amewaandikia katika nyoyo zao iymaan, na Akawatia nguvu kwa Ruwh (Wahyi) kutoka Kwake, na Atawaingiza Jannaat zipitazo chini yake mito ni wenye kudumu humo. Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hao ndio kundi la Allaah. Tanabahi! Hakika kundi la Allaah ndio lenye kufaulu". Akapumzika kuongea baada ya kumaliza kusoma aya. Akachomoa hanchifu yake mfukoni, akaanza kufuta machozi yake yaliyokuwa yanabubujika kama maji, kujionyesha amejawa na mapenzi ya Allah moyoni mwake kumbe bosheni tu, kisha akaendelea na mahubiri yake.
"Sasa kwa msingi huo mie nakuacha rasmi kwenye maisha yako ya kumtumikia Shetani, mimi sasa nimempokea Allah na kumfanya kuwa taa ya maisha yangu. Sasa wewe bado unahudhuria muziki, bado unaangalia kandanda wakati wachezaji wake wamevaa nusu uchi na dhunubu kibao ambazo zinamchukiza Allah na Mtume wake, hivyo nakuaga rasmi urafiki mimi na wewe basi, kwaheri" akaaga, akageuka akawa anajifanya anaondoka.
"Maso Square The Duduman" akawa anaona sasa anaachwa solemba moja kwa moja, hata onana tena na swahibu wake. Kuachana kwao urafiki inamaanisha hana nguzo tena ya kujishikia atakapopatwa na shida ugenini. Ndugu yake mwenye asili ya nyumbani Zanzibari, Tanzania aliyemtegemea sasa anamuacha kwenye mataa. "Mudraaaaah Mudraaaaaah....pliiiiiiz my friend don't leave me, let's talk pliiiz..!! " ilikuwa ni sauti ya kubembeleza ya Maso ikimtaka rafiki yake Mudrah arejee wayajenge. Furaha ya Mudrah moyoni mwake ilikuwa kama amepaa yupo juu ya mwezi, ndio kitu alichokuwa anakitarajia. Alikuwa tayari ameshakaribia kutaka kupotea kwenye upeo wa Maso ndio akasikia sauti inayomuita kwa nguvu zote.
Akajifanya anatikisa kiberiti kwa kujichelewesha kidogo, akasikia tena sauti ya Maso inamuita. Kiunyonge akajifanya anarudi alipo Maso. Alipofika wakakumbatiana na rafiki yake, huku anajifanya kulia kifaurongo. "Sasa inabidi nikupeleke msikitini ukatubu dhambi zako usilimu upya"
Wakakubaliana wapitiane saa kumi na nusu usiku kuelekea msikitini kwa shekhe Dawoud El-jabeer. Shekhe ambaye durusu zake za masomo ya dini baada ya sala ya alfajiri zilikuwa zinavutia vijana wengi wa Ulaya hususani nchini Uingereza. Huyo Shekhe ndio alikuwa bomu maalumu lililotegwa na Al-qaeda kuwapika magaidi wapya kwa kutumia kasumba ya Uislamu wa itikadi kali. "Maso Square The Duduman" alikuwa anaenda kulishwa itikadi kali ya kiislamu iliyopotoshwa makusudi ili kuwapotosha vijana wasio na hatia wajitoe muhanga kwa kujivika mabomu.
"Maso Square The Duduman" amesajiliwa rasmi kuwa gaidi.
Ulikuwa ni usiku wa giza nene lililoenea kila mahali. Nuru pekee iliyoangaza nchi ilikuwa ni ya nyota tu zilizoko angani ambazo zilimeremeta kwa utulivu. Watu wengi walikwisha jilalia zao usingizi wa pono kutokana na uchovu wa mihangaiko ya kimaisha ya mchana kutwa. Wakati fulani sauti za wazururaji wa usiku na walevi wenye kupenda ugomvi ilisikika mbali kabisa na karibu na kambi ya siri ya magaidi wa "Al-shabaab" iliyopo katika Milima inayoitwa 'Jabar Marrah', Magharibi mwa Jimbo la Darfur, nchini Sudani. Walevi hao walikuwa wanajiiba tu kutimiza hawaa za nafsi zao kwa kunywa pombe katika nchi ambayo inafuata utawala wa Sharia za Kiislamu, ambapo ukikamatwa umekunywa pombe unapigwa mboko hadharani.
"Maso Square The Duduman" usiku huo alikuwa amejisokota kwenye kichaka kilichopo kwenye Milima hiyo akiwa amevaa sare maalumu za "Al-shabaab", kombati za rangi ya kijani mpauko. Ghafla bin vuu bila kutegemea, katika mazingira ya ukame wa jangwani, mvua ya kidindia ikaanza kunyesha mfululizo. akaanza kulowana na akatota chapachapa mwili mzima.
Hakuwa na jinsi bali kuendelea kubakia pale pale alipohitajiwa kuwepo na wakufunzi wake. Alikuwa yupo doria ya kambi katika siku yake ya mwanzo kabisa akiwa kambini hapo kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu yatakayompika aje kuwa gaidi mahiri duniani. Alishakacha masomo kitambo na kutorokea nchini Sudani bila familia kung'amua. Siku ambazo ilikuwa hamna kulala mchana na usiku kwa muda wa miezi miwili mtawalia. Ilikuwa ni mwendo wa kunyanyua vitu vizito na kutembea navyo umbali kadhaa, kubiringika, kupiga pushapu, skwashi, kutambaa na kifua, kukimbia na kunyoosha viungo. Kambi ya 'Jabbar Marrah' ilikuwa ni pacha wa kambi kuu ya kigaidi ya "Al-qaeda" iliyopo katika mashamba ya 'Tarnak' huko 'Kandahar', Afghanistani. Hiyo ndio kambi aliyokuwa anaishi gaidi mkuu Osama Bin Laden, enzi za uhai wake wakati amejichimbia nchini Afghanistani.
Wakufunzi wake wote kijana "Maso Maso" walitokea huko 'Tarnak' wakitumia mitaala ya huko huko Kandahar iliyoachwa na muasisi wa Al-qaeda, Osama Bin Laden. Wakufunzi wa "Maso Maso" walikuwa ndio wale wale wakufunzi mahiri waliowafunza vijana hatari kwa ugaidi duniani, "Mohammed Atta" na "Ziad Jarrah". "Mohammed Atta" raia wa Misri na "Ziad Jarrah" raia wa Lebanoni wakiwa wamemaliza elimu yao ya Chuo Kikuu jijini Hamburg, nchini Ujerumani, hawa ndio walioshiriki mashambulizi ya kujitoa mhanga kwa kutumia ndege ya tarehe 11/09/2001, maarufu kwa "September 11" yaliyotokea nchini Marekani.
Bahati ilikuwa ipo upande wa Kachero Manu wakati anakaribia mlango kwa Inspekta Haroub, alimuona mhudumu nyuma yake akiwa amebeba trei lenye chakula na vinywaji akielekea usawa wa chumba cha Inspekta Haroub.
Hapo hapo machale yakamcheza, akaona ni bora atumie fursa hiyo ya kupelekwa chakula atumie kuingia kiulaini chumbani mule. Yule mhudumu alipofika usawa wa chumba mbili hizo zilizo mkabala, moja aliyokodi Kachero Manu na nyingine ya Inspekta Haroub. Kachero Manu alikuwa tayari ameshafungua mlango wa chumba chake nusu, lakini akajitia kama mle chumbani kuna jambo limejiri.
"Samahani sana kijana njoo kwanza uone dakika sifuri tu, huku anazidi kuufungua zaidi mlango" alimuongelesha mhudumu yule kwa sauti ya kubembeleza iliyojaa kweli tupu. Yule mhudumu bila ajizi akitanguliza falsafa ya mteja ni mfalme akapitiliza na trei lake mpaka ndani ya chumba cha Kachero Manu akijiamini hatopoteza hata dakika moja. Alipoingia akatua trei vizuri mezani kisha akawa anasubiria maelekezo ya alichoitiwa na mteja huyo. "Akangalia chini ya uvungu uone vumbi wewe mwenyewe" alizugwa hangaisha bwege mhudumu huyo na Kachero Manu akimfuata mpaka akawa amesimama nae uso kwa uso. Alipopotea maboya kidogo yule mhudumu na kujaribu kutaka kuangalia chini ya uvungu, akapigwa kareti moja ya shingoni, yenye vipimo maalumu itakayomfanya azimie kwa muda usiozidi dakika 40 ndipo atazinduka.
Bila kupoteza muda, mara moja akamvua nguo zake akavaa yeye. Akajiangalia kwenye kioo akaunda tabasamu pana zilimkaa vilivyo. Akabeba trei na kuurejesha mlango wa chumba chake kama umefungwa vile. Akapiga hodi chumbani kwa Inspekta Haroub akisubiria amri ya kuruhusiwa kuingia.
"Pita ndani" ilikuwa ni sauti nzito ya kigogo Inspekta Haroub Farouq, akimuamuru mhudumu wa hoteli alete chakula na vinywaji alivyoagizwa. Alikuwa amesimama takribani dakika mbili bila kupewa ruksa ya kuingia. Pua za Kachero Manu zilikuwa zinateseka kwa harufu nzuri ya kuvutia ya mahanjumati anuwai mbalimbali aliyobeba kwenye trei. Huku tezi zake za mate kinywani zikimwaga mate churururu. Kama sio kuwajibika na kazi Wallahi angedokoa kwa kuchudua chuduuu. Mpishi alikuwa amefutu ada matawi ya juu katika fani ya mapishi. Alikuwa amebeba mchapalo wa sambusa za nyama zilizochanganywa na mbogamboga kama karoti na hoho. Pia alikuwa amebeba vitumbua vya motomoto vyenye kusikika harufu yake ya hiriki na mashrabu zilikuwa ni soda za kopo mbili, "Fanta orange" na "Sprite" ambazo zilikuwa zinavuja jasho la kutosha nje ya kopo kuthibitisha ubaridi wake.
Alivyopewa ruhusa ya kuingia, hakujivunga akajibu makaribisho kwa vitendo, akanyonga kitasa mpaka chini mlango ukajimanua manuu ishara ya kumpa idhini ya kuingia ndani ya chumba. Akapiga jicho haraka haraka kwenye saa yake ya mkononi akakuta ni saa nne kasorobo usiku. Alijipa muda wa nusu saa kutoka muda huo kumaliza mchezo wote. Akajitoma ndani na kuurejesha mlango kwa kutumia mkono wa kulia huku wa kushoto umekamatia trei la mahanjumati na mashrabu.
Kisha moja kwa moja ikawa inasikika sauti ya soli ya viatu vyake, mlio wa 'do do do' inavyogonga sakafu ya chumba hicho. Mpaka akafikisha salama lile trei juu ya meza ya sehemu ya kulia chakula ya chumba kile cha kifahari. Kilichokuwa na kitanda, sehemu ya kulia chakula na sehemu ya mazungumzo.
Inspekta Haroub na sanjali wake "Maso Maso" walikuwa wamekaa kwenye meza ingine huku kuna nyaraka wamezisambaza hapo mezani, huku begi la mgongoni la "Maso Maso" likiwa lipo kitandani. Inspekta Haroub alikuwa ametingwa na uchambuzi wa nyaraka hizo alisusa hata kumuangalia mhudumu huyo. Hali ilikuwa tofauti kwa mwenza wake "Maso Maso" yeye alikuwa hadhiri kwa zaidi ya asilimia mia fil mia. Alipotupa tu jicho pogo na kumuangalia yule mhudumu, nywele zikamsisimuka, ngozi ya mwili ikamtutumuka mpaka ikatoa vipele vya baridi, machale yakamcheza. Alichunguza mambo kadhaa ndani ya sekunde chache kwa yule kijana mtoa huduma ya chakula.
Kilichomshtua kwanza shingoni hakuvaa kamba inayoning'iniza kitambulisho kama alivyowashuhudia wahudumu wengine. Pili suruali aliyovaa ya rangi nyeusi chini ilikuwa ni njiwa, haifiki mpaka chini kabisa. Na tatu kiatu alichovaa chini kilikuwa ni cha gharama kubwa kinachoweza kugharimu karibia mishahara yake ya nusu mwaka kununua. "Maso Maso" hivi viatu alikuwa anaviona kwenye maduka makubwa kipindi yupo Chuo Kikuu nchini Uingereza, iweje Tanzania viweze kuvaliwa na mhudumu wa hoteli mwenye mshahara mkia wa mbuzi.
Kachero Manu baada ya kutua mezani kile chakula akaingiza mkono wake wa kulia kiunoni upande wa kulia ili achomoe bastola yake awaweke chini ya ulinzi. Akashtukia tayari amewahiwa yeye kwa kufyatuliwa risasi ya mkono wake wa kulia iliyopiga kwenye kidole gumba chake na kuitupa bastola yake mita kadhaa. "Tumevamiwa kiongozi changamkaaaaa....tusepe mshenzi mbele yetu!" zilikuwa ni kelele za "Maso Maso" zilizomzindua Inspekta Haroub Farouq na kufahamu kuwa hali sio shwari tena mle chumbani.
Kachero Manu baada ya kutua mezani kile chakula akaingiza mkono wake wa kulia kiunoni upande wa kulia ili achomoe bastola yake awaweke chini ya ulinzi. Akashtukia tayari amewahiwa yeye kwa kufyatuliwa risasi ya mkono wake wa kulia iliyopiga kwenye kidole gumba chake na kuitupa bastola yake mita kadhaa. "Tumevamiwa kiongozi changamkaaaaa....tusepe mshenzi mbele yetu!" zilikuwa ni kelele za "Maso Maso" zilizomzindua Inspekta Haroub Farouq na kufahamu kuwa hali sio shwari tena mle chumbani.
Akaziachia zile nyaraka kisha akaruka kama samaki mkizi kumrukia Kachero Manu ambaye alikuwa anajiandaa kuifuata bastola yake. Wakaanguka wote kwa pamoja chini ya sakafu pwatwaa. Wakaanza mbiringembiringe za kufirigisana, kupapatuana na kuviringishana mieleka pale ardhini chumbani, wakawa wanapinduana kwa zamu juu chini chini juu, wanapimana ugali.
Ndio nafasi aliyokuwa anaitafuta "Maso Maso", hakutaka kupambana na vyombo vya dola muda huu, wakati kazi aliyotumwa bado mbichi hata robo hajaimaliza. Akapiga risasi moja taa ya chumbani ikamuitikia kwa mlio wa paaah...!!. Giza likatawala chumbani totorooo..!!. Kama nyani vile anavyodaka ndizi akarukia kibegi chake kitandani na kuanza kuparamia ukutani kama chui akafanikisha kutoboa dari la "gypsum" na kuingia juu ya kenchi la hoteli.
Alipoangaza chini kwa kwa tabu, macho yake yalianza kuzoea giza akaona bado Inspekta Haroub na Kachero Manu wanachuana, lakini Inspekta Haroub anaelekea kutepeta hawezi kupambana na kijana kama yule. Mara ikasikika sauti nyingine ya paaaaah...!!paaaah....!! "Aaaaaah mamaaaa naku....f...a...aaa!", ilikuwa sauti ya Inspekta Haroub akilalamikia maumivu baada ya kulambwa shaba mbili takatifu za kichwani na shingoni, zilizomfanya apoteze maisha pale pale.
"Maso Maso" aliamua kumtwanga risasi Inspekta Haroub kupoteza ushahidi, alifahamu fika akiwa hai mateso atakayopewa ataropoka kila kitu, harafu ataharibu mipango yote. Akaanza kukwava kwa kutumia msaada wa mwangaza wa tochi ya simu akiwa juu ya dari. Mpaka akafika kwenye boksi mbalimbali za kuunganisha waya toka sehemu mbalimbali za hoteli. Akawa anakata na kufumua hizo nyaya kwa kutumia koleo. Baada ya zoezi hilo hoteli nzima ikawa giza na kusababisha mlipuko ulitikisa mtaa mzima.
Kachero Manu alipowasha taa ya simu yake akapigwa na butwa baada ya kuona dari juu ya chumba limefumuliwa. Akabaki amebung'aa tu, akajiongeza tu ukiona manyoya jua ameliwa, alishatorokwa zamani. Alikuwa hajawahi kushuhudia binadamu mwenye kufanya mambo yake kwa kasi ya haraka kama alivyofanya "Maso Maso".
Akafungua mlango na kuchomoka kasi nje ya chumba huku akiwa na bastola yake mkono mmoja na mwingine kashikia tochi ya simu. Akajikuta wamekumbana mzima mzima wenyewe kwa wenyewe na Kachero Yasmine ambaye nae alikuwa anakuja wanguwangu chumbani kwa Inspekta Haroub, maana ilishapita nusu saa walioahidiana, akajua fika mambo huko yamechacha chumbani kwa Inspekta Haroub. Wakanyanyuka wote haraka haraka wakiharakisha kutoka nje ya hoteli kuzidi kuimarisha ulinzi ili asiwatoroke. Mambo yalikuwa mpwitompwito yamenoga tayari.
Alishatambaa kama dakika 12 na ushee akiwa juu ya kenchi huku jasho linamtiririka kama maji kwa joto lake lenye kushitadi haswa. Akaamua sasa liwalo na liwe lazima atoboe tundu tena hapo hapo alipo. Akaanza kupapachua tundu kwa vidole vyake. Tundu lilipokuwa kubwa lenye uwezo wa kupitisha kiwiliwili cha mwanadamu akaanza kunusa harufu ya vyakula, hisia zikamtuma huenda ikawa ni jikoni. Alipochungulia vizuri akamkuta babu mpishi kala chumvi kiasi chake akiwa kwenye sare zake za kazi anahangaika huku na kule na kutekeleza majukumu yake ya kazi. Ametingwa na kusokotwa na jukumu la kuchoma nyama huku amewasha taa za kuchaji zinazomsaidia kuona vizuri ili asiunguze nyama za wateja ikawa kesi.
Bila kufanya ajizi akateremka jumlajumla kwa kushtukiza na kutua juu ya sinki ya kuoshea vyombo. Babu wa jikoni alishtukia baada ya kuona vyombo vichafu kwenye sinki vimetoa mlio wa kuvunjika baada ya kudondoka chini. Akashindwa hata kukimbia kwa kihoro alichonacho, akaanguka ndengu chini na kuzimia kwa uoga hasa alivyoona mtu aliyeshuka kavaa nguo nyeupe, fikra zake zikamtuma huenda mzuka umemshukia.
Bila kuchelewa, akaanza kumburuza taratibu yule mpishi mpaka akamfikisha kwenye stoo ya vyakula, akamuingiza na kujifungia nae. Akatoa zana za kazi kwenye kibegi chake hima hima, akajinyoa ndevu zake haraka kwa kutumia mwangaza wa tochi ya simu, kisha akavaa sura ya bandia. Akawa amevua nusu kanzu na pajama la chini yake.
Akawa juu amebakia na singilendi nyeupe na bukta la ndani tu akavaa nguo za babu mpishi. Muda wa rakaateni usiozidi hata dakika 2 tokea amzimishe, ghafla wakaja askari njagu kama 3 kule jikoni wakiwa na tochi zao mikononi na bastola. "Aisee...lipishi hujaliona lijitu limepita huku kavaa kanzu nyeupe kama Osama?" aliuliza mmoja wa njagu wale kwa lafudhi zao za kinoko, akionekana ni mpya katika kazi ndio kwanza ametoka chuoni CCP-Moshi karibuni hivyo ana usongo wa kazi. "Maso Maso" akazuga kuchomoka na gunia la viazi jikoni anakuja nalo usoni mwa askari wanguwangu na kulibwaga kwa kishindo mbele yao.
"Hapana mkuu sijamuona kabisaaa huku nipo peke yangu" akajibu "Maso Maso" kwa kujiamini huku akijitia anakimbilia kuchukua jalo la kubebea samaki na kuwaweka samaki kwenye mafuta yaliyokuwa tayari yamepata moto yanatoa ule moshi wa kuonyesha yameshapashika moto vilivyo. Wale askari kwa pupa huku bastola zipo mkononi mwao wakaondoka jikoni mbio mbio kuelekea kusikojulikana, wakijiridhisha yule ni mpishi kutokana na nguo nyeupe aliyovaa na kigiza giza kilichopo.
Laiti wangemulika tochi zao tu darini, ndipo "Maso Maso" angetambua hamna bamvua lisilo na usubi, lakini wapi hawakupata mawazo hayo, na arobaini yake ilikuwa bado kutimu. Uamuzi wa Mungu hushinda mizungu, ahadi yake ya kukamatwa ilikuwa bado kutimu. Daima ubaya hatima yake mbaya tu. Chapuchapu kwa mwendo wa mateka, "Maso Maso" akabeba kibegi chake akatoka nje ya jiko akatembea kwenye veranda mpaka akatoka kwenye bustani ya nje iliyopo ndani ya ukuta wa hoteli.
Akakuta makundi ya wafanyakazi na baadhi ya wateja wamejikusanya vikundi vikundi wanazogoa kwa uwoga, macho yao yamepigwa na taharuki hawajui cha kufanya. Maswahibu yamewakumba Wallahi wanasubiria kudura ya Manani na nusra yake, mithili ya ng'ombe aliyeingia kwenye kumi na nane za mchinjaji anasubiria tu shingo yake itenganishwe na mwili wake watu wakajisosomole kwenye supu. Akawapuuza na kuachana nao, alipotupa jicho kwenye uwazi wa vidirisha vya ukuta akaona kuna polisi kibao na mbwa wametanda.
Akakata tamaa ya kuokoka kirahisi bila kutumia akili ya kuzaliwa,"natakiwa nicheze kama Pelle wa Brazili na timu yake ya Santos nikibugi tu wataniletea ukuda". Akiwa kwenye lindi zito la mawazo ya kujiokoa, akaanza kusikia ving'ora nje ya Hoteli vimeongezeka, akajua hapa leo hatumwi mtoto dukani. Wana usalama walikuwa wanaongezeka idadi yao, sasa walikuwa wanajeshi ndugu zao akina Marwa na Chacha ndio wanatia timu.
"Maso Maso" kwa tahadhari kubwa akaanza kurudi nyuma nyuma kwa tahadhari kubwa kwa mwendo wa kunyata huku akielekea usawa wa nje wa jiko. Akawa kama kuna kitu anakitafuta kilichopotea. Utafutaji wake ulikuwa wa umakini mkubwa utasema mgonjwa aliyeenda kutafuta tiba, kisha akaagizwa na kalumanzila wake amtafute sisimizi mjamzito aweze kupona.
Utafutaji wake alikuwa huku anamulika na mwangaza wa tochi yake ya simu. Akajawa na furaha ya ghafla baada ya kuona alichokuwa anakitafuta. Akaanza kujipiga mangumi mfululizo kifuani mwake kujipongeza kwa ushujaa wake. Kifua chake kila anapokuwa anakipiga kikawa kinatoa sauti kama taruma la reli, kuonyesha kimekubali shuruba za mazoezi magumu. Akasimama katikati na kitu alichokuwa anakitafua akatoa zana za kazi kwenye kibegi chake na kuzima simu yake. Akawa anasikia kwa mbali inatoka amri kwenye spika sasa watu waliopo kwenye jengo la Hoteli wajisalimishe, waanze kutoka nje ya jengo.
Walielekezwa kupitia magetini huku wakiwa na vitambulisho vyao rasmi vinavyowatambulisha. Taa kubwa maalumu zikiwa kwenye magari zikawashwa kuangaza eneo zima pale. Msururu wa foleni ukapangwa kwa ajili ya ukaguzi wa uso kwa uso. Huku wanajeshi waliowasili punde tu wakiamua kuanza msako wa ndani ya jengo wa chumba mpaka chumba.
Leo kwa mara ya kwanza wanajeshi na polisi walikuwa wanashirikiana kwa pamoja. Mara nyingi hawa wawili walikuwa hawapaliani moto. Akajisemea "Maso Maso" "sasa ugali moto, mboga moto, wanajiapiza lazima atiwe mbaroni "Maso Maso" mtoto wa Bi.Mwantumu, kishindo changu hawaniwezi, mpaka wataniimba jina langu usiku na mchana Bara na Visiwani nchi nzima. Kishindo changu hawakiwezi" aliwazaKkisha akatabasamu. Tabasamu la kuwazidi akili wana usalama lukuki.
SURA YA KUMI
Ijumaa ya mkono wa Tanzia nchi nzima
Kachero Manu na Kachero Yasmine walikuwa wapo kwenye viwanja vya Bunge Dodoma tokea jogoo la kwanza. Siku hiyo walilala usingizi wa mang'amung'amu wakifikiria usalama wa viongozi wao wa nchi wanaokutana leo kwenye hitimisho la maombolezo ya kitaifa yaliyodumu kwa muda wa wiki nzima. Walikatika maini juu ya usalama wa viongozi hao hasa baada ya kushindwa kumtia mbaroni "Maso Maso" usiku ule wa Jumatano pale hotelini.
"Maso Maso" aliwaporonyoka katika mazingira ya kutatanisha ya kimiujiza. Mpaka baadhi ya wanausalama wakafikia hatua ya kukufuru kuwa "Maso Maso" ni Jini la Kisomali lina uwezo wa kujigeuza upepo na kutokomea au likajigeuza mwanamke au hata mnyama kama mbwa au paka. Hawakuamini kwa ulinzi ule wa siku ile angeweza vipi kuwapotea kimaajabu kama angekuwa ni binadamu wa kawaida.
Wasichofahamu ni kuwa "Maso Maso" aliwazidi kete kwa kutorokea kupitia mfumo wa bomba la maji taka lililounganisha na hoteli hiyo na nyumba kadhaa za jirani. Bomba hilo lilikuwa linakwenda kuibukia Msalato, nje ya Jiji la Dodoma kando na barabara ya kuelekea Wilaya ya Kondoa.
Kabla hajafika eneo lolote "Maso Maso" alikuwa ni msomaji mzuri wa ramani nzima ya eneo analokwenda na namna atakavyotoroka mambo yakienda segemnege. Alhamisi yote walishinda wanamsaka kila mahali na vizuizi vya barabarani vikazidi kuimarishwa ili wamkamate lakini wakaambulia patupu.
Hitimisho likawa ni kuzuia madhara yake yasitokee hivyo walijihimu kufika eneo la tukio siku hiyo ya Ijumaa kuhakikisha mambo yanaenda vizuri kabisa. Walichokuwa hawakifahamu ni kuwa nae "Maso Maso" alikuwa yupo jirani tu jengo la Bunge, nae akiandaa shambulizi lingine la kishindo. Shambulio ambalo litasababisha kilio kingine cha kusaga na meno cha nchi nzima.
Wageni Waheshimiwa kutoka ndani na nje ya Tanzania walikusanyika ndani ukumbi maarufu kwa jina la "Pius Msekwa" kwa ajili ya kuhitimisha maombolezo ya kitaifa kwa ajili ya kuwapa heshima za mwisho wahanga wasio na hatia, Wabunge, na Mabalozi wa Nchi za Ng'ambo kutoka Marekani na Canada, waliouawa juma moja lililopita. Wingu la huzuni na majonzi lilitanda na kutamalaki katika nyuso za miongoni mwa waombolezaji.
Huku wengine wakilia kwa kwikwi hasa baada ya kuyaona majeneza ya Waheshimiwa Wabunge yanaingizwa Bungeni na kupangwa safusafu. Waombolezaji ambao walionekana nadhifu kwa mavazi yao ya suti nyeusi kuashiria wapo kwenye msiba mzito wa Kitaifa. Maafisa Usalama nao hawakuachwa nyuma walikuwa wametingwa kuhakikisha mambo yote yanaenda sawa bila kuharibika.
Ilipotimu saa nne asubuhi juu ya alama mgeni rasmi wa maombolezo hayo kutoka serikalini, Makamu wa Rais aliyekuwa anasubiriwa kwa pashau kubwa na waombolezaji aliwasili katika viunga hivyo vya Bunge. Alilakiwa na viongozi wa Mkoa wa Dodoma na wa Kitaifa kisha akasindikizwa moja kwa moja kwenda kuweka saini kwenye daftari la kumbukumbu za wageni.
Baada ya hapo akapitiliza moja kwa moja ukumbini kuchukua nafasi yake aliyoandaliwa. Mshehereshaji wa shughuli hiyo alifungua hitimisho la tanzia hiyo kwa sala ya kuwaombea marehemu kutoka kwa wawakilishi toka makundi mbalimbali ya dini, anuwai mbalimbali za madhehebu yote yaliyopo Tanzania. Kisha zikasomwa historia za marehemu kutoka mwakilishi mmoja mmoja kutoka kila familia.
Baada ya hapo wakateuliwa Wabunge wawili wa kutoa neno la shukrani kwa wageni waliohudhuria kwa niaba ya Wabunge wote. Hotuba zao Wabunge hao wawili ziliwaliza waombolezaji na kuwatonesha upya simanzi ya moyo.
Makamu wa Rais nae akatoa neno lake la faraja kwa Watanzania na kuwahakikishia msako mkali wa magaidi bado unaendelea wavute subira na wawe na imani na vyombo vyao vya usalama. Shughuli ikahitimishwa kwa kupanga mistari mirefu na kuanza kuaga maiti zikiwa kwenye majeneza yao. Mpaka kufikia saa tisa mchana shughuli zikawa zimehitimishwa na kila mmoja na wao anatawanyikia anapokujua yeye. Haikuwa shughuli ya maneno chekwachekwa kama ilivyozoeleka katika mikutano ya wanasiasa, hivyo ilihitimishwa kwa wakati. Nyuso za Kachero Manu na Yasmine zilianza kuchanua furaha kwa kubeba tabasamu hasa baada ya kushuhudia shughuli nzima imehitimishwa kwa amani na usalama bila kuchafuliwa na magaidi kama walivyoahidi kuichafua shughuli hiyo.
Lakini ilikuwa ni furaha ya muda mfupi tu, wakiwa wameshapanda kwenye gari lao wanataka kuondoka simu ya Kachero Manu ikaanza kuita. Akashtuka, mapigo ya moyo yanaanza kwenda kasi, akarukwa roho yake kwa sababu alijua ni ya Mudiru wake, Mkuu wa Usalama wa Taifa Bwana Omega Mtanika kutokana na mlio maalumu kwa ajili yake. Alipoitoa kiunoni kwa ajili ya kuipokea akaona ni kweli namba ya simu ya Bosi wake.
Akajua chuma kimeshalia huko maana simu ya Bwana mkubwa huyu ikipigwa ujue kuna lamgambo maalumu kwake la taarifa ya kazi. "Hellow...Kiongozi habari yako", alibonyeza kitufe cha kupokelea simu na kuanza kusalimia Kachero Manu. "Habari mbaya sana, nimepata taarifa sasa hivi kuwa Wabunge wengine 5 na madereva wao wote inasadikiwa kwa pamoja wamefariki wakiwa njiani kurejea Dar es Salaam muda huu, kama nusu saa iliyopita" alijibu salamu Bwana Omega Mtanika kwa kuleta taarifa mpya na mbaya kwa Kachero Manu.
Kachero Manu taarifa hiyo kwake ilipenya kwa kasi kwenye ngoma ya masikio yake na kumsababishia ahisi kama yupo kwenye njozi, tena ndoto yenyewe ni ya mchana kweupe. "Sasa kama mtahitaji msaada wa majasusi wa kigeni toka F.B.I mnijulishe haraka tujipange kuwaalika, kazi njema" akamaliza maongezi yake na kukata simu. Kachero Manu alibaki sekunde kadhaa ameshikilia simu sikioni bila kuiachia haamini kama wamepigwa tobo tena na magaidi.
"Bosi nini zaidi kimekusibu mbona kama unaweweseka sikuelewi" Kachero Yasmine alimzindua mkuu wake wa kazi ambaye alikuwa amerushwa akili na simu ile aliyopigiwa yenye taarifa kabihu isiyovutia kwa msikilizaji. "Aah..acha tu, Wabunge 5 na madereva wao kwa pamoja wamefariki dunia barabarani maeneo kati ya Ihumwe na Pandambili wakiwa njiani kuelekea Dar es Salaam" alijibiwa Kachero Yasmine kwa sauti ya unyonge.
"Huyu atakuwa mwana halula "Maso Maso" kashafanya yake, mshenzi sana" alisema Kachero Yasmine kwa sauti ya hamaki. Kachero Manu hakujibu kitu, alikuwa anaona Mkuu wake wa kazi ameshaanza kupoteza imani naye.
"Anasema anataka alete F. B. I waje kuwasaka magaidi, ni kama mshenga kumwambia mume aliyeshindwa kumpa ujauzito mkewe kuwa atamletea mume mwenza wachuane" aliendelea kuwaza Kachero Manu kiunyonge."Tuelekee hospitali ya Mkoa, tukacheki maiti zilizoletwa afu tutajua ya kufanya", alitoa amri Kachero Manu. Kachero Yasmine akatii amri ya mkubwa wake wa kazi, wakatoka mbio mbio kama watu waliopagawa.
Kachero Manu aibukia "Chops Modern Car Wash & Garage"
Ilikuwa ni kiota kipya cha kuoshea magari kilichozinduliwa jirani kabisa na Bunge, mkabala na Chuo cha Biashara "College of Business Education" (C. B. E), Dodoma. Ilikuwa ni majira ya Alasiri ya siku ya Jumapili Kachero Manu alikuwa anashuka kwenye gari yake aliloliegesha mbele ya sehemu maalumu ya kuoshea magari maarufu kwa jina la "Chops Modern Car Wash".
Lilikuwa ni eneo nadhifu linaloosha magari kwa kutumia mashine, likiwa kwa mbele yake limeungana na grereji kubwa ya kisasa ya kukarabati magari inaitwa "Chops Garage". Huku mteja akipatiwa huduma anayotaka ya kinywaji kama chai, kahawa au soda yoyote anayoihitaji wakati anasubiria gari yake.
"Bosi karibu, huduma zetu ni nzuri na nafuu sana, kuosha gari ni Tsh. 15,000/= tu" alikuwa ni kijana nadhifu mhusika wa eneo hilo akitoa makaribisho. "Ahsante sana, naomba kuonana na mhusika wa kituo" aliomba Kachero Manu. "Mhusika pita hapa ukatokezee kule mbele utaona kibao kimeandiwa kwa kimombo "Garage Manager" hapo utamkuta" alijibu kwa unyenyekevu.
"Sawa basi nioshee hilo gari yangu usichelewe sana, nitatoka ndani ya robo saa" alitoa maagizo Kachero Manu huku akimuachia funguo wake wa gari kijana huyo na kutokomea kuelekea ofisi ya Meneja wa gereji. Ilimchukua dakika 3 tu kufika mpaka mlango wa Meneja huyo. Kabla hajabisha hodi, akashtukia anafunguliwa mlango."Karibu sana ndugu" alisema yule mwarabu aliyeonekana kuwa na mwili wa kushupaa kuonyesha ni mtu wa mazoezi.
"Ahsante sana, nimekaribia" yalikuwa ndio majibu ya Kachero Manu huku anapitiliza na kwenda kukaa kwenye kiti. "Sijui nikusaidie nini rafiki yangu" aliuliza yule Mwarabu, akionekana ni mtu mkorofi. Kabla ya kujibu Kachero Manu akang'ariza macho kwenye kiofisi kie kwa haraka haraka.
Akagundua kuna CCTV-Kamera inayorekodi matukio ya eneo zima la gereji. Pia ofisi ilikuwa ni ndogo ila samani zake ni za gharama toka nchi za ng'ambo. Ukutani kulikuwa na picha kubwa ya Rais wa nchi ya Tanzania, na pembeni yake kulikuwa na mabango ya picha za maandishi ya Q'uran kitabu kitakatifu kwa Waislamu.
"Hawa wanajitia kumshiriki Mwenyezi Mungu lakini kumbe wanamshiriki Shetani" alijiwazia moyoni mwake. Kisha akavunja ukimya, "mimi naitwa Kachero Manu, nimekuja kuna maswali ningependa nikuhoji ili nipate majibu yake ya kina". Yule Meneja alikuwa anakunywa soda yake iliyokuwa mezani, ghafla baada ya kusikia maelezo ya Kachero Manu, soda ikampalia kooni akaanza kukohoa mfululizo. "Ok.....Ok...verry sorry ehee nakusikiliza, ila kwanza naomba kitambulisho chako" alijieleza yule Meneja akionyesha kujiamini. Kachero Manu akajibu kwa vitendo kwa kuonyesha kitambulisho, yule Meneja akajiridhisha, mahojiano yakaanza;
Kachero Manu: "Jina lako kamili ni nani? "
Meneja: "Naitwa Kareem Abdallah"
Kachero Manu: "Nani mmiliki wa hili eneo? "
Meneja: "Hili eneo la familia"
Kachero Manu: "Nafahamu ila nataka kujua ambaye jina lake lipo kwenye usajili kule BRELA".
Meneja: "Ni Baba yangu mzazi Mzee Hafeedh Abdallah"
Kachero Manu: "Mnazo rekodi ya magari yanayoingia kupata huduma zenu kwa siku"?
Meneja: "Tunazo rekodi na ukitaka nitakupatia bila shida yoyote"
Kachero Manu: "Ninaomba unipatie ya wiki iliyopita mpaka kufikia siku ya Jumapili"
Meneja: "Subirisha kidogo nikudurufie". Kikapita kitambo kifupi mara kompyuta yake mezani ikaanza kutoa karatasi kupitia printa yake. Akamkabidhi Kachero Manu. Akazipokea na kuanza kuzipitia, baada ya kuzipitia zile karatasi, mahojiano yakaendelea upya.
Kachero Manu: "Sioni rekodi ya siku ya Ijumaa" (akauliza huku anamkazia macho)
Meneja: "Ijumaa siku yetu kubwa ya ibada huwa hatufanyi kazi, tunamwabudu Allah tu, au nyie Jumapili mnaenda kazini?" (akauliza kichokozi kujitafutia kichaka cha kufichia uwongo wake). Kachero Manu akapotezea kujibu swali hilo la kizushi.
Kachero Manu: "Kuna magari yoyote ya Waheshimiwa huwa yanakuja hapa kupata huduma?"
Meneja: "Siwezi kufahamu kama hili ni gari la Mlalaheri au Mlalahoi, sie kazi yetu ni kuhudumia watu wote kwa usawa. Mimi nakaa tu ofisini sihusiki kazi za nje".
Kachero Manu: "Una habari kuwa Wabunge 5 na madereva wao wamefariki? "
Meneja: "Msalie Mtumee...ndio kwanza unanipasha hizo taarifa sijasikia bado". Kachero Manu alipomuangalia machoni mwake alijua fika kuna uwongo anauficha.
Kachero Manu: "Ahsante kwa ushirikiano wako, nikikuhitaji tena sitosita kukutafuta".
Meneja: "Ahsante sana, karibu tena Afande". Wakapeana mikono na kuagana. Kachero Manu akaelekea mpaka alipoaliacha gari lake. "Bosi tayari gari na risiti yako ya malipo ya EFD tayari hii hapa" alisema yule kijana huku anakabidhi risiti kwa Kachero Manu. "Ahsante sana umeosha vizuri gari yangu, kamata hii bahashishi yako" alisema Kachero Manu huku anamkabidhi mkono wa ahsante wa Sh.10,000/= yule kijana.
"Ahsante sana Bosi Mungu akubariki sana" alijibu yule kijana huku anapokea ile pesa huku akiwa na furaha fokofoko isiyo na kifani. Kachero Manu akawasha gari yake akawa anarudi kinyumenyume ili aweze kuondoka akasimamisha ghafla huku yule kijana yupo pembezoni mwa dirisha la dereva.
Akashusha kioo chake kidogo "kijana chukua hii kadi yangu ya anuani yangu na namba ya simu tuonane leo ukitoka tu uje 'Chako ni Chako Bar' saa mbili na nusu usiku tuongee nina mpango wa kufungua sehemu ya kuoshea magari kama hii hapa, uje unipe ushauri rafiki" akamrushia ile kadi huku anatimka bila kusubiri jibu toka kwa yule kijana. Alijua tu piga ua lazima aje kwenye udhia penyenza rupia, sasa kashampa kilainishi atashindwa vipi kutokea eneo la miadi.
Mauaji ya kutisha ndani ya Chako ni Chako Bar
Kachero Manu alifika muda saa mbili na dakika kadhaa huku akikuta watu wameshonana ile mbaya. Alikuwa anasikia tu "Chako ni Chako Bar" ndio mara yake ya kwanza kukanyaga. Licha ya kwamba mkewe anafanya kazi Ndani ya Jiji hili la Dodoma.
Alichoshangazwa ni kuwa jina la Baa na mandhari ya muonekano wa nje ni mbingu na ardhi. Akifananiza na kiota kama "Rose garden" ya jijini Dar es Salaam ambayo ina jina kubwa kuliko yenyewe ilivyo. Baa hiyo ya "Chako ni Chako" inapatikana maeneo ya barabara ya kuelekea uwanja wa ndege "Airport Road", eneo ambalo ni maarufu sana Jijini Dodoma.
Alikuta wateja pomoni wamejiachia ile mbaya, mambo ya nyama choma, kuku choma, mishikaki, chipsi kavu kwa mayai, supu za kongoro ndio mahali pake. Bila kusahau wanawake viruka njia hapo pia ndio eneo lao la kusaka mawindo toka kwa wanaume viruka mito. Kila mtu na lake, wengine wanakula na kunywa na baadhi yao wanacheza muziki unaopigwa kwenye santuri. Ila kuna meza moja tu yenye viti vitatu kimekaliwa kimoja tu.
Akaenda kuketi palepale, wakasalimiana na mteja aliyemkuta amekaa hapo anapiga vyombo vyake hana habari na mtu. Mara mhudumu wa kike aliyevali sare maalumu akaja kwa haraka. "Karibu sana Nakusikiliza kaka yangu!" ilikuwa ni sauti ya mhudumu ikimtaka Kachero Manu atoe oda yake. "Naomba uniletee kuku wa kuchoma wa kienyeji mzima, akauke vizuri tafadhali, bila kusahau maji ya moto aina ya 'Usambara Soft' chupa kubwa, Yale maji toka Tanga" alitoa oda yake kwa msisitizo huku anaperuzi simu yake kuangalia arafa zozote zilizoingia kwenye simu kwa muda huo.
Yule mhudumu akawa anaondoka anaondoka kwa mwendo wa njiwa, Kachero Manu akawa anamsindikiza kwa macho ya huba kuangalia miondoko ya yule dada wa Kinyaturu. Kitendo ambacho yule mteja mwenzake alishuhudia namna anavyokula kwa macho.
"Brother ni mgeni Dodoma Eeeh... Brother...?" aliulizwa na yule jirani yake kwa sauti ya kilevi. "Hapana Dodoma ni mwenyeji kiasi chake maana mke wangu anaishi hapa hapa Dodoma, ila viwanja hivi ndio mara yangu ya kwanza kutia maguu yangu alimjibu Kachero Manu jamaa yule ambaye ulevi ulishaanza kumchukua vilivyo.
"Basi Brother hapa ndio umefika kuna mabinti wengi sana 'visu' toka Singida, Babati, Mbulu, Kateshi na Arusha. Hao mabinti kwenye viunga vya 'kula bata' ndani ya Jiji hili hawakosekani. Wametamalaki kwenye lounges, clubs, pubs, local bars, restaurants, massage points na saloons za kike' hao ndio wana hati miliki hapa Dodoma. Hapa nazungumzia 15 - 23 yrs old chicks!" alizungumza kwa mbwembwe za kilevi yule jamaa huku akitia kimombo, akionekana ni mtu wa kuendekeza starehe vilivyo.
"Nashukuru kwa kunitoa tongo tongo za macho nilikuwa siyajui hayo" alimjibu kwa kumvika kilemba cha ukoka. Basi ikawa ndio kama amechochea kuni kwenye moto, wacha jamaa aendelee kubwabwaja. "Ikifika jioni watu taratibu wanaanza kujisogeza viwanja kama' Platinumz, Rainbow, Rose Garden, Maisha Club, Morena, Chako ni Chako hapa kama unavyojionea mwenyewe, African Dreams, hapa tunakuja kufuata kuku na hili giza giza la hapa ukiiba mke wa mtu, sisi wanaume virukamito unakuja kujisunda nae huku hata huonekani na kadamnasi ya watu" aliendeleza hadithi zake yule mlevi. Ikabidi Kachero Manu abakie anachekea tumboni hakutaka mazoea nae sana kwa sababu hamfahamu, huku anakunywa maji aliyoagiza wakati anasubiria oda yake ya kuku.
Haikuchukua muda akaaga yule mlevi akaondoka zake kwa mwendo wa kilevi, anapepesuka njia nzima, mezani akabakia Kachero Manu pekee anabung'aa tu. Baada ya nusu saa kuku akawa tayari ameletwa mezani, akaagiza na "Sprite" baridi akaanza kumshambulia kuku kama ana njaa ya ndovu kumla mwanawe. Kila alipokuwa akitazama saa muda ulikuwa unayoyoma kijana anayemsubiria hatokei. Mpaka saa tatu kamili alikuwa hajatokeza bado.
Akiwa bado amezama kwenye mawazo ya yule kijana waliyewekeana nae miadi akashtukia anaguswa begani. "Bosi habari yako, samahani kwa kuchelewa majukumu yaliongezeka pale kazini hata nyumbani sijafika nimeona bora tuonane na wewe kwanza ndio nichome zangu maskani" alijitetea kiustaarabu yule kijana ili asionekane mswahili, mwenye ahadi za mkahawani akiwa na mavazi yake ya kazi.
Kachero akamtoa mashaka, kisha akamkaribisha kitini. Akamuitia mhudumu na kumpa wasaa kijana yule wa kuagiza chochote anachokitaka katika maakuli na mashrabu, mazungumzo yakaanza yao yakafunguliwa rasmi.
Kachero Manu: "Kama nilivyokuambia nina mpango wa kufungua sehemu ya kisasa kama ile yenu pale, hivyo nahitaji kukufahamu kwa undani, huenda nikakupa Umeneja". Alidanganya Kachero Manu apate analolikusudia.
Kijana: "Hamna shida, tena mie nitashukuru ukinipa ajira maana wale hata siwaelewi kuhusu mustakabali wangu".
Kachero Manu: "Kivipi huwaelewi?"
Kijana: "Mfano juzi Ijumaa, waliniambia hawatofungua kwa ajili ni siku ya ibada lakini cha ajabu nina mshikaji wangu yupo jirani pale akanishtua Ijumaa hiyo wamefungua na wanafanya kazi. Ikabidi nije kisirisiri nikathibitisha kweli pamefunguliwa na nikamuona mtu anayaosha magari, nikashangaa sasa kuna nini kinaendelea nyuma yangu".
Kachero Manu: "Inaelekea watakufukuza siku za usoni, sasa huyo mtu aliyefanya Ijumaa bado upo nae au hajaja tena? "
Kijana: "Hajafika tena, ila nilishangaa sana kwa sababu ni rafiki wa Babu mmiliki wa ile "car wash" Mzee Hafeedh Abdallah, ameshawahi kuja nae pale ile wiki iliyopita zaidi ya mara tatu. Hivyo hana hadhi kabisa ya kuosha magari katu".
Kachero Manu: "Labda waliona siku hiyo kuna wageni wengi wa heshima wanaokuja kwenye maombolezo ya msiba, hivyo wanahitaji mtu makini anayejua hata kukicharaza kimombo..!"
Kijana: "Labda maana mie kwa haraka niliyaona magari ya Wabunge si chini ya saba yanaoshwa pale, achilia mbali vigogo wengine"
Mhudumu mara akafika kumletea chakula chake yule kijana. "Bosi nakuja ngoja niende msalani kwanza kibofu kitapasuka, nilindie usalama wa zege langu wasitue inzi maana nina ubao kinyama aisee... " akanyanyuka zake yule kijana kuelekea kuutafuta ulipo msala. Kachero Manu alikuwa na furaha isiyo kifani. Sasa ameshapata mtu wa kumbinya nae ni Meneja wa 'Chops carwash' mpaka watamtoa "Maso Maso" .
"Ananidanganya Ijumaa siku ya ibada hakufanya kazi kumbe hata kijana wao amethibitisha kwa macho yake palifunguliwa" alijisemea Kachero Manu nafsini mwake. Macho yake Kachero yakiwa uelekeo wa msala akimsubiria kwa hamu kijana arejee, ghafla akaona vijana wawili wanaelekea msalani kwa mwendo wa kasi. Akasisimkwa na malaika, hisia zikamtuma hao ni watu wabaya, kama ni kubanwa na haja haiwezekani wote kwa pamoja tena muwe mnakaribia kuingia chooni ndio wajifanye wamezidiwa.
Akaamua kutii hisia zake, Kachero Manu akachomoka nae kwa mwendo wa kupega huku mkono upo kiunoni tayari kwa kuchomoa bastola. Alipokata kupinda korido ya kuelekea vyooni, akamkuta mmoja wao amesimama nje ya mlango wa choo uliofungwa. Yule jamaa alipomwona tu Kachero Manu akaanza kumrushia mvua ya risasi. Lakini alikuwa anapiga ovyo kuonyesha sio mzoefu, hakuna hata moja iliyolenga shabaha. Na hata kama ingelenga shabaha, Kachero Manu daima dawamu, layla wa nahara anavaa fulana maalumu ya kuzuia risasi kupenya mwilini.
Jamaa yule baada ya kuona Kachero Manu ameshachomoa bastola yake akaona isiwe tabu akaruka ukuta na kukimbia zake, akimtelekeza yule mwenzake aliyekuja nae. Mjuba mwingine mle chooni alibaki ameduwaa baada ya kusikia shaba zinarindima nje ya choo akajua kimenuka tayari. Akatoka mkukumkuku nje ya choo huku mkononi ameshika bastola yake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment