Search This Blog

Monday, 19 December 2022

QUEEN MONICA (3) - 1

 



SEASON 3
Simulizi : Queen Monica (3)
Sehemu Ya Kwanza (1)

ILIPOISHIA SEASON ILIYOPITA “He’s here.Austin tayari amekuja.Ngoja nikamchukue yupo mapokezi “ akasema Linah na kutoka .Baada ya dakika tano akarejea akiwa ameongozana na kijana mmoja mtanashati sana mwenye sura iliyojaa tabasamu “Wow! What a handsome guy” akawaza Monica baada ya kumuona Austin.Alikuwa ni kama mtu aliyepigwa na butwaa kwa kitu alichokuwa anakitazama mbele yake. “Monica “ akaita Linah na kumstua Monica “Huyu anaitwa Austin January.Ndiye mgeni Yule niliyekueleza alikuwa anakutafuta” “Austin huyu ndiye Monica Benedict mwamsole,mkuu wa kampuni hii” LInah akafanya utambulisho.Monica akasimama na kumpa Austin mkono. “Karibu sana Austin.Nimefurahi kukutana nawe” “Hata mimi nimefurahi sana kuonana nawe Monica” akasema Austin na kuketi katika sofa.Linah akatoka na kuwaacha Monica na Austin pale ofisini. ENDELEA.................................. “ Uzuri wa Monica si uzuri wa kawaida, naweza kumfananisha na viumbe toka sayari nyingine.Ni uzuri usioweza kuelezeka kwa maneno.” Akawaza Austin huku akimtazama Monica kwa jicho la wizi. “ Austin karibu sana “ Monica akaanzisha maongezi “ Ahsante sana Monica.Pole kwa safari.Nilifika hapa jana nikataarifiwa kwamba ulikuwa safarini nje ya nchi.” “ Ni kweli Austin nilikuwa nje ya nchi nimerejea jana jioni na nilipofika nilitaarifiwa kwamba ulifika hapa kunitafuta” “Natumai msaidizi wako Linah amekwisha kueleza kwa ufupi kuhusu mimi na nini kilichonileta hapa kwako.” “ Ndiyo alinieleza” akajibu Monica “ Vizuri.Kwa ufupi naitwa Austin January,ni mtanzania lakini kwa sasa nina uraia wa Afrika ya kusini.Kikazi mimi ni mkurugenzi wa utawala na fedha katika kampuni ya kitalii ya A.A safari yenye makao yake makuu nchini Afrika ya kusini.Tunawapokea watalii toka nchi mbali mbali duniani na kuwapeleka sehemu mbali mbali za bara la Afrika.Vile vile tunazo hoteli zinaitwa AA 5 stars hotel ambazo zimesambaa katika sehemu mbali mbali za bara la Afrika.Kwa kifupi naweza kusema kwamba kampuni yetu ni moja kati ya kampuni kubwa na bora kabisa za utalii hapa Afrika” akasema Austin “Nimefurahi sana kukufahamu Austin.Mimi ni Monica Benedict ni mkurugenzi wa kampuni hii inayojishughulisha na masuala ya ubunifu na utengenezaji wa mavazi.Tunabuni mavazi hapa na kupeleka bunifu zetu katika viwanda vya ndani na nje ya nchi.Sidhani kama nitakuwa najisifu nikisema kwamba kampuni yetu ni moja kati ya kampuni bora kabisa ya mavazi katika ukanda huu wa Afrika mashariki.Mbali na mavazi ninayo pia taasisi yangu inayojisghughulisha na kusaidia jamii yenye uhitaji na hapa tumejikita zaidi kusaidia watoto na wazee wasiojiweza” “ Hicho ndicho haswa kilichonileta hapa kwako Monica “ akasema Austin kwa furaha “ Kampuni yetu ina kitengo kidogo cha kusaidia miradi mbali mbali ya kijamii katika sehemu zile ambazo tuna ofisi zetu. Tumekuwa tukichangia ujenzi wa mashule,hospitali n.k.Kwa sasa tuko katika maandalizi ya kufungua ofisi zetu hapa Dar es salaam kwa hiyo tunataka kuanza kushiriki pia katika miradi mbalimbali ya kijamii lakini kabla ya kufanya hivyo tumeona tujifunze kwanza toka kwa wenzetu ili tufahamu ni sehemu gani tunaweza na sisi kuwekeza nguvu zetu hapa Tanzania.Kwa hiyo Monica nimekuja hapa kwako kujifunza kwani wewe na taasisi yako tayari mnao uzoefu wa kutosha na mazingira ya huku Tanzania na kama itawezekana tunaweza kushirikiana katika baadhi ya miradi ya kijamii” Austin akanyamaza na kurekebisha tai yake na kumtazama Monica “ Austin nimefurahi kusikia kwamba na ninyi pia mnajishughulisha katika kusaidia jamii masikini zenye uhitaji .Hakuna shaka sisi na ninyi tutashirikiana katika miradi mbali mbali .Jamii masikni hapa Tanzania zina changamoto nyingi sana mfano elimu,afya,maji safi na salama n.k.Haya ni maeneo ambayo sisi tumeyapa kipaumbele kikubwa kwa kushjirikiana na wafadhili mbali mbali tumeweza kujenga vituo zaidi ya kumi na sita vya afya,madarasa zaidi ya hamshini,visima vya m,ai zaidi ya sitini katika sehemu mbalimbali nchini wanakopishi watu masikini .Tumekuwa tukifadhili matibabu ya wazee wasiojiweza,kuwasaidia misaada mingine muhimu kama vile chakula n.k.Tumekuwa pia tukifadhili pia elimu kwa watoto toka jamii masikini mfano kwa sasa tuko katika hatua za mwisho za ujenzi wa shule kubwa ya watoto wenye ulemavu wa kutokuona na kusikia.Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo mimi na taasisi yangu tumekuwa tukiyafanya”akasema Monica “ Hongereni sana Monica” akasema Austin.Monica akainuka akaliendea kabati na kutoa karatasi tatu kubwa akampatia Austin “ Hiyo ni shule ambayo tunaanza kuijenga hivi karibuni.Pesa tayari tumeipata na kilichobaki ni kumpata mkandarasi ili ujenzi uanze mara moja” Uso wa Austin ukapambwa na tabasamu kubwa “ Monica unastahili pongezi kubwa sana kwa hili ulilolifanya.Jamii hii ya walemavu wana uhitaji mkubwa na wamesahaulika sana katika jamii zetu.Shule hii itakuwa ni mkombozi mkubwa kwao” akasema Austin “ Ahsante Austin” akasema Monica na mara mlango ukafunguliwa akingia Linah.Akamnong’oneza kitu Monica na kutoka “Austin nimetaarifiwa kuwa ninahitajika eneo la ujenzi kuna watu toka wizarani wamefika na wananisubiri” akasema Monica “ Oh ! sawa Monica.Ninashukuru sana kwa kunipokea vizuri na nina imani tutapata wasaa mzuri zaidi wa kulizungumzia suala hili kwa upana .Nikutakie kila la heri katika kazi zako” akasema Austin huku akiinuka “Nashukuru pia kukufahamu Austin.Nitatafuta nafasi nyingine tukae tuzungumze kwa kirefu juu ya suala hili” akasema Monica wakaagana lakini kabla Austin hajatoka mle ofisini Monica akasema “ Austin kama hutojali tunaweza kuongozana kwenda eneo la ujenzi? Austin ambaye tayari alikuwa ameukaribia mlango akageuka haraka haraka na kusema “ Hakuna tatizo Monica tunaweza kwenda “ Good” akasema Monica na kuchukua mkoba wake wakatoka .Kila mmoja aliingia katika gari lake wakaondoka “ Dah ! Monica ni mwanamke mwenye uzuri wa kipekee mno.Mungu atanisamehe kwa mawazo haya lakini amempendelea mno Monica.Licha ya kumpa uzuri usioelezeka amempa pia moyo uliojaa huruma na upendo wa kipekee ndiyo maana amekuwa anajitoa mno kwa jamii masikini.Nimehisi kuguswa sana na mambo haya makubwa anayoyafanya kwa jamii.Huyu ni mwanamke wa mfano na anastahili kuwa malkia wa Afrika” akawaza Austin akiwa njiani wakielekea katika mradi wa shule ya walemavu “ Mwanaume atakayepata nafasi ya kumpata Monica atakuwa na bahati ya kipekee kabisa,atakuwa amepata kitu cha thamani kubwa kuliko hata gari lililojaa madini.Wanawake wa aina hii ni wachache mno katika dunia ya sasa.Natamani sana kumjua mpenzi wake ni nani nimpe hongera yake” akaendelea kuwaza Austin na kutabasamu baada ya sura ya Monica kumjia kichwani “ Nahisi kama vile sura ya Monica inaingia kwa kasi kubwa katika akili yangu kiasi cha kumuwaza kila sekunde.Oh no ! sitakiwi kuyaruhusu mawazo haya yatawale kichwa changu kwa sasa.Natakiwa kuelekeza akili yangu yote katika mambo mazito yaliyoko mbele yangu” akawaza na kumkumbuka mpenzi wake Maria “Nina hakika kwa muda huu Maria tayari atakuwa amerejea au anajiandaa kurejea afrika kusini.Hawezi kuja Tanzania bila ya kuwasiliana nami kwanza .Nakubali sijamtendea vizuri lakini hii ni kwa ajili ya usalama wake.Siwezi kumruhusu mwanamke nimpendaye akaingia katika hatari .Baada ya kazi kumalizika nitamuomba msamaha na nina imani atanielewa tu” Mawazo mengi yalikisonga kichwa cha Monica wakati akielekea katika eneo la ujenzi wa shule.Aliwaza kuhusu ndoa yake na David,akawaza kuhusu maisha mapya atakayoyaishi ambayo ni maisha ya kifahari mno,na mara akamkumbuka Marcelo.Alitaka sana kufahamu mahala alipo Marcelo.Alihitaji sana kumjulia hali na kuona namna ya kumsaidia “ Naamini hadi jioni ya leo,David atakuwa tayari ameelekezwa mahala aliko Marcelo ili nimjulie hali na kutafuta namna ya kumsaidia.Anahitaji sana msaada wangu na vile vile ninataka niongee naye kuhusu ugonjwa wa Pauline ,inawezekana akawa na mchango wowote hata wa mawazo” Kwa mbali machozi yakamlenga alipomkumbuka Pauline. “Mungu,akuponyePauline.Nakuombe a sana upasuaji utakaofanyiwa ufanikiwe na uendelee kuwa mzima.U mwanamke mwenye upendo wa kipekee kabisa “ akawaza Monica Waliwasili eneo la ujenzi ,Monica akakutana na wageni wake waliokuwa wanamsubiri,wakalizungka eneo lote na kuelekezana mambo kadhaa wakaondoka na kuwaacha Monica na Austin “ Monica narudia tena kusema kuwa unastahili pongezi za kipekee kwa mchango wako mkubwa kwa jamii.Jambo hili unalolifanya ni kubwa sana.Hongera kwa mara nyingine” akasema Austin .Monica akatabasamu na kusema “Ahsante sana Austin.Pamoja na kwamba mimi ndiye niliyebuni wazo hili la kujenga shule hii lakini nyuma yangu kuna kundi la wadau wanaoniunga mkono na kulifanya jambo hili liwezekane.Wamejitoa kwa hali na mali na muda wowote toka sasa mradi utaanza.Ninafurahi sana kwa mradi huu kufikia hatua hii ya kuanza.Ilikuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu na sasa inakwenda kuwa kweli” akasema Monica na ukimya mfupi ukapita “ Austin mimi ninarejea tena ofisini kama unavyoelewa sikuwepo kwa siku kadhaa hivyo nina mzigo wa kazi.Nitatafuta wasaa na tutakaa tutaongea .Kuna mambo mengi ambayo tunaweza tukayafanya kwa ushirikiano.” Akasema Monica .Austin akaitazama saa yake ya dhahabu na kusema “ Sawa Monica nikutakie kazi njema lakini hata hivyo nina ombi moja kama hutajali” “Omba Austin” “Monica una kazi nyingi zinazokukabili kwa hiyo kwa sisi kupata wasaa wa kutosha kuzungumza kwa kina mambo tunayoweza kushirikiana itachukua muda kidogo kwa hiyo kama hutajali naweza kukualika kwa chakula cha usiku na tukautumia muda huo kuzungumza? Monica akatabasamu na kusema “Usemayo ni ya kweli Austin,nina kazi nyingi lakini kuhusu ombi lako ngoja niangalie ratiba yangu endapo itaniruhusu nitakujulisha.Nipatie namba yako ya simu” walibadilishana namba za simu wakaagana kila mmoja akaingia katika gari lake wakaondoka “ Imekuwa siku nzuri,nimeanza kazi yangu vizuri .Monica tayari amenikubali na hiki ndicho nilichokuwa nakitafuta.Ninaziona kila dalili za urafiki mkubwa kati yetu.Ombi langu la kukutana naye kwa chakula cha usiku amelipokea na ameahidi kunijibu.Naamini atakubali na endapo atakubali nitajitahidi kutumia vyema kila nafasi nitakayoipata ili kuipata sampuli na hapa ninalenga zaidi nywele.Ili kuipata nywele yanipasa..oh gosh ! “ akawaza Austin na kujikuta akistuka “Ili kuipata nywele ya Monica yanipasa nijenge ukaribu naye mkubwa na hapa nina maanisha ni lazima kulala naye” Mwili wote ukamsisimka alipowaza jambo hili “Nimesisimkwa mwili wote kwa hiki ninachokiwaza.Lakini sioni njia nyingine ya kuweza kuipata nwele ya Monica bila kufanya hivi ninavyofikiri.Kulala naye ndiyo njia pekee na rahisi.Halafu ....” Austin akasita kidogo “ Baada ya kuonana ana kwa ana na Monica nahisi kama kuna kitu kimeanza kujijenga taratibu kichwani kwangu.Sura ya Monica hainibanduki kichwani.Kila dakika ninamuwaza yeye.Oh no ! sitaki kuanzisha mahusiano kwa sasa bali ninachotakiwa ni kuikamilisha kazi yangu ya kuipata sampuli na hata kama nikilala naye lengo litakuwa ni hilo tu na si vingine.” Akawaza na kutabasamu halafu akamkumbuka Maria “ Hiki ninachowaza kukifanya ni kitendo cha usaliti kwa mpenzi wangu Maria ambaye ni kwa sababu yake nimefika hapa nilipo .What am I going to do ? Austin akajiuliza “Lakini hii ni sehemu ya kazi.Ili kuikamilisha kazi niliyopewa lazima nifanye hivyo.Hata hivyo nitafanya mara moja tu .Nimekuja Tanzania kufanya kazi kwa hiyo lazima nikae kikazi.Natakiwa kumuweka pembeni Maria. Nikiendelea kumuwaza sana kila dakika nitashindwa kuifanya kazi yangu.Kwa kuwa tayari nina uhakika hataweza tena kuja Dar es salaam ninapaswa kumuweka pembeni muda huu hadi hapo kazi itakapokuwa imekamlika.Kazi hii ni muhimu mno kwangu kuikamilisha” ******************* Boaz akiwa chumbani kwake katika hoteli hii kubwa aliyofikia huku akionekana kuwa na mawazo mengi akawasha simu yake ambayo huitumia awapo Tanzania.Akazitafuta namba fulani akapiga “ Hallow Boaz.” Ikasema sauti nzito upande wa pili. “ Peter Chui.Habari ya Dar es salaam? Akauliza Boaz. “ Dar es salaam naweza kusema si kwema.Bahari imechafuka kuna upepo mbaya unavuma kwa sasa.Nimekutafuta sana jana katika simu bila mafanikio.Nimekufurahi umenipigia.Welcome home Boaz” “ Asante sana Peter.Ni upepo huo mbaya ndio ulionirejesha nyumbani mara moja.Msijali vijana wangu,baba yenu nimerudi,mawimbi na dhoruba vyote vitatulia.Neno langu moja tu linatosha kabisa kuituliza dhoruba hii.Nataka umtume kijana aje anichukue nina maongezi nawe” “Uko wapi sasa hivi? Boaz akamuelekeza mtu aliyekuwa anaongea naye simuni hoteli aliyofikia akakata simu na kuzitafuta namba nyingine akapiga “ Hallow my love.Nimestuka sana baada ya kuona simu yako.Karibu sana nyumbani mpenzi” ikasema sauti nzuri ya kike upande wa pili “ Hello Julieth.How’re you my queen” akasema Boaz “ I’m ok.Mbona umekuja kimya kimya bila tarifa? “Imenilazimu kuja kimya kimya kutokana na huu upepo mbaya unaoanza kuvuma hapa nchini kwa sasa.Uko wapi mida hii? Nahitaji tuonane ili unipatie kile kitabu.Kwa hali ya sasa ilivyo natakiwa kukihifadhi sehemu salama kwani ndilo tumaini letu la kutuhakikishia tuko salama” “ Kwa sasa niko nyumbani” akajibu Julieth “Sawa Julieth,naomba tukutane Mzizima City.Ninaelekea hapo muda si mrefu” akasema Boaz na kukata simu.Hazikupita dakika thelathini kijana aliyetumwa kuja kumchukua akawasili.Boaz akamuaga Maria na kuingia katika gari akaondoka.Kituo cha kwanza ilikuwa ni mzizima city mahala penye majengo mengi ya biashara ,akachukua simu na kumpigia Julieth “Tayari nimefika hapa Mzizima .Uko sehemu gani? akasema Julieth baada ya kupokea simu. “Njoo hapa duka la mavazi mchanganyiko utaiona gari nyeupe aina ya Jaguar na bila kuonyesha wasiwasi wowote fungua mlango wa nyuma na uingie” akasema Boaz.Baada ya kama dakika tatu mlango wa gari alimokuwemo Boaz ukafunguliwa akaingia Julieth kisha gari ikaondoka.Boaz akamvuta na kumbusu “Nafurahi nimekuona Julieth” “Hata mimi nimefurahi mno kukuona Boaz.Ila umeniudhi kwa kuja kimya kimya.Ungenitaarifu nngekuja kukupokea uwanja wa ndege” akasema Julieth na kumbusu tena Boaz “ Haikuwa katika ratiba zangu kuja Tanzania kwa sasa lakini imenilazimu kukatisha baadhi ya shughuli zangu na kuja kuweka sawa mambo kutokana na huu upepo mbaya unaoanza kuvuma.Hata ndugu zangu hapa Dar hawajui kama niko hapa.By the way kuna taarifa zozote mpya kuhusiana na Marcelo? “ Mpaka sasa hakuna taarifa zozote na bado hatujui aliko.Jeshi la polisi mpaka sasa bado halijatoa taarifa yoyote kuhusiana na kupotea kwake.” “ Damn ! he’s very smart lakini tutampata tu” akasema Boaz. “Una uhakika hajahisi chochote kuhusu wewe kwamba ndiye uliyeingia chumbani kwake na chukua kitabu ? Akauliza Boaz “Sina hakika sana .Nahisi kuna kitu anakihisi kwani alipokuwa hospitali alionyesha utofauti .Hakutaka maongezi na mimi kabisa.Kuna baadhi ya mambo ambayo hakutaka kabisa sisi ndugu zake tuyafahamu.Kuna watu wawili ambao alikuwa nao karibu na kuwasiliana nao kwa siri.” akasema Julieth “It’s ok.Where is the book? Akauliza Boaz.Julieth akafungua mkoba wake akatoa bahasha kubwa ya khaki na kumpatia Boaz “Did you open it? Ulisoma kilichomo ndani? Akauliza Boaz huku akimtazama JUlieth kwa macho makali “Hapana sijafungua kama ulivyoelekeza” “ Good” akajibu Boaz na kuifungua ile bahasha akatoa kitabu cheusi akakitazama,akamvuta Julieth na kumbusu “ Good Job Julieth” akasema na kukifungua kile kitabu ******************** Kazi kubwa aliyopanga kuifanya Austin siku hii ni kuonana na Monica.Akiwa njiani akirejea nyumbani baada ya kuachana na Monica Austin akakumbuka kitu. “Job Israel..!! akasema kwa suti ndogo “ Kwa kuwa ninao muda wa kutosha kwa nini nisimtafute huyu mtu? Ni mmoja wa watu ninaofikiria kuwajumuisha katika kikosi cha kumlinda rais.Ninafahamu uwezo wake ,nimewahi kufanya naye kazi kadhaa ni mtu mwenye uwezo mkubwa.Ni mtu hatari” akawaza Austin Alibadili uelekeo na kuelekeo mahala alikokuwa akiishi Job “ Miaka kadhaa imepita sasa Dar es salaam imebadilika mno si ile ya miaka ile.Wakati naondoka hakukuwa na majengo mazuri hivi katika mtaa huu.” Austin alikuwa anaendesha taratibu huku akitazama nje “Sijawasiliana na Job muda mrefu na inawezekana akapatwa na mstuko mkubwa kwani lazima atakuwa akiamini nilikufa Somalia.kazi ya mwisho kufanya naye ilikuwa ni ile tuliyokwenda Malawi kuwakomboa majasusi wawili waliokamatwa nchini humo.Toka hapo sikuwahi kuwasiliana naye tena .” akawaza Austin huku akisimamisha gari pembeni ya mti wa mkorosho na kutazama nyumba nzuri ya ghorofa moja “Job amejenga ghorofa ! Amejitahidi sana . Lakini ni hapa nyumbani kwa Job au nimepotea? Akajiuliza Austin. “ lakini ni hapa kwani kinachonithibitishia kuwa ni hapa ni lile duka la Mangi pale pembeni.Duka lile,lilikuwepo hapa toka wakati ule wakati ule ninakuja na Job...” Wakati akiendela kutafakari ghafla geti la nyumba ile likafunguliwa na gari zuri la kifahari lenye rangi nyekundu likatoka likiendeshwa na mwanamke mrembo .Austin akastuka “ Yule mwanamke ni nani? Mbona si mke wa Job?Au nmekosea nyumba? Lakini hapana sijakosea ngoja nikaulize pale dukani nipate uhakika zaidi” akawaza Austin na kuelekea dukani akanunua maji ya kunywa na kuuliza “ Samahani ndugu yangu naomba kuuliza” “ Bila samahani kaka” akajibu muuza duka. “ Natumai wewe ni mwenyeji sana wa eneo hili” “ Ndiyo mimi ni mwenyeji sana wa hapa.Nina miaka zaidi ya ishirini eneo hili.Baba yangu ndiye mwanzilishi wa kitongoji hiki cha mafarasi kwani zamani yeye alihamia huku kukiwa pori ili apate malisho mazuri ya farasi aliokuwa anafuga.Baadae watu wakaanza kuongezeka kwa hiyo mimi ni mkongwe eneo hili ” akajibu muuza duka “Natumai utakuwa unamfahamu mtu mmoja anaitwa Job au baba Millen huyu anaishi hapa jirani yako” “ Baba Millen ninamfahamu sana.Alikuwa rafiki yangu” Akasema muuza duka na kumstua kidogo Austin. “Mimi ni rafiki yake nilikuwa nje ya nchi kwa muda mrefu ,nimerejea na nikaona nije kumjulia hali rafiki yangu lakini nimestuka kidogo kukuta ghorofa halafu akatoka mwanamke ambaye simfahamu nikaona ngoja kwanza niulize wenyeji kama huyu jamaa bado yuko hapa au kuna mtu mwingine anaishi hapa” akasema Austin “Dah ! inaonekana hukuwepo nchini kwa muda mrefu ndugu yangu.Huyu jamaa alipatwa na matatizo ya akili.Alichanganyikiwa baada ya kukimbiwa na mke wake.Inasemekana mke wake alimpata mwanaume mwingine halafu akamtupia jini huyu jamaa akachanganyikiwa.Ndugu zake walikuja kumchukua na walimpelekea kwa mganga wa kienyeji kijiji Fulani huko karibu na Kisarawe kinaitwa Mtoka mbali.Kuna mganga anaitwa mzee Nyungu ni mganga maarufu sana kwa magonjwa hayo.Kuna ndugu yake mmoja niliyekuwa nawasiliana naye ndiye aliyekuwa akinipa taarifa za maendeleo ya baba Millen.Eneo hili wamekwisha liuza na mimi ndiye niliyewasaidia kutafuta mnunuzi.Labda nikupe mawasiliano ya huyo ndugu yake uwasiliane naye anaweza akakupa taarifa zenye uhakika zaidi kuhusu baba Millen.” Akasema muuza duka na kumpatia Austin namba za simu za ndugu yake Job.Austin akamshukuru Yule jamaa na kumpatia noti ya shilingi elfu tano akapanda gari na kuondoka “Job amekuwa chizi? Ni vigumu kuamini.Nini kimesababisha akawa chizi? Ama kweli maisha haya yana maajabu makubwa lakini sintaamini hadi hapo nitakapomtia machoni.Kama ni kweli litakuwa ni pigo kubwa kwangu kwani ni mtu ambaye nilimuhitaji sana katika operesheni yangu kutokana na uhodari wake.Ngoja kwanza niwasiliane na ndugu yake niliyepewa namba zake” Austin akasimamisha gari pembeni ya barabara akapiga zile namba alizopewa za ndugu yake Job “Hallow ndugu habari yako.Natumai naongea na Amani” akasema Austin baada ya simu yake kupokelewa “Ndiyo unaongea na Amani.Nani mwenzangu? “Naitwa Austin.Mimi ni rafiki wa ndugu yako Job.Ninaishi nje ya nchi nimerejea jana na nikataka kumjulia hali rafiki yangu ,nimefika mahala alikokuwa akiishi nikapata taarifa kwamba amepatwa na matatizo ya akili.Ninataka kufahamu anaendeleaje hivi sasa? “Ni kweli alipatwa na matatizo ya akili.Nilimchukua na kumpeleka kwa wataalamu .Kwa sasa hali yake siwezi kusema ni nzuri au mbaya ila kidogo ana unafuu” “Dah!poleni sana kwa tatizo hili.Nawezaje kuonana naye? “Kwa sasa anaishi nyumbani kwangu mji mpya Tegeta.Unahitaji mtu wa kwenda naye kwani kwa kukuelekeza katika simu inaweza kukupa ugumu kidogo kufika.Uko wapi mida hii? “Niko hapa karibu na alipokuwa akiishi Job” akajibu Austin “Sawa,Mimi niko hapa katika kiwanda cha viatu cha Ndura.Kama una usafiri njoo unichukue nikupeleke moja kwa moja.Ukifika getini uliza Amani mjeledi utanipata haraka” “Ahsante sana Amani nitafika hapo muda si mrefu” akasema Austin ******************** Msafara wa makamu wa rais uliwasili nyumbani kwa waziri mkuu aliyevuliwa madaraka na kupokelewa na mwenyeji wake akakaribishwa sebuleni. “Habari za maisha mapya? Akauliza makamu wa rais wakati wakielekea sebuleni na wote wakaangua kicheko Sebuleni alikuwepo pia bi Agatha Mkasa mke wa rais ambaye alisimama na kusalimiana na makamu wa rais halafu kila mmoja akaketi.Muhudumu aliyevalia nadhifu akawahudumia vinywaji kisha wakaendelea na maongezi. “Ndugu zangu nimewaitieni hapa kwa ajili ya kuzungumza kwa kina juu ya hiki kilichotutokea.Sote tulikuwepo katika kikao na tuliafikiana mambo ya kufanya.Ninayaheshimu maamuzi ya kikao kile kikubwa lakini ndugu zangu pale katika kikao hatukupata nafasi ya kutosha kulijadili suala hili kwa undani wake na ndiyo maana nimeona ni vyema endapo tukikutana sisi watatu kulijadili suala hili kwa kina zaidi.Baada ya kulitafakari kwa kina nimegundua kwamba hatukuchukua maamuzi sahihi kuhusiana na suala hili.Kwa ufupi naweza kusema kwamba tulikurupuka sana” “Kwa nini una sehemu hivyo Jeremiah? Akauliza Makamu wa rais “Ninasema tulikurupuka kwa sababu tulikwenda kinyume na katiba ya Alberto’s ambayo iko wazi kwamba yeyote ambaye ataisaliti jumuiya na ikathibitika hivyo basi adhabu yake ni kifo.Ernest Mkasa amefanya usaliti mkubwa na wa wazi.Ameisaliti jumuiya kwa kitendo chake cha kufuta ule muswaada na kulivunja baraza zima la mawaziri.Akaenda mbali zaidi na kumvua wadhifa mkuu wa majeshi.Ni wazi ameanzisha vita na Alberto’s na tayari ameanza kuikata mizizi yetu kwa kasi.Nyote mnafahamu muswada ule ulikuwa ni kila kitu kwetu.Endapo tungefanikisha kuupitisha muswada ule basi matrilioni na matrilioni ya fedha yangemwagika hapa Tanzania.Tungekuwa tumefanikiwa kuikomboa nchi hii toka umasikini mkubwa lakini tumeshindwa kulifanikisha hilo.Tumeshindwa kuikamilisha kazi tuliyopewa na Alberto mkuu wa tatu .Tumemuangusha sana kwani Tanzania ni nchi ambayo anaitegemea mno.Hiki ni kioo cha nchi nyingi” akanyamaza akavuta pumzi ndefu na kuendelea “ Kikao kile cha juzi cha kujadili hili lililotokea ,kumezidi kutuzamisha na kutufanya tuonekane hatufai na hatuna uwezo wa kuiongoza jumuiya.Tumeshindwa kuchukua hatua zipasazo kulikabili suala hili.Toka tulipokaa kikao hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na wala hakuna juhudi zozote zinazoonekana za kutatua jambo hili.Tumezidi kumpa nguvu Ernest ya kutudhoofisha na anazidi kufanikiwa na kama hatutachukua hatua za makusudi za haraka ndani ya muda mfupi ujao hakutakuwa na Alberto’s hapa Tanzania.Atatufagia wote na hiyo ndiyo dhamira yake.Kwa hiyo ndugu zangu nimewaiteni hapa tulijadili kwa kina jambo hili na sisi watatu tunaweza kufanya jambo la msingi sana la kuinusuru jumuiya yetu na tuzidi kuaminiwa na baba Alberto mkuu” akasema Jeremiah “ Alichokiongea ndugu yangu Jeremiah ni kitu cha msingi sana na ninaweza kukubaliana naye.Binafsi maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao kile sikuyafurahia.Hayakuwa maamuzi sahihi na muafaka kwa jambo kubwa na zito kama hili.Naweza sema yalikuwa maamuzi dhaifu mno.Sifahamu kwa nini mwenyekiti aliamua kuchukua maamuzi kama yale wakati anafahamu hali halisi ilivyo.Mimi pia naungana nawe Jeremiah katika hili.Japokuwa unaweza ukaonekana kama ni usaliti ndani ya jumuiya lakini hatuwezi kukaa kimya wakati tunaona tunakoelekea si kuzuri hata kidogo_Ofisi ya rais ilikuwa ni mhimili wetu mkuu ambao umen’goka na sasa tunayumba na tusipokuwa makini sote tutaanguka kwa hiyo ndugu zangu nakubaliana na wazo la Jeremiah kwamba tusikae kimya bali tuone namna ya kufanya .Agatha wewe una lipi la kuchangia kwa upande wako? “ Kabla sijasema lolote kuna jambo nataka kuwashirikisha.Nina chanzo changu cha taarifa ndani ya makao makuu na kwa mujibu wa chanzo hicho ni kwamba toka lilipotokea tukio hili kumekuwa na mfululizo wa vikao vya siri kati ya Alberto mkuu wa tatu na watendaji wa juu wa jumuiya.Hakuna bado taarifa yoyote iliyopatikana wanajadili jambo gani” Agatha akastuka baada ya simu yake kuita “Samahani naomba niipokee hii simu” akatoka nje akaongea kwa takribani dakika tano kisha akarejea sebuleni “Tunaweza kuendelea” akasema Agatha “Nimepata taarifa nyingine toka kwa chanzo changu kuwa mwenyekiti ameitwa makao makuu haraka.Kwa mujbu wa taarifa alizozipata huyo mpasha habari wangu ni kwamba kuna timu imeundwa ambayo itatumwa Tanzania kuja kulikabili suala hili.Endapo timu hiyo itakuja Tanzania basi sote tutawekwa pembeni kwani tutakuwa tumeshindwa kuifanya kazi yetu.Binafsi siko tayari hilo litokee hasa nikikumbuka namna nilivyojitoa kwa hali na mali kuipigania na kuipenyeza jumuiya hapa Tanzania.” Akasema Agatha “Haya yote yamesababishwa na huyu mwenyekiti wetu kwa kushindwa kuchukua maamuzi sahihi kwa wakati unaostahili” akasema Jeremiah “Kwa hiyo nini basi tunatakiwa kufanya kwa sasa? Akauliza makamu wa rais “Kuna kitu kimoja tu ambacho tunapaswa kukifanya .Tunatakiwa tumuue mwenyekiti” Ukimya mfupi ukapita halafu makamu wa rais akauliz Una uhakika na hicho unachokisema Jeremiah? Akauliza makamu wa rais “ Ndugu zangu tukitaka tulimalize suala hili lazima tumuue Obi.Baada ya kumuondoa tutafanya kampeni na kunichagua mimi niwe mwenyekiti wa muda na tukifanikiwa katika hilo nitafanya maamuzi sahihi na kitu cha kwanza nitakachokifanya ni kutoa Baraka za kumuua Ernest Mkasa.Hakuna tutakachoweza kukifanya tena bila ya kumuondoa Ernest madarakani.Tukifanikiwa kwa hilo kwa mujibu wa katiba yetu makamu wa rais utakaimu nafasi ya rais kwa muda na hapo utanirejesha katika nafasi ya uwaziri mkuu ili tuweze kuikamilisha kazi tuliyokwisha ianza.Hivyo ndivyo ilivyotakiwa kufanywa lakini tunaambiwa unatakiwa ufanyike uchunguzi kwanza kabla ya kuchukua hatua yoyote.Huo ni upuuzi


ITAENDELEA







0 comments:

Post a Comment

Blog