Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

TSSI 01 PRISONER - 3

 








Simulizi : TSS 01 Prisoner

Sehemu Ya Tatu (3)







Wakati akiwa anatoka, nje ya SuperMakert alikutana na kijana mmoja. Kijana huyu ni mmoja wapo kati ya wale wawili walioitaka kazi ya kuja kumteka TSSI 01.



“Kaka vipi?" Jamaa huyo alimsalimia Hemedy Bhachu. Usoni mwake palitangaza shida ya jambo fulani. TSSI 01 aliliona hilo.



“Safi tu. Niambie" TSSI 01 alijibu.



“Ulikuwa unaelekea wapi?" Jamaa alimuuliza.



“Naelekea Donge"



“Dah! Broo hata mimi naelekea huko huko. Samahani lakini, kama hutojali naomba unipe lifti ukaniache mitaa hiyo" Jamaa yule aliongea kwa malalamiko kiasi ili aonewe huruma. TSSI 01 alimuangalia usoni kwa mshangao. ‘Amejuaje kama mimi nimekuja na usafiri hapa?' alijiuliza mwenyewe kimoyo moyo. Ndio lazima ashangae, maana hata gari lake alilokuja nalo hapo bado lilikuwa lipo mbali nae. Labda kama angekuwa amelifikia au hata kulifungua mlango wala asinge shangaa mtu huyo kumuomba lifti. Sasa iweje mtu huyo amuombe lifti wakati yeye hakuwa na kumbukumbu kwamba mtu huyo alikutana nae mahala hapo kabla? Au labda alimuona wakati anaingia hapo.



“Aaaa! Samahani broo, nilikuona ukiingia hapa na ule usafiri wako na ndio maana nikakuomba unipe lifti kwahiyo usishangae sana kuona nimejuaje kwamba umekuja na usafiri hapa" Jamaa huyo aliongea huku akiwa anachekacheka kama mwehu ili kumzuga.



“Ok. Twende" TSSI 01 alimuambia huku akianza kupiga hatua kuliendea gari lake. Kwa kiasi fulani alikuwa na wasiwasi na mtu huyo.



“Asante kaka" Jamaa huyo aliongea huku akimfuata nyuma TSSI 01.



Walipofika kwenye gari. TSSI 01 Hemedy Bhachu aliweka mizigo yake kwenye buti la gari. Na kuenda kwenye mlango wa dereva, akaufungua na kuingia huku yule jamaa akiingia upande wa nyuma. Safari ikaanza, ndani ya gari pakiwa kimya. Walipofika maeneo ya Dunia Hoteli. Jamaa akatoa bastola yake na kumuwekea TSSI 01 kwenye shingo. TSSI 01 alishtuka ila alitulizwa na sauti ya kuamrisha ya jamaa huyo.



“Tulia hivyo hivyo ukileta tabu kidogo basi ndio utakuwa umechukua tiketi ya kwenda kuzimu. Fuata malekezo yangu ili uongeze muda wako wa kuishi kabla kifo hakija kukuta hivi punde" Jamaa huyo alimuambia na alipoona TSSI 01 yupo kimya huku akiendesha gari mdogo mdogo. Akaendelea.



“Fuata uelekeo wa shule ya sekondari Tanga School”







“Sipajui”Hemedy Bhachu alijibu. Alijibu jibu la uongo. Sio kwamba ni kweli alikuwa hapa jui. Ila alijibu hivyo ikiwa ni moja ya njia ya kutafuta kujiokoa.



“Utaenda tu hata kama hupajui. Nyoosha na hiyo njia moja kwa moja” Jamaa huyo alimuambia.



TSSI 01 alifuata kama alivyoambiwa. Wakawa wanafuata uelekeo wa njia ya sekondari ya Tanga School. Walipofika kwenye kona ya kuingilia kwenye shule hiyo kabla ya kuvuka viwanja vya mipira vya shule. Jamaa alitoa simu na mkono mmoja huku mwengine ukuwa bado umemuwekea bastola TSSI 01. Akampa maelekezo mwenzake aliekuwa akimfuata nyuma na gari kwa umbali mrefu.



TSSI 01 alipoona hivyo. Akajua hiyo ndio nafasi yake ya kupona. Akaongeza mwendo wa gari kwa ghafla na kulifanya gari hilo liende mbio mbele. Kitendo hicho kilimfanya jamaa kubwata kwa sauti ya ghadhabu huku akiiweka simu yake mfukoni. Mfuko wa shati alilovaa. Bila kutarajia. TSSI 01 alichuna breki za ghafla na kumfanya jamaa huyo aende mbele huku bastola yake ikikosa muelekeo. Hakuwa amefunga mkanda. Kosa ambalo muda mrefu TSSI 01 alikuwa akiliombea mtu wake asilikumbuke.



TSSI 01 alimpiga na kiwiko cha mkono wa kushoto baada ya sura ya jamaa kuja mbele kwa msukumo wa breki. Jamaa bastola ikamdondoka, ikaenda kwenye mapaja ya TSSI 01 huku mikono ya jamaa ikilishika pua lake kwa maumivu aliyopatiwa ya ghafla. Ngumi kali ikapenya katikati ya mikono ya jamaa iliyokuwa imeshika pua kwa maumivu na kwenda kugota kwenye koromelo la jamaa.



Jamaa alitoa macho huku mikono yake ikiwa hewani asijue afanye nini. Alaaa!! Kumbe ilikuwa ndio staili hake ya kufa hiyo. Mikono iliyokuwa hewani taratibu ikashuka chini na jamaa huyo akatulia kimya huku macho akiwa bado ameyakodoa. TSSI 01 akamvuta kwenye siti za mbele na yeye akahamia kwenye siti za nyuma upande aliokuwa amekaa marehemu jamaa. Kisha akachukua simu iliyokuwa kwenye mfuko wa shati la jamaa. Akaitafuta namba aliyotoka kuwasiliana nayo muda mfupi na kuitumia ujumbe. ‘Njoo kwenye hili gari taratibu na ficha bastola yako maana tayari nimemdhibiti’. Huo ndio ujumbe alioutuma.



Muda kidogo iliegeshwa gari pembeni ya gari la Hemedy Bhachu. Akashuka jamaa mwengine. Alishuka bila wasiwasi wowote baada ya kuhakikishiwa usalama na mwenzake kama yeye alivyodhani. Akaenda upande ule alioingia mwenzake. Upande wa kushoto siti za nyuma. Akagonga kioo ili alieko ndani afungue kioo kama sio mlango kabisa. TSSI 01 alishusha kioo huku bastola yake yake akiwa amemuelekezea jamaa huyo.



“Usilete mchechetu wa aina yoyote. Ingia kwenye gari taratibu. Usitake nilichokifanya kwa mwenzako nikifanye na kwako”



Jamaa baada ya kuchimbiwa biti hilo. Akaingia na kukaa kwenye siti. Dhahiri TSSI 01 aliuona uoga aliokuwa nao jamaa huyo baada ya kumnyooshea bastola. “Hawa wengine wala hizi kazi hawaziwezi” alijisemea mwenye kimoyomoyo.



“Najua mmetumwa na Mr Hanein si ndio?" Alimuuliza hivyo na jamaa akaitikia kwa kichwa kukubali.



“Na wale mapacha ni watoto wake si ndio?" Jamaa pia akaitikia kwa kichwa kukubali.



“Kwenye kambi yenu mpo wangapi na iko wapi?”



“Tupo sita na huyo jamaa hapo ni wa saba. Kambi yetu ipo.....” jamaa alikatishwa na sauti ya TSSI 01.



“Acha kelele bwana wewe. Alaa! Unaongea hadi ambayo hujaulizwa. Sasa umefika wakati wa kuungana na huyu mwenzako huko alipo”



Jamaa baada ya kusikia hivyo akashtuka, macho kayatoa pima asiamini aichokisikia. Akataka kuongea kitu, ila alikatishwa na ngumi iliyotua juu ya mdomo wake. Akataka kujitetea ila hakufanikiwa kwa hilo baada ya kupigwa pigo moja la ajabu la kwenye shingo. Unadhani basi hata aliweza kunyanyua kope zake? Labda kama angesaidiwa lakini sio kwa uwezo wake mwenyewe.

Alienda kuungana na mwenzake kama alivyoambiwa.

Alikuwa ni mfu tayari!.



TSSI 01 aliwatoa mmoja mmoja na kuwaingiza kwenye gari lao alilokuja nalo jamaa wa pili. Wakati akiwa katika zoezi la kumuingiza marehemu yule wakwanza kwenye gari lao. Simu ya yule marehemu ikaingia ujumbe. Akaichukua na kuufungua huo ujumbe ulioingia muda huo. ‘Tayari mshammaliza huyo mpumbavu?’ ujumbe ulisomeka hivyo. Akatabasamu na kuujibu huo ujumbe. ‘Hapana mkuu. Tumemalizwa sisi wapumbavu na hapa tulipo ni maiti. Fanyeni hima mje kuchukua mizoga yetu huku’ aliujibu hivyo na kuiacha simu hapo hapo.



Akatoka kwenye gari hilo huku akiiacha simu ile ikiita pasi na kupata wa kuipokea. Bilashaka ujumbe ule uliwachanganya walioupata. Akaingia kwenye gari lake na kulitoa mahala hapo. Akatoa simu yake na kuibonyeza bonyeza kisha akaiweka sikioni. Akatulia kwa muda kisha akasema “Nakuja” akaitoa simu hiyo sikioni na kuirudisha katika mfuko wa suruali yake.



Katika jumba la maficho lililopo Pongwe. Nyuso za waliokuwepo ndani ya jengo hilo zilionekana kusawajika kutokana na taarifa ya ujumbe walioupokea dakika chache zilizopita. Hawakuuelewa hata kidogo ujumbe huo uliotumwa na vijana walioenda kumteka au kufanya mauaji ya aliekuwa adui yao.



Swali walilokuwa wakijiuliza ni kwamba. Inawezekana vipi watu wafe halafu watume ujumbe eti wamekufa na wanaomba maiti zao ziende kuchukuliwa?.

Ajabu!

Kilichowachanganya zaidi ni vile kutopokelewa simu muda wote. Wakaona hapo kutakuwa na namna yoyote na wala si swala la kuchukulia mzaha mzaha hilo.



“Embu ‘track’ hiyo namba yao tujue wapo sehemu gani. Wasituchanganye vichwa vyetu hawa” Mr Hanein aliongea.



Atu aliiendea ‘laptop’ na kuja nayo hapo sebeleni. Baada ya kuiwasha. Akaminyaminya na kuingia sehemu anazozijua yeye. Kisha akaitia namba ya simu ya watu wale sehemu iliyomtaka kufanya hivyo. Baada ya muda ikaanza ku‘search’. Kwenye kioo cha ‘laptop’ palitokea ramani ya mji huo wa Tanga na kwenye ramani hiyo palionekana kidoti cha bluu. Sehemu hiyo yenye kidoti cha bluu. Ikajaa mbele na kuwa kubwa zaidi.



Hapo pakaonekana mistari mistari mingi inayoashiria kuwa ni barabara na vichochoro vya mtaa huo ulioko kwenye hiyo ramani. Yakatokea na majina ya mitaa hiyo hata pale pia kwenye kile kidoti palitokea jina. ‘Tanga Technical School’ palisomeka hivyo.



“Baba itakuwa kuna tatizo maana hichi kidoti hakisogei pahali popote kuashiria kwamba hii simu yao ipo hapa hapa” Atu aliongea huku akiwa bado macho yake yapo kwenye kioo cha kifaa hicho.



“Embu piga tena hiyo namba yao” Mr Hanein aliongea. Paskali akapiga tena lakini majibu yalikuwa ni yale yale kwamba simu haina mpokeaji.



“Sasa tunafanyaje?” Ata aliuliza.



“Inabidi muende mkaangalie kama kuna usalama” Mr Hanein aliongea.



“Nani na nani?” Atu alimuuliza. Kipindi hicho alikuwa ameiacha ‘laptop’ pembeni.



“Wewe na kaka yako na kuanzia sasa huyu mtu aangaliwe kwa jicho la umakini sana maana anaweza akaniharibia mipango yangu wakati sijaanza kutimiza hata lengo moja” Mr Hanein aliongea na kuwafanya vijana hao watikise vichwa kukubaliana na agizo hilo walilopewa na baba yao.



Wakatoka hapo na kila mmoja akaingia kwenye chumba chake. Walipotoka walikuwa wapo tayari kwenda huko walipo agiziwa. Wakaongea mawili matatu na kutoka nje ya nyumba hiyo huku Mr Hanein akiwasisitizia wawe makini huko wanapoenda.



TSSI 01 aliegesha gari lake nje ya kituo cha polisi Chumbageni. Akashuka kwenye gari na kupiga hatua kuingia ndani ya kituo hicho. Moja kwa moja hadi katika ofisi ya IGP Taure. Alipofika alikaribishwa kiti. Akakaa na kumueleza yote yaliyotukia kwa siku hiyo.



“Kwahiyo maiti zao umeziacha ndani ya gari lao?” IGP alimuuliza.



“Ndio. Unadhani nizichukue nizipeleke wapi?”



“Sawa. Na vipi kuhusu usalama wako? Maana inavyoonekana watu hao wana kufuatilia sana na ipo siku watakuja kukuotea tu”



“Anko kusema ukweli nipo makini sana kuliko umakini wenyewe. Hawawezi na hawatoweza kwasababu nimewazidi akili hadi uwezo”



“Sawa. Kwa sasa unampango gani. Maana naona hutaki kabisa kulimaliza hili sekeseke wakati njia tayari unayo”



“Kwasasa acha kwanza niende nyumbani nikapumzike maana jana sikupata usingizi mzuri baada ya kumuachia nyumba yule mwanamke” akainuka kwenye kiti alichokaa. Kisha akasema. “Tuma vijana wako wakachukue ile mizoga isije ikawaletea shida watu wengine” akaondoka huku akimuacha IGP Taure akisikitika huku usoni mwake pakiwa na tabasamu.

Tabasamu la hofu!



“Huyu kijana huyu!”. Alijisemea mwenyewe. Kisha akanyanyua simu yake ya mezani na kuibonyabonya.



“Niitie Inspekta Salum osifini kwangu” akakata simu na kutulia. Baada ya dakika mbili. Paliingia kijana mwenye umri kati ya miaka thelathini hadi thelathini na tano. Alikuwa mrefu wa haja. Akapiga saluti na kusubiri kuambiwa alichoitiwa.



IGP Taure akampa maelekezo yote ya kwenda kuchukua miili ya zile maiti kule shule ya sekondari Tanga School. Inspekta Salum akatoka humo. Akachukua askari watano watatu wakiwa na silaha. Wakapakia kwenye la polisi na safari ya kwenda huko walipotakiwa waende ikaanza. IGP Taure alichomuambia Inspekta salum ni kwamba. Wakifika pale wachukue hizo maiti na hiyo gari. Wasifanye uchunguzi wala mahojiano yoyote na raia watakao wakuta hapo.



Kipindi ambacho Inspekta Salum akipokea maagizo kutoka kwa IGP Taure. Ndio muda ambao Ata na Atu wanafika eneo la tukio. Wakapaki gari lao mbali kidogo kisha wao wakashuka na kuliendea gari la vijana wao lililokuwa limeegeshwa pembeni ya uwanja wa mpira wa shule hiyo. Walikuwa waangalifu na umakini juu yake. Hawakwenda hovyo hovyo. Waliangalia kila pande na kukuta wachezaji wa mpira wakiwa katika uwanja huo wakifanya mazoezi jioni hiyo kabla hawajaingia kwenye mchezo.



Hawakuwatilia shaka watu hao maana waliona kila mmoja akiwa katika mazoezi yake. Wakalisogelea lile gari kwa umakini mkubwa. Kisha wakafungua milango na walichokiona ndicho walichokitegemea. Miili ya vijana wao ikiwa humo ndani katika picha ya kifo kifo tu.



Ghafla eneo hilo likaingia gari la polisi kwa kasi kubwa huku likiacha vumbi jingi. Vijana waliokuwa wapo hapo kwaajili ya kuchukua mazoezi walipiga shangwe na kelele nyingi kwa kitendo hicho. Askari walishuka kwa haraka kwenye gari hilo na wote macho yao yakiwa kwenye gari aina ya Alteza.

Gari lililokuwa na maiti za vijana wa Hanein.



“Shit!” Ata aling'aka kwa mfadhaiko baada ya kushuhudia gari la polisi likiwa eneo hilo.







Inspekta Salum alishuka kwenye gari na kuanza kupiga hatua kuifuta ile Alteza. Alteza iliyokuwa amesimama Ata na Atu wakiwa wamegwaya na tukio hilo la kuingia askari kwa muda mfupi tu tangu wao waje. Wakajua kivyovyote kuna mtu aliwekwa kwaajili ya kuwachunguza. Wakajua huo ulikuwa ni mtego na hapo wasipofanya jambo wanaweza kwenda jela kwa kesi hiyo.



Ata alimpiga jicho dada yake na kukutana na sura iliyomuashiria kufanya kitu. Ghafla Inspekta aliekuwa anakuja upende wao alianguka chini baada ya kushambuliwa na kitu kisichojulikana. Damu kwenye bega ndizo ambazo zilionekana kwenye mwili wa Inspekta Salum aliekuwa akigaagaa chini kwa maumivu.



Muda huo Ata na Atu walikuwa wakikimbia kuizunguka ile Alteza kwenda upande wa nyuma. Upande ambao askari hawakuwepo. Hapo wale askari baada ya kuona mkuu wao akigaagaa chini. Walianza kuishambulia ile gari ambayo nyuma yake wamejificha Ata na Atu. Muda huo wale wachezaji wa mpira hakukuwa na hata mmoja hapo uwanjani aliesalia. Ndio. Wakae wasubiri nini wataki wameshuhudia na kusikia milio ya risasi ikipigwa mahala hapo?.

Wote wakatimka!.



Wale askari wakaacha ghafla kupiga risasi baada ya kugundua wanachofanya ni upumbavu. Ni upumbavu ndio. Kwasababu wanachofanya hapo ni kuliharibu lile gari na wala sio kuwadhuru wale wahalifu. Maana wahalifu walikuwa wamejificha nyuma ya hilo gari na wala hawakuathiriwa na risasi zao.



Walichofanya sasa hivi ni kulisogelea lile gari kwa uangalifu. Wakajuta. Walijuta baada ya kuja na silaha tatu tu huku wale wengine wawili wakiwa mikono mitupu. Labda ni hizo pingu zilizokuwa zikining'inia viunoni mwao. Pingu ambazo hazikuwa na maana yoyote kwa wakati huo. Hazikuweza kushambulia kwa chochote.

Duh!.



Ghafla wale askari watatu waliokuwa na silaha. Walienda chini. Sio kwamba walienda chini kwa kupenda? La hasha! Bali walienda chini kutokana na shambulizi la ghafla lililowakumba. Wale wawili ambao hawakuwa na silaha walijikuta wakirudi mbio huku wakipiga mayowe ya hofu kwa kuwaona wenzao wakiwa chini pasi na kusikika mlio wa aina yoyote. Nini hii!?. Moja kwa moja walijificha nyuma ya gari lao.

Kizaazaa!.



Ata na Atu walipoona askari wale wameingiwa na hamaniko kuu. Wakatoka nyuma ya ile Alteza waliojificha na kukimbilia mahali ambapo wameacha gari lao. Walipofika huko. Waliingia na kuliondoa gari hilo mbio mithili ya mshale uliochiwa nyikani. Wale askari wawili ambao hawakukumbwa na shambulizi. Wakabaki wakilichungulia lile gari pasi na kusoma hata namba zake. Watasomaje namba zake wakati gari hilo limeingia watu waajabu walio waangusha wenzao kimya kimya pasi na kusikika milio yoyote?.



Wakajitoa mafichoni kikakamavu baada ya kukumbuka kuwa wao ni askari. Hapo wakajicheka kwa upumbavu walioufanya wa kutotafuta mbinu yoyote hata japo ya kugundua ni wakina nani waliofanya tukio hilo. Sio kwamba walicheka kwa furaha! La hasaha! Bali walicheka kwa kutanabai kuwa wao ni askari wazembe kupata kutokea katika jeshi la polisi.

Cheko la kizembe!.



Wakajitoa pale na kuwafuata wenzao waliokuwa bado wapo chini. Ila safari hii hawakuwa wakigaagaa tena. Walikuwa wapo kimya kama wafu. Wakawakagua mmoja mmoja na kugundua kuwa bado walikuwa wakipumua. Hapo wakapiga simu kituoni kuomba msaada. Baada ya dakika kumi kuliingia gari la polisi jengine lililosheheni askari wenye silaha huku likisindikizwa na gari la wagonjwa.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wakachukua miili ya wale askari waliokuwa chini kwaajili ya kuiwahisha hospitali kwa matibabu ya haraka. Hawakusahau na zile maiti mbili kwenye ile Alteza. Wakaondoka nazo pia kwaajili ya uchunguzi. Askari waliobakia wakaondoka na ile Alteza kwenda nayo kituoni.



Ata na Atu waliegesha gari lao ndani ya uzio wa lile jumba lao la maficho. Wakashuka na kuingia ndani na kuwakuta Mr Henein, Mrutu na Paskali wakiwasubiri kwa hamu wawaeleze walichokiona huko. Kwanza kila mmoja aliingia kwenye chumba chake kwenda kutoa silaha ambazo walizipachika kwenye miili yao. Silaha hizi ndizo zile ambazo ziliwaangusha wale askari kule kwenye eneo la tukio.



Waliporudi wakawaelezea jinsi tukio lilivyotokea na walichokiona kwenye lile gari waliloondoka na wale vijana wao. Hapo wakawauliza maswali mawili matatu kuhusiana na tukio hilo lilivyotokea na wao waliwajibu. Mr Hanein alichukua simu na kupiga namba ya Mr Tanganyika. Wakasalimiana na Mr Hanein aliingia kwenye suala lililompelekea kumpigia simu mtu huyo.



“Ndugu naona mambo yananiwia vibaya baada ya kuletwa mdudu msumbufu anaefuatilia mambo yangu. Na hapa ninapokuambia wale vijana ulionipa tayari wameshataifishwa na huyo huyo mdudu. Sasa sijajua ndugu yangu utanisaidiaje hapo” Mr Hanein aliongea. Watu wote hapo ndani walikuwa kimya wakisikiliza maongezi hayo yaliokuwa yakifanyika kwenye simu. Simu iliyowekwa sauti kubwa.



“Beka mimi na wewe tumetoka mbali sana. Ulinisaidia mengi hadi hapa nilipofikia wewe ni mmoja wapo ulioniwezesha kufika. Niambie unataka msaada gani nikusaidie sasa hivi” Mtu wa upande wa pili aliongea. Mtu alietajwa kwa jina la Mr Tanganyika.



“Naomba unisaidie vijana watano waongeze nguvu kwenye kambi yangu ili tumzibiti huyu mdudu. Maana naona sasa hivi yupo miguuni kwangu nikisema niendelee kumuachia atapanda hadi kwenye sehemu za siri na hiyo itanidhalilisha sana”



“Hahahah! Usijali we niambie unataka vijana wangapi na chengine ni kipi ili nikusaidie” Mr Tanganyika aliongea. Mr Hanein aliwaangalia vijana wake usoni kwa muda kisha akasema.



“Nahitaji vijana watano na kama kuna chengine nitakuambia ndugu”



“Beka sema bwana vijana watano watakutosha kweli?”



“Nipe kwanza hao niangalie upepo kama nikitaka wengine nitakujulisha”



“Sawa. Bilashaka majira ya asubuhi mtakuwa nao hapo kwa namna ya ajabu sana. Maana hawa vijana ni vijana wa kazi sio mchezo. Naamini utaniambia hilo”



Hapo wakaongea mawili matatu marafiki hao wazamani wanaofanya biashara za haramu tangu ujana wao. Ni hivyo tu Mr Bakari Hanein aliwahiwa kukamatwa na jeshi la polisi na kuhukumiwa kifungo cha maisha kwenye mkasa uliopewa jina la UHASAMA. Kesi hizo alizofunguliwa na hukumu hiyo ndio iliyomrostisha kiuchumi na kimaendeleo hadi hapo alipofikia. Sawa biashara zake za halali zilisimamiwa na kijana wake aliemlea yeye tangia akiwa mdogo.



Paskali ndie kijana aliekuwa akizisimamia biashara za Mr Hanein tangu alipohukumiwa kifungo cha maisha hadi hapo alipokuja kutoroshwa na watoto wake mapacha waliokuwa nchini marekani tangu wakiwa na miaka saba. Aliwapeleka huko kwenda kusoma. Kusomea masuala ya ujasusi ili aje kuwatumia kwa miaka hiyo katika kazi kama hizo.



Mr Hanein hakuwa mchovu wa mali kwasababu mali zake bado zipo katika usalama. Ila kinachomnyima uhuru ni vile kutafutwa na polisi kwa kutoroka jela. Na ndio maana siku zote yupo ndani hatuki nje. Labda atoke lakini aishie ndani ya uzio wa nyumba hiyo.



Urafiki wa Mr Hanein na Mr Tanganyika ulianzia tangu walipokuwa shule ya sekondari Galanosi miaka hiyo ya Sabini. Mr Tanganyika alihamishwa na wazazi wake shuleni hapo kutokea mkoa wao Kigoma kutokana na tabia yake ya kupenda vurugu, shari na matukio ya ajabu ajabu. Aliletwa hapo akiwa kidato cha pili. Hapo aligombana na wanafunzi wenzake karibia wote huku walimu wakimchukia kutokana tabia yake mbaya. Hakuwa na rafiki yoyote zaidi ya Mr Bakari Hanein ambae waliendana kitabia. Wote walikuwa na tabia mbaya zilizowakera walimu na wanafunzi wenzao.



Walisoma hivyo hivyo kitabutabu hadi pale walipomaliza kidato cha nne na Mr Tanganyika kuhamia mkoa aliotoka akimuacha Mr Hanein akiendelea na masomo yake hapo hapo mkoani Tanga. Tangu siku hiyo urafiki wao haukufa na ndio ulizidi kukukua hadi pale walipojikuta wote wakifanya biashara za haramu ambazo serikali zinazipinga. Mr ‘Tanganyika tutakuja kumuona kwenye kisa kinachofuata.’



Hemedy Bhachu alionekana akitoka nyumbani kwake majira hayo ya jioni. Akapanda kwenye gari lake na dakika kumi na tano zilitosha kumfikisha kituo cha polisi cha Chumbageni. Huko alishuka kwenye gari na kuanza kupiga hatua kuingia ndani ya kituo hicho ilipo osifi ya IGP Taure. Ila alikatishwa safari yake hiyo baada ya kuambiwa asubiri maana IGP kuna mtu anamaongezi nae huko ofisini kwake. Akatulia na kusubiri.



Baada ya dakika tano akatoka mtu huyo aliekuwa ndani ya ofisi ya IGP Taure. Alikuwa ni askari mwenye cheo cha Konstebo. Ndio Hemedy nae akaingia. Huko alimkuta IGP akiwa na uso wa mashaka na hofu tele. Akajua kuna jambo. Ishara ya kukaa kwenye kiti ikamuongoza na yeye akakaa. Kimya kifupi kilipita na ndipo IGP Taure alipo nyanyua kinywa chake na kusema.



“Askari wangu watatu wameuawa huku mmoja akijeruhiwa begani na vijana waliosemekana ni mapacha huko shule ya sekondari Tanga Technical School leo hii jioni walipoenda kufuatilia lile gari ulilolicha na zile maiti mule ndani” IGP Taure aliongea kwa simanzi bila kukwepesha jicho kwenye macho ya Hemedy. TSSI 01 taarifa hiyo wala haikumshtua kwa nje ila ndani ilimshtua vilivyo.



“Afande naomba unifafanulie vizuri hilo tukio lilivyotokea maana kama vile sijakuelewa vizuri japokuwa nimeanza kukuelewa” TSSI 01 aliongea. IGP alimuangalia kwa sekunde kadhaa usoni na kukutana na uso wa TSSI 01 unaotaka kupewa hiyo taarifa. Kisha akamuelezea.



“Ni hivi. Wewe ulipokuja kunipa ile taarifa kuhusu wale watu wako kule shule ya sekondari. Niliwatuma vijana wangu wakaichukue ile miili na walilete lile gari hapa. Ila badala yake vijana watatu wamerudi nao ni maiti japokuwa walifia hospitalini huku mmoja hali yake sasa hivi ni mbaya sana baada ya kugundulika kuwa wamechomwa na pini au visumari vijidogo vyenye ncha kali na sumu kali. Inspekta niliemtuma kuongoza huo msafara ndie ambae hali yake ni mbaya kwasababu yeye amechomwa na visumari hivyo kwenye bega ila hao askari wengine watatu wao wamepoteza maisha kwasababu wao wamechomwa visumari vya shingo” akatulia kidogo kwa sekunde kadhaa. Kisha akasema. “Na huyo uliepishana naye hapo mlangoni ni askari mmoja wapo kati ya sita walioenda huko. Na katika hilo tukio wamepona wawili tu huyo alietoka sasa hivi humu na mwenzake mmoja” IGP Taure akamaliza kutoa maelezo yake.



Kichwa cha TSSI 01 kili waka moto kwa tafakuri nzito iliyomkumba ghafla. Alishajiapia kwamba asife mtu yoyote tangu alipopewa jukumu la kufuatilia matukio hayo. Sasa aliona lawama hivi hivi zikimjia kutoka kwa mkuu wake au kwa huyo afisa wa jeshi la polisi alieko mbele yake hapo. Hakujua kwamba tukio alilotoka kulifanya masaa kadhaa nyuma kwamba lingeweza kusababisha vifo vya askari watatu huku mmoja akiwa hali yake haieleweki. Akataka kusema kitu. Ila IGP akamuwahi.



“Najua kesi hii pia inahusina na hizo kesi unazozifuatilia wewe. Na watu unaowafuatilia wewe ndio hao hao waliofanya mauaji ya askari wangu. Kwa maelezo ya askari aliebaki hai ni kwamba watu hao walikuwa wamefanana kwa kila kitu ila jinsia tu ndio zilikuwa ni taofauti. Sasa hii ilinipa picha kwamba watu hao ndio hao vijana wa Mr Hanein au wewe unahisi nini labda?” IGP Taure alisema na kuumuuliza hilo swali. TSSI 01 alitingisha kichwa kukubaliana na wazo la IGP kuwa watu hao ndio hao hao vijana wa Mr Hanein. “Unafikiria nini hadi sasa? Maana naona tukio hili litaenda kulidhalilisha jeshi la polisi kwa mara nyengine hivi punde pindi waandishi wa habari watakapo pata taarifa hizi”



“Kwasasa siwezi kukujibu chochote. Subiri kwanza nikae nifikirie kwa kina maana sio kulidhalilisha tu jeshi la polisi bali pia nitaonekana na mkuu wangu sifanyi kazi yoyote kama ikiwa vifo vinaendelea kutokea. Naomba nionane na hao askari waliopona katika tukio hilo”



“Sawa.... Ammh! Shika na hii” akavuta droo ya meza yake na kutoka kijifuko kidogo cha nailoni. Kisha ndani yake akachomoa viji pini vijidogo au visumari. Akampatia.“ hivi ndivyo ambavyo vimeondoka na uhai wa askari wangu na kumuacha mmoja na hali mbaya” TSSI 01 alivipokea na kuviangalia vizuri. Mara moja akavigundua kuwa ni katika moja wapo za silaha hatari za kijasusi. Hapo ndipo alipopata picha ya kwamba mapacha wale pia ni majasusi kama alivyo yeye. Umakini akapanga auongeze. Hakutaka kujipa imani kwamba alivyowadhibiti kila mmoja na siku yake basi eti ndio uwezo wao wa kupambana umefikia pale. Akaaga na kutoka ndani humo moja kwa moja akamtafuta yule askari aliepishana nae wakati akitaka kuingia katika ofisi ya IGP. Askari huyo ndio huyo alieambiwa ni mmoja kati ya wawili walionusurika katika tukio hilo lililotokea saa moja nyuma. Akamchukua maelezo kidogo kisha akaondoka hapo kituoni na kuelekea anapopajua yeye.



* *



Siku iliyofuata majira ya asubuhi kwenye jumba la maficho ya Mr Hanein na kundi lake. Paskal aliinuka asubuhi hiyo kwenye chumba chake cha kulala. Akajinyoosha kidogo huku akisindikiza na muayo mrefu. Baada ya hapo akashuka kwenye kitanda hicho. Akaanza kupiga hatua za kiuvivu uvivu. Akaelekea maliwatoni ambapo kulikuwa ni humo humo ndani ya chumba chake. Akafanya ya kufanya kisha akatoka tena na kuiendea droo iliyokuwa karibu na kitanda. Juu yake palikuwa na mswaki na vikorokoro kidogo. Akachukua mswaki na dawa ya meno. Akajaribu kuminya dawa hiyo lakini hakuna kitu kilichotoka zaidi ya upepo tu ndani humo. Apiga kite cha mfadhaiko na kutoka ndani humo na mswaki wake mkononi huku lile ganda ya dawa ya meno akiliacha pale pale. Nje ya malango wake akashika uelekeo wa kwenda sebuleni.

Macho yalimtoka huku mswaki ukimdondoka mkononi mwake. Kitendo hicho kilichagizwa na yowe kubwa la hofu huku akiwa bado ameganda pale pale. Wenzake walitoka vyumbani mwao baada ya kusikia yowe hilo alilolipiga Paskali. Na wao pia walipokuja hapo wakaganda wakitazama kilichopo mbele yao..







Ni vijana watano waliokuwa wamekaa kwenye masofa hapo sebuleni wakiwa hawana wasiwasi hata punje na wala hawakuonekana kwamba walijali hamaniko la watu wale waliokuwa wakiwashangaa. Wakawa wapo kimya huku nyuso zao zikiwa na tabasamu.

Tabasamu la kebehi!.

Ndio waliwakebehi kwa tabasamu kwasababu waliingia humo ndani bila ya wenyeji kujua.



“Naitwa Denis Nduva au niite Deva kwa kifupi" Jamaa mmoja kati ya hao watano alijitambulisha huku sura yake bado ikiwa na tabasamu. Huyu alikuwa ni mweupe alieonekana kuwa na urefu wa haja na mwenye mwili uliojengeka vizuri kwa mazoezi na kichwani nywele zake alizikata kwa mtindo wa afro ya juu. Alikuwa na sura ya kike lakini ndevu zilizochongwa vizuri na timbalendi lililoko kwenye mashavu yake kuanzia mbeli kidogo ya sikio hadi kushuka kidevuni. Ndivyo vitu vilivyopunguza kidogo ile dhana kwamba ana sura ya kike.



“Naitwa Zinah Mustapha au kifupi unaweza niita Krish” Jamaa mwengine alijitambulisha jina lake. Huyu alikuwa na mwili mpana kidogo uliojengeka vizuri kwa mazoezi. Hakuwa mweupe ila alikuwa na rangi fulani inayoelekea kufikia huko. Hakuwa mrefu sana wala pia hakuwa mfupi sana, kichwani nywele zake alizikata chini chini.



“Naiwata Malikia Meena au mnaweza niita Queen" Mwanamke huyo alijitambulisha jina lake. Alikuwa ni mzuri wa sura na umbo kama hilo jina lake ila ni mwenye kumilika roho ngumu na mbaya ambayo kwake yeye kutoa roho ya mwanadamu mwenzake ni jambo jepesi kuliko yote aliyowahi kuyafanya.



“Naitwa Robert Benson au kifupi mnaweza kuniita Roben” Huyu nae alikuwa na rangi nyeusi tii isiyo na mithali. Alibeba sura iliyotangaza shari na roho mbaya aliyokuwa nayo. Sura yenye alama ya kovu la mstari ulioanzia kwenye nyusi na kushaka karibu kidogo na pua na kumalizikia kwenye kidevu. Nae alikuwa na mwili mkubwa kama hao wenzake.



“Naitwa Mr Pijo" wa mwisho alijitambulisha kwa jina hilo. Huyu alionekana kuwa na miaka mingi kuliko hao wenzake. Alionekana kumiliki miaka kati ya thelathini na tano hadi arobaini. Kichwani nywele zake zilizoanza kuota mvi huku zikifanyizwa na uwalazi na kidevuni alikuwa na ndevu alizozipaka rangi ya manjano iliyokolea. Hakuwa mrefu sana na ni mwenye mwili mwembamba uliokomaa.



Watu hao walijitambulisha wakiwa hapo hapo kwenye masofa wamekaa wakiwaangalia wenyeji wao ambao kwa sasa mshangao na hofu viliwaondoka baada ya kugundua kuwa huenda ikawa ndio waliotumwa na huyo mtu wa kuitwa Mr Tanganyika. Pakawa kimya kwa dakika kadhaa pasi na mtu yoyote kuwakaribisha ama kuwaongelesha watu hao. Simu ya Mr Hanein iliyokuwa kwenye meza ya hapo sebuleni iliita. Akaifuata na kuichukua. Alitabasamu aliposoma jina la anaepiga kwa wakati huo.



“Nadhani vijana umewapata hapo majira hayo?" mtu wa upande wa pili aliongea.



“Yeah! Nimewapata na nashukuru kwa hilo Mr”



“Watu hao ni watu hatari ambao nilikuwa nikiwamiliki mimi, ila kwasasa acha wakusaidie kazi naamini utawafurahia. Watumie utakavyo na watakuwa chini ya amri yako Mr”



“Nimekuelewa na asante kwa msaada wako” Mr Hanein aliongea huku akiwaangalia vijana hao usoni akiwa na tabasamu kuu.



“Usijali na kama ukiwa na shida yoyote usisite kuniambia” Simu ikakatwa. Mr Hanein aliwageukia vijana hao.



“Karibu vijana wangu katika himaya ya Mr Hanein”. Aliwaambia hivyo na vijana wale wakaitikia kwa kutingisha kichwa kwenda juu na chini. Hapo Mr Hanein aliwatambulisha vijana hao kwa vijana wake. Muda mwingi macho yaa Deva na ya Atu yalikuwa yakigongana mara kwa mara. Jambo hilo Ata alilishuhudia bila kificho hata pale Deva alipomkonyeza Atu.

Mmmh!

* *



Majira ya saa mbili na nusu asubuhi siku hiyo hiyo katika jiji la Daresalam. Mr Kaoneka alikuwa yupo ndani ya gari lake asubuhi hiyo akielekea kazini kwake au tuseme katika kitengo chao cha siri. Sura yake ilionekana kusawajika kwa huzuni au fadhaha flani. Mara kadhaa alionekana akikiadhibu kichwa chake hasa hasa kwenye paji la uso kwa kukigonga na kiganja cha mkono halafu anamalizia na msunyo.



Mara hii alipiga honi kwa nguvu bila kujua na kujikuta akimsababishia mtembea kwa miguu alieko sentimita chache na barabara hiyo kushtuka vilivyo kwa kelele za honi hiyo. Alipayukwa na kurusha mikono huku akisontea kidole gari la Mr Kaoneka, usoni kwake akionekana dhahiri ghadhabu zimemjaa kwa kushtuliwa na ukelele wa honi hiyo.



Mr Kaoneka hakumjali sana kutokana na yeye kuwa katika hali ambayo siyo ya kawaida. Aliendele na safari yake huku akimuacha kijana yule akisonya na kuendelea kulalamika pasi na kupata wa kumsikiliza malalamiko yake.



Dakika kumi mbele alipaki gari lake nje ya hoteli hiyo ambayo ndani yake ndipo zilipo ofisi za TSSI. Akashuka kwenye gari na kuubamiza mlango wa gari. Kisha akaanza kupiga hatua ndefu ndefu kuelekea ndani ya jengo hilo. Ni dhahiri kuna jambo limemsibu kwasababu haikuwa kawaida yake kupita na mlango wa kawaida kuingilia ndani humo. Bali yeye alikuwa akipitia na mlango wa siri unaomtokezea moja kwa moja hadi chini ya jengo hilo zilipo ofisi hizo.



Aliingia ndani ya jengo hilo na kushuka na ngazi za siri zilizomshusha hadi chini sehemu ambayo kulikuwa kuna ujia mrefu unaoelekea kushoto. Akaifuata njia hiyo na kwenda nayo huko inapoelekea. Kwa hakika jengo hilo lilikuwa ni la ajabu sana huko chini. Kulikuwa na vyumba vingi tofauti na vile ambavyo tumeviona kabla.



Baada ya mwendo mfupi. Alitokezea kwa ‘Secretary’ wake Stela. Alimpita huku akimuacha binti huyo akitoa salamu ambayo haikuletewa majibu. Moja kwa moja hadi ofisini kwake. Hapo akavua koti la suti na kulipachika kwenye kiti chake na yeye akawa amesimama huku mkono mmoja ukiwa mfukoni mwa suruali yake huku mwengine ukiwa kidevuni mwake. Akawa anatembea kwa hatua fupi fupi sana humo ofisini mwake hadi pale alipoenda kukaa kwenye kiti chake. Akachukua simu yake na kupiga.



“Habari mkuu” Sauti ya upande wa pili iliongea.



“Bhachu ni nini unafanya huko Tanga? Mbona sioni maendeleo yoyote zaidi ya vifo vya askari kuendelea kutokea tu... Leo katika taarifa ya habari imetangaza tukio la kuawa kwa askari wa tatu huko Tanga na askari mmoja kujeruhiwa. Na inavyosemekana waliofanya mauaji hayo ndio hao hao waliofanya mauaji yaliopita siku kadhaa nyuma. Embu nieleze vizuri hapo” Mr Kaoneka aliongea huku usoni mwake akiwa na mfadhaiko.



“Mkuu hata mimi sikuvifurahia vifo vya wale askari. Ila sasa siwezi kuzuia hilo.....” TSSI 01 alikatishwa na sauti ya Mr Kaoneka.



“Unasema huwezi kuzuia? Kivipi? Kwanini?"



“Kwasababu sio mimi ninaepanga watu wafe halafu pia wale wauaji bado sijawajua kiundani japokuwa tayari nimeanza kuwajua”



“Unaposema hujawajua kiundani unamaanisha nini na unaposema umeanza kuwajua napo unamaanisha nini?”



“Namaanisha kwamba sijajua makazi yao yalipo ila nimeshawajua kwa sura na nishakutana nao zaidi ya mara moja”



“Vipi lakini maendeleo ya hiyo ‘mission’?”



“Naenda nao taratibu na kwauangalifu na umakini mkubwa, kwasababu vijana hao pia wanaonekana kuwa na uweledi mzuri katika masuala ya kijasusi. Sasa inanabidi nitumie mbinu ambazo zitawachanganya na kunipa urahisi mimi wa kufanikisha kazi yangu”



“Ok. Kuna chochote ambacho ungeomba uongezewe?” Mr Kaoneka aliridhishwa na mjibu aliyopewa na TSSI 01 Hemedy Bhachu. Alimuuliza swali hilo huku akilegeza tai yake na kufungua kifungo kimoja cha juu. Kimya kilitanda upande wa pili kwa sekunde kadhaa. Kisha Hemedy Bhachu akatoa jibu kuwa kwa sasa hahitaji chochote cha kuongezewa.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Sawa.... Baada ya siku nne utaletewa gari la kazi. Atakuja Feysal na Fady( Faustin Dickson ndio wameamua kumfupisha jina na kumuita Fady) kuja kukuletea gari hilo aliloliunda Fady na baadhi ya vifaa vya kazi” Mr Kaoneka aliongea.



“Sawa mkuu hakuna shaka”



“Ukiwa na tatizo lolote usisite kunijulisha” Hapo simu ikakatwa na Mr Kaoneka akashusha pumzi ndefu huku akiigamia kiti chake.



* * * *



Siku mbili mbele jijini Tanga katika jumba la mficho ya Mr Hanein. Kulikuwa na kikao. Kikao hicho kilizungumzia juu ya kumuondoa roho mtu fulani. Mkuu wa mkoa huo wa Tanga ndie ambae anaehitajika kutolewa roho yake kwasababu ambazo hatujazijua bado.



“Kazi rahisi sana hiyo mkuu. Ni jambo la kutupa amri tu kuifanya bila tatizo lolote” Zinah Mustapha au Krishna kama mwenyewe alivyopenda kujiita. Alisema baada ya kupewa taarifa hiyo.



“Msichukulie kazi rahisi kwasababu mkuu wa mkoa analindwa na askari makini” Mr Hanein alimtahadharisha.



“Mkuu hadi nimesema hivyo ujue nimeshaiona kuwa ni kazi rahisi. We tupe ramani tu halafu matokeo utayapata”



“Ok. Baada ya kumaliza swala hilo. Sasa ndio nataka kuingia kazini rasmi maana ninacho kikosi kazi” Mr Hanein aliongea.



“Kazi hiyo inatakiwa kufanyika lini mkuu?” Deva aliuliza.



“Ikiwezekana hata leo” Mr Hanein aliongea na vijana wakakubaliana na hilo swala.



Kituo cha chumba geni katika ofisi ya IGP Taure. Kulikuwa na kikao cha dharura kati ya IGP mwenyewe, Hemedy Bhachu na Inspekta Salum Mzanzibar ambae kwa sasa hali yake inaendelea vizuri baada ya kutolea sumu ya ile sindano aliyochomwa na vijana mapacha wa Mr Hanein kule sekondari ya Tanga School siku mbili zilizopita.



IGP alikuwa akiwakutanisha TSSI 01 na Inspekta Salum Mzanzibar ikiwezekana wafanye kazi hiyo kwa pamoja. Licha ya kumtambulisha TSSI 01 kwa Inspekta Salum. Lakini IGP hakutaka kumtambulisha moja kwa moja kwamba alikuwa akitoka katika kitengo cha siri serekalini. Alichomtambulisha yeye ni kuwa mtu huyo alitumwa na ngazi za juu kuja kupeleleza vifo hivyo vinavyotokea katika mkoa huo baada ya jeshi la polisi kuzuiwa kufanya hivyo.



Hapo wakapeana mikono baada ya utambulisha huo na kupanga mikakati ya jinsi gani ya kuwadhibiti hao wauaji. Japokuwa TSSI 01 hakupenda kuifanya au kusaidiwa hiyo ‘mission’ na mtu yoyote. Ila hakuwa na uwezo wa kupinga kutokana na heshima aliyokuwa nayo kwa IGP Taure. Wakazungumza mengi kuhusiana na hilo sakata hadi pale walipoona panatosha kwa siku hiyo. Wakabadilishana namba za simu na TSSI 01 akaaga na kuondoka kituoni hapo.



Safari yake iliishia Kaskara Villa baa iliyopo maeneo ya Kiboi. Hakuwa mnywaji wa vilevi. Alichoagiza yeye ni maji safi makubwa ya kilimanjaro akiyanywa huku akiyasindikiza na muziki alioweka kwenye simu na kuunganisha na visikilizia muziki ‘earphone’ huku akiwaangalia wanaoingia na wanaotoka katika baa hiyo jioni hiyo. Nusu saa mbele aliinuka na kupotelea nje ambako alipaki gari lake. Aliingaia humo na safari ya kurudi kwake ikaanza. Hapo na nyumbani kwake hapakuwa mbali dakika tano tu zilimtosha kumfikisha.



Majira ya saa kumi na mbili za jioni katika nyumba ya Mkuu wa mkoa mama Agness Elikki mtaa wa Raskazone. Nje ya nyumba hiyo mbali kidogo kulikuwa kumepaki gari aina ya Brevees nyeusi. Gari hilo lilikuwa limepaki hapo zaidi ya dakika kumi hakuonekana mtu yoyote kushaka wala kuingia. Baada ya dakika tatu mbele akashuka Deva na Zinah. Wakaangalia huku na huko na kuanza kupiga hatua baada ya kuona mtaa huo umepoa sana na hiyo ilichangia kwakuwa nyumba za mtaa huo ni zenye mageti.



Walifika hadi mbele ya geti la nyumba hiyo na kugonga. Kwenye kijiuazi kidogo kilichopo hapo getini kulionekana sura ya mtu ikichungulia. Ikawauliza swali kuwa watu hao ni wakina nani na wanataka nini hapo? Na wao wakajibu kuwa ni watumishi katika shirika fulani na wamekuja hapo kwaajili ya kuonana na Mkuu wa mkoa. Mtu aliepo ndani akayaamini maneno hayo na kufungua mlango mdogo wa geti hilo. Punde tu mtu huyo aliekatika mazazi ya jeshi la polisi alijikuta akiwa chini kimya huku watu wale wakilirudishia geti vizuri.

Kimya cha milele!



Walishangazwa na ukimya wa nyumba hiyo na vichwani mwao wakabaki kujiuliza. Ina maana hii nyumba inalindwa na askari mmoja tu? Hawakupata jibu kwasababu hawakupata wa kulijibu swali hilo. Hata kama angekuwepo kiumbe mwengine hapo pia asingeweza kulijibu hilo swali kutokana na wao kujiuliza wenyewe nasfini mwao.



Ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na kiumbe ambacho kilikuwa kimeweka miguu kwenye mkono wa sofa huku kichwa chake akikilaza kwenye mkono mwengine wa sofa hilo hilo huku kiwiliwili kikijijaza katikati ya sofa hilo. Chini ya sofa hilo kulikuwa na glasi ya dongo ndani yake ikiwa na shurubati ya ukwaju. Ghafla kiumbe hicho kilipeleka macho yake kwenye mlango wa kuingilia sebuleni hapo. Akaona kitasa cha mlango kikizungushwa taratibu sana. Akatabasamu na kujiinua hapo kwenye sofa haraka na kukimbilia nyuma ya pazia la dirisha. Ndani humo wakaingia Deva na Zinah ambao walikuwa makini sana huku wakiangaza macho yao kwenye sebule hiyo..







Wakiwa hapo sebuleni wakiangaza macho yao huku na huko kuangalia usalama. Ndipo macho yao yakatua kwenye sofa ambapo chini yake kuna glasi yenye kinywaji. Wakajua kivyovyote humo ndani kutakuwa kuna mtu. Ghafla giza likatawala hapo sebuleni baada ya taa kuzimwa. Umakini ukaongezeka huku bastola zao wakizishikilia vizuri wakiwa hapo hapo. Hawakutaka kusogeza hata nyayo zao kwenda mbele au nyuma.

Hofu!

Wakawa na hofu kwenye mioyo yao wakajua kivyovyote wameonekana. Maana huko nje taa zilionekana kuangaza kila sehemu. Sasa iweje hapo ndani ndio zizime ghafla?



Ghafla bastola walizozishika zikawaponyoka mikononi mwao na kusambaratika sakafuni baada ya mateke mawili ya haraka kuzipiga. Papo hapo wakapokea ngumi za uso zilizowapa wenge kubwa kiasi kwamba wakabaki wakibabaika kwa kiwewe walichokipata kwa ghafla sana. Wakakaa kimapambano wasimuone wanaetaka kupambana nae. Mara kidogo mguno ukawatoka huku wakisukumwa mbele baada ya mateke mawili kuwapiga migongoni mwao. Wakajikuta wanaenda kulivamia sofa lililokuwa mbele yao, mlio wa glasi iliyovunjika ukisikika hapo.



Wakainuka kwa haraka na kukaa tena kimapigano huku wasijue wanaetaka kupigana nae ni nani.

Kizaazaa hicho!

Safari hii walipeana migongo yani kila mmoja alielekea ule upande ambao mwenzake hajaelekea.

Ghafla Deva alichotwa mtama uliompeleka chini bila kizuizi chochote na kuutuliza mgongo wake sakafuni na asimuone ni nani aliemfanya hivyo. Zinah nae alipokea ngumi za haraka zilizotua kifuani mwake na kumaliziwa na teke zito la tumbo lililomfamya kumpamia Deva pale chini na kujikuta na yeye akienda chini bila kupenda.



Kimya!



Pakawa kimya tena. Kimya kilichowafanya vijana wale pale chini wasijue wainuke au waendelee kulala vile vile. Lakini watalalaje wakati hawajamuona kama sio kutomjua kabisa anaewaadhibu? Kuna muda walidhani labda wanapambana na jini! Lakini wakalitoa hilo wazo baada ya kutoamini hicho kitu. Ni ajabu hii kupambana na kiumbe usichokina! Wakajua kivyovyote kuna mtu anawachezea mchezo wa kombolela Na wao wakapanga wamchezee mchezo wa kidali pooh.



Kwa vile adui yao anacheza mchezo wa kombolela wa kubutua halafu anawahi kujificha. Sasa na wao wakapanga wamchezee mchezo wa kidali pohh wa kupiga halafu wanawahi kukimbia.

Mchezo wa kuviziana!.

Wakainuka tayari kwa michezo hiyo. Safari hii hawakutaka tena kukaa pamoja. Wakajitenga na kukaa mbali mbali kama hatua tatu hivi. Ghafla Deva alisikia mvumo wa upepo ukija kwa kasi usoni mwake. Akataka kurudisha sura nyuma kidogo lakini alichelewa. Ngumi hiyo ilipita kwenye shavu ikamalizia kwenye pua. Haikumuacha salama. Ilimuachia maumivu. Lakini kwa wepesi wa ajabu akarusha ngumi upande uleule uliotoka ile ngumi iliotoka kumuadhibu hivi punde.



Ukasikika mguno hafifu kutokea upande ule aliorusha ngumi. Ngumi hiyo ilimpata mtu asiejulikana ya kwenye mbavu. Pakawa kimya tena. Ila hiyo ilimpa matumaini Deva na Zinah kuwa wanapambana na kiumbe kama wao ila sema yeye anatumia uwenyeji wake kuwashinda wao. Wakaongeza umakini zaidi ili wakisikia fyoko na wao wanaleta fyoko. Hilo waliliona ni jambo zuri la kupambana na huyo adui yao.



Tena ghafla Zinah alijikuta akienda chini baada ya kuchotwa mtama maridadi na adui yao. Lakini kule chini hakuenda hivi hivi. Alipotua chini na yeye akarusha teke kuenda ule upande ule mguu uliomchota mtama. Zoezi hilo lilizaa matunda kwa asilimia tisini. Maana palisikika mshindo wa mtu au kitu kilichoanguka. Hapo bila kuchelewa alijivuta mbele kidogo vile vile akiwa amelala chini na kuinua guu lake la kushoto. Kisha akalitulisha pale paliposikaka kishindo kile.



Mguno wa maumivu ukasikika tena baada ya guu hilo kutua juu ya kifua cha adui yao. Akataka kupiga kelele kumuita Deva kuwa adui yao ameshamnasa. Lakini alinyamazishwa na kisigino kikali kilichotua kwenye mdomo wake na kujikuta akiungurama kwa maumivu kama paka aliepo katika pambano kali na kiumbe kifananacho na yeye. Deva purukushani hizo alizisikia na kuanza kupiga hatua kuenda kule ziliposikika. Alipofika wala hakusubiri kuambiwa afanye nini. Shati jeupe alilovaa Zinah aliliona sasa yeye alichofanya ni kurusha teke aina ya dochi kuenda pale chini palipo na yule adui yao aliekuwa akimuona kwa ufinyu sana kutokana na giza lililomo humo ndani.



Ukelele hafifu ulisikika kisha ukafuatia na ukelele mwengine mkubwa uliosikika hapo. Ukele hafifu ulikuwa ni wa mtu asijulikana baada ya kupigwa lile dochi. Na ule mkubwa ni wa Zinah baada ya kupokea teke kali lililotua kwenye uso wake na kujikuta akirudi nyuma nyuma huku akishikilia sehemu hiyo iliyopata maafa muda mfupi uliopita.



Pakawa kimya tena baada ya adui kupotea na wasijue ameenda wapi. Wakakaa tena kimapigano huku kila mmoja akiugulia maumivu yake. Sasa kilichofuatia hapo ikawa ni kama vichekesho fulani hivi. Ndio ni vichekesho kwasababu muda huo wakawa kama matahira maana walianza kupepesuka kila waliposikia mvumo wa upepo ukipita mbele yao. Hapo ile dhana ya kwamba wanapambana na kiumbe tofauti na walivyo wao ikawarudia tena maana kila wanapojaribu kuufwatisha mvumo ule wakajikuta wakipiga hewa tu.



Pakawa kimya tena! Kimya hiki kilikuwa cha tofauti sana na vile vilivyopita. Wakaingiwa na wasiwasi. Lakini wasiwasi huo ukakatika ghafla na kuwa ni hofu iliyochagizwa na kelele nyingi zilizowatoka watu hao baada ya kupokea kichapo na wasijue kilipotoka. Kelele zilirindima humo ndani na ikawa tafrani huku watu hao wakifukuzana na wasijue ni wapi pa kujisitiri. Baada ya kupokea kichapo kingi ndipo walipokuja kuuona mlango wa kutokea sebuleni hapo.



Wakatoka hai hai na kuipita maiti ya askari waliefanya mauaji yake wakati wanaingia. Walilipamia geti na kujikuta wote wawili wakitaka kutoka kwenye kijimlango kile kwa pamoja. Mara ya kwanza waligotana. Ya pili wakagotana tena. Ya tatu wakajikuta wote wapo katikati ya mlango huo wakiminyana kutaka kutoka. Walitumia nusu dakika kuminyana katikati ya mlango pasi na mafanikio yoyote ya kutoka hapo.

Ilichekesha kuwatazama!

Walipokuja kupata akili ndipo wakarudi wote ndani na kuanza kupita mmoja na kufuatia mwengine. Wakatoka wakikimbia huku wakiuacha malango mdogo wa geti hilo ukiwa wazi. Waliingia kwenye gari yao na kupotea maeneo hayo kurudi kule walipotoka.



Huku ndani palisikika sauti ya kicheko kikuu huku ikifuatia na taa za hapo sebuleni kuwaka.

Kicheko cha Kebehi!.

Alaaaa!! Kumbe alikuwa ni Inspekta Salum Mzanzibar ndie aliekuwa akiwafanyia mchezo vijana wale. Alicheka sana huku mkononi akiwa ameshika mkia wa taa. Mkia wa taa huo ndio uliotoka kuwakimbiza vijana wale. Alicheka huku akikaa kwenye sofa jengine tofauti na lile alilokaa mwanzo. Akauweka mkia wa taa pembeni na kuchukua simu yake. Akaminya minya na kuiweka sikioni.



“Haloo” sauti ya upande wa pili iliongea.



“Bhachu tukutane Afrikana majira haya” Inspekta Salum aliongea.



“Hakuna shaka kwasababu mi mwenyewe nimekaa tu nyumbani sina pa kwenda muda huu”



“Basi fanya hivyo, kuna ishu nataka tuje kuzungumza” simu ikakatwa na Inspekta Salum akainuka huku akiendelea kucheka. Akaanza kupiga hatua kuifuata njia ya kwenda vyumbani. Mbele kidogo aligeuza na kurudi tena pale kwenye sofa. Akachukua mkia wa taa aliokuwa ameuacha pembeni ya sofa na kupotelea nao vyumbani.



Wale vijana wa Mr Hanein waliotoka nyumbani kwa mkuu wa mkoa kutaka kwenda kumuua na kinyume na matarajio yao wakakutana na kisanga kilichowaacha hoi. Majira haya walikuwa maeneo ya Tanga Pazuri wakiegesha gari lao kwenye maegesho ya baa hiyo. Walishuka na kuingia ndani ya baa hiyo. Watu walikuwa wapo wengi ndani humo wakiburudika huku wakiserebuka taratibu na muziki uliokuwa ukipigwa ndani humo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Walitafuta meza yao na kuweka kambi kwa muda wakijadili ni vipi watawajibu wanaosubiria majibu yao huko walipotumwa. Alikuja muhudumu wa kiume alievalia nadhifu na kuwataka waeleze wanachokitaka ili awahudumie. Waliagiza bia aina ya Kilimajaro na muhudumu yule akaondoka. Dakika moja alirudi na vinywaji hivyo. Akawafungulia na kuwakaribisha. Na yeye akatoweka hapo.



“Dah! Ule mzimu umeniumiza kishenzi yani” Deva aliongea huku akijikagua kwenye mwili wake. Mwili wake ulikuwa na alama nyingi za mikia ya taa waliotoka kuadhibiwa nao.



“Ila mimi sitaki kuamini kama ni mzimu ama ni shetani. Mi naamini yule ni binadamu tu kama sisi ila yeye ametumiwa uwenyeji wake kwenye ile nyumba kutuadhibu” Zinah alijibu. Kisha akapiga funda moja kubwa la kinywaji hicho.



“Ila sasa si tuliambiwa kuwa nyumba ile ni ya mkuu wa mkoa. Tena ni mwanamama. Sasa inawezekana vipi mama huyo akatuchezea michezo kama ile?” Deva aliongea kisha na yeye akapiga funda kubwa la kinywaji hicho. Alipoishusha chupa ilikuwa ipo nusu.

Sio kwamba hawakuletewa glasi za kunywea vinywaji hivyo......!



“Yule hawezi kuwa ni wakike bwana. Si unaona hata piga yake.....” waliendelea na maogezi yao na mwisho wakajadiliana ni vipi wataenda kuwajibu kule kambini kwao. Mwisho wakapanga kuwadanganya kuwa ulinzi katika nyumba ile ni mkubwa kwahiyo wameshindwa kuingia. Lakini je. Bastola zao zipo wapi? Je hayo manundu na alama za mikia ya taa? Watajibu vipi pindi wakiulizwa maswali hayo. Wakapinga wazo hilo na kupata wazo jengine la kuongea.

Wenyewe waliita. Wazo Angavu!.



Wakapanga kuwajibu kuwa. Ndio walifanikiwa kuingia ila hawakumkuta mtu waliemfuata bali walikuta kundi la watu wakiwa na sare za polisi. Na watu hao walipambana nao vya kutosha ila waliamua kukimbia baada ya kuona wakiomba msaada kwa wenzao. Ndipo hapo walipoacha bastola zao na kukimbia huku wakizawadiwa mikia ya taa kwenye miili yao.



Punde walimaliza vinywaji vyao na kutaka kuondoka mahala hapo. Ila walikuja kuzuiwa na yule muhudumu aliewahudumia akiwadai pesa zake.

La haulaa! Walijikuta hawana pesa yoyote mifukoni mwao baada ya kujisachi sana. Wakabaki wakibabaika wasijue wamjibu vipi huyo muhudumu. Unadhani muhudumu na yeye alitaka kusikiliza lolote kutoka kwa wateja hao waliokunywa vinywaji halafu wajifanye hawana pesa?.



Ilikuwa ni kizaazaa hapo. Akachachamaa alipwe pesa zake ndipo watu hao waondoke. Vijana wale wakajaribu kumuelewesha kistaarabu kuwa hawakufanya kusudi kunywa halafu na kutolipa. Bali imetokea tu kama bahati mbaya na kumuomba awaachie waondoke kisha watarudi kuja kulipa hela za watu. Lakini muhudumu hakutaka kuelewa chochote.



Akafanya kosa. Kosa kuwashika matai huku akiwadai. Sijui ilikuaje lakini tulishangaa muhudumu akigaagaa chini huku watu wale wakianza kupiga hatua kuondoka zao. Mbele walikutana na walevi watatu wanaojifanya wanataka kutetea haki ya muhudumu. Sidhani kama walifanikiwa kuwashika hata punje ya mashati waliyoyavaa vijana wale. Na wao wakajikuta kila mmoja akienda upande wake huku akipepesuka.

Sio kwamba walipepesuka kwaajili ya vilevi walivyokunywa.....!



Mara kidogo wakaja walinzi wa baaa hiyo kuja kuwadhibiti vijana hao wanaoleta tabu hapo. Nao sijui ni kipi kiliwakuta. Ila mmoja alienda kwa ghafla kuipamia meza iliyokuwa imekaa wateja huku juu yake pakiwa na vinywaji. Yowe la hofu liliwatoka wamiliki wale wa muda wa meza ile iliyopamiwa na yule mlinzi mwenye mwili mkubwa. Huku yule mwengine akienda kuwapamia watu waliokuwa wamesimama wakiuangalia mchezo huo. Bahati nzuri haikuwa upande wake maana watu wale walimpisha apite vile vile kingurue ngurue na kwenda kuipamia pikipiki iliyokuwa imepakiwa hapo. Akaenda chini yeye na jipikipiki hilo.



Ghafla kilionekana kivuli kikipotelea kizani. Kuja kutafakari vizuri kumbe alikuwa ni yule mlinzi wa tatu na wa mwisho ndie ambae amekimbia kuepuka zahma hilo lililowakumba wenzake. Hakutaka akutwe na kilichowakuta wenzake. Hapo zilisikika kelele za shangwe kwa walevi huku wengine wakithubutu kabisa kuinuka kwenye viti vyao walipokaa kuja kuwapongeza vijana wale kwa kutembeza dozi kwa watu sita huku mmoja akipotelea kizani. Kitendo cha kushangaza walijikuta wapo wenyewe walevi kwa walevi huku vijana wale wasionekane tena maeneo hayo.

Hadi sasa haijulikani ni wapi wamepotelea!.



* *



Katika mgahawa wa Afrikana uliopo maeneo ya barabara ya ishirini karibu kabisa na jengo la CCM Hall. Ndani ya mgahawa huo kulikuwa na watu wachache wakipata chakula majira hayo ya saa mbili kasoro usiku. Kwenye meza iliyoko pembeni kidogo ya malango wa kuingilia humo. Kulikuwa na watu wawili waliokuwa wamekaa huku juu ya meza hiyo pakiwa na glasi zilizo na kinywaji ndani yake. Hapakuwa na chakula chochote kwenye meza hiyo zaidi ya vinywaji tu.



Walikuwa ni TSSI 01 Hemedy Bhachu na Inspekta Salum Mzanzibar. Walikuwa wakipiga stori kabla hawajaingia katika mada iliyowaleta hapo. Muda huo huo pakaingia binti mmoja mwenye kila sifa ya uzuri. Alitembea hadi kwenye meza iliyokuwa tupu hapo na kukaa. Macho ya Hemedy na Inspekta Salum na baadhi ya wateja wengine yalimuangalia yeye. Alikaa hapo huku akichezea chezea simu yake. TSSI 01 alimminya Inspekta na kuinuka hapo kwenye meza aliyokaa na kwenda kwenye ile meza aliyokaa binti yule huku akimuacha Inspeka mdomo wazi asielewe ni kipi kimempata kijana mwenzake japokuwa yeye alimzidi umri kidogo.

“Inamaana haya ninayotaka kumuambia hayana maana tena baada ya kumuona yule mwanamke?” Alijuliza hivyo kwa sauti ya chini. Na bahati mbaya hapakuwa na wakujibu.



TSSI 01 alipofika pale akaomba ruhusa ya kukaa na mwanamke yule akamruhusu kukaa bila kinyongo. Tabasamu la binti yule lilimdatisha TSSI 01 nusuru kidogo tu aanguke baada ya kutoweka umakini na kiti anachotaka kukaa. Akakaa na kumuangalia binti huyo ambae kwa sasa alikuwa akitabasamu huku akichezea simu yake.

‘Amejileta mwenyewe’ Huo ndio ujumbe ambao alikuwa akiuandika binti huyo kwenye simu yake. Akautuma huko alipopanga kuutuma kisha akamtazama TSSI 01 kwa tabasamu kuu zaidi ya lile la mwanzo.

Ebwana eeh!.







“Habari yako malaika?” TSSI 01 alimsalimia huku mkono mmoja akiwa ameshika kinywaji chake na mwengine umeshikilia kiti kilichoangaliana na cha yule mwanamke. Tabasamu likiwa usoni kwake.



“Salama tu” Mwanadada huyo alijibu huku na yeye akiwa na tabasamu.



“Naweza nikajumuika na wewe. Au nitakuwa nimeharibu utaratibu?”



“Hapana unaweza ukakaa tu” alijibu mwanamke huyo. Kisha akahamia kwenye simu yake akimuacha TSSI 01 akikaa kwenye kiti na kuweka kinywaji chake juu ya meza. Mwanamke yule alikuwa akiandika sms kwenye simu yake. ‘Amejileta Mwenyewe’. Alipoandika hivyo. Akautuma ujumbe huo na kuinua sura yake iliyopambwa na tabasamu kuu kumuangalia TSSI 01.



“Naitwa Medy Bhachu. Sijui wewe unaitwa nani?”



“Naitwa Queen” Alijitambulisha mwanamke huyo. Queen huyu ndio yule mwanamke aliepo katika kundi la Mr Hanein. Kati ya vijana watano aliopewe na Mr Tanganyika.



“Kumbe sikukosea sana kukuita Malaika. Unakila kila sifa za kuwa malkia na kuongoza kasri yoyote ile duniani. Umzuri sana kiasi kwamba ulipoingia humu uliufanya mwili wangu ugande kwa muda. Ni macho tu ndiyo ambayo yaliweza kutembea na wewe hadi hapa ulipokuja kukaa ila nayo hayakuwa na uwezo wa kunasuka kwenye umbo lako maridhawa. Queen wewe ni Malkia kweli” TSSI 01 alianza kuchombeza kwa staili hiyo. Queen kama ambavyo amejitambulisha mwanamke huyo. Aliachia tabasamu huku macho yake yakipata tabu kukwepana na ya kijana huyo.



Muda kidogo alikuja muhudumu. Queen na yeye aliagizia juisi tu kama ambavyo TSSI 01 aliyokuwa nayo. Hapakuwa na chengine zaidi ya maongezi ya kawaida huku TSSI 01 akizidi kumchombeza mwanadada huyo. Mwisho aliaga kutaka kuondoka baada ya kumaliza kinywaji chake. Wakabadilishana namba za simu na mwanamke yule akapotelea nje ya mgahawa huo. TSSI 01 aliinuka na kurudi kwenye meza yao alipomuacha Inspekta Salum. Akakaa na kumuangalia Askari huyo anavyosikitika.



“Utakuja kufa ndugu yangu wengine sio wa kuwaamini haraka haraka namna hiyo” Inspekta alimuambia.



“Aagh! Tuachane na hayo afande, tuendelee na yaliyotuleta hapa” TSSI 01 aliongea huku akimalizia kinywaji chake ambacho kwa wakati huo kilibakia kidogo. Akamuita muhudumu aongezewe kinywaji. Na muhudumu akamuongezea yeye na Inspekta aliekimalizia haraka kinywaji chake ili aongezewe chengine. Wakaanza tena maongezi huku vinywaji vikiwa vimejaa kwenye glasi.



“Nimevamiwa masaa mawili yaliyopita nyumbani. Nafikiri walikuwa wamemfuata mama na bahati nzuri hakuwepo nilikuwepo mimi” Inspekta aliongea na kukaa kimya. Akachukua kinywaji chake na kukitia mdomoni kisha akaishusha glasi juu ya meza. Macho akayatupa kwa TSSI 01 aliekuwa kimya akimsikiliza yeye kwa umakini.

Na yeye akakaa kimya!.



“Sijakuelewa hasa. Wavamizi hao ni kina nani na walikuwa wanataka nini?” Hemedy alimuuliza baada ya kuona Inspekta nae amekaa kimya.



“Siwajui na sijajua walichokuwa wanachokitaka. Na walikuja kishari zaidi maana walikuja na silaha wakamuua na askari aliekuwa getini. Ila bahati mbaya kwao wamekutana na chuma kimewanoa na wamejikimbiza wenyewe huko”



“Kwahiyo.....aagh! kwahiyo hukufanikiwa kuziona hata sura zao ama ni vipi yani?”



“Nimewaona ila wao hawakuniona mimi kwasababu niliwahi kuzima taa za sebuleni....” Akamuhadithia ilivyokuwa na hadi watu wale wakakimbia.



“Na wewe imekuaje hadi ukaenda nyumbani kwa mkuu wa mkoa?” TSSI 01 alimuuliza baada ya kusikiliza maelezo hayo mafupi.



“Hahahaha! Mama Agness Elikki ni mama yangu mlezi ambae amenilea mimi tangua sijitambui. Kwahiyo pale ni nyumbani kwetu bwana” Inspekta Salum alijibu.



“Sawa. Sasa hapo unaweza kuhisi hawo watu itakuwa wametumwa na nani au wanataka nini?”



“Kwahapo siwezi kuhisi chochote na siwezi jua labda nimuambie mama huu mkasa huenda yeye akajua”



“Hapana usimuambie. Hilo sakata unatakiwa ulifuatilie kimya kimya hadi uwajue hao watu”



Waliendelea na mazungumzo hadi mishale ya saa tatu usiku. Wakatoka hapo na kila mmoja akaingia kwenye usafiri wake. TSSI 01 akarudi nyumbani kwake huku Inspekta nae akirudi kule Raskazone kwenye nyumba ya mkuu wa mkoa mama Agness Elikki.



Masaa kadhaa nyuma yaliyopita wakati Queen anatoka katika mgahawa huo. Alitembea hadi mbele kidogo ya jengo la CCM Hall. Hapo akaingia katika gari moja lililokuwa limepakiwa pembeni ya uzio wa jengo hilo. Gari aina ya Alteza yenye rangi nyeupe. Humo ndani ya gari kulikuwa na Ata ambae alikaa upande ulipo usukuni. Bilishaka alikuwa akimsubiria mwanamke huyo. Queen alipoingia ndani ya gari hilo, midomo yake akaikutanisha na ya Ata. Wakanyonyana mate kwa sekunde kadhaa. Kisha hapo kila mmoja akachukua nafasi yake.



“Nimeiona sms yako ila nilishindwa kuijibu nikihofia kuharibu mchezo.... Lakini mchezo si umeenda sawa bila shaka yoyote?” Ata aliongea na kuuliza. Safari hii hakuwa na tabasamu usoni kwake kuashiria yupo kikazi ziadi.



“Yeah! Hakuna kilichoharibika na amejiingiza mwenyewe mkenge, amenipa namba yake ya simu kwa minijali ya kumtafuta” Quuen alijibu na kuongezea.



“Safi. Hatua nzuri hiyo. Bilashaka kazi itakuwa rahisi sana”



“Ni kweli....” Akamuangalia usoni Ata.“Ila mbona mtu mwenyewe anaonekana hana hatari yoyote?”



“Ndio kwa muonekano anaonekana hana hatari yoyote. Ila sio mtu wa kumfikiria kirahisirahisi hivyo. Ni hatari kwa kiasi chake”



“Ok. Nimekuelewa mpenzi.... Kinachofuata?” Queen aliongea huku akimuangalia Ata kwa tabasamu kuu usoni kwake. Tabasamu lililomchanganya Ata kwa mara ya kwanza kumuona mwanamke huyo hadi akajikuta akimuapia kimoyomoyo kuwa hatomuacha mwanamke huyo hivi hivi hadi aujue uzuri wake mwengine akiachana na tabasamu. Na bilashaka adhma yake ilitimia na sasa mwanamke huyo yupo mikononi mwake.



“Kinachofuata.....” Na yeye akaongea na kuiacha kauli yake ikining'inia hewani. Kisha akamalizia. “Mapumziko baada ya kazi” akawasha gari na kuanza kulitoa sehemu hiyo.



“Wapi. Nyumbani au..? Aliuliza Queen wakati huo Ata alikuwa yupo katika barabara hiyo ya vumbi akitaka kuingiza gari barabarani baada ya magari yaliyokuwa kwenye barabara hiyo yapite.



“Nyumbani saa hizi hakuna jambo. Twenzetu ‘lodge’ tukapumzike” aliongea hivyo na kuliingiza gari barabarani kuelekea kushoto kwake njia ambayo inaelekea stendi ya zamani ya mkoa huo.



* *http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Zinah na Deva waliingia kwenye jumba la maficho majira ya saa tatu usiku. Tena hiyo ni baada ya kutembeza gari kwa mwendo mkubwa. Waliingia wakiwa wamenyongeka baada ya kushindwa kuifanya kazi kwa umakini waliyotumwa. Waliingia na kuwakuta Mr Hanein na vijana wake. Ata na Queen hawakuwepo baada ya kutumwa kazi ya kumchunguza TSSI 01 Hemedy Bhachu. Kazi hiyo ilikuwa ni kwaajili ya kuonyeshwa Queen mtu huyo maana walipanga wamnase kupitia yeye.



Na walishatoa udhuru kuwa hawatorudi tena hadi siku inayofuata. Hilo halikuwa tatizo kwa Mr Hanein kwasababu aliwaamini vijana wake. Paskal nae hakuwepo tangu majira ya mchana. Yeye alienda kufuatilia biashara za Mr Hanein zinavyokwenda huko mjini. Biashara hizo zilikuwa ni zile biashara halali ambazo zinakubalika kijamii. Na pia alienda kuhakikisha ulinzi wa nyumba ya bosi huyo iliyoko maeneo ya Raskazane.



Waliingia wakiwa wanyonye. Hapo walipokelewa na nyuso ambazo zilihitaji kujua ni kipi hasa kilichoendelea kwenye hiyo ‘mission’ waliyotoka kuifanya. Wakachukua nafasi na kuanza kuwaeleza moja baada ya jengine. Yote waliyoyaeleza yalikuwa ya uongo ili kujilinda wasionekane wazembe walioshindwa kuifanya kazi hiyo.



Mr Hanein aliwaelewa na kuwaruhusu wakapumzike. Akainuka yeye na kupotelea kwenye kordo inayoelekea vyumbani. Huku nyuma aliwaacha vijana wake wakiwa pekeao hapo sebuleni wakiongea mawili matatu. Kisha wakainuka mmoja mmoja kuelekea kwenye vyumba vyao. Kwenye jengo hilo kulikuwa na vyumba vingi sana vilivyo wawezesha vijana hao kila mmoja kulala chumba chake. Baada ya dakika moja hapo sebuleni palibakia na watu wawili tu. Deva na Atu.



Atu aliinuka pale alipokaa na kumfuata Deva pale kwenye sofa alilokaa. Alipofika akakaa karibu yake na kuanza kuukagua mwili wa kijana huyo.



“Subiri nikuchue mpenzi, unaonekana umeumia sana” Atu aliongea hivyo huku akiupapasa mkono wake kwenye mgongo wa Deva.



“Sio mahala pake hapa. Twende chumbani” waliinuka wote na kupotelea katika chumba kimoja kati ya vingi vilivyomo katika jumba hilo.



* *



Siku iliyofuata katika jumba hilo hilo majira ya saa nne asubuhi. Mr Hanein alipokea simu kutoka kwa Mr Tanganyika. Kulikuwa kuna dili kama walivyoliita. Na ndio hapo wapo kwaajili ya kulizungumza. Dili hilo lilikuwa ni la haramu kutoka kwa maharamia hao. Dili la uuzaji wa silaha.



“Lakini si una muamini huyo afisa? Maana asije akauchoma huu mpango halafu wewe mwenyewe si unajua bado wanakutafuta” sauti ya upande wa pili kwenye simu, iliongea.



“Ondoa shaka kwa hilo Mr. Huyo askari nimeshafanya nae kazi nyingi sana za haramu kipindi nilipokuwa na uhuru wangu. Naamini kwasasa hawezi kunigeuka” Mr Hanein alijibu.



“Bakari usiwaamini sana hao viumbe. Si unajua kwamba wanakutafuta kwa udi na uvumba. Sasa je ukimfikishia hizo taarifa halafu akakugeuka? Maana huwezi jua huenda ikawa ameshaiacha hiyo tabia haramu” Mr Tanganyika alionyesha wasiwasi wake.



“Kaka naomba uniamini mimi. Hapawezi kutokea jambo lolote baya. Mimi ndie ninae mjua huyo askari na mimi ndie nitakae jua namna gani ya kumdhibiti pindi akienda kinyume na maagizo yangu”



“Sawa. Basi wewe fanya kila uwezalo, kesho nitakutafuta ili nijue umefikia wapi kwa huo mpango... Ila kuwa muangalifu sana na usalama wako”



“Usijali Mr naanza harakati leo leo, nikifanikiwa nitakujulisha”



Simu ikakatwa na Mr Hanein akashusha pumzi. Tabasamu likajichanua usoni kwake. Tabasamu la furaha. Furaha ya kurudishwa tena kwenye biashara haramu alizozizoea. Biashara ambazo alizianza kipindi akiwa na umri mdogo. Biashara zilizompatia utajiri mkubwa sana na kumfanya awe ni mmoja wa matajiri katika jiji hilo la Tanga. Na biashara hizo hizo ndizo zilizomuingiza gerezani. Na biashara hizo hizo ndizo ambazo zimemtoa gerezani.

Biashara ya kupora au kuiba silaha za serikali na kuwauzia watu binafsi wenye mipango yao binafsi na silaha hizo.

Biashara Haramu!.



Mr Hanein akawaita vijana wake na kuwaeleza hilo dili lililotokea. Dili la kuuza silaha. Silaha ambazo wataziiba kwenye ghala la kuhifadhia silaha za jeshi la polisi. Ghala ambalo hadi sasa hawaja jua ni wapi lipo kwenye mji huo na vipi wataliingia. Lakini Mr Hanein aliwatoa wasiwasi na kuwaambia kuwa yupo askari mmoja atakae wapa muongozo kwenye mpango huo.



Wote walihamaki! Walishangaa si kidogo! Inakuaje kwenye mipango hiyo haramu wanawaingiza askari? Je haoni kwamba kufanya hivyo ni kujichomesha kwa hao askari? Maana yeye ni mwenye kutafutwa hadi muda huo. Kwa kosa la kutoroka gerezani kama si kutoroshwa. Kama alivyofanya kwa Mr Tanganyika. Na hata kwa hao vijana wake pia alifanya hivyo hivyo. Aliwatoa wasiwasi na kuwaambia mpango kabambe jinsi alivyouwaanda.

Wote wakakubaliana nae!.



Mpango ukaanzia siku hiyo hiyo. Queen alitumwa akamfuatilie huyo askari ambae atakae saidia mpango huo kukamilika. Akaelezwa na jina la huyo askari pasi na kuambiwa cheo chake. Na hakuna wakumuambia kwasababu hakuna anaejua cheo chake. Akasisitizwa awe makini maana kumpata huyo askari ndio mwanzo wa kuuanza mpango wao. Akamuondoa wasiwasi mkuu wake. Akatoka hapo huku nyuma akifuatiwa na Ata. Kitendo hicho hakikumfurahisha Atu hata kidogo kuona kaka yake akianzisha mapenzi na mwanamke huyo. Huku akisahau na yeye jambo lake la kuanzisha mapenzi na Deva ilihali kaka yake hataki kuona kitu hicho.



Safari yao ikaishia kituo cha polisi Chumbageni. Ata akabaki kwenye gari huku Queen akishuka na kulisogelea jengo hilo la kipolisi. Alifika mapokezi na kueleza shida yake japokuwa alieleza kwa kubabaika kutokana na kuwa hakuwa akimjua anaemuulizia. Ezekiel Kiulason ndie ambae alikuwa akimuulizia.



Afande aliekuwepo mapokezi alimsontea kidole askari ambae alikuwa akija kwa haraka mahala hapo. Bilashaka kuna kitu alikuwa anakiwahi ndani humo. Queen aligeuza shingo yake na kumuangalia askari huyo alieambiwa kuwa ndie huyo mwenye jina alilokuwa akiliulizia. Alimuangalia kwa umakini mkubwa hadi pale alipowapita hapo na kutokomea zake ndani kwa mwendo wake ule ule wa haraka. Queen alimuambia askari aliekuwepo mapokezi kuwa atamfuata baadae maana kwa sasa anaonekana kama ana haraka kwahiyo wasingeweza kusikilizana. Akaondoka hapo baada ya kushukuru na kurudi garini.



Lakini kwenye mti wa muembe uliokuwepo nje ya kituo hicho. Kulikuwa kuna askari aliekuwa akimuangalia Queen kwa mashaka tangu aliposhuka kwenye gari na hadi alipoenda kupanda kwenye gari akitokea mapokezi. Askari huyo akaanza kupiga hatua za haraka haraka kuliwahi lile gari lisije likaondoka.



..



Alikuwa ni Insepekta Salum Mzanzibar. Na alikuwa amemfananisha Queen na mwanamke aliemuona jana katika mgahawa ambao walienda kukutaniana yeye na Hemedy Bhachu. Na hapo alikuwa akimfuata kupata uhakika kama ndie ama sie. Ashukuriwe mungu maana alighairisha safari hiyo ya ghafla aliyoianzisha. Safari ambayo kama angeendelea kulifuata lile gari aliloingia yule mwanamke aliemfananisha. Basi angekutana na kijana aliewashambulia kule kwenye uwanja wa shule ya Tanga School siku kadhaa zilizopita na kusababisha mauaji ya askari wenzake huku yeye akiwa hoi taabani hajiwezi kwa sindano ile ya sumu aliochomwa nayo begani.



“Huenda ikawa nimemfananisha tu.. Hata kama angekuwa ni yeye ningeenda kumuambia nini sasa” akajiongelea mwenyewe huku akibadilisha muelekeo na kuelekea ndani ya jengo hilo.



“Huyo askari tunaemtaka nimeshamjua tayari kwahiyo tunafanyaje?” Queen alimuambia Ata.



“Inabidi tupaki gari mbali kidogo halafu tumuwinde hadi atakapotoka”



Akiangalia saa yake ya mkononi “Haaa! Yani tuanze kumsubiria saa hizi saa tano hadi muda atakaotoka zamu? Kwanza tutajua atatoka saa ngapi?” Queen aliongea kwa mshangao.



Ata alitekenya gari na kuanza kulitoa hapo huku akitabasamu. “Kanuni moja wapo niliyofundishwa na mwalimu wangu ni kutokata tamaa na jambo nilioamua kulianzisha. Acha tumsubiri hata kama atatoka usiku wa kiza” Ata aliongea hayo. Mbele kidogo, akapaki gari na wote wawili macho yao yakawa kituoni pale.



Majira ya saa saba mchana maeneo ya Tanganyika. Palionekana gari mbili zikiwa kwenye mwendo ambao hauwezi kuandikika kwa maandishi wala kusimuliwa kwa mdomo.

Mwendo wa hatari!

Gari hizo zilikuwa zikiendeshwa kwa mwendo wa kasi kuliko kasi yenyewe. Tukiachana na uajabu wa mwendo wa gari hizo. Ajabu nyengine inakuja kwenye gari hizo. Hazikuwa ni gari ambazo zimewahi kuonekana mahali popote hapa nchini.



Zilikuwa ni gari za ajabu kuwahi kuonekana. Sio kwamba zilikuwa na muundo wa kutisha au mbaya? La hashaa! Zilikuwa ni gari zilizokuwa nzuri kimuundo ila hazikuwa kama hizi nyengine ambazo zimezoeleka katika macho ya watu.



Zilipita Muheza na sasa zilikuwa Pongwe katika mwendo ule ule. Zilikuwa zikiendeshwa kasi si mchezo. Kila zilipopita watu walikuwa wakiacha shuhuli zao na kuzitazama gari hizo kwa mshangao mkubwa huku wengine wakithubutu kupiga minja na mayowe ya shangwe.



“Ebwana eee! Zile gari zimeibiwa nini?” ilikuwa ni sauti ya kijana mmoja wa makamo ambae alikuwa nyuma ya kibanda cha magazeti. Bilashaka ndie alikuwa ni muuzaji wa bidhaa hizo.



Majira haya zilikuwa maeneo ya Sabasaba baada ya kuipita Stendi mpya ya Kange. Zilipofika kwenye round about ya Kwaminchi. Zilipunguza mwendo lakini hata hivyo mwendo huo uliopunguzwa ulikuwa ukiogopesha bado. Zikakunja kushoto kama zinaelekea Kisosora. Mbele kidogo kwenye uchochoro mmoja uliokuwa umetenganishwa na nyumba mbili za ghorofa. Zikaingia kwenye uchochoro huo kwa fujo huku zikiacha vumbi kuu. Zikafunga breki na kutulia hapo.



Vumbi lilikuwa jingi kiasi kwamba hapakuweza kuonekana chochote mahali hapo zaidi ya vumbi hilo tu. Dakika tatu vumbi likaanza kupungua na sasa gari zile zikaonekana zikiwa zimesimama kwa mtindo wa kufuatana. Vumbi lilipoisha kabisa, mbele ya gari zile kwa mbali kidogo, alionekana TSSI 01 akiwa akimesimama kuziangalia gari hizo.



Milango ya gari hizo ilifunguliwa na walionekana Fady na Feysali wakishuka kwenye gari hizo. Hemedy aliwafuata huku tabasamu likiwa usoni kwake. Wakasalimiana kwa bashasha tele baada ya kutoonana kwa mwezi mmoja na siku kadhaa. Wote wakasogea mbele ya gari lile la kwanza na kusimama mbele yake. TSSI 01 alizikagua zile gari kwa dakika kumi na kurudi pale walipo wenzake.



“Aisee hizi gari muundo wake umeutolea wapi Fady?” TSSI 01 aliuliza.



“Akili tu kaka” Faustin Dickson au Fady kama wenyewe walivyamua kumkatisha, alijibu huku tabasamu likiwa usoni mwake.



“Gari za kipekee kabisa hizi. Naamini nitakapotembelea na gari hili macho yote yatakuwa kwangu aisee”



“Huyu jamaa ni nyoko. Watu wote wa kitengo walizishangaa hizi gari baada ya kukamilika. Yani huyu ni ‘genius’. Mbona huko barabarani tumeacha gumzo kubwa” Feysal aliongezea.



“Mission inaendaje?” Fady alimuuliza.



“Nilikuwa nikiigoja hii gari ili niianze rasmi. Mwambieni FATHER anipe wiki mbili tu, narudi na ushindi kitengoni” Hemedy aliongea hivyo na wote wakacheka.



“Kwahiyo muda wote ulikuwa unafanya nini? Au nyumbani ni nyumbani” Feysal aliongea na kwa pamoja wakacheka.



“Si unajua mcheza kwao hutunzwa....!” wakacheka tena. Kisha TSSI 01 akajibu lile swali aliloulizwa na Feysal. “Nilikuwa nawalia ramani na sasa ninapo pakuanzia. Soon wanangu tutakuja kuungana tena”



“Unakuja kuungana na sisi au na mtoto mzuri Hilda...” wakacheka tena kwa pamoja.



“Aaaa wapi! Nyote nimewamisi. Nimewamisi watu wa kitengo. Nimekimisi kitengo. Na pia nimemmisi FATHER.....” TSSI 01 alisema hivyo. Akaendelea.



“.......Embu majamaa tuachaneni na hayo. Nipeni maelekezo ya kuliendesha hili gari, maana bilashaka upande wangu litakua geni hili”



“Kwanza kabla ya yote, chagua kati ya haya mawili uchukue lipi kisha mambo mengine yatafuata” Medy Bhachu akayaangalia magari hayo kwa muda kisha akalinyooshea kidole lenye rangi nyekundu akiacha lile la kwanza lenye rangi nyeusi.



TSSI 02 Fady akampatia kijitabu kijidogo na kumuambia kuwa ndani humo ndio kuna maelezo yote ya jinsi ya kulitumia gari hilo. Akaongezea kwa kumuelekeza mambo baadhi kwenye gari hilo kisha akamuachia funguo na kumpa mtihani wa kujaribu hata kulisogeza hapo. Haikuwa kazi ngumu sana kwa mtu kama yeye kuelewa haraka.



Akafanya hivyo kisha akashuka ndani ya gari hilo. Hapo hapakuwa na chengine cha kufanya zaidi ya kuagana na kupeana ahadi ya kuonana tena pindi akimaliza ‘mission’ hiyo. Wenzake walimtakia kazi njema na wao wakaingia kwenye gari hilo lililobakia kwa pamoja. Gari hilo likaondolewa kwa mbwembwe nyingi mahala hapo na kuingizwa barabarani. Kisha likatokomea kusikojulikana.



Hemedy alikuwa muda wote akiwaangalia wenzake wanavyoondoka hapo. Baada ya kutokomea na yeye akaingia ndani ya gari hilo. Akafungua kile kijitabu na kuanza kukisoma. Alisoma kurasa mbili tu na kuamua kuondoka huku akiwa na wazo la kwenda kukisoma vizuri atakapofika nyumbani kwake. Akaliondoa gari taratibu na kushika uelekeo wa Kwaminchi.



Majira ya saa kumi alasiri. Inspekta Ezekiel Kiulason. Alitoka nje ya jengo la polisi Chumbageni. Mara akasikia sauti. Sauti ikimuita yeye. Akageuka kule sauti inapotokea na kukuta ni askari wa mapokezi ndie ambae alikuwa akimuita. Akapiga hatu ndogo ndogo kumfuata pale alipo huku akimuacha askari aliekuwa na jukumu la kumuendesha yeye akielekea kwenye gari ya kipolisi aina ya ‘defender’.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Afande, kuna mtu alikuja kukuulizia majira ya saa tano hivi au sita za asubuhi. Ila bahati mbaya wewe ulikuwa upo kwenye kikao. Ila mimi nilichomuambia kuwa aje baadae” mwanadada huyo aliekuwa katika vazi la kiaskari mwenye cheo cha Konstebo. Alimpa taarifa Inspekta.



“Ni nani na alikuwa anataka nini?” Aliuliza Inspekta Kiulason.



“Simjui na sijajua pia alikuwa akihitaji nini, ila alikuwa akikuulizia wewe”



“Sawa. Akija tena leo muambie aje kesho maana muda huu naelekea nyumbani” Aliagiza Inspekta na kuanza kupiga hatua akiondoka eneo hilo. Aliingia kwenye gari na safari na kuenda huko anaposema ni nyumbani kwake. Ikaanza.



Wakashika uelekeo wa Hostel za shule ya Sekondari ya Usagara. Walipofika hapo, wakakata kulia na mbele kidogo wakasimama baada ya mataa ya upande wao kuwataka wasimame. Wakasubiri kwa dakika kadhaa ndipo magari yaliruhusiwa. Wakanyoosha na njia hiyo hiyo hadi walipokuja kuipata round about ya Mabanda ya Papa. Hapo wakala kushoto kuelekea na msikiti mkubwa wa Zahrau. Wakaupita na kunyoosha na njia hiyo hiyo. Mbele wakakata kulia baada ya kuipata njia inayoelekea Mtaa wa Makorora. Wakanyoosha na njia hiyo hadi walipokuja kulipata kanisa la Angrikan lililopo mtaa wa Makorora sokoni. Wakakunja kushoto kwenye njia hiyo ya vumbi na mbele kigodo gari likasimama kwenye nyumba moja kubwa yenye rangi nyeupe. Inspekta akashuka kwenye gari na gari hilo likaondolewa kurudi walipotoka wakati huo Inspekta alikuwa kifungua geti la nyumba hiyo.



Mbali kidogo na nyumba hiyo. Gari nyengine aina ya Alteza nyeupe ilikuwa ikigeuzwa kuelekea kule lile gari la polisi lilipoelekea. Gari hilo lilikuwa lipo nyuma ya gari lile la polisi. Lilipofika kwenye mzunguko wa Mabanda ya Papa, likashika uelekeo wa njia ya mkuu wa mkoa huku lile gari la polisi likishika njia ya stendi ya zamani ya mkoa huo.



Lile gari Alteza lilikuwa ni gari ambalo ndani yake alikuwamo Ata na Queen na hapo walikuwa wakirudi kwenye jumba lao la maficho baada ya kupajua alipokuwa akiishi mtu wanaemtaka. Dakika hamsini na tano mbele, walikuwa wakiegesha gari hilo ndani ya uzio wa jumba hilo. Wakashuka wote wawili na kuanza kupiga hatua kuingia ndani ya jengo hilo.



Sebuleni waliwakuta Deva na Atu wamekaa kila mmoja kwenye sofa lake. Ata akamtolea jicho la chuki Deva na wala Deva hakuonekana kujali hilo, ndio kwanza alitabasamu. Ni dhahiri watu hao walikuwa na chuki zilizojiunda kwenye mioyo yao. Chuki ambazo mkandarasi ilikuwa ni mapenzi. Mapenzi kati ya Deva na Atu dada yake na Ata. Ata hakutaka hata kidogo dada yake awe na mahusiono na kijana huyo. Lakini dada yake alikuwa tayari ameshapenda japokuwa ana uweledi mzuri wa kijasusi.



Ni kweli alikuwa ni jasusi hatari lakini haikuwa hivyo hadi kwenye moyo wake. Pamoja na kuwa vizuri katika nyanja za mapigano. Japokuwa alikuwa ameiva kwenye mapigano. Lakini hakuweza kuuzuia moyo wake usipende. Usimpende kijana huyo mwenye sura na mwili wa ushawishi wa kimapenzi. Alijikuta akimzimia tangu siku ya kwanza kumuona na kujikuta akiangukia mikononi mwa kijana huyo.

Atu alipenda!



Ata aliinyoosha moja kwa moja kwenye chumba chake na aliporudi alikuwa amebadilika kimavazi. Akatafuta sofa lililokuwa tupu hapo na kukaa. Kipindi hicho vijana wote walikuwa hapo. Mr Hanein alienda na yeye hapo na kukaa kwenye sofa la mtu mmoja. Akapitisha macho yake kwa vijana wake wote, kisha macho yake yakaganda kwa Ata.



“Young boy niambie nini kimeendelea huko” Kinywa cha Mr Hanein kilifunguka na kuyanena hayo.



“Kazi imekamilika. Tunasubiri oda yako tu kuitekeleza” Ata aliongea.



“Sawa....” macho yake akayatupa ukutani palipokuwa na saa kubwa. Saa ambayo ilionyesha ni saa kumi na mbili na dakika tano za jioni. “Kwavile hilo dili ni la haraka, inabidi mumlete yule askari leo leo yeye na familia yake. Baada ya hapo, nitawaambia kitakachofuata”



“Lakini baba, unahakika gani kwamba huyo askari anaweza kujua ghala lolote la silaha lililopo katika mji huu? Au unabahatisha tu” Atu alimuuliza.



“Kiukweli nabahatisha tu maana mambo makubwa kama hayo hawa askari wadogo wadogo wanafichwa tu. Hawaelezwi siri kama hizo. Lakini Ezekiel Kiulason namuamini sana. Alikuwa shushushu wangu anaeniletea siri nyingi za jeshi la polisi na ndio maana nilidumu katika kazi zangu kwa muda mrefu sana bila kushtukiwa. Alikuwa ni mjanja mjanja sana ambae alipekenyua siri kubwa kubwa sana na kuniletea mimi. Sasa kwa hili sidhani kama atashindwa kujua japokuwa sina uhakika sana. Ila chamuhimu kwa sasa ni nyie kumlete hapa na familia yake. Hayo mengine yatafuata baadae”



“Sawa tumekuelewa. Tutaenda na tutarudi na ulivyotuagizia” Mzee Pijo alisema.



“Sasa.....” akawaangalia wote. Kisha akaendelea. “ Sasa inabidi muende wanne. Ata utaongoza msafara huo. Pijo, Deva na Roben mtaungana nae. Fanyane kazi kwa uangalifu, hakikisheni hamuachi alama yoyote itakayoacha wapate pa kuanzia”



“Sawa mkuu” waliitikia wote kwa pamoja.



“Mrutu, nifuate huku nje...” Mr Hanein aliongea hivyo kisha akanyanyuka pale na kutoka nje ya jumba hilo ambalo lilikuwa na wigo kubwa. Wakatoka nje na kwenda kukaa chini ya mti mkubwa wa muembe. Mahali ambapo kulikuwa na viti kwaajili ya kupumzikia.



Vijana wale walitoka na safari ya kuenda huko walipotakiwa kuenda ikaanza. Muda kidogo wakawa nje ya nyumba hiyo. Wakiwa ndani ya gari aina Pick Up. Walikuwa wakipanga ni jinsi gani wataingia ndani ya nyumba hiyo. Likatoka shauri kuwa waingie kwa kuruka ukuta maana njia ya geti inaweza isiwe salama kwao. Wakakubaliana hivyo na wakatoka watatu wakimuacha Roben ndani ya gari.







Waliruka ukuta kwa ustadi mzuri kiasi kwamba hawakuweza kumshtua mlinzi alieko getini akilinda. Ajabu hii! Watu wanaingia ndani yeye analinda geti! Hata hivyo unadhani basi alichukua hata dakika mbili za kulinda hilo geti? Alisafirishwa kwenda kulinda geti la watu wasio na fahamu huko pasipojulikana na Pijo.

Pakawa kimya!.

Kimya kikuu!.

Kimya cha nje kilimezwa na sauti ndogo ya muziki iliyokuwa ikitokea ndani ya nyumba hiyo. Pengine wenyeji walikuwa wakiangalia au wakisikiliza muziki huo. Wakatembea kwa uangalifu hadi karibu na dirisha la sebuleni.



Moja, mbili, tatu, nne, tano. Ilikuwa ni idadi ya vivuli vilivyopo ndani ya nyumba hiyo. Sebuleni! Hawakuweza kuwaona vizuri kutokana na pazia zito lililofunika dirisha. Wakashauriana kimya kimya chakufanya. Wakafikia muafaka. Wakausogelea mlango wa kuingia ndani humo. Deva na Ata wakabana pembeni ya mlango huo. Pijo akakaa katikati. Akagonga hodi kwa utaratibu.



“Musa nini tena saa hii unataka?” ikasikika sauti ya kike ikilalamika ndani humo.

Kimya! Hakuna aliejibu kitu. Mlango ukagongwa tena.



“Kwahiyo siku hizi umekuwa bubu wewe huwezi kuzungumza?” Sauti ile ilijirudia tena. Mara hii ni kwa ghadhabu kidogo. Michakacho ya mtu anaetembea kuufuata mlango huo ilisikika kwa mbali. Wakajianda kumkaribisha mwenyeji.



Mlango ulifungulia kishari huku mwanamke huyo akiendelea kulalamika. Malalamiko yalikata ghafla baada ya kupokea ngumi nzito iliyotua kwenye paji lake la uso. Papo hapo akageuzwa kwa haraka na kukabwa shingo yake.

Uoga! Hapana. Wasiwasi! Pia sivyo. Au taharuki! Pengine labda ni hofu iliwakumba wote walioko ndani ya sebule hiyo. Mayowe makubwa na madogo yaliwatoka vinywani mwao na wala wasigundue kama walitokwa na mayowe. Inspekta Kiulason alieko ndani ya vazi la fulana ya kukata mikono chini akivalia pensi kubwa. Aliingiwa na mchechetu pengine kushinda hata mkewe aliedhibitiwa na Pijo.



Bastola mbili ziliwaangalia wao huku moja ikiwa juu ya sikio la mwanamama aliedhibitiwa. Wangefanya nini zaidi ya kutulia! Hakuna walichoweza kufanya. Wakabaki kimya huku wakitetemeka kama wagonjwa wa kifafa. Inspekta ujasiri wote wa kiaskari ulimtoka mbele ya manati hiyo ya mzungu. Akatuliza akili na kuitupilia mbali hofu iliyokuwa ikimng'ang'ania isimuache. Hata hivyo hakufanikiwa.

Ujasiri mbele ya watu usiowajua!.

Ujasiri mbele ya manati ya mzungu!.



“Mna...mnataka nini kwangu?” alijitutumua kwa kiasi fulani akapata kuzungumza maneno hayo.



Kimya!



Hapakuwa na wakamjibu. Kwanza wamjibu nini? Wamuambie kuwa wametumwa kuja kumchukua yeye na familia yake? Angehoji zaidi na hapo sio sehemu ya mahojiano. Kitendo bilakuchelewa. Mwanamama yule alikuwa akishuka chini kimya kimya baada ya kuguswa sehemu nyeti kwenye shingo yake. Akawa kwenye ulimwengu mwengine. Ulimwengu wa wasiokuwa na fahamu.



Inspekta baada ya kuona swali lake limejibiwa namna tofauti na yeye alivyotegemea. Akataka kuleta purukushani ila aliwahiwa. Pigo moja tu chini ya sikio lake lilitosha kuunganishwa na mke wake huko alipo. Na yeye kimya kimya akaenda chini. Wakabaki watoto wawili na msichana mmoja waliokuwa wakigugumia kimya kimya huku machozi yakidhihirisha kile kilichopo mioyoni mwao. Pengine labda walidhani kuwa wazazi wao hawapo tena duniani au labda ni hofu imewatawala zaidi.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Watoto wale wawili na yule msichana alieonekana kama mfanyakazi wa nyumba hiyo. Na wao walifinywa sijui waliguswa kwenye shingo zao. Wakapoteza fahamu. Kazi ikawa rahisi kabisa. Wakabebelewa juu juu na kutolewa nje. Getini walimkuta mlinzi bado amelala vile vile. Wakataka wamchukue ila wakamuacha pale pale. Wakaondoka na watu wao. Walifunga geti vizuri na kuwaingiza watu wale kwenye lile gari lao. Safari ya kuondoka hapo ikaanza huku wakiacha Tv na taa za sebuleni vikiiburudishi sebule hiyo.



Hemedy majira haya alikuwa kwenye baa moja iliyopo maeneo ya Dunia Hotel. Alikuwa kwenye meza ambayo ilipata kusogelewa na mwanga wa taa kwa ufinya kidogo, ila yeye hakujali hilo. Mara kidogo Inspekta Salum aliwasili kwenye meza hiyo. Wakasalimiana kwa pamoja na Salum akakaa kwenye kiti.



“Nipe taarifa askari wangu” Hemedy alianzisha mada baada ya kimya cha muda mfupi kutawala hapo.



“Mama amerudi na amehoji kwanini askari wa getini kwake amebadilishwa”



“Askari yupi?”



“Aah Medy kwani hukumbuki kuwa nilivamiwa na wale watu na walimuua yule askari aliekuwa getini siku ile”



“Oooh! Nimekumbuka. Enhee! Niambie”



“Mi nimemdanganya tu kuwa ilibidi iwe vile na kule kituoni nimetengeneza tukio la kiujanja ujanja na wameikubali ile hali.... Ila nataka kujua kwanini umeseme iwe siri nisimuambie mama lile tukio?”



“Kumbuka wale walikuwa na nia na Mama Agness. Sasa endapo utakapompa taarifa hiyo utamchanganya sana na kusababisha mambo yawe makubwa. Kwahiyo cha msingi wewe ni kufuatilia kimya kimya mpaka uwajue watu wale walikuwa ni wakina nani na wanataka nini”



“Sasa nimekuelewa. Ila....” alikatishwa na mlio wa simu yake. Sura ilimbadilika baada ya kuitoa simu hiyo mfukoni na kulisoma jina la aliepiga. Akapiga kite cha hasira na kupokea simu hiyo.



“Sawa mkuu” alijibu kiheshima na kuirudisha mfukoni baada ya kuwa imekatwa tayari.



“Mkuu ameniita kituoni saa hizi. Sijui kuna nini tena....” akamuangalia Hemedy usoni na kumuambia. “Tutaendelea siku nyengine. Acha sasa nikamsikilize” hakusubiri jibu lolote, akanyanyuka na kutokomea nje ya baa hiyo.



TSSI 01 akaitoa simu yake na kuiminya minya. Kisha akaiweka sikioni. Akazungumza kwa muda mfupi, kisha akatoa maelekezo ya wapi alipo yeye. Alipomaliza, simu akaikata na kuiweka mfukoni. Akagida kinywaji kilichokuwa ndani ya glasi. Akachomeka visikilizia muziki masikioni mwake na kuanza kupata burudani hiyo taratibu huku akimsubiri aliemuita.



Katika jumba la maficho Pongwe. Simu ile iliyopigwa na Hemedy ilimfikia Queen. Akamueleza Mr Hanein kitu hicho na akapewa agizo kwamba aende na kama akipata nafasi nzuri basi ahakikishe anaiondoa roho ya kijana yule alionekana kuanza kuwa mwiba kwao kwenye kazi zao.



Queen alijiandaa na kutoka nje ya jumba hilo. Alitembea kwa miguu hadi alipokuja kuipata barabara kuu. Hapo akatafuta kituo cha tax na kujitoma ndani ya tax moja na safari ya kwenda mjini ikaanza. Muda kidogo, tax hiyo ikawa mbele ya baa ambayo ndani yake alikuwemo Hemedy. Queen akashuka na kumlipa dereva tax ujira wake. Akaingia ndani akimuacha dereva akiliondoa gari lake hapo.



Wanaume wakware ndani ya baa hiyo, hawakuacha kugeuza shingo zao kumuangalia mrembo huyo ambae alikuwa akiingia ndani humo muda huo. Labda mavazi ya mnyange huyo ndio yaliwachanganya, au au au labda ni umbo. Umbo la binti ndio liliwatoa akili kwa muda mfupi na kujikuta wakisahau hata vinywaji vyao vilivyokuwa mezani. Pengine hata vinywaji hiyo pia vilimshangaa mrembo huyo maana havikutingishika hata kwa bahati mbaya.

Pengine labda!



Alitembea kwa mwendo wa madaha hadi ilipo meza ya Hemedy huku macho ya wanaume wale yakiwa bado yanatembea nae utadhani wametumwa kumlinda yeye. Kipindi hiki Hemedy alikuwa amesimama pembeni ya kiti chengine tofauti na kile alichokaa yeye. Tabasamu usoni likiwa nae mithili ya mfungua mlango wa ‘Five Star Hotel’. Huenda ikawa ni kwa majivuno au labda ni ukarimu tu wakumkaribisha mgeni mahala popote awapo.



Baada ya salamu ya kupeana mikono. Hakutaka mkono huo mlaini wa mnyange huyo uishie tu kwenye mkono wake. Akaupeleka mdomoni kwake na kuutandika busu safi huku akimuangalia mnyange huyo usoni. Queen alisikitika huku tabasamu lililokuwa usoni kwake likiongezeka zaidi. Huenda amesikitika kwa furaha ya ukaribisho huo au labda amesikitika kwa kumuhurumia kijana huyo kuwa. Pamoja na mbwembwe zote hizo anazomuonyesha hapo, ila leo ndio mwisho wake umefika.

Pengine labda!.



Alimkaribisha kwenye kile kiti ambacho muda wote alikuwa amesimama pembeni yake. Alikivuta kwa nyuma na kumkaribisha Queen kama akaribishwavyo Malkia kwenye kiti cha enzi. Akakaa huku tabasamu likiendelea kuwa nae. Hemedy alizunguka na kwenda kukaa kwenye kile kiti chake alichokuwa amekaa mwanzo.



“Karibu Malikia wangu” Hemedy alimkaribisha tena.



“Asante Mr Handsome” Queen alijibu hivyo na wote wakacheka.



* *



Gari liliingizwa kwenye lile jumba lao. Wakashuka wote na kuwatoa mateka wao ambao hadi muda huo hawakuwa wamepata fahamu zozote. Waliwaingiza ndani ya jumba hilo. Mr Hanein akawaambia kuwa Inspekta Kiulason wamtenganishe na familia yake. Yani wawaweke vyumba tofauti. Agizo likatekelezeka haraka. Ezekiel Kiulason akawekwa chumba tofauti na kile kilichowekwa familia yake. Akawagiza wamletee maji kwajili ya kumzindua kwenye usingizi huo na wao wakafanya hivyo. Akawaomba wote watoke wamuache yeye na mateka wake.



Kabla ya kummwagia maji yale kwaajili ya kumzindua. Alimuangalia kwa muda jinsi afisa huyo wa jeshi alivyotopolea kwenye ulimwengu wa watu wasio na fahamu. Akatabasamu baada ya kuwaza kuwa muda si mrefu atapata kile alichokihitaji.



Inspekta Kiulason historia yake ni ndefu sana. Ila kwa ufupi ni kwamba. Yeye ni mtoto wa kwanza na wamwisho kwenye familia yao. Bahati mbaya baba yake alifariki akiwa na umri wa miaka sita tu huko kwao Bukoba. Alisoma kwa shida hadi kujakufikia kidato cha nne. Baba yake mkubwa ambae ana cheo fulani kwenye jeshi la polisi alimchukua na kumtafutia nafasi jeshini. Aliipata na kuanza kulitumikia jeshi la polisi. Miaka ishirini iliyopita. Akahamishwa mji na kupelekwa katika mkoa huo wa Tanga. Akalitumikia jeshi akiwa na cheo cha Ukonstebo. Kilichomfanya kutopanda cheo haraka ni tabia yake ya uvivu. Hakuipenda kazi hiyo. Ila alijilazimisha kuikubali kutokana na kumhudumia mama yake ambae kwa wakati huo alikuwa akimtegemea yeye.



Kutokana na kuwa hakuipenda kazi hiyo. Akawa si muaminifu tena kwenye jeshi. Aliuza siri za jeshi kwa maharamia. Ndipo alipokuja kukutana na Mr Bakari Hanein. Alimuuzia siri nyingi kipindi hicho akiwa na cheo cha Ukoplo baada ya miaka saba kupita ndipo alipo panda cheo hicho. Ikaja kugundulikana kuwa sio muaminifu kwenye jeshi. Akashushwa tena cheo. Tena hiyo ni baada ya kuombewa msamaha na baba yake mkubwa alipokuwa akitakiwa kufukuzwa kazi. Cheo cha Konstebo kikamuhusu tena.



Lakini hiyo haikumfanya kuwa muaminifu kwenye jeshi. Akaendelea kuuza siri za jeshi. Miaka mitano mbele, akapanda cheo na kuwa Koplo tena. Kipindi hiki ndio kile ambacho Mr Hanein alikuwa yupo gerezani. Akakosa wa kumuuzia tena siri za jeshi. Kiasi fulani akabadilika na kuwa muaminifu. Akapanda cheo baada ya tabia yake ya kupenda kupeleleza vitu. Akawa ni Inspekta Kiulason mpelelezi wa jeshi la polisi.



Na leo hii alikuwa mikononi mwa Mr Hanein. Mr Hanein baada ya kutosheka kumuangalia afisa huyo. Akataka kumwagia maji ili amuamshe. Ni kama vile alijuwa anataka kuamshwa. Aliamka mwenyewe. Kwanza alishangaa mazigira hayo. Akafinya macho kama mara tatu baada ya mwanga wa taa kumpiga kwenye macho yake yaliyotoka kwenye giza. Alipokuja kutulia. Akaangalia mandhari ya sehemu hiyo.



“Nipo wapi mimi!?” alijiuliza mwenyewe kwa sauti ya chini. Bado hakuwa makini kuangalia mbele yake. Akajinyanyua pale alipolala na kukaa kitako akiendelea kuangaza macho yake kwenye chumba hiko.



“Mama weee!” alipiga yowe la hofu baada ya kumuona mtu ndani humo. Mtu aliekuwa akimfananisha. Alimfananisha na mtu mmoja aliewahi kumuona miaka mingi iliyopita. Lakini mtu huyo alikuwa gerezani na ikathibitishwa kwamba alitoroka. Inamaana ndie huyu? Alijiuliza mawazoni. Mungu wangu! Anataka nini tena kwangu?.



“Bakari Hanein!” aliita kwa sauti iliyojaa taharuki ndani yake.



“Ndio mimi Koplo Kiulason” Mr Hanein alimuitikia. Alimuita kwa cheo chake alichomuacha nacho miaka kumi na tano iliyopita kabla haja enda gerezani.



* *



Kule baa. Hemedy na Queen walikuwa wakiendelea na maongezi yao. Maongezi ambayo Hemedy ndie ambae aliyatawala sana hapo. Mara kadhaa Queen alitabasamu kwa vituko na maneno ya kijana huyo. Majira ya saa tano usiku. Likapita shauri kuwa watafute pahali wapumzike. Hemedy akaomba wakapumzike kwenye ‘logde’.



“Kwani wewe huna kwako?” Queen alimuuliza.



“Kwangu kuna wageni wengi kwahiyo hakutokuwa na uhuru” TSSI 01 alidanganya. Lakini alijidanganya mwenyewe kutokana na huyo anaemdanganya anamjua yeye kuliko yeye anavyomjua. Queen alijua kivyovyote Hemedy hakutaka kupajua kwake. ‘ Sio mbaya hata huko unapopataka wewe nitakuwa huru zaidi kuiondoa roho yako’ Queen alijisemea mwenyewe mawazoni. Wakainuka hapo na kutoka ndani ya baa hiyo baada ya kuwa wameshalipa.



“Weee! Dear hili gari ni la kwako?” Queen alipayuka baada ya kuona akifunguliwa mlango kwenye lile gari la ajabu lililokuwa limepaki nje ya baa hiyo. TSSI 01 hakuongea kitu zaidi ya kumuashiria kwa macho aingie ndani ya gari hilo. Akaingia kisha mlango ukafungwa. Hemedy akazunguka upande wa pili wa dereva na kuingia. Akalitia moto na kuondoka hapo huku Queen akizidi kushangaa muundo wa gari hilo kwa ndani na uendeshaji wake pia.



Safari yao ikaishia Nyinda Hotel. Wakashuka kwenye gari na kupiga hatua kulisogelea jengo hilo la hotel. Wakapita mapokezi na kufanya itfaki zote, kisha wakakabidhiwa ufunguo wa chumba namba 76 kilichopo ghorofa ya tatu. Wakaongozana hadi walipokipata chumba hiko.





Wakajitoma ndani. Na hapo kila mmoja akichukua nafasi yake. Hemedy kitandani, Queen kwenye sofa. Ni dhahiri walikuwa wakitegeana nani aanzishe chochote kitakachowafanya kuwa pamoja kwa namna yoyote. Macho yao yalikuwa yakiangaza huku na huko ndani humo. Queen akaacha kuangaza macho yake humo na kuyahamisha kwenye simu yake kubwa. Alikuwa akiminya hapa na pale ili kuzuga.



Ghafla alishtukia mikono ikimpapasa kwenye kiuno chake. Akaifuatiliza inapotoka na kukuta ikitokea pembeni yake kwenye mwili wa Hemedy aliekuwa amehamia pembeni yake. Akakutana na tabasamu. Tabasamu lililowaacha hoi baadhi ya mabanati waliowahi kupata bahati ya kulishuhudia. Na yeye akachia tabasamu ambalo lilimuacha hoi Ata siku ya kwanza kumuona.

Ngoma droo!.



Hemedy akasogeza kinywa chake taratibu kwenye kinywa cha Queen. Alipokelewa kwa bashasha na mbwembwe nyingi. Ni kama vile Queen alikuwa akihitaji jambo hilo litokee. Alivyowaza yeye ni kuwa, uwezo wa kumuua muda huo anao. Ila alichopanga kuwa atamuua baada ya kulijua kama sio kulifaidi penzi la kijana huyo. Akajikuta anakuwa mpole ili atimize hitaji lake kabla hajatimiza lengo lake.



Walichezeana kiasi kwamba sasa wakaona huo ndio muda muafaka wa kufanya kile walichotoka nacho tangu kule baa. Kile kilichowafanya wakodishe chumba kwenye Hotel hiyo kubwa. Kile ambacho roho zao zilipenda na kuridhia kukifanya.

Ngono!.

Ngono zembe!.



“Mmm-mmh! Mbona unapapara hivyo mwanaume?” Queen aliongea hivyo huku akimuangalia Hemedy usoni. Aibu! Aibu ikawa usoni mwake baada ya kuonekana ana papara kwenye jambo hilo. Akatulia na kumuangalia msichana huyo usoni. Wakakokotana na kukiendea kitanda ambacho bila hiyana wala manung'uniko kiliwapokea. Wakafanya kile kilichopo vichwani mwao kwa muda huo.



* *



Majira haya walikuwa wapo kwenye viti viwili vilivyoangaliana katika chumba kile kile. Walizungumza kiurafiki zaidi na kukumbushina mambo mengi yaliyopita nyuma. Alimsimulia mambo aliyokutana nayo gerezani. Na yeye alimsumilia yaliyopangwa juu yake baada ya kutoroka gerezani. Ilishangaza sana. Mwanausalama kuzungumza na mhalifu. Tena alietoroka gerezani mwezi mmoja nyuma ambae jeshi la polisi linamsaka kwa udi na uvumba popote alipo.



“Sasa Kiulason kuna kazi moja ambayo nataka unisaidie rafki yangu” Mr Hanein alianzisha mada baada ya kukumbushiana ya nyuma.



“Kazi ipi?”



“Nataka unisaidie kupajua lilipo ghala la silaha kwenye mji huu. Ni hivyo tu” Kiulason macho yalimtoka pima. Hakutarajia wala kuwaza kusikia kitu kama hicho kwa mtu huyo. Ghala la silaha? La nini? Ili iweje?. Alijiuliza maswali hayo ubongoni huku akiwa bado amemkazia macho Mr Hanein.



“Ghala la silaha!” akauliza kwa sauti baada ya kuona hapati majibu ya kile ajiulizacho.



“Ndio. Na nina imani wewe unajua au kama hujui basi unaouwezo wa kupajua. Ni hilo tu”



“Unataka kufanya nini? Au kwanini?”



“Sipo hapa kwaajili ya kuulizana maswali Inspekta. Ninachotaka ni kuniambia kile nilichokuambia. Basi!”



“Ok. Sipajui” Inspekta alijibu kijeuri. Kicheko kikubwa kilimtoka Hanein na kumshangaza Kiulason. Aliwaza labda ni kwavile anajivunia kuwa yupo katika himaya yake ndio maana amecheka baada ya kusikia jibu lake.

Akaendelea kutikisa kibiriti!.



“Na usitegemee labda nitakuambia chochote kwa hayo unayoyataka. Sipo kama vile ulivyoniacha kipindi kile. Sio mpumbavu tena. Sio mjinga tena. Nikimaanisha siwezi kukuambia chochote kuhusina na siri za jeshi hata uniue” Kicheko kikubwa kikamtoka zaidi Hanein baada ya kusikia maneno hayo. Akanyamaza ghafla na kumtolea macho Inspekta huku sura yake akiileta mbele.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Sikuui wala sifikirii kukutesa ndipo uniambie. Lakini jua tu kwamba utaniambia kwa hiyari yako mwenyewe bila kukulazimisha Inspekta. Utaniambia tu” Akainuka hapo alipokaa huku akimuacha Ezekiel Kiulason akimuangalia na asielewe ni kwanini mtu huyo ameinuka hapo. Akasubiri kuona kitakachotokea.

Subiri ya vuta heri!.

Kwake ilivuta shari!.



Hakutegemea. Hakutegemea kwa alichokiona mbele yake. Familia yake yote ilikuwa mbele yake ikimtazama kwa jicho lisilo la kawaida. Jicho la huruma. Jicho la huzuni au labda jicho la wasiwasi. Au jicho la hofu. Pengine yote hayo kwa ujumla. Akataka kuinuka ila aliketishwa kwa kunyooshewa bastola na kuambiwa atulie hivyo hivyo na wala asijaribu hata kuinua vidole vyake vya miguu.



Familia ile ikaondolewa pale pasi na kuzungumzwa chochote. Wakabaki tena wawili. Mr Hanein na Kiulason, wakiangaliana kama majogoo yaliyo katika pambano la kugombea mtetea. Mr Hanein akatoa cheko jengine la kukera ilhali Inspekta akiwa kimya na mtulivu. Ujanja wote ukimuisha kama sio kumpotea kabisa na wala isijulikane ni wapi umeelekea. Mr Hanein akaongeza kicheko chake baada ya kuona mtu wake amegwaya ghafla.

Cheko la dhihaka!.

Au labda ni cheko la ujivuni.



“Sasa naomba tuongee kama watu wazima hapa. Sitaki tena mambo ya kubembelezana kama natongoza kitoto cha msingi. Kwanza nashangaa sijui jeuri hiyo unaitolea wapi wakati upo kwenye himaya yangu. Hupajui hapa ni wapi. Sehemu gani lakini bado unaleta kujiamini.. Ok. Ni wapi lilipo ghala la silaha. Ukileta jeuri, na mimi naleta familia yako naua mmoja mmoja mbele yako halafu mwisho utamalizia wewe kujiua mwenyewe.....” akatoa vitisho. “Jibu swali” akamalizia.



“Sipajui” Alijibu. Safari hii alijibu kwa adabu na kwa uhakika zaidi. Mr Hanein aliuona ukweli wa maneno hayo ndani ya uso wa Inspekta.



“Sina shaka na hilo. Ila nakuachia urudi uraiani. Nakupa siku mbili tu za uchunguzi wako kujua mahali lilipo ghala la silaha. Nakupa siku mbili tu. Ya kesho na kesho kutwa. La sivyo...” akaiacha kauli hiyo ielee hewani. “Tunaweza kuondoka humu rafiki yangu”



Akainuka pale alipokaa na kuanza kupiga hatua ndogo ndogo kuufuata mlango wa chumba hicho huku mikono ikiwa kaifumbata nyuma. Inspekta hakujua asimame au andelee kukaa pale pale. Lakini kukaa pale itasaidia nini kwake? Akainuka na kuungana na mwenyeji wake kutoka humo. Wakiwa wapo kwenye kordo wakitembea mdogo mdogo. Kiulason alijikuta ghafla akihisi maruerue. Macho hayaoni mbele vizuri na mwili ukamsaliti kusimama imara. Akaenda chini taratibu na mwisho akadakwa Mr Hanein.



Lilikuwa ni pigo ka kushtukiza alilopigwa nyuma ya kisogo na kumfanya apoteze fahama papo hapo. Akabebelewa juu juu na kupelekwa kwenye gari. Ata akazama kwenye gari na safari ya kumrudisha nyumbani kwake ikaanza.



* *



Kule Nyinda Hotel katika chumba walichokuwa wapenzi wale wa hiyari. Kilikuwa ni kipindi cha mapumziko baada ya kuwa wameshacheza mchezo wa kwanza. Walikuwa bado wapo kitandani wamejilaza chali. Hoi taabani kwa mchezo waliotoka kuufanya muda mfupi uliopita. Wakashauriana wakaoge kwanza kabla ya kuendelea na mchezo mwengine. Queen aliinuka na kujifunga taulo. Akaelekea maliwatoni akimuacha Hemedy kitandani bado.



TSSI 01 baada ya kuona mwanamke yule ameingia maliwatoni. Akawahi simu yake kwaajili ya kuipekua. Alishamtilia shaka tangu kule baa. Maana ni mara chache sana alimuona akimuangalia kwa jicho ambalo TSSI 01 alilitafsiri kivingine. Akapanga kumchunguza atakapo pata upenyo. Na upenyo wenyewe ukawa ndio huo.



Bahati nzuri ikawa kwake. Simu ile haikua na ‘password’ zozote. Ikawa rahisi kwake. Akaingia kwenye picha na kukuta ni picha za kawaida tu ambazo hakuzitilia shaka yoyote. Akatoka na kuingia upande wa ‘message’ huko alikutana na sms tatu alizokuwa akitumiana na mtu aliemsevu ‘Mkuu’. Umefanikiwa? ‘Ndio nipo nae’ basi hakikisha unaachana nae akiwa ni mfu’.



Ndizo sms alizokutana nazo. Akapiga jicho kwenye mlango wa maliwato na kukuta bado kuna ukimya. Ni maji tu yanayotiririka ndiyo ambayo yanasikika. Akarudisha macho yake kwenye ile simu na kuingia upande wa majina. Hakukuwa na majina mengi. Akaichukua simu yake na kuinakili ile namba iliyoseviwa kwa jina la ‘Mkuu’. Kisha hapo akarudisha kila kitu vile vile. Kidogo akaichukua simu yake na kuzitoa ‘password’ na kuiweka kawaida. Kisha akajilaza vile vile akisahau kuuangalia na mkoba wa mwanamke yule.

Pengine labda alidharau!.



Queen alitoka maliwatoni. Akatabasamu baada ya kukutana na tabasamu kutoka kwa kidume kilichojilaza kitandani. Hivi sasa kila mmoja alimjua mwenzake tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Akashukuru hisia zake zilizomtuma muda mrefu kumtilia shaka mwanamke yule. Na sasa alilithibitisha hilo kuwa huyo alikuwa ni hasimu wake. Inamaana hata pale mgahawani ilikuwa ni mtego wa kunitega? Duh! Kwa asilimia zote alifanikiwa hilo. Hemedy alijiwazia mwenyewe kipindi hicho mwanamke huyo alikuwa amekaa kitandani akimuangalia yeye.



“Neda kaoge mpenzi tuje kuendelea” Queen aliongea kwa sauti laini. Dhihaka hii! Ananidhihaki ndio. Alijiwazia tena mwenyewe baada ya kauli hiyo. Akajinyanyua pale kitandani na kujifunga taulo jengine tofauti na lile alilojifunga Queen. Na yeye akaingia maliwatoni.



Ikawa ni zamu sasa ya Queen kuipekua simu ya Hemedy. Aliikuta ikiwa haina ‘password’. Akafurahi kimoyo moyo bila kujua kuwa ilijulikana kuwa ni lazima angetaka kuipekuwa simu hiyo na ndio maana ikatolewa ‘password’. Akapekuwa kila sehemu lakini hakuona chochote cha maana. Akaachana nayo na kuzifuata nguo zake. Akazivaa. Kisha akarudi tena kitandani akimsubiri atoke maliwatoni. Akauvuta mkoba wake na kuitoa bastola yake. Akaiweka tayari kwaajili ya shambulizi.



TSSI 01 alipotokea kwenye mlango wa maliwatoni akakutana uso kwa uso na domo la bastola lililokuwa limeelekezwa kwake. Akatabasamu badala ya kushtuka kama Queen alivyotegemea. Kidogo hiyo ikamuondoa umakini Queen. Inakuaje namnyeshea bastola lakini ndio kwanza anatabasamu? Inamaana hajui kama hii ni bastola? Hajui kuwa ina madhara? Hajui kuwa ina ua?

Umakini ukampungua!.



“Nini tena Malikia wangu kunyoosheana mabastola tena saa hii? Au ndio mapenzi ya kwenu hayo ambayo mimi siyajui?”



“Nataka uniambie wewe ni nani na sivinginevyo” Queen aliongea kwa ujasiri.



“Inamaana jina langu umelisahau ghafla mara hii? Au unaanza kuchanganyikiwa na mapenzi niliyokupa?” TSSI 01 alimjibu akiwa bado tabasamu likiwa usoni mwake huku akianza kupiga hatua kumfuata pale alipo.



“Ukijaribu kuinua tena mguu wako natawanyisha hicho kinachokufanya ujiite mwanaume. Sitaki maelezo wala maneno. Ninachotaka uniambie wewe ni nani. Basi!”



“Basi mama, basi yaishe. Unataka nisiitwe baba? Ok. Mimi ni Hemedy Bhachu nimetoka kitengo maalumu cha siri nimekuja kuhakikisha hamuendelei tena na mauaji mnayoyafanya katika mji huu. Na nyote mnaingia gerezani kama sio kaburini mkiona sehemu hiyo haiwafai. Ni hivyo tu mrembo” TSSI 01 alijibu huku akiwa hana wasiwsi. Akapiga hatua nyengine mbili ila alikaripiwa kuwa atulie hapo hapo.



“Sasa mwisho wako umefika na utaenda kuwasalimia wenzako kuzimu” Queen aliongea huku akiikoki bastola yake.



“Nini tena Malkia? Inamaana umelisahau penzi nililokupa muda mfupi uliopita? Au ndio hiyo shukurani ya punda mateke?”



“Sihitaji ngonjera zako. Acha nifanye kile nilichokikusudia” Alizungumza hiyo na kuanza kuiminya ‘triger’ kuruhusu risasi itoke.



“Ngoja kwanza. Hiyo bastola yako haina kiwambo cha kuzuia sauti. Endapo ukinipiga risasi basi jua itatoka na sauti kubwa. Na hiyo itasababisha patokee purukushani humu na unaweza usitoke salama kutokana na hii Hotel inaulinzi mkali. Sasa chagua njia nyengine ya kuniua acha na hiyo ya hatari” TSSI 01 alimuambia. Na Queen akajikuta akikumbuka kuwa ni kweli hakuifunga kiwambo cha kuzuia sauti. Akapeleka mkono mmoja kwenye mkoba wake kwaajili ya kukichukua kiwambo huku mwengine ukiwa bado umeshika bastola. Alipapasa huku na huko lakini hakukiona. Ikabidi apeleke macho yasaidizane na mkono wake huku akiwa bado amemnyooshe bastola Hemedy.

Kosa!.



Hakupata muda wa kujua kwamba hilo ni kosa kubwa sana ambalo amelifanya. Kitendo bila kuchelewa. Bastola iliruka hewani na kuenda kusambaratika sakafuni. Ngumi mbili zikatua kwenye paji la usoni la Queen na kujikuta akiruka hadi ukutani na kusimama akiangaliana na Hemedy aliekuwa akitabasamu. Aliangalia chini ya miguu yake na kukutana na mto. Akauinua ule mto kwa haraka kwa mguu. Ukaja juu. Akaudaka na kumrushia Hemedy wa uso.



Hemedy aliupangau lakini hakuweza kulipangua teke lililotua kufuani mwake. Akapepesuka kidogo na kukaa sawa. Mara hii Queen alikuja na mapigo ya kuchanganya ya haraka na kwa kasi. Lakini yote yalionwa na kukwepwa vizuri. Hemedy akamshushia na teke la kiuno lilimtoa mguno huku akienda kuukumbatia ukuta.



Wote wakawa wanaangaliana. Queen akajaribu tena bahati yake. Akaruka juu mfano wa paka aliemuona mbwa mkorofi akilenga kuuvamia uso wa Hemedy. Hemedy alimuona na kumpisha kisha akamshushia na teke jengine la kiuno. Queen alitoa yowe dogo la maumivu huku akikunja sura. Akasimama tena kumuangalia hasimu wake. Bastola iliyoanguka ikiwa mita kadha karibu yake. Akayatupa macho yake kwa hasimu wake. Kisha akayarudisha kwenye ile bastola. Akayaondoa hapo na kumuangalia tena Hemedy. Hemedy alishajua kuwa Queen anaiwinda ile bastola. Akawa yupo makini zaidi.







Queen akaruka sarakasi kuiendea ile bastola, lakini alichokutana nacho alijuta kwannini alikuwa na wazo ya kuifuata ile bastola. Wakati Queen akiwa juu, akiwa ameruka sarakasi kuifuata bastola. TSSI 01 alichomoka kwa kasi na kumpiga teke la nguvu la tumbo kiasi kwamba Queen hakuweza kujizuia asitoe yowe kubwa kama mbwa koko aliepigwa kigongo cha kiuno. Alikwenda kujipigiza kwenye mbao ya kitanda kimgongo mgongo na kutulia chini akiwa haelewi ashike tumbo au mgongo. Akabaki kulia tu kama mtoto mdogo huku akimuangalia hasimu wake kwa hasira kuu.



“Ulitumwa kunimaliza mimi. Ila mimi nakumaliza wewe halafu ukawape salamu kuwa nimeamua kuingia kazini rasmi na yeyote atakaejipendekeza ajue kwamba hana bahati kama ambavyo huna wewe saa hii” TSSI 01 aliongea hivyo akionekana ni kweli amedhamiria kufanya hivyo. Hakuwa na tabasamu kama mwanzo na wala hakuwa akicheka tena. Aliweka sura ya kazi.



Queen bado alikuwa akitweta pale chini alipokaa kitako huku akiwa anayasikilizia maumivu kimya kimya. Hemedy alimfuata pale na kumuinua kwa kumshika kifuani kwenye nguo aliyoivaa. Queen akabaki kuning'inia kama nyama ya ng'ombe buchani. Hemedy akampiga vichwa viwili vya haraka na kushtukiza kwenye mwamba wa pua.

Damu!.

Damu zikawa zinamtoka kwenye pua zake kama mifereji ya maji machafu. Hakujizuia kulia. Alilia kwa maumivu hayo anayopatiwa na kijana huyo. Kijana alietoka kufanya nae mapenzi muda mfupi uliopita. Akatamani kumkumbushia hicho kitu. Lakini akaona atapuuzwa kama yeye alivyompuuza wakati akiwa amemshikia bastola.



Akajuta kimya kimya kwanini alimuwazia sivyo mtu huyo. Akajaribu bahati yake ya kujiokoa na kifo. Kifo alichokiona mbele yake. Pengine labda kilikuwa kimeshakaribia sasa! Akapeleka mkono wake sehemu ngeti za Hemedy. Hemedy aliligundua hilo mapema na kufanya hila ya kujirudisha nyuma kidogo na mkono wa Queen ukaondoka na taulo alilovaa. Hapo hapo kwa hasira akamrusha Queen na kwenda kujipigiza tena kwenye mbao ya kitanda kwa mara nyengine.

Ebwana ee!!



Maumivu aliyoyasikia hayakuweza kuandikika hata kidogo sembuse kusimulia tu. Akaongeza kilio. Kilio cha sasa kilikuwa ni kikubwa zaidi ya cha mwanzo. Akajuta!. Akajuta!. Akajuta kuingia anga ambazo sio saizi yake. Sasa Hemedy alikuwa akimuangalia hasimu wake kwa hasira akiwa uchi.

Uchi wa mnyama!.

Ila hakujali hilo. Alichojali yeye ni kutoa adhabu ya kimya kimya hadi kifo kimkute hasimu wake. Akamuwazia ni kipi cha kumfanya tena maana hakutaka kumuua haraka.



Wakati TSSI 01 akiwa uchi wa mnyama akimuwazia Queen ni kipi cha kumfanya kabla kifo chake. Queen na yeye alikuwa akiwaza ni vipi atajitetea kabla kifo hakijamkuta mahala hapo. Ni kweli alikuwa na maumivu mwili mzima hasa hasa sehemu ya mgongo alipopigizwa mara mbili kwenye mbao ya kitanda. Lakini maumivu hayo hayakuweza kumzubaisha na kumlaghai eti kuwa anaweza kusamehewe mahala hapo akaondoka. Akaona uzembe kufa hapo. Kufa kipumbavu. Kufa kibwege!.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mara moja akapiga jicho pembeni yake na kuiona bastola yake ikiwa mbali na yeye. Hakutaka kufanya uzembe kama alioufanya mwanzo na kumsababishia maumivu mengi kiasi hicho. Akapiga jicho kushoto kwake na kuuona mkoba wake umetulia chini ukiangalia mpambano huo. Akarudisha macho yake kule upande ulipo ile bastola. Akajua hata akifanya nini hatoweza kuiwahi. Lakini upande ulipo ile bastola. Nyuma kidogo karibu yake kulikuwa na mto. Mto ule aliojaribu kumrushia mara ya kwanza hadi akafanikiwa kumpiga teke la kifua. Pigo ambalo ndilo pekee alilobahatisha kwenye mpambano huo.





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog