Search This Blog

Monday, 27 March 2023

HADI LINI - 1

 

IMEANDIKWA NA : BISHOP HILUKA

*******************************************

Simulizi : Hadi Lini

Sehemu Ya Kwanza (1)



Yalikuwa yamemfika kooni baada ya kuitafuta haki yake kila mahali na kushindikana, akafikia uamuzi wa kuwaita wazazi wa pande zote mbili ili aweke wazi kuhusu msimamo wake juu ya ndoa yake. Kama noma na iwe noma lakini asingeweza kuendelea kuvumilia, avumilie hadi lini? ...


JUMAMOSI, saa kumi na mbili na nusu jioni, kwa saa za Burundi, sauti tamu ya muziki laini wa kubembeleza ilikuwa inasikika kutoka katika spika zilizokuwa kwenye kona za ukumbi mkubwa wa kisasa wa burudani, ndani ya Hotel Club du Lac Tanganyika.


Club du Lac Tanganyika ilikuwa hoteli yenye hadhi kubwa iliyokuwa imejengwa kwenye mandhari ya kuvutia ya ufukwe wa Ziwa Tanganyika jijini Bujumbura, Burundi. Ilikuwa hoteli ya kisasa kabisa iliyokuwa imezungukwa na mazingira yenye utulivu mkubwa ufukweni mwa ziwa, ikiwa kando ya barabara ya Chausse d'Uvira iliyokuwa inaelekea katika mji mdogo wa Uvira.


Ikiwa imezungukwa na uzio madhubuti ulioifanya kuwa mahali patulivu zaidi na penye usalama wa uhakika, ilikuwa sehemu tulivu zaidi ya kwenda kujirusha kwa watu wenye ukwasi, ikiwa umbali wa kilomita tatu tu kutoka katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Bujumbura.


Pia ilikuwa sehemu muhimu sana kwa burudani na wageni wengi kutoka nje walipenda kwenda sehemu ile, hasa mwisho wa wiki, kutokana na kuwa na kumbi mbili za kisasa. Ukumbi mmoja ulitumika kwa ajili ya mikutano, ukiwa na sifa zote, na wenye viyoyozi na umeme wa uhakika saa 24, jambo linaloufanya kuvutia wageni mbalimbali. Ukumbi mwingine ulitumika zaidi kwa ajili ya burudani na matukio.


Ukumbi wa burudani ulikuwa na kila aina ya starehe, ukiwa na madirisha makubwa ya vioo yaliyofunikwa na mapazia safi marefu, na ulikuwa na kila kionjo cha daraja la kimataifa. Ndani ya ukumbi ule kulikuwa na wahudumu wazuri wa kike, warembo kwelikweli, waliokuwa wakihudumia wateja wachache waliokuwemo ukumbini muda huo wakiwa wameketi kwenye meza nzuri za mbao ya mti wa mninga na viti vifupi vyenye foronya laini.


Muda ule wa saa kumi na mbili na nusu za jioni idadi kubwa ya wateja waliokuwemo ndani ya ukumbi ule walikuwa raia wa kigeni, hasa kutoka katika nchi za Ufaransa na Marekani. Upande wa kulia wa ukumbi ule kulikuwa na mlango na dirisha dogo la jikoni, na humo ndani kulionekana wapishi waliokuwa katika mavazi yao ya kazi, wakiandaa chakula.


Katika ukumbi ule, mmoja wa wateja Waafrika walioonekana aliitwa Ibrahim Bigirimana, alikuwa mwanamume wa Kitanzania aliyekuwa na asili ya kutoka mkoa wa Kigoma, mkoa ambao uko pembezoni mwa nchi ya Tanzania katika mpaka wa Tanzania na Burundi.


Ibrahim Bigirimana alikuwa ameketi peke yake kwenye meza moja akionekana kuzama katika fikra fulani huku akiwa na shauku kubwa ya kusubiri kitu fulani muhimu sana, ambacho, ni yeye tu kati ya watu wote waliokuwemo mle ukumbini ndiye aliyekuwa akikijua.


Ibrahim alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kutupa macho yake kuangalia nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirisha, mkono wake mmoja alikuwa ameshika bilauri ndefu iliyokuwa na mvinyo mwekundu wa Kifaransa aina ya Navette de Marseille, na mkono wake wa kushoto alikuwa kauegemeza juu ya kiti alichokalia. Ibrahim akainua bilauri ya mvinyo na kupiga funda taratibu huku akionekana kuwaza mbali sana.


Alikuwa mwanamume mrefu na maji ya kunde, akiwa na sura bashasha ya kitoto iliyokuwa na muonekano uliomfanya mtu yeyote aliyemuona adhani kuwa hangeweza kuzidi miaka therathini, ingawa alishapita miaka hiyo. Akiwa na umri wa miaka arobaini na mbili, kimuonekano, Ibrahim alikuwa na umbo kakamavu la kimichezo lililofanana na maumbo ya wachezaji wa ligi ya mpira wa kikapu wa nchini Marekani.


Alikuwa mcheshi sana na mtu wa kupenda kujichanganya na watu wengine bila kujali kipato, alikuwa muongeaji mkubwa mwenye kuzimudu vyema lugha za Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na hata Kirundi, lugha iliyokuwa ikizungumzwa zaidi na wenyeji wa nchi ile ya Burundi, jambo ambalo liliwafanya watu wengi kudhani kuwa labda alikuwa Mrundi mwenzao, hasa kwa kuwa hata jina lake la mwisho la ‘Bigirimana’ ni jina lililokuwa linatumiwa na Warundi.


Ibrahim alikuwa Muha kutoka mkoani Kigoma, kabila lililokuwa na utamaduni ulioshabihiana kwa kiasi kikubwa sana na ule utamaduni wa Warundi. Ibrahim alikuwa ameishi jijini Bujumbura kwa takriban miaka kumi sasa. Na alikuwa akifanya kazi kama Meneja Mkuu wa CRDB Bank Burundi, benki iliyokuwa na makao yake katika barabara ya Chaussée du Prince Louis Rwagasore, ploti namba 490/A, jijini Bujumbura.


Kwa nafasi hiyo, Ibrahim alikuwa mtu mwenye mafanikio mema, ingawa alikuwa na kasoro moja iliyoonekana wazi, hakuwa na wala hakupenda kuwa na kitambi. Wengi walidhani labda Ibrahim alikuwa amebebwa hadi kufikia nafasi ile, lakaini ukweli hakufikia nafasi ya ile ya umeneja mkuu wa benki hiyo kwa bahati au kama wasemavyo Waswahili ‘zali la mentali’, bali alikuwa nazo sifa zinazostahili ikiwemo elimu ya juu na uzoefu wa kazi.


Kabla hajakuwa Meneja Mkuu wa CRDB Bank Burundi, ibrahimu alikuwa amefanya kazi kama Manager Corporate Banking na baadaye akawa Senior Relationship Manager Corporate Banking katika Benki ya Biashara ya Burundi (Commercial Bank of Burundi) iliyokuwa na makao yake katika makutano ya barabara za Avenue des USA na Chaussée P.L. Rwagasore, ikiwa mkabala na jengo la CRDB Bank Burundi, jijini Bujumbura.


Ibrahim alikuwa msomi wa Shahada ya Umahili ya Business Administration aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, ambacho kilikuwa chuo kikongwe zaidi katika ulimwengu wa nchi zinazozungumza lugha ya Kiingereza, na Shahada ya Kwanza ya Banking and Financial Services aliyohitimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.


Baada ya kumaliza chuo kikuu na kabla hajaenda kufanya kazi nchini Burundi, Ibrahim alikuwa amefanya kazi kaatika Benki Kuu ya Tanzania kwa miaka miwili kisha akaacha na kwenda kuishi jijini Bujumbura ambako aliajiriwa katika benki ya biashara ya Burundi. Hii ilitokana na yeye kuamua kumfuata mke wake aliyekuwa amerudishwa nchini Burundi baada ya kukumbwa na matatizo ya uraia alipokuwa akiishi nchini Tanzania.


Alipofika Burudni na kuajiriwa Commercial Bank of Burundi Ibrahim alifanya kazi kwa miaka kadhaa, na kutokana na uwezo wake na ufanisi kazini alichukuliwa na CRDB Bank Burundi, kama mwanzilishi na Meneja Mkuu wa benki hiyo jijini humo, nafasi ambayo aliweza kudumu nayo hadi wakati huo.


Huyo ndiyo Ibrahim Bigirimana, ambaye Jumamosi hiyo alikuwa katika ukumbi wa maraha wa Hotel Club Du Lac Tanganyika akiwa mwenye shauku kubwa. Alinyanyua bilauri yake na kunywa funda dogo la mvinyo kisha akaitazama saa yake ya mkononi kwa mara nyingine tena kisha akaonekana kutikisa kichwa chake.


Alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akisonya kwa huzuni, ni wazi alikuwa hapo akisubiria kitu muhimu sana lakini hadi muda ule alionekana kuanza kuishiwa na uvumilivu. Aliitazama tena saa yake na kuminya midomo yake akionekana kuwaza mbali, akabaki akiikodolea macho ile saa kana kwamba ilikuwa mbovu.


Laiti kama ingelikuwa saa ya kawaida labda angeweza kusema kuwa ilikuwa na kasoro, lakini hiyo saa kama ilivyo kwa vitu vyake vingi, haikuwa ya kawaida kabisa!




Ilikuwa saa ya bei ghali aina ya Rolex Submariner, iliyokuwa imemgharimu kiasi cha Dola laki mbili na nusu za Marekani! Si haba, zilikuwa fedha nyingi sana kama angeamua kuzibadilisha kwa pesa za Burundi au hata za Tanzania.

Ibrahim alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu, kisha akainua tena bilauri ya mvinyo na kupiga funda ndefu huku akionekana kusisimkwa mwili, kisha aliitua ile bilauri juu ya meza na kugeuka kutazama nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha dirishani, aliitazama mandhari tulivu ya kuvutia nje ya ukumbi ule kwa upande wa nyuma wa lile jengo la hoteli.

Kule nyuma zilionekana nyasi nzuri za rangi ya kijani kibichi zilizopakana na maua ya rangi tofauti ya kuvutia, na nyasi hizo zilikuwa zimepandwa kuzunguka bwawa kubwa la kuogelea ambalo kando yake kulikuwa na viti vingi vya kupumzikia kwa waogeleaji vyenye miamvuli mizuri ya kujikinga na miale ya jua.

Katika viti hivyo walionekana baadhi ya wazungu waliokuwa wameketi wakipunga upepo na wengine walikuwa wanaogelea huku wakiwa katika mavazi maalumu ya kuogelea. Kando ya bwawa lile la kuogelea kulikuwa na bustani nzuri ya miti yenye viti vya kupumzikia visivyohamishika katika mandhari tulivu.

Upande wa pili wa bustani ile kulikuwa na baa iliyokuwa kwenye mandhari nzuri yaliyovutia ya ufukwe wa Ziwa Tanganyika, naa muda ule watu kadhaa walikuwa wameketi ndani ya baa hiyo, na pembeni kabisa ya baa ile ulikuwepo uwanja wa tennis.

Muda ule ule Ibrahim alijikuta akiyahamisha macho yake kutoka kwenye uwanja wa tennis na kumtazama mwanadada mmoja mrembo aliyekuja na kusimama mbele ya meza yake huku tabasamu kabambe likivinjari usoni pake.

Alikuwa mwanadada mrembo hasa, aliyekuwa na nywele nyingi nyeusi za kibantu zisizotiwa dawa na hivyo kumfanya aonekane mzuri wa asili. Macho yake yalikuwa makubwa na meupe yaliyokuwa yamezungukwa na kope ndefu na nyeusi ambazo alikuwa amezitinda vizuri na kuzipaka rangi nyeusi ya wanja mwembamba na kuyafanya macho yale makubwa na meupe kupendeza zaidi.

Alikuwa na pua ndefu kama ya Kihabeshi, mdomo wake wa kike wenye kingo pana kiasi na lips zake laini za kike zzilikuwa imekolea vizuri rangi ya mdomo maarufu kama lipstick, na hivyo kuifanya sura yake nyembamba kiasi yenye pua ndefu izidi kupendeza. Mdomo wake ulikuwa umehifadhi meno meupe yaliyojipanga vizuri huku yakiachia kijiuwazi kidogo kwa mbele, yaani mwanya.

Yule mrembo kama angetabasamu angeacha vishimo vidogo mashavuni vilivyochomoza haraka na kuzisulubu vibaya hisia za mwanaume yeyote aliye rijali. Masikio yake madogo yasiyochusha alikuwa ameyatoga na kuyavalisha hereni kubwa za kitamaduni zenye umbo la mviringo.

Mrembo yule aliitwa Bélise Celéstine Gatete, alikuwa binti wa kabila la Kitutsi kutoka Burundi, ambaye alikuwa na umri wa miaka ishirini na nane.

Bélise alikuwa anafanya kazi katika mgahawa wa kisasa wa La Silhouette Café uliokuwa kando ya barabara ya Chaussée du Prince Louis Rwagasore, na alikuwa anaishi katika mojawapo ya nyumba za shirika la nyumba la Burundi zilizokuwa kando ya barabara ya Ave des Patriotes, nyuma ya uwanja wa mpira wa miguu wa Prince Rwegasore Stadium.

Bélise Celéstine Gatete alikuwa amevaa blauzi nyepesi ya rangi ya bluu bahari ya mikono mirefu iliyokuwa ikiyaonesha matiti yake yenye ukubwa wa wastani na chuchu nyeusi imara zilizosimama kikamilifu.

Chini alivaa sketi yake fupi ya rangi ya pinki iliyokuwa na miraba myeupe iliyoishia juu ya magoti yake na kuifichua vizuri hazina ya kupendeza yenye mvuto wa ajabu ya miguu na mapaja yake mang’avu yenye misuli imara ya rangi maridhawa ya kibantu. Bélise alikuwa na miguu mizuri iliyokuwa ikitazamika, na alivaa viatu vya ngozi vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio.

Sketi yake ilikuwa imenasa vyema kwenye tumbo lake lililokuwa dogo na flati na kiuno chake chembamba mithili ya dondora kilichokuwa kimeshikilia mzigo mkubwa wa makalio yake imara ambao ungeweza bila ya taabu yoyote kukondesha akaunti ya mwanaume yeyote awaye rijali.

Mkono wa kulia wa Bélise alikuwa amevaa saa ndogo nzuri ya kike aina ya Swatch, ambayo bei yake ilikuwa si haba, kwani ilikuwa inauzwa Pauni mia sita za Uingereza ambazo hazikuwa fedha ndogo endapo angeamua kuzibadilisha na kupewa fedha za Tanzania, kwani zilikuwa sawa na zaidi ya shilingi milioni moja na laki nane. Saa ile ilikuwa imetengenezwa kwa namna ya kupendeza na hivyo kuongeza ziada nyingine katika uzuri wa Bélise. Mkono mwingine wa kushoto alikuwa amevaa bangili nyingi za pembe.

Kwenye bega lake la kulia alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi nyeusi, ambao wengine walipenda kuuita ‘kipima joto’. Huo mkoba nao ulimfanya binti yule kuvutia zaidi na zaidi. Itoshe tu kusema kuwa Bélise alikuwa mwanadada mrembo kweli kweli!

Kwa nukta kadhaa moyo wa Ibrahim ulisahahu mapigo yake, na yalipoanza alivuta pumzi ndefu, akazishusha. Alimtazama, akajikuta akiuajabia uzuri wa mwanadada yule uliokuwa mbele ya macho yake, akabaki akiwa amekodoa macho yake akiwa hana cha kusema, na bila hata kutegemea alianza kuzama kwenye bahari ya mawazo, mawazo yaliyomrudisha nyuma siku tatu kabla ya siku ile, siku alipokutana na mrembo yule kwa mara ya kwanza…

______

Ilikuwa siku ya Jumatano Ibrahim akiwa amevaa suti maridadi ya rangi ya kijivu alikuwa kasimama nje ya mlango wa chumba cha lifti katika ghorofa ya kumi ya jengo moja refu lililokuwa katika makutano ya barabara za Ave De Luxembourg na Avenue de Gréce, jirani na ubalozi wa Ufaransa.

Jengo lile halikuwa mbali sana na uwanja maarufu wa mpira wa miguu wa Prince Rwegasore Stadium. Ibrahim alikuwa amekwenda kwenye lile jengo kumuona rafiki na mshirika mwenza kibiashara, Adolf Ndilingiye ambaye pia walisoma pamoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Walipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Adolf Ndilingiye alisomea Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Uchumi na Takwimu (B.A. in Economics and Statistics) na Ibrahim alisomea Shahada ya Kwanza ya Banking and Financial Services.

Adolf Ndilingiye alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi mwenza wa kampuni ya ushauri wa masuala ya kibiashara na kiuchumi iliyoitwa Fleur économique et Business Consulting Ltd au Flower Economic And Business Consulting Ltd kwa Kiingereza.

Baada ya maongezi marefu ya kibiashara Ibrahim aliagana na Adolf, akatoka na kusimama pale nje ya chumba cha lifti akiwa peke yake, na muda wote alikuwa akiitupia jicho saa yake ya mkononi akionekana kuwa na haraka kidogo. Mara wakafika wanaume wengine wawili na kujiunga naye.

Kile chumba cha lifti kilipofika pale na milango ya lifti kufunguka, Ibrahim na wale wanaume wawili waliingia ndani kisha wale wanaume walibonyeza nambari sita, Ibrahim akabonyeza herufi G. chumba kile cha lifti kikaanza kushuka chini taratibu na kilipofika katika ghorofa ya tisa kikasimama na milango ikajifungua.

Hapo wakamuona msichana aliyeitwa Bélise ambaye aliingia haraka ndani ya kile chumba cha lifti na mara milango ya kile chumba cha lifti ikajifunga. Bélise aliziangalia zile namba na kutulia pasipo kubonyeza namba yoyote wala kusema neno lolote.




Bélise alikuwa amevaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu na juu alivaa blauzi ya rangi nyekundu. Kichwani alikuwa amevaa kofia ya rangi ya bluu ya kapelo na miguuni alikuwa amevaa raba za rangi nyekundu. Begani alikuwa amening’iniza mkoba mzuri wa rangi ya bluu.

Lifti ilianza kushuka hadi ilipofika katika ghorofa ya sita ikasimama na milango ya lifti ukajifungua ukiwaruhusu wale wanaume wawili kushuka huku wakiwaacha Ibrahim na Bélise mle ndani. Milango ikajifunga na lifti ikaendelea kushuka huku wakiendelea kuwa kimya. Mara Ibrahim alijikuta akimtupia jicho yule msichana na kumuona akiitupia macho saa yake ya mkononi. Moyo ukampasuka!

“Oh Mungu wangu, ni binti mrembo hasa,” Ibrahim alijikuta akiwaza huku akimtazama yule msichana kwa makini.

Wakati wote tangu alipokuwa akija mbio hadi alipoingia ndani ya kile chumba cha lifti Ibrahim hakuwa amemchanganyia macho vizuri. Kwanza kwa sababu alikuwa ameshachoka na alitaka kuwahi mapema nyumbani akapumzike, na pili hakuwa na sababu yoyote ya kumtilia maanani yule msichana.

Kumbe alikosea sana! Msichana yule hakuwa wa kawaida kama alivyokuwa amedhani, na wala hakuwa mmoja wa wale wasichana aliozoea kupishana nao kwenye korido za mahoteli au mtaani wakijigonga gonga kwake au wale aliowaona wakijiuza kwenye madanguro!

“Hujambo bibie!” Ibrahim alimsalimia Bélise kana kwamba ndiyo alikuwa akimuona kwa mara ya kwanza.

“Sijambo,” Bélise alisema huku akigeuza uso wake nusu bila kumwangalia Ibrahim huku akionekana kuyakwepa macho ya Ibrahim baada ya kugundua kuwa alikuwa anamtazama usoni kwa makini

Ibrahim alimtazama kwa makini akijaribu kumchunguza na kugundua kuwa yule msichana alikwishamshtukia dhamira yake, kwani alikuwa anamtupia jicho laa wizi mara kwa mara kumtazama katika namna ambayo kwa kweli Ibrahim hakuweza kuielewa.

Alichogundua ni kuwa macho ya yule msichana yalijaa aibu na alikuwa hawezi kumtazama mwanamume usoni kwa sekunde tatu mfululizo bila kukwepesha macho yake na kutazama kando kwa jinsi alivyojaa haiba na aibu.

“Eh, ningependa…” Ibrahim alitaka kuongea lakini alikatizwa na mlio usio wa kawaida uliosikika mle ndani ya chumba cha lifti, kisha taa ndani ya kile chumba cha lifti zikazimika na lifti ikasimama ghafla. Mara kukatokea kiza totoro ndani ya kile chumba cha lifti.

“Mungu wangu… tunakufa!” Bélise alitoa yowe kwa sauti yake iliyoonesha kujaa hofu kubwa. Aliyakodoa macho yake kwenye kile kiza huku mapigo ya moyo wake yakibadili mwendo na kuanza kwenda kasi. Alishindwa kujizuia na kuamua kumg’ang’ania Ibrahim.

“Inaelekea tumekwama, usihofu sana, bibie!” Ibrahim alisema katika hali ya kumtoa hofu yule msichana mrembo. Alisema huku akizungusha mkono wake mmoja kwenye mabega ya Bélise na mkono wa pili ulikuwa unapapasa kwenye vibonyezo vilivyokuwa ndani ya kile chumba cha lifti.

Akabahatisha kuvipata na kubonyeza kitufe kimoja ambacho kilitoa mwanga hafifu. Kisha macho yake yalitua kwenye uso wenye hofu wa yule msichana mrembo aliyekuwa akitetemeka.

“Sasa tutafanyaje, kaka?” Bélise alimuuliza Ibrahim huku akiendelea kutetemeka kutokana na hofu kubwa aliyokuwa nayo.

“Hatuna la kufanya isipokuwa tusubiri tu, huenda msaada unakuja!” Ibrahim alimwambia kwa sauti tulivu huku akimkumbatia kwa upendo. Bélise akajitoa mikononi mwa Ibrahim na kumwangalia usoni kwa mshangao.

“Unasemaje! Utakuja vipi wakati sisi tumekwama humu ndani na hakuna anayejua? Tafadhali fanya jambo, fanya jambo!” Bélise alilalama kwa sauti laini ya kubembeleza huku machozi yakianza kumlenga lenga machoni.

Ibrahim aliachia tabasamu jepesi na kuanza kulegeza tai yake, kisha akavua koti lake na kuanza kufungua vifungo vya shati lake. Bélise alimtazama Ibrahim kwa mshangao kisha akaonekana kuhamaki.

“Unataka kufanya nini?” Bélise alimuuliza Ibrahim huku akimkazia macho kwa hofu.

“Unadhani nataka kufanya nini, huoni kama navua koti langu!” Ibrahim alimwambia huku akimtazaa kwa tabasamu.

“Ili ufanye nini?” Bélise aliuliza tena kwa hofu.

“Nipate afueni kidogo, kwani huoni kuwa joto linazidi kuwa kali!”

Bélise alimtazama Ibrahim kwa hofu akionekana kubabaika sana, hofu ilikuwa imemtawala zaidi.

“Tafadhali kaka, jaribu kufanya maarifa yoyote tutakufa humu!” Bélise alilalama kwa hofu huku akionekana kuanza kukata tamaa.

“Usijali, kimoja cha vibonyezo nilivyobonyeza ni cha tahadhari kwa hiyo wahusika wamekwishafahamu kuwa chumba hiki cha lifti kimekwama na kina watu ndani yake… usihofu tutatoka salama,” Ibrahim alimwambia Bélise kumtoa wasiwasi.

Bélise alifungua mkoba wake na kutoa leso laini, akajifuta jasho usoni lililoanza kumtoka kwa wingi. Ibrahim alimtupia jicho la matamanio, akatamani kumkumbatia na kumporomoshea mabusumfululizo. Mara akashtuka kumuona Bélise akianza kulia kilio cha kwikwi.

Kabla Ibrahim hajajua afanye nini mara wakasikia sauti za watu zilizokuwa zinasikika kwa mbali.

Ibrahim akamsogeza Bélise karibu yake na kumkumbatia kwa mikono yake yote miwili ikiwa mmoja ulikuwa umeshika koti, Bélise bila hiyari yake alijikuta akijilegeza na kujilaza kifuani kwa Ibrahim huku akikiegemeza kichwa chake juu ya kifua cha Ibrahim, lakini aliendelea kulia kilio cha kwikwi.

“Usilie, binti, tutaokolewa,” Ibrahim alimwambia Bélise huku akimpapasa kwa mahaba nyama zake za mgongo.

Kisha Ibrahim alipeleka vidole vyake vya mkono wa kulia kwenye mashavu ya Bélise na kuanza kupangusa machozi yaliyokuwa yakimtoka Bélise utadhani milizamu iliyopasuka. Wakiwa katika hali ile mara chumba kile chaa lifti kinaanza kutingishika na kuteremka chini taratibu kwa kusuasua.

Baada ya kuteremka kwa muda mara wakaona chuma kikipenyezwa katikati ya ile milango ya kile chumba cha lifti na kulazimisha kuitenganisha ile milango miwili ya chumba kile cha lifti.

Kazi ile ilifanywa kwa muda mfupi, na baada ya kupata upenyo, Ibrahim na Bélise walifanikiwa kutoka ndani ya kile chumba cha lifti huku Ibrahim akimtanguliza Bélise kutoka nje.

Ibrahim akiwa kashika koti mkononi, tai shingoni ikiwa imelegezwa na vifungo vya juu vya shati vimefunguliwa na kuachwa wazi alitoka na kumkuta Bélise akiwa kazungukwa na watu wakimpa pole huku wengine wakijitokeza kumsaidia Ibrahim, na baadhi yao, hasa wadada na wanaume wakware walionekana kuwaangalia Ibrahim na Bélise kwa hisia tofauti.

Ibrahim alimsogelea Bélise ambaye alikuwa bado ana hofu na ahakuamini kama alikuwa ametoka ndani ya kile chumba cha lifti salama, akamuuliza kwa sauti ya chini, “Sijui mwenzangu unaelekea wapi?”

“Kwa hali hii niliyo nayo, kwa vyovyote itabidi niende kwanza nyumbani,” Bélise alisema huku akijiangalia.

“Unao usafiri?” Ibrahim alimuuliza huku akimtulizia macho.

“Hapana, nitakodi teksi,” Bélise alimwambia huku akiyakwepa macho yake na kutazama kando.

“Usijali, mimi nina gari, niruhusu nikusindikize hadi nyumbani kwako iwapo hutajali,” Ibrahim alimwambia huku macho yake yakiwa hayabanduki usoni kwa Bélise.

“Sitajali kama sitakusumbua,” Bélise alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Oh hapana, siwezi kusumbuka kwa hilo,” Ibrahim alisema huku akiminya midomo yake.

“Basi nisindikize kwani najisikia kizunguzungu…” Bélise alisema huku akiminya macho yake kama aliyekuwa akihisi maumivu ya kichwa.

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog