Simulizi : Nitakuua Mwenyewe
Sehemu Ya : Tatu (3)
Aliondoka na kutoka nje na timu yake nayo ilimfuata nyuma bwana Santana.
Mjini Rio Branco pilika ziliendelea kama kawaida kwa majiji makubwa kila unayekutana yuko bize na shughuli zake ziwe za halali au siyo za halali ni juu yake tofauti na kwenye vimiji vidogo dogo au uswahilini mtu akimiliki tu hata luninga au redio ndani mtamkoma na kuipata shughuli yake kwani muziki utakaofunguliwa hapo ni shida na itokee siku kadhaa nyuma walikwaruzana oohh utatamani usafiri kwa muda hasa hawa dada zetu na mama zetu hatari faya, ingekuwa ni ushauri wangu mimi ningewashauri spika nyingine ziwe zinakaa nje ili tuburudike vizuri maana huko ndani unajitesa mwenyewe kwani muziki unapopiga kwenye vispika vya sabufa vipanya vinaanguka anguka chini mara vimemdondokea mgeni mara mavi yao kwenye chakula inakuwa ni fulu tafrani. Mchina naye kama alizifahamu vurugu zetu alituletea visabufa vyenye majina ya babu zao huko ambao waliokufa wakinuna tu huko makaburini utasikia sabufa imebadili mlio na kuwa wa sadebe yaani acha tu lakini kwenye miji ya wenyewe raha tu unaweza usione jirani kaingia muda gani na katoka muda gani ni mwendo wa malengo tu. Roberto naye alikuwa ndiyo anatoka nyumbani kwake nyumba ambayo wakina Jackline waliinunua na kumkabidhi aishi na mama yake pindi akiruhusiwa kutoka hospitali na wakamwelekeza baadhi ya vyumba kama vitatu vitakuwa ni vya kwao wao wanapotoka kwenye mishe zao basi watakuwa wanafikia hapo kifupi ilikuwa ni ya kina Jackline hiyo nyumba na zile pesa walizifungia kwenye chumba kimojawapo ila walikoziweka ilikuwa ni juu kwenye ceiling board' baada ya kuziweka kwenye sanduku la chumba.
Hivyo Roberto alikuwa anawahi hospitalini kumjulia hali kisha aendelee na mishe nyingine. Lakini kilichokuwa kikimtatiza ni vile ambavyo wakina Jackline walikuwa hawapokei simu yake hilo lilimpa wasiwasi kiasi cha kuamua awahi hospitalini kisha ajaribu kuwatraki ajue wako wapi.
Alifika hospitali akamjulia hali mama yake anaendeleaje toka alivyomuacha na alizopatiwa kwani wakina Jackline walilipia gharama zote za matibabu hivyo daktari alimwelekeza hatua waliyofikia mpaka wakati huo.
"Nikushukuru mtaalam wangu kwa nguvu mnayoitumia kumpigania mama yangu."
"Ni wajibu wetu kufanya hivyo labda tu ujitahidi kuwa naye karibu ili kumpa faraja si unajua tena."
"Ni kweli kabisa daktari nitajitahidi kufanya hivyo."
Alijibu macho yakiwa kwenye simu kuona kama wanampigia wakina Jackline. Alitoka kwa daktari na kwenda kumuaga mama yake.
"Mama naomba nikuache kidogo nikawatafute wakina dada maana naona simu yao inaita tu bila kupokelewa unaweza kuona wamepata tatizo huko waliko."
Muda anaongea hayo mama yake alikuwa kalala kitambo ila tu wenzetu huamini kuwa kwenye utulivu kama huo mtu huwa anasikia vizuri tu na ndiyo maana alikuwa akimuaga hivyo hivyo.
Aliwasha GPS yake akaitraki namba ya Jackline ili aweze kujua waliko, ndani ya dakika sifuri tayari ilimuonesha location' haraka aliingia kwenye basi na kuelekea huko huku simu yake ikiwa on kwenye GPS na baada ya muda fulani aliwasili eneo hilo na kuelekea mpaka kwenye nyumba ya Melissa ambapo ndipo ilimuonesha kuwa wapo hapo hivyo aliisogelea nyumba hiyo na kupiga hodi kwa kutumia kengele ya umeme ambayo switch yake ilikuwa kwa nje. Alibonyeza na kubonyeza lakini hakuna aliyejitokeza kuufungua mlango Mahali kitu ambacho kilimshangaza sana.
"Simu hawapokei nimefika sehemu ambayo naamini ndipo walipo lakini ajabu napo pia hata mlango hawafungui kuna nini?"
Alijiuliza Roberto maswali ambayo hayakuwa na majibu, hivyo aliamua kuzunguka kwa nyuma ili aruke ukuta ambao si mrefu halafu yeye mwenyewe mtoto wa mjini vitu kama hivyo kwake ni vya kawaida sana aliruka ukuta na kutua ndani ambako huko aliambaa na ukuta wa nyumba mpaka kwenye kila dirisha hapo alikuwa akichungulia ndani kupitia kila dirisha tena kwa tahadhari kubwa na baada ya kufika kwenye dirisha la sebuleni ndipo alipokutana na vitu vilivyompa maswali.
Ni vitu gani hivyo?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA..
Baada ya kuhitimu kidato cha nne katika shule ya Sekondari Lupa Shamimu Fikirini alirejea nyumbani kwa mzee Kaaya kama ambavyo Jackline aliomba ndivyo ambavyo mzee Kaaya alifanya kwa mdogo wake, tokea waondoke kwenda nje ya nchi mzee Kaaya aliendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha Shamimu anapata mahitaji yake yote ya msingi kama mwanafunzi na Mungu saidia mpaka anahitimu hakuacha deni shuleni kitendo ambacho mzee Kaaya alipongezwa na uongozi wa shule hiyo kwani kwa mwingine angeweza kutelekeza majukumu yake.
"Karibu nyumbani mwanetu Shamimu."
Mama Robinson alimkaribisha akiwa anampokea begi.
"Asante mama nimekaribia."
Shamimu alijibu.
"Karibu sana."
"Asante mama nashukuru."
"Angalia chumba chako kama kiko vizuri si unajua tena na uzee huu nilikuwa sikihudumii kwa wakati."
"Usijali mama nitakifanyia usafi tu. Shamimu alijibu.
" Pumzika na mimi niko jikoni nikiendelea kuandaa chakula cha jioni."
"Mama bwana unapika chakula gani hicho mbona muda bado sana si ni saa kumi na mbili hii?"
"Ni kweli mwanangu nimeona niandae mapema ili muda ukifika iwe ni kula tu kwa utulivu si kuanza kutoa mijasho jikoni."
"Ni kweli kabisa mama sasa wewe kaa pembeni mwanao nimerudi hii kazi yangu."
"Hapana wewe kakiandae chumba chako usije lalia nyoka bure na kuhusu kupika wewe utaanza kesho au umesahau kama wewe ni mgeni leo?"
"Mama nawe mgeni wa wapi mimi? Basi wacha nikafanye usafi."
"Hayo ndiyo maneno mwanangu."
Shamimu aliingia chumbani kwake kufanya usafi huku akimuacha mama yake jikoni akiendelea kupika chakula kwa ajili ya jioni.
Alianza kufanya usafi wa chumba kile huku akiangalia kikae katika mkao gani ambao ataupenda.
Aliendelea kuumiza kichwa mpaka baadaye akaona atulie kwanza kitandani hapo ambapo alijilaza na kwa kuwa usingizi hauna adabu ulimchukua hapo hapo bila kumuacha amalizie shughuli yake ya usafi kwanza.
"Mambo shemeji yangu kipenzi."
Robinson alimsalimu Shamimu.
Shamimu alikuwa kajiachia mwenyewe akiwa kama alivyozaliwa akisugua miguu yake kwenye jiwe huku sehemu za nyuma zikitikisika akijua yuko peke yake pale mtoni Lupa.
"Shemeji umefuata nini huku mtoni." Shamimu alijibu huku akiwa kajirushia kwenye maji ili ajisitiri.
"Aahhh shemeji Shamy ni swali kweli hilo?"
Robinson alisogea mpaka alipokuwa kaweka nguo zake Shamimu na kuketi.
"Hivi kwa mfano dada anatokea hapa unafikiri itakuwaje shemeji?"
"Na kwa kuwa ni mfano haiwezi kutokea shemeji yangu."
Robinson alijibu huku akiziangalia nguo za Shamimu.
"Shemeji acha basi mambo yako sipendi naomba uondoke nivae nguo."
"Au nikuletee kabisa shemeji yangu kipenzi, unajua nini shemeji yangu nimeona nikufuate huku huku mtoni nije nikueleze hisia zangu juu yako mtoto mrembo kama wewe uliyeumbwa ukaumbika kwanini nisikufuate popote ulipo? Wewe ni sawa na pafyumu mpenzi."
Na muda huo alikuwa akiinusa kufuli ya Shamimu.
" Hivi unajua sikuelewi kabisa shemeji? "
" Kwa sasa huwezi kunielewa ila muda si mrefu utanielewa tu shemeji."
Aliweka chini ile kufuli ya Shamimu na kisha alisimama na kuanza kuvua nguo zake ambapo kitendo kile kilimfanya Shamimu afiche macho yake kwa mikono yake ili asione shemeji yake anataka kufanya nini. Alipomaliza kuvua nguo zote ndipo Shamimu akajua kuwa shemeji yake alikuwa kadhamiria kweli na hapo ikabidi apige mbizi kuelekea upande wa pili, lakini Robinson naye alianza kuogelea kumfuata kule kule, Shamimu alijitahidi kwa uwezo wake wote kuogelea kuhakikisha anamshinda shemeji yake huyo. Lakini ilikuwa kazi bure kwani alishtukia akidakwa miguu kwa nyuma.
"Shemeji niachie haraka kabla sijapiga kelele."
"Piga tu kama unafikiri itakusaidia shemeji."
Robinson alionekana kadhamiria kufanya jambo kwa shemeji Shamimu ambaye muda huo alianza kupiga kelele lakini ajabu ilikuwa pamoja na kupiga kelele hizo watu walikuwa wakiendelea na shughuli zao wanakuja wanachotaka maji na kuondoka zao kama hawajaona kitu vile.
"Si umeona eee ndiyo ujue hakuna mwenye shida na makelele yako hivyo ni bora utulie shemeji yako nile vyangu humu humu majini."
"Nimesema niachie huko sitakiiiiii...." Safari
hii Shamimu alifanikiwa kumsukuma Robinson kwa miguu yake ile ile na kumfanya aanguke chali na kumpa nafasi Shamimu ya kukimbia lakini alipaniwa kwani hakufika mbali kwani alipigwa bonge la mtama uliompeleka chini na kuangukia kwenye majani nje kidogo ya mto na kisha Robinson alimfuata kwa juu lakini akiwa anahangaika pale juu mara walisikia sauti ikiita.
"Shamimu, Shamimu, Shamimuuuuuuu." Ile kugeuka hawakuamini macho yao hakuwa mwingine alikuwa ni Jackline, nguvu zilimwisha Robinson akajivuta na kutoa nafasi kwa Shamimu kuweza kumsukuma pembeni.
"Shamimu, Shamimu........."
Alishtuka baada ya kuona anatikiswa mabegani mwake huku macho yakiwa yamemtoka.
"Maamaaaaa...." Aliita.
"Bee mwanangu,inaonekana ulikuwa umechoka sana maana si kwa usingizi huo nimeita na kuita wapiiiiii."
"Nisamehe mama inawezekana ni uchovu tu wa wiki mbili za mitihani."
"Amka sasa ukajimwagie maji ya baridi mwili upate nguvu na kwa kuwa usafi haujafanya itabidi ulale sebuleni ili kesho ndiyo uamkie usafi. Na baba yako kafika tayari."
"Sawa mama."
Mama yake mlezi ambaye ni mama yake Robinson aliondoka na kumuacha Shamimu akijinyooshanyoosha viungo vyake aliinuka na kujikagua vizuri kisha alikaa tena kitandani na kujishika mashavu.
"Hivi hii ndoto ina maanisha nini kwangu, yaani shemeji atake kuniingilia bila idhini yangu? Kuna nini huko waliko? Kuna usalama kweli?"
Shamimu alijiuliza huku akiinuka kutoka nje ya chumba kile.
"Mwanangu Shamimu umerudi mama?"
Mzee Kaaya aliuliza baada ya kumuona Shamimu akipita pale sebuleni.
"Ndiyo baba nimerudi tayari na hii ni baada ya kukamilisha kila kitu pale shule na kwa sababu ni jirani sikutaka kuendelea kuwepo pale shuleni."
"Umefanya jambo la maana sana Shamimu na bila shaka ungependa kujua kinachoendelea kule kituoni."
"Ni kwe..." Kabla hajamalizia neno lake mama aliingilia kati.
"Baba Robinson muache kwanza mtoto akaoge kisha hayo mengine yataendelea."
"Ohh basi sawa, kaoge kwanza mwanangu."
"Sawa baba."
Shamimu alitoka na kuelekea jikoni kuchukua maji kisha akaingia bafuni kuoga.
*******
Wakiwa na furaha ya ajabu baada ya kufanikiwa kuwatupa majini wakina Jackline, wakina Robinson walirejea kambini wakiwa wanapiga kelele za shangwe.
"Kuna nini vijana wangu?"
Mzee Bruno Gautier aliuliza baada ya kuwasikia wakina Chude wakipiga makelele ya furaha.
"Kwanza kabisa pole sana Bruno kwa kurejewa na hali ya kawaida wewe na wenzako wakina Tom."
Chude alianza kwa kumpa pole mzee Bruno Gautier.
"Asante sana kijana wangu. Kumetokea nini huko mpaka mje na mikelele yenu hapa?"
"Mzee tumefanikiwa leo kukiteketeza kizazi jeuri, kizazi cha ajabu ambacho ndani ya muda mfupi kimepelekea hasara na mambo kwenda kombo ndani ya makampuni yetu ikiwa ni pamoja na kumteka mke wa bosi wetu."
Chude aliendelea kufafanua.
"Weeeeee usiniletee mashairi yako yasiyo na kichwa wala miguu hapa unataka kunieleza nini nikuelewe maana unakoelekea usiniambie kuwa mmewaua wale mabinti."
"Ndiyo hivyo mzee unauliza tena juu ya hilo pigia mstari maana kwa muda huu nahisi misamaki itakuwa ndiyo inamalizia mifupa yao." Robinson naye aliongezea kwenye maelezo ya Chude.
"Na mke wangu je amepatikana?"
Aliuliza mzee Bruno Gautier.
"Tumefikia hatua nzuri mzee Bruno kwani mpaka sasa simu iliyokuwa ikitumiwa na wakina Jackline tayari tunayo mikononi mwetu na kesho tutakuwa eneo alilofungiwa mkeo kwa msaada wa Melissa."
Santana aliingilia mazungumzo yale ya wakina Chude na mzee Bruno.
"Naweza kuipata hiyo simu ili nianze muda huu kuyatafuta mawasiliano hayo."
"Mbona una haraka mzee Bruno kila kitu kinakwenda kwa utaratibu mzee wangu, elewa kuwa baada ya kila kukamilika kifuatacho ni kushughulikia suala la mke wako."
Santana aliendelea kufafanua zaidi.
Lakini mzee Bruno ni kama vile hakuridhishwa na namna mambo yalivyoendeshwa haraka vile hivyo kwa hasira aliamua kuondoka na kuingia ndani kulala.
" Hebu niambieni ina maana Jasmine, Jackline na Jessica mmefanikisha kuwaua?"
Melissa aliuliza swali hilo baada ya kusikia malumbano yale hivyo akaona amuulize Robinson.
"Ni kweli kabisa Melissa, inavyoonekana ile sumu iliwadhuru sana kiasi cha kutozinduka tena kama ninyi na hivyo bosi akaagiza tukawatupe ndani ya bahari kwani hakutaka kuona kitu chochote kitakachobakia kama ukumbusho wao kwake."
Robinson alimfafanulia Melissa kilichotokea siku leo na kabla.
" Aisee pole zao marafiki zangu najua huko waliko watakuwa wananichukia sana mimi ila tu naomba wanisamehe kwa kilichotokea na kupelekea kukatisha safari yao ya maisha hapa duniani kwani hata mimi mwenyewe najilaumu sana ila mbele ya mkwanja na maisha mazuri mtanisamehe sana na ninachoweza kuwaambia ni kwamba nakwenda kumteka rasmi Mr Santana kwa gharama yoyote ile ilmradi tu awe wangu."
Aliongea Melissa huku akimkodolea macho Robinson ambaye akinywa juisi.
" Ila na wewe ni mpuuzi wa tabia ndiyo nini kumsaliti mpenzi wako aliyekuonesha dunia ikoje?"
Melissa alimrushia swali Robinson ambalo hakulitegemea muda huo.
"Hata bila yeye bado hii dunia ningeifahamu tu kwani ndoto zangu zilikuwa kutoka nje ya Tanzania kutafuta maisha na kwa bahati akapita katikati ya ndoto yangu na kuwa kama ganda la ndizi vile."
"Kweli wewe una matatizo ya akili, hivi unafikiri kumtoa sadaka mpenzi wako kwa Santana utawini maisha? Hujamfahamu bado Santana wewe na endelea kumuomba Mungu asije pandwa na pepo la umwagaji damu."
"Vyovyote itakavyokuwa poa tu dada yangu."
"Okay sawa kidume mpambanaji."
Melissa alimjibu na kuelekea ndani kwenye ofisi ya Santana na kuwaacha wakina Robinson wakiendelea kuburudika.
NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
Baada ya mwendo mrefu Roberto aliwasili kwenye Ngome ya Santana maeneo ya msitu wa San Antonio ulio karibu na Ufukwe wa Marigezh na msitu huu ndani yake kuna msitu mwingine wa kupandwa ambao ulipandwa na mzee Tuyilagezi aliyekuwa zungu la Unga kwa wakati huo kabla ya kuuawa na Santana uitwao Caratons na ndani yake mzee huyu alijenga jumba lake la kifahari ambalo ukiwa ndani ya kisiwa cha Marigezh utaliona vizuri jumba hilo lillilo kwenye miamba na hivyo Santana hukitumia kwenye masuala yake na wageni ambao huwa hataki wajue anafanya nini. Na kwa kuwa analifahamu vizuri eneo hilo halikuwa tatizo kwake ni wapi apitie ili kuingia ndani ya Ngome hiyo. Lakini wakati akijipanga aingilie Ufukweni Marigezh au Caratons aliisikia gari ikitoka ndani ya Ngome ikabidi ajifiche kwenye kichaka asije onwa na wenyewe, mara ile gari ilisimama karibu na pale alipojificha kisha mtu mmoja ambaye hakumfahamu vizuri aliteremka akawa anakagua mazingira kisha mlango wa pili ulifunguliwa na Santana aliteremka.
"Hebu nisubirini kwanza nimekumbuka kule ndani kuna vitu ambavyo ni kumbukumbu za wale mizoga na kama ambavyo niliahidi kuwa sihitaji chochote cha kuwakumbuka."
Santana aliongea akimpiga bega Robinson ambaye alimfanya kama mlinzi wake wa muda wakati anamuandalia programu.
" Ni vitu gani hivyo mkuu?"
Robinson alimuuliza.
" Si zile simu zenu ambazo niliwaambia kipindi kile mziache kwa mwezi mmoja."
"Okay, kwanza nilikuwa nimeshazisahau mkuu."
"Kimbia ndani mwambie Melissa aingie ofisini kwangu kwenye droo ya meza yangu aangalie ataona bahasha ya kaki akupe ulete hapa."
Aliagiza huku yeye akijivuta kwenye kiti kiti cha gari mlango ukiwa wazi.
"Sawa bosi." Robinson aliitikia na kuondoka haraka kurudi ndani.
"Unajua nini Chude kitendo cha wanaharamu wale kufa na kutupwa baharini nimekuwa na amani sana moyoni na ni imani yangu kwa sasa yamebakia maskeletoni tu."
"Ni kweli bosi ila mimi bado nina hofu."
Chude alionesha kuwa na hofu.
"Ya nini tena Chude?"
"Si juu ya huyu Robinson?"
"Hilo hata mimi bado ninalo ila naendelea kumchunguza ikiwa ni pamoja kumshirikisha kwenye mambo yangu ya siri ili nione atafanya nini akileta ujuaji atawafuata wenzake."
Mara Robinson alifika pale akiwa na ile bahasha aliyoagizwa na huku akiwa kaongozana na Melissa.
"Hii hapa mkuu." Alimkabidhi.
"Vizuri sasa ishike toa simu yako kisha hizo nyingine chomeni moto hapo pembeni."
"Bosi hapana sihitaji hiyo simu ambayo nilinunuliwa na malaya ambaye alitaka kukuteketeza wewe kama kuchomwa zichomwe zote tu simu nitanunua kwa hela zangu mwenyewe."
"Robinson kwa sasa umekomaa hebu hii bahasha isiyo na maana kwetu itupe huko porini tunachelewa zetu mjini, na wewe Melissa vipi unaongozana nasi?"
"Bosi unanijua vizuri mambo yangu nabaki vipi halafu natakiwa kupitia pale maskani kuweka mji sawa."
"Bila shaka tunaweza kuondoka." Santana aliongea baada ya kuhakikisha ile bahasha imetupwa na Robinson.
Waliondoka zao na kutoa nafasi kwa Roberto aliyekuwa kajificha kuibuka na kuifuata ile bahasha iliyotupwa.
"Ina maana wale wadada wameuawa tayari? Na huyu aliyekuwa anaongea na Santana ni nani mbona anaonekana kuwafahamu sana wakina Jackline?" Nitakula sahani moja na Melissa mpaka nijue kisa cha wakina Jackline kuuawa na Santana."
Alijisemesha mwenyewe akiwa anaiendea ile bahasha. Aliichukua na kuifungua baada ya kuifungua alikutana na simu mbili akazitoa na kuzikagua.
"Sasa, ina maana hizi simu ni za nani sasa kati ya wale madada? Najua moja itakuwa ni ya huyu niliyemsikia akiitwa Robinson na nyingine ni ya nani? Ni ya Jackline, ni ya Jasmine au Jessica? Ngoja nitajua tu nikifika tu mjini."
Aliichukua ile bahasha na kuiweka mfukoni kisha akaondoka zake kurudi mjini kwani aliona kuendelea na zoezi la kuwafuatilia wakina Jackline ambao tayari wamekufa ni sawa na kazi bure hivyo ambacho alikiona ni kurudi zake mjini ili ajue cha kufanya japo tayari mtu wa kwanza kuanza naye alikuwa ni Melissa.
Msafara wa Santana ukiwa ndani ya msitu ule wa Amazon mara waliiona gari mbele yao ikiwa katikati ya barabara.
"Hee hii gari si ya kwangu? Mbona iko hapa?"
Santana aliuliza alipoiona.
"Ni yenyewe mkuu."
"Sasa ikoje si niliambiwa kwenye simu kuwa gari imepata ajali mbaya na dogo Hassan kafariki? Hebu simamisha gari mara moja."
Gari ilisimamishwa na kisha wote walishuka na kuiendea ile gari kuangalia kulikoni.
"Bosi hakuna mtu ndani ya gari lakini funguo iko mahala pake."
Tom alitoa taarifa baada ya kuichungulia kupitia kwenye kioo cha mlango na baada ya kuufungua mlango ulifunguka.
"Hebu jaribu kuiwasha tuone."
Santana aliagiza.
Tom aliingia na kuiwasha lakini haikuwaka, akajaribu tena lakini haikuitikia akashuka.
"Bosi inawezekana imeharibiwa makusudi hii na aliyeiacha hapa."
"Okay inawezekana lakini Hassan yuko wapi?"
Santana aliuliza akiwa kauma meno.
"Bado tuna kazi ya kufanya kijana wangu nilijua kufa kwa wale mabinti tungepumzika kumbe tulikuwa tunajidanganya muziki ndiyo kwanza umeanza."
Mzee Bruno Gautier aliongea kwa sauti ya huruma sana nafikiri hii imekuja baada ya mke wake kutoonekana mpaka sasa.
"Ingieni garini haraka hiyo iacheni hapo hapo kuna kitu tunatakiwa kufanya muda huu."
Aliongea Santana huku akiwa anakuna kichwa kwa nguvu simu ikiwa mkononi akitafuta namba fulani ambayo alipoipata aliipiga.
"Shenzi kabisa namba ya Hassan haipatikani kwa sasa ninahisi yule kijana aliyejifanya msamaria mwema ni kichomi kingine kwetu, tunaelekea kwa Melissa muda huu."
Aliingia garini na kuubamiza mlango kwa nguvu akafunga mkanda na kuruhusu gari iondoke.
Safari ilianza kuelekea North Angle kwa Melissa ambako walihisi kuna chanzo cha tatizo kwa kuwa walimtuma kufuata simu ya Jackline nyumbani kwa Melissa.
Baada ya mwendo mrefu safari yao ilitia nanga getini kwa Melissa ambako Santana alishuka haraka huku kundi lote likimfuata nyuma na alipoufikia mlango wa geti alikuta ukiwa haujafungwa kwa komeo ukiwa umeegeshwa tu na hapo akajua kuna tatizo. Akageuka nyuma kuwapa ishara ya kukamata silaha zao tayari kwa shambulizi.
"Tom na Chude ingieni ndani kwa tahadhari ninyi wengine izungukeni nyumba mimi nitabaki hapa peke yangu."
Santana alitoa maelekezo kwa watu wake.
Pasipo kupoteza muda walielekea kwenye maeneo waliyopangiwa na Santana huku Tom na Chude wakiingia ndani kwa tahadhari kubwa na baada ya kukitingisha kitasa kilifunguka bila ubishi kitendo kile kiliwafanya wakina Tom kutazamana kwanza maana ndani inaelekea kuna mtu. Hivyo waliingia kwa kupokezana na baada ya kuingia pale sebuleni walikutana na hali waliyoiacha lakini ile simu hawakuiona. Tom baada ya kuchungulia kwenye korido la kuingia chumbani aliweza kuona mtu kalala chini.
"Chude kuna mwili wa mtu kule koridoni." Tom alimnong'oneza Chude sikioni na Chude naye baada ya kuangalia alikooneshwa naye aliweza kuona na ndipo walipomfuata baada ya kumtambua ni mwenzao Hassan.
"Mungu wangu Hassan kapoteza maisha?"
Tom aliuliza huku akichuchumaa kumkagua Hassan. Na Chude hakutaka kupoteza muda alitoka nje kutoa taarifa.
"Bosi Hassan yuko ndani ya nyumba."
"Vipi hali yake?"
Aliuliza Santana.
"Kapoteza maisha kitambo kwani tayari mwili umeanza kutoa harufu."
"Buuuuu shit!!!!!!!!!! Ni kenge gani aliyepita kwenye njia yangu?"
Santana alijiuliza swali kwa sauti.
"Mimi nina mashaka na kule ambako walifikia kwani walisema kuna kijana mmoja alitaka kuwaibia hela ambazo walizipora kwenye boti lakini walimdhibiti na kumpa kichapo na ndipo alipofunguka matatizo ya mama ambapo wakina Jackline waliamua kusaidia huyo kijana hivyo asije kuwa ni huyo."
Melissa alipata mashaka kuwa inawezekana mfanya yote hayo atakuwa ni Roberto.
" Huyo kijana unamfahamu ni nani na anaishi wapi au huyo mama yake kalazwa wapi? "
Santana aliunganisha maswali mfululizo kwa Melissa.
" Hapana simfahamu kwa hawakuweza kumtaja wala sehemu ambayo anaishi huyo kijana."
Melissa alifafanua.
"Melissa unaongea nini sasa wakati huna uhakika na kauli zako?"
Santana alimfokea Melissa akiwa kamkaribia usoni kabisa.
"Nisamehe bosi wangu nilikurupuka tu kwa bahati mbaya."
Melissa alijitetea baada ya kuona kuna dalili ya kukutana na shetani mtoa roho.
"Uchukueni mwili wa Hassan na haraka sana kautupeni pembezoni mwa mji kisha rudini hapa haraka hili eneo si salama hata kidogo."
"Sawa bosi."
Waliitikia wakina Robinson na kuuchukua mwili wa mwenzao na kuupakia kwenye gari na kuondoka kutoka nje ya mji na kuwaacha wakina Santana pale ndani na huku Melissa alianza kuchukua vitu vya msingi kwake tayari kwa kuiacha nyumba yake ambayo kwa wakati huo alihisi ni jehanamu ndogo. Wakati Melissa akiwa anajiandaa mzee Bruno alikuwa katulia tu akimuangalia Santana ambaye alikuwa akichezea simu na katika piga piga namba fulani iliweza kuita.
"Santana, Santana hivi unafikiri hii dunia utaigeuza geuza unavyotaka eee?"
Roberto aliuliza baada ya kupokea simu ya Santana.
"Wewe ni nani ambaye na jina langu unalifahamu?"
Santana aliuliza.
"Ni mapema sana kunijua kwa sasa brother Santana, ila tu muda ukifika utanijua mimi ni nani na wakati huo nitakuwa mbele yako nikiichukua roho yako na usihofu katika hilo kwa sababu wewe ni utakuwa wa mwisho baada ya kushuhudia kifo cha Melissa atakayeanza, akifuata mzee wangu Bruno kisha Chude na Tom huyo boya wako mgeni yeye atauawa na aliyemleta Brazil."
Roberto alimtisha Santana kwa maneno ambayo yaliweza kumpa ubaridi.
" Wewe acha kunitisha inawezekana huna taarifa hao kenge wako kwa sasa ni marehemu na muda huu wako kwa sir God wakijibu maswali magumu."
"Ha ha ha ha ha Santana unajidanganya bro lile kundi bado lipo na kama huamini subiri hata baada ya miaka ishirini utaona mwenyewe."
Baada ya kumhakikishia Santana kuwa asifikirie wakina Jackline wamekufa bali wako hai alikata simu na kuizima kabisa.
"Huyu ni nani? Ambaye anatujua wote kwa majina yetu? Na kanihakikishia kuwa wale Pimbi hawajafa wako hai, inawezekana kweli?"
Santana aliuliza swali ambalo hakujua atalijibu nani.
"Huyo anajaribu kukutia jamba jamba tu hajui lolote inawezekana ni hawa madogo wa mjini ambao hutumia madhaifu yetu kujipatia mkwanja."
Mzee Bruno Gautier alijaribu kumtuliza mkubwa wake wa kazi.
"Sawa mzee ndiyo atufahamu wote kwa majina mpaka huyu Robinson? Hapa kuna tatizo na tunatakiwa kuwa makini kwani bila kufanya hivyo tutajikuta tukifa mmoja baada ya mwingine ikiwa aliweza kummaliza Hassan humu ndani atashindwaje kwa wengine?"
Santana alianza kuingiwa na hofu kutokana na ile simu ya Roberto.
****
Ni alfajiri na mapema ndani ya bahari ya Atlantiki kusini wavuvi wakiwa kwenye shughuli zao ndani ya boti ya uvuvi wanafanikiwa kuuona mwili wa mtu majini ukielea.
" Jamani angalieni pale si mtu yule?"
Mmoja wao aliwaonesha wenzake baada ya kuona mwili wa mtu majini.
"Ni kama mwili wa mtu ule."
Mwingine alijibu.
"Mustapha ingia haraka majini tumpe msaada huyo mtu."
Aliagiza mzee ambaye alionekana ni kama baba yao kwenye ile boti.
"Sawa mzee."
Mustapha alijibu na kuchukua boya akalivaa na kujirusha majini akapiga mbizi mpaka kwenye ule mwili na kuanza kuuvuta. Aliuvuta mpaka karibu na boti kisha akarushiwa kamba ambayo aliitumia kumviringisha na kisha wakaanza kuuvuta ule mwili mpaka juu.
Mzee yule alipiga magoti na kulitegesha sikio kwenye kifua cha yule mtu.
"Hee mapigo ya moyo yanapiga kwa mbali sana hebu tusaidiane kumkandamiza sehemu ya tumbo kumtoa maji."
"Halafu ni kamdada baba katapona kweli?"
Mustapha alimuuliza baba yake.
"Tuombe Mungu anaweza kupona tu."
Wakiwa wameelekeza nguvu zao katika kuminya tumbo la yule mwanamke waliyemuokoa mara wakaona miili mingine miwili ikiwa inaelea majini.
"Baba kuna nini leo angalia miili mingine ile pale."
Alionesha kijana mwingine.
Hapo sasa waliona haina haja ya boya tena vijana wawili walijifunga kamba viunoni na kujirusha kwenye maji na kuifuata miili ile ambayo waliifikia na kuanza kuivuta mpaka kwenye boti.
" Halafu wote ni wasichana hawa inaonekana kuna tatizo walikotoka."
Mzee yule aliongea wakati wakiwatoa maji tumboni.
"Inawezekana ndiyo hawa wakimbizi wanaotupwa majini kila kukicha."
Aliongeza mtoto wake mwingine.
"Jamani boti ielekee nyumbani ili tukawawaishe hospitali kwa matibabu zaidi."
Mzee alitoa maagizo na hapo hapo boti lilizungushwa kutoka eneo hilo na kurudi tena mpaka Namibia ambako ndiyo makazi yao. Walitia nanga ndani ya bandari ya Namport.
NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
Baada ya kutia nanga pale Bandarini Namport waliwashusha na kuwapakia kwenye Ambulance ya bandari na kuwakimbiza mpaka hospitali ya KING'S MEDICARE CENTRE. Na walipowasili walipokelewa na vijana wa mapokezi ambao walileta vitanda maalum vya wagonjwa na kuwashusha na kuwapakia juu yake na kuwakimbiza mpaka Emergency Room tayari kwa uchunguzi. Baada ya taratibu zote kufanywa na madaktari wa KMC waliwapeleka moja kwa moja mpaka kwenye chumba cha joto kutokana kugundulika kuwa wagonjwa walikuwa wamepatwa na tatizo la baridi kutokana na kukaa muda mrefu baharini na kingine kilichowashangaza kwenye vipimo ni mabinti hao kukaa majini kwa muda mrefu bila kupoteza maisha wakati si jambo la kawaida kwa binadamu na pia waliendelea kujiuliza nini kiliwakuta. Na ndipo Daktari Mkuu wa kitengo cha Dharura aitwaye Abass Mukesh alipomuomba mzee Jerome Whistle aliyewaleta wagonjwa hao kwa mazungumzo ofisini kwake.
"Ndiyo mzee wangu naitwa Daktari Abass Mukesh ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya Dharura."
"Nashukuru sana daktari, mimi naitwa mzee Jerome Whistle mvuvi na mfanyabiashara wa samaki hapa Namibia."
"Ndiyo mzee Jerome naomba unieleze ilikuwaje mpaka kukutana na hawa wagonjwa?"
"Daktari ilikuwa hivi, mimi na wanangu tukiwa majini kama kawaida yetu tukivua samaki mara tukapata kuona nguo ikielea juu ya maji na baada ya kuangalia vizuri tukagundua ni mtu ndipo nilipomtaka mwanangu Mustapha aingie majini kumpa msaada mtu huyo lakini tukiwa bize na huyu mgonjwa kumpa huduma ya kwanza ndipo tukawaona na hawa wengine wawili na ndipo wanangu tena Mustapha na Victor walipojitosa kuwaokoa na baada ya kuwaokoa na kuwapa huduma ya kwanza ndipo tulipoizungusha boti yetu na kuwakimbiza hapa kwa huduma Daktari."
Mzee Jerome Whistle alitoa ufafanuzi juu ya kile walichokifanya kwa wagonjwa.
" Aisee ni watu wachache sana wenye moyo kama wako mzee Jerome kwani angekuwa mwingine wala asingejaribu kupoteza muda wake kuwaokoa watu asiowajua na kuacha shughuli zake ila kwako imekuwa tofauti sana nikupe hongera kwa hilo mzee wangu."
"Nashukuru Daktari."
"Vipi mliweza kupata vielelezo vyovyote vinavyowatambulisha hao mabinti?"
Daktari alimuuliza mzee Jerome Whistle.
"Hapana Daktari hatukuweza kupata chochote kile nadhani iwapo watazinduka watatueleza wenyewe kipi kiliwapata huko walikotoka."
"Okay sawa mzee, itabidi iwe hivyo lakini nitakachokuomba mzee ni kwenda kutoa taarifa polisi."
Mzee Jerome alimuangalia kwa muda daktari kama alikuwa akiyachambua maneno yake na ndipo alipokuja na majibu yake.
"Kwa hilo ningeomba libaki siri kati yetu na wewe daktari kwa sababu hatujui kilichowatokea huku tuwasubiri walejewe na fahamu zao watueleze kilichowapata kisha tutajua iwapo tukaripoti au la."
"Basi sawa mzee wangu mimi nakusikiliza wewe, nikushukuru kwa kukubali kupoteza muda wako kuja kuzungumza nami."
"Daktari usijali tuko pamoja katika hili nitakuwa bega kwa bega nawe mpaka tamati."
"Bila shaka mzee Jerome."
Baada ya kuhitimisha mazungumzo yao waliagana na kisha wakatoka ofisini mzee Jerome akawafuata vijana wake huku daktari Abass Mukesh akielekea kwenye kile chumba walichohifadhiwa wakina Jackline.
"Vijana wangu tuondoke nimeshaongea na daktari tayari tutarudi kesho kuwajulia hali wagonjwa wetu kama mjuavyo hawa ni wetu kuanzia sasa."
"Baba kwani daktari kasemaje kuwahusu?"
Victor alimuuliza baba yake juu ya kile alichokiongea daktari.
"Kasema kuwa tuwaache waendelee kuwafanyia uchunguzi wa kina lakini wakianza na kuwapandishia joto kwanza na hivyo kasema mpaka kesho majibu yatakuwa yamepatikana."
Mzee Jerome alifafanua kwa watoto wake, kisha waliondoka eneo hilo la hospitali kurudi kwao.
" Wale mabinti imekuwaje mpaka wakutwe na janga lile la kutupwa baharini? Ni wakina nani hawa?"
Mzee Jerome alikuwa akijiwazia wakiwa ndani ya gari la jumuiya wenyewe wakiyaita townbus' huku Tanzania tukiyaita daladala na wenzetu kule Kenya wakiyaita Matatu.
" Wanangu hebu tushukie hapa hapa Independence Tower' "
" Baba si umetuambia tunaelekea nyumbani mbona umepingana na uamuzi wako mwenyewe?"
Mustapha alimuuliza baba yake ambaye alionekana kupata wazo jipya na hivyo kuamua kushuka kabla ya kufika nyumbani.
"Nyumbani tunakwenda ila nimeona tupitie hapo kwenye duka la Kahawa tuweze kuamsha matumbo si mnajua hatukuweza kupata chochote toka jana usiku."
"Ni kweli kabisa baba maana si kwa baridi hii ninayoisikia tumboni." Victor alionekana kuifurahia ofa ya baba yao aliyowaambia.
"Ndiyo hivyo wanangu na si kingine chochote kile."
"Tumekuelewa baba, tuwahi tusije ambulia vikombe tupu."
Victor aliona awachekeshe wenzake.
"Muuza kahawa uko wapi? Tupatie vikombe vitatu tafadhali."
Mzee Jerome Whistle aliagiza.
"Sawa mzee naleta."
Muuza kahawa alijibu huku akifungua kabati la vyombo.
"Kaka tufanyie haraka tuna majukumu mengine ya kifamilia bwana."
Victor alimharakisha muuza kahawa pale ndani.
Roberto akiwa nyumbani kwao maeneo ya Rio Branco anazitoa simu zile tatu yaani ile ya Jackline aliyoichukua kule nyumbani kwa Melissa na zile mbili alizoziokota kule porini Amazon baada ya kutupwa na Santana. Aliziweka mezani zote na kuziwasha zote na kama bahati vile zote ziliwaka ila shida ikawa kwenye ile aliyoichukua nyumbani kwa Melissa kwani ilikuwa na nywila akaona isiwe taabu kwake akaiweka kando na kuzirudia zile mbili akaanza na ile ambayo ilikuwa na picha ya Jackline akiwa kakumbatiana na Robinson.
"Nimepata jibu hapa hawa walikuwa ni wapenzi kabla ya kuchenganaaa Okey!!!!"
Aliifungua upande wa 'All calls' na kuanza kuangalia simu hiyo iliwahi kufanya mawasiliano na watu gani ndipo alipoona baadhi ya majina kama My father in-law, my young sister, na jingine lilikuwa ni la Simbozya ndiyo majina ambayo yalionekana kufanya mawasiliano na simu ya Jackline. Akaiweka kando kisha akachukua ile nyingine ambayo nayo ilikuwa na picha ile ile kama wallpaper' ya simu kitu ambacho kilimthibitishia moja kwa moja Jackline na Robinson walikuwa wapenzi.
"Mhh hayanihusu hayo mimi nifanye kazi yangu niliyoikusudia."
Alijiwazia mwenyewe baada ya kuona ile picha. Kisha akaifungua upande wa miito na kuangalia namba zilizofanya mawasiliano na simu hiyo ndipo alipokutana na majina mawili tu ambayo ni Baba na Shamimu na alipojaribu kuangalia namba ile iliyoandikwa baba akaona ni ile ile ambayo iko kwenye simu ya awali iliyoandikwa My father in-law na ile nyingine iliyoandikwa Shamimu akaona ni ile ile iliyoandikwa my young sister na hapo ndipo akapata sehemu ya kuanzia na kuona hakuna haja ya kuifuatilia ile nyingine iliyoandikwa Simbozya, akazichukua na kuziweka chaji zote kisha akatoka na kwenda kwenye kiduka kilicho karibu na nyumba yao kwa ajili ya kununua muda wa maongezi.
"Samahani jirani naomba muda wa maongezi wa shilingi elfu thelathini."
"Jirani wa hela yote hiyo unataka kuwasiliana na nani au unataka kumtumia mtu nini jiraniii?" Alitaniwa na dada yule muuza duka.
"Acha utani basi mtu wangu nifanyie hivyo basi nina haraka kidogo."
"Mmhh okay bwana naona tu siku hizi unazidi kuotesha tu kibanda cha tumbo."
Yule dada aliongea hayo akimkabidhi Roberto vocha zake. Baada ya kumkabidhi hela yake aliondoka zake kurudi nyumbani kukamilisha kile ambacho alidhamiria kukifanya. Aliingia na kuichukua ile simu ambayo alijua ni ya Jackline na kuiingizia muda wa maongezi kisha akaibonyeza namba ya mdogo wa Jackline ambayo ni ya Shamimu na kuipiga, kama bahati vile iliita.
"Jamani dada yangu Jackline ndiyo nini kupotea hivyo hata meseji kwa mdogo wako kweli? Au kwa sababu wazazi wangu hawapo ndiyo umeamua kunitenga kaka kaka? Sawa tu dada yangu ila mimi bado nitaendelea kuwa mdogo wako tu na elewa kwa sasa si mwanafunzi tena ni mhitimu tayari."
Roberto alibakia kuwa msikilizaji tu baada mpigiwa kugeuka kuwa msemaji mkuu badala ya kusikia kile kilichopangwa kuzungumzwa na mpigaji.
Hapo Roberto alibaini kitu kutoka kwa mdogo wa Jackline hivyo akaona kuwa akisema amjulishe kuwa dada yake alishafariki itakuwa nongwa kubwa hivyo aliamua kukata simu. Akaona ampigie simu mtu wa pili ambaye ni baba mkwe wa Jackline ili huyo ndiyo ampe taarifa.
"Waooo mwanangu Jackline, eeehh hujambo mwanangu? Mnaendeleaje huko ugenini na mmefikia wapi? Huku mwanangu mambo ni mazuri sana kwani yule ibilisi tayari yuko ndani akisubiri tu kukabiliana na hukumu yake pindi mkifika."
Roberto alishusha pumzi ndefu kwanza baada ya kuyasikia maelezo hayo ya mzee huyo ambaye naye hakuwa tofauti sana na mdogo wa Jackline ndipo akaona tu ajitose kufikisha taarifa kamili.
" Mzee kwanza shikamoo !!!! "
Alianza kwa kumsalimu ili kuvuta usikivu kutoka kwa mzee Kaaya.
"Hee ni nani wewe tena ambaye umetumia simu ya mkwe wangu? Au ni Robinson mwanangu?"
"Hapana mzee mimi si huyo mwanao wala si yeyote kwa Jackline bali ni msamaria mwema tu niliokota simu mbili ya mwanao Robinson pamoja na hii ya mkwe wako."
"Unasemaje wewe kijana? Umeziokota kivipi? Mbona unanipa presha?"
"Hapana mzee punguza presha niweze kukufikishia ujumbe niliopanga kukupa mzee wangu."
"Haya nakusikiliza nijuze kulikoni maana tayari jasho la pua linanitoka."
"Ni hivi mzee wangu, mimi naitwa Roberto naishi Brazil nikijuana na Jackline pamoja na rafiki zake wawili Jasmine na Jessica lakini ni kama vile Mungu alinikutanisha nao ili niwe barua yao kwenu."
"Kivipi hapo Roberto bado unaniweka gizani?"
"Baada ya siku kadhaa kupita na kuachana nao nilipata taarifa zao kuwa wameuawa na mtu ambaye ni hatari sana duniani akishilikiana na mwanao Robinson."
"Weee, wewe, weeeeeeee kijana kama ulipanga kuniletea habari za kipuuzi kama hizo jua umenoa mimi si wa aina hiyo na usitegemeee kupata chochote kwangu mimi ni mlala hoi tu kwa hiyo kama umewateka wewe waachie tu ndugu yangu."
"Mzee si..." Kabla hajamalizia neno lake Roberto alisikia simu ikikatwa na alipojaribu kuipiga tena ilikuwa imezimwa kabisa simu ya mzee huyo.
"Duuu ishakuwa tabu hapatikani tena hewani, nifanye nini sasa Roberto miye ila si mbaya taarifa ameipata kuikubali au kuikataa ni juu yake."
Roberto alijisemesha mwenyewe baada ya kukatiwa simu na mzee Kaaya na mara baada ya kuipiga tena haikupatikana tena.
******
"Dada kapatwa na nini mbona kapiga simu halafu haongei kitu na badala yake amekata simu au ndiyo kusema kachukizwa na maneno yangu?"
Shamimu alikuwa kajishika mashavu akifikiria kitendo cha kukatiwa simu na mtu aliyejua ni dada yake Jackline.
"Shamimu mwanangu mbona umejikunja hivyo hapo kulikoni?"
Mama Robinson alimuuliza baada ya kumuona akiwa kajikunja pale nje ya nyumba.
"Hamna kitu mama." Alijibu huku akijifuta machozi na pembe ya kitenge chake.
"Si kweli hata kidogo mwanangu huwezi sema hakuna kitu ilhali unatokwa na machozi?"
Mama Robinson alimuuliza tena huku akikaa karibu yake kutaka kujua kinachomliza.
"Mama hakuna kitu ni dada Jackline tu huyu."
"Kafanya nini tena wakati unajua bado hajarudi toka safari yake?"
"Amenipigia muda si mrefu mama."
"Acha uongo mwanangu Jackline huyu huyu kakupigia simu? Hajanisalimu?"
"Kukusalimu tena mama wakati nilipopokea tu nikamtolea dukuduku langu lote hee si ikawa tabu mama akanikatia na nimejaribu kumpigia tena hapatikani."
"Jamani pole sana mwanangu ndiyo kinakuliza hicho, usilie bwana si unajua kwa sasa dada yako ana msongo wa mawazo?"
"Najua mama."
"Ehhh basi ndiyo maana kakukatia simu akifikiria kuwa hujali anachokifanya na kuangalia upande wako, ila najua hajakuchukia atakupigia tu wakati mwingine tumpe muda."
"Sawa mama."
Shamimu alijibu na kuinuka kuelekea ndani akimuacha mama Robinson akiwa kaketi.
"HABARI ILIYOTUFIKIA HIVI PUNDE...
Watu watatu ambao jinsi yao ni kike wameokolewa na Wavuvi wa Kinamibia kutoka ndani ya bahari ya Atlantiki. Kwa sasa wanapatiwa matibabu ndani ya Hospitali ya KING'S MEDICARE CENTRE.
TUNAENDELEA KUIFUATILIA HABARI HII KWA UNDANI ZAIDI."
Habari hiyo kutoka Kituo kimoja cha Televisheni aliyokuwa akiiangalia iliweza kumshtua mzee Kaaya ambaye muda mfupi uliopita alipokea taarifa kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kwa jina la Roberto.
" Baba taarifa hiyo imetokea wapi?"
Shamimu aliuliza baada ya kuiona ikiishia wakati yeye akiingia ndani kutoka nje.
"Sijui imetokea wapi hiyo mwanangu hawajatoa ufafanuzi."
"Hivi kwanini siku hizi watu wanauawa sana baharini?"
Shamimu aliuliza.
"Mwanangu bara letu la Afrika lina matatizo mengi sana ambayo wengi yamewashinda na kuamua kutorokea nje ya bara ili kujaribu bahati yao lakini shida inayokuja ni njia ambazo zinatumika na wao si rasmi mwanangu."
Mzee Kaaya alifafanua kwa mwanaye.
" Ni kweli kabisa baba, kwa matatizo yanayotukumba watu wenye ngozi nyeusi unaweza jikuta ukitimkia huko na hata tukisema wafuate njia halali hawawezi kufanikiwa haraka."
"Mwanangu mbona umeniacha mwenyewe nje?"
Mama Robinson alimuuliza Shamimu.
NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
"Niliamua kuingia ndani baada ya kuona hapo nje kuna mbu mama."
Shamimu alimjibu mama yake.
"Sawa mwanangu hata mimi kimenikimbiza hicho hicho na sijajua nini kimepelekea mbu kuwa wengi mwaka huu?" Mama Robinson alirusha swali hewani ili yeyote alijibu.
"Hakuna chochote mke wangu zaidi ya madimbwi ya maji huko nyuma pamoja na majani yaliyokuwa sana ndani ya mtaa wetu."
Mzee Kaaya alimjibu mke wake.
"Tukiamka salama kesho nitaifanya kazi hiyo ya kufukia mashimo ya maji pamoja na kupalilia nyasi zote kuzunguka nyumba yetu."
Shamimu aliwaahidi walezi wake kuifanya kazi hiyo.
"Vizuri mwanangu na mimi nitakuunga mkono."
Mama Robinson alimuahidi kuungana naye kufanya usafi huo ambao utapelekea kuondoa mazalia ya mbu.
"Sawa mama." Shamimu alijibu huku akiingia jikoni kufanya maandalizi ya chakula cha usiku.
"Mume wangu leo jambo la ajabu limemtokea Shamimu ambalo sikulitegemea kabisa."
"Jambo gani hilo mke wangu."
"Si Jackline alimpigia simu lakini cha ajabu hakuongea chochote zaidi ya kumsikiliza tu mdogo wake na kisha kuikata bila kuongea chochote." Maneno yale ya mke wake yalimshtua tena mzee Kaaya na moja kwa moja akajua huyo wala Jackline bali ni yule yule aliyempigia yeye hata hivyo hakutaka kumshirikisha mke wake kile alichokisikia kutoka kwa Roberto kwa kuhofia kuzalisha tatizo kutokana na mke wake kumpenda sana mtoto wake Robinson.
"Inawezekana alikuwa kwenye eneo ambalo mtandao uko chini sana ndiyo maana aliona akate simu mpaka apate sehemu nzuri."
Mzee Kaaya alimjibu mke wake.
"Inawezekana mume ikawa tatizo likawa ni hilo sasa mwenye dada alipofanyiwa tendo hilo siyo kumwaga machozi kule."
"Utamuelekeza hivyo ajue asifikiri kila eneo lina mtandao mzuri kwa mawasiliano."
"Sawa mume wangu, basi ngoja tufanye maandalizi ya chakula maana muda nao umekimbia sana."
Alijibu mume wake na kuelekea jikoni kusaidiana na Shamimu kuandaa chakula. Na baada ya chakula kila mmoja alielekea chumbani kwake kutoa faida kwa mbu.
Kulipokucha mzee Kaaya aliona aende Internet Cafe akajaribu kutafuta mawasiliano ya mtoto wake Robinson ili aweze kujua kulikoni mpaka ahusike na kifo cha mwanamke ambaye alimpenda kutoka moyoni pasipo kuangalia maisha yao yalivyo.
"Mtoto huyu kakumbwa na mdudu gani vile mbona sikumlea hivyo na kwa Robinson ninayemfahamu hakuwahi kuua hata panya iweje aue mtu tena mpenzi wake? Nitaiweka wapi sura yangu mimi Kaaya mwenyekiti niliye mstari wa mbele kuipigania familia ya Jackline iweze kupata haki zake sasa kimetokea kidudu mtu ndani ya nyumba yangu mwenyewe daa eee Mungu wangu nipe nguvu yasiwe ya kweli haya."
Alikuwa akiongea peke njiani tena kwa vitendo vya mkono akiwa anaelekea kupata huduma.
" Baba mbona unaongea peke yako njiani?"
Shamimu alimuuliza mzee Kaaya baada ya kumuona akiwa bize anaongea peke wakati yeye akitoka kununua vitafunwa.
" Shamimu mwanangu umetoka wapi muda huu?"
Badala ya kujibu swali aliloulizwa alimtupia naye swali.
"Niliwahi kununua vitafunwa kule kwa mama Mlokozi si unajua kuwa ndiye fundi wa kupika vitumbua unavyovipendaga baba?"
Shamimu alimjibu huku akimkazia macho usoni mzee huyo ambaye alionekana kuwa na mawazo sana. Na baada ya kuona hakuna anachoongea zaidi ya kuchezesha vidole vya mkono kwa kuvipiga piga usawa wa mfuko wa suruali.
" Baaba umenisikia lakini nilichosema?"
Shamimu alimtupia swali jingine.
"Mwanangu nimekusikia sasa wewe wahi nyumbani narudi muda si mrefu kuna sehemu nafika mara moja."
"Sawa baba."
Shamimu alikubaliana na mzee Kaaya na kuachana naye.
Mzee Kaaya alifika mpaka Gomba Internet Cafe na kukutana na chifu mwenyewe wa Cafe hiyo bwana Gombanila na kumueleza dhumuni lake la kufika hapo na baada ya kusikilizwa sana mzee Kaaya kiongozi huyo wa Cafe hiyo aliingia mtandaoni na kuanza kulifanyia kazi ombi la Mzee Kaaya kumtafutia taarifa zinazomhusu kijana wake Robinson.
Gombanila alitumia zaidi ya dakika kumi tano kuweza kutafuta taarifa hizo lakini hakuweza kuzipata na ndipo mzee Kaaya akatoa simu yake na kumtajia namba ya mtoto wake Robinson na kisha ikatafuta kupitia application maalum ya mawasiliano ambayo gharama zake kwa simu za nje ya nchi si kubwa sana ukilinganisha na kwa njia ya kawaida kisha akaipiga namba ile na kama bahati vile simu iliita.
"Mzee anapatikana jiandae kuongea naye, kaa kwenye hicho kiti kisha vaa hizo headphones tayari kwa kuongea naye akipokea."
Gombanila alimwambia mzee Kaaya wakati akiendelea kufanya koneksheni ya mawasiliano.
Mzee baada ya kuvaa zile headphones system ilikubali na simu kupokelewa upande wa pili.
" Haloo, haloo mwanangu !!! "
Mzee Kaaya aliita.
" Naam mzee kwa bahati mbaya hii simu iko na yule yule aliyekupa taarifa za mwanao jana ambazo hukutaka kuzipokea kabisa na ndiyo maana ulinikatia simu."
"Ni wewe Roberto au nani?"
"Ndiye mwenyewe mzee labda niombe kukusikiliza kwa lile unalotaka kuniambia."
"Sasa kijana wangu Roberto imekuwaje ukawa na simu zote mbili? Ya Robinson pamoja na ya Jackline huoni kama unanipa mashaka?"
"Huna haja ya kuonesha mashaka kwangu mzee naomba ufungue masikio yako vizuri na unisikilize kile ninachokwenda kukuambia leo na kama hutanielewa basi usinitafute tena, mwanao Robinson anahusika na mauaji ya Jackline na wenzake wawili akishirikiana na mtu mmoja aitwaye Santana na ndiyo maana baada ya kuhakikisha zoezi lao la kuwaua limekamilika na kuwatupa baharini waliamua kuzitupa na simu hizi nje kidogo na Ngome yao na kwa kuwa sikuwa mbali na eneo lile baada ya wao kuondoka tu nilizifuata na kuziokota hizi simu na kwa taarifa yako nina mbili za Jackline na moja ya Robinson na pia naomba nikupe tu taarifa nzuri ambayo ni chungu kwako mzee, mimi ndiye ambaye nimeahidi kumkamata mwanao na si kumkamata tu bali na kumuua kwa mikono yangu miwili tena kifo kitakuwa kile kile alichofanya kwa Jackline."
"Kijana huko unakwenda mbali sana mimi nadhani unisaidie kupata taarifa ambazo zitanifanya kupata ushahidi wa mwanangu kuhusika na mauaji."
Mzee Kaaya alianza kushuka kidogo kidogo baada ya kukuta taarifa ni ile ile haibadiliki kutoka kwa Roberto.
"Mzee nakata simu na kisha nakutumia namba ya mtu ambaye anafanya kazi na mwanao."
Roberto alikata simu kisha akaitafuta namba ya Santana na kuituma kwa mzee Kaaya na baada ya kuiona Gomba aliingiza kwenye mfumo na kuipiga namba hiyo.
"Haloo naongea na nani?"
Mzee Kaaya alianza kwa kuuliza baada ya simu kupokelewa upande wa pili.
"Wewe umempigia nani?"
Santana aliuliza.
"Samahani sana kijana wangu mimi ni ndugu yake Robinson nataka kumpa tahadhari kutokana na kuuawa kwa Jackline kwani kuna mtu yuko kati yenu anawazunguka hivyo kama hutojali naomba niongee na mlengwa."
Mzee Kaaya alifanikiwa kuutengeneza uongo.
"Unaishi nchi gani?" Santana alimuuliza mzee Kaaya.
"Mimi naishi Afrika ndani ya kisiwa cha Zanzibar."
Mzee Kaaya aliendelea kudanganya.
"Okay nimekuelewa ongea na mtu wako huyu hapa."
Santana ilibidi ampe simu Robinson ili aongee na mtu huyo ambaye hakuwa kamfahamu na bila shaka iwapo angemfahamu wala asingekuwa tayari kumuunganisha na Robinson.
"Ndiyo Robinson hapa naongea, nani mwenzangu?"
Robinson alianza kwa kujitambulisha na kuuliza anaongea na nani.
"Ooohhh vizuri sana unahaja ya kutaka kujua unaongea na nani mpaka hapa Robinson?"
Mzee Kaaya alimuuliza.
"Ina maa.. ina maana naongea na baba mzee Kaaya?"
Robinson alipata kigugumizi baada ya kuitambua sauti ya baba yake.
"Vizuri kama umenifahamu mwanangu, eeh naomba kujua mnaendeleaje huko?"
Mzee Kaaya alimuuliza swali la mtego.
"Kabla ya yote mzee ningependa kujua namba hii wewe umeipataje tena ukiwa Tanzania?"
Robinson alishachanganyikiwa tayari.
"Nitakujibu kwanza jibu swali langu."
Mzee Kaaya alimrudisha nyuma.
"Huku sisi tunaendelea vizuri baba na bila shaka muda si mrefu tutarejea nyumbani."
"Mkwe wangu yuko hapo niongee naye?"
"Ame... ametoka kidogo akirudi nitampa salamu zako."
"Mbona ni kama una mashaka hivi mwanangu? Eeh simu yako iko wapi mbona haipatikani hewani?"
Mzee Kaaya alimuamua kumtega mtoto wake.
"Simu yangu baba niliibiwa siku moja nikiwa mjini."
"Okay pole sana mwanangu, lakini mbona namba yako iko na mtu ambaye ana taarifa zako zote na inasemekana simu yako na ya Jackline ulizitupa porini ukiwa na huyu mwenye hii simu?"
Mzee Kaaya aliona ampige swali litakalomshtua kidogo.
Hivyo kama alifanikiwa kwa mpango huo kwani baada ya kulisikia tu hilo swali hakuweza kulitafakari zaidi kwani alikata simu.
" Kwanini amenikatia simu huyu Robinson."
Mzee Kaaya alijiuliza swali hili akiwa anazivua zile headphones.
"Niambie mzee anasemaje mwanao mbona ni kama uliduwaa kwa muda hivi kabla ya kutoa headphones."
Gombanila alimuuliza mzee Kaaya.
"Kijana wangu naomba uniambie ni kiasi gani natakiwa kulipa haya mengine tuachane nayo nitayakabili mwenyewe."
Mzee Kaaya alimjibu kijana huyo mwenye internet Cafe baada ya kuona anatafuta ufukunyuku usiomhusu.
"Utalipia shilingi elfu tano pekee mzee wangu."
"Simu za nje hazifai hata kidogo gharama zake ni kubwa sana."
"Na hapo ushukuru nimeitumia system rafiki tofauti na hapo ungejikuta ukitoa zaidi ya shilingi elfu kumi na tano kulingana na muda ulioutumia."
Gombanila alimfafanulia mzee Kaaya.
Basi mzee Kaaya aliingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi hicho cha fedha na kumkabidhi Gombanila na kisha alitoka zake na kurejea nyumbani kwake akiwa na msululu wa maswali kichwani mwake huku akijiuliza mtoto wake amekumbwa na nini huko Brazil mpaka kufikia hatua ya kujiunga na makundi ya kihalifu.
****
Mzee Jerome na wanaye walijihimu mapema kurejea hospitalini pale KING'S MEDICARE CENTRE kuwahi kuwajulia wagonjwa wao waliowapeleka pale.
Waliwasili na moja kwa moja wakaenda kukutana na daktari bingwa Mr Abbas Mukesh ofisini kwake ili wajue maendeleo yao.
"Ooohhh mzee Jerome Whistle karibu sana naona umeongozana na jeshi lako la Ukombozi."
"Asante daktari wangu ni kweli nimeongozana nao si unajua tena mimi ni Ikulu na wao ndiyo walinzi wa hii Ikulu."
"Aisee vizuri sana mzee wangu, turudi kwenye maendeleo ya wagonjwa wetu toka mlipowaleta ile jana."
"Sawa sawa mtaalam wanaendeleaje kwa sasa?"
"Kiukweli hali yao si nzuri au mbaya sababu mpaka sasa hawajaamka ila nina matumaini makubwa ya wao kuzinduka. Ila kuna kitu ambacho nina mashaka nacho mzee."
"Kipi hicho daktari wangu?"
"Ni kuvuja kwa taarifa zao."
"Kuvuja?"
"Ndiyo mzee jana baada ya ninyi kuondoka nilifungua laptop yangu na kuangalia duniani kuna nini ndipo nikakutana na taarifa ya kuokolewa kwao ikiambatana na picha zao japo hazikuonesha sura zao."
Daktari Abbas alimwelezea mzee Jerome huku akiifungua PC yake ili awaoneshe taarifa ile ambayo ililipotiwa na blog maarufu ya habari nchini humo Namibia ya fantasticnewz.
" Walizipata wapi hizi taarifa hawa jamaa?"
" Nina mashaka na pale bandarini maana hata mazingira haya ukiyaangalia vizuri ni ya pale."
"Hebu tuone, yes daktari hapo ni bandarini kabisa daa sijui itakuwaje?"
"Mimi nina wazo ambalo litakuwa ni msaada kwako na wagonjwa wako."
"Lipi hilo daktari?"
"Ni kuwatoa hapa kwa siri kubwa na kuwapeleka ndani ya jiji la Windhoek pale kuna hospitali ya rafiki yangu inayojulikana kwa jina la Makambi Hospital pale kuna VIP room ambazo ziko chini nina uhakika watapata huduma nzuri mpaka kupona kwao."
"Sasa daktari kama ujuavyo kule Windhoek ni mbali kutoka hapa itakuwaje?"
Mzee Jerome alimuuliza daktari.
"Kuhusu hilo ondoa shaka ile hospitali ina helicopter ya huduma ya kwanza ambayo huitumia kwenye kambi mbalimbali za utalii nchini hivyo nitamjulisha na kupelekea wao kutuma ndege hiyo ambapo mida ya saa tano usiku tutawasafirisha kupitia mlango wa dharura ambao uko kwenye kitanda alicholala yule binti mwenye kidonda mguuni."
" Nitashukuru sana daktari wangu kwani baada ya blog hii kusambaza habari hii bila shaka itakuwa imesambaa sana duniani na kupelekea wabaya wao kuanza kuwafuatilia tena ila kwa plan hiyo wataambulia manyoya hapa."
"Na ndiyo maana nilipata wazo hili kwani huu mtandao una fans wengi sana duniani na nikajua moja kwa moja lazima wabaya wao wataanza kuwafuatilia."
"Nikushukuru sana daktari kwa kufikiria hilo na niko tayari kuelekea huko nikiwa na vijana wangu hawa na kama hutojali tunaomba tukawaone kisha turudi nyumbani kujiandaa na safari."
"Bila shaka mzee Jerome."
Walitoka na kuelekea kwenye kile chumba walicholazwa wakina Jackline.
*****
"Hivi Robinson unaweza kunieleza baba yako kazipata wapi taarifa hizi na si hizo tu na pia namba yangu kaitoa wapi?"
Santana alimuuliza swali Robinson mara baada ya mzee Kaaya kuwapigia simu.
"Yaani hata mimi nina mashaka na hilo japo wasiwasi wangu ni yule aliyekupigia simu kupitia simu ya marehemu Hassan."
"Yes hapo naanza kupata wasiwasi na huyo mtu ni nani na anaishi wapi?"
Na hapo hapo akapata wazo la kumpigia simu mmoja wa vijana wake kule kambini na kutaka aende pale nje kwenye vile vichaka na kuzitafuta zile simu ambazo zilikuwa kwenye kimfuko maalum. Kisha alitulia kusubiri taarifa ya huyo kijana aliyemtuma.
Na baada ya muda simu iliita na alipoipokea tu ilimfanya atokwe na jasho la ajabu.
"Kasemaje bosi?"
Chude aliuliza swali baada ya kumuona bosi wake akiitoa simu sikioni na kujishika kiuno huku akigongagonga mguu chini.
"Wamezitafuta bila mafanikio yoyote hawajaziona."
"Zimekwenda wapi sasa?"
Robinson aliuliza.
"Hilo ndiyo swali la kujiuliza vijana wangu."
Baada ya hapo waliingia garini na kurudi kambini kufanya oparesheni ya kumsaka mtu anayecheza na akili yake.
"Bosi hebu iangalie hii taarifa hapa?" Melissa alimuonesha Santana taarifa fulani hivi ambayo yeye mwenyewe Melissa ilimshtua.
"What???????? Ina maana hawa panya wameokolewa? Nooooo sikubali hata kidogo."
Santana alipiga kelele za maswali baada ya kuona taarifa ya kupatikana kwa wakina Jackline huko Namibia.
"Hivi ninyi mliwatupa kweli au mliwapakia kwenye Meli nyingine?"
Santana aliwauliza wakina Robinson.
"Bosi huo ni muujiza huwezi amini kwani sisi tuliwatupa kabisa shahidi ni giza ambalo lilikuwa linatupiga chabo."
Chude aliamhakikishia bosi wake.
"Hapa tuache malumbano jamani cha kufanya ni kupanga mkakati wa kuwapata na kuwamaliza kabla hawajapona."
Mzee Bruno Gautier aliwauliza vijana wake.
"Hilo neno mzee wangu."
Melissa alimuunga mkono mzee Bruno Gautier.
"NAITWA JACKLINE JOACHIM KUANZIA LEO NAKUWA KIVULI CHENU POPOTE MLIPO NIPO NA KAMA MLIJUA TUMEKUFA KULE BAHARINI MSAHAU KABISA TUKO HAI KABISA NA HAPA NAJUA MNAPANGA NAMNA YA KUTUKABILI KARIBUNI SANA."
Ni ujumbe ulioingia kwenye simu ya Santana kupitia mtandao wa Whatsapp na ndipo Santana alipoiangalia ile meseji akaisoma na kisha pale pale akaichunguza ile namba iliyotuma ule ujumbe, cha ajabu akakutana na namba ya Robinson.
" Jamani hebu twendeni kambini kwanza maana kichwa changu kina uma sana angalieni huu ujumbe uliotumwa kupitia namba ambayo tuliitupa pale msituni na ambayo muda mfupi uliopita wamezikosa."
Kila mmoja aliusoma ule ujumbe na kuishia kutoa macho tu wakiwa hawajui wafanye nini kwani tayari mbaya wao wanatembea naye popote walipo.
NDUGU MSOMAJI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
"Hili lishakuwa janga tayari kwetu yaani kutupwa majini kwa siku zote hizo na bado wameokolewa? Na pia naamini kuwa hawa vibwengo ni wazima na ndiyo maana wako Hospitali."
Mzee Bruno Gautier alikuwa akijiuliza swali hili mbele ya wenzake.
"Jamani kitu cha kwanza naomba mniitie mtaalam wetu wa IT aifanyie kazi taarifa hiyo kutoka huko Namibia."
Santana aliagiza.
Na hicho kilifanyika baada ya kuwasili kambini kwao.
Wakati hayo yakitakiwa kufanywa na mtaalam wa IT mzee Bruno Gautier aliomba awasiliane na rafiki yake wa kule Windhoek kuona kama wanaweza kufuatilia kujua hii Hospital ya KING'S MEDICARE CENTRE iko wapi?
"Ngoja na mimi niwasiliane na kijana wangu aliye kule Namibia tuone kama anaweza kutusaidia."
"Mzee siyo mpaka uombe ruhusa bwana hilo lifanyie kazi hata sasa nina hasira na hao viumbe mpaka naumwa."
Santana alitoa ya moyoni mwake.
Wakiwa pale ndani kuna taarifa ililetwa mmoja wao ambaye alisema kaisikia kule Ufukweni.
"Taarifa gani hiyo tuambie?"
Mzee Bruno Gautier aliuliza.
"Nasikia kuna maiti za wasichana watatu zimeokotwa baharini na wavuvi alfajiri ya leo."
"Unasemaje wewe? Usituletee habari za kusadikika hapa."
Santana aliinuka na kuuliza kwa hamaki kitu kilichomtia hofu mtoa taarifa.
"Ni kweli bosi na inasemekana wamepelekwa hospitali ya hapa misheni st. Louis Hospital."
"Wako hai au wamekufa?"
Santana alimuuliza huku akichukua koti lake.
"Nasikia wamekufa bosi."
"Tuondoke haraka mwambieni dereva awashe gari tunaelekea huko hospitali sasa hivi."
Santana hakutaka kupoteza muda wake hata kidogo akaliamuru jeshi lake kuelekea huko kwa ajili ya kwenda kuhakikisha kama ni kweli ama la. Waliondoka haraka na kuelekea St. Louis Hospital na kwa kuwa haikuwa mbali sana Msafara ule uliokuwa na magari matatu ulifunga breki zake ndani viunga hivyo vya hospitali hiyo na kuteremka kisha kuingia ndani ya hospitali hiyo.
"Habari yako daktari !!"
Santana alimsalimu daktari wa zamu waliyekutana naye mlangoni akiwa anataka kutoka.
"Salama kiongozi, karibu."
"Asante sana daktari."
Santana alijibu na muda huo wengine walikuwa na shauku ya kutaka kujua huko ndani kuna kile walichokifuata.
"Mimi natoka nina kasafari kidogo vipi sijui niweza kuwasaidia nini?"
Daktari aliuliza.
"Okay, daktari kuna vijana wetu kule baharini wamepigwa na wimbi na kuzama hatukuweza kuwaona mpaka pale tuliposikia kuwa wamepatikana na kuletwa hapa."
Mzee Bruno Gautier aliona kama Santana anachelewesha hivi akaona amsaidie.
"Mzee wangu si unajua tena hapa tuna vitengo mbalimbali vya kihuduma inawezekana naombeni muende pale kwenye ule mlango ulioandikwa 'Uliza Hapa' mnaweza kupata majibu ya maswali yenu."
Daktari alionekana kutojua hilo na hivyo kuwaelekeza mahali pa kupata majibu yao. Baada ya kuelekezwa waliongoza mpaka pale na kuingia kwenye kile chumba.
" Samahani wapendwa wa Mungu ndani ya chumba hiki huruhusiwa mtu mmoja tu, hivyo niombe abaki mmoja tu na wengine mtaingia baada ya huyu kutoka."
Daktari ambaye ni mtawa kwa muonekano wa mavazi yake aliwapa utaratibu na hivyo kutoka nje na kumuacha Santana ndani.
" Ehh kijana wangu wangu naomba nikusaidie sasa."
"Samahani daktari naomba kuuliza kama kuna miili ya watu watatu ambao jinsi yao ya kike imeletwa hapa?"
Santana alimuuliza Mtawa (Sister) huyo.
"Mmhh hebu kidogo nipekue kitabu changu kuona kama lipo hilo si unajua tena kumbukumbu ni muhimu kijana wangu?"
Alimuuliza Santana akiwa anafungua kitabu kile chenye taarifa mbalimbali za kila mgonjwa anayeletwa mle ndani.
"Ni kweli kabisa Sista."
Santana alimjibu.
"Kijana wangu hakuna kitu kama hicho hospitalini kwetu kwani kwa mara ya mwisho kupokea wagonjwa wa jinsi ya kike hapa ni mwezi jana ambao walipata ajali ya gari."
Habari hiyo ilimchanganya Santana kiasi cha kuvua miwani yake na kuiweka mezani kwa daktari.
" Daktari umeangalia vizuri kweli? Na vipi kuhusu maiti kuletwa hapa? "
Santana aliuliza maswali hayo akitoa leso yake ili afute jasho ambalo lilianza kutengeneza michirizi ya vijito usoni kwake.
"Hatuna pia kijana wangu nimeangalia kwa umakini mkubwa sana na kuhusu maiti kuletwa hapa kwetu, hatujapokea maiti yoyote ndani ya siku sita hizi."
Taarifa ile ilimchanganya kabisa na kujikuta akiomba kitanda apumzike kwa muda baada ya kuona kama kizunguzungu hivi.
" Okay hebu pita huku kijana taratibu taratibu kijana wangu eehh vizuri sana toa viatu na panda hapo kitandani."
Lakini hayo yote hayakufanikiwa kwani Santana alianza kupoteza uwezo wake wa kujitambua daktari alilibaini hilo haraka sana alimshika mgongoni na mikononi na kisha kumlaza kitandani kisha kumvua viatu vyake na alipoona kila kitu kiko sawa alitoka nje na kuwakuta wale wengine wakiwa pale mlangoni.
"Samahani vijana wangu ni nani kati yenu kaja na yule kijana kule ndani?"
"Wote hapa ni wafanyakazi wake huyo ni bosi wetu. Robinson alijibu haraka.
" Aahh vizuri sana, sasa niwaombe mtulie kidogo kwani mkubwa wenu kapata mshtuko kidogo hivyo nimempumzisha naenda kumfuata daktari amshughulikie."
"Tatizo ni nini daktari?" Mzee Bruno Gautier aliuliza.
"Tukiwa kwenye mazungumzo niliona akianza kupoteza uwezo wa kujitambua na ndipo nilipomuwahi na kumpumzisha hivyo subirini hapa nimfuate daktari aje kumshughulikia bosi wenu."
Daktari aliwapa taarifa na kuwaacha pale kisha kwenda zake kwa daktari wa magonjwa ya presha.
" Hii ishakuwa tabu yaani badala ya kuja kufuata majibu ya maswali yetu mtu anapata presha na kulazwa? "
Melissa alijiuliza baada ya ripoti ile ya daktari.
" Hivi Jamani naomba niulize swali."
Robinson kuna kitu alitaka kuuliza wenzake.
"Uliza tu Robinson."
Mzee Bruno Gautier alimpa ruhusa.
"Kabla ya leo bosi alishawahi kupata tatizo kama hili?"
"Hapana sijawahi kupata hata mimi nimejishtukia tu natokewa na hali hiyo."
Santana alitoka ndani na kukutana na swali hilo ambalo aliamua kulijibu kabla ya mtu mwingine yeyote kulijibu.
"Hee bosi vipi tena si tumeambiwa wewe umepewa kitanda na daktari na kamfuata daktari aje kumshughulikia."
Melissa aliuliza baada ya kumuona Santana katoka nje.
"Ni kweli kabisa na mimi mwenyewe nimejikuta kitandani baada ya kuamka lakini niko poa kabisa."
"Kijana wangu nakuona hauko sawa kwema kweli?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza Santana baada ya kuona anaongea lakini si yule aliyemzoea.
"Tuondoke hapa kisha kila kitu nitawaeleza mbele ya safari."
Waliondoka na kurudi zao kambini kwao baada ya Santana kuchanganyikiwa kwa kile alichokisikia kutoka pale kwa daktari.
"Dereva hebu simamisha kwanza gari hapo kwenye mti huo mkubwa."
Gari lilisimamishwa na kisha mengine nayo yalisimama ili kujua kuna nini na ndipo Santana aliposhuka garini na kukifuata kivuli cha mti ule na kukaa chini kwenye vinyasi. Wote ilibidi wamemfuate pale alipokaa na wao kuketi pia.
" Ndugu zangu katika pilikapilika zangu za utafutaji halali na usio halali sijawahi kukutana na vipingamizi visivyo na kikomo kama hivi haki ya Mungu tena."
Santana alianza kwa kuwaelezea.
"Hatujakuelewa kijana wangu kwani kulikoni?"
Mzee Bruno Gautier aliuliza.
"Mzee Bruno, kuna mengi yametokea mbele yetu ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa vijana wetu tegemezi kuanzia kambini kwangu mpaka mgodini kule na kama hiyo haitoshi tumepoteza mamilioni ya dola kuwanyamazisha askari kwenye majanga yetu ili kuwazuia wasifanye uchunguzi lakini mambo bado ni magumu tena kwetu kama vile kutekwa kwa shemeji yangu ambaye mpaka sasa hatujui kama ni mzima au kafa."
Santana aliendelea kutoa maelezo yake mbele ya wenzake.
" Kijana wangu naomba suala la mke wangu tuliache kwanza maana nimekuwa nikilia kila siku usiku kwa ajili yake na sijui huko aliko anaishi vipi?"
Alianza kulia tena pale pale.
" Jamani mzee Bruno Gautier hebu acha kulia bwana mbona mimi nina matumaini kuwa bado yu hai mpaka sasa? "
Melissa alimpa moyo mzee Bruno Gautier.
" Najua tu kuwa mnaniliwaza tu ili nisimuwaze mke wangu okay sawa tu." Mzee Bruno Gautier alifuta machozi na kukaa vizuri.
" Tunafanyaje sasa jamani kwenye?"
Chude aliuliza.
" Jamani liko hivi, huu ni mchezo tunaochezewa na mtu anayetufahamu sana."
Santana alianza kutoa maelezo kutokana na kile alichokutana nacho kule hospitali.
"Bosi kivipi mbona sikuelewi katika hili ina maana mimi ndiyo mhusika wa haya yote?"
Robinson alimuuliza Santana baada ya kusikia maelezo yake ambayo aliona kama yanamlenga yeye.
" Naweza sema ndiyo au hapana lakini kikubwa eleweni kuwa tunafuatiliwa na mtu tusiyemfahamu hata kidogo kwani ile ripoti tuliyopewa na kuamua kuifuatilia haikuwa sahihi kwani baada ya kufika kule si nikaambiwa hakuna miili iliyopelekwa pale hospitalini kwao hivyo hamuoni kama kuna mchezo hapa? "
" Bosi tumfuatilie yule kijana aliyeleta taarifa hizi pale kambini." Robinson aliwataka warudi kambini kumfuatilia aliyetoa taarifa.
" Ni kweli hilo ndilo jambo pekee la kufanya kwa sasa."
Mzee Bruno Gautier alimuunga mkono Robinson.
" Hivi huyu anayezimiliki zile simu tulizozitupa kule porini nahisi ndiye mhusika mkuu kwenye gemu hili na tusipokaa sawa atatumaliza."
Santana alionesha wasiwasi wake kwa mtu ambaye alikuwa akiwatumia meseji na kuwapigia simu kwa kutumia namba ya Robinson na Jackline.
Lakini wakiwa kwenye majadiliano ya kipi cha kufanya kwa mtu anayewafuatilia lakini hawamfahamu mara ujumbe uliingia kwenye simu mbili kwa wakati mmoja yaani ya Santana na Melissa.
"MMENASA MTEGONI KWANGU KIRAHISI SANA, NAJUA HUKO MLIKO MNAJIULIZA IKOJE BAADA YA KUKUTA TAARIFA TOFAUTI NA ZILE MLIZOZIKUTA HOSPITALI 'POLENI SANA' HILO NI GEMU TU NA KWA SASA TEGEMEENI MSHTUKO MWINGINE MKUBWA MARA BAADA YA KUFIKA NGOMENI KWENU.... POLENI SANA."
" Hee jamani si mnaona sasa ujumbe huu hapa umetoka kwa mjinga yule yule mmoja. "
Santana alihamaki baada ya kuuona ujumbe kwenye simu yake.
" Na kwangu umeingia ujumbe kutoka kwenye namba ya mtu nisiyemfahamu."
Melissa aliwaonesha ujumbe ule na baada ya kuukagua tu ilionekana ni ule ule uliotumwa kwa Santana na mtumaji alikuwa ni yule yule.
"Tuondokeni kurudi kambini nahisi kuna jambo limetokea la hatari zaidi kutokana na ujumbe huu."
Santana aliwataka waondoke haraka kurudi kambini.
***
"Afande ukuta umevunjwa na watuhumiwa wetu wametoweka hawapo."
Afande Bupe alimtaarifu mkubwa wake kwa simu hakutaka mpaka aende ofisini kwake.
"Unasemaje Afande Bupe?"
Mkuu wake wa kituo aliuliza kwa kufoka kidogo.
"Ndiyo mkuu limetokea."
"Nawahitaji haraka sana askari waliokuwa Lindo muda wote huo sasa hivi."
"Sawa mkuu nimekupata."
Afande Bupe alikata simu na kuelekea kule walikokuwa askari wenzake.
"Hivi wale askari waliokuwa lindoni wako wapi? Mkuu anawahitaji ofisini kwake kwa mahojiano muda huu."
Afande Bupe aliongea kwa sauti ya juu kidogo.
"Mbona unatugombeza hivyo Afande Bupe."
Afande mmoja alimuuliza baada ya kuona anawaambia kwa sauti ya juu.
"Afande Bupe hapa ulipotukuta tulikuwa tunalijadili hilo hilo kwani hakuna aliyesalia hapa baada ya tukio la kutoweka kwa wahalifu ila wewe umekuja na makelele utafikiri sisi pia ni wahusika?"
Askari mwingine alimfafanulia Afande Bupe.
"Naombeni msamaha jamani kwa hiyo wamewatorosha wahalifu wetu siyo?"
"Ndiyo hivyo."
"Tunafanyaje sasa kuwathibiti hawa watu?"
Afande Bupe aliuliza.
"Mpigie mkuu kumjulisha hili ili kumsikia anasemaje."
"Okay sawa."
Basi haraka sana Afande Bupe badala ya kupiga simu aliona bora aende moja kwa moja akamjulishe.
NINI KITATOKEA HUKO?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
"Hivi mnafikiri tutatoka salama kwenye misitu hii?"
Mzee Jonathan aliwauliza askari ambao walikuwa mbele yao wakiongoza njia kuelekea sehemu ambayo hawaitambui hata kidogo kutokana na ugeni wa mazingira.
"Acheni maswali huu si muda wake hata kidogo tunachokiangalia hapa ni kutoka salama tu kikubwa ni pumzi ambayo itatuwezesha kutembea umbali mrefu bila kuchoka, huku tulikopita ni vigumu kwao kuhisi kwani muda huu wao watakuwa wanapiga hesabu za kufunga barabara zote kuhusu huku hawatajaribu kuhisi hata kidogo na hata pale watakapo kumbuka watakuwa wamechelewa."
Mmoja wa askari waliokubali kuwatorosha baada ya kuahidiwa kiasi fulani cha fedha aliwaondoa hofu mzee Jonathan pamoja Masanja.
" Naomba Mungu tufanikiwe kutoka maana kwa tulilolifanya ni hatari zaidi ya lile la mwanzo."
Masanja alionesha hofu yake wakati safari ikiendelea.
Walitembea umbali mrefu sana na kisha walifanikiwa kufika sehemu moja ya machimbo ambayo ilipata umaarufu sana miaka ya nyuma na inasemekana wazungu waliitumia sana kwa starehe zao baada ya na ndiyo maana walipaita Lupa Market ni kijiji kilichojificha chini ya milima kukiwa na idadi ndogo ya watu.
"Sasa kabla ya kuingia tutatakiwa tujifiche kidogo ili giza liongezeke maana sisi tunafahamika sana maeneo haya."
Askari mmoja wao alitoa tahadhari kwa ajili ya usalama wao.
"Maulid kule chini kuna kunakuwaga na kambi za wachimbaji unaonaje kama tukienda huko tukawaibie nguo ili tubadilishe hizi za kipolisi tuwe huru zaidi."
"Ni kweli kabisa Kabuti kwa hizi sare itakuwa tatizo kwetu."
Maulid alikubaliana na Ontario na hapo waliwaacha wakina mzee Jonathan na kushuka kwenye zile kambi za wachimbaji na kuvizia zilipoanikwa nguo walianua na kuondoka zao jua lilikuwa ndiyo linaishia magharibi lakini haikuwa rahisi kwao kuonekana kwa kuwa wenye hizo kambi walikuwa kuchimba.
Walirudi na kubadilisha zile nguo kisha zile sare walizichimbia chini na kisha waliungana na wenzao.
"Kwa muda huu tunaweza kupigania chakula hivyo twendeni muda unaruhusu maana giza limetubeba."
Ontario aliwataka waanze kusogea kijijini ili wakatafute chakula.
"Hilo napingana na wewe Ontario kwa sababu tumewaibia nguo halafu turudi kwenye makazi yao hilo haliwezekani cha kufanya tutafute njia ya kutoka hapa Lupa Market tusonge mbele chakula tutapata huko."
Maulid alimpinga mwenzake Ontario na kuwataka wasiingie hapo kijijini badala yake watokomee zao mbele.
Walivuka mabonde na makorongo na kisha usiku wa manane walifika ndani ya kijiji cha Ifumbo na kwenda moja kwa moja kwenye kambi ambayo inafahamika kama STAMICO ni eneo ambalo wazungu wachimba dhahabu walikuwa na makazi yao hapo na kwa sasa lilikuwa likilindwa na walinzi ambao walikuwa na jukumu la kuhakikisha hakuna kifaa kinachoibwa hapo na hivyo wakina Ontario wakaona ndiyo sehemu salama kwa wakati huo mpaka pale ambapo hali ya utulivu itarejea ndipo kila mmoja atakapochukua hamsini zake baada ya malipo kukamilika.
"Mzee Jonathan hili eneo ni salama kwetu kwanza liko nje ya kijiji na ni eneo ambalo ni kambi ambayo zamani waliitumia kufanya process zote za madini hapa."
Maulid alifafanua zaidi kwa mzee Jonathan na Masanja.
"Okay, kikubwa ni usalama tu mengine wacha yaendelee."
Mzee Jonathan alijibu.
"Jamani yote kwa yote na mlo ni sehemu ya uhai kwetu hivyo na chakula ni muhimu kwetu."
Masanja aliwakumbusha wenzake.
"Tumekupata brother lakini elewa kuwa hapa usalama ndiyo kila kitu chakula kinafuatia tu."
Ontario alimjibu Masanja.
Walifika mpaka getini na kugonga. Ambapo kama bahati geti lilifunguliwa na kisha mlinzi alitoka kuwasikiliza.
"Nyinyi ni wakina nani? Na mmefuata nini hapa muda huu?"
Mlinzi aliwauliza.
"Samahani mzee kwa kukusumbua tunaomba hifadhi kwa muda huu gari letu limetuharibikia hapo juu kilimani."
Maulid alijitambulisha kwa mlinzi huyo.
Mlinzi kusikia hivyo ilibidi achungulie nje kuona yuko na wakina nani kwa kufanya hivyo alifanya kosa kubwa kwani alivutwa nje na Ontario kisha aligongwa na kitako cha bunduki kichwani kisha walimvutia kwa ndani na kisha kulifunga geti.
"Hebu nendeni kule kwenye majengo muangalie kama kuna wengine ili huyu nimhifadhi kwenye moja ya vyumba hivi huku."
Maulid aliwaelekeza wenzake kuangalia usalama kwa kukagua kila sehemu kule ndani kutokana na mlinzi kumdhibiti pale getini.
Walivamia kila eneo kukagua lakini hawakuweza kuona mtu yeyote zaidi ya kukuta chakula aina ya makande yakiwa yanaendelea kuiva motoni.
"Jamani mmeona hapa kama zali vile chakula kiko hapa tusubiri tu muda ufike tuweze kufanya yetu."
Masanja aliwajulisha wenzake mara baada ya kukuta makande yakiiva pale motoni.
*****
Baada ya Roberto kuhakikisha kila kitu kiko sawa ndani ya Ngome ya mzee mzima Santana aliruka ukuta bila kuonwa na yeyote kisha kupotea zake.
Ambacho alikifanya baada ya kufanikiwa kujua ambako alihifadhiwa mke wa mzee Bruno Gautier kupitia meseji ambazo alizikuta kwenye simu ya Jackline alizokuwa akichati na mtu ambaye jina lake halikufahamika zaidi ya namba yake tu kuonekana na alipoona eneo likiwa limetajwa kama bahati magofu haya anayafahamu vizuri aliamua kukodi gari kutoka kwenye kampuni ya kukodisha magari na kisha kuelekea huko. Alifika na kulisogelea eneo hilo ambalo alijua ni jepesi kumbe haikuwa hivyo bali kulikuwa na ulinzi mzito kwani kulikuwa na walinzi waliokuwa wakimlinda mke wa mzee Bruno Gautier. Na baada ya kujitambulisha na kutoa baadhi ya vielelezo ikiwa ni pamoja na taarifa ya kutoweka kwa wakina Jackline ndipo walimkaribisha ndani ya magofu hayo na kukutana na dada huyo ambaye si mkubwa kwa umri japo kaolewa na mzee. Na baada ya kupanga mikakati yao vizuri waliamua kuungana na kumbeba dada huyo kama chambo cha kuwatingisha wakina Santana na ndipo mmoja kati yao alipopenya ngomeni na kuipeleka taarifa feki huku wenzake wakiwa nje na walipoondoka tu wao walizama ndani kutokana na uchache wa walinzi kutokana na wenzao kuelekea hospitali haikuwa tatizo kwake kuingia ndani ya Ngome hiyo na moja kwa na tahadhari sana aliingia mpaka ofisini kwa Santana na kutekenya mlango na pale ulipojibu aliingia na kisha kumkalisha mke wa mzee Bruno Gautier kwenye kiti cha Santana na kumfungia kamba hapo kisha ujumbe aliuweka mezani na baada ya kukamilisha kila kitu alitoka na kuruka ukuta na kuwakuta wenzake wakimsubiri kisha baada ya hapo waliondoka na ndipo alipowatumia ule ujumbe.
Santana na wenzake walipowasili na kukagua maeneo yote waliyakuta salama kabisa ndipo aliingia ofisini kwake na huko ndipo alikutana na maajabu pale kitini kwake.
"Whaaaaaat.......!!! Hii sasa too much hata kama ni mchezo unaelekea kubaya kwanini kila ninapogusa ninafeli? Wewe mwanamke umefikaje hapa?"
Alimuuliza swali lililoambatana na kofi la kiume shavuni kwa mwanadada huyo kiasi cha kumfanya atoe kilio japo mdomoni alifungwa kitambaa ambacho hakikuzuia kilio kusikika.
" Usinitolee mimacho hapa weweeee nataka uniambie umefikaje hapa? Wewe si ulitekwa?"
Santana aliendelea kuwaka kwa maswali mfululizo huku mke wa mzee Bruno Gautier akitikisa tu kuashiria kukubali na ndipo alimfuata na kumfungua kitambaa kile.
"Haya ongea haraka kabla sijakugeuza sambusa sasa hivi mwanaharamu wewe!!!!"
Santana ni kama alichanganyikiwa vile kwani hata kabla hajasikia chochote kutoka kwa mke wa mzee Bruno Gautier alijikuta akianguka chini na kuzimia.
Hali hiyo ilimfanya mwanadada huyo kupiga kelele ambazo ziliwaibua waliokuwa nje kukimbilia ndani baada ya kusikia sauti ya kike ofisini kwa bosi wao.
"Mke wangu Claudia umefikaje hapa? Na umemfanya nini Santana?"
Mzee Bruno Gautier alimumwagia maswali mke wake ambaye ni kama alikuwa hamsikii zaidi ya kuomba kufunguliwa zile kamba mwilini.
Wakati wakimfuata Santana ili wamchukue na kumpeleka chumba maalum cha huduma ndipo Melissa alipoona karatasi chini ya kiti ikiwa ni kama ilianguka kutoka mezani na akaichukua na kumkabidhi mzee Bruno Gautier.
"Mzee angalia hii karatasi nimeikuta hapa chini inaonekana ina ujumbe ndani yake."
Aliipokea na kuiweka mezani kisha akaendelea kumfungua kamba mke wake.
"Pole mke wangu Claudia ulikuwa wapi siku zote hizi?"
"Nifungue kwanza mume wangu kisha nitakusimulia kila kitu lakini tukiwa wawili tu maana huyu bosi wako si mtu mzuri kabisa."
"Kwanini mke wangu?"
"Nimekwambia nifungue kwanza kamba mengine yatafuata."
Mzee Bruno Gautier ilibidi afanye haraka kumfungua wakati wengine walimpeleka Santana chumba maalum kwa kumpumzisha.
Na ndipo mzee Bruno Gautier alichukua ile karatasi na kuisoma kujua kilichoandikwa.
" HIYO NI SALAMU TU KWAKO SANTANA NA WATU WAKO, HUYO MTU WENU TUMEMLETA KWANI KWETU HANA FAIDA YOYOTE ILA TUNAJUA ATAWAFIKISHIA UJUMBE. UNACHOTAKIWA KUJUA SASA NI KWAMBA WANAUME TUMEKAMILIKA MUDA WOWOTE TUNAREJEA, TUTAREJEA VIPI JIULIZE TUMEINGIA VIPI MPAKA OFISINI KWAKO."
Na kilichomshangaza mzee Bruno Gautier ilikuwa ni ile alama ya damu chini kabisa ya ujumbe ule. Alirudia tena kuusoma kisha akaiweka ndani ya droo ya meza ya Santana.
" Ehh ilikuwaje mke wangu huko ulikokuwa? "
" Kama nilivyosema hapo mwanzo bosi wako si mtu mzuri kwani ameingia na kunikuta hapa badala ya kuniuliza imekuwaje yeye akaanza kunikuta mabao."
"Ndiyo ukamfanya nini tena?"
"Sikumfanya chochote bali yeye baada ya makelele yake alianguka chini na ndipo nilipopiga kelele za kuomba msaada."
"Pole sana mke wangu, lakini nini kilikukuta huko?"
"Ni hivi mume wangu, baada ya kuniacha pale nyumbani nilipokea wageni masaa kadhaa mbele wakijitambulisha kuwa ni wageni wako wa kibiashara lakini mambo yalibadilika baada ya kukupigia simu ni kama hamkuelewana ndipo waliponichukua na kunipeleka kwenye nyumba ambayo sikuitambua vizuri kwani nilifungwa kitambaa usoni na baada ya masaa kadhaa tena baadaye walirejea wale mabinti wawili na kunitoa tena eneo lile na kunipeleka eneo jingine ambalo ni magofu ya majengo ya kale huko ndiko nilikokuwa mpaka alipotokea kijana mmoja ambaye kwenye kuniweka kwenye ficho la awali alikuweko na kunichukua na kuniambia kuwa bwana yako na bosi wako wanafanya mambo ambayo si ya kiungwana kwani mpaka sasa wamewapoteza wenzetu watatu ndipo nikabaini ni wale wadada, kisha akasema hatuwezi kukuua kwa sasa ila mume wako na bosi wake wasipotekeleza mahitaji yetu tu usije kutuelewa vibaya tutakuua dada. Waliniambia hayo tu mume wangu hivyo nakuomba fanyeni kila linalowezekana mmalizane na wale watu kwani si wakawaida hata kidogo mume wangu."
Baada ya kuyasikia maneno yale ya mke wake mzee Bruno Gautier hakuongea kitu zaidi ya kumfuata Santana kule ambako alikuwa kalazwa kwa uchunguzi zaidi.
" Vipi amefungua macho? "
Mzee Bruno Gautier aliuliza.
" Bado mzee hajafanya hivyo mpaka sasa."
Alijibu Melissa.
Lakini mzee Bruno akiwa anakaa pembeni ya Santana mara simu ya Santana iliingia ujumbe. Ikabidi mzee Bruno aichukue simu ili auangalie ujumbe huo.
" NDANI YA MASAA KADHAA YAJAYO TUNAKWENDA KUKUTIA HASARA SANTANA."
Baada ya kuusoma hakuongea kitu zaidi ya kuiweka simu mfukoni na kutoka zake nje. Huku akiwaacha wenzake wakiwa hawajui kilichotokea baada ya kusoma ujumbe huo.
JE NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
Ndani ya Hospitali ya Makambi iliyo ndani ya mji wa Windhoek madaktari walikuwa kwenye kikao kizito juu ya wagonjwa watatu ambao ni Jackline, Jessica na Jasmine ambao mpaka wakati huo walikuwa bado hawajazinduka pamoja na juhudi zao zote za kuwahudumia. Mkurugenzi mkuu wa Hospitali hiyo ya Makambi bwana Hans Murray aliamua kufanya maamuzi mazito juu ya hili.
"Kwanza niwapongeze kwa juhudi zenu zote mlizozionesha kwa hawa wagonjwa tulioletewa kutoka Namport kuanzia siku ya kwanza mpaka leo hii tunapowajadili, kitu kimoja ninataka kukifanya juu yao kwani naliona kama jaribu kwetu na iwapo hatutalishinda jaribu hili tutaupoteza umaarufu wetu na Brand yetu itashuka na kupotea kabisa wataalamu wangu hivyo katika kuliona hili nimeamua kuwaleta Madaktari Bingwa kutoka Ujerumani ambao wamebobea zaidi kwenye mfumo mzima wa mwanadamu huenda watatusaidia kubaini tatizo linalowakabili."
Alifafanua Mkurugenzi.
Wakati kikao hicho kikiendelea baina ya madaktari na Mkurugenzi wao mara aliingia Nesi wa zamu kwenye chumba cha wakina Jackline na kuleta taarifa ambayo ilipelekea kusimama kwa kikao hicho huku kila mmoja akishika njia kuelekea chumbani kwa wakina Jackline na katika hilo mpaka Mkurugenzi bwana Hans Murray akishika njia mbio mbio kuelekea huko chumbani.
"Jamani ni kweli huyu hapa kafumbua macho."
Daktari mmoja aliongea kwa mshangao baada ya kumkuta Jackline akiwa kafumbua macho yake huku akiangalia huku na kule bila shaka mazingira yalimchanganya kidogo.
"Wataalamu nawaombeni tupungue kidogo ili kutoa nafasi kwa mgonjwa kutuliza akili yake kwani hapa bado anayashangaa mazingira hivyo uwingi wetu ndiyo unamchanganya kabisa, nafikiri abakie daktari husika na nesi mmoja wengine tukaendelee na majukumu mengine."
Mr Hans Murray aliwaomba wafanyakazi wake kupungua mle ndani ili kumpa nafasi Jackline ya kujenga kumbukumbu vizuri ya matukio ya nyuma kisha naye aliondoka.
" Bila shaka leo kutakuwa na taarifa nzuri kutoka kwako kaka Hans."
Daktari Abbas Mukesh aliongea baada ya kuipokea simu ya rafiki yake daktari na Mkurugenzi mkuu wa Makambi Hospital bwana Hans Murray.
"Naweza sema hivyo rafiki yangu huwezi amini dakika kumi zilizopita mgonjwa mmoja yule ambaye ni mwembamba kafumbua macho tayari ikiwa ni kama dakika kadhaa tukiwa kwenye majadiliano ya kuongeza nguvu kwa kuleta wataalamu wengine kutoka Ujerumani kwa gharama zetu ili kuilinda Brand yetu tuliyoitengeneza kwa muda mrefu."
"Brother unachokiongea ni kweli au umeamua tu leo kunijaza?"
Daktari Abbas Mukesh aliuliza baada ya kukaa kimya kwa muda akimsikiliza tu daktari Hans Murray.
"Nataniana sana na wewe Abbas lakini kwenye kumbukumbu zako unaweza kuniambia ni lini niliwahi kukutania mida ya kazi?"
"Kwa hilo nikiri halijawahi tokea kaka."
Daktari Abbas alikiri.
"Sasa iweje leo niuvae ujasiri huu wa kuinua simu na kukupigia kisha kukueleza taarifa za uongo?"
"Kulingana na jambo lenyewe lilivyochukua muda mrefu nilianza kupoteza matumaini ya kupona kwao na ndiyo maana ulivyonieleza tu nikajua unanidanganya,nisamehe bure kaka."
"Aaah achana na hizo dogo lakini weka akilini kuanzia sasa kuwa mgonjwa wa kwanza keshaamka tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu awatendee miujiza na hawa wengine wazinduke usingizini."
"Nashukuru sana kwa taarifa hizi ambazo naweza kusema ni spesho kwangu kwa siku ya leo, kesho mapema nitakuwa hapo kwa lolote litakaloendelea tujulishane kaka wala usichoke."
"Tulikubaliana toka awali na itakuwa hivyo mpaka mwisho mdogo wangu daktari Abbas."
"Mungu akubariki wewe na timu yako ya Madaktari kaka."
"Na wewe pia iwe hivyo."
"Shukrani sana."
Baada ya simu kukatwa daktari Hans aliingia ofisini kwake akaketi kitini kwake na kuipandisha miguu yake juu ya meza akiwa anaigongagonga mikono yake aliyoikunja mdomoni, kama haitoshi ni kama alikumbuka kitu aliinuka na kutoka nje ya ofisi yake na kuelekea kule kwenye kile chumba walicho wakina Jackline.
"Samahani kaka wewe ni nani na hapa ni wapi?"
Ni swali alilolikuta likitoka kinywani mwa Jackline akimuuliza daktari yule aliyekuwa akimuhudumia. Ilibidi abakie pale pale mlangoni ili asikie mgonjwa wao yuko katika hali gani ya utambuzi.
"Naitwa Daktari Ramadhan na yule pale mezani ni nesi anaitwa Mariam."
Daktari Ramadhan alijitambulisha.
"Daktari, Nesi..." Alirudia tena kutaja tambulisho hizo akiwa kama anakumbuka kitu hivi.
"Ndiyo sisi ni wahudumu wa hospitali hii ya Makambi."
Aliongeza Nesi Mariam aliyekuwa akimuandalia maji ya glucose.
"Nilifikaje fikaje hapa hospitali rafiki zangu Jasmine na Jessica wako wapi?"
Jackline aliuliza.
"Pumzika kwanza dada yangu ukiwa sawa kila kitu utakifahamu."
Daktari Ramadhan alimjibu hivyo baada ya kumuangalia bosi wake aliyetoa ishara ya kutomwambia kitu kwanza.
"Daktari unafikiri mimi ninaumwa? Siumwi hata kidogo bali nilizimia tu baada ya kuvuta hewa yenye sumu, kwanza Robinson na wenzake wako wapi? Kwa akili zenu utashangaa kuona mmewaachia."
Jackline alipoona kama vile anataka kufichwa ukweli aliwahakikishia kuwa yeye si mgonjwa na kitendo cha kulitaja jina hilo pamoja na sumu ndipo wakahisi inawezekana ulikuwa ni ugomvi wa kimapenzi.
" Nakuomba kunywa maji haya kisha pumzika kwanza..... "
Nesi Mariam alimuomba Jackline.
"Kitu kimoja tu ili nitulie nahitaji kukifahamu kutoka kwenu Jasmine na Jessica wako hai? Na wakina Robinson wamekamatwa?"
"Dada yangu hao ndugu zako ni wazima kabisa na hao wengine wako chini ya vyombo vya dola."
Baada ya kusikia hayo kutoka kwa Nesi Mariam, Jackline alipokea ile glasi ya maji akanywa na kisha akamrudishia Nesi kilichofuata alijigeuza na kulala.
Walimfunika vizuri kisha wakaviendea vitanda vya Jasmine na Jessica vilivyokuwa vimezungushwa mapazia ya rangi kuangalia kama kuna mabadiliko kwenye hali zao.
"Huyo tayari yuko vizuri kwani kwa kitendo cha kulikumbuka tukio la mwisho ni ushahidi tosha kwetu kuwa yuko vizuri, cha kufanya ni kumfanyia mpango wa lishe kisha tutapata utambulisho wao hapo kesho."
Daktari Hans alizungumza hayo baada ya kuingia kwenye vitanda walivyolazwa wakina Jessica na Jasmine ambako hata Jackline naye alikuwa huko lakini baada ya mabadiliko hayo alitolewa.
" Mkuu tunaweza kuzungumza kidogo? "
Daktari Ramadhan alimuomba bosi wake daktari Hans Murray. Aliomba wakati huo Nesi Mariam alikuwa akiwafunika vizuri wagonjwa wake.
"Daktari Ramadhan bila shaka tunaweza tu kama ni hapa au nje ni wewe tu."
Daktari Hans Murray alimkubalia Daktari Ramadhan hivyo walitoka nje ya chumba hicho na kuelekea kwenye bustani ya maua ya Hospitali hiyo na kuketi kwa mazungumzo.
"Naomba nikusikilize Mtaalam wangu."
"Nashukuru sana bosi, kuna wazo ambalo nimelipata tukiwa mle ndani."
"Wazo gani hilo Rama?"
"Ni juu ya yule binti kwa namna nilivyomuona nimebaini kuwa kuna magumu mengi ambayo kayapitia hivyo nikaona niongee na wewe uweze kuongea na mzee yule aliyewaleta ikiwezekana tumpeleke kwenye Kituo chetu cha Saikolojia na Utimamu wa Akili ili tuweze kuwajenga."
Daktari Ramadhan alimweleza bosi wake wazo lake.
" Nashukuru kwa kuliona hilo hivyo ngoja nifanye mpango wa kuwasiliana na rafiki yangu aliyewaleta huku bwana Abbas Mukesh yeye itakuwa rahisi zaidi kuongea na mzee Jerome Whistle akifanikiwa kuhusu Kituo haina shida ni chetu kile lakini wakati huo huo unatakiwa kujua kuwa mwenye maamuzi ya mwisho ni mhusika mwenyewe alikubali sawa lakini pia akikataa ni haki yake."
Daktari na Mkurugenzi mkuu wa Makambi hospitali bwana Hans Murray alikubaliana na Daktari Ramadhan lakini alitoa tahadhari pia.
Upande wa Jackline akiwa kajilaza pale kitandani mara mtiririko wa matukio ulianza kupita kichwani kwake kitu kilichomfanya kupiga kelele ambazo ni kama ziliamsha tukio ambalo halikutarajiwa na madaktari wote kiasi cha kubakia midomo wazi.
"Nasema haiwezekaniiiiii hata kidogo tunarudi tena ulingoni, wanajeshi wangu amkeeeeeniiiiiiiii..............!"
"Samahani dada tafadhali, pumzika hujapona vizuri."
Nesi Mariam alimuomba Jackline ajipumzishe baada ya kumkuta akipiga makelele.
"Bora umekuja Nesi kabla ya yote nieleze hii hospitali iko wapi?"
Jackline alitokwa na swali.
"Hii ni hospitali ya Makambi iliyoko Windhoek....."
"Ina maana hapa ni Namibia? Mungu wangu nimefikaje hapa mimi?"
" Uliletwa na mzee mmoja hivi anaitwa mzee Jerome akiwatoa hospitali ya KING'S MEDICARE CENTRE bila shaka huyo anafahamu mlifika vipi hapa nchini."
"Santanaaaaaaaaaaaaa.......................!!! Am back jiandae."
"Saa...samahani dada yangu nimekusikia ukiyataja taja majina kadhaa mara Robinson mara Santana hawa ni wakina nani?"
Nesi Mariam alimuuliza Jackline baada ya kuona akitaja jina Santana kwa hasira zaidi.
"Tuko wapiiiiiiiiiiiii........."
Sauti zilitoka kule walikokuwa wakina Jasmine. Nesi Mariam alichanganyikiwa akajikuta badala ya kwenda zinakotoka zile kelele yeye alitoka mbio kuelekea ofisini kwa Dakika wa kitengo huku nyuma akabakia Jackline ambaye naye alizisikia zile kelele na hivyo alishuka pale kitandani na kuelekea kule kwenye mapazia.
"Jasmine, Jessica na ninyi mko mahali hapa? Tumefikaje hapa?"
Jackline aliongea akiwa kawakumbatia wenzake ambao alijua katengana nao.
"Melissa yuko wapi? Na vipi kuhusu wakina Robinson na mzee Bruno Gautier?"
Jessica aliuliza swali akiwaangalia wenzake.
"Jessica achana na maswali hayo kifupi hapa hatuko Brazil tena nimeambiwa na Nesi...."
"Subiri kwanza Jackline unasema hatuko Brazil tuko wapi sasa?"
Jasmine alijikuta akiuliza.
"Hapa tuko Windhoek Namibia."
Jackline alijibu.
"Namibiaaaa !!!!!"
Walijikuta wakiuliza kwa pamoja.
"Sikilizeni mwenzenu mpaka muda huu nimefanikiwa kuwahadaa hivyo na ninyi fanyeni hivyo ili tubaini lengo lao sawa?"
Jackline aliwaambia hivyo wenzake ambao hawakuelewa alimaanisha nini.
"Waooo kama zali vile wamezinduka wote sasa na hili litapelekea hospitali yetu kujipatia umaarufu."
Daktari Ramadhan alizungumza baada ya kuwakuta wakina Jasmine nao wamezinduka.
"Samahani daktari leo jumangapi?"
Jasmine aliuliza swali.
"Leo ni Juma......" Kabla hajamalizia sentensi yake alijikuta akitemewa mate usoni na Jessica.
"Si niliwaambia kuwa noo...., sorry kumbe haukuwa wewe nilishasahau kuwa niliongea na Mkurugenzi mwenyewe."
Daktari Ramadhan alijikuta akitokwa na maneno yasiyo na utaratibu.
"Dokta mbona sikuelewi? Unasema hukuongea na mimi kitu gani?"
Nesi Mariam alimuuliza.
"Okay, okay namaanisha kuwa niliongea na Mkurugenzi kuwa hawa wagonjwa tutatakiwa kuwapeleka kwenye Kituo maalum cha Saikolojia kwa ajili ya kuwajenga Kisaikolojia hawako vizuri kiakili si umeona walichokifanya?"
Wakati Daktari Ramadhan akiongea hayo wakina Jackline wenyewe walikonyezana kama ishara ya kuanza kuishinda baadhi ya mitihani.
" Samahani daktari unaweza kutupeleka Gereji?"
Jackline alimuuliza daktari Ramadhan.
" Gereji?? "
" Ndiyo...!!! "
" Kufanya nini huko Gereji tena?"
Aliuliza Nesi Mariam.
"Hamuoni mwenzetu hapa mguu wake umewekwa rangi nyeupe hivyo inatakiwa akafanyiwe usafi na marekebisho."
Jackline alijibu na kuwafanya wale wahudumu kujivuta pembeni kidogo ili watete.
"Daktari hivi unawaelewa vizuri hawa wagonjwa?"
Nesi Mariam alimuuliza daktari Ramadhan.
"Mhh hata sina la kuongea hebu twende kwa bosi kwanza na pia itafute namba ya yule mzee mweleze kuwa watu wake tayari wamezinduka ila hawako sawa kiakili."
Sawa Daktari.
"Simnaona huu mchezo? Mmeuelewa maana yake?"
Jackline aliwauliza wenzake.
"Wala mimi sijaelewa hata moja."
Jasmine alijibu.
"Mimi ndiyo kabisaaa sijamuelewa."
Jessica naye alijibu.
"Ni hivi jamani kama nilivyowaambia kuwa huku tuko Namibia na hapa ni hospitali, kama mnakumbuka tukio la mwisho lilikuwa ni lile la pale kwa Melissa lililofanywa na wakina Robinson ambalo lilipelekea sisi kupoteza fahamu zetu hivyo hamuwezi kujua iwapo ni mchezo wa Santana huu hivyo hapa tunatakiwa kuondoka haraka sana ila kwa muda huu ambao bado hali zetu haziko sawa maigizo yawe ni asilimia mia moja."
Jackline aliwafafanulia.
" Okeeeey Hapo nimekuelewa dada yake."
Jessica alimjibu.
" Tuko pamoja tunatakiwa tusiwape nafasi ya kutujua undani wetu."
Jasmine naye aliungana nao.
Mara waliwasikia Madaktari wakija mle ndani hivyo kila mmoja alikimbilia kitanda chake.
JE NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.
"Naona wameshalala tayari, sasa angalia lala yao ilivyo yule kalala kichwa tu ndiyo kiko kitandani, huyu huku miguu juu na huyo huko yeye kaamua kulala uvunguni kabisa nafikiri maneno yangu yataeleweka vizuri mkuu hawa wamerudiwa na fahamu lakini akili zao zinagonga na kutoka."
Daktari Ramadhan tumeona hili ni tatizo tayari na kama ambavyo ulishauri nadhani iwe hivyo hawa tuwapeleke kwenye Kituo chetu cha Saikolojia inaweza kusaidia."
Mkurugenzi bwana Hans Murray aliungana na daktari Ramadhan baada ya kujionea mwenyewe hali halisi mle ndani.
" Samahani wataalamu wetu mimi nilikuwa nina ombi kidogo kama mtanielewa itapendeza zaidi."
"Tunakusikiliza mzee Jerome uko huru kabisa."
Daktari Hans Murray ambaye ndiye Mkurugenzi mkuu wa Makambi Hospitali alimruhusu.
"Kwa kuwa tayari fahamu zao zimerejea na tumepata uhakika wa kuwa wako hai ombi langu kwenu naomba niwasubiri waamke kisha niweze kuongea nao watakapokuwa wanakula chakula naweza kupata suluhisho lao kabla ya kuwapeleka huko mnakokusema ni hivyo tu japo sipingani na mawazo yenu pia."
"Hilo linawezekana tu mzee Jerome, na kama ulivyoomba iwe hivyo ili wakiamka tunaweza kupata chochote kutoka kwao kwani mpaka sasa wao ndiyo wenye undani wa yaliyowakuta na pia sifikirii kama wote akili haziko sawa lazima kati yao kuna aliyesawa. Hivyo mzee Jerome wewe endelea kuwasubiria waamke kishe utaongea nao na kwa yale ambayo mtayafikia utatujulisha na sisi."
"Bila shaka Mkurugenzi."
Mzee Jerome alimjibu daktari Hans Murray na kisha wote walitoka na kumuacha mzee Jerome mle ndani akiwa mtoto wake Mustapha.
"Hivi baba suala hili unalionaje wewe ikiwa kama watakuwa na matatizo ya akili utaendelea kuwahudumia?"
Mustapha alimuuliza baba yake walipokuwa wakisubiri waamke wagonjwa wao.
"Nisikilize mwanangu Mustapha kwa umakini sana hii ni Dunia na ina mambo mengi sana ambayo tunayafahamu na mengine tunayasikia tu, Mungu huwafanyia majaribu watu wake kila uchwao ili kuweza kujua watayakabili vipi hayo majaribu. Mfano angalia kwa upande wetu mwanangu nina miaka zaidi ya thelathini kwenye kazi yangu ya uvuvi sijawahi kukutana na tukio kama hili zaidi ya kuwakuta watu wakiwa hai wakitaka msaada au maiti tu baharini ambazo hizo zimejazana tu huko."
"Ni kweli kabisa baba lakini huoni kama kuendelea kulifuatilia hili jambo litatupotezea muda na wateja wetu wa samaki na usisahau kuteketea kwa hela zinazotumika kwenye matibabu yao mzee."
"Uko sahihi kabisa lakini tambua kuwa utu unadhani kubwa kuliko hata hizo hela unazozisema mwanangu na mwisho wa siku Mungu ndiye mwenye mamlaka atafanya kitu na mwisho tutarejea kwenye kazi yetu lakini tofauti na hapo tutaendelea kuwapa msaada wa hali na mali hawa mabinti."
"Mmhh haya sawa mzee wangu japo najua kwanini umelivalia njuga hili."
"Unajua nini Mustapha?"
Mzee Jerome aliuliza kwa ukali kidogo.
"Ni kwa sababu hauna mtoto wa kike hivyo umeona kama zawadi imeshuka kutoka juu kama zile Mana ambazo zilianguka kule Jangwani."
Mzee Jerome baada ya kusikia hivyo kutoka kwa mtoto wake alimsogelea na kumkumbatia kwa nguvu.
"Hicho nacho ni miongoni mwake mwanangu vipi hupendi kuwa na wakina dada?"
"Napenda baba ila si kama hawa nawataka kutoka kwenye uzao wako."
"Kumbuka kuwa kuna watoto wa kuasili pia ambao ni wa kimkataba."
"Samahani naomba maji ya kunywa..."
Jackline aliongea baada ya kushindwa kuingiza kwa muda mrefu.
"Baba kaamka huyu huku na anaomba maji ya kunywa."
Mustapha alishtuka baada ya kusikia sauti ikiomba maji ya kunywa.
"Mletee maji haraka Mustapha."
Mzee alimuagiza mtoto wake
huku yeye haraka sana alimsogelea Jackline pale kitandani ambapo muda huo alikuwa kakaa.
"Pole binti yangu."
Mzee Jerome alianza kwa kumpa pole.
"Asante mzee wangu, na wewe ni mhudumu hapa hospitali?"
Jackline alimuuliza mzee Jerome.
"Hapana mimi si mhudumu binti yangu bali....."
"Maji haya hapa dada." Mustapha aliingilia kati mazungumzo yao.
"Okay kunywa kwanza maji kisha tuendelee na mazungumzo yetu."
"Sawa baba yangu."
Jackline alipokea glasi ya maji na kunywa. Na baada ya kumaliza alimkabidhi Mustapha ile glasi kisha akakaa vizuri kama vile alikuwa akisubiri kitu kutoka kwa mzee Jerome.
"Binti yangu naitwa mzee Jerome Whistle mvuvi maarufu ndani ya nchi hii na makazi yangu yako ndani ya mji wa Namport huyu aliyekupa maji ni kijana wangu anai..."
"Samahani mzee." Jackline alimkatisha mzee Jerome.
"Nimeyasikia maongezi yako na mwanao kuanzia mwanzo mpaka mwisho na nimebaini kitu kutoka kwako mzee wangu, kifupi sisi hatuna matatizo ya kiakili kama mnavyozania ni wazima wa afya kabisa ila kuna mengi yako nyuma ya pazia."
Mara Jasmine na Jessica nao waliamka na kusogea kuungana nao kwenye maongezi yao.
" Ni kweli kabisa baba yetu."
Jessica na Jasmine walijibu kwa pamoja.
" Ina maana ninyi si.... "
Mzee Jerome alitaka kuuliza kitu lakini kabla hajamalizia sentensi yake waliingilia na kujibu kwa pamoja kama walijua alitaka kusema nini.
"Sisi si wagonjwa kabisa."
Walijibu kwa pamoja.
"Mungu wangu, ina maana...."
Hakumalizia Jackline alimkatisha.
"Mzee wangu kuna kauli ulimuomba Mkurugenzi wa hospitali hii sijui unaikumbuka?"
"Ipi hiyo binti yangu?"
"Okay tuache hayo, tunachokuomba kwa sasa tumia uongo wako wote kumpanga yule Mkurugenzi ukituomba kuwa unataka kutupeleka Kanisani kwa maombezi huko tutakueleza kila kitu, na kwa sasa sisi ngoja tulale vile vile kama humjaongea kitu na sisi."
"Basi sawa ngoja nimfuate Mkurugenzi nikajaribu kuongea naye."
Mzee Jerome alitoka na kuwaacha mle ndani.
"Mtafanyaje iwapo watakuja kutaka kujua hali yenu?"
Mustapha aliwauliza wakati wakijifunika mashuka.
"Brother kaa subiri uone mchezo wetu."
Jasmine alimjibu akijifunika shuka lake.
"Duuuu...."
Mustapha aliishia kushangaa tu.
Kama alijua vile mara waliingia mzee Jerome pamoja Mkurugenzi Hans Murray na timu yake.
"Vipi bado hawajaamka tu?"
Daktari Hans Murray aliuliza.
"Bado hawajaamka inaonekana wamechoka sana."
Mustapha aliwajibu.
"Kama ambavyo tumeongea Daktari nilikuwa ninaomba ulifanyie kazi ombi langu tafadhali."
Mzee Jerome aliongea wakati daktari Hans Murray akiwakagua joto la miili yao.
"Bila shaka mzee wangu hilo halina tatizo kikubwa tusubiri waamke tucheki watakuwaje kiafya kisha tutakukabidhi."
"Nasikia harufu ya damu mbele yangu Jasmine na Jessica mko wapi nileteeni kisu changu niweze kufanya yangu hawatujui eeehhh sisi ndiyo viumbe vya ajabu vinavyoishi majini nileteeni haraka wadogo zanguuuu...."
Jackline alianza kuongea maneno hayo ya ajabu huku akiwafuata wakina Hans.
" Mungu wangu nini tena hiki mbele yetu?"
Daktari Hans Murray aliuliza.
" Usihangaishe akili yako Dr Hans Murray juu yetu, sisi siyo watu wa kawaida na bahati yako tunamuona moyo wako ni wa kipekee ama sivyo tungeinyonya damu yako na ya hao waliokuzunguka na kwa usalama wako mruhusu mzee Jerome aondoke na sisi muda huu."
Jasmine aliendeleza mkwara ule mbele ya daktari Hans.
" Wakamateni hao kabla kichaa hakijawapanda kichwani haraka."
Daktari Hans Murray hakutaka kuonyesha kuwa mchovu ilibidi atumie mamlaka.
****
" Kijana wangu kwa haya yanayoendelea unasemaje?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza Santana baada ya kuzinduka.
"Da yaani mpaka sielewi nifanye lipi na lipi niliache mzee wangu, anasemaje mke wako aliletwa na wakina nani na alikuwa wapi?"
Santana alimuuliza mzee Bruno.
"Yeye kasema anachokumbuka ni kutekwa na wasichana watatu ambao walimfunga kitambaa usoni na hakuweza kujua walimpeleka wapi maana ni kama kile kitambaa kilikuwa na madawa anasema hakumbuki kilichoendelea zaidi ya siku ya leo kuzinduka na kujikuta mikononi mwa vijana waliomtishia kumuua kama ataleta jeuri hivyo ikabidi atulie tu na ndipo aliposhangaa akiletwa hapa."
Ilibidi mzee Bruno Gautier adanganye tu baada ya kuona Santana ni kama ana hasira na mke wake Bi Claudia.
" Hakuwafahamu hao vijana hata mmoja wao hivi?"
Aliendelea kumchimba maswali mzee Santana.
" Hapana kasema sura zile ni ngeni machoni kwake hakuwahi kuziona sehemu yoyote ile hapa."
"Tunafanyaje kuwapata hao Mbwa nina uhakika hawajaenda sehemu yoyote ile na ndiyo maana wanaendelea kututumia vimeseji vyao hapa."
Santana aliuliza hayo akiwa anapitia meseji mbalimbali za vitisho kutoka kwa Roberto.
"Unaonaje kama tukiongeza nguvu kwenye ulinzi ili kila kona ya Ngome iwe na walinzi halafu na kule kwenye nyumba ya Melissa nayo tupeleke walinzi nahisi itasaidia kidogo."
Mzee Bruno Gautier alipendekeza mapendekezo yake.
"Mkuu usisahau kule Mgodini nako kumesahaulika sana."
Robinson aliwakumbusha kuhusu kule Mgodini.
"Kule ondoa shaka Robinson muda mrefu sana tulishapeleka walinzi kutoka kampuni ya ulinzi ya nchini Marekani wenye Uweledi na shughuli zetu hizi."
Mzee Bruno Gautier alimuondoa wasiwasi Robinson aliyekuwa hajui chochote kinachoendelea.
"Sorry bosi nilikuwa gizani."
"Bila shaka."
Mzee Bruno Gautier alimjibu.
"Vipi hakuna taarifa zozote kutoka Afrika? Na vipi kuhusu jamaa yako mliwasiliana anasemaje?"
Santana aliuliza maswali hayo wakiwa njiani kuelekea ofisini kutokea Kituo cha tiba mle mle kambini.
"Kule bwana mdogo anaendelea na uchunguzi wake taratibu japo mpaka jana alisema hakukuwa na dalili zozote za kuwepo watu wa aina hiyo pale KING'S MEDICARE CENTRE."
"Mwambie asitupikie taarifa sisi ni Mafya hatutaangalia anatoa msaada ama la tutaondoka na roho yake iwapo tutabaini katudanganya."
"Ninamuamini sana yule dogo hawezi niletea wali uliochacha hata kidogo."
"Okay sawa, kumbe kinachotakiwa kwa sasa ni kulifanyia kazi wazo lako la sivyo tutaumbuka."
Aliongea hayo akiwa katupia macho yake kwenye ukuta wa ngome yake kama kuna kitu alikiona ambacho si cha kawaida.
Bila kuongea kitu aliitoa bastola yake na kuliendea eneo lile kitendo kilichowafanya na wakina Robinson nao kukamata silaha zao sawa na kumfuata bosi wao.
Hawakuamini macho yao baada ya kumuona Melissa akiwa chini akigugumia kwa maumivu.
"My boooss ha...ha...hali ime... chafuka tu...."
Kabla hajalimalizia neno lake alikata kauli baada ya Izrael mtoa roho kumpitia.
"Melissa, Melissa, Melissaaaaaaaaaaaaaa........!!! Nooooo amka mtu wangu unakufaje mapema hiviiiiiiiii?
Santana alipagawa kwani hakujua afanye lipi wakati huo ni tukio ambalo hakulitegemea kabisa.
" Chude, Robinson mnafanya nini hapaaaaaa tokaaaaa."
Aliwafukuza akiubeba mwili wa Melissa mwenyewe.
"Mnashangaaa nini hapa zungukeni kila kona kuwatafuta hao panya ambao wanaogopa ogopa na kuingia kwa kuvizia."
Mzee Bruno Gautier aliwafokea wakina Robinson ambao mpaka muda huo hawakujua wafanye nini.
Lakini wakiwa bado hawajui la kufanya muda huo Santana na Claudia wakikimbia kuelekea ofisini kumpeleka Melissa wakihisi wanaweza kufanya kitu kuokoa uhai wake mara walisikia mlio upande ambao ndege hupaki na walipoangalia hawakuamini macho yao baada ya kuona moshi mzito eneo hilo.
"Mzee Bruno nini tena kule kimbieni kuangalia ni nini kimetokea?"
Santana aliongea akiutua mwili wa Melissa ambao nahisi hakuona umuhimu wake muda huo na kuelekea kwenye egesho la ndege akimuacha Claudia pale na mwili wa Melissa.
"Tumevamiwa kijana wangu."
Mzee Bruno Gautier aliongea baada ya Santana kufika na kuishuhudia ndege ikiteketea kwa moto wakiwa hawajui waokoe nini kwani moto ulikuwa ni mkubwa sana.
"Haiwezekani hata kidogoooooo !!! Kwanini haya yatokee muda huu ambao nilijua kila kitu kimekwisha???"
Santana aliongea huku machozi yakimtoka bastola yake ilikuwa chini akijipigapiga vibao vya mashavu kama vile tayari alisharukwa na akili.
"Watafuteniiii haraka hao wanaharamuuuuuu wakiwa hai au wamekufa ninachokihitaji muda huu ni nyama yao tu."
Baada ya kelele hizo ambazo wakina Chude walishazizoea kazi ilikuwa kwa Robinson ambaye alikuwa hajamzoea waliondoka na kuelekea nje ya ngome ambako waliamini wanaweza kuwakamata lakini hata walipofika nje hawakuweza kuona chochote zaidi ya kukutana na karatasi iliyokuwa na ujumbe wenye sahihi ya tone la damu waliuchukua na kuupeleka kwa Santana.
"Nitawauaaaa nasema nini kimewarudisha yaani dakika moja mnarudi au mnaogopa??"
Santana alikuwa kama Kifaru muda huo hakutaka kusikia chochote macho yakiwa kwenye ndege yake ambayo muda huo ilikuwa ikisambaratika vipande vipande.
"Bosi kuna ujumbe huu tumeukuta getini umewekwa chini."
Robinson aliongea hayo akiwa anamkabidhi ujumbe huo ambao aliunyakuwa tu bila utaratibu wowote na kuanza kuusoma.
"SANTANA JITU LINALOTISHA HABARI...
NAFIKIRI SALAMU ZANGU UMEZIPATA SIKU YA LEO? KAMA AMBAVYO NILIKUAHIDI KUWA NITAKUWA NAMNYOFOA MMOJA MMOJA HUKU NIKITEKENYA KWAPA ZAKO NIONE KAMA HUWEZI KUCHEKA NA HAPO NIMELITEKENYA HILO LA KUSHOTO NDANI YA SIKU KADHAA NAHAMIA LA KULIA UMENIELEWA LAKINI? "
WAKO....... (ikawekwa alama ya tone la damu)
" Usimtishe Santanaaaaaaaaa weweeeeeeeee mimi sitishiwi kijinga hivyooooo pa pa pa pa paaaa.... "
Alipiga kelele na kuanza kupiga risasi juu bila mpangilio.
" Nasema poteeni hapa haraka sitaki kuona kiumbe chochote hapa nitamwaga damu mimiiiiii na Ole wenu mrudi mikono mitupu hapa nitawaonesha kazi."
Aliwafukuza wote safari wote mpaka mzee Bruno Gautier huku yeye alirudi ndani kwake na bila ikiwa ni kwenda kunywa mipombe mikali.
NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
Mzee Kaaya alichanganyikiwa sana kwa taarifa zile ambazo aliambiwa na Roberto kiasi cha kumfanya apange kukutana na mkuu wa kituo pale Lupa lengo ni kuweza kujua hatma ya mzee Jonathan ikoje katika hili hakutaka kabisa kumshirikisha mke wake kwani aliijua hatari ambayo ilikuwa mbele yao kwani mke wake hana kifua cha kukaa na siri na ukizingatia wanaishi na mdogo wa Jackline.
"Sasa kama kweli hilo lilitokea huko Brazil ilikuwaje miili yao ikapatikana huko Namibia? Na baada ya kupatikana ni wazima au wamekufa? Robinson kapatwa na shetani gani mpaka kufikia hatua ya kumuua mwenzake? Eee Mungu wangu niepushie mbali hili balaa."
Mzee Kaaya alitembea huku akiongea peke yake akijiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu na mwisho aliamua kumkabidhi Mwenyezi Mungu swala lake ili awe hakimu, alifika kituoni na kugonga ofisi ya mkuu wa kituo.
" Aahh mzee Kaaya pita ndani."
Mkuu wa kituo bwana Mkonge alimkaribisha baada ya kuufungua mlango.
"Asante kijana wangu." Aliitikia na kuingia ndani kisha mlango ukafungwa na mwenyeji wake.
"Kwema utokako mzee wangu?"
"Ni kwema tu Afande, nikaona leo nikutembelee kujua huko Makongolosi wanasemaje kumhusu mtuhumiwa wetu?"
Mzee Kaaya alimuuliza Afande Mkonge.
"Okay, kule taarifa zilizotufikia si nzuri mzee wangu."
"Kivipi Afande?"
"Inawezekana watuhumiwa wametoroshwa na askari wawili wa zamu na mpaka hivi bado haijafahamika waliko kutokana na geti zote tulizoweka kuripoti taarifa za kufanana kuwa hawajawaona."
"Isiwe utani Kamanda, wanawezaje kutoroka kirahisi hivyo? Au ulikuwa ni mpango na ndiyo maana waliwafuata? Mbona hapa walikaa siku nyingi lakini hawakutoroka?"
Mzee Kaaya alimtupia maswali mfululizo Afande Mkonge.
"Mzee wangu naomba nikuhakikishie kuwa hakukuwa na mpango wowote juu yao bali ni utaratibu tu wa kazi sema hilo limetokea kama ajali tu."
"Afande tulia kimya unawasemea wewe?"
"Hapana mzee wangu ila naomba nikuhakikishie kuwa Jeshi letu la Polisi halijalala mpaka sasa vijana wetu wa hapa, Makongolosi na wale wa Chunya wako porini kuhakikisha wanawapata watuhumiwa wote."
Afande Mkonge alimpa moyo mzee Kaaya.
"Afande naona mimi nikuache tu maana hapa naona naimbiwa taarabu badala ya uhalisia."
Mzee Kaaya alipata hasira na kuondoka zake na kumuacha mkuu wa kituo akiishia kumtumbulia macho tu bila kuongea chochote.
"Huu ni mkosi sasa huko nje ya nchi mauaji yamefanyika huku tena hawa nao wamemtorosha mtuhumiwa nini maana yake sasa?"
Mzee Kaaya alikuwa akijiongelesha mwenyewe akiwa njiani kurudi nyumbani.
Aliongoza moja kwa moja mpaka nyumbani kwake hakuona sababu ya kupitia sehemu yoyote ile.
"Mume wangu za matembezini huko?"
Mke wake alimsalimu baada ya kufika nyumbani.
"Huko kwema mke wangu, vipi hapa ninyi mmeshindaje?"
"Sisi tumeshinda salama tu mume wangu, lakini nakuona hauko sawa kuna nini?"
"Nani mimi?"
Mzee Kaaya alijikuta akimuuliza mke wake baada ya kuulizwa swali.
"Jamani sasa ninaongea nani hapa mume wangu?"
"Hakuna linalonifikirisha mke wangu hapa zaidi ya taarifa mbaya niliyoikuta Polisi."
"Taarifa gani hiyo tena ambayo imeichukua furaha yako mume wangu?"
Mke wake alimuuliza huku akisogeza kigoda karibu.
"Si lile shetani limetoroka kituoni Makongolosi?"
"Nani huyo Jonathan?"
"Ni swali hilo sasa mke wangu? Huyo huyo."
"Kweli ng'ombe wa masikini hazai jamani sasa mpaka anatoroka wao walikuwa wapi?"
"Hapo hata mimi sijui mke wangu."
"Mhhh..." Mke wake aliishia kuguna tu.
"Mama kuna nini mbona umejikunja hivyo mikono shavuni?"
Shamimu aliuliza baada ya kuwakuta wakiwa kwenye mawazo akiwa anatua ndoo ya maji.
"Halafu kuna kitu kilinitokea siku za hivi karibuni ndotoni sikutaka kuwashirikisha kwanza nilitaka kujua nini kitatokea lakini naona hakuna."
Shamimu aliingiza mada nyingine ambayo haikuwepo.
"Ndoto gani hiyo mwanangu?"
Mzee Kaaya aliuliza haraka kutaka kujua.
"Ni ile siku ambayo nilirejea kutoka shuleni, eti niliota niko mtoni naoga mara akaja shemeji Robinson akaanza kunitaka mimi nikajua ni utani lakini baadaye nikamuona akivua nguo zake na kujitupa majini na kuanza kuogelea kunifuata nilijitahidi sana nikiwa uchi lakini sikufika mbali akanidaka na kutaka kunifanyia kitu kibaya kama bahati vile nikafanikiwa kujitoa na kupiga mbizi mpaka ng'ambo na kuanza kukimbia uchi hivyo lakini alifanikiwa kunidaka tena na safari hii alinitupa chini kisha kuja juu yangu lakini kabla hajafanya chochote mama ulitokea na kuanza kuita na hapo hapo nikashtuka, na katika kua yangu sijawahi ota ndoto ya hivyo."
"Hiyo ni ndoto tu mwanangu hutakiwi kuichukulia maanani."
Mzee Kaaya alimjibu Shamimu.
"Pamoja na kwamba ni ndoto lazima kuna tukio baya mbele linakuja mume wangu."
Mke wake alionesha mashaka yake.
"Mke wangu hakuna kitu kama hicho labda ni hili la..."
"Lipi?" Mke wake alimkatisha baada ya kuona anataka kulizungumzia lile la polisi mbele ya Shamimu.
"Aahh la kimizimu tu hilo mke wangu si unakumbuka hatukufanya tambiko lolote kwa watoto kabla hawajaondoka."
Mzee Kaaya aliamua kutengeneza uongo unaoendana na mada ile lakini uhalisia mzee huyu aliujua vizuri na maana ya hiyo ndoto alishaijua ila ilibidi atulie hivyo kama haitoshi aliinuka na kuingia zake ndani na kuwaacha hapo hapo.
" Jamani mimi niko ndani nijipumzishe kidogo."
"Sawa baba." Shamimu alijibu.
"Na kweli muwe mnapumzika kutwa viguu na njia kaaa !!!"
Mke alimjibu mzee Kaaya na kisha kumrushia dongo.
****
Lile suala la wakina Jackline kuongea mambo yasiyo eleweka yalimtoa jasho Daktari Hans Murray kiasi cha kumuita mzee Jerome nje watete kidogo wakati huo wakina Jackline walikuwa wamedhibitiwa kwa sindano za usingizi.
"Mzee Jerome hali ni kama ulivyoiona mwenyewe ndiyo maana nimeona nikuite hapa nje tuyajenge."
Daktari na Mkurugenzi mkuu wa Makambi hospitali bwana Hans Murray alianzisha mazungumzo.
"Kiukweli daktari wangu lile suala mimi mwenyewe limenichanganya sana maana maneno yale sijayaelewa kabisa kwani alivyosema wao si watu wa kawaida na wametokea majini kuna ukweli wowote?"
Mzee Jerome alimuuliza daktari.
"Kama ambavyo nilikuambia mzee wangu ni kwamba hawa mabinti wanatatizo kubwa sana la kisaikolojia hivyo hata zile kauli zao zilikuwa ni kutishia tu kutokana na mazingira ya ugenini waliyokutana nayo."
Daktari Hans alimwelezea mzee Jerome.
"Masuala ya kitaalamu hayo Daktari kwa hiyo tunafanyaje?"
Mzee Jerome alimuuliza daktari.
"Kwa nilivyowaangalia tatizo lao halitachukua muda mrefu hivyo kuna dawa ambazo nitakuandikia utazichukua pale kwenye Pharmacy yetu na kisha tutakuruhusu uondoke nao na kwa lolote litakalo tokea utawasiliana na daktari mwenzangu bwana Abbas kwa kuwa Hospitali yake ya King's iko karibu na ninyi."
Daktari alitoa maelekezo kwa mzee Jerome
" Ina maana wakiamka hawatasumbua kweli daktari?"
"Hapana hawatasumbua mzee wangu kuwa na amani katika hilo."
"Basi daktari katika hilo hakuna tatizo kabisa kumbe niandikie hizo dawa na pia ngoja nimfuate daktari kule ofisini kwake nikachukue bill yangu nifanye malipo ili nianze maandalizi ya kurudi nyumbani."
Mzee Jerome alionekana kuichangamkia taarifa ile bila shaka muda alioupoteza ulimuuma sana.
Daktari Hans alielekea ofisini kwake naye mzee Jerome alirejea wodini na kumkuta mtoto wake Mustapha akiwa anaweka chakula mezani kwa ajili ya wakina Jackline.
" Baba hawajaamka bado?"
"Bado mwanangu nafikiri dawa walizopewa zina nguvu sana lakini najua watazinduka tu na cha kufurahisha mwanangu ni kwamba daktari yuko kuniandikia dawa watakazozitumia nyumbani na bila shaka hata wao watafurahia hili wakiamka."
"Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa tunaweza kuondoka leo baba?"
"Ndiyo hivyo mwanangu kikubwa nikamilishe malipo kwanza ngoja nikafanye malipo kisha nitamuona daktari Hans na baada ya hapo ni safari ya Namport."
"Itakuwa nzuri hiyo baba, nimelimiss boti letu si unajua tena nikiwaga mle huwa nainjoi sana."
"Usihofu mwanangu muda umewadia tayari wa kurejea nyumbani na shauku niliyonayo ni kutaka kujua kilichowasibu hawa mabinti zangu mpaka kufikia hatua ya kutaka kuondoka eneo hili la tiba wakiwa hawana imani nalo kwa usalama wao."
"Tukifika nyumbani kila kitu kitafahamika baba."
"Basi sawa ngoja niende dirishani nikaicheki bili yetu niifanyie malipo."
Mzee Jerome alitoka na kuelekea dirishani kufanya malipo ya matibabu pamoja kuchukua dawa za kutumia wakiwa nyumbani wakina Jackline.
JE, NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
Baada ya kuwasili nyumbani kwa mzee Jerome Whistle eneo la White Forest ambalo liko karibu zaidi na Bandani ya Nam walikaribishwa na Victor ambaye muda wote ambao baba yake pamoja na Mustapha walipokuwa hospitali yeye alibaki nyumbani kuhakikisha biashara hazisimami.
"Wageni haoo karibuni ndani tafadhali."
"Asante mwanangu hebu kamsaidie mwenzako kushusha mizigo kwenye gari."
"Sawa baba." Victor aliitikia na kumfuata Mustapha ambaye alikuwa akiishusha mizigo kutoka kwenye gari na kuiweka chini hivyo Victor yeye ilibidi aanze kuibebelea.
"Brother poleni sana na safari naona sasa furaha ya baba imerejea upyaaa baada ya Mungu kuyasikia maombi yake kwa kuwaamsha wagonjwa wetu."
"Ni kweli mdogo wangu kwani hata nimefurahi sana na ukizingatia dada wenyewe wana vituko haooo kwani unaweza kulala thubutuuuu...."
"Acheni stori nyinyi ingizeni mizigo ndani bwana maana nyinyi akili zenu mnazijua wenyewe, wewe Victor mama yako wapi?"
"Aliaga kuwa anakwenda kwa shoga yake mama Muddy."
"Kuna nini naye wakati nilishamwambia kuwa wagonjwa watatua nyumbani siku ya leo?"
"Baba kwenye mambo ya meza acha kabisa si unamfahamu mkeo kachafua ile mbaya."
"Nipishe na maneno yako ya uchochoroni huko ingiza mizigo haraka ndani kisha mfuate mama."
"Sawa mzee baba nimekuelewa."
"Wewe nenda kamfuate mama niachie hii kazi mwenyewe nitaifanya."
Mustapha alimwambia Victor amuachie kazi ya kuingiza mizigo ndani na yeye akamfuate mama yao.
Victor aliondoka na kwenda kumfuata mama yao kwa mama Muddy.
"Mabinti zangu karibuni sana hapa ndiyo kwangu na pia niseme kwenu pia ninyi."
Mzee Jerome alianzisha mazungumzo na wakina Jackline pale sebuleni.
"Mzee wetu tunashukuru sana kwa kila kitu hatuna cha kukulipa kwa uliyotufanyia sisi watu baki kabisa ambao tumekufanya usimamishe shughuli zako."
Jackline alianza kwa kumshukuru mzee Jerome.
"Wanangu mimi kama waafrika wengine ambao asilimia kubwa tunatokea kwenye familia za kimaskini nilitekeleza majukumu yangu tena kama mzazi pia."
"Mimi nashindwa nianzie wapi labda nitaongea baada ya kusikiliza ulitupataje sisi?"
Jasmine aliona afungue japo kinywa tu.
"Wanangu baba yenu sina mtoto wa kike hata mmoja zaidi ya yule mkubwa..."
"Mkubwa kivipi ilhali unasema huna mtoto wa kike mzee wetu?"
Jessica alimkatisha mzee Jerome kwa kumuuliza swali.
"Ninaposema mkubwa nina maanisha mke wangu kipenzi huyo ndiye mtoto wangu wa kike pekee na kwa sasa hamuwezi kuamini nina furaha ya ajabu baada ya mabinti kuongezeka na sasa ninao wanne hivyo inukeni fuateni korido hili mtakutana na vyumba viwili vinatazamana hapo chagueni cha kuwafaa pateni maji kisha mtakuja mezani tusafishe matumbo na baada ya hapo tupige stori."
Mzee Jerome aliwaelekeza wakina Jackline sehemu ambayo watalala.
" Okay sawa baba yetu."
Walijibu na kuinuka kuelekea chumbani kama walivyoelekezwa.
Waliingia na kuoga huko kisha wakabadili mavazi na kurudi sebuleni ambako muda huu walikutana na sura nyingine mpya kabisa lakini kwa muonekano wake tu walihisi ndiye mtoto mkubwa wa mzee Jerome.
"Karibuni wageni wangu, naitwa Elizabeth Mackey ndiye mke wa mzee Jerome Whistle."
"Tunashukuru kukufahamu mama yetu na sisi hapa nikianza na mimi mwenyewe naitwa Jackline, huyu hapa ni Jasmine na yule pale ni Jessica cha upole wengine hutuita 'Tripple J' mama yetu."
Jackline alijitambulisha na kuwatambulisha wenzake pia.
"Waoo mna majina mazuri sana ina maana ninyi ni ndugu?"
Elizabeth Mackey aliwauliza swali ambalo liliwafanya watazamane kwanza kisha Jasmine aliibuka na kumjibu swali lake.
"Sisi ni ndugu ndiyo."
"Okay vizuri sana, naombeni sasa tukaribie mezani tuweze kupata chochote kwanza."
Mke wa Jerome aliwakaribisha mezani.
Waliinuka na kuvifuata viti kwa ajili ya chakula bila shaka cha usiku.
"Mustapha mko wapi? Jongeeni mezani bwana mbona mnajitenga au mnawaogopa wageni?"
Mzee Jerome aliwaita watoto wake.
"Karibuni chakula jamani."
Elizabeth Mackey aliwakaribisha kwa chakula.
"Asante mama."
Jessica alishukuru.
"Mhh chakula ni kitamu sana acha kabisa vitu kama hivi tulishavisahau kitambo sana lakini leo mama yetu umeturejesha huko."
Jackline hakusita kukisifia chakula kile ambacho kilikuwa ni maalum kwao.
" Ina maana ninyi mlikuwa mnakula nini sasa ikiwa chakula kama hiki kwenu mnasema mlikula zamani?"
Mustapha aliona awaulize swali.
" Mustapha ni muda wa chakula huu usije paliwa bure hapa hayo maswali utawauliza baada ya kula."
Mzee Jerome aliona awakatishe kwanza ili chakula kichukue nafasi yake.
" Sawa baba." Victor alijibu.
Baada ya chakula familia ya mzee Jerome ikiwa na kiu ya kutaka kujua nini kiliwapata wakina Jackline mpaka kuwa hapo Jackline alimsogelea mke wa mzee Jerome na kumshukuru kwa chakula na kisha akaomba simu ili afanye mawasiliano.
" Mama kwa niaba ya wenzangu nashukuru kwa chakula na kutupokea pia watu ambao hamtufahamu kabisa."
"Inuka binti yangu sisi wote ni wasafiri hapa chini ya jua hata kama siyo sisi wazee wenu wanaweza kuwa vijana wetu wakapotea huko katika harakati za kutafuta maisha ina maana wasisaidiwe?"
"Sawa mama nimekuelewa pia nilikuwa naomba simu niweze kufanya mawasiliano kidogo."
"Bila shaka mwanangu hii hapa."
Mke wa mzee Jerome alimkabidhi simu Jackline na baada ya kuichukua aliondoka sebuleni hapo na kuelekea chumbani baada ya kuingia tu aliufunga mlango na kujitupa kitandani kisha akaingiza namba fulani kwenye simu hiyo na kupiga.
" Haloo, nani mwenzangu?"
Upande wa pili uliuliza baada ya kupokea simu.
"Shamimu naomba unisikilize."
"Naongea na dada Jackline?"
"Hujakosea mdogo wangu uko na nani hapo karibu?"
"Niko mwenyewe nimeshalala jilaza chumbani."
"Chumbani? Shule vipi?"
"Dada nawe nina mwezi sasa toka nihitimu na hapa niko kwa wakina Shem."
"Kwa kina Robinson ee?"
"Ndiyo dada."
"Okay, naomba unisikilize vizuri mdogo wangu dada yako nilipatwa na matatizo makubwa ambayo labda ungesikia tu kuwa nilishakufa ila Mungu mkubwa nimepona nini kilitokea nitakueleza siku nikirudi nyumbani la msingi ninalokuomba mdogo wangu taarifa hizi usimwambie mtu yeyote yule hapo nyumbani na pia tafuta nafasi kama itakuwa ni alfajiri sana vyovyote vile toroka hapo bila wao kujua umekwenda wapi panda basi mpaka kwa kaka Athuman Mbeya kwa usalama wako na wangu nikiwa vizuri ndani ya siku tatu nne hizi nitakutumieni fedha huku mambo yamebadilika sana na ndiyo maana hata simu nimetumia ya mtu mwingine."
"Dada mbona unanitisha mdogo wako na vipi kuhusu shemeji Robinson?"
"Naomba unielewe mdogo wangu fanya kama nilivyokueleza hayo maswali hayana msingi kwa sasa, sawa?"
"Sawa nimekuelewa dada ila sasa nitafikaje Mbeya sina nauli."
"Mpigie simu muda huu kaka Athuman mweleze haya nilivyokueleza bila shaka atakupokea tu na nauli atakulipia baada ya kufika Mbeya utamweleza mhudumu wa basi kama ni dereva na utingo wake."
"Sawa dada yangu ila nimekukumbuka sana."
Kabla hajamjibu mdogo wake aliikata simu na kisha kutuma ujumbe kwenye simu ya Roberto.
"TUMERUDI DUNIANI BAADA YA SAFARI NDEFU YA AHERA ROBERTO JIANDAE NDANI YA WIKI MOJA AU MBILI TUKO HAPO NGOJA TUFANYE MAWASILIANO NA WENYEJI WETU TUJUE ITAKUWAJE.
USIJIBU UJUMBE HUU SIMU NIMEIKODI KWA DAKIKA MOJA TU...
RAFIKI YAKO JACKLINE."
Baada ya kuhakikisha ujumbe umepokelewa alipiga ndulu ya kimya kimya kisha akaufuta ujumbe ule pamoja na namba ya Shamimu kisha akarudi sebuleni na kuwakuta wenzake wakiendelea na mazungumzo.
" Nashukuru mama simu hii hapa."
"Vipi haikukukatikia kabla hujamaliza maongezi? Maana sijaongeza salio ni miezi miwili sasa."
"Hapana mama nimemaliza bila hilo kunitokea."
"Vizuri mwanangu, ee Jasmine ikawaje?"
Alimuuliza Jasmine swali ikionyesha kuwa huku nyuma wakati Jackline kaondoka simulizi ilianza.
"Ndiyo hivyo tulishtukia tu tukivamiwa na watu hao ambao siyo wageni kama nilivyoeleza mwanzo na kuanza kutupiga lakini ni kama walijua tutawazidi kwenye mapigano ikabidi wapulize sumu kwenye kile chumba ambayo ilianza kutumaliza nguvu taratibu mpaka kupoteza fahamu mpaka kuja kuzinduka tuko hospitali halafu tukashangaa tunaambiwa ni Afrika tena Namibia? Tulichanganyikiwa sana tumefikaje tukajua wale Mafia ndiyo wametukimbizia huku kumbe masikini ya Mungu siyo."
Jasmine alihitimisha.
" Mhhh kweli ninyi si watu wa kawaida kabisa kwa muda ambao mmeusema kwa kumbukumbu zenu ni takribani miezi mitatu hivi kama siyo minne na huku sisi tuliwaokoa majini takribani mwezi mmoja na nusu kama sikosei hivi mkiwa hamjitambui ndipo tulipoona tuwakimbize hospitali moja ya hapa mjini iitwayo KING'S MEDICARE CENTRE ya rafiki yangu daktari Abbas Mukesh kwa matibabu lakini naye alinyoosha mikono juu na kuamua kuomba usaidizi kutoka kwa rafiki yake Daktari Hans Murray pale mlipozindukia Makambi Hospitali."
"Ina maana walitutupa baharini maana toka iliko ile nyumba mpaka baharini ni mbali sana hivyo waliamua kutufanyia kitu mbaya."
Jessica aliongea machozi yakimtoka.
"Nyamaza mwanangu mpaka hapo wameshindwa japo mimi nahisi wao walijua mmeshakufa tayari hivyo wakaona wafute ushahidi kabisa."
Mzee Jerome alimtuliza Jessica na kisha kutoa hisia zake.
"Dada zangu sikutarajia kuwa mnaweza kuwa mmepitia magumu kiasi hicho kwani sura zenu na mambo yenu wala hazina uhusiano kabisa."
Victor aliwapa pole wakina Jackline.
"Asante mdogo wetu ni mapito tu ya Dunia hayo lakini kwetu safari ni kama vile ndiyo imeanza upya kabisa."
Jasmine aliongea akijifuta machozi yake.
"Sasa huyo Robinson ilikuwaje mpaka akawasaliti watu ambao kwake ni kama mlikuwa wakombozi wake kimaisha?"
Elizabeth Mackey aliwauliza tena swali jingine.
"Mama yangu wee si unajua tena masuala ya mkwanja yalimfanya awe Yuda wa Kibongo baada ya yule aliyemsaliti Yesu Kristo wakati huo."
Jackline alimjibu akimuegamia Jasmine.
"Mungu awaepushie mbali na mabalaa hayo mnayopitia wanangu."
Mzee Jerome aliongea hayo kisha akawaaga na kwenda zake kulala huku akiwaacha na mama yao na wakina Mustapha na Victor wakiendelea kupiga stori za hapa na pale.
****
"Wanajeshi wangu eee kama zali vile nimepokea ujumbe unaonihakikishia Makamanda wako Hai na muda wowote kuanzia sasa tujiandae."
Roberto aliwaambia wenzake huku akiwaonesha ujumbe huo toka kwa Jackline.
"Wanaweza kuwa wenyewe kweli au ni michezo ya wakina Santana hiyo?"
Mmoja wao aliuliza kutokana na tabia za Santana kufahamika vizuri.
"Nimeifuatilia code number' na kubaini siyo ya nchi yetu...."
Kabla hajamalizia vizuri alikatishwa Roberto.
"Brother unasemaje wewe hujui mtandao wa Santana ni mkubwa na umeenea dunia nzima na ukizingatia baadhi ya mali zao tumeziharibu."
Aliendelea kuwasisitizia wenzake kutoutilia maanani ujumbe huo yule mwenzao.
"Ila kweli jamani nakubaliana nanyi katika hilo hapa sisi tuendelee na mkakati wetu wa TONE LA DAMU kwa bwana Santana."
Roberto alikubaliana nao na kuamua kuachana na ujumbe wa Jackline kisha kuendelea na mipango yao kama kawaida.
"Hebu na leo wajafanye washikwe na tumbo la kuhara brother Roberto."
Kikosi hiki kilionekana kuifurahia kazi yao ya kumnyong'onyeza Santana.
"Mnaonaje safari hii tukafanye unyimbili kule kwenye mgodi wao wa kokoto?"
Mwingine aliibua lake ambalo halikuwa kwenye mpango kabisa.
"Hapana mimi nafikiri kitu cha kufanya kwa sasa ni kwenda kuifanyia umafya Ngome yake ile ile ila safari hii ni kule chini kwenye ficho lake la siri ardhini."
Roberto aliwaeleza mkakati ambao alikuwa kaupanga safari hii ambao uliotakiwa kutekelezwa.
"Mchoree maandishi basi ili ajue wana hatuna masihara kabisa tunapopanga kitu lazima kiwe tena si kwa kificho."
Rafiki yake Roberto aitwaye Augustino naye aliona atie neno.
Bila kuchelewa Roberto alichukua simu na kuandika ujumbe.
"LEO JIANDAE KAKA YANGU SANTANA KWANI NAKUJA KUKULETEA ZAWADI NZURI SANA AMBAYO UTAIFURAHIA MWENYEWE SIYO KAMA ZILE ZA MWANZO AMBAZO ZILIKUTOA MACHOZI NA UMWAMBA WAKO HII ITAKUFANYA UTABASAMU ZAIDI, JIANDAE."
Kisha akautuma ujumbe huo kwa Santana ambaye alikuwa bado kwenye majonzi makubwa baada ya kuwapoteza watu wake na mali zake pia.
NINI KITATOKEA?
USIKOSE KUSOMA SIMULIZI HII KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
"Ndugu zangu tangia nilipoamua kuwaingiza kwenye mtego wangu Jackline na Robinson hapa Brazil kwa kuyatumia mahitaji yao kujinufahisha mimi na Makampuni lakini mambo hayakuwa hivyo yakawa kinyume kwani badala ya kunufaika imekuwa ni hasara kila kukicha mpaka kuna muda najiuliza ingekuwaje iwapo tu ningewapokea na kuwatimizia kile ambacho walikihitaji kutoka kwangu? Na kuna muda nimekuwa nikihangaika kumtafuta Simbozya kule Afrika ya Kusini labda kupitia yeye mambo yatakaa sawa lakini nimekuja kukumbuka kuwa nilimtuma mtu wangu kwenda kumuua ili iwe rahisi kuwamaliza hawa watu wawili Jackline na Robinson. Nilijidanganya mwenyewe kwani kupitia mimi nimewafanya kuwa imara sana kwani Jackline aliwachukua Jasmine na Jessica huku mimi nikiambulia kwa Robinson, angalia leo hii wao wako Namibia wakipata matibabu baada ya zoezi letu la kuwaua kushindikana huku sumu waliyoiacha ikiendelea kututafuna kila siku na leo hii nimepokea ujumbe tena kutoka kwa wale wale wanaosumbua akili zetu na safari hii wanadai tutegemee zawadi ni zawadi gani hiyo?"
Santana aliamua kuwaita wafanyakazi wake wote kutoka kwenye Makampuni yake yote.
" Samahani bosi huyo Robinson yuko wapi na anafanya kipi cha kuinufaisha kampuni yako ya Ulinzi?"
Mmoja wa wazee washauri wa Makampuni ya Santana aliinuka na kuuliza swali.
"Yupo hapa hapa na kazi rasmi hajaanza bado kufanya tukiwa kwenye kumjaribu kama atakuwa na faida, Robinson sogea hapa wazee wakuone."
Santana alimwita Robinson pale mbele ili Bodi pamoja wazee washauri waweze kumuona.
"Ndiyo huyu?" Yule mzee aliuliza.
"Ndiyo mwenyewe mzee wangu."
Santana alimjibu.
"Huoni kama umejiingiza kwenye biashara isiyo na chembe yoyote ya faida? Mtu gani huyu ambaye hana mwili wa kazi?"
"Hapana kwa hilo napingana na wewe mzee masuala ya mwili yanajengwa kituo chetu cha mazoezi na si vinginevyo kikubwa mhusika aoneshe nia ya kuwa pamoja nasi na si vinginevyo."
Santana alimjibu yule mzee kwa ukali kiasi cha kumfanya akae chini kwa kuhofia kuchafua hali ya hewa kutokana na tabia yake Santana.
" Mzee Bruno Gautier naomba ripoti kutoka Afrika inasemaje kwani kuendelea kupoteza muda hapa ni kukisubiri kifo katikati ya uwanja wa mapambano tukiwa hatuna silaha za kujitetea."
"Okay sawa." Mzee Bruno alijibu na kutoka pembeni kidogo na kumpigia simu kijana wake aliye Namibia ili kujua amefikia wapi kuwafuatilia wakina Jackline.
"Nipe ripoti kijana wangu." Mzee Bruno hakutaka kuanza na salamu badala yake alitaka ripoti ya kazi aliyoitoa kwa kijana huyo.
"Mzee huku mambo ni magumu kwani mpaka sasa ripoti niliyoipata ni kwamba pale KING'S MEDICARE CENTRE walitolewa na kusafirishwa mpaka MAKAMBI HOSPITAL mjini Windhoek ambako huko wamedumu mpaka siku mbili zilizopita ambapo walipata fahamu na kuondolewa na mzee mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja."
"Mzee? Na taarifa hizo ulizipata kwa nani?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza baada ya kusikia walipata fahamu na kuondolewa na mzee ambaye hakujulikana mara moja.
"Taarifa hizi nazipata kwa walinzi wa hospitali hizi zote mbili mzee wangu."
"Nisikilize vizuri kijana michezo kwenye kazi hii acha kabisa nafikiri unafahamu vizuri kuwa iwapo utashindwa kuwapata au taarifa zao za kueleweka hatutakuwa na huruma na uhai wako sijui unanisikia?"
"Nakusikia mzee."
"Okay vizuri, cha kukusaidia katika upelelezi wako rudi kwenye hiyo hospitali ya Makambi mtafute Mhudumu wa ndani namaanisha Daktari mvimbishie bahasha kisha mweleze shida yako sidhani kama ataikataa hiyo bahasha."
"Sawa mzee basi ngoja nielekeee huko sasa hivi."
Alimjibu kijana huyo na kisha alirudi ndani na kumpa mrejesho Santana. Mzee Bruno hakujua taarifa hiyo ataichukuliaje Santana kwani alipoambiwa tu kuwa wamepata fahamu wakina Jackline pale pale tena kwa mara nyingine alianguka chini na kupoteza fahamu.
"Mhh hali hii imemuanza lini mbona huko nyuma hakuwa nayo?"
Mwenyekiti wa Bodi ya washauri wa Makampuni aliuliza baada ya kumuona Santana akienda chini na kupoteza fahamu.
"Ni baada ya matukio haya kushamiri ambayo ndiyo yamemuweka kwenye msongo mkubwa wa mawazo."
Mzee Bruno Gautier alimjibu.
"Mpaka hapo huyu kijana anaweza kuwa kirusi kwetu naagiza mshikilieni mara moja mpaka pale haya mambo yatakapo kaa sawa. Nimeeleweka?"
"Umeeleweka ndiyo lakini ni kijana gani huyo unayemaanisha?"
Mzee Bruno aliuliza.
"Namaanisha huyo Robinson."
Pale pale Robinson alikamatwa na kupelekwa kwenye chumba cha mateso ateswe mpaka atakapoeleza anafanya kazi na wakina nani kwani kutoka yeye awepo mahali hapo siri zao zimekuwa zikivuja sana.
Walimbeba Santana na kumpeleka kwenye chumba cha huduma ya kwanza kisha wao kurudi kuhitimisha kikao chao, lakini mara alikuja daktari wao akiwa na simu mkononi ambayo ni ya Santana ikiwa inaita.
"Hiyo simu ni ya Santana mbona unakuja nayo huku tena?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza yule daktari.
"Nimeona niilete kwako baada ya kuona imeita zaidi ya mara mbili nikahisi ina umuhimu mkubwa sana ukizingatia mwenye simu bado fahamu hazijamrejea."
Mzee Bruno Gautier ilibidi aichukue ile simu na baada ya kuangalia namba ya mpigaji hakuifahamu kwani ilikuwa ni ngeni haikuwa na jina ikabidi aipokee tu.
" Habari...!!!"
Mzee Bruno Gautier alianza kwa salamu.
" Salamu yako si muhimu kwa sasa ila tu nilitaka kukufahamisha kwamba moto tumeuwasha upya kwa mara nyingine na safari wa kuuzima hayupo hata mmoja."
"Naongea nani tafadhali mbona vitisho tena?"
"Si vitisho mzee Bruno angekuwa mwenye simu angelielewa hili mara moja kifupi namhitaji Santana."
"Santana anaumwa na umejuaje kama mimi ni mzee Bruno?"
"Ni kutokana na kimbelembele chako mzee ila angalia kitakutokea puani, ulisema unataka kunijua eee?"
"Ndiyo." Mzee Bruno alijibu.
"Okay naitwa Jackline."
"Jackline???"
Mzee Bruno Gautier alijikuta akilitaja hili jina kwa mara nyingine.
Lakini muda huo Jackline hakutaka kusubiri lolote zaidi ya kukata simu.
"Mungu wangu.."
Mzee Bruno alitokwa na maneno hayo baada ya simu kukatwa na Jackline.
"Vipi ni ya heri hiyo simu?"
Mzee yule mshauri aliuliza baada ya kumuona mzee Bruno kama kapigwa na mshangao fulani hivi.
"Mzee mwenzangu si mwingine bali ni Jackline."
"Jackline? Si mlisema mmeshawatafutia dawa hao mabinti?"
"Nahisi dawa tuliyowapa haikufanya kazi."
Mzee Bruno Gautier alianza kutokwa machozi. Lakini wakati akiendelea kujifuta machozi mara simu ile ile ikiwa mkononi kwake iliingia meseji aliifungua na kuisoma.
"KESHO ASUBUHI TUTAKUELEKEZA SEHEMU YA KUIFUATA ZAWADI YAKO SANTANA."
Alipousoma ujumbe ule tu alipiga kelele zilizomshtua kila mmoja pale nje.
"Aaaaghhh kila wakati vitisho vitisho vitishooo tu mpaka lini? Santana amkaaa.."
Walikuja wenzake na kumshika na kisha kumpeleka kwenye huduma wakihisi na yeye ana tatizo kwenye ubongo wake.
****
Waliamka na baada ya kifungua kinywa walimuomba mke wa Jerome Bi Elizabeth Mackey kuwa walitaka kuingia mjini wakaupdate baadhi ya taarifa zao ili waweze kuchukua fedha kwa ajili ya matumizi yao kama watoto wa kike. Mama Jerome hakuwa na kipingamizi aliwakubalia kisha akawapa gari yake ndogo waitumie kwenye mishe zao. Walimshukuru sana mama huyo na kisha kuingia zao garini na kuondoka zao.
"Kama zali vile tumerudi na tunaianza mipango yetu upyaaa."
Jasmine aliongea kwa furaha wakati Jackline akiwa nyuma ya usukani wa gari.
"Lakini mwenzenu mguu bado hauko poa sana inaonekana ile risasi iliniingia vilivyo."
Jessica aliwaambia wenzake juu ya hali yake ya mguu baada ya kuona wameanza kuifurahia siku.
"Kama hautakuwa vizuri Jessica itabidi wewe ubaki hapa Namibia kisha sisi turudi Brazil kuimalizia kazi kisha tutakupitia hapa baada ya ushindi na kurudi zetu nyumbani Tanzania."
Jasmine alimwambia Jessica ambaye hata hivyo hakukubaliana na wazo la dada yake.
" Unafikiri itakuwaje mdogo wangu ikiwa hali yako bado si nzuri na ukizingatia vita tunayokwenda kupigana si kama ya mwanzo hii itakuwa ni ya kinyama sana ni kukamata chinja tupa kule."
Jasmine aliendelea kumweleza mdogo wake.
"Na hiyo ndiyo ninayoitaka na mimi haiwezekani vita niianze halafu niiachie njiani, nahitaji kuwaua au kuwashuhudia wakina Santana, Robinson wakifa mbele ya macho yangu."
"Usihofu mdogo wetu inabidi tukikamilisha suala la kutoa pesa tutanunua simu kwanza kisha tutarudi hapa kwa mzee Jerome na kuendelea kufanya umafia kwa kutumia simu na wakina Roberto wakitenda mpaka pale utakapokuwa kuwa sawa ndipo tutaondoka pamoja kuelekea Brazil kwa ajili ya kuumaliza mchezo, unasemaje hapo?"
Jackline aliona aondoe utata ambao ulianza kuota kati ya mtu na dada yake.
" Hayo ndiyo mambo sasa nabaki vipi mwanajeshi mwenyewe niko tayari hata kwenda kufia kwenye Uwanja wa mapambano."
Jessica alimjibu Jackline huku akimshikashika kidevu dada yake kuonesha kuwa kashindwa mtihani.
Walifika mjini na moja kwa moja waliingia Internet Cafe na kukaa kwenye PC moja ambayo ilikuwa imejitenga kidogo na kuanza kuifanyia kazi akaunti zao na baada ya kukamilika walitoka na kwenda kununua simu ambazo kwao ilikuwa kama kupata silaha kubwa ya kivita. Walizifanyia malipo ya muda wa maongezi kisha walirudi garini na Jackline kuanza kuwasiliana na Santana ambapo simu yake ilipokelewa na mzee Bruno lakini haikumkatisha tamaa aliufikisha ujumbe aliokuwa kapanga kumpa Santana.
"Kasemaje?"
Jasmine alimuuliza Jackline baada ya kukata simu.
"Watatujua tu eti kasema Santana anaumwa lakini nimempa zake mwenyewe Bruno."
"Kabisa aumwe Santana hivi inawezekana kweli?"
Jessica alishangaa baada ya kupata taarifa za kuumwa kwa Santana.
"Hivi wanajisikiaje wanaposikia tuko hai?"
Jasmine alijiuliza swali hilo wakati akicheza gemu kwenye simu yake.
"Watajua tu muda ukifika, na hapa nikiangalia kila mmoja ana mtu wa kumalizia hasira zake isipokuwa mimi lakini na mimi zitaishia kwa yule mpuuzi aliyetuuza tukiwa nyumbani kwake."
Jessica aliwaambia wenzake mtu anayemtamani siku hiyo kumpa somo.
"Nani huyo?"
Jackline alimuuliza.
"Si yule Melissa."
"Okay yule ambaye hata mimi nilikuwa nimempangia kumfanyia kitu mbaya."
Jackline alitoa ya moyoni juu ya Melissa.
Baada ya kila kitu kwenda sawa waliingia kwenye maduka ya nguo na kununua nguo ambazo zitafaa kwa kazi ngumu iliyo mbele yao ikiwa ni pamoja na viatu ambavyo ni rafiki kwa mazingira yoyote yale.
Na baada ya kila kitu waliianza safari kurudi nyumbani lakini Jackline alikumbuka kitu na kulipaki gari pembeni na kumuomba Jasmine aendeshe ili yeye afanye mawasiliano.
"Roberto mambo !!!"
Alianza baada ya upande wa pili kuipokea simu yake.
"Poa, vipi madam mnaendeleaje huko?"
"Tunamshukuru Mungu tunaendelea vizuri tu Roberto vipi mama naye hali yake?"
"Kwa kweli nisiwe muongo kuhusu mama tunasubiri tu majaaliwa ya Mwenyezi Mungu tu maana kwa sasa hali ndiyo imekuwa tete zaidi dada."
"Hee Jamani pole sana Roberto lakini hutakiwi kukata tamaa mapema hivyo kwani hiyo ni kazi ya madaktari na si wewe."
"Sawa dada nimekuelewa ila ukweli ndiyo huo."
Roberto aliendelea kuushikilia msimamo wake.
"Sasa mdogo wangu naomba kwenye simu yangu ile ya kwanza uliyoiokota kuna namba nimeisevu kamanda naomba nitumie mara moja."
"Bila shaka dada."
Kwa kuwa simu alikuwa nayo pale haikumchukua muda mrefu sana akawa kamtumia.
Kisha Jackline akaipiga ile namba ambayo ilikuwa ni ya mkuu wa kituo cha polisi Makongolosi iliita kwa muda kisha ikapokelewa.
"Jackline hapa Afande shikamoo !!"
Jackline alijitambulisha na kumsabahi.
"Wao mwanangu Jackline marahaba habari ya wapi?"
"Kwa sasa niko Afrika ya Kusini katika nchi ya Namibia."
"Kuna nini huko tena?"
"Kuna rafiki yangu nimekuja kumtembelea mara moja vipi suala langu limefikia wapi?"
Aliona maswali yamekuwa mengi akaona ampige swali.
"Kiukweli kwa kushirikiana na mzee Kaaya tuliweza kumkamata mara baada ya kuja Lupa kwa lengo la kukisambaratisha kabisa familia yako."
"Ikawaje sasa?"
"Ndipo alitiwa mbaroni akijaribu kutoroka na kisha tulimleta hapa kwa usalama wake pia kwa kuwa wananchi walikuwa wanahasira naye lakini kuna Askari wasio Waadilifu wamemtorosha na sasa bado tunaendelea kumtafuta na hivi ninavyoongea na wewe tuko pori moja la linaitwa Majimazuri kama unaelekea Mbeya kutoka Chunya tuliambiwa maeneo hao kuna maficho ya Majambazi."
"Sawa mkuu basi nitaendelea kukusumbua kupata maendeleo ya oparesheni yenu."
"Bila shaka kabisa mwanangu."
Baada ya kukata simu Jackline alikata simu.
"Vipi anasemaje?"
Jasmine alimuuliza.
"Eti walimkamata kisha katoroshwa na askari waliokuwa wakimlinda."
"Hamna lolote hapo wameshirikiana kumkimbiza hapo hiyo kazi ya kwetu tukirudi salama Brazil."
Jessica alijibu na kutoa ahadi na wakati huo gari ilikuwa getini ikipiga honi tayari kwa kuingia ndani.
JE, NINI KITAENDELEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
*TAHADHARI: CORONA IPO USIICHUKULIE POA HATA HAPO INAWEZA KUIBUKA.
Waliingia ndani wakiwa na furaha sana kitu kilichowapa faraja wenyeji wao baada ya kuwaona kwenye hali ile baada ya kurejea kutoka matembezini.
"Inaonekana safari yenu imekuwa na matokeo chanya eee."
Mrs Jerome aliwauliza baada ya kuingia ndani.
"Yaani mama acha tu tunafuraha ya ajabu baada ya vitu vyetu vya msingi kuviweka sawa na sasa tunaweza kufanya kitu chochote hofu yetu ilikuwa ni fedha."
Jackline alimjibu na kumtolea ufafanuzi kidogo mama yao huyo.
"Na kwa sasa tumekubaliana tutakuwa hapa hapa mpaka mwenzetu apone kabisa kidonda chake ndiyo tutaondoka."
Jasmine naye aliona amweleze mama yao mlezi Mrs Jerome juu ya kile walichokubaliana wakiwa njiani.
"Hilo litakuwa jambo jema sana wanangu walau mtupe faraja wazee wenu kwa kipindi hiki."
Mzee Jerome Whistle aliingilia maongezi yale.
"Mzee kumbe umerudi tayari?"
Jackline alimuuliza baada ya kusikia sauti yake akitokea chumbani kuja sebuleni walipokuwa.
"Muda mrefu tu nafikiri tulipishana kidogo tu leo hatukuwa na kazi nyingine zaidi ya kuifanyia ukarabati boti yetu maana kila baada ya miezi sita lazima tuikague."
Mzee Jerome alifafanua.
"Safi sana inaonekana unaipenda sana kazi yako ya uvuvi mzee wetu."
Jackline aliendelea kumchimba mzee Jerome kujua kama anachokifanya ni cha ndoto yake au ilikuja tu.
"Naifurahia sana kazi yangu kwani ndiyo inaniweka mjini hapa na ndiyo imenipa umaarufu."
"Na pia ndiyo hiyo hiyo imetukutanisha sisi na ninyi."
Jessica naye alichomekea utani wake na kuwafanya wote kucheka pale sebuleni.
"Umeona eee binti yangu."
Elizabeth Mackey aliingiza kibwagizo akiwa katikati ya cheko.
"Ndiyo mama bila kazi hiyo ya baba sisi labda tungekuwa na jina jipya la marehemu na ninafikiri Mungu alimuandaa kwa miaka mingi ili kuja kutuokoa sisi."
Jackline aliongeza.
"Inawezekana kabisa kwani Mungu mipango yake kwetu si ya siku moja na ndiyo maana kwenye mitihani yake wengi wetu tunafeli."
Mzee Jerome alimuunga mkono Jackline.
Wakati huo Jasmine alikuwa kapeleka vitu vyao chumbani.
"Kuna kitu ningependa kukijua kutoka kwenu wazee wetu?"
Jackline alianzisha mada nyingine.
"Kitu gani hicho Jackline?"
"Nje ya uvuvi na biashara ya samaki ni shughuli gani nyingine mnazojishughulisha nazo katika kuboresha kipato chenu?"
"Kiukweli mwanangu hakuna mara moja moja mama yenu hufanya biashara ya mazao nayo si ya kudumu mfano kwa sasa anatakribani miaka mitatu hajaifanya."
"Okay vizuri, sasa sisi tunaomba jadilianeni ni biashara gani ambayo mngependa kuianzisha ambayo haitakuwa ya kutumia nguvu sana au kusafiri sana kwa upande wa kaka zetu kwa tulivyowasoma wao biashara ya mavazi inawafaa zaidi."
"Unataka kusema kuwa baada ya kuanzisha biashara hizo boti tutaipaki?"
Mzee Jerome aliona aulize ili afafanuliwe zaidi.
"Mume wangu wamesema biashara nyingine yaani kuongeza miradi, sijui kama sijawaelewa vizuri."
Mke wake alimjibu.
"Mama uko sahihi kabisa sijamaanisha mkianza biashara hizi mpya hiyo muachane nayo hapana soko huyumba mzee wangu leo liko vizuri kesho halieleweki lakini upande wa pili linakuwa sawa."
Jackline aliendelea kuwafafanulia zaidi.
"Hapo nimekuelewa ngoja tujadiliane na kaka zenu kisha tutawapa mrejesho."
Mzee Jerome alipokea ushauri huo na kuomba ashauriane na familia yake kwanza kisha watajulishwa.
Baada ya hapo Jackline na Jessica walimfuata Jasmine chumbani ikiwa ni pamoja kuangalia vitu walivyovinunua lakini akili ya Jackline ilikuwa ni kwenye zile bastola.
"Kipi kianze Jasmine kuoga au twende kule kwenye viunga tukafanye mazoezi kidogo?"
Jackline alimuuliza Jasmine.
"Tukalitafute kwanza joto la mwili kisha maji ndiyo yafuate."
"Hapo sawa basi jiandae tutoke."
"Mnafurahia mnavyonitamanisha wenyewe?"
Jessica aliwatania japo lilitoka moyoni.
"Jessica bwana usiwe unasema hivyo hatuwezi kufanya kitu ambacho wewe huwezi kwa sasa kwani mazoezi haya yanakuhusu na wewe."
Jasmine alimuondoa wasiwasi.
"Kivipi?" Jessica aliuliza.
"Kulenga shabaha kunakuhusu Jessica."
Jackline alimjibu kwa kifupi akiwa anamalizia kuvaa raba zake. Na baada ya hapo walitoka nje na kuelekea kwenye kiunga cha nyumba hiyo.
"Vipi mnataka kufanya mazoezi ee?"
Mzee Jerome aliwauliza baada ya kuwaona wamevalia nguo za mazoezi.
"Ndiyo baba kama hutojali ungana nasi pia."
Jackline alimjibu.
Mzee Jerome aliingia ndani kubadili nguo zake tayari kwa mazoezi na wakina Jackline.
"Eeh nimekumbuka Jackline jana ulimpigia simu mdogo wako vipi alikuelewa?"
Jasmine alimuuliza Jackline wakiwa kiungani kabla ya mazoezi.
"Ni kweli kabisa wangu niliongea naye japo hakunielewa lakini kama dada yake imebidi anielewe tu na bila shaka anaweza kuwa kaondoka."
"Acha habari za kufikirika wangu mvutie waya kujua kama alishasepa au bado?"
"Kweli eee?"
"Ndiyo fanya mambo."
Moja kwa moja ikabidi Jackline arudi ndani kuchukua simu ili ampigie Shamimu ajue kama alishaondoka ama la.Alitoka nayo mpaka kule nje na kisha kumpigia.
"Shikamoo dada yangu."
Shamimu alipokea kwa salamu.
"Marahaba dogo eeh niambie ikoje !!"
"Nilifanikiwa kuondoka alfajiri na moja kwa moja nikaanza safari sikupitia stendi kwa kuhofia kuonwa na marafiki zake mzee Kaaya hivyo nikaanza mdogo mdogo kwa mguu lakini kama bahati vile nilipolifikia tu pori la Forest ikatokea pikipiki moja ambayo huleta samaki kutokea Makongolosi nikaisimamisha na kumuelekeza ombi langu na hakuwa na hiana akanibeba mpaka Makongolosi ambako nikawa nimepata basi mpaka Mbeya na hivi ninavyoongea na wewe niko na kaka Athuman hapa Mbeya Terminal alinifuata baada ya kumpigia nilipokaribia."
"Vizuri sana mdogo wangu hebu mpe simu nipate kuongea naye kaka yangu mwenyewe."
"Sawa dada huyu hapa."
Shamimu alimkabidhi simu kaka yake Athuman ili aongee na dada yao.
"Eehh dada langu lenyewe niambie habari ya wapi?"
"Kwanza habari ya siku kaka yangu?"
"Nzuri dada yangu mambo yanakwenda japo si sana lakini tunapambana sasa ndiyo nini ukaingia nje ya nchi bila kuaga au tuna ugomvi dada yangu?"
Athuman alimtupia swali Jackline.
"Ugomvi hakuna kaka yangu ila tu mambo yako yalininyong'onyeza toka ile siku ya msiba nikahisi labda hukufurahia uwepo wangu na ndiyo maana niliona nikuweke kipolo kwanza."
"Awali ya yote dada yangu naomba nikuombe msamaha kwa yote ambayo niliyafanya siku ile kama binadamu mwingine yeyote kukosea ni kawaida na ndiyo maana hata baada ya kukaa na kutafakari kwa kina nikagundua niliwakosea ndugu zangu mtihani ukaja ninaanzaje sasa kuwaomba msamaha nikiwa najiuliza hili ndipo mdogo wangu Shamimu anapiga simu kuwa umemwambia uje kwangu nilifurahi sana dada yangu."
"Usihofu kaka yangu katika hilo, sisi tulikusamehe na ndiyo maana baada ya kubaini kuna vitu ambavyo vinaweza kutuletea matatizo sisi nikaona nimwambie atoroke mara moja bila kuaga."
"Eehh dada tatizo ni nini mpaka mtu atoroke huoni kama itawachanganya pale nyumbani kwa hili la kuondoka kwa Shamimu?"
"Athuman, ni bora liwachanganye wao kuliko kutusambaratisha sisi kumbuka kuwa kuna mtu anaitwa Jonathan mtu aliyefanikiwa kuziangamiza familia zetu na tumebakia yatima sasa ni kwanini tuwafumbie macho wengine ambao wanataka kujaribu kufanya makosa yale yale na siyo kujaribu tu bali ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu."
"Una maanisha nini dada?"
"Kuna mtu anaitwa Robinson si mnamfahamu?"
"Tunamfahamu vizuri sana kuna nini?"
"Okay mtu huyo niliondoka naye kwenda Brazil kwa ajili ya kutafuta msaada wa kuja kumdhibiti Jonathan na watu wake lakini cha ajabu kufika huku kanigeuka na kuungana na maadui zangu na kisha kunifanyia umafia wa kuniua mimi na rafiki zangu lakini kwa kudra zake Allah tuko hai na hapa ni Namibia."
"Alitaka kukuua? Kisa nini?"
Athuman aliuliza swali kwa mshangao baada ya kusikia kilichofanywa na Robinson.
"Siyo alitaka bali walifanya na kujua wametuua lakini Mungu bado anatupenda tuliokolewa na wasamaria wema ambao walikuwa wakivua samaki bahari ya Atlantiki."
"Mmhh poleni sana bila shaka utatupa fulu stori siku ukija."
"Ni kweli kaka yangu ila cha kufanya kwa leo msaidie Shamimu kupata laini mpya hiyo ambayo mzee Kaaya anaifahamu aachane nayo mara moja."
"Sawa dada hata alipiga lakini hakupokea."
"Vizuri sana na wala msimueleze chochote huyo mzee hesabieni kama vile hamjawahi kukutana na watu kama hao."
"Sawa dada nimekuelewa na haitokea kumbe Robinson ni mnyama kiasi hicho?"
Shamimu alihitimisha hayo baada ya Athuman kumpa simu amalizane na Jackline.
"Ehh ikoje?"
Jasmine alikuwa pembeni akiwa na shauku ya kutaka kujua.
"Keshafika Mbeya na ni bahati pia kwani mtu niliyekuwa nina wasiwasi naye mambo freshi nimeongea naye."
"Nani Athuman?"
"Huyo huyo."
"Limekwisha hilo Jackline tuanze mazoezi sasa."
Jasmine alifurahi kusikia hayo na hivyo alimtaka Jackline waanze mazoezi kwani mzee Jerome na mke wake Bi Elizabeth Mackey walikuwa tayari wanawasubiri wao tu.
****
"Samahani Daktari kwa kukupotezea muda."
"Bila shaka brother."
Alijibu daktari Abbas alipokuwa akitoka ofisini kwake na kuliendea gari lake tayari kwa kutoka.
"Ninaitwa Muhamad Awadh ni mwandishi wa Habari kutoka blog na gazeti la NAMIBIAUPDATE."
Alijitambulisha mtu huyo na kutoa kimbulisho ambacho alimkabidhi daktari Abbas ambaye alipokiangalia alimrudishia.
"Okay naitwa Daktari Abbas Mukesh ndiye Mkurugenzi mkuu wa KING'S MEDICARE CENTRE karibu."
Alijitambulisha na kumkaribisha ofisini kwake na kuahirisha safari.
"Samahani Mkuu ni kama ulikuwa una safari hivi?"
"Yes ni kweli, kuna Seminar Elekezi ya Magonjwa ya mlipuko pale Jumba la makumbusho."
"Okay kumbe haina haja ya kuingia ofisini kilichonisogeza hapa unaweza kunisaidia hata hapa tu."
"Kama kuna uwezekano haina shida."
"Ni kuhusu wale wagonjwa ambao waliokolewa kule baharini majuma kadhaa nyuma hali zao zinaendeleaje?"
"Okay kuhusu hao wagonjwa ni kweli tuliwapokea hapa lakini kutokana na walivyokuwa ilibidi tusipoteze muda tukawapeleka hospitali ya Makambi."
"Hali zao zinaendaje huko?"
"Hapana ndugu mwandishi si jukumu langu kuelezea maendeleo ya wagonjwa wa eneo jingine ingekuwa vyema kama ungefika huko."
"Nashukuru kaka kwa ushirikiano wako basi ngoja nifike huko."
Waliagana kisha daktari Abbas Mukesh aliingia kwenye gari lake akachomoa simu yake na kumpigia rafiki yake Daktari Hans Murray.
"Ndiyo kaka za majukumu?"
Daktari Hans alipokea simu ya Abbas.
"Kwema kabisa kaka nimeona nikutaarifu juu ya wale mabinti ambao ulinieleza yaliyowakuta huko Brazil kama ambavyo mzee Jerome alipanga kutushirikisha sasa bila shaka maadui zao tayari wameanza kuwafuatilia kuna mtu mmoja anajiita Mohamed Awadh kama alivyojitambulisha kutoka gazeti na blog ya NAMIBIAUPDATE kafika hapa anawaulizia nimemwaambia aje huko cha ajabu hapa napekuapekua kwenye iPad yangu siioni hiyo blog wala taarifa za kuihusu hivyo kuwa naye makini akifika huko."
"Nikushukuru kwa umakini wako na mimi ninakuahidi kuwa akifika tu nitamuingiza kwenye kumi na nane zangu kwani nitamwambia aje tuzungumzie garini wakati huo kamera zangu zitakuwa on kisha nitamrushia video hiyo mzee Jerome ili awaoneshe mabinti zake waanze na huyo."
" Hiyo itakuwa bonge la utundu na atajuta kuvamia kazi za wenyewe."
"Basi kaka nikutakie majukumu mema mimi kuna oparesheni moja naingia kuifanya."
"Okay sawa nikutakie kazi njema."
Alikata simu akaiweka kwenye phoneholder kisha akaifunga iPad yake akawasha gari na kuondoka zake.
Upande wa pili yule mwandishi wa Habari feki baada ya kutoka pale hospitalini kwa mita kadhaa alichukua simu na kuipiga.
"Lete Habari nzuri kijana wangu."
"Mzee nimetoka ndiyo najiandaa kuelekea Makambi hospitali ambako huko ndiko walipelekwa na hizi taarifa za kweli kwani nimeambiwa na Mkurugenzi mwenyewe wa hospitali hii ya King's."
"Kazi nzuri kijana wangu lakini vipi hajakushtukia?"
"Ataweza wapi nimemwingia na gia ya uandishi wa Habari nikajitambulisha kwa jina la Mohamed Awadh wa blog na gazeti la NAMIBIAUPDATE kaingia laini na kunipa ushirikiano mwanzo mwisho."
"Vizuri sana elekea huko muda si mrefu nakuingizia kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kukusapoti utakapo kuwa huko nasikia kuna kamwendo kidogo?"
"Ni kweli kabisa kwani nitafika kesho na bila shaka kazi nayo itafanyika kesho hiyo hiyo."
"Tunakutegemea sana usituangushe."
Mzee Bruno Gautier alimjibu na kukata simu.
NINI KITATOKEA HUKO?
AMBATANA NAMI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
Kama kawaida Mohamed Awadh mwandishi wa Habari wa gazeti na blog ya NAMIBIAUPDATE kama alivyojitambulisha mwenyewe kwa Daktari Abbas Mukesh aliwasili Windhoek siku ya pili yake na moja kwa moja akapitia kwenye kijiwe cha taxi na kumvuta pembeni mmoja wa madereva ili kuongea naye.
"Mambo vipi kamanda wangu."
Alianza kwa kumsalimu.
"Poa poa kiongozi lete mchongo."
Alimjibu yule dereva taxi.
"Nahitaji kufika Makambi Hospitali."
"Haina shida kiongozi yaani hilo tu ndiyo ukanivuta mpaka huku? Ungenichana pale pale."
"Mnafanya kiasi gani hela ya mafuta?"
"Kule kiongozi kuna umbali kidogo hivyo na mkwanja wake ni mkubwa vile vile."
"Kwani kuna mile ngapi kutoka hapa kamanda maana naona kama unataka kunitisha hivi?"
"Nikutishaje kiongozi kwani wewe hii Windhoek ni mgeni?"
"Na ndiyo maana nikakuita wewe tuongee kibingwa."
"Kule kuna kama mile 53 hivi ambazo hizo utanichangia kama shilingi laki moja hivi."
"Okay sawa kamanda haina shida utanipunguzia kiasi kidogo au unasemaje?"
"Poa poa kiongozi twende zetu bwana."
Wakaondoka na kuianza safari ya kuelekea Makambi. Baada ya masaa kadhaa waliwasili na akamkabidhi nauli yake wakaachana na dereva taxi kisha akaingia hospitali na moja kwa moja akafika getini na kujitambulisha kwa mlinzi kama kawaida yake na baada ya kuruhusiwa akaingia bahati ikawa kwake kwani alimkuta Mkurugenzi Hans Murray akiwa anaongea na simu ikabidi amsubiri mpaka amalize.
"Karibu kijana."
Alimkaribisha baada ya kukata simu.
"Asante Daktari naitwa Mohamed Awadh ni mwandishi wa Habari nikifanyia NAMIBIAUPDATE blog."
"Naitwa Hans Murray ni Mkurugenzi mkuu wa Makambi hospitali sijui nikusaidie nini bwana mwandishi maana ninyi mkitiaga miguu sehemu lazima kuna jambo na kwa ninyi wa mablog taarifa zenu huwa ni mbayambaya."
"Hapana mkuu mimi nimekuja kwa taarifa nzuri tu."
"Ipi hiyo nikusaidie?"
"Ni kuhusu wale wagonjwa watatu waliookolewa baharini siku kadhaa zilizopita."
"Okay sasa nilikuwa natoka mara moja na kwa kuwa hukunitaarifu kabla inabidi mahojiano yetu yafanyike garini najua mpaka kufika mjini yatakuwa yamekwisha au unasemaje?"
"Bila shaka kiongozi tena utakuwa umenisaidia na kalifti."
"Basi nisubiri nitoe gari mara moja."
"Sawa mkuu."
Alimuacha pale na kwenda iliko gari ambako aliiandaa system yake vizuri na kulitoa gari nje ambapo hapo alimpa ishara ya kuingia garini bwana mwandishi. Baada ya kuingia safari ilianza mdogo mdogo.
"Enhh sasa tunaweza kuendelea na kilichokuleta Makambi."
"Kama nilivyokueleza hapo kabla ilikuwa ni kuja kufuatilia maendeleo yao toka walipowasili maana nilijua bado wako King's Medicare Centre ndipo nilipoelekezwa huku."
"Ni kweli waliletwa hapa kutoka King's na kuanza matibabu ambayo yaliwachukua majuma kadhaa mpaka kupata nafuu."
"Ilikuwaje maana kwa ambavyo tuliambiwa ni kwamba walizimia kabisa."
"Ni kweli ilikuwa hivyo lakini kwa Uweledi wa timu ya madaktari wangu ilikuwa ni usiku na mchana mpaka pale ambapo jitihada zilipozaa matunda."
"Hongereni sana kiongozi kwa Juhudi zenu za kuwapigania."
"Asante sana ni wajibu wetu kufanya hivyo."
"Ni kweli kiongozi na baada ya kupata nafuu ilikuwaje?"
"Matibabu yaliendelea mpaka pale tulipoona wanaweza kurudi kwao na kuendelea na dozi huko."
"Aisee kwa hiyo walisharuhusiwa tayari?"
"Ni muda sasa kama siku nne zilizopita."
"Okay ni wenyeji wa wapi wale?"
"Kazi yetu ni kuwafanyia matibabu na kutunza siri za wagonjwa na si vinginevyo."
"Naomba msaada wako lengo ni kutaka kufika huko kwao nikawafanyie mahojiano."
"Yanayonihusu nimekupa ushirikiano hayo mengine mdogo wangu hayanihusu tafuta uwezekano wa kuwapata."
"Okay nashukuru kaka yangu kwa ushirikiano wako niombe uniache hapo kwenye hilo bango la Money Express."
"Sawa sawa karibu wakati mwingine."
"Nashukuru."
Alishuka na kumuacha Daktari Hans Murray akiendelea na safari yake iliyoishia nyumbani kwake ambako baada ya kupaki gari yake aliichomoa ile kadi kwenye kamera yake pale juu kisha akaipachika kwenye iPad yake akaiangalia kwanza vipengele visivyo vya msingi alivikata kisha akamrushia mzee Jerome.
"Daktari Hans wewe ni kiboko yaani umemrekodi pasi na yeye kujua?"
Mzee Jerome alimpa sifa zake Daktari Hans baada ya kuipata video fupi ile.
"Si nilikuahidi mzee wangu?"
"Nashukuru sana ngoja niwakabidhi wenyewe."
"Wape salamu zangu na hali zao zinaendaje?"
"Kwa sasa wako vizuri na tayari wameanza mazoezi mepesi mepesi."
"Vizuri sana nikutakie majukumu mema."
Baada ya kukata simu alipandisha vioo akashuka chini na kufunga milango kisha akaingia zake ndani.
****
Mzee Jerome baada ya kuipata ile video haraka sana akawaita mabinti zake pamoja vijana wake ambao muda huo walikuwa ndiyo wamerejea kutoka kazini kwao.
"Bila shaka baba wazo letu tayari mmelifanyia kazi."
Jackline alifungua maongezi akiwa anakaa kitini.
"Kuhusu biashara mwanangu?"
"Ndiyo baba."
"Hilo tulishalimaliza muda na mama yenu labda ni kuwapa tu taarifa kaka zenu, tumekubaliana kuwa biashara ya maua itakuwa nzuri kwani bandari yetu inavusha sana kuyapeleka huko Marekani ya kaskazini hivyo tumeona kuwa kuyafuata huko yanakozalishwa au kulimwa na kisha kuja kuwauzia wageni hapa bandarini ambao hawapendi kwenda mashambani."
"Vizuri sana wazee wetu hiyo ni biashara nzuri sana kwani inapendwa sana na wenzetu wazungu."
Jasmine aliwapongeza kwa kuiona hiyo fursa.
"Baba mnataka kuanza biashara mpya inaonekana mna mkwanja eee? Si juzi juzi hapa ulikuwa unalalamika huna hela ya matengenezo ya boti?"
Mustapha aliona amtolee uvivu baba yake.
"Mwanangu ungeuliza kwanza kabla ya kuanza kulalamika."
"Wanangu baba yenu ni kweli hana salio ninyi wenyewe ni mashahidi lakini kilichotokea ni hawa dada zenu ndiyo wameamua kutusaidia mtaji na si sisi tu bali hata ninyi pia wameamua kuwafungulia duka la nguo hivyo ni kazi yenu kuwaambia mnataka la nguo gani za kike, za kiume au za watoto?"
Mama yao Bi Elizabeth Mackey aliona aingilie kati mzozo ambao ulitaka kuibuka kati ya baba na watoto wake.
" Samahani baba yetu hatukujua hilo kumbe ni kazi ya dada zetu? Kwa hiyo mnatulipa fadhila zetu dada zangu?"
Mustapha aliendelea kuwauliza.
" Mustapha naomba uelewe kuwa ninyi kwa sasa ni ndugu zetu kabisa na ndiyo maana tumeona uwezekano wa kuongeza miradi upo kwanini tusifanye hivyo?"
Jasmine alimgeuzia swali Mustapha.
" Hapana dada si hivyo niliwaelewa vibaya niombe Samahani tu."
"Haina haja ya kuomba samahani kikubwa kama umeelewa hilo limekwisha linalofuata ni ninyi kutafuta eneo linalowafaa kwa biashara kisha mtatuambia ni biashara gani mnataka."
Jasmine aliendelea kupigilia msumari kwa wakina Mustapha.
"Tunashukuru kwa jukumu mlilolibeba hakika ninyi ni watu wa kipekee sana, na kuhusu biashara gani tutawapa majibu kesho jioni baada ya kujadiliana na mwenzangu."
"Hilo ni juu yenu wanangu kwa upande wangu sina la kuwaambia ila tu Mungu anajua awatendee nini watoto wangu lakini pia nilichowaitia hapa mabinti zangu ni kazi."
"Kazi? Kazi gani hiyo baba?"
Jackline alimuuliza mzee Jerome kwa shauku kubwa.
"Sogeeni hapa niwaoneshe kitu."
Walisogea kisha akawaonesha video ikimuonesha Daktari Hans akiwa anazungumza na kijana mmoja pembeni yake.
"Huyu si Daktari Hans Murray baba sasa kuna kazi gani?"
Jessica aliuliza baada ya kuiona.
"Huyo kijana mnayemuona hapo alikwenda Makambi kuulizia hali zenu akijitambulisha kama mwandishi wa Habari lakini cha ajabu ni kwamba chombo alichokitaja kukiripotia hakifahamiki hivyo tumepata wasiwasi inawezekana akawa ni mmoja wa watu wa wabaya wenu huko Brazil wameanza kuwatafuta hivyo kwa tahadhari ni kumtafuta huyu kijana aeleze yeye ni mwandishi wa chombo gani na awapeleke kwenye ofisi zao."
"Hebu nimuone huyo kijana mwenyewe."
Mustapha aliomba amuone huyo mwandishi wa Habari.
"Mmhh mbona huyu jamaa mimi ni namfahamu si dalali wa magari na vipuri mbalimbali kutoka Japan?"
"Umeanza na wewe dalali gani choka hivi?"
Jessica alitania.
"Ni dalali na si wale wenye ofisi maalum huyu ni wale misheni town na mara nyingi anashinda nyuma pale stendi ya mabasi ya kwenda mashambani na jina lake tunamtambua kama Abdulkarim."
"Baba tunashukuru kwa kazi hii ambayo kwetu tunaiona kama uwanja wa mazoezi tu kuelekea kwenye kazi yenyewe. Kikubwa ni ninyi kaka zetu kuanza kumvizia popote alipo ikiwezekana mpaka anakolala ili sisi tukamfanyie surprise."
Jackline alishukuru kwa kumpata adui yao wa kumfanyia mazoezi.
"Dada kazi ya siku chache hiyo ninyi tuacheni matokeo mtayapata."
Mustapha alijigamba mbele yao.
"Kikubwa tu ni umakini msije ingizwa kwenye tuhuma nyingine mkajikuta mnashindwa kuyafikia malengo yenu."
Mzee Jerome aliwaasa kuchukua tahadhari.
"Baba kwenye hilo wewe tuachie majibu utayapata."
Jasmine alimtoa wasiwasi mzee Jerome.
Basi baada ya kila kitu kukaa sawa wakina Jackline walitoka na kwenda kukaa kwenye kiunga kilicho nyuma ya nyumba chini ya mpera kuendelea na stori zao.
NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.
Baada ya wiki moja ndani ya majengo ya STAMICO pale Ifumbo mzee Jonathan na kundi lake jipya ambalo ndani yake kulikuwa na wale askari waliokacha kazi kisa minoti ya mzee Jonathan waliamua kuondoka eneo hilo mida ya saa moja usiku na kuingia ndani ya kijiji kutafuta usafiri wa kuwafikisha mjini Mbeya ambako walitegemea kuingia mida ya saa sita usiku. Na kama bahati walipofika tu eneo la kisoko waliiona gari ndogo aina Eskudo ikiwa inataka kutoka.
"Samahani ndugu tuongee kidogo."
Mzee Jonathan alimuwahi dereva na kuomba kuongea naye kupitia dirishani kwani haikuwa na vioo ilikuwa wazi.
"Ongea haraka mzee baba nina haraka."
"Okay, kama unaelekea Mbeya tunaomba msaada wako tuko wanne kuna mwenzetu kalazwa Rufaa sasa tumeletewa taarifa kuwa hali yake ni mbaya sana."
"Mzee baba mbona riwaya zimeanza tena please nenda kwenye pointi iliyokusukuma kunisimamisha."
"Kijana wangu tunaomba lifti tu kwani hatuna kitu kabisa porini hakueleweki kwa sasa sijui dhahabu zimeshikwa na nani?"
"Mzee wangu unaponichosha ni pale unapochanganya mafaili, hao wenzako wako wapi mimi nina haraka ila tukifika town mtachangia hata ya mafuta."
"Haina tatizo kijana wangu."
Aliwaita wakina Masanja na kuingia kwenye hiyo gari kisha safari ikaanza kuelekea Mbeya.
"Mgonjwa wenu anasumbuliwa na nini?"
Dereva aliona avunje ukimya baada ya kutembea umbali mrefu huku kila mmoja akimvizia mwenzake.
"Mwanzo ilikuwa ni typhoid lakini baada ya vipimo zaidi pale hospitalini ikagundulika kuwa na vidonda vya tumbo vilivyokomaa."
"Da huo ugonjwa nauogopa sana mzee uliwahi kunichukulia mama yangu kipenzi miaka kadhaa huko nyuma nikiwa kijana mdogo."
"Pole sana kijana wangu."
Mzee Jonathan alimpa pole dereva.
"Tulishapoa kitambo sana na sasa maisha yanaendelea mzee."
"Aisee kweli kabisa, tumebakiwa na kilometa ngapi kufika mjini?
Maulid mmoja wa askari alimuuliza dereva.
" Tuko karibu sana kwa hapaaa tumebakiwa na kama kilometa kumi hivi kwani baada ya dakika kumi na tano tutakuwa Mbalizi."
Alimjibu akiiangalia saa yake, kigari kilikuwa kibovu lakini kilikuwa kinatembea hicho kitu kilichowashangaza wakina Masanja mwanzo walijua Mbeya wanaweza kuingia alfajiri lakini ikawa tofauti kwani kwa kilivyokuwa kinatembea kiliwapa moyo na kweli Mbeya waliingia saa sita na moja kwa moja walimuomba dereva awapeleke mpaka Uyole.
"Si mnaelekea hospitali? Sasa mbona mnakwenda Uyole tena?"
"Kule kuna mwenyeji wetu ambaye atatuhifadhi kwa usiku huu kisha asubuhi na mapema tutakuwa kwenye lango la hospitali."
Alijibu Ontario.
Basi dereva huyo alikubali kuwapeleka mpaka Uyole hivyo safari ikaendelea na baada ya kama saa hivi wakawa Uyole walishuka na mtoa kiasi kidogo cha hela na kisha waliachana.
" Nawashukuru sana jamani mtamsalimu mgonjwa."
"Bila shaka kijana."
Mzee Jonathan alimjibu huku akiwa anajifuta vumbi.
"Kinachofuata mzee?"
Ontario alimuuliza mzee Jonathan.
"Hapa cha kufanya muda huu hatutakiwi kuwepo eneo hili lenye watu wengi unaweza kukuta picha zetu ziko kila kona hivyo ninachokiona mimi tuangalie usafiri ambao unaweza kutusogeza walau Iringa."
"Mnaelekea wapi jamani kuna Fuso pale linaelekea Dar kuna siti za kuwatosha kwenye kitanda pale."
Alitokea hakuna kulala na kuwapa taarifa hiyo ambayo iliwafurahisha kwani hawakutaka hata kuuliza nauli wao walichouliza kama watatosha.
"Oya tutakaa wanne kwenye hicho kitikitanda chako kweli?"
Masanja aliuliza.
"Kaka kuna wakati huwa tunawapanga mpaka sita sembuse ninyi?"
"Basi sawa twenzao tukaone." Alijibu Maulid, na kuelekea kwenye hilo Lori na baada ya kufika tu walipanda na hakukuwa na muda wa kupoteza gari iliondoka.
"Samahani dereva niazime simu yako mara moja."
Mzee Jonathan alimuomba simu dereva.
"Tenga mpe yako yangu ilikata chaji toka tukiwa Tukuyu nikaona uvivu kuichaji."
"Gari yenu haina system charge?"
Maulid aliuliza.
"Ipo ila ilishakufa kitambo kaka."
Tenga ambaye ni kondakta wa Fuso ile alitoa simu yake na kumkabidhi mzee Jonathan ambaye aliichukua na kuingiza namba kisha akapiga.
"Nani mwenzangu?"
"Ni Mr Ubao hapa."
"Haa mkuu mbona namba ngeni tena?"
Aliuliza baada ya kulisikia jina hilo.
" Naomba nisikilize kwanza mdogo wangu."
"Nakusikiliza mkuu."
"Washa gari muda huu utufuate tuko njiani tunakuja kutokea Mbeya tuko na gari la ndizi."
"Mbona usiku sana mkuu? Mmefika sehemu gani hapo?"
Ikabidi mzee Jonathan amuulize kondakta wako sehemu gani muda huo.
"Hapa ndiyo tunaiacha Igawa tunaelekea mpakani."
Kondakta alimjulisha mzee Jonathan.
"Naambiwa tuko mpakani hapa hivyo jitahidi."
"Kama mko hapo najua dakika sifuri tunakutana njiani ngoja niwashe dude mkuu wangu."
Mzee Jonathan aliona ampigie rafiki yake aitwaye Hashimu anayeishi Makambako, alijua akifika kwa rafiki yake huyo watajificha mpaka pale watakapoianza safari ya Mwanza baada ya siku mbili.
" Asante kijana wangu simu yako hii hapa."
Alimkabidhi simu kondakta.
"Si ungebaki nayo kwanza ili uendelee kuwasiliana naye."
"Kweli kabisa kijana wangu, asante sana."
Alibaki nayo na kuendelea kufanya mawasiliano na Hashimu. Walipofika njia panda ya kuelekea hospitali ya Ilembula Lutheran walikutana na Hashimu hapo walishuka kwenye Fuso lile wakawalipa hela yao na kisha kuingia kwenye gari ya Hashimu na safari ikaendelea na muda huo ilikuwa tayari ni saa kumi na nusu.
****
"TUMEFIKISHA ZAWADI YETU TAYARI BWANA SANTANA UNAWEZA KWENDA KUICHUKUA PALE PARADISE LIGHT."
Santana akiwa na mzee Bruno wakiwa wanaliwazana kwa kucheza karata kwenye Msonge ulio katikati ya kambi yao. Mara ujumbe uliingia kwenye simu ya Santana akaichukua na kuusoma ujumbe huo. Baada ya kuusoma alisimama akazunguka huku na kule kisha akachukua siga lake na kuliwasha akalivutaa kisha akamrudia mzee Bruno pale alipokaa na kumpulizia moshi wa siga yake.
"Hivi tuna furaha gani kuendelea kukaa hapa na kucheza karata?"
Aliongea na kuzichukua zile karata na kuzichana kisha kuzitupa kitendo kilichomuacha mdomo wazi mzee Bruno kwani hakujua ana maanisha nini kwa maelezo yake na kitendo chake.
"Una maana gani Santana?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza Santana kutaka kujua.
"Unauliza mzee? Si tayari wamekuja?"
"Wamekuja? Wakina nani wamekuja?"
"Mzee amka fungua macho yako, yule kijana anayetutisha kila kukicha katuma ujumbe kuwa ameshatuma mzigo na tayari uko kule chini tena kwenye jengo letu la starehe la Paradise Light. Kwa akili yako unafikiri huko kuna zawadi gani? Na wamefikaje huko? Na wamejuaje kama chini kuna secrets rooms and services?"
" Mmhh ni hatari sana hiyo kijana wangu na mpaka hapo sioni sababu za kuendelea kumshikilia Robinson kwa sababu hiyo sehemu ambayo inafahamika na wachache tu huyo mwenyewe halijui eneo hilo."
Mzee Bruno Gautier aliona atoe pendekezo kwa Santana kwa ajili ya kumtoa Robinson kizuizini.
" Ni kweli lakini ataendelea kubaki kwanza huko mpaka tupate uhakika wa kutosha ndipo tutamuachia huru."
"Okay sawa kijana wangu."
"Jiandae mzee tuelekee huko chini tukaone kuna nini kilicholetwa lakini pia waambie walinzi wakae maeneo yao maana huyu mpuuzi anaweza kutuchezea akili zetu kama kipindi kile akatutoa kisha huku nyuma akaingia kirahisi na kufanya yake."
"Vipi kuhusu suala la wale watoto wa kike?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza swali jingine juu ya wakina Jackline.
"Mzee hiki kinachotokea kina mikono yao au umesahau kama Jasmine pekee ndiyo analijua eneo lile?"
"Okay sawa lakini unaonaje kama tukiwatuma vijana ndiyo waelekee huko chini wakaangalie kulikoni?"
"Hilo nalo neno mzee wangu ili sisi tubaki hapa kuyasoma mazingira."
Mzee Bruno alimfuata Chude na kumpa maelekezo kisha akaondoka na kuwafuata wenzake ambao kwa pamoja walielekea eneo lenye mlango wa dharura wa kushukia huko chini huku mzee Bruno akirudi alikokuwa Santana.
Baada ya muda mfupi kupita tangia washuke kule chini alirejea Chude akiwa anajifuta jasho.
"Vipi mbona umetutolea mimacho mikono mitupu uko wapi huo mzigo?"
Santana alimuuliza Chude.
"Mkuu kule kuko salama kabisa lakini kitu tulichokikuta pale mlangoni ni hiki kisu."
Alimkabidhi Santana kile kisu. Kitu ambacho kilimshangaza zaidi ni kile kisu kuwa na damu huku kwenye mpini kukiwa na kikamba kilichofunga kikaratasi ambacho alikifungua na kuusoma ujumbe ule.
" TIMU KAMILI KUKUKABILI SANTANA NA TIMU YAKO YOTE NA BILA SHAKA SAFARI HII WACHINA NA WAKOREA WATAFURAHIA VIUNGO VYENU MAANA TUMESHACHUKUA NA HELA YA AWALI YA MKATABA WA KIBIASHARA, JIANDAENI.
Ni sisi Tuliorudi kutoka Kuzimu
JACKLINE, JESSICA NA JASMINE."
" Mzee Bruno haraka sana kamfungulie Robinson aungane na wenzake kuhakikisha usalama unakuwa wa kutosha hapa kisha mpigie Afande Phillip atuongeze walinzi hapa ikiwezekana atupe zaidi ya mia moja malipo nitamuingizia jioni."
"Kwani ujumbe unasemaje huo kijana wangu?"
"Kuna lolote basi mzee wangu zaidi ya vitisho kila kukicha? Na leo wamenitumia wenyewe wakina Jasmine hivyo kuna kila dalili za wao kuwepo hapa Brazil."
"Inawezekana kwani kwa mujibu wa Abdulkarim hospitali zote walishatolewa au kutoka na mpaka sasa haijulikani waliko."
"Sisi tufanye maandalizi ya kujilinda tu ili wakitokea tu damu imwagike bila huruma hapa."
Mzee Bruno aliinuka na kuelekea alikofungiwa Robinson na kumtoa kisha kumpangia majukumu ya kufanya muda huo.
"Mzee najisikia njaa."
Robinson alimwambia mzee Bruno.
"Elekea eneo lako la kazi chakula kitakufuata huko."
"Sawa mzee." Alijibu huku akipokea silaha yake ambayo alinyang'anywa akiwa anaingizwa sero.
Mzee Bruno alirudi ofisini kwa Santana ili aweze kufanya mawasiliano na Afande Philip lakini mara hii mlinzi alimfuata mzee Bruno na kumpa ujumbe kuwa mke wake Bi Claudia anamwita nyumbani kwake, hivyo alisitisha safari ya kuelekea ofisini na kuelekea kwake, alifika na kuingia ndani.
"Karibu mzee wangu najua utakuwa umepatwa na wasiwasi mkubwa baada ya kusikia mkeo anakuita kitu ambacho hakijawahi kutokea."
Mgeni aliyemkuta pale sebuleni alimpokea kwa maneno ya kejeli.
"Wewe ni nani ndani ya mji wangu ukiwa umejiachia kama kwako?"
Mzee Bruno alimtupia swali huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio.
"Mimi ni ndugu yako mzee wangu au umenisahau?"
"Tulia wewe nani ndugu yako hapa niambie umefuata nini kwangu na mke wangu yuko wapi?"
"Mimi ni mgeni tu hapa sifahamu mkeo yuko wapi?"
Lakini wakati mgeni huyo akijieleza mbele ya mzee ya Bruno huku kajitanua kwenye sofa mzee Bruno alisikia sauti ya mtu kwa mbali kama ikilia hivi ikabidi akimbie kuelekea huko baada ya kufika hakuamini macho yake baada ya kumkuta mke wake akiwa anaogelea kwenye dimbwi la damu huku kisu kinachofanana na kile kilichokuwa kule Paradise Light kikiwa kimezama tumboni kwa Bi Claudia.
"Noooo Claudia huwezi kufa wewe nasema huwezi kufaaa amkaaa."
Mzee Bruno alipiga magoti na kuanza kujaribu kumtoa kile kisu ili ikiwezekana amkimbize hospitali, lakini alichelewa kwani tayari Roberto kijana mchafu wa matukio ya kushtukiza akawa amemfikia na kumpiga teke lililopeleka moja kwa moja kwenye kona ya jiko.
"Mzee unaonekana ni mpishi sana yaani uko tayari kufa kuliko kumuacha bosi wako Santana siyo?"
"Kwani wewe ni nani lakini?"
Mzee Bruno alimuuliza.
"Unataka kunijua siyo?"
Roberto aliongea akitoa simu mfukoni akapiga namba fulani na kumkabidhi simu mzee Bruno.
"Ongea na hiyo simu haraka na hapo ndiyo utanijua mimi ni nani."
Mzee Bruno Gautier aliipokea simu na kuiweka sehemu husika kwa kuogelea.
"Mzee Bruno Gautier mzee mpigaji mlichotufanyia hamkuridhika ukaona umuingize kwenye majanga kijana wa watu ili kujilinda siyo?"
"Naongea na nani?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza anayeongea naye.
"Naitwa Jasmine shemeji yako nikipiga simu kutoka kwenye lango la kutokea kuzimu na kurudi duniani kukabiliana na watu kama ninyi, hivi umewahi kujiuliza kuwa mtu aliyekufa akifufuka anaweza kufa tena?"
"Unataka kuniambia nini Jasmine?"
"Sijui ila tu nataka kukujulisha kuwa muda huu niko mbele ya kijana wako mwandishi wa Habari uliyempa kazi ya kututafuta na sisi kwa huruma tukaona kwanini kijana wa watu ahangaike tumejipeleka wenyewe mpe maagizo sasa huyu hapa."
Jasmine aliendelea kumtambia mzee Bruno.
" Mzee ni mimi Abdulkarim hapa."
"Nini kimekukuta kijana wangu?"
"Wameniteka mzee wangu hawa siyo watu wa kawaida kwani nimejikuta niko mikononi mwao mzee."
"Buuu shit kumbe mjinga eee yaani mpaka unashikwa ulikuwa unafanya nini?"
"Mbona na wewe kama mimi ulishindwaje kujitetea?"
Mzee Bruno kwa hasira aliikata ile simu na kuiweka chini akamgeukia Roberto.
"Sasa kwanini umuue mke wangu yeye anahusika vipi kwenye kesi hii?"
"Mzee usiwe na maswali mengi, jibu mbona ni rahisi tu nimeona nimpige kisu cha sumu ili kukupa ujumbe kuwa tumerudi upya kabisa na hizo ni salamu kwa huyo bosi wako kuwa bado tunaendelea kutekeleza ahadi zetu za kuchukua roho za wapendwa zenu na ninyi mtakuwa wa mwisho mzee."
"Unafikiri ni rahisi eee?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza Roberto.
"Majibu unayo mwenyewe mzee wangu jina langu naitwa Roberto jicho la kifo."
Roberto alijitambulisha akimfunga kitambaa cheusi usoni na kumpiga cheni mikononi.
"Kijana usijihatarishie maisha yako niachie tafadhali."
Mzee Bruno alimchimba mkwara Roberto.
Roberto hakumjibu zaidi ya kuendelea na zoezi lake na baada ya kumaliza alichomoa fataki ambayo aliipiga na kisha yeye kutokomea porini ikiwa ni ishara ya kuwaita watu wa Santana kuja kumuangalia mwenzao mzee Bruno Gautier.
"Huo mlio umetokea wapi?"
Santana aliwauliza.
"Ni kama kwa mzee Bruno hivi."
Chude alimjibu.
"Hebu kimbia mmoja kaangalie kuna nini?"
Santana aliagiza.
"Sawa mkuu."
Chude alijibu na kuelekea yeye mwenyewe kwa mzee Bruno.
NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.
Jackline aliamka siku ya leo akiwa na mawazo sana kwani alitoka nje na mswaki wake kwa lengo la kuswaki lakini cha ajabu alipofika kwenye kiunga cha maua aliutelekeza mswaki huo na kuishika simu yake na safari alikuwa akiiangalia sana namba ya Robinson kidole chake kilikuwa kikishindana na nafsi yake, kidole kilikuwa kikitamani kuigusa ile namba lakini nafsi yake ilikipiga stop kidole. Hali ile ilimchanganya sana Jackline pale kiungani.
"Robinson uliuchukua moyo wangu ukauchezea ulivyotaka na mimi kwa kuwa nilikufa na kuoza kwako sikuwa na jinsi zaidi ya kukuachia uufanye chochote kile katika kulistawisha penzi letu, lakini cha ajabu umeuchukua na kuutupa Jangwani sehemu isiyo na maji wala kivuli. Lengo lako lilikuwa ni lipi? Ina maana pesa ndiyo imeuteka mkono wako mmoja na kufikia hatua ya kuutupa moyo wangu na kisha kuokota pesa? Robinson nakuahidi katika hali ya hewa hii ya ujoto kutoka hapa Namibia kuwa nakuja Brazil kuuokoa moyo wangu hivyo jiandae, tuliingia Brazil pamoja kama wapenzi mkatufanyia yenu lakini Mungu hakuwa upande wenu katunusuru na sasa nakurudia nikiwa kama adui yako namba moja."
Aliondoka pale kama vile kuna kitu kakikumbuka na kuelekea ndani na kuuacha mswaki pale pale na moja kwa moja akaingia ndani.
" Dada Jackline umeamkaje?"
Victor alimsalimu baada ya kukutana sebuleni.
" Salama kabisa Victor vipi wewe na Mustapha?"
" Mungu ni mwema tumeamka salama japo Mustapha bado anakoroma tu kitandani."
"Inawezekana alichoka sana?"
"Wapi basi tu hajazoea mikikimikiki ya biashara yeye bahari ndiyo ya Atlantiki ndiyo sehemu yake."
"Eenh hebu niambie biashara ilikuwaje jana?"
"Unafikiri tuna cha kuongea dada Jackline, Mungu aendelee kuwapigania tu maana si kwa kuuza kule hasa viatu, t-shirts na jeans bila kusahau kadeti ndizo zilikimbiza sana jana."
"Kikubwa hakikisheni kuwa mnaikuza biashara yenu isije kufa mapema eee."
Alimshauri Victor huku akilishika korido kuelekea chumbani kwao.
"Sawa dada tutafanya hivyo."
Victor alijibu na kutoka zake nje.
"Jackline ratiba ya leo unasemaje?"
Jasmine alimuuliza Jackline akiwa bado ndani ya blanketi.
"Kwa leo naona tuchili tu japo nina hamu ya kutoka nje ya nchi."
"Nje ya nchi? Wapi huko?"
Jessica aliuliza baada ya kumsikia Jackline.
"Nahitaji kuelekea Tanzania mara moja kwa muda huu ambao wewe unaimarika kiafya."
Jackline alimjibu Jessica.
"Kuna nini tena mbona hukuwahi kuzungumzia hilo Jackline?" Jasmine alimuuliza.
"Hata sijui nini kimenitokea leo kwani huwezi amini nimetoka nje kuswaki lakini nimejikuta namuingiza mawazoni Robinson mpaka hapa mnaponiona nimeutelekeza mpaka mswaki nje."
"Usituambie kuwa hisia za kimapenzi zimeamka kwake upya?" Jasmine alimuuliza.
"Wala sielewi Jasmine katika hili japo sitaki linitokee ninamuomba Mungu usiku na mchana."
"Usizuge hapa ongea ukweli tusijejikuta tunakuwa maadui kwa jambo dogo kama hili?"
Jessica alimuuliza tena.
"Naombeni mniamini kitu kama hicho hakiwezi kutokea na ndiyo maana wazo hili lilipojiinua tu niliweka kiapo pale pale juu yake hivyo cha kufanya hapa nihakikishieni kuwa tunaongozana Tanzania au la."
"Kufanya nini huko Jackline wakati safari yetu ni kurudi Brazil?" Jasmine alimuuliza.
"Mnakwenda au mnabaki nijue?" Aliwauliza kwa ukali kidogo.
"Jackline unajua kuwa unatuchanganya wenzako? Mara Robinson, mara safari ya Tanzania. Tunakuuliza unatuwakia tunachotaka kujua Tanzania kufanya nini hutuambii hatuendi." Jasmine naye aliamua kumvimbia.
Jackline aliiona sura ya Jasmine ilivyokuwa na vituta akabaini kuwa Jasmine kachukia hivyo ikabidi ishushe jazba kidogo akaketi kitandani na kuwaeleza kile alichokifikiria kichwani.
" Nisikilizeni ndugu zangu haina haja ya kuanza kugombana kisa kutoelewana tu iko hivi baada ya kufikiria sana nimeona tuanzie nyumbani nikamalizane na mzee Jonathan kwani nasikia pamoja na kutoroka polisi lakini simu pamoja na vielelezo vingine viliachwa pale hivyo nimeona kuwa kupitia ile simu itakuwa rahisi kumnasa. Na kingine ni kwenda kumpasha ukweli wa mambo mzee Kaaya baba yake Robinson."
Alifafanua Jackline.
" Si umeona jambo lilikuwa dogo tu lakini lilitaka kutugawa." Jessica aliongea baada ya Jackline kuhitimisha maelezo yake.
" Ndiyo jamani."
Jackline aliongeza.
" Lakini Jackline unafikiri simu ile itatumikaje kumsana mzee Jonathan?"
Jasmine alimuuliza.
"Ni rahisi sana ambacho tutakifanya ni kuiingiza kwenye mfumo wetu chokozi namba ya mke wake na kumfuatilia anawasiliana na watu gani? Hiyo ni moja na pili ni kumteka mke wake, ninaamini kwa njia hizo mbili moja lazima imtie tunduni mzee Jonathan na baada ya kuweka sawa kila kitu ndipo tutarudi hapa Namibia tukiwa na bendera yetu ya kwanza ya ushindi ambayo tutaisimika hapa na kisha safari ya kuelekea Brazil itaanza mara moja kwa kutumia boti ya mzee wetu au vile atakavyotuelekeza njia ya kuitumia."
Jackline alifafanua kwa urefu.
" Hiyo imepita tayari na kwa maelezo hayo hatutakuwa na muda mrefu Tanzania, la muhimu ni kuanza kujiandaa na safari leo ili kesho mapema tutakuwa safarini."
Jasmine alimuunga mkono na kuamka kuelekea nje huku nyuma yake akifuatwa na wakina Jackline.
"Ila wewe ungebaki na mguu wako." Jackline alimwambia Jessica wakiwa koridoni kuelekea sebuleni.
"Dada umeanza sasa issue imekwisha tayari ni maandalizi ya safari juu ya mguu niachie mimi mwenyewe lakini Tanzania tunakwenda pamoja na huyo mzee wako tunakwenda kumnasa pamoja."
"Umeshinda bwana twenzetu nje kufanya usafi."
"Hayo ndiyo maneno siyo unanieleza vitu chenga dada."
Walishikana mabegani na kutoka nje wakiwa na furaha tele baada ya mkakati kukamilika.
"Halafu na ninyi mnalala sana aisee hiyo biashara mtaiweza kweli?"
Jasmine aliwaambia wakina Mustapha baada ya kuwakuta hawajaondoka bado.
"Tunakwenda muda si mrefu tulikuwa tunasubiria kifungua kinywa kisha tusepe zetu."
Victor alimjibu.
"Okay sawa vipi wazee wako ndani?"
Jasmine aliwauliza baada ya kuona kuna sura hazioni pale nje.
"Wameamka asubuhi sana kuelekea porini huko kufuatilia bidhaa zao."
Mustapha alimjibu.
"Ebwana eee mzee Jerome asije sahau biashara yake samaki?"
"Hawezi kwani kuna kampuni ambayo tumeikodishia boti kwa mkataba wa sitini kwa arobaini asilimia."
"Kivipi Mustapha?" Jackline aliuliza.
"Wao watakuwa wanachukua sitini asilimia na sisi yetu ikibaki hiyo arobaini."
Alifafanua Victor.
"Okay hiyo ni nzuri sana sasa sijui kama watarudi leo maana sisi kesho tunatoka mara moja."
Jasmine aliuliza.
"Wao kurudi itategemea na mzigo utakaopatikana, mnaenda wapi dada?"
Victor aliuliza.
"Tunatarajia kwenda Tanzania mara moja nadhani tutaongea nao kwenye simu kuwaaga."
"Mbona ni ghafla hivyo?" Mustapha aliuliza.
"Ni kweli lakini iko hivyo kutokana na simu tuliyoipokea kuna mradi wetu mmoja tumeambiwa hauendi sawa hivyo ni budi tukauweke sawa."
Jackline alitoa ufafanuzi.
"Okay ila tu isiwe moja kwa moja jamani."
"Haiwezi tokea hiyo Mustapha hapa ni nyumbani kwetu kwa sasa hatuwezi kupasahau kirahisi hivyo."
Jessica alimjibu.
Baada ya kuambiwa kuwa mzee Jerome pamoja na mke wake Bi Elizabeth Mackey wamekwenda kijijini ilibidi wao waitumie nafasi hiyo kwa maandalizi ya safari ili ikiwezekana hata siku hiyo hiyo waondoke.
****
Leo Santana na mzee Bruno waliingia St Louis Hospital kwa lengo la kumjulia hali Bi Claudia mke wa mzee Bruno baada ya siku moja nyuma kapata fahamu zake. Walifika hospitali na kufuata taratibu zote kisha kuruhusiwa kumuona mgonjwa wao.
"Mnaweza kwenda kumuona yuko chumba namba mia moja na moja kule alikokuwa tulimtoa baada ya kuona hali yake inazidi kuimarika."
Daktari aliwapa maelekezo.
"Tunashukuru daktari kwa maelekezo." Santana alimjibu daktari na kisha wakashika njia kuelekea kwenye chumba chenye hiyo namba.
Walifika na kuingia humo ambamo walimkuta akiwa anaongea na mwanamke mmoja ambaye hawakumjua mara moja ni nani.
"Unaendeleaje kipenzi wangu?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza mke wake.
"Kwa kweli namshukuru Mungu naendelea vizuri tofauti na ilivyokuwa mwanzo."
Wakati Bi Claudia akimweleza mume wake juu ya hali yake ilivyo yule mwanamke aliyekuwa naye aliinuka na kuaga.
"Sasa dada Claudia ubaki salama kikubwa usiache kumuomba Mungu kila wakati kwani yeye ndiye aliyekufikisha hapo ulipo sasa."
"Nakushukuru sana dada yangu kwa upendo wako uliouonesha kwangu Mungu akubariki."
Bi Claudia alimshukuru mwanamke huyo ambaye hakufahamika mara moja ni nani, mwana mama huyo aliondoka zake. Lakini Santana aliona amuulize maswali kidogo.
" Samahani dada ningependa kukufahamu maana tumekukuta na mgonjwa wetu ukiwa unaongea naye na sisi tumefika wewe unataka kuondoka."
"Shemeji huyo ni mtumishi wa Mungu kazi yake ni kupita kwenye mawodi kuwatia moyo wagonjwa ambao huamini kuwa kuletwa kwao hapa ni mwisho wao kumbe huwa tunajidanganya sana na kupitia yeye na mafundisho yake nimejikuta mwili unapata nguvu mpaka kufikia hatua ya kukaa hivi." Bi Claudia akaona isiwe shida amjibie mgeni wake kwani anamfahamu vizuri Santana asije muwashia moto mama wa watu.
" Sawa shemeji nashukuru kwa ufafanuzi wako kwa kile anachokifanya lakini nilitaka kumsikia yeye mwenyewe, eti..... "
Hakuweza kumalizia sentensi yake kwani alipomgeukia hakuweza kumuona.
"Yuko wapi huyu mwanamke?"
Santana aliuliza baada ya kutomuona alipogeuka.
"Aliondoka wakati ukitoa maelezo kwa Bi Claudia."
Alijibu Chude.
"Kwanini aondoke ghafla hivyo amekwepa nini? Hebu mtafuteni mara moja."
Aliuliza Santana na kisha kutoa maagizo ya kumtafuta.
Walitoka wakina Robinson na kuanza kumfuatilia yule mwanamke waliyemkuta mle wodini huku Bi Claudia akimuelezea mwanamke huyo lakini baada ya kufika huko nje waliweza kuiona gari ndogo aina ya Nissan G5 ikitoka kwa kasi na kuliacha geti la hospitali hiyo na kuishia zake. Spidi ile baada ya kufika nje ya geti iliwapa mashaka wakina Robinson na kuwafanya kurudi ndani kutoa taarifa kwa Santana. Na walipoingia ndani ya lile wodi ambalo halikuwa na wagonjwa wengi kuna kikaratasi kilichofinyangwa finyangwa hivi kilionwa na Chude chini ya kitanda kwenye mguu wa nyuma wa kitanda akakiokota.
"Hatujampata mkuu lakini kuna gari ndogo imeondoka kwa kasi sana ilipofika nje ya geti na hivyo tumelitilia mashaka gari hilo halafu kuna hiki kikaratasi."
Chude alimweleza Santana na kisha kumkabidhi kile kikaratasi alichokiokota pale chini.
Santana alikipokea kile kikaratasi na kukikunjua kisha akaanza kukisoma. Sura yake ilionesha fika kilichoandikwa mle hakikuwa kizuri.
" Si unaona sasa nilijua tu mtu gani kutoka kusikojulikana aje kukufanyia maombi wewe?"
Aliongea kwa kufoka baada ya kukisoma kile kikaratasi.
"Kuna nini kijana wangu?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza baada ya kuona anaongea kwa sauti ya juu.
"Si huyo mtumishi wenu aliyekuja kutoa mahubiri kwa mkeo." Alijibu huku alimkabidhi kile kikaratasi mzee Bruno asome mwenyewe kilichoandikwa mle. Mzee Bruno alikipokea na kukisoma.
"NI WAKATI WETU WA KUWAONESHA SISI NI WAKINA NANI, NA BAADA YA KUPATA UJUMBE HUU TEGEMEENI TAARIFA KUTOKA KWENYE MOJA YA MILIKI ZENU. ILA MUDA SI MREFU TUTAKUWA NDANI YA NGOME YAKO SANTANA. MPE POLE BI CLAUDIA ANAYEENDELEA KUYABEBA MAUMIVU YASIYOMUHUSU HATA CHEMBE ILA AVUMILIE TU.
NI WALE WALE UNAOWAFIKIRIA MUDA WOTE."
Baada ya kuusoma ujumbe huo mzee Bruno alitoa kitambaa na kujifuta jasho ambalo lilivamia uso wake bila hodi, hali iliyomtisha kila aliyemtazama mzee Bruno.
" Umeona ee, si umeona mzee Bruno?"
Santana alimuuliza mzee Bruno aliyekuwa akiendelea kufuta jasho.
"Nimeona kijana wangu, ee nimeona sijui nini kifanyike hapa maana mpaka wametoa taarifa hii ujue tayari kuna sehemu wameshaharibu."
"Mimi nadhani wewe na Robinson elekeeni kule mgodini halafu mimi na hawa wengine nirudi kambini kuona kuna nini kikubwa tupeane taarifa kwa lolote ambalo litakuwa limetokea."
Santana alitoa mgawanyo wa majukumu pale pale kila mmoja aelekee kambini kwake.
"Na vipi kuhusu mke wangu?"
Mzee Bruno Gautier alimuuliza Santana kuhusiana na mke wake kwani alishakuwa na hofu juu ya usalama wake.
"Tunapotoka tutawaelekeza uongozi wa Hospitali ili waweze kuchukua hatua za kiusalama kwenye wodi hili ikiwezekana hata kumhamishia kwenye private room'"
Hapo hapo waliagana na mgonjwa wao kisha wakatoka nje ili kufanya yale waliyokubaliana. Lakini mzee Bruno na Robinson walionekana kuwa na mawazo sana kwani wao utokaji wao ulikuwa ni wa utofauti na wenzao kwani walitoka vichwa vikiwa chini kama kuna vitu wanavifikiria.
"Mungu wangu hivi Robinson mimi ni nini kilinisukuma kuwasaliti wenzangu? Maana toka nimeungana na hawa mbona sijaweza kuiona furaha zaidi ya kukurukakara za huku na kule? Na itakuwaje siku wakirejea wakina Jackline nitasalimika? Mhh nimepatikana sijui nifanyeje hapa... "
Kabla hajamaliza mzee Bruno alimshika begani na kumfanya kushtuka kidogo kutoka kwenye lindi la mawazo.
" Kijana wangu tufanye haraka kuelekea kule mgodini japo naona mwili ni kama vile umepigwa barafu hivi sijui itakuwaje na kwa hakika kijana wangu Robinson toka tuanze hizi biashara za kimagendo hatujawahi kukutana na upinzani mkubwa kama tunaokutana nao sasa kutoka kwa hawa ndugu zako. Santana ni wa moto sana lakini kwa sasa namuona kama vile majivu yenye joto la moto na si kama zamani ilikuwa ukigusa ardhi au njia yake lazima uonje mauti."
"Lakini mzee uonavyo wewe kuna dalili za ushindi kwenye vita hii inayoendelea kututesa kila kukicha?"
Robinson aliuliza.
"Ushindi ni mkubwa sana ila tu kinachonitia hofu ni wakina nani walio nyuma yao? Maana namna wanavyotuotea ni kama vile kuna mtu anayetufahamu kiundani zaidi."
"Si mlisema anaweza kuwa Jasmine?"
"Ni kweli lakini nahisi kuna kundi jingine la watu."
Mzee Bruno Gautier alimjibu Robinson huku wakiingia kwenye gari tayari kwa safari yao.
****
"Mzee Mkonge shikamoo."
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment