Simulizi : Mbwa Wa Getini
Sehemu Ya : Pili (2)
Akachumpa hadi chini na kisha akaanza kukimbia kusonga mbele kulikokuwa na miti mingi iliofunga na tayari kiza kilianza kukolea wadudu wa usiku walikuwa wanapiga miluzi kushangilia muda wao,lakini si wote waliokuwa wakishangilia kwa furaha maana wengine walijikuta wakishangilia kwa woga baada ya kusikia vishindo vya kitu kizito kikipita karibu yao,alikuwa ni Zedi akikimbia katikati ya pori asililolijua na tayari sasa nyuma yake alikuwa akikoswakoswa na risasi za waliokuwa wakimkimbiza huku wakiwa na amri moja tu wakimpata wamuue.
Zedi alipiga hesabu maana risasi zinatoka kwenye bunduki moja,hivyo mtu aliekaribu yake bila shaka ni mmoja haraka akatoka kwenye uelekeo ule aliokuwa anaendea na akajibanza kwenye mti,lakini akagairi kujificha hivyo na kama paka akauparamia mti ule kisha kama nyoka akajigeuza na kichwa kikatazama chini huku mikono ikiwa imeukama vyema mti ule mrefu,alitulia hata pumzi zake mwenyew hakuzisikia.
Mtu yule aliekuwa anamkimbiza Zedi,akashangaa kuona anakimbia peke yake,akajua anategwa au amepigwa changa la macho usiku ule.
Akaanza kunyata huku sasa hofu ikiwa dhahiri moyoni mwake.
Alihofu vitu viwili,mosi alihofu viumbe ambao aliamini watakuwapo ndani ya pori lile usiku ule na pili alihofu kukutana na mtu yule aliemwona akidondoka kutoka juu ya paa la kambi yao,lakini kubwa zaidi akiogopa maana hakuwa na ruhusa ya kukimbiza mtu usiku ule na hata radio yake ya upepo ilikuwa haijapata uhai,hivyo ilimaanisha kazi alioifanya haikuwa na baraka zote kutoka kwa mkubwa wao.
Akagairi kuendelea mbele,
Ni wakati mlinzi yule akigeuka ili arudi alikotoka,hapo ndipo akakutana na kivuli cha mtu kikiwa kimesimama bila kutikisika.
Wakati mlinzi yule akiwa anajiandaa kushambulia,hakujua hata kimetokea nini akajikuta anaelekea kuanguka,lakini hakufika chini mkono wake wa kushoto ulikuwa umejaa kwenye mkono imara wa kivuli kile.
Mlinzi yule akavutwa kwa kasi kurudi juu na bila kutarajia akajikuta akipewa kichwa cha uso hadi akaona nyotanyota kisha likafuatia swali ambalo hakulitarajia kutoka kwa kivuli kile .
“Nioneshe njia ya kutokea katikati ya pori hili”
Mlinzi yule akawa hana cha kubisha akamweleza kinaga ubaga ya kuwa,eneo walilopo kilomita mbili mbele kuna ukuta mrefu sana,na hakuna aliewahi kuuvuka na huko pia kuna askari wengi sana.
Zedi akapagawa kuyasikia yale kutoka kwa mlinzi yule,akayarudisha macho yake kwa mlinzi yule na hapo masikio yake yakapata kusikia habari njema kidogo kutoka kwa mtu yule aliekuwa anaongea kiswahili na kiingereza kwa lafudhi ya kikenya.
Mtu yule alimwambia kuwa,njia pekee ni kupita kwenye mkondo wa maji machafu,mkondo ambao unapeleka maji yake kwenye mto Sariza,na chemba ya kupita ni moja na ipo hatua mia kutoka walipo.
Zedi ni mwanaintelejensia aliebobea,akayapima maelezo ya mtu yule na hapo akagundua jambo,mtu yule alisema ukweli,lakini kuna kitu zaidi kwenye macho ya mtu yule,alionekana kuutapika ukweli makusudi ili amwokoe Zedi,lakini kwanini atake kumsaidia,likabaki swali kichwani kwa Zedi na hakutaka kulipata,akasimama na kumwachia mtu yule kisha akaanza kupiga hatua kufuata uelekeo alioelekezwa.
Hakupiga hatua nne,akasikia mtu yule akimpa tahadhari
Hakupiga hatua nne,akasikia mtu yule akimpa tahadhari
“Huwezi kupata huo mlango wa chemba..”
Yule mtu hakungoja swali kutoka kwa Zedi,taratibu akaanza kumfuata Zedi kisha akampita na kumuomba wafuatane,Zedi akatii lakini hakuwa na imani sana na mtu yule hivyo akawa makini sana na nyendo zake na za mtu yule.
Safari yao ilikuwa ni ya kimyakimya,katikati ya pori lile na nusu walitembea nusu walikimbia ili mradi lengo lao lilikuwa ni wawahi kufika.
Safari yao iliwafikisha kwenye mfuniko wa mkubwa wa chemba ya maji machafu yatokayo ndani ya ngome ile ya Kabah,walishirikiana kufungua chemba ya ile na kabla ya Zedi hajajitosa ndani,mtu yule akamshika bega la kulia kisha akasema
“Naitwa Mao Waira,nikutakie safari njema na tukutane Nairobi…””
Alimaliza kuongea mtu yule aliejitambulisha kwa jina la Mao Waira.
Zedi akaliweka kichwani jina lile kisha akazama chembani na Mao Waira akaifunga kwa juu na kuanza kurudi kambini kwao kwa kasi ya umeme.
*****
Kitu ambacho Kabah hakutaka kuamini ni kusikia eti Zedi hajaonekana kote ndani ya ukuta unao izunguka ngome ile ile iliokatikati ya pori nene la Kenya national park.Kichwa kilimuuma,aliiona hatari ya kuanzisha Vita na Zedi aliehuru,na mara kwa mara alijilaumu kwa kushindwa kumuua Zedi mapema.
Hadi inafika ahsubuhi Kabah alikuwa hajapata kusikia habari yoyote kutoka kwa vijakazi wake ya kuwa Zedi ameonekana au mwili wake au hata nyayo zake,Kabah alijikuta akizunguka peke yake pasi kufanya kitu ndani ya ofisi yake,hakuwa amedhania Zedi aweza kuwa na uwezo wa kuruka ngome ile au Zedi anao uwezo wa kuwapiga chenga vijana wake mahiri kwa namna ya ajabu kiasi kile.
Kabah hakutaka kushindwa,aliagiza vijana mahiri waingie msituni kumsaka Zedi,lakini pia alinyakuwa simu yake iliokuwa mezani na kupiga pahali na kutoa maelekezo Zedi atafutwe Nairobi nzima ikibidi na viunga vyake.
Zedi alihisi kama kuna kitu kinamtekenya ndani ya sikio,na kwa pupa akakurupuka,lakini halikuwa sikio tu baadhi ya maeneo ya mwili yalikuwa yameanza kushambuliwa na sisimizi waliokuwa wameanza kumtambaa mwilini baada ya kukaa eneo lile la pango kwa muda mrefu.
Akasimama na kujikung’uta,kisha akaanza kufuata njia ile ya kipango kile ambacho hakujua kinaishia wapi.
Akasonga mbele hatimae akajikuta akitabasamu peke yake,mbele aliona mwanga, hivyo aliamini huko mbele ataiona dunia na ndivyo ilikuwa,alijikuta akaitokeza nje ya pango lile na kwa mbali aliona makazi ya watu na barabara iliokuwa ikipitisha magari.
Taratibu akaanza kufuata uelekeo wa barabara,na hapo akaamua kujitizama na akaona hatamaniki kwa mavazi na uchafu,lakini pia alijiona alivyo konda.
Alizifikia nyumba za wakazi wa eneo lile,na kilionekana kuwa ni kijiji cha wafugaji kilichokuwa pembezoni mwa hifadhi ile ya Nairobi.
Waliowengi kijijini pale,walionekana kumshangaa,lakini macho ya huruma yalikuwa yakimlaki kwa viulizo,hatimae Zedi alimfikia mzee mmoja na kuuliza,aliambiwa yupo Nanyuki nje kidogo ya jiji la Nairobi na pembeni ya hifadhi ya Nairobi national park.
Zedi alidanganya masahibu yaliomkuta na alidai yeye ni mtalii kutoka Tanzania na aliachwa na wenzie baada ya Simba kuwakimbiza huko porini.
Kama ujuavyo jamii nyingi za wafugaji,roho ya upendo imewajaa,ndivyo walivyo mwamini Zedi na wakampa chakula na kisha vijana rika sawa na Zedi wakavunja mabegi yao na kumpa Zedi nguo za nzuri na viatu,na Zedi alishukuru kwa ukarimu wa watu wa Nanyuki.
Ni wakati anaaga ili aondoke ndipo akapata jambo jipya kutoka kwa wakazi wa Nanyuki,wakazi wale walimpa tahadhari,maana kumekuwa na upotevu wa watu kijijini pale hasa vijana tena wengi hupotea nyakati za jioni na usiku,lakini kubwa zaidi ni kuwa hivi sasa serikali imetangaza hali ya hatari kwa wakazi wote wa nchi ya Kenya,ya kuwa kuna jamii ya wadudu wasioeleweka chanzo chake wamekuwa wakishambulia wanyama na binadamu kwa muda mchache sana.
Zedi hakuwa mgeni na wadudu wale,aliwajua na hapo akaona anakazi ya kufanya ili kulipa wema wa Wakenya.
Akawatoa hofu,na kisha akasaidiwa kupata usafiri wa kumfikisha jijini Nairobi kwa kupitia Nyeri,jambo moja hakujua aendako si salama kwake na Kama angelijua ni heri angelitafuta njia ya kurudi Tanzania kumsaidia mwanae anae teseka mikononi mwa ***** Tausi.
****
Tausi kilio kwake kilikuwa ni kama ratiba ya kila saa kwake,na sasa alikuwa analia kwa kuingiliwa kimwili na rafiki wa kabah.
Kabah na rafiki zake walimgeuza mtumwa wao wa ngono,kila walipojisikia walifika na kumwingilia kimwili Tausi,iwe kwa lazima ama hiyari,rafiki huyu wa Kabah alikuwa amemlagai kwa paketi mbili za madawa ya kulevya aina ya heroine na kwa kuwa Tausi aliyahitaji basi akafanya vile rafiki yule alivyotaka,hakuwa na pa kusemea wala hakuwa na kulilia maana Kabah alijua rafiki zake wanamwingilia mpenzi wake huyo na yeye alibariki,pengine ndo ilikuwa ni tabia yao,lakini Tausi aliona ule ni udhalilishaji kwake lakini anelikwenda wapi,ikiwa hakuna mtu anae msikiliza au kumruhusu japo kutoka nje ya geti ya jumba lile la kifahari.
Alijinyanyua kutoka pale alipokuwa amelazwa na rafiki wa kabah ambae yeye alimtambua kama Burizozo.
Akaelekea sebuleni na huko akatoka nje ya jumba lile na kisha akamuita mlinzi mmoja aliekuwa eneo lile.
“Temba!! Mwanangu yuko wapi!?”
“Tausi mimi kwa sasa sijui ila atakuwa anamezeshwa mzigo huko ili,,,,,”
Tausi hakutaka Temba amalize kuongea,akaweka viganja vya mikono yake mdomoni,kuziba sauti ya kilio isitoke,kisha akakimbia kurudi ndani,na huko kilifuatia kilio kingine cha kwikwi na akasahau kama aliingiliwa kimwili na rafiki wa kabah dakika chache zilizopita.
Temba alibaki akimtizama mwanamke yule akiishia ndani,na hapo akili yake ikaingiwa na roho ya huruma,alitamani kumsaidia,lakini aliona sio muda sahihi wa kufanya hivyo,akageuka ili arudi lindoni kwake na bila kutarajia akijikuta akitazamana na Kabah aliekuwa ameingia pale uwani kwa kutumia mlango mdogo wa geti uliokuwa wazi.
Temba alitoa heshima kwa bosi wake huyo,ambae kiumri alikuwa ni mdogo kwa Temba,lakini shauri ya pesa ilimfanya Kabah atukuzwe na kila mtu akiwemo Temba aliekuwa mlinzi mkuu wa mali za magendo za Kabah na siku ambayo hawakuwa na kazi basi Temba alisimamia ulinzi ndani ya jumba lile la kifahari lililokuwa mjini Dodoma maeneo ya area c.
Kabah alimtizama Temba kwa dakika moja bila kusema kitu na kisha kama aliegutushwa kutoka usingizini alimwambia Temba wanakazi ya kufanya muda huo na haraka Temba aandae vijana mahiri wa kazi.
Temba alijua ni nini walipaswa kufanya wakati huo nae hakuwa na namna akaingia kazini muda huo huo na vijana wake wa kazi ambao walijipachika jina la MBWA WA GETI wakiwa na maana wanasimamia masilahi ya bosi wao na hakuna mtu wa kuingilia awe askari au mtu wa kawaida ni lazima achungulie kaburi akikutana na vijana hawa.
*****
Kabah aliingia ndani huku akimwacha Temba ama Mbwa wa geti akiandaa vijana kwa kazi maalumu,alipoingia ndani tu moja kwa moja alielekea chumbani kwake na huko akachukua simu yake aliotumia kuwasiliana akiwa Tanzania na akampigia mtu anaemfahamu yeye akamweleza kupotea kwa Zedi na kisha akaagiza mipaka yote iwekwe nzi wa kunusa harufu ya mtu kama Zedi,vijana wakapangwa wakamgojea Zedi.
Alishuka chini na kumkuta Tausi akiwa amejiinamia sebuleni
Itaendelea
Alishuka chini na kumkuta Tausi akiwa amejiinamia sebuleni,akamtazama kwa dharau kisha akamsabahi,lakini salamu yake haikuitikiwa na Tausi,Kabah akakaa kwenye sofa huku akimtizama Tausi.
“naomba umuache mwanangu Kabah,mateso unayonipa yanatosha kuwa adhabu ya ujinga wangu,lakini mwache mwanangu aishi kwa amani..”
Tausi alikuwa anaongea na Kabah
“mwanao anafanya kazi kwa malipo,na malipo yake ni kete ninazo kupa kila siku,”
Yalikuwa majibu ya Kabah kwenda kwa Tausi.Tausi alinyanyua macho na kumtizama Kabah kama vile haamini alichokisikia kutoka kwa Kabah
“Naomba umwache mwanangu,kama kete ndo malipo basi naomba usinipe tena ili mwanangu aishi kwa amani Kabah please…..”
“are you sure kwamba huhitaji tena kete zangu?
“Ndio kabah”
“basi sawa mi naondoka na mwanao anakuja” kabah hakungoja neno kutoka kwa Tausi akasimama na kuchukua briefcase yake na kuondoka sebleni pale.
*****
Rpc Kambi Mabeyo,alikuwa ameshika faili maelezo kadhaa kuhusu mkakati wa ukomeshaji uuzaji wa dawa za kulevya mkoa wa Dodoma ikiwa ni kutekeleza agizo la rais la kupambana na uuzaji wa dawa za kulevya nchini.
Rpc Kambi Mabeyo alilifunga faili lile kisha akamtazama askari mkakamavu aliekuwa amesimama mbele yake akiwa ndani ya vazi lake la kazi.
“una hakika ndani ya Wiki hii utakuwa umekamilisha ushahidi wa kuwatia hatiani hawa wauzaji wa dawa hizi?!”
Lilikuwa swali la Rpc kambi kwenda kwa kijana wake aliekuwa anaongoza mpangao mzima wa kuwakamata wauzaji wa dawa za kulevya mjini Dodoma.
“Ndio afande na tumebakiza hatua ndogo sana kumjua papa wao hawa jamaa” lilikuwa jibu la Inspector Makasi kwenda kwa mkubwa wake wa kazi.
Rpc Kambi Mabeyo akimtizama kwa makini kijana wake,na hapo akaona ari ya kijana yule ndani ya uso wake,akampa nasaha kidogo na namna ya kuendesha mkakati ule bila kusingizia watu au kubugudhi watu wasio husika.
Inspector Makasi alipiga salute na kisha akaondoka ofisini pale ili kuwahi majukumu mengine ya kikazi na tayari alikuwa na kibali cha kuwakamata watu kadhaa waliokuwa wakihusika na tuhuma za uingizaji dawa za kulevya ndani ya mji ule wa Dodoma,huku maeneo kama hazina na airport yakiwa ndio senta ya biashara ile.
Jambo moja ambalo Rpc na inspector hawakujua ni kuwa muda wote wa ukusanyaji na uwasilishaji ripoti kuna mtu alikuwa akifuatilia kila hatua ya maendeleo ya kazi ile na hata wakati Inspector Makasi anatoka ofisini kwa Rpc,mtu yule aliona na aliona pia wakati Inspector Makasi anapanda gari yake aina ya Noah na vijana wengine watatu huku wakiwa na silaha za moto mikononi mwao,mtu yule aliamua kupiga simu pahali kisha akatoa maelezo machache tu na kukata simu kisha akaendelea na kazi yake.
Inspector Makasi alikuwa anaendesha noah ile tangu walipotoka ofisini kwa Rpc na sasa walikuwa wanazunguka mzunguko wa jamatini kisha wakanyoosha na barabara,wakaipita Nyerere square na wakawa wanakaribia Bank ya NBC ndipo walipata mgeni nyuma.
Ilikuwa ni pikipiki iliokuwa imebeba watu wawili na pikipiki ile ilikuwa ni BMW yenye namba za usajili kutoka uganda,watu kadhaa barabarani walikuwa wakishangaa ukubwa wa pikipiki ile.
Inspector Makasi aliiona pikipiki ile lakini hakuitilia shaka akaendelea na Safari yake huku akipanga mikakati na vijana wake.
Gari inayoendeshwa na Inspector makasi ilisimama kwenye njia panda ya dar es laam road ili kusubiri taa za kuongozea magari ziruhusu ni wakati huo ambapo kilitokea kitendo ambacho hakuna aliekitegemea.
Ile pikipiki ilikuwa ipo nyuma haraka ikapita upande wa pili kulia mwa gari ya Inspector ambako kulikuwa na magari machache sana na hapo ukasikika mlio wa risasi kutoka kwenye bunduki iliokatwa mbele na askari waliokuwa kwenye Noah ile wakashuhudia kichwa cha Inspector Makasi kikisambaratika huku damu iliochanganyikana na ubongo ikiruka huku na huko na hata waliposhuka walikuwa wamechelewa tayari pikipiki ile ilikuwa imeondoka eneo lile na wao wakaanza kushambulia kuielekea lakini tena bila kutarajia wakajikuta wakioga risasi kutoka kwenye gari nyingine iliokuwa ipo upande wa pili kama inarudi mjini huku wao walikuwa wakitoka mjini.
Kutoka kwenye gari ile walishuka watu watatu na wakaanza kushambulia kwa weledi kuelekea kwa askari wale waliokuwa wametoka ndani ya Noah na ndani ya dakika mbili tu eneo la mataa lilikuwa limebakia na maiti nne za askari polisi huku wauwaji wakiwa wanagawana njia za kukimbia.
***
Simu ya Rpc Kambi Mabeyo iliita na akaipoea,ililuwa ni sauti ya askarI wa barabarani alie kuwa pale mataa ,alieleza kwa kifupi namna tukio lilivyotokea.
Kambi mabeyo Rpc wa mkoa wa Dodoma alichanganyikiwa kusikia taarifa za kuuwawa kwa Inspector Makasi na askari wengine watatu,haraka akatoka ofisini kwake huku simu yake ikiwa sikioni alikuwa anatoa taarifa vikosi vya uchunguzi vifike eneo la tukio haraka sana.
Ndani ya dakika kumi tu tayari magari ya polisi zaidi ya manne yalikuwa yamesimama eneo lile huku magari yanayoingia na kutoka mjini yakiwa yamezuiwa kuvuka eneo lile jambo lililopelekea kuwe na foleni ndani ya mji wa Dodoma.
Hakuna askari ambae alikuwa eneo lile hakuwa na silaha,huku wakiwa wameweka ulinzi mkali eneo lile,Kambi Mabeyo haraka akaagiza kijana mmoja achukue faili ndani ya noah ile,lakini akarejeshewa taarifa ya kuwa hakuna faili hata moja ndani ya gari lile ,hapo akachanganyikiwa na akaagiza uchunguzi ufanyike kwa kina kujua wauaji na kwanini waliua japo jinsi alivyojua yawezekana ni ripoti ya madawa ndio imegarimu maisha ya vijana wake.
Swali moja lilibaki kichwani ni kwanini taarifa za kijana wake ziliwafikia wauaji ikiwa swala lile walilipeleka kwa siri mno.
Rpc akaelekea kituo kikuu cha polisi Dodoma na huko akataka apewe majalada yote ya kesi zinazohusu uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya,lakini ajabu nako hakukua na jalada hata moja,akaondoka bila kusema kitu hadi mkoani zilipo ofisi zake na huko akahitaji kupata jalada la mwisho lililokuwa linaandaliwa na Inspector Makasi,taarifa ikarudi ya kuwa hakuna kilichoachwa na inspector.
Rpc akachanganyikiwa na hapo akaona anachezewa shere ndani ya mkoa wake,hiyo ni dharau akanyanyua simu na kupiga makao makuu
Rpc akachanganyikiwa na hapo akaona anachezewa shere ndani ya mkoa wake,hiyo ni dharau akanyanyua simu na kupiga makao makuu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment