Search This Blog

Saturday, 5 November 2022

TSSI 01 PRISONER - 4

 








Simulizi : TSS 01 Prisoner

Sehemu Ya Nne (4)







Ghafla akauvuta ule mto na kumrushia tena usoni. TSSI 01 akababaika kidogo kuukwepa ule mto. Queen akatumia nafasi hiyo kutoroka. Hakuitumia tena nafasi hiyo kwaajili ya kupambana. Akaona kufanya hivyo ni kama vile kusubiri kifo chake. Pale pale akauvuta mkoba wake na kupanda kitandani haraka. Ashukuriwe ‘Disgner’ wa chumba hicho kwa kukiweka kitanda karibu na dirisha. Dirisha la vioo. Queen hakupata tabu kukivunja kioo hicho na kuupata upenyo ambao ungemuwezesha yeye kupenya.



Akaurusha mkoba wake na nje kisha akapitisha mguu wake mmoja na kuingiza kichwa. Mguu mmoja ukabaki ndani. TSSI 01 kuona anataka kutorokwa. Akawahi kupanda kitandani na kuudaka mguu mmoja wa Queen uliokuwa umebakia ndani bado. Wakawa wanashindani. Hemedy anauvuta kuingia ndani na Queen nae anauvuta kuutoa nje. Ikawa ni vuta nikuvute. Quuen akauvuta mguu wake na kuusukukuma kwa nguvu nyuma. Mguu ule ukamponyoka Hemedy na kufanikiwa kuutoa na nje.



Huko akatambaa na nguzo ya matofali iliyokuwa imeshuka chini pembeni ya dirisha. Alipofika chini kabisa. Akachukua mkoba wake ambao ulikuwa umenasa kwenye maua. Akaruka ukuta kwa kudandia mapipa ya maji yaliyokuwa karibu na ukuta huo.



“Shit!” TSSI 01 aling'aka kwa hasira baada ya kuona hasimu wake amemtoroka. Akavaa nguo zake haraka haraka. Akaiokota bastola ya Queen na kutoka nayo pale pela dirishani. Akazunguka kwa mbele ya Hotel hiyo. Akaingia kwenye gari lake na kutokomea zake hapo.



Safari yake iliishia kwenye nyumba yake. Akaingiza gari ndani baada ya kuwa ameshalifungua geti. Akashuka na kuanza kupiga hatua kuingia ndani humo kwa mwendo wa haraka. Alipofika sebuleni, akakaa kwenye sofa na kuanza kutafakari hili na lile. Hiki na kile. Akaitoa bastola iliyoachwa na Queen kule Hotelin na kuiangalia. Kisha akatabasamu.

Tabasamu la uchungu!.

Uchungu wa kumkosa hasimu wake!.



“Kumbe nilikuwa nimekaa na nyoka muda wote ule?”



Alijisemea mwenyewe akiwa bado anaiangalia bastola ile. Akazitoa risasi na kuziweka pembeni kisha na ile bastola pia akaiweka. Hivi sasa aliishika simu yake. Akiwa anaiangalia ile namba. Namba ambayo kwenye simu ya Queen iliseviwa ‘Mkuu’. Aliiangalia kwa muda utafikiri alikuwa akijaribu kuinakili kichwani, lakini sivyo. Alikuwa akiwaza. Huyo Mkuu anaweza akawa ni yule mfungwa alietoroka kwa jina la Bakari Hanein?.

Hakupata jibu!.



Akaachana na ile namba. Akaingia upande wa majina yaliyoseviwa kwenye simu yake. Baada ya kupata jina alilolitafuta. Akapiga. Lakini jibu lililokuja ni kuwa mtumiajia wa namba hiyo hakuwa akipatikana kwa muda huo. Akapewa ushauri kwamba labda ampigie tena baadae. Akaiweka simu pembeni na kutoka hapo sebuleni. Akapandisha ngazi hadi chumbani kwake. Huko moja kwa moja akajitupa kitandani baada ya kuwa ameshazipunguza baadhi ya nguo zilizokuwa mwilini mwake. Akalala huku akiacha simu na ile bastola vikimsubiri pale sebuleni alipoviacha.



* *



Queen baada ya kuponea chupuchupu kwenye tundu la kifo. Majira haya alikuwa maeneo ya Chuda relini karibu na Pweza Club. Alikuwa akijikokota mithili ya ajuza atembeleae fimbo. Hasira, Ghadhabu na Maumivu, Pengine na uchovu pia ulichangia kuwa hivyo. Alitoa simu yake na kumpigia Ata. Majira haya Ata ndio alikuwa anarudi baada ya kumpeleka Inspekta Kiulason nyumbani kwake.



Akiwa kwenye gari maeneo ya ya msikiti wa Madina. Simu yake ilipata uhai. Akaangalia anaempigia ni nani kisha akaipokea baada ya kujua kuwa ni Queen ndie ambae alikuwa akimpigia.



“Ata uko wapi saa hii?” Queen aliuliza kwa sauti ya uchovu na ya maumivu. Sauti hiyo ilimfanya Ata apunguze mwendo wa gari na kusikiliza vizuri.



“Nipo mjini huku. Kuna nini? Kwani wewe uko wapi?” Ata alijibu kisha akauliza.



“Mimi nipo sijui wapi hapa. Nimepatwa na makubwa” Ata baada ya kusikia hivyo. Akaegesha gari mkabala na ‘Garden’ ya Madina apate kumsikiliza mwanamke huyo. Anashangaa sana. Inakuaje Queen aseme yupo pahali lakini hapajui ni wapi wakati yeye kumbukumbu zake alimuacha kwenye lile jumba lao?.

Wivu!.



“Queen mbona sikuelewi? Uko wapi wewe na unafanya nini huko saa hizi?” Ata alimuuliza.



“Sipajui, wewe njoo unichukue nitakuambia kila kitu”



“Ooh! Sasa nije kukuchukua wapi ikiwa wewe mwenyewe hupajui?”



“Subiri basi niulize kisha nitakujulisha” Simu ikakatwa. Baada ya dakika mbili simu ya Ata ikaita tena. Akaipokea.



“Nipo Chuda relini karibu na Club moja ya zamani inayoitwa Pweza. Ukifika nipigie simu maana sio sehemu salama kwangu.....” akamalizia. “Na usichelewe”



Ata sehemu hiyo alikuwa akiijua. Akaondoa gari na kwenda kuizunguka ‘round about’ ya Mabanda. Kisha akashika uelekeo wa njia iendayo stendi ya zamani. Alikuwa kwenye mwendo wa kasi si kidogo. Akanyoosha na njia hiyo hadi alipokuja kuipata barabara ya kwanza. Akakunja kushoto na kunyoosha na njia hiyo. Punde alikuwa karibu na Club ya zamani iitwayo Pweza. Akasimamisha gari na kuangaza huku na huko kabla hajatoa simu yake na kuzipiga namba za Queen.



“Uko wapi? Mi’nshafika hapa Club” Ata aliongea huku akiangaza angaza macho yake huku na huko akiwa bado ndani ya gari.



“Rudi nyuma kidogo karibu na hii Bakery ya mikate” Queen alijibu hivyo. Ata alirudisha gari kinyume nyume simu ikiwa bado iko hewani. Hapo Club na hapo kwenye hiyo Bakery hapakuwa mbali sana. Ni kama mita mia na hamsini tu. Akafika na kabla hajaongea kitu. Akashangaa mlango wa gari upande wa abiria ukifunguliwa.



Queen aliingia huku akiwa anatweta kwa hofu na uoga. Maana mahala hapo hapakuwa mbali sana na ile Hotel waliyofikia yeye na Hemed. Alikuwa akihisi maumivu hata pale alipokaa pia aligugumia. Muda wote Ata alikuwa akimuangalia kwa mshangao asielewe ni kipi hasa kilichompata mwanamke huyo.



“Mpenzi nini kimekukuta? Umepatwa na nini? Na kwanini saa hizi upo huku?” Ata alimuuliza baada ya Queen kupata utulivu. Queen alimueleza yote tangu alivyokuwa kule kwenye jumba lao na alivyopigiwa simu na Hemedy. Alimueleza yote lakini alimficha jambo la kufanya mapenzi na kijana huyo.



“Pole sana mpenzi” Ata alimpa pole. Kisha akaliwasha gari na kuelekea huko walipotaka waende. Safari ya kwenda kwenye jumba lao ikaanza.



Majira ya usiku mwingi na isijulikane ni saa ngapi. Alijikuta kwenye chumba chenye giza. Giza kuu asiloweza kuona chochote kile hata rangi ya nguo alizovaa. Alijaribu kufumbua macho. Giza ndio lilizidi kuongezeka.

Ebwana eee!.

Kaburini!. Kuzimu! Au labda ni Jahannamu!. Hapana. Sio Jahannamu. Mbona sisikii hata mvuke wa moto? Pengine labda ni peponi!. Eeeh si unaona hata huo upepo unaovuma na hiyo mivumo ya miti?

Pengine labda!.



Lakini patakuaje peponi? Mbona sasa sioni chochote zaidi giza tu? Au labda sikustahili kuingia kwa wakati huu? Alijiuliza maswali hayo. Akajiinua pale alipolala na kuanza kupapasa ardhini. Mama wee! Pepo gani hii ina sakafu? Tena sakafu ya marumaru? Au labda nipo kwenye kibaraza cha pepo?



Akatambaa pale alipo kama mtoto mdogo. Akipapasa huku na huku. “Mama wee nakufaaaa!.” Yowe kubwa lilimtoka baada ya kupigwa na kitu kama shoti ya umeme. Akajirusha na kwenda kujipigiza na mgongo sakafuni. Akatulia kimya. Sio kwamba alikufa au alizimia? La hashaa!. Alikuwa akisikilizia sauti mfano wa viatu vya mtu akija pahali hapo ambapo yeye yupo. Sauti zile za viatu zilikuwa zikija kwa kasi na hicho ndicho kilichomfanya kutulia kimya hata yale maumivu aliyoyapata muda mfupi asiyahisi tena.



Malaika!. Hapana kwani malaika nao wanavaa viatu? Sasa hiki ni kiumbe gani kinachokuja upande huu? Alijiuliza mawazoni huku akiendelea kuzisikilizia sauti zile za viatu. Sasa iliongezeka sauti nyengine. Sauti ya kufunguliwa kwa mlango. Akazidi kustajabu. Mstajabu wake ukaondoka ghafla baada ya kusikia akiitwa.



“Bosi... Bosi nini tena? Mbona hivyo?” Ebwana eee!. Bosi hadi peponi?. Alijiuliza. Lakini sauti hii mbona kama vile naijua?. Maswali yake ya kujiuliza mwenyewe yakakoma ghafla baada ya kuanza kuhisi akipapaswa. Akipapaswa kichwani. Mara kidogo nuru ikaja Ghafla.



Alaaaa!.



Kumbe alikuwa amefungwa kitambara machoni. Ili chekesha na hata yeye mwenyewe pia alijiona ni mpumbavu. Kumbe muda wote huo alikuwa yupo nyumbani kwake tena sebuleni akiwa amefungwa kitambara. Akafinya finya macho kuminyana na mwanagaza ule wa taa. Akatulia na kumuangalia mlinzi wake wa getini alivyogwaya kumuangalia yeye. Maumivu kwenye mkono wake yakarudi tena. Akauangalia mkono wake na kuangalia upande palipokuwa na Tv, Redio na Deki. Chini yake palikuwa na kebo ya umeme iliyoonekana kubenuka. Akajua kivyovyote maumivu yale yametokana na shoti ya umeme pale alipokuwa anapapasa sehemu ile.



“Bosi nini mbona hivyo? Umelala sakafuni. Umejifunga tambara kwenye macho. Unapiga kelele mwenyewe. Nini tatizo?” Mlinzi wa getini alikuwa akimuuliza Inspekta Ezekiel Kiulason aliekuwa amekaa bado chini.



“Nini kwani? Embu toka hapa nenda kaendelee na shuhuli zako. Usinisumbue mimi. Alaah!” Alibwata kwa hasira na hiyo ni baada ya kukumbuka kilichomkuta masaa kadhaa yaliyopita. Alikumbuka kwamba alitekwa na kupelekwa sehemu asiyoijua. Huko alipewa kazi na rafiki yake wa zamani. Kazi ambayo alipewa siku mbili tu za kuikamilisha vinginevyo familia yake hatoipata. Huenda na yeye pia akaunganishwa na familia yake huko ilipo baada ya kushindwa kufanikisha kazi hiyo.



Kazi ya kuwajulisha ghala la silaha la mji huo lilipo. Ilikuwa ni kazi kubwa sana kwake ila atafanya nini sasa ili kuikomboa familia yake? Kujikomboa na yeye kwenye zahma litakalomjia baada ya kushidwa kuifanya kazi hiyo? Hakuwa na lakufanya zaidi ya kufanya kile alichoamrishwa. Akafikiria kumuambia mkubwa wake wa kazi. Lakini akaona njia hiyo ni mbaya sana kwa usalama wake.

Akawaza kuifanya kazi hiyo kimya kimya!.



“Tokaa unaniangalia angalia nini?” alibwata kwa hasira na sauti kuu kumuambia mlinzi wake baada ya kuona akimshangaa tu hapo. Mlinzi alitoka kimya kimya hadi nje sehemu yake ya kazi. Akatulia kwenye kiti na kuwaza yaliyotokea punde tu.



“Bosi nini kipi kimemkuta? Au anaaza kuchanganyikiwa? Au ndio majukumu yake ya kazi yamemzidi? Sasa mbona alikuwa amejifunga kitambara machoni? Alikuwa akifanya mazoezi ya hisia nini?...” Akatoa cheko dogo kisha akatulia kimya. “Lakini mbona hata mimi sielewi nilikuwa kwenye mazingira gani?” Mmmh!. Akaguna.









Inspekta Kiulason alipobaki pekeake pale chini sebuleni. Aliangalia saa iliyoko ukutani na kukuta ni saa kumi na moja alfajiri. Akapiga kite cha ghadhabu. Akajiinua kiuvivu uvivu na kusimama. Kichwa kilikuwa kikimuuma. Hakujua ni kwaajili ya uchovu au ndio homa hiyo inamnyemelea. Pengine labda ni wasiwasi wa kuifanya hiyo kazi aliyokabidhiwa.



Akaingia chumbani kwake. Huko akajiandaa kwenda kazini asubuhi hiyo. Japokuwa aliwahi sana ila hakutaka kujali hilo. Alitumia nusu saa kujianda na muda huu alikuwa akitoka kwaajili ya kwenda kazini kwake. Alipofika getini akapita bila ya kumpa salamu mlinzi wake. Mara kidogo akarudi tena pale alipo mlinzi.



“Usiruhusu mtu yoyote kuingia humu ndani na...na..... Aaa ni hivyo tu” akageuka kuufuata mlango. Mara akageuza kurudi tena pale alipo mlinzi. “Hii nyumba ndani haina mtu yoyote. Jana wote walisafiri wameenda huko kusalimia. Kwahiyo uwe makini na huko ndani pia” Akaondoka akimuacha mlinzi mdomo wazi.



“Wamesafiri? Lini? Saa ngapi?... Si jana usiku walikuwepo wote humu ndani, sasa ni vipi aseme eti wamesafiri? Wamepitia wapi?” Alikuwa akijiuliza mwenyewe kwa mshangao. “Lakini mimi kuna muda nililala usingizi wa mashaka, huenda ikawa ndio wameondoka muda huo. Lakini ndio wasinijulishe?” Akabetua mabega yake juu huku sura yake akiikunja kimbea. Akajiegemeza kwenye kiti cha plastiki alichokalia akiusaka usingizi.

Akalala!.



* *



Inspekta Kiulason alifika kituoni mapema sana. Moja kwa moja hadi ofisini kwake. Hapo akakaa kwenye kiti chake cha kuzunguka na kutulia kimya akitafakari kazi iliyoko mbele yake. Ni kweli tabia yake ya zamani ya kuuza siri za jeshi aliiacha. Lakini hakuwa na budi kuirudia tabia hiyo ili kuokoa familia yake pengine na uhai wake pia.



“Shit! Ningekuwa saa hii nina cheo kikubwa kuliko hiki nilichokuwa nacho.. Kushushwa cheo kama si kufukuzwa kazi kulee nakuona kunanijia sasa. Aargh! Ee mungu ninusuru mimi” Aling'aka kwa ghadhabu huku akiiadhibu meza yake kwa kuigonga na upande wa ngumi pasi na kosa lolote iliyotenda. Mafaili na Kompyuta vilivyokuwa juu ya meza hiyo vilitikisika kwa uzito wa ngumi. Akatulia huku akivitolea macho vilivyoko juu ya meza hiyo utafikiri ndivyo ambavyo vinampa ghadhabu hiyo.



“Aargh! Sasa nitafanya nini ili kujua ilo ghala lilipo? Nimuulize mkuu.....? Hapana hiyo ni njia mbaya sana kwasababu lazima atahoji juu ya hilo. Sasa nifanye nini?..” Akajiinua pale kwenye kiti na kuliendea kabati lililokuwa na mafaili mengi yaliyo katika mpangilio mzuri. Akachagua chagua kutokana na namba zilizokuwa kwenye ubavu wa mafaili hayo. Kisha akaondoka na mafaili mawili na kwenda nayo mezani kwake. Akalifungua moja na kulisoma kidogo kidogo kwa takribani nusu saa. Kisha akahamia kwa kile jengine nalo pia alilisoma. Kisha akayarudisha sehemu yalipokuwa.



Akarudi tena mezani kwake na kukaa hapo. Viwiko vya mikono yake vikiwa vimekita kwenye meza huku viganja vyake vikiwa kwenye kidevu. Alitulia hapo kwa zaidi ya dakika tano kisha akainuka na kutoka nje ya ofisi yake.



“Koplo Zubeda. Mkuu ameshafika tayari?” alimuuliza askari wakike aliekuwa ni ‘Secketary’ wa IGP Taure.



“Hapana. Bado hajafika” Askari huyo alijibu huku akiendelea kuminyaminya Kompyuta iliyoko mbele yake. Insepekta akataka kusema kitu. Ila alighairisha. Akaondoka hapo hadi ofisini kwake. Huko alikaa tena kwenye kiti kwa dakika mbili. Alionekana akiwa na uso wa mashaka na msawajiko usio wa kawaida. Akainuka tena na kutoka moja kwa moja hadi kwa Koplo Zubeda.



“Aaaa! Sasa Koplo naomba ukanichukulie vitafunwa mara moja hapo nje halafu uniletee ofisini kwangu”. Koplo Zubeda aliinua uso wake kwa ghafla toka pale alipokuwa na kumuangalia Inspekta Kiulason kwa mshangao. Tangu lini ameanza kunituma huyu? Akawaza kimoyo moyo akijiuliza mwenyewe. Lakini kwavile alikuwa ni mkubwa wake wa kazi, hakuwa na budi kukubali. Akajiinua pale alipokaa akiwa bado na mshangao wake. Akapokea pesa aliyokuwa akipewa na Inspekta. Akauliza ni vitafunwa gani ambavyo alikuwa akitaka Inspekta. Akapokea jibu kuwa alete vyovyote vitakavyo patikana. Akatoka nayo akimuacha Inspekta akipiga hatua kwenye kordo inayompeleka kwenye ofisi yake.

Alizuga!.



Ilikuwa ni zuga kumtoa Koplo Zubeda nje ili yeye afanye kitu. Akarudi pale alipokaa Koplo Zubeda kwa haraka na kuanza kufungua droo yake. Hapo akatoka na funguo. Akatoka nazo mbio hadi kwenye mlango wa ofisi ya IGP Taure. Akajaribu kufungua huku mikono ikimtetemeka. Ni mara kadhaa alikuwa akikosea kuchomeka funguo kwenye tundu kutokana na kutetemeka mikono. “Aargh” akapiga kite cha hasira na kutuliza wenge kwanza. Ndipo alipofanikiwa kufungua. Ofisi ya IGP Taure ikawa wazi!.



Presha ilizidi kumpanda hadi akataka kughairisha kile alichotaka kufanya. Akapiga moyo konde na kuliendea kabati lililokuwa na mafaili mengi. Akaanza kuyachangua haraka haraka huku akipitishia macho juu juu ndani ya mafaili hayo.

Akapata analotaka!.



Akatoa simu yake kubwa haraka na kuanza kupiga picha kwenye kurasa za faili hilo. Kisha akalirudisha sehemu lilipokuwa huku akijitahidi kupanga vile vile alivyokuta ili asije akaleta mshtuko ama wasiwasi wowote kwa mkuu wake pindi atakapoingia na kukuta ndivyo sivyo.



Akatoka ndani humo na kuufunga mlango kama alivyokuta. Akarudisha funguo sehemu alipoikuta na kurudi ofisini kwake haraka huku akiwa bado anatetemeka. Akakaa kwenye kiti chake na kukilaliza kichwa chake juu ya meza. Alipokuja kuinua kichwa. Tabasamu lilionekana usoni mwake.

Tabasamu la ushindi!.

Ndio alikuwa na haki ya kutabasamu kama si kucheka kabisa au kufurahi kwa kazi aliyoiona ni kubwa lakini sasa inakwenda kukamilika muda mfupi.



Akatoa simu yake na kuingia upande wa picha. Akaangalia picha zile alizopiga kwenye lile faili. Akayasoma maandishi yale kwa kuya ‘zoom’ ili apate urahisi mzuri wa kuyaona. Akayosoma mwanzo mwisho huku tabasamu likiwa linazidi usoni mwake kila baada ya kusoma. Alikuwa na furaha ya ajabu kwa kupata kile alichokua anakitaka.



Alishtuka. Mshtuko ulimpata baada ya kusikia mlango wake ukigongwa. Hofu, Uoga, wasiwasi vyote vilikuwa nae sambamba kwa wakati huo. Akawasha data na kuingia upande wa ‘Whatsapp’ haraka na kuzituma picha zile kwa mtu anaemjua yeye. Kisha akafuta zile picha kila sehemu na kuitia simu yake mfukoni ndipo hapo alipotoa ruhusu kwa huyo anaegonga aingie ndani.



Alikuwa ni Koplo Zubeda na mkononi alibeba mfuko mweusi ulionekana kuvimba kidogo. Akamletea vitu vyake na yeye akaondoka. Inspekta alishusha pumzi ndefu kisha akauangalia ule mfuko kwa muda. Akanyanyuka pale na kutoka nje ya kituo. Huko aliingia kwenye gari lake na kuondoka akiuacha mfuko wenye vitafunwa ukiwa juu ya meza yake.



Safari yake iliishia nyumbani kwake. Huko aliingia ndani akiliacha gari lake nje ya uzio wa nyumba. Moja kwa moja hadi sebuleni na kuiendea meza. Juu ya meza hiyo kulikuwa na vitu baadhi ila aliachana navyo vyote na kuchukua simu iliyokuwa juu ya meza hiyo kati ya vitu baadhi. Simu hiyo ilikuwa ni ya mkewe. Akatoa ‘password’ na kuwasha data kisha akaingia upande wa ‘Whatsapp’. Alikutana na ‘Massage’ nyingi ila zote hakuwa na shuhuli nazo. Akatafuta zile ambazo amezituma yeye muda mfupi uliopita na kuzipata. Akahakikisha kama ndizo kisha akatabasamu na kuizima kabisa simu hiyo. Akaichukua na kuificha chini ya sofa. Akatoka huku nafsi yake ikiwa na amani tele.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Majira ya mchana yalimkuta Hemedy Bhachu akiwa nyumbani kwa afisa wa zamani wa jeshi la polisi. Mzee Ganjo. Walikuwa wakipata chakula kwa pamoja majira hayo huku wakizungumza hili na lile. Hiki na kile. Sana sana Ganjo alikuwa akimuuliza maswali Hemedy Bhachu kuhusiana kazi yake aliyokuwa akiifanya na ambayo imemfanya muda huu kuwa katika jiji hilo. Kazi ya usalama wa taifa.



“Mlikuwa wangapi huko mafunzoni?” Ganjo alimuuliza baada ya kupewa histori fupi ya huko walipoenda kuchukua mafunzo ya ujasusi.



“Tulikuwa wengi sana takribani watu Arobaini ama Thelathini hivi”



“Na wewe umeniambia ulishika nafasi ya tatu kati ya wote hao. Na je Hilda nae alishika nafasi ya ngapi?”



“Ishirini na nane alikuwa nafasi hiyo”



Waliendelea na maongezi hadi pale jua lilipozama na mwezi kuchukua nafasi yake. Majira ya saa tatu usiku Hemedy aliaga na kuondoka baada ya kuwa ameshakula chakula cha usiku hapo hapo. Siku hii Ganjo alimshinikiza sana TSSI 01 aende kwake ili wakazungumze mengi maana kijana huyo tangu alipofika katika mji huo hakuwa akipata muda mzuri wa kumpumzika kutokana na kazi iliyomleta. Na siku hiyo akaamua kuvunja ratiba zake zote na kuamua kwenda kwa Mzee huyo baada ya kung'ang'anizwa sana aende.



* * * *



Ikiwa ni siku ya pili baada ya iliyopita kupita. Siku ambayo Inspekta Kiulason alihitajika kupeleka mrejesho wa kazi aliyopatiwa na Mr Hanein siku mbili nyuma. Kazi ya kuhakikisha anawatafutia taarifa za ghala la silaha la mji huo. Mwanzo ilikuwa ni kazi ngumu sana kwake. Ila kwa sasa imekuwa ni rahisi kuliko vile alivyodhani yeye. Ndio ilikuwa ni rahisi kweli baada ya kupata taarifa za siri na muhimu kuhusu sehemu lilipo ghala hilo.



Na hivi sasa taarifa hizo muhimu alikuwa nazo zote baada ya kuzikopi kwa kupiga picha faili lenye taarifa hizo. Akawa anasubiri muda tu utakapofika awakabidhi kazi yao kwa waliyomtuma kisha hapo aikomboe familia yake iliyokuwa chini ya mikono ya Mr Hanein. Labda pengine angeweza kuvamia na kikundi cha askari mahala ambapo familia yake imetekwa ama imehifadhiwa. Lakini hilo halikuwezekana kutokana na kuwa sehemu hiyo hakupajua ni wapi katika mji huo. Labda huenda ikawa ni nje ya mji huo kwa mawazo yake.

Pengine labda!.



Maana yeye alivyopelekwa hakuwa akijitambua. Hakujua ‘A’ wala ‘B’. Alikuja kushtuka akiwa kwenye himaya ile ambayo hadi sasa alikuwa akijiuliza ni wapi mahala pale. Labda angesema angekadiria mwendo waliokuwa wakiutumia kutoka huko hadi hapo nyumbani kwake au kwake hadi huko. Lakini hilo pia halikuwezekana kutokana na alivyopelekwa na alivyorudishwa hakuwa na utimamu.



Majira haya ya jioni katika jumba la maficho ya Hanein lililoko Pongwe. Ndani ya jumba hilo kama kawaida hapakuishiwa na vikao. Na hata sasa palikuwna kikao. Kikao ambacho kilikuwa kikizungumzia juu ya mipango au mpango wa kuteka ghala ya silaha za jeshi la polisi na kujichukulia silaha wazitakazo kisha kwenda kuziuza kwa wanaozitaka. Waliahidiwa pesa nyingi sana na kwa namna moja ama nyengine hawakutaka kuzikosa pesa hizo.



“Nadhani leo ndio ile siku ambayo tulimtumikisha yule askari msaliti atuletee taarifa za wapi lilipo ghala la silaha. Sasa Zinah na Robart mtaenda kumchukua kama mlivyomchukua siku ile na kumleta hapa. Umakini unahitajika zaidi maana hatujui ana mipango gani juu yetu. Huenda ikawa ameweka mtego endapo atajitokeza yoyote basi wamkamate na kumfanya kama njia ya kutupata sisi wengine. Umakini una hitajika vijana wangu” Akatulia kimya kama sio yeye aliekuwa akiongea kabla. Alitulia kwa dakika isiyozidi moja. Kisha akawaangalia vijana wake wote na macho yake yakaganda kwa Zinah na Robart. Akaongea.



“Mtaenda saa hii. Tena saa hii ilikumuwahi mumfuatilie au mumchunguze kabla ya kumteka na kumleta hapa. Na sisi wengine tutakuwa tukiwasubiri. Na kama pakiwa na tatizo lolote basi msisite kutujulisha haraka kabla halijawa kubwa. Silaha mtachukua ndogo ndogo kwaajili ya kujihami na chochote. Mnaweza kwenda” alipoongea hivyo, akanyanyuka pale alipokaa. “Atu tuongozane sehemu” alimalizia na hivyo kisha akapiga hatua kuuendea mlango wa kutokea hapo na kutoka nje ya nyumba hiyo huku akifuatiwa na Atu. Huko aliingia kwenye gari moja wapo kati ya mengi yaliyokuwa kwenye banda maalumu la kuegeshea magari. Atu alikaa upande wa dereva na safari ya kutoka hapo kuelekea huko wanapopajua wao ikaanza.



Zinah na Robart kila mmoja aliingia chumbani kwake na walipokuja kutoka walikuwa tayari kuenda huko walipohitajika waende. Wakatoka na kupakia kwenye gari moja na kuondoka hapo.



Ndani humo kulibakia vijana watano. Ata, Pijo, Deva, Mrutu na Queen. Deva aliinuka kwenye sofa alilokaa na kuliendea friji lililopo hapo Sebuleni. Akachukua machungwa mawili na kuchukua na kisu kilichokuwa juu ya meza. Akatoka navyo nje na kwenda kwenye bustani iliyopo ndani ya uzio wa jumba hilo. Huko alikaa kwenye kiti na kuliweka chungwa moja chini huku lile jengine akilimenya taratibu.



Mbele yake akawapo Ata na asijue mtu huyo amefika hapo saa ngapi. Alipomuangalia mkononi alimuona akirusharusha chungwa huku akimuangalia kwa jicho flani la dharau. Akampuuza na kuendelea kumenya chungwa lake. Lakini alipoangalia pale chini alipoweka lile chungwa jengine. Hakuliona!. Akarudisha macho yake haraka hadi kwenye mkono wa Ata. Akaliona lile chungwa ambalo mwanzo alikuja nalo. Na hivi sasa likiwa mikononi mwa Ata. Akamuangalia usoni kwa macho ya mshangao. Hapo akakutana na tabasamu. Akampuuza tena na kuendelea kumenya chungwa lile lililokuwa mkononi mwake.



“We shoga naomba hicho kisu” Ata aliongea hivyo. Deva ghafla alivamiwa na hasira ambazo hakujua zimetoka wapi au zilikuwa wapi. Alimuangalia usoni kwa ghadhabu kuu lakini alikutana na tabasamu kama vile Ata alivyomuita ni sawa tu. Akampuuza kwa mara nyengine. Lakini kumpuuza huku kulikuwa na namna ya kuvuta subira akisubiria kusikia neno jengine la kuudhia kutoka kwa kijana huyo ili amjibu kwa vitendo.



“We mtoto mzuri hujaniskia ama? Mwanaume gani unasura ya kike kama si ushoga ni ni.......” Hakumalizia sentensi yake baada ya kisu kukita ghafla pembeni ya mguu wake. Sio kwamba kisu kile kimekitwa pembeni ya mguu wa Ata kwa makusudi. Bali Ata aliuondoa mguu wake haraka maana kisu kile kililenga kuutoboa kama si kuudhuru mguu wake kabisa.



Ata akaupiga mkono wa Deva uliokuwa umekishika kile kisu na kisu kile kikaruka mbali. Deva akapokea teke la kifua na kurushwa kwa kubenjuka kwenye kiti alichokaa kwenda nyuma huku kiti kikimfuata. Akakizuia kile kiti na kumrushia Ata ambae alikuwa anamjia mbio yeye. Ata akanyoosha teke kali kukipiga kile kiti. Kiti kikasaliti amri na kuvunjika mbele yao vipande vipande.



Wanaume wawili wakawa wamesimama kimapigano huku kila mmoja akimuangalia mwenzake kwa ghadhabu. Kisa kilichopelekea kuwa mahasimu kiasi hicho ni kidogo tu. Kisa ni Deva kutoka kimapenzi na dada wa Ata ambae ni Atu. Ata alikuwa akichukizwa sana kuwaona wawili hao wakiwa wapenzi. Hakutaka kumuona dada yake akitoka na mtu ambae wao kupitia baba yao ndie ambae alikuwa akimlipa. Yani ni kama mfanyakazi. Sasa iweje dada yake atoke na mfanyakazi wao?.

Dharau!.







ENDELEA..



Ata alimuendea Deva kwa kasi huku kasi hiyo ikiwa na mapigo mengi ya kuchanganya. Maana alijua Deva hata afanye nini hawezi kufua dafu kwake. Ni kweli Deva hakuwa na ujuvi mkubwa kumshida Ata kimapigano. Kutokana na yeye ngumi zake alijifunzia mtaani na mwisho wa mchezo akajakuchukuliwa na Mr Tanganyika. Huko ndipo alipoongezewa ujuvi wa kupigana baada ya Mkuu wao huyo kuwatafutia mwalimu ambae alikuwa na uweledi mzuri kwenye mapigano. Ila hata hivyo uwezo wake haukuweza kuwa mkubwa kama wa Ata ambae hata shule aliyokuwa akisoma ilikuwa ikiwafunza hayo tangu wakiwa na miaka saba.



Mapigo yale yalimpa wakati mgumu Deva kuyapangua japokuwa alifanikiwa hilo kwa asilimia chache. Ila kupangua huko hakukuzuia mapigo mengine yasimpate. Mapigo hayo yalimfanya aende chini huku akiambatana na maumivu. Ata alimfuata kwa kasi pale chini na kushusha guu lililolengwa kifuani. Deva aliliona na kujivingirisha pembeni. Guu ile likatua ardhini na kuchangua baadhi ya majani yaliyokuwa kwenye bustani hiyo. Ata akageuka ule upande ambao Deva alikuwa anajitahidi kujiinua kabla pigo jengine halijaletwa.



Ata akarusha dochi kali lililompata Deva kwenye mbavu. Lakini ndio lilimsaidia kuinuka japokuwa maumivu aliyapata. Akakaa sawa huku akikunja sura kwa maumivu. Ata akiwa na ghadhabu za waziwazi. Alimfuata Deva pale aliposimama kwa kasi. Ila kabla hajamfikia. Deva chini ya mguu wake kulikuwa na kipande cha mguu wa kile kiti kilichosambaratika baada ya kuvunjwa kwa teke kali la Ata. Deva aliuinua ule mguu wa kiti kwa mguu wake wa kulia kwa utaalamu mzuri. Mguu wa kiti ukaja juu na sasa ukawa mkononi mwake.



Ata kitendo kile cha Deva kuinua ule mguu wa kiti hakukitarajia. Badala yake alikuja kushtuta akiwa na maumivu kwenye paji lake la uso huku tumbo lake likiwa na maumivu kama hayo. Ni kitendo cha haraka sana Deva kuupigiza ule mguu wa kiti kwenye tumbo la Ata na papo hapo akaupigiza kwenye paji la uso wa Ata.

Alooh! Maumivu aliyoyasikia Ata hayakuwa madogo tena si haba. Alirudi nyuma huku akishika kwa mikono yake paji lake la uso akiwa mgogo kaupinda kwa mbele kudhihirisha maumivu aliyonayo.



Deva muda huo ule mguu wa kiti aliokuwa ameushika mkononi mwake ulikuwa ni kipande baada ya kuvunjika kwenye komo la Ata. Alikuwa akimuangalia Ata kwa ghadhabu pale alipoinama. Akatupa kile kipande kisha akamuendea Ata kwa nia ya kumpiga teke kali la ‘kata funua’. Ambalo hupigwa mtu chini ya kidevu na kupelekea kurushwa nyuma huku ukiachiwa maumivu makali. Sasa si bora yawe maumivu tu. Pengine linaweza likaondoka na meno ya barazani na kubaki kibogoyo.



Dhamira ile ya Deva haikufana baada ya Ata kurudi nyuma na teke lile likapita kwa kasi kwenda juu. Ebwana eee!. Kama ulivyokuwa mguu wake upo juu baada ya kukosa lengo. Hivi sasa alikuwa juu mwili mzima baada ya kuchotwa mtama maridadi na Ata aliegeuka mboga ghafla. Deva akiwa bado anaelea juu. Alipokea teke jengine la kiuno lililomtupa mbali na kutoa kishindo kikuu huku kikichagizwa na yowe la maumivu. Yowe ambalo lilifananiana na mlio wa mbwa aliepigwa jiwe.



Unadhani basi aliweza tena kuinuka pale alipoangukia? Hapana. Na atawezaje kuinuka wakati amepokea kipigo sehemu mbaya ya kiuno? Akabaki kugugumia pale chini huku akimuangalia Ata kwa hasira. Ata wala hakujali hasira alizokuwa nazo Deva. Kwanza atajali vipi hasira za hasimu wake wakati yeye mwenyewe alikuwa na hasira dhidi ya huyo hasimu.



Akamfuata kwa kasi na alipofika karibu yake. Akajirusha juu akiwa na dhamira ya kummaliza kabisa Deva. Pigo ambalo kama angefanikiwa kumshushia Deva pengine masaa mawili mbele wangekuwa wanachimba kaburi kuufukia mwili wa Deva. Ata akiwa juu akiwa na dhamira ya kumshushia Deva pigo la kifo. Pijo alitokea pasipojulikana na kwenda kumvamia Ata kule kule juu na kumkumba kama kimbunga na wakajikuta wote wakienda chini huku Pijo amemkumbatia Ata.



Ata akataka kujitoa kwenye kumbato hilo. Ila nguvu iliongezwa na Mrutu ambae alikuja pia kutoa msaada kwa Pijo ili kumdhibiti Ata. Ata alibweka kwa hasira akitaka aachiwe ili amuonyeshe kazi Deva. Muda huo Deva alikuwa akikokotwa na Queen kuingizwa ndani ya nyumba. Nusu saa mbele ndipo Ata akatulia. Akaondoka kwa hasira na kuingia ndani moja kwa moja hadi chumbani kwake. Aliubamiza mlango baada ya kuwa ameshaingia huku akimalizia na tusi la nguoni na isijulikane amemtukana nani.

Pengine limeelekezwa kwa Deva.



Kituo kikubwa cha polisi Chumbageni. Mbali kidogo na kituo hicho. Zinah na Robart walikuwa wapo ndani ya gari lao wakitega Inspekta atoke wamuungie mkia. Walijihiridhishia kuwa bado yuwamo humo ndani kituoni kutokana na gari lake binafsi lipo nje ya kituo limepaki. Haikuchukua muda sana wakamuona Inspekta akitoka huku akiwa ameongozana na askari mwengine. Walipofika kwenye gari la Inspekta. Inspekta aliegemea gari lake huku yule askari mwengine akiwa amesimama wima kumuangalia Inspekta. Walikuwa wakiongea. Ila kilichoongelewa hakikuskiwa na kina Zinah kutokana na wao kuwa mbali na watu hao.



Baada ya dakika tatu. Walipeana mikono na Inspekta akaingia kwenye gari lake huku yule askari mwengine akirudi ndani. Inspekta aliondoa gari lake mdogo mdogo kituoni hapo akishika uelekeo wa Hostel za Usagara. Nyuma yake kulikuwa kuna gari jengine likimuungia mkia bila yeye kujua. Gari zile zilipofika Hostel. Zikakata kulia. Mbele kidogo kwenye makutano ya barabara zikasimama baada ya ‘trafic light’ kusimamisha gari za upande wao.



Rabart akaona hapo hapo ndipo pakumchukua mtu wao. Akashuka kwenye gari haraka na kuliendea gari la Inspekta Kiulason lililokuwa mbele yao. Akafungua mlango wa upande wa kushoto na kuzama ndani. Inspekta akashtuka. Lakini mshtuko wake ulipotezwa na bastola iliyo mbavuni mwake.



“Broo tulia hivyo hivyo ulivyo. Chakufanya ni kufuata maelekezo yangu na si vinginevyo” Inspekta akashusha pumzi ndefu na kutulia kimya. Taa ya kuwaruhusu upande wao ikawaka na magari yakaanza kuondoka moja moja.



“Kunja kushoto” Robart alimuambia na yeye akakunja na barabara ya Mkwakwani. Wakaupita uwanja huo wa mpira hadi walipokuja kuzipata osifi za magari ya abiria waendao mikoani za Ratco. Akaamriwa asimame nje ya osifi hizo na yeye akafanya hivyo.



“Nadhani kazi yetu imekamilika” Robart aliongea hivyo huku akimuangalia usoni. Inspekta akaitikia kwa kichwa kukubali.



“Unavyo hapa au hadi uzifuate sehemu?”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Zipo nyumbani” Inspekta aliongea hivyo na safari ya kuelekea nyumbani kwake ikaanza tena akiwa chini ya ulinzi na Robart.



Walipofika nyumbani kwa Inspekta. Robart aliingia na Inspekta ndani ya nyumba hiyo kwa amani na utulivu ili asije akazua hofu kwa majirani au mlinzi wa nyumba hiyo. Walipita getini na kumsalimia mlinzi na moja kwa moja wakaingia wote ndani. Baada ya dakika tatu wakarudi tena garini.



“Sasa Afande inabidi nikufunge macho ili tuweze kuenda huko” Robart aliongea na wala hakutaka kusubiri jibu. Akatoa kitambara cheusi na kumfunga machoni. Kisha akatoa na kamba ngumu ambazo alimfunga mikononi kwa kuiweka nyuma ya mgongo. Safari ikaanza ya kuelekea huko wanapotakiwa waende.



Dakika kadhaa mbele. Inspekta alikuwa mbele ya Mr Hanein katika chumba kile kile alichokuwemo siku ya kwanza kuletwa pale. Hakuwa na kitambara usoni kama alivyoingia. Hivi sasa walikuwa wakiangaliana uso kwa uso.



“Natumai kazi niliyokupa umeifanya.....” Mr Hanein aliongea kisha aka kaa kimya. “Embu naomba unidhihirishie kama ulivyo niahidi siku mbili zilizopita bwana mdogo” akamalizia.



Inspekta ni dhahiri hakupenda kushurutishwa. Lakini sasa atafanyaje ilhali yupo mikononi mwa mtu? Akatuliza munkari wake. Kimya kikachukua nafasi wakati huo Inspekta Kiulason akivuta begi dogo lililoko mgongoni mwake. Akaliweka juu ya mapaja yake na kuanza kulifungua pasi na kuliangalia. Macho yake yalikuwa yanatazamani na macho ya Mr Hanein. Halikuwa ni jambo alilolipenda kama ilivyokuwa miaka mingi iliyopita.



Akatoa jarida flani mfano wa faili na kumtupia Mr Hanein aliewahi kulidaka huku tabasamu usoni likijiunda. Akalifungua faili lile lenye kurasa mbili tu. Moja ikiwa na maandishi huku nyengine ikiwa na ramani. Mr Hanein aliyasoma yale maandishi kwa dakika tatu ama nne kisha akaamia kwenye ule ukurasa wenye ramani. Akaiangalia ile ramani baada ya hapo akalifunga lile faili na kumuangalia usoni Kiulason akiwa na tabasamu pana zaidi.



“Nikushukuru kwa kukamilisha kazi niliyokupa...” akarudisha macho yake kwenye lile faili na kuliangalia mbele kisha akaligeuza nyuma. Akainuka taratibu na kuuendea mlango wa chumba hiko. Akagonga mara mbili na kurudi pale alipokaa.



Mlango ukafunguliwa na Atu akaingia humo ndani mkononi mwake akiwa na bahasha kubwa ya khaki. Akampatia Mr Hanein kisha akarudi nyuma yake na kusimama mikono akiwa ameifungamanisha kwa mbele. Mr Hanein hakujishuhulisha kuiangalia bahasha ile ina nini ndani. Pengine huenda ikawa alishajua kabla kilichomo ndani ya bahasha ile. Kama alivyotupiwa lile faili. Na yeye akamrushia ile bahasha Kiulason. Akaidaka na kuitazama ndani. Kulikuwa na maburungutu kadhaa ya pesa yaliyopangwa vizuri ndani yake. Inspekta Kiulason alitabasamu na kuifunga vizuri ile bahasha. Kisha nae akairusha alipo Mr Hanein.



“Naitaka familia yangu na si vinginevyo” aliongea maneno hayo na kurudisha mgongo wake nyuma kuegemea kiti alichokaa. Atu alitaka kuiokota ile bahasha, ila alizuiwa na Mr Hanein. Kisha hapo Mr aliiokota mwenyewe na kumpa Atu.



“Si kama familia yako usingeipata. Ila kwa vile umetaka kufanya kazi bila malipo pia sio mbaya. Familia yako utaipata na uhuru wako na wao pia utapatikana....” Akamgeukia Atu na kumuambia. “Fanya kinachopaswa”



Atu alimpa ishara kwa kichwa Inspekta kuwa amfuate. Inspekta akamuangalia usoni Mr Hanein na kumuona mtu huyo akimtingishia kichwa ishara ya kuwa afanye kile alichoambiwa. Inspekta Kiulason aliinuka pasi na kusema lolote akimfuata Atu aliekuwa ameshatoka nje ya chumba hiko. Aliongozwa hadi nje ya nyumba hiyo na kutakiwa aingie ndani ya gari. Akafungua mlango na kuikuta familia yake yote ikiwa imelala ndani humo.



Kiroho kikamruka kwa hofu. Inamaana wamewaua watu wangu? Alijiuluza mwenyewe. Akataka kuhoji kwa hasira ila alikutana na ishara ya kutulia kimya aliyopewa na Ata.



“Hatuwezi tukapindisha ahadi bwana mkubwa tuliowekeana hata mara moja. Familia yako iko hai ila kwa sasa ipo ulimwengu wa watu wasio na fahamu. Na inakubidi na wewe uwapo huko ili tuwasafirishe kwa amani hadi kwenye makazi yenu” Baada ya kusililiza maelezo hayo. Kidogo moyo wake ukapata unafuu. Ila akataka kupinga na yeye kusafirishwa huko kwenye ulimwengu wa wasio na fahamu. Ila hakuweza hata kunyanyua mdomo wake. Majira haya alikuwa akikokotwa kuingizwa garini baada ya kuwa amezimishwa na Atu. Safari ikaanza kurudishwa familia hiyo iishipo.



Majira haya Hemedy Bhachu alikuwa yuwamo ndani ya gari lake jipya lenye muonekano wa tofauti na magari mengine. Gari lile lilimpendeza yoyote aliefanikiwa kuliona. Alikuwa yupo maeneo ya Kaskaravilla akiwa ndani ya gari yake akisililiza muziki ya wa Hip Hop kutoka kwa msanii maarufu nchini anaejulikana kama Young Killer nyimbo ikiitwa Popote Kambi. Alikuwa akiufuatisha wimbo huo kwa sauti ya chini. Akaipita Hospital ama Chuo cha Besha. Akanyooka na barabara hiyo ya lami hadi pale alipokuja kuipata Baa moja iitwayo Ubaiya. Akakunja kulia na kuingia kwenye njia ya vumbi. Mbele kidogo akapaki gari nje ya nyumba moja kati ya nyingi zilizopo kwenye mtaa huo.



Akashuka kwenye gari baada ya kuwa amekwishalizima. Akaanza kupiga hatua kuiendea nyumba hiyo. Jirani na nyumba hiyo kulikuwa na wanawake wanne wamekaa. Wawili walikuwa wakisukana, mmoja alikuwa akifumua nywele zake huku yule mwengine akiwa bize na simu yake tamba. Akawasalimia, wawili kati yao wakaitikia salamu ile. Akiwa ni yule aliekuwa bize na simu na yule aliekuwa akisukwa. Wale wawili wengine walibetua midomo na isijulikane nini kimesababisha kuwa hivyo.



Hemedy hakujali chochote. Aliingia ndani ya nyumba hiyo. “Hee heeeee! Halloooo na tutakoma mwaka huu” Vicheko vya kishangingi na kimbea vilisikika kutoka kwa wanawake wale kule nje.

Uswahilini bwana!. Sasa ni kipi kimefanya watoe vicheko hivyo? Haikujulikana. Pengine labda ni Hulka yao tu.



Ndani ya nyumba hiyo alimkuta mwanamke wa makamo kidogo akiwa amekaa juu ya mswala alioutandika nje ya baraza yake. Pembeni yake pakionekana mboga aina ya mchicha na kwenye sahani iliyokuwa karibu na mwanamke yule pakiwa na mboga zile zikiwa zimekatwakatwa. Mwanamke yule alipomuona Hemedy Bhachu aliinuka pale alipokaa huku tabasamu likiwa usoni mwake.



“Karibu kaka. Karibu ukae, ngoja nikuletee kiti” Aliongea mwanamke yule huku akipiga hatua kukiendea kiti cha plastiki kilichokuwa kimekaa pweke chini ya mti.



“Usijali dada nitakaa tu hapa hapa ulipokuwa umekaa wewe nikusaidie kutengeneza mboga” Hemedy aliongea hivyo kisha akavua viatu vyake na kukaa kwenye mswala ule. Mwanamke yule alighairisha kukifuata kile kiti na kurudi pale alipo Hemedy na yeye akakaa.







“Za saa hizi Shemeji, maana nimeingia tu bila ya kukusalimia” TSSI 01 alisema.



“Salama tu. Tupo hapa tunaanda andaa mboga tupate chakula cha mchana” Mwanamke yule aliongea.



“Sawa....” akatulia. “Sasa shemu nadhani jana hatukupata maelewano mazuri ila leo bilashaka yatakuwepo”



“Usijali shemu tuongee tu”



“Sawa. Nadhani ungenieleza kabla ya kifo cha mume wako. Nini kilitukia huku nyuma, maana inavyojulikana kuwa mume wako alifia ndani ya nyumba ya marehemu mama Mpito” TSSI 01 dhumuni la kuja kwenye nyumba hii ni kuja kupata chochote kutoka kwa mke wa Inspekta yule wa mwanzo kabisa aliekabidhiwa kesi hii ambayo hadi sasa inasumbua vichwa vya wakubwa. Inspekta yule ambae alifia kwenye nyumba ya Mama hakimu siku kadhaa nyuma kabla ya kuletwa TSSI 01 kuja kuifuatilia. Mwanamke yule alifuta machozi yaliokuwa yamekwishaanza kutoka kwenye macho yake na kusema.



“Mume wangu siku ambayo tunaletewa taarifa kwamba amekufa nyumbani kwa yule marehemu hakimu. Jioni yake alikuja hapa nyumbani alionekana kama mtu aliechanganywa na jambo fulani. Mimi kama mke wake nikajaribu kumfuata na kumuuliza kulikoni lakini akanijibu kuwa nimuache kwanza kwa muda ule, mi nikaondoka nikatoka nje nikimuacha mwenyewe chumbani. Sasa majira ya usiku sikumbuki ilikuwa ni saa ngapi. Akatoka tena na kuondoka bila kuniambia chochote. Nikiwa nina wasiwasi kuwa mume wangu ameenda wapi, najakuletewa taarifa kuwa amekutwa amekufa pamoja na yule mlinzi kwenye nyumba ya yule mama hakimu. Mume wangu amekufaa bila ya kula chakula cha usiku. Chakula nilichokipika mwenyewe kwaajili yake maana mchana hakuwa amekula piaa” Mwanamke yule akajikuta akidondosha machozi ya uchungu baada ya kukumbuka kifo cha mume wake. Hemedy akajitahidi kumtuliza. Hakutumia nguvu sana akawa amenyamaza.



“Pole sana Shemeji. Hivi walikuja watu wangapi kukuhoji chochote hadi muda huu?”



“Ni askari wa wiwili tu akiwemo yule afande Salum na wewe ukiwa ni wa tatu basi. Zaidi ya hapo hakuna tena mwengine. Halafu mkija kama hivyo hao wanawake hapo nje wanadhani labda kama natumia nafasi ya kutokuwepo kwa mume wangu kufanya mambo ya kishenzi na ndio maana hata ulipokuja wewe nimesikia wakicheka. Kiukweli mimi mume wangu nampenda japokuwa hayupo tena, kwahiyo siwezi kufanya ushenzi kisa yeye hayupo” Akamaliza kutoa maelezo na kujifuta machozi na upande wa khanga yake. Kisha akamuangalia Hemedy usoni na kumuuliza.



“Kwani mmeshawajua waliosababisha kifo cha mume wangu?” Akauliza huku akiwa mkavu usoni. TSSI 01 Akababaika kidogo kujibu hilo swali.



“Aaaa bado ila sasa tumeshaanza kupata mwanga. Usijali, acha niende ila nitarudi tena siku yoyote kuja kukutembelea” Hemedy akainuka na kumfanya yule mwanamke nae pia ainuke.



“Sawa. Acha nikutoe kidogo” Akamsindikiza hadi karibu na getini. Hemedy akaondoka na yule mwanamke akarudi pale kibarazani kuendelea na shuhuli yake.



Hemedy akatoka nje na kuingia kwenye gari akiwaacha wanawake wale wakicheka tena vicheko vya umbea. Hakujali baada ya kuhisi huenda hawakuwa na shuhuli za kufanya na ndio maana wamekaa vibarazani kazi kuwasongondoa watu wapitao na njia hiyo. Akawasha gari na kundoka hapo. Akiwa kwenye gari simu yake iliita. Akaangalia nani anaepiga na kukuta ni Inspekta Salum ndie ambae alikuwa akimpigia. Akaipokea na kuiweka sikioni.



“Nipo huku Mikanjuni naelekea nyumbani” “Poa tukutane hapo” simu ikakatwa na safari ikaendelea.



* *



“Nadhani kazi inaenda kuanza baada ya kupata ramani nzima ya lilipo ghala” Mr Hanein aliongea kisha akaiangalia ile ramani kwa mara nyengine. Akagutushwa na swali lilitoka kwa Mr Pijo.



“Mkuu tuna uhakika gani kwamba hiyo ramani ndio yenyewe. Je kama tumeuzwa?” Pijo aliongea kitu kilichowafungua ubongo watu wote waliokuwa hapo. Kila mmoja akayapa uzito maneno ya Pijo na kuona kwamba wao mwanzo walikuwa wakishadadia tu bila kufikiria jambo hilo. Wakakuna vichwa vyao huku wakijaribu kulifikiria vizuri jambo hilo.



“Ni kweli uyasemayo Pijo, lakini sasa....” Nikama vile alikosa cha kuongea Mr Hanein akajikuta akikaa kimya kwa muda akiyaacha maneno yake yakielea. Akapata cha kuongea na kusema. “Inabidi kwanza uchunguzi ufanyike kabla ya kuenda huko kufanya uvamizi” akatulia kimya huku akiiangalia tena ile ramani.



“Ufanywe uchunguzi upi Baba?” Ata aliuliza. Mr Hanein aliinua kichwa na kumtazama yeye.



“Inabidi waenda vijana wawili hadi hiyo sehemu inayodaiwa kuwa lipo ilo ghala kufanya uchunguzi. Kisha hapo wakishagundua uwepo wa ilo ghala kweli, basi mtaenda sasa kufanya kazi iliyokusudiwa” Wakaliunga mkono wazo hilo. Sasa kilichobakia ni kuwa nani na nani wataenda kufanya uchunguzi huo. Mr Hanein akamchagua Ata awe wa kwanza huku akimpa nafasi achague mwenzake atakaeongozana nae. Ata aliwaangalia wenzake mmoja mmoja na macho yake yakatua kwa Deva.



“Nitaenda na Deva” Ebwana eee! Deva alishtuka si masihara. Na si yeye tu alieshtuka, na wengine wote waliokuwako siku hiyo wakati mpambano kati ya Deva na Ata ukiendelea pia walishtuka. Wakajua kwamba huko pataenda kufanyika jambo zaidi ya uchunguzi uliokusudiwa. Mr Pijo akaomba badala ya kwenda Deva basi aende yeye.



“Hata mimi nilidhamiria uwende wewe. Ila pia sio mbaya. Deva utabaki hapa na Pijo utaongozana na Ata....” Akaangalia saa na kukuta ni saa kumi na nusu jioni. “Kama itawezekana mkienda saa hizi itakuwa vizuri zaidi ili kesho tufanye kazi iliyokusudiwa. Mr Tanganyika anasubiria neno langu tu ili tufanye biashara” Akahitimisha. Bila kuchelewa. Ata na Mr Pijo waliinuka kwenda kujiandaa baada ya hapo wakaianza safari ya kwenda huko kulipodaiwa kuna ghala la silaha za jeshi la polisi.



Ndani ya Baa ya G Motel iliyoko mtaa wa Magaoni. Katika meza moja kulikuwa na vijana wawili wamekaa kwenye viti kuizunguka meza hiyo. Alikuwa ni TSSI 01 Hemedy Bhachu na Insepekta Salum Mzanzibar. Juu ya meza hiyo kulikuwa na vinywaji vya aina mbili. Kulikuwa na chupa ya mvinyo aina ya Castal Lite na chupa ya maji safi ya kilimanjaro.



“Kwahiyo huwezi kabisa kunywa pombe?” Salum alimuuliza Hemedy huku akimimina kinywaji hicho kwenye glasi.



“Sijawahi kunywa na nadhani nikisema ninywe wala hatutosikilizana hapa”



“Ok. Ulienda kwa yule mwanamke leo?” Salum alimuuliza.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Yeah! Nimefika ila ameonyesha kwamba hafahamu chochote kuhusiana na kifo cha mume wake. Sasa kazi nauona ugumu wake na uwepesi wake” Hemedy aliongea.



“Kivipi? Ugumu uko wapi na wepesi uko wapi?” Inspekta alimuuliza kisha akagida ile glasi yenye kilevi.



“Ugumu unakuja kwamba hatujui wahusika wa vifo vile wako wapi na wepesi wake ni kuwa tumeshawajua baadhi”



“Tuachane na hilo...” Akanywa tena kinywaji kile na kukisikilizia kikishuka taratibu hadi tumboni mwake. Akaendelea. “ Leo Inspekta Kiulason alinifuata na kuniambia maneno tatanishi sana hadi sasa naumiza kichwa sijui pia ni nini amemaanisha. Labda nikikuelezea na wewe huenda ikawa ukang'amua lolote kwenye maneno hayo..” Akatulia tena na kuvuta pumzi. Kisha akasema “ Ameniambia kwamba kuna uvamizi utakao tokea kwenye ghala la silaha na hajui ni lini, ila ameniambia kwamba kati ya siku hizi mbili jambo hilo linaweza likafanyika. Nikamuuliza kajuaje na watu hao ni wakina nani. Akajifanya kupotezea ile mada. Akaniambia kwamba alikuwa akizungumza lakini hajui ni nini alichozungumza. Mwisho wakati tuaagana akaniachia maeneno ambayo mimi nayaita ni tata na ndio yanayonifanya hata sasa nichanganyikiwe. Ameniambia. Lisemwalo lipo, na kama halipo basi litakuja” Akahitimisha maelezo yake na kumuachia nafasi sasa Hemedy ayafikirie na yeye maelezo hayo.



“Sasa... Kwani wewe umemuelewa vipi huyo Inspekta?” Ikabidi aulize baada ya kuhisi huenda ikawa hajaelewa vizuri au kama ameelewa basi anahitaji mawazo ya Salum ili na yeye achangie yake.



“Wakati akinipa maelezo hayo mwanzo. Alikuwa yupo ‘serious’ nikama mtu aliekuwa amechanganywa sana na jambo hilo hadi akaamua kulitoa kwangu na ndio maana nilipomuuliza kwamba amejuaje na hao watu ni akina nani. Ndipo alipokurupuka na kunijibu kuwa alikuwa akiongea lakini hakujua aliongea nini halafu akanizuga na tabasamu. Huoni kwamba hilo nila kweli na analijua vizuri tu ila sema alilificha na kwangu alilitoa tu kwa bahati mbaya baada ya kuchanganywa sana au kuwaza sana bila kupata ufumbuzi” Aliongea Inspekta muda huu akiwa amekisahau kabisa kinywaji chake baada ya kutingwa na maongezi hayo.



“Mi nadhani tungeanza kufanya kwanza uchunguzi kabla hatujalipa uzito sana hili jambo”



“Tunaanzia wapi huo uchunguzi? Kwa Inspekta Kiulason au wapi?”



“Yeah inabidi tuanzie kwake kwasababu yeye si ndo kalileta hili jambo”



“Basi inatubidi tumfuate saa hii nyumbani kwake” Wakakubaliana hivyo na kuondoka hapo. TSSI 01 alijitoa kulifuatilia hilo jambo bila kujua kwamba kuna uwiano kati ya jambo hilo na lile analolifuatilia yeye.



Majira haya walikuwa ndani ya nyumba ya Inspekta Kiulason. Walikaribishwa vizuri na mke wa Kiulason. Waliletewa vinywaji japokuwa mwanzo walivikataa. Wakazungumza mawiwili matatu kabla ya kuingia kwenye jambo lililowaleta.



“Hivi huyu bwana mkubwa tumemkuta?” Salum aliuliza.



“Mmmh! Yani tangu alipoondoka hapa asubuhi hadi sasa hajarudi tena. Na bahati mbaya pia simu yake haipatikana sasa” Mke wa Inspekta aliongea huku akionekana dhahiri akiwa na hofu.



“Mi nilimuacha kituoni. Embu acheni kwanza niwaulize huko” Akatoa simu yake na kupiga namba ya askari mmoja wanaofanya wote kazi kituo kile. Na jibu alilopewa baada ya kuuliza ni kuwa, mtu huyo aliondoka kituoni tangu majira ya mchana. Akakata simu na kuwapa taarifa hiyo.



“Sasa itakuwa ameenda wapi?” Mke wa Inspekta aliuliza. Kila mmoja akawa kimya kwasababu hakuna aliekuwa akijua. Vijana hao wakaaga na kuondoka huku wakimuahidi mke Kiulason kwamba watajitahidi kumtafuta kadri ya uwezo wao.



“Sasa tunafanyaje?” Hemedy alimuuliza Salum walipokuwa ndani ya gari.



“Ngoja kwanza nifanye uchunguzi wa jambo fulani kisha nitakujulisha ifikapo kesho nini tunafanya” Wakakubaliana hivyo na Hemedy Bhachu akampeleka Inspekta nyumbani kwake na yeye akarudi nyumbani kwake.



* *



Majira ya saa kumi na moja jioni. Yaliwakuta Ata na Pijo katika kituo kikubwa kilichopo Muheza. Ramani yao iliwaonyesha kwamba hapo ndipo kwenye hilo ghala la silaha. Hawakushangaa sana kukuta ghala la silaha kuwa katika kituo cha polisi. Walikuwa mbali sana na kituo hicho. Hapo walijadili ni jinsi gani ya kujua kama ni kweli ni hapo ama sipo. Wakapanga kufanya mchezo. Mchezo ambao utawawezesha kunga'amua jambo wanalolihitaji.



Pijo akashuka kwenye gari akiwa na begi kubwa kiasi kama yale wanayoyatumia wanafunzi. Akapotelea kichakani na kama dakika tano. Akarudi akiwa tofauti sana. Alionekana kama mzee aliechanganyikiwa au mwendawazimu fulani ambae umri umemtupa mkono. Mgongoni akiwa na safleti kubwa lililojaa vitu na isijulikane limejaa kitu gani. Mkononi akiwa ameshika mua ulioanza kuharibika akiula taratibu huku yale maji maji ya ule mua yakimdondokea kwenye nguo zake chafu. Kamasi lilikuwa likimtoka tundu ya pua yake moja na wala asifanye jitihada zozote za kuliondoa.



Akapiga hatua za hovyo hovyo kuelekea na kule kilipo kile kituo. Wakati akiwa anatembea. Alikuwa akiongea mwenyewe huku mara kadhaa akicheka. Alipofika karibu kidogo na kituo kile. Akaweka lile fuka lake chini na kutoa chungwa lililooneka kuanza kuoza. Akalitoa maganda na kucha zake huku mara kadhaa sana akipiga jicho ndani ya kituo hicho. Aliona askari wakizurura ndani humo wengine wakiwa wamekaa. Walionekana hawakuwa na shuhuli nae hata kidogo.



Akainuka na kubeba fuko lake huku akilifyonza lile chungwa na kuendelea na safari yake. Akapita mbele ya kituo na muda huu alikuwa nyuma ya kituo. Hapo akauacha uchizi wake na kungalia huku na huko ndani ya kituo hicho. Palionekana kupoa sana. Akatoa koleo la kukatia nyaya na kuziendea seng'enge. Akazikata uwazi ambao anaweza kupita yeye. Akaingia yeye na fuko lake. Akarudishia vizuri ule uzio wa seng'enge na kuangaza macho yake huku na huko muda huu akiwa ndani ya kituo.







ENDELEA.



Macho yake yakatua kwenye jengo moja kubwa lililokuwa nyuma ya kituo hicho. Lakini ni ndani ya uzio. Akapiga hatua zake zile zile za hovyo huku akiendelea kulifyonza lile chungwa lake. Akawa analikaribia kabisa lile jengo.



“Hey! Embu simama hapo” Ilisikika sauti ikiongea hivyo. Akaipuuza ili kudhihirisha uendawazimu wake kwa yoyote amuonae. Sauti ile ikajirudia tana na sasa ikimkaripia kwa nguvu zaidi ya ile ya mwanzo. Pijo akasimama na kisha kugeuka tatatibu huku tabasamu lililoelekea kucheka likiwa usoni mwake. Yule askari akamfikia hadi pale aliposimama.



“We vipi?” Akauliza kwa mshangao askari yule huku akimuangalia kwa tuo Pijo. Pijo hakujibu kitu badala yake akashusha lile fuko lake chini na kulifungua. Ebwana ee! Lilitoa harufu kali mithili ya mzoga wa mnyama iliyomfanya yule askari kuziba pua zake. Ndani ya fuko lile alitoa muwa ulioanza kuharibika na kuanza kuula mdogo mdogo. Majira haya alikuwa akicheka huku akimuangalia askari yule alivyo gwaya.



Yule askari akataka kuongea kitu ila akanyamaza baada ya kuona kitendo kichafu kilichofanywa na yule mwendawazimu. Pijo lile kamasi lililokuwa likining'inia kwenye tundu yake ya pua. Alilipangusa na viganja vyake kisha viganja vile akavilamba.



“Toka, toka mkicha wewe. Unaleta uwendawazimu mbele ya askari. Embu toka kabla sijakushushia kipigo saa hii” Askari yule alifoka huku akiangalia huku na huko kutafuta hata fimbo ya kumfukizia mwendawazimu yule. Hakuiona. Ikabidi amfukuze tu kwa kuendelea kumfokea. Pijo alikuwa akimcheka tu kisha akaanza kupiga hatua ndogo ndogo kuondoka hapo mara kadhaa aligeuka nyuma na kumuangalia yule askari huku akicheka. Akapita mbele ya kituo na kuwaacha askari midomo wazi. Huyu si mwendawazimu? Amepitia wapi? Maswali kama hayo walikuwa wakijiuliza. Wakabaki na mshangao wao huku Pijo akiendelea kupiga hatua akikiacha kituo hicho mbali.



Alipofika mbali na kituo hicho. Akaingia tena kichakani na baada ya dakika kadhaa akarudi kama alivyokuja. Akaingia garini. Huko alimfanya Ata kufungua vioo vya gari huku akiziba pua zake.



“Nini tena kaka mbona unanuka namna hiyo?” Atu alimuuliza kwa sauti ya kupana pua baada ya kuwa pua zake amezibana ili kujikinga na harufu aliyoingia nayo Pijo.



“Embu acha uboya wako, twenzetu” Pijo aliongea.



“Hapana kaka. Embu njoo uendeshe wewe acha mimi nikae nyuma huku” akashuka na kuhamia siti za nyuma. Pijo akahamia upande wa dereva huku akicheka. Na safari ya kuondoka hapo ikaanza. Njiani alimueleza wasiwasi wake kuwa lile jengo lililokuwa nyuma ya kituo kile huenda ikawa ndio hilo ghala wanalolitafuta. Wakapanga wakajadiliane vizuri wafikapo maskani kwao.



“Mnasema nyuma ya kituo kuna jengo ambalo mmelitiliashaka huenda ikawa ndio hilo ghala?” Mr Hanein aliwauliza badala ya kuwa wameshafika na kuwatolea maelezo ya kile walichodai ni kufanya uchunguzi.



“Yeah! Ni kama hivyo ila hatuna uhakika sana” Mr Pijo aliongea. Majira haya alikuwa tayari ameshabadili zile nguo zilizokuwa zikinuka. Sio nguo tu. Hata mwili ameshaufanyia usafi pia.



“Mnaonaje. Nimpe taarifa Mr Tanganyika kuwa mpango unaenda kukamilika na awaandae hao wanaotaka huo mzigo au tusubiri kwanza hadi tutakapo kamilisha mpango?” Mr Hanein aliwauliza.



“Mi nahisi ungempa taarifa kabisa ili hata kama kuna jengine la kuongezea basi afanye mapema kabla hatujakamilisha kazi” Pijo alitoa rai. Rai hiyo ikaungwa mkono na watu wote. Mr Hanein akachukua simu na kumpigia Mr Tanganyika. Baada ya simu ilipokwisha kupokelewa. Wakasalimiana na Mr Hanein akaenda kwenye lengo lililomfanya kupiga simu hiyo.



“Sawa kama uhakika upo. Sasa cha kufanya baada ya kukatika kwa hii simu. Ni kuwajulisha hao wanunuzi wa huo mzigo ili wajiandae na nadhani hiyo kazi itafanyika kesho...?” Mr Tanganyika kabla ya kumaliza sentensi yake. Akakomea hapo kwanza na kuuliza. Jibu likatoka kuwa ni kesho ndio imeonelewa kazi hiyo ifanyike. Akaendelea.



“Basi nitawajulisha kuwa kesho kutwa ndio waje wafuate mzigo wao. Bakari hiyo kazi ni rahisi sana kwa maono yangu. Sasa sitegemei vijana wako kuishindwa. Au labda nikuongezee vijana wakusaidizana kuifanya hiyo kazi?”



“Hapana kaka mbona kazi nyepesi sana hii” Hanein alijibu.



“Basi acha niwajulishe sasa ili na wao wajue wanajiandaaje” Simu ikakatwa.



Majira ya saa nne usiku katika gesti moja iliyopo maeneo ya Majengo. Ndani ya chumba kimoja. Inspekta Kiulason alikuwa amejilaza juu ya kitanda. Uso wake ulionekana kusawajika kwa jambo fulani. Mawazo ima uchovu au labda pengine ni vyote. Macho yake alikuwa akiyapepesa pepesa huku akiyaangaliza juu lilipo dari. Unaweza ukahisi labda alikuwa yupo hapo kwaajili ya kumkosoa au kumsahihisha fundi wa hilo dari.



Kilichomfanya kuyakimbia makazi yake na kuja kujichimbia katika gesti hiyo. Ni kile alichokiita usumbufu. Hakutaka usumbufu wowote kutoka kwa mtu yoyote kwa kitu chochote. Mawazo yake yalikuwa ni juu ya kuvujisha siri ya jeshi kwa kutoa maelezo na ramani ya wapi lilipo ghala la silaha za jeshi la polisi. Aliwaza mambo mengi. Je wasipofanikiwa katika huo mpango wao. Si wataona nimewauza? Au labda katika hiyo ‘mission’ akishikwa mmoja wao na kubanwa aeleze nani yupo nyuma ya mpango huo si nitatajwa mimi? Familia yangu nitaiweka wapi? Nitajificha wapi?



Alijilaumu sana ni kwanini hakumueleza mkuu wake kuhusiana na hilo? Pengine labda lingefanyika jambo jengine mbadala. Kwasababu kulikuwa na nafasi nyingi sana za kuwakamata wahalifu hao kupitia yeye. Akawaza sana na mwisho akaonelea aache kujiumiza kichwa chake. Akajaribu kufumba macho ili ausake usingizi. Usingizi nao ukamsaka. Sasa ikawa ni msakano kati yake na usingizi. Usingizi ukatwaa taji la ushindi baada ya kufanikiwa kumpata.

Akalala!.



* * * *



Siku iliyofuata jijini Daresalam majira ya saa nne asubuhi. Katika mgahawa wa Hoteli ambayo ndani yake ndipo zilipo ofisi za TSSI. Kulikuwa na watu wengi sana asubuhi hiyo waliokuwa wakipata staftah kwenye mgahawa huo. Kwenye meza moja wapo kulikuwa na vijana wawili ambapo ni Hilda na Fady walikuwa na wao wakipata kifungua kinywa asubuhi hiyo. Wakiwa wanaendelea kupata kifungua kinywa muda huo huku wakiongea. Hilda alimnyamazisha Fady ghafla na kumtaka asikilize kwa umakini maongezi yaliyokuwa yakizungumza na watu waliokuwa meza ya jirani nayo. Fady akakaa kimya kusikiliza huku umakini ukiwa nae.



“Bado sijajua ni za aina gani, lakini hata kama zikiwa sio zile tuzitakazo sie, basi tutawaambia watupunguzie bei. Hatuwezi tukaacha mzigo” Aliongea kijana mmoja kutoka meza hiyo ya pembeni. Ambae alionekana ujana unaanza kumtupa mkono kiumri. Walikuwa wapo wawili. Na yule mwenzake alikuwa ni mzee kiasi ambae ki muonekano bado alikuwa na nguvu zake.



“Kwanza uhakika wa kupatikana upo? Maana jana Mr alinipigia simu tu nakuniambia nijiandae kesho kutwa ambayo ni kesho mzigo utakuwa tayari. Sasa nina wasiwasi hao watu waliopewa hiyo kazi wanaweza kutuzingua...” Mzee yule akakatishwa na yule kijana.



“Na ndio maana hatukuta kuwapa ‘advance’ kwasababu hatujawahi kufanya nao kazi” Akazungumza yule kijana.



“Umeandaa usafiri wa kwenda kuchukua huo mzigo huko mkoani hiyo kesho?” Akauliza yule mzee.



“Kila kitu tayari na hata vijana wengine pia nimeshawaandaa. Yani hapa kilichobakia ni simu yao tu”



“Lazima umakini utumike si unajua kazi yenyewe hii haikuwii kunuka?” Yule mzee alizungumza.



Waliangaliana Hilda na Fady. Kisha macho yao wakayahamisha tena kisirisiri kwa watu wale ambao hadi muda huo walikuwa wakiendelea maongezi yao bila kujua kwamba yalikuwa yakinaswa na watu wengine ambao hawakupaswa kuyasikia.



“Ni lazima tujue wanampango gani hawa maana nishaanza kuwa na wasiwasi nao” Aliongea Hilda huku jicho lake pembe likiwa bado kwa watu wale.



“Wasiwasi umetoka wapi ilhali wanaongea mambo ya kawaida tu?” Fady aliongea kikawaida kisha akanyanyua kikombe chake cha chai na kunywa kidogo na kukishusha. Hilda alimuangalia machoni kwa mshangao.



“Inamaana hukuyatilia shaka maongezi yao?” Hilda alimuuliza.



“Sikuyatilia shaka yoyote na ninayaona kama maongezi ya kawaida tu”



“Tatizo hukuwasikiliza tangu wanakuja hapa” Hilda aliongea kisha akanyanyuka. Fady akataka kuhoji lakini alikuwa ameshachelewa. Hilda alipiga hatua za haraka haraka na kupotelea ndani ya Hotel hiyo. Baada ya dakika nne alirudi akiwa tofauti sana na alivyokuwa mwanzo. Hivi sasa alikuwa amevaa sare za wahudumu wa mgahawa huo. Akapiga hatua za kimadaha huku tabasamu likiwa nae hadi kwenye ile meza waliokuwa wamekaa wale mabwana. Muda wote Fady alikuwa akishangaa tu mambo anayoyafanya Hilda.



“Samahanini wakaka..” Akanyamaza kisha akawatupia macho wote wawili na kukuta wakiwa na umakini nae. Akaendelea. “Kaka hapo kuna mtu anakuita kule” Akaongea hivyo huku akielekeza kwa kidole sehemu ambayo inatumika kama jiko. Wote macho yao wakayapeleka huko walipoelekezwa na kukuta hakuna chochote cha maana zaidi ya wahudumu kupita pita tu mahala hapo.



“Nani anaeniita?” yule kijana akauliza kwa wahka huku akimungalia machoni Hilda.



“Ki ukweli kaka yangu simjui ila ameniambia tu nije nikuchukue anakuhitaji mara moja”



“Wakike au wakiume?” Akauliza tena yule kijana.



“Ni mdada. Ameniambia ni mara moja tu anakuhitaji” Yule jamaa bila kuhoji tena. Alimminya mguu yule mzee aliemuita kwa jina la Koja. Kisha akainuka na kumfuata Hilda nyuma wakielekea huko wanapoenda. Fady akataka kuunga ili akatoe msaada wowote kama utahitajika. Ila akajipa moyo wa subira akasubiri pale pale akitaka kuona mchezo utakavyoenda.



“Alooh! Dada unanipeleka hadi wapi wewe?” yule jamaa alihoji baada ya kuona wanapita ile sehemu aliyoelekezwa na kuzidi kutokomezwa ndani zaidi. Hilda hakumjibu kitu zaidi aligeuka baada ya kuona sehemu hiyo waliyopo itamuwezesha kufanya kile alichokipanga.



“Hakukuwa na mtu yoyote aliekuwa akikuita. Bali mimi ndio nilikuwa na shida na wewe..” Hilda alijibu. Yule kijana akatabasamu baada ya kuhisi muhudumu huyo ni malaya na amemzimia na hapo amemuita waje kufanya uchafu.



“Wewe ni nani?” Hilda alimuuliza. Kijana yule akastaajabu. Inakuaje malaya aniulize jina? Anashida gani nyengine zaidi ya kunipa mzigo? Akajiuliza kimya kimya.



“Naongea na wewe broo. Wewe ni nani na ulikuwa ukiongea nini na yule mzee pale nje. Na mlikuwa mkizungumzia kuhusu nini?” Hilda akaona aende moja kwa moja kwenye lengo lake baada ya kuona kijana huyo huenda hakumuelewa mwanzo. Mshtuko ulimkumba yule kijana baada ya kumtazama vizuri Hilda. Akamkumbuka!. Huyu mwanamke ndio yule aliekuwa amekaa na yule jamaa kwenye meza ya pembeni yetu. Iweje awe muhudumu ghafla mara moja hii? Na kwanini ameniuliza maswali haya? Kumbe alikuwa akitusikiliza muda wote? Ni nani huyu? Askari? Jamaa yule alijiuliza maswali yote hayo.



“Kwani wewe ni nani na unataka nini?” Jamaa yule aliuliza kwa dharau.



“Hilo ndio janga ambalo linasumbua sana hapa bongo. Unaulizwa swali badala ya kujibu na wewe unaliza. Jibu kwanza swali langu” Hilda aliongea. Jamaa aliona hakuna cha maana kinachoendelea hapo. Akageuka kutaka kuondoka. Aligeuka tena baada ya kuguswa bega. Aligeuka na ngumi iliyodhamiria kumpiga nayo Hilda ya shavu. Hilda akabonyea chini kisha akampiga jamaa ngumi ya tumbo. Jamaa akagugumia na kukaa sawa.



Wote wawili wakawa tayari kwaajili ya mpambano. Jamaa alikuwa bado akimdharau Hilda baada ya kuhisi ni lege lege na ngumi ile aliipiga tu kwa kubahitisha. Jamaa akamuendea Hilda na kurusha ngumi za kawaida sana ambazo zote Hilda alizihepa na kumpiga ngumi mbili za kifua. Jamaa akarudi nyuma na sasa akawa makini na mwanamke huyo baada ya kujua yupo vizuri kwenye mapigano. Mara hii Hilda akamuendea yeye na mapigo ya haraka yenye ustadi mzuri. Jamaa akababaika kidogo huku akijitahidi kuhepa mapigo hayo. Mawili kati ya matano yalimpata kwenye uso maeneo ya mdomo.



Jamaa akatema damu. Akamuangalia Hilda kwa hasira huku akiwa aamini kwamba kuna mwanamke yoyote anaweza kumdhibiti yeye. Akajipanga upya. Sasa akawa anajipanga na mapigo ya kareti. Alikuwa akinesanesa huku na huko huku akiwa mikono yake ameikunja kimapigano. Hilda akawa anamuangalia jinsi jamaa anavyonesanesa. Ghafla kuja kushtuka alijikuta akitupwa ukutani baada ya kutokuwa makini na jamaa yule. Hilda aliwahi kuinuka baada kuona jamaa akimuendea yeye akiwa hewani yupo kwenye pigo la kumtengua.



Hilda akabenjuka kiutaalamu na kumpisha. Jamaa akatua hola na muda huo huo Hilda akampiga teke kali la mgongo na kumfanya jamaa akumbatie ukuta huku akitoa mguno wa maumivu. Hilda akarudi nyuma. Akajishika maeneo ya shingo pahali palipotua pigo alilopigwa. Jamaa akageuka. Akajifuta damu zilizokuwa zikitoka puani baada ya kujipigiza ukutani. Akameza mate na hivi sasa akaanza kuingiwa na wasiwasi na mwanadada huyo. Akaomba kimya kimya Koja atokee mahali hapo aje kutoa msaada. Hilda muda alikuwa akitabasamu baada ya kuuona uoga ulioonekana dhahiri usoni mwa jamaa.









“Naomba uniambie wewe ni nani na ule mpango wenu mliokuwa mkiongea ni wa nini? La sivyo..... Hutobaki salama” Hilda alijitoa kwenye mkao wa mapigano na kuongea hivyo. Jamaa ni kama vile hakuyasikia maneno hayo. Akayajibu. Lakini sio kujibu kwa maneno, badala yake aliyajibu kwa matendo. Alichomoka mbio kwa nia ya kwenda kumkumba Hilda. Hilda aliliona hilo na kumpisha. Jamaa akapita hola. Alipokuwa nyuma ya Hilda. Akaachia teke kali la shukurani ya punda. Hilda alilipisha na kuudaka mguu wa jamaa akiwa vile vile bado amempa mgongo. Yani jamaa alikuwa nyuma ya Hilda.



Ule mguu wa jamaa ambao kwa sasa upo mikononi mwa Hilda. Hilda aliupiga pigo moja juu ya goti. Jamaa alitoa ukelele mkubwa baada ya pigo hilo. Papo hapo alimpiga tena na kiwiko cha mkono kinywani. Ukelele ukakoma ghafla, damu tu ndio zilidhihirika kinywani. Hilda aliuachia ule mguu na kumpiga ngumi ya taya. Jamaa akaenda chini huku damu zikizidi kutoka. Ni dhahiri kwamba hakuwa akiweza tena kuongea chochote baada ya pigo lile lililotua kwenye taya. Yule mtu akajiburuza hadi ukutani na kuegamia. Sasa alikuwa akimuangalia Hilda huku akitabasamu. Tabasamu ambalo halikujulikana chanzo ni nini.



Hilda alimfuata taratibu hadi pale alipo na kukita goti moja chini. Akamuangalia usoni jinsi uso ulivyochafuka kwa damu. Akatabasamu na kumuuliza tena maswali yale yale kuwa yeye ni nani na walikuwa wakiongea mpango gani na yule mzee pale nje? Jamaa hakujibu. Tungesema bado anakiburi lakini hata hivyo pia taya zake zilivunjwa. Sasa vipi ataongea? Haikujulikana! Au labda ilijulikana lakini Hilda alimuuliza kwa kumkejeli.



Wakati Hilda akiwa bado anauliza maswali yasiyotolewa majibu. Mkono wa jamaa kipindi hiki ulikuwa nyuma ya mgongo wake. Haikujulikana anatafuta nini huko. Ila ghafla aliibuka na kisu alichokipitisha kwa kasi usoni mwa Hilda. Ni vile tu Hilda aliwahi kukiona na kukipisha. Ila bilashaka kingeondoka na macho yake. Ngumi tatu za haraka zikatua kifuani mwa jamaa. Alicheua damu zilizoruka kwa kasi kidogo na kumchafua Hilda kifuani kwenye vazi lake lililofanana na wahudumu wa huo mgahawa.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Jamaa akacheua tena damu nyengine, ila hizi hazikutoka kwa kasi. Badala yake zilidondokea kidevuni na kuangukia kifuani. Akakodoa macho kwa muda kisha shingo yake akailaza juu ya bega lake. Hapakuwa na ubishi kwamba jamaa alikuwa tayari ameshakufa baada ya kupokea mapigo yale. Hilda akajiinua pale na kuondoka. Akapitia chooni, alisafisha lile vazi lake pale kifuani zilipokuwa zile damu kisha akapakausha na kitambara.



Akatoka sehemu ile na kuelekea kule alipokuwa yule mzee alietajwa kama Koja na yule jamaa marehemu. Alipofika kama kawaida tabasamu usoni. Alimuambia Koja kuwa alikuwa akihitajika na yule jamaa alieondoka nae muda mfupi. Yule mzee alianza kuingiwa na wasiwasi. Ni vipi waingie kwenye mgahawa huo halafu waanze kuitwa mmoja mmoja kuelekea pasipojulikana? Akamuuliza ni pahala gani ambapo alipo yule mwenzake. Hilda akajibu kuwa ni ndani ya Hotel na huko yule jamaa alimuagiza aje kumuita yeye aende huko. Akaongezea kuwa yule jamaa amekutana na mtu ambae walikuwa wakifahamiana kwahiyo amemtuma yeye aje kumuita.



Kidogo wasiwasi ukamuondoka. Akaainuka pale na kumfuata Hilda ambae alikuwa akiongoza njia pasi na shaka yoyote itakayomfanya yule mzee kumshtukia. Hilda alimpa ishara ya siri Fady kua afuate nyuma. Aliielewa na yeye alifuata. Muda huu hawakuwa wakielekea kule Hilda alipoelekea mwanzo na yule jamaa. Hivi sasa walikuwa wakizunguuka nyuma ya jengo la Hotel ile. Yule mzee akataka kuhoji ni kwanini wanaelekea huko ilhali aliambiwa kuwa ni ndani ya Hotel hiyo. Akapitisha wazo la kuwa kimya ila akijiandaa na lolote baya.



Safari ikaendelea. Hivi sasa walikuwa ndani ya jengo hilo baada ya kupita kwenye mlango wa nyuma wa Hotel hiyo. Huko kulikuwa na watu wachache ambao walikuwa wakipata staftah asubuhi hiyo huku wengine wakiwa wamepumzika tu kwenye viti vilivyokuwepo sehemu hiyo. Kuna mambo yalimshangaza Koja. Kwanza, kuna mtu tangu walipokuwa kule mgahawani alikuwa akiwafuata nyuma lakini alikuwa akizuga kama hayupo kwenye msafara huo. Ni nani huyo? Hakupata jibu. Pili ni safari gani hiyo isiyofika mwisho? Akajiuliza.



Wakachepuka kwenye njia iliyokuwa kushoto kwao. Hapo Koja akabana kwenye kona na kuchungulia kule walipotokea ili kumchunguza Fady. Alimuona mtu huyo akiongea na simu tena akiwa anacheka si mchezo ila hakuwa akija tena na njia hiyo waliyo chepukia wao. Akajiondoa wasiwasi huenda ikawa yule mtu alikuwa na yake. Butwaa lilimpiga baada ya kugeuka na kule walipokuwa wakielekea na asimuone yule muhudumu. Inakuaje asionekane ilhali njia ni ya kunyooka?

Ajabu hii!.



Akageuka kule walipotoka ili arudi. Ebwana eee!. Yule kijana aliekuwa akimshuku kuwa alikuwa akiwafuatilia. Hivi sasa alikuwa mbele yake tana akiwa ana tabasamu. Hii inakuaje? Hakupata jibu. Nyuma yake alihisi harufu ya manukato. Akageuka haraka ili kumjua huyo mwenye kunukia hivyo. Alaa! Alikuwa ni yule mwanamke ambae yeye alimjua kama muhudumu wa ule mgahawa. Hivi sasa alikuwa yupo ndani ya mavazi tofauti na yale aliyokuwa ya kihudumu. Akajua sasa moto umewaka.



Akachomoa bastola yake haraka na kumnyooshea Fady. Mara akaihamishia kwa Hilda. Kisha tena akairudisha kwa Fady. Mara tena akaihamisha kwa Hilda. Hakuwa na chaguo maalumu la nani amuelekezee bastola hiyo. Alikuwa amepagawa si mas'hara. Hakuwajua watu hao ni akina nani. Licha ya kutowajua tu. Pia hakujua walikuwa na shida nae gani. Je yule mzwenzake yupo wapi. Au na yeye alifanywa kama yeye anavyofanyiwa?

Hakujua!.



Wakati akiwa bastola amemnyooshea Hilda. Fady alifanya kitendo cha ghafla sana kilichomuacha jamaa hoi na kujikuta akiwa mtupu mikononi bastola ikiwa mikononi mwa Fady. Akaingiwa na mchechetu baada ya kutoelewa ni vipi asiwe na bastola ilhali ilikuwapo mikononi mwake sekunde kadhaa nyuma. Akamuendea Hilda kwa kasi ya ajabu na kumdhibiti vema kwa nyuma kwa kumkwida roba akitumia nafasi hiyo kujiokoa.



“Shusha bastola chini vinginevyo namuua huyu malaya wako” Alisema Koja huku akihakikisha roba yake inakuwa sawa kwenye shingo ya Hilda. Hilo lilimpa wakati mgumu Fady kufanya chochote akizingatia Hilda alikuwa amekedwa shingoni. Roba ile haikuwa kali sana kwasababu ilikuwa ni roba ya onyo japokuwa ilikuwa na maumivu yake.



Hilda alimpa ishara ya macho Fady. Ishara ambayo Koja hakuiona. Na ataionaje wakati alikuwa nyuma ya Hilda? Hakuiona!. Fady akaishusha taratibu bastola ile chini huku akiwa anaiangalia ile miili miwili iliyoko mbele yake. Kidole chake cha shahada kikiwa kwenye ‘trigger’. Aliishusha bastola ile hadi ilipofikia usawa wa miguu ya watu wale. Hilda alibananisha miguu yake akiipa nafasi miguu ya Koja kuonekana bila shida.



Mlio wa risasi ukasikika na Koja alishuka chini huku akiwa anapiga mayowe ya uchungu. Mguu wake wa kushoto ukitoa damu kwenye ugoko. Kazi ikawa rahisi kabisa!. Wakamchukua mtu wao wakimkokota kumpeleka ndani ya jengo hilo. Koja alikuwa akilia kwa uchungu huku akitukana matusi kwa watu hao. Hawakujali!. Walimpitisha njia hii na kutokea ile hadi walipofika chini ya jengo lile ambapo ofisi za TSSI zilikuwepo. Walimfikisha ndani ya chumba kile ambacho miezi miwili nyuma walielekezwa kama ni chumba cha mateso ama mahojiano.



Wakamfunga vizuri kwenye kiti na wala wasijali lolote kuhusiana na maumivu ayapatayo mtu huyo ile sehemu yenye jeraha. Hilda akasema anaenda kumpa taarifa mkuu wao kuhusiana na mtu huyo. Akapiga hatua kutoka ndani humo. Alipofika mlangoni alishtuliwa na sauti ya Fady aliekuwa akimtaka amsubiri. Akasimama. Fady akamuendea mpaka pale.



“Hilda unajua tumemchukua huyu mtu ila hadi sasa sijajua ana shida gani?” Fady alionyesha wasiwasi wake. Hilda akamuangalia yule Koja pale walipomfunga. Akamuona akitokwa na machozi huku akinung'unika chini chini. Akamuangalia Fady.



“Tatizo hukuyazingatia maongezi yao wakati wakiwa wanaongea pale. Na maongezi yao ndio yamenifanya niwe na shaka nao”



“Shaka kivipi? Na yule mwengine umempeleka wapi?” Fady alihoji.



“Nimemuua. Subiri nakuja” Akajibu na kuondoka akimuacha Fady kinywa wazi. Iweje aue mtu asie na kosa? Akajiuliza Fady. Au uwezo wake anataka kuutumia vibaya huyu mwanamke?. Akabetua mabega yake na kurudi pale alipo Koja. Akavuta kiti kingine na kukaa akisubiri aone mwisho wa huo mchezo tatanishi.



“Inakuaje ukamate na uue watu ambao umewatilia shaka wewe kama wewe bila kuonyesha madhara yoyote juu yako? Au unadhani kitengo hiki ni cha jeshi la polisi kwamba yoyote anaeitiliwa shaka hata kwa kuonekana kwamba huenda ameiba kuku akamatwe?” Kaoneka aliwaka kwa hasira baada ya kusikiliza maelezo ya Hilda aliyoyatoa kuhusu watu wale aliosema ati amewatilia shaka na asijue ni shaka kuhusiana na nini hadi amuue mmoja na amkamate mmoja.



“Mkuu lakini ungenipa walau nafasi ya kwenda kumuhoji, naamini utayaona haya ninayo yaongea kwasababu wakati wanaaza kuongea mimi niliwasikia mpak.....” Akanyamazishwa na sauti kali ya Kaoneka.



“Nisipoyaona....?” Akauliza Kaoneka. “Unajua hiki kitengo sio cha kipolisi kwamba kitahusika na majambazi ama watekaji wa kawaida kawaida. Hiki ni kitengo kinachotenda kazi kwaajili ya Taifa zima na sio sehemu fulani tu.” Akamuangalia Hilda usoni. Muda huu Hilda alikuwa amegwaya baada ya kufikiria maneno hayo ya mkuu wake na kukuta yana tija ndani yake. “Ameshakufa mmoja na mmoja yupo chumba cha mateso akisuburi ahojiwe na sijui utaenda kumuhoji kuhusiana na nini. Je kama ukipata kujua watu hao hawana hatia yoyote we utafanya nini ilhali huyo mwengine ushamuondoa kwenye uso wa dunia?” Mr Kaoneka alihoji huku akiwa anamuangalia Hilda machoni. Hilda alitahayari!. Hakujua kama mwanzo alichokuwa akikifanya ni makosa. Akashindwa ajibu vipi swali hilo. Akabaki kimya akifikiria cha kujibu. Wakati akijiandaa kujibu. Alikatishwa na sauti na mkuu wake akimtaka aende akafanye vile atakavyo.



Aliinuka na kutoka kinyonge sana ndani humo. Roho ilimuuma baada ya kukaripiwa na mkuu wake kiasi hicho. Ni kweli alifanya makosa kuwashuku watu wale na kusababisha kifo cha mmoja wapo. Lakini angepewa nafasi nzuri ya kumhoji yule aliebakia ili awadhihirishie kwamba hakufanya makosa kuwashuku watu wale kama mawazo yake yalivyomtuma.



Akaingia ndani ya kile chumba cha Mateso na kumkuta Fady akiwa amekaa kwenye kiti tuli akisubiri aone nini kitatukia. Koja alikuwa kimya muda huu hakuwa akilia tena. Huenda ikawa mguu wake umepata ganzi au kama sio ganzi basi ameshayazoea maumivu. Hilda alienda mpaka pale alipo Koja. Akavuta kiti na kukaa. Akawa anaangaliana na Koja. Kule kwenye ofisi ya Mr Kaoneka alikuwa anaona kila kinachoendelea na kusikia pia kwa kutumia Kompyuta yake maana iliunganishwa na kamera na vinasa sauti vilivyokuwa ndani ya chumba hicho.



“Hunijui sikujui. Naomba unijibu kila nitakalo kuuliza. Vinginevyo sitatumia nguvu kukuuliza bali utanijibu kinguvu” Hilda alionya. Koja alikuwa akimuangalia usoni na isijulikane kama ameyaelewa maneno hayo ama laa!. Hilda alianza kwa kuuliza jina la mzee huyo na alijibiwa kuwa alikuwa akiitwa Koja. Akamuuliza tena iwapo anajua mwenzake alipo hadi muda huo na Koja akajibu kuwa hajui na anachokijua yeye ni kuwa mwenzake ameondoka na yeye.



“Mlikuwa mkizungumza kuhusu kufanya biashara na watu fulani. Je unaweza kuniambia ni bishara gani ambayo mlikuwa mkizungumza?” Hilda aliuliza. Jamaa akakaa kimya na isijulikane ni ugumu wa swali au hakuelewa swali lile. Hilda akamuonya tana na kurudia swali lake. Koja akakaa kimya tena.



“Nadhani nimeshakuonya mara mbili na sitaki kurudia tena kukuonya kwasababu wewe si mtoto na unaelewa nini ninacho maanisha” Akainuka kwenye kiti kama anataka kuondoka hapo.



“Ni biashara za kawaida tu mama” Koja alijibu. Hilda akarudi tena kitini.



“Biashara za kawaida. Ni biashara gani hizo?”



“Tulikuwa tukipanga kusafirisha bidhaa za mananasi kutoka hapa Dar kwenda Tanga” Koja alijibu.



“Mananasi ee? Mananasi ndio mseme kwamba hamjajua ni ya aina gani na hata kama yakiwa sio hayo mnayotaka ninyi mchukue hayo hayo mtakayoyakuta halafu mdai kupunguziwa bei? Mananasi ndio utumike umakini mkubwa sana kuyasafirisha huku mkihofia usalama barabarani? Nadhani haupo tayari kuniambia ukweli. Subiri nifanye kile unachotaka wewe” Hilda alinyanyuka na kuliendea kabati lilipo humo humo ndani.







Akatoa sufuria kubwa na kulipeleka kwenye jiko la gesi. Akawasha jiko na kuchukua dungu lililokuwa na mafuta na isijulikane ni mafuta gani. Akayamimina kwenye ile sufuria na kuwasha jiko. Hilda alimuangalia Koja aliekuwa amehamaki asijue nini atakachoenda kufanyiwa muda mfupi ujao. Mafuta yale yalichemka mule ndani kwa muda mfupi tu hadi yakawa yanatoa moshi.



Akaepua ile sufuria na kwenda kuiweka karibu na alipo Koja. Koja alishuhudia mafuta yale yakitokota kwa moto. Hofu!. Alikuwa na hofu baada ya kuhisi ukali wa mafuta yale. Hilda akarudi kwenye lile kabati na kutoa kisu kilichokuwa kikimeremeta kwa makali. Akachukua na pamba ngumu na kwenda navyo. Akaviweka chini na kuuvuta ule mguu wa Koja uliokuwa na jeraha. Kile kiti alichofungiwa Koja kilikuwa ni kwaajili ya mateso. Hilda aliuvuta ule mguu wa kiti ambao ulikuwa umefungwa na mguu wa Koja. Mguu wa Koja ukawa mbele sambamba na mguu wa kiti. Akachana suruali ya Koja sehemu ile palipo na jeraha alilopogigwa risasi na Fady. Sehemu ile ikawa wazi.



Hakuongea kitu. Badala yake alikwangua ile damu iliyonganda pembeni ya lile jeraha. Kisha akaichukua ile pamba na kuichovya kwenye yale mafuta ya moto. Kuja kuitoa ilikuwa ikivuka moshi utafikiri ilichemshiwa mule mule ndani. Bila huruma yoyote wala utaratibu wa kuchua kidonda. TSSO I 03 alibandika ile pamba kwenye lile jeraha kwa nguvu na kukandamiza.



“Aaaaaaaaaaa!! Nasemaa! Nasemaaa!!” Koja alipiga yowe la uchungu na kumalizia kwa kusema atasema hicho alichotakiwa kukisema. Hilda aliondoa ile pamba na kumtaka Koja aseme kama alivyosema atasema. Ila Koja alikuwa akigugumia kwa maumivu huku mara kadhaa akitukana matusi ya nguoni.



Hilda akamuonya tena kwa mara nyengine kwamba alitakiwa aseme ukweli na asidanganye chochote. Koja akamtukania mama yake huku akisema kwa hasira kwamba hajui aseme nini na hapo alikuwa akionewe tu.



“Anhaa! Nadhani nimekuchua hilo jeraha lako na sasa umepata afueni kidogo ndo unaleta dharau. Subiri nikuonyeshe tena. Bilashaka hivi sasa utasema ukweli wote maana naenda kukuvunja kiungo kimoja kimoja hadi uwe mlenda” Akainuka na kuelekea kwenye droo iliyokuwa humo humo. Akatoka na kitu kama rimoti. Akaenda ukutani na kuwasha swichi iliyokuwa hapo. Kiti kile kikatoa mlio fulani kama wa ‘Alarm’ uliolia mara tatu tu na kuzima ghafla. Kisha kikawaka taa nyekundu na kuzima.



Hilda alisogea karibu na kilipo kiti kile ambacho walikuwa wamemfunga Koja kwa kutumia ‘Lock’ zilizopo kwenye kiti kile. Akabonyeza kitufe fulani kwenye ile rimoti na mikono ya kiti kile ikaanza kuzunguka taratibu. Hilda akatabasamu ilhali Koja na Fady wakishangaa. Ila Koja alishangaa zaidi. Nini hii? Akajiuliza huku akiangalia mikono yake ikizunguka taratibu kiasi ambacho ilianza kumletea maumivu.



Akamuangalia Hilda kwa uso wa hamaniko na asijue alikuwa na dhamira gani. Au ndio anataka kunivunja viungo kama alivyo sema? Akajaribu kutingishika kama ataweza kujinasua hapo. Ila alishindwa. Hivi sasa mikono yake ilikuwa ikimuuma baada ya kuzungushwa kiasi fulani. Zoezi hilo liliendelea hadi pale Koja alipopiga mayowe ya uchungu. Fady akataka kumuambia Hilda aache hivyo anavyotaka kufanya maana anaona kama anamuonea tu mtu huyo. Ila akasita. Mr Kaoneka alikuwa akishangaa yanayofanywa na mtoto huyo wa kike. Ana kichaa huyu? Alijiuliza huku akiitolea macho kompyuta yake.



Kule kwenye chumba cha mateso. Koja alipiga kelele kiasi ambacho ilikuwa ni kero ndani humo. Fady akashindwa kuvumilia na kumpazia sauti Hilda kuwa aache zoezi hilo. Hilda alimuangalia kwa jicho baya huku akitetemeka mwili mzima na hiyo ilitokana na hasira alizokuwa nazo baada ya kuonekana na mkuu wake amefanya uzembe kwa mara ya kwanza kitengoni.



“Nasemaaaaa!. Nasema ukweliiii!. Basiiii!! Basiii” Koja alipaza sauti huku akitetemeka mwili mzima kwa maumivu ya kuelekea kuvunjika mikono yake. Hilda ni kama vile hakusikia hicho alicho sema Koja. Akakaa kimya huku akiendelea kuangalia mikono ya Koja inavyo nyongorotwa pale kitini. Muda huu Koja alipaza sauti kuu huku akiomba kusamehewa kwa kitendo chake cha kudanganya na kuahidi kusema ukweli wote anaoujua. Fady alimuangalia usoni Hilda kwa wasiwasi akiwa haamini kama msichana huyo mrembo anaweza kufanya kitendo cha kikatili kama hicho. Akaminya kitufe kwenye ile rimoti yake na mikono ile ikaacha kuzungushwa.



“Tafadhali naomba uiweke mikono yangu sawa nipo tayari kusema ukweli wote” Koja alisema huku akilia. Hilda aliminya kitufe kwenye ile rimoti na mikono ile ikazungushwa taratibu kuwekwa sawa.



“Naitwa Koja. Mimi na yule mwenzangu tulikuwa tukizungumza mpango hasi ambao ulikuwa ni kuenda kununua silaha ambazo zitaporwa kwenye jeshi la polisi huko Tanga. Na pale tulikuwa tukijadili ni jinsi gani ya kuendesha ‘operesheni’ hiyo mpaka ikamilike. Ni hivyo tu hakuna vingine” Koja alieleza mpango wao waliokuwa wakiuzungumza. Hilda akamuuliza kuwa ni nani wanunuzi wa silaha hizo na Koja alijibu kuwa ni wao wenyewe wawili.



“Nani ambae alikuwa akienda kuwauzia hizo silaha na watazipata wapi?” Hilda aliuliza. Majira haya Fady na Mr Kaoneka walikuwa makini kusikiliza. Wote wakiwa hawaamini kwamba watu hao wanaweza kuwa na mpango mkubwa kiasi hicho.



“Hatukuambiwa kuwa tutazipata kwa nani na tuliambiwa tutaambiwa kila kitu baada ya mpango wa kuteka silaha hizo ukamilike”



“Hamkuambiwa!? Hamkuambiwa na nani ilhali umesema kwamba ni nyie ndio wanunuzi wa hizo silaha? Unaleta tena uongo sio?” Hilda alimuuliza.



“Hapana sidanganyi. Ni kweli tupu”



“Ndio useme sasa ni nani aliewaambia kuwa mtazipata kwa huyo anaetarajia kuwauzia?”



“Ni mtu mmoja anaitwa Mr Tanganyika ndie ambae alituelekeza kwa huyo tunaetaka kufanya nae biashara” Kaoneka aliposikia jina hilo lililotajwa na mtu huyo. Akatoka haraka ndani humo na kuelekea kwenye kile chumba ambacho walikuwamo watu wale. Ila hakuingia ndani badala yake alisimama mlangoni akisikiliza kitakachongelewa zaidi..



“Lini biashara hiyo mlipanga mkaifanye?” Sasa Fady nae aliuliza.



“Ndio tulikuwa tunasubiria simu yao” Wakati wakiwa wanaendelea kumuuliza maswali. Fady alimuona Mr Kaoneka pale mlangoni na Mr Kaoneka alipoona ameonewa na Fady. Akampa ishara kuwa wamfuate muda huo yeye na Hilda. Kisha akanza kupiga hatua kuondoka hapo. Fady akamuambia kuwa mkuu wao alikuwa akiwaita muda huo. Wakaacha kumuhoji na kutoka hapo kuelekea kwenye ofisi ya Mr Kaoneka. Walipofika walikaa kwenye viti kumuangalia mkuu wao. Mr Kaoneka alimtazama Fady kwa sekunde kadhaa kisha macho yake akayahamishia kwa Hilda. Hapo alimtazama kwa kitambo kidogo kisha akaachia tabasamu dogo. Akasema.



“Sikutegemea kama utakuwa na mafikirio makubwa kiasi hiki na utambuzi wa haraka kiasi ambacho umehisi tu na halafu ikawa kweli...” Akatulia kama si yeye aliekuwa akiongea maneno yale. Akainuka pale alipokaa na kuliendea friji. Akatoa chupa kubwa ya maji safi na kuchukua glasi. Akarudi navyo pale mezani na kumimina yale maji kwenye glasi. Akapiga funda moja na kuishusha juu ya meza.



“Nadhani hakuna yoyote kati yenu anaemjua huyo mtu alietajwa kwa jina la Mr Tanganyika. Mtu huyo aliwahi kuwa kiongozi katika sekta fulani kubwa serikalini. Ila alifukuzwa kazi baada ya kufanya hujuma kwenye hiyo sekta aliyowekwa. Hadi sasa haijulikani ni wapi makazi yake yalipo. Nikimaanisha tangu alipofukuzwa kazi hakuwahi kuonekana tena sehemu yoyote ile. Sasa kama hao vijana wamesema kwamba muasisi mkuu wa huo mpango ni yeye. Basi ni dhahiri yupo hapa Tanzania au kama sio hapa, basi atakuwa Afrika Mashariki hii...” Akatulia tena na kumalizia yale maji yaliyokuwa kwenye ile glasi. Akaendelea.



“Huyo mtu kwa sasa hatuna shuhuli nae kwasababu pamoja na kuwa yeye ndie muasisi. Lakini amewahi kujitoa na kuwapa dili hilo watu wengine kama maelezo ya yule kijana alivyosema. Sasa ni hivi. Nendeni mkam'bane vizuri hadi awatajie hao watu wengine” Akamaliza hivyo na kuwaruhusu waende. Wakati wakiwa wanataka kufungua mlango ili watoke. Waliashtuliwa na sauti ya Mr Kaoneka. Wakageuka wote na kumuangalia. “Hii kazi ya kwenu” Akasema hivyo na kuwaruhusu waende.



Ebwana wee!.



Mshtuko uliwapata baada ya kumkuta Pijo akiwa na dalili zote za kutokuwa na uhai. Shingo akiwa ameilaza begani kwake huku mdomoni akitoka mapovu. Walienda mbio hadi pale alipo. Hilda akawahi kusikiliza mapigo ya moyo na kukuta yakipiga kwa chini sana. Akatoka mbio ndani na humo na aliporudi. Alikuwa ameongozana na Trace Daniel TSSI 04 mwenye taaluma ya utabibu. Wakasaidizana kumtoa haraka chumbani humo na kumpeleka kwenye chumba ambacho ilikuwa ni ofisi ya TSSI 04 Trace ambayo pia kilikuwa ni chumba maalumu kwaajili ya matibabu. Huko walimuingiza na Trace aliwataka wampishe ili afanye kazi yake kwa ufasaha. Wakatoka nje wakiwa wanyonge.



Walikuwa wakimuombea kimya kimya Koja apate siha njema ili waingie kazini. Walikuwa na mori wa kufanya kazi kwa hakika. Maana kama Koja atafariki basi itawabidi watulie waendelee na majukumu mengine kwasababu hawatakuwa na pakuanzia popote zaidi ya maelezo ya Koja. Hofu ilikuwa sambamba nao. Hawakutaka kupokea taarifa ati ya kwamba Koja amefariki. Maswali yalikuwa mengi vichwani mwao. Nini kimemkuta? Mbona hali yake imekuwa vile ghafla? Atapona kweli.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mara kidogo Trace alitoka chumbani mule. Sura yake ilisawajika kwa huzuni kutangaza hali mbaya huko alipotoka. Haikuwa yenye kutangaza furaha hata kidogo. Akawaangalia kina Hilda waliokuwa wakimuangalia yeye kwa nyuso za hamaniko wakitaka kujua nini kimetukia ndani humo.



“He's gone!” Macho waliyatoa pima wasitake kuamini walioyasikia. Wakazidi kumuangalia Trace kwa macho ya kuuliza. Kivipi? Mbona mapema hivyo?.



“Amekufa!?” Hilda aliuliza tena kupata uhakika zaidi. Trace akatingisha kichwa chini juu kukubaliana nae.



“Nini kimemuua?” Fady akamuuliza.



“Sumu” Alijibu. Wote wakalitamka neno hilo kwa pamoja. Wakaangaliana usoni kisha macho yao wakayarudisha kwa Trace.



“Mkuu anatuita. Twendeni” Alisema hivyo na kuanza kuondoka hapo mdogo mdogo. Huku nyuma Hilda na Fady walifuata huku nyuso zao zikiwa na huzuni tele. Waliingia kwa mkuu wao na kila mmoja akachukua nafasi yake.



“Hii kazi imeishia hapa kwasababu hamna pa kuanzia tena. Au mnapo?” aliwauliza. Wakaangaliana na wakarudisha tena macho yao kwa Mr Kaoneka.



“Sasa basi. Kinachofuata sasa hivi ni kuifuata maiti ya huyo mwengine huko Hilda alipomuulia na muinganishe na hiyo nyengine mzifanyie utaratibu wowote. Maana italeta hofu endapo mtu yoyote akiiona ile maiti kule...” Akamgeukia Hilda.“ Nakupongeza kwa umahiri wako” Alimuambia hivyo huku akitabasamu. Hilda nae alitabasamu. Wakaruhusiwa kutoka na Fady akatafuta vijana wawili wanaofanya kazi kwenye kitengo hiko. Lakini ikiwa ni tofauti na zile wanazozifanya wao. Akawambia kuwa kuna mwili wa mtu ndani ya mgahawa wa hoteli hiyo unatakiwa uchukuliwe na uletwe humo ndani. Lakini wawe makini wasije wakasababisha hofu yoyote kwa mtu yoyote. Vijana hao wakatii na kuenda huko walipotakiwa waende.



Hilda akiwa ofisini kwake. Alikuwa na furaha muda wote baada ya kuondoa ile hofu iliyokuweko moyoni kwake pindi alipoonekana na mkuu wake amefanya jambo la kipumbavu kuwadhuru watu ambao wao mwanzo waliwaona hawana hatia yoyote. Alichukua simu yake na kumpigia Hemedy. Wakazungumza kidogo na Hilda akamuelezea tukio alilotoka kulifanya muda mfupi uliopita. Hemedy alishangazwa na taarifa hiyo. Ati kuna watu walikuwa na mpango wa kuja Tanga kuja kununua silaha. Kivipi? Mbona maelezo ya Hilda yanafanana na ya Inspekta Salum aliyoelezwa kiutata na Inspekta Kiulason? Akaficha mshangao wake kwa Hilda akijifanya hajui chochote kuhusiana na taarifa hiyo. Akampongeza kwa hatua aliyofikia. Mwisho wakaagana.



Hemedy majira hayo alikuwa nyumbani kwake. Akifikiria hili na lile. Hasa hasa ile taarifa aliyotoka kupewa hivi punde na Hilda. Hili jambo inabidi lisidharauliwe hata kidogo. Alijiwazia. Akachukua simu yake na kumpigia Salum. Akamtaka afike nyumbani kwake muda huo. Inspekta Salum akamuambia kuwa hapajui nyumbani kwake. Hemedy akamuelekeza hadi pale Salum alipokiri kupafahamu. Akamuambia kuwa ndani ya dakika thelathini atakuwa hapo. Simu ikakatwa Hemedy akimngojea Salum.



Nusu saa mbele. Kengele ya geti lake ililia kuashiria kuwa kuna mtu nje ya geti. Akatoka na kwenda kufungua. Alikuwa ni Inspekta Salum Mzanzibar. Wakaingia ndani wote na kukaa sebuleni. Hemedy Bhachu akamuelezea kila kitu juu ya taarifa aliyotoka kuipokea kutoka kwa Hilda. Hofu ikazuka kwa Inspekta Salum juu ya Hemedy. Huyu mtu ni nani? Alijiuliza akiwa na hofu na Hemedy. Lakini alipokumbuka kuwa aliwahi kuambiwa na IGP Taure kuwa Hemedy ni mpelelezi aliekuja kupeleleza vifo vinavyotukia kwenye mji huo. Akashusha pumzi ya ahueni na kumuambia.



“Leo nimepokea simu kwa mke wa Inspekta Kiulason akidai kuwa mume wake amerudi nyumbani lakini hamuelewi-elewi”



“Inabidi tuanzie nyumbani kwake kabla hatujaenda eneo la tukio” Hemedy aliongea na wakajianda kwenda nyumbani kwa Kiulason.







Walipofika. Waliingia ndani na kumkuta mke wa Kiulason akiwa amekaa kwenye sofa sebuleni akiwa na mfadhaiko uliojidhihirisha usoni. Kila mmoja akamsalimia kwa wakati wake na yeye akaitikia salamu hizo. Nao waka kaa kwenye masofa yaliyokuwepo hapo.



“Vipi shem. Huyu jamaa yupo?” Inspekta Salum alimuuliza kwa wasiwasi kidogo baada ya kuona sura ya mke wa Kiulason ikiwa si yenye tabasamu kama alivyodhani yeye. Maana yeye alitegemea kumkuta kawaida au akiwa na furaha baada ya mume wake kurudi nyumbani baada ya kutoonekana kwa siku iliyopita.



“Hayupo...” Akameza mate. Na kuendelea. “Hayupo. Ametoka tena bila kunisemeza chochote na sijui ameenda wapi” Mke wa Kiulason aliongea kwa masikitiko.



“Amekuja saa ngapi na ametoka muda gani?” TSSI 01 alimuuliza.



“Alikuja hapa kwenye majira ya saa kumi na moja alfajiri na akaingia ndani, akabadilisha nguo na kutoka tena. Ametoka muda si mrefu” Akajibu. Hemedy na Salum wakaangaliana na macho yao wakayahamisha kwa mke wa Kiulason.



“Sasa shem embu jaribu kumpigia simu” Salum alitoa wazo. Mke wa Inspekta Kiulason akajibu kuwa muda wote alikuwa akijaribu kumpigia lakini hakuwa akipatikana. Aliyaongea hayo huku akijaribu kuipiga tena namba ya mume wake. Majibu yakarudi yale yale kuwa namba anayoipiga haipatikani. Wote wakachoka. Wakamuaga na kumuachia maagizo kuwa muda wowote atakaporudi basi awajulishe maana kuna mazungumzo muhimu wanataka kuzungumza nae.



“Kwani mwenzenu ana nini mbona amekuwa hivi ghafla?” Mke wa Kiulason aliyasema hayo wakati huo Hemedy na Salum walikuwa tayari mlangoni kwaajili ya kuondoka. Salum akamjibu kuwa hata wao hawajui na hapo wapo katika harakati za kumtafuta yeye. Wakatoka nje baada ya kumpa moyo kuwa atapatikana na watamrudisha akiwa sawa kabisa.



Kipindi wakina Hemedy wakiwa wanatoka nje ya nyumba hiyo. Kule sebuleni mke wa Inspekta Kiulason alikuwa akijishauri jambo. Kwanini nisiwaambie ule utata uliotukia juzi? Huenda ikawa ile ndio imemfanya mume wangu kuwa katika hali ya kuchanganyikiwa. Kwanza sijajua ni kipi kilichotufanya tukawa kwenye lile jumba kule sijui ni wapi. Na hata mume wangu pia nilimuona mara moja tu kule na sijui pia alikuwa anafanya nini kule. Au na yeye walimteka kama tulivyoteka sisi? Aargh! Acha niwaambie hili huenda wakapata njia ya kumuweka sawa mume wangu.



Baada ya kujishauri hayo. Akatoka mbio kuwawahi kina Salum. Bahati nzuri aliwakuta wakiwa kwenye gari ndio wanajiandaa kuondoka. Akawaomba warudi ndani kuna jambo anataka kuwaeleza. Na wao wakashuka kwenye gari na kurudi ndani huku vichwani mwao wakiwaza ni jambo gani mwanamke huyo anataka kuwaeleza.



Wakakaa kwenye masofa wakiwa tayari kusikiliza hilo jambo wanalotakiwa kuelezwa. Mke wa Kiulason kwanza kabla ya mazungumzo. Akawaandalia chai tupu baada ya wageni hao kukataa vitafunwa. Na yeye akakaa kwenye sofa jengine tayari kuwaambia kila kitu kilichotokea siku tano nyuma.



“Mume wangu nahisi kuna jambo linamsumbua. Kwasababu kabla ya hilo tukio kutukia alikuwa sawa kabisa, ila baada ya kutukia tu ndio akawa kama hivi alivyokuwa sasa...” Akanyamaza kidogo. Macho yake akayahangaisha kwenye sebule hiyo kama ndio mara yake ya kwanza kuiyona. Alipoyatuliza macho yake. Akaendelea. “Siku hiyo tulikuwa wote hapa sebuleni. Nakumbuka ni majira ya saa tatu au nne za usiku. Ghafla tu wakaingia watu tusiowajua. Mikononi wakishika silaha za moto. Wakatushurutisha tuwe kimya na tusithubutu kufanya chochote maana walikuwa na uwezo wa kutudhuru kivyovyote vile. Sisi tukawa kimya. Sijui nini kilitukia. Ila nilipokuja kushtuka nilishanga nikiwa katika chumba fulani sehemu nisiyoijua. Nikiwa mimi na watoto wangu na mfanyakazi wetu mmoja. Wote tulishangaa kujikuta katika sehemu ile ambayo hata sasa ukiniuliza ni wapi sijui pia nitakujibuje. Tulikaa humo nadhani ni kwa dakika kama ishirini ama thelathini hivi. Ndipo mlango ukafunguliwa na akaingia mwanaume mmoja. Huyu alikuwa tofauti na wale waliokuja kututeka hapa. Akatuamuru tumfuate nasi bila kujua tupelekwapo. Tukamfuata nyuma nyuma hadi huko tulipoishia. Tuliishia kwenye chumba kimoja chengine. Huko tulimkuta mume wangu na mwanaume mwengine. Huyo mwengine hakuwa kijana bali alikuwa ni mzee. Nadhani walipanga kutukutanisha tu maana hatuku semezana chochote kile. Muda kidogo wakatuondoa tena na kuturudisha kule kwenye kile chumba tulichokuwamo mwanzo. Hadi hapo hatukuonana tena na mume wangu mpaka juzi tulipojikuta tena hapa katika namna ile ile tuliyoondokea. Sasa baada ya matukio hayo ndipo hali ya mume wangu ilipoanza kubadilika na kuwa kama hivi alivyokuwa” Mke wa Kiulason akahitimisha maelezo yake. Wote wakashusha pumzi ndefu na kuangaliana usoni.



“Hukumuuliza chochote Kiulason tangu mliporudishwa hapa kuhusina na tukio hilo?” Hemedy alimuuliza.



“Sikupata muda huo kwasababu hakutaka tuzungumze chochote. Yani hata masuala ya familia pia hakutaka tuzungumze kwa siku hizi mbili”



“Kwahiyo unasema huko mlipopelekwa haupajui?” Inspekta Salum alimuuliza.



“Sipajui shem. Yani ni kama ajabu hivi maana tulitolewa hapa tukiwa hatujielewi na tumerudishwa hapa pia tukiwa katika hali hiyo hiyo”



“Kwahiyo unadhani labda Kiulason atakuwa akipafahamu huko?” Salum alimuuliza.



“Sijajua. Labda mkimpata mumuulize yeye huenda akawa ana vingi anavijua kuhusiana na hilo tukio. Maana hata sasa bado sijajua tulipelekwa kule kwaajili gani”



Walizungumza machache kuhusina na hiyo mada iliyoanzishwa hapo. Baada ya hapo wakaaga tena kwa mara ya pili na kuondoka. Wakiacha chai kwenye vikombe ikiwa nusu nusu baada ya kuinywa kidogo tu. Wakatoka na kuingia kwenye gari.



“Mi nadhani kwanza tuingie kituoni tukamuangalie kama atakuwa kule” Inspekta Salum alitoa rai.



“Kwanini usimuulize askari yoyote ambae atakakuwepo kituoni muda huu kwenye simu kama amefika huko kuliko kuenda” Hemedy nae akatoa rai yake. Salum akaiunga mkono. Akatoa simu yake na kumpigia huyo anaetaka kumpigia. Wakazungumza machache na kukata simu. Akamgeukia Hemedy na kumuambia kuwa. Hadi muda huo hakuwa amefika kituoni tangu jana alipoondoka. Wakashauriana waende nyumbani kwa TSSI 01 wakajiandae na safari ya kwenda huko kwenye ghala la silaha ambapo walishapatilia mashaka huenda pakavamiwa siku hiyo au siku inayofuata.



Kule kwenye jumba la maficho. Mr Hanein alikuwa akiwapanga vijana wake kwa tukio ambalo wamepanga wakalifanye siku hiyo majira ya usiku. Walikuwa wakizungumza na kupanga ni jinsi gani ya kuingia mahala pale na kufanya walichopanga kukifanya. Wakapanga kwamba muda huo wa mchana waende ama aende mtu mmoja akachunguze mazingira mahala pale hadi pale muda pangwa utakapotimia wa kufanyika tukio.



Ikaonelewa atangulie Zinah kwenda kula rada huku wengine wakijianda na kusubiri muda wakafanye tukio. Zinah akaenda chumbani kwake kujianda na alipotoka alikuwa tayari kwa safari. Akachukua pikipiki kubwa aina ya XLR na kulidanda. Akatoka nalo kwa mbwembwe nyingi mahala hapo na kupotelea nje ya jengo hilo.



* *



Majira ya saa sita na dakika arobaini na mbili. TSSI 01 na Inspekta Salum Mzanzibar. Walikiwa ndani ya gari la Hemedy maeneo ya Sabasaba wakielekea Muheza. Gari ambalo amepewa na kitengo afanyie kazi. Hawakuwa kwenye mwendo mkubwa sana wala pia haukuwa mdogo. Gari hilo lilikuwa likitoa sauti nzito kama yale ya mashindano. Muda wote Inspekta Salum alikuwa akiushangaa uendeshajwi wa gari hilo. Ulikuwa ni wa tofauti na haya magari aliyoyazoea yeye.



Dakika kadhaa wakawa wamefika Muheza mjini. Wakakunja kulia wakiiacha stendi ya Muheza. Walinyoosha na njia hiyo. Kona mbili tatu wakawa wanakiona kituo cha Polisi kwa mbali. Kituo ambacho kwa maelezo waliyoyapata ni kuwa hapo ndipo lilipo ghala la silaha. Wakiwa hapo wamesimamisha gari. Pikipiki kubwa aina ya XLR likawapita na kupotelea kwenye kona iliyokuwa mbele yao. Hawakuitilia mashaka hata kidogo.



Baada ya kushauriana nini wafanye kwa wakati huo. Wakaonelea bora wapaki gari lao mbele kidogo palipokuwa na mgahawa. Sehemu ile ilionekana kuchangamka kutokana na wingi wa watu mahali hapo. Ila walichoamua wao ni kila mmoja kuwa kivyake kwa muda huo. Ili wasije wakaleta hofu kwa watu waliokuwepo hapo maana ni lazima wawe hapo kwa muda mrefu wakitegea windo lao wasilolijua kama linaweza likaja kwa siku hiyo ama laa!



Pamoja na kuhofia kuleta hofu kwa raia wa kawaida. Pia walihofia kugundulika mapema ikiwa kama kuna mtu amewekwa hapo kwaajili ya kula rada. Inspekta Salum akashuka kwenye gari na kuchepuka kwenye kipori kilichokuwa karibu na barabara hiyo. Na TSSI 01 Hemedy Aliendesha gari lake hadi pale karibu na ule mgahawa. Akatafuta sehemu nzuri na kupaki gari lake. Watu wote mahala pale walikuwa wakilishangaa gari lile. Hata Inspekta Salum aliekuwa ameshafika kwenye mgahawa ule pia alionekana kulishangaa gari lile.



Wakawa wanasubiri waone ni nani atakaeshuka kwenye gari. Baada ya dakika tano kupita, alishuka Hemedy. Alionekana ni Sharobaro ama bishoo flani. Kijana wa kileo anaeenda na wakati. Alivalia kileo zaidi huku nywele zake kichwani akiziachia timtim ila sio kwa namna ya kumkera mtazamaji. Zilikuwa katika mpangilioa mzuri japokuwa zilionekana zipo hovyo hovyo. Masikioni alichomeka visikilizia muziki.



Akapiga hatua ndogo ndogo ambazo hazikuonyesha majivuni yoyote ya ufahari. Alipofika ndani ya mgahawa ule. Alisalimia na baada ya salamu yake kupokelewa na vijana baadhi ya waliokuwa ndani ya mgahawa huo. Wengi walistaajabu. Inakuaje kijana kama huyo mwenye kuonekana kuwa poa kifedha aje kula katika mgahawa huo? Wapo waliopuuza na wapo walioendelea kuwa na mawazo kama hayo. Na yeye akaagiza ugali samaki huku Salum muda huo alikuwa na sahani iliyojaa wali na mchuzi akiendelea kula taratibu.



Mbali kidogo na mgahawa huo. Sehemu ambayo kulikuwa na kibanda cha magazeti pembeni yake kukiwa na kijiwe cha kahawa. Sehemu hiyo nayo kulichangamka kutokana na wazee wale waliokuwa wakinywa kahawa pale huku wakibishaniana maswala ya mpira na siasa. Zinah alikuwa amekaa kwenye moja ya mabenchi manne yaliyoizunguka meza ambayo juu yake kulikuwa na chupa kadhaa za kahawa na vikombe vingi vya kunywea kahawa. Alikuwa kimya huku akisoma gazeti lake alilolinunua jirani na hapo alipokaa. Mbele yake kukiwa na kikombe cha kahawa aliyokuwa akiinywa taratibu.



Hemedy alieshuka muda mchache uliopita kwenye gari alimuona. Ila hakumtilia mashaka sana japokuwa viulizo vya maswali kichwani kwake vilikuwa vingi kama wale watu waliokuwa ndani ya mgahawa wakati Hemedy akiingia pale. Akampotezea na kuendelea na uchunguzi wake. Mara kadhaa alikuwa akipiga jicho kituo kile cha polisi kilichokuwa mbali na pale alipo yeye. Ni kama mita mia mbili hivi umbali uliopo kutoka pale alipo hadi kituo kile cha polisi kilipo.



Waliomaliza kula ndani ya mgahawa ule wengi wao walionekana wakitoka nje na kwenda kutulia kwenye kijiwe chengine ambacho hiki kilijaa vijana zaidi. Walionekana wakicheza michezo wa drafti na keramu huku pembeni yao kwenye banda kubwa la wazi kukiwa na mchezo wa ‘POLTABLE’. Huko ndio kulionekana kundi la vijana wengi wakiwa humo. Wengine wakicheza huku wengi wao wakiwa ni watazamaji tu.



Inspekta Salum yeye ndie alikuwa wakwanza kumaliza kula kabla ya Hemedy. Akatoka nje ya mgahawa huo. Akaangalia huku na huko akitafuta sehemu ya kwenda kuweka pozi. Pale kwenye kijiwe cha kahawa aliona patafaa zaidi. Akapiga hatua na kuenda mahala pale. Alipofika alitoa salamu kwa watu waliokuwepo pale. Wote wakaacha walichokuwa wakikiongea na kumtazama yeye. Wakajibu salamu yake na kuendelea na mazungumzo yao. Salum akakaa kwenye benchi ambalo liliangaliana na lile alilokaa Zinah. Kila mmoja akiwa hajui nia ya mwenzake. Kila mmoja akamdhania mwenzake kuwa ni mwenyeji wa mtaa huo.



Dakika kumi mbele, Hemedy nae alimaliza kula. Akatoka baada ya kuwa ameshalipa. Akazungusha macho nje ya mgahawa ule na kumuona Salum akiwa amekaa kwenye kijiwe cha kahawa. Yeye akapiga hatua kuliendea lile banda ambalo ndani yake kulikuwa na vijana waliokuwa wakicheza mchezo wa ‘Poltable’. Akatoa salumu tena na kutafuta sehemu nzuri ambayo itamfaa kwa uchunguzi wake. Baada ya mchezo ule uliokuwa ukiendelea pale kuisha. Akaomba na yeye acheze. Akalipa mchezo na akataka mtu yoyote acheze nae. Mchezo ukaanza baada ya kujitokeza mtu wa kutaka kucheza nae.



Mara kadhaa alikuwa akichangia mada zilizokuwa zikiongelewa na vijana wale. Wote wakajikuta wakimzoea kwa muda mfupi baada ya kuiondoa ile dhana waliokuwa nayo mwanzo juu ya mtu huyo. Na sasa wote wakamuona wa kawaida. Alicheza michezo karibia mitatu. Akaacha huku akiwaachia vijana wengine waendelee kucheza baada ya hela yake aliyoitoa kumtaka kuendelea kucheza. Akatafua sehemu mule mule bandani na kukaa. Sehemu ambayo ilimuwezesha kukiona kituo cha polisi na kukiona kijiwe kile alichokuwa Inspekta Salum.



‘Umegundua nini hadi sasa?’ Inspekta Salum alipokea ujumbe huo kwenye simu yake kutoka kwa TSSI 01. Akajibu hakuna alichogundua na hadi majira hayo anaona pako sawa tu. ‘Embu muangalie vizuri huyo mtu aliekuwa mbele yako. Mara kadhaa anaonekana kutotuliza macho yake sehemu moja. Anaonekana kama kuna kitu anakichunguza hivi’ Salum akapokea ujumbe mwengine kutoka kwa Hemedy baada ya ule wa mwanzo kuujibu. Akampiga jicho Zinah na kumuona akiwa makini zaidi na sehemu kilipo kituo cha polisi. Na yeye akaangalia huko kwa kificho zaidi. Akaona askari tu waliokuwa wakipishana kwenye kituo kile.



Ujumbe mwengine kwenye simu yake ukaingia. ‘Hushangai hilo gazeti analolisoma? Ni muda sasa tangu nimuone akilisoma. Inamaana hamalizi tu? Kuwa nae makini maana nishaanza kumtilia shaka’ ujumbe ukamalizika hivyo. Ni kweli hata yeye alivyo chunguza vizuri. Ni muda sasa tangu amekwenda kwenye kijiwe hicho. Ni kama dakika arobaini na kuendelea tangu amefika hapo. Na alimuona mtu huyo akilisoma gazeti hilo. Huenda ikawa ni kweli? Akajiuliza.







Huenda ikawa ni kweli? Akajiuliza. Hakupata jibu!. Akawa makini na Zinah huku Zinah asiweze kumtilia shaka hata kidogo Inspekta Salum.



* *



Majira ya saa mbili kasoro usiku. Mtaa ule ulianza kupoa. Vijana walianza kuondoka mmoja mmoja na kupotelea pasipojulikana. Giza zaidi ndio lilitawala eneo hilo. Mwangaza ulikuwa ni hafifu uliotoka kituo cha polisi na baadhi ya nyumba chache zilizokuwa eneo hilo.



Pale kwenye banda la mchezo wa ‘Poltable’. Vijana waliokuwa wakicheza na wengine wakiwa ni watazamaji. Pia walipungua. Walibakia wachache kiasi. TSSI 01 hakuonekana maeneo yale na asijulikane ni wapi alipo. Hata lile gari lake alilokuwa amelipaki karibu na ule mgahawa pia halikuwepo. Hakuna aliejali wala kuhoji. Watu walidhani ni mpita njia tu maeneo hayo.



Kwenye kile kijiwe cha kahawa. Wazee waliendelea kupiga soga zao. Inspekta Salum hakuwepo. Zinah nae pia hakuwepo. Pia hakuna aliejali wala kuhoji kutokuwepo kwa vijana wale wawili wageni machoni mwao.



Kule kituoni. Kulibaki askari waliokuwa zamu siku hiyo ya lindo la kituo. Waliokuwa wakizunguukazunguuka kituoni hapo huku wakiwa na silaha za moto. Kiufupi hali ilikuwa shwari kama siku zote. Ni kama vile hakukupangwa kufanyika tukio mahala hapo. Kila mmoja alikuwa na shuhuli zake alizozoea kuzifanya kila siku.



Majira ya saa nne usiku. Majira hayo mtaa huo ulikuwa umepoa sana. Watu wote walikuwa wameshatawanyika mahala hapo. Mbali kabisa na eneo lile. Gari aina ya Toyota PickUp ilipaki kando ya barabara inayoelekea eneo lile lenye kituo kile cha polisi. Wakashuka watu watano ambao sura zao waliziziba na soksi kubwa kwaajili ya kuziba uso. ‘Max’ Mikononi mwao walikuwa wamebeba silaha za moto. Kila mmoja akachepuka kwenye vichaka vilivyokuwa karibu na barabara hiyo. Ndani ya gari. Nyuma ya usukani. Kulikuwa na Queen ndie ambae alikuwa dereva wa gari hilo. Akarudisha gari nyuma na kuliweka sawa tayari kwa safari yoyote ya ghafla.



Nyuma ya kituo kile ambapo kulikuwa na nyumba za kota za polisi. Watu wawili waliojiziba nyuso zao kwa soksi walikuwapo huko. Wakapeana ishara wanazozijua wao na kila mmoja akaizunguka nyumba hiyo kwa upande wake. Punde wakawa wanatazamana na uzio wa seng’enge uliozungushiwa kwenye kituo hicho. Muda huo wakiwa wameshazivunja taa zilizokuwepo nje na nyuma ya nyumba zile. Giza liliongezeka kwa kiasi kikubwa na kuwapa nafasi nzuri ya kufanya kile walichotaka. Watu hao walikuwa ni Pijo na Deva.



Ubavuni mwa kituo kile. Sehemu ambayo Robart alipenya kwenye uzio ule wa Seng'enge na kuzama ndani siku iliyopita alipokuja kufanya uchunguzi. Kulikuwa na watu wawili waliofananiana na wale waliokuwa kule nyuma kwa mavazi. Maana wote walivaa mavazi meusi marefu huku kwenye nyuso zao wakiziziba na soksi. Hawa nao walikuwa wamejibanza kwenye miti mirefu wakisoma ramani ya eneo hilo. Hawa walikuwa ni Robart na Atu.



Kule ubavuni mwengine mwa kituo kile. Kulikuwa na watu wawili pia. Walikuwa wamejibanza kwenye jengo dongo lililotumika kama sehemu ya bomba la kuchota maji ya kunywa kwenye mtaa huo. Nao walikuwa kimya wakisoma ramani ndani ya kituo hicho. Hawa walikuwa ni Ata na Zinah. Katika mpango huo. Hawakutaka kuingilia na upande wa mbele wa kituo hicho. Walitaka kufanya uvamizi upande wa nyuma ilhali askari waliokuwa upande wa mbele wasijue chochote kinachoendelea.



Kwenye mti mrefu wa muembe uliokuwa karibu na kituo hicho. Juu kwenye mti huo kulikuwa na watu wawili waliokuwa wamejituliza kimya wakiusoma mchezo mzima uliokuwa ukifanywa na watu wale sita kule chini. Watu hao walikuwa ni Inspekta Salum na Bhachu TSSI 01. Wote walijikuta wakitabasamu baada ya kuona kumbe walichokuwa wakikidhania kimetukia kweli. Ama kweli subira huvuta heri. Walikuwa wamekata tamaa baada ya kukaa kwa muda mrefu juu ya mti huo pasi na kuona chochote cha kutilia shaka.



Walipanda saa ngapi juu ya mti huo? Haikujulikana!.

Hata pale Zinah alipowapotea kwenye kile kijiwe cha kahawa pia hawakutambua ni uelekeo upi aliuchukua. Ila furaha yao kwa sasa ni kuona mtego wao umetimia. TSSI 01 Alifungua begi lake ambalo mwanzo aliliweka mgongoni mwake. Humo kulikuwa na vifaa vichache vya kazi. Akatoa visu vitatu na kuvipachika nyuma ya mgongo wake kwenye nguo aliyoivaa. Mara hii hakuwa tena na zile nguo za ‘kibishoo’ alizokuwa nazo mchana wa siku hiyo.



Akachomoa bastola ndogo mbili na kuzipachika ndani ya nguo aliyoivaa upande wa mbele. Haikujulikana vitu hivyo vilienda kujishikiza kwenye nini ila vilikaa bila shida. Akatoa na soksi kubwa kama walizokuwa nazo wale watu sita na kuivaa usoni. Akafunga begi na kumuachia Inspekta Salum. Akawa tayari kuteremka kule juu. Alidandia matawi ya mti huo kwaajili ya kushuka chini. Tawi moja, la pili alirudi tena juu kule alipo Salum. Akazitoa zile bastola na kumkabidhi Salum. Akamuambia kuwa hizo silaha zitamletea kelele kwenye kazi yake huko chini. Zaidi ya hapo alimuambia kuwa amtolee visu viwili vyengine kwenye lile begi.



Inspekta akalifungua lile begi kwaajili ya kutoa visu. Chaajabu. Hakuona chochote ndani ya begi hilo zaidi ya kukutana na zile nguo alizokuwa nazo mchana Hemedy. Akamuangalia kwa mshangao. Hemedy akamuelewa. Akatabasamu na kulivutia kwake lile begi. Akaingiza mkono na kutoka na visu viwili. Akavichomeka kwenye viatu alivyovivaa kila kimoja na mguu wake. Akarudisha zile bastola kwenye begi na sasa akawa tayari kushuka chini.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Akadandia matawi ya mti huo. Alifananiana na nyani jinsi alivyokuwa akicheza na matawi hayo kimya kimya bila kutoa mchakacho wa sauti kubwa. Muda huu alikuwa chini akitembea kwa umakini kuziendea zile nyumba za kota. Upande ambao alikuwapo Pijo na Deva . Kule juu ya mti Inspekta Salum alibaki kusikitika kwa mshangao huku akitabasamu kutokana na uajabu wa Hemedy. Akaweka bunduki yake sawa kwaajili ya kuwa mlinzi wa Hemedy popote pale aendapo. Sehemu hiyo ilimuwezesha kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea ndani ya kituo kile na nje ya kituo.



Kule nyuma ya kituo ambapo kulikuwa na jengo ambalo lilidhaniwa kuwa ndio ghala la silaha. Pijo na Deva majira haya walikuwa ndani ya uzio baada ya kuzikata zile seng'enge. Walikuwa wakinyata kimya kimya kila mmoja upande wake akiangalia mazingira. Huruma zimuendee askari aliekuwa upande wa Pijo akiranda randa bunduki yake ikining'inia mgongoni. Alionekana akitafuta mahala pazuri pa kutoa haja ndogo.





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog