Search This Blog

Tuesday, 20 December 2022

KWA AJILI YENU WANANGU, NITAMWAGA DAMU - 5

  



Simulizi: Kwa Ajili Yenu Wanangu, Nitamwaga Damu 

Sehemu Ya Tano (5)


"Bora yenu wenzenu tumekwama huku ndani mambo ni magumu kwani inavyoonekana wakina Jasmine wametekwa kwa mujibu wa Nawane ambaye tumemmaliza na tukipiga simu zao hawapat....."

Kabla hajamalizia sentensi yake Roberto alimkatisha.


"Wewe hebu punguza utani basi wanatekwaje ni nani anayekufahamu kule kijijini."

Roberto hakutaka kuamini alichoambiwa na mpenzi wake Titiana.


"Nat......" Alitulizwa na sauti ambazo walizisikia zikija upande wao na kumfanya Titiana kumkatia simu Roberto na kumgeukia Jackline ambaye alikuwa amebana karibu na mlango tayari kwa shambulizi kama itabidi kufanya hivyo.


NINI KINAKWENDA KUTOKEA NDANI YA KAMBI HIYO?




Jackline alishindwa kuvumilia pale mlangoni alisogea mpaka dirishani na kuchungulia dirishani ili aweze kuona kuna kitu gani ambacho kimepelekea makelele hayo. Na baada ya kuchungulia hakuamini macho yake kwa ambacho alikiona nje. Hali ile ilimfanya Jackline kuchukua bastola yake na kuielekeza pale dirishani huku mwili wake ukimtetemeka.


"Unataka kufanya nini hapo?"

Titiana alimuuliza.


"Siwezi kuvumilia jiandae ni muda wetu wa kuwaonesha uwezo wetu hebu wajulishe kwa ujumbe mfupi wakina Roberto kuwa huku hali tete wajiandae kujibu mashambulizi."

Jackline alimuagiza Titiana huku yeye jicho lake likiwa kwenye range.


"Sawa ngoja nimuelekeze."

Titiana alimjibu.

Wakiwa bado wanashangaa kupitia dirishani huku Titiana akihangaika na simu mara aliletwa mtu ambaye hawakuamini macho yao.


"Haiwezekani nasema haiwezekaniiiiiiii......"

Jackline alipiga kelele ambazo ziliwashtua pale nje na kupelekea kiongozi wa genge lile bwana Mackdone ambaye ndiye alimfanya Jackline kutoa bastola mwanzo kutoa amri kwa vijana wake.


"Masikio yangu yanaumia sana mko wapi ninyi?"

Mackdone aliwaambia vijana wake ambao hawakusubiri amri yoyote walijua kuwa Bosi wao anahitaji kitu gani hivyo waliufuata mlango ule ili kuwatoa watu walio ndani yake.


"Nifuate Titiana hilo kundi siyo la kitoto."

Jackline alimwambia Titiana huku akilifungua kabati kubwa ambalo lilikuwa nyuma yao. Haraka sana walijificha nyuma ya lile kabati kisha bastola zao wakazielekeza kule walikotokea.


"Ukiwaona wanakuja upande wetu hakuna kusubiri oda ni kufyatua kwani bila kufanya hivyo tunatiwa mikononi."

Jackline alimjulisha Titiana.


"Nimekuelewa wifi yangu."

Alipokamilisha kutuma ujumbe alitoa bastola yake na kufanya kama alivyofanya Jackline.


"Wako wapi mbona hakuna watu? Watafute kila sehemu humu ndani hawawezi kutoka kienyeji."

Kiongozi wao aliwaamrisha vijana wake huku yeye akiliendea kabati ambalo alihisi kitu.

Baada ya kulifikia alichungulia kupitia nafasi iliyopo kati ya ubao na ubao lakini kabla hajafanya chochote Jackline alimfanyia mchezo wa kikubwa baada ya kumchapa risasi ya paji la uso iliyompeleka chini kiongozi huyo na haraka sana Jackline akawa keshatoka na kumuinua japo alikuwa tayari keshaanza kulegea huku Titiana akitoka na kujificha ubavuni mwa kabati hilo ambalo ukubwa wake ni mita nne kwa mita nane urefu.


"Kwa usalama wenu tueni silaha zenu chini kisha mikono juu kabla sijammaliza kiongozi wenu."

Jackline aliwaamrisha vijana hao ambao walikuja na kutaka kuwashambulia. Hawakuwa na la kufanya zaidi ya kuziweka silaha zao chini, walifanya kosa kwani kitendo cha kuinama tu chini Titiana na Jackline waliwamiminia risasi mfululizo na vijana wote nane kwenda chini na kuwapa urahisi wakina Jackline kumtua chini kiongozi wao ili watoroke kutoka humo ndani kabla hawajakamatwa. Lakini kabla hawajafanikiwa kutekeleza kile ambacho walitaka kukifanya walichelewa kwani kijana mmoja ambaye bila shaka alikuwa hajazimia au kufa aliinua silaha yake na kuwamiminia wakina Jackline.


"Aaaaaaaaaghhh........."

Hizo ni kelele zilizotolewa na Jackline akiwa anaanguka chini huku Titiana akianguka kama gunia bila kupiga kelele yoyote.

Na muda huo huo waliokuwa nje waliingia mle ndani mara baada ya kusikia mlio wa risasi ambazo ziliwashtua ila baada ya kusikia kelele za mtu wao akiwaita ndipo walipoingia ndani.


"Kamata wote hao na funga kamba wengine wabebeni vijana wetu kwa ajili ya huduma ya kwanza."

Vivian alitoa amri baada ya kuwakuta wakina Jackline wakiwa chini hawajitambui. Waliwachukua na kuwafunga pingu kisha waliwaingiza chumba cha mateso walichofungiwa wenzao.


" Tulia wewe unamtolea macho nani? Ninyi si ni miamba tulienk tulieni humu msubiri chakula chenu."

Mmoja wa vijana waliowaingiza wakina Jackline mle ndani alimwambia Jasmine ambaye aliduwaa baada ya kuona wakina Jackline wakiingizwa mle ndani wakiwa hawajitambui huku damu zikiwatoka bila kupatiwa huduma yoyote.


" Maskini ndugu zangu safari hii sijui itakuwaje?"

Jasmine aliongea huku akibubujikwa na machozi na miguu yake pamoja na mikono yake ikiwa imefungwa kwa cheni nene.


"Kelele wewe!!!!"

Kijana huyo alimtisha Jasmine na kisha alitoka nje na kuufunga mlango kwa nje.


"Hakikisheni jengo hilo linalindwa vilivyo maana hao mliowaweka humo ndani si watu wa kawaida ni mizimu hiyo."

Jasmine alitulia baada ya kuisikia sauti hiyo iliyokuwa ikitoa maelekezo.


"Mmmh si Bi Elizabeth huyo? Maana hiyo na ujanja wetu wote tumenaswa na Bi Elizabeth?"

Jasmine aliongea kwa sauti ya chini na alipojaribu kujivuta ili alisogelee zaidi dirisha alishindwa kutokana na uzito wa cheni zilizokuwa zimemfunga. Lakini akiwa hajui afanye nini mara simu ya Titiana iliita na hapo hakuwa na namna zaidi kujivuta kwa tumbo kama nyoka kumfuata Titiana ambaye alikuwa kimya kabisa hajui kinachoendelea, alijivuta na kufanikiwa kumfikia Titiana swali likaja ataitoaje simu kutoka mfukoni mwa Titiana.


"Mungu wangu nisaidie nifanikiwe kuitoa simu hii ambayo ni msaada kwetu kabla haijakata."

Jasmine alijisemea mwenyewe huku akitafakari namna ya kuitoa simu ile lakini baada ya kuona kuwa hataweza kuitoa mfukoni wazo ambalo lilimuijia kichwani ni kuubonyezabonyeza ule upande wenye simu mpaka ijipokee yenyewe na kweli alifanikiwa katika hilo.


" Nani?"

Jasmine aliuliza lakini kabla hajajibiwa simu ile ilikata kitendo kile kilimchanganya Jasmine na kushindwa kuelewa ataganyaje ili kufanya mawasiliano.


"Aghhhhhh nini hiki tena? Kwanini umekata kabla hujaongea shida yako?"

Swali hilo alijiuliza mwenyewe huku akijipigiza kichwa pale chini. Lakini mara simu ile iliita tena na safari hii aliupiga upande ule wenye simu haraka haraka kabla haijakata na Mungu alimsaidia kwani alifanikiwa kuipokea.


" Halo halo naomba nisikilize, tumekamatwa hali zetu ni mbaya sana Jackline hajitambui, Titiana sijui naye kama ni mzima, Jessica tuko naye humu ndani lakini toka siku zile hajazinduka mpaka leo watoto waliwachukua na sijui waliwapeleka wapi tafadhali fanyeni mnachoweza kutusaidia tuko kwenye jengo lililoandikwa 'NILO' "

Jasmine hakutaka kusubiri kitu kingine zaidi ya hapo alijivuta pembeni kwani hakuwa tayari kuendelea kuifuatilia simu ile kikubwa alichoamini yeye ni kuwa ujumbe umefika japo hakujua kama ametoa siri kwa watu sahihi au siyo sahihi.


" Sijui potelea mbali liwalo na liwe."

Jasmine alijisemea mwenyewe kisha akajilaza pale pale baada ya giza kuingia.


Upande wa pili mateso yalipelekea Daktari Abbas kuzimia mara kwa mara kutokana na mateso makali aliyokuwa akiyapata kwenye kile chumba chenye kila aina ya mateso, kwake mateso ilikuwa kama dozi ya malaria kutwa mara tatu.


"Pwaaaaaaa......."

Walikuja na kummwagia tena maji baada ya kuona amechukua muda mrefu bila kuzinduka.


"Aaaaaaaaagh mnaonaje mkiniua tu kuliko kunipa mateso makali kiasi hiki."

Daktari Abbas alilalamika.


"Kwani hapa kuna mateso yoyote tuliyokupa Daktari? Tena usijejaribu kuongea mbele ya mkubwa wetu itakuwa balaa kwako."

Kijana huyo alimjibu Daktari Abbas.


"Nimechoka jamani nioneeni huruma japo kidogo tu."

Daktari Abbas aliendelea kulalamika.


"Kelele wewe nitakugeuza kitoweo muda si mrefu shauri yako."

Kijana yule aliendelea kumtisha.


"Ni bora iwapo itakuwa hivyo maana si mateso haya."

Daktari Abbas alishajikatia tamaa hivyo alikuwa tayari kwa lolote litakalotokea mbele yake.


"Samani ndugu yangu unaweza kunisaidia japo maji ya kunywa?"

Daktari Abbas aliomba msaada wa maji ya kunywa.


"Ohhh umekaukiwa maji ya kunywa siyo?"

Mlinzi yule alimuuliza.


"Ndiyo ndugu yangu."

Daktari Abbas alijibu.


"Okay vizuri, hilo tu limepita ila kwa masharti kidogo tu."


"Sharti gani hilo?"

Daktari Abbas aliuliza.


"Uko tayari?"

Mlinzi aliuliza.


"Niko tayari tu ndugu yangu."

Daktari Abbas alikubali pasipo kujua ni sharti gani.


"Utatakiwa kufumba macho na kisha kuasama mdomo na mimi nitakuwekea kile unachokitaka."

Mlinzi huyo alimwambia Daktari Abbas ambaye bila kusubiri alifanya kama alivyoambiwa bila kutarajia mlinzi alifungua zipu yake na kumkojolea mdomoni.


"Aaaaaaaaagh..."

Daktari Abbas alipiga kelele baada ya kugundua ni mikojo.


JE UNAFIKIRI NINI KITATOKEA?





Kitendo cha mlinzi kumkojolea mdomoni kilimkwaza sana Daktari Abbas mpaka kufikia hatua ya kuanza kulia,alilia sana hasa baada ya kuyakumbuka maisha yake ya nyuma kabla ya kukutana na mrembo Jackline ambaye ujio wake umekuja na majanga kwenye maisha yake.


"Mungu wangu hivi ni kwamba nilikosea kumuoa Jackline? Kwanini haya yote yatokee mara baada ya kumuoa yeye lakini?"

Daktari Abbas alianza kulia tena akiamini Jackline ndiye sababu ya yote yanayoendelea juu yake.


"Kwa...kwa....kwanini lakiniiiiiiiiiii?????"

Daktari Abbas alizidi kulia na kulia mpaka pale alipoingia mwanamama Bi Elizabeth ambaye alifurahi sana baada ya kumkuta Daktari Abbas akilia bila mpangilio kama vile kapewa taarifa za msiba.


"Kweli nimeamini kuwa Dunia hii ni tambala povu yaani Daktari Abbas pamoja na umaarufu wako wote ule leo unacheza na kula na vidudu kama chawa, utitiri na kunguni? Ha ha ha ha ha ha ha...."

Bi Elizabeth akiwa kwenye dela lake nadhifu la rangi ya pink aliongea kwa dharau huku akinywa juisi yake ya muwa.


" Bi Elizabeth hivi kwe....kwe....kweli unafurahia hili na wewe nimekukosea nini mimiiii..."

Daktari Abbas aliongea kwa shida kutokana na hasira ambayo alikuwa nayo juu ya watu wote wa kwenye jengo lile.


"Jamani poleeee.. Pole sana Daktari Abbas kwa haya unayoyapitia hata mimi mwanzo nilipata kuwa mhanga wa matatizo ya mume wangu pamoja na wakina Jackline ambao wao hawakujali nini kinatokea kwa wengine wao waliangalia mafanikio ya Oparesheni yao ambayo ilipelekea familia yangu yote kufariki na mimi kuutumia muda wangu mwingine jela. Eti Daktari Abbas kwanini nisilipe kisasi kwa watu kama hao? "

Bi Elizabeth alimwambia Daktari Abbas kwa sauti ya upole kama vile alitaka kumuachia huru lakini katika kumuonesha Daktari Abbas ni kwa namna gani anamchukia yeye na familia yake alimwagia ile juisi baada ya kumfikia na kisha alikabidhiwa mkanda wenye visindano na mlinzi wake na kuanza kumtandika nao Daktari Abbas maeneo mbalimbali ya mwili.


"Bi Elizabeth se..se...sema cho...cho...cho...chochote nitafa...fanya lakini si kwa hiki kichapo."

Daktari Abbas alijitetea.


"Nataka unieleze Daktari hivi wewe ndiye unayemfadhili Jackline toka kipindi kile mpaka sasa?"

Bi Elizabeth alimuuliza Daktari Abbas.


"Aaaaaghh Mungu wangu naomba unisaidie katika hili nateseka tu kwa kosa ambalo silifahamu hata kidogo, naomba uniamini Bi Elizabeth mimi sijawahi kumfadhili Jackline hata siku moja zaidi ya kumuoa tu au nalo ni kosa?"

Daktari Abbas alimuuliza Bi Elizabeth.


" Ninyi vibwengo mnacheza tu hapa mbona huyu mtu hajachakaa hata kidogo au hivyo vimachozi vyake ndiyo vinawachanganya mpaka mnashindwa kufanya kazi yenu? "

Bi Elizabeth aliwauliza walinzi wao ambao badala ya kujibu swali la Bi Elizabeth walibaki kujiumauma tu.


" Hapana Bosi si hivyo."

Mlinzi mmoja alimjibu Bi Elizabeth.


" Unasemaje wewe? "

Bi Elizabeth alimgeukia yule mlinzi na kumuuliza swali ambalo hakutaka kusubiri jibu badala yake alimtandika risasi kitendo hicho kiliwashangaza walinzi wengine pamoja na Daktari Abbas na kisha akamsogelea Daktari.


"Daktari naomba nikupe tahadhari moja usije ukaleta jeuri yako ndani ya majengo haya hakika itakugharimu.."

Bi Elizabeth alimtaharisha Daktari Abbas akiwa kamuinamia na kumshika kidevu kilichokuwa na mindevu mingi ambayo haijawahi katwa tokea akamatwe na mwisho alimsukuma.


" Bi Elizabeth nikuombe kitu kimoja tu. "

Daktari Abbas alimwambia Bi Elizabeth.


" Kitu gani hicho?"

Alimuuliza akiwa kamgeukia kwa dharau.


"Naomba mniue tu hakuna haja ya kuendelea kuishi."

Maneno ya Daktari Abbas yalimrudisha tena Bi Elizabeth na kucheka sana.


"Kazi yangu moja tu iwapo utaifanya jioni ya leo hapo ndipo utachagua tukuue na uendelee kuishi, umenielewa?"

Bi Elizabeth alimwambia Daktari Abbas na kisha alitoka zake nje na kuwaacha walinzi wakiufunga mlango. Lakini wakiwa wanamalizia kufunga mlango mara kuna kishindo kilisikika pale mlangoni na kisha mlango ulifunguliwa na kisha kuna watu waliingia ndani.


"Mahmoud umekujaaaaa? Roberto hivi kweliiiii? Nimekosa nini mimi jamaniiii.... "

Daktari Abbas alipatwa na mshangao na kujikuta akitokwa na maneno baada ya kuwaona wakina Roberto mle ndani.


" Tutaongea tu kaka cha kwanza tukutoe hapa ndani ni hatari sana."

Mahmoud alimjibu huku wakina Ryan wakihangaika kumfungua minyororo ile aliyokuwa kafungwa.


"Fanyeni haraka hatuna muda wa kupoteza hapa."

Roberto aliwaambia wenzake huku macho yakiwa nje kupitia dirishani. Walifanikiwa na kuondoka naye bila kuonwa na yeyote huku wakiziacha zile maiti za walinzi pale mlangoni.

Muda mfupi baadaye alikuja Vivian kwenye kile chumba.


" Mamaaaaaaaa........ "

Alipiga kelele na kurudi mbio alikotoka baada ya kuwakuta walinzi wote watatu wakiwa chini wanavuja damu hovyo.


"Kuna nini tena weweeeee?"

Bi Elizabeth alimuuliza Vivian ambaye alifika pale akiwa anatweta mapigo ya moyo yakiwa juu juu.


"Mama ma...ma....mbo yameharibika huko."

Vivian alimwambia Bi Elizabeth huku akinyoosha mkono kuonesha alikotoka kama msisitizo.


"Yameharibikaje? Hebu funguka wewe Kamanda gani goigoi hivyo."

Bi Elizabeth aliuliza akiinuka kutoka kwenye kiti alipokuwa kaketi.


"Walinzi wameuawa na kisha Daktari Abbas kabebwa."

Vivian alimjibu huku naye akiinuka.


"Wamefanya nini? Hebu waite walinzi wote na mtanikuta kwenye jengo la tulilowahifadhi wakina Jackline, umenielewa?"

Bi Elizabeth kama vile alichanganywa kwani alimpa maelekezo Vivian huku akielekea kwenye eneo la tukio na wakati huo huo akaitoa simu na kutafuta namba kutoka kwenye phonebook' na baada ya kuipata aliipiga.


" Habari yako mama la mama. "

Mackdone alianza mara baada ya kuipokea simu.


"Kwa hiyo ulivyoona nimeubaini unyama wako umeamua kunichezea mchezo ili nirudi kukupigia magoti siyo?"

Bi Elizabeth alimuwakia Mackdone ambaye alijua kuna mazuri mara baada ya kuiona namba ya Bi Elizabeth.


"Kukuchezea mchezo gani tena mama la mama?"

Mackdone alimuuliza Bi Elizabeth.


"Si umewatuma watu wako kuja kumtoa Daktari Abbas? Na kama unafikiri hiyo ndiyo njia ya kunivuta umechelewa kwani bado nina wahusika wenyewe Jackline na wenzake na muda si mrefu kile kiganga nakwenda kukitia adabu si kinajifanya jeuri kwa kuendelea kuwaficha watoto wa Jackline. "

Bi Elizabeth aliendelea kumshushia lawama Mackdone kiasi cha kumfanya abaki kushangaa tu kwani yeye alijua ni utani tu.


" Nisikilize kwanza Bi Elizabeth.... "

Lakini kabla hajamaliza kuongea Bi Elizabeth akamkatia simu.

Na baada ya kufika eneo lile akakutana na miili ya walinzi wakiwa kwisha habari yao.


"Hivi mnafikiri hawa waliocheza huu mchezo wanaweza kuwa wakina nani?"

Bi Elizabeth alimuuliza Vivian ambaye aliwasili akiwa na baadhi ya walinzi.


"Hofu yangu ni kundi la Jackline tu hakuna mwingine."

Vivian alimjibu bila hata kupepesa macho.


"Una uhakika na unachokiongea? Hujashirikiana na Mackdone kumtorosha?"

Bi Elizabeth alivurugwa alimuuliza Vivian akiwa kamuelekezea bastola yake.


"Huko unakoelekea siyo kabisa yaani sisi leo hii tukugeuke kwa lipi hilo yaani yote tuliyokufanyia ni utumbo eee..."

Vivian alimjibu kwa kujiamini huku akikisogeza kifua chake karibu zaidi na mdomo wa ile bastola.


"Piga basi si umeamua kuniua piga piga sasa mbona unanitumbulia mimacho yako kumbe wewe kibibi huna Asante?"

Vivian aliendelea kumuwakia Bi Elizabeth aliyekuwa akitokwa na jasho huku bastola ikiwa bado imemuelekea Vivian.


"Okay sawa hakuna tatizo."

Bi Elizabeth aliishusha bastola yake na kutaka kuingia ndani lakini alisita baada ya kuwaona walinzi ambao walikwenda kuwaona wakina Jackline wakiwa wanakuja huku wakiteta jambo.


"Na ninyi mnateta nini huko?"

Bi Elizabeth aliwauliza.


"Hatujawak........"

Kabla mlinzi yule hajamalizia kuongea Bi Elizabeth alimkatisha.


"Hakikisha kila kona ni yenu asipite mtu nawataka wakiwa hai au wafu."

Bi Elizabeth aliamurisha watu wake kusambaa kuwatafuta wakina Jackline.


"Na wewe utakuwa nami eneo la mbele kule kwa ajili ya usalama zaidi."

Bi Elizabeth alimwambia Vivian huku akiondoka eneo hilo huku wengine wakitoa ile miili ya wenzao.


****


"Jamani vipi huko kuna usalama? Huku ni kwema kabisa."

Mzee Minyetye aliongea mara baa ya kuipokea simu ya Roberto.


"Unaongea kweli mzee Minyetye? Mbona tunaambiwa mlikamatwa?"

Roberto aliuliza.


"Ni kweli kabisa kijana wangu tulinaswa lakini kama ujuavyo nilitumia taaluma yangu kuwatoroka pamoja na wajukuu zangu na mwisho wa siku tuko salama kabisa ila ni eneo jingine tumejificha."

Mzee Minyetye alimjibu Roberto.


"Vizuri mzee wangu basi nitakucheki muda si mrefu ngoja kwanza kuna kitu tunafanya hapa."

Roberto alimwambia mzee Minyetye na kisha alimkatia simu.


"Mambo freshi??"

Mahmoud alimuuliza Roberto.


"Wako salama kabisa."

Roberto alimjibu.


"Afadhali kama iko hivyo, sasa hapa tunaelekea njia gani?"

Jasmine aliwauliza wenzake.


"Hapa tutaendelea kupambana na hiki kimsitu cha matete mpaka kule kwenye yale majaruba ya mpunga ambako kuna kinjia cha kutokea kwenye vyombo vyetu vya usafiri."

Ryan alimjibu Jasmine akiwa mbele ya wenzake akiongoza msafara. Wakiwa wanaendelea na safari kwenye maji huku Jackline akiwa kabebwa na Mahmoud, Titiana akiwa mgongoni kwa Roberto huku Ryan aliyekuwa akiongoza msafara alimbeba Jessica wakati huo Daktari Abbas akikongojwa na Jasmine.

Lakini wakiwa wamejiamini kuwa hawatafikiwa na kundi la Bi Elizabeth mara walishtukia wamewekwa mtu kati na wale walinzi.


"Kwa hiyo mlijua mmeshinda huu mchezo siyo?"

Mmoja wa walinzi aliuliza kwa kebehi huku akiwasogelea pale walipokuwa.


"Kwa usalama wenu wenyewe tunaomba mgeuze hivyo hivyo mlivyo na mizigo yenu bila kugusa chochote tofauti na hapo mtakuwa nyama zetu."

Mlinzi mwingine aliwatisha wakina Roberto lakini katika hali ambayo haikutarajiwa Roberto alimtupa majini mpenzi wake Titiana na kuwafanya maadui kupigwa na butwaa kwa kilichotokea na hapo wakawa wamefanya kosa kwani Roberto alitoa bastola yake na kuanza kuwamiminia risasi mmoja baada ya mwingine na ndipo na wakina Mahmoud wakakaa sawa kuwashambulia maadui zao.


"Mahmoud na Ryan nendeni mkasogeze usafiri maana eneo hili tulipo ni karibu na barabara kuliko kwenda mpaka kule."

Roberto aliwajulisha wenzake huku akimkimbiza mlinzi mmoja ambaye alifanikiwa kuwakimbia.


"Sawa kaka lakini hakuna haja ya kufukuzana na huyo rudi bwana."

Daktari Abbas alimwambia Roberto ambaye hakutaka kuacha hata mmoja atoke salama kule mtoni.


"Bahati yako wewe chizimaji mnajidai mnajua sana ee sasa jiandaeni tunarudi upya si mlituvizia.."

Roberto alikuwa akiongea peke kama vile aliyekuwa akimwambia alisikia tambo zake. Walijikongoja na kufanikiwa kuyafikia magari yao na Bajaj yao na baada ya kupanda waliondoka haraka eneo kabla ya maadui zao hawajakuta.


" Kama utani vile.... "

Daktari Abbas aliongea huku akianza kutokwa na machozi na hii ilikuja mara baada ya kujiangalia hali yake na kisha kumuangalia Jackline ambaye alikuwa hajazinduka.


"Pole sana kaka mkubwa kwa yaliyokukuta."

Mahmoud alimpa pole Bosi wake ambaye ni Daktari Abbas kwa aliyopitia.


"Asante sana mdogo wangu lakini ni changamoto tu katika maisha."

Daktari Abbas alimjibu.

Safari ilishika kasi huku mbele akiwa katangulia na Bajaj maana yeye ni mwenyeji wa mazingira yale.


JE NINI KITAENDELEA?




Baada ya kupata taarifa za kutoroka kwa mateka wao pale Dighton Sunset Mackdone aliamua kuelekea huko kwa usafiri wa ndege yake binafsi kutoka Afrika ya Kusini japo muda mfupi uliopita alipokea malalamiko kutoka kwa Bi Elizabeth ambaye aliamini aliye nyuma ya tukio la kutoroka kwa mateka wao ni Mackdone, hii ni baada ya Bi Elizabeth kugundua kilichotokea mwilini mwake baada ya kupata fahamu. Kitendo cha Mackdone kuutumia mwili wake kusafirisha madawa ya kulevya kilimuuma sana ukizingatia kuwa Mackdone alikuja kwake kwa lengo la kurudisha mahusiano yao ya miaka kadhaa nyuma ambayo yalivunjwa na wazazi wao. Hivyo Mackdone aliona aende Dighton Sunset kwa ajili ya kuyaweka sawa mambo haya kabla hayajawa magumu kwao.


"Naomba usimwambie huyo bibie kuwa niko njiani kuja huko."

Ni ujumbe mfupi ambao uliotumwa na Mackdone kwa Vivian akimtaka asimtaarifu Bi Elizabeth juu ya ujio wake kambini hapo Dighton Sunset.


"Kama ulivyoagiza Mkuu."

Vivian alimjibu Mackdone mara baada ya kuusoma ujumbe ule.

Na dakika chache toka ujumbe utumwe kwa Vivian ndege ya Mackdone ilikuwa ikilizinguka anga la kambi ya Dighton Sunset ikiashiria kutaka kutua, muungurumo wake ulimtoa ndani Bi Elizabeth ambaye alikuwa kachanganyikiwa kwa kitendo cha watu wake kutoroshwa na watu ambao hakuwajua kwani upande wa kundi la Jackline hakuwa na shaka nalo kutokana na idadi kubwa ya kundi hilo kuwa mikononi mwake hivyo kuwa na mashaka na mfadhili wake Mackdone. Maandishi ya ubavuni mwa Helicopter ile ambayo ilikuwa tayari imetua yalimshtua Bi Elizabeth kwani hakutarajia. Ilikuwa imeandikwa MACKDONE na hivyo kumfanya Bi Elizabeth kupandwa na hasira badala ya kwenda kumlaki mgeni wake yeye alirudi ndani.

Baada ya mlango kufunguka Mackdone na timu yake walishuka na kulakiwa na mwenyeji wao Vivian.


"Niambie jembe langu upo? Mmeshindwaje kuwathibiti panya kama wale mpaka waingie ndani na kuwatorosha mateka?"

Mackdone alimuuliza Vivian akimkamata mkono na kuelekea ziliko ofisi bubu za kambi hiyo isiyo rasmi.


"Tulikuwa imara masaa yote kumbe wenzetu wakawa wamekitumia kijito kile kule(akimuonesha kuliko) wakati sisi nguvu yetu tuliielekeza kwenye mageti yote ya kuingia ndani."

Vivian alimjibu Bosi wake huku akiwakaribisha ndani kwa ishara mara baada ya kuufungua mlango.


" Kwa miili yote ya wapendwa wetu mliichoma moto?"

Mackdone alimuuliza Vivian.


" Ndiyo Bosi tuliichoma na majivu yao kuyahifadhi kwenye kabati hilo mbele yako isipokuwa tu mwili wa Nawane hatujauchoma kama ambavyo uliagiza japo Bi Elizabeth hakutaka iwe hivyo."

Vivian alimjibu Bosi wake na wakati huo aliingia Bi Elizabeth ofisini mle na kwenda moja kwa moja kuketi kwenye kiti kilicho karibu na kabati ambalo limehifadhi kumbukumbu mbalimbali kama vile majivu ya marehemu wao.


" Umeona uje uone niko na hali gani mara baada ya kunifanyia mchezo wako mchafu siyo?"

Bi Elizabeth alimuuliza Mackdone ambaye alikuwa akitoa heshima zake kwenye vichupa vya majivu.


"Unaongea nini wewee mwanamke? Najua una hasira tu juu yangu na wala hakuna kingine. Kuna kosa nililifanya hilo halina ubishi lakini kumbuka nilifanya hivyo kwa ajili yako."

Mackdone alimjibu Bi Elizabeth huku akiomba akabidhiwe handbag' ambayo ilikuwa imeshikwa na mmoja wa walinzi wake aliokuja nao.


" Hapa kuna zawadi yako ambayo nilikuwa nimelenga mara baada ya kukubebesha madawa yale na siyo kwamba nilidhamiria la hasha..."

Wakati akiyapamba maneno yake mbele ya Bi Elizabeth juu ya kile ambacho alikifanya mara Bi Elizabeth alimkatisha.


"Kwa hiyo uliona kutoa msaada kwa umpendaye haiwezekani mpaka ukaamua kunibebesha midawa yako siyo?"

Bi Elizabeth alimuuliza Mackdone.


"Noooo Bi Elizabeth usinifikirie hivyo tafadhali inawezekana nilijua niko sahihi kumbe nilikosea..."

Mackdone aliendelea kujitetea mbele ya Bi Elizabeth.


"Huna lolote Mackdone ni tabia zako."

Majibu ya Bi Elizabeth yalimfanya Mackdone kumtoa nje ili wakaongee wakiwa wawili maana pale alihisi kushushiwa heshima yake.


"Ni kweli nilikosea Bi Elizabeth na ndiyo maana nikaona kukaa mbali na tatizo siyo njia ya kulitatua lakini njia pekee ni kulikabili na ndiyo maana niko hapa, naomba unielewe kwa hilo na ndani ya ile handbag kuna kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya dola milioni hamsini ambazo kwa kipindi hiki cha pilika kitasaidia na kwenye akaunti yako nimeingiza dola milioni ishirini na sita."

Mackdone alimwambia Bi Elizabeth akiwa kampigia magoti.


" Nashukuru sana kwa kunilipa ujira wangu kwa kazi niliyokufanyia. "

Bi Elizabeth alimwambia Mackdone huku akitokwa machozi ambayo alishindwa kuyadhibiti.


" Bi Elizabeth naomba unisamehe kwa hilo najua limeshatokea kikubwa ni kuhakikisha kuwa hawa wakina Jackline wanapatikana wakiwa hai au wafu na unionavyo hivi nimekuja rasmi kwa ajili ya suala hili."

Mackdone alizidi kumshawishi Bi Elizabeth ambaye alikuwa kakaa chini akiendelea kulia tu kwani kitendo ambacho alifanyiwa na Mackdone hakupendezwa nacho kwani hakushirikishwa.


" Naomba uinuke nimekusamehe katika hilo lakini nataka uniambie kwenye shambulizi hili unahusika au?"

Bi Elizabeth alimuuliza akiwa karibu yake kamkazia macho kama vile alikuwa halii.


"Nakuhakikishia katika hilo sihusiki hata kidogo na nina uhakika waliofanya hivyo ni watu wao kwani kundi lao siyo dogo na ukumbuke kuwa hata kule Australia walikuja wakiwa na lengo la kukushambulia hivyo siyo watu wa kubeza hata kidogo."

Mackdone alimjibu.


" Ok nimekuelewa Mackdone hebu turudi ofisini tukaandaye mipango ya kuwashughulikia."

Bi Elizabeth alikubali yaishe na kumtaka kurudi ofisini kwa ajili ya kupanga mikakati. Walirudi na kuwakuta wakiwa wanawasubiri kama walivyowaacha.


"Bosi zoezi letu limekwama."

Vivian alimjulisha Bi Elizabeth.


"Kivipi Vivian?"

Bi Elizabeth alimuuliza.


"Zile nyaya ambazo zilikatwa kwenye yale magari pamoja kulegeza nati kwenye limu za magari na ile Bajaj havijazaa matunda, wamepata ajali lakini hakuna walioumia kutokana na eneo ambalo ajali imetokea kuwa ni la tambarare na mchanga wa kutosha na hivyo wamefanikiwa kutoka salama na kutokomea msituni.. "

Vivian alifafanua baada ya kupata ujumbe mfupi kutoka kwa watu wake ambao wako porini wakiwafuatilia kuona kama watawakamata.


" Kwa hiyo wako msituni? "

Mackdone aliuliza.


" Ndiyo Bosi."

Vivian alijibu.


" Huo ni uzembe Vivian ilikuwaje wakafanya hivyo ilitakiwa wawategeshee hata bomu ni huruma gani mnayowaonesha?"

Bi Elizabeth alimlaumu Vivian kwa mipango mibovu iliyofanywa na vijana wake.


" Hebu twendeni huko huko."

Mackdone aliwaambia huku akimkabidhi ile handbag Bi Elizabeth na kuwapa ishara kuelekea kwenye helicopter tayari kwa safari.


" Nisubirini basi nihifadhi huu mzigo."

Bi Elizabeth aliwaambia akitoka na kuingia ndani kuhifadhi ule mkoba.


" Fanyeni haraka bwana hatuna muda wa kupoteza."

Mackdone aliwaambia wenzake ambao walikuwa hawajafika kwenye ndege.


****


"Hivi tutatoka salama kweli kwenye pori hili?"

Jasmine ambaye alikuwa kachoka kutembea aliuliza baada ya kuona giza linazidi kukomaa lakini kukiwa hakuna matumaini ya kufika kwenye makazi ya watu.


"Dada Jasmine usichoke ongeza mwendo Mungu atasaidia tutalivuka salama hili pori."

Ryan alimjibu Jasmine huku naye akitokwa jasho japo kulikuwa baridi kali kwani mgongoni kulikuwa na Jackline huku Roberto akiwa kambeba Jessica safari hii na Titiana alikuwa mgongoni mwa Mahmoud huku mtu mzima Daktari Abbas alikuwa akikokotana na Jasmine.


"Anachoongea Jasmine ni sahihi kabisa tupumzike ndugu zangu mwenzenu nimechoka na sidhani kama ninauwezo wa kuendelea na safari."

Daktari Abbas aliongea huku akikaa chini.


"Shemeji jitahidi bado tuko kwenye maeneo ya wabaya wetu kwani hatujui wako wapi muda huu."

Jasmine alimuomba Daktari Abbas asikate tamaa wasonge mbele.


"Habana siwezi kuendelea na safari ninyi nendeni tu mtaniagia kwa wanangu kama mtakutana nao maana sina uhakika kama wako hai lakini pia mfikishieni salama mke wangu kipenzi Jackline pindi atakapozinduka bila kumsahau rafiki yangu Daktari Hans. Mahmoud unafahamu kila kitu kiliko utamwelekeza Jackline afanye taratibu zote za kisheria... Jamaani nawashuru kwa wema wenu kwangu lakini mimi mwenyewe nimeshindwa kuimaliza safari.... "

Jasmine akiwa bado anamshangaa usoni akimsisitiza ajikaze Daktari Abbas aliivuta bastola ya Jasmine na kujipiga risasi ya kichwa ambayo iliwashtua wakina Ryan.

Wakiwa wamewatua waliokuwa migongoni mwao walimfuata na kumvuta Jasmine aliyekuwa kamlalia akilia kwa nguvu kwani ni tukio ambalo hakulitarajia hata kidogo.


"Mungu wangu keshatuacha."

Mahmoud aliwaambia wenzake baada ya kumuwekea vidole karibu na tundu za pua.


"Kweli safari yetu ni ngumu nimeamini."

Roberto aliongea huku akimpekua mifukoni kuangalia kama anachochote.


"Tuondokeni ndugu zangu."

Baada ya kujiridhisha kuwa hakuwa na chochote aliwaambia waondoke.


"Kwa hiyo tunamuacha?"

Jasmine aliuliza.


"Jasmine siyo hivyo lakini jiulize tunafanyaje hapa hatuna kingine zaidi ya kunusuru roho za walio hai kwanza huyo keshakufa hawezi badili maana."

Roberto alimjibu Jasmine ambaye alikuwa bado akiendelea kulia huku akitaka waubebe mwili wa Daktari Abbas.


"Ni kweli hatuwezi kuuchukua cha kufanya hapa tuondoke iwapo huko mbele tutakutana na makazi ya watu tutaomba msaada wa kuja kuufuata mwili huu kwa maziko."

Mahmoud aliunga mkono kauli ya Roberto ambaye alikuwa akimlaza vizuri pembeni ya mti.


"Jackline rafiki yangu pole unaachana na mumeo ukiwa gizani."

Jasmine aliongea hayo akimpigapiga Jackline mgongoni kama vile alikuwa akisikia maneno kwani mara akapiga chafya.


"Makubwaaa..."

Jasmine alipiga kelele ya mshangao.

Ikabidi wote watulie kwanza na kumfuata Jackline pale chini na baada ya kumuangalia wakakuta amelala vile vile.


"Jamani tuwahini huyu tayari kazinduka ni muda tu hapa."

Mahmoud aliwaambia wenzake huku akimuinua na kumbeba mgongoni.

Safari ilianza mara moja huku mwili wa Daktari Abbas ukiwa umeachwa pale porini na kabla hawajafika mbali mara wakajikuta wako katikati ya miale ya tochi zilizokuwa na mwanga mkali uliofanya mpaka macho kushindwa kuona vizuri.


"Jitambulisheni hapo hapo mlipo kabla mishale yetu haijala nyama zenu."

Sauti nzito na kavu yenye madaraka iliwaamrisha wakina Jasmine.


"Sisi si watu wabaya ndugu zetu tumepata ajali ya gari hivyo tumeona tupite huku kutafuta njia ya mkato kufika mjini."

Jasmine alimjibu mtu huyo aliyekuwa na kundi la watu kadhaa.


"Mjini? Mnaumwa nini aliyewaambia huku kuna njia ya mkato ya kuelekea mjini ni nani?

Mmetokea wapi?"

Wakati mtu huyu anawauliza maswali hayo mara angani ikaonekana helicopter ambayo haikuwa juu sana huku taa yake yenye mwanga mkali ikimulika chini.


"Na hawa wanatafuta nini?"

Mtu huyo aliuliza macho yake yakiwa juu.


"Mkuu hao watakuwa ni askari wa Wanyamapori wakitutafuta hivyo hatuna muda wa kupoteza hapa."

Mmoja wao alimjibu mkuu wao na hapo hapo wakaanza kukimbia wakiwaacha wakina Roberto.


"Tunaomba msaada wenu ndugu zetu sisi huku siyo wenyeji hatujui tunakoelekea, msaada wenu tafadhali."

Sauti ya Roberto iliwafikia vilivyo wale wawindaji na hivyo kufikia hatua kusimama na kujadiliana kwa muda kisha wakarejea walipokuwa wakina Jasmine.


"Mtaondoka nasi lakini mkileta jeuri tutawafundisha adabu."

Kiongozi huyo aliwatahadharisha wakina Jasmine.


"Wala msihofu sisi siyo watu wabaya hata kidogo."

Jasmine alimjibu huku ile helicopter ikirudi maeneo yale kuendelea kuyamulika.


"Kuna mwili wa mwenzetu kule nyuma kama kilometa moja kutoka hapa tunaomba tuuchukue."

Mahmoud aliwaomba huku akitangulia kuelekea uliko.


"Rudi wewe unalijua hili pori vizuri? Wewe na wewe nendeni naye mkauchukue huo mwili mtatukuta mbele tukiwa taratibu."

Kiongozi wa wale wawindaji aliagiza ukafuatwe mwili huo huku wengine wakichukua jukumu la kuwachukua wakina Jackline, Jessica na Titiana na wakina Roberto wakipata ahueni ya kupumzisha migongo yao ambayo ilikuwa imebeba wenzao kwa umbali mrefu.


JE NINI KITAENDELEA KATIKA SAFARI HIYO YA WAKINA JASMINE?





Safari ile ya kutoka ndani ya msitu ule iliendelea huku wakiwa wameufuata mwili wa Daktari Abbas, wakina Jasmine walikuwa wamechoka sana kutokana na kutembea mwendo mrefu bila kupumzika japo wale Wawindaji waliwapokea wagonjwa wao lakini bado walikuwa wachovu sana hivyo kupelekea kusubiriwa na wale wenyeji wao kila baada ya umbali fulani na kuna wakati fulani walishindwa kutembea na kufikia hatua ya kukaa hasa Jasmine ambaye kila baada ya mwendo fulani alikuwa akiomba wapumzike kidogo.


"We binti unajua kuwa unatupotezea muda hapa?"

Kiongozi wa Wawindaji alimuuliza baada ya kuona kakaa chini tena.


"Ni kweli lakini nimechoka sana najiona kukosa nguvu."

Jasmine alimjibu.


"Wenzenu wako zao huko majumbani wanalea watoto na huku porini wakisalia vidume wa kazi nakushangaa uliianzaje hii safari badala ya kubaki nyumbani."

Kiongozi yule alimshambulia Jasmine kwa maneno yale.


"Naomba nipumzike kidogo ndugu zangu."

Jasmine aliomba msaada.

Roberto kwa kuwa hakuwa mbali alimfuata Jasmine na kuongea naye.


"Panda mgongoni Jasmine tusije waudhi hawa wenyeji wetu."


"Nashukuru sana kaka yangu."

Jasmine alimjibu Roberto huku akijipandisha mgongoni. Lakini wakiwa wanasubiriwa na wenyeji wao wabebane ili safari iendelee mara wale vijana ambao waliambiwa wakaufuate mwili wa marehemu Daktari Abbas walirudi kasi kiasi cha kuwapita wakina Roberto bila kuongea chochote hali ile ilimshtua kila mmoja pale mpaka kufikia hatua kwa Jasmine ambaye alikuwa amechoka badala ya kupanda mgongoni kwa Roberto ambaye alitaka kumbeba aliunga mbio kuwafuata vijana wale bila hata kugeuka nyuma kujua wanakimbia nini hilo hakutaka kujua.


"Ninyi kuna nini huko mbona mbio hivyo?"

Mkuu wao aliwauliza vijana wake. Badala ya kujibu wao waliendelea kukimbia na kwa tendo hilo kila mmoja ikabidi aunge azimio kwani walihisi kuna hatari nyuma yao na kazi ikawa kwa wale vijana ambao waliwabeba wakina Jackline.


" Oya ongeza spidi bwana mbona uko hapo hapo unakimbiaje hivyo?"

Mmoja wa vijana waliowabeba wakina Jackline alimwambia mwenzake aliyekuwa akikimbia taratibu.


"Unauliza nini wewe huoni mgongoni kwangu kuna nini? Unajitoa fahamu ee hebu acha hizo bwana kama una haraka si upite pembeni huko."

Kijana aliyeambiwa mwanzo alimjibu.


"Nipishe huko wewee."

Alimpita kasi na kumsukuma mwenzake lakini kama bahati vile hakuweza kuanguka mpaka chini badala yake alijishikiza kwenye mti uliokuwa pembeni yake.


"Mshikaji ee pole pole basi tutauwana ujue?"


"Tembea kimlendalenda hivyo hivyo majibu utayapata."

Alimjibu mwenzake akimuacha. Safari ile ngumu sana ukizingatia kuwa giza lilikuwa limetanda kila mahali na kuzifanya tochi za Wawindaji kufanya kazi ya ziada kuweza kumulika njia.


"Zimeni tochi haraka tunafuatiliwa."

Mmoja wa wale vijana waliowapita alipaza sauti kwa wenzao akiwa mita kadhaa mbele na pasipo kuuliza kila mmoja aliweza kutii agizo lile mpaka mkubwa wao naye kwenye hilo aliweza kutii hivyo kuanza kutembea giza. Walitembea kwenye hali ile ya giza mpaka walipofika kwenye mbuga ambayo ni chepechepe.


"Nifuateni mimi huku."

Kiongozi yule aliwaelekeza wenzake huku yeye akiwa mbele yao kuonesha kuwa ni mwenyeji wa eneo hilo. Walimfuata taratibu kwa kuwa lilikuwa lina tope ambalo liliwafanya kutembea kwa tahadhari kuepuka kutitia. Wakiwa katikati ya ile mbuga oevu waliweza kuziona tochi nyuma yao zikimulika eneo lile huku zikienda huku na kule bila shaka walikuwa wakiangaza walikoelekea.


"Mkuu angalia nyuma."

Kijana mmoja alimwambia kiongozi wake aangalie walikotoka aweze kuona zile tochi.


"Jamani kazeni mwendo si muona kule wale watu wakijua kuwa tumeingia huku hawawezi kutuacha salama hivyo ongezeni mwendo."

Kiongozi wao aliwapa tahadhari wenzake baada ya kugeuka nyuma na kuziona zile tochi zinavyohaha huku na kule kuwatafuta.


"Lakini mkuu watakuwa wakina nani hao watu?"

Mwingine aliuliza swali ambalo halikuwa na maana kwani hakuna aliyejishughulisha kumjibu kwa hata aliyeulizwa alikuwa bize kuzamisha fimbo yake kukagua sehemu ya kupita. Na hatimaye walifanikiwa kutoka ndani ya mbuga ile yenye matope.


"Mkuu tupumzishe migongo si kwa uzito huu aisee."

Kijana aliyekuwa kambeba Titiana aliomba wapumzike kidogo.


"Bora umesema dogo maana si kwa uzito huu utafikiri tayari wamekufa?"

Aliyekuwa kambeba Jackline alidakia.


"Eti ninyi au nao hawa ni marehemu?"

Kiongozi aliwageukia wakina Roberto na kuuliza.


"Hapana ni wazima."

Ryan alimjibu kiongozi yule ambaye alikuwa kaketi karibu na Jasmine.


"Haka kabinti kiboko aisee kelele nyingi kumbe kalitaka kubebwa tu si mmeona namna ambavyo kametupita kwa mbio wakati kalidai kamechoka."

Kiongozi wao aliongea hivyo kumtania Jasmine ambaye aliomba wapumzike kidogo mpaka pale alipojitokeza Roberto na kutaka kumbeba kabla halijatokea la kutokea.


" Ni nani anayependa kufa kienyeji hivyo? "

Jasmine alimjibu.


" Ila yako kama ingepimwa na vifaa maalum nakueleza kabisa ungevunja rekodi zilizowekwa na wanariadha mbalimbali duniani hasa wale wa Kenya."

Kiongozi yule aliendelea kumtania Jasmine.


"Kwanza mimi naomba kujua kilichowakuta kule mpaka kufikia hatua ya kurudi mkukumkuku bila kile mlichoagizwa?"

Roberto aliwauliza wale vijana.


"Wee acha tu yaani kama bahati vile kwani ile tunakaribia tu jamaa hawa hapa wakiwa wanamulika mulika karibia na eneo lile ambalo mlisema kuna mwili wa mwenzenu hivyo katika kuokoa maisha yetu si ndiyo tukapotea zetu kabla ya kuotewa."

Mmoja kati ya vijana wale waliokuwa wamekwenda kuubeba mwili wa marehemu Daktari Abbas.


" Kwa hiyo hamkufanikiwa kuuchukua mwili? "

Mahmoud alimuuliza.


" Kaka hivi ungekuwa ni wewe ungekaa usubiri kuubeba mwili ambao tayari si hai? "

Kijana huyo alimuuliza.


"Mhhh jamani tuondokeni hatujui kama hawa watu wamekata tamaa kutufukuzia."

Kiongozi wao aliwaambia waondoke sehemu hiyo ambayo si salama sana.


"Ni kweli kabisa maana hao watu wanaweza kuwa ni wale wa maliasili hivyo jamani tuishie zetu kabla hawajatutokea hapa."

Kijana mwingine alichangia wazo na hivyo kuondoka zao hapo. Waliondoka moja kwa moja mpaka walipofanikiwa kufika kwenye kijiji fulani ambacho kilionekana ndiko waishiko wale wawindaji.


" Hodi hodi bibi, hodi bibi wajukuu wako tumefika fungua mlango."

Yuke kiongozi wao alifika na kupiga hodi kwenye jengo ambalo kwa kijijini lilionekana la maana kwani lilinakshiwa kwa mataa ya rangi rangi kulizunguka.


"Mbona usiku hivi? Mmesahau niliwaambia nini?"

Yule bibi ambaye hakuonekana mzee sana kama alivyoitwa aliwauliza.


"Tukaribishe ndani kwanza mengine tuongee tukiwa huko."

Kiongozi alimwambia bibi huyo.


"Sawa lakini ninyi wageni hamruhusiwi kuingia kwenye nyumba yangu."

Maneno ya yule bibi yaliwashangaza wakina Jasmine.


"Kwanini bibi?"

Kijana mmoja wapo aliuliza akiwa anaingiza silaha zao.


"Mimi ndiye niliyesema hivyo wewe unatakia nini?"

Bibi huyo alimjibu kijana wake akitoka nje na kuwapa ishara wakina Roberto wawabebe wakina Jackline na kumfuata alikokuwa anakwenda.


"Ingieni humu ndani mtalala humo kisha kesho ndiyo tuongee."

Aliwaambia huku akiwaonesha mlango wa kijumba chenye bati chakavu na taa hafifu ya chemli ndani yake japo nyumba kubwa ilikuwa imefungwa taa za Sola lakini kijumba kile hakikuwa na umeme huo wa Sola.


" Samahani bibi.... " Ryan alitaka kuuliza lakini alikatishwa na bibi yule.


"Binti unataka kuongea nini wakati mimi nimemaliza kama hauko tayari pisha kwenye jengo langu na ujue kuwa mmenikatisha usingizi wangu."

Majibu ya bibi yule yalitosha kabisa kumfanya Ryan kuwapa ishara wenzake kuingia ndani na kisha mlango ulifungwa kwa nje na kisha yeye akarudi zake ndani.


" Jamani hivi mnafikiri tutatoka salama humu ndani kweli? "

Jasmine aliuliza.


" Tumuachie Mungu aamue hili maana sisi hatujui ya mbele yetu."

Roberto alimjibu Jasmine huku akiwa anamuangalia mpenzi wake kama ana dalili za kuzinduka.


"Hii jamani vitu gani hivi tena vinaminyaminya miili?"

Ryan aliuliza akiwa anajikagua mkono wake kuashiria kang'atwa na kitu.


"Hebu ngoja kwanza."

Roberto Mahmoud aliongea akijaribu kuwasha simu yake ambayo aliizima mara baada ya kuona inakaribia kukata moto.


"Jamani angalieni hapa."

Mahmoud aliongea baada ya kumulika chini na kukutana na vidudu vidogodogo.


"Kweli huyu mama ana roho mbaya sana yaani kutuweka kwenye chumba chenye kunguni? "

Jasmine aliongea akiinuka huku akijikagua na yeye kama amepandwa na hao kunguni.


" Mnajua nini hapa cha kufanya? "

Roberto aliwauliza.


" Hatujui twambie!!! "

Mahmoud alimjibu.


" Tufumbeni macho kisha tuvute pumzi ya kutosha na kuishusha kwa utuo na baada ya hapo tuivute picha mpya kuwa chumba hiki ni salama kabisa hakina tatizo lolote kisha tulale hakuna kunguni ambaye atajaribu kutuuma. "

Aliwaambia wenzake Ryan.


"Unachekesha wewe nani alale na kunguni wote hawa? Ninyi laleni tu tukutane asubuhi."

Roberto alimjibu.

Walilala na wengine kusalia macho kwa hofu ya kunguni mpaka kulipopambazuka na hiyo ni baada ya kumsikia jogoo akiwika kuashiria kuwa kumekucha japo Jasmine alipojaribu kuangalia nje kupitia kwenye Ufa wa ukuta alikutana na kigiza chembamba ambacho kilikuwa kikishindana na nguvu ya jua.


"Jamani mwenzenu nimevimba karibia mwili wote afadhali kumekucha."

Mahmoud aliongea.


"Aliyekwambia kumekucha nani? Hao ni wale vijogoo ambao ni wazurulaji kupita kiasi mpaka kufikia hatua ya kulala na njaa mwisho wa siku wanaishia kutuamsha hata ikiwa ni saa sita usiku kokolikoooooo aaah wacha nilale kidogo."

Jasmine aliwajibu na kuwafanya wote kuangua kicheko kilichowafanya kusahau madhila ya kunguni.


" Hao watakuwa ni Majogoo wa sehemu moja ya Tanzania iitwayo Singida maana nasikia kule kuna kuku kushinda watu sijui no kweli? "

Roberto alichomekea.


" Muongo mwingine huyo sijui katokea wapi au ndiyo ming'ato ya kunguni imemchanganya akili maana yeye na Tanzania wapi na wapi labda angeongea Jackline ambaye kule ni kwao."

Jasmine aliongea baada ya kuona kama vile Roberto anataka kuwatanguliza.


"Nathan mfuate Natalie chakula kiko tayari mle kabla ya hakijapoa."

Kila mmoja alishikwa na mshangao na kusogea kuangalia kama alichokisikia anaota au ni kweli.


"Wanangu acheni kelele basi mama yenu nina usingizi bado nendeni huko nje mkamsaidie baba yenu kuosha gari."

Kila mmoja mle ndani alitulia kimya kuyaacha maneno yale yaendelee kupenya masikioni mwao na kuziacha bongo zao ziendelee kuchakata sentensi zile.


JE NINI KINAKWENDA KUTOKEA? NA MANENO HAYO YALIYOWACHANGANYA WAKINA JASMINE YAMESEMWA NA NANI?




Maneno yale yaliyokuwa yakisemwa na Jackline yalimfanya kila mmoja mle ndani ya kile kibanda kutokwa na machozi ambayo hakuna aliyeweza kuyazuia hata kidogo japo kila mmoja yalimtoka kwa sababu yake kuna ambao yaliwatoka kwa kumuonea huruma Jackline ambaye akili yake inaamini Daktari Abbas yu hai ilhali keshapoteza maisha kutokana na mateso ambayo alikutana nayo kwenye ngome ya Bi Elizabeth kiasi cha kumkatisha tamaa na kufikia hatua ya kujipiga risasi wakiwa kwenye harakati za kuwatoroka wakina Vivian na wengine walitokwa machozi ya furaha kutokana na Jackline kuzinduka.


"Kazinduka tayari hakika Mungu ni mwema."

Jasmine alimshukuru Mungu kwa muujiza uliofanywa kwa Jackline.


"Tuko wapi hapa?"

Jackline aliuliza baada ya kufungua macho yake na hii ilikuja baada ya kelele walizopiga wakina Ryan wakati akiongea akiwa ndotoni.


"Tulia kwanza Jackline akili ikaye sawa utajua tu."

Jasmine alimjibu.


"Naombeni mniambie basi mbona mnanifanyia hivyo lakini?"

Jackline alilalamika.

Lakini kabla hajajibiwa swali lake mara mlango ulifunguliwa.


"Ninyi wakimbizi tokeni nje haraka."

Yule bibi mwenyeji wao aliwataka kutoka nje.


"Sawa bibi."

Roberto alimjibu.


"Fanyeni haraka bwana bibi bibi nani bibi yako unanifahamu mimi wewe?"

Bibi huyo aliyeonekana kuwa mtata alimjoboa Roberto.


"Nisamehe kwa hilo."

Roberto alimjibu akitoka nje kutoka kwenye kijumba kile.


"Hee mbona mko hivyo jamani?"

Jackline aliwauliza wenzake baada ya kuwaona namna walivyokuwa wamechafuka kwa matope yaliyokaukiana kwenye nguo.


"Unawashangaa wenzako? Kwa kuwa wewe ulibebwa unajisikia rahaaa mwenyewe."

Yule bibi alimjibu Jackline aliyetaka kujua kwanini wenzake wako kwenye hali ile.


"Ina maana mlizama kwenye matope?"

Jackline alizidi kuwatupia maswali ambayo alihitaji kujua kilichowatokea.


"We binti acha maswali yako ya kijinga kwenye makazi yangu unauliza nini si na wewe ulikuwa huko unachotaka kujua ni nini? Nifuateni huku."

Bibi yule alimzodoa kwanza Jackline kisha akawataka wamfuate alikokuwa kawaongoza.

Ilibidi Jackline awe mpole na kumsikiliza mwenyeji wao anasema nini.


" Samahani mama vipi kuhusu wagonjwa wetu? "

Jasmine alimuuliza.


" Wagonjwa? Wananihusu nini mimi waache huko huko bandani nawataka ninyi wenye akili zenu timamu."

Bibi yule alimjibu Jasmine japo majibu yale yalimuumiza sana Jackline ambaye alikasirika na kutaka kufanya jambo lakini Mahmoud alimzuia.


"Unataka kufanya nini shemeji? Kumbuka hujapona vizuri na pia kuwa mpole tuko kwao hawa."

Mahmoud alimwambia Jackline maneno ambayo yalimwingia vilivyo na kutulia huku wakimfuata bibi yule aliyekuwa mbele akiwa kashika usinga mkononi na akiongea maneno ambayo wao hawakuyaelewa hata kidogo.


" Unaelewa anazungumza nini? "

Jasmine alimuuliza Ryan.


"Ni maneno ya kimizimu hayo, anawasiliana nayo bila shaka yuko kuomba kibali cha kutupokea sisi."

Ryan alimjibu Jasmine.


"Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa huyu bibi ni mganga wa jadi?"

Jasmine alimuuliza tena Ryan.


"Naweza sema hivyo japo sina uhakika ila si mtu mbaya kwa namna anavyoongea na hiyo mizimu yake."

Ryan alimjibu Jasmine na muda huo walikuwa mlangoni mwa jengo la bibi huyo ambalo kwa asubuhi hiyo lilionekana vizuri lilikuwa ni jumba la kifahari sana kwa eneo ambalo lilikuwa. Kwa kijijini kuwa na jengo la ghorofa moja si mchezo.


" Karibuni ndani."

Bibi huyo aliwakaribisha wageni wake.


"Asante."

Roberto aliitikia kwa niaba ya wenzake. Waliingia ndani ambako aliwakaribisha mpaka kwenye chumba ambacho hakikuwa na kiti chochote zaidi ya mikeka iliyokuwa imetengenezwa kiasili.


"Tulieni hapo chini vijana."

Aliwataka wakaye chini huku yeye akiwa anaketi kwenye kigoda alichoingia nacho.


"Karibuni sana vijana."

Aliwakaribisha tena huku akimuangalia mmoja mmoja.


"Asante tunashukuru."

Jackline alijibu.


"Vizuri, naitwa Blandina Collins mimi ni mzaliwa wa jiji la Paris nchini Ufaransa lakini asili yangu ikiwa hapa hapa Gaborone. Nilizaliwa na kukulia kule pia elimu yangu nimeipatia kule kule Ufaransa wazazi wangu wakiwa ni wafanyabiashara. Lakini baada ya kuhitimu kozi zangu mbalimbali kule Ufaransa nilirejea nyumbani kwa wito maalum kutoka koo yangu ya Kiwindaji kunitaka nirudi kuiongoza jamii hii kwa sababu mimi nilikuwa chaguo la bibi yangu ambaye alikuwa ndiye malkia wa ardhi hii yote na jamii yake hivyo sikuona sababu ya kukataa japo kwa mtu niliyekulia Ulaya ingekuwa ngumu sana lakini nilikuja na kuvikwa hili vazi maalum la Utawala. Naitwa bibi lakini mimi si wa umri huo kwani sijafikisha hata miaka arobaini limekuja kutokana na majukumu yangu."

Blandina Collins alijitambulisha kwa wageni wake ambao walibaki wameduwaa wakimsikiliza tu alivyokuwa akielezea historia yake.


" Kwa hiyo wewe ni nani? "

Jackline alimuuliza Bi Blandina.


" Mimi ni mtawala wa jadi wenyewe Wananiita Malkia Amashabho kwa heshima ya jamii yangu lakini watu ambao si wahusika kwenye jamii yetu hunitambua kama Blandina Collins ambaye nje ya utawala katika eneo hili mimi pia ni mfanyabiashara wa nyamapori ambayo huwa naisafirisha nje ya nchi hasa katika nchi ya Ufaransa japo serikali kwa sasa inasema haiutambui Utawala wetu kwenye eneo hili hivyo tumeingia kwenye mgogoro nao lakini tutashinda tu."

Blandina Collins aliwafafanulia wageni wake.


" Tunafurahi kukaa karibu nawe dada Blandina mtu ambaye toka jana tulikuchukia kwa kitendo cha kutulaza kwenye kijumba kile chenye kunguni na pia bila hata kutupa maji ya kuoga na chakula lakini kwa sasa tumeanza kuwa wapole."

Jasmine aliongea kile ambacho walijisikia kwa yale waliyofanyiwa pale.


" Vizuri mdogo wangu kwanza kabisa naomba nieleweke wazi kuwa nisingewalaza ndani ikiwa siwafahamu vizuri hata mlikotokea hivyo ilikuwa ni lazima niwalaze kwenye kijumba kile ambacho hutoa majibu kwangu na kile mlichokutana nacho mle siyo kunguni bali ni mizimu ambayo ilikuwa ikichukua taarifa zenu."

Bi Blandina aliendelea kuwastaajabisha wakina Jasmine.


" Taarifa zetu? Kivipi? "

Roberto aliuliza.


" Tulieni nitawaeleza kila kitu kuwahusu,nafikiri hamuwezi kunielewa mapema lakini mtanielewa tu. Kwanza kabisa niwape pole kwa majanga mnayokutana nayo kila kukicha."


"Hatujapoa bado Bi Blandina."

Mahmoud alijibu haraka.


"Najua, Najua vizuri sana yote haya yanatokea kwa sababu ya mdogo wangu huyu hapa (aliongea huku akimgusa bega Jackline) sababu kubwa ikiwa ni kurejesha haki zake zilizoporwa na rafiki ya baba yake bwana Jonathan katika hangaikahangaika akajikuta akiangukia mikononi mwa yule muujiza mkubwa wa madawa ya kulevya kule Blazil na sasa vita imehamia kwa Mackdone na Bi Elizabeth. Ninachoweza kuwaambia ni kwamba vita ya kwanza ilikuwa nyepesi lakini hii ya sasa ni ngumu sana kwani mnapambana na mtu hatari sana ambaye ana mbinu nyingi za kupambana na maadui zake na ndiyo maana jana kawafuatilia mpaka mbugani na alipowakosa akaondoka japo hakuondoka hivi hivi aliubeba mwili wa mpendwa wenu mliokuwa mmeuacha kule porini. "

Bi Blandina aliendelea kuelezea kile akijuacho juu ya ile timu ya wakina Jasmine.


" Unasema mpendwa wetu? Yupi huyo? "

Jackline alipata shaka akaona aulize juu ya huyo mtu anayezungumziwa pale lakini Blandina alishajua nini kinakwenda kutokea hivyo alichokifanya alichukua kibuyu kidogo kilichokuwa pembeni yake akakitikisa huku akiongea maneno ambayo hayakujulikana maana yake japo Ryan aliokotaokota baadhi kisha akamimina kwenye glasi ambayo alimkabidhi Jackline.


"Kunywa hiyo dawa ni nzuri huponya hitilafu zote mwilini hasa vidonda vya ndani ya mwili na pia inasaidia kukufanya kuwa mkakamavu."

Bi Blandina alimkabidhi ile dawa na Jackline naye aliipokea na kuinywa. Baada ya kunywa alianza kuona kizunguzungu kisha akajikuta anaanguka chini.


" Msimguse muacheni kwanza hiyo itamfanya kutoteteleka atakapopata taarifa ya familia yake ambayo ameipoteza."

Bi Blandina alimkataza Jasmine ambaye alitaka kumzuia asianguke.


"Ameipoteza familia yake?"

Roberto aliuliza.


"Ndiyo kaipoteza kwani si mlishuhudia mume wake akijipiga risasi?"

Bi Blandina Collins aliwauliza.


"Ndiyo tulishuhudia."

Jasmine alijibu.


"Haswaa, lakini pia watoto wake wakiwa wanatoroshwa na mzee Minyetye kutoka kule kijijini kwake akiwatorosha kwenda kijiji kingine kilicho porini ambako alihisi anaweza kuwaficha huko wakabaki salama bila kukutwa na Bi Elizabeth lakini hakufanikiwa kwani ile ndege ilipokuwa ikirudi kutoka hapa kwenye pori letu iliweza kuwaona wakiwa kwenye Oparesheni ya kuwatafuta ninyi hivyo walitua na kuanza kuwafuatilia wakijua ni ninyi kumbe alikuwa ni mzee Minyetye na wale mapacha na baada ya kuwafikia Bi Elizabeth hakutaka kusubiri aliwafyatulia risasi kisha kuwabeba na kurudi nao kambini....."


"Hapana haiwezekani hata kidogo wale mapacha hawawezi kufa kienyeji hivyo dada utakuwa umekosea."

Jasmine alimkatisha Bi Blandina.


"Siwezi kubadili nyeusi kuwa nyekundu lakini ukweli ndiyo huo wale watoto na mzee Minyetye wameuawa japo huyu Natalie nikiangalia vizuri bado anapumua japo kwa shida ila sijui kama mtafanikiwa kumfikia na kumuokoa."

Bi Blandina aliwafafanulia.


"Wamepelekwa wapi?"

Ryan aliuliza.


"Wako pale pale kambini kwao wamewaweka kwenye lile ghala wakiamini kuwa wote wamekufa na lengo likiwa ni kuwatafuta ninyi pia."

Bi Blandina aliongeza kitu ambacho kiliwafanya wakina Jasmine kuangaliana kwa muda.


"Nendeni kwanza kwenye yale mabafu pale nje mkaoge kwanza mpate nguvu kisha mpate chakula na baada ya hapo nitawaelekeza cha kufanya."

Bi Blandina Collins aliwaelekeza wakina Jasmine ambao walikuwa wamelowa kwa jasho ambalo hawakujua limetoka wapi huku kila mmoja macho yakiwa pale chini ambapo alikuwa kalala Jackline bila shaka ilikuwa ni kumuonea huruma namna atakavyokuwa baada ya taarifa hizi kumfikia.


JOTO LIMEPANDA EEE?





Baada ya kuoga walirudi ndani ambako Bi Blandina aliwaandalia mavazi ambayo yalikuwa mbadala wa yale waliyokuwa wameyavaa huku yeye akiingia kwenye kile kijumba walichokuwa wakina Titiana na Jessica wakiwa hawajitambui huko aliiwasha dawa iliyokuwa kwenye vichungu viwili na kuwawekea kila mmoja wao usawa wa kichwa ambayo ilianza kutoa moshi mwingi kisha yeye alitoka na kufunga tena mlango kwa kufuli kisha akarudi ndani na kuwakuta wakina Jasmine wakiwa tayari sebuleni lakini kila mmoja alikuwa na sura ya huzuni sana tofauti na kabla ya kupata taarifa za kuuawa kwa watoto mapacha na wakiwa hawajui kama ni kweli kile walichokisikia kutoka kwa mwenyeji wao Bi Blandina.


"Hivi wenzangu hili la kushambuliwa mzee Minyetye na watoto mmekubaliana nalo kweli?"

Roberto aliwauliza wenzake.


"Mimi hata sielewi maana kichwa kinaniuma tu hapa."

Jasmine alijibu akiitoa simu yake mfukoni.


"Endeleeni hapo mezani kupata chakula hayo mengine ukweli mtaupata mkifika huko huko kwa sasa najua itakuwa ngumu kunielewa."

Bi Blandina aliwakaribisha kwa chakula lakini akisisitiza juu ya kile ambacho aliwaelekeza mwanzo.


"Sawa dada tunashukuru kwa chakula na haya tunayoyaongea no hofu tu wala si kingine."

Mahmoud alimjibu Bi Blandina.


"Samahani dada vipi kuhusu wenzetu ambao bado hawajazinduka."

Jasmine alitaka kujua hali za wakina Titiana.


"Kuleni chakula kisha mtaongozwa na vijana wangu mpaka njiapanda ambako mtaelekezwa njia ya kutokea pale Dighton Sunset."

Bi Blandina aliwaelekeza wakina Roberto ambao walikuwa wakiendelea kula chakula. Lakini wakiwa wanaendelea kula mara kuna gari lilisikika nje.


" Msitoke subirini kwanza asitoke mtu nje."

Bi Blandina aliongea akiwa anachungulia dirishani kuangalia ni watu gani hao. Alipoangalia vizuri aliona gari dogo aina ya Toyota Land Cruiser likisimama na kikundi cha watu wakishuka kwenye gari.


"Watakuwa wapi?"

Alimsikia mmoja wao ambaye alionekana ndiye kiongozi akiangalia huku na kule kisha kuuliza.


"Madam tusipoteze muda toa amri tufanye yetu si unayakumbuka maagizo ya Bosi?"

Kijana mwingine alimuuliza Vivian na kumtaka awaamuru wafanye upekuzi kwenye mjengo huo.


"Mmh hapana hatuwezi kufanya hivyo kabla hatujaongea na wenyeji wa hapa na wakitulazimisha kutumia nguvu tutafanya hivyo."

Vivian alimjibu huku akiangaza huku na kule.


"Karibuni wageni, karibuni sana."

Alitokea Bi Blandina na kuwakaribisha wageni hao akiwa hana wasiwasi hata kidogo.


"Asante, afadhali umetokea mwenyeji wetu shida yetu ni moja tu hapa."

Vivian alimjibu.


"Shida gani hiyo binti?"

Bi Blandina alimuuliza.


"Tunaomba ututolee watu wetu uliowahifadhi ndani ya nyumba yako kabla hatujaisambaratisha nyumba yako dada yetu."

Vivian alimtisha Bi Blandina ambaye alikuwa akiwaangalia kwa dharau.


"Mna uhakika kuwa nimewahifadhi watu wenu?"

Bi Blandina alimuuliza Vivian.


"Uhakika tutaupata ukituruhusu kufanya msako."

Vivian alimjibu Bi Blandina.


"Na nikisema kuwa sitaki muingie kukagua mtafanya nini?"

Bi Blandina aliuliza tena.


"Itafahamika hapo hapo."

Vivian alimjibu.


"Halafu wewe mwanamke mbona una mashauzi hivyo unajiamini nini hivi unatuonaje sisi?"

Mmoja wa walinzi alimuuliza Bi Blandina huku akimsogelea.


"Unataka kufanya nini?"

Bi Blandina alimuuliza kijana huyo baada ya kuona anamfuata.


"Unauliza?"

Vivian alimuuliza huku akimnyooshea bastola Bi Blandina kuashiria kuwa wako kikazi.


"Ninyi ni wakina nani mpaka kuninyooshea bastola ndani ya Himaya yangu? Okey inawezekana ninyi ni watemi huku porini siyo? Sasa nakuruhusu fyatua hizo risasi zako."

Kwa hasira Bi Blandina aliongea hayo huku akimsogelea Vivian karibu zaidi na ile bastola kumuonesha kuwa haogopi kitu lakini ni kama akawa kama ameuwasha moto kwani kijana mmoja aliyedhani kuwa Bi Blandina anakwenda kupambana na Vivian alimfuata na kumpiga ngumi ya kichwa ambayo ilimpeleka chini Bi Blandina.


"Mshenzi wewe unafikiri tutaufurahia huo upuuzi wako? Nafikiri bado hujatujua vizuri sasa kwa usalama wako tuoneshe ulikowaficha watu wetu."

Vivian alimwambia Bi Blandina Collins huku akiwa kamuwekea bastola kichwani pale chini. Lakini Bi Blandina hakujibu chochote zaidi ya kuanza kuongea maneno ambayo hayakueleweka mbele ya wakina Vivian kiasi cha kubaki wakimshangaa tu kwani akiwa anaongea maneno yale alikuwa akitetemeka kama vile anaugonjwa wa kifafa.


"We dada tuondolee maigizo yako hapa hebu tekeleza maagizo yetu kabla sijausambaratisha ubongo wako."

Vivian aliendelea kumshinikiza Bi Blandina aoneshe waliko wakina Jasmine, Bi Blandina aliendelea kuongea maneno yale ya kimizimu bila kujali kitu na muda huo nyuma ya pazia la dirisha kule ndani wakina Jasmine walikuwa wakishuhudia kila kitu kilichokuwa kikiendelea pale nje mara waliweza kuwaona baadhi ya vijana wa Vivian wakiongoza ndani walimokuwa wao.


"Tunafanyaje hapa jamani?"

Ryan aliwauliza wenzake.


"Tujifiche kwenye moja ya chumba humu humu ndani."

Jasmine alijibu.


"Mimi nafikiri tutoroke zetu kabla hawajatukuta."

Roberto alitoa wazo ambalo lilipingwa na Mahmoud pamoja na Jasmine.


"Hatuwe...."

Kabla hajamaliza kuelezea mara hali ilibadilika mle ndani na kufanya giza nene lililopelekea kutoonana kati ya mtu ya mtu na hata Jasmine alipojaribu kuchungulia nje kupitia pale dirishani hakuweza kuona chochote zaidi ya kusikia makelele ya watu waliokuwa wakisikika kwa mbali wakiimba nyimbo ambazo zilionekana kuwa za makabila ya kule porini.


"Jamani hebu angalieni kule."

Jasmine aliwaita wenzake wasogee pale dirishani kuona kile ambacho yeye alikiona. Walikuja na kuwaona watu hao waliokuwa wamevalia mavazi ya kiasili huku wakiwa na mienge ya moto.


"Haya ni maajabu ndugu zangu hivi si ni mapema kabisa sasa hili giza limetokea wapi?"

Aliuliza Ryan. Lakini kabla hajapata majibu kutoka kwa wenzake mara ilisikika sauti kubwa ambayo ilisikika kama mwangwi kutoka nje.


"Enyi wanaharamu, wanaharamu mliovamia eneo hili takatifu na kumshambulia Malkia wetu bila sababu yoyote mnakwenda kuyajutiaaaaaaaa......"

Baada ya sauti ile kumalizika giza lilianza kutoweka taratibu eneo lile lakini ajabu lile kundi la watu halikuondoka badala yake waliwakamata wale wakina Vivian na kuanza kuwaviringisha kamba kwenye mti uliopo karibu na nyumba ya Bi Blandina. Hali ile iliwashangaza sana wakina Jasmine.


"Angalia walivyovalia mavazi yao."

Jasmine alionekana kushangazwa na mavazi ya wale watu ambayo yaliwafanya ni ya ngozi za wanyama ambayo yaliweza kuwaziba maeneo ya sehemu za siri tu.


"Waadhibuni hao mpaka nitakaposema basi."

Bi Blandina alitoa maagizo kisha yeye aliondoka na kurudi ndani ambako hakuongea chochote zaidi ya kumfuata Jackline alikokuwa kamlaza.


"Amka Jackline, amka Jackline muda wako wa kuelekea vitani umefika, amka Jackline !!!"

Maneno yale waliyasikia moja kwa moja kutoka kwenye kile chumba kisha Bi Blandina alitoka.


"Ondoeni hofu kila kitu kiko sawa na mwenzenu anaungana nanyi muda si mrefu."

Bi Blandina aliwataka wasiwe na wasiwasi juu ya kilichotokea muda mfupi uliopita japo wakina Jasmine waliendelea kuchungulia nje kuona kinachoendelea na mara Jackline alitokea pale sebuleni.


" Jasmine mume wangu amepatikana? "

Lilikuwa ni swali ambalo liliulizwa na Jackline akiwa anajikongoja taratibu kutoka kwenye kile chumba na kwa namna alivyokuwa akitembea ni dhahiri hakuwa vizuri sana kutokana na kuchechemea.


"Mdogo wangu usijali mumeo yupo lakini kikubwa kwa sasa angalia hali yako kwanza."

Bi Blandina alimjibu huku akiwa kamkumbatia Jackline na wakati huo alikuwa akiwakonyeza wakina Jasmine kuashiria kutojibu chochote.


"Malkia wetu kazi yako iko tayari."

Mmoja wa watu wale alisogea karibu na dirisha na kutoa taarifa ile ambayo ilimfanya Bi Blandina kulisogelea dirisha ili kujiridhisha kama ni kweli kwa aliloambiwa.


"Vizuri, mnaweza kuondoka sasa."

Baada ya kujiridhisha aliwaamuru watu hao kuondoka na haikuchukua muda waliondoka kwa staili ile ile ya kuimba na kucheza ngoma huku wakiondoka,kisha aliwataka wakina Jasmine kutoka nje.


***


Mackdone aliangaza huku na kule kuona kama anaweza kuwaona wakina Vivian kwani ilikuwa ni muda mrefu umepita na kwenye simu zao walikuwa hawapatikani.


"Watakuwa wapi hawa?"

Mackdone alijiuliza huku akiiangalia simu yake.


"Au watakuwa wamekutana na majanga nini mpaka sasa? "

Bi Elizabeth aliuliza akimsogelea Mackdone pale nje alipokuwa kasimama.


" Unashauri nini katika hili Bi Elizabeth? "

Mackdone aliuliza huku akiiwasha sigara yake.


"Bosi !! yule mtoto mwingine kafumbua macho yake."

Henry alikuja na kutoa taarifa ya kilichotokea kule kwenye chumba walichokuwa wamewahifadhi.


"Yupi huyo?"

Bi Elizabeth aliuliza huku akigeuka kuelekea kwenye chumba kile.


"Yule wa kike."

Henry alimjibu.


"Mtoto ana roho ngumu kama ya mama yake? Ngoja nikamuoneshe kazi."

Bi Elizabeth aliongea huku akiongeza hatua zake.


"Enhh imekuwaje eti?"

Bi Elizabeth alimuuliza Hamza ambaye alikuwa kakaa kwenye kiti kutokana na hali yake kutokuwa vizuri sana.


"Ndiyo kama alivyowaeleza Henry mimi sijapata nafasi ya kuangalia huko ndani."

Hamza alimjibu.


"Fungua mlango haraka!!"

Bi Elizabeth aliamrisha mlango ufunguliwe lakini kabla hilo halijafanikiwa mara Mackdone alifika na kumzuia Bi Elizabeth kutoingia kwenye kile chumba.


"Bi Elizabeth hebu usimuue huyo mtoto kwanza anaweza kutusaidia kwenye Oparesheni yetu ya kumtafuta mama yake na watu wake na itakuwa vizuri mama huyo akiyashuhudia mauaji ya mtoto wake. Unaonaje hilo?"

Mackdone alimuuliza huku akimshika mabega.


"Eti eee?"

Bi Elizabeth aliuliza huku akirudisha mguu nyuma.


"Ndiyo itakuwa nzuri sana Mpenzi wangu."

Mackdone alimjibu huku akimpa ishara Henry kuufunga mlango ambao alikuwa keshaufungua. Kisha wao walirudi tena kule walikokuwa huku wakiwaacha wakina Hamza.

Lakini mara simu ya Bi Elizabeth iliita na kuichukua haraka kutoka kwenye mfuko wa suruali yake.


"Huyu hapa kapatikana."

Bi Elizabeth alimwambia Mackdone mara baada ya kuona aliyepiga ni Vivian.


"Okay msikilize anasemaje."

Mackdone alimtaka amsikilize anasemaje Vivian hivyo aliipokea.


"Nakusikia Vivian."

Aliongea Bi Elizabeth mara baada ya kuipokea simu.


"Wala si Vivian Bi Elizabeth najua hili litakushangaza lakini ndivyo ilivyo, naomba nikuahidi kuwa moto uliouwasha nakuja kuuzima."

Upande wa pili ulimpa taarifa hiyo na kisha simu ile ilikata. Bi Elizabeth aliishia kumtolea macho Mackdone kama vile ndiye aliyekuwa akiongea naye.


JE SIMU HIYO ALIYOIPOKEA BI ELIZABETH ILITOKA KWA NANI? NA KWANINI ITUMIKE SIMU YA VIVIAN? YEYE YUKO WAPI?


KUPATA MAJIBU YA MASWALI HAYA TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.





Hali ile ilimshtua Mackdone ambaye alikuwa pembeni ya Bi Elizabeth aliyeduwaa baada ya ile simu kukatwa. Si kwamba hakuifahamu ile sauti iliyotoka kuongea naye la hasha kilichomshangaza ni kwa namna gani ameweza kuitumia simu ya Vivian? Akajikuta akiishia kuiangalia simu yake.


"Nini kimetokea Bi Elizabeth?"

Mackdone alimuuliza baada ya kuona kaduwaa.


"Mmh sijui nini kimetokea huko kwani simu ya Vivian imetumiwa na Jackline na akiongea kwa kujiamini sana.


" Inawezekana wametekwa? "

Mackdone aliuliza.


" Ndiyo hicho najiuliza hapa au aliiangusha nini? "

Bi Elizabeth aliendelea kujiuliza swali hilo.


" Hebu ngoja kwanza mpenzi."

Mackdone aliongea hayo akiitoa simu yake mfukoni kwake ambayo aliibonyeza namba fulani na kisha kuiweka sikioni.


"Halo Bosi naku..nakusikia."

Vivian aliongea baada ya kukabidhiwa simu na Jackline aliyeweza kuliona jina la Bosi likitokea simu ilipoita na huku akipewa masharti juu ya simu hiyo.


"Mko wapi Vivian mbona muda unakwenda bila taarifa yoyote?"

Mackdone aliuliza.


"Bado shughuli ni ngumu Bosi hawa watu hatujafanikiwa kuwakuta hawa wa...wa...watu."

Vivian alimjibu kwa hofu fulani hivi.


"Hamjawapata? Kwanini? Mbona simu yako imetumiwa na Jackline?"

Mackdone hakutaka kuamini kile alichokisikia kutoka kwa Vivian na ukizingatia muda si mrefu simu hiyo hiyo imetoka kutumiwa na Jackline.


"Labda kama kuna kitu kimefanyika kwenye simu yangu lakini simu yangu haijashikwa na mtu yeyote ninayo mwenyewe."

Majibu ya Vivian yaliendelea kumshangaza Mackdone.


"Unauhakika kwa hicho unachokiongea kweli?"

Bi Elizabeth alimuuliza Vivian swali mara baada ya kuchukua simu kutoka kwa Mackdone.


"Ni kweli kabisa mama ina maana hamniamini?"

Vivian alimuuliza Bi Elizabeth.

Lakini Bi Elizabeth hakutaka kuelekea kubishana naye alichokifanya ikawa ni kuikata simu ile na kisha kumkabidhi simu Mackdone.


"Kwamba huyo Jackline kaichezea simu ya Vivian?"

Mackdone alimuuliza Bi Elizabeth akiiwasha sigara yake.


"Kwa akili ya yule binti anaweza Mackdone maana kile kichwa huwa sikiamini hata kidogo."

Bi Elizabeth alimjibu.


"Kama ndiyo hivyo tunafanyaje hapa unafikiri?"

Mackdone alimuuliza Bi Elizabeth.


"Tuvute muda kidogo tukiona kimya tuingie msituni kuwatafuta maana mimi moyo wangu unadunda sana na hii si ishara nzuri kwangu hata kidogo."

Bi Elizabeth alimjibu Mackdone akiiangalia saa yake. Baada ya mazungumzo ya muda mfupi waliondoka mahali hapo na kuingia ndani. Lakini ni muda huo huo walipoingia ndani tu kuna watu wawili walifika na kuelekea upande waliokuwa wakina Hamza wakilinda jengo ambalo lilikuwa limehifadhi miili ya watu wa Jackline pamoja na Natalie ambaye alishapata fahamu lakini alikuwa hawezi kufanya chochote kutokana na namna ambavyo alikuwa kafungwa kamba mwili mzima huku eneo lenye majeraha akiwa kawekewa kichuma chenye ncha kali karibu kwamba akitingishika kidogo tu chuma kile kinamchoma. Na baada ya kuwafikia hawakuwa na mazungumzo nao kwa kutumia silaha zao zenye viwambo vya sauti waliwamiminia risasi ambazo hazikuwaacha salama Hamza na mwenzake Henry na kuwapeleka chini na kutoa nafasi kwa watu hao kuingia ndani na kuanza kumfungua kama zile Natalie ambaye alikuwa hoi sana na hiyo ilikuwa ni kutokana na kuchoka pamoja na njaa kwani miongoni mwa mateso ambayo walipanga kumfanyia yule mtoto ilikuwa ni kumuua kwa njaa.


"Fanya haraka Mahmoud kabla haijawa tabu."

Ryan alimwambia Mahmoud huku yeye macho yakiwa kuelekea kwenye milango inayotazamana na kile kijumba.


"Vuta subira ndugu yangu hizi kamba zilifungwa kama vile wanafunga gogo? Hawa jamaa hawana huruma kabisa."

Mahmoud alimjibu akiendelea kuzifungua taratibu pasipo kumuumiza mtoto Natalie. Hali hiyo ilimfanya Ryan kuondoka pale alipokuwa na kumfuata Mahmoud pale chini ili kumsaidia, walianza kulifanya hilo kwa haraka kabla hawajashtukiwa na wakina Mackdone.


" Wao wao inapendeza karibuni wageni."

Mackdone alitokea na kuwashtua na walipogeuka kuangalia nyuma walikutana na sura ambayo ilikuwa na tabasamu pana huku akiwa kawaelekezea bastola.


"Ningependa tufahamiane wageni wangu japo mmeingia bila taarifa lakini siyo kesi. "

Mackdone aliendelea kuwatia wazimu hali ile ilimfanya Mahmoud ageuke na kumtazama Mackdone.


" Unafikiri tunakuogopa Mackdone?"

Mahmoud alimuuliza.


" Enhh una maanisha nini? "

Mackdone aliuliza akiiweka sawa bastola yake.


" Unaonaje kama ukiiweka chini hiyo bastola kisha tuucheze mchezo kavu kavu siyo unaongea kibezi mbele ya vidume kisa una chuma mkononi, thibitisha ubabe wako sasa tuone."

Ryan aliamua kumpandisha hasira Mackdone ambaye alikuwa bado kawaelekezea bastola.

Lakini kabla hajafanya chochote Mackdone alijikuta akitazamana na mdomo wa bastola ya Mahmoud aliyoichomoa kwa staili ya aina yake.


" Sasa unaweza kuamua kutekeleza kile tulichokuambia au fyatua nifyatue."

Mahmoud alimpiga mkwara.


"Unaonekana kujiamini sana kijana lakini nikuambie tu kuwa hapa kuingia ni rahisi sana kama mlivyo fanya ila kutoka shughuli ipo."

Alipomaliza kuongea hivyo tu mara nyuma yao alitokea Bi Elizabeth kwa kupitia mlango wa nyuma ambao hawakuutilia shaka hata kidogo walipokuwa mle ndani.


" Weka chini silaha yako kabla sijausambaratisha ubongo wako."

Bi Elizabeth alimuamuru Mahmoud kuiweka chini bastola.


"Nafikiri maana yangu mmeielewa sasa mnaingiaje kwenye makazi ya watu bila hodi na kuanza kufanya kazi ambazo hamjatumwa?"

Mackdone alianza kutamba wakati huo Mahmoud alikuwa akiiweka bastola yake chini kusalimu amri.


"Mnafikiri leo mtasalimika? Hebu angalieni kule nje muone kuna nini."

Ryan alimjibu Mackdone na kuwataka waangalie nje kitendo ambacho wakina Mackdone na Bi Elizabeth walikifanya pasipo kufikiri.

Kwa kasi ya ajabu Mahmoud aliuinua mkono wenye bastola na kummiminia risasi Mackdone lakini alichelewa kwani Bi Elizabeth alijibu mashambulizi kitendo kilichomfanya Ryan kutoroka mle ndani kwani hali ilikuwa siyo yenyewe. Mahmoud na Mackdone wakiwa wanakwenda chini Bi Elizabeth alitoka mkuku kumfukuzia Ryan kabla hajafanikiwa kutoka ngomeni.


***


Baada ya kila kitu kwenda kama walivyopanga Bi Blandina alitoka ndani akiwa na vitu fulani kama unga unga hivi na kuupuliza juu kisha akawageukia wakina Jackline waliokuwa kwenye gari la wakina Vivian tayari kwa safari.


"Mnaweza kuondoka sasa lakini wagonjwa nitaendelea kuwahudumia."

Bi Blandina aliwaruhusu kuondoka.


"Sawa dada wacha tukaifanye kazi yetu huko Dighton Sunset."

Jackline alimjibu huku Jasmine akijiweka sawa kwenye usukani.


"Ok safari njema."

Aliwajibu kisha akarudi ndani na wakina Jasmine wakaondoka.


"Mahmoud hapokei simu yake."

Roberto aliwaambia wenzake mara baada ya kumpigia mara kadhaa Mahmoud lakini simu yake haikupokewa japo ilikuwa ikiita.


"Inawezekana kaondoa mlio kwenye simu yake ili isiwaletee hatari mle ndani."

Jackline alimjibu.


"Labda."

Roberto alijibu akiwa anajaribu tena kumpigia Mahmoud lakini mara iliingia namba ya Ryan.


"Ndiyo Ryan."

Alijibu Roberto baada ya kupokea simu.


"Hali ni mbaya huku."

Ryan alimjibu Roberto.


"Mbaya kivipi?"

Roberto aliuliza.


"Mahmoud na Mackdone sina uhakika kama wako hai maana kilichotokea mpaka nashindwa kuelezea."

Ryan aliendelea kumuweka njia panda Roberto.


"Nyoosha maelezo basi nini kimempata?"

Roberto aliuliza tena.


"Baada ya kuingia kwenye jengo lile ambalo amehifadhiwa Natalie tukamkuta na kuanza kumpa msaada wa kumfungua kamba lakini walitokea na kutuweka chini ya ulinzi lakini kama ujuavyo Mahmoud hakutaka kushindwa si akamshambulia Mahmoud ndipo alipotokea Bi Elizabeth aliyemshambulia naye, mimi sikutaka kujua nini kimetokea nilichokifanya ni kukimbia mara baada ya kuona Bi Elizabeth akili yake kaielekeza kwa Mackdone."

Ryan alisimulia kilichotokea.


" Kwa hiyo Mahmoud kafariki? "

Roberto aliuliza.


" Sina uhakika kwa asilimia kwani baada ya kutoka Bi Elizabeth naye alitoka kunifukuzia hivi ninavyoongea nawe tunatafutana ndani ya huu msitu ulio pembeni ya majaruba ya Mpunga."

Ryan alimjibu kisha simu yake ilikatwa.


" Anasemaje? "

Jasmine aliuliza.


"Ndiyo kama hivyo Mahmoud kafa au hajafa kulingana na maelezo ya Ryan hivyo tufanye haraka tunaweza kufanya chochote kwa Mahmoud."

Roberto alimjibu.


"Mungu asaidie tuwahi kufika pale japo najua wamejipanga."

Jasmine aliongea akiwa anapishanisha tu miguu kwenye pedali za gari hilo.


"Roberto na wewe Jasmine mtapitia lango kuu na mimi nitawazunguka kwa nyuma kuhakikisha tunawatia nguvuni bila kutumia nguvu."

Jackline aliwapa maelekezo wenzake wakiwa wamelikaribia jengo la Dighton.


"Uko wapi sisi tushafika tayari?"

Roberto alimuuliza Ryan mara baada ya kumpigia simu.


"Nimewaona nisubirini hapo hapo."

Ryan alimjibu mara baada ya kuliona gari likiwa limesimama kutoka pale alipokuwa yeye hivyo alitoka kwenye kile kichaka na kuwafuata pale walipokuwa.


"Ryan pole kwa majanga."

Jasmine alimpa pole baada ya kuwafikia.


"Asante dada Jasmine ndiyo hivyo yametokea lakini tunaweza kumuokoa kama watakuwa hawajammalizia."

Ryan alimjibu.


"Jamani tusipoteze muda wetu hebu Ryan tupe picha ya kule ndani ilivyokaa kabla hatujaingia."

Jackline alimwambia Ryan huku akiiweka sawa bastola yake tayari kwa kazi iliyowapeleka pale.


"Kule ndani hakuna walinzi wengi wamebakia wachache tu na katika hao hakuna vinara waliobaki ni hawa wazembezembe tu lakini la msingi ni kuingia kwa tahadhari kubwa kwani Mackdone keshajua kuwa muda wowote kambi yake itavamiwa hivyo kajiandaa kwa lolote. Tunachotakiwa kukifanya ni kugawanyika wengine wapitie nyuma ya ngome na wengine watapitia getini kwa kushambulia ili pale watakapokuwa wakielekeza mashambulizi getini hawa wa nyuma watahamisha mateka na kutokomea."

Ryan alitoa maelekezo ambayo walikubaliana nayo kwani hata kabla ya Ryan kuongea hivyo walikuwa wameshajipanga kutumia mbinu hiyo, lakini wakiwa bado wanaendelea na mikakati ya namna ya kuingia mle ndani mara angani waliweza kuiona helicopter ambayo ilitokea kambini na kuzunguka maeneo yote ya karibu na kambi hiyo kitendo hicho wakajua tayari ulinzi umeimarishwa zaidi.


"Jamani tunafanyaje hapa?"

Roberto aliuliza huku akiwaongoza wenzake kuelekea vuchakani kuepuka kuonwa na walio kwenye helicopter.


"Mnaonaje kama tukiitungua ndege hiyo maana bila kufanya hivyo itatusumbua sana."

Jackline alitoa pendekezo.


"Ipo juu sana tutatumia silaha gani?"

Ryan aliuliza.


"Ondoa shaka kuhusu hilo Ryan kwani Bi Blandina alitukabidhi mtambo wake huu hapa."

Jackline alimjibu akimkabidhi kiboksi Roberto ambaye alitakiwa kuanza kuunganisha silaha hiyo. Aliiunganisha na baada ya kukamilika aliielekeza kule ilikokuwa ile helicopter lakini kabla ya kufanya lolote Jackline akaona amtumie kwanza ujumbe Bi Elizabeth.


"MIAMBA YA PORI IMEWASILI NDANI YA NGOME YAKO HIVYO ANDAA VIKOSI VYAKO VYOTE TAYARI KWA MAPAMBANO LAKINI KWA USALAMA WENU ISHUSHENI HIYO HELICOPTER YENU."

Baada ya kuutuma ujumbe walisubiri kwa dakika kadhaa kusubiri majibu na ndani ya muda mfupi ujumbe uliingia kwenye simu yake.


" HATUTISHIWI NYAU KAMA NINYI NI VIDUME JITOKEZENI HADHARANI TUPAMBANE NA KINGINE KUMBUKENI KUWA HAMUWEZI KUINGILIA MAJUKUMU YETU."

Alipousoma ujumbe ule alitabasamu kisha akawaelekeza wenzake kisha akampa ishara Roberto ya kushambulia ile ndege huku wao wakiwa wamejificha.


" Niko tayari Jackline nasubiri amri yako."

Roberto alimwambia Jackline.


" Okay jiandae kwa shambulizi ikiingia kwenye tageti yako ishambulie."

Wakati Jackline akimjibu Roberto mara ile helicopter iliweza kuwaona pale walipokuwa na kuanza kuwashambulia mfululizo.


JE NINI KITAENDELEA?





Mackdone akiwa ndani ya helicopter aliweza kushuhudia kila kitu kilichokuwa kikifanywa na vijana wake kwa kulishambulia eneo lile ambalo walijificha wakina Jackline. Kwa hakika alifurahi sana kwa kile kilichokuwa kikiendelea na kumpa imani kuwa ndani ya muda mfupi ujao watakuwa wamemsambaratisha adui yao na kisha kuyaanza maisha mapya na mwanamke aliyempenda tokea kitambo hicho. Wakati huo yeye akiwa kwenye sigara Bi Elizabeth yeye aliongoza mashambulizi kutoka juu na kwa hasira alizokuwa nazo alitamani kushambulia mpaka udongo wa eneo hilo.


"Bosi kama unavyoliona eneo hapo chini kazi kwisha."

Mmoja wa vijana wao aliyekuwa kwenye kitengo cha mashambulizi mle kwenye ndege alimjulisha Bi Elizabeth kuwa hakuna kiumbe aliyesalia hapo na hilo lilikuja mara baada ya kushuhudia gari ambalo walilitumia wakina Jackline likiwaka moto.


" Kazi nzuri vijana wetu kichotakiwa sasa ni kushuka chini na kulikagua eneo lote kama kweli tumewamaliza wajinga hawa."

Bi Elizabeth alimjibu kijana wake huku akimgeukia Mackdone.


"Si ndiyo Mackdone?"

Bi Elizabeth alimuuliza Mackdone.


"Kweli kabisa bibie hatuwezi kusema tumeshinda wakati hatujajiridhisha."

Mackdone alimjibu Bi Elizabeth akichungulia nje.


"Nimewaelewa wakuu katika hili tuko tayari kushuka. Rubani tafuta namna ya kutuwezesha kutua."

Kijana huyo ambaye ni kiongozi wa vijana wapambanaji mle kwenye ndege alimwambia Rubani.


Baada ya kuzunguka juu kwa muda kuangalia eneo ambalo halina madhara kisha ilitua, Mackdone aliwaongoza vijana wake kushuka chini kutoka kwenye helicopter lao ambalo lilikuwa bado likipiga kelele huku vumbi likitimka kutokana na yale mapanga ya ile helicopter kuendelea kuzunguka kwa nguvu ikiwa ni kuwa tayari iwapo litatokea lolote.


"Mackdone njoo uone huku."

Bi Elizabeth alimwita Mackdone kuja upande wake mara baada ya kukutana na mwili uliochakaa kwa risasi na baadhi ya maeneo ya mwili wake yakiharibiwa kwa moto na kuufanya kutotambulika vizuri.


"Waoo huyu si ni mwanamke? Bila shaka ni Jackline huyu na kama yeye tayari ni marehemu aliyesalia ni nani?"

Mackdone aliongea kwa bahasha kubwa baada ya kuukagua mwili ule walioukuta pale chini karibu zaidi na majaruba ya mpunga.


"Ni kweli kabisa Bosi lakini hatuna uhakika wa asilimia mia kama ni mwenyewe kwa sababu ameharibika sana na kuifanya sura yake kutoeleweka."

Kijana mmoja wapo alikubaliana na Bosi wake lakini pia hakuacha kuonesha mashaka yake.


"Ukisemacho kijana wangu ni cha kweli kwani hapa nilikuwa naangalia vizuri vitu fulani fulani kutoka kwenye huu mwili mmh hapana huyu si yeye labda watu wake ambao aliongozana nao."

Bi Elizabeth naye hakuweza kukubaliana na Mackdone mara baada ya kufanya uchunguzi wake kwenye mwili waliokuwa wakidhani ni wa Jackline. Kisha waliondoka eneo hilo na kusogea mbele zaidi lengo likiwa ni kutafuta miili ya maadui wao pamoja na kuwafikia ambao hawajafa na kuwamalizia. Walizunguka kwa masaa zaidi ya sita lakini walikutana na miili michache ambayo pia waliitilia mashaka kutokana na mavazi yao.


"Hapa nimepata mashaka kidogo kwenye miili yote niliyoiona."

Bi Elizabeth aliendelea kuonesha hofu yake juu ya uchunguzi wao.


"Mashaka gani hayo Bi Elizabeth?"

Mackdone alimuuliza.


"Nahisi hawa tuliowaua ni wafanyakazi kwenye mashamba haya ya mpunga lakini wenyewe hapana labda tukalikague lile gari kama kuna mabaki ya miili ya watu ndani yake."

Bi Elizabeth alimjibu Mackdone na hivyo walirudi kwenye gari ambalo muda huo lilikuwa limebakia vyuma chakavu na baada ya kufika pale napo hawakuambulia chochote hivyo wakajikuta wakipata mashaka mapya kuwa Jackline na kundi lake wametoroka eneo lile au wamejificha japo kwenye kujificha hawakuamini kutokana na kuzunguka eneo lote bila mafanikio hivyo imani kubwa ikawa wametoroka.


"Rubani na vijana wawili ingieni kwenye ndege rudini kambini wacha sisi tuendeleze uchunguzi kwenye eneo lote."

Mackdone aliagiza hilo na kumfanya Rubani kukaa sawa na vijana wale wawili kuondoka sehemu ile kurejea kambini. Wenyewe walibaki na kuendelea kuwatafuta maadui wao na safari hii waligawanyika kwenye makundi huku kundi la Mackdone likielekea kule mtoni ambako kuna vichaka na vinjia vingi vya kuelekea kambini. Walipoyafikia maji ya kijito kile kuna vitu ambavyo viliwatisha kidogo navyo ilikuwa ni maji kwenye kimkondo kimojawapo kuwa na rangi nyekundu kwa mbali.


"Sambaeni eneo lote hili nahisi huku kuna waliojeruhiwa wamejificha. Hakikisheni hamuachi kichaka chochote ndani ya mto huu."

Mackdone alitoa maagizo kwa vijana wake ambao bila kusubiri walitawanyika na kumuacha Mackdone akihangaika kuchomoa sigara kwenye pakiti.


" Shiiiit kumbe kiberiti kimeishiwa gesi? Nitafanyaje sasa na moto wenye harufu za mizoga ya watu siwezi tumia."

Mackdone alijikuta akiongea peke yake mara baada ya kukosa kiwasha sigara. Lakini kuna hali fulani ilimuijia pale alipokuwa na kuufanya mwili wake kusisimka kitu ambacho si kizuri kwa mtu yeyote awapo porini.


" Mimi ninacho kiberiti kama hutojali naweza kukupa."

Ni sauti ambayo iliongea kutoka nyuma yake na huko kulikuwa na vichaka na kumfanya Mackdone kuduwaa kwanza kabla ya kugeuka kumuangalia mtu huyo. Akili iliyomuijia kichwani ikawa ni kuchomoa bastola yake kwa ajili ya kujihami hivyo akaupeleka mkono kwenye kikasha kilichohifadhi bastola na kuanza kukifungua akiwa bado hajageuka na kuichomoa bastola yake. Lakini alipogeuka nyuma hakuweza kuona mtu sehemu ile.


"Unacheza na akili yangu ee jitokeze nikusambaratishe mjinga wewe."

Mackdone aliongea kwa sauti baada ya kutomuona mtu aliyemsemesha dakika chache zilizopita.


"Kuna nini Bosi?"

Kijana wake alifika na kumuuliza baada ya kuyasikia makelele ya mkubwa wao.


"Unauliza nini wewe? Ondoka hapa hakikisha mnawapata wanaharamu hawako mbali nasi, Umenielewa wewe?"

Mackdone alimfokea kijana huyo.


"Nimekuelewa Bosi."

Kijana huyo alimjibu na kuondoka zake akaona isiwe tabu. Baada ya kuondoka yule kijana wake Mackdone alienda mpaka kwenye eneo ambalo alihisi kuwa yule mtu aliyemsemesha alikuwepo na baada ya kulifikia eneo lile alichuchumaa na kulikagua vizuri na kama bahati vile alifanikiwa kuziona alama za buti ambalo mtu yule alikanyaga ndipo akaona aanze kuzifuatilia. Alizifuatilia zile buti mpaka kwenye vichaka vya mtoni ambavyo hutengenezwa na matete.


"Okay zilielekea hukuuu na kisha zikaelekeaaa....." Kabla hajamalizia sentensi yake alishtukia akiitwa kwa nyuma.


"Mackdone, Mackdone umeamua kunifuata mpaka huku?"

Mahmoud aliongea hayo akiwa amemnyooshea bastola Mackdone huku akiwa katapakaa matope mwili mzima na kuachia macho, mdomo na pua tu sijui ilikuwa ni katika kujiepusha na maadui. Ndipo Mackdone alipomgeukia mtu huyo.


" Wewe ni nani? Na umenijuaje mimi? "

Mackdone alimuuliza Mahmoud .


"Unataka kuni...kuni...jua?"

Mahmoud alimuuliza badala ya kumjibu.


"Ndiyo kwani kuna ubaya wowote wa mimi kutaka kukujua?"

Mackdone aliendelea kumuuliza.


"Oohhoo! Usivute hatua yako hata chembe nitakufanya kitu kibaya."

Mahmoud alimtaka Mackdone asisogee mbele kumfuata kwani itakuwa hatari kwake kwani alijua anaweza kusababisha majanga lakini kabla hata Mackdone hajajibu chochote alishtukia kuona risasi kadhaa zikimiminwa kuelekea kwake kiasi cha kumpeleka chini na kuzimia lakini baada ya kuzinduka alijikagua na kujikuta yuko vizuri na baada ya kumaliza kujikagua aliinua kichwa na kuangalia pembeni yake hakuamini macho yake baada ya kumuona Mahmoud akiwa kaketi akiwa anamuangalia tu huku akiwa anaichezea bastola.


"Kumbe ni muoga hivyo bwana mkubwa? Umezimia wakati nikimuua kijana wako yule pale (akimuonesha kijana huyo ambaye alishakuwa marehemu) sasa ningekumiminia risasi hizo wewe ingekuwaje?"

Mahmoud alimuuliza akiwa kamsogezea mdomo wa bastola. Kwa hasira Mackdone aliinuka na kutaka kumvaa Mahmoud lakini alichelewa kwani Mahmoud alimmiminia risasi zaidi ya tatu kwenye bega ambazo zilimpeleka chini na kumfanya Mahmoud kumfuata kwa lengo la kutaka kumtandika nyingine za kifuani lakini alichelewa kwani kabla hajafanya hivyo alijikuta akipoteza fahamu na kuanguka. Hiyo ilikuja mara baada ya kijana mwingine wa Mackdone kuja kwa nyuma na kumtandika risasi ya mgongoni ambayo ilimpeleka chini.


"Bosi, Bosi, Bosi unanisikia? Bosi ni mimi kijana wako inuka basi. "

Kijana huyo alimsemesha Mackdone ambaye hakujibu chochote zaidi ya kupiga kelele za maumivu ya bega lake.


" Bosi inuka tuondoke basi hapa si salama." Kijana huyo aliendelea kumshawishi Mackdone ambaye kama vile hakumsikia.


" Kelele bwana unaongea nini wewe huoni kama nimeumizwa na mjinga huyo hebu hakikisha unamdhibiti haraka."

Mackdone alimfokea kijana huyo na kumpa maelekezo ya nini cha kufanya hivyo kumfanya kijana huyo kumuacha Mackdone na kumfuata Mahmoud ili kummaliza lakini alifanya kosa kwani Mahmoud alishapata fahamu na kuikamata bastola yake vizuri kisha kumshambulia kijana yule kwa risasi za kifuani mfululizo ambazo zilimpeleka chini na kisha alielekeza kwa Mackdone ambako alimfyatulia risasi kama mbili hivi lakini Mackdone naye hakumuacha salama Mahmoud kwani kwa tabu hivyo hivyo aliichukua bastola yake na kummiminia risasi zilizompeleka chini.


JE MAHMOUD NA MACKDONE WATAKUWA WAMEKUFA?




Baada ya kushambuliwa kwa mara ya kwanza na Bi Elizabeth na watu wa Mackdone kuamini kuwa wameshammaliza Mahmoud na kumuacha ndani bila uangalizi wowote kisha wao kuelekea kumsaka Ryan na baadaye wakina Jackline huku nyuma kwa tabu sana Mahmoud alirudiwa na fahamu zake na kuingia porini kuhakikisha anayasalimisha maisha yake lakini bado akajikuta mikononi mwa Mackdone japo aliamua kumshangaza. Lakini hakufanikiwa kumuangamiza baada ya kushambuliwa na kijana wa Mackdone ambaye alimtandika risasi za mgongoni na safari hii hakuweza kuinuka tena alipoteza maisha yake. Mackdone na kijana wake walikokotana kurejea kambini kwa ajili ya matibabu.


"Bosi jikaze najua maumivu ni makali sana lakini huna jinsi zaidi kujikaza tuweze kufika kambini."

Kijana yule alimwambia Bosi wake baada ya kuona anataka kukaa chini wakati wakiwa bado mbali na kambi yao.


"Hebu mpigie Bi Elizabeth tuone kama wanaweza kufanya jambo maana hali yangu si nzuri."

Mackdone alimtaka mlinzi wake amtafute Bi Elizabeth kwa msaada.


Aliichukua simu kutoka kwenye mfuko wa Mackdone na kuitafuta namba ya Bi Elizabeth na baada ya kuipata aliipiga lakini haikupatikana, hakuchoka akarudia tena kuipiga lakini haikubadilisha maana yoyote.


"Hapatikani Bosi."

Alimtaarifu Bosi wake.


"Hapatikani?"

Mackdone alipata shaka kwani si kawaida ya Bi Elizabeth kutopatikana hewani hivyo akahisi kuwa anaweza kuwa kapata tatizo hivyo aliangaza huku na kule kisha akaomba msaada kwa kijana wake.


"Naomba ikague bastola yangu kama iko vizuri ikiwezekana niongezee risasi kisha nisaidie nikakae pale kwenye chaka lile pale nikiliangalia limekaa vizuri sana kiasi kwamba ni vigumu kwa mtu kuniona kirahisi."

Mackdone alimwambia kijana wake.


"Hilo ni suala ambalo haliwezekani bosi hapa wewe jikaze tu mpaka tufike kambini kama ni kumhusu Bi Elizabeth ninaamini yuko salama."

Kijana wake alimgomea na kumuahidi kuwa ni lazima wafike kambini.


"Kwa hiyo unabishana na mimi siyo?"

Mackdone akapandisha sauti kwa lengo la kumtisha.


"Hapana Bosi lakini elewa kuwa sehemu hii si salama kwa muda huu."

Kijana wake aliendelea kusisitiza kuwa ni lazima waondoke kwa kuhofia usalama wa Bosi wake.


"Unaonekana kunijali sana mimi siyo?"

Mackdone alimuuliza.


"Ndiyo mkuu."

Alimjibu.


"Vizuri sasa niisikilize nikiwa kama mkuu wako nakuagiza, utaniacha hapa na kisha wewe utaelekea kambini kumuangalia Bi Elizabeth ili kujua kilichompata mpaka asipatikane hewani, umenielewa?"

Mackdone aliongea maneno hayo akiwa kamkazia macho kuonesha kuwa alikuwa akimaanisha katika hilo.


" Nimekuelewa mkuu."

Alimjibu huku akimsogelea ili kumsogeza sehemu ambayo aliitaka.


" Panatosha hapa hapa wewe fanya kama nilivyokueleza."


"Sawa mkuu."

Kijana yule alimjibu Mackdone na kuondoka zake. Lakini wakati hayo yakifanyika kulikuwa na warembo wawili waliochakaa hovyo hovyo kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na wakina Mackdone na kupelekea miili yao kuvuja damu kila eneo la miili yao na kuwafanya kutembea kwa tabu. Hilo lilitokana na Jackline kushambuliwa eneo la mguuni huku yeye Jasmine akipata majeraha ya kichwani kutokana na kuchomwa na kisiki ambacho alikiangukia wakati akianguka na hivyo kujifunga t-shirt yake kuzuia damu zaidi, kwa hiyo wakati Mackdone na kijana wake wakipanga yao wao walikuwa wamejificha kwenye chaka la jirani yao bila kuonwa.


"Ujanja wako wote, jeuri yako yote tumekunasa kichakani? Niliambiwa wewe ni mtata kukufikia tu shida sasa mbona imekuwa tofauti? Au siyo wewe Mackdone?"

Jasmine akiwa kabana tu maziwa yake kwa sindiria huku t-shirt yake ikiwa imekifunga kichwa chake aliongea nyuma ya Mackdone bastola ikiwa kisogoni kwake. Hali ile ilimshtua sana Mackdone ambaye hakutarajia kukutana na mtu yeyote mahali pale.


" Wewe ni nani?"

Mackdone alimuuliza.


"Nakuruhusu kugeuka lakini kitu cha kwanza irushe mbele bastola yako ili tuongee vizuri."

Jasmine alimjibu. Mackdone hakuwa na ubishi tena alichokifanya aliirusha mbele yake ile bastola kama alivyoambiwa.


"Sasa unaruhusiwa kugeuka ili unitazame inawezekana utanitambua."

Jasmine alimwambia Mackdone na wakati huo Jackline alikuwa akijivuta kwa sapoti ya kigogo ambacho alikuwa nacho. Mtu wa kwanza kumuona alikuwa ni Jackline na hapo akajua kuwa ameshapatikana kwani Jackline anamfahamu vilivyo tofauti na Jasmine.


" Mbona umeduwaa bwana mkubwa?"

Jasmine alimtoa kwenye mawazo.


"Ninyi wanawake ni mashetani kabisa mmefuata nini hapa?"

Mackdone aliwauliza.


"Tumetumwa na marehemu Daktari Abbas pamoja na watoto wake Natalie na Nathan."

Jasmine alimjibu huku akiinama kuichukua ile bastola ya Mackdone.


"Hao watu wamewatuma kufanya nini?"

Mackdone aliuliza swali ambalo jibu lake alilifahamu bila shaka ni kutokana na kuchanganyikiwa.


"Kile mlichowafanyia ndicho hicho hicho tumeagizwa kwenu."

Jackline alimjibu na kuliinua lile gongo lake na kumpiga nalo kichwani Mackdone.


"Haaaaaa kichwa changu, watu wenu wameshakufa na sidhani kama mtaonana labda kama mtakufa kama wao hapo sawa japo yule wa kike mkimuwahi mnaweza kumkuta akiwa hai japo ni asilimia chache sana."

Jackline alimshushia jingine ambalo hilo lilitua utosini na kumpasua na kupelekea damu kumwagika lakini hilo Jackline hakujali aliinua kwa mara nyingine ili amgonge nalo lakini Jasmine alimzuia.


"Haiwezekani umfaidi peke yako wacha na mimi nipooze machungu kwa huyu mwanaharamu."

Jasmine aliongea akimsachi mfukoni ambako alitoa kila kitu kuanzia hela mpaka simu na alichokifanya zile hela alimrushia Jackline kisha yeye akaifungia ile simu na kuanza kutafuta majina na bila shaka alikuwa akilitafuta majina ya washirika wa Mackdone na kama bahati vile alikutana na jina la Bi Elizabeth ambalo liliseviwa 'Mama la mama' na hapo aliipiga ilipoita aliikata na haraka sana akaingia na upande wa ujumbe mfupi na kumuandikia.


"Uko wapi? Mimi hali yangu siyo nzuri niko huku mtoni kwenye haya matete yaliyostawi sana nimejificha siwezi hata kuvuta hatua."

Alipoituma tu hazikupita hata dakika mbili simu iliita aliiangalia tu bila kupokea.


"Ni nani?"

Jackline alimuuliza.


"Achana naye nimemuingiza kwenye mtego ni Bi Elizabeth."

Jasmine alimjibu.


"Nina hamu na huyo binamu yake Shetani? We acha tu ngoja aingie kwenye hamsini zetu."

Jackline alimjibu Jasmine huku akibubujikwa na machozi bila shaka ni kutokana na kuzisikia kwa mara nyingine taarifa za wapendwa wake. Hilo lilimfanya Jasmine kumsogelea na kuanza kumtuliza rafiki yake ambaye kwa wakati huo ungemuona sijui kama ungemfahamu. Lakini wakati akimtuliza rafiki yake mara ujumbe uliingia kwenye simu ya Mackdone ambayo ilikuwa mikononi mwa Jasmine muda huo.


"USIONDOKE TUNAKUJA SASA HIVI KWANI HATA MIMI PAMOJA NA DOGO MMOJA TUMEJIFICHA HUKU HUKU PEMBEZONI MWA MTO KUTOKANA NA KUVAMIWA NA VICHAA WA KUNDI LA JACKLINE AMBAO WALITAKA KUMCHUKUA NATALIE LAKINI NIMEFANIKIWA KUTOROKA NAYE."

Ujumbe huo ulisomeka hivyo na kisha Jasmine alimjibu haraka sana.


" SASA HUYO MTOTO WA NINI SI UMMALIZE TU. "

Jasmine alimtega.


" HAPANA SIWEZI KUFANYA UJINGA HUO KWANI NATAKA KUMUUA MBELE YA MACHO YA MAMA YAKE ILI AUONE UCHUNGU WA MWANA."

Bi Elizabeth alimjibu na kumfanya Jasmine kumuonesha ujumbe huo Jackline ambao uliwafanya kutabasamu maana walishajua ushindi unasogea kwao.


"Lete nimjibu na mimi."

Jackline aliichukua simu na kuujibu ujumbe huo.


"Itakuwa vizuri sana njoo naye ili waje washuhudie kifo chake kabla ya wao kumfuata mtoto wao."

Baada ya kuituma walitazamana na kucheka tena kisha Jackline alisimama kwa lengo la kuujaribu mguu wake.


HAYA SASA UHONDO UMEFIKIA HAPO SIJUI KATI YA JACKLINE NA KUNDI LAKE PAMOJA NA BI ELIZABETH NA KUNDI LAKE ATAYEIBUKA MSHINDI MAANA HALI NI TETE KWA WOTE.


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.





Wakiwa pale wamejituliza kwenye kile kichaka ambacho waliuficha mwili wa Mackdone walisikia vishindo vya watu wakija upande ule na hivyo kubaini kuwa wanaweza kuwa ni watu wa Bi Elizabeth hivyo walijiweka sawa kwa kila kitu kinachokwenda kutokea.


"Kaa sawa Jackline hao lazima ni wenyewe ngoja mimi nitoe mlio wa hii simu ya mtu wake Mackdone isije tuumbua."

Jasmine alimwambia Jackline akiichomoa ile simu haraka.


"Fanya haraka naona wanakaribia isije tuumbua."

Jackline alimjibu akiliweka sawa gongo lake. Na hata dakika tatu hazikupita simu ya Mackdone iliyokuwa mikononi mwa Jasmine ikiita na haraka sana aliikata badala ya kupokea kisha akamtumia ujumbe mfupi.


"Umefika wapi?"

Alimuuliza kwa ujumbe mfupi.


"Nimefika hapa korongoni tayari nimeingia majini sijui nielekee wapi? Na mbona unakata simu?"

Bi Elizabeth akiwa kamshikilia Natalie aliyekuwa akilia kutokana na maumivu ya mguu.


"Acha ujinga wewe hebu songa mbele unafikiri kwenu hapa? Alaaa!!"

Ni maneno ambayo waliyasikia yakisemwa na Bi Elizabeth kwa Natalie ambaye walimsikia akilia, kitendo hicho kilimuuma sana Jackline na pale alipotaka kujitokeza tu kukabiliana na Bi Elizabeth Jasmine alimzuia.


" Unataka kufanya nini sasa hebu tulia kwanza kuku ni wetu wenyewe manati ya nini? Ngoja asogee karibu maana hatujui ameongozana na kundi gani."

Jasmine alimtuliza Jackline na kwa wakati huo alikuwa akiijibu jumbe ya Bi Elizabeth.


"Ngoja nikupe ishara ujue niliko."

Baada ya kumtumia ujumbe huo alichukua jiwe na kulirusha majini. Na bila kuchelewa Bi Elizabeth aliongoza eneo lile lilipotua jiwe na kuanza kuangaza alipo mtu ambaye aliamini ni Mackdone lakini hakuweza kumuona na ndipo alipotoa simu ili aweze kumpigia.


"Hebu mkamate panya huyo kwanza."

Bi Elizabeth alimsukumiza Natalie kwa mmoja wa vijana wake ili ampigie simu Mackdone lakini kilichomshangaza ni baada ya kutoipata hewani simu ya Mackdone.


"Mmh mbona haipatikani tena itakuwa chaji nini? Tumefika jitokeze bwana hebu acha utoto."

Bi Elizabeth baada ya kumkosa hewani aliamua kuita kwa sauti ili aweze kusikia kama yuko sehemu ile. Aliendelea kuita kwa muda lakini hakuweza kujibiwa wala kumuona Mackdone na hapo wakaingiwa na wasiwasi.


" Madame kutakuwa kumetokea jambo hapa mbona hii si kawaida ya Bosi kucheza michezo kama hii...." Kijana wake mmoja alionesha hofu yake baada ya kuona Mackdone hajitokezi lakini kabla hajamalizia kauli yake wakasikia sauti ya mamlaka ikitokea nyuma yao.


"Karibuni sana kwenye mtego wetu tulijua mtakuja tu na ndivyo mlivyofanya hivyo msifanye chochote ambacho kitasababisha mumfuate mkubwa wenu Mackdone."

Jackline akisogea aliongea kwa sauti ya kukwaruza bila shaka ilikuwa ni mchanganyiko wa kilio mara baada ya kumuona mtoto wake Natalie.


" Mamaaaaa... " Natalie alipaza sauti mara baada ya kumuona mama yake na hivyo akaanza kujivuta kutoka kwenye mikono ya yule kijana ambaye alimshikilia.


"Kwa hiyo ndiyo mchezo mliotuchezea siyo?"

Bi Elizabeth aliuliza huku akimvutia kwake Natalie na kumfanya ngao yake.


"Muachie mwanangu haraka kabla sijausambaza ubongo wako Bi Elizabeth."

Jackline alimuamuru Bi Elizabeth ambaye naye alikuwa kawaelekezea bastola kama walivyofanya wao huku mbele yake akiwa kamtanguliza Natalie.


"Fanya chochote kile Jackline wala siogopi kwanza nitakuwa nimefurahi sana kuungana na wanangu lakini vipi kuhusu wewe ambaye utakishuhudia kifo cha mwanao muda si mrefu?"

Bi Elizabeth aliongea kwa dharau pasipokuwa na shaka yoyote mbele ya watukutu ambao hata yeye anaufahamu mtanange wao ukianza lakini hakujali.


" Narudia tena Bi Elizabeth, muachie mwanangu kama wewe ni shujaa kwanini unajificha kwenye kivuli cha mwanangu? Muachie ili tuoneshane umwamba maana nikikuangalia nakuona ni yule yule wa zamani huna chochote kipya."

Jackline aliendelea kumtisha Bi Elizabeth.


" Ukitaka hilo nilifanye nitafanya ila siyo kwa sasa bali ninachoweza kukuambia muda huu wewe na huyo mbwa wako wekeni silaha zenu chini kwani mfuga mbwa hapa ni mmoja tu wengine wote hapa ni mbwa tu."

Bi Elizabeth aliwaambia huku akimuelekezea bastola


Natalie sehemu ya sikio kwa juu huku wale vijana wake wakiwa wamewaelekezea wakina Jackline bunduki zao.


"Huwa sirudii mara mbili mbili kuongea neno moja kwa watu wenye masikio mawili fanyeni kile nilichowaambia tofauti na hapo hamtaamini kitakachotokea hapa."

Bi Elizabeth alikazia maneno yake huku akiisogeza karibu zaidi bastola yake kwa Natalie lakini pamoja na mikwara ya Bi Elizabeth wakina Jackline walikuwa bado kuweka silaha zao chini kwani walitazamana kwa muda bila shaka kuna jambo ambalo walikuwa wanajadili kwa ishara wakiwa tayari wameinama kuziweka chini silaha zao. Kwa kasi ya ajabu Jasmine alikwenda juu huku akizimimina risasi kwa vijana wa Bi Elizabeth ambao aliweza kuwaona wamejisahau huku Jackline naye akilitimua vumbi kumpoteza maboya Bi Elizabeth na kisha kupotelea kwenye matete. Risasi ziliendelea kulia kwa vijana wa Bi Elizabeth na Jasmine ambaye alikuwa kajitoa mhanga kuhakikisha anafanya kitu na kwa hilo aliweza kufanikiwa lakini mwisho wa siku akiwa anatua chini aliweza kushambuliwa na risasi ya mguu kutoka kwa Bi Elizabeth na kwa wakati huo alikuwa akitoroka eneo hilo baada ya kuona vijana wake wote wamelazwa chini na Jasmine hivyo akaona kuwa imebakia zamu yake.


"Unakwenda wapi Bi Elizabeth?"

Akiwa anauvuta mguu wake Jasmine alisimama hivyo hivyo na kumtuliza Bi Elizabeth kwa nyuma akiwa kamshikilia mtoto Natalie.


"Usijidanganye Jasmine utakufa kifo kibaya sana mimi siyo yule unayemfahamu shauri yako."

Bi Elizabeth alimjibu akiwa hajageuka kampa mgongo na mkononi akiwa kamshikilia Natalie.


"Muachie huyo mtoto haraka."

Jasmine alimuamuru Bi Elizabeth.


"Aaagh......" Bi Elizabeth alisugua meno yake kwa hasira kisha aligeuka kwa kasi na kuanza kumimina risasi kwa Jasmine ambaye tayari aliiona hiyo na kwenda chini kisha akamjibu Bi Elizabeth kwa kuzimimina risasi na moja ilikwenda kutua kwenye mkono ambao ulimshika Natalie na kupelekea kumuachia. Kitendo hicho kama vile kilileta uhuru kwa Natalie ambaye alitimua mbio kuelekea vichakani na kumuacha Bi Elizabeth akigalagala kwa maumivu.

Na alipogeuka nyuma aliweza kumuona Jackline akija pale alipolala wakati Jasmine akiugulia maumivu akajua mtoa roho yake sasa anakuja hivyo akafikiria haraka cha kufanya akaona hakuna nafasi nyingine zaidi ya kujiviringisha kuelekea vichakani kabla hajamfikia na ndicho alichokifanya.


"Huwezi kuelekea kokote Bi Elizabeth naomba usimame tu maana hili ndilo chaguo ambalo uliona linakufaa kuweza kuwafikia wapendwa wako."

Jackline alimwambia Bi Elizabeth huku akimfuata kule vichakani bastola ikiwa mkononi kwa tahadhari zaidi. Lakini Bi Elizabeth hakuweza kumjibu wala kujitokeza hivyo ikawa ni kazi kwa Jackline kumsaka alikojificha. Alimtafuta na kumtafuta lakini hakuweza kumuona hivyo akaendelea kumsaka lakini kabla hajavuta hatua mbele zaidi akashtukia akiguswa kisogo na kitu cha baridi hivyo ikabidi awe mpole.


"Leo ni siku yako Jackline na ninajisikia faraja sana kukuua kwa mkono wangu mwenyewe hivyo usipoteze muda wako juu yangu Jackline ninachokuomba ni kuiachia bastola yako taratibu ili nikuue kwa amani binti yangu."

Bi Elizabeth alijinasibu nyuma ya Jackline ambaye alikuwa keshapiga magoti huku akiwaza afanye nini kujinasua kwani moja ilikuwa haikai wala mbili.


" Fanya haraka wewe alaa unafikiri natania eee."

Bi Elizabeth alimfokea Jackline baada ya kuona hakuna anachokifanya kwenye yale aliyomuagiza afanye na kisha akamfyatulia risasi ya mguuni ambayo ilimfanya Jackline kuachia kilio.


"Aaagh mamaaaaa.....!!!!"

Kilio hicho cha Jackline kilimfanya Bi Elizabeth kumsogelea karibu akijua tayari keshamuweza lakini baada ya kumfikia tu Jackline alijigeuza kwa staili ya ajabu na kummiminia risasi Bi Elizabeth ambazo zilimkuta vilivyo eneo la kifuani na kwa kitendo hicho Jackline aliinuka kwa tabu hivyo hivyo akiwa kachafuka kwa damu na kumsogelea Bi Elizabeth ambaye hakuwa na jeuri tena.


"Mama yangu Bi Elizabeth, mama ambaye nilikupenda sana katika maisha yangu na huwezi amini mara baada ya kukutana nanyi huwezi amini nilifurahi sana kwani nilijua nimepata wazazi wapya mara baada ya kupoteza wazazi wangu na ndiyo maana wanao pamoja mumeo walijitoa mhanga kunisaidia Mungu azilaze roho zao mahala pema peponi kuhakikisha nawashinda maadui zangu lakini Mungu akawapenda zaidi. Mama yangu kwako ikawa tofauti kwanini mama yangu? "

Jackline alipiga magoti pembeni ya Bi Elizabeth na kuanza kumuelezea kile kilichokuwa moyoni kwake huku machozi yakimmwagika.


" Jack..... Jack.....line mi...mi si ndu...ndugu yaa..... " Hakuweza kumalizia kauli yake alikata roho. Kitendo kile cha kufa kwa Bi Elizabeth pamoja yote yaliyotokea Jackline alilia sana huku akiutingisha mwili wa mama huyo.


"Mama, mama, mama unamliliaje huyo bibi? Humjui tu ni mtu hatari sana huyo kwani kashiriki kumuua kaka yangu na baba yangu muacheee..."

Natalie alifika na kuanza kumlaumu mama yake kwa anachokifanya kwa Bi Elizabeth.


"Ni kweli mwanangu usemacho hujui tu kinachoniliza mama yako."

Jackline alimjibu mtoto wake akimbeba japo kwa shida hivyo hivyo lakini wakati Jasmine akimkagua Bi Elizabeth mara walitokea wakina Ryan jasho likiwatoka huku wakiwa wamechafuka kitu kilichowafanya wakina Jasmine kuanza kucheka.


" Poleni mlikuwa wapi? Mbona mlipotea hewani?"

Jackline aliwauliza.


"Wee acha tu kilichotukuta huko ilikuwa zaidi ya vita ya tatu ya dunia hata hivyo tunamshukuru Mungu tumeibuka kidedea. Tulijua kuwa wangekuwa kambini kumbe hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya wale walinzi zaidi ya kumi waliokuwa wamejificha na tulipotokea tu bila sisi kuwaona wakatuanzia sema tu Mungu alikuwa upande wetu."

Alijibu Roberto.


" Na Mahmoud yuko wapi? "

Ryan aliuliza.


" Ameuawa wakati wa mapambano na Mackdone ambaye naye kafariki. "

Jasmine alimjibu.


" Kwa hiyo wote tumewamaliza? "

Roberto aliuliza huku akimuangalia Bi Elizabeth pale chini kwa hasira.


" Ndiyo hivyo kilichobaki ni kurudi kule kambini kwao tukauchukue mwili wa mwanangu Nathan pamoja na wa baba yao kisha wa Mahmoud safari ianze kurejea Namibia kwa maziko. "

Wakati Jackline akiwapa maelekezo ya namna itakavyokuwa mara simu ya Jasmine iliita.


" Whaaaaaat?????? "

Jasmine aliuliza tu na kisha alianguka chini na kuzimia hapo hapo wakamfuata na kuanza kumpepea na kwa kuwa simu ilikuwa bado haijakata Ryan alichukua.


"Kumetokea nini tena Bi Blandina?"

Baada ya kuuliza ndipo alipoambiwa kuwa Titiana na Jessica wameshindwa kuupigania uhai wao hivyo wameaga dunia.


"Mungu wangu."

Ryan aliishia kusema hivyo tu huku akiwaangalia wakina Jackline kisha aliikata simu na kuizima kabisa kisha akaiweka mfukoni.


****


Baada ya taratibu zote kukamilika waliweza kuilaza miili ya marehemu kwenye makazi yao ya kudumu ndani ya nyumba ya Daktari Abbas kama kumbukumbu ya wapigania haki wote ambao walikuwa ni Daktari Abbas mwenyewe, mtoto wake Nathan, Jessica, Mahmoud, pamoja na Titiana. Na baada ya kumalizika maziko ya wapendwa wao waliweza kukaa hapo kwa miezi miwili kwa kuomboleza kisha Jasmine na Roberto walirejea nchini Brazil huku Jackline yeye na mtoto wake walisalia kwa muda pale Windhoek pamoja na kijana Ryan ambaye alikubali kuishi na Jackline kama msaidizi wake hasa kwa kipindi hicho ambacho kilikuwa kigumu sana kwa Jackline na mtoto wake Natalie.


* MWISHO *


JIANDAE KWA HADITHI MPYA YA 'MAISHA BAADA YA KUTUMBULIWA' PAMOJA NA 'NANI ABEBE LAWAMA (Ambayo ni hadithi ya kweli kabisa)


ZITAKUIJIA BAADA YA KUTOKA MAPUMZIKO AMBAYO YATACHUKUA WIKI MBILI.

NAWASHUKURU KWA USHIRIKIANO WENU WADAU WANGU HASA MAMA YANGU MSHAURI KUTOKA ARUSHA BI GLAD'S KABUTA AMBAYE ULIACHA SHUGHULI ZAKO NA KUJITOA KWA HALI NA MALI KUHAKIKISHA KIJANA WAKO SITOKI NJE YA MAADILI KWENYE TUNGO ZANGU, NAKUSHUKURU SANA MAMA YANGU MUNGU AENDELEE KUKUTIA NGUVU KWANI SAFARI BADO CHANGA SANA.


* MWISHO *


0 comments:

Post a Comment

Blog