Search This Blog

Wednesday, 22 March 2023

NITAKUUA MWENYEWE - 4

   

Simulizi : Nitakuua Mwenyewe 

Sehemu Ya : Nne (4)


Jackline alimsalimu Afande Mkonge.


"Marahaba binti yangu bado zoezi linaendelea la kumsaka mtu wako."

Alijibu na kueleza kinachoendelea.


"Niko Chunya hapa ndiyo tunakuja huko Makongolosi bila shaka baada ya dakika kadhaa hivi tutakuwa hapo."

Jackline alimwambia.


"Umeingia lini Tanzania mwanangu Jackline?"


"Tumeingia leo hii mishale ya saa tatu hivi usiku tukiutumia uwanja wa Ndege wa Songwe."


"Aisee poleni sana bila shaka hapa itakuwa saa saba usiku."


"Mzee Mkonge kuhusu hilo usijali hata kidogo kikubwa tu niandalie simu yake najua kupitia hiyo nakwenda kumnasa mimi mwenyewe kwani itakapo fika asubuhi tutakuwa njiani kuelekea Tabora hii inaitwa hakuna kulala."

Jackline alitamba simuni wakati akiongea na mkuu wa kituo mzee Mkonge.


" Kila kitu kiko sawa mwanangu ni wewe tu."

Afande Mkonge alimjibu Jackline. Lakini wakati huo akawa anawaza ni kwa namna gani ameweza kufika nchini ghafla kiasi hicho.Ni kweli kama ambavyo walisema waliwasili Makongolosi wakiwa na gari ya kukodi. Walimkuta mzee Mkonge akiwasubiri na muda huo ilikuwa yapata saa sita na unusu hivi usiku.


"Mmejitahidi sana kutembea yaani muda huu mmefika?"

Aliuliza Afande Mkonge.


"Si sana ilikuwa kawaida tu mzee wangu. Hawa ni rafiki zangu huyu anaitwa Jasmine na yule pale anaitwa Jessica."

Jackline aliwatambulisha wakina Jasmine kwa Afande Mkonge.


"Nashukuru kuwafahamu rafiki zako, wanangu karibuni sana Makongolosi mimi ni Afande Mkonge ni mkuu wa kituo cha Polisi." Alijitambulisha naye mzee Mkonge.


"Asante sana Afande."

Walijibu kwa pamoja.


"Nilipopata simu yako ilibidi niende kituoni kuichukua simu ya mzee Jonathan ili ukifika nikukabidhi lakini bado kuna vitu vyake vingine tunavishikilia ikiwa ni pamoja na gari zake mbili ambazo ziko pale Kituoni Lupa na baadhi ya dokumenti zake ziko hapa."

Afande Mkonge alitoa ufafanuzi huku alimkabidhi ile simu Jackline.


" Asante sana baba yangu lakini kwa sasa simu hii ni muhimu sana kwangu na kama nilivyokueleza kwenye simu sisi hakuna kulala muda huu tunaunga safari kuelekea Tabora na baada ya kufika huko ndipo nitaanza kuifanyia kazi hii simu na ninakuhakikishia Afande tutamtia mikononi mwetu mzee Jonathan na hautoamini."


"Mimi niwatakie kila lenye heri katika zoezi hili na niwahakikishie kuwa bega kwa bega nanyi pale mtakapohitaji msaada wetu."


"Tunashukuru sana mkuu."

Jasmine alijibu huku wakipeana mikono na Afande Mkonge kuagana naye na kisha kutoka hapo nyumbani kwa mkuu huyo wa kituo na kurudi kwenye gari iliyokuwa pale nje ikiwasubiri na safari ikaanza kuelekea Tabora wakipita njia ya Lupa.


Nini kitaendelea?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.




Baada ya mwendo mrefu waliwasili mkoani Tabora ikiwa ni saa kumi na mbili asubuhi. Kabla ya kufanya chochote kile walimuomba dereva wao atafute Hotel apate kupumzika na kuwaacha wao kufanya kitu kilichowaleta Tanzania.

Waliachana naye kisha wao wakatembea kwa mguu mpaka sehemu moja iitwayo Cheyo ambapo hapo waliingia Grocery ya Double Star ambayo inajina sana na inasifika kwa kuwa na Bustani ya maua mbalimbali ya kuvutia na hapo walitafuta viti vilivyokuwa havina watu wakatulia hapo.


"Karibuni Double Star kwa huduma." Mhudumu huyo aliwakaribisha.


"Asante Kaka yetu kwa asubuhi hatuhitaji chochote kile ila tutalipia viti tu baada ya kuhitimisha maongezi yetu."

Jackline alimjibu mhudumu aliyefika pale kuwasikiliza.


"Bila shaka dada zangu." Alijibu na kuondoka zake akiwaacha waendelee na zao.


Alipoondoka wao walianza kupanga mipango yao ya namna ya kumkabili mzee Jonathan.


"Halafu na wewe Jackline mpana sana aisee kona hii uliijuaje mwenzetu?"

Jessica alimuuliza.


"Unajua ikoje rafiki zangu?"


"Hatujui ndiyo utuambie mwenzetu."

Walimjibu kwa pamoja huku wakitazamana.


"Kipindi hicho nikiwa katika Ulimwengu wa ukungu na giza nilikuwa nikiletwa eneo hili na mzee Jonathan. Na wakati huo nilikuwa nikiamini kuwa ni mtu pekee aliyeipatia nafasi ya marehemu baba yangu licha ya kuwa wao walikuwa ni marafiki tu. Yaliyotokea baadaye mpaka sasa ni kitendawili rafiki zangu na ndiyo maana nimeona asubuhi ya leo tuanzie hapa."

Alitoa kitambaa na kujifuta machozi ambayo yalianza kuchukua nafasi machoni kwake.


" Tusamehe bure Jackline kukurudisha nyuma hatukuwa tukijua hili inawezekana haraka zetu zimeleta haya labda ungetujulisha kwa nafasi yako."

Jasmine aliomba msamaha baada ya kumuona Jackline akidondosha machozi japo alifuta lakini bado yaliendelea kutoka. Jackline aliwaangalia kwa muda rafiki zake kisha aliinuka na kuwakumbatia wote kwa pamoja.


" Msijali rafiki zangu niko sawa kwa sasa japo ni kumbukumbu zisizo futika kichwani mwangu lakini yote kwa yote tuanze."

Aliwaambia rafiki zake.


"Usijali Jackline tuko pamoja tuanze sasa."

Jessica alimuondoa hofu Jackline.

Lakini wakiwa kwenye harakati za kuanza mchakato wao mara kuna ujumbe uliingia kwenye simu ya Jackline kwa njia ya Whatsapp.


"Roberto kanitumia ujumbe hapa sijui kuna nini?"

Jackline aliwaambia wenzake akifungua ujumbe ule.


"Ufungue tujue kuna jipya gani leo huko maana sio kwa kuwapeleka puta wakina Santana kama nawaona vile."

Jasmine aliongea huku akigonga mkono na Jessica.


"Habarini dada zangu! Mnaendeleaje huko kwa upande wangu mdogo wenu naendeleza mapambano ya kuhakikisha nawarudishia furaha iliyopokwa na Santana mpaka kufikia hatua ya kuyaishi maisha ambayo hamkuwahi kuyafikiria. Ni jana tu nimefanya janga kule mgodini baada ya kutuma vijana wangu kwenda kupiga moto ghala la kuhifadhia mitambo mbalimbali kama salamu tu kwao na mkumbuke pia hata lile Helicopter la Santana nilishalitia moto pia."


Kila mmoja aliupitia ujumbe ule wa Roberto na kisha kwa pamoja walisimama na kuruka juu kwa furaha kisha wakajirekodi video fupi ambayo walimrushia Roberto na ilikuwa na ujumbe huu ;-


SANTANA TUNAOMBA UJIANDAE JESHI KAMILI LIKO MAZOEZINI NA MWAMBIE HUYO ANAYEJIITA ROBINSON KUWA TUKO HAI NA HAPA NI TANZANIA.


Na chini ya video hiyo kulikuwa na ujumbe uliokuwa ukimshukuru Roberto kwa anachoendelea kukifanya.


"Brother tunashukuru kwa kujitoa mhanga kwa ajili yetu na muda si mrefu tutaungana nawe kwenye vita hii inayoelekea ukingoni."


Roberto aliurudisha ujumbe muda mfupi baada ya wao kuutuma ule wao.


"Nipo kwa ajili yenu dada zangu I miss you."

Aliandika hivyo kisha naye Jackline akaujibu mara moja.


"We miss you too brother."


Kisha waliachana na Roberto wakaanza mchakato uliowafikisha Tabora muda huo. Jackline alitoa simu ya mzee Jonathan akaifungua na kutafuta namba ya mzee Jonathan na baada ya kuipata aliipiga na kumkabidhi Jasmine aongee naye.


"Habari yako mama ni Ofisa wa Polisi kutoka kituo kikuu hapa Chunya, tumeona tukupigie simu hii kukufahamisha kuwa mumeo katoroka sero ya Makongolosi. Na tumevichukua vitu vyake vyote ikiwa ni pamoja na hii simu. Hatujui amejificha wapi mume wako ila tu tunahitaji msaada wako."


"Jamani Afande mlimfanya nini mpaka akafikia hatua hiyo ya kutoroka?"


"Hakuna ambacho tulimfanya isipokuwa tu yeye mwenyewe kwa kushirikiana na maaskari wawili."


"Jamani kwanini mimi lakini? Sasa Afande mnanisaidiaje kumpata maana nimjuavyo asije vaa tai ya kifo shingoni?"

Mke wa Jonathan alilalamika simuni.


"Tunashukuru kwa ushirikiano wako mama yangu tutakujulisha kinachoendelea hapa."


Jasmine aliongea hayo na kisha kukata simu ambayo alimrudishia Jackline.


"Waoo dada yake yaani kama Afande kweli kumbe mlalahoi mwenzangu tu."

Jessica alimpongeza dada yake na kuweka utani kidogo.


"Aisee umefanya zaidi ya nilivyofikiria Jasmine Safi sana."

Jackline naye alimpongeza kwa alichokifanya.


"Jamani acheni kunijaza mwenzenu nisije ota mapembe bure eenh kifuatacho baada ya hiki? Maana mama yako mlezi siyo kujiliza simuni utafikiri mpambe wa malaika kumbe jini mnyonya damu."


"Kwanza ukimuona alivyo na yanayotokea huwezi amini ndugu yangu."

Jackline aliongeza kwenye maelezo ya Jasmine.

Baada ya hapo walimuomba Jessica aifungue application ya kufuatilia simu ya mtu anafanya mawasiliano na watu gani kuzijua namba hizo na kisha kuzifuatilia katika GPS.


" Kwa hiyo mimi nitakuwa IT wenu siyo?" Jessica aliuliza.


"Kama kawaida."

Jasmine alimjibu huku akimkabidhi iPad ambayo itatumika kwenye zoezi hilo.


"Na kwa kuanza anza kuiangalia namba ya huyu mama tuliyeongea naye iko mkoa gani?"

Jackline alimwambia Jessica huku akiinuka pale alipokuwa kaketi na kumfuata Jessica pale alipokuwa kaketi akiifuatilia namba ya mke wa mzee Jonathan.


"Hii namba haiko mbali dada zangu inaonekana ikihama na eneo hili ni karibia na mkoa wa Tabora."

Jessica aliwaambia wenzake.


"Unasemaje Jessica?"

Jackline alimuuliza Jessica kama hakumsikia vile awali.


"Ndiyo hivyo na inavyoonekana yuko safarini kwani haijatulia eneo moja namba yake."

Jessica alimjibu.


"Nimegundua kitu huyu inawezekana kuna sehemu anakwenda au kawasiliana na mume wake ndiyo anakoelekea nini?"

Jackline alijiuliza huku akiwa kamkazia macho Jasmine na hapo hapo akawaambia wenzake watoke eneo hilo mara moja. Hukukuwa na la kusubiri muda huo zaidi ya kumfuata yule kijana mhudumu wa pale na kumkabidhi hela yake kisha wakaishika njia kutoka eneo hilo huku Jessica akimpigia simu dereva wao awafuate walipo.

Alipofika dereva wao waliingia garini na kuishika barabara ya kuelekea Wilaya ya Manyoni kupitia Nyahua ya Itigi inayokwenda kutokea Manyoni nje ya makao makuu ya mkoa wa Singida.


"Kwa hiyo tunaelekea wapi Jackline maana tunaona huku Tanzania unatukimbiza tu mara ingia hivi mara kata kushoto kama ilivyokuwa upande wetu Brazil."

Jasmine alimuuliza baada ya kuona namna anavyomuelekeza dereva njia ya kupita.


"Hii njia tunakwenda kutokea mbele ya Singida namaanisha kuwa hatuingii Singida mjini bali tunakwenda kutokea wilaya ya Manyoni ambayo hii ukiipita tu unaanza kuutafuta mkoa wa Dodoma na baada ya kufika Manyoni Jessica utaifanya kazi yako ili tujue kama tuko mbele yake au tuko nyuma yake?"

Jackline alihitimisha maelezo yake kwa kumtaka Jessica kuendelea na kazi yake watakapofika Manyoni.


" Mimi si ndiyo mtaalam wenu wa tiba ninyi tegemeeni matokeo mazuri ya huduma yangu."

Jessica alijisifia.


" Basi mwenyewe bichwa hilooo kama nakuona vile."

Jasmine alimtania mdogo wake.


Ndani ya masaa mawili walikuwa ndani Manyoni na kama ilivyo kawaida yao walimtaka dereva apeleke gari kulifanyia chekapu Gereji na wao wakashuka na kuingia ndani ya Hoteli iitwayo Highway ambayo ipo kilometa chache kutoka barabara kuu iendayo Dodoma.


"Samahani dada wasikilize ndugu zangu pale."

Jackline alimuagiza mhudumu wakati yeye akielekea chooni.

Baada ya kurudi alikuta wenzake wakimshughulikia kuku mzima pale mezani huku kukiwa na chupa kubwa ya juisi hivyo akaona achukue glasi ilikuwa ikimsubiri na kujimiminia ile juisi na kisha kuungana nao kumsambaratisha yule kuku.


"Yaani Jackline huku maisha yako chini sana aisee si kama Brazil na maeneo mengine tuliyotembelea eti kuku mkubwa hivi wametuambia shilingi elfu ishirini na tano wakati Namibia tu tuliambiwa dola elfu mbili mia tatu?"

Jessica aliyasifia maisha ya Singida baada ya kukutana na bei ya chini kwenye kuku waliyemnunua.


" Sikieni huu ndiyo mkoa unaoongoza kwa kuwa na bei ya chini kwa kuku sijajua wanafuga sana au vipi lakini iko hivyo."

Jackline aliwaeleza wenzake huku akitupia kipande cha nyama mdomoni.


"Jamani tufanyeni haraka tuendelee na kazi yetu huyu kuku asije tuchelewesha kwa tunachokifuata."

Jasmine aliwakumbusha baada ya kuona habari ya kuku inataka kuwa kubwa sana.


"Kweli dada yangu."

Jessica alijibu na kuinuka akaelekea chooni ambako huko hakuchukua muda alirejea na kulifuata buyu chirizi lililokuwa karibu nao akanawa mikono yake na kujikausha vizuri akaungana na wenzake pale mezani akaichukua iPad yake na kuanza kazi.


" Hee hebu angalieni jamani haya si maajabu kweli?"


Bila hata kuuliza wote walimsogelea na kuangalia alichokuwa akiwaonesha, hawakuamini macho yao baada ya kuiona GPS ikionesha namba ya mke wa mzee Jonathan ikiwa karibu zaidi na pale walipo na hivyo kubaini kuwa mama huyo hayuko mbali na pale walipo ndipo jackl alipoinuka na kuelekea nje jengo lile la Highway na hakuna kingine alichokifanya zaidi ya kukagua magari yote yaliyokuwa yamepaki pale kwenye eneo la maegesho. Wakati akiwa anaangalia lile eneo mara aliwasikia watu wakija upande wake kutokea kwenye ngazi za kutokea ghorofa ya juu na ndipo alipojificha kwenye nguzo mojawapo ya jengo hilo ili aweze kuwaona vizuri watu hao kwani sauti ya mama huyo si ngeni sana masikioni mwake,ndipo alipoweza kumuona mbashara kabisa mama huyo akiwa na kijana mmoja ambaye alimhisi kama dereva wake wakiwa wanatoka na kuelekea lilikopaki gari lao na bila shaka walipita hapo kupata chakula. Haraka sana alirudi ndani na kuwaita wenzake huku simu ikiwa sikioni kumwita dereva wao.


"Uko wapi kaka?"

Jackline alimuuliza.


"Niko hapa mliponiacha nang'arisha buti langu."

Alijibu dereva huyo.


"Usiondoke tunakuja kuna gari jeusi aina kluga linatoka kwenye geti la Highway Hotel mbele yako unaliona?"


"Hebu ngoja kwanza niliangalie dada, yapu naliona ndiyo linatoka getini."

Alimjibu dereva wao.


"Hakikisha halitoki machoni kwako hilo gari."

Jackline alimpa maagizo hayo huku na wao wakiwa karibu na geti hilo la Hoteli ya Highway.


"Vipi umemuona tayari?"

Jasmine alimuuliza Jackline ambaye ni kama alichanganyikiwa hivi kwani aliwaita bila kuongea chochote.


"Ndiyo yuko ndani ya Kluga nyeusi na imeshatoka tayari."

Alijibu huku akihesabu hatua zake kuifuata gari iliyokuwa ng'ambo ya Hotel hiyo. Waliingia ndani ya gari na kisha iliondoka.


"Vipi imeelekea wapi?"

Jackline alimuuliza dereva.


"Iko mbele yetu haina hata dakika kumi toka imeondoka."

Dereva alimjibu.


"Basi jitahidi tulikaribie maana ni kama bahati vile kuliona."

Jackline alimuomba dereva alifukuzie.


"Sawa dada."

Dereva alimjibu.

Hivyo njia ilishikwa kuelekea Dodoma kulifukuzia Kluga hilo alilomo mke wa mzee Jonathan.


WATAFANIKIWA KUWAKUTA ?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.





Mzee Bruno Gautier na Robinson waliwasili Mgodini walikoondoka muda mrefu sana hii yote ilikuwa ni katika kukabiliana na wakina Jackline na leo wanarejea wakiwa hawajafanikiwa kuwatokomezea mbali mabinti hao badala yake ni kama vile wamewaimarisha zaidi kwani wamekuwa hatari zaidi ya walivyokuwa mwanzo. Walipoingia walikutana na hekaheka za watumwa pamoja na walinzi kubebelea maji kwenda nayo kwenye jengo la chini ambalo huhifadhi vipuri na mitambo mbalimbali.


"Mbona sielewi elewi kulikoni huko?"

Mzee Bruno Gautier aliuliza.


"Mambo si shwari mkuu ghala letu la mitambo limewaka moto."

Alijibu kijana wake ambaye aliachiwa mgodi wakati huo.


"Unasemaje weweee yaani umeangalia weeee ukakosa cha kunidanganya umeona uuguse mtima wangu siyo?"

Mzee Bruno Gautier alitokwa na maneno baada ya kusikia kuwa ghala limewaka moto.


"Mkuu nikudanganye ili itokee nini au nifaidike nini? Ukweli uko hivyo mkuu tumejitahidi kuuthibiti moto huo kwa kasi yetu lakini asilimia sabini ya vifaa vimeteketea na hii yote ni kutokana na kushindwa kufanya mawasiliano na jeshi la zimamoto."

Alifafanua kijana wake.


" Kwanini mlishindwa kufanya mawasiliano na jeshi la zimamoto pamoja na sisi?"

Mzee Bruno aliendelea kumtwanga maswali na muda huu walikuwa wanaelekea kule kwenye tukio.


" Mkuu system ya mtambo wetu wa mawasiliano uliharibiwa kwanza ndipo hili likafanywa kwani mawasiliano hakuna mpaka sasa ndiyo maana hatukuweza kufanya hivyo ikabidi tupambane kwa kushirikiana na watu wako."


"Wacha uswahili wewe hebu Robinson nenda ofisini kaangalie signo kama iko chini tuone."

Haraka sana Robinson alikwenda kuangalia signo kule kwenye ofisi ya mzee Bruno Gautier.


"Na kingine mkuu mfumo wa mawasiliano mlikosea sana namna mlivyouseti."


"Unataka kuniambia nini wewe?"


"Kukataza matumizi ya simu za mkononi zaidi yako mwenyewe na kuiruhusu simu ya upepo tu maana hata hawa walinzi wa kukodishwa tulipowaelekeza juu ya hili walidai hawana mamlaka walichosaidia ni kushiriki pamoja nasi na kwa utaalam wao ndiyo hali hii unayoiona."


"Ni kweli ukisemacho lakini hii ni kwa usalama wetu na mgodi wetu kwani kuruhusu ninyi kumiliki simu za mkononi ni kukaribisha majanga kwani hatujui nani mzuri na nani mbaya ambacho tutarekebisha zaidi ni kuboresha tu mfumo na si vinginevyo."

Mzee Bruno Gautier alishikilia msimamo wake na aliongea haya akiwa anashika shika mabaki ya vipuri huku moshi ukiwa ni mkubwa sana ndani ya jengo lile.


" Mkuu huu moshi si mzuri kwa afya naomba tutoke nje kwanza tutarudi baadaye."

Kijana wake aliongea hayo baada ya kuona mkuu wake kaanza kupiga chafya mfululizo kwa shingo upande alikubali kwani alikuwa akitoka huku kichwa kikiwa kwenye mabaki mle ndani.


"Mkuu system ya mawasiliano iko chini sana inaonekana mbaya wetu alifanikiwa kuingia mpaka ofisini kwako maana hata ofisi haiko kwenye mpangilio mzuri."


"Eti ni kweli kinachozungumzwa na Robinson?"

Mzee Bruno Gautier alimuuliza kijana msaidizi wake baada ya kusikia maelezo ya Robinson.


"Ni kweli kabisa mkuu na hatujui alipita wapi kwani Ngome muda wote ilikuwa imara."


"Unasema nini? Hebu niitie mkuu wa kikosi saidizi cha ulinzi aje mara moja ofisini kwangu."

Aliagiza akiwa anapanda juu iliko ofisi yake.


"Sawa mkuu."

Alijibu Robinson na kuondoka.


"Huu kweli ni mwaka wa shetani."

Mzee Bruno Gautier aliongea akiwa kajishika kiuno ni baada ya kukuta droo za meza na kabati zimefumuliwa na makaratasi kutupwa hovyo chini.


"Huyu mvamizi alikuwa anatafuta nini kwenye droo hizi?"

Mzee Bruno Gautier aliendelea kujiuliza maswali haya akiwa kainama kukusanya na kuzikagua zile karatasi kuona kama zipo zote.


"Kulikuwa na maana gani kuongeza nguvu hapa, tumelipa hela nyingi kwenu kuhakikisha usalama unaimarika hapa kumbe tulijidanganya."

Mzee Bruno alianza baada ya mkuu wa kikosi saidizi cha Ulinzi kuingia mle ofisini.


"Mkuu ulinzi ni kama ulivyouona uko imara sana lakini kwa kilichotokea ni dhahiri wahusika wana mtandao wao humu humu ndani na ninachohisi humu ndani kuna simu ya mkononi japo mmezuia."


"Unataka kuniambia kuwa kuna simu iliyoingizwa humu ndani kinyemela?"


"Ndiyo mkuu."


"Iliingiaje sasa hapa sasa?"


"Hilo ndiyo la kujiuliza yawezekana iliingia kabla ya sisi kufika hapa."


"Robinson haraka sana kapige king'ora cha dharura."

Mzee Bruno Gautier aliona njia pekee ni kuwaita wote ili kuweza kumbaini mtu aliyefanya tukio hilo.


"Mkuu mle ndani ya ghala baada ya moshi kupungua tumeuona mwili wa mtu mmoja ukiwa umeteketea kabisa na kuwa mkaa sijui ni miongoni wetu tuliokuwa tunaokoa au la."

Kijana mmoja aliyekuwa kwenye eneo la tukio alileta taarifa iliyowachanganya mzee Bruno na mkuu wa kikosi cha ulinzi.


" Hebu twende mara moja huko tunaweza kubaini kitu kutokana na mwili huo."

Aliongea mkuu wa kikosi saidizi cha ulinzi na kutoka nje mara moja na kuelekea ghalani.


Upande wa Santana na watu wake waliwasili kambini kwao wakitokea St Louis Hospital kumuangalia mke wa mzee Bruno na baada ya kufika tu aliwaita watu wake wote kuanzia walinzi mpaka wafanyakazi wa vitengo vyote.


"Poleni na majukumu ndugu zangu ni muda mrefu sana umepita hatujakaa pamoja kuangalia changamoto zinazowakuta sehemu zenu za kazi kama ilivyokuwa hapo awali sababu ya haya yote nadhani mnafahamu wenyewe hatujaweza kutulia kabisa na hata hivi tunavyoongea nimepata taarifa kutoka kwenye mgodi wetu wa kuchimba kokoto kuwa ghala la vipuri limewaka moto pamoja na nyaraka muhimu za mgodi kutoweka hivyo bado tunaendelea na uchunguzi. Na kwa sasa tunabadilisha utaratibu wa kazi humu ndani. Kila mmoja pamoja na kuwajibika sehemu yake ya kazi lakini pia atawajibika kama mlinzi nafanya hivyo baada ya kubaini kuwa kuna wageni wanaingia wakiwa kwenye mazingira ya kutotiliwa mashaka na wafanyakazi humu ndani na kufanya matukio na baada ya kutokea tukio ndiyo tunaanza kulabudisha labda ni yule aliyeingia muda ule, hivyo kwa sasa kila sura itakayotia mguu humu ni kuikamata tu nimeeleweka?"

Alihitimisha Santana kwa wafanyakazi wake."


"Umeeleweka mkuu."

Walijibu.


"Vizuri kama nimeeleweka, kila mmoja aelekee sehemu yake ya kazi."

Waliondoka na kuelekea sehemu zao za kazi huku kila mmoja akionekana kutafakari kile kilichoelezwa na mkuu wao.


"Tom hivi wewe unayaonaje haya matukio?"

Chude alimuuliza wakiwa wanatoka nje.


"Kuna jingine hapo zaidi ya mtandao wa Jasmine na wenzake kuhusika? Yaani hapa mkuu anajitafuna mwenyewe kutokana na matendo yake kwa yule mke wake na pia hata huyu Robinson ingekuwa amri yangu ningemtungua kitambo sana."

Tom alieleza lake.


"Kwanini unasema hivyo?"


"Wewe huoni toka mshikaji aungane nasi kuna matukio yasiyoisha?"


"Hilo na ninalihisi na inawezekana anatuchora weee kisha anawataarifu watu wake."


"Haswaa, tunafanyaje sasa kulinusuru hili?"


"Tunafanyaje? Nenda kaeleze kwa Santana hilo uone kama hujatunguliwa mwenyewe maana wenzako wanamuamini balaa."


"Mhhh nikae zangu kimya kwanza sina hata hisa moja kwenye kampuni hii sasa kihelehele cha nini?"


"Ndiyo nakushangaa sasa?"


Santana akiwa kabaki mwenyewe ofisini mara iliingia meseji kwenye simu yake na baada ya kuifungua aligundua ni Whatsapp kuna kuna video imeingia aliifungua hakuamini alichokiona kwa mara ya kwanza anaziona sura za wakina Jackline tena zikiwa zenye afya tele huku wakimwambia kuwa watarejea huko kumalizia kazi yao kwa muda huo wako zao Tanzania.


"Shiiiiit !!! Hivi hawa ni viumbe wa namna gani lakini maana nilijua kuwa hata wangerejea tena wangekuwa wameharibika zaidi kama si sura zao basi afya zao lakini ndiyo wamekuwa watamu zaidi?"

Santana alisimana na kujiongelesha mwenyewe huku akikizunguka kiti chake.


" Wana uhusiano gani na huyu ajiitaye Roberto mpaka wao kumtumia hii video na yeye kunitumia mimi?"

Aliendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu. Alichoamua kukifanya ni kuipiga hiyo namba ya Roberto. Kama bahati vile iliweza kuita.


"Santana 'a Big boss' nikusaidie nini?"

Roberto alimuuliza baada ya kupokea tu simu.


"Nataka kujua wewe kijana mdogo usiyejaa hata kwenye kiganja changu unapataje ujasiri wa kunitingisha?"


"Kwanza rekebisha kauli yako mimi si kama unavyonifikiria Santana, nipe sifa zangu kwanza mimi ndiyo kiboko yako na kama huamini niruhusu safari hii nije nikuchukue wewe mwenyewe badala ya Bi Claudia ambaye muda si mrefu tutamuajiri kwenye timu yetu. Halafu kaka yangu Santana huna shukrani kabisa yaani kazi yote niliyoifanya Mgodini kwenu hata kunishukuru hakuna? Mungu hapendi hivyo kaka."

Maneno ya shombo ya Roberto yalimfanya Santana aikate simu maana aliona kijana anavuka mipaka na kumtia wazimu.


****


Mchuano ulikuwa mkali sana kati ya gari ya wakina Jackline pamoja na ile mke wa Jonathan kwani dereva wa gari ya wakina Jackline alikuwa na kazi ya kutoipoteza gari ya mbele yake na walikuwa umbali ambao usingewafanya wawashtukie. Baada ya masaa kadhaa waliwasili jijini Dodoma lakini gari ya mke wa Jonathan haikutia kituo ilipita na kuwafanya nao wakina Jackline kuunga hivyo hivyo na walipofika kwenye mchepuko wa kuingia Mtela Kluga iliingia huko na wao kama kawaida waliifuata.


"Hii njia inaelekea wapi?"

Jackline alimuuliza dereva.


"Inaelekea mkoani Iringa ikipita Mtela."


"Ndiyo hii husema ni ya mkato Iringa to Dodoma?"

Jackline aliendelea kuuliza.


"Mbona wanaingia barabara ya vumbi?"

Aliuliza Jasmine baada ya kuiona Kluga ikiacha lami.


"Inaonekana huko kuna sehemu wanaelekea na unaweza kuona mzee Jonathan kajificha huko hebu sisi tusonge mbele kidogo kisha dereva weka triangle mbele na nyuma sijui kitaalamu mnaziitaje ila umenielewa kuashilia gari imepata hitilafu kisha utakuwa kama unalitengebeza hivi utakuwa na Jessica hapa mimi na kamanda mkuu Jasmine tutaivizia hiyo gari kupitia vichaka hivi hapa."

Jackline alitoa maelekezo ambayo yaliungwa mkono na kila mmoja mle garini kisha ikafanyika kama ilivyopangwa.


" Njoo kwa huku Jasmine naiona imesimama pale kwenye mti ule sijui kuna nini?"


" Na sisi tubaki hapa hapa tuendelee kuitazama uzuri tunaliona vizuri eneo lile."


"Ni kweli."


Basi waliendelea kubakia pale ili waone nini kinafanyika na wachukue hatua gani kwani wao hisia zao ziliwapeleka kuwa eneo hilo wamejificha wakina mzee Jonathan kwani wasingekuja tu huku porini bila sababu maalum. Wakiwa bado pale wale waliokuwa kwenye gari walirejea na kuingia garini ila kuna kitu kiliwashtua,walioingia kwenye gari siyo waliofikiria kwani walikuwa ni vijana wa kiume wawili ambao ni kama walikuwa wanatokea kwa mganga kwani kuna mbibi ambaye waliongozana naye alikuwa kavalia nguo za kaniki akiwa na usinga mkononi.


"Jackline hiki ni kiini macho au nini mbona wale ni vijana wa kiume na hakuna mwanamke pale zaidi ya yule bibi sijui mchawi?"


"Tumechezewa picha hapa Jasmine tunatakiwa kuondoka hapa mara moja."

Jackline aliongea akiinuka pale walipokuwa wamefichama.


"Subiri kwanza waondoke kisha tumfuate yule bibi atatueleza ni wakina nani wale."

Jasmine alitoa wazo.

Na baada ya ile gari kuondoka wao walimfuata yule bibi na kuongea naye.


"Bibi shikamoo."

Jasmine alimsalimia.


"Marahaba wajukuu zangu karibuni."

Aliitikia na kuwakaribisha.


"Samahani bibi sisi ni waandishi wa Habari tulikuwa tunafuatilia tukio moja la mauaji huko ndani kabisa kuna kijiji cha wafugaji kiko huko sasa tumetembea muda mrefu tumechoka sana lakini tumeona kuna gari limetoka hapa linaelekea wapi hilo huna namba zao tupate lifti?"

Jackline alimdanganya mganga huyo.


" Poleni sana mabinti zangu kwanza mna bahati sana eneo hili siyo zuri kiusalama kwani kuna matukio mengi ya ajabu na mshukuruni Mungu wenu kwa kuwafikisha hapa salama, ile gari ni ya wateja wangu walikuja kwenye huduma wao wanaishi Singida."


"Huduma gani hiyo bibi?"

Jasmine alitaka kujua.


"Mimi ni mganga wa kienyeji najihusisha na Mali za Kafara hata ninyi mkitaka kuwa mamilionea sasa hivi nawapa tu."

Bibi alifafanua zaidi kitu kilichowashtua wakina Jackline ni baada ya kusikia bibi huyo ni mganga wa Mali za Kafara waliogopa sana.


"Bibi sisi tunashukuru sana tulijua wanaelekea Iringa kama ni huko Singida achana nao uzuri tumeshafika barabara kuu tutapata tu magari."

Jasmine alimshukuru bibi yule.


"Bila shaka kama mtakosa usafiri mnaweza kuja kulala hapa kwani ulinzi ni asilimia mia moja."


"Sawa bibi kwa heri."

Jackline alimuaga na wakarudi kwenye gari yao na kuwakuta wakina Jessica na dereva wakiwa wamekunjua siti wamelala.


"Oya amkeni amkeni." Jasmine aliwaamsha.


"Vipi tayari tuwafuate?"

Dereva aliuliza.


" Tumechemka kaka tuliifuata gari isiyokuwa yenyewe rangi na aina ilituchanganya."

Jackline aliongea huku akipiga bodi ya gari.


" Mimi sikuona umuhimu Tracking maana nilijua ni yenyewe."

Jessica aliongea baada ya kujua wamechemka.


" Ni kweli uhakika ulikuwa asilimia mia moja na ndiyo maana tulikuwa tumerilaksi wenyewe."

Jasmine aliobgeza.


"Jessica hebu rejea kwenye ofisi yako icheki namba yake iko maeneo gani?"

Jackline alimuomba Jessica aikague tena ile namba ya mke wa Jonathan.


"Sawa." Alijibu na kuiwasha iPad yake.


"Tumefeli dada zangu."


"Nini tena?"

Jackline alimuuliza.


"Network iko chini sana hapa hivyo tunatakiwa kwenda mbele au kurudi nyuma."


"Okay turudi nyuma."

Jasmine alipendekeza.

Dereva aliwasha gari na kuligeuza kurudi nyuma huku kila mmoja akiwa kachoka hajui aanzie wapi kwani walijua mchezo umekwisha kumbe wapi hakuna kitu.


JE, NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA





Walirudi mpaka Dodoma mjini lakini kitu cha ajabu ni kwamba Jessica hakuweza kuipata namba ya mama Jonathan kwenye system yake kitu kilichowashangaza sana. Wakaona isiwe tabu wapate pumziko ndani ya mji huo na kwa kuwa tayari Jackline alishanunua nyumba mjini na ndipo aliiacha gari yake wakati wakiondoka kuelekea Brazil. Nyumba hiyo yenye hadhi yake kiasi iko katikati ya mji maeneo ya Area C na kuzama ndani. Jasmine aliishangaa nyumba hii ambayo haikuwa kubwa sana kwani ilikuwa na vyumba vinne tu vya kulala ambavyo ni self pamoja na Dining room na Sitting room, Store na Jiko.


"Hapa ni kwa nani Jackline?"

Aliuliza Jasmine.


"Jamani mimi nimeona tuitumie nyumba hii kwa kipindi hiki ambacho tutakuwa hapa Tanzania."

Jackline aliwaeleza wenzake.


"Sawa lakini tuambie hii nyumba ni ya nani?"

Jessica naye aliendelea kukazia swali.


"Jamani jamani mweee, ni kanyumba ketu haka ndugu zangu ambako nilikanunua mara baada ya kukosa mawasiliano na familia ya mzee Jonathan baada ya kurejea kutoka Afrika ya Kusini."


"Waoo hongera sana kwa kufanya maamuzi yako Jackline ni Mjengo wa maana kwa eneo hili."

Jasmine alimpa sifa zake.


"Asante jamani kwa hiyo tuondoe mashaka juu ya nyumba hii tuko huru kabisa."


"Kwa hiyo hata gari hilo hapo nje ni la kwako?"

Jessica alimuuliza swali jingine.


"Ni kwangu na msisahau kama nilivyowaambia kuwa kila mnachokiona ni cha kwetu."


"Hongera sana kwa hiyo ni mwendo wa kukandamiza tu."

Jasmine alitania.


"Kaka karibu ndani bwana nilikuwa najibu maswali ya waandishi wa habari."

Jackline alimkaribisha dereva wao.


"Asante na hongera pia kwa hatua hii."

Dereva alimpongeza.


"Kidogo kaka yangu."


Waliingia ndani na kuchukua nafasi kisha yeye Jackline alimfuata dada mmoja ambaye alimpa nyumba ndogo ya pembeni yake aishi kwa lengo la kufanya usafi kipindi chote ambacho hakuwepo ili kupata dondoo kidogo.


"Dada Juliana, dadaa!!"

Alimuita.


"Abee." Aliitikia akitoka ndani na kumuangalia anayemwita nje.


"Jamani mdogo wangu wa nguvu Jackline umerudiii?"

Alimkimbilia na kumlaki kama kawaida ya watanzania walikumbatiana kwa furaha zote.


"Nimerudi dada yangu nambie za siku nyingi?"


"Nzuri mdogo wangu ndiyo nini kupotea hivyo sasa?"


"Majukumu tu dada kikubwa nimekukuta mzima, vipi lakini kazi?"


"Mungu anasaidia zinakwenda ila tu upande ule kule wa kiunga alishindwa kumalizia kwani tulikuwa tunabishana yeye akitaka kufanya anavyotaka yeye tofauti na maelezo yako hivyo nikamsimamisha nikamwambia mpaka urudi."

Alimweleza Juliana.


"Usijali dada kikubwa nimerejea tutalishughulikia mwambie kesho aje tuelekezane."


"Sawa mdogo wangu, ila nilikukumbuka acha tu."


"Huna lolote dada Juliana."

Alimjibu huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa noti saba za shilingi elfu kumi na kumkabidhi.


"Bila shaka zitakusogeza kidogo dada."


"Mwee kama ulijua vile mdogo wangu ndiyo maana nilikukumbuka mpaka basi."


"Haya bwana niko ndani nina wageni wangu huko."


"Basi wewe nenda kaungane nao kama kuna chochote ambacho mtakihitaji msisite kuniita."


"Sawa dada."

Alimjibu na kurudi ndani kuungana na wenzake.


"Huyo dada ni nani?"

Jasmine alimuuliza.


"Ni dada ambaye alinipa ushirikiano mkubwa wakati naipigania nyumba hii kuinunua hivyo nikampa nyumba hiyo ndogo aishi huku akiihudumia nyumba yangu kipindi chote ambacho sipo."


"Safi sana."

Alijibu Jasmine.


"Sasa kaka naona kesho wewe urejee Mbeya ili sisi tuendelee na mpambano si unajua gari la kukodi linavyokomba mpunga?"

Jackline alimgeukia dereva wao waliyetoka naye Mbeya.


"Sawa dada ila sema tu kwa sababu ni ya kampuni na mimi mwenyewe ni mwajiriwa ingekuwa tofauti na hapo ningebaki nanyi kwani kupitia ninyi kuna vitu nimejifunza kwa muda mfupi huu."

Dereva aliwaeleza wakina Jackline.


"Kweli kabisa hata sisi wenyewe tulikuwa huru sana ila ndiyo hivyo lakini wakati wowote utakapotaka kufanya kazi na sisi karibu sana."

Jasmine alimtia moyo kama vile wataendelea kuwepo Tanzania.


"Nawashukuru sana dada zangu."

Basi harakati nyingine ziliendelea mle ndani ikiwa ni pamoja na kufuata chakula cha jioni hiyo


ambapo waliona wakanunue nyama na ndizi kwa kuusukuma usiku huo.


Wakati Jackline akishughulikia suala la chakula Jessica alikuwa bize na iPad yake kuendelea kumtafuta mke wa mzee Jonathan huku Jasmine na dereva wao wakiwa wanaangalia televisheni.


"Nimepata jibu la huyu mmama kwanini hapatikani."

Jessica alivunja ukimya uliokuwa umetawala katikati yao.


"Kwanini dogo?"

Jasmine aliuliza.


"Wakati nafuatilia hapa kuna kama signo ilitaka kushika ikatoka bila kulocate eneo."


"Okay kumbe endelea au iache on ili kama system itakuwa poa tutabaini."


"Poa." Alijibu na kuendelea.


Jackline alirudi na chakula ambacho alikiandaa na kuwakaribisha mezani kupata chakula na mara baada ya kupata waliendelea na stori za hapa na pale. Wakiwa wana angalia Televisheni huku wanapiga stori mara kuna ujumbe uliingia kwenye simu ya Jackline, aliifuata pale mezani na kuangalia umetoka wapi ujumbe huo, alipoutazama aliona umetoka kwa Roberto ulisomeka;-


"DADA ZANGU NAPENDA KUWAPA TAARIFA YA KIFO CHA MAMA YANGU MPENDWA KILICHOTOKEA LEO MARA BAADA YA HALI YAKE KUBADILIKA GHAFLA IKIWA ZIMEBAKIA SIKU MBILI KURUHUSIWA KUTOKA."


Aliwafuata wenzake huku akiendelea kuisoma ile sms kuhakikisha kama yuko sahihi alivyousoma.


" Jamani hebu na ninyi usomeni huu ujumbe yawezekana nikawa nimekosea."

Jackline aliongea huku akimkabidhi simu Jasmine.


"Mungu wangu Roberto kafiwa na mama yake?"

Jasmine aliongea kwa sauti ya juu.


"Maskini Roberto wa watu mama yake kipenzi ambaye alikuwa tayari kufanya kila tukio ilmradi tu mama yake apate tiba na sasa amemuacha da."

Aliongea Jackline kwa sauti ya huruma akiwa kajishika mashavu.


"Ninyi ongeeni tu lakini mwenzenu hapa nimevuta picha ile siku ambayo tulimbananisha pale mlimani mpaka akaanza kujitetea na leo hii anampoteza? Imeniuma sana ndugu zangu."

Jessica aliwaambia wenzake akitokwa na machozi.


Hali ya hewa ilibadilika ghafla mle ndani mara baada ya ile taarifa ya msiba wa mama Roberto kitu ambacho kilimfanya dereva wao kushangaa kwani toka achukue kazi ya kuwazungusha hakuwahi waona kwenye hali ya huzuni kama ile. Jackline aliona amtumie ujumbe wa kumfariji mdogo wao.


"MDOGO WETU ROBERTO POLE KWA MSIBA WA MAMA YETU KIPENZI HATUNA CHA KUSEMA KWANI MUNGU KAVUNA MAVUNO YAKE JAPO ILIKUWA NI MAPEMA SANA KUMCHUKUA NA HATUJUI ANA MAKUSUDI GANI JUU YETU KWANI MPAKA SASA WOTE TUMEPOTEZA WAZAZI WETU WOTE KUANZIA MIMI, JASMINE NA JESSICA NA SASA WEWE NA ALIYEKUWA NA WAZAZI WOTE ALITUASI. INAWEZEKANA KUNA JAMBO ANATUANDALIA. #RIPMAMA_YETU.

TUKO PAMOJA MDOGO WETU."


Kisha alimtumia na baada ya kumtumia aliinuka na kuwaaga wenzake kuwa hajisikii vizuri.


" Kaka utaingia chumba hicho pembeni yako mwenzenu siko vizuri ndugu zangu mtanikuta chumbani."


Akawaacha hapo hapo wakiwa kama wamepigwa na ganzi kwani walishindwa hata kumjibu Jackline.


LEO NIMEPOST EPISODE FUPI BAADA YA KUONA MIKONO INATETEMEKA BAADA YA KAMANDA WANGU KUPATA PIGO LA MOYO, TUKUTANE KESHO.


NINI KITAENDELEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.





Roberto aliuchukua mwili wa mama yake na kwenda nao kwao kwa ajili ya maziko, wanajamii wa kijijini kwao Marty waliungana naye kumhifadhi. Kiukweli walijitokeza maelfu kwa maelfu katika safari hiyo ya mwisho ya mama Roberto na kama ilivyo Mila na desturi za kabila lao waliuchoma mwili na kisha majivu yake wakayahifadhi kwenye jengo maalum ambalo hutumika kuhifadhia ambalo lilijengwa karne ya tatu likiwa na zaidi ya miaka elfu mbili lakini limekuwa likiendelea kuhimili kazi hiyo.

Roberto akiwa mwenye huzuni na sauti yake kukauka kutokana na kulia aliyahifadhi sehemu iliyoandaliwa kazi ambayo ingefanywa na baba yake kama angekuwepo kwa kuwa yeye ndiye aliyebakia alitakiwa kuifanya. Baada ya kuyahifadhi ibada maalum ilifanyika mahali hapo ya kumuombea marehemu na baada ya kumaliza watu walitawanyika eneo hilo na kumuacha Roberto akiwa na mpenzi wake Titiana ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo kikuu cha Sanaa Marina. Alikuja kuungana na mpenzi wake kwenye msiba wa mama mkwe wake.


"Baby pole sana kwa donda hili ambalo litachukua muda mrefu kupona."

Titiana alimpa pole mpenzi wake ambaye muda huo alikuwa kaegemea fensi ya jengo hilo akiwa anaangalia wanaopita nje ya jengo hilo.


"Asante mpenzi wangu ni kazi yake Mola hatuna budi kumshukuru yeye, mwache mama yangu apumzike kapata mateso sana."

Alianza kulia tena baada ya kuongea hivyo. Ikabidi Titiana achukue nafasi yake kumtuliza.


"Mtulize mama unavyolia hivyo unampa mateso huko aliko jambo la msingi ni kuendelea kumuombea aliko apumzike salama."


"Nimekuelewa mpenzi wangu, najitahidi lakini ndiyo hivyo tena nashindwa wewe mwenyewe unafahamu vizuri nilivyoishi na mama yangu."


"Naelewa vizuri sana mpenzi lakini kuwa kwenye hali hiyo haimaanishi kubadilisha kilichotokea."


"Nashukuru mpenzi kwa upendo wako tuondoke sasa nahitaji kuwa eneo lenye utulivu." Waliondoka na kuelekea nyumbani na wakiwa njiani mara ujumbe uliingia kwenye simu yake Roberto.


"Watakuwa dada zangu hawa." Roberto aliongea akiufungua ujumbe huo.


"Dada zako gani tena?"


"Niliokueleza kipindi kile kuwa nimekutana nao sehemu fulani hivi nilikokuwa nikawaeleza full life yangu ndipo walipojitoa kumlipia mama hela ya matibabu pamoja na kunikabidhi nyumba ile tunayoishi kwa sasa."

Roberto alimfafanulia mpenzi wake mara baada ya kuuliza.


" Okay ndiyo wale ambao ulisema wana kisanga na Genge la Santana?"


" Hao hao mpenzi."


"Ujumbe wao unasemaje?"


"Ndiyo naufungua hapa."

Aliufungua kisha kuanza kuusoma.


"BILA SHAKA TAYARI UMESHAMZIKA MAMA SIKU YA LEO KAMA AMBAVYO ULISEMA, BAADA YA MUDA WA MAOMBOLEZO UNATAKIWA KUUNGANA NASI HUKU TANZANIA KUIKAMILISHA HII KAZI YA KITOTO KISHA TUJE HUKO KUMALIZA MCHEZO AMBAO BILA SHAKA UTAMPA TABASAMU MAMA YETU HUKO ALIKO."

Baada ya kuusoma alitabasamu kitendo kilichomshtua Titiana kwani kwa muda wote huo hakuweza kuliona hata jino moja la mpenzi wake.


" Vipi mbona meno nje tena? "


" Soma ujumbe huu wewe mwenyewe mpenzi."

Alimpa simu ausome yeye mwenyewe ujumbe huo na baada ya kuusoma alimgeukia na kumuuliza Roberto.


"Usemaje kwenye hili sasa?"


"Hakuna la ziada mpenzi zaidi ya kusafiri kwani kama nilivyokueleza hapo kabla kuwa nahitaji kupata eneo tulivu la kutuliza mawazo hivyo najua tutakapokuwa Afrika akili itakaa sawa kwanza nitakutana na Crew niliyoizoea au unasemaje baby?"


"Sina neno itabidi iwe hivyo ili na mimi iwe kama Tourtime kwa kipindi hiki cha likizo."


"Tuko pamoja baby hivyo tukifika nyumbani fanya maandalizi ya pamba tutakazotumia tukiwa huko na siwaambii kuwa kesho tunaingia huko nataka iwe bonge la surprise fulani hivi kwao."

Roberto alimkumbatia mpenzi wake baada ya kukubaliana naye juu ya safiri ya Tanzania na kumpa kazi ya kufanya maandalizi ya safari huku yeye akisema ataelekea mjini kwa ajili ya kushughulikia suala la tiketi na taratibu zote za safari.


****


Waliamka na kuelekea katika Benki ya Global kufanya malipo kwenye kampuni ya Mbeya Kwetu Transport&Co.Ltd ambayo ndiyo iliwakodishia gari hilo pamoja na dereva. Hivyo kwa kuwa tayari walikuwa kwao na usafiri wanao wakaona haina haja ya kuendelea kutumia gharama kubwa wakati gari ipo kwani mpaka hapo walikuwa tayari wanadaiwa kiasi cha shilingi milioni tatu na laki sita. Walifika Benki wakafanya muamala kwenda kwenye akaunti ya Kampuni hiyo kisha wakamkabidhi payslip dereva aende nayo na kisha nakala nyingine wakaituma kwa njia ya email. Kama uungwana walimpa naye kiasi cha shilingi laki nne kama akiba yake njiani kisha waliagana naye yeye akaianza safari ya kurejea Mbeya na wao wakaendelea na zoezi la kumfuatilia mama Jonathan.


"Wacha weee, ngoma si hii hapa chezea mimi wewe?"

Jessica aliongea baada ya kuinasa signo.


"Umempata tayari?"

Jackline alimuuliza.


"Jibu hilo dada Jack."

Alimjibu.


"Inasoma sehemu gani leo maana kwa sasa hatutakiwi kucheza faulo."

Jackline aliuliza.


"Hapa inasoma ni Idofi sijui ndiyo wapi huko?"

Jessica alimjibu.


"Idofi tena mbona giza Mungu wangu iko mkoa gani hiyo hebu ifuatilie kwa upana wake."

Jackline alichanganywa na jina hilo kwani hata yeye si mwenyeji sana wa maeneo ya Tanzania.


"Okay nimelipata eneo hilo tayari dada."


"Enhh liko wapi?"


"Inaonekana liko mkoa wa Njombe katika halmashauri ya mji mdogo wa Makambako."

Alimjibu Jessica.


"Vizuri nalipata hilo eneo, hatuna muda wa kupoteza twendeni nyumbani tukajiandae kwa safari kwani hapo ni njia ya kuelekea Mbeya kupitia njia ile ile ambayo tuliipita kabla ya kupotea."

Jackline alifafanua akikunja kona kurudi nyumbani kwake kwa maandalizi.


" Jackline haina haja ya kurejea nyumbani tukafanye nini huko sisi jeshi kamili mpigie simu dada Juliana afunge milango pale na kufanya usafi, sisi tuianze safari sasa hivi kona kona hizi tutawapoteza tena hao."

Jasmine alitoa wazo ambalo halikupingwa na hivyo alimpigia simu Juliana kumfahamisha hilo.


" Ila dogo wewe kiboko tayari safari na vipi kuhusu yule kiunga? "


" Mwambie afanye kama ulivyomwelekeza hapo awali sisi tunarudi kati ya kesho au keshokutwa ni dharura ya kikazi dada."

Jackline alimjibu dada yao Juliana.


"Haya mdogo wangu safari njema kikubwa usisahau kuniletea zawadi za huko."


"Haya dada." Jackline alimjibu na kugeuza gari kuelekea Iringa road kwa safari ya Makambako. Mashine kubwa Honda jet5 iliatamia barabara kuelekea Iringa.


"Natamani tuwakate wakiwa wote?"

Jackline aliongea.


"Kwanza mimi ninahisi huyu kamfuata mume wake si nasikia Njombe ndiyo eneo linaloongoza kwa kuwa na misitu mikubwa ya kupandwa?"

Jasmine aliuliza.


"Sijui maana kuna Iringa na Njombe hapo sijajua ni upi zaidi ya mwingine."

Jackline alimjibu.


"Naiona signo inasogea upande wetu hii ina maana kuwa wanarudi huku tuliko."

Jessica aliwaeleza kinachoendelea mtandaoni.


"Sisi ni kusonga mbele tu itafahamika mbele kwa mbele kikubwa ni kuwa makini wasitupotee kwa kupita ile ya Morogoro."

Jackline alimjibu Jessica.


"Jackline Tanzania ni nchi nzuri sana na ndiyo maana Watalii huutumia muda wao wa likizo kuja kutembelea Vivutio vyetu vya Utalii."


Jasmine aliisifia Tanzania kwa kuwa na Uoto wa Asili mzuri ambao ni wa kipekee zaidi Ulimwengu.

Honda jet5 ilikuwa ikiingia mjini Iringa muda huu na kuanza kushuka kimlima kutoka Iringa mjini kuja Ipogolo kuishika barabara kuu ya Dar to Mbeya.


" Hebu simamisha kwanza inaonekana signo iko karibu zaidi."


Jessica alimtaka Jackline kusimamisha gari.

Aliipaki gari karibu na kituo cha mafuta cha Ipogolo na kutulia.


"Ngoja nichukue walau biskuti na juisi hapo supermarket."

Jasmine alishuka na kuingia kwenye Kimin supermarket kilichopo pale kituo cha mafuta.


"Ninyi si ni wajanja bila shaka mtu wenu kawataarifu kuhusu kifo cha mama yake na bila shaka kilichobakia ni kukikata kichwa chake na kuwatumia huko huko mliko."


Ujumbe huu uliingia kwenye simu ya Jackline aliusoma akaona haina haja ya kuwaeleza wenzake zaidi ya kuujibu tu.


" Kwa hiyo unataka kunieleza nini Santana? Yule mama kwanza alikuwa mgonjwa kajiishia zake hivyo hata kama umehusika unajisumbua tu kwani mpaka sasa hujui tunachofanya juu yako."


Baada ya dakika moja ujumbe ulirudi tena kutoka kwa Santana.

Aliusoma Jackline kisha akaujibu tena.


UNAFIKIRI ALIUJIBU VIPI ?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.





Ilikuwa ni mchana wa saa saba jua likiwaka kwa kuibiaibia huku wingu likiwa limechukua nafasi kubwa na kuifanya hali ya hewa kuwa ya ubaridi sana, kila mtu alionekana akiwa ndani ya nguo nzito ambazo muda wote ni kupambana na baridi kali ya mkoa huu. Lakini cha ajabu ilikuwa ni kwa baadhi ya vijana walioonekana kuifurahia hali hii ya hewa kwani walikuwa vifua wazi wakibebelea mizigo kutoka kwenye jengo moja ambalo ni kama ghala ya kuhifadhia mizigo na bidhaa mbalimbali likiwa nje kidogo ya Uwanjani wa Ndege wa Songwe.

Hii iliwafanya wapita njia kuwashangaa muda wote. Kwenye gari ndogo aina ya Toyota Brevis nyekundu yenye chapa maalum ya usafirishaji abiria kutoka Uwanja wa Ndege kuwapeleka katikati ya mji na nje kidogo ya mji wa Mbeya, pembeni ya dereva huyu mtanashati alitulia mrembo mmoja ambaye kwa muonekano tu alikuwa ni mgeni wa jiji la Mbeya kutokana na kushangaa kila alichokuwa anakiona mbele au pembeni yake na muda mwingi alionekana kuiangalia sana simu yake ambayo masikioni kulikuwa na wireless phones ambazo ukizitazama kwa haraka unaweza kusema ni hereni kumbe la.


"Tutachukua muda gani kutoka hapa mpaka Forest mpya?"

Mrembo huyo alimuuliza dereva ambaye muda mwingi alikuwa akiibia kwa jicho la pembeni kuuangalia uzuri wa abiria wake.


"Samahani umesemaje dada yangu?"

Ilibidi aulize kwa kuwa alipokuwa akiulizwa swali yeye alikuwa safarini kimawazo na kwa inavyoonekana tayari alishapata ugonjwa wa matamanio.


"Nimeuliza hivi, itatuchukua muda gani kufika Forest mpya?"

Ilibidi arudie tena swali lake.


"Ni dakika ishirini tu ila lingekuwa ni gari bovu bovu mwenyewe ungeisoma mngechukua hata masaa mawili au zaidi."

Dereva alitamba mbele ya mrembo kwa kuisifia gari yake.


"Ni kilometa ngapi?"

Alipigwa swali jingine tena.


"Ni kama kilometa nane mpaka kumi hivi ila sina uhakika sana."

Majibu ya dereva yalimfanya mrembo huyo kutabasamu kidogo bila shaka alibaini kitu.


"Naitwa Mwakapera dereva mashuhuri hapa Songwe Airport nikihudumia abiria wa ndani na nje ya Tanzania nikihakikisha usalama wao kwa asilimia mia moja sijui mwenzangu wanakuitaje?"


"Naitwa Titiana Thompson."


"Aisee jina zuri kama wewe mwenyewe."


"Nashukuru sana."

Alijibu huku akiiangalia simu yake ambayo ilikuwa kwenye tracking system na alipoiangalia vizuri ikamuonesha kuwa ni mita kadhaa mbele anatakiwa kusimama.


"Samahani kaka yangu naomba unishushe hapo mbele kwenye hilo bango kubwa."


"Mbona bado si umesema Forest mpya?"

Dereva alimuuliza baada ya kuona akitaka kushushwa eneo la Maghorofani.


"Ni kweli lakini naomba uniache hapo hapo nadhani unaiona hiyo Corolla nyeupe pale mbele ya lile bango."


"Ndiyo nimeiona."


"Vizuri hapo ndipo usimame tafadhali."


Dereva ilibidi awe mpole kwani hakuwa na la kufanya zaidi ya kutekeleza matakwa ya abiria wake na baada ya kufika pale gari lilisimama kisha akatelemka mrembo Titiana kisha dereva naye akatelemka na kushusha mizigo yake. Baada ya kupokea hela yake alimshukuru na kugeuza gari kurudi alikotoka huku ndani ya ile Corolla alishuka kijana mmoja mweupe na mwembamba mwenye nywele nyingi kiasi zikiwa ndani ya kofia aina ya cap nyekundu na machoni akiwa katupia miwani mikubwa myeusi kwa upande wa miguuni alikuwa na Raba nyeupe ambazo hazikuwa na nembo yoyote ile huku jeans ya rangi ya nyeusi na t-shirt nyeupe ikiwa ndani ya Kikoti cha rangi ya kijivu vikiupamba mwili wake. Walikumbatiana na kisha waliingiza mabegi kwenye gari hiyo na wao wakaingia zao na safari ikaanza.


"Nipe habari mpenzi?"


"Freshi tu baby niliingia hapa usiku wa saa tisa mvua ilikuwa ikipiga balaa baridi usiseme, nchi hii si ya kawaida nishukuru Mungu dereva huyu alinipa kampani ya nguvu sana kwani alinifikisha MBEYA SMILE HOTEL iliyo Forest mpya nilijitupa bila kula kitu chenye chochote kile mpaka asubuhi nikapata chochote kitu ndiyo kuwa sawa."

Roberto ambaye alitangulia kwa masaa kadhaa mbele ya mpenzi wake Titiana Thompson alikuwa akimpa mchapo wa safari yake ilivyokuwa.


" Pole sana mpenzi wangu lakini hali hii inakaribiana na ya kwetu Brazil sema hapa ni kama imezidi kidogo."


"Hapana ya hapa ni zaidi."

Alimjibu Roberto.


"Nambie sasa kifuatacho maana uliniambia nikifika tu kuna jipya ni lipi hilo?"

Titiana alimuuliza.


"Baada ya kuitrack namba ya Jackline jana usiku na leo kwenye mida ya saa tano niliibaini kuwa haiko mbali sana kutoka hapa Mbeya na nilipoiconvert kwenye mwendo nikaona ni kama masaa matatu hivi kwa mpiga gia mzuri na nilipomshirikisha dereva wangu akasema hiyo kazi ndogo sana kwake."


"Kwa hiyo tunaanza kuifuatilia?"

Titiana alimuuliza.


"Kama kawaida mpenzi."

Alimjibu.


"Okay sawa japo mwenzako nimechoka sana ila usijali."

Titiana alikubaliana na matokeo safari ilianza kuelekea Makambako road.


"Suka mpaka hapo Makambako tutaingia saa ngapi maana hii ni saa kumi na nusu."

Roberto alimuuliza dereva.


"Hapo ongeza masaa matatu kamili."

Dereva alijibu huku akipangua mitaa ya makunguru kukwepa msongamano wa magari maeneo ya Mafiati mpaka Kabwe hivyo yeye aliingia njia ya kutokea Soweto. Maana anaufahamu msongamano wa Mbeya ulivyo unaweza poteza hata masaa mawili usipokuwa makini.


" Inaonekana wewe ni jeuri sana ee unaukimbia msongamano hapo mataa?"

Titiana alimuuliza dereva baada ya kuona anachepuka.


****


Baada ya kusubiri sana pale Ipogolo bila mafanikio yoyote waliona haina haja ya kuwafuatilia kule Makambako wakaona warudi Iringa mjini ndani ya TRAVETA HOTEL ambako walilala huku macho yao yakiwa kwenye system. Na kulipokucha asubuhi baada ya kupata kifungua kinywa na kuona bado system inaonesha wako ndani ya Makambako wakaona kuwa kwa hapo hakuna jinsi zaidi ya kuwafukuzia huko huko. Hivyo jet5 liliungurumishwa kushuka mteremko wa kuelekea Ipogolo kisha kuishika barabara kuu ya Dar - Mbeya.


"Wameshtukia nini? Mbona wanatukwepa sana hawa?"

Aliuliza Jackline akiwa nyuma ya usukani.


"Hawana janja hiyo nahisi hapo walipo wanasubiria kitu na hata siku ambazo alipotea hewani nahisi ilikuwa mtandao au chaji tu na si vinginevyo."

Jessica aliwapa moyo wenzake huku jet likiendelea kukata mbuga na mabonde kuitafuta Makambako.


"Nina hamu nao hao hasa huyo anayejiita Jonathan? Nitahakikisha tunazipiga kavu kavu naye kabla ya kuanza kutenganisha viungo vyake."

Jackline aliwaeleza wenzake atakachomfanyia baba yake mlezi.


"Endesha gari huko usije ishia kulia tu utakapomuona."

Jasmine alimtania na wote wakacheka.


"Siwezi kubisha yote yanawezekana maana nina hasira sana na matokeo ya hasira hayanaga adabu eti."

Jackline alimjibu


Hatimaye waliwasili mjini Makambako na kutafuta sehemu ambayo hawataweza kuipoteza signo na hivyo kutafuta Hotel ambayo iko karibu na barabarani hivyo wakakunja barabara kuelekea Songea road na kupaki nje ya hotel ya KIBADAMO hapo walichukua vyumba na kisha walipumzika kidogo. Lakini Jessica alitoa pendekezo kuwa wasikae vyumbani bali washuke chini na kutulia ndani ya gari ili iwe rahisi kuwakabili. Wakafanya hivyo na baada ya muda kidogo wakiwa ndani ya Honda jet5 waliona signo inatembea wakaanza kuifuatilia mpaka eneo la Majengo huko signo ikawaonesha kuwa wako karibu zaidi na maghala ya nafaka ikabidi waende maeneo yale kuangalia kama kuna nyumba ambayo itakuwa na gari ile ya Kluga. Walipaki gari lao karibu kidogo na Maghala na kisha kushuka na kuifuatilia.

Walizunguka kwa muda na kama bahati vile ndani ya nyumba moja waliiona ile gari ikiwa imepaki ndani yake wakaona isiwe shida wakarudi garini na kutulia hapo huku macho yakiwa kwenye kile kinjia cha kuingia mle ndani. Masaa yalipita lakini hakuna kilichotokea labda ile gari itatoka lakini wapi na hatimaye saa moja jioni iliwakuta wakiwa pale pale na kuamua kuondoka eneo lile kuhofia kushtukiwa na wenyeji wa maeneo yale hivyo wakapita na kwenda upande wa ambako walipaki lakini macho yakiwa pale pale.


"Mnaonaje gari tukalipaki barabarani kisha sisi turudi kwa mguu mpaka hapa na tukakae pale kwenye kile kiduka."

Jackline alitoa wazo na hivyo kuwaacha wenzake na kwenda kulipaki gari kando ya barabara ya Mbeya - Iringa kisha yeye akarejea kwa mguu kuungana na wenzake.

Ila kuna kitu kilimshtua kidogo kwani wakati akiwafuata wenzake aliiona gari ndogo taxi ikielekea pale pale walipo na kupaki nyuma kidogo ikiwa imezima taa.


Hapo ikabidi apunguze mwendo na kuanza kuivizia kujua wanatafuta nini eneo lile na kwanini watembee giza, akaona pia atoe simu kuwataarifu wenzake juu ya watu hao lakini simu hakuwa nayo alimuachia Jasmine aliyekuwa akiitumia kucheza gemu.


"Mungu wangu itakuwaje sasa?"

Jackline alijiuliza swali hilo baada ya kuikosa simu.

Akaona isiwe tabu akaanza kuwavizia mdogo mdogo na baada ya kuwakaribia akawaona watu wawili wakishuka kutoka kwenye gari hilo na kurudisha milango kisha kuanza kuelekea walikokuwa wakina Jasmine. Na kwa kuwa ilikuwa ni giza kutokana na kukatika kwa umeme hakuweza kuwaona vizuri hivyo ikabidi yeye alivizie hilo gari kuona kuna nini ndani yake. Alipofika kwenye ile gari alichungulia ndani na kumuona mtu ndani yake akaugonga mlango huku yeye akiwa kauficha mwili wake ubavuni mwa gari asionwe na mtu huyo aligonga tena ikabidi mtu yule ashushe kioo ili achungulie nje kuna nani aliyegonga gari. Alipochungulia na kuona hakuna mtu wakati huo Jackline akiwa amelizunguka gari ikabidi mtu yule ashuke chini kitendo cha kukanyaga tu ardhi alikutana na mdomo wa baridi wa bastola uliokuwa tayari kisogoni kwake.


"Tafadhali kwa usalama mkubwa weka mikono yako juu kabla sijakufanyia kitu mbaya."

Jackline alimuweka mtu kati kijana wa watu na kisha kumsogelea karibu zaidi ili kumtwanga maswali yatakayomuweka huru kijana huyo au kumchukulia uhai wake.


JE, NI NINI KITATOKEA?


USIKOSE KUSOMA HADITHI HII KATIKA SEHEMU ITAKAYOFUATA KUJUA KILICHOJIRI.





Kwa kujitetea ilibidi aeleze anachokijua mpaka hapo alipo muda ule.


"Dada yangu usiniue nitakwambia kila kitu ninachokijua."

Alianza dereva.


"Haraka nakusikiliza kabla ubongo wako haujawa halali yangu."

Jackline aliongeza mkwara.


"Mimi ni dereva Taxi tu kutoka mkoani Mbeya, nimekodiwa tu hao wageni waliotokea sijui Brazil? Kwa maelezo yao."


"Brazil? Ina maana ni Roberto?"

Jackline alishangaa kusikia wageni kutoka Brazil hivyo hakutaka kusubiri haraka sana alimtaka wafuatane kule walikoelekea wale wageni.


"Si kweli aise hebu ongoza kuelekea kule walikoenda na ole wako iwe ni habari ya uongo utajuta kuisikia sauti hii."

Waliondoka na kuelekea kule walikoelekea wageni wa yule dereva Taxi. Walitembea na kuwakuta wakiwa wamekaa pamoja wakipiga stori kitendo kilichomfanya aamini na kufikia hatua ya kumsukuma pembeni yule dereva na kukimbia huku akiita.


" Robertoooooo........."

Roberto naye baada ya kuisikia sauti hiyo naye aliinuka na kumfuata Jackline.


"My sister Jeyiiiiiiiiiiiiii....."

Walipofikiana walirukiana na kukumbatiana kitendo kilichowapeleka mpaka chini.


"Kwanini umetufanyia hivi lakini Roberto?"

Jackline alimuuliza huku wakisogea pale walipokuwa wenzao.


"Nilitaka kuwaonesha mimi ni mtu wa namna gani?"

Roberto alijibu kwa kujiamini zaidi cheko likiwa limetawala uso wake.


"Njia uliyotumia ni nzuri lakini ni hatari sana kwani hapa tuko windoni na ninyi mmetokea unafikiri nini kingetokea mdogo wangu?"

Jackline alimuuliza Roberto.


"Surprise zina sehemu zake Roberto shauri yako."

Jessica aliingiza neno lake naye na kama bahati vile umeme nao ulirejea kama kawaida.


"Jamani eee dogo lenu limetua ni kosa limefanyika lakini lengo langu limetimia kikubwa ni kujua mnatafuta nini hapa maana si kwa baridi hii."

Roberto aliomba msamaha kiaina na kuuliza kilichowaweka pale.


"Hapa ndipo kazi yetu iliyotuleta Tanzania inapokwenda kuanzia kwani ndani ya jengo lile kuna gari ambayo ilimbeba mke wa Jonathan Ubao."


"Kwa hiyo mnataka kuniambia nimeuvaa mkenge kwa kufikia kazini?"

Roberto aliuliza.


"Ni kweli kabisa Roberto karibu sana lakini hujaniambia uko na nani?"

Jackline alijibu na kuuliza.


"Anaitwa Titiana Thompson ni mchumba halali wa kaka Roberto."

Jessica alilijibu swali la Jackline.


"Waoo safi sana mdogo wangu, Titiana karibu mzigoni naitwa Jackline Kamanda wa kikosi nchini Tanzania."

Jackline aliwachekesha wenzake kwa namna alivyojitambulisha.


"Asante dada yangu nipeni jukumu langu nilifanyie mchakato mara moja."

Roberto tayari hakutaka kupoteza muda na stori ambazo zinaweza kuwapotezea windo lao.


"Kama tulivyosema kuna watu tunawavizia hivyo tuko hapa kwa staili ya fisi."

Jasmine alimwambia Roberto.


"Sawa sawa ila naomba tuongozane na mmoja mpaka karibu zaidi na hiyo nyumba ili kujua tuanzia wapi kuliko kuwa hapa unajuaje kama wameshtukia mchezo na kuiacha system pale na wao kuishia zao?"

Roberto aliwapa neno ambalo liliwaingia vilivyo wakina Jackline. Hivyo haraka sana ikabidi waondoke wote kuelekea kwenye nyumba ile. Walifika mpaka pale wakiwa wote watano huku dereva akisalia kwenye gari. Na baada ya kufika pale kila mmoja alibana kwenye kona yake ili kutowapa nafasi wenyeji wa maeneo hayo kuwashtukia na hivyo kumfanya Roberto kusogea zaidi mpaka kwenye nyumba ile na kuchungulia ndani na baada ya kuona hakuna kitu cha kumsumbua akaamua kuruka ukuta na kutua ndani. Na kwa kuwa nyumba ile haina ulinzi wowote ikiwa ni ya mtu wa kawaida tu haikumpa changamoto sana kuweza kuingia ndani. Lakini akiwa kwenye nguzo ya nyumba ile mara alitoka mtu mmoja ambaye aliangalia huku na kule kisha akarudi tena ndani, kitendo kile kilimfanya Roberto kupata hamu ya kutaka kujua huko ndani kunafanyika vitu gani na ni wakina nani hao. Aliusogelea zaidi ukuta wa nyumba ile na kulikaribia dirisha ambalo ndani yake kulikuwa na sauti zilizokuwa kwenye mjadala ambao ulimvuta zaidi Roberto kusikiliza.


"Unajua nini jamani muda wa kuondoka unakaribia kwani hii ni saa tatu by saa nne tunatakiwa kuwa barabarani na tunakiwa kuingia njia ya Mtera to Dodoma kisha Mwanza lakini itatuchukua siku sita kutokana na kutafutwa kila kona."

mmoja wao akizungumza hayo kitu kilichomfanya Roberto kuchungulia ndani kupitia dirisha na kubaini ni mtu mmoja mwenye minywele mirefu.


" Ila ninyi jamaa zangu maafande tutaachana hapa hapa kwa sababu tumeshamalizana tayari huko mbele mtajua wenyewe, lakini tu niwatahadharishe mkikamatwa kufeni kivyenu hakuna kumtaja mtu sijui kama hili mmelisikia?"

Aliendelea kuongea yule yule mwenye minywele mirefu.


" Huyu mtu mwenye minywele mirefu ni nani mbona anaonekana kusikilizwa zaidi?"

Roberto alijikuta akijiuliza swali hili na hivyo kuamua kuondoka hapo kwa kuruka ukuta na kutokomea zake kwa wenzake.


" Jamani kule ndani kuna kundi kubwa na bila shaka mpaka mzee Jonathan inawezekana akawa mle ndani kwani nimesikia wakitajwa maafande na pia kuna mtu mmoja mle ndani anasikilizwa sana hivi na ndiye alisema kuwa muda wa wao kuondoka ni saa nne na pia kuwataka wale maafande kuachana pale pale."


"Mhh yukoje huyo mtu kimuonekano?"

Jackline alimuuliza.


"Ni mtu mmoja mwenye minywele mirefu hivi ni kama Rasta."


"Ana Rasta? Hebu ngoja kwanza nifanye jambo moja hivi."

Pale pale Jackline alichukua simu yake kwa Jasmine na kuitafuta namba ya mkuu wa kituo cha polisi Makongolosi Afande Mkonge na kumpigia.


"Samahani mzee wangu hivi kwenye misheni zako umewahi kukutana na mtu ambaye ni Rasta?"


"Jackline uko wapi na kwanini umeuliza hivyo?"


"Nataka kujua tu mzee wangu sababu kuna ndoto huniijia ya mtu mwenye muonekano huo."


"Pole sana binti yangu huyo si mwingine bali ni mzee Jonathan alibadili muonekano wake ili kutoshtukiwa na vyombo vya dola."


"Asante mzee wangu."

Jackline alikata simu yake na kuwataka waondoke sehemu hiyo na kurudi Hotelini kuchukua kilichochao na kuondoka zao. Walifika pale Hotelini kisha waliamua kumalizana na dereva wa Taxi kwa kumpa chake kisha waliingia ndani ya dude lao la Honda jet5 na kisha kutimua vumbi.


"Tunaanzia wapi kamanda wetu?"

Jasmine alimuuliza Jackline ambaye alisahau mpaka kuwajulisha wenzake alichoambiwa na mkuu wa kituo.


"Tunawatangulia mbele hawa watu, Jessica washa kifaa chako kisha tutawasubiri nje ya mji kidogo na watakapotukaribia tunaondoka ili kutowapa nafasi ya kutuona mpaka pale tutakapowatia mikononi mwetu, hamuwezi kuamini ndugu zangu huyo mwenye minywele ndiyo mzee Jonathan mwenyewe."

Jackline aliwafafanulia wenzake.


" Kwa hiyo mtu wetu tunamkaribia kumtia mdomoni?"

Jessica aliwauliza wenzake.


" Kama kawaida hana jeuri tena mzee Jonathan dakika zinahesabika."

Jackline alimjibu.


Baada ya dakika kadhaa walifunga breki maeneo ya Iramba (Makambako) na kuwasubiri watu wao.


" Yote kwa yote Roberto tunakupa pole tena kwa kifo cha mama na ilikuwaje mpaka ikawa hivyo ilhali alianza kuwa fiti?"

Jasmine alimpa pole Roberto na kumtwisha swali.


"Asanteni dada zangu naelewa msiba huu wa mama ni wetu sote ila tu kuna ujumbe niliupata kutoka kwa Santana akijitapa kuwa amehusika."

Aliongea hivyo huku akiufungua ujumbe ule na kuwaonesha wausome wenyewe.


"Kwa hiyo Santana aliamua kutupa kidonda kingine ee? Haina shida katupiga goli la kuongoza lakini ajue sisi ndiyo tutatwaa ubingwa."

Jasmine aliuliza na kutoa matokeo yake huku akijifuta machozi.


"Ni matarajio yangu kuwa ndani ya siku zisizopungua kumi tutakuwa ndani ya msitu wa Amazon tukizisaka roho zao. Kwa sasa ni zamu ya hili zee ambalo lina uhakika kuwa kutoroka kwake polisi baada ya kuhonga linajua limeshinda kumbe halijui nini kiko mbele yake."

Aliongea Jackline huku akisafisha kioo cha simu yake akiwa kaegemea usukani wa gari.


" Jackline jiandae signo iko nyuma yetu mita chache."

Jessica alimpa taarifa Jackline.


Na kweli waliiona gari inakuja nyuma yao kwa kasi kitu kilichomfanya Jackline kulirudisha barabarani Honda lake na kuatamia njia huku macho yake yakiwa kwenye site mirror ili kuhakikisha hawaachi mbali watu hao.


" Mimi nafikiri tuondokane na utumwa huu, mnaonaje kama tukienda kuwasubiri pale njia panda ya kuingia Iringa mjini maeneo ya Ipogolo?"

Jasmine alitoa wazo lake ambalo kila mmoja alikubaliana nalo hivyo kumfanya Jackline kukandamiza gia zaidi.


Waliwasili Ipogolo na kuipaki gari pembeni mwa barabara karibu zaidi na mchepuko wa kuelekea Iringa mjini. Na baada ya dakika kadhaa Kluga ilitia timu na kuingia sheli ambako ilikula mafuta ya kutosha na kuondoka tena na safari hii waliuanza muinuko wa kuingia mjini na kisha wakina Jackline nao wakaanza kuwafuata nyuma taratibu mpaka walipoifikia njia au barabara ya kuelekea Dodoma ambako gari lilishika kasi na nyuma yao wakina Jackline wakafanya hivyo hivyo.


Ndani ya gari la wakina mzee Jonathan stori ziliendelea kama kawaida huku wakiwa hawajui kama wanafuatiliwa nyuma na watu hatari ambao hawakati tamaa mapema kama wanajeshi wa Vietnam ambao ukiua kumi wanaongezeka hamsini.


"Nambie mke wangu.."

Mzee Jonathan alimuuliza mke wake.


"Usingiza ulikuwa haupiti kwa kukuwaza mume wangu kipenzi."


"Tuko pamoja tena mke wangu na baada ya kufika Mwanza ni maandalizi ya safari ya kuelekea Uganda kuna sehemu nimeshapata jumba la kupanga nje kidogo ya mji wa Entebe huko tukifika tu kwa heri mkono wa sheria."

Mzee Jonathan alimtambia mke wake mipango ya baadaye ambayo alikuwa ana uhakika kama vile kaongea na Muumba wake.


" Ni kweli kabisa mume wangu tutatakiwa kufanya hivyo mapema kwani siku za hivi karibuni moyo wangu umekuwa ukinienda mbio sana wala hata sijui ni kwa ajili ya nini?"


"Ni kwa sababu ulikuwa mbali nami na sasa Ondoa shaka kidume wako nimekuja."


Lakini wakati wakiwa katikati ya maongezi kuna gari liliwapita kwa kasi na kwenda kusimama mbele kisha milango ilifunguliwa na kushuka watu wapatao watano wakiwa ndani ya maski huku mikononi wakikamata silaha.


" Mungu wangu kuna nini tena mume wangu?"

Mke wa mzee Jonathan alipatwa na mshangao uliomfanya kumuuliza mume wake ambaye walikuwa pamoja ndani ya gari moja.


"Wala hata sijui, bila shaka hawa ni Majambazi tu kwanini wavalie maski usoni wanaficha nini?"

Mzee Jonathan alijibu huku mwili wake ukiwa umetokwa na vipele vingi vya uoga kitu ambacho mke wake alikiona kitu hicho akajua kumekucha. Lakini wakati wao wakiulizana maswali yasiyo na majibu kijana mtukutu Masanja alifungua mlango na kujitupa kwa staili ya kuviringika kuelekea porini huku akimimina risasi kutoka kwenye moja bunduki ambazo mke wa mzee Jonathan alikuja nazo lakini ni kama alinyang'anya nyama kutoka mdomoni kwa simba mwenye njaa kwani alichokutana huko ulisikika mlio tu makelele ya maumivu na kisha alionekana mmoja akija mbele yao na kuwaonesha ishara ya kushuka chini huku mwingine akimfuata Masanja alikoingia.


"Mume wangu inakuwaje hapa?"


"Tujifanye wajinga tushuke tu kwani tukileta jeuri hapa yanatukuta ya Masanja."

Mzee Jonathan alimsihi mke wake kutii amri kabla ya kukutwa na makubwa. Mtu wa kwanza kutoka garini mikono ikiwa juu alikuwa ni dereva wao ambaye hakutaka kujiuliza mara mbili mbili. Mzee Jonathan na mke wake walifuata na wao wakifanya vile vile.


" Funga pingu hao fasta !!"

Jackline aliwaamuru wakina Jasmine kuwafunga pingu huku Roberto akiwa anakuja na Masanja ambaye alikuwa tayari kapoteza fahamu akiwa kambeba begani na kumpakia kwenye gari ile ile ya mzee Jonathan. Na baada ya kuwafunga na kuwafunga plasta midomoni waliwarudisha ndani ya Kluga na kisha Roberto alikaa nyuma ya usukani kisha magari yalikunja kona kurudi yalikotoka, kitendo hiki kilikuwa ni haraka sana na hakuna aliyepoteza muda. Mpaka yanafanyika haya si mzee Jonathan au mke wake aliyewatambua Watekaji wao.


SAFARI HII NI YA KUELEKEA WAPI?


USIHOFU, TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA.




Santana baada ya kufanikisha kumuua mama Roberto kupitia kwa Nesi Suzanne ambaye ni rafiki yake wa muda mrefu walianza oparesheni ya kuisaka nyumba ya Roberto ili kumfungia kazi kabisa. Walihangaika kwa muda mrefu sana bila mafanikio yoyote ya kumpata. Hivyo kuamua kutuma timu ya watu wawili Robinson na Tom kuelekea nchini Namibia kuwasaka wakina Jackline na kuwatia nguvuni au kuwamaliza kabisa kwa kushirikiana na kikundi cha kihalifu kiitwacho 'The Black Eyez" kinachoongozwa na mwanamama Nafiwe kikiwa na maskani yake jijini Windhoek. Kundi hili limekuwa tishio sana ndani na nje ya Namibia kwa kufanya matukio ya kiporaji kwa kutumia Silaha na kufikia hatua ya kufungiwa misaada kutoka nje ya nchi kwenye mataifa makubwa kama Uingereza na Ujerumani kutokana na mauaji yalifanywa na kundi hili kwa kuwaua Watalii zaidi 20 kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo hayo mawili ambao walifika Namibia kwa shughuli za Kiutalii ndipo walipovamiwa na kundi hili na kuporwa kila kitu na kisha kuuawa. Lakini pamoja na harakati zote zilizofanywa na jeshi la Polisi la nchi hiyo la kuwakamata hazikufanikiwa kwani kwa mujibu wa habari za chini ya kapeti ni kwamba kundi hilo lina ushirika na baadhi ya viongozi wenye vyeo vya juu serikalini. Na ndiyo maana kila wanapojipanga kuwakamata taarifa zao huwafikia haraka 'The Black Eyez' na kuchukua tahadhari za haraka.

Robinson na Tom waliwasili nchini humo masaa ya magharibi kwa kutumia usafiri wa anga wakiwa na Jukumu moja tu la kuwasambaratisha wakina Jackline na kisha kurejea Brazil kuendelea na shughuli zao haramu.


"Karibuni sana vijana wa Santana Cruise katka ardhi ya watu weusi wenye roho za Kizungu kama sisi."

Nafiwe aliwakaribisha wageni wake muda huo wakiwa ndani ya gari kutoka Airport kuelekea nyumbani kwake.


"Asante sana madam."

Alijibu Tom.


"Naitwa Madam Nafiwe maarufu kwa jina la Iron Lady' nikiwa ndiye Rais wa The Black Eyez' na Mfanyabiashara mkubwa sana hapa Namibia."


"Tunashukuru kukufahamu Madam, mimi naitwa Tom na mwenzangu hapa ni Robinson."

Tom naye alifanya utambulisho.


"Oohh jina kama la mwanangu wa kwanza Safi sana."

Aliwajibu wakina Tom.


"Jina gani hilo madam Tom au Robinson?"

Robinson aliuliza.


"Anaitwa Robinson na siyo Tom."

Aliwajibu Nafiwe.


Safari iliishia kwenye jengo moja la kifahari ambalo liko nje kidogo ya mji na kuingia moja kwa moja mpaka ndani na kupaki wakateremka na kukaribishwa ndani.


"Karibuni ndani wageni wangu."


"Asante sana."


Waliingia ndani na kupokelewa na dada wa kazi aliyekuwa kwenye maandalizi ya chakula cha jioni. Baada ya kuwakaribisha alirudi jikoni na kuelekea na mapishi.


"Jamani eehh hapa ndiyo nyumbani kwangu wenyewe wanasemaga Maskani na kama mjuavyo hapa ni kibabe tu hatulembi kwenye pazia jekundu pale ndiyo malalo yenu kwa siku mtakazokuwa hapa hivyo mnaweza kupeleka mabegi yenu kisha mengine yafuate."

Waliinuka na kupeleka mizigo yao chumbani huku mwenyeji wao madam Nafiwe akiingia chumbani kwake huku akilivua koti lake. Alibadilisha nguo zake na kurudi akiwa na katupia traki ya nyeupe yenye michirizi ya rangi ya bluu na tshirt nyeusi juu na kisha kurejea sebuleni ambapo aliwakuta wageniu wake wakiwa wanatazana Televisheni.


"Nilipewa taarifa zenu na dada yangu Nesi Suzanne kuwa siku za hivi karibuni utapokea ugeni kutoka kwa mtu tuliyemfanyia kazi pale hospitalini."

Alifungua mazungumzo madam Nafiwe.


"Ni kweli madam Uongozi umeamua kututuma huku Namibia baada ya watu ambao tulidhani kuwa tumewamaliza kumbe haikuwa hivyo waliweza kuokolewa na kisha kufanyiwa matibabu na sasa ni wazima wa afya. Mbaya zaidi wanaendelea kutekeleza mauaji yao kutokea huku wakimtumia kijana aitwaye Roberto ambaye tulikatisha uhai wa mama yake hivi karibuni kwa ushirikiano wako na dada yako Suzanne."

Alieleza Tom na kuinua glasi ya maji na kuipeleka mdomoni.


" Kwa hiyo mnataka kuniambia kuwa hao watu na timu yao wako hapa Namibia wakiendelea kuratibu mipango yao?"

Madam Nafiwe aliuliza.


" Ndivyo tunavyoamini madam."


"Labda tuichore ramani baada ya Mbwa wangu kufika baadaye kidogo kwani sikumbuki kama kuna kundi pinzani hapa."


"Madam tunakutegemea sana katika kulifanikisha hili kwani watu tunaokwenda kupambana nao ni hatari sana wana kila aina ya mbinu."

Robinson alimtahadharisha madam Nafiwe.


"Robinson umekwisha fika mikononi mwa Iron Lady hivyo shaka ondoa kabisa labda ninachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kuongea na Bosi wenu Santana kila kitu kikae sawa kabla mtanange haujaanza."

Aliongea madam Nafiwe na kuiangalia namba ya Santana kwenye simu yake kisha kuipiga.


" The Iron lady." Alianza Santana baada ya kuipokea simu ya madam Nafiwe.


" Ndiyo mimi mwenyewe nambie kamanda wangu."


"Nakusikiliza wewe kwani ni matumaini yangu kuwa tayari timu yangu imewasili hapo kwani niliamua kuwasafirisha pasipo kufanya mawasiliano nawe kwanza nikiwa nimejazwa matumaini na dada yako Suzanne hivyo tunaweza kuongea sasa."

Alifafanua Santana.


"Nashukuru kwa kuniamini mimi na kundi langu nakuhakikishia asilimia mia ya kufanikisha jambo lako kikubwa ni mkwanja na si wa kitoto."


"Kama bei gani vile Iron Lady?"

Santana aliuliza.


"Mpaka unawatuma vijana wako kuja kwangu maana yake tayari ulishajipanga."


"Ni kweli lakini nitaanza na asilimia kumi na tano ya mkataba na kazi ikifanikiwa tu iliyobaki namalizia."


"Santana mimi ni tofauti na wengine, mara nyingi huwa nataka fedha zote mkononi kisha kazi ianze sababu natumia rasilimali watu, fedha na vifaa tukifeli zoezi na kila kitu kimesambaratishwa na maadui itakuwa hasara ya nani Santana? Ni kazi yangu mimi?"

Madam Nafiwe alifunguka.


" Okay tuachane na hayo nipe bei mara nifanye muamala leo hii hii ila tahadhari usipofanikisha tu umekwisha mdada."

Santana alimjibu.


" Sipigwi mkwara kihivyo Santana ulizoea kuwaonea hao hao hapa ni Himaya nyingine kabisa na kama una nguvu si ungekuja mwenyewe na ukileta za kuleta naanza na hawa kisha unafuata wewe, umenielewa?"

Nafiwe alimpakia Santana.


" Okay tuachane na hayo nipe bei."

Ilibidi Santana ashuke chini kiume.


" Nahitaji akaunti yangu isome kiasi cha shilingi milioni mia saba bila senti kisha kazi ianze leo leo."


"Hicho kiasi ni kikubwa sana Iron Lady."


"Yaani kwa sifa nilizoambiwa juu yako na umaarufu wako leo hii unalialia kama vile hujawahi fanya mishe za hivi?"


"Usininange hivyo wewe mwanamke, hela yako naingiza leo kabla ya jua kutua na kwa kukuonesha Santana ni nani naweka milioni mia saba na ishirini."

Madam Nafiwe alicheka sana baada ya kusikia majigambo ya Santana kisha akamjibu.

"Huo ndiyo umwamba Santana siyo unajilizaliza hapa."


Kisha alikata simu na kuingia ndani ambapo aliwaambia wakina Tom waoge kisha wapige msosi na baada ya hapo waingie matembezini kidogo mpaka usiku huko wanaweza pata pa kuanzia.


****


Waliwasili jijini Mbeya na kwenda moja kwa moja mpaka wilayani Chunya na kwa kuwa ilikuwa ni saa mbili ya asubuhi waliona wapumzike kwanza kwenye kona za mkoa eneo ambalo hutumiwa na Watalii mbalimbali kufurahia mandhari ya bonde la Usangu (View Area) na kupaki magari hapo huku mateka wao wakibakia ndani ya gari wakiwa bado kwenye sintofahamu ya wakina nani waliowateka.


"Vipi kwanini tunapaki hapa?"

Aliuliza Roberto baada ya kushuka kutoka kwenye gari.


"Kwa kuwa kumeshakucha inatubidi tuzuge hapa kwa masaa haya mpaka Magharibi ndipo tutaianza tena safari yetu kwani tuna kilometa mia na zaidi mbele."

Jackline alimjibu Roberto akiwa bado ndani ya Maski kitu ambacho ilikuwa ni ngumu kwa mzee Jonathan na mke wake kumtambua kutokana na kupungua mwili na kumfanya kuonekana mrefu na bado isingekuwa rahisi kwani siti ambazo walifungwa zilikuwa zimeteguliwa na kuwa kama zimelala vile.


"Jackline mkoa wa Mbeya una mandhari nzuri sana aise cheki hili eneo lilivyo utafikiri tuko Amerika au Afrika ya Kusini?"

Jasmine alilisifia eneo lile baada ya kushuka.


"Ni sehemu tu naambiwa ina maeneo mengi sana ya Kitalii ambayo hayajafikiwa bado wala kufanyiwa matangazo."

Jackline alimjibu Jasmine huku akiwa kamshikilia mkono Titiana na kusogea mbele karibu kabisa na kingo ya chuma ambapo bonde la Ufa linaonekana vizuri sana.

Aliipekua simu yake na kisha kupiga namba ambayo aliitaka.


" Shikamoo dada yangu."

Upande wa pili ulianza na salamu baada ya kupokea simu.


"Marahaba mdogo wangu, sasa nisikilize. Tuko huku Kona za Mkoa tunaelekea Lupa tukiwa na watu ambao huwezi kuwafikiria hata kidogo namaanisha kuwa mzee Jonathan pamoja na mke wake, tunawapeleka wapi haihusu kwa sasa mwambie Athuman akupe shilingi laki mbili au muongozane mpaka Supamaketi mkatununulie vyakula idadi yetu ni nane mjitahidi."

Jackline alimuagiza mdogo wake Shamimu.


" Makubwa, yaani mmemkamata mzee Jonathan?"

Shamimu alishangaa baada ya kusikia taarifa hizo.


" Kwani yeye ni nani mpaka tushindwe kumkamata?"

Jackline alimuuliza mdogo wake.


" Haya dada ngoja nikaongee na kaka Athuman juu ya hili ili tuje huko, na kaka si anaweza kuja pia?"

Shamimu alimuuliza Jackline.


"Ni yeye tu kikubwa tunahitaji vyakula msisahau maji na juisi pia msijisahau mkabeba na miwali maana mmekaa hapo Mbeya nina mashaka nanyi."


"Dada na wewe kwani sisi tumekuwa washamba kiasi hicho? Halafu pia matokeo yameshatoka dada."

Shamimu alimchomekea na ishu ya matokeo yake ya kidato cha nne.


"Fanya kwanza nililokuagiza tukilimaliza hili lillilo mbele yetu litakalofuata ni hilo la kwako na la kaka Athuman."

Jackline alimjibu Shamimu aliyeonekana mwenye furaha baada ya kutaja neno matokeo.

Baada ya kumaliza kuongea na simu alimgeukia Titiana na wakati huo Jasmine na Jessica walikuwa wakiwafuata na Roberto akibakia kama mlinzi pale kwenye magari.


" Umeona hili bonde linavyoonekana?"

Jackline alimuuliza Titiana akimshika begani.


"Vinyumba vinaonekana vidogo utafikiri hakuna watu wanaoishi huko?"

Titiana alimjibu Jackline na kuendelea kuyafurahia mazingira yale, kiuhalisia Titiana hakuwa muongeaji sana mara nyingi alionekana kuwa msikilizaji tu zaidi zaidi utamsikia akijibu tu maswali anayoulizwa na wenzake.


" Jackline wenzako tunatamani kama vile tuwashushe mle kwenye gari tuanze kuwasukumizia mijeledi ya maana ila basi tu."

Jessica alimwambia Jackline kile walichokuwa wakijadiliana na dada yake.


"Kuwa mpole Jessica hao ni wetu haraka za nini kwanza hapa ni barabarani si tutashangawa na wanaopita hapa tulipo ni salama kwani wao wanajua sisi ni Watalii kumbe tunaisubiri Magharibi ili tupite vizingiti vyote vya Polisi bila tabu yoyote."

Jackline aliwataka wenzake wasiwe na haraka kwani muda unakuja ambao kila mmoja ataifurahia show ya bure.


JE NINI KITATOKEA?


SEHEMU YA 66 INAKUSUBIRI KUPATA JIBU LA SWALI LAKO.




Athuman na Shamimu waliwasili pale kona za mkoa karibu na kijiji cha Lwanjiro kilicho Mbeya vijijini wakiwa na vyakula vyao. Baada ya kutelemka kutoka kwenye basi linalofanya safari zake Mbeya kwenda Chunya waliungana na wakina Jackline pale walipokuwa.


"Wao ndiyo maana ninawapendaga ndugu zangu asanteni kwa kunijali dada yenu."

Jackline aliongea akiwakumbatia Athuman na Shamimu.


"Usijali dada yetu wewe mwenyewe unafahamu tumebakia wangapi? Lakini kuna muda hutushangaza sana dada Jack."

Athuman aliongea.


"Kivipi Athuman?"


"Si kuwa ndani ya Mbeya bila sisi kujua chochote."

Shamimu aliingilia.


"Naombeni mnisikilize wadogo zangu, nayafanya haya yote ili kurahisisha maisha yetu ya baadaye kama mnavyojua hatuwezi kuishi maisha ya ndoto zetu kama mzee Jonathan na wengine waliojitokeza kuendelea kuishi hapa duniani na ndiyo maana nikaamua kuibeba hii vita kwa gharama yoyote ile, na wale pale ni rafiki zangu waliojitoa kunisaidia japo nao wametendwa pia hebu tusogee niwatambulishe kwao."

Aliongea hayo huku akisogea nao pale walipokuwa wameketi wakina Jasmine.


" Naona uko na ndugu zako, yaani mmefanana sana aisee."

Jessica aliongea baada ya kufika wakina Jackline.


" Ni kweli Jessica hujakosea sisi ni ndugu na huyu hapa ni Shamimu na huyu ni Athuman taarifa zao nilishawaeleza."

Jackline aliwatambulisha wadogo zake kwa timu yake.


" Wadogo zangu hawa ni rafiki zangu kama nilivyowaambia huyu ni Jasmine na huyu hapa ni Jessica nao ni ndugu wa damu lakini pia tuko na Roberto kama mnavyomuona pale kwenye ile gari akiwa anahakikisha mzee Jonathan hainui hata kichwa chake na huyu hapa ni Titiana mpenzi wa Roberto naye kaamua kuachana na likizo pamoja na masomo na kuungana basi kwenye oparesheni yetu."

Alimaliza utambulishi wake.


" Ndugu zetu mnavyotuona hivi sisi ni ndugu wapya kutokana na familia zetu kusambaratishwa na wabaya wetu katika Mazingira tofauti ya kiutafutaji."

Jasmine alijazia maelezo ya Jackline.


" Jamani sisi tumefurahi kuwaona na kuwafahamu tunaamini baada ya hii oparesheni kuna hadithi mmeibeba ambayo mtatusimulia kwa sasa hatupendi kuwasumbua kutaka kujua nini kinaendelea."

Athuman aliongea hayo huku akimpa ishara Shamimu ya kumuonesha Jackline vile walivyovinunua.


" Usijali Athuman kama tulivyosema kuwa sisi ni familia moja kwa sasa tunaipigania haki yetu iliyopokwa na watu wenye roho mbaya lakini tunachowaomba ni kuendelea kutuombea kwani vita hii ni kubwa sana na msije shangaa leo hii mnatuona watano kwa idadi lakini baada ya vita hii tukawa hivi hivi au pungufu hivyo kwa kila hatua yenu kila siku hakikisheni mnatuombea turudi salama kwani baada ya hapa tunarejea Brazil."

Maneno hayo yalizungumzwa na Roberto ambaye alifika pale baada ya kuwaona wakina Athuman wakiwa na mifuko ya mapochopocho na mwishoni mwa nasaha yake alimwaga machozi kitendo kilichoungwa na kila mmoja pale na kuwaduwaza wakina Shamimu ambao wao hawakujua chochote kilichopelekea waanze kulia lakini baada ya kufuta machozi yao walisogea na kukumbatiana kwa pamoja kama ishara ya umoja kwenye vita ulivyo mbele yao.


"Tunawapenda sana lakini ndiyo hivyo bado tuko kwenye Uwanja wa vita kwenye hiyo gari hapo mbele ndimo tulimowafungia mzee Jonathan na mke wake ikiwa ni dalili njema kuelekea kuishinda vita hii."

Jackline alijazia nyama kwenye maneno ya Roberto.


"Tutaendelea kuwaombea kuanzia leo kesho na wakati wote wa zoezi hili."

Shamimu aliona naye azungumze yake yaliyo moyoni mwake.


"Kwa upande wangu naomba niongozane nanyi kwenye vita hii mliyoianzisha ndugu zangu."

Athuman aliomba kuingia vitani,lakini hakuwa kuikuwa rahisi kwake kukubaliwa katika hilo.


"Kama tulivyosema hapo awali kuwa hii vita ni yetu wote kila mmoja anapigana kwa njia yake na ndiyo maana tukawaomba mtuombee tu hiyo nayo ni shirika katika vita hii lakini kusema tuongozane hapana Athuman kwa hapa tulipofikia ni pabaya sana kwani mimi mwenyewe nimeingilia katikati mpaka naogopa hivi lakini namshukuru mpenzi wangu kanitia moyo hivyo naombeni mrudi nyumbani tuombeeni tuishinde hii vita ili siku ya mwisho tufungue shampeni ya ushindi."


Maneno ya Titiana yalimuacha mdomo wazi kila mmoja kwani si mtu wa kuongea ongea sana lakini akifungua mdomo wake hutema madini.


"Tumewaelewa ndugu zetu, tunawatakia mafanikio mema katika hili na nina Imani kubwa mnakwenda kuishinda kwa mlipofika tu ni ushindi tayari."

Shamimu aliwajaza matumaini.


"Tuendelee kumuomba Mungu atende miujiza katikati yetu."

Roberto aliongea hao akiondoka kuelekea kwenye gari anayoifanyia ulinzi.


"Dada tuongee mara moja."

Athuman alimtaka dada yake waongee kidogo.


"Okay sawa." Walisogea pembeni kidogo kuteta.


"Najua tuko kwenye kipindi gani dada lakini kwa kuwa nimepata nafasi ya kuonana nawe na kuuona muonekano wetu ulivyo, kifupi dada yangu mambo si shwari kabisa kwani biashara zangu zilisimama muda mrefu kinachoniweka mjini ni kuotesha maua ambayo kwa sasa soko limeshuka nadhani ni kutokana na mtaji kwani wengi wetu wanaofanya shughuli hii wamewekeza kweli kweli hivyo niombe kama una salio kidogo nipige kampani dada ili mambo yaende."

Athuman aliongea kile ambacho alipanga kumwambia dada yake.


" Usijali mdogo wangu nimekuelewa katika hivyo kuna kahela kidogo nitakuingizia kwenye akaunti yako kikubwa unipe akaunti namba yako na hapa kuna kiasi kidogo kitasaidia kwa siku kadhaa."

Jackline aliongea akiingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi cha fedha na kumkabidhi Athuman kisha walikumbatiana na kurudi kwa wenzao. Na kwa kuwa ilikuwa tayari ni magharibi waliagana na wakina Shamimu walisimamisha basi na kupanda wakaondoka zao huku nyuma wakina Jackline nao walitulia kupata chakula tena na kuwasha magari yao na kutimua vumbi ila pamoja na yote kitu walichowafanyia wakina Jonathan ni kuwanyima chakula bila shaka adhabu imeanza kufanya kazi yake.

Safari iliendelea na hatimaye waliwasili mjini Lupa na kukita breki zake nyumbani kwa mzee Kaaya nyumba ambayo miaka kadhaa Jackline aliiishi akiwa kama mmoja wa wanafamilia kama mkwe na sasa kaja tena kama nani hapo. Mzee Kaaya akiwa ndani kalala alisikia mlio wa gari nje ya nyumba yake na baada ya kuchungulia nje kupitia dirishani aliweza kuona taa za gari nje. Alimuamsha mke wake na kumuonesha kilichopo nje mara mlango uligongwa. Bado walibaki kuulizana ni wakina nani hao wanaogonga mlango nje? Kelele za mlango ziliwaibua na kuufungua lakini kitu walichokutana nacho hawakuamini macho yao kwani walikutana na tochi iliyowamulika machoni kitendo cha kutoona mbele na hapo walidakwa na kufungwa vitambaa usoni na kupigwa cheni mikononi na kupakiwa garini kwani Roberto aliifanya kazi yako bila woga wowote huku akisaidiana na Jasmine na Jackline akisalia garini. Baada ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa Jasmine aliifunga milango ya nyumba ile kisha alirudi garini na kisha waliondoka zao na safari hii ilikuwa ni kuelekea njia ya njia ya Tabora.


"Jamani huku kuna baridi kuliko hata ile ya Mbeya mjini?"

Titiana aliona aongee baada ya kuona baridi inapuliza sana na muda huu ilikuwa ni usiku mnene wa saa sita usiku.


"Mkoa mzima wa Mbeya unabebwa na baridi kama hivi."

Jackline alimjibu Titiana ambaye walikuwa naye kwenye Honda jet5.


"Hivi dada Jackline safari hii tunakwenda kuishia wapi?"

Jessica aliuliza.


"Tunakaribia kufika unajua nini? Kuna pori moja linaitwa Kipembawe huko kuna ndiko tunakwenda kufanya yetu."

Alijibu Jackline huku akiendelea kupiga gia.


"Na hawa wazee inakuwaje?"

Jessica aliuliza tena.


"Kuwa mpole mdogo wangu muda ukifika utajua subiri tushuke."

Alimjibu tena na ikabidi Jessica awe mpole na baada ya kufika ndani ya msitu wa Kipembawe gari ziliacha njia na kuingia porini huko walitia breki karibu zaidi na kilima na kisha kuwashusha watu wao na kuwapeleka moja kwa moja mpaka kwenye pango moja ambalo linaonekana hutumiwa na Majangili kwani japo liko ndani sana lakini lilikuwa lina joto la kutosha na kulikuwa na vitu kama mikeka, ngozi ngozi za wanyama kwao haikuwatisha waliwaingiza ndani watu wao na kuwafunga cheni nyingine miguuni na kisha kuwafungua vitambaa na pale ndipo mzee Jonathan hakuamini macho yake baada ya kukutana na sura ya Jackline.


"Mzee mbona unatoa mimacho kiasi hicho?"

Jessica aliongea wakati huo akisaidiana na Titiana kuwaweka kila mmoja sehemu yake huku Roberto akiwa nje ya pango kwenye gari kuutoa mwili wa Masanja ambaye tayari mwili uliachana na roho kwani risasi ambazo zilimtwanga hazikumuacha salama alishakufa hivyo Roberto alimtoa na kwenda kumtupa mtoni. Na kisha kurejea kuungana na wenzake.


"Jackline ni wewe kweli?"

Mzee Jonathan aliuliza kwa mshangao mkubwa.


"Unashangaa nini mzee wangu si ulisema kuwa uko China? Na kwanini umebadili muonekano wako? Nilisikia kuwa ulimwaga mihela kunitafuta mimi ili iweje?"

Jackline alimjibu na kumtwanga maswali mfululizo.


"Mwanangu na mimi mbona umenileta huku?"

Mzee Kaaya alimtupia swali Jackline kabla mzee Jonathan hajajibu maswali ya Jackline.


"Mzee naomba ukae kimya wewe na mkeo kesi yenu inakuja kwa sasa niko na huyu Rastaman na mke wake haka kadereva kameingia mkenge kwenye kesi isiyokahusu."


"Mwanangu naomba naomba sana unisamehe kwa niliyokufanyia najua una hasira na mimi."

Mzee Jonathan alianza.


"Naomba uyajibu maswali yangu sihitaji kingine."

Jackline alimkatisha maneno yake ya maigizo.


"Mwanangu nisamehe tu yote haya ni kwa ajili ya Uroho wa Mali si kingine."


"Unasemaje mzee?"

Roberto alimsogelea mzee Jonathan na kumpiga swali akiwa kamshika mashavu.


"Mwanangu naomba nihukumiwe mimi na mume wangu aachiwe sababu mimi ndiye chanzo cha yote haya maana nilimshawishi kwenda kwa mganga wa kienyeji ili kuzipora Mali zenu na ndicho kilichotokea na kusababisha ajali iliyowaua wote na sisi kujibebea Mali zenu zote na kujifanya watu wema kwako na kukupeleka nje ya nchi kwa masomo na huku nyuma ilikuwa ni nafasi yetu kujiimarisha kumiliki Mali zenu... "

Kabla hajamalizia neno lake alikutana na ngumi ya mdomo kutoka kwa Jasmine iliyompeleka chini na kuanza kutoa damu mdomoni kitendo kilichomfanya mzee Jonathan kuanza kutokwa jasho kwani alishajua nini maana ya kuletwa mle Pangoni.


NINI KITATOKEA HUMO?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.




Kundi la Black Eyez likiongozwa na mama lao Nafiwe sambamba na Tom pamoja na Robinson waliingia mtaani kuanza mchakato wao wa kuwasaka popote walipo wakina Jackline na hii ilichochewa na kiasi cha mkwanja kilichomwagwa na Santana kwenye akaunti yao kilichofikia shilingi milioni mia saba na ishirini. Hivyo kila mmoja alikuwa na moto wa hatari kuhakikisha wakina Jackline wanapatikana wakiwa hai au wafu. Baada ya pekua pekua mtaani walipata nyepesi nyepesi kuwa wagonjwa hao baada ya kuokolewa na mzee mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja lakini akiwa ni mvuvi maarufu ndani ya nchi hiyo. Hivyo basi hii ikawa taarifa nzuri kwao kwani 'The Black Eyez' waliamua kushika njia mpaka hospitali ambayo iliwapokea kwa mara ya kwanza wakina Jackline ya KING'S MEDICARE CENTRE ili kwenda kuupata ukweli wa mambo na ambao utawasaidia katika kazi yao na moja kwa moja waliwasili hospitalini hapo na wakati wengine wakibaki nje ya Hospitali hiyo kiongozi wao madam Nafiwe aliingia ndani na kukutana na Mganga mkuu wa hospitali hiyo ndugu Abbas Mukesh kwa ajili ya kuongea naye. Na kwa bahati nzuri alimkuta daktari Abbas Mukesh akiongea na simu alimsubiri amalize na kisha aongee naye.


"Karibu dada yangu, naweza kukuhudumia sasa." Alimwambia madam Nafiwe baada ya kukata simu.


"Nashukuru sana daktari sipo hapa kwa matibabu au nini zaidi nimefika kwa kitu kimoja tu."

Alianza madam Nafiwe.


"Samahani dada yangu sasa kama hauhitaji huduma zetu za kitabibu unahitaji nini? Na kama huduma nyinginezo unaweza kwenda kwenye dirisha letu la 'customercare' ambao wanaweza kukusaidia kabla ya kufika kwangu."

Daktari Abbas alimfafanulia madam Nafiwe.


"Nashukuru kwa mashairi yako mazuri japo hayana vina ila tu naweza kukuweka wazi kuwa sina mpango wa kukutana na Mbwa na ndiyo maana niko hapa kwa mfugaji mwenyewe."

Aliendelea kujigamba mbele ya meza ya daktari Abbas.


"Mbona sikuelewi dada yangu?"

Daktari Abbas alimuuliza.


"Na huwezi kunielewa mpaka nikufungue loki za ubongo wako kwanza kisha utanielewa, kifupi nahitaji kujua waliko wale wagonjwa waliookolewa kule baharini na si kingine."

Alimaliza kuongea akalivutia pembeni koti lake na kuionesha bastola yake kisha akaketi. Na kitendo cha kuiona bastola ile daktari Abbas alijihisi kutokwa na jasho la baridi kutoka kila sehemu ya mwili wake. Na hapo hakujua afanye nini mbele ya mwana mama huyo aliyekuwa kavalia sura ya kazi akiwa anasubiri maelezo.


"Dada yangu kifupi watu hao walisharuhusiwa kutoka hapa muda mrefu sana baada ya kuendelea vizuri."

Daktari Abbas alijitahidi kutoa maelezo.


"Waliondoka kuelekea wapi na ni nani aliwafuata hapa?"

Madam Nafiwe alimuuliza tena.


"Walikoelekea sifahamu dada siwezi kukudanganya ila tu walifuatwa na mzee aliyewaleta hapa."


"Mzee gani huyo?"

Aliuliza madam Nafiwe.


"Alijitambulisha kwa jina moja tu la Jerome zaidi ya hapo sifahamu chochote."

Aliendelea kujitetea mbele ya jimama.


"Okay vizuri daktari wangu wacha mimi nitoke lakini nitarudi tena maana nahisi harufu ya kifo ya damu yako."

Aliongea hayo akiufungua mlango na kuishia zake nje na kumuacha daktari Abbas Mukesh akiwa katokwa na macho kama vile kafumaniwa vile.

Njia aliyoiona ni okozi kwake kwa wakati huo kuepukana na kikombe kilichokuwa mbele yake ni kutoa taarifa polisi kwa ajili ya usalama wake.


"Afande nahitaji ulinzi wenu kwani kuna mwanamke kafika hapa kazini na kunitishia maisha kisa tu ni wale wanadada ambao waliletwa kwa matibabu baada ya kuokolewa majini."

Daktari alitoa maelekezo.


"Anataka nini kutoka kwa hao wanawake?"

Lilikuwa ni swali kutoka upande wa pili wa simu.


"Sijui ila nahisi watakuwa ni wale ambayo waliowafanyia unyama na kuwatupa baharini kwa huyu si wa kwanza kuna ambaye aliwahi kuja hapo kabla na yeye alikuwa akiwauliza hao hao mabinti."

Alieleza Daktari Abbas Mukesh kwa Afande aliyempia simu.


"Basi kuna vijana watakuja hapo ndani ya dakika kadhaa na nikuombacho muda huu usiondoke hapo na kwa lolote lile litakalotokea usisite kututaarifu Daktari."

Afande alimtahadharisha Daktari Abbas Mukesh.


"Nikutegemea sana Afande katika hili kwani kwa namna ambavyo alikuwa akinitazana usoni mwanamke yule ooohhh si wa kawaida hata kidogo."


"Usijali Daktari wangu."

Afande alimjibu Daktari.


Na kwa kuwa Nafiwe alikuwa mlangoni alisikiliza kila kitu kutoka kwa daktari kisha aliondoka zake na kuwakuta vijana wake wakimsubiri pale nje. Akatoa ishara ya kuondoka hivyo wakaingia garini na kuondoka zao na wakiwa nje kidogo ya viwanja vya hospitali ya King's Medicare Centre alimtaka dereva asimamishe gari.


"Kuna kitu tunatakiwa kukifanya kwa huyu daktari kwani kuna mazungumzo yake nimeyanasa nahisi alikuwa akiwasiliana naye na bila shaka ni askari hivyo nataka mmoja abaki kwa kazi maalum ya kumfuatilia huyu daktari kuna kitu tutakipata cha kutusaidia kwenye zoezi letu."

Hivyo alishuka dada mmoja ambaye siku zote kwenye misheni zao hutumika kama chambo kuwanasa maadui zao. Na baada ya kushuka tu wao waliendelea na safari yao kurudi maskani kwao.


Mara ujumbe ulioambatana na video fupi uliingia kwenye simu ya Robinson kutoka kwa Santana na ulisomeka hivi;


"Vichwa vyao vitakuwa halali yetu iwapo tu mtakwenda kinyume na makubaliano baina yetu na yatafuata kama mtakuwa tayari kuyasikiliza."


Robinson akapata shauku ya kuifungua ile video ajue ni nini hicho kinachozungumziwa. Baada ya kuifungua hakuamini macho yake baada ya kukutana na nyuso za wazazi wake wakiwa kwenye mateso makali huku nyuso zao zikiwa zimetapakaa damu na kuwafanya kutotamanika machoni pa mwanadamu.


"Mwanangu popote ulipo mimi baba yako nakuomba badili mawazo yako hatukukulea katika mfumo huo uliojiingiza wewe siye yule Robinson tunayemfahamu mnyenyekevu mbele ya kila aliyemzidi, mtoa msaada kwa kila mwenye tatizo ilmradi tu unaweza kufanya."

Yalikuwa ni maneno ambayo aliyazungumza mzee Kaaya baba yake Robinson kwa taabu sana kwenye ile video fupi.

Mikono yake ilikosa ushirikiano baada ya kukiona kile alichokiona kwenye simu yake lakini hakujaribu kumuonesha yeyote mle garini japo Tom alimshtukia lakini hakutaka kumuuliza. Pale pale alimtumia ujumbe Santana akitaka kujua ile video ameitoa wapi.


"Bosi ni nani kakutumia hii video ya wazazi wangu wakiteswa namna hii?"


Haikuchukua muda Santana aliujibu ujumbe ule.


"Imetumwa kwa njia ya Facebook messenger na mtumaji hakujipambanua na tulipojaribu kuifuatilia akaunti hiyo yenye utambulisho wa jina la Mafia na profaili picha ya Duma tulibaini kuwa imehakiwa tu."

Alijibu Santana kwa njia ya Ujumbe.

Kimoyo moyo Robinson alianza kujiwazia juu ya hiyo video.


" Ina maana wazazi wangu wametekwa? Na watekaji wanahitaji nini sasa? Au ni wakina Jackline? "


Hapo hapo Robinson aliamua kumpigia simu Santana baada ya uzalendo kumshinda.


"Mkuu wanahitaji nini watekaji?"


"Hata sijui kwani hawajaacha mawasiliano na kwenye akaunti waliyoitumia hawapatikani tena."


"Masikini wazazi wangu itakuwaje sasa mkuu wangu?"

Robinson alimuuliza Santana.


"Tuko hapa tukiisubiri simu yao au email ya ofa kama watafanya tofauti na hapo hatuna ujanja mdogo wangu."

Santana aliongea.


"Sawa lakini sijui itakuwaje kwa sababu wazazi wangu wanaonekana kupitia wanayopitia kwa ajili yangu na hao si wengine bali ni wakina Jackline."


"Tuwe na subira yataongeleka tu hayo Robinson hata kama ni wakina Jackline kikubwa kuwa na moyo wa kiume najua ni namna gani umeumia baada ya kuiona hiyo video ya wazazi wako."


"Sawa mkuu nimekuelewa ngoja tuendelee kuwasikilizia."


Simu ilikatwa na Robinson aliungana na wenzake kuingia ndani ya jengo la madam Nafiwe.


NI NINI KITATOKEA?



"Jackline mwanangu naomba niongee kitu ili baada ya hapo chukua uamuzi."

Mke wa mzee Jonathan aliongea, muda huo wote walikuwa wamefungwa kwenye mizizi ya mti ulio ndani ya kimto kilichokatisha ndani ya pango hilo na kuifanya sehemu ya miili yao kuwa majini na kuanzia kifuani kuja kichwani kuwa nje ya maji. Na wakati huu mzee Kaaya ya mke wake walishatolewa ndani ya maji wakiwa hawajitambui kabisa japo ilikuwa kwa mzee Jonathan ambaye naye alikuwa amekata kauli lakini hawakumtoa ndani ya maji,aliendelea kusalia humo.


"Unasema nini wewe Shetani? Au unafikiri sijui ambacho ulikifanya na mumeo kwa wazazi wangu, wewe si ndiye ulimshawishi mume wako kuwaendea kwa mganga ili muweze kumiliki Mali zetu? Kwa mfano mngechukua tu mali na kuwaacha wazazi wangu tusingefika huku."

Jackline alimkatisha mama yake mlezi huku akiwa kajifunga jaketi lake kiunoni na kuuacha mwili wake ukisitiriwa na kibana maziwa tu na kuliacha tumbo lake likiwa wazi nafikiri ni kutokana na shughuli pevu waliyokuwa nayo mle pangoni. Na muda huu wengine kama Jasmine, Jessica, Roberto na Titiana wakiwa wanamuandaa swala ambaye alikuwa kanaswa na mtego wa Titiana ambao alikuwa kautega nje ya pango.


"Mwanangu ni kweli kabisa na yote hii ilikuwa ni kutokana na uroho wa mali ambazo tuliamini zingekuwa mikononi mwetu baada ya kukumaliza wewe lakini hali ya hewa imebadilika na sasa wewe umegeuka kuwa hakimu wa haya, tunaomba huruma yako mwanangu usiibebe roho ya kikatili ambayo hukuwahi kuwa nayo.. "

Aliongea huku akilia mama huyo.


"Kaa kimya mwanaharamu wewe, mchawi usiye na tunguli wala ofisi elewa kuwa Jackline umuonaye hapa si yule uliyemfahamu kipindi iko huyu ni mwingine kabisa ambaye hujawahi kumuona wala kumsoma kwenye kitabu chochote kile, ninachokuomba ni kufunga hili domo lako lililosheheni kila aina ya unyang'anyi."

Jackline aliongea hayo huku akimgusa mdomo kwa bastola yake.


" Oho! oho! oho!..... "

Mzee Jonathan alizinduka na kuanza kukohoa.


" Roberto njoo umfungue Rastaman naona tayari karudi duniani baada ya kuona alikokuwa ni afadhali ya duniani."

Jackline alimwambia Roberto baada ya kumsikia mzee Jonathan akikohoa.


"Naja kamanda wangu mwenyewe."

Roberto alijibu akikata kipande cha nyama na kukitupia mdomoni.


"Mwanangu naomba usiniite hivyo hii yote ni katika kujaribu kuukwepa mkono wa sheria yote kwa yote ninaomba uukunjue moyo wako uliojikunjakunja kutokana na niliyokufanyia, kisha tuliweke sawa hili niko tayari kwa lolote."


"Unaongea nini wewe mwanaharamu usiye na haya wala aibu, nisikilize kwa makini wewe mzee mali zetu utazitoa kwa hiari au kwa lazima. Unanielewa?"

Jackline alimuuliza mzee Jonathan ambaye muda huo alikuwa taabani kwa mateso.


"Mzee acha kusinzia unamsikia Malkia wa Haki anayokwambia?"

Roberto alimuuliza akiwa anamfungua pingu za miguuni.


"Nimemsikia kijana wangu tena vizuri tu."

Mzee Jonathan alimjibu Roberto.


"Kwa hiyo unasemaje katika hili au unasubiri mpaka tukufanyie umafia?"

Jackline alimuuliza swali kutokana na majibu yake kwa Roberto.


"Niko tayari kurudisha mali zako binti kikubwa tu uniahidi kuwa utaniacha huru na mke wangu tuanze maisha mapya."


Mzee Jonathan alimjibu akiwa anajiinua ili apige magoti kuomba msamaha, lakini ikawa tofauti kwani Roberto alijua anataka kuinuka ili aanze vurugu hivyo alichokifanya ni kumtwanga bonge la teke lililomkuta kifuani na kumpeleka ndani ya kijito cha maji na kujigonga gonga huko na kusababisha kichwa chake kupasuka sehemu ya paji lake na kupelekea damu nyingi kumtoka.


"Jamani mbona hivi? Basi kama lengo ni kuniua naombeni mfanye hivyo mapema kuliko haya mnayoendelea kunifanyia."

Alipaza sauti akiwa majini akijivuta kutoka nje.


"Mzee nakuonea huruma sana ni bora ufanye fasta tumalize mchezo wetu."

Roberto alimwambia akiwa anampa sapoti ya kumtoa majini kwa staili ya tanganyika jeki.


"Jackline tufanye fasta hili eneo tuondoke maana si salama tena kwetu si mnawakumbuka wale wawindaji wa jana mnafikiri watakaa nalo hili pamoja na mkwara tuliowachimba?"

Jasmine alikuja akila nyama na kuwataka zoezi liende haraka ili waondoke zao hapo.


"Nakumbuka vizuri sana ndugu yangu si hawa washenzi wanajitia ugumu wakati tayari washaanza kuwa mkate mbele ya Chai."

Jackline alimjibu Jasmine.


"Eti mzee kuna ugumu unaouleta mpaka muda huu? Mimi nilikuwa kimya kwa sababu ya njaa na kwa sasa niko fiti kukipokea kijiti hiki hivyo basi unaweza tu kurahisisha mambo mwenyewe ili tusifike huko na haya yote yanatokea kutokana jeuri yako mzee sisi hatuna roho mbaya kiasi hicho ila wewe ndiyo unafanya tuwe hivyo."

Jasmine alimsogelea mzee Jonathan na kuanza kumtisha kiaina.


" Mbona mimi sina tatizo kabisa hata hapo awali nimeongea jamani?"

Mzee Jonathan alitokwa na maneno.


" Huna tatizo ee basi tuuanze mchezo wetu pasipo sababisha majanga zaidi mzee manywele."

Jasmine aliona ubebe msala baada ya kuona wakina Jackline kama vile wamevurugwa.


Wakati Jasmine akiuanza mchezo na mzee Jonathan kwa kumfanya kukubali kumkabidhi Jackline kila kilicho chake simu ya Jackline iliita na hivyo kuichukua na kuangalia mpigaji hakuwa mwingine bali Santana.


"Nakusikiliza Mwanaizaya usiye na haya."

Jackline alianza baada ya kupokea simu ya Santana.


"Nisikilize wewe mrembo, na waambie na hao Warembo wenzako kuwa ninyi bado sana kwenye hili gemu. Na kuhusu lile deo lenu mlilomrekodi mzee wa Robinson wala halitustui hata chembe kwani hao muda wao wa kuishi umefika ukingoni na Robinson anachokiangalia ni maisha yake kwani kwa sasa hana mpango wa kurudi Tanzania sijui Afrika hivyo msijidanganye na vimichezo vyenu visivyo na kichwa wala miguu, umenielewa? "

Santana alihitimisha kwa kuuliza swali.


" Umeshamaliza ambayo ulipanga kuyaongea kwetu?"

Jackline naye alimtupia swali.


" Pigia mstari kama bado au la."

Amjibu Santana.


" Kata simu basi sisi huku tuna majukumu ya kifamilia na si kitu kingine wewe Mbwamwitu."

Jackline aliona ampakie Santana.


"Na muda si mrefu mtapokea matokeo ya gemu linaloendelea kuchezwa hapo hapo Namibia."


"Unasemaje?"

Jackline aliuliza kwa hamaki swali ambalo hata hivyo halikupata jibu kutokana na simu kukatwa na Santana, kitendo kilichoshuhudiwa na Jasmine pamoja Roberto baada ya kumuona Jackline ameishiwa pozi baada ya kukatwa simu.


"Anasemaje huyo Santana?"

Jasmine alimuuliza Jackline.


"Kuna tatizo tayari Namibia kwani inavyoonekana tayari Santana na watu wake wako Namibia na hofu ni kwa familia ya mzee Jerome, ya Daktari Abbas Mukesh na ya Daktari Hans Murray."

Jackline aliongea kwa yale aliyoyaamini kumhusu Santana.


"Tunafanyaje hapo?"

Roberto alimuuliza Jackline na Jasmine.


"Hebu ngoja kwanza."

Jasmine aliongea hivyo huku akiipekua simu na baada ya kuikuta namba aliyokuwa akiitafuta na aliipiga.


"Halo baba shikamoo!"


"Marahaba mwanangu Jasmine wazima huko?"

Mzee Jerome alimuuliza Jasmine.


"Sisi tu wazima kabisa vipi kuhusu ninyi?"

Jasmine alimjibu na kumuuliza swali.


"Sisi ni wazima kabisa na biashara zetu zinakimbia kama upepo sijui kwanini mlichelewa kuja kwenye familia yetu hakika ninyi ni Malaika wetu."

Mzee Jerome aliongea kwa furaha.


"Hongereni sana lakini kuna janga linawavizia na ndiyo maana nimekupigia mzee wangu."


"Janga gani Jasmine mbona unataka kuniweka kiroho juu mzee wako?"

Mzee Jerome alichanganyikiwa baada ya kusikia hivyo.


"Mzee ni hivi hapo Namibia kuna watu wamekuja kututafuta baada ya yule mwanzo kuminywa mdomo wakaona hakuna jingine zaidi ya kuwatuma wengine hivyo hofu yetu ni kama wakitukosa."


"Hofu ya nini mwanangu huoni kama wakiwakosa wataondoka zao."


"Si hivyo baba, tunahisi wanaweza kuwakamata ninyi na ikiwezekana kuwafanya kitu mbaya."


"Inawezekana eti eee??"


"Ndiyo hivyo baba hivyo kuanzia sasa chukueni hatua rafiki ya kujilinda."


"Nashukuru kwa ushauri mwanangu kwa hilo ondoa shaka si unatufahamu wavuvi tulivyo zaidi ngoja niwajulishe wakuu wa hospitali zile za Makambi na King's pia wadogo zenu."

Mzee Jerome hakuonyesha wasiwasi wowote japo alipata mshtuko mwanzoni. Hivyo Jasmine hakuona sababu ya kuendelea kuongea na mzee Jerome alimkatia simu.


" Vipi anasemaje mzee wetu? Maana kwa ubishi wake sijui."

Jackline alimuuliza japo alisikia kila kitu kutoka kwa Jasmine.


"Eti tumuani kwani yeye hawaogopi ila atafanya maandalizi na vile vile kasema ngoja awasiliane na Madaktari pamoja na wakina Victor juu ya hili."


"Shauri yake aendelee kupingana na anachoambiwa hivi anaijua akili ya Santana?"

Jackline alimjibu Jasmine.

Kisha alimfuata mzee Kaaya ambaye akili ilikuwa iko sawa baada ya kurejewa na akili yake sasa na kumtupia swali.


"Hivi mzee wangu hujawahi kusikia lolote kutoka kwa mwanao?"


"Wacha nijilaumu mwenyewe kwa haya yanayotokea kwangu na familia yangu."

Mzee Kaaya alimjibu Jackline.


"Kivipi mzee Kaaya?"


"Utu wangu unanimaliza mwenyewe, hivi Jackline wewe ni wa kutufanyia haya kweli?

Tule nyama basi si tayari umetuivisha."

Mzee Kaaya aliongea kwa hisia kali na kuanza kulia kwa kwikwi.


"Labda nikuulize swali jepesi tu mwanangu Jackline."

Mzee Kaaya aliinua kichwa na kumuomba amuulize swali.


"Uliza tu mzee kama ukiweza."

Jackline alimjibu mzee Kaaya.


"Hivi huyo mwanangu mnayemwita msaliti mara jambazi ambaye mnasema lazima mmuue usingeondoka naye kwenda huko mlikokuwa angekuwa hivyo alivyo?"


"Mzee Kaaya kumbe bado unajeuri kama mwanao eee?"

Mzee alijikuta alikutana na kofi la machoni baada ya kumuuliza swali Jackline ambalo bila shaka lilimwingia na kujikuta akifanya kitendo hicho ambacho kilipelekea mzee Kaaya kwenda chini.


"Sawa nifanye chochote Jackline lakini kumbuka kuwa mimi ni mtuhumiwa nisiye na hatia mwenyewe mnamfahamu fika na hata kama nitakufa leo hii lakini ukweli utabakia pale pale."

Aliongea maneno hayo ambayo yalimwinua Jackline na kutoka mpaka nje ya pango lile na kwenda kukaa karibu zaidi na magari huko alianza kulia kwa sauti ya chini kwani alichoambiwa na mzee Kaaya ilikuwa kweli tupu japo yeye alijua alichokuwa anakihitaji kutokana na kuwashikilia wazee hao.


NI NINI KITATOKEA HUKO PORINI NA NAMIBIA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.



Alikaa kwa muda pale nje karibu kabisa na gari lake na alipoona yuko sawa kiakili alifungua mlango wa gari kisha akaingia humo na kuchukua baadhi ya nyaraka zake zilizokuwa kwenye whitebox ambayo inapatikana chini ya kiti cha dereva akazipitia kwa muda mrefu kidogo moja baada ya nyingine na aliporidhika alishuka garini akiwa nazo kisha akaingia tena mle pangoni kuungana na wenzake.


"Mzee majibu ya maswali yako yote utayapata muda si mrefu hivyo tulia tu hapo."

Jackline alimwambia mzee Kaaya huku akimsogelea mzee Jonathan pale alipokuwa katulia.


"Nizifanyaje hizi karatasi unazonipa?"

Mzee Jonathan aliuliza baada ya kuona akikabidhiwa rundo la mikaratasi.


"Zisome kisha umwage wino sehemu inayokuhusu."

Jackline alimjibu huku akimfuata Jasmine.


"Kama ni za kubadili umiliki wa Mali sahau kabisa kuhusu hilo Jackline."

Mzee Jonathan alimjibu kisha akazirusha karatasi zile ambapo moja wapo ilipeperuka na kuangukia majini, kitendo kilichokwenda kuuvuruga kabisa mfumo wa mawasiliano wa kichwa cha Jackline kwani pale pale aliichomoa bastola yake kutoka kiunoni kwake na kuielekezea kwenye paja la Mzee Jonathan na kumtwanga risasi moja iliyomfanya kushtuka.


"Jackline hutaniwi? Kidogo tu ushanishuti kweli?"


"Narudia tena zisome kisha mwaga wino wako sehemu inayokuhusu sawa?"

Jackline hakumjibu chochote zaidi ya kumuelekezea tena ile bastola na kurudia maelezo ya mwanzo.


"Sawa niko tayari kufanya hivyo kikubwa unihakikishie uhai wangu na wa mke wangu."

Alikubali japo aliweka masharti yake kabla ya kusaini zile nyaraka. Lakini mara aliingia Titiana akiwa macho juu juu.


"Vipi honey kuna nini?"

Roberto alimuuliza baada ya kumuona akihema juu juu huku akiwa anaangalia kule alikotokea.


"Kuna watu wako kwenye vichaka vile pale mbele kidogo na yalipo magari."


"Umewaonaje Tity?"

Jasmine alimuuliza.


"Nikiwa napitia mitego yangu pale karibia na kimbuga kile kule juu si ndiyo nikasikia kama sauti za watu na baada ya kuangalia huku na kule si ndiyo kuona watu wamejificha eneo lile pale."


"Watakuwa wakina nani hao?"

Jasmine aliuliza swali ambalo alilirusha hewani ili yeyote alijibu.


"Nahisi watakuwa ni wale waliokimbia hivi karibuni."

Roberto alihisi kitu juu ya wale wawindaji waliokimbia karibuni.


"Nahisi hivyo na mimi."

Jessica alimuunga mkono Roberto.


Hapo hapo walitoka nje wakiwa na silaha zao mkononi na kulivizia lile eneo kisha walianza kulishambulia bila kuuliza na baada ya kujiridhisha kuwa hakuna aliyepona walisogea ili kuangalia ni wakina nani na walikutana na mtu mmoja akiwa akiwa anagugumia kwenye dimbwi la damu na hapo Jasmine akainama kutaka kumjua ni nani huyo lakini alichelewa kwani aliagana na dunia.


"Nini tena?"

Jackline aliuliza swali.


"Ameshakufa tayari."

Jasmine alijibu.


"Kuna mchezo hapa hebu turudini tukafanye maandalizi ya safari hili eneo si rafiki kwetu."

Jackline aliwaambia wenzake na kuondoka zao kurudi pangoni ambako waliwakuta wote isipokuwa mzee Jonathan.


"Shenzi huyu hajafika kokote na lile donda hebu tugawanyike hili eneo na ninyi Titiana na Jessica bakini na hao wengine."

Jasmine alitoa maelekezo kisha wakasambaa kumsaka mzee Jonathan ambaye alitumia nafasi ya wao kwenda kupambana na waliowahisi wabaya wao. Mpaka inatimia saa sita usiku hakukuwa na matumaini ya kumpata mzee Jonathan wakaona warudi mle pangoni na kuwabana wakina mzee Kaaya kutaka kujua ameondokaje mzee huyo ndipo mke wake aliwajibu.


"Kajikongoja mwenyewe na hakuna aliyeingia humu."


"Ni ya kweli hayo yanayozungumzwa na huyu mama?"

Jackline aliwauliza wengine ambao nao walijibu kuwa aliondoka mwenyewe na hakuna aliyemtorosha. Ndipo walitoka tena na kuuzunguka mlima ule kuona kama kuna sehemu anaweza kujificha. Na kulipoanza kupambazuka tu wakiwa wamekata tamaa ya kuendelea kumsaka hamadi walimkuta akiwa juu ya mti mmoja mkubwa wenye majani mengi ambayo juu huu huwezi kujua kuna nini juu yake wao kilichowashtua ni baada ya kipande cha kimti kudondoka karibu ya Roberto na ndipo walipoangalia juu na kumuona. Walimshusha na kisha kumshambulia kwa migumi na mateke kisha kumbeba juu juu tena mpaka pangoni. Huko walianza upya kumkabiri kwa kichapo hevi kilichopelekea mzee Jonathan kuchakaa si kwa nguo tu bali mpaka sura na baada ya kutosheka ndipo walianza upya mahojiano naye.


"Sina cha kuwasaidia mimi fanyeni mnalotaka kunifanyia bora nife tu."

Mzee Jonathan aliwaambia kwa shida kutokana na maumivu ya mwili.


"Unasemaje wewe mzee?"

Jasmine alimuuliza mzee Jonathan.


"Sirudii tena mimi siyo matangazo ya vifo."

Mzee Jonathan alijibu kishomboshombo.


"Anasema yeye si matangazo ya vifo sasa niachieni mimi huyo."

Roberto aliomba ruhusa kwa wenzake.


"Kazi kwako Roberto."

Jackline alitoa ruksa.


Kisha alimchukua mzee Jonathan na kutoka naye nje kisha alimfunga kwenye mti mmoja uliokuwa karibu na lango la kuingia pangoni na kumfunga hapo kisha akaanza kumsukumia mijeredi ya kutosha.


"Ngoja nikupe stata ya kuufungua mdomo wako mzee mwenye misimamo yako."

Roberto alimwambia mzee Jonathan huku mifimbo ikiendelea kuushambulia mwili wake.


"Kijana wangu nina hakika una wazazi waliokulea kwa maadili mema kabisa na wala hawakukufundisha haya unayonifanyia leo."

Mzee Jonathan alimwambia Roberto.


"Sina wazazi na watu kama wewe ndiye waliosababisha niwe hivi hivyo pona yako ni kusaini dokumenti zetu umepona tofauti na hapo umekwisha."


"Ninusuru na hili toto kijana wangu na iwapo utafanikisha tu hili nakwenda kukumwagia minoti ya kutosha."

Mzee Jonathan alianza mambo yake ya kumtongoza Roberto ili apate pona.


"Unaweza kufanya hivyo kweli?"

Roberto alimuuliza.


"Ndiyo na ndiyo maana nakuomba msaada."


"Vizuri, cha kufanya sasa turudi ndani kasaini nyaraka kisha nakutorosha kwenda kufanya uhamisho wa mkwanja wako ikiwa ni pamoja na kumilipa zangu na Jackline atakapofikia hatua ya kuhamisha salio tu atakutana na salio empty, uko tayari?"


"Niko tayari kwa hilo."

Mzee Jonathan alikubaliana na maneno ya mzee Jonathan ya kumzunguka Jackline. Na kweli baada ya hapo aliwekewa nyaraka tena kisha akasaini zote na kisha Roberto akamtumia Jackline ujumbe mfupi ulioeleza mchongo mzima aliopanga na mzee Jonathan, akawa ameshauelewa vizuri kisha Jackline, Titiana na Jessica walitoka kwenda kuangalia mitego aliyotega Titiana ili kumpa nafasi Roberto kufanya yake.

Huku nyuma Jasmine aliyekuwa hajui lolote alishangaa Roberto anamdaka na kumfunga kamba kisha kumfungulia kamba mke wake mzee Jonathan na kuondoka nao mpaka kwenye gari yao Kluga na kuondoka zao. Huku nyuma Jasmine alianza kupiga mikelele iliyowashtua wenzao kule nje na kurudi haraka na kumkuta akiwa kambani wakazikata na kumwinua kisha akawasimulia kilichotokea hapo wakati wao wametoka nje.


"Dada yangu utakufa bure kwa ubishi wako nilikwambia twende ukajidai umechoka kumbe Izrael mchezea roho za watu alikuwa anakuvizia."

Jessica alimwambia ndugu yake.


"Roberto kapatwa na nini mpaka kufanya hivi ama kweli dunia ina mambo alikuwa Robinson sasa ni huyu kinyago."

Jasmine aliongea huku akipukuta machozi yaliyokuwa yakimwagika mashavuni bila breki.


"Roberto amekuwaje? Ina maana hata mimi sina maana kwake?"

Titiana naye aliuliza swali huku akiangua kilio.


"Jamani nyamazeni kuendelea kulia si suluhisho dawa ni kuanza kuwafukuzia tu."

Jackline aliwaambia wenzake wakakubaliana na kisha wakawafungua pingu wakina mzee Kaaya, mke wake na yule kijana dereva wa mke mzee Jonathan ambaye alikuwa bado kazimia hajitambui kutokana na kichapo kingine hevi siku moja iliyopita na kuwapakia kwenye gari na safari kuanza haraka.


"Haki ya Mungu naapa tukiwakamata hasa Roberto atajuta kuungana nasi."

Jasmine aliongea akirekebisha mkanda wa kiti huku Titiana akiwa analia tu.


"Unaona sasa mlivyosema mwanangu amewasaliti? Ndiyo mjue kwenye hela hakuna mkamilifu."

Aliongea mzee Kaaya ambaye hata hivyo hakuna aliyemsikiliza maneno yake kwani kila mmoja alikuwa akiwaza lake wengine wakivuta tu makamasi. Walipofika barabara kuu ya Mbeya kwenda Tabora na Singida Jackline alisimamisha gari na kushuka kisha akaufungua mlango wa nyuma huku wenzake wakimshangaa tu kisha akawataka mzee Kaaya na mke wake kushuka haraka. Kauli hiyo iliwafanya watazamane kwanza kisha walikumbatiana huku machozi yakimwagika kwani walijua mwisho wao umefika.

Walishuka chini na hapo hapo Jackline pasipo kuongea chochote alirudi kwenye usukani na kutimua vumbi na kuwaacha wakiwa wanaishangaa gari linavyopotea kwenye upeo wa macho yao.

Walikumbatiana tena mzee Kaaya na mkewe wakiwa hawaamini tena kilichotokea mbele yao. Huku wakina Jackline wakiviacha vijiji vya Mafyeko, Bitimanyanga na Kambikatoto na kisha kuingia Rungwa ambapo hawakutaka kupoteza muda waliikamata njia na kuendelea na safari yao na baada ya kuingia ndani ya pori la Rungwa walimshusha yule kijana dereva na kutimua zao vumbi kuendelea na safari ya kuitafuta Sikonge.


"Mbona hao wote umewashusha?"

Jessica aliuliza baada ya kuiona kazi ya Jackline kama vile kavurugwa.


"Huyu tayari ni nusu mfu maeneo haya ni salama kwake na wale wengine waache waje washuhudie kifo cha mtoto wao Robinson muda ukifika."

Jackline alimjibu Jessica huku miguu ikicheza na pedali za gari.


"Unasema hivyo wakati tayari kazi mpya imezaliwa."

Jasmine aliongea baada ya kuona Jackline akiwa anazungumzia suala la Robinson.


"Roberto tutamdhibiti mapema tu ondoeni shaka rafiki zangu."

Jackline alijibu huku akikanyaga mafuta.


"Wewe rahisisha tu unafikiri ndiyo yule miaka ile huyu ni mwingine kabisa."

Aliongea Jessica aliyeonekana kumhofia zaidi Roberto.


"Kumbuka kuwa hata sisi si wale wa kipindi kile tumekuwa strong' zaidi."

Jackline aliendelea kuwapa imani.


"Hivi utafanya nini ikitokea tumemkuta Roberto?"

Jasmine alimgeukia Titiana na kumuuliza swali hilo ambalo lilikuwa kama moto kwake.


"Wala hata sijui itakuwaje labda nitakufa."

Alijibu Titiana huku akiachia tabasamu lililobebwa na machozi.

Baada ya mwendo mrefu hatimaye waliwasili Sikonge na kuamua kupata chakula kabla ya kuendelea na safari yao hivyo walitafuta Hotel moja ambayo iko nje kidogo ya mji unapoingia Sikonge ukitokea Tabora iitwayo Mtemi Hotel na kupaki hapo.


"Jamani hapa nafikiri ni sehemu nzuri kwa chakula kwanza iko nje na makelele ya mji zaidi ya yale ya wateja pia Jessica itabidi umtraki Roberto tujue kaelekea tusije ingia njia ambayo siyo yenyewe."


Baada ya kukubaliana nini cha kufanya waliagiza chakula na kuanza kula na hapo hapo Jackline akaitumia nafasi hiyo kuwapa ukweli ulivyo kati ya Roberto na mzee Jonathan na ndipo akawaonesha ile meseji ambayo alitumiwa na Roberto na kila mmoja aliisoma na kubaki mdomo wazi hasa Titiana ambaye alianza kutoa machozi ya furaha kwani alianza kuwaza mambo mengine kabisa kichwani mwake.


"Huyu ndiyo kidume anayejua nini maana ya kampani na ushirikiano siyo yule kenge Robinson."

Aliongea maneno yale Jessica na kuwafanya wote kuangua kicheko.


"Kwa hiyo kunifanyia vile ilikuwa ni triki tu ya kuwazuga wale wazee?"

Jasmine aliuliza huku akiendelea kucheka.


"Unauliza majibu Jasmine."

Jackline alimjibu huku wakiwa wapiga selfie wakiwa na minyama mikononi kama furaha kuashiria mkakati wa Tanzania unaelekea ukingoni.


JE NI NINI KITATOKEA?


SEHEMU INAYOFUATA INAKUHUSU NI KAZI YAKO KUWEKA BANDO LA MAANA.




Mrembo yule ambaye alipewa kazi ya kumfuatilia Dr Abbas Mukesh alimpa mrejesho kwa njia ya simu madam Nafiwe kuwa kila kitu kiko sawa. Na kitu ambacho kiliwafurahisha zaidi 'The Black Eyez' chini ya madam Nafiwe ni baada ya kusikia kuwa Dr Abbas Mukesh mida hii yuko nyumbani kwake. Hivyo ikabidi madam awajulishe wenzake juu ya hili na hivyo kuingia kwenye gari mbili za kazi na kuelekea mitaa ya 'Old Town' anakoishi Dr Abbas Mukesh. Walipofika maeneo haya na kukutana na chawa wao ambaye aliwapeleka mpaka mitaa hiyo na kuifikia nyumba ya Daktari na kwa kutumia upande wa nyuma ambako kuna mabanda ya kuku na Sungura walipanda na kutua ndani na wengine wakabakia nje kucheki ustaarabu wa nje. Tom na Robinson ndiyo walitinga ndani na kundi la 'The Black Eyez' kusalia nje na baada ya kutua ndani waliunyemelea mlango wa kuingia ndani pale Tom alinyonga kitasa kwa kutumia ufunguo wa bandia na kisha kuingia ndani kwa tahadhari kubwa.

Walikagua kila kona ya nyumba hii lakini walitoka patupu kwani hakukuwa na chochote zaidi ya wale kuku, sungura na paka waliyemkuta sebuleni.


"Brother hii hali umeielewa?"

Robinson alimuuliza Tom baada ya kutokupata kile walichokuwa wanakihitaji.


"Mimi mwenyewe wala sielewi kabisa kama haka kadada kalifuatilia kwa umakini iweje tusimkute ndani yaani hata familia yake? Kwamba hajaoa hana hata ndugu yeyote?"

Tom naye aliuliza tena swali ambalo halikuwa na majibu.


"Kaka hapa kuna mchezo umefanyika na tusipoangalia tutaangukia shimoni, na kama ambavyo nilisema awali kuwa wakina Jackline si watu wa kuwachukulia poa ni hatari sana wanaotakiwa kufanyiwa shambulizi la maana na si staili kama hizi."

Robinson aliongea huku akitoka nje ya nyumba ile huku nyuma yake Tom alikuwa anaangalia nyuma kama anaweza kuona kitu cha kuwasaidia.


" Nakuelewa sana dogo langu kwa unachokiongea hapa ni kweli tumebugi na kwa mbali naviona vivuli vya wakina Jackline kwenye hili cha msingi hapa ni kwenda hospitali moja kwa moja tukamvizie inawezekana akawa kule."


"Ni kweli kaka lakini sioni kama linafaa hilo, ninachokifikiria mimi ni kumtaarifu Bosi awatafute wakina Jackline kwa kutumia GPS finder' itasaidia na kingine ninachokiona mimi kwa nini tusiende pale Namport tukapige kambi pale tunaweza kumpata aliyewaokoa majini maana nasikia ni mvuvi."

Robinson alitoa mawazo yake ambayo alihisi yanaweza kusaidia. Hivyo walipanda ukuta na kuishia zao nje na kuungana na wenzao ambao walikuwa wakiwasubili na walipowaambia juu ya walichoambulia huko ndani waliamua kuondoka kuelekea hospitali ya 'King's Medicare Centre' kwenda kumuangalia Dr Abbas Mukesh.


"Madam unaonaje kama tukigawanyika makundi mawili moja likapige kambi kule bandarini na lingine liendelee kumtafuta huyu Daktari kule tunaweza kupata taarifa za kumhusu yule mvuvi aliyewasaidia."

Robinson alitoa wazo lake wakiwa njiani kuelekea hospitali.


" Robinson acha kutuwekea vikwazo na pia nimepewa taarifa zako na Santana kuwa huyu Kidudumtu Jackline ni demu wako uongo au kweli? Usije ukawa unatoa ushauri hapa kumbe ndiyo unawasaidia kiaina."

Madam Nafiwe alimuuliza Robinson baada ya kutoa ushauri.


"Ni kweli usemacho Madam lakini kumbuka kuwa alikuwa na si kwa sasa na vile vile kumbuka kuwa kuwatumia watu wake kawateka wazazi wangu hivyo nisemavyo haya nina hasira nao sana na sivyo unavyofikiria wewe madam."


"Nimekuelewa Robinson ila muda huu ni usiku itakuwa ngumu kwenda bandarini ni vyema kama tutaendelea na safari mpaka hospitali pale tutampa chochote kitu mlinzi aweze kutunyetishia ratiba nzima ya Bosi wake."

Madam Nafiwe alikubaliana na Robinson lakini akitaka kwanza wamalize zoezi la kule hospitali kwa usiku ule na kesho yake ndiyo watege mitego mingine.

Waliwasili pale KING'S MEDICARE CENTRE na kisha alishuka Tom na kumfuata mlinzi wa hospitali na kuongea naye kwa muda kisha akatoa bahasha yenye chochote na kumkabidhi mlinzi yule ambaye alikubali kumpa ushirikiano kwa kutoa taarifa za siri za bosi wake, waliondoka zao na kurudi nyumbani.


"Mzee wewe ni kiboko ya njia."

Dr Abbas Mukesh alimpigia simu mzee Jerome.


"Kwanini Daktari wangu?"

Mzee Jerome Whistle alimuuliza Dr Abbas Mukesh.


" Si wamefika leo watu wako wakiwa na magari mawili na wawili kati yao haraka walikwea ukuta na kuzama ndani na baada ya kunikosa waliondoka zao."


"Unasema kweli Daktari?"


"Kwanini nikudanganye mzee wangu usiku wote huu?"


"Aisee pole sana daktari ikawaje baada ya kuja hawakukudhuru?"


"Hapana hakunifanya chochote kwani baada ya kunipigia simu na baada ya mkwara ambao nilichimbwa na yule mwanamke ilibidi nichukue hatua za kiusalama haraka sana na kwa kuwa karibu na kwangu kuna Lodge' ilibidi nihamishie familia yangu pale kwa usalama na hivyo kwa kupitia dirishani nikiweza kuuona mchezo mzima kwa kutumia kiona mbali changu ambacho kilinifanya kucheka sana."


"Kwanini ulicheka badala ya kusikitika?"

Mzee Jerome alimuuliza.


"Kwa sababu walikuja kwenye mawazo yetu kama ambavyo tulihisi na pia nahisi baada ya kutoka hapa watakuwa walienda kazini kwangu."


"Shauri yao bwana, cha kuangalia hapo na usalama wetu tu mengine yafuate na vipi kuhusu Dr Hans Murray ulimpata hewani?"


"Nani mzee wa Makambi? Namkosaje tena Swahiba wangu mwenyewe. Nilimpata na kumuelekeza na aliniambia kuwa kwa upande wake wasijaribu kuigusa Makambi kwani tayari Hospitali yake imeshazungukwa na Kampuni ya Ulinzi kutoka Ujerumani."


"Vizuri sana vijana wangu kwa kujiandaa hivyo na mimi mzee wenu siko nyuma katika hilo kwani nimeshaipiga marufuku familia yangu kuzurura bila sababu."


"Tumekamilika kwa vita mzee, nikutakie usiku mwema na mimi ngoja niwapigie simu wafanyakazi wangu kule Hospitali wawe makini na kila mtu wanayemtilia shaka."


"Asante kijana wangu na kwako pia."

Alijibu mzee Jerome na kisha simu ilikata na kuiweka kwenye Bedtable na kisha kulala zake.


***


Baada ya kupata chakula pale Sikonge waliendelea na safari yao ambayo safari hii ilikuwa ikiongozwa na Jessica aliyekuwa na iPad yake akiwa kawatraki wakina Roberto. Walifika Tabora mjini na kwa kuwa signo ilikuwa ikiendelea kusonga mbele waliona wasipoteze muda pale zaidi ya kusonga mbele hivyo mafuta yalikanyagwa ilikuwa ni sekunde ikawa dakika na baadaye masaa na hatimaye waliwasili jijini Mwanza na kuelekea moja kwa moja maeneo ya Nyakato ambako ilionekana ile signo ilionekana kustop na wao walisimama na kwa kuwa gari yao wanaifahamu wakina Jonathan waliamua kupaki sehemu moja yenye kituo cha mafuta hapo kuna kijana muosha magari ambaye walimkabidhi ile gari aifanyie kazi ya usafi na wao walishuka wakaanza kutembea kwa mguu kuifuata ile signo ambayo iliwapeleka moja kwa moja mpaka kwenye majengo yaliyokuwa na jina la MARIMBE HOME APARTMENT (MHA) hapo waliweza kujua fika ndipo anapoishi mzee Jonathan hivyo hawakuwa na haraka waliingia kwenye duka moja linalotazamana na geti la kuingia kwenye majengo hayo na kuketi hapo lengo likiwa ni kufuatilia kila anayeingia na kutoka ndani ya majengo hayo. Waliagiza vinywaji vyao pale huku Jessica macho yakiwa kwenye signo yake ambayo hakutaka kuipoteza kama ilivyowatokea Dodoma.


"Hapa tayari tumewanasa watu wetu kiulaini kabisa."

Jasmine aliongea akipiga fundo la sprite ya baridi huku wenzake wote wakicheza na pepsi za baridi pia.


"Ni kweli lakini tuwe makini tusijeingizwa mjini."

Jessica aliongea na kuonesha kutomuamini kwa asilimia zote Roberto.


"Hapa kazi imekwisha kikubwa ni kumsikilizia Roberto akisema kushineyi wazee wa kazi tunajaa ndani."

Jackline aliwajibu wenzake.

Walikaa pale kwa muda kidogo kisha ujumbe ukaingia kwenye simu ya Jackline ambao ulitoka kwa Roberto nao ulisema,


"MAMBO YANAENDELEA HUKU NDANI BABU JINGA AMESHANIPA HUNDI YA SHILINGI MILIONI MIA MBILI SABINI, NA HIVI NAMSUBIRI AOGE NA KUTOA UCHAFU WAKE KICHWANI BAADA YA HAPO TUTAONDOKA NA KUELEKEA ENEO LA ILEMELA HAPO KUNA OFISI ZAKE TUNAKWENDA KUUMALIZA MCHEZO HIVYO KAMA HAMKO MBALI JIANDAENI KAZI KWISHA."


Walipoisoma hiyo jumbe walisimama na kugonga cheers' mpaka muuzaji aliwashangaa kwa namna ambavyo walikuwa wamefurahi wateja wake.


" Si mnaona namna ambavyo tunakwenda kuumaliza mchezo kisha tunamchukua na kuondoka naye huku mke wake akiwa harufu ya wenyeji."

Jackline aliwaambia wenzake kinachofuata.


"Itakuwaje hapo sasa tunaongozana au tunafuata nyuma?"

Jasmine alimuuliza Jackline.


" Simpo tu hiyo kwani wakitoka tu tunachukua gari la kukodi ambalo litatupeleka huko wanakoelekea na baada ya kufika huko tutauvamia mkutano wake na wafanyakazi wake kisha tutamteka na kuongea na wafanyakazi wake na kuwaelekeza kuwa Makampuni ya Ubao yote yako chini ya mmiliki mpya ambaye ni Jackline kisha ngoja kwanza.... "

Jackline ni kama alikumbuka kitu hivi akachukua simu na kuitafuta namba fulani na kisha kuipiga.


"Mzee Jerome tunaelekea kukamilisha kazi yetu masaa kadhaa yajayo na baada ya hapo tutambeba mtu wetu na kwenda kumuulia porini huko na mke wake kisha tutaianza safari yetu kurudi Brazil na misheni ikikamilika tu tutarejea Namibia kuungana nanyi."

Jackline aliona amtaarifu mzee Jerome kinachoendelea muda huo.


" Nawatakia mafanikio mema mabinti zangu."


"Asante baba."

Jackline alimjibu mzee Jerome.


"Jamani inukeni tuondoke zetu gari ndiyo ile inatoka ni wakati wetu sasa wa kufanya na kutekeleza kilichotuleta Bongo."

Jasmine aliwaambia wenzake baada ya kuyaona magari kama matatu yakitoka getini.

Walikimbia haraka mpaka yalipopaki magari ya kukodi na kuingia kwenye gari mojawapo na kuingia ndani yake.


" Dereva tafadhali ufuatilie Msafara ule uliopita hapa dakika chache zilizopita."

Jackline alimuamuru dereva wa gari waliyoingia.


"Yale matatu?"

Hayo hayo dereva jitahidi kabla hayajapotea mbele ya mboni za macho yako.


"Shaka ondoeni mmekutana na dereva mwenye uchizi na kazi yake mara moja tunawafikia na hata mkitaka niwapite."

Dereva huyo mwenye mbwembwe alijinadi mbele yao na kisha aliwasha gari na kuondoka kwa kasi na kuwafuata walengwa ambao ni kikosi cha mzee Jonathan waliokuwa mbele yao.


JE, NINI KITAENDELEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.




"Mke wangu kipenzi Dorothy baada ya mateso makubwa ni muda wetu wa kutanua ndani ya nchi ya Uganda na mambo yakiwa sawa tutawarudia wabaya wetu kwa kushirikiana na kikundi cha TIA CHATA cha mzee wa kazi Rogers maarufu kama Karatu huku tukipewa nguvu na Jabali la Kibrazil hili hapa (akimuonesha Roberto) "

Mzee Jonathan alikuwa akimwambia mke wake Dorothy mipango yake mara baada ya mtu wake wa fedha kumletea zile briefcase zenye mkwanja zilizokuwa kama nne akiwa tayari kutimkia nchini Uganda.


" Lakini mume wangu una uhakika na maamuzi yako?"

Mke wake alimuuliza.


"Kwanini unaniuliza hivyo mke wangu?"

Alimtupia swali badala ya kumjibu swali.


"Basi maana naona mapigo ya moyo yananienda mbio sana na hali hii huwa ikitokea lazima kuna jambo baya mbele linakuja."

Mke wake alimwambia anachokihisi.


"Mke wangu achana na mawazo hayo bwana hapa ni safari tu hata nyumbani haturudi tunaondokea hapa hapa."

Muda huo wakiwa wanajipa matumaini ya kuiacha ardhi ya Tanzania pembeni yao alikuwa katulia tuli Roberto akiwachora tu na stori zao.


Mara simu ya Mzee Jonathan iliita na baada ya kuiangalia aliipokea.


" Niambie Rogers?"


" Nikwambie nini mzee Jonathan wakati unajua kuwa kazi yetu hatujaimaliza? Mpaka sasa hujanipa mrejesho."

Rogers (Karatu) alimwambia.


"Kijana wangu ni kweli kabisa sikuweza kukwambia chochote kwani nilikuwa nataka nipumzike kwanza ndipo nikucheki lakini kwa kuwa umeshapiga ngoja niunganishe tu ni hivi kazi ni ngumu sana kila kunapokucha na vijana ambao ulinipa ni waoga sana."


"Waoga kivipi?"

Rogers alimkatisha mzee Jonathan.


"Si kama unavyojua Black alinikimbia huku Masanja akiuawa na maadui ninaowatafuta mara baada ya kutuzidi kwenye Uwanja wa mapambano."

Mzee Jonathan alitoa ufafanuzi.


"Kwanini hukunipa taarifa mpaka nikupigie mimi?"


"Ningekupigiaje wakati mimi mwenyewe nilitekwa huoni hata hiyo namba ni mpya? Nimshukuru huyu dogo wa Kibrazil aliyeamua kunisaidia na huyu atakuwa msaada mkubwa kwetu iwapo tutamtumia vizuri."


"Ongea yote mzee lakini ninachokitaka mimi ni vijana wangu tu, namhitaji Masanja na Black hapa hao sijui wakina nani siwatambui hata kidogo umenielewa?"

Rogers alimuwakia mzee Jonathan baada ya kupata taarifa za kufa kwa Masanja.


"Ninachokuomba kijana wangu punguza hasira haya yameshatokea tuangalie ya mbele kwa sasa kundi litakuwa imara zaidi tofauti na mwanzo na kwa kila tutakapokanyaga tutaweza kuibuka Mashujaa kwani si huyu tu bali wapo na Maaskari wengine wawili ambao waliniokoa kutoka sero kule Makongolosi nao wako tayari kuufanya kazi na sisi.... "

Mzee Jonathan alikatisha mazungumzo yake na Rogers kwenye simu baada ya kusikia makofi yakipigwa mbele yake hivyo ilibidi aiachie simu kutokana na kile alichokiona kwani hakutegemea kabisa kitu kama kile.


" Jackline???? "

Alitaja jina la Jackline kwa mshangao huku akiinuka kitini macho kwa Jackline.


"Ndiyo mimi mzee wangu, ulijua umefanikiwa kunitoroka? Unafikiri ni rahisi eee?"

Jackline aliongea kwa dharau ya hali ya juu huku akimsukuma pembeni na kuketi kwenye kiti ambacho alikalia mzee Jonathan.


"Roberto unawaangalia tu fanya kazi yako wakujue."

Mzee Jonathan alimwambia Roberto akiwa anajiinua kutoka pale chini ambapo alikuwa kaangukia.


"Paaaa........"

Mlio wa risasi ulisikika mle ndani, mzee Jonathan hakuamini alichokiona mbele yake.


"Roberto mshenzi wewe mjaa laana umemfanya nini mke wangu?"

Mzee Jonathan alimbwatukia Roberto huku akijivuta kumfuata mke wake aliyekuwa chini ya sakafu akitokwa na damu eneo la kifuani.


"Nimetekeleza maagizo yako mzee Jonathan umeshasahau mara hii kuwa nifanye kazi yangu wanijue na ndicho nilichokifanya mzee Jonathan."

Roberto alimjibu Jonathan akiwa kamkamata mashavu kwa staili ya kuyaminya kisha akamtemea mate usoni.


"Bado sijakuelewa kijana wangu umepatwa na nini hadi uuchukue uhai wa mke wangu Dorothy?"


"Mzee Jonathan huu ni uthibitisho kuwa mimi nani kwako kikubwa nikuombacho sasa ni kukiri madhambi yako yote kwa Mwenyezi Mungu kabla hujaongea na risasi."

Roberto aliongea hayo huku akizichukua zile briefcase na kuwakabidhi wakina Jasmine na Jackline alikuwa bize kwenye makabati akipekuapekua baadhi ya nyaraka za mzee Jonathan. Kilio cha mzee Jonathan kiliongezeka baada ya kumshuhudia mke wake akimalizikia pale chini huku baadhi ya wafanyakazi wake waliokuwepo pale ofisini wakiwa bado hawajui wafanye kipi kwa yale waliyokuwa wanayashuhudia pale ofisini.


"Na ninyi ongoza kwenye chumba kile pale haraka sana na hakikisheni kila kitu mnaweka hapo mezani sasa fanya kinyume chake uone."

Roberto aliongea hayo huku akiwaonesha kwa kuingia.


"Hebu subirini kwanza ninyi msije fanya yenu, inueni mikono juu haraka."

Titiana aliwaamrisha na kuwafuata kisha akaanza kuwacheki mifukoni na kutoa kila walichokuwanacho na kisha kuwaamrisha waingie kwenye chumba ambacho walioneshwa na Roberto kisha wakawafungia huko na kumrudia mzee Jonathan.


" Mzee Jonathan Ubao inuka na mchukue mkeo na muingize kwenye kile chumba kile pale ambacho ni chumba chako cha mambo yako ya siri."

Mzee Jonathan aliposikia maneno yale ya Roberto hakuamini macho yake kwani hakutegemea kuwa ndani ya muda mfupi Roberto alikuwa ameshasoma mazingira ya jengo lile lote.


" Naombeni mnisaidie nimzike mke wangu kwanza ndipo mengine yafuate nawaombeni sana."

Mzee Jonathan aliongea akiwa kashika Raba ya Jackline akiomba msaada.


"Inauma sana eee? Hata mimi baada ya kufiwa na wazazi wangu wote pamoja na walezi wangu ilikuwa hivyo hivyo na baadaye hali ilikuwa zaidi ya hiyo baada ya kugeukwa na mtu ambaye nilimpa maisha yangu yote nikiamini ndiyo jicho langu la tatu kumbe nilijidanganya mzee lakini namshukuru Jasmine, Jessica pamoja na Roberto bila kumsahau mpenzi wake Titiana kwa kujitoa kwao kwangu hivyo simama haraka mbebe mnyang'anyi mwenzako mfungie mle kisha tuianze safari."

Jackline aliongea kwa huzuni sana kwani alitokwa na machozi kiasi kwamba alishindwa kujizuia na kujikuta akikaa chini na kuegemea ukuta na kuanza kulia kwa sauti kitu kilichomsogeza Titiana na kuanza kumtuliza huku Jonathan akiinuka kwa kujikongoja macho yakiwa kwa Roberto na kuanza kumuinua mke wake alijikaza akafanikiwa kumbeba na kumuingiza mle chumbani kisha akatoka na mlango ukafungwa na Jessica.


"Mzee ni muda wa kuondoka sasa."

Jessica alimwambia mzee Jonathan akiwa anampita.


"Pakieni kila kitu kinachotuhusu kwenye gari, Roberto mpige blackeye' huyo."

Jackline aliwataka wapakie vitu kwenye gari huku akimtaka Roberto amfunge kitambaa cheusi usoni na kisha cheni miguuni na mikononi. Zoezi lilifanyika na kisha walitoka na kuingia kwenye magari mawili Nissan Veto G8 na ile Kluga na kuondoka zao kuelekea kule ambako waliiacha Honda jet5 na hapo safari ya kuelekea Tabora ilianza.


****


Ikiwa ni usiku wa saa tano usiku kundi la 'The Black Eyez' walikuwa nje jumba la daktari aliyewashughulikia wakina Jackline kutoka hospitali ya Makambi Hospitali iliyoko Windhoek anayeitwa Ramadhan. Na baada ya kupaki gari yao tu mwanadada Nafiwe aliteremka na kulifuata lango la kuingia ndani na kubonyeza kengele na baada ya dakika kama mbili hivi lango lilifunguliwa na kutoka kijana ambaye ni mtoto wa daktari Rama na kumkaribisha ndani.


"Hujambo kijana mzuri."

Madam Nafiwe alimsalimu kijana huyo.


"Sijambo mama mdogo karibu ndani."


"Asante kijana wangu unafikiri hata niingie ndani? Hapana nina shida na Daktari Ramadhan."


"Okay yuko ndani anajiandaa kutoka kuelekea kazini kapigiwa simu kuwa kuna mgonjwa wa dharura."

Mtoto wa Daktari Ramadhan alimfafanulia madam Nafiwe bila kujua anayemwambia ni nani.


"Aisee kumbe nimefikia penyewe kwani huyo mgonjwa ni wa kwangu mwenyewe."

Madam Nafiwe alidanganya.


"Jamani pole sana mama mdogo kumbe ngoja nikamfuate."


"Sawa sawa si vibaya tukiongozana."

Aliongea hivyo na kuingia ndani kisha lango likafungwa kitendo cha geti kufungwa tu wakina Tom na wenzake wakauparamia ukuta na kuzama ndani kupitia kwenye maua kuogopa kumulikwa na mataa.


"Unasemaje mwanangu?"

Daktari Ramadhan alimuuliza mtoto wake inaonekana kama taarifa aliyopewa hakuielewa.


"Mbona nimeongea na wenye mgonjwa ni wa kiume na huyo mwanamke ni nani?"


"Yuko sebuleni hapa anakusubiri utamsikia mwenyewe inawezekana nimefikisha taarifa isivyo."

Mtoto yule alimjibu baba yake baada ya kubaini kuwa kachukia.


"Nakuja."

Alijibu Daktari.


"Kasemaje?"

Madam Nafiwe aliuliza baada ya kumuona mtoto yule anakuja sebuleni lakini akionekana kufikiria kitu.


"Kasema anakuja mama mdogo."


"Vizuri sana, nakushukuru sana kijana wangu."

Alijibu madam Nafiwe na kutoa sigara yake ambayo aliiwasha pale sebuleni.


"Hee dada yangu vipi tena na masigara kwenye majumba ya watu hebu angalia nyuma yako ukutani."

Daktari Ramadhan alimuuliza madam Nafiwe baada ya kumkuta akiwa anaipuliza kwa raha zake. Na baada ya kuangalia nyuma yake alikutana na mchoro ukimuonesha mtu anavuta sigara na huku alama ya usivute sigara hapa ikiwa imeizunguka.


" Samahani Daktari sikuiona na nilifanya hivi nikijua Madaktari wengi huvuta sigara kumbe nilikuwa najidanganya mwenyewe."

Aliomba msamaha baada ya kuona kakosea.


"Okay bila shaka, eenh niambie kuna nini na usiku wote huu dada yangu?"

Daktari Ramadhan hakutaka kupoteza muda.


"Samahani naomba tuongee hapo nje tafadhali."


Madam Nafiwe alikubali kutoka nje ili amsikilize mgeni wake ana mpya gani iliyomleta usiku huo. Lakini kitendo cha kumalizia kukanyaga ngazi ya mwisho tu walitokea Tom na Robinson na kumnyakua juu juu mpaka nje ya geti na hilo wakati hilo linatokea lilishuhudiwa na mtoto wake ambaye alikuwa kafunua pazia la dirisha, hivyo kuchukua simu na kuanza kuipiga lakini alichelewa kwani madam kitendo kile alikishuhudia hivyo hakutaka kupoteza muda wake alinyoosha bomba na kumfuatilia pale pale dirishani bila shaka ilimkuta kwani kilichosikika ni kelele za maumivu lakini Madam Nafiwe hakujali alitoka nje haraka na kuungana na kundi lake.


"Bila shaka umeshajua ni nini tumekifuata kwako."

Tom alimwambia daktari Ramadhan baada ya kumuona akigeuka nyuma alikousikia mlio wa risasi.


"Hiyo risasi amepigwa nani mbona ni kama sauti ya mwanangu?"

Daktari Ramadhan alimuuliza Tom na Robinson.


"Usalama wako Daktari ni kutuambia wale mabinti watatu walielekea wapi na ni nani aliwafuata."

Madam Nafiwe alimuuliza baada ya kuwafikia.


"Yaani hilo tu mpaka mtumie nguvu nyingi kiasi hicho? Angalia sasa mmemuua mwanangu."

Aliwauliza daktari Ramadhan.


"Unaona dogo eee, sasa jidanganye Daktari na wewe utamfuata mwanao sasa hivi jibu maswali yetu ngonjera waachie wenye shughuli zao."

Robinson alimpiga biti Daktari wa watu.


"Ninachokifahanu ni kwamba wale mabinti walipopona waliruhusiwa kuondoka na mtu aliyewachukua ni mzee mmoja hivi aitwaye Mzee Jerome inasemekana ndiye aliwaokoa kwani hata kuwaleta alihusika pia."

Daktari Ramadhan alieleza hayo baada ya kusikia kitu cha baridi kimeligusa paji la uso wake.


" Huyo mzee anapatikana wapi kwa namna ambavyo ulisikia au kuambiwa naye maana wewe ndiye ulikuwa karibu naye."

Madam Nafiwe alimuuliza.


" Si sana ila nasikia alitokea kilometa nyingi kutoka hapa kwani nasikia anatokea Namport na shughuli zake ni mvuvi."

Aliendelea kutoa maelezo daktari.


" Vizuri Daktari unaelekea kuyashinda mauti iwapo tu utafanikisha hili la mwisho."

Akitamba mbele yake madam Nafiwe.


" Lipi hilo?"

Daktari Ramadhan aliuliza huku uso wake ukiwa umechakaa kwa mijasho.


" Tupe mawasiliano yake kisha tukusindikize kazini kwako na sisi tuendelee na yetu."


"Namba yake ninayo ngoja niwape."

Alijibu huku akiitoa simu mfukoni na kumkabidhi Tom atafute namba hiyo.


"Umeisevu kwa jina gani?"


"Kwa jina la Mzee Mtanashati."


"Kwanini jina hilo na si jina lake halisi?"

Madam Nafiwe alimuuliza baada ya kulisikia jina hilo.


"Nilisevu jina hilo kutokana na muonekano wake."

Daktari Ramadhan alimjibu huku akiwa kajishika mikono yake huku akitetemeka.


"Tayari Madam."

Tom alimwambia madam Nafiwe baada ya kuiandika kwenye simu yake na kumkabidhi simu hiyo madam Nafiwe.


"Vizuri mpakieni kwenye gari tuondoke."

Alijibu huku akiipiga namba ile kuona kama ni yenyewe na kama bahati hivi iliita na kisha ilipokelewa upande wa pili.


"Ndiyo Daktari wangu ni muda sasa toka tuachane."

Mzee Jerome Whistle aliongea baada ya kuipokea.


"Ni ni kweli mzee wa-wangu naomba tuonane... Hapana usije nimetekwa."

Alikutana na ngumi kutoka kwa Tom iliyomfanya aidondoshe simu chini.


"Umesemaje Daktari? Kumbe wewe ni jeuri? Nafikiri umeegemea mlango wa jela kwa makusudi."

Tom alimuuliza huku akimuinua pale chini alipokuwa kalala huku damu zikimtoka puani na mdomoni.


"Paaaaa......."

Alichapwa risasi ya kichwani na kutulia kimya kuashilia kuwa ameachana na dunia.


"Mnamchelewesha pimbi kama huyu wakati tayari ameshaharibu plani yetu? Endesha gari mpaka kazini kwake hapo tutautelekeza mwili wake na kwa kutumia simu hii tunakwenda kumnasa mzee huyu kabla asubuhi haijafika."

Aliongea madam Nafiwe baada ya kumsambaza ubongo Daktari Ramadhan.

Hivyo magari yalishika njia mpaka Makambi hospitali ambako kweli waliutelekeza mwili huo karibu kabisa na geti la hospitali hiyo ambapo waliusukumiza chini mwili huo na wao kupotea zao.


"Tom itafute namba hiyo mtandaoni fasta tuimalize kazi yetu kabla ya mwezi kumalizika."

Nafiwe alimpa kazi Tom wakiwa njiani kutoka Windhoek kurejea Namport kumtafuta mzee Jerome.


"Sawa Madam."

Alijibu Tom na kutoa simu yake ambayo alianza kuifanyia kazi ile namba kwenye GPS.


NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.





"Mke wangu hawa watoto wako wako wapi? Maana hali si shwari."

Mzee Jerome alimuuliza mke wake Elizabeth.


"Hawajarudi bado kwani kuna nini mpaka useme hivyo?"

Mke wake alimuuliza mume wake kutokana na hali ambayo alimuona nayo.


"Leo nikiwa kwenye pilika pilika zangu nilipokea simu kutoka kwa Daktari ambaye aliwashughulikia wakina Jasmine kule Makambi Hospitali aitwaye Ramadhan lakini kilichonitisha zaidi ni baada ya kumsikia akiongea kwa wasiwasi akinitaka tuonane lakini baadaye alibadili kauli na kusema hapana usije nimetekwa.... "


" Ametekwa...? "

Mke wake alimuuliza.


" Ndivyo alivyohitimisha mbaya zaidi haikuchukua muda nikasikia mlio wa risasi na kufuatiwa na makelele hivi."

Mzee Jerome alimfafanulia mke wake tukio lilivyotokea.


" Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa Daktari Ramadhan kauawa?"


" Bila shaka mke wangu naweza sema hivyo."


"Maskini Daktari wa watu kazi yake imempeleka kaburini kama naiona familia yake kwenye dimbwi la huzuni nzito. Lakini hapa kuna kitu mume wangu naomba kama kuna uwezekano jaribu kuwasiliana na wanao wote ukianza na hawa wakina Mustapha na Victor kisha wakina Jackline hapa kuna tatizo mume wangu hawa watu wanaonekana kupania haswaa."


"Kuhusu wakina Jackline nimeshawatumia ujumbe juu ya hili linaloendelea huku na muda huu ngoja niwapigie wakina Victor."


"Fanya hivyo mume wangu naanza kupata hofu."

Mke wake aliendelea kusisitiza.


Hivyo aliwapigia wakina Victor na kuwajulisha kinachoendelea mtaani na hivyo kuwataka kuchukua hatua za kiusalama kwani wanaofanya haya hawajulikani. Mara simu yake iliita na alipoangalia mpigaji ni nani aligundua ni Dakika Abbas hivyo alipokea.


"Mzee wangu umetuletea janga nchini."

Daktari Abbas Mukesh alianza kwa kumuambia mzee Jerome baada ya kupokea simu.


"Janga gani tena Daktari wangu?"

Mzee Jerome alimuuliza daktari Abbas.


"Wale mabinti walimopitishwa mote wakati wa matibabu yao maadui wao wanapita humo na si kupita tu bali wenyewe wanapita na roho zao kwa kila wanayekutana naye hivi tunavyoongea tayari yule daktari aliyewatibu wakina Jackline kule Makambi ameuawa pamoja na mtoto wake ni taarifa ambayo nimeipata kwa mkuu wake Daktari Hans Murray."

Daktari Abbas alifafanua zaidi.


" Mhh kwa hiyo lawama zote zinakuja kwangu Daktari katika hilo? "

Mzee Jerome alimuuliza daktari.


" Hapana mzee wangu ilikuwa ni katika kuitengeneza stori vizuri mzee wangu lakini hali si shwari hawa watu ni hatari sana na unaweza sikia lolote kuanzia sasa kikubwa ni kuchukua tahadhari."

Daktari Abbas alimaliza.


" Nakushukuru kwa taarifa mtaalam wangu sijui itakuwaje lakini nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa ila tu tusisahau kupeana taarifa kwani huyo daktari Ramadhan mpaka mlio wa risasi niliusikia kwa masikio yangu kwani alinipigia kabla na inavyoonekana hawa watu wananitafuta mimi."

Mzee Jerome alimwambia Daktari Abbas kwa kile ambacho kilitokea.


" Aisee kazi tunayo, basi mzee ndiyo hivyo wacha mimi niingie kazini."


"Sawa sawa Daktari wangu nikutakie siku njema."

Mzee Jerome aliagana na daktari Abbas.

Na kisha aliwatafuta watoto wake hewani ili kuongea nao kwa kilichopo mtaani.


"Mko wapi ninyi muda huu?"


"Baba mimi niko huku dukani lakini Mustapha toka alipoondoka ile asubuhi hajarudi mpaka muda huu."

Alimjibu Victor.


"Unasemaje Victor? Na vipi kuhusu simu yake?"

Mzee Jerome alimuuliza mtoto wake baada ya kusikia kuwa Mustapha hajarudi toka asubuhi na baada ya kuangalia saa yake na kugundua kuwa ilikuwa ni saa tisa alasiri.


"Simu yake iko chaji hapa dukani aliiacha baba hivyo hana mawasiliano yoyote yale."


"Ooohhh Mungu wangu nifanyie muujiza katika hili mwanangu asiingie kwenye mikono ya watoa roho za watu, mwanangu hebu wasiliana na rafiki zake wa karibu tujue yuko wapi."


"Sawa baba."

Victor alimjibu baba yake na kisha akakata simu na kumpigia rafiki yao ambaye mara nyingi huwa karibu sana na Mustapha. Kilichotokea ni taarifa iliyozua maswali kwani rafiki yao huyo alimwambia Victor kuwa walikuwa pamoja lakini kuna msichana mmoja ambaye sura yake ni ngeni na kumuita pembeni hapo waliongea kwa muda kidogo kisha Mustapha akaniaga kurejea muda si mrefu na kisha wakaondoka zao na mpaka sasa hawajarejea.


"Kwa hiyo hakusema anaelekea wapi?"

Victor alimuuliza rafiki yao huyo.


"Hapana Victor hakusema zaidi ya kuniambia kuwa atarejea."

Hapo hapo Victor alikata simu na kumpigia simu baba yake tena.


"Nipe ripoti mwanangu."

Mzee Jerome aliongea baada ya kupokea simu.


"Baba kaniambia kuwa walikuwa pamoja lakini baadaye aliondoka na msichana ambaye hakufahamika mara moja na toka muda huo hakurejea."


"Okay vizuri mwanangu bila shaka huyo ni mpenzi wake ni mtu mzima yule lolote litakalomwendea hovyo atatoa taarifa."

Mzee Jerome aliridhika baada ya majibu ya mtoto wake na kisha alirejea ndani kuungana na mke wake aliyekuwa roho juu kusubiri taarifa ya watoto wake.

Alimjulisha kila kitu alichoambiwa na mtoto wao pamoja na Daktari Abbas na hapo ndipo Bi Elizabeth alipochanganyikiwa kabisa na kuchukua simu yake ili awajulishe wakina Jackline kinachoendelea Namibia.


****


Baada ya kufika Nzega waliona wasiingie Tabora badala yake wakanyoosha kuelekea Igunga tageti yao ikiwa ni kuingia Singida na baadaye iwe Dodoma kwa ajili ya kukamilisha mambo yao machache yaliyo mbele yao kwani mpaka muda huo mzee Jonathan walikuwa naye kwenye gari akiwa kafungwa cheni za miguu na mikono huku machoni kapigwa kitambaa cheusi.

Kuna ujumbe uliingia kwenye simu ya Jackline akiwa nyuma ya usukani. Aliichukua simu na kumkabidhi Jessica aliyekuwa naye mbele ausome unataka nini kwani aliona mtumaji ni mzee Jerome.

Jessica aliichukua na kuifungua ile meseji, alitokwa na maneno mdomoni.


"What !!!!!!!!!!!!!!!!!"


"Nini Jessica mbona makelele?"

Jackline alimuuliza Jessica baada ya kuona kaitolea macho meseji ile.


"I can't believe that, mzee kakosea kutuma ama vipi?"

Jessica alibaki kuongea peke yake.


"Nini bwana nijuze mbona unaniweka kiroho juu?"

Jackline aliendelea kuuliza kutaka kujua kulikoni.


"Eti Daktari Ramadhan kauawa na watu wasiojulikana na si peke yake bali hata mtoto wake naye kisha wakautelekeza mwili wake nje geti la hospitali ya Makambi."


"Daktari Ramadhan kauawa? Mungu wangu hapo hakuna mwingine bali ni Santana na wenzake tusipokuwa makini tutapoteza watu wetu wa karibu wote."

Jackline aliongea hayo akifuta machozi kwa kiganja chake cha mkono.


"Jessica nakwambia siko tayari katika hili hata kidogo lazima tufanye jambo mapema."

Jackline aliapia katika hilo huku akiugonga gonga usukani.


"Ni kweli Jackline nahisi kitu hasa familia ya mzee wetu Jerome."


"Ndiyo, sijui hata nini kifanyike katika hili okay lakini bado tuna muda."


Waliendelea kuumiza vichwa kutokana na ujumbe huu walioupata kutoka Namibia na muda huu walikuwa ndiyo wanaiacha Igunga na sasa ilikuwa ni pori kwa pori. Simu ya Jackline iliita na muda huu mpigaji alikuwa ni Bi Elizabeth mke wa mzee Jerome.


" Nani huyo?"

Jackline alimuuliza Jessica.


"Ni mama Jerome."

Jessica alimjibu huku akimkabidhi simu.


"Ndiyo mama yangu shikamoo na pole na majukumu."

Jackline alianza kwa kumsabahi.


"Marahaba mwanangu, huku mambo si shwari kama mlivyoambiwa na baba yenu ila kuna jingine limezaliwa hapa."


"Lipi hilo mama?"


"Mdogo wenu Mustapha toka alipoondoka asubuhi hajarejea mpaka sasa na mbaya zaidi inasemekana aliondoka na msichana mmoja ambaye ni mgeni katika eneo letu."

Bi Elizabeth alifafanua.


"Mmejaribu kumtafuta hewani mama?"

Jackline alimuuliza Bi Elizabeth.


"Hewani wapi mwanangu, simu aliiacha dukani kwao ikichajiwa hivyo sijui kapatwa na nini huko?"

Bi Elizabeth aliendelea kutoa maelezo.


"Mama naomba punguza mawazo Mustapha ni mtu makini sana hivyo sidhani kama kuna lolote baya lililompata kikubwa tuendelee kumfuatilia tujue yuko wapi kwa sasa na pia wasijisahau kama ambavyo tulisema awali."

Jackline alimuuliza mama yao juu ya hilo japo hofu ilianza kumuingia.


" Sawa mwanangu, kwa hiyo mnakuja lini huku Jackline? "


" Ni ndani ya siku hizi nne mama yetu tuombe Mungu."

Jackline alimjibu mama yao huyo mlezi Bi Elizabeth.


Baada ya simu kukatwa Jackline aliipaki gari pembeni na kuteremka akifuatwa na Jessica, kwa kuwa walikuwa mbele ilibidi na wakina Roberto nao wasimame baada ya kuona wenzao wamesimama hivyo wakataka kujua kulikoni.


"Jackline kuna nini?"

Jasmine alimuuliza baada ya kumuona kakaa kwenye jiwe akiwa kajishika kichwa.


"Jasmine tuna muziki mnene mbele ya safari."


"Kwanini?"


"Daktari wetu aliyetuhudumia kule Makambi...."


"Nani? Daktari Ramadhan? Kafanya nini?"

Jasmine alimkatisha kwa maswali mfululizo.


"Kauawa yeye na mtoto wake na tayari kuna hofu kwa Mustapha kwani toka asubuhi hajarudi nyumbani na kwa mara ya mwisho alionekana na msichana ambaye ni mgeni pale Namport."

Jackline alifafanua.


"Jackline hakuna kuumiza kichwa juu ya hili huyu ni Santana hakuna mwingine."

Jasmine alimjibu Jackline pasipo kuwa na shaka yoyote ile.


"Inauma sana Jasmine hebu twendeni."

Jackline aliinuka na kuingia kwenye gari na kuondoka zake huku nyuma akifuatwa na wakina Jasmine na gari lao. Baada ya mwendo mrefu walifika mlima Sekenke mwinuko wenye historia kubwa sana kwa Jackline kutokana na kilichotokea miaka kadhaa nyuma. Hivyo walisimamisha magari na kushuka kisha Jackline aliwafuata wakina Jasmine ambao kwenye gari lao ndiyo walimbeba mzee Jonathan.


"Mshusheni huyo mzee."

Jackline aliagiza huku yeye akielekea kieneo ambacho inasemekana ndipo ilipotokea ajali ambayo ilichukua uhai wa wazazi wake wote yaani Bi & bwana Joachim. Hivyo walimshusha na kisha walimfungua kitambaa pamoja na zile cheni.


"Mzee Jonathan unalikumbuka eneo hili?"

Jackline alimuuliza akiwa juu ya jiwe huku mzee Jonathan akiwa kwenye jiwe jingine akiwa anatazama kule alikokuwa anatazama Jackline.


"Nalikumbuka vizuri sana eneo hili binti kwani ni eneo lililobeba historia kubwa ya rafiki yangu kipenzi...."

Mzee Jonathan aliongea.


"Unasemaje wewe? Umejiachia kabisa unasema rafiki yako kipenzi kweli? Huoni aibu mzee wewe?"

Jackline alimuijia juu mzee Jonathan Ubao.


"Kwanza naomba unisamehe mwanangu, najua unanichukia sana lakini kwa yote ambayo yalitokea hayawezi kubadili ukweli huu na utabaki kuwa hivyo."

Mzee Jonathan aliendelea kumwambia Jackline.


"Okay vizuri kwa kulitambua hilo na ndiyo maana nikaona nikulete eneo hili hili ambalo rafiki yako aliachana na uso wa dunia na sihitaji kingine zaidi ya kukuongoza kwa rafiki yako."

Jackline aliongea hayo akiwa kashikilia bastola yake ambayo alikuwa kaielekeza kwa mzee Jonathan.


" Jackline pamoja na kwamba Joachim alikuwa rafiki yangu enzi za uhai wake sijamaanisha na mimi nimfuate kwa njia ambayo unataka kuitumia."

Mzee Jonathan alianza kujitetea na huku akipiga magoti.


"Unanipangia cha kufanya siyo?"


"Hapana binti yangu sina uwezo wa kukuzuia kufanya kile ulichopanga kukifanya ninachokuomba ni kunipa nafasi nyingine ya kuishi niweze kukuthibitishia namna nilivyo mpya."


"Okay sawa nimekuelewa mzee Ubao lakini kwa sasa hebu ongea na hii kwanza ' pa pa paaaa'"

Zilisikika risasi ambazo zilikwenda moja kwa moja kwa mzee Jonathan na kumpeleka chini huku akiugulia maumivu kwa kilio baada ya risasi zile kutua kifuani na kichwani na kuifanya damu kutawanyika eneo lote lile ambalo alikuwepo. Walimchukua na kwenda naye mpaka kwenye gari la Jackline na kumfunga kamba shingoni na kuifunga kwa nyuma kwenye gari la Jackline kisha aliingia ndani na kuondoka kwa kasi kupandisha mlima huo wa Sekenke na baada ya kufika juu alirudi tena mpaka chini mpaka walipokuwa wenzake.

Sura yake, mavazi yake hayakutamanika hata kidogo kwani alikuwa kachakaa walimfungua tena na kumbeba tena mpaka kule bondeni ambako walimrusha huko huku Roberto akifuata na dumu lililokuwa na mafuta ya Petrol na kuyamwagia eneo lile kisha Jackline akapiga kiberiti moto ulilipuka. Wakati huo wote Jasmine alikuwa anarekodi matukio yote yaliyotokea hapo Mlimani Sekenke.

Hawakuondoka mpaka pale waliposhuhudia moto wa mwisho eneo lile na kuwa majivu hivyo Roberto na Jackline pamoja na Jasmine walisogea kuangalia mzee Jonathan yuko kwenye hali gani lakini kabla hawajafika ulisikika mlio mkubwa sana ambao uliwafanya warudi nyuma.


"Kwisha historia yake huyo, naona bichwa limejibu hapo."

Jasmine aliongea akiwa anarudi nyuma.


"Nenda zako mzee Jonathan, kisasi changu nimekimaliza kama ambavyo niliwaahidi wazazi wangu ni wakati wao sasa kumuhukumu kwa upande wao huko waliko, bila shaka mnachekelea wazazi wangu kwa kuwaletea mbaya wenu."

Jackline aliongea hayo kisha alipiga risasi za kutosha tena eneo lile huku akipiga makelele ambayo yaliwafanya waliokuwa wanapita eneo lile kushangaa.


" Twenzetu."

Jackline aliongea baada ya kuingia kwenye gari na muda huu Jackline alimpisha Jessica kuukalia usukani wa gari kwani Jackline hakuwa poa kwani mpaka hapo alikuwa bado analia.


JE, NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA KUJUA KINACHOFUATA BAADA YA KIFO CHA KIKATILI CHA MZEE JONATHAN.





Mpaka inafika usiku wa saa saba Mustapha alikuwa hajapatikana wala taarifa zake hali hii iliichanganya sana familia ya mzee Jerome hasa mke wake Bi Elizabeth ambaye alianza kutoa shutuma kwa mzee Jerome Whistle kuwaleta wakina Jackline kwake ambayo ndiyo chanzo cha yote hayo.


"Katika hili mume wangu katu huwezi kujitoa hata kidogo wewe ndiyo chanzo cha yote yanayotokea huwezi kuwaokota tu watu ambao hujui historia zao na kwanini wako majini? Kingine huoni kama wale mabinti wana laana mpaka kifo kinawaogopa huwezi ukuzamishwa Brazil na kuokolewa Namibia na bado mkaendelea kuishi."


"Unaongea nini Elizabeth? Hivi unafikiri ni muda muafaka wa kulalamikiana? Badala ya kujiuliza mwanetu yuko wapi muda huu wewe umekomaa na shutuma juu ya watoto wa watu umesahau kuwa ulikuwa namba moja kuwakaribisha baada ya kuuona msaada wao leo umeona nini?"

Mzee Jerome alimshukia mke wake baada ya kuona ni kama anataka kuvuka mipaka.


" Babu wee hata uongee nini sikuelewi hata nukta ninachokitaka hapa ni mwanangu tu haijalishi wamefanya nini hao Mbwa wako haiwezekani watu waendelee kupoteza maisha kisa wao, wamekuwa wakina nani? Na ninakuahidi kuwa iwapo mwanangu hata patikana nitauwasha moto usiozima hata kwa mitambo ya jeshi la Zimamoto."

Bi Elizabeth aliendelea kumtisha mume wake.


" Inatosha sasa mama unaongea vitu gani? Mbona umekuwa hivyo? Huu ni muda wa kumtafuta kaka hao unaowalaumu wako Tanzania na kaka kapotea huku huku Namibia na kingine mwanenu mnamfahamu vizuri sana hufanya maamuzi yake bila kushirikisha yeyote yule au umesahau kuwa ni mtu mzima yule?"

Victor alimaliza kwa kumtupia swali mama yake ambaye muda huo japo ilikuwa ni usiku wenye baridi kali lakini mama huyo alikuwa akitokwa na jasho lisilo na kikomo, huku akiwa hana kituo maalum mara aende huku arudi kule ilmradi tu kupata suluhisho la mwanaye Mustapha.


"Ngoja nipumzike kidogo kwani makelele haya hayataleta muafaka hata kidogo zaidi tuisikilizie kesho itakuwaje na iwapo itakuwa tofauti itabidi nikatoe ripoti polisi kwa msaada zaidi."

Mzee Jerome aliona amkatishe mke wake baada ya kuona hakuna hitimisho lolote kwenye hilo.


" Wewe jishaue tu lakini bado nitausimamia msimamo wangu, iwapo mwanangu hatapatikana nitalisimamisha jua kwa muda."

Aliongea hivyo na kumpita mume wake kwa kasi na kuelekea chumbani huku wakimuacha Victor sebuleni akiwa hajui lipi lifanyike kwa familia yake ambayo alihisi kupata mushkheri muda si mrefu. Alitulia pale sebuleni mpaka usingizi ulimpitia hapo hapo na kilichokuja kumshtua ni simu yake ambayo ilikuwa ikiita na baada ya kupokea ndipo alibaini kuwa mpigaji alikuwa ni Jackline kwani iliingia namba bila jina.


"Victor kuna usalama kweli hapo nyumbani?"

Jackline aliuliza.


"Mbona umetumia namba tofauti na niliyonayo hapa dada Jackline?"


"Hii ni yangu pia nimeona niitumie baada ya kuona nampigia baba lakini anaikata simu yangu."


"Anakata simu?"

Victor aliuliza kwa mshangao ambao ulikuwa wazi kabisa.


"Ndiyo nimempigia karibia mara nne hivyo lakini inafanywa hivyo hivyo ndiyo nikaona nitumie namba nyingine nikupigie wewe nijue kuna nini?"

Jackline alimfafanulia Victor.


"Kwa hiyo umenipigia kwa namba nyingine ukiamini na mimi nitakukatia simu dada Jackline?"

Victor alimuuliza Jackline.


"Ndivyo akili yangu ilivyonidanganya hivyo kutokana na matokeo ya awali."


"Sina uhakika kama baba kakukatia simu ila kutokana na mzozo wa masaa yaliyopita nahisi aliyefanya hivyo ni mama wala si baba."


"Kwanini afanye hivyo?"

Jackline aliuliza tena swali.


"Kifupi Mustapha hajaonekana kama ambavyo tuliwataarifu mpaka sasa kimya kabisa kitu hicho kimemuibua mama na kuonesha hasira za wazi juu yenu kuwa bila ninyi haya yote yanayotokea yasingetokea hivyo mpaka wanaingia kulala hakukuwa na maelewano yoyote."

Victor hakuona sababu ya kuendelea kumficha Jackline juu ya yale yanayotokea nyumbani.


" Yuko sahihi kabisa mama."

Jackline alimuunga mkono mama Victor.


" Kwanini unasema hivyo dada Jackline?"


" Victor acha tu lakini ninaimani yatapita tu kama ulivyopita upepo wa kisulisuli. Toka tuingie kwenye haya mapambano tumekuwa wabaya kutoka kwa watu wetu wa karibu kifupi hatujawahi pendwa zaidi ya kuchukiwa."


"Dada usiseme hivyo mbona baba na mimi bado tuko pamoja nanyi?"

Victor alimwambia Jackline baada ya kumsikia akilia wakati akiongea hayo, lakini hakukuwa na mrejesho wowote zaidi ya simu kukatwa bila kufikia muafaka. Hali hiyo ikamfanya Victor aangalie muda kwanza ajue ilikuwa ni saa ngapi na baada baada ya kuangalia akabaini kuwa ilikuwa ni saa kumi na mbili asubuhi hivyo aliinuka pale kochini na kuuendea mlango wa wazazi wake na kutaka kuugonga, mara ulifunguliwa kabla hajafanya vile.


"Vipi mbona mapema mlangoni kwetu Victor au kuna lolote umesikia juu ya kaka yako?"

Lilikuwa ni swali kutoka kwa mama yake mara baada ya kukutana mlangoni.


"Hapana mama yangu nimeona nije kutaka kuwajulia hali kwani siku ya jana hamkuondoka vizuri na pia nilitaka kuongea na baba."

Victor alitengeneza sentensi ambazo zisingekuwa kikwazo kwa mama yake ambaye hakujibu chochote zaidi ya kuurudisha mlango na kisha kumfuata mume wake na baada ya dakika chache alirejea pale na kumkuta Victor akiwa bado kasimama pale pale.


" Anakuja mwanaume mwenzako maana naona mmenitenga na kuamua kukaa vikao vya kunijadili, siyo mbaya ongezeni kasi lakini muda ukifika mtanitafuta wenyewe."

Bi Elizabeth aliongea hayo akimsukuma kidogo mtoto wake na kuelekea zake sebuleni tayari kwa kuiandaa asubuhi.


" Mwanangu huyo ni mama yako ambaye ulimfahamu miaka kadhaa nyuma hajabadilika bado hapa katikati aliamua kufanya maigizo tu kuna nini mbona asubuhi hivi?"

Mzee Jerome alimtuliza mwanaye ambaye alikuwa akimsindikiza mama yake kwa macho yenye maswali kibao.


" Naomba tuelekee kule bustanini tukaongee kidogo baba."

Victor alimwambia baba yake ambaye hakusita alirudi ndani akavalia koti huku chini akiwa na msuli wake kisha wakatoka nje.


"Baba kwanini ulimkatia simu dada Jackline? Ina maana umefikia hatua hiyo kweli?"

Victor hakutaka kupoteza muda wake alianza na maswali yake.


"Nimemkatia simu?"

Mzee Jerome alimuuliza swali mtoto wake huku akijipapasa mifuko ya koti lake na baada ya kubaini kuwa anachokitafuta hakioni aliondoka haraka kuelekea ndani ambako hakuchukua muda mrefu alirejea akiwa na simu mkononi akiwa anaipekuapekua.


" Ya ni kweli alinicheki Jackline na bila shaka huyu atakuwa ni mama yako tu aliyefanya huu upuuzi."

Mzee Jerome aliongea hayo huku akiieweka sikioni simu yake kuashiria kuna namba alikuwa ameipiga.


"Mmhh hapatikani hewani."

Aliongea hivyo mzee Jerome baada ya kutompata aliyempigia.


"Nani huyo?" Victor alimuuliza baba yake.


"Nilimpigia Jackline kutaka kuongea naye na kumtoa hofu juu ya kilichotokea."

Mzee Jerome alimjibu mtoto wake.


"Usijali baba katika hili nitaongea naye mwenyewe na nitamuweka wazi hili wewe kawekane sawa na mama kwani nina hofu na maneno yake."


"Sawa mwanangu fanya hivyo basi wacha mimi nimfuate mama yako ndani."

Mzee Jerome alijibu na kuondoka kurudi ndani huku mtoto wake Victor akiondoka kuelekea zilizokuwa gari bila shaka alikuwa anatoka nje ya nyumba yao.


****


"Jamani ee hali si shwari Namibia kwani kutokana na yaliyotokea na kuendelea kutokea mama yetu katubebesha zigo la lawama na hakuliki hapo home kwani fikiria mpaka nakatiwa simu."

Jackline aliwaambia wenzake mara baada ya kuachana na Victor.


"Nadhani jambo la msingi ni kufika huko na kuanza michakato yetu, hao tukutane baadaye na ikiwezekana tusiwataarifu kuwa tunaikaribia Namibia ila sisi tutafanya kazi ya kupambana na wabaya wetu ikiwa ni pamoja na kuwalinda pasipo wao kujua kama tunafanya hivyo."

Jasmine alimjibu Jackline baada ya kuona kuna tatizo baina yao na familia ya mzee Jerome hasa Bi Elizabeth.


" Ni kweli kabisa Jasmine."

Roberto aliunga mkono hoja hiyo.


" Jessica naomba ufanye shughuli yako ikiwa ni pamoja na kunasa mawasiliano ambayo yalifanywa kwa mzee Jerome, mke wake na watoto wao najua hapo tutapata pa kuanzia au mnasemaje makamanda?"

Jackline alimtaka Jessica afanye kazi yake na kisha aliwauliza wenzake juu ya plani yake hiyo ambayo haikupingwa na mtu yeyote zaidi ya kuungwa mkono na wote. Hayo walikuwa wakiyapanga ndani ya ndege ya South Airways' ya nchini Namibia ambayo hufanya safari zake kati ya Tanzania na nchi za kusini mwa Afrika. Hawakuwa na muda wa kupoteza kwani mara baada ya kufika jijini Dodoma waliweza kila kitu sawa ndani ya jumba la Jackline na nyaraka nyingine zilikabidhiwa kwa mwanasheria wake aishiye nchini Afrika ya Kusini si unajua tena siku hizi Dunia imekuwa kijiji kila kitu Mtandaoni na kisha waliondoka kuelekea jijini Dar es Salaam ambako waliwasili asubuhi sana na kuondoka zao na ndege hiyo ya South Airways ambayo ilitokea Zanzibar na kisha kuanza kulitafuta anga la Namibia.


"Kwa hiyo tutafikia wapi jamani?"

Roberto aliuliza baada ya kusikia kuwa kuna tatizo na sehemu ambayo waliishi awali wakiwa kwenye matibabu.


"Tutafikia pale pale Namport lakini tutakuwa kwenye Hotel yoyote ambayo ni ya Hadhi yetu."

Jackline alimjibu Roberto.


"Nafikiri 'The Camel Hotel' ni mahali poa sana kwa ajili yetu."

Jessica alitoa pendekezo lake.


"Ni ipi hiyo Hotel?"

Jasmine alimuuliza mdogo wake.


"Si ile ambayo inatazamana na ile kampuni ya kuuza magari?"

Jessica aliwaelekeza wenzake inakopatikana hiyo Hotel.


"Mmhh kweli bwana ile ndiyo yenyewe itatukaa kwa kipindi chote cha oparesheni yetu."

Jackline aliungana na Jessica kufikia kwenye hotel hiyo ya 'The Camel Hotel' ambayo iko karibu na Kampuni ya uuzaji magari ya mjini Namport.

Na baada ya masaa kadhaa ya kuwa angani hatimaye waliwasili Namibia na haraka sana walichukua gari ndogo ambayo inafanya kazi ya kusafirisha abiria wanaokodi maarufu kwa jina la Taxi na kuitaka iwapeleke mpaka Namport kutoka Windhoek kwani waliamini huko ndiko kutatoa majibu ya kazi yao.


"Kuna vitu vya kufanya kabla ya kufika last point?"

Jasmine aliwauliza wenzake mara baada ya kuwasili Namport.


"Tukapate chakula kwani hapa mwenzenu nina njaa sana na pia tunatakiwa kufanya manunuzi ya vitu vya kutusaidia maskani."

Jackline alijibu haraka na kisha alimtaka dereva huyo awashushe Kabega Supermarket kwani hawakutaka dereva huyo ajue ni wapi wanakoelekea kwa sababu hawajui ni nani ni mzuri au mbaya kwao.


" Kwanini tumeshukia hapa?"

Jessica alimuuliza Jackline mara baada ya kushuka.


" Ni kumzingua dereva Taxi ili asijue tunafikia Hotel ipi na sisi ni watu gani si unajua tena tuna maadui kila kona."

Jackline alijibu huku akibeba begi lake huku na wakina Roberto nao wakafanya hivyo na kuiita Taxi nyingine ambayo hiyo iliwapeleka mpaka kwenye lango la Kampuni ya magari kisha wakatembea kwa mguu mpaka kwenye hotel hiyo ya 'The Camel Hotel' na kufanya booking ya vyumba na baada ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa walielekea sehemu ya Restaurant kwa ajili ya chakula na muda huo ilikuwa tayari ni saa kumi na moja ya jioni. Wakiwa pale wanapata chakula chao mara Roberto alimuona mrembo mmoja akiwa kakaa kwenye meza ya pembeni akiwa anaongea na simu kilichomchanganya ni namna alivyokuwa anaongea na simu kwani alikuwa akiongea huku kauziba mdomo wake uelekeo wa wakina Roberto akiwa anawaangalia kwa macho ya kuibia hivi hiyo ilimfanya Roberto ainuke na kuelekea kule alikokuwa yule mrembo ambaye hakufahamika ni nani na alikuwa akiwasiliana na nani.


MREMBO HUYO NI NANI?

NA VIPI KUHUSU MUSTAPHA ATAPATIKANA AKIWA HAI?


ILI KUPATA MAJIBU YA MASWALI HAYA NA MENGINE MENGI TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAFUATA YA HADITHI HII.





Roberto alimpita na kuwa kama anaelekea chooni alipofika kwenye korido alibana hapo na kumtumia ujumbe Jasmine.


"Huyo binti aliye mbele yako ni kama anatufuatilia hivyo kuweni makini naye na huyu ndiye atakuwa chambo chetu."


Jasmine baada ya kuusoma ujumbe huo alimtazama yule binti na kumuona hivyo hakuongea chochote pale kwani alijua Jackline akilijua hili lazima atafanya jambo, akaona amtumie ujumbe Roberto.


" Tunafanyaje hapa sasa mtu wangu?"


" Hiyo kazi naimaliza mwenyewe niachie."


"Poa."


Roberto alijisogeza karibu zaidi na nguzo ambayo inamtenganisha na huyo dada na kisha alijibana hapo.


"Ndiyo ni wenyewe kabisa ila tu idadi yao ndiyo inanitia shaka hapa wako mabinti wanne na mwanaume mmoja."

Alionekana akiongea na simu upande wa pili huyo dada.


"Na mimi nimechukua chumba kwenye hotel hii hii ya 'The Camel Hotel' nashangaa ninapoingia Restaurant nawakuta hawa viumbe, niko chumba namba 107 utanikuta tu."

Alipomaliza kuongea hayo aliinua glasi ya juisi akakata yote akaiweka mezani akainuka na kuondoka zake. Hiyo ikawa nafasi kwa Roberto kumfuata kwa nyuma lakini kabla haufikia mlango wa kutokea nje akashtukia anashikwa bega ikabidi ageuke kumwangalia aliyemshika.


"Mbona sikuelewi Roberto toka tumeingia humu uko bize na yule mwanamke na sasa unataka kumfuata anakokwenda?"

Titiana aliona amfuate baada ya kuona imekuwa too much' na hivyo kuufanya uchunguzi wake kuishia njiani.


"Baby kuna kitu nakifuatilia si mtu wa kawaida ni kama anatufuatilia hivi."


"Kiachie kivuli cha kazi yenu, usikitumie kama kinga Roberto kumbuka ahadi yetu."


"Kwa hiyo hauniamini Tity si ndiyo?"

Roberto alimuuliza huku alirejea walipokuwa wakina Jackline na kuketi huku macho yake pima kwa Titiana aliyekuja naye na kuketi.


"Jamani kulikoni tena?"

Jackline aliuliza swali.


"Sijui Tity anataka nini? Naona kashadadia jambo ambalo halina maana."

Roberto alimjibu huku akiinuka na kutoka zake.


"Nikiwa kama mke wivu lazima mtu gani toka tuingie humu macho yote kwa yule mwanamke aliyekuwa pale anatoka naye anataka kumfuata nyuma nikae tu naangalia, haiwezekani jamani."

Titiana aliwaka na wote wakajikuta wakimtolea macho tu wasijue waongee nini kwani hawajawahi kumuona Titiana kwenye hali hiyo.


" Hebu jitulize mdogo wangu Roberto ninayefahamu mimi si mambo hayo kwa vyovyote vile kuna jambo hapo namfahamu vizuri Roberto hebu tumsubiri arudi."

Jackline aliamua kumtuliza Titiana aliyekuwa kavurugwa tayari na Roberto.


"Ni kweli hata mimi sikumbuki kama hilo limewahi kutokea bila shaka kuna kitu anakifuatilia hapo tusubiri kwanza."

Jessica aliungana na Jackline kumtetea Roberto huku Jasmine akiwaangalia tu ndipo alipoamua kukata mzizi wa fitina kwa kuwaonesha ujumbe ambao alitumiwa na Roberto kabla ndipo kila mmoja akapumua hasa Titiana aliyekuwa kuwa kafura kwa hasira.


" Sasa si angeniambia kuliko kuondoka tu bila kulijenga?"

Titiana aliongea akikaa vizuri kitini.


"Lazima kamfuata yule msichana, hapa cha kufanya ni kumfuatilia kwa nyuma."

Jackline aliongea hayo baada ya kuona hatokei Roberto.


"Hapana tumsubiri hapa hapa atatuletea majibu yake."

Jasmine aliwatuliza wenzake ambao walionekana kuwa kasi kwenye hili.


Roberto baada ya kutoka nje hakuweza kujua yule msichana kaelekea wapi hivyo akaona njia pekee ni kukifuata kile chumba namba 107 na alipokiona kilipo alitoka na kuelekea mapokezi ambako alimuwekea shilingi elfu ishirini mezani mhudumu yule kisha akamweleza shida yake.


"Sorry madam, naweza kupata jina la mgeni aliyeingia chumba namba 107 tafadhali?"

Yule mhudumu bila kujibu chochote aliichukua ile hela na kuiweka kwenye mfuko wake wa koti kisha kumfunulia kitabu cha wageni ambapo moja kwa moja Roberto aliifuata namba ile na kisha kuangalia lile jina na hapo ndipo alipobaini kuwa ni Carolina Oklam hakuwa na kingine zaidi ya kuichukua namba ya simu na kuachana na jina kwani alijua watu kama hawa hudanganya taarifa.


"Asante sana madam ila naomba taarifa zake kila umuonapo akiingia au kutoka nje ya chumba chake."

Roberto alimuomba mhudumu huyo ambaye akiwa na sura ya furaha alimjibu kwa kutikisa kichwa tu Roberto alimuelewa kisha akaondoka zake.


"Nani mwenzangu?"

Yule msichana aliuliza baada ya kupokea simu iliyopigwa na Roberto.


"Naitwa Gift."

Roberto alijitambulisha


"Gift gani huyo, mbona sikufahamu."


"Hunifahamu? Mimi mbona nakufahamu vizuri sana na hata hii namba ulinipa wewe mwenyewe siku kadhaa nyuma."

Roberto aliendelea kumchezea msichana yule.


"Hapana sikumbuki hata kidogo."

Alivyomjibu hivyo alimkatia simu. Roberto hakuchoka alimuandikia ujumbe.


"Kama hutojali lakini naomba tuonane leo labda ukiniona utanikumbuka tu."


Baada ya dakika chache alijibu ujumbe huo.


"Okay sehemu gani hiyo tuonane?"


"Chagua wewe."

Roberto alimjibu.


"Okay fanya hivi leo usiku mida ya saa tatu usiku nitakuwa pale TSWANAH NIGHT CLUB ni sehemu tulivu sana."


"Kumbe vizuri nitafika muda huo."


"Poa."

Alijibu msichana yule.


"Umekwisha mrembo."

Roberto alijisemesha mwenyewe huku akirusha mikono juu na kurejea kuungana na wenzake.


"Lete matokeo ninja wetu."

Jasmine alimuanza Roberto.


"Mambo freshi kabisa nimeongea naye na tumekubaliana kuwa tuonane TSWANA NIGHT CLUB."


"Si mnaona nilikwambia mimi."

Titiana aliibuka na kuongea hayo.


"Ulituambia nini Titiana?"

Jackline alimuuliza.


"Muulizeni yeye hiyo namba kaitoa wapi mpaka wamewasiliana kwenye simu?"

Titiana aliendelea kuonesha wivu wa wazi kabisa.


"Mpenzi wangu, punguza wivu kila kitu nimekipata kwa mhudumu wa Hotel cha kushangaza tunaye humu humu Hotelini ila tu alitangulia siku kadhaa nyuma."


"Nimekuelewa kipenzi lakini wivu ni lazima hilo nielewe wangu."

Titiana alijitetea kitu kilichopelekea wakina Jackline kuangua kicheko.


"Si tulikuambia Titiana hili ni jembe la kazi muda wowote liko active' halichagui ardhi."

Jasmine alommwagia sifa Roberto.


"Tupe mpango."

Jackline alimtaka Roberto awape kile alichokipanga kichwani kuhusiana na usiku huo.


"Tutakwenda wote lakini ninyi mtakuwa kwenye gari jingine na mimi nitakuwa kivyangu ili iwe rahisi kumnasa, na ninyi hamtaingia ndani mtabaki nje mpaka pale nitakapowatumia ujumbe kuwajulisha kinachoendelea ndipo mtaingia."


"Hiyo imekaa vizuri nafikiri muda huu tukajipumzishe kidogo kusubiri muda huo wa kumnasa panyabuku wetu."

Jackline alikubaliana na maelezo ya Roberto na hivyo kuwataka wakapate pumziko la muda.


Ulipofika usiku wa saa mbili Roberto alitoka na kukifuata chumba alichopanga Carolina kama alivyoandika kwenye kitabu. Alikifikia chumba na kuchungulia ndani kupitia tundu la kitasa ila hakuweza kuona vizuri kwa kuwa kulikuwa na ufunguo kwa ndani.


"Shiiiiiiiit...."

Alijisemea mwenyewe. Lakini katika hangaika haingaka alimuona kwa mbali akiwa anapaka mafuta japo kwa shida sana.


Aliondoka na kuchukua simu yake kisha akamtumia ujumbe mfupi.


"Nimefika mapema, nakusubiria wewe tu."


"Umeishi Ulaya nini maana si kwa kuwahi huko."

Aliujibu ujumbe huo na hapo Roberto akajua muda si mrefu atatoka akajificha kwenye korido la upande wa pili. Mara mlango ulifunguliwa akatoka na kuondoka haraka huku nyuma Roberto aliutekenya mlango ukakubali kwa masterkey zake akazama ndani na kuufunga kwa ndani. Akiwa ameanza kukikagua kile chumba mara mlango uliguswa kitendo kile kilimfanya Roberto kujificha uvunguni haraka na Carolina aliingia ndani akiwa anaongea na simu.


"Unajua nini bosi kuna mtu kajitambulisha kwa jina Gift anasema tunafahamiana."

Akawa kimya akimsilikiza anayeongea kwenye simu.


"Ndiyo lakini nina mashaka namba yangu yangu aliitoa wapi? Kwa tahadhari nipatiwe vijana wawili wa kunipa sapoti japo najiamini."

Alikata simu kisha akaiweka kitandani na kuvuta droo ya kitanda akatoa bastola na kuiweka kiunoni kwake akalivaa koti lake akaichukua simu yake na kutoka zake huku chini Roberto aliizima kabisa simu yake kuhofia kuita kisha kubainika.

Alipohakikisha kila kitu kiko poa kabisa alitoka uvunguni na kuiwasha kisha akawatumia ujumbe wakina Jackline.


"Kule tunakwenda kwa tahadhari kubwa kwani wameishtukia issue hivyo wamejipanga."

Akaiweka simu mfukoni akatekenya loki ya droo ya kitanda kisha akapekuwa na kukuta kikaratasi kidogo kilichokuwa na maandishi mengi kidogo yaliyochanganywa na ili uweze kuyasoma ni lazima uwe umepitia elimu hiyo ya maandishi ya siri. Alikiangalia akaona hakuna anachokielewa akakirushia pembeni na kuendelea na kazi yake ndipo alipokutana na kikasha kidogo kikiwa kimefungwa na kikufuli hapo akahisi kitu ndani yake ndipo haraka sana akakichukua na kufunga ile droo akauendea mlango lakini akakikumbuka tena kile kikaratasi akakichukua na kutoka zake. Alimfuata yule mhudumu pale mapokezi na kumuomba kitu.


"Hivi mmefunga kamera kwenye vyumba vyenu?"


"Kwanini kaka umeuliza hivyo?"


"Nataka kujua tu dada yangu."


"Kwa Hotel kama hii inakosaje CCTV Camera?"

Yule mhudumu alijibu kwa madaha yote bila kujua majibu yale hayakuwa mazuri kwa upande wa Roberto.


"Okay sawa."

Alijibu lakini akionekana kukuna kichwa kitu kilichomshtua yule mhudumu.


"Kama kuna kinachokusumbua niambie nikusaidie."


"Hapana hakuna kitu ngoja niende."

Alijibu akiiangalia saa yake na kuishia zake. Baada ya kufika chumbani kwa Jackline alimuonesha kile kisanduku na ile karatasi ajabu Jackline aliisoma haraka sana na ilikuwa na ujumbe huu;- "HUYO DOGO AONDOLEWE HAPO NA APELEKWE KWENYE YALE MAJENGO CHAKAVU YA KULE UFUKWENI GEZRA HAPO USALAMA SI MKUBWA SANA."


Baada ya kuusoma Jackline alimgeukia Roberto na kumwambia.


"Huyu si mwingine bali ni Mustapha tu."


"Tunafanyaje sasa hapo?"


"Waite wakina Jasmine tupangane hapa."

ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog