Search This Blog

Thursday 23 March 2023

CABO' DELGADO - 3

  

Simulizi : Cabo' Delgado


Sehemu Ya : Tatu (3)


Kachero Manu akawa anachuchumia kwa ncha ya vidole vyake ya viatu vyake vyepesi alivyovaa. Kama umeme Kachero Manu akarushwa nje ya gari na kudakwa juu juu na askari waliobakia nje ya gari. Wakaanza kumgombania kama mpira wa kona, huku askari mmoja wapo akienda kumshusha dereva Masebbo chini ya gari. Wakaanza kumgombeza Mzee Masebbo kwa kuwapa taarifa za uwongo kuwa hajambeba Mtanzania kwenye gari lake.
Mzee Masebbo katika kujiokoa roho yake akajitetea kwa kumkana kuwa hamfahamu Kachero Manu, na sio jukumu lake kukagua abiria ila ni jukumu la Taniboi. Baada ya majadiliano mafupi baina yao wakamruhusu Mzee Masebbo aondoke zake pale na wamuache Kachero Manu wamchezeshe kindumbwendumbwe. Wakati Mzee Masebbo anataka kuondoka eneo lile wakagonganisha macho kati yake na Kachero Manu, kana kwamba kuna ishara alipewa Mzee Masebbo na Kachero Manu.
Askari wale wakamkwida Kachero Manu na kutokomea nae porini kidogo, nje ya barabara. Siku zote mdharau mwiba, guu huota tende, dharau zao kwa Kachero Manu ziliwaponza wale Askari. Walipomsachi na kumuona hana kitu chochote, wakajua ni mtu wa kawaida tu mwenye nia na madhumuni ya kwenda Msumbiji kiholela.
Askari wawili tu ndio wakabakia kutaka kumuadabisha Kachero Manu huku wengine wakibakia kutega pale barabarani. "Leo takuwa chakula cha simba wewe...!" alifoka mmoja wapo kwa kiswahili kibovu. Alikuwa tayari ameshachomoa bastola yake ipo hewani hewani tayari kwa kuifyatua, wakiwa sasa wameshazama kwenye kimsitu chepesi.
Askari mwingine alionekana yupo kama hayupo anayumba kama vile kazidiwa na kileo. Kachero Manu alikuwa anaongoza mbele amenyoosha mikono juu kuomba amani huku wale askari wanamfuata kwa nyuma. Kadri walivyokuwa wanaelekea kichakani ndipo harufu kali kama ya maiti zilizoharibika ilikuwa inafika katika pua za Kachero Manu ikitokea kule machakani wanakoelekea.
Akaanza kupatwa na kihoro kuwa huenda anapelekwa kuuliwa kwenye chimbo lao maalumu la mauaji. Akajiongeza kichwani mwake kuwa hana budi kuzichanga vyema karata zake za kujiokoa. Alitanabahi akili mwake kuwa anatakiwa apate nafasi moja tu ya wale maadui kufanya makosa halafu yeye aitumie vizuri kujiokoa. Kachero Manu alijua hana muda wa kupoteza, begi lake na kila kitu chake kilikuwa kwenye Lori la Mzee Masebbo hivyo alitakiwa afanye juhudi kuliwahi njiani.


Bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi, yule Askari mlevi ambaye alikuwa ameikamatia tochi akaliparamia jiwe na kujikuta anakula mwereka kwa kuserereka mpaka chini kwa kishindo kikubwa. Bila kufanya ajizi, kosa moja goli moja, Kachero Manu akajipindua hewani kinyumenyume na moja kwa moja teke lake lenye nguvu la mguu wa kushoto likaenda kutua kwenye mkono wa Askari mwenye kushikilia bastola, mpaka ikamponyoka kiganjani. Akiwa bado amepigwa na butwaa hajui kinachoendelea Kachero Manu akaiwahi ile bastola na kuwafyatulia risasi mbili za haraka haraka na kuwaua pale pale.
Risasi zile mbili mlio wake uliiwashtua wale Askari wengine waliobakia barabarani na kuwafanya waje wanguwangu bila kuchukua tahadhari ya kutosha. Walitaka kujihakikishia kama wenzao wapo salama. Kachero Manu bila kufanya ajizi tena kwa mara ya pili akawa anawatungua akiwa amebana pembezoni ya kichaka mmoja baada ya mwingine kama nyumbu vile mpaka akawamaliza.
Na kwa bahati risasi zikawa zimeishia zake, akairushia porini bastola hiyo. Akajipa muda wa matazamio kama wa dakika 5 anapima upepo, baada ya kuona hali ni shwari hamna shari wala rabsha zozote, akachomoka zake toka porini. Akaiokota ile tochi ikawa msaada kwake anaitumia kusogea mbele kidogo kule porini alikokuwa anapelekwa. baada ya mwendo wa kama dakika 5 akakutana na maiti zilizoharibika zinazotoa harufu mbaya zimetapakaa ovyo.
Alivyozidi kuchunguza akaona wawili kati yao pembeni yao kuna hati ya kusafiria ya nchi ya Tanzania, ikiwa imelowanishwa na maji ya mvua. Akamshukuru Mungu wake kwa kumuokoa kutoka kwenye bonde la mauti alilokuwa anapelekwa kuuliwa muda mfupi uliopita. Hima hima akashika uelekeo wa kutoka kule bondeni akawa anaelekea barabarani anafuata uelekeo wa Lori la Mzee Masebbo.
Alipotupa jicho lake kwenye mishale ya saa yake ilikuwa inaonyesha kuwa zimepita takribani dakika kama 22 tokea lile Lori limtelekeze pale porini. Hapo ndipo alipoona faida ya mazoezi ya mbio anayoyafanya kila siku. Akaamua aanze kufyatuka nduki kwa kasi kubwa. Alikuwa na uwezo wa kutimua mbio kwa spidi ya dakika 4 kwa kila kilometa 1.
Hakujali hofu ya wanyama wakali katika giza lile totoro la porini usiku ule, hamu na shauku yake ilikuwa ni kuliwahi Lori lile kabla halijamuacha njiani.
Alifahamu akikosa usafiri ule ndio amekwisha habari yake hamna tena usafiri mwingine. Na kama alikamatwa kwa kuhusishwa na vifo vya wale Askari 6 aliowateketeza porini kwa mtutu wa bunduki hatosalimika tena, watamshukia kama mwewe anavyokishukia kifaranga cha kuku.

Kachero Manu baada ya kutoka nduki kwa zaidi ya dakika 45 bila kupumzika tena akiwa ameshakimbia kwa zaidi ya kilometa 17 kwa mbali sana alipotupa macho akaona kitu kama taa nyekundu zinawaka mbele yake. Alikuwa anatweta kwa uchovu kama swala anayemkimbia simba mkali mwenye uchu wa kutaka kumshambulia.
Akashusha pumzi na kuanza kujipa matumaini huenda hilo ni gari la Mzee Masebbo hivyo azidi kuongeza kasi alifikie kabla halijang'oa nanga. Akashukuru kwa jinsi Mzee Masebbo alivyokuwa makini kuzisoma ishara alizompa kuwa amsubirie mbele pale alivyokamatwa na Askari pale kizuizini.
Baada ya mbio za kama dakika 10 zaidi, akawa ameshalifikia lile gari. Abiria wote watoto wa madrasa na Maustadhi wao walikuwa ndani ya gari wanakoroma kwa usingizi wa uchovu. Mzee Masebbo na taniboi wake wapo chini ya gari wanalikorokochoa gari likae sawa safari iweze kuendelea.
"Uuukh.....Uuukh.......Uffff......Uffff... Afadhali nimewakuteni, maana nisingewapata sijui ningekuwa mgeni wa nani...! " alisema Kachero Manu kwa uchovu huku mikono yake imekamatia kiuno, jasho jekejeke linamchuruzika mwilini mithili ya mchoma mikate kwenye tanuri la kuni.
Moyoni Kachero Manu alijisifu kwa maamuzi yake ya kuvaa viatu vyepesi vilivyomrahisishia mbio zake ndefu alizozikata mbuga.
"Ooh.....pole sana una bahati sana, tungeshakuacha ila gari imepata hitilafu katika mfumo wa breki ndio narekebisha hapa tuondoke, Chikulubu wewe lete grisi, acha kulala muda unayoyoma...!" aliongea Mzee Masebbo kumjibu Kachero Manu kisha akaanza kumpigia makelele Taniboi wake achangamkie kazi.
Yule Taniboi alikuwa hataki hata kumuangalia Kachero Manu usoni baada ya kuona unaa wake kwa wale Askari umefeli. Kachero Manu akampuuza tu akadandia ndani ya Lori, na kuwakuta watoto wale wamelewa usingizi wa fofofo hawajitambui.
Kachero akaenda moja kwa moja mpaka kwenye begi lake na kuanza kulifanyia speksheni ya usalama wa vitu vyake alivyoviacha. Akajikuta anafyonya peke yake kwa hasira baada ya kugundua kuwa begi lake limepekuliwa. Akili yake ikamtuma kuwa hamna mshenzi mwingine yoyote mwenye kiherehere cha kumchunguza zaidi ya huyu Taniboi kijana Chikulubu.
Akazigusa silaha zake kwenye mfuko wa ndani kwa ndani alipozihifadhi, akazikuta zipo salama. Kama angezikuta zimechokonolewa, pasingetosha lazima angemtia adabu huyo kijana. Kabla hata hajatulia vizuri akamuona Mzee Masebbo ameshapanda ndani ya gari na kuliwasha akiwa bado amevalia bwelasuti yake ya gereji zikiwa zimechakazwa kwa uchafu wa grisi na mafuta machafu.
Gari likaanza kuondoka huku sasa Chikulubu akiwa ameamua kukaa mbele na dereva wake. Kachero Manu akatanbahi kuwa hizo ni dalili za kumkwepa kwa kuona aibu kutokana na kitendo chake cha kumchomea utambi mbele ya wale Askari.
Barabara ilikuwa na utelezi uliotokana na mvua iliyokuwa imenyesha hivyo Mzee Masebbo alikuwa anatembea kwa tahadhari kubwa asije kuwabwaga barabarani yakaibuka majanga mapya. Kachero Manu hakuchukua raundi kutokana na uchovu wake akajikuta analala usingizi mzito wa pono.
Ni Mwenyezi Mungu pekee ndio ambaye hakumshiki kusinzia wala kulala, lakini binadamu wote hata uwe komandoo au Amiri Mkuu wa Majeshi yote lazima utafika wakati ambao mwili utahitaji mapumziko ili kuhuisha nishati mpya.
Walifanikiwa kufika salama safari yao saa 11:30 ya alfajiri, walishushwa nje ya jengo la Madrasa ambapo pembezoni kuna msikiti mdogo. Watoto wa madrasa wakaanza kuhangaika kushusha mizigo yao pamoja na ngoma zao za dufu walizokuwa wanazipiga kule Maulidini.
Baada ya mizigo kushushwa Mzee Masebbo alionekana ana haraka sana hana tena muda wa kupoteza eneo lile huku yule kijana wake Chikulubu akiwa haonekani eneo lile.
Kachero Manu hakuwa tena na pupa ya kuongea na Mzee Masebbo, aliona mustahabu zaidi kwenda kuonana nae Mzee Masebbo nyumbani kwake kama walivyopeana miadi. Walipowasili tu sauti ya adhana "Allahu Akbar Allahu Akbar..." ya wito wa swala ya alfajri ulikuwa unatolewa kwenye kipaza sauti cha msikitini.
Wito ulikuwa unawatangazia Waislamu wake kwa waume kuwa wakati wa kuitekeleza ibada ya swala ya alfajiri umewadia Hivyo wanatakiwa waviachie vitanda vyao kwa ajili ya kujiandaa na swala.
Mtoa adhana bila kusahau, akaweka na vikorombwezo vya kuwafanya waumini hao waingiwe na woga waamke kwa haraka, akaanza kuongea kwenye kipaza sauti "Eeeh...Muislamu wewe kitanda chako hicho ndio jeneza lako, shuka hiyo uliyojifunika ndio sanda yako, Swali leo Baba, swali leo Mama, swali leo Kaka, swali leo Dada, kesho kesho kila siku kesho kiama".
Yalikuwa ni maneno ya kuogofya ambayo mtu mwenye roho ngumu tu ndio ataendelea kuuchapa usingizi, lakini mtu swalihina lazima anayanyuke kuswali hata kama amezidiwa na usingizi.
Kachero Manu nae haraka haraka akajiunga na kundi la waumini wachache waliokuwa wanatia udhu kwenye mabomba ya maji nje ya msikiti kujiandaa na sala hiyo ya asubuhi. Alikuwa mjanja anatia udhu taratibu sana huku anapiga jicho upembe anaigizia namna waumini wa kweli wanavyoosha mikono yao, nyuso zao, vichwa vyao na kumalizia miguu yao.
Hakutaka kujitia kimbelembele halafu ashtukiwe hajui kutia udhu wakati amevalia kiislamu na kuwatia ndimu kuwa yeye ni Mzanzibari. Waislamu wa Msumbiji ukiwaambia unatoka Zanzibari wanakuheshimu kama kile unatokea Mji wa Maka alipozaliwa Kiongozi wa waislamu duniani Mtume Muhammad (S. A. W).
Hivyo ingekuwa ni kituko cha karne kwao uwe Mzanzibari halafu hujui jambo dogo katika dini ya Uislamu kama kutia udhu. Wakati anamalizia udhu wake, akasikia mnadi wa sala anasoma maneno ya kiarabu ya ikama kuashiria sala inataka kuanza, hivyo waumini hao wajipange safu safu tayari kwa swala kuanza.
Imamu aliposimama na kuelekea kibla kwa ajili ya kuanza kuswalisha na kutamka maneno ya "Allahu Akbar" kisha akafunga swala na kuanza kusoma sura ya ufunguzi wa swala, ikiwa ndio sura ya kwanza kwenye Kurani, kitabu kitakatifu kwa waislamu.
Kachero Manu hakutaka kuremba, alichofanya ni kutoka nje ya mlango mdogo wa nyuma ya msikiti na bila kusitasita akavaa viatu vyake vilaini vya "Kung-Fu" vilivyokuwa vimechafuka vumbi haswa kutokana na mbio zake ndefu alizozitimua.
Kisha akatokomea mtaani, akawa anatembea mashimashi huku anaelekea sehemu asiyoifahamu ikiwa ni saa 11:40 za alfajiri alipoiangalia saa yake ya mkononi. Ilikuwa ni asubuhi ya tarehe 15/02/2016 ndani ya viunga vya Cabo-Delgado ameshawasili, tayari kwa mapambano.
Akamshukuru Mungu kwa kumfikisha salama katika uwanja wa mapambano. Akajikuta anaropoka tu kimoyomoyo "Hapa kazi tu...!" kwa lengo la kujishajiisha na kujipa morali ya mapambano na mahasimu zake anaotarajia kuonana nao.


SURA YA SITA
Mafioso wa Biashara haramu ya madini hadharani
"Alfredo Afonsio Alexis" ni jina ambalo kwanza ukitaka kulitamka kwa ufasaha zaidi inabidi upitie masomo ya ziada ya lugha ya Kihispaniola, vinginevyo ujiandae kupata ajali ya ulimi wakati wa matamshi.
Alikuwa ni chotara, mchanganyiko wa Kireno na Kimakonde, kijana mwenye kukimbilia kwenye rika la utu uzima. Ulikuwa kama ukibahatika kuonana nae mubashara unaweza kumkadiria umri takribani wa miaka 55 na fauka ya hapo, lakini utakuwa umemkosea sana.
Umri wake halisi ulikuwa hauzidi miaka 48. Ila kutokana na mwili wake mkubwa, wa nyama uzembe, ukijumlisha na pesa sufufu anazomiliki wengi walikuwa wanajua ni mtu shaibu kiumri. Tabia yetu Waafrika mtu akimiliki uchumi wa kutosha hata kama ni mdogo kiumri tunamzeesha hapo hapo kwa majina kama Mzee, Mshua, Bosi Kubwa na mengineyo kedekede ya kumpamba.
Baba yake mzazi, Mzee "Afonsio" alikuwa ndio mmiliki wa kampuni kubwa ya ukoo inayoitwa "Monte Branco Ltd" iliyoanzishwa tokea 1885 ikijishughulisha na biashara ya kununua na kusafirisha korosho na mihogo mikavu nje ya Msumbiji tokea enzi hizo za mkoloni.
Biashara ambayo ilimuingizia pesa sufufu kuliko matajiri wengi wa Msumbiji wa wakati huo. Baadae kampuni hiyo ikajitanua ikawa inajishughulisha pia na uvuvi katika bahari kuu na uchimbaji na uuzaji wa vito vya madini. "Alfredo" alizaliwa na pacha mwenzake akiitwa "Negredo" ambaye kwa bahati mbaya sana alifariki akiwa mtoto mchanga kwa ugonjwa wa Nimonia "Pneumonia".
Mama yao ni mmakonde aliajiriwa kama mpishi katika hekalu la Mzee Afonsio ambaye aliwapata mapacha hawa akiwa na umri wa miaka 50 mwaka 1970.
Inasemekana huyo mama wa kimakonde alibakwa na Mzee Afonsio Alexis lakini katika kutaka kuficha aibu ilipogundulikana mpishi wake ni mjamzito akampa ahadi ya kutunza watoto wake ila asivujishe siri yoyote ya tukio hilo.
Alipata kuwa na mke wa Kireno siku za nyuma lakini hawakujaaliwa kupata mtoto, na mkewe huyo alifariki wakati wa mapambano ya vita vya ukombozi mwaka 1966, alipigwa risasi kwa bahati mbaya na wapiganaji wa FRELIMO akiwa dukani kwake Jijini Maputo.
Siku ya mazishi ya mkewe, Mzee Afonsio aliweka nadhiri hadharani mbele ya sahibu zake ya kulipiza kisasi kwa damu iliyomwagwa ya mkewe kupitia kwenye kizazi chake kwa serikali ya FRELIMO kama itafanikiwa kuchukua madaraka ya nchi.
Inasemekana Mzee Afonsio ndio alikuwa mmoja wa wafadhili wakubwa wa kikundi pinzani za FRELIMO cha RENAMO. Hii yote ni katika harakati zake za kuwaadabisha FRELIMO kwa kusababisha kifo cha mkewe.
RENAMO ni ufupisho wa maneno yafuatayo ya lugha ya Kireno, (Resistência Nacional Moçambicano ), kikianzishwa 1975 kwa ufadhili wa matajiri wa Kireno, Rhodesia (Zimbabwe) na Afrika ya kusini mara tu baada ya Msumbiji kupata uhuru wake.
Malengo ya kuanzishwa kwa RENAMO yakiwa ni kuhujumu maendeleo ya Msumbiji, na pia kuzuia serikali ya Msumbiji kutoa misaada kwa wapigania uhuru wa Rhodesia na Afrika ya Kusini.
Hujuma zote ndani ya Msumbiji zilizokuwa zinafanywa na chama cha RENAMO za kulipua mashule, mahospitali, na kuharibu miundo mbinu ya reli na barabara zilikuwa zinafadhiliwa na Mzee Afonsio na genge lake.
Pia inasemekana kifo cha Samora Machel Rais wa kwanza wa Msumbiji mwaka 1986 kina mkono wa Mzee Afonsio na genge lake.
Jumba bovu la tuhuma linamuangukia yeye kwa sababu miezi miwili kabla ya kifo cha Rais Samora Machel inasemekana Mzee Afonsio alijichimbia zake nchini Malawi na Mafioso wenzake kwa ajili ya kupanga na kupangua mikakati mizito ya kuiangamiza FRELIMO na Rais Samora Machel.
Ilipotimu mwezi mmoja kabla ya kifo cha Samora Machel, viongozi wa Zimbabwe, Zambia na Msumbiji, Bwana Robert Mugabe, Keneth Kaunda na Samora mwenyewe walikwenda Malawi kwa Rais Kamuzu Banda kumtaka aache kufadhili kikundi cha uasi cha RENAMO.
Kwa hasira Rais Kamuzu Banda aliwajibu "hakuna Rais wa nchi asiyekufa". Wadadisi wa mambo wanajenga hoja kuwa jeuri ya Rais Banda kutabiri kifo cha Samora dhahiri shahiri tena mbele ya vigogo wazito ilitokana na mikakati mizito iliyowekwa na akina Afonsio.
Moja ya mikakati yao ilikuwa ni kufunga kifaa chenye nguvu ya kuingilia mawasiliano ya ndege "Decoy beacon", hivyo kuipoteza dira ndege aina ya Tupolov 134A ndege ya kirusi iliyokuwa inatumiwa na Rais Samora Machel.
Siku ya tukio la kifo cha Samora tarehe 19/10/1986, siku ambayo ni ya huzuni na majonzi makubwa kwa wazalendo wa bara zima la Afrika. Lakini kwake Mzee Afonsio siku hiyo ilikuwa ni sikukuu kubwa kwa kufanikisha kulipiza kisasi cha kifo cha mkewe aliyeuliwa na wanamgambo wa FRELIMO.
Siku hiyo alisafiri asubuhi na mapema kwenda nchini Afrika ya Kusini kuungana na Mafioso wenzake kusubiria taarifa za kifo kitakachoitikisa Afrika. Rais Samora alisafiri kwenda kwenye mkutano wa nchi za mstari wa mbele katika ukombozi wa bara la Afrika.
Mkutano huo ulikuwa unafanyikia nchini Zambia katika eneo la Mbala, kwa bahati mbaya sana mkutano huo uliisha muda wa saa 12:45 magharibi, giza likiwa linaanza kutamalaki angani.
Kiusalama Rais Samora alishauriwa asisafiri usiku huo na rubani wake wa Kirusi lakini waswahili wanasema siku ya kifo marehemu anakuwa mbishi mbishi sana. Rais Samora akapingana vikali na rubani wake, akamtaka waondoke usiku huo mbichi kwa sababu kesho yake alikuwa na mkutano mwingine muhimu sana.
Rubani yule kwa shingo upande akapeperusha mwewe angani, wakaondoka kwenye ndege moja na msafara wa Maofisa 33 wazito wa Msumbiji. Kutoka kwenye taarifa zilizodukuliwa za jeshi la anga la Afrika ya Kusini (SAAF) zinasema 2:45 usiku, ndege iliyombeba Samora ilikuwa tayari imeshafika mpakani mwa Msumbiji na Afrika ya Kusini.
Kwenye muda wa kati ya saa 3:00 na saa 3:15 usiku ndege hiyo ikalipuliwa katika eneo la Mbuzini, Afrika ya Kusini meta 200 kutoka mpaka wa Msumbiji na Afrika ya Kusini. Mlipuko ambao ulimpelekea jongomeo Rais Samora Machel na Maofisa wake waandamizi serikalini, bila kusaza mtu yoyote.
Mzee Afonsio alizipata taarifa ya kifo cha Samora Machel saa 4:00 usiku baada ya Majasusi wao waaminifu kwenda mpaka eneo la tukio na kujiridhisha kuwa kwa namna ndege ile ilivyolipuliwa ni ngumu kwa Rais Samora kutoka salama kama ilivyokuwa ni vigumu kumpata mwanamke bikira kwenye wodi ya wazazi.
Furaha fokofoko aliyojawa nayo Mzee Afonsio ilikuwa haiwezi kupimika katika mizania ya kawaida ya vipimo vya furaha. Walikesha na Mafioso wenzake wakisheherekea usiku kucha kwenye ufukwe wa bahari wa Clifton kwa kula kunywa na vinywaji anuwai mbalimbali.
Ufukwe huo maridhawa unapatikana ndani ya Jiji la Capetown. Mvinyo wa gharama ya juu kabisa aina ya "Cheval Blanc" unaouzwa zaidi ya Sh. milioni 300 pesa za Kitanzania kwa chupa moja nao ulikuwepo kwenye sherehe hiyo.
Kifo cha Rais Samora Machel kilikuwa ni kipigo kitakatifu cha Mafioso hawa kwa Nchi Huru za Kiafrika. Lengo ni kwamba nchi hizo zijione kuwa bado wao ni dhaifu, hawawezi kupiga hatua mbele katika mambo ya kiuchumi, kilimo, kisiasa, kiutamaduni na mambo mengineyo bila kuwahusisha wao wakoloni.
Baada ya sherehe hiyo, Mzee Afonsio na wenzake wakapanga mipango mipya ya kuandaa mapigo matakatifu zaidi ya kiuchumi ili kuzifanya nchi za Kiafrika zisiweze kujitegemea zenyewe. Ndipo ilipopangwa mipango ya kutekelezwa miaka 30 ijayo kutoka mwaka 1986.
Mipango ya Mzee Afonsio ilikuwa ni kumuachia mamlaka yote ya kampuni ya "Monte Branco Ltd" mwanawe Alfredo. Hivyo akaamua kumuandaa kielimu, hivyo alimpeleka mtoto wake Marekani kusoma elimu bora kuanzia elimu ya sekondari mpaka alivyohitimu chuo kikuu cha "Chicago" moja ya vyuo bora nchini Marekani.
Hakutaka mtoto wake asome Afrika kwenye elimu za kubahatisha. Alisomea Shahada ya Utawala wa Biashara akibobea kwenye sekta ya mafuta na gesi kwa mwongozo wa baba yake kuwa asomee masomo hayo. Tofauti na watoto wa Walalahoi mpaka wanafika hadi Chuo Kikuu hawajui hata wakasomee kitu gani, hawana mtu wa kuwaongoza.
Kwa sababu utakuta baba kazi yake ni ngariba, mama mkulima, mjomba ni dobi, shangazi ni kungwi. Pia inasemekana Alfredo alipikwa akapikika vilivyo katika mafunzo ya ujasusi wa kiuchumi katika kuzitafuta na kuzivumbua fursa mbalimbali zilizomo barani Afrika.
Mwaka 1993 akiwa na umri wa ujana mbichi wa miaka 20 tu, Alfredo akakabidhiwa mikoba rasmi ya madaraka yote ya kampuni. Wakati watoto wa kiswahili miaka 20 bado ni mtoto wa kimawazo, ni kiongozi tu wa makundi ya mitandao ya kijamii kama Facebook, Whatsapp na mingineyo.
Mzee Afonsio kwa kujiamini kabisa, akamrithisha mikoba ya kuiendesha kampuni mtoto wake kisha akarejea kwao Ureno kwenda kumalizia uhai wake. Huku akiyakinisha kuwa ameacha Msumbiji mtoto, ambaye ni Kirusi kibaya kwenye mambo ya ufisadi wa kiuchumi zaidi ya Kirusi cha Corona kinachowatesa Wachina.
Mtoto ambaye atakayekuja kumiliki njia kuu za uchumi za Msumbiji hasa katika sekta ya mafuta, gesi na madini. Haraka haraka kwa kutumia mbinu za kijasusi alizojifunza nchini Marekani.
Ndani ya miaka 2 tu ya uongozi wake wa kampuni, Alfredo alitengeneza mchanganuo wa kujua kiasi cha utajiri wa madini, gesi na mafuta kilichopo nchini Msumbiji na nchi za jirani na Msumbiji.
Kisha akatengeneza mtandao uliokita mizizi yake kuanzia serikalini, vyombo vya dola na mahakama mpaka bungeni ili kuhakikisha zabuni kubwa kubwa zote za serikali lazima zipitie kwenye mgongo wake.
Akafanikiwa kutengeneza mtandao na makampuni makubwa duniani ambayo yakawa yanamtumia kama kibaraka wao kutafuta fursa mbalimbali za kiuchumi kusini mwa janga la Afrika kisha kupanga mipango ya kimafia namna watakavyonufaika na hizo fursa kwa kupewa kamisheni yake nono kama nundu la ng'ombe.
Sasa taarifa za kiintelijinsia za kampuni ya Alfredo zilionyesha tishio la Wafanyabiashara wa kutoka Tanzania namna wanavyohamia Cabo-Delgado kwa kasi na kushika njia kuu za kiuchumi katika nyanja za biashara ya madini, vituo vya mafuta na biashara ya vyakula.
Kibaya zaidi taarifa zilieleza asilimia tisini (90%) ya wazawa Cabo-Delgado hawana elimu ya kutosheleza katika kukabiliana na ushindani wa soko la utandawazi hivyo ujanja ujanja wa raia wa Tanzania ulimtisha sana Alfredo.
Hivyo akaandaa mikakati kwa kutumia viongozi wa dola la Msumbiji ambao wapo mfukoni mwake waandaae mipango ya kuwavuruga, kuwatisha na kuwafyekelea mbali Wafanyabiashara wa Kitanzania ili waogope kuwekeza nchini Msumbiji.
Ili kuendelea kuacha mirija ya uchumi chini ya kibaraka Alfredo na mabwana zake wa nchi za ng'ambo. Hivyo kudhoofisha ndoto za waasisi wa Msumbiji za kuhakikisha kunakuwa na Msumbiji huru kiutawala na kiuchumi.

Inspekta "Mark Noble" ni wakala wa Alfredo toka jeshi la polisi
"Mark Noble" akiwa kama Afisa Mkuu wa Jeshi la Polisi katika Jimbo la Cabo-Delgado alikuwa ndio mkono wa kuume wa Alfredo katika utekelezaji wa operesheni mbalimbali haramu.
Hata ule mkutano wake wa kujadili machafuko ya Cabo-Delgado na kigogo mwenzake, Inspekta Jenerali wa upande wa Tanzania alikuwa analeta unafiki tu. Anajifanya hapendezwi maswahibu wanayowasokota Watanzania waishio Cabo-Delgado kumbe yeye ndio mratibu mkuu wa vitendo hivyo haramu.
Akiwa kijana mdogo wa makamo mwenye ubongo unaochaji haswa utasema utotoni amelishwa vichwa vya samaki. Alipanda vyeo haraka haraka kama umeme kutokana na elimu yake, nidhamu na kujituma kwake katika kazi.
Alikuwa ndio kwanza amehamishiwa kikazi akitokea Wilaya ya Montepuez. Waswahili wanasema ujana ni kaburi la tamaa zote, unazozijua wewe duniani.
Ukiwa kijana damu inachemka ndio unatamani kila msichana mrembo awe wako wewe, kila gari zuri la fasheni mpya lililoingia katika Mji ulimiliki wewe na hawaa kedekede za nafsi zenye kutamanisha katika starehe za duniani.
Mark Noble alikuta vijana wenzake wadogo tu Jimboni Cabo-Delgado wanamiliki biashara kubwa kubwa za madini. Walikuwa wanaishi kifahari na wanamiliki mali za gharama kubwa.
Alfredo mmiliki wa "Monte Branco Ltd" akamsoma pupa yake ya utajiri wa njia za mkato, akapenyeza rupia kwa kwenye udhia kwa Afisa Mkuu wa polisi huyo Mark Noble. Chambo alichorushiwa Mark Noble kikafanikiwa kumuingiza kwenye ndoano mzimamzima na kumnasa kooni vilivyo.
Wakamkalisha kitako chini wakimsomesha madhumuni yao "Monte Branco Ltd" namna wanavyotaka kuliteka soko la biashara ya madini, mafuta na gesi. Akakubali kuwa mmoja wa washirika wao katika kutekeleza mikakati yao haramu. Wakafanikiwa kutengeneza mfumo wa siri ndani ya mfumo rasmi wa serikali.
Mfumo ambao ulikusanya vibaraka wao, waliokosa soni na uzalendo wa nchi yao kuanzia kwenye Mabenki, Polisi, Mahakama, Hospitali, Vyombo vya habari na sekta zote muhimu unazozijua wewe wakahakikisha wanaweka mtu wao wa kuyatelezesha mambo yao kiulaini bila kikwazo.
Ndani ya muda mfupi tu Inspekta Jenerali Mark Noble akaanza kumiliki mali za kifahari karibia kwenye Wilaya zote za Cabo-Delgado. Kutimiza msemo kuwa ukila na kipofu usimshike mkono asije kukushtukia kuwa unampunja, basi mali nyingi za Mark Noble ziliandikishwa kwa majina ya ndugu na marafiki kukwepa mkono mrefu wa sheria siku za usoni usije ukamkamata.
Ndio ikawadia hii operesheni ya kuwafagia Watanzania wote wanaomiliki biashara za madini. Inspekta Jenerali Mark Noble akapewa jukumu hilo zito la utekelezaji wa kuwafurusha na Bwana Alfredo. Mark Noble akaliendesha zoezi hilo kwa umakini na ufanisi mkubwa sana tena bila chembe ya huruma.
Aliwachakaza kichapo kizito cha mbwa koko Watanzania walioingia kwenye rada zake. Wakubwa zake akina Alfredo walifurahishwa na utendaji wake wa kazi ikawa huwambii chochote juu yake wakuelewe, na hawafanyi kitu chochote bila kumshirikisha Mark Noble.
Huku wakimpa ahadi ya kumpigia chapuo kwa wakuu zake wa kazi apandishwe Cheo na kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi 'IGP' wa nchi ya Msumbiji. Mark Noble akaota mapembe, mgema ukimsifia tembo hulitia maji, ikafika hatua analeta ushawishi serikalini wa kuupanua mpaka wa nchi ya Msumbiji uishie mkoani Mtwara, Tanzania.
Huku vijana wake wa kazi akiwatuma mpaka ndani ya mipaka ya Tanzania kufanya uhalifu wanavyojisikia wao. Vijana wa Inspekta Jenerali Mark Noble ndio waliofanya mauaji ya Profesa na mwanafunzi wake kijana Alex katika Hoteli ya 'New Star Hotel'.
Kama hiyo haitoshi vijana wa Inspekta Mark Noble ndio hao hao waliovuka mpaka kinyemela na kwenda mpaka kijijini Mahiwa Mkoani Lindi kwenda kumkata kichwa kikatili mama mzazi wa Kachero Manu.
Lakini kitendo cha Kachero Manu kuwaswaga bila huruma, Askari 6, vijana wa Mark Noble kule barabarani kuliibua mshtuko wa mwaka. Kwa mara ya kwanza tokea ajiunge na jeshi la polisi Inspekta Jenerali Mark Noble alikoseshwa usingizi.
Alipewa penyenye za uhakika kuwa Kachero Manu ni mtu wa hatari sana, mwenye uwezo wa akili wa zaidi ya makomandoo 10. Alishatambua uzembe wa aina yoyote ile utamsababishia kitumbua chake kuingia mchanga na hata kupoteza mali zake na uhai wake.
Alishatambua kuwa Kachero Manu tayari kashatua nchini Msumbiji kwa njia ya barabara, tofauti na matarajio yao kuwa atatua kwa njia ya anga.
Machale ya Kachero Manu kutumia usafiri wa nchi kavu yalimbeba sana vinginevyo angetiwa mikononi na maadui zake hata kabla hajaikanyaga ardhi ya nchi ya Msumbiji.
"Huyu mtu ni hatari sana, kama amefanikiwa kutupiga chenga ya mwili na kufanikiwa kutuvamia nyumbani kwetu basi na sisi tumpe somo takatifu, lakini kabla hamjamuua, akamatwe akiwa hai, Wakubwa wanataka waonane nae...!" yalikuwa ni maigizo ya wazi ya Inspekta Mark Noble kwenda kwa Makamanda wake walioteuliwa kuendesha operesheni ya kumdhibiti Kachero Manu.
Sasa rasmi msako wa Kachero Manu ukawa ni operesheni ya kufa au kupona iliyozinduliwa.


SURA YA SABA
Kachero Manu anasakwa na mabaradhuli kwa udi na uvumba
Kachero Manu baada ya kufanikiwa kuondoka pale msikitini wakati wa sala ya alfajiri bila kuonekana na mtu, sasa alikuwa anakata mitaa bila wasiwasi utasema ni mzawa wa Cabo-Delgado na kibegi chake.
Alitembea katika mtaa ule ule wa msikiti mpaka karibu kufikia nyumba ya nane kutoka pale msikitini, huku kukiwa na giza giza kwa mbali akatoa miwani yake maalumu yenye uwezo wa kukuza vitu na pia kupiga picha kisha akaivaa.
Akapinda kulia kwake, kulikuwa na ushoroba mwembamba ambao unaenda kutokeza kwenye kituo cha madereva taksi. Akatembea mpaka akawa amewasili kituoni hapo. Kwa muda ule wa saa 11:50 za asubuhi zilionekana zimebaki taksi chache zisizozidi 6, huku ikionekana wengi wameenda kujipumzisha maskamoni mwao baada ya pilikapilika za usiku kucha.
Akaifuata teksi ya mwanzo mwanzo na uelekeo wake, cha kwanza alichokumbuka ni kukariri namba za taksi hiyo kichwani mwake kwa tahadhari tu kisha akasogelea mpaka usawa wa mlango wa dereva ambao kioo chake kilikuwa kimeshushwa nusu.
Akaugonga mara tatu, bila kuitikiwa na mtu. Alipogonga mara ya nne tu, dereva akakurupuka toka kwenye usingizini mzito. "Samahani sana, nina uchovu mwingi, Karibu mteja wangu, nikupeleke wapi..?", alisema dereva kwa sauti yenye viashiria vya uchovu wa usingizi.
"Usijali naelewa, nipeleke nyumba ya kulala wageni tulivu lakini ipo katikati ya Mji", alisema Kachero Manu huku akilinyanyua begi lake tayari kujiandaa kuingia nalo ndani ya gari, kisha akafungua mlango mlango wa nyuma ya dereva akaingia.
"Nitakupeleka nZuwa Lodge, ni sehemu tulivu na ni ya kisasa...!", kisha baada ya dereva kusema hivyo akatia gari moto na kuanza kuondoka kwa mwendo wa wastani.
Kwa taaluma yake ya upelelezi, Kachero Manu alikisoma kitu toka kwa dereva yule, alikuwa anamuangalia kwa wasiwasi kwa jicho la kuibia kwa kutumia kioo chake cha juu kinachompa uwezo wa kuona nyuma ya gari kinachoendelea.
Kachero Manu hakujali, baada ya kama umbali wa kutembea robo saa wakawa wameshafika kwenye nyumba hiyo ya wageni. "Kiasi gani cha pesa unanidai?" aliuliza akiwa bado hajashuka nje ya gari. "Mpaka hapa gharama ni mitikashi 100" alisema yule dereva kwa kujiamini.
Mitikashi ni aina ya pesa zinazotumika nchini Msumbiji, kama ilivyo Ksh. ya kule nchini Kenya na Tsh. ya nchini kwetu Tanzania. Hilo ni jina lenye asili ya lugha ya kiarabu, "Mithqal" kizio kinachotumika kupimia uzito wa dhahabu na kilikuwa kinatumika sana katika nchi nyingi za Afrika mpaka kwenye karne ya 19 mwanzoni.
Kachero Manu hakutia neno lolote zaidi ya kuchomoa noti toka kwenye pochi lake, akalipa kisha akashuka chini.
Dereva yule akasema huku akiwa tayari anajiandaa kuondoka ameshawasha motakaa yake, "Mzee ukinitaka muda wowote nipigie simu chukua namba yangu ya simu basi..!". "Sina laini ya simu bado sijanunua laini mimi ni mgeni hapa..", akadanganya Kachero Manu.
Maana alivyokuja, alikuwa anayo simu yenye laini aliyopewa ofisini ikiwa na laini ya simu ya mtandao wa "Mcel" aliyopewa na Kokunawa Sekretari wa Bosi wake.
Ili asimkatishe tamaa akamwambia "ila nitajie yako niiandike nitakupigia, nikinunua laini..!". "Natumia "mtandao wa "Mcel" namba zangu ni +258 44526378 nipigie muda wowote nitakupeleka popote unapotaka ndani ya Jimbo hili, nalijua nje ndani...! " alisema dereva teksi.
Kachero Manu akazuga kama anaandika kweli ile namba lakini hakuwa anaandika hakuwa na haja ya kumtumia tena dereva mmoja isije ikawa rahisi maadui zake kumfuatilia.
Baada ya hapo akaagana nae kwa kupungiana nae mkono wa kwaheri. Akachomoa mshikio wa begi lake na kuanza kuliburuta kwa kutumia matairi ya begi lile. Akafika mapokezi na kueleza shida yake ya kupata sehemu ya kulala kwa siku kadhaa.
Akapokelewa kwa bashasha na mhudumu wa mapokezi kisha akaingia kwenye mfumo wa kompyuta iliyopo mezani kwake ili kuangalia chumba kilicho tupu. Akapewa chumba kwenye roshani ya pili, akakilipia na kusindikizwa mpaka chumbani.



Alipoingia akakikagua vizuri na kuridhishwa nacho kisha akamwambia mhudumu yule, "nitaandikisha taarifa zangu nikiamka, sasa nataka nipumzike kwanza nimechoka sana".
Mhudumu akajibu "hamna shida ila usiache kuandika ukiamka maana sasa kila baada ya masaa huwa wanapita polisi kukagua wageni waliofika katika Mji wetu, tusipokuandika tutaingia matatizoni". "Don't worry..!, nitaandika" alisema huku akiubugaza mlango wake.
Moyoni mwake aliweka nia ya kutafuta nyumba ndogo ya kukodi kuepusha usumbufu wa polisi kabla hajamaliza kazi yake iliyomleta. Kazi ambayo alitaka kuimaliza ndani ya wiki moja tu isizidi awe ameusambaratisha mtandao wote.
Akaingia chumbani akapangilia vitu vyake kiumakini mkubwa kisha akalala usingizi mzito wa masaa yasiyopungua saba. Aliamka saa 7:15 mchana akiwa na njaa kali sana ndipo akakumbuka hajatia chochote kitu tumboni kwa muda mrefu tokea alivyokula Mtwara mjini.
Ila anachokumbuka ni kuwa alimeza vidonge vyake anavyotumia kupoteza njaa aina "Phentermine" akiwa yupo ndani ya "pick-up" ya Halmashauri ya Nanyumbu baada ya hapo hakusikia njaa tena.
Harakaharaka akajizoa kitandani akaanza mazoezi mafupi ya viungo ya muda wa robo saa kama kawaida yake kila anaposhtuka usingizini. Baada ya hapo akakimbilia maliwato kujimwagia maji ili achangamke na kujisikia vizuri.
Baada ya kuvaa akatoka nje ya nyumba hiyo ya wageni ya "Nzuwa lodge". Alipotokeza hapo nje akaona bango kubwa la mgahawa ambalo linaelekeza kuwa kando ya Lodge kama meta 20 ndipo ulipo.
Ulikuwa ni mgahawa uliojikita zaidi kwente kupika maakuli ya asili. Wageni wengi hasa watalii waliokuwa wanatembelea Cabo-Delgado walikuwa wanapenda kwenda kula vyakula vya kienyeji kwenye mkahawa huo.
Hapo ukifika asubuhi ukihitaji kifungua kinywa utapata uji wa totori. Huo ni uji unaotengenezwa kwa kutumia unga unaoitwa "Nalungutu".
Unga wa Nalungutu unaotokana na makapi ya mwanzoni ya nafaka ya mtama. Matayarisho yake makapi hayo ya mtama huwa yanafunikiwa kwenye kinu ili yavunde kidogo afu yanachanganywa na mabibo ya korosho wakati wa kupika au unaweza kuchanganya jivu la majani ya ufuta ili kuleta uchachu.
Uji huo wakati unakunywa unapewa utumie majani ya mnazi kuchotea. Hapo ndio utamu wake unazidi kuliko kunywa na kijiko. Uji huo ni shibe ambayo ukila sasa hivi unaweza kukaa masaa mpaka 8 shambani unalima tu bila kuhisi njaa.
Kachero Manu akakata shauri ya kwenda mgahawani huko akapate maakuli ya asili. Alipofika tu Mkahawani bila hata salamu akaagiza kwa mhudumu uji wa Totori, Machoba na Pure, usicheze na njaa wewe. Hayo Machoba ni futari ya mihogo mikavu iliyoungwa na nazi. Na pure ni chakula mchanganyiko wa mahindi na maharage, maarufu kama Makande.
Alipoletewa chakula chake tu akaanza kufakamia chakula hicho kwa pupa kutokana na njaa yake huku akijua usiku mwingine wa misuko suko unakuja. Chakula hicho alikuwa amewahi kula sana utotoni mwake, hivyo kilikuwa kinamkumbusha mbali sana. Alipomaliza mlo wake akaagiza juisi ya dafu baridi sana kwa ajili ya kushushia mlo wake.
Alipomaliza kula akatoka nje ya mgahawa akakaa kwa nje kwenye kiti uzembe cha kujikunja akipunga upepo na kuruhusu vimeng'enyo vya mwili vifanye kazi yake maridhawa ili viupe mwili virutubisho stahiki. Wakati huo huo macho yake yamekodoa kodo uelekeo wa Nzuwa Lodge pale alipofikia.
Hakuwa amekaa kiboyaboya, kwenye usalama wake alikuwa makini sana. Baada ya dakika kadhaa akawa amefungua gazeti la lugha ya kireno liitwalo "Domingo" linalotoka kwa wiki mara moja anazuga anasoma kumbe anapoteza watu maboya tu, kwa sababu hakijui Kireno hata tone.
Gazeti ambalo alilichukua mapokezi kule nyumba ya wageni alipofikia, wakati anaacha funguo wa chumba chake wakati anatoka kuja kula. Kwa mbali maeneo ya pale "Lodge" akaona gari "Toyota Land-cruser" rangi nyeupe limepaki kwa nje bila kufuata utaratibu wa kukaa kwenye maegesho.
Hisia zake zikamtuma awe makini nalo hilo gari, kwa vyovyote vile itakavyokuwa linaendeshwa na dereva mjuba asiye na chembe ya ustaarabu. Kwa Kachero mzoefu kila kitu unachokitilia mashaka lazima uwe makini nacho usikipuuzie hata kidogo.
Akiwa bado ametumbua macho uelekeo wa pale iliposimama ile gari, fajaa kwa mshangao mkubwa akaona linatoka lile gari kwa kasi kuja uelekeo wa njia ile ile ya mgahawa aliopo. Tumbo lake likaanza kupata joto na kumvuruga, akidhania labda anafuatwa yeye pale alipo.
Akajigusa maeneo ya tako lake la kushoto akauhisi mguu wake wa kuku alioufumbata kiunoni upo, akatulizana. Alichofanya ni kulinyanyua gazeti lake juu zaidi ya uso wake kujificha nalo lakini huku anatupa jicho pembe aweze kuzisoma namba za gari kama ataweza.
Kwa kasi iliyopita nayo aliambulia namba mbili za mwanzo tu "MBA-08.." likawa limeshatimuwa vumbi limetokomea mitaani. Akashukuru uamuzi wake wa kubeba gazeti ambalo limemsaidia kujificha nalo licha ya kwamba hafahamu kabisa lugha hiyo ya kireno.
Hima hima akafunga gazeti lake akamuita mhudumu kisha akalipa pesa ya chakula chake alichokula na kinywaji chake na kurejea "Lodge" kuangalia usalama wake.
Alipofika mapokezi kuchukua funguo wakati anaelekea kwenye chumba chake akasikia sauti ya mhudumu wa mapokezi, "kaka samahani asubuhi hakuandika kwenye kitabu cha wageni, ulisema umechoka sana" alisema dada yule.
"OK... sawa" akarejea Kaunta pale na kujaza jina lake la uwongo la kizanzibari "Hasan Ibn Hussein" kama linavyoonekana kwenye hati ya kusafiria aliyokuja nayo Msumbiji.
Alivyomaliza kujaza akaelekea chumbani kwake na alipoingia tu kengere ya hatari ikagonga kichwani akawa anajiuliza "kuna watu wameingia chumbani, je ni wahudumu wa usafi? hapana sio wahudumu alijiambia maana wamefanya upekuzi lakini huwezi kufahamu mpaka uwe mtaalamu".
Akaurudishia mlango wake akatabasamu baada ya kukiona kitabu chake alichokiacha kipo mezani. Nyaraka zake muhimu zote kama hati ya kusafiria, kadi za benki, baadhi ya pesa zake na vinginevyo vilikuwa kwenye kitabu hicho maalumu cha kijasusi kinaitwa kitaalamu "Hollow Book Safe".
Kitabu ambacho ukikiona kijuujuu utadhania ni kitabu tu cha kujisomea kama vilivyo vitabu vingine lakini katikati ya kitabu hicho kilikuwa hakuna kurasa bali kuna uwazi unaoweza kutunzia vitu vyako muhimu.
Kisha akaelekea kwenye kingo ya dirisha akachomoa kiberiti chake cha kuwashia sigara aina ya "HDALTH" lakini hakikuwa kiberiti cha kawaida, ni kiberiti cha kijasusi ambacho kina uwezo wa kurekodi video. Akatoa "chip" kutoka kwenye kiberiti hicho akahamishia kwenye kompyuta mpakato yake ndogo aliyoitoa kwenye begi lake.
Akaiwasha Kompyuta na kuanza kuangalia wavamizi wake. Akaanza kuona watu wawili wote wamevaa miwani nyeusi na suti za rangi bluu wapo chumbani wakiwa na haraka na sura za wasiwasi wanapekuwa pekuwa mpaka chini ya godoro.
Wakaingia bafuni wakatoka na sabuni ya kuogea wakaikata katikakati kutafuta kitu wanachokitaka kisha wakaweka sabuni mpya kama ile ya mwanzoni wakaenda kwenye pipa dogo la taka la chumbani nako hawakuona chochote.
Baada ya hapo wakatoka kwa haraka wakafunga chumba. Baada ya kumaliza kuangalia video ile fupi, akashusha pumzi ndefu, ya kushukuru Mungu.
Akaanza kuwaza kuwa kazi imeanza na wameshajua kuwa yupo Cabo-Delgado, je wamejuaje? ndani ya masaa machache tu wameshafanikiwa kufika mpaka alipofikia, akajiapiza lazima agangamale na awe makini.
Anapambana na genge la watu makini na hatari sana tena wanaoijua vizuri kazi yao. Hivyo akaweka nia ya kwenda haraka nyumbani kwa mzee Masebbo mtaa wa Ruvuma nyumba namba 23B huenda akapata dondoo za kuwasaka wabaya wake.
Lakini kwanza atahitaji msaada wa Mzee Jacob Steven maarufu kama "Komandoo JS", komandoo mstaafu aliyepewa mawasiliano yake na Bosi wake kazini, kuwa lazima amsake Komandoo JS aweze kumuwekea ganda la ndizi la kutekeza nalo.
Alikuwa anataka kumtafuta Mzee Jacob kwanza amsaidie kupata gari la kutumia la kukodisha mwezi mzima, pili amsaidie kupata namba za usajili wa gari za kufoji hizo ndio atazitumia kwenye gari ili kuwapoteza vyombo vya dola kufuatilia nyendo zake za nyendo za hilo gari.
Na tatu alitaka apate msaada wa nyumba ya kupanga kwa muda wa mwezi mzima, hakutaka tena kuwindwa windwa kwenye nyumba za wageni kama changudoa.
Akajiandaa kuondoka kwa kuvaa nguo zake za kazi akaitoa bastola yake kiunoni na kuibusu. Akapiga magoti chini akasali sana kwa muda wa robo saa mpaka machozi yakawa yanabubujika kwenye paji lake la uso kama maji.
Huyu ndio Kachero Manu anakuwa karibu sana na Mungu hasa kwenye wakati mgumu.
Daima Mseminari atabaki kuwa Mseminari tu huyu ndio Manu yule wa Namupa Seminari ni Padre aliyegeukia gwanda za kuleta amani ya mwili kwa mtutu wa bunduki kwa watu ambao ni vichwa maji kama akina Alfredo na vibaraka wenzake.
Akafunga chumba chake na kurudisha funguo mapokezi mgongoni akiwa na begi dogo huku akitia nia kutokurudi tena pale.



Chikulubu, Utingo msaliti hana fadhila
"Chikulubu Wa Chipoku" ni kijana aliyechukuliwa na dereva Masebbo tokea akiwa ghulamu wa miaka 15, na kwa bahati mbaya sana hakujaaliwa kusoma hata darasa moja maishani mwake, mbumbumbu mzungu wa reli hana lolote alijualo hapa duniani kuhusu elimu ya darasani.
Wazazi wake walikuwa ni Wamakonde Chale wa Msumbiji ambao kipindi cha msimu wa kilimo wanavuka mpaka na kwenda Tanzania kufanya vibarua vya kilimo katika vijijini vya mpakani kwa malipo ya mshahara tonge, mkia wa mbuzi usiokidhi mahitaji yao ipasavyo.
Msimu wa kilimo ukiisha wanarejea kwao Msumbiji kusubiri msimu ujao wa kilimo. Hayo ndio yalikuwa maisha yao daima dawamu wanacheza katika mnyororo wa umasikini.
Ilitokea siku moja isiyo na jina dereva Masebbo akiwa na Lori lake alipata pancha ya lori lake jirani na kijiji cha akina Chikulubu na utingo wake wa kawaida hakuwepo kwenye safari bila kutoa taarifa kwa dereva Masebbo hivyo kumpelekea dereva kusafiri bila Utingo.
Chikulubu ndio alimsaidia dereva Masebbo kubadili tairi la gari pamoja na kumtafutia chakula na maji. Kama zali la mentali vile, hiyo ikawa ni sababu ya Chikulubu kula maisha akapata ajira kama Taniboi wa Mzee Masebbo.
Sasa safari za mipakani kwenda Tanzania, Zambia na Zimbabwe zikawa kama kuingia chooni kwa Chikulubu, kismati kinamtembelea. Maisha yake sasa yakapata naizesheni na nafuu kubwa na akahama kijijini na kupanga chumba katika Mji wa Cabo-Delgado.
Amedumu na dereva Masebbo kwa muda wa miaka 10 mtawalia. Lakini hivi karibuni akaanza kubadilika tabia mambo yake yakaanza kuwa tumbitumbi yasiyo na kichwa wala miguu. Hasa baada ya kuanza kukaa vijiweni, akaanza kupenda wanawake, pombe na kila aina ya starehe za vijana wa Mjini.
Vijiwe vya vijana wa kihuni wenye hadithi za kwenda kutafuta maisha bora Afrika ya kusini na ulaya kwa kuzamia meli, na kupata maisha bora bila kufanya juhudi na maarifa. Akaanza tabia ya kuiba mafuta kwenye gari la Mzee Masebbo. Vijana wa mjini wanaita "kupiga nyoka" gari.
Mzee Masebbo alimuonya sana zaidi ya mara tatu hasa akimchukulia kama mtoto wake aliyemtoa kijijini zaidi ya miaka 10 iliyopita mpaka amebaleghe mikononi mwake. Lakini kama ujuavyo mtoto akinyea kiganja hakikatwi kinasafishwa tu, ndivyo namna Mzee Masebbo alivyokuwa anamvumilia Chikulubu.
Sasa kilichomzuzua Chikulubu ni tukio la hivi karibuni la Taniboi mwenzake ambae ni rafiki yake kipenzi cha kuwasakizia Wafanyabiashara wa madini kutoka Tanzania waliokuwa wamewapakiza kwenye gari lao kwa Mafioso wa Alfredo. Ambapo baada ya wale Wafanyabiashara kuporwa madini yao Taniboi huyo alilipwa pesa nzuri sana.
Pesa ambayo iliyomuwezesha kupanga nyumba nzima na kununua bodaboda mbili zinazovuka mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji kubeba mizigo. Toka siku hiyo Chikulubu nae akawa ni mtu wa macho juu juu, shingo feni mwenye wahaka mkubwa kwa kila abiria anayehisi ni Mtanzania wanayempakia kwenye gari lao.
Sasa siku ile ya safari nadhani unakumbuka alikuwa anamtazama sana Kachero Manu mpaka Kachero akashtukia. Sasa hisia zake kuwa Kachero Manu ni mtu muhimu na anaingia nchini mwao Msumbiji kinyemela ni pale waliposimamishwa na askari barabarani halafu alipoulizwa dereva Masebbo kama wote ni raia wa Msumbiji, na dereva Masebbo akajibu wote ni raia hapo hapo akaanza kushikwa na tamaa ya utajiri kupitia Kachero Manu.
Akajua ni mtu muhimu ndio maana Mzee Masebbo anamficha kwa wale askari wasimkamate. Pia kitendo cha Mzee Masebbo kuzuga gari limeharibika ili kumsubiria Kachero Manu, Taniboi Chikulubu alishtukia mchezo mzima.
Kitendo hicho cha usanii wa dereva Masebbo kilimpa maono kuwa Kachero Manu sio mtu mzuri ndio maana analindwa na dereva Masebbo kwa hali na mali. Na kama akifikisha taarifa zake kwa Mafioso wa Alfredo chini ya uongozi wa Inspekta Mark Noble atalipwa pesa sufufu za kumfanya aishi maisha mazuri.
Hivyo walipofika tu Cabo-Delgado, pale Msikitini hakupata hata muda wa kuagana hata na dereva wake kwa kile kimuhemuhe na kiroho papu cha pesa ya madili. Akatokomea zake mtaani kumtafuta yule rafiki yake ampeleke kwa Mafioso wa Cabo-Delgado ili awape penyenye za Kachero Manu kuwa amebebwa kwenye gari la Bosi wake Mzee Masebbo.
Vijana wa kazi wa Inspekta Jenerali Mark Noble walivyoletewa taarifa tu kitu cha kwanza walienda kwenye kituo cha taksi na kuwaelezea wajihi wa mtu wanayemtafuta bahati nzuri wakampata yule dereva aliyempeleka Kachero Manu pale Nzuwa Lodge.
Mafioso walipofika Nzuwa Lodge, walijitambulisha kama maafisa usalama wakakagua kompyuta inayorekodi taarifa za wageni. Bahati mbaya mlengwa wao hakuandika taarifa zake mapema hivyo ikazidi kuwatia mashaka kuwa Kachero Manu sio mtu mzuri.
Hivyo wakaingia chumbani kufanya upekuzi nako hawakupata wanachokikusudia. Wakiwa mule chumbani wakapigiwa simu na kupewa taarifa mbaya ya kuuliwa Askari 6 wanaokagua Watanzania wanaoingia kupitia mpakani.
Pale pale ndio wakaondoka mbio mbio kuelekea nyumbani kwa dereva Masebbo kumfanyia mahojiano juu ya yule mgeni aliyembeba kwenye gari ni ni nani na kaja kufanya nini Cabo-Delgado, kama walivyopewa taarifa na Taniboi wake Chikulubu.
Taniboi msaliti asiyejua kulipa fadhila, ama kweli "shukrani ya punda ni mateke, daima tenda wema uende zako usingoje shukrani, fadhila mfadhili mbuzi utaambulia mchuzi, binadamu ana maudhi".

Mauaji mtaa wa Ruvuma nyumba namba 23B
Mzee Masebbo aliporudi safari yake baada ya kufikisha mzigo wa magendo wa watu salama alienda kwenye kampuni ya tajiri wake akaliegesha gari na kurudi nyumbani kwake kupumzika. Nyumbani kwake alikuwa amebaki peke yake, mkewe na watoto wake watatu wanaosoma sekondari walikuwa wamekwenda likizo eneo la Muidumbe moja ya Wilaya za "Cabo-Delgado".
Huko Muidumbe ndipo ambapo ndio walipo wakwe zake Mzee Masebbo. Alivyofika nyumbani kwake kwanza alikunywa chai kwa mkate alionunua njiani wakati anarejea nyumbani kisha alipitiliza kuoga. Baada ya hapo akaingia kulala kwa nia ya kuamka mchana, afanye usafi wa nyumba na kupika chakula ale.
Alivyopanda kitandani hii asubuhi Mzee Masebbo alikuwa na mawazo mengi sana, hasa juu ya uamuzi anaotaka kuchukua wa kuacha kazi. Alikuwa hapendezwi na namna kampuni yao ya usafirishaji ilivyoanza sasa kushiriki kubeba mizigo haramu ya Mafioso wa Alfredo.
Kitu ambacho hakupendezwa na dhulma anazoshiriki kufanya kwa kuiba Maliasili za Tanzania na kuwafanyia vitendo vya kikatili Watanzania. Aliweka nia mwisho wa mwezi ukifika akipokea mshahara wake tu, ndio utakuwa mwisho wa ajira yake.
Lakini pia akawa anawaza ataendeshaje familia yake bila kazi, hasa katika Mji mkubwa kama huu wa Cabo-Delgado ambao gharama za maisha zipo juu kupitiliza kutokana na ujio wa Watalii toka pande mbalimbali za dunia. Watoto wake bado wanasoma sekondari kwenye shule za kulipia gharama kubwa na mkewe ni mama wa nyumbani, golikipa maarufu mtaani hawezi hata kujitafutia senti tano nyeusi.
Pia na kijijini wazee wake wameshakuwa watu wazima wanamtegemea yeye kwa hali na mali, hawajiwezi kwa sukari wala si kwa chumvi. Fikra hizo zikamfanya ajiweke njia panda, achague mwenyewe kusuka ama kunyoa.
Lakini mwishowe akapiga moyo konde kuwa lolote liwalo na liwe atapeleka barua ya kuacha kazi itakapofika mwisho wa mwezi, hilo ndio likawa hitimisho lake.
"Penye nia pana njia, nitakapoacha kazi nitatafuta sehemu nyingine ya kupatia mkate wangu wa siku na Mungu atanifungulia njia", aliujaza moyo wake ushujaa. Akajikuta anapitiwa na usingizi muda huo wa saa 4 asubuhi.
Mzee Masebbo aliamshwa usingizini na sauti za vishindo vya kugongwa kwa mlango wake kwa nguvu. Mwanzoni alidhania kama yupo ndotoni lakini aliposhtuka akajua kuna watu wanagonga kiukweli sio njozi.
Akapatwa na hofu ya kutaka kufahamu nini kimetokea mpaka anaongewa mlango wake kibabe. Maana namna alivyokuwa anaishi na majirani zake kila mtu anashika hamsini zake.
Huwa wanaonana kwenye matukio ya msiba au sherehe lakini hawana utamaduni wa Kitanzania wa kutembeleana kujuliana hali hujambo sijambo. Akakurupuka toka kitandani, kitambi wazi na pajama yake mbio mbio kwenda kwenda kufungua.
"Nani mwenzangu"? aliuliza Mzee Masebbo wakati anajiandaa kukitegua kitasa cha mlango kwa funguo. Akajibiwa toka nje ya mlango "fungua sisi ni wana usalama tuna mahojiano na wewe". Mwili wake ukapigwa na ubaridi wa ghafla kwa sekunde kadhaa, haja zote kubwa na ndogo anazihisi zinagonga chupi kwa uoga.
Akaanza kutetemeka, kijasho chembamba kinamvuja huku akijiuliza bila kupata majibu kafanya kosa gani. Akapiga moyo konde, akajikaza kisabuni akaamua awafungulie maadamu dhamira yake ipo safi moyoni na hana kosa lolote.
Alipofungua tu wakaingia vijana wawili kwa kishindo. Walivalia suti za bluu na miwani.
"Yupo wapi abiria wako toka Tanzania uliyekuja nae leo usiku?" aliulizwa swali la kushtukiza Mzee Masebbo kwa ukali tena kuwa na ustaarabu. Akajibu kwa sauti ya kitete "mie sijapakiza Mtanzania, walikuwa wanafunzi wa madrasa na Maustaadhi wao basi", alidanganya Mzee Masebbo, huku akiomba Mungu kimya kimya uwongo wake ukubalike.
Hakujua kama wanazo taarifa zake zote, nje ndani toka kwa Taniboi wake Chikulubu. "Mzee mzima kama wewe unasema uwongo hata huoni aibu? Taniboi wako katueleza kila kitu usicheze na akili zetu wewe kikaragosi", alisema mmoja wao wale majambazi kwa hasira, huku akimsogelea amuadabishe.
Mzee Masebbo uso wake ukavaa taharuki, sasa akijua Chikulubu ameshamuuza. Chikulubu aligeuka zigo la misumari habebeki tena. Sasa tutakufundisha namna ya kusema ukweli, alisema mmoja wapo huku anamfuata Mzee Masebbo na kumpiga ngwara, Mzee Masebbo alianguka mzima mzima kama gunia la mahindi toka Zimbabwe la uzito wa kilo mia.
Akaangukia mdomo na kuvunja meno kadhaa. Damu zikaanza kumchuruzika kinywani bila kizuizi. Kisha akamkaba roho kwa kabali juu kidogo ya koo la Mzee Masebbo. Akaanza kukosa hewa safi, "mtani...u....aa.. bu... r.... .......e, mi...mi... simf....a.... h... a..... mu" alisema Mzee Masebbo kwa tabu sana, akikataa kuwa Yuda dhidi ya Kachero Manu.
"Jimmy muache kwanza huenda atasema, eheee wewe babu eleza haraka hatuna muda wa kupoteza tutakupoteza sasa hivi ukifanya mchezo" alisema mmoja wa wajuba wale aliyejipambanua kama ni kiongozi wa mwenzake.
Jimmy akamuachia koo Mzee Masebbo, akaanza kuhema kwa tabu kisha akakohoa makohozi yaliyochanganyika na damu, kisha akaanza kujieleza. "Ni kweli nilimpakia Mtanzania lakini simfahamu kiukweli shughuli zake, nilimsaidia tu kiubinadamu, kwa sababu hamna usafiri wa uhakika kwa sasa. Huo ndio ukweli wangu mtaniua bure lakini sina ninachokijua juu yake", alijieleza Mzee Masebbo kwa uchungu akijua fika anataka kutolewa sadaka bila kosa lolote.
"Kwanini sasa walipokuja Askari kukuuliza kama wote ni raia wa Msumbiji uliamua kumficha mgeni wako?" aliendelea kusailiwa na Jimmy. Mzee Masebbo akawa hana la kujibu anaangalia chini tu, amepatwa na fadhaa huku anajifuta damu kwenye ncha mdomo wake.
"Je unafahamu kuwa huyo mgeni wako uliyemleta mpaka Cabo-Delgado ameua askari wetu 6?, Sasa malipo ya umamluki ni risasi ya ubongo ukasimulie huko jongomeo unakokwenda kuwa usaliti haufai", bila kuchelewa Jimmy akafyatua risasi iliyompata Mzee Masebbo kisawasawa kwenye paji lake la uso na kukifumua kichwa chake kama tikitimaji lililopasuka.
Mzee Masebbo akaanguka chini na kuanza kufafaruka kwa kutupa tupa miguu yake kama mgonjwa kifafa akipigania roho yake. Bila kuchelewa wakatoka nje na kupanda gari lao wakatokomea zao, na kumuachia Mzee Masebbo anapigania uhai wake katika dakika za mwisho mwisho kabla hajaelekea jongomeo.


"Mwiba wa Tasi" kazini
Kachero Manu baada ya kutoka nje ya Nzuwa Lodge akiwa na kibegi chake alielekea upande wa kushoto wa barabara akatembea kama meta 70 na ushee hivi akakatiza barabara ya kushoto kwake. Akajikuta ametokezea stendi ya daladala ya kuelekea Pemba, makao makuu ya jimbo la Cabo-Delgado.
Nyuma ya stendi hiyo kulikuwa na vibanda vingi vya biashara vilivyochangamka ikiwemo kibanda cha "Internet Cafe" kinachotoa huduma za wavuti. Mlango wake kibanda hicho ulikuwa umetengenezwa kwa mbao ya Mninga, ukiwa umenakshiwa kwa marembo marembo ya maua yenye kupendezesha.
Alikata shauri kwanza awasiliane na Mzee Jacob Steven au ukipenda muite Komandoo "JS", Komandoo mkongwe na tegemeo wa nchi ya Msumbiji, lakini alikuwa ni kama lulu iliyotupwa jangwani, hatumiki tena. Ni mmoja wa Makomandoo watano bora barani Afrika waliofuzu mafunzo pamoja na Bosi wake Kachero Manu, Mzee Mathew Kilanga.
Kwa sasa alikuwa anafanya kazi zake binafsi za uvuvi na pia alikuwa na kampuni binafsi ya upelelezi ambayo aliwaachia vijana wake aliowapika kwenye upelelezi waiendeshe. Alipoingia kwenye "Internet-Cafe" akalipia muda wa nusu saa wa kuperuzi mtandao.
Akafungua barua pepe yake ili kurambaza taarifa zozote muhimu alizotumiwa kisha alituma ujumbe wa barua pepe kwa komandoo JS. Kwa bahati nzuri Komandoo JS alikuwa yupo kwenye mtandao muda huo huo hivyo wakaanza kuchati.
Akajitambulisha kwa kutuma namba za siri maalumu alizopewa na Bosi wake za utambulisho, hivyo komandoo Jacob Steven akamtambua Kachero Manu kuwa ni kijana wa komandoo mwenzake wa Tanzania Bwana Mathew Kilanga. Gari aliloomba apatiwe kwa kukodi akapewa ahadi kuwa baada ya dakika 45 atalikuta gari kwenye maegesho ya duka la mikate "Bakery padaria".
Pia ndani yake atakuta namba za gari feki mbili za kubadilisha zipo kwenye gari pamoja na funguo za nyumba ya vyumba viwili ambayo ipo katika mtaa wa "Stadium". Pia akapewa ahadi ya kusaidiwa vijana wa kazi wawili kama atawahitaji.
Akafanya malipo ya gharama zote kwa njia ya mtandao kwa kuhamisha pesa kutoka kwenye akaunti yake kwenda kwenye akaunti ya Komandoo Jacob Steven. Ndani ya dakika 25 tu akawa ameshamalizana na Komandoo JS.
Alipomaliza huduma ya wavuti aliyotumia akatoka nje ya "Internet Cafe" akawasha data ya simu yake ya mkononi yenye namba iliyosajiliwa kabisa ya mtandao wa "Mcel" ambayo alipewa Tanzania na Sekretari wa Bosi wake Mathew Kilanga. Akaingia kwenye ramani ya kimtandao ya "google map" akaitafuta wapi ilipo "Bakery padaria".
Akajikuta anatabasamu mwenyewe na kujiona mjinga, akazima data ya simu yake. Kumbe hakuhitajika hata kukodi taksi ni mtaa wa tatu tu kutoka pale alipo ndio ilipo "Bakery Padaria". Zilikuwa zimebaki dakika chache tu kutimia muda alioahidiwa kulikuta gari. Akaanza kutembea mdogo mdogo huku akibarizi Mji, kuelekea "Bakery padaria".
Alipofika hapo moja kwa moja akapitiliza ndani ya duka kwa ajili ya kununua mchapalo wake. Humo akakuta aina mbalimbali za mikate karibia ya sehemu tofauti za dunia kwa mapishi yake. Alikuta mikate ya boflo iliyotengenezwa kwa ngano ina umbo la mstatili, pia kulikuwa na mikate ya mofa yenye umbo la duara inayotengenezwa kwa unga wa mtama, uwele au mahindi na akakuta mikate ya unga wa ngano iliyochanganywa na unga wa mhogo.
Akachagua mikate mitatu iliyokatwa silesi ya mchanganyiko wa unga wa ngano na unga wa muhogo. Moja ya mikate mitamu sana na inapendwa sana maeneo ya Afrika magharibi hasa nchini Naijeria. Alijua huenda akakosa muda wa kula usiku huu, hivyo akiba haiozi akabeba na juisi ya chupa ya plastiki ya machungwa yenye ujazo wa lita moja pamoja na paketi moja la mboga mbichi mchanganyiko zilizofungashwa.
Akalipia akatoka nje jengo haraka. Alivyotoka tu akaona gari aina ya "Volvo S60" imejitenga peke yake akatambua ndio gari yake aliyoletewa kwa sababu alivyokuja pale hakuiona hiyo na ndio hiyo aliahidiwa na Komandoo JS. Haraka haraka akaenda kwenye lile gari alivyolikaribia tu gari hilo akashuka kijana mwenye umbile la miraba minne, kifua cha mataruma ya reli, kavaa fulana nyeupe amevaa miwani.
Wakasalimiana kwa bashasha, kisha kijana yule akajitambulisha kwa Kachero Manu. Kisha akakabidhiwa kila kitu na yule kijana wa Komandoo Jacob Steven wakaagana. Akaingia ndani ya gari akaanza kuikagua, akaipenda sana ilikuwa ni gari toleo la kisasa na inakwenda mpaka mwendokasi wa 230km/hr kitu ambacho Volvo nyingi za zamani zilikuwa hazifikii mwendokasi huo.
Uzuri wake ni kuwa adui yako ni rahisi kukupuuza anapokukimbiza kama haijui vizuri "Volvo S60" ambayo ina silinda nne na nguvu ya "450hp". Akaweka vizuri vitu vyake kwenye gari akaiwasha gari akaanza kuelekea mtaa wa Ruvuma nyumba namba 23B nyumbani kwa Mzee Masebbo lakini hakujui.
Gari ilikuwa imejazwa mafuta ya kutosha akaenda mpaka karibu na mwisho wa mtaa wa "Bakery padaria" akakutana na mataa akayavuka mataa na kusimamisha gari pembeni ya kijana ambaye ana kibanda cha kuuza vocha za simu na vifaa vya simu.
Akashuka kwenye gari akamsalimia kwa nidhamu "habari yako kijana, samahani nataka kwenda mtaa wa Ruvuma ila sipafahamu naomba unielekeze" alisema Kachero Manu huku anachezesha funguo za gari mkononi.
"Ahaaa..... bila samahani kaka yangu sio mbali sana kutokea hapa tulipo. Unaona ile Hoteli kwenye lile jengo refu rangi nyeupe mbele yako?sasa ile Hoteli inaitwa "Complexo Hoteleira". Ukifika pale kata barabara ya pili yake kulia kwako, ni barabara ya vumbi ndio mtaa huo huo unaotakiwa kwenda" alielekeza kijana yule kwa uchangamfu mkubwa huku akitumia mpaka na ishara ya vidole.
"Ahsante sana, kazi njema" alishukuru kisha akapanda ndani ya gari yake akawasha akaanza kuelekea mtaa wa Ruvuma nyumba namba 23B kwa mwendokasi wa wastani.


Mtaa wa Ruvuma ulikuwa ni mtaa wa watu wa kipato cha kati, na inasemekana baadhi ya wapigania Uhuru wa Msumbiji waliokwenda Msumbiji wakitokea nchini Tanzania kusaidia vita vya ukombozi baadhi yao waliishi mtaa huu na familia zao za wanawake raia wa Msumbiji.
Hivyo waliupa jina hilo la utani ili wajihisi kama bado wapo nyumbani Tanzania. Nyumba namba 23B ilikuwa ipo upande wa kushoto wa njia aliyoingilia Kachero Manu, ilikuwa imezungukwa na fensi ya michongoma mirefu iliyokosa matunzo kutokana na ukosefu wa kumwagiliwa maji ya kutosha.
Kachero Manu aliwasili nyumbani kwa Mzee Masebbo saa kumi kasorobo alasiri. Alipofika akagesha gari yake mwishoni kabisa mwa fensi. Mgeni yoyote asingefahamu kama anakusudia kuingia nyumbani kwa Mzee Masebbo kwa jinsi gari lililovyoegeshwa kijanja. Kisha akashuka nje ya gari, akajongea taratibu mpaka akaifikia baraza ya simenti iliyojaa vumbi zito linalotokana na kukosa kupigwa deki kwa siku kadhaa.
Ilikuwa ni nyumba ambayo mazingira yake ya nje kwa ujumla yalikuwa mchafukoge. Hapo Kachero Manu akatambua nyumba hii haina mwanamke ndani, fikra zake zikimtuma labda Mzee Masebbo hajaoa, au ni mgane au mkewe kasafiri, vinginevyo baraza isingekuwa chafu kiasi hicho cha kutisha. Alipofika mlangoni tu akagonga hodi. Kimya kikatawala bila kujibiwa kitu.
Akagonga tena zaidi ya mara tatu, lakini ukimya ukatawala, bila kujibiwa. Kachero Manu akataka kurudi kwenye gari amfanyie subira kidogo huenda ametoka nyumbani na mbaya zaidi hakumpa namba yake ya simu huenda angemtafuta. Ghafla alipoangalia chini ya mlango aliposimama akapatwa na mshtuko asioutegemea.
Alipatwa na wasiwasi juu ya usalama wa dereva Masebbo baada ya kuona kuna damu imechuruzikia mpaka mlangoni pale aliposimama. Akapigwa na taharuki kubwa, kwa sekunde kadhaa asijue la kufanya. Akafanya maamuzi ya kuingia ndani liwalo na liwe, akajaribu kushika kitasa cha mlango kikakubali kufunguka akazidi kustaajabisha, akaingia ndani.
Alichokiona ndani kwa macho yake hakuamini, alijiona kama yupo ndotoni vile. Alimkuta Mzee Masebbo, rafiki yake waliyejuana masaa machache yaliyopita amelala kifudifudi huku ametumbua macho juu ishara ya kwamba amepoteza uhai wake. Hapo hapo akachomoa bastola yake toka kiunoni mwake akaishika mkononi huku anaisogelea maiti ya Mzee Masebbo kwa tahadhari kubwa.
Alipoifikia ile maiti, akatoa kinga mpira "gloves" mfukoni mwake akazivaa mikononi kisha akaanza kuikagua ile maiti. Damu yake akakuta bado ina ubichi ubichi kwa mbali, kuonyesha mauaji hayajafanyika muda mrefu sana. Akaanza kujilaumu kuchelewa kwake kuja kumuona Mzee Masebbo ndio kumesababisha kifo chake.
Akawa anajiambia kimoyomoyo kuwa huenda angeharakisha kuja huku kabla hajaenda "Internet-Cafe" angeweza kuokoa uhai wake. Alipoliangalia jeraha ilipoingilia risasi akaona alama ya nyota akatambua kuwa mpigaji alipiga kwa ukaribu zaidi, na kwa kuwa kapiga risasi ya kichwani akatambua mpigaji sio mzoefu katika fani.
Maana walifundishwa kwenye kozi ya ulengaji shabaha ukitaka kumpoteza mtu maisha kwa haraka mpige risasi ya kwenye moyo au unatengeneza shabaha ya pembe tatu kutoka kwenye usawa wa pua na pembe ya mdomo, ili risasi ikaharibu neva za uti wa mgongo "spinal cord".
Akawa anajiuliza "kwanini kauliwa kinyama Mzee Masebbo? kosa lake hasa ni nini? labda wananitafuta wamenikosa wameamua kumfuata Mzee wa watu awaelekeze nilipo na maadamu kashindwa kuwapa taarifa zangu wamemuua kikatili" akajikuta anashikwa na hasira zisizo kifani.
Akaamua ailaze chali maiti ya Mzee Masebbo kupunguza usambaaji wa damu sakafuni akawa anamvuta kwa tahadhari asijichafue damu. Alivyomsogeza kidogo tu akaona kitambulisho cha kazi kwa pembeni kuna kikaratasi kimechomekwa.
Akakivuta kile kitambulisho alipokifungua kina jina la "James Penteleo" ni muajiriwa wa jeshi la polisi Msumbiji, na kikaratasi kidogo cheupe lakini kigumu kimeandikwa NAUTILUS HOTEL-"PEMOVACHA" saa 3:00 usiku.
Akachukua kitambulisho na kile kikaratasi akavisunda kwenye suruali yake ya kazi ambayo ina mifuko ya siri. Akaendelea na ukaguzi ndani ya nyumba ya Mzee Masebbo kutafuta kitu kitakachomsaidia kwenye upelelezi wake hakupata kitu chochote cha maana.
Wakati anajiandaa kutoka asije akakutwa ndani akasingiziwa yeye ndio aliyefanya mauaji, maana anayekutwa na ngozi ndio mwenye kesi. Alipofika mlangoni anajiandaa kushika kitasa cha mlango atoke nje akasikia mlio wa bodaboda kwa nje usawa wa mlango wa mzee Masebbo akachomoa bastola yake haraka haraka akasitisha zoezi la kutoka nje kisha akarudi ndani.
Akakimbilia kwenye sofa kubwa la ukumbini akajibanza pembeni mwake upande wa nyuma, anasubiria kama mtu huyo anakuja kwa Mzee Masebbo au ni mpita njia tu. Ghafla mlango ukafunguliwa kwa nguvu moja kwa moja, mtu aliyevaa suti na miwani nyeusi akaingia ndani. Kachero Manu mara moja akamtambua kuwa ni mmoja wa wale waliokuja kupekua chumba chake kule Nzuwa Lodge.
Akapata jibu la asilimia mia moja kuwa kifo cha Mzee Masebbo kina uhusiano wa moja kwa moja na msako wake yeye. Yule jamaa alivyoingia akaenda kwenye maiti ya Mzee Masebbo akaipindua pindua kama kuna kitu anakitafuta. Kwa jinsi alivyojawa na taharuki hakuwa hata na umakini wa kuangalia jinsi maiti walivyoiacha ipo kifudifudi na sasa ameikuta imelala chali, hivyo ilitakiwa awe na tahadhari.
Akaanza kuzunguka sebuleni kama mwendawazimu alipokuwa anatembea simu ya mkononi ya yule mtu ikaanza kuita. Akaipokea baada ya kuitoa mfukoni, akaanza kuongea huku anazunguka ukumbini pote pale.
"Hellow...! Kamanda Mark, kitambulisho changu cha kazi sikioni aisee na kile kikadi cha kuniruhusu kuingia kwenye chumba maalumu pale Nautilus Hotel nacho sijakiona, kijasho kinanitoka hapa nilipo maana bila kadi siwezi kuruhusiwa..! ". Akawa amefika karibu na usawa wa sofa ambalo amejificha Kachero Manu.
"Nyanyua mikono yako juu na tupa simu yako chini, usijaribu kuleta ujanja wowote...!" alitoa sauti ya amri Kachero Manu isiyo na chembe ya masihara. Yule jamaa alipatwa na mshtuko kama amepewa taarifa ya msiba wa mtu wake wa karibu, hakutegemea kama kulikuwa na mtu mle ndani, hapo hapo akatii amri na kunyoosha mikono juu huku akiitupa simu yake kwenye sofa.
"Haya geuka nyuma kisha anza kwenda mbele" alitoa maelekezo Kachero Manu. Hilo lilikuwa ni kosa kubwa, kwani alipogeuka yule jamaa alirukia sofa lililopo mbele yake kisha akajigeuza juu kwa juu utasema mtoto wa marehemu 'Bruce Lee' kisha akaachia teke moja matata sana lililotua sawia kwenye mkono wa kushoto wa Kachero Manu.
Mkono ambao ulikuwa umeshikilia bastola yake na kusababisha bastola kudondokea pembeni mwa sofa. Kachero Manu hakutaka kumkawiza, akajongea pembeni kidogo, akamuona anakuja kwa kasi kama mbogo ili amvamie, alichofanya Kachero ni kumkwepa kisha akamtega kwa mguu akaanguka kifudifudi hapo hapo hakumchelewesha akamrukia kwa kabali ya miguu, ikawa baradhuli yule anafurukuta lakini hawezi kutoka, mpaka pumzi zake za uhai zikaanza kukata zikawa zinapita kwa shida.
Kachero Manu akamuachia kidogo kisha akachomoa kisu kidogo cha kukunja akamuwekea shingoni. Akaanza kumfanyia mahojiano, "kwanini mmemuua Mzee Masebbo bila kosa lolote mbwa nyie? na nani amewatuma?". Kabla hajaanza kujibu akaanza kumkata ngozi laini ya kwenye koo ili kumtia uoga aropoke kila kitu, lakini yule jamaa akaonyesha haogopi, akajibu "siwezi kukujibu chochote, fanya utakacho mbwa mwenyewe...! ".
Kachero Manu akajua hana muda wa kupoteza akamshika mikono yake huku goti amelikandamiza kwenye shingo ya mwanaharamu yule, akaivuta mikono kwa kasi kuelekea mgongoni kwa kasi mpaka akategua viungo vya mabegani.
Jimmy akagugumia kwa maumivu makali, haraka haraka Kachero Manu akachomoa kichupa kidogo cha dawa mfukoni mwake na sindano ndogo. Kichupa cha dawa kimeandikwa "PENTOTHAL" akavuta dawa kwenye sindano akamdunga nayo mwilini. PENTOTHAL ni dawa ambayo ukidungwa inakufanya uongee ukweli tupu huwezi kuficha kitu. Ukiulizwa hata idadi na majina ya michepuko yako unaotaka bila hofu hata mbele ya mkeo.
"Jina lako ni nani?" aliuliza Kachero Manu ili kupata uhakika kile kitambulisho kama ni kweli cha jeshi la polisi. Akajibu "naitwa "James Penteleo" alijibu. "Kwanini wewe ni polisi lakini unashirikiana na wahalifu"? aliulizwa huku akirekodi mahojiano hayo kwa kutumia kalamu yake maalumu.




Kachero Manu akajua hana muda wa kupoteza akamshika mikono yake huku goti amelikandamiza kwenye shingo ya mwanaharamu yule, akaivuta mikono kwa kasi kuelekea mgongoni kwa kasi mpaka akategua viungo vya mabegani.
Jimmy akagugumia kwa maumivu makali, haraka haraka Kachero Manu akachomoa kichupa kidogo cha dawa mfukoni mwake na sindano ndogo. Kichupa cha dawa kimeandikwa "PENTOTHAL" akavuta dawa kwenye sindano akamdunga nayo mwilini. PENTOTHAL ni dawa ambayo ukidungwa inakufanya uongee ukweli tupu huwezi kuficha kitu. Ukiulizwa hata idadi na majina ya michepuko yako unaotaka bila hofu hata mbele ya mkeo.
"Jina lako ni nani?" aliuliza Kachero Manu ili kupata uhakika kile kitambulisho kama ni kweli cha jeshi la polisi. Akajibu "naitwa "James Penteleo" alijibu. "Kwanini wewe ni polisi lakini unashirikiana na wahalifu"? aliulizwa huku akirekodi mahojiano hayo kwa kutumia kalamu yake maalumu.
"Mimi sijui chochote, ila yule mkuu wangu wa kazi Mark ndio anawajua hao wakubwa wanaotutuma akina ALF....... aaaah nakufw......a.. a..aaaa.." aligugumia Jimmy kwa maumivu makali ya risasi aliyopigwa usawa wa moyo kupitia dirishani.
Kachero Manu alijitupa pembeni kama samaki mkizi akachukua ile bastola yake iliyokuwa imedondokea pembeni ya sofa kisha akaharakisha kufungua mlango wa mbele. Akasikia muungurumo wa gari linaondoka kwa kasi ya ajabu linatimua vumbi katika barabara ya vumbi ya mtaa wa Ruvuma. Akaegesha mlango akatoa kijitabu kidogo mfukoni mwake akaangalia namba ya kutoa taarifa polisi akapiga 10111 kuwapa taarifa hiyo ya mauaji.
Akazima simu yake na kupanda gari huku akienda kujiandaa na usiku wa mapambano. Lakini akawa anatafakari "huyu ALF.. ni nani? mzee Masebbo kafariki na siri yake moyoni ya huyu ALF..., na huyu baradhuli Jimmy nae kafa na siri ya huyu ALF.., huyu ni nani na ana nguvu gani, mpaka ukitaka kumtaja tu jina lake huwezi kumalizia na Malaika mtoa roho anakujia ghafla kuchukua roho yako..!.. "Dawa yake inachemka, supu ya mbwa yanywewa ikiwa ya motomoto....", aliwaza kimoyomoyo huku anachochea mwendokasi wa gari lake anapasua mitaani.


SURA YA NANE
Mkutano wa siri Nautilus Hoteli
'Nautilus Hotel' ni moja ya Hoteli yenye hadhi ya nyota 5 iliyojengwa katika ufukwe wa bahari ya Wimbi katika wilaya ya Pemba. Pemba ndio Wilaya kubwa kuliko zote katika Wilaya za Jimbo la Cabo-Delgado nchini Msumbiji. Huu Mji kuanzia mwaka 1904 ulikuwa unaitwa kwa jina la "Porto-Amelia" kwa heshima ya Malkia wa Ureno. Baada ya uhuru wa Msumbiji mwaka 1975 ndio Mji huo ukaitwa Pemba.
Moja ya kivutio cha Mji wa Pemba ni uwepo wa wazawa halisi wa Mji huo ambao wametunza utamaduni wao mpaka leo. Makabila wazawa wa Pemba ni Wamakonde, Wamakuwa na Wamwani. Ni jambo la kawaida kukutana na mwanamke wa Kimakonde amejichora tatoo mwilini, amejipaka rangi nyeupe usoni au kukutana na ngoma za asili zinazoitwa "Mapico" au kukutana na watu wanachonga vinyago.
Vitu ambavyo vilikuwa vinawavutia watalii kutoka pande mbalimbali za Ulaya kumiminika Wilayani Pemba. Kuifikia Hoteli ya Nautilus kutokea uwanja wa ndege wa Pemba ni kilometa zisizopungua 3. Hivyo ingekuchukua robo saa kwa mwendo wa wastani. Ilikuwa ni Hoteli ya kisasa yenye vyumba vya kulala zaidi ya 21 na kumbi mbalimbali za mikutano zisizopungua 7.
Kila chumba cha kulala kilikuwa kimeunganishwa na waya wa DSTV, runinga ya kisasa za inchi 32, waya wa mawasiliano ya kieletroniki na kipoza hewa. Pia vyumba vilikuwa vimenakshiwa vinyago vya urembo wa asili wa tamaduni za Kimakonde. Kulikuwa na mabwawa makubwa ya kuogelea, vyumba vya kisasa vya mazoezi 'Gym', Mkahawa wa kulia chakula pamoja na Baa.
Kwa uzuri wake tu ni moja ya fahari za Mji wa Pemba, ambayo kila mwananchi wa Pemba alikuwa anajivunia nayo.
Kampuni ya "Monte Branco Ltd" iliukodisha ukumbi 'Na. 03' wa mikutano katika Hoteli hiyo kwa muda wa siku 2. Wakaulipia kwa muda wa Juma zima huku wakiwa hawataki Mfanyakazi yoyote wa Hoteli hiyo kusogelea ukumbi huo. Kila kitu walijiandaa kivyao, kuanzia vyakula na vinywaji vyao. Waliweka walinzi wao na kufunga mitambo yao ya kuzuia udukuzi wa kikao chao cha siri kinachotegemea kufanyika saa saa 3:00 usiku.
Ilikuwa kuanzia meta 100 kutoka ukumbi wa mkutano kuna walinzi wao wenye vifaa vya kisasa. Asiyehusika na kikao kile kufanikiwa kuwapenya walinzi wale mpaka uingie kwenye chumba cha mkutano ilikuwa ni sawa na muujiza wa ngamia kupita kwenye tundu la sindano. Mkutano huo ulihusisha Wakurugenzi Wakuu wa Kampuni ya Monte Branco Ltd, Inspekta Jenerali Mark Noble na baadhi ya vijana wake na baadhi ya Vigogo wa serikali ya Msumbiji wasio waaminifu ambao ni washirika wao.
Kulikuwa kunapangwa mikakati ya kufanikisha dili haramu lenye pesa ndefu la ujenzi wa barabara unaogharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika 'ADB'. Kama ujuavyo Alfredo na Mafioso wenzake walikuwa wapo kwenye harakati za kujinufaisha kiuchumi kwenye dili lolote lile lenye pesa.
Usiri mkubwa ulihitajika sana kutokana na maamuzi yatakayopitishwa na kikao hicho. Maamuzi ambayo yangeweza kugharimu maisha ya baadhi ya vigogo wanaokwamisha kufanikiwa kwa dili hilo haramu. Mkutano huo pia ulikuwa upitie taarifa ya udhibiti wa wahamiaji toka Tanzania, na ripoti ya uchimbaji wa madini ya rubi katika machimbo yaliyopo Jimboni Cabo-Delgado. Kilikuwa ni kikao ambacho moto mkali wa majadiliano ulitegemewa kuwaka.

Kachero Manu atinga mkutanoni kwa teknolojia
Alivyotoka nyumbani kwa Marehemu Mzee Masebbo kule mtaa wa Ruvuma, moja kwa moja aliekea kwenye nyumba yake aliyotafutiwa ya kupanga. Aliwasili nyumbani hapo muda wa saa 10:45 alasiri, alipofika akazunguka mazingira yote ya nyumba kujiridhisha na usalama wake.
Kisha akaanza kuhisi njaa akakumbuka alinunua mkate, juisi ya matunda chupa bonge na saladi alivyovihifadhi ndani ya gari. Akala mkate alioununua kisha akashushia na juisi. Baada ya hapo akafanya maamuzi ya kujinyoosha usingizi wa muda mchache, tayari kwa safari ifikapo saa 12 magharibi kuelekea mji wa Pemba.
Kabla hajalala aliingia kwenye mtandao wa simu yake ya kiganjani kuitafuta ilipo "NAUTILUS HOTEL" kupitia wavuti wa "Google Map". Akapata majibu ni hoteli ya kitalii ipo wilaya ya Pemba, umbali wa kilometa takribani 185 kutoka mji alipo wa Montepuez.
Akajiapiza lazima aende akafahamu kuna mafungamano gani yaliyojificha kati ya wale mabaradhuli waliofanya mauaji ya Mzee Masebbo na mkutano huo. Na pia hilo neno "PEMOVACHA" kwenye kikaratasi cha marehemu Jimmy alikuwa anataka kufahamu undani wake. "Majibu nitayapata Nautilus hoteli sina haja ya kuumiza kichwa", alijiambia mwenyewe kimoyomoyo Kachero Manu.
Ilipofika saa 11:45 alasiri alikuwa tayari ameshajiandaa kwa ajili ya safari hiyo. Hivyo akapitia kituo cha mafuta cha jirani na alipo akajaza mafuta yaliyojaa tenki. Akang'oa nanga kuelekea Pemba akiwa ndani ya gari alilokodi la 'Volvo s60' toleo jipya la mwaka 2012. Ilikuwa ni safari ya umbali kama wa Dar es Salaam kwenda Morogoro ukifananisha kwa hapa kwetu Tanzania. Ni safari ambayo kwa mwendo wa kawaida ilitakiwa atumie saa 4. Hivyo anavyotoka hiyo saa 12 itambidi aingie saa 4 usiku nyuma ya muda wa mkutano anaotaka kuhudhuria kwa lisaa limoja.
Akaamua aende kwa mwendo wa kasi huku akiomba Mungu asipate ajali yoyote au kukamatwa na askari usalama barabarani. Mipango yake ilifanikiwa mpaka saa 1:15 usiku mbichi alikuwa tayari kashafika katika kijiji cha Metoro umbali ambo ni nusu ya safari. Alisimama kukagua gari na kuchimba dawa kidogo ili kukipa ahueni kibofu chake cha mkojo.




Akaamua aende kwa mwendo wa kasi huku akiomba Mungu asipate ajali yoyote au kukamatwa na askari usalama barabarani. Mipango yake ilifanikiwa mpaka saa 1:15 usiku mbichi alikuwa tayari kashafika katika kijiji cha Metoro umbali ambo ni nusu ya safari. Alisimama kukagua gari na kuchimba dawa kidogo ili kukipa ahueni kibofu chake cha mkojo.
Aliondoka Metoro saa 1:25 usiku huku mvua ya mkaragazo ikinyesha kwa kishindo, lakini hakuijali sana. Malengo yake yalikuwa afike saa 2:45 usiku. Kwa mwendokasi aliokuwa anaenda nao utadhania ni mshindani wa mashindano ya mbio za magari za "Dacar Rally", mbio ambazo ni za hatari sana na hutokea mara nyingi baadhi ya madereva kupoteza uhai. Mashindano hayo ya "Dacar Rally" huanzia Jijini Paris, Ufaransa mpaka kuishia Jijini Dakar, Senegali.
Alipofika kitongoji cha Nanlia bado kama kijiji kimoja afike Pemba kutokana na utelezi wa barabara uliosababisha na mvua kali aliwakosa kosa kuwagonga kundi kubwa la ng'ombe waliokuwa wanaswagwa kurudisha nyumbani, akanusurika na ajali mbaya sana. Alipofika kijiji cha Murrebu akapata pancha ya tairi lake, hapo sasa safari ikabidi isimame kwa muda.
Ilikuwa ni muda wa saa 2:25 usiku. Bahati nzuri kulikuwa na tairi la akiba akabadililisha haraka haraka tairi lenye pancha na kuendelea na safari yake. Mpaka kufika majira ya 3:05 usiku ndio alikuwa anapaki gari lake kwenye maegesho ya magari ya Nantilius Hoteli tayari kashaingia kwenye himaya ya mabaradhuli wake anaopambana nao.
Akashuka akajikagua vitu vya kazi alivyonavyo kuanzia bastola yake kibindoni ndani wa suruali yake ya dangirizi, pia kuna bisibisi, mkasi, mkungu wa funguo bandia na koleo. Akaenda mapokezi pale Hotelini akawa anazuga kuulizia bei ya vyumba na gharama mbalimbali za vyakula na gharama za kukodi ukumbi wa mikutano huku anasoma ramani nzima ya jengo la Hoteli iliyowekwa pale mapokezi.
Alipoielewa ramani vizuri akaomba aelekezwe chooni. "Tembea na hii veranda kisha utakata kushoto utakutana na vyoo vya wanaume" alielekeza mhudumu wa Hoteli kwa sura ya bashasha, akijua ni mmoja wa wateja wao wapya bila kuelewa mipango ya Kachero Manu, kuwa yupo kazini wala hana haja na chumba wala chochote. "Ahsante sana, ngoja niwahi kwanza maliwatoni" alisema Kachero Manu huku akaondoka kwa mwendo wa haraka.
Alipofika usawa wa maliwato, kulia kwake kulikuwa na lifti inayokupeleka mpaka roshani ya 3 ambapo ndio kuna vyumba maalumu vya mikutano. Akaita lifti ilivyokuja akapanda haraka akabonyeza kitufe cha kuifanya isimame ghorofa ya 3. Bahati nzuri alikuwa yupo peke yake ndani ya lifti ile akashukuru Mungu, bahati bado ipo upande wake.
Aliposhuka tu akaipa ubavu wa kushoto lifti aliyoshukia kisha akatembea kuelekea mbele kwa mwendo wa kunyatia kwenda kwenye chumba cha kudhibiti umeme wa jengo zima la Hoteli. Alipofika akakuta chumba hicho, kimefungwa. Akatoa mkungu wa funguo malaya toka mfukoni mwake, akaingiza funguo moja wapo, kisha akaitekenya kufuli kidogo tu ikafunguka.
Bila kufanya ajizi akaufungua mlango kisha akaingia zake bila kusahau kuurudishia mlango wa chumba hiko. Humo ndipo akaanza vimbwanga vyake tatanishi. Akafungua mfumo wa kukata umeme kwa kutumia bisibisi yake akaunganisha waya wa "earth" na "neutral" kwa pamoja hapo hapo umeme wa jengo zima la hoteli ukazimika kwa kupiga shoti ya kubutuka kwa kishindo kikubwa.
Giza totoro likatawala ndani ya jengo zima la hoteli. Akatabasamu kuwa mbinu yake namba moja imetimia, akatoka nje ya chumba akafunga kufuli na kurudi kujibana kwenye ukuta wa pembeni unaotenganisha chumba cha kudhibiti mfumo wa umeme na stoo ndogo ya kutunzia vifaa vya usafi, sehemu ambayo sio rahisi kwa anaekuja kumuona.
Alijua tu lazima fundi umeme wa hoteli atakuja kwenye chumba cha mfumo wa umeme kuja kuangalia chanzo cha tatizo, akawa anamsubiria afike. Akaangalia saa yake ikawa inasoma ni saa 3:30 usiku. Akajipa matumaini kuwa kikao hakijaanza na kama kimeanza basi kwa kuchelewa kama Waafrika ilivyo tabia yetu hatuwezi kuchunga muda. Mungu si athumani hazikupita hata dakika 5 akasikia lifti inagota ghorofa ya 3.
Akaombea awe ni fundi umeme ndio anayekuja na hiyo lifti. Kweli bana lifti ilivyofunguka akashuka kijana wa makamo ana mwili wa wastani amebeba sanduku lake la vifaa vya ufundi alivyoshuka tu na tochi yake akawa anaelekea upande wa chumba cha kudhibiti mfumo wa umeme. Akamsubiria afike mpaka aufikie mlango huo ndio amfungie kazi. Alipofungua tu mlango na kuingia kwenye chumba, fundi hakuubugaza mlango aliuacha wazi. Kachero akamfuata taratibu kwa mwendo wa kunyatia bila kumshtua.
Alipomfikia akamgusa begani, ile kugeuka tu akampiga kareti moja matata sana ya shingoni, fundi umeme akaanguka chini pale pale kama gogo la mti. Akamvuta pembeni ya chumba akajua atakuwa amezimia atakuja kuzinduka masaa mawili mbele. Haraka haraka akamvua nguo yake ya kazi, bwelasuti rangi buluu. Nguo maalumu wanayovaa mafundi yenye nembo ya jina la Hoteli akavaa yeye Kachero ikamkaa vizuri kama vile fundi nguo alimpimisha yeye vipimo wakati wa kushona vazi lile.
Haraka haraka akatoka na lile sanduku la vifaa la fundi akaongoza mwendo kuelekea veranda ya upande wa vyumba vya mikutano, ambao ni kinyume na kile chumba alichotoka. Akakutana na walinzi kama watano walipomuona na vazi la fundi umeme wakaharakisha kumlaki, "fundi tatizo nini? kuna mkutano muhimu chumba namba tatu umeshindwa kuendelea kwa sababu ya umeme na tumelipia fedha sufufu ili tupate huduma za viwango", alisema mmoja wa walinzi akionyesha kukasirishwa na kitendo cha kukatika umeme ghafla.
"Poleni sana huenda katika moja ya soketi za chumba hicho cha mkutano ina shoti maana nimetoka kukagua chumba cha kudhibiti umeme wa jengo zima sasa hivi hamna tatizo lolote, na chumba cha mkutano pekee kinachotumika kwa sasa ni hiki namba 03" alijibu Kachero Manu kwa unyenyekevu mkubwa.
Akaruhusiwa kuingia chumba kile bila kizuizi wala kikwazo chochote. Alivyoingia tu, akakuta watu wamekaa kwa mtindo wa mduara huku mbele kuna projekta kubwa ya kuwasilishia mada iliyounganishwa na kompyuta. Kwa haraka haraka hakuweza kuwaona vizuri sana kutokana na mwanga hafifu wa taa za kuchaji iliyowashwa.
Akawa anazungukia kwenye soketi zote akazuga anazikagua kwa kutumia bisibisi "testa" kisha kwenye baadhi ya soketi akavisha kifaa kinachofanana na soketi lakini chenye kazi ya kudukua mawasiliano yoyote ya simu itakayochajiwa eneo hilo. Baada ya hapo akaenda kwenye meza ambayo kuna projekta ya kuwasilisha maelezo ukutani akaikagua kisha akatoka haraka nje ya chumba cha mkutano.
Akarudi katika chumba cha kudhibiti umeme, baada ya dakika tano tu umeme ukarudi kwenye jengo zima la hoteli. Akavua nguo za yule fundi, akaegesha mlango akatoka haraka haraka akaifikia lifti akaidandia na kushuka nayo mpaka sakafu ya chini.
Akapitiliza moja kwa moja mgahawani na kuagiza soda aina ya Coca-Cola baridi sana ya kopo. Akalipia na kurejea kwenye gari yake huku ameshika kinywaji chake mkononi anatabasamu, tabasamu la ushindi wa kishindo. Akajisifu kimoyomoyo ujanja mwingi na wa hali ya juu aliioutumia.


?Dr.Muganyizi Lazima afe
"Dr.Fredrick Muganyizi" ni Mkurugenzi Mkuu, mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kanda ya kusini mwa jangwa la Sahara. Alikuwa ni shaibu wa makamo mwenye umri usiopungua 55.
Ni Daktari wa Falsafa aliyebobea katika fani ya maendeleo vijijini "Rural Development" aliyehitimu katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA)-Morogoro. Mwanzoni alikuwa ni mhadhiri katika Chuo cha Mipango, Jijini Dodoma.
Mara tu alivyomaliza masomo yake ya Uzamivu akapata ajira Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kama Meneja Miradi Kanda ya Afrika Magharibi kuanzia mwaka 2005-2013. Kabla ya mwaka 2014 kupandishwa Cheo na kuwa Mkurugenzi Mkuu mwakilishi kanda ya kusini mwa jangwa la Sahara na kituo chake cha kazi kipya kikawa ni nchini Botswana.
Miongoni mwa tabia za Dr.Muganyizi ni uwazi, uwajibikaji na ukweli. Tabia ambazo zilimtengenezea maadui wengi na kumpatia marafiki wachache. Hasa ukichukulia serikali nyingi za Afrika zilikuwa zinanuka rushwa na ufisadi.
Watendaji katika serikali za Kiafrika tabia zao wakipata nyadhifa nyeti za uteuzi kama Uwaziri au Ukurugenzi wa Shirika fulani basi wanapongezana na familia zao kuwa wameula maisha. Kwa Tanzania Ikaibuliwa misamiati mitaani ya kurathimisha ufisadi wao, ikawa yakipita mitaani magari yenye namba za shirika la umma (SU) wao wakatafsiri maana yake ni "SOMA ULE".
Na ikiwa kiongozi kapata madaraka na hataki kupokea rushwa wala kutengeneza mirija ya ufisadi atapachikwa maneno ya kebehi kama anajifanya "Mnyerere", wakifananisha uzalendo wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Sasa Dr.Muganyizi alikuwa "Mnyerere" haswa, alikuwa hataki kutumia senti hata moja katika njia ya ubadhirifu.
Alikuwa hata akisafiri kikazi pesa za masurufu zote zinazobakia anazirudisha kwenye idara ya uhasibu. Tokea anafundisha Chuo Kikuu hakuwahi kufaulisha wanafunzi waliofeli, alikuwa tayari hata kama ni darasa zima wafeli mtihani wake lakini sio kuwapa alama za bure bure bila kutolea jasho.
Hii ilimfanya achukiwe na Wanachuo wasiopenda kujisomea walio wengi na apendwe na wanafunzi wachache wanaopenda kujituma kimasomo.
Siku aliyowaaga wanafunzi wake kuwa amepata kazi benki ya "ADB" baadhi ya wanachuo walifanya sherehe ya kufurahi kuondoka kwake. Walikesha usiku kucha wanacheza muziki na kunywa pombe kudhihirisha furaha yao ya kuondoka kwa mhadhiri wao mnoko.
Alivyokwenda Afrika Magharibi, moja ya miradi iliyompatia sifa ni ujenzi wa barabara ya juu kwa juu kuunganisha jiji la Dakar na mji wa Diamnadio. Mradi uliofadhiliwa na Benki ya Afrika kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dakar, Senegal. Alisimamia kwa umakini na uaminifu mkubwa mchakato wote wa kumtafuta mkandarasi bila ufisadi wowote.
Kabla mradi hujaanza kutekelezwa akahamishwa baada ya kunusurika kupigwa risasi zaidi ya mara mbili kutoka kwa majambazi waliotumwa na wakandarasi waliozoea kupata tenda kifisadi. Akahamishiwa kusini mwa jangwa la Sahara sasa akiwa kama Mkurugenzi na ofisi yake ikiwa Jijini Gaborone, Botswana.
Toka mwaka 2015 alikuwa anasafiri mara kwa mara kutoka Gaborone kuja Pemba, Msumbiji kwa ajili ya ujenzi wa barabara na bandari. Barabara ambayo itaunganisha miji ya Pemba, Montapuez, Vanduzi na Changare kwa kifupi "PEMOVACHA-PROJECT".
Ni mradi ambao asilimia tisini (90%) ya pesa zingetolewa na Benki ya Afrika (ADB) na asilimia kumi (10%) ya pesa zingetolewa na serikali ya Msumbiji kutoka kwenye makusanyo yake ya mapato ya ndani. Ulikuwa ni mradi wenye lengo la kuboresha miundombinu iliyoharibiwa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya serikali ya FRELIMO na waasi wa RENAMO.
Kutokana na umuhimu wa mradi na gharama za ujenzi kuwa kubwa ilibidi umakini mkubwa uhitajike hivyo Dr. Muganyizi akaamua kuhamishia makazi yake katika Mji mkuu wa Cabo-Delgrado, Pemba, ili kusimamia mchakato wa ujenzi kwa umakini na ukaribu zaidi.
Huo ukaribu katika ufuatiliaji akagundua madudu makubwa ya ufisadi yanayotaka kufanyika na watendaji wa serikali ya Msumbiji ambao sio waaminifu, wa kutaka kuipa tenda ya utengenezaji barabara hiyo kampuni ya "Monte Branco Ltd" ambayo haijawahi hata kutengeneza barabara sehemu yoyote ile Msumbiji.
Dr.Muganyizi akawa anakataa kuidhinisha kampuni hiyo ipewe tenda hiyo, msimamo uliomtia matatizoni, mpaka kuwekwa kwenye orodha ya wanaotakiwa kuonja kifo kutoka kwa Mafioso wa Alfredo.

Mkutano uliokuwa unatakiwa kufanyika kuanzia saa tatu chumba namba 03 pale Nautilus Hoteli ulichelewa kuanza kwa sababu mbili.
Kwanza ilikuwa ni kukatika kwa umeme kwa ghafla kusikotarajiwa, lakini jambo la pili ilikuwa ni taarifa ya mauaji ya James Penteleo mwana usalama ambaye alikuwa kwenye kikosi cha kudhibiti wimbi la wahamiaji kutoka Tanzania, ambaye alipewa jukumu la kuondosha uhai wa dereva Masebbo.
Taarifa hiyo ya mauaji toka kwa Inspekta Jenerali Mark Noble ilileta mshtuko na taharuki kubwa kwa vigogo hao. Hawakutegemea kama kuna mtu anayejipenda na kuuthamini uhai wake anaweza kujaribu kutia mkono wake kwenye mzinga wao wa nyuki, Mafioso uliojaa asali inayolindwa na nyuki wakali wanaokula maua ya bangi.
Ilipofika saa 4:00 usiku baada ya majadiliano ya hapa na pale ndipo kikao ndio kikao hicho kikaanza kwa kufunguliwa rasmi.
"Ndugu wajumbe wa kamati ya siri ya "Monte Branco Ltd" na washirika wetu waalikwa, tumeitana usiku huu kujadili mchakato wa utekelezaji wa ajenda zetu za kikao kilichopita. Ajenda ya kwanza ni kupokea ripoti ya utekelezaji wa zoezi la kuwafukuza Watanzania nchi Msumbiji hasa maeneo ya machimbo ya madini ya Montepuez na kuhakikisha biashara na njia zote kubwa za kiuchumi zinakuwa chini ya kampuni yetu ya "Monte Branco Ltd". Ripoti hii itawasilishwa na Inspekta Jenerali Mark Noble karibu sana....!", alimaliza kuzungumza mwakilishi wa mmiliki wa kampuni akimuwakilisha Bosi mkubwa Alfredo kwenye kikao hicho.
Muwakilishi huyo aliyekuwa amevalia kaunda suti ya kijivu akazima maiki yake na kukaa chini ya kiti chake. Inspekta Jenerali Mark, aliandaa hotuba yake kwa mtindo wa kugotoa bila kurefusha mazungumzo yasiyo na msingi asije kuwachosha vigogo wenzake ambao hawana muda wa kusikiliza porojo.
ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog