Search This Blog

Saturday 5 November 2022

MAUAJI YALIYOJAA UTATA - 2

 






Simulizi : Mauaji Yaliyojaa Utata

Sehemu Ya Pili (2)





“Umefikia wapi David?” aliuliza Benjamin kwenye simu.

“Nilisahau, ila hilo si tatizo kaka, muda wowote ule nitalifanyia kazi,” alijibu David.

“Umejisahau sana kaka, wanataka kumuua Vivian,” alisema Benjamin.

“Unasemaje?”

“Ndiyo hivyo, ninataka kujua alipo kwa sasa na ndiyo maana nikakwambia lile jambo linatakiwa kufanyika kwa haraka sana,” alisema Benjamin.

“Basi sawa, nipe saa moja tu.”

Simu zikakatwa, Benjamin akatulia kitandani huku akionekana kuwa na mawazo tele, bado kichwa chake kilichanganyikiwa mno, hakuamini kilichokuwa kikiendelea maishani mwake.

Wakati mwingine aliwaza kutoroka lakini hilo lisingekuwa suluhisho hata kidogo, ilikuwa ni lazima kama kuondoka, aondoke na Vivian lakini si kumuacha.

Kumuua Carter lilikuwa jambo gumu sana lakini mpaka kufikia kipindi hicho, hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kumuua ili aweze kuyaokoa maisha ya mpenzi wake ambaye mpaka kipindi hicho bado alikuwa mateka.

Watu hawakupungua hotelini hapo, walilala huku kila mmoja akitaka kumuona Carter ambaye ndiye alikuwa gumzo duniani kwa kipindi hicho. Benjamin akasimama dirishani na kisha kuchungulia nje, watu waliolala pale nje ya hoteli ile walimfanya kuwa na huruma kumuua Carter, alijua ni kwa namna gani angewaumiza watu hao, si wao tu bali hata watu wengine duniani kote, hakika yangekuwa maumivu makubwa sana mioyoni mwao.

Kwa hatua aliyofikia, hakutakiwa kujali kitu chochote kile, kama alivyoambiwa kwamba asipofanikisha kumuua Carter basi mpenzi wake angeuawa, hivyo alitakiwa kupambana mpaka mwisho wa siku kuhakikisha kwamba mtu huyo anauawa.

Siku iliyofuata ilikuwa ni ya kihistoria hapo Miami, watu walikusanyika katika Ukumbi wa Carthebian uliokuwa katika ufukwe wa Salvador hapohapo Miami kwa ajili ya kuangalia shoo iliyoandaliwa na wanafunzi waliowahi kusoma na Carter.

Shoo ilikuwa nzuri, watu waliifurahia sana tena wengine wakichukua nafasi hiyo kupiga picha na msanii huyo huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha mno.

Wakati shoo hiyo ikiendelea huko, huku hotelini Benjamin alikuwa bize, alitamani sana kuingia chumbani kwa Carter lakini hakujua ni kwa namna gani angeweza kuingia.

Milango yote haikuwa ikitumia ufunguo, kulikuwa na kadi maalumu ambayo ulitakiwa kuichukua na mlangoni kulikuwa na sehemu ya kupitishia kadi hiyo na hatimaye mlango kufunguka.

Alichokihitaji kilikuwa ni kadi malaya ambayo angeweza kufungua kila chumba na kufanya kile alichotaka kufanya. Kabla ya kuitafuta, akaandaa sindano yake iliyokuwa na sumu ambayo aliiona kufaa sana kuchomwa Carter, baada ya kuiweka vizuri, akaanza mishemishe za kumtafuta msichanaMercy kwa kuamini kwamba alikuwa na kadi ya kufungulia milango yote kwani ndiye msichana aliyekuwa akifanya usafi wakati wageni hawapo vyumbani mwao.

Huyo ndiye alikuwa mtu muhimu, ilikuwa ni lazima kumtafuta, alichokifanya, akatoka chumbani humo na kuanza kumtafuta Mercy. Hakumuona na hakujua alikuwa wapi. Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, aliamini kwamba msichana wa mapokezi, Rose alikuwa akifahamu msichana huyo alipokuwa, hivyo akaenda huko kumuuliza.

“Mercy yupo wapi?” alimuuliza Rose.

“Wewe wa nini?” aliuliza Rose huku akionekana kuona wivu, kwa kifupi alishaanza kumpenda Benjamin.

“Nataka nimuone tu.”

“Kuna nini?”

“Kwani si kumuona tu jamani, au kuna tatizo?” aliuliza Benjamin.

“So ili mkeo nijue jamani,” alisema msichana huyo, Benjamin akamwangalia kwa macho makini, uzuri wake yeye mwenyewe ulimchanganya, ila hakutaka kujionyesha kama alipagawa.

“Kumbe tatizo lipo wapi? Si nataka kumuona shemeji wangu,” alisema Benjamin.

Rose akashusha pumzi, alimwangalia Benjamin kwa umakini, alimpenda mwanaume huyo na hakujua alikuwa akiishi wapi na alifika mahali hapo kufanya nini.

Kwa sababu kwa maneno ya Benjamin alionekana kama kukubaliana naye, akamwambia kwamba inawezekana Mercy alikuwa katika chumba cha usafi akifua mashuka kwa mashine pamoja na vitu vingine. Chumba hicho kilikuwa ghorofa ya sita, hakutaka kusubiri, akaelekea huko.

Alipandisha ngazi, hakutaka kutumia lifti kwa kuhisi kwamba angeweza kukutana naye hata kwenye korido za ghorofa nyingine. Alipofika katika ghorofa hiyo aliyoambiwa, akaelekea katika chumba kilichoandikwa laundry mlangoni, akafungua.

Mbele yake kulikuwa na mashuka mengi yakiwa yameanikwa, yalikuwa zaidi ya mia moja. Kumuona mtu wa upande mwingine ilikuwa ngumu sana hivyo alichokifanya Benjamin ni kuanza kuita.

“Mercy...Mercy...” aliita mwanaume huyo.

“Helo...” aliita msichana huyo.

Benjamin akaenda huko alipoitikiwa, alipofika, akamkuta Mercy akiwa peke yake, alikuwa akitoa mashuka kutoka kwenye tenga na kuweka kwenye mashine moja ya kufulia, hapohapo akamsogelea.

“What are you doing here?” (Unafanya nini hapa?) aliuliza Mercy huku akimwangalia mwanaume huyo machoni.

“I am here to see you baby! Is anyone here?” (Nipo hapa kukuona! Kuna mwingine hapa?) alijibu Benjamin na kuuliza.

“Nobody...” (Hakuna mtu)

Kabla ya kufanya kitu chochote kile alitakiwa kutafuta mahali kadi ilipokuwa, kwenye kuangalia huku na kule, pembeni akauona mkoba wa Mercy, akajua kwamba ni lazima ndani ya mkoba huo kulikuwa na hiyo kadi, hivyo akamchukua msichana huyo na kumpeleka kule kulipokuwa na mokoba ule.

“Kuna nini?” aliuliza msichana huyo.

“Nataka nikuone jinsi ulivyo, umezishtua hisia zangu,” alisema Benjamin huku akijifanya kuhema juujuu kimahaba.

“Jamani ndiyo unataka hapa?”

“Kwani kuna tatizo? Kuna mtu anatuona?” aliuliza Benjamin huku tayari mikono yake ikiwa imeanza kazi ya kufungua vifungo vya blauzi ya Mercy.

“Aishiiii...” alianza kutoa kelele za mahaba.

Akili ya Benjamin ilikuwa kwenye ule mkoba tu, aliihitaji kadi iliyokuwa katika mkoba ule na hakukuwa na njia nyingine ya kuipata kadi ile zaidi ya kufanya kile alichokuwa akikifanya.

Akaanza kumvua msichana huyo suruali ya jinzi aliyokuwa ameivaa na kubaki na nguo ya ndani tu, akaanza kuutalii mwili wake kwa kupanda huku na kule, kwa jinsi Mercy alivyochanganyikiwa, akaanza kufumba macho kimahaba, alichanganyikiwa mno.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Unanukia vizuri sana...” alisema Benjamin kwa sauti ya chini karibu na sikio la Mercy.

“As..an..t..e..” aliitikia msichana huyo, mwili wake ulikuwa hoi.

Kitendo cha kufumba macho tu, Benjamin hakutaka kuchelewa, hapohapo akaupeleka mkono ule kisiri tena huku kichwa chake kuyaficha macho ya msichana huyo.

“Hii hapa...” alijisemea moyoni mara baada ya kuigusa kadi hiyo mkobani, alichokifanya ni kuichukua, akaiingiza mfukoni kisiri, kilichofuata ni kufanya mapenzi na msichana huyo ndani ya chumba hichohicho cha kufulia.





.Walichukua dakika arobaini na tano mpaka kumaliza. Mercy alikuwa hoi, hakuamini kama angeweza kukutana na mwanaume anayeweza kufanya mapenzi kama ilivyokuwa kwa Benjamin.

Hapohapo wakaanza kuvaa nguo zao na kisha kubaki wakiangaliana tu. Hakukuwa na mtu aliyesema chochote kile zaidi ya kusogeleana na kukumbatiana tu.

“Ninakupenda...” alisema Benjamin.

“Nakupenda pia.”

Benjamin hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka kurudi chumbani kwake huku tayari akiwa na kadi ile mfukoni mwake, alipofika, akaingia chumbani na kutulia.

Mpango aliokuwa nao ilikuwa ni lazima akalale chumbani kwa Carter usiku huohuo ili iwe rahisi kwake kukamilisha mpango wake. Muda ulizidi kwenda mbele, kuna kipindi alihisi kwamba angeweza kuchelewa, hivyo akaamka, akachukua kitambaa kilichokuwa na dawa za usingizi na kisha kutoka mule huku mfukoni akiwa na bomba la sindano.

Kwenye korido, hakukuwa na kamera za CCTV hivyo ilikuwa ni rahisi kwake kuingia humo ndani. Akachukua kadi yake na kuipachika katika kimashine kidogo, zikawaka taa nyekundu kwa zamu kisha kubadilika na kuwa za kijani, mlango ukafunguka.

Akaingia chumbani mule, hakikuonekana kuwa tofauti na chumba chake, vyote vilikuwa vya bei kubwa, alibaki akizungukazunguka mule, aliporidhika, akakifuata kitandani, kwa sababu kilikuwa na uvungu mkubwa kidog uliomuwezesha kupenya japo kwa tabu, akaingia humu huku akiwa na bomba la sindano na kitambaa ambacho alikiwekea dawa za usingizi.

“Ngoja nisubiri...Mungu, sifanyi hivi kwa kupenda, nimelazimishwa kwa ajili ya mpenzi wangu,” alisema Benjamin kwa sauti ndogo huku akivaa glovu mikono mwake.

Hakulala hata kidogo, alikuwa macho huku akiendelea kumsubiri Carter ambaye aliamini hakuwa mbali mpaka kufika mahali hapo. Huko uvunguni, alizima simu yake, hakutaka kufanya kosa lolote lile na kuonekana kabla hajakamilisha mpango wake.

Muda ulizidi kwenda mbele, ilipofika saa kumi alfajiri, akasikia sauti za watu nje, kwa kukadiria zilikuwa kama za watu sita, watu wale wakasogea mpaka mlangoni na kisha kuufungua.

Alikuwa Carter na wapambe wake, wakaingia ndani huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha. Muda ulikuwa umekwenda sana na hawakuwa na muda wa kupoteza, Carter akaenda bafuni, akaoga na kisha kurudi chumbani pale.

Wakapiga stori, nyingi walizozipiga hapo zilikuwa ni za kumsifia Carter kwamba alifanya kazi nzuri sana, aliwaonyeshea watu yeye alikuwa nani. Walikaa kwa dakika kadhaa mpaka muda ule ambao wengine wakaenda kulala na yeye kutulia kitandani ambapo baada ya dakika chache, akapitiwa na usingizi.

Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi kwa Benjamin kumuua Carter, hakutaka kuchelewa kule uvunguni, harakaharaka akatoka na kisha kumwangalia Carter kitandani pale, alichokifanya ni kuchukua kitambaa kile kilichokuwa na dawa ya usingizi na kisha kumkandamiza Carter kitandani pale huku kitambaa kile kikiwa usoni mwake.

Carter hakukubali, alijitahidi kuhangaika huku na kule ili kujinasua lakini ilishindikana kabisa, alikandamizwa kitandani pale na kadiri alivyovuta pumzi na ndivyo alivyokuwa akiivuta dawa ile na sekunde chache mbele, akatulia kitandani pale.

“Kazi imekwisha...” alisema Benjamin.

Mara baada ya kufanikiwa kumlevya kwa yale madawa yaliyokuwa kwenye kitambaa kile akachukua bomba la sindano aliyokuwa nayo na kisha kumchoma katika mshipa mmoja mkononi mwake ili aweze kumuua kitandani pale.

Alipohakikisha sumu ile imeingia vilivyo mwilini mwake, akachukua fedha ambazo aliambiwa aziweke ikiwepo euro, dola, yen na paundi kisha kuanza kufanya mikakati ya kutoka ndani ya chumba kile.

Hakukuwa na shida kwenye kutoka, akaufungua mlango ule na kutoka. Hakutaka kuingia chumbani kwake, akaelekea katika chumba kile cha kufanyia usafi kwa kufua mashuka na nguo kisha akaitupa ile kadi chini, pembenipembeni na kisha kurudia chumbani kwake, akavuta shuka na kutulia.

****

“Umenionea kadi yangu?” aliuliza msichana Mercy huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Kadi gani?”

“Ya milango!”

“Hapana! Kwani wewe uliiweka wapi?”

“Niliiweka kwenye huu mkoba.”

“Sasa iko wapi?”

“Ndiyo siioni.”

“Umeangalia vizuri?”

“Ndiyo! Hakuna!”

Mercy alichanganyikiwa, alikumbuka vilivyo kwamba aliiweka kadi ndani ya mkoba wake, lakini katika kipindi hicho alipokuwa akiitafuta, hakuwa akiiona. Akaondoka mahali hapo na kwenda sehemu zote alizopita lakini huko hakuona kitu.

Mercy alizidi kuchanganyikiwa, hakukumbuka kama aliuacha mkoba ule sehemu yoyote ile, mtu pekee na wa mwisho kumjia kichwani mwake alikuwa Benjamin.

“Inawezekana anajua...”

Alichokifanya Mercy ni kumpigia simu ya mezani chumbani kwake, kitu kilichomshtua ni kwamba simu iliita lakini haikupatikana. Mercy hakutaka kukata tamaa, aliendelea kupiga zaidi na zaidi lakini majibu wala hayakubadilika, bado simu ile haikupokelewa kitu kilichomtia wasiwasi mwingi.

“Au ameshaondoka?” alijiuliza.

Akaondoka na kuelekea mapokezini na kumuuliza dada aliyekuwepo hapo, hakuwa Rose, yeye aliondoka na kumuacha msichana mwingine, akamuuliza kama mteja aliyepanga chumba namba tisini na mbili alikuwa ameondoka.

“Hapana! Bado yupo,” alijibu msichana huyo.

“Mbona nampigia simu simpati?”

“Sijui! Inawezekana amelala, ila hapa inaonyesha yupo, hajaondoka,” aliongeza msichana huyo.

Mercy hakutaka kusubiri, alichokifanya ni kwenda wenyewe mpaka katika chumba kile, alipoufikia mlango, akaanza kugonga kwa nguvu, aligonga zaidi na zaidi lakini mpango wala haukufunguliwa kitu kilichoendelea kumpa maswali mengi.

“Mmh! Mbona naanza kuwa na wasiwasi...” alisema msichana huyo, akahisi akichoka, kilichobaki mbele yake kilikuwa ni kufukuzwa kazi tu, hakukuwa na kitu kingine zaidi ya hicho kwani kupoteza kadi, tena ile masta kabisa lilikuwa kosa kubwa mno.

Akaondoka na kuelekea nyumbani kwake, hakuwa na raha, alipanga siku inayofuata kuwa asubuhiasubuhi kuzungumza na Benjamin kwani bado moyo wake ulimwambia kwamba mwanaume huyo aliiona ile kadi aliyokuwa akiitafuta.

***

Asubuhiasubuhi msichana Mercy akafika hotelini hapo, bado akili yake haikuwa sawa hata kidogo, alikuwa na mawazo mengi, kadi ambayo aliipoteza usiku uliopita ilimchanganya mno.

Alipofika hotelini, hata kabla ya kufanya kitu chochote ilikuwa ni kwenda katika chumba cha Benjamin ili aonane naye na kumuuliza kuhusu kadi hiyo. Alipofika, akagonga mlango ambapo baada ya sekunde kadhaa, mlango ukafunguliwa, mwanaume aliyesimama mbele yake alikuwa Benjamin.

“Kumbe wewe...karibu mpenzi,” alisema Benjamin huku akimkaribisha msichana huyo huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

“Ahsante! Nimekuja kukuuliza kitu,” alisema msichana huyo.

“Kitu gani?”

“Nilipoteza kadi jana!”

“Kadi gani?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Alijifanya kutokufahamu chochote kile, hata macho yake yalionyesha kabisa kwamba hakujua kilichokuwa kikiendelea. Mercy akaanza kumwambia kuhusu kadi ile ambayo aliipoteza katika mazingira ya kutatanisha huku muda wote huo akionekana kuwa na majonzi tele usoni mwake.

“Pole sana, ila umeangalia vizuri kwenye kile chumba?” aliuliza Benjamin.

“Nimeangalia kila kona.”

“Umetoa nguo zote na kuangalia vizuri?”

“Ndiyo!”

“Mmh! Sasa iweje isionekane?” aliuliza Benjamin.

“Ndiyo nashangaa!”

Alichokifanya Benjamin ni kumwambia waende kwenye kile chumba cha kufanyia usafi, alikuwa na uhakika kwamba kadi ile ilikuwa mule kwani alfajiri ya siku hiyo aliirudisha na kurudi chumbani kwake.

Mercy alikuwa na uhakika kwamba kadi hiyo haikuwepo huko, aliangalia kila kona, alitoa nguo zote na kuzirudisha lakini hakufanikiwa kuiona kadi hiyo. Benjamin alipomaliza kujiandaa, wakaelekea katika chumba hicho na kuanza kuitafuta kadi hiyo.

Kwanza Benjamin hakutaka waende kwenye ule upande alioiweka kadi ile, alimwambia Mercy waende kwenye upande mwingine kitu ambacho kikafanyika kikamilifu. Walipokosa na ndipo walipokwenda kwenye ule upande uliokuwa na kadi, kweli wakaikuta.

“Ni hii hapa,” alisema Mercy huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.

“Wewe si ulisema umeikosa?”

“Ndiyo! Nilitafuta sana, nafikiri huku sikuja,” alisema msichana huyo.

Wakabaki wakiangalia tu, tayari miili yao ikaanza kuwasiliana mahali hapo, walikuwa wawili tu kama jana na kila mtu alionekana kumtamani mwenzake. Wakiwa wanaangalia kama mbuzi, wakaanza kusikia mlango mmoja huko nje ukigongwa, uligongwa huku sauti za watu zikisikika mahali hapo.

Kwanza wakashtuka, haikuwa kawaida kabisa, wakatoka chumbani humo na kwenda kwenye korido, marafiki zake Carter walikuwa katika mlango wa chumba alichochukua Carter na kuanza kugonga huku wakitaka wafunguliwe.

“Jamani, si jana amechelewa kulala, ataweza kuamka muda huu?” aliuliza Mercy huku akionekana kuwashangaa.

“Hatuna muda, tunatakiwa kuondoka sasa hivi,” alijibu jamaa mmoja.

Alichokifanya Mercy ni kwenda mapokezini ambapo huko akaanza kupiga simu ya mezani ndani ya kile chumba cha Carter, alipiga simu, iliita na kuita lakini haiupokelewa.

Hilohilo ndilo lililotokea kwa Benjamin usiku wa jana, hata naye alipojaribu kupigiwa simu hakuipokea. Wote wakaanza kushikwa na wasiwasi, wafanyakazi wa hoteli hiyo hawakutulia, wakaanza kupandisha juu mpaka kwenye korido iliyokuwa na chumba kile na kuanza kugonga.

Wakati huo Benjamin alikuwa chumbani kwake, alifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kutoka nje, alitaka kuona kitu gani kingeendelea.

Mara akasikia mlango ukianzakupigwa, watu hao waligonga na kugonga, mlango haukufunguliwa na hivyo kuanza kuuvunja. Ilikuwa kazi kubwa, mlango ulikuwa imara sana, walifanya hivyo kwa zaidi ya dakika nne, mlango ukafunguka na kuingia ndani.

Picha waliyoiona, hakukuwa na mtu yeyote aliyeiamini, Carter alikuwa juu ya kitanda chake, sindano iliyokuwa na madawa ilikuwa katika mkono wake, tena ikiwa imechoma katika mshipa wake, kwa jinsi picha ilivyoonekana ilionyesha kabisa kwamba mtu huyo alikuwa amejidunga madawa ya kulevya.

“What the fuck is this?” (Ndiyo nini hiki?) aliuliza jamaa mmoja huku akionekana kushtuka.

Wakamsogelea kitandani pale, wanawake waliomuona Carter wakaanza kupiga kelele, waliokuwa wamelala katika vyumba vyao wakaamka na kwenda chumbani humo kushuhudia ni kitu gani kilikuwa kimetokea.

Mbali na mwili huo, pembeni yake kulikuwa na fedha za noti, dola, yeni, euro na paundi. Hilo wala halikuwafanya kuhisi chochote kile kwani kwa mtu kama Carter, kuwa na fedha mbalimbali lilikuwa jambo la kawaida sana.

“Was he cocaine addicted?” (Alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya?) aliuliza jamaa mmoja huku akimwangalia Carter pale kitandani.

Marafiki zake walibaki wakiashangaa, hawakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, rafiki yao wa muda mrefu, Carter eti alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya.

Hawakutaka kuamini hilo, pale kitandani alipokuwa, alikuwa kimya kabisa na hata mapigo yake ya moyo hayakuwa yakidunda hali iliyoonyesha kwamba alikuwa amekufa.

Walichokifanya ni kupiga simu polisi ambapo baada ya dakika ishirini walikuwa mahali hapo. Moja kwa moja wakaenda mpaka katika chumba hicho huku wakiwataka watu wote watoke nje na wao kufanya kazi yao.

Tayari mpiga picha wa polisi pamoja na mchoraji walifika mahali hapo na kuanza kuuangalia mwili wa Carter, alionekana kutumia kiasi kikubwa cha madawa mpaka kufariki pale kitandani.

Si marafiki zake walioshangaa tu bali hata polisi wenyewe nao walishangaa. Walimfahamu Carter, alikuwa mmoja wa wanamuziki wadogo ambao walitumika hata na kampuni mbalimbali kutokomeza utumiaji wa madawa ya kulevya, sasa iweje mtu huyo leo afe kwa kuzidisha utumiaji wa madawa hayo? Kila walichojiuliza, walikosa jibu.

Stori juu ya kifo chake zikaanza kusambazwa kwa kasi, hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba mwanamuziki aliyekuwa na jina kubwa, Carter alikuwa amefariki dunia tena kwa kujidunga madawa ya kulevya kwa kiasi kikubwa.

Kila mtu aliyesikia taarifa hizo alibaki akishangaa, wengi wakajiuliza na mwisho wa siku kuja na majibu kwamba Carter alifanya siri utumiaji wa madawa ya kulevya.

Ulikuwa msiba mkubwa, kijana huyo, mwanamuziki huyo alikuwa na jina kuubwa, alikuwa kipenzi cha watuu wengi kitendo cha kusikia kwamba alikuwa amekufa ndani ya chumba hicho, hakika yalikuwa majonzi makubwa mno kwa kila mtu.

Taarifa hizo ziliendelea kuwekwa katika mitandao ya kijamii, kila aliyeziona, hakuamini, ndani ya saa moja tu, dunia nzima ilijua kile kilichokuwa kimetokea nchini Marekani huko Miami.

Watu walilia sana, wengine walijiuliza maswali mengi juu ya sababu iliyomfanya Carter kutumia madawa ya kulevya kwa kiwango kikubwa hicho mpaka kufa ndani ya chumba hicho.

Kila mtu alilaumu, wengine wakamuonea huruma. Mpaka mwili wake unaingizwa katika Hospitali ya St. Martin Luther King, tayari watu wengi walikusanyika hospitalini hapo, walitaka kusikia kile kilichokuwa kikiendelea, walitaka kuamini kama kweli msanii huyo alikufa baada ya kutumia madawa ya kulevya kupita kiasi.

***

“Nimefanya mlichotaka nikifanye, naomba mmuachie mpenzi wangu,” alisema Benjamin, alikuwa akizungumza na mtu fulani katika simu.

“Sawa! Tumeona, umefanya kazi nzuri sana...” ilisikika sauti upande wa pili.

“Kwa hiyo?”

“Kuhusu?”

“Mpenzi wangu! Si tayari nimekwishafanya kazi yenu, muachieni sasa,” alisema Benjamin.

Alikuwa akizungumza na mwanaume wa upande wa pili, alikuwa akimpa taarifa kwamba kazi aliyokuwa amepewa tayari ilikuwa imefanyika na hivyo alitaka mpenzi wake aachiwe huru kama yalivyokuwa makubaliano yao kabla.

Kwanza mwanaume huyo alikataa, kwa jinsi ilivyoonekana, alitaka kumuongezea kazi nyingine, ila alipotaka kufanya hivyo, aliona haikuwa sahihi kwani makubaliano ambayo waliwekeana mwanzo yalikuwa ni kumuua Carter na hakukuwa na jingine.

Walichokifanya huko walipokuwa ni kumfunga kitambaa cheusi Vivian na kumpakiza ndani ya gari, wakaanza kuondoka naye huku waliomsindikiza wakiwa wanaume wawili, waliokuwa na miili iliyojazia.

Njiani, Vivian alikuwa akilia, moyoni mwake aliumia mno, hakujua sababu iliyomfanya kutekwa na watu hao, kila alipouliza, hakupewa jibu bali aliambiwa asubiri mpaka atakapokutana na mpenzi wake.

Safari hiyo iliendelea mpaka walipofika katika kituo cha mafuta cha Total ambapo hapo ndipo walipomkabidhi Benjamin msichana Vivian ambaye hakuonekana kuwa sawa kabisa, kila wakati alikuwa akilia tu.

“Wamekufanya nini? Wamekupiga?” aliuliza Carter.

“Hapana! Kwa nini wamefanya hivi?” aliuliza Vivian.

“Sijajua! Acha tuondoke,” alisema Benjamin huku akionekana kutokujiamini.

“Benjamin, bosi amesema uchukue hii simu,” alisema mwanaume huyo huku akimpa simu aina ya iPhone 7.

“Ya nini?” aliuliza Benjamin huku akiichukua simu hiyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kama zawadi yako!”

“Nashukuru!” alisema Benjamin na kisha kumrudishia mwanaume huyo kwani alihisi kwamba simu hiyo ilikuwa na kifaa cha GPS ambacho kingemfanya kuonekana kila alipokuwa.

“Basi hakuna tatizo!”

Hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuingia ndani ya gari na kuanza kuondoka mahali hapo. Alichokifikiria Benjamin ni kuondoka na mpenzi wake kwenda mbali kabisa kujificha, hakutaka kuonekana kwani kile alichokuwa amekifanya chumbani kwa Carter, alikuwa na uhakika kwamba watu hao wangemtafuta na kumuua tu.

Walipofika katika apartment waliyokuwa wakiishi, Benjamin akamwambia Vivian wachukue kila kitu chao na kuondoka mahali hapo, kweli wakafanya hivyo.

“Ila kwa nini?” aliuliza Vivian.

“Wewe tuondoke, watatutafuta hawa.”

“Kisa?”

“Nimewachezea mchezo!”

“Mchezo gani?”

“Usijali, nitakwambia nini kilitokea,” alisema Benjamin huku akiendesha gari kwa kasi ya ajabu, alikuwa katika barabara ya St. Johnson ya magari yaendayo kasi kwa zaidi ya 180, ilikuwa ni lazima waondoke na kuelekea Alexandria, mji uliokuwa pembeni mwa jiji hilo la Washington DC.





Madaktari waliendelea na tiba yao kama kawaida, mwili wa Carter uliwekwa kitandani huku ukiwa umetundikwa na dripu kadhaa. Japokuwa taarifa za awali zilisema kwamba mwanamuziki huyo alikuwa amekufa lakini walipomchunguza, wakagundua kwamba hakuwa amekufa bali mwili wake uliwekewa dawa Declophine, dawa ambayo mtu akiwekewa katika mishipa yake husimamisha mapigo ya moyo kwa muda.

Madaktari walikuwa wakiingia kwa zamu, walikuwa bize wakiendelea kumpa matibabu mwanamuziki huyo kwa kumwekea dawa iitwayo Anti-Declophine ambayo ndiyo ilikuwa na uwezo wa kuyarudisha mapigo ya moyo ya Carter.

Mpenzi wake alifika hospitalini hapo, muda wote alikuwa mtu wa kulia tu, hakuamini kama kweli siku ile aliyoagana naye na kwenda Miami ndiyo ingekuwa siku ya mwisho kuonana naye.

Ndugu zake ndiyo waliokuwa msaada, walimshika huku na kule, kila alipotaka kufanya jambo baya, walimzuia kwani walijua kabisa kwamba katika kipindi kama hicho angeweza kufanya jambo lolote baya.

Kama dunia ilivyokuwa ikishangaa, hata naye alikuwa akishangaa, mpenzi wake kufa huku akiwa amejidunga madawa ya kulevya ilimshangaza sana. Alikuwa naye kwa kipindi kirefu, walifanya mambo mengi walizoeana sana lakini hakukuwa hata na siku moja ambayo alimuona mpenzi wake akitumia madawa ya kulevya, si kutumia tu, hata kumuona akiyasifia madawa hayo, hakuwahi kusikia kitu kama hicho.

Kazi ilikuwa kubwa, kiasi cha dawa hiyo ambacho alipewa Carter ilionyesha kwamba angechukua saa arobaini na ndipo angerudiwa na fahamu hivyo. Nje ya hospitali hiyo, kulikuwa na watu wengi wakiwemo waandishi wa habari, kila mtu alitaka kusikia madaktari wangesemaje kuhusu afya ya Carter ambayo ilikuwa tata sana.

Madaktari hawakutaka kuzungumzia chochote kile, walikwishajua kile kilichokuwa kimetokea lakini hawakutaka kumwambia mtu yeyote kwa kuhisi kwamba kama wangefanya hivyo basi amtu aliyekuwa amemchoma sindano hiyo angeweza kumrudia hapo hospitalini na kufanikisha mpango wake.

Saa ziliendelea kusonga mbele, saa arobaini zilipofika, Carter akaanza kutingisha viungo vyake pale kitandani alipokuwa. Kiungo cha kwanza kabisa alichokitingisha kilikuwa ni vidole kisha kuyafumbua macho yake.

“He is back...” (Amerudi...) alisema Dk Phinias.

Kila mmoja akaonyesha tabasamu pana, kitendo cha Carter kurudiwa na fahamu kiliwafurahisha mno na hivyo kuwasiliana na wazazi wake ambao walikuwa nje na kuwapa taarifa juu ya kile kilichokuwa kimetokea.

“Unasemaje?” aliuliza baba yake huku akionekana kutokuamini.

“Carter amerudiwa na fahamu!” alijibu Dk. Phinias.

“Inawezekana vipi?”

“Subirini kwanza, tunahitaji kuzungumza na polisi!”

Kila mmoja aliyesikia jibu la daktari alibaki akiwa na furaha mno, hawakuamini kile walichokisikia kwamba Carter alikuwa amerudiwa na fahamu. Ilikuwaje arudiwe na fahamu na wakati ukweli ulijulikana kwamba alikufa baada ya kujidunda madawa ya kulevya hotelini?

Hawakuamini hivyo wakataka kumuona. Kutokana na furaha walizokuwa nazo, wakashindwa kuvumilia na hivyo kuwataarifu watu wengine, hapo ndipo stori zilipoanza kuvuma kwamba kumbe Carter hakufa bali alikuwa amezimia.

“Sasa kwa nini polisi walisema kwamba alikufa? Kama alikufa si inamaana walisikiliza mapigo ya moyo lakini hayakuwa yakidunda, kama hayakuwa yakidunda, kwa nini yupo hai?” yalikuwa maswali kadhaa waliyojiuliza watu mitaani, maswali yalikuwa mengi mengi lakini hakukuwa na aliyepata jibu.

****

Bwana David Seppy alikasirika, hakuamini kile alichokisoma kwamba mtu aliyetaka afe, hakuwa amekufa, alichukuliwa kutoka hotelini na kupelekwa hospitalini na madaktari wakamtibu na hatimaye kupona.

Hakujua ni kitu gani kilitokea, hapo ndipo alipogundua kwamba Benjamin hakuwa mtu wa kawaida, alitumia ujanja ambao mpaka wao wenyewe hawakuuelewa ulikuwa ujanja upi ambao ulivizuga mpaka vyombo vya habari na kuripoti kwamba Benjamin alikuwa amekufa.

Hapohapo akawapigia simu vijana wake, kwa jinsi walivyomuona siku hiyo, hakuonekana kuwa katika hali ya kawaida hata kidogo, alionekana kuwa na hasira sana na hata alivyokuwa akizungumza alionekana kuwa mtu ambaye hakuleta utani hata mara moja.

Aliwaangalia vijana hao kwa zamu, aliwalaumu kwa kuwa walipewa taarifa kwamba Carter alikufa, hawakutaka kujiridhisha, wakakubaliana na Benjamin kwamba kijana huyo alikufa.

“Nani ana uhakika kwamba Carter amekufa?” alianza kwa kuuliza swali huku akiwaangalia vijana hao watatu kwa zamu, wote wakanyoosha mikono juu.

“Mna uhakika kwamba amekufa?” aliuliza Bwana Seppy.

“Ndiyo bosi!”

“Umesikia wapi?”

“Kwenye vyombo vya habari, na hata wewe tulikuja kukwambia kwamba kijana huyo amekufa, ukatuambia tumeona wapi, tukakuonyesha picha katika mitandao, ilionyesha kabisa kwamba alikufa, ukakubaliana nasi,” alisema kijana mmoja huku akimwangalia Bwana Seppy usoni.

Mzee huyo hakutaka kuzungumza kitu, akabaki kimya, ni kweli alikumbuka kwamba aliwaambia vijana hao maneno hayo kwamba mtu huyo alikuwa ameuawa, lakini kwa nini naye alikubaliana moja kwa moja kwamba mtu huyo alikuwa ameuawa, kila alipojiuliza, akakosa jibu.

“Sasa sikilizeni, ninataka muhakikishe kwamba hawa watu wawili wanauawa haraka iwezekanavyo,” alisema Bwana Seppy huku akiwaangalia vijana wake hao kwa zamu.

“Wawili tena?”

“Ndiyo! Carter na Benjamin, hakikisheni kabla mwezi huu haujakwisha, wanauawa wote,” alisema mzee huyo.

“Sawa mkuu!”

****

Maofisa wa upelelezi nchini Marekani, FBI (Federal Bureau Investigation) walitaka kufuatilia kuona ni kitu gani kilitokea mpaka hali iliyomkuta Carter imkute huku ulimwengu mzima ukijua kwamba mwanamuziki huyo alikufa hotelini baada ya kujiovadozi madawa ya kulevya.

Walitaka kupata ripoti kamili kutoka kwa madaktari, walikuwa na uhakika kwamba walijua kuwa mtu huyo alikufa kutokana na mapigo yake ya moyo kusimama, sasa ilikuwaje mpaka awe hai kipindi hicho, wakahisi kwamba kulikuwa na kitu kilitokea ambacho nao walitaka kukifahamu.

Harakaharaka wakawasiliana na uongozi wa Hospitali ya Martin Luther King na kutaka kuzungumza na daktari mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Terry. Walitaka kusikia kila kitu, walijua kwamba piga ua madaktari walifahamu ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka hali hiyo kuwa hivyo.

Hawakutaka kuchelewa, wakawatuma maofisa wawili ambao walikwenda moja kwa moja mpaka katika hospitali hiyo na kukutana na Dk. Terry ambaye mara baada ya kuambiwa dhumuni la maofisa hao kufika hospitalini hapo, akaahidi kutoa ushirikiano wote.

“Tunahitaji kufahamu kuhusu Carter,” alisema ofisa mmoja.

“Hakuna tatizo! Kipi mngependa kufahamu?” aliuliza Dk. Terry.

“Kuhusu kile kilichotokea, kuna ripoti yake?”

“Ndiyo! Ila bado sijaletewa ofisini!”

“Tunahitaji kuiona, na tunataka kujua nini kilitokea, ikiwezekana tuzungumze na madakatri wa kwanza ambao waliupokea mwili wake,” alisema ofisa mmoja.

Hilo wala halikuwa tatizo, alichokifanya daktari huyo ni kuwasiliana na daktari mmoja miongoni mwa madaktari waliompokea Carter na kumuhitaji ndani ya ofisi yake huku akiwa na ripoti kamili mara baada ya mwili wake kuchunguzwa na madaktari wa hospitali hiyo.

Ni ndani ya dakika kumi tu, mlango wa ofisi hiyo ukaanza kugongwa, Dk. Terry akamkaribisha mgongaji, mwanamke mmoja wa makamo akaingia ndani ya ofisi hiyo huku akiwa amevalia koti refu jeupe, shingoni alining’iniza mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo, alipoingia ndani ya ofisi hiyo, akasalimia na kisha kumpa ripoti ile Dk. Terry ambaye akaanza kuiangalia.

“Mmh!” aliguna Dk. Terry.

“Kuna nini?” aliuliza ofisa mmoja.

“Ripoti inaonyesha kwamba alichomwa sindano iliyokuwa na Declophine, hii ni dawa ya kusimamisha mapigo ya moyo kwa muda,” alisema daktari huyo, maofisa wale wakajiweka vizuri vitini.

“Declophine! Ina maana alichomwa?”

“Hatuna uhakika, inawezekana alijichoma pia, hatuwezi kufahamu hilo,” alijibu daktari huyo.

“Kuna kingine?”

“Ndiyo! Sasa hapa nimepata uhakika kwamba alichomwa kwa sababu ripoti inaonyesha kwamba puani alipuliziwa dawa kali ya usingizi,” alisema daktari huyo.

“Na nani?”

“Hilo hatufahamu! Limetokea huko hotelini!’

“Kwa hiyo kulikuwa na mtu alitaka kumuua?”

“Sijajua! Mpaka hapa ripoti inashangaza! Hivi kweli mtu ambaye alitaka kumuua angeweza kumchoma sindano yenye Declophine?” aliuliza daktari huyo.

Hakukuwa na mtu aliyejibu swali hilo, kila mmoja alikuwa kimya. Swali alilouliza Dk. Terry lilikuwa kweli kabisa, kama kulikuwa na mtu aliyekuwa ameingia ndani ya chumba hicho kwa ajili ya kumuua, asingeweza kumchoma sindano iliyokuwa na Declophine, kama kweli alidhamiria kuua, basi angemuua kwa kumchoma sindano yenye sumu kali.

“Kwa nini huyo mtu alifanya hivi?” aliuliza ofisa mmoja.

“Hatujui!”

“Au Carter mwenye alitaka kutengeneza jina zaidi?”

“Nalo hatujui!”

“Ni lazima tufanye naye mahojiano, nadhani kuna jambo kubwa limejificha nyuma ya pazia,” alisema ofisa huyo, hawakutaka kubaki ofisini humo, wakaondoka zao kurudi makao makuu huku wakiwa na kopi ya ripoti hiyo.

“Hapana! Haiwezi kuwa hivi!” alisema mkuu wa upelelezi kitengo cha FBI.

“Hiyo ndiyo ripoti tuliyopewa!”

“Yaani mtu atokee tu na kumchoma sindano yenye Declophine, hivi inawezekana kweli? Ausimamishe moyo ili iweje? Kama angetaka kumuua si angemuua tu!” alisema mkuu huyo.

Ripoti hiyo ikaanzisha maswali mengi vichwani mwa FBI hao, kila mmoja alijiuliza sababu ya mvamizi kutumia sindano yenye Declophine lakini wakakosa jibu kabisa.

Walijua kwamba inawezekana mvamizi huyo alikuwa akimfuatilia Carter tangu kitambo lakini swali kubwa lilikuwa ni sababu gani ilimfanya kutumia Declophine kuusimamisha moyo wake na wakati alikuwa na uwezo mkubwa wa kumuua?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hapo ndipo wakapata jibu kwamba wamfuate Carter hospitali na kuzungumza naye, awahadithie ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka kuchomwa sindano iliyokuwa na Declophine.

FBI hao hawakutaka kuchelewa, harakaharaka wakaondoka na kwenda hospitalini huko, walipofika, kwa kuwa tayari Carter alikuwa akijisikia nafuu, wakaruhusiwa kwenda kuzungumza nao, Carter alipowaona tu, akashtuka.

“Unaweza kutuambia nini kilitokea ndani ya chumba kile cha hotelini?” aliuliza ofisa mmoja mara baada ya salamu, muda huo, macho yake yalikuwa usoni mwa Carter tu.

“Naweza!”

“Nini kilitokea?” aliuliza ofisa huyo na Carter kuanza kuelezea kila kitu kilichotokea siku hiyo, mpaka aliporudi hotelini, alipolala na kisha kushtukia akiwa ameshikwa na mtu na kuanza kuvutishwa madawa ya usingizi, baada ya hapo, hakujua kitu gani kiliendelea kwani alipofumbua macho, alijikuta akiwa hospitalini.

****

Carter akaanza kuhadithia kila kitu kilichotokea hotelini katika usiku ambao alimaliza shoo yake na kurudi huko. Hakutaka kuficha, yeye mwenye alibaki akishangaa mara baada ya watu kumwambia kwamba alikufa, alikufa vipi na wakati alipewa tu madawa ya uzsingizi?

Wakati akisimulia hivyo, maofisa wa FBI walikuwa kimya wakimsikiliza, simulizi yake ilisema kwamba alivamiwa chumbani na mtu ambaye alikuwa na uhakika alikuwa ndani ya chumba hicho, baada ya kumvamia kitandani, akamkamata vilivyo na kumnusisha kitambaa kilichokuwa na madawa, baada ya hapo, hakujua nini kiliendelea zaidi ya kujikuta akiwa hospitali.

“Kwa hiyo hukumuona kabisa huyo mtu?” aliuliza ofisa mmoja wa FBI.

“Kwa kweli sijamuona.”

“Kuna nini kilitokea kabla, kuna ugomvi wowote, labda na mtu yeyote unayemuhisi?” aliuliza ofisa huyo.

“Hapana! Sina ugomvi na mtu yeyote yule, nina urafiki mkubwa na kila mtu, sijui kama kuna mtu niligombana naye, kilichotokea, inawezekana ikawa wivu tu wa watu wengine,” alijibu Carter.

Huo ndiyo ulikuwa ukweli, Carter alikuwa mtu wa watu, alipendwa na kila mtu, hakuwa mgomvi, watu wengi walimheshimu kwa kuwa hakuwa mbaguzi kama watu wengine.

Kila kona jina lake lilisikika na ndiyo maana hata taarifa za kifo zake zilipoanza kusikika kila kona, kila mtu alikuwa na huzuni tele. Aliendelea kubaki hospitalini hapo, hakuwa mzima kiafya na alitakiwa kusubiri kwa siku tano na ndipo arudi nyumbani.

Watu waliendelea kumiminika hospitalini hapo, wengine walileta maua, kadi na vitu vingine huku wakimpa pole kwa kila kitu kilichotokea.Mpenzi wake, kila siku ilikuwa ni lazima afike hospitalini hapo, alimpenda sana carter na hakuwa tayari akimuona akipitia katika kipindi kigumu peke yake, alimpenda na kumthamini zaidi ya mtu yeyote yule.



Bwana Seppy alituli chumbani kwake, alionekana kukasirika mno, mchezo aliofanyiwa na Benjamin ulimfanya kujona hana akili, kuwaona vijana wake hawakuwa siriazi kwa kazi kubwa aliyokuwa amewapa.

Alichotaka kuona ni Carter anakufa, tena hapohapo hospitalini kwani kama angeendelea kubaki hai ilimaanisha kuwa kuna siku angekuja kugundulika kwani huyo Carter angesema kilichotokea na hatimaye kufungwa pingu na kupelekwa jela.

“Ni lazima auawe hapohapo kitandani,” alijisemea.

Tayari aliwaambia vijana wake kwamba kitu hicho kilitakiw akufanywa haraka iwezekanavyo, ila alitaka kuwasisitizia kwamba kifo cha Carter kilikuwa muhimu sana kwa wakati huo kuliko kitu chochote kile. Hata alipowapigia simu, aliwasisitizia kwamba jambo hilo lilitakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo, hata kama lingehitaji kiasi kikubwa cha fedha, bado lilitakiwa kufanyika.

Vijana hao, watatu wakajiandaa, iliwapasa waingie ndani ya hospitali hiyo na kujifanya madaktari, wajifanye wanakwenda katika chumba alicholazwa Carter na hatimaye kumuua, hivyo ndivyo walivyotakiwa kufanya.

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kununua makoti makubwa ya kidaktari, mashine za kupimia mapigo ya moyo na mafaili ambayo yangewafanya kuonekana kama madaktari na kuingia ndani ya chumba hicho kirahisi.

Wakafanikiwa kupata vitu vyote na hivyo kufanya kile walichotaka kukifanya. Kabla ya kwenda hospitalini huko kutekeleza kile walichotaka kukifanya, kwanza wakampigia simu Bwana Seppy.

“Ndiyo tunakwenda kiongozi, kuna lolote?” aliuliza kijana mmoja, huyu alijiita Dracula, kijana mwenye roho mbaya, mwanaume mwenye kuua watu kama alivyoua panzi.

“Kwa sababu huyu Benjamin alijifanya mjanja, sasa inabidi mkimuua muhakikishe mnaacha alama za vidole vyake, mmenielewa?” alisema na kuuliza.

“Ndiyo mkuu!”

Suala la kupata alama za vidole vya Benjamin wala halikuwa tatizo, walikuwa nazo katika kinailoni kidogo. Walizichukua alama hizo kipindi kile walipomkabidhi mpenzi wake kwake, walimpa simu aina ya iPhone 7, alipoishika, alama za vidole vyake zilibaki katika kioo cha simu.

Hawakukigusa kioo hicho, waliishika simu kwa tahadhali kubwa, walipofika katika chumba ha wataalamu wao, zile alama zikaanza kutolewa kifundi na mwisho wa siku kufanikiwa, wakawa nazo na hivyo kuziweka kwenye nailoni, yaani hapo popote pale ambapo wangefanya kitu chochote, wangeweka kile kinailoni katika sehemu yoyote, alama za mikono za Benjamin zingeonekana.

“Fanyeni hivyo, ni lazima dunia ijue kwamba yeye ndiye aliyehusika,” alisisitiza Bwana Seppy.

“Sawa mkuu!”

“Na kingine msisahau kuacha fedha, hiyo ni kwa ajili ya kuwachanganya FBI,” alisema mzee huyo.

“Sawa mkuu!”

Hicho ndicho kilichotakiwa kufanywa. Kinailoni ambacho kilikuwa na alama za vidole vya Benjamin (Fingerprints). Walipoanza kuingia ndani ya hospitali hiyo, wakajigawa, isingekuwa rahisi kufikiri kwamba watu hao hawakuwa madaktari kwani mavazi yao, muonekano ulionyesha kabisa kwamba walikuwa madaktari.

Waliwekeana muda kwamba ndani ya hospitali hiyo kubwa wangetumia dakika ishirini na kisha kuonana nje, wangeingia ndani ya gari lao na kisha kuondoka pasipo kugundulika, wakaelewana.

Muda ulikuwa ni saa moja usiku, muda ambao si watu wengi waliokuwa hospitalini hapo. Ndugu wa Carter walikuwepo mahali hapo, si ndugu bali hata polisi nao walikuwepo kuhakikisha ulinzi unafanyika, asiingie mtu yeyote ambaye si mhusika.

Wakati Dracula anapiga hatuia kuelekea katika chumba kile, hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule, hata ndugu zake Carter walipomuona akisogea kule walipokuwa, hawakuwa na hofu hata kidogo, walijua kwamba naye huyo alikuwa daktari kwani hospitali kubwa kama hiyo, ilikuwa na madaktari wengi mno.

“Poleni sana jamani...” alisema Dracula hata kabla ya kuingia ndani ya chumba hicho. Kwa kumwangalia tu, usingejua kama alikuwa muuaji, na kama ungeambiwa umpe kazi, harakaharaka ungempa uchungaji au upadri, alijiweka katika sura ya kipole mno.

“Asante sana...”

Hakutaka kubaki hapo nje, kila mtu aliyemwangalia, alikiri kwamba hospitali hiyo ilikuwa na daktari aliyekuwa na huruma kuliko madaktari wote duniani. Kabla ya kuingia ndani ya chumba kile, akaonyesha alama ya msalaba kama wanayofanya Waroma, yaani kwenye paji, kifuani na mabegani.

Alipofanya hivyo tu, watu wote wakajawa na tabasamu pana, mbali na kuwa daktari, wakagundua kwamba Dracula aliyekuwa na kichuma kilichoandikwa Dr. Kevin kifuani alikuwa mtumishi wa Mungu, hivyo walikuwa na uhakika kwamba mambo yangekwenda salama.

“Unajisikiaje Carter?” aliuliza Dracula mara baada ya kuingia ndani ya chumba hicho, Carter alikuwa kitandani akisubiri muda wa kuona wagonjwa ufike ili ndugu zake waingie.

“Najisikia vizuri kidogo...”

“Sawa! Ngoja nipime mapigo ya moyo,” alisema Dracula na hapohapo akatoa mashine ya kupimia mapigo ya moyo, stethoscope na kuanza kumpima.

“Mapigo ya moyo yapo vizuri kidogo,” alisema Dracula na kumwambia Carter ageuke, mgongo uwe juu.

Carter hakubisha, alimwamini Dracula na kuona kwamba alikuwa daktari wa ukweli hivyo akageuka. Hilo lilikuwa kosa kubwa sana kulifanya, hapohapo Dracula akaanza kumkaba Carter palepale kitandani.

Carter alijitahidi kuitoa mikono ya Dracula, akashindwa, alijitahidi kupita kelele, sauti haikutoka kabisa. Alihangaika na kuhangaika lakini hakufanikiwa hata kidogo.

Dakika moja nzima bado Dracula alimkaba mahali pale vilivyo. Nguvu zikaanza kumuisha Carter, akachoka na hapohapo pumzi ikaanza kukata, mbele yake akaona giza, hazikupita sekunde nyingi, akafa hapohapo kitandani.

Dracula hakutaka kuchelewa, akachukua kile kinailoni, akakiweka shingoni mwa Carter, akakikandamiza vilivyo na alama zile kubaki shingoni mwa Carter, alipomaliza, hakutaka kubaki, akatoka nje ya chumba kile, akawaambia ndugu zake Carter kwamba mgonjwa wao aliendelea vizuri hivyo wasubiri, wote wakamshukuru Mungu, Dracula akaondoka zake huku akiwa amekwishakamilisha kazi yake.

“It’s done,” (Kazi imefanyika) alimwandikia ujumbe mfupi Bwana Seppy ambapo alipoisoma, tabasamu pana likajaa usoni mwake.

****http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Kila mtu alikuwa na uhakika kwamba Carter alikuwa amepona na hivyo alitakiwa kurudi nyumbani. Watu walimkumbuka, kazi zake alizokuwa akizifanya zilimfurahisha kila mmoja na hivyo kutamani kuona mwanamuziki huyo akirudi tena nyumbani na kuendelea kuwabuirudisha.

Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba kulikuwa na kitu kimetokea ndani ya chumba alicholazwa Carter, hata madaktari na manesi wa hospitali hiyo hawakuwa wakijua chochote kile.

Baada ya dakika kadhaa tangu Dracula aondoke ndani ya chumba kile na kufanya mauaji, Dk. Rafael akatokea na kwenda ndani ya chumba kile, kama kawaida aliwakuta ndugu zake Carter wakiwa nje, nyuso zao tu zilionyesha furaha tele, mioyo yao ikajazwa na nguvu.

Dk. Rafael akawasalimia na kisha kuingia humo ndani, kwanza jinsi alivyomkuta Carter kitandani pale, akashikwa na wasiwawasi kwa kuhisi kulikuwa na kitu kimetokea, akasoegea na kumwangalia vizuri, hakuwa akipumua, macho yalimtoka na muonekano wake tu ulionyesha kwamba alikuwa amekufa.

Akajaribu kuvipeleka vidole vyake karibu na pua ya Carter, hakuwa akipumua, hakuridhika, akachukua mashine yake na kusikiliza mapigo ya moyo ya stethoscope na kuanza kuyasikiliza mapigo ya moyo wa Carter, hayakuwa yakidunda.

“Mungu wangu!”

Hakutaka kubaki chumbani humo, alichokifanya ni kutoka huku akikimbia, ndugu waliokuwa nje walipomuona, wakashangaa, hawakujua sababu ya daktari yule kukimbia hivyo.

Kule alipokwenda, karudi na madaktari wawili ambao wakaingia ndani ya chumba kile, walichoambiwa ndicho walichokutana nacho ndani, Carter alikuwa kimya kitandani, wakampima kila kipimo lakini hakushtuka, dalili zote zilionyesha kwamba alikufa.

“Nani amefanya hivi?” aliuliza Dk. Michael.

Madaktari waliulizana lakini hakukuwa na mtu mwenye jibu, walichanganyikiwa, hawakujua kama kulikuwa na mtu mwingine alikuwa ameingia ndani ya chumba kile au la.

Mbali na mwili ule, pembeni kulikuwa na fedha za nchi tofauti, yaani dola ya nchini Marekani, paundi ya Uingereza, Euro ya Ulaya na Yeni ya China. Hawakujua kwa nini fedha zile zilikuwa mahali pale.

Walichokifanya ni kutoka nje na kuwauliza ndugu wale ni nani alikuwa ameingia ndani ya chumba kile, ndugu wale wakasema kwamba kulikuwa na daktari mmoja aliyekuwa ameingia kabla.

“Yupi?”

“Ni daktari mmoja, mrefu, ana shingo ndefu, ana sura ya kipole sana,” alijibu ndugu mmoja.

Jinsi walivyomzungumzia huyo daktari, hakukuwa na daktari aliyekuwa na sifa hizo hivyo wakajua kwamba kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa ameingia. Hawakutaka kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea ndani bali wakawasiliana na polisi, baada ya dakika kadhaa, polisi wakafika hospitalini hapo.

Kitu cha kwanza kabisa, hawakutaka mwili uguswe kwa ajili ya kutokupoteza alama za vidole kama zipo, madaktari walilifahamu hilo na tangu walipohisi kwamba alikuwa ameuawa, hawakuugusa mwili huo.

Walipoona kwamba mwili haujaguswa, hawakutaka kuchelewa, wakaharakaiisha vipimo vichukuliwe harakaharaka na kama kuna alama za vidole viangaliwe ni vya nani ili muuaji huyo atafutwe haraka iwezekanavyo.

Kilichowashangaza polisi ni kwamba walikuta fedha kitandani, hawakujua zilikuwa na maana gani lakini walipokumbuka, hata siku ambayo Carter alisadikiwa kuwa aliuawa kwa kuchomwa na sindano, pia palepale kitandani kulikuwa na fedha, hilo likawapa maswali, je kulikuwa na mtu aliyekuwa akifanya hivyo?

“Hivi mmejiuliza kuhusu hizi fedha?” aliuliza polisi mmoja.

“kivipi?” akauliza mwingine.

“Siku ile taarifa ziliposema kwamba Carter alijidunga sindano, pembeni kulikuwa na fedha kama hizi, leo ameuawa, pia kuna fedha, hamuhisi kitu chochote hapa?” aliuliza polisi huyo.

“Mmh!” Polisi wengine wakaishia kuguna tu.

Kama Carter kuuawa, aliuawa, mtu wa kwanza kabisa aliyeshukiwa ni mlinzi ambaye aliwekwa mahali hapo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kila kitu kinakuwa sawa, akachukuliwa na kupelekwa kituoni kwa mahojiano maalumu.

Ndugu zake waliokuwa nje, wakaambiwa kweli kile kilichotokea, kwanza hawakuamini, inakuwaje ndugu yao auawe na wakati muda wote wao walikuwa nje ya chumba kile na hakukuwa na adui yeyote aliyeingia zaidi ya madaktari tu?

“Mmoja wa watu walioingia hawakuwa madaktari, alikuwa muuaji,” hilo ndilo jibu alilolitoa daktari hivyo kuibua vilio mahali hapo.

Taarifa zilitolewa kwamba mwanamuziki Carter alikuwa ameuawa ndani ya chumba cha hospitali, kwanza watu hawakuamini, walihisi kwamba taarifa hizo zilikuwa ni uongo kwani kipindi cha nyuma, taarifa zilitoka hivyohivyo kwamba alikuwa amejichoma sindano na kujiovadozi madawa ya kulevya.

Katika kuuchunguza mwili ule wakagundua kwamba muuaji wa mauaji hayo hakuwa amevaa glavu kitu kilichoifanya alama za vidole vyake kubaki shingoni mwa mwili wa Carter.

Walichokifanya madaktari ni kuwasiliana na polisi ambao wakafika mahali hapo na kuchukua alama zile na kurudi nazo ndani ya kituo chao. Huko, kwa msaada wa mashine walizokuwa nazo, wakaziscan alama zile na kisha kuziingiza katika kompyuta zao, kilichoendelea ni kuanza kutafuta Marekani nzima juu ya mtu aliyehusika katika mauaji yale.

Picha zilipita nyinginyingi na tena kwa haraka mno, zilikwenda na kwenda, kama dakika kumi na tano hivi na ndipo picha moja ikasimama huku neno 100% MATCH likionekana kuonyesha kwamba picha ya mtu aliekuwa akionekana na alama alizoziweka wakati akisajiri kitambulisho cha taifa, alama zile alizokuwa nazo ndizo zilizoonekana katika mwili wa Carter.

“Anaitwa nani huyo?” aliuliza ofisa wa FBI.

“Benjamin Saunders.”

“Yupo wapi?”

“Cambridge, Boston ni mwanachuo wa Chuo Kikuu cha Harvard,” alijibu ofisa mmoja.

“Ni lazima twende huko, ni lazima huyu muuaji apatikane. Wasiliana na polisi wa Cambridge, inawezekana hayupo huko ila ni lazima tuweke mitego, mbali na hivyo, pelekeni picha zake kila kona, kwenye vituo vya habari na sehemu nyingine. Gideon, hakikisha mtu huyu anapatikana,” alisema mkuu wa FBI, Bwana Solomon Kane, hivyo picha zake kuanza kutumwa sehemu tofautitofauti, kila mtu akajua kwamba Benjamin ndiye aliyemuua Carter.





Watu walilia na kuhuzunika, taarifa zilizokuwa zimesambaa kwamba muimbaji mkali wa miondoko ya Pop, Carter aliuawa ndani ya chumba cha hospitalini ilimshtua kila mtu.

Wengi walijiuliza maswali kwamba ilikuwaje muuaji kuingia ndani ya chumba hicho na kumuua Carter huku kukiwa na ulinzi ulioimarishwa ndani ya hospitali hiyo? Kila mtu aliyejiuliza, alikosa jibu ila ripoti ambayo ilitoka hospitali ilisema kwamba muuaji aliingia ndani ya chumba hicho baada ya kujifanya daktari.

Maofisa wa FBI walichokitaka ni kuangalia kwenye kamera za CCTV ambazo walizifunga humo ndani, walitaka kumuona mtu aliyeingia alikuwa nani. Wakaenda katika chumba kilichokuwa na televisheni na kuhitaji kuona hizo video ambazo zilipigwa, wakawekewa, walifanikiwa kumuona muuaji, sura yake ilikuwa ngeni na haikuonekana vizuri kutokana na udogo wa upigaji picha wa kamera hizo hivyo kila mtu akaamini kwamba yeye ndiye huyo Benjamin, kwani walifanana ngozi, wote walikuwa weusi.

Picha za Benjamin zikaanza kuwekwa mitaani, kila mtu aliyemuona, hakuamini, alikuwa kijana mzuri, mdogo lakini kitu kilichowashangaza watu kwa nini alifanya mauaji, tena kwa mtu waliyekuwa wakimpenda mno?

Benjamin alitakiwa kutafutwa kila kona, hakutakiwa kuachwa kwani yeye ndiye aliyefanya mauaji kwa mtu aliyekuwa kipenzi cha watu. Mitaani, picha zake zikasambazwa, si kwenye vituo vikubwa vya kwenye mabasi bali hata kwenye vituo vya treni, kote huko picha za sura yake zikabandikwa.

FBI walitaka kuionyeshea dunia kwamba walikuwa siriazi katika kila wakifanyacho, hivyo wakatengeneza ‘apprication’ maalumu na kuziweka katika simu zote za Android na iPhone, apprication hiyo ilikuwa ni kuwahamasisha watu kumtafuta huyo Benjamin ambaye kwa kipindi hicho alipata umaarufu mkubwa hata zaidi ya rais.

Baada ya wiki, hatimaye watu wakakusanyika nyumbani kwa Carter, kila mmoja alikuwa akilia, walihuzunika lakini hakukuwa na kitu kilichomrudisha hai mwanamuziki huyo, ukweli ulibaki palepale kwamba aliuawa na asingeweza kurudi tena.

Mpenzi wake na ndugu zake, kila mmoja alionekana kuwa na huzuni mno, kama kulia mpaka kuzimia, hiyo ilitokea mara nyingi sana lakini bado ukweli wa kifo chake ukaendelea kubaki palepale.

Siku mbili baadaye, ndugu, marafiki na watu wengine wachache wakakusanyika katika makaburi ya First Calvary Cementary yaliyokuwa katika mji wa Brooklyn jijini New York nchini Marekani. Hapo, mchungaji aliyeandaliwa kwa ajili ya ibada ndogo akaanza kutoa maneno ya mwisho na hatimaye mwili wa Carter kuzikwa, huo ukawa mwisho, yule mwanamuziki mdogo, mwenye umaarufu mkubwa akawa amezikwa huku akiwa na ndoto nyingi kichwani mwake.

Siku iliyofuata, magazeti yote nchini Marekani na nchi nyingine zilitoa taarifa juu ya kifo cha mwanamuziki huyo, watu hawakuwa wakiamini, walihisi kwamba angeweza kurudi tena kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Tasnia ya muziki Marekani ikapata pengo, hakukuwa na msanii ambaye alikuwa na jina kubwa ambaye aliupaisha muziki wa Pop kama alivyofanya Carter, leo hii, Carter huyohuyo akaondoka na muziki wake, tuzo zake alizochukua katika mashindano mengi zikabaki kama mapambo ndani ya nyumba yake.

“Huyu Benjamin ni lazima apatikane, kuna taarifa yoyote?” aliuliza Bwana Kane.

“Bado ila taarifa zinasema kama alionekana chuoni, bado tunaendelea kufuatilia mkuu!” alisema ofisa mmoja wa FBI.

****

Ilikuwa ni lazima Benjamin aondoke kuelekea Boston kuendelea na masomo yake, hakutaka kubaki New York kwa kuamini kwamba watu wale waliokuwa wamemteka wangeweza kumrudia tena.

Mara ya kwanza alimwambia mpenzi wake, Vivian waondoke na kuelekea Los Angeles lakini huko hakukuonekana kuwa na usalama wa maisha yao, hivyo ilikuwa ni lazima arudi Boston ambapo angechukua apartment sehemu fulani na kisha kuendelea na maisha yake na si kukaa chuo kama alivyokuwa akifanya.

Kutoka New York mpaka Boston ilikuwa ni mwendo wa saa tano kwa treni ya umeme, hiyo ilimaanisha kwamba kama wanaondoka muda huo ambao ulikuwa ni saa tatu asubuhi basi wangeweza kufika Boston majira ya saa saba.

Wakaingia ndani ya treni, macho yao hayakutulia, kila wakati walikuwa wakiangalia huku na kule. Waliogopa, hawakutaka kumuamini mtu yeyote kwa kipindi hicho, kila aliyeonekana mbele yao, walimuona kama muuaji ambaye walikuwa na uhakika kwamba wangetafutwa sana mara baada ya kugundua kwamba Benjamin hakuwa amefanya kile alichokuwa ameambiwa akifanye.

Baada ya saa nne, wakaingia Boston, ilionekana kuwa furaha kwao, kidogo kwa Benjamin akaonekana kujiamini kwa kuhisi kwamba asingeweza kuonekana kwani wauaji hao wasingediriki kusafiri kutokana New York mpaka Boston kumtafuta yeye tu.

Baada ya siku mbili, masomo yakaanza kama kawaida, hakumwambia Vivian arudi jijini Los Angeles kwa kuhisi kwamba kama angekuwa mbali naye basi binti huyo angeweza kuuawa, alichomwambia ni kwamba aishi naye hapo Boston huku akifanya mipango ya kumtoa hapo na kumpeleka Atalanta walipokuwa wazazi wake.

“Hautakiwi kuwa na hofu yoyote ile, wewe kaa hapa, baada ya miezi kadhaa, itakubidi uende Atalanta, huko, nitakupangia apartment,” alisema Benjamin hivyo kukubaliana na Vivian.

Siku tatu baada ya kufika Boston, wakiwa chumbani wamekaa ndipo wakapigwa na mshtuko mara baada ya kuona taarifa ya habari katika Kituo cha CNN ikisema kwamba mwanamuziki aliyekuwa na jina kubwa, Carter alikuwa ameuawa ndani ya chumba alichokuwa amelazwa.

Wakashtuka, hawakuamini walichokuwa wakikiangalia, Benjamin akatulia na kuiangalia taarifa ya habari ile kwa umakini, aliangalia picha, kweli alikuwa Carter na taarifa za awali zilisema kwamba aliuawa baada ya kukabwa kitandani tena huku pembeni kukikutwa fedha za za mataifa mbalimbali.

“Wamemuua Carter,” alisema Benjamin huku akionekana kushtuka.

“Mungu wangu!” alisema Vivian huku akionekana kuumia moyoni mwake.

Benjamin akachukua simu yake na kuanza kumpigia rafiki yake David, akamuelekeza kila kitu alichokifanya hivyo kutaka afanye kila liwezekanalo kuhakikisha ile namba aliyokuwa amempa ilikuwa ikipatikana wapi.

“Ila Vivian si umempata?” aliuliza David.

“Ndiyo! Ila nataka nijue ni nani anahusika katika mauaji haya, David, tafadhali naomba unisaidie,” alisema Benjamin.

“Usijali, nipe muda,” alisema David na kisha kukata simu.

Hiyo ilikuwa ni taarifa ya majonzi waliyokuwa wameipata, hawakuamini kama kweli watu hao baada ya kugundua kwamba Carter hakuwa ameuawa basi wangemtafuta mpaka wampate na kumuua, hakujua tatizo lilikuwa nini ila kitu alichohisi ni kwamba kulikuwa na siri kubwa sana nyuma ya pazia.

Baada ya kukaa kwa huzuni usiku huyo, asubuhi ikaja taarifa nyingine, hii ilikuwa ni juu ya muuaji aliyekuwa amemuua Carter. Benjamin na Vivian wakabaki wakiangalia, hawakuamini walichokuwa wakikiona kwamba Benjamin ndiye aliyemuua Carter tena huku alama za vidole vyake zikiwa zimeonekana katika shingo ya Carter, picha zake zilionyeshwa kwenye kila televisheni, alipoziona, hakuamini, akapiga magoti na kuanza kulia.

“Sikuua, sikuua,” alisema Benjamin, alikuwa akimwambia mpenzi wake huku akilia kwa uchungu.

“Ngo ngo ngo...” mlango ulisikika ukigongwa, kila mtu akaogopa kwa kuhisi kwamba aliyekuwa akigoga mlango alikuwa polisi.

****

Maofisa wa FBI wakafika katika Chuo cha Harvard kilichokuwa Cambridge jijini Boston kwa ajili ya kumkamata Benjamin ambaye alihusika katika mauaji ya Carter. Walivalia suti nyeusi, miwani myeusi, kwa kuwaangalia tu ilikuwa rahisi kugundua kwamba watu hao walikuwa maofisa wa FBI kwani hata masikioni mwao walikuwa na vispika ambavyo viliunganishwa moja kwa moja mpaka kwenye maiki zilizokuwa mdomoni.

Wakaelekea mpaka katika ofisi ya mkuu wa chuo ambapo baada ya kufika huko, wakamwambia kitu walichokifuata kwa kuamini kwamba taarifa kuhusu muuaji, Benjamin zilikuwa zikijulikana kila kona.

“Alikuwa hapa...” alijibu mkuu wa chuo.

“Bado yupo au?”

“Hapana! Aliondoka!”

“Kwenda wapi?”

“Anapoishi! Hakuna anapopajua kwani tangu arudi kila kitu amekuwa akikifanya kwa siri sana, hayupo kama zamani, nahisi kuna kitu kinaendelea,” alisema mkuu wa chuo.

“Una namba yake ya simu?”

“Ndiyo! Niliichukua kwa ajili ya kuzungumza naye juu ya kilichokuwa kikiendelea kwani alibadilika, alionekana kuwa na mawazo kitu ambacho hakuwa nacho kabla, ila bahati mbaya sikuweza kuwasiliana naye,” alisema mkuu wa chuo na hivyo kuwapa namba yake ya simu.

Hawakutaka kuendelea kubaki hapo ndani, walichokifanya ni kuondoka na kuelekea ndani ya gari lao. Ilikuwa ni lazima waitraki simu yake, wajue mahali alipokuwa hivyo kuchukua laptop yao na kuiunganisha na simu zao kisha kuanza kumpigia.

Kitendo cha simu kuita tu, ilionekana kuwa kosa kwani tayari kompyuta yao ikaanza kusoma, ikaanza kuwapa maelekezo juu ya mahali alipokuwa Benjamin kwa kipindi hicho. Waliangalia vizuri, hakuwa mbali na mahali hapo alipokuwa, hivyo wakaanza safari ya kuelekea huko, GPS ilionyesha kwamba alikuwa katika chumba kimoja kilichokuwa katika apatimenti za St. Monica ambazo hazikuwa mbali kutoka hapo chuoni.

“Tumfuateni,” alisema ofisa mmoja, wakaingia ndani ya gari na kuanza kuelekea huko.

****

Kila mmoja ndani ya chumba kile alionekana kuwa na wasiwasi mkubwa, kitendo cha kugongwa hodi ndani ya chumba kile kila mmoja akahisi kwamba walikuwa ni polisi.

Kitu cha kwanza kabisa alichokifanya Benjamin ni kuanza kutafuta sehemu ya kujificha, hakutaka kuchelewa, ilikuwa ni lazima afanye haraka kwani pasipo kufanya hivyo ilikuwa ni lazima kukamatwa.

Akachukua simu yake iliyokuwa mezani, akaona kulikuwa na mtu aliyekuwa akimpigia, namba ilikuwa ngeni, hakujali, alichokifanya ni kuanza kuangalia sehemu nzuri ya kujificha, hata kama ingekuwa kuruka dirisha na kutokea upande wa pili, ilikuwa sawa ingawa chumba hicho kilikuwa katika ghorofa ya tatu.

“Who is it?” (Nani?) aliuliza Vivian.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Me!” (Mimi!)

“You got no name buddy?” (Huna jina mshikaji?)

“Marie...”

“Who is Marie?” (Marie ndiye nani?)

Maswali yote hayo alikuwa akiuliza Vivian, mtu huyo bado aliendelea kupiga hodi ili mlango ufunguliwe. Hakukuwa na aliyekuwa radhi kuufungua mlango huo, kitu ambacho kilikuja moja kwa moja vichwani mwao ni kutoroka ndani ya chumba hicho, hivyo wakafanya hivyo.

Wakaufungua mlango wa nyuma ambapo kulikuwa na sehemu kubwa ya kupumzikia, walichokifanya ni kuanza kutembea pembezoni mwa ghorofa hilo kwa kwenda upande wa chumba kingine ambapo pembeni yake kulikuwa na bomba refu la choo lililoelekea mpaka chini.

“Ni lazima tuteremke kwa kutumia bomba lile,” Benjamin alimwambia Vivian.

“Nitaweza?”

“Utaweza tu, hatuna jinsi, mtu anayegonga mlango hatumfahamu, inawezekana akawa mmoja wa wale wauaji,” alisema Benjamin, tayari walilifikia bomba lile na hatimaye kuanza kuteremka nalo chini.

Ilikuwa ni lazima kuondoka mahali hapo, hawakutakiwa kumuamini mtuu yeyote yule. Hawakuwa wakiiogopa serikali ila watu waliokuwa wakiwaogopa zaidi walikuwa hao wauaji na ilikuwa ni lazima kuwakimbia.

Walipotua chini tu, hawakutaka kukimbia kwani kwa mbali waliliona gari moja likiingia mahali hapo hivyo kujificha. Gari liliposimama, wanaume wawili waliovalia suti nyeusi wakateremka.

Benjamin aliwajua, mavazi mengi hayo huvaliwa na maofisa wa FBI, hivyo akamwambia Vivian wajifiche zaidi kwani watu waliokuwa wamefika hawakuwa watu salama kwao, walikuwa FBI.

Walibaki wakiwaangalia mpaka walipokwenda ndani, walijuaje kama walikuwa humo na wakati hawakuwa wamemwambia mwanachuo yeyote yule? Wakajua kwamba watu hao walitraki simu yake, hivyo alitakiwa kuiacha hapohapo.

Huo ndiyo ulikuwa umamuzi waliochukua, hawakutaka kwenda na simu ile sehemu yoyote kwa kuona kama wangekamatwa, hivyo Benjamin akaiacha hapohapo walipokuwa wamejificha huku akifuta meseji zote, simu zilizotoka na kuingia, akazikariri namba zile za wauaji na kisha kuondoka huku akiwa na laini.

****

Bwana Seppy alizidi kuchanganyikiwa, hakuamini kama kweli vijana wake walishindwa kabisa kumpata Benjamin japokuwa walikuwa wametega mitego mbalimbali kumnasa.

Alichanganyikiwa kwa sababu kumuacha mtu huyo akiwa hai lilikuwa kosa kubwa, inawezekana likawa kubwa kuliko makosa yote aliyowahi kuyafanya tangu azaliwe.

Aliwaagiza vijana wake waendelee kumtafuta Benjamin lakini kila siku majibu yalikuwa yaleyale kwamba hakupatikana, ilikuwaje wasimpate na wakati walijua hakuwa mjanja, atakuwa amejificha wapi kwani nchi nzima ilikuwa ikimtafuta yeye.

“Hakikisheni mnampta kabla ya FBI kumpata,” aliagiza Bwana Seppy.

“Sawa mkuu!” alisikika Dracula.

Bado kazi ilikuwa kubwa, Marekani ilikuwa kubwa sana na hawakujua ni mahali gani walitakiwa kwenda. Kwa sababu fedha ilikuwepo, walichokifanya ni kuwapa kazi vijana wengi wamtafute Benjamin na kumpata kisha wangepewa malipo makubwa ya fedha, vijana hao kutoka sehemu mbalimbali wakaingia kazini na kuanza kumtafuta.

Zoezi hilo lilidumu kwa kipindi cha wiki nzima, hakuwa amepatikana wala kusikia tetesi kwamba likuwa sehemu fulani, hiyo iliwachanganya sana na hivyo Bwana Seppy kuamua kujiongeza kwamba kulikuwa na kitu kilitakiwa kufanyika.

“Naamini kwamba kuna watu wanawasiliana na Benjamin,” alimwambia Dracula aliyekuwa na vijana wenzake.

“Kivipi? Kwenye simu hapatikani kabisa!”

“Najua ila naamini kuna sehemu yupo, anawasiliana na ndugu zake bila hofu! Sasa naagiza kwamba ninamhitaji kijana yeyote anayejua sana kimpyuta aletwe mbele yangu, kuna kazi nataka kufanya naye,” alisema Bwana Seppy, hayo yalikuwa maagizo hiyo yalitakiwa kufanyika haraka iwezekanavyo.

Baada ya saa tatu Dracula akarudi mahali hapo huku akiwa na kijana mmoja mtanashati, alivaa kwa kuchomekea shati lake, uso wake ulikuwa na miwani, kwa kumwangalia tu ungegundua kwamba kijana huyo alikuwa na uwezo mkubwa sana kichwani mwake.

“Huyu ni Cosmas, mmoja wa vijana wenye ujuzi sana katika masuala ya kompyuta,” alisema Dracula.

“Sawa! Mlete ndani!”

Muda wote Cosmas alionekana kuwa na hofu moyoni mwake, hakuamini kama sehemu aliyokuwepo mahali hapo ilikuwa salama kwa maisha yake au la. Alimwangalia Dracula, alimfahamu kupitia kaka yake na ndiye alikuwa mtu pekee ambaye kila wakati alimtoa hofu kwa kumwambia kuwa sehemu hiyo ilikuwa salama kwake kwa asilimia mia moja.

“Una uwezo gani wa kutumia kompyuta?” aliuliza Bwana Seppy huku akimwangalia Cosmas kwa macho yaliyoonyesha kutaka kupewa jibu lae haraka iwezekanavyo.

“Nina ujuzi mkubwa sana, wewe niambie unataka nini na mimi nitakufanyia,” alisema Cosmas huku akionekana kuwa makini na majibu yake.

“Kuna mtu ninataka kufahamu anawasiliana na nani katika simu yake,” alisema Bwana Seppy.

“Nani?”

“Anaitwa Benjamin Saundres!”

“Huyu anayetafutwa?”

“Ndiyo!”

“Mungu wangu! Yupo wapi?” aliuliza Cosmas huku akionekana kushtuka.

“Hatujui! Ndiyo tunataka wewe utuambie yupo wapi,” alisema Bwana Seppy.

“Nitajuaje?”

“Tuna namba yake ya simu, tunataka tujue mawasiliano yote aliyowahi kufanya kwa njia ya simu,” alisema Bwana Seppy.

“Hakuna tatizo!”

Alichokifanya Cosmas ni kuchukua begi lake na kisha kutoa laptop yake na kuiwasha. Kitu alichokihitaji kilikuwa ni namba ya mtu aliyekuwa akihitajika, akapewa na kisha kuiingiza katika kimpyuta yake.

Kitu pekee alichokuwa akicheza nacho kilikuwa ni codes mbalimbali za kompyuta, alikuwa akiingia katika system mbalimbali na kuanza kucheza na codes hizo. Haikuwa kazi nyepesi, ilikuwa ngumu lakini mwisho wa siku akakamata namba zote ambazo zilikuwa zimeingia katika simu ya Benjamin kwa mara ya mwisho ambayo kwa tarehe iliyoonyesha, ilikuwa kama wiki moja iliyopita.

“Namba ambayo mara kwa mara imekuwa ikiwasiliana naye ni hii hapa,” alisema Cosmas huku akiwapa namba hiyo.

“Ni ya nani?”

“Mnataka niangalie?”

“Ndiyo!”

“Sawa.!”

Hilo nalo halikuwa tatizo hata kidogo, kwa Cosmas hiyo ilionekana kuwa kazi ndogo mno hivyo alichokifanya ni kuanza kuangalia usajiri wa namba ile ambayo mwisho wa siku ikamuonyesha kwamba ilikuwa ni ya mtu aliyejulikana kwa jina la David Belshaaz.

“Anaishi wapi?”

“Washington DC!”

“Sehemu gani?”

“Livingstone. System inaniambia yupo katika nyumba moja namba 2789W ambayo pia imepakana na hoteli kubwa ya Salander Hill!” alijibu Cosmas.

“Ni lazima huyo mtu apatikane, bila shaka atakuwa anafahamu mahali Benjamin alipo. Watume vijana waliopo Washington waende, tena hakikisha na wewe unachukua ndege na kwenda huko! Huyu David naye ni mtu muhimu, hakikisha anakamatwa, anateswa na kutambia Benjamin yupo wapi,” alisema Bwana Seppy.

“Sawa mkuu!” aliitikia Dracula, hapohapo akachukua simu na kuanza kuwapigia vijana wake waliopo Washington pia kumpigia simu rubani na kumwambia aandae ndege kwani kulikuwa na safari ya dharura ya kwenda Washington DC.





“Nimekuja kutoa taarifa...”

“Taarifa ya nini?”

“Ya huyu Benjamin Saunders...”

“Unajua alipo?”

“Hapana! Ila kama mkimpata mtu fulani, kazi ya kumpata itakuwa rahisi sana...”

“Nani?”

“Rafiki yake anaitwa David Belshaaz, yupo Washington Dc.”

“Una uhakika?”

“Asilimia mia moja, alikuwa akiwasiliana naye sana!”

“Wewe umejuaje?”

“Kwani nyie mnahisi nimejuaje? Kwanza niambieni, hela zipo?”

“Hizo zipo, ila mpaka ufanikishe kukamatwa kwake!”

“Hakuna tatizo! Fedha kwanza...”

“Fedha kabla ya mzigo?”

“Mzigo kabla ya fedha?”

“Sisi ni serikali, wewe tuamini! Tuambie tunaweza kumpata vipi!”

“Sawa! Ila mkichelewa, hamtompata huyu David kwani kuna mtu pia anamuhitaji kwa nguvu zote...”

“Nani?”

“Nyie fanyeni haraka! Ngoja niwape maelekezo,” alisema kijana mmoja.

Huyo alikuwa Cosmas ambaye aliamua kwenda polisi na kutoa taarifa katika kitengo cha FBI na kuwaambia kila kitu kuhusu kupatikana kwa rafiki wa Benjamin, David ambaye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwasiliana na Benjamin, bila shaka alikuwa akijua mtu huyo alikuwa mahali gani.

Alipowapa maelezo waliyokuwa wakiyahitaji, wakawapigia simu maofisa wa kitengo hicho waliokuwa Washington kwa ajili ya kwenda walipoelekezwa kwa ajili ya kumpata David, sehemu hiyohiyo ndipo nao vijana wa Bwana Seppy walikuwa wakienda kwa ajili ya mtu huyohuyo.

****

David alikuwa ametulia chumbani kwake, alikuwa mbele ya kompyuta yake huku akihangaika kufanya kazi aliyopewa na Benjamin, ilikuwa kazi kubwa lakini ilikuwa ni lazima ahakikishe anampatia majibu juu ya mahali mpigaji wa namba aliyompa alipokuwa akiishi.

Hakuwa akiwasiliana naye kupitia namba yake, alimwambia mapema kwamba angeitupa simu na hata kuwasiliana naye asingewasiliana kwa kupitia namba yake bali angeitumia namba ya mpenzi wake, Vivian, hivyo ndivyo alivyofanya.

Hiyo ilikuwa siku ya saba, bado alikuwa na kazi moja ambayo ilikuwa ngumu na hakujua ni kwa wakati gani angeweza kuikamilisha. Kilichokuwa kikimshinda, hakuweza kuipata namba hiyo ikiwa hewani, ilikuwa imezimwa jambo ambalo lilimpa ugumu mkubwa mno.

Wakati akiendelea na kazi hiyo, ghafla akasikia kama vishindo vya mtu kwa nje, akashtuka, haikuwa kawaida kwani nyuma aliyokuwa akikaa, kwa muda kama huo, saa saba usiku ilikuwa vigumu sana kuwa na mtu mwingine nje.

Haraka sana akaifunika laptop yake, akazima taa na kisha kuelekea chumbani kwake ambapo kwa juu kulikuwa na tundu, akalifungua na kuingia humo.

Hicho kilikuwa chumba kingine cha kujificha, huku hakukuwa kama dali la nyumba za Afrika, kulionekana kama chumba kingine ambapo kulikuwa na kitanda na vitu vingine, akatulia huku akisikilizia kuona ni kitu gani kingetokea huko chini alipokimbia.

“Hebu subiri!” alijisemea, harakaharaka akawaisha kompyuta yake ya huko ambapo aliiunganisha na kamera ndogo za CCTV ambazo aliziweka kwenye kona kadhaa ndani ya nyumba hiyo.

Akaanza kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea, wanaume watatu waliovalia nguo nyeusi tupu walisimama katika mlango wa kuingilia ndani, walikuwa wakijadiliana ni kwa namna gani wangeweza kuingia ndani.

Hakujua watu hao walikuwa wakina nani na walikuja hapo kufanya nini, aliogopa, alibaki akitetemeka kule juu kwani kwa jinsi alivyowaona, watu hao hawakuonekana, hawakuonekana kuwa watu wazuri hata mara moja kwani mikononi mwao walikuwa na bastola.

“Ni wakina nani?” alijiuliza lakini hakupata jibu.

Watu hao wakafungua mlango na kuingia ndani, kule alipokuwa, David alikuwa akitetemeka lakini alikuwa na wasiwasi wa kukamatwa na watu hao, kuwa huko dalini hakukusaidia, alichokifanya ni kujificha chini ya kitanda kilichokuwa hukohuko huku kompyuta ile akiielekezea kule alipokuwa kwa ajili ya kufuatilia kilichokuwa kikiendelea.

“Yupo wapi?" aliuliza jamaa.

“Hebu tutafuteni,” alisema jamaa mwingine na hivyo kuanza kumtafuta.

Waliangalia kila kona, hakukuwa na mtu yeyote, walikuwa na maswali mengi kwamba David alikuwa wapi kwani kwa jinsi hali ilivyoonekana ndani ya nyumba ile, alikuwa sehemu fulani ambayo hawakuifahamu ilikuwa sehemu gani.

Walimtafuta kwa zaidi ya dakika tano lakini hawakuweza kumuona kabisa. Wakati wakiendelea kuchunguza huku na kule, ndipo mmojawao akasema kwamba inawapasa kuangalia juu ya dali kwani kulikuwa na nyumba nyingi hapo Marekani ambapo juu kulikuwa na sehemu nyingine ya kukaa.

“Tuangalieni juu kule, nahisi anaweza kuwa huko,” alisema mwanaume mmoja.

“Una uhakika?”

“Tunatakiwa kujaribu, tutafuteni mlango wa kuingilia juu,” alisema mwanaume huyo.

Hakukuwa na cha kusubiri, ushauri huo uliotolewa ulitakiwa kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo hivyo kuutafuta mlango wa kuingilia huko. Wala hawakupata kazi kubwa, wakaupata na kisha kuufungua.

Kama walivyohisi na kama ilivyokuwa kwa nyumba nyingine, hata huko juu kulikuwa na chumba kingine kikubwa, mmojawapo akapanda na kuingia huko kisha kuanza kumtafuta david.

“Najua upo humu! Najua upo humu, jitokeze mwenyewe,” alisema mwanaume huyo, alikuwa huko huku bastola ikiwa mikononi mwake.

“Hutaki kutoka?” aliuliza huku akiikoki bastola ile.

Kule uvunguni alipojificha David alikuwa na presha kubwa, mapigo ya moyo yalikuwa yakimdunda mno, kitendo cha kusikia bastola ile ikikokiwa, tayari jasho lilimtiririka kwa kuhisi kwamba mwanaume huyo angeanza kupiga risasi ovyo.

Hakutaka kusubiri huko, ili kujiokoa, harakaharaka akajitoa huku akimuomba asimpige risasi.Hicho ndicho alichokuwa akikitaka, hapohapo akamchukua na kumwambia ashule chini, David akafanya hivyo haraka sana, huko chini, akapokewa na wale wanaume wawili.

“Safi sana....hebu piga magoti hapo,” alisema mwanaume mmoja, David hakutaka kubisha, akapiga magoti huku machozi yakianza kumtiririka mashavuni kwani hakujua kama angeweza kupona mahali hapo.

“Unaweza kutuambia mahali alipokuwa Benjamin?” aliuliza mwanaume mmoja.

“Benjamin yupi?” aliuliza David.

“Humfahamu?”

“Ndiyo! Sina rafiki anayeitwa Benjamin!”

“Acha utani kijana, hebu tuangalie vizuri, unatuonaje? Tuna utani au?” aliuliza mwanaume mmoja.

“Kweli tena, simfahamu!” alisema Benjamin.

Watu hao waliona kama wanataniwa, walimwangalia vizuri David, majibu yake na uso wake ulionekana kuwa tofauti na kile alichokisema. Kitu cha kwanza kabla ya kuuliza zaidi ilikuwa ni kumpiga kofi zito shavuni mwake, David akaanguka chini.

“Tuambie ukweli!”

“Huo ndiyo ukweli!”

“Upi?”

“Kwamba simfahamu m...” alisema lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, akashtukia akipigwa tena.

“Umekataa?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Kweli simjui!”

“Basi sawa...” alisema mwanaume huyo na kisha kuikoki bunduki yake.

Kitendo cha bunduki ile kukokiwa, tayari David alijua ni kitu gani kilitakiwa kufuata mahali hapo, alibaki akitetemeka kwani hakujua kabisa kama watu hao wangeweza kuchukua uamuzi wa harakaharaka wa kummaliza hapohapo nyumbani kwake.

Akaomba sana msamaha lakini hakukuwa na aliyemjali, ili wasimuue, basi ilikuwa ni lazima aseme mahali Benjamin alipokuwa, vinginevyo, roho yake ilikuwa mikononi mwao.

“Muue haraka tuondoke zetu, hatuna muda wa kupoteza,” alisema mwanaume mwingine ambaye tangu aingie ndani ya nyumba hiyo hakuwa amezungumza lolote lile.

“Hakuna noma...” aliitikia huyo mwenzake, hapohapo akamnyooshea bunduki David tayari kwa kumuua mahali hapo.

****





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog