Simulizi : Nitakuua Mwenyewe
Sehemu Ya : Tano (5)
Jackline alimwambia Roberto ambaye alitoka kuwafuata vyumbani kwao.
Baada ya kurudi majadiliano yalianza haraka sana juu ya ujumbe huo ulioletwa na Roberto.
Roberto aliitoa simu yake na kuitoa ile chipu aliyoitumia kuwasiliana na Carolina kisha akaiweka nyingine na ile akaiweka kwenye kimkebe chake kisha akakiweka mfukoni.
"Jamani hatuna muda wa kupoteza tunatakiwa tuwahi kuelekea kwenye majengo haya haraka sana kabla hawajafanya lolote."
Jackline aliwaeleza wenzake.
"Imepita hiyo ni utekelezaji tu hapo."
Alijibu Jasmine na kuanza kuvaa raba zake huku Jackline akikihifadhi kwanza kile kisanduku. Walipojiandaa walitoka na kuisimamisha taxi iliyokuwa inapita na kuingia ndani yake.
"Tunaelekea Gezra mara moja."
Jackline alitoa maelekezo kwa dereva Taxi ambaye aliitikia kuashiria kuwa sehemu hiyo anaifahamu. Walitembea kwa mwendo mrefu kidogo kisha walifika karibia na eneo hilo ambapo walimsimamisha dereva Taxi huyo wakamlipa ujira wake kisha wao wakaanza kulifuata eneo hilo lenye majengo hayo chakavu na kama bahati vile waliweza kuliona na ndipo walipogawana majukumu ya kuyafanya kisha kila mmoja akachukua njia yake kuingia ndani bastola mkononi.
KULIKONI HUKO?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA NITAKUUA MWENYEWE TUPATE KUJUA KULIKONI HAPO GEZRA.
Wakiwa wamejibana kwenye vyumba vya majengo hayo mara ilitokea gari likiwa kasi na kupaki kwenye uwanja wa eneo hilo na kisha walishuka vijana wanne wakiwa na silaha zao mikononi wakaangalia huku na kule kisha mlango wa mbele ukafunguliwa akashuka mwanamke mmoja ambaye alionekana ndiye kiongozi wao na kuongoza mpaka ndani ya jengo lile ila kilichowashangaza wakina Jackline na kuwafanya kutoa macho ni baada ya kumuona Robinson akiwa ni miongoni mwa wale vile vidume.
"Hili eneo mmelikagua vizuri? Litafaa kweli bila kutuletea shida?"
Mwanamke yule aliwauliza wakina Robinson swali hilo wakiwa wanaingia ndani na bila kujua hapo hapo mlangoni kwa juu alikuwa kajificha Roberto akiwachora tu.
"Hili litatufaa sana kwani mpaka waje wajue tumemuweka mtu wao hapa itakuwa imekula kwao."
Alijibu Robinson na kuwaongoza wenzake sehemu ambayo wanatarajia kumficha Mustapha.
"Hivi mnafikiri kwa kumteka kijana huyu tutapata kile tunachokitaka kweli?"
Madam Nafiwe aliendelea kuuliza maswali kama hajiamini kwa walichokifanya.
"Mkuu hebu kuwa na imani na kile tunachokifanya kwani kupitia huyu najua tutamnasa mama yake, baba yake, Jackline, Jasmine, Jessica pamoja na wengine wote walioshiriki na bila shaka ndani ya siku nne kama siyo tano tutakuwa tena Brazil tukimalizia shughuli kwa yule dogo msumbufu."
Tom alimhakikishia madam Nafiwe ni kwa namna gani wamejiandaa vizuri na mpango wao.
" Okay vizuri basi wapigie fasta wakina Carolina wamlete huyo kijana maana nasikia kaenda kule TSWANA NIGHT CLUB kukutana na huyo Gift anayedai kufahamiana naye lakini kaangukia pua kwani hajafika yeye wala hiyo simu yake haipatikani hewani."
Madam Nafiwe aliwaeleza wakina Tom kilichomtokea Carolina.
" Mimi nilijua tu kuwa huo ni mchezo na anatakiwa kuwa makini tayari wajanja walishamng'amua yeye ni nani na mbaya zaidi mtoto yule anajiamini sana."
Robinson aliungana na maneno ya madam Nafiwe huku akieleza kinachotakiwa kufanywa na Carolina.
"Kikubwa kazi iende mbele hayo mengine yatafahamika mbele kwa mbele si ni mtu mzima na anajitambua yule?"
Madam Nafiwe alimjibu Robinson huku akionesha kutomjali mtu zaidi ya kufanikisha zoezi lake. Hivyo simu ilipigwa upande wa pili kuwataka wamlete Mustapha kule ili waweze kumpa adhabu na mateso ya maana ilmradi aeleze ni wapi waliko wanaowahitaji.
" Fanyeni haraka jamani, huku baridi ni kali sana bwana na hakikisheni hakuna anayewafuata nyuma yenu."
Nafiwe alitoa maelekezo kwa wakina Carolina.
"NINYI TOKENI HUKO KWA TAHADHARI MUIVIZIE GARI ILIYOMBEBA MUSTAPHA KABLA YA KUFIKA HUKU."
Roberto alimtumia Jackline hiyo meseji wakati yeye akiwa bado pale juu ya ukuta ule ambao umetenganisha korido la kuelekea kwenye chumba walichopanga kumhifadhi Mustapha na lile korido la kuingia eneo la wazi kama vile Resting room.
" OK KUMBE WEWE ENDELEA KUWACHORA HAPO HAPO ILI SISI TUKAUZIME MOTO HUKO HUKO."
Jackline alimjibu kisha wao wakataarifiana wote na kuondoka zao kuifuata njia ambayo watapita waliombeba Mustapha.
Wakina Jackline walifika nje kidogo ya majengo yale na kujificha kwenye vichaka vilivyostawi vizuri na kuelekeza silaha zao barabarani. Na ndani ya muda mfupi ilisikika gari ikija upande wao.
"Jasmine jiandae hilo gari bila shaka ndiyo lenyewe."
Jackline alimtaarifu Jasmine ambaye alikuwa mbele yao kidogo ambaye alipewa jukumu la kuhakikisha anazitungua tairi za gari hilo na ilifanywa hivyo kutokana na shabaha aliyonayo Jasmine.
"Pyuuu pyuuuuuuuuuu.........."
Ulikuwa ni mlio mkubwa wa matairi ya gari hiyo aina ya Toyota Noah, hiyo ikiwa ni kazi ya Jasmine ambaye alitumia silaha yake aina ya tigashoot 101 yenye kiwambo cha kuzuia sauti kusikika huku lenzi yake ina uwezo mkubwa sana wa kukisogeza kilicho mbali na kufanya chochote kile anachokitaka huku ikiwa na bomba mbili za kutema risasi.
Dereva ilibidi ashuke chini kuangalia ni nini alikikanyaga mpaka tairi zote kupiga mlio huo uliopelekea upepo kwisha.
"Suka umebaini nini kwenye hili kwanini imekuwa hivi?"
Carolina aliuliza akiwa na tochi yenye mwanga mkali sana akisaidiana na dereva kumulika eneo lile kuona kama wanaweza kuona chochote cha kusaidia lakini hawakuweza kuona chochote kile ndipo Carolina kama alishtuka hivi alirudi mpaka kwenye gari na kumulika tairi la mbele.
"Shabash....."
Alijisemesha mwenyewe kwa ambacho alikiona kwenye lile tairi.
"Kuna nini madam?"
Dereva aliuliza baada ya kusogea hapo na kumkuta Carolina akitamka neno hilo la mshangao.
"Angalia hapa."
Carolina alimuonesha sehemu iliyotobolewa na hivyo kubaini kuna mchezo wamefanyiwa ndipo wakaona waangalie na matairi mengine kama yana matundu hayo waliyoyaona kwenye tairi la kwanza. Lakini kabla hawajafanya lolote walijikuta wakiwekwa mtu kati kwa kupigwa na vitu vizito vichwani kwao na kuwafanya kupoteza fahamu.
"Haraka jamani mshusheni chini huyo dogo huko ndani ya gari tuna muda mchache wa kuwepo eneo hili."
Jackline alitoa maagizo hivyo wakina Titiana walifungua mlango na kumtoa Mustapha ambaye alikuwa kafungwa pingu mikononi na miguuni huku akiwa kazibwa mdomo na soltepu nyeupe iliyomfanya ashindwe kufanya lolote kama kupiga kelele za kuomba msaada.
Walimfungua kamba na ile soltepu na ndipo alipopigwa na butwaa mara baada ya kuwaona wakina Jackline wakiwa kwenye sura za kazi.
"Dada Jackline !!!!! Hee na wewe dada Jasmine uko hapa? Mmerudi lini kutoka Tanzania?"
Mustapha alijikuta akitokwa na maneno baada ya kuwaona wakina Jackline.
"Ni baada ya kutengwa na familia yako kutokana na kupotea kwako Mustapha hasa mama yako ilibidi tuje kuupigania uhai wako kabla hujafanywa lolote, tumefika leo."
Jessica alimjibu Mustapha huku akisogea pale kutoka porini akiwa na tochi mkononi.
"Kutengwa na familia yangu? Dada Jessica na wewe uko hapa? Na mlijuaje kama mimi niko huku?"
Mustapha aliendelea kuuliza maswali yake.
"Utapata majibu ya maswali yako yote muda ukifika kwa sasa bado tuna kazi ya kufanya."
Jessica alihitimisha kwa kusema hivyo kisha akaungana na wakina Jackline kuwapiga pingu Carolina na dereva yule kisha wakarudi zao porini na kutulia. Jackline akachukua simu na kumtumia ujumbe Roberto.
" Dogo huku kazi kwisha hivyo unaweza kuondoka hapo haraka sana kabla hawajakushtukia tulipo hapa si mbali sana kutoka hapo utaiona gari aina ya Toyota Noah njiani angalia chini kuna alama tumeichora ifuate."
Roberto alipoisoma meseji haraka sana alishuka kwa tahadhari pale juu na kuanza kuondoka eneo lile.
" Usivute hatua nyingine kwenda mbele au nyuma tulia hivyo hivyo mwanaharamu wewe."
Sauti ilitoka nyuma kwa Roberto na kumfanya kushindwa kuvuta hatua mbele na kujikuta jasho likipishana mwilini japo kulikuwa na baridi kali eneo hilo.
Hivyo akajikuta akienda chini na kupiga magoti.
" Unajidai jeuri kufuatilia mambo yasiyokuhusu siyo?"
Aliulizwa swali na mtu aliyemfuata pale alipokuwa, Roberto aligeuka nyuma kuangalia mtu huyo yuko na wakina nani japo kulikuwa na giza lakini hakuweza kuna mtu mwingine yeyote. Hivyo hakuona sababu ya kutumia nguvu wakati huo hivyo akajipanga kumkabili adui wake kwa namna ya kipekee.
"Nakuuliza tena umefuata nini hapa na wewe ni nani?"
Yule mtu alimuuliza tena Roberto akiwa anamsogelea pale alipokuwa. Lakini hakumjua anayemchezea na vimaswali vyake ni nani? Roberto alimuangalia usoni jamaa yule kabla ya kumjibu na alichokifanya ni kumtemea mate usoni.
" Unafanya nini wewe mjinga unaweza kunitemea mate yako machafu mimi............"
Lakini kabla hajafanya chochote alishtukia alikutana na mchanga machoni kwake uliomfanya aangue kilio kutokana na maumivu ya macho yaliyotokana na mchanga kuingia machoni.
"Macho yangu, macho yangu jamani nisaidieni mwenzenu....."
Alipiga kelele kuomba msaada na wakati huo Roberto aliinuka na kutokomea gizani.
Kelele zile ziliwashtua wakina Robinson kule ndani na kutoka haraka zilikotokea kelele hizo. Walifika nje na kumkuta mwenzao akiwa anagalagala chini kwa maumivu ya macho na mikono ikipishana machoni.
"Umepatwa na nini wewe?"
Nafiwe alimuuliza mlinzi huyo baada ya kumfikia.
"Madam tumebainika, kuna mtu alikuwepo ndani ya jengo na akiwa anatoka nje niliweza kumuona ndipo nikamfuta kumkabili kabla ya kufika popote hilo nilifanikiwa kwani alitii amri ya kuweka mikono juu hivyo nikabaini ni mchovu tu haina haja ya kuwaiteni ninyi kumbe nilijidanganya akanitaimu na kunimwagia mchanga machoni na kukimbia."
Alitoa ufafanuzi wake mbele ya wakubwa wake.
" Kelele wewe nyang'au mkubwa usiye na haya, hivi unafikiri maneno yako ya kijinga nitayakubali kijingajinga hivyo siyo? Na kwa kuwa umesababisha adui yetu atoroke mikononi mwetu hauna sababu ya kuendelea kuishi kwani wewe ni askari mzembe. Robinson muongezee safari yake huyo akawasalimu wote walio kuzimu."
Madam Nafiwe alionyesha roho yake mbaya kwa mlinzi ambaye alitakiwa kupatiwa msaada lakini yeye akaamuru auawe na Robinson alipatiwa jukumu hilo ambalo hakulilazia damu akamsambaza ubongo wake pale pale na kisha wakamvutia ndani ya jengo lile na kuondoka zao.
"Halafu na wakina Dorine (Carolina) wanacheza na akili zangu haiwezekani mpaka sasa wawe hawajafika."
Nafiwe aliendelea kuwaka baada ya Dorine aliyejitambulisha kwa Roberto na Hotel aliyofikia kama Carolina kutotokea mpaka muda huo.
"Inawe........." Tom kabla hajamalizia kuongea alikatisha maneno yake baada ya kuliona gari mbele yao.
"He gari si hilo hapo mbele?"
Aliwaambia wenzake waangalie gari lao ambalo lilikuwa mbele yao.
"Simamisha gari dereva hapa hapa kwanza."
Nafiwe alimuamuru dereva kulisimamisha gari huku yeye akiichomoa bastola yake na kuishika mkononi huku na wakina Tom na wenzake wakifanya hivyo hivyo. Baada ya kushuka walilifuata lile gari kwa tahadhari kubwa sana na baada ya kulifikia walikutana na milango ikiwa wazi huku matairi yakiwa hayana upepo na chini yake kukiwa na kamba ambazo zilitumika kumfungia Mustapha pamoja na soltepu zilizotumika.
"Washenzi wameshajua uwepo wetu hapa Namibia, na si wengine hawa kwa vyovyote vile ni wakina Jackline tu hawa Madam tuna kazi ya ziada kuhakikisha Dorine anapatikana."
Tom alimwambia Nafiwe juu ya hisia zake kwa kilichotokea hapo.
"Liacheni hilo tuondoke zetu tukajipange upya maana kazi imerudi mwanzo kabisa."
Madam Nafiwe aliwaambia wenzake na kuondoka zao eneo hilo na kurudi maskani kujipanga upya.
****
Mzee Jerome alikuwa anatoka nyumbani kwake kuelekea kwenye majukumu yake mida ya asubuhi akashtushwa na honi iliyopigwa nje ya geti hivyo aliuendea mlango akachungulia nje kupitia nafasi ya mlango hakuona chochote ndipo alipoona afungue mlango na kuchungulia nje. Hakuamini macho yake kukutana uso kwa uso na mtoto wake Mustapha.
"Hee Mustapha mwanangu !!!"
Mzee Jerome alijikuta akitaja jina la mtoto wake huku akiangalia nyuma yake kuna nani kaongozana naye.
"Naam baba ni mimi mwanao."
Alimjibu baba yake huku wakikumbatiana kwa furaha.
Mzee Jerome alijitoa kwa mwanaye na kurudi ndani huku akipiga makelele.
"Mwanangu Mustapha amerudi jamani, amerudi, amerudiii mke wangu njoo umuone mwanao."
Hali ile ilimshangaza sana Mustapha akiwa haamini anachokiona kwa baba yake kwa anayoyafanya ambayo hakuwahi kuyaona hapo kabla na ndipo mama yake alipotoka nje kuhakikisha anachokisikia kwa mume wake.
Hakuamini macho yake baada ya kumuona mwanaye Mustapha.
Kutokana na kupata furaha iliyopitiliza ilimfanya Bi Elizabeth kuanguka kwa mshtuko.
"Mama, mamaaa, maaamaaa......... Noooooooo wake up ma mum.."
Mustapha alijikuta akipiga kelele huku akikimbia kumuwahi mama yake huku mzee Jerome akiwa naye kapigwa na butwaa pale pale alipokuwa kasimama akiwa hajui afanye nini, amfuate mke wake au afanye nini akaishia kuduwaa tu.
Hivyo ikabidi Mustapha ambebe juu juu mama yake na kumkimbiza mpaka chini ya mti wa kivuli ulio kwenye bustani ya maua na kuchukua kipepeo kisha kuanza kumpepea.
JE, NI NINI KITAENDELEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA MPENZI MSOMAJI WA HADITHI YETU HII YA NITAKUUA MWENYEWE.
Baada ya kumpeleka Mustapha kwao wao hawakutaka kuonesha sura zao hivyo waliondoka na kuelekea kule kule Gezra forest ambako waliwafunga wakina Dorine ambako walimuacha Titiana na Roberto kuhakikisha kuwa iwapo watazinduka wawaanzie suluba ya maana mpaka waongee wanayemfanyia kazi na wapi anakopatikana. Kabla ya kuelekea huko porini Jackline aliona warudi kwanza Hotelini kukifuata kile kisanduku ambacho Roberto alikichukua chumbani kwa Dorine.
"Unajua nini, tupitie kwanza Hotelini tukakichukue kile kisanduku kisha tuelekee porini au mnaonaje?"
"Ni kweli kabisa kwanza mimi njaa imeuma toka tulipopiga msosi jana jioni, inabidi asubuhi hii tule kabisa then tuwabebee na wenzetu mishe nyingine ziendelee."
Jessica alijibu haraka haraka kama vile aliisubiri kwa hamu kubwa kauli hiyo itamkwe.
"Haina tabu tufanye hivyo tu kikubwa tuwe vizuri si mnanajua usiku wa leo inawezekana ukawa ni wa kikazi zaidi."
Jackline alimuunga mkono Jessica kwa wazo lake la kupiga chakula kabisa kabla ya kurudi Gezra forest. Walifika Hotelini wakala chakula cha asubuhi ambacho wenyewe wanakiita kifungua kinywa kisha wakachukua vitu na vyakula kama walivyokubaliana kisha wakatoka.
"Jamani mnaonaje tubadilishe utaratibu badala ya kutumia gari la kuendeshwa na mwenye gari twendeni tukakodi gari ambayo tutaitumia kwa siku zote ambazo tutakuwa hapa Namport ambalo tutakuwa nalo huru kuliko haya ya kulipia kila siku."
Jasmine alitoa pendekezo juu ya kubadili mfumo wa usafiri kwa ajili ya matumizi ya kipindi chote hicho.
" Ni kweli lakini kwanini tusiifuate gari yetu kwa mzee Jerome?"
Jessica alikubaliana nao lakini yeye akaona ni vyema walifuate gari lao lililoko kwa mzee Jerome kuliko kuendelea kupoteza hela kukodi magari ya Makampuni.
"Lile tutalifuata tukimaliza misheni yetu wasifikiri sisi tunawategemea sana wao na hata kutuona kama vile tuna magunia ya mikosi ambayo tuliwapelekea kwao."
Jackline alilikataa wazo la kulifuata gari kwa mzee Jerome Whistle hivyo wakakubaliana kwenda kukodi kwenye kampuni moja maarufu ya kukodisha magari ambayo hukodisha magari yao kwa watu tofauti tofauti. Walifika pale kwenye hiyo kampuni na kuchagua mashine moja matata sana inayokwenda kwa jina Land Rover New Model (Pilotgear) ambayo ni Six yenye milango minne nyeusi, baada ya taratibu zote kukamilisha waliondoka nalo na safari hii nyuma ya usukani alikuwa Jessica baada ya mguu wake kupona vizuri.
"Hili dude naliita kiboko yao lazima wanga wote wakae aisee."
Jessica aliisifia gari hili akiwa analitoa yard na kuikamata barabara ya kuelekea Gezra Forest' ambako walikuwako wakina Roberto.
"Hapa itatusaidia sana kwa safari zetu za hapa na pale siyo tuna mishe zetu za siri tunamkodi mtu tusiyemjua Je naye ni adui yetu?"
Jackline alimuunga mkono Jessica kwenye kuipamba gari hiyo. Baada ya mwendo mrefu waliwasili porini na kuwakuta wakina Dorine wakiadhibiwa na Roberto.
" Narudia tena wewe ni nani na kwanini ulianza kutufuatilia pale restaurant ya The Camel Hotel?"
Roberto alimuuliza huku akiwa anampiga kwenye vidole vya mguuni na kifaa ambacho upande ni kisu na upande mwingine ni kinyundo.
"Mtaniua tu mimi sijui lolote na pale hotelini nilikuwa mteja na sikuwahi fikiria kuwafuatilia hata siku moja jamani."
"Kumbe mbishi eee vipi kuhusu yule dogo mliyekuwa naye kwenye gari?"
Titiana alimuuliza huku akiwa anasaga magome fulani ya miti.
"Kiukweli mimi nilikuwa natoka Hotelini ndipo nikakutana na kijana mmoja ambaye aliniambia niambatane na huyu dereva mpaka huko ambako sikujui na nilipojaribu kukataa akanitishia kuniua hivyo nikawa sina jinsi."
Dorine aliendelea kujitetea muda huo yule dereva alikuwa kalalia damu kwenye majani kuashilia kuwa alikuwa kauawa tayari.
" Anasemaje huyo mrembo?"
Jackline aliingilia mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea kati ya Roberto, Titiana na Dorine.
" Anazingua huyu maana kila analoulizwa anakataa."
Titiana alimjibu Jackline.
"Vizuri hebu na mimi niachieni niweze kumhoji."
Jackline aliwaomba wamuachie na yeye.
"Enhh mrembo naomba unieleze ukweli wako wote wewe ni nani na kwanini unatufuatilia?
Na unamfanyia kazi nani? Ni hayo tu na ukitaka kujua jina langu naitwa Jackline, huyu ni Roberto wale pale ni Jasmine na Jessica. Nakusikiliza sasa."
Jackline alimaliza na kumuachia ulingo Dorine.
" Dada yangu mimi ni mwandishi wa Habari tu huku nimeingizwa mkenge tu na watu nisiowajua."
Alianza Dorine.
" Naomba ujibu maswali nilivyokuuliza tafadhali kabla sijayaharibu mapokezi yako."
"Dada yangu mtaniua tu mimi sijui lolote."
Aliendelea kugoma kuongea ukweli.
"Vizuri inawezekana ni kweli tunakuonea mrembo."
Jackline aliongea huku akichukua kisanduku kutoka kwa Jasmine.
"Enhh hiki kisanduku unakifahamu? Au hiki kikaratasi?"
Aliviangalia vitu vile mara mbili mbili huku akishusha macho chini kwa aibu.
"Sivijui na wala sijawahi kuviona popote dada yangu"
Alibisha kwamba havijui vitu hivyo.
"Ni kweli huvijui vitu hivi?"
Jasmine aliingilia kati.
"Kweli tena sivijui ndugu zangu."
"Vizuri."
Jackline alijibu huku akikifungua kile kisanduku kwa kutumia lundo la funguo alilokabidhiwa na Roberto ambaye naye alitoa kwenye mifuko ya koti la Dorine. Baada ya kulifungua walikutana na picha zao wote isipokuwa za Roberto na Titiana huku zikiwemo za Dr Hans Murray na Dr Abbas Mukesh kilichowaacha midomo wazi ni baada ya kuzikuta picha za mama yake Roberto na Dr Ramadhan zikiwa na alama ya X hiyo ni kuashiria Dorine ni mtu hatari sana ambaye amekuwa akimsaidia kwa siri sana Santana kuwatafuta wabaya wake na kuwaangamiza kwa siri kubwa. Na hapa ndipo walipobaini kuwa huyu ndiye aliyehusika na vifo vya watu aliowawekea alama ya X.
"Haya kila kitu kiko hapa kuanzia nyaraka zako za utambulisho wako mpaka mambo uliyoyafanya kwa hiyo tunatoa nafasi ya mwisho kwako kujieleza kabla hatujafungua bucha."
Roberto akiwa anasaga meno kwa hasira baada ya kuiona picha ya mama alimsogelea Dorine na kumuwekea kwenye jicho moja unga uliokuwa unasagwa na Titiana. Kutokana na maumivu aliyoyapata kutokana na Unga ule kupenya vilivyo jichoni kwani inavyoonekana mti uliotumika kuzalisha Unga ule unaasili ya pilipili kwani hata wao pale walianza kupiga chafya mfululizo.
"Aaaaghhh jicho langu jamani hakukuwa na haja ya kunifanyia haya mimi ningeongea tu."
"Fanya haraka kabla sijaanza kula kidole chako kimoja baada ya kingine."
Roberto alimsogelea na kumvuta masikio yake huku chafya na machozi vikiwa vimembana vilivyo Roberto.
"Nitaongea, nitaongea jamani, Santana ndiyo chanzo cha haya yote jamani, mimi jina langu halisi naitwa Dorine Conrad Wangey nina asili ya Marekani lakini nimekuwa nikifanya kazi na makundi mbalimbali ya Kijasusi na Kimafia bila kujulikana kutokana na Elimu ya Sayansi ya binadamu pamoja na Mahusiano ya Kimataifa ambayo hunifanya kuingia sehemu yoyote kuomba kazi kama kuna suala nalifuatilia. Na ndiyo maana ilikuwa rahisi kuingia kwenye hospitali ambayo alilazwa mama yake Roberto na kufanikisha mauaji yangu nikiwa nimefanya kazi pale kwa miezi miwili kwanza nikisoma mazingira. Na pale nilitumia kitambulisho chenye jina la Suzanne ambalo lilikuwa feki na baada ya kufanikisha hilo na kupokea malipo yangu kutoka kwa Santana nilikimbia huku kujificha kwa ndugu yangu Nafiwe ambaye unaweza kusema ni ndugu na mara nyingi amekuwa akiwaambia watu hivyo lakini si kweli, pia mimi ndiye niliyechora mchoro mzima wa mauaji ya Dr Ramadhan yaliyofanywa na wakina Nafiwe baada ya kumkosakosa Dr Abbas pale KING'S MEDICARE CENTRE aliyeushtukia mchezo mzima. Ni hivyo tu ndugu zangu ni umaskini tu umeniletea yote haya naombeni msiniue."
Alihitimisha kusimulia Dorine.
Muda huo Roberto alikuwa akilia tu baada ya kuisikia simulizi iliyochukua uhai wa mama yake,ilibidi Titiana afanye kazi ya ziada kumtuliza mpenzi wake.
" Vizuri kazi yako iliyopita ni kutufikisha kwa ndugu yako Nafiwe ndipo hatma ya maisha yako itakapofahamika, sawa?"
Jasmine alimsogelea karibu Dorine na kumweleza jukumu lillilo mbele yake.
"Jamani mimi nina hasira na huyu Mwanaharamu aliyeyachukua maisha ya mama yangu naombeni ruhusa ya kummaliza huyo Nafiwe tutampata tu iwe isiwe lakini siyo kuendelea kumuona machoni kwangu huyo Shetani."
Roberto aliongea hayo huku akiiweka sawa bastola yake ambayo alishaikoki tayari wakati wakina Jackline wakijaribu kumzuia walichelewa kwani alishaifyatua iliyomkuta kichwani.
JE, NI NINI KITATOKEA?
"Mdogo wangu umeuaaa? Umemrahisishia kifo huyu mimi nilitaka afe taratibu kwa mateso makubwa ambayo yangemfanya ajutie kwa maovu aliyoyafanya ila ndiyo hivyo tena umeshindwa kuzuia hasira zako."
Jackline alimlaumu Roberto kwa alichomfanyia mtu ambaye walitegemea kumtumia kama daraja la kuwafikia wabaya wao.
" Dada Jackline nakuhakikishia kuwakamata hawa Washenzi mmoja baada ya mwingine kwa kutumia Weledi wangu lakini si kumtumia Nyang'ao mlaaniwa na kama nimewakosea naombeni mnisamehe lakini Roho yangu saafi kwa sasa japo bado waliokuwa nyuma yake."
Roberto alimjibu Jackline na kumhakikishia kuwa kazi ndiyo imeanza na ameahidi kuwanasa mmoja baada ya mwingine na katika hilo hakukuwa na la kufanya zaidi ya kuangalia mbele.
" Usihofu Roberto wala kujutia ulichofanya juu ya adui yako kwani hata ningekuwa mimi nisingevumilia hata kidogo kumuona adui mbele akivimba ilhali yeye mwenyewe kakiri kuhusika na mauaji ya mama. Pia tuliongea vile kwa kuangalia mafanikio ya haraka lakini kwa maneno yako tu tunaamini tutafikia tageti yetu."
Jasmine alimuondoa hofu Roberto na kumuahidi kushirikiana kwa kila kitu na hakuna haja ya kuleta mgawanyiko baina yao kisa tu hiki kilichotokea. Hivyo waliinuka na kukumbatiana pamoja kuashiria kuwa jeshi linaanza upya kisha Roberto na Titiana walikabidhiwa chakula wale huku wakina Jackline waliichukua miili ya wakina Dorine na dereva wake na kuipeleka kwenye kichaka kilichokuwa karibu na barabara kisha walirudi.
"Roberto mnaonaje muendelee kupata chakula garini huku tukipiga hatua mbele?"
Jackline aliwauliza wakina Roberto kama kuna uwezekano wa wao kupiga chakula kwenye gari ili sehemu hiyo waondoke mara moja.
"Why not?' inawezekana kabisa."
Alijibu Titiana na kuinuka kisha kumvuta mkono Roberto aliyekuwa bado kainamia chakula na kisha kuliendea gari. Waliingia na safari ilianza mara moja.
"Turudi Hotelini kwanza tukavute muda pale mpaka itakapofika usiku ndipo tuingie mtaani kuendelea na oparesheni yetu ya mtaa kwa mtaa."
Jackline aliwaelekeza wenzake wanaenda wapi muda huo. Kila mmoja alimuunga mkono na Jasmine alitoa pendekezo lake wakiwa pale Hotelini.
" Mnajua nini, tukifika pale inabidi turudi tena kwenye chumba cha mpuuzi Dorine tunaweza ambulia chochote na pia kama itawezekana itatubidi tukaonane na 'Operator Manager' wa kitengo cha Security tuweze kuzipitia zile CCTV Camera za chumba kile lazima tutapata pa kuanzia."
"Kweli kabisa hiyo yenyewe ila sijui kama watakubali kuturuhusu kuingia mimi nafikiri kuwa tunatakiwa kuharibu mfumo wa CCTV kama itatulazimu kufanya hivyo but nina uhakika kile chumba kitatupa majibu ya mahitaji yetu."
Jasmine aliunga mkono hoja ya Roberto lakini akatoa maoni yake yaliyopingana na Roberto. Waliwasili 'The Camel Hotel' na kuingia kwenye vyumba vyao na baada ya kuoga walikutana Restroom na kuanza kujadiliana ni kwa namna gani walianze zoezi lao kwani muda huo tayari ilikuwa ni Magharibi tayari.
Baada ya majadiliano hayo ndipo walikubaliana kuwa Roberto na Jasmine waende kwenye chumba cha Dorine huku Jackline, Jessica na Titiana wao waelekee Restaurant kuusoma mchezo kwa kila sura itakayokuwa mle ndani. Walitawanyika na kuelekea sehemu zao walizokubaliana. Baada ya kufungua mlango wa chumba namba 107 kwa kutumia funguo walizozichukua kwa Dorine ambaye tayari ni marehemu na kuingia ndani humo moja kwa moja walianza kukikagua chumba kile. Wakiwa wanakikagua kuna utofauti ambao waliuona mle ndani, kwanza kitandani kulikuwa na laptop ambayo inaonesha kuna mtu alikuwa akiitumia kwani haikuwa imefungwa pia ndani ya kabati kulikuwa na kimkoba cha kike ambacho baada ya kukikagua walipata hofu kidogo kama ni cha Dorine au kuna mtu mwingine ndani ya chumba hicho.
"Jasmine tutoke humu nahisi kuna mtu yuko ndani ya chumba hiki kutokana na mazingira ninayoyaona na kama sikosei anaweza kuwa katoka nje kwa muda."
Jasmine hakujibu kitu zaidi alimpa ishara ya kukikagua chumba kwanza kabla ya kutoka ndipo Roberto aliingia maliwatoni huku Jasmine aliangalia uvunguni na maeneo mengine ambayo alihisi anaweza kuona chochote lakini wote hawakuona chochote hivyo waliamua kutoka zao.
"Hapa tunatakiwa kubana sehemu tuchunguze ni nani alikuwa humu ndani."
Jasmine alimwambia Roberto huku akiufunga mlango.
"Ni kweli lakini pia ngoja nimpigie simu Jackline kumtaka awachunguze watu waliomo Restaurant."
Roberto alimjibu Jasmine.
"Okey fanya hivyo na mimi ngoja nikaifanye kazi yangu kwa mhudumu wa mapokezi."
Basi kila mmoja alifanya shughuli yake muda huo huku Roberto akimpigia simu Jackline.
"Dada Jackline chumba namba 107 kina mtu alikuwa mle ndani na ninahisi katoka mara moja hivyo jaribu kuwachunguza watu walio humo mlimo ninyi..."
"Hebu ngoja kwanza Roberto nakupigia sasa hivi."
Jackline alimkatisha Roberto baada ya kumuona dada mmoja ambaye alikuwa anakunywa juisi lakini baada ya kutazamana na Jackline dada huyo aliinuka na kutoka haraka nje ya Hotel na kuingia kwenye Taxi ambayo Jackline aliiona naye alikimbilia gari lao na kuanza kuifukuzia ile taxi. Na kwa kuwa giza lilikuwa limeanza kushika kasi haikuwa rahisi kwa watu waliokuwa ndani ya Taxi ile kujua kama nyuma yao kuna gari inawafuatilia. Taxi ile ilitembea na kutoka nje ya mji na kuelekea sehemu moja ambayo ni kama kijiji fulani hivi na huko gari liliingia ndani ya jengo moja lilionekana si la mtu wa mashaka kwani lilikuwa ni la kisasa zaidi na baada ya kufika dada yule alishuka akamlipa ujira wake kisha yeye akaingia zake ndani na geti likafungwa na ile taxi ikageuka na kuanza kurudi. Jackline akapiga hesabu akaona hakuna jinsi zaidi ya kumsimamisha dereva Taxi huyo hivyo akashuka na kuipiga mkono bila shaka gari ilisimama kabla dereva hajajua ashuke au ashushe kioo aongee na msimamishaji alishtukia tu mtu kashaingia ndani ya gari lake.
"Habari yako mpambanaji?"
Jackline alianza kwa kumsalimu dereva huyo.
"Nzuri dada yangu lakini mimi siyo mpambanaji."
"Hujanielewa maana yangu, mpambanaji ni yeyote anayepigania haki yake iwe ni chakula, uchumi au chochote kwa njia halali au siyo halali."
"Okay hapo mimi niko wapi?"
"Unataka uniambie kuwa kupitia hii Taxi huingizi chochote?"
Jackline alimtupia swali dereva huyo ambaye alionekana kuwa na mashaka hivi.
"Naingiza."
"Sasa hiyo ni nini?"
"Okay tuachane na hayo naomba nikusaidie dada yangu."
Dereva Taxi huyo alimkatisha Jackline ambapo alitaka kumsaidia.
"Huwezi kunisaidia wewe tatizo langu."
"Hee sasa kama siwezi kukusaidia kwanini umenisimamisha?"
Dereva huyo aliongea kwa kufoka kidogo kutokana na maneno ya kuudhi ya Jackline.
"Unaongea sana eee!!!"
Jackline aliongea hayo huku akiwa kaielekeza bastola yake sikioni kwa dereva Taxi huyo ambaye baada ya kuona kitu cha baridi kikigusa sikio lake alichanganyikiwa.
"Dada yangu kwa utani wewe umekubuhu aise."
"Unasemaje wewe?"
"Naomba unisamehe dada yangu."
"Naomba unisikilize vizuri mimi si mtu wa kawaida hata kidogo na ndiyo maana nimekufuata hapa bila wewe kujua. Wewe unafanya kazi na wahalifu huku ukijidai dereva Taxi."
"Hapana dada mimi ni dereva Taxi kabisa."
"Kelele !!!! yule uliyemleta huku ni nani na hii nyumba ni ya nani?"
"Hapo ni moja ya nyumba ya Tajiri mmoja mwanamke anayekimbiza kwa sasa hapa Namibia anaitwa Nafiwe."
"Ohhh vizuri unaweza kunikutanisha na huyu mfanyabiashara au ukanipa mawasiliano yake?"
Jackline alimuuliza dereva huyo.
"Huwezi kuonana na huyu Tajiri kirahisi hivyo."
"Okay vizuri naomba simu yako haraka."
Dereva huyo alitoa simu yake na kumkabidhi Jackline ambaye aliikagua na baada ya kukutana na majina ambayo aliyatilia mashaka aliiweka mfukoni kisha alimtaka ashuke garini huku naye akifanya hivyo baada ya kushuka.
"Haya changanya miguu haraka."
Kusikia hivyo tu dereva hakutaka kupoteza muda alianza mbio japo haikuwa bahati kwake kwani Jackline alimtandika risasi ya mgongo na kisha alirudi ndani ya gari na kuipiga namba ya Jessica.
"Jessica chukua bodaboda hapo njoo eneo moja hapa (huku akimulika kama ataona utambulisho wowote wa eneo hilo ndipo alikiona kibao kilichoandikwa 'White Color Supermarket'") kuna kibao cha 'White Color Supermarket' pembeni yake utanikuta."
****
Baada ya kupigwa na upepo wa kutosha Bi Elizabeth alipata fahamu na muda huu aliungana na familia yake sebuleni kutaka kujua ni nini kilimtokea Mustapha mpaka kufikia kutorudi nyumbani kwa muda wote huo.
"Mwanetu ulipatwa na nini mpaka kutoonekana kwa kipindi chote hiki?"
Mzee Jerome alimuuliza mtoto wake kwa niaba ya mke wake na Victor.
"Ni kweli kabisa kaka tuambie maana kuna kutoelewana humu ndani."
Victor alishindilia msumari kwenye swali la baba yao.
"Baba, mama na mdogo wangu Victor niweze kumshukuru aliyejuu kwa kuniweka hai mpaka leo hii, lakini kifupi ni kwamba nilitekwa na watu ambao wanawatafuta wakina Jackline."
"Unaona mume wangu si nilisema, si nilisemaaa? Yako wapi sasa yaani h....."
"Mke wangu hebu subiri amalizie kwanza hayo mengine ya nini?"
Mzee Jerome aliamua kumkatisha mke wake baada ya kuona anaingiza vitu vingine kabisa.
"Mwanangu endelea ikawaje?"
Mzee Jerome alimtaka Mustapha aendelee kusimulia mkasa wake.
"Hivyo baada ya dada yule ambaye aliniteka akiwa kama mteja wetu pale dukani kwetu alikwenda kunipeleka kwenye nyumba moja ambayo ilikuwa kama sehemu ya kuhifadhia vyuma chakavu, alinifungia kwenye chumba kimojawapo na humo kulikuwa na kila aina ya uchafu huku kila siku asubuhi na jioni nikitandikwa bakora za maana huku maji yenye barafu yakimwagwa mwilini mwangu. Na waliniambia kuwa nikiwapa ushirikiano kwa kutaja uliko wewe baba na wakina Jackline ndipo wataniachia lakini kwa upande wangu sikuwa tayari kueleza hayo nilikuwa tayari kupoteza maisha baba. Kuna kipindi walikuja watu wengine hasa dada mmoja hivi ambaye sura yake si ngeni sana ambaye alikuwa akinipiga sana (huku akiwaonesha vidonda vilivyokuwa mgongoni na miguuni) kitu ambacho kilimfanya azidi kupoteza matumaini ya kuishi."
"Pole sana mwanangu yaani ulikuwa tayari kufa kuliko kuyataja mashetani?"
Bi Elizabeth aliendelea kuonesha chuki ya wazi kwa wakina Jackline.
"Mama hebu tulia basi mbona hivyo?"
Victor aliona mama yake kazidi akaamua kumtuliza.
"Mama kuna nini mbona naona kama kuna kitu kiko moyoni mwako?"
Mustapha alimuuliza mama yake.
"Hana lolote mama yako, unafiki tu na roho mbaya imemjaa hapo."
Mzee Jerome alimjibia kitu kilichomfanya asimame na kuondoka zake kuelekea chumbani kwake.
"Okay hivyo baada ya kuona kama hakuna mafanikio kwenye kunibana waliamua kubadilisha eneo la kunitunza bila shaka waliamua kutafuta sehemu ambayo hata wakiniua haitawapa tabu kunificha lakini hamuwezi amini Ukuu wa Mungu ulionekana pale kwani hata walikotokea sijui si wakanisaidia na kisha kunileta mpaka hapo nje kisha wao wakaondoka zao na nilipojaribu kuwataka waingie ndani walikataa wakaondoka zao."
"Pole sana mwanangu kwa yote uliyofanyiwa kikubwa Mungu kakuokoa kupitia kwa hao waliokuokoa ila hujasema ni wakina nani?"
Mzee Jerome alimpa pole na kisha kumtaka awataje ni wakina nani waliomuokoa.
"Si wengine bali ni wakina Jackline."
"Unasemaje Mustapha, wakina Jackline ndiyo waliokuokoa? Au umechanganyikiwa?"
Mzee Jerome hakuamini alichokisikia.
"Ndiyo hivyo baba, kwani hamjui kama wako hapa mjini?"
Mustapha alimtupia swali baba yake.
"Acha tu mwanangu wala sijui nisemeje juu ya hawa mabinti ambao mama yako hata kuwasikia hataki kabisa."
Mzee Jerome aliamua kufafanulia Mustapha.
"Wamekosa nini mpaka awachukie hivyo?"
"Tuachane na haya kikubwa umerudi tunamshukuru Mungu kwa hilo, hili la mama tuachane nalo watalimaliza wenyewe."
Mzee Jerome aliinuka na kumfuata mke wake ndani huku Mustapha na Victor nao wakibaki sebuleni kucheza games.
"Unawafahamu waliomuokoa mwanao?"
Mzee Jerome alimuuliza Bi Elizabeth baada ya kumkuta chumbani akiwa ananyoosha nguo zao.
"Hata nikijua itasaidia nini kwa upande wangu kikubwa mwanangu karudi salama nashukuru."
Bi Elizabeth alimjibu bila kumtazama usoni akiwa bize na nguo zake.
"Ila mke wangu una roho mbaya sana wewe maneno gani hayo? Na siku utakayojua kuwa maadui zako ndiyo waliomuokoa mwanao sijui utasema nini?"
Mzee Jerome Whistle aliongea hayo huku akiinuka na kutoka nje ya chumba hicho baada ya kuona hakuna ushirikiano wowote baina yake na mke wake.
" Sasa unakwenda wapi mume wangu si uniambie ni wakina nani hao?"
Bi Elizabeth alimkimbilia mume wake na kumshika mkono kumzuia kuendelea na safari akimtaka arejee chumbani amwambie ni wakina nani hao waliomuokoa Mustapha. Lakini mzee Jerome Whistle hakuwa tayari kurejea tena chumbani badala yake alimwambia kuwa mtoto wake atamwambia yeye anataka akapunge upepo nje, kitendo kilichomfanya Bi Elizabeth kuishiwa pozi na kurejea chumbani akiwa anajisugua vidole vya mikono huku macho yakiwa kwa mume wake aliyekuwa akiendelea kutoka akidhani atabadili mawazo.
JE, NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
Taarifa za kupatikana miili ya Dorine na dereva wake vichakani akiunganisha na tukio la mlinzi wake kupigwa kwa kumwagiwa mchanga machoni lilimchanganya zaidi Madam Nafiwe kiasi kwamba siku ya leo hakutaka kutoka kabisa nyumbani kwake.
"Ina maana hili kundi lisilo na jina limeshajua uwepo wetu kwenye misheni yao? Na kama siyo wao ni wakina nani hawa? Dogo Dorine ndiyo alikuwa na majibu yote ya hawa watu na kama siyo wao kwanini wamemuokoa yule kijana ambaye ilikuwa ndiyo tageti yetu ya kuwanasa?"
Madam Nafiwe alikuwa akijiuliza maswali yasiyo na majibu baada ya kusikia kuwa kuna miili imepatikana karibu na eneo ambalo gari lao lilishambuliwa. Alikata mafundo kadhaa ya maji huku akitembea tembea sebuleni kwake.
" Madam inakuwaje sasa?"
Tom alimuuliza baada ya kumkuta akihesabu hatua kama vile anahakiki ukubwa wa sebule yake ambayo siku zote huitumia yeye mwenyewe.
"Kuhusu nini Tom?"
Alimuuliza na yeye kama vile hakumsikia mwanzo.
"Unauliza tena kwani tulikuwa tunapitia taarifa gani kabla?"
"Si ilikuwa taarifa ya kuokotwa miili ya watu wetu kule porini?"
Madam Nafiwe alimjibu akiketi kitini.
"Na ndiyo maana nakuuliza iwapo kama kuna mpango mpya umeufikiria wa kuwakabili maadui."
"Siyo siri Tom unajua nini? Kazi hii niliiona ndogo sana ukilinganisha na vigongo ambavyo nimewahi kukutana navyo lakini kitendo cha kuuawa kwa Dorine ni dalili mbaya sana kwani kwa uimara wa Dorine lakini kathibitiwa ujue tuna kazi kubwa sana."
Nafiwe aliongea akiwa kasimama tena na kusogea mpaka dirishani ambako alikuwa sijui anaangalia nini nje.
" Wale madada ni moto mbaya madam ukiona Santana na jeuri yake yote kapaki na kuamua kukodi jeshi jingine ujue si mchezo."
Tom ndiyo alizidi kumchanganya kabisa Nafiwe.
"Kwa kauli hiyo unataka nikate tamaa?"
Nafiwe alimsogelea karibu Tom na kumuuliza swali la kibabe.
"Si maanishi hivyo bali ninachokitaka ni kujua tunaanzia wapi maana mpaka sasa maadui wametuotea na kupelekea watu wetu watatu kupoteza maisha huku wao wakipoteza wawili tu tena wa familia moja."
Tom bado aliendelea kumuelewesha madam Nafiwe ambaye moja wala mbili zilikuwa hazikai.
" Tom nimepata wazo hapa hebu tumsubiri kwanza Asnat si unajua tulimtuma kule Hotelini akakichunguze chumba cha Dorine kuona kama kuna anaweza kupata chochote ambacho kiliachwa na marehemu kinachoweza kutusaidia kwenye zoezi letu."
Nafiwe alimwambia Tom wasubiri taarifa ya Asnat inaweza kuwasaidia. Wakiwa kwenye majadiliano mara simu ya Asnat iliingia na Nafiwe aliipokea.
" Asnat kuna mpya yoyote ambayo umeipata huko?"
Madam hakusubiri mahubiri yaanze yeye alitaka kupata taarifa tu.
"Madam hali ni tete sana maadui zetu wameshatapakaa kila sehemu kwani ukirusha hatua tu wako nyuma yako hivi ninavyokupigia simu tuko hapa nje ya ofisi kuna mwili wa dereva Taxi ambaye nimemtumia muda mchache uliopita unachunguzwa na askari baada ya kukutwa hapa huku wahusika wakiwa wametokomea na gari lake."
"Mhh hii kali hivi hawa watu ni majini au ni watu wa kawaida kwanini sasa? Mbona ishakuwa hatari kuna biashara kweli hapa mbona naona dalili za umauti mbele?"
Madam Nafiwe anajikuta akiropoka tu baada ya kupata taarifa za kuuawa dereva aliyetumiwa na shushushu wake Asnat.
" Lakini Bosi tumaini lipo kwani wakati nikiwa pale 'The Camel Hotel' kuna dada mmoja alikuwa anaongea na simu huku akinitazana sana kitu ambacho kilinifanya niondoke haraka pale na ndipo nilipochukua Taxi ambayo dereva wake kauawa hivyo moja kwa moja nahisi yule dada anaweza kuwa ndiye mhusika."
Asnat alimweleza Madam Nafiwe juu ya mtu ambaye alimuona Hotelini kuwa huenda akawa ndiye aliyehusika na tukio hilo.
" Uliweza kuimaki sura yake ili tuingie mtaani kumtafuta ikiwezekana tuanzie mtego wetu pale pale hotelini."
"Sura yake sikuweza kuimaki kutokana muda wenyewe lakini kama lile eneo kalizoea tutamnasa tu na mimi bado sijaondoa vitu vyangu kwenye chumba cha marehemu Dorine kwani nilikuwa sijamaliza shughuli yangu nilitoka mara moja kupata chochote si ndiyo nikakutana na Mwanaharamu ikabidi nimpoteze maboya asijue niko wapi lakini alivyokuwa makini kumbe alicheza na akill yangu."
"Sasa hilo eneo halikuhusu waachie polisi wewe sogea karibu na hotel ili uweze kukutana na mtu ambaye mtasaidiana kulindana au polisi umewaeleza kuwa huyo mtu ulikuwa naye wewe?"
"Hapana nifanye hivyo naumwa mimi wala na hata hivyo nimeshatoka hapo ndiyo nakaribia kufika Hotelini."
"Basi nampa namba yako ili akifika hapo mtawasiliana maana yeye si mwenyeji sana hapa mjini."
Baada ya maongezi ya muda kidogo waliachana na ndipo madam Nafiwe akamgeukia Tom na kumuelekeza cha kufanya kisha akamkabidhi namba ya simu na bila kupoteza muda Tom aliondoka zake. Huku nyuma baada ya Tom kuondoka tu simu ya Madam Nafiwe iliita lakini alipojaribu kuiangalia ile namba hakuona kitu zaidi ya 'unknown caller' ikabidi apokee hivyo hivyo.
"Nani mwenzangu?"
Alianza kwa kuuliza swali.
"Naongea na Nafiwe? Kiongozi wa kundi la 'The Black Eyez?"
"Wewe ni nani?"
Nafiwe alimuuliza tena mpigaji.
"Jibu swali langu acha jeuri mwanamke."
Sauti ile ya upande pili iliendelea kumtia presha Madam Nafiwe.
"Ndiyo mimi kuna nini na wewe ni nani?"
Ilibidi akubali kisha naye akampiga swali.
"Utanifahamu tu mimi ni nani siku nikija kwako kwani muda huu ninaoongea na wewe niko mlangoni kwako hapa."
Kusikia hivyo tu ni kama alishtuka hivi akatoka haraka kwenda getini huku akiangalia huku na kule kumuangalia aliyempigia simu yuko wapi na alipolifikia geti alichungulia kwanza kupitia matundu ya milango ya geti lakini hakuona kitu ikabidi afungue geti na kutoka nje, baada ya kufika nje aliishuhudia gari ikitimua vumbi kutoka eneo hili, ikabidi achukue simu na kutaka kuipiga ile namba lakini hakuweza kuiona ikabidi arudi ndani kwa hasira na kubamiza geti.
"Ni nani huyu? Au tayari wameshapafahamu hapa? Mhh hapana hakai mtu hapa ngoja nitoke nikatembee kidogo washenzi hawa wasicheze na akili yangu mimi ndiyo Nafiwe Malkia wa The Black Eyez. Aliondoka zake mpaka mtaa wa pili lakini akaona apaki gari pembeni ampigie simu Santana kumjulisha juu ya hii hali inavyoendelea asikae tu huko Brazil akijua mambo yanakwenda kumbe hali tete.
"Mama la mama mwenyewe nambie."
Santana alipokea simu kwa mashamsham yote akiwa hajui kwanini kapigiwa.
"Nikwambie? Huku mambo si mambo wale watoto wa kike hawafai wamejitanua hao ni kundi kubwa hatari ni tofauti na nilivyotarajia mpaka sasa wametafuna watu wangu watatu wakati sisi tumewafumua wawili tu na wenyewe siyo wao ni wa kule hospitali yaani Daktari na mtoto wake."
"Unasemaje Kamanda wangu unamaanisha kazi imekushinda niingie mwenyewe kazini? Na vipi kati ya hao waliokufa vijana wangu wamo?"
"Kumbe huna akili wewe yaani unauliza watu tu si ndiyo? Sasa sikwambii kuhusu umenikwaza, kifupi kazi haijanishinda hata kidogo ila ninachotaka ni wewe kuja huku tuunganishe nguvu."
"Mungu wangu yaani kwa unavyoongea tu inaonesha fika umekata tamaa, Nisamehe kama nimekukwaza kwa kuulizia waliokufa kama ni wa kwangu ama wako please niambie nimefuta kauli ya mwanzo."
"Santa ee ni hivi, waliokufa mpaka sasa ni Afisa mipango wetu Dorine....." Kabla hajamaliza alikatishwa na Santana.
"Unasemaje Nafiwe? Suzanne kauawa? Usiniambie ndiyo tafadhali."
Santana alichanganyikiwa baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa Dorine (Suzanne).
"Nisikwambie vipi wakati tayari nishakupa taarifa Santa? Wengine ni dereva wake Dorine pamoja dereva Taxi aliyekuwa akitumiwa na kipanga wetu mtaalam wa IT Asnat."
"It's too much aisee kama hali ndiyo hiyo tunatakiwa kufanya kitu ama sivyo watatukalia kichwani hao."
"Na ndiyo maana nikaona nikupigie nikujulishe bro."
"Nimekupata ila endeleeni na michakato tutajua la kufanya."
"Poa poa bosi."
Baada ya kumaliza kuongea na Santana alikata simu na kisha akaliwasha gari na kuondoka zake lakini hesabu za kurudi nyumbani hakuwa nazo akanyoosha mguu.
"Uko wapi kiongozi wangu, yule dada tumemuona tena hapa lakini ametupotea sijui kaingia wapi?"
Ulikuwa ni ujumbe ambao uliingia kutoka kwa Asnat akimjulisha Madam Nafiwe kuwa kamuona tena Jackline pale 'The Camel Hotel' lakini hajafanikiwa kumuona kaelekea wapi.
" Msiondoke endeleeni kumchunguza maeneo hayo hayo anaweza kuwa kajificha tu na mimi niko njiani nakuja huko huko tuungane kumsaka mshenzi huyo mpaka kieleweke."
Alimjibu baada ya kuusoma ujumbe ule na kisha akaongeza kasi ili awahi kufika huko.
Kutokana na mwendo mkali aliokuwa nao ukichanganya na mawazo ya shughuli iliyokuwa mbele yake gari lilikwenda na kugonga kingo ya barabara na kuangukia mtaroni.
" Nini tena jamani mbona nakutana na majanga tena mimi, aghh mguu wanguuu ashiiiiiiii...." Akiwa anajichomoa kutoka kwenye gari ambalo lilikuwa limebondeka sana show ya mbele ilikuwa haitamaniki.
Alijivuta mpaka akachomoka na kusogea pembeni ambapo alikaa na kujifungua kitambaa kichwani ambacho alikitumia kujifutia damu iliyokuwa kwenye mguu wake wa kushoto pamoja kidole cha mguu wake wa kulia vilivyokuwa vinabubujika damu. Alijitahidi kuifuta na kisha akachana kipande cha kitambaa hicho na kujifunga kwenye goti sehemu ambayo ilionekana kuchubuka zaidi na alipomaliza aliinuka na kuondoka zake huku akiliacha gari lake lililokuwa halitamaniki kuliangalia tena kisha alitoa simu yake na kumpigia Asnat.
"Nakusikia Madam umefika?"
"Hapana nimepata ajali hapa karibia na hili daraja la kuchepuka kuja huko The Camel hivi niko mdogo mdogo nikiwa nakuja huko."
"Basi tulia hapo hapo nikufuate usije tonesha madonda yako."
"Okay basi fanya hivyo utanikuta njiani nikiwa nakuja taratibu Asnat."
Asnat alikata simu na kuchukua Taxi haraka iliyokuwa imepaki pale nje na kumuelekeza dereva wa taxi hiyo ni wapi wanatakiwa kuelekea na baada ya kuelewana safari ilianza mara moja. Gari lilishika kasi na kuifuata njia ambayo alielekezwa dereva lakini mambo yakawa tofauti kwani baada ya kumfikia tu Nafiwe gari lilimfuata na kutaka kumgonga ikabidi arukie pembeni kulikwepa na bila kusimama lilishika kasi pasipo kupunguza kasi hata kidogo.
"Weee mkaka huyo uliyetaka kumgonga ndiye tunayemfuata mbona unapitiliza tena?"
Asnat aliuliza akiwa kashika kichwa chake baada ya kuona mwendo si wa kawaida na dereva wa taxi hiyo alikuwa hamjibu chochote kile zaidi ya kuendelea kukanyaga mafuta.
"Ufanye chochote kile mrembo kama unayapenda maisha yako sijui umenielewa?"
Ilikuwa sauti nyororo na yenye kumaanisha kutoka siti ya nyuma ambayo ilimfikia vizuri sana Asnat huku kitu cha baridi kikimgusa kisogoni.
"Kuna nini jamani mbona sielewi wee kaka sinilikwambia kuna mtu tunamfuata kapata ajali mbona inakuwa hivi tena?"
Hakujali kama chuma kinacheza na kichwa chake yeye aligeuka na kumuuliza dereva ambaye hakuwa na habari naye zaidi ya kupambana kupishana na miti iliyokuwa ikirudi nyuma na kuufanya mpishano wa aina yake.
" Nimesema kimya na hutakiwi kufanya chochote mrembo kichwa kigumu eee nitakisambaza sasa hivi, kwanza nipe simu yako haraka."
Muda bastola ilikuwa ikikisuguasugua kisogo cha Asnat na kumfanya kuogopa sana pasipo na ubishi wowote ule aliitikia kwa kichwa na kuitoa ile simu na kumkabidhi Jackline kisha akamuamuru Roberto kuelekea kule kule kwa Gezra, hivyo hakukuwa na majadiliano zaidi kuelekea huko. Kwa ambaye angekutana na taxi hii kwa vyovyote angempa krediti kwa dereva huyu kutokana na mwendo wake na wengine wangekwenda mbele zaidi na kusema taxi hii imebeba magendo na ilikuwa ikifukuzana na maaskari wa kuzuia magendo.
"Shuka haraka wewe mrembo uliyeshindwa kuutumia uzuri wako kufanya kazi ambayo ingekuletea heshima kwa jamii na iwapo ungeenda mbali zaidi ungeweza hata kugombea Ulimbwende wa Dunia na bado taji hilo lingekuwa la kwako ila kwa kuwa ulichagua kufanya shughuli hii ngoja sisi tukuvishe taji la Umauti ambalo hutolivua maishani.
"Pa pa pa paaaaa................"
Ulikuwa ni mlio wa risasi mfululizo zilizosambaratisha kichwa cha Asnat ambaye aliangukia uwanja ule ule ambao uliyachukua maisha ya mlinzi aliyetaka kupambana na Roberto. Na baada ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa walipongezana kwa hatua waliyoifikia kisha waliingia garini.
"Roberto unafahamu kuwa kila hatua tunayoifikia tunakaribia ushindi?"
"Ni kweli kabisa Jackline na nina uhakika kwa mbinu hii watakufa kama kuku kama siyo panya."
Wakiwa wanaendelea kupongezana mara simu ya Asnat iliita.
"Asnat mbona kimya mpaka sasa hujaondoka tu au kuna lolote umefanikiwa kuliona? Na pia ni kama mkosi vile huwezi amini Asnat kuna taxi imepita hapa kwa mwendo mbaya sana almanusra nigongwe."
Nafiwe alijiachia akifikiri kuwa anaongea na Asnat kumbe simu ilikuwa sikioni kwa Jackline.
" Nafiwe, Nafiwe, Nafiwe huyo uliyefikiri kuwa ni Asnat umechelewa sana muda tayari anasalimiana na Dorine huko kuzimu muda wa wewe kuitwa Nafwa na siyo Nafiwe wala Nafiwa umewadia jiandae, mimi ndiyo kubwa la Maadui."
Alikata simu na kuitupa pale pale karibu na ulipo mwili wa Asnat na kumtaka Roberto aendeshe gari waondoke eneo hilo.
" Tukikaribia makazi ya watu simamisha gari tulitelekeze kisha tutatembea mpaka tupate usafiri wa kukodi."
"Sawa sawa Jackline."
Roberto alimjibu na kukanyaga mafuta kuelekea mjini.
JE, NI NINI KITATOKEA?
Waliwasili karibia na makazi wakasimama pembeni ya barabara na kushuka garini na kuliacha hapo na kwa kuwa lilikuwa ni gari la dereva aliyeuawa na Jackline wakati akiwa kampeleka Asnat ofisini kwao wakaona kuwa kazi yake imekwisha wakaondoka eneo hilo na huku Jackline akiitoa simu yake na kumpigia Jasmine awafuate hapo walipo kwa kuwa walikuwa mbali kidogo na Hotel. Kwa muda huo baridi lilikuwa limekolea hivyo ikawafanya waanze kupasha kwa kukimbia mdogo mdogo ili kupunguza baridi.
"Unajua nilipuuzia kuchukua koti muda sasa muziki nimeanza kuuona."
Jackline alishindwa kuvumilia ile hali ikabidi aongee tu na kwa kuwa Roberto naye ilikuwa ni vivyo hivyo ikabidi wawe wanakimbia kidogo wanatembea kidogo hii walikwenda nayo mpaka pale walipokutana na Jasmine, Jessica pamoja na Titiana.
" Vipi kwema huko Hotelini?"
Jackline aliuliza mara tu baada ya kuingia garini.
"Hakuna chochote kile tulipatwa na hofu baada ya kuona kimya hamtupi taarifa kwa kinachoendelea."
Jessica alimjibu na kuelezea hisia zake.
"Acheni kabisa watu wangu kwani ilikuwa ni gemu ya kibabe kwani tuliamua kufanya umafia bila hata kuangalia kuna nani anatuangalia lakini yote kwa yote tumefunga ukurasa huu na kwa sasa tunauangalia ukurasa unaofuata."
Roberto aliwajibu huku meno yote yako nje kuashiria ushindi kwenye vita ambayo walitoka kupambana. Na zaidi ni triki ambayo waliamua kuitumia ya kuegesha pale hotelini kama dereva Taxi huku Jackline akiwa siti ya nyuma.
" Niwachekeshe sasa tukiwa pale kuna wateja walikuwa wanakuja kutaka usafiri Roberto siyo kujiumauma kule ashukuru nilikuwepo ikawa ndiyo kisingizio 'sorry nina mteja tayari' mimi siyo kucheka kule."
Jackline aliamua kuwachekesha wenzake ndani ya gari wakiwa wanarejea Hotelini.
" Sasa jamani ningefanya nini ikiwa kazi yenyewe niliibaka tu niliifanya wapi?"
Roberto alijibu baada ya kuona Jackline amemgeuza agenda.
" Jamani mwenzenu nina wazo kidogo japo ni usiku."
Roberto aliwaambia wenzake juu ya kile alichokuwa anakiwaza peke yake.
" Jambo gani hilo tena?"
Jasmine alimuuliza.
" Mnaonaje muda huu tuelekee nyumbani kwa mzee Jerome Whistle tukawafanyie surprise'?"
" Ishia hapo hapo Roberto, twende ili nini kikatokee? Wao si wametuona sisi gonjwa la mlipuko? Haina haja kikubwa sisi tumemrudisha mtoto wao inatosha."
Jackline aliweka mgomo bila kupepesa macho.
" Sisi wote ni wahanga au naweza sema sisi ni Mayatima na baada ya kuungana tulikubaliana kuishi maisha yenye furaha, hebu twendeni kwao tukawaoneshe sisi si watu wa taipu yao na kingine gari letu liko kule tunatakiwa kulichukua na kulirudisha hili ambalo tumelikodi."
Jasmine alionesha kutofautiana na Jackline juu ya kukataa kwenda kwa mzee Jerome Whistle eti kwa sababu wamewakosea akaona wala siyo poa wao waende wakafanye yao mengine yatajulikana huko huko, hivyo walikubaliana na kwenda huko lakini walienda kwanza Hotelini kuchukua majaketi na masks ili waingie pale wakiwa na sura za kazi ili muda wowote ikitokea issue waingie kazini. Basi baada ya kufika Hotelini kila lililotakiwa kufanyika hapo lilifanyika na kila mmoja alitoka akiwa kamili na waliingia kwenye gari na safari ikaanza huku stori za hapa na pale kuhusiana na changamoto walizokutana nazo toka wafike Namibia. Lakini kwenye site mirror' Jasmine aliyekuwa akiendesha gari wakati huo aliweza kuiona gari ikija kwa kasi nyuma yao na hivyo kumfanya kupunguza mwendo kama vile amegundua tatizo kwenye gari hivyo akapunguza mwendo kabisa na kusimama, wakati akifanya hivyo hakuweza kumueleza yeyote mle ndani alitaka ajiridhishe kwanza. Na baada ya kushuka aliizunguka gari akawa anaicheki ile gari ambayo nayo ilipoikaribia ilipunguza mwendo lakini baada ya taa kumulika mbele na kubaini kuna mtu kaegemea gari iliongeza mwendo na kuwapita kwa kasi. Jasmine aliiangalia akagundua plani yao ni ipi kwani kwa mbele kulikuwa na majengo mengi mengi yenye viuchororo vya kutosha hivyo akaona aingie kwenye gari na kuwadokeza wenzake juu ya alichokishtukia.
"Umejuaje kama tunafuatiliwa Jasmine?"
Roberto aliuliza.
"Nimechezwa na machale kwenye hii gari iliyopita kasi muda huu."
"Kama ndiyo hivyo tunafanyaje sasa?"
Akauliza Jessica.
"Mimi nafikiri tugeuze ili tuwachore kwanza au mnasemaje?"
Jasmine aliwaeleza alichokifikiria.
"Hapana Jasmine tukifanya hivyo watajua tumewashtukia cha kufanya sisi tuendelee na safari lakini tukifika mbele tu tunabadili njia maana kama wanatufuatilia sisi lazima watakuwa wamepaki mbele wanatusubiri."
Roberto alipendekeza safari iendelee na hivyo hakukuwa na la kujadili ikabidi Roberto mwenyewe aukalie usukani na kusonga mbele.
" Enhh angalia kule ile gari pale ni yenyewe kwa kuwa eneo hili halina magari muda huu na pale siyo sehemu ya kuegesha magari lenyewe linafanya nini?"
Jasmine aliwaonesha kwa kidole.
"Hapo Roberto punguza mwendo nenda pole pole kwanza tukipita hapa utaongeza mwendo kisha kwa mbele utajua tufanye nini ili tumkabili adui."
Jackline alimuelekeza Roberto ambaye aliitikia kwa kichwa.
Walisonga mbele kwa mwendo wa pole pole na baada ya kuifikia barabara ya mchepuko inayokwenda madukani na ile inayokwenda kwa mzee Jerome Whistle hapo Roberto akaingia ya kuelekea madukani na kuongeza mwendo ambao mpaka Jessica alipiga kelele kuomba mwendo upungue lakini haikuwa hivyo alichokifanya ni kukata kona kwenye kiuchochoro kilichokuwa karibu na barabara kisha akaipaki na bila kuongea chochote alishuka haraka bastola ikiwa mkononi. Wakina Jackline nao walifanya hivyo hivyo na baada ya muda ile gari ilikuja njia ile ile na kupita kwa kasi bila shaka hawakuiona gari ya kina Jackline ilipopaki na hapo bila kupoteza muda waliingia kwenye gari na kurudi nyuma haraka kabla ile gari haijageuza. Kama bahati vile mpaka wanaingia barabara inayokwenda kwa wakina Mustapha hakukuwa na gari inayokuja nyuma.
"Roberto huo mwendo hapana aise unataka utumbo ukatikekatike?"
Jasmine alimuuliza Roberto aliyekuwa akicheka tu huku mafuta yakiendelea kukanyagwa.
"Hivi saa ngapi saizi jamani?"
Alichokifanya ni kubadilisha mada badala ya kujibu swali yeye akauliza muda.
"Roberto una makusudi sana wewe yaani unaturusha roho juu juu mwendo wako halafu unatupooza na swali lako la muda."
Titiana aliona apigilie msumari wa lawama kwa mpenzi wake ambaye muda huo alikuwa akipiga honi getini kwa wakina Mustapha.
"Hivi ninyi mna utani sana kuna mwendo hapo aliotembea?"
Jackline aliwauliza waliokuwa wakilalamikia mwendo.
"Waambie hao wanalia na mwendo wa bibi harusi, je nikitembea mwendo wa wavusha magendo itakuwaje jamani?"
Roberto alivyosifiwa akapata pa kujipamba zaidi akiwa anashuka baada ya kuona hakuna dalili za geti kufunguliwa hivyo akaifuata kengele na kuipiga.
"Hivi inawezekana ni usiku sana ee yaani nyumba imepoa kiasi hiki?"
Titiana aliuliza huku akiiangalia saa yake mkononi.
"Ninyi hivi mnajua ni saa ngapi saizi?"
Akawauliza wenzake.
"Hatujui Tity twambie."
Jessica alimjibu huku akimrukia mgongoni.
"Ni saa nane na robo hii."
Mara geti lilifunguliwa huku kukiwa hakuna anayechungulia kutoka ndani. Ikabidi waingie huku Roberto akisalia kwanza nje kuangalia usalama. Na alipojiridhisha hakuna mnyatiaji nyuma yao akaingia garini na kuliingiza ndani.
"Ninyi watoto ndiyo nini kutuvalia hivyo?"
Mzee Jerome aliuliza akitokea kwenye maua alikokuwa kajificha baada ya kufungua geti.
"We mzee uking'atwa na wadudu huko?"
Jackline alimuuliza huku akimkumbatia mzee Jerome Whistle.
"Karibuni wanangu, karibuni sana ndani ndiyo nini mkamleta mwenzenu na kuondoka bila hata kutakiana hali?"
Mzee Jerome hakusubiri mpaka wafike ndani akaona awaulize tu wakiwa wanasalimiana.
"Ndugu zangu haoooo... Karibuni jamani mbona usiku hivyo?"
Victor aliwalaki baada ya kutoka chumbani na kuwakuta wakikaa vitini.
"Jamani kwanza tunaomba radhi kwa kuwatembelea usiku huu tunajua mlikuwa mmejipumzisha."
Jackline alianza kwa kuwataka radhi wenyeji wao.
"Wala msihofu wanangu kwangu ni baraka tu nikiwaona mko salama, mengine mnayoyasikia mtusameheage bure tu si mnajua tunavyozeeka na akili nazo huzeeka hivyo hivyo."
Mzee Jerome aliomba msamaha kikubwa kwani anafahamu alichokifanya mke wake.
"Baba sisi tulishasamehe na ndiyo maana tulipomaliza shughuli yetu Tanzania tulikuja mara moja kuhakikisha kuwa Mustapha anapatikana na tunashukuru Mungu tulifanikiwa katika hilo na kwa kuwa tulijua tunaingia vitani hatukutaka kuja mapema tulitaka kuhakikisha kuwa wale wote wanaowavizia tunawamaliza."
Jasmine alimfafanulia mzee Jerome ambaye muda huo alikuwa anafuta tu machozi na wakati huo Victor alikuwa kamfuata Mustapha aliyekuwa kalala.
" Baba usiogope kuiona hii timu iliyo mbele yako na popote unapoiona ujue usalama upo, ukituacha sisi hawa wawili ni Roberto na Titiana ambao ni rafiki zetu waliokuwa wamesalia Brazil na sasa wamekuja kuungana nasi na toka wamekuja kuongeza nguvu habari wanayo."
Jackline aliwatambulisha wakina Roberto na Titiana kwa familia ya mzee Jerome Whistle.
" Msiseme kuwa ninyi ndiyo mliohusika na vifo vya wale watu waliokutwa kule Gezra?"
Mustapha aliuliza wakati akikaa.
" Mustapha unaendekeaje kwa sasa? Hayo ya Gezra achana nayo kwani kuna mengi mtasikia."
Jessica alimuuliza hali yake ikoje toka wamemwacha siku kadhaa zilizopita.
" Mhh haya dada, mimi naendelea vizuri namshukuru Mungu katika hilo kwani nashindwa kuelewa msingekuwa ninyi siku ile sijui ingekuwaje mimi kidume wa mzee Jerome."
Maelezo ya Mustapha yalimfanya kila mmoja kuangua kicheko kwani aliongea huku akishika mashavu yake. Lakini kilichowashangaza wakina Jackline ni kutomuona Bi Elizabeth wakati huo pale ndani kitu kilichomfanya Jessica kumuuliza mzee Jerome.
" Mama yenu kama mnavyomjua kwa muda huu mfupi aliondoka jana mchana kuelekea South Africa' kwa Shangazi yake na bila shaka atarejea baada ya majuma matatu hivi."
Mzee Jerome aliwaeleza maelezo ambayo kila mmoja aliyaelewa vizuri.
Basi maongezi yaliendelea pale sebuleni huku Roberto akiwavunja mbavu kwa stori zake.
" Mzee wangu mimi ndivyo nilivyo ukiiangalia utafikiri umekutana na Jini mtoa damu lakini wala kazi yangu ni kutoa somo la maisha kwa wale wanaopita kwenye mapito yangu kama unafikiri utani mzee wangu hata wewe jaribu."
"Wee na mimi ni hatari kijana wangu? Uliza wavuvi kule Pwani watakueleza vizuri au waulize wanangu."
Mzee Jerome naye alivimba.
"Baba acha uongo mbona ulivyofungua geti ulijificha kwenye maua?"
Titiana alimuuliza baada ya kumuona anavyojigamba kwa vitendo.
"Ile ni mbinu ya kivita, nilifanya vile baada ya kuchungulia na kukutana na minguo myeusi nje nikajua ndiyo wenyewe wamekuja. Sasa mlianzaje kuvaa minguo hiyo?"
"Wewe mwenyewe umesema mbinu za kivita si ndiyo hizi sasa?"
Wakati Jackline akimjibu mzee Jerome mara ukasikika mlio kama wa gari nje kitu kilichomuinua Roberto haraka kitini na kutoka nje kuangalia kulikoni.
JE, KUNA NINI HUKO?
Baada ya kutoka nje Roberto alizunguka nyuma ya nyumba hiyo huku Jackline na kundi lake lote walijificha kwenye maua tayari kwa kupambana na yeyote atakaye ingia ndani. Roberto kule nyuma alipanda ukuta na kurukia nje huko alianza kuambaa na ukuta kwenda uelekeo wa getini. Giza lililokuwa limetanda muda huo lilikuwa ni ulinzi tosha kwa Roberto ambaye hakuweza kuonekana. Alipochungulia getini aliweza kuona kuna gari liko pale huku kuna tochi zinamulika mulika eneo hivyo akajua moja wamevamiwa hivyo alichokifanya ni kumtumia ujumbe Jackline kule ndani wajiandae kwa mpambano ambao yeye aliamua kuwasambaratisha kwa kuwatoa kwenye lengo lao hivyo alichofanya ni kukimbilia upande wa pili kuliko kuwa na jengo jingine ambalo lenyewe taa zake zilikuwa ni za ndani nje ilikuwa giza.
"Kwisha habari yenu subirini muone."
Roberto alijisemesha akiwa anajiandaa kufyatua risasi kuelekea kule huku akiangalia atakimbilia wapi baada ya kufyatua.
Alichokifanya ni kufyatua risasi moja ambayo ilikwenda na kugonga kioo cha gari hiyo. Mlio huo uliwaondoa kwenye plani kwani waliokuwa chini ilibidi wakimbie huku aliyekuwa kwenye gari akiliondoa kwa kasi. Hiyo ikawa nafasi kwa Roberto kuendelea kumimina risasi ambazo zilikuwa zikitua kwenye kioo cha nyuma cha gari hiyo.
"Maamaaaaa nakufaa....." Ni ukelele uliotokea ndani ya gari.
"Nyambafuuu mnabipu vipaji vya watu..."
Roberto alisema huku akihama ukuta baada ya kuona risasi zinamiminwa kuja upande wake. Na alipoona amekaa sehemu salama alitoa simu na kumpigia Jasmine.
"Toeni gari haraka hatuna muda wa kupoteza hawa Nguruwe nimemjeruhi mmoja sijui ni nani ila nimesikia sauti ya ukelele kutoka kwenye gari tunatakiwa tuwafukuzie kabla hawajafika mbali."
"Okay."
Jasmine alimjibu na kukata simu akawafuata wenzake na kuwaelekeza alichoambiwa na Roberto. Hakukuwa na mjadala waliingia kwenye gari huku wakina Victor nao wakitaka kupanda.
"Victor ninyi bakini hapa hapa huko kuna hatari ninyi lindeni nyumba chochote kitakachotokea tujulisheni haraka."
Hakukuwa na namna ikabidi Mustapha afungue geti na gari kutoka nje ambako walimpitia Roberto na kuondoka zao. Gia zilipigwa huku macho ya kila mmoja yakiwa mbele pembeni na nyuma ili kuona kama wanaweza kuona chochote lakini hakukuwa na dalili ya gari wala watu.
"Watakuwa ni wenyewe au ni wengine tu?"
Jessica aliwauliza wenzake.
"Wale ni wenyewe kwa walivyokuwa na pilika pale getini sema tu risasi zangu zimewatoa kwenye njia."
Roberto alimjibu Jessica.
"Watakuwa mbali mpaka huku kimya?"
Jasmine aliwaambia wenzake baada ya kuona hakuna dalili.
"Nafikiri sisi tukajibu shambulizi kwa bosi wao Nafiwe au mnaonaje?"
Roberto damu ilikuwa imeshachemka akawataka wawafuate huko huko kwa bosi wao.
"Haitakuwa hatari kujipeleka kwao wakati wametoka hapa sasa hivi? Mimi nadhani tuelekee Hotelini tukamalizie masaa yaliyosalia ili asubuhi tuamke na mipango mipya."
Jackline alipingana na kauli ya Roberto na kutoa ushauri wake.
"Ni kweli kabisa hatuna haja ya kuwafuata sisi tukawaandalie shambulizi la kushtukiza."
Titiana ambaye muda wote si muongeaji sana alikubaliana na mawazo ya Jackline.
****
Nyumbani kwa Nafiwe kulikuwa hakukaliki kila mmoja kiti kilikuwa cha moto hali ya mgonjwa ilikuwa tete alikuwa anakoroma kutokana na risasi ambayo ilimpata kwenye kwenye uti wa mgongo. Nafiwe kwa kuhofia maswali ambayo hakuwa tayari kuyajibu kutoka kwenye vyombo husika aliamua kumuita daktari ambaye humtumia likitokea la kutokea kwenye mishe mishe zake.
"Nambie Daktari kuna uwezekano wa kupona mgonjwa kweli?"
Aliingia tena ndani na kumuuliza daktari ambaye muda huo alikuwa katingwa kuupigania uhai wa mgonjwa.
"Madam tulia, si uliniamini kuwa naweza kuifanya kazi yako? Sasa niachie mimi ndiyo nitakwambia ikoje."
Daktari huyo alimjibu Nafiwe kwa ukali kidogo ikiwa ni dalili kuwa shughuli ni pevu.
"Okay ok endelea mtaalam.." Nafiwe akatoka nje mikono kiunoni na kuelekea ukumbini walipokuwa vijana wake wengine.
"Hivi ilikuwaje mpaka mkaotewa kiasi hicho? Kila kukicha ninyi ni wa kushindwa tu kwanini?"
Madam Nafiwe aliwaijia juu wakina Robinson ambao walikuwa kwenye vamio nyumbani kwa mzee Jerome Whistle.
"Madam unajua nini?"
Robinson alimuuliza Nafiwe.
"Mimi sijui, wewe ndiyo uniambie Robinson."
"Kila kitu tulikiweka sawa na hakukuwa na mtu yeyote ambaye alituona sababu tuliwashuhudia wakiingia ndani na kufunga geti na bado hatukuishia hapo tulichungulia ndani tukawaona wakiingia ndani ndipo tulipowapigia simu wenzetu waje lakini ajabu mshambuliaji alitokea nyuma yetu kwenye jengo lillilo karibu na yule mzee."
Robinson alimfafanulia madam Nafiwe ambaye muda huo alikuwa amevurugwa kutokana na kupoteza watu wake na yeye mwenyewe kuponea chupuchupu kufa kwenye ajali ya gari na pia kukoswa na gari.
" Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa mwenye hiyo nyumba anahusika katika hili?"
"Sina uhakika katika hilo kwani unaweza kukuta ni mbinu iliyotumiwa na mvamizi wetu."
Robinson hakuwa na uhakika katika hilo hivyo hakutaka kulipa asilimia zote. Akatoka daktari kitambaa mkononi kikitembea usoni kufuta jasho lililokuwa likimtiririka. Nafiwe hakutaka kupoteza muda akamsogelea kutaka kujua kulikoni.
" Daktari anaendeleaje mgonjwa wetu?"
"Madam, nimejitahidi sana kwa uwezo wangu wote lakini imeshindikana amekata roho."
Daktari aliwafafanulia, taarifa hiyo iliwatia simanzi sana Robinson alijikuta akikaa chini kwa kuishiwa nguvu kutokana na kumpoteza mtu wake wa karibu. Alipojiunga na Santana mtu ambaye alitokea kuendana naye alikuwa ni Tom. Kifo chake kilimnyong'onyeza sana kiasi kwamba aliona miguu yake ikiishiwa nguvu kwa kukosa ushirikiano.
"Mkuu ni kweli kabisa kaka Tom hatuko naye?"
Robinson alimuuliza madam Nafiwe.
"Kama ulivyosikia Robbie hatuko naye tena."
Madam Nafiwe alimjibu Robinson huku akimshika begani.
Alitoa simu mfukoni na kuitafuta namba ya Santana ili amtaarifu tukio la kufa kwa Tom.
"Brother mambo yanazidi kuwa magumu kila kukicha."
"Una maanisha nini?"
Santana alimuuliza baada ya kusikia kauli ya Nafiwe kuwa mambo yanazidi kuwa magumu.
"Tom anaongeza idadi ya watu ambao tunaendelea kuwapoteza kila kukicha, ka......" Kabla hajamalizia kauli yake Santana alimkatisha.
"Unasemaje wewe mwanamke? Hebu rudia tena sentensi yako? Wafe wote huko lakini Tom aniletee ripoti ya ushindi na si vinginevyo."
Santana alimuwakia madam Nafiwe kwenye simu kama yuko nae karibu vile.
"Mkuu wangu ukweli ndiyo huo siwezi kukudanganya hata robo."
Nafiwe aliendelea kusimamia msimamo wake kwenye taarifa yake.
"Okay nadhani kazi nilimkabidhi mtu asiye na uwezo, nisikilize mwendawazimu wewe nakuja huko kesho naomba msifanye chochote kile kwa jembe langu mimi ndiye nitakaye simamia mazishi yake,jiandae kurudisha asilimia arobaini ya mkataba wetu na hiyo oparesheni nitaisimamia mwenyewe nakuja na kosi langu lote ninaloliamini kikazi."
Santana aliamua kumfungukia Nafiwe kuwa anaianza safari akiwa na vijana wake wa kazi kumkabili Jackline na wenzake akiwa na imani na mzee Bruno Gautier na Chude ambao walikuwa wakiingia mzigoni na Tom kazi inakuwa pevu sasa wamepungua hali hii iliwachanganya wote Namibia na Brazil.
"Itakavyokuwa poa tu hata ukitaka nirejeshe yote niko tayari kazi gani ngumu utafikiri nini kwanza haiendani na malipo tuliyokubaliana kwa hiyo usinitishe brother."
Nafiwe naye akaamua kumtunishia msuli Santana kitu kilichomfanya kukata simu.
"Hawa wote waliohusika na tukio hili wajiandae kwa kisasi."
Nafiwe aliongea hayo akiingia ndani kumhifadhi vizuri marehemu Tom akisaidiana na Robinson aliyekuwa akitiririkwa na machozi muda wote hasa baada ya kuuona mwili wa marehemu ndiyo ikawa maradufu.
" Brother, nitahakikisha nailipia damu yako iliyomwagwa na mafedhuri wasio na haya."
Robinson aliongea akitokwa na machozi yakiambatana na makamasi. Baada ya kila kitu kukamilika daktari aliaga na kuondoka zake. Geti lilifunguliwa akatoa gari na kuishia zake. Lakini kabla hajafika mbali na jengo la Nafiwe alitokea mama mmoja aliyekuwa kajifunga lemba kubwa kichwani akisimamisha gari. Daktari alimpita lakini mbele kidogo alisimama baada ya kujifikiria akarudi rivasi. Alipomfikia aliisimamisha gari na kuteremka chini, alifanya makosa yule mwanamke alimshuti risasi ya kichwa na kukimbia zake huku akimuacha daktari akidondoka kwenye lami. Mwanamke yule alipofika mbele kidogo alitoa simu akamtumia ujumbe Nafiwe.
"Kuna mzoga wako nje ya jengo lako njoo uuchukue kabla haujaharibika."
Kisha akaizima simu yake na kuingia kwenye gari yake aliyokuwa kaiegesha kando ya barabara ya vumbi na kuondoka zake Hotelini na kuiacha simanzi nyingine kwa madam Nafiwe.
Alifika Hotelini na moja kwa moja aliingia mpaka chumbani kwake.
"Asante Mola kwa hatua hii muhimu, kwa sasa wanahesabika."
Jackline aliongea akiwa anavua viatu na nguo nyingine kupunguza uzito mwilini, akiwa anaziweka zile nguo kabatini alicheka sana kwa sauti ya chini kiganja kikiwa mdomoni baada ya kujitazama kwenye kioo.
" Hivi Jackline umekuwaje kwa sasa? Umekuwa katili kiasi hicho? Lakini hapana wewe siyo katili bali unaifundisha dunia kuwa hakuna mnyonge chini ya jua ni kutia nia tu. Na haya manguo yanasubiri kufuliwa lini?"
Aliendelea kucheka na kujitupa kitandani mzima mzima. Na muda huo tayari ilikuwa ni alfajiri na walikuwa wamekubaliana kuwa kukicha wataandaa plani ya kuwakabili maadui wao na kila mmoja aliingia kula lakini hali ikawa tofauti kwa Jackline kwani akili yake haikutulia ndipo alipotoka na kwenda nyumbani kwa Nafiwe kufanya shambulizi lakini baada ya kufika alipanda ukuta na kuchungulia ndani akakuta ulinzi mkali akaamua kurudi nyuma na kujificha kando ya barabara. Na baada ya muda ndipo alipoiona gari likitoka ndani hesabu zake alijua ni mmoja kati wa watu walio kwenye tageti yake lakini akawa ni mtu mwingine hiyo pia hakujali akaamua kupeleka ujumbe kwa Nafiwe.
Alijigeuza geuza pale kitandani hakupata usingizi akaona hakuna haja ya kuendelea kulala akaamka na kumfuata Jasmine shoga yake kipenzi akamgongea na kuingia baada ya kufunguliwa mlango.
"Kwanza nikuombe msamaha rafiki yangu najua nimefanya jambo ambalo hatukulijadili pamoja lakini nimshukuru Mungu nimefanikiwa kiasi kuongeza presha."
"Sijakuelewa Jackline ikoje kwani?"
Jasmine aliona amuulize ili amueleweshe vizuri baada ya kuona anamwaga maneno tu.
"Ni hivi tulipoingia kulala kwani mimi nililala aa wapi nilishika njia na kuelekea kwa Nafiwe kufika kule nilitaka kuingia ndani kupitia ukuta nikakuta ulinzi mkali nikashuka na kurudi kwenye gari lakini nikaona siwezi kuondoka bila kuacha alama ya maumivu nikaona nijifiche kando kidogo na ndipo ilipotoka gari mle ndani nikaipiga mkono nikijua anaweza kuwa ni mmoja wao kumbe ni sura nyingine lakini mpaka ilikuwa mle ndani lazima anaushirika na kundi lile."
Jackline alimuelezea kwa kirefu Jasmine.
" Ikawaje sasa Jackline una mambo wewe?"
" Si ndiyo nikampa ya kichwa na kuondoka zangu huku nyuma nikimtumia ujumbe Nafiwe."
Alimaliza na kujilaza kitandani kwa Jasmine.
" Pole sana shoga yangu lakini wakati mwingine usirudie kwenda sehemu bila kushirikisha wenzako."
"Asante kwa kunielewa ila sijui kama watanielewa wakina Jessica."
"Tutakuelewa tu kwanini tusikuelewe ikiwa tunakufahamu kwa sasa mambo yako ya fasta fasta dada Jackline?"
Alimjibu Jessica akiwa anaingia chumbani kwa dada yake ikiwa ni utaratibu wake kumjulia hali dada yake kila asubuhi.
"Nashukuru mnanielewa kwa sasa."
Jackline aliongeza.
Walijiandaa na kuelekea Restaurant kwa ajili ya kupata kifungua kinywa.
"Jamani kutokana na yaliyotokea jana usiku najua kuna jambo litafanywa na Santana hivyo kwa sasa tuwe makini zaidi kwa kila hatua zetu."
Jasmine aliwaambia wenzake wakiwa wanafungua vinywa. Na hii ilikuja baada ya Jackline kuwasimulia kilichotokea na wakina Roberto.
" Mimi nafikiri tufanye kila tunaloweza kulipata lile gari kule kwa mzee Jerome na hili lirudi kwa wahusika kwani Mashaka yangu ni kwamba wameshaikariri hivyo itakuwa ni rahisi kutufuatilia.Au tutafute gari ndogo mbili za hela chini kutoka kwenye Gereji za uswahilini ambazo zitakuwa ni kuukuu lakini tutazifunga injini mpya zenye uwezo mkubwa."
Roberto aliwapa mbinu wenzake ambayo itawaweka salama kwa kuwa gari wanalolitumia linafahamika sana kwa sasa.
" Wazo lako la kupata hizo gari mbili ni bab'kubwa sana watakuwa wanajua kigari chenyewe ni kibovu lakini kila wakikanyaga mafuta sisi tunawatimulia vumbi tu chezea nini."
Jasmine alimuunga mkono Roberto na wote walikubaliana na baada ya chai waliondoka kuingia mtaani kutafuta gereji zilizo uswahilini ambazo zinaweza kufanya kama wanavyotaka wao.
JE, NINI KITATOKEA?
Santana na watu wake wa kazi mzee Bruno na Chude waliwasili nchini Namibia na kupokewa na timu ya Nafiwe ambayo ni ya siri sana iliyoandaliwa na Nafiwe kufanya mapokezi hayo kwa kuhofia kuonwa na kundi la Jackline hivyo aliona wale wote wanaofahamika na kundi hilo si vizuri kama watakwenda Bandarini kuwapokea watu wao hao. Hivyo baada ya kupokewa waliwasili nyumbani kwa Madam Nafiwe.
"Siamini macho yangu, karibuni sana viongozi wangu, karibuni sana Namibia."
Nafiwe aliwakaribisha wageni wake.
"Asante sana Madam Nafiwe tunamshukuru Mungu tumewasili salama pasi kuwa na tatizo lolote, Nafiwe poleni kwa yote mnayokutana nayo kwenye zoezi hili ambalo nilijua litachukua muda mfupi kumbe nilijidanganya kwani sikufikiria maadui zetu wamejipangaje."
Santana aliwapa pole kwa yaliyotokea mpaka kufikia kumpoteza Tom na si Tom pekee bali kuna Suzanne (Dorine), Dereva wa Asnat pamoja na mlinzi wa kule Gezra aliyeuawa na Nafiwe lakini chanzo kikiwa ni kundi la Jackline.
" Asante sana Santana naweza sema hili ni letu sote lakini pia kuna daktari aliyemhudumia mgonjwa wetu mpaka anakata roho naye alipotoka tu humu aliuawa na hao watu mita chache kutoka hapa nadhani unakumbuka nilivyokuambia kuwa hawa watu kama Wavietnam wametapakaa kila kona."
Nafiwe akiwa anatokwa na machozi aliwasimulia yale yanayofanywa na kundi la Jackline na mwenzake Jasmine.
" Mhh kweli hii imekuwa ni zaidi ya Umafia yaani mauaji yanafanywa mpaka mlangoni kwako Nafiwe? Mbona siyo yule ambaye huwa hakubali kupigwa kijinga hivyo? Nafiwe ni wewe kweli au nimjuaye alishakufa?"
Santana aliinuka na kuanza kumshambulia madam Nafiwe akiwa kashikiria koti lake mkononi.
" Santana hivi unafikiri huu ni muda wa kulaumiana kweli? Kumbuka Tom yuko ndani anaendelea kuharibika tu, unaonaje tumalize hili kwanza kisha mengine yafuate."
Nafiwe alimtuliza Santana na kumkumbusha kilicho ndani. Hivyo ikabidi Santana atulie na kumuomba wakamuone alipohifadhiwa. Waliingia kwenye chumba hicho na kutoa heshima zao kwa kamanda wao aliyelazwa chali na Roberto.
" Vipi eneo la kuuchomea mwili wake limeandaliwa tayari? Maana majivu yake baada ya oparesheni hii tutayachukua na kurudi nayo Brazil ambako atahifadhiwa na eneo letu maalum."
"Liko tayari si unajua kuwa inatakiwa jamii isijue hili hivyo tutamchomea nje kidogo ya mji kwenye kipori cha kuelekea Windhoek na tutafanya hivi itakapofika usiku."
Madam Nafiwe alitoa maelekezo ya itakavyokuwa kwenye maziko ya Tom.
"Kwa hiyo mwili wa Dorine ulizikwaje?"
Santana alitaka kujua hilo pia maana huyu naye alikuwa ni mtu muhimu kwenye shughuli zake kule Brazil.
"Tulichelewa serikali walifika mapema na kuubeba hivyo kujitokeza nilishindwa si unajua tena wanafahamu upande wa pili nafanya nini hivyo ningeonesha pua yangu pale wangehisi kitu hivyo nilikuwa mpole lakini kwenye maziko ya Jumuiya yaliyofanywa na jiji tulihudhuria kama watu maarufu wa eneo hili. Mwisho niliagiza vijana wangu wazoe mchanga ambao niliuhifadhi humu ndani kwenye kiunga kile pale ndipo nilipomlaza Dorine."
Baada ya Nafiwe kutoa maelezo hayo waliongoza mpaka kwenye kiunga hicho kilichojengwa kaburi la Dorine na kutoa heshima zao na kisha kurejea ndani.
Chakula kiliandaliwa mahali hapo wote wakajumuika kupata chakula pamoja na wageni wao.
" Hivi kwa ulivyo Madam Nafiwe wamekuoteaje wajinga wale?"
Santana alimtazama Nafiwe kisha akamtania.
"We acha tu vile Vibinti si vya mchezo kwani nakumbuka siku niliyokuwa namsubiri Dorine aje anichukue nilikoswa kugongwa na waliomteka hivyo muda huu tunaoongea na kucheka isingekuwa hivi bali ingekuwa kinyume chake huku jina nalo likiwa limebadilika.
" Acha uoga binti Namibia, Simba kaingia kazini nitakuonesha namna ya kuwakabili vichaa."
Santana alijigamba mbele ya Nafiwe.
"Haya tusijeanza kukimbiana hapa Santana wewe vimba tu humu ndani."
"Najua huniamini muulize mzee wangu Bruno kazi yangu anaifahamu vizuri sana, kwanza naomba niwaulize kwa siku zote hamjaweza kuyafahamu makazi yao?"
Santana aliendelea kujisifia mbele ya Nafiwe na watu wake lakini pia alitaka kujua wanaishi wapi wakina Jackline.
"Bado haijafahamika wanaishi wapi maana huibuka tu na kufanya mashambulizi ya kushtukiza na kupotea,lakini tulichokibaini ni makazi ya mzee aliyewaokoa."
Nafiwe alimweleza Santana kile anachokifahamu kuwahusu wakina Jackline.
"Vizuri, kuifahamu nyumba ya mzee huyo na hatua moja kuelekea kwenye mafanikio yetu andaa utaratibu natakiwa kufika kwenye makazi ya mzee huyo kabla ya jua kuzama."
Santana aliagiza kuongozwa kwa mzee Jerome Whistle kabla ya Magharibi.
"Ni Santana kwanini isiwe usiku wakiwa wamejisahau?"
Robinson alimtahadharisha Santana kwenda magharibi au mchana.
"Robinson unaongea nini kijana? Ninyi si mlikwenda usiku na si usiku tu bali ule wa manane lakini mliambulia nini kama siyo kumpoteza Tom tu."
Santana alimkumbusha Robinson juu ya anachokiongea.
"Sawa Santana itakuwa hivyo lakini tahadhari inatakiwa kuchukuliwa."
Ilibidi Nafiwe akubaliane naye lakini akionya kuchukua tahadhari.
Baada ya maandalizi ya kutosha mchana huo walipata kupumzika kidogo kuusubiri muda ufike wa kuelekea kwa mzee Jerome Whistle.
****
" Habari yako kaka."
Jackline alimsalimu fundi makanika waliyemkuta akipuliza rangi kwenye moja ya gari aina Suzuki 56 ambayo ni ya wazi gari ya kazi.
"Nzuri dada zangu, karibuni kwa huduma."
Aliitikia baada ya kuwatazama bila shaka ni kutokana ugeni wa sura hizo.
"Asante sijui tunaweza kuongea mara moja kaka yetu?"
Jasmine alimsogelea na kumtaka waongee kidogo.
"Bila shaka dada lakini isiwe muda mrefu si unajua tena mida ya kazi hii jioni hesabu kwa bosi."
Fundi huyo alimjibu huku akiachia mashine yake ya rangi na kuchukua kitambaa ambacho alikuwa akijifutia marangi ya mkononi.
"Usijali kuhusu hilo kwani sisi tunaweza kukupa likizo ya siku nzima na bado tukakupa mkwanja mrefu ambao unaweza kuutumia kwa muda mrefu zaidi."
Jackline alimjibu baada ya kuona anaongea kwa mashaka.
"Acheni utani ninyi kwa maisha gani mliyonayo mbona nikiwacheki naona mmepauka sana sasa huo mkwanja mtautoa wapi ili mnipe mimi mtoto wa mjini?"
Fundi magari huyo aliwajibu kwa dharau kutokana na muonekano wao kwa wakati huo, na kweli kwa wakati huo walikuwa wamefubaa sana mpaka rangi yao asilia ilianza kufifia.
Kauli ile ilimchukiza Roberto ambaye alimsogelea yule fundi na kumpiga na kibunda cha hela usoni.
"Acha dharau kijana, usimjadili mtu kwa muonekano wake."
Fundi hakuamini alipokiangalia kitita kile bila shaka toka aanze kazi hiyo ya ufundi hakuwahi kukishika hivyo aliwaangalia kwa zamu kisha zile hela lakini hakujua azifanyaje akaishia kuziangalia tu.
" Bosi unashangaa nini furahia maisha yako kuanzia sasa ni zako hizo na ukitaka zaidi utazipata zaidi ya hizo."
Roberto aliendelea kumtamanisha kijana wa watu wa Kinamibia.
"Zaidi ya hizi? Kwa kazi gani mpaka mnipe zaidi ya hizi?"
Fundi yule aliwauliza baada ya kuyasikia maelezo ya Roberto.
"Ni hivi fundi, tunahitaji magari mawili kama hilo unalolitia rangi lakini yasiyo ya wazi, inaitwaje hiyo?"
Jasmine alimweleza hitaji lao lililowapeleka hapo kwake.
"Hiyo ni Suzuki 56 injini kubwa hiyo ilitolewa maalum kwa ajili ya kupita sehemu yoyote ile mpaka Jangwani si unaiona tairi zake?"
Fundi huyo aliielezea gari hiyo huku akiipigapiga kwa mbele akiwa na ujanja wa kutosha mfukoni.
"Sawa vipi uwezekano upo wa kuzipata?"
Jasmine aliendelea kumuuliza maswali.
"Kwa ajili yenu zitapatikana tu tena nitawaachia bure kabisa najua mkimaliza mishe zenu mtanirudishia mwenyewe kwani mara nyingi watu wajao kwa ajili ya kutembelea vivutio vyetu huyakodi hayo na ndiyo maana hapa yamejaa hayo tu kifupi gereji yetu inajihusisha na magari haya ya Suzuki 56."
Dereva aliwaelezea juu ya gari hilo.
" Fanya mambo tunazihitaji kufikia kesho ziwe kamili na la muhimu hatutaki kusikia chochote kutuhusu kutoka kwa mtu mwingine sawa."
Jackline alimsogelea fundi na kumweleza zinatakiwa lini na pia alimpiga mkwara mzito huku akimuonesha bastola iliyokuwa kiunoni.
Baada ya kuiona alichanganyikiwa fundi magari yule na kutoa macho yasiyo na kipimo.
" Wala msijali ndugu zangu nawezaje kutoa siri hii na mihela yote hii mliyonipa, sijui mna kiwanda cha kutengeneza hela daa."
Fundi aliongea hayo wakati wakina Jackline wakiishia zao.
"Kazi ya kwanza imekamilika tunachotakiwa kukifanya ni kwa sasa ni kupata vitendea kazi vya maana, mnaonaje kama tukienda kwa Daktari Abbas Mukesh pale KING'S MEDICARE CENTRE tukamuombe sindano ndogo pamoja na sumu ambayo tukimdunga mtu anakufa taratibu ndani ya masaa mawili."
Jessica alitoa pendekezo kwa wenzake kipi kifanywe muda huo.
" Kabla hujaendelea Jessica naomba nikukatishe kwa hilo, kwanini tutafute sumu isiyo na maumivu kwa huruma gani tuliyonayo ikiwa wao waliwaua wapendwa wetu kwa maumivu makali zaidi."
Roberto alilikataa wazo la Jessica na kutaka njia ya kuitumia njia ya risasi tu.
" Ni kweli jamani dawa ya moto ni moto kwanini tuingiwe huruma?"
Titiana naye alichangia wazo lake.
" Kwa hiyo tunaelekea wapi muda huu kumbukeni tuna la kufanya kila hatua ipitayo."
Jasmine aliwauliza baada ya kukaribia Hotelini.
"Kama ilivyokuwa kwa mama yake Roberto muda si mrefu tunaleta anguko jingine la moyo miongoni mwenu jiandaeni kwa maumivu."
Ujumbe uliingia kwenye simu ya Jasmine, aliusoma kisha akawaonesha wenzake wakiwa wanashuka kwenye gari kilichowastaajabisha zaidi ni namba iliyotuma ujumbe huo ilikuwa ni mpya na ina kiunganishi cha nchi ya Namibia ambacho ni +264 hapo wakapagawa.
" Atakuwa nani huyu aliyetuma huu ujumbe?"
Jackline aliuliza ujumbe huo utakuwa umetoka wapi na kwanini imetumika namba mpya.
"Nahisi huyu Santana kwa namna ambavyo hii meseji imeandikwa kwani kama mtakumbuka ujumbe uliowahi kutumwa huko nyuma ulikuwa kama huu."
Jasmine alihisi ulikotoka ujumbe huo.
"Naomba Jessica ingia mtandaoni itraki hiyo namba hiyo mara moja tutambaini tu muda si mrefu."
Jackline alimuomba Jessica aiangalie hiyo namba ili wambaini mtumaji wa huo ujumbe.
Na pia Jasmine alipata wazo la kumpigia Santana ili ajue yuko wapi kwa sasa. Baada ya kupiga simu ya Santana iliita lakini cha ajabu ilikatwa mara moja. Hali hiyo ilimfanya Jasmine aiangalie namba hiyo kabla ya kupiga tena.
"Mungu wangu !!!!!"
Jasmine alipiga kelele baada ya kuiangalia namba hiyo.
"Nini tena Jasmine?"
Roberto aliuliza baada ya kuuona mshangao huo machoni kwa Jasmine.
"Hamuwezi kuamini namba ya Santana imeita kwenye kiunganishi cha Namibia(+264) hivyo ndiyo kusema kuwa jamaa yuko ndani ya nchi hii."
Jasmine aliwaeleza wenzake alichokibaini baada ya kumpigia simu.
"Kwa hiyo ndiyo kusema kuwa Santana kesha kuja kutukabili sisi si ndiyo?"
Jackline alijikuta akijiuliza swali hilo ambalo kila mmoja alijiuliza swali hilo hilo.
"Tusimameni upya makamanda wangu vita ndiyo kwanzaaa tumeianza 'tupigeni cheers' kama ishara ya kuliamsha upya."
Jackline aliwaambia wenzake na kisha walipiga cheers la maana kwa kutumia Silaha zao.
Hilo lilifanyika ndani ya chumba cha Jackline hivyo baada ya zoezi hilo kila mmoja alivalia mavazi ya kazi tayari kwa kuelekea nyumbani kwa Nafiwe kwani walijua kuna jambo linaweza kutokea baina yao au kwa watu wao wa karibu.
Safari ilianza mara moja kuelekea kwa Nafiwe na wakiwa njiani kuna gari moja iliwapita kasi kutoka wanakoelekea wao na baada ya kuitazama ndani waliweza kuwaona watu wapatao kama watatu hivi lakini pamoja na kuwa ilikuwa ni usiku lakini waliweza kuziona sura zao zikiwa ndani ya surauficho na bila shaka walisahau kuzima taa ya ndani ya gari hiyo ndiyo iliwafanya waonwe na wakina Jackline.
"Roberto geuza gari ifuate hiyo gari au hujaziona hizo sura zilizomo humo?"
Jackline alimwambia Roberto ageuze gari na kuwafuata.
"Kwani wakoje nilikuwa bize na usukani tu?"
Roberto alimuuliza Jackline.
"Utajua tukiwafikia ila tu wanaonekana si watu wazuri kwani mwendo wao, sura zao zilivyofichwa ni dhahiri kuna jambo huko."
"Wameficha sura zao?"
"Ndiyo Roberto."
Jackline alimjibu.
Hapo ikawa kama ameyaamsha mashetani ya Roberto kwani aliongeza mwendo mara dufu kiasi ambacho wakina Jasmine walikasirika sana lakini hiyo hakuiona Roberto.
JE UNAFIKIRI NINI KITATOKEA?
Wakiwa bado njiani Jackline akapata wazo la kumpigia simu mzee Jerome Whistle kujua yuko wapi ili ampe angalizo juu ya wageni wasio rasmi. Simu iliita na kisha aliipokea.
"Mwanangu vipi mlifika salama? Na mnaendekeaje lakini."
Mzee Jerome alianza baada ya kupokea simu.
"Tulifika salama na tuko salama mzee wangu, uko wapi muda huu?"
Jackline alimtupia swali mzee Jerome.
"Niko nyumbani hapa kuna kikazi nakifanya si unajua tena wadogo zako wako kwenye shughuli zao na leo walijihimu bandarini kuangalia mzigo kwa tuliowakabidhi boti hivyo nafuafua vinguo maana vimechafuka sana."
Mzee Jerome alimwambia Jackline akiwa na furaha zote akiwa hajui nini lengo la kupigiwa simu.
" Okay pole sana baba yangu, ila nikuombe rudisha nguo ndani na kisha hapo nyumbani ondoka na jifiche nyumba ya jirani uwe unaangalia getini kwako nahisi kuna watu wanakuja kwako si watu wazuri na sisi tuko njiani kuja huko, sijui umenielewa mzee wangu?"
"Kweli huu ni mwaka wa shetani, hivi wananitaka nini mimi lakini? Nimewalia nini ambacho kinawakosesha amani kiasi hicho? Sawa mwanangu ngoja nijikusanye haraka."
Mzee Jerome alikata simu na Jackline aliiweka simu mfukoni baada ya kuhakikisha kila kitu kiko vizuri.
Safari iliendelea lakini kwa spidi yote hiyo hawakuweza kuwaona hiyo ikatoa picha kuwa wamedhamiria si kwa mwendo huo.
" Hawa jamaa kiboko yaani kwa mwendo wangu huu sijawaona hata vumbi lao?"
Roberto ilibidi aongee baada ya kuona hakuna dalili ya kuwakuta wala kuwaona.
"Tufanye hima tutawakuta wamefika au tunaweza kuwaona mbele."
Jasmine alimtia moyo Roberto aliyekuwa kakitolea macho kioo cha mbele ya gari kama vile atoke awe mbele kabisa kwani alihisi ni kama vile haikimbii.Wakiwa umbali wa kama mita mia tano hivi kutoka kwenye nyumba ya mzee Jerome waliweza kuiona ile gari ikiwa imepaki mita chache kutoka getini kwa mzee Jerome.
"Ni kweli aisee gari lile pale tunafanyaje hapa?"
Roberto aliongea baada ya kuiona ile gari pale nje.
"Sogea mbele kidogo kisha paki pembeni tujue tunafanyaje, hofu yangu ni kama wamemkuta ndani."
Jackline alimuelekeza apaki kwani kwa kuiona ile gari tayari hakuna jema ndani ya nyumba ya mzee Jerome.
Jackline aliipiga namba ya mzee Jerome iliita lakini haikupokelewa, akaipiga tena lakini mwendo ni ule ule iliendelea kuita tu bila kupokelewa. Hisia ziliwaijia kuwa tayari mzee Jerome kapatwa na tatizo.
"Kuna shida ndugu zangu simu yake inaita tu bila kupokewa sijui ikoje?"
Jackline aliwaambia wenzake huku akiiangalia simu yake kama vile kuna kitu anakitarajia kukipata muda mfupi ujao kutoka kwenye simu hiyo.
Jasmine na Roberto walishuka na kuanza kutembea kuielekea nyumba ya mzee Jerome kupitia sehemu nyingine ili wasishtukiwe na walioko pale. Jackline naye akaona kwanini asalie kwenye gari akaona hapana akashuka na kujiweka sawa na kisha akaanza kuifuata barabara kwa maana ya kulifuata geti pasipo kujifichaficha kama wakina Jasmine ila tu kwa namna alivyokuwa kajifunga mwenyewe ingekuwa ni kazi kwa yeyote kumtambua kwa haraka. Aligeuka na kuwapa ishara wakina Jessica na Titiana kubaki garini.
"Tumeufikia ukuta lakini kuna milio ya risasi kutoka ndani."
Roberto alimtumia ujumbe Jackline.
"Kupitia huo ukuta tafuteni tageti haraka muwakabili kutokea nje."
Jackline alimjibu na kisha kuiweka simu mfukoni.
Muda huo Jasmine alikuwa kesha jiongeza na kulifikia eneo lilikuwa na urembo fensi ambazo ni ruvazi na kuchungulia ndani, kwa bahati aliweza kuona kinachoendelea mle ndani.
" Roberto njoo haraka uone kule."
Jasmine alimwita Roberto aliyekuwa akiiweka simu yake mfukoni.
Alisogea na kuchungulia ndani ambako waliwaona watu wawili wakipambana kuuvunja mlango wa kuingia ndani.
"Tunafanyaje hapa?"
Jasmine alimuuliza Roberto ambaye alikuwa bado akiendelea kuchungulia ndani wala hakuweza kumsikia Jasmine anazungumza nini. Jasmine aliona anachelewa alichokifanya alichukua bastola yake na kuilengesha kwenye kitundu kile na kuiseti vizuri kuwaelekea walipo wale watu kisha akaachia risasi mbili mfululizo. Kwa bahati mbaya hazikuwapata walishtuka na kuangalia huku na kule wakiwa wanakimbia kujificha.
"Sister vipi tena?"
Roberto alimuuliza Jasmine ambaye alikuwa anaitoa bastola pale huku akitukana.
"Wana Mungu wao washenzi wale, halafu nimeiona sura ya Chude pale."
Jasmine alimjibu Roberto huku akiondoka eneo lile kutafuta sehemu nyingine ambayo anaweza kufanya jambo.
"Baki hapo hapo endelea kuwacheki pale walipojificha wanafanya nini?"
Jasmine alimwelekeza Roberto huku yeye akiendelea kuizunguka nyumba kuufuata upande waliojificha.
"Mko wapi wanangu huku mambo si mazuri waliniwahi kabla sijatoka."
Mzee Jerome alimpigia simu Jackline kumweleza kinachoendelea.
"Hawajakudhuru mzee wangu?"
"Hapana bado wanapambana kuuvunja mlango wa kuingia ndani na mimi nimejificha stoo kwenye yaliko magunia ya nafaka na siyo kizembe niko na sub-machine gun yangu ambayo huitumia nikiwa kwenye uvuvi."
"Vizuri huko usitoke sisi tayari tuko nje tunajaribu kuwadhibiti."
"Sawa binti yangu, nawaaminia sana."
Jackline aliikata simu na kumpigia Jasmine ili kujua kinachoendelea, lakini badala ya kupokea simu Jasmine aliikata kitendo kilichotafsiriwa na Jackline kuwa kazi inakaribia kuiva haraka sana na yeye akalifuata gari la wale wabaya wao bastola ikiwa mkononi na kuipiga risasi za kwenye matairi ya mbele kisha akatulia akiwa katikati ya barabara kuona kama kuna anayeweza kujitokeza akaona kimya ndipo alipolisogelea na kufungua mlango na kuingia sijui alilifanya nini humo ndani lakini alitoka na kupiga tairi za nyuma na kujificha nyuma ya mti uliokuwa karibu na pale. Akiwa pale alisikia milio ya risasi kutoka ndani hivyo akaona atoke pale na kuufuata ukuta ili aupande lakini mara alisikia geti likigongwa kisha akatoka mtu akiwa kama kachanganyikiwa, Jackline akauachia ukuta na kuivuta bastola yake na kumtageti mtu yule ambaye alimpa mgongo.
Lakini kabla hajafanya lolote ashtukia jamaa akitoa ukelele huku akilishika bega lake na kutokomea ng'ambo ya barabara na kukimbia na kuliacha gari. Jackline alianza kumfukuzia yule mtu kule alikokimbilia.
"Hee nini kimetokea huko ndani?"
Jackline aliuliza baada ya kukutana na Roberto akiwa na anahema kwa nguvu huku kainama na kujishika magoti.
"Achana na huyo mshenzi kimbilia ndani kampe msaada Jasmine."
Jackline kusikia hivyo hakutaka kungojea maelezo mengi alitimua mbio ndani kuona kilichotokea. Baada ya kuingia alishangazwa kumkuta Jasmine akiwa chini anatapatapa kwa maumivu huku damu nyingi zikimtoka kwenye bega lake la kulia.
Haraka sana Jackline alimwinua na kumbeba kuelekea iliko gari yao ambayo inakaa kwa mzee Jerome, lakini akakumbuka kuwa funguo ziko ndani akatoa simu na kumpigia mzee Jerome.
"Toka na funguo ya gari haraka mzee huku nje Jasmine kajeruhiwa na risasi."
Akakata simu na kumshika vizuri Jasmine lakini wakati huo huo tayari wakina Jessica wakawa wameshafika na gari hivyo ikabidi wampakie baada ya kuona mzee Jerome anachelewa.
"Mshikilieni hivyo hivyo."
Jackline aliongea huku akiuendea usukani na kwa kasi ya ajabu aligeuza gari na kutimua vumbi.
Mzee Jerome anatoka anaambulia vumbi tu akatembea kulifuata geti lakini sijui nini kikamwambia geuka nyuma alipogeuka akamuona mtu kalala chini upande wa maua, akaangaza huku na kule kuona kama kuna yeyote alipoona hakuna alimfuata na kumuangalia. Muda huo huo akaingia Roberto akiwa na ile gari iliyoachwa pale nje.
"Mzee vipi uko salama? Hofu yetu ilikuwa ni kwako wewe."
Alimuuliza huku akishuka kwenye gari na kumfuata pale alipo.
"Huyo kachapwa risasi na Jasmine akiwa anashuka kwenye ukuta kabla hajaotewa na risasi iliyomjeruhi lakini nashukuru Mungu nilimshtua na risasi yangu iliyompata sijui ni mkono au bega maana alitoka mbio akiwa kashika sehemu ya mkono nimemkimbiza akawa kanizidi mbio."
"Mimi nilikimbilia ndani baada ya kusikia geti linavunjwa na kwenda kujificha stoo."
Mzee Jerome alimjibu huku akiendelea kumchunguza aliyelala kama bado anapumua.
"Mungu wangu huyu si ni mtu wa Santana?"
Roberto aliongea baada ya kumuona vizuri sura mtu yule.
"Vipi unafahamiana naye?"
Mzee Jerome alimuuliza baada ya butwaa la Roberto kutokea.
"Hapana lakini tumekutana mara nyingi kwenye mipambano kipindi wakina Jackline wako huku."
"Kwa hiyo unataka kuniambia wamekuja kufanya wanayoyafanya kwetu?"
"Mzee wangu unavyomuona huyu jua hata kiongozi wao asiyekubaligi kushindwa yuko hapa Namibia pia."
Roberto alimjibu mzee Jerome Whistle huku akimuinua na kumpakia kwenye gari lao lililotelekezwa na kisha kutoka naye wakiwa na mzee Jerome.
"Tunaelekea wapi kijana wangu?"
"Huu mwili tunatakiwa kuuacha nje na makazi yako kwa usalama zaidi na vile hatuwezi kujua iwapo gari hili ni lao au ni la wizi hivyo maiti na gari tunakwenda kuviacha huko."
Roberto aliongea huku akipambana na gari ambalo matairi yake hayana upepo hivyo kumvuta huku na kule barabarani lakini aliweza kuliwini. Baada ya kufika mbali kidogo alilipaki kando ya barabara na kumchukua marehemu na kumuweka siti ya dereva na kumuegesha kwenye usukani na kisha kufunga milango na kuondoka zao na kwa wakati huo hakuna watu waliokuwa wakitumia njia hiyo hivyo kuwa rahisi kwao kufanikisha zoezi lao. Mzee Jerome alitoa simu na kumtumia ujumbe mtoto wake Mustapha.
"Nyumbani tulivamiwa leo hivi ninavyowatumia ujumbe huu tuko barabarani tunataka kuelekea hospitali alikopelekwa dada yenu Jasmine kaumizwa vibaya na risasi."
Alipohakikisha ujumbe umemfikia mhusika aliiangalia namba ya Jackline na kuipiga.
"Mwanangu mmeelekea hospitali gani?"
"Tuko njiani kuelekea KING'S MEDICARE CENTRE."
"Okay na sisi tuko njiani kuja huko."
Alimjibu na kukata simu kisha akamgeukia Roberto na kumuelekeza walikoenda wakina Jackline.
"Safari ni KING'S MEDICARE."
Mzee Jerome aliongea kwa kifupi akiwa anaiweka simu mfukoni.
"Tuwahi tukachukue gari tuwawahi huko."
"Bila shaka kijana wangu."
Mzee Jerome alimjibu huku akiitoa simu mfukoni iliyokuwa inaita.
"Unasemaje Mustapha?"
Aliuliza baada ya kupokea simu.
"Hakuna mwingine aliyeumia baba?"
"Hakuna mwanangu ila tu tulifanikiwa kumuua mmoja wa Majambazi na mwenzake tulimjeruhi akakimbia. Si unanijua baba yako kwa shabaha."
Mzee Jerome alitumia nafasi kujivika kitambaa ya ustaa akimdanganya mtoto wake kuwa yeye ndiye aliyemuua jambazi.
"Baba umeanza uongo wako sasa ni nani asiyekufahamu kwa uongo wako. Ninaye kufahamu wewe kwa uoga wako kama hukujificha chooni."
Mzee Jerome alivyoona kashtukiwa na mtoto wake akamkatia simu. Lakini Mustapha akapiga tena.
"Ukweli mchungu eee? Tuache hayo dada kalazwa hospitali gani niende?"
"Ninyi rudini nyumbani mfanye usafi huko idadi yetu inatosha sana. Sawa kijana wangu? Ila uwe na adabu kwa baba yako."
"Sawa baba nimekuelewa."
Alikata simu na kuchukua funguo ya gari iliyokuwa mfukoni na kumkabidhi Roberto aliyekuwa akilikagua gari mara baada ya kulifikia lilipokuwa mle ndani.
Aliliwasha na kuondoka zao kuwafuata wakina Jackline hospitali.
***
"Unasemaje mkuu wangu?"
Lilikuwa ni swali la Nafiwe kutoka kwa Santana baada ya kupokea simu aliyopigiwa.
"Acha maswali mwanamke wewe nimesema nifuateni sijui niko sehemu gani hapa na giza hili."
"Mbona sikuelewi tukufuate kivipi wakati mna gari?"
"Mpaka nasema hivyo ujue mambo hayako sawa huku hata kidogo."
"Kivipi au mlipotea njia?"
"Unaonaje kama ukinifuata ujue nikoje kuliko kuendelea kunitwisha maswali yako bibie?"
Santana aliona amkatishe Nafiwe baada ya kuona maswali yamezidi.
"Nimekuelewa mkuu jitahidi usizime simu ili anayekufuata aweze kuitraki."
"Najua bwana."
Santana alijibu kwa ukali na kukata simu.
Nafiwe alimgeukia mzee Bruno na kumjulisha alichoambiwa na Santana.
"Mzee wangu nahisi Santana kapatwa huko naona anaongea kwa ukali tu mara kapotea na yuko sehemu gani yeye ni mgeni."
"Inawezekana waliwazidi au hawakufika kutokana na ugeni wake."
Mzee Bruno Gautier aliongea alichokihisi.
"Inawezekana ikawa hivyo, lakini shida ya Santana ni ubishi si unakumbuka nilimwambia aongozane na mwenyeji akatuchamba kuwa sisi ni timu ya washindwa atakwenda na Chude kwa kutumia GPS yako wapi sasa hawajafika na GPS yao wamepotea na sasa timu ya washindwa inakwenda kumpa msaada."
Nafiwe aliyakumbuka maneno aliyoambiwa na Santana kabla ya kuondoka.
" Msamehe tu bila shaka kapata somo kikubwa wafuatwe huko maana giza limeanza kukolea hili."
"Ni kweli kabisa mzee wangu, Robinson jiandaeni mkafuate bosi wenu huko aliko sijui ni wapi lakini najua njia pekee ni kuitraki simu yake."
"Sawa mkuu."
Walijibu na kuliendea gari na kuwasha lakini mzee Bruno akaomba kuongozana nao huko hivyo hakukuwa na pingamizi lolote wakaondoka kuelekea huko.
JE NI NINI KITAENDELEA HUKO?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA KUJUA KILICHOJIRI.
Waliingia mpaka ndani ya KING'S MEDICARE CENTRE baada ya geti kufunguliwa na gari liliposimama wahudumu wa kupokea wagonjwa walifika na wheel chair na kumchukua Jasmine na kuingia naye kitengo maalum huku nyuma yao Jackline akiwa sambamba nao. Wakati wakiingia ndani Jessica na Titiana walisalia nje kusikilizia kitakachoendelea huko ndani na baada ya dakika chache Jackline alitoka nje kuungana na wenzake na kuwaeleza kinachoendelea.
"Kila kitu kinakwenda vizuri wameshaingia naye chumba cha upasuaji."
Jackline aliwataarifu wenzake akikaa kwenye kiti.
"Mungu ampiganie dada yangu apone."
Jessica aliongea huku chozi likimtoka, Titiana alimfuata na kumtuliza.
Wakiwa pale mara alifika Daktari Abbas Mukesh na kushuka garini, aliongoza ofisini kwake huku akiitazama saa yake kwani kwa namna ambavyo alivyokuwa akitembea kwa kasi kidogo ni dhahiri kabisa alikuwa amechelewa. Lakini alipowakaribia wakina Jackline pale walipokaa aliwaangalia kidogo na kwa kutaka kupata uhakika zaidi alishusha miwani yake.
"Ni macho yangu au ni kweli ninachokiona?"
"Daktari Abbas wala huna sababu ya kujiuliza mara kumi kumi uko sahihi kabisa macho yako hayajakudanganya sisi ndiyo wale wale uliojaribu kuokoa uhai wao."
"Yes, Jackline?"
Daktari Abbas Mukesh aliuliza kwa hamaki kidogo.
"Ndiye mwenyewe mimi na pembeni yangu hapa ni Jessica pamoja na friendmate wetu Titiana."
Jackline alitoa utambulisho.
"Wao nafurahi kuwaona mkiwa katika nyuso za furaha kiasi hicho, bila shaka kuna jambo mpaka mko hapa kwetu?"
"Ni kweli daktari tumepata tatizo."
"Hebu nifuate ofisini kwangu tukaongelee hilo tatizo lako tafadhali."
Daktari Abbas alimtaka Jackline aongozane naye ofisini kwake ili akajuzwe hicho kilichowaleta pale. Hivyo alinyanyuka na kuongozana naye.
"Karibu Jackline, kulikoni huko?"
Daktari Abbas Mukesh alimkaribisha Jackline na kutaka amweleze kilichomleta King's Medicare Centre.
"Kama ujuavyo majanga yaliyo nyuma yetu."
"Ndiyo nafahamu."
"Basi jana lile kundi linalotuwinda lilifika nyumbani kwa mzee Jerome kwa kutaka kufanya umafia wao lakini kwa bahati nzuri tukawa tumewawahi na kutokea majibishano ya risasi yaliyopelekea Jasmine kupigwa risasi."
"Jasmine kapigwa risasi? Ya wapi? Na vipi hali yake?"
Daktari Abbas alijikuta akitokwa na maswali mfululizo ambayo hayakusubiri majibu.
"Tumekuja naye yuko chumba cha upasuaji kwani alipigwa ya begani ambayo hatujui imemuadhiri kiasi gani?"
"Okay hebu ngoja kwanza."
Daktari Abbas alimwambia Jackline asubiri kwanza alichukua simu na kupiga kitengo cha upasuaji ili kujua nini kinaendelea kwa mgonjwa wanayemfanyia upasuaji.
"Enhh vipi upasuaji unaendeleaje kwa huyo binti."
"Mkuu ndiyo tunamalizia haikuwa mbaya sana kwani ilikuwa ni begani na tumefanikiwa kuitoa risasi moja na hapa ndiyo tunammalizia kumshona."
Daktari mkuu wa kitengo cha upasuaji alimweleza mkuu wake kinachoendelea muda huo.
"Poleni sana Jackline kwa majanga mnayopitia, Jasmine yu buheri wa afya na upasuaji umekwenda vizuri ametolewa risasi moja begani."
"Mungu mkubwa, lakini haya yote yatapita na maisha mengine yataendelea. Kikubwa tufahamishane kinachoendelea kwani wale watu siyo wazuri najua watataka kufanya mauaji kwa wote walio karibu na sisi."
Jackline alitoa tahadhari kwa daktari kutokana na kilichotokea kwa mzee Jerome Whistle hakutaka kitokee kwa wengine.
" Usijali Jackline toka tulipolijua hilo tulichukua tahadhari zote lakini ni vyema kukumbushana hili."
"Sawa sawa na pia nakushukuru kwa msaada wako uliotufanyia kwa kushirikiana na daktari Hans Murray wa Makambi hospitali kule Windhoek hakika ninyi ni wa thamani sana kwetu na Mungu aendelee kuwapa uhai zaidi ili msaada mliotufanyia sisi mfanye na kwa wengine pia."
Jackline hakusita kutoa pongezi zake kwa daktari Abbas.
" Jackline usijali kabisa katika hilo kwani ni jukumu letu kufanya hivyo maana ndiyo taaluma yetu."
Daktari Abbas alipokea pongezi hizo na kumuahidi kuwa watafanya zaidi ya hayo kwa kuwa ndiyo shughuli yao. Wakiwa wanaendelea na mazungumzo mara aliingia mzee Jerome Whistle akiwa kaongozana na Roberto.
" Karibu mzee Jerome, vipi na wewe ulikuwepo pale nje?"
Daktari Abbas alimuuliza mzee Jerome kwani hakumbuki kama alimuona pale nje.
"Hapana daktari mimi ndiyo nimeingia muda huu na nilipokuulizia pale nje nikaambiwa uko ofisini hivyo nikaona si vibaya kama nikiungana nanyi."
"Karibu sana mzee wangu."
"Asante sana daktari vipi mgonjwa wetu anaendeleaje?"
Mzee Jerome alimuuliza daktari.
"La kumshukuru Mungu ni kuwa Jasmine anaendelea vizuri na oparesheni imeenda vizuri na kwa sasa bila shaka atakuwa yuko wodini."
"Da afadhali maana kwa namna tukio lilivyotokea lilimchanganya kila mmoja ila zuri kwetu ni kwamba yule ambaye alimchapa risasi amekufa na kwa ushirikiano na kijana wangu hapa tumemchukua na kwenda kumtelekeza mtaani huko."
Mzee Jerome alitoa maelezo ya kilichotokea.
" Vipi mliweza kumjua ni nani huyo?"
Jackline aliwauliza kama wamemtambua mtu huyo.
" Hapana ila sura yake si ngeni ni kama mtu wa Santana hivi."
Roberto alijibu huku akiitoa simu mfukoni ili awaoneshe picha ambayo alimpiga mtu huyo.
"Ni kweli Santana yuko nchini kwani huyu ndiye kijana wake wa karibu kuliko wote kwenye timu yake hivyo kama kafa huyu lazima kachanganyikiwa na hivyo anaweza kufanya jambo baya lolote lile. Huyu anaitwa Chude."
"Na ukumbuke pia aliyekuwa naye naye ana jeraha la risasi mkononi hivyo ni kuendelea kufanya uchunguzi kaenda kutibiwa hospitali gani?"
Roberto aliongeza. Baada ya maongezi yao waliongozana kuelekea chumba alikuwa Jasmine ili kujua hali yake na ikiwezekana awekwe chumba maalum chini ya uangalizi mkali kama hali yake itakuwa si nzuri kwa kuhofia kuingiliwa na mtu wa Santana.
" Baba dada Jasmine anaendeleaje?"
Ulikuwa ni ujumbe wa Mustapha akitaka kujua hali ya Jasmine.
Mzee Jerome hakusita kumjibu mtoto wake.
"Keshafanyiwa upasuaji anaendelea vizuri kwa sasa."
Waliwakuta wakina Jessica pale nje na kisha kuongozana nao mpaka wodini alikolazwa Jasmine baada ya upasuaji.
"Dada unajisikiaje kwa sasa?"
Lilikuwa ni swali la Jessica baada ya kuingia tu wodini na kumkuta akiwa kajilaza.
"Namshukuru Mungu, Madaktari na ninyi kwa kunipigania kwani kwa maelezo ya Madaktari ni kuwa kama ningecheleweshwa basi kama siyo kuupoteza mkono ingekuwa ni kupooza kutokana na risasi ilipokuwa imekaa."
Jasmine aliwaeleza kile alichoambiwa na Madaktari waliomfanyia oparesheni.
" Pole sana Jasmine, nakuahidi utakuwa poa muda si mrefu na utarudi kwenye majukumu yako."
Daktari Abbas alimhakikishia kuwa sawa muda si mrefu.
" Nashukuru sana daktari Abbas Mukesh natami hata iwe leo kwani baada ya kumuua Chude nilipigwa risasi hii na Santana baada ya kunifahamu na tayari nilikuwa nimemtageti hivyo hata alivyonipiga alikuwa anajihami tu kwani kitendo cha Chude kwenda chini kilimshtua hakukitarajia hata kidogo."
Jina la Santana kuhusika na kumpiga Jasmine liliwachanganya wote mle wodini kwani hawakutegemea kama angekuwa ni yeye wao walijua ni miongoni mwa vijana wao.
" Bad news' kama Santana ameingia mzigoni yeye mwenyewe basi ni habari nyingine hiyo tunatakiwa kupanga mkakati mpya wa kupambana nao."
Jackline aliongea baada ya kujua Santana ndiye aliyehusika na tukio lile.
"Ni kweli Jackline wakati Jasmine anaendelea na matibabu yake, tunatakiwa kuendelea na maandalizi ya shughuli mpya iliyo mbele yetu."
Roberto aliongea hayo naye baada ya kusikia kuwa Santana kaingia mzigoni.
****
Mzee Bruno Gautier na Robinson na kundi la walifanikiwa kumkuta Santana akiwa anatembea taratibu kwenye kibarabara cha vumbi huku akiwa hajui anaelekea wapi kwani hata watu aliokuwa anakutana nao njiani alishindwa hata kuwauliza uelekeo wake kwani alikuwa hajui chochote.
"Pole mkuu kwa majanga yaliyokukuta."
Robinson alimpa pole baada ya kukutana naye.
"Asante Robbie hali si nzuri kwetu kwani maadui wetu wamejizatiti vilivyo kila unayekutana naye si mzembe hivyo tuna kazi ya ziada ya kufanya."
Santana kwa mara ya kwanza alikiri udhaifu wao mbele ya wakina Jackline.
"Aisee inabidi tukuwahishe kwenye tiba kijana wangu kabla sumu haijatembea zaidi mwilini. Na Chude yuko wapi na gari?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza Santana baada ya kuona yuko pekee yake.
"Mzee wangu kwa hali hii unapata picha gani juu ya swali lako? Kifupi ni kwamba Jasmine kamuua Chude na mbaya zaidi alitaka kuniua na mimi nikamuwahi na ndipo nikapata upenyo wa kukimbia ile nafika nje nikakutana na chuma kilichocheza na mkono wangu, nilijikuta napotea mpaka gari ilipo."
"Pole sana kijana wangu kwa janga lililokukuta, kwa hiyo ndiyo kusema Chude hatuko naye tena?"
Mzee Bruno Gautier alijikuta akiuliza swali tena.
"Ndiyo hivyo mzee wangu."
"Kumbe tulifuate gari mlipoliacha na kisha tuufate mwili wake...."
Kabla Robinson hajamaliza maneno yake alikatishwa na Santana.
"Unasemaje Robinson? Mrudi kule nilikotolewa nduki mimi mnafikiri kuna usalama huko? La muhimu nimepona tuondokeni vyuma vinanunuliwa lakini si uhai."
Hakukuwa na la kufanya zaidi ya kuondoka eneo hilo kutokana na Santana kutoa tahadhari. Lakini wakiwa wanaiacha barabara ya vumbi na kuingia barabara ya lami waliweza kuiona gari kwa mbele mita kadhaa inayofanana na ya kwao ikiwa kando ya barabara.
" Hee mbona gari liko huku tena?"
Santana alijikuta akiuliza swali baada ya kuliona gari likiwa eneo tofauti na kule ambako aliliacha.
"Labda limefanana tu mkuu inawezekana siyo lenyewe."
Robinson alimjibu Santana.
"No, ni lenyewe si unaona namba yake pale ni ile ile niliimaki 'N... 0'
Santana aliwaambia hiyo gari ni yenyewe na si kwamba labda giza limemchanganya la hasha hivyo walipolisogelea aliagiza kijana mmoja waliyekuwa naye aende kwa tahadhari akaliangalie.
Baada ya kulifikia na kukuta hakuna pingamizi lolote aliwapa ishara ya usalama hivyo nao walisogea mpaka pale na kuteremka.
"Shiiiiiiii... t !!! Si unaona hawafai wale Chude wamemuweka humo na kuyashuti matairi yote."
Santana alifoka baada ya kumuona Chude akiwa kalalia usukani huku matairi yakiwa hayana upepo.
"Mshusheni huyo humo mpakieni kule, Robinson lete waya tulifunge na kulivuta mpaka nyumbani hakiwezi kubaki hapa."
Mzee Bruno Gautier aliagiza hayo baada ya kuona kiongozi wake kama kachanganyikiwa vile akiwa anaongea peke yake.
Walifanya hivyo kisha Robinson aliingia kwenye gari bovu na mzee Bruno akaingia kwenye ile aliyokuwa akiiendesha, safari ikaanza.
Waliwasili kambini na haraka sana Santana aliingizwa ndani kwa matibabu huku mwili wa Chude ukitolewa na kupelekwa chumba maalum.
"Santana pole sana kwa kilichokukuta."
Nafiwe alimpa pole Santana kwa hali ambayo alikuwa nayo huku akitafuta namba ya daktari wake mwingine baada ya yule wa awali kuuawa na Jackline.
"Nakuona unavyochekelea mwanamke?"
Santana aliongea huku akivua koti na shati lake.
"Una maanisha nini Santana?"
Madam Nafiwe alimgeukia kumuuliza Santana baada ya kuikata simu ya daktari.
"Kwani siioni sura yako ilivyo?"
Santana alimjibu.
"Shida yako Santana hakuna jema ambalo umewahi kuniambia na sina uhakika iwapo kama kuna kijana wako yeyote umewahi kukubali kile anachokifanya."
Nafiwe alimfungukia Santana baada ya kuona kuwa imekuwa 'too much' kwa maneno yake ya shombo.
"Hebu tuachane na hizo mambo zako hebu mwambie huyo daktari afanye haraka maumivu yameanza."
Ilibidi Santana abadilishe mada ili kuepusha mgongano baina yao. Madam Nafiwe alitoka nje kwa hasira na kumuacha ndani Santana na kuingia kwenye gari ili kwenda kumchukua daktari ambaye alidai usafiri wake uko matengenezo.
" Punguza maneno, si unaona umemkwaza tayari Nafiwe kitu ambacho si kizuri kuwa nacho kipindi hiki cha matatizo."
Mzee Bruno Gautier alimtahadharisha Santana kwa mambo yake ambayo huyafanya pasipo kuangalia nyakati.
" Achana naye mzee wangu, huyo ni mwanamke tu siwezi kumnyenyekea hata mara moja wewe mwenyewe unakumbuka kipindi kile namnyenyekea Jasmine lakini leo hii si huyu kanikosakosa risasi."
"Ni kweli lakini angalia huyo naye unayemsema ana hasira na wewe kwa mambo uliyomfanyia unafikiri itakuwaje siku ukikutana naye face to face?"
"Mzee wangu kwa hiyo unanitisha na wewe?"
Santana aligeuka na kuwa mkali.
"Si hivyo nakuambia tu kuna wakati unatakiwa kubadilika kijana wangu nyakati zinabadilika."
"Aaaaghhh, unanipanda kichwani unaacha kuangalia kile kilichotuleta huku gizani mzee wangu unageuka babu mshauri au unamtaka Nafiwe?"
Santana aliongea hayo huku akiitoa bastola yake kiunoni akitaka kumshuti mzee Bruno lakini hiyo ilionwa na Robinson ambaye aliuwahi mkono ule.
" Mkuu unataka kufanya nini sasa hujionei huruma kwa hali yako? Kufanya hivyo hujui unatoa ushindi kwa mpinzani?"
Alimnyang'anya bastola hiyo na kumpiga maswali ambayo badala ya kujibu Santana alianza kulia kwa kwikwi.
"Robinson ume..ume....kua ee mpaka una...unachukua bast..."
Kabla hajamalizia maneno yake aliyokuwa akiyaongea kwa kuyakatakata kutokana na hasira zake aliingia Nafiwe akiwa kaongozana na mtu mmoja ambaye bila shaka ndiye Daktari aliyefuatwa kwa ajili ya kumtibu Santana.
JE, NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI YETU.
Nafiwe alimuangalia Santana kisha akacheka kicheko cha dharau, akimkaribisha kiti daktari.
"Karibu mtaalam, mgonjwa ndiyo huyu lakini kama tulivyoongea ya humu ndani yabakie humu humu na si vinginevyo."
Nafiwe alimsisitizia daktari kwa yale ambayo waliongea kabla ya kufika pale.
"Wala usijali Madam shughuli kama hizi nimezifanya sana hivyo muwe na amani juu yangu."
Daktari alimjibu Nafiwe.
"Mnasemaga hivyo hivyo lakini dakika tatu mbele mlishabadilika."
Santana aliongea huku alikaa karibu na daktari kumpa nafasi ya kukiangalia kidonda chake.
"Hao ni wengine ila siyo kwangu mimi, naijua mipaka yangu ya kazi kwa hali zote lakini kabla sijaanza kazi mnaweza kuongea chochote kile kama nianze au niache na kuondoka maana ni kama vile mna wasiwasi na mimi."
Daktari aliona aoneshe msimamo wake mbele ya miamba hiyo.
" Unasemaje wewe? Uondoke kwenda wapi? Kama haukuwa tayari kwanini ulikubali kuja au ndiyo ulikuja kutuchunguza kisha upeleke ripoti huko siyo?"
Santana alisimama na kumkunja daktari ambaye alijua anaongea na watu wa kawaida hivyo kuweka utani wake.
"Brother ndiyo nini sasa tunakunjana namna hii wewe ni mtu wa namna gani usiyeujua utani?"
Daktari aliongea akiwa kasimamia ncha za viatu angekuwa peku tungesema kasimamia kucha kutokana na kabali ambayo alikuwa kakunjwa na Santana.
"Unasikia wewe daktari mimi siyo binadamu wa kawaida ni mtu hatari sana hivyo jiangalie na maneno yako? Utaokotwa mtaani ukiwa marehemu shauri yako."
Aliongea hayo na kumuachia, kitendo kile kilimfanya daktari kutokwa na jasho huku kikohozi kikiwa kimemkamata cha bila kutarajia.
" Nisamehe kaka sikujua kama vitu vidogo kama hivi vingetufikisha huku."
"Unanishangaa nini sasa tukiwa njiani nilikwambia nini? Na wewe umefanya nini? Nimekwambia kabisa kuwa mgonjwa wangu kavurugwa hivyo ukifika pale fanya kazi yako basi kujuana juana achana nako lakini wewe kichwa maji umekutana na kubwa yako, anza kazi bwana."
Nafiwe naye badala ya kumsaidia akaendelea kumsakama na maneno ya maudhi kitendo kilichozidi kumkwaza daktari.
" Okay sawa lakini laiti kama ningejua kuwa nitapatwa na haya wala nisingeingiza mguu humu kwenu."
Daktari aliongea huku akitoa vitendea kazi kwenye kibegi chake.
"Na wewe muda mwingine uwe unakuwa mstaarabu bwana mambo gani hayo sasa, kwani daktari alikutuma kwenda huko bila kampani ya kutosha?"
Madam Nafiwe alitupa shambulizi kwa Santana.
"Kwa hiyo unanisema siyo?"
"Siyo hivyo mimi nakuambia ukweli Big mambo yako siyo bwana."
"Haya bwana umeshinda wewe."
Aliongea hayo huku akiwa kakunja sura kutokana na vifaa vya daktari kuanza kazi yake ya kukisafisha kidonda bila shaka alikuwa akifidia aliyofanyiwa na Santana. Wakati matibabu yakianza Nafiwe aliwaita watu wake na kutoka nao nje kupanga yao na huku wakitoa nafasi kwa daktari kufanya kazi yake kwa uhuru.
"Kama mnavyoona hali si shwari hawa watu wametufikia kila kona, tusipochukua hatua za haraka tutaaibika nadhani ninyi wenyewe mnaona kila tukishambuliwa lazima mtu wetu apoteze maisha kitu ambacho siyo kizuri hata kidogo."
Madam Nafiwe hakutaka kuficha hisia zake juu ya kinachoendelea kati yao na wakina Jackline.
" Ni kweli kabisa Madam lakini bado tuna muda wa kufanya marekebisho na kuwarudi."
Robinson aliongeza.
" Halafu mimi nina mashaka na Robinson kwenye oparesheni hii, hivi ukikutana na Jackline uso kwa uso unaweza kumkabili kweli?"
Madam Nafiwe alimuuliza swali Robinson.
" Kuhusu hilo ondoa shaka kabisa kwa tumeshamfanyia majaribio mengi sana kwenye hilo baada ya kuwa na wasiwasi naye."
Mzee Bruno alimtoa wasiwasi Madam Nafiwe juu ya Robinson.
" Halafu kingine Madam unachotakiwa kukijua kwa sasa ni kwamba mtu huyo si mpenzi wangu na mbaya zaidi aliwaongoza wenzake kuwateka wazazi wangu na kuwatesa hivyo bado nina hasira nao sana."
Robinson alimfungukia Madam Nafiwe katika kuhakikishia kuwa hana mpango nao zaidi ya hasira nao.
" Okay vizuri kama uyasemayo ni ya kweli. Kumbe tunatakiwa kuchunguza uwepo wao kwenye maeneo matatu kisha tuwafanyie shambulizi, na maeneo hayo ni ile Hoteli ya The Camel ambayo mara nyingi wameonekana hapo, pili ni nyumbani kwa yule mzee walikoshambuliwa wenzetu nako wanaweza kuwa wameweka makazi yao na mwisho ni kwenye mahospitali wanaweza kuwa huko kwa matibabu ya mgonjwa wao hivyo tunatakiwa kutuma watu wetu kufanya uchunguzi mara moja kuanzia asubuhi."
"Bila shaka binti yangu mimi pia nitakuwa sambamba nanyi katika hili."
Mzee Bruno alijitoa kuungana nao kwenye mpango wao huu mpya ambao wanahisi unaweza kuwaletea matokeo chanya.
"Kumbe itakuwa vizuri mzee wangu, sasa Robinson na Malaika mtakwenda King's Medicare na Makambi hospitali kuwatafuta huko na pia mimi nitakuwa na mzee wangu kule The Camel Hotel na nyumbani kwa mzee Jerome na ninyi hapa Paul na wenzako mtakuwa na Santana kuilinda ngome sawa jamani?"
Alihitimisha Madam Nafiwe kwa swali la msisitizo ambalo mara nyingi jibu lake huwa ni ndiyo.
" Umeeleweka mwanangu hapo kila watu wajiandae kwa shughuli kama walivyopangwa."
Mzee Bruno aliungana na Madam Nafiwe katika hilo kisha daktari alitoka ndani akiwa na mkoba wake kuashilia kuwa kazi yake imekamilika na nyuma yake alikuwa Santana akiwa na sigara mdomoni.
" Kazi yangu imekwisha madam naomba mimi niende."
Daktari alitoa taarifa ya kazi yake.
"Okay sawa mtaalam wangu ingia tu kwenye gari nikukimbize mara moja."
Madam aliongea hayo huku akiifuata gari yake tayari kwa kumpeleka daktari.
"Vipi mambo yamekwenda vizuri?"
Mzee Bruno alimuuliza Santana.
"Yuko vizuri sema tu ujingajinga wake ndiyo sijaufurahia hata kidogo."
"Kijana wangu tulichokuwa tunakihitaji ni hicho tu hayo mengine unataka undugu kwake?"
"Yaishe mzee."
Santana aliona ahitimishe baada ya kuona mzee Bruno naye ni kama alikuwa amekwazika na yale ambayo alimfanyia daktari.
****
Jackline na Roberto walitoka pale hospitali na kuwaacha Jessica, Titiana na mzee Jerome kuendelea kumuangalia Jasmine. Safari yao muda ule ilikuwa ni kule uswahilini kwenye ile gereji ambayo walitoa oda ya gari mbili aina ya Suzuki 56 kwa ajili ya oparesheni maalum ambayo walikuwa wameipania hivyo waliamini wakipata magari hayo itakuwa poa sana. Hivyo kabla waliamua kwanza watie kwenye ile kampuni ambayo walikodi ile gari ili kuirudisha hivyo tairi ziliongoza huko na baada ya taratibu zote za kimalipo kukamilika walitoka na kuchukua Bajaj kuelekea kule gereji. Walifika na kumkuta kipanga wao ambaye waliongea naye na kwa kuwa kila kitu kilienda sawa walikabidhiwa kila mmoja yake kilichofuata hapo lilikuwa ni vumbi tu maana gari hizo zilikuwa vizuri barabarani. Breki ya kwanza ilikuwa ni Hotelini ambako waliingia ndani na kuchukua kila kilicho chao na kupakia kwenye magari yao rasmi ya kazi tayari kwa kuondoka.
"Tunakwenda wapi sasa maana na wewe dada yangu maamuzi yako yanakuwaga ya ghafla kama mganga wa kienyeji vile."
Roberto alimuuliza Jackline baada ya kuona wamepakia kila kitu chao kwenye magari huku akiunganishia na kiutani ndani yake.
"Nimehisi kuwa eneo hili litakuwa si rafiki kwetu kwa sasa maana nina imani baada ya tukio hili lazima wataanza kutuwinda tu."
"Ni kweli dada katika hili hata mimi nilikuwa nina hofu hiyo ilmradi umelibaini ni vyema kutokomea hapa. Sasa makazi mapya yatakuwa wapi?"
Roberto alimuuliza Jackline wakati huo akifunga buti la gari.
"Kuna sehemu moja nimeipata nasikia ni nzuri sana iko karibu kabisa bahari, hoteli hiyo inaitwa Flamingo Villas Boutique Hoteli naambiwa ni miongoni mwa hoteli ghali hapa Namibia."
"Kama umeipenda wewe basi na sisi tumeipenda vile vile tuanze safari."
"Poa."
Kila mmoja aliingia kwenye gari lake na safari ilianza mara moja, hoteli hii iko pembeni mwa Namport kwa kilometa za kutosha hivyo spidi za magari zilihusika. Wakiwa tayari nje ya mji wakingua msitu huu wenye hali Ujangwa mara Roberto aliyekuwa nyuma aliweza kuiona gari ndogo kupitia site mirror zake hivyo akawa amepata kazi mpya ya kuichunguza gari hiyo kama inawafuatilia au ina safari zake. Akamtumia ujumbe Jackline.
"Kuna mbwa ananusa mapito yetu huku nyuma."
Jackline alipousoma ujumbe ule akayapeleka macho kwenye site mirror ili kuiangalia gari hiyo lakini hakuweza kuiona kutokana na umbali kati yao hivyo ilibidi apunguze mwendo kwanza.
"Tusimame kwanza tuone uelekeo wao au ni bendera fuata upepo. Kama ni bendera lazima wapoteze mwelekeo."
Roberto alipoupata ujumbe huo ikabidi amuangalie Jackline atasimama sehemu gani ili naye afanye hivyo hivyo na baada ya mwendo kidogo walitia nanga. Walishuka na Roberto akatoa triangle zake na kuziweka kuashiria gari limepata tatizo kisha akaliegemea huku Jackline akiwa ng'ambo ya barabara akiongea na simu. Ile gari ilikuja na kuwapita kwa kasi na walivyoiangalia waliibaini ni gari ya kukodi si ya mtu binafsi hivyo wakawa wamebaini kitu, wakapeana ishara ya kuanza kuifuata nyuma gari hiyo. Roberto alitoa alama zake kisha kwenye gari safari ikaanza upya na safari hii ikiwa ni kasi kidogo kuhakikisha hawaipotezi ile gari.
"Kwa vyovyote vile lazima watatafuta uchochoro wa kujificha ili watutangulize mbele kama ni wenyewe hivyo hakikisha tunawaweka kati."
Roberto alimpigia simu Jackline kumuelekeza hilo.
"Hapa wamekosea njia lazima wagawane vipande vya ardhi na hapo ndipo watajuta kutufutilia."
Jackline alimjibu Roberto na kukata simu kisha kuelekea kukanyaga mafuta.
Baada ya mwendo mrefu gari ile iliacha barabara kuu na kuchepuka na kuwafanya wakina Jackline kuendelea na safari yao hilo halikuwasumbua kwani walijua ni janja tu hiyo hivyo hawakuweza kupunguza mwendo bali waliongeza mwendo kuwazuga. Na kama waliotea vile kwani walipofika kitongoji fulani cha wafugaji waliweza kuiona tena ile gari ikija nyuma yao kwa mwendo ule ule Jackline akamtumia ujumbe Roberto.
"Andaa mashine yako tukifika kwenye msitu ulio mbele yetu tunawasimamisha watuambie wanaelekea wapi?"
"Bila shaka, huwa haichezi mbali." Roberto alimjibu.
Na kweli walipofika tu kwenye kimsitu kile Jackline aliipeleka gari yake kulia na kuisimamisha huku Roberto kutokea kushoto aliikata barabara akasimama kisha wote kwa pamoja walishuka bunduki zao mkononi na kusimama katikati ya barabara na kuzielekeza kwenye ile gari iliyokuwa inawafuata, na katika kuwatia hofu maadui Roberto alipiga za juu futi chache kutoka sehemu ya juu ya gari hilo.
Jackline naye hakutaka kusubiri yeye alizichapa tairi zote mbili za mbele kama kawaida yake na kuifanya gari hiyo kuanza kuyumbayumba na kupoteza mwelekeo.
JE, UNAFIKIRI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA.
Gari ilikwenda na kugonga kingo za barabara, show ya mbele ilipoteza mvuto wake na kuifanya kuwa kituko. Roberto aliisogelea huku mkononi akiwa na mashine yake jasho likimtoka usoni mithili ya kijito kinachotiririsha maji.
"Fanya haraka tokeni humo ndani fasta kabla sijawasambaratisha sura zenu."
Huku mmoja akiwa anatokwa na damu kutokana na kupasukiwa na kioo baada ya gari kugonga ukingo walitazamana mle ndani ya gari kisha wakafungua milango kwa taabu sana na kushuka chini na moja kwa moja walikwenda na kulala kifudifudi mikono ikiwa mgongoni ambapo Jackline alifika na kuwapiga cheni maalum mikononi mwao wakiwa pale chini.
"Ninyi ni wakina nani? Na kwanini mnafuata kivuli chetu?"
Jackline aliwauliza akiwa kawaelekezea bastola yake tayari kwa kufanya kitu iwapo wataleta jeuri.
"Sisi tulikuwa na safari yetu wala hatukuwa tukiwafuata ninyi."
Aliyekuwa akiendesha gari hilo alijibu huku akijitingisha mikono yake kuashiria kuwa zile cheni zilikuwa zimembana sana.
"Una uhakika na unachokiongea brother?"
Jackline alimuuliza swali jingine tena dereva huyo ambaye sura yake ilikuwa imejaa makovu ya kutosha huku mwenzake akiwa katulia tu pale chini akiwa hajui afanye nini kujinusuru na janga hilo.
"Kweli kabisa dada yangu huo ndiyo ukweli wangu kwanini nidanganye?"
Dereva yule alishikiria msimamo wake pasipo kupepesa macho yake.
"Na itakuwaje iwapo tutabaini kuwa mmetudanganya?"
Roberto alimuuliza huku akimsogelea karibu yule dereva.
"Fanyeni chochote kile ambacho mtaona kinatufaa kama adhabu."
Alipojibu hivyo tu Jackline akampa ishara Roberto ya kuwasachi mfukoni huku yeye akilifuata gari lao kuchungulia kuna nini ndani ambacho kinaweza kuwasaidia. Basi Roberto aliaanza kuwakagua lakini hilo halikuwa jepesi kwani alipomsogelea tu yule jamaa mwingine ambaye alikuwa kimya muda wote alijipindua kutoka pale chini na kumtandika teke maridhawa la ikulu kunako via vya uzazi na kumfanya Roberto kuachia ukelele mkali kuashiria maumivu ambayo aliyapata na kumpeleka moja kwa moja mpaka chini huku bunduki yake ikienda kuanguka pembeni. Kitendo kile kiliwafanya wale jamaa wakiwa na cheni walizofungwa mikononi kwa nyuma kusimama huku mmoja akiifuata ile bunduki na mwingine akimrukia Roberto huku goti lake kalikunja na kwenda kumkita kifuani Roberto kabla hajafanya chochote kile,lakini kama vile walijisahau kwani Jackline kwa kasi ya upepo aligeuka na kumtandika risasi ya mguu wakati akihangaika kuichukua ile bunduki kwa staili ya kipekee wakati mikono imefungwa. Hiyo ilimpeleka kando ya ile bunduki na kumfanya Jackline kuichukua na kisha kumfuata yule aliyekuwa kamng'ang'ania Roberto na kumpiga kichwa na kitako cha bunduki.
"Aaaaghhh.....mamaaa kichwa changu."
Alipiga kelele hiyo akiviringika pembeni na kumpa nafasi Roberto kuamka haraka na kukimbilia nyuma ya gari kukojoa.
"Washenzi ninyi mtajuta kutufuatilia haki ya Mungu, kama mlikuwa na safari zenu iweje muanzishe ugomvi wakati tukitaka kuwakagua?"
"Jackline hao wameamsha mashetani yangu ngoja niwaoneshe..."
Alikuja Roberto na kuingilia mahojiano yale na kumfuata yule ambaye alimpiga teke la dolani na kumpiga ngumi nzito iliyokwenda kumpata vilivyo mdomoni.
"Aaaaghhh meno yangu....."
Alipiga yowe hilo huku akitema meno mawili chini kama haitoshi alimfuata na yule mwingine na kumtwisha kichwa kilichokwenda kutua usoni na kumfanya kupasuka paji lake. Roberto alionekana kama kupagawa hivi baada ya kukutana na upinzani ule lakini Jackline aliiona hiyo akamtuliza.
"Haya kwa usalama wenu ingieni kwenye magari pale mbele."
Jackline aliongea huku akimkamata Tanganyika jeki yule dereva na huku huyu mwingine akipambana kuinuka mwenyewe baada ya kumuona Roberto akimsogelea kwa kuhofia labda anataka kumgonga kichwa kingine cha usoni.
" Hakuna shida kaka mimi naenda mwenyewe."
Maneno yake yalimfanya Roberto kucheka kwani mtu mwenyewe anayeongea hivyo kuinuka ilikuwa kazi pale chini akamsogelea na kumuinua na kwenda kumtupia kwenye gari lake na kuwafanya kila mmoja kumbeba mmoja kisha kuishia zao na kuliacha lile gari lao pale pale. Walipofika eneo fulani hivi ambalo ni karibu na majengo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo ya Namibia walisimamisha magari na kuwatowa kisha kuwavuta mpaka kwenye miti ambayo iko karibu na majengo hayo na kisha wakawaweka kati.
"Tulieni hapo mna dakika chache za kuendelea kuvuta hewa hii kabla hatujawapeleka kuzimu, haiwezekani mcheleweshe safari yetu bila sababu haya salini Sala zenu za mwisho."
Jackline alidhamiria kufa jambo kwa jamaa hawa kwani muda huo alikuwa ameshakoki mashine yake tayari.
" Dada yangu punguza jazba mbona hili linaongeleka tu."
Dereva aliona wanakoelekea siyo kule ambako walitarajia akaona afungue kinywa.
" Kelele weweee huna muda huo wa kuongea na sisi tekeleza nilichokuagiza ufanye pekee na si vinginevyo sijui tumeelewana?"
Jackline mpaka kufikia hatua hiyo alikuwa hana utani kabisa kwani alishaanza kufumba macho kuonesha kwamba hataki kukishuhudia kile anachotaka kukifanya.
" Heeey mko chini ya ulinzi hamtakiwi kufanya chochote."
Ni sauti iliyowaamrisha kutoka kizani kwani muda huo tayari ilikuwa ni usiku na hawakuweza kumjua mtu huyo aliyekuja kwa kujiamini akiwa kawamulika tochi yenye mwanga mkali. Jackline hakuwa na la kufanya ikabidi atii amri kwa kuinama kuweka bunduki chini huku Roberto naye akifanya hivyo hivyo. Lakini Jackline alichokifanya kikawa tofauti kwani kwa kasi ya ajabu aligeuka akiwa kainama hivyo hivyo na kummiminia risasi mfululizo mtu yule kitu kilichosababisha wale mateka kutimua mbio kwani wakati Jackline akimshambulia yule aliyewavamia Roberto naye aligeuka kumuangalia kama amepigwa ama la ili aweze kummaliza.
"Roberto unashangaa nini Mijusi inakimbia kule wafuate !!!"
Jackline alimfokea Roberto baada ya kugeuka na kukutana na miti tu jamaa hawapo.
Roberto alipogeuka tena na kutoona watu alitoka mbio kuwatafuta jamaa ambao alijua atawanasa tu kwani hawawezi kukimbia vizuri kutokana na cheni walizofungwa mikononi kwa nyuma.
Yeye Jackline alimfuata aliyempiga risasi na kumkuta kalalia dimbwi la damu na baada ya kumsachi akakutana na vitambulisho vinavyomtambulisha kama mlinzi wa majengo hayo kutoka kampuni ya Ulinzi ya Home Security' hilo likamshtua Jackline akaangulia pande zote kama kuna mwingine anayekuja eneo hilo na baada ya kujiridhisha hakuna alitimua mbio kwani alijua ameharibu hivyo akaungana na Roberto kuwatafuta wale waliokuwa wamewakamata lakini bahati nzuri akamkuta tayari ameshawaweka chini ya ulinzi.
"Roberto tumeharibu huku fasta wape wanachostahili hao tuishie zetu."
Jackline aliongea huku akiwa juu juu huku macho yakiwa alikotoka hivyo Roberto akawa amoeba initially kitu hivyo bila kuuliza kulikoni alimimina risasi kuwaelekezea wale jamaa ambazo ziliwakuta vilivyo miilini mwao na kuwalaza chini na bila kusubiri chochote toka kwa Jackline aliwafuata na kuwakagua mifukoni ambako alikutana na vitu mbalimbali vikiwemo vitambulisho ambazo alimuonesha Jackline kisha waliingia kwenye gari zao na kutimua vumbi kuendelea na safari yao.
***
"Jessica umewasiliana na wakina Jackline?"
Jasmine aliuliza baada ya kuona kimya toka walipoondoka kuyafuata magari kule Gereji.
"Mpaka sasa hakuna lolote nililoambulia maana simu zao wote zinaita tu lakini hazijibiwi."
"Watakuwa wapi hao hebu jaribu kuwapigia tena."
Mzee Jerome alimtaka Jessica awapigie tena ili wajue waliko maana hali si nzuri kwa wakati huo.
"Inaita, baba inaita ya Roberto hii."
Titiana alisema huku akiwa kalitegesha sikio kusikilizia kama inapokelewa au la.
"Nambie mpenzi wangu."
"Mko wapi mbona mnatutia hofu kihivyo jamani?"
Titiana alimuuliza Roberto kwa sauti ya huruma sana.
"Baby huku tuliko ni nje ya mji na ni mbali sana kuna jambo tunalivizia bila shaka kufikia asubuhi tutakuwa na la kuwaeleza. Msiwe na hofu nasi tuko salama kabisa."
"Sawa mpenzi lakini jua mimi ni mwanamke nina wivu kama wanawake wengine. I love you."
"Niamini mpenzi nalijua hilo na katu siwezi kukusaliti nafikiri unalijua hilo."
Roberto alimjibu mpenzi wake na kukata simu.
"Nipe simu niongee naye."
Jasmine alimuomba Titiana simu aongee na Roberto.
"Amekata, lakini kasema wako nje ya mji kuna issue wanaifuatilia ambayo kufikia asubuhi watakuwa wana la kutueleza."
Titiana aliwaeleza wenzake kutokana hofu waliyokuwa nayo juu ya wakina Jackline.
"Itakuwa ni issue gani hiyo mpaka waondoke kimya kimya bila kutujulisha? Au Santana kalianzisha huko nini?"
Jasmine alionesha wasiw wake baada ya kusikia hayo kutoka kwa Titiana.
Wakiwa wanajulishana yawahusuyo wakina Jackline mara simu ya mzee Jerome iliita.
" Unasemaje mwanangu?"
" Kimenuka hapa baba."
Victor alimjibu baba yake baada ya kuulizwa.
" Kimenuka? Kuna nini Victor funguka?"
Mzee Jerome aliuliza kwa sauti ya juu iliyomfanya kila mmoja mle ndani kutega sikio kujua kulikoni.
"Baba hapa ninapokupigia hii simu tumeruka ukuta baada ya kutokea mlango wa nyuma, tulisikia kelele ya geti ikipigwa tukasikilizia kwanza kwani tulijua wewe huwezi kurudi leo lakini tukiwa bado tunaulizana atakuwa ni nani huyo? Si ndiyo tukasikia geti likivunjwa ile kuchungulia nje tukashuhudia watu wengine wakiwa juu ya kuta na tochi zokimulika huku na kule si ndiyo tukaiona hatari ndiyo kukimbia?"
Mustapha alimjulisha baba yake baada ya kumnyang'anya simu Victor aliyekuwa akikata kona kumwelekeza baba yake.
" Mungu wangu watakuwa wakina nani hao tena? "
Mzee Jerome aliuliza baada ya kukata simu.
" Nini tena mzee? "
Jasmine alimuuliza mzee Jerome Whistle baada ya kumuona akijikuna kichwa huku akiuliza swali lisilo na jibu.
"Nyumbani kwangu kumevamiwa wanangu na hata sijui itakuwaje?"
"Wamevamia? Wakina nani? Na wakina Mustapha wako salama?"
Jasmine aliuliza huku akijiinua pale kitandani.
"Dada sasa unakwenda wapi kwani umeambiwa huwezi kuuliza ukiwa hapo kitandani umejilaza?"
Jessica alimuuliza dada yake baada ya kuona anataka kuinuka pale kitandani kitu ambacho hakuwa tayari kukishuhudia kikitokea pale ndani japo habari waliyoipata haikuwa nzuri kwao.
NINI KITATOKEA NYUMBANI KWA MZEE JEROME WHISTLE? NA VIPI KUHUSU KWA UPANDE WA WAKINA JACKLINE?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
"Mdogo wangu Jessica hivi unataka nifanye nini kwa ambalo tumelisikia hapa na ukizingatia wakina Jackline wako kwenye oparesheni ambayo undani wake wanaujua wao."
Jasmine aliongea kwa machungu makubwa huku akiwa analiangalia bega lake huku machozi yakifanya usafi kwenye mashavu yake. Hakuna ambaye alimuangalia Jasmine akaachwa salama na machozi mpaka Jessica mwenyewe uzalendo ulimshinda akajikuta anamsogelea dada yake na kumkumbatia huku akiiungana naye kwenye majonzi hayo.
"Dada yangu simaanishi kukuzuia kufanya lolote kwenye hili ambalo limetokea lakini ninachokiangalia ni afya yako ambayo bado haijatengamaa, kule nyumbani wakina Victor wameokoa maisha yao kwa kukimbia kwanini tuwe na presha kiasi hicho?"
Jessica alimwambia dada yake akiwa anamshikashika bega lenye bandeji.
" Nalijua hilo mdogo wangu lakini hapa ninatamani niende nikawaoneshe kuwa mimi ni nani?"
" Nakujua dada yangu hebu jilaze kwanza tuwasubiri Madaktari tusikie nini kinaendelea kwanza mengine yatafuata."
Jessica alimkazia dada yake kwa kuwa anayajua maamuzi yake akikomalia kitu.
" Dada Jasmine msikilize mdogo wako afya yako ni muhimu sana kwa sasa na kama tulivyoambiwa wakina Mustapha wametoroka hiyo tu ni taarifa nzuri kwetu hapa ni kuendelea kufuatilia baada ya kuwakosa walifanya nini kingine."
Titiana aliongeza baada ya kumuona Jasmine akilala kwa hasira huku akigeukia ukutani kuashiria kuwa kachukia na hataki kuongea chochote na yeyote. Na hata baada ya kuambiwa hayo na Titiana hakujibu chochote zaidi ya kujifunika shuka mpaka kichwani.
" Wanangu naomba muacheni apumzike dada yenu."
Mzee Jerome Whistle aliongea hayo huku akiweka kitambaa chake mfukoni kikiwa kimeloa baada ya kulia sana na kilitumika kujifutia machozi. Hivyo walikubaliana na kumuacha apumzike na wao walitoka nje.
"Kwa muda huu ambao dada kalala mnaonaje sisi tukienda kuangalia usalama kwani sikutaka kumuonesha hisia zangu maana namfahamu yule anaweza kutoka hivyo hivyo na akaliamsha vile vile."
Jessica alitoa wazo kwa wenzake wakiwa nje ya chumba alicholazwa Jasmine.
" Ni usiku sana Jessica hauoni kama ni hatari kwetu na mgonjwa kwani wanaweza kutumia uzembe wetu kutushambulia kwani muda huu tuko hapa tuna uhakika gani kwa watu walio hapa kama ni wazuri?"
Titiana alionesha hofu yake na hivyo kutoungana na Jessica kutaka kutoka hapo na kumuacha mgonjwa wao.
" Tufanye kitu kimoja jamani, mimi na mzee Jerome twende tukaangalie usalama nyumbani na wewe Titiana bakia hapa na dada tutaungana na wewe baadaye kidogo."
Jessica alitoa wazo ambalo liliungwa mkono na wote hivyo mzee Jerome ambaye muda huo alikuwa kama kamwagiwa maji ya barafu aliingia kwenye gari tayari kwa kuondoka na Jessica baada ya kupeana moja mbili tatu na Titiana aliingia kwenye gari na safari ya kuelekea nyumbani kwa mzee Jerome Whistle ilianza.
"Mzee wangu punguza mawazo ni mapito tu haya tunayapitia kuna muda yatakwisha na maisha mapya yataanza upya."
Jessica alimwambia mzee Jerome Whistle baada ya kuona kila wakati kitambaa kinatembea machoni.
"Usihofu mwanangu tuko pamoja."
Alimjibu hivyo tu na kutulia kimya akiwa amegeukia kwenye kioo cha mlangoni kuangalia kinachoendelea nje. Lakini wakiwa katikati ya safari waliweza kupishana na gari ambayo kwa namna ilivyowapita walipata hofu maana miendo ya kundi la Nafiwe pamoja na Santana wanaijua vizuri.
"Samahani mzee wangu."
Jessica alimwambia mzee Jerome na kusimamisha gari pembeni kisha akatoa simu na kumpigia Titiana.
"Nambie wangu mmefika?"
Titiana aliongea baada ya kupokea.
"Bado wangu ila naomba unisikilize."
"Nakusikiliza."
Titiana alimjibu.
"Kuna gari limetupita kasi sana hapa nina mashaka nalo naomba hivyo naomba mfanye mchakato wa kutoka humo na kujificha wodi jingine au sehemu yeyote ambayo ni salama."
"Poa nimekupata ngoja tupotee zetu watakutana na manyoya na lazima tuwaoneshe mlango wa kutokea."
Titiana alimjibu Jessica kwa kujiamini kisha simu ilikatwa na Jessica akalirudisha gari barabarani na safari ikaendelea.
Baada ya kufika waliiacha gari mbali kidogo kisha walitembea kwa miguu kuifuatilia njia ya uchochoroni inayokwenda nyuma ya nyumba ambako watauruka ukuta na kuingia ndani kupitia mlango wa uliotumiwa na wakina Mustapha.
Wakiwa wanaukaribia ukuta ule mzee Jerome alitoa simu na kumpigia Victor.
"Eenhh vipi mko wapi?"
"Bado tuko hapa hapa nje ya jengo tunachungulia kinachoendelea ndani."
"Msitoke tunaukaribia huo ukuta au mnaweza kutuona upande wa mashabiki huku."
"Okay sawa baba nimeuona mwanga wa simu yako zima sasa ni hatari huo mwanga."
Victor alimshauri baba yake kuzima simu baada ya kuuona mwanga ambao unaweza kuwapa ishara maadui pia kama ilivyotokea kwake hivyo mzee Jerome Whistle alifanya hivyo na kuwasogelea pale walipo.
****
Ikiwa ni majira ya alfajiri wakina Jackline wakiwa wamechoka baada ya safari ya usiku kucha iliyoambatana na purukushani za hapa na pale njiani zilizopelekea kuchelewa kufika, waliingia ndani ya Flamingo Villas Boutique Hotel ambayo imejengwa kwa Ustadi wa hali juu huku parking ya magari ikiwa imeongeza uzuri wa Hotel hii kutokana na jinsi ilivyojengwa.
"Wao bonge la Hotel uliijuaje hii kitu dada Jackline?"
Roberto aliuliza wakiwa wanatoa mabegi yao kwenye magari.
"Kuna sehemu moja pale Namport wana Wakala wao ambaye ndiye hushughulikia kila kitu hivyo hapa tunapelekwa tu kwenye room zetu malipo na mambo mengine nilishakamilisha siku tatu nyuma."
Jackline alimjibu Roberto ambaye muda huo alikuwa bize kukagua mazingira kwa staili ya kuzungusha macho kama kinyonga.
" Okay nafikiri hili ni eneo zuri kwetu."
Roberto aliunga mkono huku akiliweka sawa begi lake begani.
Waliingia ndani na kumkuta mhudumu wa Mapokezi aliyewakaribisha kwa bashasha kubwa.
"Karibuni sana wageni wangu naitwa miss Angel karibuni Hotelini kwetu, Hoteli yenye hadhi ya kimataifa."
"Asante sana Angel naitwa Jackie na huyu hapa ni kaka yangu anaitwa Rob, hii hapa kadi yetu tulishafanya kila kitu kwa Wakala wenu kule Namport."
Jackline aliongea huku akimkabidhi ile kadi mhudumu yule wa Mapokezi. Baada ya kuangalia ile kadi aliwachukua na kuwapeleka kwenye vyumba vyao.
Walipooneshwa vyumba walihifadhi vitu vyao na baada ya kila kitu walitoka na kupumzika sebuleni kwa kuwa vyumba walivyochukua vinaunganishwa na hiyo sebule juu kabisa kwenye ghorofa la kumi na tatu.
"Lete vile vielelezo ulivyovichukua kwa wale panya."
Jackline alimwambia Roberto baada ya kuketi kitini.
"Okey ni kweli kabisa hebu tuvipitie tuweze kuwajua vizuri wale jamaa."
Roberto aliongea huku akivitoa vitu hivyo mfukoni kwake.
"Umeonaaa dada Jackline hii si ni businesscard ya Santana?"
"Okay sawa kumbe hawa mbwa walitumwa na Santana kutufuatilia sisi alijuaje kama sisi tutakuja huku? Hebu washa simu zao tuangalie kwa mara ya mwisho waliwasiliana na nani?"
Jackline alimtaka Roberto aziwashe simu za wale watu ili wajue mawasiliano yao ya mwisho yalikuwa baina yao na nani.
Baada ya kuzikagua vizuri walibaini mtu wa mwisho kuwasiliana nao alikuwa ni Madam Nafiwe na ilionekana kila wakati waliwasiliana naye hivyo kuubaini kuwa ni mtu ambaye aliwapa kazi japo walikuwa na kadi ya Santana.
"Kumbe Nafiwe ndiye aliyetuchora sisi ni nani aliyempa mchoro? Hapa tunatakiwa turudi haraka Namport tukampe kazi Jessica afuatilie mawasiliano ya Nafiwe."
Roberto alimwambia Jackline wafanye mchakato wa kurudi Namport.
"Hapana suala la kumpa kazi Jessica tutalifanya leo hii hii kwa kumtumia ujumbe tu ili sisi tuendelee kuyasoma mazingira hapa huwezi jua inawezekana wengine wako hapa."
Jackline alimtaka watumie ujumbe Jessica ili wao wabaki Flamingo kuendelea na uchunguzi wao.
" Itakuwa nzuri kumbe mjulishe ili muda huu tupate chochote tumboni kisha tuanze mambo yetu."
Roberto alikubaliana na wazo la Jackline ambalo lilikuwa ni kumjulisha Jessica aifuatilie namba ya Nafiwe na Santana kujua wanawasiliana na nani na ndivyo ilivyokuwa na baada ya hilo waliagiza chakula kiletwe kule juu. Lakini mara simu iliingia kutoka kwa Jasmine ambayo Jackline aliipokea baada ya kumfahamu mpigaji.
"Halo Jasmine unaendeleaje?"
"Naendelea vizuri japo hali si shwari huku mko wapi?"
"Tulikuja kuandaa mazingira ya kambi mpya ndani ya hotel ya Flamingo Villas Boutique ambayo tulijua itakuwa sehemu poa kwa misheni yetu lakini mambo yamekuwa tofauti baada ya kukutana na watu waliokuwa wakitufuatilia kwa nyuma Mungu ni mwema tumewazima wote wawili lakini tuliwakuta na businesscard ya Santana pamoja na simu zao zikiwa na namba zao pia hivyo tumempatia Jessica aifuatilie kujua ni nani yuko nyuma yao anayevujisha siri zetu ni hivyo na umesema hali si shwari kulikoni?"
Jackline alihitimisha maelezo yake kwa swali.
" Kwanza poleni sana kwa majanga mliyokutana nayo huko lakini huku jamaa wamevurugwa balaa jana walivamia nyumbani kwa mzee Jerome usiku lakini hawakuambulia chochote kwani wakina Mustapha waliruka ukuta na kupotea zao gizani na baadaye Jessica na mzee Jerome walikwenda kuangalia kinachoendelea lakini kilichotokea huko asikwambie mtu pambazuko liliamlia wakakimbia lakini Nyumba ya mzee Jerome imechakaa hasa vioo vya madirisha kutokana na kushambulia wakiamini wahusika wako ndani kumbe wakina Jessica walishambulia kutoka nje upande wa nyuma hivyo kama vipi hebu rudini tufuatilie hili ili tunapoondoka tuondoke timu yote."
Jasmine alitoa maelezo marefu ambayo yaliwatoa machozi wakina Jackline.
" Poleni sana vipi lakini hakuna aliyeumia? "
Jackline aliuliza hilo tena.
" Amewaficha lingine ni kwamba walikuja hapa hospitali kututafuta ila tuliwawahi na kufichama wakatoka patupu."
Titiana alimnyang'anya simu Jasmine na kuongeza lile ambalo Jasmine alitaka kulificha.
" Titiana poleni sana nawahakikishia kuwa tunaingia barabarani kwa ajili yao hao wajinga."
Jackline alimwambia Titiana na kukata simu huku akiinuka na kuvaa jaketi, kitu kilichomtoa macho Roberto.
"Wapi tena si tumeagiza chakula?"
Roberto aliona aulize swali baada ya kuona Jackline kama alichanganyikiwa baada ya kukata simu.
"Hakuna haja kusubiri chakula ilhali wenzetu kule wamevamiwa na Santana cha kufanya kawaambie watufungie kama hawataenda na muda tunawaachia tunaondoka zetu."
Jackline alimjibu huku akiiangalia bunduki yake kama iko vizuri na kuingia chumbani kuchukua vitu ambavyo vitatumika mbele ya safari.
Walitoka na kushuka ngazi haraka huku Roberto akimwelekeza mpishi awafungie chakula na kuwawekea na juisi kisha awaletee kwenye maegesho ya magari.
JE, NINI KINAKWENDA KUTOKEA?
Mpishi yule alimkabidhi Roberto vile viboksi vya vyakula na kuviweka ndani ya gari yake kisha kuingia na kufunga mkanda na muda huo Jackline alikuwa tayari nje ya jengo akiwa mdogo mdogo kumsikilizia Roberto na baada ya kutokea tu safari iliinza huku miendo ya gari zao ikiwa utafikiri kulikuwa na mashindano ya magari kitu ambacho kilipelekea kila aliyepishana nao njiani hakusita kuwaangalia kupitia 'site mirror' zao bila kusahau waenda kwa miguu ambao hawakusita kugeuza vichwa vyao kuwaangalia. Safari ilikuwa ni ndefu sana safari hii ukizingatia walishaijua vizuri lakini walipofika lile eneo ambalo walipambana na vibaraka wa Nafiwe na kupelekea gari kupata ajali waliwakuta askari wakiendelea na uchunguzi wa tukio lile huku miili ya wahusika wakiitoa kule ambako ilikuwa na kuisogeza kwenye gari la wagonjwa, askari wengine waliendelea kuyasimamisha magari na kuyafanyia ukaguzi lakini wakina Jackline walivuka kizingiti hicho na kuendelea na safari.
Simu ya Jackline iliingia ujumbe ambao ulitoka kwa Jasmine baada ya kuuangalia.
"Jackline tumeruhusiwa kutoka hivi tunaelekea kwa mzee Jerome tukiwasubiri mfike tujue tunafanya lipi."
Baada ya kuusoma akaona ampigie tu hivyo ili kuepusha ajali barabarani kutokana na mwendo waliokuwa nao.
"Halooo...."
Aliita Jackline.
"Niambie Jackline umeupata ujumbe?"
Jasmine alimuuliza Jackline.
"Yes nimeupata daktari Abbas kasemaje? Na tayari mmeondoka?"
"Yeye kasema kwa sasa niko vizuri naweza kurudi tu nyumbani kuendelea na dawa ambazo kanipatia na hapa tuko njiani tunaelekea kwa mzee Jerome."
"Basi vizuri na sisi tuko njiani tunakuja kikubwa ni kuwa makini hao panya lazima watarudi leo usiku au alasiri si unajua zao ni kuvizia tu."
Jackline alimtahadharisha Jasmine kutobweteka wawapo kwa mzee Jerome.
Kisha aliikata simu na kuiweka pembeni mkono ukarudi kwenye usukani na kuanza kumtafuta Roberto ambaye muda huo alikuwa mbali sana lakini alikuwa akimuona kwa mbali.
" Dada mbona hampatikani huku kulikuwa na majanga usiku wa kuamkia leo."
Mustapha alimtumia ujumbe Jackline ambao aliuangalia na kisha kuusoma na hapo hapo aliichukua simu na kumpigia naye.
"Mustapha tutaungana nanyi muda si mrefu tuko njiani naendesha."
"Sawa dada nimekuelewa."
Mustapha alimjibu kisha simu ilikatwa na hapo Jackline akaona aizime kabisa ili kumfikia Roberto.
Na baada ya masaa kadhaa waliwasili ndani ya Namport na hapo Jackline aliiwasha simu yake ili kuwasiliana na Roberto kujuzana wanaelekea wapi.
" Nisubiri hapo kwenye hicho kituo cha mafuta cha 'LA Oil'
" Okey sawa."
Roberto alimjibu lakini wakati huo huo Jackline alikuwa ameshafika na kuliingiza gari kituoni hapo.
" Hebu tuwekee mafuta kiasi cha lita ishirini kila gari, tufanyie haraka tafadhali."
Jackline alimweleza mhudumu wa kituo hicho cha mafuta, wakati mafuta yakiwekwa Jackline alimfuata Roberto na kupanga naye mkakati.
"Unaonaje tukamchukue yule dogo aliyetuuzia haya magari, nina wasiwasi naye huenda ndiye aliyetuuza nahisi hivyo."
Jackline alimwambia Roberto kile anachokihisi juu ya mtu aliyetoa siri kwani hakuna mtu ambaye alijua safari yao inaanzia wapi baada ya kutoka pale Gereji.
" Unajua nini? Hata mimi hofu yangu ilikuwa pale pale kwa yule jamaa maana safari yetu ilitokea pale."
"Au haya magari yalitegeshewa kifaa cha kuwafuatilia?"
Jackline aliuliza.
"Upande wa divice' kufungwa sina uhakika ila tukambebe yule dogo."
Baada ya majadiliano hayo waliondoka mpaka pale Gereji ambapo waliingia mpaka kwenye maegesho ya magari ya wateja na kusimama.
Walishuka na kuelekea ndani iliko ofisi ya Gereji hiyo.
"Wewee dogo uko wapi?"
Jackline aliita baada ya kukuta ukimya umetawala mle ndani hakukuwa na shughuli yoyote iliyokuwa ikiendelea pale.
"We Roberto mbona hakuna dalili ya mtu humu ndani au dogo kasafiri nini?"
"Mimi mwenyewe nashangaa hii hali kama ameondoka mbona geti lilikuwa wazi huku kila kitu kiko sehemu ya kazi yaani kama vile kuna kazi ilikuwa ikiendelea, hebu cheki hii injini ni kama ilikuwa ikitengenezwa hapa."
Roberto alimjibu Jackline.
"Mmhh mbona kuna matone ya damu?"
Jackline alimuonesha Roberto matone ya damu yaliyoanzia pale ilipokuwa ile injini na kisha kukaonekana mbuluzo wa kitu hali iliyowashtua na kuwafanya kila mmoja kuchomoa bastola yake na kuiweka sawa kisha kuufuata mbuluzo ule.
Waliufuatilia mpaka kwenye magari mabovu yaliyokuwa yamewekwa upande wa nyuma.
"Ohh my God , njoo uone dada Jackline."
Roberto alimwita Jackline aje aone kilichokuwa ndani ya moja ya magari yale.
"Kuna nini?"
"Wewe njoo na angalia ndani ya gari hili."
Roberto alimuonesha Jackline ndani ya gari lile bovu na kitu alichokiona kilimfanya atoe ukelele.
"Mamaaaa nini hiki? Noooo haiwezekani, nasema haiwezekani !!!"
Hapo hapo walitoka eneo hilo haraka bastola mkononi na kurudi kwenye magari yao.
WAMEKUTANA NA NINI?
"Robinson umefanya nini sasa kule?"
Madam Nafiwe alimuwakia Robinson baada ya kupokea taarifa kuwa badala ya kumkamata yule fundi magari yeye akafanya maamuzi yake pasipo kuwa na subira.
"Naomba unisikilize madam."
Robinson aliomba asikilizwe kabla ya kulaumiwa.
"Nitasikiliza nini Robinson kutoka kwako, hivi unafahamu maana ya kuzingatia maelekezo?"
Nafiwe alikuwa hakaliki kitini hii ilionekana kumchanganya sana.
"Bibie hebu mpe nafasi ajieleze inawezekana anayo sababu ya kuchukua maamuzi yale."
Mzee Bruno aliingilia mazungumzo yale ambayo hayakuwa na muafaka wowote zaidi ya kupandishiana tu.
"Mzee wangu katika hili unafikiri nitamuelewa Robinson hata kidogo hivi anamfahamu yule dogo mimi hunisaidia vipi katika mishe zangu?"
"Ni kweli inawezekana sisi tukawa hatujui lakini tujiulize kwanini aliwakodishia magari watu ambao tunapambana nao? Huoni kama alikuwa katusaliti?"
Santana aliona asimame baada ya kumaliza kuvuta sigara yake kubwa iliyochanganywa na madawa ya kulevya na kumuanzia madam Nafiwe.
" Kwa hiyo unataka kusema nini hapo Santana au wewe ndiye ulimuamuru amshambulie akimkuta? "
Madam Nafiwe alimpiga swali Santana huku akiwa kamfuata karibu zaidi.
"Ha ha ha unauliza kuhusu hilo, kwani sisi huku tumefuata kutengeneza undugu na mtu? Imetuleta kazi tu ya kuwamaliza panya wote wanaopita kwenye njia zangu na si vinginevyo Nafiwe na ukinivuruga nakupoteza mara moja."
Santana aliona amvimbie Nafiwe baada ya kuona anataka kumpanda kichwani hilo lilipelekea Nafiwe kuchanganyikiwa kwani Santana aliongea hayo akiwa kamshika kidevu chake kama vile anataka kumkisi kumbe zilikuwa ni hasira zilizopitiliza kwani baada ya kumwambia hayo alitoka zake nje.
Robinson alimfuata madam Nafiwe na kumuelekeza ilivyokuwa kabla ya kuchukua maamuzi magumu.
"Madam sikutaka kufanya vile lakini ilinilazimu baada ya kutaka kunishambulia na nilivyomdhibiti alipokonyoka na kukimbilia sehemu alipokuwa ameiweka injini aliyokuwa anaitengeneza akachomoa simu na kuanza kumpigia mtu ambaye sikumjua na kwa kuwa tayari mlinieleza kuwa anafanya kazi na wakina Jackline nikajua moja kwa moja anawapigia hivyo nikaona kabla hajamaliza nimnyamazishe kabla hayajawa makubwa wala si vinginevyo Madam."
Robinson aliuhitimisha uongo wake ili mradi tu nafi amuelewe.
Lakini badala ya kumjibu kama ameelewa au la Nafiwe alimuangalia Robinson kuanzia juu mpaka chini kisha akasonya na kuondoka zake kuingia chumbani kwake na kuwaacha mzee Bruno na Robinson wakitazamana bila kujua wafanye nini.
"Kijana wangu ulichofanya ni chenyewe huyo mpuuzi achana naye hizo hasira zake zitamgharimu tu tuangalie kinachofuata."
Mzee Bruno alimfuata na kumnong'oneza sikioni Robinson kisha akampiga begani na kuondoka kutoka nje kumfuata Santana alipokuwa kakaa huku Robinson akiachwa pale sebuleni akirusha mikono juu kushangilia ushindi. Lakini mara akashtukia akiguswa kisogoni na kitu cha baridi.
"Mnafikiri mmeshinda siyo? Watu wangu wafe hovyo kisa kazi yenu ifanikiwe siyo? Sasa nisikilize Robinson kwa ulilolifanya la kumuua chawa wangu utalipia nakwambia, nasema utalipia tu jiandae."
Nafiwe aliitoa ile bastola kisogoni kwa Robinson kwa staili ya kuiburuza kisha akaipachika kiunoni na kuondoka zake. Robinson alibaki pale kaduwaa akiwa haamini kama kapona, pamoja na kumuona Nafiwe mbele yake akitoka nje lakini yeye alipeleka mkono kisogoni kuhakikisha kama kapona kweli.
Na baada ya kuhakikisha yuko salama alipumua kwa nguvu na kujitupa kochini huku akiiweka bunduki yake pembeni. Alijishika kichwa chake akiwa kalala pale kwenye kochi macho juu mawazo ya kutosha kwani pamoja na yote alikuwa akifikiria iwapo kama atakuja kutoka salama ndani ya hao jamaa kutokana na vituko vyao ambavyo huvifanya hata uwafanyie kazi vizuri namna gani lazima wazue jambo.
"Hivi maisha haya mpaka lini? Toka nimejiunga nao hakuna kazi ambayo niliifanya iwe kwa Santana au Nafiwe nikasifiwa na kupongezwa zaidi ya kuzodolewa tu, kwanza sijui nilifuata nini huku si bora nimebakia na mrembo wangu."
Robinson alipofikia wazo hilo ilibidi asimame kabisa na kuliendea dirisha lililokuwa karibu yake na kuanza kuchungulia nje.
" Hivi kuna siku itatokea mimi na Jackline kuwa pamoja tena kama zamani na kuitimiza ndoto zetu kweli? Kwanini mimi? Tom chali, Melissa chali, Kamanda mwenyewe mbishi kama nini lakini naye chali sasa mimi ni nani mpaka nipone kwenye uwanja huu wa vita na mimi si watanila nyama siku wakinikamata? Masikini Robinson mimi sijui hata nifanye nini? Lakini haiwezekani mimi ndiyo mwamba wao nasema haiwezekaniiiii !!!!!!!!!!........ "
Mawazo yalipitiliza na kujikuta akipiga kelele huku akivisambaratisha vioo vya dirisha lile kwa ngumi za hasira kitu ambacho kiliwashtua wakina Santana kule nje na kuja mbio ndani kujua kilichompata Robinson.
" Wewe kuna nini mbona makelele?"
Santana alimuuliza baada ya kumkuta akiwa katulia dirishani kashikilia Nondo huku damu zikitiririka mikononi baada ya kukatwa na vipande vya vioo.
Badala ya kujibu swali aliloulizwa na mkubwa wake yeye alianza kulia na tena siyo kulia kimya kimya bali kwa sauti iliyowafanya watazamane kwanza kabla ya kuchukua hatua.
"Robinson umepatwa na nini wewe mbona hivyo?"
Mzee Bruno alimuuliza tena swali ambalo lilimfanya ageuke huku akilia na kumkamata koti mzee Bruno na kuanza kumtingisha kwa nguvu.
"Hivi nifanye nini mpaka mjue nimewafanyia kazi? Nifanye nini mzee? Si unijibu sasa? Nijibu mzee maana sioni sababu ya kuendelea kuishi na kama tageti yenu ni kuniua si mfanye hivyo sasa kuliko ninayofanyiwa! Niuweni sasaaaa?"
Aliongea hivyo huku akimuachia mzee Bruno na kuichukua bunduki iliyokuwa kwenye kiti lakini kabla hajafanya lolote Santana alimuwahi na kuipiga teke ile bunduki ambayo ilimtoka na kuanguka chini kisha akaiokota.
" Unataka kufanya nini Robinson? Au madawa yamekuchanganya siyo? Unahitaji kukifuata kifo chako eee unajilaumu nini hapa kwani sisi tulikuita kuungana nasi si njaa njaa zako? Sasa nisikilize ukirudia kutupigia mikelele yako utanijua Kimburu wewe."
Santana alimwambia Robinson akiwa kamuelekezea bastola usoni na baada ya kukamilisha mkwara wake aliitoa bastola yake na kuiweka kotini na kumgeukia mzee Bruno.
" Ongea naye kijana wako kabla sijabadilika."
"Nitaongea tu baadaye, Robinson hebu nenda kalale kwanza upumzishe ubongo."
Robinson hakujibu chochote zaidi ya kumuangalia tu mzee Bruno na kuingia zake chumbani kwake.
Mzee Bruno Gautier alimsindikiza kwa macho mpaka alipoishia chumbani kisha alitingisha kichwa chake kama vile kumuonea huruma Robinson kisha naye alitoka nje na kumfuata Santana pale alipokuwa kakaa.
"Nafiwe kamfanya nini Robinson?"
Mzee Bruno alimuuliza Santana akiwa anakaa naye pale alipokuwa Santana.
"Unafikiri anaweza kumfanya nini hakuna chochote ushenzi wake tu kwanza naanza kuwa na mashaka naye huko mbele anaweza kuja kutugeuka na kutuuza kwa panya wale."
Santana alionesha hofu yake juu ya Robinson.
"Siwezi kuungana na wazo lako hilo kwani hata huko nyuma niliwahi kukuambia hili na pia kumbuka kuwa huyu ndiye tuliyebaki naye ambaye ni strong kuliko madogo wengine tulionao."
"Okay sawa nimekuelewa mzee wangu tuangalie mpango wa baadaye unaendaje."
Santana alikubaliana na mzee Bruno kwa ambacho aliambiwa.
***
Waliendesha magari yao mpaka karibu nyumba ya wakina Santana kisha walisimamisha magari yao kwenye kiuchocho ambacho kwa haraka haraka asingeweza kujua wamefuata nini kwani ni kieneo ambacho kina pilika nyingi za biashara ndogo ndogo na hapo walitelekeza magari na kisha kutembea kwa mguu mpaka lilipo jengo la madam Nafiwe ambalo waliamini ndipo wanapoishi na kuanza kulizunguka kwa nyuma.
"Hapa tuachane tutakutana karibia na tulipoacha magari, angalizo tunakwenda kutumia dakika kumi na tano tu ukiona kimya baada ya hapo hakuna kusubiri sawa?"
Jackline alimpa maelekezo Roberto wakati wakitakiwa kuachana pale kila mtu akitakiwa kuingia ndani kwa ajili ya kuchukua taarifa ambazo zitaweza kuwasaidia kwenye zoezi lao.
" Nimekuelewa."
Roberto alimjibu wakagonga kisha wakaachana kila mmoja akachukua njia yake.
Jackline alielekea mwelekeo ambao kulikuwa na mti wa mpapai kwa ndani hivyo alichokifanya ilikuwa ni kuupanda ukuta na kisha kuurukia mpapai kwa spidi ya ajabu alijiburuza na kutua chini na kwa kuwa ilikuwa ni jioni kivuli kikiwa kimechukua sehemu kubwa mle ndani, hivyo alikimbia na kuufuata mlango uliokuwa kule nyuma na kuugusa kama uko wazi lakini ulikuwa umefungwa kwa ndani. Ikabidi atoke pale na kuliendea dirisha lililokuwa karibu yake na kuchungulia ndani, hakuamini macho yake kwa ambacho alikiona.
"Mshenzi wewe sijakukuta leo, mbio zako zote zimeishia hapa."
Aliongea hivyo Jackline baada ya kumuona Robinson ndani akiwa kalala hivyo akailengesha bastola yake pale dirishani ili amsambaratishe mle mle ndani.
"Robinson hii ndiyo dawa ya msaliti utanisamehe kwa hili wasalimie wazazi wangu wote huko kama mtaonana."
Akiwa anajiandaa kufyatua mara mlango wa chumbani kwa Robinson ulifunguliwa na kumfanya asitishe zoezi na kubonyea chini kabla hajaonwa.
"Hebu amka Robinson tunatakiwa kwenda mjini mara moja tukafanye manunuzi si unaona vitu vimepungua humu ndani?"
Ilikuwa ni sauti ya mwanamke ikimtaka Robinson aamke hivyo Jackline akiwa pale chini alisikia kila kitu hiyo ikampa hamu ya kumfahamu mwanamke huyo ambaye alihisi kuwa aweza kuwa ni Nafiwe. Lakini kabla hajafanya lolote alishtukia akiguswa bega lake hiyo ilimshtua ikabidi ageuke kumuangalia aliyemgusa.
"Jackline karibu kwetu, kwanini ujisumbue kupita uchochoroni huku si ungepita tu mlangoni?"
Maneno hayo ya kuudhi yaliyomkwaza Jackline mpaka kushindwa kufanya kazi yake yalisemwa na mzee Bruno. Akiwa kamuelekezea bastola kwa umbali kama wa mita tano hivi alimpa ishara asimame.
" Ukijaribu kufanya lolote umekwenda na maji hivyo uwe mpole kama maji ya mtungini mama."
Jackline hakuwa na jinsi zaidi ya kutii amri huku mikono ikiachia bastola yake na kwenda hewani kuashiria kusalimu amri.
"Ipige teke kwangu hiyo bastola haraka."
Jackline alifikiria hilo haraka akaangalia umbali aliokuwepo kati yake na mzee Bruno aliona hawezi kufanya lolote ikabidi awe mpole kwanza.
Kule ndani wakina Robinson wakawa wamesikia kelele zilizokuwa nyuma ya chumba walichokuwemo hivyo wakatoka haraka kujua kuna nini kwani pamoja na kuchungulia walimuona mzee Bruno lakini aliyekuwa akiongea naye alizibwa na nguzo ya nyumba hivyo hawakumuona vizuri.
"Mzee Bruno ni nani huyo?"
Nafiwe aliuliza baada ya kumuona mzee Bruno kaelekeza bastola mbele akiwa makini sana lakini mtu huyo hawamuoni.
"Huyu si ni....."
Kabla hajamalizia kujibu swali ambalo aliulizwa na Nafiwe alikutana na risasi moja ya kichwa iliyopelekea kuangua chini huku damu zilimwagika kama vile zilikuwa zimehifadhiwa kwenye moja ya kiungo kichwa. Jackline naye hakujua ni nani aliyepiga risasi mzee Bruno ikabidi ageuke nyuma uelekeo wa ukuta ndipo alipomuona Roberto wakapiga dole lakini alichelewa kugeuza kichwa akakutana na teke lililompeleka chini. Nafiwe akajua amemuweza akamfuata na kutaka kumuinua ili ampige tena lakini naye alijisahau kwani alikutana na teke lililotua vilivyo mbavuni kwake na kumpeleka chini akiwa anapiga mikelele ya maumivu, hapo ndipo Robinson alipokuja kama mbogo baada ya butwaa la muda la kutoamini kumuona Jackline ambaye hakukutana naye kwa muda toka walipowatupa baharini na baada ya kukumbuka kuwa ni mtu mbaya kwake ndipo alimfuata kwa lengo la kumshambulia lakini na yeye kabla hajafanya lolote alikutana na risasi ya mguu iliyompunguza kasi na kupiga magoti kwa maumivu makali kitendo hicho kikatoa nafasi kwa Jackline kumfuata na kumpiga teke takatifu la kichwa lililomfanya kutema damu za kutosha.
"Hiyo ni breakfast' tu Robinson lunch' inaandaliwa kwa ajili yako mshenzi usiye na ukoo wewe."
Jackline alimwambia huku akiwa kamkanyaga pale pale alipopigwa risasi na Roberto na kupelekea kupiga makelele mwenzake Nafiwe alikuwa keshadhibitiwa na Roberto.
" Dada twende zetu kabla Santana hajakurupuka kule alikolala."
Roberto alimwambia Jackline ambaye alinogewa na mchezo wa kucheza na mwili wa Robinson.
"Yuko wapi?"
Jackline alimwachia Robinson na kuinuka huku alimuuliza Santana kama vile alikuwa anataka kumfuata aliko.
"Twenzetu ni kama kazidiwa na miunga yake, muda wao unakuja walau rumewagusa."
Roberto alimwambia Jackline akiwa anamvutia kule ambako alipita. Na kuwaacha wakina Robinson kwenye maumivu makali huku mzee Bruno akiwa hajitambui hata chembe.
MUZIKI HUU NI NANI ATAUCHEZA?
Walijikongoja mpaka kwenye magari yao bila kusubiri waliondoka kurudi kwa mzee Jerome Whistle huku nyuma wakiacha wingu zito lililotanda ndani ya jumba la Madam Nafiwe kwani tayari mzee Bruno roho yake ilishaachana na mwili huku Madam Nafiwe pamoja na Robinson walikuwa hoi baada ya kukutana risasi zilizoingia kwenye sehemu tofauti za miili yao. Machungu yalikuwa zaidi kwa Robinson ambaye muda mfupi kabla ya tukio alikuwa akiyawazia maisha anayoyaishi ndani ya jumba hilo. Baada ya kupata fahamu kutokana na kujidunga midawa ya kulevya Santana alijiinua taratibu mpaka ndani ambako hakukuwa na mtu yeyote yule kitendo kilichomchanganya ikabidi atoke nje na kumuuliza mlinzi ambaye ambaye yeye mara zote hulinda geti la kuingilia.
"Wako wapi hawa?"
Santana alimuuliza mlinzi yule.
"Wamekwenda kupata tiba."
"Tiba? Ya nini"
Aliuliza baada ya kusikia kupata tiba.
"Mkuu wewe ulilala wakati tumevamiwa..."
"Mlivamiwa na nani?"
Alimkatisha na kumtupia swali jingine.
"Tulivamiwa na wale wakina... Sijui wakina nani wale?"
Mlinzi aliishia kujikanyagakanyaga tu bila kuwaelezea vizuri.
"Wakina nani? Au wakina Jackline?"
"Enhhh hao hao mkuu."
Alidakia mlinzi baada ya Santana kulitaja jina la Jackline.
"Shabashhhh..... Mlikuwa wapi mpaka likatokea hilo tukio?"
Santana alipagawa baada ya kusikia waliokuwa wamevamia.
"Mkuu mimi nilikuwa hapa getini nikiendelea na ulinzi wangu lakini mara nilisikia milio ya risasi ikilia sikuchukulia uzito kwa sababu ni eneo ambalo ninyi hulitumia kufanyia mazoezi ya shabaha hivyo nilichukulia poa."
"Unasemaje? Ulichukulia poa? Nyangalika wewe yaani unalidhika tu majibu yanayotolewa na bichwa lako lenye mikona hilo siyo? Na wengine walikuwa wapi?"
"Kwanza naomba unisamehe kwa kosa hilo wenzangu walichelewa kurudi kutoka ambako walitumwa na Madam, lakini mzee Bruno yeye yuko kwenye jengo lile pale."
Baada ya kutoa maelezo kwa Santana alimuonesha alikohifadhiwa mzee Bruno.
"Kakaa kule anafanya nini huyu mzee naye siku hizi kawa mzembe sana kapatwa na nini? Hebu kaniitie aje hapa tuwafuate hao walio kwenye matibabu."
"Nikamwite?"
Mlinzi alimuuliza Santana.
"Kwamba hujasikia au basi nifundishe lugha yenu ili niongee kilugha."
"Bosi mzee Bruno kalala usingizi mzito."
"Unasemaje wewe? Yaani mzee Bruno ninaye mfahamu mimi alale usingizi mzito? Haiwezekani hata kidogo nasema haiwezekaniiiiiiii....."
Santana aliondoka pale kasi huku akipiga kelele kuelekea kwenye kijumba alichohifadhiwa mzee Bruno.
"Mzee wangu umewezaje kufa kizembe kiasi hicho? Kwanini lakini au umepumzika tu kisha utaungana nami kijana wako? Niambie basi kwamba haujafa bali umelala tu, niambie.. Niambieeeeee......."
Santana aliongea kwa machungu makubwa huku machozi yakimmwagika alimtikisa mzee Bruno lakini jibu lilikuwa ni moja tu amefariki. Alimuangalia tena kisha akapiga magoti na kumfunika vizuri blanketi kisha akajiweka sawa na kutoka zake akaingia chumbani kwake na kufungua kabati lililokuwa na vifaa vyake vya kazi. Aliviangalia kwa muda kisha akavichukua na kuviweka kitandani na yeye akafuata hapo akachukua bastola yake ambayo huiamini sana na visu kama vitatu kisha akaliangalia bega lake kwenye kioo akatikisa kichwa. Akavalia buti zake tayari kwa kuondoka. Mara akaingia dereva wa madam Nafiwe.
"Unasemaje?"
"Mkuu unaitwa na Madam."
"Mwambie nakuja."
Alimjibu kwa mkato huku akichukua vitu vyake pale kitandani.
Alimaliza na kuondoka kuelekea kwenye banda walikokuwa wakina madam Nafiwe.
"Hatuwezi kukaa kimya katika hili ni lazima tufanye jambo ambalo nao litawaumiza mioyo yao kama sisi."
Madam Nafiwe aliongea huku akipulizia marashi mwili wa marehemu mzee Bruno.
"Roho yangu imepata jeraha kubwa sana hamjaniona tu ndugu zangu yaani katika kundi nililoongozana nalo nimebaki mimi tu?"
Alianza kulia tena Santana huku akipokea kile kikopo cha marashi na kupulizia mwili wa marehemu.
"Na hata kundi la Robinson nalo kasalia peke yake na upande wangu wenye akili ya mapambano wote wamekwenda nimesalia mimi tu hivyo tuna deni kubwa mbele ya hawa wapendwa wetu na ndiyo maana kila
timu imebakiwa na kamanda mmoja hii ni ishara nzuri kwetu."
Nafiwe alizungumza hayo huku akiwa kamshika begani Robinson katika kutafuta msawazo kwa maumivu aliyokuwa nayo ubavuni.
" Ila Santana na wewe punguza dozi zako za madawa zisizo na maana laiti ungekuwa vizuri tulikuwa tumeshawashinda wale kwani mzee Bruno aliwadhibiti tayari uchache wetu wakautumia."
"Kwa hiyo unanilaumu mimi?"
Santana alimuuliza Nafiwe akiwa kamkazia macho.
"Naongea na nani hapa acha kujitoa fahamu wewe kubali madhaifu yako tu."
Nafiwe alikazia maelezo yake.
"Bwana ee limeshatokea tayari hapa cha kufanya ni kujipanga kufanya shambulizi la kushtukiza ambalo hawatokaa wasahau tena maishani mwao."
Santana aliona ajishushe kikubwa na kutaka mikakati iandaliwe ya kuwakabili wakina Jackline.
***
Waliwasili na kuingia ndani baada ya geti kufunguliwa na kuwakuta wenzao wakiendelea kufanya usafi kwa kuyaweka mazingira sawa kutokana na kuharibiwa na wakina Robinson.
"Pole sana Jasmine kwa majanga yaliyokukuta."
Jackline alimpa pole Jasmine aliyekuwa kakaa kwenye maua.
"Asante wangu, nashukuru Mungu niliponea chupuchupu kwani jamaa ni kama alishanijua hivyo alitaka kunimaliza pale pale."
Jasmine aliwaelezea kilichotokea.
"Enhh vipi na ninyi mlikokuwa kwema?"
Mzee Jerome Whistle alitaka kujua ilivyokuwa huko.
"Mzee tunalomshukuru Mungu tu wazima si kwa jeuri yetu ila ni yeye mwenyewe aliye juu ndiye aliyetunusuru kwa majanga kuanzia kule Flamingo mpaka hapa, Jessica mnaweza kuamini kuwa yule dogo wa Magari kauawa na wakina Santana?"
"Acha utani basi, wamemuua kwa sababu gani?"
"Sijui ila ndivyo ilivyo mpaka ninahisi alikuwa akifanya nao kazi."
Wakati wao wakiendelea na mazungumzo Roberto yeye alikuwa pembeni kidogo na mpenzi wake Titiana wakipeana taarifa za hapa na pale ilmradi kuhakikisha penzi lao haliingii doa lolote.
"Lakini kwa ajili yako tulijitoa mhanga kupambana nao tukawa tumewafuata kwao huko huko na kuliamsha mpaka mnatuona hivi shukuruni Mungu ilikuwa mmoja wetu aage dunia lakini Mungu bado anatupenda, tumewashambulia na kuwaweka majeraha huku mzee Bruno akipoteza maisha kwa risasi ya kichwa."
"Mbona mnanitamanisha jamani !!! Ningekuwepoooo wangejuta hata hao mliowapa majeraha mimi ningewamwaga bongo zao maana kwa hasira nilizonazo acha tu."
Jasmine aliongea hayo huku akisimama kujipima kama yuko fiti kwa mpambano.
"Unakwenda wapi bado wewe?"
Mzee Jerome alimwambia Jasmine aliyekuwa akiinuka pale alipokuwa kaketi.
"Tunafanyaje hapo kwani kama mmeliamsha huko lazima wanajiandaa kutuvamia mnaonaje kama tukielekea huko ambako mlikwenda kutafuta Hotel ambayo ni salama japo mlisema tayari walishaidukua nayo lakini siyo mbaya."
Jessica alitoa wazo lake baada ya kulisikia sakasaka lililotokea huko kwa madam Nafiwe.
" Hatuwezi kuamini nilikuwa nammaliza pale pale Robinson amshukuru Nafiwe aliyetokea pamoja na mzee Bruno waliorudisha nyuma kidole changu cha kazi."
Jackline aliendelea kuwaelezea wenzake waliyokutana nayo huko.
"Jamani hebu tukaeni chini tupange mikakati kuhakikisha kuwa tukiingia ulingoni safari hii hatufanyi makosa zaidi ya ushindi sababu mpaka sasa tumeshinda kwa asilimia sitini na saba hizo thelathini na tatu ni chache sana lakini zinaweza kutugharimu."
Jasmine aliwasogeza wenzake kujadili mkakati ambao utawapa ushindi bila kufanya makosa. Mzee Jerome naye hakusalia nyuma safari hii alichokifanya ilikuwa ni kuingia chumbani kwake huko alichukua boksi lake ambalo huhifadhia silaha yake ambayo alipewa na rafiki yake kutoka Afrika ya Kusini kama zawadi mara baada ya kumuuzia samaki wazuri ambao waliweza kumpa jina nchini mwake na hivyo kuamua kumpa silaha hiyo kwa ajili ya kujilinda dhidi ya maharamia wa majini, aliitazama bunduki hiyo aina ya SMG kisha akairudisha kwenye boksi na kulibeba lakini akalitua chini na kutoa simu mfukoni mwake na kuitafuta namba ya mke wake Bi Elizabeth na kuipiga bila shaka alimkumbuka sana baada ya kuondoka kisa tu wakina Jackline.
"Halo mke wangu Habari ya siku."
"Salama mume wangu wazima huko wewe na familia yako yote?"
Bi Elizabeth alimjibu baada ya kuipokea.
"Una maana gani kusema yangu yote?"
Mzee Jerome alichukizwa na kauli ya mke wake kwani alijua ni wapi alikokuwa anaelekea kwenye swali lake.
" Mume wangu kwani kuna ubaya wowote kuwaulizia wanao wote wakina Jackline na wakina Mustapha?"
" Mmhh haya bwana hebu tuachane na hizo mambo kwanza kifupi huku ni kwema japo siyo sana....."
"Najua hilo mume wangu kutakuwaje kwema wakati bado ndani kuna siafu?"
Mke wake alimkatisha mume wake.
"Ni kweli kama unavyoamini,lakini unarudi lini nyumbani?"
Mzee Jerome aliona amuulize mke wake juu ya mustakabali mzima wa kurejea kwake.
"Hata kesho tu mume wangu niko tayari kurejea....."
"Ni nini sasa kimekukalisha mpaka sasa ni nauli?"
Mzee Jerome alimkatisha baada ya kusikia kuwa yuko tayari kurejea.
"Mbona tunakatishana hivyo si unisikilize mume wangu kwanza? Nitarejea nyumbani ikiwa tu hao siafu wataondoka hapo na si vinginevyo."
Mzee Jerome akaona hakuna haja ya kuendelea kumuuliza maswali ikiwa mtu mwenyewe bado kasimamia msimamo wake ule ule wa kuwachukia wakina Jackline pasipo sababu ya maana hivyo alikata simu akabeba boksi lake na kutoka nalo sebuleni.
" Wanangu niko tayari kuingia uwanja wa mapambano hebu iangalieni mashine yangu hiyo."
Aliwakabidhi wakina Jackline boksi lile kisha yeye akawaita watoto wake pembeni wazungumze kidogo.
"Wanangu naombeni mnisikilize baba yenu inawezekana nikawa nina mapungufu yangu lakini mimi ni baba yenu tu."
"Kivipi baba mbona umetuanzia na mafumbo?"
"Ni hivi wanangu mama yenu nimempigia simu muda si mrefu nikiwa chumbani kutaka kujua atarejea lini nyumbani, lakini alichonijibu ni kuwa atarejea iwapo tu wakina Jackline wataondoka hapa nyumbani. Hivi haya wanayopitia walipanga yawatokee?"
"Baba wala usipate tabu katika hilo kwani mimi mwenyewe niliongea naye jana lakini majibu yake hayakunifurahisha hata kidogo nilitaka kukuambia lakini nikajua ni mkeo kwanini niwatie kwenye misukosuko lakini kama na wewe ikiwa umeambiwa hivyo baba tuachane naye kuna siku atarejea tu hapa si ni kwake?"
Mustapha aliungana na baba yake na kisha kumuachia swali ambalo hakutaka jibu.
" Baba tuachane na hili hebu tuangalie lililo mbele yetu huyo ni mke wako na pia ni mtu mzima mwenye mitoto mikubwa kama sisi bado anataka kubembelezwa hivyo?"
Walikumbatiana kisha wakarejea pale walipokuwepo wakina Jasmine na kuungana nao.
"Mzee wangu hii ni bonge la mashine lakini zito mzee sisi tumeshazoea hivi vimiguu vya kuku unacheza navyo unavyotaka mwenyewe."
Roberto aliisifu lakini akamwambia ilivyo ni ngumu kuingia nayo kwenye mikikimikiki.
"Sikiliza Roberto hii ndiyo yenyewe, mimi nafichama sehemu huku ninyi mkiwafukuzia kule niliko na mimi kama naoga vile namtungua mmoja mmoja mpaka inabaki ziro mpooo...."
Mzee Jerome aliwafanya waangue vicheko kwa mbinu ambayo aliileta. Basi walifanya maandalizi yao ya mwisho mwisho kabla hawajaingia barabarani kuelekea Flamingo ambako wanaamini litakuwa eneo zuri la kuanzishia mashambulizi yao.
" Ila mimi nina wazo ndugu?"
Titiana aliwataka wamsikilize wazo lake.
"Wazo gani hilo Titiana?"
Jasmine alimuuliza.
"Kwanini tuelekee huko wakati tayari maadui zetu walipo tumepajua na nzuri zaidi tumeshawagusa kidogo bila shaka watakuja tu hapa kwanini tusiwasubiri hapa hapa? Au tuwafuate huko huko waliko."
Wazo la Titiana lilionekana kuwashika hivyo wakakubaliana nalo na hivyo kubadili gia hewani.
" Hiyo imepita kwa upande wangu sijui kwa upande wenu kwani kuelekea huko ni kumkimbia adui cha kufanya hapa ni kuandaa vidude vya kuwalisha wao si wana njaa na sisi?"
Jasmine aliunga mkono wazo la Titiana, hivyo kila mmoja alikuwa tayari kwa mpambano mpaka wakina Victor.
" Na mimi bega kwa bega nanyi wanangu hapa cha kufanya ni kila mmoja alijue eneo lake ambalo atakuwa wakati ukiwadia."
Mzee Jerome aliwaunga mkono na alionekana kuwa furaha sana muda huo huku akiwaonesha maeneo ambayo ni rahisi maadui kuyatumia kutokana na ufupi wa ukuta upande wa nyuma.
Waliweka mazingira yao sawa kisha mzee Jerome alitaka watoke wakalifanyie ziara tena eneo la Nafiwe ili ikiwezekana wawafanyie sapraizi la maana.
"Mzee unataka uende kule unaliweza?"
Jessica alimuuliza mzee Jerome baada ya kutoa wazo lake hilo.
"Unauliza kuhusu mimi? Waulize wanangu nikoje nikivurugwa."
"Mzee wangu wewe bado unahitajika sana acha uswahili bwana."
Victor alimkana na kumtaka aache uswahili kwani bado anahitajika sana asije sambaratishwa huko.
"Jamani ee mimi nafikiri......"
Kabla Roberto hajamalizia mara waliona mwanga kama wa tochi hivi ukimulikamulika nje hasa eneo la getini na ukutani hilo liliwafanya watulie kidogo na kutazamana kabla ya kufanya maamuzi.
Waliondoka haraka na kuzunguka nyuma ya nyumba huku wengine wakirudi ndani. Kule nyuma ya nyumba Roberto safari hii akiwa na Mustapha pamoja na Victor walipanda ukuta na kuanza kuvizia kule ambako mwanga ulikuwa ukitokea.
RAFIKI NI WAKINA NANI HAO NA TOCHI ZAO?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA KUPATA MAJIBU YA MASWALI HAYA.
Mustapha na Victor wao walipita upande mwingine wa nyumba yao na kumuacha Roberto naye akipita upande wake lengo likiwa ni kuwashtukiza waliokuwa eneo la getini bastola ikiwa mkononi Roberto aliendelea kuambaa na ukuta ule kulisogelea geti kule wakina Mustapha nao wakiwa makini vipande vya nondo mkononi nao waliendelea kusogea mpaka karibu na geti. Cha kushangaza baada ya kufika pale getini hawakuweza kumuona mtu yeyote wala ule mwanga tena kiza kilitanda. Walikagua geti vizuri na kukuta liko salama na kisha pale chini ili kuona kama wanaweza kuona makanyagio ya miguu au viatu au chochote cha kuwasaidia lakini hawakuona kitu.
"Ilikuwa ni nini sasa?"
Akiwa kashikilia kiuno chake Roberto aliwauliza wenzake.
"Maajabu kaka, kwa mwanga kama ule uliashiria kabisa kuna watu wenye nia fulani walikuwa nje ya nyumba sasa iweje?"
Victor alimjibu Roberto baada ya kutoona chochote pale, ndani ya geti Jackline alisogea mpaka karibu ya geti na kuchungulia nje kupitia nafasi za geti na kuwaona wakina Roberto wakiwa wanaongea ndipo naye akaufungua mlango mdogo wa pembeni na kutoka nje akiwa na mzee Jerome pamoja na Jessica.
"Imekuwaje?"
Mzee Jerome aliwauliza baada ya kuwakuta wakiwa wanajadiliana juu ya lililotokea.
"Wala hatuelewi baba hatujakuta mtu yeyote yule hapa."
Mustapha alimjibu huku akijaribu kuangaza maeneo ya jirani kama anaweza kuwang'aza.
"Basi watakuwa wamekimbia na kujificha tu, kwanini watoweke ghafla hivi? Kuna sehemu wapo hawa."
Jackline aliwaambia wenzake kuwa lazima wamejificha sehemu na katika kutaka kulihakikisha hilo alisogea pembeni na kuanza kuchunguza mazingira yale.
"Wakina nani ninyi hapo?"
Ilisikika sauti kutoka gizani ambayo iliongea kwa kujiamini sana.
Walikaa kimya kumsikilizia aliyewauliza swali hilo, na kwa kuwa Jessica alikuwa na tochi alimulika kule lilikotoka swali.
"Mbona mnanimulika pasipo kujibu swali langu?"
Aliuliza swali tena baada ya kumulikwa mwanga usoni, ule mwanga ulimfanya mzee Jerome kumtambua mtu yule na hakuwa peke yake alikuwa kaongozana na vijana wengine kama watano hivi.
"Mzee mwenzangu kwema kweli? Umenishtua sana unajua."
"Ni mzee Jerome?"
"Ndiye mwenyekiti karibu."
"Asante mzee Jerome, unajua nini tulikuja hapa kutaka kukujulisha kuwa usiku wa leo unatakiwa kutupa msaada kwenye ulinzi wa mtaa wetu kwani mzee mwenzetu Changalawe kapata tatizo la msiba huko kijijini leo ni siku ya tano lakini tulivyoona kengele haitupi mrejesho tukaona tuondoke zetu."
"Pole sana mwenyekiti mwanga tumeuona tukahisi labda ni Majambazi wametuvamia tena si unakumbuka walionivamia siku ngapi hizi."
"Nakumbuka vizuri sana mzee Jerome sasa hapo sijui tufanyaje?"
Mwenyekiti alimuuliza mzee Jerome juu ya suala la Ulinzi.
"Kwanza nikupe pole kwa msiba wa bwana Changalawe lakini pia kwa leo nitaungana nanyi kwenye zoezi hili la Ulinzi kwani nina ugeni hapa ndani lakini pamoja na ugonjwa hivyo niombe mimi nitafanya hivyo tu kwenye zamu yangu na kingine kabla sijasahau mwenyekiti waambie vijana kuwa hata huku ulinzi ni muhimu vile vile siyo wawe kule kwenye mataa kwani kuwa na silaha siyo ulinzi umoja wetu ndiyo silaha si ulishuhudia mwenyewe nilichofanyiwa siku ile laiti kama ulinzi ungekuwa kwenye maeneo yote ingekuwa vile?"
Mzee Jerome alimfafanulia mwenyekiti wa eneo lile kile kilicho moyoni mwake.
" Mzee mwenzangu nimekuelewa katika hilo na ndiyo maana nimewapa utaratibu mpya ambao utaanza kufanya kazi wiki ijayo kwa kipindi hiki nilishawaelekeza maeneo yanayotakiwa kushughulikiwa kiulinzi."
"Iwe hivyo mwenyekiti si unajua tena dunia hii si kama ile ya wakati wetu."
"Ni kweli kabisa, kumbe mzee Jerome mimi nimekuelewa wacha sisi tuendelee na kibarua hiki ambacho natakiwa kuichukua nafasi hii ya bwana Changalawe."
Wakashikana mikono kuagana lakini Jackline aliwasogelea na kutaka kuongea na mwenyekiti.
"Samahani mwenyekiti mimi ninaweza kusaidia ulinzi lakini ngoja kuna mambo fulani hivi nayakamilisha yakiwa tayari nitaungana nanyi."
Jackline aliongea na mwenyekiti huku akimshikisha hela mkononi kitu kilichomfanya mwenyekiti kufurahi sana.
"Binti wala usijali sana sisi tuko kamili lakini pia huku sisi suala la Ulinzi halifanywi na wanawake."
Alimjibu huku akitupia hela ile mfukoni mwake.
"Basi tunashukuru na tuwatakie majukumu mema."
Jackline aliwatakia kazi njema huku wao wakiingia ndani na kufunga geti.
"Yaani nilikuwa nina mzuka wangekuwa ni wale panya ningewachezesha Samba ambalo wasingelisahau aslani."
Victor alijigamba huku akimpigapiga Mustapha mgongoni.
"Taratibu sasa mgongo wa mtu huo."
Jibu hilo liliwafanya wote kucheka wakiwa pale varandani.
"Hivi dada Jackline hatuwafuati wakina Nafiwe?"
Mustapha alimuuliza Jackline wakiwa pale pale nje varandani.
"Si hawa wametuchanganya? Lakini kama kawaida vamio liko pale pale usiku huu huu na kwa kuwa kila kitu kiko tayari nafikiri tuianze safari."
Jackline aliwaeleza.
"Ila mimi ningeomba wakina Mustapha wangesalia na Jasmine hapa pamoja na Titiana sisi wengine ndiyo tuelekee huko."
Jessica alitoa pendekezo.
"Dada Jessica una....."
Mustapha kabla hajamalizia kauli yake ilikatishwa na Jackline.
"Sikiliza Mustapha siyo kwamba tumewadharau la hasha kubaki hapa pia ni kazi, hebu fikiria tukipishana nao wakaja huku ni nani wa kuwadhibiti?"
"Kwa hapo tumewaelewa dada, kazi na ianze."
Victor alimjibu. Hapo kila mmoja alichukua zana yake tayari kwa kwenda kwa madam Nafiwe kufanya shambulizi. Lakini wakiwa ndiyo wanatoka na kuelekea kwenye gari ambalo alikabidhiwa ufunguo mzee Jerome mara simu ya Jackline iliingia ujumbe, aliichukua na kuufungua ujumbe huo.
"NASHUKURU MMEUGUSA MOYO WANGU KWA KUWAANGAMIZA WAPENDWA WANGU LAKINI NATAKA KUWAHAKIKISHIA KUWA USIKU MMOJA UTATOSHA KULIPA KILE MLICHOKIFANYA KWANGU JIANDAENI."
Jackline aliusoma ujumbe ule na kuubeza akaiweka simu yake mfukoni na kuingia garini, safari ikaanza. Mzee Jerome kwa kuwa mitaa anaijua vizuri alitumia muda mfupi sana kufika kwenye mtaa liliko Kasri la Madam Nafiwe hapo aliegesha gari kando ya barabara kwenye kiuchochoro ambacho kipo mita kadhaa kutoka kwenye jumba hilo. Hapo waliacha gari na kila mmoja alichukua zana yake kisha wakapeana majukumu ya namna ya kuingia ndani ya jengo lile na kwa kuwa Jackline na Roberto waliingia kwenye jengo mwanzo haikuwa ngumu kwao hivyo waliwaelekeza wenzao namna ya kukaa kwenye tageti.
"Jessica wewe utapitia mlangoni kwa mbinu yoyote ile kwani pale getini hukaa mlinzi mmoja tu, mzee Jerome wewe utasalia hapa hapa kwenye gari kazi yako ni kuliangalia geti na kuchukua hatua stahiki. Roberto utapita njia yako ile ile na mimi kule kule ila kabla ya kila kitu kufanywa mmoja wetu anatakiwa afike pale afanye doria kwanza maana hawa kwa sasa hatujui wamejiandaaje? "
Jackline alihitimisha kugawa majukumu kwa wakina Jessica.
" Nakwenda mimi kuangalia naleta majibu muda si mrefu."
Roberto alimjibu akiondoka kwa mwendo wa kunyatia kuelekea upande wa nyuma wa jengo lile na baada ya kulifikia aliupanda ukuta na kuchungulia ndani, aliangaza huku na kule lakini hakuona hata kivuli cha mtu japokuwa kulikuwa na mwezi muda huo.
" Watakuwa wamekaa upande gani? Mbona kimya kiasi hiki? Au wako ndani hebu ngoja kwanza."
Alijiuliza maswali bila majibu na mwisho akaona ateremke pale juu na kuangukia ndani ambako alitua kwa staili ya kuviringika kisha akajiinua na kupiga goti kisha akachomoa kisu na kuirudisha bastola sehemu yake. Kisu kikiwa mkononi alianza kutembea kusonga mbele akiwa kainama, alifika mpaka kwenye ukuta wa jumba lile na kulifikia dirisha ambalo lilionekana lina taa iliyokuwa inawaka, alifika akainuka kwa kuibia na kuchungulia ndani lakini hakuona mtu yoyote ndani yake. Aliondoka na kulifuata dirisha la upande mwingine nako alichungulia ndani lakini hali ilikuwa ni ile ile.
"Washenzi hawa watakuwa wapi?"
Alijiuliza tena baada ya kuangukia pua. Ikabidi arudi nyuma na kuuendea mlango wa kuingilia ndani kwa mwendo wa kunyata alifika mlangoni ambapo alinyonga kitasa kikakubali akaingia ndani ambako huko alikagua kila chumba na kona zote lakini hakuambulia kitu chochote. Alitoka nje na kuurudisha mlango kama ulivyokuwa na kuondoka akalifuata jengo dogo lililokuwa upande wa kulia kwake na kuanza kulinyatia kama kawaida kwenye madirisha ambako alichungulia ndani lakini hakuweza kuona mtu.
"Buu shiiiit.....!! Watakuwa wapi hawa au wametuchezea picha nini?"
Alipojiuliza swali hili akajikuta mwili kama unapata ubaridi hivi, vipele vya baridi vikamtoka mwili mzima hapo kengele ya hatari ikamgonga kichwani.
"Mhh kwanini hivi, noo hapa kuna mchezo tumechezewa."
Aliondoka eneo lile na kwenda kuuparamia ukuta haraka na kurukia nje na kutoka mbio kuwafuata wakina Jackline.
"Tumechezewa mchezo hapa ndugu zangu jengo liko kimya sana hata panya tu hachezi humo ndani na katika kujiridhisha nimeingia mpaka ndani lakini hali ni ile ile."
Maneno ya Roberto yakawa kama yameongea na ubongo wa kumbukumbu wa Jackline ambaye aliukumbuka ujumbe wa Santana, na hapo hapo akamtaka mzee Jerome ageuze haraka gari na kurudi nyumbani.
" Umehisi nini mwanangu? "
Mzee Jerome aliuliza huku akigeuza gari.
"Hapana ila ni kama nahisi wale washenzi wameelekea nyumbani."
Jackline alimjibu mzee Jerome.
"Hata mimi nahisi hivyo hivyo na kwanza nina mashaka hata na yule mwenyekiti anaweza kuwa alitumiwa tu bila kujua na Santana."
Roberto alionesha hisia zake kwenye hilo.
"Acheni basi kubashiri mambo tusubiri kwanza tufike mengine yatajulikana huko huko."
Jessica aliona awakatishe maongezi yao kwani hawakujua ni namna gani alikuwa akiumia juu ya dada yake kumkuta salama au la. Huku Jackline naye aliendelea kujiuliza juu ya ule ujumbe aliotumiwa ulitoka kwa nani maana haukuwa na jina la mtumaji na hapo akaitoa simu na kuuangalia tena ujumbe ule lakini ilikuwa vile vile namba iliyotumika ilikuwa ngeni, hivyo akaona haina haja ya kuendelea kuwa nao akaufuta na hakutaka kumwambia mtu yeyote mle kwenye gari akaiacha ibakie siri yake. Walipoukaribia mtaa wao kama nyumba ya nne hivi nyuma walisimama na kila mmoja silaha mkononi na kuanza kuelekea nyumbani.
"Jamani nyumba kila mmoja anaifahamu ilivyo hivyo cha kufanya ni kupita pande mbili tu yaani kulia na kushoto. Roberto na Jessica piteni kulia halafu mimi na mzee hapa tutapita kushoto."
Jackline alitoa maelekezo kwa wenzake kisha minyatio ikaanza. Walitembea mpaka karibu na nyumba kwa kila watu upande wao na kuufikia ukuta ambao kwa tahadhari kubwa waliupanda na kuingia ndani. Na baada ya kutua walikwenda moja kwa moja mpaka kwenye madirisha kuchungulia ndani lakini kwa upande wa Jessica na Roberto wao baada ya kuingia ndani walikwenda kupitia kwenye maua ambako walikutana na mshangao baada ya kukutana na mwili wa Victor ukiwa karibu na ukuta wa nyumba ukiwa umeshambuliwa na visu vya kutosha.
"Mungu wangu Victor kashambuliwa tayari na hawa Wendawazimu?"
Aliongea Jessica ambaye hakutaka kupoteza muda alikimbilia ndani akipiga kelele za kumuita dada yake hakujali wameondoka au bado wapo yeye akili zake zikawa kwa dada yake.
Aliingia ndani na kukutana na wakina Jackline wakiendelea kuwatafuta baada ya kukuta vitu vimevurugwa si mchezo.
"Victor yuko huko nyuma kalalia midamu kibao!!!"
Jessica aliongea bila kujali kama kuna mtu ataumizwa na kauli yake.
"Unasemaje Jessica?"
Mzee Jerome alimgeukia Jessica na kumuuliza swali ambalo kabla hajajibiwa alitokea Roberto akiwa kambeba Victor ambaye alikuwa amelegea kuashiria kuwa amekufa huku Roberto akilia. Kila mmoja alimfuata ili kuhakikisha kama ni kweli. Wakiwa bado wanamshangaa Victor kwa namna alivyouawa mara mlango wa chumba cha mzee Jerome ulifunguliwa.
JE NI NANI KAFUNGUA MLANGO WA CHUMBANI KWA MZEE JEROME?
JASMINE, TITIANA NA MUSTAPHA WAKO WAPI?
MAJIBU YA MASWALI HAYA NI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA USIKOSE.
Wote waligeuka kumuangalia Mustapha aliyetoka humo chumbani akiwa anavuja damu puani na mdomoni na kutokana na kuvuja damu nyingine alipofika tu sebuleni alianguka chini na kuanza kukoroma. Wote walitazamana kwa kinachoendelea pale, mzee Jerome hakusubiri alimfuata mtoto wake pale chini na kuanza kumtingisha.
"Must.. Must... Mustaphaaaaa amka ulale kama ndugu yako."
Mzee Jerome alipiga kelele na kuanza kulia kwa sauti kubwa. Roberto alikwenda mpaka kwenye kiti kikubwa na kumlaza Victor pale kisha alimfuata mzee Jerome pale chini na kumuondoa, alimuangalia Mustapha kukagua mapigo ya moyo akayasikia kwa mbalii yakifanya kazi hivyo alimbeba na kutoka naye nje huko alikwenda naye moja kwa moja mpaka kwenye gari akampakia kisha akarudi ndani.
"Kwanini tuendelee kujikunyata kiasi hiki kuna kosa limefanyika tayari hatuna budi kuyaokoa maisha ya ambao bado wanapigania uhai wao."
Roberto aliongea hayo baada ya kuona kila mmoja mle ndani kama kapigwa shoti hivi wameduwaa tu, Jackline alikuwa kasimama karibu na dirishani akiangalia nje machozi yalimtoka mpaka yakakata yenyewe. Roberto alimuangalia kwa muda kisha akamfuata pale na kumshika bega lakini cha ajabu naye alikwenda chini na kuzimia, tendo hilo liliwachanganya hasa Roberto ambaye muda huo hakujua atoe msaada kwa nani? Ilibidi atoe simu mfukoni mwa Jackline na kuitafuta namba ya simu ya daktari Abbas wa 'THE KING'S MEDICARE CENTRE na kumpigia.
"Daktari huku mambo si yenyewe nyumba nzima imezima baada ya kuvamiwa na Santana aliyefanya mauaji na kuna wengine hatujui waliko, hivyo kama hutojali naomba gari la wagonjwa."
Roberto aliongea na daktari Abbas baada ya kupokea simu.
"Mmevamiwa na Santana? Mko wapi?"
Taarifa ile ilimshangaza sana daktari Abbas kiasi cha kujikuta akiuliza maswali ambayo hakuwa na uhakika wa kupata majibu kwani wakati anauliza hivyo tayari simu ilikuwa imekatwa. Baada ya kukata simu Roberto aliiweka mfukoni simu ya Jackline na kumbeba akamtoa nje na kumlaza kwenye kiunga ile apigwe upepo kisha alirudi ndani akamkongoja mzee Jerome aliyekuwa kama kachanganyikiwa kwa tukio lililofanyika nyumbani kwake huku Jessica yeye alikuwa hataki kuongea na yeyote mle ndani alikuwa kajikunja tu kwenye kiti.
"Jessica njoo ukae nje sehemu yenye hewa nzuri ili akili ikae sawa."
Roberto alimwambia Jessica huku akijaribu kumwinua pale kitini.
"Hebu niache huko unanipeleka wapi? Unanijua mimi wewe tena usiniguse Roberto."
Maneno yale yalimshangaza sana Roberto hakuamini kama yakitoka mdomoni kwa Jessica ama la.
"Jessica ina maana mi...." Kabla hajaimalizia sentensi yake Jessica alimkatisha.
"Naomba unisikilize kwa umakini mkubwa wewe panya, wewe na huyo mshenzi mwenzio Jackline nitawafanya kitu mbaya asipopatikana dada yangu Jasmine tena nitaua mtu kweupe."
"Lakini siyo sisi tuliofanya haya wewe mwenyewe unalijua hili na ukisema kuhusu Jasmine kumbuka mpenzi wangu mimi mwenyewe sijajua yuko wapi mpaka sasa hivyo ukisema hayo utakuwa unakosea Jessica."
"Narudia tena mimi sina undugu na ninyi hata kidogo ninachokihitaji hapa ni dada yangu na si vinginevyo zaidi zaidi nitaua mtu kwa mkono wangu mwenyewe."
Wakati Jessica akiongea hayo tayari Jackline alikuwa amerejewa na fahamu zake na aliinuka pale na kuja ndani lakini kabla hajakanyaga kizingiti cha mlango alisikia yaliyokuwa yanazungumzwa ndani hivyo ikabidi abane pale kusikiliza kinachoongelewa.
" Naomba tushirikiane pamoja kwani hata mimi najishangaa kwanini nitumikishwa na Jackline kwa manufaa yake? Kwani ukiangalia kama ni mama alishakufa haya mpenzi wangu naye ndiyo kama hivi......" Lakini kabla hajafikia mwisho wa maelezo yake mara kilisikika king'ora nje kuashiria kuwa gari la wagonjwa lilikuwa limeshafika tena hakukuwa moja yalikuwa mawili,haraka sana walitoka nje kwa ajili ya kutoa ushirikiano kwa Madaktari hao waliofika. Jackline alirudi alipokutana kalazwa na kujilaza vile vile kama awali baada ya kusikia kila kitu kilichokuwa kikizungumzwa na Roberto pamoja na Jessica hivyo akaamua atulie.
"Wagonjwa wako wapi Roberto?"
Daktari Abbas aliuliza akiwa anashuka kwenye gari lake binafsi.
"Mmoja yuko kwenye gari lile pale, Jackline yuko pale chini na mzee Jerome yule pale lakini pia ndani kuna mwili wa Victor."
Baada ya kuonesha Madaktari waliwabeba na kuwapakia kwenye magari yale mawili huku daktari Abbas yeye alimfuata Jackline na kumbeba na kumpakia kwenye gari lake.
" Roberto, ninyi njooni mpande huku."
Daktari Abbas aliwaita Roberto, Jessica na mzee Jerome ili wapande kwenye gari lake lakini cha ajabu wote walikataa kupanda gari lile wakapanda gari lao na kuondoka zao kufuatana na gari la wagonjwa. Daktari Abbas aliachana nao na kuingia kwenye gari lake na kuondoka, lakini akiwa anaendesha mara Jackline aliinuka.
"Daktari Abbas pole kwa usumbufu."
Jackline aliongea akikaa vizuri pale kitini kwani alilazwa kiti cha nyuma.
"Jackline umezinduka?"
Daktari Abbas alimuuliza huku akilipaki gari pembeni.
"Nimezinduka muda mrefu sana daktari ila kuna vitu ambavyo wenzangu walikuwa wanaongea vilinishtua kidogo ikanilazimu niigize kulala vile vile."
"Ulisikia nini? Hebu njoo ukae huku mbele."
"Nitakwambia wakati mwingine daktari ila ninachokiomba kutoka kwako ni kutonipeleka hospitali maana sihitaji kuonana nao kwa sasa."
"Sikuelewi Jackline unaongea nini au kichwa hakijakaa vizuri?"
"Hapana niko vizuri kabisa daktari Abbas ila kama hutojali naomba nipelekwe Makambi kwa daktari Hans Murray kikubwa ni kuwa mbali na hawa wenzangu."
"Sawa nimekuelewa, lakini wakitaka kujua nimekuacha wapi nitasemaje?"
"Ni rahisi sana wewe utawaambia kuwa nilizinduka na kutaka kushuka chini kupata haja ndogo ndipo nilipokimbia."
"Mhh sawa kumbe inabidi nikushushe hapa hapa nikukodie gari la kukupeleka huko."
"Sawa nashukuru."
Daktari Abbas alipaki gari pembeni na kumfungulia mlango baada ya kuteremka aliita taxi akampa maelekezo dereva huyo na kisha Jackline akapanda na kuondoka.
Safari iliendelea huku Jackline akiwa katika lindi kubwa la mawazo juu ya alichokisikia kutoka kwenye vinywa vya Jessica na Roberto kijana ambaye alimuamini katika harakati zake za kuipigania haki.
"Ni kweli mimi ndiyo chanzo cha haya yote lakini mbona wakina Jasmine nao waliapa kulipa kisasi kwa Santana pia Roberto aliungana nasi kutokana na historia mbaya iliyosababishwa na Santana kwa familia yake? Kwanini leo hii nionekane mimi ndiyo ninawapelekesha kwa ajili ya manufaa yangu? Siamini kwa kweli, pole sana mzee Jerome kwa familia yako kuingia kwenye matatizo kisa sisi ila nina imani Mungu atafanya jambo kwao na kuondokana na roho za kipepo zilizowaingia."
Alipofika hapo alianza kulia kwa kwikwi kitu kilichomfanya dereva Taxi kusimamisha gari pembeni.
" Dada vipi kuna tatizo?"
" Usihofu kaka yangu wewe tuendelee na safari haya ni masuala yangu binafsi."
"Ni kweli lakini kama hutojali unaweza kuniambia maana kama ni heri usingeanza kulia dada yangu."
"Uko sahihi kaka yangu lakini haya naomba uniachie mwenyewe nashukuru kwa moyo wako wa huruma."
Jackline alimjibu dereva Taxi akaona isiwe tabu akawasha gari na safari ikaendelea huku akiendelea kumuangalia kwa jicho la kuibia kwani Jackline hakuacha kulia.
" Nooo silii tena mzigo ni wa kwangu nitaubeba mwenyewe na si mtu mwingine hapa na kwanini niende mbali nao? Haiwezekani natakiwa nikawaambie ukweli ili mbele yangu waniambie hawako tayari kuendelea nami ili mwisho wa yote nijue la kufanya."
Wazo hili lenye nguvu lilivyotembea kichwani aliona haina haja ya kuendelea na safari hivyo akamuomba dereva Taxi ageuze gari kuelekea 'THE KING'S MEDICARE CENTRE'
" Samahani kaka yangu naomba ugeuze gari turudi tulikotoka."
"Kuna nini dada yangu si yule daktari alisema nikufikishe Makambi hospitali?"
"Ni kweli na mimi ndiye msafiri na nimeona hakuna haja ya kwenda huko natakiwa kurudi."
"Mhhh haya nimekuelewa."
Dereva hakuwa na la kufanya zaidi ya kugeuza gari kama mteja wake alivyoamuru.
"Natakiwa kuwarudisha mikononi mwangu Jasmine na Titiana, na ninaahidi kuwa Robinson nakurudia jiandae na utajuta kuungana na hao panya."
Alisema hayo huku akijifuta machozi yake kwa kiganja cha mkono wake.
****
Walifikishwa hospitali na mara moja matibabu yalianza kwa Mustapha na baba yake huku mwili wa Victor ulipelekwa kuhifadhiwa chumba maalum cha kuhifadhia maiti, Jessica yeye akipewa dawa za kutuliza maumivu ya kichwa.
"Unajisikiaje sasa?"
Daktari Abbas alimuuliza Jessica baada ya kumkuta akiwa anatembeatembea pale koridoni.
Jessica aligeuka kumuangalia daktari Abbas kama vile kuna swali alihitaji kumuuliza.
"Naendelea vizuri daktari vipi Jackline yuko wapi?"
Swali hilo halikumshtua daktari Abbas kwani alilitegemea, hivyo alichokifanya ilikuwa ni kumshika mkono Jessica na kutembea naye kuelekea nje huku Roberto akiwafuata nyuma.
"Hivi Jackline ni mtu wa namna gani?"
"Kwanini unauliza hivyo daktari?"
"Nauliza tu kwani wakati nikiwa naendesha alizinduka na kunitaka nisimame kwanza apate haja ndogo nikafanya hivyo lakini cha ajabu aliposhuka tu aliniambia safiri salama yeye akaanza kurudi tulikotoka."
"Kwa hiyo unataka kuniambia Jackline hujaja naye hapa?"
Jessica alimuuliza daktari Abbas.
"Kama uonavyo ndivyo ilivyo Jessica."
"Ana Mungu wake angetia miguu yake hapa angenitambua walahi."
"Jessica usiongee maneno hayo yaliyojaa laana, wewe ni binti mrembo sana hustahili kabisa maneno hayo, kumbuka kuwa mliamua kwa sauti moja kuungana kuisambaratisha Ngome ya adui yenu mpaka mwisho mkiwa hai au mmekufa,si ndiyo?"
"Ni kweli kabisa daktari."
Jessica alimjibu.
"Vizuri sasa iweje uibue mpasuko katikati ya vita ambayo hamjaimaliza? Najua unateseka na kutekwa kwa dada yako Jasmine pamoja na mpenzi wa Roberto lakini kwa kutengana na Jackline mtafanikiwa kuwakomboa?"
Daktari Abbas alipomaliza kuongea hayo alimgonga mgongoni Jessica na kuachana naye kisha akarejea ofisini kwake kuendelea na majukumu yake.
" Kasemaje daktari? "
Roberto alimuuliza Jessica baada ya kuona wameachana na daktari Abbas.
" Ni juu ya Jackline, inasemekana kuwa kashukia njiani haijulikani kaelekea wapi? Na pia kauliza kuwa mgawanyiko wetu katikati ya uwanja wa mapambano utaleta matokeo mazuri?"
" Kwa hiyo atakuwa kaenda wapi? Au kaamua kuwafuatilia wakina Robinson?"
"Hata sifahamu ndugu yangu ila maneno ya daktari yana kitu ndani yake? Kwanini tumemchukia Jackline ghafla kiasi hicho?"
"Wewe ndiye uliyemchukia mimi aka sijamchukia pale zilikuwa ni hasira baada ya kumuona Mustapha kwenye hali ile huku ndugu yake akiwa kafa."
Wakiwa wanaulizana maswali hayo mara kuna gari ndogo taxi iliingia mle ndani ya Hospitali na wakati wanaishangaa kwa mwendo iliyoingia nao mle mara mlango ulifunguliwa na ndipo walipomuona Jackline akishuka. Baada ya kushuka aliwafuata pale walipo.
" Najua mnionapo chuki yenu imeongezeka mara dufu, lakini niwaombe tu mnisamehe kwa yote mabaya niliyowafanyia mpaka kufikia hatua ya kunichukia kiasi hicho."
Jackline aliongea hayo huku akiwa anafuta machozi ambayo yalisheheni mashavuni na machoni.
"Jackline mbona hatukuelewi katika lipi?"
"Naomba mwenye simu yangu anipe kuna mtu nahitaji kuwasiliana naye."
Roberto aliitoa na kumkabidhi.
"Umesema tukusamehe kwa lipi dada Jackline?"
Roberto alimuuliza swali baada ya lile la Jessica kupotezewa.
"Niliwasikia yote mliyoyaongea muda ule kule nyumbani juu yangu na kweli mlikuwa na kila sababu ya kunitupia zigo la lawama na mimi nina waahidi kuwa nitahakikisha nairejesha furaha yenu."
Jackline aliwajibu huku akiendelea ofisini kwa daktari Abbas na kuwaacha na maswali wakina Jessica ambao waliduwaa baada ya kusikia kuwa aliwasikia ikiwa wao walijua kuwa kazirai. Baada ya muda kidogo alirejea kutoka ofisini kwa daktari Abbas na kuwaaga.
"Dada Jackline unachokifanya siyo kabisa, naomba usiondoke kwanza tulizungumze hili mbona ni suala dogo sana na linazingumzika."
Roberto aliongea huku akimfuata Jackline kwa nyuma huku Jessica akiwa ameduwaa mikono kichwani.
"Roberto narudi sasa hivi tutaongea tu ngoja nikafuate mzigo fulani hivi niliuacha nyumbani kwa mzee Jerome."
Jackline alimwambia Roberto huku akiwa kaufungua mlango tayari kwa kupanda.
"Basi tuongozane wote huko nyumbani."
"Hapana wewe baki tu umpe kampani Jessica."
Alimjibu na kuingia kwenye gari alilokuja nalo na kuondoka zake. Roberto na Jessica walitazamana kama vile kila mmoja alikuwa ana swali kwa mwenzake.
"Hivi ni kweli atakuwa anaelekea nyumbani?"
Jessica alimuuliza Roberto.
"Wewe na mimi hatujui anaelekea wapi tumeyakoroga wenyewe Jessica hasira hasara."
"Ni kweli kabisa Roberto hata sijui itakuwaje siku dada akirudi na kuambiwa kuwa tulifanya ujinga kama huu."
Alikuja daktari aliyekuwa akiwashughulikia wakina Mustapha na baba yake mzee Jerome na kuwapa taarifa kuwa wagonjwa wao wanaendelea vizuri na mzee Jerome keshapata fahamu tayari ila Mustapha atatakiwa kuachwa apumzike mpaka kesho.
" Lakini naye atazinduka daktari?"
Jessica alimuuliza daktari.
"Ndiyo na ataendelea kubakia chumba maalum lakini mzee Jerome mnaweza kwenda kumuona."
Daktari aliwaelekeza na kuachana nao wakielekea kumuona huku naye daktari akielekea ofisini kwa daktari Abbas kupeleka taarifa ya wagonjwa wake.
Jackline alifika nyumbani kwa mzee Jerome akashuka getini na kumshukuru yule dereva Taxi na kuachana naye kisha yeye akaingia ndani ambako alienda mpaka ndani akachukua kila kilicho chake na kupakia kwenye moja ya gari ambayo walichukua kwa yule kijana aliyeuawa na Robinson, lakini kabla hajaondoka alichukua kisu chake pamoja na bastola yake akatoka zake na kuelekea nyumbani kwa mwenyekiti na kwa kuwa alikuwa hapajui aliweza kumuuliza mama mmoja aliyekuwa akiuza maandazi mtaani pale.
"Mwenyekiti wa mtaa wetu anaishi kwenye nyumba ile pale yenye geti la kijivu."
"Nashukuru mama."
Alimshukuru na kuongoza mpaka kwenye nyumba ile aliyoelekezwa na mama muuza maandazi na kugonga geti. Alipoona kimya aligonga tena lakini hali ilivyobaki vile vile aliona apige kengele ambayo ilipelekea mlango mdogo wa geti kufunguliwa.
"Karibu binti pita ndani."
Alikaribishwa na mama mmoja wa makamo ambaye bila shaka alikuwa ni mke wa mwenyekiti.
"Asante mama, mimi si mkaaji ninahitaji kuonana na mwenyekiti."
Alimjibu baada ya kuingia ndani.
"Wewe ni nani? Mbona sura yako ni ngeni machoni pangu."
"Ni kweli lakini hata nikikaa kuanza kukuelezea mimi ni nani huwezi kunifahamu, naomba uniitie mwenyekiti au unahisi na mimi ni mke mwenzako?"
Jackline alimjibu jeuri.
Mama huyo hakujibu kitu zaidi ya kuingia chumbani kwake.
JACKLINE KAFUATA NINI KWA MWENYEKITI?
NA VIPI KUHUSU VITA MPYA BAINA YA JACKLINE NA WENZAKE ITAKUWAJE NA WAKINA JASMINE WATAPATIKANA?
USIKOSE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA KUJUA KILICHOJIRI.
Huku nyuma Jackline aliitoa bastola yake na kuivisha kiwambo tayari kwa kuzuia mlio kusikika kisha akairejesha kwenye koti lake. Mara alitokea mwenyekiti akiwa kaongozana na mke wake, alipokutana na sura ile ya Jackline ni kama alihisi kitu.
"Karibu binti."
"Asante."
Aliitikia Jackline.
"Ndiyo sijui nikusaidie nini binti."
Mwenyekiti alimuuliza Jackline.
"Sidhani kama unaweza kunisaidia kitu chochote mwenyekiti."
Jackline alimjibu huku akikaa vizuri kitini.
"Hudhani kama naweza kukusaidia?"
"Ndiyo huwezi kunisaidia chochote."
"Heee !! Sasa kama sina cha kukusaidia umefuata nini kwangu muda huu?"
"Nimekufuata wewe, unakumbuka jana uliniambia una tatizo gani?"
Jackline alimjibu huku akiinuka pale alipokuwa kakaa.
"Wewe binti hebu kuwa na adabu unapoongea na kiongozi mkubwa wa eneo hili, sawa !!"
Mwenyekiti aliongea kwa hasira kidogo huku akiwa kamtolea macho Jackline.
"Niwe na adabu ninapoongea na kiongozi mkubwa wa eneo, nani huyo wewe au mwingine?"
Hapo Jackline alimsogelea mwenyekiti na kumkamata kidevu huku akimuuliza maswali kwa sura iliyojaa hasira.
Kitendo kile kilimkwaza mke wa mwenyekiti aliinuka pale alipokuwa kakaa na kumfuata Jackline bila kuuliza aliinua mkono ili ampige lakini alikutana na teke ambalo lilimpeleka mpaka kwenye meza na kujipigiza huko.
"Mume wanguuu.....niokoee....!!"
Alipiga kelele hizo huku akibubujikwa na damu kichwani. Mume wake alitaka kumfuata mke wake ili atoe msaada lakini alishangaa kukutana na mdomo wa bastola.
"Sasa unaweza kupata majibu ya maswali yako kwanini niko ndani ya nyumba yako, ili kuokoa uhai wako na wa mke wako ongea mwenyewe ulichokifanya nyumbani kwa mzee Jerome."
"Binti mbona sijafanya lolote mimi huko?"
Alijitetea mwenyekiti.
"Ohh vizuri sana kumbe siyo wewe....!!"
Jackline aliongea na kumtandika risasi ya kidole cha mguuni.
"Mwenyekiti unaweza kuongea sasa bila uoga wowote."
Kabla hajajibu chochote mwenyekiti alichomwa kisu cha kwenye paja ambacho kilimfanya kupiga ukelele wa maumivu huku mke wake naye alikuwa akiendelea kuvuja damu bila msaada wowote.
"Vipi mwenyekiti bado huna majibu ya swali langu?"
Alimuuliza huku akiwa kamsogelea karibu zaidi.
"Nitaongea ukweli wote ila naomba usiniue binti yangu."
"Unanichelewesha mzee ongea haraka."
"Usiku ule nilifuatwa na mwanadada aitwaye Nafiwe akiwa kaongozana na watu wengine wawili wa kiume ambao sikujua majina yao lakini walikuwa wageni machoni pangu na kisha kunishinikiza nije pale niwazubaishe kisha niondoke, lakini sikujua nini maana yake na mara baada ya mimi kufanya vile na wale vijana tulirudi majumbani na baada ya kama dakika thelathini hivi alirejea Nafiwe peke yake akiwa na furaha kubwa hakusema kitu zaidi ya kunikabidhi bahasha ya kaki iliyokuwa na hela ndani yake."
"Ni hivyo tu?"
Jackline alimuuliza tena.
"Ni hivyo binti yangu lakini anapotoka alisema nisiwe na wasiwasi juu ya usalama wangu kwani wao wanaelekea mafichoni Brazil kwani walichokuwa wanakihitaji wamekipata."
"Walichokuwa wanakihitaji wamekipata?"
"Ndiyo."
"Kitu gani hicho?"
"Hapo ndiyo sifahamu chochote."
Majibu ya mwenyekiti yalipiga kengele ya hatari kwa Jackline akiamini kuwa kwa vyovyote vile wamewachukua Jasmine na Titiana kwa ajili ya kwenda kuwatoa viungo vyao vya mwili kama ilivyokuwa ahadi ya Santana ili wakaviuze kwa Wahindi huko India hivyo hakuona sababu ya kuchelewa kubaki alimchapa risasi mbili za utosini mwenyekiti huku mke wake akimshindilia kisu cha tumboni kisha kutoka zake. Alitembea haraka sana kuelekea nyumbani kwa mzee Jerome tayari kwa safari. Lakini alipofika nyumbani kwa mzee Jerome Whistle aliwakuta Jessica na Roberto nao wakiwa tayari na mizigo yao kwenye gari alilopakia yeye.
"Enhh mbona mko hapa?"
Jackline aliwauliza baada ya kuwakuta wakiwa wameegemea gari.
"Tulikuwa tunakungojea wewe hatuko tayari kutengana na wewe katika hili hivyo na sisi tunaambatana pamoja huko uendako."
Roberto alimweleza Jackline kile walilokuwa wamejadiliana baada ya yeye kuondoka pale hospitali.
"Vizuri lakini mimi siko tayari kuongozana na ninyi popote naogopa kuwaharibia mikakati yenu bwana, nilianza tukakutana njiani naomba tuachane njiani safari nitaimaliza mwenyewe."
Jackline aliongea na kuingia kwenye gari lakini kabla hajaondoka wakina Roberto waliingia garini.
" He vipi ninyi naomba mshuke mnanichelewesha jamani!!!"
" Fanya chochote juu yetu lakini hatuko tayari kufanya kosa jingine ambalo litasababisha tukupoteze."
Jessica alimjibu Jackline majibu ambayo yalimchosha na kupelekea kupiga mikono yake kwenye usukani kisha akageuka kuwaangalia kwa macho ya hasira kisha alijifunga mkanda na kuwasha gari safari ikaanza. Walianzia kwenye makazi ya Madam Nafiwe kwanza ambako baada ya kufika kila mmoja alikamata silaha mkononi na kugonga geti la nyumba hiyo humo kila mmoja alielekea upande wake lakini mwishoni walikutana wakiwa hawana walichokiona kwenye jengo hilo hivyo waliingia kwenye gari na kuelekea kwenye jengo jingine la Nafiwe.
"Tumefika kwenye jengo hili ambalo Nafiwe hulitumia kama ofisi za kampuni yake hivyo tuweni makini wanaweza kubadili matumizi kwa muda."
Jackline aliwatahadharisha wakiwa wanashuka kwenye gari.
"Tufanye kipi dada Jackline?"
Jessica aliuliza swali.
"Tutaingia kwa pamoja silaha zikiwa mifukoni kisha upepo ukibadilika tu ni kuzichomoa na kucheza nao."
"Bila shaka."
Roberto alijibu kisha wakashuka kwenye gari na kuliendea geti ambalo halikuwa mbali na pale walipokuwa, walifika na kugonga. Mlinzi alifungua na kuwaruhusu waingie ndani walitazamana na kuingia Jessica akiwa mbele Roberto akifuata na Jackline akawa wa mwisho na baada ya kumpita tu mlinzi Jackline aligeuka na kumpiga teke la kidevu ambalo lilimpeleka chini mlinzi na bila kuchelewa alimfuata na kumkita kisu cha kifuani wakina Jessica walipogeuka na kuushuhudia mchezo ilibidi wafichame kwa lengo la kumlinda ili alitokea mjinga yeyote wacheze naye.
"Niambie Nafiwe yuko wapi na watu wake?"
Jackline alimuuliza mlinzi huyo huku akikizungusha kile kisu alipomchoma.
"Aghh.. Si..si...ju..ju.. Mamaaaa nitaongea usinifanye hivyo wewe mwanaizaya."
"Ongea haraka kabla sijaanza kuondoa vidole vyako."
"Wam...wam....eondoka muda si mrefu kue...kuelekea bandarini wanataka kuiwahi Meli ya usiku."
"Wameondoka wangapi?"
"Waliku...wali...wa...wakuwa wote na wa...wal...."
Hakumaliza sentensi yake alikata kauli.
Aliinuka na kuwapa ishara wenzake ya kuondoka mle ndani.
"Tunaelekea bandarini muda huu inasemekana wako huko wanajiandaa kusafiri na Meli ya usiku ila haijulikani ya saa ngapi, muda huu ni saa moja hebu tuwahi huko."
Aliwaelekeza alichoambiwa na mlinzi kisha walitoka na kuelekea walikokuwa wamepaki gari lakini walipolikaribia gari Jackline alilishtukia baada ya kuona ni kama kuna kivuli cha mtu hivyo aliwazuia wenzake wasilisogelee.
" Jessica msilisogelee hilo gari ni kama kuna mtu kwa nyuma."
"Kuna mtu?"
Roberto aliuliza huku akiliangalia gari hilo pale lilipokuwa kama kuna mtu kweli.
NINI KITAENDELEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA.
YA KUTAFUTIA USINGIZI HIYO.
Baada ya kuangalia vizuri ni kweli kulikuwa na kivuli cha mtu upande wa nyuma wa gari hilo hivyo haraka sana waliondoka eneo hilo na kwenda kujificha kando kidogo ili kuweza kumuangalia mtu huyo anafanya nini hapo kwenye gari lao. Walijibana pale kwa muda lakini mtu yule aliendelea kukaa pale na pia hawakujua wafanye nini kwa mtu huyo.
"Mimi nina wazo jamani."
Jessica aliwaambia wenzake.
"Wazo gani hilo?"
Jackline alimuuliza Jessica juu ya kile alichokifikiria.
"Mnaonaje kama mmoja wetu akienda pale kwa staili ya kuviringika mpaka pale na kuingia uvunguni mwa gari na kumshambulia kutoka uvunguni kwani mpaka sasa hajaweza hajatuona kwani ingekuwa hivyo lazima angechukua hatua juu yetu."
Wazo lile la Jessica lilipitishwa bila pingamizi na haraka sana Roberto hakutaka kusubiri uchaguzi ufanywe nani aende yeye akajitosa kuelekea kwenye gari kwa staili ya kuviringika kama gurudumu. Baada ya kufika alijitosa uvunguni mwa gari na kutokea pale alipokuwa kasimama mtu yule ambaye hakufahamika ni nani na anasubiri nini pale.
Alipomfikia alimpiga mtama maridhawa uliompeleka chini yule mtu na kumfanya Roberto kumkalia juu yake bastola ikiwa kwenye paji la uso.
"Niambie wewe ni nani na umefuata nini hapa?"
"Wewe ni nani?"
"Nimekuuliza wewe ni nani na umefuata nini hapa sihitaji maswali bali majibu."
Roberto alimuuliza huku akiisugua bastola kwenye paji la uso wa yule mtu.
"Samahani kaka mimi naitwa Mahmoud ni dereva Taxi niliyekuwa nimemleta ndugu yenu pale hospitali."
"Dereva Taxi? Sasa umefuata nini hapa muda huu?"
Roberto alimuuliza swali baada ya kujua mtu huyo ni dereva Taxi ambaye alimbeba Jackline mchana.
"Toka nilipoachana naye sikutaka kumuacha peke yake kwani hakuwa sawa hivyo niliamua kumfuatilia nyuma kwa kila hatua yake mpaka anakwenda kumuua mzee yule kule bondeni ambaye ni kiongozi wa eneo lile nilikuwepo na sasa huku."
"Kwa hiyo wewe unatuchunguza sisi siyo?"
Roberto alimuuliza huku akimsindikiza na ngumi ya kichwani.
"Kaka hujui tu ndiyo maana unanipiga hivi."
"Roberto tunakwenda na muda mnaongea nini na huyo?"
Jackline alimkumbusha Roberto wakiwa wameshafika pale.
"Huyu ni yule dereva Taxi uliyekuwa naye mchana."
"Dereva Taxi? Kafuata nini huku au naye ni Kibaraka wa Santana?"
Jackline aliuliza.
"Tulipoachana muda ule niliondoka zangu lakini sikufika mbali nikawa nimekutana na Daktari Abbas akanisimamisha na kunipa kazi ya kukufuatilia kwa lengo la kukulinda bila wewe kujua hivyo niligeuza gari na kurudi mpaka pale nilipokuacha ndipo ulitoka na kuelekea kwa yule kiongozi nikiwa nyuma yako mpaka unafika na kufanya mauaji yale mimi nilikuwa dirishani kifupi ni hivyo tu na kule mlikokuwa mmeingia kulikuwa na walinzi wawili ambao walijificha mlipoingia tu walianza kuwavizia mimi nilicheza nao na kuwavutia pembeni bila ninyi kuona, na hapa ikawa hivyo hivyo njooni muone."
Alipoinuka huku akiwasimulia aliwaita kuwaelekea gizani ambako huko aliwaonesha miili ya watu watatu aliowaua.
" Hawa walikuwa nje ya geti mlipoingia ndani waliwasubiri hapa nje mkitoka tu wawashambulie lakini niliwamaliza."
"Mbona hatukusikia mlio wa risasi yoyote?"
Roberto alimuuliza.
"Bastola yangu ina kiwambo cha sauti hivyo huwezi sikia sauti."
Maelezo ya dereva Taxi yule yaliwachanganya kiasi cha kuwa na mashaka naye.
"Unatuchanganya Mahmoud kwa hiyo wewe ni dereva Taxi au nani? Tupe utambulisho wako."
Jackline alimuuliza.
"Mtanijua tu baadaye siyo sasa, mnaweza kuendelea na misheni yenu mimi nitakuwa nyuma yenu nikitekeleza wajibu wangu kwenu kama niliagizwa na bosi Abbas."
Hakuwa tayari kuwaeleza yeye ni nani kwa wakati huo na aliwaahidi kuwa watamfahamu hapo baadaye.
"Okay sawa."
Jackline alimjibu.
Waliondoka na kuelekea bandarini kwa ajili ya kumwagiwa Santana na watu wake. Kwa kuwa hapakuwa mbali waliweza kufika karibu na bandari hiyo ya Namport na kusimamisha gari.
"Jamani ndiyo tumefika eneo la mapambano si eneo zuri kwani linamilikiwa na serikali hivyo tukifanya kosa tunakamatwa na kama ambavyo niliwahi ambiwa huko nyuma wakati naichunguza hii bandari ni moja maeneo yanayolindwa sana serikali hivyo basi huko ndani tutaingia kwa staili ya panya hii staili ya kupenya popote pale hata pawe na ulinzi kiasi gani na tulifika huko ndani hatuwezi kutumia bastola zetu tutatumia visu tu."
Jackline alitoa maelezo.
" Sasa kama kuna ulinzi mkali tutapenyaje kuingia ndani?"
Jessica aliuliza.
" Kuhusu kuingia wala msijali nilishawahi fanya uchunguzi kwa kumtumia mfanyakazi wa humu ndani, kuna chemba moja ambayo tutaitumia hiyo kuingia ndani ni njia majitaka."
"Santana atakuwa alipitia wapi kuingia huko ndani?"
"Jamani tunapoteza muda andaeni vitendea kazi tuanze zoezi la kuingia ndani."
Walijiandaa wakashuka kwenye gari na kuanza kuufuata uchochoro ambao ulikuwa na hiyo chemba ya majitaka. Walifika kwenye hiyo chemba Jackline akatoa mfuniko na kuanza kuingia ndani, Roberto alikuwa wa mwisho hivyo akaurusha mfuniko kwa staili ya kuuweka kichwani kwake alivyoshuka chini wenyewe ulibaki sehemu yake huko chini ilikuwa ni visu mkononi. Walitembea na kutokea ndani sehemu ambayo ilikuwa ni kama barabara ya viberenge ya kupitishia mitambo na bidhaa mbalimbali kutoka kwenye Meli.
"Hapa tulipo kabla hatujaonwa tufichame sehemu tulivu ambayo hawawezi kutuona Jessica utaitraki namba ya Santana au ya Nafiwe tujue wako upande gani?"
"Sawa lakini hapa nina namba ya Santana tu."
"Siyo mbaya anza na hiyo asipoonekana nitakupa namba ya Nafiwe."
Jessica aliitoa simu yake na kuiingiza namba ya Santana kwenye mfumo na kama bahati ilikuwa hewani, walipoangalia vizuri umbali wakifurahi sana kwani wahusika hawakuwa mbali na pale walipo hivyo walianza kunyata kuufuata ukuta wa lile jengo. Na mwisho iliwaonesha sehemu walipo kwa usahihi na ndipo Jessica alipoizima simu huku Roberto akifanya kazi ya kuchungulia kila dirisha la chumba walichokuwa wanakifikia.
"Wanasema tuendelee kuwepo hapa kwani Meli hiyo itaondoka hapa mnamo saa nane usiku kwani bado wanamalizia kupakia mzigo."
"Ina maana tunaondoka na Meli ya mizigo?"
"Unataka tuondoke na boti ili tudakwe? Meli ya mizigo inahusika na uzuri wa hii Meli ni ya Kampuni ya jamaa yangu hivyo usalama ni asilimia mia moja."
Maongezi yale kutoka ndani ya chumba kimoja waliweza kuyasikia yaliyokuwa kati ya Santana na Nafiwe wakiwa na uhakika zoezi lilikuwa limekamilika kwa asilimia zote.
" Tunafanyaje hapa kuwavamia Jackline?"
Jessica aliuliza.
" Hapa tulipo ni moja ya mafanikio yetu hatuna haja ya kuwa na haraka, hapa kazi tunayoianza ni kuanza kuua mlinzi mmoja baada ya mwingine mpaka tuwafikie."
"Sawa sawa tuanzeni sasa."
Roberto aliwaharakisha wenzake, hivyo walianza kuwanyatia walinzi waliokuwa wanalinda jengo ambalo ndani yake ndiyo walikuwamo wakina Jasmine. Wakiwa wanaendelea kuvichunguza vyumba vile kupitia madirishani mara walikifikia chumba ambacho hicho waliweza kusikia watu wakiongea kwa taabu sana.
"Na..na..naom...ba wai...waite wani...ue nime....choka kwa mateso."
Sauti hiyo ilikuwa ni ya Titiana ikiongea kwa shida kwa ilivyoonesha walikuwa wameteswa sana mpaka kufikia hatua ya kukata tamaa. Kitendo hicho kiliamsha hasira za Roberto na kujikuta akiligonga dirisha lile ili waweze kusikia, na kweli walisikia kwani Jasmine aliyekuwa kafungwa kamba za kutosha kwenye kiti cha chuma aliweza kugeuka kutazama dirishani.
"Tumekuja kuwaokoa ndugu zetu msikate tamaa."
Jackline aliongea kwa sauti ya kunong'ona lakini iliyosikika mle ndani.
"Naomba sigara yako niwashe yangu."
Roberto aliambiwa na mlinzi aliyefika kuomba kuwasha sigara baada ya kumuona Roberto akivuta sigara akajua ni mlinzi mwenzake, Roberto aligeuka kumpa mkono wenye sigara kitendo cha kupokea ile sigara alimdaka na kumvutia kwake na kumpiga kichwa kilichomfanya apepesuke na kabla hajafanya chochote alimuwahi na kumkita kisu cha kifuani kisha kumvutia gizani na kusonga mbele. Visu viliendelea kutembea mle ndani mpaka alipoukaribia mlango wa kile chumba lakini akiwa anataka kugusa kitasa cha mlango huo mara mlango wa chumba cha pili ulifunguliwa haraka sana alikimbia na kujificha. Alimchungulia aliyetoka ni nani japo lilikuwa ni giza aliweza kumfahamu kutokana na mwanga wa simu ambayo mtu huyo alikuwa akiiangalia.
"Shiiiit si Nafiwe huyu?"
Roberto alijiuliza baada ya kumuona vizuri.
"Nakula naye sahani moja huyu kabla hajazima simu yake."
Alimfuata na nyuma nyuma mpaka alipoufungua mlango wa chumba cha wakina Jasmine huku ule mwanga wa simu ukimpa msaada kutokana na giza lililokuwa sehemu ile. Alipofungua tu mlango kabla hajafanya chochote Roberto alimfuata na kumuwekea bastola kichwani kwake.
"Nafiwe kuwa mpole tofauti na hapo ubongo wako halali yangu, naiomba simu yako."
Nafiwe hakuwa na jinsi alimkabidhi ile simu na kuweka mikono juu.
"Ingia ndani haraka."
Madam Nafiwe aliingia ndani ya kile chumba Roberto naye akafuata na kuufunga mlango kwa ndani.
Humo hakutaka kuchelewa aliona amlegeze kwanza ili asipate jeuri kuleta jeuri yake hivyo Roberto alianza kumshushia kichapo hasa baada ya kumuona mpenzi wake akiwa kwenye hali ile.
"Niko tayari kufanya chochote kile lakini usiniue."
Kichapo kilipokolea alianza kuomba msaada kutoka kwa Roberto ambaye muda huo hakuwa akiongea chochote zaidi ya kutoa kamba mfukoni na kuanza kumfunga Nafiwe karibu kabisa na Jasmine.
"Wala usihofu huwezi kufa saizi muda wako bado haujafika."
Alimjibu huku akiinuka na kumfuata Titiana ambaye muda huo alikuwa akikoroma tu hali ilikuwa tete.
"Mpenzi wangu usiniache nimefika kukuokoa."
Roberto alimwambia Titiana asimuache muda huo akimfungua kamba alizofungwa na baada ya kumaliza alimfuata Jasmine ambaye hali yake haikuwa mbaya sana zaidi ya maumivu ya bega ambalo lilipigwa tena pamoja na kichwa ambacho alikuwa akilalamika kutokana na kipigo cha kugongeshwa ukutani.
"Nafiwe utalipia na wenzako Ole wenu Titiana afe."
Jasmine alimwambia baada ya kufunguliwa pale. Na baada ya hapo mlango ulifunguliwa na kumtoa nje Titiana kisha wakamfungua kamba Nafiwe kumfunga kitambaa usoni kisha kamba za mikono na kuondoka naye. Zoezi likawa wanafikaje nje kwa kupitia kwenye ile chemba wakiwa na wagonjwa. Hivyo waliamua kumchukua Nafiwe na kutaka ataje njia ya kutokea nje.
"Taja njia ya kutokea nje ambayo ni salama."
Jackline alimuuliza huku akimchoma kisu cha kwenye paja.
"Nitawaambia tu msinifanyie hivyo mwenzenu."
"Nani mwenzako mshenzi wewe usiye na haya onesha njia haraka."
Roberto alimkatisha.
"Fuateni hayo makontena mpaka mwisho mtaikuta barabara hiyo ndiyo muifuate itawatoa nje bila kuonwa na walinzi."
Hapo hapo Roberto akambeba Titiana huku Jackline naye akimchukua Jasmine huku Jessica yeye akisalia nyuma kuangalia usalama.
NINI KINAKWENDA KUTOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.
Muda ulipita bila Madam Nafiwe kurudi toka alipotoka kwenda kuwaangalia Jasmine na Titiana kama wamezinduka baada ya kupokea kipigo kikali kutoka kwao, ikabidi Santana amwambie Robinson akaangalie nini kimetokea huko kwani hata namba yake ya simu ilikuwa ikiita tu bila kupokewa.
Robinson aliondoka na kuelekea kwenye chumba ambacho waliwahifadhi mateka wao lakini alibaki mdomo wazi baada ya kukuta chumba kiko wazi na ndani hakuna mtu si Jasmine wala Titiana na hata Nafiwe mwenyewe hakuwepo. Alitoka na kumfuata Santana jasho likimtoka na halikuwa jasho la kawaida bali la hofu juu ya kilichotokea.
"Bosi tumechezewa mchezo na Nafiwe."
Robinson alimwambia bosi wake Santana.
"Tumechezewa mchezo? Una maanisha nini Robinson kusema hivyo?"
Santana alitoa sigara yake mdomoni na kumuuliza Robinson anamaanisha nini kusema wamechezewa mchezo.
"Unauliza? Twende ukajionee mwenyewe nisije ongeza chumvi bure ukanigeuza bucha."
Robinson alimjibu huku akimshika mkono kutoka naye nje mpaka kwenye kile chumba ili akajionee mwenyewe.
"Haaa nini kimetokea Robinson? Unajua msijaribu kunichanganya mimi ni chizi kitambo ohooo..."
Santana alishangaa baada ya kukuta chumba kitupu hakina mtu yeyote yule.
"Na ndiyo maana nikakwambia tumechezewa mchezo na Nafiwe, kama si yeye yuko wapi sasa?"
Robinson alimuuliza maswali ambayo inawezekana Santana hakuyahitaji zaidi ya majibu.
"Hebu ngoja kwanza Nafiwe anawezaje kunifanyia kitu cha kishenzi kama hiki?"
Santana alichanganyikiwa kitambaa kikiwa mkononi kufuta jasho ambalo sijui lilitoka wapi kwani muda huo kulikuwa na baridi kali,ikabidi atoke nje kwanza kuangalia chochote kile kinachoweza kumsaidia kubaini waliko watu wake. Hakuweza kuamini alichokutana nacho nje ya jengo lile miili kadhaa ya walinzi walikuwa wameuawa.
"Ahaa ina maana huyu Nafiwe ni mshenzi kiasi hiki? Haiwezekani hata kidogo mimi ndiyo Santana kiboko yao nitamuonesha."
Akiwa ameshika kichwa chake alijisemea maneno hayo huku akishuhudiwa na Robinson.
"Bosi hivi waliohusika na huu mchezo hawawezi kuwa wakina Jackline kweli?"
Robinson alimuuliza huku akimfuata nyuma kwani Santana hakuona sababu ya kuingia ndani ikabidi awafuate walinzi wa geti kuu la kuingilia mle ndani.
"Ngoja kwanza niwafuate walinzi kule geti kuu watanieleza ni nani aliyefanya hivi."
Walitembea haraka kulifuata lango kuu ambalo lilikuwa na walinzi wa kutosha.
"Hee hiki si ni kiini macho kweli? Wako wapi hawa mbona geti liko tupu?"
Santana aliuliza baada ya kukuta geti halina mtu na mlango mdogo wa pembeni uko wazi.
"Nafiwe kafanya yake bosi hapa hakuna cha kuendelea kujadili zaidi ya kumtafuta popote pale alipo."
Robinson aliyekuwa na uhakika kuwa Nafiwe ndiye mhusika wa kuwatorosha wakina Jasmine aliongea kwa kujiamini huku akilifuata gari lao walikokuwa wamelipaki.
" Nitakula nyama ya mtu ikiwa mbichi iwapo nitamkamata huyu mwanaharamu."
Santana aliongea akifunga mkanda wake huku Robinson akiwa nyuma ya usukani tayari kwa safari ya kuanza kumsaka Madam Nafiwe.
"Tunaanzia wapi mkuu?"
"Breki ya kwanza iwe nyumbani kwake kwanza japo sina uhakika kwani kwa alilolifanya hawezi kuwa kwake lakini tuanzie huko."
"Sawa mkuu."
Robinson alimjibu na kukanyaga mafuta kutoka mle bandarini. Wakiwa nje ya lango hilo simu ya Santana iliita akaichukua na kuangalia mpigaji ni nani alipombaini akapokea.
"Haloo Santana."
"Umeona unifanyie Umafia baada ya kulisikia dili la Wahindi siyo?"
Santana aliuliza kwa ghadhabu baada ya kuisikia sauti ya Nafiwe.
"Ulijua wewe ni mjanja baada ya kuyafanya uliyofanyia siyo? Sasa nakuahidi kuwa wewe na huyo mshenzi wako uliyebaki naye muda wenu umefika tayari."
Jackline aliichukua simu ambayo alimuwekea Nafiwe aongee na Santana.
"Mwanaharamu wewe usiye na kwenu kumbe ndiye uliyenichezea kauntataki hii?"
"Usiulize kuhusu hilo jiulize nikikukamata nitakuuaje? Kwani mpaka sasa uko kiganjani kwangu pamoja na huyo nyangarika mpenda kifo."
"Unajidanganya Jackline huwezi kufanya unachokifikiria kwani nitakuangamiza kabla ya kutekeleza ulichokipanga kwetu."
"Vizuri sana Santana, unajua nini mimi siku zote hupenda kucheza michezo kama hii na adui anayejiamini kama wewe, na kama uko tayari kwa hilo niambie tuuanze huu mchezo sasa hivi."
Jackline aliendelea kumchimba mkwara Santana ambaye muda huo alikuwa katota kwa jasho kwani hakutegemea kama aliyewatorosha mateka wake anaweza kuwa Jackline.
" Mshenzi huyu atanitambua, hawezi kucheza na akili yangu namna hii."
Santana alikuwa akijiwazia hayo kabla ya kumjibu Jackline aliyekuwa hewani akisubiria jibu.
"Mbona kimya Kamanda? Au ndiyo ule msemo wa kiswahili usemao kuwa 'ukiona kimya pigia mstari' na mimi nifanye hivyo?"
Jackline alimtupia swali jingine baada ya kuona kimya.
"Jackline ninakuapia haki ya mama yangu mzazi aliyelala pale makaburini Brazil nitakuua."
"Maneno ya mfa maji hayo huna lolote lile unaloweza kulifanya, hivi kati yangu na wewe ni nani awezaye kummaliza mwenzake?"
"Mimi ndiyo nitakayekuua kabla yako."
Santana alimjibu huku akimuashiria Robinson apunguze mwendo.
"Mimi ndiye niliyekuwa na nafasi ya kukuangamiza lakini niliona niwaache mvute hewa ya mwisho mwisho na ikiwezekana muwapigie simu ndugu zenu kuwaaga na kuwaambia kuwa muda si mrefu bara la Afrika linakwenda kuwameza."
"Kelele wewe unazungumza hayo kwa mamlaka ya nani?"
Santana aliona aongee kiume baada ya kuona sauti ya kike inataka kumpanda kichwani.
"Hapo ulipo unaweza kuangalia nyuma ukipenda lakini."
Jackline aliongea hayo na kumkatia simu,na hapo Santana aligeuka nyuma kuangalia kuna nini alichoambiwa na Jackline akiangalie.
"Mwanahizaya huyu kuna nini sasa mbona sioni chochote huko nyuma? Hebu paki gari pembeni tuone kuna nini."
Walitelemka baada ya kupaki gari na kurudi nyuma kuyakagua maeneo yote kama aliambiwa kwenye simu lakini hakuna walichokiona.
"Unajua huyu mwanamke anaendelea kunipandisha hasira zangu atajuta kuingia anga zangu."
Santana aliongea hayo baada ya kutokuona chochote kile eneo lile ikabidi wageuze kurudi kwenye gari kuendelea na safari lakini hawakuamini kilichotokea mbele ya macho yao, gari liliondolewa kwa kasi ya ajabu na kuwaachia vumbi pale walipokuwa.
" Bosi mbona gari linaondoka?"
"Kweli tunachezewa akili zetu na huyu Mwanaharamu yaani atushushe kwenye gari kisha yeye aondoke nalo?"
"Kinachonishangaza kafanyaje wakati funguo ninayo hapa?"
Robinson alimuonesha funguo ile ya gari Santana huku akilishuhudia gari likipotea mbele ya upeo wa macho yao.
"Yaani wewe kweli bado sana kwenye fani hii unauliza funguo? Watu wana taaluma zao hebu tufanye utaratibu wa kuwafukuzia."
Santana alimshangaa Robinson baada ya kuuliza wamefanyaje ilhali funguo anayo yeye.
"Umeona sasa namna ninavyoweza kuwasambaza kama upepo wa kimbunga? Nakuangamiza kidogo kidogo nimeanza na watu wako wa karibu, nimechukua gari lililokuwa linakupa jeuri mpaka kufika kwa mwenyekiti na kufanya naye umafia ule lakini napenda kukujulisha kuwa naye pamoja na mke wake wako kukuandalia makao yenu wewe na Robinson."
Ilikuwa ni simu kutoka kwa Jackline moja kwa moja.
" Hivi we..... "
Kabla hajamaliza kuongea simu ilikatwa.
"Shabash, nitakukamata tu hata kwa kuchelewa lakini lazima iwe hivyo haiwezekani Santana nionekane hayawani nisiye na dhamani mbele ya waonao."
Aliongea hayo na kuchomoa sigara mfukoni na kuiwasha huku nyuma Robinson akiwa kavua na koti lake japo ilikuwa ni baridi.
***
" Pole sana Jasmine Mungu bado ni mwema anakupigania."
Daktari Abbas aliongea baada ya kumpatia huduma Jasmine alipofikishwa na pale hospitali na Jessica akiwa sambamba na Roberto ambaye muda huo alikuwa hatuii mlangoni kusubiri ni taarifa gani atakayoambiwa kwenye oparesheni inayoendelea kwa mpenzi wake Titiana ambaye hali yake ni mbaya sana.
"Ninakushukuru sana daktari Abbas kwa kujitolea kutupigania."
"Usijali nilijitolea kwenu kwa hiyo bado nina deni ambalo litakamilika baada ya maadui zenu kusalimu amri."
Daktari Abbas alimtia moyo Jasmine aliyekuwa katika tabasamu kubwa baada ya kupata matibabu.
"Kwa uweza wake Mungu tutaishinda hii vita ikiwa nilipoteza matumaini ya kuishi tena baada ya kutekwa na kuteswa lakini Jackline alitokea na kutusaidia."
"Mungu awasimamie muishinde hii vita mapema."
Daktari Abbas aliongea hayo na kumuomba apumzike kisha alitoka nje kuendelea na majukumu mengine.
Jessica aliendelea kumliwaza mzee Jerome Whistle ambaye giza zito la huzuni lilitanda mbele yake mara baada ya kuwapoteza watoto wake wote Victor na Mustapha ambao muda huo walikuwa wamehifadhiwa Mochwari wakisubiri kuhidhiwa kaburini.
"Binti yangu, wanangu wameniacha peke yangu nitaishi vipi mimi bila wao?"
Mzee Jerome aliendelea kuomboleza huku machozi yakimtiririka machoni.
"Mzee Jerome jipe moyo utayashinda haya yote yanayokutokea kipindi hiki kumbuka kila jambo hutokea kwa sababu chini ya jua."
Daktari Abbas alimwambia mzee Jerome baada ya kumkuta akiomboleza mbele ya Jessica aliyekuwa akimpa sapoti kwenye kutembea.
"Eee Mungu wangu nisimamie katika hili jaribu niweze kulishinda, nakuomba ukaniepushe na fikra mbaya juu ya vifo vya watoto wangu."
Mzee Jerome aliendelea kusali kimya kimya huku machozi yakiendelea kumwagika.
"Mzee Jerome naomba urudi wodini muda wa mazoezi umeisha."
Alifika Nesi na kumtaka mzee Jerome kurejea ndani maana muda ambao alipewa kufanya mazoezi umeisha. Jessica alimuongoza mzee Jerome kuingia wodini, alimkongoja taratibu mpaka wodini na kumpa sapoti kupanda kitandani.
" Jessica mwanangu hali yangu kwa sasa si mbaya sana nikiamka salama kesho au keshokutwa niwazike wanangu."
"Sawa baba tutalifanyia kazi hilo naomba upumzike sasa."
Jessica alimuomba apumzike ili kuupa nguvu mwili ambao bado haujawa sawa. Na wakati huo huo Roberto aliingia mule wodini.
ROBERTO ANA TAARIFA GANI?
JACKLINE ATAFANIKIWA KUWANASA WAKINA SANTANA? KAA TAYARI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
MWISHO WA SEASON 1
ENDELEA KUFUATILIA SEASON 2
MWISHO
0 comments:
Post a Comment