Simulizi : Ukurasa Wa Gaidi
Sehemu Ya : Tatu (3)
wa idara ya kupambana na ugaidi Tanzania yaani
C.T.I(Counter Terrorism Intelligence). Ni ajenti
namba moja kati ya maajenti wanaokwenda mstari
wa mbele kufanya kazi kwa vitendo (field agent) na
ni ajenti pekee aliyekuwa na uwezo wa kufanya
upelelezi na hata mapambano peke yake bila ya
kuwa na usaidizi.Mick ni ajenti namba moja kati ya
Maajenti sita wa idara ya C.T.I, maajenti watatu
wakiwa ni wa mstari mwa mbele kivitendo(field
agents) na watatu wakiwa ni maajenti wa usaidizi
(back up) waliofanya kazi zao nyingi ndani ya ofisi
na mara chache sana nje ya ofisi.
JIONI YA SIKU HIYO
Katika moja ya hoteli zilizopo katika kisiwa hiki cha
Ibiza, Mick anaonekana akipata chakula cha
jioni.Wakati huu ndipo alipowasha simu yake ya
mkononi aliyoifunga wiki nzima.Hakutaka
kusumbuliwa katika likizo yake.Hata televisheni na
kompyuta yake,alivitumia kwa nadra sana wakati
kama huu anapokuwa likizo.Alipenda kuishi kiasili
sana anapokuwa likizo. Muda mwingi
alijishughulisha kutembelea vivutio mbali mbali vya
Hispania ikiwapo majumba ya makumbusho ya
kihistoria na kujifunza mambo mbalimbali ya
kihistoria. Wakati mwingine alitembelea nchi
nyingine mbali mbali kama Italia,Ugiriki,
Korea,China na hata Japan.Yaani moja ya starehe
zake ilikuwa ni kujifunza historia mbali mbali na
hasa kwa nchi zilizokuwa na historia ndefu sana
tangu zama za kale(ancient time).Moja ya historia
aliyoipenda sana ni ile ya Korea ya kale na Mataifa
matatu yaliyowahi kuwapo katika nyakati hizo yaani
Koguryeo, Baekje na Silla.Lakini pia aliipenda
historia ya tawala za kirumi.
Wakati huu Mick alipoiwasha simu yake, message
mbalimbali ziliingia katika simu yake.Kulikuwa na
meseji mbali mbali kutoka mitandao ya kijamii na
zile za kawaida. Moja ya message iliyomvutia zaidi
ni ile ya kawaida iliyoingia katika laini yake namba
mbili ambayo hakupenda kuitumia sana na ni watu
wachache sana walioifahamu. Message ilisomeka
kwa Lugha ya kiingereza 'When the house is
burning call the resque team' (nyumba inapoungua
wapigie zimamoto).
"Kumekucha".Alijisemea Mick mara baada ya
kupata meseji hiyo.Dakika kadhaa baadaye Mick
alikwisha kufuatilia habari zaidi na kujua kinaga
ubaga nini kimetokea nchini.Baada ya kufuata
taratibu za kukodi ndege,saa chache baadaye
alikuwa yuko ndani ya 'pipa' ngani akielekea
nyumbani Tanzania, kuungana na idara nzima
kufanya kazi ngumu iliyokuwa mbele yao.
*********************************************
*****************************************************
Ndege aliyopanda Mick iliwasili uwanja wa ndege
wa JKIA(Julius Kambarage International Airport)
saa sita mchana.Mara baada ya kukamilisha
taratibu zote za ukaguzi wa uwanja wa ndege,
alielekea sehemu ya maegesho ya magari ambako
alikuta magari mbali mbali yakiwa yamepaki lakini
yeye akaliendea gari aina ya Range rover sport
nyeusi.Mick alikwenda moja kwa moja eneo la
matairi ya nyuma ya gari hilo, akapenyeza mkono
katika mlsehemu ya juu ya moja kati ya matairi
hayo kisha akapapasa katika.eneo hilo.Hapo
alifanikiwa kupata ufunguo wa gari hilo.
Moja kwa moja Mick alifungua mlango wa gari hilo
na kuingia ndani ambako alifungua droo katika
'dash board' ya gari hilo.Hapo akakuta bastola
mbili moja aina ya Beretta na nyingine ndogo aina
ya 'colt 45', pia kulikuwa na kiwambo cha kuzuia
sauti kwa jija lingine 'sailensa', magazine nne za
'beretta' zilizosheheni risasi, kiboksi cha risasi za
'colt 45'. Pia chini kabisa ya vitu hivyo alikuta
kikaratasi kimeandikwa 'Mahali salama Iringa.
Wengine watafuata'.Hapo Mick aliwasha gari na
kuondoka kwa kasi kuelekea Iringa.
Message iliingia katika simu ya Makassy "IRINGA".
Hapo hapo Makassy akamuita katibu muhtasi wa
C.T.I, Clara Makene. Sekunde chache baadaye
Clara alikuwa mbele ya mkuu wake wa kazi
akipewa maagizo. "Andaa kikao Maajenti wote
wahudhurie.Pia wasiliana na Kamanda wa E.C.S
( Elite Combat Squad). Mwambie nahitaji kuonana
naye masaa matatu kuanzia sasa.Ila kikao hiki
kiandae sasa hivi. Ndani ya nusu saa maajenti
wote muwe ndani ya chumba cha mikutano."
Alizungumza Makassy.
"Sawa boss". Alijibu Clara,katibu muhtasi wa C.T.I.
Wakati ambao idara ya C.T.I haikuwa na kazi
maalum zaidi ya upelelezi ule wa kung'amua kama
kuna tishio lolote la ugaidi linalotishia taifa, Clara
Makene alifanya kazi kama katibu muhtasi wa
C.T.I. Lakini kwa nyakati kama hizi ambazo
kulikuwa na kazi maalum iliyohitaji kupewa
kipaumbele , Clara alikuwa ni ajenti aliyepewa
namba nne katika idara ya C.T.I na namba moja
katika utaalamu wa teknolojia ya kompyuta.Clara
alikuwa na shahada ya pili ya teknolojia ya habari
na mawasiliano (information and communication
technology) aliyoipata katika chuo kikuu cha M.I.T
huko Marekani.Pia alikuwa ni mtaalamu wa 'data
analysis' kwa hiyo alikuwa ni data analyst
(mchambua data) wa C.T.I .Wataalamu wengine wa
kompyuta walikuwa ni ajenti Morris ambaye pia
alibobea katika masuala yote ya maabara na ajenti
Rachel ambaye pia alikuwa Daktari wa idara.
*************************************
Nusu saa baadaye, chumba cha vikao ndani ya
ofisi za C.T.I, maajenti wote kasoro ajenti Mick,
walikwisha kufika na kukaa katika viti vilivyomo
humo ndani. Zaidi ya ajenti Clara, Ajenti Morris na
Ajenti Rachel ; pia alikuwemo Paul Kumwembe,
ajenti namba mbili wa C.T.I ambaye alikuwa ni
ajenti wa mstari wa mbele(field agent) ambaye pia
alikuwa ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya
ulengaji wa shabaha, na mwisho alikuwepo ajenti
Jackline, ajenti namba tatu kati ya maajenti wa
mstari wa mbele( field agent) ambaye pia ni
mtaalamu wa kupangilia vikosi vya kimapigano.
Jukumu namba mbili Jackline lilikuwa ni kumsaidia
kiongozi wa kikosi maalum cha mapigano cha
C.T.I cha E.C.S kamanda Joshua Mwambinga
katika uwanja wa vita.Kwa lugha ya kitaalam
Jackline alikuwa ni 'Second in comand' wa E.C.S.
"Nadhani wote mumekwisha kuhisi sababu ya
kuwaita katika kikao hiki. Tukio lililotokea hapa
nchini ni tukio linalotuhusu sisi kuliko mtu
mwingine yeyote. Idara hii ilianzishwa ili ilifae taifa
kwa nyakati kama hizi.Kwa sababu hiyo ,tuna
sababu ya kuanza kazi mara moja.Tunaachana na
masuala mengine yote ya kiusalama na tunalipa
suala hili kipaumbele. Tuna chini ya miezi mitatu
kukamilisha kazi iliyo mbele yetu. Nimeongea juu
juu kwa kuwa Clara atatueleza mambo haya yote
kwa kina."Aliongea Mkurugenzi Eliackim Makassy.
Clara Makene, binti mzuri na mrembo kwelikweli,
alitembea kutoka alipokaa na kwenda katika meza
iliyokuwa mbele yake umbqli wa mita kama sita
hivi mbele yake. Juu ya meza hiyo kulikuwa na
kompyuta mpakato pamoja na 'projector'.Clara
akachomeka waya maalum wa 'AVG' upande
mmoja katika 'projector' na upande mwingine
katika kompyuta mpakato. Kisha akabonyeza hapa
na pale katika vifaa hivi vilivyokuwa mbele
yake,'projector' na kompyuta vikawaka.Taa katika
chumba hicho zikazimwa nakufanya 'projector'
kufanya kazi yake vizuri zaidi. Kilichokuwa
kikionekana katika kompyuta ile kilionekana katika
ukuta mweupe , mbele walikokuwa wanatazama
maajenti wote wa C.T.I.Taswira mbili zilionekana
ukutani kwa msaada wa 'projector'.Picha za Omar
AL-Mahmood na Abdallah Yusoof zilionekana
vizuri kabisa mbele yao wote.
"Omar Al Mahmood,mrefu wa futi nane,mtaalamu
wa kutengeneza milipuko ya aina mbalimbali
kutoka huko Urusi.Amewahi kufanya kazi katika
idara ya kipelelezi ya KGB enzi za serikali ya ki-
SOVIET. Alikuwa ni 'special agent' na pia 'head of
field operations' ndani ya KGB kabla ya
kubadilishiwa majukumu na kuwa mkufunzi wa
'martial arts' na matumizi ya silaha kwa maajenti
wanafunzi.Aliondoka katika nchi ya Urusi mara tu
baada ya USSR( United States ofSoviet Repablic)
kuvunjika mwanzoni mwa miaka ya 90 kwa kuwa
alikuwa mkereketwa wa sera za ki-soviet.Alirudi
katika asili yake na alikozaliwa nchini
Afghanistani.Alipotea machoni pa wengi kabla ya
baadaye kusemekana kuwa amejiunga na kikundi
cha kigaidi cha Alquaeda.kisha baadaye kuhamia
Somalia kama moja ya viongozi wa ngazi za juu
na waanzilishi wa kikundi cha kigaidi cha
Alshabaab." Aliongea Clara kisha akakohoa kidogo
kuiandaa sauti yake kuanza kutoa maelezo
mengine tena.
Ajent Clara akaanza kubonyeza keyboard ya
kompyuta ile tena.Mara baada ya kubonyeza hapa
na pale,picha ya Omar Al Mahomood
ikapotea,picha nyingine ikajitokeza kwa ukubwa
kama ile picha iliyopita.
"Mtuhumiwa namba mbili, Abdallah Yusoof
Fatawi.Mtaalamu wa teknolojia ya habari na
mawasiliano ama 'ICT' aliyebobea sana na
mtaalam wa mambo yote ya kompyuta
kiujumla.Amekwisha wahi kufanya kazi idala ya
inteligensia ya ISI(Inter Service Intelligegence) ya
huko Pakistani.Alitoroka na kukimbilia India baada
ya kugundulika kuwa anavujisha siri za ki-
intelijensia za Pakistani kwa idara ya kipelelezi ya
nchi ya india 'RAW'.Baada ya kukaa kwa muda
nchini India, Yusoof alihamia Afghanistani na
kulowea huko kwa muda mrefu kabla hajajiunga na
kikundi cha kigaidi cha Alquaeda. Mara utaalamu
na ujuzi wake ulipoonekana kuwa na tija ndani ya
kikundi hicho,alipandishwa na kuwa katika uongozi
wa juu wa Alquaeda. Alikuja kuhamishiwa Somalia
baada ya miaka kadhaa ili kukiongeza nguvu
kikundi cha Alishabaab. Yusoof ni mtaalamu pia
wa mapigano ya mwili kwa mitindo ya
karate,taekwondo na kick-box , mrefu wa futi 7.8
na kati ya waharifu hatari zaidi na asiyewahi
kukamatika duniani".Akamaliza kuongea
Clara,kisha akarudi mahali alipokaa mwanzoni.
Kikao kiliendelea kwa kuongelea na kupanga
mambo mbalimbali kuhusiana na kazi iliyokuwa
inaikabili idara hii nyeti.
"Jambo la muhimu ni kuwatambua hawa walengwa
wetu wakuu kwa sasa.Tufanye jitihada za hali ya
juu kuwatambua mahali walipo ili hatua nyingine
zifuate.twapaswa kutambua kuwa tunaenda
kupambana vita nzito sana na hawa wahalifu wa
kimataifa."aliongea mkurugenzi kisha akaendelea
"Kwa kuhitimisha naomba tujiandae kwa safari ya
kwenda 'safe house' ya Iringa ambako ndiyo
kitakuwa kituo chetu kikuu katika kesi hii.Tukutane
Iringa kesho asubuhi na pia bila kusahau,tumepew
a miezi mitatu tu kukamilisha suala hili.Miezi hii
ikiisha basi tutanyang'anywa hili suala na kisha
litakuwa mikononi mwa Taifa la Marekani.Hii
itakuwa aibu kwetu.Kwa hiyo kabla miezi mitatu
haijaisha angalau tuwe na uelekeo wa kung'amua
wahalifu hawa walipo."Alimaliza kuongea
mkurugenzi na kikao kikaahirishwa.
Baada ya muda mkurugenzi Makassy alikuwa na
kikao na kamanda wa kikosi cha ECS , Kamanda
Joshua. Waliongea wakipanga hili na lile kisha
wakaagana.Kamanda wa ECS(Elite Combat Squad),
akaenda kupangilia askari wake wa weledi kwa ajili
ya safari ya kuhamia Iringa pamoja na kuwaweka
tayari kimapigano wakati watakapohitajika kufanya
hivyo
IRINGA
SAFE HOUSE
Hadi kufikia siku iliyofuata asubuhi, idara yote ilikuwa imehamia Iringa katika moja ya nyumba ambazo inazimiliki Tanzania. Katika mikoa yote iliyo jirani na mikoa iliyo mpakani mwa nchi,C.T.I ilimiliki nyumba moja kama hii. Kwa kuwa mkoa wa Mbeya unapakana na nchi ya Malawi na Zambia, nyumba ilijengwa katika mkoa jirani wa Iringa.
Kiuhalisia si kwamba nyumba ilikuwa mpya. Nyumba ile ilikuwa imefanyiwa ukarabati kutoka kuwa ghala la chakula na kurekebishwa kuwa jumba la kisasa sana.Jumba hili lilikuwa na vyumba kadhaa vya kulala pamoja na ofisi kubwa na ofisi ndogo ndogo pamoja na vitu vingine vingi sana.Hata namna ya kuingia katika nyumba ile haikuwa kazi nyepesi. Kulikuw na vitasa vya kisasa katika nyumba hii ambavyo vilihitaji namba ya siri, alama za vidole pamoja na mtazamo wa mboni ya jicho ili kufungua.Walio weza kuingia ndani ya nyumba hii ni wale wahusika tu. Hawa ndio pekee ambao teknolojia inayohusika kwa sababu za usalama katika nyumba hii ilikuwa imelishwa taarifa zao.
Maajenti wa idara hii ya CTI,walikuwa wamekusanyika katika ofisi kubwa ya pamoja wakifanya hili na lile pamoja na kupanga hiki na kile ili mradi kuweka mambo sawa.Chumba hiki cha ofisi, kilikuwa kimetawaliwa na kompyuta kadhaa zilizounganishwa kwa utaalamu wa hali ya juu huku zikitumia 'soft wares' za kisasa kabisa zinazohusika na kazi hii ya upelelezi. Yaani kwa kifupi kazi ilikuwa inaanza kuoamba moto rasmi wakati huu.
********************************************************
"Clara, hebu jaribu ku-hack mfumo wa kamera za CCTV za jeshi kikosi cha jkt Mafinga uangalie kilichorekodiwa kwa muda wa wiki moja nyuma kabla ya tukio kutokea." Aliongea Mick na kusikika kwa ajenti Clara upande wa pili kupitia kifaa cha mawasiliano alichokivaa sikioni.
"Ok acha nifanye yangu ".Alijibu Clara kutoka upande wa pili na kisha sauti ya vitufe vya kompyuta ikaanza kusikika ikibonyezwa bonyezwa kwa kasi ya ajabu.
Wakati huu ambao wawili hao walikuwa wanawasiliana, Clara alikuwa yupo ofisini wakati Mick yupo msituni,mahali ambapo palitokea tukio siku mbili tatu nyuma.Tukio lililosababisha wanaidara wa C.T.I kujikuta wana jukumu zito la kufanya mara baada ya kuwa na majukumu ya kawaida tu kwa muda mrefu.
Tangu asubuhi,wakati idara yote ya C.T.I ilipokuwa imewasili katika eneo hili, Mick alikwenda mahali pale na kuanza kazi yake eneo la tukio mara moja.Akiwa amekwishapata taarifa za awali za nini kilichojiri,moja kwa moja Mick alijua ni wapi pa kuanzia. Alikumbuka moja ya kauli mbiu ya idara yake iliyosema "katika tukio lolote, ni vizuri na lazima upelelezi uanzie eneo la tukio kwa sababu ndiyo mahali pekee ambapo utapata ushahidi au fununu zitakazokupeleka kwenye ushahidi". Na ni ukweli mtupu unaoongelewa katika kauli mbiu hii.Idara yoyote ya usalama duniani inapofanya upelelezi wa tukio fulani,ni lazima itafika eneo la tukio kwa sababu ya mambo mawili.Ushahidiau fununu au kama mataifa ya magharibi yaliyotufundisha mambo haya wanavyosema kwa lugha yao 'either clue or evidence'.
Kwanza kabisa baada ya kufika eneo la tukio,ajenti Mick alimuhoji mmoja wa askari waliokuwa wanalinda eneo hilo.Wakati alipomuhoji,Mick aliweza kung'amua kuwa magaidi wale walikhwapo muda mrefu,pengine masaa mawili matatu kabla ya msafara kupita na kushambuliwa.Aling'amua kuwa magaidi wale walikuja kwa pamoja eneo hilo na kisha wakatawanyika kila upande nyuma ya misitu ya eneo lile la tukio na ndiyo maana ilikuwa vigumu kupambana nao.Pia alihisi,kwa jinsi eneo lilivyokuwa msituni basi magaidi hawa yawezekana waliletwa eneo lile kwa usafiri fulani mahali pale.Kwa maelezo ya askari aliyehojiwa Mick ,aliweza kung'amua upande ambao inawezekana ndiko magaidi wale walikoikia kabla ya kutawanyika kuzingira eneo lote.
Ndiyo.Ilikuwa ni rahisi kwa Mick kung'amua mambo haya kutokana na maelezo ya askari yule wa weledi wa E.C.S waliokuwa chini ya C.T.I ambaye alikuwa miongoni mwa askari waliokuwa wakilinda eneo lile la tukio ili ushahidi usipotee.Kilichopelekea askari yule kutoa maelezo kwa kina ni kwa kuwa pia alikuwa ni miongoni mwa askari waliosindikiza msafara uke uliovamiwa.Askari yule alimueleza ajenti Mick upande ambao risasi nzito zaidi kutoka kwa adui ziliwashambulia.Na ni upande huo huo ambako upinzani mkubwa ulitokea kuliko upande wowote.Mick aliposikia hayo aliweza kuhisi kuwa yawezekana upande huo ndiko upande ambao adui walikuwa wengi zaidi.Pia yawezekana risasi nzito kwa maelezo ya askari,zilitokea katika bunduki nzito nzito zilizofungwa katika magari ya adui.Basi kwa kusikiliza hayo na kuyachambua kichwani Mick aliuhisi upande huo na kuanza kufuatilia,akitokea barabara ya lami na kuingia msituni.
Mick alipasua msitu na kuukabili hadi kilometa moja na nusu msitu ukipoishia. Wakati huu wote,alikuwa anafuata njia za vumbi ambazo zilitawaliwa na tope katika msimu huu wa mvua Akitumia gari alilokabidhiwa,aina ya Range rover sport nyeusi iliyong'ara sana,Mick alifuatisha barabara ya vumbi iliyokuwa inapita nyuma,upande wa pili wa msitu huu kwa umbali wa kilomita moja tena. Kama ingepigwa picha kutoka juu sana,ama kama ilivyoonekana kwa picha za satelite, barabara hii ilikuwa upande wa pili wa msitu huu wa 'mipaina' ikionekana kwenda ki-msambamba na barabara ya lami.
Kilomita moja mbele ,Mick aliweza kung'amua alama za matairi ya magari zinazoingia msituni.Kilichompa dukuduku zaidi kuwa huenda hicho ndicho alichokuwa ankitafuta,ni kuwa alama zile zilizojichora katika tope zilionesha kuwa magari zaidi ya nane yalipita eneo hili na kuchepuka kuingia msituni.Alama hizi zilinoga zaidi eneo la miti michanga ambapo miti ilikanyagwa sana.Akiwa ameshuka kutoka garini,kwa miguu yake Mick alipasua pori na kuanza kufuatilia matairi hayo huku bastola yake aina ya bereta ikiwa kiunoni na ile ndogo ya 'colt 45' ikiwa imepachikwa katika soksi mguu wa kulia.Kufuatilia huku kulimpeleka hadi mita 300 ndani ya msitu ule,eneo ambalo alama za matairi ya magari yale ziliishia.Hapo Mick aliona kitu ambacho kilimuhakikishia kuwa adui walifikia katika eneo hili na kisha kutawanyika.Eneo lilikuwa limetawaliwa na maganda ya risasi kwa uwingi hasa. Maganda ya risasi kutoka katika bunduki nzito nzito yalikuwa yametawanyika katika eneo hili.Bunduki ambazo aidha zilikuwa zimefungwa kwenye magari au hata kama zilibebwa na magaidi wale basi wasingeweza kutembea nazo kwa umbali mrefu kutoka katika gari kutokana na uzito wake.Hili nalo lilizidi kumthibitishia kuwa hapa ndipo maadui walifikia nakutawanyika kufanya mashambulizi.
Baada ya kujihakikishia kwa hili,Mick alirudi katika gari lake na kuanza kufuatilia alama zile.za magari zilizokatisha msituni na kuishia mahali alikokuta maganda ya risasi mengi,upande zilikotokea kabla yakukatisha porini hapo.
Akiwa anaendesha gari lake huku akifuatilia alama za matairi za magari haya mahali zilikotokea, alama hizi zilimpeleka kilomita nane mbele,mahali ambako barabara hii ilipita nyuma ya kambi la jeshi la kujenga taifa.Kambi ya Mafinga.
Hapa Mick aliona alama za matairi zikiwa zimechepuka kidogo na kisha mbele kurudi usawa wa mwanzo.Alama hii ilikuwa ni ya matairi ya gari dogo.Mick alipaki gari pembeni, akashuka na kuchuchumaa kuangalia kwa umakini alama zile huku akionekana kutafakari jambo.
"Hapa yalipita magari madogo mawili na makubwa au labda malori sita.Kati ya haya magari makubwa kulikuwa na magari aina ya TATA mawili, IVECO mawili na ISUZU mawili.Hapa alama za matairi zinazoonekana kwenda pembeni kidogo nakisha kurudi usawa wa mwanzo na kutengeneza 'curve', kuna gari moja kati ya magari makubwa lilipaki kando na kisha kuendelea na safari,labda kuna jambo wahusika walifanya nje ya gari."Aliwaza ajenti Mick ndani ya kichwa chake.Kisha akageuka nyuma na kuona ukuta wa fensi upande wa nyuma wa kambi hilo ulivyo mrefu.Kisha baada ya ukuta huo kwa ndani kulikuwa na msitu wa miti mingi aina ya milingoti na miti ya matunda mingi. Majengo hayakuonekana labda utumie kiona mbali kutokana na msitu ulivyoshona mahali hapo,hivyo Mick akatambua kuwa si rahisi kwa walio ndani kujua nini kinaendelea nje.Lakini alipokaza macho vizuri, aliona kamera za CCTV zilizofungwa kwa juu katika jengo hilo ambapo kama si utaalamu na uzoefu wa kazi yake pengine asingeziona.
Na hapo ndipo alipowasiliana na ajenti Clara ili amsaidie kwa utundu wa kompyuta kuingilia mfumo wa kamera hizi na ikiwezekana kuibia mambo yaliyorekodiwa nyakati za tukio lile lilipotokea.
Mara baada ya kuwasiliana na ajenti Clara,Mick alirudi katika gari lake na kuendelea kufuatilia alama za matairi alizokuwa anazifuatilia tangu mwanzo.Alifuatilia zilikotokea kabla ya eneo hili alikotoka.Mbelealimaliza eneo la usawa wa jeshi.Mbele kidogo ya hapo alikutana na magari yanayobeba mbao yakitokea katika upande mmoja wa barabara hii ya tope na kwenda porini kwa kufuata barabara nyingine.Hii barabara iliyofuatwa na malori haya na ile inayotoka nyuma ya jeshi zimeunganishwa kwa barabara moja huko zilikotokea.Kwa sababu hiyo ikawa siyo rahisi kwa Mick kuweza kuendelea kung'amua alama zile za matairi alizokuwa anazifuatilia kwani zilichanganyika na alama za matairi za malori yale naa pengine zilifutwa kabisa na kubaki alama za malori yale.
Akiwa amekata tamaa ya kufuatilia kile alichokuwa anakifuatilia,akaona si vibaya akiuliza kitu kutoka kwa bwana mmoja aliyekuwa akibadilisha tairi katika roli lake lililokuwa tupu.Bwana huyu alionekana kama ndiye dereva wa gari lile na kwa upande ambao gari lake lilitazama,ilionekana kuwa ndiyo anaenda kufuata mzigo wa mbao.
"Samahani braza".Mick alianzisha mazungumzo na dreva yule ambaye ndiyo kwanza alikuwa amegundua kuwa kuna mtu nyuma yake.
"Bila samahani kaka sijui nikusaidie nini".Alijibu kwa staha dreva yule hasa kutokana na unadhifu wa huyu mgeni wa ghafla(Mick).Ama kwa hakika jinsi dreva huyu alivyoongea kwa adabu ungeweza kudhani kuwa madreva wa malori ni watu wa staarabu sana.Lakini kumbe...........
"Hivi ni kwa nini mnapita njia ndefu na malori yenu. Mbona kuna njia fupi hii inayopita nyuma ya jeshi au wajeda wanamaindi nini.?" Alihoji Mick.
Yule dreva aliyeulizwa swali hili akamuangalia Mick usoni kwa sekunde kadhaa kwa kukereka kisha akafungua mdomo wake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment