Simulizi : Mauaji Yaliyojaa Utata
Sehemu Ya Tatu (3)
Filamu nyingi ziliigizwa kila mwaka, watu walifuatilia filamu hizo katika kumbi mbalimbali, kila mtu alizipenda, kuna wengine, kabla ya kuagiza filamu hizo katika makampuni husika, kazi yao ilikuwa ni kwenda kwenye majumba ya kuangalia na kuziangalia filamu hizo.
Achana na za mapenzi, kulikuwa za mapigano ambazo kwa kipindi hicho ndizo ziliteka hisia za watu wengi, kulikuwa na waigizaji wengi, wenye uwezo ambao waliigiza filamu za mapigano na kupendwa sana lakini filamu ya Knock Out 3D iliyoigizwa na muigizaji chipukizi, Todd Lewis ndiyo ilionekana kuwa kali zaidi ya filamu za mapigano zilizotangulia.
Todd Lewis alikuwa kijana mdogo lakini kutokana na matangazo ya filamu hiyo (Trailers), watu wengi nchini Marekani walitaka kuiona, mapigano aliyokuwa akiyatumia ndani ya filamu hiyo yalimchengua kila mtu ambaye alitazama matangazo ya filamu hiyo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku ambayo ilipangwa kuzinduliwa kwa filamu hiyo watu waliona ikiwa mbali, waliiona ikichelewa kufika hivyo kutaka ifike haraka ili waingie na kisha kuiangalia.
Si Marekani tu waliobabaika na matangazo ya filamu hiyo bali hata katika nchi nyingine, kote huko waliisubiria filamu hiyo kwa hamu kubwa, tiketi zaidi ya milioni kumi, sehemu zote duniani ziliuzwa na kuisha na bado watu walihitaji zaidi kwani matangazo ya filamu hiyo katika sehemu mbalimbali zilionyesha kabisa kwamba hiyo haikuwa filamu ya kukosa kuiyazama.
Siku zilikatika na hatimaye siku hiyo kuwaidia, watu walijazana katika Ukumbi wa Stapple Center, Los Angeles nchini Marekani tayari kwa kuishuhudia filamu hiyo ambayo ilisubiriwa kwa kipindi kirefu na ndiyo filamu ya kwanza kuuza tiketi nyingi katika siku ya kwanza ya uzinduzi wake.
Filamu ilipoanza kuonyeshwa katika mfumo wa 3D, kila mtu alisisimka, miwani ilikuwa nyusoni mwao huku wakiangalia namna Todd alivyoigiza kwa umahiri mkubwa.
Mpaka filamu hiyo inamalizika, kila mtu aliridhika, hawakuamini kama kungekuwa na muigizaji chipukizi ambaye angeweza kuigiza kwa ustadi mkubwa kama ilivyokuwa kwa Todd.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mafanikio yake, alikuwa na miaka kumi na saba tu lakini alitabiriwa kuwa muigizaji mkubwa hapo baadaye. Kila sehemu alipopita watu walimuita, walimpa vitabu vyao kwa ajili ya kuvisaini, alipendwa na kila mtu, yaani kila alipokuwa, alinukia fedha.
Siku zikaendelea kukatika, huo ulikuwa mwanzo wa mafanikio yake mengi, akaigiza filamu ya pili na ya tatu, ya nne na ya tano, mpaka anafikisha umri wa miaka ishirini, alikuwa na jina kubwa, alitengeneza sana fedha na watu wengi walitamani kuwa kama yeye.
“Inakuwaje?” aliulizwa na mwandishi wa habari, tena alikuwa amekaa ndani ya gari lake.
“Safi...”
“Mimi ni mwandishi wa habari...”
“Najua, unaitwa Ester kutoka Independent...” alisema Todd huku akitabasamu.
“Ndiyo! Nimesikia umenunua gari jipya, ni kweli?”
“Umesikia wapi?”
“Ni taarifa tu kutoka sehemu mbalimbali, kuna ukweli?” aliuliza Ester.
“Ndiyo! Ila umezipata wapi?”
“Hii ndiyo kazi yangu Todd...” alisema msichana huyo.
Baada ya kupata mafanikio makubwa, alichokifanya Todd ni kununua jumba la kifahari lililokuwa Los Angeles hapohapo nchini Marekani, lilikuwa jumba la kifahari lililomgharimu dola milioni nne, zaidi ya bilioni nane za Kitanzania.
Hakuishi hapo, alichokifanya ni kununua gari la kifahari aina ya Ferrari Testarossa kutoka nchini Italia. Gari hilo alilinunua baada ya kutoa oda kwani katika kipindi hicho magari hayo yalikuwa nane tu, yeye akawa miongoni mwa watu waliokuwa wakimiliki gari hilo.
Kuwa na gari hilo, tayari aliandikwa kila kona, hakukuwa na siri tena, alikuwa staa hivyo kila kitu alichokifanya, watu walikifahamu. Todd hakuwa mtu wa starehe, hakuwa mtu wa kwenda klabu au kutumia pombe yoyote ile, pamoja na ustaa wake huo, alikuwa mtu wa kusali sana, alikwenda kanisani kila Jumapili kitu kilichowashangaza watu wengi.
Wanawake walimpapatikia, hakuwa na nafasi nao, aliwajua, aliwakumbuka watu wengi ambao walipoteza fedha zao, umaarufu wao mara baada ya kuweka ukaribu wanawake, hakutaka kitu hicho kitokee kwake na ndiyo maana kila siku alijitahidi kuwaepuka.
Baada ya siku kadhaa, yeye na Kampuni ya Filamu ya Marvel wakaondoka na kuelekea nchini Ukraine kwa ajili ya kuingiza vipande vya filamu iliyotarajiwa kutoka baada ya miezi sita, filamu kali iitwayo Around ambayo ilisemekana kuwa filamu kali kuliko zile zilizopita.
Watu walitulia majumbani mwao, walitaka kufahamu filamu hiyo ilikuwaje na ilifananaje kwani waliiamini kampuni ya Marvel, ilikuwa kampuni kubwa, iliyotengeneza filamu nyingi kama Spiderman, Captain America, Thor na nyingine nyingi, hivyo waliamini kwamba hata Around ingekuwa moja ya filamu kali, tena iliyokuwa ikiigizwa na muigizaji mwenye jina na uwezo mkubwa, Todd.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
David alikuwa akitetemeka, kitu alichokuwa akikiona mbele yake kilikuwa kifo tu, hakuamini kama watu wale wangeweza kumuacha kwani walimtaka kusema ukweli juu ya mahali alipokuwa Benjamin, ila hakutaka kusema, alifanya siri kitu kilichowakasirisha wanaume hao.
Bado walimtaka kuzungumza, kusema ukweli juu ya mahali alipokuwa Benjamin lakini bado msisitizo wa David ulikuwa palepale kwamba hakuwa akimfahamu mtu huyo, ndiyo kwanza alimsikia siku hiyo.
Hawakutaka kusubiri zaidi, David alionekana kuwa jeuri hivyo walichoamua ni kummaliza tu. Huku bastola zikiwa zimekokiwa tayari kwa kufyatuliwa, ghafla wakasikia dirisha la kioo likivunjwa, risasi mfululizo zikaanza kupigwa kuelekea ndani humo, tena kwa ustadi mkubwa kabisa.
Wanaume wawili miongoni mwa wale watatu wakaanguka chini, damu zilikuwa zikiwatoka migongoni mwao, walirusharusha miguu na mikono yao, walihangaika katika hatua za mwisho kabla ya kukata pumzi na kufariki dunia.
Mwanaume mmoja, yeye na David ndiyo waliobaki ndani ya nyumba ile, alikuwa na wasiwasi mkubwa, bastola ilikuwa pembeni yake na hata kuichukua, hakudiriki.
Alikuwa akitetemeka muda wote, macho yake yalipotua kwa wenzake ambao walipigwa risasi na kufa, alizidi kuogopa na kuona kwamba muda wowote ule hata yeye mwenyewe pia angeweza kufa.
Wakati wote wawili wakiwa wamelala chini, ghafla mlango ukafunguliwa na maofisa watatu wa FBI kuingia huku wakiwa na bastola zao mikononi mwao, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwaweka wote chini ya ulinzi.
“Sijafanya kitu,” alisema David huku akitetemeka, ndiyo kwanza walikuwa wakimfunga pingu.
“Tutajua...”
“Lakini hawa ndiyo walikuja kunivamia,” alisema.
“Tutajua tu, twendeni!”
Wote wakafungwa pingu na kutolewa ndani ya nyumba ile, muda wote David alikuwa akilia, hakuamini kama kweli alifungwa pingu. Watu walioingia walikuwa ni maofisa wa FBI, walijuaje kama alikuwa amevamiwa? Na wale watu waliokuwa wameingia na kumuweka chini ya ulinzi wao, walijuaje kama yeye alikuwa akimfahamu Benjamin? Kila alilojiuliza, alikosa jibu kabisa.
****
Wote wakachukuliwa, wakaingizwa ndani ya gari na safari ya kuelekea katika kituo cha polisi kuanza mara moja. Njia nzima David alionekana kuchanganyikiwa, hakujua kitu gani kilichokuwa kikiendelea, mawazo mengi, maswali yalimtinga lakini yote hayo hayakuwa na majibu yoyote yale.
Walichukua muda wa dakika ishirini ndipo gari lao likaanza kuingia katika jengo ambalo alikuwa na uhakika halikuwa jengo la polisi. Kwa muonekano wake tu, kwa kuliangalia harakahara lilionekana kujengwa kwa ajili ya kazi maalumu, nje hakukuwa na magari, na sehemu hiyo ilionekana kuwa tofauti kabisa na sehemu nyingine.
Hakukuwa na mtu aliyezungumza kitu chochote kile, wakalipeleka gari katika sehemu ya kuegeshea na kisha kuwataka wote wateremke, wakafanya hivyo. Wakawachukua na kwenda nao ndani, huko, wakatenganishwa vyumba, David alipelekwa katika chumba kingine na yule mwanaume mwingine akapelekwa katika chumba kingine.
Huko, David alikuwa akitetemeka, hakujua ni kitu gani kilichowafanya maofisa hao wa FBI kumchukua na kumuingiza ndani ya chumba hicho badala ya kumuacha nyumbani kwake kwa kuwa alikuwa amevamiwa.
Akawekwa mbele ya meza kubwa, kulikuwa na viti viwili chumba kizima, mbele yake kulikuwa na kioo kikubwa, akajua tu kwamba nyuma ya kioo kile kulikuwa na watu waliokuwa wakimwangalia.
Mbali na hivyo, pia kulikuwa na kamera ndogo mbili za CCTV zilizokuwa zimewekwa katika pembe mbili ndani ya chumba hicho. Alikaa huku akionekana kuwa na hofu, akahisi kwamba kulikuwa na jambo zito mbele yake.
Wakati akiwa kwenye mawazo, mara wanaume wawili wakaingia ndani ya chumba hicho, mmoja akakaa katika kiti kimoja na mwingine kusimama huku bastola ndogo aina ya 45 Automatic ikiwa kiunoni mwake.
“Unamfahamu mtu anaitwa Benjamin?” aliuliza ofisa huyo aliyejitambulisha kwa jina la Gregory.
“Hapana!” alijibu.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“David Belshaaz, hatupo hapa kama watu wabaya, unajua dhahiri kwamba tunamtafuta mtu huyo, kwa nini unatuficha, kuna nini? Hutuamini?” aliuliza Gregory.
“Simfahamu! Watu wale walionivamia, walikuja na kuniuliza kuhusu Benjamin, mmewaua, na nyie mnakuja na kuniuliza kuhusu Benjamin, huyu Benjamin ni nani na amefanya nini?’ aliuliza David huku akimkazia macho Gregory.
“Ina maana haumfahamu Benjamin?”
“Ndiyo! Au naweza nikawa namfahamu kwa kumwangalia, ila jina, ni geni kwangu,” alijibu David.
“Una uhakika?”
“Ndiyo ofisa...”
Alijua fika hakuwa na kosa lolote lile, hata kama angekataa kusema mahali alipokuwa Benjamin, asingepigwa wala kuuawa, au hata kutishiwa. Alizungumza kwa kujiamini kwani alijipa uhakika kwamba mahali alipokuwa palikuwa salama kabisa.
“Unamfahamu marehemu Carter?” aliuliza Gregory.
“Ndiyo! Kuna mtu asiyemfahamu mtaalamu wa Pop?”
“Unajua nini kuhusu yeye?”
“Kwamba alikuwa mwanamuziki mkali, labda kingine, alipenda sana kucheza chess,” alijibu David.
“Na kuhusu kifo chake?”
“Nitajua nini kuhusu hilo? Nafuatilia vyombo vya habari, nadhani waandishi watakuwa wanajua zaidi kuliko mimi,” alijibu David.
“Sawa. Naomba simu yako!”
“Ya nini?”
“Hakuna ubaya. Naweza kuipata?”
“Unaweza ukaipata kama ukiniambia ya kazi gani, ila vinginevyo, hautoweza kuipata,” alijibu David.
Gregory akabaki akimwangalia David, kwa namna alivyokuwa akizungumza, alionekana kuwa mtu makini, hakuingiza utani, kila alichokiongea, uso wake ulimaanisha kila sentensi kwamba hakuwa akileta utani hata mara moja.
Gregory akabaki akimshangaa, katika kufanya naye kazi hakuwahi kukutana na mtu aliyekuwa akijiamini kama ilivyokuwa kwa David. Si yeye tu aliyeshangaa bali hata wale waliokuwa wakifuatilia nyuma ya kioo, walishangaa, huyu David alikuwa mtu mwingine kabisa.
“Si kwa lengo baya!”
“Najua ofisa. Naweza kuondoka?”
Gregory akashusha pumzi nzito, akayapeleka macho yake kwa mwenzake aliyekuwa amesimama pembeni, wakapeana ishara fulani, David aliiona ila hakutaka kujali kwani bado akili yake ilimwambia kwamba alikuwa katika mikono salama kabisa.
“Oooh! Samahani ofisa, mlisema kwamba mnaitaka simu yangu, si ndiyo?’ aliuliza David.
“Ndiyo!”
“Mtaweza kuitumia?”
“Ndiyo!”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa! Naombeni niwape kwa masharti.”
“Yapi?”
“Nikiwapa niondoke zangu, mtaniletea mkishamaliza kazi nayo,” alisema David, maofisa hao wakaangaliana.
“Sawa!”
Alichokifanya David ni kuichukua simu hiyo kutoka mfukoni na kisha kumgawia Gregory ambaye akaipokea huku macho yake yakiwa usoni mwa David.
Maswali mengi yakaanza kumiminika kichwani mwake, kwamba ilikuwaje David atake kumpa simu baada ya kujifikiria kwa muda mrefu lakini pia kumuuliza kama angeweza kuitumia?
Hakupata jibu ila alijua kwamba kwenye kutumia simu hakukuwa na tatizo lolote lile na ndio maana akakubaliana naye. Alipopewa, hakuwa na jinsi, alitakiwa kutekeleza ahadi yake hivyo wakamruhusu kuondoka na kuahidi kumrudishia simu ile pindi watakapomaliza kuitumia.
Kitu cha kwanza kabisa walichotaka kukifanya ni kuipekua simu ile. Haikuwa rahisi kama walivyofikiria, kwanza sehemu ya simu zilizopigwa na kuingia hazikuwa zikionekana. Walishangaa, haikuwa simu ya kawaida, ilionekana kuingizwa programu ambayo hawakuwa wakiifahamu.
Wakaipeleka kwa watu wao wa masuala ya kompyuta (IT), walipowapa ile simu na kuanza kuichezea ili kujua ni simu zipi zilikuwa zimepigwa na kutoka, hawakuweza kuona chochote kile.
Walihitaji muda wa saa moja huku wakiishughulikia simu ile, maofisa wengine wa FBI waliwasubiri zaidi lakini mpaka saa moja linafika, hakukuwa na kilichowezekana, bado majibu yalikuwa yaleyale kwamba simu haikuweza kufunguka sehemu ya simu zilizoingia na kutoka.
Ilikuwa ni usiku sana, walikuwa safarini kuondoka walipokuwa wakiishi na kuelekea sehemu ambayo hawakuifahamu. Walembea kwa mwendo wa harakaharaka, hawakutaka kusimama, kila walipoangalia nyuma, walihisi kwamba kulikuwa na watu walikuwa wakiwafuata hivyo ilikuwa ni lazima kukimbia.
Walikwenda mpaka walipofika sehemu iliyokuwa na kituo cha mafuta, kitu walichokihitaji ni chakula, kilipita kipindi fulani hawakuwa wamekula chakula chochote kile, walihisi njaa hivyo ilikuwa ni lazima kununua chakula.
Wakaingia katika supamaketi iliyokuwa katika kituo hicho cha mafuta na kuanza kuzunguka huku na kule kutafuta chakula. Hakukuwa na mteja yeyote, walikuwa wao na muuzaji mwanamke ambaye kila wakati alibaki akimwangalia Benjamin kama mtu aliyekuwa akimfahamu.
Benjamin hakujua hilo, alikuwa bize kuangalia huku na kule, walipomaliza kuchagua vyakula walivyovitaka, wakaenda mpaka katikasehemu ya kulipia tayari kwa kumlipa mwanamke huyo.
“Kuna nini?” aliuliza Benjamin kwa sauti ya chini, alikuwa akimuuliza Vivian.
“Kivipi?”
“Huoni jinsi anavyotuangalia huyu mwanamke?”
“Mmh!”
“Nahisi kuna kitu!”
Wakati wamesimama hapo, mwanamke huyo hakuonekana kuwa na haraka, alikuwa akiwahudumia taratibu huku chini ya meza yake kukiwa na kitufe ambacho kama ungekibonyeza, kilipeleka taarifa katika kituo kidogo cha polisi kilichokuwa karibu na supamaketi hiyo kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Alimfahamu Benjamin, picha yake ilikuwa maarufu hata zaidi ya Gazeti la New York Times na zilibandikwa kona nyingi hapo Marekani. Alikuwa akimchelewa mahali hapo kwa kuwa alijua kwamba tayari polisi walipokea taarifa hivyo wangefika mahali hapo muda wowote ule.
“Tunaweza kuondoka?” aliuliza Benjamin, alimshangaa namna mwanamke huyo alivyokuwa akijichelewsha.
“Subirini kwanza...”
“Tusubiri nini?” aliuliza Vivian, mwanamke huyo hakujibu, aliendelea kujifanya anapanga baadhi ya bidhaa zake, hivyo Benjamin na Vivian wakasubiri pasipo kujua kwamba polisi walikuwa njiani kufika mahali hapo.
Walionekana kukasirika lakini hawakutaka kuondoka, kwa jinsi mwanamke huyo alivyoonekana bize, ilionyesha kuwa hakuwa akifanya kusudi, kweli alikuwa bize.
Huku wakiendelea kuwa mahali hapo, ghafla wakaanza kusikia ving’ora vya gari la polisi likija kule walipokuwa. Kwanza wakashtuka, walipoyapeleka macho yao kwa mwanamke yule, alionekana kabisa kushtuka.
“Umeita polisi?” aliuliza Benjamin.
“Nani?”
“Umeita polisi...umeita polisi wewe...” alisema Benjamin huku akimshika mkono Vivian na kuanza kuondoka naye mahali hapo.
Tayari gari la polisi lilikaribia kabisa karibu na kituo hicho cha mafuta, waliona kabisa kama wangepita kwa kutumia mlango wa mbele ingekuwa rahisi sana kuonekana, hivyo ilikuwa ni lazima waondoke kwa kupitia mlango wa nyuma.
Hakukuwa na muda wa kujifikiria mahali hapo, wakaanza kuondoka kupitia mlango wa nyuma, mwanamke yule akatoka nje, alionekana kuwa na haraka, akaanza kuwahimiza polisi wale wafike haraka mahali hapo kwani mtu waliyekuwa wakimtaka, alikuwa akikimbia.
Baada ya polisi kufika mahali hapo, wakasimamisha gari lao na kisha kuteremka, hawakutaka kuzungumza na mwanamke yule, walichokifanya ni kuingia ndani moja kwa moja, bastola ndogo zilikuwa mikononi mwao, wakaanza kuangalia huku na kule wakimtafuta.
“Yupo wapi?’ aliuliza polisi mmoja huku akiwa makini kuangalia huku na kule.
“Aliondoka kupitia mlango ule,” alisema mwanamke yule, polisi wakaanza kuelekea huko.
Sehemu walipotokea ilikuwa ni stoo, kulikuwa na bidhaa nyingi, hawakutaka kusimama mahali hapo, ilikuwa ni lazima wakimbie, mbele yao kulikuwa na mlango mkubwa wa chuma, wakaufuata na kisha kuufungua.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sehemu waliyotokea ilikuwa na mifuko mingi iliyokuwa imefungwa, wakapita katikati mpaka walipokutana na mlango mwingine ambapo baada ya kuufungua, wakakutana na gari aina ya Jeep.
“Tuingie garini,” alisema Benjamin huku akilifuata gari hilo.
“Hatuna ufunguo...”
“Wakati mwingine si lazima uwe na ufunguo...” alisema Benjamin huku akikivunja kioo cha gari lile.
Akaingia ndani, akamfungulia mlango Vivian na kuingia ndani. Alichokifanya ni kuifungua sehemu iliyokuwa chini ya usukani na kisha kuanza kuziunganisha nyaya zilizokuwa mahali hapo, tena kwa kasi ya ajabu.
“Fanya haraka....wanakuja...”
“Najitahidi...nipe sekunde tano...” alisema Benjamin huku akizichuna zile nyaya kwa meno yake na kisha kuanza kuziunganisha, yote hiyo ilikuwa ni harakati za kuwasha gari hilo.
Wakati akiendelea kuliwasha lile gari kwa kutumia nyaya kadhaa, polisi wale walikuwa wakikaribia, muda huo nao walikuwa stoo, walikimbia kuelekea kule walipoelekea Benjamin na mpenzi wake, Vivian.
Wakati wameufikia mlango, ghafla wakasikia mlio wa gari likiwa limewashwa, wakati wameufungua mlango huo, wakaliona gari hilo likiondoka kwa kasi mahali hapo, hata mlango mkubwa wa nyuma haukufunguliwa, Benjamin akaufunja mlango huo kwa gari lile na kuanza kuondoka.
“Tuwakimbize, twende garini,” alisema polisi mmoja.
Wakatoka nje, wakalifuata gari lao, wakaingia na kuanza kuondoka kulifuata gari lile ambalo lilikuwa mbali kama mita mia moja na hamsini kwani injini yake ilikuwa na nguvu kubwa.
“Tunahitaji msaada Barabara ya St. Joseph 45W, tumemuona mtuhumiwa wa mauaji, Benjamin, tunahitaji msaada....ova..” alisema polisi mmoja, alikuwa ameshika redio call, mwenzake alikuwa akiendesha gari hilo kwa kasi kubwa.
****
Bwana David Seppy alichanganyikiwa, hakuamini zile taarifa alizokuwa amepewa kwamba vijana wake waliokuwa jijini Washington DC waliuawa huku mmoja akikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi chini ya maofisa wa FBI.
Hakutaka kuona hilo likitokea, alijua vilivyo jinsi maofisa hao walivyojua kuzungumza na mtu, kumuuliza maswali ya mitego na hatimaye kuwaambia mtu aliyekuwa amewatuma.
Kwa kijana huyo kushikiliwa na FBI lilionekana kuwa jambo bata sana, hakutaka kuona akigundulika kwamba yeye ndiye aliyekuwa akihusika na mauaji yaliyokuwa yakitokea, hivyo ilikuwa ni lazima ahakikishe kijana huyo anauawa.
Akawasiliana na Dracula ambaye naye tayari alifika huko, akampa amri kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kijana huyo auawe kwa kuwatumia baadhi ya maofisa waliokuwa ndani ya jengo hilo kumuua kijana huyo kwa kumchoma sindano.
Hilo likachukuliwa na Dracula, akawasiliana na maofisa wawili wa FBI ambao walikuwa upande wao na kuwalipa kiasi kikubwa cha fedha, akawaambia kwamba kijana huyo alitakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo, hivyo mishemishe zikaanza.
“Imekuwaje?” aliuliza Bwana Seppy.
“Vijana wanafuatilia, bila shaka watafanikiwa,” alijibu Dracula.
Alikaa na kusubiri, alitaka kujua kama maofisa hao walifanikiwa au la, baada ya saa nne, akapigiwa simu na kupewa taarifa kwamba kijana yule aliyenusurika kuuawa, aliuawa katika chumba kimojawapo katika kituo cha polisi baada ya kuchomwa sindano.
“Safi sana,” alisema Bwana Seppy huku akionekana kuwa na furaha kubwa.
Baada ya wiki moja, akaamua kumuita kijana wake, Dracula na kumpa mpango kabambe uliokuwa mbele yake, alimwambia wazi kwamba alitaka kuzitangaza biashara zake kupitia watu maarufu hivyo mtu ambaye kwa kipindi hicho alikuwa juu ambaye ilikuwa ni lazima kuonana naye, alikuwa muigizaji, kijana mdogo, mwenye uwezo mkubwa, Lewis Todd.
Kumpata Todd halikuwa tatizo hata kidogo kwani kwa sababu mambo ambayo walitakiwa kuzungumza naye yalikuwa ni biashara, wakawasiliana na meneja wake na kumwambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea hivyo aliakiwa kuzungumza mtu wake.
“Hakuna tatizo, nitazungumza naye,” alisema meneja huyo, Bwana Oswald Genz.
Genz alikuwa mtu wa fedha, kila alipokaa, kitu alichokifikiria kilikuwa fedha tu. Kulikuwa na madili mengi yaliyokuwa yakija mezani kwake kwa ajili ya mtu wake, hivyo kupewa taarifa kwamba Bwana Seppy alitaka kuingia mkataba wa kufanyiwa matangazo na mwanamuziki aliyekuwa akimsimamia, kwake ilikuwa dili nzuri.
Kitu cha kwanza akawasiliana na Todd na kumwambia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, akampa mchakato mzima kuhusu dili hilo ambapo kwa upande wa Todd, hakukuwa na tatizo lolote lile, alitakiwa kurudi kutoka nchini Ukraine na ndipo angesaini mkataba huo.
“Ila walikwambia ni kiasi gani?” aliuliza Todd kwenye simu.
“Hapana!”
“Ni lazima tujue. Bila dola milioni ishirini, hakuna biashara hapo,” alisema Todd.
“Nadhani inaweza kuwa zaidi ya hapo, si unajua jinsi Seppy alivyokuwa na fedha?”
“Ndiyo! Najua hilo! Kama itakuwa ni zaidi, basi hilo ni bonge la dili,” alisema Todd na simu kukatwa.
Baada ya wiki tatu, Todd akafika nchini Marekani, kitu cha kwanza kabisa kukifanya ni kupanga mikakati ya kuonana na Bwana Seppy, mikakati hiyo ikafanyika na ndani ya siku mbili, walikuwa katika hoteli ya kifahari ya Leopard Vile iliyokuwa ikimilikiwa na mzee huyo kwa ajili ya kuingia mkataba.
“Nitakulipa dola milioni tano,” alisema Bwana Seppy.
“Unasemaje?” aliuliza Todd huku akionekana kutokuamini kile alichokisikia.
“Dola milioni tano! Unaonaje?” aliuliza.
Todd akaangaliana na meneja wake, hawakuamini walichokuwa wamekisikia kutoka kwa mzee huyo. Walitegemea kwamba wangepata zaidi ya dola milioni ishirini kutokana na jina kubwa alilokuwa nalo kipindi hicho, sasa iweje apewe milioni tano na wakati nyuma yake kulikuwa na watu wengi, waliofanya alichokifanya?
“Haiwezekani,” alisema Todd.
“Kivipi?”
“Bila milioni thelathini, hakuna kinachofanyika,” alisema Todd, alionekana kumaanisha haswa.
“Nisikilize Todd.....”
“Hakuna suala la kusikiliza. Kiasi hicho nilikuwa nikipokea miaka miwili iliyopita, si sasa, kuna watu wengi mno nyuma yangu, kiasi hicho kidogo,” alisema Todd.
Bwana Seppy akakasirika kama kawaida yake, kwake, mtu kukataa kuingia mkataba na yeye, tena kwa fedha alizozitaka yeye ilionekana kuwa dharau kubwa, akabaki akimwangalia kijana huyo, hasira kali iliyomkaba kooni ikamwambia kwamba ilikuwa ni lazima amuue kijana huyo, yaani kama ilivyotokea kwa Carter.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bwana Seppy alitumia muda huo kumbembeleza Todd akubaliane naye lakini kijana huyo akakataa kabisa kwa kusema kwamba kiasi kilichotolewa, kisingeweza kumfikisha kokote kule kwani mbali na yeye, kulikuwa na watu wengi nyuma yake.
Bwana Seppy hakutaka kuzungumza tena, moyo wake ulimuuma sana kwa kuona kama akilazimishwa kumuua kijana huyo, hivyo alichokifanya ni kuondoka kuelekea nyumbani kwake.
Alikuwa na mawazo mengi, hata mkewe alipomuona, aligundua kwamba mume wake hakuwa sawa kichwani hivyo akamlazimisha kumwambia ukweli lakini akasema kwamba kulikuwa na vitu vidogo vya kibiashara vilivyokuwa vikimsumbua.
“Kweli?” aliuliza mkewe.
“Ndiyo mke wangu! Kichwa changu hakipo saa, biashara zangu zinasumbua sana,” alisema mzee huyo.
Hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kumwambia Dracula kwamba Todd alitakiwa kuuawa kama kawaida, hakutaka kumuona mtu huyo akiendelea kuishi, alimpa muda wa mwezi mmoja kijana huyo afe.
“Tumuue kwa risasi?” aliuliza Dracula.
“Itagundulika kama ameuawa...” alijibu.
“Au ajali?”
“Napo itagundulika kama ilivyokuwa kwa Princess Diana...”
“Sasa tumuue vipi?”
“Kama ilivyokuwa kwa Carter. Mfanyeni aonekane kama amejidunga madawa ya kulevya, tena iwe ndani ya nyumba yake,” alisema Bwana Seppy.
“Sawa! Tutafanya hivyo mkuu!”
“Tena ni vizuri ikiwa ndani ya gari lake,” alisema Bwana Seppy.
“Ila....”
“Ila nini bosi?”
“Isiwe mwezi huu, acheni mpaka mwezi ujao,” alisema.
“Sawa!”
“Natumaini mtaifanya kazi yangu ipasavyo!”
“Ndiyo mkuu! Hela zitahitajika kuwekwa?”
“Kama kawaida. Kama ilivyokuwa kwa Carter, acha iwe kwa Todd pia, na msisahau kuweka na alama za vidole vya Benjamin,” alisema Bwana Seppy.
“Hakuna tatizo!”
Benjamin alikuwa akiendesha gari kwa kasi kuwakimbia polisi ambao nao walikuwa wakija nyuma yake, alichanganyikiwa, kitendo cha kukimbizana na polisi barabarani lilikuwa kosa kubwa ambalo lingemfanya kuadhibiwa kwa kupigwa faini au kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani.
Ilikuwa ni afadhali kwa kipindi hicho kukimbizwa na polisi hao kuliko kukamatwa na kufikishwa mahakamani. Dunia nzima ilijua kwamba yeye ndiye alikuwa muuaji, hakukuwa na aliyejua lolote kwamba kilichokuwa kimetokea nyuma ni yeye kuyaokoa maisha ya Carter na hata zile alama za vidole vyake, zilikuwa zake ila hakuwahi kuingia ndani ya chumba kile.
Akakanyaga mafuta, gari ile ilikuwa na injini kubwa hivyo aliweza kuwaacha mbali polisi wale, hakutaka kusimama na kujisalimisha, alipoona kwamba inawezekana polisi wale walikuwa wamewasiliana na polisi wengine, akamwambia Vivian kwamba ashikilie usikani.
“NA wewe?” aliuliza msichana huyo.
“Ni lazima niondoke garini, siwezi kuendelea mbele,” alijibu.
“Uondoke?”
“Ndiyo! Vinginevyo nitakamatwa...” alisema Benjamin.
“Unataka kuniacha?”
“Ndiyo! Vivian, unajua ukweli, nataka unisaidie kuiambia dunia ukweli,” alisema Benjamin.
“Sawa! Ila unakwenda wapi?”
“Popote pale, nitajifiicha, sitotaka kuonekana mpaka hapo dunia itakapofahamu ukweli kwamba sikuua,” alisema Benjamin.
Hakukukuwa na muda wa kupoteza, mahali walipokuwa, ilikuwa ni kwenye kijiji cha Hertrown ambacho kilikuwa pembezo mwa Jiji la Boston, barabarani kulizungukwa na miti, sehemu hiyo ilikuwa kama na pori fulani.
Gari likasimamishwa, harakaharaka Benjamin akamsogelea Vivian, akambusu na kisha kuteremka, alichokifanya ni kuingia ndani ya pori lile, Vivian akapiga gia na kuondoka mahali hapo.
Benjamin akaanza kukimbia kwa kasi kubwa, akiwa huko, akasikia king’ora cha polisi, akajua kabisa kwamba tayari gari hilo lilikuwa likipita mahali hapo.
Benjamin akaondoka mpaka katika mlima mmoja mkubwa, huko, kulikuwa na mawe mengi kama milima ya jijini Mwanza, akasimama kwenye kilele na kuanza kuangalia chini, aliliona gari lile alilopanda na Vivian likiwa limesimamishwa na magari matatu ya polisi yaliyokuwa mbele, aliweza kumuona mpenzi wake, Vivian kwa mbali akiwa ameteremka garini na kuongea na polisi waliokuwa wamemsimamisha, hakutaka kusubiri, alichokifanya ni kuanza kushusha mlima ule upande wa pili na kutokomea zake, hakutaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea huku nyuma.
****
Vivian aliendesha gari lile huku akiwa na maumivu makubwa moyoni mwake, kitendo mcha mpenzi wake, Benjamin kutafutwa kwa kosa la mauaji kilimuumiza sana kwani aliujua ukweli kwamba mpenzi wake hakuhusika katika mauaji hayo bali nyuma ya pazia kulikuwa na watu wengine ambao walihusika.
Hakuendesha gari kwa mwendo wa kasi kama ilivyokuwa kwa Benjamin, aliendelea kusogea mbele mpaka pale alipokutana na magari ya polisi ambapo akapigwa mkono na kuambiwa apaki pembeni, hakubisha, akafanya kama alivyoambiwa.
Polisi wale walipoliangalia gari lile, lilikuwa lilelile waliloambiwa kwamba ndani yake kulikuwa na Benjamin, mwanaume aliyekuwa akitafutwa sana kipindi hicho, wakaingia ndani ya gari na kuanza kupekua kila kona, mtu huyo hakuwepo.
“Benjamin yupo wapi?” aliuliza polisi mmoja.
“Benjamin yupi?”
“Ulikuwa na nani kwenye gari?”
“Peke yangu!”
“Haukuwa na mtu?”
“Hapana!”
Wakati mahojiano yakiendelea, lile gari la polisi lililokuwa likiwakimbiza likafika mahali hapo, moja kwa moja polisi hao wakateremka na kuanza kuelekea kule walipokuwa polisi wenzao na Vivian.
“Alikuwa humu,” alisema mmoja wa polisi waliofika mahali hapo.
“Benjamin alikuwa humu, huyu binti ni lazima atuambie yupo wapi,” alisema polisi mwingine, alikuwa miongoni mwa wale waliofika mahali hapo ambao ndiyo waliokuwa wakiwafukuza.
“Hakukuwa na mtu zaidi yangu!”
“Hapana! Tuambie yupo wapi!”
Japokuwa walimlazimisha Vivian kusema mahali alipokuwa Benjamin lakini msichana huyo hakutaka kuzungumza kitu chochote kile, msimamo wake ulikuwa uleule kwamba hakukuwa na mtu mwingine ndani ya gari lile zaidi yake.
Walichokifanya ni kumchukua na kumpeleka kituoni, walidhani kwamba angebadilisha msimamo wa majibu yake lakini aliendelea kusisitiza kwamba hakukuwa na mtu yeyote ndani ya gari zaidi yake kitu kilichowaweka polisi katika wakati mgumu wa kumpata Benjamin.
****
David hakutaka kutulia, bado mbele yake kulikuwa na kazi kubwa ya kujua yule mtumiaji wa namba iliyokuwa ikitumika kuwasiliana na Benjamin ilikuwa ni ya nani na ilitoka wapi.
Japokuwa simu yake ilichukuliwa lakini data zote za simu ile alikuwa amekwishazituma katika email yake hivyo akaingia na kuanza kuangalia. Alipoipata namba ile, akachukua programu aliyoitengeneza mwenyewe iliyoitwa Davy Hack kisha kuanza kuipekua simu iliyotoka namba ile.
Hukondipo alipopata majibu ya maswali yote aliyokuwa akijiuliza, akakutana na namba nyingi zilizokuwa zikiingia na kutoka ila kitu kilichompa uhakika kwamba mtu aliyekuwa akihusika zaidi alikuwa ni mtu ambaye namba yake inaishia na 69 kwani ndiye mtu aliyekuwa akipiga mara kwa mara.
“Huyu ni nani?” alijiuliza.
Hakutaka kuchelewa, kila swali alilokuwa nalo kichwani mwake ilikuwa ni lazima kupata majibu yake hivyo alichokifanya ni kuanza kuangalia usajili wa namba ile.
Kazi wala haikuwa kubwa, japokuwa watu pekee ambao wangeweza kuangalia namba ya usajili kwa undani zaidi walikuwa ni wale wenye mtandao husika lakini yeye akafanikiwa kwa asilimia mia moja, mtumiaji wa namba hiyo iliyokuwa ikipigwa mara kwa mara katika namba ya simu ya huyo aliyekuwa akimsumbua Benjamin aliitwa David Seppy.
Taarifa hizo hazikuishia hapo, ziliendelea kutoa zaidi taarifa na kuonyesha mahali alipokuwa akiishi, kila kitu kuhusu yeye ambacho hakikuwa na siri yoyote vilionekana.
David akashusha pumzi ndefu, hakuamini kwamba matukio mengi yaliyokuwa yakitokea yalipangwa na mzee huyo. Hakujua tatizo lilikuwa nini, alimfahamu rafiki yake, hakuwa mtu mwenye ugomvi na mtu yeyote, na hakujua kama kulikuwa na ulazima wa Benjamin kufahamiana na mzee huyo kwani walikuwa watu tofauti kabisa, sasa kwa nini kulikuwa kama na ukaribu fulani?
Alichokifanya cha zaidi ni kuangalia meseji zilizokuwa zikiingia na kutoka katika namba hizo mbili. Alipoziona, akashtuka kwani meseji hizo ndizo zilizoonyesha kila kitu kilichokuwa kikiendelea, David akashusha pumzi ndefu, akachoka, hakuamini kama mzee aliyekuwa akiheshimika, David Seppy ndiye aliyekuwa akihusika kwenye mauaji ya Carter, pia, mbali na hivyo, alijipanga kumuua Todd baada ya mwezi mmoja.
****
“Benjamin, niambie ukweli kuhusu hili linaloendelea,” alisema Harry, rafiki mkubwa wa Benjamin.
“Hakuna jipya, sikuhusika kumuua Carter.”
“Una uhakika?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo!”
“Mbona alama zako za vidole zimeonekana katika mwili wa Carter?” aliuliza Harry.
“Huwezi kuamini Harry, ila jua kwamba sikuhusika na chochote kile,” alisema Benjamin.
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
Benjamin aliamua kufunga safari kuelekea katika Mtaa wa Augestberg uliokuwa hapohapo Boston nchini Marekani. Hakuwa na sehemu nyingine ya kwenda zaidi ya hapo.
Alimwamini sana Harry, alikuwa rafiki yake mkubwa, walikuwa pamoja kila kona katika kipindi walichokuwa chuo. Hakuwa na sehemu nyingine ambayo aliona kustahili kukimbilia zaidi ya hapo, kwa Harry ndipo kulikuwa kila kitu kwa kipindi hicho.
Maneno aliyosema Benjamin bado yalimuweka Harry katika wakati mgumu, hakujua kama alitakiwa kumwamini Benjamin kama kweli hajaua au la, kila alipojiuliza swali hilo, alikosa jibu.
“Kwa hiyo tufanye nini?” aliuliza Harry.
“Nahitaji unisaidie.”
“Nikusaidie nini?”
“Nataka niwe na nawasiliana na David mara kwa mara, kuna kazi nimemwambia anisaidie. Harry, nimechanganyikiwa, sina hatia, sijui ni kwa nini muuaji aliamua kumuua Carter,” alisema Benjamin huku akionekana kuvurugwa kabisa.
Hakuwa na jinsi, kwa sababu alikuwa rafiki yake na alikuwa akikumbana na matatizo mengi, akaamua kuishi naye kwa kumficha, humo alipokuwa, hakutaka hata marafiki zake wengine wafahamu kama Benjamin alikuwa ndani kwake, si hao tu, bali hata mpenzi wake, Shakira naye hakutakiwa ufahamu kitu chochote kile.
Siku ziliendelea kukatika, Benjamin akaamua kuwasiliana na David juu ya mahali alipofikia hasa baada ya kumpa namba ile ambayo alitakiwa kuifuatilia, majibu aliyopewa, hakuyaamini kwamba nyuma ya kila kitu, alikuwepo mzee mwenye utajiri mkubwa nchini Marekani, Bwana David Seppy.
“Unasemaje?” aliuliza Benjamin huku akionekana kushtuka, Harry alikuwa pembeni yake.
“Nimefuatilia mawasiliano, nimegundua hilo, ushahidi upo, tena nikwambie kitu?’ aliuliza David.
“Niambie!”
“Anayefuata ni muigizaji Todd!”
“Unasemaje?”
“Hiyo ndiyo taarifa, kila kitu kinachoendelea kinajionyesha hapa, wanatumiana meseji pasipo kugundua kwamba ninafuatilia kila kitu,” alisema David kwenye simu.
Maneno aliyoyaongea yalikuwa mazito mno, yaliwachanganya wote wawili lakini pia walitaka kufuatilia kama kweli walivyokuwa wamewasiliana kwenye simu, Todd angeuawa kweli au la.
Wote wakabaki kimya, wakaenda pembeni ya chumba hicho na kubaki kimya kabisa. Vichwa vyao vikaanza kuwafikiria watu wawili, Bwana Seppy na Todd.
Kulikuwa na maswali mawili yaliyokuwa yakivitesa vichwa vyao, sababu ya Bwana Seppy kufanya mauaji hayo kwa watu waliopendwa na watu wengi, hawakujua kitu chochote kile.
“Kwa nini?” aliuliza Benjamin.
“Hata mimi najiuliza hilohilo! Kwa nini?”
“Ni lazima tukatoe taarifa polisi,” alisema Benjamin.
“Hapana! Ukifanya hivyo tutakuwa tunakosea,” alisema Harry.
“Kwa nini? La sivyo Todd atakufa, huoni kama itanisaidia hata mimi mwenyewe kuwa huru?” aliuliza Benjamin.
“Una ushahidi kama Bwana Seppy ndiye muuaji?” aliuliza Harry.
“Si David anao!”
“Sawa! Wewe unao?”
“Sina, mpaka David atakaponipa!”
“Nisikilize Ben, hatutakiwi kufanya mambo kwa kukurupuka, ni lazima twende kama wasomi, tukusanye ushahidi wa kutosha, hata kama Todd atauawa, si tatizo kwani kupitia kifo chake tutazidi kujikusanyia ushahidi wa kutosha, tukicheza, hatutoweza kumtia hatihani huyu mtu, tuwe na subira,” alisema Harry.
“Mpaka lini?”
“Sijui! Ila tuwe na subira!”
“Kwa hiyo tuache Todd auawe?”
“Kama inawezekana, tuache, haina jinsi,” alisema Harry, Benjamin akashusha pumzi ndefu.
Kuanzia siku hiyo, hakukuwa na mtu mwenye furaha, wlaimchukia sana Bwana Seppy ambaye mara kwa mara alikuwa mtu wa kuwasaidia watoto yatima na kufungua taasisi zake za kuwasaidia masikini huku nyuma ya pazia akiwa mtu wa matukio ya kikatili.
Hakukuwa na mtu aliyemshtukia, ilikuwa ngumu kugundua kwa sababu muda wote alijifanya kuwa mtu wa watu. Matendo yake maovu aliyaficha kwa kutumia kivuli cha misaada kwa watu masikini na wengine ambao hawakujiweza.
Serikali iliendelea kumwamini huku ikimpa tenda nyingi. Kwa watu watatu, Bwana Seppy alionekana kuwa mtu katili ambaye iliwabidi wamfikishe mahakamani haraka iwezekanavyo.
“Ni lazima huyu mtu ahukumiwe,” alisema Benjamin.
Kuanzia siku hiyo, wala hawakukaa sana, wakapata taarifa ambayo waliitegemea kuisikia siku za karibuni kwamba muigizaji chipukizi aliyekuwa na kipaji cha hali ya juu katika mapigano, Todd Lewis alikutwa akiwa amejiua ndani ya gari lake baada ya kujidunga dawa za kulevya aina ya Cocaine.
Taarifa ziliendelea kusema kwamba mara baada ya polisi kuingia ndani ya gari hilo, pembeni ya mwili wa Todd kulikuwa na fedha za noti, dola, yeni, euro napaundi.
Hawakujua sababu ya Todd kujidunga sindano hiyo, mwili wake ulichukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Calvary ambapo huko ndipo madaktari pamoja na polisi wangejua ni kitu gani kilichokuwa kimemuua, kama ni madawa ya kulevya peke yake au kulikuwa na kingine.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Todd Lewis, muigizaji aliyekuwa na jina kubwa duniani alikuwa akitoka katika Uwanja wa Kikapu wa Stapple Center kuangalia mechi ambayo iliwakutanisha wenyewe, La Lakers ikiongozwa na Shaq O’ Neil ambayo ilikuwa ikipambana na Chicago Bulls.
Alikuwa ameamua kusafiri kutoka jijini New York mpaka Los Angeles kwa ajili ya kuangalia mechi hiyo. Alipenda mchezo wa kikapu na hakutaka kabisa kukosa mchezo huo ambao ulikuwa ukizikutanisha timu kongwe, kali ambazo zilikuwa na nguvu mno katika kipindi hicho.
Nje ya uwanja huo, watu wengi walikuwa wakimsubiri, alikuwa na jina kubwa, ukiachana na mastaa wengi wa mchezo wa kikapu, pia siku hiyo Todd alikuwa gumzo kubwa, ndani ya uwanja huo, watu wengi walitaka kupiga naye picha, pale alipokuwa amekaa, watu walimsogelea na kuanza kujifotoa picha kadhaa na mpaka mchezo huo unamalizika, kulikuwa na watu wengi waliopata nafasi ya kupiga naye picha.
Wengine hawakuridhika, hata walipokuwa wakitoka, bado mashabiki walikmfuata Todd, walitaka kupiga naye picha huku wengine wakitaka kusainiwa vitabu vyao.
Hayo yalikuwa maisha ya usupastaa, walimheshimu kwa kuwa aliifanya kazi yake ipasavyo, wengi walipenda kutazama filamu zake, kwa kifupi, Todd aliwavutia watu wengi mno.
Alipomaliza kuwasainia watu vitabu vyao na hata kupiga nao picha, kama kawaida akaifuata gari yake ya kifahari, Ferrari nyekundu na kisha kuingia, kilichofuata ni kuanza safari ya kuelekea hotelini kabla ya kurudi New York alipokuwa akiishi siku inayofuata.
Akaliwasha gari hilo na kuondoka mahali hapo. Moyo wake ulijisikia faraja, hakuamini kwamba mwisho wa siku angekuwa na umaarufu mkubwa kama aliokuwa nao katika kipindi hicho.
Katika kipindi cha nyuma alipokuwa akianza, mambo yalikuwa magumu mno, alipambana usiku na mchana lakini mwisho wa siku, alifanikiwa kuwa kama alivyokuwa, hakukuwa na kitu kingine kilichokuwa kikiendelea zaidi ya kukusanya fedha na kuwa nazo zaidi ya zile alizokuwa nazo.
Wakati safari ikiendelea na kuyakuta makutano ya Barabara za St. Barnaba na Morovian ambayo ilikuwa ikienda mpaka katika Mtaa wa Butterfly uliokuwa umbali kama wa kilometa tatu, akashtuka baada ya kuona gari moja likija kwa kasi nyumba yake, lilikwenda mbele yake kwa mwendo wa kasi na kisha kusimama kwa katikati ya barabara, tena kiubavuubavu.
Kama haukuwa umakini wake mkubwa, basi angeweza kuligonga gari hilo. Kwa ustadi mkubwa, Todd akafunga breki na kisha kusimama, alibaki akihema kwa nguvu, mbele yake ilionekana ajali kubwa ambayo pasipo kutumia uwezo wake basi angeweza kuligonga gari hilo.
Huku akijiuliza ni kitu gani kinaendelea, wanaume wawili wakateremka kutoka kwenye ile gari na kuanza kuelekea kule alipokuwa. Hakujua watu hao walikuwa wakina nani na walihitaji nini kutoka kwake.
Mahali hapohakukuwa na magari, ilikuwa usiku sana na magari hayakuwa yakipita mara kwa mara, hasa katika barabara hiyo ya magari yaendayo kasi. Akashindwa kuliwasha gari lake, watu wale walikwenda kwa kasi mpaka pale lilipokuwa gari lake, wakamwambia afungue mlango vinginevyo wangempiga risasi humohumo.
Hakuwa na jinsi, hakutaka kupinga, kitu cha kwanza kabisa, akashusha kioo cha mbele cha mlango wa upande mwingine, mwanaume mmoja akaingia na kumwamuru aendeshe mpaka sehemu waliyotaka wao waelekee.
“Naomba uniache, kama unataka gari chukua,” alisema Todd huku akitetemeka.
“Unadhani sisi tunataka gari?” aliuliza mwanaume huyo huku akiwa na bastola mkononi mwake.
“Hata kama unataka kiasi chochote cha fedha, nitakupa, naomba uniache...” alisema Todd, tayari machozi yakaanza kububujika mashavuni mwake.
Mwanaume yule mwingine akapita upande wa pili, akaufungua mlango na kumshusha Todd kisha kumpeleka katika gari lao walilokuja nalo huku yule mwingine akiachwa katika gari lile kwa ajili ya kuondoka nalo.
Kila kitu kilichokuwa kikifanyika mahali hapo, kilifanyika kwa haraka sana, tukio zima lilichukua sekunde arobaini na tano tu, tayari wakaondoka huku wakiwa na Todd ndani ya gari.
“Naombeni mniacheee...” alisema Todd.
“Hutakiwi kupiga kelele...” alisema mwanaume mmoja huku akimnyooshea bastola.
“Nimefanya nini? Naombeni msiniue..” alisema Todd.
“Kwani kila anayeuawa kuna baya amelifanya? Hakuna kitu kama hicho, kuwa mpole,” alisema mwanaume huyo.
Baada ya hapo, hawakutaka kuongea kitu chochote kile, wakaondoka naye huku garini wakiwa kimya, kwani hata Todd naye aliyetaka kuzungumza maneno mengi aeleweke na hivyo kuachwa, aliambiwa akae kimya kwani suala la kumuua lisingeweza kuzuilika hata kidogo.
Walikwenda mpaka katika barabara nyingine ya Queen Elizabeth I ambayo ilikuwa ikienda moja kwa moja mpaka kwenye jumba la makumbusho ya Lincoln, hawakufika huko, wakakata kulia na kisha kuchukua barabara nyingine ambayo iliwapeleka mpaka katika sehemu ambayo haikuwa na watu, giza lilitawala, gari likasimamishwa mahali hapo.
“Naomba mnisamehe....”
“Halafu?”
“Niondoke, nitawalipa kiasi cha fedha chochote mnacholkitaka....”
“Halafu?”
“Naomba mnisamehe...”
Hawakutaka kupoteza muda, saa zao zilionyeshwa kwamba tayari ilikuwa ni saa nane za usiku hivyo walitakiwa wafanye haraka, wamuue na kisha kuendelea na mambo yao.
Walichokifanya ni kumkaba kooni, tena kwa nguvu kuhakikisha anakufa na kisha kufanya kile walichoambiwa kukifanya. Mwanaume mmoja mwenye nguvu ndiye aliyetumika kumuua Todd ndani ya gari hilo.
Dracula hakutaka kwenda katika lile gari kwani aliamini kwamba vijana wale wangefanya kama jinsi alivyowapa maagizo, kweli wakafanya. Kilichofuata baada ya kuhakikisha kwamba Todd amekufa ni kumchoma sindano iliyokuwa na madawa aina ya cocaine, walipomaliza, wakachukua nailo zenye unyevuunyevu ambazo kwa kutumia utaalamu wao waliweza kuweka alama za vidole za Benjamin na kisha kuziweka katika shingo ya Todd na sehemu nyingine za mwili.
“Vipi?”
“Tayari!”
“Mbebeni mkamuweke ndani ya gari lake, pia wekeni na hizi fedha,” aliagiza Dracula huku akiwapa noti ambazo zilitakiwa kuwekwa ndani ya gari hilo, vijana wale wakafanya kama walivyoagizwa, wakaubeba mwili wa Todd na kisha kuupeleka garini mwake na kuziweka noti zile.
“Tuondokeni!” alisema Dracula baada ya kumaliza kila kitu. Wakaondoka mahali hapo huku kila mmoja akiwa na furaha ya kukamilisha kazi waliyokuwa wamepewa.
****
Hakukuwa na mtu aliyeamini mara baada ya taarifa juu ya kifo cha Todd zilipotolewa katika vyombo mbalimbali vya habari nchini Marekani. Wengi walipigwa na bumbuwazi, kile walichokisikia, hakikuaminika kwao kwamba yule muigizaji, mwenye jina aliyekuwa akivuma sana kipindi hicho, Todd Lewis alikutwa amejidunga madawa ya kulevya kwakujiovadozi.
Watu wakapigiana simu, kila aliyesikia, hakutaka kukubaliana na habari hiyo kwani miongoni mwa watu waliokuwa wakifanya vizuri kipindi hicho, alikuwa huyo Todd, sasa kwa nini afe mapema hivyo? Tena mbaya zaidi alikutwa akiwa amejiovadozi madawa ya kulevya kitu ambacho kiliwachanganya watu wote kwani Todd hakuwa mtumiaji wa madawa hayo hata mara moja.
Wengi wakaenda katika Hospitali ya Calvary kujionea, huko, watu walikuwa wakilia kwani ndipo walipopata taarifa kamili kwamba muigizaji huyo alikutwa ndani ya gari yake ya kifahari ya Ferrari akiwa amejiovadozi madawa ya kulevya.
“Haiwezekani Bwana! Huyu jamaa hakuwa mlevi kabisa,” alisema jamaa mmoja.
“Ndiyo! Hata mimi nimeshangaa sana, yaani Todd awe mlevi wa madawa ya kulevya! Haiwezekani hata kidogo,” alisikika jamaa mwingine.
Kila mmoja alikuwa sahihi kabisa, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa na shaka na Todd kwamba alikuwa mtumiaji wa madawa hayo, taarifa hizo zikaendelea kusambaa kila kona mpaka ndani ya saa moja tu, dunia nzima ilijua nini kilitokea nchini Marekani.
Hofu zikaanza kutanda, taarifa zilizosema kwamba ndani ya gari la marehemu kulikutwa noti za fedha kutoka nchi mbalimbali ziliwashtua sana kwani hata siku ambayo Carter alikutwa akiwa amekufa ndani ya chumba cha hoteli, fedha kama hizo zilikutwa kitu kilichowafanya watu kuona cha kawaida ila baada ya fedha hizo kukutwa ndani ya gari hilo, wakagundua kwamba inawezekana hizo fedha zilibeba ujumbe fulani.
“Kama huyu Benjamin ndiye aliyemuua Carter, basi inawezekana akawa amemuua na Todd pia,” alisema jamaa mmoja wakati alipokuwa supamaketi, katika sehemu ya kuuzia magazeti na majarida mbalimbali.
“Inawezekana kabisa...hebu tuwasikilizie polisi tuone watasemaje,” alisema jamaa mwingine.
Hilo ndilo lililokuwa vichwani mwa watu wengi, kila aliyesikia namna gari hilo lilivyokutwa, alikuwa na uhakika kwamba muuaji alikuwa yuleyule, kijana wa chuo mwenye akili nyingi, Benjamin Saunders.
Hilo ndilo lililotokea, baada ya siku mbili, taarifa zikatolewa kwamba alama za vidole vya Benjamin vilikuta katika mwili wa Todd, yaani kabla ya kumchoma sindano, alimkaba kooni na kumuua na ndipo alipofanya mambo mengine likiwepo lile la kumchoma sindano ya madawa ya kulevya ili ionekane kwamba alikuwa amejiovadozi.
Hakukuwa na mtu aliyejua sababu ya Benjamin kuwaua watu maarufu, wengi waliuliza, kwenye mitandao wakatoa maoni yao lakini hakukuwa na mtu aliyefahamu lolote lile juu ya sababu ya Benjamin kuwaua watu maarufu na kisha kuacha noti za fedha mbalimbali karibu na miili yao.
“Ila kwa nini anawaua watu maarufu?’ aliuliza mwanamke mmoja.
“Hata mimi sifahamu! Kwanza nashangaa...”
“Halafu nasikia huyu Benjamin mwenyewe ana akili sana darasani.”
“Hata mimi nimesikia hivyohivyo na watu walipokwenda, wakakuta kweli ana akili sana, inawezekana ndiyo ikawa sababu ya kuwasumbua polisi na wananchi kumtia nguvuni,” alisema jamaa mmoja.
Bado watu walitakiwa kumtafuta Benjamin lakini hakukuwa na yeyote aliyempata, kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya dola milioni ishirini na tano ambazo zilikuwa ni zaidi ya bilioni hamsini kilitolewa lakini bado majibu yalikuwa yaleyale kwamba mitaani hakuonekana kabisa.
Maofisa wa FBI walikuwa na kazi kubwa, hakukuwa na aliyeamini kwamba mpaka muda huo Benjamin hakuwa amepatikana. Taarifa zilizopelekwa katika meza ya mkuu wa kitengo chao zilisema kwamba walitakiwa kupewa muda zaidi kwani inawezekana kulikuwa na mtu hatari ambaye alikuwa akimlinda Benjamin ili asiingie katika mikono yao.
“Kwa hiyo tumeshindwa?” aliuliza mkuu wa FBI, Bwana Connery Gibson.
“Hapana!”
“Sasa mbona hapatikani?”
“Ngoja tuendelee nadhani kuna kipindi tutampata tu.”
Hakukuwa na muda mwingine wa kupoteza, kama kusubiri, walisubiri kwa kipindi kirefu lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale, kuna kipindi walijiona kama kushindwa hivyo walitakiwa kuwasiliana na Shirika la Kijasusi la FBI ili wawasaidie kwani huyu Benjamin, japokuwa walijua kwamba hakuwa polisi au mtu yeyote mwenye uwezo wowote wa kijeshi lakini alikuwa mgumu mno kupatikana.
Walichokifanya ni kujiongeza tu, wakawagawa vijana wao katika miji mingine kama Los Angeles, Miami, Texas na sehemu nyingine ili kuhakikisha Benjamin anapatikana haraka iwezekanavyo.
“Nadhani hatotushinda tena, si ndiyo?”
“Tutegemee hilo mkuu!”
****
Harry alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokuwa amekiona kwamba muigizaji maarufu duniani kwa kipindi hicho, Todd Lewis aliuawa ndani ya gari lake huku wauaji hao wakitaka kuionyeshea dunia kwamba alijiovadozi madawa ya kulevya kitu ambacho hakikuwa kweli kabisa.
Kilichomchanganya zaidi ni alama za vidole zilizopatikana ndani ya gari lile na hata katika mwili wa Todd ambazo zilionyesha kwamba ni Benjamin ndiye aliyefanya mauaji hayo.
Hapo ndipo alipoamini kwamba Benjamin hakuhusika katika mauaji, kulikuwa na watu wengine waliokuwa wakiyafanya huku wakiweka alama za vidole vyake katika kila tukio walilolifanya.
Alimwangalia Benjamin mara mbilimbili, hakuamini kilichokuwa kimetokea, alimuonea huruma sana kwamba inawezekana vipi mtu auwe na kisha kuweka alama za vidole vyake? Alimuuliza Benjamin lakini mwanaume huyo alimwambia ukweli kwamba hakujua kitu chochote kile.
“Sifahamu!” alisema Benjamin.
“Kuna kitu unajua!”
“Harry! Sifahamu chochote, huyu mzee Seppy ndiye anahusika, yaani ni lazima dunia ijue kwamba yeye ndiye anahusika, vinginevyo, nitahukumiwa kwa mauaji ambayo sikuyafanya,” alisema Benjamin.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tutatoa vipi taarifa polisi? Watakukamata!”
Huo ndiyo ulikuwa mtihani mwingine, hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya, hawakuwa na ushahidi wa kutosha hivyo kama wangekosea sehemu moja basi lingekuwa tatizo kubwa kwao, walitakiwa kujipanga ili hata kama watakwenda kutoa taarifa polisi basi kusiwe na tatizo lolote lile.
David ndiye alikuwa na ushahidi kamili lakini bado kulikuwa na kitu kimoja kilichokuwa kikiwatatiza, kila mauaji yalipotokea, kulikuwa na fedha zilizokuwa zikiachwa, zile fedha zilimaanisha nini? Kila walichojiuliza, walikosa jibu.
“Sijui zinamaanisha nini, ila kama nikipewa muda, nitaweza kufahamu tu, kuna kitu,” alisema Benjamin huku akionekana kama mtu aliyekuwa akijifikiria sana.
“Hili ndilo la msingi, sidhani kama hata FBI watakuwa wanajua maana, huu utakuwa ni ujumbe, ujumbe gani sasa? Hebu tuhangaike mpaka tufahamu,” alisema Harry.
Wote wakakubaliana na kuingia kazini kuhakikisha wanajua kwanza maana ya zile fedha za noti zilizokuwa zikiwekwa katika mauaji yaliyokuwa yakitokea.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment