Simulizi : Hadi Lini
Sehemu Ya Tatu (3)
Major Ferdinand Niyongabo akamruhusu Ibrahim aondoke na kuwapa ishara askari wengine waliokuwa wamesimama kwenye kile kizuizi kuondoa kile kizuizi. Askari hao walitii amri ya Major Ferdinand Niyongabo na kuondoa kile kizuizi cha barabarani na kumruhusu Ibrahim kupita.
“Ukipata tatizo njiani nipigie, maana si salama sana saa hizi!” Major Ferdinand Niyongabo alimwambia Ibrahim na kumwashiria kuwa anaweza kuondoka.
Ibrahim alikubali kwa kichwa huku akimshukuru, na muda huo huo akaingiza gia na kuliondoa gari lake akiifuata barabara ile ya Avenue de I'OUA iliyompeleka hadi kwenye mzunguko (roundabout) uliokuwa unaziunganisha barabara za Avenue de I'OUA, Boulevard Mwambutsa, RN 9 na Chaussée du Peuple Murundi. Akauzunguka ule mzunguko akiingia upande wa kulia kuifuata barabara ya Chaussée du Peuple Murundi iliyopita katika kituo cha mafuta cha Top One PC Station.
Barabara ile ya Chaussée du Peuple Murundi ilikuwa barabara iliyokuwa inakatisha katikati ya makazi ya watu na ofisi kadhaa na mbele kidogo Ibrahim akalivuka daraja la mto Ntahangwa, mto wenye urefu wa kilomita 10.75 uliokuwa unapeleka maji yake katika Ziwa Tanganyika, kisha mbele kidogo akalipita Kanisa la Pentekoste, lililokuwa upande wa kulia wa barabara ile.
Baada ya kulipita lile Kanisa la Pentekoste, mlevi mmoja aliyekuwa anatembea kando kando ya ile barabara ya Chaussée du Peuple Murundi alianza kuvuka ile barabara kuelekea upande wa pili wa barabara bila kutazama kama kuna gari lililokuwa likija, huku akiyumba.
Ibrahim alimuona yule mlevi na kuliyumbisha gari lake huku na huko ili kujaaribu kumkwepa. Sauti ya msuguano wa matairi kwenye lami kutokana na breki kali ilisikika na kumfanya yule mlevi kujikunja na kuruka kurudi alikokuwa ametoka huku akiwa kafumba macho yake. Pombe yote ilionekana kumtoka kichwani!
Ibrahim alimudu kumkwepa yule mlevi, na pasipo kusimama aliendelea mbele na kuanza kupunguza mwendo kisha akachepuka na kuingia upande wake wa kulia akiifuata barabara ya Avenue de I’Hopital, iliyokuwa inapita jirani na majengo ya hospitali maarufu ya Prince Régent Charles.
Prince Régent Charles Hopital ilikuwa moja ya hospitali tatu kubwa za umma jijini Bujumbura, ikiwa na hadhi ya hospitali ya wilaya. Mahali kulipokuwa na hospitali ile lilionekana kuwa eneo tulivu mno kwa muda ule wa usiku, ni ndege pekee waliokuwa wamejazana kwenye mti mmoja mkubwa ndio walioonekana kuendelea kulipa uhai anga lililotanda kwa mwanga hafifu uliokuwa unatokana na taa za nyumba kadhaa zilizopo jirani na eneo lile huku nyota za angani zikionekana kushindwa kufua dafu katika kuileta nuru.
Ibrahim alipunguza mwendo kisha akafunga breki na kuliegesha gari lake chini ya mti ule mmoja mkubwa ambao ulikuwa mita chache kutoka kwenye nyumba moja iliyokuwa kando ya barabara ile ya Avenue de I’Hopital.
Ibrahim alitulia akionekana kulichunguza lile eneo kwa makini huku akiitazama ile nyumba huku wasiwasi ukijionesha kwenye uso wake, alishusha pumzi na kutoa simu yake ya mkononi na kuanza kutafuta namba fulani haraka haraka, lakini kabla hajabofya namba yoyote ili kupiga, kijana mmoja mrefu alijitokeza haraka na kwenda moja kwa moja kwenye lile gari la Ibrahim.
Alisimama karibu na mlango wa gari wa dereva, kisha akampa ishara fulani Ibrahim kumuonesha kuwa kulikuwa na mtu ndani ya ile nyumba ambayo Ibrahim alikuwa akiitazama kwa wasiwasi.
Yule kijana ndiye aliyekuwa amempigia simu Ibrahim kumtaka awahi kuja kumfumania mtu aliyekuwa akiishi ndani ya ile nyumba, Jeanine Kanyameza ambaye alikuwa mpenzi wa Ibrahim. Ibrahim alikuwa amempangishia nyumba Jeanine na alikuwa akigharamia mahitaji yote ya mwanamke yule.
Jeanine alikuwa mwanamke wa miaka kati ya ishirini na nane na therathini na alikuwa na umbo kubwa la kuvutia. Alikuwa mweupe kwa asili, lakini pamoja na urembo ule wa asili bado alikuwa anajiongezea kwa mapambo mengine ya gharama yaliyomfanya kuvutia zaidi. Hakuwa mwanamke wa kumtizama mara moja tu ukamwacha kwani alikuwa anavutia sana kutokana na umbo lake lililokuwa mfano wa umbo la nyigu.
Jeanine na Ibrahim walikuwa wamefahamiana baada ya kukutana katika hospitali ya Prince Régent Charles, ambayo Jeanine alikuwa anafanya kazi ya uuguzi. Walifahamiana baada ya Ibrahim kwenda katika hospitalini ile kumjulia hali mfanyakazi mwenzake aliyekuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.
Jeanine ndiye aliyekuwa muuguzi wa zamu wa wodi ile aliyokuwa amelazwa yule mgonjwa na alijitoa kwa kila hali kumhudumia, jambo ambalo lilionesha kumvutia sana Ibrahim.
Kukutana kwao ndiyo ulikuwa mwanzo wa kufahamiana zaidi, kisha urafiki ukazaliwa na baada ya wiki chache wakawa wapenzi. Kilichofuata baada ya hapo lilikuwa penzi lililokua taratibu, na baada ya miezi michache Jeanine akawa nyumba ndogo rasmi ya Ibrahim na kuanza kupata huduma zote alizostahili kupewa mke.
Ibrahim alitokea kumpenda sana Jeanine na kumhudumia kwa kila kitu, ikafikia wakati akawa katika mchakato wa kutaka kumuoa ili awe mke wake wa pili, na hata ikibidi kumwacha mkewe ili aishi na Jeanine.
Kitu ambacho Ibrahim hakuwa akikifahamu ni kwamba, Jeanine alimhitaji Ibrahim kwa kuwa alitaka kumtumia kama chombo cha kumtoa kwenye maisha ya chini na kumpeleka hatua nyingine, lakini hakuwa mwanamke wa kutosheka na mwanamume mmoja.
Jambo ambalo Jeanine hakujua ni kwamba hakukuwa na siri duniani, taarifa zilimfikia Ibrahim ingawa Ibrahim hakutaka kuziamini kwa kuwa alikuwa akimpenda sana na kumwamini Jeanine. Hata hivyo, ilifika wakati Ibrahim aliamua kumuuliza Jeanine kuhusu taarifa zile lakini Jeanine ‘aliruka kimanga’ na kudai kuwa hizo zilikuwa njama za wabaya wake kutaka kumfitinisha naye.
Pamoja na kukataa lakini habari zile zilizidi kumuumiza sana Ibrahim na ndipo alipoamua kumtafuta mtu ambaye angekuwa mpelelezi maalumu wa kufuatilia nyendo za Jeanine na kumpa taarifa pindi angemuona akiingiza mwanamume mwingine ndani ya ile nyumba.
Alikuwa akimlipa pesa nyingi kwa ajili ya kufanya uchunguzi juu ya mwenendo wa Jeanine. Haikupita hata wiki, hatimaye Jeanine alikuwa kaingia kwenye ‘kumi na nane’ za Ibrahim, na sasa Ibrahim alikuwa amesimama nje ya ile nyumba ya Jeanine tayari kufanya fumanizi.
Ibrahim alishuka haraka kutoka kwenye gari lake na kuifuata ile nyumba huku akimwacha yule kijana aliyempa taarifa akiwa amesimama pale pale kwenye lile gari lake. Ibrahim alifika mbele ya ile nyumba na kushika kitasa cha mlango wa mbele, akakinyonga taratibu na mlango ukafunguka.
Aliusukuma ule mlango taratibu na kuingia ndani akiwa na wasiwasi kidogo kisha aliurudisha ule mlango nyuma yake taratibu na kutokea kwenye sebule nadhifu.
Taa ya pale sebuleni ilikuwa imezimwa na kuifanya ile sebule kuwa na mwanga hafifu sana, hasa kutokana na mwanga uliokuwa unapenya na kuangaza humo ndani kutoka kwenye taa za nje.
Ibrahim alisimama na kuzungusha macho yake akijaribu kulizoea giza la humo ndani, alitazama huku na huko akijaribu kusikiliza kwa makini na kuupimia utulivu wa humo ndani, huku sebule ile ikionekana kuwa tulivu mno na hakukuwa na sauti yoyote ya maongezi iliyokuwa inasikika mle ndani.
Ile sebule ilikuwa pana ikiwa na zulia zuri zuri la manyoya lililokuwa na mchanganyiko wa maua ya rangi nyeusi na nyeupe sakafuni na kulikuwa na seti moja ya makochi ya sofa yaliyokuwa yamepangiliwa vizuri upande wa kushoto wa sebule hiyo. Yale makochi yalikuwa yanatazamana na seti moja ya runinga bapa aina ya Sonny Blavia ya inchi 28 iliyokuwa imefungwa vizuri ukutani na kuunganishwa na decorder ya StarTimes yenye chaneli nyingi za kimataifa.
Upande huo huo wa kushoto wa ile sebule kwenye kona kulikuwa na meza fupi ya mapambo na jokofu kubwa. Katikati ya ile sebule kulikuwa na meza nzuri ya kioo na stuli ndogo nne zilizokuwa zimepangwa kuizunguka meza hiyo.
Ukutani kulikuwa na saa kubwa na kulikuwa na picha mbili kubwa, picha moja ilikuwa ikimuonesha mwanadada mrembo, Jeanine Kanyameza, akiwa amepozi kwa ajili ya picha katika siku ya kuhitimu mafunzo yake ya uuguzi. Picha ya pili ilikuwa inamuonesha Ibrahim akiwa kamkumbatia Jeanine katika picha aya pozi la kimahaba iliyokuwa imepigwa kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika.
Upande wa kulia wa ile sebule kulikuwa na ukumbi mdogo wa chakula wenye meza kubwa ya mninga ya chakula ya umbo la yai ambayo ilikuwa imezungukwa na viti sita vya mbao ya mninga vilivyokuwa na foronya laini. Jirani na ule ukumbi wa chakula kulikuwa na mlango uliokuwa unaelekea kwenye korido iliyoelekea kwenye milango mitatu. Milango miwili ikiwa upande wa kushoto na mlango mwingine ulikuwa upande wa kulia.
Mlango wa kwanza upande wa kushoto ulikuwa mlango wa kuingia kwenye maliwato ya pamoja, mlango wa pili ulielekea kwenye chumba cha kulala wageni, na mlango mwingine uliokuwepo upande wa kulia ulikuwa mlango wa chumba kikubwa chenye maliwato ndani (master bedroom).
Ibrahim alizungusha tena macho yake akitazama pale sebuleni kwa udadisi zaidi kisha alikunja uso wake. Akaanza kupiga hatua taratibu kuuendea mlango uliokuwa unaelekea kwenye korido iliyokwenda vyumbani.
Ibrahim alikwenda moja kwa moja hadi kwenye mlango wa upande wa kulia wa korido ile na kusimama mlangoni, alikishika kitasa cha ule mlango akitaka kuufungua lakini akasita na kusimama huku akisikiliza kwa makini.
Sauti ya kilio cha mwanamke aliyekuwa akilia kwa mahaba mazito ilikuwa inasikika kutokea mle chumbani huku ikiambatana na miguno ya ajabu ajabu ya mwanaume. Ibrahim alionekana kupandwa gadhabu, akashindwa kuvumilia na kumeza funda la mate kutowesha donge kubwa la hasira lililomnasa kooni.
Ibrahim alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu, akajishauri kwa kitambo kifupi akiwaza endapo afungue ule mlango au la, kisha akaonekana kushindwa kuvumilia na kukishika kile kitasa cha mlango kwa nguvu kisha akakinyonga huku akiusukuma ule mlango lakini haukufunguka.
Sauti za kilio na miguno ndani ya kile chumba zikanyamaza ghafla na kufuatiwa na sauti ya mwanamke iliyokuwa inauliza kwa hofu kutokea chumbani, “Nani?”
Kama mtu aliyepandwa na wazimu, Ibrahim akaanza kubamiza ule mlango kwa ghadhabu akitaka kuuvunja. Hasira sasa zilikuwa zimempanda kichwani kama mbogo aliyejeruhiwa, akarudi nyuma hatua kadhaa na kuurukia ule mlango kwa teke moja la nguvu, mlango ukasalimu amri na kufunguka, nguvu aliyokuwa ameitumia ilimtupa na kumwangusha kwa kishindo katikati ya kile chumba.
Mwanadada Jeanine Kanyameza alikuwa na mwanaume kitandani, wakakurupuka kutoka pale kitandani kwa hofu, Jeanine aliinuka na kupiga magoti juu ya kitanda kwa hofu, uso wake ulikuwa umejawa hofu, jasho lilikuwa linamtiririka na macho yake alikuwa kayatoa utadhani alimuona mtoa roho. Akapiga kelele kwa hofu.
Yule mwanamume aliyekuwa Jeanine kitandani alisimama wima bila kutingishika pembeni mwa kitanda kama aliyekuwa amepigiliwa misumali huku akiwa ameshikilia nguo zake mkononi, uso wakeulikuwa umejawa hofu. Wote wawili walikuwa watupu kama walivyozaliwa.
Mkono wa kushoto wa Jeanine uliokuwa umevikwa bangili za rangi ya dhahabu ulikuwa umekunjwa ukishikilia upande wa kanga ili kujaribu kujisitiri sehemu ya utupu wa mbele na eneo la kifuani, huku akiacha sehemu kubwa ya mwili wake kubaki tupu na hivyo kuonesha mapaja yake yaliyonawiri vizuri na kulidhirisha umbo lake lake la nyigu.
Nywele zake ndefu zilikuwa zimesukwa kwa mtindo wa rasta na kuning’inia hadi kwenye mabega yake na mkono wake wa kulia ulikuwa umekunjwa kwenye kiwiko na kuziba mdomo wake ambao ulikuwa umemdondoka kwa hofu ungedhani alikuwa amemuona ziraili mtoa roho.
Chumba kile cha Jeanine kilikuwa kikubwa na chenye nafasi ya kutosha. Upande wa kulia kulikuwa na kitanda kikubwa cha mbao chenye godoro la foronya laini na shuka za rangi ya bluu bahari. Mashuka juu ya kitanda yalikuwa yamevurugika kutokana na purukushani iliyokuwa imefanyika hapo kitandani. Sakafu ya kile chumba ilikuwa imefunikwa kwa zulia zuri la rangi ya kijivu lenye maua mekundu.
Upande wa kushoto wa kitanda kulikuwa na kabati zuri la nguo la ukutani lililokuwa pembeni ya dirisha kubwa ambalo lilifunikwa kwa mapazia marefu na mepesi yaliyokuwa yanaruhusu hewa safi kupenya na kuingia mle ndani.
Upande wa kulia wa kile chumba kulikuwa na meza ya vipodozi (dressing table) iliyokuwa na kioo kirefu cha kujitazama na aina mbalimbali za vipodozi vikiwa juu ya meza ile, na pembeni ya meza kulikuwa na mlango wa kuelekea kwenye chumba cha maliwato.
Ibrahim akiwa hayaamini macho yake, aliinuka kutoka pale sakafuni alipokuwa amedondoka huku akimkodolea macho yule mwanamume mgoni wake na kujiandaa kumvamia, lakini hakuwa amejua kilichokuwa kikiendelea kwenye mawazo ya yule mwanaume. Hivyo likatokea jambo la ghafla ambalo hakuwa amelitarajia, yule mwanaume alichomoka kwa kasi ya ajabu na kutimka kama mkizi huku akiwa ameshika nguo zake mkononi.
Wakati alipokuwa anatoka nduki alimpiga kikumbo Ibrahim ambaye alikuwa amesimama wima na kumwangusha chini, msukumo wa nguvu ukamtupa Ibrahim chini kwa mshindo mkubwa na kumfanya kugaragara pale sakafuni mithili ya mgonjwa mwenye kifafa.
Jeanine alipiga kelele ya hofu huku akiiachia kanga yake iliyodondoka sakafuni na kumwacha akiwa mtupu kabisa.
Ibrahim hakukubali kumwachia mgoni wake aondoke kirahisi, alijinyanyua haraka kutoka hapo sakafuni na kuchomoka kwa spidi kumfuata yule mwanamume kabla hajafanikiwa kutoka nje, na alipomfikia ndipo vita kuu kati ya Ibrahim na mgoni wake ilipoibuka.
Yule mwanamume alikuwa anakukuruka kushika kitasa cha mlango wa mbele wa nyumba ili afungune mlango lakini kabla hajaufungua, Ibrahim aliruka kama mkizi na kumkumba, wote wawili wakapiga mwereka sakafuni. Ibrahim akawahi kusimama huku hasira zikiwa zimempanda kichwani kama mbogo aliyejeruhiwa.
Yule mwanamume naye alisimama akiwa mtupu na kumtupia Ibrahim mapigo mawili ya kushtukiza ya ngumi kavu za tumbo, mapigo yale yalimkuta Ibrahim akiwa bado hajakaa sawa na kumpata kisawasawa, kaguna.
Yule mwanamume alirusha teke lililompata Ibrahim sawasawa kwenye kinena na kumrusha kisha kumtupa sakafuni huku akihisi maumivu makali yasiyoelezeka.
Yule mwanamume akiwa amepandwa na hasira alipanga kumfuata Ibrahim hapo hapo sakafuni ili amfundishe adabu na kumuonesha kilichomtoa kanga manyoya ya shingoni.
Ibrahim alimuona na kuinuka haraka kisha alijipanga tayari kwa mapambano akionekana kujihami zaidi kwa kufanya mashambulizi ya nguvu. Aliruka na kumvaa yule mwanamume, akampiga kichwa kikavu kinachompata barabara katikati ya macho na pua na kumvunja mshipa wa pua, pigo hilo likafanya yule mwanaume kupepesuka.
Damu zilianza kumtoka kwenye pua yake mfano wa mrija wa maji uliokatika. Yule mwanamume alijishika pua yake na kuiminya akijaribu kuzuia damu isiendelee kumtoka, na kabla hajakaa sawa Ibrahim alimrukia tena na kumkaba kabali ya nguvu iliyomfanya kukukuruka akitaka kujitoa kwenye ile kabala, lakini Ibrahim alizidisha kabali yake na kumfanya yule mwanamume kuanza kuishiwa nguvu.
Kuona vile Jeanine akaanza kupiga kelele kwa hofu akimsihi Ibrahim kumwaachia yule mwanamume, kelele hizo ziliwavuta watu wengi kutoka katika nyumba zilizokuwa jirani na hata wapiti njia, ambao walisogea katika eneo lile kushuhudia kilichokuwa kinaendelea. Ibrahim akiwa amepandwa na gadhabu alimbeba yule mgoni wake juu juu na kumtupa sakafuni kama vile alikuwa anabwaga mzigo.
Yule mwanamume alianguka na kuunguruma kwa maumivu makali kisha akatulia tuli kama mfu. Ibrahim alimtazama kwa hasira na kugeuka kuwatazama watu waliokuwa wamejazana kwenye madrisha na mlangoni kushuhudia ule mpambano, kisha akajiandaa kumkamata tena yule mwanamume ili kumpaa adhabu zaidi.
Bila kutegemea yule mwanaume alikurupuka na kumkumba Ibrahim, akamwangusha chini na kumwacha akigaragara, yeye akatoka nduki na kukimbilia nje kwenye giza akiwa mtupu.
Ibrahim alijiinua kutoka pale sakafuni alipoangushwa huku akiwa ana hasira, akageuka kumtazama Jeanine huku donge la hasira likiwa limemkaba kooni. Jeanine alimtazama kwa hofu huku akitokwa na machozi. Ibrahim aliendelea kumtazama kwa hasira kwa kitambo kisha akamnyooshea kidole. Jeanine alikuwa anatetemeka kwa hofu huku akiwa amekunjia mikono yake kifuani kaatika hali ya kuomba msamaha.
“Nisamehe mpenzi, sitarudia tena,” Jeanine alisema huku akigeuka kuwatazama watu waliokuwa wamejazama kwenye madirisha wakishuhudia kila hatua ya ule ugomvi mle ndani.
Alikuwa anaona haya lakini hakuwa na namna nyingine ya kufanya ila kujikaza kisabuni na kuendelea kumbembeleza Ibrahim ili apewe nafasi nyingine.
“Nikusamehe! Si nilikuuliza ukakataa, msamaha upi unautaka malaya mkubwa!” Ibrahim alimfokea Jeanine kwa hasira huku akimsukuma.
“Nisamehe mume wangu!” Jeanine alisema huku akianguka na kupiga magoti kwenye sakafu miguuni kwa Ibrahim. Hata hivyo, kauli ya kumwita Ibrahim mume wake ikaonekana kuzidisha hasira za Ibrahim.
“Nani mume wako, kafilie mbali!” Ibrahim alimwambia Jeanine na kumsukuma Jeanine, kisha aligeuka na kuanza kupiga hatua akielekea nje ya ile nyumba.
Jeanine alijua wazi kuwa alikuwa amelikoroga kweli kweli, uchungu ulimpanda na donge la hasira ya kumpoteza Ibrahim likamkaba shingoni. Alijiuliza angempata wapi tena mwanamume kama yule aliyekuwa msaada mkubwa kwake na kwa familia yake?
Alisimama huku mikono ikiwa kichwani, akaanza kujihisi kujidhulumu kitu kikubwa na cha thamani na kuona kuwa alikuwa anastahili adhabu hiyo kali. Alitamani amkimbilie Ibrahim na kuanguka miguuni kwake kumwomba radhi na ikibidi kugaragara.
Sasa akili yake ilianza kwenda kasi, alianza kujiuliza ni shetani gani aliyekuwa amemwingia hadi kujikuta akishindwa kutosheka na mwanamume mmoja? Ni shetani gani aliyempitia kiasi cha kujikuta akitamani kila mwanaume anayekutana naye? Akahisi kizunguzungu.
Kama mtoto mdogo Jeanine aliketi na kujikunyata kisha akaanza kulia kwa uchungu mkubwa pasipo kujali watu waliokuwa wakimtazama kwa mshangao na wengine kwa huruma. Taratibu wale watu waliokuwa wamesimama akishuhudia lile tukio wakaanza kuondoka huku wengi wakimuonea huruma na wengine wakimcheka kuwa alikuwa “amejitakia” mwenyewe. Wachache hawakuficha dhihaka yao kwake, kwani walikuwa wanacheka hadharani.
Ibrahim alipotoka mle ndani alifika kwenye gari lake na kuliondoa kwa kasi ya ajabu akiwa na hasira kisha akaifuata barabara ya Avenue de I’Hopital hadi kwenye makutano ya barabara za Avenue de I’Hopital, Avenue Foreami, Avenue de la Tanzanie na Avenue du Stade, akakata na kuingia kushoto akiifuata barabara ya Avenue du Stade.
Hapo akaongeza tena kasi na kulipita soko maarufu la Congolese Market lililokuwa kushoto kwake na mbele kidogo aliyapita majengo ya Bujumbura Apartments Services.
Haraka alipunguza mwendo wa gari lake baada ya kuwaona wanajeshi wawili wa doria wakijitokeza mbele yake na kusimama katikati ya ile barabara ya Avenue du Stade huku wakimuonesha ishara kwa mkono kuwa asimame. Alipowatazama vizuri akaona kuwa mikono yao ilikuwa imekamata vyema bunduki aina ya SMG.
Eneo lile lilikuwa tulivu sana lililokuwa jirani kabisa na Uwanja mkubwa wa Golf ambao ulikuwa umezungukwa na sehemu nzuri zenye viti visivyohamishika vya kupumzika vilivyokuwa chini ya miti mikubwa na mirefu ya vivuli na kuyafanya mandhari yake kupendeza sana.
Wakati akipunguza zaidi mwendo na kujiandaa kusimama mara akawaona askari wengine wawili wakijitokeza na kujongea katikati ya ile barabara kisha wakasimama nyuma ya kizuizi kilichokuwa katikaati ya ile barabarani huku nao wakiwa wameshika vyema bunduki zao mikononi.
Ibrahim alisimamisha gari lake kando kando ya ile barabara ya Avenue du Stade, akatazama vizuri eneo lile huku roho ikimdunda kwa nguvu na kugundua kuwa mbele yake kwenye kile kizuizi cha barabarani kulikuwa na magari mengine mawili yaliyokuwa yamesimamishwa kando ya barabara yakipekuliwa na askari wengine wa doria.
Ibrahim aliitazama saa yake ya mkononi na kugundua kuwa ilikuwa imeshatimu saa tano usiku, akashusha pumzi na kutulia ndani ya gari lake akiamua kubaki ndani ya gari lile, kisha akashusha kioo cha dirishani kwake huku akijiandaa kutengeneza tabasamu la kirafiki pindi askari mmoja alipomfikia.
Askari wawili walimsogelea huku wakimnyooshea mtutu wa bunduki, kisha wakalizingira lile gari. Askari mmoja aliyekuwa na cheo cha Inspekta, Medico Nzitunga alikwenda moja kwa moja pale dirishani, akamtazama Ibrahim na kumtambua mara moja, kisha akaachia tabasamu la kirafiki.
“Oh, Bosi… kumbe ni wewe?” Inspekta Medico Nzitunga alisema kwa furaha huku akinyoosha mkono wake kumsalimia Ibrahim.
Ibrahim hakujibu neno bali alinyoosha mkono wake kumpa yule askari huku akibetua kichwa chake. Donge la hasira za kumfumania mwanamke aliyekuwa anampenda lilikuwa bado limemkaba kooni. Muda huo huo askari wengine walisogea pale kwenye gari la Ibrahim kama ambao walikuwa wanalichunguza kwa makini, lakini Inspekta Medico Nzitunga aliwampa ishara ya kumuacha Ibrahim kisha akamuashiria Ibrahim kwa kichwa kuwa aendelee na safari yake.
Ibrahim aliachia tabasamu la kirafiki na kumpungia mkono Inspekta Medico Nzitunga katika namna ya kumuaga kisha akatia moto gari lake na kuliondoka kutoka eneo lile akiwaacha wale askari wanaendelea na ukaguzi wa magari mengine.
Ibrahim aliendesha kwa kasi na baada ya dakika chache alikata kushoto akaingia katika barabara pana ya kisasa iliyokuwa na sifa zote sawa na zile barabara nyingine za kisasa za jiji lile la Bujumbura, barabara ya Boulevard du 1er Novembre. Barabara hii ilikuwa inapakana na makazi ya kisasa yenye nyumba nyingi za ghorofa na ofisi chache zenye nidhamu kiuchumi.
Ibrahim aliendelea kuendesha kwa mwendo wa kasi huku akipishana na magari machache muda ule huku akiwa bado ana donge la hasira na kuufikia mzunguko wa barabara za Chaussée P.L. Rwagasore, Chaussée du Peuple Murundi na Avenue de la Revolution, akaifuata barabara ya Chaussée P.L. Rwagasore huku akilivuka jengo la Ofisi za Taifa za Utalii Burundi (Office National du Tourisme du Burundi).
Hapo akapishana na kundi la askari kama sita wa serikali waliokuwa wakielekea kule alikouwa akitoka, hakusimama bali aliendelea mbele na kuvuka majengo mengine marefu ya ghorofa yenye ofisi za kisasa za watu binafsi na ofisi za mashirika mbalimbali ya serikali ya Burundi.
Kisha akaupita mgahawa maarufu wa La Silhouette Café uliokuwa kando ya barabara ile ya Chaussée P.L. Rwagasore, Ibrahim aliutazama kwa makini na kumkumbuka Bélise. Kisha akasonga mbele na kuuvuka mgahawa mwingine wa Tropicana Net Café ambao pia ulikuwa kando ya barabara ile ya Chaussée P.L. Rwagasore upande wa kulia na kushoto kwake kulikuwa na barabara ya Rue de la Victoire.
Ibrahim aliongeza mwendo huku akiipita barabara ya Bvd. Patrice Lumumba kisha mbele kidogo akayakuta makutano ya barabara za Chaussée P.L. Rwagasore na Avenue Du Commerce.
Akataka kuingia Avenue Du Commerce lakini akasita na kuendelea mbele huku akikosa kumgonga mtu mmoja aliyekuwa akitembea kando ya ile barabara, kisha akaanza kuyapita majumba ya kifahari yaliyokuwa yamezungukwa na miti mirefu na kuta zenye usalama wa uhakika katika barabara ile tulivu ya Chaussée P.L. Rwagasore.
Eneo lile lote lilikuwa eneo ambalo limezungukwa na makazi ya kisasa kabisa ya viongozi wa kitaifa na wa kimataifa walioishi jijini Bujumbura. Vitongoji vyake vilikuwa vimeunganishwa kwa barabara nzuri za lami zenye taa za barabarani.
Ibrahim akaanza kupunguza mwendo huku akiwa na mawazo mengi, alianza kuendesha taratibu katika ile barabara ya Chaussée du Prince Louis Rwagasore iliyokuwa tulivu mno huku ikimulikwa na taa nzuri zenye mwanga mkali. Mtaa ule ulikuwa kimya sana katika nyakati zile za usiku, isipokuwa sauti kali za mbwa waliokuwa wanabweka katika nyumba za jirani kwa mbali.
Ibrahim akazidi kupunguza mwendo huku akiyavuka makutano ya barabara za Chaussée du Prince Louis Rwagasore na Avenue de L'Enseignemen. Kuanzia pale, hakwenda mbali sana mara akaifikia anaifikia nyumba nzuri ya kifahari iliyokuwa imezungukwa na miti mizuri ya vivuli na sehemu za wazi zenye bustani nzuri ya maua na nyasi za kijani kibichi zilizokatwa vizuri.
Ukuta wa ile nyumba kuizunguka ulikuwa mrefu uliokuwa umefungwa mfumo maalumu wa umeme wa kuzuia wezi juu yake usiomwezesha mtu kuona ndani. Ilikuwa moja ya majumba makubwa ya kisasa ya watu wakwasi yaliyokuwa yamezungushwa uzio na mageti makubwa yenye vifaa vyote vya usalama vya kuwahakikishia wakazi wake usalama wa hali ya juu.
Hapo ndipo ambapo Ibrahim alikuwa akiishia akiwa amepangishiwa na benki ya CRDB Burundi. Ibrahim alifika mbele ya geti kubwa jeusi la nyumba ile na kupiga honi mara mbili. Mlango mdogo wa geti ukafunguliwa kidogo, kisha mlinzi mmoja kutoka kampuni ya ulinzi ya KK Security Burundi ya jijini Bujumbura akatoa kichwa chake kuchungulia nje na kumuona Ibrahim.
Akaachia tabasamu na kulifunga lile geti dogo, kisha akalifungua lile geti kubwa na kuliruhusu gari la Ibrahim kuingia ndani ya ule uzio wa nyumba. Ibrahim aliliingiza gari lake ndani ya ule uzio wa nyumba na kuliegesha sehemu maalumu ya maegesho ya magari, jirani na gari jingine aina ya Landcruiser GX V8 lililokuwa na rangi nyeusi.
Baada ya kuunguruma kwa kitambo fulani Ibrahim alilizima gari lake na kuteremka kisha akachukua ile briefcase yake na simu zake mbili na kushika mkononi. Akafunga vizuri milango ya lile gari na kutupa macho yake kuangalia huku na huko. Mara mbwa mkubwa aina ya Rottweiler akamkimbilia na kumrukia huku akirusharusha mkia wake mfupi.
Ibrahim alampungia mkono yule mlinzi wa getini, mlinzi naye akapunga mkono huku akiwa kasimama kikakamavu kwenye kibanda maalumu cha mlinzi ambacho kilikuwa kimejengwa kando ya lile geti kubwa la nyumba hiyo. Kisha Ibrahim akaanza kupiga hatua zake kuelekea ndani ya ile nyumba huku akipiga mluzi kwa kujiamini zaidi.
Yule mlinzi wa getini alimtazama Ibrahim kwa wasiwasi mkubwa, kama aliyekuwa akijishauri akaanza kunyoosha mkono wake akitaka kumwita Ibrahim ili amwambie jambo lakini akasita na kushusha pumzi huku akitingisha kichwa chake kwa masikitiko.
Ibrahim aliendelea kupiga hatu zake taratibu pasipo kuelewa kile kilichokuwa kinaendelea kwenye mawazo ya yule mlinzi na kuisogea baraza ya nyumba yake ambayo ilikuwa kubwa ya kisasa, katika ile nyumba ya ghorofa moja.
Nyumba hiyo ilikuwa na madirisha makubwa ya kisasa na baraza kubwa mbele yake iliyopangwa seti moja ya makochi ya sofa. Nje ya ile nyumba upande wa kushoto kulikuwa na banda la wazi la kuegeshea magari.
Sehemu nyingine ya mandhari ya ile nyumba ilikuwa imezungukwa na miti mirefu na mikubwa ya kivuli, huku sehemu ya mbele ya ile nyumba ikiwa imezungukwa na bustani nzuri ya maua ya kupendeza na katikati ya bustani hiyo kulikuwa kumetengenezwa njia nzuri ya kutembea kwa miguu kwa vitofali vidogo vilivyokuwa vinavutia.
Kwa upande wa kulia wa ile nyumba kulikuwa na bwawa kubwa la kuogelea lililokuwa limezungukwa na vitanda vizuri vya kujipumzisha chini ya miamvuli mikubwa ya kivuli. Nyuma ya nyumba ile kulikuwa na tenki kubwa la maji na kando yake kulikuwa na karo kubwa la kuoshea vyombo na kufulia.
Ibrahim aliifikia ile baraza ya nyumba hiyo na kuacha kupiga mluzi, badala yake akaanza kuimba kwa sauti ya kawaida wimbo ule ule ambao mwanzoni aliuimba kwa kupiga mluzi, tena aliimba kwa kujiamini mno. Alikuwa akiimba kibwagizo kutoka katika wimbo wa Les Mangelepa, “Utakuja nitafuta mashariki na magharibi, utakujalia aah, kisha mama usinione… utaliaa, utalia aah, usionionee…”
Aliendelea kuimba maneno yale huku akikung’uta viatu vyake kwenye zulia dogo lililokuwepo pale mlangoni kwa kupigapiga miguu yake, kisha akashika kitasa cha mlango na kukinyonga, akausukuma ule mlango ambao ulisalimu amri na kufunguka.
Ibrahim alisimama pale akishangaa ilikuwaje hadi muda ule ule mlango wa nyumba ulikuwa haujafungwa kwa funguo? Aliinua mkono wake na kuitazama saa yake ya mkononi, ikamuonesha kuwa ilikuwa imeshatimia saa tano na dakika therathini na tano za usiku!
“Hii si kawaida!” Ibrahim aliwaza huku akikunja sura yake kwa hasira. Aliona kuwa alikuwa amepata sababu ya kumgombeza mkewe, hivyo alitulia kidogo pale barazani huku akiyatembeza macho yake kuangalia mazingira ya ile nyumba.
Yule mbwa mkubwa alikuwa bado anamfuata na kumrukia. Ibrahim alimfukuza yule mbwa na kuingia ndani huku akiendelea kuimba wimbo kwa kujiamini zaidi, akatokea kwenye sebule kubwa yenye samani zote muhimu za kisasa.
Ile sebule ilikuwa imepambwa kwa seti mbili za makochi ya sofa ya kifahari yaliyokuwa yamepangwa katika mtindo wa kuizunguka. Sakafuni kulikuwa na zulia zuri la rangi nyekundu huku katikati ya ile sebule kukiwa na meza nzuri ya kioo iliyokuwa na umbo la yai ikizungukwa na stuli ndogo nne za sofa.
Upande wa kulia wa ile sebule kwenye kona kulikuwa na runinga pana aina ya Samsung iliyofungwa ukutani na chini yake kulikuwa na meza fupi nyeusi yenye sistimu ya muziki, decorder na deki moja ya Dvd.
Ukutani kulikuwa na picha mbalimbali zilizokuwa zinamuonesha Ibrahim akiwa na familia yake, na picha zingine za kuchorwa zilizokuwa zinavutia sana. Upande wa kushoto wa ile sebule kwenye kona nyingine kulikuwa na meza fupi ya mapambo na jokofu. Pembeni ya meza ile kulikuwa na rafu kubwa iliyopangwa vitabu na majarida mengi na juu ya rafu hiyo kulikuwa na vinyago vya Kiafrika vilivyopangwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Upande wa kushoto kulikuwa na ngazi zilizokuwa zinaelekea juu na upande mwingine kulikuwa na ukumbi mdogo wa chakula wenye meza kubwa ya chakula yenye umbo la yai iliyozungukwa na viti sita nadhifu vyenye foronya laini. Jirani na ule ukumbi wa chakula kulikuwa na mlango mwingine upande wa nyuma wa ile sebule uliokuwa unaelekea kwenye vyumba viwili vya chini vya ile nyumba.
Ibrahim alishtuka sana na kusimama ghafla, aliacha kuimba na kubaki mdomo wazi huku macho yake yakimtoka pima kwa mduwao. Akili yake ilikuwa kama iliyopigwa shoti kali ya umeme hatari wenye nguvu nyingi, na hivyo kuzifanya shughuli za mwili wake kusimama kwa ghafla kama aliyekuwa amepigwa kumbo na ugonjwa hatari wa kiharusi.
Alibaki amesimama pale pale jirani na mlango akiwa ameduwaa, kilichokuwa kimemshtua sana ni kuona ugeni mzito ndani ya nyumba yake ambao hakuwa ameutarajia kabisa na wala hakuelezwa kama wangefika siku ile. Alipatwa na hisia mbaya kuwa kwa vyovyote ugeni ule haukuwa umekuja pale kwa ajili ya kusalimia, bali kulikuwa na jambo zito lililokuwa limetokea!
Ibrahim akawaza haraka haraka huku akiwa ametahayari sana. Aliwakodolea macho wazazi wake na wazazi wa mke wake ambao walikuwa wameketi kwenye makochi ya sofa huku wakimtazama kwa makini.
Ibrahim alishtuka sana na kusimama ghafla, aliacha kuimba na kubaki mdomo wazi huku macho yake yakimtoka pima kwa mduwao. Akili yake ilikuwa kama iliyopigwa shoti kali ya umeme hatari wenye nguvu nyingi, na hivyo kuzifanya shughuli za mwili wake kusimama kwa ghafla kama aliyekuwa amepigwa kumbo na ugonjwa hatari wa kiharusi.
Alibaki amesimama pale pale jirani na mlango akiwa ameduwaa, kilichokuwa kimemshtua sana ni kuona ugeni mzito ndani ya nyumba yake ambao hakuwa ameutarajia kabisa na wala hakuelezwa kama wangefika siku ile. Alipatwa na hisia mbaya kuwa kwa vyovyote ugeni ule haukuwa umekuja pale kwa ajili ya kusalimia, bali kulikuwa na jambo zito lililokuwa limetokea!
Ibrahim akawaza haraka haraka huku akiwa ametahayari sana. Aliwakodolea macho wazazi wake na wazazi wa mke wake ambao walikuwa wameketi kwenye makochi ya sofa huku wakimtazama kwa makini.
ENDELEA...
Baba yake, Mzee Hussein Bigirimana alikuwa ameketi kwenye sofa kubwa, aliinua mkono wake na kutazama saa yake ya mkononi kisha akainua uso wake na kumkazia macho Ibrahim yaliyokuwa na maswali lukuki, pembeni yake alikuwa ameketi mke wake, Mama Mariam Bigirimana, wote walikuwa wakimtazama Ibrahim kwa makini.
Ibrahim aliwakodolea macho na kuhisi kijasho chembamba kikimtoka mwilini. Akafungua mdomo wake kutaka kusema neno lakini maneno hayakutoka, mdomo wake ulimdondoka kwa hofu utadhani alikuwa amezingirwa na wanamgambo wa al-Shabab waliokuwa tayari kujilipua wakati wowote.
Ibrahim akayahamisha macho yake kutoka kwa wazazi wake hadi kwa wazazi wa mke wake, Mzee Diomede Tugiramahoro na Mama Ninziza Bernice, ambao walikuwa wameketi kwenye sofa jingine kubwa, nao pia walikuwa wanamwangalia Ibrahim kwa makini.
Ibrahim akaona kama vile macho yote yaliyokuwa yakimwangalia pale sebuleni yalikuwa yanamsuta, akavuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani na kuzishusha taratibu huku akijipa ujasiri, akalazimisha tabasamu na kuyahamisha macho yake kutoka kwa wakwe zake hadi kwa watoto wake wawili, Nduwimana, mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 10, na Samantha, mtoto wa kike aliyekuwa na umri wa miaka 7.
Nduwimana na Samantha walikuwa wameketi kwenye meza kubwa ya chakula, nao walikuwa wakimtazmana baba yao kwa wasiwasi.
Ibrahim akaangalia saa yake ya mkononi na kuwatupia tena jicho wazazi, akalazimisha tabasamu huku akijaribu kujiamini zaidi. Aliwasalimia wazazi wake na wazazi wa mke wake kwa unyenyekevu. Na wote bila hiyana waliitikia salamu yake huku wakiendelea kumtazama kwa makini.
Ibrahim akapiga hatua kuwasogelea watoto wake Nduwimana na Samantha huku akiwaangalia kwa upole.
“Nyinyi, mbona hamjalala mpaka saa hizi saa tano na ushee? Kalaleni tafadhali,” Ibrahim alisema huku akiwashika kichwani kwa upole. Kisha aligeuka kuwatazama tena wazazi wake haraka haraka na kuanza kuziendea ngazi za kuelekea juu ya ile nyumba, lakini kabla hajaanza kupanda zile ngazi Mzee Bigirimana akawahi kumsemesha.
“Bwana mdogo, ukipumzika kidogo nina mazungumzo na wewe,” Mzee Bigirimana alisema huku akijiweka sawa pale kwenye sofa alipokuwa ameketi.
“Mazungumzo usiku huu!” Ibrahim alimuuliza baba yake kwa mshangao huku akiitazama saa yake ya mkononi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment