Search This Blog

Thursday 23 March 2023

HUJUMA NZITO - 3

  

Simulizi : Hujuma Nzito

Sehemu Ya : Tatu (3)

"Mtakunywa vinywaji vyovyote tafadhali?" walitibuliwa mazungumzo yao na mhudumu wa mkahawa baada ya kuwaona wamekaa muda mrefu baada ya kumaliza kula bila kupata vinywaji. Hivyo hisia zake zikamtuma ajiongeze tu kwa kuwafuata na kuwauliza.

"OK...ahsante bila samahani hamna shida, tena umetufaa mie naomba "Grand Reserve ya Wine list" nichague kwanza kabla sijakuagiza" alizungumza Nathanieli huku akinyoosha mkono wake wa kulia kupokea karatasi ya orodha ya vinywaji aliyoiomba toka kwa yule mhudumu. "Nipatie glasi ya mvinyo wa "Bovlei Cape classic dry red" tafadhali" alimpa oda mhudumu huku nae Yasmine akiwa ameikamatia ile karatasi aliyoichukua toka kwa Nathanieli nae akawa anaperuzi kwa haraka haraka orodha ya vinywaji ili achague.

"Nipatie "Pearly Bay Sparkling" niijaribishe sijawahi kuinywa hiyo" alitoa oda yake Kachero Yasmine. "Aaah..bora ungeagiza "Swartland Bay Sparkling" nayo pia haileweshi ni katika kundi moja la vinywaji visivyo na kilevi, vinywaji vyenu watoto wa Masheikh lakini mie naona ndio ina ladha tamu kuliko uliyoiagiza, lakini ni ushauri wangu tu... ..! " aliingilia kati Nathanieli uchaguzi wa kinywaji wa Kachero Yasmine huku wakiangua kicheko kutokana na utani huo.

"Wewe ondoa hofu mie leo naenda kulala kwako leo laazizi, Baba mdogo amesafiri kikazi toka juzi anarudi kesho, maana naona unavyohangaika kutaka kunichagulia vilevi vikali vikali, ili niangushe gari hapa hapa mkahawani ujiokotee embe dodo chini ya mwarobaini..!" alijibu Yasmine, jibu ambalo lilisababisha wote wafe kwa kicheko kwa mara ya pili huku Nathanieli akiwa haamini kama kweli mambo yamekuwa mepesi kuliko alivyotegemea.

Akawa anavuta taswira Yasmine ndio kashafika nyumbani kwake wako wawili tu, jinsi nyasi za uwanja wa fundi seremala zitakavyowaka moto, kwenye pambano la patashika nguo kuchanika hakuna kulala hiyo mpaka lyamba. Kuna kipindi wakati vinywaji vyao vimeshaletwa, Nathanieli akajiroga kwenda msalani, Kachero Yasmine hakupoteza fursa aliyokuwa anaisotea kwa muda mrefu.

Akachomoa kichupa kidogo toka kwenye mkoba wake, akanyunyizia dawa za kulevya kidogo tu kwenye kinywaji cha Nathanieli, na kukirudisha haraka haraka kichupa chake kwenye mkoba wake. Dawa hizo alizonyunyiza zilikuwa zinatenza nguvu taratibu na kukufanya uwe unaonekana umelewa maradufu bila kukuchosha. Baada ya kuburudika kwa vinywaji kwa muda fulani tokea arudi msalani, Nathanieli taratibu bila kujielewa akaanza kujiskia vibaya.

Hiyo ilikuwa ni ishara ya kuzidiwa na mtindi alioutwika kichwani, akajikuta anaanza kulalama. "Aiseeh...Mpenzi tuondoke haraka tukalale, ila gari yangu utaendesha wewe najiskia vibaya sana, pombe zimenielemea vibaya leo kuliko kawaida yangu mpaka najishangaa.. !".
Yasmine akachangamkia fursa haraka kwa kulipa bili za gharama ya huduma ya vinywaji na chakula walivyokula na kunywa. Kisha Yasmine akachukua funguo za gari za Nathanieli zilizokuwa zipo mezani kwa ajili ya kuondoka. Akafanya maamuzi ya kuiacha gari yake pale pale Hotelini kwa minajiri ya kuwa atalifuata kwa muda wake.

Sasa alikuwa anajua anakwenda nyumbani kwa Nathanieli kufanya taftishi ya chochote kitakachomsaidia kwenye upelelezi wake kwa raha mustarehe bila usumbufu. Kwa mihadarati aliyomchanganyia, alijua fika muda sio mrefu atalala fe fe fe, aweze kujimwayamwaya anavyotaka yeye.

"Toka lini paka na panya wakapendana kwa mapenzi ya maki! Huo ni ujuha, imekula kwake" aliwaza Kachero Yasmine kwa furaha ya ushindi huku akiwa anaendesha gari kwa ustadi mkubwa kuelekea nyumbani kwa Nathanieli.


Kachero Manu mikononi mwa adui zake nchini Afrika ya Kusini..

Ilikuwa ni majira ya 4:00 ya asubuhi mwanana, Kachero Manu alikuwa ndio kwanza anatua katika uwanja wa Kimataifa wa "Cape Town" nchini Afrika ya Kusini na ndege ya shirika la ndege la nchini Angola, "TAAG Angola Airlines", akitokea Jijini Dar es Salaam.

Kibaridi cha Bondeni kwa Mzee Madiba kilikuwa kinapuliza sana asubuhi hiyo utadhania bado ni usiku. Hivyo hakusahau kabisa kutupia jaketi la rangi ya kahawia na kofia ya mzula nyeusi kichwani mwake walau kupunguza makali ya baridi hiyo.

Alijibadilisha muonekano wake akionekana kama mtu mzima kiumri kutokana na ndevu bandia na masharafa bandia aliyojibandika nayo usoni.
Kwa muonekano wake tu jinsi alivyofanikiwa kujibadilisha hata mama yake mzazi Kachero Manu Kama angepitishiwa mwanawe amtambue asingeweza kumtambua hata kama angepitishwa zaidi ya mara 100 mbele ya uso wake.

Aliposhuka tu kwenye ndege pale uwanjani moja kwa moja akaelekea kwenye dawati la idara ya uhamiaji kwa ajili ya ukaguzi wa kina na maswali mepesi mepesi ya kizushi.
Alichokuwa hakifahamu Kachero Manu ni kuwa pale kwenye dawati la uhamiaji kulikuwa na kibaraka wa kundi la "Nyasa Empire Supporter" (NES) mwenye ujuzi wa hali ya juu wa mambo ya ujasusi ambaye alimgundua kwa baadhi ya viashiria tu. Kwanza matumizi ya mkono wa kushoto kama walivyotonywa na Afisa wa juu wa jeshi la polisi Bwana Chew Master.

Pili alijisahau kubadilisha sauti yake ili iendane na umri wake kiasi kwamba kwa uzoefu wake baada ya kumchunguza usoni akaona viashiria vya uwekwaji wa ndevu, masharafa na kionja mchuzi bandia.
Alipotoka tu Kachero Manu pale dawatini, kibaraka akawatonya wenzake kuwa mshukiwa wao wanayemhisi, tayari kashatua nchini Afrika ya Kusini na anategemea kufikia nyumba ya kulala wageni inayoitwa "New Salama Lodge Milnerton" umbali wa kama kilometa17.7 kutokea uwanja wa ndege wa "Cape Town".

Kabla hajaondoka uwanjani kwenda alipotarajia kupata malazi akaonana na rafiki yake wa kitambo anaitwa Dr. Edson Nkube ambaye nae alikuja kumlaki pale uwanjani. Alikuwa anafanya kazi katika kituo cha kimataifa cha harakati za amani, "International Peace Support Training Centre" (IPSTC) kilichopo nchini Afrika ya Kusini, wakitoa mafunzo maaalumu kwa nchi za SADC.

Dr. Edson Nkube alizaliwa Tanzania katika kambi ya wakimbizi wa Afrika ya Kusini iliyopo Mazimbu, Morogoro. Alikuwa anakicharaza kiswahili utasema ni Mluguru wa Matombo kumbe ni Mzulu wa baba na mama.

"Nikupunguzie mizunguko na sampuli yako, nitaipeleka maabara sasa hivi na majibu ni ndani ya siku mbili. Wewe nenda kapumzike jioni jioni tutakutana saa 1 usiku shapu tupange mikakati ya kesho" alizungumza Dr.Edson huku Kachero Manu akiwa hana neno la kutia akionyesha amekubaliana uamuzi huo wa kumsaidia kazi hiyo hasa ukichukulia yeye ndio mwenyeji wake.

"Hey...Shoo Shoo...!" "OK....Sharp.. Sharp..!", alisalimia Kachero Manu salamu ya lugha ya kimtaani ya nchini Afrika ya Kusini kumsalimia dereva teksi, nae akamjibu kuwa mambo yako safi. "Can you take me to "New Salama Lodge"?". "Yes...just prepare 25 Rand..!". Wakawa ndani ya dakika chache wameshaelewana wakaanza msafara wa kuelekea huko.

Alikuwa amechoka vibaya hasa akichukulia usiku wake uliopita alikuwa nyumbani kwa Meja Marwa akarejea nyumbani muda mbaya kabla ya alfajiri yake kuanza msafara wa kuja nchini Afrika ya Kusini. Ilimchukua takribani dakika 20 kufika hapo New Salama, ambayo lilikuwa ni jengo jipya la roshani 12, pembeni yake kukiwa na "Salama Lodge" ya zamani.

Mmiliki wa hizi nyumba zote mbili za kulala wageni alikuwa ni mtu mmoja. Alipowasili tu pale kwenye nyumba ya kulala wageni kabla hata hajafika mapokezi, wakaingia watu watatu waliokuwa wanaonekana wana haraka, ambao moja kwa moja wakapitiliza pale mapokezi wakaelekea kwenye lifti na kupandisha juu.

Kachero Manu hakuwajali sana akajua labda ni wageni wenzake. Akafika ofisi ya mapokezi na kupokelewa kwa bashasha na mhudumu, wakasalimiana kisha akaeleza shida yake ya kuhitaji chumba.
"Chumba kipo roshani ya 12, kimebaki chumba namba 126 tu" alijibu mhudumu kwa kutumia Kiswahili fasaha kabisa kuthibitisha kweli nchi za SADC zimeamua kukifanya kiswahili ni lugha yao ya mawasiliano kwa kuhakikisha kinatumika kwenye nyumba zote za kulala wageni.

Bila kufanya majadiliano mengi akakamilisha taratibu zote za usajili na malipo, akaelekea kwenye lifti kwa ajili ya kupandisha ghorofani. Alipo bonyeza kitufe cha kuita lifti haikuchukua muda mrefu ikaja na kufunguka, akaingia na kufunga mlango wa lifti kwa kubonyeza kitufe maalumu.

Kisha akabonyeza namba 12 kwenye lifti ile kuipa maelekezo kuwa anakusudia kwenda mpaka roshani ya 12. Lifti ikakubali maelekezo na kuanza kupanda kwa kasi kuelekea juu kabisa ya jengo.
Ndani ya dakika moja na sekunde kadhaa akawa ameshafika roshani ya 12. Akajizoazoa na kutelemka nje ya lifti ile akiwa na begi lake dogo la safari alilolifumbata mgongoni mwake.

Akaanza kutembea kwenye korido ya vyumba kukisaka chumba namba 126 alichokilipia.
Punde si punde akakiona, akasogelea mlango na kuchomoa mfukoni mwake kikadi kidogo cheupe chenye ukubwa ukubwa sawa na kadi ya ATM ya kutolea pesa benki. Kikadi hicho kilibandikwa lebo ndogo yenye tarakimu 126 juu yake.
Akakisogeza kikazi hicho karibu kabisa na kitasa cha mlango, rangi nyekundu ikawaka juu ya kitasa kisha ikawaka rangi ya bahari buluu kuashiria unaweza sasa kufungua mlango.

Aliponyonga kitasa na kuingia ndani ya chumba, kengele ya tahadhari ikalia kichwani mwake, kuashiria mambo hayapo sawa kuna jambo lisilo la kawaida. Wakati anajiandaa kutaka kuchomoa bastola yake toka kiunoni mwake alishachelewa, wakamuwahi yeye.

"Nyoosha mikono yako juu mara moja, usilete ghiliba zozote, nitasambaratisha ubongo wako mara moja" ilikuwa ni sauti kali na nzito, isiyo na chembe ya masihara ya mtu aliyejificha ndani ya chumba kile.
Kachero Manu akatii amri huku akiwa ameshikwa na butwaa, anajiona kama yupo ndotoni. Ghafla akiwa bado yupo kwenye taharuki ukapigwa mluzi wakajitokeza watu wengine wawili mule chumbani.

Alipoziona tu sura zao, akawakumbuka kuwa alipishana nao chini pale karibu ya ofisi ya mapokezi. "Ha.. ha... ha... ha.. ha....kwisha habari yako mbwa jike wewe..!" aliongea kwa kicheko cha kebehi mmoja wao wale wajuba huku wengine wakimzingira na kufanikiwa kumpokonya silaha.

Sasa alikuwa yupo kilingeni, yupo mikononi mwa mahasimu zake watatu na wote wana silaha zao. Kachero Manu alikuwa anasubiri muujiza tu wa Mola wake, alijua fika saa ya kifo chake imekaribia, hana ujanja tena.


Kachero Yasmine afanikiwa kudukua taarifa nyeti za Dola ya Nyasa

Mpaka nyakati za mafungulia ng'ombe, jua angani limeshaanza harakati zake za kusimama dede, bado Nathanieli alikuwa yupo usingizini anakoroma zake. Kachero Yasmine, akijifanya mchumba mwema, alikuwa amedamka, ameshafanya usafi wa nyumba nzima huku akiwa tayari ameshaandaa staftahi maalumu kwa ajili yao.

Baada ya hapo akafanya mazoezi mazito ya dakika 45 kwenye chumba kidogo chenye mashine zote muhimu za kufanya mazoezi kilichopo ndani ya jumba hilo la kifahari. Kisha akaelekea bafuni kujiandaa kwa ajili ya kurudi nyumbani kwake. "Nath...Nath...Nath...!" aliita kwa nguvu huku anamtikisa pale kitandani.

"Eeeeh....Eeeeh....Daaah.....kumekucha hivi siamini macho yangu..!" alijikuta anaitika huku anakurupuka usingizini na kuufikicha uso wake na kiganja chake cha mkono wa kulia. Kisha akajizoazoa kitandani na kukaa kitako pembezoni mwa kitanda, miguu yake ikiwa imegota chini huku anapiga miayo ya uchovu.

"It's time baby.....amka Bwana mpaka umeniogopesha umepatwa na maswaibu gani, jana umezidisha sana mipombe yako sijui kwanini uliamua kufanya hivyo?" alizidi kujifaragua Yasmine, akiwa amevaa taulo tu mwilini mwake alilolifunga mpaka usawa wa juu ya matiti yake na kuacha sehemu kubwa ya mapaja yake wazi akiwa ndio kwanza ametoka maliwatoni kujimwagia maji. Alikuwa anamuangalia kimahaba mpenzi wake mpya feki pembezoni mwa kitanda.

"Daah..I'm sorry sifahamu nini kimenitokea ndio mara yangu ya kwanza kukumbana na hali kama hiyo. Nashukuru Mungu sana nilikuwa na wewe vinginevyo ningeadhirika vibaya sana mbele ya watu pia ningechafua taswira nzima ya taasisi yetu..!" alijitetea huku akiwa amejiinamia pale pale kitandani alipoketi kwa majonzi makubwa.

"Tena ulivyofika tu nyumbani ukapata nguvu za ghafla ukaenda kule kwenye baa yako ya nyumbani ukachukua mvinyo wako wa nyumbani nadhani unaitwa "Simonsig Redhill Pinotage" kama sijasahau jina ukachanganya na konyagi, ukazidi kujidunga hapo ndipo ulipozidi kukoroga mambo ukakata mawasiliano kabisaaaa...!" alikoleza uwongo wake Kachero Yasmine alioutunga ili kumfanya asitie hisia kuwa kuna hila chafu kafanyiwa ili kutimiza malengo maalumu asiyoyafahamu.

"Aaaah...Samahani naahidi haitajitokeza tena hili tatizo usije ukanipiga chini bure kwa kuhofia kuolewa na mume mlevi buda..!" alijitutumua kujitetea huku akijilazimisha kujichangamsha lakini nafsini kwake kulikuwa na majuto makubwa hasa ya kushindwa kuitumia fursa ya ujio wa mrembo nyumbani mwake kisha akatoka salama kama alivyokuja.

"Nenda basi kajimwagie maji fasta tupate kiamsha kinywa cha pamoja nataka niwahi uwanja wa ndege Baba mdogo anarudi leo, kanipigia simu inabidi nikampokee, nikichelewa patachimbika" aliongea Yasmine huku akiwa sasa amempa mgongo Nathanieli akiwa anaanza kulifungua pochi lake aanze kujipodoa ili ajiandae kuondoka. Akawa anajitikisa mwili wake kiuchokozi ili kumtia shemere Nathanieli.

"Sawa mpenzi sina jinsi ya kukuzuia mie nilijua leo Jumapili yote unashinda na mimi humu ndani ili tupande na kushuka pamoja kwenye vilima vya huba, unanikatili mahabubu wangu" aliongea kwa sauti ya kubembeleza huku akiwa tayari ameshajinyanyua toka kitandani amemkumbatia kwa nyuma Yasmine na kumbembeleza abakie akijaribu bahati yake aliyoipoteza.



"Sawa mpenzi sina jinsi ya kukuzuia mie nilijua leo Jumapili yote unashinda na mimi humu ndani ili tupande na kushuka pamoja kwenye vilima vya huba, unanikatili mahabubu wangu" aliongea kwa sauti ya kubembeleza huku akiwa tayari ameshajinyanyua toka kitandani amemkumbatia kwa nyuma Yasmine na kumbembeleza abakie akijaribu bahati yake aliyoipoteza.

"Usihofu mimi ni wako, usiwe na papara na mimi, fursa ikijitokeza siku nyingine nitakuja kupika na kupakua pamoja..ila kwa leo niruhusu tu nikampokee Baba yangu siwezi kuvunja miadi nae tunaheshimiana sana..!" alijitetea Yasmine huku akifanikiwa kujibandua mikononi mwa Nathanieli ambaye ilibaki kidogo abadili zoezi, alishaanza harakati za kutaka kumdondoshea taulo lake.

Uzuri wake Yasmine alikuwa kazini sio kahaba anajua hatua zote za kujilinda anapokuwa sehemu hatarishi na mwanaume. Nathanieli kiunyonge akaweka taulo lake begani akaanza kuelekea maliwatoni bila kutia neno lolote.
Alishakubali matokeo kapoteza pambano tena akiwa uwanja wa nyumbani kwa uzembe wake mwenyewe wa kufakamia pombe kindezi.

Baada ya kitambo kama cha nusu saa akawa tayari ameshaoga na kuvaa pajama lake, wakaelekea wote mesini kwenda kupata mlo.
"Mhhh...chapati tamu na laini kama sufi huku zinazukia marashi ya karafuu, hongera sana kumbe Zenji nako mnatisha kwa mapishi mie nilidhania Tanga peke yake, jicho langu halijakosea kuchagua Visiwani" alitania kusifia mapishi wakati wanaendelea kuishambulia meza ile iliyochafuka mapochopocho ya kila sampuli, kuanzia michapalo ya kila aina mpaka supu na rosti mbalimbali.

"Sasa hizi ni mvua za rasharasha tu, mvua yenyewe ya kidindia ukileta barua ya posa ndio itanyesha kabisa, kila mwishoni mwa juma utakuwa unashinda ndani tu umevaa msuli.....hutoki nje kabisa...!" alijibu mapigo ya utani Yasmine wakabaki wamekufa kicheko huku uma, vijiko na visu vikitoa sauti ya kugongana kwenye sahani zao.

"Gari yako uliiacha wapi?" sasa Nathanieli fahamu zilikuwa zinaanza kumrudia taratibu anaanza kuunganisha matukio kiufasaha. "Niliiacha pale pale Hotelini ili nikulete wewe huku, leo ndio nitaifuata..!" alijibu Yasmine wakati sasa akijiandaa kuondoka wakiwa tayari wameshamaliza staftahi yao.

"Hamna, ngoja nikukimbize mara moja mpaka pale Hotelini uchukue gari yako, mie nitarudi nyumbani leo sitoki sina pa kwenda" aliongea Nathanieli, kisha wakakubaliana na Yasmine. Wakapanda kwenye gari wakiwa wanatoka getini, Yasmine alikuwa na furaha sheshe kwa kufanikisha kilichomleta. Alijiapiza kuwa huu ndio mwanzo na mwisho kukanyaga kwenye kizingiti cha mlango wa nyumba hiyo.
.
Kachero Yasmine alipotoka "Hyatt Regency" kuchukua gari lake akapitiliza moja kwa moja nyumbani kwake Mbweni. Hakuwa na mgeni yeyote uwanja wa ndege, ilikuwa ni danganya toto tu. Alishukuru Mungu kwa kumaliza salama speksheni yake nyumbani kwa Nathanieli bila vikwazo vyovyote.

Alipofika nyumbani alikuta ujumbe wa barua alioachiwa na Kachero Manu ukimtakia kazi njema na ukimpa taarifa kuwa ameelekea nchini Afrika ya Kusini, ambapo anategemea kukaa kwa muda wa wiki mbili tu. Akampa ahadi kuwa akifika tu atampa taarifa Kachero Yasmine kuwa ameshawasili salama.

Kachero Yasmine alifanikiwa kudukua mafaili mengi tu kwenye kompyuta ya nyumbani ya Nathanieli kwa njia zake za utundu. Alifyonza mafaili ya kutosha kwenye flashi yake kwa ajili ya kuja kuyasoma vizuri baadae. Pia alikuta mafaili mengine yamedurufiwa akayaskani kwa kutumia simu yake.

Moja kwa moja alipofika nyumbani akapitiliza kwenye maktaba yao ndogo ya pale nyumbani.
Akaketi kitini na kuwasha kompyuta yake ya mezani. Akaanza kuyadurusu mafaili yake aliyoyadukua kwa Nathanieli. Faili la kwanza kumvutia kulisoma liliandikwa kwa maandishi makubwa yaliyokolezwa MAN-TEMBA FILE?S/N: 532- "THREE IN ONE-SOWETO-HOUSE NO. 29, SINZA-MORI ?ATM-ISSUES". Akapatwa na mshawasha wa kulifungua faili hilo, lakini kwa mshangao mkubwa akakuta faili halijaandikwa chochote. "Bull Shit..! Huu ni ufala sasa..!" alijikuta anaropoka tusi bila kupangilia kutokana na hasira zilizomsokota.

Akafungua faili lingine, nalo akakuta tena jina lile lile, "MAN-TEMBA, FILE S/N: 189- SANDTON CITY CODING SYSTEM" alipopaparika kulifungua faili hilo, mambo yakawa ni yale yale faili lipo kavu halina chembe ya maandishi yoyote.
Akafungua mafaili lukuki aliyoyanyonya lakini hakuambulia kitu zaidi ya mafaili yenye usiri mkubwa sana. "Hawa watu kiboko, wapo makini na shughuli zao, kazi ipo!" aliwaza Kachero Yasmine fikra tasa zisizo na majibu. Mwangaza kidogo akaanza kuupata kwenye baadhi ya nyaraka zilizokubali kufunga na kuwa na maelezo kiasi fulani, yaliyomsaidia kuunganisha matukio.

"Kinachoonekana kuna chumba maalumu kilichopo hapa Tanzania kinachorusha mafaili nje ya nchi. Nchi Yenyewe ni Afrika ya Kusini kwa ajili ya kuchakatwa na ndio ufisadi wote unapikwa huko, huku wanakuja kupakua tu ufisadi wao ukiwa umeshaiva huko" alijikuta anaropoka taratibu kwa furaha akiwa peke yake kwenye chumba cha maktaba.

Pia aligundua kuna miamala mingi ya pesa inafanyika kupitia jina la Mohammed Mtoni kwenye kupitia akaunti ya "JUAKALI GENERAL SUPPLIES" iliyopo mtaa wa Mkwepu, maeneo ya Mjini Posta, Jijini Dar es Salaam. Kila tarehe ambayo nyaraka inatumwa nchini Afrika ya Kusini basi kesho yake kulikuwa na muamala wa Bwana Mohammed Mtoni utatumwa kupitia "JUAKALI GENERAL SUPPLIES" Hilo ndio hitimisho lake alilotoka nalo baada ya kusoma baadhi ya nyaraka zikiwa zina muelekeo huo.

Akamshukuru Mungu angalau kwa fununu alizopata zinazompa mwangaza mweupe kwenye kiza kinene. Akawa anakumbukia jinsi alivyokesha usiku kucha kupekenyua mle maktaba ya nyumbani kwa Nathanieli kwenye vitabu na makabrasha mengi mengi kwa matarajio huenda akaambulia chochote kitu.

Akatuma taarifa nzima ya kiuchunguzi wake kuanzia alipoanzia mpaka alipofikia kwenye barua pepe ya Kachero Manu huku akisubiria simu yake aliyoahidiwa kupigiwa pindi akitua nchini Afrika ya Kusini. Kwenye Kompyuta ya Nathanieli alidukua pia picha za siri alizopiga na wanawake mbalimbali huko Ughaibuni akiwa nusu utupu anakula nao bata.

Hizo picha alipanga azitumie kama tiketi ya kuvunja uhusiano wao, ili kuepusha usumbufu wake. Sasa alikuwa tayari ameshamaliza kazi yake pale Benki Kuu kwa karibia nusu nzima ya kazi aliyoagizwa kwenda kuikamilisha.

Muda sasa ulikuwa umeyoyoma akaanza kuhisi njaa inamkwangua. Mubashara akaelekea jikoni kwenye jokofu lake kuangalia mbogamboga za kupika kwa ajili ya maakuli ya mchana. Akiwa anajiandaa kufungua mlango wa jokofu akaisikia simu yake inaita mlio uliomshtua.

Mlio ambao ulimfanya asitishe zoezi zima analotaka kulifanya kule jikoni na kumfanya atoke mbiombio kama mtu aliyepagawa kuikimbilia simu hiyo. Alipoikaribia tu simu hiyo ikakata. Alipoichukua kuiangalia ikabidi ajifyonye mwenyewe kwa ujinga wake.
Simu ilikuwa imeisha chaji, tokea alivyoipa chaji jana yake mchana na usiku kucha ilikesha nyumbani kwa Nathanieli kuskani na kupiga picha nyaraka mbalimbali.

Hofu sasa ilizidi kushamiri nafsini mwake, kwani alijua fika aliyepiga simu ni Bosi wao wa idara Bwana Omega Mtanika kutokana na mlio maalumu aliouweka kwa ajili yake. Akajutia kwanini alizembea kuiweka kwenye chaji pindi tu alipowasili nyumbani kwake. Haraka haraka akautafuta waya wake wa "USB" maalumu kwa ajili ya kuichaji simu yake kwa bahati nzuri akaupata.

Akaichomeka simu yake kwenye soketi kwa kutumia waya ule ili walau kuiamsha chaji itakayomuwezesha kufanya mawasiliano na Mkuu wake wa kazi. Alijua huko aliko atakuwa amefura shingo kwa hasira kama samaki bunju.

Baada ya dakika kama tano za kuiamsha simu yake akaiwasha tayari kwa kujiandaa kumpigia. Ghafla ikaanza kuita tena, hakujivunga himahima akabonyeza kitufe cha kupokelea simu. "Hellow....wewe binti unajitambua kweli kwenye kazi yako?" alichapwa na swali zito toka kwa Bosi wake.

"Shikamoo Bosi" alijitutumua Yasmine kusalimia huenda akamlainisha moyo wake.
"Hujalisikia swali langu.... mbona haunijibu?. Nyie kizazi cha Singeli mna shida sana, mnaleta utani kazini, hayaa shauri yako wewe endelea tu kudharau kazi yako nitakuonyesha siku moja kilichomnyoa kanga manyoya....!!" aliendelea kutapika nyongo yake mpaka akapoa, hapo ndipo Yasmine akapata nafasi ya kuzungumza.

"Nisamehe Kiongozi...simu iliisha chaji jana usiku nimekesha nayo inapiga mzigo kama unavyoijua simu yangu ni zaidi ya Kompyuta kiufanisi..!". "Yameisha, sitaki utetezi wowote, Eheee..una taarifa zozote za mwenzako Kachero Manu?? alipigwa swali lililompa mshtuko kidogo.

"Hapana..tena alinipa ahadi ya kunipigia simu mara tu akitua nchini Afrika ya Kusini lakini mpaka sasa sijapokea hata meseji yake sembuse kupigiwa simu !". "Nimepigiwa simu na wakala wetu Dr. Edson Nkube kuwa Kachero Manu amenaswa na wahalifu nchini Afrika ya Kusini.

Tuendelee kusubiria huenda sudi ikawa upande wake na wetu akajitokeza. Ila ujiandae kwa lolote hata ikibidi kwenda kumsaka na kama amekufa uendeleze pale alipoachia yeye. Aluta Kontinua Kanyaga Twende hamna kulala mpaka lyamba..!!" alizungumza Bosi Omega Mtanika maneno ya hamasa kwa kijana wake.

"Ehee....nawe umefikia wapi kwenye taftishi zako? Maana sijapata ripoti yako yoyote mpaka sasa, hujapelekwa pale kwenda kuuza sura tu, upo kazini pale Benki Kuu mama umeskia eeeh..huwezi kazi kaa pembeni!!" aliendelea kuchimbwa mkwara mzito na Bosi.

"Mambo yanaenda aste aste lakini kwa uhakika, nimetoka kutuma ripoti hivi punde tu kwa Kachero Manu. Maana ingependeza ikija ripoti ya pamoja na sio vipande vipande!!" alijitetea Kachero Yasmine huku akijua fika leo Bosi wake kalalia ubavu wa kushoto ana hasira kama kapandisha Jini kisirani kichwani mwake.

"Mfanye haraka mlipewa mwezi mmoja lakini sasa mwezi wa pili, na tayari Benki moja kati ya zile tatu zilizotapeliwa imefunga shughuli zake rasmi nchini Tanzania imehamia nchini Burundi. Hivyo ni pigo kubwa kwa nchi yetu kwa kupoteza mwekezaji kama ujuavyo sera ya Tanzania ya Viwanda inaenda sambamba na mikopo ya Benki inayotumika kujengea viwanda. Hivyo ongezeni bidii usalama wa nchi upo mikononi mwenu" alitoa ufafanuzi wa umuhimu wa kazi yao kwa uchumi wa nchi.

"Shaka Ondoa, wote wahusika tunawatia mbaroni muda sio mrefu. hakuna atakayesalimika na tufani tutakayoifungulia" aliongea Yasmine kwa ujasiri na uzalendo kwa nchi yake, akijiamini na kazi yake. Wakaagana baada ya maelezo mawili matatu, ya Bosi na mtumishi wake.

Yasmine alipokata simu akacheki muda, tayari adhuhuri ilikuwa imeshaingia. "Chipsi kiepe kinanihusu huko mtaani muda sasa umekwenda sana siwezi kupika chochote" alijisemea moyoni huku akiingia ndani kujiandaa ili atoke kwenda kula.

Mipango yote ya kujipikia alishaipiga mkasi. Wakati anatoka ndani wasiwasi juu ya Kachero Manu kupatwa na jambo ovu ukaanza kumuingia maana sio kawaida yake kutotimiza ahadi anayoipanga.




Kachero Manu ajiokoa mbele ya midomo ya bastola za maadui..

"Usipotueleza ukweli ulipoficha sampuli ulizokuja nazo toka Tanzania,?tunakuua humu humu chumbani kwa kutumia bastola yenye kiwambo cha kuzuia sauti kisha tunaucharanga mapanga mwili wako na kwenda kuuyeyusha kwenye pipa la tindikali, habari yako inakuwa imekwisha" alisema huku anafoka kwa hasira mmoja wa maadui waliomkamata Kachero Manu. Sura yake ilionyesha anachokisema ndicho anachokimaanisha.

"Mimi sijaleta sampuli yoyote, begi langu ndio hili la mgongoni mmelipekua kila kona hamjakuta kitu, sasa sijui niwasaidiaje...!" alijibu Kachero Manu kwa kujiamini huku akiwa amepigishwa magoti, mikono yake ipo juu. Maadui zake walionekana wamechanganyikiwa vilivyo hasa baada ya kukosa kitu walichokusudia kukipata toka kwake.

Alishawapiga chenga ya mwili pale pale uwanja wa ndege wa CapeTown. Kachero Manu alimshukuru vilivyo kimoyomoyo Dr.Edson Nkube kwa maono yake ya mbali vinginevyo sampuli toka kwenye maiti ya anayedhaniwa kuwa ni ya Dr.Pius Chilembwa ingetua mikononi mwa adui zake.

"Sasa kama wewe kweli umekuja kwa wema kwanini uliamua kujibadilisha umbile lako?" alipigwa swali lingine na mmoja wa wale maadui zake. Kachero Manu alibaki kimya ameinamisha kichwa chake chini hana cha kujitetea kwa hilo, ameshikwa na pumbao la nafsi. Maana tayari walishafanikiwa kumnyofoa kila kitu chake feki kichwani na kumuacha akiwa yupo halisi.

Akachomoka wanguwangu yule mjuba sana na kumsogelea Kachero Manu na kumuwasha vibao vya nguvu mtawalia. Akaanza kuona maruweruwe na nyota nyota kutokana na maumivu yake makali.

"Hauna jibu eeeh...ulijipanga kupotoa mipango yetu eeeh...Sasa hukumu ya mwenye kuingia Mji wa watu bila kubisha hodi, adhabu yake ni kifo, sali sala ya mwisho kabla ya kifo chako..!!" alizungumza yule adui mkuu kwa sauti ya kuunguruma kama simba inayonuka mauti ndani yake.

Kachero Manu aliishiwa maarifa yote, alikufa moyo kabisa, na kukatika maini. Laiti angekuwa ni adui mmoja tu ndio anamiliki silaha na wengine wapo mikono mitupu angejaribu kupambana nao.

Machozi ya hasira yakaanza kutiririka mashavuni mwake kama anavyofanya ngamia anayesubiria kuchinjwa, hasa baada ya kugundua hana ujanja tena wa kuwachoropoka hata kidogo. Aliona kabisa saa ya kifo chake imeshawadia, malaika mtoa roho, "Ziraeli" yupo jirani kabisa na chumba chake

Mitutu mitatu ya bastola ilikuwa imeelekezwa kwake yeye, hivyo ungekuwa ni muujiza wa Mitume ya kale kuweza kupambana na watu hao watatu wenye silaha na kuwashinda. Kila alipotupa macho yake kuwatazama kwa huruma ili huenda akatokea mmoja wapo mwenye sura ya huruma akabadilisha hukumu yake ya kifo, lakini wapi wote walivaa sura za kazi, macho yao makavu hawataki utani hata chembe.

Hotelini pale kulikuwa na utulivu wa hali ya juu kiasi kwamba kulikuwa hamna kabisa hata michakato ya miguu ya watu iliyokuwa inasikika karibia na chumba ili huenda akapata matumaini ya msaada wa kuokolewa na janga zito lililopo mbele yake.

"Ha...ha...ha...ha...Kachero bobezi tena jasusi wa kimataifa unatoa michozi kama mtoto wa Chekechea kwa uwoga wa kifo..!!. Sasa mkeo huko Tanzania ajiandae kupachikwa jina jipya la Mjane, na watoto wako kama unao kweli nao wataitwa kwa lakabu ya Yatima. Kama hiyo haitoshi na wewe mwenyewe pia utapata jina jipya la ubatizo la Hayati..ha.. ha..ha...kamsosi maji ya baridi mkubwa wewe..!!" alichambwa Kachero Manu na yule mkuu wa maadui, vichambo vya kuchoma moyo haswa.

Vichambo vile vilimuingia kwelikweli, na kumfanya afumbe macho na aanze kuvuta taswira mwili wake upo ndani ya jeneza huku ndugu zake na mkewe Bi Faith Magayane namna wanavyomwaga machozi na kugalagala sakafuni kwenye sanduku lake alilohifadhiwa tayari kwa ajili ya kwenda kuzikwa kama wataipata maiti yake.

Sauti ya Padri iliyojaa majonzi inayosema "ulikuja kwa udongo na utarejea kwa udongo" ikaanza kuvuma masikioni mwake akiwa chini ya ardhi futi saba, amefungiwa ndani ya sanduku la mbao na juu yake kuna tani za kutosha za mchanga zimemwagwa juu yake.

Akiwa kwenye bahari hiyo ya mawazo hasi, akashtukizwa na sauti ya yule jambazi mkuu ambaye wakati wote mle chumbani yeye ndio alikuwa muongeaji mkuu akianza kuhesabu namba kwa sauti kali kabla hawajafyatua risasi kwake wote watatu kwa mpigo.

Hesabu ambazo zilimzindua na kumkurupua Kachero Manu kwenye lindi la mkururu wa mawazo ya huzuni lililokuwa linamkabili. Sauti hiyo ikamfanya aanze kuisalimisha nafsi yake kwa muumba wake kujiandaa kuelekea jongomeo kwa kuanza kutubia dhunubi zake kwa Mwenyezi Mungu zile alizowahi kufanya duniani zile za siri na za dhahiri, alizowahi kufanya kwa makusudi na kwa bahati mbaya.

"Mojaaaa .....Mbiliii.... Taaa.....!" kabla hajamaliza kuitaja namba tatu ili wote kwa pamoja wafyatue risasi kwa pamoja kikasikika kishindo kizito kama cha bomu kilichosababisha mlango kuvunjika vipande vipande kama umecharangwa na shoka.

Kachero Manu hakulaza damu ndio fursa ya pekee aliyokuwa anaisubiria kwa hamu itokee kwa upande wake. Bila kufanya ajizi akalala chini na kuanza kuviringika sakafuni akitafuta mlango wa kutokea huku mvua ya risasi ikimnyeshea pale sakafuni na kufanikiwa kuzikwepa zote.

Alipofanikiwa kufika nje ya mlango akachomoka nduki huku akiacha nyuma yake mashambulizi ya risasi ya msamariamwema wake na maadui zake yakirindima kwa mapambano. Hakutaka kutumia lifti kushuka chini badala yake akawa anatumia ngazi kushuka.

Alipofika roshani ya 8 akahisi vishindo vya watu wanaomfukuza kimya kimya, kugeuka nyuma kweli akawaona wapo wawili. Akaongeza kasi ya kukimbia kama vile mshindani wa mbio za meta 100 anayeikaribia kamba ya kuhitimisha mbio.

Alipofika roshani ya 5 akaona kuna kabati la umbo la mstatili lenye matairi, la kukokotwa likiwa limeegeshwa mkabala na lifti huku likiwa limeegemezwa ukutani. Bila kujiuliza mara mbili mbili akafungua kabati na kuingia ndani yake na kujifungia.

Punde si punde akasikia vishindo vya wale maadui wanaomkimbiza wakiharakisha kushuka ngazi kuelekea ghorofa ya 4. Akamshukuru Mungu kimoyomoyo kwa kujaribisha mbinu iliyokubali kufanya kazi.
Alikuwa amejifungia kwenye kabati lenye kutumika kusambaza mataulo na mapochopocho kama pipi, chokoleti, biskuti kwenye vyumba vya wateja.

Lilikuwa limeegeshwa na mtumishi wa vyumba hivyo akisubiria lifti ije kumfuata ashuke nalo chini ya jengo.
Mtumishi huyo alikuwa amechepuka eneo hilo mara moja kwa dharura hivyo kumpa nafasi Kachero Manu ya kujipenyeza.

Mara akawa anasikia sauti ya michakato ya mhudumu huyo akija kulifuata kabati lake.
Alipolifikia akaanza kulisukuma lile kabati na kuja kuliegesha pua na mdomo na mlango wa lifti. Baada ya kupita kama sekunde 48 tu mlango wa lifti ukafunguka. Ndani yake kulikuwa na vijana wawili ambao ndio wale waliokuwa wanamfukuza Kachero Manu wamkamate.

Wakamuongelesha lugha ya Kizulu yule mhudumu kabla hajaingiza kabati lake kwenye lifti. "Ubani ombonile lana?" (Umemuona mtu hapa?"). "Akukho muntu lana..!"(Hakuna mtu yoyote hapa). "Asimbheke ngalena"( Twende kule), walijibizana huku wakichomoka nje ya lifti kwa kasi kuanza kumsaka adui yake. "Umklinyeee Umklinyeeee..!!"(Ondosha uhai.. wake Ondosha uhai wake...!!") walikuwa wanafoka kwa sauti ya juu kutiana hamasa ya kufanya mauaji, huku bastola zao sasa zinapepea hewani.



Kachero Manu alikuwa anayasikiliza mahojiano yote baina ya mtumishi huyo wa Hoteli na maadui zake akiwa ndani ya kabati lile ingawa alikuwa haelewi lugha inayozungumzwa. Alikuwa anaomba dua tu kwa kila aina ya sala anayoijua yeye kuwa wasimshtukie kuwa yupo mule, vinginevyo anajiona angekwisha kabisa.
Mtumishi yule akaipa ruksa lifti, ikaanza kushuka taratibu, hapo Kachero Manu akapata upenyo wa kudokoa ndani ya kabati lile biskuti. Zikamsaidia kupoza njaa yake iliyokuwa inamkwangua tumboni mwake kisawasawa.

Lifti Ilipofika chini kabisa ya jengo, mtumishi yule akaanza kulikokota kabati lile anaelekea stoo.
Akawa yupo makini kuchunguza nyendo za wapi wanapoelekea kwa kuchungulia kwenye upenyo wa kabati. Walipoingia stoo kabisa, yule dada akaanza kuvua nguo zake za kazi ili avae za nyumbani. Alikuwa amelipa mgongo lile kabati huku akiwa anaimba na kucheza hana habari yoyote. Kachero Manu akafungua taratibu kabati lile bila kuzalisha kelele zozote akawa yupo nyuma ya mgongo wake.


Kwa jinsi alivyokuwa ameumbika dada yake wa Kizulu nusra atoke nje ya lengo lililomleta nchini Afrika ya Kusini. Ikabidi ampunge Ibilisi wake na tamaa za kimwili, na kumuapiza kuwa yupo kazini hajaja kukimbizana na wanawake wa "Banyalabanyala" kwa Mzee Madiba.

Akamsogelea kwa kunyatia na kumgusa begani, alipogeuka na kugonganisha sura zao, mshtuko alioupata hapo hapo yule dada alianguka chini na kuzimia. Hakutegemea kukutana na mwanaume ndani ya chumba kile tena akiwa katika hali ile ya nusu uchi anataka kuvaa kwa raha zake.

Kachero Manu hakumjali akaangaza mle stoo na kuziona sare za rangi kijivu wanazovaaga wafanya usafi wa mazingira ya nje hapo Hotelini. Akazichagua kwa kipimo cha macho zinazoweza kumtosheleza hatimaye akazipata sare hizo.

Akazijaribisha zikamtosheleza vyema kabisa. Akalisogelea kabati la ukutani ambalo mlango wake ulikuwa umeegeshwa tu alipolifungua akakuta kuna madaftari, peni na baadhi ya vitambulisho vya wafanyakazi wa hapo Hotelini. Akakichukua kitambulisho kimoja wapo na kujivika shingoni na kuanza kutoka nje ya mlango wa stoo huku anapiga miluzi mikono ipo mfukoni mwake.

Alipotokeza nje ya jengo lile na "New Salama Lodge" akakuta baadhi ya askari wametanda eneo lile na mitutu yao begani huku gari lao la polisi lenye mbwa kama watatu limeegeshwa pembeni. Akapiga moyo konde, bila kuwajali akawapita bila kutazamana nao usoni, akatoka nje ya geti na kuanza kutokomea zake mtaani.

Mbwa wale walikuwa wanabweka huku wanamuangalia Kachero Manu kwa uchu na matamanio. "Inaonyesha labda wametoa taarifa kuwa kuna jambazi ndio maana polisi wamekuja wanguwangu, namshukuru Mungu wangenitia mbaroni ingekuwa ngumu kuwachoropoka maana picha ya hati yangu ya kusafiria na nilivyo hivi sasa ni tofauti kabisa" alijiwazia nafsini mwake.

Moja kwa moja akapanga kuelekea kwenye ofisi anazofanyia kazi Dr.Edson Nkube wakajipange upya. Kachero Manu hakujua kwamba Dr.Edson ndio aliyetuma msamaria mwema mwokozi wake baada ya kuhisi dalili kama kuna watu kama wanamfuatilia Kachero Manu mara baada ya kutoka tu pale Uwanja wa ndege bila yeye mwenyewe kufahamu. Bila umakini wa Dr.Edson Nkube sasa hivi Kachero Manu angekuwa ameshatangulizwa jongomeo.
.
Siri ya kifo cha Dr.Chilembwa ipo Adolf Goertz Street

Kachero Manu, usiku wa Jumapili ukamkutia ndani ya nyumba ya Dr.Edson Nkube iliyopo ndani ya mtaa maarufu wa "Rahima Moosa Avenue". Mtaa ambao umepewa jina kwa heshima ya mwanamama huyo mwanaharakati wa kutukuka wa chama cha "African National Congress" (ANC).

Bibi huyo anakumbukwa kwa ushupavu wake wa kuongoza maandamano ya wanawake ya tarehe 9/08/1956 ya kupinga matumizi ya hati ya kusafiria ndani ya nchi.

Nyumba yake Dr.Nkube ilikuwa na vyumba vitatu vinavyojitegemea huku kwa nje kuna nyumba ndogo ya mfanyakazi wake wa kazi za nyumbani.
Alikuwa anaishi peke yake ndani ya nyumba hiyo huku familia yake yote kuanzia mke na watoto wakiwa Jijini Gaborone, nchini Botswana.

Waliketi sebuleni na mwenyeji wake wanabadilishana mawazo namna ya kuboresha taratibu zao za upelelezi huku wanaangalia televisheni ya Taifa, "South African Broadcasting Corporation" (SABC).
Ukafika muda wa kurushwa kwa taarifa ya habari wakawa wameongeza umakini kwenye runinga ili kufahamu kinachoendelea nchini Afrika ya Kusini kwa ujumla.

Taarifa ya kwanza ilikuwa ni tukio linalosemekana la ujambazi lililotokea katika nyumba ya kulala wageni ya "New Salama Lodge Milnerton". Ikaripotiwa kuwa majambazi wawili walimvamia mteja Hotelini, mmoja ameuawa na mwingine ametoroka. Ikaripotiwa kuwa juhudi zinafanyika za kumsaka jambazi aliyetoroka.

"This is non-sense and fooolish..kabisa!!" aling'aka Dr.Edson Nkube hasa baada ya kijana wake kusakiziwa tuhuma za ujambazi.
"Nilishampa taarifa mkuu wa kituo juu ya tukio lako zima la kuvamiwa lakini nashangaa jinsi taarifa ilivyoripotiwa ndivyo sivyo...This is Africa every where corruption..corruption..... corruption!!" aliendelea kubwabwaja Dr.Edson Nkube hadi mapovu meupe ya hasira yakimtoka mdomoni.

"Mungu wangu..!! ina maana msamaria mwema wangu ameaga dunia.!! Mungu amuweke mahali pema peponi kwa sababu amefia kazini akitimiza wajibu wake" aliongea Kachero Manu kwa huzuni huku machozi yanamlengalenga.

Akachomoa hanchifu yake kwenye mfuko wake wa sarawili ya dangirizi na kujifuta machozi na mafua mepesi kisha akarudisha mfukoni mwake kitambaa kile.
Wakamezwa na mazungumzo mengine huku taarifa ya habari ikiwa inaendelea. Walishachefukwa na ile habari ya kijana wa Dr Nkube kusingiziwa skendo ya ujambazi hawakutaka hata kuendelea kuiangalia.

Baada ya muda Kachero Manu akanyanyuka kuelekea jikoni kuchukua maji ya vuguvugu ya kunywa. Muda huo huo Dr.Nkube nae akanyanyuka kuelekea chumbani kwake. Sebule ikabaki tupu haina mtu yoyote kwa kitambo fulani kifupi.

Wakati Kachero Manu anarejea toka jikoni akiwa karibu kabisa na runinga hiyo iliyoning'inizwa ukutani, akakutana na habari iliyovuta na kuteka hisia zake. Himahima akajikuta anashawishika kuchukua 'kitenda mbali' cha ile runinga na kuongeza sauti ya runinga hiyo huku akitazama na kusikiliza kwa umakini mkubwa.

Akajikuta anachomoa kalamu yake mfukoni na kidaftari kidogo ananukuu maelezo yanayoelezwa kwenye runinga na mtangazaji mshereheshaji wa hiyo taarifa mpaka ilipofika mwisho akajikuta anashusha pumzi ndefu kama tairi la gari lililopata pancha.

"Vipi unaumwa mbona unashusha pumzi kwa sauti kama umechoka vile, na umesimama hujakaa kwenye sofa, nikukimbize hospitalini?" aliongea Dr.Nkube kwa wahaka na mshawasha mkubwa wa kutaka kujua hali ya kiafya ya mgeni wake. Dr.Nkube alikuwa ndio kwanza anarejea toka chumbani kwake alipojisunda kwa zaidi ya dakika tano.

"Aisee...kesho asubuhi tukitoka kuchukua vipimo vya DNA itabidi unipeleke mtaa unaitwa "Adolf Goertz Street'...!!" aliongea huku ana kimuhemuhe kikubwa Kachero Manu.
"Kunani huko mbona hatukupangilia kwenye ratiba ya mpango kazi wetu wa kesho?" alidadisi Dr.Nkube huku akiwa kama hamuelewi mwenzake. "Najua huwezi kunielewa lakini wakati upo chumbani kuna habari fumanizi nimeikutia kati, hivyo ningependa kwenda kwenye duka moja linaitwa "Bhatti Shop" linamilikiwa na Muasia mmoja nimemuona hivi punde akihojiwa na mwandishi wa habari za kiuchunguzi, na mimi ningependa kuongea nae pia..!" alitilia msisitizo ombi lake la kutakwa kupelekwa dukani kwa ponjoro huyo.

Dr.Nkube Akang'amua rafiki yake ana hamu na hamumu ya kwenda dukani kwa mhindi. Akaepusha malumbano yasiyo na tija na rafiki yake wa chanda na pete. Hisia zikamtuma huenda kuna jambo ameliona kwa huyo mhindi linaloweza kusaidia katika upelelezi wake.

"Ngoja nikalale nimeanza kusinzia kichwa kinayumba yamini wa yasari kama bendera ya taifa mlingotini" alianza kuaga mapema Kachero Manu, na kutilia tashididi kuwa anaenda kweli kulala akajinyanyua pale kochini.
"Aaah..sijui una haraka gani saa haijatasa, kungali mapema sana. Ujue hatujaonana siku nyingi sana" alijaribu kumbembeleza Dr Nkube, rafiki yake asimuache mpweke pale sebuleni waendelee kusogoa maana hakuwa na hata chembe ya lepe la usingizi.

"Sasa wewe endelea tu kung'atwa na mbu wenu wa kikaburu hapa sebuleni. Maana ni wabaguzi kama Mabwana zao wananing'ata mimi, wewe wanakuacha. Mie sijalala vizuri muda mrefu, Usingizi wangu ni wa mang'amung'amu...ngoja nikapumzike Tchaooo Usiku mwema.." aliaga kwa msisitizo kwa mara ya pili na kuchanganya miguu yake kuelekea chumbani kwake.
Dr. Nkube akabakia anatabasamu kwa vibweka na chombezo za rafiki yake. Nae bila kuchelewa akazima taa za sebuleni na kuingia chumbani kwake.



SURA YA NANE

Kachero Yasmine aanza kuwatia mbaroni wanamtandao wa NES..

Tayari kulishakucha na makucha yake, ikiwa ni Jumatatu tulivu yenye mambo mengi sana Jijini Dar es Salaam. Pilikapilika na hekaheka zilipamba moto kila kona, watu wakiharakia kufika kwenye shughuli zao katika siku ya kwanza ya mwanzo wa Juma.

Kachero Yasmine siku hiyo alidamka asubuhi na mapema kuliko kawaida yake kuwahi kazini. Ilikuwa ni siku aliyoichagua kukamilisha mambo mengi sana aliyojipangia hasa ukichukulia siku zilikuwa zinayoyoma na bado mpaka sasa walikuwa hawajamtia mbaroni mtuhumiwa hata mmoja wa dawa.

Alipika na kupakua mbinu zote zinazofaa kuzitumia ili kufanikisha kuwakamata wana mtandao wote wa "Nyasa Empire Supporter" (NES). Hii wiki alipanga iwe ni wiki ya lala kaburiani anayestahiki kulala rumande aanze kunyea mtondoo. Alitaka wahalifu wote wapigwe zii wasing'aze kabisa sura zao uraiani.

Alifika kazini kwake pale BKT majira ya saa 1:15 asubuhi kisha baada ya kubonyeza kitufe cha kurekodi mahudhurio kazini akaelekea moja kwa moja kwenye ofisi ya Afisa Rasilimali Watu kwa ajili ya kuomba ruhusa na kuchukua fomu ya kwenda kutibiwa hospitalini.

Alipotoka hapo akaingia ofisini kwake, kwa bahati Bosi wake Nathanieli alikuwa bado hajawasili kazini. "Flora hii ni bahasha ya Bosi Nathanieli akifika umkabidhi" aliongea Kachero Yasmine kumpa maagizo mfanyakazi mwenzake.

"Hamna shida Shosti ila wewe mvivu kutembelea watu, nyumbani kwangu umekuja mara moja tu vibaya hivyo Shosti...!" alijibu Flora huku akimvurumishia lundo la lawama rafiki yake waliyeshibana ndani ya muda mfupi tu.

"Usijali, leo sijisikii vizuri kiafya ila nikipata nafuu nitakuja tu, ila sikuambii siku wala saa ya ujio wangu utanishtukia tu ghafla bin vuu..nipo maskamoni kwako" alijibu Kachero Yasmine huku wakiagana haraka haraka akiwa hataki kabisa Nathanieli amkute mule ofisini, asije akaanza hadithi za kutaka kusindikizana hospitali akaharibu mipango yote.

"Haina shida ugua pole, ukapime hospitali nzuri upate matibabu bora, pia karibu nyumbani muda wowote ukipata nafuu, pale ni kwako tena nitafurahi maana najisikia upweke wa kupitiliza" alijibu Flora kwa sauti yenye bashasha huku akimpa ushauri mbaraka Yasmine.

Mpaka kufika saa 1:45 asubuhi akawa yupo huru kuingia mtaani akafanye vitu vyake kwa uhuru wote. Alipanga kuomba mapumziko ya kazi ya wiki nzima, afanye vitu vyake kwa uhuru wote bila kusumbuliwa kazini.

Wakati anatoka na gari lake kwenye maegesho ya pale ofisini, Nathanieli akawa ndio nae anaingia kwenye maegesho hayo. Yasmine akamchunia akajifanya kama hamuoni vile alikuwa hataki usumbufu usio na faida yoyote kwa sasa toka kwa mtu kama Nathanieli ambaye zilikuwa zinahesabika siku tu nae atakuwa mkazi wa gerezani.

Akamuacha amepigwa na mzumbao haamini kama Yasmine amemkaushia, kamnyima hata salamu tu. Yasmine alielekea na gari yake mubashara mpaka Mtaa wa Mkwepu, maeneo ya Posta. Ndani ya muda wa dakika zisizozidi 10 akawasili eneo alilolikusudia. Akatafuta sehemu makini ya kuegesha gari yake kwa bahati akaipata. Akashuka kwenye gari yake akafunga milango na kuanza kutembea kwa miguu huku akipepesa pepesa macho yake huku na kule kuitafuta ofisi ya "JUAKALI GENERAL SUPLLIES" mahali ilipo.

Alikuwa anapishana na makundi ya watu, wengine wamejikusanya kwenye kijiwe cha mng'arisha viatu, na wengine wamezunguka kijiwe cha kuuzia magazeti. Cha kushangaza walikuwa wapo nadhifu, wengine wametinga suti zao za gharama, lakini wanapiga soga kijiweni muda wa kuwajibika kazini. Wanahamisha mada tu wakitoka kwenye siasa, wanahamishia mjadala wa burudani na michezo, mara wanahamia kwenye mijadala ya mambo ya kijamii ili mradi majilisi wakati wote inakuwa imechangamka mtindo mmoja.

Kimuonekano wa nje, walionekana hawafanyi kazi yoyote wanavuta muda tu hapo kijiweni, lakini maajabu makubwa ni kuwa vijiwe hivyo wanavyoshinda vilikuwa vinawapa maisha mazuri kuliko hata wale wenye vibarua serikalini au taasisi binafsi, wanaojitutumua kuwa ni watu mufti kimaisha, kumbe wanakufa na tai zao shingoni.

Vijiwe hivyo vilikuwa vinawawezesha baadhi yao wenye maono, kusomesha watoto wao mpaka ngazi ya Chuo Kikuu. Vijiwe hivyo viliwapa nafasi ya kusarifu wake zao mahitaji yote muhimu katika maisha kama malazi, mavazi na chakula kiuhakika tena sio kisudisudi. Vijiwe hivyo vilikuwa vinawawezesha kumudu kulipa gharama za matibabu za familia zao katika hospitali kubwa.

Siri kubwa iliyojificha baina yao inayowapa pesa za kutosha ni kuwa walikuwa na ofisi za mfukoni. Mwajiri wao midomo yao kwa ujanja wa kusarifu maneno tepetepe yaliyojaa ghiriba kubwa. Wapo waliokuwa wanamiliki kampuni za kupakua mizigo bandarini, wapo pia wenye kampuni za kupeleka tenda ya chakula mashuleni, hospitalini na magerezani. Wapo ambao walikuwa ni baraza la mitihani 'NECTA' inayotembea, kwa maana shughuli yao kubwa ni kutengeneza vyeti feki vya kumaliza elimu ya sekondari na vyuo Vikuu.

Wapo ambao walikuwa ni madalali wa mashamba, viwanja na nyumba, ramani ya Jiji zima la Dar es Salaam ipo viganjani mwao. Wapo ambao ni wapambe wa viongozi wa serikalini, kiasi kwamba ukiwa na shida ya kuonana na kiongozi yoyote unayemtaka wewe wa serikali wana uwezo wa kuunganishiwa madili mpaka unaonana nao kwa kulipia kwao gharama fulani.

Walikuwepo pia washenga wa Madaktari, Mahakimu na Polisi. Kiasi kwamba kama una mgonjwa wako na kapangiwa kufanyiwa upasuaji tarehe ya mbali, ukiwaona wao tu wanasuka mipango upasuaji unafanyika mara moja. Pia ukiwa na mtuhumiwa wako yupo rumande kanyimwa dhamana, wanasuka mipango kuanzia polisi mpaka mahakamani kisha dhamana inakuwa nje nje hadharani kwa jamaa yako.

Dunia siku zote haikosi vituko, wapo ambao kazi yao maeneo hayo ya Posta ni ukuadi tu. Mwanamke yoyote maarufu unayemjua wewe walikuwa wana mawasiliano yake. Ukiwataka kingono unawapa tu kazi ya uwakala wa kukutongozea kwa niaba yako, ukifanikisha lengo lako unawalipa dau lao.

Ule msemo ukisikia Mjini akili tu, nguvu zako peleka shamba ndio maeneo ya hapa Posta ulikuwa ndio unafanya kazi. Watu walikuwa wanajaza matumbo kwa kusugua vichwa vyao kwa kuzusha matukio mapya ya utapeli kila kukicha ili mradi mkono uende kinywani, bila kujali kuwa wamejaza matumbo yao kwa pato la dhunubi.

Kachero Yasmine akaachana nao na anuwai ya maisha yao waliyoyachagua, akashika hamsini zake. Baada ya uliza ya hapa na pale, huyu na yule akafanikiwa kuonyeshwa ilipo ofisi za "JUAKALI GENERAL SUPPLIES". Alipatwa na mshtuko baada ya kuziona ofisi hizo, kwa jinsi ilivyokuwa ni chakavu kwa mwonekano wake wa nje.

Alipoingia ofisini akaigundua kuwa ni ofisi yenye samani kuukuu kuanzia makabati yake ya kutunzia vifaa vya ofisini mpaka kompyuta yake inayotumiwa na tarishi wake. Ilikuwa ni ofisi inayojishughulisha sana na uuzaji wa vifaa vya maofisini na mashuleni.

"Karibu sana dada yangu nikusaidie nini?" alikaribishwa Kachero Yasmine kwa uchangamfu na yule dada mhudumu wa ile ofisi, akifuata sharuti za ukumbi katika maongezi. "Ahsante sana.. mie shida yangu ni kuonana na Mkurugenzi wa kampuni, nina dili na yeye la pesa ndefu sana" alizungumza Yasmine kwa mtindo wa kumtia mtegoni kwa kumtamanisha aingie kichwa kichwa.




Karibu sana dada yangu nikusaidie nini?" alikaribishwa Kachero Yasmine kwa uchangamfu na yule dada mhudumu wa ile ofisi, akifuata sharuti za ukumbi katika maongezi. "Ahsante sana.. mie shida yangu ni kuonana na Mkurugenzi wa kampuni, nina dili na yeye la pesa ndefu sana" alizungumza Yasmine kwa mtindo wa kumtia mtegoni kwa kumtamanisha aingie kichwa kichwa.

Mbinu hiyo ilionyesha kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Uso wa yule tarishi ukavaa tabasamu sheshe na bashasha ya hali ya juu. Kachero Yasmine aliusoma mchezo mzima, akafanya hitimisho kuwa ile ofisi ni geresha tu lakini kazi yao kubwa ni kuchonga dili za pesa haramu.

Kwa tathmini ya haraka aliyoifanya kwa mauzo pekee ya ofisi ile kwa mwezi hayawezi kabisa kulipa pango ndefu ya fremu katikati ya Jiji kama Posta. Mapato ya ofisi yalikuwa hayawezi kutosha kulipia gharama ya usafiri wa gari ya Mkurugenzi na kujilipa mishahara yao wenyewe.

"Hellow...Bosi njoo haraka ofisini, kuna rosti ya maini ya ngamia..njoo na pilipili kabisa ujisosomole...!!" aliongea kwenye simu yule mhudumu na Bosi wake kwa lugha ya mafumbo wanayojuana wenyewe tu ili mradi kumtamanisha afike haraka.
Kachero Yasmine nusra aangue kicheko kwa sauti, lakini akajibana na kujifanya ametingwa na zoezi la kuangalia vifaa mbalimbali vinavyouzwa mle ofisini na bei zake huku anasikilizia jibu atakalopewa na yule mhudumu.

"Msubirie kwenye kiti hapo kiduchu tu, hachukui muda mrefu anakuja sasa hivi myajenge, natumaini hamtoshindwana...!! " alitoa maelezo kwa lugha ya kimjini mjini kuonyesha ni mzoefu na shughuli zile za mazabe ya pesa haramu.

Yasmine akaitikia makaribisho yale kwa vitendo bila kuongea chochote, akajongea zake kuketi kitini kisha akachomoa simu yake kwenye mkoba na kujitia kuchati huku anachunguza uingiaji na utokaji wa wateja mbalimbali ndani ya ile ofisi. Punde si punde akaingia kwa pupa kibonge cha mtu, kibushuti, ana kitambi mithili ya ngoma kubwa ya bendi ya shule anatembea kwa madaha huku anatupa mikono, kwa ujumla alishiba siha.

Alikuwa amevalia nadhifu, suti rangi nyeusi na tai yake. Akasalimia na yule mhudumu kisha wakawa wanaonyeshana kidole mahali alipo Kachero Yasmine. Yasmine akawaona akaunda tabasamu feki usoni kwake, hisia zikamtuma huenda ndio Mkurugenzi mwenyewe wa "JUAKALI GENERAL SUPPLIES".

Yule mbaba akamuita Kachero Yasmine kwa kutumia ishara ya kiganja chake kumtaka amfuate alipo. Yasmine akanyanyuka huku anamfuata kwenye kichumba kingine kidogo tu kinachotenganisha na chumba kila cha ofisi kwa mgawanyo wa mbao nyepesi. Alipoingia akakaribishwa kitini huku yule Mkurugenzi akikaa kwenye kiti cha kuzunguka cha matairi.

Ilikuwa ni ofisi ndogo isiyo na vikorombwezo vingi, zaidi ya meza, viti viwili, kompyuta mpakato' na mafaili machache pale mezani, huku feni ya mezani chakavu ikipuliza hewa huku inatoa makelele mtindo mmoja. Ukutani kulitundikwa vyeti vya ithibati ya usajili wa kampuni hiyo toka BRELA. Pia kulikuwa na picha kubwa za viongozi mbalimbali wa kitaifa ukutani.

"Mhhh...mie shida yangu moja tu, namhitaji Mohammed Mtoni nimeelekezwa nitampata hapa" aliongea Kachero Yasmine baada ya kusalimiana baina yao huku akiwa anaifunga vizuri hijabu yake nyeusi kichwani bila kumtazama usoni Mkurugenzi yule.

"Sikuelewi wewe mama umeambiwa huyo mtu anapatikana hapa ofisini kwangu?" aliuliza huku akiwa amekunja ndita usoni kwake, kuonyesha hajapendezwa na swali aliloulizwa. "Ndio mimi sio kichaa kuja kumuulizia hapa, najua unamfahamu fika tena kinagaubaga Mohammed Mtoni" aliweka msisitizo wa swali lake huku uso wake ukionyesha hayupo kwenye mchezo asubuhi ile.

"Weeee Suziiiii.... Suziiii...njoo mtoe nje kichaa wako, ndio umeniambia kuna dili mtu kaleta kumbe kichaa!!" alilalama Mkurugenzi kumshitaki Kachero Yasmine kwa yule mhudumu aliyemkaribisha pale ofisini, akionekana kabisa ameshatiwa kitumbo maji na swali alilopigwa ila anajitutumua tu.

"Samahani Bosi wangu, maelezo yake ya awali alionyesha kabisa kama ana jambo la msingi na wewe....Shosti toooka.. toooka mama usinitilie mchanga kitumbua changu, mambo ya kunukishana kidagaa asubuhi sio mazuri, nitakupasua" alifoka Suzzy kwa lugha iliyojaa nyodo huku anamvuta kwa nguvu Kachero Yasmine kwa mikono yake miwili ajipapachue kitini.

Kachero Yasmine alishindwa kujidhibiti hasira zake akajikuta amejigeuza kimaajabu na kuunyonga mkono wa Suzzy. "Mama nakufaaaaaaaaah....!" alipiga makelele huku akiwa anagaragara sakafuni kwa uchungu wa maumivu anayoyasikia.

Yule Mkurugenzi alibaki ametumbua macho kama samaki wa kwenye barafu akiwa haamini anachokishuhudia kwa macho yake alichokifanya Yasmine. Masikini Suzy alijua Yasmine ni mwanamke mwenzake wa kawaida tu ambaye mazoezi yake ni ya mdomo kupitia umbea.

Hakutanabahi kuwa anamchokoa komandoo mwenye uwezo wa kuvunja nazi kwa kichwa chake na kuvunja tofali kwa ngumi moja tu. Yasmine akanyanyuka kitini na kufunga mlango kisha akamrudia yule Mkurugenzi ambaye sasa alikuwa amesimama haelewi kinachomtokea ofisini mwake.

"Mpigie simu haraka sana Mohammed Mtoni unipe niongee nae...!' alitoa maelekezo kwa sauti ya kufoka huku akimuonyesha kitambulisho chake cha kazi. Yule Mkurugenzi aliaanza kutetemeka baada ya kukiona kitambulisho kile utasema yupo Wilayani Mafinga asubuhi kwenye baridi halafu anatembea kifua wazi. Jasho jekejeke lilikuwa linamvuja mwilini, suti aliyovaa alitamani aivue na kuitupa.

Kiunyonge akaichukua simu yake ya mkononi pale mezani na kuanza kupekenyua majina aliyoyahifadhi mpaka akaliona jina la Mohammed Mtoni. Akabonyeza kitufe cha kuruhusu kupiga simu na kuanza kusikiliza kwa sauti kubwa ili na Kachero Yasmine asikilize kila kitu bila mficho.

"Hellow....Muddy upo wapi?". "Ndio natoka nyumbani naenda kwanza Wizara ya Mambo ya Ndani kuna vimeo vyangu pale sijavikamilisha huko kitaa mpaka adhuhuri nadhani, vipi ulikuwa unasemaje au jamaa wameniingizia mzigo wangu uliobaki ule kwenye akaunti yako tena?" aliongea kwa sauti ya kujiamini, kujionyesha ni mtoto wa Mjini, maisha ameyapatia tayari anatengeneza madili atakavyo.

"Hapana kuna mgeni wako amekuja ofisini kwangu, ongea nae kwanza...!" aliongea kiunyonge sana huku anasalimisha simu yake kwa Kachero Yasmine. Alipoipokea tu ile simu akabinya kitufe cha kutoa sauti kubwa ili yule Mkurugenzi asisikie kinachozunguzwa.

"Hellow..Bwana Mohammed habari yako,, eeh... eeh...bora tukutane hapo nitakusubiria, nakutumia namba yangu sasa hivi ukifika unipigie...!" akakata simu baada ya kuelewana nae.
Alipokata simu tu hapo hapo akapiga simu nyingine kwa kutumia simu yake kuwasiliana na idara ya polisi huku akiwapa maelekezo ya kuja kuwatia mbaroni Mkurugenzi yule na Suzzy.

Yule Mkurugenzi alikuwa anamuomba vilivyo msamaha Kachero Yasmine huku anatambaa kwa magoti, lakini haikufaa kitu siku zote majuto ni mjukuu. Suzzy kilio chake cha maumivu kilikata kabisa mara moja haswa baada ya kusikia mambo ya polisi. Kidagaa kile alichokuwa anakataa kisimuozee, sasa kimemuozea kweli.

Haikupita hata robo saa polisi watatu wakatia timu pale ofisini. "Huyu akatibiwe lakini akitoka hapo ndani, pamoja na huyu Bosi wake wote waswekeni lupango kwa usalama wa nchi mpaka yatakapokuja maagizo mengine dhidi yao" Kachero Yasmine alitoa maagizo mafupi yenye kueleweka.

Kilichofuatia ni utekelezaji tu, huku vilio vikitawala eneo lile utasema kuna msiba wa tegemeo la familia fulani umetokea. Kachero Yasmine akaondoka zake akielekea Wizara ya Mambo ya Ndani kujipanga kumtia mbaroni Mohammed Mtoni.

Mohammed Mtoni au lakabu yake maarufu kwa wanakijiwe wenzake ilikuwa ni "Muddy Comp", Comp wakifupisha neno la Kiingereza "Computer" wakifananisha namna kichwa chake kinavyochaji kama Kompyuta kwenye madili ya wizi.
Ni mtoto alwatani wa Magomeni Mapipa, kazaliwa hapo, kakulia hapo na mwenyewe alikuwa anajiapiza atajukuu na kufia Magomeni. Daima alikuwa anajitapa ya kuwa starehe za Magomeni ladha yake haiwezi kupatikana sehemu yoyote katika kipande cha dunia hii.

Ukianzia kwenye sekta ya burudani, muziki wa aina yoyote unaoutaka wewe kuanzia Mdumange, Baikoko, Mdundiko, Mchiriku, Mnanda, Taarabu, Singeli, Kibaokata na nyinginezo nyingi katika aina ya miziki ya uswahili ilikuwa inapatikana Magomeni usiku kucha kila siku za juma.
Kwa ujumla vijana wa Magomeni walikuwa wanajihesabu wao ni wajanja kupitiliza hasa kutokana na wengi kuwahi kusafiri kwenda Ughaibuni kubeba mihadarati. Tumrudie huyu Bwana "Muddy Comp", yeye vimeo vyake vikubwa alikuwa anavifanyia kwenye ofisi za serikali na taasisi zake.

Waliosoma nae shule ya msingi pale Mzimuni, Magomeni wanakuambia hawaamini kama ndio huyu Mohammed Mtoni mjanja wao wa Jiji kwa sasa. Wanasema darasani alikuwa kilaza wa kutupwa kwenye kilinge cha darasa lao.
Lakini maajabu wale wale waliokuwa wanamkanyagia darasani na kufanikiwa hadi kufika Chuo Kikuu kwenda kutabahari kwenye fani, na kupata vyeo vikubwa vikubwa serikalini, leo ilikuwa mambo yao ya ufisadi wa pesa za serikali hayawahi bambam mpaka "Muddy Comp" kilaza wao wa darasa aweke mkono wake.

Siri kubwa iliyokuwa inawaunganisha hawa Wasomi na "Muddy Comp" ni kuwa alikuwa mtaalamu wa risiti feki, hivyo Mabosi wakichukua masurufu ofisini wakitaka kufanya marejesho ya taarifa ya matumizi ya pesa walizoomba ofisini lazima wamuone yeye arekebishe mambo.
Vinginevyo bila "Muddy Comp" kutia mkono wake, mambo yanabuma walikuwa wanaumbuka vibaya mbele ya wakaguzi wa mahesabu.

Alikuwa ana mtambo wake wa kufyatua risiti za mashine za "EFD" achilia mbali hizi risiti za mkono. Mpaka Wakurugenzi wa Wizara wakiwa na safari zao za Ulaya wakitaka risiti za magumashi za Hoteli za hadhi ya juu za huko Ughaibuni, jamaa alikuwa anawapatia bila shida yoyote.
Hiyo tisa, kumi na la kutisha kuliko yote alikuwa ni mtaalamu wa kufoji saini za watu. Alikuwa akifanikiwa kuoneshwa saini yako mara moja tu mchezo umekwisha. Wenyewe wakimtania kuwa saini anayoshindwa kuigiza ni ile tu ya Malaika mtoa roho tu.

"NYASA EMPIRE SUPPORTERS" (NES) kikundi haramu chenye madhumuni ya kupindua utawala wa nchi, walimtumia sana "Muddy Comp" kwenye utapeli wa bilioni za pesa zilizoibwa kwenye Mabenki. Kuna pesa zilihamishwa kwa kibali cha Gavana wa Benki Kuu, hivyo yeye ndio alihusika kughushi saini ya Gavana.

Hilo dili la saini ya Gavana ndio lilisababisha awe analipwa mamilioni ya pesa kupitia akaunti namba ya "JUAKALI GENERAL SUPPLIES" ofisi zilizopo mtaa wa Mkwepu.
Maisha yake binafsi, alikuwa mtu rahimu na raufu, hana makeke. Sio mlevi wa pombe, hapatani na mtindi asilani. Lakini chambilecho asiye na hili ana lile, ulevi wake mkubwa, uliokuwa unamtoa roho ni kupenda vidosho kupitiliza utasema ana Jini Mahaba.

Licha ya mamilioni yote ya pesa anayochuma kwenye utapeli wake hata msingi wa nyumba alikuwa hajafanikiwa kujenga. Pesa yake yote Mzaramo huyu ilikuwa inaishia kwa virukanjia wake kutimiza hawaa za nafsi.
Kila kitongoji unachokijua wewe cha Jiji la Dar es Salaam alikuwa ana kimada wake. Tena alikuwa sio machaguchagu, yeye kuanzia Mama Nitilie, Watembeza matunda mitaani mpaka Wadada warembo wa kwenye maofisi akinogewa nao tu lazima arushe nyavu zake.

Kwa ujumla Mohammed Mtoni alikuwa anaishi maisha mchafukoge ili mradi siku imepita tu, yasiyo na malengo marefu ya uzeeni.
Sasa alipowasili pale makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani muda wote alikuwa na furaha tu. Aliona kabisa asubuhi yake ya leo imeangaziwa na nyota jaha, maana dili za pesa zinatiririka kwa upande wake mithili ya maporomoko ya maji.

Asubuhi hiyo alikuwa ameitwa kuja kusaidia upatikanaji wa risiti za safari feki ya nchini Uingereza, dili ambalo alitegemea litampatia zaidi ya milioni moja taslimu, halafu hapo hapo inaunganika na dili lingine lililoungwa juu kwa juu toka ofisi yake ya kupigia pesa ya "JUAKALI GENERAL SUPPLIES".
Moja kwa moja alipotua maeneo yale akaelekea kwenye ofisi aliyoitwa kwa ajili ya tenda hiyo chafu. Huko akakaa kama saa moja na dakika kadhaa, ndipo akawa amemalizana nao wapigaji wenzake. Alipotoka tu akaanza kuipiga namba ya simu ya Yasmine aliyotumiwa.



Asubuhi hiyo alikuwa ameitwa kuja kusaidia upatikanaji wa risiti za safari feki ya nchini Uingereza, dili ambalo alitegemea litampatia zaidi ya milioni moja taslimu, halafu hapo hapo inaunganika na dili lingine lililoungwa juu kwa juu toka ofisi yake ya kupigia pesa ya "JUAKALI GENERAL SUPPLIES".

Moja kwa moja alipotua maeneo yale akaelekea kwenye ofisi aliyoitwa kwa ajili ya tenda hiyo chafu. Huko akakaa kama saa moja na dakika kadhaa, ndipo akawa amemalizana nao wapigaji wenzake. Alipotoka tu akaanza kuipiga namba ya simu ya Yasmine aliyotumiwa.

"Hellow...sistery, upo wapi mbona sikuoni?...usiulaze usiku mapema mapema, wakati ni ukuta..hapa sasa hivi nimepigiwa simu Ikulu kuna issue natakiwa nikarekebishe huko....Oooh OK. Sawa nisubiri hapo hapo nje !!" akakata simu yake.

Alikuwa anafanya mawasiliano na Kachero Yasmine huku akimtia ndimu kuwa ameitwa Ikulu wakati ni uzushi mtupu, lengo ni kujionyesha yeye ni mtu wa thamani sana anasakwa kila kona kama lulu vile, ili akikutajia dau lake usichomoe.
Yasmine hakutaka wakutane ndani ya jengo la Wizara, alitaka wamalizane nae nje ya jengo. Hivyo akamfahamisha yupo nje ya jengo kwenye kiduka cha Mangi anapoza koo kwa kujiburudisha kwa soda.

"Habari Aisee, Salaamu aleikum Bibie hongera kwa kupendeza.....!!" ilikuwa ndio salamu yake kwa Yasmine mara tu baada ya kuonana uso kwa uso. Tayari sura ya mrembo Yasmine ilishamchanganya, kumvuruga na kumkoroga vilivyo. "Vitu vya rangi ya Mtume ndio ugonjwa wangu huu....!!" alijiwazia kichwani mwake "Muddy Comp" huku wakipeana mikono ya salamu na Yasmine.

"Mie habari yangu ni nzuri, yaani nimefurahi sana kukutia machoni mjuba wewe. Maana ulivyo adimu kama mguu wa sisimizi uliodumbukizwa kwenye mchuzi wa rosti" alijishebedua Yasmine mbele yake na kumfanya Muddy ajione ni mtu wa thamani sana, kumbe anampaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

"Acha tu mrembo, kwanza hapa nikitaka nipige chini dili lako maana Ikulu nasumbuliwa sana, kuna Afisa mmoja ananisumbua sana, namdanganya foleni kali. Alikuwa tayari atume gari zao zile na eskoti juu ya polisi ili mradi tu niwahi kufika, lakini wale JUAKALI naheshimiana nao sana nikaona sio vizuri kumuangusha yule Mkurugenzi" alizidi kujifagilia na kujikweza matawi ya juu.

"Jamani ahsante kwa kujali, Mungu atawalipa kwa upendo wenu, sasa tunaweza kwenda kuzungumzia ndani ya gari?" alibadilisha mada Yasmine sasa akimvuta taratibu kwenye lengo lake mahususi analolikusudia.
Nalo ni kumchukua "Muddy Comp" mpaka nyumbani kwake Mbweni. Alitaka ampeleke akamsulubishe, na kumpa mfueni vilivyo mpaka aropoke kila kitu pesa alizokuwa anapokea toka "Nyasa Empire Supporters" (NES) zilikuwa na madhumuni gani haswa. Kama zilikuwa ni mahari ya binti yake, au mchango wa matibabu atapike kila kitu anachokijua juu ya pesa zile kodi ya walalahoi, wavuja jasho wa Tanzania.

"Hamna shida tena itakuwa bora maana jua limeanza kunoga huko angani Malaika msimamizi wake hatuonei huruma, yeye analichochea tu makali yake" alijibu Muddy huku anamfuata sako kwa bako Kachero Yasmine kuelekea kwenye gari lake.

"Kaka yangu, mimi nafanya kazi Benki Kuu sasa kuna dili fulani inabidi ifojiwe saini ya Rais wa Benki Maendeleo ya Africa "ADB" ndio liweze kukamilika, naomba sana msaada wako kuna chambichambi ya kutosha usiwe na hofu na mgao wako..!" alizungumza kwa sauti ya kubembeleza huku amemlegezea macho "Muddy Comp", kwa mtindo wa kurembua.
Akajitia kushusha pumzi ndefu, kuonyesha amepewa mtihani mzito kuukabili. Kisha akaa kimya kitambo kifupi anajifanya anatafakari, halafu akafungua mdomo wake.

"Mie kweli ni mpigaji madili kama ulivyoelekezwa pale "JUAKALI GENERAL SUPPLIES" lakini dili sampuli hiyo unayonieleza ya kufoji saini za watu nimeachana nazo kitambo kirefu sana. Nilishawahi kupata matatizo na vyombo vya dola siku za nyuma ilibakia chupuchupu nikanyee mtondoo gerezani" alijitia kubadilika na kuipanjua dili hilo hadharani mchana kweupe.

Kachero Yasmine alipomuangalia "Muddy Comp" wakati anajieleza aligundua fika kwa kumuangalia uso wake, kuwa anaongopa mchana kweupe, ni ndumilakuwili tena mnafiki mkubwa hasa kutokana na elimu yake ya saikolojia ya wahalifu wanayofundishwa katika Vyuo vya Ukachero.

"Jamani weweeh...kaka yangu Muddy nisaidie kwa leo tu mara moja mwenzako..chonde chonde tafadhali" alizidi kubembeleza Yasmine huku sasa akiwa amekifumbata kiganja cha mkono wake wa kushoto kwenye mkono wa "Muddy Comp". Kitendo cha kushikwa kiganja cha mkono tu, akaanza kulainika kama siagi kwenye uji wa moto, huku anajichekesha chekesha tu kama mwehu.
Jinsi Kachero Yasmine alivyo mjanja akawa anamchezea vidole vyake huku anambembeleza kwa maneno matamu yenye kumtoa nyoka pangoni. Mawazo mwake Muddy alishakubali waondoke alitamani sana wapite nae maskani Magomeni walau awaongopee rafiki zake kuwa leo kaopoa kifaa kipya.

"Daah..majaribu haya unaniletea binti, jela inaniita hivi hivi nitakuwa peke yangu ujue, huku wewe unakula mbwanda na familia yako uraiani" aliongea kwa sauti ya chini, akiwa ameshagandishwa ulimi kuonyesha yupo tayari kuifanya hiyo kazi.
Baada ya mazungumzo mafupi wakakubaliana na kufikia muafaka yupo tayari kufanya kazi hivyo waelekee huko Mbweni akakabidhiwe mchongo mzima. Kachero Yasmine alikuwa anaendesha gari lake kwa mtindo wa halambe halumbe.

Mara amekosa kugongana na gari hili, mara kamkosa kumgonga mtu ili mradi tafrani njia nzima. Alishavurugwa tayari alikuwa anataka mambo yaende haraka haraka. Walishakuwa wapo nyuma ya muda kuwatia mbaroni wahalifu wa "Nyasa Empire Supporter" (NES).
Muddy alikuwa muda wote ana furaha ghaya, akiona kabisa anaenda kupiga pesa ndefu na huenda akikomaa akang'oa kabisa mtoto wa Kizenji, Yasmine. Kumbe hakujua anaenda kupata suluba na kalinyekalinye za kufa mtu mpaka atajuta kuzaliwa.


Ratiba ya Kachero Manu na rafiki yake Dr.Edson Nkube ilibidi ipinduliwe kichwa chini miguu juu. Mishemishe zao badala ya kuanzia kwenye ofisi ya "DNA Diagnostics Centre" (DDC) walipopeleka sampuli ya mwili unaodhaniwa wa marehemu Dr.Pius Chilembwa, kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba vya marehemu, wakabadilisha kibao wakaamua waanzie kwanza mizunguko yao mtaa wa "Adolf Goertz Street", kule dukani kwa Mhindi "Bhatti Shop".

Sababu ya mabadiliko hayo ya ratiba yalitokana na taarifa walizopokea toka kwenye vyanzo vyao vya Kiintelijinsia. Penyenye ziliwafikia kuwa kuna ghasia na machafuko yanayotarajiwa kuanzia kurindima nchi nzima ya Afrika ya Kusini.
Wazawa walikuwa wanataka kuandaa maandamano kushinikiza serikali yao kuwafukuza Wafanyabiashara wa kigeni ambao ndio wamekamatia asilimia 80% ya Uchumi wa Afrika ya Kusini. Wakileta madai ya kuwa wageni hao wamekimbia nchi zao zenye hali ngumu za kimaisha wamekimbilia nchini Afrika ya Kusini, nchi yenye neema ya asali na maziwa.

Iliwachukua kama nusu saa tu wakiwa na usafiri binafsi, kuwasili dukani kwa Mr.Bhatti. "Good Morning Mr.Bhatti, How are you?" alianza kusalimia Kachero Manu kwa uso wa bashasha, akafuatia Dr.Nkube nae kusalimiana naye huku wanapeana nae mikono ya salamu.

"Habari yangu nzuri sana iko karibuni sana" alijibu salamu kwa lugha ya kiswahili jambo ambalo liliwafanya Dr.Nkube na Kachero Manu waangaliane usoni na kutabasamu wakiwa hawamini kama Mhindi yule anaweza kuongea Kiswahili fasaha kiasi chake.

"Nashangaa nini, mimi meishi Tanzania miaka zaidi ya 20, wazazi iko kule wekeza zamani kiwanda cha kusindika nyanya, Dumila-Morogoro. Hivyo najua swahili na mlipoingia dukani nilikusikieni naongea swahili nikafurahi sana, nikajua nyie ni dugu zangu toka nchi ya Nyerere" alijieleza Bwana Bhatti wapi alipojulia lugha ya kiswahili.

Baada ya mazungumzo ya hapa na pale, wakajitambulisha kuwa wao ni waandishi wa habari wa kimataifa wa kujitegemea. Wapo nchini Afrika ya Kusini kutafuta habari za kichaa aliyepotea kwenye mazingira ya kutatanisha anayetafutwa kwa udi na uvumba na ndugu zake. Mr.Bhatti kwanza alionekana kuhuzunishwa sana na taarifa kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha kwa majinuni huyo. Pia alionyesha kufurahishwa na ujio wa Wanahabari wale ili huenda Kichaa huyo akaonekana.

"Van-Dubbe kama alivyokuwa anajiita mwenyewe alizoea sana hapa mtaa wa Adolf Goertz Street. Tazunguka huku na kule lakini lazima rejee hapa. Menyewe penda jiita Rais wa Mtaa". Alifungua utangulizi wa mahojiano baina yao Mr.Bhatti kwa kuelezea namna alivyokuwa anamjua Majinuni aliyetoweka Van-Dubbe. Kachero Manu akafungua rasmi mahojiano baina yao.

Kachero Manu: "Kwanini alikuzoea wewe na sio wana mtaa wengine?, maana hata taarifa ya SABC-News ilionyesha polisi wamekuja kukuhoji wewe! "

Mr.Bhatti: "Swali zuri, watu wa huku roho baya sana, sasa mie iko mpa yeye chakula, maji na hata mavazi ndio maana Van-Dubbe iko hakauki hapa dukani kwangu! "

Kachero Manu: "Je siku chache kabla hajapotea, kuna mienendo yoyote ya hatari dhidi yake ulinusa hasa kutokana na ukaribu wenu?"

Mr.Bhatti: "Eeeh...iko watu wageni jitokeza ghafla jifanya nampenda sana kuja hapa nunulia mikate, soda naondoka nae kisha namrudisha, karibia wiki zima hivi..!!". Jibu la Mr.Bhatti likawafanya Dr.Nkube na Kachero Manu waangaliane usoni na kupeana ishara kuashiria kuwa hao watu huenda ndio wahusika wakuu.

Kachero Manu: "Unaweza kutuonyesha video zilizorekodiwa na CCTV-Camera ya hapa dukani kwako za wiki za mwisho mwisho kabla hajapotea?"

Mr.Bhatti:"Hamna shida mie CCTV yangu natunza matukio mpaka miezi tatu kisha nafuta, twende mkaone" alisema yule Mhindi huku wakisimama kuelekea nyuma ya duka lile, pembe za chaki kabisa, wakimuacha mtumishi wake mmoja Mr.Bhatti kuendelea kutoa huduma kwa wateja wake wachache waliokuwa wanaingia na kutoka hapo dukani.



Walikaa kwenye mtambo wa CCTV-Camera kwa zaidi ya dakika 45 wakichambua picha na video hizo kwa umakini mkubwa mpaka wakafanikiwa kumgundua mtu mmoja kati ya washukiwa wa mauaji ya Kichaa Van-Dubbe.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog