Search This Blog

Saturday 5 November 2022

SAUTI YAKE MASIKIONI MWANGU - 5

 







    Simulizi : Sauti Yake Masikioni Mwangu

    Sehemu Ya Tano (5)





    “Hilo niombi?”

    “Ndiyo ni ombi; na itapendeza kama jibu litakuwa ni ndiyo.” Akasema Leehom.



    Mkuki alitazamana na Mei Lee kana kwamba walikuwa wakiulizana kuhusu kukubali ombi la jamaa huyo; na kupitia macho yao wakaonekana kukubaliana jambo ambalo ni wenyewe tu walielewa—hata hivyo  walikubali ombi la Leehom.

    Leehom alikuwa ni msanii wa muziki mkubwa zaidi nchini China, amabye pia alikuwa ni maarufu hata nje ya taifa hilo. Tayari alishawahi kufanya kazi na wasanii wakubwa wa muziki hasa kutoka Marekani; amewahi kufanya kazi na mtu kama marehemu Michael Jackson na wengine wengi. Yeye alipendezwa sana na jinsi ambavyo Mei Lee alikuwa akiimba lakini zaidi alijikuta anatamani kuwa karibu naye mara baada ya kufanyiwa upasuaji wa kusafisha uso. Alivutiwa sana na jinsi ambavyo uso wa Mei Lee unaonekana bila yale makunyanzi; hivyo alikuwa na mpango wa wa hata kufanya naye kazi pamoja.

    Yote hayo Leehom alikwenda kuyazungumza walipofika kwenye kasri lake, wakiwa wanapata chakula cha jioni.

    “Nataka shindano likiisha nifanye kitu kikubwa na wewe, nataka nikutangaze duniani.” Alimwambia na alifafanua zaidi.

    Hiyo ilikuwa ni kama ngekewa kwa Mei Lee, msichana ambaye kwa kipindi chote alikuwa akiota kuwa msanii mkubwa, kuzungumza na dunia kupitia sauti yake aitosayo ndani ya mashahiri matamu ayaundayo kwa kutumia akili yake ya kawaida lakini ya pekee. Alitamani hata shindano liishe leo, sasa hivi, ili apate nafasi ya kufanya kazi na Leehom na amtangaze duniani kote kama ambavyo yeye alikuwa akifahamika.

    Kwa upande wa Mkuki pia aliona hiyo ni heri na neema inazidi kuja upande wake kwa sababu kama Mei Lee atafanikiwa kwa kiasi kikubwa namna hiyo basi ni wazi kwamba yeye atakuwa mtu wa kwanza kufaidi matunda ya mafanikio hayo.

    Basi baada ya chakula Leehom aliwachuka hadi kwenye maegesho ya magari ya nyumbani kwake, huko kulikuwa na magari yapatayo sita ya kifahari lakini alichagua moja ambalo alipanga kulitumia kuwarejesha nyumbani kina Mei Lee kwa kuwaendesha yeye mwenyewe.

    Ilikuwa hivyo, aliwarudisha huku safari nzima wakizungumza na kucheka; walizoena naye mapema sana kwa sababu Leehom alikuwa ni mzungumzaji sana na mcheshi.

    Aliwafikisha hotelini, akaawaacha hapo na yeye akarejea nyumbani huku akimtaka Mei Lee anapopata muda awe anamtafuta kwa ajili ya kumnoa na kumfua zaidi kama sehemu ya maandilizi ya fainali ya mashindano yale.





    **********************************

    Mei Lee na Mkuki walikuwa ndani ya chumba cha hoteli walimopanga, punde walisikia hodi mlangoni, Mkuki akasimama kwenda kufungua. Alikutana na mgeni, mwanamke wa kichinia ambaye hakuwa akimfahamu.

    “Karibu.” Alisema Mkuki.

    “Asante. Naitwa Yin, ni afisa mratibu matangazo wa kampuni ya fenicha ya Beijing, nina shida na Mei Lee. Naweza kumuona.” Akajitambulisha mwanamke huyo na kuweka wazi adhma ya ujio wake.

    “Ndiyo.  Karibu ndani.” Akasema Mkuki huku akimpisha. Yule mwanamke akaingia na hapo Mkuki akafunga mlango.

    Dada huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Yin alimuona Mei Lee mara tu baada ya kuingia ndani, akamsogelea na kumsalimu kwa kumpa mkono kisha akaelekezwa akateti kwenye kiti; akafanya hivyo.

    “Karibu.” Mei Lee akasema, kwa wakati huo Mkuki alikiwa ameshakuja, ameketi pembeni yake.

    “Asante Mei Lee,” akasema yule msichana na kujitambulisha zaidi kama alivyofanya kwa Mkuki na akaendelea. “Kampuni yetu inataka kufanya tangazo kwa ajili ya mtindo mpya wa fenicha zetu, kwahiyo tulimtafuta Leehom ili tumtumie katika tangazo hili lakini yeye alikataa na akapendekeza tukutumie wewe; na kimsingi vigezo unavyo; kwahiyo nimekuja hapa ili tufikie makubaliano ya awali, tujue kama na wewe unapenda kufanya kazi na sisi kama ambavyo sisi tunapenda kufanya na wewe. Na kama jibu litakuwa ndio, basi tunaweza kutoka sote, mimi na wewe, twende ofisini tukaweke sawa baadhi ya mambo kisha tupange ni lini tutafanya hilo tangazo kabla ya siku ya fainali ya shindano lako.” Akasema Yin.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mei Lee na Mkuki wakatizamana kana kwamba walikuwa wakiulizana kitu kuhusu taarifa ile na kupitia ishara za macho Mkuki akamshauri Mei Lee akubali.

    “Sawa. Hakuna shida.”

    “Kwahiyo tunaweza kwenda?” akauliza Yin kuthibitisha.

    “Sawa.”Akajibu Mei Lee kisha akamgeukia Mkuki na kumuuliza na kumuuliza kama watakwenda pamoja na Mkuki akajibu ndiyo.

    “Samahani Mei Lee. Hili jambo ni la kiofisi zaidi, kwahiyo ni vyema kama tutaenda na wewe peke yako.” Ghafla Yin akaingilia mazungumzo yao kina Mei Lee na kutoa taarifa ya namna hiyo.

    “Kwanini!? Hapana haiwezekani. Kwani tunakwenda kujadili nini  ambacho mpenzi wangu hastahili kukisikia?” akahoji Mei Lee na swali lake lilionesha kumkata maini Yin ingawa bado hakuonekana kuridhishwa na kwamba waondoke pamoja na Mkuki.

    Mtoto wa kiume aligundua hilo, akapiga mahesabu ya haraka, akagundua kwamba hata kama Mei Lee atakwenda peke yake pesa atakayolipwa kwa ajili ya kufanya tangazo hilo haitapungua; kwahiyo  kimantikki yeye hakuwa wa muhimu sana kwenye suala zima la maslahi. Haraka akatumia akili hiyo, akamtaka Mei Lee akubali bila kinyongo huku akimuhakikisha kwamba hakuna kitakachoharibika, na kwa sababu binti alikuwa akimsikiliza sana Mkuki hakuweka kipingamizi katika hilo, alifanya kama alivyoelekezwa.

    Basi baada ya pale Yin akamchukua Mei Lee mpaka nje ya hoteli yao ya gharama za chini waliyokuwa wakiishi. Huko kulikuwa na gari safi ya kifahari sana ikiwasubiri kwa ajili ya safari. Walipoifikia wakaingia na safari ya kuelekea zilipo ofisi za kampuni ya fenicha inyomuhitaji Mei  Lee katika tangazo lao ikaanza.

    Ilikuwa ni safari iliyogharimu robo saa tu, walipofika wakashuka garini na Yin akamuongoza Mei Lee ndani ya jengo ambalo bila shaka ndilo lilikuwa  na ofisi za kampuni yao. Alimpeleka hadi ndani ya ofisi moja kubwa ya kisasa, na mara tu baada ya wao kuingia  humo Mei Lee alimuona Leehom kwenye moja ya picha kubwa zilizobandikwa ukutani; jambo hilo lilimshangaza lakini alijitahidi kujiaminisha kwamba huenda picha zile zilikuwa pale kwa sababu Leehom alikuwa ni msanii mkubwa na maarufu hivyo mtu yeyote aliweza kuweka picha yake ofisini.

    “Karibu.” Alisema Yin huku akimuelekeza Mei Lee aketi kwenye kochi; binti akafanya hivyo.

    “Naomba dakika moja nakuja.” Akaomba Yin kisha akatoka nje akimuacha Mei Lee peke yake pale kwenye kochi, mle ofisini.

    Punde mlango ilifunguliwa, akaingia Yin, lakini hakuwa mwenyewe safari hii, alikuja na mtu mwingine—alikuwa amekuja sambamba na Leehom. Mei Lee akamtazama, wakatazama, Leehom akatabasamu kidogo huku akimsogelea binti pale kwenye kochi na alipomfikia akampa mkono wa salamu.

    “Karibu.” Akasema Leehom huku akiendeleza lile tabasamu lake, binti akampa mkono pia kama ishara ya kuipokea karibu yake huku na yeye akionesha tabasamu kwa mbali.

    “Nawaacha.” Mara Yin akawaaga, kisha akatoka ofisini humo na kumuacha Mei Lee na Leehom, huku Mei Lee asielewe nini kinachoendelea, kwa sababu aliambiwa anapelekwa kwenye makubaliano ya kufanya tangazo na sio hiki anachokiona—lakini alijitahidi kuwa mpole kusubiria matokeo ya kile kinachoendelea.

    Leehom akamuachia mkono Mei Lee baada ya kumganda kwa sekunde kadhaa, kisha akazunguka na kwenda kuketi kwenye kiti kukubwa cha kibosi kilichopo nyuma ya meza ya kisasa ya ofisi hiyo ambayo juu yake  ilikuwa na kompyuta na makabrasha mengi.

    “Karibu Mei Lee. Hapa ni ofisini kwangu pia.” Akasema Leehom, jambo hilo lilitabiriwa na Mei Lee lakini aliigiza kushangaa ili aonekane kwamba hakutarajia kupelekwa hapo na hata alipolekwa hakugundua kwamba kuna uhusiano wa aina yoyote na Leehom.

    “Asante.” Akajibu Mei Lee.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Najua labda unaona kila kitu hakifanani na jinsi ambavyo Yin amekueleza. Lakini ilivyo ni kwamba mimi ndiye mmiliki wa Beijing Furniter na nimependa kufanya kazi na wewe; ningependa utokee kwenye tangazo la fanicha za mtindo mpya ambazo tutaziingiza sokoni hivi karibuni.” Akafafanua kwa uzuri Leehom huku akijizungusha-zungusha kwenye kiti chake cha kunesanesa.

    Kampuni ya Beijing Furniter ilikuwa chini yake, yeye ndiye alikuwa mmiliki mkuu na ndiye aliyekuwa na mamlaka ya kufanya vyovyote atakavyo, na ndiyo maana hata alikuwa na nguvu ya kumchagua Mei Lee katika tangazo hilo bila kupingwa na mtendaji yeyote aliyemuajiri.

    Hata hivyo kumchagua Mei Lee hakukuwa ni bure-bure tu, isipokuwa moyo wa Leehom ulikuwa ukifurukutwa ndani kwa ndani na jambo fulani la kiutu uzima zaidi, jambo zito mno. Hata hivyo hakutaka kuruka hatua hata moja katika kulifanikisha, kwahiyo ili kuhakikisha ujumbe unafika mahala pake kwa utulivu na usahihi aliamua kuanzia mbali namna hiyo.

    *****************************



    ngumzo ya hapa na pale kuhusu lile tangazo Mei Lee alikubaliana na Leehom kwamba atafanya wakati bosi Leehom yeye aliahidi kumwaga pesa nyingi sana kwa mwanadada huyo kama malipo ya kazi hiyo.



    Ili kutimiza ahadi, mara tu baada ya mazungumzo Leehom akanyanyua simu ya mezani na kumpigia Yin, akamuomba amuandalie Mei Lee hundi ya malipo ya kiasi kikubwa cha pesa na alipomaliza kutoa maagizo alimrudia Mei Lee.

    “Tutatoka hapa nitakupeleka kwa watu watakaokutengezea nguo kwa ajili ya tangazo, na kesho kutwa asubuhi utapigwa picha za video za tangazo.” Akaeleza Leehom huku akionekana kujipa majukumu mengi ambayo hata hakuwahi kuyafanya kwa kazi nyingine za kufanana na hiyo zilizowahi kufanyika kipindi cha nyuma.

    Baada ya pale Leehom alimchukua Mei Lee hadi kwenye gari ile ile waliyokuja nayo akiwa na Yin; na walikuwa wao wawili tu pamoja na dereva. Basi mwendo ukaanza kuelekea kwa mbunifu wa mitindo maarufu nchini China aitwaye Hannuo. Huko Mei Lee alifanyiwa vipimo kwa zaidi ya dakika 30 na baada ya hapo kazi ikawa imekamilika kwamba binti angeweza hata kurejea nyumbani.

    Lakini Leehom hakutaka kuzitumia vibaya nafasi za kuwa karibu na Mei Lee namna hiyo, alihakikisha anautumia muda wake kwa ufasaha ili ikiwezekana atimize lengo lake ndani ya muda mfupi. Ili kufanikisha hilo alimuomba Mei Lee kwamba kabla hajamrejesha nyumbani ampelekee kwenye mgahawa, wapate mlo wa mchana wa pamoja kisha amrejeshe hotelini kwao; na kwa kuwa binti hakuwa akifahamu chochote, au labda kuhisi ile adhma ya Leehom alimkubalia kwa wepesi sana.

    Basi Leehom akamtaka dereva awapeleke kwenye moja ya migahawa mikubwa ya jijini Beijing; mgahawa uitwao ‘Luminax’ ambao wenyewe ulikuwa ukishika nambari mbili kwa kupika vyakula vitamu sana na vya gharama kubwa. Huko Mei Lee alinunuliwa ‘msosi’ wa maana, chakula ambacho dhumuni lake kuu si kushiba tu, bali pia kufanyiza tafrija ndani ya kinywa cha mlaji.

    Lakini haikuwa chakula tu, pia Leehom na Mei Lee walizungmza mengi mno, na kwa muda ule mfupi tu walianza kuhisi kuzoena sana hata wakajikuta soga walizokuwa wakipiga zilitawaliwa sana na vicheko  vikubwa.

    Baada ya yote hayo Leehom alimchukua Mei Lee na kumrejesha nyumabni, hakuwa akiendesha yeye gari hivyo hata njiani pia walipata nafasi ya kuzungumza mengi kwa uhuru pia.

    **************************************

    Muda uliyoyoma kwa Mkuki, alipigwa na sintofahamu kwa sababu kwa jinsi alivyokuwa akifikiria yeye ni kwamba zoezi lile lingefanyika mara moja kisha Mei Lee angerudishwa nyumbani, lakini mambo yalikuwa kinyume chake.

    Wote wawili hawakuwa na simu hivyo haikuwa rahisi kumtafuta; mtoto wa kiume alibaki akiugulia maumivu ya wivu mle chumbani hata asijue nini cha kufanya.

    Punde mlango ulifunguliwa, akaingia Mei Lee mwenye furaha kweli kweli. Akapita moja kwa moja hadi kitandani alipokuwa Mkuki, akamrukia na kumkumbatia na kumbusu huku akisema maneno ya kuthibitisha kwamba walikuwa wanaelekea kuachana na umaskini lakini mwenzake hata hakutaka kuwa mshabiki katika jambo hilo—yeye alikuwa akifikiria ni kwanini Mei Lee alichelewa sana kurejea nyumbani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mbona umechelewa?” Akauliza Mkuki.

    “Nilikwenda ofisini kwao, kumbe Leehom ndiye bosi wao, basi tukafanya mazungumzo pale, kisha Leehom akanichukua kwenda kupima nguo kwa ajili ya tangazo, halafu tukaenda kula, kisha akanirejesha hapa.” Akaeleza Mei Lee na kuongoza. “Mkuki, Leehom ni mtu safi sana. Nimekaa naye kwa muda mfupi tu lakini nimegundua hilo.” Akasema Mei Lee; yeye hakuwa akiona tatizo lolote juu ya kila kitu kilichokuwa kinaendelea.

    Mkuki alibaki kimya huku akitafunwa na hasira ndani kwa ndani; maelezo na sifa alizozitoa Meu Lee juu ya Leehom zilimkera, zilimuumiza na kumfanya ahisi wivu uliopitiliza.

    **************************************

    Siku ya kutengeneza tangazo iliwadia, Mei Lee akafuatwa asubuhi na hata  sik hiyo aliondoka peke yake bila Mkuki. Lakini leo mambo yalikuwa tofauti kwa Mkuki, hakuwa mwenye furaha kama ilivyokuwa siku ya kwanza Mei Lee alipofuatwa na Yin, na yote hiyo ni kwa sababu tayari alianza kuingiwa na uoga, alikuwa na mshaka kwamba huenda kulikuwa na maagano fulani ya siri kati ya mpenzi wake na Leehom.

    Basi binti alichukuliwa hadi studio litakapofanyika zoezi za upigaji picha za video za tangazo, huko Leehom alikuwepo kama kawaida. Kazi ya uchukuaji picha hizo iligharimu saa tatu tu na huwezi kuamini kwamba Mei Lee alifanya vizuri mno kama ambavyo muelekezi (Director) alitaka iwe.

    Baada ya pale Leehom alimchukua Mei Lee lakini kwa hiari; alimuomba kwa siku hiyo akamtembelee kwake, kwenye jumba lake jipya, si lile ambalo walikwenda akiwa  na Mkuki; na kisha atamrejesha nyumbani.

    Mei Lee hakuwa na tatizo juu ya hilo, kwa mtazamo wake yeye aliomuona Leehom kuwa ni mwanamume mkarimu sana mwenye lengo la kumsaidia kumvusha daraja la maisha—kutoka umasikini uliomlea kwenda utajiri anaouota.

    Kutoka pale studio lilipokuwa likifanyika zoezi la uchukuaji picha za tangazo hadi nyumbani kwa Leehom ilikuwa ni safari ya dakika kumi na tano tu; jumba jipya la Leehom lilikuwa huko Henshuu, kitongoji ambacho kilikuwa ni makazi ya wanasiasa wakubwa, wasanii maarufu nchini China na wafanyabiashara mamilionea—binti alipelekwa huko. Nakwambia alichanganyikiwa na kila jumba alilokuwa akiliona, hata akashikwa na wasiwasi ya kwamba inawezekana ile ilikuwa ni safari ya kuelekea paradiso.

    Punde gari yao ikasimama mbele jumba la Leehom; jumba kubwa la kifahari lililojengwa kwa mtindo unaowapendeza matajiri wengi nchini China. Jumba hilo lilivutia mno, liliupendeza moyo wa Mei Lee na hata macho pia kiasi kwamba alihisi kutamani kuwa mmiliki wa kasri lile kwa namna yoyote ile—hata kwa kupewa kama zawadi.

    Basi baada ya pale lango kubwa la jumba hilo likafunguliwa, Leehom akaingiza gari yake ndani na kwenda kuituliza kwenye maegesho maalumu, kisha akateremka, akazunguka na kwenda kumfungulia mlango Mei Lee pia.

    “Tumefika.” Akamwambia huku akiachia tabasamu kubwa.

    Binti akateremka polepole huku bado akiendelea kushangaa huku na huko, Leehom akafunga mlango kisha akamshika mkono na kumuongoza kuelekea ndani zaidi ya jumba lile.

    Walipoingia ndani ndo Mei Lee alizidi kupata wazimu, sebule ya jumba lile ilikuwa ni zuri hakika, ilikuwa na kila kitu chenye kupendeza macho na kumfanya mgeni ajihisi mwenye thamani kubwa kuwa pale.

    “Karibu. Keti hapa.” Alisema Leehom kumwambia Mei Lee huku akimulekeza kwa mkono ni wapi pa kuketi. Binti akafanya kama alivyoombwa, akaketi taratibu huku bado akiigeza shingo yake huku na huko ili ayaridhishe macho.

    Leehom naye akaketi, kisha baada ya pale alifanya npango wa wote wawili kupata kinywaji laini kwa ajili ya kusindikiza mazungunzo yao—alimuagiza kijakazi wake kuhakikisha hilo linfanikiwa.

    Basi baada ya kuletewa vinywaji yalizungumzwa mengi sana siku ile lakini Leehom hakudiriki kuweka wazi hisia zake kwa Mei Lee. Alitaka kutumia vitendo tupu, au kama ni maneno basi yawe mwishoni sana, kipindi ambacho binti atakuwa tayari amegundua kila kitu kupitia matendo yake. Alikuwa akimpenda, tena mapenzi kweli, sio kumtamani au kumchezea, lengo lake lilikuwa ni kumuoa mara moja pindi tu binti atakapomuelewa na kumkubali.

    Usiku uliingia, hapo ndipo Leehom aliamua kumchukua Mei Lee kwa ajili ya kumrejesha nyumbani. Walitoka hadi nje, hadi kwenye maegesho ya magari. Huko akachukua pikipiki kubwa ambalo alipanga kulitumia siku hiyo. Basi mwanamume akapanda, binti akapanda nyuma pia na kumshika kiuno Leehom huku akimlalia kidogo kwa mgongoni; si kwamba alidhamiria kufanya hivyo isipokuwa pikipiki lenyewe lilimlazimisha kwa jinsi ambavyo sehemu ya nyuma ya ilivyokuwa imeinuka—hapo wote wawili walikuwa wamevalia kofia ngumu kichwani.

    Safari ikaanza, Leehom aliendesha kwa kasi kubwa sana kama ambavyo ilikuwa kawaida yake. Yeye alikuwa ni chizi wa vyombo vya moto, alipenda magari mazuri ya michezo na mapikipiki pia na ndiyo maana alikuwa akimiliki mashine hizo nyingi huku akizitumia kwa kuzibadilisha mara kwa mara.

    Mwendo alioendesha ulifupisha mno safari, walifika nje ya hoteli aliyokuwa akiishi Mei lee na Mkuki, akasimamisha hapo na binti akateremka, kisha akavua na Helmet na kumkabidhi Leehom. Mwanamume akaipokea huku akimtazama jicho kavu Mei Lee, uso kwa uso bila kupepesa.

    “Vipi?” Akauliza Leehom.

    “Vipi vipi?” Akauliza  Mei Lee huku akitabsamu.

    “Kuna kitu nakiona... machoni mwako.”

    “Kitu gani?”

    Akashusha pumzi Leehom kabla ya kuzungumza. “Macho yako yanambia unataka niseme nilichokibeba moyoni.”

    Akacheka kidogo Mei Lee. “Tufanye ni kweli....  Haya nataka kusikia ulichokibeba moyoni.” Akazungumza Mei Lee; yeye kila kitu alichukulia masihara kwa sababu walishazoeshana kutaniana namna hiyo.

    “Natamani kukubusu kabla sijaondoka.” Akasema Leehom kwa kujiamini. Mei Lee akamtazma usoni asiamini kile alichokisikia, na si kile alichokisikia tu, bali kwa jinsi ambavyo Leehom alikizungumza kwa utulivu na hisia.

    Hapo kimya kikachukua nafasi, kimya cha zaidi ya sekunde kumi. Si Mei Lee si Leehom, wote walivipa likizo vinywa vyao huku wakitazama machoni.

    “Naweza?” Akaamua kuuliza Leehom, lakini binti hakumjibu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Basi alichoamua ni kuteremka kwenye pikipiki, akaweka ‘helement’ yake aliyokuwa ameishika mkononi kwenye mkono wa kushoto wa ‘motosaiko’ hiyo kisha akapiga hatua mbili kumuelekea Mei Lee—wakawa umbali mdogo sana. Akamshika mikono yote miwili, akamtazama usoni kwa jicho lililonena, jicho lililozungumza yaliyomoyoni mwake hasa kuhusu lile ombi lake la kumbusu kabla ya kuondoka.

    Basi taratibu Leehom alianza kujisogeza karibu na Mei Lee ili ambusu kinywani, binti aliishia kufumba macho tu, aliishiwa nguvu, alishindwa kupinga lolote juu ya kila kilichokuwa kinaendelea ingawa alikuwa akifahamu kwamba lile halikuwa ni jambo la kiungwana.

    Lakini kabla hata ya Leehom hajafanikisha lengo alisukumwa ghafla na kuangukia huko; alikuwa ni Mkuki aliyefanya hivyo, kumbe alishuhudia kila kitu tangu Leehom na Mei Lee wanafika pale hotelini, alikuwa juu kwenye chumba chao, hivyo alitazama sinema nzima kupitia dirishani na sasa ndiyo alishuka chini kuja kuharibu mchezo

    ************************





    Lakini huyu hakuwa Mkuki mtulivu yule unayemfahamu, alikuwa ni mkuki mwenye roho ya mbogo. Alikuja akiwa ni mwenye hasira na ghadhabu kweli kweli ya kuweza hata kuua mtu, hasira ambayo ilianzia ndani tumboni kwenye bandama na kupanda mpaka kooni—angeweza kufanya lolote kwa hali ile.

    Basi kwa hasira hizo hizo alisogea karibu na pikipiki la Leehom, akalisukuma kwa mguu wake na likaanguka chini hata kioo cha pembeni (Side Mirror) kikavunjika; wakati huo Leehom ndiyo alikuwa akiamka pale chini alipoangukia baada ya kusukumwa.

    Leehom akafanikiwa kunyanyuka kabisa, akasimama akijitazama mwili kwa mtindo wa kujikagua, kisha akajipangusa vumbi au chochote kile alichoona kinafaa kupanguswa kutoka mwilini mwake na baada ya hapo akaanza kumfuta taratibu Mkuki pale alipokuwa, na kwa jinsi alivyokuwa anakwenda Leehom, ilionekana waziwazi kwamba mpambano mkubwa ungeibuka kati yao.

    Mkuki naye akajiweka tayari kwa lolote, alifahamu kwamba kama mwanaume alistahili kupigana mpaka hatua ya mwisho ili kuthibitisha uanaume wake. Hakutakaa kuwa mnyonge, aliamini katika msemo wa mtaani usemao ‘Pesa huna, nguvu huna, hata mkwara?’

    Basi Leehom alizidi kumfuata Mkuki, lakini kabla hata hajamfikia, Mei Lee alichomoka pale alipokuwa na kwenda kusimama katikati yake yao akinyoosha mikono kama ishara ya kuwazuia. Leehom akawa muelewa, hakutaka kufanya kinyume na jinsi ambavyo Mei Lee alitaka na huenda alikubali kwa urahisi hivyo ili labda Mei Lee amuone kwamba ni mwanamume muelewa; Mkuki yeye bado alikuwa ni kama mbogo mwenye uwendawazimu, alifura kweli kweli huku akiropokwa maneno  ya ovyo ambayo yalimkera hata Mei Lee pia.

    “…usije ukafikiri mimi ni mjinga. Naweza nikakunyoosha hata kama upo kwenye ardhi ya mama yako.” Akabwata Mkuki.

    “Kuninyoosha!? Unaweza?  Unaweza nikuruhusu ufanye sasa hivi?” akauliza kwa dharau Leehom, tena polepole kana kwamba hawakuwa wakigombana.

    “Sishindwi. Sina ninachoogopa kutoka kwako. Sijali kuhusu pesa zako wala umaarufu wako.”

    “Unaigiza kijiamini sana, lakini kwa taarifa yako tu ni kwamba umewasha moto ambao hautazimika kwa namna yoyote ile.”

    “Kuzimika? Hata mimi najua kwamba hautazimika kwa sababu kabla ya wewe kuuzima nitakuwa nimeshakuzima.” Akazidisha jeuri Mkuki.

    Leehom akacheka kabla ya kujibu tena, “Hii vita unayoinzisha ni nyepesi sana, inatabarika mno, najua siwezi kushindwa kuwa mshindi ninapotupwa ulingo mmoja na nguruwe wa aina yako.”

    “Washindi hawaongeiongei, wanashinda.” Akasema Mkuki, kisha kabla hata ya Leehom hajatoa neno la kumjibu Mei Lee akaingilia kati; si kwa  kuzungumza, bali alimshika mkono Mkuki na kumuongoza kurudi hotelini—wakaondoka hivyo wakimuacha Leehom akiwatizama tu.

    ***************************

    Ndani hakukukalika; Mkuki alihitaji majibu yaliyonyooka juu ya kile alichoshuhudia, na ingawa binti alimjibu lakini kilichosemwa aliona ni kama porojo za kumlanghai tu.

    Aliongea maneno mengi sana mkuki juu ya lile tukio, hata mengine yalikuwa ni mbaya kuyasikia lakini tamati alikuwa mpole; aliamua kumsahamehe Mei Lee kwa sababu alikuwa akimfahamu uzuri, alijua kwamba hata kama alikuwa anafanya jambo mbaya ilikuwa ni kutokana na vishawishi, hivyo alimtaka kuwekeza nguvu nyingi kwenye mazoezi kwa ajili ya fainali ya shindano badala ya kupoteza muda mwingi akiwa karibu na Leehom.

    Lakini asubuhi ya siku ya tukio lile magazeti yote yaliandika habari za  ugomvi mkubwa kati ya Leehom na Mkuki ambao chanzo chake kilifahamika haraka kwamba walikuwa wakigombania mwananamke; yaani Mei Lee. Tena habari hiyo haikwenda kavu, bali na picha za tukio zilizopigwa kwa utaalamu wa hali ya juu huku picha ambayo ilitumika sana ikionyesha wakati ule Leehom aliposukumwa na Mkuki. Picha zote zilipigwa na mtu mmoja isipokuwa aliziuza kwa kila gazeti na alipata pesa nyingi sana kwa kuwa Leehom alikuwa ni mtu maarufu mno pale China. 

    Ile ikawa ni ‘skendo’ kubwa sana na huenda ilikuwa na madhara kwa watu wote watatu lakini hilo halikuwa rahisi kuonekana kwa mtu mwenye upeo wa kawaida. Watu wengi walidhani kwamba taarifa ile ililenga kumchafua Leehom kwa sababu tayari yeye alikuwa ni nembo ya Taifa la China.

    Hata hivyo ni kama ilikuwa kweli, habari zile ilimuumiza sana Leehom kwa sababu baada ya kusambaa huku na huko kuna baadhi ya makampuni aliyokuwa akifanya nayo kazi kama balozi yalimpiga chini mara moja kwa madai kwamba kwa kile alichokifanya kilikuwa ni hatari kwa taswira ya makampuni hayo. Hapo sasa ndipo Leehom akaketi chini, meza moja na watu wake wa kazi ili kuangalia jinsi ya kutafuta utatuzi wa haraka wa  sauala hilo kabla mambo hayajaoza kabisa.

    ***********************************

    Usiku wa deni hauchelewi kucha, siku ya fainali ya yale mashindano iliwadia kana kwamba ni kufumba na kufumbua tu. Mashabiki waliolipa viingilio vikubwa walijazana ukumbini huku wengi wakiwa ni wapenzi wa dhati wa Mei Lee na muziki wake; na hii ilikuwa ni wazi kwamba binti alikuwa anakwenda kutwaa ushindi utakaobadilisha maisha yake kuanzia siku hiyo.

    Mkuki alikuwepo pia ukumbini pamoja na adui yake Leehom; tena Leehom yeye alikuwepo hapo kama mgeni maalimu wa shindano ambaye ndiye atakayekuwa na jukumu la kumtangaza mshindi mara baada ya washiriki wote, akiwemo Mei Lee watakapotumia kete zao kwa kuimba kwa mara ya mwisho. Hata hivyo suala hilo la Leehom kumtangaza mshindi lilishapingwa na baadhi ya wataalamu wa mambo ya burudani wakidai kwamba litapunguza mvuto wa shindano kwa kuwa tayari Leehom alishaonekana kuwa na mtafaruku na baadhi ya mshiriki ambaye kwa namna moja ama nyingine anaonekana kuwa na dalili zote za kutawazwa mshindi. Lakini kila kitu kilishindikana kubadilishwa kwa sababu mgogoro wa Leehom na Mei Lee uliibua kipindi cha mwisho kuelekea fainali ya shindano hivyo mambo yaliachwa yaendelee kama yalivyopangwa.

    Basi hakukuwa na cha kupoteza muda, mshiriki mmoja baada ya mwingine kati ya wale watano waliosalia alipanda jukwaani na kujaribu kuwashawishi mashabiki kwa mara ya mwisho kwamba alikuwa na uwezo mkubwa zaidi na alistahili kushinda.

    Kila mshiriki alipewa fursa ya kuimba nyimbo tatu kwa siku hiyo, lakini ni kwa mtindo wa kuimba moja na kumpisha mshiriki mwingine hadi pale wote watakapotimiza hivyo vibao vitatu.

    Kila Mei Lee alipopanda jukwwani shagwe zilitawala ukumbini, watu walisimama na kufatisha kila alichokiimba kuashiria ni jinsi gani alikuwa akiwakosha. Masaa mawili baadae kila msanii akawa ameshaimba nyimbo mbili na sasa ikawa ni zamu ya kutumia kete yao ya mwisho—kuimba wimbo wa tatu.

    Wote wakaimba, na tamati ilikuwa ni zamu ya Mei Lee na alipanga kuimba wimbo aliouimba mara ya kwanza alipokuwa akitafuta nafasi ya kushiriki katika shindano hilo, wimbo alioutunga maalum kwa ajili ya Mkuki; wimbo wenye kubeba hisia nzito za mahaba alizonazo juu ya mwanaume huyo; wimbo uitwao RANGI YA HUBA.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mashairi yake yalimkuna kila mtu pale ukumbini lakini sanasana ni kwa jinsi ambavyo mwenyewe aliimba, aliyatamka  kwa ufundi maneno ya kwenye kila mstari wa shairi hilo kiasi  kwamba masikio ya wote yalipenda kile kitu bila kuchoka. Mioyo ya mashabiki pale ukumbini ilitetemeshwa, walisikia raha mno kumsikia Mei Lee, ni kama sauti yake ilivujiza asali na maziwa masikioni mwao. Walitamani shindano lisiishe, na pia walitamani liwe shindano la mshiriki mmoja ambaye ni Mei Lee ili awaimbie yeye muda wote na si vinginenvyo.

    Baada ya Mei Lee kumaliza kuimba hadhira ilitulizwa na maneno ya kuchombeza ya mshehereshaji wa onyesho lile, kisha Jaji Mkuu akapewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya majaji wenzake wawili na baada ya hapo mshehereshaji akamkaribisha mgeni maalum; Leehom kwa ajili ya kuja kumtangaza mshindi wa shindano.

    Huo ulikuwa ndio wasaa mahususi kwa ajili ya kuthibitisha umahiri wa Mei lee na jinsi ambavyo alifanikiwa kuziteka roho za mashabiki kwa sababu iko wazi kwamba atakayetangazwa kuwa mshindi pale atatafsiriwa kama mtu aliyekuwa bora kwa kuimba zaidi ya washiriki wote. Na ilikuwa ni Mei Lee kwa sababu mpka hatua ya mwisho, kabla ya fainali kura zilionesha kwamba anaongoza, isipokuwa inapofikia siku ya fainali kura huwa ni siri, haziwekwi wazi tena hadi pale anapotangazwa mshindi.



    **********************





    Basi Leehom akapanda jukwani kuungana na washiriki wote watano, majaji na mshehereshaji, huku mkononi akiwa na karatasi yenye jina la washindi watatu kati ya wale watano pamoja na kipaza sauti. Alikuwa amevalia nadhifu mno siku hiyo—suti matata iliyobuniwa na mbunifu wa mavazi maarufu nchini humo aitwae Xiaomi. Watu walimshangilia mara tu alipopanda jukwaani kwa sababu hata yeye alikiwu ni kipenzi cha wapenda muziki wa nchini China, tena walimpenda zaidi ya ambavyo wanampenda Mei Lee sasa hivi.



    “Habarini za jioni.” Akasalimu na baada ya kujibiwa akaendelea kwa ujumla, “Leo ni siku kubwa sana, siku kubwa kwa sisi kushuhudia ushindi wa wenzetu hawa walioshiriki shindano, lakini ni siku kubwa  kwao kwa shuhudia ushindi walioupigania miaka nenda rudi. Kama ningetaka nisitumie maneno ningesema leo ni siku ya fainali, na maana ya fainali ni kumjua mshindi.

    Kimsingi wote watano ni washindi, lakini kwa bahati ni kwamba karatasi niliyoishika hapa mkononi ina nafasi ya majina matatu tu. Kwanini nasema hivi? Nasema hivi kumaanisha kwamba hata kama wewe mshiriki mmoja hutatajwa humu bado una nafasi ya kutimiza ndoto zako kwa sababu hata mimi sikupitia mashindano ya hivi, lakini leo nina nafasi niliyokuwa nikiiota kuwa nayo.

    Kama nilivyokwishasema, nina majina ya watu watatu hapa mkononi  ambao ni mshindi wa kwanza, wa pili na watatu, na nitamtaja mshindi wa tatu, kisha wa pili na wa kwanza. Lakini kabla sijaanza kutaja nataka nikumbushe kitu kimoja kwamba; WASHINDI HAWAONGEI, WANASHIDA.” Akazungumza Leehom na watu wakashangilia kana kwamba walipenda sana kile alichokizungumza.

    Basi Leehom akaanza kutaja majina, akaanza na mshindi wa tatu kama alivyofafanua mwanzo na hapo akaja mvulana aliyeshika nafasi hiyo. Watu wakamshangilia kwa kiasi chake wakati anatoka alipokuwa amesimama na washiriki wenzake pale jukwaani na kusogea karibu na majaji kwenda kupokea anachostahili—alipiga picha kadhaa na Leehom, na majaji wote ambao pia walikuwa pale jukwaani kisha zawadi atakayopata ikatangazwa hadharani kisha akasimama palepale jukwaani, karibu na majaji.

    Kisha wapili pia akatajwa, mashabiki wakaangua shangwe kubwa ingawa hazikufikia kiasi  cha ambavyo huwa wanamshangilia Mei Lee japo zilizidi shangwe alizopata mshindi wa tatu. Mshiriki huyu naye alikuwa ni mvulana, akasogea kwa majaji na kufanyiwa kama ilivyokuwa kwa mshindi wa tatu—yaani kupiga picha kisha mwishowe zawadi yake kutangazwa hadharani kisha akasimama karibu na majaji pia.

    Sasa homa ikawavaa mashabiki ulipofika muda wa kumfahamu mshindi wa kwanza wa shidano hilo; kwa sababu nafasi ilibaki moja wakati bado Mei Lee na mtu aliyekuwana akimfuata kwa kura walikuwa hawajatajwa. Hii ni sawa na kusema kwamba, mmoja kati yao ni lazima atatoka kapa.

    Leehom akapewa ruhusa ya kuendelea.

    “Mshindi wa shindano letu kwa mwaka huu ni....” akazungumza Leehom, kisha akapiga kimya akiwatazama mashabiki kana kwamba alikuwa akiwauliza ‘mnanfahamu?’

    Akaendelea.

    “Mshindi ni…. Liu Kang.” Akasema kwa sauti kubwa na hapo ziliibuka shangwe za watu waliokuwa wakimkubali Liu Kang huku mashabiki wengine hasa wanaompenda Mei Lee wakishindwa kuamini kile kilichotokea—inakuwaje mshiriki ambaye alikuwa akionekana kukubalika zaidi amekosa hata nafasi ya tatu.

    Zogo kubwa lilizuka papo hapo bila kuchelewa, mashabiki wa Mei Lee walianzsha fujo wakilaani vikali na kupinga matokeo yale kwa madai kwamba yalichakachuliwa. Fujo zikapamba moto kiasi kwamba sasa watu walianza kupigana kwa kurushiana chupa na kadhalikaka. Ilikuwa ni mshikeshike kweli kweli ambao pengine hakuna hata aliyetarajia, lakini kwa sababu waliuanzisha basi shetani naye akakamatia katikati yao.

    Ilibidi askari wapewe taarifa wakati huo tayari walinzi wa kawaida walianza kutumia nguvu kutuliza zile ghasia na pia kuwalinda watu waliokuwa pale jukwani ili wasidhurike na walifanikiwa katika hilo kwa kuwatorosha majaji wote, washindi wa kwanza hadi wa tatu na Leehom pia ambaye kimsingi ndiye alikuwa amepaniwa zaidi na mashabiki wa Mei Lee .

    Mkuki hakujihusisha na gomvi lolote kule alipokuwa, alitulia akiugulia maumivu yaliyosababishwa na kile kilichotokea. Roho ilimuuma sana kwa sababu alifahamu fika kwamba yale hayakuwa matokeo halisi kwa maana ya kwamba lazima kuna mchezo mchafu utakuwa umefanyika na bila shaka mpango huo uliratibiwa na Leehom kama sehemu ya vita aliyoitangaza mara baada ya kuibuka kwa mgogoro wao. Alipoteza matumaini hata alijikuta akijuta kuwa mjinga kiasi cha kukubali kuacha kazi yake kwenye mgahawa kule Hong kong ili amlete Mei lee kuja kushiriki shindano la kishenzi namna hii, shindano lisilozingatia misingi ya haki kabisa—na hapa sasa ndiyo alizidi kujiona ni mtu wa ‘fungu la kukosa’.

    Mei Lee yeye ndiyo alishindwa hata kujizuia, alilia sana kwa sababu alikuwa na imani sawasawa na Mkuki. Aliamini kwamba ule ushindi ulikuwa wake, na si wa Liu Kang kama ilivyotangazwa, isipokuwa kile kilichotokea ilikuwa ni dhuluma iliyofanywa na Leehom akishirikiana na waratibu wa shindano hilo. Basi akiwa bado palepale jukwaani ghafla alianza kuhisi kizunguzungu; aliona ni kama dunia inarukaruka hivi, inakwenda mrama. Taratibu giza likaanza kuivaa nuru ya macho yake, miguu ikapoteza nguvu na uwezo wa kusimama na punde akaanguka chini kama mzigo, akazimika.



    **************************





    Fahamu zilimrejea Mei Lee saa tatu baadae na alipozinduka tu alijikuta amelazwa kitandani ndani ya chumba cha hospitali. Pembeni yake alikuwepo Leehom, ambaye mara tu alipogundua kuwa Mei Lee amerejewa na fahamu alimsogelea.



    “Vipi? Unajisikiaje?”

    “Mkuki. Mkuki yuko wapi?” Akauliza Mei Lee.

    “Tulia kwanza, kila kiti kuhusu Mkuki utafahamu baadae.”

    “Hapana. Sitaki. Nataka kumuona Mkuki sasa hivi.”

    “Tulia kwanza.”

    “Sitaki...” akasema Mei Lee huku akionesha kwa vitendo kwamba kweli alikuwa hataki kutulia; akataka kuinuka pale kitandani lakini Leehom alimzuia kabla hajafanya hivyo.

    “Ngoja. Tulia. Mkuki huyupo.” Akasema Leehom huku akimtuliza Mei Lee kwa kumzuia asiinuke.

    “Yuko wapi?”

    “Amekamatwa.”

    “Amekamatwa? Kwa Kosa gani"? Akahoji kwa mshangao Mei Lee.

    Leehom akatulia kidogo kabla ya kijibu. “Kumbe alikuwa akiishi hapa bila kibali, na si unajua kuwa yeye si mchina wala Mthaiwan.” Akasema na hapo ndipo alizidi kumchanganya zaidi Mei Lee na nusura apoteze fahamu kwa mara nyingine.

    Alichofikiria kwa haraka ni kwamba mara baada ya taarifa ile asingeweza tena kumuona Mkuki kwa sababu kwa kosa ambalo Leehom alimueleza ni wazi kuwa uhamiaji wangemrudisha Mkuki nchini kwao tu.

    Kile alichokisema Leehom kilikuwa ni kweli tupu, lakini hata hivyo kila kitu kilikuwa ni mpango wake yeye mwenyewe kama sehemu ya kuhakikisha anashinda ile vita aliyoitangaza dhidi ya Mkuki. Aligundua kuwa si rahisi kwa Mkuki kuwa na kibali na hii kutokana na historia ya Mkuki aliyoipata kutoka kwa Mei Lee mwenyewe; alimsimulia kipindi kile walichokuwa na ukaribu. Leehom akatumia upungufu huo, akatoa taarifa uhamiaji na wao wakaishuhulikia mapema taarifa hiyo kwahiyo walipomkamata Mkuki walimchukua na kumfanyia mahojiano ambapo alieleza kila kitu, kwamba yeye alikuwa ni Mtanzania na hata alifikaje China. Hii ilikuwa ni sawa na kusema kwamba baada ya taarifa hiyo uhamiaji walifanya mawasiliano na ubalozi wa Tanzania nchini China ambao walifanya mpango wa kumrejesha nyumbani na hilo lilifanikiwa-- Mkuki alirejeshwa kwao.

    “Nadhani watakuwa wameshamrejesha kwao” alieleza Leehom kumwambia Mei Lee ambaye kwa muda huo alikuwa ameshikwa na uchungu usiosemekana, uchungu ambao hakuna msamiati kutoka kwenye lugha yoyote ile yenye kuweza kuelezea. Aliona dunia na kila kilichomo ndani yake vimekosa kumjali, alihisi kuonewa na alitabiri jinsi ambavyo ataishi maisha ya masumbuko bila ya uwepo wa karibu wa Mkuki; mwanamume ambaye kwa mtazamo wake Mei Lee alikuwa ni mwenye vigezo vyote vya kuitwa SHUJAA. Mwanaume ambaye alimfanya aishi upande wa raha wa dunia, akampa kila kitu ilihali hakuwa na kitu, mwanaume aliyemfundisha mapenzi, aliyemfundisha kupenda na kupendwa, mwanaume alimuonyesha RANGI YA HUBA.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alifikiria mengi akiwa pale lakini tamati alinyanyua kinywa chake na kuzungumza sentensi moja yenye maneno mawili tu ambayo ilikuwa ni swali kwa Leehom.

    “Kwahiyo umeshinda?” Aliuliza hivyo Mei Lee.

    “Kushinda nini?” Leehom akahoji. Hakuwa amelielewa swali kwa sababu lilikuja tofauti kulinganisha na mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.

    “Vita. Vita yako dhidi ya Mkuki.”

    “Hapana. Sikuwa na vita naye. Nilishamsamehe.”

    “Sawa. Naomba mniruhusu kutoka hapa.”

    “Kutoka uende wapi? Afya yako bado haijatengemaa Mei Lee.”

    “Niko vizuri.”

    “Bado.”

    “Lakini ni mimi. Mimi ndiye nahusika, ndiye nafahamu kuhusu Afya yangu, unasemaje siko vizuri wakati mwenyewe najiona niko sawa? Nataka kuondoka.” Akafoka Mei Lee lakini Leehom hakutaka kuonekana mwepesi, hakutaka kukubali kirahisi kila kilichosemwa na msichana huyo.

    “Kwenda wapi?”

    “Mbali. Mbali na wewe shetani, mshindi wa vita kwa njia za haramu.” Akang'aka kwa maneno makali namna hiyo ambayo yalimfanya Leehom  apoe akimtazama Mei Lee kwa hasira za ndani kwa ndani.

    “Lakini hupaswi kuzungumza hayo Mei Lee. Unatakiwa ufahamu hisia zangu. Unielewe. Nakupenda.” Akaropoka Leehom lakini Mei Lee aliishia kumtazama tu, wakatazamana kwa zaidi ya sekunde kumi kisha msichana akafungua kinywa chake kuzungumza sentensi fupi yenye maneno matatu tu.

    “Nina mimba ya Mkuki.” alizungumza Mei Lee tena hapa akiwa na uso wenye kumaanisha kile alichokizungumza. Taarifa ile ilimuacha kinywa wazi Leehom ambaye alifanya hila zote ili kumpata Mei Lee. Alikuwa akimpenda sana lakini je ni kweli angeweza kuendelea kumpenda hata kama mwanamke huyo atakuwa na ujauzito wa Mkuki kama alivyoeleza.

    Akandelea kuzungumza Mei Lee.

    “Najua nia yako Leehom. Nafahamu kila kitu unachowaza kuhusu mimi. Najua umempoteza Mkuki ili nihamie katika dunia yako, lakini ukweli haitawezekana. Umemuondosha mtu mwenye moyo wangu, kwahiyo hata nikisema nikupende nitatumia akili. Nitakupenda kwa ujanja ujanja. Ahadi ulizokuwa ukinipa za kunisaidia kutimiza ndoto zangu si ngeni, yote hayo Mkuki alishayafanya, kwahiyo nguvu unazotumia ni kazi bure. Ni sawa na kumwaga sukari katikati ya bahari ili maji chumvi yafanane ladha na asali.”

    Leehom aliganda kama sanamu, maneno ya Mei Lee yalimchoma mno kwa sababu alikuwa na matarajio makubwa juu ya msichana huyo na ndiyo maana alifanya figisu zote za kuhakikisha anampoteza Mkuki.

    Basi baada ya pale Mei Lee alilazimisha kuondoka na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Hakurejea Thaiwan, alibaki pale pale China na aliendesha maisha yake kwa kuimba nyimbo mtaani ambapo wapita njia walimtunza sarafu ambazo alizichannganya na kupata pesa ya kutosha kumsukuma kimaisha. Lakini alifanya hivyo kwa wiki moja tu, baadae alipata mtu wa kumshika mkono, akamsaidia kurekodi nyimbo nyingi na alifanikiwa sana kimuziki ndani ya muda mfupi tu kwa sababu tayari alikuwa na kundi kubwa la mashabiki aliowavuna katika lile shindano la kusaka vipaji lilikuja kuharibiwa na hila za Leehom.

    Mei Lee sasa akawa ni miongoni mwa wasanii wakubwa nchini China, wasanii wa kutumainiwa na taratibu akaanza kufika ‘level’ za Leehom. Alimfikia kabisa na akawa ni mpinzani wake mkubwa mno na hiyo ikaandika historia kubwa katika tasnia ya muziki nchini China.

    Kuhusu mimba ya Mkuki ilikuwa ni kweli kabisa na Mei Lee aligundua hilo muda mrefu isipokuwa aliliweka akiba, alipanga kumwambia Mkuki siku ya fainali, baada ya yeye kutangazwa mshindi kwa sababu alikuwa na imani kubwa katika hilo.

    Basi aliulea ujauzito huo lakini kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu alijua kuwa mtoto wake atazaliwa, na hatokuja kumjua baba yake kwa sababu hata yeye hakuwa akijua alipo kwa kuwa kwa kipindi chote walichoishi na Mkuki hakuwai kufahamu mpenzi wake anatiokea wapi; si unakumbuka Mkuki alikuwa anaficha kila kitu kwa madai kwamba hana kumbukumbu yoyote ya anapotokea.

    Kuna wakati Mei Lee alijaribu kufuatilia lakini alishindwa kabisa kupata jibu la uhakika, na hapo ndipo alipokata tamaa kabisa na kuamua kumshukuru Mungu tu kwa kila kilichotokea huku akijitahidi kumuombea sana mwanaume huyo huko alipo.





    ************************************

    “Nilirudishwa nyumbani na kuendelea na maisha ya kifukara yaleyale niliyoyakimbia, hakuna kitu kilichobadilika, sanasana mambo yalizidi kuwa magumu, kwa sababu kwanza nilikuwa kama mgeni, sijui fursa ziko wapi  na pia nilikuwa sina maisha ya amani kabisa kabisa. Watu wananidhihaki kwamba nilizamia lakini nimerudi sina kitu, lakini ndo ukweli, kwahiyo sina sababu ya kuwachukia, labda  nijichukie mimi na maamuzi yangu niliyoyafanya.” Anaeleza mzee Mkuki Salum Goigoi. Hapa akiwa katika kituo cha redio akifanyiwa mahojiano ya moja kwa moja juu ya ile safari ya maisha aliyopitia-- hii ni baada ya miaka takribani 20 tangu kutokea kwa tukio lile.

    “Bado unaikumbuka sura ya Mei Lee? Yaani unaweza kutuambia alikuwa anaonekanaje?” mtangazaji anamuuliza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana, sio rahisi kukumbuka kiasi cha kuweza kumuelezea alikuwaje; lakini kwa kifupi alikuwa ni mzuri, mrembo. Isipokuwa kitu kimoja kutoka kwake ndo siwezi kukisahau.”

    “Kitu gani?”

    “Sauti yake. Sauti ya Mei Lee bado ipo masikioni mwangu. Nikilala, nikiamka, nikitembea, popote huwa naisikia. Mungu alinipa tuzo kumpata yule mwanamke.” Anashindwa kuendelea kuzungumza mzee Mkuki, anahisi uchungu sana, na kooni ni kama amemeza chuma cha moto kinachoteremka taratibu kwenda tumboni.  Anaanza kulia kwa kugugumia.

    “Okey.  Msikilizaji mzee Mkuki anashindwa kuendelea kuzungumza. Naomba tupate mapumziko mafupi kutoka kwa mdhamini, ili na yeye apate muda wa kutulia, tutakoporejea ataendelea kutueleza mengi zaidi kuhusu hii safari ya maisha aliyopitia. Tutarejea.”

    ******************************

    MWISHO WA MSIMU WA KWANZA


0 comments:

Post a Comment

Blog