Search This Blog

Thursday 23 March 2023

CABO' DELGADO - 5

  

Simulizi : Cabo' Delgado


Sehemu Ya : Tano (5)


Dr.Anabella ashikie hiyo nafasi.
Alimdanganya hiyo ni kambi ya serikali ya Msumbiji kitengo cha Usalama wa Taifa, hivyo asikatae hayo majukumu na iwe ni siri yake akitoa anaweza kuupoteza hata uhai. Waswahili walisema 'mla kunde husahau ila mtupa maganda hawezi kusahau', Mark alishasahau kuwa Dr.Anabella anawajua NACATANAS ambao waliteketeza baadhi ya wanakijiji, na sare za kambi zilikuwa na maandishi yenye maneno hayo.
Tahadhari waliyokuwa wanaichukua ni kumfunga kitambaa cha usoni mpaka ndani ya kambi kisha wanamfungua ili asijue kambi ipo eneo gani. Lakini siku ya kwanza kuwaona wale watesaji wakuu wamevaa zile fulana nyeusi zimeandikwa NACATANAS akajua hawa ndio wahalifu wake aliokuwa anawatuhumu kwa mauaji ya familia yake na baadhi ya wanakijiji.
Mwanzoni alikuwa anasindikizwa na baradhuli mpaka selo wakati wa kutoa huduma, walipomzoea Dr.Anabella hasa walipojua ni mchumba wa Bosi wao Mark Noble wakaanza kumuamini na kuvunja miiko ya kazi, wakawa wanamuacha aingie peke yake kwa masharti asichelewe kutoka. Wao wanakuwa kwenye sehemu yao ya mapumziko wanakunywa pombe kali na kufurahia starehe. Hilo likawa ni kosa la mwaka kwao, ambalo hawakujua kuwa watakuja kujutia milele.
Kuna siku walipopelekwa kuhojiwa akina Koplo Hamduni, aliyewarudisha selo alifuatana na Dr.Anabella akiwa na pombe yake mkononi, alipokuwa ameshughulishwa na kuwadhibiti akina Koplo Hamduni, Dr.Anabella alifanikiwa kuchanganya vidonge aina ya “Amoxapine” kwenye pombe ya baradhuli yule mlevi buda.
"Amoxapine" ni vidonge vinavyotumika kumrudishia mtu uchangamfu akiwa hana furaha sasa vikichanganywa na pombe vinasababisha usingizi uje kwa haraka. Baradhuli alipokunywa tu akapatwa na usingizi mzito, hapo Dr. Anabella akafanikiwa kuongea na Koplo Hamduni kinagaubaga sababu za kukamatwa kwao. Koplo akamueleza kwa ufupi maana Koplo alikuwa na maumivu makali anaongea kwa shida na Dr.Anabella alijua muda sio mrefu watafuatwa wakiona wanachelewa kurudi.
Hivyo Dr.Anabella pindi alivyokamatwa Kachero Manu, alipatwa na hisia ni washirika wa Koplo Hamduni, ndio maana akamuambia ile siku ya kwanza kazinduka kutoka kuzimia alimuambia kwa NACATANAS watakufuata kukuhoji ili kumpa fununu juu ya watu waliomteka. Ili kama hawajui ila ameshawahi kusikia habari zao apate kutanabahi.
Nafasi ya mwisho ya dhahabu aliyoitumia Dr.Anabella ni kujaribu kuwakutanisha kati ya Koplo Hamduni na Kachero Manu. Alipewa amri Dr.Anabella awachome sindano za sumu Koplo Hamduni na wenzake wakiwa wamefungiwa kwenye majeneza, huku Koplo Hamduni akiwa amefungwa kitandani.
Wale mabaradhuli walikuwa wanamuogopa sana Koplo Hamduni huenda akifungiwa kwenye jeneza anaweza kujitoa kutokana na ukakamavu wake alioonyesha wakati wanamtia mbaroni. Alichofanya Dr.Anabella ni kumchoma Koplo Hamduni sindamu ya sumu chini ya dozi inayotakiwa, ili Koplo Hamduni na Kachero Manu waweze kukutana, na dhana yake njema alijua wakikutana watabadilishana taarifa za kipelelezi, huku akiombea mabaradhuli watakaomleta Kachero Manu selo kubwa wasiwe makini kuchunguza kama Koplo Hamduni na wenzake wamekufa au bado wapo hai.
Lengo la Dr. Anabella lilifanikiwa, Kachero Manu na koplo Hamduni walikutana na kuongea maongezi yaliyokuwa na tija sana kwa Kachero Manu kwa kumpa mwangaza halisi wa upelelezi wake.


SURA YA KUMI NA TANO
Kachero Manu bado hali tete
Kachero Manu usiku ule baada ya maongezi na marehemu Koplo Hamduni, alipigwa na baridi kali hasa ukichukulia alikuwa hajavishwa nguo yoyote mwilini mwake. Akafanikiwa kusota mpaka jirani na jeneza moja akaliegemea ikamsaidia kupunguza joto.
Akapatwa na usingizi mzuri sana uliosaidia kupumzisha mwili wake kiasi fulani. Aliamshwa toka usingizini na mionzi ya jua iliyokuwa inapenya kwenye vidirisha vidogo vya mule chumbani. Akakisia huenda ikawa ni saa mbili na nusu au saa tatu kasoro asubuhi. Sasa akawa ametimiza siku nzima kamili ndani ya selo kuu.
Akaanza kuhisi njaa kali inatafuna utumbo wake, mpaka akaanza kutetemeka kwa njaa. Baada ya kupita kama nusu saa akasikia nyayo za watu zinakaribia mlango wa ile selo kuu alipofungiwa.
Likafunguliwa lango kuu wakaingia watu kama 7 pamoja na Dr. Anabella akiwemo. Walipoingia hawakumsemesha chochote wengine wakashughulishwa na kutoa nje majeneza ambayo sasa yalikuwa na maiti zilizofia ndani yake, na mmoja wao akaenda kwenye kitanda alichofia Koplo Hamduni akamfungua kamba zake na kuiburuta maiti yake nje ya chumba, kitendo ambacho kilimfanya Kachero Manu amuangalie Dr.Anabella kwa umakini akamuona kwa mbali machozi yanamlenga lenga alivyokuwa anaangalia maiti ya Koplo Hamduni. Ila usingeweza kugundua kwa haraka kwa sababu alikuwa amevaa miwani.
Dhamira ya Dr.Anabella ilikuwa inamsuta kwa kufanya mauaji ya Koplo Hamduni kutokana na sindano ya sumu aliyomchoma. Katika maisha yake yote alikuwa hajawahi kuua kiumbe chochote zaidi ya kuua mbu wa Malaria, hata kuua mende alikuwa anaogopa hivi leo baradhuli Mark amempelekea mpaka kuua binadamu wenzake.
Baada kama ya nusu saa wakaondoka na kufunga mlango wa geti la selo. Kachero Manu akazidi kuchanganyikiwa akawa anajiuliza, "hawa watu ni binadamu kweli au ni roboti? Hata chembe ya utu mbona hawana. Wamenichukua toka jana hawajali hata kama nina njaa au hapana". Alikuwa hajawahi hata siku moja maishani mwake kukata tamaa ya kuokoka lakini alianza kuhisi hatopata njia ya kutoroka ndani ya selo hiyo.
Na Dr.Anabella aliyeanza kuwa na matumaini nae kuwa huenda akamukoa nae hakuona kama ana msaada wowote. Maana hata kumuongelesha kuhusu namna ya kutoroka hajawahi. Wala hajawahi kuonyesha ishara yoyote kuwa wapo pamoja kama alivyosimuliwa na Koplo Hamduni.
Akaanza kuiona kurunzi ya mule chumbani kama inaanza kufifia kutokana na kuanza kuishiwa kwa mafuta ya taa. Baada ya kupita kama saa moja kwa kukadiria ni kama saa nne asubuhi akaanza kusikia tena michakato ya miguu ya watu wanakuja tena kwenye selo yake. Ila idadi yao kwa makadirio ilionyesha ni wachache sio kama wale wa mwanzoni, akaanza kufufua matumaini ya kuokoka.
Wale watu walipofika wakafungua lango la selo na kuingia ndani. Alikuwa ni tena Dr.Anabella tena na vijana wa kundi hatari la NACATANAS wapatao wawili. Mmoja alikuwa amebeba trei ya chakula, ilikuwa ni supu ya nyama, matandu meusi ya wali yale ya juu na mkate wa boflo mmoja. Huku mwingine amebeba bunduki aina ya SMG begani hana hata chembe la tabasamu utasema malaika wa motoni kwa jinsi alivyokunja ndita usoni.
Dr.Anabella alikuwa amevaa shingoni mwake kifaa cha kupimia mapigo ya moyo huku koti lake jeupe mifuko yake ikionekana imetuna tuna. Yule aliyebeba trei la chakula akaenda mpaka kwenye meza chakavu iliyokuwa na kurunzi ya mafuta ya taa inayosaidia kueneza mwanga katika selo yenye mwanga khafifu, akaweka trei mezani kisha akamfuata Kachero Manu kumfungua kamba zake za mikononi pekee, kisha akamletea chakula ale.
"Usijaribu kuleta ujanja wowote, jaribio lolote utakalofanya litagharimu uhai wao, kula ujisosomole kuondosha njaa yako" alisema yule baradhuli aliyebeba SMG huku akiwa amemuelekezea Kachero Manu mdomo wa bunduki. Dr.Anabella akawa nae kaisogelea meza ile chakavu akatoa baadhi ya chupa za madawa, mkasi na pamba akaweka juu ya meza kisha akaegemea meza anamuangalia Kachero Manu anavyopokea chakula.


Usijaribu kuleta ujanja wowote, jaribio lolote utakalofanya litagharimu uhai wao, kula ujisosomole kuondosha njaa yako" alisema yule baradhuli aliyebeba SMG huku akiwa amemuelekezea Kachero Manu mdomo wa bunduki. Dr.Anabella akawa nae kaisogelea meza ile chakavu akatoa baadhi ya chupa za madawa, mkasi na pamba akaweka juu ya meza kisha akaegemea meza anamuangalia Kachero Manu anavyopokea chakula.
Kwa njaa aliyokuwa nayo, aliuchovya ule mkate wa Boflo wote kwenye supu kisha akaula kama uji, kisha akaanza kuokoteza marapu rapu ya nyama akichanganya na matandu akawa anakula. Nyama ambayo harufu yake inaonyesha kama imekaa muda mrefu kwenye friza ambalo lilikuwa halifati kanuni za uhifadhi kwa kufunguliwa ovyo mara kwa mara hivyo kusababisha nyama kuanza kupoteza ubora wake. Kwa njaa aliyokuwa nayo Kachero hata kama ungempa nyama iliyotupwa jalalani wiki moja angekula, kisha akakombelezea mchuzi wa supu na kuiacha sahani ya matandu na bakuli la supu likiwa halina hata chembe ya mabaki ya chakula zaidi ya mifupa michache.
Baada ya kumaliza mlo wake akaomba apelekwe chooni. Choo kilikuwa upande mkabala na meza aliyoegemea Dr.Anabella, akasindikizwa huku ameshika bega la yule mbeba chakula huku anaruka ruka katika kutembea kama mtu mwenye mguu mmoja huku baradhuli aliyebeba bunduki anawafuatia kwa nyuma kwa umakini mkubwa bila kupepesa macho kama mpambe wa Rais anavyokuwa makini.
Kilikuwa ni choo ambacho hakifai kwa matumizi ya binadamu. Tundu la choo cha sinki lilikuwa limeziba na kusababisha uchafu wa haja za wanaotumia kuelea juu juu, huku mikojo ikiwa imetiririka kila kona. Sakafu yake ilikuwa imesakafiwa na marumaru nyeupe ila kutokana na ukoko wa uchafu zilikuwa mithili ya sakafu ya rangi njano na kijani kutokana na kuunguzwa na chumvi chumvi ya madini ya urea inayotoka kwenye mikojo ya binadamu. Huku inzi wenye ukubwa kama nyuki walikuwa wanasheherekea rundo la uchavu katika tundu la choo.
Ila hilo halikumshtua Kachero Manu kwani huwa Makomandoo wanapitia mazingira magumu ya kukujengea ujasiri zaidi. Alishawahi kusimama kwenye shimo la kubeba uchafu wa choo muda wa siku mbili huku uchafu umefika mpaka kifuani mwako. Hivyo kwa choo hicho kwake kilikuwa ni kama choo cha Ikulu kwa upande wake akilinganisha na mazito aliyopitia.
Wakati anarudishwa toka chooni, alitupia jicho mezani na kufanikiwa kuona miongoni mwa baadhi ya chupa za dawa. Aliona kuna spiriti, na chupa zinginezo ambazo hazifahamu. Alikuwa anajaribu kuangalia labda kuna kitu kitakachomsaidia, kama ujuavyo "mfa maji haachi kutapatapa". Alipotulia sakafuni, akafungwa tena kamba za mikononi, kwa ustadi mkubwa zaidi mpaka akahisi damu haipiti vizuri. Baada ya harakati hizo akaitwa Dr.Anabella ili ampe huduma ya kwanza. Akaja akamsafisha vidonda vyake na kumpaka dawa kisha akamchoma sindano ya kupunguza maumivu. Baada ya kumpa huduma ya kwanza akabeba vifaa vyake akaelekea usawa wa lango la kutokea akamuona anatupa vitu kama takataka kwenye pipa dogo la takataka. Baada ya hapo akageuka kumuangalia Kachero Manu kisha akamkonyeza ukope kwa jicho legevu la mahaba na kutabasamu, halafu akaongoza njia ya kutoka. Kitendo hicho cha kukonyezwa kilimfanya asisimukwe mwili na kuanza kuwaza mambo mengi sana.
"Ina maana huyu Dr.Anabella amenizimia kimapenzi ameamua kuelezea hisia zake kwangu kwa ishara mpaka ananilegezea jicho kiasi kile na kunikonyeza" mawazo machafu yalipata katika fikra zake. Akaanza kujiuliza tena nafsini mwake "ametupa takataka gani mule mpaka akaamua anigeukie, anikonyeze na kutabasamu".
Wale mabaradhuli wawili wakashika uelekeo wa kutoka nje ya selo kuu wakimfuata Dr.Anabella. Walipofika mlango wakati wengine wameshatoka, akageuka nyuma yule aliyebeba bunduki akamuangalia Kachero Manu kisha akampayukia "Leo ndio siku yako ya mwisho kuishi duniani, usiku huu utakuja kuchukuliwa ukawaone hao unaowatafuta kabla hujatolewa roho yako, kwaheri ya kuonana wasalimie huko akhera ukienda" akabamiza geti na kuanza kufunga lango lako na kufuli na kwenda zao.
Kwa makadirio Kachero Manu akajua inaweza kuwa ni saa sita mchana, hivyo apumzishe mwili kisha aanze kuwaza njia za kutoroka vinginevyo wakija mara ingine ni kwenda kupelekwa kufa mbele ya vigogo wa Monte Branco Ltd.
Akaegemea ubavu mmoja huku uso wake unaitizama kurunzi ya karabai ambayo kioo chake kina nyufa za mpasuko. Ni kurunzi ambayo daima haizimwi kutokana na giza la ndani ya selo ile. Kachero Manu akapitiwa na usingizi mdogo wa mchana, akisubiri miujiza ya kuokoka.

Anasakwa Kachero Manu na Komandoo mstaafu 'JS'.
Wakati anapewa maagizo ya kwenda Jimboni Cabo-Delgado, Msumbiji Kachero Manu aliambiwa akiwasili salama awasiliane na Komandoo mstaafu wa Msumbiji Bwana Jacob Steven (JS), mmoja wa makomandoo watano bora katika bara la Afrika. Kachero Manu alitii maagizo ya Mkuu wake wa kazi, hakuleta ujuaji, alifanya nae mawasiliano kupitia wavuti.
Huyo ndiye yule aliyemsaidia Kachero Manu kupata nyumba Montepuez na kukodishiwa gari aina ya Volvo s60 anayoitumia kwenye misafara yake mbalimbali ya hapa na pale. Kampuni ya kukodisha magari ya "PAPADIOT". Kampuni ambayo magari yake yote yamefungwa mfumo wa kufuatilia wapi lilipo (car tracker) ili kuchunga usalama wa gari na mtumiaji.
Hivyo kitendo cha gari alilokodishwa Komandoo Jacob Steven (JS) kuonekana limeegeshwa pembezoni mwa ukumbi wa maonyesho kwa zaidi ya saa 12 bila kutembea kiliwapa mashaka. PAPADIOT wakaamua kumpa taarifa Bwana Jacob Steven (JS).
Alipofuatilia ndipo akalikuta gari kwenye maegesho. Akafanikiwa kufungua ndani akahisi yumkini Kachero Manu atakuwa matatizoni, kwa sababu alikuta zana za kazi zimefichwa ndani ya gari kwenye makanyagio ya miguu ya dereva.
Kwa utundu wake wa kipelelezi na kutoa mlungula au chauchau kwa mfanyakazi wa ukumbi wa maonyesho ilipoegeshwa gari anayedhibiti CCTV-Camera, akafanikiwa kumuona Kachero Manu namna anavyoegesha gari na kutokomea mtaani usiku wa manane akielekea upande wa "Pemba Magic Lodge". Akafanya mbinu tena kutoa chauchau kwa mdhibiti wa "CCTV-Camera" wa Pemba Magic Lodge, hapa hakufanikiwa kitu aliwekewa ngumu, waliogopa rungu la Mafioso wa Alfredo litawashukia wakigundua kuwa wao ndio wameuza mechi. akatengeneza mbinu ya pili ya kudukua "CCTV-Camera" ya nyumba hiyo ya kulaza wageni. Akatengeneza utundu wa njia tano kwa kutumia vifaa maalumu, kitaalamu vinaitwa "DVRs" na "IP" Camera, kisha akazielekeza kwenye mtandao wa wazi (open internet) hapo ndipo alipofanikiwa kuona tukio zima namna alivyotekwa Kachero Manu na gari lililotumika kumteka.
Haya mafunzo ya kudukua nyaraka za siri, mitandao na "Camera" kama "CCTV Camera" kwa Komandoo mzoefu kama yeye ni kitu cha nusu saa tu. Hapo sasa ikabaki kufuatilia hilo gari lililomteka limeelekea nae wapi.
Ilimchukua masaa kama mawili ya upelelezi na kulikuta gari hilo limeegeshwa kwenye kiwanda cha korosho kinachomilikiwa na kampuni ya Monte Branco Ltd anapofanyia kazi Dr.Anabella. Lengo lake halikuwa kumpata mmiliki ila ilikuwa ni kumpata kachero Manu yupo wapi tena akiwa hai.
Akatumia akili za kuzaliwa kwa kuchukua sampuli za vumbi la mbele ya gari chini ya boneti kijasusi bila kujulikana kisha akatuma sampuli kwenye maabara ya vijidudu inayoitwa "MICROCHEM" iliyopo nchini Afrika ya Kusini kutambua vijidudu wanaopatikana kwenye udongo uliokutwa kwenye gari ni wa maeneo gani. Ili iwe rahisi kujua wapi gari lililomteka Kachero Manu lilitembelea kwa mara ya mwisho.
Baada ya kupita saa 10 majibu kutoka "MICROCHEM" yakaanikwa hadharani. Yakaonyesha wadudu waliopatikana kwenye sampuli ya vumbi la gari wapo kwa wingi mbugani, na yakaonyesha gari inaweza kuwa ilikwenda maeneo ya Gorongosa.
Komandoo Jacob Steven (JS) ilipotimu saa kumi alasiri, saa 3 kabla ya Kachero Manu kuja kunyakuliwa mafichoni kwa ajili ya kupelekwa mbele ya mkutano wa Mafioso wa biashara ya rubi, akawa nae anaelekea kwenye kampuni ya helikopta ya kukodi. Lengo lilikuwa aweze kwenda maeneo ya Gorongosa maana asingeweza kwenda na gari akafika mapema kutokana na umbali huo.
Lakini bado Komandoo JS alikuwa kwenye kizungumkuti, hafahamu ni wapi atampata kijana wake. Ila akajipa moyo bahati itaangukia kwake. Akajisemea mwenyewe nafsini mwake "daima Mwenyezi Mungu huupigania upande wa wenye haki, na shetani husaidia upande wa waovu, maandiko ya dini ndivyo yanavyofundisha".


Akakaa kitambo kifupi akifikiria mbinu nyingine ya kufanya, akaamua aanze kuvingirika kuelekea kwenye pipa la takataka. Matarajio yake huko yalikuwa huenda akakuta mkasi umetupwa ili ukiwepo aubane kwenye meno kisha autumie kukatia kamba ya mikononi. Akajipa matumaini atapata kifaa cha kujifungua.
"Kwa namna Dr.Anabella alivyokuwa anatupa kitu kwenye pipa, alivyoniangalia sana ile ni ishara kuna kitu cha kuniokoa aliniwekea" mawazo chanya yalipita kwenye fikra zake. Akaanza kujisogeza huku jasho linamtiririka mwilini kama maji kutokana na joto la mule selo.
Alipokuwa yupo karibu na nusu kufikia kwenye pipa la taka, ghafla akasikia vishindo vya mabaradhuli wanakuja selo kuu, hapo hapo akaanza kukata tamaa ya kutoroka akajua amekwisha wanakuja kumchukua. "Lakini mbona mapema sana wanakuja kunichukua kulikoni!" aliwaza sana Kachero Manu. Akaanza kusali sala maarufu kwa Wakatoliki, ya Baba yetu wa mbinguni akijua hapa tena hana ujanja alishakubali shingo upande kushindwa na maadui zake. Wakati amefunga macho yako yuko katika hisia nzito ghafla lango likafunguliwa wakaingia mabaradhuli wawili wapya ambao hawafahamu wakiwa wamembeba mzobe mzobe mtu mmoja.
Alikuwa ni shaibu wa makamo hakosi miaka 55 kwenda juu ukimkadiria. Alikuwa kirambi cha mtu, mfupi kama mbirikimo ana tumbo kubwa ambalo linatokana na ulaji mbovu wa vyakula na uvivu wa mazoezi na kujisaidia haja kubwa mara kwa mara. Cha kusikitisha huyu Mzee alikuwa yupo uchi wa mnyama analia kwa sauti mbaya kama ya punda kilongwe wa majumbani. Alitoa kilio mpaka sauti yake ikampwelea kabisa.
Walipoingia wale mabaradhuli hawakumjali kabisa Kachero Manu ambaye alijikunyata na kujifanya tongo hajui chochote kinachoendelea. Wakamfunga juu kwa juu yule Mzee kama nyama ya mbuzi wa ndafu anayesubiri kuliwa na maharusi. Mzee wa watu ukawa inamtoka mikojo ya uoga mfululizo utasema anaumwa ugonjwa wa kisukari hawezi kujizuia mkojo, au anaumwa ugonjwa unaoitwa nasuri uwapatao akina mama waliotoboka tundu la mkojo maarufu mtaani kama fisitula.
Kumbe kihoro chake ni cha uoga wa kifo cha kishenzi na cha kidhalili ugenini. Kachero Manu akawa anajichekea kimoyo moyo kuwa huyu Mzee atakuwa yupo ndani ya kumi bora ya watu waoga duniani. Kisha walivyomfunga wakamuacha anabembea huku kichwa kinaning'inia halafu wakafunga mlango na kuondoka. Mzee uso wake ulivimba vimba kidogo ulikuwa na manundu, inaonyesha alikuwa kuna kitu anakaidi kutekeleza wakamnasa mambata ya haja ya usoni. Na mdomo wa chini ulipasuka kidogo ukawa unamwaga damu.
Kachero Manu akavuta taswira ya huyu Mzee, akili yake ikamwambia kuwa anamfahamu vilivyo tena anamjua sana na ni mtu maarufu ila tu kupondeka kwa sura yake ikawa sura inaingia na kuondoka. Mwishowe Kachero Manu akaanza kuangua kicheko cha sauti kubwa na dharau mpaka Mzee wa watu akaanza kuogopa kuwa huenda kaletwa gereza la vichaa.
"Kumbe ni Mzee Andenga Kazimoto, kaletwa selo kuu, kazi ipo mwaka huu" alijiwazia baada ya kumtambua. Waswahili walisema "shukrani ya punda ni mateke. Amekipata alichokitafuta kwa mafia Alfredo. Inaonyesha Alfredo kaona hana umuhimu wa kuingia kwenye kikao wakati nyaraka wameshazipata" akazidi kuwaza Kachero Manu.
Kweli tamaa ilimuua fisi, 'kakosa mwana na maji ya moto'. Maana kwa Cheo cha huyu Mzee Andenga, alikuwa amebakiza miaka michache ya kustaafu angepata kiinua mgongo na pensheni nzuri tu ya kula na familia yake mpaka mwisho wa uhai wake.
"Komandoo Mstaafu uso kwa uso na NACATANAS"
Komandoo mstaafu Jacob Steven (JS) alipofanikiwa kugundua gari lililowapeleka akina Kachero Manu 'Gorongosa Camp', akaenda moja kwa moja kwenye kampuni ya helikopta ya kukodisha ili aelekee Gongorosa kumkomboa kijana wake.
Masaa matatu tu ya kufa au kupona yalikuwa yamebaki kabla ya Kachero Manu kuletwa kiwanda cha Korosho cha Monte Branco Ltd. Ilitakiwa komandoo 'JS' atumie 'kipawa cha liwa kutibu harara', afanye vyovyote iwavyo amnasue kijana wake. Kama angekwenda na gari asingeweza kufika wakati muafaka wa kuweza kumuokoa.
Umbali wa kutoka Pemba mpaka Gongorosa ni kama kutoka Dar esalaam mpaka Mbeya kwenda na kurudi. Eneo la Gongorosa lipo jimbo la kati la Sofala zaidi ya kilometa 1635.
Bahati nzuri akapata nafasi kwenye helikopta hiyo ya kukodi inayoelekea "Gongorosa National Park" (GNP) inayopeleka watalii mbugani. Mpaka saa 11 jioni akawa ameshawasili Gongorosa. Sasa kilichokuwa kinachomsumbua kichwani mwake ni kufahamu Kachero Manu kafichwa wapi?. Maana ni sawa na mwenyeji wako akuambie nipo Dar es salaam, lakini Sinza, Manzese, Mbagala, Kawe, Goba, Mbezi, Rehema, Masaki zote ni Dar es Salaam. Lakini bado hata ukifahamu ni Sinza bado Sinza ni kubwa sana, Kwa Remmy, Kumekucha, Palestina, Madukani, Shekilango bado vyote hivyo ni vitongoji vya Sinza.
Akaumiza kichwa akapata jawabu ni kuuliza wapi kuna Ukumbi wa starehe maarufu kuliko zote, huko ndio atapata majibu. Maana haiwezekani viongozi wa Gorongosa Camp wanaolipwa pesa nzuri sana washindwe kustarehe. Tabia za watu majambazi na maharamia ni kustarehe sana, ndio maana pesa wanazopata hazina fidi. Ukitaka kumsaka mtu swalihina basi ni kwenye nyumba ya ibada, lakini mtu fedhuli pesa zake huwa zinaishia kwenye pombe, muziki na kustarehe na vidosho.
Akauliza uliza kwa wenyeji klabu za fauka kwa starehe, wengi wao walimtajia kiwanja cha kisasa cha kujivinjari ukiwa Gongorosa kinaitwa "Montebelo Pub". Akafanikiwa kufika "Montebelo Pub" anayasoma mazingira.
Ilikuwa ni "Pub" yenye kuvutia kimazingira, ilijengwa ikajengeka vilivyo. Geti la kuingilia lilipambwa na bango kubwa lenye maandishi makubwa lililoandikwa jina la "Montebelo Pub". Kisha ilizungukwa na fensi fupi ya ukuta iliyopandwa miti iliyoshonana kuzunguka ukuta wote. Kwa ndani kulikuwa na midule mingi mingi iliyozungukwa ukumbi mzima kwa umbo la duara huku katikati kukiwa na ukumbi wa wazi uliozibwa kwa paa la makuti yanayotokana na mti wa mnazi.
Pia kulikuwa na wahudumu ambao ni wasichana wabichi na vipusa ambao wengi wao wapo katika rika la kufanana la kuanzia miaka 20 mpaka 25 wakiwa wamevalia mavazi yao ya sare za minisketi zenye kuacha sehemu kubwa ya mapaja yao nje nje bila kufunikwa vizuri, juu wana fulana nyeupe zilizowabana na kuzichongoa vilivyo chuchu zao konzi.
Alipoingia alikuta nje kuna magari mengi ya kifahari yameegeshwa kwenye maegesho kuonyesha kuwa ni "Pub" ya watu wazito wa Mji. Alipofika akachagua meza iliyokaribu na ukumbi wa kutumbuizia akavuta kiti na kukaa. Maana kulikuwa na "LIVE BAND" kutoka kwenye bendi maarufu ya "DJAAKA BAND".
Hiyo ni bendi ya muziki ya vijana wa Jimboni hapo hapo la Sofala. Bendi hiyo iliwahi kushinda tuzo ya "Crossroads in Southern Africa mwaka 2001. Watu walijaa pomoni kuja kuwaona vijana wao wakiwa wamerudi toka ziara za kimuziki nchi za ng'ambo za Uholanzi na Denmark ambapo walikuwa wamekaa huko zaidi ya mwezi mmoja huko Ughaibuni.
Alipotulia kwenye kiti akaja dada mmoja mrefu kavalia sare ambazo zilikuwa zinamtambulisha kuwa ni mhudumu wa hapo akiwa ameshika karatasi ngumu ya "MENU za aina na bei za vyakula na vinywaji" alipofika karibu na Komandoo mstaafu akamsalimia kwa unyenyekevu kisha akamkaribisha na kumpa Komandoo Jacob Steven (JS) ile karatasi ya orodha ya vinywaji na vyakula.
Komandoo akaipokea na kuisoma kimya kimya kisha akamwambia mhudumu "Naomba uniletee "Limoncello" ya baridi sana na maji ya moto ya kuzimulia tafadhali" alisisitiza Komandoo Jacob.
"Limoncello" kilikuwa ni kinywaji kimachotengenezwa kwa kutumia ndimu. Asili yake kinywaji hiki ni Italia ya kusini. Yule mhudumu akawa anaondoka kuelekea kaunta huku anatembea kwa madahiro huku anatikisa makalio yake kiufundi anayapandisha juu na kuyashusha kwa kuyapishanisha. Lakini madahiro hayo hayakumzuzua komandoo 'JS' alishazoea kukutana na vishawishi vya warembo mbalimbali tena wa nchi mbalimbali duniani. Akili yake ilikuwa inawaza kazi tu kwa sasa sio kitu kingine alitambua mshika mawili moja humponyoka.
Baada ya dakika kama tano, yule mhudumu akawa amesharudi mezani kwa Komandoo Jacob, wakati yule mhudumu anasaidia kumfungulia kinywaji komandoo ghafla umati wa watu wakawa wanashangilia kwa nderemo na vifijo huku macho yao yanaelekea mlango wa kuingilia. Kulikuwa na kipande cha mtu kibushuti mfupi kanyoa upara kichwani anatembea mguu mmoja kama mfupi huku amevaa miwani nyeusi, na pembezoni ana wapambe kama wawili wamenyoa nywele zao katika mtindo wa kishungi wanamsindikiza. Miondoko yao ilitambulisha kuwa ni watu mafedhuri na wajuba.
Huyu jamaa ndio yule aliyemtesa Kachero Manu katika handaki la mateso la "Gongorosa Camp" siku ya kwanza alivyopelekwa. Wakapita jirani kabisa na meza ya Komandoo Jacob kisha wakasogea jirani na meza ya kaunta ya "Pub".
Walipopita tu Komandoo Jacob akapatwa na hisia hawa ni mabaradhuli wa tabia sio watu wazuri hata kidogo. Akakata shauri amuulize yule dada mhudumu, "samahani mwanangu huyu ni nani aliyeingia hapa hivi sasa, naona watu wanashangilia kama mpira". Akaongea kwa sauti ya kumnong'oneza yule mhudumu.
"Babu wewe ni mgeni kumbee, yatakukuta mambo usiingie ngomani ukashindwa kuicheza bure, huyo ndio "Bob Chinanga" tunaskia tu ni Bosi wa kambi inayosemekana ni ya Usalama wa Taifa, anaogopwa zaidi ya kifo kinavyoogopwa hapa Sofala..!". Kisha haraka haraka akaondoka yule mhudumu kwa mwendo wa madaha akiwafuata wateja wengine aweze kuwahudumia.
Komandoo 'JS' akawa anaendelea kunywa kinywaji chake huku anafuatilia nyendo za yule "Bob-Chinanga", jitu katili lenye kuogopwa. Wakati muziki wa bendi unazidi kupamba moto, akamuona yule "Bob Chinanga anaelekea stejini kuwatunza pesa wanamuziki wa bendi huku wanamtaja taja jina na kumsifia sifia maneno ya kumpamba kama vile "Boob-Chinanga baba ya mapesa mengi, mlezi wa wana" na maneno kedekede ya kumsifu na kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa, ili mradi wamle pesa zake.
Alikuwa anawapa pesa za kigeni mfano wa dola au paundi maana stejini kulikuwa na mwanga khafifu. Kilichomshangaza Komandoo Jacob no kumuuona yupo peke yake wale wapambe wake wawili hawapo.
Akajiuliza wameenda wapi, kengele ya tahadhari ikagonga kichwani mwake akahisi kuna jambo wanafanya wale wapambe wake. Alipotupa macho kwenye meza waliyokuwa wamekaa hakuona mtu zaidi ya msitu wa bia zilizoachwa bila kuwa na mnywaji. Machale yakamcheza akaamua anyanyuke aende chooni huenda atakutana nao huko halafu atajua mbivu na mbichi wakikutana huko huko. Akanyanyuka kuelekea uelekeo wa chooni, huku akiiweka vizuri bastola yake yenye kiwambo cha kuzuia sauti.
Alipofika karibu na vyoo vya wanawake akasita kidogo kwenda, akawa anasikia kama kuna sauti ya kike inalalamika kwa maumivu makali. Akaichomoa kiunoni bastola yake tayari kwa matumizi itakapobidi. Akaanza kujongea taratibu akawa sasa amekaribia kabisa anaskia sauti ya mtu anayeugulia maumivu. "Naku....f...waaaa nisa..i... di... eeee...!" akakaza mwendo kusogelea inapotokea ile sauti.
Lahaula! alitanabahi kuwa yule dada mhudumu wa "Pub" aliyempa huduma ya kinywaji amechomwa kisu cha kwenye titi la kushoto, kimepenya kisawa sawa chini ya ziwa huku damu zinachuruzika kama bomba la maji la DAWASCO lililopasuka mtaani kutokana na shinikizo kubwa la maji. Akamfikia akamshika kichwani kwenye nywele zake na kuanza kumhoji.
"Umepatwa na nini mwanangu..nani kakufanyia unyama huu..."?. Akajibu yule dada kwa tabu sana huku pumzi zake za kuokoteza okoteza, "wame... n.. i...uaaa wame....ni...uli... zaaa we... we ni nanii...na nimeku....ku.... a.. mbi... a nii...ni, niokooooee pliiz". Komandoo Jacob Steven akapatwa na taharuki akajua hapa akijifanya msamaria mwema itakula kwake, atashushiwa jumba bovu la mauaji, akaondoka kama mwehu anarudi ukumbini kuwatafuta wale wapambe wa Bob Chinanga akimuacha yule dada anapigania roho yake.
Akakuta meza yao ipo tupu hawapo wameshasepa na hata Bob Chinanga mwenyewe karibu na pale stejini anapowatazama waimbaji hayupo. Haraka haraka akatoka nje ya lango la kuegesha magari, akaona kwa mbele yake kuna gari limewasha indiketa linataka kuondoka huku Bob Chinanga ndio anafungua mlango wa nyuma kuingia kwenye gari huku mkononi ameshika chupa yake ya pombe kali.
Hapo hapo akajikuta anapigiwa honi na gari aina ya "Range Rover" rangi nyeusi inataka kuegeshwa pale aliposimama Komandoo Jacob. Akili ya Komandoo ikachemka haraka haraka akaona fursa imejitokeza katika wakati muafaka, hakuondoka akazidi kulisogelea lile gari kisha ghafla akashtuka pembeni mwa upande wa mlango wa dereva, hapo hapo dereva akashusha kioo chake kisha akaanza kuporomosha bomba la matusi akamnyambua komandoo "JS" kwa kadri alivyoweza.
Komandoo Jacob hakuwa na muda wa kujibizana nae alimpa kisogo, alichofanya ni kuchomoa bastola yake na kumuamrisha yule dereva, "shuka chini haraka sana usilete utani na wanaume wakiwa kazini" alisema Komandoo Jacob huku anatishia kama anaweka sawa bastola yake kufyatua risasi. Bila ubishi yule baba cha matusi, akawa amegwaya akafungua mlango wake wa dereva. Alikuwa mpole ghafla kama "Mmasai anayesifika ushujaa wa kuua simba lakini anaogopa kula samaki eti macho ya samaki yanamtisha".
Aliposhuka tu kwenye gari yule jamaa, kufumba na kufumbua Komandoo Jacob akaingia kwenye gari na kuligeuza kuelekea uelekeo wa inapoelekea gari ya akina Bob Chinanga. Akaanza kuwakimbiza wabaya wake akina Bob Chinanga, akiwa ndani ya "Range Rover" huku wanatokomea nje ya Mji. Akimuacha yule baba wa kuporomosha matusi akiwa mikono kaweka kichwani, ametaharuki nusu majinuni hajui afanye kitu gani kuipata gari yake tena.




Hapo hapo akajikuta anapigiwa honi na gari aina ya "Range Rover" rangi nyeusi inataka kuegeshwa pale aliposimama Komandoo Jacob. Akili ya Komandoo ikachemka haraka haraka akaona fursa imejitokeza katika wakati muafaka, hakuondoka akazidi kulisogelea lile gari kisha ghafla akashtuka pembeni mwa upande wa mlango wa dereva, hapo hapo dereva akashusha kioo chake kisha akaanza kuporomosha bomba la matusi akamnyambua komandoo "JS" kwa kadri alivyoweza.
Komandoo Jacob hakuwa na muda wa kujibizana nae alimpa kisogo, alichofanya ni kuchomoa bastola yake na kumuamrisha yule dereva, "shuka chini haraka sana usilete utani na wanaume wakiwa kazini" alisema Komandoo Jacob huku anatishia kama anaweka sawa bastola yake kufyatua risasi. Bila ubishi yule baba cha matusi, akawa amegwaya akafungua mlango wake wa dereva. Alikuwa mpole ghafla kama "Mmasai anayesifika ushujaa wa kuua simba lakini anaogopa kula samaki eti macho ya samaki yanamtisha".
Aliposhuka tu kwenye gari yule jamaa, kufumba na kufumbua Komandoo Jacob akaingia kwenye gari na kuligeuza kuelekea uelekeo wa inapoelekea gari ya akina Bob Chinanga. Akaanza kuwakimbiza wabaya wake akina Bob Chinanga, akiwa ndani ya "Range Rover" huku wanatokomea nje ya Mji. Akimuacha yule baba wa kuporomosha matusi akiwa mikono kaweka kichwani, ametaharuki nusu majinuni hajui afanye kitu gani kuipata gari yake tena.
Bob Chinanga na mabaradhuli wenzake walifanikiwa kupandikiza uoga katika nyoyo za raia wa maeneo yote ya Gorongosa. Walikuwa wanajitangaza kuwa wao ni wasimamizi wa kambi ya usalama wa taifa kwa watu wanaotishia maslahi ya nchi ndio huletwa kwao. Ilikuwa mgeni yoyote akifika Gorongosa maeneo ya karibu na kambi yao lazima wapewe taarifa na kama usipotoa taarifa basi wanakupa tiketi ya kuelekea kaburini.
Makondakta wa daladala za Mji, Wapiga kiwi viatu, Wauza magazeti, Wahudumu wa baa, Machinga wa bidhaa mitaani wote walikuwa ni "askari vidole wao", wakipata taarifa tu wanaifikisha kwa mawakala wao akina Bob Chinanga wanalipwa chao.
Sasa Komandoo Jacob Steven alivyokuwa pale "Pub" wakati anaongea na mhudumu wa "Pub", meza ya nyuma yake kulikuwa na muuza vitu vidogo vidogo anayetembeza kwenye kadamnasi ya watu akawa anaskiliza mazungumzo yao. Alivyonasa kila nukta ya mazungumzo yao haraka akapeleka taarifa kwa wakala wake ndio habari zilivyofika kwa wapambe wa Bob Chinanga.
Bila kuchelewesha wakamvutia chooni yule mhudumu na kumhoji kwanini hakutoa taarifa za yule Mzee aliyemuuliza habari za Bob-chinanga, hivyo adhabu yake ya usaliti ni kisu cha chini ya ziwa. Na kwa kuwa muda wa kumpeleka Kachero Manu kwenye mkutano ulikuwa umekaribia wakaona hawana muda wa kumkamata na kumhoji Komandoo Jacob Steven.
Walifahamu akipata taarifa za mauaji ya mhudumu aliyeongea nae zitakuwa ni salamu kwake hivyo atapatwa na uoga na hata kama alikuwa na nia ya kuwafuatilia atasitisha mipango yake. Ndio maana walipofanya mauaji wakatokomea kambini tayari kumsafirisha Kachero Manu kwa helikopta.

Kachero Manu ushindi unanukia kwake
Baada ya kuachwa mule selo kuu Kachero Manu saa kadhaa akiwa na sanjali wake msaliti Meneja Andenga Kazimoto. Kachero Manu akaachana na vilio vya Bwana Andenga akaanza kupanga mikakati upya ya kujiokoa.
Akafahamu mlango wa selo ukifunguliwa tena kwa mara ingine ni kuja kutolewa yeye kwa ajili ya kupelekwa mbele ya Mafioso wenye kiu ya damu za watu na pesa. Akajongea kwa bidii mpaka akalifikia pipa la taka la bati lililokuwa lina kutu kutu. Alipofika akalichota mtama kwa miguu yake yote miwili iliyofungwa lile pipa likaanguka chini na kumwaga vitu chini, mwaaaaah.
Akatawanya tawanya kwa kusasambua vitu vilivyomo kwa mikono yake miwili iliyofungwa. Kwa bahati mbaya hakuona chochote chenye uwezo wa kukata kamba ya mikononi mwake. Kijasho chembamba cha mpaka kwenye meno kilianza kumvuja. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake Kachero Manu akaingiwa na hofu ya kifo.
Baada ya kuchemsha ubongo wake kwa dakika kadhaa akapata wazo jipya la kulifanyia kazi, akapiga moyo konde, akaanza kubiringika kuelekea kwenye ile meza chakavu iliyowekwa kurunzi ya karabai ya kutumia mafuta ya taa. Alipoikaribia meza hiyo, akaiona taa yake inaanza kuripuka ripuka dalili ya uchache wa mafuta ndani yake. Akajifikiria tena kama dakika 3, akapata wazo jipya la la kuyafuata mabaki ya pamba zilizotumika kwenye pipa la taka aliloliangusha. Kisha akiyapata aje nayo karibu na meza afu aifyatue meza ile kurunzi ikianguka chini kioo kikipasuka ule moto wake ukichanganyika na mafuta ya taa pamoja na pamba moto utawaka ndani ya selo halafu ukiwaka atatumia moto kuunguza kamba za mikononi. Akatabasamu kwa namna alivyopanga na kupangua mpaka amepata mbinu yenye matumaini kwake ya kujiokoa.
Akabiringika kwa kasi ya matumaini mapya ndani ya moyo wake ya kuokoka. Alipolifikia pipa la taka, akabana lundo la pamba chafu kwa kutumia mdomo wake kutoka kwenye takataka zilizotawanyika chini. Ilikuwa inahitaji uvumilivu maana ya pamba zilikuwa zinatoa harufu ya uvundo unaotokana na usaha wa kwenye vidonda vya mateka. Akavumilia kubana zile pamba mdomoni huku anasota mpaka akazifikisha salama chini ya meza ile yenye kurunzi. Sasa ikabaki pata potea ya mwishoni ya kuiangusha kurunzi ili ilipuke. Bahati nasibu ambayo kama akishindwa kuzichanga vyema karata zake, itakuwa imekula kwake kimoja.
Akavuta pumzi ndefu ndani kwa nguvu, akasali kimoyomoyo kisha akahesabu moja, mbili, tatu...kisha akaivuta ile meza kwa miguu yake, kurunzi ikaanguka chini ule msukumo wa mafuta ya taa ukasababisha mlipuko mkubwa ambao ukadaka zile pamba mlipuko ukazidi. Haraka haraka akasogeza mikono yake kwenye muwako ule. Zikaanza kuungua zile kamba za mikononi, maumivu yalikuwa makali sana kwa sababu ni kamba za plastiki hivyo zilikuwa zinaganda kwenye mikono lakini akawa anajitahidi kuzichambua huku amekaza roho yake kwa ujasiri mkubwa. Baada ya muda mfupi akafanikiwa kuifungua mikono yake na kamba.
Hima hima akaanza kujifungua kamba za miguuni, ili awe huru asilimia 100%. Yule msaliti bwana Andenga alikuwa ametumbua macho kama maiti iliyowekwa kwenye barafu akisubiri wazishi wake, huku anaangalia maajabu tu aliyokuwa anasoma kwenye vitabu vya riwaya na kuangalia kwenye filamu za maajabu ya Makomandoo. Lakini leo hii ndio kashuhudia mubashara bila chenga namna Komandoo alivyokuwa anaungua mikono bila hata kupiga kelele utasema ameng'atwa na mbu.
Kachero Manu akampuuza Bwana Andenga akaelekea tena kwenye pipa la taka akaanza kupekua pekua tena huenda akapata kitu cha kumsaidia. Imani yake ilikuwa bado inamtuma lazima Dr.Anabella afanye jambo la kumsaidia kutokana na shuhuda aliyopata toka kwa marehemu koplo Hamduni. Na pia Dr.Anabella mara ya mwisho alitupa kitu kwenye pipa la taka na alimtazama sana, hivyo lazima afuatilie hisia zake. Alivyopekua pekua akaanza kukata tamaa, maana takataka zilikuwa nyingi na mwangaza ulianza kuzidi kuwa khafifu kutokana na kuvunjwa kwa kurunzi na vidirisha kuwa viko juu sana. Wakati amekata shauri aachane na kuchakua chakua takataka ghafla akashika kitu kigumu kama chuma kimevirigiwa karatasi na mfuko wa plastiki.
Haraka haraka akaifungua ile plastiki akakutana na funguo tatu zilizochongwa na karatasi kubwa nyeupe ina michoro ya ramani ambayo haionekani vizuri kutokana na kagiza giza cha selo kilichoanza kushamiri. Akaamua kwenda kuchukua moja ya jeneza lililomo kwenye kile chumba akalisimamisha kiurefu. Kisha akaliparamia kama nyani mpaka juu kisha akarukia kwenye kidirisha akawa ananing'nia kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ameshika ramani akaanza kuipitia kwa umakini mkubwa. Ilimchukua takribani dakika 20 tu kuielewa kuwa kuikariri ramani ya jengo zima la "Gorongosa Camp". Baada ya kumaliza kuisoma akatikisa kichwa na kumshukuru sana Dr.Anabella, maana bila ramani ile angetumia muda wa chini hata siku tatu ndio angetoka, lakini kupitia ramani ile alishazigundua njia za panya za kutoroka kwa haraka. Kwa kutumia ramani alikuwa na uhakika wa kutoka na kuwahi kikao kule kiwanda cha korosho kwa gharama yoyote.
Akaporomoka mpaka chini akachanachana ile ramani akaitafuna na kuimeza kama tonge la ugali ili kupoteza ushahidi na akaanza kusaka nguo ya kujisitiri kama atapata. Akakosa akaenda kwenye kile kitanda kupumzisha mgongo akiwasubiri waje awachakaze.



Alivyokaa kama dakika 5 kitandani akapata mawazo mapya kuwa aanze kuchukua maelezo kwa Bwana Andenga Kazimoto ambaye ni mshirika mwenzao hawa mabaradhuli toka Tanzania. Akamsogelea Bwana Andenga akamkuta anaanza kusinzia, Kachero Manu akatabasamu akafikiria ule msemo kuwa usingizi ni mwanaume kweli, hamna kiumbe mgumu mbele ya usingizi katika mazingira yoyote lazima utalala tu hata ukalazwa sehemu mbaya kama chooni. Kama ulivyo mkate wa boflo kiboko yake chai ya rangi, unene wote wa mkate ukiingizwa kwenye chai unabwaka. Akakumbuka picha za Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe zilizokuwa zinasambaa mitandaoni zikimuonyesha anasinzia mkutanoni hali ya kuwa akiwa macho ni mkali kama mbogo, mpaka wazungu wenyewe wanaufyata mkia.
Akamshtua kwa kibao matata sana cha kwenye mafuta ya kitambi, sauti iliyotoka kwenye kitambi kilichochapwa kofi utasema "mpira wa baiskeli uliopata pancha, ilisikika paaaaah..!. "Amka haraka sana haupo Kempisiky Hotel hapa nyamafu wewe" alisema Kachero Manu kwa sauti ya ukali kumuambia Bwana Andenga, ambaye alikuwa hamuoni vizuri Kachero Manu kutokana na giza.
Muda wakati huo ulikuwa ni saa 12:30 magharibi ila kiza chake sasa, utasema kama saa 2 za usiku. "Umefikaje toka Tanzania mpaka humu selo?" aliulizwa Bwana Andenga na Kachero Manu wakati anafanyiwa usaili. Akajibu Bwana Andenga bila kufanya ajizi, "niliitwa kuhudhuria kikao cha leo usiku saa 4:00 usiku" alimalizia Bwana Andenga. "Unadhani kwanini msaliti umesalitiwa na wenzako?, ni kama umelipa pesa bandia kununua bidhaa feki!" alisema Kachero Manu kwa dhihaka.
"Wamenisaliti kwa sababu wamekipata walichokitaka, mikataba yote ya siri ya nchi yetu ambayo haitakiwi ijulikane na nchi zingine wameipata, hivyo hawana tena umuhimu na mimi, wamenifanyia ghiliba nami nikadanganyika. Malipo niliyopata ni matunda ya usaliti wangu, tamaa mbele mauti nyuma" aliongea Meneja Andenga kwa uchungu na masikitiko makubwa huku machozi yanamtiririka kama ngamia.
" Acha kulia kwa unafiki mtovu wa haya wewe, ulikamatajwe"? aliendeleza mahojiano yake Kachero Manu huku akiwa amekasirika kisawasawa. "Nilipotua uwanja wa ndege wa Pemba, nilipokewa vizuri tu sasa njiani wakati wananipeleka hoteli waliyoniandalia kufikia ndio wakanipokonya brifkesi langu la nyaraka zote. Kisha wakanipiga, nikafungwa kitambaa usoni na kupandishwa helikopta mpaka kuletwa huku" alijibu kwa umakini Bwana Andenga.
"Nani alikupa hii kazi ya kudukua na kuvuruga maslahi ya Tanzania kwenye sekta ya gesi na mafuta" aliuliza Kachero Manu huku akiyasimamisha dede masikio yake.
"Ni Bwana Alfredo mmiliki wa Monte Branco Ltd, tulijuana alipokuja Tanzania na msafara wa Wafanyabiashara wa Msumbiji katika kuangalia fursa za uwekezaji nchini Tanzania wakati wa sherehe za uzinduzi wa daraja la Umoja la Mtambaswala". Akapumzika kuongea ili ameze mate Bwana Andenga kisha akaendelea.
"Sasa yeye alijifanya anataka fursa za uwekezaji kwenye gesi na mafuta. Na akanitembelea ofisini kwangu mara kadhaa ndio maelewano yetu na urafiki wetu ukapelekea nijiingize kwenye haya majanga. Aliniahidi mengi sana ikiwemo kunipa ushirikiano wa kuja kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2025, ndio maana ukaona kila tukio naonekana kwenye vyombo vya habari huku wahariri wakubwa wote wakiwa mfukoni mwangu kuhakikisha habari inayonihusu mimi lazima itafutiwe nafasi ukurasa wa mbele wa gazeti" aliongea Bwana Andenga kwa uchungu sana huku ameinika kichwa chake chini kama kobe anayetunga sheria.
"Haya wewe subiri hukumu yako, ukipona hapa utapelekwa Tanzania kwenye mikono ya sheria ukajibu tuhuma zako. Waswahili wanasema kiendacho mavani "makaburini" hakina marejeo, ulikuwa ni mtu mahashumu sana lakini heshima na hadhi yako Tanzania uliyoijenga kwa miaka mingi ya utumishi wako imekufa kabisa huwezi kuirudisha tena, kwa taarifa yako "TAKUKURU" na "Tume ya kudhibiti ufisadi Tanzania (TKUT) wamekamata mali zako zote na akaunti zako za benki za nje na za ndani zimegandishwa kwa maombi ya serikali ya Tanzania kwa nchi husika na wamekubali hivyo hapo ulivyo bila nguo ndio hata Tanzania upo hivyo hivyo huna chako. Umechezea kamari maisha yako, na kawaida ya kamari ina pande mbili, kuvuna au kuparia, sasa wewe wamekuparia. Tanzania mliigeuza shamba la bibi, mkageuza gesi na madini kuwa mali za mahonyo mnaiba mtakavyotaka, mlikuwa mnaishi maisha ya fawaishi mnaenda likizo Ulaya, watoto wenu mnawasomesha nje ya nchi, mnajenga makasri ya ajabu kwa jasho letu walalahoi, sasa chamoto utakiona, humu utaishi maisha ya paka na mbwa hamna tena utukufu humu, pole sana" aliongea Kachero Manu kwa nyodo bila kupindisha maneno wala kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa, akimchamba utasema Kachero ni Mzaramo kwa ufundi wa kuzodoa mtu kwa maneno.
Kauli hizo zilimshtua sana Bwana Andenga, ghafla akaanza kutokwa na mapovu puani na kinywani huku damu ikitiririka masikio, halafu akawa anaugulia maumivu, kisha akatulia kama mzoga. Kachero Manu akatambua, Bwana Andenga amepatwa na shambulio la ghafla la moyo na shinikizo la damu kutokana na kupata taarifa ya mali zake kuzuia kwa amri ya serikali.
Akaamua kumfanyia ubinaadamu wa kumfungua kutoka juu ya vyuma na kuilaza maiti ya Bwana Andenga juu ya kitanda, huku anaisimanga ile maiti na kuisoza kwa vidole utasema inasikia vile.
"Wewe utakuwa chakula kitamu kwa samaki wa mto Ruvuma hatutopoteza kodi za Watanzania kusafirisha maiti ya msaliti, umekufa polo huna hata senti moja uliyowaachia familia yako kwa tamaa zako. Umesomeshwa kwa kodi za Watanzania wa jembe la mkono wewe umeamua kuwasaliti, sasa mshahara wa dhambi ni mauti" aliongea Kachero Manu kwa sauti kubwa kama vile Bwana Andenga anamsikiliza kumbe anaongelesha mzoga wa jana.

Komandoo mstaafu "JS" majaribuni
Bob Chinanga na wenzake walipotoka pale "Montebello Pub" walikuwa wamepigiwa simu kuwa helikopta iliyokuja kumchukua Kachero Manu akahojiwe mbele ya Alfredo ilikuwa imeshawasili "Gorongosa Camp" hivyo waje kumpakiza adui yao haraka apelekwe wilaya ya Pemba, makao makuu ya Jimbo la Cabo-Delgado akahojiwe.
Hivyo mwendokasi aliotoka nao dereva mmoja wa wale wapambe ulikuwa ni wa kuwahi kambini hawakutegemea kama kuna mtu atakuwa anawafukuzia kwa nyuma. Bob Chinanga na wenzake walikuwa wanatumia gari aina ya "Subaru Forester" toleo jipya ambazo zina zinatimua kasi kama gari za mashindano.
Walipotembea kama umbali wa dakika dakika 45 tu mshale wa mafuta ya gari ukaonyesha mafuta yanakaribia kwisha, Bob Chinanga alivimba kwa hasira kama kichwa cha chura mpaka akawa anataka kupasuka kisha akampasha makavu dereva wake.
"Uzembe wa kijinga sana, huwezi kuniendesha mimi Bosi wa kambi halafu hujui kama gari inatakiwa ijae mafuta muda wote" kisha akamalizia hasira kwa kumtukana tusi kwa lugha ya kireno akamwambia "estúpido" akimaanisha mpumbavu au kwa lugha ya kimombo "stupid". ""Samahani Bosi tutawahi tu usiwe na hofu" alijibu dereva yule akijitetea huku akifahamu fika Bosi wake kashazidiwa na kileo ndio maana anatukana ovyo matusi ya nguoni.
Baada ya dakika chache dereva akaanza kupunguza mwendokasi wa gari akawasha indiketa ya kushoto kuonyesha anaingia kituo cha mafuta. Kilikuwa ni kituo kikubwa cha mafuta kimeandika maandishi ya kireno kwa rangi nyekundu "Unidade estação de petróleo" ikimaanisha " ni kituo cha mafuta jina lake ni "umoja".
Komandoo mstaafu hakutegemea upunguzaji ule wa mwendokasi alikuwa anakimbiza asije akaachwa maana hakujui hawa wanapokwenda hivyo kwa kupitia kioo cha pembeni Bob Chinanga akaliona gari "Range Rover" kwa nyuma yao, hakujali sana. Wao wakaingia kituo cha mafuta ile "Range Rover" ikapita kwa kasi ya mshale. Wakajaza mafuta yao wakaondoka kwa kasi dereva akili yake yote asije kumchelewesha Bob Chinanga kibarua chake kikaota nyasi bure.
Walipotembea kama umbali wa nusu saa tu hivi, Bob Chinanga alipoangalia kwenye kioo akaona kama kuna gari linafanana la lile aliloliona pale kituo cha mafuta, imeegesha porini kidogo na wameipita. Inabidi uwe mtaalamu sana kugundua maana iliegeshwa kuficha viakisi mwanga (reflector) na komandoo mstaafu, ni mzoefu wa shughuli sio mnemba kwenye fani.
Walipotembea kama dakika 20 tu, Bob Chinanga akamwambia dereva punguza mwendokasi wa gari nahisi kuna mjinga anatufuatilia Dereva kupitia vioo vyake vya pembeni akaanza kuliona gari la Komandoo mstaafu kwa mbali nalo likawa linapunguza mwendokasi. Bob Chinanga akamwambia dereva wake ongeza mwendokasi wa juu sana halafu tafuta kichochoro chochote uliingize gari kisha tumvizie.
Mbinu yao ilifanikiwa vizuri maana komandoo Jacob Steven (JS) hakutegemea kama atakimbiwa namna ile. Nae ilibidi aongeze kasi akawa haoni gari yoyote akaanza kupunguza kasi ya gari kuangalia labda kuna kuna njia ya mchepuko kuona kama labda gari ya Bob Chinanga imekata huko.
Ghafla akaona ile gari "Subaru Forester" imesimama kwa pembeni kabla hajamaliza taharuki yake akashtukia mvua ya zinarushwa usawa wa kioo chake cha dereva.


Ghafla akaona ile gari "Subaru Forester" imesimama kwa pembeni kabla hajamaliza taharuki yake akashtukia mvua ya zinarushwa usawa wa kioo chake cha dereva. Zikapasua kioo cha mbele kwa bahati nzuri zote zilimkosa. Alichofanya ni kuinamia na kuishikilia steringi la gari yake ili lisiyumbe barabarani asingeweza kufunga breki ya ghafla lazima angekula dafrao mbaya.
Haraka haraka akachomoa bastola yake halafu akawashtukiza alivyofika usawa wa lile "Subaru Forester" kwa kupiga risasi tairi la kushoto la mbele. Akasogea kwa kulipita kidogo kisha akasimamisha gari na kushuka kwa kupitia mlango wa abiria wa mbele, kama alijua maana risasi zilirushwa bila mpangilio usawa mlango wa dereva.
Alichofanya ni kutambaa chini kwa chini mpaka nyuma ya gari lake kisha akamlenga mmoja wao risasi usawa wa kifua na ilimpata kisawa sawa akafa pale pale. Ghafla likawa linakuja lori wangu wangu nyuma yake kwa hiyo akaogopa kumulikwa na mwanga aonekane kirahisi hivyo akaamua aingine chini ya gari atambae kwa chini kisha Lori likipita awashambulie kwa kushtukiza tena.
Alichokiona hakuamini macho yake. Lile Lori lilipofika usawa wa gari la Bob Chinanga alimuona Bob Chinanga anatoka mbio za ajabu na anadandia Lori kwa nyuma, huku nae mpambe wake anamfuata kwa nyuma haraka haraka.
Kachero Manu akafanikiwa kumpiga risasi ya mguu yule mpambe wake. Lakini Bob Chinanga akawa amesalimika ila yule mpambe alianguka chini anagaa gaa chini kwa maumivu. Kilichomchekesha Komandoo JS ni zile mbio za Bob Chinanga mithili ya bingwa wa nchi wa mbio za meta 100 na ule mguu mmoja mrefu na mwingine mfupi basi ilikuwa burudani sana kumuangalia anavyokimbia.
Inaonyesha akina Bob Chinanga waliishiwa na risasi maana walikuwa wanarusha bila mahesabu yoyote. Akatulia kidogo kabla hajamfuata akiogopa huenda ukawa ni mtego anategwa ili wamkamate kirahisi alivyoona kimya kama dakika 5 akachomoka chini ya gari akawa anamfuata yule mpambe alipomfikia akamkwida shati lake na kumnyanyua juu huku amekandamizia mguu wake kwenye jeraha la risasi la mguuni. Yule mpambe wa Bob Chinanga alikuwa anapiga yowe la maumivu makali.
"Kwanini mmemuua yule mhudumu wa Pub" aliuliza Kachero mstaafu kwa hasira. Kwa jeuri yule mpambe akakusanya makohozi kinywani kisha akamtemea usoni komandoo mstaafu.
Akajibu mapigo kwa kumpiga yule mpambe kichwa cha kwenye mwamba wa pua. Tahamaki damu zikawa zinamchuruzika usoni yule adui. Kisha akampiga makofi ya kubambanya sikio la kushoto na kulia. Yule mpambe alipiga kelele kama mtoto mdogo anayetahiriwa jandoni na ngariba mwenye kisu butu.
Kisha ghafla yule mpambe akawa anamung'unya kitu kama pipi. Komandoo akawahi kumkaba shingoni kumzuia asimeze ila alikuwa ameshachelewa kwani kilishapita ilikuwa ni sumu inayotumiwa na majasusi kujipoteza uhai ili wasitoe siri. Ni vidonge vidogo vinazungushiwa glasi nyembamba kisha vinazungushiwa juu yake raba ya rangi ya udongo, halafu zinatengenezwa kama umbile la jino bandia. Kwa hiyo ile raba inamlinda kama amemeza kwa bahati mbaya haimdhuru inapita tumboni bila madhara. Ila anapokusudia kujiua inabidi aitafune tafune kuivunja ile glasi ili sumu iliyowekwa ndani aina ya "Potasium Cyaninde" ifanye kazi.
Hii sumu inaua ubongo ndani ya dakika moja tu na inasababisha moyo wa mwanadamu usimamishe mapigo yake kwa muda mfupi sana.
Haraka haraka akaingia kwenye gari lao lile akaanza kupekua kupekua huenda atapata kitu cha kumsaidia akakuta bastola tupu zisizo na risasi. Wakati anataka ashuke aondoke akakumbuka kitu akapanda tena akatafuta "Log book" inayotumiwa na dereva. Akaifungua akapitia pitia akapata anachokitaka. Alikuwa anaangalia umbali wa kutoka pale "Pub" mpaka "Gorongosa Camp". Akawasha gari na kuongeza mwendokasi kuwahi kambini kabla Kachero Manu hajachukuliwa.

SURA YA KUMI NA SABA
Mlima Gorongosa, kichaka cha waovu tokea asili na jadi.
Wilaya ya Gorongosa katika Jimbo la Sofala, Kaskazini mwa Wilaya hii kuna Mlima Gorongosa ambapo kilele chake cha Mlima kinaitwa Gogogo. Mashariki yake ndio kuna mbuga ya wanyama ya Gorongosa (Gorongosa National Park). Hiyo ni moja ya mbuga iliyobarikiwa sana kwa urithi wa asili wa Afrika.
Mbuga hiyo ina zaidi ya aina za wanyama elfu sabini na mbili (72,000). Na imezungukwa na zaidi ya mito minne kama mto Vunduzi, Chitunga, Muera na Nhandare. Mito hiyo ndio chanzo cha maji ya kunywa katika Wilaya nzima ya Gorongosa na inamwaga maji yake Bahari ya Hindi.
Licha ya utajiri huu wa asili, bahati mbaya sana hili ni eneo ambalo lina mikosi ya kutokupata amani ya kudumu. Kipindi cha vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya FRELIMO na RENAMO, Mlima Gorongosa na mbuga yake ndio ilikuwa uwanja wa vita. Kwa muda wa miaka 16 mtawalia kuanzia 1976-1992, eneo hili lilikuwa linashuhudia ulipuaji wa mabomu, uwindaji haramu wa wanyama kwa ajili ya kutorosha maliasili kama pembe za ndovu, ngozi za simba na nyara zinginezo. Hali ilikuwa mbaya zaidi mwaka 1983 mpaka serikali ya FRELIMO ikaamua kufunga shughuli za kitalii eneo la Gorongosa hasa baada ya tukio la kutekwa kwa watafiti wa maliasili wazawa na wanasayansi wawili wa kigeni.
Baada ya mkataba wa amani wa mwaka 1992 hali ya usalama ilirejea na Benki Maendeleo ya Afrika (ADB) pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Shirika ya Kimataifa Ulinzi wa Mazingira (IUCN) wakaaanda mpango mkakati na utekelezaji wake wa kurudisha hali ya kawaida katika mbuga ya Gorongosa.
Mwaka 2014 eneo hili tena likakosa amani baada ya aliyekuwa kiongozi wa RENAMO Bwana "Afonso Dhlakama" kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu baada ya kushindwa uchaguzi na chama cha FRELIMO, hivyo kuamua yeye na jeshi lake kuhamia mlima Gorongosa hivyo kuzua tena hali ya taharuki.
Hali hiyo tete ya eneo la Gorongosa kwa Tanzania unaweza kufananiza na hali tete na taharuki ya eneo la Kibiti na Ikwiriri namna magaidi walivyotawala eneo hilo kipindi cha nyuma na kuendesha mauaji ya kutisha kwa viongozi wa vijiji na polisi, kabla hawajadhibitiwa na jeshi la wananchi. Ni eneo ambalo ukiamua kufanya makazi basi roho yako umeiweka rehani inatakiwa uwe na tahadhari ya hali ya juu.
Kibaraka wa wazungu katika kuchota utajiri wa Msumbiji na Afrika kwa ujumla Chotara Alfredo alikuwa ni mtu wa maneno machache sana lakini mipango mingi sana. Kila kitu kinachopita mbele yake yeye alikuwa anaangalia atapata fursa gani hapo aitumie kujinufaisha. Inasemekana alikuwa hata akiliona gari la kubeba vinyesi vya binadamu linapita barabarani alikuwa anasikitikia sana kinyesi hicho kumwaga bure. Mawazo yake ni kutaka kuzalisha mbogamboga na matunda ya kulisha Afrika nzima kwa kutumia mbolea ya kinyesi cha binadamu.
Hivyo alivyorudi masomoni na kukabidhiwa umiliki wa kampuni ya Monte Branco Ltd, machafuko ya Gorongosa ikawa fursa kwake ya kufanya uwindaji haramu hivyo akajenga ndani ya milima, kambi ya kuhifadhia nyara haramu kama meno ya tembo na nyinginezo. Kisha nyara hizo zilikuwa zinasafirishwa kupitia bandari ya Beira iliyopo hapo hapo jimbo la Sofala, moja ya bandari tegemezi kwa nchi za Zimbambwe, Zambia na Malawi.
Baada ya amani kurudi Msumbiji akawa anawazuga watu ni ghala la kutunzia mazao kama korosho na mihogo mikavu kumbe ikawa ni kambi ya mateso kwa wabaya wake. Akaajiri vijana ambao zamani kazi yao ilikuwa ni wapiga mapanga watu mitaani na machimboni maarufu "NACATANAS" ambao kwa Tanzania ni mfano wa "KOMANDO YOSSO" walivyosumbua miaka ya 90's na kiongozi wao akijiita "Jenerali Nyau". Hawa KOMANDO YOSSO walisumbua sana kuanzia Manzese, Tandika mpaka bonde la Mwananyamala. Ndio kama hawa NACATANAS huko Msumbiji na kiongozi wao Bob-Chinanga chini ya uratibu wa Inspekta Jenerali Mark Noble.
Bob Chinanga yeye matumizi ya akili kwake ni madogo sana kwake kila kitu anatumia nguvu, hivyo Inspekta Jenerali Mark Noble askari polisi mwenye cheo cha juu kabisa akawa ni kibaraka wa Alfredo (under cover) katika kuijenga NACATANAS kisasa.
Mark akawa anaunganisha ujuzi wake kwa hawa NACATANAS, akawapika wakaiva mafunzo. Kuingia kambini kwao hawa NACATANAS kama walivyomuingiza Kachero Manu kisha ukatoka salama inabidi uwe na roho saba kama za paka. Maana ukikosea njia ya kuingia milimani unatokeza kwenye msitu wa wanyama wakali kama simba na chui au kwenye majoka yenye sumu kali. Huo ulikuwa ni ulinzi wa asili wa kambi hiyo.
Iwapo ukifanikiwa kuvuka vikwazo hivyo unakutana na fensi ya waya za senyenge za umeme uliozunguka kambi yote ambao usipovaa nguo zao maalumu kwa kupita eneo lisiloruhusiwa unakauka kama mkaa ukiwa umbali wa meta 5 kutoka kwenye fensi. Ulinzi mkubwa ulikuwa ni wa teknolojia za kisasa.
Pia kulikuwa na ulinzi wa kutumia mbwa maarufu kama mbwa wa polisi wanaitwa K-9 aina ya "German sherphed", mbwa ambao walikuwa wanaelewa alama za ishara na maneno. Walipitia mafunzo maalumu na walikuwa wanatibiwa vizuri na wanalishwa vyakula vya kwenye Masupamaketi sio makombo ya kwenye migahawa kama hawa mbwa koko wetu wanaotusumbua majumbani kuiba kuku wetu.
Kisha ndani kulikuwa na wafanyakazi maalumu kwa mateso ya watu wanaokamatwa. Watesaji hao wanaishi kwenye nyumba zao za kota ndogo za kisasa, wakiwa na viwanja vya mazoezi, mabwawa ya kuogelea na vikorombwezo kibao vya kunakshi nakshi mazingira yao. Kutwa nzima walikuwa wanashindana wenyewe kwa wenyewe kufanya mazoezi kama kunyanyua vyuma, kucheza karate, mieleka, judo, kukimbia na mazoezi mengineyo na huku wanashindana kula vyakula mbalimbali. Vifua vyao vilikuwa vimejaa kama mataruma ya reli kwa wingi wa nguvu walizonazo.
Mfano Bob Chinanga alikuwa akimaliza mazoezi ya asubuhi ana uwezo wa kunywa supu ya kuku mzima lile jogoo la kienyeji linalowika kuanzia saa 9 usiku kwa chupa nzima ya chai kwa mikate ya Boflo mitano, kama marehemu Pepe Kalle mwanamuziki wa Congo alivyokuwa na mshipa wa kula.
Selo zao zilikuwa za aina tatu tu, Kulikuwa na selo ya mateso ya kuanzia watu watano afu kulikuwa na selo kubwa inayoweka zaidi ya watu kumi na selo ya mtu mmoja mmoja, kutegemeana na makosa ya mkosaji. Hizi selo zote zilikuwa na kuta ngumu za plastiki kuzuia mateka kujiua wenyewe kama ataamua ajigongeshe kichwa ukutani na zilikuwa na vifaa vya mateso ikiwemo viti vya umeme kwa ajili kupiga shoti ya umeme.
Gharama ya siku moja tu kwa ajili ya kuendesha shughuli zote za usalama, umeme, maji, mawasiliano na vyakula ilikuwa si chini ya milioni tano za Kitanzania kwa siku. Hapo ndio utaona kwa namna gani Bwana Alfredo alijipanga haswa kutikisa uchumi wa Msumbiji na nchi za kusini mwa jangwa la Afrika kwa ujumla.


Bob-Chinanga katimba kambini tayari kumnyakua Kachero Manu
Bob Chinanga alifanikiwa kumtoroka Komandoo mstaafu Jacob Steven (JS) katika sekeseke la kurushia risasi, kwa kurukia lori la mizigo.
Lori hilo la mizigo kwa bahati nzuri lilikuwa linaelekea karibu kabisa na kambi ya "Gorongosa Camp" kwa karibia kilomita 7 Lilikuwa ni Lori la "Gorongosa National Park" likiwa linatoka bandari ya Beira kubeba mizigo ya vifaa mbalimbali vya kutumiwa mbugani kwa ajili ya ofisi na wataliii.
Dereva wa Lori aliziona zile gari mbili akawa yupo makini katika kuongeza mwendokasi wa gari lake hakutaka kusimama maana anafahamu njia ya kuelekea mbuga ya Gorongosa haikuwa nzuri sana kiusalama. Hivyo Bob-Chinanga alipodandia lori alifanikiwa kupasua turubai lililoziba mizigo kwa kisu chake cha kukunja ambacho ni moja ya silaha zake anazolala na kuamka nazo.
Akafanikiwa kujisweka katikati ya lundo la mizigo kukwepa baridi kali ya milimani. Wakati wote alikuwa anaangalia saa yake maana alijua uzembe wowote wa kumchelewesha kachero Manu kufikishwa mbele ya Bwana mkubwa Alfredo ungepelekea kupoteza kazi na hata kupoteza uhai wake.
Kama kuna mtu NACATANAS wote mpaka Inspekta Mark mwenyewe walikuwa wanamuogopa basi ni Alfredo. Inasemekana Alfredo alipoenda kusoma Chicago, Marekani alipitia pia mafunzo ya kijasusi ila wengi walikuwa hawajui na alikuwa hapendi ajulikane kama ni bobezi kwenye fani. Inasemekana siri hii ilitolewa na majambazi wa Cabo-Delgado waliwahi majambazi kama 6 waliwahi kuvamia nyumbani kwake usiku wa manane alichowafanyia ni gumzo mpaka leo.
Wenyewe walijua ni tajiri kibonde kibonde nyama uzembe, mwili yai kama hawa matajiri wetu wanavyojiweka. Inasemekana aliwaona kwenye mifumo yake ya ulinzi wakati wanaingia ndani ya nyumba akawaagiza walinzi wake wakiwakamata wawany'ang'anye silaha kisha wawaache waje ndani, alipokutana nao alipigana nao wote majambazi 6 kwa pamoja, akawafirigisa sawia. Ambapo 3 kati yao walivunjwa viuno vyao na mmoja alikufa palepale hawa 2 waliponea tundu la sindano lakini wakiwa wamevunjwa mikono. Hao ndio walioenda kuvujisha siri kwenye vijiwe kuwa hawajawahi kuona mtu mtaaalamu wa sanaa za mapigano kama Bwana Alfredo.
Hivyo Bob Chinanga alifahamu hana uwezo wa kumuepuka Alfredo bali ni kutekeleza maagizo yake kama anavyotaka. Alipokaribia karibia na mbuga, Bob Chinanga aliteremka bila kuonekana na dereva wa lori.
Kwa mtu kama Bob Chinanga ilimchukua nusu saa tu kupata usafiri wa kufika kambini, ni hivi alienda kwenye vichochoro vinavyotumiwa na wawindaji haramu wanaotumia bodaboda kusafiri mizigo usiku usiku kuipeleka Gorongosa mjini. Huko akafanikiwa kupora bodaboda moja bila hata kuua inzi maana dereva bodaboda alivyomuona tu aliachia mwenyewe funguo maana alijua kubishana na Bob Chinanga ni sawa na kujitafutia kifo cha makusudi.
Mpaka kufika muda saa tatu kasoro usiku Bob Chinanga alikuwa anaingia kambini, huku akiacha maagizo makali ya ulinzi wa kambi kuimarishwa maradufu na kutoa onyo kuwa uzembe wowote utakaoruhusu kambi kuvamiwa haotuvumilika kwa mhusika yoyote kwenye idara yake.
Baada ya kutolewa amri hiyo mkuu wa kikosi cha mbwa alikuwa yupo nje na wasaidizi wake kuimarisha ulinzi, wale wanaozunguka ukuta wa kambi kila mmoja akiwa na silaha yake iliyojazwa risasi alikuwa kwenye eneo lake ili mradi ulikuwa ni usiku wa hekaheka mtindo mmoja. Na kila mmoja alikuwa kwenye sare zao za rangi ya kaki, kofia na buti nyeusi ili iwe rahisi kutambuana inapotokea tatizo.
"Showdown" ya kibabe "Mwiba wa Tasi" vs "Bob-Chinanga"
Kachero Manu aliona giza linazidi kuwa totoro mule selo kuu huku hamna dalili yoyote ya kuja kwa mabaradhuli wale. Alipoisogelea maiti ya msaliti Bwana Andenga Kazimoto alikuta imeanza kufutuka. Akajisema ndio kawaida ya maiti za watu wenye vitambi huwa zinavimba sana. Akapatwa na huruma ya mzazi kwa mtoto akawa anawafikiria watoto wa Mzee Andenga watakuwa wanamsubiria baba yao arudi safari toka Msumbiji na zawadi za kutambishia watoto wenzao shuleni. Lakini ndio basi tena hawatamuona baba yao ataishia kuwa chakula cha ndege na fisi porini, au chakula ya samaki mtoni.
Akiwa amezama katika dimbwi lenye kina kirefu la fikra, akapata wazo la kukitega kile kitanda cha chuma mlango na kwa kuwa wakiona giza wataingia kwa pupa watakapojikwaa watapoteza umakini hapo hapo itakuwa rahisi kuwavamia na kuwamaliza. Akakisogeza kitanda kwa kutumia nguvu zote huku juu yake kuna maiti ya Bwana Andenga mpaka akafanikiwa kukitega kitanda meta chache kutoka kwenye geti la kuingia kwenye selo kuu, kisha yeye akajibanza pembeni. Akasikia kama mlango unagongwa akajiweka tayari kwa lolote. Lakini kumbe walikuwa ni popo wa ndani ya selo wanajigonga kwenye kwenye mlango.
Kumbe popo walikuwa wanamletea habari njema haikuzidi hata dakika 5 akawa anaskia nyayo za vishindo vya viatu vinatembea akajisemea kazo iliyonileta Cabo-Delgado ndio inaanza. Akajibana vizuri pembeni mwa kitanda, na kwa haraka alivyopima mlio wa zile nyayo za viatu akaamini hawazidi zaidi ya kati ya watu wawili au watatu. Mlango ukawa unafunguliwa kwa vishindo vyote huku wanajiamini adui yetu Kachero Manu yupo mahututi kwenye kamba alizofungwa hajiwezi kumbe "Mwiba wa Tasi" alikuwa anawasubiri tu waingine kichwa kichwa awafunze adabu. Awaonyeshe cha mtema kuni kilichomnyoa kanga manyoya.
Wa kwanza kuingia alikuwa ni Bob Chinanga na bangi yake mkononi analipuliza ili kujipa stimu za kuwajibika. Alipagawa baada ya kuona giza nene akaingia ndani kichwa kichwa akajikuta anaparamia kitanda mpaka kaparamia maiti ya Bwana Andenga Kazimoto. "Fyatua risasi" alipiga kelele Bob Chinanga kwa hamaki kama mwehu, alishajua maji yamezidi unga tayari.
Alikuwa ameshachelewa, kwani Kachero Manu alishamrushia teke la mkononi yule mwenye bunduki mkononi ikamponyoka lakini akawahi yule msaidizi wa Bob-Chinanga kuchomoa tochi kiunoni na kuwasha, ilikuwa ni zile tochi kubwa sana chumba kikaenea mwangaza.
Ule mwangaza ukawa kosa kwao sasa Kachero Manu akawa anawaona wote vizuri. Haraka haraka Kachero Manu akaruka kurukia tumbo la maiti ya Bwana Andenga kisha akajibinua hewani na kumchapa teke moja matata sana la kifuani Bob Chinanga ambaye alikuwa ametoka kujizoazoa chini. Lakini licha ya ukali wa lile teke la Kachero Manu lilipofika kifuani kwa Bob Chinanga hakutikisika hata kidogo.
Isipokuwa alichezesha matiti yake kifuani huku anacheka mithili ya wale wacheza mieleka wa miaka ile ya 90's walivyokuwa wanachezesha matiti yao akina "Power Bernado", "Power Marungusi", "Power Bukuku" au "Power TX-Chaka".
Yule msaidizi wa Bob Chinanga akawa anatambaa kiujanja kwenda kuiwahi bunduki iliyodondoka. Kachero Manu hakumchelewesha alimuwahi akamrukia mgongoni kisha akakamata shingo yake na kuinyonga mara moja, akafa pale pale bila kuomba maji.
Kitendo cha kupoteza uhai wa msaidizi wake, Bob Chinanga kilimkasirisha vibaya sana, alipandisha morali na kumfuata Kachero Manu pale alipo kama mbogo huku anapiga ukelele wa hasira mithili ya Morani wa Kimasai. Wakawa sasa wamekaribiana wanaviziana, Bob Chinanga akawa anaruka ruka kama nyani, mara amerukia zile bomba zinazoning'inia za kutesea mateka mara ameshuka anavizia ashambulie kwa kushtukiza.
Hapo Kachero Manu akajua huyu anatumia staili ya kizamani kabisa za akina "Koo Ting Sang" alizokuwa anazitumia katika filamu ya "Snake in the monkey's shadow". Kachero Manu akaamua kutumia staili ya "Chang Quan" ambayo ni mpya kabisa haujazoeleka na wengi. Mtindo ambao unapoanza unasimamisha mguu wa kulia na unaukunja mguu wa kushoto mpaka maeneo ya goti la mguu wa kulia huku mkono wa kulia unanyooka huku wa kushoto unakuja chini, ni staili ambayo ilikuwa ni ngeni kabisa machoni kwa "Bob Chinanga".
Alivyokunja ule mguu Kachero Manu, Bob Chinanga akaona kapata nafasi ya kushambulia akaruka kumrukia Kachero mzima mzima, lilikuwa ni kosa baya sana kwake. Alipokuja Kachero aliukunja mguu wa kulia kisha ule mguu wa kushoto ambao ulikuwa upo juu ukapita kwenye shingo la Bob Chinanga, ikawa sinema ya mbwa aliyeingiza kichwa kwenye ndoo yenye mdomo mdogo anashindwa kutoa kichwa chake. Ikawa kila anapojichomoa ndio kabali ya mguu inazidi kujikaza mpaka Bob Chinanga aanza kuhisi anataka kuishiwa pumzi, huku anatoa mishuzi ovyo.
Alichofanya Bob Chinanga ni kujisukuma kichwa kwa nguvu zote kikachomoka na kupiga sehemu za siri za Kachero Manu. Jaribio lake lilifanikiwa kwani Kachero Manu aliachia mguu na kupiga kelele utasema amekanyagwa na tairi la trekta. Bob Chinanga bila kuchelewa akampiga Kachero Manu farasi teke la nguvu eneo la tumboni ambalo lilimfanya kachero Manu apepesuke kama mlevi wa gongo. Bob Chinanga akajua ameshamaliza kazi akawa anamfuata Kachero Manu kizembe bila kuchukua tahadhari.
Kachero Manu akazuga kama amezidiwa na kipigo cha Bob Chinanga kumbe anamvizia asogee karibu amalize kazi. Alipomsogelea karibu zaidi akawa anajiandaa kumsukumizia makonde ya usoni Kachero Manu, aliporusha konde la mkono wa kushoto, Kachero Manu akaliona akakwepesha kichwa chake kuelekea kushoto kidogo tu, konde likapita patupu hewani. Bob Chinanga akapoteza uelekeo kutokana na kuyumba.
Hapo ndipo Kachero Manu akatupa konde la nguvu la mkono wa kulia, konde ambalo lilimuangusha chini Bob Chinanga kwa kishindo. Haraka haraka akajinyanyua chini akajifuta kwenye pembe ya ncha ya mdomo wake akaona damu zinachuruzika. Akaanza kurusha ngumi mtawalia bila umakini, ambazo ngumi zote Kachero Manu alikuwa anazikwepa huku anarudi nyuma nyuma. Kitendo cha kuona damu yake inamwagika kilichochea hasira za Bob Chinanga na kupunguza uwezo wake finyu wa kufikiri akawa anakuja kumvamia Kachero Manu kama anakuja kubeba gunia la viazi lumbesa.
Kachero Manu hakumkawiza, akajipindua sarakasi kurudi nyuma kisha akaruka na teke moja kali sana la mguu wa kushoto lililotua kwenye usawa wa koo la Bob Chinanga ambalo lilimtupa chini kwa mara ya pili akafikia chali upande wa kisogoni akawa anajaribu kunyanyuka anashindwa.
Hapo hapo Kachero Manu akamrukia na kumkaba kabali ya mbao huku magoti ya Kachero Manu yamekanyaga tumbo la Bob Chinanga, akawa kila Bob Chinanga akijaribu kujitoa hawezi kujitoa, mpaka akaanza kukoroma kwa kukosa hewa, akanyonga kwa nguvu shingo ya Bob Chinanga mpaka akapoteza uhai. Kachero Manu akawa anahema kwa nguvu huku jasho linamtiririka haamini kama amemuangamiza Bob Chinanga.




Komandoo "JS" ndani ya Gorongosa Camp"
Komandoo "JS" alijaribu kulifukuzia lile lori la mbuga ya wanyama ya Gorongosa, lakini hakufanikiwa kulipata. Mpaka alipoifuata barabara ya vumbi ndipo alianza kuona alama za matairi ya Lori na bahati kulikuwa kumenyesha mvua nyepesi hivyo ilikuwa rahisi kuona alama za matairi ya gari. Mpaka akafika njia panda ambayo ukiifuata kulia unaelekea mbugani na kuna kibao cha kuonyesha unaelekea mbugani.
Hapo akasimama kutafakari uelekeo wa yule Bob-Chinanga ni wapi amepita kuelekea kambini kwao alipowekwa Kachero Manu. Wakati hajui aelekeee uelekeo gani ghafla akamuona kijana wa makamo anatimua mbio kwa taharuki kuelekea uelekeo wa gari la komandoo "JS".
Komandoo "JS" akachomoa bastola yake na kuelekeza usawa wa yule kijana, kisha kwa sauti yenye maamrisho ndani yake yenye kuonyesha usipotii utakipata chamoto. Akanena Komandoo "JS", kumwambia yule kijana, "simama hapo hapo ulipo, unatoka wapi na unakwenda wapi usiku huu"?. Kijana alipigwa na bumbuwazi na kugwaya, kulikojionyesha dhahiri usoni kwake.
Alifahamu hiyo ni kauli mutlaki isiyo na chembe ya mashaka kuwa akibishia kutii atauliwa. Mwenyewe alijua anakimbilia kwenye usalama kumbe anakwenda kukutana na mtihani mwingine.
Huyu kijana ni wa bodaboda ni yule kijana anayevusha nyara haramu za asili ambaye alipokonywa bodaboda yake na Bob Chinanga. Hapo alikuwa amekimbia karibia kilometa 2 na ushee ili kuokoa uhai wake na hakuamini kama kafanikiwa kumchoropoka Bob Chinanga. Mtu ambaye hamna asiyemfahamu katika mji wa Gorongosa awe mtoto au mkubwa juu ya ukatili wake.
Alikuwa ameshachoka vibaya sana kutokana na mbio. Sasa alipoona taa za gari kwa mbali akapata nguvu mpya za kuongeza mwendokasi ili aweze kupata msaada. Lakini alivyokaribia akashtushwa na sauti ya kuamrishwa kusimama. Pale pale kijana yule akasimama huku amenyoosha mikono juu.
Komandoo JS akaanza kujongea anamfuata kwa tahadhari akihofia huenda akawa ni adui. Mpaka alipofika usawa wa karibu zaidi, akamhoji "wewe ni nani? na unatokea wapi usiku huu"?."Mimi ni dereva bodaboda, nilikuja mbugani kubeba mzigo", alijibu kijana yule kwa sauti ya uoga.
"Bodaboda yako umeacha wapi, na mbona unakimbia kama wewe sio mhalifu na ni raia mwema"? aliendelea Komandoo "JS" na mahojiano yake. "Nimeporwa bodaboda na Bob-Chinanga" alijieleza kijana yule. Komandoo "JS" kusikia jina la Bob Chinanga, vinyweleo vya mwili vikamsisimuka akatambua ameshazidiwa akili na akizubaa itakula kwake.
Anaweza kumpoteza Kachero Manu na yeye pia akaingizwa kwenye mtego wa kukamatwa kisha kupotezwa pia. "Haya twende haraka tuondoke na gari, hii sio sehemu salama hata kidogo" alisema Komandoo "JS". Chapuchapu kijana yule na komandoo "JS" wakakimbilia kwenye gari.
Mwanzoni yule kijana alidhania wanaondoka kuelekea Mjini, lakini akashangaa kuona gari linaenda uelekeo wa kule kule alipotoka kuporwa bodaboda yake na Bob Chinanga. Ikabidi awe mpole tu asiulize ulize maana hata huyu alikuwa hajui kama ni shirika moja na Bob Chinanga au ni watu tofauti.
"Na kama ni watu tofauti kwanini anamiliki silaha? na kwanini anaenda kule kule alipotoka yeye ambapo maadui zake ndipo walipo?" ni maswali ambayo alikuwa anajiuliza hapati majibu.
Walipoenda kama dakika 10, Komandoo "JS" akavunja ukimya, "Nimekuja kumsaka Bob-Chinanga kanitoroka huko njiani ndio maana kakupora bodaboda yako. Hivyo naomba msaada wako wa kunielekeza kambini kwao".
Kijana yule akavuta pumzi ndefu za uoga na kuzishusha kisha akakohoa kidogo akaanza kuzungumza "kwa kweli huko kambini kwao sijawahi kufika ila kuna siku katika harakati zetu hizi za magendo wakati tunapita njia za panya kuwakwepa askari wanyama pori waliokuwa wanatufukuza tumeshawahi kuona helikopta ndogo inatua kwenye kiwanja kidogo, ilibidi tujifiche na bodaboda zetu kwa kuogopa tusije tukakamatwa tulikuwa tunajua ni askari wanyama pori wa anga.
Lakini tulivyochunguza wakati abiria wanashuka alikuwa ni Bob Chinanga na hawara zake kama wawili na rubani wa helikopta wanashuka. iIikuwa ni usiku wa manane na tuliweza kuwatambua kwa sababu waliwasha taa za hapo kiwanjani. Hivyo inaonyesha kambini kwao sio mbali na huo uwanja mdogo wa ndege vinginevyo wasingeshukia hapo.
Pia baadhi ya askari wa hiyo kambi yao tunashirikiana nao kwenye biashara za magendo huwa wanatupa mizigo ya dili tunawapelekea Mjini, sasa mmoja wao kuna siku alilewa sana akaanza kuropoka ropoka mazingira ya kambi yao, akafikia hatua ya kusema hawezi kiumbe yoyote kukanyanga kambini kwao akatoka salama akaleta kejeli kuwa hata kama jeshi zima la Marekani, litafanikiwa kufika kambini kwao basi halitoweza kutoka salama wote watateketezwa hivyo imaonyesha ni kambi iliyojitosheleza kwa kila namna ya ulinzi na vifaa", akamaliza maelezo yake marefu yule kijana yaliyovuta hisia za Komandoo "JS".
Maelezo ambayo yalimpa mawazo mapya Komandoo "JS" ya kuwa kwa muda mchache uliobaki asingeweza kupambana na kikosi chote cha kambi akiwa peke yake, ila anachoweza kufanya ni kwenda kuvizia kwenye huo uwanja wa ndege, ili kama atajitokeza hapo Bob Chinanga aweze kupambana nae kwa kumteka na kumtumia kama ngao ya kuingia kambini kirahisi ili kumkomboa Kachero Manu.
Lakini alikuwa anajua anacheza bahati nasibu ya pata potea. Maana Bob Chinanga anaweza kuondoka kambini kwa kutumia usafiri wa gari, lakini hisia zilimtuma hawezi kutumia tena gari kwa sababu anafahamu kuwa anaviziwa na adui yake, hivyo atataka kuondoka kwa helikopta akiwa na yakini asilimia mia kwa mia kuwa Komandoo "JS" hafahamu uwepo wa kiwanja kidogo cha ndege kwa namna kilivyojificha.
Akakumbuka kanuni yake muhimu inayomuongoza kwenye kazi zake za kijasusi alifundishwa na mwalimu wake toka CUBA kuwa ukitaka kuwa mpelelezi mahiri heshimu sana hisia zako na pia kila kitu unachokutana nacho usikipuuzie hata kidogo. Mwalimu wake huyu toka CUBA alikuwa anampenda sana Komandoo "JS" hasa akikumbuka kwenye jaribio la siku ya kwanza tu ya somo lake, Komandoo "JS" alipata alama 99/100.
Yule Mcuba aliingia darasani siku ya kwanza afu mbele kulikuwa na ubao na meza iliyojaa vitu aina tofauti tofauti zaidi ya ishirini kama boksi la biskuti, chupa ya maji, daftari na vinginevyo halafu kabla hajaanza kufundisha akaomba dharura ya dakika tano akatoka nje ya darasa. Halafu kabla hajarudi vile vitu vikatolewa pale mezani alivyorudi yule mwalimu darasani akaanza kugawa karatasi nyeupe zimeandika jaribio la kwanza, wanafunzi walishangaa hawajafundishwa kitu wanaanza kupewa mtihani!.
Swali lilikuwa moja tu utaje vitu vilivyowekwa pale mezani kabla havijaondolewa. Komandoo "JS" alifanikiwa kutaja vitu kumi na tisa kati ya ishirini vilivyokuwa vimewekwa mezani. Kitu ambacho toka siku ya kwanza alitabiriwa na Mwalimu huyu toka Cuba kuwa atakuja kuwa jasusi mahiri sana. Na ndio ilivyokuja kutokea, ukitafuta Makomandoo watano bora barani Afrika huwezi kumuweka pembeni Komandoo "JS" hata kidogo. Utakuwa umetenda dhambi kubwa sana ukimtenga kwa sababu ya kijiba chako cha roho na chuki binafsi.
"Basi nipeleke karibia na huo uwanja tukifika karibu niambie tulifiche gari mimi nitakwenda wewe utabaki humu ndani ya gari ukinisubiri. Usijaribu kutoka, na kama utaona helikopta inapaa ikipita nusu saa sijarudi, basi fahamu usalama wangu upo hatarini ondoka mara moja na hili gari ukaliache popote pale katikati ya Mji na upotee zako. Wenye gari lao watalipata kwa sababu linauwezo wa kujulikana lilipo kwa njia za kimtandao". Kijana alipewa maelekezo fasaha na Komandoo "JS".
Komandoo "JS" akaendesha gari kwa maelekezo ya yule kijana kuelekea kwenye uwanja mdogo wa ndege. Walipokaribia na uwanja wa ndege ambao upo meta kama 600 kutoka kwenye lango kuu la kuingilia kambi ya Gorongosa. Kijana yule wa bodaboda alimuelekeza Komandoo "JS" ukaribu wao na uwanja hivyo wakatafuta kichaka kimoja makini sana wakalisekwa gari. Kisha wakazifunika viakisi mwanga vya gari kwa kitambaa ili lisionekane kirahisi.
Kijana akabakizwa ndani ya gari akiwa kaachiwa funguo za gari na bahati nzuri alikuwa ni kijana wa mjini anajua vizuri tu kuendesha gari. Kisha Komandoo "JS" akaelekea uelekeo wa uwanja wa ndege mdogo ili kujaribu bahati yake ya kumvizia Bob Chinanga.

Kachero Manu katika harakati za kuisambaratisha "Gorongosa Camp"
Baada ya kuhakikisha ameshawaua Bob Chinanga na msaidizi wake, haraka haraka akavua nguo za yule msaidizi wa Bob Chinanga akazikung'uta kuondosha mavumbi kisha akazijaribisha kuvaa. Zikawa zimemkaa vyema kama amepimishwa yeye na fundi nguo. Akavaa na kofia yake na viatu vya yule msaidizi ingawa vilimbana kiasi ila vilimuenea kwa dharura vilikuwa vinavalika.
Kisha akampekua Bob Chinanga akakuta anazo bastola mbili za kisasa moja ina kiwambo cha kuzuia sauti, na vipisi kadhaa vya bangi kwenye pensi yake ya dangirizi na rundo la funguo. Akazichukua zile funguo na bastola zote mbili akajimilikisha kisha akaokota tochi ya yule msaidizi wa Bob Chinanga kisha akaiweka vizuri miili yao kisha akatoka nje ya selo na kufunga lango kuu kwa nje.
Nje kulikuwa ni giza totoro lakini kwa msaada wa tochi mkononi aliyoichukua selo, akawa anaweza kuona anapoelekea umbali wa mpaka meta 10 mbele yake. Kutokana na namna alivyoisoma ramani ya selo kuu kutoka kwenye karatasi aliloletewa kijanja kwenye pipa la kutupia takataka na Dr.Anabella, aligundua kuna njia kama sita za kutoka nje ya Selo. Lakini njia nyepesi zaidi ya kutoka kwa haraka kwa muda mfupi ni kwa kupitia handaki lililochimbwa karibu na chooni ambalo linakuja kuibukia karibu na lango kuu la kutokea nje linalotumiwa na magari kutoka nje ya kambi.
Hivyo alivyotoka tu selo alitembea kama hatua 30 kwa makadirio akaanza kushuka ngazi kuelekea chini ya jengo akaanza kukumbuka siku aliyopelekwa kwenye mateso akajipigiza kiwambazani ilifanana na njia hii kisha alipofika chini ya ngazi ya mwisho akaona kwa mbele yake kuna bwawa la matope lenye kutoa harufu mbaya ambalo alipitishwa siku ile ya mwanzoni.
Akasimama kidogo kutafakari njia ya kupita akawa anafanya kumbukizi ya ramani maana kulikuwa na njia ya kushoto na kulia, baada ya muda akachukua maamuzi ya kufuata njia ya kulia ilikuwa ni njia nyembamba yenye kokoto ndogo ndogo akatembea kama takribani dakika 5. Baada ya hapo, njia ikaanza kuwa pana kwa mbele akaanza kuona mwangaza wa taa akazima tochi yake na kujibana kwenye nguzo kuchungulia ni eneo linalohusika na kitengo gani.
Akawa anaona watu wanapishana kila wakati huku na kule wakiwa wamevalia makoti rangi nyeupe na kofia nyeupe wamebeba maboksi kichwani, wanayatoa chumba kimoja wanapeleka kwenye chumba kingine.
Akasita kidogo huku akijiuliza aendelee kwenda mbele au asitishe kwa sababu njia ya kuelekea kwenye handaki ipo katikati ya vile vyumba viwili vinavyotazamana kwa mbele yake ndio kuna vyoo kisasa moja ya kile choo sio choo cha kweli bali ni njia ya chini kwa chini ya handaki.
Njia hiyo huwa inatumika mara chache chache kwa dharura kufika kwa haraka karibu na lango kuu la kutokea. Eneo lile lilikuwa ni kiwanda kidogo cha kufungasha madawa ya kulevya yanayoletwa kupitia bandari ya Beira nchini Msumbiji yakitokea nchi za Pakistani na Brazili kisha yanafungashwa hapo "Gorongosa Camp" na kusafirishwa kwa boti za kasi kuelekea sokoni nchini Afrika ya kusini kwa njia za panya.
Wakati anatafakari kitu cha kufanya akaona mtu ambaye ni mmoja wa walinzi, kavaa nguo kama zake ameshika bunduki anatoka chumba kimoja kwenda kingine akashukuru Mungu kwa uamuzi wake wa kuchukua nguo za yule mlinzi wa Bob Chinanga. Hivyo akajihakikishia kuwa sasa anaweza kusonga bila kushtukiwa kirahisi.
Akaanza kuvuta hatua zake taratibu kuelekea mbele kule kwenye vyumba viwili mkabala kwa kila kimoja, mpaka alipowakaribia wale watu akaanza kukatiza katikati yao huku anapiga miluzi, ameweka viganja vya mkono mfukoni kuonyesha kujiamini.
Mbinu yake ikasaidia sana akakatisha bila kikwazo chochote. Alikuwa anasikia miungurumo ya mashine zinatoa mlio kiwandani huku masikio yametega kwa kusikiliza chochote kitakachotokea, alivyowapita tu akaanza kuongeza kasi ya mwendo wake.
Alipofika kwa mbele kidogo akaanza kukanyaga marumaru nzuri zilizosakafiwa kwenye korido yote iliyo nyembamba. Akazidi kusonga mbele kidogo kisha akapinda kulia akaanza kusikia sauti za vyombo vya muziki akafahamu kuna ukumbi wa disco maalumu kwa wafanyakazi wa kambi ya Gorongosa wapate sehemu ya kujiliwaza baada ya masaa ya kazi.
Akasogelea uelekeo wa ule ukumbi kisha alipoenda kushoto kidogo akaupa mgongo mlango wa kuingilia kwenye ukumbi akakuta kuna mlango wa lifti. Bila kupoteza muda akabonyeza kitufe kitakachompelekea roshani namba 03.
Ikaanza kuja ile lifti mpaka ikafika usawa wake ulivyojifungua mlango wa ile lifti kulikuwa na mtu ndani yake alivyomuona akajiskia kama mapigo ya moyo yanataka kusimama kwa muda kutokana na mshtuko alioupata. Miguu na mwili wake vinakosa ushirikiano msawazo wa kumuwezesha kutembea kuingia kwenye lifti.




Alikuwa ni mwanamke mrembo ambaye macho yake yalipomuona yalipata nuru ya matumaini. Alikuwa ni Dr.Anabella anataka kushuka kwenye lifti kwa haraka haraka na ilibaki kidogo wagongane kwa haraka ya Dr.Anabella. Dr.Anabella hakumtambua kwa haraka Kachero Manu alijua ni mmoja wa askari wa mule kambini yupo katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Alichofanya ni kumshika mkono mmoja kwa nguvu Dr.Anabella kumzuia asiende kisha mkono mwingine akabana mlango wa ile Lifti isijifunge. “Daktari ahsante sana kwa ile ramani uliyoiacha kule selo kuu kwenye pipa la takataka” alisema Kachero Manu huku akiunda tabasamu jembamba kwenye uso wake na kukenua meno yake yaliyopangika vizuri kwenye kinywa chake.
Dr.Anabella akageuka na kutumbua macho yake akiwa haamini alichokisikia na kukiona toka kwa yule kijana aliyedhania ni mlinzi wa “Gorongosa Camp”
"Siamini mboni za macho yangu na ngoma za masikio yangu alisema Dr.Anabella. Kachero umefanikiwa kujiokoa?, nilishapatwa na wahaka wa moyo juu ya usalama wako, hapa nilikuwa nakuja kwa haraka huko selo kuu kuangalia labda umezidiwa nikupe huduma ya kwanza. Maana tunamsubiria Bob Chinanga kwenye helikopta iliyokuja kukuchukua ikupeleke mbele ya mkutano mkuu wa genge la Monte Branco Ltd. Sasa imepita zaidi ya dakika 45 Bob Chinanga haonekani, na simu zinapigwa toka mkutanoni na mchumba wangu Inspekta Mark Noble anaulizia kama tumeanza safari ya kwenda Pemba. Hivyo nilikuwa na hofu huenda umejaribu kupambana nae amekujeruhi hivyo nije kukupa huduma ya kwanza, nilishakata tamaa kama unaweza kufanikiwa kuchomoka kutoka kule na hata ungechomoka huo ulinzi wa ndani na nje ya kambi sijui ungetokaje humu kama usingeiona ile ramani. Sasa twende haraka tutoroke kikubwa ni kumteka rubani atupeleke mkutanoni huko tutajua namna tutakavyoingia" alisema Dr.Anabella akiwa na uso wa bashasha isiyo na kifani.
"Ila kuna kitu nimekumbuka kabla ya kutoka nataka niingie kwenye chumba kimoja jirani na lango kuu, utanisubiri kwa dakika zisizozidi dakika 10 kisha ndio tutatoka kupanda gari kuelekea uwanjani" alisema Kachero Manu kumwambia Dr.Anabella. "Muda mfupi tu unapajua kila kona ya kambi? nimekuvulia kofia kipenzi changu, kweli ramani umeisoma ukaielewa kila kichochoro cha kambi" alisema Dr.Anabella kwa sauti nyororo yenye utani kumwambia Kachero.
"Bila msaada wako wa kuniletea ramani ya kambi ningekuwa nasubiriwa kwenye karamu ya fisi kama mzoga tu, lakini mbinu zako zimeniokoa leo, ahsante sana" alijibu kachero Manu. Bila kupoteza muda Kachero Manu na Dr.Anabella wakapanda ile lifti na kuelekea kwenye gari linalomsubiri Bob Chinanga karibu na lango kuu.
Alikuwa anakusudia kwenda kutega mabomu kwa ajili ya kuyalipua na kuitekeza kabisa kambi hii ya wahalifu wa Gorongosa.
*************************************************************
Komandoo "JS" anateka Helikopta
Alfredo aliujenga uwanja mdogo wa ndege ulio umbali mchache kutoka kambi kuu ya "Gorongosa Camp". Ulikuwa umezungushiwa fensi waya uwanja wote kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wake. Kulikuwa na taa nne kubwa kwenye kila kona mithili ya taa za uwanja wa mpira maalumu kwa kuchezea mechi za usiku. Huku geti la chuma la kuingilia uwanjani likiwa limeelekezwa upande wa mashariki ya uwanja huo.
Uwanja huu ulijengwa maalumu kwa kutorosha nyara haramu kutoka mbuga ya Gorongosa na kupokea mizigo mingine haramu ya Bwana Alfredo kutoka pande mbalimbali za dunia.
Pia viongozi wa kambi akina Bob Chinanga, Inspekta Jenerali Mark Noble na wenzake walikuwa wanautumia mara kwa mara wanapokuwa wanahitaji kufika kambini wa haraka bila kutumia usafiri wa gari.
Siku hiyo ya kusombwa Kachero Manu na kupelekwa mbele ya Mafioso, helikopta maalumu iliyomfuata ilikuwa imefika uwanjani toka saa 12:30 jioni. Ndani yake ikiwa na rubani, Dr.Anabella na msaidizi mmoja wa Bob Chinanga wote wakitokea Pemba. Bob Chinanga yeye alikuwa anaishi huku huku kambini Gorongosa kama Mkuu wa mateso kwa mateka na operesheni zote chafu. Pemba alikuwa anaenda mara moja moja kwa wito maalumu. Msaidizi wa Bob Chinanga ilivyofika helikopta alishuka haraka na kuelekea kambini kwa ajili ya kumchukua Kachero Manu akisaidiana na Bosi wake Bob Chinanga huku Dr.Anabella akiwa amebaki kwenye helikopta akiwasubiria akina Bob Chinanga wamlete Kachero na ampe huduma ya kwanza kama atakuwa katika hali mbaya kabla ya kuanza msafara.
Dr.Anabella alivyoona muda unazidi kwenda imefika saa mbili kasorobo bado Bob Chinanga hajatokea wala msaidizi wake, akaanza kupatwa na wasiwasi juu ya usalama wa Kachero Manu. Hivyo akamuambia rubani kuwa huenda Kachero amezidiwa hivyo ngoja aende kambini haraka kuwafuatilia hivyo kwenye helikopta akawa amebaki rubani peke yake.
Jambo ambalo lilimrahisishia Komandoo "JS" kufanya utekaji kilaini sana. Komandoo "JS" alivyomuacha kijana wake wa bodaboda ndani ya gari, aliambaa ambaa na vivuli vya miti iliyoshonana kuzunguka uwanja huo mpaka akakaribia geti la kuingia uwanjani. Alipotupa macho getini, akaona wapo walinzi wawili tu, mmoja amesimama ametundika bunduki yake begani huku mwingine akiwa amekaa kwenye kiti bunduki yake kaisimamisha pembeni kama mchongoma tena akiwa anasinzia.
Komandoo "JS" akafanya maamuzi ya kuparamia juu ya mti uliokaribu yake ili aweze kuwalenga shabaha ya risasi kwa kutumia bastola yenye kiwambo cha kuzuia mlio wa risasi na awamalize mara moja, bila kupoteza muda wa mapigano na kuwashtua waliopo ndani ya helikopta kwa purukushani za mapigano. Kwa bahati mbaya sana akakanya vibaya tawi la mti ambalo lilikuwa kavu hivyo likavunjika na kutoa sauti.
Yule mlinzi aliyesimama aligutushwa na sauti ya mlio wa lile tawi ikabidi afuatile kujua kulikoni, isije ikawa mdudu kaingia ndani ya kokwa tayari. Hasa ukichukulia kuwa mapema kabisa walipewa tahadhari na Mkuu wao Bob Chinanga ya kuimarisha ulinzi wa maeneo yote. Akataka amuamshe mwenzake toka usingizi lakini akasita, akaamua kwenda peke yake uelekeo wa mti aliouparamia Komandoo JS.
Akaukaribia karibu kabisa mti huo ambao juu yake yupo Komandoo "JS" amejibanza. Akazidi kusogea zaidi kutokana na giza lililoshamiri kwenye ule msongamano wa miti akaamua achomoe tochi yake iliyopachikwa kiunoni mwake. Akawasha, sasa akawa amefika tayari chini ya mti alikuwepo Komandoo "JS", ambaye alikuwa makini kufuatilia nyendo za yule mlinzi wakati anakuja. Mpaka alipofika chini ya mti aliokuwa Komandoo "JS" akasimama sekunde kadhaa anatupa macho yake kiudadisi huku na kule kama indiketa za taa za taa za gari.
Yule mlinzi hakuwa makini kabisa kuangalia juu ya mti, yeye akili yake ilikuwa ni kusaka kama kuna mtu amejificha kwenye fukuto la miti na nyasi mbele yake. Alipoanza kupiga hatua kuelekea mbele na kuuacha ule mti lilikuwa ni kosa la majuto kwake, kwani Komandoo "JS" alijirusha toka juu ya mti huku akiwa mikono yake inabembea kwenye tawi la mti na kufanikiwa kumbana Yule mlinzi kwa kabali ya miguu miwili.
Yule mlinzi kwake lilikuwa ni shambulio la ghafla asilolitegemea hata kidogo, hivyo hakuwa na namna ya kujitetea. Alijitahidi sana kufurukuta ili kujitoa kwenye kabali miguu ile lakini miguu ya Komandoo "JS" ilikuwa migumu kama chuma.
Miguu ambayo miundi yake unaweza hata kuvunjia nazi na ikavunjika bila kuleta madhara kwenye mifupa hiyo. Hivyo mlinzi yule akapoteza uhai wake na kuelekea jongomeo kwa kukosa pumzi. Alipohakikisha amekufa tayari akashuka haraka haraka kutokea juu ya mti na kuuvuta mwili wake vichakani. Kisha kwa mwendo wa minyato akaanza kusogea jirani kabisa na getini huku mlinzi aliyebaki akiendelea kuuchapa usingizi wake, habari hana kama tayari wameshavamiwa.
Akawa anajificha kwenye vivuli vya miti mpaka alipokaribia meta chache kutoka kwa mlinzi anayeuchapa usingizi, akajibanza kwenye mti kisha akapiga mbinje kwa mluzi. Yule mlinzi akakurupuka usingizini mvangemvange kama mwehu huku amebeba bunduki yake. Akaanza kumtafuta mwenzake, akawa hamuoni kwenye upeo wa macho yake. Hofu na wasiwasi ukaanza kutamalaki nafsini mwake, akaanza kuita jina la mwenzake huku anakuja uelekeo aliojibanza Kachero Manu.
Hakuitikiwa kabisa na mwenzake, hali ambayo ikamzidishia uoga na kumfanya azidi kujihami. Alipokaribia zaidi, Komandoo JS akajitokeza ghafla kwa mbele yake kitendo ambacho hakutegemea yule mlinzi. Akashikwa na butwaa, akiona kama vile ametokewa na mzimu wa Mlima Gongorosa.




Bila kumchelewa Komandoo JS akamrusha teke la mguu wa kushoto kwenye mkono wa adui aliokuwa amekamatia bunduki ikamdondoka chini. Yule mlinzi akajibu mapigo akafanya kama anageuka nyuma kama anataka kukimbia lakini akajigeuza kwa haraka na kurusha teke moja maridhawa la mguu wake wa kulia kuelekea kwenye tumbo la Komandoo "JS". Teke ambalo lilimpata sawia maeneo ya tumboni, kwa sababu Komandoo "JS" alishindwa kujilinda.
Aliingia kwenye mtego wa kuzania adui yake anakimbia hivyo hakujiandaa na shambulio lile na ghafla. Teke lile lilimyumbisha Komandoo "JS" vilivyo na kumfanya mwili wake ukose uwiano linganifu. Yule mlinzi akamfuata Komandoo "JS" wakati amejiinamia kuugulia maumivu. Akamkamata mabega kwa nguvu kisha akamuinua kwa haraka halafu akamuinamisha kwa haraka na kumpiga vifuti viwili vya nguvu usoni mwake. Vifuti vile vilimuingia kisawasawa Komandoo "JS", akaanza kuona nyota nyota usoni. Alivyopeleka vidole vyake usoni na kujishika puani, akaona damu zinachuruzika churu churu kwenye mwamba wa pua yake.
Kitendo ambacho kilichochea hasira na kumpa hamasa ya kujibu mapigo kwa haraka na kwa umakini. Akaanza kujilaumu kimoyomoyo kwa kumdharau adui yake ambaye alimchukulia kuwa ni mzembe "lalavi buda", anayezembea lindoni kwa kulala. Kumbe adui yake ni mzuri sana kwenye mapambano ya ana kwa ana. Komandoo "JS" akaigiza kama amezidiwa sana akawa anayumbayumba mtego ambao aliuingia yule mlinzi akajua Komandoo "JS" ameshaelekea kibla mwenyewe anasubiri kuchinjwa tu.
Sasa akawa anamfuata bila kuchukua tahadhari yoyote, utasema anapambana na Bi.Harusi. Alipomkaribia tu yule Mlinzi akarusha teke la mguu wa kushoto la mbavuni.
Komandoo "JS" akaliona lile taka akalikwepa kisha akaudaka mguu na kuukunja kwa mbele, ilikuwa ni kitendo cha haraka ndani ya sekunde kadhaa. Mfupa wa maungio ya goti ulivunjika kama unavyovunjika muwa bungala, kwa kutoa sauti ya taaaah..!.
Mlinzi yule akawa anapiga kelele za maumivu utasema amejikwaa jiwe na kung'oa ukucha wa dole gumba la mguuni. Komandoo "JS" akamuwahi kumziba mdomo asije akawashtua waliomo kwenye helikopta pale uwanjani. Kisha akampiga kareti moja ya shingoni, akafa pale pale bila hata kuomba maji ya kunywa. Akamburuza yule mlinzi kwenye kichaka cha pembeni yake, akatoa kitambaa kidogo mfukoni mwake akajifuta damu za puani mwake kisha akamvua sare zake yule mlinzi na kuzivaa yeye na kofia yake ili aweze kwenda kwenye helikopta bila kutiliwa mashaka.
Alivyovaa alijicheka kidogo maana hazikumtoshea vizuri hasa suruali ya yule mlinzi ilikuwa fupi wakati Komandoo "JS" alikuwa ni mrefu. Alikuwa anaonekana kama wanamuziki wa Kikongo wale wanaovaa suruali pana za mabwanga kama mifuko ya mashineni. Baada ya kuvaa akaelekea getini na kuelekea ilipo helikopta. Akawa anatembea kuelekea kwenye helikopta bila wasiwasi wowote na ilikuwa ipo mbele ya upeo wa macho yake. Alipoikaribia akaongeza umakini lakini aliona taa za ndani za helikopta zimezimwa ila za nje zinawaka. Kumbe rubani alikuwa amejipumzisha yupo peke yake lakini anamuona jinsi komandoo "JS" anavyokuja.
"Mbona Bob Chinanga anazidi kuuweka usiku, hapa Inspekta Mark anapiga simu kila wakati na kachukia sana kitendo chetu cha kuchelewa kumpeleka mateka wetu" alisema yule rubani kumueleza Komandoo "JS" alipofika usawa wa kioo cha rubani.
Laiti rubani angefahamu kuwa anauza siri za kambi kwa adui hatari sana, angejifia kihoro kwa uoga. "Nadhani wanakuja muda sio mrefu maana nimeona gari linajiandaa kuja" alidanganya komandoo "JS" na kujisifu kimoyomoyo kuwa mbinu yake imefanikiwa. "Samahani naomba kuazima kiberiti nataka kuvuta sigara sasa kiberiti changu kimepotea sikioni " alisema Komandoo "JS".
"Ngoja basi nishuke tuvute wote maana na mie sijavuta muda mrefu nina kiu ya sigara balaa nilikuwa nategemea watakuja kwa haraka" alisema rubani yule huku akishuka nje ya helikopta.
Wakati anazunguka kwa mbele ya helikopta yule rubani kumfuata Komandoo "JS", lilikuwa kosa kwake alipotokeza mbele ya komandoo "JS" akakutana na mdomo wa bastola unamtazama. "Nyoosha mikono juu na usijaribu kuleta ujanja wowote ambao utagharimu uhai wako uende ukasalimie kuzimu usiku usiku kabla jogoo la asubuhi halijawika" alifoka Komandoo "JS" huku anamsogelea. Kiuhalisia alikuwa anamtisha tu hakupanga kabisa kumuua bali alipanga kumtumia rubani huyu huyu aendeshe hiyo helikopta.
Komandoo "JS" alikuwa mtaalamu wa kurusha helikopta na hata ndege ndogo ila tatizo alikuwa hayafahamu vizuri mazingira ambayo hiyo helikopta inatakiwa kutua. "Ongoza njia urudi ndani" alisema Komandoo "JS" kwa sauti ya ukali. Bila kuleta kukurukakara rubani yule akatii sheria bila shuruti akiongoza njia huku amenyoosha mikono juu.
Walipoingia ndani akamuamrisha akae kwenye siti ya urubani na kumfunga mikono na miguu kwa kamba ya manila, na kumshindilia matambala kinywani Kisha akampokonya simu zote za mawasiliano ya mkononi.
Akajipa nusu saa kama hatumuona Kachero Manu atamfuta kichwani mwake kwenye hesabu za watu hai, hivyo itabidi aingie kambini kuiteketeza kambi ili awatie hasara haswa mpaka wajute kumfahamu.

Tukutane kiwandani mkutanoni
Kachero Manu na Dr.Anabella walifanikiwa kufika kwenye gari linalowasubiri lango kuu bila kikwazo chochote na bila kutiliwa mashaka. Kwa sababu Dr.Anabella alikuwa anajulikana kinagaubaga, kambi nzima kuwa ni mchumba wa Bosi wao Mark na pia ni Daktari wa mateka mule kambini.
Walipofika geti kuu Dr.Anabella akapanda kwenye gari siti ya mbele jirani na dereva, huku Kachero Manu akizunguka kibanda cha walinzi wa getini akatokomea kwenye stoo za silaha zilizojipanga pembezoni umbali mchache kutokea kwenye kibanda cha walinzi.
Alipofika stoo kwa kutumia funguo alizochukua mfukoni kwa Bob Chinanga, akajaribisha mara kadhaa mpaka ufunguo mmoja wapo ukakubali kufungua. Kilikuwa ni chumba cha zana za kivita za kisasa, ni chumba ambacho walikuwa wanaingia watu watatu tu, ambapo kila mmoja alikuwa na funguo zake binafsi anazotumia. Watu hao ni Bob Chinanga, Inspekta Jenerali Mark na Bwana mkubwa Alfredo.
Bila kuchelewa akatafuta yalipo mabomu na rimoti za kulipulia mfano wa saa za mkononi akazipata, akayatega vizuri tayari kwa kulipuka. Akatoka na mabomu mawili madogo mfano wa ukubwa wa nazi za pemba zilizotolewa maganda yake lakini yana uwezo wa kuteketeza kijiji kizima ukiamua. Baada ya dakika 10 akawa kamaliza kazi ya kutega milipuko.
Akaharakisha kurejea kwenye gari na kudandia nyuma tayari kwa kutoka lango kuu lililokuwa likimsubiria yeye tu. "Ondosha gari haraka tumechelewa" alisema Kachero Manu kwa sauti ya juu akiwa amepakia nyuma ya "Pick-up". "Tunaondoka sawa lakini simuoni Bob Chinanga wala mlengwa mkuu wa safari wapo wapi? "alisema yule dereva kwa sauti ya wasiwasi huku mkono wake wa kulia unawasha gari.
"Mateka wetu ana hali mbaya sana, hawezi hata kuongea hivyo Bob Chinanga kamtuma huyu mwenzako akatoe taarifa kama kuna uwezekano ibadilishwe siku ya mahojiano ili apate nafuu na pia mimi nakwenda kufuata dawa za kumtibia huyo mgonjwa" alidanganya Dr.Anabella uwongo mkongwe kwa kutumia sauti ya huzuni. Uwongo ambao msikilizaji yoyote atadhania kuna ukweli ndani yake kutokana na sauti hiyo ya kubembeleza kubeba ujumbe wa huzuni.
Dereva yule hakutia neno lolote, ishara ya kukubaliana na maelezo ya Dr.Anabella akawa anaingiza gia na kuliondosha gari kwa mwendo wa wastani mpaka walipofunguliwa geti kuu na kutimua vumbi kuelekea uwanjani ilipo helikopta tayari kwa safari ya Pemba usiku huo. Bila kujijua kuwa wanaenda kukutana na Komandoo "JS" anayewasubiria kwa hamu kubwa waende kuanzisha vagi mkutanoni.
Komandoo "JS", macho yake yalikuwa hayabanduki kila wakati kwenye saa yake ya mshale ya gharama sana aina ya "Patek Philippe" kutoka Uswisi, aliyoivaa mkono wake wa kushoto. Saa ambayo mishale ya dakika na sekunde ilikuwa inashindana kujizungusha ili iweze kuleta mabadiliko ya muda. Muda ulikuwa unasomeka saa 2:45 usiku mbichi ikimaanisha zimebaki dakika zisizopungua 5 tu kutimia saa tatu kasoro dakika kumi ikiwa ndio muda wa mwisho aliojiwekea wa kuvumilia kuwangojea akina Kachero Manu na watekaji wake. Akiwa amezama kwenye tafakari ya mishale ya saa yake na kuanza kujiweka tayari kushuka kwenye helikopta akashtukia gari inakuja usawa wa ile helikopta kwa kasi kisha ikaenda kwenye maegesho madogo ya hapo uwanjani.
Wakashuka watu watatu, mwanamke mmoja akiwa amevaa koti la kidaktari na walinzi wawili wakiwa kwenye sare zao wakawa wanakuja kwenye helikopta alipo Komandoo "JS" na rubani ambaye sasa ni mateka wake. Komandoo JS alikuwa anausoma mchezo mzima kupitia kwenye kioo cha helikopta kwa kutumia mwangaza wa taa za uwanjani pia taa za helikopta zilikuwa zinawamulika vizuri sana. Ila wao walio nje walikuwa hawawezi kumuona kwa sababu alizima taa za ndani ya helikopta.
Komandoo "JS" akawa amepagawa hamuoni Kachero Manu ambaye alitegemea ataletwa na hawa walinzi. "Lakini mbona hawajafika nae?, kauliwa? au wamemfanya nini?", ni maswali aliyojiuliza lakini yakawa yanakosa majibu muafaka. Hivyo akajipanga wakiingia ndani ya helikopta lazima alianzishe varangati kwa kuwashtukiza kabla hawajamshtukia yeye uwepo wake ndani ya ile helikopta.
Mipango ya Kachero Manu na Dr.Anabella ilikuwa ni kuondoka na rubani na yule mlinzi ambaye ndio dereva wa Bob Chinanga mpaka Pemba, kisha watakapofika wawageuke na kuingia na mlinzi mkutanoni.
Hivyo walikuwa wanakuja ndani ya helikopta kizembe zembe bila kuchukua tahadhari yoyote bila kujua ndani ya helikopta kuna komandoo "JS" Ambaye malengo yake na yao yanashabihiana ila hawatambuani. Komandoo "JS" alijibanza chini ya kiti nyuma kabisa, huku akiwa ameshikilia bastola zake mbili mkononi.
Wa kwanza kuingia ndani ya helikopta alikuwa ni Dr.Anabella, akachagua siti akakaa tuli. Kisha akaingia mlinzi yule na akafuatia Kachero Manu akiwa wa mwisho kuingia. Wote kwa pamoja wakapatwa na mshtuko baada ya kumuona rubani amefungwa kamba za miguuni na mikononi na kazibwa na matambala kinywani mwake.
Kabla hawajatanabahi maamuzi ya kufanya walishtuliwa na sauti nzito toka kwa mwanaume wa kazi, Komandoo "JS". "Nyanyueni mikono yenu wote, msilete ujanja wowote utakaonilazimisha kulipua vichwa vyenu kwa risasi" alifoka Komandoo "JS", sauti ambayo haikuwa na chembe ya utani ikimaanisha anachokizungumza ndicho aatakachokifanya kwa kuwatwanga risasi mmoja mmoja kama wakileta ukaidi mbele yake.
Bila ubishi wowote wote kwa pamoja wakanyanyua mikono juu, huku tayari komandoo "JS" ameshajitokeza juu, kutokea chini ya siti ya nyuma.



Komandoo "JS" akauliza, "Kachero Manu mmemuacha wapi? toeni jibu nyinyi makhabithi la sivyo na nyie naondosha roho zenu sasa hivi". Hapo hapo Kachero Manu akatambua huyu yupo upande wake kwa sababu kama angekuwa upande wa adui angekuwa anajua kila kitu kinachoendelea na asingemteka rubani yule. Akaibia Kachero Manu kumtazama kwa jicho pembe, akaona ni mtu aliyefuga masharafa mashavuni mwake yenye mvi nyeupe, akakumbuka Komandoo "JS" anafuga masharafa kutokana na picha aliyopewa ofisini Dar es salaam na Bosi wake.
Alichofanya Kachero Manu ni kujitambulisha kwa lugha ya siri (SPY-CODE) aliyopewa ya kuwasiliana na Komandoo "JS" pindi alipojitambulisha ujio wake na uhitaji wa gari na nyumba ya kukodi. Akasema kwa sauti ya juu "wewe ni CUT-OUT?" akimaanisha anamuuliza Komandoo "JS" ni kiunganishi kati ya ofisi ya Makachero wa Tanzania nchini Msumbiji?.
Makachero wazoefu wana lugha zao ambazo wanazitumia kuwasiliana ambazo ni ngumu kwa asiyemhusika kuzifahamu. Mfano ukiskia msemo, "EARS ONLY" maana yake ni taarifa ya siri mno haitakiwi kuandikwa ila inafikishwa kwa maneno pekee, au ukiskia "DEAD DROP" maana yake ni mzigo ambao Kachero mmoja ataupeleka sehemu fulani atauacha kisha mwingine ataupitia kuuchukua mzigo huo bila Makachero wawili hao kuonana uso kwa uso.
Hivyo kitendo cha kutumia neno "CUT OUT" hapo hapo wakatambuana, Komandoo "JS" akashusha bastola zake chini, na Kachero Manu akachomoa bastola yake na kumuweka chini ya ulinzi yule dereva wa Bob Chinanga na kumpa amri ya kumfungua kamba rubani wa helikopta.
Baada ya pilikapilika hizo za dakika chake safari ikaanza muda wa kama saa 3:05 usiku. Hawakuwa na muda wa kupoteza huku rubani akipewa tahadhari ya kutoleta ujanja wowote wa sungura utakaogharimu maisha yake. Wakati wakiwa juu angani wameanza kupaa meta chache tu ikasikika milipuko mikubwa ya mabomu huko chini kambini, 'Gorongosa Camp' inateketea kwa moto.
Dr.Anabella na Kachero Manu wakatazamana huku kila mmoja akitabasamu, alikuwa Kachero Manu amelipua mabomu aliyoyatega pale kambini kwa kutumia kitendambali (rimoti) ya mkononi mwake aliyovaa kama saa mkononi. Kiwingu kizito cha moto mwekundu kilitanda kuizunguka kambi ya Gorongosa usiku huo utasema siku ya kiama ndio imetoka. Kambi hiyo iliteketezwa kabisa bila kusaza kitu chochote.

SURA YA KUMI NA NANE
Mwisho wao Mafioso wa Cabo-Delgado umewadia
Soko la Baraca maana yake ni soko la vitu vya bei rahisi. Hili soko lipo katikati ya Mji wa Pemba kilometa takribani kama 2 tu kutokea barabara ya pwani (Coastal Road). Ni soko ambalo wakati wote limefurika limefurika Wafanyabiashara na wateja wao. Sokoni hapo ni maarufu pia kwa bidhaa za vinyago vya Kimakonde vya kila sampuli ikiwemo na bidhaa za baharini. Ni soko ambalo aghalabu utakutana na watalii wa kutoka nchi za ng'ambo kama China, Japani, Marekani na mataifa mengineyo ya kigeni wakiwa wametingwa kujitafutia zawadi za bidhaa asilia za kurejea nazo nchini kwao.
Waswahili wanasema kila kwenye msafara wa mamba na kenge nao hawakosekani, kwani katika harakati hizi za soko la Baraca za watu kujitafutia riziki zao za halali za kujiendeshea maisha kwa ajili yao na familia zao, kampuni ya "Monte Branco Ltd" nao walijichomeka katika eneo hili kwa kuwekeza kiwanda cha daraja la kati cha kusindika korosho, lakini ndani yake ilikuwa ni ofisi yao kuu ya kupanga mipango haramu yote ya kuhujumu nchi ya Msumbiji. Chini ya kiwanda inasemekana kulikuwa na ofisi za wapanga madili na wizi wa kila aina ambao walikuwa wanalipwa mishahara minono na mmiliki wa kampuni Bwana Alfredo.
Dr.Anabella ameshawahi kupelekwa huko chini ya kiwanda zaidi ya mara moja na mchumba wake Inspekta Jenerali Mark enzi mapenzi yao yamepamba moto. Mark katika kutaka kujionyesha kuwa ni mtu muhimu sana mbele ya Bwana Alfredo, siku ya kwanza alimchukua Dr.Anabella usiku wa manane siku ambayo Dr.Anabella alikuwa na zamu ya usiku katika hospitali ya kiwandani hapo akampeleka huko kwenye mahandaki chini ya kiwanda kumtembeza. Yalikuwa ni mahandaki yenye maofisi na chumba zenye starehe zote na mahitaji yote muhimu yanapatikana. Milango yake ilikuwa ni ya kufunguka kwa rimoti inayofunguliwa na namba za siri maalumu. Inspekta Mark alimdanganya Dr.Anabella kuwa anazitumia ofisi hizo za siri kupangia baadhi ya operesheni dhidi ya wahalifu.
Kiwandani hapo ndio palipangwa kufanyika mkutano wa Mwisho ambao utahitimisha uhai wa Kachero Manu, na kutoa onyo kali kwa wote wenye kufuatilia nyendo za Bwana Alfredo katika biashara zake za rubi na nyinginezo.
Mkutano ulipangwa uanze saa 4:00 kamili usiku, huku ukumbi ulikuwa umepambwa vikorombwezo vyote muhimu kwa mahitaji ya mkutano huo muhimu. Na washirika wote wa Bwana Alfredo, Mafioso wenzake kutoka Ureno na Afrika ya kusini walikuwa wameshawasili Pemba tayari kwa mkutano. Wengi walikuwa ni vigogo wana hisa wa kampuni na watendaji wakuu wa shughuli za kila siku za kampuni. Inspekta Jenerali Mark Noble alikuwa hatulii kama mbwa koko jike mwenye joto anayehitaji kupandwa. Alikuwa kama mtu mwenye mazonge yanayotokana kuelemewa na majukumu. Yeye kama akiwa Afisa Usalama Mkuu wa kampuni na kiongozi wa kikundi cha mateso cha "NACATANAS" alikuwa anahaha kuhakikisha mambo yanaenda kama yalivyopangwa bila kuharibiwa na mtu yoyote.
Lakini kilichokuwa kinamnyima raha ni kitendo cha helikopta kutokea Gorongosa kambini kuchelewa kufika Pemba. Alikuwa amempa maagizo Bob Chinanga ya kuhakikisha wanafika Pemba ifikapo saa 2:00 usiku. Sasa muda huo wa saa 3:15 usiku muda ukiwa unayoyoma haonekani Bob Chinanga wala wasaidizi wake. Mbaya zaidi ilikuwa mwanzoni anawasiliana na rubani na kule kambini lakini sasa alikuwa akipiga simu zote hazipatikani kabisa.
Kijasho chembamba kikaanza kumtiririka usoni na kwenye makwapa ya mikono yake jasho jekejeke likawa linamtiririka. Kengele ya hatari ikagonga kichwani mwake kuwa huenda Kachero kawazidi nguvu. Lakini kwa upande mwingine anajipa matumaini haiwezekani mtu mmoja aweze kuteketeza kikosi kizima cha zaidi ya watu elfu na ushee na kama akiweza basi itakuwa ni zaidi ya miujiza hashara ya Mtume Musa kwa Farao alipoenda kuwakomboa wana wa Israeli.
Inspekta Jenerali Mark Noble alikuwa ameshachoshwa na maisha haya ya mikiki mikiki. Aliweka nia na adhima ya kuacha kazi katika idara ya Polisi ya Msumbiji, kisha pia astaafu kazi kutoka "Monte Branco Ltd" kazi ambayo ilishakuwa hatarishi kwake. Ambapo suala la kupoteza uhai ilikuwa ni dakika sifuri. Alipanga achukue mafao yake kisha aondoke na mchumba wake Dr.Anabella kwenda kuishi kwenye visiwa vya Madagascar. Kwa mafao yake atakayopewa na Bwana Alfredo yalimpa jeuri na kiburi cha kuweza kuishi nchi yoyote ya Kiafrika bila kufanya kazi kwa muda hata wa miaka 50.
Inspekta Jenerali Mark akiwa amezama kwenye dimbwi la mawazo nje ya sehemu ya kuegeshea magari akiwa anawasubiri akina Bob Chinanga akasikia mlio wa simu yake unaita akaanza kupagawa. Akadhani anataka kuulizwa kuhusu ujio wa Kachero Manu. Ulikuwa ni mlio maalumu kwa ajili ya Bosi wake Bwana Alfredo, akajidhania kama yupo ndotoni maana hakutegemea kupokea simu ya Bwana Alfredo katika kipindi kigumu kama hiki. Alipoitoa simu yake akaipokea huku vidole vinatetemeka kama mlevi gongo.
"Habari za siku BIG BOSS" alisema Mark kwa sauti ya kujifaragua na kujilazimisha furaha. "Njoo ofisini mara moja kabla ya kikao nina mazungumzo nyeti na wewe...!" kisha kabla ya kujibu kitu chochote ikawa tayari simu imeshakatwa na Bwana Alfredo. Moyo wa Mark ukalipuka, na kuanza kwenda mbio kama mwanariadha anayeshindania medali ya dhahabu katika mbio za meta 100 moja. Akapiga moyo konde kuwa liwalo na liwe ngoja aende akamsikilize Bosi wake.
Akaanza kutembea kuelekea kwenye ofisi ya Bwana Alfredo iliyoko chini ya kiwanda kwenye handaki kwa kupitia kwenye maegesho ya magari, huku anajifanya kutikisa funguo za gari yake kupotezea hofu yake kuonyesha anajiamini. Lakini mawazoni alikuwa anajiambia leo kazi ipo kusuka au kunyoa.



Dr.Anabella akili yake ilifanya kazi haraka sana baada ya kukataliwa kuingia pale getini. Alifahamu taarifa zake za usaliti zitawafikia wakubwa zake na haitachukua muda atakamatwa kilaini. Hivyo moja kwa moja alikimbilia kwenye ofisi ya mchumba wake Inspekta Mark Noble. Alipoingia alimkuta Katibu Muhtasi wake Edina ameinamia kompyuta anaandika andika nyaraka mbalimbali.
Katibu muhtasi Edina na Dr.Anabella walikuwa wanafahamiana kitambo hasa kutokana na Dr.Anabella kuja ofisini kwa Mark mara kwa mara. "Samahani naingia ofisini kwa Mark kuna nyaraka za kumsafirishia mgonjwa, Mark kanielekeza nizifuate huku, zinahitajika haraka sana" aliomba Dr.Anabella kwa yule sekretari. Bila kipingamizi alijibiwa "hamna shida shemeji ingia tu kuwa na amani tu bila samahani, unataka nikuzuie kesho nikute barua ya kuachishwa kazi" wote kwa pamoja wakaangua kicheko cha nguvu, huku Dr.Anabella akielekea kufungua mlango. Dr.Anabella alitumia mwanya huo huo kujipenyeza ofisini kwa Mark.
Alipoingia moja kwa moja akaelekea kwenye kabati la mtoto wa meza karibu na kiti cha Mark, akavuta droo akautana na funguo nyingi pamoja na rimoti ndogo rangi nyeusi akaibeba akaihifadhi kwenye koti lake kisha akakizunguka kiti cha Mark. Akavuta kwa mbele kabati dogo la kuwekea mafaili ya taarifa za kipolisi alizokuwa anazishughulikia na vitabu mbalimbali.
Chini ya lile kabati kulikuwa na mfuniko wa chuma kama wa kufunikia chemba za choo. Akazitoa marumaru zilizoegeshwa juu ya ule mfuniko akaziweka pembeni. Akavuta ule mfuniko ukafunguka kisha akaingia kwenye shimo lile mpaka alipogusa ngazi ya kwanza ya kushukia chini akarudishia ule mfuniko vizuri kisha akaanza kuteremka ngazi kuelekea kwenye ofisi ya Mark ingine ambayo ipo chini ya handaki. Kwa msaada wa tochi ya simu yake akawa anashuka kwa haraka. Alipofika ngazi ya mwisho akazima tochi yake akajibanza dakika moja kuangalia kama kuna mtu yoyote, bahati ilikuwa kwake. Hakukuwa na mtu yoyote na korido nzima akawa akitembea taa zinawaka wenyewe kwenye korido.
Kulikuwa na mfumo wa kuleta mwanga pindi zinapohisi kuna binadamu anatembea. Akafika mpaka kwenye ofisi ya Mark ambayo ilikuwa ipo mkabala na ofisi ya Bwana Alfredo. Alipofika mlango akatoa rimoti mfukoni mwake akaanza kubonyeza bonyeza tarakimu za siri haikuchukua muda mrefu mlango ule uliotengenezwa kwa madini ya "aluminium" ukaachia ukaa wazi akaingia akaufunga tena kwa rimoti.
Kisha akaelekea kwenye runinga kubwa iliyopo ndani ya kile chumba akawasha umeme ukutani. Akaruhusu umeme uingie kwenye runinga hiyo kisha akaanza kuona kila kinachoendelea kwenye ukumbi wa mkutano mubashara.
Akashtushwa sana na alichokishuhudia kwa macho yake. Alikuwa hasikii sauti yao kinachozungumzwa mle ndani ya chumba cha mkutano ila aliwaona washirika wake, Kachero Manu na Komandoo "JS" wakiwa wamefungwa kwenye viti kwa kutumia mikanda, wakiwa hawana matumaini ya kujiokoa wao wenyewe.
Alivyowasoma wale walinzi wa ukumbi ndani ya muda mfupi namna walivyojipanga matumaini ya kuwaokoa yakaanza kufufuka upya.
Haraka haraka akatoka nje ya chumba cha Mark bila hata kuzima Televisheni. Akakimbilia ngazi za kupanda juu kuelekea kwenye chumba cha mkutano kutokea kule kwenye handaki akiwa na hamasa zote. Huku bastola yake ikiwa mkononi tahadhari kwa lolote litakalotokea, akaanza kupanda ngazi kwa kasi ya ajabu.

Kachero Manu alizindukia ukumbini akijikuta amemwagiwa maji ya baridi akiwa amefungwa kwenye kiti, pembezoni mwake yupo Komandoo "JS" nae akiwa amefungwa mikanda.
"Kachero Emmanuel Joseph" na "Komandoo Jacob Steven" karibuni sana kwenye mkutano ambao mlikuwa mnatamani mhudhurie, nadhani maombi na dua zenu zimekubaliwa na Mungu mmefika salama" alifungua mkutano huo Bwana Alfredo mwenyewe akiwa na kiko yake pembeni ameikamatia kwa mkono wa kushoto.
Kachero Manu na Komandoo "JS" wakatazamana wakionyeshwa kushangazwa kwa wao kujulikana majina yao kiufasaha. Walichokuwa hawakijui ni kuwa kulikuwa na "CCTV-Camera" zenye uwezo wa kuchukua matukio yote pale kiwandani kwa ufasaha. Hivyo ilivyojulikana kuwa kiwandani pamevamiwa, zilienda kuchukuliwa picha za maeneo yote wakaonekana namna walivyoingia, kisha picha za Kachero Manu na Komandoo "JS" zikatumwa kwa washirika wao Tanzania yakaja majibu ya utambuzi wa Kachero Manu lakini Komandoo "JS" hatambuliki. Zikatumwa picha ya Komandoo "JS" kwa washirika wao wa Msumbiji yakaja majibu ya kila kitu kinachomhusu Komandoo "JS".
"Pia nachukua fursa hii kukupongeza Komandoo Jacob Steven kwa kuteuliwa kwako kuiongoza Idara ya Usalama wa Taifa nchi ya Msumbiji, najua kuwa huna hizo taarifa kutokana na kujishughulisha na mambo yasiyokuhusu, mtaka nyingi nasaba hupata mengi majanga hivyo nasikitika huo uteuzi wako na pongezi zako zitaifikia maiti yako. Kesho asubuhi utaokotwa ukiwa maiti na hilo litakuwa ni onyo takatifu kwa wote wanaojifanya wazalendo wa nchi ya Msumbiji" alisema Bwana Alfredo kwa mbwembwe huku anaanza kuvuta kiko chake.
"Mwisho wako na vibaraka wenzako wa wakoloni Bwana Alfredo umefika, Msumbiji huru yenye kujitoa kwenye makucha ya wanyonyaji inakuja. Msumbiji yenye neema ya uchumi wa gesi, mafuta na madini inakuja, hata kama utatumaliza sisi lakini tutakuwa tumekufa kishujaa, aheri kufa mwili lakini mawazo yako yakawa hai vizazi na vizazi ...!" aliropoka Kachero Manu bila kupewa ruksa kwa kudakiza maneno kwa lengo la kupoteza muda ili kuangalia kama kuna fursa yoyote ya kujiokoa itajitokeza.
"Kelele wewe mbwa koko unaropoka bila kupewa ruksa ya kuongea ngoja tukutie adabu kidogo" alifoka Mark kwa hasira huku anamfuata Kachero Manu kwenye kiti chake kwa.
"Mark achana nae, daima mfa maji haachi kutapatapa hata ukimpiga ni kazi bure huyo ni maiti hai inayosubiri kutolewa roho tu" alisema Bwana Alfredo kwa sauti ya dharau. "Nyinyi ni waoga sana mnapambanaje na sisi hali ya kuwa mmetufunga mikono na miguu? mwanaume wa kweli hawi muoga kiasi hiki Bwana Alfredo, tambueni mshahara wa dhambi ni mauti mtakamatwa mapema iwezekanavyo " alisema Komandoo "JS", nae akijaribu kuvuta muda ili kuona kama kuna fursa yoyote ya kujiokoa itajitokeza.
Bwana Alfredo hakujibu kitu bali alikuwa anaangalia mlango wa mbele yake, alikuwa anaingia kipande cha mtu mrefu, amesokota rasta nywele zake, huku mkononi ameshika shoka kubwa limelowa damu damu iliyogandiana, kuonyesha sio shoka la kibisa ni shoka la kazi.
Mtu huyo alikuwa anatembea kwa mikogo analizungusha hewani shoka lake kwa mitindo tofauti tofauti kama Msolopagazi na Inkosikazi yake. Kachero Manu kwake sura hii haikuwa ngeni kwenye mboni zake za macho, akawa anajaribu kufikiria wapi alimuona huyu mtu. Lakini kutokana na maumivu ya kichwa anayohisi akashindwa kupata majibu ya fikra zake.
"Kachero Manu umefanya mauaji ya kikatili kwa Bob Chinanga, sasa rafiki yake kipenzi anaitwa "Nanga Boy" ameomba aje kutenganisha shingo yako kwa shoka yeye mwenyewe kulipiza kisasi cha rafiki yake" alisema Inspekta Mark Noble huku anacheka kicheko cha kebehi na dharau. Yule rafiki wa Bob Chinanga alikuwa anatokwa machozi ya uchungu mkali wa hasira. Kachero Manu akakumbuka yule jamaa alionana nae kambi ya mateso Gorongosa, ndio walimtesa yeye na Bob Chinanga.
Komandoo "JS" alikuwa ameinamisha kichwa chini kama kobe anayetunga sheria vile, huku Kachero Manu akiangaza angaza kwenye chumba kama mtu asiyekata tamaa akisaka fursa yoyote ya kujiokoa, akili yake ilikuwa inampa asilimia 98% kuwa ataokoka na asilimia 2% ndio ilikuwa inampa hofu ya kupata madhara.
"Ndugu wajumbe Kabla hatujaanza mkutano wetu hawa wawili wauwawe kikatili kwa shoka huku Mark nikikupa jukumu la kumtafuta hawara yako Dr.Anabella na kumpoteza haraka sana baada ya kikao hiki kama hatopatikana kwa haraka, jiandae kufa wewe kwa niaba yake kwa kosa la kutupandikizia kirusi kwenye kundi letu...! " alitoa amri Bwana Alfredo kwa sauti yenye hasira na hamaki kali akionyeshwa kuchukizwa na Mark.
"Sawa Bosi wangu nitatekeleza kwa uaminifu mkubwa" alijibu Inspekta Mark huku anatetemeka sura yake imemsawijika vilivyo, akijuta kumfahamu Dr.Anabella.
"Salini sala zenu za mwisho kabla Nanga Boy hajavunja shingo zenu" alisema Inspekta Jenerali Mark huku akimuangalia Nanga Boy ambaye alikuwa akisogelea kwenye kiti alichofungwa Kachero Manu. Alipofika karibu yake kabisa akanyanyua shoka juu kusubiri amri ya kukata shingo ya Kachero Manu. Ukumbi mzima ukapewa amri ya kusimama, kisha Mark akasogea karibu ya Nanga Boy, akaanza kuhesabu ili akifika tatu Nanga Boy ashushe shoka shingoni.
"Moja, mbili, taa....." kabla hajamalizia kuhesabu tatu, ghafla mlango wa nyuma ya kiti cha Bwana Alfredo ukavunjwa kwa kishindo kikubwa, huku Kachero Manu akitumia nguvu zake zote kujitupa pembeni. Shoka lile lililotupwa na "Nanga-Boy" likatua kwenye kingo ya kiti na kukata mikanda iliyomfunga Kachero Manu.
Ambapo bila kuzubaa Kachero Manu akaanza kujifungua mikanda iliyobakia. Risasi ya kutoka kwa Dr.Anabella ilitua sawia kwenye bega la mchumba wake Mark na kusababisha bastola yake kumponyoka. Kachero Manu akawa kashajifungua tayari. Kutupa macho pembeni akamuona Inspekta Jenerali Mark anajivuta kwa kutambaa kuifuatilia bastola yake iliyomponyoka huku damu zinamchuruzika.
Kachero Manu hakumkawiza akamchapa teke la begani mahali pale pale alipopigwa risasi na Dr.Anabella kama kulitonesha jeraha tena, akawa anagugumia kwa maumivu makali. Kisha akaiwahi yeye ile bastola sasa ikawa mikononi mwake. Akawa anamkinga nayo Dr.Anabella asishambuliwe ambaye alikuwa anamalizia kumfungua mikanda Komandoo "JS". Tayari, Nanga Boy alikuwa anakimbilia upande wa Bwana Alfredo kwenda kuwalinda baadhi ya viongozi.
Kabla Nanga Boy hajaifikia meza kuu ya viongozi, Bwana Alfredo akamrushia bastola, ghafla wakashtukia Dr.Anabella anagugumia kwa kali sauti ya maumivu, "Maaaamaaaaah naaa..kuf............ aaaaaaaah....!" alikuwa amepigwa risasi ya tumboni na Bwana Alfredo, akakaa chini kwa kupweteka.
Komandoo "JS" akawa anatambaa chini kwa chini akiwa anamvizia Bwana Alfredo huku Kachero Manu akiwa tayari ameshawachakaza kwa risasi Mafioso kama 6 kitendo ambacho kilimgutusha Bwana Alfredo na kujiona yumo hatarini. Huku mkono wake wa kulia akiwa amebeba faili rangi nyeusi, na mkono wa kushoto ana bastola yake na shingoni amening'iniza "USB-flash" akawa anamwaga risasi ovyo huku anaelekea upande wa kulia wa jengo.
Alipofika kwenye makutano ya kuta mbili, akarusha risasi iliyompata Inspekta Jenerali Mark kwenye usawa wa moyo wa Mark. "Aaaaaaaah.......My Boss you are killing me Whyyyyyy.....!" alilalama Inspekta Jenerali Mark kwa uchungu mkubwa wa maumivu. Risasi ambayo ilipoteza kabisa uhai wa Mark, asingeweza kupona hata kama apelekwe kwenye hospitali bora kama ile ya Apollo iliyopo nchini India.
Bwana Alfredo alikuwa anathibitisha ukomavu wake kwenye ujasusi hakutaka Mark akamatwe kirahisi aweze kuropoka siri zake. Kisha akatoa kitu kidogo mfukoni mfano wa rimoti ghafla kuta mbili zikatengana akatokemea na kuta mbili zikajifunga. Ilikuwa ni kama kiini macho kinafanyika mbele yao kitu ambacho hawakukitegemea. Ilikuwa ni jambo la sekunde kadhaa tu.
"Anatooo...ro...ookaaa...muwa...aaaa.... hini kw... eny....e... maaaeg...esh... o... ya maag...ariii...!" alitoa maelezo Dr.Anabella kwa sauti ya shida ya maumivu. Komandoo "JS" akampa ishara Kachero Manu kuwa anamfuatilia Bwana Alfredo yeye apambane na Nanga Boy.
Nanga Boy akajikuta bastola yake imeishiwa na risasi, Kachero Manu akatupa chini bastola yake akampa ishara wapambane kwa mikono. Ikawa wameshasogeleana kama mahasimu wawili wa kwenye masumbwi ni fursa adhimu ambayo Kachero Manu alikuwa anaitamani ya kulipiza kisasi cha mateso ya kifo aliyopewa kambini na mbwa hawa "Bob Chinanga" na "Nanga Boy".
Alikuwa ni Nanga Boy kuwa wa kwanza kutupa konde la mkono wa kushoto likatua sawia kwa Kachero Manu usawa wa shingo yake. Ilikuwa ni katika harakati za kujaribu kukwepesha konde hilo lisitue kwenye taya zake likaharibu mpangilio mzuri wa meno yake. Nanga Boy akarusha kombora la teke kali la usawa wa mbavuni, bahati nzuri Kachero Manu akakaza misuli ya tumboni. Teke hilo lilimyumbisha Kachero Manu akafanikiwa kujizuia asianguke chini. Akajibu mapigo kwa kurusha teke la sehemu za siri za "Nanga Boy". Nae akawa mwepesi akawahi kulipangua kwa mikono yake, vinginevyo angekuwa mgumba maisha yake yote yaliyobakia.
Kachero Manu hakuwa na muda wa kupoteza na huyu "Nanga Boy" hasa ukichukulia mlengwa wao, Bwana Alfredo hawajamkamata bado, kashawatimulia vumbi. Hivyo akaanza kuruka ruka huku amekunja ngumi mithili ya BRUCE-LEE huku anarudi nyuma nyuma, Nanga Boy akapotea maboya akadhani kurudi nyuma nyuma Kachero Manu anamuogopa akawa anakuja mzobe mzobe ili ambebe Kachero Manu na ampigize chini.
Alivyombeba tu Kachero Manu akampiga na vifuti vya mikono juu ya utosi wa Nanga Boy, damu zikaanza kumchuruzika kama bomba, akamtupa chini. "Nanga Boy" akawa amelewa kutokana na kupoteza kwa damu nyingi kwa wakati mmoja ikawa kila anavyokuja, Kachero Manu anamkwepa, anakwenda kujigonga kwenye viti vya kwenye chumba cha mkutano. Mara ya mwisho baada ya kuona anachezewa hangaisha bwege na Kachero Manu, akaliokota shoka lake akawa anakuja nalo kwa kasi ampige nalo Kachero Manu huku anapiga kelele za kupandisha mori kama morani wa Kimasai aliyepewa ahadi ya kupewa mke kama akiua Simba.
Kachero Manu akasimama wima huku akiwa ameipanua kidogo miguu yake kupata uimara wa mwili. Alivyofika kushusha shoka lake, Kachero Manu akaudaka mkono wake na kuuzungusha kidogo tu, Nanga Boy alipiga yowe la nguvu. Mfupa wake wa maungio ya bega ulikuwa umechomoka begani, kirungu cha maungio ya mfupa begani kinaning'inia nje ya bega.
Hakumkawiza akamchota mtama akaangukia kisogoni chini ya sakafu, akawa anatupa tupa miguu ya kushoto na kulia alikuwa anakata roho.
Kachero Manu akapata nafasi ya kukimbilia kwa Dr.Anabella ambaye alikuwa yupo kimya kama amefariki vile. Alikuwa amezimia kutokana na kupoteza damu nyingi sana. Alichofanya ni kushika maeneo ya kifuani, akabinya kwa nguvu kwa kutumia vidole vyake akawa anasikia mapigo ya moyo kwa mbali. Akaenda kwenye simu ya mezani kwenye kila chumba cha mkutano na kupiga simu ya dharura ili gari la kubeba wagonjwa mahututi lifike kuwapeleka majeruhi hospitalini. Pia akapiga simu idara ya usalama Ikulu moja kwa moja waje haraka sana kuwakamata watuhumiwa, kisha akakata simu na kukimbilia nje kusaidiana na Komandoo JS.


Komandoo "JS" alipotoka nje akaelekea kule alikoelekezwa na Dr.Anabella kwenye maegesho ya chini kwa chini ya magari. Ilionekana hamna njia ingine ya kutokea kule kwenye handaki isipokuwa kwenye maegesho haya.
Akawa anatambaa chini kwa chini kuelekea kule kwenye magari ya thamani kubwa ambapo alihisi gari mojawapo ni la Bwana Alfredo. Ghafla mvua ya risasi ikaanza kumfuata, salama yake kulikuwa na kigiza giza hivyo walengaji wakawa wanakosa risasi akabingirika mpaka akafanikiwa kuingia chini ya uvungu wa gari.
Kisha akapata wazo la kuwachanganya, akatoa rimoti kama saa mfukoni mwake, akabonyeza bonyeza vitufe vyake. Ghafla bin vuu mabomu aliyotega nje ya ukuta wa jengo la kiwanda yakanza kulipuka. Mbinu ambayo ilifanikiwa wale washambuliaji wake wakawa wanakimbizana kuokoa maisha yao, wengine walitupa mpaka silaha zao.
Bwana Alfredo nae akatimka mbio na faili lake mkononi na bastola akitokea kwenye karakana alikokuwa amejichimbia kwenye mashine mbovu na kukimbilia kuingia kwenye gari lile lile ambalo chini yake kuna Komandoo "JS".
Komandoo akawa anatambaa chini ya chasesi ya gari alipofika mwishoni kwenye buti gari ikaanza kuondoka. Komandoo "JS" akafanikisha kushika chuma cha kingo za nyuma kinacholinda gari na ajali akawa anaburutwa chini lakini haliachii gari.
Kachero Manu akiwa anatokeza kwenye maegesho akawa anaona gari inakuja usawa wake akarusha risasi moja iliyotua kwenye tairi la kushoto la gari ikaanza kuyumba huku tayari Komandoo "JS" yupo juu ya gari kashaipandia anatambaa kwenye bodi ya gari mpaka akafika usawa wa siti ya abiria kiti cha nyuma.
Bwana Alfredo alikuwa ametingwa na kujibizana risasi na Kachero Manu akajisahau kuwa kuna namba ingine chafu sana kuliko hata huyo Kachero Manu nayo inamuwinda imfikishe katika mikono ya sheria.
Alichofanya Komandoo "JS" ni kutoa kioo cha dirisha la gari kwa kutumia pete yake ya almasi aliyovaa mkono wake wa kushoto, kisha akaingia kwenye kupitia dirishani kisha akajikohoza. Bwana Alfredo akageuka, mshtuko alioupata hakuamini mpaka bastola yake ikamponyoka ikaingia chini ya uvungu wa siti ya kiti cha dereva.
Alikuwa haamini anachokia kwenye mboni za macho yake. Akawa anachochea mwendokasi wa gari kuelekea kwenye tanki la mafuta mkabala na geti la kutokea. Akili ya Komandoo "JS" ikausoma mchezo wote kuwa ana lengo la kujitoa mhanga kama magaidi kwa kwenda kulipigiza gari kwenye tanki la kuhifadhia mafuta na kusababisha mlipuko ili wafe wote.
Komandoo "JS" akarukia kiti cha mbele wakawa wanapimana ubavu wa nguvu za mikono kwa kugombaniana usukani wa gari, mpaka walipokaribia meta chache kulifikia tenki la mafuta, Bwana Alfredo akafungua mlango wa dereva na kurusha nje faili lake jeusi kisha yeye mwenyewe kuruka nje ya gari.
Kishindo kikubwa cha mlipuko kilisikika baada ya gari kwenda kujibamiza kwenye tenki na kushika moto. Wakati huo huo gari ya kubeba wagonjwa mahututi na gari za polisi zikawa zimewasili kiwandani.
Dr.Anabella na Komandoo "JS" ambaye nae alifanikiwa kuruka nje ya gari walikuwa wamepoteza fahamu hivyo wakawa wa kwanza kupakizwa na kuwahishwa hospitali kwa matibabu. Bwana Alfredo alikuwa amevunjika kiuno kutokana na risasi tano alizopigwa kiunoni akiwa hewani na Kachero Manu alipokuwa anaruka nje ya gari, akapigwa pingu za mikononi na miguuni tayari kwa safari ya kituo cha polisi. Shughuli yote ya kuwashikisha adabu vibaraka wa wakoloni ilikamilika saa saba kamili usiku.

SURA YA KUMI NA TISA
La Mgambo limelia Ushindi hadharani
Asubuhi ilipambazuka kwa Kachero Manu akiwa amelala katika moja ya hoteli kubwa na ya kifahari inayoitwa "Cardoso" iliyopo Jijini Maputo. Ilikuwa ni hoteli ambayo hawafikii hapo ila watu wenye sharafu na pesa nyingi. Alipelekwa usiku usiku na ndege binafsi ya Rais wa Msumbiji na kupewa ulinzi wenye hadhi ya kibalozi.
Rais wa Msumbiji alikuwa amefurahishwa na ushujaa wa Kachero Manu kwa kufanikiwa kukisambaratisha kikosi cha Mafioso waliokuwa wanachafua jina na hadhi ya Msumbiji kitaifa na kimataifa.
Mafioso ambao kama wangechekewa wangeziingiza kwenye uhusiano tete nchi za Msumbiji na Tanzania na kuvunja misingi ya waasisi wa mataifa hayo.
Hivyo akaagiza Kachero Manu apewe ulinzi mkubwa asije akapata madhara kutoka kwa wanyonya mirija waliobaki kwenye mfumo wa vibaraka walioujenga toka enzi za mapambano ya kudai uhuru wa Msumbiji. Akaenda kuwekwa kwenye hoteli ambayo usingizi wake kwa siku ni zaidi ya milioni mbili kwa pesa za kitanzania.
Aliamshwa Kachero Manu asubuhi hiyo na miale ya jua isiyo na makali iliyokuwa inapenya katika vioo vya dirisha lake ambalo hakufunga pazia lake kutokana na uchovu wa mapambano ya usiku kucha. Alitupa pembeni blangeti lake la kujifunika na baridi akachukua rimoti ya kipoza hewa cha chumba akazima. Kisha akapiga magoti akaanza kusali kumshukuru Mungu kwa kumpa nafasi ingine ya kuwa hai hasa ukichukulia kwenye majukumu haya mazito aliyopewa nchini Msumbiji ndani ya siku kadhaa hizi amechungulia mdomo wa kifo mara nyingi sana kisha anaponea chupuchupu.
Baada ya kumaliza sala fupi akanyanyuka akapiga simu jikoni kuagiza kifungua kinywa, kisha akawasha runinga iliyotundikwa juu katika ukuta wa chumbani kwake, ilikuwa ni saa mbili asubuhi akakutana na taarifa ya habari ya Shirika la Habari la Afrika ya Kusini (SABC). Akawa anajongea mlango wa maliwatoni kwenda kuoga maji ili mwili upate nguvu mpya alipofika mlango wa maliwato kabla hajaingia, akamsikia msomaji wa taarifa ya habari anaelezea habari zilizowafikia hivi punde, akasimama kuangalia hiyo taarifa.
"Kachero bobezi kutokana nchini Tanzania kwa kushirikiana na Komandoo mkongwe wa nchini Msumbiji wamefanikiwa kuwatia mbaroni viongozi wahalifu wa kundi la NACATANAS lililokuwa linaongoza mauaji ya raia wasio na hatia pamoja na uporaji katika machimbo mbalimbali ya madini nchini Msumbiji. Pia jeshi la Msumbiji limefanikiwa usiku wa kuamkia leo kukamata shehena ya madawa ya kulevya na kontena mbili za madini ya rubi ziliyokuwa zimefichwa katika kiwanda cha korosho tayari kwa kusafirishwa nje ya nchi. Pia jeshi la polisi linamshikilia mmiliki wa kampuni ya Monte Branco Ltd Bwana Alfredo kwa tuhuma za kuendesha shughuli mbalimbali haramu nchini Msumbiji ikiwemo kufadhili kikundi cha "NACATANAS", na atapandishwa kizimbani mara tu baada ya upelelezi kukamilika. Pia jeshi la polisi limefanikiwa kunasa majina ya washirika wote wa Bwana Alfredo waliopo serikalini na kwenye taasisi binafsi. Uchunguzi bado unaendelea nao watafikishwa mahakamani mara moja baada ya upelelezi kukamilika. Wakati huo huo Rais wa Msumbiji amemteua ndugu Jacob Steven kuwa mkuu mpya wa Idara ya Ujasusi na Usalama nchini Msumbiji. Uteuzi huo unaanza mara moja kuanzia leo. Pia mheshimiwa Rais amemuagiza katibu mkuu wa Wizara ya Afya kumpangia mara moja kituo cha kazi Dr.Anabella katika hospitali yoyote nchini Msumbiji atakayopenda kufanyia kazi".
Kachero Manu akatabasamu, akiacha na habari hiyo na kufungua mlango wa maliwato kwenda kumwaga maji. Alikuwa akijiandaa aelekee hospitalini kabla hajapaa kurejea Tanzania.
Baada ya kupata staftahi yake akiwa tayari amevalia mavazi yake nadhifu, saa 4:00 kamili juu ya alama za asubuhi, Kachero Manu alikuwa ndio anawasili katika viunga vya hospitali binafsi ya kisasa inayoitwa "Hospital Privado de Maputo" iliyopo eneo la "Ruo do Rio Inhamiara", Jijini Maputo. Alikuja kuwazuru wenzake Dr.Anabella na Komandoo "JS", wenzake ambao alishirikiana nao bega kwa bega katika misheni takatifu ya kuwaangamiza wahujumu wa uchumi wa nchi ya Msumbiji. Dr.Anabella na Komandoo "JS" nao walikimbizwa usiku usiku Jijini Maputo kwa ndege maalumu ambayo inavifaa vyote vya kuhudumia wagonjwa mahututi.
Kachero Manu alisindikizwa pale hospitalini na msafara wa ulinzi madhubuti wa Jeshi la Msumbiji utasema Rais wa Taifa kubwa kama Marekani ametua nchini Msumbiji. Komandoo "JS" hakufanikiwa kuongea nae alimkuta yupo kwenye chumba cha wagonjwa mahututi 'ICU' amezinduka tayari, lakini ana maumivu makali. Hivyo alishauriwa na Daktari amuache mgonjwa apumzike vya kutosha. Ila Dr.Anabella alifanikiwa kuongea nae kwa tabu sana, huku akionekana kuwa na furaha sheshe inayotokana na kushiriki kulipiza kisasi cha walioua familia yake.
Baada ya kutoka hospitali akarudi hotelini kujiandaa na safari ya kurejea Tanzania usiku wake. Alishaongea na kwenye simu na Bosi wake wa Idara ya Usalama wa Taifa Bwana Mathew Kilanga, huku akimpongeza na kumuahidi mapokezi ya kishindo ya kishujaa.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog